Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

ROMAN ABRAMOVICH: UTAJIRI WA DAMU, RISASI NA UMAFIA - 2

 





    Simulizi : Roman Abramovich: Utajiri Wa Damu, Risasi Na Umafia

    Sehemu Ya Pili (2)











    Hapa nieleze kidogo,







    Sehemu kubwa ya Urusi (kwa maana ya ardhi) ni jimbo kubwa linaloitwa Siberia. Siberia inajulikana kutokana na hali yake ya hewa ya baridi kali kupitiliza pamoja na barafu kwa muda mwingi wa mwaka. Lakini pia Siberia ina kitu kingine adhimu zaidi duniani… “dhahabu nyeusi”… mafuta. Jimbo la Siberia lina utajiri mkubwa mno wa mafuta na sehemu kubwa ya utajiri huu wa mafuta unamilikiwa na kampuni yenye kuitwa Sibneft ambayo wanamiliki eneo la visima vya mafuta lenye eneo kubwa zaidi ambalo linaweza kulingana kabisa na ardhi yote ya nchi ya Wales kama tukilinganisha kwa ukubwa wa ardhi.







    Hapa ndiko hasa ambako Abramovich alikuwa amepalenga.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Baada ya uchaguzi kuisha na serikali kuanza kufanyakazi, Abramovich akamfuata Rais Boris Yeltsin na kumkumbusha kwamba wakati wa ‘kuwakumbuka’ ma-oligarch waliowasaidia kwenye uchaguzi umewadia. Kama ambavyo yeye Abramovich hakutaka kupewa cheo chochote kile serikalini ndivyo vivyo hivyo pia alipendekeza kwamba ma-oligarch wengine ‘wakumbukwe’ kwa namna nyingine badala ya kufikiria tu kuwapa vyeo vya kiserikali.







    Ukawekwa utaratibu wa kubinafsisha makampuni mengine ya umma ambayo bado yalikuwa chini ya serikali. Makampuni yakabinafsishwa kwa ma-oligarch. Abaramovich hakuzuzuka na kutaka kudandia hisa kwenye kampuni nyingine hizi, kichwani alikuwa na lengo moja tu… target moja tu ambayo alitaka kuifikia.







    Visima vya mafuta ni rasilimali adhimu kwa nchi yeyote ile. Kwa hiyo japokuwa Russia ilikuwa kwenye uwendawazimu wa ubinafsishaji kiholela lakini ilipofika kwenye visima vya mafuta ilikuwa ni suala lilifanyika kwa tahadhari kubwa zaidi. Naam, viko visima vya mafuta ambavyo vilibinafsishwa lakini visima vya mafuta vya kumilikiwa na kumpuni ya Sibneft viliwekewa utaratibu maalumu na ikulu.



    Uzuri au ubaya ni kwamba katika kipindi hiki ulikuwa ukiongelea ikulu ya Russia unaongelea ‘Utatu Mtakatifu’, Abramovich, Tatyana na Yumachev.







    Watatu hawa wakaandaa utaratibu maalumu wa namna ya kuibinafsisha kampuni ya Sibneft. Nisisitize tena, Sibneft wanamiliki ‘oil fields’ kubwa kuzidi ardhi yote ya nchi kama Wales. Na katika miaka hii kampuni ya Sibneft ilikuwa na thamani ya zaidi ya dola Bilioni 50 za kimarekani (zaidi ya trilioni 120 za Kitanzania).







    Utaratibu ukaandaliwa. Roman Abramovich akahakikisha anaweka vigezo na masharti kadhaa ya mtego mtego ili kukwamisha wengine. Hatimaye mnada wa kuiza Sibneft ukafanyika lakini ajabu ni kwamba katika mnada alijitokeza ‘bidder’ mmoja tu. Ni nani huyu? Nitaeleza…



    Bidder huyu alitoa ofa ya kuinunua Sibneft kwa kiasi cha dola milioni 150.!! N



    Nisisitize na kukumbusha tena, Sibneft walikuwa na ‘oil fields’ ukubwa zaidi ya nchi ya wales na ‘valuation’ yake ilikuwa ni zaidi ya dola bilioni 50. Auction ikafanyika… Sibneft ikauzwa kwa mwekezaji huyu.



    Naamini tayari tunaweza kubashiri kwamba ‘bidder’ alikuwa ni Roman Abramovich. Lakini swali ni kwa namna gani Abramovich anaweza kuwa na dola milioni 150 kwa kipindi kile kuinunua Sibneft??







    Nilieleza awali kuhusu kikao cha Abramovich na Berezovsky wiki kadhaa baada ya uchaguzi mkuu. Katika kikao kile Abramovich alimpa ‘ofa’ mentor wake huyo kwamba kwa ushawishi alionao sasa kwa Rais Yeltsin anaweza kutengeneza mazingira wao wawili wauziwe visima vyote vya mafuta na mali za kampuni ya Sibneft lakini akamweleza kuwa anahitaji kitu kimoja tu kutoka kwake… fedha. Makubaliano yao ni kwamba Berezovsky atatoa rasilimali fedha na Abramovich atahakikisha anatengeneza mazingira Ikulu na kuhakikisha kwamba kampuni hiyo inatua kwenye mikono yao.







    Ndio kusema kwamba Sibneft kampuni yenye kumiliki visima vya mafuta kwenye eneo kubwa sawa na chi ya Wales, kampuni ambayo ‘valuation’ yake inanesa kwenye dola bilioni 50 ikauzwa kwa Abramovich na Berezovsky kwa dola milioni 150 tu… hela ya ugoro kama asemavyo mzee Rugelamarila. Yaani kitendo cha wao kukabidhiwa tu kampuni siku hiyo hiyo uwekezaji wao uliwalipa faida karibia 400%. Miaka miwili baadae uwekazaji wao huu ulikuja kuwalipa karibia mara 1000 ya fedha waliyonunulia kampuni?

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Lakini kama ambavyo nilieleza awali kwamba Abramovich alikuwa mahiri wa mifumo ya kibepari inavyofanya kazi kuwazidi watu wengi nchini Russia kipindi kile na hata serikali yenyewe ambayo bado ilikuwa na tongotongo za ujamaa machoni. Kwa hiyo hata kwenye ununuzi wao wa Sibneft hawakununua tu kichwa kichwa kwa kuweka majina yao kwenye makaratasi ya umiliki bali aliweka mfumo complex wa umiliki kuhakikisha kwamba ni ngumu kufahamu hasa nani anamiliki hisa kiasi gani kwenye kampuni,na nani anapokea dividends kiasi gani na bila kusahahu kuhakikisha wanalipa kodi ndogo iwezekanavyo kwenye mapato.







    Nitoe mfano kidogo kabla ya kwenda mbali zaidi… sijui ni wangapi wanakumbuka mwaka 2013 mwishoni ndugu Rostam Aziz alipouza nusu ya hisa zake za kampuni ya Vodacom kwa karibia bilioni 400 za Kitanzania. Jambo la kufurahisha ni kwamba tulipata kodi kiduchu mno, yani kiduchu haswa kutoka kwenye uuzaji huo wa hisa tofauti na ambavyo tulitegemea. Tukabaki tumeduwaa tu wengine wakimnyooshea kidole Rostam kuwa pengine ‘amecheza rafu’ na watu wa system. Yes, hatukupata kodi lakini Rostam hakuvunja sheria na wala hakucheza rafu kwenye ile deal. Alitumia umahiri tu wa kibiashara… hisa zake alikuwa anazihold kupitia ‘private Trust’ ambayo imesajiliwa nchini Mauritus kama nakumbuka vyema. Tunafahamu namna ambavyo sheria za kodi za nchi ya Mauritus zilivyo ‘loose’. Kutoka hapo mtoto wa mjini Rostam akacheza na loopholes za sheria za kimatafa na hata za nchi yetu wenyewe na deal ikafanyika huku vibunda vikibaki mfukoni mwake na vingine kwenda serikali ya Mauritus na kiduchu tukapata sie akina yakhe. Maarifa… maarifa… maarifa.







    Hii ndio sababu huwa naamini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa wanapaswa kufanya mageuzi ya kusudi kabisa kuhakikisha wanaenda na kasi ya ulimwengu. Kwa mfano maafisa kwenye ‘directorate’ ya Collection wengi ni watu wazima. Mindset zao bado zimejiseti kana kwamba tunakabiliana na adui aliyebeba AK47. Zama zimebadilika mno, adui sasa habebi guruneti… adui sasa hivi anaweza kuwa amejificha tu mahala fulani chumbani na laptop mkononi kama silaha yake na akaitikisa nchi. Adui sasa hivi hawazi tena kupindua nchi bali anafanya hila kuhujumu mfumo wa uchumi… adui sasa hivi hataki madaraka bali anataka kumiliki njia na nyenzo za uchumi wa nchi. Tuko kwenye zama ambazo maafisa wetu wa Idara ya usalama wa Taifa wanapaswa kujua namna ya kunyumbulika na kizazi hiki cha sasa na changamoto zake.



    Idara yetu kwa sehemu kubwa inafanya kazi kwa kutegemea ‘Humint’ kama waitavyo wenyewe na ‘open source intelligence’ kitu ambacho sio kibaya sana kutokana na uhalisia wa nchi yetu na uwezo wetu kama nchi na rasilimali tulizonazo. Kwa hiyo ni muhimu sana sana, kuwa na maafisa ambao wanaweza kunyumbuka na uhalisia wa nyakati tulizonazo pamoja na kuwa na mindset sahihi. Unapokuwa na maafisa wenye mindset ya enzi zile za kupambana na adui amebeba AK47 akitaka kushika dola ni ngumu kwake kung’amua vipaumbele anavyotakiwa kujishughulisha navyo na mwisho wake tutahoji juu ya ubora wa intelligence tunayoipata na mwisho wa siku itaathiri hata ufanyaji kazi wa watu wa ‘directorate’ inayosimamia processing. Kinachokuja kutokea ni kwamba pale kitengoni, idara inayohusika na Tasking inajikuta ina-allocate resources nyingi (kwa maana ya maafisa, muda, wataalamu mahususi ) kwenye masuala ambayo pengine hayakupaswa kuwa vipaumbele. Lakini mzizi unaanzia wapi? Idara inayohusika na Collection… tupunguze maafisa watu wazima au kwa usahihi zaidi niseme tuhakikishe tuna maafisa ambao wanaendana na kizazi cha sasa na mnyumbuliko wake… sioni faida au ufanisi unaopatikana kwa kuweka watu wazima wengi kwenye idara hii. Sio kwamba wasiwepo, la hasha… mtu mzima dawa bhana… lakini tupunguze. Lazima watu walioko kwenye kitengo mahususi kwa ajili ya idara hiyo waweze kunyumbulika na zama tulizonazo… nature ya adui imebadilika mno… na sisi tunapaswa kujiboresha.







    Kuna mtu atasema “…wewe The Bold unajifanya unajua kuliko Usalama wenyewe…?” tabia na swali kama hili ndio kwa umombo tunasema kuwa ni “Obnoxious”.



    Hivi EPA, Richmond, Escrow n.k. hizi ‘abracadabra’ zilivyotokea tulikuwa wapi? Hatukujua kabla ya kutokea? Tulijua. Tulikuwa na nia ya kuzuia. Yes tulikuwa na nia… kwa nini hatukufanikiwa?? Ndio maana tunashauri, kwenye hili suala la Collection ya intelijensia hebu tufanye mageuzi makini pale… nature ya adui imebadilika lazima tujue namna ya kunyumbulika na zama hizi.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Tuache hayo, nahisi naanzisha mada ndani ya mada…







    Lakini nimetoa mfano huu ili kuelewa namna ambavyo Abramovich aliweza kucheza na nyakati… wananchi, serikali na hata Idara zake bado walikuwa na ‘hangover’ ya ujamaa wakati ambao Abramovich alikuwa tayari ana umahiri wa namna ubepari unafanyakazi.



    Nimeeleza kwamba ili kuhakikisha yeye Abramovich na mentor wake Berezovsky wanaficha kiwango chao cha umiliki wa Sibneft, lakini pia kuhakikisha wanalipa kodi kiduchu iwezekanavyo na ‘kucheza’ za mfumo wa mgawanyo wa dividends (kiasi kidogo kilikuwa kinapaswa kwenda serikalini) Abramovich na mwenzake hawakuweka majina yao moja kwa moja kwenye nyaraka za umiliki. Je, nyaraka zilionyesha nani wamiliki wa Sinbeft.







    Kipindi hicho ilikuwa ukichimba kwenye nyaraka za ulipaji wa dividends wa Sibneft unakutana na majina matano tu… CarbonRow ltd, Craven Investments, Gemini Co., MarteChelo Plc na White Pearl ltd. Makampuni manne kati ya haya matano yalikuwa yamesajiliwa nje ya Russia nchini Cyprus, moja ya nchi inayojulikana ulimwenguni kwa kuwa na sheria loose mno za masuala ya kodi na benki. Swali ni akina nani hasa wanamiliki makampuni haya? Tuchukue kwa mfano CarbonRow ukiitazama kwenye nyaraka za kumbukumbu inaonyesha kwamba CarbonRow inamilikiwa na ‘private trust’ inayoitwa MERITSERVUS (TRUSTEES) LIMITED. Nani anamiliki Meritservus Ltd? Dimitris Yunidis…ni nani huyu? Ukichimba ndani zaidi ni kwamba Dimitris ni Accountant ammbaye anamiliki kampuni inaofanya ‘flagging’ ya ‘shell companies’. Kwa kifupi tu ni kwamba kadiri unavyochimba ndio unazidi kuchanganyikiwa na huwezi kuliona jina la Abramovich au Berezovsky na hata ukifanikiwa kuliona huwezi kuona kiwango cha dividends anacholipwa yeye binafsi au kiwango cha umiliki wake wa Sibneft.







    Lakini inakadiriwa kwamba Abramovich alikuwa anamiliki 51% ya Sibneft na asilimia zilizobaki walimiliki Berezovsky na serikali ya Russia. Kisheria kwa sababu yeye ndiye alikuwa anamiliki hisa nyingi zaidi, kwa maneno mengine yeye ndiye alikuwa mwenye kauli ya mwisho ndani ya Sibneft , na kwa maneno mengine Sibneft ilikuwa ni kampuni yake.







    Ndani ya mwaka mmoja tu baada ya yeye na Berezovsky kununua Sibneft, Roman Abramovich, kijana yatima aliyekulia kwenye umasikini wa kutupwa ambaye miaka mitatu tu nyuma alikuwa anauza wanasesele na matairi chakavu, mara moja alipanda chati na kufikia status ya ubilionea ambapo kwa kipindi kile utajiri wake ulikuwa unafikia dola 3.4 bilioni za kimarekani (kama trilioni 7 za kitanzania) na hii ikamfanya kuwa oligarch kijana zaidi kipindi hicho nchini Russia akiwa na miaka 31 tu.







    Lakini wanasema penye riziki hapakosi fitina… Naam, kitendo hiki cha Abramovich kutumia ushawishi alionao Ikulu kujilimbikizia utajiri wa kutupwa kiliwaudhi baadhi ya watu wa ‘system’. Kuna watu waliumia pia mtoto mdogo wa miaka 31 hata harufu ya maziwa haijamuisha ati leo anakuwa oligarch. Ikaanza minong’ono na vuguvugu la chini kwa chini kuwapiga vita Abramovich na Berezovsky.



    Vuguvugu hili likaenda mbali zaidi ambapo mwendesha mashtaka mkuu wa serikali kipindi hicho Bw. Yuri Skuratov alifanya mkutano na wanahabari na kusema kwamba anakusanya ushahidi ili afungue mashtaka dhidi ya baadhi ya ma-oligarch. Japo hakuwataja majina lakini kila mtu alijua anamlenga nani.







    Lakini Abramovich alikuwa mboni ya Rais Yeltsin. Rais akamuita Mwendesha Mashtaka mkuu wa serikali na kumtaka aachane na jambo hilo… Yuri Skuratov akakataa.



    Yeltsin akajaribu kumfukuza kazi, lakini bunge likapinga uamuzi huo wa Rais na kumrejesha kazini Bw. Yuri Skuratov. Wabunge walikuwa na vihoro… roho ziliwauma kijana mdogo kama Abramovich kuwa na ushawishi mkubwa hivyo kwenye nchi ambayo miaka si mingi ilikuwa ndiyo ‘superpower’ ya ulimwengu.







    Yuri Skuratov aliporejeshwa kazini na bunge kiburi kikamjaa zaidi… akaitisha mkutano mwingine na wanahabari na kuwaeleza kuwa ana ushahidi wa kutosha dhidi ya Roman Abramovich na Berezovsky na anakusudia kuwafungulia mashtaka ya kuhujumu uchumi. Watu wa system walifurahi kweli kweli wakijua huo ndio mwisho wa Abramovich… kama wangelijua kipindi kile Abramovich ni mtu wa namna gani wasingelithubutu kumtikisa. Walikuwa wanapima kina cha bahari kwa goti la mguu…







    Mara ya mwisho nilieleza kuhusu mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Bw. Yuri Skuratov akijitapa kuwa ana ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka oligarch Roman Abramovich na ameweka nia kumburuza mahakamani siku si nyingi.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Kuna suala moja la msingi sana… katika nchi za Ulaya mashariki pamoja na nchi za ulimwengu wa tatu, ukiona mtu amechuma utajiri mkubwa wa kutisha basi ufahamu kuwa si mtu wa ‘mchezo mchezo’. Kwa namna ambavyo serikali zetu na biashara zetu zinaendeshwa katika nchi za ulimwengu wa tatu namna pekee unaweza kuushinda ‘uhuni’ ni kwa kuwa ‘muhuni’ wewe mwenyewe pia. Mambo kwenye nchi hizi hayaendeshwi kwa kanuni za ustaarabu kama kwenye ulimwengu wa kwanza… kwa hiyo ni eidha ujifunze kula nyama za watu au usubiri wewe ufanywe kitoweo.







    Ndio maana utaona kuna mjasiriamali maarufu na mwenye mafanikio makubwa sana hapa nchini, tumuhifadhi jina maana ni marehemu kwa sasa amefariki kama miezi mitatu iliyopita… alikuwa yuko vizuri haswa na kitengo chake binafsi cha ulinzi na ‘intelijensia’. Kuna watu watashangaa, ati yule mzee mwenye media house kubwa nchini ana kitengo binafsi cha intelijensia? Naam, na kiko vizuri haswa… well, si kitengo kikubwa haswa kufananisha na jamaa zetu wa Oysterbay au makumbusho, bali ni kitengo cha ulinzi haswa lakini kiko very well equipped kufanya ushushushu wa kibiashara na hata mwenendo wa nchi na viongozi wake.



    Na ndio maana pia Askofu maarufu sana hapa nchini ambaye hakauki kutoa matamko yenye utata unaweza kujiuliza anawezaje ‘ku-survive’ na hata muda mwingine vyombo vya usalama kupigwa chenga… jawabu ni hilo hilo, ana kitengo maridhawa mno cha ulinzi na usalama ambao pia wako vyema mno kwenye kufanya ushushushu. Tena huyu askofu nimeshuhudia kwa macho yangu na naweza kusema kabisa kwamba ni kitengo chake cha usalama kiko mbali zaidi kushinda hata wafanyabiashara wengi hapa nchi… kiko very sophisticated.







    Kwa nini nasema haya? Ni kwa sababu sisi wafanyabiashara wetu wanayafanya haya leo hii, Roman Abramovich alikuwa ameshaanza kukifanya kitu hiki tangu miaka ya mwanzoni mwa tisini na alikuwa anakifanya kwa ufanisi mkubwa haswa.



    Ndani ya kampuni ya Sibneft alikuwa ameunda kitengo maalumu cha ulinzi na usalama. Kazi ya kitengo hiki, Mosi, kilihusika na ulinzi wa kawaida wa mali za kampuni. Lakini pia ndani yake kulikuwa na idara maalumu ya siri ambayo Abramovich mwenyewe aliita SUR ambayo ilikuwa inahusika na ukusanyaji wa intelijensia juu ya washindani wao wa kibiashara pamoja na viongozi wa serikali na hapa hasa ndiko ninapotaka kupaongelea.







    Kitengo hiki cha SUR kama ambavyo Abramovich mwenyewe alipendelea kukiita walikuwa na intelijensia ya kutosha juu ya viongozi wengi wa serikali na mmojawapo akiwa ni mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Bw. Yuri Skuratov.







    Wanasema kila binadamu chini ya jua kuna ‘mafuvu’ ameyaficha kabatini. Kila mtu ana siri ambayo anatamani afe nayo. Siku ambayo adui zako wakigugundua siri hiyo ndio inakuwa kiama chako kama ambavyo ilimtokea mwendesha mashtaka Skuratov.







    Baada ya joto la mwendesha mashtaka wa serikali kutaka kumshtaki Abramovich kupanda, Oligarch Berezovsky alikaa na Abramovich kumuuliza ana mpango gani na hicho ambacho kinaelekea kutokea. Abramovich akamuondoa wasiwasi, akamwambia tu anahitaji msaada mmoja kutoka kwake.







    “Anything you want.!” Berezovsky akamjibu .







    Abramovich akamuomba Berezovsky ampatie nusu saa tu katika televisheni yake muda wa usiku, kiandaliwe kipindi maalumu kwa ajili yake. Nilieleza kwamba kwa kipindi hicho Berezovsky alikuwa anamiliki kituo cha televisheni ambacho ndicho kilikuwa kinatazamwa zaidi nchini Russia. Berezovsky bila kusita akawasiliana na meneja wa kituo chake cha televisheni na kumueleza kwamba atenge muda huo wa nusu saa majira ya usiku ndani ya siku mbili zijazo kwa ajili ya Oligarch Abramovich kuongea.







    Muda ukapangwa na siku ya Abramovich kuongea ikawekwa kwenye ratiba.











    Ikapigwa ‘promo’ ya kutosha kutangaza siku hiyo husika na muda husika ambao Oligarch Roman Abramovich ataongea kupitia televisheni kujibu shutuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuhujumu uchumi wa nchi. Ajabu ni kwamba muda huu ambao ulitangazwa Abramovich ataongea ilikuwa ni saa tano usiku na kuna angalizo lilitolewa kwamba wazazi wahakikishe asiangalie mtoto mwenye umri chini ya miaka 18.



    Watu walikumbwa na butwaa… Abramovich anataka kuongea nini hicho ambacho watoto hawapaswi kukisikia.?

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Yuri Skuratov mwenyewe alifahamu ni ‘tsunami’ gani ilikuwa inakuja japo hakutaka kuamini.







    Siku ikawadia, muda ukawadia… saa tano kamili usiku, Abramovich alikuwa mubashara kwenye runinga kujitetea tuhuma zake. Nadhani wengi tunafahamu namna ambavyo Abramovich anaongea, anaongea taratibu mno na kwa sura ya upole haswa. Upole wake anapoongea unaweza kumfananisha na kijana Jared Kushner, mastermind aliyemuingiza Trump whitehouse. Hapa kwetu waweza kumfananisha na marehemu mzee wetu Mengi labda au Ruge Mutahaba… wote hawa mastermind wa masuala mengi ya nchi japo kwa namna wanavyoongea taratibu na kwa upole unaweza kudhani ni magoigoi tu. Lakini waguse uone cha mtema kuni…







    Kipindi kilipoanza Abramovich akajieleza kwamba anaonewa wivu na wanasiasa kutokana na mafanikio yake ya kibiashara. Abramovich akajitetea kwamba mafanikio yake hayo si kwa ajili yake tu bali pia ni kwa ajili ya familia nyingi masikini ambao nao watanufaika (miaka michache baadae Abramovich alitumia fedha zake binafsi zaidi ya dola bilioni tatu (zaidi ya trilioni 6.7 za Tanzania) kwa ajili miradi ya maendeleo kwenye moja ya majimbo masikini zaidi nchini Russia, nitaeleza).



    Akajitetea zaidi kwamba wanasiasa hao wanamtumia mwendesha mashitaka Yuri Skuratov ili amchafue na kumuondolea imani kwa wananchi wenzake. Kisha Abramovich akamalizia kwa kusema kwamba anao ushahidi kuthibitisha kwamba Skuratov ni mtu wa hovyo kabisa ambaye hapaswi kuaminiwa na jamii.







    Alipomaliza kusema hayo mkanda wa video ukaanza kuchezwa kwenye runinga. Video hiyo ilikuwa inamuonyesha Yuri Skuratov akiwa uchi wa mnyama kwenye chumba cha hoteli akifanya ngono mabinti wadogo wawili waliokadiriwa mmoja kuwa na miaka kumi na mitano na mwingine miaka kumi na sita. Video inamuonyesha binti mmoja akimfanyia kitendo cha ngono kwa kutumia midomo yake na huku mwingine akimpapasa mwilini na kubusiana.







    (natamani kuiweka hapa video lakini sidhani kama itakuwa sawa kwa sababu za maadili na sidhani kama ni lazima sana kuitazama… nimepiga ‘screenshots’ tu ili walau upate picha wa kilichotokea)







    Ilkuwa ni tsunami na ambayo haikutegemewa… Abramovich akaongeza kuwa anao ‘ushahidi’ wa wanasiasa wengi wanaompinga kuwa ni watu wa hovyo na mafisadi waliojawa wivu. Kwa maneno mengine alikuwa anatoa ‘warning’ kwa wapinzania wake kwamba anao ushahidi wa mauzauza wanayoyafanya gizani.







    Nchi ya Urusi ilitetema usiku mzima. Kesho yake asubuhi Skuratov akajaribu kujitetea kwamba mkanda huo wa video ni feki lakini hakuna ambaye alimuamini. Yeye ambaye alikuwa kwenye harakati za kumfungulia kesi Abramovich kibao kiligeuka kwake, akafunguliwa mashataka ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto ambao hawajafikia umri halali kisheria kujihusisha na vitendo vya ngono. Kutokana na kushtakiwa kwa kesi hiyo akashinikizwa pia kujiuzulu wadhifa wa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali.







    Skuratov akapotea kwa namna hiyo na hata tuhuma zake dhidi ya Abramovich zikafa kibudu kwa mtindo huo pamoja naye.







    Abramovich sasa akawa anaogopwa pale Moscow. Wapinzani wake wakikutana naye walitamani hata wamuamkie japo ni kijana mdogo kwao. Walifahamu kuwa ana ushahidi wa mauzauza yao na anaweza kuyaachia kwa umma muda wowote ule. Hiyo ilikuwa ni kinga tosha kwake Abramovich.. sasa alikuwa ni ‘untouchable’. Hakuna ambaye alikuwa anathubutu kumnyooshea kidole…







    Hii ilikuwa ni fursa adhimu kwake kutimiza lengo lake la pili kwenye kujilimbikizia mabilioni ya dola. Lengo hili la pili lilikuwa ni kushikilia sekta ya uzalishaji Aluminum. Rusia ni mzalishaji mkuu wa Aluminium duniani na kipindi kile miaka ya tisini asilimia kubwa ya aluminium ambayo ilikuwa inatumika duniani ilikuwa inatoka nchini Rusia. Abramovich alikuwa anataka kuweka mguu wake kwenye sekta hii… mguu mmoja tayari alikuwa ameuweka kwa uthabiti kabisa kwenye sekta ya mafuta na gesi.







    Lakini kulikuwa na tatizo kubwa zaidi linawakabili ma-oligarch. Na lilikuwa tatizo kubwa zaidi ambalo lilikuwa linatishia utajiri wao kupotea na hata uhai wao… kulikuwa na kila dalili kwamba Rais Boris Yeltsin alikuwa amekumbwa na tatizo la ugonjwa fulani wa akili.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Mwanzoni watu walidhani ni ucheshi tu lakini kadiri siku zilivyoenda kulikuwa hakuna ubishi kwamba Yeltsin alikuwa amekumbwa ghafla na tatizo la akili. Kwanza alikuwa amekuwa mlevi kupindukia… alikuwa analewa mpaka muda wa kazi. Kuna siku alikuwa anahutubia taifa akiwa amelewa chakali. Alikuwa anasoma sentesi moja dakika tano nzima. Siku nyingine alihudhuria mazishi ya jenerali wa jeshi akiwa amelewa chakali tena. Hata ulipofika muda wake wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu ambapo unasogelea jeneza na kupiga saluti, Yeltsin aliposogelea jeneza ili apige saluti nusura adondoke kwa kupepesuka. Ilibidi mpaka walinzi wake wamshike kama mtoto ndio asimame sawasawa na kupiga saluti.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog