Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (2)
Sehemu Ya Tano (5)
Emilio, mwanaume mrefu kuliko wenzake aliuliza akijitahidi kuonyesha hana hofu yoyote.
“We want your life.” Kaguta alijibu moja kwa moja kwa ufupi.
Sauti za ving’ora vya polisi zilisikika nje ya uwanja. Magari kadhaa ya polisi yalifika mengine yakiwa njiani kuja na mapolisi lukuki. Sauti hizo za ving’ora ziliwapa matumaini wakina Emilio, kwa namna moja ama nyingine wakajihisi wanaweza wakawa salama. Labda Mungu anaweza tia mkono, eidha waliwaza.
“Do you hear that? … Police are here. They are going to catch you!” Santanna alitishia. Bakari akamjibu akitabasamu:
“So you think you are going to escape just like how you did in Venezuela?”
Emilio na wenzake wakatizamana. Hawakuwahi kudhani kama kuna mtu yeyote anafahamu juu ya matukio yao huko Venezuela. Walipigwa na butwaa.
“Who are you people?” Cruz aliuliza, Vitalis akajibu:
“We are the guests – the guests who have no invitation.”
“Please, don’t kill us. Don’t uncover our identity. We will give you money. How much do you want? Enh?” Emilio alijikomba.
Jibu alilopata lilikuwa ni vyuma vya risasi kupenya kichwani mwake pamoja na mwa wenzake. Hawakupata hata muda wa kuugulia maumivu. Tiketi zao za kwenda jehanamu zilikuwa VIP.
WAGENI isijulikane wapi wamepitia, waliyoyoma wakiwaachia polisi maiti zikitapakaa ndani ya uwanja. Siku iliyofuata picha za marehemu Emilio na wenzake zikatumwa kwenye tovuti rasmi ya usalama wa taifa zikiambatana na maelezo yaliyojitosheleza.
Kama vile haitoshi, makabrasha hayo yalitumwa Interpol. Ndani ya siku tatu mbele, taarifa za magaidi hao zikaanikwa na kurusha kwenye vyombo vikubwa vya habari kama vile CNN, BBC na Al Jazeera huku waziri wa mambo ya ndani akiwa na mengi ya kujieleza juu ya uwepo wa watu hao nchini pasipo kuwa na taarifa.
****
Hamilton, Bermuda.
Uso wa Kim Salvatore, mwanaume chotara wa kizungu na kiafrika, ulikuwa mwekundu mkono wake ukitetemeka na kumwaga kahawa aliyojaziwa kikombeni.
Ilikuwa ngumu kwake kuamini anachokiona kwenye televisheni – taarifa ya habari ya CNN ikionyesha miili ya Emilio, Cruz na Santanna – Wanaume aliokutana nao miaka mitano nyuma kipindi alipokwenda Venezuela kwa biashara ya madawa kulevya kabla ya miaka miwili mbele wanaume hao kumtaka awasitiri kwa miaka kadhaa mpaka pale nyuso zao zitakaposahaulika wakiahidi kumlipa fadhila wasimuache mikono mitupu.
Kim alitupa kikombe chake cha kahawa chini akibinua mdomo. Nyuma yake walisimama wanaume wawili wazungu wakivalia suti. Punde alitokea binti mrembo akiwa ndani ya sare nyeusi na nyeupe akasafisha eneo lililotapakaa vipande vya chupa na kahawa alafu akaondoka upesi. Alirudi ndani ya muda mfupi akibebelea kikombe kingine cha kahawa akaweka mezani.
Kim alizima televisheni akawatizama wanaume wawili walionyuma yake. Hakusema kitu bali aliwapa ishara kwa kuonyesha kidole kwenye televisheni kisha akachinja shingo yake na mkono. Wanaume wale wakaitikia kwa kutikisa kichwa. Kim akapiga ngumi kiganjani mwake akisaga meno. Alinyooshea kidole nje akikunja sura, upesi wanaume wale wakatoka nje pasipo kuaga.
Kim alishusha pumzi ndefu akachezea sharubu zake kwa muda. Alinyoosha mkono akateka simu pana nyeusi iliyoketi kushoto kwake. Hapo mkono wake wa kushoto ukaonekana mchoro mkubwa wa kisu kikichuruza damu. Mchoro huo ulifunikwa na koti la suti pale Kim alipoweka simu yake sikioni, akateta kwa ufupi:
“Njoo nyumbani kwangu upesi.”
Sauti yake nzito iliyoenda moja kwa moja ilitosha kumtisha mtu yeyote.
Asiwe mpweke kwa muda mrefu, akafika mwanaume mzee mwenye asili ya India. Alivalia joho rangi ya kahawia na nyeusi. Kichwa chake ambacho hakikuwa na nywele kilikuwa kimechorwa mistari miwili meupe kuanzia nyuma ya shingo ikiishia kwenye paji la uso kwa kutengeneza kaduara kadogo chekundu. Macho ya mwanaume huyo yalipakawa wanja mweusi, shingoni akivalia kamba iliyobebelea madunguli rangi ya kijivu yenye ukubwa sawa.
Rajul – mwanaume huyo aliitwa Rajul.
“Wito wako wa ghafula, mheshimiwa. Vipi kuna tatizo?”
Aliuliza Rajul akiketi.
Tangu aje, Kim hakumtizama kabisa, alikuwa anatizama televisheni yake aliyoizima kana kwamba kuna jambo nyeti anafuatilia.
“Nahitaji msaada wako wa hali na mali” Alisema Kim bado akitizama televisheni yake.
“Mambo yangu yanakuwa mabaya kadiri siku zinavyoenda mbele. Najiuliza ni wapi nilikosea hatua lakini nakosa majibu kabisa.”
Rajul alijitengenezea vizuri akisikiliza kwa makini.
“Mambo yangu yanapanguliwa kila siku huko upande wangu wa pili wa dunia. Watu wangu wanatishiwa, wanakamatwa, wanauwawa. Sasa imekuwa ngumu hata kuingia ubia na baadhi ya viongozi kwasababu tu wanahofia usalama wao. Pesa yangu imekuwa dhaifu, dhaifu, dhaifu.” Kim aliweka kituo akamtazama Rajul.
“Kuna shida gani? Wapi nimekosea? Tafadhali unaweza ukaniambia?”
Rajul alitikisa kichwa chake akakumbatisha viganjavye.
“Mr Kim, unajua kabisa ya kwamba tokea mwanzoni nilikusaidia kwa uwezo wangu wote pasipo kufinya wala kubana jambo. Nilikupa michoro iliyo hai, michoro mitakatifu, michoro inayoweza kuadhibu. Unafahamu ni jinsi gani michakato ile ilivyotafuna watu, muda na pesa. Ilipelekea mpaka nikafukuzwa kwa kukiuka maadili na miongozo ya matumizi ya nguvu zetu. Sasa nini wataka tena toka kwangu? Unadhani nawezaje tena kukusaidia?”
“Rajul!” Kim alipaza sauti yake. “Unajivunia michoro uliyonipa? Ajabu kweli!”
Akatikisa kichwa.
“Unafahamu kabisa michoro yako ilikuwa ni kwaajili tu ya kuwaongoza wafuasi wangu. Haiwezi kutambua adui na kumteketeza bali inawateketeza watu wangu tu pale wanapokiuka masharti …”
“Bwana Kim kwani kipi ulitaka?” Rajul alikatiza kauli ya Kim. “Wakati unanifuata uliniambia wazi kabisa lengo lako la kwanza ni kuhakikisha watu wako wanakuwa na maadili ya kazi. Wanatii miiko yao. Wanatii amri yako. Wanaficha siri za oganaizesheni kwa njia yoyote ile. Si ndio nikakupatia hiyo michoro na viapo vyake?”
Kim kimya.
“Uliniambia endapo tu watu wako watatii maadili na maagizo, mengine yatamalizwa na pesa zako. Nami nikafanya hivyo. Leo unaiona michoro haina mana? … na nilikuweka wazi, wazi kabisa. – michoro ni kinga lakini pia inaweza kuwa silaha hatari ya kuwaangamiza maadui wako pale utakapomwaga damu ya mtoto wako wa kiume kisha ukanuwia unachotaka. Hukufanya hivyo kwa mtumishi mweusi? Lawama zinatoka wapi tena mheshimiwa?”
Kim kimya. Alikuna sharubu zake akifikiria anayoambiwa. Yalikuwa ni ukweli mtupu na hakuwa na lolote la kumsukuma kutema cheche. Aligonga meza yake mara tatu akaja mwanamke mrembo ndani ya sare akimletea maji ya kunywa kwenye glasi kubwa. Aliyaweka mezani akatokomea.
Kim alinyanyua glasi ya maji akanywa mafundo matatu kupoza nafsi. Alinyamaza kwa sekunde kadhaa alafu akashusha pumzi na kusema kwa sauti ya upole:
“Sawa, Rajul, nimekuelewa. Unakumbuka niliweza kumtumikisha mtumishi mweusi baada tu ya mwanangu pekee wa kiume kupata ajali na kuwa kwenye hali mbaya. Nilishindwa kumuona akiteseka vile hospitali. Niliamua kumuua na hapo ndio nikateka damu yake nitimize adhma. Sasa sina mtoto yeyote kwahiyo unaniambia hakuna nafasi yoyote ya mimi kufufua na kuipa nguvu michoro tena?”
“Unayo.” Rajul alijibu na kuongezea: “Ila nafasi hiyo ni finyu mno na yenye kuhitaji juhudi za dhati. Lakini kabla sijaendelea yanipasa kutizama kwenye ramli zangu umebakiza michoro mingapi kwa sasa ambayo twaweza kuipa nguvu zaidi.”
Kim alitikisa kichwa kuafiki. Rajul alinyanyuka akatoka, baada ya dakika mbili alirudi ndani akishikilia chungu kidogo kilichojengwa na malighafi ya mbao. Alimtaka Kim avue viatu aketi kitako chini. Kim akatii.
Rajul akiwa amesimama alitoa kiwembe pasipojulikana akakata nywele za Kim na kuzitia ndani ya kichungu. Alichanja mgongo wa kiganja cha mkono wa Kim wa kushoto akakinga damu. Aliweka kichungu juu ya kichwa cha Kim alafu akakifunika na kiganja chake kipana akifumba macho na kuteta maneno kadhaa yasiyoeleweka.
Alitoa kiganja chake akaona michoro miwili ndani ya chungu: Simba na mistari mitatu ya mawimbi kuwakilisha maji.
Aliketi kitako akimtizama Kim, akamwambia:
“Una michoro miwili tu iliyobaki: simba na maji. Unaweza ukaipa nguvu tena ikakulinda na kutekeza maadui zako kufumba na kufumbua.”
“Niambie cha kufanya.” Kim alisema kwa kujiamini.
“Mbadala pekee wa damu ya mtoto wa kiume, ni damu ya familia ya kifalme, royal blood.” Rajul alieleza.
“Damu ya familia ya kifalme? Kivipi?” Kim aliuliza.
“Unatakiwa utafute damu ya familia ya kifalme. Familia yoyote ambayo inatoa viongozi wanaotawala, namaanisha sio kama Uingereza na Spania ambazo zina wafalme na malkia lakini hawana nguvu za kisiasa kama mawaziri wao wakuu. Inatakiwa damu ya familia zinazotawala kisiasa, kijamii na kiuchumi.”
Kim alinyamaza kwa muda akitizama chini. Rajul akamuuliza:
“Utaweza ama tuache?”
Kim akanyanyua uso wake akiukunja.
“Hakuna lisilowezekana, Rajul. Niitafanya hivyo.”
Rajul akatabasamu.
“Nilitegemea hilo jibu. Kim ninayemjua mimi hapendi kushindwa … haina shida, utakapopata hiyo damu, unajua wapi pa kunitafuta.”
Rajul alijikusanya akaondoka zake. Kim aliketi kitini akifikiria. Mtihani uliosimama mbele yake haukuwa wa kitoto hata kidogo. Kijasho chembamba kilimchuruza lakini bado alijikuta akitabasamu alipogundua bado ana mwanya mwingine wa kuweka mambo yake mujarab.
Giza lilitwaa jiji la Hamilton ambalo ukiachana tu na umaarufu wake wa kuwa na fukwe za bahari zinazovutia basi utakutana na bandari yake asili inayofanya kazi usiku mchana. Meli za makampuni makubwa kama DryShips Inc, Frontline Limited na Dockwise zilikuwa zinapishana kuingia makaoni mwake.
Sauti za mawimbi ya bahari, upepo mwanana na milio ya mabasi makubwa ya abiria ambayo bado yalikuwa yanatoa huduma ndio hasa zilikuwa zinasikika zikitumia utulivu wa usiku kwa faidaze. Mbali na hapo labda sauti za watu wachache hapa na pale.
Ndani ya jengo jeupe la ghorofa kwenye uwanja mkubwa walisimama wanaume wapatao themanini kwa idadi. Walichanganyikana wanaume weusi na wazungu. Vifua vyao vilivyojengeka kimazoezi vilikuwa wazi wakivalia suruali nyeusi za jeans. Migongoni mwao walibebelea mchoro mkubwa wa kichwa cha simba.
Mbele ya wanaume hao kulikuwapo na kiti kikubwa kirefu chenye rangi ya dhahabu. Hakikuwa na mtu lakini wanaume wote walikuwa wanakitizama kana kwamba kuna mtu asiyeonekana amekaa hapo.
Kim alitokea mlango wa kushoto wa uwanja, akanyookea kitini na kuketi. Wanaume wote nao wakaketi kitako chini wakimtizama.
“Nimewaita hapa kwa dhumuni la kuwataarifu kazi iliyopo mbele yetu. Ndani ya siku nne zijazo tunatakiwa tutengeneza msiba mkubwa. Msiba wa kifalme. Msiba utakaotikisa vichwa vya habari.”
Kim alisema kwa kujiamini akikaza macho yake.
“Nitawateua wanaume watano miongoni mwenu. Wanaume hao wataenda Oman. Wataenda huko kwa dhumuni moja tu: kummaliza Sultan Absaedy Omar ama mwanawe yeyote wa kiume. Nataka damu zao hapa kwa gharama yoyote ile … kwa gharama yoyote! … Wanaume hao watakaofanikisha hilo, watazawadiwa maradufu kwa ushujaa na ufanisi wao.”
Kim alinyanyuka akaweka mikono yake nyuma. Alitembea akipita katikati ya mistari ya wanaume waliokuwa wamejipanga akiendelea kumwaga maneno.
“Hakuna nafasi ya kufanya makosa katika hili. Ni eidha kufa ama kupona. Ni eidha wao wafe ama sisi tufe. Hatujawahi kushindwa vita yoyote ile na hii siyo ya kwanza na wala haitakuwa ya mwisho. Nawaamini.”
Baada ya maneno hayo aliwateua wanaume watano kwa kuwagusa mabegani. Wanaume hao wakasimama na kwenda mbele, wengine wakasimama na kutokomea.
Katikati ya wanaume hao watano walioachaguliwa, walikuwepo pia wanaume wale wawili waliokuwa na Kim wakati anatizama televisheni, walijulikana kwa majina ya Panther na Jaguar.
Kim aliwatizama akawapa ishara huku wengine akiwaambia kwa maneno:
“Nimewachagua nyie kwasababu naamini kwa dhati mnaweza mkafanya hii kazi. Nataka damu ya kifalme ije hapa ndani ya siku tatu tu. Siku tatu! Nataka mkajadili na kupanga usiku huu. Kesho asubuhi mnieleze nini mnahitaji kukamilisha hili zoezi.”
Wanaume hao wakaondoka wakimuacha Kim mwenyewe ameketi kwenye kiti chake kikubwa. Alifikira kwa muda kisha akatabasamu akitikisa kichwa.
“Nadhani hili litakuwa kisasi kizuri dhidi ya yule mshenzi aliyeninyima fursa ya kuwekeza kwenye biashara yake ya mafuta … Sultan, nipo njiani nakuja. Ulinihukumu kwa uchotara wangu, mimi nitakuhukumu kwa ncha ya upanga.”
***
Bakari akiwa pamoja na Miraji walitizama kioo cha tanakilishi mpakato kilichokuwa kinaonesha michoro ya simba na alama za maji kwa makini kana kwamba wanatafutia suluhisho hesabu ngumu.
Bakari alitikisa kichwa chake akauliza:
“Sijui hii michoro ina maanisha nini?”
Ukimya ulikatiza kwa sekunde kabla Bakari hajaendelea kunena:
“Ina mana kuna watu wengine wenye hii michoro, sio?”
“Nadhani.” Miraji alijibu.
“Sasa tutawapataje hao watu? Au tutawangoja mpaka watushambulie?”
“Inabidi tuwagundue mapema. Tofauti na ilivyokuwa kwa kundi la nyoka, wenyewe walitutafuta. Hatujajua hawa wenye hii michoro watatutafuta ama tutawatafuta. Ila tutakuwa salama zaidi endapo tutawatafuta kabla wao hawajafanya hivyo.”
Vitalis na Kaguta waliingia wakaungana na wakina Bakari. Waliendeleza mjadala wakijaribu kufumbua fumbo ambalo lilikuwa gumu kufumbuliwa.
Marietta aliingilia mjadala huo akamuiba Vitalis. Alitaka akacheze naye fukweni kwani alimkumbuka sana tokea yupo shuleni bweni. Vitalis alishindwa kukataa. Alimnyanyua Marietta akamuweka begani wakaenda zao kuchezea maji ya fukweni.
Walirushiana maji wakikimbizana. Walioga michanga. Waliogelea wakishindana kukaa muda mrefu majini. Mwishowe walilala kwenye mchanga mlaini wa fukwe wakitizama jua la saa mbili asubuhi. Hapo Bernadetha akajitokeza na kujiunga nao baada ya kukaa muda mrefu pembeni akiwatizama pasipo wao kujua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Macho yake yalikuwa mekundu akitabasamu. Kwa muda wakati anamtizama Vitalis akicheza na mwanae, Marietta, alimkumbuka mume wake, Malale. Kila mwisho wa juma walikuwa wanaenda ufukweni kama familia. Huko walicheza na kufurahia kisha wanarudi nyumbani jua likizama.
“Karibu!” Vitalis alimkaribisha Bernadetha.
“Ahsante.” Bernadetha alijibu akimtizama mwanae.
“Vipi, kuna tatizo?” Vitalis aliuliza.
“Hapana. Hamna tatizo!” Bernadetha alijibu akilazimisha tabasamu. Alimbeba mwanae akamuuliza:
“Mlikuwa mnafanya nini?”
“Tunacheza! … Nilikuwa nacheza na anko!” Marietta alijibu kwa maajivuno.
“Alafu mama, nimemuambia anko anifundishe ngumi!”
“Ngumi?” Bernadetha alitabasamu. “Nani kakuambia anko anapigana ngumi?”
“Nilimuona! … siku moja nilimuona akipigana na anko Kaguta.”
Baada ya kucheka, Bernadetha akauliza:
“Wewe unataka ukampige nani?”
“Kule shuleni kuna mijitu migomvi!” Marietta alijibu. “Nataka niwapige mpaka wakome!”
Wote walicheka wakaondoka kurudi kwenye makazi yao.
Siku hiyo ilikuwa ni ya kupumzika. Hakuna kazi waliyofanya zaidi ya kupika na kula kisha kufurahia mandhari ya bahari. Waliogelea, walicheza mpira mpaka jua linatuama.
Kaguta akiwa pamoja na Sandra, Miraji, Jombi na Bakari waliaga wanatoka kwenda kujirusha nje ya kisiwa. Waliahidi kurudi siku inayofuata mapema, wanahitaji kupumzisha na kubadilisha mazingira mara moja.
Baada ya mvutano wa hapa na pale, walikubaliana waende.
“Kuweni makini.” Bernadetha aliwahasa.
“Usihofu. Wapo na mimi.” Kaguta akajibu akijinyooshea kidole.
Walitumia boti yao ndogo wakakata maji kwenda jiji la Dar, wakawaacha Bernadetha, Vitalis na Marietta kisiwani.
Haukupita muda mrefu baada ya kula chakula cha usiku, Marietta akapitiwa na usingizi. Vitalis alimbeba akampeleka chumbani alipomlaza na kumfunika na shuka.
Alirudi sebuleni akamkuta Berbadetha ametulia akijikunyata. Alikuwa anafikiria jambo ambalo halikuchukua muda mrefu akamshirikisha Vitalis:
“Samahani, Vitalis. Kuna muda naona picha ya mume wangu pale ninapokutizama. Sijui kwanini inakuwa hivyo. Haijalishi mara ngapi najitahidi kujizuia lakini haisaidii katu.”
Bernadetha aliweka kituo akitizama chini, mara chozi likaanza kumshuka.
“Leo wakati nakuona na mwanangu nili …”
“Sshh! …” Vitalis alimkatiza. Alimfuta chozi akamnyanyua uso.
“Usihofu. Haina haja ya kuomba samahani, Bernadetha. Naelewa. Naelewa unachojihisi … kuna mambo yakupasa uyaache yaende ili upate amani moyoni.”
Vitalis alimbusu Bernadetha shavuni kisha akambeba akimlaza mikononi mwake.
“Nataka uwe na furaha. Sipendi kukuona ukifadhaika.”
Bernadetha alipeleka mdomo wake kwa Vitalis wakanyonyana ndimi. Walielekea chumbani wakazima taa.
****
Muziki ulizidi kunoga ndani ya klabu. Huku mataa ya rangi mbali mbali yakimulika mulika hovyo, watu walikuwa wanajichengua kwa miondoko mbali mbali kutokana na midundo ya muziki iliyokuwa inaita muda huo kwenye vipaza. Walicheza kana kwamba kuna mtu anawalipa, ama labda kuna shindano la kumtafuta gwiji la miondoko.
Wadada walivalia nguo fupi na za kubana. Wanaume wengine nao walivalia nguo zilizobana miili yao hali iliyopelekea ugumu kuwatambua jinsia endapo ukiwatizama kwa nyuma.
Kila mtu alicheza na mtu wake, ikiwemo pia na wakina Kaguta waliokuwemo humo ndani. Wakati Kaguta anacheza na Sandra, Miraji, Bakari na Kaguta walishapata wenzi waliokuwa wakisakata nao rhumba.
Wakati hayo yanaendelea, mwanaume mmoja akiwa amevalia tisheti nyeusi yenye maandishi ya lugha ya kifaransa, Mon frere, alikuwa anawatizama wakina Kaguta na macho yasiyopepesuka. Mkono wake wa kulia alibebelea kinywaji cha BALTIKA ya kopo. Mkono wake wa kushoto alikuwa akiutumia kukunia ndevu zake kidevuni.
Baada ya dakika kadhaa, Miraji alitoka kwenye uwanja wa kucheza akaelekea chooni. Mwanaume yule aliyekuwa anawatizama akanyanyuka na kumfuata. Akitembea kuelekea huko, alichomoa kisu kidogo mfuko wa nyuma wa suruali, akakiweka vema mkononi.
Watu wengi walikuwa wanaelekea huko chooni. Haswa walevi ambao walikuwa wanaenda kupunguza wakapate kuongeza tena. Katikati ya nyomi hiyo iliyokuwa inaenda na kurudi, Miraji alipotelea asijulikana wapi alipo. Giza lilifanya ugumu kuonekana. Kwakuwa wengi wao waliokuwa wanaenda huko maliwatoni ni walevi na hawapendi mwanga, walizima taa.
Mwanaume yule alirudi sehemu yake alipokuwa ameketi awali akasubiri hapo. Muda ukazidi kuyoyoma. Alitizama saa yake mara kwa mara mwishowe akaamua kunyanyuka akafanye tukio vivyo hivyo.
Taratibu alitembea akiwapisha watu. Macho yake yalimtizama Jombi kwa umakini asimpoteze. Alipofika karibu na tageti yake akachomoa kisu chake, ila kabla hajafanya tukio, alishitukia mtu akimsukumiza tokea nyuma yake. Ulikuwa ni ugomvi wanaume wawili wakimgombea mwanamke.
Haraka mabaunsa walikuja kutuliza fujo. Mwanaume yule akarudisha kisu chake mfukoni upesi, akatoka na kurudi alipokuwa ameketi. Sasa aliwapoteza watu wake na hakujua wapi walipo. Alirusha macho yake huku na kule asione kitu. Alikunja sura. Alisaga meno kwa hasira. Aliminya kopo la kinywaji chake akakitupia chini.
Alitoka ndani akaenda nje, huko akawa anangoja walengwa wake watoke apate kuwashughulikia.
Haukupita muda mrefu, akawaona wanatoka wakicheka na kulonga. Taratibu akaanza kuwasogelea.
Kosa alilofanya ni kutopiga mahesabu. Walengwa wake walikuwa wanne badala ya watano. Kuna mmoja hakuwepo na hakujua wapi alipo.
Wakati akijongea kusogea zaidi alisikia mkono begani. Aligeuka akakutana uso kwa uso na ngumi moja nzito iliyompeleka chini kama mbuyu. Alinyanyuka upesi apambane ila akarudishwa chini na teke liliofyatukia hewani likimtengua taya na kumwacha hoi.
“Bado unataka tena?” Kaguta alimuuliza mwanaume yule aliyekuwa chini hajiwezi. Punde wakina Miraji na baadhi ya watu wengine wakajongea karibu.
Kabla hawajafanya lolote, mwanaume yule alijichoma kisu shingoni akafa.
****
“Kwahiyo hamkupata chochote toka kwake?” Vitalis aliuliza akimtizama Kaguta.
“Hatujapata kitu kutoka mdomoni mwake … zaidi alikuwa ana mchoro wa simba mgongoni.”
“Ina mana tayari hili kundi la simba limeshaanza kutufuatilia.” Alisema Bakari. “Inashangaza ni kwa namna gani wanapata taarifa zetu.”
Kaguta alinyanyua kikombe cha maji akanywa. Alizungusha macho yake kuwatizama wenzake wote waliokuwepo mezani kisha akashusha pumzi ndefu. Wote walimtizama kana kwamba wanategemea atie neno.
“Inabidi tuongeze umakini.” Alisema Kaguta akinyanyuka. Alitoka ndani akivua shati akaelekea baharini.
“Ok. Tutaendela kujadili baadae.” Vitalis aliwatawanyisha wenzake. Kila mmoja alitoka akaenda upande wake wakimuacha Vitalis na Bernadetha ndani peke yao.
“Sasa tunafanya nini, Vitalis?” Bernadetha aliuliza kwa sauti taratibu. Aligeuza shingo yake nyembamba akamtizama Vitalis aliyekuwa anawaza na kuwazua.
“Bado sijajua kwa sasa.” Vitalis alijibu. Aligeuza naye shingo yake akamtizama Bernadetha. Walitizamana machoni kwa dakika moja kana kwamba kuna vitu wanaona kwenye viini vyao vya macho. Walishituliwa na mtoto, Marietta, alipokuja akiwaita.
Vitalis alimkwapua Marietta akambeba mgongoni kwa furaha. Huku akimchezea mashavu mwana huyo akaenda naye nje baada ya kumuaga Bernadetha kwa kumkonyeza.
Mpaka jua lazama kuhitimisha hiyo siku hakuna lolote lililogundulikana isijalishe ni mara ngapi walijadili ama kwa muda gani Bakari alikaa karibu na tanakilishi yake kupembua na kuchambua.
Ngoma bado ilikuwa nzito …
***
Muscat, Oman.
Tangu karne ya kwanza jiji hili, Muscat, limekuwa ni jiji muhimu sana kama kitovu cha biashara kati ya ulimwengu wa mashariki na magharibi. Kwa mujibu wa historia kitambo huko nyuma, tunaelezwa ya kwamba waarabu hawa wa Oman walikuja mashariki ya Afrika wakaweka makazi yao katika mji wa Zanzibar wakiboresha mji huo kwa majengo na kuupa umilki wa dini ya kiislamu inayotawala mpaka sasa.
Uwepo wa mazao kama karafuu na majengo yenye asili ya mashariki ya mbali, uarabuni, yamesimama mpaka sasa kama kiashiria cha makazi ya watu hao hapo zamani.
Jiji la Muscat kwa kiasi kikubwa limetawaliwa na milima ya Al Hajar. Barabara na majengo yake yamezungukwa na milima hii ya wastani ambayo pia huwa ni kivutio cha utalii. Mbali na hapo ni mojawapo ya jiji lenye joto kubwa na pia vile vile kavu kama majiji mengi ya mashariki ya mbali, uarabuni, kwasababu ya ukosefu wa mvua za kutosha. Ila hilo si kigezo cha ukosefu wa maji katika jiji hilo, mabomba ya maji yametambaa kila kona yakimimina maji freshi masaa ishirini na manne.
Wageni wa jiji hili watumiao ndege, hupokelewa kwenye uwanja mkubwa wa ndege Muscat International Airport. Uwanja huo upo umbali wa kilometa takribani ishirini na tano kutoka kwenye wilaya ya biashara ndani ya jiji, Ruwi, huku uwanja huo ukiwa takribani kilometa kumi na tano mpaka kwenye makazi ya Sultan.
Jengo la Al Alam, makazi ya Sultan wa Oman, ni mojawapo ya jengo linalowavutia watali kwa muundo na muonekano wake wa kuvutia. Jengo hilo lililojengwa mwaka alfu tisa mia sabini na mbili ndilo ambalo limekuwa likisimama kama alama ya utawala wa Sultan, ambaye ni miongoni mwa viongozi walioshikilia madaraka kwa muda mrefu sana duniani.
Watumishi watano wa Kim Salvatore, wakivalia suti nadhifu, walishuka kwenye ndege kubwa Qatar Airways wakaongozana mpaka nje walipochukua taksi ikawapeleka moja kwa moja kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tatu.
Waliandikisha majina bandia hapo wakichukua vyumba viwili baada ya kukataliwa kurundikana kwenye chumba kimoja kwa mujibu wa idadi yao. Wakiwa ndani ya chumba kimoja walianza kupanga yale waliyodhamiria kuyafanya kama vile walivyoagizwa kutenda.
Wakiwa wana ramani ya jiji zima la Muscat, pamoja pia na ramani ya jengo la Al Alam, wakaanza kupanga wapi waingilie, wapi watokee, wapi wafanye hiki na wapi wafanye kile. Watatu walielekezana kwa maneno huku wale wenzao wawili, mabubu, wakielekezwa kwa ishara ya mikono. Ndani ya begi lao kubwa walitoa sura za bandia, shuka kubwa rangi ya dhahabu, tiketi za kurudi walipotoka pamoja na kifaa cha kukingia damu. Kifaa hicho kilikaa kama birika lakini lenye mdomo ulichongoka.
“Tutafanya kazi yetu ijumaa, yani kesho. Ni siku ambayo Sultan hutoka kwenda msikitini. Tutatumia nafasi hiyo kuingia ndani ya jengo lake kwakuwa ulinzi utakuwa hafifu. Na pale tu atakaporudi, tutatumia dakika ishirini tu kumaliza kazi yetu na kuondoka. Hatuna muda wa kupoteza!”
Walimaliza usiku wao kwa hayo maagano.
***
Wakati adhana inalia kila upande wa jiji la Muscat, tayari magari yaliyombebelea Sultan pamoja na familia yake yalikuwa yapo barabarani kuelekea msikitini. Magari meusi. Magari ghali. Magari yasiyo na uwezo wa kupenyeza vyuma vya risasi. Barabara yote ilikuwa nyeupe kupisha msafara huo wa kiongozi mkubwa.
Wakati huo huo, watumishi watano wa Kim wakiwa na nyuso bandia waliwasili mbele ya jengo kubwa, Al Alam. Mmoja alibebelea begi mgongoni, wote wakibebelea kamera shingoni mwao. Walivalia kana kwamba ni watalii – bukta za timberland, nguo nyepesi za kurandana na joto, miwani ya kupambana na jua kali, raba na viatu vya wazi.
Walizunguka huku na kule wakitizama tizama jengo hilo na kulipiga picha. Walizidi kusogea zaidi na zaidi, mwishowe mlinzi akawafuata. Alikuwa amevalia kofia nyekundu yenye mkia mweusi mithili ya kaufagio. Nguo zake zilikuwa za kaki zikiwa zimenyooshwa vema na kupendeza. Usoni mwake alikuwa na mustachi mpana na macho yenye nyusi nyeusi zilizokoza.
“Hamruhusiwi kusogea zaidi, tafadhali.”
Alisema mlinzi akiunyoosha mkono wake.
Watalii hao feki wakaafiki maelezo. Waliendelea na safari yao wakizunguka jengo kubwa la Al Alam. Walipofika nyuma ya jengo hilo, huko kulipokuwa kimya na tulivu, walirudia tena zoezi lao la kusogelea jengo kwa karibu. Walinzi watatu waliwafuata wakiwakataza, hapo wakawakaba walinzi hao kwanguvu na kuwapokonyauhai. Haraka aliyebebelea begi akatoa kitambaa cha rangi ya dhahabu akawafunika walinzi waliouwawa. Kufumba na kufumbua walinzi hao wakapotea isijulikane wapi walielekea. Kilibakia tu kitambaa ambacho kilichukuliwa haraka kikarejeshwa begini wanaume wengine wakitwaa nguo za walinzi na kujivika.
Wanaume watatu waliovalia nguo za walinzi walisogelea jengo la Al Alam wenzao, wawili, wakienda kwa mbali kidogo kama watizamaji. Ila wote wakiwa wanawasiliana.
“Bado dakika tano Sultan atoke msikitini.” Alisema mtumishi mmoja wa Kim aliyekuwa nje ya jengo huku akitizama saa yake mkononi.
Ijumaa si tu kwamba ni siku maalum ya kuswali kwa waislamu ambao dhahiri ndio idadi kubwa ya wananchi wa Oman, bali pia ni siku ya mapumziko. Watu hawaendi kazini siku hiyo, wanakaa majumbani na familia zao. Baada ya kuswali, ijumaa huwa inashuhudia idadi kubwa ya watu wakiranda randa mitaani. Ni siku nzuri kwa kufanya tukio na kutoroka, labda ni sababu nyingine ya tukio hili la kutafuta damu ya Sultan kufanyika siku hii.
Zilikamilika dakika tano, magari ya msafara wa Sultan yakaanza kushika njia kurudi makaoni. Kama kawaida barabara ilikuwa nyeupe. Magari yalikuwa yanakimbia kwa kasi yakijipanga kwenye mpangilio wa moja. Gari la Sultan lilikuwa katikati likitanguliwa na kufuatiwa na magari ya walinzi.
Kuna walinzi waliovalia nguo za sare pia wakiwemo na wale waliovalia suti nyeusi pamoja na miwani. Hawa wa suti nyeusi, wanaume sita, ndio walikuwa karibu sana na Sultan. Walihusika kumfungulia Sultan milango ya gari na nyumba pia kuongozana naye kwa ukaribu.
Ndani ya jengo la Al Alam, mahali pa mfalme, kila eneo kuliwekwa kamera zikimulika huku na kule. Sehemu pekee palipokuwa hapana kamera ni vyumba vikubwa vya Sultan na familia yake. Sehemu zingine zote, kuanzia jiko kubwa lililopo ndani ya jumba hilo, korido pana safi za jengo hilo, sebule nene za jengo na sakafu zake zote palikuwa na kamera zilizokuwa zinaonekana na kusomwa ndani ya chumba cha teknishiani ambaye alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na walinzi wa jengo hilo.
Kama vile haitoshi, walinzi walitapakaa ndani ya jengo wakiwa wamesimama kama minara na silaha zao. Hata kama nzi angelikatiza mbele ya macho yao wasingelipepesuka kamwe. Walisimama kwa ukakamavu na utulivu kana kwamba wametiliwa gundi hapo.
Sultan pamoja na familia yake walikuta meza ya chakula ikiwa imejaa chakula na matunda ya kila aina. Wahudumu wa chakula walisimama pembeni wakingojea kupewa amri.
Familia hiyo iliketi wapate kula ila Sultan hakuwapo bali mkewe na wanawe wanne. Sultan alipoingia tu ndani alinyookea chumbani kwake na sasa ilipita dakika kadhaa hajaja mezani kupata chakula.
Mke wa Sultan baada ya kula matonge kadhaa, alimuita mlinzi kwa ishara akamuagiza aende kumtizama mume wake chumbani. Mlinzi alipokea amri hiyo akaenda kuitimiza. Aligonga mlango wa chumba cha Sultan pasipo majibu.
Alichungulia tundu la ufunguo akaona miguu ya Sultan ikiwa inatapatapa juu ya kitanda. Alivunja mlango akaingia ndani. Alimkuta Sultan akiwa anamimina damu ubavu wake wa kushoto kukiwa na tundu kubwa.
Sultan alinyanyua mkono akioneshea nyuma ya mlinzi. Mdomo wake ulikuwa unateta kitu ambacho hakikusikika vema. Mlinzi aligeuka kutizama nyuma akakutana na teke kali. Alidondoka chini akazirai.
Mwanaume aliyefanya hayo akatoka chumbani akiwa ameficha kitu ndani ya shati lake.
Teknishiani wa chumba cha kamera alimuona mwanaume huyo aliyeficha kitu akitoka ndani ya chumba akitembea haraka. Alipovuta picha yake kwa karibu, aliona mwanaume huyo ana damu mkononi. Haraka akatoa taarifa kwa walinzi wote juu ya mwanaume huyo.
Familia ya Sultan iliwekwa chini ya ulinzi kwa usalama. Walinzi wote waliokuwepo nje walikaa tenge kwa vita. Walinzi waliokuwepo ndani wakaanza kumfukuzia mwanaume aliyetokea chumba cha Sultan wakiongozwa na teknishiani wa chumba cha kamera.
Kutokana na jumba kuwa kubwa ilikuwa ngumu kwa mtuhumiwa kukamatwa kirahisi.
Kabla hajatiwa nguvuni, teknishiani alivamiwa ndani ya chumba chake akauwawa. Mwanaume mwingine, mtumishi wa Kim, akaanza kuwapoteza walinzi kwa kuwaelekeza muelekeo usio sahihi huku akiwasiliana na wenzake akiwataka wakutane chumba cha teknishiani.
Ndani ya muda usiofika dakika, wote watatu walifika ndani ya chumba cha teknishiani. Walijifunika na shuka lao rangi ya dhahabu, kufumba na kufumbua wakapotea. Walinzi walipokuja, walikuta tu shuka wavamizi wasionekane wapi wameenda, mlango upi wametokea.
Wanaume watatu wavamizi walitokea ufukweni mwa bahari. Walijikusanya wakiwasiliana na wenzao wakutane hotelini. Walivua nyuso zao za bandia wakazitupia baharini. Kando kando yao kidogo tu palikuwepo na maiti zile tatu za walinzi waliowaua.
Haraka walitoka eneo lile wakaelekea hotelini walipokutana na wenzao.
“Umefanikiwa?”
“Ndio! … hii hapa!” Mwanaume mwenye kibirika alioneshea.
“Sasa nini kinafuata?” Mmoja aliuliza.
“Tusiwe na haraka ya kuondoka.” Mmoja alijibu, mmojawapo wa wale walioachwa nje ya jengo. “Taarifa imeshatolewa mipaka yote ya jiji ifungwe asitoke mtu yeyote. Kila chombo pamoja na watu wake watakaguliwa kabla ya kutoka nje ya jiji.”
Mmoja alifungua dirisha akachungulia. Huko nje akaona magari ya wanajeshi yakizunguka zunguka huku na huko.
***
“Wametokea wapi?” Mkuu wa ulinzi wa jengo la Al Alam aliuliza akiwa ameshikilia shuka lilioachwa na wavamizi.
Hakuna aliyejibu. Kila mtu alikuwa amebung’aa.
“Kuna sehemu yoyote iliyovunjwa?”
“Hapana!”
“Sasa wametokaje?”
Kimya. Mara …
“Watakuwa wametumia hilo shuka!” Alisema mlinzi mmoja akioneshea shuka aliloshika mkuu wake.
“Wametumia nini?”
“Hilo shuka!”
“Sijakuelewa.”
Mlinzi huyo alisogea karibu akalitizama shuka.
“Watakuwa wametumia hili shuka kupotea hapa. Hili shuka la Wadhaab, jinni la baharini, ukijifunika unatokea fukweni.”
Upesi walinzi watatu walijifunika hilo shuka, wakapotea. Walitokea ufukweni palepale walipotokea wavamizi. Pembeni waliona wenzao watatu waliouwawa. Lakini pia kabla hawajaondoka eneo hilo wakaona sura za bandia zilizotupwa.
Walizikusanya sura hizo wakazipeleka maabara. Isichukue hata muda sura za wale waliokuwa wamejivika sura hizo za bandia zikaonekana kwenye tanakilishi baada ya vinasaba vyao kupembuliwa.
Picha hizo zilisambazwa kwa wanajeshi, hivyo sasa kila sehemu haswa za wageni, kama vile hotelini na sehemu zingine za kupumzikia, wanajeshi wakasambaa. Uwanja wa ndege na mipakani pia ulinzi ukawekwa wa kutosha picha hizo zikitumika.
Hoteli zote zilianza kufanyia upekuzi wa wageni. Orodha ya kusajilia wageni ya hoteli ilitumika wanajeshi wakipita kila chumba kukagua wakazi. Kila mgeni aliombwa atoe pasipoti yake akiulizwa maswali kadhaa juu ya lini kafika na anafanya shughuli gani.
Haikuchukua muda mrefu kwa wanajeshi hao kufika ndani ya hoteli ya nyota tatu walimo walengwa wa mauaji – chumba 277. Waligonga mlango kwa muda kidogo, ukafunguliwa na mwanamke. Mwanamke mfupi aliyevalia hijabu na baibui nyeusi. Wanajeshi wakaguzi walitizamana na msimamizi wa hoteli kabla hawajaanza kuuliza maswali.
“Tunaomba pasipoti yako.”
Mwanamke akatoa.
Wanajeshi waliitizama pasipoti ile. Ila kana kwamba hawajaridhishwa na maelezo yale ya pasipoti, wakauliza:
“Unaitwa nani?”
“Fatuma Saed.”
“Unatokea wapi?”
“UAE … United Arab Emirates.”
“Unafanya nini Oman?”
“Nimekuja kutalii … kutizama michanga ya Wahiba.”
“Upo mwenyewe?”
“Hapana. Nipo na mume wangu ametoka kidogo.”
Wanajeshi walitizama tena pasipoti kisha wakatizamana kana kwamba wana mashaka. Waliingia ndani ya chumba wakapekua kila sehemu wasione kitu. Walitoka wakaendelea na upekuzi vyumba vingine.
Mwanamke yule mwenye hijab alivua sura yake ya bandia akipiga mluzi, wakatokea wanaume wengine wanne juu ya dari walipokuwa wamejishkiza. Baada ya kuhakikisha mlango umefungwa na madirisha pia walianza kujadili:
“Tuondoke hapa, si salama tena kukaa. Hatuna tena nyuso za kujifichia.”
“Sawa, tutaondokaje na sehemu zote zimebanwa?”
“Mkuu amenitumia ujumbe. Usafiri wetu upo tayari, cha kufanya ni kuelekea kusini mwa mji kesho asubuhi … huko pana watu wachache.”
****
Asubuhi ya saa mbili, tayari wanaume watano wakiwa wamevaa baibui walitoka nje ya hoteli wakajipaki kwenye taksi.
Walitoa maelekezo waelekee kusini mwa mji. Ila baada ya muda tu kidogo, walimkaba dereva wakashika wao usukani. Dereva wa taksi alitupiwa nje ya gari huku wakiwa kwenye mwendo.
Gari hiyo ilienda kwa takribani dakika ishirini pasipo kusimama. Wakiwa wanatafuta dakika ya ishirini na moja, wakakutana na kizuizi. Wanajeshi kumi wakiwa na magari yao walifunga njia huku wanaopita hapo wakikaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.
Kabla wanaume wale watano hawajajua cha kufanya, gari lao lilishafika mbele ya wanajeshi waliolisimamisha kwa kunyoosha mkono.
“Shukeni!”
Wakaamriwa.
Walitizamana wakashuka. Wakaja wanajeshi wawili wanawake wakaanza kuwapapasa papasa maungo yao. Wanajeshi wengine watatu walifuata gari wakaanza kulipekua pekua.
Wanaume wale hawakuweza kustahimili upekuzi ule. Walijua fika kibirika kile cha damu kitaonekana kwenye gari na pia hata jinsia zao zitatambulika kutokana na upekuzi waliokuwa wanafanyiwa. Vile vile haitochukua muda wataamriwa wafunue baibui zao kuhakikiwa nyuso.
Watafanyaje?
Walitizamana wakakonyezana. Isichukue hata dakika mbili kila mmoja akatumia utaalamu wa mapigo yake kuwatengua na kuwavunja wanajeshi wakaguzi na kuwapokonya silaha.
Ni kabla mwanajeshi yeyote hajachukua hatua ya kutetea roho yake, wanaume wale walisharuka na kumfikia ama kumtumia teke wakijitumia wao wenyewe kama ngazi, muda mwingine huyu akimbeba yule na kumrusha kisha kumvuta tena nyuma. Unaweza sema ni maonyesho ya sarakasi, kumbe ni mapigo ya ajabu yatakayokuacha ukibung’aa huku ukichakazwa.
Wanaume wale watano walichukua magari ya wanajeshi wakayeya. Walipofika walipotakiwa kufika, walikuta helikopta hapo na dereva wake. Walipanda wakaondoka ndani ya nchi ya Oman.
Baada ya nusu saa wanajeshi walifika hapo wakakuta gari tu.
***
Ukiwa ni usiku wa saa saba, boti ndogo nyeupe inayosukumwa na mashine ilisogelea kisiwa cha wakina Vitalis kwa mwendo wa taratibu.
Kwenye boti hiyo walikuwepo wanaume wanne waliovalia nguo nyeusi juu mpaka chini. Kati yao watatu walikuwa wazungu huku mmoja akiwa mtu mweusi.
Boti hiyo ilizunguka kisiwa hiko mara mbili alafu mashine ikazimwa. Mwanaume mmoja akasema:
“Hakuna kumuacha mtu yeyote hai.”
Baada tu ya hiyo kauli, wanaume watatu waliopewa maagizo walirukia ndani ya maji wakaogelea kama samaki. Punde tu walishika nchi kavu na kuanza kusogelea nyumba pekee hapo kisiwani.
Baada ya sekunde kadhaa, sauti kali ya kiume ilisikika, Vitalis akashituka usingizini. Alitulia kwa sekunde tatu akisikilizia, akajikuta akisema:
“Jombi! … Jombi!”
Akili yake ilimuambia hiyo sauti ni ya Jombi. Upesi alifungua dirisha akachungulia nje, kwa mbali akaona kitu cheupe baharini.
Kama vile haitoshi, alisikia sauti ya kishindo nje ya chumba chake. Haraka akanyanyuka na kutwaa bunduki yake aliyoiweka chini ya godoro. Aliikoki bunduki hiyo akatoka ndani kwa kupitia dirishani.
Taratibu alinyata akifuatisha sauti mojawapo ya kiume iliyokuwa inafoka ikimuamuru mtu atoke alipojificha.
Alipofika karibu na sauti hiyo alichungulia dirishani akamuona Bernadetha anatoka ndani ya kabati pamoja na mwanaye, Marietta. Mikono yao waliiweka juu nyuso zao zikitandazwa hofu.
Pasipo kusubiri, Vitalis alipitisha mkono wake dirishani akafyatua risasi ikambanjua adui kichwani. Kufumba na kufumbua alitokea adui mwingine akaingia ndani ya chumba hiko kwa pupa. Alifyatua risasi ikamkita Marietta kifuani na kumwaga chini. Kabla hajafyatua nyingine Vitalis alimuwahi kwa kumlenga risasi ya mkono kisha akarukia ndani upesi kwenda kumjulia hali Marietta.
Alikuwa hapumui. Damu zilikuwa zimemjaa kifua kizima. Macho yake yalikuwa wazi pamoja pia na mdomo. Alikuwa amekufa, Marietta. Lakini mama yake hakuamini hilo, aliendelea kumuita akilia. Alimtikisa tikisa kama kibuyu cha maziwa.
Chozi likamshuka Vitalis. Alimfunika macho Marietta akamshika bega Bernadetha. Aliogopa hata kumbembeleza. Aliishia tu kumtizama kana kwamba amepigwa na butwaa. Alisahau ya kwamba hakumuua yule adui aliyemfyatulia risasi zaidi tu ya kumjeruhi mkono, maeneo ya begani. Adui huyo aliyekuwa nyuma yao alisogeza bunduki yake akawanyooshea pasipo wao kutambua.
Kabla hajafyatua, alifumuliwa ubongo na risasi iliyotokea nyuma yake, mlangoni, habari yake ikaishia hapo. Alitokeza Kaguta akibebelea bunduki anaongozana na Miraji na Bakari.
***
“Walikuja wanaume wanne na boti. Hatujajua ni kwa njia gani wamefahamu tunapoishi. Hatupo salama tena hapa!” Alisema Kaguta kimsisitizo wote wakimtizama.
Macho ya Bernadetha bado yalikuwa mekundu. Alikuwa makini akitazama bahari kupitia dirishani. Alitizama huko kana kwamba anamuona mwanae Marietta juu ya uso huo wa bahari ya bluu uliokuwa unamulikwa vema na jua la mchana. Mtoto wake pekee aliyebakia, Miraji, alikuwepo pembeni yake akimuwekea mkono begani kwa kumbembeleza. Pembeni zao walikuwapo Bakari, Kaguta na Sandra. Mbele zao wote alikuwepo Vitalis.
“Nini kingine umekipata?” Vitalis aliuliza. Bakari akasafisha koo lake.
“Kama unavyojua, wavamizi wote walikufa kwahiyo hakuwepo hata mmoja wa kutupa taarifa. Mmoja tuliyekuwa tunamtegemea ni yule ambaye alipigwa risasi ya mguu na Kaguta, tukimfunga kamba kwa kutegemea atakuwa rasilimali baadae ila naye tulipotoka tu ule upande wenu tukamkuta amejiua kwa kujibamiza kichwa chini.”
Bakari alisema kisha akaweka kituo. Wote walikuwa wanamtizama.
“Tulipofuatilia huko tulipotoka, tumegundua watu hao walikodisha boti kwenye kampuni ya Suleiman Fishing, wakipatana kuirejesha muda si mrefu. Walitoa pesa za kutosha hivyo kampuni ikashindwa kuwakatalia kwani hata kama wangetokomea nayo wangeweza kupata nyingine mpya …”
“Kwahiyo wametokomea nayo?” Vitalis alimkatisha Bakari.
“Ndio, wameondoka nayo. Ila itakuwa ahueni kwetu kuwapata kwa urahisi.”
“Kivipi?”
“Tutatumia tracking device ya kampuni. Suleiman Fishing huwa wanaweka vifaa kwenye kila chombo chao ili hata pale vinapopotea ama kuibwa basi inakuwa rahisi kuvipata. Tutatumia mwanya huo kuwapata.”
“Kwanini wameondoka na boti hiyo?” Vitalis aliuliza kisha akang’ata ngumi yake akitizama pembeni.
“Labda watakuwa na matumizi nayo hapo baadae.” Sandra alijibu. “Na hayo matumizi yanaweza yakawa mabaya zaidi upande wetu.” Akaongezea.
“Hatuna budi kufanya upesi kabla hawajafanya wao.” Vitalis alisema. “Hiyo ndio itakuwa njia nzuri kuenzi wapendwa wetu waliotutoka wakati bado tunawahitaji na kuwapenda.”
Aliweka kituo akawatizama wenzake wote usoni. Alifumba macho kwanguvu akayafumbua akisema:
“Muda umewadia. Twende tukafanye sala.”
Walizunguka matuta mawili makubwa yaliyokuwa umbali mchache toka yalipo makazi yao. Walitulia hapo kwa muda wakiwa kimya nyuso zao zikitizama chini.
Hawakudumu sana, Bernadetha akaanza kulia. Alidondoka chini akipiga yowe. Machozi yalimmiminika kama maji. Japokuwa alibembelezwa, hakunyamaza abadani. Uchungu aliokuwa nao ulizidi matumaini na pole alizopewa.
“Nitawaua tu na mimi … hak’ya Mungu!” Bernadetha aliapa kilioni.
***
Hamilton, Bermuda.
Walikusanyika wote kwenye uwanja wao kama walivyofanya hapo awali. Wanaume kama themanini kwa kuhesabu kwa macho wakiwa vifua wazi na wamevalia suruali za jeans nyeusi waliujaza uwanja. Mbele yao hakuwepo mtu yeyote bali viti viwili vikubwa ambavyo kimoja wacho kilijazwa dakika moja mbele na Kim Salvatore.
Alikuwa amevalia suti nyekundu na tai nyeusi. Mgongo wake ulikuwa umefunikwa na joho kubwa la manyoya lenye vidoti doti vyeusi. Kiatu chake cheusi kilikuwa kinameta meta kama nyota. Nywele zake za mchanganyiko wa mweupe na mweusi zilikuwa zinang’aa kwa kupakwa na kushiba mafuta. Ndevu zake zilichongwa vema huku nyusi zake zikiwekwa sawia na wanja.
Kwa mbali mdomo wake ulikuwa unameta mithili ya saa yake ya dhahabu aliyoivaa mkononi. Pete yake rangi ya fedha yenye kito cha almasi, aliivalia kidole cha mwisho. Alikuwa anatumia kidole hicho kugongea gongea mkono wa kiti taratibu kana kwamba anajaribisha kipaza sauti cha sherehe.
Kwa mazingira tu yaliyopo yalionyesha siku hiyo haikuwa ya kawaida. Sio tu uwepo wa viti viwili ulisema hivyo, bali hata mavazi na maandalizi. Uwanja mzima ulipambwa na bendera nyekundu zenye mchoro mweusi – mchoro wa mikono iliyopishana ikitengeneza umbo la ‘x’ – mchoro wa mikono ya chuma.
Kila nguzo ndani ya uwanja huo ulifunikwa na kitambaa chekundu kirefu, sakafu ikifunikwa na zulia jeusi.
Kim alitoa ishara kwa kuinamisha kichwa chake, wanaume wote wakaketi kana kwamba wapo masjid – mkao mmoja. Kulikuwa kimya, tuli. Kim akanyanyuka akatizama pande zote na kusema:
“Vema!”
Akatikisa kichwa kimakubaliano.
“Naona vyote vimekuwa vema. Na hivyo ndivyo inatakiwa iwe.”
Alitabasamu akatizama upande wake wa kushoto. Huko akatokea Rajul akibebelea kibakuli kidogo cha mbao. Alivalia nguo nyeupe ndefu ikimfunika miguu kabisa. Shingoni mwake alikuwa amevalia cheni yake ya madunguli ya mbao. Kichwa chake kisicho na nywele kilikuwa kimechorwa michoro miwili meupe zigzag.
Alitembea kwa umakini akifuata kiti kitupu. Aliketi akipakata kibakuli chake, akamtazama Kim na kumpa ishara ya kuinamisha kichwa. Kim akawatazama wafuasi wake.
“Leo ndio ile siku maalum. Siku adhimu kabisa. Leo ni siku ya kurudi utotoni. Leo ni siku ya kuzaliwa upya!”
Kim alisema kisha akaweka kituo. Akatabasamu.
“Nitakaowaita watakuja hapa mbele. Watakunywa damu ya kifalme, damu ya baraka, damu ya uongozi, damu ya nguvu. Punde tu damu hiyo itakapoingia kwenye mishipa yao, hawatokuwa binadamu tena bali simba kamili. Si panga wala risasi, si mikuki wala mishale zitawamaliza.”
Alipomaliza kusema hayo akaita majina ya wanaume watano. Kati ya wanaume hao watano, wanne walikuwa ni miongoni mwa wale wanaume watano waliotumwa Muscat, Oman, kuteka damu ya mfalme.
Mwenzao mmoja hakuitwa. Aliachwa akiwa ameketi, uso wake ukibeba ndita ametoa macho kana kwamba haamini. Alikunja ngumi yake akisaga meno. Alijikuta akinong’oneza akiwatizama wenzake wakinywa walichopewa kwenye kibakuli.
“Kwanini? … Kwanini?”
Alijaribu kukumbuka yote yaliyotukia Muscat, Oman. Jinsi alivyojituma akijifanya mwanamke. Jinsi alivyowaokoa wenzake kwa shuka la Wadhaab. Na jinsi alivyorusha mateke na ngumi za adabu kwa wanajeshi wa Oman.
Kote huko hakuona kosa alilolifanya. Kwanini hajaitwa na yeye? Aliwaza.
Mkutano ulidumu kwa dakika ishirini na tano kabla watu hawajatawanyika. Kim na Rajul waliongozana wakaelekea ofisini. Nyuso zao zilikuwa na furaha, zilipambwa na matabasamu. Waliketi wakawa wanapongezana kwa kupeana mikono na kutikisa vichwa vyao.
“Sasa yamekwisha, bwana Kim. Unaweza ukatawala ulimwengu tena kwa kuwasambaratisha maadui zako.” Alisema Rajul akitabasamu.
“Ahsante sana, Rajul. Nafikiria nikulipeje lakini nakosa majibu kabisa.”
“Hamna shida kabisa bwana Kim una …”
Mlango uligongwa.
“Nani?” Kim aliuliza kwa kupaza sauti.
“Stanis!”
Sauti ikamjibu toka mlangoni.
“Ingia!”
Mlango ulifunguliwa akaingia mtumishi wa Kim. Mtumishi aliyeona amenyiwa fursa ya kuitwa na kutunukiwa kama wenzake.
“Karibu, Stanis. Naweza kukusaidia?”
Kabla Stanis hajajibu, Rajul alisimama akamtizama Kim.
“Naomba niende. Nitakuja siku nyingine tuongee zaidi.”
Kim akampa ishara ya kuinamisha kichwa, Rajul akaondoka zake. Stanis akaketi alipokuwa amekaa Rajul.
“Nimekuja kuuliza, mkuu.”
“Kuuliza nini?”
“Kwanini umenibagua wakati nami nilitumia akili na nguvu zangu zote kukutumikia. Kwanini?”
Kim alitabasamu na shavu la upande mmoja. Aligonga meza yake mara mbili akaja mwanamke mrembo ndani ya sare nyeusi na nyeupe akibebelea chupa ya mvinyo na glasi. Alimmiminia Kim kinywaji kisha akaenda zake. Kim alikunywa mafundo mawili akimtizama Stanis. Aliweka glasi yake chini akauliza:
“Ulivyorudi toka Muscat, sikukupa mifuko miwili ya dhahabu?”
“Ulinipa.”
“Sikukupa wanawake watano warembo toka Brazil ukalale nao?”
“Ulinipa.”
“Sikukupatia nafasi ndani ya mamlaka yangu?”
“Ulinipa lakini …”
“Lakini nini? Unadhani yale niliyoyafanya pale yalikuwa ni zawadi tena?”
“Ni nini?”
“Stanis! … labda umesahau wewe ni nani na mimi ni nani. Naweza nikafanya lolote lile ninalolitaka, wewe ni nani uniulize na kutilia mashaka ninachokifanya? Wewe ni mtumishi tu. Huna haki yoyote ya kutaka mimi nifanye unavyotaka. Wewe ndio unafanya mimi ninavyotaka.”
Kim alisema kwa sauti ya chini yenye mkazo. Alijimiminia mvinyo kwenye glasi yake akanywa mafundo matatu.
Stanis alinyanyuka akataka kwenda. Kim akamuita.
“Unaenda wapi Stanis? … kaa hapo, bado tuna mengi ya kuongea.”
Stanis alirudi akaketi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kutembea kwa takribani dakika tatu akitoka kwenye jumba la Kim, Rajul alifika kwenye kituo cha mabasi. Kwakuwa ni muda wa mchana, hakukuwa na watu wengi kituoni. Eneo hilo hujaa haswa muda wa asubuhi na jioni – watu wakienda na kurudi makazini.
Rajul aliketi kungojea usafiri papo. Ilipita dakika moja basi likaja. Rajul alinyanyuka taratibu kufuata basi hilo, alipokaribia mlangoni kondakta alimnyooshea mkono akimkataza kupanda, basi lilijaa.
Rajul alitikisa kichwa chake akarudi kungojea. Aliketi hapo sasa akiwa na mtu mmoja tu, wengine walipata nafasi ya kukwea basi lililopita.
Mtu huyo aliyeketi naye alikuwa ana nywele nyeusi za singa. Hakuwa mweupe wala mweusi – maji ya kunde. Alivalia shati jeupe na kikoi cheusi. Hakuonekana kama muongeaji wala sura yake haikuwa karimu. Alikuwa ameufumba mdomo akiuvuta kana kwamba anambusu mtu.
Rajul alimtizama akampuuzia. Aliendelea kutazama tazama barabara akingojea basi. Alionekana ana haraka na swala la kungoja lilimbughudhi.
Baada ya dakika tatu, basi lingine liliwasili. Rajul alinyanyuka upesi akimtangulia mwenzake kana kwamba yu mashindanoni. Aliingia kwenye basi moja kwa moja akaenda kuketi kwenye kiti kando na dirisha. Hakujali wala kutizama nyuma kama yule mwenzake aliyekuwa naye kituoni amepanda ama lah. Hakujali alimradi yeye keshapata nafasi.
Ila yule mwanaume aliyekaa naye kituoni, naye alipanda basi hilo hilo. Alikuwa nyuma yake upande huo huo wa karibu na dirisha.
Basi lilipotembea kwa muda wa dakika sita, Rajul akabonyeza kengele kuashiria anashuka kituo kinachofuata. Alishuka akashika njia nyembamba inayopanda juu palipo na maghorofa kadhaa.
Alitembea taratibu na mwendo wake wa kizee.
Nyuma yake yule mtu mwenye nywele singa alikuwa anamfuatilia taratibu. Kila Rajul alipogeuka, mwanaume huyo alijibanza aidha kwenye jengo ama beneti na mtu mwingine, Rajul akaendelea kusonga mbele.
Alisonga hatua kadhaa, alipowadia kwenye kona ambayo aliikata ghafula akitizama nyuma, alimuona mwanaume yule anayemfuatilia. Hakujali sana. Alipuuzia akaendelea na safari yake. Ila alipata hofu zaidi pale alipokata kona mbili na zote akimuona mwanaume huyo nyuma yake akiigiza anafanya shughuli fulani kana kwamba hana muda naye.
Rajul aliongeza mwendo maradufu. Asifike mbali, akakabwa katikati ya kichochoro alichojaribu kukatiza awahi aelekeapo. Mwanaume yule mwenye nywele singa alitokea mbele yake akamziba pumzi na kitambaa.
Gari dogo aina ya Volkswagen lilijiri haraka, mwanaume yule mwenye nywele za singa akambeba Rajul na kumwagia ndani ya gari hilo. Wakatokomea.
***
Bakari alitandaza ramani ya Dar es Salaam juu ya meza akanyooshea kidole sehemu palipotiwa alama nyekundu, akasema:
“Boti ipo Whitesands hotel.” Alisema kwa uhakika akiwatizama wenzake. “Kwa mujibu wa tracker ya kampuni, boti ipo hapo, ila hatujajua haswa wahusika watakuwa eneo gani.”
“Twende!” Vitalis alitoa agizo.
Akiwa ameongozana na Jombi na Kaguta walielekea kwenye boti ndogo iliyokuwa imepaki baharini. Vitalis aliwasha mashine ya boti wakaanza safari kwa mwendo wa kasi.
Walikata mawimbi mithili ya papa upepo ukiwapuliza zaidi ya viyoyozi.
Bakari akitumia tanakilishi yake alikuwa anawaona kwenye ramani kwa mtindo wa kidoti cha bluu kilichokuwa kinasonga kwa kasi kuitafuta Whitesands hotel. Alitumia radio call kuwaelekeza upande upi waelekee, nao wakafuata.
Walipoitia machoni Whitesands hotel, mafuta yalikwisha kwenye boti. Kwa mahesabu ya haraka haraka bado walikuwa wana kama kilomita moja na nusu kuingia eneo la Whitesands hotel. Walitumia mikono yao kama mapakuo wakapakua maji mpaka ufukweni walipoificha boti yao kisha wakabadili nguo wakivalia za kuogelea.
Vitalis aliwasiliana na Bakari kupata taarifa zaidi juu ya eneo walilopo na wanapoelekea. Alipopata taarifa za kukidhi haja aliacha hapo redio call kwenye boti wakaanza kutembea kwa miguu kuifuata hotel.
Walipokaribia kwakuwa hawakuwa na tiketi wala kuponi ya kuingilia ndani ilibidi watumie njia mbadala, waliogelea wakaibukia ndani ya eneo la bahari ya hotel wakachangamana na wateja.
Kama samaki walizamia wakitumia vema pumzi zao zilizojaza vifua. Hakuna aliyechomoza kichwa nje ya maji mpaka pale walipoibuka. Hapo taratibu wakaanza kujongea kuifuata fukwe. Hawakusahau kuhakikisha macho yao yanatizama usalama kwa kuwaweka karibu walinzi na macho yao.
Walipokanyaga fukwe, Vitalis alijigawa akamfuata mlinzi mmojawapo aliyemtambua kwa sare yake. Akamuuliza akinyooshea kidole boti iliyoegeshwa kwa mbali kidogo.
"Ile boti ni ya nani, afande?" Aliongea kwa lafudhi ya kiswahili cha Kenya.
Mlinzi alitizama kule alipoelekezwa akauliza:
"Kwani kuna nini?"
"Naihitaji nikodishe!" Vitalis alijibu.
***
Mwanaume mmoja akiwa kifua wazi, amevalia tu bukta alitoka eneo la wazi la la bahari akitembea kuelekea ndani ya jengo la hoteli ya Whitesands.
Mgongoni mwake alikuwa ana mchoro mkubwa wa kichwa cha simba. Kichwa chake hakikuwa na nywele. Mwili wake ulijaza vya kutosha kufanywa mlinzi. Alikuwa mrefu akitembea kwa kudunda mithili ya kitenesi.
Alikata korido akinywa kinywaji chake cha kopo taratibu mpaka pale alipowadia mbele ya mlango uliopachikwa namba 609. Hapo akagonga mlango mara tatu.
Mwanaume aliyekuwa ndani alichungulia kwenye kitundu kilichokuwepo mlangoni kwanza kabla hajaufungua mlango. Aliporidhika na alichokiona aliufungua mlango kisha akasimama kando kumngoja mwenzake aingie.
Ajabu akashangaa kuona mwili wa mwenzake huyo unadondokea ndani kama zigo. Kufumba na kufumbua akaingia Vitalis. Mwanaume yule aliyekuwepo ndani asipate hata nafasi ya kufanya kitu, haraka kama mwanga wa radi alikitwa teke la shingo akarushwa mbali.
Alidondokea kwenye meza ya kioo akaivunja vipande milioni.
Alijifyatua na mikono yake akasimama tena wima. Aliruka hewani akituma teke lakini lilidakwa na mkono wa kuume wa Vitalis kisha akarushwa akibamiziwa ukutani.
Asikome, alinyanyuka tena akiwa anavuja damu puani akakunja ngumi.
Mara hii Vitalis alihakikisha mwanaume huyo hasimami tena kwa kumpachika teke ubavu wa uso akitumia mguu wa kushoto baada ya kumhadaa kama vile anatumia mguu wa kulia.
Mwanaume huyo alidondoka chini akicheua damu. Alirembua macho akiachama mdomo. Alionekana tayari amekubali sheria, hana madhara tena.
Vitalis alimsogelea karibu mwanaume huyo akamtizama. Mara mwanaume huyo akaupeleka mkono wake nyuma ya kiuno akatoa bunduki na kumnyooshea Vitalis.
Alitabasamu kujipongeza. Alijua sasa anamaliza habari iliyoonekana awali kumshinda.
"Vitalis?"
Aliuliza mwanaume huyo.
Kabla Vitalis hajasema neno, mlio wa risasi ulivuma mara tatu mwanaume yule akitobolewa fuvu la kichwa. Risasi ilitoka kwa Kaguta ambaye alikuwa amesimama mlangoni.
"Mara ya pili hiyo!"
Kaguta alimwambia Vitalis akitabasamu kisha akaongezea:
"Tumeshawamaliza wote. Tunaweza tukaondoka sasa upesi kabla hayajageuka mengine."
"Hamna chochote mlichopata?"
"Kipo."
Kaguta alipomaliza kusema hilo, sauti ya king'ora ilianza kulia ndani ya hoteli. Miraji aliyekuwa amesimama nje ya mlango aliingia chumbani akawaambia:
"Tuondokeni haraka!"
Kaguta alisogelea dirisha la chumba akachungulia nje. Aliona walinzi kadhaa wakijipanga na kuwatuliza wageni, aligeuka akawaambia wenzake:
"Hatuwezi tukatoka hapa kirahisi, watakagua kuponi kabla ya kumruhusu mtu atoke nje."
"Vipi na baharini?" Vitalis aliuliza.
"Hamna mtu baharini. Hatutaweza kutumia njia hiyo, tutakamatwa kiurahisi!"
"Kwahiyo?" Miraji aliuliza.
"Inabidi tuunde tukio!" Kaguta alijibu. "Tukio litakalotufanya tuondoke kwa urahisi!"
Dakika tano tu kupita baada ya hiyo kauli, moto ulizuka hotelini. Hapo sasa vurugu ikawa kubwa. Watu ambao walikuwa wamejifungia ndani ya vyumba vyao waliposikia habari za moto, walizuka wakakimbia kama wehu.
Katikati ya watu hao walojichopeka wakina Vitalis wakatoka getini kiurahisi. Nani angekagua kuponi ilhali watu wanakimbia huku na huko kuokoa roho zao?
***
Taa iliwashwa kummulika Rajul aliyeketi kwenye kiti akiwa amefungwa kamba nzito. Alifichama macho yake kwa mwanga huo mkali akitizama pembeni. Alitulia kwa sekunde tano asisikie majibu, akauliza:
"wewe nani ... unataka nini kwangu?"
Kimya.
Alisikia vishindo vya miguu vikimsogelea na mara taa zikawashwa. Alijaribu kufungua macho yake kutizama lakini mwanga mkali wa taa ulimuumiza. Alifunga na kufungua macho taratibu taratibu mpaka pale yalipozoea mwanga.
Hapo ndio akaona watu nane wamemzunguka. Wote walikuwa wamenyoa vipara kama yeye, wakivalia nguo ambazo na yeye huvaa na pia shingoni wakibebelea cheni za madunguli makubwa ya mbao.
Utofauti ni kwamba yeye alivalia nguo nyeupe wakati wenzake wakivalia nguo rangi za kahawia na michoro yao kichwani haikuwa zigzag bali iliyonyooka ikikomea utosini na nukta nyekundu.
"Rajul, umepungukiwa imani na hekima kiasi hiki?" Sauti moja ilisikika ikiuliza. Haikujulikana ilitokea wapi mpaka pale mzee mmoja mwenye asili ya India alipotokezea nyuma ya wale wengine nane. Alikuwa ni mzee mrefu mwenye ndevu nyingi nyeupe kama sufi.
"Kwanini umebadili adhma ya nguvu zako ukitekwa na tamaa za dunia dhalimu, katili na ovu?" Aliuliza yule mzee akijongea karibu zaidi.
"Unafahamu fika, malengo yetu ni kusaidia walio wanyonge, walio masikini, wasio na nguvu. Tulikula kiapo hiko nawe pia wajua tukiahidi kuacha maisha yote na anasa zake ili tukapande mbegu ambayo itazaa mema duniani. Umesahau kiapo kile?"
Rajul alitikisa kichwa akitizama chini.
"Umetusaliti. Umesaliti imani yako. Umesaliti kiapo chako. Umemsaliti muumba wako na tutamuachia yeye akuhukumu. Sisi si chochote mbele zake bali wanaohitaji msamaha na upendo wake."
Alihitimisha yule mzee. Rajul akapaza sauti:
"Naomba nitizamwe kwa jicho la huruma! ... mtamuacha kondoo huyu aliyepotea ingali maisha yake yote tokea ujana alimtumikia Mungu wake kwa nia ya dhati?"
Aliwatizama waliomzunguka akiendelea kuongea.
"Mimi naliumbwa na damu na nyama. Ni binadamu. Natenda makosa. Napitiwa. Naomba nipewe nafasi nyingine ya kufuta makosa yangu. Najutia nilichokifanya."
"Rajul!" Mzee aliita. "Hakuna msamaha kwa mtu anayekiuka kiapo chake. Uliweka maagano na Mungu wako, na umeyavunja maagano hayo ukiwa na akili zako timamu. Ulituficha sisi binadamu, hukujua Mungu anaona kila sehemu, kila eneo, kila tukio na kila mtu. Hatuna la kusema wala kuamua juu yako, bali Mungu pekee. Tunatimiza yale uliyoyaingia maagano."
Alisema mzee yule kisha akawatizama wanaume waliokuwepo pale na kuwapa amri:
"Mpelekeni anapostahili. Hakikisheni anapata anayostahili."
Baada ya maneno hayo mzee akaondoka. Rajul alifunguliwa kamba akabebwa akipiga makelele ya kuomba msamaha.
****
Hamilton, Bermuda.
Mawimbi ya bahari yalichapa fukwe taratibu yakisukumwa na upepo.
Siku hiyo maji yalikuwa machache, kwa kuyatizama tu ungaligundua hilo. Yalisonga mbali tofauti na kawaida yake. Hiyo ikawa fursa nzuri kwa watoto kuchezea maji na hata pia kwa watu kutembea tembea fukweni wakanyage mchanga ambao huwa unamezwa na maji mara nyingi.
Miongoni mwa watu hao, alikuwapo Stanis. Suruali yake ya jeans aliyoivaa aliikunja vema mpaka magotini akivalia shati jeupe jepesi lililokuwa linapeperushwa na upepo wa bahari.
Asionekane na furaha aliranda randa huku na kule akiyapiga maji teke. Ila mara kadhaa alitizama kushoto na kulia kama anatafuta kitu kisha akaendelea na shughuli yake ya kuzurura.
Baada ya dakika kama nne mbele simu yake ilitetemeka mfukoni. Aliitoa akaitizama. Alitabasamu akajongea kutoka eneo la bahari akielekea upande wake wa kushoto.
Huko akakutana na mwanaume chotara ya mweupe na mweusi mwenye nywele ndefu nyeusi ti. Walikumbatiana wakasonga mbali zaidi wakiteta;
"Yuko wapi Fraud?" Stanis aliuliza.
"Wote wameshafika, wanakungoja." Alijibu mwanaume yule mwenye nywele ndefu, Gog.
Walifika mahali fulani palipoezekwa makuti mepesi, wakajumuika na wanaume wengine watatu, jumla wakawa watano: Stanis, Gog,Fraud, Nun na Adrian.
Baada ya kutizama kushoto na kulia, Stanis akasema:
"Nimewaita hapa kwasababu najua ninyi ni marafiki zangu, watu wangu ninaowaamini, na ninatumai hamtoniangusha kamwe."
Alitizama tena kushoto na kulia kisha akaendelea:
"Bila shaka wote mnakumbuka jinsi nilivyowaunganisha kwa Kim baada ya kuhangaika sana. Nisingependa tujadili sana mambo ya nyuma, ila nadhani sasa ni muda wa kunigawia kidogo fadhila. Si tu kwasababu ya urafiki, bali pia fadhila hiyo yenu itawarejeshea fadhila kubwa sana."
"Kipi unataka tufanye Stanis?" Nun aliuliza wakimkodolea macho Stanis kwa makini.
"Nataka tuchukue huu ufalme!" Stanis alisema akitumbua macho.
"Nataka tuukwapue, tuuweke mikononi mwetu!"
"Kivipi?" Fraud aliuliza na kuongezea, "Sidhani kama hilo jambo ni rahisi hivyo."
"Si rahisi ila inawezekana!" Stanis alijibu kimkazo. Akaongezea:
"Nina mipango yote. Kila kitu nimeshakianisha, ni utekelezaji tu ndio unaotakiwa."
Akanyamaza akiwatizama wenzake kwa macho ya ufahamu.
"Nani atakuwa na mimi?" Aliuliza.
"Tupo pamoja." Gog akajibu akitikisa kichwa.
"Na mimi pia." Fraud akadakia akimaliziwa na wengine wawili.
Stanis akatabasamu.
"Ahsanteni sana." Alisema kisha akachuchumaa chini, akachora ardhi na kidole.
"Tizameni hapa mniambie ..."
***
Hakukuwa salama tena kisiwani. Boti ilishatua karibu na fukwe Vitalis na wenzake wakijipakia wapate kuyeya.
Walifanya hivyo baada ya kutoa heshima zao za mwisho kwenye makaburi ya wenzao waliotangulia mbele za haki. Baada ya kila mmoja kusali kwa imani yake, walibeba walichokiona cha muhimu wakatia moto boti mpaka walipokutana na kisiwa ambacho hata jina hawakukifahamu.
Hakikuwa kikubwa kama cha hapo mwanzo. Kilifungwa na misitu mingi kikitengeneza giza hata wakati wa mchana.
Kwa kutizama haraka haraka, hakukuwepo na dalili yoyote ya viumbe kuishi hapo. Palikuwa kimya, kimya mno. Hata milio ya ndege haikuwepo. Labda tu sauti ya mawimbi yakichapa fukwe.
Kabla basi ya jua kuzama, wanaume wakachakarika kukata miti, kusafisha vichaka watengeneze mahali pa kupumzikia.
Kwa ugumu wa kazi, mpaka jua lazama hawakuwa wamefanikiwa. Ila walipiga angalau hatua. Walishapata eneo safi ambalo walichopeka mistimu ya miti hapo na paa la majani majani kuvutia muda.
Kupambana na giza na ubaridi wakawasha moto wakiketi kwa kuuzunguka.
"Nini kinachofuata sasa?" Sandra aliuliza. Kana kwamba wamepanga, wote wakajikuta wakimtazama Vitalis.
"Kuna wengine wapo nchini, itabidi tuwamalize mapema. Bahati nzuri kwa upatikanaji wa simu ya mmojawao kutatusaidia kuwatambua wapi walipo. Hatuna muda mwingi, lakini pia hatupo mbali sana na mkuu wao, Kim." Alisema Vitalis. Akaendelea kuhutubia:
"Tumepewa sababu nyingine ya kupambana - kuwapumzisha wenzetu mahali salama. Kama tusipofanikiwa basi hawatokuwa na amani huko walipo. Tumebakiza michoro miwili tu, mmoja kati yao tumeshaanza kuhangaika nao. Hatutakiwi kuchoka bali kuongeza nguvu zaidi. Tuwe waangalifu sana tunapotoka nje ya hili eneo kwasababu yoyote ile, iwe ni kwaajili ya kufuata vifaa vyetu vya umeme ama kufuata mahitaji. Keshokutwa tutatoka huku mafichoni twende bara. Na hatutorudi mpaka pale tutakapohakikisha hakuna yeyote kati yao anayevuta pumzi tena.
"Kwanini keshokutwa si kesho?" Bernadetha aliuliza.
"Kwasababu kesho tuna kazi kubwa ya kufanya hapa." Kaguta alimsaidia Vitalis kujibu kisha akaongeza:
"Vipi tukienda huko bara, tutapata vinywaji? Nina kiu sana aisee! Sijaonja kitambo."
Sandra akamzaba Kaguta kofi dogo mgongoni.
"Umeanza. Hakuna kunywa tena!"
"Kidogo tu nisafishe koo." Kaguta alijitetea wakaendelea kuzozana na Sandra kiutani.
Giza lilisonga mwishowe wakapitiwa na usingizi. Moto ulivuma mpaka ukatika pakawa giza kamili ambalo lilishinda mwanga wa mwezi kwa kishindo kikuu.
Masaa matano mbele wote wakiwa wamedidimia ndani ya usingizi mzito, wanaume wasiopungua kumi na mbili wakiwa vifua wazi, wamebebelea mishale, mikuki na mapanga, waliwazingira katika hali ambayo hakuna sauti yoyote ilisikika – kama mizuka.
Wanaume hao walikuwa wamejichora chora michoro ya ajabu miilini mwao. Si kaptula wala suruali walivaa, bali ngozi zilizofungiwa vema viunoni mwao vipate kuwasitiri nyeti. Miguuni walikuwa peku. Kwenye mapaja ya mikono yao ya kushoto walifunga kamba isipokuwa mwanaume mmoja tu ambaye yeye pekee ndiye aliyevalia kofia kubwa la manyoya kichwani, shingoni akivalia cheni ya mifupa.
Mwanaume huyo alikuwa ana macho makubwa meupe yaliyokodoa. Aliwatizama wenzake akapandisha kichwa, wote wakasogea zaidi wakinyanyua mikono yao kana kwamba wanataka sasa kushambulia ndani muda mfupi ujao. Kabla hawajatimiza adhma, Vitalis alishituka usingizini mithili ya mtu aliyeona mzimu.
Alihema kama mbwa mwitu akitizama pande zake zote pasipo kuona kitu. Hakukuwa na lolote isipokuwa giza tu. Hakutosheka, alinyanyuka akatembea hatua kadhaa kila upande kabla hajarudi alipokuwa ameketi na kuanza kupekenyua mkoba mmoja uliokuwa kando, akatoa sindano.
Alishusha pumzi ndefu. Alipapasa papasa mkono wake wa kulia maeneo ya mkunjo akitafuta mshipa wa damu, taratibu akapeleka hapo sindano na kujidunga kwa uangalifu mkubwa wa vidole vyake kwenye uhakiki.
Alirudisha sindano mkobani, akajaribu kujilaza tena. Isichukue muda mrefu, akasikia sauti ya majani yakimwendo. Alikaa kitako akatizama tizama, mwishowe alipuuzia akaacha usingizi umbebe.
Watu wale waliokuwa wanataka kuvamia walikaa umbali wa mita kadhaa wakitizama yote anayofanya Vitalis. Japokuwa kulikuwa na giza totoro, kwao haikuonekana shida, walimuona vema Vitalis akihangaika hangaika mpaka pale alipoamua kujilaza.
Mwanaume yule mwenye shungi la manyoya alipiga kamluzi kadogo, wote wakaondoka eneo hilo wasijulikane hata wapi walielekea.
Masaa yalisonga, jua likachomoza. Kaguta alikuwa wa kwanza kuamka kabla ya yeyote. Alijikongoja akaenda baharini kupata maji, baada ya muda mfupi aliungana na Bakari na Miraji majini. Sandra naye na Bernadetha wasichukue muda wakaamka wakatengenezea kuni na kuwasha moto kwa ajili ya kuandaa chai. Muda wote huo, Vitalis alikuwa bado yu usingizini. Tena si usingizi mwepesi, bali ule wa kukoroma hoi bin taabani.
Sandra alimtizama Vitalis akamwambia Sandra:
“Sandra, unadhani ni kawaida?”
“Nini?” Sandra alijibu kwa kuuliza.
“Vitalis kulala mpaka saa hizi wakati yeye ndiyo huwa wa kwanza kuamka kila siku?”
“Labda kachoka. Kazi ya jana ilikuwa pevu.”
“Sidhani. Mbona wenzake wamekwisha amka? … huwa ikifika saa kumi na moja tu, Vitalis anaamka. Haijalishi amefanya kitu gani jana yake.”
“Kwahiyo wewe unahisi nini?”
Bernadetha alirusha macho yake vema akaona mkoba mmoja uliokuwa karibu na Vitalis ukiwa wazi. Alinyanyuka upesi akafuata mkoba huo alioutwaa na kutizama ndani. Akaona sindano tupu.
“Nilijua tu.” Alijisemea mwenyewe. Alichuchumaa akapachika kiganja chake kwenye paji la uso la Vitalis.
“Mmmh … wa moto.” Akasema tena. Alimtizama Vitalis kwa macho ya huruma, akatikisa kichwa.
“Nini kimetokea Vitalis? …” Alinong’oneza. Mara Vitalis akakurupuka. Bernadetha alimshika mabega akimtuliza.
“Tulia Vitalis … tulia, tupo hapa. Tupo wote.”
Vitalis alishusha pumzi akatizama chini. Bernadetha akamuuliza:
“Imekurudia jana, sio?”
Vitalis akatikisa kichwa kukubali.
“Ulijis’kiaje?”
“Nilihisi kuna watu wamekuja kutuvamia … nilisikia sauti za ajabu na vishindo vyao vikisogea tokea mbali. Nilipoamka sikukuta yeyote. Ila bado nilikuwa nasikia sauti … sauti kana kwamba wanatembea.”
“Haukuwaona kabisa?”
“Sikuwaona! Labda kwasababu sikugeuka mnyama kabisa. Niliwahi kujidunga sindano ndipo nikapata ahueni. Nikalala.”
“Pole sana. Ila upo sawa sasa.”
Alisema Bernadetha kwa tabasamu la matumaini. Vitalis alishika kichwa akalalama:
“Kichwa kinanipasua.”
Bernadetha akamlaza akimwambia:
“Pumzika. Mwili wako umetoka kwenye kazi kubwa ya kurudi kwenye hali yake.”
Vitalis akajilaza tena.
Bernadetha alinyanyuka akamrudia Sandra. Alimueleza yale yote aliyoyasikia toka kwa Vitalis, na kipindi wanapata chai akawaeleza na wanaume: Kaguta, Bakari na Miraji juu ya habari hizo.
Walipomaliza kunywa chai, Kaguta aliwaaga anaelekea bara kuleta mahitaji yaliyopungua, akilenga kwenda mapema hiyo ili awahi kurudi waendeleze zoezi lao la ujenzi lililokomea jana. Bakari alimpatia Kaguta tanakilishi pamoja na simu akazitie moto huko penye umeme.
Kaguta aliwasha boti akaondoka zake, baada ya nusu saa akakanyaga ardhi ya jiji la Dar es Salaam. Alipeleka simu na tanakilishi sehemu za kutia moto kisha akaelekea maeneo ya soko la kariakoo ambapo ndipo anachukulia mahitaji yake.
Hakuwa na papara, kwakuwa alilazimika kungoja vifaa vile vya umeme alivyovipeleka vipate moto, basi akaamua kutafuta mahali atulizane kidogo akinywa vitu vyake.
Akielekea kwenye mgahawa mmoja hapo hapo maeneo ya Kariakoo, alikatiza eneo la magazeti aoshe macho kwa kufahamu yanayoendelea ulimwenguni. Hapo vichwa viwili vya magazeti vikamteka fahamu:
MAJAMBAZI YATOROKA KIJASUSI!
MAJAMBAZI WAUA MAGEREZA NA KUTOKOMEA!
Vichwa hivyo vya habari viliambatana na picha kadhaa za gari la wafungwa likiwa lina matundu kadhaa ya risasi – damu zimetapakaa zikifanya barabara nyekundu ya bendera. Kando kando ya picha hizo, kulikuwepo na picha ndogo ya wanaume watatu, mmojawapo Alphonce Mwamtembo, almaarufu Mamba.
Kaguta alitoa pesa mfukoni akanunua magazeti hayo. Alipoenda mgahawani akawa anayapitia taratibu akishushia na Tusker baridi.
Habari ni kwamba wafungwa watatu wakiwa njiani kuhamishwa gereza baada ya kutokea kwa vurugu kubwa gereza walilokuwepo hapo awali, walifanikiwa kuwapiku maaskari baada ya gari hilo kuvamiwa ghafula pale liliposimama ili maaskari watoe magogo kadhaa yaliyotandikwa barabarani.
Watu nane wakibebelea bunduki ‘SMG’ walichomoza vichakani wakawateka maaskari waliokuwemo ndani ya basi la wafungwa na wale wasindikizaji walikuwemo ndani ya defender. Wakawalaza barabarani na kuwamiminia risasi kisha wakawafungua watuhumiwa na kutokomea.
Maelezo hayo yalikuwa ni kwa mujibu wa askari aliyenusurika kufa, akiachwa na majeraha makubwa mwilini.
Kaguta aliyaweka magazeti hayo chini akanywa fundo moja la bia yake kisha akasema:
“Karibu tena mtaani Mamba. Ni kifo tu kinakuita.”
***
Hamilton, Bermuda: Saa kumi jioni.
Kim akiwa ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka, anaenda kushoto na kulia, aliwatizama wanaume wake wa kazi watano, wale ambao walinyweshwa damu ya mfalme wakiwa wamesimama kwa ukakamavu wanamtizama kwa makini, akatekenya ndevu zake za kidevuni akisema:
“Kwa siku tatu sasa namtafuta pasipo majibu. Kama mnavyojua, bado kuna kazi yangu ndogo sijamaliza naye alafu nimpotezee mbali. Nashindwa kuelewa wapi alipo na anafanya nini. Nataka mumtafute popote alipo, mji mdogo huu. Namuhitaji hapa kabla jua la kesho halijakucha. Mnaweza mkaenda.”
Waliitikia kwa kuinamisha vichwa vyao kisha wakashika njia kwenda nje. Kabla hawajatoka mlangoni, Kim aliita akauliza:
"Mmemuona Stanis leo?"
Walitazamana wakakanusha. Kim akawaruhusu waende.
Baada ya dakika ishirini wanaume hao wa kazi wakafika mbele ya tempo kubwa lenye rangi nyeupe.
Hapo wakaangaza angaza macho yao kabla ya mwanaume mmoja akivalia joho hajaja na kuwauliza:
"Naweza nikawasaidia?"
"Tunamtaka Rajul." Akajibiwa kiufupi pasipo babaisho.
"Samahani, hamuwezi kumpata huyo mtu kwa sasa." Alisema mwanaume yule pasipo kupepesa macho.
Hakujua kauli hiyo ingekuwa ya mwisho kwake kabla hajaiaga dunia. Alijikuta hewani baada ya kutandikwa teke kali la kifua. Alipotua chini hakusema hata 'mama!' pumzi haikuwa yake tena. Alitawanywa mbavu, kifua kikatengeneza shimo.
Mara kengele ikalia keng! Keng! Keng! Keng! Keng! Mwanaume mmoja aliyekuwa ameketi juu ghorofani aliiliza kwanguvu. Ndani ya dakika chache wakajaa wanaume sio chini ya hamsini. Wote walikuwa wamevalia sare za majoho ya kaki, vichwa vyao vikiwa vitupu kwa ukosefu wa nywele.
Walitapakaa uwanjani wakiwatizama wageni wao walioleta shari.
"Tunamtaka Rajul! Tupatieni na hamtopata kadhia yoyote. Kinyume na hapo tutabadili majina yenu muitwe marehemu ndani ya dakika!" Alitishia mwanaume mmoja wa kazi. Akajibiwa na mwanaume mlinzi:
"Hakuna chochote mtakachopata hapa! Unadhani tunawahofia?"
Mwanaume yule wa kazi alitabasamu kwanza kisha akawatizama wenzake. Kufumba na kufumbua macho yao yalibadilika yakawa ya simba.
Walinguruma kama simba mwituni. Walinzi walitazamana kwa hofu lakini hawakwenda popote, walisimama palepale wakiwazuia wageni kusonga ndani.
Hiko kikawa kifo chao. Ndani ya dakika tano tu walitenguliwa, wakavunjwa na kuchanwa chanwa, wakaachwa kwenye dimbwi la damu.
Wanaume wa kazi waliingia ndani wakamsaka Rajul mpaka wakapata chumba alimofungiwa. Walivunja mlango kwa teke moja tu, wakamkuta muhindi huyo akiwa hoi bin taaban ameng'ang'aniwa na minyororo. Mwili wake ulikuwa mwekundu kwa kuvujia damu. Alikuwa ana mashimo mashimo mwili mzima kwa kunyofolewa nyofolewa nyama na tai kila siku baada ya kuchapwa mijeledi hamsini kama dozi.
Ilikuwa ngumu kumtambua mpaka pale alipoitika kwa taabu sana alipoitwa jina lake.
"Tumekuja kukuokoa."
"Hapana. Hapana ... naomba mniache. Nataka ... kutumikia adhabu yangu..."
"Mkuu ametuagiza tukupeleke."
"Mmmh mmh ... siwezi kwenda. Mimi na ... mimi na yeye ... hatuna ... cha kufanya."
Wanaume wale wa kazi walivunja minyororo na mikono yao, mmoja akambeba Rajul begani wakaondoka zao.
Majira ya saa nne usiku, pembezoni mwa bahari.
Stanis alichomoa sigara toka kwenye pakti, akaiwasha na kuiweka mdomoni. Alivuta mapafu matatu kabla hajawaona watu kadhaa wanakuja kwa mbali.
Watu hao waliposogea karibu alipata kuwahesabu na kugundua wapo kumi, akatabasamu. Alifahamu sasa kazi inaelekea kuwa nyepesi zaidi. Kwa watu wengi kama hao, hakuna kisiki kigumu.
Watu hao walikaribia, Gog akawatambulisha kwa Stanis kama wahusika wapya waliopendezwa na wazo lake la kuleta mabadiliko. Mmoja alisogea mbele akaongea kwa niaba:
"Tunatumai utafanya maisha yetu yawe bora zaidi kuliko afanyavyo Kim. Tumeamini hivyo na ndio maana tupo hapa."
Walipeana mkono na Stanis, Stanis akawapa pia neno lake:
"Naahidi hilo kwa moyo wangu wote. Ameshindwa kuthamini mchango wetu, basi hatuna budi kujilipa fadhila wenyewe..."
Akakatizwa:
"Unataka tufanye nini?" Mwanaume aliyeongea kwa niaba aliuliza.
Stanis akatabasamu kwanza.
"Nataka kuwapa kazi moja tu, vingine nitavimaliza mwenyewe."
“Kazi gani hiyo?”
“Msiwe na haraka. Ni moja ila kinataka uangalifu mkubwa sana. Endapo tukiwa na papara basi tutagundulikana na kuishia kwenye vitanzi.”
Wote walikaa kimya wakiskiza.
“Mbele yetu kuna mlima mmoja tu, kama tukiupanda huo basi kote ni tambarare. Mlima huo una vilele vitano, kila kilele kina ncha na baridi kali. Ila ndio njia yetu pekee. Lazima tuupande tuikute tambarare.”
“Sijaelewa, unamaanisha nini?” Mwanaume mmoja mgeni aliuliza.
“Namaanisha kwamba, ili tupate yale tunayoyahitaji basi lazima tuwamalize watu wale watano waliokunywa damu ya simba. Kim hana chochote wala lolote la kutuzuia, ni tambarare tu.”
“Kim ni tambarare?” Aliuliza tena mwanaume yule. Stanis akatikisa kichwa.
“Ndio, ni tambarare. Najua udhaifu wake upo wapi. Hana nguvu yeyote kama vile anavyotudanganya kila siku, hilo nina ushahidi nao wa kutosha. Juzi nilimsikia anaongea na wale watu wake aliowanywesha damu ya kwamba anangoja na yeye apate kutimizwa na mganga ili wawe familia kamili isiyozuilika. Ina mana Kim anapelea, kuna jambo bado hajatimizwa isipokuwa tu wale watano. Kwahiyo dhumuni letu ni kumshambulia haraka kabla hajaonana na Rajul.”
Fraud alikohoa kidogo, wote wakamtizama. Akasema:
“Kim atakuwa tayari ameonana na mganga wake. Leo nimeshuhudia akiletwa jengoni.”
Nun akadakia:
“Ila alikuwa na hali mbaya sana, hata kuongea shida. Sidhani kama watakuwa wamefanya lolote. Mwili wake wote umejaa majeraha na damu. Wanasema alikuwa matesoni huko walipomtoa.”
“Basi kesho itabidi tufanye tukio letu.” Stanis akapendekeza.
“Kazi yenu itakuwa moja tu ya kuwahadaa watu wale watano kwamba mmevamiwa. Mtafanya hayo kwa malengo ya kuwavutia ndani ya chumba cha mateso na kuwafungia humo. Tayari nimeshaandaa gesi ya sumu kwa ajili yao, mtapenyeza bomba chini ya mlango. Kwa dakika moja tu watakauka kama mabua. Mimi nitaenda kumalizana na Kim.”
Wakaridhia. Stanis akawageukia Gog, Nun, Fraud na Adrian.
“Nyie kazi yenu ni kukata viherehere wote wataokuwa kinyume na sisi. Hakikisheni hawaponi kwa njia yoyote ile.”
Nao wakaridhia.
“Tukutane kesho asubuhi ya saa kumi na mbili, hapahapa.” Stanis alitoa tamko, wakatawanyika kuondoka.
Juu ya meza ya Kim, ofisini, kifaa kimoja cha bluu mithili ya redio ndogo kilitoa sauti ya vishindo vya watu wakitembea. Baada ya muda sauti hizo zilififia, ikasikika sauti moja ikisema:
“Nadhani umesikia yote yaliyopangwa, mkuu.”
Kim akatikisa kichwa akisema:
“Nimeyasikia yote. Umefanya kazi njema, kapumzike sasa tukutane kesho.”
“Mamba yupo mtaani.” Vitalis alijikuta akitabasamu. Alirushia chini gazeti alilokuwa analisoma akitikisa kichwa.
“Ndio.” Kaguta alidakia, “Amerejea uwanjani, hatujui ni nini atakuwa amepanga kufanya sasa hivi.”
“Ila nani kamuokoa?” Bakari aliuliza. “Hawezi akajiokoa mwenyewe toka kwenye mikono ya polisi!”
Kaguta akaeleza: “Mpango wao huo ulisukwa vema tokea polisi kwenyewe. Kwanza, vurugu iliyotokea huko jela ilikuwa ni ya kupanga ili kufanikisha hili. Pili, baada ya hiyo vurugu na mpango huo wa kuhamishwa kufanikiwa, taarifa ikatolewa kwa hao waokozi juu ya wapi gari litaelekea, hivyo wakajipanga na kumuokoa mtu wao.”
“Lakini kwanini wameamua kumuokoa Mamba?” Miraji alistaajabu.
“Swali zuri sana, Miraji.” Vitalis akateka zamu. “Hawa watu waliobebelea mchoro wa simba migongoni mwao sio watu wa hapa nchini, unaweza ukaona hata makazi yao ni kwenye hoteli za kitalii. Ni wageni, hivyo wanatafuta mwenyeji anayeielewa vema ardhi hii. Kwao uchaguzi bora wa mwenyeji ukawa ndio huu, Mamba. Wanajua fika wakiwa na Mamba itakuwa rahisi kukamilisha misheni zao.”
“Kwa njia yoyote ile, Mamba na wenzake inabidi watawanyishwe haraka iwezekanavyo.” Kaguta alisisitiza. “Tukivuta tu muda zaidi, watafanya jambo ambalo litagharimu nchi nzima.”
“Ni kweli.” Vitalis aliridhia, akamgeukia Bakari. “Kuna vitu ambavyo Bakari amevipata toka kwenye ile simu tuliyoiopoa kule hotelini … Bakari, unaweza ukatushirikisha sasa.”
Bakari akatikisa kichwa kuafiki. Alivuta mkoba wake ulioketi pembeni akafungua na kuchoropoa tanakilishi. Aliingiza tena mfuko mkobani humo akatoa karatasi nyeupe iliyobebelea maandishi kadhaa. Alifungua tanakilishi hiyo akabofya baadhi ya vitufe akifuatisha namba fulani kwenye karatasi yake, baada ya muda kidogo akasema:
“Kuna mojawapo ya namba ambazo mwenye hii simu alikuwa anazoza nazo. Hiyo namba wakati natizama hapo awali … naona kwa sasa mtandao unasumbua sana … ilikuwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, karibu kabisa na Bahari Beach Resort.”
Bakari aliachana na namba hiyo akaenda kwenye maandishi mwengine karatasini.
“Lakini pia kwenye rekodi ya mawasiliano, nimekuta namba yenye ‘code’ 441. Namba hii ni ya nchini Bermuda. Nilipofuatilia zaidi kwa mujibu wa ujumbe, nikagundua ni namba ambayo ilipewa taarifa ya tukio lile la kuvamiwa. Zaidi kuna picha kadhaa ambazo mnaziweza mkaziona …”
Bakari aliwakabidhi wenzake simu wakawa wanatizama kwa zamu.
“Huyu ni mmojawao wa wale tuliowaua.” Vitalis alisema akioneshea kidole simuni. Mpaka zoezi hilo na kuonesheana picha linakoma, wanaume wote waliomalizwa Whitesands Hotel siku ile walionekana. Lakini pia na zaidi wakiwepo wanaume wanne ambao walikuwa wapya machoni.
“Hawa wanne ndio watakuwa wamehusika na kumuokoa Mamba.” Vitalis alisema kama mtu mwenye uhakika, kisha akamuuliza Bakari:
“Kuna lingine zaidi ya hayo?”
“Yapo, ila sidhani kama yanaendana na shughuli yetu.”
Kabla hawajafanya lolote zaidi ndani ya banda lao kubwa jipya lililoezekwa na kusukwa vema na majani ya minazi, papo hapo wakiwa kwenye viti vilivyoundwa kiustadi na miti mikavu na meza ndogo katikati, walisikia sauti ya mtu anayegugumia huko nje. Punde mlango ukafunguliwa akaingia Bernadetha akiwa kamshikilia Sandra anayetembea kwa kuchechemea.
Kaguta alinyanyuka upesi akawafuata wanawake hao na kumtwaa Sandra akimbebelea.
“Kuna nini?” Aliuliza.
“Amejichoma na mti huko porini tukitafuta kuni.” Bernadetha alijibu akifuata kiti na kuketi. Alikuwa anavuja jasho haswa.
“Amejichoma sana?” Bakari aliuliza.
“Kiasi chake.” Bernadetha akajibu kisha akamtizama Kaguta. “Mpeleke chumbani nakuja kumshughulikia.”
Kaguta akatii amri. Alichukua hatua kuelekea chumbani akirusha macho kwenye mguu wa kushoto wa Sandra unaochuruza damu.
****
Hamilton, Bermuda: Saa kumi na mbili asubuhi.
Stanis alitizama saa yake ya mkononi mara mbili kisha akatizama kushoto na kulia kwake. Ni kama vile abiria anayesubiria ‘treni’ la mwendo kasi akiwa anadhani aidha litakuwa limemuacha. Hakutulia.
Dakika kumi mbele akaungana na wanaume wanne: Gog, Fraud, Nun na Adrian. Bila ya kupoteza muda wakaanza kujongea kuelekea upande wao wa kaskazini.
“Wengine wapo wapi?”
“Wametangulia.” Fraud alijibu. “Tumeona kuongozana kwa wingi itapelekea kugundulikana kwa urahisi.”
“Ila hayo hayakuwa makubaliano yetu.” Stanis alitamba. “Sikupanga twende wote ila kuna baadhi tu ya mambo ningependelea kuyaweka sawa.”
“Kwani kutakuwa na shida yoyote kubwa kwa wao kutokuwepo hapa muda huu?” Gog aliuliza.
“Inaweza ikawepo, inategemea na huko tuendako.” Stanis akajibu.
“Ila sisi tupo, unaweza tu ukatujuza hayo mambo.” Gog alipendekeza. Stanis akatikisa kichwa chake.
“Tuachane nayo. Tuzingatie tu yale tuliyoyapanga awali.”
Walitembea kwa muda wa dakika ishirini kamili mpaka kufikia kwenye jengo lao la kazi. Palikuwa kimya na tulivu. Wakati wanaingia, Stanis aliwatizama wenzake na kuwapa ishara ya ngumi akinong’oneza:
“Kama tulivyokubaliana.”
Gog na wenzake wakamuacha Stanis aende mbele wakati wao wakijigawa kushoto na kulia kwenda kukutana na wengineo ambao walikuwapo kwenye mkutano siku iliyopita.
Stanis asiwe na hofu bali papara, akatembea akiwa amepachika macho yake kwenye mlango wa ofisi ya Kim. Hatua zake ndefu zilimuwia muda mfupi tu kumkutanisha na mlango huo ambao aliugonga kistaarabu, akatulia kusikiliza majibu.
“Ingia!”
Sauti toka ndani ikamkarimu. Alitabasamu kwanza kabla hajazungusha komeo na kuzama ndani alipomkuta Kim akiwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa akibembea kwa kwenda kushoto na kulia.
“Karibu, Stanis. Vipi mbona mapema hivi?” Kim aliuliza na uso wenye hamu ya kufahamu. Kabla Stanis hajajibu, Kim alidaka simu yake ya mezani akamuita mhudumu.
“Kuna jambo nimekuja kumalizana na wewe.” Stanis aligamba.
“Jambo lipi tena hilo? Kuna lolote jipya?” Kim aliuliza.
Kabla Stanis hajajibu, mhudumu akaingia ndani akibebelea vikombe viwili ya kahawa. Alivisambaza vikombe hivyo kisha akaondoka zake.
“Fukuza uchovu na kahawa, Stanis.” Kim alimkaribisha mgeni wake baada ya kunywa mafundo mawili.
Stanis akanyanyua kikombe apeleke kinywani, ila alipofikisha nusu safari akashindwa. Alisikia maumivu makali ya kichwa akarejesha kikombe mezani.
“Vipi, kuna tatizo?” Kim aliuliza akitabasamu.
Stanis alinyanyua mkono wake akitaka kumkamata Kim, lakini zoezi lake hilo likashindikana haraka. Kichwa kilimgonga mithili ya nyundo akabaki akilaumu huku akipapasa papasa kichwa chake mithili ya mama kipofu anayejitahidi kumgundua mwanaye kwa kutumia viganja.
Kadiri muda ulivyozidi kusogea, maumivu yakazidi.
“Stanis … Stanis … Stanis. Unadhani ni rahisi kiasi hiko? Yani ulale tu na kuamka utake kunipindua? Unajua ni kwa nguvu gani nilitumia kujenga hiki unachokiona sasa? Unajua imenigharimu kiasi gani kuwepo hapa? … Hakika nakwambia, njia zangu si rahisi hivyo. Kiatu changu ukitumbukiza mguu basi hautoweza kuunyanyua.”
Maneno hayo yalikuwa kama mwangwi kwenye masikio ya Stanis, aliyasikia yakijirudufu kana kwamba yumo ndani ya chungu. Hata macho yake sasa hayakuona vema, yalimuona Kim wakiwa wanne tena akielea elea kama mtu anayeogelea.
“Nini kinatokea?” Stanis alijiuliza akitetema maneno kama ‘teja’.
“Unasema?” Kim aliuliza akijinywea kahawa.
“Nini … nini kinan’tokea mwilin … mwangu.” Stanis aliongea kwa shida. Si kichwa kilikuwa kinauma sasa bali kilikuwa kizito kama vile amebebelea kichwa cha gari moshi.
“Pole sana. Ulikosea. Kaa ukijua siku zote waweke marafiki zako karibu, ila maadui zako karibu zaidi. Nilitambua wewe ni adui yangu tokea siku ya kwanza ulipokuja ofisini kwangu kulaumu. Niliona ndani ya macho yako ari na matamanio makubwa, hivyo nikakuweka karibu zaidi nijue kila unalofanya, kila ulipo. Hatimaye kama unavyoona, nimefanikiwa.”
Kim alikunywa fundo moja la kahawa kisha akanyanyua mkonga wa simu yake na kupiga simu, punde Fraud na Gog wakaja ofisini.
“Mpelekeni anapostahili. Nina maongezi naye baadae.”
Fraud na Gog wakambeba Stanis kwa kumburuza mpaka kwenye chumba kimoja kilichojitenga kikitawaliwa na giza totoro. Humo wakamrushia Stanis na kuufunga mlango.
***
Masaa kadhaa huko nyuma …
“Nimekuja kukufikishia habari kama ulivyoniagiza, mkuu. Leo pia anataka tukutane naye.” Gog alisema kwa kujiamini akimtizama Kim.
“Unataka tufanye nini? Sema nasi tutafanya … tummalize?” Fraud aliuliza. Kim akatikisa kichwa.
Aliwatizama kwanza wanaume wake wa kazi, Gog na Fraud kisha akasema:
“Hapana. Nataka nimmalize kwa mikono yangu mwenyewe. Fanyeni kama aliyowaagiza, ila hakikisha na mimi nasikia kila kitu kwenye hayo maongezi.”
Kim alifungua droo akatoa kifaa kidogo rangi ya zambarau akamkabidhi Gog. Gog na mwenzake wakanyanyuka na kuaga. Nje wakakutana na Nun na Adrian walioongozana nao mpaka kwa wenzao wengine walioongea nao kwa dakika kadhaa kabla ya kukubaliana jambo kwa kutikisa vichwa vyao na kupeana mikono.
Baadae jua lilipozama na hata kusahau lilipotokea, wanaume hao wakaongozana kwenda kukutana na Stanis maeneo ya ufukweni. Hapo wakati wote wakiwa wanalonga, Kim akawa anasikia kila jambo kwa kifaache.
Stanis asiwe na hili wala lile, aliagana na wenzake akaenda. Wenzake walizunguka nyuma na kukutana. Gog akawasiliana na Kim.
“Nadhani umesikia yote yaliyopangwa, mkuu.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimeyasikia yote. Umefanya kazi njema, kapumzike sasa tukutane kesho.”
“Sawa, mkuu. Ila unaonaje tukarahisisha kazi zaidi?” Aliuliza Gog kabla hajamuelewesha Kim nini wamedhamiria kufanya.
Baada ya maongezi hayo, Gog alimteua Fraud kwa ajili ya kazi ya ziada. Alimpatia chupa kubwa ya kijani akisema:
“Hakikisha anakuwa salama. Ulisikia mkuu anataka ammalize kwa mkono wake mwenyewe.”
Wakati wenzake wanaelekea kwenye makazi yao, Fraud akashika njia kwenda kwa Stanis. Kwa kunyata na kwa uangalifu mkubwa alifuata dirisha la chumba alalacho Stanis akapulizia dawa humo taratibu akiwa amejifunga kitambaa kuziba mdomo na pua.
****
“Mwili wake unachemka sana. Hajisikii kula wala kunywa chochote. Kama kuna uwezekano, apelekwe hospitali.” Bernadetha alishauri akiwatizama wanaume waliomzingira.
“Yote haya ni kwasababu ya kujichoma na mti?” Kaguta aliuliza.
“Ni ajabu lakini kweli.” Bernadetha akajibu. “Hakuwa hivi kabisa kabla ya hiyo ajali … embu tizameni hapa …”
Bernadetha alifungua jeraha la Sandra akawaonyeshea wanaume. Jeraha lilikuwa limezungukwa na rangi ya kijani. Hata damu iliyokuwa imetapakaa kwenye bandeji hiyo nyepesi iliyofunga jeraha ilikuwa ni ya kijani.
“Kuna mtu yeyote aliyewahi kuona kitu cha aina hii?” Bernadetha aliuliza. Wote wakatikisa vichwa vyao – kilikuwa ni kitu kigeni machoni.
“Unadhani inaweza ikawa ni nini?” Vitalis aliuliza.
“Itakuwa alikanyaga mti wa sumu.” Miraji akadakia. “Kuna aina ya mimea yenye sumu, ila inatofautiana kwenye utapakaaji wake mtini na madhara yake mwilini. Kuna baadhi ya miti matunda yake yana sumu, mengine mbegu, mengine mizizi, na mengine kila kitu kinakuwa na sumu mfano mti wa ‘manchineel’. Tunda lake tu laweza kuua watu wazima ishirini, au endapo tu mtu atakapogusana na unyevu au maji tu ya mvua yaliyogusa mti huo, atapata malengelenge makali papo. Sasa hatujajua atakuwa amekanyaga mti wa aina gani.”
“Sasa tunafanyaje?” Bakari aliuliza. “Tumpeleke hospitali?”
“Sidhani kama hilo la hospitali ni jema kwa sasa.” Alisema Vitalis akitizama saa yake ya mkononi. “ Sasa hivi ni saa tano kasoro usiku na kama tunavyojua njia yetu ni kwenye maji, inaweza ikawa hatari zaidi. Tumpe tu huduma tunayoweza alafu asubuhi na mapema tudamkie hospitali.”
Baada ya mabishano madogo wakakubaliana juu ya hilo. Walizima moto waliokuwa wanautumia kama taa ndani ya banda lao kisha wakajilaza tayari kwa ajili ya kuvuta pumzi na nguvu za kutosha kwa siku inayofuata ambayo ilionekana itakuwa ndefu sana kwa majukumu.
Katikati ya usiku huo mpevu, watu wa ajabu, wakiwa wamevalia ngozi zilizositiri sehemu zao za siri tu, walikuja na kuzingira makazi ya ‘wageni’. Watu hao walikuwa ni wale waliokuja siku moja nyuma. Walikuwa wamejichora chora mwilini. Mikononi mwao walibebelea mikuki, marungu na mishale. Kwa idadi walikuwa wanaume mia moja.
Mwanaume aliyevalia kishungi cha manyoya kichwani, alisogea mbele zaidi akikodoa macho kana kwamba anatafuta funguo gizani. Alitizama kushoto na kulia kwake akaupeleka mkono wake wa kushoto nyuma ya kiuno na kutoa kibuyu kidogo.
Alikitizama kibuyu hiko kama vile anatafuta jambo la kukosoa. Kisha akakitikisa na kumkabidhi mmojawao ambaye alizunguka makazi ya ‘wageni’ akinyunyuzia yaliyotoka kibuyuni. Alipozunguka mara tatu alirejesha kibuyu kwa aliyempa naye akakirudisha nyuma ya kiunoche kisha akaelekezea kichwa chake kwenye makazi yale. Wanaume kumi wakafuata makazi ya wageni na kutoka na wote waliokuwemo ndani kisha hao wakatokomea nao msituni wakiimba nyimbo za ajabu wakicheza na kuruka kwa furaha.
****
Hamilton, Bermuda.
Mlango wa chumba hicho kilichokuwa giza totoro kilifunguliwa na kuruhusu angalau mwanga upenye na kummulika Stanis aliyelala chini kama goigoi.
Kim akiongozana na wanaume watatu, miongoni mwa wale waliokunywa damu ya Sultan, alisogea karibu kabisa na Stanis akachuchumaa. Mwanga uliongia tokea mlangoni ulimfanya amuone Stanis vema, huku Stanis akibughudhiwa na ukali wa mwanga huo mgeni machoni, akajitahidi kuukinga na mkono yake.
“Unaendeleaje Stanis?” Kim alichombeza kwa kebehi.
Stanis alisogeza pembeni mkono wake umkingao na mwanga akajitahidi kumtazama Kim.
“Unajulia hali yangu yanini? Niue upate kuridhika!” Alisema kwa jazba. Kim akatabasamu.
“Tatizo siwezi kukuua haraka haraka hivyo. Nataka nitengeneze somo zuri sana kwa wenzako wote wajue ya kwamba kunisaliti mimi si kitu wanachotakiwa kukiota kamwe. Nitakutengenezea ratiba nzuri sana ya mateso ya kila siku washuhudie …. Washuhudie jinsi mwili wako unavyovuja damu, jinsi unavyolia kwa uchungu na kumwaga machozi … washuhudie jinsi ilivyo chungu njia ya kwenda kombo na mimi. Nataka kifo kiwe kitu cha mwisho kabisa kwako baada ya kupata kila aina ya maumivu ninayoyataka. Baada ya hapo nitakutupa uliwe na mbwa wangu kama chakula cha mchana.”
Baada ya kusema hayo Kim alisimama akawatizama wanaume wale wa kazi aliokuja nao. Wanaume hao wakasogea na kumnyanyua Stanis, wakambeba na kumpeleka upande wa nyuma wa jengo lao kubwa. Huko wakamfungia kwenye mstimu mkubwa mweusi kisha akaadhibiwa kwa kutandikwa mijeledi ya nguvu iliyotumwa vema na mwanaume mmoja wa kazi.
Wakati hayo yanajiri, wafuasi wote wa Kim, pamoja na yeye mwenyewe, walikuwa wanashuhudia.
Macho yao yaliona damu zinavyoruka kwa hasira toka mgongoni mwa Stanis. Masikio yao yalisikia vema jinsi mwanaume huyo anavyolia kwa uchungu kana kwamba mtoto. Mgongo wake wote uliharibiwa ukawa mwekundu kwa majeraha yanayomwaga damu kwa mashindano.
Hakuachwa kutandikwa, mpaka pale alipopoteza fahamu kwa kushindwa kuhimili maumivu anayoyapata. Hapo ndio Kim akasimama na wote wakahamishia macho kwake.
“Hakuna jambo linalofanywa kwa bahati mbaya ulimwenguni hapa. Kila jambo lina sababu na msukumo wake … kama pia mnavyoliona hili lililotukia mbele yenu.”
Kim aliweka kituo akiwatizama wafuasi wake kwa macho makali na uso uliokunjamana. Akaendelea kulonga:
“Wote mnajua ni wapi nilipowatoa … jinsi mlivyokuja kwangu na nikawapokea kwa mikono yangu miwili tukiapa kutunzana na kamwe kutosalitiana. Je, kinatokea nini pale mmoja wetu anaposaliti maagano?”
“Kifo!” Wote wakajibu.
Kim akatikisa kichwa chake kuafiki.
“Kifo! … ndio, ni kifo. Na hicho ndicho anachostahili mtu huyo.” Alisema hayo akimtizama Stanis mstimuni.
“Mtoeni na mumrudishe kwenye makazi yake. Kesho tutakutana tena hapa kuendeleza yale anayostahili.”
Stanis alibanduliwa mstimuni akiwa hajitambui akapelekwa kwenye chumba chake cha giza. Alitupiwa humo kama mzigo, mlango ukafungwa na komeo, nje ya mlango wakasimama wanaume wawili kumlinda mgoigoi huyo asije kwenda popote kabla hajakutana na kifo chake.
Lakini ndani ya chumba hicho cha giza, Stanis akiwa amelala akichuruza damu na fahamu zake zikiwa ng’ambo, kuna sauti ilimuita mara tatu kwa kunong’oneza pasipo na majibu.
Kumbe kwenye ukuta upande wa kulia, palikuwa na tobo dogo lililotokezea chumba cha pili. Ndani ya chumba hicho, palikuwa na mtu … ndani ya chumba hicho palikuwa na Rajul.
Naye alikuwa amefungiwa humo pakiwa ni giza haswa. Hata hali yake ya mwili bado haikuwa imetengemaa toka kwenye mateso na adha alizozipata tempo kwa utovu wake wa nidhamu.
****
“Ulifanya kile nilichokuagiza?” Mamba alimuuliza mwanaume mmoja chotara kwa kumkazia macho.
Walikuwa ndani ya chumba kikubwa cha kuvutia chenye kila aina ya vikolombwezo vya gharama. Kwa kukisia haraka kilikuwa ni chumba cha hoteli. Tena hoteli ya nyota nyingi tu.
Mwanaume huyo chotara alitikisa kichwa akajibu:
“Ndio nimefanya.”
“Umegundua hiyo simu yako ipo wapi?”
“Ndio. Ipo kwenye kisiwa fulani bahari ya Hindi.”
Mwanaume huyo alisema akimkabidhi Mamba simu yake kubwa rangi nyeusi.
Mamba alitizama simu hiyo akaona ramani iliyotoholewa mtandaoni. Katikati ya ramani hiyo palikuwapo na kidoti chekundu ‘kikimwekamweka’ kama taa ya ishara ya gari. Chini ya kidoti hicho palikuwapo na maelezo ya nyuzi za longitudo la latitudo ya mahali hapo.
“Ulipapataje?” Mamba aliuliza.
“Simu yangu ina program ya kujikinga dhidi ya virusi.” Chotara akajibu.
“Programu ya virusi imepelekeaje wewe kupata mahali hapa?” Mamba aliuliza.
“Ndani ya programu hiyo unaweza pia ukatenga mahesabu ya kupata simu yako iliyopotea kwa kuamrisha simu nyingine utakayoichagua iwe inakupa taarifa ya simu yako. Na simu yenyewe ndiyo hiyo hapo. Hata mwizi atakapotoa laini haitosaidia kumficha.”
Mamba akatabasamu.
“Nalijua hili eneo.”
“Ndio mana tukakutafuta kwa hali na mali.” Chotara akadakia, “Sasa tunaweza kwenda na kumaliza biashara yetu?”
“Ndio twaweza kwenda. Ila sio kwa haraka kiasi hiko.”
“Kivipi?”
“Yatupasa kujikamilisha kwa silaha na mipango. Kisiwa hiki kipo pweke hivyo ni rahisi kwa mgeni kuonekana akija tokea upande wowote. Na pia hatujajua wao wamejipangaje. Huwezi jua labda wanategemea ujio wetu.”
“Kwahiyo tunafanyaje?”
“Waite wenzako kwanza tuyajenge.”
Baada ya nusu saa, wote watano wakawapo ndani ya chumba hicho wakapata kupanga na kupangua, Mamba akiwa kiongozi.
Walipomaliza kuainisha mipango yao, Mamba akawaambia.
“Huyo Vitalis mumuache. Nataka nimshughulikie kwa mikono yangu mwenyewe.”
Wote wakaafiki kisha wakajipumzisha na mipango yao waliyokuwa wanaisuka kwa kuzoza na mengine ya dunia, huku wakishushia na vinywaji vikali vilivyotapakaza meza. Huenda mawazo yao ya sasa yalichombezwa na mwenendo mkali wa vileo vichwani. Walicheka hovyo na kupaza sauti pasipo na mahitaji.
“Mlienda wapi, mbona hamkutuaga?” Mamba aliuliza wanaume watatu ambao hawakuwepo hapo awali. Mmoja wao akacheka kidogo na kujibu:
“Tulikuwa huko mtaani tukionja ladha ya wanawake wa Tanzania.”
Wote wakajikuta wakicheka.
“Umeionaje ladha yao?” Mamba alichokoza huku wakiendelea kutandika vileo.
“Aaah! Kusema ukweli haielezeki.” Mwingine alijibu. “Unajua kule kwetu Bermuda, hamna wanawake wenye shepu nzuri kama huku. Wengi wao wanafanana tu na sisi pindi wakivua nguo, lakini hapa ni tofauti kabisa!”
Wakacheka.
“Ni kweli.” Mwingine akatia neno, “Waweza vunja shingo ukikatiza barabarani mana kila mmoja ana mvuto wake wa kushangaza. Mapaja yao ya moto na meupe. Matiti yao makubwa yakujaza. Makalio ndio doh …”
Wakacheka tena.
“Sasa mbona hata hamkunambia kama mlienda huko?” Chotara aliuliza kwa kulaumu. “Mbona ni wabinafsi sana nyie ndugu zangu?”
“Sasa hivi tutaenda sisi na nyie mbaki hapa.” Mamba akasema akioneshea kidole sakafuni.
“Kwanini tusiwaite hapa wakatufuata? Nilichukua namba zao za simu. Nitawaambia waje na wenzao, au mnasemaje?” Mwanaume mmoja miongoni mwa wale waliotoka huko nje alitoa wazo. Likaonekana kukonga nafsi zao.
Mamba akasema:
“Utanipa niongee nao. Wakijua nyie wageni watatupiga pesa ndefu sana.”
Simu ikanyanyuliwa na kupigwa, Mamba akatoa oda ya wanawake nane ambao alihadiwa kufika walipo kwenye majira ya saa nne usiku, ila hilo likifanyika baada ya malipo ya awali kutumwa.
Mamba alituma pesa hizo kisha wakakaa tenge sasa kungoja raha.
Raha toka kwa wanawake walionona haswa.
Raha toka kwa wanawake wa danguro ghali na maarufu jijini Dar lipatikanalo maeneo ya Mbezi beach.
***
Muda si barafu ukaganda.
Majira ya saa nne usiku yalijongea na kuwaleta wanawake warembo haswa ndani ya chumba namba 321 walimokuwemo Mamba na wenzake wakijiliwaza kwa kutizama televisheni na kunywa pombe kali.
Wanawake hao walipambwa na shepu barabara zikibanwa na nguo fupi. Nywele ndefu za kisasa isipokuwa mmoja tu mwenye nazo fupi. Nyuso zilizokozwa ‘make up’ za kulaghai. Michuchumio ya hatari ya kumetameta bila kusahau mapochi makubwa ya bei ghali.
Kila mwanamume alijichagulia wa kwake akanywa na kucheza naye. Mamba alitwaa wanawake wanne peke yake wenzake wakigawana mmoja kwa kila mmoja.
Baada ya kucheza na kuwehuka kwa muda, wakaanza ‘kuchojoana’ nguo na kufanya mapenzi mbele ya kila mmoja kana kwamba kuna mashindano.
Usipite muda mrefu, wanaume hao wakajikuta wazito mno. Waliamka majira ya saa nne asubuhi wakiwa peke yao ndani ya chumba.
Walikombwa pesa zote na vitu vya thamani: saa, viatu na nguo. Hata ramani waliyoikuwa wamepangia mambo yao haikuwapo.
Mamba alishika kichwa chake akapiga ukunga wa hasira.
“Uliwatoa wapi? Hawa wanawake sio wa danguro la Mbezi! Hawana tabia hizi za kishenzi!” Mamba alifoka.
“Ila walisema ni wa Mbezi!” Aliyetoa namba alijitetea.
“Lakini mbona kama kunywa tulikunywa wote. Walituwekea madawa sehemu gani?” Mwingine aliuliza.
“Hawa malaya huwezi ukashindana nao kwa kunywa.” Mamba aling’aka. “Wana vichwa vigumu sana kulewa … itakuwa kuna mahali tu walitupatia wakatuweza. Si kwasababu ya pombe. Tusingeweza kuzima vile.”
“Sasa tutafanyaje na pesa zote wameondoka nazo? Tuwasiliane na mkuu atuwezeshe?” Mmoja alitoa wazo.
“Hapana! Hapana!” Mwenzake akadakia haraka. “Hatuwezi tukaomba pesa nyingine wakati alizotupa zilikuwa ni nyingi mno, na tumezimaliza kabla hatujafanikisha alichotuagiza.”
“Kwahiyo unashaurije?”
“Tupambane kwanza kufanikisha hili jambo mbele yetu kwa njia yoyote ile. Hapo mkuu anaweza akatuelewa na kutupatia pesa. La sivyo hakuna tena njia.”
****
Masaa kadhaa nyuma …
“Wamepiga simu, wanataka wanawake nane. Sasa hilo dili vipi?” Aliuliza mwanamke mmoja mwenye nywele fupi na hereni kubwa za mviringo masikioni.
Ndani ya chumba hicho walikuwepo jumla ya wanawake watano waliojilaza na kuketi kwenye godoro lililolazwa chini. Wote walivalia nguo za ‘hasara hasara’, watatu miongoni mwao wakipasha mapafu kwa sigara.
“Huo sio mchongo wa kuuacha kabisa. Watakuwa ndio wale wale wageni tuliowapa namba za simu. Wana madola ya kumwaga. Kama vipi wash’tue wakina Shamira tukachukue pesa hizo.”
“Ila kabla ya kwenda umewaambia watoe pesa ya advansi?” Mmoja aliuliza.
“Sasa tutaendaje kichwa kichwa bila kuwaambia hivyo?” Aliyeongea na simu akajibu kwa swali. Mwingine akachangia:
“Na kama unavyojua walituonea maeneo ya Mbezi kwahiyo wanajua sisi mambo safi, sio wale wa mitaani. Kwahiyo kama tunaenda basi tuwaambie wakina Shamira waje na mitupio ya hatari.”
“Poa poa!”
Simu ikapigwa na kutoa maelekezo yote. Baada ya punde Shamira na wenzake wakafika chumbani hapo na mikoba ya gharama iliyobebelea nguo za maana.
Baada ya kujivesha na kujitathmini, wakasuka mipango yao.
“Kama mnavyoelewa, sie ni watoto wa mbwa. Hapa hatulazi damu wala hatuzubai. Inabidi tuwakombe kila kitu.” Alisema yule mwanamke mweye nywele fupi na hereni kubwa. “Kila mmoja ahakikishe anapaka dawa yake kama kawa. Au sio?”
“Poa.”
Wakati wanajiandaa kwenda kutoa huduma kwa wanaume waliowaita kwa kujikwatua na kujipulizia manukato ya Paris, walipakaa pia unga fulani mweupe kwenye chuchu za matiti yao kwa kuzungusha kidole.
Walipomaliza, mmoja wao akasema kwa kebehi:
“Wakinyonya tu imekula kwao.”
Wote wakacheka na kugongesha viganja vyao.
Baada ya mwanaume aliyevalia kiremba cha manyoya kunyoosha juu mkono wake uliobebelea panga, ngoma zote ziliacha kupigwa, kukawa kimya. Sauti pekee ya moto mkubwa uliowashwa kando ndio ikawa inavuma kwanguvu.
Watu wote wale wa ajabu waliovalia ngozi na michoro ya ajabu miilini mwao wakawatizama wakina Vitalis waliokuwa wamening’inizwa kwenye miti, kila mmoja na mti wake wakifungwa kamba miguuni, viunoni na mikononi.
Mwanaume yule mwenye kiremba cha manyoya akasogea karibu na kuanza kuwatizama mateka wake mmoja baada ya mmoja. Alifika kwa Sandra aliyekuwa wa mwisho upande wake wa kulia, akamtizama mwanamke huyo kana kwamba kuna jambo analitilia shaka.
Mwanamke huyo alikuwa amedhoofu mno. Macho yake yalikuwa yameingia ndani huku yakitengeneza uzio wa kijani. Pua yake ilikuwa inachuruza damu ya kijani. Mdomo wake ulikuwa umekauka sana ukichuruza udenda. Mguu wake uliopata jeraha ulikuwa kana kwamba umeoza, ulikuwa wa kijani mpaka maeneo ya ‘enka’, tena uking’ong’wa na nzi wengi.
Mwanaume huyo aliyevalia kiremba cha manyoya akatikisa kichwa chake akibinua mdomo. Mara sauti ya Kaguta ikapaza na kumshitua:
“Tafadhali, naomba umsaidie. Anaumwa sana!”
Kitendo cha Kaguta kumaliza tu hiyo kauli, alipokelewa na fimbo nane alizotandikwa kwa fujo na kuamriwa anyamaze kimya kwa ishara.
“Utakapoongea tena hayo maneno yako, hautochapwa, bali utauwawa.” Aliongea mwanaume yule mwenye kiremba cha manyoya kwa lafudhi ya mithili ya mtu aongeaye kiarabu, kisha akawaita wanaume wawili kwa ishara wakaja, akawanyooshea kidole kwa Sandra.
Wakamfungua Sandra na kumbebelea mpaka karibu na moto. Ngoma zikaanza kupigwa tena watu wakicheza na kuimba nyimbo zao kwa lugha ngeni. Japokuwa Kaguta na wenzake walipiga kelele kuomba Sandra aachiwe, haikusaidia. Sauti zao zilimezwa na sauti ya ngoma na nyimbo zisisikike kabisa.
Sandra akiwa hajiwezi kwa lolote akafungiwa kwenye mti mwembamba ila mkomavu na mgumu, tayari kwa ajili ya kutundikwa kwenye vishikizo vilivyosimama pembeni ya moto ili abanikwe kwa ajili ya nyama.
Kabla zoezi hilo halijakamilika, Bernadetha akamgeukia Vitalis akimtizama kwa sura yenye macho matulivu. Akamuita:
“Vitalis.”
“Naam!” Vitalis akaitika.
“Huu ndio muda wako. Muokoe Sandra.”
“Nitamuokoaje?” Vitalis aliuliza. Bernadetha akamjibu:
“Najua unaweza. Unajua unaweza. Muokoe kabla hatujachelewa.”
Wakati wanaume wale wakinyanyua mti uliombebelea Sandra wapate kumuweka motoni, wakasikia sauti kali ya mngurumo iliyowashitua.
Wote walitizama sauti hiyo ilipotokea, wakakutana na mnyama mkubwa mweusi akiwa amevimba.
Mnyama mkubwa akiwa ameshajiandaa kwa kufanya shambulizi.
Mnyama mkubwa akionesha meno yake makubwa na makali.
Mnyama mkubwa mwenye macho mekundu kama damu.
Mnyama huyo akiwa ni mbwa mwitu. Ila asiwe mbwa mwitu tunayemjua, bali yule mpana na mrefu, anayeogofya hata kumtizama.
Mwanaume yule mwenye kiremba cha manyoya akiwa ametoa macho ya kuduwaa, akapaza sauti kwa lugha ngeni. Mara watu wake wote pamoja na yeye wakatupa silaha zao pembeni na kuinama haraka kusujudu.
Mnyama alibadilika taratibu akawa Vitalis. Alimkimbilia Sandra na kumfungua toka kwenye ule mti aliofungiwa. Akamuuliza:
“Sandra, upo sawa?”
Sandra akatabasamu akiwa amefumba macho. Akasema:
“Ahsante, Vitalis. Ila nahisi muda wangu umefika.”
Vitalis aliwageukia watu wale wa ajabu waliokuwa bado wameinama, akawapazia sauti:
“Msaidieni, ana hali mbaya!”
Mwanaume yule mwenye kiremba cha manyoya akasogea karibu na kumwambia Vitalis kwa lafudhi yake kana kwamba anameza maneno:
“Tumechelewa, hatuwezi tukafanya lolote likamsaidia. Alitobolewa na mti wa mfofo. Ukitobolewa na mti huo inabidi utibiwe kabla haijapita dakika moja. Ikipita tu hakuna tena namna.” Vitalis aliporudisha tena macho yake kwa Sandra akamkuta mwanamke huyo akiwa ametulia tuli, mdomo wake unamimina damu ya kijani.
Alimuita lakini hakupata majibu. Aliweka sikio lake kifuani lakini hakusikia mapigo ya moyo.
Aligeuka akamtizama Kaguta na kumwambia:
“Ameenda.”
Kaguta akatizama chini na kudondosha chozi. Hakutia neno zaidi ya kusaga meno yake kwa uchungu usiomithilika.
***
“Kila kitu kipo sawa. Tunaweza tukaenda sasa.” Mwanaume mwenye kiremba cha manyoya alimwambia Vitalis aliyekuwa ameketi na Kaguta kwenye kitanda cha ngozi.
Macho ya Kaguta yalikuwa mekundu lakini pia uso wake ukiwa haba na furaha. Alinyanyuka akaongozana na Kaguta mpaka huko nje walipokutana na wanaume kadhaa wakaanza kusonga nao kuelekea upande wa mashariki.
“Kwanini umenikarimu ghafla hivi?” Vitalis alimuuliza mwanaume mwenye kiremba cha manyoya. Mwanaume huyo akatabasamu na kuuweka mkono wake begani mwa Vitalis. Akajibu:
“Kwasababu wewe ni kiongozi.”
“Kiongozi wa nini?”
“Katika mila na desturi zetu, mbwa mwitu ni mnyama mtakatifu anayeabudiwa. Huko nyuma, mababu zetu walipata kuwa kama wewe. Uwezo wao wa kugeuka na kuwa mbwa mwitu uliwafanya waheshimike na kulinda jamii yetu dhidi ya maadui.”
“Kwahiyo kwa sasa hakuna tena mtu anayegeuka na kuwa hivyo?”
“Hamna tena. Wote wameenda na kile kizazi cha mababu zetu. Hali hiyo imesababisha tuishi kwa mashaka lakini pia tukose mifano halisi ya kuwaelezea wajukuu zetu juu ya mambo hayo.”
“Lakini kwanini watu hao wamepotea na hakuna wengine? Ilikuwaje wakawepo?”
“Walituambia ni kwasababu walikuwa na mawasiliano na wanyama hao kipindi hiko cha zamani. Watu pekee waliopata uwezo huo ni wale tu waliokuwa shupavu na majasiri, wale waliojitolea kupambana na hao wanyama kwa ajili ya kulinda jamii zao. Hao wanyama ndio wakawapa huo uwezo. Ndivyo tulivyohadithiwa.”
Wakiwa wanamalizia maongezi hayo, wakawa tayari wameshakaribia eneo lililokuwa na watu wengi wakijikusanya, watu hao wakiwa ni wakazi wale wa kisiwa ila miongoni mwao wakiwapo pia Bernadetha, Bakari na Miraji.
Mwili wa Sandra ukiwa umefunikwa na majani mithili ya sanda ulishushwa na kufukiwa shimoni ngoma zikipigwa na nyimbo zikiimbwa. Juu ya kaburi hilo yakawekwa majani pamoja na nyoya moja lililotoka kwenye kiremba cha kiongozi. Baada ya hapo, watu wote wakarudi kwenye makazi yao na kuliacha kaburi nyuma.
Huko nyumbani siku ikajazwa na shughuli nyingi. Wakina mama wakawasha majiko yao na kuinjika vyungu motoni. Wanaume wakafyagia uwanja, wakaleta matunda mbalimbali nyumbani pamoja na kutengeneza uwanja mpana kwa ajili ya shughuli.
Wakati jua laelekea kuzama, sherehe kubwa ikazuka eneo hilo. Ngoma na nyimbo zikarindima kila eneo. Vitalis na wenzake walitengewa eneo maalumu la kuketi, karibu kabisa na kiongozi, hapo ndio wakaelekezwa dhumuni la tafrija hiyo.
“Ni mila na desturi zetu kushehereka pale ambapo mmoja wa familia ya kifalme anapofariki, kwasababu tunaamini anaenda mahali bora kuliko hapa. Marehemu ni miongoni mwa familia yenu, miongoni mwa kiongonzi wenu, anastahili heshima hii.”
Alisema kiongozi akimtizama Vitalis na kumuonesha kidole.
Walipewa chakula wakala, vinywaji wakanywa. Watu waliimba na kucheza kwa furaha.
Siku hiyo Kaguta akanywa pombe kupita kiasi asimsikie yeyote aliyemwambia aache hilo zoezi. Kwake aliona hiyo ndio njia mbadala ya kumtoa Sandra aliyeng’ang’ania kichwa chake haswa.
Alikunywa na kunywa mwishowe ‘akazima’. Akabebwa kama mtoto na kupelekwa ndani kulazwa.
***
“Upesi! Hatuna muda wa kupoteza.” Mamba alifoka akiwaambia wenzake wanaoshuka kwenye boti ndogo nyeupe. Wote walivalia sare za wahudumu walizozipatia hotelini huku mikononi wasiwe hata na silaha yoyote.
Baada ya wote kushuka wakiwa wamekanyaga maji na moka zao, Mamba aliwaamuru:
“Nifuateni.”
Wakatembea hatua kadhaa kufuata nchi kavu. Macho yao yaliranda randa huku na huko lakini hawakuona kitu. Walisimama, Mamba akashusha pumzi ndefu akibinua mdomo wake.
“Hii ndio kazi ya kupoteza ramani. Hatujui tunaelekea wapi.”
Waling’aa ng’aa macho hapo kwa sekunde kadhaa, Mamba akasema:
“Twende mbele kwa mbele kabla tuliowaibia boti hawajatukuta hapa.”
Walisonga mbele kidogo wakaona ‘kijumba’ walichokuwa wanatumia wakina Vitalis. Waligawana pande wakavamia kijumba hicho ambamo ndani hawakukuta yeyote. Zaidi kwenye upekuzi huo walikuta simu na tanakilishi, bahati mbaya kwao, vyote navyo vilikuwa vimezima moto.
“Inabidi tusake kisiwa kizima. Haitotuchukua muda mrefu kutimiza hilo.” Mamba aliwaambia wenzake. Pasipo kubisha wakaanza kutimiza agizo hilo kwa kutembea huku na huko macho yao yakiwajibika haswa kutoa salamu kila pande ya dunia.
Baada ya mwendo wa dakika kumi na tano, chotara alipata ajali. Mguu wake wa kushoto ulichanwa pajani na mwiba. Pasipo kujua, ama kupuuzia madhara ya mwiba huo wakaendelea kutembea kutafuta wahusika wao.
Punde tu ilipopita dakika moja, chotara akaanza kuona kizungu na joto kupanda mwilini. Mwili mzima ulimvuja jasho kana kwamba amemwagiwa maji. Jeraha lilimimina damu haswa na kuchafua suruali, ila ajabu ni kwamba, damu ilikuwa ya kijani.
Mwishowe chotara akashindwa kutembea na kudondoka chini. Macho yake yalilegea mithili ya mtu anatekenywa na upamba sikioni, huku mwili ukifuka jasho kweli.
Haraka wenzake wakamsogelea kumjulia hali.
“Najisikia joto kali. Kizunguzungu, na macho hayaoni vizuri.” Alisema chotara kwa shida.
“Inabidi tumuache twende. Hatuna muda wa kupoteza.” Mamba akawaambia wenzake.
“Hapana. Hatuwezi tukamuacha hapa mtu tuliyekuja naye.”
Wengine wakamkatalia katu juu ya hilo.
“Nimesema tunamuacha hapa. Atakuwa tu mzigo kwetu huko mbele ukizingatia tuna kazi nzito.”
“Hapa tunamuacha na nani? Ingelikuwa wewe ungelitaka tukuache?”
Kishingo upande Mamba akaridhia waende naye. Wanaume wawili wakambebelea mwenzao safari ikajongea kuzidi kuzama ndani ya kisiwa ila sasa mwendo ukipungua kutokana na mzigo wa mgonjwa huyo.
Wanaume hao wasitembee muda mrefu, wakafika eneo dogo lililokuwa wazi lakini likizingirwa na miti mirefu kama sehemu zingine za kisiwa. Walikatiza eneo hilo, ghafla udongo ukatitia na kutengeneza shimo kubwa, wote wakazamia humo asiwepo hata wa kuwaokoa.
Kulikuwa ni giza na joto humo ndani. Mwanga wa jua uliokuwa unaangaza muda huo haukutosha kupenya shimoni na kuwamulika. Wakawa wanapapasa.
“Tupo wapi humu?”
Mmoja aliuliza. Badala yake sauti ya mwangwi ikamjibu:
“Tupo wapi humu?”
***
Mlango wa chumba afungiwacho Stanis ulifunguliwa wakaingia wanaume wawili. Wanaume hao walimfuata Stanis wakambebelea mithili ya kuku mwenye mdondo na kumburuzia nje mpaka eneo la mateso.
Walimfunga mikono na miguu kwenye mti kisha wakampisha mwenzao aliyeyebelea mjeledi apate kufanya kazi yake.
Sehemu zile zile zilizokuwa zina ‘madonda’ ya mijeledi ya jana, ndipo hapo pakafumuliwa na mijeledi mipya, damu zikamwagika kama maji.
Tofauti na siku iliyopita, Stanis hakupiga kelele kabisa siku hiyo. Macho yake yalikuwa yamechoka, mwili wake ukisukumwa na nguvu ya mijeledi mbele na nyuma. Mdomo wake mkavu ulinyamaza kimya usifunguke mpaka zoezi linakoma.
Watu wote wakiwa wanashuhudia, Stanis akabanduliwa toka kwenye mti aliofungiwa kisha akaburuzwa kama kiroba cha viazi kwenda kwenye makazi yake ya giza.
Huko, kama ada, akatupiwa ndani na mlango kufungwa.
Chumba kizima kilikuwa kinanuka damu kana kwamba ni machinjioni. Stanis akiwa kama mtu asiyejielewa, alilala humo kana kwamba hakusikia wala kujali harufu hiyo. Labda haikuwa inamkifu na kumbugudhi tena kama hapo awali. Aidha aliizoea sasa maana hakuwa na jinsi nyingine.
“Stanis! … Stanis!”
Sauti iliita. Stanis hata hakushituka wala kujisogeza.
Kwenye ukuta tunduni, Rajul akaendelea kuita jina hilo pasipo kukoma. Aliita mara kumi ila majibu yakiwa ni yale yale tu, kimya.
“Tafadhali Stanis, amka! … utakufa humu! Amka!”
Kimya.
Rajul alipiga piga ukuta mwishowe akachoka. Aliegemea ukuta akashusha pumzi.
“Lazima nifanye jambo kumuokoa huyu kiumbe. Hii inaweza ikawa sehemu yangu ya kwanza kutafuta rehema za Mungu wangu niliyemkosea.”
Alipenyeza kidole ndani ya shati aliyoivaa akatoboa mojawapo ya jeraha lake na kulichuruzisha damu. Alikinga damu hiyo na kuiweka kwenye kiganja cha mkono wake wa kushoto. Alinyanyua mkono wake wa kulia akaupeleka utosini na kufuta unga wa mchoro wake kwa kutumia kidole. Kisha kidole hicho akakidumbukiza kwenye damu kiganjani.
Kabla hajaendelea na kingine, akasikia mlango wa chumba chake unafunguliwa. Haraka akamwaga damu na kujifutia ukutani.
Waliingia wanaume wawili chumbani wakasimama mbele yake.
“Mkuu anataka kuonana na wewe.” Alisema mwanaume mmoja. Kabla Rajul hajasema lolote, alikwapuliwa na kubebwa mpaka ofisini kwa Kim alipokalishwa kwenye kiti kinachomtizama ‘Mkuu’, kisha wanaume hao wakatoka ndani na kusimama nje ya ofisi.
“Karibu, Rajul.” Kim alisema kwa tabasamu, Rajul asitie neno lolote.
“Bila kupoteza muda ningependa kwenda kwenye mada niliyokuitia. Na najua unaifahamu … Nadhani sasa ni muda wa kutimiza yale tuliyoyabakiza.”
Rajul alimtizama Kim kwa macho yaliyochoka, akasema:
“Siwezi. Sina nguvu ya kutimiza hayo. Unaj … hali yangu … si nzuri.”
“Bwana Rajul! Siwezi nikasubiri milele! Inabidi tumalize kazi yetu!” Kim alifoka.
“Najua … najua kitu ninachotakiwa kufanya. Ila kwa sasa … kwa sasa, sina ngu … vu hiyo.”
Rajul alijibu kisha akanyanyua sehemu yake ya shati yenye damu na kuipeleka puani. Harufu hiyo ikamchefua na kumtapisha.
Kim akakunja sura kwa kinyaa. Alimuita mfanyakazi wake aje kusafisha upesi. Akawaita na walinzi pia wamtoe Rajul na kumrudisha kwenye chumba chake.
Aligonga meza kwa hasira, akafoka:
“Ushenzi gani huu!”
Alishika kiuno akazunguka ofisi nzima huku na kule.
***
Baada tu ya mlango wa chumba kufungwa, Rajul alijaribu tena kuita jina la Stanis mara tatu pasipo majibu. Alichungulia kwenye kitundu lakini hakuona kitu kwa sababu ya giza lililokuwepo kwenye chumba cha Stanis.
Alipiga piga tena ukuta, mara hii Stanis akashituka, ila hakutoa sauti yoyote.
“Stanis! … Stanis upo?” Rajul alinong’oneza baada ya kusikia sauti ya mtu akisogea.
“Eeeiiigh …” Stanis aliitikia kwa kukoroma. Rajul akatabasamu.
“Stanis, inabidi utoroke, la sivyo utauwawa. Unanisikia?”
“Eeeeiggh …”
“Inabidi uondoke humo kwa njia yoyote. Inabidi tutoroke la sivyo, Kim atafanikiwa adhma yake.”
“Eeeeiigghhh …”
“Ili Kim afanikiwe anahitaji damu. Na endapo nikimwambia hilo basi atakufanya sadaka. Akikufanya sadaka, atapata nguvu. Akipata nguvu, hakutokuwa na wa kumzuia tena.”
“Eeeigggh …”
“Una wazo lolote la kutoroka?”
“Eeeiigggh …”
“Stanis, huwezi kuongea neno lolote?”
“Eeeiiggh …”
“Mungu wangu!” Rajul alijibamiza kichwa akaegemea ukuta.
“Nifanye nini sasa? … Nifanye nini?”
Aliwaza na kuwazua kwa dakika kadhaa, mara akatikisa kichwa na kusema:
“Hii sasa ndio njia. Hii ndio njia pekee.”
Aligeukia kwenye kitundu, akamuita Stanis.
“Stanis, nina njia ya kututoa humu. Upo tayari?”
“Eeeiggh …” Stanis akaitikia kwa kukoroma kama ada.
***
Sauti kubwa ya mlio wa pembe la ng’ombe ililia na kumshitua Vitalis aliyekuwa amelala.
Ilikuwa ni asubuhi sasa ya saa kumi na mbili hata jua halijasimama. Vitalis alimtizama Kaguta aliyelala upande wake wa kushoto akamuona yu hoi usingizini. Asimsumbue hata, akanyanyuka na kutoka nje atizame kunani. Huko akakutana na Bernadetha, Bakari na Miraji, wote walikuwa wametoka nje kushangaa. Kama wehu, wenyeji wao walikuwa wanatoka kwenye makazi yao wakikimbia kuelekea msituni sauti inapotokea. Wakiwa wamebung’aa wasipate hata mtu wa kumuuliza, wakamuona kiongozi. Upesi, Vitalis alimkimbilia akamwambia:
“Unajua ni wewe tu ndiye unayeongea lugha tunayoielewa.”
Kiongozi akaitikia kwa kutikisa kichwa.
“Kuna nini?” Vitalis aliuliza. “Mbona watu wanakimbia?” Kiongozi akatabasamu.
“Kuna taarifa ya mateka wamekamatwa mtegoni.” Alisema. “Usiwe na hofu.”
Kauli yake hiyo ikafungwa kwa kuingizwa kwa mateka hao ndani ya kijiji wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi mkali. Vitalis alimuona Mamba pamoja na wenzake, akajikuta anatabasamu na kusema:
“Mungu mkubwa. Amenipa nafasi ya kutimiza ahadi yangu.”
“Vitalis!” Mamba alishangaa kumuona adui yake. Alijikuta anacheka kwanza kisha ndiyo akaendelea kunena:
“Sikujua kama ulikuja kuomba msaada wa watu hawa washamba ... wa kale ... wasiojua ulimwengu unaendaje.”
Alicheka tena alafu akaendelea:
“Sikujua kama wewe ni muoga kiasi hiki. Sikujua kama wewe ni mwanamke kiasi hiki. Vitalis, watu wanavyokudhania huko nje ni tofauti na ulivyo. Hawajui jinsi gani ulivyo mtu wa kujificha na kukimbia kama panya."
Mamba aliongea kwa kejeli akiupindisha mdomo wake. Vitalis akamuuliza:
"Unakumbuka ahadi yangu niliyoiweka mbele yako kule kiwandani?"
"Ahadi gani wewe mwanamke?" Mamba akauliza pia. Vitalis akamsogelea karibu zaidi.
"Nilikuambia siku nikikutia mikononi nitahakikisha nakuharibu mpaka mama yako mzazi ashindwe kukutambua. Siku yenyewe ndiyo leo."
"Karibu!” Mamba alisema akimuita Vitalis kwa ishara ya ulimi. “… sasa nitapambanaje na nimefungwa kama mzigo wa msafiri?" Akauliza. Vitalis akamuomba kiongozi ampatie mtu huyo, kiongozi akaridhia. Mamba alifunguliwa kamba, wakapewa uwanja.
La haula, kabla Vitalis hajajiweka sawa, Mamba alijitosa hewani akamgawia teke zito lililomzoa na kumbwaga chini mwanaume huyo.
Upesi Vitalis aliamka kwa sarakasi akajiweka sawa kisha akatulia kungojea tena shambulizi.
Mamba akatuma tena teke, mara hii likadakwa na mkono wa kuume wa Vitalis. Teke hilo likavutwa karibu kisha Vitalis akaruka na kujigeuza akimtandika Mamba kisigino cha taya. Mithili ya mzigo, Mamba akarushiwa kando.
Aliponyanyuka kwa hasira aonyeshe ubabe wake, akaula tena wa chuya, kila ngumi na teke alilorusha zikakwepwa kisha akazawadiwa ngumi nzito chini ya kifua, akacheua damu.
Mamba alifuta damu yake kwa kiganja kisha akaguna. Alikimbia kumfuata Vitalis, ila Vitalis akamkwepa haraka na kumuwekea goti la mguu wa kushoto mwanaume huyo aliyegota hapo kama gari la mwendo kasi. Kama haitoshi, Vitalis akarusha mguu wake wa kulia na kumkita nao Mamba shingoni. Sasa Mamba akadondoka chini ila akiwa katikati ya miguu ya Vitalis. Miguu ikabanwa kwanguvu na kumnyima Mamba hewa. Alirusha ngumi kwa fujo ajiokoe, Vitalis akakamata mikono hiyo na kuivunja kisha akavuta jabali lililokuwa pembeni akaponda uso wa Mamba mpaka pale ulipokuwa chapati.
Damu zilimrukia Vitalis kwa fujo. Shati lake lote na hata suruali vilichafuka damu. Wakati anafanya tukio hilo la kuponda kila mtu alimshangaa. Ni kama vile alikuwa anaponda mawe kumbe kichwa cha mtu. Hakuwa na roho ya ubinadamu hata kidogo muda huo bali ya shetani, tena shetani mwekundu. Hakuacha hilo zoezi mpaka pale alipokuja kutolewa na Kiongozi aliyemvutia pembeni na kumtaka apunguze jazba.
Aliwatizama wenzake na Mamba akawaambia:
“Nyie ndio mnafuata!”
Watu hao, isipokuwa chotara, walimtizama Vitalis kana kwamba wanatizama pundamilia akimla simba. Chotara yeye alikuwa hoi asijali hata kinachoendelea. Alisimama kama mgomba ulioelemewa na mkungu wa ndizi. Alikuwa ametota jasho mdomo ukiwa mkavu mno. Macho yake yalikuwa yamelegea yakiwa mekundu ya kutisha.
Vitalis alijikwamua toka mikononi mwa Kiongozi akajiendea ndani asiwaone watu hao. Mateka walitundikwa mitini, watu wakaendelea na shughuli zingine kama ada. Baada ya muda mfupi, Bakari aliwafuata hao mateka waliotundikwa mitini akawapekua mifukoni. Miongoni mwa mmoja wao alikuta simu. Aliitia mfukoni mwake akawauliza:
“Mmetumwa na nani?”
Mateka wale watatu, walio wazima wa afya, wakatabasamu.
“Usitegemee kupata jibu lolote toka kwetu.” Mmoja alijibu.
Bakari alimfuata chotara akamtizama kwa karibu. Aliona mishipa ya shingoni ya mwanaume huyo imegeuka kuwa rangi ya kijani. Alimfungua macho akamtizama, napo akaona macho ya mwanaume huyo yakiwa na umbijani kwa mbali, akaishia kutikisa kichwa na kusema:
“Mwenzenu atakufa muda si mrefu.”
“Tunaomba umsaidie.” Mmoja akasema. “Tafadhali naomba umsaidie.”
Bakari akatabasamu.
“Usitegemee kupata msaada wowote toka kwangu.”
Alisema kisha akajigeuza aondoke. Akaitwa.
“Tafadhali msaidie. Tutakuambia unayoyataka.”
“Vipi kama mkiniambia alafu ndiyo niwasaidie?” Bakari alisema akisogea karibu kwa aliyemuita.
“Hapana! Tutajuaje kama unatulaghai?”
“Na mimi nitajuaje kama mtanilaghai?”
“Hatuwezi kufanya hivyo. Tukikulaghai, tutaondokaje na mmetufungia mtini?”
“Siwezi jua. Ila ingekuwa vema kama mngeniambia upesi ili mwenzenu apate tiba upesi, yupo kwenye hali mbaya. Si mnamuona?” Bakari alimtizama chotara.
Alikatizwa zoezi lake hilo na sauti ya Bernadetha iliyomuita. Aliaga akaahidi kurudi upesi kumalizana nao. Aliondoka, Kaguta akasogea karibu na mateka. Muda wote Bakari aliokuwepo hapo, Kaguta alikuwa akimtizama kwa karibu.
Sura yake ilikuwa imekunjamana. Macho yake yalikuwa yamevimba na mekundu. Mdomo wake ulibinuliwa kwa kebehi ama hasira. Nyuma ya mgongo wake alikuwa amefichama mkono uliobebelea kisu. Aliwatizama mateka akawaambia kwa sauti ya chini:
“Nimekuja kudai uhai wenu.”
Bakari aliporejea baadae kwa mateka hao, akawakuta wote wamekufa. Kila mmoja alikuwa anachuruza damu kifuani mwake akiwa na matundu ya visu si chini ya mawili.
“Samahani kwa kuingilia maongezi yako.” Sauti ya Kaguta ilimfikia Bakari na kumshitua. Aligeuka akamkuta Kaguta nyuma yake.
“Kwanini umewaua?” Bakari aliuliza. “Kuna taarifa muhimu walikuwa wanataka kunipa!”
“Unadhani wangekuambia kitu?” Kaguta aliuliza. “Kama ulitegemea kitu toka kwa watu waliokula viapo vya kutosema lolote, pole sana. Hawa watu hawastahili huruma yoyote.”
Baada ya kusema hivyo Kaguta aliondoka akaelekea ndani ya kijumba. Alinyofoa mtungi wa pombe uliokuwepo chini ya kitanda cha ngozi alaliacho, akamwagia kinywaji hicho ndani yake mpaka pale alipozima akalala. Hakutia tumboni kitu chochote isipokuwa pombe hiyo ya kienyeji. Hata pale jioni alipoamka, aliamkia na pombe hiyo. Ni Vitalis ndiye aliyekuja kumuokoa toka kwenye hiyo shughuli.
“Inatosha!” Vitalis alisema akimpokonya Kaguta mtungi wa pombe kwanguvu.
“Unadhani itasaidia?” Vitalis aliuliza. “Haitosaidia zaidi ya kutuongezea msiba mwingine, Kaguta!” Alifoka. Aliweka kituo akapunguza sauti.
“Tuna maongezi. Tunakungojea nje, fanya uje.”
Alitoka ndani ya chumba, Kaguta akamfuata baada ya muda mfupi.
Wakiwa watano, WAGENI, wamekaa kwenye benchi refu, waliteta:
“Sasa ni muda wa kwenda kumalizana na adui yetu mkubwa.” Vitalis alifungua maongezi. “Kila tunachokihitaji tunacho. Hatuna tena muda wa kungoja.” Alimtizama Bakari, Bakari akachukua zamu:
“Nilifanikiwa kwenda town kuchaji simu. Bahati nzuri baada ya simu kuwaka, barua pepe toka kwa Mr Kim ziliingia. Nilichat naye nikijifanya mimi ni mtumishi wake, nikapata taarifa muhimu za kutufikisha alipo.”
“Basi twende!” Kaguta aliropoka. “Tunangoja nini?”
“Tulia Kaguta.” Vitalis akasihi. “Si tu kwenda, tupange kwanza. Unajua tutafikia wapi? Unajua tutafanyaje kumpata Mr Kim?”
“Haya, tuendelee.”
Kaguta alisema kwa sauti ya chini isiyoridhia.
Hamilton, Bermuda.
Milango iliyokuwa imewafungia ndani wafungwa wawili, Stanis na Rajul, ilikuwa wazi. Pembeni ya milango hiyo ilikuwepo miili miwili ya wanaume waliokufa.
Taarifa hiyo ya vifo, ama kutoroka kwa wafungwa hao, haikuwa imesambaa popote pale. Hakuna yeyote ndani ya jengo hilo kubwa aliyefahamu kilichojiri isipokuwa tu akili za wafu waliolala hapo, akili zisizo na umuhimu tena juu ya ulimwengu wa walio hai.
Muda uliposonga, ukawadia wasaa wa Stanis kupokea adhabu yake ya muendelezo. Ndani ya muda huo ndipo taarifa ikatapakaa – Wafungwa wametoroka.
Kim alikuwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa akiwa tayari kushuhudia tena mgongo wa mwanaume aliyejaribu kumpindua ukifumuliwa na mijeledi. Akiwa anakunywa Vodka iliyotunzwa kwenye chupa ndogo yenye urembo wa kuvutia, mtumishi wake alifika mbele yake akamnong’oneza. Kim alimsukuma mtumishi huyo kisha akanyanyuka upesi na kwenda huko wahifadhiwapo wafungwa.
Kama vile milango ilivyokuwa wazi, naye mdomo wake ukabaki wazi aliposhuhudia. Alitoa macho ya butwaa. Aliuliza waliokuwa zamu ya lindo, wote wakaitwa mbele yake. Aliagiza wanaume hao wafungwe kamba na waadhibiwe mpaka kifo. Pasipo huruma, wanaume hao wanne wakafungwa na kuchapwa mijeledi ya nguvu. Kama vile haitoshi, Kim akafumua bongo zao na bunduki kisha akawaita wanaume wake watano wa kazi, akawaagiza wawatafute wafungwa hao.
“Kwa njia yoyote, kwa gharama yoyote ile, nataka hao watu warudi hapa!”
Wanaume hao watano walijipaki kwenye gari wakatoka nje ya uzio wa jengo tayari kwenda kuwatafuta Rajul na Stanis kwa udi na uvumba.
***
Basi lilisimama wakashuka wanaume wawili, Stanis na Rajul. Stanis alikuwa hoi kutembea mwenyewe asiweze ila kwa msaada wa Rajul alijikokota kwa mwendo wa kinyonga wakielekea upande wa kaskazini mwa barabara.
Kwa mazingira ya eneo walilopo, haikuhitaji elimu kung’amua ni ya kijijini. Japokuwa nyumba zilikuwa nzuri na za kuvutia, zilikaa mbali mbali huku zikiambatana na maghala ya chakula ama zizi la ng’ombe au farasi. Mashamba yalikuwa mengi yakizunguka makazi. Na ndani ya mashamba hayo walikuwepo watu wakichakarika kutimiza majukumu.
Baada ya mwendo wa dakika kumi, Rajul na Stanis walifika mbele ya nyumba nyeupe saizi ya kati. Rajul aligonga mlango wakafunguliwa na mwanamke mzungu mzee, Kelly, ambaye alishangazwa na hali ya wageni wake.
“Rajul, kuna nini?” Mwanamke huyo aliuliza.
“Naomba niingie ndani kwanza.” Rajul akasema. Mwanamke huyo akasaidiana na Rajul kumshikilia Stanis mpaka ndani walipomlaza mwanaume huyo kifudifudi. Rajul alimvua shati Stanis, Kelly akafunika mdomo wake na kiganja.
“Oh my God!” Kelly aliduwaa.
“Naomba umsaidie.” Rajul akamwambia mwanamke yule mzee.
“Amefanyaje?”
“Ni stori ndefu. Usijali, nitakuambia.”
“Ni bora ungempeleka hospitali, Rajul. Sio kwangu.”
“Hapana. Hospitali ni hatari kwake na kwangu pia.”
“Kivipi?”
“Nimekuambia ni stori ndefu, nitakuambia. Msaidie kwanza.”
“Nitamsaidiaje, Rajul?”
“Vyovyote. Ulishawahi kuwa nesi, tumia ujuzi wako.”
“Nilikuwa nesi kitambo.”
“Najua … najua. Ujuzi haufutiki, Kelly. Msaidie.”
Kelly alinyamaza kwa sekunde chache alafu akasema:
“Ok, ningojee hapa.”
Aliondoka akaelekea chumbani. Alirejea akiwa na kiboksi chekundu kilichoandikwa ‘First Aid’, akakifungua na kutoa pamba na chupa mbili za dawa.
“Hizo dawa za nini? Rajul aliuliza. Kelly akatabasamu.
“Tatizo umezoea dawa zako za mitishamba. Nashangaa huyu hujaenda kumtibia na madawa yako.”
“Ni stori ndefu, Kelly.”
“Ok ok … Mr. stori ndefu. Ni dawa ya kumsafisha na kumkausha majeraha. Hawezekani kushonwa tena huyu.”
“Ahsante sana kwa kumsaidia.”
“Usijali. Unajua wewe ni rafiki yangu, na ulijua kabisa nisingeweza kukukatalia kukusaidia ndio maana ukaja.”
“Ndio. Mume wako yupo wapi?”
“Ameenda kunywa … kama kawaida yake.” Alijibu Kelly akimshughulikia mgongo wa Stanis.
“Pole.” Rajul alimwambia Kelly. Kelly akamtizama mwanaume huyo kisha akarudisha macho yake mgongoni mwa Stanis.
“Pole ya nini na ni wewe ndiye ulitaka niishi maisha haya.”
“Hapana, Kelly.”
“Hapana nini? Kama ungelikubali kunioa na kuwa na mimi, nisingeishia kwenye mikono ya huyu mlevi. Lakini kwasababu uliona dini yako ni bora kul …”
“Ishia hapo Kelly.” Rajul alimkatisha Kelly maneno. “Tafadhali tusianze kujadili yaliyopita. Hatuwezi kuyabadilisha abadani.”
Kelly hakutia tena neno. Alitikisa kichwa akaendelea na zoezi lake la kucheza na majeraha ya Stanis.
***
“Hatujafanikiwa, mkuu.” Alisema mwanaume mmoja wa kazi. “Tumetafuta jiji zima lakini hatujampata kabisa.”
“Mnasemaje?” Kim aliuliza akiwatizama watumishi wake watano. “Hamjawapata kivipi?”
“Tumetafute kote mheshimiwa. Kote!”
Kim alibamiza meza kwanguvu, akafoka:
“Hamjatafuta vya kutosha! Nendeni mkatafute kwa mara nyingine. Haraka!”
Wanaume wale walitizama kisha wakatoka ndani ya ofisi ya bwana Kim na kwenda kwenye gari lao. Kwa mara ya pili walizunguka jiji zima wakitumia picha za watu wanaowatafuta kuulizia kila mahali lakini wasifanikiwe kabisa. Mpaka jua linazama na usiku unautwaa ulimwengu, walikuwa kapa. Walirejea ofisini kwa mkuu wao wakampasha habari – Rajul na Stanis hawapo jijini.
“Naombeni mnipishe.” Kim aliwaambia watumishi wake. Walitoka ndani ya ofisi wakamuacha mkuu wao akiwaza na kuwazua.
Baada ya muda mfupi aliwaita wanaume hao wa kazi, akawapatia ujumbe na kuwataka waupeleke makao makuu ya polisi. Ujumbe huo ulipofika, matangazo yakaanza kurushwa redioni na kwenye chaneli za televisheni yakiambatana na picha za Rajul na Stanis.
‘Watuhumiwa hawa wa mauaji wanatafutwa na jeshi la polisi. Popote watakapoonekana tafadhali tunaomba utoe taarifa kwenye namba zifuatazo: Zawadi zitatolewa kwa yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa sahihi.’
***
“Fungua mlango wewe mbwa jike!” Sauti ya nzito ya kiume ilipaza toka mlangoni.
Kelly alitazama saa ya ukutani akaona ni saa saba usiku. Alijinyanyua toka kwenye kochi alipokuwa amelala akauendea mlango na kufungua.
“Nini kilichokufanya uchelewe kufungua mlango?” Aliuliza mwanaume huyo aliyefunguliwa. Alikuwa ni mzee wa makadirio ya miaka sitini na mbili mpaka na tano. Alivalia kapelo iliyochoka. Mkononi alibebelea chupa ya bia. Macho yake yalikuwa mekundu yanarembua. Alikuwa hawezi kusimama vizuri bali anayumba yumba kana kwamba miguu imepoteza balansi.
“Nimekuuliza kwanini umechelewa kufungua mlango?”
“Johnny, nilikuwa nimelala.”
“Umelala?” Mwanaume huyo aliuliza alafu akacheka. “Umelala na mumeo hajarudi nyumbani?”
Kelly hakusema kitu. Alitoka hapo mlangoni akaenda kukaa kwenye kochi.
“Kwahiyo ninayoyaongea siyo ya maana, umeamua uondoke?”
“Tafadhali, nakuomba unyamaze.” Kelly alisema kwa upole.
Mwanaume yule akaingia ndani pasipo kufunga mlango. Alimsogelea Kelly akamuuliza:
“Unaniambiaje we mwanamke?”
Kelly kimya.
“Unaniambia ninyamaze? Kwangu?”
Mwanaume huyo alimzaba kibao Kelly, Kelly akapiga kelele kali za maumivu. Kelele hizo zilimshitua Rajul toka usingizini akaketi na kutega sikio lake. Aliendelea kusikia kelele za kilio za Kelly, mwishowe uvumilivu ukamshinda akaenda huko sebuleni.
“Inatosha!” Rajul alifoka akimtizama mume wake Kelly, Johnny.
“Wewe ni nani? Na unafanya nini nyumbani kwangu?” Johnny aliuliza.
“Mimi ni Rajul. Nimekuja kwa rafiki yangu Kelly kumuomba msaada wa kitabibu. Nimekuja na rafiki yangu anaumwa.”
“Oooh Rajul!” Johnny alisema kwa kebehi kisha akamtizama Kelly.
“Kumbe huyu ndio Rajul? Naona amekufata sasa, unh? Umeamua kumleta huyu malaya wako mpaka nyumbani!”
Kelly kimya.
“Sina mahusiano yoyote na Kelly.” Rajul alijitetea. “ Ni rafiki yangu tu!”
“Naona!” Johnny akasema. “Naona kweli ni rafiki yako.”
Alinyanyua mkono wake ampige Kelly ila ghafla akavamiwa na Rajul akamwagiwa chini. Walipambana wakirushiana huku na huko. Kelly aliwataka waache kupigana lakini hakuna aliyemsikia, waliparangana mpaka pale Johnny alipotulia kimya kama mtu aliyekufa.
“Rajul, umemuua?” Kelly aliuliza.
“Hapana.” Rajul akamjibu. “Atakuwa amepoteza fahamu tu.”
“Sasa?”
“Itabidi niondoke kabla hajazinduka.”
“Utaenda wapi usiku huu?”
“Popote pale.”
“Hapana. Kaa hapa hapa mpaka asubuhi ndio uende.”
Kelly aliposema hayo alimkumbatia Rajul kwanguvu akambusu shavuni.
“Ahsante.” Alisema.
“Karibu.” Rajul akamjibu. “Nenda kalale sasa.”
Kelly na Rajul walienda kwenye vyumba vyao wakafunga mlango na kuzima taa.
Baada ya masaa kadhaa, Johnny aliamka akishikilia kichwa chake kwa maumivu. Alijikokota akaenda chumbani kwake alipogonga mlango pasipo majibu. Alirudi sebuleni akawasha televisheni na kujilaza kwenye kochi. Kabla usingizi haujamkomba, akaona tangazo la Rajul na Stanis.
‘Watuhumiwa hawa wa mauaji wanatafutwa na jeshi la polisi. Popote watakapoonekana tafadhali tunaomba utoe taarifa kwenye namba zifuatazo: Zawadi zitatolewa kwa yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa sahihi.’
Macho yalimtoka kwa mshangao, akajilamba kwa tamaa.
“Mungu wangu. Huyu atakuwa Rajul na mwenzake bila shaka!”
Haraka alifuata simu ya mezani akatia namba alizoziona kwenye kioo cha televisheni na kuweka simu sikioni.
“Nimewaona hao watu mnaowatafuta … wapo nyumbani kwangu …”
Alipomaliza kutoa taarifa zote muhimu akarudi kwenye kochi na kujilaza. Alitabasamu muda wote kila alipokumbuka lile donge nono la pesa lililoahidiwa. Hata pale alipolala aliota yu tajiri haswa, akitapanya pesa anavyotaka.
Alikunja kushtushwa na hodi mlangoni ikiwa ni majira ya saa moja asubuhi. Alinyanyuka upesi akauendea mlango na kufungua, akakutana na wanaume watano wa bwana Kim.
“Bila shaka ni wewe uliyetoa taarifa polisi.”
“Ndio! Ndio mimi.”
“Wapo wapi?”
“Wapo chumbani. Twendeni.”
Waliongozana mpaka chumba cha wageni wakafungua mlango na kuingia ndani.
“Wapo wapi?”
Aliuliza mwanaume mmoja akimtizama Johnny.
“Walikuwepo humu.” Johnny alisema. “Watakuwa wametoroka.”
Mwanaume mmoja aliona tone la damu sakafuni, alichuchumaa akafuta tone hilo na kidole chake kisha akailamba.
“Wapo karibu.” Aliwaambia wenzake. “Damu bado fresh, hawajatoka muda mrefu.”
Haraka wanaume hao wakatoka ndani ya chumba, Johnny akawaita.
“Pesa yangu?”
Wanaume wale watano wakatazamana kisha mmoja akajiteua na kumfuata Johnny.
“Unasema?”
“Pesa yangu.” Johny alirudia kauli. “Si nimewapa taarifa.”
Mwanaume yule alimzawadia Johnny teke zito la kifua. Johnny akarushwa na kujibamiza ukutani kwanguvu. Alidondoka chini damu zikimtoka mdomoni na puani. Kifua kilikuwa nyang’anyang’a.
Wanaume wale watano walitoka ndani ya nyumba hiyo wakagawana pande za kusaka watu wao. Kwa kutumia pua kunusa kama wanyama, kwa kutumia mbio zao kama simba, walitawanyika kutekeleza walichoagizwa.
Umbali wa nusu kilomita wa mwanaume aliyeelekea upande wa mashariki ndipo alipokuwepo Rajul, Stanis na Kelly. Walikuwa wanatembea taratibu wakimsaidia Stanis kutembea. Walikuwa kwenye barabara nyembamba ikomeayo baharini baada ya mwendo wa kama dakika thelathini.
Wakiwa wamebakiza mwendo wa robo saa kufikia maji ya bahari, mlio wa bunduki uliwashitua, mlio huo ulienda sawia na kilio cha Kelly. Risasi ilikuwa imekita kwenye mgongo wa mwanamke huyo. Alidondoka chini akiachama mdomo. Rajul alipotizama ilipotokea risasi hiyo, akamuona mwanaume mmoja wa kazi akija kwa kasi.
“Ondoka, Rajul!” Kelly alipaza sauti. “Nenda, nitakuwa sawa.”
“Hapana siwezi nikakuacha hapa.” Rajul alisema akimtizama Kelly kwa huruma.
“Rajul, kama wakikukuta hapa nini itakuwa juhudi zako zote hizo tokea mwanzo?” Kelly aliuliza. “Nenda. Najua hawanihitaji mimi bali wewe na mwenzako. Nenda uttizame chini ya mnazi mrefu kuliko yote utaona mtumbwi. Nenda!”
Kishingo upande Rajul akaondoka. Alimbeba Stanis mgongoni akakimbia naye mpaka baharini akipunyuliwa na risasi. Huko alivuta mtumbwi na kujiweka na Stanis akawasha mashine na kuanza kukata maji.
Mwanaume wa Kim alifika ukingoni mwa bahari akiwa amechelewa. Alirusha risasi lakini hazikusaidia, Rajul na Stanis walilala ndani ya boti hivyo wakawa salama. Hata pale risasi zilipolenga kuitoboa boti hiyo, ilishindikana kwa kwenda kando.
Mwanaume huyo aliposhindwa kumalizana na kazi yake hiyo aligeuza shingo yake akamtazama Kelly. Upesi alimrudia mwanamke huyo. Kelly alijivuta akirudi nyuma. Aliomba aachiwe uhai wake lakini haikumsaidia. Alimiminiwa risasi na mwanaume huyo pasipo tone la huruma, hiyo ikawa salamu kwa Rajul aliyeishia kutoa machozi akitizama tukio hilo kwa mbali.
Mwanaume huyo akachomoa simu yake mfukoni na kuwataarifu wenzake upande walengwa wao walipoelekea. Hakuchukua tena muda hapo, akajiondokea.
Ndani ya muda mfupi, kundi la wanaume watano wa Kim likawa tayari limewasili kwenye mwambao wa bahari unaoshukiwa kuwapokea wageni wanaowatafuta – Rajul na Stanis. Waliona boti iliyowasafirisha watu hao lakini ndani hakukuwa na mtu isipokuwa tu mabaki ya damu yaliyotapakaa sehemu mbali mbali. Walijigawa wakaelekea pande tofauti kwa ajili ya kuwatafuta watu hao, ila mpaka yafika jioni hakukuwa na matokeo mazuri – wanaowatafuta hawakuonekana popote.
Kwenye majira ya saa kumi jioni uwanja mkubwa wa ndege wa Bermuda ulipokea ndege mbili kubwa: Emirates Airways na British Airlines. Toka ndani ya ndege kubwa nyeupe yenye rangi ya kijani na nyekundu mkiani, Emirates Airways, Vitalis akiongozana na wanakundi wenzake: Kaguta, Miraji, Bakari na Bernadetha walishuka wakiwa wamebebelea mabegi ya kukidhi juhudi za mikono yao.
Waliongozana mpaka nje ya uwanja wakajiweka ndani ya taksi iliyokomea kwenye mojawapo ya hoteli ya hadhi ya kati, huko wakachukua vyumba viwili tu wakikukabaliana kujigawa watatu kwa wawili, Vitalis akiangukia kukaa na Bernadetha chumba kimoja baada ya majibizano ya sekunde kadhaa.
Hawakulenga kufanya lolote kwa hiyo siku zaidi ya kupumzika waondoe uchovu wa safari iliyowagharimu siku mbili njiani. Bernadetha akiwa amejilaza kwenye kitanda kikubwa ameshapotelea usingizini, Vitalis alikuwa ameketi sofani miguu yake imepandia mezani kwa kunyooshwa. Ilikuwa ni saa mbili sasa ya usiku. Televisheni kubwa iliyobandikwa ukutani ilikuwa inaonyesha matukio kadhaa ya siku hiyo iliyokuwa inaelekea kuisha. Angalau kwa kuikodolea macho, Vitalis alijipata akiwa na kitu cha kumsogezea muda baada ya kukosa kabisa usingizi.
Aliendea jokofu akatoa kinywaji cha rangi nyekundu iliyoiva kikiwa kimewekwa kwenye chupa ya kioo mithili ya bilauri. Aliitizama chupa hiyo akabinua mdomo, itakuwa tu ni kiywaji hawawezi kutia sumu ndani ya jokofu la wageni. Aliweka chupa hiyo juu ya meza ndogo ya kioo iliyokaa karibu na sofa akaendelea kukodolea televisheni akinywa kinywaji hicho mafundo ya mbalimbali. Isimchukue muda mrefu akaona habari iliyokamata muda wake – kifo cha watu wawili: mtu na mkewe, siku moja maeneo tofauti.
Taarifa hiyo ilionyesha miili ya marehemu hao huku washuhudiaji wakieleza yale waliyopata kuyaona ama kuyasikia. Mwanaume alitapanywa kifua huku mkewe akishindiliwa risasi zisizo na idadi.
“Tuliwaona wanaume watano majira ya asubuhi. Hatukujua nini walifanya humo ndani ila tokea walivyoondoka hatukumuona tena Johnny mpaka sasa tulipopata taarifa amekufa.” Alisema shuhuda mmoja.
“Asubuhi ya mapema wakati mimi na mke wangu tunajiandaa kwa ajili ya kwenda shambani, tulimuona Kelly akitoka na wanaume wawili ndani ya nyumba yake. Walikuwa wanatembea kwa kujikongoja wakielekea upande wa baharini, hatokumuona tena mpaka pale tulipokuja kuambiwa ameuwawa.” Alisema shuhuda mwingine.
“Japokuwa niliwaona hao wanaume kwa mbali majira hayo ya asubuhi, ila nina uhakika ndio wale wanaotangazwa kwenye Tv kama watuhumiwa wa mauaji.” Alisema shuhuda mwingine.
Vitalis alifuatilia habari hiyo kwa makini. Alijikuta akiamini kuna jambo ambalo ataling’amua na likawa na umuhimu kwenye kile walichokuja kukifanya ndani ya nchi hiyo. Hii ni nchi ndogo yenye jiji dogo, kila la uhalifu linalojiri humu basi lazima litakuwa na mkono wa mtu mkubwa, aliamini. Na mtu huyo mkubwa anaweza kuwa Kim.
Kwa usiku wote hata pale taarifa ya habari ilipokoma, aliendelea kuwaza na kuwazua juu ya kile alichokiona. Nani wale waliouwawa? Kwanini wameuwawa? Nani kawaua? Wakina nani wanaotafutwa kwa kesi ya mauaji? Mbona wanatafutwa kinyemela? Maswali hayo yalisindikiza usiku wake barabara mpaka asubuhi alipoamka na kwenda kutwaa mojawapo ya gazeti apate habari kwa undani.
Kitu kipya alichokipata gazetini ni kuhabarishwa kuwa mmojawapo wa wanaume wale wanaotafutwa kwa kutangaziwa kesi ya mauaji kwenye televisheni, aliwahi kuwa mfanyakazi wa Kim Salvatore – Stanis Laughen. Hapo Vitalis akapata walakini zaidi na msukumo wa kufuatilia hilo. Alipata maswali zaidi ambayo aliona jukumu la kuyatafutia majibu.
“Nataka utafute chochote unachoweza kupata juu ya watu hao wanaotafutwa kwa kesi ya mauaji pia matukio yote ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ndani ya jiji.” Vitalis alimuagiza Bakari.
Pasipo kukawia, Bakari alivalia njuga swala hilo kwa kuanza kuperuzi mitandaoni. Kwa msaada mkubwa wa mtandao wa Youtube, alipata video za taarifa za nyuma akapakua video hizo na kuzitunza kisha akaziwasilisha kwa Vitalis.
“Sioni haja ya kujivuta, Vitalis!” Kaguta alifoka. “Muda unaenda na hatuna muda wa kupoteza zaidi. Tunafahamu mahali alipo Kim, tunangoja nini kumfuata?”
Uso wa Kaguta ulikuwa umejazwa nondo za hasira, hata matendo yake aliyokuwa anayaonyesha wakati akiongea yalisema hayo. Aliona ni upotezaji wa muda, ya nini kuperuzi na mnajua chaka la adui yenu? Huko si kuuzunguka mbuyu? Aliwatizama wenzake akawaona waoga.
“Kaguta, si kila jambo latibiwa na hasira, mengine yahitaji akili.” Vitalis alihasa. “Huwezi kwenda tu kumvamia Kim kwakuwa unafahamu anapokaa, la hasha! Unajua amejipangaje? Unajua udhaifu wake? Unajua wapi umpige akaumia?”
Kaguta aliutupa mkono wake wa kuume kwa kupuuza.
“Unadhani itatuchukua muda gani kuyajua yote hayo? Tutakaa tungoje?”
“Haitochukua muda mrefu. Tunajua hatuna muda mrefu wa kukaa hapa. Hata pesa tuliyonayo ni haba.”
“Nanyi wote mnaaminii hilo?” Kaguta aliuliza akiwatizama wengineo: Bernadetha, Miraji na Bakari. Hawakujibu lakini sura zao zilionyesha wapo pamoja na Vitalis. Kaguta alitikisa kichwa akisaga meno, alitoka ndani akaubamiza mlango kwanguvu. Vitalis alishusha pumzi ndefu akawatizama wenzake.
“Najua wote hapa tumepoteza watu wetu tunaowapenda kwasababu ya huyu mdhalimu, Kim. Lakini kama tukiacha hasira zikashika uwezo wetu wa kufikiri, basi nasi tutaishia huko walipoishia waliotutangulia.”
Alifuatilia video zote alizokabidhiwa na Bakari, akapata yale aliyokuwa anayataka. Hakusita kuwashirikisha wenzake.
“Kuna wanaume wawili wanatafutwa na polisi kwa kesi ya mauaji, ila nachelea kusema wanaume hao wanatafutwa na Kim kwasababu ambayo bado hatujaijua. Kwanini nasema hivyo na kwanini hili jambo ni muhimu kwetu? Kwa mujibu wa taarifa ya habari ya jana usiku, mwanaume mmoja aliyeshutumiwa kuwapokea wanaume hao wawili wanaotafutwa, aliuwawa kwa kuvunja mbavu nyang’anyang’a. Pigo hilo la kuvunjwa mbavu liliwahi kujiri hapo awali kwenye Temple mojawapo hapa jijini ambapo ndipo mmojawapo wa wanaume anayetafutwa alikuwa anaishi. Kwahiyo mtu aliyefanya mauaji hayo huko temple ndiye aliyefanya mauaji hayo huko kijijini, lengo likiwa ni lile lile la kumtafuta mtu wao. Hili jambo la polisi kuwatafuta ni ghelesha tu, kwani kwenye matukio yote hayo hakuna tukio hata moja polisi walipohusika zaidi ya wanaume watano wanaotajwa, na hapa ndipo ninanapopata uhakika wa kusema ni Kim anahusika kwasababu ya nguvu yake ya kutawala vyombo vya dola. Kim anatumia ushawishi wa polisi kuwapata anaowatafuta. Swali la kujiuliza ni kwamba, mtumishi wa Kim kwanini yupo na huyo mtu wanayetafutwa naye? Na kwanini Kim anawatafuta kwa hali na mali?”
Miraji alisafisha koo lake akauliza:
“Kwahiyo unaona kuna umuhimu wa kuwatafuta watu hao?”
“Hakika!” Vitalis alijibu. “Kim hatafuti watu ambao sio hatari kwake. Hatafuti watu ambao hawana umuhimu kwake. Kuna jambo ambalo hawa watu wawili wanalo, laweza likaturahishia kazi zaidi.”
“Sasa tutawapatia wapi hao watu?” Bernadetha aliuliza.
“Popote pale.” Vitalis akajibu. Alimtizama Bakari akamwambia:
“Nahitaji picha za hao watu zikiwa manipulated. Wakiwa wana ndevu, wakiwa na nywele ndefu, wakiwa hawana nywele kabisa, wakiwa wamevaa kofia, wakiwa wamesuka, na kadhalika. Nataka nipate picha zao wakiwa kwenye mazingira yoyote ambayo wanaweza wakajivika.”
Bakari akatabasamu.
“Hilo tayari lishakwisha.” Alisema kwa kujiamini.
Saa kumi jioni, ghorofa ya tano Fade Tourism Hotel.
Meza moja iliyokaa katikati mwa uwanja iliambatana na viti vyake vinne vilivyopendeza kwa kufungiwa urembo wa riboni. Meza hiyo ilikuwa pweke wakati uwanja wa hoteli ukiwa umejazwa na watu toka mataifa mbalimbali, wengi wao walikaa kwenye ukuta wa hoteli hiyo ili wapate mwanya wa kutizama na kuona mandhari ya nje yaliyokuwa yanavutia kwa majengo na muonekano ang’avu wa bahari.
Ndani ya majira hayo hayo, Vitalis akajiri kwenye hoteli hiyo akiongozana na Bakari, Miraji na Bernadetha. Alitizama kutafuta nafasi ya kuketi akaiona moja tu, ya katikati, hawakuwa na budi walifuata nafasi hiyo wakajiweka kabla ya muda mfupi mhudumu kuwasili na kuwauliza haja zao. Waliagiza vyakula vya bahari ‘sea food’ pamoja na vinywaji vyepesi, baada tu ya muda mfupi wakaletewa mahitaji yao wakikaribishwa kwa ukarimu.
“Kwahiyo Kaguta amegoma kabisa?” Vitalis aliuliza akila.
“Ndio.” Miraji alijibu. “Amesema hatoenda wala kushiriki chochote isipokuwa tu kwenda kumuua Kim.”
Kukawa kimywa wakila.
“Unajua Kaguta ameathirika na kifo cha Sandra. Amekuwa mpweke sana na hataki juhudi za kutafuta furaha. Amekuwa akiwaza kumuua Kim tu mara mia ya mwanzoni.” Bernadetha alisema. Wote walimtizama kisha wakaendelea kula.
“Namjua Kaguta, ni rafiki yangu tangu utotoni. Natumai hasira zake hizi za sasa hazitomponza.” Alisema Vitalis kisha akashushia maneno hayo na kinywaji. Hakuna mtu mwingine aliyeongea tena kwa dakika kama tano, mpaka pale Miraji aliponong’oneza:
“Tayari kuna nafasi.”
Waligeuka wakatazama ukutani, wakaona kuna watu wananyanyuka wapate kuondoka. Vitalis alitikisa kichwa akasema akinyanyuka:
“Twende.”
Waliendea meza hiyo wakakaa. Nyuso zao zilielekea nje ya jengo hilo wakitazama mandhari – ila si ya majengo ama bahari kama walivyokuwa wanafanya wengineo, bali wakitazama jengo kubwa la Kim Salvatore lililopakana na hoteli hiyo. Bakari alitumia simu yake kupiga picha kwenye kila pande ya hilo jengo akihakikisha hakuna analojinyima.
“Ni eneo kubwa, muda si mrefu litakuwa mahali petu pa kuchezea.” Vitalis alisema akiendelea kukodolea.
“Itakuwa rahisi kama tukija wakati wa usiku.” Miraji alitoa wazo. “Tutaingilia mlango ule wa nyuma kisha tutatumia ile miti na yale majengo kama sehemu za kujifichia …”
Walishituliwa na sauti ya mhudumu ambaye alihaha kwa sekunde kadhaa kuwatafuta. Alikuwa ameleta ‘bill’ ya chakula, Vitalis alitoa fedha akamkabidhi. Mhudumu aliondoka upesi akikunja shingo yake kuwatizama wageni wake kwa macho ya shaka. Alielekea eneo la mapokezi ya uwanja huo akamnong’oneza mwenzake huku akiwaonyeshea kidole wakina Vitalis. Pasipo kukawia, aliyepewa habari alinyanyua simu ya mezani akapiga. Wakati anaongea macho yake yalikuwa yakiwatizama wakina Vitalis kwa umakini. Alitikisa kichwa mara mbili akairudisha simu mezani.
Baadaye ndani ya siku, kukiwa tayari giza, wanaume watano wa Kim walifika eneo hilo wakakutana na mhudumu wa mapokezi. Walitumia kamera za ndani ya jengo kuwatizama wakina Vitalis, wakachukua huo mkanda na kuupeleka kwa mkuu wao, Kim.
Baada ya mkanda huo kukoma, Kim alijikuta akicheka kwanguvu ila macho yake yakiwa wima. Alipiga meza yake kwanguvu nusura ipasuke, akafoka:
“Nataka watu hawa mikononi mwangu!” Alisema na macho mekundu yaliyotoka nje. Uso wake ulibadilika rangi ukawa mwekundu. Alihema kama ametoka mbioni, akaongezea:
“Kwatafuteni hoteli zote! Zote! Nawataka hapa! Mmenisikia? Nawataka hapa!”
Baada ya kusema hayo, wanaume wale watano wakatoka nje. Kim aliketi kwenye kiti uso wake bado ukiwa mwekundu. Alijimiminia kahawa kikombeni apate kunywa kushusha ghadhabu. Alinyanyua kikombe akaona mikono inatetemeka. Alitupia kikombe chini kwanguvu kikapasuka. Alisaga meno akisema:
“Kwahiyo wameona wanifuate kabisa mpaka kwangu.”
Alishika peni akaiminya kwanguvu mpaka ikapasuka.
“Nitawaonyesha mimi ni nani. Nitahikisha wanaomba kifo wakilia na kusaga meno.”
Alikosa pumzi kwa jazba kumjaza kifua. Alinyanyua chupa ya kahawa akajimiminia mdomoni.
***
Ni majira ya saa tatu usiku Kaguta akitoka nje ya hoteli wanayoishi akiwa amevalia sweta jepesi, suruali nyeusi ya kadeti na viatu vya wazi.
Kulikuwa kuna kaubaridi kalichofanya watu waheme moshi na kutia mikono yao mifukoni. Kwa mbali pia kulikuwa na vimanyunyu vya mvua vilivyowafanya watu wasio na miamvuli watembee upesi kwenda waelekeapo.
Kaguta alitazama kushoto na kulia kwake kisha akasugua viganja vya mikono yake na kuvitia ndani ya mifuko ya suruali. Alitembea kuelekea upande wa kushoto wa hoteli kwa mwendo wa ukakamavu akielekezea kichwa chini.
Nyuma yake, ng’ambo ya barabara, kulikuwa na gari nyeusi Range modeli mpya. Ndani ya gari hilo alikuwepo mtu aliyemtazama kwa ukaribu pasipo yeye kujua.
Baada ya kutembea kwa dakika kama ishirini kwa kufuata barabara ya lami, Kaguta aliingia kwenye kibanda kilichoandikwa ‘LOL Café! – Delicious food’, aliendea kwenye meza moja pweke akaketi baada ya kuagiza chakula chepesi.
Macho yake yalikuwa meupe lakini yaliyoundwa kwa huzuni na upweke, hayakufurahia mandhari nzuri ya eneo hilo kwa kuyatazama bali kwa kuyakwepa yakitizama meza kana kwamba ni mchanga uliomeza shilingi yake iliyopotea.
Alikaa hivyo mpaka pale aliposhituliwa na sauti ya kike iliyomsalimu. Alinyanyua uso wake akakutana na mwanadada mrembo aliyevalia koti la kijivu lililombana, macho yake makubwa ya kurembua na mdomo mdogo uliojikusanya vema ukizungukwa na mashavu mekundu. Nywele za mwanamke huyo zilikuwa rangi ya ‘gold’ zikichomoza toka kwenye kikofia cha koti alilovaa. Alikuwa ananukia vizuri. Aliminya lips zake akaachama mdomo wazi akimngojea Kaguta ajibu salamu yake.
“Safi, habari yako?”
“Poa, kuna mtu hapa?”
“Hapana, hamna mtu.”
“Naweza nikakaribia?”
“Bila shaka.”
Mwanadada alikaa akafungua begi lake dogo na kutoa simu yake, muda huo Kaguta alikuwa anamtizama kwa kubutwaa. Ni kana kwamba alikuwa anampekua mwanamke huyo kama ni binadamu ama malaika. Alikwapuliwa kwenye butwaa hilo na mhudumu aliyeleta chakula chake.
“Karibu.”
“Ahsante.” Kaguta alijibu akitikisa kichwa chake kisha akamtazama mwanadada aliyeketi karibu yake.
“Karibu.”
“Ahsante, changu kinakuja.” Alijibu mwanadada kwa kutabasamu. Meno yake yalikuwe meupe yakipangana kwa adabu.
Mwanaume mmoja aliyevalia suti nyeusi pasipo tai aliingia kwenye kibanda hiko maridadi akaketi karibu na mlango. Macho yake yalikuwa yanamtizama Kaguta na yule mwanadada. Si bure alikuwa ndiye yule aliyekuwa anamchora Kaguta akiwa ndani ya gari. Mhudumu alimfuata bwana huyo na kumuuliza mahitaji yake, akaagiza kahawa pekee.
“Unaweza tu ukala cha kwangu wakati unasubiri chako.” Kaguta alisema kwa ukarimu. Sura yake ilikuwa imetua yale aliyokuwa ameyabebelea hapo awali. Kabla mwanadada hajajibu, mhudumu aliwasili akamkabidhi chakula, akiwa anakula wakawa wanateta na Kaguta ya hapa na pale. Walifanya hivyo mpaka pale walipomaliza chakula na kupeana namna za kuwasiliana.
Kabla hawajatoka ndani ya kibanda, mwanaume yule aliyekuwa anawatizama aliwatangulia kwa kutoka. Haikujulikana wapi alielekea. Kaguta alitoka na yule mwanadada wakaongozana kwa hatua kadhaa kabla hawajaachana. Walipeana mikono kila mtu akaenda upande wake.
“Umefanikiwa?” Aliuliza mwanaume yule aliyekuwa anamfuatilia Kaguta. Alikuwemo ndani ya gari aina ya Range nyeusi akiwa ameketi kiti cha mbele kabisa.
“Ndio, nimefanikiwa.” Sauti ya kike ilijibu. La haula! Alikuwa ndiye yule mwanamke aliyeketi na Kaguta kibandani.
Gari liliwashwa likasonga. Baada ya sekunde kadhaa walimtia Kaguta machoni akiwa anatembea. Ilichukua muda mfupi, Kaguta akadondoka chini kama mzigo. Haraka gari lilisimama, mwanaume yule na mwanadada wakatoka kwenye gari, wakambeba Kaguta na kumtia kwenye gari kisha wakaondoka kwa kasi.
Ndani ya ‘supermarket’ iliyokuwa kando kando ya barabara, kulikuwa na mwanaume aliyeshuhudia mambo hayo yakichukua nafasi kwa haraka. Alikuwa mwanaume mfupi mnene mwenye kiwaraza. Alivalia shati jeupe na tai yenye mistari mekundu na bluu, suruali yake ya kijivu. Macho yake yalikuwa yanasaidiwa na miwani ndogo ya macho. Mkononi alikuwa ameshikilia chocolate ambayo haikupelekwa mdomoni kwasababu alikuwa ameduwazwa na kilichokuwa kinatokea mbele ya macho yake.
Alivuta droo akatoa bunduki ndogo ‘mguu wa kuku’. Alifuata mlango wa kioo wa supermarket akatoka nje na kuchungulia. Macho yake yalitwaa hofu. Hakudumu kuchungulia akarudi ndani. Alinyanyua simu ya mezani akaiweka sikioni baada ya kutia namba kadhaa.
“Nakuomba uje haraka ofisini tufunge … Ndio, sasa hivi. Usiniulize maswali mengi.”
Alirudisha simu mezani akaketi.
Mara kwa mara alirushia macho yake kule nje aliposhuhudia ya kushuhudia, ni kana kwamba aliambiwa tukio hilo laweza kujirudia tena. Mara chache alipotazama ndani basi alikodolea saa yake ya mkononi. Kutokana na upungufu wa wateja kutoka na usiku kuwa mwingi, alijikuta akifanya hayo mazoezi mara kwa mara.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilichukua muda mrefu sasa Kaguta hajarejea, Miraji na Bakari wakapata mashaka. Kwa mujibu wa saa ya ukutani alikuwa anatimiza masaa matano sasa akiwa nje. Sio masaa matano ya kawaida, masaa matano ya usiku tena kwenye nchi ngeni, nchi ya adui.
Waliona yapaswa Vitalis kushirikishwa. Miraji aliendea chumba alalacho Vitalis na Bernadetha akabofya kengele. Baada tu ya muda mfupi, Vitalis akafungua mlango. Alikuwa amevalia bukta fupi tu. Kifua chake cha mazoezi kilichobebelea nywele kadhaa kilikuwa wazi. Macho yake yalikuwa yamepooza ila si kwa kulala, aidha kuna kitu alikuwa anafanya ama anakitizama.
“Kaguta hayupo ndani, na hajarudi mpaka sasa hivi tokea alivyotoka jioni hii.” Alisema Miraji. Uso wake ulieleza shaka.
“Ameenda wapi?” Vitalis aliuliza. Alikuwa ametoa macho yake nje, uso wake ameukunja. Haikuwa habari njema hiyo.
“Alituaga anaenda café kubadili chakula.”
‘Café ipi?” Vitalis aliwahi kuuliza. Alionekana kupoteza subira.
“Sijui! Alisema tu café.”
Vitalis aliingia ndani ya chumba, baada tu ya dakika moja alitoka nje akiwa amevalia suruali ya jeans na raba huku akifunga vifungo vya shati.
“Acha niende. Bakia hapa hapa utizame usalama, sawa?”
“Kwanini tusiende wote?”
“Miraji, ni hatari. Nisingependa kumhatarisha ama kumpoteza yeyote kabla ya kuanza kutimiza mipango yetu. Baki hapa, huwezi jua labda ni mchezo wa kututawanya. Inabidi tuwe wa tahadhari sana.”
Kishingo upande, Miraji aliridhia. Vitalis aliondoka upesi akimuacha mwanaume huyo akimtazama anavyoyoma, hata mlango hakuufunga.
Alipopotea, Miraji alitazama ndani kwa kupitia mwanya ulioachwa na mlango akaona karatasi kubwa jeupe limelazwa mezani. Alijaribu kulivutia taswira ila hakuipata vema kutoka na umbali aliopo. Hakuingia ndani, labda alihofia anaweza mkuta mama yake ameketi vibaya. Alifunga mlango akarejea chumbani kwake alipompasha Bakari habari.
Vitalis alishuka ngazi upesi akajikuta kaunta alipotoa taarifa ya kutoka kwake. Akiwa kwenye mwendo wa kasi, alitoka nje ya hoteli.
Watu walikuwa wachache sana mtaani, pia na magari. Ungeweza kuyahesabu pasipo shida. Hali ya ubaridi bado iliendelea kutawala na kila mtu aliyeonekana basi alikuwa amevalia nguo nzito ya kumsitiri, isipokuwa Vitalis.
Vitalis aliperuzi huku na huko asione cha maana. Alimuuliza mtu mmoja aliyekutana naye barabarani kuhusu café iliyoko karibu akaelekezwa. Alikata mtaa mpaka ilipo café hiyo. Ilikuwa ndiyo ile aliyokuwamo Kaguta masaa kadhaa nyuma. Alikuta imefungwa tayari.
Alishusha pumzi ndefu akitafakuri. Hakuwa na pa kwenda wala cha kufanya zaidi. Moyo wake ulijazwa na hofu juu ya wapi alipo Kaguta, na usalama wake.
Alishika kiuno akawa anarejea alipotokea taratibu. Uso wake aliuelekezea chini akitazama sakafu iliyopokea lami pana ya njia nne. Alipofika maeneo ya supermarket akaona kitu. Ilikuwa ni bangili ipo chini. Malighafi yake ya metali iling’aa na kudaka macho ya Vitalis.
Aliinama akaiokota na kuitizama vema.
“Kaguta.”
Vitalis alijikuta akisema kwa bumbuwazi. Aliikumbuka ile bangili, ndio. Kaguta aliinunua bangili hiyo nje ya airport baada tu ya kutua. Sasa aliikuta barabarani na si mkononi mwa Kaguta. Yupo wapi?
Vitalis alitazama kushoto kwake akaona jengo la supermarket lililo gizani, lilikuwa tayari limefungwa. Hakuwepo wa kumuuliza chochote.
Alifuata barabara usawa wa eneo bangili ilipodondokea, akatizama vema. Hakuona kitu. Alitoa simu mfukoni akamulika barabarani hapo akaona alama za mchubuko wa matairi ya magari. Hapo akawa tayari amegundua jambo.
Kitu pekee alichokipata sasa ni kwamba Kaguta ametekwa. Hakukuwa na namna kwamba alidondosha bangili ile mpya aliyovutiwa nayo pindi tu alipoitizama. Hakuingia akilini pia kwamba mwanaume huyo alidondoka chini akaiacha bangili hapo. Kilichooneka kina maana kichwani mwa Vitalis ni kwamba kulikuwa na pambano, Kaguta alishindwa kwa kudondoshewa chini kisha akakwapuliwa na kuingizwa kwenye gari lililoondoka kwa kasi ya kuchubua barabara.
Alisimama akajiuliza:
“Wakina nani watakuwa wamemteka? … Kim? … Ina maana anajua tulipo? Anajua tunapoishi? … Ina mana anatufuatilia?”
Alijikuta anapata hofu. Vipi kama kule hotelini atakuwa ame …?
Alitoa macho kwa uoga.
Haraka alikimbia kwenda hotelini pasipo kuweka kituo popote. Alienda haraka chumbani kwake akafungua mlango, hakukuta mtu. Chumba kilikuwa kitupu lakini kikiwa hovyo, kila kitu kilikuwa shaghalabaghala.
Jasho lilimtoka Vitalis na moyo ulienda mbio kupita kiasi.
Aliendea milango ya bafu na choo akaifungua pasi hodi, napo hakukuta mtu. Alitoka upesi akaenda chumba cha wakina Miraji. Napo huko alikuta kama vile alivyokuta chumba chake, hakukuwa na mtu na kulikuwa hovyo hovyo. Hapo akachoka zaidi. Alihisi ‘joint’ zimepoteza nguvu ghafla.
Alizidiwa kete. Adui alimtangulia mbele hatua moja.
Aliketi kitandani akiwa kama mtu asiyeamini. Kwa muda kidogo akili iligoma kuchambua mambo. Baada ya dakika kumi ama zaidi alinyanyuka akaenda kaunta kukutana na mapokezi na wahudumu.
Aliwaulizia wenzake pasipo mafanikio, hakuna mhudumu aliyesema ameshuhudia chochote. Hata pale Vitalis alipoomba kamera zitumike, hakupewa majibu ya maana.
Haikumuwia vigumu kuelewa hali aliyomo. Kwa yale aliyoyashuhudia aliishia kutambua kwamba: yupo kwenye nchi ya adui, na si tu kwamba yupo ndani ya nchi hiyo, bali yupo ndani ya nchi iliyoshikiliwa na mikono ya adui; mikono yake ipo kila eneo; mikono yake ina nguvu ya kunyonga na kukata hata akiwa ofisini. Mikono yake ni ya chuma.
“Tuwataarifu polisi?” Mwanamapokezi aliuliza.
“Hapana.” Vitalis akajibu. Hakuwa na imani na polisi pia.
Alirejea chumbani akapekenyua kwenye mojawapo ya begi na kutoa fedha alizozitia mfukoni. Kabla hajatoka nje ya chumba hicho aliona kiasi kidogo cha damu chini ukutani, mbali kidogo na mlango. Alisogea eneo hilo akaona damu zaidi kwa chini, ila haikuwa nyingi kiasi cha kumfanya mtu aone upesi ukizingatia ilikuwa zuliani.
Vitalis alitazama damu hiyo ya ukutani akaona imechorewa jambo. Ilikuwa ni kama ka alama ka paa mbili za nyumba zikigusana.
Alitafakari alama hiyo inamaanisha nini kwa dakika moja. Alikuja kugundua baada ya kufananisha taswira ya muonekano wa jengo la Mr Kim na mchoro ule.
likumbuka mojawapo ya eneo waliloliona vema walipokuwa kwenye ile hoteli wakitazama jengo la Kim, ni majengo mawili ya mshenzi uyo yakiwa yamepakana paa. Ina maana Bernadetha na wenzake wamepelekwa huko?
Pasipo na shaka Bernadetha alipigwa kwanza kabla ya kubebwa, hii ni damu yake. Na inaelekea aliambiwa wapi anapelekwa kabla hajabebwa. Hiki alichokiandika ukutani atakuwa alikifanya kwa umakini mkubwa asionekane ili anifikishie mimi taarifa, Vitalis aliwaza.
Alisaga meno yake akikunja ndita kabla hajanyanyuka na kupotelea kusikojulikana.
***
Ilikuwa asubuhi sasa ya saa mbili, jiji la Hamilton lilikuwa bize magari na watu wakipishana.
Miongoni mwa watu walioujaza mji, alikuwamo Vitalis. Alikuwa amevaa koti refu jeusi na kofia ‘cowboy’. Mikono yake aliidumbukiza mfukoni kama mtu anayehisi baridi akitembea kuelekea upande wake wa kaskazini.
Aliona taksi akainyooshea mkono, taksi ikasimama. Aliingia ndani ya taksi hiyo akampa maelekezo dereva ampeleke nje kabisa ya jiji, huko vijijini. Dereva, mwanaume mzee mweusi aliyevalia kapelo iliyochoka na shati la bluu iliyopauka, alimtazama mteja wake huyo kwa mashaka. Alimuuliza:
“Una pesa ya kunilipa kukupeleka kote huko?”
Vitalis alitoa pesa kwenye koti lake, noti kadhaa za dola za kimarekani akamuonyesha dereva, dereva akatikisa kichwa akitabasamu. Alipangua gia akakanyaga mafuta.
Kwa muda wa dakika kama ishirini ama zaidi walitembea pasipo yeyote kuongea. Dereva alimtazama mteja wake kwa kupitia kioo kilicho juu ya kichwa chake mara mbili akamuona mteja wake huyo akitazama nje. Alionekana kuboreka. Alipomtazama kwa mara ya tatu kiooni na kumuona yu vile vile, alimuongelesha.
“Pasipo mashaka, wewe ni mgeni, sio?”
Vitalis alimtazama mzee huyo akatikisa kichwa kukubali.
“Nilivyokuona tu ukinielekeza nikajua wewe ni mgeni. Kama ungekuwa mwenyeji ungepanda basi na si taksi. Ila sio mbaya, umemsaidia mzee wako kuona siku njema leo.”
Vitalis hakusema kitu. Aliendelea kutazama nje.
“Kwanini umeamua kwenda huko?” Dereva aliuliza akimtazama Vitalis kiooni. “Hakuna kitu cha utalii huko zaidi tu ya mashamba.”
“Najua.” Vitalis alijibu kiufupi akiendelea kutazama nje.
Dereva alilazimisha kutabasamu, akaendelea kuongea:
“Kama ukitaka nikutembeze sehemu za utalii, nitakufanyia kwa bei poa sana. Najua sehemu zote za kuvutia ndani ya hii nchi. Umeona namba yangu nyuma ya kiti nilichokaa? Ukintafuta muda wowote siku yoyote nitakufanya ufurahi sana kuwepo hapa.”
“Ahsante.” Vitalis alijibu akitazama nje.
Dereva alibinua mdomo wake akapandisha mabega. Alikaa kimya kwa dakika kama tatu kisha akaanza kuongea tena:
“Kwanini umeamua kwenda huko kijijini? Sio salama sana. Muda si mrefu kuna watu wawili waliuwawa huko. Mmojawao aliuwawa kwa risasi.”
Vitalis kimya.
“Ni tahadhari tu.” Dereva alijitetea kisha akafunga mdomo wake. Baada ya dakika moja, Vitalis aliuliza:
“Watu hao waliofanya mauaji wamekamatwa?”
Bado uso wake ulikuwa unatazama nje.
“Wakamatwe wapi!” Dereva alihororoja. “Tokea mamlaka haya ya nchi yaingie kwenye dola, hakuna muuaji yeyote aliyewahi kukamatwa nchi hii. Hakuna! Tunafanya tu kusikia watu wameuwawa huku na kule. Lakini hakuna aliyewahi kutiwa nguvuni. Hata pale wananchi wanapotoa taarifa, inakuwa kazi bure. Sana sana huyo aliyetoa taarifa naye hatochukua zaidi ya siku moja kuuwawa.”
Hapo Vitalis alihamisha uso wake kutoka nje akamtazama dereva. Macho yake yalionyesha amevutwa hisia.
“Sio kwamba nakutisha.” Dereva alijitetea, “Ila nakupa hali halisi ya nchi hii. Kwa miaka kadhaa tumekuwa tukihofia sana usalama wetu.”
Walikuwa sasa nje ya jiji. Waliacha majengo mazuri marefu mbali wakishika njia kuelekea kijijini.
Dereva bado alikuwa anaongea, Vitalis asitie neno bali tu kumsikiliza.
Haikumchukua muda mrefu baada ya kuacha jiji, Vitalis akagundua wanafuatiliwa. Nyuma yao kulikuwa kuna gari ‘cadillac’ nyeusi ‘tinted’ inakuja kwa kasi. Aliitazama gari hiyo kwa macho makini akitumia vioo vya gari.
Gari hiyo ilipunguza mwendo ilipokaribia taksi, kisha vioo vya viti vya nyuma vikashuka chini wakatoka wanaume wawili kila pande wakiwa wamebebelea bunduki kubwa nzito. Walikuwa wamevalia suti na miwani nyeusi.
“Inama chini!”
Vitalis akamuamuru dereva. Dereva asijue linaloendelea, aliuliza:
“Niiname? Sasa nitaendeshaje?”
Alipomaliza tu hiyo kauli, risasi zilizorushwa hovyo kulenga gari zilimpasua bongo. Gari liliyumbayumba. Vitalis alinyoosha mikono yake akashika usukani, akajaribu kulimudu gari hilo lililozidi kumiminiwa risasi za kutosha.
Alimvutia dereva kiti cha kando, akapata kukaa nafasi nzuri aliyoweza kulimudu gari vema. Mkono wake mmoja ulishikilia usukani huku mwingine ukikanyagia mafuta.
Wanaume wale waliokuwa wanamimina risasi waliacha hilo zoezi wakaingia ndani ya gari na vioo vikafungwa. Sasa gari liliongeza kasi likagonga taksi kwa nyuma kwanguvu. Taksi lilienda mbele mputa mputa. Vitalis alijitahidi sana kulibakiza barabarani. Haraka alijivuta toka nyuma akakaa kwenye kiti cha dereva. Vioo vya pembeni vya gari vilikuwa tayari vimeondolewa na risasi. Vitalis alikuwa anatumia kioo pekee kilicho juu yake kuwatizama maadui.
Alikanyaga mafuta kwanguvu, taksi ikapepea. Nyuma yake ‘cadillac’ nayo iliongeza kasi maradufu ikawa inamfukuzia.
Ilibidi akili itumike sasa. Alikuwa mwenyewe pia akiwa hana silaha. Silaha pekee aliyokuwa nayo ni akili kichwani ambayo kwa muda huo ilikuwa inahangaika kutafuta jibu la jinsi gani atajinasua kwenye janga hilo. Hakukuwa na muda, ilibidi akili ifanye kazi mara mbili ya kawaida.
Kwa kasi kubwa, cadillac ilisogelea taksi. Ilibakia kaumbali kadogo sana gari hilo kubwa libamize taksi. Vitalis alitazama kiooni kwa makini kana kwamba kuna kitu anangojea.
Cadillac ilipomsogelea zaidi, akasema:
“Tayari.”
Ghafla alisogeza taksi pembeni kidogo upande wa kulia kwa kasi ya ajabu kisha akapiga breki kali.
Bodi ya pembeni ya taksi ilimezwa na gari kubwa la Cadillac ambalo liliparamia bodi hiyo na tairi lake moja la kulia. Kutokana na kasi lilikuwemo, cadillac lilinyanyuka juu juu na kupinduka vibaya likibiringita mara sita. Hakuna aliyetoka hai.
Vitalis alikanyaga mafuta ndani ya taksi akaisogelea hiyo cadillac. Alisimamisha kando yake akalitizama kwa kinyaa.
Alitema mate nje ya gari, ptuuh!, akasema akibinua mdomo:
“Wasalimie kuzimu.”
Kisha akatia moto taksi na kutimka zake.
Ilimchukua dakika chache tu kuwasili eneo alilokuwa analihitaji – lile aliloliona kwenye taarifa ya habari.
Kwa msaada wa maelekezo ya hapa na pale aliyopewa na wenyeji, hatimaye alifika mbele ya nyumba ya marehemu Kelly na Johnny.
Ilikuwa pweke kwa kuitazama tu hata kwa nje.
Vitalis aliitazama kisha akashusha pumzi ndefu kabla hajaanza kuchukua hatua kusogea mlangoni.
Pasipo kugonga hodi wala kuhangaika na mlango huo uliokuwa umefungwa, alichambua mazingira. Kwa haraka akaona mkanda wa njano uliosomeka – Police, don’t cross the line, ukiwa kando kando umeachwa pasipo mashiko. Haukuwa na maana tena, ndivyo ambavyo ungesema kutokana na kutokuwepo kwake mahala husika wakati husika.
Vitalis alibinua mdomo wake akijisogeza dirishani mwa nyumba hiyo na kuchungulia ndani.
Sebule ilikuwa shaghalabaghala. Hakukuwa na dalili yoyote ya binadamu.
Vitalis alikunja shingo yake akatazama kushoto mwa nyumba hiyo alipoona nyumba iliyokuwa karibu zaidi zikiwa zinatazamana madirisha ya pembeni.
Alisogelea nyumba hiyo akagonga mlango. Punde akatoka mwanamama mfupi mzee. Nywele zake zilikuwa nyeupe pe uso wake ukikunjamana vilivyo.
Alimtazama Vitalis na macho yake ndani ya miwani kubwa kama vile anajitahidi kuing’amua sura hiyo aliyowahi kuiona hapo nyuma.
Vitalis alitabasamu kidogo kabla hajamsalimu kwa kumpa mkono.
Bibi huyo asipokee mkono wa Vitalis, aliuliza kwa sauti yake kavu:
“We ni nani? Mbona kama nakujua?”
Vitalis akatabasamu zaidi, ila akiwa na uso wa tahadhari.
“Kweli?”
“Ndio. Kwani wewe haunijui?”
“Mama, umeanza!”
Sauti nyembamba ya kike iliita tokea ndani.
Mlango ulifunguliwa akatokea mwanamama mwekundu mnene kiasi. Nywele zake ndefu za kahawia na mwenye macho ya ukali. Alikuwa amevalia gauni refu la maua maua lililobanwa kiunoni na kamba ya nguo hiyo.
Alitabasamu kumtazama Vitalis, akasalimu.
“Tafadhali, karibu ndani. Samahani kwa usumbufu wa mama yangu, kila mtu akija hapa lazima amwambie maneno hayo hayo.”
“Usijali.”
Alisema Vitalis akipiga hatua kuingia ndani wakati yule bibi akitokomea kufuata ngazi na mwendo wake wa kinyonga.
Ilimchukua Vitalis dakika mbili kumtambua yule mwanamke aliyekamrimu ndani. Alikuwa ni mmojawao wa wale waliotua ushuhuda wao kwenye televisheni juu ya kifo cha Kelly na mumewe.
Jambo hilo lilimpa afueni, uso wake ukawa mwepesi zaidi.
“Samahani sana kwa usumbufu, naitwa Vitalis. Nimekuja hapa kwa ajili ya kupata taarifa zaidi juu ya kifo cha majirani zako. Naomba ushirikiano wako.”
“Wewe ni mwandishi wa habari?” Aliuliza mwanamke yule akimtazama Vitalis na macho yaliyoboreka punde tu kusikia.
“Yah! Ni mwandishi wa habari, ila ni wa upelelezi.” Alijibu Vitalis kwa kujiamini lakini mama yule hakuonyesha kushtushwa na hilo.
“Unajua wamekuja waandishi wengi sana wa habari hapa, na mapolisi pia wakitaka kufahamu yaliyotukia. Ila ninachokijua ni kwamba hakuna lolote litakalotokea. Ni upepo tu utakaopita kama pepo zingine. Sioni kama kuna haja ya mimi kuongea tena na tena kila siku kwa kitu ambacho hata kama nikiongeaje hakitaleta mabadiliko yoyote.”
“Lakini muda huu haitokuwa tena kama huko mwanzoni.” Vitalis alisema akimtazama mwanamke anayeongea naye. Macho yake yalionyesha ni namna gani anamaanisha kile kilichotoka mdomoni.
Hapo mwanamke yule akavutiwa. Macho yake yaliwaka hamu ya kutaka kufahamu.
“Una maanisha nini?”
“Sasa hivi wauaji watakamatwa. Nao watauwawa.”
Kwa muda mfupi kidogo kukawa kimya wakitazamana.
“Nakuhakikishia hiki ninachokuambia. Maneno yako hayataenda bure.” Vitalis alitia msisitizo.
Ni kama vile alimpa nguvu fulani mwanamke yule aliyekuwa anatazamana naye. Mwanamke huyo alimtazama Vitalis machoni kisha akaurushia uso wake chini na kuanza kueleza yote kwa pande ambayo aliliona tukio.
Sauti yake yembamba ilikuwa nyembamba zaidi akisimulia. Ila haikusita pia kukwaana na kilio pale palipokuwa pagumu kueleza. Mpaka anamaliza kusema yote uso wake ulikuwa umelowana machozi na sauti yake ilikuwa imefifia zaidi.
Vitalis aliweka mkono wake kwenye bega la mama huyo, akamuuliza:
“Unadhani kwanini Kelly na hao watu walienda uelekeo huo?”
Mwanamke yule akavuta kwanza makamasi mara mbili. Akiwa anaminyaminya vidole vyake, alijibu:
“Sijui ni kwanini. Ila huko walipokuwa wanaelekea ni njia karibu na bahari, itakuwa aliwatoroshea huko.”
Alijifuta pua na mgongo wa kiganja chake, kisha akaendelea:
“Walitumia boti ya Kelly kutoroka nayo maana polisi walisema hawakuikuta hiyo boti huko ufukweni.”
“Kelly alikuwa ana boti?”
“Ndio, alikuwa nayo. Si tu boti bali pia nyumba japokuwa amefariki ameiacha bado haijakamilika … Unajua Kelly alikuwa na wakati mgumu sana kuishi na mumewe, Johnny. Mume wake hakuwa mtu wa kuwaza maendeleo bali pombe na wanawake. Kidogo alichokuwa anapata kwenye kilimo alikuwa anawekeza pasipo mumewe kujua.”
Kuna kitu kikagonga kichwani mwa Vitalis.
“Unaweza ukanielekeza hiyo nyumba yake ilipo?”
Mwanamke alisita.
Alimtazama Vitalis machoni kama mtu anayewazua jambo. Baada ya muda mfupi, akatua zigo lake la hofu.
“Ndio, naweza.”
Vitalis akatabasamu.
Mwanamke huyo alimuelekeza Vitalis akitumia mikono yake kama ramani. Kwa muda wa kama dakika tatu, alifanya tukio hilo kufanikiwa pasipo kujua kama Vitalis ni mgeni nchini.
Kwa kutazama na kusikiliza kwa makini, Vitalis aliweka maelezo kichwani, akamuaga mwenyeji wake kabla ya kujirudisha kwenye gari alilokuja nalo lililokuwa na majeraha karibia kila pande na kuondoka eneo hilo.
Alichukua takribani masaa mawili na nusu kufika alipolenga.
Ilikuwa ni nyumba yenye ukubwa wa kati ikiwa haijamaliziwa kupakwa rangi wala kuezekwa paa. Ilikuwa imekaa mbali kidogo na shurba za watu – sehemu tulivu ambapo pangekuhitaji sababu kubwa kukufanya uende hapo.
Nyumba ilikuwa imezingirwa na majani marefu ambayo yalichora njia zinazotumika kuingilia ndani ya nyumba. Njia hizo nazo hazikuwa safi kama tujuavyo, zilikuwa na majani pia lakini yakiwa mafupi kuliko ya kando kando.
Vitalis alipekua eneo hilo na macho upesi. Hakuona dalili ya yeyote kuishi hapo. Aliegemea gari akaendelea kupekua eneo hilo kwa dakika kama mbili ama zaidi kabla hajaanza kuchukua hatua kwenda ndani.
Alifika sebuleni pasipo kuona kitu. Alipita vile vile chumba cha kwanza, pili na tatu pasipo kuona mtu.
Lakini baada ya muda mfupi akaona alama za unyayo wa kiatu koridoni. Hakukuwa na sakafu. Ardhi ilikuwa rafu na ngumu hivyo kuona jambo kama hilo ilihitaji umakini mno kwenye utazamaji.
Vitalis alichuchumaa akatazama alama hiyo kwa karibu. Alirusha macho yake aone kama ataona nyingine, hakufanikiwa.
Kabla hajajua achukue hatua gani ya pili, alishituka kusikia kishindo nyuma yake. Aligeuka upesi akakutana na teke lililokita chini ya taya bila huruma na kumrushia mbali.
Kabla hata hajafungua macho alishaamriwa ageukie ukutani na anyooshe mikono juu kabla hajalipuliwa na risasi. Haraka aliusogelea ukuta akipeleka mikono yake juu.
“Mimi sio adui yenu!”
Vitalis alijitetea.
Kivuli cha mwanaume aliyemnyooshea bunduki kilijongea kumfuata.
Mwanaume huyo alisimama nyuma yake, akamuuliza akiwa ameweka mdomo wa bunduki kisogoni.
“Wewe ni nani na unafanya nini hapa?”
Sauti haikuwa ngeni.
Ilikuwa na ka-lafudhi ka-kihindi ndani yake japokuwa ilisema kwa mkazo usio na tone la utani.
Likiwa jibu langojewa, mdomo wa bunduki uliendelea kushindiliwa kwenye kichwa cha Vitalis kwanguvu.
“Naitwa Vitalis – Vitalis Byabata toka Tanzania.”
Vitalis alijieleza. Alikuwa anatota jasho.
Muda mfupi mdomo wa bunduki uliondolewa kichwani kwake swali likiulizwa:
“Vitalis?”
“Ndio.” Vitalis akajibu akitikisa kichwa.
“Umekuja kufanya nini huku?”
“Kumuua Kim.”
Kimya.
“Umejuaje kama tupo hapa? Nani kakuambia?”
“Nilifuatilia kwa Kelly. Jirani yake alinambia ana nyumba yake maeneo haya nikajua fika mtakuwa huku.”
“Hakuna mtu anayekufuatilia?”
Rajul aliuliza akiangazaangaza.
“Hamna mtu yoyote. Nilihakikisha nipo mwenyewe.”
Rajul alirudisha bunduki kiunoni akamtaka Vitalis anyanyuke.
Alikuwa amevalia suruali nyeusi ya kadeti pamoja na shati jeupe, miguuni alikuwa peku. Kichwa chake kilichozoeleka kutokuwa na nywele, kilikuwa kimeshamiri kedekede pamoja pia na ndevu.
Ni macho na sauti yake ndivyo bado vingekufanya umgundue. Tena baada ya kumfanyia uchambuzi yakinifu.
Aliongozana na Vitalis kwenda chumba cha kwanza kabisa ambapo alijongea karibu na kona ya dirisha akakanyaga chini kwanguvu mara tatu na mara kukafunguliwa.
Ilikuwa ni kama andaki. Mlango wake ulikuwa ngumu kutambuliwa kwasababu ya kutandazwa udongo juu yake ambao haukonyesha tofauti yoyote na wa kando kando.
Waliingia ndani wakamkuta Stanis. Alikuwa kifua wazi akiwa amevalia suruali pekee. Mwili wake ulikuwa na makovu mengi kama kenge ila lisionekane jeraha hata moja. Alikuwa anamimina jasho jingi. Kwa hali ya joto mule ndani ya handaki halikuwa la kushangaza hilo.
Kwa chini kulikuwa kumetandazwa jamvi na ndilo hilo lilikuwa linatumika kama kitanda. Kwenye jamvi hilo konani pia kulikuwa na kofia la nywele, na pasipo shaka lilikuwa ni mahususi kwa ajili ya Stanis kujifichia uso asijulikane.
Rajul alivua nywele na ndevu zake za bandia, akamwambia Stanis:
“Tumepata ugeni kutoka kwa wageni.”
Stanis alimtazama Vitalis kwa macho ya kutafuta. Rajul alimsogelea karibu akamwambia:
“Anaitwa Vitalis, toka Tanzania. Nafikiri hilo si jina geni kwako.”
“Vitalis?” Stanis alishangaa akimtazama Vitalis. Ni kana kwamba alikuwa anajaribu kuvuta kumbukumbu yake juu ya hilo jina.
“Ndio, Vitalis. Amemsumbua sana mkuu wako, Kim, huko Tanzania. Kim alikuwa akiniambia sana habari za huko nyumbani kwake kwa pili. Sasa amekuja Bermuda kumaliza biashara yake aliyoianza.”
“Nini kinakufanya udhani utafanikiwa, Vitalis?” Stanis aliuliza.
Vitalis alimtazama na macho yaliyoonyesha hamu ya damu. Aliminya lips zake akasema:
“Sina kitu wala kazi nyingine kwa sasa zaidi ya Kim. Alichonipotezea hakiwezi kurejeshwa kwa njia yoyote ile na moyo wangu hautotulia kamwe mpaka pale nitakapohakikisha hayupo tena duniani.”
Kulikuwa kimya kidogo kama vile kuna kitu kimepita. Stanis na Rajul walimtazama Vitalis na ni wazi waliona jinsi kiu yake ya kisasi ilivyo kali usoni.
“Amepoteza familia yangu. Amepoteza rafiki zangu. Amepoteza kazi yangu. Amepoteza na anaendelea kupoteza watu kila kukicha kwenye nchi yangu aidha kwa madawa, ama kafara. Amekuwa mchango mkubwa wa kudorora kwa serikali na maendeleo ya nchi yangu. Hastahili kuishi kwa amani. Hastahili kuwepo duniani. Kuendelea kwake kuvuta pumzi ni mzigo na adhabu kwa wengi.”
Stanis na Rajul walitazamana. Ni kama kuna jambo waliteta na macho yao kabla ya Rajul kuuliza:
“Wenzako wapo wapi? Najua haupo peke yako.”
“Wametekwa wote na Kim.” Vitalis alijibu upesi. “Alinitangulia hatua moja mbele, akafanikiwa kunizidi kete.”
“Vitalis.” Rajul aliita. Uso wake ulikuwa na miale ya huruma.
“Huku si Tanzania. Kim anajua kila sehemu ya nchi hii, kila sehemu. Hakuna mahali ambapo hana mtu wake wa kumuangalizia jambo. Iliwapasa kuwa makini sana. Si tu kwamba ana ushawishi kila Nyanja, lakini pia ana mkono kila mahali. Ni ngumu sana kupambana naye.”
Akamshika Vitalis bega la kuume.
“Ila ujio wako umenipa nguvu. Sitosita kusaidia nguvu ama akili kwenye kulifanikisha hili. Nimetenda makosa makubwa sana huko nyuma kwa kumsaidia. Nadhani ni wakati sasa wa mimi kulinywa nililolikoroga.”
Kimya kidogo.
“Pumzika kwa sasa, uso wako unaonyesha umepitia mengi. Tutajadili zaidi baadae.”
Aliposema hayo alipanda juu na baada ya muda mfupi akarejea na majani fulani aliyoanza kumkanda nayo Stanis mgongoni.
Japokuwa hakuwa na majeraha, Stanis alikuwa analalamika kwa maumivu.
Aidha bado alikuwa ana maumivu ya ndani kwa ndani.
Vitalis aliyekuwa amekaa kandokando alitazama zoezi hilo likifanyika akiwa na macho ya maswali.
Labda alikuwa anajiuliza nini kilijiri kwenye mgongo ule uliokuwa hautamaniki kwa makovu. Ila hakuuliza.
‘Tutajadili zaidi baadae’ ya Rajul labda itahusisha na hilo jambo, aliwaza.
***
Joto kali la ndani ya Handaki lilimbughudhi Vitalis na kumfanya aamke. Alitazama pembeni yake lakini hakuona mtu, alikuwa peke yake.
Haraka alinyanyuka akifikicha macho.
Akiwa anajinyoosha mwili, alisikia kelele za kiume toka juu, akajawa na tahadhari.
Taratibu aliusukuma mlango wa handaki akatoka ndani.
Ilikuwa ni jioni sasa. Kwa macho ilikuwa ni kama saa kumi na moja ama kumi na mbili. Kwa nje kulikuwa kuna kaubaridi ukilinganisha na ndani ya handaki kulimokuwa kama tanuru.
Vitalis akiwa na sura ya mashaka, alifuata sauti aliyokuwa anasikia ikampeleka mpaka nyuma kabisa ya jengo. Huko alikuta wenyeji wake wakijipasha kwa mazoezi.
Aliketi akawatazama kwa muda kabla hawajamuona na kumtaka ajiunge nao.
Baada ya kufanya hilo zoezi kwa muda wa kama nusu saa ama zaidi, walishitushwa kuona kivuli cha nyumba kinasongeshwa na mwanga ambao waliujua ni wa gari baada ya kusikia sauti ya mngurumo.
Walitazamana kwa mshangao. Ni kana kwamba walikuwa wanajiuliza nini cha kufanya na wakina nani hao wamekuja maskani mwao.
Haraka Rajul aliwaonyesha upande wa kwenda. Ilikuwa ni kwenye nyasi ndefu zilizosimama wima. Pasipo kupoteza muda, wakaeleka huko na kujificha.
Walisikia milango ya gari inafunguliwa na wanaume wakiteta. Punde wakasikia vishindo vikizama ndani. Kisha kukawa kimya kidogo.
“Tunafanyaje sasa?” Stanis alinong’oneza.
“Tatizo hatujajua wapo wangapi na wana nini.” Vitalis alimjibu kisha kimya kikatawala kwa dakika kadhaa. Sauti tu za mioyo yao iliyokuwa inaenda mbio ikivuma.
“Wamejuaje tulipo lakini?” Rajul aliuliza kana kwamba haitaji jibu.
Kulikuwa kimya kwa sekunde kadhaa, Vitalis akasema:
“Itakuwa wameifuatilia ile taksi niliyokuja nayo.”
“Kivipi?” Stanis aliuliza.
“Wakati naelekea kule kwa Kelly walikuwa wananifuatilia ili nilifanikiwa kuwamaliza wote. Itakuwa walitoa taarifa kuhusu lile gari kabla sijawamaliza na labda baada ya kuona kimya kirefu, wakaanza kufuatilia.”
Milio ya risasi ikavuma.
“Inabidi tufanye jambo, hatuwezi tukakaa hapa muda wote!” Alisisitiza Rajul.
Kupambana na watu wenye silaha, tena bunduki, yahitaji uangalifu mkubwa. Ndani ya jengo walikuwepo wanaume watatu waliovalia suti na kubebelea bunduki aina ya SMG mikononi mwao. Miongoni mwa wanaume hao alikuwepo mwanaume mmoja wa kazi. Mwili wake uliojaa ulibana suti. Walikuwa wanatazama huku na kule wakiwa na sura za kazi.
Vitalis alijongea akachungulia mlangoni, akawaona wanaume hao wakiingia kwenye chumba kimoja kabla ya sauti kusikika muda mfupi:
“Kuna handaki!”
Wanaume wawili waliingia kwenye handaki hilo kwa tahadhari ya kutosha mmoja akabakia juu.
Ndani ya muda mfupi yule aliyebakia alivunjwa shingo na Vitalis pasipo kusema chochote. Kabla hajadondoka na kusababisha sauti ambayo ingeweza kuwagutua wenzake, Vitalis alimdaka na kumlaza taratibu kabla hajafunga mdomo wa handaki na kuwashitua wenzake kwa mluzi, wakafika ndani ya muda mfupi.
“Wamo ndani!”
Alisema Vitalis aliyekuwa amebebelea bunduki sasa mkononi.
Mara milio ya bunduki ikaanza kurindima. Mdomo wa handaki ulikuwa unapokea risasi mfululizo zikitoka kwa wale waliofungiwa humo.
Rajul alimtazama Vitalis akamshika mkono.
“Nadhani ni muda wa kuondoka. Tutatumia usafiri wao.”
“Kwanini tuondoke kabla hatujawamaliza?” Vitalis aliuliza.
“Bado hatujajiandaa vya kutosha.” Rajul akajibu akimvutia Vitalis nje ya chumba.
Vitalis hakuelewa kilichokuwa kinaendelea na kwa namna moja ama nyingine alishangazwa kuona wameridhia kile alichokisema Rajul kwa wepesi.
Waliingia ndani ya gari la maadui wakakuta hamna funguo. Stanis alikata waya alizoziunganisha gari likawaka. Ila kabla chombo hakijaondoka, walisikia sauti kubwa ya kushtua. Haikuwa ya mlio wa bunduki, la hasha! Ilikuwa ni sauti ya kishindo kilichoashiria kufunguliwa kwa mdomo wa handaki.
Tena kwa nguvu mno.
Rajul alimtazama Stanis aliyekuwa amekalia kwenye kiti cha dereva, akamuamuru:
“Ondoa gari!”
Stanis alikanyaga mafuta gari likatimka likiacha vumbi jingi.
Hawakufika mbali gari likaanza kulengwa na risasi kwa pupa. Alikuwa ni yule mwanaume wa kazi akiwa anakimbiza gari hilo kwa hatua zake pana na ndefu. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea bunduki aliyokuwa anaifyatua pasipo kukosea. Kwa shabaha yake hiyo, vioo vyote vya gari walilokuwemo Vitalis na wenzake vilitawanywa na kumwagwa.
Mwanaume huyo alikimbia kwa mwendo mkali akajiweka karibu na gari. Alimiminia risasi gari hilo dereva asipate muda wa kuzingatia barabara kwa umakini, gari likawa linaenda kwa pupa huku na kule. Watu wote ndani ya gari walikuwa wameinama kujificha dhidi ya risasi.
Endapo kama mwanaume yule wa kazi angeendelea kushambulia gari hilo basi si muda mrefu angekuwa amemaliza kazi yake, ila zoezi lake hilo lilikwamishwa pale risasi zilipokauka bundukini.
Alisimama akaitazama na kuikagua bunduki kabla hajaivunja na mikono yake kwa hasira. Kwa muda huo gari likajichanua kumuacha. Alilitazama gari likiyoyoma, mara akaanza tena kukimbia ila mara hii akielekea upande tofauti na ule gari lilipoelekea.
Hakuonekana mwehu, hapana, uso wake ulionyesha anajua anachokifanya japo kwa namna moja ama kingine kingekustaajabisha kama Vitalis.
“Anaenda wapi?”
Vitalis aliuliza. Hakuna aliyemjibu. Aidha hawakuwa na majibu ama bado walikuwa katika ombwe la mshangao kwa namna gani wamepona.
“Yule mtu ni nani? – si wa kawaida!” Vitalis aliongezea swali.
Hapo Rajul akamjibu upesi:
“Ndio mana nilikwambia bado hatujajiandaa.”
Kimya kidogo.
“Ni bahati yetu alikuwa mmoja, kama wangelikuja wote basi tusingelikuwa na nafasi ya kuishi leo hii.” Rajul aliendelea kuongea.
“Wapo watano na wana nguvu ya ajabu. Wote nyota zao ni simba. Wamepewa madawa yaliyojumuisha damu ya mtawala wa kifalme. Ni ngumu sana kuwazuia kwa uwezo wa binadamu wa kawaida.”
“Kwanini nyota ya simba?” Vitalis aliuliza.
Rajul akashusha pumzi ndefu.
“Kwasababu ni mojawapo ya alama ya nguvu aliyobakiwa nayo Kim mbali na ile ya maji. Watu waliotakiwa kupewa nguvu hiyo ni wale tu wenye nyota hiyo, si vinginevyo.”
Rajul alimaliza kwa kumtazama Stanis.
Vitalis alikumbuka ile michoro waliyoiona na wenzake kule kisiwani kwenye ukuta wa yule mganga.
“Kwahiyo? Hakuna lolote la kufanya kuwakabili?”
“Lipo, ila linataka muda, nguvu naa … wizi vilevile.”
“Wizi?”
“Ndio. Kupata mkabala wa kuwakabili kuna ulazima wa kuiba jambo fulani sehemu fulani. Kama tusipofanikiwa hatuwezi kumpata Kim.”
“Tunaiba sehemu ga …”
Waliona kitu mbele yao!
Alikuwa ni yule mwanaume wa kazi. Hawakujua amefikaje pale ila sasa ilikuwa na mantiki kusema na kuamini kwamba alikuwa amewapitia njia denge. Njia ile waliyokuwa wanaitumia ilikuwa na kona kadha wa kadha na mwanaume huyo alionekana kufahamu kwa undani ramani ya eneo hilo.
Stanis alikanyaga moto zaidi. Kabla mwanaume yule wa kazi hajazolewa, aliruka juu akanasa paa la gari. Vidole vyake vilitoa kucha ndefu zikang’ang’ania paa kwanguvu. Haikujalisha ni kwa kiasi gani Stanis aliyumbisha gari, mwanaume huyo hakuachia paa sembuse kutetereka.
Vitalis alifyatua bunduki kulenga paa. Risasi za mfululizo zikamtoboa mwili wa mwanaume huyo lakini asikome. Sasa alikuwa anapiga ngumi paa na imebakia kidogo tu alitoboe. Vitalis alichomoza dirishani upesi akamfyatulia risasi kadhaa mwanaume huyo kabla bunduki haijapigwa kofi ikarukia mbali.
Mwanaume huyo alituma teke lake kumzoa Vitalis akiwa amejishikiza na mkono mmoja. Vitalis alikwepa teke hilo kisha akalidaka na kulivuta. Hakufua dafu. Aligeuziwa kibao kwa kukandamizwa mateke mawili ya haraka. Ilikuwa ni wakati ameshika mguu ule uliorusha teke, mwingine ulimuadhibu kisha akaachia ule wa awali ambao nao pia ukamsigina.
Isingekuwa Rajul basi angelidondoka toka kwenye gari lile lillokuwa linaenda kwa kasi, muhindi huyo aliwahi kumdaka Vitalis na kumvutia ndani kwa kutumia nguvu zake zote. Vitalis hakuwa hata na muda wa kujiuguza maumivu, paa la gari lilichanwa kama karatasi mkono wa mwanaume yule ukapenya kushika kichwa cha dereva – Stanis. Vidole viliziba uso wa dereva huyo na kumpotezea uwezo wa kuona.
Gari likawa linaenda alimradi laenda.
Rajul alidaka usukani kusaidia kubaki barabarani pia kukwepa magari mengine.
Stanis akiwa anahangaika kujikomboa, alikamata mkono wa adui akaujeruhi kwa kuuachana na bati la paa baada ya kuugandamizia hapo. Mwanaume yule wa kazi akauvuta mkono wake na kuutazama kwa ghadhabu. Ulikuwa unachuruza damu toka kwenye jeraha kubwa.
Breki kali ilikanyagwa, akarushiwa mbali.
Isingelikuwa alizingatia mkono wake zaidi ni wazi asingelirushwa. Kucha zake ndevu ziling’ata paa ya gari vizuri. Na kama tu zingepata msaada wa akili yake nzima, kubanduka hapo ilikuwa ni ndoto isiyotekelezeka.
Mwanaume huyo alibiringita mara mbili tu kabla viganja vyake havijakita juu ya lami kucha zikazama. Alijisogeza kando upesi kupisha gari la wakina Vitalis kisha akafanya jitihada ya kupata usafiri mwingine, akapata pikipiki.
Vitalis alipogundua wanafuatwa na usafiri huo, aliomba akalie yeye usukani, Stanis akampatia hiyo fursa. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kutazama kioo cha juu akiwa anasaga meno yake na kubinua lips. Kinyume na matarajio akapunguza mwendo kwa kiasi fulani. Pikipiki ikajongea karibu zaidi.
Baada ya kujihakikishia pikipiki ipo karibu na kingo ya bampa la gari, taratibu Vitalis akaongeza kasi ya gari. Ilikuwa bado kidogo mwanaume wa kazi aitie gari mkononi. Pikipiki nayo ikaongeza kasi.
Baada ya dakika kama moja likatokea jambo haraka sana!
Ni baada ya kuona gari lingine, Noah rangi ya silver, laja kwa nyuma na kusonga karibu, ndipo Vitalis akakata kona ghafula akiwa amekamata breki. Kama fagio, gari likamzoa mwanaume juu ya pikipiki na chombo chake kwa pamoja wakamwagiwa mbele ya Noah.
Mwanaume yule alitupwa kando na pikipiki yake ikamfuata pia kumkanyagia juu. Noah iliyomgonga ilisimama dereva akiwa na nyuso ya huruma na mshangao. Alikuwa anatetemeka asijue la kufanya.
Tusijue hata kama mwanaume yule aliyegongwa amepona ama ameenda, Vitalis alirudisha gari nyuma akampanda mwanaume huyo kana kwamba mlima. Alifanya zoezi hilo mara nne, akikanyaga mafuta kwenda na kurudi, kabla hajajiweka sawa na kuondoka kwa kasi.
Dereva wa Noah kushuhudia hayo, alizirai. Barabara ilitapakaa damu mhanga akiwa ameachwa amepasuka kichwa na viungo vimevunjwa kwanguvu.
Kwa muda kukawa na foleni eneo hilo.
Vitalis alifuatisha maelezo aliyopewa na Rajul baada ya muda mfupi akawasilisha gari karibu na eneo la ‘temple’. Rajul alitazama eneo hilo kwa haraka akashusha pumzi.
“Ni hapa.” Alisema. “Ni hapa ndipo tunatakiwa kuiba kitu fulani.”
“Utahitaji msaada wowote?” Stanis aliuliza.
“Hapana.” Rajul akajibu. “Tangu walipovamiwa na kuuwawa kwa ajili yangu, sidhani kama kutakuwa na watu wengi. Naweza nikafanikisha hili mwenyewe.”
Alipomaliza kusema hilo alifungua mlango akatoka ndani.
“Nipatieni kama nusu saa hivi.”
Alielekea nyuma ya temple alipodandia ukuta na kujimwagia ndani. Kwa uangalifu mkubwa akiwa amebonyea alitembea haraka kuliendea jengo. Alijibanzia ukutani akachungulia korido kama ina watu, akaona hewara.
Alitembea upesi upesi, aliposikia sauti za watu alijifichia kwenye kuta ama kwenye vyoo kisha akaendelea na safari mpaka alipofika kwenye mlango fulani mkubwa uliokuwa unaong’aa kwa matirio yake ya mbao yenye polishi. Alijaribu kuufungua akashindwa, ulikuwa umebanwa na komeo. Funguo atatoa wapi?
Alisaga meno yake kabla hajatwanga kiganja chake na ngumi nzito kisha kuendea ngazi apande juu. Ilibidi sasa aende chumba kinachotunza funguo. Alifika hapo baada tu ya sekunde chache. Ndani ya chumba hicho kulikuwamo na mwanaume mmoja mzee aliyekuwa amevalia shuka la kahawia na cheni ya madunguli meusi. Alikuwa ameketi akisoma kitabu kikubwa chenye jarada jeupe. Macho yake ndani ya miwani kubwa ya macho yalikuwa yanaenda kushoto na kurudi kulia, kulia yakirudi kushoto.
Hakukuwa na muda wa kupoteza kwa Rajul, lakini pia hilo halikutosha kumfanya asiwe muangalifu. Korido haikuwa na mtu ila si kwamba itakuwa hivyo milele hivyo ilibidi achakate akili yake kwa upesi.
Akigonga mlango ataambiwa karibu. Akiingia uso wake ukionekana atajulikana, si ndio? Hakutaka kujulikana. Alibisha hodi mara tatu, mzee yule aliyekuwemo ndani akapaza sauti yake kumkaribisha pasipo kutazama mlangoni.
Mtu hakuingia.
Mzee alibandua macho yake kitabuni akatazama mlangoni. Baada ya dakika moja ya kutosikia tena hodi alinyanyuka akauendea mlango. Alipoufungua tu, Rajul aliusukuma mlango kwanguvu ukamgonga mzee huyo na kumlaza hajitambui. Aliingia ndani akufuata ubao wa funguo na kuchukua ufunguo anaouhitaji na kutokomea eneo hilo akifunga mlango na kumuacha mzee huyo chini.
Alirejea mlango ule akaufungua na kuingia ndani. Humo ndani hakuchukua muda mrefu akatoka na bilauri refu la kioo.
Kitendo tu cha kuufunga mlango huo, sauti kubwa ya king’ora ikaita! Jengo zima lilikuwa kelele ghafula.
Tayari mzee yule aliyeziraishwa kule ofisi ya utunzwaji funguo alikuwa ameonekana. Ni punde tu baada ya Rajul kutoka, watu wawili walikuja na kumkuta katika hali ile. Kutokana na kitendo cha kuvamiwa kwa jengo hilo siku za nyuma na kupelekea mauaji, hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa zaidi mahali hapo. Wanaume waliobebelea silaha mathalan jambia, marungu na mapanga walitapakaa kuitikia wito wa king’ora kile.
Rajul akiwa amebebelea bilauri lake alikimbia kurejea njia yake aliyoingia nayo jengoni humo, bahati mbaya akakuta tayari maeneo yale yashatwaliwa na walinzi. Alirudi upesi kwenda upande mwingine ila huko kabla hajafikia ukuta aliamriwa na sauti nyuma yake asimame la sivyo atatapanywa!
Walikuwa wanaume watatu waliobebelea mapanga mikononi. Nyuso hazikuwa rafiki hata kidogo. Vichwa vyao havikuwa na nywele na walivalia mashuka ya kahawia. Walikuwa wanamsogelea Rajul taratibu.
Rajul alisimama akiwa hajui la kufanya. Macho yalikuwa yamemtoka na mdomo ulikuwa umeachama. Alitazama bilauri alilobebelea akameza mate ambayo hayakuwepo hata mdomoni. Mdomo wake ulitetema mambo ambayo hayakusikika.
Ghafla, geti lililokuwa karibu yake lilivunjika likaingia gari lililowabebelea Vitalis na Stanis kwa kasi kubwa!
Gari hilo likiwa linaendeshwa na Vitalis liliwafyagia wanaume wale wenye silaha kisha likajitenga mbele ya Rajul.
“Ingia fasta!” Vitalis alimuamuru Rajul.
Rajul aliingia ndani ya usafiri, gari likatimka upesi!
Baada ya masaa mawili walikuwa fukweni mwa bahari ila fukwe iliyojitenga na purukushani za dunia. Kulikuwa kimya upepo ukipuliza. Mawimbi yalikuwa yanapiga taratibu na yakivutia kutazama.
Walikuwa wameegemea gari wakitazama jua likizama. Anga lilikuwa jekundu. Kulikuwa kimya kana kwamba walipeana tahadhari ya kutoongea. Wakati jua likiwa jekundu mno na limebakiza punde ndogo ili lipate kupotea kwenye uso wa dunia, Rajul alijikuta anakohoa kusafisha koo lake kisha akasema:
“Kesho ni siku muhimu sana.”
Aliposema hivyo kulikuwa tena kimya kwa dakika kama mbili. Jua lilizama kukawa na kakiza kepesi.
“Ni siku yangu ya kubeba adhabu halisi ya yale yote niliyoyatenda. Ila nafurahi mana nitakuwa huru. Nafurahi maana nitakuwa nimelinywa nililolikoroga.” Alisema Rajul.
“Naomba nirudie kuuliza, ina maana hamna njia nyingine kabisa?” Stanis alivuma. Sauti yake ilikuwa ya kuguswa.
“Hamna njia nyingine. Endapo kama sitofanya hivyo si tu kwamba nitakuwa nimekimbia jukumu langu, bali itawawia vigumu kushinda” Rajul akajibu kwa sauti kakamavu kisha akanyooshea kidole baharini. “Mtanitupia kule mkiwa mmenifunga jiwe kubwa shingoni.”
Alishusha kidole chake akasisitiza:
“Naomba mfanye hivyo maana sitakuwa binadamu wa kawaida tena. Nitakapokunywa hizo dawa nitauchukua uovu wote nilioupandikiza na hivyo nitakuwa shetani haswa. Sitakuwa namjua wala kumkumbuka yoyote yule mbele yangu, nitakuwa hatari. Hivyo muwe mmenifunga na kunijaladia vema.”
Hakuna tena aliyesema kitu. Ni upepo tu ulipuliza.
Na hapo ndipo tuliporudi nyuma kwa lisaa limoja kushuhudia mabaki ya damu ya mwanaume yule wa kazi yakipatikana ndani ya gari mahali pale alipokatwa mkono, yakachanganywa na damu ya Rajul ndani ya bilauri kabla ya kufungwa upesi na kuchimbiwa chini ya bahari.
Ilitosha kupata na kutumia damu ya mwanaume yule kama alama ya kumuwakilisha Kim, utawala na mabadiliko yake, wakati damu ya Rajul ikitumika kumwakilisha aliyechagiza mabadiliko hayo.
Tayari bilauri hilo lilikuwa linatetemeka ndani ya ardhi ya bahari kana kwamba simu iliyonyimwa mlio. Ila muda wake wa kuopolewa ulikuwa bado. Ni siku inayofuata majira ya tatu asubuhi.
***
Jua la siku hiyo lilikuwa kali kupitiliza. Wakati ikiwa tu ni saa sita, tayari miale yake ilivuma kiasi cha kukufanya uwe na sababu mujarabu ya kubebelea mwamvuli, kuvaa shati jepesi na kaptula.
Ilikuwa kinyume kabisa na siku za nyuma ambapo kaubaridi kalitawala kwa mujibu wa majira ya mwaka. Jua lilikuwa linaonekana kwa wazi saa saba na saa nane mchana kabla ya tena kupotezwa na mawingu mazito yaliyotawala anga. Labda kibahati ungekuja kuliona majira ya jioni likizama huku likirandana na sifa yake ya kugeuza anga jekundu.
Siku hiyo ilikuwa tofauti. Tunaweza kuhitimisha kwa kusema hivyo. Lakini kipi kilichofanya ikawa tofauti?
Ndani ya majira ya saa kumi na mbili asubuhi pasingekuwepo na kiumbe ndani ya jiji la Hamilton ambaye angeweza kubashiri siku hiyo. Ilikuwa ni kama siku zingine za kawaida. Manyunyu yalikuwa yanadondoka. Baridi likishika kila kona. Lami ilikuwa imelowana na kama ungetoka nyumbani kwako pasipo kubebelea chanzo cha joto, watu wangekuona mgonjwa. Na ilikuwa hivyo mpaka saa tatu ya asubuhi.
Lakini haikuwa hivyo kuanzia hapo na kuendelea.
“Samahani sana, Rajul.” Alisema Vitalis akimtazama Rajul aliyekuwa amefungwa kamba mwili mzima. Si kamba za kawaida, bali zile nene zikiwa zimeshindiliwa na kukazwa vizuri. Pembeni ya Stanis alikuwa amesimama Stanis mkononi akibebelea bilauri la kioo, wote walikuwa wanamtazama Rajul kwa uso wa huruma. Wote walikuwa wamesimama kwenye ardhi ya juu ya fukwe upepo ukiwapuliza.
Rajul ambaye alikuwa na macho mekundu, alikuwa amelazwa au amejilaza kwenye uso wa fukwe hiyo ya bahari asionekane kujitambua. Uso wake ulikuwa mweusi. Nywele zake zilisimama wima. Mdomo wake ulikuwa unachuruza mate macho yake yakimimina damu. Mishipa ilikuwa imemsimama usoni na jasho likimtiririka pia.
Si tu kwamba alionekana mithili ya mwendawazimu, alionekana kama shetani. Alikuwa ananguruma kama simba dume akionekana ana uchu wa nyama.
Stanis alitazamana na Vitalis kisha akaliendea jiwe kubwa lililokuwa pembeni. Alilifunga jiwe hilo na kamba na kulifungia kwenye shingo ya Rajul kwanguvu. Rajul alihangaisha kichwa chake huku na kule mwishowe akamng’ata Stanis kidole cha mwisho.
Damu zilimchuruza Stanis wakati Rajul akijilamba kana kwamba mwehu. Stanis asijali sana, alimalizia kazi yake.
Baada ya kulifunga jiwe hilo, Stanis akatazamana na Vitalis. Ni kama vile walipeana ishara, Vitalis akaweka bilauri chini wakambeba Rajul na kumrushia baharini. Walipofanya hivyo waligeuza migongo yao wasione Rajul anavyozama.
Kama kipande cha chuma, mwili wa Rajul ulizama majini ukichukua dakika moja kugota sakafuni mwa bahari. Mwanaume huyo alihangaika kujikwamua asiweze abadani. Alikunywa maji na kukosa hewa. Alihangaika ndani ya kamba zake kama samaki nchi kavu. Macho yalimtoka na aliachama mdomo ambao kwa bahati mbaya badala ya kumpa hewa ukamnywesha maji. Ilipopita dakika moja, akatulia tuli.
Alikuwa ameenda.
Ilikuwa ni saa tatu na dakika ishirini na tano.
Mawingu yalitawanyika na kuliacha jua uchi. Hali ya hewa ikabadilika kabisa.
“Yamekwisha.” Stanis alisema.
“Naam, naona yameisha.” Vitalis akaitikia na kuongezea. “Sasa tumebakia wanadamu pekee.”
Stanis akatazama saa yake ya mkononi na kusema:
“Tufanye upesi. Si unajua ratiba inatutaka mida ya mchana tuwepo eneo la tukio?”
Walifuata chombo chao cha usafiri – lile gari walilohangaika nalo na kulichakaza jana yake. Walikwea ndani ya gari hilo na kutimka upesi. Walifuata barabara wakakomea kwenye makazi ya zamani ya Stanis. Huko walijiweka sebuleni na kuanza kusuka cha kufanya ndani ya jumba kubwa la Kim.
Ramani ikiwa mezani walielekezana wapi pa kuingilia na pa kutokea. Ufahamu mdogo wa Vitalis juu ya jengo hilo ukapanuliwa na Stanis aliyemdadavulia kila korido, kila chumba asiache hata kitu kikielea.
Kisha hapo Stanis akaenda chumbani kwake na kusogeza kitanda pembeni. Sakafu mwa uvungu wa kitanda akapandakamiza na mguu wake pakatengeneza shimo. Humo ndani alitoa vidude vitano vyeusi vya pembe nne na rimoti yake. Alitabasamu akivitazama vitu hivyo kabla hajarudi sebuleni kukutana na Vitalis.
Sasa ulikuwa ni muda wa kutenda.
Wakiwa na pesa walizokabidhiwa na Rajul kabla hajapata kunywa dawa ndani ya bilauri, waliendea kununua visu vingi na vibegi vya kubebea visu hivyo. Hawakuona umuhimu wa kuwa na bunduki. Kudhamiria kufanya mambo yao kwa ukimya kuliwachangia wasipate presha kubwa ya kutafuta silaha hiyo ya moto. Haikuwa mipangoni.
Walivitia visu hivyo kwenye gari wakatia moto chombo na kuondoka. Ndani ya dakika chache wakawa karibu na jengo kubwa la bwana Kim. Waliruka ukuta wakazama ndani, vibegi begani. Kwa maelekezo ya Stanis walifuata jengo hilo wasionekane.
Walielekea chumba cha kuongozea na kutizamia kamera zilizosambazwa karibia maeneo yote ya jengo. Huko walimnyonga mwanaume aliyekuwemo humo kisha wakatazama jengo zima.
Kwa mujibu wa video za kamera hizo wakajua wapi pa kupita na wapi pa kupaacha. Ila pia wakaelekezana zaidi kwa msaada wa picha zitembeazo.
“Kila kitu kwenye hili jengo kinaendeshwa na umeme.” Stanis alisema huku akitazama video za kamera.
“Umeona hapo? Hapo ndipo zilipo stoo za utunzaji wa silaha.” Stanis alionyeshea video moja kiooni. “Ndipo napotakiwa kupachika mabomu haya niliyoyabeba.”
Akaonyeshea video nyingine.
“Hii ni mojawapo ya maeneo mateka wanapofungiwa. Haipo mbali saana na stoo za silaha na uwanja wa mateso. ”
“Sasa tukilipua maeneo hayo, mateka hawawezi wakauwawa?” Vitalis aliuliza.
“Hapana.” Stanis akajibu. “Umbali huo si wa karibu kiasi hiko.”
“Lakini vipi kama tukiwafungua mateka hao ndipo tukapambane na Kim?” Vitalis aliuliza.
“Tummalize kwanza Kim.” Stanis akajibu msisitizo kisha akaongezea: “Unajuaje kama hao mateka watakuwa hoi kwa kupewa mateso. Wanaweza wakawa mzigo tukashindwa kuhitimisha kazi.”
Kwa namna moja ama nyingine ikamuingia Vitalis kichwani.
“Hawatokuwa wameuwawa?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana. Kim si mtu wa kuua upesi kiasi hiko, tena watu ambao anajua anaweza akawatumia kutimiza jambo lake fulani. Alisita kuniua mimi kwasababu tu ya kunitumia kama sampo ya kuwafunzia wengine.”
Walikubaliana wakatoka ndani ya chumba hicho na kufuatisha maeneo yale waliyoyaona ni salama. Korido waliyoichukua waliifuata kwa hatua thelathini kabla hawajakata kona ya kushoto. Huko napo walitembea hatua chache kabla hawajakata kona ya kulia.
Wakamuona mwanaume mmoja akiwa anafungua chumba. Alikuwa mfupi ila aliyejaza misuli kiasi cha kubana shati lake jeusi alilolivaa.
Kabla mwanaume huyo hajakukuruka kufanya kitu, Vitalis alichomoa na kurusha kisu kilichotoboa koo la mwanaume huyo na kumdondosha chini kama mzigo.
Walimjongelea upesi wakafungua kile chumba na kuufungia mwili huo ndani. Kabla ya kuendelea na safari yao, Stanis alibandika vile vidude vyeusi viwili ndani ya chumba hicho kisha wakaendelea na korido hiyo kwa hatua kama kumi. Walipotaka kukata kushoto, walisita upesi, walisikia sauti za watu zinakuja.
Walijibanza na kuwangojea watu hao ambao walichukua sekunde kama kumi kuwafikia. Walikuwa wawili kwa idadi. Walikuwa warefu wenye miili iliyojaza. Mmoja alikuwa mweupe ya uzungu wakati mwingine akiwa chotara.
Walidakwa wakakatwa shingo wakifunikwa midomo, kisha wakaachwa hapo Stanis na Vitalis wakaendelea na safari yao.
Walitembea hatua chache tu ndani ya hiyo korido kabla hawajakumbana na wanaume watano waliotokeza ghafula konani. Upesi wanaume hao walipata kuona wenzao waliouwawa umbali wa hatua kadhaa hivyo haikuwia vigumu kukokotoa wale walipo mbele yao walikuwa ni maadui, tena hesabu hiyo ilirahisishwa zaidi kwa uwepo wa Stanis.
Walitazamana kisha wakawafuata maadui zao kwa mkupuo.
Wepesi ulikuwa ni kwamba wanaume hao hawakuwa na silaha yoyote.
Stanis na Vitalis walitumia visu vyao vema kuwamaliza kwa urahisi. Ndani ya muda mfupi walitengeneza dimbwi la damu maeneo hayo kwa kuwachanachana na kuwachoma wanaume hao pasi na huruma kisha wakaendelea na safari, ila sasa wakiwa wameongoza zaidi kasi ya mwendo wao.
Wakiwa njiani, Stanis alibandika vidude vyake mpaka pale vilipoisha.
Kitendo cha kuwamaliza wanaume kadhaa na kuwaacha koridoni ilikuwa ni hatari kwa usalama wao ukizingatia bado walikuwa na safari ndefu kufikia ofisi ya Kim, na safari ilikuwa ndefu zaidi kutokana na uchaguzi wao wa njia salama.
Sasa ilibidi wafanye mambo yao kabla maiti zile hazijagundulikana na taarifa ikasambaa kote. Na kuonekana kwa maiti zile si jambo ambalo unaweza sema kwa uhakika litachukua muda fulani, ni muda wowote tu laweza likachafua mazingira!
Walisonga wakapanda ngazi nne. Walikamata korido waliyoenda nayo ndani ya muda mfupi kabla hawajakata kona ya kushoto iliyowaongoza mpaka eneo la kupatia chakula. Lilikuwa ni eneo kubwa lenye madirisha makubwa ya vioo. Humo ndani palikuwemo na watu hamsini ama zaidi kidogo. Miongoni mwao wakiwemo wahudumu na wapambanaji wa bwana Kim waliokuwa wanapata chakula cha mchana.
Kwa mujibu wa saa ya ukutani ndani ya jengo hilo ilikuwa ni saa nane na nusu mchana. Televisheni kubwa iliyokuwemo humo ilikuwa inaonyesha michezo ya olimpiki: watu wakishindana kukimbia, kuruka, kuogelea, kutupa tufe na kadhalika. Watazamaji walikuwa wamegawana watu wa kuwashabikia kwahiyo wakati wanakula macho yao yalikuwa yameganda kwenye kioo cha kideo.
Hiyo ikawa fursa nzuri kwa Stanis na Vitalis.
Muda wa kuingia ndani ya jengo hilo ulikuwa maridhawa. Kama ingelikuwa ni muda mwingine basi bila shaka wangekuta wanaume hao wote ambao wamekusanyana ndani ya jengo hilo wakiwa wanarandaranda huku na kule. Ingekuwa hatari zaidi.
Wakiwa wamechuchumaa wasionekane kwenye madirisha, walipita upesi na korido hiyo kabla mbele ya hatua kama kumi hawajajificha upesi waliposikia sauti ya viatu ikisonga.
Walijibana kwenye kingo moja ya ukuta, akapita mwanamke aliyekuwa amevalia kinadhifu; suti nyeusi na viatu vyenye kisigino kirefu. Alikuwa anatembea kana kwamba hakanyagi chini.
“Ni sekretari wa Kim.” Alisema Stanis. “Anaenda kuchukua chakula chake na cha bosi wake.”
Walitoka kingoni wakaendelea na kutembea.
Baada ya dakika mbili za kujificha kuibuka, waliikaribia ofisi ya Kim. Mbele ya ofisi hiyo walikuwa wamesimama wanaume wawili: wale wanaume wa kazi, wakiwa wamevalia suti na miwani nyeusi tayari kwa ajili ya kufanya kazi zao. Walikuwa na miili mikubwa, mabega na vifua vipana. Walikuwa wamevimba kana kwamba ndani ya muda mfupi wanapasuka. Ingawa walikuwa wanalinda mahali na mtu mwenye mashiko makubwa, hawakuwa na silaha yoyote mikononi. Labda walikuwa wanaamini uwezo wao. Silaha ya nini?
Stanis na Vitalis wasipoteze muda, wakatokeza mbele ya wanaume hao.
“Ni muda sasa wa kujaribu kile alichokisema Rajul.” Alisema Stanis.
Wanaume wale wawili waliwafuata Stanis na Vitalis kwa mbio, ila kabla hawajafika walikutana na visu njiani vilivyokita na kuzama kifuani, ni mipini tu ndiyo ilibakia nje.
Wanaume hao wa kazi wakistaajabu hayo ya Musa, walidondoka chini habari yao ikaishia hapohapo.
Kabla Stanis na Vitalis hawajasogeza miguu, ving’ora vikaanza kuita!
“Hata hivyo tuna bahati!” Alisema Vitalis.
Haraka waliufuata mlango wa ofisi ya Kim, Vitalis akamwambia Stanis:
“Lipua!”
“Bado.” Stanis akajibu. “Watakuwa ndio wapo njiani kufuata silaha zao.”
Ni kweli. Wanaume wale waliokuwa wanapata mlo waliacha mara moja walichokuwa wanakifanya wakakimbia kuelekea kwenye stoo zao za utunzaji wa silaha punde tu baada ya kusikia king’ora. Sio wao peke yao tu, ikiwemo pia na wengineo waliokuwa wanarandaranda.
Stanis na Vitalis walivunja mlango kwa mateke ya nguvu, uso kwa uso wakakutana na Kim. Mkononi alikuwa amebebelea bunduki yake ndogo lakini uso wake ukijawa na woga.
“Sta – nis!” Kim alishangaa. Alimtazama na Vitalis akabakiwa ameachama mdomo kana kwamba anatafuta cha kusema.
Stanis, kwa siri asionekane, alibonyeza kitu kilichokuwa mfukoni mwake. Ghafla milipuko kikubwa ikasikika! Jengo lilitikisika likipitia tetemeko kubwa la ardhi.
Wanaume wale waliokuwa wanajihudumia silaha stoo hawakutoka salama hata kidogo. Aidha walipokonywa uhai wakitawanywa vipandevipande ama walibakizwa wakiwa na majeraha makubwa.
Ofisi ya Kim iligeuka shaghalabaghala. Alikuwa ameinama baada ya kusikia tetemeko hilo. Alipotazama awaone maadui zake waliokuja kudai roho yake, alikutana na kisu kilichotoboa mkono wake uliobebelea bunduki. Bunduki ikadondoka chini.
Sasa alikuwa analia kwa maumivu machungu aliyokuwa anayasikia.
Stanis alichukua bunduki ndogo ya Kim kisha kwa kushirikiana na Vitalis wakamtwaa mlengwa wao huyo na kumpeleka uwanja wa mateso walipomfunga kamba kwenye mstimu, kama vile alivyoamuru Stanis afanyiwe kipindi cha nyuma.
Walipomaliza kumfunga, walisogea mbali kwa hatua kadhaa wakipuuzia sauti ya mwanaume huyo iliyokuwa inapaza kuomba msamaha huku machozi yakimtiririka.
Walimtazama kwa sekunde kadhaa, Vitalis akatikisa kichwa chake alipokumbuka yale yote aliyoyapoteza kwasababu ya mwanaume yule.
Alijikuta anabinua mdomo wake, akafoka:
“Huwezi ukafa kirahisi Kim. Japokuwa hauwezi kusikia maumivu yale yote uliyoyasababisha juu ya ulimwengu huu, basi angalau kuyasikia kwake kidogo kutanipa ahueni ya moyo.”
Aliposema hayo alimtazama Stanis.
Ajabu akamkuta mwanaume huyo amemnyooshea mdomo wa bunduki.
“Samahani sana, Vitalis.” Alisema Stanis. “Inabidi nifanye hivi.”
Ghafla uso wa Vitalis ukanywea. Macho yalikuwa mekundu na mdomo wake mkavu ukaachama kabla hajajikuta akiuliza:
“Kwanini unafanya hivi Stanis?”
“Kwasababu ya pesa.” Stanis akamjibu kwa wepesi kisha akamuamuru aweke kibegi cha visu chini na kusogea mbali. Vitalis akatii.
Kwa kutumia bunduki yake, Stanis alimuamuru Kim ataje alipoweka nyaraka zake zote za siri pamoja na taarifa za benki kwa ahadi ya kumuachia uhai. Kim akamtajia pasipo kusita.
Alipopata taarifa hizo alirudisha mdomo wa bunduki kwa Vitalis akamtaka asali sala zake za mwisho. Vitalis akatema mate pembeni na kusema kwa kiburi.:
“Niue wewe malaya msaliti. Unasubiri nini?”
Stanis akacheka.
“Nilipokuwa nasikia matendo yako, nilidhani una akili sana, kumbe hamna lolote! Nimefanikiwa kukupata kwa akili ndogo sana. Ndogo sana!”
Akacheka tena.
“Okay, tuanze mwanzo kwanza. Tokea mara ya kwanza nilipokuona nilijua sasa ndoto zangu zinaenda kutimia kwa kukutumia wewe, lakini wewe mwenyewe haukujua, si ndio?”
Akabinua mdomo wake.
“Moja, ulidhani ni bahati mbaya nilipong’atwa na Rajul. Hapana, nilikuwa nimepanga. Ile ndiyo ilikuwa fursa yangu adhimu kupata nguvu nilizonyimwa kwa muda wote huo. Na kupata nguvu zile maana yake naenda kuwa Kim mpya, na bahati mbaya ama nzuri hatokuwepo tena Rajul wakunisimamisha.”
Akabinua tena mdomo wake.
“Pili, nilipokukataza usiwafungulie wenzako kabla ya kumaliza tulilopanga, ulifikiria nini? Haukuona hiyo ilikuwa ni njia rahisi ya kukufanya uwe mpweke nikumalize upesi? Kama kweli uliamini watakuwa waliteswa na wamechoka, kwanini haukuomba hata utizame zile video zilizotunzwa na kamera kwa kurudisha nyuma ili uone? Uliniamini sana, si ndio?”
Akabinua mdomo wake.
“Na tatu basi, ulipoona nimekimbilia bunduki ya Kim uliwaza nini? Bila shaka ulidhani nilifanya vile kwa sababu ya usalama wetu, eti enh?”
Akacheka kwa dharau.
Ila hakuchukua muda uso wake ukanywea. Vitalis alikuwa anatabasamu akishika kiuno.
“Sawa, naona ulikuwa umepanga mengi sana na ukatumia akili nyingi sana.” Alisema Vitalis. “Ila kamwe usidhani huwa naacha akili yangu nyuma ninapopanga jambo, kwahiyo acha na mimi nikukumbushe vitu.”
Stanis akanyamaza kimya akitoa macho.
“Moja, ulinambia kila kitu kwenye jengo la Kim kinaendeshwa na umeme, maana yake hata lile lango la wafungwa pia. Sasa ulivyolipua mabomu yale yote bado ulidhani umeme ndani ya jengo upo? Na kama haupo, maana yake nini? Acha nikusaidie kujibu; maana yake mateka wapo huru. Kwahiyo bado hakukuwa na sababu ya kuhofia ukizingatia ulinipa sababu ya kuamini kwanini watakuwa salama hata baada ya mabomu kulipuka.”
Vitalis akabinua mdomo wake na kuendelea:
“Pili, ulivyokuwa mjinga ukasahau na uliniambia wazi kabisa kwamba sehemu ya mateka ipo karibu na uwanja wa mateso. Kwahiyo ukichanganganya na ile ya kwanza kwamba wateka sasa wapo huru, maana yake watakuwa na uwezo wa kujongea eneo hili kwa wepesi kuliko maeneo mengine. Na sasa mateka hao wapo nyuma nyuma yako umbali si mrefu.”
Stanis akageuza macho yake kutazama.
Hilo likawa kosa.
Kwa kasi ya radi, Vitalis aliinama akachomoa kisu kwenye kibegi na kukirusha kulenga mkono wa Stanis. Pasipo kukosea aliutoboa mkono huo ukadondosha bunduki chini.
Stanis akiwa anagugumia maumivu, alijaribu kuokota bunduki na mkono wake wa kushoto ulio salama, ila nao kabla haujafanikiwa ukatobolewa na kisu kingine kilichorushwa upesi. Sasa akawa analia kwa maumivu makali.
“Tatu, ulivyo zuzu ukaamini ninayoyasema.” Alijigamba Vitalis.
“Sasa kama lango la wafungwa linaendeshwa kwa umeme ndio lifunguke umeme ukikatika?”
Akaacheka kwa dharau.
“Mbali na hayo naomba nikushukuru kwa kunisaidia kupata taarifa nyeti za Kim, pamoja pia na taarifa za benki. Nikutakie usiku mwema.”
Alipomaliza kusema hayo alimkandika Stanis teke zito la kichwa likamrusha mwanaume huyo samasoti kabla hajatua chini kama furushi na kupoteza fahamu.
Baada ya hapo juu ya nini kilitokea huko jiji la Hamilton, Bermuda, kilikuja kusemwa na muda. Vyombo vya habari nchini Tanzania vilieleza kinaganaga picha zikipendezesha majalada.
‘KIM ATOBOLEWA VISU MWILI MZIMA NA KUNYONGWA!’
‘KIM AUWAWA KINYAMA NA WATU WASIOJULIKANA: Kundi la ‘Wageni’ lahusishwa.
‘MWEKEZAJI MKUBWA NCHINI AUWAWA KIKATILI: Polisi washutumiwa kuchelewa kutoa msaada.’
‘MAOVU YA KIM YAANIKWA BAADA YA KUUWAWA KIKATILI: Nyaraka zake zawekwa wazi mitandaoni.’
‘VIGOGO SERIKALINI WAFA KWA PRESHA: Ni baada ya nyaraka za siri za Kim kuwahusisisha.’
Kila nakala ya magazeti hayo ilikuwepo mezani wakati Kaguta akiwa anakunywa chai majira ya asubuhi ndani ya nyumba kubwa ya kifahari.
Alijikuta anakunja sura yake alipoutazama mwili wa Kim kwenye picha mojawapo gazetini kabla hajatikisa kichwa chake na kusema:
“Kitendo cha kumuacha baradhuli huyu akiwa anatambulika kwa kumtazama usoni ni kosa kubwa sana. Sijui kwanini Vitalis alinizuia?”
Akashushia maneno hayo na chai.
Hakukaa hapo muda mrefu Miraji na Bakari wakajiri. Walikuwa wamevalia suti safi nyeusi, tai nyekundu na viatu vya ngozi vilivyokuwa vinametameta.
Kaguta aliwatazama vijana hao vizuri kama anawachambua kisha akatabasamu.
“Mmependeza!”
Mara wakatokea Vitalis na Bernadetha. Vitalis alikuwa amevalia suti taxedo iliyomkaa vema huku Bernadetha akiwa amevalia gauni jeupe lililominya kiuno chake na kujimwaga kwenye nyonga. Alikuwa kama malkia ingawa hakuwa amejipara na pembeni yake Vitalis alionekana kama mfalme.
Kila mtu aliwasifia wamependeza na kushauri kwanguvu nguo hizo zivaliwe siku ya harusi yao.
Wakati furaha hiyo ikiwa imewatawala huku, ilikuwa kinyume kwa Stanis, kule Hamilton, Bermuda.
Hakuwa amekufa, la hasha! Bali alikuwa mwendawazimu asiyeelewa nini anafanya, kula ama kunywa. Alikuwa hivyo punde tu baada ya kuzinduka toka kwenye usingizi mzito aliopewa na teke la Vitalis.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Roho ya mashetani aliyopandikizwa na meno ya Rajul ndiyo pekee ilikuwa imebakia juu ya uso wa dunia ikidai na kushikilia taasisi za Kim.
Na kama waswahili wasemavyo; mtoto wa nyoka ni nyoka, basi ndivyo ilivyokuwa kwa wale wote waliokuwa kwenye makampuni ama mashirika ya baradhuli yule mfu. Waliishia kuchanginyikiwa wakikimbia hovyo. Wengine waliishia kujiua ama kufa kwa kugongwa na magari.
Hakuna aliyebaki salama.
***
MWISHO
0 comments:
Post a Comment