Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

TAXI (2) - 2

 







    Simulizi : Taxi (2)

    Sehemu Ya Pili (2)





    Barabara ile haikuwa na msongamano, hivyo mwendo wao uliongezeka kidogo, wakakatiza katikati ya makazi ya watu wakikutana na kona kadhaa na hatimaye wakaanza kupita katika eneo la viwanda. Lile gari Toyota Verossa lilipofika mwisho wa barabara ile ya lami likakunja kona na kuingia kulia likiifuata barabara ya vumbi iliyoelekea eneo la Karakata.



    Likaanza kushusha mteremko katika barabara ile ya vumbi likipita katikati ya makazi ya watu yenye nyumba mchanganyiko, za kawaida na za kisasa na baada ya mwendo wa dakika tano lile gari likakomea mbele ya nyumba moja kubwa ya kisasa iliyojitenga, ikiwa na uwanja mkubwa kwa mbele. Ilikuwa ni nyumba tulivu sana na mahala pa kifahari.



    Ile taxi aliyopanda Tunu ilikuwa kwa mbali nayo ilikunja na kuelekea upande ule ikiifuata barabara ya vumbi na kwenda kusimama kwenye uwanja mpana wa mchanga uliokuwa mbele ya baa moja iliyokuwa inapiga muziki laini muda huo huku watu wakionekana kuburudika. Baa hiyo ilikuwa umbali wa mita mia moja toka pale ilipokuwa ile nyumba.



    Tunu akamtaka dereva wake azime injini ya gari, yule dereva alikuwa mwepesi kuelewa, akafanya kama alivyoagizwa. Kisha Tunu akamuuliza kuhusu kiasi cha fedha alichokuwa anadai kama malipo ya umbali wa kutoka Ilala alikokodiwa hadi pale.



    Yule dereva akamwambia kiasi cha fedha na bila kupoteza muda Tunu alimlipa na kumzidishia ili kujenga uaminifu kwa yule dereva. Yule dereva alizipokea zile fedha huku akishukuru sana. Tunu alitulia mle garini kwa muda akijaribu kulichunguza eneo lile kwa makini na mara akamwona yule mrembo akifungua mlango na kushuka toka kwenye lile gari Toyota Verossa, akaliendea geti la mbele la ile nyumba na kutoa ufungo, akafungua na kuzama ndani ya ile nyumba huku geti likifungwa haraka.



    Muda huo huo lile gari Toyota Verossa likaonekana kugeuza na kuondoka likirudi lilikotoka na kuwapita kwa kasi, kisha likatokomea kizani. Tunu aliiangalia ile nyumba kwa shauku, akageuza shingo yake kumwangalia yule dereva wa taxi na kumwahidi kuwa angerudi baada ya dakika therathini ila endapo asingetokea katika muda huo basi angekuwa huru kuondoka zake.



    Akiwa katikati ya udadisi na shauku alishuka toka ndani ya ile taxi, na kuanza kupiga hatua taratibu na kwa tahadhari kuelekea kwenye ile nyumba huku moyo wake ukienda mbio sana, hakuweza kuhisi nini ambacho kingemtokea mbele yake, hata hivyo, hilo halikumzuia kuendelea na harakati zake.



    “Liwalo na liwe,’ Tunu aliwaza huku akizidi kujongea kwenye ile nyumba.







    Kabla hajafika mbali akasikia sauti fulani ya tahadhari ikimwita nyuma yake, “Sister!” Alipogeuka akamwona yule dereva wa taxi iliyomleta akimjia haraka. Tunu alisimama akamtazama kwa mshangao. Yule dereva alikuwa akimjia haraka.



    “Kuwa makini sana, Sister,” yule dereva alimwambia Tunu sentensi fupi yenye uzito kisha akaanza kurudi haraka kwenye gari lake. Tunu alibaini kuwa alikuwa anamaanisha anachokisema kwa namna alivyomtazama. Naye kwa kumwonesha kuwa wapo pamoja, alibetua kichwa chake kukubali kisha akaanza kuondoka.



    Wakati akitembea, aligeuka tena kutazama nyuma, akamwona yule dereva akiwa ametulia kwenye gari lake lakini akiwa makini kufuatilia kule alikokuwa Tunu.



    Tunu aligeuka kutazama pembeni yake, hakuweza kumwona mtu yeyote aliyemtilia shaka. Akashusha pumzi na kuendelea na safari yake bila kuonesha wasiwasi wowote akiwa kama mtu aliyekuwa anapita zake. Aliitupia jicho la wizi nyumba ile kuutathmini usalama wa eneo lile. Mwanga wa taa kubwa juu ya ukuta wa ile nyumba ulimwezesha kwa kiasi fulani kuyasoma mazingira ya eneo lile.



    Aliziona kamera mbili zilizokuwa juu ya geti zenye uwezo wa kunasa picha ya kitu chochote mbele ya nyumba. Alipofika mwisho wa ule ukuta, akachepuka na kuzunguka upande wa nyuma ambako nyumba ile ilikuwa imezungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli ambayo matawi yake yalikuwa makubwa yaliyokuwa yametengeneza vichaka vilivyosababisha kiza fulani.



    Alisimama kwenye kiza kwa tahadhari akaendelea kuitazama ile miti mikubwa kwa utulivu huku hisia zake zikimweleza kuwa mtu yeyote mwenye hila angeweza kujibanza nyuma ya miti ile na kuitimiza adhma yake mbaya.



    Alipojiridhisha kuwa hali ilikuwa salama, akaukwea kwa tahadhari mti mmoja mkubwa na kufanikiwa kufika juu, akachungulia ndani. Akayaona mazingira mazuri ya nyumba ile. Ilikuwa nyumba ya kisasa iliyozungukwa kwa bustani nzuri ya maua na nyasi zilizokatwa vizuri. Kulikuwa na magari mawili yaliyokuwa ndani ya banda la wazi la kuegeshea magari.



    Gari moja ni aina ya Mercedes Benz E-class limousine jeusi lililokuwa na milango sita na gari jingine ni Nissan Patrol jeupe. Akiwa pale juu alichagua tawi moja zuri lililokuwa limening’inia ndani ya ukuta wa ile nyumba kule nyuma ya nyumba. Alijilaza juu ya tawi lile na kuanza kusota kwa tumbo taratibu akishuka kuelekea mle ndani ya ule ukuta.



    Kiza kilichosababishwa na matawi makubwa ya miti ya vivuli iliyoizunguka nyumba ile kilimpa nafasi nzuri ya kufanya mjongeo makini na wa utulivu akionekana kama kivuli kwani alitembea kwa tahadhari kubwa, akiwa na uhakika kuwa ingehitaji mtu makini sana kugundua uwepo wake.



    Alifika kwenye varanda ndogo katika sehemu ya nyuma ya ile nyumba na kusimama huku macho yake yakiwa makini kuangaza huku na huko, varanda ile ilikuwa na mlango wa nyuma wa kuingilia jikoni. Aliusogelea mlango na kusimama kwa utulivu akitazama huku na kule katika namna ya kusikiliza kama angeweza kusikia kitu lakini hali bado ilikuwa ya ukimya mno.



    Pembeni ya ule mlango kulikuwa na dirisha moja la sehemu ya jiko la ile nyumba upande wa kushoto. Tunu alilisogelea lile dirisha na kuchungulia ndani, japo dirisha lilikuwa limefunikwa na pazia kwa ndani lakini kupitia uwazi mdogo pembeni ya dirisha lile aliweza kuona mle ndani. Hakuona dalili ya kuwepo mtu yeyote.



    Alijaribu kulifungua lile dirisha lakini hakufanikiwa kwani lile dirisha lilikuwa limefungwa ndani kwa komeo. Hakuona kama kulikuwa na namna nyingine yoyote ya kuweza kuingia mle ndani isipokuwa kuvunja sehemu ndogo ya kile kioo cha lile dirisha.



    Mara akahisi uwepo wa kiumbe kingine eneo lile, akashtuka na kugeuka kutazama nyuma yake na macho yake yakakutana na macho ya yule mrembo akiwa ameshika bastola mkononi akimwelekezea. Tunu alishikwa na taharuki ambayo hakuitarajia kabisa.



    Yule mrembo alikuwa bado amevaa nguo zilezile alizotoka nazo kule ELLI’S, sketi fupi nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi nyeupe ya mikono mirefu na viatu vya flati, na alikuwa amekunja sura yake huku akimtazama Tunu kwa macho makali.



    Tunu alimtazama kwa makini, sura yake ikajaa usoni kwake, ghafla akaonekana kumkumbuka.



    “Lisa!” Tunu aliita kwa mshangao mkubwa.



    Yule mrembo kwanza hakumjibu, aliendelea kumnyooshea bastola huku akiwa amekunja sura yake. Akili ya Tunu ikaanza kufanya kazi haraka akitafuta namna ya kujinasua toka katika mikono ya Lisa. Alitazama kando yake na kuliona kopo dogo lililopandwa maua.



    “Niambie, Tunu, nini kilichokuleta hapa?” Lisa aliuliza kwa ukali.



    “We need to talk, Lisa, nilikuja hapa kuongea na wewe na tumalize tofauti zetu...”



    “Usinifanye mimi ni mjinga, Tunu! Natambua kinachoendelea,” Lisa alisema na kuendelea, “Nilifahamu tu kuwa ungenifuata hapa na ulivyo na kichwa cha panzi umeshindwa hata kuushtukia mtego hafifu kama huu. Dereva wako uliyemkodi kakuchuuza. Yule ni mwenzetu.”



    “Umekosea sana, Lisa, kwa hiki unachotaka kukifanya, we are friends...” Tunu alisema huku akimwangalia Lisa kwa uchungu, moyoni alijua kuwa amenasa kwenye mtego kwa kumwamini yule dereva kirahisi. Lisa aliangua kicheko cha dharau.



    “Tunu, Nafahamu vyema wewe ni nani, unamfanyia nani kazi na upo hapa Dar es Salaam kwa kazi gani! Sishangazwi na hilo kwani hata mimi nipo hapa kwa maslahi ya ninayemfanyia kazi kama ilivyo kwako,” Lisa alisema kwa kujiamini.



    “Kwa hiyo bado unamfanyia kazi Mr. Oduya? Hivi unaamini kabisa atakuwa rais wa nchi hii?” Tunu aliuliza huku akimkazia macho Lisa.



    “Mimi huwa sina kawaida ya kujibu maswali ya kipumbavu toka kwa watu wa sampuli yako,” Lisa alisema kwa dharau. Kisha kikatokea kitambo kifupi cha ukimya.







    “Sasa nataka uyajibu vizuri maswali yangu na usilete hila yoyote kwani nakuhakikishia kuwa mimi si Lisa yule uliyekuwa ukimfahamu. Kwa sasa hakuna kiumbe yeyote msumbufu anayeweza kuingia anga zangu akaniponyoka,” Lisa alimwonya Tunu huku akiachia tabasamu la dharau.



    * * * * *



    Gari aina ya Cadillac DeVille lilifunga breki mita therathini kabla halijaifika nyumba ya Sammy baada ya kusimamishwa na askari mmoja aliyekuwa amebebelea bunduki na kifua chake kikiwa kimekingwa na vazi maalumu linalozuia risasi. Kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wamejazana eneo lile wakiwa na nyuso za huzuni.



    Wakati huo aliwaona askari wengine wawili ambao pia walivaa mavazi ya kuzuia risasi na kubebelea bunduki waliokuwa wanaweka utepe maalumu wa njano katika eneo lile kuashiria hali ya hatari. Walikuwa wanapashana habari na watu wengine ambao hawakuwepo eneo lile kwa vifaa maalumu vya kisasa vya mawasiliano. Wale askari wenye silaha walikuwa wanajitahidi kuwazuia watu wasisogee katika eneo lile huku nyuso zao zikionesha wazi kuwa walikuwa tayari kwa lolote, tayari kuua, tayari kufa.



    Sammy alishikwa na bumbuwazi, aliteremka toka kwenye gari lake na kusimama akiwatazama wale askari kwa makini, alipouona ule utepe wa njano ukizingushwa katika eneo la nyumba yake moyo wake ukapiga kite, ukaanza kwenda mbio isivyo kawaida na mwili ukaishiwa na nguvu.



    “Kuna nini?” Sammy aliwauliza wale askari wenye silaha kwa wasiwasi huku akili yake ikikataa kuamini kama kulikuwa na tatizo nyumbani kwake. Askari yule alikuwa anakagua eneo lile huku akiwasiliana na watu ambao hawakuwepo eneo lile.



    “Majambazi,” yule askari alimjibu kwa kifupi huku akiendelea kukagua eneo lile.



    “Wako wapi?”



    “Wametoroka na pikipiki.”



    Kauli ile ikamfanya Sammy amkumbuke yule mtu aliyekuwa anaendesha pikipiki kwa mwendo wa kasi ya ajabu kama mwendawazimu na kuingia upande wake akitaka kumgonga, akashusha pumzi.



    “Kwa hiyo kumetokea nini huko ndani?” Sammy alizidi kuuliza huku wasiwasi ukimtawala.



    “Kwani wewe ni nani unayeniuliza maswali ya kipolisi?” yule askari alimuuliza Sammy huku akimkazia macho.



    “Mimi ndiye mwenye nyumba hii, nilipigiwa simu nirudi haraka kuna tatizo,” Sammy akasema huku akianza kukereka.



    “Basi ndiyo kama ulivyosikia,” yule askari akamwambia Sammy.



    “Kusikia nini! Unajua hadi sasa sielewi kilichotokea?”



    “Ni kwamba majambazi walivamia nyumba hii, hatujajua bado walichokuwa wakikitaka ila kuna mwanamke, sijui kama ni mkeo amepigwa risasi...” askari mmoja alimwambia Sammy.



    Moyo wa Sammy ukapiga kite kwa nguvu kama aliyepigwa konde zito kichwani bila kutarajia. Hakusubiri tena kuambiwa, alichomoka na kukimbilia ndani kama mtu aliyepagawa. Askari mmoja akataka kumzuia lakini alishachelewa kwani Sammy alishafika getini na kuzama ndani. Pale sebuleni alimkuta Joyce akiwa sakafuni amelalia dimbwi la damu huku akikoroma kwa maumivu. Upesi Sammy alimkimbilia na kutaka kumnyanyua bila kujali damu.



    “Mama Pendo! Mama Pendo!” Sammy aliita huku akimgeuza Joyce. Wale askari walimshika Sammy na kumzuia. Sammy akaanza kuleta purukshani huku akipiga kelele kama aliyepandwa na wazimu kichwani lakini wale askari walidhibiti kisawasawa.



    “Mama Pendo! Please don’t die!" Sammy aliita na Joyce akafungua macho lakini hakuweza kusema chochote. Mwili wake haukuwa na nguvu kwani alipoteza damu nyingi.



    “Mama Pendo, tafadhali usituache, bado tunakuhitaji. Siwezi kuishi bila wewe, Mama Pendo!” Sammy alisema kwa uchungu huku akimtazama Joyce kwa huzuni, machozi yalikuwa yanamtoka. “Ee Mungu baba, nakuomba usimchukue mke wangu,” Sammy aliomba kimyakimya huku akishusha pumzi za kukata tamaa,



    Alitupa macho yake kando na kuwaona Winifrida na Pendo wakiwa wamesimama wanalia kwa uchungu. Sammy aliwasogelea, akambeba Pendo huku akiwakumbatia wote kwa uchungu. Hakika lile tukio la kupigwa risasi Joyce lilikuwa pigo kubwa kwao wote, ni kama pigo la kisu lililopenya mwilini na kujeruhi mioyo yao.



    Akiwa bado amewakumbatia Pendo na Winifrida, Sammy aliwashuhudia watu wawili waliovalia makoti marefu meupe na glavu nyeupe mikononi wakiingia haraka mle ndani wakiwa wamebeba machela, wakambeba Joyce na kumlaza kwenye ile machela kisha wakatoka naye na kupeleka katika gari la wagonjwa lililokuwa limeegeshwa nje.



    Sammy hakutaka kubakia pale, aliwakabidhi Winifrida na Pendo kwa wale askari aliowakuta mle ndani kisha akatoka kumfuata Joyce kule kwenye gari.



    * * * * *



    “Nilihisi tu kuwa mtafanya makosa… nilijua tu, we are fucked up!” sauti ya Mr. Oduya ilisikika kwenye simu, ikapenya katika ngoma ya sikio la Spoiler hadi kwenye ubongo wake na kumfanya asisimkwe mwili kwa hofu.



    “Lisa aliponipigia simu kunieleza kuwa Sammy yupo na Tunu nikajua kila kitu kimeharibika...” Mr. Oduya alisema kwa sauti yenye mtetemo na kuendelea, “Mbaya zaidi, Sammy aliondoka na watu wawili ambao kwa vyovyote walipandikizwa na Tunu ili kumlinda ndiyo maana hakufika nyumbani. Sijui huyu Tunu ametokea wapi baada ya miaka yote hii na ilikuwaje mkashindwa kubaini kuhusu uwepo wake?”



    Kwa mara ya kwanza katika harakati za namna ile Spoiler alianza kuhisi hofu ikimtambaa mwilini mwake.



    “Sasa, hakuna haja ya Sammy kukamatwa na kupelekwa kule Kinondoni, ninachotaka ni kifo tu, afe tu basi! Tena siyo yeye tu, nataka Tunu naye afe, halafu niletewe vichwa vyao hapa!” Mr. Oduya alisema kwa ghadhabu.



    “Nitakuongezea watu, sijui umenielewa!” Mr. Oduya alipaza sauti kwa ukubwa kiasi cha kumfanya Spoiler aisogeze simu yake mbali na sikio kwa kuhofia kuleta madhara kwenye ngoma ya sikio.



    “Nimeelewa!” Spoiler alisema na kushusha pumzi.



    Spoiler alikuwa amesimama katika eneo la makaburi ya Vingunguti yaliyopo katika bonde la Mto Msimbazi baada ya kutoka nyumbani kwa Sammy eneo la Tabata Chang’ombe. Eneo lile la makaburi ya Vingunguti lilikuwa moja ya maeneo yaliyotisha sana kutokana na sifa yake ya kuwa eneo hifadhi la wahalifu waliokuwa wakivizia wapita njia ili kuwakaba na kuwaibia mali zao.



    Spoiler alifika eneo lile baada ya purukshani nyingi barabarani, laiti kama asingekuwa mzoefu wa harakati kama zile angekamatwa au angeuawa. Nguo zake zilikuwa zimetapakaa damu. Aliutazama mwili wa Dulla Mcomoro ambao haukuwa na uhai jinsi ulivyolala kifudifudi juu ya pikipiki. Alitamani kuutupa pale makaburini lakini aliogopa ingeweza kuwaletea shida baadaye kwa kuwa Dulla alikuwa anafahamika kuwa na ukaribu na Mr. Oduya.







    Spoiler alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiwa makini sana kuhakikisha hakuna mtu aliyekuwa anamwona pale kizani alipokuwa amejificha.



    Sasa alianza kumfikiria Tunu. Alikuwa na uhakika kuwa Tunu hakuwa mwanamke wa kawaida. Alikuwa ni zaidi ya vile walivyokuwa wakimchukulia, alikuwa ni shushushu aliyebobea ambaye mara nyingi aliutumia uzuri wake kuwaingia wanaume na kupata taarifa alizozihitaji.



    Spoiler aliyakumbuka maneno ya Mr. Oduya kuwa Sammy aliondoka na wanaume wengine wawili ndani ya gari lake baada ya maongezi yake na Tunu, Spoiler akaamini kabisa kuwa sasa kazi ilikuwa ngumu tofauti na alivyodhania mwanzo kwani ingehitajika nguvu ya ziada. Kama mwanzoni walimchukulia Sammy kama mtu mmoja sasa hakuwa peke yake, waliongezeka Tunu na watu wengine wawili ambao hakuwajua.



    Spoiler alihisi mwili wake ukimsisimka, kwa hasira akageuka nyuma na kutaka kuanza kuondoka pale alipokuwa amejificha lakini akasita baada ya kukutana na sura za wanaume wawili walioonekana wamebobea kwa uhalifu. Wale wanaume walikuwa na miili iliyojengeka imara na walikuwa wakimtazama Spoiler kwa tabasamu la kifedhuli.



    Mmoja alikuwa mrefu na mweusi kama Mjaluo, macho yake yalikuwa makubwa na mekundu yenye uchovu lakini yaliyokuwa makini sana. Alikuwa na kovu kubwa chini ya jicho lake la kushoto. Alivaa suruali ya jeans iliyochanwachanwa sehemu ya mapaja na fulana nyeusi, kichwani alijifunga kitambaa chenye rangi mchanganyiko wa nyekundu, njano na kijani kikiwa na alama ya mche wa bangi.



    Mwingine alikuwa mfupi lakini mwenye mwili uliojengeka, alikuwa na uso mrefu uliotulia kama maji mtungini, alivaa magwanda mfano wa kombati na kichwani alikuwa na upara unaowaka na usiokuwa na unywele hata mmoja. Kichwani alikuwa na ngeu na mishipa ya damu ilionekana kutuna na kusambaa kichwani kama mizizi ya mmea wa nafaka. Uso wake pia ulikuwa na makovu.



    Spoiler aliwatazama kwa makini huku akijaribu kuwapima. Mapigo ya moyo wake yalianza kumwenda mbio huku baridi nyepesi ikisafiri katika maungo yake. Hali ile ilimfanya ahisi kuwa maficho yale hayakuwa salama tena, hivyo angelazimika kuondoka pale haraka iwezekanavyo na kutafuta chimbo jingine.



    Wale watu walimsogelea taratibu, mikononi walikuwa wameshika silaha kama jambia na nondo tayari kwa lolote. Akili ya Spoiler ikafanya kazi haraka, bila kuchelewa alichomoa kisu chake kwenye ala, akakirusha kiustadi na kwenda kumchoma yule mtu mfupi upande wa kushoto wa kifua kwenye moyo. Alianguka chini huku akipiga yowe dogo.



    Kabla yule mwanamume mrefu na mweusi kama Mjaluo hajakaa sawa wala kuelewa kilichotokea, Spoiler tayari alishadaka kisu kingine kutoka kwenye begi lake dogo la mgongoni na kuruka sarakasi ya chinichini kisha akamcharanga shingo yake na kukichomoa kile kisu kwa fujo huku akimwacha yule mwanamume akidondoka kama mzigo wa gunia la mahindi akiwa tayari maiti. Spoiler akakifuta damu na kumfuata yule mtu wa pili, akakichomoa kile kisu kilichokita kwenye moyo kwa fujo huku akihakikisha kuwa wote hawataamka tena.



    Sasa alikuwa amepandwa na hasira kali ambazo zilimfanya kuanza kuzungukazunguka eneo lile. Mara simu yake ikaanza kutetema. Aliitoa na kuitazama kwa makini, ilikuwa ni simu kutoka kwa Mr. Oduya. Spoiler aliipokea haraka na kuiweka kwenye sikio. “Ndiyo, Boss!” Spoiler alisema huku akishusha pumzi ndefu.



    “Una uhakika hapo upo sehemu salama ambayo huwezi kushtukiwa?” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti ilionekana kuwa ‘serious’ tofauti na mwanzo, kwa mbali tumbo lake lilikuwa linamuuma.



    “Si mahala salama sana, nipo makaburini na nimetoka kupambana na wahalifu wawili sasa hivi waliotaka kunidhuru,” Spoiler alisema huku akishusha pumzi.



    “Okay, nimemtuma Job anakuja, atakupigia simu akikaribia hapo ili akupeleke Karakata ukaungane na kina Lisa na Uledi. Uledi kanipigia simu, ameniambia Tunu alikuwa anawafuatilia lakini tayari ameingia kwenye mtego na Lisa ameshamdhibiti,” Mr. Oduya alisema kisha akakata simu.



    Mzuka wa unyama ukazidi kumpanda Spoiler, alijikuta akisisimkwa zaidi mwili wake tayari kwa mapambano. Alitamani aote mabawa ili apae angani na kumfikia Tunu kisha amwoneshe kile kilichomnyoa kanga manyoya ya shingoni.



    * * * * *



    “Tupa chini mkoba wako na ugeuke ukutani wewe kahaba na unyanyue mikono yako juu, utulie hivyo hivyo, ukijitikisa tu nitakifumua kichwa chako,” Lisa alimwonya Tunu huku akiwa ameshika vyema bastola yake akiielekeza kichwani kwake.



    “Sawa, kahaba mkubwa!” Tunu alijibu kwa jeuri na kuutupa chini mkoba wake huku akigeuka.



    “Sasa utafuata kile nitakachokwambia na usijidanganye kufanya utundu wa namna yoyote kwani sitokuvumilia,” Lisa alifoka.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Sawa!” Tunu alijibu tena.



    Lisa alimsogelea kwa tahadhari huku akiwa yupo makini zaidi, akaanza kumpekua mwilini huku mkono wake mmoja ukiwa bado umeielekeza bastola yake kisogoni kwa Tunu tayari kufyatua risasi endapo angeleta utata. Katika upekuzi wake alipata bastola moja ndogo aina ya Glock 19M ambayo hutumiwa na wapelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI). Bastola hiyo Tunu alikuwa ameifutika kiunoni.



    Alipomaliza kumpekua akauchukua ule mkoba na kumwamuru aanze kupiga hatua. Tunu alibaki akiwa amesimama asijue anatakiwa kupiga hatua kuelekea wapi!



    “Tembea mbele kahaba mkubwa wewe!”



    “Natembea kuelekea wapi? Kwenda kujiuza!” Tunu aliuliza kwa kebehi akijifanya haelewi somo.



    “Fuata ninachosema, mimi huwa sipendi maswali maswali ya kijinga. Nataka uelekee ndani, umenielewa?” Lisa alisema kwa kufoka.







    “Nimekuelewa!” Tunu alisema na kuanza kupiga hatua.



    Safari ya kueleka ndani ikaanza, Tunu alikuwa ametangulia mbele akiwa amenyanyua mikono yake juu na wakati huo bastola ya Lisa ikiwa nyuma yake ikiendelea kumgusa kisogoni. Hasira zilikuwa zimemshika kwa kuingia mikononi mwa Lisa, hata hivyo aliendelea kujifanya ameishiwa ujanja ili aweze kulichunguza vyema lile jumba.



    Wakati wanatembea alifikiria kufanya shambulizi la kushtukiza lakini akajionya kuwa kufanya uamuzi wowote wa kukurupuka kwa kipindi kile usingekuwa na tija yoyote na badala yake alitakiwa kusubiri kwanza hadi hapo ambapo muda mwafaka ungewadia.



    Walizunguka kutoka kule nyuma ya nyumba na kutokezea upande wa mbele wa ile nyumba na wakati wote huo Tunu alikuwa akiyachunguza mandhari ya nyumba ile huku pia akiupima uimara wa Lisa. Walipofika kwenye mlango wa mbele Lisa akamwamuru Tunu ausukume ule mlango na kuingia, kwani ulikuwa umerudishiwa tu, haukuwa umefungwa kabisa.



    Wakaingia na kutokea sebuleni. Ilikuwa ni sebule kubwa yenye samani zote za kisasa. Tunu aliendelea kupiga hatua huku macho yake yakizunguka kulichunguza eneo lile kama kulikuwa na watu au mtu mwingine yoyote.



    “Simama,” Lisa aliamuru na Tunu akasimama huku akiyazungusha macho yake, hakuweza kumwona mtu mwingine pale sebuleni ingawa hali hiyo haikumshawishi aamini kuwa Lisa alikuwa peke yake mle ndani.



    “Kwani wengine wako wapi?” Tunu aliuliza huku anatafuta namna ya kujiokoa toka mikononi mwa Lisa, alitazama kando kwenye dirisha na kuachia tabasamu.



    “Sikukwambia kuwa sipendi maswali ya kijinga, we kahaba?” Lisa alifoka.



    “Sawa, kahaba mwenzangu!” Tunu alisema huku akiangalia kwenye dirisha na kubetua kichwa chake kwa tabasamu la chati kana kwamba alikuwa anampa mtu fulani ishara. Lisa akageuza shingo yake haraka kutazama upande ule wa dirisha, hilo likawa kosa kubwa. Tunu alimvaa Lisa na kumkumba. Wakapigwa mwereka sakafuni huku bastola zikimtoka Lisa na kuangukia kando.



    Lisa akainuka haraka kuifuata bastola yake lakini kabla hajaifikia Tunu akajitupa tena na kuunyoosha mguu wake kuipiga teke, ikasogea mbali, halafu akaunyanyua ule mguu kutaka kumtandika teke la kifuani lakini Lisa akawa mwepesi na kulikwepa, kisha akajirusha kwa mgongo kumfuata Tunu.



    Alipokuwa hewani Tunu alitupa ngumi lakini Lisa akaiona na kuikwepa, ya pili akaidaka na kuuviringisha mkono wake huku akijizungusha na kutupa kiwiko lakini Tunu akakikwepa na kumdaka shingo yake, akamkaba kwa nguvu zake zote.



    Lisa akaanza kutapatapa akitupa viwiko vyake ili kujikwamua toka kwenye ile kabali, kimoja kilimpata Tunu na kutua kwenye mbavu zake kikamwachia maumivu makali, akayavumilia na kuendelea kumkaba. Lisa akatupa tena kingine, hakikumpata, cha tatu kikampata tena na kumtia maumivu makali zaidi. Tunu akashindwa kuvumilia na kumwachia!



    Bila kutarajia Lisa alirusha konde lililotua barabara kwenye shavu la kulia la Tunu. Tunu akatema damu. Lisa akainuka kuifuata bastola yake lakini Tunu hakumruhusu achukue bastola. Akawahi kumvuta. Kuona hivyo Lisa alitupa teke lakini Tunu akaudaka mguu na kumvuta kwa nguvu huku akimrukia mgongoni na kumkaba tena. Safari hii aliikandamiza mikono ya Lisa kwa magoti yake na Lisa hakuweza kufurukuta, akaanza kuishiwa nguvu.



    “Sasa zamu yako kujibu maswali yangu, mlimfuata nani pale Elli’s?” Tunu alimuuliza Lisa huku kamkaba.



    “Sijui,” Lisa alijibu kwa jeuri. Tunu akamtwanga ngumi kali iliyompa maumivu makali. Lisa akagugumia kwa maumivu. Akazidi kumkaba hadi alipoona anaanza kukoroma, akamwachia na kuziwahi bastola zote mbili, ile ya kwake aliyonyang’anywa aina ya Glock 19M na ile ya Lisa aina ya 45 Colt.



    Akazishika vyema zote mbili, moja mkono wa kulia na nyingine mkono wa kushoto na kuzielekeza kwa Lisa ambaye alikuwa anatapatapa pale sakafuni kwa maumivu.



    “Mlimfuata nani pale Elli’s?” Tunu alirudia tena swali lake. Lisa akacheka kwa dharau.



    “Hayo maswali yako ya kijinga sidhani kama nipo kwenye mood ya kuyaji...” Lisa hakumaliza kujibu, akakatishwa na mvumo wa risasi mbili toka kwenye bastola ya Tunu yenye kiwambo cha kuzuia sauti. Tunu alikuwa amefyatua risasi mbili za upesi upesi zikapita pembeni ya kichwa cha Lisa na kumtengenezea maumivu makali sikioni. Lisa akaonekana kuogopa sana.



    “Kama hutonijibu unajua kitakachokutokea, you know me, Lisa. You know me very well,” Tunu alifoka. Sasa sura yake ilikuwa imebadilika, aliuvua ubinadamu na kuuvaa unyama, macho yake yalikuwa yanawaka kama kaa la moto.



    “Hata kama nikikujibu swali lako haitasaidia kitu...” Lisa alisema huku akicheka kwa dharau.



    “Mambo ya kunisaidia au kutonisaidia nayajua mwenyewe. Nijibu kabla sijakifumua kichwa chako kwa risasi! Wala usijidanganye kuwa unachelewesha muda ili wenzako wafike kutasaidia, sina muda wa kumbembelezana kwa sasa,” Tunu alisema na kupeleka tena kidole chake kwenye kilimi ili kufyatua risasi, alimaanisha alichokuwa akikizungumza.



    “Usidhani kuniua mimi ndiyo umeshinda, bado una kazi ngumu sana, Tunu.”



    “Kazi ngumu ndizo ninazozipenda! Sasa nijibu, mlimfuata nani?” Tunu alifoka. Kisha akaachia risasi moja iliyoparaza kichwani ikazipunyua nywele za Lisa. Lisa akatoa ukelele wa hofu, “Nasema! Nasema!”



    “Sema haraka!” Tunu akamkaripia.



    “Tulimfuata Sammy!” Lisa akaropoka.



    “Mnamtakia nini?”



    “Mzee katutuma tumteke na lile gari lake...” Lisa alianza kuropoka kwa hofu lakini akaonekana kusita huku hofu kubwa ikitanda usoni kwake. Tunu akahisi uwepo wa kitu kilichomwogofya Lisa. Hakujiuliza mara mbili, alijirusha na kujitupa chini nyuma ya sofa moja dogo na muda ule ule kichwa cha Lisa kilifumuliwa na risasi zilizotoka kwenye bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.







    Tunu aliviringika na kutambaa kama nyoka akihama kutoka sofa lile dogo na kwenda kwenye sofa kubwa. Akajilaza kimya akijaribu kusikilizia lakini akahisi chuma kikielekezwa kichwani kwake, moja kwa moja akatambua kuwa ulikuwa ni mtutu wa bastola na aliyeshika bastola hiyo alikuwa hatua moja tu toka alipolala. Mwili wake ukaingiwa na baridi.



    Tunu hakutikisika wala kuinua mikono yake iliyoshika bastola. Alijua wazi kuwa alikuwa amepatikana. Hakuwa na ujanja na wala hakutakiwa kufanya lolote lile kwa pupa isipokuwa kuutii kila atakachoambiwa na mtu yule.



    “Weka bastola zako chini na uinuke taratibu,” sauti ya ukakamavu ya yule mtu ilimwamrisha Tunu. Taratibu akaziweka chini bastola na kusimama akiwa amenyoosha mikono yake juu.



    Alihisi kama ameona mzimu, alijikuta akitazamana na mtutu wa bastola aina ya FNX 45 Tactical yenye kiwambo cha kuzuia sauti. Bastola ile ilikuwa imeshikwa na mwanamume mfupi mwenye umbo lililojengeka kwa misuli kutokana na ratiba nzuri ya mazoezi. Mwanamume yule alikuwa amevaa fulana nyekundu iliyombana na kulionesha vyema umbo lake lililojengeka kwa misuli, suruali ya bluu ya jeans na miguuni alivaa raba nyeusi.



    Tunu alimtazama kwa wasiwasi. Macho ya yule mwanamume yalikuwa na dalili zote za ukatili, uwendawazimu na unyama uliokubuhu.



    “Uledi!” Tunu alimaka kwa mshangao. Alikuwa akimfahamu vyema Uledi Mkama tangu alipokutana naye katika ofisi ya Mr. Oduya wakati huo yeye Tunu akifanya kazi hapo. Alifahamu kuwa Uledi alikuwa mmoja wa vijana wawili waliokuwa wakitumwa kufanya kazi maalumu na za siri za Mr. Oduya, yeye na Dulla Mcomoro. Alikumbuka kuwa ni hawa wawili wakishirikiana na Spoiler waliohusika kwenye mauaji ya Jaji Lutego.



    “Uledi!” Tunu aliita katika namna ya kutaka kumzubaisha lakini Uledi hakutaka maongezi yoyote na Tunu, yeye alidhamiria kuua na kupeleka kichwa kama alivyoagizwa na Mr. Oduya.



    Alianza kuvuta ndimi ya bastola, Tunu akafumba macho kwani alijua kile ambacho kingetokea na hakutaka kuona. Mara ukasikika mlio mkubwa wa risasi kutoka kwenye bastola isiyo na kiwambo cha kuzuia sauti, damu zikamrukia Tunu ambaye alianguka sakafuni huku akihisi moyo wake ulikuwa umepoteza mapigo yake, kisha akatulia kama mfu akiwa hajui iwapo alikuwa amekufa au alikuwa ndotoni.



    “Sister! Sister!” Tunu akasikia sauti ya mwanamume ambayo haikuwa ngeni masikioni mwake, alihisi kuitambua vyema. Akajiuliza ameisikia wapi?



    “Sister... ni mimi dereva wako. Inuka tuondoke haraka kuna wenzao wataingia hapa dakika yoyote kuanzia sasa,” ile sauti ilisema tena kwa wasiwasi. Sasa aliikumba vyema. Ni kweli ilikuwa ni sauti ya yule dereva wa teksi aliyoikodi. Hata hivyo hakujitokeza kwa kuogopa kuwa huenda ulikuwa ni mtego.



    Tunu aliinua uso wake kwa wasiwasi na kumwona yule dereva akiwa ameshika bastola akiangalia kule kwenye mlango mkubwa wa kuingilia sebuleni kwa wasiwasi na kuanza kutoka haraka. Tunu hakutaka kuwa mbishi, akainuka na kuokota haraka bastola yake na mkoba wake, akautupia jicho mwili wa Uledi na kuona jinsi kichwa chake kilivyokuwa kimefumuliwa kwa risasi, hakutaka kuzubaa akatoka kuanza kumfuata nyuma yule dereva.



    Walielekea nyuma ya ile nyumba na wakati huo huo ukasikika muungurumo wa gari lililokuwa linaikaribia ile nyumba na kukomea mbele ya geti kubwa la nyumba ile. Hawakusubiri, wakarukia matawi ya mti yaliyokuwa yameinamia mle ndani na kupanda haraka kisha wakajirusha na kuangukia nje ya ukuta wa ile nyumba. Yule dereva akaanza kutimua mbio kuelekea bondeni. Tunu akamfuata. Baada ya mwendo mfupi wakaanza kuambaa na ule Mto Msimbazi kabla hawajaanza tena kupandisha kama wanarudi juu lakini wakiwa mbali na eneo la ile nyumba waliyotoka.



    “Tunu, are you okay?” yule dereva alimuuliza Tunu wakati wakikimbia. Tunu akashtuka sana kusikia yule dereva akimwita kwa jina lake, muda huo walikuwa wanapita katika vichochoro vya nyumba za eneo lile.



    “I’m okay!” Tunu akamjibu yule dereva kwa ufupi huku akiwa katika tahadhari kubwa. Bastola amezishika mkononi tayari kwa lolote.



    “Endelea kunifuata, gari nilikwenda kulificha sehemu huko mbele ili wasinishtukie.” yule dereva alisema huku akiendelea kukimbia.



    Pamoja na kuendelea kumfuata yule dereva lakini Tunu bado alikuwa katika mawazo kumuhusu yule dereva. Alikuwa anajiuliza yule nin nani hasa? Kwa nini amemwokoa toka kwa wale watu wakati inasemekana yeye pia ni mmoja wao? Je, katumwa na nani aje amwokoe? Au yeye pia ni undercover? Tunu alijiambia kuwa alikwisha hisi tangu mwanzo kuwa yule dereva hakuwa wa kawaida kama walivyo madereva wengine, alionekana mwelewa sana wa mambo na mwepesi wa kushika maelekezo.



    Waliendelea kukimbia kwa kasi, yule dereva akiwa mbele na Tunu akiwa nyuma ingawa kwa upande fulani alianza kumwogopa sana. Jasho jingi lilikuwa linamtoka kwa kukimbia. Baada ya dakika kadhaa za kukimbia wakatokea kwenye kichochoro kimoja na kuikuta ile taxi ikiwa imeegeshwa hapo. Yule dereva akageuka kumtazama Tunu kwa macho makali.



    “Pole sana, huo ndiyo uzalendo kwa nchi yako,” yule dereva alisema lakini Tunu hakumjibu. Alimtazama usoni kwa makini.





    “Panda tuondoke, hapa pia si mahala salama. Bado tunakabiliwa na hatari kubwa,” yule dereva alisema huku akifungua mlango na kuingia ndani ya gari. Tunu naye akaingia na gari likaondoka kwa mwendo wa kasi.



    * * * * *

    Saa saba usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ilala, ya Amana, Sammy alikuwa amesimama jirani na mlango wa chumba cha upasuaji uliokuwa umefungwa na hakuruhusiwa mtu asiyehusika kuingia ndani ya chumba kile, aliamua asubirie pale nje huku akijaribu kuchungulia mle ndani kupitia kioo kikubwa cha mlangoni.



    “Ee Mungu, naomba umponye mke wangu, Joyce,” Sammy alikuwa akiomba Mungu kimoyomoyo na aliendelea kuyatamka maneno hayo mara kwa mara.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Elli alikuwa ameketi kando kwenye benchi akiwa amejiinamia kwa huzuni, mambo mengi yalipita kichwani kwake akijaribu kuwaza na kuwazua hili na lile pasipo kupata majibu.



    “Maskini mke wangu, tafadhali usiniache... Tafadhali usiondoke na kuniacha na mtoto!” Sammy aliwaza huku akichungulia ndani ya kile chumba cha upasuaji kupitia kile kioo.



    Hadi muda ule hali ya Joyce iliendelea kuwa tete na Sammy hakuwa ameketi wala kubanduka pale karibu na mlango, alikuwa akifuatilia kwa karibu sana kila hatua akihofia hali ya mkewe.



    Alianza kujiuliza, ni nani waliomshambulia Joyce? Je, shida yao ilikuwa kuiba au kuna kitu walikuwa wakikihitaji? Nini walikuwa wanakihitaji kutoka kwake? Je, kulikuwa na uhusiano wowote kati ya simu aliyopigiwa na Joyce kuwa Pendo amezidiwa na tukio lile la kuvamiwa na kupigwa risasi? Kilichomshangaza ni pale alipofika nyumbani akamkuta Pendo mzima wa afya akiwa hana dalili yoyote ya kuumwa.



    “Hii inaweza kuwa nini maana yake?” Sammy akajiuliza. Akiwa ametulia akitafakari mara akaona mlango wa kile chumba cha upasuaji ukifunguliwa na mhudumu mmoja wa chumba cha upasuaji akatoka. Alikuwa mwanamke mrefu aliyekuwa amevaa mavazi rasmi ya hospitali. Alipotaka kupiga hatua Sammy na Elli wakamkabili ili kujua hali ya Joyce.



    “Bado yuko kwenye upasuaji. Endeleeni kusubiri hadi upasuaji ukimalizika mtajulishwa kila kitu,” yule mhudumu alisema na kuendelea na safari yake.



    Sammy alishusha pumzi na kushika kiuno chake kwa mikono yote miwili, ni wazi alionekana kukata tamaa. Elli alimtazama Sammy kwa huzuni na kumshika kwenye bega.



    “Sammy, hebu kaa utulie, ukiendelea kusimama hapa utachoka sana kwani hatujui upasuaji utachukua muda gani, yawezekana ukachukua muda mrefu,” Elli alimsihi Sammy.



    “Nashindwa kukaa, Elli. Ninapata wakati mgumu sana ni kwa vile hujui tu,” Sammy alijibu huku machozi yakimlengalenga machoni na mara akakumbuka jambo na kuchukua simu yake, akatafuta namba fulani na kupiga, kisha akaweka simu kwenye sikio lake. Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokewa hadi ikakata. Akapiga tena, simu ikaita mara moja tu na kupokewa.



    “Hallo!” sauti ya mwanamume upande wa pili wa simu ikasikika mara baada ya simu kupokewa. Sammy aliitambua sauti ile, ilikuwa sauti ya Rafael Jengo, baba’ake Joyce.



    “Shikamoo, mzee wangu!” Sammy alisalimia kwa unyenyekevu, hata hivyo uso wake haukuficha wasiwasi wake.

    “Marhaba, mwanangu, vipi mbona usiku sana, kwema huko?” sauti ya upande wa pili wa simu ikasikika ikiuliza kwa wasiwasi.



    “Kuna tatizo, mzee wangu... niko hapa hospitali, Joyce amepigwa risasi na watu wasiojulikana...” Sammy alianza kuelezea lakini sauti upande wa pili wa simu ikamkata kauli.



    “Tafadhali usinitanie,” Mzee Jengo alisema kwa sauti ya kutetemeka akionekana kushtushwa sana na taarifa zile.

    “Si utani, baba’angu, ni kitu cha kweli kabisa. Tupo hapa hospitali ya Amana na Joyce yupo katika chumba cha upasuaji,” Sammy alisema huku hofu ikimtambaa mwilini mwake.



    “Mungu wangu!” Mzee Jengo alimaka kwa mshtuko, alihisi moyo wake ukipoteza mapigo yake. Kikatokea kitambo fulani cha ukimya. “Amepigwa risasi saa ngapi na imetokeaje?” hatimaye Mzee Jengo aliuliza baada ya kile kitambo cha ukimya.



    “Mimi sikuwepo nyumbani, ilikuwa around saa nne usiku kuelekea saa tano, watu wawili walivamia nyumbani wakiwa na pikipiki, inasemekana walikuwa wamevaa mavazi yaliyoficha sura zao zisiweze kutambulika...” Sammy alisema na kushusha pumzi, akafuta machozi yaliyokuwa yakimlengalenga machoni.



    Kikapita tena kitambo kingine cha ukimya, kisha Mzee Jengo akashusha pumzi ndefu, “Ahsante sana kwa taarifa hii. Ngoja nimwambie na mama’ake, kesho mchana tutakuwa hapo,” alisema na kukata simu.



    Sammy alibaki akiitazama simu yake kana kwamba alikuwa akiiona kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, mawazo hayakuwa kwenye ile simu. Baada ya kitambo aliirudisha simu yake mfukoni kisha wakaendelea kukaa pale nje kwa muda mrefu. Ilipotimia saa kumi na moja alfajiri ndipo daktari mmoja alitoka na kuwapa taarifa.



    Aliitwa Daktari Mshana, alikuwa mtu mzima, mrefu wa futi sita na ushee, mweupe na mwembamba aliyekuwa na macho ya upole. Aliwatazama Sammy na Elli kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Vipi, daktari, vipi hali ya mgonjwa wetu?” Elli aliuliza kwa wasiwasi.



    “Poleni sana kwa kusubiri. Upasuaji umefanikiwa kwa asilimia mia moja, tumeweza kuondoa risasi mbili mwilini mwake zilizopigwa mgongoni lakini hazikuleta madhara makubwa kwake wala kwa mapacha aliowabeba tumboni. Kwa sasa atapelekwa katika chumba cha uangalizi maalumu huku tukiangalia hali yake kwa ukaribu zaidi,” yule daktari alisema.



    Sammy na Elli wakatazama, ulikuwa mtazamo wa matumaini. Hata hivyo, suala la Joyce kuwa na mimba ya mapacha lilikuwa geni kwa Sammy. Alifumba macho yake na kushusha pumzi.



    “Daktari tunakushukuru sana kwa kazi kubwa mliyoifanya, sijui tunaruhusiwa kumwona?” Sammy alisema huku akiwa bado ameyafumba macho yake. Machozi ya furaha yalionekana machoni pake.







    “Kwa sasa hamtaruhusiwa maana bado yupo kwenye coma na anaandaliwa kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu. Ila kutakapokucha huenda mkaruhusiwa kutegemeana na hali ya mgonjwa itakavyokuwa,” Daktari Mshana alisema.



    Sammy alitaka kusema neon lakini akasita baada ya kuona mlango mkubwa wa chumba cha upasuaji ukifunguliwa. Macho yao yakaelekezwa kule mlangoni ambako kitanda alicholazwa Joyce kilitolewa, kikasukumwa taratibu na wauguzi wa chumba cha upasuaji.



    Juu ya kitanda kile alikuwa amelala Joyce akiwa hana fahamu. Dalili pekee ya uhai katika mwili wake yalikuwa macho yake yaliyokuwa wazi kidogo, yakiwa yamejaa kila dalili ya maumivu na mateso makubwa. Sammy na Elli wakasimama wakimtazama Joyce kwa huzuni.



    Sammy alihisi kisu cha moto kikipenya tumboni mwake na kuanza kumkatakata maini, akili yake ilikuwa imepoteza uhai wake na mwili wake ulikuwa umekufa ganzi. Kisha kwa uwezo ambao hakujua ulikotokea alianza kupiga hatua kuwafuata wauguzi wale hadi katika chumba cha uangalizi maalumu ambako hakuruhusiwa kuingia kwa usiku ule.



    Wakati akitembea kukifuata kile kitanda alikuwa akiita kwa sauti ya upole huku machozi yakimtoka. “Joyce! Mama Pendo!” lakini Joyce hakuonesha dalili zozote za kuitika wala kumsikia.



    “Sammy, hakuna tunachoweza kukifanya kwa sasa, kwa kuwa tumefahamu kuwa hayupo tena kwenye hatari kama mwanzo, twende nyumbani ukapumzike, tutakuja tena kutakapokucha ili kujua maendeleo yake. Kama kutakuwa na mabadiliko yoyote simu zetu zipo wauguzi watatujulisha,” Elli alishauri.



    “Nyumbani kufanya nini! Nitabaki hapa hapa hadi kunakucha nijue...” Sammy alisema lakini Elli akamkatisha.



    “Huwezi kuendelea kukaa hapa, rudi nyumbani ukajue hali ya watoto. Wanahitaji pia faraja yako. Hujui wana hali gani kwa sasa, huenda wameathirika kisaikolojia kutokana na tukio hili na huenda wakatakiwa kupelekwa kwa mwanasaikolojia kwa ajili ya ushauri nasaha,” Elli alisema. Sammy akaonesha kumwelewa na kubetua kichwa chake kukubali.



    “Ni kweli. Hata hivyo, bado najiuliza... nimejiuliza sana sababu ya Joyce kupigwa risasi lakini nimekosa majibu. Ni kwa sababu gani hasa haya yakatokea?” Sammy aliuliza.



    “Nadhani tutapata majibu yote baada ya kuongea na Winifrida au pale Joyce atakapozinduka. Pia jeshi la polisi wakikamilisha uchunguzi wao wanaweza kuwa na jibu zuri zaidi hasa wakiwapata watu waliofanya shambulio hili,” Elli alisema kisha akamshika Sammy mkono na kuanza kuondoka eneo lile.



    * * * * *



    Saa sita usiku katika nyumba moja iliyopo eneo la Kinyerezi, Tunu alikuwa ameketi sebuleni akimwangalia kwa makini Tom ambaye alikuwa anaongea na mtu fulani kwenye simu. Tom kama alivyojulikana kwa wengi ingawa jina lake halisi aliitwa Faustine Thomas Ndejembi, ndiye yule dereva wa taxi aliyoikodi Tunu. Tom alikuwa amejitambulisha kwa Tunu wakati walipokuwa wakielekea katika nyumba ile aliyodai ni mahali salama zaidi kwao.



    Ile ilikuwa nyumba yake aliyoijenga kwa siri na ilikuwa bado haijaanza kukaliwa na mtu, walikuwa amefika kwenye nyumba ile baada ya mizunguko ya hapa na pale ili kuwachanganya watu ambao wangeweza kuwa wanalifuatilia gari lao.



    Nyumba ile ilikuwa kubwa na nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri. Ilikuwa imezungukwa na ukuta mrefu uliofungwa mfumo maalumu ya umeme wa kuzuia wezi juu yake na kulikuwa na vibao vidogo vyenye maandishi mekundu ya tahadhari yaliyoandikwa: ‘Nyumba hii inalindwa na mitambo maalumu ya kuzuia wezi’ huku ikionesha kuwa inalindwa na kampuni ya ulinzi ya Darforce 1.



    Urefu wa ukuta ulioizunguka nyumba ile haukumwezesha mtu yeyote aliyepita nje kuona mle ndani na ulikuwa umekorezwa kwa nakshi za hapa na pale zilizoifanya nyumba kuvutia zaidi. Kwa ujumla ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa iliyokuwa na madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa iliyokuwa mbele yake ikipangwa seti moja ya makochi ya sofa.



    Muda ule Tunu alikuwa bado katika fikara nzito kumuhusu Tom aliyekuwa ameyaokoa maisha yake toka katika mtutu wa bastola ya Uledi, mwanamume aliyeonekana kuwa na kazi moja tu ya kutaka kuutoa uhai wake. Tunu alijikuta akimshukuru Mungu kwa kumleta Tom katika maisha yake.



    Muda huo hakuwa na wasiwasi kwani alishapata majibu ya yale maswali aliyokuwa akijiuliza kabla kumuhusu Tom, kama: yule dereva ni nani? Kwa nini aliamua kumwokoa toka kwa wale watu ingawa ilisemekana kuwa na yeye alikuwa mtu wao? Alikuwa ametumwa na nani amwokoe?



    Tunu alikiri kuwa hajawahi kumwona Tom miongoni mwa mashushushu wa Tanzania ingawa alihisi kuwa alikuwa amemkodi mtu mwenye ujuzi wa ziada katika shughuli za aina ile.



    Tom alikuwa mzaliwa wa Dodoma na alikuwa na umri wa miaka thelathini. Alisoma Shule ya Sekondari Ilboru hadi kidato cha nne na baadaye kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya Sayansi ya Jamii. Alipohitimu akapata udhamini wa kwenda nchni Ubelgiji kwa masomo ya saikolojia kabla hajajiunga na mafunzo ya awali ya ujasusi nchini Ufaransa na baadaye akaelekea nchini China ambako alihitimu vyema.



    Tangu ajiunge na Idara ya Usalama wa Taifa, Tom alionekana kuwa na uwezo mkubwa sana na mbinu nyingi za kiupelelezi, akipenda kufanya kazi zake kama undercover (akijifanya dereva wa taxi na kazi nyingine za kujishusha ili kukamilisha majukumu yake). Kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi, kujichanganya na watu, kutokubagua kazi na heshima kwa kila mtu ilikuwa rahisi sana kwa Tom kupata taarifa nyingi na haikuwa rahisi kushtukiwa.







    Likiwa gari lenye miaka minne katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam, Tom alipata kuchukua abiria wa aina mbalimbali ndani ya gari hilo, akiwatoa hapa na kuwapeleka pale. Wapo wenye tabia za ajabu, wenye maneno ya ajabu, wenye mipango ya ajabu, wapiga dili na matapeli, wazinzi wa wake au waume wa watu n.k. ili mradi kila abiria alitofautiana na mwingine kwa hili na lile. Hata hivyo, wote walikuwa abiria wake.



    Ni katika kazi hiyo amekuwa akipata taarifa nyeti za kiintelijensia kutoka kwa abiria wake, kwani alizifahamu lugha nyingi. Ukiacha lugha za kimataifa za Kiingereza, Kifaransa, Kihispaniola na Kichina, aliweza pia kuongea lugha za makabila mbalimbali ya Tanzania. Ni katika kazi yake ya kuendesha taxi ndipo alipoweza kukutana na akina Lisa, Uledi na Dulla Mcomoro.



    Mwanzoni hakuwa akiwaelewa kabisa, walikuwa ni watu wenye maneno na vitendo visivyoeleweka wala kuelezeka. Japo walikuwa na magari yao, tena ya kifahari, lakini walipenda kukodi taxi kwa mambo yao ili kupoteza lengo la waliokuwa wakiwafuatilia.



    “Tunu!” Tom alimwita Tunu baada ya kumaliza kuongea na simu, maongezi yaliyomchukua zaidi ya dakika ishirini. “Umepata taarifa yoyote kuhusu Sammy?” Tom alimuuliza Tunu huku akimkazia macho.



    “Hapana, Tom, sijapata taarifa zozote. Kwani kuna taarifa gani?” Tunu aliuliza huku uso wake ukionesha mashaka makubwa.



    “Chanzo changu cha taarifa ndani ya jeshi la polisi kinanieleza kuwa watu wawili walimteka wakati akirudi nyumbani kwake baada ya kupigiwa simu na mkewe, wakalipekua gari lake, inaonesha kuna kitu walikuwa wanatafuta lakini hawakukipata...”



    “Hilo nalifahamu,” Tunu alisema kwa sauti tulivu huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Tom.



    “Unalifahamu!” Tom akauliza kwa mshangao.



    “Yeah! Walikuwa watu wangu. Niliwatuma kuitafuta memory card yenye ushahidi muhimu sana kuhusu kifo cha Jaji Lutego,” Tunu alisema.



    “Ushahidi wa mauaji ya Jaji Lutego upo kwenye memory card! Imefikaje kwenye gari la Sammy?” Tom alionesha kuchanganyikiwa. “Tunu, naona unazidi kunishangaza! Naomba nikiri katika kazi zangu sijawahi kukutana na shushushu wa aina yako, haukuwepo nchini kwa kipindi kirefu lakini unaelewa mambo mengi!”



    “Suala la memory card nitakueleza baadaye lakini kwanza naomba unisaidie kupata taarifa zote kuhusu mikakati ya Mr. Oduya,” Tunu alisema huku akiachia tabasamu. “Narudia tena kukushukuru kwa kuniokoa, najua umehatarisha maisha yako ili kuhakikisha ninakuwa salama. Wakati nakukodi sikuwa najua kabisa kuwa nimemchukua mtu hatari lakini ni muhimu sana kwenye mission yangu...”



    “Usijali, nilipokuona unakimbilia taxi nilihisi wewe ni mtu wa kitengo na una mission muhimu sana ya ku-accomplish, ndiyo maana ilibidi nikuwahi kabla mtu mwingine hajakuwahi. Mimi pia siko tayari kuona Mr. Oduya anakuwa rais wa nchi hii,” Tom alisema na kuendelea, “Kwa kuwa sasa nimekupata wewe, sina hofu tena ya kitu chochote. Natumai tutafanikiwa kulizima jaribio hilo…”



    “Siyo tu kulizima, bali pia maisha ya mzee huyo yanaishia gerezani,” Tunu alidakia. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya.

    “Kwa hiyo na hili la Sammy kuvamiwa nyumbani kwake na mkewe kupigwa risasi pia unalijua?” Tom alimuuliza Tunu huku akimkazia macho baada ya kitambo kifupi cha ukimya.



    “Unasema nani kavamiwa nyumbani kwake?” Tunu aliuliza huku akionesha mshtuko mkubwa.



    “Sammy,” Tom alisema, macho yake alikuwa ameyatuliza usoni kwa Tunu.



    “Oh my God!” Tunu alimaka kwa mshtuko huku akihisi kuchanganyikiwa. Alikuwa anapumua kwa nguvu. “Kwa vyovyote waliofanya hivyo watakuwa ni watu wa Mr. Oduya,” Tunu alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    * * * * *



    Saa kumi na moja alfajiri usiku Mr. Oduya alikuwa amesimama jirani na dirisha ndani ya ofisi yake binafsi kwenye jengo lake la kifahari la ghorofa mbili lililopo Mikocheni jirani na Rose Garden. Hadi muda huo hakuwa ameambua japo lepe la usingizi kutokana na taarifa alizokuwa akizipata kutoka kwa watu wake aliowatuma kukamilisha kazi maalumu.



    Alikuwa amefika katika nyumba hiyo baada tu ya kupata taarifa ya kile kilichotokea kule Karakata nyumbani kwa Lisa. Kama kuna siku aliumia sana basi ni siku hiyo, vifo vya watu wake muhimu watatu: Dulla Mcomoro, Uledi na Lisa vilikuwa vimemchanganya kupita maelezo. Hawa watatu pamoja na Spoiler walikuwa watu wake muhimu sana katika oparesheni zake za siri.



    Tangu afike katika nyumba hiyo saa mbili zilizopita alikuwa anavuta sigara mfululizo na hadi muda huo alikuwa tayari amekwisha maliza pakti mbili na nusu za sigara akiwaza na kuwazua pasipo kupata majibu. Alikuwa amekanganyikiwa, mambo hayo hayakuwa yamemwingia kichwani kabisa! Ni vipi Tunu akafanikiwa kutoroka kwenye mikono ya Lisa na Uledi? Watu wenye mafunzo ya mapigano, wenye silaha na wafanisi?



    Aliwatazama Spoiler na Job walioketi mbele yake huku wamejiinamia. Walikuwa na nyuso zilizoonesha wasiwasi mkubwa.



    “Kwa hiyo?” Mr. Oduya akauliza. Alikuwa bado amesimama jirani na dirisha kandokando ya meza yake akiwa ameshika kiuno. Mche wa sigara ukiwa umebanwa kwenye pembe ya mdomo wake na uso wake ukiwa umemezwa na fikra lakini pia sononeko.



    “Kwa hiyo si Sammy wala gari lake vilivyopatikana hadi muda huu! Na Tunu naye amefanikiwa kutoroka,” Mr. Oduya alisema kwa sauti ya chini kama aliyekuwa akiwaza. Akatingisha kichwa. “Sielewi, ninaomba maelezo mafupi sasa hivi kwa nini umeshindwa kukamilisha kazi hii.”



    “Nadhani, bosi, nadhani hatutakuwa na maelezo ya kukuridhisha kwa nini hadi sasa hatukufanikiwa katika msheni, kwa sababu...”



    “Ni wazembe!” Mr. Oduya alimkatiza kwa kufoka, uso wake kaukunja. “Au kuna sababu nyingine?”

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Spoiler alimtupia jicho Job mara moja kisha akajiweka vizuri kitini. Alishaanza kuingiwa na hofu iliyochanganyika na woga. Alikuwa na kila sababu ya kujisikia vile. Mr. Oduya hakuwa tu mfanyabiashara na mwanasiasa wa kawaida, alikuwa mafia na katili kupindukia asiyeruhusu makosa ya kipumbavu yaliyoashiria uzembe yatokee kwenye mipango yake.



    Kwa macho ya kawaida ungeweza kudhani Mr. Oduya ni mfanyabiashara wa kawaida kama walivyo wafanyabiashara na mabilionea wengine lakini huyu ni mtu ambaye kwa sifa zake za umafia angeweza kumfuatilia hata shetani katika harakati zake za kuharibu misheni zake, akamtia adabu... alikuwa na watu wa kuifanya kazi hii wa nyanja zote, kuanzia kwenye taasisi nyeti serikalini hadi watoto wa kihuni, ambao wala wao wenyewe wala hawakujuana. Spoiler alitambua alikuwa anaongea na mtu wa aina gani.



    “Siyo wazembe, boss,” Spoiler alisema kwa sauti ya chini.



    “Kumbe nini?” Mr. Oduya alimuuliza Spoiler huku akimtolea macho.



    “Kama ulivyosikia kuhusu Sammy, wakati sisi tukiwa nyumbani kwake yeye alikuwa na Tunu kule ELLI’S, kama ni kufeli ni Lisa na Uledi ndio waliotufelisha...” Spoiler alisema na kutowesha koo lake lililokauka. “Nitajitahidi ku...”



    “Kufanya nini?” Mr. Oduya akafoka. “Hivi kinachowashinda kumaliza kazi hii tukakaa kwa amani ni kitu gani? Mbona mnaanza kuwa wajinga kiasi hiki?” Mr. Oduya alifoka na kufoka huku mate yakiruka. Alikuwa ameghafirika kweli kweli. Mikakati ya muda mrefu kuutaka urais wa nchi lakini mwisho wa siku anapewa taarifa za upuuzi. Inamaana kazi yake nzima ilikuwa imeharibika!



    “Wangefanya wengine ningeweza kuelewa lakini siyo wewe Silas, hivi ni wewe wa kushindwa kumpata Sammy eti kwa sababu alikuwa na Tunu? Ni wewe wa kushindwa kuliteketeza gari lake?” Mr. Oduya alifoka kwa hasira. “Unajua upo hapa kwa sababu una uwezo mkubwa, kwa sababu ninakulipa fedha nzuri sana ambayo hata mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano hawalipwi! Sasa unapoanza kushindwa kwenye kazi ndogo kama hii unanifanya nianze kukutilia mashaka. Ina maana unazidiwa akili na Tunu? Hii ni mara ya pili sasa Tunu amekutoa knock out!”



    “Hapana, si...”



    “Ni nini basi? Kweli upo hapa kuniambia eti binti shushushu amekushinda?”



    Spoiler alimlaani Mr. Oduya kimoyomoyo, kisha akasema, “Mkuu… mkuu, hai...”



    “Hai kitu gani?”



    “Ni kweli kosa limefanyika lakini sisi si wazembe, kama unavyotutuhumu. Tumefanya kazi ngapi kubwa na za hatari zaidi ya hii?” Spoiler alisema huku akijitahidi kuzuia hasira zake zilizoanza kumpanda. Hakuwa mtu wa kudharauliwa kiasi hicho. Kitu fulani cha moto kilikuwa kinauchemsha mwili na joto kali likaibuka ndani yake. Lakini alijizuia kufanya chochote mbele ya Mr. Oduya.



    Mr. Oduya alishusha pumzi, akaketi juu ya kiti na kuegemea. Ni kweli kabisa Spoiler ni mtu shupavu, anayefanya kazi kwa kujituma bila ya kuhitaji kusimamiwa au kuhimizwa. Mr. Oduya mwenyewe humtegemea yeye katika kazi zake zote hatari.

    “Okay!” Mr. Oduya alisema, safari hii sauti yake ilikuwa yenye utulivu, na mikunjo ya hasira usoni mwake ilipungua.



    Alianza kuwaza, sasa mambo yalizidi kuwa magumu. Hakuwa amelichukulia suala la Sammy kwa uzito mkubwa kwa kujua alikuwa anadili na Sammy peke yake, mtu wa kawaida ambaye angeweza kummudu pasipo kuhitaji kutumia nguvu na rasilimali zake nyingi. Lakini sasa kulikuwa na huyu Tunu, hata hakujua alitokea wapi na kuja kutibua mipango yake! Huyu Tunu hakuwa mwanamke wa kawaida.



    Mr. Oduya aliona anatakiwa kutafuta njia mbadala za kuwapata wote, Tunu na Sammy. Kwa Sammy isingeweza kazi ngumu kumpata na kumyamazisha pamoja na makosa yaliyofanyika, lakini huyo Tunu angempataje? Alihisi kama kichwa chake kinapasuka. Njia mbadala ya kumpata binti huyo ingekuwa ni kwa kupitia Nelson Mtokambali, aliyekuwa boyfriend wake, lakini walishatibuana. Ni Nelson ndiye aliyewashtua kuwa Tunu ni shushushu aliyebobea ambaye alikuwa pale kuchunguza nyendo za Mr. Oduya.



    Aliamini kuwa Tunu alikuwa anajua kila mbinu za kiintelijensia. Alikuwa anajua michezo yote ya silaha na amefundishwa namna gani ya kutumia akili yake mara tatu zaidi ya shushushu wa kawaida. Ni mtaalamu wa mapigano ya silaha na pia pasipo silaha. Kwake yeye, Tunu ni adui mkubwa kuliko gaidi yeyote toka kwenye makundi hatari ya kigaidi, kwani alimfahamu vizuri yeye (Mr. Oduya) na kampani yake karibu yote.



    Tunu aliifahamu mifumo, mipango na harakati zake kama kiganja cha mkono wake wa kuume. Hivyo Mr. Oduya alijionya kuwa makini sana anapotaka kudili na binti huyo.



    “Nataka kusikia habari za kifo cha Tunu, sijui mmenielewa!” Mr. Oduya alipaza sauti kana kwamba alikuwa anaongea na watu waliokuwa mita hamsini mbali na yeye. Aliposema hayo alitulia tena akafikiria kidogo, mdomo wake ulikuwa mkavu kwa sababu ya moshi wa sigara.



    “Atakayefanikiwa kumuua Tunu, ama kuniletea hapa mwili wake nitamlipa shilingi bilioni hamsini papo hapo! Cash!” Mr. Oduya alisema kwa msisitizo, na kuendelea, “Kama mnadhani ni kazi ngumu semeni niwatume watu wengine kuifanya, maana nina watu wengi wa kuifanya kazi hii.”



    Spoiler na Job wakatazamana kama vile wakiulizana nani hawezi kufanya kazi ile. Kisha wote wawili wakashusha pumzi kwa pamoja.



    * * * * *



    Saa tatu na nusu asubuhi Sammy alikuwa ameketi nje ya chumba cha uangalizi maalumu katika hospitali ya Amana, alikuwa amefika hapo mara tu alipoweka mambo sawa nyumbani kwake. Kwa kushirikiana na Elli, Sammy aliwahamisha Winifrida na Pendo na kuwapeleka Kurasini, nyumbani kwa Elli.



    Alichokikuta pale hospitali baada ya kufika kilimmaliza nguvu. Joyce alikuwa amewekewa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua baada ya hali yake kubadilika ghafla. Muda ule madaktari na wauguzi walikuwa wanahangaika kuokoa maisha yake, Sammy hakuruhusiwa kuingia wodini.





    Akiwa ameketi pale nje ya chumba alimolazwa Joyce mara simu ya Joyce ikaanza kuita, simu hiyo alikuwa nayo Sammy akiwa ameichukua asubuhi ile. Aliitoa toka mfukoni na kuitazama kwa makini, akaliona jina la mpigaji na kushusha pumzi. Ilikuwa ni simu kutoka kwa Madame Norah.



    “Hallo!” Sammy alisema mara tu alipoipokea na kuiweka sikioni huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Hallo!” Madame Norah alisema kwa sauti iliyoonesha shaka kidogo baada ya kuisikia sauti ya kiume ikizungumza badala ya sauti ya Joyce, “Madame Norah hapa, sijui nazungumza na nani?” akauliza kwa mshangao.



    “Sammy, mume wa Joyce,” Sammy alijibu kwa sauti tulivu huku akilamba midomo yake.



    “Ooh, Sammy! Hujambo baba?”



    “Sijambo, mama, shikamoo!”



    “Marhaba! Samahani kwa usumbufu nahitaji kuongea na Joyce sijui yupo karibu?” Madame Norah alisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.



    “Bila samahani, mama, nipo hapa hospitali ya Amana, Joyce alipigwa risasi usiku wa kuamkia leo,” Sammy alisema huku akijitahidi kuzuia machozi yaliyokuwa yakimlengalenga machoni.



    “Oh my God!” Madame Norah alimaka kwa mshtuko, kisha kikatokea kitambo fulani cha ukimya. Alihisi dunia yote ikizunguka kwa kasi ya ajabu na kumtia kizunguzungu. “Nani kampiga risasi?” Madame Norah alimudu kuuliza baada ya kitambo fulani cha ukimya.



    “Bado haijafahamika nani waliompiga risasi na kwa sababu gani?” Sammy alisema, Madame Norah akavuta pumzi ndefu.



    “Vipi hali yake?”



    “Hali yake si nzuri, anapumua kwa msaada wa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua.”



    Madame Norah alitaka kusema lakini maneno hayakutoka, alihisi donge fulani likimkaba kooni, akashusha pumzi na kubaki kimya. Alihisi kupata pigo kubwa sana kwa kuwa alimtegemea sana Joyce kwenye mradi wake mpya. Alishindwa kuvumilia, akaanza kulia. Alikuwa analia kilio cha kwikwi kilichosikiwa vyema na Sammy. Sammy alipigwa na butwaa, hakujua afanye nini.



    Wakati huo huo gari dogo la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i jeusi lilikuwa linapita kwenye geti la kuingilia la hospitali ya Amana na kwenda hadi katika viunga vya maegesho vya hospitali hiyo, likaegeshwa hapo jirani na gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille. Gari hili liliendeshwa na Tunu.



    Alibaki kwenye gari kwa dakika chache huku gari likiunguruma kisha akazima inji na kufungua mlango, akashuka huku akilitazama kwa makini gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille kisha akatazama pande zote kuhakiki usalama.



    Alipohakikisha kuwa kulikuwa na usalama wa kutosha akaanza kupiga hatua taratibu kuelekea katika jengo la mapokezi. Kabla hajafika mapokezi aligeuza shingo yake kutazama kule kwenye maegesho na kuridhika kuwa hali ilikuwa shwari. Akashusha pumzi. Tunu alikuwa amevaa suti ya kike ya bluu ya kitambaa ghali na shingoni alivaa mkufu wa dhahabu wenye kidani chenye herufi “G”.



    Pale mapokezi aliwakuta wahudumu kadhaa akawauliza mahala kilipo chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu, akaelekezwa na bila kupoteza muda akaelekea huko. Alipokuwa mbali alimuona Sammy akiwa ametulia, simu ikiwa kwenye shavu.



    “Sammy!” Tunu alishindwa kujizuia akaita hata kabla hajamfikia.



    Sammy alishtuka na kumtazama Tunu kwa makini, akamtambua na kuinuka huku akimkodolea macho kwa mshangao.

    “Gift!” Sammy alisema kwa sauti ya chini iliyojaa simanzi.



    “Pole sana kwa yote yaliyotokea, I feel sorry for you,” Tunu alisema kwa huzuni huku akimkumbatia Sammy katika namna ya kumfariji. Wakakumbatiana kwa kitambo huku Sammy akilengwa na machozi, kisha akambusu Tunu kama shukrani ya kwenda hospitali kumfariji.



    Baada ya maongezi mafupi ya kujuliana hali Sammy alimsimulia Tunu yote yaliyomtokea siku iliyotangulia, tangu walipoachana pale katika mgahawa wa Elli’s, njiani akatekwa na watu waliokuwa wanatafuta memory card hadi alipofika nyumbani na kukuta askari wametanda nyumbani kwake baada ya kupewa taarifa za uwepo wa watu hao nyumba yake. Alimweleza Tunu pasipo kubakisha kitu hadi jinsi alivyopishana na watu waliompiga risasi mkewe na kukosa kuwagonga kwa gari, na baadaye kumkuta mkewe kalalia dimbwi la damu baada yakupigwa risasi.



    Tunu alimsikiliza Sammy kwa makini, alihisi donge la huzuni likimkaba kooni kwake. Machozi yalimlenga machoni na alijikuta akitamani sana kumweleza ukweli Sammy kuhusu akina Bob waliomteka kuwa ni yeye aliyewatuma, lakini si kwa nia mbaya.



    “Pole sana!” hatimaye Tunu alimudu kutamka, na kuendelea, “Wakati mkeo anapigwa risasi hakukuwa na watu wengine nyumbani?” Aliuliza huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy akijaribu kuyasoma mawazo yake.



    “Mbali na mke wangu, pia walikuwepo mtoto wangu wa miaka mitano, Pendo na mdogo wangu Winifrida anayesoma kidato cha nne,” Sammy alisema.



    “Vipi kuhusu wao, hawakudhuriwa?” Tunu aliuliza kwa wasiwasi huku akimkazia macho Sammy.



    “Hawakudhuruiwa ingawa Pendo walimfunga plasta mdomoni ili asipige kelele. Winifrida hawakumwona kwani aliwahi kujificha juu ya kabati la ukutani kabla hawajaingia chumbani na aliweza kusikia baadhi ya maneno ya vitisho waliyokuwa wakiyatoa...”



    “Alibahatika kuwaona sura zao?”



    “Tumejaribu kumuuliza lakini haelezi vizuri, ni kama vile kuna mambo anaogopa kuyasema au pengine hana uhakika!” Sammy alisema kisha akamsimulia



    “Kwani ni nani aliyewajulisha polisi kuhusu uwepo wa watu hao nyumbani kwako?” Tunu alizidi kumsaili Sammy akionesha shauku ya kutaka kujua.



    “Hapo ndipo penye kizungumkuti, hajulikani nani aliwapigia simu, tumemuuliza Winifrida lakini amekana kupiga simu, ingawa polisi wanadai kuwa mpigaji alikuwa mwanamke na aliwaambia kuwa alikuwa amejificha ndani ya nyumba hiyo iliyovamiwa!”



    “Kwani Winifrida ana simu?”



    “Hana,” Sammy alijibu pasipo kufikiri.



    “Una uhakika?” Tunu aliuliza kwa sauti iliyoonesha shaka fulani, bado alikuwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Sammy katika namna ya kuyasoma mawazo yake.



    Sammy alifikiria kidogo na kushusha pumzi, akatingisha kichwa chake taratibu kushoto na kulia kukataa. “Hata sijui!”



    “Kwa hiyo polisi wanasemaje, wamekwisha wabaini waliofanya tukio hilo?” Tunu aliuliza baada ya kufikiria kwa kitambo kidogo.



    “Bado wanaendelea na upelelezi, ila nilipozungumza nao leo asubuhi walisema kuwa wamebaini vitu vichache, hususani alama za viatu walivyokuwa wamevaa watu hao na maganda ya risasi.”







    “Nadhani huo ni mwanzo mzuri...” Tunu alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. “Hata hivyo, itakuwa vizuri ukifahamu kuwa mlengwa wa tukio hilo ulikuwa ni wewe na wala siyo mkeo.”



    Sammy alionesha kushtuka kidogo, alimtazama Tunu kwa kitambo kirefu bila kusema neno na kushusha pumzi. Kisha alimudu kuuliza, “Kwa nini unasema hivyo?”



    “Fikiria mwenyewe, umepigiwa simu kuwa mwanao amezidiwa jambo ambalo ni uongo, ukiwa njiani unatekwa na watu wanaotafuta memory card ambayo kwa vyovyote itakuwa na siri fulani, unapofika nyumbani unakuta mkeo kapigwa risasi na mambo mengine mengi yanayokifanya kisa hiki kuwa katika mlolongo mrefu! Hudhani pengine simu uliyopigiwa ilikuwa ndiyo simu ya kifo chako mwenyewe?” Tunu aliuliza na kushusha pumzi. “Kuwa makini Sammy, usimwamini mtu yeyote kirahisirahisi, hata kama ni mimi!”



    Sammy alimtazama Tunu kwa mshangao kama aliyeona kiumbe cha kushangaza toka sayari za mbali, akajikuta akifikiria kidogo na kushusha pumzi. Alihisi kuwepo kwa ukweli kwenye maneno ya Tunu, maana alivyokuja kuambiwa bi kwamba hata simu aliyokuwa amepigiwa na Joyce usiku kuhusu ugonjwa wa Pendo ilikuwa ni maelekezo toka kwa watu waliovamia nyumbani kwake.



    “Kwa mlolongo huo naweza kukubaliana na wewe, hata hivyo, sioni kama nina maadui kiasi cha kutaka kuniua, kwani nimewakosea nini!” Sammy alisema baada ya kitambo kifupi cha ukimya.



    “Huwezi kujua, unaweza kudhani huna adui kumbe wapo, tena maadui wenye nguvu kubwa kiuchumi na hata kisiasa! Na huenda katika shughuli zako ukawa umeingilia maslahi ya watu fulani wakubwa...” Tunu alisema huku akimkazia macho Sammy kuona kama maneno yale yalikuwa yanamwingia. “Na inaonekana kabisa watu hao wanahisi kuwa una kitu au taarifa fulani nyeti zinazowahusu.”



    Sammy alihisi jasho jepesi likimtoka mwilini na ubaridi wa woga ukimwingia na kupenya hadi kwenye mifupa yake. Maneno ya Tunu yalimpeleka mbali, yalimrudisha kwenye mzozo wake na Spoiler baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa amesikia siri za Mr. Oduya.



    “Ni Mr. Oduya!” Sammy aliwaza. “Huyu mzee si wa kumfanyia mchezo hata kidogo. Mambo machache niliyoyasikia kutoka kwake yananipa picha tosha kuwa huyu mzee ni mafia na ndiye amehusika kwenye tukio hili. Hata hivyo, kupambana naye inataka ujasiri mkubwa.”



    Alipowaza mara picha ya Spoiler akimfuata pale nje ya ukuta wa Udzungwa Beach Resort siku ile alipopewa barua ya kusimamishwa kazi ikamjia Sammy kichwani. Akakumbuka kila neno la kitisho aliloambiwa na Spoiler, hasa kuhusu familia yake: “very soon nitapafahamu nyumbani kwako, nitamfahamu mkeo na hata shule wanayosoma watoto wako, kama unao… hivyo usinilazimishe kufanya kitu utakachokuja kukijutia baadaye...”



    Sammy akajikuta akisisimkwa mwili wake huku damu ikianza kumchemka na kukimbia kwenye mishipa yake ya damu, aliikumbuka vyema kauli hiyo na roho ilimuuma sana kwa kutochukua tahadhari, aliuma meno yake kwa hasira. Alikuwa anahofia. Moyo wake ulikuwa unakita kwa nguvu na kwa kasi. Haya mambo hayakuwa katika nyanja yake kabisa!



    “Kwa kitendo hiki walichomfanyia mke wangu ni lazima walipe na ikibidi wafikishwe katika vyombo vya sheria kujibu mashtaka dhidi yao,” Sammy aliapa kimoyomoyo. Ni wazi ujio wa Tunu ulikuwa umemfumbua macho.



    “Jaribio lao la kwanza lilikuwa kuniteka mimi ili wapate memory card ambayo hata sijui inahusu nini, limegonga mwamba. Jaribio la pili la kumtumia mke wangu anipigie simu pia limegonga mwamba, lakini wamefanikiwa kumpiga risasi na sasa anapumulia mashine... nina hakika hawataishia hapo, lazima watatafuta namna nyingine ya...” Sammy aliyekuwa ametopea kwenye lindi la mawazo alikatishwa na sauti ya Tunu.



    “Sammy!” Tunu aliita. “Najua una maswali mengi unayotaka kuyafahamu kuhusu hao waliompiga risasi mkeo. Nitakusaidia kupata majibu yote lakini nakuomba usiniulize chochote kuhusu namna nitakavyofanya. Kitu cha msingi ni kufahamu tu kwamba nipo hapa kukusaidia,” Tunu alisema na kushusha pumzi.



    “Gift, ni kweli nina mengi sana ninataka kuyafahamu. Mengi sana yanayohusu huu mlolongo wa visa na mikasa hadi mke wangu kupigwa risasi. Lakini pia ninataka kufahamu mengi yanayokuhusu wewe, kuanzia usiku wa siku ile tuliokuwa pamoja kisha ukatoweka kama moshi na kuniachia maumivu yaliyochukua miaka mingi kupoa, hadi jana ulipotokea tena.”



    “Usijali, Sammy, tuna mengi ya kuzungumza ila kwa sasa tuangalie kwanza afya ya mkeo, pia mazingira haya si rafiki sana kuzungumza mambo hayo,” Tunu alisema na kulamba midomo yake na ukimya mfupi ukapita.



    “Kikubwa kwa sasa ni kumwombea mgonjwa apone, mambo mengine ya nani walimpiga risasi yatajulikana. Ni yeye ndiye mwenye majibu ya waliompiga risasi walikuwaje na yawezekana labda alizifahamu sura zao ndiyo maana wakafanya hivyo ili kupoteza ushahidi,” Tunu alisema baada ya kitambo kile cha ukimya.



    “Halafu ninahitaji kuzungumza na Winifrida, sijui nitampataje?” Tunu aliuliza na kumfanya Sammy amwangalie kwa udadisi zaidi.



    “Gift, naomba uniambie ukweli wewe ni nani hasa! Are you a cop?” Sammy aliuliza huku akimkazia macho Tunu.



    “Kwa nini umeuliza hivyo?”



    “Nataka tu kufahamu, maana hata maswali yako yote uliyoniuliza ni ya kipolisi. Ni ya mtu mwenye taaluma ya intelijensia anayetafuta taarifa za kiuchunguzi ili azifanyie kazi.”



    Tunu aliachia tabasamu lililozaa kicheko hafifu huku akiyaondosha macho yake toka usoni kwa Sammy, akakaa kimya kwanza kwa sekunde kadhaa kisha akamtazama tena Sammy huku akishusha pumzi. Alionesha kuwa na jambo zito sana ndani yake ambalo asingependa kuliweka wazi.



    “Hamna shida kama haujisikii kuniambia,” Sammy alisema huku akitabasamu. “I can understand. Ila siku utakayojisikia kuniambia ukweli you know how to get me.”







    “Wala siyo hivyo, ukweli ni kwamba mimi siyo polisi. I'm just concerned as a close friend... Nataka nionane na mdogo wako kwa kuamini kama kweli ana jambo analijua basi ataniambia, I know how to deal with...” Tunu alisema na kuachia tabasamu pana.



    “Sina sababu ya kutokukuamini, hata hivyo, nimefurahi sana kukuona tena after so many years. Nimefurahi japo imekuwa ni kipindi kigumu na cha mshtuko mkubwa. Sikutegemea kabisa kama...” Sammy alisema kwa huzuni lakini akasita baada ya watu watatu kufika.



    Walikuwa wanawake wawili na mwanamume mmoja, jirani zao kule Tabata Chang’ombe, waliopita kumjulia hali Joyce.



    * * * * *



    Saa nne kamili asubuhi, katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, magurudumu ya ndege aina ya Bombardier DASH8 Q400 ya shirika la ndege la Tanzania yaligusa ardhi kwenye kiwanja hicho huku tayari abiria wakiwa wamejiandaa kwa tukio lile la kutua kwa ndege. Ndege hiyo ilikuwa inatokea jijini Tanga.



    Muda mfupi baada ya ndege ile kusimama, milango ya ndege ilifunguliwa na hapo abiria wakaanza kushuka. Kati ya abiria hao walikuwepo abiria wawili mume na mke waliokuwa na sura zilizosawajika zikiwa na huzuni isiyoelezeka. Hawa walikuwa ni Rafael Jengo na Bi. Pamela Jengo, wazazi wa Joyce.



    Rafael Jengo alikuwa mrefu mwenye sura ya ucheshi na umbo kubwa lililopendeza. Alikuwa amevaa suti nadhifu ya rangi ya kijivu na shati jeusi lililomkaa vyema na kumpendeza. Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi vya ngozi na mkono wake wa kushoto alivaa saa nzuri ya mkononi. Umri wa Rafael Jengo wa miaka hamsini na nne bado ulikuwa haujatosha kabisa kuzipokonya nguvu zake mwilini.



    Bi. Pamela alikuwa mnene wa wastani, hakuwa mfupi wala mrefu bali alikuwa na kimo cha wastani na alikuwa mweupe. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na nane. Wakati wanashuka toka kwenye ndege Rafael Jengo alikuwa akimtazama mkewe Bi. Pamela akiwa na uso uliosawajika kidogo pasipo kusema neno lolote huku akionekana kuipa utulivu akili yake.



    Mara waliposhuka kwenye ile ndege wakaingia kwenye jengo namba mbili la kiwanja kile cha ndege cha kimataifa lenye migahawa ya kisasa na ofisi mbalimbali za utawala. Kwa kuwa hawakuwa na mizigo yoyote mikubwa waliwatangulia abiria wengine wenye mizigo wakapenya haraka na kutoka nje ya jengo la kiwanja kile cha ndege cha kimataifa.



    Dereva mmoja wa teksi mjanja akawawahi haraka kabla ya wenzake baada ya kuhisi hitaji lao. Dereva yule alikuwa mzee wa makamo, mrefu na mwembamba mwenye sura ya ucheshi akiwa amevaa kofia nyeusi ya kapelo, shati jeupe, suruali ya nyeusi na makubasi ya ngozi miguuni, aliwahi kuwapokea mizigo waliyokuja nayo na kuwafungulia mlango wa taxi yake hata kabla hawajaafikiana naye au kumweleza hitaji lao. Kwa ushawishi ule hawakuwa na pingamizi, hivyo wakaingia ndani ya gari.



    Mara tu walipoingia ndani ya ile taxi yule dereva akawatazama kwa makini huku akiachia tabasamu la kirafiki. “Sijui niwapeleke wapi, ndugu zangu?” yule dereva taxi aliwauliza huku tabasamu la kindugu likiendelea kutawala usoni kwake.



    “Tupeleke Amana,” Rafael Jengo alisema, na muda huo huo ile taxi ikaondoka na kuanza kuyaacha maegesho ya magari ya kile kiwanja cha ndege, kisha ikaingia katika barabara ya Nyerere na safari ya kuelekea Amana ikaanza.



    * * * * *



    Kwenye viunga vya maegesho vya hospitali ya Amana, Tunu alikuwa ameketi kwa utulivu ndani ya gari dogo la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i jeusi alilokuja nalo. Gari lile lilikuwa haliungurumi. Alikuwa nyuma ya usukani wake akionekana kutafakari sana juu ya kazi iliyokuwa mbele yake. Alikuwa analitazama kwa makini gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille.



    Alikuwa na mambo kadhaa ya kuyashughulikia na hakujua angeanza na lipi, hata hivyo alikuwa amepata mahali pazuri pa kuanzia baada ya mazungumzo yake na Sammy, mwanamume aliyemwondolea utoto wake na kumwingiza katika dunia ya watu wazima.



    Hakutegemea kabisa kukutana na Sammy katika mazingira yale ya utata. Alijihisi alikuwa na jukumu la kumsaidia Sammy kama njia ya kudumisha uhusiano wao uliopotea kwa takriban miaka kumi na moja. Siyo Sammy aliyekuwa ameathirika na kupotezana kwao, hata yeye pia alikuwa katika wakati mgumu, alishindwa kabisa kumtoa Sammy moyoni mwake.



    Aliikumbuka vyema siku aliyokwenda nyumbani kwa Sammy, yale waliyoyafanya na ahadi walizopeana baada ya hapo, na wakati akiondoka hakujua kama wasingeonana tena kwani aliporudi nyumbani kwa shangazi yake huko Sinza alikuta taarifa za kifo cha baba yake aliyekuwa mwanasiasa maarufu mjini Tabora. Alitakiwa kusafiri kwenda Tabora asubuhi ya siku iliyofuata na hakuweza tena kuwasiliana na Sammy kwani hakuwa amechukua namba yake ya simu.



    Tunu alikuwa amezaliwa mkoani Tabora akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne, yeye akiwa mtoto pekee wa kike. Baada ya mazishi hakurudi jijini Dar es Salaam, alibaki Tabora kumsaidia mama yake hadi matokeo ya mtihani wake wa kidato cha sita yalipotoka ambapo Tunu alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kitaifa, na hivyo kupata udhamini wa kusomeshwa bure chuo kikuu.



    Siku alipofika jijini Dar es Salaam alimtafuta Sammy bila mafanikio, nyumba aliyokuwa akiishi alikuwa amehama na hakuna aliyejua alihamia wapi. Baada ya kuhangaika kumtafuta kila alikodhani angemwona hatimaye Tunu alikata tamaa ya kumpata, kwani pia alikuwa na muda mfupi sana wa kujiandaa kabla ya safari.



    Muda ulipofika aliondoka kwenda masomoni nchini Marekani katika Taasisi ya Teknolojia ya Georgia (Georgia Tech). Huko Marekani Tunu alisoma kwa miaka minne akibobea na kuhitimu Shahada ya Kwanza katika Computer System Analysis.



    Aliporudi nchini alichaguliwa kujiunga na programu maalumu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya vijana wasomi walioandaliwa kwenda kuchukua mafunzo ya awali ya ujasusi. Baada ya kumaliza mafunzo ya kijeshi Tunu alilitumikia jeshi kwa muda mfupi na kituo chake kilikuwa Lugalo jijini Dar es Salaam.





    Akiwa Lugalo alipata pia mafunzo maalumu ya kijeshi (Special Forces and Tactical Weapons Training) na baadaye kupelekwa nchini Israel katika taasisi ya IDC Herzliya (ICT International Institute for Counter-Terrorism) ambako alihitimu shahada ya umahiri ya ujasusi ikihusisha pia masuala ya usalama wa ndani na mapambano dhidi ya ugaidi na teknonojia ya habari na mawasiliano.



    Akiwa huko huko Israel alipata pia mafunzo ya kujihami katika michezo ya karate and judo na kufanikiwa kupata mkanda mweusi. Aliporejea nchini alianza kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa na muda mfupi tu tangu alipojiunga idarani hapo alionesha uwezo mkubwa sana kiasi cha kuaminiwa na kupewa nafasi mbalimbali za kufanya kazi ndani na nje ya nchi.



    Pamoja na kusafiri sehemu mbalimbali duniani, akikutana na watu mbalimbali na wakati fulani aliangukia kwenye uhusiano na mmoja wa mabosi wa mamlaka ya mawasiliano nchini, Nelson Mtokambali, bado hakuweza kumtoa Sammy moyoni mwake. Na sasa alikuwa amekutana naye katika mazingira yale, ingawa hakujua kama bado alimhitaji, lakini aliapa kumsaidia ili wote waliofanya kitendo kile walipe gharama za uhalifu wao.



    Alizinduka toka katika mawazo yale, akatazama kushoto kwake kulikokuwa na gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille. Akashusha pumzi na kuwasha injini ya gari lake kisha akaliondoa taratibu na kutoka kwenye geti la kuingilia na kutokea la hospitali ya Amana, halafu akakata kushoto akiifuata barabara ya lami iliyokwenda kuungana na barabara ya Uhuru.



    Tunu alilipita gari moja jeusi aina ya Toyota Alphard jeusi lililokuwa na vioo vyenye tinted nyeusi iliyomzuia mtu kuona waliokuwemo ndani, likiwa limeegeshwa kando ya barabara ile ya lami, jirani na mgahawa mmoja uliopakana na ukuta wa hospitali ile ya Amana. Gari lile lilikuwa linanguruma taratibu. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wawili, wanaume wa kazi. Spoiler na Job.



    Spoiler na Job walikuwa makini wakifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea eneo lile, ni kama vile walikuwa wanangoja kitu. Masikioni mwao walikuwa wamevaa vifaa maalumu vya usikivu na mawasiliano. Waliliona lile gari BMW X6 xDrive 50i jeusi wakati liliwapita, wakamtambua Tunu aliyekuwa akiendesha lile gari. Walimwona akikunja kuingia upande wa kushoto na kuifuata barabara ya Uhuru.



    “Leo ndiyo leo,” Spoiler alisema akiwa anatafuna Big G. “Endapo tukimpata Tunu, kazi yetu itakuwa imekwisha...” Spoiler alisema na kumpa ishara Job ambaye aliliondoa gari kuelekea kule lilikoelekea gari la Tunu.



    Tunu alikuwa ameshazipita kona kadhaa za mitaa ya Ilala ili kukwepa foleni katika barabara ya Uhuru wakati alipoukumbuka wajibu wake. Alikizungusha kichwa chake taratibu kutazama nyuma na hapo mwili wake ukajikuta ukiingiwa na ubaridi wa ghafla.



    Moyo wake ukaanza kupiga kite kwa nguvu huku mwenendo wa mapigo yake ukianza kwenda katika utaratibu usiozoeleka, koo lake nalo likakaukiwa na mate. Gari aina ya Toyota Alphard jeusi lililokuwa na vioo vyenye tinted nyeusi iliyomzuia kuona waliokuwemo ndani lilikuwa limemfungia mkia kwa nyuma.



    Tunu alikuwa na uhakika kuwa wale watu walikuwa wakimfuata yeye, kwani alikuwa ameliona lile gari nje ya hospitali ya Amana likiwa limeegeshwa kando ya barabara ya kutokea hospitali.



    Lile gari Toyota Alphard jeusi lilikuwa nyuma yake kiasi cha umbali wa mita hamsini hivi likiwa limeacha gari moja katikati yao, na alihisi kuwa namba zake zilikuwa za bandia. Hata hivyo, kwa uzoefu wake aliweza kugundua kuwa dereva wa gari hilo hakuwa mzoefu mzuri katika kufuatilia windo.



    Tunu alilitazama lile gari kwa makini huku akijiuliza kuwa watu wale ni akina nani na kwa nini wamfuatilie. Je, ni watu wa Mr. Oduya? Akaanza kushikwa na wasiwasi, hata hivyo aliamua kuachana nao na kuyakaza macho yake kutazama mbele huku akijitahidi kulisahau gari lile kwa muda, aliipa utulivu akili yake ianze kufanya kazi.



    Tayari muda wa dakika takribani kumi na tano ulikwisha yeyuka tangu Tunu alipotokhttp://pseudepigraphas.blogspot.com/a pale hospitali ya Amana, aligundua hivyo baada ya kuitazama saa yake ya mkononi iliyoonesha vizuri kupitia mishale yake ya dhahabu ilivyokuwa ikimetameta.



    Baada ya sekunde chache alifikia uamuzi wa kuwapoteza kwa kuwa hakutaka watu wale wafahamu ni wapi alipokuwa akielekea. Akapanga kubadilisha mwelekeo. Aliutazama mshale wa mafuta ukamwonesha kuwa alikuwa na mafuta ya kutosha kuweza kuzunguka jiji la Dar es Salaam mpaka jioni bila kusimama. Akatabasamu na kuongeza mwendo.



    * * * * *



    Katika hospitali ya Amana, Sammy alikuwa ametulia nje ya chumba alimolazwa Joyce, alikuwa akitafakari kuhusu mazungumzo yake na Tunu huku akijaribu kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Alitamani sana kufahamu kilichotokea kwa Tunu, alikuwa wapi siku zote? Anafanya kazi gani?



    Alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufahamu mengi kuhusu Tunu, ni wapi alikuwa katika kipindi hiki chote cha miaka kumi na moja tangu walipoachana! Pamoja na kupotezana miaka yote hiyo lakini bado Tunu aliendelea kuonekana mrembo sana. Alikuwa bado ni Gift yule yule mwenye mvuto wa ajabu.



    Wakati akizidi kuwaza mara akawaona watu wawili wakija na walipofika karibu akawatambua mara moja, walikuwa wazazi wake Joyce, Bwana na Bibi Jengo. Akasimama na kuwalaki.







    Bi. Pamela alipomwona Sammy alishindwa kujizuia, alifungua mdomo wake kutaka kusema lakini maneno hayakutoka, akabaki mdomo wazi akimkodolea macho Sammy huku donge la fadhaa likimkaba kooni. Akaangua kilio kwa uchungu.



    “Mama Davie, usilie tafadhali. Joyce anatuhitaji sana hivyo tunatakiwa tuwe na ujasiri,” Jengo alisema huku akimkumbatia mkewe na kumpigapiga mgongoni.



    “Baba Davie, hujui tu ninapitia kipindi gani kwa sasa, mwenyewe unajua tangu nilipopata taarifa hizi nimeshindwa hata kula...” Bi. Pamela alisema na kuchukua kitambaa laini, akafuta machozi.



    “Mama, Joyce ni jasiri, naamini atashinda vita hii ya kupigania maisha yake, cha msingi tu tumuombee,” Sammy alisema huku akiwatazama wakwe zake kwa makini.



    “Najua mwanangu, lakini nina uchungu, kwa nini wamfanyie hivi kwani kawakosea nini jamani!” Bi. Pamela alisema kwa huzuni. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, Sammy akawataka waketi kwenye benchi lililokuwepo pale.



    “Nataka kufahamu tukio hili limetokeaje?” Rafael Jengo alimuuliza Sammy baada ya kuketi.



    “Ni kama nilivyokueleza kwenye simu, mimi sikuwepo nyumbani ila kwa maelezo ya mdogo wangu Winifrida, watu wawili walifika na kuwaweka chini ya ulinzi, shida yao kubwa ilikuwa ni mimi. Hadi sasa sijajua nani aliwapa polisi taarifa, ila wale watu walipogundua askari wameizingira nyumba ndipo wakampiga risasi Joyce na kutoroka,” Sammy alisema kwa huzuni.



    “Muda huu nilijaribu kupiga tena simu polisi kujua kama kuna hatua yoyote waliyopiga au kuna mtu yeyote aliyekamatwa lakini mpaka sasa hawajafanikiwa na uchunguzi bado unaendelea,” Sammy alisema.



    “Lakini, vipi hali ya Joyce?” Rafael Jengo aliuliza kwa wasiwasi.



    “Tuendelee tu kumwombea aweze kupata nafuu maana hadi sasa hajazinduka, usiku walimfanyia oparesheni na kufanikiwa kutoa risasi mbili...” Sammy alisema na kusita kidogo. “Daktari ameniambia ukweli kwamba hali aliyo nayo sasa kupona ni hamsini kwa hamsini hivyo tujiandae kwa lolote litakalotokea,” Sammy alisema huku machozi yakimlengalenga machoni.



    “Joyce wangu jamani!” Bi. Pamela alisema kwa uchungu mkubwa huku akishika kichwa, alionekana kusononeka sana. Mara kikohozi kidogo kikamtoka na nyuma yake wimbi la machozi lilikuja mbio. Alishindwa kujizuia na akapiga yowe dogo la kilio. Rafael Jengo na Sammy wakawa na kazi ya kumbembeleza.



    Kwa muda wa dakika kadhaa hali ya mahali pale ikageuka kuwa ya simanzi kubwa. Kilio cha Bi. Pamela kikawafanya Rafael Jengo na Sammy wajikute wakitokwa na machozi pasipo kupenda.



    “Mama Davie, tafadhali piga konde moyo ujizuie kumwaga machozi. Nimekwambia tunahitaji sana kuwa watu jasiri kwani Joyce anatuhitaji,” Rafael Jengo alimwambia mkewe huku akimfuta machozi. Akamshika bega, “Listen, ninamfahamu Joyce ni mpambanaji. She’ll fight this!”



    “I know, and I’m trying my best... lakini sina uhakika na hali ya mwanangu hadi nimuone. Oh jamani mimi!” Bi. Pamela alisema huku akiendelea kulia.



    “Please, Mama Davie, eneo hili halihitaji kelele! Please!” Rafael Jengo alisema kwa ukali kidogo. “Usikate tamaa kirahisi hivi, naamini Mungu atamsaidia, si vyema kumwaga machozi eneo hili. Ningejua hali itakuwa hivi ningekuacha Tanga, na kama hautakuwa na ujasiri nitakurudisha Tanga leo hiihii!” Rafael Jengo alisema huku akishusha pumzi.



    “Samahani, Baba Davie, nimekuelewa. Nitajitahidi ingawa inaniwia vigumu,” Bi. Pamela alisema huku akifuta machozi. “Ah, machozi yangu yawe dawa ya mwanangu na Mungu amponye,” alisema kwa sauti ya chini huku akishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.



    “Kwa hiyo, wanasemaje? Tunaweza kumwona mgonjwa?” Rafael Jengo alimuuliza Sammy.



    “Mpaka sasa madaktari hawajaanza kuruhusu mtu kumwona, nadhani wanafanya utaratibu wa...” Sammy alikatishwa na simu ya Joyce aliyoishika iliyoanza kuita.



    Aliitazama kwa makini na kuliona jina la Madame Norah kwenye kioo cha simu. Akashusha pumzi za ndani kwa ndani. “Samahani, ngoja nipokee kwanza hii simu,” Sammy alisema na kuipokea ile simu, akaipeleka kwenye sikio lake. “Hallo, Madame!”



    “Hallo, baba, tayari nimeshafika hapa hospitali, sijui uko kwa wapi?” Madame Norah aliuliza.



    “Njoo moja kwa moja huku chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu.”



    “Okay, nipe dakika moja tu siko mbali na hapo,” Madame Norah alisema na kukata simu.



    Sammy alishusha pumzi na kuitazama ile simu kwa makini kisha akairudisha mfukoni. Kabla hajajua aseme nini mara akamwona Madame Norah akipiga hatua zake haraka haraka kuelekea pale walipokuwa.



    Madame Norah alionekana nadhifu sana akiwa amevaa suti ya rangi ya zambarau ya kitambaa ghali toka nchini Italia; suruali na koti, na ndani alikuwa amevaa blauzi nzuri ya rangi ya samawati. Usoni alivaa miwani mikubwa ya jua iliyoyafunika macho yake, mkufu wa dhahabu shingoni na miguuni alivaa viatu vya zambarau vyenye visigino virefu.



    Akiwa takriban hatu kumi kabla hajawafikia, alisimama ghafla baada ya kuwaona watu wengine wawili wakiwa na Sammy, kilichomshtua zaidi ni yule mwanamume aliyekuwa amevaa suti nadhifu ya rangi ya kijivu na shati jeusi.



    “Jengo?” Madame Norah alijiuliza kwa sauti ndogo huku akihisi miguu yake ikiishiwa nguvu. Aliivua miwani yake na kuishika mkononi. “Ni yeye kweli au nimemfananisha? Ni yeye, naamini macho yangu bado yana nguvu ya kutosha na sina shaka na kile ninachokiona,” Madame Norah alizidi kuwaza huku akimtazama Rafael Jengo kwa makini.



    Sammy alishangaa kumwona Madame Norah akiwa amesimama akishangaa kama aliyeona kitu kigeni. “Vipi, mama, mbona unashangaa?” Sammy aliuliza kwa mshangao na kuwafanya Rafael Jengo na Bi. Pamela wageuze shingo zao kutazama kule ambako macho ya Sammy yalikuwa yanaangalia.





    Macho ya Madame Norah yakagongana na yale ya Rafael Jengo na kumfanya Madame Norah ashushe pumzi na kuanza kupiga hatua taratibu kuwasogelea huku akiwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Jengo.



    “Mungu wangu! Nuru!” Rafael Jengo alimaka kwa mshtuko mkubwa. Alikuwa ameshika simu mkononi, ikamponyoka. Wakabaki wametazamana kwa sekunde kadhaa.



    Bi. Pamela pia alionesha mshtuko mkubwa sana kumwona Madame Norah akiwa pale, alikuwa akimfahamu, siyo kwa kumwona kwenye runinga tu bali alishawahi kuambia habari zake na mumewe, Jengo. Bi. Pamela aliminya midomo yake yenye maki na mashavu yake yakapiga misingi, pembe za midomo zikafinya, akajitahidi kuficha wivu ulioanza kumkaba kooni.



    Ni Sammy pekee ambaye hakujua kilichokuwa kinaendelea pale, alikuwa katika mshangao mkubwa.



    Madame Norah aliwatazama Jengo na mkewe Bi. Pamela kwa zamu huku akihisi donge la fadhaa likianza kumkaba kooni. Kwa dakika kadhaa alishindwa kabisa kuongea na badala yake alisimama akiwa kimya kama aliyekuwa akisubiri kusomewa hukumu yake, machozi yalikuwa yanamlengalenga machoni.



    “Hallo Nuru! Au sijui nikuite Madame Norah?” Jengo alisema baada ya kumwona Madame Norah akiwa amesimama kimya, uso umesawajika.



    “Je-je-jeng…” Madame Norah alitaka kuita lakini akashindwa kutamka, mdomo wake ulikuwa unatetemeka. Kikapita kitambo kingine cha ukimya. “Dah! huu kwangu ni muujiza mkubwa sana, sikuwa nimetarajia kabisa kukukuta hapa!” Madame Norah alimudu kusema akiwa bado katika mshangao.



    “Hukutarajia! Basi karibu. Kuna nini mbona uko hapa?” Jengo alimuuliza Madame Norah huku akimkazia macho.



    “Nimekuja kumwona mwandani wangu Joyce. Na wewe unafanya nini hapa?” Madame Norah alimuuliza Jengo huku akimkazia macho.



    “Joyce! Inamaana tayari mnafahamiana?” Jengo aliuliza kwa mshangao mkubwa.



    “Of course! Ni mwandani wangu na mshirika wangu, kwani vipi! Kuna tatizo lolote?” Madame Norah aliuliza huku akishindwa kuuficha mshangao wake.



    Jengo alitaka kusema neno lakini akasita na kumtazama mkewe Bi. Pamela, macho yao yakakutana. Hakuna aliyesema neon, Jengo akashusha pumzi za ndani kwa ndani. Alikuwa amepatwa na mshtuko mkubwa sana asioutarajia. Alionekana kama mtu aliyepigwa na shoti kali ya umeme na hakuamini alichokisikia toka kwenye kinywa cha Madame Norah.



    Madame Norah aliugundua mshtuko huo, akamtazama Sammy huku akishindwa kuuficha wasiwasi wake. “Kwani kuna nini kinaendelea hapa, baba’angu?”



    “Sijui, lakini hawa ndio wazazi wake na Joyce,” Sammy alijibu kwa sauti tulivu huku mshangao ukiwa haujamtoka usoni.



    “Jengo ndiye baba’ake na Joyce!” ikawa zamu ya Madame Norah kupatwa na mshangao mkubwa. Sammy alibetua kichwa chake kukubali.



    Madame Norah alimtazama Jengo kwa makini pasipo kupepesa macho yake. “Is Joyce our daughter?” alimuuliza huku akihisi kuchanganyikiwa. Alikuwa bado amemtulizia macho usoni.



    “Not our daughter, she is my daughter,” Jengo alijibu kwa sauti kavu huku akiwa amekunja sura yake.



    “Na binti yetu yuko wapi?” Madame Norah akauliza huku akizidi kumkazia macho Jengo. Safari hii alionekana kuwa serious zaidi.



    “Huoni aibu kuuliza swali kama hilo! Siye wewe uliyembwaga na kupotelea kusikojulikana? Leo unathubutu vipi kuuliza habari ya mtoto! Shame on you!” Jengo aliongea kwa hasira huku akimkazia macho Madame Norah.



    “Stop! Ni wewe chanzo cha yote haya. Kumbuka nilikuwa msichana mdogo wakati huo, ni wewe uliyenilaghai na ulipogundua nimepata ujauzito ukanifukuza nyumbani kwako kama mbwa, mbele ya malaya wako. Unajua ni mateso gani niliyoyapata? Unajua kuwa nilikaribia kujiua baada ya kuona dunia yote imenitenga, ukiwemo wewe?” Madame Norah alikuja juu, aliongea kwa uchungu na hasira.



    “Nimeteseka miezi tisa na ujauzito, isingekuwa rafiki yangu kunifadhili hadi nikajifungua salama hata sijui ingekuwaje, lakini bado hukujali. Leo hii unaweza kusimama hapa na kunitukana kiasi hiki! Inatosha, naomba tuheshimiane,” Madame Norah alizidi kuongea kwa uchungu na hasira, safari hii kwa sauti ya juu iliyokaribia kupiga kelele.



    Jengo alitaka kusema neno lakini akahisi hatia ikimkaba kooni, alishindwa kutamka neno na kugeuza shingo yake kumtazama mkewe kwa wasiwasi. Bi. Pamela alikuwa yupo kimya kabisa muda wote kana kwamba mambo yale yalikuwa hayamhusu kabisa. Uso wake ulionesha kukwazika ingawa alijizuia kusema lolote. Kikatokea kitambo kirefu cha ukimya, kila mmoja alikuwa anawaza la kwake.



    “Mzee, samahani... kwani Joyce ni mtoto wa Madame Norah?” Sammy alimuuliza Jengo kwa mshangao huku akionekana kuchanganyikiwa kidogo.



    Jengo alishindwa kujibu, alimtazama kwanza mkewe Bi. Pamela kisha akayahamisha macho yake kumtazama Madame Norah na mwisho akamalizia kwa Sammy na kushusha pumzi ndefu, akabetua kichwa chake kukubali na kuinamisha kichwa chake chini.



    “Oh my God!” Sammy alimaka kwa mshtuko mkubwa. “Dah! Hili kwangu ni jambo jipya kabisa,” Sammy alisema huku akishindwa kabisa kuuficha mshangao wake. Hakuamini kabisa kile alichokishuhudia mbele yake. Kikatokea tena kitambo kifupi cha ukimya kila mmoja akijaribu kutafakari hili na lile.



    “Nahitaji kumwona binti’angu. I need to talk to her,” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu huku akimwangalia Sammy.



    “Sijui kama wataruhusu, hadi sasa hakuna aliyeruhusiwa kumwona...” Sammy alisema kwa wasiwasi.







    “They must,” Madame Norah alisema huku akiwaashiria wamfuate. Walielekea moja kwa moja kwenye ofisi ya wauguzi. Madame Norah akagonga mlango mara moja na kuufungua, akachungulia ndani ya ofisi na kuachia tabasamu, kisha akaingia akiwaacha akina Sammy wakisubiri nje ya ofisi.



    Mle ndani ya ofisi aliwakuta wauguzi waliokuwa wanaongea na Daktari Mshana. Madame Norah alikuwa akifahamiana na Dk. Mshana na baadhi ya wauguzi, hivyo hakupata taabu kujieleza. Baada ya dakika chache za maongezi walitoka nje na kuelekea moja kwa moja katika chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu.



    Jengo na mkewe Bi. Pamela walifuata nyuma kimyakimya, hakuna aliyesema neno kati yao hadi muda ule. Sammy alikuwa bado anashangaa. Walipofika kwenye kile chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu, wote walivalishwa mavazi maalumu mfano wa majoho, ya rangi ya samawati, kofia maalumu na vitambaa vya kufunika mdomo na pua, kisha wakaingia ndani.



    Kilikuwa chumba kikubwa chenye vitanda viwili maalumu kwa wagonjwa mahututi, kikiwa na mitambo maalumu ya kupima mwenendo wa mapigo ya moyo, mashine maalumu za kuwasaidia wagonjwa kupumua na vifaa vingine vingi.



    Walisimama wakimtazama Joyce aliyekuwa amelala kitandani kama mfu akiwa amevalishwa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua huku skrini kubwa ya ukutani ikionesha mwenendo wa mapigo ya moyo wake. Mwili wake ulikuwa umezingirwa na nyaya mbalimbali zilizounganishwa na kompyuta kubwa. Kutokana na hali aliyokuwa nayo Joyce, watu wote walijikuta wakipatwa na simanzi kubwa.



    Madame Norah alimsogelea Joyce, akamtazama kwa kitambo huku akilengwa na machozi, alijitahidi kuangua kilio na kushusha pumzi. “Please God, help her. We still need her,” Madame Norah aliomba kimya kimya huku akiyatuliza macho yake kumtazama Joyce na kuvuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu.



    “Joyce, najua unanisikia. Ni mimi Madame Norah... ni mimi mwandani wako, mama’ako, rafiki’ako na mentor wako. Najua wewe ni mpiganaji na hutakubali kushindwa. Najua bado unayo ndoto ya kufikia mafanikio yako katika maisha. Tafadhali usiondoke ukatuacha. Utakapoamka na kutoka hapa nitakueleza kwa nini tangu siku ya kwanza nilijihisi nina mzigo mkubwa sana wa kukusaidia kufanikisha ndoto yako, sikuwa najua lakini sasa najua. Ninakuhtaji sana mwanangu...” Madame Norah alisema kwa huzuni. Alishindwa kuendelea kumtazama Joyce na kuinamisha kichwa chake.



    Kidevu chake kilianguka kifuani kwake, msirimbi wa kipaji cha uso wake ukaumuka, milizamu ikatutusika chini ya masikio yake kama iliyopulizwa, shingo yake ikavimba, mara kikamtoka kikohozi kikubwa na michirizi ya machozi ikapasuka machoni mwake. Sasa Madame Norah alishindwa kabisa kujizuia, akalia japo alijaribu sana kuyazuia machozi yasitoke lakini hakuweza. Sauti ya kilio chake ikaongezeka na sauti kubwa ya kilio ikasikika na kuwafanya wengine pia waanze kulia.



    Kwa kitambo kifupi hali ndani ya kile chumba cha wagonjwa mahututi ilibadilika na kuwa ya simanzi kubwa, chumba kizima kikachakatika vilio vya kwikwi na nyuso zikafirigiswa katika viganja vya mikono.



    Madame Norah alitoa leso yake iliyokunjwa kwa umaridadi na kupangusa macho yake akifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka utadhani milizamu iliyopasuka. Alikuwa hajiwezi, alipenga kamasi zilizoanza kumtoka na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.



    Dk Mshana hakupenda hali ile iendelee ndani ya kile chumba kilichohitaji utulivu wa hali ya juu, alimshika mkono Madame Norah na kumtoa nje ya kile chumba huku akiwata na wengine kutoka. Akina Sammy pia walishindwa kuidhibiti fadhaa iliyowajaa katika mioyo yao, walitoka nje ya kile chumba huku wakilia.



    Kule nje ya kile chumba Madame Norah alisimama huku akiendelea kufuta machozi yaliyoendelea kumtoka. Dk. Mshana alimtazama kwa makini. “Ndiyo maana sikupenda kuruhusu watu kwa sasa kuingia mle ndani,” Dk. Mshana alisema huku akimtazama Madame Norah kwa makini.



    “Dah! Imeniumiza sana... kwa kweli hali ya mwanangu inakatisha tamaa sana lakini naamini ni mpiganaji, nimemwambia apambane aamke ili tuendelee na miradi tuliyoianzisha, ninaamini amenisikia!” Madame Norah alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Hata mimi naamini kuwa ataamka muda si mrefu kutokana na ujasiri wake,” Sammy alisema huku akifuta machozi.



    “Hivi ni nani hasa waliompiga risasi?” Madame Norah aliuliza.



    “Mpaka sasa haifahamiki,” Sammy akajibu.



    “Siku nikimjua aliyefanya hivi, nitakachomfanya naomba Mungu anisamehe...” Madame Norah alisema kwa hasira huku akipitisha kidole chake cha shahada shingoni na kukikung’uta hewani, kisha akamtazama Dk. Mshana. “Dokta, nakuomba fanya kila uwezalo kuhakikisha anaamka. Kama unadhani anahitaji kupelekwa Muhimbili utaniambia...” mara simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Madame Norah aliitazama kwa makini na kushusha pumzi kisha akaipokea na kuiweka kwenye sikio.



    “Hello, Mr. Mafuru, nipigie baadaye siko kwenye mood,” Madame Norah alisema kwa sauti yenye kitetemeshi.



    “Madame... lakini tulikubaliana kukutana saa hizi kwa ajili ya kuandaa ile...” Mr. Mafuru alianza kujieleza lakini Madame Norah akamkatisha.



    “Nisikilize, siwezi kufanya lolote kwa sasa wakati mwanangu yupo kitandani anapigania uhai wake. Sijui umenielewa?” Madame Norah aliongea kwa sauti kali iliyoonesha kukerwa.



    “Oh samahani, sikujua. Kwani nani anaumwa maana sina taarifa?” Mr. Mafuru aliuliza kwa sauti iliyoonesha mshangao.



    “Binti’angu, anaitwa Joyce. Walivamia nyumbani usiku na watu waliokuwa wanamtaka mumewe kisha wakampiga risasi. Hali yake siyo nzuri hivyo siwezi kufanya lolote kwa sasa...”



    “Oh my God!” Mr. Mafuru alisema na kuongeza, “Dah, ngoja nimweleze Mr. Oduya. Umesema yupo hospitali gani?”



    “Amana.”



    “Okay, nashukuru kwa taarifa. See you later,” Mr. Mafuru alisema na kukata simu.







    * * * * *



    Tunu akiwa katika mwendo wa kasi alijikuta akikanyaga breki ya ghafla na kupunguza mwendo baada ya kuliona daladala linalofanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Viwandani likiingia katika mtaa wa Lindi pasipo kusubiri magari mengine yaliyokuwa yanapita katika mtaa huo. Gari hilo lilikuwa linatokea eneo la Ilala Boma likiwa katika mtaa wa Tabora.



    Tunu alisonya na kulisubiri lipite kisha akakanyaga pedeli ya mafuta kwa nguvu na kulifanya gari lake liserereke na kuongeza mwendo, akalipita gari moja aina ya Nissan Caravan la rangi nyeupe lililokuwa mbele yake na hivyo kufanya uwepo wa magari mawili katikati yake na gari aina ya Toyota Alphard jeusi lililokuwa kiasi cha umbali wa mita sabini.



    Muda huohuo simu yake ya mkononi iliyokuwa imewekwa kwenye dashbodi ikaanza kuita, Tunu aliitupia jicho na kuliona jina la Victor, rafiki yake na shushushu mwenzake, Victor alikuwa anafanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunu akaachia tabasamu na kushusha pumzi, alikuwa amepata wazo la kumtumia Victor kufanikisha misheni yake.



    “Hallo, Victor, uko wapi!” Tunu aliuliza mara baada ya kuiweka simu sikioni, muda huo alikuwa ameifikia barabara ya Kawawa iliyokuwa inakatisha mbele yao ikitokea eneo la Chang’ombe kuelekea Kinondoni.



    “Unanitenga, Tunu, unanitenga...” Victor alianza kulalamika.



    “Uko wapi, Victor, I want to see you right now,” Tunu aliuliza tena kwa sauti iliyoonesha kuwa na haraka, muda huo alikuwa anavuka barabara ya Kawawa na kuufuata mtaa ule wa Lindi. Alikuwa usawa wa Machinga Complex.



    “Nipo hapa MAK Books and Brains katika jengo la Mkuki ila nataka kuelekea bandarini mara moja...” Victor alisema.



    “Usiondoke, nisubiri hapo nje ya jengo, natokea huku Shaurimoyo,” Tunu alisema kwa sauti iliyomfanya Victor kushikwa na mshangao.



    Tunu akapunguza mwendo na kumkwepa mtu mmoja aliyevuka barabara pasipo kuangalia, alikuwa akitokea katika duka moja la vipuri vya magari eneo lile na kuelekea lilipo jengo la Machinga. Lile gari aina ya Toyota Alphard jeusi nalo lilikuwa linavuka barabara ya Kawawa na kuufuata mtaa ule ule wa Lindi, japokuwa lilikawia kidogo kuvuka.



    Hadi hapo Tunu alikwishapata uhakika kuwa walikuwa wakimfuata yeye, hata hivyo kwa namna nyingine ile ilikuwa ni ishara mojawapo ya kumtahadharisha kuwa hakupaswa kujiamini sana bali alitakuwa kuwa makini zaidi.



    Aliongeza mwendo hadi alipofika kwenye makutano ya mtaa ule wa Lindi na Shaurimoyo, akaiacha barabara ya Lindi na kungia upande wa kulia kuufuata mtaa wa Shaurimoyo na hapo mwendo wake ukaongezeka tena huku akiyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yake. Alikuwa mjanja sana na anayeijua vizuri kazi yake.



    Aliivuka reli na alipowa mbioni kufika mwisho wa mtaa ule akageuza shingo yake kutazama nyuma na kuliona lile gari aina Toyota Alphard jeusi likiwa limeingia katika barabara ile ya Shaurimoyo. Muda huo huo akaliona treni la abiria lifanyalo safari zake ndani ya jiji la Dar es Salaam maarufu kama “Treni la Mwakyembe” likiwa linapita na kuyafanya magari yote kusimama, hiyo ikawa nafuu kwa Tunu.



    Tunu aliingia katika barabara ya Nyerere na kupitiliza moja kwa moja hadi lilipo jengo la Mkuki, akamkuta Victor akiwa amesimama amejiegemeza katika gari lake aina ya Toyota Prado la rangi nyeupe.



    “Nina haraka kidogo, niazime gari lako halafu tumia hili langu, kuna sehemu naenda nikimaliza nitakutafuta tuongee vizuri,” Tunu alisema mara baada ya kushuka toka kwenye gari lake ambalo lilikuwa bado linanguruma taratibu. Victor akaonesha mshangao.



    “Unanitenga, Tunu. Umekuja jana tu leo naona una ndinga mpya, tupeane michongo basi, mshikaji wangu,” Victor alisema kwa utani huku akimpa Tunu ufunguo wa gari lake.



    “Tutaongea bwana, ngoja niwahi sehemu,” Tunu alisema na kuingia ndani ya lile gari la Victor, akaliwasha na kuliondoa kwa mwendo wa kasi akiifuata barabara ya Nyerere kuelekea eneo la Chang’ombe, alimwacha Victor anashangaa.



    Kama kawaida yake, Victor alikuwa amevaa shati zuri la kitenge la mikono mirefu, kofia ya pama, suruali ya dengrizi na miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za ngozi. Alishusha pumzi na kuingia ndani ya lile gari aina ya BMW X6 xDrive 50i jeusi aliloachiwa na Tunu kisha akaliondoa toka katika lile jengo la Mkuki na kuingia katika barabara ya Nyerere, akaelekea uelekeo wa eneo la Kamata. Hakuwa na wasiwasi wowote.



    Wakati akiwa analikaribia jengo ambalo awali lilikuwa likitumika kama Shoprite Supermarket gari aina yaToyota Alphard jeusi lililokuwa likiendeshwa na Job ndiyo lilikuwa linaingia katika barabara ya Nyerere.



    Victor alipofika katika taa za kuongoza magari barabarani eneo la Kamata akaiacha barabara ya Nyerere na kuingia kulia akiifuata barabara ya Gerezani, kisha akanyoosha moja kwa moja hadi katika mzunguko unaozikutanisha barabara za Gerezani na ile Bandari iliyokuwa inaelekea bandarini.



    Wakati huo lile gari aina yaToyota Alphard jeusi nalo lilikuwa limezivuka taa za kuongoza magari barabarani za Kamata na sasa lilikuwa katika mwendo wa kasi zaidi kuelekea kule liliko gari aina ya BMW X6 xDrive 50i. Victor aliuzunguka mzunguko wa barabara na kuelekea kulia kuifuata barabara iliyokuwa inaelekea bandarini kisha akaanza kulivuka daraja ambalo chini yake kulikuwa na reli.







    Akiwa anamalizia kulivuka lile daraja na kabla hajayafikia maeneo yaliyokuwa yamehifadhi makontena ghafla lile lile gari aina yaToyota Alphard jeusi likampita kwa kasi na kumzuia kwa mbele. Kilikuwa ni kitendo cha kushtukiza na Victor hakuwa na namna, akakanya breki huku akilipeleka gari lake kando ya barabara na kulifanya gari lake liserereke kisha likasimama hatua tano toka lilipokuwa limesimama gari aina yaToyota Alphard. Alipiga ngumi kwenye usukani huku akitweta kwa hasira, akalitazama lile gari lililomzuia kwa hasira zilizochanganyika na mshangao.



    Kitendo cha haraka sana kikafanyika, Spoiler na Job walishuka toka kwenye gari lao na kulifuata lile gari aina ya BMW X6 xDrive 50i alilokuwemo Victor. Spoiler akauvuta mlango wa dereva. Akajikuta akipigwa na butwaa baada ya kumwona Victor badala ya Tunu! Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa kwa namna ambayo ni wao wawili tu walioelewa maana yake.



    “Shit!” Spoiler alisema huku akishusha pumzi kisha akageuza shingo yake kutazama huku na huko. Tunu alikuwa kawapiga chenga ya akili na mwili.



    “Kwani vipi, wazee, mbona sielewi!” Victor aliuliza kwa mshangao huku akiwatazama Spoiler na Job kwa zamu.



    “Victor, kwani... hili si gari alilokuwa nalo Tunu leo, au yanafanana?” Spoiler alimuuliza Victor akiwa haamini alichokuwa akikiona mbele yake.



    “Ndiyo hili, kaniachia sasa hivi na yeye kachukua la kwangu,” Victor alisema na kushusha pumzi, “Kwani kafanya nini?” akauliza akiwa bado anashangaa.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Muda huo magari mengine yakaanza kupiga honi kumtaka dereva gari aina ya yaToyota Alphard kuliegesha kando ya barabara. Job hakuwa mbishi, aliingia ndani ya gari kisha akalisogeza pembeni kabisa ya barabara ili kuyapisha magari mengine yapite.



    “Tayari tumeshachezewa shere!” Spoiler alisema huku kashika kiuno chake kwa mikono yote miwili, alionekana kukata tamaa.



    “Haha! Kama mlikuwa mnafuata Tunu, mmeshapotezwa!” Victor aliongea huku akiangua kicheko na kuongeza, “Kwani kuna ishu gani, mzaee, mbona husemi pengine naweza kusaidia.”



    “Hayo ndo maneno, ngoja nije nikupe mkanda mzima,” Spoiler alisema huku akizunguka upande wa pili wa lile gari, akafungua mlango na kuingia ndani ya gari, akaketi huku akimkabili Victor.



    * * * * *



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog