Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

NYUMA YAKO (4) - 3

 





    Simulizi : Nyuma Yako (4)

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Basi kidogo mlango ukafunguliwa na mmoja wa watu wa usalama. Bwana huyo alikuwa amevalia sare za jeshi na mkononi alikuwa amebebelea bunduki - SMG. Bwana huyo akampasha Azizi kuhusu yale yalotokea kule kwenye kasri la Abdulaziz.



    “ … watu wote wapo hoi. Wanapata shida kuhema na miili yao imekuwa ya baridi kana kwamba barafu!”



    Haabri hizo zikamchanganya sana Aziz. Mawazo yake yalitambua kuwa ni mdogo wake ndiye aliyafanya hayo. Ameua watu wake!



    Basi akakung’uta ngumi nzito mezani mpaka kuivunja.



    “Nalijua haya!” akafoka. Akanyanyua simu yake na kumtaarifu Jamal kwamba anamtaka Abdulaziz haraka! Haraka iwezekanavyo kabla hajasababisha maafa mengine.



    Aliposema hayo akashika kiuno kwa mkono wake wa kulia wa kushoto akiweka tama. Alimezwa na mawazo.



    Punde kidogo akaingia bwana aliyebebelea sinia lenye vikombe vya kahawa. Meza haikuwapo. Bwana huyo aliyekuwa amejawa na ndevu akarusha macho yake huku na kule asitambue la kufanya.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Alipotaka kuondoka afanye mbadala mwingine, Aziz akamwita na kumtaka ampatie kahawa yake mkononi.



    “Muda wote huo mlikuwa mnafanya nini?” Aziz akauliza kwa hasira, akagida kinywaji chake na kuweka kikombe chini.



    “Nenda sasa!” akamwambia mhudumu. “Wangoja nini hapa?”



    Lakini mhudumu hakwenda. Badala yake akasimama hapo kumtazama Aziz. Naye Aziz alipomtazama vema mhudumu huyo akatambua machoye hayakuwa mageni.



    Ngoja …



    Yalikuwa ni macho ya Abdulaziz!



    **





    Hakika moyo wake ukapiga fundo kubwa akitaharuki. Mlango ulifungwa na Abdulaziz akatoa bunduki na kuwaweka chini ya ulinzi Aziz na Ramadan.



    “Mtatulia kama maji mtungini na basi haya yote yataisha vema. La sivyo, maiti zenu zitaokotwa msituni. Ni kheri kama zikikutwa na binadamu kabla ya wanyama.”



    Basi Aziz na Ramadan wakatii amri. Hawakuwa na la kufanya na wala nguvu zao hazikuwa na msaada mahali hapo.



    “Wewe ni shetani!” Aziz akafoka. “Uroho wa madaraka ndo unakufanya uwe mnyama kiasi hiki?”



    Abdulaziz akatabasamu. “Nadhani umesahau, Aziz. Mimi na wewe ni watu tofauti kabisa. Siwezi nikakubali wewe ukae kwenye kiti ilhali nipo hai.”



    Kusikia maneno hayo, Aziz akamtemea mate Abdulaziz na kufoka kumtusi. Akimlaani na kumtupia maneno makali. Basi kidogo tu, Abdulaziz akakoki bunduki yake na kutungua kichwa cha kaka yake.



    Aziz akalala mfu!



    “Nisamehe!” Ramadan akabweka. “Nisamehe, naomba usiniue!”



    Bwana huyo alikuwa anatetemeka kweli. Moyo wake ulikuwa unakita haswa. Alikuwa anatokwa na jasho akiwazia kifo. Abdulaziz akamtazama bwana huyo na kisha akaketi kitini.



    Kuna jambo alikuwa analiwaza. Alikuna kichwa chake kwa bunduki yake alafu akamuuliza Ramadan maswali kadhaa kuwahusu Marietta na wenziwe.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Kama unataka uendelee kuhema, basi yakupasa ufanye kama ninavyokuagiza,” akasema Abdulaziz. Huko nje watu walikuwa wakiendelea na mambo yao kama kawaida. Hawakuwa wanajua kinachoendelea ndani kwani Abdulaziz alitumia kiwamba cha kumeza sauti kwenye mdomo wa bunduki alotumia.



    “Sawa!” akabwatuka Ramadan. Alitazama mwili wa Aziz uliokuwapo chini ukiwa hauna uhai akachanganyikiwa zaidi. Alikuwa anahofia sana. Kama angeendelea kuwapo kwenye hali hiyo basi angejikojolea si muda.



    “Usidhani kunidanganya kabisa. Ukifanya hivyo utajikuta unakufa na kuacha familia yako.”



    Baada ya vithisho hivyo bwana Abdulaziz akampatia Ramadan kazi ya kufanya na kumpa onyo kabisa kwamba familia yake itakuwa chini ya uangalizi mpaka pale atakapomaliza kazi.



    **



    Saa moja jioni …





    Kila mtu ndani ya kasri alishafahamu kwamba Aziz amefariki dunia. Japo bado habari hiyo haikuwa imevuja kwenda popote pale. Ilikuwa ni habari ya simanzi sana na kila mmoja aliyekuwapo hapo kundini alikuwa ameguswa nayo kwa kiasi kikubwa, ilikuwa ni tishio kwa ajira zao.



    Lakini mbali na hapo Aziz alikuwa ni mtu ambaye aongea na kila mmoja. Kiongozi ambaye hakuwa na makuu wala karaha. Japo ni vijakazi lakini walifurahia uwepo wake kasrini na walitarajia makubwa zaidi endapo bwana huyo ngeingia madarakani.



    Sasa inakuaje?



    “Inabidi tufikishe taarifa kwa mfalme. Hatuwezi liweka hili zaidi!” alisema kiongozi mkubwa wa wajakazi wa kasri. Bwana huyo alikuwa ni mnene lakini asiye na kitambi. Kichwa chake kilikuwa kimefunikwa na kofia nyekundu yenye utepe mweusi.



    “Lakini yatupasa tuwe makini sana,” akasema bwana mwingine, yeye alikuwa naibu wa yule kiongozi mkuu wa vijakazi. “Kama tukilipeleka hili jambo upesi tunaweza kumuua Mfalme mara moja. Mnajua vema hali yake ilivyo. Ni mwezi sasa yupo hospitalini akisaidiwa na mashine.”



    “Ni kweli,” akasema kijakazi mkubwa. “Lakini nina hofu sana juu ya hili. Litatuweka matatani haswa sisi vijakazi. Tutasema nani kamuua mwana wa mfalme?”



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    **





    “Hamna kitu!” Marietta alisema akitikisa kichwa. Sasa walishasaka nyumba zote za Abdulaziz pasipo mafanikio. Hawakumwona mlengwa wao popote pale.



    “Sasa tunafanyaje?” akauliza Kelly. “Hamna mtu mwenye makisio ya ziada?”



    “Tutamfute Abdulaziz popote alipo!” akasema Marshall. “Kama tukimpata basi atatuelekeza wapi.”



    “Si rahisi kumpata Abdulaziz kwa sasa,” Mahmoud naye akatia neno. “Anajua kuwa anatafutwa, unadhani atakuwa karibu?”



    “Na vipi kuhusu familia yake?” akauliza Marshall. “Tunaweza kuitumia familia yake kama chambo cha kumpata!”



    Wakiwa hapo wanaendelea kuteta, simu ya Mahmoud ikaita. Alipotazama akabaini ni Ramadan. Upesi akapokea.



    “Tafadhali tuonane upesi.”



    “Kuna nini?”



    “Tukikutana tutaongea. Hakikisha mmekuja nyote.”



    Bwana huyo akataja na mahali pa makutano kisha akakata simu. Mahmoud akawajuza wenzake juu ya makubaliano hayo na basi upesi wakaanza mkakati wa kwenda huko walipoelekezwa.



    Wakiwa njiani, wamepakia taksi, wakasikia habari za kifo cha Aziz. Habari hizo zilikuwa zinatangazwa na kituo cha kuaminika cha redio, na kwa taarifa zaidi muuaji hakuwa bado amegundulikana.



    Vijakazi wote wamewekwa chini ya ulinzi kwa mahojiano zaidi.



    “Ni Abdulaziz!” akafoka bwana Mahmoud akibonda ‘dashboard’. Alipatwa na mawazo. Kama Aziz amekufa basi nini hatma yao na nchi kwa pamoja?



    Mahali walipopakimbilia napo pamemezwa!



    “Sasa tutafanyaje?” Marietta akauliza upesi. “Ndo’ maana Ramadan akataka kutuona?”



    “Inawezekana,” Mahmoud akajibu. Hakuongezea neno jingine kwani alikuwa amebanwa na mawazo, alikuwa anafikiri kuliko kuteta. Alihisi kichwa kimekuwa cha moto.



    “Lakini,” Danielle akapaza sauti yake. Yeye alikuwa ana hofu na Ramadan. Kwa mujibu wa akili yake aliona yawapasa kuwa makini kwani kama vijakazi wote wamewekwa chini ya ulinzi na tukio kubwa kama hilo limetokea, vipi kuhusu Ramadan?



    Yeye alikuwapo wapi? Kama alikuwapo eneo la tukio, kitu ambacho kina asilimia kubwa, imekuaje yeye akanusurika na kifo?

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Kwa muda kidogo gari likawa kimya. Watu walikuwa wamefumba vinywa vyao lakini akili zikiwa zinaongea na kupiga kelele.



    Marshall akamtazama Danielle na kumuuliza,



    “Wewe unawazaje?”



    “Chochote kinaweza kutokea hapa,” Danielle akajibu. Marshall akaelewa ni nini mwanamke huyo anamaanisha, basi akajikuta akitabasamu na kutupia maneno kadhaa,



    “Pengine njia imepatikana!”



    **



    Bwana Ramadan alitazama saa yake ya mkononi kisha akarusha macho yake barabarani. Juu ya ‘dashboard’ alikuwa ameweka kikombe cha ‘take away’ chenye kubebelea kahawa nyeusi ya moto.



    Uso wake ulikuwa mzito na kwa kumtazama tu ungalijua yu shidani. Kahawa yake ambayo ameiweka kwenye dashboard hakuinywa hata kidogo.



    Koo lake lingepitishaje kahawa hiyo ingali familia yake ikiwa kifungoni? Na bwana aliyekuwa anamtumikia miaka yote hiyo amekufa, tena mbele ya macho yake?



    Aliegemeza kichwa chake kwenye kiti. Alitamani kulia lakini haikuwa sahihi. Aliporejesha macho yake barabarani ndipo akaona taksi ikiwa inakuja kwa mbali.



    Akachukua simu yake kutuma ujumbe fulani upesi kisha akaweka simu yake mbali.



    “Imetumwa ujumbe hivi sasa,” sauti ndogo ilisikika kwenye sikio la Marshall kwa kupitia kifaa sauti. Bwana huyo alikuwa anawasiliana na Jack ambaye alikuwapo nyumbani mbele ya kitu anachoweza kutumia kushinda vyote duniani: tarakilishi.



    Mmarekani huyo mwenye asili ya China alikuwa tayari ameshadukua njia za mawasiliano ya Ramadan punde tu alipopewa namba na bwana Mahmoud muda si mrefu.



    Sasa alikuwa anaona kila ujumbe na kusikia kila sauti atakapoongea.



    “Unasemaje?” Marshall akauliza.



    “Wameshafika,” Jack akamjibu na basi Marshall akatulia na kuwajuza wenzake. Punde taksi ikasimama, kulikuwa na umbali toka kwenye usafiri wa Ramadan, bwana Mahmoud akiongozana na Kelly na Marietta wakashuka toka kwenye gari na kumfuata Ramadan.



    Walijikwea kwenye gari bwana Ramadan akilazimisha tabasamu usoni.



    “Nafurahi mmeitikia wito wangu,” aliposema hayo akatazama ile taksi na kuuliza, “Hamna wengine?”



    “Hapana. Ni sisi tu,” bwana Mahmoud akajibu.



    “Mbona taksi haiondoki?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Punde taksi ikageuza na kwenda. Ni kama vile ilisikia kile kilichosemwa. Taksi ilivyopotelea, kwa mbali yakaonekana magari mengine mawili. Kelly alitambua ujio wa magari hayo.



    “Nadhani mmesikia habari za msiba. Hapa tuongeapo bwana Aziz ameaga dunia kwa kufyatuliwa na risasi kichwani … sina haja ya kuwaeleza nani muuaji, mnamfahamu vilivyo.”



    Bwana huyo akaweka nukta kwa sekunde tatu. Wakati huo Mahmoud akafanikiwa kutazama nguo ya Ramadan na kubaini kuwa na mabaki ya damu upande wa kushoto wa kanzu yake.



    “... Nimeumiza sana. Sikutaraji kama haya yangetokea,” akasema Ramadan jicho likiwa jekundu. Akatoa leso yake na kujipangusa. “Samahanini sana lakini jambo hili ni kubwa sana kwangu. Sijui nitalibebaje.” akavuta kamasi nyepesi puani na kuendea kwenye lengo lake sasa,



    “Najua mahali alipo yule kiongozi. Nipo radhi kuwapeleka ili mkamuokoe kabla ya Abdulaziz hajatimiza adhma yake!”





    **





    “Sasa wanaanza kusogea,” sauti ilisikika kwenye sikio la Marshall. Ilikuwa ni sauti ya Jack aliyekuwa anatazama kioo cha mashine yake kutazama mwelekeo wa namba aliyoidukua.



    Akawaelekeza wenzake mwelekeo kwa kutumia majina ya barabara na ncha za dira, upesi Marshall akamtaka dereva wa taksi aelekee huko maelekezo yanapotaja lakini kwa kutumia njia nyingine kuepusha kugundulikana upesi.



    Kila walipotembea kwa muda fulani Jack akawa anawajuza zaidi na zaidi nao wakazidi kusonga kufuata maelezo. Walipokaribia na eneo la tukio wakawa wanapunguza mwendo kutoa nafasi ya usalama.



    “Itakuwa wanaelekea jangwani,” sauti ya Jack ikasema kifaani.





    **



    Kelly alikunja shingo yake kutazama nyuma. Hakuyaona yale magari mawili tena na hakuwa anajua wapi yalielekea.



    Alirusha macho zaidi asipate kitu. Kuangazangaza kwake kukamfanya Ramadan amtilie shaka. Alikuwa anamwona mwanake huyo kwenye ‘sight mirror’.



    “Vipi? Kuna tatizo?”



    “Hapana. Hamna!”



    Wakaendelea kutembea. Kwa kama baada ya dakika sita, Kelly akayaona yale magari mawili kwa mbele. Kila moja lilikuwa limechipukia njia yake yakakutana kwenye njia kuu.



    Mwanamke huyo akamtazama Marietta kwa macho ya ujumbe. Lips zake hazikusema jambo.



    Aliporudisha macho yake mbele, akakutana na mboni za Ramadan kwenye ‘sight mirror’.





    **





    Basi baada ya kitambo kifupi wakafika mahali ambapo Ramadan amewapeleka. Ilikuwa ni jangwani, makazi yalikuwa machache na kumetulia. Hapo kulikuwa na nyumba kubwa kiasi mithili ya kiwanda kwa umbo.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Humo ndo’ Ramadan akawaambia yu mlengwa wao.



    “Siwezi kwenda huko, mnaweza kuingia sasa kwenda kuhakikisha wenyewe. Tafadhalini, hakikisheni mmemuua Abdulaziz kwa namna yoyote ile!!”



    Basi wakashuka wakimwacha Ramadan kwenye gari, hata hawakumbughudhi, kidogo waliposonga Ramadan akapiga simu kutaarifu utendaji wake wa kazi.



    “Nadhani nipo huru sasa!”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog