Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

ROMAN ABRAMOVICH: UTAJIRI WA DAMU, RISASI NA UMAFIA - 5

 





    Simulizi : Roman Abramovich: Utajiri Wa Damu, Risasi Na Umafia

    Sehemu Ya Tano (5)







    Nilieleza kwamba mwaka huo alipopewa Baraka na Putin kuingia kwenye biashara ya Aluminium, Abramovich alifungua kampuni iliyoitwa Millhouse Capital ambayo ilisajiliwa nchini Uingereza. Kampuni hii ilikuwa inatrade commodities. Tufahamu kwamba mpaka muda huu kampuni hii haikuwa lolote wala chochote. Haikuwa na ‘volumes’ kubwa kwenye kutrade hizo commodities wala assets za maana. Thamani pekee ya kampuni hii iliyokuwa nayo ni ile u kwamba inamilikiwa na Roman Abramovich.



    Abramovich alipotambulishwa kwa Deripeska alikuwa na ombi moja tu kwake… waunganishe kampuni zao Millhouse Capital ya Abramovich na Sibirsky Aluminium Group ya Deripaska na iwe kampuni moja. Kwa umombo dili kama hii wanaita ‘merger’.

    Unaweza kuona kwamba ombi hili lilikuwa ni la kijinga… Sibirsky Aluminium Group ilikuwa kwa muda huo ni kampuni kubwa sana ndani ya Russia inayomiliki smelters kadhaa kubwa kubwa ndani ya Russia na pia ilikuwa kampuni mama ya trading companies kama vile ile VTK ambayo deripaska aliinzisha na wanasayansi wenzake. Wakati ambapo Millhouse Capital ya Abramovich ilikuwa kama ni kampuni jina tu yenye ofisini bila mali kubwa kubwa kulinganisha na Sibirsky Aluminium Group.



    Ajabu ni kwamba Deripaska hakusita hata kwa sekunde kukubali ombi hilo. Alikubali mara moja waunganishe kampuni hizo mbili kuwa moja ambayo watakuwa wanaimiliki wote.

    Kwa nini akubali kirahisi hivi? Wendawazimu?... hapana, kama ilivyo kwa Abramovich ndivyo hivyo hivyo pia ilivyo kwa Deripaska… ni mtu wa mikakati. Anaiona miaka ishirini ijayo leo.



    Kuna mambo mawili…



    Thamani halisi ya kitu haitokani na hali yake ya sasa bali thamani yake ni ile ‘potential’ iliyonayo kuleta mafanikio huko mbeleni. Yaani kwamba tukiwaza kibiashara… kwa mfano utajiri au umasikini wa mtu haupimwi kwa kile alichonacho sasa bali ‘potential’ aliyonayo kupoteza zaidi au kuingiza zaidi kwa siku na miaka ijayo. Unaweza kuwa na milioni mia moja leo hii lakini kuna mtu akikuangalia anakuona masikini. Labda kwa namna fulani amegundua ndani ya miezi michache tu utazipoteza zote. Na unaweza kuwa na elufu kumi tu mfukoni na mtu mwingine akakuona tajiri kwa sababu anahisi potential uliyonayo mwakani tu unaweza kuwa na bilioni umelaza benki.



    Napenda mifano hai, nitoe mfano mfupi halisi…

    Mwaka 2008 nilikuwa na rafiki yangu tulikuwa darasa moja Tambaza High school. Huyu kwao walikuwa na haueni sana. Mzee wake alikuwa afisa mwandamizi wa serikali kwenye kitengo fulani. Alikuwa na safari za mara kwa mara nje ya nchi. Kuna safari moja aliporejea alimletea zawadi ya simu ya iPhone. Hiyo ni mwaka 2008 ambapo unaweza kutembea mjini kutwa nzima bila kuona mtu hata mmoja mwenye simu aina ya iPhone. Unaweza kupata picha ni kiasi gani yeye mwenyewe na sisi 'washkaji' zake tulikuwa ‘tunavimba’ shuleni… ndio hata sisi wapambe wake tulikuwa tunajiona kama simu yetu. Loooh.!!

    Basi tukaanza ‘uzungu uzungu’ hivi… kutaka kujua mambo ambayo yanatrend huko duniani. Mara tukafahamu kuhusu facebook… hu ni mwaka 2008… sikumbuki kuwahi kumsikia mtu yeyote kabla akitaja facebook. Kilikuwa ni kitu kipya ambacho hapa nchini kilikuwa hakijulikani kabisa kabisa. Kipindi kile ‘chat rooms’ ndio zilikuwa maarufu sana hapa nchini. Pale shuleni kwetu ni ‘genge’ letu tu nadhani ndio ambao tulikuwa na akaunti za facebook na hata sisi ni baada ya kusikia ni kitu ‘hot’ huko duniani.



    Kutokana na udadisi sikuishia tu kuitumia facebook bali nikaanza kuichimba. Ndio nikafahamu kuhusu mmiliki wake bwana Mark Zuckerberg na kipindi kile akisemwa kuwa ndio Bilionea kijana zaidi duniani akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.4 akiwa na umri wa miaka 26 tu. Nikawa najiuliza sana… huyu mtu anawezaje kuwa tajiri mkubwa kiasi hicho wakati huduma hiyo tunaitumia bure? Kipindi kile facebook haikuwa na matangazo kama sasa na ilikuwq sehemu ya sera yao kutokuweka matangazo kwenye mtandao wao… hakukuwa na tangazo hata moja na wala walikuwa hawapokei matangazo. Na pia wala walikuwa hawajafanya ile IPO… ile kuirodhesha kwenye soko la hisa na kuanza kuuza shares kwa umma. Kipindi kile hata financial documents za kampuni zilikuwa zinaonyesha kwamba kwa mwaka wanapata zero revenue? Inakuwaje huyu mtu awe tajiri hivi? Hizi hela zinatoka wapi? Hawa wazungu wanatuzuga na uongo au nini?



    Wewe unadhani hela za Mark zilikuwa zinatoka wapi kipindi kile? Kwa nini kipindi kile waseme ana utajiri wa dola bilioni 2.4?



    Jawabu ni 'Speculation'… ‘potential’ ambayo watu wanaiona kwa kitu hicho kutengeneza faida kubwa kwa wakati ujao. Sikumbuki sawasawa lakini nadhani kipindi kile Facebook ilikuwa na watumiaji kama milioni 300 hivi duniani. Kwa hiyo kulikuwa na speculation kubwa kwamba hii kampuni siku yoyote ile ‘ita-boom’ na kuleta fedha nyingi. Na hii ndio ilikuwa inafanya thamani ya kampuni ya facebook kuwa kubwa na kumfanya Mark kuwa na utajiri wote ule. Lakini kiuhalisia kwa kipindi kile hawakuwa wanaingiza revenue hata kipande ukiachaa hela za investors.



    Sasa hiki ndicho ambacho Deripaska alikuwa anakiona kwa Abramovich… potential. Potential gani? Abramovich alikuwa ni ‘mtoto’ pendwa wa Putin. Putin alikuwa anamuamini Abramovich kuzidi mtu yeyote yule. Kwa hiyo kama akiwa mmiliki mwenza wa kampuni moja na Abramovich, basi hakuna anga ambalo litawashinda kulivuka na wanaweza kutengeneza moja ya kampuni tajiri zaidi duniani.



    Nilisema kuna mambo mawili… hiyo ilikuwa sababu ya kwanza. Sababu ya pili ilikuwa ya busara zaidi. Isingelikuwa busara kwake kumkatalia Abramovich kwasababu, ‘If Roman wants something… Roman gets something.!” Kama angemkatalia ofa hiyo Abramovich, basi Abramovich angetafuta namna nyingine ya kukipata kiwanda hicho na njia hiyo nyingine ingekuwa hasara kwa Deripaska. Abramovich ni aina ya watu ambao lazima wapate wanachokitaka… hakuna kiunzi ambacho atashindwa kukiruka.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Kwa hiyo wakaunganisha kampuni zao, Millhouse Capital na Sibirsky Aluminium Group na kuunda kampuni mpya inayoitwa RUSAL (siku hizi inaitwa United Company RUSAL).



    RUSAL ilikuwa kwa haraka sana. Walichokuwa wanakifanya… walikuwa wananunua viwanda vingine na migodi ya boksiti ndani ya Russia na nchi jirani. Maoligarch ambao walikuwa wanamiliki viwanda hivyo na migodi ilikuwa ni eidha uwauzie RUSAL kiwanda chako kwa hiari au wakichukue kwa lazima. Ukikubali kuwauzia wanakulipa hela… ukikataa kuwauzia kesho kutwa tunaokota mwili wako jalalani.

    Kuna ‘transcript’ za mahakamani kutoka Uingereza za mwaka 2010 ambapo Abramovich aliitwa kutoa ushahidi kwenye kesi fulani, anakiri kwamba hizi aluminium wars zilikuwa moto kweli kweli kiasi kwamba yeye binafsi anakumbuka kwa miaka ya 2000 na 2001 kwa wastani wa kila baada ya siku tatu ulikuwa unasikia mwii wa oligarch fulani umeokotwa.



    Na hapa ndipo ambapo ulikuja umuhimu wa Badri Patarkatsishvili yule jamaa wa kwanza aliyetambulishhwa na Berezovsky. Unapojihusisha na sekta ambayo kila kukicha unasikia wenzako wanakufa lazima uwe na tahadhali makini haswa. Huyu Badri nilieleza kwamba alikuwa anajua kudili na Mafia.

    Unapomwaga damu za wenzako lazima kuna marafiki zao na ndugu zao na hata wale wengine wanajihisi nao siku utawamaliza, wote hawa watajihami kwa kutaka kukumaliza wewe. Ilifika kipindi ndani ya Russia Abramovich alikuwa hawezi hata kuonekana hadharani… kila oligarch aliyekuwa bado hai alikuwa ameweka vijana kumuwinda na kutaka kumuua. Ndio hapa ambapo Abramovich ilimbidi kulipa zaidi ya dola milioni 500 kupitia kwa Badri kwenda kuhonga kila kikundi cha mafia ndani ya Russia ambacho kilitumwa kumuua yeye na kisha kuwapa agizo jipya wakawamalize wale ambao waliwatuma awali.



    Nchi ilichafuka haswa kwa vifo vya maoligarch… lakini RUSAL ilizidi kupaa. Ndani ya miaka miwili tu walikuwa wana-control karibia migodi yote muhimu ya boksiti na viwanda vyote vikubwa vya Aluminium ndani ya Russia na nchi jirani. Kuanzia viwanda vya Armenal foil mill nchini Armenia mpaka Belaya Kalitva Metallurgical plant na Novokuznetsk aluminium smelter nchini Russia. Uje migodi ya boksiti ya Friguia bauxite na Alumina complex mpaka Kindia Company. RUSAL ilipaa juu kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi ya uzalishaji wa aluminium duniani. Lakini hapana… Abramovich hakutaka kuwa ‘moja ya’ kampuni kubwa duniani. Alitaka kuwa kampuni kubwa zaidi duniani ya uzalishaji aluminium.



    Afanyeje? Kulikuwa na ‘terget’ ya mwisho… Krasnoyarsk.



    Kipindi hicho jimbo la Krasnoyarsk ndilo lilikuwa na hifadhi kubwa zaidi ya migodi ya boksiti. Sasa pale Krasnoyarsk kulikuwa na kiwanda cha aluminium kinachoitwa Krasnoyarsk Aluminium Smelter. Kiwanda hiki kilikuwa kinamilikiwa na oligarch anaitwa Anatoly Bykov. Huyu oligarch alikuwa ni kijana kama wao akina Abramovich japo alimzidi Abramovich miaka miwili kwa kuzaliwa. Kampuni yake ambayo ndiyo ilikuwa inamiliki Krasnoyarsk Aluminium Smelter kwa kipindi hicho iikuwa inashika nafasi ya pili nyuma ya RUSAL kwa uzalishaji Aluminium. Abramovich tayari alikuwa amemfuata na kumpa ofa mara kadhaa kuwauzia kampuni lakini Bykov alikataa. Mpaka muda huo alikuwa amefanikiwa kukwepa majaribio 26 ya kumuua.



    Kwa hiyo huyu oligarch biashara alikuwa anaijua kama wao na uhuni wa kimafia pia alikuwa anaujua.



    Kama Abramovich akifanikiwa kuchukua kiwanda hiki cha Krasnoyarsk Aluminium Smelter maana yake ni kwamba atafanikiwa kuifanya RUSAL kuwa kampuni kubwa zaidi ya uzalishaji aluminium duniani.



    Lakini Bykov alikuwa amejiapiza kutowauzia kiwanda chake na majaribio ya kumtoa roho yalishindikana mara 26.

    Abramovich si mtu wa kukubali kushindwa vita… “Roman wants something… Roman gets something.”



    Alikuwa anahitaji mbinu mpya… Abramovich alijiapiza kuwa hataki tu kuwa na ‘moja ya’ kampuni kubwa zaidi duniani ya kuzalisha aluminium...alitaka kuwa na kampuni kubwa zaidi duniani ya kuzalisha aluminium.



    Alikuwa anahitaji ‘kuchemsha muarobaini’ mpya wa kumnywesha Bykov.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/









    Kiunzi pekee ambacho kilikuwa kimebaki mbele ya Abaramovich kuifanya RUSAL kuwa kampuni kubwa zaidi ya uzalishaji wa Aluminium ilikuwa ni deal ya kiwanda cha Krasnoyarsk kinachomilikiwa na Anatoly Bykov.



    Baada ya kila mbinu kutofanikiwa Abramovich akapata wazo lingine. Mbinu hii ambayo aliitumia mara ya pili inatoa picha ni kwa namna gani Abramovich alikuwa na nguvu ndani ya Russia kipindi kile.



    Kama ambavyo nimeeleza kwa msisitizo kwenye sehemu zote zilizopita… biashara aluminium ilikuwa ni sekta ya hatari mno kipindi kile nchini Russia. Maana yake ni kwamba mtu yeyote yule ambaye ameweza 'ku-survive' na kushamiri ndani ya biashara hiyo maana yake ni kwamba alikuwa ni mtu hatari zaidi. Hii ilikuwa inamaanisha kwamba Anatoly Bykov kama wenzake wengine wote, pia hata yeye alikuwa na madudu mengi sana ameyafanya ili kuweza kushamiri kwenye biashara hiyo. Na hii ndio ilikuwa silaha ya mwisho ya Abramovich.



    Sasa,



    Katika jimbo la Krasnoyarsk ambako Anatoly Bykov alikuwa anaishi, kutokana na utajiri mkubwa aliofanikiwa kuuchuma huku akiwa ni kijana wa umri mdogo tu, ilimfanya kuwa kama 'celebrity' kwenye mji wao. Vyombo vya habari vilikuwa havikauki ofisini kwake.

    Siku hiyo alikuwa anafanya mkutano na wanahabari ofisini kwake… kama kawaida pia kulikuwa na kundi la wananachi wakishangaa shangaa.

    Kufumba na kufumbua gari tano zikiwa na wanajeshi karibia thelathini wa 'special forces' ziliingia kwa ghafla kwenye eneo la ofisi. Kundi la wananchi waliokusanyika walitawanywa kwa risasi kupigwa juu hewani huku walinzi wa Bykov wakiwekwa chini ya ulinzi. Bykov akanyakuliwa mzobe mzobe kama kuku na kupakiwa kwenye gari na kuondoka naye.



    Jioni ya siku hiyo serikali ikatangaza kupitia vyombo vya habari kwamba wamemkamata Anatoly Bykov kwa shutuma ya makosa ya utekaji na mauaji.

    Nchi nzima ilizizima… sintofahamu ilitanda kila mtu akijiuliza kwa nini iwe Bykov pekee wakati ni suala linalofahamika wazi kabisa kwamba maoligarch wote wanaojihusha na sekta ya aluminium mikono yao imejaa damu za roho za watu.



    Wiki moja baadae Bykov alipandishwa kizimbani. Hati ya mashtaka ilisema kwamba anakabiliwa na kosa la "Kupanga njama ya kuua na utekaji". Kesi iliunguruma na kuteka vyombo vya habari.

    Ndani ya miezi miwili kesi ilikuwa imemalizwa kusikilizwa na mahakama ilimkuta Bykov na hatia na kumuhukumu kwenda jela miaka sita.



    Miaka sita… ilikuwa inatosha kabisa kwa Abramovich kufanya kile alichokusidia.



    Baada ya miezi mitatu tu kwa kutumia mwanya wa Bykov kuwa jela, Abramovich na Deripaska waliishawishi bodi ya wakurugenzi ya Krasnayorsk Aluminium Smelter kuwauzia kiasi kikubwa cha hisa ambacho kiliwafanya kuwa "majority share holders". Na mwanya huo wa wao kuwa wanahisa wakuu wa kampuni wakautumia kushinikiza uamuzi wa kampuni hiyo ya Krasnoyarsk kuuzwa kwa RUSAL.



    Lengo likatimia…



    Kwa akili ya haraka haraka tu suala kama hili haliwezekani likafanyika kwenye nchi za magharibi au hata hapa Afrika leo hii. Lakini hivyo ndivyo mambo yalivyoendeshwa kihuni nchini Rusia miaka ya tisini na mwanzo mwa 2000. Hiyo ndio maana hasa ya 'Wild Wild East.!"



    Hii ilikuwa ni mwezi July mwaka 2002. Ndio siku ambayo RUSAL ilipanda ngazi Rasmi kuwa kampuni inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa Aluminium. Utajiri wa Abramovich ukapaa kwa kasi ya ajabu. Na ndio hapa kwa mara ya kwanza jina lake likaanza kutajwa tajwa sana hata nje ya Russia.



    Ni wazi sasa kwamba Abramovich alikuwa ni Oligarch namba moja ndani ya Rusia. Mtu pekee ambaye alikuwa na nguvu ndani ya Russia kumzidi Abramovich alikuwa ni Putin pekee. Lakini hakukuwa na mwingine yeyote yule ambaye alikuwa ana hata nusu tu ya ushawishi ambao Abramovich alikuwa nao.



    Waswahili tuna msemo tunasema kwamba "mti wa riziki, ficho kivuli cha husda." Kwamba ukipata uwe makini maana kuna watu watahisi kupata kwako kunaziba riziki zao.



    Kitendo cha kijana aliyetoka familia masikini wa kutupwa. Kijana ambaye alikuwa anauza wanasesere. Kijana aliyeuza matairi chakavu leo hii kuwa mfanyabiashara mwenye ushawishi zaidi na si hivyo tu bali kuwa 'right hand man' wa Rais wa taifa la urusi kiliwaudhi baadhi ya maoligarch.

    Abramovich alikuwa anaogopwa pale Moscow na maoligarch waliudhika sana na kitendo hiki. Yaani kinyago walichokichonga wenyewe leo hii kinawatisha?



    Ajabu ni kwamba mpaka Berezovsky alichukia.

    Yes, Berezovsky mentor wa Abramovich naye alichukia… sijui kama ilikuwa ni wivu au vipi. Maana Abramovich sasa alikuwa na utajiri mkubwa maradufu zaidi ya Berezovsky. Yawezekana ni wivu, au labda ni woga… Berezovsky alikuwa amechukia haswa kitendo cha Abramovich kuwa Oligarch namba moja ndani ya Urusi na ushawishi wa kupitiliza alionao mtaani na ndani ya serikali.



    Vikakaliwa vikao vya siri vya maoligarch… wakafikia azimio. Azimio ambalo naamini maoligarch walioko hai mpaka sasa ambao walikuwepo kwenye kikao kile wanatamani hata kurejesha muda nyuma na kufanya azimio tofauti na lile.

    Walifikia uamuzi kwamba, kama ukomunisti uliweza kudondoka ndani ya Urusi, na kama juzi juzi tu hapo waliweza kushawishi kuondoka madarakani kwa Rais Boris Yeltsin… Je, huyu anayemkingia kifua Abramovich, anayemlea na kumpa meno ya kutafuna maoligarch wengine… huyu Putin.. Putin ni nani hata wasiweze kumng'oa ili wawe wamekimaliza kabisa kinyago chao walichokichonga, Abramovich, ambacho sasa chawatisha hata usingizi hawalali kwa raha??



    Kipindi hiki vita ya Chechenya ilikuwa ndio imepamba moto na Putin alikuwa anafanya ile tunaita "full scale war".

    Jamii ya kimataifa ilikuwa inapiga kelele kwamba Putin anavunja haki za binadamu na kufanya uhalifu wa kivita kutokana na ile vita ambayo alikuwa anaiendesha Chechenya.



    Tunakumbuka nilieleza kuwa ile televisheni ya taifa Perviy Kanal ambayo ndio yenye kutazamwa zaidi ndani ya Rusaia ni Berezovsky alibinafsishiwa kipindi kile na utawala wa Rais Yeltsin.



    Maoligarch waliompinga Abramovich mpango wao ukaanzia hapa.



    Televisheni ya Perviy Kanal ikaanza kuandaa makala na chambuzi kumkosoa Rais Vladmir Putin na mbinu na nguvu anazotumia kwenye vita ya Chechenya.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Tukumbuke kwamba vyombo hivi hivi vya habari ndivyo ambavyo vilitumika kufanya propaganda ya kuijenga 'image' ya Putin kwa wananchi kipindi kile alipochaguliwa na Rais Yeltsin kuwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo walidhani kwamba kama waliweza 'kumchonga' kwa vyombo vyao vya habari wanavyovimiliki basi wanaweza kumbomoa 'image' yake taratibu kwa umma na hatimaye kumuondoa madarakani.



    Was a big mistake…. Ni kweli wao walikuwa na vyombo vya habari, lakini mwenzao Putin alikuwa na kitu muhimu zaidi pembeni yake… Roman Abramovich.









    Mara ya mwisho nilieleza kuhusu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na maoligarch wakiongozwa na Berezovsky walinyoanza kumkosoa Putin kwa lengo la kumuharibia kwa wananchi na hatimaye iwe rahisi kwao kumuondoa madarakani. Baada ya ukosoaji huu Putin kwenye moja ya hotuba zake aliwaambia wananchi kwamba kuna ‘genge’ la maoligarch wanaomiliki vyombo vya habari wanaendesha kampeni ya kumchafua kwa malengo yao ya kisiasa.



    Unakumbuka nilieleza kwamba katika kipindi hiki Berezovsky alikuwa amejiingiza kwenye siasa. Alikuwa ni mwakilishi kwenye Bunge la Duma (GosDuma). Kwa hiyo madai haya ya Putin kwamba Berezovsky na wenzake wanamchafua kwa malengo ya kisiasa yalipata mashiko kwa sababu Berezovsky alikuwa ni mwanasiasa. Kwa hiyo wananchi waliona hii ilikuwa kama ni ‘move’ ya Berezovsky kuutaka urais wa Urusi. Wengi hawakupendezwa na hili maana walihisi huu haukuwa wakati sahihi kubadili Rais wa nchi kwa kuzingatia kwamba nchi ilikuwa kwenye mzozo mkubwa huko Chechenya na pia ulikuwa umepita muda mchache tu tangu kumbadilisha rais wa awali, Boris Yeltsin.



    Ajabu ni kwamba baada ya hotuba hii ya Putin, safari hii sio tu kwamba Berezovsky alitumia vyombo vyake vya habari kumpinga Putin bali aliitisha mkutano na wanahabari na kumkosoa Putin na sera zake wazi wazi.



    Putin na Abramovich hawakutaka kukurupuka kumshughulikia Berezovsky. Walikuwa na uwezo wa kutumia vyombo vya ulinzi kumkamata na kumtia gerezani Berezovsky lakini hii isingekuwa na ufanisi sana kwa sababu tatizo halikuwa Berezovsky peke yake bali ni yeye na genge lake. Na isingekuwa busara kuwakamata maoligarch wote na kuwatia gerezani kwani kutokana na ushawishi wao ingeweza kuzua taharuki kubwa kwenye nchi. Sasa wanafanyaje? Wamuache Berezovsky aendelee kutamba kwenye vyombo vya habari na kumchafua Rais?



    Hapana… nyoka akiingia ndani ya shimo usizame na wewe kumfuata… msubiri juu. Hawezi kukaa shimoni milele… msubiri atokeze kichwa juu… mfyeke na upanga.



    Usiwe na pupa,

    Subiri…





    Nilieleza kuhusu Badri Patarkatsishvili rafiki mkubwa wa Berezovsky ambaye alimletea Russia kusimamia Televisheni yake. Berezovsky na Badri walikuwa marafiki haswa lakini kulikuwa na mtu ambaye alikuwa rafiki mkubwa zaidi wa Berezovsky, rafiki wa kushibana haswa, rafiki wa damu haswa, mboni ya jicho kweli kweli ya Berezovsky. Huyu alikuwa anaitwa Nikolai Glushkov. Licha ya urafiki wao lakini pia walikuwa washirika wakubwa kwenye biashara.



    Sasa turudi nyuma kidogo,

    Pale Russia kuna shirika la ndege la umma linaitwa Aeroflot. Shirika hili ni moja ya mashirika kongwe zaidi ya ndege duniani. Mwaka 1995 Glushkov aliteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Aeroflot. Baada ya mwaka mmoaja tangu kuteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu kuna skandali kubwa aliibua japo haikufika kwa umma wakati ule lakini ilikuwa tafrani kubwa ndani ya ‘system’ ya serikali ya Russia.

    Kipindi hicho ndani ya shirika kulitokea mkanganyiko mkubwa sana juu ya mapato ya shirika na matumizi yake. Glushkov akajipa jukumu la kuchimba ni nini hasa kilikuwa kinaendelea. Baada ya uchunguzi wake wa miezi kadhaa akang’amua kwamba fedha zote za shirika ambazo zilikuwa zinapatikana kutokana na mauzo ya tiketi ya ndege zilikuwa zinapelekwa kwenye zaidi ya akaunti 352 zilizotawanyika sehemu mbalimbali duniani. Akaja kugundua kuwa akaunti hizi zilikuwa zinatumiwana mashirika ya Usalama ya FSB, SVR na GRU kw ajili ya kugharamia shughuli za ujasusi nje ya Russia. Nilieleza kuhusu FSB, hawa wanahusika hasa na Couter-Intelligence na usalama wa ndani ya Russia na mipakani. SVR hawa wanahusika hasa na ujasusi nje ya Russia. GRU wao kwa kifupi twaweza kusema ni kama chombo cha intelijensia ya jeshi.

    Glushkov akagundua kuwa pia waajiriwa 3,000 katiya waajiriwa wote 14,000 wa shirika la Aeroflot walikuwa ni mashushushu wa FSB, SVR na GRU.



    Glushkov akakasirika na kuwaandikia barua vyombo hivyo vyote vya ujasusi. Katika barua hiyo kwanza aliwalalamikia vyombo hivyo kutumia rasilimali vya Aeroflot kwa shughuli zao za ujasusi bila ruhusa ya bodi ya Aeroflot wenyewe. Pili, aliwapa ‘bili’, Kiasi chote cha hela ambao mashirika ya ujasusi yalipokea kutoka Aeroflot na kuwataka warejeshe kwenye shirika.



    Glushkov hakuishia hapo tu bali pia alihakikisha fedha zote ambazo zililipwa kwenye akaunti zile 352 ambazo zilikuwa bado hazijatolewa, utaratibu unafanyika akauti wakazi-freeze na kuhakikisha zinatolewa kwenye akaunti hizo. Makosa makubwa yalifanyika hapo…



    Unaweza kujiuliza Glushkov aliwezaje kufanya haya dhidi ya shirika la ujasusi kama FSB, SVR na GRU? Lakini tukumbuke kwamba hii ilikuwa ni mwaka 1996 kwenye utawala wa Yeltsin ambapo maoligarch ndio walikuwa ‘wenye nchi’. Glushkov alikuwa anaweza kujitutumua na kufanya yote haya kwa mgongo wa oligarch Boris Berezovsky rafiki yake wa damu wa kufa na kuzikana.



    Turudi tulipoishia…. Nyoka akiingia shimoni hatumfuati… tunasubiri atokeze kichwa nje tumfyeke.



    Baada ya Berezovsky kuendelea kumkosoa kwa kutumia vyombo vyake vya habari… Abramovich akaja na mkakati wa kumdhibiti.



    Abramovich akafukua kaburi skandali ile ya Nikolai Glushkov rafiki kipenzi wa Berezovsky. Jambo moja ambalo kipindi kile mwaka 1996 halikufuatiliwa kwa kina ilikuwa ni namna gani fedha zile zilizobakia kwenye akaunti 352 zilitolewa. Kwa sababu kipindi kile Abramovich alikuwa ni kipenzi pia cha Berezovsky kwa hiyo kuna siri nyingi alikuwa anazijua. Mojawapo ya siri hizi zilikuwa ni nini ambacho kilitokea kwenye fedha ambazo zilihamishwa kutoka kwenye akaunti zile 352.



    Fedha zili kwa maelekezo ya Glushkanov zilihamishwa kutoka kwenye akaunti zile 352 za idara za ujasusi na zote kuwekwa akaunti ya kampuni iliyosajiliwa nchini uswisi inayoitwa Andava. Kampuni hii ya Andava ilikuwa inamilikiwa na watu wawili, Nikolai Glushkov na Berezovsky. Kwa maana nyingine ni kwamba Nikolai Glushkov na Berezovsky walikuwa wamejichukulia fedha za kampuni ya umma ya Aeroflot ambazo zilikuwa zimelengwa zitumiwe na FSB, SVR na GRU.



    Hii ilikuwa silaha ya kwanza ya Abramvich kumshughulikia Berezovsky.



    Polisi walimkamata Glushkov na kumfungulia mashtaka ya ubadhirifu wa mali za umma. Siku chache baada ya Glushkov kukamatwa Berezovsky alikimbia Russia na kuomba ukimbizi wa kisiasa nchini Uingereza kwa maana alijua kuwa yeye pia alihusika kwenye kosa hilo ambalo Glushkov alishtakiwa nalo.



    Hii haikuwa muarobaini kamili wa kumshughulikia Berezovsky kwani japo alikimbilia Uingereza lakini bado alikuwa anamiliki kituo kile cha televisheni na kampuni nyingine kadhaa ambazo zilikuwa na ushawishi kiuchumi na kisiasa ndani ya Russia.



    Abramovich akapiga hatua ya pili ya mkakati wake na kusafiri moja kwa moja hadi Uingereza ambako Berezovsky alikuwa amekimbilia…













    Safari ya Abramovich kwenda London ilikuwa mahususi kwa ajili ya kwenda kuonana na mentor wake huyo wa zamani akiwa na maagizo kutoka juu kwa bwana mkubwa… Putin. Maagizo haya yalikuwa ‘straight’ bila kupiga piga chenga. Kwamba Berezovsky anafahamu kuwa hakuna mahala ambako anaweza kujificha na mkono wa Putin ukashindwa kumfikia. Kwa hiyo Putin alikuwa anampa sharti moja tu… kwamba Berezosky amuuzie Roman Abramovich kituo cha televsheni na akikubali kufanya hivyo Putin atamuacha aishi.

    Kituo hiki cha televisheni kilikuwa na thamani ya mabilioni ya dola lakini Abramovich alimuambia Berezosvky kwamba atakinunua kwa dola milioni 150 tu. Berezovsky akakataa.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Abramovich akarudi Russia kupeleka mrejesho kwa Putn kwamba Berezovsky amekataa. Putin akamtuma tena Abramovich kwenda London na ofa nyingine mpya.

    Safari hii alipokutana na Berezovsky alimueleza kwamba yeye mwenyewe yuko tayari kupandisha kidogo dau lake la kununua kituo cha televisheni na atampa dola milioni 175. Na si hivyo tu bali pia kama atakubali kumuuzia kituo hicho cha televisheni basi Putin atamuachia huru rafiki yake kipenzi Glushkov ambaye tayari alikuwa anatumikia kifungo jela.

    Kitendo cha kusikia kuwa rafiki yake kipenzi Glushkov ataachiwa huru, Berezovsky hakuwa na nguvu tena ya kukataa ofa ya Abramovich, akakubali kumuuzia kituo chake cha televisheni. Na huo ndio ukawa mwisho wa uhuru wa habari nchini Rusia mpaka leo hii maana kituo cha Berezovsky ndio kilikuwa na ushawishi zaidi nchini Russia. Na Abramovich baada tu ya kukinunua kutoka kwa Berezovsky alikikabidhi mikononi mwa Putin akitumie anavyotaka.



    Jambo baya zaidi ile ahadi yao ya kumuachia Glushkov hawakuitimiza. Glushkov akaendelea kusota jela. Kuna kipindi akawekewa mtego akiwa amepelekwa hospitali kutibiwa maaskari magereza wakamuacha chumbani peke yake na akataka kutoroka. Akakamatwa tena na kuongezewa kifungo. Maoligarch kadhaa nao wakakamatwa kwa tuhuma za kupanga njama ya kumtorosha Glushkov. Ule mtandao wa maoligarch uliokuwa unaongozwa na Berezosvky ambao ulikuwa unampiga vita Putin na Abramovich ukasambaratishwa wote. Maoligarch wengine waliosalia wakaelewa somo… ukitaka kusurvive kibiashara ndani ya Russia kuna mtu mmoja haupaswi kumgusa… Roman Abramovich.



    Nilikuwa natamani niishie hapa lakini kuna kionjo kidogo wacha nikisimulie pia ili uone uwezo wa Abramovich kucheza na ‘system’ ya dunia. Hata ‘wazungu’ wa magharibi amewahi kuwafanyia uhuni ambao hata sasa hawaamini macho yao.



    Pale ulaya wana benki yao, European Bank. Mwishoni mwa mwaka 1998 kuna benki ya kirusi inaitwa SBS Agro ilichukua mkobo wa hela nyingi sana, mabilioni ya Euro. Ikapita kama miaka miwili hivi pasipo SBS Agro kulipa deni lake. Baada ya kuona deni hilo halilipwi European Bank wakahitaji dhamana ya mkopo huo kutoka kwa SBS Agro. Kama dhamana, SBS Agro wali-plegde deni la dola milioni 14 ambalo wanadai kwa kampuni inaitwa RUNICOM S.A. ambayo imesajiliwa nchini Uswisi. Na hapa ndipo ambapo jina la Abramovich linatokea… kampuni hii ya RUBICOM S.A faida yake kubwa walikuwa wanaipata kwa kuuza mafuta ya kampuni ya Sibneft kwenye nchi za ulaya. Katika kipindi hiki pia benki ile ya SBS Agro ilitangaza kufilisika. Lakini European Bank hawakuwa na wasiwasi kwa sababu deni lao lilikuwa ‘guaranteed’ na RUNICOM S.A… sijui kama naeleweka sawasawa…



    Sasa basi,



    European Bank wakaanza kuwadai RUNICOM S.A. Wakadai sana bila mafanikio… ikabidi uitishwe uchunguzi kuangalia mali za kampuni ili wajue namna gani wanaweza kurudisha fedha zao. Katika uchunguzi wao huu mkazo mkubwa uliwekwa kwenye kuingalia biashara ya mafuta ambayo RUNICOM walikuwa wanaifanya kwa sababu nyaraka zilionyesha kwamba faida yao kubwa ilitoka huko. Hawakuamini macho yao walipogundua kuwa biashara ile ya mafuta ya Sibneft kama miezi sita iliyopita ilikuwa imehamishiwa kwenye kampuni nyingine iliyosajiliwa nchini Cyprus ikiitwa RUNICOM LIMITED.



    European Bank wakafura kweli kweli… hii ndio ile kwa umombo wanaita ‘sleight of hand’. Ushawahi kuona mchezo wa karata tatu… anazivuruga vuruga unahisi umeona sawia kuwa shupaza iko pale mkono wa kulia lakini akifunua unakuta kuna dume la kopa. Hii iliyokuwa inafanyika twaweza kusema ilikuwa ‘financial sleight of hand’… abracadabra.



    Kuna kitu gani ambacho kinafanana kwenye huu msululu wote? SBS Agro waliokopa awali ni kampuni ya kirusi (Roman Abramovich ni mrusi). Walio gurantee huo mkopo RUNICOM S.A faida yao kubwa walikuwa wanaipata kwa kuuza mafuta ya sibneft kwenye nchi za ulaya (Roman Abramovich ndiye mmiliki wa Sibneft). RUNICOM LIMITED walirithishwa biashara ya mafuta ya sibneft kutoka RUNICOM S.A (Sibneft… Abramovich).



    European Bank wakafura zaidi… ilikuwa wazi kwamba ujanja huu walikuwa wanafanyiwa na Roman Abramovich lakini ubaya ni kwamba huwezi kumshtaki kwa kuwa siye uliyemkopesha… walimkopesha nani? SBS Agro… European Bank wakaenda mhakamani. Kesi ikaunguruma kwa miaka miwili. Hukumu ikatolewa kwamba European Bank walipwe kiasi cha dola milioni 24. Lakini nani akulipe?? SBS Agro walishatangaza kufilisika miaka miwili iliyopita na kampuni haipo tena… nani atakulipa hela hizo? Mpaka leo hii ninapoandika makala hii deni hilli halijalipwa na kamwe halitolipwa na ubaya ni kwamba muhusika mkuu na aliyenufaika na mkopo unamjua lakini huwezi kumshitaki kwa sababu hakuna jina lake halijatokea popote kwenye nyaraka na wala hukumkopesha. Tangu kipindi hicho wazungu wanalijua vyema jina la Abramovich na ni mtu wa namna gani.



    Kuna watu ukiwasimulia upande huu wa pili wa Abramovich ambao hawajawahi kuusikia watakwambia kuhusu miradi mikubwa ya kijamii ambayo aliifanya akiwa kama gavana wa Chukokta. Jibu langu siku zote ni kweli kwamba Abramovich alitumia fedha zake binafsi karibia dola blioni 3 kwa muda wote aliokuwa gavana wa Chukokta… lakini je unafahamu alinufaikaje?

    Baada ya Putin kuwa Rais akampa Baraka Abramovich kuingia kwenye siaisa. Ukitoka pale Kremlin, mwendo wa ndege kama masaa tisa hivi kuna jimbo masikini mno mno linaitwa Chukokta. Hili ndilo ambalo Abramovich aligombea ugavana na kushinda. Alitumia mabilioni ya hela zake kwa ajili ya maendeleo lakini wengi wasichojua ni kwamba alinufaika zaidi. Akiwa kama gavana alikuwa anashawishi sheria ndogo za kodi na misamaha ya kodi kwa kampuni wanazoziona zinafaa. Sasa ile kampuni yake ya Sibneft visima vyake vya mafuta viko Siberia. Walichokuwa wanafanya walikuwa wanauza mafuta yao ya Sibneft kwa bei ya kutupa kwa kampuni ambazo walizisajili kwenye jimbo la Chukokta. Kisha kampuni hizi za Chukokta wanauza mafuta hayo nje ya Russia kwa kampuni dada ya Sibneft kama vile RUNICOM S.A. na walifanya hivi kwa kuwa mafuta haya yakitokea Chukokta yalikuwa na msamaha wa kodi.



    Kwa hiyo ni kweli Abramovich alikuwa anasadia lakini papo papo alikuwa ananufaika zaidi.





    Wale ‘maswahiba’ wake wa zamani wako wapi?



    Mentor wake Boris Berezovsky ambaye alikuja kuwa adui mkubwa siku ya March 23 mwaka 2013 alikutwa amefariki bafuni nyumbani kwake Barkshire, Uingereza. Kifo chake bado kina ubishani mkubwa baadhi ya wachunguzi wa masuala ya post mortem wakisema amejiua wengine wakisema ameuwawa. Wengine wanadai alijiua baada ya kuandamwa na madeni kutokana na kushindwa kesi ambayo alimfungulia Abramovich kugombea umiliki wa Sibneft akitaka kulipwa fidia ya dola bilioni 6 kesi ambayo ilisikilizwa nchini Uingereza na Abramovich kushinda. Hili suala la kugombea Sibneft sijalieleza humu… ila kwa kifupi tu Abramovich alimpiga mchanga wa macho mentor wake… unakumbuka nilieleza kwamba enzi zile za utawala wa Yeltsin Abramovich na Berezovsky walinunua kwa pamoja Sibneft kwenye mnada wa ulaghai ambao wao pekee ndio walikuwa ‘bidders’. Nadhani tunakumbuka vyema… sasa baada ya Berezovsky kukimbia Urusi, Abramovich akafanya janja janja na kumuondoa Berezovsky kwenye umiliki. Berezosvky akafungua kesi.



    Abramovich alishinda kesi.



    Wanadai kwamba kesi ile ilimfilisi Berezovsky kwa kulipa gharama kubwa za mawakili.



    Lakini tukitazama nyuma kidogo tuna pata picha ya tofauti na pengine kutupa dalili kuwa Berezovsky aliuwawa. Novemba mwaka 2006 mshirika wake wa karibu sana Alexander Litvinenko aliuwawa kwa Polonium hapo hapo Uingereza.

    Miaka miwili baadae yule rafiki yake Badri ambaye kipindi wako Russia alikuwa anasimamia televisheni yake alikutwa amefariki chumbani kwake hapo hapo Uingereza.

    Kama hiyo haitoshi yule rafiki yake kipenzi Nikolai Glushkov alimaliza vifungo vyake na kutoka jela na kukimbilia nchini Uingereza. Huyu naye mwaka jana tu hapa 2018 mwezi March amekutwa amefariki nyumbani kwake hapo hapo Uingereza.



    Kwa hiyo maoligarch wote ambao walianzisha vita dhidi ya Putin na Abramovich wote wamefariki vifo vya utata wakiwa na afya njema kabisa… lakini wale wote ambao walikuwa wapole na kumuunga mkono Abramovich kama vile akina Deripaska wako hai hata sasa na utajiri wao ukizidi kupaa kila uchwao.



    Mwanzoni mwa makala hii nilijenga hoja kwamba si jambo jepesi sana kuwa bilionea. Unaweza kuwa tajiri… milionea, hakuna shida wala shaka. Lakini kutengeneza utajiri wa kufikia dola bilioni moja na zaidi ni lazima ukubali mikono yako kuchafuka ‘vumbi’ kidogo. Muulize Mo Dewji, msome Gates na alichowafanyia IBM na Steve, chunguza vifo vilivyotokea mwanzoni kwa kuanzishwa kwa Facebook na alichokifanya Mark, muulize Aliko Dangote, teta na akina Motsepe na familia ya Gupta pale Afrika Kusini.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Wote hawa hawawezi kukataa kwamba “behind every great fortune lies a great crime.” Kila utajiri una ukafiri nyuma yake.











    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog