Search This Blog

Sunday 20 November 2022

TAXI - 2

 





    Simulizi : Taxi

    Sehemu Ya Pili (2)





    “Oh… Madame Norah! Samahani mama’angu, kwa kweli sikutegemea kabisa kupata simu yako…” Joyce alisema huku akibabaika kidogo.







    “Ooh… usijali,” Madame Norah alijibu, na papo hapo akauliza, “Kesho Jumapili utakuwa na ratiba gani?”



    “Kesho muda gani?” Joyce aliuliza kwa shauku kubwa.



    “Jioni.”



    “Nitakuwepo tu nyumbani, sina pa kwenda.”



    “Naomba uje ofisini kwangu Mikocheni tuongee, japo maongezi yangu yanaweza yasiwe matamu kama ya mumeo! Au wasemaje?” Madame Norah alisema kwa madaha na kuachia kicheko hafifu.



    “Sawa tu nitafika muda huo, sijui saa ngapi?” Joyce aliuliza huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Saa kumi na mbili…” Madame Norah alisema na kuongeza, “See you at that time.”



    “Okay, Madame!” Joyce alisema huku akipitisha ulimi wake kwenye mdomo wake ulioanza kukauka, na hapo simu ikakatwa. Joyce hakuamini, alibaki akiitazama simu yake huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu bashasha. Alionekana kuwa na furaha isiyo kifani.



    Kisha alijiegemeza kwenye sofa huku akiendelea kutabasamu, na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Muda huo kipindi cha “Madame Norah Show” kilichokuwa kinaendeshwa na Madam Norah mwenyewe kilikuwa kinarushwa kwenye runinga, Joyce alichukua rimoti ya runinga akaongeza sauti.



    Muda wote tabasamu lake lilikataa kwenda likizo, alimwangalia Madame Norah kwenye runinga kwa makini sana na kuonekana kuvutiwa naye. Pendo alikuwa ameketi kwenye sofa jirani na mama yake akifuatilia kwa makini kila kilichokuwa kinaendelea pale sebuleni. Hakusema neno bali alikuwa anamwangalia mama yake kwa makini.



    Winifrida aliingia pale sebuleni akitokea jikoni na kuketi juu ya mkono wa sofa huku akimwangalia Joyce kwa makini, kisha akaguna.



    “Wifi, mbona umefurahi sana, inaonekana unampenda sana Madam Norah!” alisema Winifrida.



    “Madame Norah ni mfano mzuri wa mwanamke mjasiriamali… natamani sana kufikia mafanikio kama yake,” alisema Joyce huku akishusha pumzi ndefu.



    “Mama, kwani na wewe unataka kuwa kama Madam Norah?” Pendo alimwuliza mama yake huku akimkazia macho kwa makini.



    “Ndiyo mwanangu, natamani sana na ninaamini Mungu atanisaidia.”



    “Kwa hiyo na wewe utamwacha baba yangu?” Pendo alimwuliza tena Joyce na kumfanya amtazame kwa mshangao.



    “Kwa nini nimwache baba yako? Kwani haya maneno huwa unayapata wapi we mtoto!” Joyce alimwuliza pendo huku akiendelea kumtazama kwa mshangao.



    “Si wanasema Madam Norah hataki wanaume!” Pendo alisema kwa kujiamini na kuwafanya wote wamkodolee macho kwa mshangao. Winifrida aliziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono.



    “We mtoto wewe… ni nani kakwambia maneno haya?” Joyce aliuliza huku mshangao ukiwa bado haujamtoka usoni kwake. Winifrida aliachia kicheko hafifu na kumfanya Pendo naye acheke.



    “Watu wanasema, hata anti Winnie alikuwa anasema…” Pendo alisema huku akinyoosha kidole chake kumuonesha Winifrida.



    “Aka! Lini mimi nimekwambia? Utakuja kusutwa we mtoto!” Winifrida alimkata kauli Pendo na kumruka huku akiinuka na kubetua mabega yake juu. Joyce aliguna tu na wala hakujua la kufanya wala kusema.



    * * * * *



    Sammy alikuwa ameketi kwenye kiti kifupi chenye foronya laini ndani ya mgahawa mkubwa wa kisasa wenye kuta safi za vioo, uliokuwa ukimilikiwa na rafiki yake, Elli Kiango, na juu ya meza ya mbao ya mti wa mpodo kulikuwa na chupa kubwa ya maji baridi ya Kilimanjaro na bilauri ndefu.



    Nje ya ule mgahawa kulikuwa na bango kubwa jeupe juu yake lililokuwa na maandishi makubwa ya rangi nyekundu yakisomeka ‘ELLI’S’. Pia kulikuwa na eneo la maegesho ya magari na kulikuwa na takriban sabini yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari na mengi yalikuwa ya watu wenye vipato vya juu.



    Elli’s ulikuwa mgahawa wa kisasa kabisa wenye kila aina ya vionjo vya daraja la kimataifa, ukifananishwa na migahawa mikubwa duniani kama McDonald; Royal Dragon; West Lake ulioko Mji wa Changsha, China; Varsity Downtown wa Atlanta, Georgia; Lundy’s wa Brooklyn, Newyork; Cosmo wa Croydon, Uingereza n.k.



    Kutokana na umaarufu wa mgahawa huo, Elli’s ulikuwa na uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 2,000 kwa siku na uliajiri wafanyakazi zaidi ya 200 waliotoa huduma mbalimbali katika mgahawa huo.



    Mgahawa huo ulikuwa na mandhari yenye ubora iliyowafanya wageni wengi kuingia kwa wingi na kujionea mandhari yake na vivutio vilivyopo kwenye mgahawa huo.



    Pia ukubwa wa majengo yake yaliyotengenezwa kwa ustadi wa hali juu yakiambatana na nakshi zilizochorwa na kutengenezwa kwa ustadi zikiashiria mila na tamaduni za makabila yaliyopo Tanzania ndiyo sababu zilizowafanya watu wengi pamoja na wageni mbalimbali kutembelea mgahawa wa Elli’s.



    Ulikuwa na ukumbi maalumu mkubwa wa vyakula mbalimbali (dining hall) vya watu wa mataifa tofauti uliokuwa na utulivu wa kutosha, ukiwa na meza ndefu za kisasa zilizozungukwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini. Ukumbi huo ulikuwa na uwezo wa kubeba takriban watu 500, ambapo wateja walikaa kwa vipindi fulani (shifting zone).



    Pia kulikuwa na ukumbi mwingine mkubwa wa kisasa uliotumika kwa ajili ya burudani au mikutano mbalimbali, ukumbi ule ulikuwa na jukwaa zuri la kisasa lililokuwa likitazamana na viti vingi vya kisasa na ulikuwa na uwezo wa kuingiza watu wasiopungua 1,000 kwa wakati mmoja bila bugudha yoyote.



    Huduma ya mtandao wa intaneti ya WiFi (Wireless Fidelity) haikukosekana ndani ya ukumbi ule, hasa kwa mtu mwenye kifaa kilichoweza kunasa taarifa za kimtandao wa intaneti, kama simu za kisasa za mkononi, kompyuta na kadhalika.



    Muda ule wa mchana kulikuwa na sauti ya muziki laini wa taratibu iliyosikika kutoka katika spika zilizokuwa sehemu fulani ndani ya ule mgahawa na kuzikonga vizuri nyoyo za watu waliofika kwa ajili ya chakula, vinywaji au huduma zingine muhimu.







    Ndani ya ule mgahawa kulikuwa na wahudumu wa kike warembo kwelikweli waliokuwa wakihudumia wateja. Wahudumu wale walikuwa wamevaa sare za kazi, sketi fupi nyeusi zilizoishia juu ya magoti, makoti ya suti ya rangi nyeupe yenye kola nyeusi na kofia nyeusi kichwani, na walikuwa na nyuso zilizopambwa na tabasamu la kirafiki muda wote.



    Ukumbi ule wa chakula na vinywaji ulikuwa na meza nyingi ndogo fupi na pana zilizozungukwa na viti vifupi vyenye sofa laini, na muda ule wa mchana kulikuwa na watu wasiopungua mia moja walioketi kwa utulivu kwenye viti vyao huku wakijipatia chakula na vinywaji, wengi wao wakiwa Wazungu na Waasia.



    Sammy alikuwa ameketi kwenye kile kiti kifupi chenye foronya laini kwa utulivu mno akionekana kuwa mbali kimawazo, muda ule ule mwanamume mmoja mrefu na mwenye mwili uliojengeka kwa mazoezi, alifika pale na kuketi kwenye kiti kingine kifupi chenye foronya laini kilichokuwa mkabala na kile alichoketi Sammy.



    Mwanamume yule mcheshi na mwenye macho ya upole alikuwa amevaa suti nadhifu ya rangi ya kijivu ya ‘single button’ na shati jeusi lililomkaa vyema na kumpendeza. Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi vya ngozi kutoka Italia na mkononi alivaa saa aina ya Rolex Submariner.



    Aliitwa Elli Kiango na alikuwa rika moja na Sammy, huyo ndiye aliyekuwa mmiliki wa ule mgahawa wa kisasa. Yeye na Sammy walifahamiana tangu utoto wao, walikuwa ni zaidi ya marafiki, walikuwa ni ndugu hasa.



    Wakati Sammy alikuwa msomi wa ngazi ya Uzamili aliyesomea biashara ya kimataifa na lugha (M.A. in International Business With Languages), Elli pia alikuwa msomi wa ngazi ya Uzamili aliyesomea Uongozi wa Biashara (M.A. in Business Administration).



    Tofauti kubwa kati yao ilikuwa katika misimamo, wakati Sammy alikubali kuajiriwa, Elli hakupenda kabisa kuajiriwa na aliona kuwa elimu yake ingemletea mafanikio makubwa akiamini katika falsafa kuwa: ‘huwezi kutimiza ndoto yako kama utakuwa chini ya mtu mwingine, ukimfanyia kazi na yeye akikupangia na kukulipa mshahara’.



    Elli alipoketi kwenye kiti aliweka miguu yake juu ya kiti kingine kilichokuwa mbele yake, akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akimtazama Sammy kwa makini kwenye jicho lake la kushoto lililokuwa na jeraha. Sammy alijaribu kuyakwepa macho ya Elli kwa kutazama kando huku akiilamba midomo yake.



    “Samahani kuna mambo yalinitinga kidogo nikalazimika kukuacha peke yako, I hope you are not bored,” Elli alisema huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti.



    “I’m not bored at all,” Sammy alisema huku akiachia tabasamu na kutazama kando. Kilipita kitambo fulani cha ukimya kila mmoja akionekana kutafakari.



    “Kama ulivyoniambia, bado sioni mantiki ya wewe kusimamishwa kazi kwa utovu wa nidhamu, mbona kama hainiingii akilini! Au kuna kitu wewe na bosi wako mmepishana au kuchukuliana?” Elli alivunja ukimya huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Sammy na kumtazama kwa makini.



    “Wala hatujapishana au kuchukuliana chochote, yeye tu na roho yake!” Sammy alisema na kushusha pumzi. Usoni wake haukuonesha tashwishwi yoyote na badala yake alikaa kimya akiupisha utulivu kama afikiriaye jambo fulani.



    Jibu lile lilimfanya Elli amtazame Sammy kwa mshangao kisha akamuuliza kwa sauti tulivu, “Inaonesha kama kuna jambo fulani unalijua ila hutaki kuniambia, don’t you trust me?”



    “Kwani lini nimewahi kukuficha jambo, ndugu yangu?” Sammy naye aliuliza huku akimkazia macho.



    “Sikumbuki… lakini niseme tu ukweli nilishtushwa sana pale mkeo aliponipigia simu asubuhi kunieleza kuwa ulirudishwa nyumbani usiku wa saa 7 ukiwa umebebwa kwenye mkokoteni chakari hujitambui,” Elli alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Sammy hakusema neno, alibaki kimya akiwa ameinamisha uso wake akiangalia chini kwa fadhaa, ni wazi alionekana kuwa na huzuni.



    “Anasema ulipoingia ndani ukaiangukia meza ndogo ya kioo na kuivunja, kisha ukatapika kwenye korido na ulipotaka kukimbilia kwenye mlango ukabamiza jicho… mkeo akakuburuza kukupeleka chumba cha kulala, na alipoanza kukuvua nguo ukapiga kelele ‘niache, mi nimeoa’,” Elli alisema na kuangua kicheko hafifu.



    Sammy alitamani kucheka lakini alionekana kujizuia na kuangalia kando kwa aibu. Alishusha punzi za ndani kwa ndani na kukunja sura yake akijaribu kukumbuka, hata hivyo hakuonekana kukumbuka chochote.



    “By the way… sidhani kama kulewa ni suluhisho la matatizo yako, unatakiwa kuyakubali matokeo na uwe tayari kwa chochote, kwa sababu kilichotokea siyo mwisho wa dunia,” Elli alisema na kumwita mhudumu mmoja mrembo sana aliyekuwa akipita eneo lile.



    “Hamisa, naomba uniletee juice ya avocado,” Elli alimwambia yule mhudumu ambaye aliitikia kwa kubetua kichwa chake huku akitabasamu, kisha akageuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile huku mtikisiko wa mzigo wa makalio yake ukiwafanya wateja kugeuza shingo zao kumtazama kwa matamanio.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Baada ya yule mhudumu kuondoka Sammy alishusha pumzi za ndani kwa ndani. “Kwa kweli nipo njia panda,” alisema kwa huzuni.



    “Nadhani sasa utakuwa umepata funzo, usikubali tena kuwafanyia kazi watu wasioona umuhimu wa wengine, bali wanachojali wao ni kutengeneza fedha tu na kutunisha mifuko yao,” Elli alisema kwa msisitizo na kuongeza.



    “Kwa nini usifikirie kuanzisha kampuni ya kukodisha magari, a car rental… naamini unao uzoefu wa kutosha kwa kuwa uliwahi kufanya kazi ya kutembeza watalii kabla hujafanya kazi katika hoteli.”



    “Ninatamani sana kumiliki kampuni yangu tatizo fedha ninayoitegemea haitatosha.”



    “Si lazima kuanza na magari mengi, hata moja au mawili yanatosha na utakuwa unaongeza kadiri biashara inavyochanganya… tafuta gari zuri na lenye utofauti ili kukabili ushindani,” alisema Elli na kumfanya Sammy ashushe pumzi huku akionekana kukosa uthubutu. Alitazama kando akionekana kufikiria jambo kwa kitambo fulani.





    “Itakuwaje iwapo nitatumia akiba yangu yote na mambo yasiende vyema?” Sammy aliuliza.



    “Tatizo lako kwa kuwa umesomea biashara ya kimataifa basi unafikiria kimataifa badala ya kufikiria huku chini, wewe amua mimi nipo nitakusaidia kusajili kampuni, unajua inapendeza zaidi kufanya kazi unayoipenda, ambayo wewe mwenyewe ndiye bosi,” Elli alisema huku akimtazama Sammy kwa makini na kutabasamu.



    “I’m still in dilemma, nahisi nnaweza kupoteza thamani kwa familia yangu pindi ikibainika kuwa nimepoteza kazi, japo nina ndoa thabiti, lakini hali hii inaweza kubadili kila kitu kwenye uhusiano wetu,” Sammy alisema kwa wasiwasi.



    “Mwambie Joyce ukweli na umdokeze kuhusu wazo la kuanzisha kampuni,” Elli alimwambia Sammy na kuongeza, “Ila tafuta njia nzuri ya kumweleza na umpe nafasi aongee ili usikie mawazo yake.”



    “Mmh!” Sammy aliguna huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, akaminya midomo yake.



    “Kuambiana ukweli ni muhimu sana katika kuijenga familia…”



    “Nakubaliana kabisa na wewe, ukweli ni mzuri lakini si kwa mwanamume kumwambia mwanamke kuwa amesimamishwa kazi eti kwa madai ya utovu wa nidhamu!” alidakia Sammy.



    “Unadhani utaendelea kumficha hadi lini? Huoni kama siku akigundua mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi?” Elli alijaribu kumtahadharisha Sammy.



    “Ndiyo hapo sasa! Nadhani natakiwa kukubaliana na wewe na nimweleze tu ukweli, tena nitamweleza leo hii hii.”



    “Fanya hivyo, mara nyingi ili kushinda vita ni lazima ukubali ukweli, usahau yaliyopita na uyaishi yaliyopo,” Elli alishauri na kumfanya Sammy kubetua kichwa chake huku akiachia tabasamu.



    “Nitazame mimi, nilikataa utumwa wa kuajiriwa na kuamua kufungua biashara yangu mwenyewe kwa sababu sipendi kutumika kumuingizia mtu mwingine fedha nyingi ili anilipe mshahara,” Elli alisema na kuongeza, “Pia ninapenda nifanye kitu ninachokipenda na niwe bosi wa kazi yangu mwenyewe.”



    Japo Sammy alikuwa bado ana wasiwasi lakini alianza kupata matumaini kwa mbali, sasa shauku ya kuanzisha biashara yake ilijionesha waziwazi usoni kwake, alinyanyua uso wake kuangalia juu kwa kitambo akitafakari sana kuhusu hatma yake, kisha alishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    * * * * *



    Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kilikuwa na pilika pilika nyingi sana jioni hiyo, kulikuwa na hali ya mawingu kiasi. Watu mbalimbali walikuwa katika pilika pilika za kusafiri au kupokea wageni wao kutoka ndani na nje ya nchi.



    Gari la kifahari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi, mali ya Mr. Oduya lililokuwa likiendeshwa na Madjid Chege liliwasili katika kiwanja hicho cha ndege saa 10:30 za jioni, likaelekea katika kituo namba tatu (terminal III) cha kiwanja cha ndege.



    Mr. Oduya alikuwa ameketi kwa utulivu ndani ya lile gari na alikuwa amekuja kumpokea mgeni wake binafsi na muhimu sana, mwanadada Zainab Semaya, hiyo ilikuwa nusu saa kabla ya mgeni huyo kuwasili na ndege ya shirika la ndege la Ujerumani la Lufthansa.



    Mipango yote ilikuwa imepangwa kwamba mgeni huyo akiwasili tu katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere apelekwe moja kwa moja Paradise Club alikotakiwa kufikia, kabla wafukunyuku wenye kufuatilia mambo yasiyowahusu hawajamtia machoni.



    Madjid Chege, dereva wa Mr. oduya aliyedumu naye kwa miaka kumi na mbili sasa, aliliegesha lile gari kwenye eneo maalumu la maegesho ya magari la kile kituo namba 3 cha JNIA, kituo kilichokuwa na uwezo wa kuruhusu ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja na abiria milioni 6 kwa mwaka kikiwa na mandhari ya kupendeza, yaliyomvutia kila aliyefika pale kwa mpangilio wake mzuri.



    Mr. Oduya aliangaza macho yake huku na kule akionekana kutafuta kitu kisha alitoa simu yake lakini kabla hajapiga alimuona Mafuru akielekea pale walipoegesha gari lao. Kumbe muda wote Mafuru alikuwa ameliona gari la Mr. Oduya tangu lilipokuwa likiingia pale kiwanjani.



    Waliongea kwa dakika chache, kisha Mafuru aliondoka haraka akimwacha Mr. Oduya ndani ya gari, akavuta hatu zake kuelekea ndani ya lile jengo la kituo namba 3, hasa katika eneo la kusubiria wageni. Akajichanganya na watu waliokuwa katika eneo hilo wakisubiri ndugu na jamaa zao.



    Muda wote Mr. Oduya alionekana kuwa na wasiwasi, alijiegemeza kwenye siti yake na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha alifumba macho na kuanza kutafakari.



    Ingawa hakupenda kabisa Zainab aje Tanzania lakini hakuwa na namna nyingine ya kumzuia, alihofia kuwa endapo wapinzani wake kisiasa wangejua kuhusu uhusiano wake na Zainab na ujio wa Zainab nchini wangeweza kutumia kama silaha ya kumharibia katika harakati zake za kutaka kuwa Rais wa Tanzania, nafasi aliyoitamani kwa miaka mingi.



    Zainab alikuwa ameng’ang’ania kuja jijini Dar es Salaam na kama Mr. Oduya angekataa basi angetakiwa yeye aende nchini Canada alikoishi Zainab na watoto wake wawili, Jasmine na Latifah. Ilikuwa imeshapita takriban mwaka mmoja na ushee bila Mr. Oduya kwenda nchini Canada kuwaona, japo walikuwa wanawasiliana kwa simu na njia ya skype takriban kila siku.



    Mr. Oduya alishindwa kwenda Canada kwa kuwa alikuwa kwenye harakati za kuweka mambo yake sawa kabla ya pazia la kampeni za uchaguzi halijafunguliwa, hivyo hakuwa na namna nyingine isipokuwa kukubali kwa shingo upande Zainab aje ili asimuudhi, lakini kwa sharti kuwa safari hiyo iwe ya siri sana na asije na watoto, pia asikae muda mrefu arudi Canada.



    Zainab na Mr. Oduya wamekuwa na uhusiano wa siri na mapenzi yao waliyafanya kuwa ya siri sana kwa zaidi ya miaka kumi na miwili, Mr. Oduya alikuwa amempora Zainab kutoka kwa mumewe, Hemed Kimaro, aliyekuwa mfanyabiashara wa madini.







    Hemed alikuwa shemeji wa Mr. Oduya, kwani alikuwa ndugu wa tumbo moja na Dk. Salma K. Oduya, mke wa Mr. Oduya. Ilitokea wakati ndoa yao ikiwa katika mgogoro ndipo Mr. Oduya alipopata mwanya huo kumshawishi Zainab kwa kila njia ikiwemo kumpa fedha nyingi ambazo hakuwahi kuota kuzipata. Hatimaye waliingia kwenye uhusiano wa mapenzi.



    Kabla, Zainab alikuwa mwanamke mtulivu na mwaminifu sana kwa mumewe licha ya urembo na upole wake, lakini Hemed alikuwa ‘bize’ na biashara zake na muda mwingi aliutumia kusafiri huku na huko au kuwa na washirika wake wa kibiashara, jambo lililosababisha mgogoro wa mara kwa mara kwenye ndoa yake.



    Kabla ya uhusiano na Zainab, Mr. Oduya alishakuwa na uhusiano na wanawake kadhaa warembo akitumai kupata faraja aliyoikosa kutoka kwa mkewe Dk. Oduya, ambaye alikuwa ana gubu na alijaa kisirani. Ilifika kipindi Mr. Oduya alijilaumu kwa nini alimwoa.



    Kwa Zainab alijikuta akiweka kituo, na wote wawili (Zainab na Oduya) walijikuta wakihitaji faraja nje ya ndoa zao, ndiyo maana mapenzi yao ya siri yalichipua na kumea kama mche kwenye udongo wenye rutuba, japo kulikuwa na tofauti kubwa ya umri kati yao.



    Mr. Oduya alikuwa akimpatia Zainab chochote alichokitaka ikiwemo kumnunulia kwa siri jumba la kifahari eneo la Kijitonyama na penzi lao kukua kwa kasi mithili ya moto mkali ulao nyika.



    Kwa kuwa Zainab hakuwahi kuwa na uhusiano mwingine wowote wa kimapenzi kabla na hata baada ya ndoa yake, hivyo alijikuta akilivamia penzi la ‘shuga dadi’ kwa miguu yote miwili, alikuwa ni kama aliyepatwa na wazimu wa mapenzi na pepo la uzinzi lilikuwa limeingia kazini.



    Hatimaye Hemed alianza kuzishtukia nyendo za mkewe, alianza kuhisi kuwa mkewe alikuwa akiisaliti ndoa yake na mwanamume mwingine, ingawa hakujua ni mwanamume gani. Aliumia sana na kuanza kufuatilia, siku moja alirudi ghafla nyumbani usiku na kumfumania Zainab akiwa na Mr. Oduya kitandani, akaishiwa nguvu na kupoteza fahamu.



    Mr. Oduya alihofia mambo hayo kumfikia mkewe, isitoshe Zainab alishakuwa na ujauzito. Kesho yake asubuhi mwili wa Hemed ulikutwa kwenye mtaro wa maji machafu nyuma ya nyumba yake ukiwa umetapakaa damu baada ya kuchakazwa risasi tatu kifuani...



    “Naona ndege ndiyo inaingia,” sauti ya Chege ilimzindua Mr. Oduya kutoka kwenye mawazo. Alichungulia dirishani na kuiona ndege kubwa ya shirika la ndege la Lufthansa ikishuka taratibu katika Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.



    Mawazo yalikuwa yamemteka Mr. Oduya, alikwishaanza kuchoka kuishi mbali na Zainab na aliazimia kuwa baada ya kushinda uchaguzi na kuwa Rais wa nchi, asingeendelea kuficha bali angefanya kila njia, hata ikibidi kusababisha kifo cha mkewe ili Zainab awe mkewe rasmi ‘first lady’.



    Aliamini kuwa mambo yalikwisha isha kwani miaka mingi ilikwishapita tangu mauaji ya mumewe Hemed Kimaro na baadaye jaji aliyekuwa kimbelembele katika ile kesi kabla hajapandishwa cheo kuwa jaji mkuu, Sylvester Lutego. Hata hivyo alikuwa na uhakika faili la kesi ya mauaji ya Hemed halikuwepo tena, kwani waliliteketeza kwa moto na hakukuwa na kumbukumbu zozote zilizoachwa...



    _____



    Saa kumi na moja kamili, ndege kubwa ya shirika la ndege la Lufthansa ilikuwa ikikimbia kwa kasi kwenye barabara ndefu ya lami maarufu kama ‘runway’ iliyokuwa imewekwa alama elekezi za kuwaongoza marubani wa ndege, katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.



    Baada ya muda ilipunguza mwendo na kugeuza, kisha ikaingia katika barabara nyingine ya lami ambayo pia ilikuwa imechorwa alama elekezi za kuwaongoza marubani wa ndege kisha aliingia kwenye maegesho tayari kwa kuteremsha abiria waliokuwa wameabiri katika shirika hilo.



    Muda mfupi baada ya ile ndege kusimama na abiria kuruhusiwa kufungua mikanda ya siti zao milango ya ndege ikafunguliwa na ngazi zikiwekwa sawa, abiria walikuwa katika foleni ya kushuka. Mmoja wa abiria wale aliitwa Zainab Semaya.



    Zainab alikuwa mwanamama mrembo kwelikweli, alikuwa na umri wa miaka therathini na nane, mrefu na mweupe kiasi mwenye umbo la kuvutia, nywele ndefu na laini alizokuwa amezifunika kwa kofia ya kapelo na alivaa miwani mikubwa myeusi iliyoyaficha vyema macho yake makubwa ya kike yenye ulegevu.



    Sura yake ilikuwa ndefu kiasi, midomo laini yenye kingo pana kiasi zilizopakwa rangi nzuri ya mdomo ya chocolate, pua yake ilikuwa ndefu na vishimo vidogo mashavuni mwake viliwafanya wanaume wababaike kila walipomtazama.



    Alivaa suruali nyeusi ya jeans, iliyoshikiliwa na kiuno chembamba kiasi mithili ya dondola lakini imara kilichoshikilia minofu laini ya mapaja yake yaliyonona, fulana nyepesi nyekundu iliyoyaficha vyema matiti yenye ukubwa wa wastani na juu yake alivaa jaketi jeusi la jeans. Miguuni alivaa raba ngumu za rangi nyekundu.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Baada ya taratibu zote za uhamiaji hatimaye alishika uelekeo wa upande wa kulia akifuatana na abiria wengine, wakaifuata korido ndefu iliyokuwa ikipakana na ofisi mbalimbali za utawala wa kile kituo namba 3, na kutokea eneo maalumu la kuchukulia mizigo yao iliyokuwa ikipita kwenye mikanda maalumu.



    Alichukua begi lake kubwa la magurudumu na kuelekea kwenye korido nyingine upande wa kushoto iliyokuwa ikipakana na ofisi mbalimbali za mashirika tofauti ya ndege, migahawa ya kisasa, maduka ya kubadilishia fedha za kigeni, ofisi za mawakala wa kampuni za utalii na kadhalika.



    Mwisho wa ile korido wakatokea kwenye eneo pana la mbele sehemu kulipokuwa na watu wengi waliokuja kupokea wageni wao na nyuma yao kulikuwa na maegesho ya magari. Mafuru alikuwa amesimama huku akiangaza macho yake huku na kule kumtazama mgeni aliyepewa maagizo na Mr. Oduya kumpokea.



    Mkononi alikuwa ameshika bango dogo jeupe lililoandikwa maandishi makubwa ya: “Welcome Suzanne Ross”.



    Zainab alikuwa akijongea eneo lile taratibu huku akitazama huku na kule akiwa anaburuta begi lake kwa mkono mmoja na begani akiwa ametundika mkoba mdogo mzuri wa kike wa rangi nyekundu. Mara alimuona mwanamume mmoja aliyekuwa ameshika bango dogo lililoandikwa jina la Suzanne Ross.







    Alishtuka kidogo na kumtazama kwa makini yule mwanamume huku akijiuliza kama kulikuwa na mtu mwingine aliyeitwa Suzanne Ross aliyekuwa akiwasili katika kiwanja kile cha ndege. Hili lilikuwa jina lake alilobadilisha ili kukwepa utambulisho wake baada ya kuhamia Canada.



    Alimtazama yule mwanamume kwa makini, akakumbuka kuwa alikuwa ameambiwa na Mr. Oduya kuwa mwanasheria wake aliyeitwa Adam Mafuru angempokea pale kiwanjani na kumpeleka sehemu salama, hivyo akaamua kumkabili.



    “I’m Suzanne Ross,” Zainab alijitambulisha kwa Mafuru huku akinyoosha mkono wake kumsalimia. Mafuru alionekana kubabaika sana na uzuri wa Zainab.



    “I’m Adam Mafuru,” Mafuru naye alijitambulisha huku akimpa mkono wake. Kisha kwa unyenyekevu Mafuru alimwambia Zainab kuwa Mr. Oduya alikuwepo pale kiwanjani ila kwa sababu maalumu asingeweza kujitokeza kumpokea, na kumtaka amfuate.



    Walianza kutoka huku Mafuru akiliburuta lile begi la Zainab kuelekea kwenye gari aina ya Toyota Lexus RX la rangi nyeupe lililokuwa na vioo vya ‘tinted’ nyeusi isiyomruhusu mtu kuona waliokuwemo ndani, ambalo lilikuwa likitumiwa na Spoiler.



    Spoiler aliwaona na kufungua sehemu ya nyuma ya gari, akaweka lile begi la Zainab na kwa heshima zote na tabasamu la kirafiki Mafuru alimfungulia Zainab mlango wa nyuma wa gari na kumkaribisha aingie.



    Muda wote Mr. Oduya alikuwa ametulia kwenye gari akishuhudia kila kitu, hakutaka kabisa kushuka kwa kuwa hakupenda watu waliomfahamu wamuone au wajue nini kilikuwa kinaendelea kati yake na Zainab.



    “I see! Nimeimisi sana nchi yangu, ni bahati iliyoje kurudi tena baada ya miaka mingi ya kuishi uhamishoni,” Zainab alijiambia nafsi mwake huku akishangaa kuona kulikuwa na maendeleo makubwa tofauti na wakati alipokuwa akiondoka.



    Gari lilianza kuondoka kutoka eneo lile na safari ya kuelekea mjini ikaanza. Aligeuza shingo yake kuyatazama mandhari ya kupendeza ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere yaliyomvutia sana kwa mpangilio wake mzuri wa majengo.



    * * * * *



    Saa 12:30 jioni gari dogo la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi nyeupe likiwa na vioo vilivyowekwa ‘tinted’ nyeusi isiyomruhusu mtu kuona waliokuwemo ndani, lilikuwa kwenye foleni likizivuka taa za kuongozea magari barabarani za Buguruni Shell.



    Gari lile lilikuwa linatokea katika barabara ya Uhuru na lilipozivuka taa za kuongozea magari barabarani liliingia barabara ya Mandela likielekea eneo la Tazara.



    Ndani ya lile gari kulikuwa na watu watatu, Elli, aliyekuwa akiendesha lile gari na mwanadada mrembo sana alikuwa ameketi pembeni yake kwenye siti ya abiria. Kwenye siti ya nyuma aliketi Sammy akionekana mtulivu sana. Lile gari lilipokivuka kituo cha daladala cha Buguruni Chama likasimama kando ya ile barabara ya Mandela.



    Sammy alishuka huku akimshukuru Elli, wakaagana kisha alianza kutembea taratibu kando ya ile barabara na kukivuka kituo cha daladala cha Buguruni Chama akielekea ziliko taa za barabarani za kuongozea magari.



    Pale kwenye kituo cha daladala abiria walikuwa wengi wakiwa wanakimbilia kupanda magari ya Gongolamboto na Mbagala yaliyokuwa yamejaza abiria. Sammy aliendelea kutembea taratibu na kuwapita vijana waliokuwa wanauza maji na wengine wakiwa wamebeba madeli ya barafu (ice cream) za Ukwaju.



    Yeye alitembeaa taratibu pasipo kujishughulisha na mambo ya watu wengine, alionekana kuwa na mawazo. Muda huo jua lilikwishaanza kuzama na kiza kuanza kuchukua nafasi ya mchana, hivyo magari yalianza kuwasha taa.



    Sammy aliangalia huku na huko na kuvuka barabara ya Mandela iliyokuwa na magari yanayoelekea Tazara kisha akapanda juu ya ukuta wa katikati uliotenganisha magari ya kuelekea Tazara na yale yaliyokuwa yakielekea Ubungo, akitaka kuelekea upande wa pili wa barabara.



    Wakati akianza kuvuka barabara upande wa pili sauti ya breki kali za gari ilisikika na kumshtua sana, alijikunja na kuruka huku akiongeza mwendo. Dereva wa lile gari alijitahidi kumkwepa kisha gari lilisimama katikati ya barabara. Sammy aligeuka kutazama kule kwenye gari huku mwili wake ukitetemeka kwa hofu.



    Aliliona gari la kifahari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi likiwa limesimama huku dereva akimtazama kwa hasira, kisha macho ya Sammy yakatua moja kwa moja kwenye uso wa Mr. Oduya aliyekuwa ameketi kwenye siti ya nyuma akiangalia nje kupitia kioo cha dirisha.



    Japokuwa Mr. Oduya alionekana kutafakari jambo fulani kwa kina lakini alikuwa makini sana kumtazama Sammy. Waliangaliana kwa kitambo na Mr. Oduya akaachia tabasamu.



    Sammy alionekana kushtuka sana na kukimbilia kwenye baa ya Kimboka lakini akaona haitoshi, akajichanganya na watu wengine akiwapita wauzaji wa biashara ndogo waliopanga biashara zao kando ya barabara ya waenda kwa miguu na kuifuata njia nyembamba iliyokuwa ikielekea kwenye hoteli ya New Popex.



    Mr. Oduya alibaki akiwa mtulivu huku akitazama kule alikokuwa amekimbilia Sammy huku akiendelea kutabasamu, muda huo huo magari mengine yaliyokuwa nyuma ya lile gari la Mr. Oduya yalianza kupiga honi ya kumtaka dereva aondoe gari.



    Dereva wa Mr. Oduya aliangalia nyuma kupitia kioo cha gari cha katikati na kuyaona yale magari yaliyokuwa nyuma yake yakimuwashia taa kumuashiria aondoe gari, alitii na kukanyaga pedeli ya mafuta, magurudumu ya gari yakaserereka kwenye lami huku gari likiondoka kwa kasi.



    Wakati lile gari likiondoka kwa kasi eneo lile Mr. Oduya aligeuza shingo yake kutazama kule alikokuwa amekimbilia Sammy, lakini hakumuona.







    * * * * *



    Saa 1:00 jioni gari aina ya Toyota Lexus RX la rangi nyeupe lililokuwa na vioo vya ‘tinted’ nyeusi isiyomruhusu mtu kuona waliokuwemo ndani lilikuwa linaukaribia uzio wa hoteli ya Udzungwa Beach Resort katika barabara ya Ufukweni, eneo la Oysterbay.



    Lilikata na kuingia kulia likishika barabara iliyoelekea nyuma ya majengo ya hoteli ya Udzungwa Beach Resort, kisha liliingia kushoto na kuishika barabara maalumu iliyoelekea Paradise Club.



    Eneo lile lilikuwa na ulinzi mkali nje na ndani ya uzio, na walioruhusiwa kuingia ndani ya Paradise Club ni wanachama waliosajiliwa tu au wageni wao maalumu, lakini kwa utambulisho maalumu.



    Barabara ile ilipambwa na maua mazuri ya ‘Magnolia grandiflora’ yaliyokuwa na rangi ya maziwa na maua mengine aina ya ‘lotus’ yaliyokuwa na rangi mchanganyiko nyeupe, pinki na zambarau, pia ilikuwa imezungukwa na taa nzuri za rangi mbalimbali na maua ya kupendeza.



    Lile gari lililokuwa likiendeshwa na Spoiler lilikaribia kwenye kizuizi cha barabarani kilichokuwa na maandishi makubwa yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza: ‘Security Check Point’, na kwenye kizuizi hicho kulikuwa na askari maalumu watano wa kampuni ya ulinzi ya Spark K7, watatu kati yao walikuwa na silaha.



    Spoiler alikanyaga breki na kupunguza mwendo na hatimaye kusimamisha gari lake umbali wa mita kumi kutoka kilipokuwa kizuizi huku walinzi wenye silaha wakiwa wamenyoosha silaha zao kumuelekea. Walinzi wawili kati yao walianza kupiga hatua zao kulisogelea lile gari huku wakiwa wameshika vyema bunduki zao wakizielekeza kwenye lile gari.



    Mlinzi mmoja alielekea kwenye dirisha la Mafuru, akamsalimia kwa adabu sana na kumuomba kadi yake. Wakati huo huo mlinzi mwingine alizunguka akaelekea upande wa nyuma wa lile gari huku akiwa analichunguza kwa jicho la hadhari.



    “Mgeni wa PC.008.19, nadhani taarifa zote mnazo!” Mafuru alimwambia yule mlinzi huku akionesha kadi maalumu ambayo walipewa wageni, kisha aliachia tabasamu.



    Yule mlinzi aliwapa ishara walinzi wengine waliokuwa wamesimama kwenye kile kizuizi kuondoa kile kizuizi, wale walinzi walitii na kuondoa kizuizi wakimruhusu Spoiler kupita.



    “Madame, hivi sasa Tanzania imeendelea sana tofauti na ulivyoiacha, unaona kama hapa kuna ulinzi mkali sana, kwa kuwa wanaokuja hapa ni mabilionea na watu wenye nyadhifa kubwa serikalini,” Mafuru alimwambia Zainab aliyekuwa kimya muda wote akionekana kushangaa sana.



    Baada ya mita hamsini walikutana na kizuizi kingine kilichokuwa na askari maalumu watano wa kampuni ya ulinzi ya Spark K7 huku wawili wakiwa na silaha. Spoiler alisimamisha gari lake na Mafuru akatoa kichwa chake nje.



    Alitaja tena namba ya utambulisho huku akiwaonesha ile kadi na wale walinzi walimruhusu kupita, walikwenda mita therathini tu mbele wakakutana na kizuizi cha tatu, ambacho pia kulikuwa na askari maalumu watano wa kampuni ya ulinzi ya Spark K7 huku watatu wakiwa na silaha.



    Mafuru alitaja tena namba ya utambulisho huku akionesha ile kadi na mara mlinzi mmoja alibonyeza kitufe fulani, geti kubwa likajifungua na kuwaruhusu kuingia ndani. Walijikuta wametokea katika eneo zuri mno lenye bustani nzuri ya nyasi laini aina ya ‘Citronella’ na mandhari ya kuvutia sana yaliyopambwa na mazuri aina ya ‘Magnolia grandiflora’ na ‘lotus’.



    Waliegesha gari lao kwenye maegesho maalumu ya magari, na kulikuwa na magari mengine kadhaa ya kifahari yaliyokuwa yamejipanga.



    “Madame, tumefika,” Mafuru alimwambia Zainab huku akishuka na kumfungulia mlango wa gari kisha alishusha begi lake.



    Zainab alishuka na mara moja akatokea mwanadada mmoja mrembo sana aliyekuwa amevaa gauni zuri lililochanganywa kitenge cha fabric na kitambaa cha rangi ya pinki ndani ya kitenge, lenye mshono mzuri wa kisasa. Nywele zake ndefu nyeusi alikuwa amezisuka mtindo wa mkia wa pweza.



    Midomo yake alikuwa ameipaka rangi ya pinki na macho yake alikuwa ameyatia wanja mzito na kumfanya aonekane kama malkia wa uzuri katika njozi ya alfajiri.



    “Naitwa Lilian Japhet, sina shaka ni Madame Suzanne Ross wa PC.008.19…” yule mrembo alijitambulisha kwa kina Mafuru huku akiachia tabasamu pana na kusalimia kwa adabu.



    “Yeah, ni mgeni wa PC.008.19,” Mafuru alisema huku akimtambulisha Zainab kwa Lilian. Mara moja Lilian aliachia tabasamu na kupokea begi la Zainab.



    “Karibu sana Madame, mimi ndiye nitakayekuhudumia muda wote utakaokuwepo hapa, naomba nifuate,” Lilian alisema na kupiga hatua zake taratibu na kwa madaha akitangulia mbele huku akiburuta begi.



    Zainab alimfuata nyuma taratibu hadi kwenye mlango mkubwa wa mbele wa Paradise Club, Lilian akausukuma taratibu na kumruhusu Zainab aingie ndani. Lilian akaurudisha ule mlango nyuma yake kisha taratibu akaanza kupiga hatua zake kwa utulivu huku akifuatwa na Zainab, wakakatisha katikati ya ukumbi.



    Zainabu alitembea huku akiyatembeza macho yake taratibu kutazama huku na huko, mazingira aliyoyaona yalimuashiria kuwa eneo lile lilikuwa ni klabu ya kisasa kabisa yenye vionjo vyote vya burudani kwa watu wenye ukwasi wa daraja la kimataifa, walikuwa wakipishana na sura zilizoonekana za watu wenye ukwasi mkubwa na kulikuwa na burudani ya kila aina.



    Kisha walikatisha kwenye korido pana iliyopita kwenye ukumbi mkubwa wa baa ya kisasa uliokuwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini pamoja na meza fupi na pana zenye umbo duara. Zainab aliyatembeza macho yake taratibu kuwatazama mabilionea wachache, wengi wakiwa wageni wa kutoka nje ya nchi ya Tanzania, na zaidi kabisa nje ya bara la Afrika, waliokuwa mle ndani na wenzi wao.



    Kisha waliufikia mlango mwingine mkubwa uliokuwa na maandishi makubwa ya ‘VVIP’, nje ya ule mlango kulikuwa na walinzi watatu wa kampuni ya Spark K7 waliokuwa nje ya ule mlango, wawili kati yao walikuwa wameshika silaha.









    Lilian alimtambulisha mgeni wake. Wale walinzi walimsalimia Zainab kwa adabu na mmoja wao alichukua kifaa cha kukagulia na kuwakagua Zainab na Lilian kuona kama yeyote kati yao alikuwa na silaha yoyote. Kisha walilichukua lile begi lake na kulipitisha kwenye mtambo maalumu na walipohakikisha kwamba hana silaha yoyote, waliufungua mlango na kuwaruhusu waingie.



    Lilian na Zainab wakaingia na kutokea kwenye korido pana iliyokuwa ikielekea kwenye vyumba vya VVIP, wao waliifuata korido nyingine fupi kushoto kwao na kukuta vyumba viwili vya lifti upande wa kushoto na upande wao wa kulia kulikuwa na ngazi za kuelekea juu.



    Lilian alibonyeza kitufe chenye alama za mshale unaotazama juu na mwingine ukitazama chini kilichokuwa pembeni ya milango ya lifti na mara milango ya kile chumba cha lifti ikafunguka na kuwaruhusu kuingia ndani.



    Walipoingia Lilian akabonyeza nambari mbili kwenye kitufe fulani kilichokuwa humo ndani kikiwa na namba kadhaa pembeni ya mlango, milango ya kile chumba cha lifti ikajifunga kisha lifti ikaanza kupanda juu taratibu na ilipofika katika ghorofa ya pili ikasimama na milango ikajifungua yenyewe.



    Walipotoka tu wakakuta korido nyingine pana na mlango mkubwa wenye maandishi ya ‘Presidential Suites’. Hapo waliwakuta walinzi wengine watatu wa kampuni ya Spark K7 waliokuwa nje ya ule mlango, wawili kati yao walikuwa wameshika silaha.



    Lilian alimtambulisha tena mgeni wa PC.008.19. Wale walinzi walimsalimia Zainab kwa adabu na kuwafanyia ukaguzi. Waliporidhika kuwa hawakuwa na silaha waliwaruhusu kuingia ndani



    Lilian alimuongoza Zainab, wakafuata korido nyingine pana iliyopita katikati ya vyumba kadhaa, mbele yao wakaingia kushoto wakiifuata korido nyingine fupi iliyowapeleka hadi mbele ya mlango madhubuti wa mbao uliokuwa na maandishi: PC.19.



    Lilian aliufungua ule mlango kwa kadi maalumu ya kielektroniki aliyoigusisha juu ya kitasa cha mlango kisha wakaingia na kutokea kwenye sebule pana. Lilian alibonyeza swichi zilizokuwa ukutani na kuwasha taa na kiyoyozi kilichokuwa sehemu fulani kwenye kona ya kile chumba, na hapo hewa safi ya ubaridi ilianza kusambaa mle ndani.



    Sakafuni kulikuwa na zulia nene la rangi nyekundu na upande wa kushoto kulikuwa na runinga pana aina ya Sony iliyofungwa ukutani na chini yake kulikuwa na meza fupi nyeusi yenye kisimbusi chenye chaneli nyingi za kimataifa.



    Upande wa kulia kwenye kona kulikuwa na meza fupi ya mapambo na jokofu na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza ya umbo duara ya chakula iliyokuwa imezungukwa na viti vinne nadhifu vyenye foronya laini.



    Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na mlango ulioelekea kwenye chumba cha kulala. Lilian alimwelekeza Zainab ule mlango huku akiufungua, wakatokea kwenye chumba kikubwa cha kifahari chenye nafasi ya kutosha na kilichokuwa na kitanda kikubwa cha samadari katikati.



    Mbele ya kitanda kulikuwa na seti nzuri ya runinga pana aina ya Sony na chini ya ile runinga kulikuwa na meza fupi nyeusi ya kioo, na juu ya meza kulikuwa na simu ya mezani na kitabu chenye orodha ya majina ya watu na kampuni zilizotumia huduma ya simu hiyo ya mezani.



    Pia kulikuwa na kabati kubwa la kisasa la nguo lililokuwa ukutani, kando yake kulikuwa na meza ya vipodozi yenye kioo kirefu cha kujitazama na kochi moja kubwa la sofa.



    Kulikuwa na madirisha mawili mapana ya vioo yaliyokuwa yamefunikwa kwa mapazia mazito na marefu yenye nakshi za kupendeza. Kwa kutokea kwenye lile dirisha mtu angeweza kuona mandhari nzuri ya kuvutia, na kwenye kona ya chumba kile upande wa kushoto kulikuwa na mlango wa kuelekea kwenye maliwato.



    * * * * *



    Sammy alifika nyumbani kwake muda wa saa moja na ushee za jioni akiwa amebeba mkoba wake mdogo wa kiofisi aina ya Pad & Quill wa rangi ya hudhurungi aliokuwa ameusahau pub ya Barakuda usiku wa siku iliyokuwa imetangulia.



    Aliupitia baada ya kukumbuka, na alipoingia ndani ya nyumba yake alimkuta Joyce akiwa mwenye furaha mno, Sammy alimtazama kwa makini huku mshangao wa wazi ukijitokeza usoni kwake, kisha aliwatupia macho watu wengine waliokuwepo pale sebuleni.



    Pale sebuleni walikuwepo Joyce, Pendo na Winifrida waliokuwa wanafuatilia marudio ya mchezo maarufu wa kuigiza wa runinga ulioitwa ‘Gereza la Kifo’ kutoka kwa mtunzi mahiri wa michezo ya kuigiza, Hamisi Kibari.



    Hata hivyo, mawazo ya Joyce hayakuwa kwenye ule mchezo wa kuigiza bali alikuwa anawaza kuhusu ahadi yake ya kwenda kuonana na Madame Norah, huku akianza kuiona njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa kimataifa. Muda ule alikuwa amejiegemeza kwenye sofa huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu muda wote.



    Joyce alimuona Sammy na kuinuka, akamkaribisha huku akiupokea mkoba wake, hata hivyo tabasamu pana usoni kwake lilishindwa kabisa kwenda likizo. Sammy aliguna huku akimkazia macho Joyce kwa umakini zaidi.



    “Mwenzetu vipi, mbona naona leo una furaha kupita maelezo, au umeshinda jackpot?” Sammy aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Joyce.



    “Kapigiwa simu, kipindi chake cha mitindo kimekubaliwa,” Winifrida alidakia huku akiachia tabasamu.



    “Kapigiwa simu na nani?” Sammy aliuliza huku akiwa bado ana mshangao, alimkodolea macho Joyce huku akiwa na maswali lukuki kichwani kwake. Joyce alibaki kimya, lakini sasa hakuwa anatabasamu tena!



    “Kapigiwa na Madam Norah…” Winifrida alisema bila wasiwasi wowote huku akionesha kufurahishwa sana na hatua ya Madam Norah kumpigia simu Joyce.



    Sammy alishtuka kidogo, alibana taya za midomo yake akionekana kuzuia hasira huku akimkazia macho Joyce. Hakuonesha kufurahishwa kabisa na zile taarifa.



    “Madam Norah ndiyo habari ya mjini… anamiliki vituo vya radio na televisheni na ana kipindi cha “Madame Norah Show” cha kuhamasisha harakati za wanawake,” Winifrida alizidi kuongea kama ametiwa ufunguo na kumfanya Sammy akunje sura yake, kisha aliondoka taratibu na kuelekea chumbani kwake bila kusema neno.



    Joyce alimsindikiza Sammy kwa macho na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha aligeuka kumtazama Winifrida huku akiwa amekunja sura yake, alitaka kusema neno lakini akasita.







    Joyce alimsindikiza Sammy kwa macho na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha aligeuka kumtazama Winifrida huku akiwa amekunja sura yake, alitaka kusema neno lakini akasita.



    * * * * *



    Saa 2:30 usiku ilimkuta Mr. Oduya akiwa amesimama chumbani kwake mbele ya meza nzuri ya kisasa ya vipodozi maarufu kama ‘dressing table’ iliyokuwa na vioo virefu vitatu vilivyowekwa kuizunguka ile meza na kumfanya mtu ajione mara tatu, alionekana yupo katika harakati za kujiandaa ili atoke.



    Mr. Oduya alikuwa amevaa suti ya bei ghali nyeusi aina ya Kenzo, shati jeupe la mikono mirefu na viatu vyeusi vya ngozi, alikuwa anachana nywele zake taratibu huku akijitazama kwenye vile vioo, kisha mikono yake ilianza kurekebisha tai yake ya rangi nyekundu shingoni.



    Alionekana kuwa mtulivu sana huku akiwa amezama katika lindi la fikra, hata hivyo, alikuwa makini akimtupia jicho la wizi mkewe, Dk. Salma Oduya aliyekuwa amesimama kando yake akimtazama kwa makini huku amekunja sura yake.



    Dk. Oduya alikuwa mwanamke mnene wa wastani, hakuwa mfupi wala mrefu bali alikuwa na kimo cha wastani na rangi ya maji ya kunde iliyokuwa ina mng’aro wa aina yake.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Akiwa na umri wa miaka hamsini na tano, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mama wa watoto wawili: Omari Oduya aliyekuwa na miaka 30 na kwa wakati huo alikuwa anaishi nchini Marekani, na Zuhura Oduya aliyekuwa na miaka 26 na wakati huo alikuwa anachukua Shahada ya Umahili ya Maendeleo ya Uchumi wa Kimataifa nchini Uingereza.



    Usiku ule Dk. Oduya alikuwa amevaa nguo nyepesi ya kulalia maarufu kama ‘night dress’ ya rangi ya samawati na alijifunga kitenge kiunoni, juu alivaa sweta la mikono mirefu na kichwani alikuwa amevaa kofia laini maalumu kwa kukinga nywele.



    Muda ule wa saa mbili na nusu usiku upepo ulikuwa unavuma na kutengeneza sauti ya mvumo wa kustaajabisha kwenye matawi ya miti mikubwa ya kivuli iliyozunguka jumba la kifahari la Mr. Oduya, kadiri matawi ya miti yalivyocheza huku na kule kwa utulivu ndivyo mvumo ule ulivyosikika na kutengeneza sauti kama ya chatu mkali aliyehisi hatari kichakani.



    Upepo ulivuma ukayasonga songa mapazia marefu yaliyokuwa yamefunika madirisha mawili makubwa mle chumbani.



    Jumba la Mr. Oduya ambalo lilistahili kuitwa kasri, lilikuwa katika eneo la ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Mbezi Beach, eneo lililokuwa na makazi ya watu wenye ukwasi mkubwa au viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Tanzania. Katika eneo lile tulivu yalionekana majumba kadhaa ya kifahari yaliyozungukwa na kuta ndefu na mageti makubwa mbele yake.



    Lilikuwa jumba kubwa la ghorofa mbili lenye vyumba saba vya kulala kila kimoja kikiwa na maliwato yake, sebule tatu kubwa, kumbi mbili za chakula, majiko mawili ya kisasa, kaunta ya baa iliyokuwa katika sehemu ya chini ya jengo na sehemu mbili za ghorofani za kubarizi zenye kochi safi za sofa.



    Eneo lile lilikuwa na barabara pana ya lami yenye usafi wa hali ya juu, iliyopandwa miti mizuri ya kivuli kando ya barabara. Muda ule wa usiku eneo lile lilikuwa na utulivu mkubwa sana huku likimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali. Ni sauti kali za mbwa waliokuwa wakibweka eneo lile bila sababu za msingi ndizo zilizokuwa zinasikika kwa mbali na magari machache sana yalipita barabarani.



    Ndani ya lile jumba waliishi watu kumi, watu wazima wanane na watoto wawili: Mr. Oduya mwenyewe na mkewe Dk. Oduya, ndugu watatu wa familia ya mkewe na watoto wao wawili, wahudumu wawili wa kike wa ndani na mhudumu mmoja wa kiume aliyesaidia shughuli za mifugo na shamba. Pia kulikuwa na walinzi watatu waliolinda kwa kupokezana, lakini hawakuwa wakiishi pale.



    Hata hivyo, lile jumba lilikuwa na ulinzi madhubuti kwa kujengewa ukuta mrefu uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake na usiomwezesha mtu yeyote kuona mle ndani.



    “Hivi wewe mwanamume, unajua mimi sikuelewi kabisa!” sauti ya Dk. Oduya ilimgutusha Mr. Oduya kutoka kwenye lindi la mawazo.



    Muda wote Dk. Oduya alikuwa anamwangalia mumewe akionesha wazi kuwa alikuwa na hasira na sura yake alikuwa kaikunja na kutengeneza matuta madogo usoni.



    “Kwa nini hunielewi?” Mr. Oduya alimwuliza mkewe bila kugeuka ingawa alikuwa akimtazama kupitia vioo vya kwenye meza ya vipodozi.



    “Eti eeh! Unajifanya huelewi ninachomaanisha!” Dk. Oduya aliongea kwa hasira huku sasa akiwa ameshika kiuno chake kwa mikono yote miwili na kumkazia macho mumewe.



    “Hapana naelewa,” Mr. Oduya alimjibu huku akigeuza shingo yake kumtazama kwa makini.



    “Unaelewa nini?” Dk. Oduya alihoji huku macho yake yakiwa hayabanduki usoni kwa mumewe.



    “Naelewa kwamba hunielewi kabisa!” Mr. Oduya alijibu huku hasira zikianza kuchipua ndani yake.



    “Haya wewe endelea tu… huo umalaya wako wa uzeeni utakugharimu siku moja… ila usisahau kutumia condom usije ukaniletea maradhi,” Dk. Oduya alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Naomba tusianze kuharibiana siku, unaropoka tu wala hujui naenda kukutana na kina nani saa hizi, hivi kwa mwendo huu nitaweza kweli kushinda uchaguzi wa urais kama hata kwenda kukutana na washirika muhimu wa kisiasa inakuwa nongwa!” Mr. Oduya alianza kulalamika.



    “Wadau gani wa kisiasa? Hivi unaniona mimi mtoto mdogo siyo! Wewe si umetoka huko huko muda huu! Hata hujapumzika vizuri unataka kuondoka tena, eti kuwaona wadau wa kisiasa, ni wadau gani wasiokupa hata muda wa kupumzika na familia yako?” Dk. Oduya alizidi kuhoji,



    Mr. Oduya alimtazama kwa makini, akataka kumjibu lakini alisita na kuamua kumpuuza, ni mwanamke aliyeishi naye katika ndoa kwa miaka therathini na moja. Alimchukulia kama mwanamke wa kawaida tu ambaye hakuwa na jipya zaidi ya maneno mengi mithili ya chiriku kila uchao.



    Badala yake Mr. Oduya alichukua mkoba wake wa kiofisi na kugeuka, akaanza kupiga hatua za taratibu kuondoka, aliazimia kwenda kuumaliza usiku wa siku ile akiwa na Zainab, mwanadada mtundu mno na aliyekuwa amemuonesha ulimwengu mpya wa mapenzi, pamoja na umri wake mkubwa, alikiri kuwa hakuwa mjuzi kabisa.









    Zainab Semaya, mtoto wa ki-Tanga, alikuwa binti mwenye busu za kusisimua sana na kila mara walipomaliza mchezo alimwachia Mr. Oduya maswali kibao na kubaki akijiuliza alijifunzia wapi yale mahaba! Kwani Zainab alikuwa wa aina ya pekee, mwenye majibu yote ya maswali yahusuyo mapenzi.



    Hivyo, Mr. Oduya aliona kuwa hakutakiwa kumpa nafasi mkewe aharibu utaratibu mzima wa siku ile wa kwenda kufurahia penzi la mrembo asiyechuja, bibie Zainab, kwani lingekuwa kosa kubwa sana kumwacha alale peke yake wakati alikuja kwa ajili yake.



    “Sawa bwana, endelea kunidharau… lakini nakwambia mbio za sakafuni huishia ukingoni,” Dk. Oduya alisema huku akiwa bado kakunja uso wake kwa hasira, alikuwa anamsindikiza mumewe kwa macho.



    Mr. Oduya hakugeuka wala kusema neno bali alitoka nje ya chumba kile na kuufunga mlango nyuma yake kisha alizifuata ngazi za kuelekea sehemu ya chini ya lile jumba la kifahari huku akiwa amechefukwa kweli kweli.



    Asingeweza kuahirisha safari yake ya kwenda Paradise Club kufurahia maisha na kipenzi cha moyo wake, hakuwa na shaka kuwa suala la mkewe angelimaliza kiutu-uzima kwani alijua namna nzuri ya kumdhibiti.



    * * * * *



    Saa tatu na ushee usiku Joyce alikuwa amekaa kwenye kona ya kitanda chumbani kwao, alikuwa amevaa nguo nyepesi nyeupe ya kulalia iliyolichora vizuri umbo lake zuri na kuifichua nguo yake nyeusi ya ndani.



    Joyce alikuwa ameketi akimtazama mumewe Sammy kwa wasiwasi lakini kwa macho yaliyojaa ubembe wa huba huku akihisi moyo wake ukienda mbio kama saa mbovu! Hata hivyo, moyoni alionekana wazi kusimamia kile alichopanga kufanya na hakuwa tayari kuyumbishwa, kwani aliamini kuwa bahati kama iliyomtokea siku ile haiji mara mbili!



    Ni kweli alimpenda sana na kumheshimu Sammy, lakini isingekuwa rahisi kwake kuachana na mpango wake wa kwenda kumuona Madame Norah.



    Kilipita kitambo kirefu cha ukimya, Joyce alikuwa akimwangalia Sammy kwa makini. Macho yake yalishatoa taswira ya kilichokuwa moyoni mwake. Alishajua kabisa kuwa mwenzake alikuwa katika hasira, alikasirishwa na jambo ambalo lilikuwa na faida, si kwao wawili bali kwa familia nzima.



    Tangu Sammy aliporudi nyumbani na kuelezwa na Winifrida kuhusu simu ya Madame Norah aliyompigia Joyce, alionekana kutokufurahia jambo hilo, kwani siku zote hakukubaliana na mkewe kutaka kuonana na Madame Norah. Alikuwa na wasiwasi kuwa Madame Norah angeweza kumwambukiza tabia zake Joyce.



    Muda ule kila mmoja alikuwa na mawazo yake, Sammy alikuwa amejiegemeza ukutani pale kitandani alipokaa na kutazama juu ya dari kwa muda mrefu. Joyce naye alikuwa na mawazo yake, alijaribu kufikiria ni kwa namna gani angemlainisha Sammy akubali kumruhusu kwenda kuonana na Madame Norah.



    Kwa hakika ilikuwa kazi ngumu, tena ngumu kweli kweli! Pengine ingekuwa rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko kumlainisha Sammy, maana alikuwa na msimamo thabiti! Sammy alimtazama Joyce kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Sijakuelewa kabisa, Baba Pendo! Kwa nini hutaki niende kuonana na Madame Norah?” Joyce alimwuliza Sammy kwa mara nyingine tena baada ya kitambo kirefu cha ukimya na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Kwani hujaelewa nini katika yote niliyosema?” Sammy aliuliza huku akipitisha ulimi wake kulamba midomo yake iliyoanza kukauka.



    “Yote uliyosema ni uvumi tu, hayana ukweli wowote. Mambo mengi dhidi ya Madame Norah ni ya kuzushwa tu, tena yanazushwa na watu wenye wivu, wasiopenda maendeleo yake,” Joyce alisema.



    “Ya kuzushwa ki-vipi wakati kila kitu kinajionesha?” Sammy alihoji huku akimtazama Joyce kwa mshangao.



    “Mimi siamini! Isitoshe mimi siyo mtoto mdogo useme kwamba naweza kushikiwa akili, ninatambua mabaya na mazuri,” Joyce alisema huku akitingisha kichwa chake taratibu.



    “Hata kama huamini lakini kumbuka kuwa hakuna moshi bila moto!” Sammy alisema kwa sauti tulivu akijitahidi kuizuia hasira iliyokuwa imechipua ndani yake.



    Joyce alimtazama Sammy kwa makini kwa kitambo kifupi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Usidhani kuwa nazuia maendeleo yako bali nafanya hivi kwa sababu nakupenda…” Sammy alisema huku akijiweka vizuri pale kitandani.



    “Unafanya hivi kwa sababu una wivu. Kwa sababu Madame Norah ana misimamo juu ya wanaume na anaelimisha wanawake!” Joyce alisema kwa unyonge huku akiinamisha kichwa chake kutazama chini. Sammy alishtuka sana, hakutegemea jibu kama lile kutoka kwa mkewe.



    “Sijawahi kukudharau hata siku moja na wala sifikirii kuja kukudharau, lakini nalazimika kufuata ndoto zangu,” Joyce alisema na kuinua uso wake kumtazama Sammy.



    Sammy alionekana kuchukizwa sana na ile kauli, alikunja sura yake na hasira ikaanza kuibuka upya ndani yake. Alikunja ngumi ya mkono wa kushoto na kwa kutumia vidole viwili; kidole gumba na kidole cha shahada akaibana pua yake na kuvuta hewa ndani kama aliyekuwa anavuta kamasi.



    Joyce aligundua kuwa alikuwa amemuudhi sana mumewe, aliamua kumsogelea na hapo hapo mikono yake yote miwili ikaanza kufanya ziara kwenye mwili wa Sammy, huku mkono wa kulia ukienda moja kwa moja kwenye kifua chake na kuanza kukipapasa kile kifua chenye vinyweleo vingi.



    “Can you please stop this?” Sammy alisema kwa sauti iliyoonesha hasira huku akikunja sura yake, pumzi zake zilianza kumpaa.



    “Stop what?” Joyce aliuliza huku akimwangalia Sammy moja kwa moja machoni.



    “Niangalie machoni,” Joyce alisema kwa sauti ya upole na kwa utulivu mkubwa huku akiendelea kumpapasa kifuani kwake. Sammy akamwangalia. Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa, Sammy akakiona kile ambacho hakutarajia kukiona katika macho ya Joyce.



    “Nisamehe sana mume wangu, sikukusudia kukukwaza wala kukuhuzunisha, unajua ni kiasi gani nakupenda sana na kukuheshimu, lakini sijui kwa nini wewe hutaki kuniamini!” Joyce alisema kwa sauti ya mhemo huku mikono yake ikiendelea kujivinjari kwenye mwili wa Sammy.



    Sammy hakusema neno bali alibaki kimya huku akifumba macho yake kuusikilizia ule mpapaso wa mikono ya Joyce kwa makini. Hata hivyo, Joyce hakusubiri jibu la Sammy, alipeleka mkono wake wa kushoto ndani ya bukta ya Sammy na kuanza kuvinjari eneo la ikulu huku mkono wa pili ukienda moja kwa moja mgongoni.







    Wakati akiendelea kumpapasa, Sammy aliamua kuvunja ukimya huku akimtazama Joyce usoni.



    “Joyce!” Sammy aliita kwa sauti tulivu.



    “Abee, mume wangu,” Joyce aliitikia kwa sauti laini iliyokuwa na kila aina ya kiashiria cha kuhemkwa na tamaa za kimwili.



    “Nimekuelewa,” Sammy alisema huku akihema kwa nguvu.



    “Kweli?”



    “Ndiyo.”



    Joyce alitabasamu, mikono yake iliendelea kujivinjari kwenye mwili wa Sammy, macho yake bado yalikuwa usoni kwa Sammy yakimwangalia kwa makini, Sammy naye alikuwa akimwangalia Joyce kwa makini. Macho ya Joyce yalipepesa, kope zikacheza kidogo kuruhusu usafi wa macho yake. Kisha taratibu alianza kufumba macho yake.



    “Nenda kazime taa,” Sammy alimwambia Joyce huku akijinyoosha na kujilaza chali kitandani, alionekana kusubiri kile ambacho kila mmoja wao alikihitaji kwa wakati huo. Joyce aliinuka haraka na kwenda kuzima taa.



    Muda mfupi uliofuata walikuwa wamehama kabisa kutoka katika sayari hii, wakajikuta wakiwa katika sayari nyingine ya mbali, sayari ya mahaba mazito yenye kila aina ya vionjo vya kumtoa nyoka pangoni.



    _____



    Ilikuwa imetimu saa sita na nusu za usiku, Sammy na Joyce walikuwa wamelala kitandani na kupitiwa na usingizi mtamu wa uchovu baada ya kwenda mizunguko miwili iliyowafanya washindwe hata kujimudu, wote walikuwa hoi.



    Sammy alikuwa amelala chali na Joyce alikuwa amelala kifuani kwake kama kifaranga cha kuku kilichokuwa kimekumbatiwa na mama yake. Mguu wake mmoja ulikuwa katikati ya mapaja ya Sammy huku mkono wake mmoja akiwa ameuzungusha shingoni kwa Sammy na alikuwa akikoroma kwa sauti hafifu ya uchovu.



    Mara mlango wa chumba chao ulianza kugongwa taratibu, Joyce alishtuka na kufumbua macho yake kivivuvivu, alimtazama Sammy usoni kisha alinyanyua kichwa chake na kugeuza shingo yake kutazama kule kwenye mlango huku akipiga miayo ya uchovu.



    Alijaribu kumpuuza mgongaji wa mlango na kukilaza tena kichwa chake kifuani kwa Sammy, lakini mlango ulizidi kugongwa, safari hii uligongwa kwa nguvu zaidi na kusababisha kero masikioni mwake. Joyce aliposikiliza kwa makini aliweza kuisikia sauti ya Winifrida nje ya mlango ikiita kwa hofu.



    Kabla hajajua cha kufanya, yeye na Sammy kwa apamoja walijikuta wakikurupuka kutoka pale kitandani na kusimama kwa wasiwasi huku wakilitupa shuka walilokuwa wamejifunika. Walitazamana lakini hakuna aliyekuwa na jibu.



    Winifrida aliendelea kugonga mlango huku akiwaita kwa nguvu, Joyce alichukua haraka khanga yake akajifunga kifuani na kuelekea mlangoni akiwa na wasiwasi, wakati huo Sammy alikuwa amekwishavaa bukta na fulana, akaelekea mlangoni na kusimama nyuma ya Joyce.



    “Pendo amezidiwa hawezi kupumua vizuri, anatapatapa huku akilalamika maumivu…” Winifrida alisema kwa hofu huku akilia kilio cha kwikwi baada ya mlango kufunguliwa na kuwaona Sammy na Joyce wakimtazama kwa wasiwasi.



    Bila kusubiri, Joyce na Sammy walikimbilia kwenye chumba alikokuwa amelala Pendo na kumkuta akiwa anatapatapa huku akihema kwa shida. Pendo alipowaona alianza kulalamika maumivu ya mikono na miguu.



    Kwa kuwa Sammy alielewa zile dalili ziliashiria tatizo gani kwa Pendo, hakusubiri, alichukua haraka simu yake na kumpigia dereva mmoja wa teksi jirani yao ili wamkimbize Pendo hospitali.



    * * * * *



    Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu ya asubuhi, sauti ya aina yake iliyoburudisha ya maji ya baharini yaliyokuwa yanachapa kingo za baharini ilipenya kwenye madirisha makubwa ya chumbani hadi pale kitandani walipolala Zainab na Mr. Oduya.



    Mr. Oduya alijigeuza na wakati huo huo Zainab naye alijinyoosha kisha akamkumbatia. “Good morning, my darling!” Zainab alimsalimia Mr. Oduya huku akikishika kidevu chake kwa utani kama vile mjukuu akimtania babu yake.



    “Morning, my darling!” Mr. Oduya aliitika huku akipiga miayo na kuachia tabasamu, kisha akaongeza, “Mungu ni mwema, tumeamshwa salama.”



    “Mungu ni mwema kweli kweli,” Zainab naye aliirudia ile kauli huku akiachia tabasamu.



    Mr. Oduya alijinyoosha kisha akainuka na kuketi pale kitandani, miguu yake ikakanyaga sakafuni, alishusha pumzi na kuinuka huku akiendelea kujinyoosha na kusogea upande wa pili ilipokuwa simu yake ya mkononi, akaichukua na kuiwasha, kwani ilikuwa imezimwa.



    Alikuwa amelazimika kuizima simu yake kwani shughuli iliyofanyika usiku wa kuamkia siku ile ilikuwa supa. Zainab alikuwa amemtaka aizime ili kusiwe na kitu chochote cha kuingilia faragha yao, naye akatii.



    “Sihitaji simu yoyote saa hizi, nimekuja kwa ajili yako, ni mimi na wewe tu hadi lyamba…” Mr. Oduya alikumbuka kuambiwa na Zainab usiku kabla hawajalala.



    Usiku wa kuamkia siku ile Mr. Oduya alipofika Paradise Club ilikuwa imeshatimu saa nne za usiku. Alimkuta Zainab akiwa amejifunga khanga moja tu nyepesi na alipogonga mlango haraka Zainab alimfungulia na kumrukia, akakumbatia kwa mahaba.



    “Waoo… pole mpenzi wangu, naona umechoka sana,” Zainab alimwambia huku akiupokea mkoba wa kiofisi aliokuwa kaubeba na kuupeleka moja kwa moja chumbani.



    “Asante sana, mke wangu mpenzi,” Mr. Oduya alisema huku akimfuata Zainab kule chumbani, kisha akajipweteka juu ya kitanda.







    Zainab alimsogelea akaimvua koti lake kisha alimvua viatu na soksi, halafu akamfungua tai yake shingoni na kufungua vifungo vya shati lake huku akimtazama usoni kwa tabasamu.



    “Samahani mpenzi, naomba nikufungue mkanda wa suruali,” Zainab alisema kwa sauti tamu ya mahaba akiomba ruhusa kwa Mr. Oduya.



    Mr. Oduya alimtazama kwa makini na kuachia tabasamu huku akishusha pumzi.



    “Darling!” Mr. Oduya aliita kiwa sauti ya kunong’ona.



    “Abee!”



    “Unaweza kufanya chochote, mwili huu ni mali yako.”



    “Asante sana mpenzi, unapaswa kuhudumiwa maana unachoka na kazi nyingi, una mambo mengi ya kufanya, pole sana ninajua akili yako haijatulia.”



    “Asante sana, mpenzi wangu, ndiyo maana nakupenda kuliko kitu chochote,” Mr. Oduya alisema na kupitisha mkono wake kichwani, kuanzia kwenye paji la uso kuelekea usogoni na alipofika mwisho wa kichwa alipitisha mkono wake shingoni mwake na akawa kama anayejinyoosha.



    Kisha aligeuka upande wa kushoto na kulia huku akitoa miguno ya uchovu hasa.



    “Pole sana. Umeshakula?” Zainab alimuuliza Mr. Oduya huku akiivua suruali yake na kumwacha akiwa na boksa tu.



    “Hapana sijala,” Mr. Oduya alijibu huku akijilegeza.



    “Sijui utakula kwanza ndiyo ule au unakula kwanza halafu ndiyo utakula?” Zainab alimuuliza Mr. Oduya kwa sauti laini ya mahaba na kumfanya Mr. Oduya amwangalie kwa makini kabla ya kuachia tabasamu lililozaa kicheko hafifu.



    “Kabla hujajibu ngoja kwanza nikupunguze uchovu,” Zainabu alisema kabla hata Mr. Oduya hajajua ajibu nini.



    Haraka bila kuchelewa, Zainab alimsukuma Mr. Oduya, akaanguka chali pale kitandani kisha alimgeuza vyema akalalia tumbo lake kisha alipanda juu yake akakaa vyema, alichukua mafuta laini (lotion) aliyokuwa ameyaandaa na kuanza kumpaka Mr. Oduya eneo la mgongoni na shingoni kisha akaanza kumsinga kwa ufundi wa hali ya juu. Wenyewe huita kumfanyia masaji.



    Mr. Oduya alitulia kimya wakati Zainab akifanya kazi yake kwa ufundi, alikuwa akifurahia sana kila kitu alichokuwa anafanyiwa na Zainab.



    “Darling, yaani namna unavyonikanda najisikia burudani hasa, kwa kweli nimemisi sana kufanyiwa haya mambo,” Mr. Oduya alisema huku akihisi faraja ya aina yake.



    “Usijali mpenzi, nimekuja Tanzania kwa ajili yako… hii ndiyo kazi yangu,” Zainab alisema huku akiendelea kuukanda kanda mgongo wa Mr. Oduya, kisha akashuka mapajani na baadaye akapanda hadi shingoni, mpaka kichwani.



    Hadi muda huo Mr. Oduya alikuwa kazidiwa, kwani macho yake yalishabadilika na kuwa mekundu kabisa. Hii ndiyo faraja aliyokuwa akiikosa ndani ya ndoa yake na kuamua kuitafuta nje ya ndoa yake. Hakika kwenye ndoa nyingi mambo kama haya hukosekana.



    Wanawake wengi ni wavivu sana kwenye ndoa zao, na ndiyo maana shetani ameweza kutumia mbinu hii kusambaratisha ndoa nyingi… cha ajabu wanawake hawa wanajituma sana kwenye uzinzi lakini kwenye ndoa zao wala hawajitumi!



    Baada ya kazi ile ya kusingwa, kilichofuata kiliiongeza njaa ya Mr. Oduya mara dufu, alihisi kizunguzungu kutokana na garidwe la aina yake alilochezeshwa na Zainab, gwaride lililomuacha akihema ovyo kama bata.



    Walipomaliza waliingia maliwatoni, kilikuwa chumba kikubwa cha maliwato yenye hadhi yake yaliyoweza kumsahaulisha majonzi hata aliyefiwa na ampendaye.



    Waliingia kwenye jakuzi na kutulia humo miili yao ikiwa inakandwa na maji ya uvuguvugu…



    “Unawaza nini, mpenzi?” sauti ya Zainab ilimzindua Mr. Oduya aliyekuwa amesimama wima akimkodolea macho Zainab pasipo kumuona.



    “Ah, wala usijali… nilikuwa nayakumbuka mautundu yako,” Mr. Oduya alisema huku akipiga miayo mfululizo na kuchukua taulo lake, akajifunga kiunoni kisha akaelekea jikoni. Alitengeneza vikombe viwili vya kahawa na baada ya dakika chache alirudi chumbani, kikombe kimoja akampatia Zainab.



    “Welcome, my darling,” Mr. Oduya alisema kwa mahaba huku akiachia tabasamu pana usoni kwake.



    “Thank you,” Zainab alisema huku akiinuka, akajifunga kipande cha khanga nyepesi kifuani na kukaa pembeni ya Mr. Oduya.



    “No, darling…” Mr. Oduya alisema huku akitingisha kichwa chake taratibu. “Ukiona nimekaa, unatakiwa kukaa hapa,” alisema huku akijipigapiga juu ya paja lake.



    “Kaa hapa mpenzi wangu…” Mr. Oduya alisisitiza na kumfanya Zainab aangue kicheko hafifu cha mahaba huku akiinuka na kumkalia juu ya paja lake, kisha wakawa wanakunywa kahawa taratibu.



    Walipomaliza kunywa kahawa wakaelekea maliwato, walijimwagia maji na kurudi chumbani wakiwa wamepata nguvu mpya. Mr. Oduya alivaa bukta na kukaa kitandani kisha akaanza kuvuta mkoba wake wa kiofisi, Zainab alimtazama kwa makini na kuufuata ule mkoba.



    “Darling, nikusaidie?” Zainab alimuuliza kwa sauti ya mahaba.



    “No… unajua sipaswi kukusumbua na kukuchosha, wewe ni malkia… isitoshe mwanamke siyo roboti, relax…” Mr. Oduya alisema huku akimpapasa Zainab mgongoni kwa mahaba.



    “Wala hunisumbui mpenzi, it’s just loves, najisikia tu kukusaidia…” Zainab alisema lakini akakatishwa na mlio wa sauti ya kengere ya mlangoni iliyoita kwa fujo huko sebuleni na sauti yake kupenya hadi chumbani, wakatazamana. Ni kama walikuwa wanaulizana ‘ni nani?’



    Zainab alitoka chumbani akaelekea sebuleni na kuchungulia kwenye tundu maalumu la mlangoni lenye kioo cha lenzi, akamuona Lilian akiwa amesimama nje ya mlango. Akashusha pumzi na kuufungua mlango.



    “Ooh, Lilian… karibu mdogo wangu, naona umeniwahi,” Zainab alisema huku akisogea kando kumpisha Lilian aingie.



    “Asante sana madame, habari za asubuhi?” Lilian alisema huku akiingia na kusimama pale sebuleni.



    “Nzuri Lilian… unaweza kuendelea na kazi, kama kutakuwa na chochote utaniita nipo chumbani,” Zainab alimwambia Lilian na kurejea chumbani alikomwacha Mr. Oduya.









    “Nzuri Lilian… unaweza kuendelea na kazi, kama kutakuwa na chochote utaniita nipo chumbani,” Zainab alimwambia Lilian na kurejea chumbani alikomwacha Mr. Oduya.



    * * * * *



    Saa nne asubuhi siku ya Jumapili, katika chumba kikubwa cha wadi maalumu ya VIP ya Hospitali ya Dar Group iliyopo barabara ya Nyerere jirani na Tazara, jijini Dar es Salaam, Sammy alikuwa amesimama kando ya kitanda alicholala Pendo, akionekana mwenye huzuni.



    Chumba kile kilikuwa kikubwa chenye vitanda viwili na dirisha kubwa lililokuwa linaingiza hewa safi, na juu kulikuwa na dari nzuri iliyotengenezwa kwa gypsum ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kulining’inizwa taa nzuri na pangaboi.



    Kitanda alicholala Pendo kilikuwa cheupe cha chuma chenye godoro nene la foronya laini na mto laini wa kuegemeza kichwa. Pendo alikuwa bado anapumua kwa shida kutokana na kusumbuliwa na tatizo la seli mundu lililosababisha kupungukiwa damu na matatizo ya kupumua.



    Kando ya kile kitanda kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyokuwa imetundikiwa chupa ndogo ya damu na mrija wake ukipeleka damu kwenye mshipa wa damu mkononi kwa Pendo.



    Kando ya ile stendi ya chuma kulikuwa na meza ndogo na juu yake kulikuwa na trei ndogo ya chuma iliyokuwa na vifaa-tiba kama mkasi, plasta, bomba la sindano, glovu, chupa kubwa ya maji, bilauri na dawa za vidonge kwa ajili ya tatizo la seli mundu.



    Baadhi ya vile vifaa vilikuwa vimefunguliwa na kuachwa wazi kitendo kilichoashiria kuwa tayari vilikuwa vimekwisha tumika.



    Winifrida alikuwa ameketi kwa utulivu juu ya kitanda cha pili mle chumbani akimtazama Pendo kwa huzuni, alionekana mbali kimawazo na machozi yalikuwa yanamlenga machoni. Chumba kilikuwa na ukimya wa aina yake.



    Muda ule ule mlango wa kile chumba ulifunguliwa, Daktari wa magonjwa ya watoto, Daktari Beda Msimbe aliingia akiwa ameongozana na muuguzi wa wodi ile ya watoto



    Daktari Msimbe alikuwa mwanamume mfupi mnene na rangi ya ngozi yake ilikuwa ya maji ya kunde, akiwa na umri wa miaka hamsini na saba alikuwa na nywele fupi zenye mvi kiasi na uso wake ulikuwa mpana huku miwani yake mikubwa ikiwa imeyahifadhi macho yake makubwa.



    Alikuwa amevaa suruali ya kitambaa cha kadeti cha rangi ya khaki, shati kubwa jeusi lililokuwa na mistari myeupe ya pundamilia na juu yake alikuwa amevaa koti refu jeupe la kidaktari na kuning’iniza shingoni kwake kifaa maalumu cha kupimia, kwa kitaalamu kiliitwa ‘stethoscope’.



    Daktari Msimbe alikwenda moja kwa moja kitandani kwa Pendo akapishana na Winifrida aliyeinuka na kutoka nje. Daktari Msimbe alisimama akimchunguza Pendo kwa macho na kumgusa kwenye paji la uso wake, kisha aliiangalia kwa makini damu iliyokuwamo ndani ya chupa aliyotundikiwa Pendo.



    Aliangalia kwa makini jinsi matone ya damu yalivyokuwa yakidondoka na kuingia kwenye mrija maalumu uliopeleka damu kwenye mshipa wa damu mkononi kwa Pendo na kuonekana kuridhika kisha alipeleka macho yake kusoma maelezo kwenye faili la ugonjwa wa Pendo alilokuwa amelishika mkononi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Baada ya kusoma maelezo kwa kitambo kifupi aliinua uso wake kumtazama muuguzi mmoja aliyefuatana naye, wakaonekana kuongea jambo fulani kwa lugha ya kitabibu, kuhusiana na tatizo la Pendo. Yule muuguzi alibetua kichwa chake kukubali.



    Muuguzi alikuwa mwanamke wa umri wa kati ya miaka ishirini na nane na therathini, mrefu wa wastani, si mweusi wala si mweupe kwa rangi. Alikuwa na mashavu mfano wa chungwa na alikuwa na nywele nyingi kichwani, nyeusi fii.



    Alikuwa amevaa gauni jeupe refu na pana kiasi lakini lililokuwa limeushika vyema mwili wake na kulichora vyema umbo lake kubwa. Kiunoni alikuwa amevaa mkanda mpana mweusi na kofia ndogo nyeupe ya kiuguzi yenye lesi iliyofunika sehemu ya utosi wa mbele kichwani kwake.



    Baada ya mazungumzo mafupi ya kitabibu kati ya Daktari Msimbe na muuguzi, Daktari Msimbe aliandika taarifa fulani kwenye lile faili la ugonjwa wa Pendo kisha alimgeukia Sammy aliyekuwa amesimama kando ya kile kitanda akionekana mwenye huzuni.



    “Poleni sana na kuuguza, Mungu atamsaidia mtoto na atakuwa sawa,” Daktari Msimbe alisema na kuachia tabasamu.



    “Asante sana daktari,” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani na kumeza mate kutowesha koo lake lililokauka.



    Kisha Daktari Msimbe aliachia tabasamu pana la kufariji na kuanza kupiga hatua kuondoka, alifungua mlango na kutoka huku akifuatwa na yule muuguzi.



    Kule nje Winifrida alikuwa amesimama na kujiegemeza kwenye ukuta wa korido pana na ndefu iliyozitenganisha zile wodi, alionekana kutafakari sana. Aligeuka kumwangalia Joyce aliyekuwa ameketi kwenye benchi huku akiongea na simu.



    Muda huo huo alimuona muuguzi mmoja wa kiume aliyekuwa akipita eneo lile akisukuma kiti cha magurudumu kilichokuwa kimekaliwa na mgonjwa mmoja aliyeonekana kama nusu mfu huku akiwa ametundikiwa chupa ya maji na mrija wake ulipeleka maji kwenye mshipa wa damu wa mkono wake wa kulia.



    Joyce akiwa na uso wenye huzuni aligeuza shingo yake kumwangalia yule mgonjwa na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiendela kusikiliza simu. Alionekana kukubali jambo kwa kubetua kichwa chake na kuvuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu. Muda mwingi alionekana kama aliyekuwa katikati ya mtihani mgumu sana.



    “Ni kweli mama, lakini hapa nipo njia panda… hali ya mjukuu wako hadi sasa siyo nzuri kabisa…” Joyce alisema huku akivuta kamasi nyepesi kutokana na machozi mepesi yaliyokuwa yakimtoka machoni.



    Aliyazungusha macho yake na kumwona Winifrida akiwa amejiegemeza kwenye ukuta huku akifuta machozi yaliyomtoka, Joyce alimtazama kwa makini na kuonekana kusita kidogo, kisha alishusha pumzi za ndani kwa ndani.







    “Haya mama, ngoja nione itakavyokuwa halafu nitakupigia simu kukujulisha… lakini nisingependa kabisa kuikosa fursa hii muhimu kwangu!” Joyce alisema na kukata simu yake akionekana kuchanganyikiwa.



    Aliinuka na kuondoka haraka eneo lile, akaingia wodini na kusimama karibu na Sammy huku akimwangalia Pendo kwa makini, huzuni ilikuwa inajionesha waziwazi kwenye macho yake. Sammy aligeuza shingo yake kumtazama Joyce, wakatazamana bila kusema neno. Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubetua juu mabega yake.



    * * * * *



    Saa saba mchana Paradise Club, Zainab alikuwa ameketi kwenye sofa sebuleni akisoma magazeti ya siku ile, uso wake ulikuwa umeliinamia gazeti moja la kila siku lililokuwa limeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hali iliyoonesha kuwa alikuwa amenogewa na habari iliyoandikwa gazetini.



    Ilikuwa ni habari-muendelezo iliyohusu kutoweka kwa mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi wa gazeti la MamboLeo, Abbas Dalali, ambaye hakuna yeyote aliyejua yupo wapi, na kama ni mzima au mfu.



    Kabla ya hapo, Zainab alikuwa amesoma habari nyingine mbili, moja ilihusu mke kumuua mumewe kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali, na nyingine ilihusu mume kumuua mkewe kwa kumbanika kwenye mkaa wa moto kama ndafu. Hizi ni habari alizokutana nazo kwenye magazeti karibu yote ya siku ile.



    Hii ndiyo Tanzania ambayo utafiti ulionesha kuwa ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoongoza kwa watu wake kutokuwa na furaha! Ndiyo maana kila kukicha habari za matukio ya wenzi kuuana zilitawala!



    Lakini… mbona hata nchi zilizoendelea zenye watu wanaoishi kwa furaha bado matukio kama hayo yalikuwepo, tena ni kwa kiwango kikubwa? Zainab alikumbuka kushuhudia matukio mengi ya mke kumuua mume au mume kuua familia yake yote, au mtoto kuua wazazi wake nchini Canada na hata Marekani!



    “Sasa nini kifanyike?” alijiuliza bila kupata jibu huku akiyatupa yale magazeti kando. Alikumbuka kuwa hata yeye aliwahi kutuhumiwa kumuua mumewe Hemed miaka kumi na miwili iliyopita, na vyombo vya habari viliandika sana kuhusu hilo.



    Zainab alimeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokuwa limekauka, alitamani sana habari ile ya mauaaji ya Hemed ibaki kuwa hadithi ya kutunga, hakupenda kukumbuka, lakini haikuwa hivyo. Mawazo sasa yalianza kupita kichwani kwake utadhani alikuwa akitazama sinema, aliyakumbuka maisha ya kijijini Mkuzi katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, alikozaliwa akiwa mtoto wa tatu na wa mwisho kwa mama, Bi Rehema, ambaye hakuwahi kuolewa.



    Zainab ndiye mtoto pekee aliyesoma hadi kumaliza kidato cha nne ingawa hakuwa na ujuzi wowote wa maana, kwani hata hiyo elimu ya kidato cha nne aliimaliza kwa mbinde baada ya baba yake mzazi, Adam Semaya kufa na mama yao kuugua ugonjwa wa ajabu.



    Zainab alipozaliwa aliwakuta dada zake wawili waliomtangulia, Nuru Mhina na Zuena Shauri ambao kila mmoja alikuwa na baba yake na hakuna kati yao aliyewahi kumfahamu baba yake, ni Zainab pekee aliyebahatika kumfahamu baba’ake, ingawa hata yeye alikuwa mtoto wa nje ya ndoa, kwani Bi Rehema hakuwa mmoja wa wake wanne wa Adam Semaya.



    Japo maisha ya Bi Rehema hayakuwa mazuri lakini alijitahidi sana kuhakikisha binti zake wanasoma. Alikubali kufanya kazi dhalili katika mazingira magumu mno, kiasi cha kumuondolea utu na heshima kwa jamii ili tu binti zake wapate elimu aliyoamini ingewakomboa toka katika lindi la ufakiri.



    Aliwahimiza sana binti zake kusoma kwani hakutaka na wao waishie alikoishia yeye, akiwa na wasiwasi kuwa kama angekufa wasingepata msaada kwa ndugu, kwa kuwa yeye alikuwa na ndugu wachache sana aliowafahamu upande wa mama yake, ambao hawakuwa ndugu wa damu, na hakumjua ndugu yeyote upande wa baba.



    Bi Rehema hakujua alikotokea mama yake wala ndugu wa baba’ake, na siku zote alikuwa akisononeka zaidi, kwa kujua kuwa binti zake pia wangefuruka na kuishi maisha ya kubangaiza kijijini kama yeye endapo wasingetia bidii kusoma, ndiyo maana aliwahimiza sana kusoma.



    Lakini maisha yalibadilika sana baada ya binti zake wakubwa, Nuru na Zuena kupachikwa ujauzito, kwa nyakati tofauti, wakiwa sekondari na kufukuzwa shule. Nuru hakurudi nyumbani, alitorokea kusikojulikana! Lakini Zuena alirudi kulea ujauzito wake nyumbani, na alipojifungua mtoto hakukaa hata mwezi akafa. Zuena akawa amekosa mwana na masomo, hivyo aliondoka nyumbani na kuelekea Arusha na kuanzia hapo hakuna tena aliyejua taarifa zake.



    Kuanzia hapo Bi Rehema alianza kuumwa hiki na kile na miaka kadhaa baadaye Mzee Semaya alikufa ghafla baada ya kuanguka chooni, wakati huo Zainab alikuwa kidato cha kwanza. Hali ya Bi Rehema ilibadilika zaidi, alianza kuwa mtu wa kuuguzwa. Hakuna aliyejua alikuwa anaumwa ugonjwa gani, walipima na kupima lakini hawakuona ugonjwa wowote.



    Aliendelea kuugua tu. Mara alalamike kuhusu miguu, mara alalamikie maumivu ya mgongo, mara kichwa! Ili mradi, hakukuwa na machweo yaliyopita asiwe katika hali ya kulalamikia maumivu. Katika kuhangaika huku na kule ikasemekana kuwa alikuwa amelogwa. Waliambiwa kuwa mchawi wake alikuwa ni mke mkubwa wa Adam Semaya



    Lakini Daktari wa afya ya akili wa Hospitali Teule ya Muheza aligundua kilichokuwa kinamsumbua na kuwaeleza kuwa alisumbuliwa zaidi ni msongo mkali wa mawazo. Hili la msongo mkali wa mawazo hakuna aliyelielewa, hivyo walichagua kuamini katika ushirikina kuwa alilogwa, kwani ilikuwa rahisi kwao kuelewa hilo kuliko kuambiwa mawazo yakizidi huleta ugonjwa.



    Zainab alikuwa na miaka kumi na nane alipomaliza kidato cha nne huko Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe. Rafiki wa baba yake aliyeitwa Julius Mhilu, ambaye alikuwa mhariri wa gazeti moja maarufu jijini Dar es Salaam, alimfanyia mpango wa kumpatia kazi katika hoteli ya kitalii ya Kilimanjaro, kwani alikuwa akifahamiana na wakubwa wengi serikalini.



    Zainab hakwenda popote kwa ajili ya mafunzo ya kazi hiyo kama wafanyavyo wasichana wengine, kwa kuwa alipenda sana kufanya kazi, hivyo ilimchukua muda mfupi tu kuimudu kazi hiyo.



    Alifanya kazi kwa bidii huku akijitahidi sana kumsaidia mama yake mgonjwa, kwa kutuma fedha kidogo nyumbani kila mwezi, kwani wakati huo ni yeye pekee aliyebakia kumsaidia mama yake kwa kuwa dada zake wote hawakuwepo nyumbani na hakuna aliyejua walikokuwa, isitoshe hakukuwa na mtu mwingine wa kumsaidia mama yao.



    Ni katika hoteli ile ya Kilimanjaro ndipo siku moja alikutana na Hemed Kimaro, mfanyabiashara wa madini. Kama ilivyokuwa kwa dada zake, Zainab alikuwa msichana mrembo kweli kweli na kila mwanamume alikuwa yuko tayari kutoa roho yake ili amuoe.







    Hemed alishindwa kuvumilia baada ya kumwona Zainab na kuamua kuingia mzima mzima kwenye mbio za kumfukuzia. Aliporusha ndoano hakuamini baada ya kuona akiibuka na ushindi. Hawakuwa na muda mrefu wa mazungumzo, na huo mfupi ulitosha kabisa kuwajulisha kuwa kila mmoja alitokea kumpenda mwenziwe. Miezi michache baadaye wakafunga ndoa.



    Miezi ikaanza kusonga na hatimaye mwaka mmoja ukakatika lakini Hemed hakuwa mjuzi wa masuala ya ndoa, aliyachukulia kama jambo la kawaida sana na hakujali hisia za mwenzi wake wala kumfikisha alikotaka kufika kimapenzi. Muda mwingi alikuwa ‘bize’ na biashara zake na akirudi nyumbani amechoka, analala, wakati Zainab alitaka kufurahia ndoa yake…



    Miaka mingine miwili ikapita tangu na hali ilikuwa ile ile, hatimaye mwaka wa nne ukafika lakini mambo haya kubadilika, yalibaki kuwa yale yale! Tena yalianza kuwa mabaya zaidi. Hemed alikuwa bize zaidi kiasi cha kuchelewa hata kurudi nyumbani na wakati mwingine hadi usiku wa manane. Siku moja Zainab alilala sebuleni kumsubiri mumewe kwa saa nyingi lakini hakurejea kabisa.



    Hata aliporejea siku iliyofuata Zainab alimkabili kumuuliza alilala wapi, lakini alijibiwa kirahisi rahisi tu, Zainab kwa kumpenda mumewe alijitahidi kuvumilia akiamini kuwa huo ulikuwa ni upepo mbaya tu uliokuwa ukipita na muda si mrefu maisha yangesonga vyema.



    Kutahamaki mwaka wa tano! Zainab alishangaa, mwaka wa tano katika ndoa lakini mambo ni yale yale na hawakuwa na mtoto, wala Hemed hakuonesha kushtuka. Ni wazi Hemed aliendelea kuchukulia mambo ya ndoa kirahisi rahisi.



    Usiku Zainab alikuwa hapati usingizi, muda mwingi alikuwa anawaza kuhusu hatma ya ndoa yake, akibaki peke yake alikuwa analia tu, donge la hasira lilimkaba kooni na hakuweza kulihimili mpaka atoe kilio. Siku moja alijiuliza sana na kuamua kupeleka shauri lao kwa wifi yake mkubwa, Dk. Salma Oduya.



    Hapo ndipo mume wa wifi yake, Mr. Oduya alipopata mwanya wa kuwa na ukaribu na Zainab na baadaye kupenyeza ushawishi wake, haikuchukua muda wote wawili wakagundua kuwa kila mmoja alihitaji faraja lakini wote walionekana kuikosa katika ndoa zao. Hawakuwa na njia nyingine isipokuwa kuitafuta nje ya ndoa na hatimaye Zainab akapata ujauzito…



    _____



    “Madame, kuna tatizo lolote?” sauti laini ya Lilian ilipenya hadi kwenye ngoma ya masikio ya Zainab na kumzindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Aliinua uso wake kumtazama Lilian aliyesimama mbele yake na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilazimisha tabasamu.



    Lilian alikuwa amesimama pale kwa kitambo kirefu akimsemesha Zainab lakini ilionesha kuwa Zainab alikuwa mbali kimawazo. Alimtazama Zainab kwa macho yenye udadisi na mkononi alikuwa ameshika bilauri na chupa ndefu ya mvinyo mwekundu wa bei ghali aina ya Romanee-Conti uliotengenezwa nchini Ufaransa.



    “Kinywaji chako hiki hapa, madame,” Lilian aliongea kwa sauti tulivu huku macho yake yakiendelea kuweka kituo kwenye uso wa Zainab.



    Na hapo Zainab akakumbuka kuwa alipokuwa anasoma magazeti alimuagiza Lilian kumtafutia mvinyo mwekundu wa Kifaransa aina ya Navette de Marseille au Romanee-Conti.



    “Ah, usijali mdogo wangu… weka hapo,” Zainab alisema huku akimuonesha Lilian ilipo meza, alijitahidi kuupamba uso wake na tabasamu na kuyakwepa macho ya Lilian. Alikuwa analengwa na machozi kutokana na kukumbuka mengi katika maisha yake ya zamani.



    Kumbukumbu zile zilikuwa zimemuumiza sana, hasa kwa kuwa mama yake Bi Rehema alikufa kwa msongo mkali wa mawazo miezi miwili tu baada ya yeye Zainab kutuhumiwa kushiriki katika mauaji ya mumewe, Hemed.



    “Asante sana mdogo wangu, unaweza kuendelea na kazi zako kama nikihitaji kitu nitakujulisha,” Zainab alimwambia Lilian baada ya kuona alikuwa bado amesimama mbele yake akisubiri maagizo. Lilian aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile, akaelekea jikoni huku akiwa na wasiwasi.



    * * * * *



    Saa saba mchana katika ofisi za Mr. Oduya zilizo ghorofa ya sita ya jengo la ghorofa kumi na mbili lililomilikiwa na Mr. Oduya, jengo lililokuwa katika barabara ya Bagamoyo eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo na mgeni wake, Balozi Aldolf Mageuzi, walikuwa wanabadilishana mawili matatu.



    Ni Balozi Mageuzi aliyeomba kuonana na Mr. Oduya mchana ule, na yeye hakuweza kukataa ombi lake kwa kuwa alikuwa mmoja kati ya watu muhimu na walioheshimika sana. Balozi Mageuzi alikuwa kati ya washauri muhimu sana wa Rais wa Tanzania, Dk. Yohana Funguo, hasa katika masuala ya diplomasia, ulinzi na usalama wa taifa.



    Ni kwa sababu ya kutambua umuhimu wake ndiyo maana mchana wa Jumapili ile Mr. Oduya aliondoka Paradise Club akimwacha kipenzi chake Zainab, badala yake alitenga muda ili aweze kuonana na Balozi Mageuzi.



    Balozi Mageuzi alifika pale kuongea na Mr. Oduya ili kujua upepo wa kisiasa kwa upande wake ulikuwaje, hasa baada ya kushuhudia vuguvugu la urais ndani ya Chama Cha Ukombozi (CCU) likizidi kupamba moto, kwani Rais Yohana Funguo alikuwa mbioni kumaliza muhula wake wa pili.



    “Niseme ukweli, upepo wa kisiasa si mbaya, unavuma vizuri sana licha ya changamoto za hapa na pale kutok kwa washindani wangu lakini nimekwisha jiweka vizuri sana kwani nina sapoti kubwa ya mabilionea wa Paradise Club na wamekubali kufadhili kampeni zangu nchi nzima,” Mr. Oduya alimwambia Balozi Mageuzi.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Ni jambo zuri lakini kumbuka awamu hii siyo ile ya Rais Sakaya Mkiete, hii ni ya Dk. Funguo, na mfumo wote ndani ya CCU umebadilika, sidhani kama hao mabilionea wana ushawishi mkubwa ndani ya chama, labda nje ya chama. Hata hivyo, bado sina wasiwasi na nguvu yako ingawa hupaswi kujipa uhakika sana,” Balozi Mageuzi alisema huku akimwangalia Mr. Oduya kwa makini.



    “Kwa nini unasema hivyo, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.



    “Kwa hali ilivyo, hamasa ya kuwania uteuzi imeongezeka sana ndani ya chama. Ila bado imeendelea kuwa siri ni nani na nani watajitosa kuwania uteuzi. Lakini najua mheshimiwa Tumbo na Dk. Hussein Abbas watawania…” Balozi Mageuzi alisema na kuongeza.







    “Dk. Hussein Abbas japo anaonekana kama asiye na nia lakini kwa taarifa nilizonazo atawania nafasi ya kuteuliwa na chama, ni mmoja kati ya wanachama wenye nguvu kubwa kwenye chama na kwa siku za hivi karibuni nguvu yake imeongezeka na kutishia vigogo wenzake serikalini ambao nao wana dhamira kama yake…”



    “I see! Kumbe mambo ni moto moto kiasi hicho!” Mr. Oduya alionesha kushangaa sana.



    “Hivi nikuambiavyo tayari mheshimiwa Tumbo ameanza kampeni za chini kwa chini ili kutafuta uungwaji mkono katika zoezi la kura za maoni na katika vikao vya juu vya uteuzi ndani ya chama…”



    “Niseme ukweli, sikutegemea kama Dk. Hussein Abbas angeonesha nia ya kutaka kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taarifa nilizo nazo ni kwamba anaandaliwa kuwa Rais wa Zanzibar, ndiyo maana nilifikiria kumshirikisha kwenye mikakati yangu ya urais!” Mr. Oduya alisema kwa mshangao.



    “Hakuwa akitaka ila wazee wamemuomba. Na jambo hili limesababisha makundi ndani ya chama, lipo kundi linalomsapoti Dk. Hussein Abbas na lingine linamshabikia Mheshimiwa Tumbo, kwa hiyo kuna mchuano mkali wa chini kwa chini kati ya vigogo hawa wakubwa serikalini. Kumbuka hawa waliwahi kuwa maswahiba wakubwa lakini kwa sasa wamekuwa mahasimu wakubwa. Kwa ufupi hiyo ndiyo hali halisi ilivyo ndani ya Chama,” Balozi Mageuzi alisema na kutingisha kichwa chake kwa huzuni.



    “Nimekuelewa Balozi, kama Dk. Hussein Abbas naye anatafuta nafasi ya kuungwa mkono kugombea urais basi tutegemee mnyukano mkubwa kati yake na mheshimiwa Tumbo. Wawili hawa watakigawa chama katika sehemu mbili, sipati picha mtikisiko utakaokuwepo ndani ya chama katika uteuzi, ndiyo maana naamini kuwa mwisho wa siku ni mimi nitakayeibuka mshindi, japo shaka yangu kubwa ni mheshimiwa Tumbo kutumia siasa za majitaka…” Mr. Oduya alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.



    “Kweli kabisa, kuna kila dalili za mpasuko ndani ya chama, hawa vigogo wameanza kukigawa chama katikati na hilo ndilo hasa limenifanya nitake kukuona. Cha kwanza nijue msimamo na pili nikupe taarifa ambazo naamini bado hujazipata,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Zipi hizo?” Mr. Oduya aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.



    “Sipendi kukuficha rafiki yangu lakini ni ukweli usiopingika kuwa utapata wakati mgumu sana kuteuliwa ndani ya chama kwa sababu ya vigogo hawa wawili kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama na wewe nguvu yako kubwa iko nje ya chama. Hivi sasa kuna mkakati maalumu wa kumshawishi Rais ili jina lako likatwe kabla ya kufika Halmashauri Kuu. Juzi usiku kulikuwa na kikao cha siri Chattle Hotel na mwenyekiti wake alikuwa Katibu Mkuu wa Chama, Dk. Bazil Uledi…” Balozi Mageuzi alisema na kunyamaza kidogo, akailamba midomo yake iliyoanza kukauka.



    “Ninazo taarifa za uhakika kuwa mheshimiwa Tumbo tayari ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama na wajumbe wengi wa kanda yote ya kusini, pwani na kwa sehemu kubwa ya kanda ya magharibi. Kuna mtandao makini na wa siri umeundwa ili kuhakikisha wanashinda, kusema kweli hawalali, wanafanya kazi usiku na mchana…” Balozi Mageuzi aliongezea.



    Maneno yale yalimshtua sana Mr. Oduya, alibaki ameduwaa huku akihisi joto kali mwilini na jasho jepesi likianza kumtambaa sehemu mbalimbali za mwili wake, koo lake lilikauka ghafla na nywele zikamsimama kichwani kwa hofu.



    “Wanahangaika usiku na mchana kwa kuwa hofu yao kubwa ni wewe, wanaogopa wakikuachia upenyo kidogo utawashinda kwani jina lako linatajwa sana katika orodha ya watu wenye sifa na uwezo wa kuiongoza nchi hii, kutokana na misaada mbalimbali ambayo umekuwa ukiitoa kwa vikundi vya walemavu, akina mama na vijana,” Balozi Mageuzi alisema baada ya kuona Mr. Oduya yupo kimya akimtumbulia macho.



    “Kwani mheshimiwa Rais anasemaje kwenye hili? Umebahatika kusikia chochote kuhusu mtu anayemuunga mkono?” hatimaye Mr. Oduya alimudu kuuliza, hata hivyo bado alikuwa na wasiwasi.



    “Sijamsikia kusema chochote, lakini natambua urafiki wenu ulivyo mkubwa, yeye ni mmoja wa watu wanaokukubali, na wapinzani wako wanajua hilo, ndiyo maana hawapati usingizi… hivi sasa wanawatumia watu wa Usalama wa Taifa kukusanya kila taarifa ya kashfa inayokuhusu ili wampelekee Rais,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Kilipita kitambo kirefu cha ukimya, kila mmoja alikuwa kimya akitafakari. Sasa Mr. Oduya hakuhisi tena joto kali mwilini bali alianza kukihisi ubaridi mkali ukimtambaa mwilini mwake.



    “Lakini usihofu, najua yupo mtu mmoja muhimu sana, kama utaweza kumshawishi ajiunge na upande wako utakuwa umemaliza vita kabla hata hujafika kwenye uwanja wa mapambano…”



    “N-nani?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku uso wake ukianza kuonesha matumaini.



    “Makamu Mwenyekiti wa Chama, mzee Fabian Magulu… kama umegundua huyu mzee anakubalika sana, ndiye mwenye ushawishi mkubwa siyo tu ndani ya chama bali hadi serikalini na ndiye alikuwa nguzo muhimu ya ushindi na mafanikio yote ya Rais Funguo, wakati akiwania kipindi cha pili cha urais. Unakumbuka alipigwa sana vita ili aishie kipindi kimoja,” Balozi Mageuzi alisema na kumfanya Mr. Oduya avue koti lake na kulitundika kwenye kiti chake, sasa hakuwa akihisi tena baridi.









    “Unajua sina ukaribu sana na mzee Magulu japo tunafahamiana, sijajua nitamuingiaje!” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti tulivu.



    “Usipate taabu, ndiyo maana nipo hapa kukusaidia, nipe wiki moja tu nitakuelekeza nini cha kufanya ila kama utakuwa tayari kufuata ushauri wangu…”



    “Kwa nini nisifuate ushauri wako wakati ni wewe ndiyo umenifumbua macho?” Mr. Oduya alisema huku akionesha uso wenye matumaini mapya, sura yake sasa ilikuwa imejenga tabasamu pana.



    * * * * *



    Saa kumi na moja na dakika arobaini jioni ilimkuta Madame Norah akiwa ameketi kwenye kochi kubwa la sofa ndani ya ukumbi mkubwa wa kisasa wenye jukwaa zuri la kisasa lililokuwa linatazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya burudani au kufanyia mikutano. Kulikuwa na seti moja ya masofa yaliyokuwa yamepangwa kwa namna ya kulizunguka lile jukwaa.



    Ukumbi ule ulikuwa katika jumba zuri la kifahari la ghorofa tatu lililokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi katika eneo la Mikocheni, likiwa limezungukwa na miti mirefu ya kivuli. Eneo lile lilikuwa la majumba ya kifahari ya makazi ya kisasa ya watu wenye ukwasi, yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika.



    Jumba lile lilikuwa limezungukwa na ukuta uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake na lilikuwa na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri.



    Madame Norah alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza japo alikuwa na umri mkubwa, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza kutokana na mazoezi.



    Miguuni alikuwa amevaa viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio vya rangi ya bluu na harufu nzuri ya manukato ghali aliyokuwa amejipulizia mwilini ilitamalaki mle ukumbini



    Japo alijitahidi kuonekana mchangamfu sana lakini macho yake yalionesha huzuni fulani, hakuwa na furaha kabisa. Alikuwa mbali kimawazo japo alionekana kama alikuwa anamwangalia msaidizi wake na mtayarishaji wa kipindi chake maarufu cha Madame Norah Show, Jessica Walari.



    Wakati huo Jessica alikuwa anatoa maelekezo kwa wapigapicha za mnato na video wakati wakichukua picha za matukio mbalimbali za wabunifu wa mavazi waliokuwa wakiandaa mavazi na kuivalisha ‘midoli’ mikubwa iliyokuwepo eneo lile.



    Pale kwenye masofa alipoketi Madame Norah pia kulikuwa na wageni wachache mashuhuri waliofika kumuunga mkono Madame Norah katika shughuli zake za kusaidia jamii. Kushoto kwa Madame Norah aliketi kijana mmoja mtanashati asiyezidi miaka therathini na tano, aliitwa Florian na alikuwa mpenzi wa Madame Norah.



    Florian alikuwa mweupe, mwenye ngozi nyororo na umbo kakamavu la kimichezo, alikuwa amevaa fulani nyekundu na suruali ya jeans ya rangi ya bluu. Kichwani alivaa kofia nyekundu aina ya kapelo na miguuni alivaa raba ndefu na ngumu za rangi nyekundu.



    Kama walivyo vijana wengi wenye tabia ya kupenda wanawake waliowazidi umri kwa sababu ya kutaka fedha zao, Florian hakuona aibu kuambatana na Madame Norah kila alipokwenda, na muda ule alikuwa amejiegemeza kwenye sofa katika hali ya mahaba.



    Kuna muda alimnong’oneza jambo Madame Norah wakati akiongea na wageni wake, Madame Norah aligeza shingo yake kumtazama Florian na kuachia tabasamu pana la kimahaba, kisha alinyoosha mkono wake na kumgusa shingo yake.



    Florian alikuwa ameweka mkono wake wa kulia juu ya paja la Madame Norah kisha aliuchukua mkono wa kushoto wa Madame Norah, moja kwa moja akaupeleka kwenye uso wake, aliupitisha kwenye paji la uso wake na kumfanya Madame Norah kuligusagusa paji lake.



    Muda ukafika wapiga picha wakaweka tayari kamera zao kuzielekeza jukwaani kwa Madame Norah, kisha Jessica alitabasamu na kumpa ishara ya dole gumba kuwa wapo tayari kuanza kuchukua picha ya kilichowaleta pale.



    Madame Norah alinong’ona jambo kwenye siko la Florian na kumfanya aachie kicheko hafifu cha mahaba. Madame Norah alitabasamu na kumpiga piga Florian mgongoni kwa mahaba, kisha Florian aliinuka taratibu na kuondoka akimwacha Madame Norah na wageni wake pale jukwaani.



    Madame Norah alishusha pumzi za ndani kwa ndani, akaketi vizuri kwenye sofa, na baada ya kupewa ishara na Jessica, alianza kwa kujitambulisha na kuwatambulisha wageni wake kisha akaeleza lengo lake.



    “Kwanza niweke wazi, maonesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti kidogo na miaka mingine, tumeandaa kitu kinachoitwa Live from the Red Carpet kitakachowafanya watu wote wawe sehemu ya onesho. Litakuwa onesho kubwa kuwahi kufanyika Afrika kwani tumewaalika wabunifu na wanamitindo wakubwa duniani na lengo likiwa kutunisha mfuko ili kuwajengea makazi bora wazee wasiojiweza sambamba na kituo na shule ya watoto wenye ulemavu na waishio katika mazingira magumu chenye miundombinu rafiki kwa elimu yao na makazi. Itakuwa shule ya aina yake na ya kimataifa kwani baadaye tutaweza kupokea hata watoto kutoka maeneo mengine ndani na nje ya nchi…” Madame Norah alisema huku akiachia tabasamu.



    “Kupitia Madame Norah Foundation tutazidi kutatua matatizo mbalimbali ya watoto na wazee wasiojiweza ambao ni kundi linaloonekana kusahaulika sana. Tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwenye vituo vya yatima na hospitalini kusaidia watoto wadogo na hata wazee, tumekuwa tukisaidia huduma za afya, chakula na mambo mengine. Katika utafiti tulioufanya mwaka jana tumegundua kuwa kundi moja limesahaulika sana, ni la watoto wenye ulemavu. Kundi hili linazidi kuongezeka na wanakumbana na changamoto nyingi sana…” Madame Norah alinyamaza kidogo na kumeza mate ili kutowesha koo lake lililoanza kukauka.







    “Kwa miaka kumi sasa tangu niingie katika tasnia ya ubunifu na mitindo, mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa kukusanywa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.” Madame Norah alimaliza hotuba yake na kuachia tabasamu.



    Baada ya kutambulisha lengo lake waandishi wa habari walimuuliza maswali ambayo aliyajibu kwa ufasaha kisha alianza kuwatembeza waandishi na wageni kuwaonesha sehemu mbalimbali na kazi walizokuwa wanazifanya pamoja na hatua mbalimbali za ubunifu wa mavazi ndani ya lile jumba.



    Baada ya kuwatembeza eneo lote Madame Norah aliagana na wageni wake kisha akaelekea kwenye ofisi yake binafsi iliyokuwa juu kabisa, kwenye ghorofa ya tatu ya lile jumba la kifahari.



    Aliingia ofisini kwake na kuketi kwenye kiti kirefu cha kuzunguka cha kiofisi cha ngozi halisi kilichokuwa na magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea.



    Ilikuwa ofisi nzuri yenye samani za bei ghali, ikiwa na kiyoyozi aina ya Boss kilichokuwa kikisambaza hewa safi mle ndani, zulia nene la manyoya la rangi nyekundu sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta moja aina ya IMac Retina 5K ya inchi 27, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.



    Pembeni kulikuwa na meza nyingine ndogo ya kioo ya pembe nne na juu yake kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu aina ya Navette de Marseille na bilauri, chini ya ile meza kulikuwa na magazeti na majarida mbalimbali ya mitindo.



    Meza hiyo ilikuwa mbele ya kochi moja kubwa jeusi la sofa na ukutani juu ya ile meza ya kioo kulikuwa na shubaka la vitabu lililokuwa na vitabu na mafaili yenye nyaraka mbalimbali yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa.



    Upande wa kulia kulikuwa na madirisha mapana ya kioo yaliyokuwa na mapazia mepesi marefu ya rangi ya samawati, na pembeni kabisa kulikuwa na mlango ulioelekea kwenye maliwato maalumu ndani ya ofisi ile.



    Pia kulikuwa na kabati kubwa la ukutani lenye mbao zilizosanifiwa kwa ustadi wa hali ya juu na kulikuwa na kioo kirefu cha kujitazama, pembeni yake kulikuwa na jokofu ukubwa aina ya BOSS lililojazwa vinywaji mbalimbali vya kumchangamsha yeyote aliyeingia humo, hata kama angekuwa amechoka sana baada ya kazi ngumu.



    Akiwa na huzuni, Madame Norah alivuta droo moja ya meza yake na kutoa picha tatu, aliziangalia kwa kitambo na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionekana kukata tamaa.



    Zilikuwa picha zake za zamani, akiwa bado binti tineja. Picha moja ilimuonesha akiwa na wadogo zake wawili, wote wa kike, wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao ndogo ya nyasi kijijini kwao Mkuzi Wilaya ya Muheza. Picha hiyo ilipigwa kama kumbukumbu baada ya kupata matokeo mazuri ya darasa la saba.



    Madame Norah alikuwa amevaa gauni refu la zambarau lenye maua ya rangi mchanganyiko na alikuwa na miaka kumi na tano, wadogo zake mmoja alikuwa na miaka kumi na moja na mwingine alikuwa na miaka mitatu.



    Picha ya pili aliipigia shuleni wakati huo akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Usagara jijini Tanga, alikuwa na wanafunzi wenzake na picha ya tatu alikuwa na kijana mmoja mtanashati wakiwa katika mkao wa kimahaba.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Aliitazama kwa kitambo kirefu ile picha ya tatu, mara matukio fulani ya zamani yakaanza kumjia akili kwake, alikuwa kama aliyekuwa anaangalia kipande cha filamu ya kuhuzunisha. Ilikuwa ni mchanganyiko wa picha mbalimbali za msichana mrembo wa miaka kumi na nane akiwa analia kwa uchungu katika chumba kidogo chenye mwanga hafifu wa taa.



    Msichana huyo alikuwa mwenye huzuni nyingi na alitazama mbele yake kwa huzuni, wakati huo sauti ya mwanamume ilisikika ikimtaka aondoke haraka na haakutakiwa kuonekana tena pale. Kisha sauti ya mtoto mchanga akilia nayo ikasikika…



    Madame Norah alizinduka kutoka kwenye yale mawazo, akaangaza macho yake huku na huko na kugeuka kujitazama kwenye kioo kirefu cha kujitazama, alijitazama kwa kitambo akionekana mwenye huzuni kubwa.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog