Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NYUMA YAKO - 3





    Simulizi : Nyuma Yako

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Saa tano asubuhi …

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Nilifunga mlango wa taksi baada ya kukamilisha malipo yangu. Nikatengenezea koti langu mwilini na kutazama mtaa ambao nilikuwa nimeshushwa. Hapo kulikuwa na nyumba kadhaa zikiwa zimesimama kwa kufuatisha barabara hii ya lami.

    Na kama nilivyokuwa nimemuelekeza dereva taksi, alikuwa amenishusha mbele ya nyumba ninayotakiwa kushukia. Nyumba yenye anwani 2345!

    Nikaitazama nyumba hii kabla ya kuijongea. Ilikuwa ni nyumba tulivu isiyo na dalili ya makazi. Madirisha yake yalikuwa yamejaladiwa na vioo yakiwa hayana mapazia.

    Nikanyanyua miguu mpaka mlangoni, nikagonga mlango na kutulia nikiskizia. Hamna kitu. Nikagonga tena na tena, hamna kitu! Sasa nikaanzaa kuamini kuwa humo ndani hamna watu. Nikachungulia dirishani kwa ufupi alafu nikaujaribisha kuusukuma mlango. Haukufunguka.

    Nikausukuma kwa nguvu kidogo, ukatenguka na kufunguka! Taratibu nikausogeza na kuzama ndani. Nikarusha macho yangu huku na kule kwa tahadhari huku mkono wangu wa kuume ukiwa karibu na nyonga ya mguu, kwa tahadhari ya kuchoropoa silaha.

    Ndani ya nyumba hii kulikuwa na samani za zamani, buibui na vumbi. Ni nyumba iliyotelekezwa, tena si karibuni. Niliingia mpaka chumbani na hata jikoni nisikute alama yoyote ya uhai au uwepo wa binadamu. Nikiwa nimerejea hapo sebuleni, kwa chini mbali ukutani, nikaona vipandevipande vya vyupa.

    Nikavisogelea na kuokota kipande mojawapo na kukitazama. Kilikuwa ni kipande cha picha. Nikajaribu kuonganisha vipande kadhaa vya vyupa hivyo, nikapata kuona picha ya mwanamke mwenye nywele nyeusi na macho yalopoa.

    Lakini sura yake sikuweza kuiona vema kama nilivyotaka. Vipande vingine vya chupa vilikuwa vimesagika vibaya hivyo kupoteza kabisa maana zake. Na nilipotazama vema, nikabaini kuwa katika picha hiyo, huyo mwanamke alikuwa ameketi na mtoto.

    Sasa ni kheri ya picha ya huyo mwanamke, ya mtoto ndiyo ilikuwa haionekani kabisa, nyang’anyang’a! Nisingeweza kutambua lolote lile isipokuwa rangi ya nywele zake. Rangi ya dhahabu.

    Basi nikapiga picha kadhaa kwa kutumia simu yangu alafu nikazama ndani kule chumbani kwa nia sasa ya kukagua makabati nione ni nini nitapata. Nikaona nguo za mtoto waa kiume, na za mwanamke. Lakini zaidi nikaona kifaa cha kusaidia kupumua kwa watu wanaosumbuliwa na tatizo la pumu!

    Hapa sasa nikapata kukumbuka kuhusu kifaa hicho. Kifaa alichonionyeshea Daniele kuwa wamekiokota uwanja wa ndege wakidhania ni cha Raisi. Ina maana ile ilikuwa ni ishara au?

    Nikakiweka kifaa hicho kibindoni, lakini kabla sijaendelea na kazi ya upekuzi, nikasikia gari ikisimama kwa ‘kuchuna’ breki kali huko nje. Haraka nikajongea dirisha na kutazama.

    Nikaona wanaume watatu wakiwa wamevalia nguo nyeusi wakishuka toka kwenye Volkswagen modeli ya zamani. Gari hiyo kwa ubavuni ilikuwa na chapa ya samaki na maneno ya kijerumani yakimaanisha kampuni ya uvuvi.

    Wanaume hao walikuwa na sura ya kazi, na nikadhani huenda wakaja mule nilipokuwapo, ila lah! Wakanyookea nyumba ya pili na kuzama humo. Sikujua walienda kufanya nini, na sikujua kwanini niliwatilia shaka. Nilihisi tu si watu wema.

    Basi nikapiga moyo wangu konde na kuendelea kusaka. Sikupata cha maana, baada ya kama dakika kumi, nikaona nitoke humo ndani niende zangu nikiwa nimelenga kutafuta serikali ndogo ya eneo hilo ili nipate walau taarifa juu ya wakazi wa hapa.

    Nilipotoka nikatazama ile nyumba jirani ambayo iliwameza wale watu niliokuwa nawatilia mashaka. Sikuona jambo. Muda si mrefu,, kwa mwendo wangu wa haraka, nikawa nimefika kituoni ambapo nilipanda gari nikilenga kuelekea kwenye ofisi ndogo za wilaya. Ikanichukua kama dakika kumi tu kufika hapo. Nikazama ndani na kueleza shida yangu.

    Nilijitambulisha kama James Tuck toka Marekani na nimefika hapo kumuulizia ndugu yangu ambaye anakaa Munich kwani nimefika kwake sikumkuta.

    Mhudumu akaniuliza kuhusu anwani yake, nikamtajia. Muda si mrefu akanielekeza mahali pa kwenda, yaani kama balozi wa mtaa, huko nitapata majibu kamili na ya uhakika.

    Kwahiyo nikajiresha tena kituoni na ndani ya muda mfupi nikawa nimefika nilipoelekezwa. Nikamkuta mzee mmoja mnene mfupi akiwa anakunywa bia aliyoitunza kwenye glasi kubwa. Nikamsalimu na kumweleza shida yangu. Akaniambia ya kuwa mwanamke huyo aliyekuwa anakaa kwenye yale makazi alipotea na hakuna mtu anayejua wapi alipo hata sasa.

    “Ni kama miezi mitano sasa. Taarifa pekee tuliyonayo ni kwamba jirani yake aliona gari aina ya van ikimpakia na kwenda naye, yeye pamoja na mtoto. Hakumuaga mtu yeyote, hivyo hamna anayefahamu.”

    “Vipi kuhusu namba ya usajili ya van hiyo?” nikauliza.

    “Hamna mtu aliyeijali,” akanijibu huyo mzee. “Nani atasumbuka na kunakili namba za magari na ingali haikuonekana kama ni tukio la shuruti?”

    “Na vipi kuhusu huyo jirani? Yupo?”

    Mzee akatikisa kichwa na kunambia, “naye hayupo!”

    “Amehama?”

    “Hakutoa taarifa kama anahama. Sijui alipoelekea.”

    Nilipompeleleza zaidi nikagundua kuwa huyo jirani anayemwongelea alikuwa anakaa kwenye ile nyumba ambayo niliwaona watu wakiingia humo. Nikamuuliza, “Ina maana hapo pana wakazi wapya?”

    “Ndio, kuna wanaume wa kiwanda cha mbao hapo,” akanijibu kishaa akagida fundo la bia. Lakini …

    Wale wanaume mbona hawakuonekana kama wafanyakazi wa kiwanda cha mbao? Nilijikuta nikitia shaka. Mbona gari yao ilikuwa na chapa ya samaki kama ni hivyo?



    **



    Maswali hayo yalibaki kichwani hata wakati natoka kwenye jengo hilo. Nilikuwa nawaza na nikaona endapo nikiendeleza mawazo hayo basi naweza jikuta nagongwa na gari barabarani.

    Nikatembea zangu mpaka kituoni na kukwea basi. Kama nipendavyo nikaenda kukaa nyuma, kichwa nikakiegeshea kitini na huku macho yangu yakiwa yanatazama mji. Namna vitu viendavyo nyuma wakati sisi tukienda mbele.

    Wakati huo pia nikiwa nawaza kumwambia Jack Pyong juu ya yale niliyoyakuta kule kwenye nyumba yenye anwani elekezi ili anambie kama kuna kingine cha kufanya baada ya hapo kama vile alivyoniahidi hapo awali.

    Nikiwa katika ombwe hilo, basi likasimama na kunifanya nizingatie. Kwa macho yangu ya kipelelezi nikayarusha kutazama nani anashuka kana kwamba namjua mtu huyo, kabla sijatoa huko macho nikaona wanaume wawili wakiwa wanapanda basi. Wanaume hawa walinifanya niwatazame zaidi kwa namna walivyovaa na hata mwonekano wao maana nilihisi walikuwa wakifanania na wale niliowaona kwenye ile nyumba ya pembeni na 2345!

    Wakati nikiwatazama, mmoja wao akanitazama pia tukakutana macho kwa macho! Tukatazamana kwa kama sekunde tatu kabla hajageuza uso wake kutazama kando. Mimi nikaendelea kumtazama zaidi na zaidi, na hata yeye alilitambua hilo.

    Niliwakagua kwa macho yangu na kujiridhisha kuwa huenda wakawa na silaha ndani ya makoti yao. Basi nikaanza kufikiria namna ya kuwakabili kama ni mimi wananifuatilia …

    Tukaenda kwa mwendo wa kama dakika sita, nikasimama na kutoa ishara kuwa nashuka kituo kinachofuata kwa kubinya kamba ya kumshtua dereva.

    Hivyo tukasonga kidogo tu, na basi likaanza kupunguza mwendo kuashiria laenda kusimama. Liliposimama, nikanyanyuka na kushuka.

    Hapa sio nilipotakiwa kushuka ila niliona panastahili mimi kushukia kwasababu ya uwingi wa watu. Hiyo ni kwasababu za kiusalama.

    Nikazama ndani ya watu na kujichanganya lakini kwa wakati huohuo nikiwa natazama kama nyuma yangu nafuatwa. Sikuona watu. Wanaume wale hawakushuka. Nikaendelea kuzamia na kuzamia huko hata mahali ambapo sipajui alimradi kujihakikishia usalama. Nilipoona ni salama sasa, nikatulia kwenye benchi na kutoa simu yangu mfukoni, nikawasiliana na Jack.

    “Jack, nimetoka kwenye ile anwani! … sijakuta mtu huko!”

    “Kabisa?”

    “Ndio. Ni samani za zamani na mabaki ya nguo na picha … na kifaa cha kuhemea!”

    “Unaweza kun’tumia hiyo picha?”

    “Sidhani kama utaielewa, ilikuwa condensed kwenye kioo, imevunjikavunjika.”

    “Haionekani hata kidogo?”

    “Kwa mbali, ila ni ya mwanamke tu. Ya mtoto haionekani kabisa!”

    “Gosh!” Jack akalaumu. Nikamuuliza,

    “Vipi, hamna namna ya pili kama ulivyonieleza?”

    “Ipo, ila hiyo ya pili nilikuambia itakuwa confirmed na hiyo ya kwanza. Sikukuambia hivyo, we fala?”

    “Sasa nifanyeje?”

    Akanielekeza mwonekano wa mtoto, kisha akanisihi nirudi kule kwenye anwani 2345 ili nikahakikishe kama huyo mtoto alikuwa anaishi hapo kwa kutumia taarifa za majirani.

    Nikamuuliza, “Jack, huyo mtoto ana nini? Kwanini yeye?”

    “Sijui, Tony. Ila fanya nilichokuambia kwa maana hiyo MUNICH 2345 itakuwa ni yeye.” Aliponieleza hayo akasema, “Nipo busy na shemeji yako, baadae!” kisha akakata simu.

    “Pumbavu!” nikalaani nikiiweka simu kibindoni, kisha nikatoa kile kifaa cha kuhemea ambacho nilikiokota kule kwenye anwani 2345 na kukitazama kwa umakini.

    Nikagundua kifaa hicho kilikuwa kimechorwa katuni kwa kutumia ‘marker pen’ rangi ya bluu. Marker pen inayoelekea inaelekea kufifia sasa.

    Mchoro huo wa katuni ulikuwa ni wa mwanaume aloyechorwa kwa mtindo wa njiti na nywele zake zikisimama kama vijiti. Nikawaza atakuwa nani huyo? Huenda akawa ni huyo mtoto ambaye Jack anamwongelea?

    Sikuwaza sana juu ya hicho, nikakiweka kile kifaa kibindoni kisha nikatazama kushoto na kulia alafu nikaanza kuchukua tena hatua kutoka jengoni humo.



    **

    Saa tisa alfajiri …



    Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!

    Punde mlango ukafunguliwa, akatoka mwanamke mzee ambaye alinikagua upesi kwa macho yake ndani ya miwani yenye lenzi kali kisha akaniuliza haja yangu.

    Tulikuwa tunatumia lugha ya kijerumani.

    “Tafadhali, naomba kuulizia,” nikasema kwa sauti ya upole. Mwanamke huyo akatambua, nadhani kwa lafudhi yangu, kuwa mimi mgeni. Akafungua mlango na kunikaribisha ndani.

    Nilipoketi akaniuliza kama ningependelea maji ama bia. Ni tamaduni ya wajerumani kunywa bia. Nikamwambia nahitaji maji na ndani ya muda mfupi mkononi mwangu nikawa nimeshikilia glasi ya maji safi.

    Kwa muda huo mdogo niliokuwa nimekaa hapo, niligundua kuwa mzee huyo anaishi mwenyewe. Nyumba ilikuwa pweke japo safi na ipo kwenye mpangilio mzuri.

    Akaketi na kuniuliza wapi nilipotokea, nikamlaghai natokea Uingereza, alafu pasipo kupoteza muda nikamuuliza juu ya jirani yake, yule anaekaa kwenye anwani 2345. Hii nyumba ya huyu mzee ilikuwa ni ya tatu toka pale kwenye nyumba namba 2345.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Basi huyo mzee akajaribu kuvuta kumbukumbu, ungeliona hilo kwa macho yake, kisha akanangalia na kunieleza yale anayoyajua kuhusu jirani huyo, yaani mwanamke na mtoto wake.

    Kwa mujibu wa maelezo yake nikagundua kuwa mwanamke aliyekuwa anakaa kwenye ile anwani alikuwa anaishi mwenyewe pamoja na mtoto wake wa kiume. Na pia alikuwa mgeni, kutokea Marekani.

    “Mara kwa mara nilikuwa namsikia akiongea na mwanae kwa kiingereza safi, ila alikuwa anajua pia na kijerumani!”

    Hapa sasa ndiyo nikaanza kujenga picha. Kama wakazi hao walikuwa ni wamarekani kwanini walikuwa wanaishi Ujerumani? Na watakuwa na mahusiano gani na Raisi aliyepotea mpaka kumpatia rafiki yake anwani ya nyumba?

    Nikamdadisi huyo mzee juu ya mwonekano wa mtoto huyo aliyekuwa anakaa na huyo mama, akanieleza kuwa mwenye nywele nyekundu na mashavu makubwa na macho ya dhani ya paka.

    Kwa maelezo zaidi, nikapata kujiuliza kwanini mtoto yule alichora picha ya njiti kwenye kifaa chake cha kuhemea. Yule hakuwa yeye. Sikujiuliza sana nikaaga niende zangu nikiwa sijayanywa yale maji niliyopewa.

    Nilifanya hivyo kwasababu za usalama, huwezi jua anaweza akawa ametia nini. Kila mtu ni wa kumtilia mashaka kwenye ulimwengu wa kiitelijensia.

    Nilipotoka , nikarusha macho kwenda kwenye ile nyumba ya kando ambayo nilikuwa nikiitilia mashaka. Ile nyumba ambayo iliwameza wale watu ambao walikuwa wakivalia nguo nyeusi. Hapo sikuona mtu, lakini kabla sijageuza shingo yangu nikamwona mtu dirishani akichungulia.

    Mtu huyo upesi alitoka dirishani na kupotea!

    “Hawa watu ni wakina nani?” nikajiuliza nikitembea zangu kuelekea kituoni, ila mara hii, tofauti na ya kwanza, nikahisi nafuatiliwa kwa mapema zaidi! Kwa mahesabu yangu ambayo yalikuwa sahihi, kulikuwa na gari linalokuja nyuma yangu, tena kwa kasi!

    Basi nikaongeza kasi ya mwendo wangu na alafu ile kona ya kwanza nikaikata na kuanza kukimbia upesi. Na kabla gari hilo linifuatalo halijachomoza, nikawa nimejibana nyuma ya nyumba!

    Nikachomoza kichwa changu kwa udogo na kuangaza. Punde lile gari likapita hapo likiwa katika mwendo wa pole. Ilikuwa ni Volkswagen modeli ya zamani. Madirishani niliwaona wanaume wakiwa wanachungulia na kurusha macho yao kutafuta jambo. Nyuso zao hazikuwa za amani.

    Vuuuuuuupp! Wakapita! Lakini ikiwa imepita kama sekunde mbili tu, mara nikasikia sauti ikifoka kwa kijerumani, “Unafanya nini hapo!” kutazama alikuwa ni bwana wa kijerumani ambaye amevalia kaptula tu, kifua wazi.

    Sauti yake ilikuwa kali sana, na majibu yake niliyaona punde tu maana nilisikia sauti ya gari ikivuma na mara ikaja kutuama mbele ya ile nyumba! Kutazama, nikaona mwanaume akitokea na mkono wa bunduki, akayaftua risasi mfululizo! Nilikwepa kwa kujibana kwenye nyumba. Yule mwenyeji aliyenifokea nikamwona akiwahi haraka kuzama ndani!

    Kidogo nikasikia milango ya gari ikifunguliwa, hapo nikaona tena si pa kukaa. Kutazama nyuma yangu, yaani ya nyuma ya nyumba ile, kulikuwa na ukuta wa mbao, haraka nikaufata na kuukwea kama nyani!

    Nilipotua upande wa pili, nikaanza kukimbia kuufuata ukuta mwingine wa nyumba niliyozamia. Kidogo, nikasikia watu wengine wakitua, walikuwa ni wanaume wawili ambao wananifukuzia! Wakaanza kurusha risasi kwa fujo! Kwa pupa!





    Basi haraka nikachumpa kuuvuka ukuta mwingine, hapa hata sikuushika ukuta huu bali kuruka kama samaki. Nikatua kwa ustadi na kisha kukimbia upesi kwanguvu zote kuufuata ukuta mwingine, nao nikiwa nimeukaribia, wanaonikimbiza wakawa wametua. Wakaendelea kufyatua risasi kama njugu!

    Hapa moja ikanipunyua mkono na kunisababishia jeraha. Ila sikukoma kukimbia kuokoa nafsi yangu. Nikaruka tena kwenye ukuta mwingine na mwingine na mwingine, alafu nikajificha pahala.

    Wale watesi wangu wakasonga wakiwa wameduwaa. Wakatazama kushoto na kulia mimi nikiwa nawachora toka kwenye ua kubwa. Hawakuwa wananiona. Ila kama sijakosea, mmoja wao akahisi huenda naweza nikawa nimejibana nyuma ya ua. Nikaona akimshtua mwenzake akitazama eneo nililopo.

    Kuona hivyo, basi upesi nikachomoka na kuwafyatulia risasi. Wote wakalala chini na kunipa amani kwa muda. Nikatoka hapo nyuma ya ua na kukimbia upesi. Nikaruka ukuta mwingine na kuzama barabarani, sikuona mtu nyuma, nilikuwaa mwenyewe sasa. Kidogo nikakutana na gari, nikasimamisha na kumwamuru dereva atoke ndani, alipotii nikazama ndani ya gari na kutimka.

    Ila sikufika mbali sana na hilo gari, nikaliacha na kudaka lingine. Nalo liliponisogeza umbali kidogo, nikaliacha na kupanda basi la uma. Nikaenda kabisa nyuma ya basi na kusimama huko. Nilijihisi salama sasa.

    Nikafika hotelini na nikiwa naelekea chumbani mwangu, dada wa mapokezi akaniita. Mwanamke mwenye sura pole na mashavu mapana ndani ya sare. Nikamjongea taratibu nikiwa najiuliza nini shida? Akanitazama na kisha akaangalia tarakilishi yake na kuniuliza, “Kuna mgeni wako ulimtuma?”

    “Mgeni?”

    “Ndio! Kuna mwanaume alikuja hapa kukuulizia.”

    “Aliniuliziaje?” nikatahamaki. Basi yule mhudumu akanambia kuwa alitumia maelezo ya mwonekano wangu, na hivyo alivyoniona tu akapata kujua kuwa ndiye mimi. Nami nikamuuliza mtu huyo aonekanaje? Akanieleza.

    Maelezo yake yakajenga picha kichwani mwangu kuwa mtu huyo atakuwa ni miongoni mwa wale wajamaa ambao nilipanda nao basi kabla sijawapotea.

    Ina maana wameshajua makazi yangu mapya? Nikaona hapa si mahali pa kukaa tena. Nikanyookea chumbani mwangu na kuanza kukusanya vitu muhimu kutoka kwenye begi, haswa pesa na kadi. Lakini kabla sijatoka, nikasikia hodi mlangoni! Nikatulia tuli nikipepesapepesa macho yangu. Kidogo sauti ya kiume ikasema, “mhudumu!” kisha kugonga tena mlango.

    Sikusema kitu. Nikaweka silaha yangu mkononi na kujongea mlango. Sijaufikia, nikastaajabu mlango umekumbwa na teke! Ukang’oka na kunivamia na kunidondosha chini!

    Kutazama, nikamwona mwanaume akiwa amevalia nguo nyeusi. Sura yake haikuwa ngeni. Alikuwa ni miongoni mwa wale wanaume niliopanda nao basi kabla sijawapotea. Mkononi mwake alikuwa amebebelea bunduki!

    Basi haraka nikaunyanyua mlango na kujikinga nao. Bwana yule akatupa risasi kama tano vile pasipo kupumzika, zote zikaishia mlangoni. Mimi nilipochomoza na kumtwanga yangu moja, akawa amekwisha! Alidondoka chini kama mzigo akiwa ameachama mdomo.

    Upesi nikanyanyuka na kumtazama. Punde nikasikia sauti kali ya mwanamke ikipiga yowe huko mbali. Hapa nikahisi hamna tena usalama, huenda kuna wavamizi wengine! Nikatoka ndani kushika korido, ila uso kwa uso, umbali wa kama hatua kumi na nane, nikaonana na wanaume wawili wakiwa wanakuja wamebebelea bunduki!

    Upesi nikarudi ndani. Nikasikia vishindo vya watu vikikimbia kuja. Nikavunja dirisha na kutokea nje. Chumba changu kilikuwa ghorofa ya kwanza, nikarukia huko chini nikitulia pazia lililokuwa limefunikia magari yaliyoegeshwa, kisha nikajitupia chini na kukimbia!



    **



    “Kama nisipofanya mambo haya upesi, nadhani yatazidi kuniwia vigumu zaidi na zaidi!” niliteta na Jack nikiwa nimeketi kwenye kiti ndani ya nyumba ya kupumzikia. Niliongea naye kwa muda sana na mwishowe alipokata simu nikajilaza kitandani na kuwaza mambo kadha wa kadha.

    Kwa maelezo ambayo nilimpatia Jack, aliniambia yanasawiri na namna alivyokuwa anawaza lakini asiniweke bayana kipi ambacho kipo kichwani mwake, akataka ningoje kwa muda kidogo. Hivyo hapo nilipokuwa nimejilaza nilikuwa namngoja.

    Zikapita kama dakika sita, usingizi ukaanza kuninyemelea. Nilisinzia nikipambana na macho yangu mazito. Ikiwa kama dakika ya nane kama niko sahihi, simu yangu ndiyo ikaita Jack akirudi tena hewani.

    “Sasa sikia …” akaanza kwa kauli hiyo kisha akanambia kuhusu yule mtoto ambaye alikuwa anakaa na mama yake kwenye nyumba yenye anwani 2345. Kumbe alishamtambua mtoto huyo na kunituma kwenda kumuulizia mwonnekano wake ilikuwa ni kwa ajili ya kuthibitisha tu.

    Lakini mtoto huyo ni nani haswa? Hakuwa anafahamu japo nishamwambia kuwa ni Mmarekani. Na kuhusu mama yake, Jack hakuwa na taarifa naye hata kidogo!

    Ilikuwa ni ajabu kidogo kwani Jack aliniambia alifanikiwa kum – trace mtoto huyo kupitia game la ‘Subway Surfers’ ambalo humo ndani, kwa ridhaa, wachezaji huweza kuunganisha na mtandao wao wa Facebook ili washindane na marafiki zao.

    Lakini zaidi, unaweza ukatazama kuona wachezaji gani wana points nyingi ulimwengu mzima. Basi kwa kupitia huko, Jack Pyong akakuta jina la MUNICH 2345. Na aliposaka jina hilo mtandaoni akitumia picha aliyoiona humo mchezoni, akafanikiwa kulipata. Kwa ufupi, jina la mtoto huyo huitwa Brussels, lakini jina lake la mchezoni hutumia MUNICH 2345, yaani jina la anwani ya nyumba alokuwa anakaa.

    “Sasa tunaweza tukampata wapi yeye na mama yake?” nikamuuliza Jack.

    “Usijali,” Jack akan’toa hofu. “Mpaka kufikia kesho n’takuwa nishapata!” tukamaliza maongezi na mie nikajilaza sasa.

    Nikiwa usingizini, nadhani kwasababu ya kupitia purukushani hapa karibuni za mara kwa mara, nikaota ndoto ya kunishtua. Nilijikuta nikinyanyuka upesi na kushikilia bunduki yangu lakini nilipotazama huku na kule sikuona kitu. Nilikuwa mwenyewe!

    Kidogo usingizi ukawa umenitoka. Nikashika simu yangu na kuperuzi, nikaukuta ujumbe toka kwa Daniele. Alikuwa akinijulia hali na kuniuliza wapi nilipofikia. Ujumbe huo ulikuwa umetumwa dakika tisa nyuma.

    Nikaujibu kisha nikaweka simu pembeni. Sikutarajia kama Daniele angeujibu kwani ilipita muda kidogo tangu autume lakini kinyume na matarajio yangu, akajibu punde tu. Na hapo ndipo nilipoingia naye kwenye uwanja wa kuchat kw muda kidogo akinieleza mambo kadha wa kadha.

    Lakini zaidi lililokamata hisia zangu ni mashambulio mawili ambayo Daniele na timu yake waliyapitia ingali wakiwa kazini. Kwa mujibu wa Daniele, walishambuliwa na mwanamke mmoja na wanaume watatu. Ingawa walikuwa wameficha nyuso zao lakini waliwatambua kutokana na maumbo yao ya mwili.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Shambulio la kwanza lilitokea wakiwa wametoka kwenye nyumba ya Makamu wa Raisi na ya pili wakitoka kwenye ofisi ya Wizara ya usalama wa ndani!

    “Watu wangu wawili wameuawa kwasababu ya mashambulizi hayo, na hata kupotea kwa baadhi ya nyaraka. Nimepeleka taarifa kwenye uongozi, wakaniongezea ulinzi.”

    Nami nikamshauri kushirikiana na Jack Pyong kwenye mambo kadhaa haswa ya kiteknolojia kwani anaweza kumsaidia. Kwa mawasiliano zaidi nikampatia namba za Jack na hata kumtaarifu Jack juu ya swala hilo.

    Baada ya hapo, nikalala.



    **



    Saa kumi na moja asubuhi…



    Nina uhakika simu ilinguruma mara moja tu kabla sijaamka. Niliitazama nikiwa nimekunja uso wa usingizi, kwenye kioo nikaona nimetumiwa na Jack ‘location’ ya eneo ambalo naweza kumpata yule mtoto ambaye tulimjadili.

    Basi usingizi ukanikata papo hapo, nikanyanyuka nikaoga na kuvaa kisha kushika barabara kwenda huko ambako Jack alikuwa amenielekeza. Mahali mbali kabisa na jiji la Munich. Tena msituni. Ulikuwa ni kama mwendo wa masaa matano kasoro kwa basi mpaka kufika huko. Huko wenye msitu huo wa ‘Black forest’ ambapo ndipo location ilipoongoza.

    Mpaka kupata na kupanda basi ikawa tayari ni saa moja asubuhi, safari ikaanza. Kama kawaida nilikuwa nimekaa nyuma ili nipate nafasi ya kutazama abiria wote ndani ya basi, watakaoshuka na wale watakaoingia.

    Nikiwa nimekaa huko nikawa nawaza sana kichwani mwangu, mtoto huyo atakuwa anafanya nini huko Black Forest?

    Yupo mwenyewe au na mama yake?

    Je wapo wenyewe au na watu wengine?





    Basi mawazo hayo yakanifanya nisisinzie ndani ya basi nikawa natazama dirishani na muda mwingine mlangoni pale ambapo basi lilikuwa linasimama.

    Tulipotembea kwa muda wa kama lisaa limoja, basi likasimama nasi, watu ndani ya basi, tukapata wasaa wa kununua vitu vya kuchangamsha kinywa na kujaza matumbo kisha safari ikaendelea.

    Hapo tukatembea kwa lisaa limoja tena tukawa tumefika Black Forest. Nikashuka na nikiwa natazama simu yangu nikaanza kusonga.

    Haki ulikuwa ni msitu mkubwa sana. Sikujua kwanini uliitwa Black Forest, yaani msitu mweusi, na kwa muda huo bado sikuwa najua kwanini msitu huo ni maarufu nchini Ujerumani.

    Ulikuwa umeota mgongoni mwa safu ya milima. Hapa kukiwa kimya na kwa mtu mwenye woga akikaa mbali aogope hata kukatiza.

    Basi kwakuwa maelekezo ya kwenye simu nilishayameza, nikaweka simu mfukoni na kuendelea kuzama msituni. Nikatembea kwa kama kilomita moja na nusu, bado milima tu ilikuwa imenizingira, mbele na nyuma yangu kwa sana.

    Nilipomaliza kilometa mbili, kwa mahesabu ya harakaharaka, nikaanza kujiuliza kama kweli nitakuwa nimefuata maelekezo ninayotakiwa kwani sikuwa naona alama wala ishara yoyote ya binadamu.

    Nikatoa simu yangu mfukoni nitazame. Nilikuwa sahihi. Nikairejesha na kuendelea kukwea. Kidogo kwa umbali, nikaona kijumba cha rangi nyeupe. Kilikuwa ni kijumba pweke maana kikipakana na miti pekee.

    Basi nikazidi kusonga na kusonga, nikiwa naamini sasa kile kijumba ndipo mahali ninapotakiwa kufika. Na niliposonga zaidi na zaidi nikagundua kuwa kile hakikuwa kijumba bali nyumba, ni unbali tu ndio ulikuwa unafanya paonekane padogo.

    Lakini … nikapata maswali. Mtoto yule atakuwa anafanya nini huku msituni kwenye nyumba ile? Na kama yupo na mama yake, kwanini wanaishi huku? Mbali kabisa na dunia?

    Mawazo haya yakanipa hoja niliyotokea kuiamini. Kuna kitu hakipo sawa. Na hivyo natakiwa kubeba kila aina ya tahadhari ninapoelekea kwenye nyumba hiyo.

    Niliposonga, nikiwa nimebakiza umbali wa kama robo kilometa kuikuta ile nyumba, nikatulia na kuitazama vema kuikagua. Nilipokuwa nimekaa palikuwa ni eneo la juu kidogo hivyo palinipa fursa ya kutazama vema.

    Kwa usalama zaidi nikalala chini na nikatenga dakika kama kumi za kukagua eneo hilo kabla ya kupasogelea zaidi.

    Basi nikiwa hapo, nikatulia tuli sana. Palikuwa ni eneo tulivu mno ukiondoa upepo usukumao matawi ya miti.

    Ikiwa kama imepita dakika tano tangu nilale hapo, nikastaajabu kichwa changu kikisukumizwa na kitu kigumu kisha sauti ya kijerumani ikaniamuru, “Tulia hivyo hivyo!”

    Nami nikatii nikiamini kuwa mtu huyo amenishikia bunduki.

    Akaniuliza mimi ni nani na hapo nafanya nini, tena akiwa ananisisitizia nisigeuke kumtazama. Kwa taratibu nikamjibu mimi ni mtalii na nalishangaa kuona nyumba hiyo msituni.

    Akaniamuru nisimame nikiwa nimenyoosha mikono juu. Nikatii. Bado nikiwa simtazami. Akanipekua upesi kwa mikono, akahisi nina silaha. Akaichomoa, ilikuwa ni bunduki yangu. Hapo ndiyo nikaona akitupa mti kando na kutumia silaha yangu kuniwekea kichwani!

    Kumbe hata silaha hakuwa nayo.

    Sasa akaniamuru nigeuke. Nilipofanya hivyo nikakutana na mwanaume aliyevalia hovyo, ndevu nyingi na kofia ya soksi nzito kichwani. Mkononi mwake alikuwa amebebelea tunda, papai, akila kana kwamba sokwe mtu.

    Akaniuliza, “unataka kufa?”

    Sikumjibu. Akarudia tena swali lake, “Unataka kufa?”

    “Hapana!” nikamjibu, asiniongeleshe kitu akashika njia kwenda zake. Alipopiga hatua tatu akanigeukia na kunambia, “kama hutaki kufa, nifuate!”

    Basi mimi nikamfuata. Njiani nikamuuliza yeye ni nani na anafanya nini humo msituni. Hakunijibu. Alikuwa kimya akiwa anakula tunda lake ambalo halijamenywa!

    Baada ya kama dakika kumi za kutembea, tukafika mbele ya kijumba dhoofu, kimesanifiwa kwa magogo na majani. Humo akazama ndani na kunitaka mimi nikae pale nje. Kidogo akatoka akiwa amebebelea kikombe cha bati ambacho sikujua mule ndani ameweka nini. Akawa anakunywa.

    Akanitazama kana kwamba ndo’ mara ya kwanza ananiona alafu akaniuliza, “wewe ni nani?”

    “Nishakwambia hapo awali,” nikamjibu. Akakunja uso na kuuliza, “muda gani? Nimekutana na wewe popote pale?”

    Nikastaajabu. Nikadhani ananifanyia utani.

    “… hata silaha yangu umechukua wewe!” nikamweleza. Akajitazama na kujikuta na bunduki. Haraka akanirushia akinitazama kwa mashaka. Hapa nikafahamu na kuthibitisha kuwa mtu huyu hakuwa sawa.

    Nikamweleza mimi naitwa Jerry na nilikuwa nataka kufahamu juu ya nyumba ile iliyopweke msituni!

    “Nyumba ipi hiyo?” akaniuliza akiwa ameweka kituo kutafuna.

    “Ile ambayo ulinikuta naitazama,” nikamjibu. Akan’tazama kwa mashaka kisha akaniuliza, “ipi hiyo?”

    Nikaona isiwe tabu nikamwelekeza. Ajabu alikuwa anaifahamu. Kumbe bwana huyu ana tatizo la kupoteza kumbukumbu za karibu. Alipojua ninachokiongelea, akaendelea kutafuna kisha muda si mrefu akaniuliza, “Una biashara gani hapo?”

    “Nataka tu kujua,” nikamjibu na kuongezea, “Ni wakina nani wanaishi hapo?”

    “Sijui nani anaishi hapo!” bwana yule akan’jibu. Kabla sijaongea, akaendelea, “Huwa naona watu kadhaa hapo. Sijui nani anapaishi?”

    “Unaweza kunambia watu hao ni wa aina gani? Yaani wapoje?”

    “Wapo kama wewe!”

    “Kivipi? Namaanisha mwonekano wao? …” nikamwona akifikiria pasipo malengo. Nikamkatisha kwa kumuuliza, “Vipi, ushawahi kumwona mtoto hapo? Mvulana mwenye nywel nyekundu?”

    Akanitikisia kichwa kukataa.

    “Na je mwanamke? Hujawahi mwona mwanamke hapo?”

    Akanitikisia tena kichwa akibetua mdomo. Alafu akang’ata tunda lake na kutafuna.



    **



    Baada ya dakika nane …



    “shhhiiii!” nikamwonya yule jamaa yangu mwehu niliyemkuta ndani ya msitu. Alikuwa nyuma yangu wakati mimi nikiwa nimejibanza mtini natazama nyumba ninayotaka kuelekea.

    Nilipomwonya hivyo, akafunga mdomo wake, nami nikarusha macho yangu kutazama ile nyumba ambayo kwa muda huo ilikuwa ipo kama hatua kumi na mbili tu tokea tulipo. Bado palikuwa kimya. Ni kama vile hakukuwa na mtu hapo.

    Nami nilikuwa nimevalia mavazi ya hovyo sana kama mtu yule niliyeongozana naye. Nilimwomba mavazi yake ili basi yakanisaidie pale mambo yatakapokuwa yamenielemea.

    Nilipoona ni kimya tu, nikatoka hapo mtini nikiwa nimemwelekeza yule jamaa wangu abakie hapohapo mtini nami nitarejea. Nikaelekea mbele kabisa ya ile nyumba na kujifanya nikiimba wimbo ambao hata siujui na huku nikitazamatazama huku na huko na kuokotaokota vitu vya ajabu.

    Punde akatoka mwanaume mmoja aliyekuwa amevalia sweta nyeusi inayokaba koo na suruali jeans ya bluu mpauko. Mkononi alikuwa na bunduki ndogo. Akan’tazama na kuniuliza kwa amri, “wewe nani?” Alikuwa anatumia lugha ya kijerumani.

    “Mimi Jerry!” nikamjibu, kisha nikampuuzia na kuendelea kuokotaokota vitu. Akapaza sauti, “hey! Sikia!” nikamtazana.

    “Hapa si mahali pa kuchezeachezea, sawa? … potea!”

    Kabla sijasema kitu, yule jamaa wangu niliyemwacha mtini akatoka na kupaza sauti akiuliza, “Ninyi! Mnafanya nini hapo?”

    Nikamwona yule jamaa aliyetoka ndani ya nyumba akishikwa na tahadhari. Akaikamata silaha yake vema akiwa amekunja sura. Mara akaninyooshea na kuniuliza. “mnafanya nini hapa?”

    Yule jamaa kule pembezoni mwa mti akapaza sauti, “muue huyo! Kwanza amevalia nguo zangu! Sijui kazitoa wapi?”

    Yaani alikuwa ameshasahau kuwa yeye ndo’ kanipa!

    Nikamtazama kwa kushangaa lakini huku nikijipapasa kufuata silaha yangu. “Phili, unasemaje?” nikamtunga jina upesi. Kabla jamaa yule hajajibu, nikawa nimeshapata silaha yangu kiunoni, nikaichomoa upesi na kumwonyeshea yule jamaa aliyetoka ndani ya nyumba.

    “Weka silaha chini!” nikamwamuru. Akawa mbishi. Naye alikuwa ameninyooshea bunduki akiwa amen’tolea macho.

    “Siweki, weka wewe!”

    Nikamwambia, “unajua sisi tuko wawili. Unadhani yule ni chizi sio?”

    Akageuza shingo yake kumtazaama yule jamaa wangu kule pembeni ya mti. Jamaa akatabasamu kama mdoli.

    “pale ana silaha, anasubiri nimpe amri tu. Usiwe mjinga, weka silaha chini nyoosha mikono juu!” nikamsihi. Akafikiri kidogo.

    “Wewe ni nani?” akaniuliza. “Muamerika?”

    Sikumjibu.

    “Hautatoka ndani ya msitu huu salama. Hata kama ukiniua.” Akasema akinitikisia kichwa. Mimi nikaendelea kumsihi, “weka silaha chini! Mara hii sitaongea tena, sina muda wa kupoteza!”

    Basi akatii amri yangu baada ya kun’tazama kwa sekunde tatu.



    ***





    Nikazama naye ndani nikiwa nimemwekea bunduki kichwani. Sebuleni nikawakuta wanaume wawili ambao nikawaamuru waweke silaha chini la sivyo nitammaliza mwenzao. Ajabu wakatii. Nikasonga kidogo na kumwamuru mmoja wao akafungue milango, nipate kuona yaliyondani.

    Wakati anafanya hivyo nikawa nawataza kiumakini wasifanye jambo lolote. Ndani ya chumba cha kwanza nikampata mtoto na mama yake. Mtoto yule ambaye nilishaambiwa na Jack Pyong.

    Nikawaamuru wasonge mbele na kwa tahadhari nikawafyatulia risasi wale wanaume watatu miguuni washindwe kunifukuza nitakapotoka hapo kisha nikamwamuru yule mtoto ambaye nimemtoa humo ndani aziokote silaha na kunipatia. Baada ya hapo tukatoka ndani na kuzama msituni, hamaki yule bwana mwehu naye akaungana na sisi. Tukawa tunakimbia.

    Sikujua tunaelekea wapi, ila nilitaka tu twende mbali na lile eneo kwa usalama wetu. Lakini tukiwa tunasonga, kidogo yule mama, mama ambaye nimetoka kumwokoa kwenye mikono ya wale wadhalimu, akanishauri tuelekee upande wetu wa mashariki.

    Nami pasipo kubisha, maana sikuwa na huo muda, tukaongoza kwenda huko tukiwa tunakimbia. Kidogo, tukasikia sauti za pikipiki nyuma yetu. Tulipogeuka na kuangaza hatukuziona. Zilikuwa mbali ila kiuhakika zikija uelekeo wetu.

    Tukakazana kukimbia, na kama baada ya dakika mbili, sasa tukaanza kuona pikipiki zikija kwa kasi nyuma yetu. Zilikuwa tatu kwa idadi. Kila moja ikiwa imebebelea watu wawili wawili, wa nyuma akiwa amebebelea bunduki!

    Nikapaza sauti, “kimbiaa! Kimbia!” lakini ni wazi tusingeweza kimbia zaidi ya kasi ya pikipiki. Na nilihofia endapo watu wale wangeanza kufyatua risasi ingetuwia vigumu kupona.

    Kweli, risasi zikaanza kurushwa kwa fujo! Zikapasua na kutoboa miti huku zikitupunyua na kupita kando za masikio yetu. Kidogo, yule jamaa mwehu tuliyekuwa tunaongozana naye, akabamizwa risasi ya mgongo! Niliona damu zikowa zinaruka kama vumbi, na mara akadondoka chini!

    Ulishawahi mwona farasi akidondoka ingali yu kwenye kasi? Namna anavojikita na kujivunjavunja? Naam ndivyo ilivyokuwa kwa bwana huyu. Alidondoka vibaya mno, nahisi alivunjika vibaya sana haswa uti wake wa mgongo na shingo.

    Nilitamani sana kumtazama kwa kujali lakini sikuwa naweza maana kufanya hivyo kungekuwa ni kutaka kifo. Nikaendelea kukimbia pamoja na wale niliowaokoa, lakini sasa mambo yakiwa magumu zaidi. Niligundua risasi zote zilikuwa zimenielekea mimi, kuniangusha chini, kwani zilinipita pembeni ama kupasua miti niliyokuwa nayo karibu, na hatimaye moja ikan’tifua begani!

    Bahati haikunipasua mfupa, bali ilizama kwenye nyama na kunifanya nivuje damu kwa wingi. Vitu vingine ni kama bahati tu. Muda mwingine Mungu humsaidia mja wake pale anapokuwa anatenda lile lililojema, huwa naamini hivyo. Kuna muda niligeuka kutazama nyuma na kumbe muda huohuo risasi ilitupwa kunipasua kichwa, hivyo kugeuka kwangu kukawa kumeniokoa!

    Risasi ikaparasa shavuni kwa upesi na kwenda kukomea mtini! … pah! Hata nikatahamaki.

    Ila nilikuja kujifunza kuwa, watu wale waliokuwa wanatukimbiza walikuwa wamedhamiria kunimaliza mimi na si yule mwanamke na mtoto. Niliona wao wakiwa hawalengwi wala kudhamiriwa. Risasi hazikuwa zikiwapunyua na kuwawinda bali mimi na yule jamaa yangu ambaye tayari ameshalambishwa vumbi!

    Basi kujua hilo, nikaanza kujisogeza kwa yule mwanamke na mtoto mpaka kujiweka mbele yao ingali sijui wapi tunapoelekea. Kwa kufanya hivyo, ghafla risasi zikakoma kurushwa. Kumbe nilikuwa sahihi!

    “Usifyatue! Usifyatue!” nilisikia sauti ikiamuru kwa kijerumani. Hapa ndiyo nikajua na kuthibitisha kumbe wale mateka bado walikuwa wa thamani kwa wale wadhalimu. Bado walikuwa wanawahitaji na hiyo ni kumaanisha bado kuna kazi hawajaimalizia.

    Lakini kukaa huku mbele ya mateka kusingelidumu kwa muda! Pikipiki zilikuwa zinakuja kwa kasi nyuma yetu na sasa ungeweza kusema kwamba, baada ya kama dakika moja tu, tutakuwa tumeshafikiwa na kunyakuliwa!

    Kwahiyo basi hapa ilinilazimu kutafuta namna ya kutuweka salama. Nikachomoa bunduki mbili toka kiunoni mwangu na kuanza kuwatupia risasi wale waliokuwa wanatukimbiza. Kwa kufanya hivyo wakapunguza kasi na hata kuzubaa kwa kujikinga dhidi ya risasi!http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Na kumbuka wao walikuwa hawawezi tena kunitupia risasi kwakuwa najifichia kwa watu wasiotaka kuwaua.

    Nikawadungua watatu, wawili walikuwa madereva, mmoja akiwa abiria. Nikawa nimebakiza pikipiki moja. Nayo baada ya kusonga karibu zaidi, nikamfyatulia dereva risasi, akaikwepa na kumpata abiria wake. Akadondoka chini dereva akiendelea kutufuata.

    Basi baada ya kuona amebakia mmoja, tena dereva ambaye alikuwa ameweka nguvu zake kwenye usukani, nikasimama na kumweka vema kwenye rada alafu nikamfyatulia risasi mbili kwa wakati moja, nikapasua mabega yake na kumfanya achie usukani! Kabla hajadondoka chini, nikamtupia tena risasi nyingine, ikatoboa kofia yake ngumu na kumpasua kichwa, akajifia.

    Basi mimi nikarudi nyuma, nikawamalizia wale wengine walioko chini kwa mbali, kisha nikachukua pikipiki ya yule aliyekuwa mbele kabisa, niliyetoka kumuua punde, kisha nikambeba yule mwanamke na mwanaye na kutimka kwa kasi!

    Nikaendesha pikipiki hiyo kana kwamba nacheza mchezo wa kwenye kompyuta ama simu. Nilikwepa miti kama mchezo huku nikisababisha hofu kubwa kwa wale niliowapakia. Walikuwa wakipiga yowe na kunisihi nipunguze kasi lakini sikuwaskiza kwani nilikuwa najua ninachofanya. Nilitaka kuumaliza msitu huu angalau niikute lami na kunyoosha nayo.

    Kidogo tena tukasikia sauti za pikipiki zatujia. Nikaongeza kasi zaidi, punde tu, tukafika mpakani! Hapa tulikuwa tumesimama juu ya korongo, na huko chini, kama mita mia tano, kukiwa na mto mkubwa wenye maji ya kasi!

    Nikakunja kona na kuanza kuambaa ambaa na hili korongo kwenda upande ambao mto unaelekea. Kama dakika tatu, kwa nyuma, wakatokea watu waliokuwa juu ya pikipiki sita! Wakawa wanatukimbiza kwa kasi sana, kasi zaidi ya pikipiki yetu.

    Na kidogo tu, wakaanza kutupa risasi kwa fujo. Hawakuwa wanalenga watu bali pikipiki, nadhani lengo lao lilikuwa ni kupasua matairi ama kutusababishia ajali watukamate. Nilijitahidi kuiyumbisha pikipiki kuwakwepa ila napo nikaona kuna hatari ya kuwabwaga abiria.

    Nikaendelea kukazana na mwendokasi. Lakini napo nisifike mbali, mbele yetu tukaona watu wakiwa wamesimama, watano kwa idadi, wakiwa wameziba njia na pikipiki zao. Mikononi wamebebelea bunduki na wamezielekezea upande wetu!

    Hapo nikamsikia yule mwanamke niliyembeba akisema, “tunakufa!” naye mtoto wake akadakia kwa kusema vivyo hivyo, “tunakufa!” Mimi nikawaambia, “nishikeni kwanguvu!”

    Kisha nikaminya mafuta na kuelekezea pikipiki korongoni! Tukashika ardhi kwa muda mdogo tu kabla pikipiki haijapaa hewani kwa muda wa kama dakika moja na kisha kutumbukia kwenye maji!

    Waaah!!



    **

    Nilipoyazidi nguvu maji, nikatoa kichwa changu na kutafuta watu niliozama nao. Sikuwaona! Si kwamba maji hayakuwa na nguvu, hapana, bali angalau niliweza kuyamudu tofauti na mwanzoni tulipozama, yalikuwa na nguvu mno!

    Nilitazama kushoto na kulia, bado tulikuwa ndani ya msitu, na bado sikuwa nawaona ‘watu wangu’. Nilipiga mbizi nikijitahidi kwa nguvu kuelekea maji yanapotokea, ila kidogo nikasikia sauti ya kike toka nyuma yangu, “msaada!”

    Nilipopinda shingo kutazama, nikamwona yule mwanamke akipambana kumsaidia mwanaye. Lakini maji yakimzidi nguvu, akizama na kunyanyuka na kunywa maji!

    Basi upesi nikarudi na kumfikia. Nikamnyakua mtoto na kumtaka anishike wakati mimi nikiwa natumia mkono wangu mmoja kupiga mbizi twende pakavu. Mtoto hakuwa ana ufahamu. Kichwa chake kilikuwa kinavuja damu.

    Tulipofika pakavu, nikamtazama mtoto na kubaini alikuwa amejigonga kwenye jiwe ingali tu mtoni. Na kwa namna alivyokuwa anatoka damu, inabidi ifanyike namna upesi ya kumsaidia, la sivyo alikuwa anatuacha!

    Nikamwambia mama yake, “gandamizia mahali pa jeraha, nakuja!” mimi nikaenda kutafuta majani yatakayoweza kumsaidia jerahani.



    ***





    Nilifahamu ndani ya msitu ule sitakosa ninachotaka. Nikakimbia upesi na kufanya jitihada za kuangaza macho yangu nikitumia stadi niliyonayo juu ya madawa ya asili. Tulifunzwa hii. Tulifunzwa namna ya kudumu na kumudu kwenye hali mbalimbali kama hizi.

    Ndani ya muda mfupi, nikapata kuona kichaka chenye majani membamba na ncha kana kwamba sindano. Nikajongea hapo na kuchuma majani kadhaa na kuyatia mdomoni kutafuna alafu nikaanza kurudi upesi kule kwa yule mwanamama na mwanaye.

    Nilipofika majani mdomoni mwangu yalikuwa tayari yashalainika vya kutosha. Nilikunja sura kwa uchungu wake mithili ya shubiri. Nikayatema na kumpachika yule mtoto eneo lake la jeraha alafu nikachana sehemu ya shati langu kutengeneza bandeji, nikamfungia hapo kichwani na kumweka mtoto huyo begani tuendelee na safari.

    Tukiwa tunatembea, nikapata sasa wasaa wa kumuuliza maswali kadhaa. Niliona huu ni muda muhimu wa kufanya hivyo maana lolote linaweza kutokea muda wowote. Basi likitokea, angalau niwe nimetimiza robo ya haja yangu.

    “Wewe ni nani? Kwanini watu hawa wamekuteka?” Niliuliza nikimtazama mwanamke huyo ambaye alikuwa akitembea kwa ukakamavu. Alikuwa na ushupavu ndani yake.

    Akanitazama na kunyamaza kwanza akipiga hatua. Alipovuta pumzi ndefu ndipo akanijibu pasipo kunitazama, “Nilidhani utakuwa unanijua ndo’ maana ukaja kuntafuta.” Kisha akaniuliza, “Ajenti, umekujaje kumtafuta mtu ambaye humjui?”

    “Umejuaje kama mimi ni ajenti?”

    Akatabasamu. “Anayeweza kuyafanya yote haya, ni raia wa kawaida?” kabla sijanena akaendelea kunena, “Umefanya kazi kweli kujua wapi nilipo. Hata sasa kuwa hai unastahili pongezi.”

    Nikamtazama na pasipo kuongea nikarudisha macho yangu mbele tuendako nikitarajia mwanamke huyo ataendelea kunena.

    “Mimi ni raia wa kawaida kabisa. Ni mmarekani ninayeishi Ujerumani pamoja na mwanangu. Sina shida nyingine na mtu!”

    “Huku Ujerumani unafanya nini? Na kwanini Ujerumani?”

    “Una maswali mengi sana. Sidhani kama nipo kwenye mood ya kukata kiu chako. Pengine baadae nikiwa nimetulia.”

    “Wamekufanya lolote ulipokuwa chini yao?”

    Akatikisa kichwa. “wasingeweza kunifanya kitu.”

    Nikamtazama kwa maulizo pasipo kusema kitu. Nadhani yeye mwenyewe akajiongeza na kunijibu swali langu la kimya. “Bado wananihitaji. Mimi ni asset kwao. Hawawezi kunidhuru.”

    “Unamaanisha nini wewe ni asset?”

    “Nimekuambia una maswali mengi. Najua. Tutakapotulia nitakuambia, pengine nitakata kiu chako.”

    “Hauwezi ukanambia hata machache?”

    “Naitwa Britney. Ni raia wa Marekani. Nadhani hayo yanakutosha.”

    Sikutaka kusumbuana naye. Niliona ninyamaze kimya, kweli hayupo kwenye mood, japo kifuani mwangu nilikuwa nalaumu sana kutokujua kinachoendelea ingali tulipokuwa kitu chochote kingeweza kujiri.

    Tukatembea kwa kama dakika kumi, akantazama kisha asiseme kitu akatazama zake mbele. Nadhani alikuwa anajiuliza maswali kichwani. Baada ya sekunde kadhaa, akasema, “Naomba umtazame mwanangu. Yeye ndo’ kitu pekee nilichonacho kwa sasa.” Kisha akasimama na kun’tazama. Nami nikasimama. Akaniambia, “Niahidi hilo … niahidi mtoto wangu atakuwa salama.”

    “Nakuahidi,” nikasema kwa sauti ya kutikisika. Akaniuliza, “Unaniahidi?”

    “Ndio, nakuahidi,” saa hii nikasema kwa kujiamini. Basi akaridhika tukaendelea na safari. Akaniambia kama tukitembea kwa takribani robo saa tutakuwa tumefika barabarani.

    Tukatembea kwa kama dakika sita, yeye mwenyewe akaanza kuongea. “Nimemkumbuka sana mama yangu,” sauti yake ilikuwa ya mtu anayekaribia kulia.

    “Kama ningalifuata alichonambia, nisingalikuwa hapa.”

    Nikamtazama nisimsemeshe kitu. Nilihofia maneno yangu yangeweza kumkatiza. Nilimwacha afanye vile alivyokuwa anataka.

    Akavuta makamasi mepesi kisha akaendelea, “Sasa nimekuwa mkimbizi nisiye na makazi. Toka kwenye kamera za mwanga mpaka kujificha chini ya uvungu na nyuma ya milango. Ama kweli maisha huweza badilika ndani ya sekunde moja tu!

    Ndani ya sekunde moja mtu akawa kilema. Akapoteza alivyovipata kwa masaa. Ndani ya muda huo mchache akawa amebadili mwelekeo wa maisha yake.”

    Nikaendelea kumtazama pasipo kutia neno. Niliona uso wake ukiwa umebadilika rangi kuwa mwekundu. Alikifikicha pua yake na kumwaga tena maneno, “Hakuna anayejua kesho yake, sio? … mimi sikudhani kama siku moja ntakuja kuwa na familia. Sikuwa nawaza hilo jambo kabisa, labda kwasababu ya aina ya maisha niliyoyachagua.

    Maisha yalonifanya ninyooshewe kidole kila nilipopita nikionekana laana, mchafu na niliyelaaniwa. Sikutaka mwanangu aje kushea laana yangu. Ashindwe kupita mtaani kwasababu ya mama yake. Ni adhabu. Najua ukubwa wa adhabu hiyo maana nimeibeba mgongoni kwa muda mrefu. Inachosha na kuumiza.

    Watamani kukaa mbali na walimwengu ambao ni wepesi wa kuhukumu na wachoyo wa fadhila. Lakini ajenti, wawezaa kukaa mbali na dunia?”

    Aliniuliza akintazama. Nikamtikisa kichwa kukataa pasipo kutia neno. Basi akatabasamu kwa mbali na kisha akakaa kimya kidogo. Tukatembea kwa kama dakika moja asinene jambo ila nikiamini ataendelea tu kusema.

    Nilihisi ana kitu kifuani. Atajihisi mwepesi endapo atakitoa.

    Akajifuta machozi na mikono ya sweta lake alafu akatazama juu kwenye matawi ya miti, pembeni na kisha mbele.

    “Hata kama niki –”

    “Shhh!” nikamzuia upesi nikimwonyeshea ishara ya kidole mdomoni. Kuna kitu nilihisi. Tulisimama tukatulia tuli na kutazama kushoto na kulia. Masikio yangu yalinambia nimesikia sauti ya watu wakiteta. Na sikuwa nimekosea, lah! Nyuma yetu kwa umbali, tukawaona wanaume wawili waliokuwa wamevalia nguo nyeusi na mikononi mwao wana bunduki ndefu!

    Wanaume hawa hawakuwa na usafiri, bali wakitumia miguu yao.

    Haraka nikamtaka Britney akimbie na mie kabla sijafungua miguu yangu nikafyatua risasi kuwalenga wanaume wale kuwapumbazisha kwa muda kidogo.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Tukakimbia na kukimbia. Nao wale wanaume wakawa wanaendelea kutukimbiza, wakawa pia wanatupa risasi wakijaribu kunilenga.

    Nikiwa nimembebelea mtoto, nikakimbia kwa kasi na kwanguvu mpaka kumwacha Britney nyuma. Si kwamba alikuwa anakimbia taratibu, hapana! Na wala hakuonekana mtu anayehitaji msaada. Alikuwa anajimudu kukimbia.

    Hatukudumu muda mrefu mbioni, nikasikia risasi ya karibu zaidi na kisha sauti ya kike ikilalama! Kutazama, nikamwona Britney akidondoka chini!

    “Shit!” nikamsikia mmoja wale wajamaa wanaotukimbiza akilaani, kisha kwa punde akamlaumu mwenzake kwa kumfyatulia risasi Britney. Hapa nikatumia nafasi hiyo upesi kuwamiminia risasi na kuwalaza chini.

    Nikamtazama Britney. Alikuwa amelengwa kwenye shina la nyuma la shingo. Risasi ilivunja uti wake wa mgongo! Ilikuwa ngumu kwake kupona. Damu zilimtiririka. Macho yake yalimwaga machozi akinishika kwanguvu na kung’ata meno yake.

    “Ajenti, mtazame vema mwanangu,” akasema akikwamakwama. Kisha akaninong’oneza, “Naitwa Juliette Simpson. Natumai utakuwa unanijua.” Alafu akajifia.

    Akafa mbele ya macho yangu. Akafa mwanaye akiwa bado hajitambui.

    Nikawaendea wale wanaume niliowaua na kuwapekua. Sikuwakuta na kitu zaidi ya bunduki na risasi kadhaa. Nikazichukua. Nilipomrudia Britney ambaye kabla hajafa alinipa jina lingine, naye nikampekua kama ana kitu. Alikuwa mtupu.

    Nikapata maswali juu ya nini cha kufanya. Haraka nikatoa simu yangu na kumchukua picha kadhaa, nashukuru simu yangu haikuwa simu inayoingiza maji.

    Nikiwa nimempiga picha mbili tu, nikasikia tena sauti ya watu, hiyo ikawa ishara kuwa sitakiwi kukaa hapo tena. Nikaanza kukimbia. Huko nyuma nikasikia, “Yule!” na vishindo vya watu vikinifuata kwa kasi!

    Nikakimbia sana lakini nguvu zangu hazikuwa kama za hapo awali, nilichoka mno. Kumbeba mtu kwa muda wote ule huku nikikimbia na kutembea haikuwa jambo jepesi. Hivyo basi nikaanza kupunguza kasi ya mwendo wangu na kupelekea wale maadui wanikaribie zaidi!

    Wakatupa risasi kadhaa. Nashukuru miti ilinikinga. Nilisikia zikipasua na kugotea mitini. Nilipoona maji yanazidi kupiku unga, nazidi kukaribiwa na hali ni mbaya, nikakimbilia mtoni na kujitosea humo!

    Nilizama maana kina kilikuwa kirefu. Risasi zikatumwa kunifuata ndani ya maji, zikanipitia kupunyua, lakini kwakuwa maji yalikuwa na nguvu na mengi ya kutosha kunipeleka, yakaniepushia na balaa!

    Yakanisomba kunisafirisha.



    Maji yalipotuama, tukiwa tumesafiri kwa kama robo saa, nikachoropoka toka mtoni kuitafuta barabara.

    Haikuwa safari ndefu sana. Sidhani kama nilichukua zaidi ya dakika kumi, nikawa tayari nimefika kwenye lami ambapo niliomba msaada na upesi nikapatiwa. Nadhani ilikuwa ni sababu ya mtoto niliyekuwa nimembeba. Mama mmoja ambaye alikuwa anasafiri na mbwa wake, alisimamisha akiwa ananitazama kwa huruma kisha akaniuliza naelekea wapi kabla hajaniruhusu niingie ndani na kuendelea na safari.

    Nikiwa ndani akawa ananidadisi nini kimenitokea, na kwasababu sikutaka kumsababishia taharuki, nikamlaghai kuwa tumepata ajali. Akanipeleka mpaka mjini kabisa na kuniacha hospitalini. Mtoto akatazamwa jeraha na kupatiwa dawa za kumsaidia dhidi ya maumivu na kumkausha jeraha.

    Baada ya hapo nikatafuta mahali pa kupumzikia. Nikamlaza mtoto na mimi kufanya utaratibu wa chakula maana njaa nayo ilikuwa inauma. Kila kitu kilipokuwa sawa, nikajilaza kitandani nikiwa nawaza.

    Mwanamke yule aliyefia mikononi mwangu, mtoto huyu ambaye yupo pembeni, watu wale waliokuwa wanatufukuza na mahusiano yao na Raisi! Nilihisi mambo yamechangamanaa sana.

    Sikudhani kama msako wangu wa Raisi ungenisafirisha ukubwa huo. Nikanyanyua simu na kumpigia Jack Pyong kumweleza yote yaliyojiri. Naye akashangaa sana lakini lile la Britney likamshangaza zaidi. Akanisihi nimtumie picha za mwanamke huyo na kisha jina lake hilo la mwisho ambalo alilisema kabla hajafariki, yaani Juliette Simpson.

    Nikafanya hivyo, akaniambia nimpatie muda kidog basi atanirejeshea majibu. Nikaendelea kujilaza kitandani. Kama baada ya dakika tano, mtoto yule akaamka akilalamikia maumivu makali kichwani.

    Nikampatia dawa na kumhasa apumzike zaidi. Lakini kabla hajafanya hivyo, akaniuliza mama yake yupo wapi? Hapa nikapata kigugumizi.

    “Unaitwa nani?”

    “Henessy,” akanijibu akiwa ananitazama kwa kufinya macho.

    “Henessy, Mama ametangulia Marekani. Marekani si ndo’ nyumbani?”

    Akasita kisha akaniuliza, “Kwanini ameenda mwenyewe?” kisha macho yake yakalowana machozi. “Kwanini ameniacha?’

    “Hajakuacha,” nikasema nikimkodolea macho. Nikamfuta machozi na kumpoza, “ilibidi atangulie kwenda huko maana ndege ilijaa. Nasi tutamfuata, usijali.”

    Akan’tazama kwa maulizo. Akafuta machozi kwa mgongo wa kiganja chake kisha akaniuliza kwa sauti ya kubashiri, “Tutaenda lini?”

    “Usijali, tutaenda. Kuna mambo kadhaa namalizia kama kesho ama keshokutwa. Sawa?” akatikisa kichwa kuafiki lakini kishingo upande. Kidogo simu yangu ikaita, alikuwa ni Jack Pyong, nikapokea akaanza kunambia nini amepata.

    “Tony,” akaanza kwa kuniita jina. Sauti yake ilikuwa ya chini na msisitizo. Akanambia, “Huyo mdada ni mwigiza picha za ngono!”

    “Yupi?”

    “Huyo Juliette! Namaanisha Juliette Simpson!”

    “Huyo niliyekutumia picha?”

    “Acha basi kuniuliza maswali ya kijinga. Kwani tumetoka kuongelea nini hapa muda si mrefu?”

    “Kuna mtu mwenye maujinga kama wewe?”

    “Nitaacha kukwambia! Ohoo!”

    “Sema basi. Unajua credit inaenda!”

    “Sasa nikitaka kusema wewe unaanza mambo yako. Tulia kama unanyolewa.”

    “Sawa, nimetulia. Kwahiyo unanambia—” kabla sijamalizia nikamtazama yule mtoto, sikutaka asikie. Nikasonga kando kidogo.

    “…kwahiyo Juliette huyo ni pornstar?” Pornstar maanaye mcheza sinema za ngono.

    “Ndio. Ni maarufu tu. Sikuwa najua hilo mpaka nilipoingia mtandaoni!”

    “Sasa Jack, mcheza sinema za ngono atakuwa ana mahusiano gani na kupotea kwa Raisi?”

    “Tony, hiyo ni kazi yako. Unanipachikia mimi sasa?”

    “Sasa we fala, huko mtandaoni ulikuwa unafanya nini?”

    “Nakutafutia huyo mtu wako. Ebu sikia, kesho kama nikipata muda nitaenda kwenye kampuni aliyokuwa anafanyia kazi. Pengine nitapata baadhi ya majibu. Baadae!”

    Akakata simu na kuniachia maswali lukuki kichwani. Niliona mambo yanazidi kuwa magumu. Nikazama mtandaoni na kuandika jina la yule mwanamke, punde nikaona majibu ya ajabu. Kweli mwanamke yule alikuwa mcheza sinema za ngono.

    Lakini kwa taarifa zaidi, alikuwa mstaafu! Lakini kwa kazi hii kuna mstaafu kweli ilhali video zake bado zipo hewani na watu wanaweza kuzipakua na kuzitazama?

    Nilipofuatilia zaidi nikabaini na hiyo kampuni aliyokuwa akifanyia kazi. Kwa jina, LEXANDER PLEASURE ikiwa inasimamiwa na mwongozaji mwenye asili ya kilatini aitwaye jina la utani, Bomboclat!

    Hapa sasa nikapata kujua kwanini mwanamke yule alishangaa nilipomwambia simfahamu. Huenda alidhani umaarufu wake kwenye michezo hiyo ungelinigusa hata mimi. Lakini pia nikafahamu kwanini alinipatia majina mawili, mosi Britney, pili Juliette. Ina maana Britney lilikuwa ni jina lake la uhalisia wakati Juliette Simpson likiwa ni la ‘kazini’.

    Nikashusha pumzi ndefu nikimtazama yule mtoto. Nilikuwa nawaza kama atakuwa anajua kuwa mama yake huko mtandaoni yupo uchi. Nikajikuta natikisa kichwa kisha nikaanza kusuka tu mipango ya kurudi Marekani maana sikuwa na cha ziada cha kukifanya tena hapa Ujerumani.

    Hivyo nikaona ni stara kufunga safari, kesho asubuhi na mapema, kwenda jiji la Berlin ambapo ndipo kuna ubalozi wa Marekani.

    Siku hiyo nipumzike tu kwakweli. Nilikuwa nimechoka mno. Shurba nilizopitia zilikuwa zatosha kunifanya nijilaze.



    **



    Kesho yake …



    Berlin, Ujerumani.



    Nilitoka ndani ya balozi nikiwa na uhakika wa safari yangu jioni. Na kwakuwa nilijitambulisha na kuthibitisha humo ndani kuwa mimi ni ajenti wa CIA, basi mambo hayakuniwia sana ‘ugumu’.

    Nikaongozana na Henessy mpaka mgahawani kujipatia chakula. Hapo tukakaa kwa muda wa kama nusu saa kabla hatujajiweka kwenye basi na kwenda mpaka beach. Nilitaka angalau nifurahie ujio wangu hapo Ujerumani japo ulikuwa ni wa kikazi.

    Walau nipate muda wa ‘kuenjoy’ kabla sijaacha ardhi hiyo kurejea nyumbani. Nikiwa hapo nikapata nafasi ya kuzoezana na Henessy ambapo tulicheza na kufukuzana pamoja tukiwa tunapigwa na pepo ya bahari.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Tukiwa tumechoka, tukawa tunatembeatembea tu fukweni. Lakini kama baada ya hatua zetu kadhaa, paliongokea mwanamke mmoja ambaye amevalia ‘casual’. Uso wake ulikuwa umefichwa na miwani meusi na miguu yake imebanwa na jeans iliyopauka. Begani ananing’iniza mkoba mdogo uliobana kwapa lake.

    Mwanamke huyo akiwa anapunga mkono wake na kutabasamu, aliita, “Heneessyy!” tukageuka wote kutazama. Alikuwa anatokea upande ilipo barabara kuu.

    Nikamuuliza Henessy, “Unamjua huyo mwanamke?”

    Henessy hakunijibu, badala yake akawa anamtazama kwa umakini mwanamke huyo pengine akumbuke kama alishawahi kumwona mahali. Hivyo kabla hajanipa majibu, mwanamke huyo, kwakuwa alikuwa anakimbia na kutembea kwa kasi, akawa ametufikia.

    Akan’salimu kwa upesi, akitumia kiingereza, kisha akainama kumtazama Henessy akitabasamu. “Hujambo Henessy? … unaendeleaje muda wote huo?”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog