Simulizi : Urithi Wenye Umauti
Sehemu Ya Tatu (3)
"Hamjambo ndugu zangu"niliwasalimu,"safi tu bratha"mmoja wao,bonge la mtu akatangulia kunijibu baada yao kugeuka."Naomba kuonyeshwa nyumba za gesti"nikawauliza."Nyoosha upande ule mbele kidogo utakutana na hoteli Kisha fuata uchochoro wa kushoto.Utaona majumba ya kukodi"mtu yule akanielekeza.Baada ya kuwashukuru,nilifuata njia niliyoelekezwa na wale wahandisi wa magari.Mbele kidogo hatua Kama hamsini hivi nikakutana na bango lililokuwa na mchoro wa binti aliyekuwa nusu uchi ikiwa na maandishi ya kichina ambayo sikuielewa ng'o.Kuliwacha bango lile nyuma nikakutana na uwanja wenye upana sawa na ule wa mchezo wa miguu lakini ikiwa imejaa vyuma na magurudumu mabovu.
Sehemu kadha wa kadha za magari zilikuwa zimekusanywa upande wa kulia zikingoja ukarabati au kubadilishwa skrepu.Kando na kelele zilizokuwa zikitokea nje ya uwanja ule,pahali pale palikuwa na ukimya wa ajabu.Mbele sikuona uchochoro wowote ambao ungenifikisha kwenye gesti za kulala jinsi lile bonge la mtu lilivyonielekeza.Ghafla kengele ya hatari ikagonga kichwani,uwezekano wa asilimia mia kuwa nilikuwa nimejiingiza kwenye domo la mamba-mtegoni!!Nilijipenyeza katikati ya vyuma vile Kisha nikaiona gari aina ya Toyota,muundo wa kizamani, iliyokuwa imeng'olewa gurudumu zote na kusimamishwa juu ya bati gumu kuzuia kutu kuharibu mwili wake.Niliichagua kwani ndiyo iliyokuwa karibu na nilipokuwa na kwa vile sikutaka kupoteza muda,nikaiendea.Nilipata ugumu wa kufungua milango yake kwani ilikuwa imeathirika na kutu lakini dakika chache tu nikawa nimejitoma ndani.Viti vya gari ile vilikuwa bado kwenye hali yake ya upya.Nilijirusha upande wa nyuma na kujilaza kwenye viti.Mwili wangu ukawa umepata burudisho ambayo nilikuwa nimeikosa kwa muda mrefu.Nilitazama saa yangu ya mkononi iliyoonyesha kuwa ni saa kumi usiku.Alfajiri ilikuwa karibu kuigubika nchi.
Kivuli kutokana na kiwiliwili cha mtu ndiyo ilinishtua kutoka kwa starehe zangu.Nilichungulia dirishani kwa umakini bila kusababisha kelele yoyote mle ndani.Watu wawili,mmoja wa kiume na wa kike,walikuwa wamesimama karibu na gari lile nililokuwamo.Mwanamke alikuwa na mkoba mweusi ulioshabihiana na wangu Kisha mwanamume yule akawa ameikamata bunduki kubwa ya AK-47 mkononi kwa ukakamavu."Akina Jonah wamesema amekuja huku.Mbona hatumwoni?"Mwanamume yule alisema kwa sauti ndogo lakini niliyoisikia vizuri."Yawezekana ametorokea upande ule,kuliko na lori bovu lile"mwanamke yule akamjibu mtu yule.Ukapita muda mfupi kabla ya wawili wale kuzungumza tena kisha yule wa kike akasema,"mbona usimwulize mkuu 'atrack' simu yake Kisha atupe ramani ya aliko huyu kijana?
"Mara moja nikajua kuwa wale watu walikuwa wakinifuata kwa kutumia GPS ya simu yangu.Haraka sana nikachomoa simu yangu na kutoa betri Kisha nikaitoa pia kadi ya mawasiliano na kuvihifadhi kwenye mifuko midogo iliyokuwa kando ya begi lile.Wale watu wawili walikuwa wamesogea umbali wa mita tatu hivi Kisha yule wa kiume akawa akibonyeza rununu Kisha akaiweka kwenye sikio."Hatujampata kwa sababu amepotelea sijui wapi…ndio…tupo kwenye gereji hivi sasa…hapana…tusimwue?Sawa Sawa"yule mwanamume akawa akizungumza na mtu mwingine upande wa pili ambaye sikuwa namjuwa.Ilikuwa ni Kama anapewa amri kuhusiana na mimi."Wanasemaje Ethan?"yule mwanamke akamwuliza yule wa kiume ambaye nikamjua, Ethan."Mkuu anasema wamepoteza mawimbi ya simu yake hivyo tuendelee na msako kote mjini hata kwenye majumba ya kulala ila akipatikana tusimwue."Ethan akamjibu."Tusimwue!!Hukumbuki Jana akina Liam wamepoteza mmoja wao kutokana na huyu bwege?"yule mwanamke akamaka."Nani aliuawa kwenye kundi hilo?Mbona sijapata taarifa yoyote?
"Ethan akauliza,"akina Liam walikuwa wamerudi kwa yule bilionea kutafuta ufunguo wa lile kasha kisha wakampata mwanawe,mkuu anashuku alikabidhiwa ufunguo ule na babake kwa siri.Katika harakati za kuipekua jumba lile na pia kumsaka yule kijana,mmoja wao akawa amemkaribia lakini akaambulia kusafirishwa kuzimu kwani alipigwa kininja"yule mwanadada akamjibu Ethan kwa maelezo marefu.Kwa kweli moyo wangu uligubikwa na furaha kwa kugundua kuwa hata wale watu walikuwa wananiogopa kufikia hatua hiyo."Lakini Ava yabidi ugundue kuwa bosi na huyu kijana ni wa damu moja hivyo hatutakikani kumwua.Ni sisi tutimize kazi,tulipwe na turudi nchini kwetu."Ethan alimwambia yule mwanadada ambaye pia nikamjua alikuwa anaitwa Ava.
Maneno ya Ava yakawa yameniacha njia panda.Ni nani yule ambaye tulikuwa na unasaba alikuwa akinisaka?Wale watu walichukua muda mfupi tu pale kisha wakaondoka huku nikikosa kusikia mazungumzo yao vyema kwani mwendo wao haukuwa wa polepole.Tayari kutokana na maongezi ya wale watu wawili; Ethan na Ava,vita rasmi kati yangu na mkuu wao ambaye sikuwa nikimjua ikawa imetangazwa rasmi.Simu yangu ya mkononi ambayo ilikuwa ikitumika kunifuatilia nikawa nimeizima hivyo kuwapoteza.Kitambo miale hafifu ya jua ilianza kujipenyeza kupitia kwenye vioo vya gari lile.Kutoka mle ndani nikapata fursa ya kusaili mazingira pahali pale.Ulikuwa uwanja mkubwa uliokuwa umezungushiwa ukuta wa mabati.Upande wa juu kulikuwa na lori moja bovu lililokuwa limetelekezwa la kubebea mchanga lakini lenye muundo wa kisasa.Kwa muonekano wake ni kama lilikuwa limehusika katika ajali mbaya sana kwani mbondeko ubavuni ulidhihirisha hivyo.
Sikupenda kuendelea kukaa mle ndani zaidi kwani kitambo niligundua kuwa wale wahandisi wa magari Yale walikuwa washirika wa kuniwinda au labda wakukodiwa kunipokonya uhai wangu.
Upekuzi nilioufanya mle ndani haukufanikisha kupata chochote cha umuhimu kwani lilikuwa gari bovu tu.Kwa utaratibu,nikausukuma mlango wa lile gari na kujitoa huku begi nikilivaa mgongoni.Hali ya anga ilikuwa shwari kabisa,mwanga na joto kutoka kwa jua ikawa imeruhusiwa kuibusu dunia.Mwili wangu ulianza kurudiwa na uhai huku shati na suruali zikiendelea kukauka.Nilianza kutembea nikienda uelekeo wa nyuma ya uwanja wa gereji lile bila ya kusahau kusaili usalama wa pahali pale.Kufikia uzio ule wa mabati,nikauruka kwa kujivuta na mikono.Ulikuwa uzio imara sana tofauti na nilivyofikiri mwanzo.Nilifikia nyuma ya duka la nguo ambapo sikupata ugumu wa kuendelea mbele baada ya kupata uchochoro ulionifikisha upande wa mbele.Wazo lilinijia la kununua nguo pale kwani nguo zangu zilikuwa zimechakaa na kuchafuka kupita kiasi.Mwanadada mmoja mrembo akanipokea mpaka ndani ambapo nilianza kupekua hapa na pale nikitafuta suruali na shati ambazo zingenipendeza.Baada ya upekuzi wa hapa na pale,nilivutiwa na suruali moja yenye muundo wa kikombati na tisheti moja nyeusi.Suruali ile pia ilikuwa yenye rangi ya weusi ila iliyokolea.
Nikaendelea mpaka upande kulikokuwa na viatu,nikachagua buti moja ngumu ya kijeshi.Kwisha maliza kununua mavazi Yale,nilipachika kadi yangu ya mawasiliano na kuiwasha rununu kisha haraka nikaingia sehemu ya Mpesa nilikodhamiria kulipia.Muda mfupi tu nikawa nimemaliza kumlipa yule mwanadada kisha nikaizima tena rununu ile na kuchomoa kadi ya mawasiliano na betri.Nikaondoka eneo lile baada ya kuulizia zilipokuwa vyumba vya kukodi.Nilifululiza mpaka sehemu niliyoelekezwa na binti yule,nikakodi chumba kimoja.Kwisha kuoga,nikavaa suruali na shati niliyokuwa nimenunua muda mfupi tu nyuma.Kwenye kioo nikadhibitisha kuwa nilikuwa tayari kukabiliana na misukosuko yoyote.Usingizi ukanipitia nikiwa pale kitandani huku nikiwa nimevaa viatu vile.
Ubishi wa sauti ya juu kati ya watu ambao walikuwa upande wa mbele ndiyo iliyonigutusha."Sisi hatuwaruhusu wateja wengine kuingilia starehe za wenzao.Hivyo nambari ya chumba mnachokitaka hamtapewa"sauti ya mwanadada wa mapokezi ikasikika."Sisi Hatuna shida nawe ila yule mvulana aliyechukua chumba humu"sauti ya kiume ikasikika.Machale yakanicheza,wale watu walikuwa wamenifikia tena mle niliokuwa nimejificha.Walipokuwa wakiendelea kubishana,nilishuka kutoka kitandani na kuvaa begi langu baada ya kuchomoa bastola niliyowaibia wale watu nyumbani kwetu.Sikujua ilikuwa imebakia na risasi ngapi ila hilo halikunibughudhi,ilmuradi tu nilitaka itumike kuwaogofya wale watu.Kwa uangalifu na polepole nikakinyonga kitasa cha mlango na kutoka Kisha nikaurudisha polepole.Kando na mabishano kule mapokezi,wapangaji wengine walikuwa kimya,kila mmoja akijihusisha na ya kwake.
Nilitembea kwa kunyata nikichukua uelekeo wa zilipokuwa vyoo.Nikakata kona upande wa kushoto, nikawa nikiangaliana na mlango wa chuma uliokuwa umefungwa na kwa uchunguzi wa haraka,nikagundua kuwa mlango ule ulikuwa umefungwa kwa muda mrefu kutokana na kutu iliyokuwa imeanza kuiharibu kufuli ile.Haraka nikauparamia mlango ule na kutokea sehemu zilikokuwa vyoo ambavyo navyo havikuwa vimetumika kwa muda mrefu mpaka misitu midogo midogo ikawa imeanza kuota kwenye kuta.
Mipasuko ya hapa na pale kwenye kuta ikawa dhihirisho tosha kuwa vyoo vile vilikuwa vimetumiwa miezi kama si miaka ya nyuma sana.Nyuma ya vyoo vile kulikuwa na uzio wa mbao ambao ulikuwa na urefu usio wa kawaida mpaka sikuweza kuona nini kinaendelea upande ule.Nilitembea haraka mpaka kwenye uzio ule Kisha nikaanza kuuparamia kwa ustadi na umakini.Kabla ya kufika upande wa juu,nikasikia sauti mbovu ya bastola isiyo na kiwambo cha kuzuia sauti ikifuatiwa na ukemi wenye kuashiria maumivu.Sikutaka kupoteza muda pale hivyo nikamaliza kuupanda uzio ule na kurukia upande wa pili.Nikawa na uhakika kuwa wale watu walikuwa wamempa mwanadada yule wa mapokezi tiketi ya kwenda kuzimu.Eneo nililotua lilikuwa uwanja wa kutupa taka taka.
Kulikuwa na chupa za pombe, karatasi zilizorushwa ovyo ovyo,nguo kuukuu,mipira ya kondomu zilizotumiwa kwenye mapenzi ya kununua.Almuradi eneo lile lilikuwa na kila aina ya uchafu.Niliambaa ambaa kwenye ukuta ule wa mbao huku nikitoka nyuma ya vyoo vile, nilikuwa nafuata uchochoro ambao ulielekea kwenye mabanda ya walalahoi.Nikawa nimeiacha eneo lile kwa mbali sana.Jua lilikuwa linachoma kwelikweli mpaka jasho ikawa ikinitiririka.Vibanda vile nilipovifikia,nikakutana na kundi la vijana wakibugia makombo ambayo sikujua vilikuwa mabaki ya vyakula gani.Waliponiona wakasimama huku wakianza kupiga kele kwa lugha ya sheng',ambayo sikuielewa katu.
Mmoja wao akaanza kunikaribia kwa kasi ya ajabu huku akiwa na kipande cha chupa amekiinua mkononi nami bila kupoteza wasaa nikajitayarisha kwa vurugu lile.Muda wote ule wale wenzake walikuwa wakishangilia.Nikaona uwezekano wa kumdhibiti yule ombaomba ilikuwa ni kwa kumkita teke la nguvu tumboni.Aliposogea nilipokuwa,nikajipinda na kumchapa teke moja maridadi ikijulikana kana 'roundhorse kick'.Kutokana na ugumu wa viatu nilivyovivaa,mvulana yule akajishika pale teke lilikita Kisha akapiga ukemi.Wale wengine kuona hivyo wakaokota vifaa vyovyote vilivyokuwa vigumu ardhini na kuanza kunitupia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment