Search This Blog

Friday 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (1) - 3

 






Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (1)

Sehemu Ya Tatu (3)









Ujumbe haukwenda. Raheem akalaani kwa tusi. Alifungua kidroo kilichopo pembeni ya usukani akatoa bunduki yake ndogo.





Baada ya dakika kadhaa, Raheem alifika hospitalini. Alishuka akaweka silaha yake nyuma ya kiuno akaifunika na koti. Akatoa simu.







“Mko wapi? ... Nakuja.”







Alisonga asichukue hata dakika tatu akawa ameshafika. Alikuta wenzake pamoja na inspekta Vitalis wakiwa wameketi kwenye mabenchi ya hospitali kama watu wangojeao taarifa na maelekezo toka kwa daktari.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Karibu!” Mtemvu alimpokea.

“Ahsante. Vipi anaendeleaje?”

“Daktari kasema anaendela vizuri, japo kavunjika mikono na uso umeharibika vibaya mno.”

“Kilichosababisha ajali ni nini?”

“Kwa mujibu wa mashuhuda, Bwana Filbert aliacha barabara yake akaparamia upande wa pili.”

“… Ila mimi siamini hilo.” Pius alidakia. “Yani aache barabara yake afuate barabara ya upande wa pili! Kutakuwa kuna jambo tu.”







Raheem akatikisa kichwa chake kwa masikitiko.







“Na hicho ndo’ kinakutesa. Filbert amepata ajali sababu ya stress zake. Anyway, mwambie huyo mtu wenu anayewatisha tisha aache kunifuatilia. Nitampoteza katika huu uso wa dunia!”







K square, Mtemvu na Pius wakatizamana kwa kuduwaa.







“Naondoka, nitakuja baadae nikipata muda. Kwa sasa sipo vizuri. Mtanifikishia pole zangu kwa huyo majeruhi wa kujitakia.”







Aliaga hivyo akanyanyua mguu wake kuondoka. Alifika kwenye uwanja wa kutunzia magari lakini hakuona gari lake popote. Alitizama huku na huko pasipo kuona kitu. Akibung’aa hapo, akamuona bwana Pius akishuka. Haraka akamkimbilia.







“Unaenda wapi?”

“Kwangu, si unajua nina msiba.” Alisema Pius akitembea kana kwamba hana muda wa kupoteza.

“Mbona hujaondoka. Kuna mtu unamngoja?”

“Hapana. sioni gari langu!”

“Uliliweka wapi?”

“Pale! Nyuma ya ile Escudo nyekundu!”

“Una uhakika?”

“Asilimia zote! Lilikuwa pale kabisa!”







Waliongozana kumfuata mlinzi getini kumuuliza, mlinzi akasema hajaona gari la aina hiyo likipita getini isipokuwa tu kwenye kuingia kwake.







Raheem alichanganyikiwa. Pius alimshika bega akamwambia:

“Nadhani na wewe utakuwa mepata matatizo ya kisaikolojia.”







Akatabasamu kwa mbali.







“Nenda kalitafute vema.”







Pius alisema akiondoka zake.







Kwa mara ya kwanza Raheem alianza kuhisi wanayoyaongea wenzake yanaweza yakawa na chembe za ukweli ndani yake. Kuna mauzauza. Kuna mtu anawatafuta. Kuna mtu anawadai roho zao.





Ilikuwa ni picha mbili tofauti kipindi kile cha msiba na hiki cha sasa. Nyumba ya marehemu Malale sasa ilikuwa pweke. Hakukuwa na gari lolote nje, wala mtu. Kwa haraka haraka mpita njia anaweza sema hakuna mtu kwa jinsi kulivyokuwa kimya na kulivyochoka haraka.







Ndani ya sebule kulikuwa patupu. Kochi moja tu ndilo lilibakia na meza mbili, mojawapo ikiwa imebebelea televisheni. Kwenye hilo kochi moja aliketi Miraji, mtoto pekee wa kiume wa marehemu.







Taratibu televisheni ilikuwa inapiga muziki wa rege, muimbaji akiwa anajirusharusha pamoja na wenzake wakitengeza mithili ya wehu fulani wasiojali.







Miraji akishika tama, macho yake yalikatiza kwenye televisheni hiyo yakatizama meza kwa uso wa fikra.







Picha ya baba yake ilimjia kichwani tena ikisindikizwa na maneno ya mama yake ambayo tokea apate kuyasikia kwenye kikao hayakukoma kumrudia. Aliyafumba macho yake kwanguvu na kuyafumbua akashusha pumzi ndefu akitengua tama.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





Pembeni yake upande wa kushoto kulikuwa na kijitabu kidogo cheusi juu yake ikiketi simu ndogo aina ya nokia, maarufu kama ‘nokia tochi’. Baada ya wimbo uliokuwa unapiga kwenye televisheni kukata, ujumbe uliingia kwenye simu kwenye simu hiyo haraka Miraji akadaka simu aufungue.







‘Nimeshaipata. Njoo hapa kona, nimepaki.’







Tabasamu likachipuka kwenye uso wa Miraji baada ya kusoma ujumbe huo. Ni kama vile alikuwa anausubiria kwa hamu zote.







Alinyanyuka akazima televisheni na kubeba kijitabu na simu yake akatoka nje kuelekea kona alipokuta gari aina ya Toyota altezza rangi ya silva. Alifungua mlango akaingia ndani.







“Niaje Jombi?”

“Poua. Mzigo huu hapa.”







Mwanaume aliyekuwa amekaa kiti cha dereva, Jombi kwa jina, alimkabidhi Miraji mfuko mweusi. Miraji akaupokea na kuuchungulia, kisha akatabasamu.







“Ina risasi ngapi?”

“Tano.”

“Mbona chache?”

“Chache? Kuuwa watu watano ni wachache?”

“Una uhakika gani itauwa watu watano?”

“Ndio uhakikishe sasa. Pesa yangu ipo wapi?”







Miraji alimnyooshea Jombi mkono alioutoa kwenye mfuko wake wa suruali, Jombi akapokea na kutizama. Ilikuwa ni pesa, elfu kumi kumi zilizojikunja zikirundikana.







“Hapa fresh. Nitalipitia gari langu kesho asubuhi.”







Jombi alisema akitoka nje ya gari na kumuacha Miraji ambaye alisogea kwenye kiti cha dereva akafunua kijitabu chake asome. Ndani kulikuwa na orodha ya watu ikiwa imejipanga kwa mujibu wa tarakimu.







Pius – Mbezi kimara, nyumba no. 501.





Katende – Bahari beach, nyumba no. 222





Raheem – Mbezi beach, Tangi bovu. Nyumba no. 123





Filbert – Mikocheni A, nyumba no. 335.





Mtemvu – Mbezi beach, nyumba no. 203.







Aliweka kialama cha nukta kwa mlengwa wa kwanza, Pius, kisha akaondoa gari kuelekea upande wake wa kusini, bunduki na kitabu vikijilaza kwenye kiti cha kando huku muziki wa fujo ‘get out of the way’ wa mwanamuziki maarufu Ludacris ukifunguliwa na kupigwa kwa sauti ya juu.







Ilifikia pahala, gari likasimama. Kulikuwa na foleni kama ilivyo ada kwenye jiji la Dar.







Miraji alishika tama akisubiria foleni liende. Alitizama tizama mandhari ya ndani ya gari na mara akaona mfuko mweusi umetokezea toka kwenye droo ndogo. Alifungua akatizama, ndani akakuta majani ya bangi na misokoto kadhaa, ikiwa pamoja na kiberiti cha gesi.







Aliwasha na kuanza kuvuta. Taratibu macho yakageuka rangi nyekundu. Foleni iliporuhusiwa aliondoa gari kwa kasi ya ajabu akiyavuka na kuyapisha magari mengine mithili ya mashindano. Moja kwa moja alienda kupaki gari mbele ya nyumba ya bwana Pius. Akatulia hapo kwa dakika kadhaa asome mazingira.







Alishuhudia umati wa watu ukiwa unaingia ndani. Vilevile na magari mengi mengi yakiwa yamejipanga kwa nje. Akajiuliza:

“Kuna nini hapa?”







Alitoka ndani ya gari akaingia ndani ya nyumba. Alinyookea kwenye viti vya plastiki akaketi. Mazingira yaliyopo ndani yalitosha kumuonyesha kwamba kuna msiba. Alimuuliza jirani yake.







“Samahani, nilikuwa nina shida na bwana Pius. Wapi naweza kumpata?”

“Nadhani atakuwepo sebuleni. Amerudi muda si mrefu.” Jirani alimjibu. Alikuwa ni mzee mwenye mvi tele kichwani na miwani kubwa usoni.







Miraji alinyanyuka akaenda sebuleni. Alifika akaketi kwenye kiti akijaribu kupiga mahesabu Pius ni yupi. Bahati nzuri, punde tu aliingia mgeni akamnyookea bwana Pius kumsalimu na kumpa pole. Miraji akatabasamu.







“Kumbe ndiye yeye.”







Alinyanyuka akafuata gari lake achukue bunduki.







“Wacha nitengeneze msiba mwingine.”







Alijisemea mwenyewe akitabasamu na kukoki bunduki. Alitoka kwenye gari akarudi ndani akiwa ameificha bunduki kwenye koti lake la ngozi alilojivika, akaenda kuketi kwenye kiti alichokuwa amekaa hapo kabla.







Macho yake yalimtizama bwana Pius kana kwamba hataki kumpoteza. Bwana Pius naye akamtizama Miraji kana kwamba anamfananisha. Mwishowe Pius alisimama akamfuata Miraji.







“Habari yako kijana?”

“Njema, shikamoo.” Miraji alisalimu bila ya kumtizama mlengwa.

“Wewe ni Miraji?”







Miraji akashtushwa. Hakutegemea kama angeligundulikana kwa wepesi hivyo.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Ndio. Umenijuaje?”

“Wewe ni mtoto wa Malale, sio?”







Kabla ya kujibu, Miraji alimtizama Pius usoni na sura kavu kisha akatizama chini.







“Ndio.” Akajibu kwa sauti ya kiburi.

“Karibu sana. Mimi na baba yako tulikuwa marafiki sana. Alikuwa ananiambia sana juu yako.”







Miraji hakusema jambo. Alibaki kimya kana kwamba hakusikia alichoambiwa. Uso wake aliulekezea chini.







“Okay. Kama utakuwa na tatizo lolote utanambia.” Pius aliaga akaondoka kabisa sebuleni akitoka ndani. Miraji alivuta visekunde kadhaa kisha naye akatoka kumtafuta bwana Pius.







Bahati haikuwa kwake. Alimkuta akiwa ameketi na watu kadhaa. Akasonya.







“Hapa kazi ipo. Sidhani kama nitafanikisha.” Aliongea mwenyewe. Alitoka eneo lile akarudi kwenye gari lake.







“Siwezi kurudisha gari kesho bila ya kutimiza adhma. Lazima nimuue hata mmoja.” alijongelesha mwenyewe akiwasha msokoto wa bangi. Alinyonya mara moja akamimina moshi nje.





Alishika usukani akakanyaga mafuta mpaka Bahari beach, mbele ya jengo namba 222, Mali ya bwana Katende, ama K square. Jengo kubwa lenye ukuta mpana na mrefu, juu yake kukiwa na nyaya zilizoshikilia bango lililosomeka:







HATARI, NYANYA ZA UMEME!







Alikaa hapo kwa muda kidogo. Mlinzi akamfuata na kugonga kioo cha dirisha.







“Wewee! Wewe!”







Miraji akashusha dirisha chini. Mlinzi akakunja sura akipepea hewa.







“Kijana, unafanya nini hapa na mibangi yako?” Mlinzi aliuliza. Alikuwa ni mbaba mweusi mwenye mwili kiasi, akiwa kavalia sare za rangi ya kahawia na kofia ya kiaskari, begani ukikatiza mkanda uliobebelea bunduki kubwa kuukuu.







“Nipo tu, nimekaa.”

“Umekaa! Umekaa kwako hapa?

“Kwani kuna shida gani?”







Mlinzi akamnyooshea Miraji bunduki yake.







“Tokomea kabla sijakufanya historia sasa hivi!” Alitoa kitisho.







Miraji alitizama mlinzi kana kwamba anapanga kumvamia. Aliwazana kuwazua afanyaje akaona hana ujanja zaidi ya kutokomea. Aliwasha gari akayeya.







Alienda kwa Raheem, Filbert, na kwa Mtemvu akashuhudia mandhari zinazofanana; nyumba kubwa, kuta ndefu na pana, pamoja na walinzi wenye silaha za moto, huku asiwaone hata wahusika wake anaotaka kuwamaliza.







Alirudi nyumbani akapaki gari. Akiwa ndani ya nyumba alitulia tuli akitafakuri mambo. Baada ya muda alimpigia Jombi na kumuomba aje eneo alilopo.







Ndani ya muda usiozidi lisaa, Jombi alikuwa tayari ameshafika. Wakajiweka ndani ya gari.







“Ndugu yangu, tatizo ulikurupuka. Haukuwa na mipango yoyote. Ulienda kichwa kichwa kwa kudhani ni rahisi.”

“Mbona hukunambia, Jombi?”

“Nilitaka ukajionee mwenyewe. Kwani haujui kwamba watu unaoenda kuwawinda ni watu wazito? Wakubwa? Wana pesa ushawishi na nguvu?”

“Najua.”

“Sasa? Ulitegemea utawaua kama kuku, sio?”

“Nipe basi maujanja, Jombi. Mbona kama unaninanga?”

“Ni hivi, kwanza inabidi usome maeneo wanaoishi wahusika wako, kivipi unaweza ukayaingilia. Pili, uwe na mavazi ya kuficha utambulisho wako. Tatu, ujue ni maeneo gani wanapenda kuyatembelea, kama yapo. Nne, ufahamu udhaifu wao kama inawezekana, si wote wanaweza uwawa kwa risasi, inaweza ikawa sumu au chochote!”

“Sawa. Nisaidie.”

“Utan’lipa kiasi gani?”

“Embu sahau kwanza kuhusu mambo ya pesa. Huwezi kunisaidia kama rafiki yako?”

“Urafiki utanunua vifaa?”

“Tutachangiana, Jombi. Ile pesa yenyewe niliyokupa nimemwibia mama. Kuna kazi ananitafutia, mambo yatakaa vyema tu.”

“Poua, isiwe kesi. Tunahitaji kununua vifaa vifuatavyo; Darubini, Mkasi mkubwa wa kukatia nyaya, vinyago, buti na nguo kadhaa."

“Sawa. Lini sasa tutafanya hivyo?”

“Utakapokuwa tayari.”

“Hata leo?”







Jombi asijibu, alikanyaga mafuta na kupotea lile eneo moja kwa moja mpaka madukani waliponunua mahitaji yao.







Giza lilipoingia walipitia nyumba za walengwa wao, mmoja baada ya mmoja huku wakiandika baadhi ya taarifa kwenye kijitabu walichokuwa wamekibebelea; ulinzi wa eneo husika, idadi ya taa, eneo la kujificha na sehemu pa kutorokea.







Walipomaliza walijirudisha majumbani kwa miadi ya kuanza kazi baada ya wiki moja, waache kwanza mambo ya msiba yapite kando.







Miraji alimkuta mama yake akiwa amesimama nje ameshikilia kiuno. Ni kama vile alijua mtoto wake anakuja muda si mrefu.







“Ulikuwa wapi?” sauti ya mama Miraji – Bernadetha – iling’aka.

“Nilikuwa kwa rafiki yangu.”

“Rafiki yako yupi? Unaondoka unamuacha mdogo wako mwenyewe wewe unazurura! Nimemkuta mtoto ana njaa, hana wa kumuhudumia!”

“Samahani, mama.”

“Baba yako alikuambiaje kuhusu huyo rafiki yako?”

“Mama, unajua ni nani?”

“Kwahiyo unadhani sijawaona?”

“Mamaaa! … Mbona hana shida?”

“Hana shida? Mvuta bangi?” Bernadetha alibinua mdomo akikunja sura.

“Mama umeshaanza sasa. Kwani mimi sijui kizuri na kibaya lakini?”

“Asiyesikia la mkuu huvunjika guu Miraji. Pesa yangu niliyoweka kwenye droo nayo ipo wapi?”







Bernadetha sasa akamtizama Miraji kana kwamba anamtizama mtoto anayedai hajala sukari ilhali chembechembe zaonekana mashavuni.







“Sijui!” Miraji alijibu akipandisha mabega.

“We mtoto wewe. Ndio pesa ya kula hiyo. Unataka kuniambia Marietta ndiye kachukua?”

“Sijui, mama! Si nimeshakuambia?” Alilalamika Miraji akienda chumbani kwake na kumuacha Bernadetha nje ameduwaa. Bernadetha akiwa naye anaenda ndani asibaki nje mwenyewe wakati huo wa usiku, simu yake iliita akaitizama ufupi na kuipokea akiendelea na mwendo.

“Haloo … Salama, mnaendeleaje? ... Tunaendelea vizuri … Filbert? ... Amepata ajali lini? ... Hospitali gani? … Wodi namba ngapi? … Sawa, nitajitahidi nikipata muda.”







Simu ikakatwa, Bernadetha akasonya.







“Hivi hawa wananitakia nini? Wamemuua mume wangu na bado wananifuatilia tu! Si wakae na hiyo misiba yao na maajali yao. Na bado, Mungu atawataabisha!”



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Wakati huo Miraji alikuwa ametega masikio kwenye mlango wake akisikiliza yote yanayoendelea.





Giza liliingia. Vibao vya kukataza wageni kutembelea wagonjwa vilianikwa. Watu walipungua kwenye korido za hospitali, walioonekana walikuwa ni eidha madaktari au manesi, ama watu maalumu wa kulala na wagonjwa.







Taa ziliwashwa kila eneo na kufanya hospitali ing’are na kupendeza machoni. Kadiri giza lilivyozidi kukua na muda kusogea, ukimya ulitawala. Lakini muda mwingine ulivunjwa na makelele ya magari ya wagonjwa na wakati mwingine watu waliokuwa wanawaingiza wagonjwa wapya hospitalini.







Muda huo ulikuwa ni muafaka kwa walinzi kuanza kuzunguka zunguka kutizama usalama. Mikononi mwao walibebelea kurunzi na virungu, hawakuwa na silaha moto, labda kwasababu hakukuwa na cha kuiba hospitalini.







Chumba alicholazwa Filbert kilikuwa kwenye ghorofa ya tano. Kulikuwa kimya. Alikuwa yupo peke yake chumba kizima.







Chumba kilikuwa kikubwa mno, kitanda kimoja tu kikiwa kimetawala. Kabati kubwa la nguo lilikaa mashariki yake. Sinki la kunawia mikono upande wa kusini likiwa linashea ukuta na maliwato. Madirisha yalikuwa makubwa na wazi yakipitisha hewa ya baridi iliyokuwa inapuliza muda huo.







Bwana Filbert alikuwa amelala, miguu na mikono yake ilikuwa imefungwa P.O.P kwa ajili ya viungo vilivyovunjika. Kichwa chake kilikuwa ndani ya plasta kubwa rangi ya maziwa. Ni macho pekee yalikuwa wazi na sehemu ndogo ya mdomo kwa ajili ya kula na kupumua.







Pembeni yake kulikuwa na meza ya wastani, juu yake ikikaa redio ndogo ikiruruma kwa sauti ya chini. Pembeni kidogo kulikuwa na ukuta uliobebelea saa kubwa iliyosema ni saa nane ya usiku kasoro dakika tano tu.







Dakika tano hizo zilipohitimu, saa ilitoa mlio mdogo ti! ti! Ghafula umeme ukakatika hospitali nzima. Sauti za walinzi wakishangazwa na hiyo hali ikamshitua bwana Filbert aliyekuwako usingizini. Kulikuwa ni kiza totoro asione hata chochote.







“Nesi! Nesi!” Filbert aliita kwa woga. Mdomo wake haukuweza kufunguka kwa upana kwa sababu ya bandeji. Lipsi na ulimi tu ndivyo vilisogea taya zikiwa palepale. Hakuna sauti yote iliyomjibu zaidi ya mwangwi tena kwa mbali.







Sauti pekee iliyokuja masikioni mwake muda mfupi ikawa ni ya vyombo kabatini kang! – kang! Akashituka kwa kuhema.







“Nani?”

Hakuna majibu. Zaidi mlio wa vyombo ulijirudia kwa mara ya pili. Filbert akatambua kuna tatizo. Ingawa alikodoa macho yake ashuhudie, hakuona chochote.







“Mr Filbert Waziri. Mimi ni mgeni wako usiku wa leo.” Sauti nzito iliita isijulikane imetokea upande upi na imetemwa na nani.

Moyo wa Filbert ukaanza mbio.

“Mgeni?” Filbert aliuliza kwa shida akijitahidi hata akae kitako.

“Ndio. Unataka kuniona?” Sauti iliuliza na kuongezea: “Nilidhani utaogopa ndio maana nikaja kizani.”







Kabla Filbert hajajibu, umeme ulirudi chumba kizima kikawa cheupe mithili ya jua la saa nane. Macho ya Filbert yakaona mtu mrefu mweusi akiwa kavalia joho jeupe akimpa mgongo. Mtu huyo alipogeuka kikaonekana kichwa cheusi. Macho mekundu na mdomo mpana uliotoa tabasamu kubwa likionyesha meno chonge.







Filbert akapiga kelele. Pap! Umeme ukakatika.







Kufumba na kufumbua kitanda cha Filbert kilianza kusonga kuelekea dirishani. Kilipofika, dirisha likafunguka na kuwa wazi. Kitanda kikaanza kunyanyuka kama vile kinataka kumwagia Filbert nje.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Filbert alipiga makelele huku akiomba msamaha. Mlango wa chumba chake ulifunguka, daktari na nesi wakaingia kwa pupa. Hapo hapo umeme nao ukarudi.







Mtu mweusi hakuonekana. Alibaki Filbert pekee akilia.







“Mr Filbert what happened?” Daktari mwenye asili ya kihindi aliuliza na lafudhi yake ya lugha mama huku akisaidiana na nesi kurudisha kitanda sehemu stahili.







Filbert hakusema kitu, zaidi aliendelea kulia tu kama mtoto. Alipotizama dirishani alimuona yule mtu mweusi akitabasamu. Kwa woga alioneshea uso na macho yake huko dirishani huku akitikisa kichwa kumuoneshea daktari lakini daktari na nesi walipotizama hawakuona kitu. Mtu mweusi alipotea.







“Come down mr Filbert. Come down!” Daktari alihasa. Nesi alimtizama bwana Filbert na macho yenye weledi wa mashaka. Alitengenezea vizuri mkono wa mgonjwa, akagundua unavuja damu.

“Doctor, he is bleeding!”

Daktari akautizama mguu kwa macho makini. P.O.P ilikuwa inaloana damu taratibu bwana Filbert akitetemeka na kukunja sura kimaumivu.

“We have to check him in, go bring some tools.” Dokta alitoa amri, nesi akaitikia na kutoka chumbani.

Filbert alimtizama daktari akamuoneshea simu yake iliyokuwa mezani kwa ishara ya macho. Daktari akampatia Filbert simu, Filbert akaipokea kwa mkono uliokuwa na unafuu, wa kushoto. Alitafuta jina la Mtemvu, akapiga.







“Hali si nzuri, brother, kile kiumbe cha ajabu kimenitokea muda si mrefu alikuwa anataka kunimwagia nje! … Mmefikia wapi kuhusu ule mpango wa mtaalamu? ... Kesho? ... Fanyeni hivyo ndugu zangu … Hamna shida mimi nitaongeza ulinzi kwenye chumba changu, ila kuweni makini sana.”

Akakata simu na kumtizama daktari aliyekuwa bado anaupekua mkono wake wa kuume, ni wazi daktari alikuwa hana cha kufanya zaidi ya kusubiria nyenzo alizomtuma nesi.

“Daktari, kuanzia kesho nitalala na mtu humu ndani. Nipo mpweke sana na nahisi sipo salama.”







Daktari akamtizama Mtemvu kwa macho ya maulizo. Hakuelewa kitu – hajui Kiswahili. Mtemvu alisahau kabisa kuhusu hilo jambo. Alipomuona daktari anatoa macho akakumbuka ikambidi amtafsirie kwa kiingereza. Daktari akaafiki hilo ombi.







Mlango wa chumba ulifunguliwa nesi akaingia na kisahani cha bati kilichobebelea nyenzo kadhaa.







“Here they are, doctor.” Nesi alisema huku akitua sahani juu ya meza. Daktari akatikisa kichwa akimuuliza Filbert:

“Are you ready?”







“Kwa Raheem?”

“Yap!”

“Enhe, nini ulipata huko?”







Sauti ya Jombi na Miraji zilisikika zikitokea ndani ya Toyota Altezza.







“Kuna vitu tulivirekodi. Nyuma ya nyumba yake kuna bomba kubwa la kutolea uchafu, ni sehemu nzuri ya kuingilia.” Miraji alieleza.

“Kingine? Kuna taa ngapi?”

“Taa kubwa zilizo juu ya ukuta zipo nane, nyuma nne, mbele nne. Zingine ni za nyumba ambazo ni za kawaida tu.”

“Kwahiyo utapitia kwenye bomba alafu?”

“Nitaelekea kujibanza kwenye zizi. Lipo kwa mbele kidogo.”

“Na mbwa?”

“Nitabeba sumu.”

“Mlinzi?”

“Nitafuata kibanda chake taratibu na kumpulizia dawa ya usingizi.”

“Vizuri. Hakikisha hufanyi makosa. Kaweke kila kitu tayari, mida ya saa mbili usiku nitakupitia.

“Poa, baadaye mwana.”







Mlango wa gari ulifunguliwa Miraji akatoka na kwenda nyumbani akitembea haraka.







Jombi alimsindikiza Miraji kwa macho mpaka anazama ndani kisha akatoa simu yake mfukoni akampigia mwanaume aliyemtunza kwa jina fupi – ‘Mkuu’:

“Tayari kila kitu, kuanzia kesho anaanza kufanya mauaji ya hao watu wetu.” Jombi alisema kwa kujiamini akipandisha vioo vya gari.







“Hakikisha hajui wala kuhisi chochote juu yako.” Sauti toka simuni ilinena. “Malengo yetu yawe yake pasipo yeye kujua lolote lile.”

“Halina shaka hilo, mkuu.” Jombi aliteta. “Nitahakikisha chuki yake inakuwa upofu wake. Ila vipi je kama hatutofanikisha kama vile tulivyopanga?”

“Kwanini msifanikishe? … Dark man yupo na atafanya yale ambayo yapo nje ya uwezo wenu. Nadhani unajua kazi yake si kuwaua hao walengwa, bali ameagizwa kuwakosesha raha na hizo pesa walizozipata.”

“Ndio.”

“Kwahiyo ufanye kazi.”







Simu ikakata. Jombi akawasha gari na kutimka.







Miraji akiwa tayari amehakikisha usalama kwa kufunga mlango, madirisha na mapazia yake, alipaki vitu kwenye begi lake dogo jeusi; mkasi, kamba ndefu yenye kishikizi cha chuma, kinyago, spray, kisu na bunduki ndogo.







Alifungua droo ya kitanda akatoa picha ya baba yake akaitizama na kuibusu kwenye paji la uso kabla hajafungua mdomo wake;

“I miss you, Dad.” Alisema kwa kunong’oneza.







Machozi yalijaa machoni. Aliyafuta na kiganja chake akaiweka picha pia kwenye mkoba wake na kuufunga. Alijilaza juu ya kitanda usingizi ukampitia.







Hakulala kwa muda mrefu, Bernadetha akaingia ndani ya nyumba akitokea mihangaikoni. Usipite pia muda mwingi mtoto wake wa mwisho, Marietta, naye akarudi akiwa amevalia sare za shule.







Uso wake haukuwa na furaha. Hakutoa tabasamu analolitoa pindi aingiapo nyumbani, Bernadetha aligundua hilo haraka.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





“Shikamoo, mama.”

“Marhaba, hujambo mwanangu?”

“Sijambo.”

“Mbona umenuna baby wangu? Njaa?”

“Hamna.”

“Nini shida, mama?”

“Shule.”

“Kuna nini?”

“Siipendi hii shule, mama.” Marietta alilia. “Nataka nirudi shule yangu.” Alisema huku akipiga miguu yake chini.

“Vumilia mwanangu.” Bernadetha alimshika mwanaye mkono. “Utazoea, ni ugeni tu. Tafuta marafiki uwe unacheza nao.”







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog