Search This Blog

Friday 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (2) - 4

 






Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (2)

Sehemu Ya Nne (4)





Alisema kisha akashika njia ya korido, lakini mara akarudi mapokezi.

“Sorry, madam. May I have your phone number if you don’t mind?”







Mdada wa mapokezi alitabasamu na kumwangalia mwenzake kwa macho yenye jazba la furaha, alichana karatasi haraka toka kwenye counter book lililokuwepo mezani akaandika namba yake na kumkabidhi Kaguta.









“Here it is.”







Kaguta alitabasamu ishara ya shukrani alafu akaondokaze.









“Sasa wewe Rhoda, umechana kitabu cha wageni jinsi ulivyokuwa huna akili!”

“Aaah bwana! Ulitaka nilaze damu tena. Watu tunatafuta fursa.”

“Nani kakuambia huyo mkaka anakutaka?”

“Hujaona alivyokuwa ananitizama? … hehehe! Kalaghabao dada. Nitaenda zangu America we uendelee kusugua gaga manzese.” Alijinadi mdada wa mapokezi, ama Rhoda. “Na hapa akitoka tu huko namwambia anibip. Yani nishajiona Amerika mie. Mungu mkubwa jamani!”

Mwenzake na Rhoda alibinua mdomo akaendelea na kazi yake ya kupanga panga mafaili.









----





Ngo! Ngo! ngo!

“Welcome!”





Mlango ulifunguliwa na Kaguta akaingia.







“Habari yako?” Kaguta alisalimu.

“Njema tu, naweza kukusaidia?”

“Unaweza haswaa kunisaidia.” Alisema Kaguta huku akiketi kwenye kiti. Mkurugenzi aliacha shughuli zake akamtizama. Kaguta alitoa kitambulisho chake akamuonyesha mkurugenzi. Mkurugenzi alitizama kitambulisho na macho yake ndani ya miwani kisha akatabasamu.

“Nikusaidie nini, afande?”







Kaguta alibinua mdomo, akanyanyua briefcase yake na kuiweka mezani. Alipofungua alitoa faili moja rangi ya kahawia likiwa limeandikwa na wino mweupe, ‘SENSITIVE CASE’. Alilifungua na kulipitia kwa haraka haraka kisha akamuuliza mkurugenzi:









“Mzee, bila ya kupoteza muda. Una kesi ya kujibu.”







Mkurugenzi alitambaa na uso wa shaka. Aliubandua mgongo wake kitini akauliza:

“Kesi gani afande?”

Kaguta alitoa miwani yake akaiweka mezani.

“Tangu mwaka jana. Tangu lini mkurugenzi?”

“Mwaka jana.”

“Haswaa. Tangu mwaka jana hii hospitali chini ya uangalizi wangu. Umeona hapo?” Kaguta alionyesha mojawapo ya picha ya jengo la hospitali likiwa kwenye ukarabati wa wodi ya wanawake.

“Ndio, nimeona afande.”

“Sawia. Nimekuwa nikitembelea hii hospitali mara kwa mara na ungependa kuniuliza kwasababu gani, sio?”

“Ndio, afande. Kwasababu gani?”

“Ni kwasababu ya ukuaji wa urasimu hasa kwenye hizi hospitali binafsi. Unamjua huyu?”







Kaguta alionyeshea picha ya Bernadetha kwa kufungua upande wa pili wa faili. Mkurugenzi akaguguma na kifuache.









“Ndio, namjua. Ni mfanyakazi wa hapa.”









Kaguta alifunga faili kisha akamtizama mkurugenzi machoni kwa dakika bila ya kusema jambo.









“Kwani kuna nini, afande?”









Kaguta hakusema kitu, aliendelea kumtizama mkurugenzi na macho sh’takizi kwa dakika moja nyingine. Hatimaye mkurugenzi akapakua mdomowe:

“Afande, sijamaanisha. Nilikuwa namtania tu nipime msimamo wake.”

“Eti enh? … Ulijua haitojulikana, sio?”

“Hapana, afande. Nani kakuambia? Yeye au?”

“Camera yangu niliyoipachika kwenye korido na pia ofisini kwako, haisemi hivyo, mkurugenzi.”

“Umeweka lini camera ofisini kwangu?”

“Rudi kwenye mada, mkurugenzi. Hiyo ni kazi yangu.”







Mkurugenzi alishusha pumzi ndefu akatizama meza yake. Ni kama vile hakuwa na la kunena. Alifungua droo yake akatoa bahasha ya kaki na kuiweka mezani kisha akaitelezesha kumfuata Kaguta.









“Chukua hiyo basi, afande. Yaishe.”









Kaguta alivuta ile bahasha karibuye akatoa marker pen na kuiandika kwa juu, ‘USHAHIDI WA HONGO’. Macho yakamtoka mkurugenzi.

“Una kesi mbili sasa za kujibu, mkurugenzi.”







Mkurugenzi alitota jasho. Akabanwa na kigugumizi.







Ilikuwa ni mida ya saa moja ya usiku. Sandra akiwa katika kimini cha pink na top nyeusi, alikuwa akibofya simu yake huku akielekea upande ilipo nyumba yake. Kabla hajafikia mlango, alisikia honi nyuma ikiita. Akageuka.







“Shit! Isaac.”









Sandra alilaani huku akitengua lips zake. Kama mtu aliyelazimishwa akatembea kufuata gari lililopiga honi. Lilikuwa ni gari aina ya VX nyeusi. Vioo vilishushwa na aliyekuwemo ndani alikuwa ni Isaac na mzungu mmoja anayerandana ukaribu na mtu mwenye ulemavu wa ngozi, albino.







“Panda basi nikutoe!” Isaac alisema kwa majivuno.

“Hapana, Isaac. Kwa sasa siwezi, nimechoka.” Alijitetea Sandra.

“Aaah mrembo! Sasa leo mie nitakuwa na nani? … twende enh, kesho hautoenda job.”

“Hapana, Isaac. In fact, sijiskii vyema pia. Nahisi tumbo na kichwa vyaniuma.”

“Ok … ok. Basi kapumzike, nitakucheki morning, sawa?”







Gari liliondoka, Sandra akalisindikiza kwa sonyo kisha hatua kuelekea nyumbani. Aliingia ndani ya nyumba ila punde tu akabanwa na tapishi, alikimbilia bafuni akatapika. Alirudi chumbani akiwa ameshika kiuno na akitembea kiuchovu. Alijitupa kunako kitanda akaweka kiganja chake juu ya paji la uso.









“Mungu wangu, Sandra. Nini hiki?”









Baada ya dakika moja ya tafakuri, Sandra alinyanyuka akaenda nje famasi. Alinunua kifaa fulani alichoweka ndani ya kamfuko keusi kisha akarudi nyumbani kwake. Alikifunua hicho kifaa na kukitizama. Kilikuwa ni cha kupimia mimba. Sandra alishusha pumzi ndefu akatikisa kichwa chake kama mtu asikitikaye. Ghafla akiwa hapo, mlango ulifunguliwa akaingia Roby.









“Surpriseee baby!”









Roby alipiga kelele. Haraka Sandra alipeleka mkono wake nyuma ila kasi ikadondosha kifaa chake chini.











“Nini hiyo, Sandra?”







Sandra aliinama haraka akaokota kifaache, Roby akampokonya na kumtizama.







“Sandra, hiki si cha kupimia mimba? Una mimba, Sandra?”









Sandra alitoa chozi badala ya kujibu. Roby alinyanyua mkono wake wa kuume akamzaba Sandra kofi shavu la kushoto. Sandra akadondokea kitandani.







“Malaya mkubwa wewe! Mbwa! … Umemuuzia nani huo uchi wako?” Roby alitema cheche. Sandra hakujibu, alilia tu. Roby alivuta mkanda kiunoni mwake akautengenezea vizuri mkononi.

“Nimekuuliza umelala na nani? Nani kakupa mimba?”









Sandra aliendelea kulia. Roby akamcharaza mikanda minne ya nguvu na kufoka:









“Sijawahi kufanya mapenzi na wewe bila kinga hata siku moja. Unaenda kupima mimba umelala na nani?”

“Na Isaac! Nimelala na Isaac!” Sandra alilia. Mwili wake ulikuwa na mistarii mine mekundu ikiwa imekatiza mgongoni na mkono wake wa kushoto. Roby alimezwa na butwaa. Macho yalimtoka na pia mdomo ukaachama. Mkanda ulimponyoka ukadondoka chini pasipo kuonyesha kama anajua huo muamala.

“Unasemaje, Sandra?”

“Nililala na Isaac. Bosi wako.”

“You are lying!”

“Kweli! Ni kweli, Roby. Sikuweza kumkataa Isaac. Unajua ana nguvu gani.”









Roby aling’ata meno. Aliinama akateka mkanda wake na kutoka ndani ya nyumba ya Sandra kwa pupa. Sandra alibakia akiwa analia huku akitizama mistari aliyopachikwa na mkanda.











Macho yake yalimimina machozi na mdomo wake ulipokea mapokeo ya kwikwi za kilio. Alishika nywele zake kwanguvu akazifumua fumua. Aligara gara huku na kule kitanda kizima hata shuka na bedcover zikachomoka. Ilimchukua masaa mawili kutulizana na kupitiwa na usingizi.







Ikiwa ni asubuhi ya saa mbili watu walikuwa wamejazana kwenye kijiwe cha magazeti kilichokuwa kimejiweka pembezoni mwa barabara kuu ya lami. Walikuwa wanateta juu ya vichwa vya habari pasipo kuonekana hata mmoja akiwa amebebelea gazeti mkononi.







Kundi hilo lililokuwa na watu wanne liliongezeka baada ya Kaguta kusogea na kurusha macho yake kwenye vichwa vya habari, gazeti moja likakamata macho yake.







‘SIMANZI: KIJANA MMOJA AUWAWA KINYAMA KWA RISASI KUMI’









Kichwa cha habari kilijieleza kikiambatana na picha ya kijana huyo ambaye alikuwa amechafuka damu. Kaguta alitoa shilingi elfu moja mfukoni mwake akampatia muuzaji na kumnyooshea kidole gazeti atakalo, muuzaji akampatia.











Kaguta akalisogeza gazeti machoni na kuanza kuitizama ile picha ya muhusika aliyeuwawa kwa risasi kumi. Mara mmoja wa wale waliokuwa wanajadili vichwa vya habari akaanza kuhororoja:









“Unamtizama huyo jamaa? … Unaweza ukamuona huruma ila mshenzi kama nini!”

Mara mwenzake akauliza:

“Nani huyo?”

“Si Roby!” Jamaa akajibu. Basi majadiliano yote yakahamia kwenye lile gazeti alilonunua Kaguta.

“Muuaji kauwawa hatimaye. Ila nani atakuwa kamuua?”

“Watakuwa wameuana wenyewe hao. Si unajua hawa madili yao ya madawa?”

“Kweli, hata mimi nahisi hivyo. Unakumbuka siku ile huyu jamaa alipita na gari kwa kasi tulipokuwaga kule magomeni?”

“Alikuwa anaendesha Prado?”

“Ndio, nyeusi hivi.”

“Eeeh … nakumbuka!”

“Sasa pale si alikuwa anaenda kwa yule Niga c. He! Baadae nakuja kusikia Niga c kauwawa na risasi mwanangu!”

“Walimuua yule!”

“Ndio mana yake, cha kushangaza hata mshkaji hakufuatiliwa wala nini!”









Kaguta alifunga gazeti lake akaondoka lile eneo. Alielekea hospitalini kwenda kumjulia hali Vitalis, alipomkuta mlengwa wake kalala alifungua gazeti lake akawa anasoma habari ya Roby. Alizama gazetini mpaka pale alipokuja kushtuliwa na Bernadetha.











“Umekuja saa ngapi?”

“Muda si mrefu sana. Vipi unaendeleaje?”

“Safi tu. Mbona hujamuamsha Vitalis?”

“Sijataka kumsumbua, mwache tu apumzike.”

“Hapana. Anatakiwa aamke anywe chai saa hivi.”

“Iko wapi?”

“Namletea hivi punde.”











Bernadetha alimuamsha Vitalis akaketi kitako. Baada ya kujuliana hali, Kaguta alimuonyesha Vitalis gazeti aliloninunua, Vitalis akapitia yaliyomo, alipomaliza Bernadetha naye akalichukua na kulisoma.











“Nani atakuwa kamuua?” Vitalis alimuuliza Kaguta kwa mshangao.

“Watakuwa ni wakina Isaac Makongo.” Kaguta alijibu.

“Umejuaje?”

“Hujaona pale kwenye gazeti?”

“Sijaona sehemu iliyosema kauwawa na wakina Isaac.”

“Kauwawa maeneo Oysterbay na huo mtaa naujua. Pembezoni mwake mbele kidogo kuna nyumba kubwa ina namba 898.”

“Ila Isaac anaishi Kurasini.”

“Basi jua kati ya yule muhindi ama yule mzungu, Ford, atakuwa anahusika na kifo hiko.”

“Ila kwanini wamuue?”

“Hapo ndipo kuna la kutafuta. Inabidi tufanye utafiti.”

“Tufanye? … mmh mmh hapana! Sijihusishi tena na mambo ya hao watu. I am done, Kaguta.”

“You are done kivipi, Vitalis?”

“Sitaki tena kujihusisha na mambo yoyote ya upelelezi. Sasa hivi mimi ni mwananchi wa kawaida, acha iwe hivyo tu. Kama Mungu akinijalia nikatoka hapa, basi nitaenda kufanya biashara zangu basi.”









Kaguta alimtizama Bernadetha, Bernadetha akapandisha mabega. Kaguta alishusha pumzi ndefu kisha akanyanyuka.











“Nitakuja baadae mida ya jioni. Ila Vitalis, fikiria maamuzi yako mara mbili.”









Kaguta akatoka. Bernadetha akamtizama Vitalis na kutabasamu.











“Mbona unatabasamu?”

“Nimefurahi.”

“Umefurahishwa na nini?”

“Kujua kuanzia sasa utakuwa salama.”







Vitalis alitabasamu akaunyanyua mkono wa Bernadetha na kuuweka kifuani kwake.





****





Gari la Kaguta lilipaki pembezoni mwa baa iliyobebelea jina la Karunde. Ni mida ya saa mbili ya usiku. Kaguta alishuka akiwa kavalia suruali nyeusi ya kadeti, shati jeupe la kubana na koti single button rangi nyekundu aliyoifananisha na viatu vyake vya kuchomeka.









Alinyookea glocery akaagiza kinywaji, alibebelea glasi akapeleka mdomoni na kuria mafundo mawilikabla hajatoa simu yake mfukoni na kutuma ujumbe kwa Sandra.









‘Nipo hapa bar karibu na kwako njoo basi’









Alimaliza kinywaji chake lakini bado Sandra hakutokea. Alinyanyuka akalipa akatoka nje ya bar mpaka kwenye gari lake, akarusha macho yake barabarani pasipo kuomuona mtu. Alianza kutembea taratibu taratibu mpaka nyumbani kwa Sandra.











Aligonga mlango lakini hakuruhusiwa aingie ndani. Aligonga na kugonga lakini hakukuwa na majibu yoyote. Alizunguka nyuma ya nyumba akachungulia kupitia dirishani, akaona miguu ya Sandra ikiwa imelala chini. Alijitahidi auone mwili mzima lakini haikuwezekana, pazia la dirisha lilimkinga.









Haraka Kaguta alirudi mlangoni, alichomoa earphone ya simu mfukoni akaing’ata na kutengeneza waya mnene kiasi alioupenyeza kwenye kitasa akadondosha ufunguo uliokuwemo humo. Akautoa waya na kuupindisha alama ya saba, akaungiza ndani ya tundu ya kitasa na kuuchezesha, mara ikasikika sauti ‘tas!’ mlango ukafunguka.













Kaguta aliingia ndani akamkuta Sandra uchi wa mnyama, pembezoni mwake kulikuwa na pakti ya madawa ya vidonge, mashavu yake yalikuwa na alama nyekundu za vidole, uso umevimba na kuvijilia damu na mdomo wake ulikuwa una mabaki ya mapovu.











Kaguta alikimbilia kabatini akatoa gauni. Alimvika Sandra kisha akambeba na kumkimbizia garini kwake haraka. Aliondoa gari mpaka hospitalini ndani ya dakika mbili tu, alishuka akambeba Sandra na kumuingiza ndani. Alitolewa nje ya chumba cha wagonjwa akaambiwa angoje majibu nje.











Aliketi kwenye mabenchi, akawa amefungamana mikono yake na kuiweka mbele ya mdomo wake. Alikaa hapo kwa muda, hakuna dokta aliyekuja kumpa majibu. Mwishowe alilala kabisa. Alikuja kuamshwa na daktari usiku ukiwa mzito.









“Mgonjwa wako amekunywa madawa: alikuwa anafanya jaribio la kujiua. Na inaelekea alipta kipigo kabla hajachukua maamuzi hayo.”

“Anaendeleaje kwa sasa?”

“Anaendelea vizuri. Tumempa huduma ya kwanza tu. Tunaomba uende kituo cha polisi ukaripoti, hatuwezi mtibia bila hivyo.”









Kaguta alitoa kitambulisho chake cha kazi akamuonyesha daktari. Daktari akasema:

“Okay. Ameomba aonane na wewe.”









Daktari aliposema tu hivyo, Kaguta alianza kutembea. Daktari alimshika mkono akamwambia:











“Fanya haraka. Inabidi apumzike.”









Kaguta alitikisa kichwa akaendelea na safari yake. Alipoingia chumba cha Sandra alikutana macho kwa macho na mwanamke huyo. Sandra akaanza kulia. Kaguta alimsogelea akambembeleza anyamaze.











“Niambie nani kakufanyia hivi?”









Sandra akiwa amekabwa na kilio alisema:











“Isaac … Isaac Makongo. Amemuua Roby, amenipiga na kusema hatambui ujauzito nilio nao. Hataki kuniona tena! Sikudhani kama angekuja kunifanyia unyama kiasi hiki!”









Baada ya hayo maneno, Sandra aliangua kilio kama aliyefiwa. Kaguta alitikisa kichwa chake akamvuta Sandra na kumkumbata. Ila punde, Sandra alizirai. Kaguta alikimbia kwenda kumtafuta dokta akaja naye upesi, daktari alimtoa Kaguta nje afanye kazi yake, baada ya muda daktari alitoka chumbani akampasha Kaguta habari.











“Amezirai tu. Nadhani sasa ni muda wa kumuacha apumzike.”











Kaguta alitoka hospitali akaeleka bar. Alinunua chupa moja kubwa ya konyagi akaiweka mezani taratibu akawa anamiminia kooni kwake kwa pozi. Kabla ya chupa kufika nusu, Bhoke alisogea eneo alilopo Kaguta. Alitabasamu kisha akapaza sauti yake laini:









“Mambo handsome!”











Kaguta alimtizama Bhoke kisha akapandisha nyusi zake.









“Poa, karibu.”











Bhoke alivuta kiti akaketi.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Niambie, handsome. Kitambo sijakuona.”









Kaguta alitabasamu tabasamu lililo kinyume na macho yake. Alikunywa fundo moja kisha akajibu:

“Mbona nipo tu. Mambo yamebana.”

“Nimekumisi sana. Nichukue kinywaji.”

“Chukua.”









Bhoke aligeuza shingo yake akatazama kaunta.









“We Mishiii naomba castle nyongaa!”











Haraka mhudumu alikuja na sahani inayobebelea castle, akaiweka mezani na kuifungua. Bhoke akaidaka castle akaipeleka mdomoni na kunywa mafundo manne kama vile maji.











“Sasa, leo twaenda wote ama?”

“Hapana!”

“Kwanini? … Umepata mwanamke mwingine baba?”

“Hapana. Nimechoka tu.”









Baada ya kusema hivyo, Kaguta alisimama akamiminia kinywaji chake mdomoni kama vile si konyagi bali juisi au energy drink, alafu akaaga:











“Sasa mi naenda. Tutaonana.” Alisema huku akitoa pesa kwenye pochi yake na kuilaza mezani. Bhoke akabaki akimtizama Kaguta kama mtu anayeshuhudia mtu akimla simba.









Kaguta akautoa mwili wake pale bar na kufuata gari lake, wakati yu njiani kwenye lami mara simu yake ikapokea ujumbe. Mkono moja ulibeba simu na kuipeleka usoni wakati mwingine ukiwa umeshikilia usukani, akausoma ujumbe:









“Hi Peltridge! ts me Rhoda from hospital.”









Kaguta alisonya akaitupia simu yake kwenye kiti cha kando.





Ilikuwa ni jioni, si tu saa ilisema hivyo bali hata nguvu ya jua ilikuwa imepungua na giza lilianza kusogelea uso wa ulimwengu. Mataa ya hospitali yalikuwa yameanza kuwashwa sehemu mbalimbali wakati huo Bernadetha alikuwa nje akimfanyisha mazoezi Vitalis wakitembea toka eneo moja kwenda lingine,Bernadetha alikuwa amemshikilia mkono Vitalis aliyekuwa anachechemea akitembea.









“Sasa hivi angalau sasa, napata moyo.”

“Kwanini?”

“Unajitahidi kutembea. Mara ya kwanza nilikuwa nahofia kweli, nikadhani unakuwa kilema sasa.”

“Kwahiyo tusema Mungu yu pamoja nami, sio?”

“Kabisa.”

“Nashukuru sana. Ila najisikia vibaya kwa kilichotokea leo.”

“Nini?”

“Marietta kuja na kunikuta nimelala. Kwanini hukuniamsha?”

“Sikutaka kukusumbua. Atakuja hata siku nyingine, usihofu.”

“Sijamuona kitambo. Umenikatili, mama.”

“Usifadhaike bwana, atakuja. By the way, umeona zawadi aliyokuletea?”

“Hapana.”

“Nimeiweka kwenye droo. Tukirudi nitakuonyesha.”

“Aisee! Sikupata hata muda wa kumshukuru.”









Vitalis alilalama. Wakati wanaongea, Bernadetha alijisahau akamuachia Vitalis mkono.











“Zawadi yenyewe pipi!”

“Ndio hiyo hiyo! Kwani nilikuwa nayo?”











Mara Vitalis akagonga jiwe na mguu wake wa kulia, alikosa balansi akataka kudondoka, upesi Bernadetha alimdaka na kumvuta kwanguvu akamkumbatia wakawa wanatizamana uso kwa uso, macho kwa macho. Kwa sekunde tano hakuna aliyesema kitu, macho yaliteta. Walikuja kurudishwa fahamuni kwa sauti ya mtu asafishaye koo. Walipokengeuka kutizama wakamuona Miraji.









“Umejuaje tupo huku?”

“Nimeelekezwa na wafanyakazi wenzako mpo mazoezini.”

“Karibu.”

“Ahsante! Sh’kamoo.”

“Marhaba!” Bernadetha na Vitalis waliitikia.

“Nimekuja kumjulia hali mgonjwa, naona anaendelea vyema sasa.”

“Mungu anasaidia. Naendelea vizuri sana tu.” Vitalis alijibu. Walitafuta eneo moja tulivu wakaketi na kuanza kuteta wakiwa wanapata vinywaji vilaini.

“Umesikia habari za mauaji ya yule mtu maeneo ya Oysterbay?” Miraji aliuliza.

“Ndio, nimesikia. Niliona kwenye gazeti.” Vitalis alijibu.

“Yani haijapita hata muda, wameuwawa wengine watatu kama huyo wa Oysterbay.”

“Wapi?”

“Inasemekana maeneo ya Bunju, nyumba namba mia tatu na mbili hivi kama sikosei. Wameshindiliwa risasi za kutosha. Na mashuhuda wanasema waliwaona watu watatu wameingia katika hiyo nyumba wakiwa wamevalia suti kabla ya mauaji hayo kutokea.”

“Umesema Bunju?”

“Ndio!”

“Nyumba namba mia tatu na mbili?”

“Yap! Kama kumbukumbu zangu ziko sawa.”











Vitalis akatulia kwa muda kidogo akiwaza. Picha ya nyumba aliyoingia Bakari kipindi kile wakiwa wanamfuatilia yeye na Kaguta, ilikuja kichwani. Ndio, ilikuwa ni nyumba namba mia tatu na mbili maeneo ya Bunju. Sasa nani kauliwa? Bakari? Vitalis alijiuliza nafsini, mara akakurupushwa na Miraji.













“Vipi? Kuna shida?”

“Hapana! Hamna shida.”

Vitalis alikurupuka. Alipitisha kiganja chake usoni akashusha pumzi ndefu.

“Embu tuachane na hizo habari. Tuongelee mengine.”







Vitalis aliomba.







****







Siku mbili zilipita. Ikiwa ni wasaa wa saa nane ya mchana ikishuhudiwa na jua lililosimama utosini, alikuja mgeni maeneo ya nyumba ya Vitalis. Aligonga hodi mara tatu, sauti toka ndani ikaitikia. Mlango ulipofunguliwa mgeni akaingia.









“Hah! Bakari!”











Jombi alipaza sauti akishangaa. Bakari aliingia ndani akauliza:

“Inspekta Vitalis yupo wapi?”

“Yupo hospitali.”

“Kaguta je?”

“Naye hayupo!”

“Tafadhali, naomba unisaidie. Nina shida nao kubwa sana.”

“Shida gani?”

“Tafadhali naomba unisaidie kuwapata.”

“Ok, karibu, ingia ndani.”









Bakari aliingia akaketi kwenye kochi. Alisalimiana na Miraji kisha akarudisha macho yake kwa Jombi.











“Tafadhali, nakuomba ufanye upesi.”







Jombi alitoa simu yake mfukoni akampigia Kaguta na kumtaka afike nyumbani kwa Vitalis haraka. Alipokata simu akamwambia Bakari.











“Kama dakika kumi na tano hivi, Kaguta atakuwepo hapa.”









Bakari akaridhika. Alilaza kichwa chake kwenye kochi, baada ya muda mfupi akapitiwa na usingizi. Miraji na Jombi wakamuacha apumzike, wao wakawa wanatizama runinga. Ila mara kwa mara Bakari alikuwa akishtuka toka usingizini pale sauti yoyote kubwa kiasi ya runinga ilipokuwa inamfikia.











Kila aliposhtuka alikuwa anakimbizia macho yake dirishani kuchungulia nje kisha anatulia na kulala tena. Hali hiyo ikawa inawatisha Jombi na Miraji. Baada ya muda wa dakika ishirini na tano, Kaguta aliwasili. Bakari aliamka akatoka na Kaguta nje.











“Bakari, umepajuaje hapa?”

“Tuachane na hayo, Kaguta. Nina shida.”

“Shida gani?”

“Wanataka kuniua! Naomba unisaidie.” Bakari alilia.

“Wakina nani wanataka kukuua?”

“Jeshi la Mr Kim. Wameshawaua wenzangu watatu. Wanan’tafuta na mimi waniue!”

“Kwanini wakuue?”

“Nimetoa siri yao kuhusu kisiwa cha Alwatan Kombo. Wanataka kutumaliza wote!”

“Usihofu, nitakusaida. Lakini, kwanini haukumwambia Jombi hizi habari, umeamua kunambia mie tu?”









Kabla Bakari hajajibu, alitizama kushoto na kulia kwake kwanza ndipo akasema:









“Najua Jombi ana tattoo. Ni hatari, kwani nikimuambia taarifa zitawafikia ninaowakimbia.”

“Umejuaje hizo habari za tattoo, Bakari? Umejuaje kama hao watu ni jeshi la Mr Kim?”

“Najua kwasababu namimi nilishawahi kuwepo huko. Nilishawahi kuwa mfuasi wa hilo genge. Nilishawahi kuwa na hiyo tattoo kabla sijaiondoa karibuni.”

“Kuiondoa?”

“Ndio!”

“Umeiondoaje? Pasi?”

“Hapana! Niliiondoa na chumvi.”

“Chumvi?”

“Ndio!”

“Chumvi?”

“Ndio! Mimi ni zaidi ya mnijuavyo, Kaguta.”

“Wow! Inaonekana.”

Kaguta alisema na kutabasamu.







Ikiwa ni saa tisa ya alasiri, Kaguta alikuwa yu njiani beneti na Bakari wakiwa wanaelekea hospitalini alipolazwa Sandra. Kaguta alikuwa kavalia koti la suti, jeans na moka nyeusi wakati Bakari alikuwa kavalia shati jeupe la Jombi na suruali ya kaki ya kadeti.









Walipoingia ndani ya geti Kaguta aliona gari moja jeusi aina ya range rover, alipolitizama vyema akaona ubavuni mwa gari limepachikwa stika ya tattoo, tattoo ya nyoka, nyoka aliyemuona kule kwenye kijumba cha Alwatan Kombo. Kaguta akamvuta Bakari na kulifuata lile gari. Aliuingiza mkono wake chini ya gari akasema:











“Bado lina joto, wamekuja muda si mrefu.”

“Wakina nani?”

“Bila shaka watakuwa jeshi la Kim.”

“My God! Wanafanya nini hapa?”

“Hiko ndicho nataka kujua.”











Kaguta alisema, alitoa peni mfukoni mwake akatobolea tairi moja la gari. Alimshika mkono Bakari wakaanza kutembea haraka kuelekea wodi ya Sandra. Wakiwa koridoni, Bakari aliona wanaume watatu waliovalia suti mbele yao hatua chache. Akamshtua Kaguta:











“Hao hapo mbele.”

“Umewajuaje?”

“Ndio hao. Wote hawana nywele na wanatembea pamoja. Ndio hao! Ndio hao!”

“Ssshh! ... Taratibu.”









Kaguta alitizama mikononi mwa wale wanaume watatu akaona wamefichilia bunduki. Alimtizama Bakari akamuambia:









“Tafuta batan ya hatari popote pale humu hospitalini, bonyeza. Hakikisha king’ora kinalia. Fanya haraka! Hatuna njia yoyote zaidi ya hiyo, hatuwezi kuanzisha vita hospitalini.”

“Sawa!”











Bakari aliachana na Kaguta akaenda kufanya alichoagizwa. Kaguta akabakia akitembea nyuma ya wale watu watatu ambao walikuwa wanaelekea wodi ya Sandra.











Dakika zikapita pasipo king’ora kulia na wale wanaume wakazidi kusogea zaidi na zaidi. Kaguta aliangalia huku na huko kwa hofu. Akaanza kujisemea:









“Bakari … Bakari … Bakari, please.”









Mara king’ora kikalia kwanguvu. Watu walipatwa na taharuki wakaanza kukimbia huku na huko, walinzi nao wakaanza kupandisha kwenye majengo kutizama usalama. Wanaume wale watatu ndani ya suti wakatizamana, walipeana ishara ya kichwa wakageuka na kuanza kurudi.











Hapo Kaguta akaona sura zao, loh! Walikuwa wamefanana kila kitu usoni.Walipopita, Kaguta alitoka alipokuwa amejificha akabaki anawatizama kwa kuduwaa.













Walinzi walipomfikia aliwaita akawaonyeshea kitambulisho chake cha kazi na kuwaelekeza wawakamate wale wanaume watatu mapacha wapo chini yalipopakiwa magari. Walinzi wakashuka upesi kwenda walipotumwa, bahati mbaya wakakuta wanaume wale wameshatoweka na gari lingine.











Bakari na Kaguta wakaendelea na safari yao kwenda chumba alicholazwa Sandra. Walimkuta wakamjulia hali yake, lakini pia wakampasha habari juu ya yaliyotokea. Bakari akasema:









“Ni kwasababu ya tattoo yako. Watakufuata popote utakapokuwa.”









Sandra akashangazwa na hizo habari.











“Umejuaje?” Alimuuliza Bakari.









Kaguta akatabasamu na kumjibu:









“Ni simulizi ndefu. Kwanza inabidi utoke hili eneo, si salama tena.”







Ilichukua siku tatu tokea Sandra alipofuatwa na wanaume mapacha watatu ndani ya suti. Siku ya nne Vitalis akiwa kwenye kitanda chake cha hospitali, wageni watano walikuja kumuona: Jombi, Miraji, Sandra, Kaguta na Bakari, pamoja nao alikuwepo pia Bernadetha, jumla wakawa sita. Baada ya kujuliana hali, Kaguta alichukua fursa kumwambia Vitalis kile kilichowaleta:











“Vitalis, hawa unaowaona hapa mbele yako kwa njia moja ama nyingine wameathirika na Mr Kim. Wamepoteza wazazi wao na hata watu wao wa karibu kwasababu ya huyo mshenzi. Wamenifuata na kunieleza adhma yao, nami nikaona ni busara kuja kukueleza, kwamba wanataka kushiriki kuhakikisha wanampoteza Mr Kim. Wanataka kusaidia pia kuwaokoa wengine wasije wakawa kama wao. Tafadhali wape nafasi.”









Vitalis kimya.









“Kumbuka Vitalis, familia yako ipo wapi sasa? Mkeo, watoto wako? Je ni wangapi huko wanaendelea kupoteza wapendwa wao? Kama tusipochukua hatua leo, kesho itakuaje? Vilio vingapi vitaendelea huko mtaani? Wangapi watapoteza ndoto zao?”







Vitalis kimya. Bakari alisonga mbele akampokea Kaguta:

“Najua hunifahamu vyema, Vitalis, ila natumai hiki nitakachokuambia kitakugusa kwa njia moja ama nyingine.”









Bakari aliweka kituo kisha akaendelea:









“Miaka mitano nyuma ya hapa nilikuwa mfanyakazi wa kampuni kubwa ya mawasiliano Afrika ya mashariki. Kazi yangu ilikuwa ipo chini ya kitengo cha taarifa na teknolojia. Kipindi hiko, si tu niliweza kumudu maisha yangu bali pia ya wazaziwangu waliokuwa wananitegemea.Lakini baadae mambo yalikuja kubadilika baada ya Mr Kim kumuua bosi wetu kwa kile kilichosemekana ni kugeukana kwenye biashara.











Baada ya hapo maisha yakawa magumu, alikuja bosi mwingine lakini alishindwa kumudu kampuni mwishowe kampuni ikapata hasara na kulazimu kupunguza wafanyakazi, mmojawao kati ya waliofukuzwa ni mimi. Sikuja kupata kazi tena baada ya hapo haikujalisha mara ngapi nilizunguka na vyeti. Wazazi wangu nao je?











Maisha yalikuwa magumu kupita kiasi, mwishowe mama yangu alijiingiza kwenye biashara ya kujiuza tupate kula. Bahati mbaya alikuja akaukwaa ukimwi na kumuambukiza na baba pia, wote wakafa. Kwakuwa sikuwa na mbele wala nyuma, ikabidi nijiunge kwenye kundi la Mr Kim baada ya kushawishiwa na mwenzangu niliyefukuzwa naye kazi. Nikajiingiza humo, tukawa tunatumwa kuua watu mbalimbali.











Ila ilifikia muda nikachoka kufanya mauaji, nilifuta tattoo mwilini wangu pasipo yeyote kujua. Yote nilifanya ili niachane na matendo yao, lakini kabla sijakamilisha misheni yangu ndipo nikafanya kosa la kuwavujishia siri ya Alwatan Kombo. Mpaka sasa ninapoongea na nyie wenzangu watatu wameshauwawa na mimi natafutwa kwa udi na uvumba niuwawe. Najua nitakufa, ila basi nife nikiwa napigania dhamira safi, hata mara moja.”









Bakari alimaliza kueleza simulizi yake akakaa kando. Wote wakaamtizama Vitalis kwa macho yanayongoja jibu.









“Sawa. Naombeni nipate wasaa wa kufikiri.” Vitalis alisema kwa upole. Wageni wakaaga akabakia Bernadetha peke yake. Vitalis akamuuliza Bernadetha:

“Wewe unasemaje? Maoni yako ni yapi?”







Bernadetha akabanwa na kigugumizi.







Ilipita wiki moja, Vitalis akaruhusiwa kurudi nyumbani. Baada tu ya siku moja kikao kiliitishwa kati ya Vitalis, Kaguta, Miraji, Jombi, Bernadetha, Sandra na Bakari. Katika kikao Vitalis akatoa jibu lake kwamba ameridhia kurudi katika uwanja wa mapambano. Ila akatoa usia:







“Itatakiwa tutumie njia za kisasa zaidi kwa sasa.”









Kutimiza hilo, siku iliyofuata vifaa vilinunuliwa; vinyago, gloves, darubini, nguo nyeusi, mikasi, visu, kamba, vinasa sauti, radio call, tracker, mabuti na hata ramani kubwa ya Tanzania. Pia vikainishwa vipaumbele vya mapambano:









Kwenda kisiwani kukata mzizi wa fitna





Kutafuta na kuwakamata maaskari wanaoshirikiana na kundi la Mr Kim.





Kutafuta mawakala wote wa Kim. Wakianza na Isaac Makongo.





Kuwabana mawakala waeleze Kim alipo.





Kuwatafuta wanaume mapacha watatu.





Kukamata simu na vifaa vyovyote vya mawasiliano vya maadui kwa ajili ya kuwapa taarifa wazitakazo. Mtendaji akiwa Bakari.





Kumaliza na kufunga kila jengo linalotoa mafunzo ya kumtumikia bwana Kim.





Baada ya hapo kundi likapewa jina la THE GUESTS, yani kumaanisha ‘wageni.’









*** NDANI YA MDOMO WA MAUTI ***





Ilichukua juma moja kufuzu mafunzo ya kufyatua na kulenga risasi kwa wasio weza, Sandra na Bernadetha. Baada ya hapo, ikachukua tena majuma mawili kuwekana sawa kwa mazoezi mbalimbali kama vile kukimbia, kuruka, na hata kubana pumzi ndani ya maji, Vitalis na Kaguta wakiongoza wenzao. Walipomaliza hapo, sasa ikachukua tena juma moja kuelekezana jinsi ya kutumia kisu kama dhana pekee iliyo mkononi.













Kurusha kisu kwenye miti, kukata na kufunga na kuchimba kwa kutumia kisu. Hapo sasa ikawa imechukua mwezi mmoja rasmi kumaliza hayo. Siku iliyofuata wakiwa ndani, Bakari aliwafungia vifaa vya umeme mwilini kwa ajili ya mawasiliano. Kila mtu aliwekewa track na kupewa kisafirisha sauti kwa ajili ya kuwasiliana na wenzake.













Walivaa nguo nyeusi za kubana miili, gloves mikononi, na kofia za kufunika vichwa vyao, miguu yao ikaezekwa na viatu vikubwa vilivyobanwa vyema na kamba. Mabegi yao madogo yakajazwa kamba, risasi, mikasi, darubini, na chakula kidogo kilichofungwa kwenye kikontena kidogo cha kubana. Mikanda yao ikabebelea vifuko vya visu vikubwa. Kisha wakajiweka kwenye gari la Kaguta na kuanza safari ya kuelekea bwagamoyo.











Bakari pekee ndiye alibaki, alikaa na tanakilishi yake akiitumikisha satelaiti impe madadavuo ya maeneo yote ambayo wenzake wanakatiza, na hata kuwaelekeza pale panapohitajika. Kisafirisha sauti chake kilikuwa mdomoni, na pembeni yake aliweka kikombe cha kahawa alichokuwa anakipeleka mdomoni mwake kumpasha joto na kumfanya mchangamfu.









Kwakuwa gar aliendesha Kaguta, ndani ya muda mfupi ‘wageni’ walikanyaga ufukwe wa bwagamoyo. Walikodi boti ikawapeleka kisiwani na kuondoka zake. Hakukuwa na maajabu ya boti kupotea wala kuondoka yenyewe, labda kwakuwa jitu halikuwa na taarifa. Kabla ya kuenenda ndani ya kisiwa, Vitalis aliwasogeza wenzake karibu wakapeana maneno mawili matatu.











“Tunaweza tukapoteana humo ndani, hakikisha unawasiliana na wenzako kadiri inavyowezekana. Sawa?”

“Sawa!”

“Na pale utakapopotea, wasiliana na Bakari. Sisi tunamsikia lakini yeye anatuona pia. I know we can make it. Hii ndiyo hatua yetu ya kwanza, hatutakiwi kuipoteza kwa gharama yoyote.”









Waliweka mikono yao katikati wakigusana viganja. Wote wakasema:









“Sisi ni wageni wasio na mualiko. Mwenyeji umejiandaa?”











Walipeana matabasamu wakaifuata njia nyembamba iingiayo ndani. Baada ya hatua kadhaa, upepo ulitokea kusipojulikana ukawazoa na kumsambaratisha kila mtu sehemu yake. Baada ya kudondokea sehemu mpya, Vitalis alituma sauti yake kuuliza hali ya kila mmoja, wote wakasema wako sawa.









“Hakikisha unashikilia bunduki yako vyema. Focus!” Vitalis alisema kwa kujiamini. Wote wakafuata maelekezo. Macho yalitoka na mkono ukashikilia dhana kwanguvu.









“Kila mtu aende upande wake wa kaskazini, mtakutana baada ya kilometa mbili.” Taarifa ilitoka kwa Bakari, wote wakaipata na kuanza kuifuata.









Sandra alikuwa wa kwanza kujaribiwa. Akiwa anatembea kwa umakini, masikio yake yalimpa taarifa kuna kitu kinasogea. Alituma kichwa chake kila upande lakini hakuona kitu zaidi tu ya miti, miongoni mwao ukiwa wa mchungwa.











Basi akaendelea kutembea mbele akielekea kaskazini, ila hakupita muda mrefu, akasikia tena sauti na alipogeuka kutizama hakuona kitu, ila kuna jambo aligundua, mti wa mchungwa ulikuwa umesogea, haukuwepo pale alipouona mara ya kwanza. Kama vile hakugundua hilo, Sandra akaendelea kujongea kwenda mbele.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





Punde sauti ya kitu kusogea iliita tena. Sandra aligeuka haraka kutizama na kuelekeza bunduki yake kwenye mti wa mchungwa, kabla hajafyatua risasi, mzizi wa mchungwa ulitambaa haraka ukakamata miguu ya Sandra na kuivuta, Sandra akadondoka, bunduki ikarukia kando. Mzizi ukaanza kumvuta Sandra karibu na mti. Sandra alitoa kisu haraka kiunoni mwake, akakata mzizi unaomvuta kisha akataarifu wenzake hali aliyopo.









“Hold on, nakuja muda si mrefu!” Sauti ya Kaguta ilimwambia Sandra.











Mzizi mwingine ulikuja haraka ukamchapa kibao Sandra na kumchana shavu. Ulimshika mkono wenye kisu ukaugongesha kwenye mti, Sandra akaachia kisu. Mzizi mwingine ukaja haraka ukakamata mguu wa Sandra na kuanza kumvuta tena kusogelea mti, wakati Sandra anavutwa alinyoosha mkono atwae bunduki yake iliyokuwa chini hatua kadhaa, mzizi mwingine ukasukumiza bunduki mbali.











Sandra akasogezwa karibu na mti, mizizi mingine ikachipuka na kumviringita kisha ikamnyanyua juu na kumtupia kwenye mti mwingine, Sandra akafikia mgongo na kudondoka kama mzigo. Alitoa sauti kali ya maumivu huku akiukunja mgongo wake.













“Nakuja Sandra, nipo karibu!” Sauti ya Kaguta ilisikika masikioni mwa Sandra.

“Kaguta fanya haraka!” Sauti ya Vitalis nayo ikasikika.

“Umekaribia kumfikia. Kimbilia upande huo huo.” Bakari naye alisikika akitoa maelezo.











Wakati Sandra akiwa anaugulia mgongo chini ya mti alikotupiwa, mzizi wa mchungwa ulikuja kwa kasi kama mkuki ukifuata kichwa chake, alikwepa mzizi ukachoma mti. Alitaka kunyanyuka, mzizi mwingine ukakamata mguu wake na kumdondosha kisha ukaanza kumburuza tena kufuata mti.









Wakati anasogezwa Sandra alipitishwa juu ya kisu chake, alikichukua kwa siri akaficha mkono nyuma, mzizi ulipomsogeza karibu na mti kama awali mizizi mingine ikaamka na kuanza kumpanda Sandra kuanzia miguuni huku ikimbinya kwanguvu. Ilipofika kiunoni, Sandra alipiga kelele kali ya maumivu, kabla ya mizizi kummalizia kumfunga tumboni na kifuani ilimsogeza karibu zaidi, Sandra akaona macho ya mti huo.













Yalikuwa makubwa na ya kijani mfumo wake ukiwa wa kenge.Hapo hapo Sandra akatoa kisu chake na kukikita kwenye macho hayo kwanguvu. Maji ya kijani yakaruka kama mafataki. Mti ukalalamika kwa kuyumba yumba huku na huko. Mizizi ikafunguka na kumuacha Sandra akadondoka chini, Sandra akiwa amebung’aa hapo, mti wa mchungwa ulidondoka na kumfunika. Alijitahidi achomoke lakini haikuwezekana, alibanwa.











Aliishia kupiga makelele ya kuomba msaada. Bahati njema Kaguta akawasili. Alimvuta akamchoropoa toka chini ya mti.

“Upo sawa?”

“Yah! Nipo okei.”

Kaguta aliutizama mti wa mchungwa kisha akamtizama Sandra.

“Upo vizuri, mama.”

“Ahsante.”











Sandra alichomoa kisu chake akakirejesha kiuoni. Mara sauti ya kelele ikawafikia masikioni kupitia earphone zao. Ilikuwa ni sauti ya Miraji ikiomba msaada. Ikafuatiwa na sauti ya Bakari.











“Miraji amebebwa. Anapelekwa upande wenu wa magharibi kwenu Bernadetha, Vitalis na Jombi, na kwa Kaguta na Sandra ni upande wa kaskazini magharibi. Fanyeni haraka!”











Haraka wote wakaanza kukimbia kuelekea kule walipoelekezwa.











Miraji alikuwa hewani akiwa amebebwa na ndege wa ajabu, alikuwa ni mweusi ti mwenye mdomo mrefu kama chuchunge. Mabawa yake yalikuwa mapana na yenye nguvu ingali macho yake ni mekundu yenye muundowa paka. Miraji hakuweza kufurukuta kwa ndege huyo aliyekuwa kamkamata mkono wake wa kuume na kucha zake zikiwa zimemtoboa.













Alijaribu kuutuma mkono wake wa kushoto kwenda kwenye mfuko wa suruali uliokaa upande wa kulia ili atoe kisu, lakini akashindwa. Upepo ulikuwa mkali na alihisi kupata maumivu zaidi. Hakukata tamaa, alijaribu tena akafanikiwa.











Alikata mguu wa ndege, ndege akamuachia akadondoka chini. Alifikia ubavu akalalamika kwa maumivu makali begani na kiunoni. Alitizama juu kumtizama ndege, ajabu akaona ndege watatu wakiwa wamefanana kama yule aliyembeba. Na mara wale ndege wakaanza kushuka kwa kasi wakimfuata Miraji. Miraji alinyanyuka akaanza kukimbia. Aliweka mkono wake sikioni akamuuliza Bakari:











“Nipo wapi?”

“Unaelekea kusini.” Bakari alijibu. “Nenda upande wako wa mashariki, wenzako wapo upande huo!”











Miraji aligeuza akaanza kuelekea upande wake wa mashariki. Hakufika mbali ndege mmoja alimsukuma na miguu akadondoka chini. Miraji kunyanyuka akakuta kazungukwa na ndege watatu.











Alivua begi lake akataka kuingiza mkono, ndege mmoja akatuma bawa lake likamzaba Miraji na kusogeza begi kando, kisha akamrukia Miraji na kumdonyoa shingoni kwanguvu huku miguu yake ikiwa juu ya kifua cha Miraji. Miraji alifurukuta kumtoa ndege juu yake lakini haikuwa rahisi kwani ndege aliweza kujibalansi na mbawa zake huku akimdonyoa maeneo mbalimbali.













Ilimchukua muda Miraji kuweka kisu chake vizuri mkononi na kukisokomeza kifuani mwa ndege aliyekuwa anamshambulia. Ndege akapiga kelele kali za kulalamikia maumivu aliyoyapata, Miraji akanyanyua mguu wake na kumsukumizia pembeni kisha akanyanyuka na kuanza kukimbia mbio za sakafuni ambazo hazimkufikisha mbali. Ndege wawili waliobakia walimuangusha chini, mmoja akakanyaga mikono ya Miraji na mwingine miguu, Miraji akabakia pasipo ujanja.











Ndege mmoja alipiga kelele za nguvu kwenye uso wa Miraji. Mate yalimtoka na kuingia mdomoni mwa Miraji aliyekuwa ameachama kwa mduwazo. Japokuwa Miraji alitema, lakini alikuwa kachelewa. Ndege alinyanyua shingo yake kwanguvu ammalize mhanga wake, ila mara sauti ya mlio wa bunduki ikavuma, kufumba na kufumbua ndege wote wakamdondokea Miraji wakiwa wafu.





“Upo sawa?” Sauti ya Vitalis ilimuuliza Miraji aliyekuwa kabakizwa uso tu, mwili mzima ukiwa umefunikwa.

“Watoe hawa wadudu juu yangu!” Miraji aliropoka. Vitalis alitabasamu akamsaidia kuwaondoa ndege. Miraji alinyanyuka akamshukuru. Hawakukaa hapo muda, taarifa ikaingia toka Bakari:

“Bernadetha yupo matatizoni, Vitalis na Jombi rudini mashariki yenu mpo karibu naye!”

Vitalis alimtizama Miraji akamwambia;

“Acha niende!”

“Twende wote!” Miraji aliroroja.

“Hapana, umejeruhiwa. Niruhusu niende haraka. Utakuja nyuma yangu.”









Baada ya kusema tu hayo, Vitalis alifunguka haraka kurudi mashariki yake. Alikimbia kwa nguvu zake zote, mikono na miguu yake vikipishana kama treni ya umeme.











Baada tu ya punde alikuwa kamuacha Miraji mbali mno. Ila mara akasikia sauti ya Jombi, ikabidi asimame na kutizama pande zote kuona yupo wapi atoaye sauti. Punde akamuona Jombi anatokeza upande wake wa kushoto akikimbia kama mwehu.







“Kimbia, Vitalis. Kimbia!”









Kabla Vitalis hajachukua hatua yoyote, aliona mbwa mwitu wakubwa weusi wakimfuata Jombi kwa kasi. Vitalis aliwapiga risasi mbwa mwitu wawili na kuwaua akachelewa kumlenga mwingine ambaye alimrukia na kumdondosha chini, akamng’ata mkono wake wa kushoto.









Vitalis alimpiga ngumi mbwa mwitu kwa kutumia mkono wake wa kulia kisha akaishika shingo ya mbwa huyo na kujinyanyua akakaa juu ya mgongo wa mnyama huyo. Aliweka bunduki yake kiunoni. Alichomoa kisu chake akamchanja mbwa mwitu, mbwa mwitu akaanza kukimbia.











Vitalis akakamata masikio ya mbwa huyo na kuyatumia kama usukani akimuelekeza mbwa kuelekea upande wa mashariki. Mithili ya farasi, Vitalis alimtumia mbwa mwitu. Baada ya muda mfupi Vitalis akafika eneo alilopo Bernadetha, alichomoa kisu akamchoma mbwa mwitu mgongoni kisha akajirusha kando.











Mbwa mwitu alidondoka akafa. Vitalis akakimbia kumfuata Bernadetha aliyekuwa anakimbizwa na jitu lililofanania na mti mkavu. Lilikuwa na matawi na hata majani.









“Wewee!” Vitalis alipaza sauti. Mti ukageuka na kumtizama.

“Unanikumbuka? … Nimekuja tena. Unakumbuka nilichokufanya?”









Mti uligeuka ukaanza kumfuata Vitalis.











“Yeah! … Njoo kama una jiamini mti usio chimbwa dawa wewe!”









Mara mti ukaanza kukimbia. Vitalis aligeuka naye akaanza kukimbia.









“Bakari, nielekee wapi?” Vitalis aliuliza.

“Endelea kwenda mashariki yako, utakutana na Kaguta na Sandra.” Sauti ya Bakari ilijibu. Vitalis akaelekea upande huo.

“Kaguta!”

“Yeah!”

“Nakujaa na mti mkavu upande wako. Andaa moto, haraka!”

“Nitapatia wapi moto sasa?”

“Utajua. Andaa moto haraka!”







Kaguta alimtizama Sandra akamuuliza;







“Tunafanyaje sasa? Vitalis anakuja!”







Sandra alitizama kushoto na kulia kwake, akaanza kukusanya miti na majani makavu.







“Tunapata wapi moto sasa?” Kaguta alimuuliza Sandra. Sandra akamuonyeshea Kaguta saa yake ya mkononi.

“Tutatumia saa yako. Si ina lenzi?”









Kaguta aliitizama saa yake akajibu;









“Nadhani.”

“Chuchumaa, kioo cha saa yako kielekezee juani na kwenye majani haya makavu. Haraka!”









Kaguta alifanya kama alivyoelekezwa, mara moshi ukaanza kutoka baada ya dakika. Kabla moto haujakoza, Vitalis akatokeza.









“Tayari?”

“Bado kidogo!”

“Fanyeni haraka!”









Vitalis alisema huku akiendelea kukimbia kuwapita wenzake, nyuma yake mti ukiendelea kumfukuza. Baada ya muda akarudi tena.









“Kaguta, tayarii?!”

“Ndio!”

“Tumia kamba. Upesi!”









Kaguta alitoa kamba akafunga kitanzi kisha akairusha kwa mtu mti na kuanza kumvutia kwenye moto ambao ulikuwa umekoza sasa. Sandra naye alishika kamba akawa anamsaidia Kaguta, Vitalis naye akawaunga mkono wakamvuta mtu mti mpaka kwenye moto. Mti ukashika moto, ila nayo kamba ikakatika. Mtu mti ukaanza kukimbia hovyo hovyo ukielekea kaskazini.









“Kaskazini kuna kitu gani, Bakari?”









Vitalis aliuliza.









“Kuna mto!” Sauti ya Bakari ilijibu. Vitalis akawatizama Kaguta na Sandra akawaambia;

“Anaelekea mtoni kuzima moto. Inabidi tumzuie!”









Haraka wakaanza kukimbia kumfuata mtu mti. Vitalis alitoa kamba yake akatengeneza kitanzi. Aliirusha kwa mtu mti ikamkamata wakaanza kuivuta kwanguvu. Baada ya muda kidogo kamba ikakatika tena, mtu mti akaendelea kukimbia, ila hali yake ikiwa mbaya, matawi yalipukutika na moto ulizidi kumtafuna.











Mpaka anafika mtoni alikuwa tayari ameishakwisha. Vitalis alishusha pumzi akashika kiuno. Waliwasiliana na wenzao, wote wakakutana kwenye kingo ya mto kasoro Jombi.









“Upo wapi, Jombi?” Kaguta aliuliza kwenye kisafirisha sauti.







Kimya.







“Bakari, Jombi yupo wapi?”

“Yupo upande wenu wa magharibi.” Sauti ya Bakari ilijibu. Wote wakaanza kuelekea upande huo. Wakamkuta Jombi amelala chini hoi, pumzi tu ikionyesha yu hai.

“Jombi, kuna nini?” Kaguta aliuliza. Jombi akajibu;

“Saa … Saa imeanza kutoa majaribu yake.”

“Imetoa muda gani?”

“Dakika kumi kumi. Tayari jaribio la kwanza limeshapita, nimepambana nalo.”









Kaguta alitizama saa yake akaona haisemi majira. Vitalis alitizama na ya kwake pia, akaona haisemi majira sahihi.









“Inabidi tumtafute huyo mtu anayetoa hayo majaribu.” Vitalis aliwaambia wenzake.

“Tutampatia wapi?” Kaguta aliuliza.

“Lazima tu kuwe na njia.” Vitalis alijibu, “Tuifuatishe hii barabara.”









Kabla hawajachukua hatua, jaribio lengine la saa lilitokea. Upande wao wa kushoto walitokea watu wanane mbilikimo, nyuso zao zilikuwa zimepambwa na michoro ya ajabu, walikuwa wamevaa sketi za makuti, miongoni mwao wawili tu ndio walikuwa wameshikilia panga kila mkono.











“Nini hiki?” Sandra aliuliza. Bernadetha akaachama mdomo kwa mshangao.









Mara wale mbilikimo wakajitenga katika mafungu ya watu wanne wanne, wakabebana mabegani na kutengeneza watu wawili warefu, wale mbilikimo wenye mapanga wakawa ndio wapo juu. Vitalis na Miraji wakachukua kundi moja la mbilikimo, Kaguta na Jombi wakachukua kundi lililobakia.









Vitalis alirusha ngumi, mbilikimo wa kati akainama na kumfanya wa juu akwepe kisha panga likarushwa na kukata shati la Vitalis. Vitalis alipotizama pembeni yake akaona Kaguta na Jombi wamerushwa chini.









“Wow! Kumbe its serious.” Alisema Vitalis.









Miraji alirusha teke kumpiga mbilikimo wa juu, wa katikati akamrusha juu mwenzake, teke likapita, aliporejea mwenzake akamdaka mikono na kumrusha kwa Miraji, Miraji akasombwa na teke akarushwa huko. Vitalis akamnyanyua na kumnong’oneza;









“Focus na wa katikati, mimi nitadeal na wa chini. Wa juu hana kitu.”









Miraji aliitikia, wakaanza upya mchezo wakilenga mashambulizi kwa mtu wa chini na katikati, mbilikimo wa juu akawa mzigo kwa wenzake. Ndani ya muda mfupi wakawamaliza. Kaguta na Jombi wakatumia risasi kuwamaliza wa kwao baada ya kushindwa kuwamudu.













“Sasa tunafanyeje?” Miraji aliuliza.

“Unadhani tutafanikiwa?” Bernadetha naye akauliza.









Vitalis alitizama saa yake ya mkononi akaona mshale wa dakika unasogea tokea ilipokuwa namba tatu kwenda namba nne.Alimfuata Jombi akamuuliza;

“Jaribio la kwanza lilitokea upande gani?”









Jombi akanyooshea kaskazini. Vitalis akatabasamu.









“Yes! Sasa nimeelewa. Wakati unapata jaribu la kwanza mshale wa dakika ulikuwa juu, ndio maana jaribu likatokea kaskazini. Mshale ulipofika mashariki, yaani namba tatu, jaribu likatokea upande huo.”









“Kwahiyo?” Kaguta aliulza.







“Kwahiyo haya majaribu yanarandana na muelekeo wa mshale wa dakika. Sasa hivi jaribu linalokuja litatoka mashariki kusini kwakuwa dakika kumi zingine mshale wa dakika utakuwa kwenye namba tano. Kwahiyo ili tupate chanzo chake lazima tujue dakika zinaanzia wapi na kukomea wapi.”









“Kwenye kumi na mbili!” Sandra alilonga.







“Yap! Kwahiyo tuelekee kaskazini yetu haraka kabla mshale haujafika kwenye tano.” Vitalis alitema maneno. Upesi wakaanza kukimbia kwenda upande wa kaskazini. Ikiwa imebakia sekunde kadhaa mshale wa dakika ufike kwenye tano, wakawa wamefika sehemu moja walipokuta jicho kubwa la kijani. Vitalis akatabasamu na kusema;











“Here we are! Hapa ndipo majaribu yanapotokea. Hili ndilo jicho linaloona kila pande kwa ajili ya jitu jeusi.”









Walishindilia risasi kwenye hilo jicho likapasuka na kutoa ute wa kijani. Walikumbatiana na kupongezana. Hatimaye wakawa wametoka kwenye mdomo wa mauti.





*** HUNA HAKI YA UHAI ***





Glasi za vinywaji ziligongeshwa … Klang! Klang! … Zikafuatiwa na kelele sasa za binadamu zikishangilia … Hureeeee! Hawakuwa wengine bali wahusika wa kundi la WAGENI. Nyuso zao zilijaa tabasamu. Baada ya kunywa vinywaji, waliketi chini wakamuacha Vitalis pekee akiwa amesimama.

“Ni jambo la kufurahia kufanikiwa kwa hatua yetu ya kwanza tangu tukutane na kuunda familia hii. Nadhani wote hapa mnaamini msemo wa nyota njema huonekana asubuhi, hatua yetu hii ya kwanza ni nyota njema na tunaamini tutamaliza kama tulivyoanza.” Vitalis aliweka kituo, wenzake wakapiga makofi kisha akaendelea;

“Sasa ni wakati wa kujipanga kukabili hatua yetu ya pili. Kazi iliyo mbele yetu ni kuhakikisha tunasafisha uchafu wote uliopo kwenye jeshi la polisi. Sisi wote hapa ni mashahidi kwamba kwa njia moja ama nyingine ujihusanishaji wa polisi na kundi hili haramu la bwana Kim inawia vigumu mapambano ya kufuta uhalifu huu juu ya uso wa dunia. Kwahiyo basi, nguvu ile ile tuliyoiweka kwenye pambano letu la kwanza tutaihamishia huku. Tutatumia nguvu na akili zetu zote kunyofoa mizizi mirefu ya uhalifu huu bila kujali utatugharimu nini. Hatuna cha kupoteza zaidi ya hofu zetu. Sisi ni wageni wasio na mualiko, mgeni njoo mwenyeji apone kwetu hilo ni mwiko.”

Makofi yalipigwa tena baada ya Vitalis Byabata kumaliza kunena. Wote waliweka ngumi zao hewani wakasema kwa pamoja:

“Hakuna wa kutuzuia!”

Wakagongesha tena glasi zao kisha wakazipeleka mdomoni.

Masaa matatu baada ya tafrija hiyo fupi, Bakari alikuwa yupo kwenye kiti cha kazi mbele yake ikiwa imeketi tanakilishi mpakato. Pembeni ya tanakilishi hiyo kulikuwapo na karatasi nyeupe ikiwa imeandikwa namba ya simu na maneno yasomekayo ‘OCD’. Bakari aliiweka hiyo namba ya simu kwenye tanakilishi yake ndani ya kichumba kidogo cha bluu kilichotokea kwenye skirini, alafu akabonyeza kitufe kikubwa kilichoandikwa ‘enter’. Mara ramani ya Dar es Salaam ikaja na kuonyesha kidoti chekundu eneo fulani mtumiaji wa namba hiyo anapopatikana. Bakari akatabasamu,punde tu Vitalis akatokea chumbani akaungana na Bakari.

“Umeipata?”

“Ndio, nimekwishaipata. Eneo alilopo ni hilo hapo kwenye ramani.”

“Vyema. Sasa mtumie ujumbe wake aupate.”

“Sawa, mkuu.”

Ndani ya muda mfupi simu ya OCD iliwaka taa na kutoa sauti ndogo … Ting! Ting! OCD alifungua simu yake akakuta ujumbe: “Maisha yako yatapotea muda si mrefu endapo hautotubu maovu yako unayoyafanya na Bwana Kim.”

OCD akashtuka kwa kuachama mdomowe. Alitoa macho akatizama kando yake kama vile kuna mtu ilhali yupo chumbani. Ujumbe haukuonyesha umetoka namba gani, OCD alikosa cha kufanya zaidi ya kutupa simu yake pembeni na uso wake kuunda ndita.

“Mshenzi gani huyu ananifuatilia?” OCD alijiuliza, alitabasamu kisha akabinua lips za mdomo wake.

“Amekosa watu wa kuwatishia. Kama ni kifo anatafuta atakipata.”

Usiku ukaenda.

Kesho yake nyumba ya OCD ikawa imezungukwa na walinzi kumi. Wote walikuwa wamebebelea bunduki mikononi mwao huku wakiwa wanatizama huku na kule kuhakikisha usalama. Kuanzia getini mpaka ndani ya uzio ulinzi ulikuwa kabambe.Umbali wa kilomita moja toka nyumba hiyo ya OCD ilipo, lilisimama gari la Kaguta. Ndani yake walikuwepo Jombi na Miraji wakiwa wamevalia ovaroli la bluu likiwa na chapa ya DAWASCO vifuani mwao.Walishuka garini wakavisha vichwa vyao kofia. Walitoa jembe, shoka na chepe kwenye gari kisha wakasogea hatua kama saba, wakatizamana.

“Itakuwa ni hapa.” Jombi alisema huku akionyeshea kidole chini. Miraji akatikisa kichwa kukubali. Eneo walilokuwepo lilikuwa na ubichi kidogo tofauti na sehemu zingine za kando. Waliinamisha migongo yao wakaanza kuchimba lile eneo kwanguvu wakitumia jembe na chepe. Baada ya dakika chache wakakutana na mabomba matatu chini. Jombi akakata mabomba hayo kwa jembe mara moja, maji yakaanza kumwagika. Walirudishia kifusi walichokiweka pembeni wakapanda gari na kuondoka.

Baada ya muda mfupi.

“Haloo! … Eeeh nyie Dawasco, mbona mmenikatia maji?” OCD alifoka. “Nipe niongee na meneja wenu … Hayupo? … Anakuja saa ngapi? … Mje haraka iwezekanavyo! … Natumai mtakuwepo hapa ndani ya muda mfupi!”

OCD alisonya baada ya kukata simu. Kitu ambacho hakujua ni kwamba alikuwa anaongea na Bakari ambaye pembeni yake alikuwa ameketi na Vitalis. Vitalis alimgusa begani Bakari, Bakari akampigia simu Jombi.

“Nendeni sasa.”

Taratibu Jombi na Miraji wakiwa wamebebelea mfuko wao wa vifaa wakaanza kusogelea jengo la OCD. Walifika getini wakaonyesha vitambulisho vyao vya DAWASCO, walinzi wakapiga simu ndani na kuuliza kuhusu huo ugeni, wakaambiwa wawaruhusu. Miraji na Jombi wakaingia ndani walipokutana na OCD.

“Nini shida?” OCD aliuliza.

“Itakuwa humu ndani kwako.” Miraji akajibu, “Bomba la kuleta maji lipo salama tokea huko tulipotoka, na majirani zako wanapata maji kama kawaida.”

“Embu tengenezeni basi haraka.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sawa. Usihofu mheshimiwa.”

Miraji alitangulia mbele akielekea jikoni lakini Jombi alisita kumfuata hivyo wakampa fursa OCD kuwa wa pili kwenye msafara na kutimiza adhma yao ya kumuweka polisi huyo katikati. Baada ya hatua kadhaa wakiwa koridoni, Jombi alimkaba na kumziba mdomo OCD, Miraji akageuka na kutizama uso wa OCD uliokuwa umekunjamana ukisikilizia maumivu ya kubanwa kwa mishipa ya shingo;

“Mkuu, huwezi ukakimbia wala kujificha. Tubu maovu yako unayofanya na bwana Kim mbele ya kadamnasi. La sivyo pumzi yako itaacha mwili muda si mrefu. Huu ni ujumbe wako wa mwisho.”

Baada ya kusema hivyo, Jombi alipiga shingo ya OCD, OCD akadondoka na kuzirai. Jombi na Miraji wakapachika kamera kwenye nyumba ya OCD kila kona, walipomaliza wakaondoka wakipita kwenye msitu wa walinzi ambao walikuja kufahamu kilichoendelea dakika kumi baada ya wahusika kupotea.



Saa tano na robo usiku.

Vitalis alikuwa juu ya kitanda akiwa amefunga macho kama mtu aliyelala. Alikuwa amevaa kaptula fupi huku kifua chake kikiwa wazi. Ni kama vile kuna kitu kilikuwa kinamsumbua kwani alikuwa akijigeuzia huku na huko huku akiwa amekunja sura yake. Baada ya muda mfupi akiwa anajibiduabidua Vitalis alianza kutota mno. Jasho lilimvuja na kulowanisha kitanda. Kama hilo halitoshi alianza kugugumia lakini ajabu sauti aliyokuwa anaitoa haikuwa iliyozoeleka, bali ya kunguruma kama simba. Jeraha lake la meno ya mbwa mwitu mkononi nalo lilianza kuvuja likitoa ute mzito wa maji maji, na wakati yote hayo yanafanyika macho ya Vitalis yalikuwa yamefumba.

Zilichukua dakika tano zoezi likiwa ni hilo hilo lajirudia. Vitalis alikuja shtuka akawa anahema kwanguvu. Alitizama viganja vyake na miguu, mishipa ilikuwa imedinda. Alijishika shingo kama vile anaugulia. Alinyoosha viungo vya mwili huku akiwa amekunja sura. Akajiuliza,

“Nini kimetokea?” huku akitizama vinyweleo vyake vilivyokuwa vimesimama dede.



Saa moja na nusu asubuhi.



Bakari alikuwa anapiga mswaki huku akiwa anatizama tanakilishi yake iliyokuwa inamuonyesha ndani ya nyumba ya OCD. Baada ya punde alimuona OCD akiwa anamkaribisha mtu ndani kwake. Bakari alivuta karibu picha ya kamera, akamuona bwana Isaac Makongo akiingia ndani na kuketi kwenye kochi akifuatiwa na OCD aliyeketi kando naye. Hapo Bakari akaamua kufuta picha za kamera zingine kwenye kioo cha tanakilishi yake na kukuza picha ya kamera moja tu ambayo ilikuwa karibu na wahusika wake. Alipofanya hivyo, alitoa mswaki mdomoni mwake akapaza sauti kumuita Vitalis, Vitalis akaja punde.

“Rekodi, haraka!” Vitalis alimuagiza Bakari, haraka zoezi hilo likaruhusiwa kisha wote macho yao yakawa yanatizama.

“Naomba mnipatie ulinzi ndugu zanguni nipo hatarini.” Sauti ya OCD ilivuma ikimuambia Isaac.

“Usihofu, tupo na wewe mwanzo mpaka mwisho. Fadhila zako kwetu si za kusahaulika. Umetusaidia sana kukamata hii nchi na tunakuahidi kukulinda.”

“Ahsante sana, Isaac. Ila unadhani ni nani aliye nyuma ya mpango huu wa kuniua?”

“OCD, Mr Kim ni mtu mkubwa sana ulimwengu mzima. Ni mtu mwenye mafanikio na kama unavyojua biashara zake, hawezi akakosa maadui. Maadui hao ndio wanaokutafuta kwakuwa wanajua mchango wako kwa bwana Kim. Ila ondoa hofu ushanipa taarifa.”

“Sawa. Nakuamini.”

“Mengineyo?”

“Hakuna lingine, mkuu. Labda tu niliulizie fungu langu, umepita mwezi sasa.”

“Lingine?”

“Hakuna.”

“Ok. Pesa yako itakuja kesho, kuna kijana wangu atakuletea ofisini kwako. Ila kumbuka kuna mzigo unakuja ukitokea Brazil, hakikisha unapita airport pasipo na shaka. Ni mzigo wa milioni mia tano, unga wa high class.”

“Niachie hiyo kazi, mkuu. Unajua huwa sikuangushi.”

Baada ya maongezi hayo walinyanyuka wakapeana mkono kisha wakatoka ndani. Bakari alimtizama Vitalis wote wakajikuta wanatabasamu.

Siku iliyofuata saa kumi na moja na dakika tano jioni, mlango wa OCD uligongwa. OCD alpofungua alimkuta mlinzi wake akiwa amebebelea kasha la CD. Mlinzi akamkabidhi kasha hilo na kumuambia:

“Kuna mtu amepitisha nje, amesema ni mzigo wako.”

“Nani?” OCD aliuliza.

“Simjui.” Mlinzi akajibu.

“Unaruhusuje mtu usiyemjua akupe kitu na ulete kwangu? Kama bomu je?”

“Hapana, mkuu. Nimekikagua nikaona ni CD tu.”

OCD alichukua ule mzigo akauweka ndani ya DVD player alafuakaketi pembeni ya runinga yake. Baada ya CD kucheza machozi yalianza kumtoka OCD. Aliona kila kitu ambacho alikifanya na kuongea na Isaac. Picha ya CD ilipokwisha, maandishi yalijionyesha yakisomeka: TUBU MAOVU YAKO KABLA HATUJASAMBAZA KANDA HII KWENYE VITUO VYA HABARI.

Uso wa OCD ukabadilika ghafla na kuwa mweusi zaidi. Alidondosha runinga yake akaipasua. Akatafuta kamera zote zilizopachikwa ndani kwake akazitoa na kuzipasua. Ujumbe ukaingia kwenye simu yake;

“It is too late.”

Nayo simu akairushia ukutani na kuipasua. Akapiga yowe kali la hasira. Jasho la hamaki na woga likamtoka. Machozi yakazidi kumbubujika, mwishowe akakaa kwenye kiti na kushika tama uso wake ukiwa na mikanganyiko ya hofu na hasira. Hakika ndege alikuwa tunduni sasa. Tena tundu bovu.

Baada ya masaa kumi na mbili, chaneli za runinga zikaanza kurusha matangazo ya moja kwa moja. Kanda ya OCD ilisambazwa kwenye kila kituo cha chaneli za runinga. Kwenye kila kioo cha runinga picha ya OCD na Isaac Makongo ikatapakaa, wananchi wakaona kwa macho yao. Haikuchukua muda mrefu, magari ya polisi yakaongozana kwenda kwa OCD. Walikuta mwili tu, OCD akiwa tayari ameshajimaliza kwa kunywa madawa. Ni msiba ndio ukafuata baada ya hapo, watu wengi wakahudhuria ikiwemo waliokuwa wafanyakazi wenzake na OCD, lakini wengiwao walikuwa wananchi wa kawaida ambao waliguswa na taarifa za OCD na eidha walitaka kumuona mtu huyo kwa sura kabla hajamezwa na udongo wa dunia.

Vitalis Byabata alikuwa ni miongoni mwa wahudhuriaji wa msiba. Alikuwa amevaa nguo nyeusi na miwani yenye vioo vya kahawia. Kidogo alikaa mbali na wenzake, alikuwa ametulia tuli akitikisa kichwa chake. Kulikuwa na makelele mengi watu wakiruruma huku na kule, ila kuna sauti fulani iliteka masikio Vitalis.

“Hili jambo linatutisha sasa, nani atakayefuata baada ya mkuu wetu? … Inabidi sasa tujitizame vizuri ndugu yangu bila hivyo tutakwisha.”

Vitalis akageuza shingo yake kutafuta makazi ya hiyo sauti. Kwa mbali toka kwake akaona watu wawili wananong’onezana. Kabla ya kujiuliza kwanini wale watu wanaongelea yale mambo, Vitalis alishangaa amesikiaje sauti toka mbali vile, tena ya watu wanaonong’onezana? Haikuwa kawaida. Badala ya kushughulikia wale watu Vitalis akaanza kukumbuka usiku ule aliokuwa anahangaika kitandani, je una mahusiano na yale mabadiliko yake? Mwishowe akaamua kupuuzia na kuweka akili yake kwa wale watu wawili ambao muda mfupi baada ya kuaga mwili wa marehemu waliagana na kuondoka. Mmoja wao aliyekuwa mfupi, jina Morgan, akiwa amevalia shati jeusi na suruali ya jeans alifuata gari lake Harrier akaingia ndani. Kabla hajaipa moto gari, alikabwakwanguvu na mtu tokea viti vya nyuma. Akaulizwa;

“Wewe ni nani? Na OCD na Bwana Kim ni nani zako?”

Morgan akaleta ngumu kusema kitu. Alikabwa kwanguvu zaidi, akaamua kusema;

“Naitwa Morgan, ofisa wa polisi.”

“OCD na Kim ni nani zako?”

“Mabosi wangu … Ni mabosi wangu.”

“Sawa sawa. Sasa basi, tunakupa nafasi ya kutubu ili uwe hai. La sivyo uhai wako utakuwa haki yetu.”

Baada ya hicho kitisho, mkabaji alishuka gari likaondoka. Kumbe alikuwa ni Vitalis Byabata, alitoa simu yake mfukoni akampigia Bakari.

“Nimepachika kifaa kwenye mojawapo ya gari, unaweza ukakiona hapo kwenye mashine yako? … Hakikisha unaifuatilia hiyo gari, naamini baada ya kumtishia atafanya move itakayotusaidia kuwapata wote.”

Simu ikarudishwa mfukoni. Kaguta akaondoka kurudi nyumbani, alimkuta Bernadetha akiwa chumbani pamoja na Kaguta. Walikuwa wamevaa gloves nyeupe. Juu ya meza kulikuwapo na sindano nyingi, madawa yaliyokuwa yamepondwa na kabeseni ka maji. Kaguta alikuwa anatwanga madawa, wakati Bernadetha akichukua madawa na kuyaweka kwenye maji kisha anayafyonza na sindano na kuziweka pembeni. Vitalis akawapa pole kwa kazi. Alivua miwani yake akasema;

“Kuna mambo nahisi hayapo sawa mwilini mwangu.”

Kaguta na Bernadetha wakaacha kazi yao na kumtizama Vitalis.

“Mambo yapi?” Bernadetha akauliza.

“Usiku nimekuwa nahangaika sana, natota jasho. Alafu ajabu, nimekua na uwezo mkubwa wa kusikia. Sijui imekuaje?”

“Vipi jeraha lako limepona?” Bernadetha akauliza, kabla Kaguta hajajibu, Bernadetha akanyanyua mkono wa Vitalis na kuutizama. Jeraha halikuwapo. Lilikuwa limekauka pasijulikane hata kama kuna kitu kilitokea. Bernadetha alimtizama Vitalis kwa uso wa butwaa. Akauliza;

“Imekuaje jeraha limepotea haraka hivyo?”

Mara sauti ya Bakari ikaingilia ikiwaita. Wote walitoka wakaenda sebuleni.

“Lile gari limeelekea msitu wa Pande!” Bakari alitoa taarifa. “Kutakuwa kuna kitu kinafanyika huko.”

Vitalis akamuita Jombi na Miraji akawataka wajiandae waende kazini.

Huko ndani ya msitu wa pande, Morgan akiwa na wenzake wanne walitoka kwenye gari wakatembea hatua kadhaa. Kisha wakaanza kujadili. Waliona msituni ni salama kuliko ndani ya nyumba kutokana na yale yaliyomkuta OCD. Ila baada tu ya muda mfupi, WAGENI wakawa tayari wamewasili eneo la tukio. Vitalis alisafisha koo lake, wakina Morgan wakageuka na kuwakuta wanaume wawili ndani ya vinyago; Kaguta na Vitalis. Morgan akatabasamu.

“Hatimaye mpo kwenye mikono yetu. Mlidhani sisi wajinga, sio? Kuja huku msituni huku mkiwa mmepachikatracker kwenye gari letu?Poleni sana. Kwa taarifa yenu tuliona mlichokiweka kwenye gari, na tumewavuta huku ili muwe historia. Tutawaua na kuwazika huku huku, hakuna atakayewajua.”

Vitalis akatikisa kichwa naye akasema:

“Unadhani hilo linawafanya msiwe wajinga? Bado nyie ni wajinga kwasababu, moja; mmesahau kwamba mmeacha alama za matairi ya magari matatu manne, alafu mkaacha moja hapo ili ionekane mpo wenyewe wakati mmekuja wengi, matokeo yake tumeshaharibu magari hayo. Pili, mmesahau kufuta nyayo zenu zilizoingia humu msituni, inaonekana mpo watu hamsini tano na hapo mnajidanganya kwa kutuonyesha mpo watano. Sasa unadhani na sisi ni wajinga kiasi cha kuja kupambana na watu hamsini na tano kwa wawili?”

Morgan alitizama wenzake, alafu akapiga mluzi. Mara wakatokea watu hamsini tokea gizani waliobebelea bunduki. Wote wakanyooshea bunduki kwa Vitalis na Kaguta. Vitalis naye akapiga mluzi, mara taa za gari zikawaka na kuwamulika wakina Morgan na kuwafanya vipofu kwa muda. Milio ya risasi ikavuma. Taa zilipozima, watu wote hamsini waliobebelea bunduki wakawa wapo chini wamekufa. Walibakia Morgan na wenzake wanne tu. Walipepesa macho yao huku na huko, waliposikia kishindo wakaelekezea bunduki zao huko na kufyatua risasi. Mara taa za gari zikawamulika tena usoni na kuwafanya vipofu, zilipozima wote wakawa wameuwawa kasoro Morgan ambaye alichomekwa sindano ya dawa shingoni na kupokonywa bunduki.

“Sasa sikia.” Kaguta alimwambia Morgan. “Dawa uliyowekwa mwilini itakumaliza pole pole. Bahati nzuri dawa ya kukuponya tunayo. Ila ili uipate, nenda katubu maovu yako mbele ya kadamnasi, la sivyo uhai wako utakuwa mali yetu.”

Baada ya hapo, Vitalis na Kaguta wakapotea.

Kwa siku mbili Morgan akawa mtu wa kukakamaa na kutema mapovu macho yakiwa yamemtoka na jasho likimchuruza. Siku ya tatu akaita vyombo vya habari akaeleza ushiriki wake na OCD na bwana Kim. Baadae mzigo wa boksi ukatumwa nyumbani kwake ukiwa umeandikwa ‘antidote’ kwa juu. Ndani yake alikuta kichupa kidogo chenye kinywaji rangi nyekundu. Akanywa.

“Mmmh … Mbona kama Fanta?”

Alipotizama kwa makini akakuta ujumbe kwenye kikaratasi cha chupa … HUNA HAKI YA UHAI. Polisi walipokuja kumkamata Morgan walimkuta tayari yu mfu. Alikuwa chini amekakamaa kama gogo kavu.





**** MSAKO WA MAHAYAWANI ****



Mada moto katika vyombo vya habari ilikuwa ni kuhusu kujitokeza na kuuwawa kwa wahalifu. Picha ya OCD na wenzake kama Morgan na wengineo waliouwawa zilikuwa zaonyeshwa ama kuongelewa na wachambuzi mbalimbali. Lakini je kwanini wahalifu hao wamevuliwa nguo na kupokonywa uhai kwa muda huo? Nani yupo nyuma ya huo mchezo ambao ulionekana kukamata hisia za watu wengi? Hakukuwa na majibu. Vitalis alitabasamu akazima runinga kisha akawageukia wenzake waliokuwa wameketi wakielekeza macho yake kwake.

“Hongereni sana kwa kazi kubwa mliyoifanya. Sasa tunahamia kazi kwenye kazi nyingine pevu: Msako wa mahayawani. Wapo watatu, tutaanza na bwana Isaac Makongo. Lazima tumkamate ila akiwa hai kwasababu tunahitaji maelezo mengi toka kwake ambayo yatatusaidia kumpata mlengwa wetu, Kim Salvatore.”

“Kwahiyo tunapitia mpango gani?” Miraji akauliza. Vitalis akamgeukia Kaguta na kusema.

“Plan yetu ya sasa itaanza na Kaguta. Anajua sehemu ambayo Isaac huenda kumtizama mpira mara kwa mara. Pazuri kuanzia hapo.”

“Naomba na mimi nihusike!” Sandra akapendekeza, “Nataka na mimi nimshikishe adabu huyo mpumbavu!”

“Najua una hasira na Isaac, ila sidhani kwa sasa kama ni wasaa wa kuruhusu hasira hiyo iokoteze vya kutosha ndani yako.” Kaguta akashauri alafu akamgeukia Vitalis.

“Kwahiyo what’s the plan?”

“Plan ni kuhakikisha unatia pin kwenye tairi la gari la Isaac.” Vitalis akaonyesha pini ndogo nyembamba ndefu. “Pini hii itakuwa inapenya taratibu kwenye tairi na mwishowe tairi litapasuka, hapo atakuwa tayari ametoka eneo la mpira, matumaini yetu atakuwa mwenyewe na hivyo tutatokea na kumkamata. Cha umuhimu kuwasiliana.” Vitalis akaeleza, Kaguta akatikisa kichwa kukubaliana.

Siku tatu baadae ndani ya Samaki-Samaki Makonde, Mbezi beach, kukiwa ni usiku, Kaguta na Isaac wakawepo hilo eneo. Isaac alikuwa amejitenga kidogo na umati wa watu, alijiweka kando akiwa anatizama vyema runinga na kuishushia na bia baridi. Kaguta alikuwa ameketi upande wa kushoto wa Isaac, hakuwa naye amejichanganya na watu, zaidi alikuwa anamtizama Isaac katika kila tendo alilokuwa anafanya. Punde akanyanyuka na kwenda nje sehemu ya kupaki magari, akapepesa macho yake kushoto na kulia kutafuta gari la Isaac, hakuona kitu. Akarejea ndani na kuketi sehemu yake.

“Hajaja na gari leo?” Kaguta akajiuliza. Alipeleka mkono wake kidevuni akawa anajikuna-kuna huku akitafakuri. Alimtizama Isaac akaona anaagiza kinywaji kingine baada ya cha mwanzo kuisha, hiko kitu kikampa mawazo Kaguta ambaye aliishia kutabasamu na kuanza kuzingatia kinywaji cha Isaac huku pia akichungulia dakika za mpira uliokuwa unaonyeshwa.

Ikiwa ni dakika ya hamsini na tano ya mpira, chupa ya kinywaji ya Isaac ilikuwa tayari imeteremka karibia na sakafu yake. Kaguta alinyanyuka akatokomea. Isaac akanywa fundo moja la mwisho alafu akanyoosha mkono kutaka kuita muhudumu, haraka Kaguta akatokea akiwa amevalia sare za wahudumu na mkononi mwake ana sahani iliyobebelea bia baridi. Aliweka bia mezani akaifuta na kuifungua kisha akaondoka, Isaac akadaka kinywajiche na kuanza kukishughulikia. Kaguta aliyetokomea akarejea akiwa na nguo zake za awali, aliketi eneo lake moja kwa moja akatizama dakika za mpira zasemaje, dakika sabini kamili, akatabasamu.

“Okay, sasa tutizame mpira.” Kaguta akajisemea.

Ilipofikia dakika ya themanini na tano ya mpira, Isaac akaanza kuona giza. Alitikisa kichwa chake huku akikipiga lakini haikusaidia kitu. Macho yalikuwa mazito hata kichwa pia, akaishia kulala juu ya meza. Alipokuja kufungua kope zake, alijikuta yupo kitini amefungwa ndani ya jengo kuukuu. Vitalis na Kaguta wakatokea na kumsogelea.

“Pole sana mheshimiwa.” Kaguta alisema huku akiigiza sura ya mtu anayesikitika, “Hatimaye upo mikononi mwetu. Tunaweza kukufanya lolote lile kuanzia sasa, ila tusingependa kufikia huko kwakuwa najua tutamalizana kwa amani. Mr Kim Salvatore ni nani kwako?”

Isaac akatabasamu.

“Kama mmenikamatia hilo, nawapa pole maana sitasema lolote. Nawashauri mniue msipoteze nguvu zenu.”

Vitalis akatabasamu.

“Tunajua haitokuwa rahisi kwako kusema. Ila nasi tumejiandaa sana kwa hilo.”

“Narudia tena, mnapoteza nguvu na muda wenu bure, sitosema chochote.” Isaac akasisitizia. Vitalis akakunja shati lake akamtandika ngumi Isaac tumboni. Tena na tena, tena na tena, Isaac akatema damu.

“Utasema husemi?” Vitalis akauliza kwa ukali. Isaac akatabasamu na kutikisa kichwa chake kukataa. Vitalis akamuwasha kofi kali Isaac kisha akasonya.

“Huu ni mwanzo tu, utasema nakuambia!”

Ghafla vikopo vitatu vya chuma vikarushwa ndani ya chumba walichokuwepo wakina Vitalis na mateka wao. Havikujulikana vimetokea wapi. Vikopo vile vilianza kutema moshi mzito mweupe na haikuchukua muda mrefu kutapakaa, wakaingia wanaume watatu wenye kimo sawa waliovalia suti nyeusi na vinyago vya kuzuia gesi usoni, wakapambana na Vitalis na Kaguta ambao walikuwa dhaifu kila walipozidi kuvuta hewa. Ndani ya sekunde chache tu, Vitalis na Kaguta wakawa wameshalazwa chini, hawajielewi. Wanaume wale watatu wakamfungua kamba bwana Isaac Makongo, mmoja akamuweka begani na kutangulia kutoka nje, wengine wawili wakasogelea miili ya Vitalis na Kaguta, wakaionyeshea midomo ya bunduki. Kabla ya kufyatua risasi, sauti ya gari inayoserereka ilipasua masikio yao, wakashtuka. Punde wakasikia vishindo vya miguu na sauti za watu, haraka wanaume wale wawili wakaondoka lile eneo.

Kwenye mida ya saa tisa ya jioni, Bakari kama afanyavyo mara kadhaa alikuwepo mbele ya tanakilishi yake. Alifungua mtandao akapachika jina la Isaac Makongo kisha akabofya kitufe cha kutafuta majibu, muda mfupi picha za Isaac, anwani na maelezo kadhaa yakajiri yakisema ni mfanyabiashara wa nyama za kusindika na mchezaji wa zamani wa mpira. Bakari akaandika maelezo hayo kwenye notebook yake kisha akanyanyuka na kuondoka.

Kwenye mida ya saa kumi na robo ya jioni, Vitalis alianza kugugumia akiwa kitandani amelala. Jasho lilikuwa lamchuruza. Alikuwa anakunja-kunja uso wake kama mtu asikiliziaye maumivu makali. Aling’ata meno akaamka kwa pupa. Alijitizama mikononi mwake akaona kucha zake zimekuwa ndefu kuliko kawaida. Kifuani kulijaa nywele. Meno yake chonge yaliongezeka urefu, ya chini na juu. Ila punde akarudi katika hali yake ya kawaida, kila kiungo kikaa sawa. Vitalis akanyanyuka toka kitandani akavaa shati na kwenda nje. Kibarazani akamkuta Miraji anacheza na mdogo wake, Marietta.

“Shikamoo Uncle!” Marietta alimsalimu Vitalis kwa sauti ya juu. Vitalis akaitikia kwa furaha kisha akamnyanyua binti huyo juu juu na kumrusha-rusha. Alimkabidhi shilingi mia tano akamtaka aende kununua anachokitaka, Marietta akaondoka upesi kuelekea dukani.

“Nini kilitokea asubuhi baada ya kupoteza fahamu?” Vitalis aliuliza. Miraji akamtizama Vitalis.

“Waliondoka na mateka, tulishindwa kuwafukuza kwasababu hali yenu haikuwa nzuri.”

Vitalis akashusha pumzi ndefu. Miraji akauliza:

“Unadhani gesi waliyoitumia itakuwa na madhara kwenu?”

Vitalis akatikisa kichwa. “Sidhani. Hawawezi wakafanya hivyo kwasababu mkuu wao naye alikuwemo ndani. Mlipata kuona nyuso za hao watu waliovalia suti?”

“Hapana!” Miraji akajibu, “Ila tulichokigundua ni ufanano wao wa kimo na rangi pia.”

“Walijuaje kama tupo ndani ya lile jengo?”

“Hapo ndipo hatujapatia jibu.”

Kimya kikakatiza katikati yao. Mara kwa mbali akaonekana Bakari akija na Marietta. Bakari alikuwa amebebelea mkoba mweusi wakati Marietta akiwa ameshikilia pipi kubwa ya kijiti mkononi.Marietta alipitiliza mpaka ndani, Bakari akajiunga na Vitalis na Miraji kibarazani.

“Kuna kitu nataka muone.” Bakari alisema huku akiufungua mkoba wake. Alitoa karatasi nne nyeupe zenye picha na maandishi akawakabidhi Vitalis na Miraji, wakaanza kuzipekua na macho yao. Baada ya sekunde chache Miraji akalipuka kwa kusema:

“Namjua huyu!”

Alionyeshea picha moja karatasini. Vitalis na Bakari wakaitizama.

“Huyu ni baba yangu mkubwa! Anaitwa Tahid. Mara yangu ya mwisho kumuona ni kipindi kile cha msiba wa baba.” Miraji akasema kwa tahamaki.

“Huyu ni mshirika wake Isaac Makongo!” Bakari akasema, “Ni mshirika wake mkubwa wa biashara yao ya nyama.”

“Wanasindikia hizo nyama zao wapi?” Vitalis aliuliza.

“Eneo lao la kiwanda ni Tegeta.” Bakari akajibu.









“Baba mkubwa yako alikuwa ni mfanyabiashara tangu muda gani?” Vitalis alimuuliza Miraji.

“Sijui.” Miraji akajibu, “Ninachojua ni kwamba alikuwa mwalimu. Habari za kuwa mfanyabiashara ndio nazisikia hapa!”

“Basi atakuwa anafanya kwa siri.” Vitalis akabashiri kisha akaongezea; “Hii kazi nadhani itafanywa vyema na wewe, Miraji, na mama yako. Yatupasa tuutumie huo udugu wenu kama njia ya kumvuta Tahid kwenye mwanga na ya kutupatia Isaac Makongo.”

“Sawa.” Miraji akaitikia.

Siku iliyofuata asubuhi Bernadetha akiwa amejivika khanga alienda nyumbani kwa shemeji yake, bwana Tahid. Alikaribishwa na mke wa shemeji wake, akaketi sebuleni, punde akaungana na mlengwa wake ambaye alikuwa anajiandaa apate kwenda kazini.

“Karibu sana, shemeji.”

“Ahsante.”

“Mbona ghafla hivyo?”

“Nimekukumbuka tu. Ni kitambo sasa tangu mume wangu amefariki na hatujapata kuonana kabisa.”

“Kweli kabisa, ni muda mrefu: kazi zinabana. Hapa yenyewe ungechelewa, usingenikuta. Vipi maisha lakini?” Tahid aliuliza huku akitengenezea tai yake shingoni.

“Maisha hivyo hivyo tu, yanasonga.”

“Ashukuriwe Mungu. Karibu sana.”

“Nimeshakaribia, shemeji. Lengo langu kubwa la kuja hapa ni kupata kufahamu mambo kadhaa toka kwako.”

Tahid akakaza macho.

“Yapi tena?”

“Ya kawaida tu, shemeji. Kwani kuna shida?”

“Wala!” Tahid alipandisha mabega yake.

“Sawa. Nataka tu kufahamu kama umepata taarifa yoyote juu ya wale waliomuua mume wangu. Hakuna chochote ulichopata? Hakuna yeyote unayemjua anahusika kwa njia yeyote ile?”

Tahid akatikisa kichwa chake huku akiubinua mdomo wake.

“Kusema ukweli hakuna ninachokifahamu … Hakuna nilichokipata!”

“Kabisa?”

“Kabisa! Ningepata kujua chochote nisingesita kukujuza.”

Bernadetha akashusha pumzi ndefu.

“Sawa, shemeji. Naomba nikuache, tutaonana kadiri muda unavyotaka.”

Bernadetha akaondoka. Tahid akabakia kwenye kiti uso wake ukiwa umetulia tuli. Ni kama vile alisahau kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini mpaka pale mke wake alipokuja kumshtua.

Zikapita siku mbili.

Siku ya tatu, Bernadetha akarudi tena kwa shemeji yake, bwana Tahid. Ilikuwa ni jioni kavu, anga lilikuwa jekundu kwasababu jua lilikuwa lazama hivyo hata mawingu yalikuwa na rangi nyeusi. Bernadetha alikuwa kavalia suruali ya jeans isiyombana, pamoja na shati jeupe lililobebelea tangazo la bia, huku miguuni akijivika raba nyeupe.

“Karibu.” Bwana Tahid alisema huku uso wake ukiwa na makunyanzi. Bernadetha akaingia na kwenda kuketi pale alipoketi mara yake ya mwisho. Bwana Tahid akaungana naye huku akiwa analazimisha tabasamu.

“Karibu tena shemeji.”

“Ahsante, nimekaribia. Samahani sana kwa ugeni wa ghafla.”

Tahid akacheka kiuongo alafu akauliza:

“Hapana, unakaribishwa muda wote, shemeji.”

“Ahsante. Nimekuja kwa suala langu lile lile, shemeji.”

“La kifo cha mumeo?”

“Haswaa.”

Tahid akatikisa kichwa.

“Nadhani shemeji huu ni muda wa kusahau yaliyopita na kuganga yajayo. Sioni kama kuna haja ya kufukua tena maiti ambayo imeshasagwa na kumumunywa na udongo.”

“Shemeji, mume wangu aliuwawa. Siwezi kulala wala kukaa kwa amani mpaka pale nitakapohakikisha wote wanaouhusika wanaenda kaburini.”

“Umepangaje kuhakikisha hilo, shemeji?”

“Lipo kapuni.”

“Nakutakia kila la kheri.”

“Ahsante. Nimekuja kwako kwa mara ya mwisho, bwana shemeji. Naomba uniambie kama kuna lolote unalolijua kuhusu kifo cha mume wangu.Lolote ambalo unajua silijui.”

Uso wa Tahid ukaumuka.

“Unadhani nakuficha kitu, shemeji?”

“Labda.” Bermadetha akajibu kwa macho makavu.

Tahid akatabasamu kwa dharau. Akakuna kidevu chake mara tatu na kusema kwa sauti ya taratibu.

“Naomba uondoke, shemeji.”

Bernadetha akanyanyuka.

“Naenda. Ila jua utamfuata kaka yako muda si mrefu.”

Mwanamke akaondoka akitembea kwa kujiamini. Tahid akamsindikiza kwa macho makali akiwa amevimba kama mtu aliyekabwa na gunzi la moto kooni. Bernadetha alipotoka tu mlangoni, Tahid akanyofoa simu yake mfukoni, akaweka namba na kuiweka sikioni.

“Listen Puzo. Kuna mtu nataka mummalize haraka iwezekanavyo! … Hilo swala la pesa, niachie mimi.” ….

Siku iliyofuata watu wawili wakiwa ndani ya gari aina ya Noah walipaki karibu kabisa na nyumba ya marehemu bwana Malale. Kabla hawajatoka ndani walificha nyuso zao na vinyago vyeusi, wakakoki bunduki zao na kushuka haraka kwenda ndani. Hatua kadhaa mbele ya Noah kulikuwepo na gari la Kaguta, ndani walikuwepo Kaguta mwenyewe na Vitalis. Walikoki bunduki zao, Vitalis akasema:

“I love you Bernadetha. Mtego umekubali.”

Wakashuka wakitembea kwa tahadhari, waligawanyika mmoja akaenda mbele mwingine nyuma. Wakavamia ndani na kuwaweka watuhumiwa wao chini ya ulinzi. Waliwaweka kwenye gari na kuondoka nao mpaka kwenye jengo lao la maumivu. Wakawafunga kamba kwenye nguzo, wakavaa vinyago na kuwapa kipondo kizito kabla hawajakiri aliyewatuma ni bwana Tahid.

“Mmemfanyia kazi ngapi bwana Tahid mpaka sasa?” Kaguta aliuliza.

“Tumefanya kazi mbili tu.” Mateka mmoja akajibu kwa huruma huku akichuruza damu mdomoni.

“Ipi na ipi?”

“Kazi ya kumuua bwana Yudu Makombo na hii.”

“Kwanini mlimuua Yudu?”

“Bosi wetu Tahid aliambiwa afanye hivyo ili apate tenda ya nyama kwa bwana Isaac Makongo.”

Vitalis akatikisa kichwa chake. Alimtizama Kaguta na kumpa ishara ya kuondoka. Walifuata kamera yao iliyokuwa inarekodi kila kitu walichokuwa wanakifanya, wakaizima.

Jua la siku iliyofuata likachomoza, Tahid akiwa anataka kwenda kazini alitoka ndani kwake akajiweka ndani ya gari. Ila ghafla kabla hajatimka, kioo chake juu ya kichwa kikamjulisha kuna mtu kwenye viti vya nyuma. Aligeuka haraka akakutana na Miraji.

“Unaendeleaje baba mkubwa?”

Tahid akatoa macho ya hofu.

“Umeingiaje humu? Unataka nini?”

“Si la muhimu sana kujadili hilo, ila kwakuwa umeniuliza nitakujibu. Nimekuja kukuchukua, na kwasababu huko tunapoenda tunahitaji gari ili tuwahi ikabidi nikungojee humu uje na ufunguo.”

Miraji akatoa kitambaa cheupe mkononi akamziba nacho pumzi bwana Tahid. Kitambaa kilikuwa kina dawa, Tahid alipovuta pumzi mara moja tu, akazirai. Miraji akahamia viti vya mbele, gari likaondoshwa.

Tahid alikuja kujikuta ndani ya jengo kuukuu akiwa amefungwa kamba kwenye nguzo. Alipotizama pembeni yake akawaona watu wake aliowatuma, akashtuka. Walikuwa wamechoka mno kwa kipigo. Nyuso zao zilikuwa zimetapakaa damu, haikueleweka wamekufa ama wamezirai.

“Puzoo!” Bwana Tahid aliita, lakini ikawa bure. Punde akaja Vitalis, Kaguta, Miraji na Bernadetha, wakasimama mbele ya bwana Tahid.

“Kumbe ni wewe mshenzi Bernadetha na mwanao! Nitawafunda adabu, nitawaonyesha nawaambia!”

Bernadetha akasogea mbele zaidi kumkuta Tahid. Akamuwasha kofi matata alafu akamuuliza:

“Utaninyoosha kama mume wangu?”

Tahid akaishia kutoa macho.

“Unadhani sijui kwamba ulihusika na kifo cha mume wangu? Unadhani sijui kwamba wewe ndiye ulikuwa unatoa taarifa za mdogo wako kwa maadui auwawe ili upate ujira na kujikomboa toka kwenye kazi uliyoidharau ya ualimu? Sio wewe uliyeshauri mdogo wako ahamishiwe Royal hospital kwa usalama? Sio wewe uliyekuwa karibu na Dokta Rajesh? Unadhani sikukuona wakati mnapongezana wakati mimi nalia na kusaga meno? Yote hayo ili upate hisa tu kwenye kiwanda cha nyama cha baradhuli Isaac? Mshenzi wewe!”

Bernadetha akamtandika kibao kingine bwana Tahid, tena na tena. Miraji akaja kumtoa na kumpeleka nje.

“Kwahiyo kulikuwa na haja gani kwa wakina Mtemvu kumuhonga dokta asiseme ukweli wakati dokta mwenyewe yupo upande wa Mr Kim?” Kaguta alimuuliza Vitalis.

“Dhamira ya bwana Kim ni kufanya na kutengeneza mazingira ya kisasi kwa mauaji ya wakina Mtemvu, watu wasijue kama ni yeye yupo nyuma ya huo mchezo. Lakini kiuhalisia yeye ndiye aliyekuwa anapanga na kufanya kila jambo.” Vitalis akajibu kisha akamfuata bwana Tahid.

“Sisi hatuhusiani na mambo yenu ya kifamilia, sisi tunamtaka Isaac Makongo. Tunajua wewe unaweza ukatupatia.”

“Mimi?”

“Ndio!”

“Kivipi?”

“Tunajua Isaack ni mshirika wako kibiashara. Ukimuhitaji, unampata.”

“Samahani, siwezi kufanya hivyo.”

Vitalis alinyoosha mkono wake kwa Kaguta, akapewa kamera. Aliifungua kamera akamuonyesha video bwana Tahid jinsi vijana wake walivyokiri maovu yake. Baada ya hapo, Vitalis akamuambia:

“Hii video itasambazwa kwenye vituo vya habari. Bado hutofanya tunayoyataka?”

Tahid kimya.

“Okay. Labda hilo halijakugusa. Umeona hii?” Vitalis akaonyesha picha kwenye kamera ikiwa inaonyesha bomu lililopandikizwa nyumbani kwa Tahid.

“Endapo tukibofya kitufe tu, nyumba yako yote pamoja na mke na watoto wako wataenda, hutopata hata majivu yao. Vipi hapo, bado?”

Uso wa Tahid ukanywea.

“Nitawasaidia. Lakini naomba msijeruhi familia yangu.”





Kesho yake ndani ya asubuhi Tahid akiwa amevaa suti yake nyeusi alikutana na bwana Isaac Makongo kwenye mgahawa mmoja uliokuwa na watu wachache. Walikuwa wanapata kifungua kinywa huku wakipeta soga. Kila walichokuwa wanakiongea kilikuwa kinasikika na Vitalis, Kaguta, Jombi na Miraji waliokuwa wapo ndani ya gari aina ya van iliyosimama umbali wa kama mita mbili toka eneo la mgahawa.

Uso wa Tahid haukuonyesha woga wala tafakuri tatanishi yoyote lakini mikono yake ilikuwa inatetemeka. Hakuweza kubeba kikombe cha chai, kila alipojaribu aliishia katikati na kukirejesha mezani. Isaac akagundua hilo.

“Vipi kuna tatizo?”

“Ndio.”

Tahid akatoa bunduki yake na kumuonyeshea Isaac huku akiwa ameificha na koti, akamuamuru afuate gari aina ya van iliyoko kando, Isaac akatii, wakasogea mpaka garini. Gari likafunguliwa Isaac akaingia ndani. Tahid akasema:

“Nimemaliza kazi yenu sasa, naomba video na remote ya bomu niende.”

Mara ghafla gari likatokea kwa nyuma, Tahid aligeuka kushangaa akakutana na risasi tatu zilizokita kifuani mwake, akadondoka chini kama gogo. Vitalis akafunga milango ya gari, mafuta yakakanyagwa kwanguvu. Barabarani ikawa mfukuzano, gari la wakina Vitalis mbele, nyuma yao wakiwa wanakimbizwa na Range rover nyeusi, risasi zikirushwa kama njugu. Magari yalipelekwa kwa kasi mno kama vile game. Kaguta aliyekamatia van alihakikisha habandui mguu wake sehemu ya kukanyagia mafuta, hata pale konani. Lakini hata waliokuwa wanawakimbiza walifanya vivyo hivyo.

Kaguta akatoka barabara kubwa ya njia nne, akaingia ya njia moja. Ila punde kwa mbele yakatokea magari mawili makubwa, yakaziba njia. Kaguta alipotaka kurudisha nyuma akashindwa, alibanwa na Range rover hatua kadhaa nyuma. Wanaume watano: mapacha watatu na wengine wawili wakashuka toka kwenye magari yao wakiwa wamebebelea bunduki wakawaamuru wote waliokuwepo ndani ya van washuke chini haraka kabla namba zinazohesabiwa hazijafika kumi.

Wakiwa katika mahesabu hayo, Vitalis akawaambia wenzake:

“Muda wa plan B sasa.”

Jombi akachomoa solo tape mfukoni akamfunika mdomo Isaac alafu wakashuka watu wanne tu: Vitalis, Kaguta, Jombi na Isaac. Miraji akabakizwa ndani. Mapacha wale watatu na wenzao wawili wote wakajongea sehemu moja, nyuma ya van, kumpokea Isaac. Vitalis na wenzake walikuwa wamenyoosha mikono juu, lakini muda huo huo wote walikuwa wanahesabu namba kwa kunong’oneza tokea wametoka ndani ya van. Ilipofika namba tano, wote wakarukia pembeni, ghafla van ikarudi nyuma haraka na kuwasukuma maadui wote kwanguvu wakarukia huko, wakina Vitalis wakawahi silaha za maadui na kuwaweka chini ya ulinzi. Wakawaamuru wote wapande ndani ya van. Wakapanda na kuondoka.

Wakiwa wametembea kwa dakika moja barabarani, mapacha watatu wakatizamana kwa macho yanayowasiliana. Mmoja akasema kwa kunong’oneza:

“Plan b.”

Wote wakapeleka mikono kwenye saa zao za mikononi na kuzibofya, moshi ukaanza kutoka taratibu. Wao wakabana pumzi huku wakiwatizama wengine ambao haikuchukua muda wakalewa na kulala. Baada ya lisaa limoja, macho ya Kaguta yakafunguka. Mapacha watatu, Isaac na wenzao wawili hawakuwepo, walibakia wahusika wanne wa kundi la WAGENI tu. Van ilikuwa imesimama kandokando ya barabara ikiwa wazi.

“Amkeni!” Kaguta aliwaamsha wenzake. Vitalis akapepesa macho kisha akauliza:

“Wapo wapi?”

“Hawapo. Wameondoka.” Kaguta alijibu huku akiwa amekunja sura. Vitalis akapiga ngumi gari.

“Shit! … Shit!”

Alishia tu kutikisa kichwa na kushika tama. Gari liliwashwa wakaondoka. Walipofika nyumbani, Bakari akawahabarisha.

“Nilifunga kamera ndani ya gari, nadhani inaweza kutusaidia kutupa baadhi ya taarifa.”

Wakaketi na kuanza kusoma matukio yote yaliyotukia ndani ya gari kwa kupitia tanakilishi ya Bakari. Wakaona jinsi mapacha wale watatu walivyopeana taarifa na kubofya saa zao. Wakaona pia jinsi walivyonusurika kufa baada ya jaribio la kupigwa risasi kushindikana pindi wakiwa wamelala kilevi baada ya mapacha wale watatu kukosa risasi za kufanyia tukio. Video ilipoisha, Kaguta akasema:

“Nadhani tulikosea target. Kumpata Isaac yatupasa kwanza kuwauwa hawa mbwa watatu. Wao ndio kila kitu. Na inawezekana Isaac ana chip ndani ya mwili wake, popote atakapokuwepo, hawa mbwa watatu watafahamu.”

“Kweli.” Vitalis akaunga mkono hoja.

“Ila kati ya hao watu watatu wanaofanana kuna ambaye anaongoza wenzake.” Miraji alichangia, “Wote hawa ni mtu mmoja tu ambaye amegawanywa, inaitwa Human Plurality Modification, ama HPM. Ukitizama vema video utaona kuna ambaye anatangulia kufanya kitu alafu wengine ndio wanafuata. Hata pale kwenye kunong’oneza huyo anayetangulia yeye ndiye aliyefanya hilo tukio, wengine wakafuata, huyo kiongozi anaitwa ‘the brain’ama ubongo. Kama tunataka kuwamaliza hawa watatu inabidi kwanza tumjue kiongozi wao, na huyo ndio awe primary target.”

“Miraji, Umejulia wapi haya mambo?” Kaguta aliuliza, Miraji akatabasamu kisha akamtizama Vitalis huku akitabasamu. Vitalis naye akarejesha tabasamu kisha akasema:

“Tuna bahati sana kuwa na wewe kwenye kundi letu. Sasa umetupa matumaini mapya. Naamini ukikaa na Bakari mnaweza mkafanya kazi nzuri tukakamilisha misheni yetu kwa ufanisi.”

Miraji akamtizama Bakari alafu wote wakatabasamu na kutikisa vichwa.

“Okay jamani. Naomba nitoe udhuru.” Kaguta akasema huku akisimama. “Leo nina mtoko na bibie Sandra usiku huu, naomba nikajiandae wandugu, si unajua tena?”

“Unaweza tu ukaenda, take care!” Vitalis akamsabahi rafiki yake. Kaguta akampa mkono kila mtu na kuwatakia kazi njema. Kaguta alipotoka ndani Miraji na Bakari wakamtizama Vitalis kwa macho yenye mshumbusi wa tafakuri.

“Vipi? … Mbona mnanitizama hivyo?” Vitalis aliuliza.

“Wewe hautoki na mwenzako?” Miraji akasema. Vitalis akaigiza.

“Nitoke na nani?”

“Kwani hujui nani?”

“Sijui nini mnaongelea.”

Bakari na Miraji wakatabasamu.

“Tunadhani na wewe ni muda muafaka wa kwenda mtoko na Miss Bernadetha.” Bakari akapasua jibu.

“Tafadhali mfanye mama yangu afurahi.” Miraji akashindilia msumari. Vitalis akakosa cha kusema, alibakia tu akitabasamu. Alinyanyuka akaenda chumbani kwake. Miraji na Bakari wakagongesha viganja vyao.

Baada mida ya saa mbili ya usiku gari la Kaguta likatua kwenye uwanja wa nyumba ya Vitalis. Ndani yake alikuwemo Kaguta na Sandra wakiwa wamependeza haswa. Honi ilipigwa na punde wakatoka Vitalis akiwa ameongozana na Bernadetha. Vitalis alivalia suti nyeusi wakati Bernadetha akiwa amevalia gauni refu jeupe lenye maua mekundu shingoni na mabegani. Walikuwa wanang’aa. Kaguta alitabasamu akamwambia Sandra:

“Yeyote aliyewapa hawa watu wazo la kufanya hivi, abarikiwe na mwenyezi Mungu mwenye enzi.”

Vitalis na Bernadetha wakapanda garini wakaondoka kwenda moja kwa moja KACHIKA BEACH HOTEL. Waliketi meza moja kila mtu akiwa karibu na mwenza wake. Vinywaji vikaletwa na kuchafua meza, mhudumu akamimina kinywaji kwenye kila glasi kisha akaondoka na kurudi na sahani zenye chakula laini.

Bakari na Miraji bado hawakuwa wamelala. Wote walikuwa wameketi karibu na tanakilishi wakiperuzi mambo. Miraji alishikilia usukani kwa kuweka vidole vyake juu ya vibofyeo akiweka maneno na kuyatafuta mtandaoni. Alama za fomula za kisayansi zilikuwa zinawekwa na kutafutwa mara kwa mara, mara zingine vitabu vya mambo ya uzalishaji na uzazi vikitafutwa na kusomwa na Miraji huku akiwa anaandika baadhi ya taarifa kando. Bakari alipiga mhayo akauliza:

“Uliyajulia wapi hayo mambo, Miraji?”

Miraji akaandika kwanza kitu kando alafu akamtizama Bakari aliyekuwa anarembua kiusingizi akamwambia:

“Haya ndiyo mambo niliyoyasomea India. Kabla sijaacha shule na kurudi nyumbani nilikuwa kwenye utafiti juu ya hii sayansi ya kugawanya watu na wakafanana vilevile.”

Bakari akapiga mhayo tena. Miraji akarejesha macho na vidole vyake kwenye tanakilishi akaendelea. Baada ya muda akasikia mtu anakoroma, aligeuza shingo kutizama akamkuta Bakari ameweka kichwa chake juu ya meza, amelala. Akanyanyuka akambeba akamlazia kwenye kochi kisha akarudi kuendelea na kazi yake.

Vicheko vilitawala meza ya wakina Vitalis. Nyuso za furaha zilitawala huku hakuna aliyeonekana kama anafikiria ulimwengu mwingine mbali na ule waliokuwemo. Kaguta na Vitalis walikuwa wanashindana kuimba huku wanawake wakiwa mahakimu kwa kutoa point. Kwakuwa hakuna aliyekuwa na sauti nzuri ya kuimba, basi lile tendo likawa kama mchezo wa futuhi, wote wakawa wanacheka na kusemana hapa na pale. Tafrija ilikuja kukatishwa pale alipokuja mwanamke mmoja akiwa kavalia nguo za wahudumu. Mwili wake ulikuwa umejaa kwa shepu ya kibantu, alitembea kwa madaha yote akasimama nyuma ya Kaguta kisha akainama na kumnong’oneza.

“Helo mpenzi!”

Kaguta akashtuka na kutizama sauti ilipotokea.

“Bhoke!” Kaguta akatahamaki. “Unafanya nini hapa?”

“Kwani vipi, hukutegemea kuniona, mpenzi?”

“Mpenzi wako nani? … Embu tafadhali nenda, hivi ndivyo mlivyofundishwa kuhudumia wateja?”

Bhoke akaguna.

“Leo unaniona takataka enh? Leo sina maana kwako, sio?”

“Kaguta, huyo nani?” Sandra akaingilia.

“Usihofu, mpenzi. Nitakuelezea.” Kaguta alijitetea.

“Utaeleza nini?” Bhoke akauliza, “Kumbe hata jina ulin’danganya ukanambia unaitwa Benson? Mwanaume wewe!”

Kaguta alinyanyuka akamtoa Bhoke lile eneo. Alimvutia mbali kabisa na eneo walilopo wenzake, akashusha pumzi ndefu na kutikisa kichwa chake.

“Unafanya nini, Bhoke? Tangu lini mimi na wewe tulikuwa wapenzi? Si tulikuwa tunamalizana tu kila mtu anaenda na zake?”

“Nilikudai pesa mara ngapi? Nilikudai pesa mara moja tu ile siku ya kwanza, siku zingine nilikuwa nakupa penzi bure kabisa. Unavyosema tulikuwa tunamalizana unamaanisha nini?”

Kaguta akatoa pochi yake mfukoni.

“Unanidai shilingi ngapi?”

Bhoke akasonya.

“Unadhani kama nilikuwa nataka pesa nisingekuambia muda wote huo? … Nakutaka wewe Benson, sijui Kaguta, vyovyote vile.”

“Unan’taka mimi?”

“Ndio. Nataka penzi ulilonipa liwe la kwangu tu.”

“Una wazimu wewe enh?”

“Ndio. Penzi lako lanipa wazimu.”

“Bhoke, tafadhali naomba uende. Unajua wale ni watu wa heshima sana. Unaniharibia picha yangu kwa kabisa.”

“Kwahiyo?”

“Nenda, tutayamaliza baadae.”

“Ole wako usinitafute.”

Bhoke akaondoka. Kaguta akashika kiuno.

“Aisee! Yani nimekimbia kule nije huku kumbe ndiyo nimeyakuta huku huku.”

Alitikisa kicha chake akang’ata lips.

“Kaja lini huku huyu mwanamke? … Mungu wangu!”

Aligeuza akawarudia wenzake akakuta kiti cha Sandra kitupu. Vitalis akamwambia:

“Ameondoka. Pole kwa maswahibu.” Kisha akatabasamu.

Hawakuchukua tena muda mrefu hapo, wakalipia bili na kuondoka zao. Kaguta aliwarudisha Vitalis na Bernadetha nyumbani yeye akaenda zake kwa madai ya kumfuata Sandra. Vitalis na Bernadetha wakaingia ndani wakawakuta Miraji amelala pembeni ya tanakilishi huku Bakari akiwa hajielewi usingizini kwenye kochi. Vitalis alimnyanyua mmoja mmoja akawapeleka chumbani na kuwafunika na shuka. Bernadetha alisimama mlangoni akimtizama Vitalis akiwafunika shuka wanausingizi. Vitalis alitoka chumban akamtizama Bernadetha kwa sekunde kadhaa, Bernadetha akasema:

“Una nguvu kweli. Umewabeba watu wazima hivyo.”

Vitalis akainama na kumnyanyua Bernadetha.

“Hata wewe naweza kukubeba.”

Alimpeleka chumbani akamlaza.

“Nakutakia usiku mwema. Nimefurahi sana kuwa na wewe usiku huu.” Kaguta alisema kisha akatoka chumbani. Bernadetha akavuta mto na kuukumbatia kwanguvu. Alitabasamu mwenyewe akajisemea:

“Ahsante kwa kurudisha furaha yangu.”

Masaa yakakimbia usiku ukakata. Asubuhi ya saa tatu, Miraji na Bakari walikuwa pamoja na Vitalis kwenye meza ya tanakilishi. Miraji akachukua karatasi yake aliyokuwa anaiandikia, akasema:

“Kuna habari nzuri na mbaya. Nianze na ipi?”

“Mbaya.” Vitalis akajibu.

“Habari mbaya ni kwamba, hatujapata njia ya kuwakamata mapacha watatu.”

“Na nzuri?”

“Habari nzuri, tumepata watu ambao kwa njia moja ama nyingine wanahusika na tendo hili la kisanyansi.”







“Wakina nani?”

“Tafiti hii imefanywa na watu wawili tu ulimwengu mzima: Profesa Kumar wa India na Profesa Hox wa Bermuda. Kama ningelifanikiwa basi nami ningekuwa wa tatu. Watafiti hao wawili ndio ambao wamefanikiwa kufikia tamati lakini kukiwa na utofauti mdogo, profesa Kumar wa India yeye alifanya practice yake kwenye mimea wakati profesa Hox yeye akifanya practice kwa wanyama akitumia panya. Wote walifanikiwa kwa kuunda vitu vipya vilivyofanana. Shida hatujui nani ndiye mhusika mkuu.”

“Ni profesa Hox.” Vitalis akajibu kwa kujiamini.

“Umejuaje?”

“Bermuda ni makao ya Mr Kim Slavatore. Ni lazima kutakuwa na mahusiano.”

“Kwahiyo?”

“Inabidi twende huko. Hakuna namna.”

Baada ya siku mbili ndege kubwa ya British Airways ikatua ndani ya uwanja wa kimataifa wa L.F. Wade, Vitals na Kaguta wakashuka. Walichukua taksi ikawapeleka hotelini wakapumzika kwa siku hiyo waliyofikia. Siku iliyofuata wakaanza msako wa kumtafuta profesa Hox kwa kwenda Bermuda College. Walitizama ratiba ya profesa huyo kwenye ubao wa matangazo, wakarejea siku ya maonano.

“My name is Vitalis, from Tanzania. And this fellow of mine, called Kaguta from the same country.”

“What can I help you?” Profesa Hox akauliza. Alikuwa ni mzee mwenye uwaraza na nywele zenye mvi. Macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani kubwa ya macho. Alikuwa na mustachi mweupe kwa mbali, alivalia shati lililojikunjakunja na suruali mpauko ya jeans.

“We are in need of your assistance and your cooperation, professor. There are some sensitive matters we want to discuss with you.”

“What matters?”

“Its about HPM: Huma Plurality Modification research.”

“What about it?”

“Can we discuss it further out of here?”

“No. And I’m not in the mood of talking about such matters. Just leave, please. Don’t ever come back here. Leave or I will call security.”

Vitalis akamtizama Kaguta.

“Tuondoke.”

Wakanyanyuka na kuondoka.

Wakati jioni imefika profesa Hox akafunga ofisi yake na kufuata gari lake. Alikwea akaondoka toka eneo la chuo, nyuma yake kuna gari likawasha taa na kuanza kumfuata profesa kwa umbali kidogo. Ikiwa ni kasoro lisaa, profesa akafika aelekeapo. Aliingia kwenye nyumba moja yenye ukubwa wa kati, geti likafungwa.

Siku iliyofuata na iliyofuata mchezo ukawa ndio huo huo wa profesa kufuatwa na gari nyuma yake pasipo kujua. Siku ya tatu, Kaguta akauliza:

“Kuna haja gani ya kufanya hivi, Vitalis? Huoni kama tunapoteza pesa kila siku kwa kukodi gari na kukaa hotelini?”

“Kaguta, inabidi tujue kwanza maeneo anayopenda kwenda huyu mlengwa wetu. Tujue kama huwa anafuatiliwa au anakutana na nani muda fulani ama mara kwa mara kabla ya kuchukua hatua yoyote. Kumbuka tupo kwenye makao ya adui. Kuwa mvumilivu.”

Siku ya nne baada ya Profesa kuingia ndani kwake akitokea kazini, Vitalis naye akaruka ukuta na kuingia ndani. Profesa akiwa sebuleni akasikia mbwa anabweka sana huko nje. Alitoka akiwa amebebela bunduki kubwa ‘gobore’ akatizama huku na kule pasipo kuona kitu.

“Shut up you dog!” Profesa alifoka. “I will kill you if I will hear your stupid barks again, fool!”

Akarudi ndani na kujilaza kwenye kochi ambapo napo hakukaa sana akaendea jokofu na kutoa chupa ya kilevi akawa anaigigidia mdomoni mithili ya kwamba yupo mashindanoni. Wakati anafanya yote hayo Vitalis akawa anamtizama kwa kumchungulia, baada ya muda mfupi Vitalis akatoka na kumrudia mwenzake aliyekuwa ameketi kwenye gari.

“Umepata nini?”

“Kuna kitu nimegundua. Profesa anaishi mwenyewe na ni mtu ambaye anasumbuliwa na msongo wa mawazo. Anakunywa na analala na picha kubwa iliyo ndani ya fremu.”

“Sasa hiyo itatusaidia nini, Vitalis?”

“Kaguta, inabidi tujue udhaifu wa profesa. Unadhani kila kitu kitaendeshwa na mdomo wa bunduki?”

Hawakuongea tena, gari lilitiwa moto wakahepa.

Siku iliyofuata Vitalis akafanya kile kile alichofanya siku iliyopita. Alizamia ndani ya nyumba ya profesa Hox akachungulia ndani. Akamuona profesa Hox anakunywa pombe huku akiwa anatizama picha kubwa akilia. Mara kadhaa alikuwa majina ya watu yakiambatana na vyeo vya mtoto na mke. Baada ya muda Vitalis akamrudia mwenzake, wakaondoka.

Siku iliyofuata Vitalis na Kaguta wote wakaingia ndani ya nyumba ya profesa punde tu baada mwenyeji kuingia, walimuweka profesa chini ya ulinzi na kumkalisha kitini. Kaguta akamnyooshea bunduki profesa.

“Tell us everything about HPM before I send you to hell.”

Profesa akatabasamu,

“Just kill me, unknown friend. Stop wasting you time.”

Vitalis akashusha mkono wa Kaguta.

“Si kila kitu kinaenda na risasi, Kaguta. Acha niseme naye.”

Vitalis akamtizama profesa machoni na kusema:

“I am sorry for all of our troubles. It is just we are in great need of your valuable explanations about HPM. Our country is in trouble because of it. Please help us.”

Profesa Hox alinyamaza kimya. Aliwatizama Kaguta na Vitalis kisha akatizama chini. Vitalis alishusha pumzi ndefu akamtazama tena profesa machoni.

“What about your family?”

Profesa akakunja sura yake.

“What do you know about my family?”

“Nothing.” Vitalis akajibu, “But what I know is that you are lonely and somehow you wish they could be here with you.”

Macho ya profesa yakaanza kubadilika rangi na kuwa mekundu. Vitalis akaendelea kuongea:

“There are many families in Tanzania that are in risk of becoming like yours because of HPM mis-use. Please help us, please save other families.”

Profesa hakuongea kitu, machozi yalimtiririka. Vitalis alinyanyuka akamuachia namba yake na kumtaka amtafute atakapokuwa tayari. Usiku huo wote mzima profesa akaumaliza kwa kulia.

Siku iliyofuata saa kumi na mbili jioni, profesa Hox akakutana na Vitalis pamoja na Kaguta maeneo ya ufukweni. Wakiwa wanakunywa vinywaji laini, profesa akaeleza yote anayoyajua kuhusu HPM. Haikuwa amri yake kupelekea matumizi mabaya ya teknolojia aliyoigundua bali ilikuwa ushawishi wa nguvu wa bwana Kim akiwa kateka familia yake na kuwapa madawa ya kuwaua kwa kumlaghai atawaponya pale tu atakapokabidhi tafiti yake nzima. Kwa kutumia teknolojia yake hiyo akatengeneza viumbe vyenye nguvu na uwezo wa ajabu baada ya kuchanganya vinasaba vya wanyama tofauti wa mazingira mbalimbali na wenye fiziki kubwa. Vinasaba hivyo vikawekwa kwenye miili ya wakina mama wajawazito na pindi walipojifungua wakatoka watoto mapacha. Ila miongoni mwao ni yule pekee aliyekuwa tumboni ndiye atakuwa na uwezo mkubwa wa kuliko wenzake. Na mara nyingine wenzake watakuwa wanafuatisha kile afanyacho. Atakapouwawa ama kujeruhiwa, wenzake wote watapata matokeo sawasawa na hayo.

Kaguta akataka kujua zaidi kuhusu udhaifu wao na kivipi wanaweza kuuwawa kwa wepesi. Profesa Hox akataka apewe muda zaidi arudi maabara kufanya utafiti.

“We don’t have time, professor. Please hurry up.” Vitalis akausia.

“I will try my level best.” Profesa akawapa moyo.

Zikapita siku tatu profesa Hox akiwa anashinda maabara usiku mzima. Siku ya nne akakutana na Kaguta na Vitalis akiwa amebebelea briefcase. Walikutania palepale walipokutana mara ya kwanza. Akiwa ameshikilia briefcase lake kwanguvu na mara zingine akitizama tizama usalama kwa kuangaza huku na huko, profesa akasema:

“Make sure you put this liquid inside of their body, it will either weak them up fast or kill them as well.”

Wakati profesa anatoa briefcase ikatokea gari moja jeusi Jaguar, lilikuwa latembea kwa kasi mno, mtu mmoja akachomoza ndani ya hilo gari na kurusha risasi nyingi mno kuwafuata wakina Vitalis. Profesa Hox akamiminiwa risasi za tumboni na kifuani. Briefcase nalo likachakazwa. Vitalis na Kaguta wakapona baada ya kulala chini upesi. Gari likatokomea haraka na kupotea machoni. Vitalis na Kaguta wakaharakisha kumtizama profesa Hox, wakamkuta ameshakufa, walipofungua na briefcase hawakukuta kitu, vyote vilivyokuwemo vilikuwa vimevunjika na kumwagika. Kaguta alishika kichwa chake kama mtu aliye msibani akapiga yowe:

“Uuuuuuuuuwiii!”

Alipiga magoti akamtizama Vitalis.









“Sasa tumekuja kufanya nini huku, Vitalis? Dah!”

Vitalis akashika kiuno chake akashusha pumzi ndefu.

“Nyanyuka twende, Kaguta.”

Kaguta akanyanyuka wakaondoka. Wakaenda nyumbani kwa profesa Hox.

“Unadhani tutapata kitu huku?” Kaguta aliuliza.

“Ndio. Nina hisia hizo kabisa.”

Walizunguka nyumba ya profesa wakatokea maabara. Baada ya kupekuapekua wakaona kuna kamera, walizivunja zote kisha wakaendelea kutizama tizama. Punde Kaguta akaona karatasi moja kubwa jeupe likiwa limeandikwa fomula za kikemia. Akamuita Vitalis na kumuonyesha. Vitalis akatabasamu na kumkumbatia Kaguta.

“Tumeipata! … Hii ndo’ yenyewe.”

“Umejuaje?”

“Huoni ameandika hapa HPM demise formula?”

Haraka wakatoka ndani. Walikata tiketi ya ndege Siku ya pili kufuata wakawa tayari wapo ndani ya ndege kurudi nyumbani. Ila kuna watu walikuwa wanawafuatilia. Bahati nzuri waliwahi, kabla hawajakutwa ndege ilikuwa tayari ipo angani.

Baada ya siku moja wakawasili Julius. K. Nyerere Airport. Miraji na Bakari wakaja kuwapokea. Vitalis alimuonyesha ile karatasi Miraji, akamuulza:

“Unaelewa chochote hapo?”

Miraji akatizama karatasi kwa umakini alafu akajibu:

“Ndio.”

Vitalis akaangua kicheko. Walipofika nyumbani Miraji akamuonyesha karatasi mama yake, akaitizama kisha akamtikisia kichwa. Miraji akamuambia Vitalis:

“Tunaweza kutengeneza ila kuna mahitaji yanatakiwa yawepo.”

“Hakuna shida kuhusu hilo.” Vitalis akawatoa shaka. “Nitazitafuta na kuzileta, tajeni tu.”

Baada tu ya siku moja kazi ya kutengeneza dawa ikamalizika. Lakini bado ikawa haitoshi.

“Tutawapata wapi sasa?” Miraji aliuliza.

“Hiyo ni kazi yangu.” Bakari akajibu. Alivuta tanakilishi yake akacheza video iliyorekodiwa kwenye van. Ilipofikia sehemu gari la mapacha lilipoonekana likiingia, akasimamisha video. Akanakili plate number za hilo gari, akalichora na kuli-scan. Alifungua mtandao wa Dar city center akatuma gari alilochora na kulitafuta, punde taarifa zikaja.

“Lipo maeneo ya Kijitonyama kwa sasa pembeni ya Exim bank kwa mujibu wa kamera zilizo karibu.”

Kaguta, Vitalis na Miraji wakabebelea sindano za dawa wakapanda gari kuelekea Kijitonyama. Walipofika wakaliona gari lengwa ila wenye nalo hawakuonekana wapo upande upi wa dunia. Kaguta akapaki kando kwa lengo la kungojea.

Baada ya dakika moja lilitokea gari kubwa aina ya Scania likagonga gari walilomo wakina Kaguta kwanguvu upande wa nyuma na kulifanya nyang’anyang’a. Kabla wakina Kaguta hawajafanya lolote, gari likasukumwa kwanguvu kufuata ukuta mkubwa ulio mbele. Kaguta alijitahidi kukamata breki lakini haikusaidia kuwasimamisha wakazidi kusogelea ukuta kwa haraka. Kaguta aligeuka akapaza sauti:

“Tushuke upesi!”

Milango ya gari ikafunguliwa watu wakajirusha nje. Gari la Kaguta likaburuzwa na kwenda kubondwa ukutani likageuzwa chuma chakavu kufumba na kufumbua macho. Kaguta alishika kichwa chake, akalalama:

“Gari langu!”

Mapacha watatu wakashuka toka kwenye gari lao kubwa na kuanza kuchukua hatua kuwafuata WAGENI. Kaguta alishindwa kusubiria akawakimbilia mapacha adui akamvaa mmoja wao na kumbwagia chini, kabla mapacha wengine wawili hawajafanya kitu nao wakavamiwa na Vitalis pamoja na Miraji. Mapigano yakazuka lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na uwezo wa kumshinda pacha aliye naye. Mapacha walikuwa na nguvu, wepesi na wenye kufikiria kwa haraka zaidi. Kabla Vitalis hajanyanyua ngumi yake na kuituisha kwenye uso wa pacha, tayari mkono ulikamatwa na kutenguliwa. Kabla Kaguta hajanyanyua teke mguu ulishapanguliwa na kurudishwa. Kabla Miraji hajatuma kichwa chake, pacha alishawahi na kupeleka kichwa chake haraka. WAGENI hawakupata hata muda wa kutoa sindano kwenye mikanda yao iliyobebelea vifuko. Walichakazwa ndani ya muda mchache, wakiwa wamelala chini kwa kuchoka, mapacha walisonga karibu yao wakawanyooshea midomo ya bunduki. Mmoja aliyekaa katikati akasema kwa kubinua mdomo:

“Sali sala zenu za mwisho.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kabla vidole vyao havijabinya vitufe ghafla likatokea gari aina ya defender rangi ya kijivu likiwa katika mwendo wa kasi sana. Mapacha wote waligeuza shingo zao kutizama hilo gari. Liliwasomba kama fyagio likawatupia mbali mithili ya mipira. Gari lilisimama wakachomoza Jombi, Bernadetha na Sandra wakiwa katika nguo za kazi.

“Mpo okay?”

Jombi aliuliza kwa sauti.

“Tupo sawa!” Vitalis akajibu, Kaguta akaongezea:

“Tupo fresh.” Huku akimpa mkono Miraji na kumnyanyua. Mara sauti ya Scania ikapasua ngoma zao za masikio. Walistaajabu kuona Scania linakuja kwa kasi kufuata gari walilokuja nalo wakina Jombi. Jombi aliondoa gari lao haraka kurudi nyuma. Bernadetha na Sandra walichomoza madirishani wakaanza kumwaga risasi wakilenga Scania. Baada ya muda mfupi Scania lilisukuma defender ikageuzwa upande unaoelekea Scania. Bernadetha aliendelea kumwaga risasi akapasua kioo cha pembeni na kumjeruhi pacha mmoja wapo begani. Jombi alishika usukani na mkono mmoja mwingine akatolea bunduki akapasua matairi ya Scania. Scania likasimama tuli. Jombi akasogeza gari na kulipaki mbele kidogo mwa Scania, yeye na wenzake wote wakaelekezea bunduki zao kwenye Scania wakingoja yeyote atakayetokea awe mali yao. Punde Kaguta na Miraji nao wakafika eneo la tukio. Macho yao yote yalielekezwa kwenye gari kubwa jekundu, Scania.

“Vitalis yupo wapi?” Bernadetha alimuuliza Kaguta. Kaguta aligeuza geuza shingo yake pasipo kumuona Vitalis, alistaajabu:

“Wote tulikuwa tunakuja hapa …. Sijui wapi ameelekea. Miraji umemuona Vitalis?”

“Hapana.”

Wakiwa kwenye bumbuwazi wakasikia sauti za watu wanaolia kwa maumivu ndani ya Scania. Mara wakaona damu zachafua kioo cha mbele cha gari hilo kubwa, ndani ya sekunde chache pacha mmoja akatupwa nje akiwa anavuja damu, amechanwa chanwa usoni na shingoni, punde tena akatupwa pacha mwingine na mwingine alafu kukabakia kimya kama vile hakuna kilichotokea. Kwa dakika nzima hakuna aliyefanya lolote zaidi ya kubung’aa. Bernadetha alishuka akakimbilia kwenye Scania. Alichungulia ndani akaona mwili wa binadamu umejikunyata mfumo wa coil u-uchi wa mnyama. Akaita kwa uso wenye wenye mushkeli:

“Vitalis!”

Mara yule mtu akatizama sauti inapotokea. Loh! Alikuwa ni Vitalis. Bernadetha akatabasamu kisha akawatizama wenzake waliokuwa wanajongea. Akasema kwa furaha:

“Vitalis! Vitalis yupo humu!”

Baadae giza likiwa limetawala na Vitalis akiwa amejipumzisha kitandani, Bernadetha akafungua mlango na kuingia ndani. Aliketi kitandani akamgusa bega Vitalis.

“Unaendeleaje?”

Vitalis alijinyoosha akajibu:

“Naendelea vizuri. Wewe je?”

“Nipo poa. Nini kilitokea, Vitalis?”

Vitalis alishusha pumzi ndefu kwa kutumia pua yake alafu akatikisa kichwa:

“Bernadetha.” Aliita, “Mimi sio binadamu tena.”

“Kwanini unasema hivyo, Vitalis?”

“Mimi ni mnyama sasa. Tena mnyama wa ajabu. Nimeshuhudia kwa macho yangu nabadilika, natokwa manyoya kama simba!”

“Usihofu, Vitalis. Pumzika kwa sasa. Tutaongea baadae, hakuna lisilowezekana.”

Bernadetha alisema huku akimfunika shuka Vitalis alafu akatoka na kwenda sebuleni alipowakuta wenzake wakiwa wanamsubiri.

“Anaendelea vizuri. Nimemtaka apumzike kwa sasa.” Bernadetha alisema kwa sura yenye uhakika. Kaguta akauliza:

“Amekuambia lolote kuhusu mabadiliko yake?”

Bernadetha akakuna nyusi kwanza alafu akajibu:

“Ameniambia kwamba aligeuka na kuwa mnyama. Yupo katika hali ya hofu ndio mana nikamtaka apumzike tuyapanga baadae.”

“Unadhani nini litakuwa tatizo kwenye mwili wake?” Miraji aliuliza. Jombi akawahi kujibu:

“Pasi na shaka ni wale mbwa mwitu wa kisiwani- walimng’ata mkono wake. Huwa nasikia mate yao si mazuri kwa kiumbe kama binadamu, yaweza pelekea akapata mabadiliko sometimes.”







“Sasa tutafanya nini kama hayo anayoyaongea Jombi yakisadikika?” Sandra akauliza. Watu wakakaa kimya kwa dakika kadhaa, pumzi tu ndizo zikisikika. Hakuna aliyeonekana ana majibu, hata wenye nayo labda walihofia kuyasema mbele ya kadamnasi. Mwishowe waliamua kufunga kikao mpaka pale watakapolipatia ufumbuzi linalowatatiza.

Siku iliyofuata saa tano na dakika ishirini na tatu asubuhi, Bakari alisimama mbele ya wenzake wote wakiwa sebuleni. Mkononi mwake alikuwa kabebelea kafimbo kadogo keupe akiwa anakatumia kuonyeshea kilichoandikwa ama kuchorwa kwa kugusia ubao mweupe uliokuwa umesimama na miguu minne mbele yake. Juu ya ubao kulikuwa na tarakimu kadhaa pamoja na mchoro mkubwa wa nyoka aliyejiviringita kwenye mti na kusimamisha vichwa vyake vitatu juu. Bakari alisema akionyeshea mchoro wa nyoka:

“Huu ndio mchoro waliokuwa nao mapacha watatu kwenye migongo yao. Ni tofauti kabisa na michoro mingine tunayoifahamu. Bila shaka utakuwa na maana yake ambayo tunahitaji kuifanyia ufumbuzi.”

Kaguta akakohoa kidogo kukamata atensheni za watu alafu akasema:

“Bakari, huo mchoro si mara ya kwanza kwetu kuuona. Kama una kumbukumbu nzuri kwa mara ya kwanza tuliushuhudia ukutani mwa yule mzee wa Bwagamoyo.”

Vitalis akatikisa kichwa chake kama mtu anayekubali kilichosemwa.

“Ni kweli anachokiongea Kaguta, tuliuona huo mchoro huko. Utakuwa una maana gani? Kuna haja ya kuurejelea kwa bwana Alwatan Kombo?”

Sandra akaguna. Watu wote wakampa nyuso zao.

“Kwa bwana Kim hakuna kundi moja linaloweza kumlinda na kuhakikisha matakwa yake yanatimia. Ni lazima awe na mianya na fursa nyingi kufanya hayo. Je kwenye huo ukutwa wa bwana Kombo, mlipata kuona michoro mingapi?”

Kaguta na Vitalis walitazamana kama vile kila mtu anamngoja mwenzake aanze. Vitalis akajibu:

“Nadhani kama nakumbuka vema, ni michoro mitano.” Alafu akauliza, “Au sio Kaguta?”

Kaguta akatikisa kichwa. Sandra akaendelea kutema maneno:

“Basi tukae tukijua kwamba kuna makundi matano yanayomlinda Mr Kim. Kila kundi litakuwa na miiko yake pia wajibu wake, na vile vile viongozi. Kuna haja ya kung’amua hilo.”

“Ila hatuoni kama hapo tunajiingiza kwenye msoto mwingine mpya kabla hatujaumaliza huu uliopo?” Bernadetha aliuliza kisha akaongezea:

“Mi nadhani kuna haja kwanza ya kumalizana na hawa mawakala wanaobebelea mchoro wa jitu. Baada ya hapo tuhamie kwenye hilo kundi jingine. Kwa maono yangu naona kama vile haya makundi yanategemeana kwa njia moja ama nyingine, na yana hulka ya kusaidiana. Kundi hilo la nyoka limewasaidia wenzao eidha sababu wameombwa wafanye hivyo ama wameona wenzao wapo taabani.”

“Naunga mkono shauri.” Jombi alisema. “Tulinywe kwanza tulilolikoroga kabla ya kuomba kopo lingine la togwa.”

Wazo likapewa fursa. Bakari akaendelea na ubao wake, sasa akagusisha ki-fimbo chake kwenye tarakimu zilizoandikwa pembeni ya mchoro wa nyoka: 25119-20.

“Nyuma ya shingo ya pacha mmoja kuna nambari hizi. Kuna yeyote mwenye utambuzi kuhusu hili?”

“Naomba hilo liwe homework. Tuanze kupanga jinsi ya kuwakamata mawakala kwa kuanza na Isaack.” Kaguta alitoa wazo. Vitalis akatabasamu.

“Hapo ndio patamu sana. Hakuna sehemu napapenda kama hapo. Tuanze sasa.”

Bakari akafuta ubao na kuandika kichwa cha habari ‘THE PLAN’.

Ilikatiza siku moja baina yao. Siku iliyofuata ikiwa ni jioni Isaac alikuwa kwenye gari lake akirudi nyumbani. Alifika getini akapiga honi lakini hakuna aliyekuja kumpokea wala kumfungulia geti. Alikunja sura yake akalaani huku akishuka garini:

“Pumbavu sana huyu. Kaenda wapi muda huu?”

Alisogelea geti akajaribu kulisukumiza likafunguka.

“Yani hata geti kaacha wazi. Jinga kabisa! Naona amechoka kazi sasa.”

Aliingiza gari lake ndani, akarejea kwenye geti lake na kulifunga. Moja kwa moja akaenda ndani. Hakuona pembezoni mwa kibanda cha mlinzi kulikuwapo na matone ya damu yakielekea nyuma ya kibanda hiko. Labda angelijua angelisita kwenda ndani.

Mlango wa sebule ulifunguka pasipo kelele Isaack akaingia ndani. Kabla hajafanya lolote alinyoosha mkono wake akawasha taa. Uso kwa uso akakutana na njemba mbili zikiwa zimejaa kwenye kochi, nyuso zao zilikuwa zimevikwa vinyago vyeusi, macho tu yakiwa wazi. Isaack akakodoa macho.

“Wakina nani nyie?”

Njemba mmoja akatoa bunduki yake na kumnyooshea Isaack. Akamuamuru:

“Kaa chini!”

Isaac akatii.

“Sisi ni wageni wako wa leo.” Sauti ya Vitalis ilisikika toka kinywani mwa yule aliyebebelea bunduki.

“Mnataka nini kwangu?”

“Tunataka uhai wako. La sivyo utupe taarifa tunazozitaka.”

Isaack akatabasamu.

“Kumbe ni nyie. Bado hamjachoka kunifuatilia? … Labda tu niwasaidie kuokoa muda wenu kwa mara nyingine kwa kuwapa jibu la moja kwa moja – sitosema lolote, msitegemee kupata taarifa yoyote toka kwangu.”

Njemba aliyeshikilia bunduki akamtizama mwenzake na kumpa ishara ya kichwa. Mwenzake akanyanyuka na kwenda mbele kidogo akifuata chumba cha kulia chakula. Kilikuwa ni giza tupu hakuna kinachoonekana. Njemba yule akawasha taa tap! Mara ikaonekana miili mitatu mfu ya mapacha wakiwa na majeraha ya kina kirefu. Isaack akapigwa na butwaa. Alitaka kunyanyuka lakini akaamriwa na njemba mwenye bunduki:

“Tulia hapo hapo!”

Akatulia. Uso wake ulibebelea tambara la wasiwasi mkubwa.

“Najua ulikuwa unaleta kiburi kwasababu ulidhani watu wako wa kukusaidia wapo. Pole sana, najua umeshtushwa. Sasa vipi utatupatia majibu yetu?”

Isaack alikunja sura akaropoka:

“Laiti mngejua mnachohangaika nacho ni kikubwa kuliko nyie, msingediriki kuhatarisha maisha yenu kiasi hiki. Hamtofika popote, nawahakikishia. Hakuna atakayewatambua nyie kama mashujaa. Kwani mnataka shilingi ngapi? Semeni niwape. Mmenisababishia hasara kubwa sana. Mmekamata unga wangu wa pesa ndefu mkauharibu, bado hamjatosheka?”

Njemba mwenye bunduki hakusema kitu, alibinya kifyatulio taratibu risasi ikaenda kwa kasi na kutoboa goti la Isaack. Isaack akapiga kelele kali za maumivu.

“Nishakuambia nini nataka. Ulisikia nikisema pesa?” Njemba mwenye bunduki akauliza. “Sasa basi utanipa ninachokitaka au lah?”

Isaack aliendelea kulia na maumivu. Njemba mwenye bunduki akafyatua tena risasi kulenga ugoko wa mguu mwingine, Isaack akalia kama mtoto.

“Please stoop! … Please naumiaa!”

“Utakapokuwa tayari kusema utaniambia. La sivyo tutaendelea na zoezi letu hatua kwa hatua.” Alisema njemba mwenye bunduki kisha akalenga risasi kiatu cha Isaack. Isaack akaendelea kumwaga kilio. Jasho lilimvuja. Damu zilimtapakaa miguuni. Machozi nayo yalimtiririka. Hakujua ashike wapi aache wapi. Njemba mwenye bunduki akanyooshea bunduki kwenye ugoko wa mguu ulitobolewa goti. Isaack akanyoosha mkono mmoja akimpa ishara ya kumkataza.

“Nasema! … Nitawaambia mnachokitaka! Nakuomba usiendelee, nakuomba!”

Njemba mwenye bunduki akapumzisha mkono wake juu ya mapaja, akauliza:

“Umeanza biashara ya madawa ya kulevya kuanzia lini? Unauingizaje nchini? Na unapouleta, unampelekea nani?”

Isaack akameza kwa mate alafu akaongea akiwa anatetemeka.

“Nimeanza miaka mitano iliyopita. Nahonga vyombo vya usalama na wao ndio wanaonipitishia, bandarini au uwanja wa ndege.”

“Na soko?”

“Soko langu hasa hasa ni vijana. Pia napeleka kwa wale vijana ambao wapo kwenye kambi zetu za mafunzo.”

“Mr Kim Salvatore ni nani kwako?”

“Simjui.”

Njemba mwenye bunduki akanyanyua mkono wake uliobebelea silaha. Isaack akapayuka:

“Nasema! Nasema! Nakuomba usifyatue! Nasema!”

“Mr Kim Salvatore ni nani kwako?”

“Ni boss wangu. Yeye ndiye mkuu wetu.”

“Na wewe una nafasi gani kwake?”

“Mimi ni wakala. Nahusika kusajili wale wote wenye ngozi nyeusi Tanzania kujiunga na jeshi la Mr Kim.”

“Vipi kuhusu mtandao wenu hapa Tanzania, ni mpana kiasi gani?”

“Hakuna sekta ambayo hakuna mtu wetu. Zote zina mtu wetu kwa njia moja ama nyingine. Tafadhali naomba niende hospitali, nimepoteza damu nyingi mno.”







Njemba mwenye bunduki akatikisa kichwa kukataa.

“Hakuna haja ya kwenda hospitali wakati utakufa tu. Nashukuru sana kwa ushirikiano wako, kwa sasa unaweza ukapumzika kwa amani.” Alisema njemba mwenye bunduki alafu akahitimisha uhai wa bwana Isaac kwa kumdidimizia risasi kwenye paji lake la uso.

Video ya kila kitu kilichotokea ndani ya nyumba ya bwana Isaack ikasambazwa kwenye mitandao ya jamii, watu wakatumiana kama bidhaa. Hatimaye ikachukua nafasi mpaka kwenye vyombo vikubwa vya habari. Mwisho wa video maandishi mekundu yalijiandika yakiuliza: Who’s next?

Baada ya siku mbili:

Uso wa bwana Wyne ulikuwa mwekundu. Alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake kubwa maeneo ya Masaki akiwa kabebelea sigara kubwa. Saa yake kubwa ya ukutani yenye rangi ya kijivu na urembo wa maua ilikuwa inasema ni saa tisa huku mshale wa dakika ukiwa katikati ya namba tano na nne. Palikuwa patulivu sana kiasi kwamba hata nzi akikatiza inakuwa ni kelele kubwa. Ila punde sauti ya honi ya gari ikaharibu utulivu huo. Ndani ya dakika chache wakaingia watoto wawili wa kike waliovalia sare za shule, kwa makadirio ya miaka saba kwa kila mmoja, walimparamia bwana Wyne wakipayuka:

“Daaaddyyy!”

Bwana Wyne akawatizama kwa sura kavu isiyo na mapokezi.

“Go change your clothes, faster!”

Watoto wakanywea. Wakiwa wameelekeza sura zao chini waliondoka kuelekea chumbani. Bwana Wyne akaendelea kuvuta sigara yake kubwa kwa hisia. Alitoa simu yake akaipachika namba na kuita.

“Borg, for how long should I wait for the number? … Send me the number immediately!” Wyne alifoka akakata simu. Baada tu ya muda mfupi, ujumbe ukaingia kwenye simu ya Wyne, namba za mawasiliano zikiwa na jina la ‘White Mask’. Wyne akapiga hiyo namba.

“Hey Whitey! … Please I need your help … You know what has been happening to our crew at this time, we are at risk, please protect me and my family, I need your assistance … Okay, thanks.”

Wyne alipokata simu akatabasamu. Alitegemea sasa kuanzia muda ule kikosi cha ulinzi kitakuja na kumuhakikishia usalama. Aliweka sigara yake kubwa kwenye ki-sahani maalum alafu akajilaza kwenye kochi. Bakari alitua simu mezani akawatizama Kaguta, Vitalis, Jombi na Miraji, akawaambia:

“Mnaweza mkaenda sasa. Anahitaji ulinzi toka kwa wenzake.”

Baada ya dakika kadhaa wanaume wakavalia suti kali, wakajiweka kwenye defender moja kwa moja mpaka getini kwa Bwana Wyne.Walipofika mlinzi akataka maelezo.

“We are here for the sake of protecting Mr Wyne.” Miraji alieleza kifupi. Mlinzi akapiga simu ndani kumuuliza mkuu wake kama ana miadi, Bwana Wyne akamtaka awaruhusu, WAGENI wakaingia ndani.

“Karibuni sana. Karibuni!” Bwana Wyne aliongea kwa lafudhi ya kimarekani.

“Ahsante sana.” Vitalis akasema huku wakiketi.

“Nilikuwa navategemea kujha.” Wyne aliongelea puani. “Lakini sikujua kama mtawahi. Mpo njema kweli.”

“Yah! Tupo njema kweli. Hii ni kazi yetu na tunaipenda.”

“Nafurahi kusikia.” Wyne akajibu, “Natumai mtahakikisha nakuwa salama na family yangu. Hali imekuwa very worse nowadays. I wonder nani anafanya haya.”

Hakuna aliyemuongelesha. Kaguta alinyanyuka akapanda juu ya meza na kufunga kamba yenye kitanzi hapo. Vitalis akatoa bunduki nyuma ya kiuno chake akamnyooshea bwana Wyne. Miraji akatoa vinyago akawakabidhi wenzake. Miraji akatoka nje kwenda kumalizana na mlinzi na kuteka kamera.

“What’s happening?” Wyne alitahamaki. Kaguta, Vitalis na Jombi wakamtazama wakiwa tayari wamefichama sura zao kwenye vinyago. Miraji aliporudi akawasha kamera na kuanza kurekodi.

“Leo ni zamu yako kutembelewa na wageni, bwana Wyne.”

“What the **** is this? Nyie ni nani? Mnataka nini?” Wyne aliuliza kwa mkupuo na sauti yake inayopitia kwenye tundu za pua.

“Sisi ni WAGENI. Ulidhani unaweza kutukwepa? … Pole sana, sisi hatuhitaji mualiko.”

Vitalis alisema alafu akamtizama Kaguta. Kaguta akaenda vyumbani kufunga milango yote na komeo ikiwemo na chumba walichopo watoto.

“Tell me what you want. Nitawapa. Msiniuwe!” Wyne aliongea kwa huruma.

“Tunataka tu taarifa.” Vitalis alisema kwa ufupi. “We need only information from you.”

“Nitawaambia everything. But don’t kill me as you did kwa Mr Isaack.”

“Isaack tulimuua kwasababu alijifanya mjanja. Hakuweka wazi kila taarifa na alithubutu kutaka kutudanganya. So if you don’t wanna die, be honest.”

“I will! Kweli kabisa.”

“Wewe ni nani kwa Mr Kim Salvatore?”

“Just agent. Nipo kama kiongozi wa white people wote ndani ya Tanzania.”

“Najua mbali na agency, kuna kazi mnakuwa mnafanya. Wewe majukumu yako mengine ni yapi?”

Wyne akasita kidogo kujibu. Kaguta akamnyanyua na kumsimamisha juu ya meza, akamvesha kitanzi.

“I will answer.”

“Then do it before it’s too late.” Vitalis alitishia. Bwana Wyne akafungua mdomo wake kusema:

“Apart for being agent. Pia nafanya kazi ya porching, ujangili. Natafuta meno ya tembo, vifaru na ngozi za wanyama then I transport kwenda kwenye ghala ya Kim.”

“Kampuni yako inaitwaje?”

“Deep Africa wildlife.”

“Na huwa unashirikiana na nani kufanya your deals successful?”

“Katibu ya wizara ya maliasili.”

“Okay. Thanks for your information.”

Vitalis alinyanyuka akamtizama Kaguta na kumpa ishara ya kumtikisia kichwa. Kaguta akatengua meza iliyombeba bwana Wyne. Kitanzi kikadaka koo la mzungu huyo na kuling’ang’ania mpaka pumzi ikakata. Wakafanya msako ndani ya chumba cha bwana Wyne wakabeba baadhi ya nyaraka, wakaondoka.

Baadae video ikaanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii mpaka kwenye luninga zikiwa zimeambatana na picha za nyaraka za bwana Wyne. Ndani ya muda mfupi katibu wa maliasili akakamatwa, kampuni ya Deep Africa ikafungiwa kwa uchunguzi, wahusika wa ulinzi bandarini na kwenye uwanja wa ndege wakasimamishwa kazi na kusekwa ndani kwa upelelezi zaidi.

Swali likazuka: nani atakayefuata kutembelewa na WAGENI? Hakuna yeyote aliyejua nani atafuata, mitandao ya kijamii ilikuwa inatizamwa mara kwa mara. Matumbo ya wafanyakazi wa serikali yalipashwa joto. Polisi walitangaza donge nono kwa yeyote atakayetoa taarifa ya upatikanaji wa WAGENI kwa kigezo cha kuvunja sheria kwa kufanya mauaji.

Japokuwa hakuna mwananchi aliyebashiri nani atakuwa mhanga ajaye wa WAGENI, bwana Rajesh Deepti yeye aliona ndiye atakayefuata pasi na shaka. Kila kitu chake alichokihitaji kiliwekwa ndani ya mabegi. Akiwa na miadi ya kupaa na ndege ya jioni na muda ukiwa umebakia masaa manne, alishasimama mbele ya geti lake kungojea taksi. Muda tu mfupi taksi ikafika, akaweka mabegi yake na kumuamuru dereva aelekee Mwalimu Nyerere Airport haraka sana. Wakati dereva anaendesha akawa anaongea na simu.

“Yes, I’m on my way to Airport now. I’m heading directly to New Delhi, India. Okay see you!”

Alikata simu akairejesha mkobani. Alitoa tiketi yake ya ndege akaitizama kisha akairudisha mkobani. Akashusha pumzi ndefu. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa taksi ikakunja kona na kuacha barabara kuu. Rajesh akawaka:

“Hey! Nimekuambia twende Airport. Wapi unaenda huko?”

Mwendo kasi ukazidi kuongezwa kuelekea maporini. Rajesh akatoa simu yake mfukoni, taksi ikapiga breki kali simu ikadondoka chini, Rajesh akajigonga kwenye kiti cha mbele kwanguvu. Dereva taksi akashuka akaenda viti vya nyuma, kumbe alikuwa ni Kaguta, alimpiga Rajeshi kichwani na kitako cha bunduki, Rajesh akazirai.

Baada ya masaa mawili Rajesh alirejewa na fahamu akajikuta yupo kwenye kiti kilichozungushiwa nyaya uchi za umeme. Alikuwa amebanwa haswa kufurukuta hawezi. Mbali yake hatua kama tano, kulikuwepo na kebo ya umeme. Bernadetha pamoja na Vitalis walitokea wakajongea karibu yake. Bernadetha akamuuliza:

“Nadhani unakumbuka hii sura.”

Rajesh akabinua mdomo wake kwa dharau pasipo kusema kitu.

“Leo utakuwa mwisho wako. Kama wageni ni wako, ni wako tu. Huwezi kuwakimbia.” Alisema Bernadetha alafu akaondoka zake akimuacha Vitalis ambaye aliungana na Miraji baada ya muda mfupi akiwa amebebelea kamera.

Siku ikaenda. Kesho yake ikakaribishwa kwa kusambaa kwa video za mauaji ya Rajesh kwenye kiti cha umeme. Huku taarifa zake za uwakala wa watu wa Asia na kuwa kwenye kitengo cha sayansi na tiba zikitapakaa. Akiwa mshiriki mkubwa wa kuua watu makusudi kwa dhumuni la kufanyia tafiti madawa yao na huku maiti zikisafirishwa kwenda nchi mbalimbali zikiwa zimepandikizwa madawa ya kulevya.









MAHAYAWANI WAKAWA WAMEENDA NA MAJI.







*** SHETANI MPYA ***





Ilikuwa usiku wa saa mbili wakati Vitalis akiwa sebuleni anatizama taarifa ya habari runingani. Baada ya taarifa moja kukatiza ikiwa inaongelea ziara ya raisi wa Tanzania nchini China, ilifuatia taarifa iliyogutusha uso wa Vitalis. Aliona picha yake kwenye kioo cha runinga huku maelezo yakielezwa kama mshutumiwa nambari moja wa mauaji yaliyotukia ndani ya muda mfupi, waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa ameuwawa kwa kudidimiziwa kisu shingoni.

La haula!

Kitambulisho cha kazi cha Vitalis kilionyeshwa na kamanda wa kanda maalum akisema kwamba kimepatikana eneo la tukio. Na mtuhumiwa anashukiwa anaweza kuwa mhusika wa kundi linalotafutwa kwa udi na uvumba, WAGENI.

Vitalis alisimama akiwa ameshika kiuno na macho yake yakiwa yametoka nje. Alizunguka sebuleni kwa hatua kadhaa akienda na kurudi. Taarifa ya habari ilikuwa imepita na zingine zaendelea lakini kichwani kwake bado alikuwa anasikia jina lake kama mtuhumiwa wa kwanza kwenye mauaji ya mtu mkubwa serikalini.

“Nani kaniset kwenye haya mauaji? … Wametoa wapi kitambulisho changu? Ila si alikichukua OCD? …Kwanini waziri wa mambo ya nje?” Maswali yalimtafuna Vitalis.

Wakiwa kwenye kikao juu ya jambo hilo la mauaji, Bakari alitoa maono:

“Itatulazimu twende eneo la tukio, tunaweza tukapata jambo huko likatusaidia kusafisha jina lako kwa watu.”

“Ila unadhani itakuwa ni rahisi?” Jombi aliuliza, “Hilo eneo bila shaka litakuwa kwenye uangalizi mkubwa.”

“Si lazima tuingie eneoni.” Bakari alisema na kuongezea kwa kuuliza, “Kwani makazi ya marehemu ni wapi?”

“Msasani, ama tunaweza sema mpakani mwa Msasani na Oysterbay.” Vitalis alijibu. Bakari akavuta tanakilishi yake na kwenda kwenye ramani moja kwa moja, Vitalis akamuonyeshea makazi ya marehemu kwa kidole.

“Hapa!”

Bakari akatikisa kichwa, akavuta picha kwa ukaribu na kuitizama kwa umakini huku wenzake wakiwa wanamngojea aseme kitu.

“Tunaweza tukapata data.” Bakari alisema huku akihamisha macho yake toka kwenye tanakilishi mpaka usoni mwa Vitalis. “Pembeni kidogo ya jengo la makazi ya marehemu kuna duka kubwa la vifaa vya kisasa vya kompyuta.”

“Kwahiyo?” Miraji alidakia.

“Kwahiyo jengo kama hilo ni lazima tu litakuwa na kamera za ndani na nje. Tutatumia kamera za nje kutizama juu ya hilo tukio kwa kuzingatia muda wa tukio tuone kuna wageni gani walitembelea hapo muda mfupi kabla ya tukio.”

“Ni wazo zuri.” Sandra alichangia, “ila inabidi pia tufanye juhudi ya kuingia ndani, kuna mambo ambayo hatuweza kuyapata kwa kamera pekee.”

“Nitafanya hiyo kazi.” Vitalis alihakikisha, “Kazi hiyo kamera nitakuachia Bakari, Miraji na Jombi, najua hamtoniangusha.”

Saa nane mchana gari lililowabebelea Jombi, Bakari na Miraji lilitua kwenye kiwanja cha duka kubwa la vifaa vya tanakilishi. Wanaume walishuka wakiwa wamevalia ovaroli na kapero za bluu. Ndani ya dakika chache wakafika eneo la ulinzi, wakaketi kwenye viti nyuma ya tanakilishi zote za kamera baada ya kuwafunga wahusika midomo, mikono na miguu.

Bakari alirudisha video nyuma akaanza kuangalia yaliyotukia jana mida ya saa kumi ya jioni kwa mujibu wa kamera za nje zilizokuwa zinatizama jengo la marehemu waziri. Katika wasaa huo kwenye dakika za ishirini, wakaona gari aina ya Mark X nyeusi ikiwa inaingia ndani. Bakari alisimamisha video alafu akaivuta kwa ukaribu zaidi taratibu taratibu, akaandika chini namba za usajili na tarakimu: 25119-20, zilizokuwa zimeandikwa kwenye stika upande wa kushoto wa kibao cha usajili. Alijaribu kuvuta picha zaidi na zaidi lakini hakuona nyuso za waliomo ndani.

Baadae wakiwa ndani ya nyumba ya Vitalis, Bakari akaonyesha yale waliyoyapata. Vitalis aliweka karatasi ya nailoni mezani ndani yake kukiwa na risasi mbili na sigara kubwa.

“Haya ndiyo ambayo nimeweza kuyaokoteza ndani ya uzio wa nyumba ya marehemu.”

Bakari alishika karatasi ya nailoni akaipeleka machoni kwake kwa ukaribu. Aliitizama riboni kubwa nyeupe iliyoizunguka sigara ile kubwa, akasoma maandishi yaliyoandikwa hapo.

“Lugha gani hii?”

Kaguta alichukua huo ushahidi akausoma.

“Ni kiitaliano.” Alisema na kuongezea, “Imetengenezwa Italy, ni sigara ya watu wa daraja la juu.”

Bakari alipokea tena ushahidi huo akaupiga picha kisha akasogelea tanakilishi yake na kuiunganisha na kamera. Akatafuta majibu ya sigara mtandaoni.

“Hiyo sigara uliikuta wapi Vitalis?” Bernadetha aliuliza.

“Mlango wa kuingilia sebule ya marehemu.” Vitalis akajibu.

“Kwanini unadhani inaweza ikatusaidia?”

“Kwasababu naamini ni lazima itakuwa imeachwa na wauaji. Sidhani kama mwenye nyumba anaweza akavuta sigara na kuitupia mlangoni kwake.”

“Ni kutoka Italy!” Sauti ya Bakari ilipasua anga, wote wakamtizama. “Inatengenezwa Italy na inasafirishwa kwenda nchi chache sana Afrika. Wateja wake wengi wapo Ulaya na Marekani. Ni ghali mno, na ndio mana inachukuliwa kama ni ya watu wa tabaka la juu.”

“Kwahiyo kwa Tanzania inapatikana wapi?” Vitalis alidadisi.

“Kuna wakala mawili tu wanaouza hizo sigara kwa Dar es Salaam. Wote wapo Posta, wanauza pia na vinywaji vikali kama vile spirits, wines na whisky.”

“Nataka hayo maduka yafuatiliwe. Tupate majina ya wateja na makazi yao. Bakari, Jombi na Miraji, hiyo kazi naacha mikononi mwenu. Sandra na Kaguta nitawataka kesho muende msibani, Sandra, nitataka uwe karibu mno na mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu, mchimbe unavyoweza. Najua tutapata kitu toka kwake. Naamini unaweza.”

Baada ya kupeana majukumu, walikula na kunywa. Kaguta na Sandra wakaondoka. Vitalis alitoka nje kuvuta hewa safi, Jombi akamfuata huko.

“Hatujapata muda wa kuongea tokea nimetoka maeneoni, mkuu.” Jombi alisema huku akitizama tizama mazingira. Vitalis alitabasamu akasema:

“Ni kweli.” Alivuta pumzi ndefu na matundu yake ya pua, akamgeukia Jombi.

“Naomba unipe mrejesho wa miradi. Inaendeleaje?”

“Inaendelea vyema tu. Baada ya kuwekeza pesa ile tuliyoikwapua kwa Isaac na Mr Wyne, imefufua na kuipa nguvu kubwa. Kwa sasa faida ni kubwa. Tunaweza tukafanya mambo yetu pasipo na shida kabisa.”

Vitalis akatabasamu.

“Hongera sana! Sasa tuna kazi moja tu ya kuusogeza huu mlima mbele yetu, baada ya hapo kila mtu akaishi maisha yake.”

“Tutaweza tu. Dhamira safi siku zote hushinda.” Jombi alikazia uzi.

Gari safi Toyota Rav4 modeli mpya rangi ya kijivu ilisimama kando kando ya uzio mkubwa wa nyumba ya marehemu waziri. Magari yalikuwa mengi mno watu pia. Sandra na Kaguta walishuka toka kwenye Rav4 wakiwa wamevalia nguo nyeusi na miwani ya rangi hiyo hiyo. Wakiwa wanaongozana wakaingia ndani na kuketi kwenye mojawapo ya viti vilivyokuwa vimetandazwa uwanja mzima. Shingo zao zilizungusha vichwa wakitizama kule na kule, Kaguta akamgusa Sandra.

“Yule pale.”

Alionyeshea kwa kutumia kichwa chake. Sandra akaelezea uso wake kule alipoonyeshewa, akamuona mwanaume mmoja mwenye uso mchanga wenye ndevu zilizojaa kidevuni.

“Anaitwa Morris. Ndiye tageti yetu.” Kaguta alieleza. Sandra akataka kunyanyuka, Kaguta akamzuia.

“Ngoja kwanza tusome mazingira.”

Waliendelea kutizama huku na kule. Kaguta akawaona wanaume wanne waliovalia suti na miwani zenye vioo vyeusi. Masikioni mwao walikuwa na viwaya vyeupe vilvyokuja mpaka mdomoni. Kazi yao ilikuwa kuperuzi peruzi huku na huko. Kaguta aliingiza mkono wake mfukoni akatoa miwani. Aliibinua akawatizama wanaume wale kwenye kioo akawaona kwa ukaribu zaidi, shingoni mwao walikuwa na tarakimu 25119-20.

“Utakapoenda, hakikisha unakuwa makini kuwatizama wale watu. Inaonekana wapo hapa kwa malengo fulani kinyume na ya kwetu.”

“Sawa.”

Sandra alinyanyuka akasogea mbele kidogo. Akasogea tena na tena kila alipoona walinzi hawamjali, mwishowe akamfikia Morris. Alimpa mkono wa kuume akisema:

“Pole sana, Morris.”

“Ahsante, nishapoa.” Morris aliitikia huku uso wake ukiwa umebebelea ka-wasiwasi.

“Samahani. Nakujua?” Morris aliuliza.

“Sidhani kama unanijua.” Sandra alijibu. “Ila mimi nakujua, wewe ni mtoto wa kwanza wa Mheshimiwa Johnson Machibya, aliyekuwa mfanyakazi mwenzangu kipindi tunafanya kazi pamoja ubalozini Australia. Ndani ya ofisi yake alikuwa ana picha kubwa ya familia yake, na huko ndipo nikaona uso wako, hata nilipokuona hapa nikakutambua.”







Morris alitabasamu kidogo, akauliza:

“Na wewe je, unaitwa nani?”

“Dakota.” Sandra akajibu, “Dakota Sean.”

“Okay. Karibu Tanzania.”

“Nipo Tanzania kwa miaka mitatu sasa, sistahili kukaribishwa. Ila sasa naona mahitaji makubwa ya kurudi Australia.” Sandra alieleza.

“Mahitaji gani?” Morris akauliza.

“Upungufu wa amani nchini kwetu - inantisha sasa. Kama mfanyakazi mwenzangu ameuwawa kiukatili hivyo nani anajua atakayefuata? Kama ni mimi?”

“Unadhani suluhisho ni kukimbia tatizo?” Morris aliuliza huku akimtizama Sandra. Wakati wanaendelea kuongea, Kaguta akaona walinzi ndani ya suti wakimtizama Sandra. Punde wakapeana habari na kuanza kuchukua hatua kuelekea alipo mlengwa wao kwa hatua kubwa kubwa. Kaguta alimuita Sandra kwa kunong’oneza lakini haikusaidia. Ilibidi atumie njia mbadala. Alidondoka chini akaanza kujirusha rusha kama mtu mwenye kifafa huku akitoa sauti ya kugugumia. Watu wote walitekwa na hilo tukio. Walinzi wakamsahau Sandra kwa dakika na kumkimbilia Kaguta.

Baada ya dakika kama mbili Kaguta alitulizana na kuwaomba radhi walinzi kwa usumbufu, walinzi walimuacha wakaenenda kwa mlengwa wao, Sandra, ila walipofika walimkuta mtoto wa marehemu pekee, Sandra hakujulikana wapi alienda. Walinzi walipomrudia Kaguta naye hawakumkuta, alishayoyoma. Wakabaki kwenye mduwazo.

Ndani ya Rav4 Kaguta na Sandra walijiweka wakatoka eneo la msiba. Wakiwa njiani wakawa wanateta:

“Vipi umefanikiwa?” Kaguta aliuliza.

“Ndio. Nimempatia namba yangu. Anaonekana ana kiu ya kutaka kufanya kitu juu ya kifo cha baba yake.”

“Safi sana.”

Walinzi walitoka nje kutizama kwenye paki ya magari, napo hawakuona gari lolote lililotoka, Kaguta na Sandra walikuwa tayari wameshapotea. Walinzi walitizama kushoto na kulia wasione kitu, wakaamua kurudi ndani ya uzio.

“Tumepata orodha ya wateja toka kwenye duka moja la sigara.” Bakari alimwambia Vitalis wakiwa wameketi sebuleni pamoja na wahusika wote wa kundi la WAGENI.

“Katika orodha hiyo wateja wa Dar wapo wawili tu, waliobakia wote ni kutoka Arusha wateja wengi wakiwa ni watalii.”

“Na vipi kuhusu duka la pili?” Vitalis aliuliza.

“Hatukuangaika nalo maana wao ni wakala tu wa kupokea sigara hizo na kuzipeleka Zambia na Uganda. Hawasambazi hapa Tanzania.”

“Sawa. Hao wateja wawili nahitaji uwafuatilie zaidi na tufahamu nani anahusika na hayo mauaji. Sawa?”

“Sawa. Hesabia kama tayari.”

Siku iliyofuata wasaa wa mchana Sandra alikuwa na Kaguta mgahawani wakipata chakula cha mchana huku wakilonga hili na lile. Haikuchukua muda mrefu kabla ya simu ya Sandra kuita, namba mpya kiooni. Sandra akapokea:

“Haloo! … Okay okay, nakuja.”

Alipokata simu akamtizama Kaguta.

“Morris anataka tukutane sasa hivi, acha niende.”

“Poa, see you!”

Muda mfupi tu baadae Sandra akawa ameketi na Morris kwenye uwanda wa nyasi kijani kibichi.Mkononi mwa kila mmoja wao kulikuwa kuna kinywaji kilaini rangi ya maji ya machungwa.

“Sijui nani wa kumuamini, kuna baadhi ya mambo nakinzana kabisa na jeshi la polisi.”

“Unaweza ukaniamini mimi. Tunaweza tukawatumia Interpol kama polisi hauwaamini. Ni mambo yapi unayokinzana na polisi?”

“Wanadai aliyefanya tukio ni mtu aliyeacha kitambulisho eneo la tukio. Sidhani kama ndiye.”

“Unadhani ni nani?”

“Mida ya saa kumi ya jioni tulivamiwa na watu watatu wakiwa wamevalia suti na vinyago usoni. Mmoja wao alikuwa anavuta sigara kubwa. Walimuua mlinzi na kumuweka baba chini ya ulinzi, wakamuuliza kama kuna mtu yeyote ndani, akajibu hapana. Walifanya msako lakini hawakunipata nilikuwa nimejificha nyuma ya kabati. Hawakuchukua chochote zaidi ya kumuua baba kwa kumchoma kisu shingoni - nilipata kushuhudia kwa macho yangu mwenyewe. Walipomaliza wakaondoka zao, mmoja wao akatupa kitambulisho kwa makusudi kabisa.Nadhani lengo lao lilikuwa ni kum-frame huyo anayetafutwa sasa.”

“Unaweza ukaniambia muonekano wa hao majambazi watatu?”

“Walikuwa wanaume warefu, mmoja wao alikuwa mrefu zaidi na mwenye mwili mpana, kinyago chake cha usoni kilipoishia ilitokezea alama ya kovu la kisu pembeni ya sikio. Ndiye aliyekuwa anavuta sigara na ndiye huyo aliyemchoma baba kisu cha shingoni, na ni yeye ndiye aliyewaamuru wenzake waondoke.”

Morris alinyamaza kimya huku macho yake yakiwa yanalenga machozi. Alitoa simu mfukoni akamkabidhi Sandra.

“Hii ni simu ya baba - password yake ni 18821. Kabla hatujavamiwa nilimsikia anaongea na mtu dakika chache tu nyuma. Inaweza ikasaidia kwenye upelelezi.”

Sandra aliitizama ile simu akaiweka mkobani.

“Ahsante. Ila sasa nahitaji namba yako.”

Morris alimpa namba Sandra, Sandra akainakili kwenye simu yake kisha wakaagana.

“Nitakutaarifu kila nyendo.”

Sandra alimtoa shaka Morris.

“Naamini itakuwa hivyo. Hakikisha inakuwa siri, nahisi kuna watu wananifuatilia.”

“Sawa, Morris.”





Saa tatu na nusu usiku:



Sandra alimkabidhi simu Bakari, akamwambia:

“Hiyo ni simu ya marehemu. Kuna mtu aliwasiliana naye kabla ya tukio, unaweza ukatizama.”

Bakari alipokea simu akaiweka mezani kisha naye akalonga kuwaambia wenzake:

“Tumepata mtu ambaye tunahisi ndiye mlengwa wetu.” Alimeza mate alafu akaendelea:

“Kati ya wale watu wawili, kuna mmoja ambaye ndani ya uzio wa nyumba yake kuna magari mawili yenye tarakimu sawa sawa na zile ambazo zilikuwa ubavuni mwa gari linalohusika na tukio la mauaji – 251 19-20.”

“Maeneo gani?” Kaguta aliuliza.

“Kijitonyama.” Bakari akajibu.

“Tupo pazuri sasa.” Vitalis akasema, “Ila kwanza track hiyo namba ya mwisho kuongea na waziri. Nataka kufahamu inapatikana maeneo gani. Endapo ikirandana na hilo eneo basi huyo ndiye mlengwa wetu. Kama sio, basi sio yeye, itakuwa tu ni watu wengine wanaoshabihiana nao kidhalimu.”

“Naomba nifanye hiyo kazi sasa.”

“Sawa, hakuna shida.”

“Kuna yeyote mwenye uelewa kuhusu tarakimu hizo zilizo kwenye gari na miili ya hawa watu?” Vitalis aliuliza. Hakuna aliyejibu.

“Inabidi tujue. Kuna kitu kitakuwa kimejificha nyuma ya hizo tarakimu.” Vitalis alisema kisha soga zingine zikachukua nafasi huku Bakari akiperuzi kwenye tanakilishi yake. Baada ya muda Bakari akapiga ngumi hewani.

“Zina-match!” Alipayuka. Vitalis akasogea karibu.

“Namba ya simu inarandana na hilo eneo!” Bakari alisema kwa furaha, “Patakuwa ndio penyewe!”

Vitalis akatikisa kichwa.

“Sasa tunavamia ama?” Kaguta aliuliza.

“Hapana.” Vitalis aliwahi kujibu. “Inabidi kwanza tusome hilo eneo kwa muda kama wa wiki, tujue nani anaingia nani anatoka, wapo wangapi, ulinzi upoje, na wapi tunaweza tukapatumia kuingilia.”

“Tutafanyeje sasa kufanya yote hayo?” Bernadetha aliuliza.

“Kwa kupeana shift ya kutembelea eneo hilo. Eidha kwa njia ya kufanya mazoezi, ama mpita njia, ama mkazi jirani.” Vitalis alijibu.

Kuanzia siku iliyofuata vikaanza kutekelezwa vilivyopangwa - Sandra na Bernadetha wakawa wanapita kila siku asubuhi wakifanya mazoezi. Bakari, Jombi, Miraji na Kaguta wakawa wanagawana majukumu, leo ikiwa mpita njia kesho utakaa kando kusoma gazeti, ama kufanya mzozano wa mpira ama tamthilia kando kando ya nyumba. Wiki moja ilipopita wakapeana taarifa.

“Eneo lina ulinzi. Walinzi wawili mpaka watatu wanalinda geti kwa siku na wanapeana zamu kila asubuhi.” Bernadetha alisema.

“Magari yanayoingia hapo ndani ni Mark X nyeusi tu, ikiwemo lile linalohusika na mauaji.” Kaguta alitoa taarifa.

“Ila ndani ya juma kuna siku mbili ambapo gari la kuleta sigara laja. Kama tunataka kuingia ndani huo ndio mwanya mzuri.” Miraji alichangia.

“Hapana, bado hatuwezi kuvamia hilo eneo.” Vitalis alitoa angalizo, “Yatupasa turudi kwa Alwatan Kombo. Yatupasa tufahamu nini kinachounda huyu mnyama, nyoka, kama vile tulivyofanya kwa lile jitu. Tusipofanya hivyo, hatuwezi kufanikiwa abadani.”

“Wazo zuri. Lini tunaenda?” Kaguta alichombeza.

“Kesho.” Vitalis akajibu.



Saa sita na dakika mbili mchana siku iliyofuata:



Kaguta na Vitalis aliyekuwa amevalia kofia kubwa ‘cowboy’ walikuwa wapo eneo la nyumba ya Alwatan Kombo. Milango yote ilikuwa umefungwa na kufuli kubwa. Hata ndani kulikuwa kweupe pe! Kaguta alipopaza sauti yake kuita dirishani alijibiwa na mwangwi mkavu.

Walisogea nyuma ya nyumba kwenda kufuata kijumba cha kazi cha Alwatan Kombo, wakakuta nacho kimefungwa. Majani yalikuwa yameota mpaka mlangoni. Walivunja mlango wakaingia ndani, wakakuta kumejazwa na majani, hata ukuta ukiwa umefifia na michoro haionekani. Walipangusa pangusa ukuta kwa mbali wakaona mchoro wa nyoka.

“Huu hapa!” Vitalis aliropoka. Waliutizama vyema mchoro wakaona kwa mbali kuna visu tisa juu ya kichwa cha nyoka huyo mwenye vichwa vitatu. Ila ghafla wakasikia sauti za watu huko nje.

Wanaume watano waliovalia suti walikuwa wamebebelea bunduki mikononi wakirusha macho yao huku na huko. Waligawana wawili wakaelekea kushoto na watatu wakaelekea kulia. Wote walikuja kukutana kwenye kijumba, walipoingia ndani hawakukuta mtu. Walipekua pekua huku na huko ila hawakuona yeyote.



Saa nane mchana:



Kaguta na Vitalis walifika nyumbani wakamkuta Bakari akiwa ameketi kwenye tanakilishi yake. Vitalis alivua kofia akairushia kwenye kochi, wakamjulia hali Bakari.

“Kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu.” Bakari aliwaambia huku akimkabidhi simu Vitalis.

“Aliyetuma huo ujumbe ni yule yule tuliyem-track!” Vitalis alijazishia habari. Kaguta na Vitalis wakausoma ujumbe … WE ARE IN THE WAR: HUNT OR BE HUNTED. Vitalis alishusha pumzi ndefu, Kaguta akamuuliza Bakari:

“Unaweza ukaniambia huyu jamaa yupo wapi kwa sasa?”

“Ndio. Yupo nyumbani kwake.”

“Gari la sigara huwa linapita kila lini hapo nyumbani kwake?”

“Jumanne na Alhamisi.”

“Tunaenda kuvamia!”

“Hapana!” Vitalis akadakia. “Hatutakiwi tuwe na haraka kiasi hiko, Kaguta. Tuwe na plan kwanza!”

“Tukichelewa wataanza wao ku-hit!” Kaguta alitoa angalizo.

“Na tukiwahi bila ya plan tutaishia wapi?” Vitalis aliuliza, Kaguta akabakia kimya.

“Kwanza tunatakiwa kujua, maana vichwa vitatu vya nyoka ni nini? Na maana ya visu tisa pia. Na zile tarakimu pia. Tukifahamu hivyo, tutakuwa tuna nafasi kubwa ya ushindi.”

“Sawa.” Kaguta akaitikia.



Siku iliyofuata mshale wa saa kumi na mbili asubuhi:



Kaguta na Vitalis wakiwa wamevalia traksuit na makoti ya hood walikuwa wanafanya mazoezi ya kukimbia. Vitalis alikuwa amevalia kofia ya koti uso wake ukiwa chini huku Kaguta akiweka kichwa chake wazi na akitizama mbele. Haikuchukua muda mrefu lilitokea gari aina ya van kwa kasi likasimama mbele wakashuka wanaume watano waliobebelea bunduki, wakawateka Kaguta na Vitalis, gari likatokomea.

Zilipita siku mbilia Vitalis na Kaguta hawakuonekana wala kujulikana walipo. Bakari pamoja na wenzake wakamezwa na maswali.

“Sasa tunafanyaje?” Bernadetha aliuliza.

“Tatizo ni kwamba hatujui tunawatafutia wapi!” Sandra alijibu kwa kuduwaa.

“Inabidi tuitafute ile namba. Ni wao pekee ndio watakuwa wanahusika, hakuna mwingine. Mnakumbuka ule ujumbe niliowaonyesha?” Bakari aliuliza alafu akaendelea:

“Ama twende tukavamie nyumba yao.”

“Una uhakika gani watakuwa wamewaweka humo?” Jombi aliuliza. Wote wakawa kimya kwa muda kabla Bakari hajatizama vibonyezeo vya simu yake Nokia tochi kwa sekunde kadhaa kisha akachukua peni haraka na kuanza kuandika kitu kwenye karatasi. Aliandika: ‘BEAST’ alafu akawaonyeshea wenzake.

“Ndio nini?” Jombi aliuliza.

“Maana ya tarakimu: 251 19-20.” Vitalis akajibu. “Hizo namba walizoziweka hapo zina maana ya BEAST, yani mnyama. Badala ya kuandika herufi, wao wakatumia namba za herufi. A = 1, B = 2, C = 3 na kuendelea. 2 maana yake B, 5 maana yake E, 1 maana yake A, 19 maana yake S, na 20 maana yake T.”

“Sasa itatusaidiaje kuwapata wenzetu.” Jombi aliuliza. Sandra akalipuka:

“Najua! Najua walipo!”

“Wapi?”

“Kuna jengo! … Kuna jengo kubwa njiani kuelekea Arusha. Nakumbuka Isaac alishawahi kunionyesha kwa mbali. Limeandikwa BEAST kwenye paa. Isaac aliniambia ni sehemu ya mateso na mateka, ila yeye mwenyewe hawezi kufika huko!”

“Na ni kwasababu hakuwa kwenye kundi la nyoka!” Bakari alidakia.

“Twendeni!” Miraji akapaza sauti.

Jengo la BEAST lilikuwa maili kama thelathini toka ulipo mkoa wa Dar Es Salaam. Lilikuwa ni jengo pweke lisilo na jirani isipokuwa tu uwanda wa msitu na vichaka. Ukuta mkubwa na mrefu ulikuwa umelizunguka jengo hilo pamoja na geti refu jekundu. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anafahamu nini kinachoendelea ndani ya jengo hilo isipokuwa tu wahusika. Hakuna unyama ambao uliachwa kutendeka ndani ya jengo hilo ambalo halikuwahi kushuhudia mateka yeyote akitoka na pumzi yake aliyoingia nayo. Kilikuwa ni kiwanda cha kupokonya uhai wa watu na kuwageuza wafu waliofukiwa kwenye mashimo kadhaa yalikuwa umbali mdogo tu na jengo hilo. Baada ya muda mashimo hayo yalifukuliwa na kutoa mbolea ambayo ilichanganywa na madawa kisha kusafirishwa nje ya nchi. Ni ngumu kuyafahamu yote hayo kutokana na ulinzi mkali unaobana eneo hilo. Ni jengo pekee tena likiwa limekaa mbali na barabara hivyo kufanya usalama kuwa imara tangu kunawapa fursa walinzi kutizama pande zote za jengo na kugundua hatari mapema iwezekanavyo.





Mahali hapo kabla hapajageuka jehanamu ndogo palikuwa ni mali ya bwana Msolasa aliyetumia eneo hilo kama kiwanda cha tumbaku. Tamaa yake ya pesa ilimpelekea akauza eneo hilo kwa mwanaume mmoja mwenye asili ya Amerika ya kusini, Emilio Diego, kwa shilingi milioni mia tisa. Kabla ya pesa hiyo kutumiwa hata thumni, Msolasa akavamiwa na watu wasiojulikana wakamnyonga na kumtupia baharini pesa yote ikikombwa na kurudi mkononi mwa Emilio. Japokuwa kifo cha Msolasa kiliteka vyombo vya habari, hakuna lolote lililofanywa na polisi zaidi tu ya ahadi lukuki ambazo ziliishia kutotekelezwa. Sasa habari yake ilikuwa ni tungo ambayo ilipeperushwa na upepo, hakuna tena aliyemkumbuka bwana huyo isipokuwa familia yake iliyoachwa na ukata mkali, mjane na watoto wakibangaiza.

“Kabla hatujaenda inabidi tufahamu hilo eneo vizuri.” Jombi alitoa angalizo.

“Ni eneo ambalo limejitenga mbali na barabara. Hakuna jengo lingine lolote lililo karibu yake kwa kilomita si chini ya kumi ukiwa unatokea Dar, na kumi na tano ikiwa unaelekea mbele na barabara hiyo kuu.” Sandra alieleza.

“Kwahiyo Sandra, unataka kunambia haujui lolote juu ya yale yanayoendelea ndani ya jengo hilo japokuwa wote mpo chini ya Kim?” Miraji aliuliza.

“Kama alivyosema Bakari, huwezi jua yale yanayoendeshwa na makundi mengine isipokuwa tu la kwako. Kila kundi lina viongozi, miiko na taratibu zake japokuwa viongozi wote huwa wanakutana mara mbili kwa mwaka kuelezeana mafanikio na changamoto zao.” Sandra alitoa maelezo.

“Sasa unaweza ukatupa maelezo kidogo juu ya hilo eneo ili tupate kufahamu pa kuanzia?” Jombi aliuliza, mara hii Bakari akadakia:

“Tutatumia Google map kusoma hilo eneo. Nadhani ni njia nzuri zaidi ya kufahamu eneo lolote kinaga ubaga.”

Hilo halikuhitaji mzozo likapita. Walimuacha Bakari acheze na mashine yake kwa dakika kadhaa kisha akawapa jibu:

“Kuna njia tunaweza kutumia pasipo kugundulika kwa wepesi.”



****



Kulikuwa ni giza totoro hakuna kilichokuwa kinaonekana kwa macho ya kawaida. Ndani ya giza hilo kulikuwa kukisikika pumzi za watu zikihema taratibu mara zingine zikikatizwa na kwikwi. Kwa muda kidogo sauti ikanong’oneza:

“Kagutaa … Kagutaa.”

Hakukuwa na jibu. Ni giza kali tu ndilo lilijibu. Sauti ile ya kunong’oneza haikukata tamaa, ikaita tena:

“Kagutaa … Kagutaa.”

Kimya.

Mara mtu akaguna kama aliyezidiwa.

“Kaguta, upo sawa?” Sauti ya kunong’oneza iliwahi kuuliza baada tu ya kusikia mguno. Akajibiwa tena na mguno.

“Upo sawa? … Enh? … Kaguta?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hakuna jibu lolote zaidi tu ya mguno.

Mara taa zikawashwa ghafula, kiza chote kikapotea kufumba na kufumbua. Palikuwa peupe peh mithili ya mchana wa jua la utosi. Kaguta na Vitalis walikuwa wamekalishwa kwenye viti wakiwa wamefungwa mikono, miguu, kichwa na kiuno kwa kamba nene. Nyuso zao zilikuwa hazitamaniki kwa majeraha na kuvimba vimba. Midomo na pua ilikuwa inachuruza damu huku wakionekana kuchoka mno hasa Kaguta ambaye alikuwa amefumba macho na mdomo wake ukiwa wazi kama mtu aliye jangwani akibanwa na kiu kikali mno hamna hata tone la maji ya kunywa. Nguo zilikuwa zimechanwa chanwa hazitamaniki, hazikufaa tena kuitwa nguo bali matambara.

Wanaume watatu waliovalia suti nyeusi walionekana punde baada ya taa kuwaka wakiwa wamekaa kwenye viti virefu kidogo vilivyokuwa vinawatizama mateka wao. Kabla ya kunyanyuka na kuwasogelea mateka walitizamana alafu wote wakanyanyuka na kutembea taratibu mpaka karibu kabisa na Vitalis ambaye aliwapokea kwa macho ya kifedhuli. Hawakujali, badala yake walitabasamu mmoja akauliza:

“Unadhani mwenzako anaweza kuongea baada ya kile kipigo kitakatifu alichokula?”

Wote wakacheka kana kwamba wanatizama futuhi. Kwao kuua ilikuwa ni kama kunawa mikono – kitu wanachoweza kufanya bila ya kujifikiria mara mbili. Mmoja wao alikuwa mrefu zaidi mwenye uso wenye kovu la kisu pembeni kidogo ya sikio, mwingine alikuwa ana kipara kichwani kwake akiwa ana kumbukumbu kubwa ya alama ya mkato wa kitu cha ncha kali. Wa mwisho yeye alikuwa na mdomo wenye kovu la jeraha lililokula nyuzi za kutosha upande wake wa kulia – alishawahi kuchanwa mdomo, haliitaji akili nyingi kugundua hilo.

“Sasa mpo tayari kutuambia nani anawafadhili ama tuendelee kuwashibisha kipigo?” Alinguruma mwanaume mwenye kovu la kisu pembeni ya sikio. Hakuonyesha anatania bali anayemaanisha kile anachokisema. Uso wake ulikuwa unatisha haswa, kama ana mke ama mpenzi basi bila shaka atakuwa ni miongoni mwa wa wanawake wenye uvumilivu wa hali ya juu.

Vitalis alimtizama mwanaume huyo kwa macho yake yaliyovimba na kuchuruza damu akamwambia kibabe mdomo ukipinda kwa hasira na kebehi:

“Muda utakaoingia mikononi mwangu, ndio utakuwa muda wako wa mwisho juu ya uso wa dunia. Sitabakiza mfupa wako wowote mzima. Nitahakikisha hata mama yako mzazi hawezi kukutambua hata!”

Akamtemea mate yake ya damu usoni mwa mwanaume aliyemuuliza, mwanaume huyo akajipangusa huku akitabasamu.

“Naona somo halijakuingia kijana. Wacha nikufundishe kile ambacho mama yako ameshindwa.”

Alituma ngumi yake nzito kwenye uso wa Vitalis damu zikaruka kama maji yanayotoka kwa kasi bombani. Alimpiga Vitalis ngumi tano za tumbo, Vitalis akatapika damu huku puani nako kukichuruza. Kabla hajaendelea kushambulia, wenzake walimkamata na kumtaka aache, inatosha.

“Utamuua sasa. Si unajua mkuu anamtaka akiwa hai?” Mwanaume mwenye kovu kichwani alitahadharisha. Mwenzao akajibandua toka kwenye mikono yao kwanguvu.

“Hawezi akaniletea dharau za kijinga nikabaki namtizama!”

“Sasa ukimuua je, unadhani utamwambia nini mkuu?” Mwanaume mwenye kovu la kichwa aliendelea kunena huku mwenzake mwenye kovu la mdomo akitikisa tu kichwa.

“Mkuu! Mkuu naye mpumbavu tu. Aliwaamini sana wale triple badala yangu, mbona wamekufa sasa? Wako wapi sasa? Na anawatakia nini hawa mbwa wakiwa hai wakati tayari wameshaua triple power yake? Mkuu mwenyewe sasa hivi anaishi chini ya kivuli vya wenzake ambao bado wana power zao. **** off!”

“Unamaanisha nini kusema hivyo jembe?”

Kabla hajajibu aligeuka kwanza kumtizama Vitalis akamuona hajielewi mdono wazi anachuruza tu madamu.

“Kwani nyie hamjui kama triple yake imeshakufa? … Maana yake Emilio atalamba miguu ya Cruz na Santanna.” Alipomaliza kusema hivyo walisikia kelele kali ya mtu akilalamikia maumivu. Walitizamana, mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio akatoa ishara, mmoja akabakia na wakina Vitalis, wawili: mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio na kichwani, wakagawana muelekeo – kulia na kushoto. Baada ya muda wakajikuta wapo nje ya jengo upande wa kushoto sauti ilipokuwa inatokea, walikuwa wanaume wawili mmoja akiwa kamlalia mwenzake kwa juu, mwanaume wa chini akiwa analia kwa sauti ya maumivu. Mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio akajongea kwa tahadhari akamsogeza mwanaume aliyekuwa juu ilia pate kumtizama alalamikaye. Ajabu akamkuta amekufa, alipomgusa mwili wake alihisi ubaridi mkali kuonyesha ya kwamba amekufa kwa kitambo kidogo. Alipotizama pembeni akaona kirekodi sauti na kumbe hicho ndio kilikuwa kinapiga kelele kwa muda wote huo.

“Pumbavu!” Mwanaume amwenye kovu pembeni ya sikio alilalamika. “Bode tumevamiwa. Bonyeza alarm washtue wote!”





Kabla amri haijatimizwa wakasikia sauti ya mtu mwingine anapiga kelele. Mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio akaropoka:

“Huyo sio Gongo!”

“Ndiye yeye! Wavamizi watakuwa wanawaokoa mateka. Twende haraka!”

Jengo lao lilikuwa limegawanywa katika vipengele vikubwa vitatu kila kipengele kikiwa kimekaa mbali kidogo na chenzake na kutenganishwa na kuta pana refu. Kipengele cha kwanza kilikuwa ni kwa ajili ya mateso kwa mateka. Cha pili ambacho kilikuwa kikubwa kuliko vyote, ni kwa ajili ya kuchanganyia mabaki ya binadamu na makemikali, watu wa hapo walikuwa wanavaa makoti meupe marefu, wanabana nywele zao na kofia na kuziba midomo na pua zao kwa vinyago. Kipengele cha tatu kilikuwa cha uhifadhi wa mifuko ya mbolea ambazo tayari zilikuwa zimeshamalizika. Kile kipengele kilikuwa kina ulinzi wake ila kwa nje pia kulikuwa na ulinzi wa jengo zima kwa pamoja. Walinzi wote hao wa nje pamoja na wa kipengele cha mateso walikuwa wameshauwawa, walikuwa chini wakimiminika damu sehemu kadha wa kadha za miili yao. Ila ajabu ni kwamba hakuna yeyote aliyekuwa ndani aliyefahamu kwamba wamevamiwa. Tendo hilo lilifanyika kwa ukimya mno na utaalamu wa hali ya juu huku silaha zilizotumika zikiwa ni visu na kamba ambazo ziling’ang’ania shingo za walinzi na kuwaacha wakiwa wafu. Wavamizi walitembea kwa tahadhari na walionekana wanalijua jengo hilo vyema wakifahamu waingilie na kutokea wapi.

“Bonyeza alarm. Harakaaa!” Mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio alifoka baada ya kuona mateka wote hawapo, juu ya kiti kimoja akiwa amekaa mwenzao waliyemuacha awatizame meteka, damu zikiwa zinammiminika shingoni toka kwenye matundu mawili ya kisu. Wavamizi walitumia mlango huo huo ambao ulitumiwa na wanaume wale wawili baada ya kuuacha wazi wakifuata sauti.

Alarm ilibonyezwa sauti kubwa ikalia na kuwakusanya wanaume wote waliokuwepo hai ndani ya jengo. Walikuwa wanaume thelathini na saba kwa idadi. Miili yao ilikuwa mikubwa na wenye sura mbaya, wote walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai nyembamba nyekundu. Mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio alisimama mbele yao akafoka:

“Kuna watu wamevamia ngome na kuwaokoa mateka. Najua hawajafika mbali, nawataka hapa ndani ya dakika tano tu!”

Wanaume wale walitapakaa kila upande kusaka.

***

Kaguta na Vitalis walikuwa wamebebelewa migongoni mwa wanaume wawili ambao walikuwa wamevalia kombati nyeusi wakiongozana na wanawake wawili waliokuwa kama walinzi wa wale wanaume waliobebelea wenzao. Walikuwa wanatembea haraka haraka wakiacha jengo la BEAST umbali wa nusu ,maili moja nyuma yao wakielekea upande wa magharibi.

Majani yalikuwa marefu mno kiasi cha kuleta ugumu kutembea. Lakini kwa njia moja ikawasaidia wavamizi kujificha mara tu walipoona mwanga mkali wa kurunzi unataka kuwamuliza. Mwanga huo mkali ulikuwa unatoka kwenye kibanda ambacho kilikuwa kipo juu kabisa kwenye jengo la BEAST, humo alikuwepo mwanaume aliyekuwa ameshikilia kurunzi kubwa akilepeleka huku na huko kutafuta walengwa wao.

Baada ya muda mfupi wana-BEAST walimaliza kusaka, hawakuona mtu yeyote. Walirejea wakamwambia mkuu wao – mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio – kwamba hawajamuona mtu yeyote kote kabisa.

“Wapumbavu nyie! Mnashindwaje kuwakamata watu ndani ya eneo kubwa kama hili?”

Mwanaume huyo alichomoa bunduki yake kwenye koti akalenga vichwa viwili vya wenzake, wakafa papo hapo.

“Nendeni mkawatafute! Mkirudi hapa bila ya watu hao, nasambaratisha bongo zenu!”

Wanaume walisambaratika kwenda kusaka tena, pamoja nao sasa nyuma yao wakaongozana na mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio. Ndani ya dakika chache walifika eneo moja lenye shimo ambalo lilikuwa limefunika funikwa na nyasi. Waliingia ndani ya shimo hilo wakagundua ni njia ambayo ilienda kuchomoza kando kando mwa barabara kuu. Walichokuta ni alama tu za matairi kabla hazijapotelea kwenye uso mweusi wa lami.

“Nataka hawa mbwa wapatikane ndani ya masaa ishirini na nne! Nimesema nawataka hawa mbwa ndani ya masaa ishirini na nneeee!” Aliwaka mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio.

***

Sauti ya ndege pori zilimfanya Vitalis ashtuke toka kwenye usingizi mzito wa maumivu. Alikuwa amelala kwenye kitanda kidogo chembamba ndani ya nyumba ndogo iliyofumwa fumwa na miti ya mianzi. Aligeuza uso wake huku na huko akajaribu kunyanyuka, ila mara akasikia sauti ya Bernadetha ikimkataza kufanya hivyo. Bernadetha alitokea akiwa anatabasamu akaketi karibu yake.

“Unaendeleaje?”

Kabla Vitalis hajajibu, aliuliza:

“Kaguta yupo wapi?”

Bernadetha akamtoa hofu: “Amempumzika. Anaendelea vizuri.”

“Na hapa tupo wapi?”

“Kisiwa kando ya Mafia. Nyumbani si salama tena.”

Kichwa kilimuuma Vitalis akashindwa kuendelea. Alilaza kichwa chake kilichokuwa kimefungwa bandeji kwenye godoro na kufumba macho kupumzika.

Ilikuwa ni siku ya pili tangu watoroke kwenye jengo la BEAST. Ndani ya muda huo Vitalis na Kaguta walikuwa wanatafutwa kwa hali na mali ndani ya jiji kwa gharama yeyote ile. Nyumba ya Vitalis ilichomwa moto na kuteketezwa mpaka kuwa majivu baada ya msako kufanyika. Huku Marietta akinusurika kutekwa kwenye bweni la shule yao kabla ya kuokolewa na Miraji punde tu baada ya wana-BEAST kuwasili eneo hilo. Jiji halikuwa salama tena kwa WAGENI, ilikuwa ni kisiwani tu ambapo walikuwa wanaishi wenyewe wakiwa wamejenga makazi ya muda.

Baada ya siku tatu, Vitalis na Kaguta walipata unafuu japokuwa si kuwa sawa kamili. Bado miili yao ilikuwa na maumivu ambayo yaliwapasua eidha wakiwa wanatembea, kuongea, kuruka ama kujihusisha na shughuli yoyote ya viungo. Lakini kazi lazima ifanyike hivyo hakukuwa na muda wa kubweteka. Wana-BEAST waligeuza mji na kuufanya uwanja wao kwa kufanya mauaji na kuwatesa watu kama salamu kwa Vitalis na Kaguta. Ndani ya muda huo watu nane waliuwawa ikiwemo majirani wa Vitalis, walimu wa Marietta na hata wafanyakazi wenzake na Bernadetha, wale aliofanya nao kazi kwa kipindi kifupi kule hospitalini. Haikujulikana wana-BEAST walipatia wapi taarifa zote hizo. Hayo yalizidi kuwapa hofu WAGENI juu ya BEAST.

Mwanaume mwenye kovu pembeni ya sikio, ajulikanae na wahalifu wenzake kwa jina Mamba, ni miongoni mwa watu hatari juu ya uso wa dunia. Anapotembea katikati ya jiji hakuna anayejua ya kwamba ndiye mwanaume yule yule aliyepata kutikisa Tanzania kwa ujambazi wake wa silaha za moto miaka ya 1980 mpaka 1990 akiwa kama mhusika wa kundi maarufu la kijambazi lililojipachika jina la WANYAMA, kila mhusika ndani akiwa amebebelea jina la mnyama anayempenda. Kwenye miaka ya 2000 kundi hilo lilisambaratishwa na jeshi la polisi, wahusika wote walikamatwa na kutupiwa jela kwa kifungo cha maisha isipokuwa Mamba ambaye alitorokea msitu wa Pangani, Tanga, huko akaishi kama mnyama kwa miaka kumi na tano kabla ya kurejea tena mjini akiwa amebadilika kabisa, uso wake ukiwa umefichwa na ndevu na nywele nyingi. Hata mwili wake ulikuwa mpana zaidi kutokana na mazoezi aliyokuwa anayafanya kutwa kucha. Mjaa asili haachi asili, Mamba alitafuta tena kundi la kijambazi na kujiunga nalo aendeleze kipaji chake. Kutokana na mahusiano makubwa na kundi la bwana Kim ambaye aliitawala serikali ya Tanzania kwa kiasi kikubwa, Mamba alifanikiwa kufuta rekodi yake ya ujambazi na kuwa raia kama wengine. Sasa yupo mtaani kuendeleza mkono wake damu. Amepewa nafasi kubwa na bwana Emilio Diego katika kundi lake la BEAST chini tu baada ya mapacha watatu ambao tayari wameshauwawa, hivyo sasa kumfanya awe juu kuliko wengineo. Na sasa anahaha kumthibitishia mkuu wake kuwa yeye ni bora kuliko hata wale mapacha watatu. Ingetakiwa ampe nafasi na kumuamini zaidi.



***





Baada ya kupata chakula cha usiku, WAGENI wakiwa wamekaa kwenye mkeka walianza kuteta juu ya nini cha kufanya. Karatasi kubwa ilikuwa imetandazwa chini Bakari akiwa ameshikilia marker pen. Wote walikuwa wametulia kwa utulivu na baada ya kusali, Vitalis akaanzisha mjadala.

“Hatuna muda wa kupoteza ndugu zanguni. Nini ambacho mlikipata kwenye upembuzi wenu mpaka mkafahamu tulipohifadhiwa?”

“Tulichambua zile namba na kugundua zina maanisha neno BEAST. Sandra akatuamabia anafahamu jengo la mateso na mateka linaloenda kwa hilo jina, ndipo tukawapata.” Bakari alidadavua.

“Kwahiyo ina maanisha hili kundi la BEAST lina maeneo yake ya kufanyia unyama wao.” Kaguta alieleza alafu akauliza: “Kwahiyo lile eneo la kwanza litakuwa ni nini?”

“Bila shaka itakuwa ni ofisi.” Vitalis alijibu. “Na vipi kuhusu alama ya nyoka na visu?”

Kimya kikawashika kwa muda kabla Vitalis hajafungua mdomo wake kuuliza:

“Ujanja wa nyoka upo kichwani kwake, sio?”

“Ndio.” Wote wakamjibu.

“Sasa kidogo napata picha. Nyoka tuliyemuona kwenye kuta, ni mwenye vichwa vitatu, kwanini? … Kwasababu BEAST wana viongozi watatu.” Vitalis alijibu alichojiuliza na kuendelea:

“Nakumbuka wakati tupo kule kwenye lile jumba, mmoja wao alisema kwakuwa wao wamepoteza triple yao, ambayo ni wale mapacha, Emilio atalamba miguu ya Cruz na Santanna. Kwahiyo ina maanisha kuna watu watatu hapa: Emilio, Cruz na Santanna. Na wale mapacha watatu, yani triple, waliokufa walikuwa ni wa Emilio. It means kuna mapacha wengine watatu mara mbili, wa Cruz na wa Santanna, ndio kwa jumla wanaunda idadi ya visu tisa juu ya vichwa vile vitatu vya nyoka. Kwahiyo sasa hivi kwenye vichwa vya nyoka hawa watatu kuna visu tisa tu.”

“Na kwanini ni visu si risasi wala mabomu juu ya vichwa vya nyoka hao?” Miraji aliuliza.

“Nadhani pia hapo pana siri ya kuifunua.” Vitalis alitanabahi. “Watu watatu ambao walikuwa wanahusika na kututesa, wote walikuwa na kovu za kisu sehemu mbalimbali, hasa za vichwa vyao. Kwanini si za risasi ama kitu kingine?”

Kimya kilitawala kwa muda kidogo. Jombi akachangia:

“Ila mnakumbuka wakati tunaenda kuwaokoa wenzetu tulitumia silaha gani?” Aliwatizama Sandra, Bernadetha na Miraji.

“Tulitumia visu kwasababu ya kutowashtua wenzao.” Sandra alijibu.

“Kuna kitu gani kilitokea tulipotumia visu hivyo?” Jombi aliuliza. Bernadetha akajibu:

“Waliwahi kuwa wa baridi baada tu ya muda mfupi kisu kugusa nyama na damu zao.”

“Sasa kwanini wawe na makovu ya visu wao wenyewe?” Vitalis aliuliza.

“Itakuwa ndio mtindo wao wa kiapo.” Sandra akajibu. “Kwenye kila kundi wana miiko na taratibu zao. Kile kinachowekwa kwenye tattoo lazima kiwe kina mahusiano na viapo. Na pale wanapovikiuka, ni hivyo viapo ndivyo vitawahukumu.”

“Yani kumaanisha nyoka kama vile ilivyokuwa jitu?” Kaguta aliwahi kuuliza.

“Ndio!” Sandra akajibu.

“Kwahiyo kwa sasa tuna shetani mpya wa kuhangaika naye, sio?” Vitalis akauliza kama mtu asiyetegemea jibu. Kisha akatabasamu utadhani ni mazuri.



****



Baada ya kuvuta sigara aliumeza moshi akautolea puani. Akaagiza tena kinywaji kingine kikali na kuendelea kujipa huduma taratibu akiwaza jinsi gani atawatia mikononi mateka wake waliotoroka. Hakutaka kushindwa kabisa – hiyo si asili ya Mamba. Yeyote atakayeingia kwenye maji basi ni halali yake na hakuna cha salia mtume. Alinyonya tena sigara yake akarusha moshi juu, mara hii akadidimiza mkono mfukoni akatoa simu ndogo nyeusi akaweka namba na kuipachika sikioni.

“Upo wapi? … Fanya upesi ni pakti ya sigara sasa namaliza na bado hujafika.”

Alirudisha simu mfukoni akabeba kinywaji amwagie mdomoni. Baada ya dakika chache akawasili mwanaume mwenye kovu kichwani, Bode. Alikuwa amevalia shati la kitenge linaloendana na suruali yake. Huwezi ukabashiri ya kwamba ni muuaji mkubwa ndani ya nguo hizo nadhifu zenye rangi zisizoita macho kwa ukaribu.

“Umepata nini?”

Mamba alimpokea mgeni wake na swali. Bode akashusha pumzi kwanza.

“Hakuna kipya, mzee. Nimejaribu sana kuulizia kwa kutumia picha lakini sijafanikiwa.”

Kimya kikakatiza katikati yao mpaka pale mhudumu alipokuja kumuuliza Bode angependelea huduma gani, akaagiza pombe yoyote kali.

“Kuna haja ya kurudi ofisi ya taarifa?” Bode aliuliza.

“Hapana.” Mamba akajibu kisha akatulia kwanza akichakaza kichwa. Mhudumu akaja akiambatana na kinywaji alichoagizwa, akakiweka mezani na kukifungua, alipoondoka Mamba akasema:

“Nadhani kuna njia nzuri zaidi ya kuwatafuta watu wetu. Hatutohangaika tena, bali wao ndio watakaotutafuta.”

Bode akapiga fundo moja na kutabasamu kana kwamba kinywaji kimegusa penyewe.

“Hapo ndipo nakukubali, Mamba. Upo fasta kuchonga mawazo. Embu nishirikishe hilo wazo lako. Njia gani hiyo?”

Mamba akajibu huku akikuna kidevu.

“Tutakachokifanya sasa hivi ni kuvamia shule na kuwateka wanafunzi kadhaa. Kwa kuwa wale wapumbavu wanataka sifa, watajaribu kuwaokoa na hapo ndipo watakaporudi mikononi mwangu na sitawaletea tena mzaha, nitawapa usafiri mzuri wa kwenda kuzimu.”

Bode akatikisa kichwa kuafiki wazo. Akanywa chupa yote ya pombe na kuagiza nyingine ambayo nayo aliinywa kwa pupa ingali kichwa ki chepesi. Baada ya dakika kadhaa mbele pombe zilianza kumgonga kichwa akasahau ya kwamba yupo bar na wanaongelea mambo ya hatari, sauti yake ikapanda. Mamba kuepusha adha alilipa bili akamnyanyua Bode na kuondoka naye kuelekea garini akimkokota. Waliwasha chombo wakayeya. Ila punde tu akatokea mwanamke aliyevalia nguo za wahudumu akaitizama gari lile likitokomea. Alikuwa ni Bhoke. Hakubanduka kando ya barabara mpaka pale taa za gari lile zilipopotelea. Lakini pia Mamba alimuona mwanamke huyo kwa kutumia kioo cha gari kilichoketi juu ya paji lake la uso. Alipata walakini lakini haukumkonga sana moyo wake, labda mhudumu yule alikuwa anataka kumrudishia chenji yake, aliwaza.





Bhoke alirejea ndani ya bar akiwa ametwaliwa na uso wa fikra. Mkononi mwake alikuwa amebebelea chenji ya mteja ambaye badala ya kumuita na kumpatia alibakia akimsikiliza kwa butwaa. Wanataka kumuua nani? Wanataka kuvamia shule? Kwanini? Hawa watu ni wakina nani? Kichwa cha Bhoke kilivuma. Mwishowe aligongana na mteja kwasababu ya mawazo. Aliomba radhi haraka akakimbilia kaunta. Alishika simu yake akitaka kumpigia mtu amwambie, ila ampigie nani sasa? Alimuita mwenzake karibu akamshirikisha, hapo akapata wazo.

“Si umpigie yule bwana ‘ako mwanajeshi?”

Haraka Bhoke akatafuta namba ya Kaguta na kuipigia.

“Samahani, namba ya mteja unayempigia haipatikani kwa sasa.” Alikatishwa hamu na ujumbe huo. Uso akaukunja.



***



Haikuwa usiku wala mchana mazoezi yasifanyike ndani ya kisiwa kando na Mafia. WAGENI walikuwa wanajinoa haswa ndani ya maji na nchi kavu wakijifua zaidi namna ya kutumia silaha, kutunza pumzi ndani ya maji, kuongeza pumzi mapafuni na kutafuta ustahimilivu. Waliamka saa kumi na moja alfajiri wakilala saa saba ya usiku. Walitota jasho wakati wa mchana jua likiwa kali huku miili ikisinyaa wakati wa usiku baridi likipiga. Lakini hiyo ikawa haitoshi kwa Kaguta na Vitalis ambao waliendelea kujifua hata pale wenzao walipopumzika. Mara kadhaa walikuwa hawalali kabisa wakishinda wakikimbia ama kuogelea, au wakipambana wenyewe kwa wenyewe. Vita iliyokuwa mbele yao ilikuwa ni kubwa – halikuanduka hilo kichwani mwao.

Wakati sasa yapata kuelekea jioni ndani ya siku ambayo haikuonyesha dalili zozote za mvurugo, Kaguta alikuwa anajiandaa apate kwenda mjini Mafia kuchukua mahitaji ya kuwasogeza siku kadhaa mbele. Mwili wake uliojaza ulikuwa umeshikwa na shati la kijani lililombana huku miguu yake ikifichamwa na kombati na buti la jeshi. Kichwani alikuwa amevalia pama ikiwa na maandishi … can you suck me?

Haikupita hata dakika nyingi Kaguta akawa tayari yupo ndani ya kamji kadogo ka Mafia. Hakuonekana kama mtu mwenye wasiwasi wowote mpaka pale alipotikiswa na mngurumo wa simu mfukoni mwake. Hakuzoea hiyo hali, kukaa sana kisiwani kusipo na mtandao kulimfanya asahau kidogo simu. Alipoitoa na kuitizama, akasonya.

“Huyu Bhoke anataka nini lakini?” Alilaumu akisoma ujumbe toka kwa Bhoke ukimtaka aonane naye haraka iwezekanavyo. Alipuuzia akarudisha simu mfukoni na kuendelea na mambo yake. Kabla ya jua kuzama alisharejea kisiwani. Bahati nzuri ama mbaya, Sandra akashika simu ya Kaguta na kuukuta ujumbe wa Bhoke. Alifura. Moja kwa moja alidhani Kaguta alienda kuonana na malaya huyo.

Alipanua kifua chake kwa kuficha jambo hilo kifuani. Kesho yake akatoroka na kwenda mjini Mafia, akampigia simu Bhoke. Baada ya kubishana kwa sekunde kadhaa juu ya Kaguta, Bhoke akampasha habari Sandra.

“Kuna majambazi wawili wanataka kuvamia shule ya Kwembe kesho wawateke wanafunzi. Walikuja hapa bar juzi wakaongea hayo mambo. Naomba umfikishie Kaguta hizi habari. Umesikia?” Bhoke aliuliza kwa nyodo kisha akakata simu. Sandra hakuamini, aliona ni janja tu ya Bhoke kukwepa mashtaka ya kudandia wanaume wa watu. Alisonya na kulaani kana kwamba Bhoke anamsikia. Alirudi zake kisiwani akajitahidi kukaa na hilo jambo kwa dakika chache tu kabla ya kufunguka kwa hofu ya usalama. Aliweka aibu yake ya kuchukua simu ya Kaguta bila ya taarifa, akafikisha habari.

“Hili si jambo la kupuuza. Watakuwa ni wana BEAST sasa wanatutafuta kwa njia mbadala. Nadhani wametupa sehemu nzuri ya kuanzia.” Vitalis aliwika. “Kaguta, nenda ukutane na Bhoke. Hakikisha anakupa kila elezo muhimu.”

Sandra hakufurahishwa sana na hayo maamuzi. Labda alitamani aende yeye na si Kaguta. Ama waende wote basi.



***



Mida ya jioni ndiyo bar hufurika wateja wakiwa wametoka vibaruani. Wahudumu wanakuwa wapo bize wakizunguka huku na huko na sketi zao fupi zinazotekenya mapaja. Mbali na kufungua vizibo vya vinywaji walikuwa pia wanafungua matabasamu na kutembea kwa madaha wang’oe wanaume ama wahongwe bia mbili tatu.

Miongoni mwa wateja hao alikuwamo Kaguta. Alikuwa ameketi mwenyewe kando kando ya bar, juu ya meza chupa ya Grants ikiwa imesimama wima pasipo na glasi. Macho yake yalikuwa lindo akitizama huku na huko. Baada ya muda Bhoke alijiunga naye.

“Sina muda wa kukaa sana hapa, si unaona wateja ni wengi.” Bhoke alijibaraguza. Kaguta akatabasamu kisha akanywa fundo moja la Grants.

“Punguza hasira na mimi, mama. Nambie kinagaubaga nini ambacho ulikiona na kukisikia.”

“Nimeshamwambia hawara ‘ako. Hajakuambia?” Bhoke alibetua mdomo.

“Bhoke, ndio mana nimekuja hapa. Najua kuna mengi ya kupata toka kwako. Kama basi hunipendi, fikiria kidogo kuhusu usalama wa watoto hao watakaoenda kudhuriwa.”

Baada ya nyodo za hapa na pale, Bhoke akaeleza yote aliyoyaona.

“Unaweza ukaniambia plate number ya hiyo gari waliloondoka nalo?”

“Sikumbuki. Ila lilikuwa ni gari jeusi lenye vioo vyeusi. Na limeandikwa be-a-st kwenye kioo cha nyuma.”

“Sura zao je?”

“Mmoja ambaye ndiye aliyetangulia, ana kovu kando ya sikio na macho yake ni makali mno na ya kutisha. Mwenzake ana kovu kubwa kichwani, ana mwili wa kawaida.”

“Kipi ulisikia?”

“Baada ya kupeleka kinywaji cha pili kwa yule mwanaume mwenye kovu kichwani, muda mfupi tu akaanza kuropoka ropoka mwenzake akijitahidi kumnyamazisha. Alisema hakuna wa kuwazuia huko Kwembe na watamuonyesha mkubwa wao kwamba wao ni wa maana pia.”

Baada ya maelezo hayo, Kaguta alimaliza kinywaji chake akaaga akimtaka Bhoke awe makini mno maana hao watu ni hatari. Na atakapowaona tena popote atoe taarifa hata polisi.

“Sasa huniachii hata tip?” Bhoke alimuuliza Kaguta kabla hajayoyoma.



****



Shule ya Kwembe ilikuwa imejitenga kidogo na purukushani za jiji la Dar es Salaam. Kwa mtu kupata kuifikia ilimpasa aache barabara ya lami kwa umbali usiopungua kilomita tatu alafu akatishe kwenye barabara iliyofunikwa na miti mbalimbali na kutengeneza kiza hata pakiwa mchana. Upande wake wa mashariki ilikuwa imepakana na maji ya bahari ya hindi. Kaskazini imepakana na misitu ya mikoko huku magharibi vijumba hoi vya wavuvi. Si bure wadhalimu walichagua hiyo shule. Ni rahisi kutoweka. Sehemu za kupotelea zi kedekede pia ni ngumu kwa msaada kupatikana kwa wahanga. Japokuwa shule ina wanafunzi wa msingi na upili bado haikuonekana kufurika. Watoto walikuwa wengi maeneo ya ufukweni na baharini wakivua samaki na kuogelea kuliko wale waliopo madarasani.

Wakati kengele ikitangaza kikomo cha mapumziko na kuwataka wanafunzi warejee madarasani, gari nyeusi aina ya van ilitokeza ikiwa katika mwendo wa kawaida usiomshangaza yeyote. Ndani walikuwemo wanaume wanne wa kazi: Mamba, Bode, Shaziri – mwanaume kijeba aliyenyoa ‘kiduku’ akiendesha gari na Yosso, mwanaume mwembamba aliyejichora chora mwilini. Waliposhika barabara ya kuelekea shuleni hapo kwa mbele kidogo wakakutana na gogo kubwa katikati ya barabara. Gari likasimama, Shaziri akashuka. Baada ya muda kidogo Mamba na wenzake wakaona kimya, Shaziri hakurudi na gogo bado lilikuwa barabarani.

Mamba akiwa na uso wa mashaka alimuamuru Bode pamoja na Yosso washuke kutizama usalama. Wakashuka wakiwa wamebebelea bunduki. Walitizama kushoto na kulia kwao pasipo kuona mtu yeyote, walipotizama juu ya mti ikawa kosa. Walimwagiwa unga rangi ya manjano usoni wakapiga mayowe ya maumivu wakirusha silaha kando. Kufumba na kufumbua mwili wa Shaziri ukadondoka toka juu ya mti alafu wakashuka wanaume watatu wakiwa wamevalia nguo za jeshi na kofia za kuficha nyuso wakaanza kumiminia risasi van kwa fujo. Kwa pupa van ikarudi nyuma na kuondoka kwa kasi mno ikiwaacha watu iliokuja nao mahututi. Kabla watu hawajajaa eneo la tukio likaja gari ‘defender’ likiendeshwa na Bakari, wanaume wale watatu wakapanda pamoja na mateka zao wakapotea haraka.

Ila Mamba bado alikuwa hai!









Hilo jambo lilimuumiza sana Vitalis. Alijihukumu kushiriki uzembe wa kumruhusu mshenzi kama yule atoroke mbele ya macho yake. Alijua fika uhai wa mamba ni vifo vya wasio na hatia. Hakuna yeyote anayejua ataenda kufanya nini baada ya jaribio lake la kuteka wanafunzi kushindikana. Ni lazima atiwe mikononi haraka! Afunzwe adabu! Mwili wake uvunjwe vunjwe na umeze risasi si chini ya tano! Aliwaza Vitalis mwenyewe akiwa amebinua mdomo wake na amekunja sura kama mtu aliyekunywa dawa chungu.

Sasa ni fursa ya kuvamia ofisi yao na kuisambaratisha. Tusimpe muda wa kupanga mambo yake zaidi.



****



Baada tu ya muda mchache baada ya tukio la utekaji wa wanafunzi kushindikana, Mamba alishakuwa mtu tofauti kwa kubadilisha mavazi na hata usafiri – haikuwa tena van wala mark X aliyokuwa anaendesha bali range rover nyekundu aliyoisogeza mpaka eneo la bar. Uso wake ulikuwa umebeadilika kwa kupachikwa ndevu za bandia na macho kufunikwa na miwani meusi.

Alishuka akatembea taratibu mpaka ndani ya bar, punde akatoka na Bhoke akiwa kamkamatia kiuno wakitabasamu na kuongea. Alimfungulia mwanamke huyo mlango akaingia ndani, gari likang’oa nanga.

Baadae mida ya saa kumi na moja jioni, Bhoke akakutwa akiwa mfu ndani ya Limpopo guest house, Sinza, kifua chake kikiwa kimetobolewa na risasi tatu. Mdomo wake umeachama na macho yapo wazi. Shuka limetapakaa damu. Si mapokezi wala yeyote aliyesikia milio ya risasi wala kelele zozote, zaidi maelezo yalisema mwanaume aliyeingia na marehemu aliondoka baada tu ya dakika chache walipoingia chumbani.

Habari hizo zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii. Na hata zikachukua nafasi kwenye taarifa za habari. WAGENI walifahamu fika ni nani aliyefanya huo unyama. Kukaa kwao kimya kungeendeleza matukio hayo ya umwagaji damu. Siku inayofuata ilikuwa ni alhamis – siku adhimu kwa shambulizi la ofisi ya BEAST. Sandra akishirikiana na Kaguta na Vitalis walitega gari lao pembeni kidogo ya barabara umbali wa kilomita moja tokea ofisi za BEAST zilipo. Punde wakiwa hapo wakaona gari la kusambaza sigara laja, wakaliteka na kwenda nalo mpaka mbele ya uzio wa jengo hilo lenye ulinzi mkali. Wakiwa wamevalia nguo za wahudumu, ilikuwa ngumu kugundulikana. Walitumia bunduki zao zenye viwamba vya kumeza sauti wakawamaliza walinzi wote wa nje kisha wakagonga geti na kuingia ndani ya uzio kwa urahisi mno.

Ndani ya sekunde kumi tu, walinzi wote wakawa wamelala chini wakivuja damu waliokuwemo ndani wasijue kinachoendelea huko nje. Vitalis na wenzake wakajigawa mmoja akaenda upande wa kushoto, mwingine kulia na mmoja katikati. Ufahamu wao juu ya hilo eneo kwa kutumia teknolojia ya google map uliwasaidia kunyambua mazingira vema. Mikono yao mepesi iliyokomaa kwa mazoezi na mateke yao mazito yenye nguvu yalirahisisha sana kazi – haikuonekana ngumu hata kidogo ukilinganisha na mazoezi yao wanayoyafanya kila uchwao. Mpaka wanaingia kwenye chumba cha mkuu, hawakuwa hata na mchubuko. Walisimama wima mbele ya mwanaume wa kilatini aliyelaza nywele zake nyuma kwa ustadi mkubwa, mdomoni mwake akiwa ana sigara kubwa. Macho yalikuwa yamemtoka kwa butwaa – wazi hakutegemea watu kuvamia ngome yake na kuingia kwa urahisi hivyo, tena bila hata ya kutambua.

“Who are you?” Mlatini aliuliza kwa uso uliokuwa unajitahidi kufichama hofu. Alitoa sigara yake akailaza kisosini.

“We are your angels of death.” Vitalis alijibu kwa kebehi kisha akamuamuru mlengwa wake asimame upesi kabla hajammwaga ubongo. Mlatini akawa mkaidi kidogo, alijaribu kufungua droo yake atwae bunduki, kabla droo haijasogea risasi ikapiga kando yake na kumshtua.

“Don’t even dare to try!” Kaguta alisema na uso wa kazi ‘uso wa mbuzi’ kisha akamtwaa Mlatini huyo na kutangulia naye nje pamoja na Sandra, Vitalis akibakia kidogo ofisini macho yake yakitembea tembea huku na huko.

Juu ya ukuta mdogo wa ubao wa matangazo, Vitalis aliona picha kadhaa za mifuko ya mbolea na matangazo ya biashara hiyo. Aliposogea na kutizama kwa ukaribu picha hizo za mbolea, chini yake akaona tarehe 8/8/2014 – Ilikuwa siku ya nanenane! Siku ya wakulima! Bila shaka BEAST walikuwepo kwenye maadhimisho ya sherehe hiyo wakitangaza bidhaa yao. Na pasipo kujua wakulima wakanunua bidhaa zao – mabaki ya binadamu wenzao waliouwawa na kuzikwa kimakundi kisha kuchanganywa na kemikali mbalimbali.

Bila shaka BEAST watakuwepo tena kwenye maadhimisho ya sherehe hiyo karibuni. Vitalis aliwaza. Bado wiki moja tu sikukuu ya nanenane ifikie kilele. Huo ndio muda muafaka sasa wa kuwatia wadhalimu hawa mikononi na kumsaidia Mungu kuwahukumu.



***



Hali ya utulivu na pilikapilika za hapa na kule zilimeza jiji la Dar es Salaam. Maduka yalifurika watu wakikatiza kule na kule katika mitaa ya Kariakoo. Kama kawaida kila mtu alikuwa ameshika yake, ukitizama kwa juu unaweza ukasema ni sisimizi wamemwagwa eneo hilo, kumbe ni watu! Katikati ya watu hao alikuwemo mwanaume mmoja aliyevalia suti nyeusi mkononi amebebelea briefcase. Alikuwa yu nadhifu mno. Kichwa chake kilikingwa jua na kofia safi nyeusi yenye ufito mwekundu. Macho yalizibwa na miwani nyeusi huku mdomo ukiwa umezungukwa na ndevu nyingi. Hakuwa mwingine, bali Mamba. Lakini kumfahamu ilihitaji uchambuzi wa hali ya juu. Dhahiri shairi alikuwa ana tukio la kufanya eneoni hapo. Laiti kama wananchi wangelikuwa wanafahamu wangelikimbia kuokoa pumzi zao.

Alitembea kwa wima pasi na hofu. Alikata mitaa akiwa anapiga mluzi taratibu kama njiwa pori. Kichwani kwake alikuwa amelaza ramani nzima ya tukio analotaka kulifanya – kulipua soko kuu! Alizama ndani ya jengo hilo mpaka chini kabisa kana kwamba ni mteja. Akiwa anatembea tembea na kutizama tizama hali ya usalama, mwanaume mmoja alimsimamisha, alikuwa ni mlinzi. Mamba alipata shaka lakini hakuruhusu hilo jambo liteke uso wake. Alitabasamu akauliza:

“Kuna shida afande?”

Huku mkono wake ukiwa tayari umeshakakamaa kufanya tukio lolote litakaloamuliwa na akili yake iliyokuwa inachemka.

“Vipi, wewe ni mgeni humu?” Mlinzi aliuliza. Mamba akatabasamu, alijua mlinzi alimuona wakati anayasoma mazingira. Japokuwa yeye ni mwenyeji huwezi mdanganya lolote kuhusu Dar, aliamua kujifanya mjinga.

“Ndio, mimi ni mgeni.” Alisema na sauti yenye mkandamizo wa kisukuma kwa mbali. Hilo likatosha kumfanya mlinzi ajue ni mtu toka kijijini.

“Nimekuja natafauta mbolea nzuri ya mahindi yangu.”

“Oooh! Nenda mbele kidogo alafu ukunje kushoto, utaona duka la mbolea na madawa ya shambani. Sawa mzee?”

“Sawa. Nashukuru gete!” Alisema Mamba kasha akafuatisha ushauri aliopewa. Alinyookea dukani hapo akajifanya mteja anayeulizia bidhaa. Aliweka mkoba wake chini kisha akaondoka kama mtu anayejinasibu kuusahau mzigo huo. Alitembea kwa kasi mno akielekea kutoka nje. Mlinzi aliyemuelekeza duka la mbolea alimuona mtu wake huyo akitembea haraka huku mkononi akiwa mtupu – akapata shaka. Eidha ameibiwa na watoto wa mjini – aliwaza. Haraka alianza kumfukuzia Mamba huku akijaribu kumuita. Mamba alizidi kusonga asigeuke nyuma kabisa ingawa alisikia sauti ya mlinzi ikimuita. Alipoacha jengo la soko nyuma kwa hatua kadhaa mlipuko mkubwa ukamrusha mbele akadondokea kwenye gari. Jengo lote la soko lilikuwa linawaka moto kama vile tanuru. Taharuki ilikamata watu wakakimbia huku na huko. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa ndani ya soko akatoka mzima. Mlinzi pekee aliyekuwa anamkimbiza Mamba ndiye aliyepona. Aliamka akarusha uso wake kwa mbali akamuona Mamba akiyoyoma katikati ya umati wa watu unaokimbia. Alinyanyuka akamkimbilia lakini hakumuona abadani. Mamba alikuwa tayari ameshavua na kutupa kofia yake na ndevu zake bandia zilikuwa tayari zimeshatupwa kando. Ilikuwa ni ngumu tena kudhani kama ni yuleyule aliyekuwa amebeba mkoba awali. Alikuwa ni mtu mwingine akiwa tayari ameshawateketeza watu 250 ndani ya dakika, sasa akiwa tayari yupo ndani ya taksi akisepa. Huo ulikuwa ni ujumbe maridhawa sana kwa WAGENI. Wameuwa watu wake watatu na kumteka mkuu wake, sasa yeye ameua watu 250. Nani zaidi? Alijikuta akitabasamu.



***



Zilipita siku tatu za vuguvugu la tukio la ugaidi Dar es Salaam, Kariakoo. Bado watu wa Dar hawakuwa na amani, maongezi yao yalitawaliwa sana na hilo tukio la kutisha mno kuwahi kutokea katika nchi ya Tanzania. Japokuwa jeshi la polisi lilitoa tamko lake likijinasibu kufuatilia na kumtia mikononi mhalifu aliyeshiriki, bado haikutosha kuondoa ukakasi wa hofu uliowaganda wananchi waliokuwa kwenye maombolezo. Mbona siku zazidi kuyoyoma na mtuhumiwa hajakamatwa? Hilo swali lilihukumu kazi ya polisi.

Kando kando ya bahari ya hindi iliyokuwa inapuliza kwa mawimbi madogomadogo, Vitalis aliketi akiwa ana mawazo. Kwa mara ya kwanza alijihisi hana mchango wowote kwa wananchi wa Tanzania. Kama watu 250 wanakufa na yeye yupo hai, ana faida gani sasa? Alijiuliza. Alijihisi si lolote si chochote. Alijiona ngoma yake ya kitoto haswa.

Mawazo yake yalitambaa juu ya maji ya bahari. Upepo mkali uliokuwa unampuliza haukusaidia chochote kuondoa zigo la tafakuri alilonalo kichwani. Alijikuta akisaga meno yake huku akikunja ngumi kakamavu. Alitamani Mamba atokee ili apate kumtia adabu na kumvunja vunja bila huruma. Aliishia tu kutamani na kutamani, hakujua wapi atampata adui wake huyo – hawezi akakaa tena na kule kiwandani – anajua yupo mtaani kuonyesha umwamba wake dhidi ya mapacha watatu, ila haswa ni wapi aende ili amkamate baradhuli huyo amuonjeshe kifo? Alibaki anawaza mpaka pale aliposhtuliwa na mkono begani.

“Usiwaze sana, Vitalis.” Sauti ya Bernadetha ilimkarimu. Alinyanyua uso wake akamtizama mwanamke huyo mwenye sura tamu. Akajikuta anatabasamu kwa mbali. Bernadetha aliketi karibu na Vitalis, akamshika mkono.

“Unadhani huyu muuaji ndiye Yule aliyemuua Waziri?” Bernadetha aliuliza.

“Bila shaka ndiye yeye akiwa ametumwa na mkuu wake tuliyemkamata.” Vitalis akajibu kisha akaongezea: “Kwa mujibu wa maelezo ya mlinzi wa soko, kimo cha mtuhumiwa na sifa za mwili wake ni sawa na zile za yule aliyemuua waziri kutokana na maelezo ya mtoto wa marehemu. Ametusakizia kifo cha waziri na sasa anachokifanya ni kuzidi kuwafanya wananchi waamini kile walichokianzisha, uongo. Pia kututaabisha.”

Bernadetha alitizama maji ya bahari akisema:

“Ndiye yeye pia aliyemuua Bhoke … Ila si ulisema umepata nafasi nzuri ya kuwakamata?”

“Ndio, sikukuu ya nanenane, ila naona mbali. Mpaka pale siku hiyo itakapowasili atakuwa kaua wananchi wangapi wasio na hatia?”

Walinyamaza kwa muda, Bernadetha akasema:

“Labda nina wazo.”





Vitalis akamuazima masikio yake.

“Kesho kuna mkutano mkubwa wa polisi, wadau na wananchi kujadili swala la usalama kutokana na matukio ya hapa karibuni. Nadhani lazima mtuhumiwa wetu afike hilo eneo. Unaonaje?”

Vitalis alitulia kwa muda kidogo akatikisa kichwa chake.

“Wazo zuri sana. Lazima awepo hilo eneo. Ni muhimu sana kuwepo hapo.”

Baada ya muda mfupi Bakari alisonga karibu akiwa amevalia bukta na shati jepesi lililokuwa linarushwa na upepo wa bahari mithili ya tiara. Mkononi mwake alikuwa ameshikilia simu yenye kioo kikubwa na juu ya kioo hiko palikuwepo na picha ya mwanaume mzungu mwenye masharubu marefu.

“Samahani kwa kuingilia maongezi yenu.” Bakari alijitambulisha kwa hiyo kauli kisha akaendelea:

“Nimefanikisha ile kazi mkuu.”

“Sawa sawa. Niambie ambacho umekipata.” Vitalis alisema akijitengenezea.

“Mtu huyo ambaye tumemteka ni moja kati ya washiriki wa lililokuwa kundi maarufu la uhalifu huko Venezuela. Kundi hilo lilikuwa linahusiana na usambazaji wa madawa ya kulevya lakini pia likihusika na mauaji ya watu wasiopungua mia tatu kwa sababu mbalimbali. Kwa pamoja, serikali ya Venezuela ikishirikiana na ya Marekani walifanikiwa kuliangamiza kundi hili kwenye miaka ya 2004. Wahusika kadhaa walikamatwa na wengine wakafungwa kifungo cha maisha. Ila viongozi wa hilo kundi ambao walikuwa ni watatu, walitoroka na mpaka leo haijulikani walipo. Wanatafutwa kwa udi na uvumba na zawadi nono kupatikana kwa atakayefanikisha hilo.”

Bakari alimuonyesha Vitalis picha iliyokuwepo kwenye kioo cha simu, akasema:

“Huyo ndiye tuliyemkamata.”

Vitalis akasataajabu: “Mbona hafananii?”

“Mtizame macho yake vizuri. Wanafahamu ya kwamba wanatafutwa hivyo amebadilisha kabisa mionekano yao iwe ngumu kutambulika. Amepunguza nywele zake, amenyoa masharubu na kukuza ndevu za kidevuni kwa wingi. Ila yeye hakuwa kiongozi wa hilo kundi, bali hawa hapa.”

Bakari akafagia simu yake zikaja picha zingine tatu.

“Huu ndio muonekano wao wa awali, hatujajua kwa sasa watakuwa wanaonekanaje. Na watakuwa wanatumia majina gani.”

“Print hizo picha zote unikabidhi. Tutazihitaji sana, hasa tarehe nane.”

“Sawa, mkuu.”



***



Washikadau pamoja na waandishi wa habari mbalimbali walikuwa tayari wamefurika kwenye uwanja wa jengo la LAPF Tower wakati muda ukiwa unajongea kabisa kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uliotishwa na mamlaka ya usalama. Kamera zilikuwa zi tayari, na baadhi ya waandishi wa habari walikuwa wanawahoji watu waliokuwepo hapo kabla ya uongozi wa usalama kuwasili muda mfupi ujao.

Katika hali hiyo hiyo ya zaga zaga na zogo zogo, mwanaume mmoja aliyevalia koti jepesi refu la kaki, kofia pamoja na miwani nyeusi ya jua alipenya akaingia ndani ya uwanja wa mkutano ambamo alikuta watu wachache tu. Aliketi kwenye kiti cha nyuma kabisa akaanza kupepesa macho yake huku na huko ayasome mazingira.

Mwanaume huyo alipovua kofia yake hapo ndipo taswira ya Mamba ikaonekana kwa kujitosheleza – uso na kichwa chake visivyovutia ambavyo havikupoozwa na ndevu za bandia alizokuwa amejivika.

Alikunja nne akitizama saa yake kisha akabinua mdomo kana kwamba analaumu kutozingatiwa kwa muda. Alipotizama saa yake mara ya nne akasikia ving’ora huko nje na mara watu wakaanza kuingia ndani wakiongozana na viongozi wa usalama. Ndani ya dakika kumi na tano mbele mhadhara ukaanza kwa kutambulishwa kwa viongozi kisha kupewa nafasi kwa mkuu wa jeshi la polisi kutoa maneno.

Eneo zima la mhadhara lilikuwa limezingirwa na maafisa usalama wakiwa wametulia ndani ya sare za polisi na wengine ndani ya nguo za kiraia. Kwa haraka haraka Mamba aliwahesabu maafisa hao akapata idadi ya watu ishirini. Alisonya akichezea chezea ndevu zake bandia alafu akarusha macho yake kwa mkuu wa jeshi la polisi aliyekuwa anaendelea kubwabwaja kwa hisia za ukali na huruma juu ya usalama wa nchi, mkono wake wa kushoto akiwa ameshikilia kitambaa cha kujikaushia jasho.

Mamba alimtizama mkuu huyo wa jeshi la polisi kana kwamba anatizama katuni. Alididimiza mkono ndani ya koti akagusa bunduki yake na kifaa kidogo cheusi chenye umbo la mraba ambacho alikibonyeza na kutoa mkono mfukoni haraka, kifaa hicho kikaanza kuhesabu kuanzia dakika thelathini kushuka chini. Mamba akatabasamu alafu akaanza kuwatizama watu waliokuwa wamejaa humo kwa macho ya huruma. Moyoni alijua anawateketeza watu hao ndani ya muda mfupi tu ujao kama vile alivyofanya kwenye soko kuu, Kariakoo, na hii itaendelea kuwa salamu tamu kabisa kwa wale waliomteka mkubwa wake. Na hatoacha kufanya mauaji hayo mpaka pale wanaojiita WAGENI watajisalimisha.

Kwahiyo wakati dakika za kifaa cha mraba zaendelea kuyoyoma kushuka chini, Mamba alikuwa akifuatisha dakika hizo kwa kuzihesabu mdomoni akisubiria zibakie dakika chache tu apate kuyoyoma na kuwaachia wahanga msala.



****



Dakika za kwenye saa ya Vitalis zilikuwa zinaenda kwa kasi kwa mujibu wake. Aliona anachelewa kuwepo eneo la tukio kiasi kwamba akaona gari linanyata wakati alikuwa anaendesha kwa kasi yote. Mithili ya mtu anayeendesha gemu, Vitalis alikwepa magari mengine barabarani na kuyavuka. Alikuja kukanyaga breki kali mbele ya uwanja wa hoteli ya LAPF Tower, kabla hajashuka akapachika mustachi wa bandia na kujiveka miwani meusi ya jua.

Alitembea kwa kasi akaingia ndani ya jengo la hoteli lakini akapanda ghorofa la juu hivyo akawa anatizama mkutano ukiendelea kwa chini. Macho yake hayakutulia kwa kutizama. Alikuwa anamtafuta Mamba amekaa upanda gani ili apate kumshughulikia. Kwa dakika tatu alitafuta bila ya mafanikio, baadae macho yake yakatuama kwa mwanaume aliyekuwa amevaa koti na kofia.

Alimtilia shaka.

Alimchambua kwa macho yake makini akajidhihirishia kuwa ndiye mlengwa wake, Mamba, lakini akiwa katika muonekano tofauti. Alipomtizama zaidi akagundua ya kwamba Mamba alikuwa akinong’ona kana kwamba kuna kitu anasoma, na mkono wake wa kuume ulikuwa umetuama juu ya kitu fulani cha mraba.

Vitalis akazidi kupata shaka. Alihisi kabisa kile kitu ni bomu na vile anavyonong’ona Mamba basi atakuwa anahesabu muda. Lakini kabla hajafanya kitu, aliona Mamba akinyanyuka na kuondoka anaelekea chooni. Haraka Vitalis akashuka na kwenda huko.

Akiwa ananyata alirusha macho yake kumtafuta Mamba ameingia mlango gani wa choo. Alifungua mlango mmoja mmoja na kutizama asione kitu. Ulipobakia mlango mmoja tu, Vitalis akashusha pumzi kwanza kisha akaupiga teke mlango huo lakini namo hakukuta kitu, patupu!

Hapo hapo ghafla akahisi kitu cha baridi kisogoni kwake. Moja kwa moja akatambua ni mdomo wa bunduki. Mamba alikuwa amemzidi ujanja kwa kujibandika juu kisha akashuka taratibu nyuma yake.

“Ulidhani sikukuona?” Mamba aliuliza kwa dharau. “Kaa ukijua kwamba unapoishia wewe kufikiri ndipo mimi naanzia. Leo umejileta mwenyewe na nitakugeuza kuwa mshkaki pamoja na nyumbu zako wote waliopo humu ndani.”

Kisha akacheka kibabe.

“Kabla sijaondoa uhai wako, nakuahidi nitamaliza kikundi chako chote tena ndani ya juma moja tu.”

Wakati Mamba anahororoja Vitalis alinyanyua macho yake kutizama juu akaona bomu limepachikwa na lasoma dakika kumi na tano. Ni dakika chache mno kabla eneo hilo lote halijageuzwa kuwa tanuru. Hakukuwa na muda wa kupoteza kabisa, Vitalis aliwaza.

Kwa wepesi wa ajabu akageuka na kupangua mkono wa Mamba uliobebea bunduki kisha akafyatua mateke mawili makali yaliyomsomba Mamba na kumtupa chini huku bunduki ikirukia pembeni. Alirukia bomu na kulibandua kisha akaanza kuhangaika nalo alizime. Mamba akiwa amejawa na hasira akanyanyuka kwa pupa akikunja ngumi. Alirusha mateke mazito Vitalis akayakwepa huku akiendelea kuhangaika kuzima bomu. Alirusha ngumi mbili za mfululizo, moja ikamkosa Vitalis lakini nyingine ikatua tumboni na kumfanya Vitalis augulie vikali huku akimpa nafasi nzuri Mamba kumzabua tena na teke zito la mguu wake wa kulia. Vitalis akatupwa kando bomu likiruka upande wake wa kushoto.

“Huwezi kupambana na mimi wewe. Mbona hauna kitu kabisa!” Mamba alisema kwa kebehi. Sekunde moja tu mbele alijikuta yupo hewani baada ya kulambwa mtama mkali na Vitalis, kabla hajatua chini aliongezewa teke kali la mbavu likamcheusha damu na kumuacha akiugulia kwa maumivu makali. Vitalis akaendelea na shughuli yake ya kulizima bomu.





***





Baada ya dakika moja Mamba akanyanyuka tena apambane. Mara hii alitaka kuifuata bunduki yake ili amalize kazi kwa wepesi, ila kabla hajaifikia Vitalis aliilenga bunduki hiyo kwa bomu, bunduki ikaenda mbali zaidi. Ile Mamba kumtizama Vitalis akashangaa mtu yupo hewani kufumba na kufumbua akazawadiwa mateke mawili kwa pigo la kisigino, chali akaachwa hoi, mdomo wazi. Vitalis akaokota bomu na kuendelea kushughulika nalo sasa muda ukiwa umebakia dakika tano tu lilipuke na kugeuza eneo lote bahari ya moto.

Kwa uangalifu mkubwa, Vitalis akafukunyua bomu hilo na kukuta waya tatu zenye rangi tofauti tofauti. Aligusa kila waya na kusikilizia kwa muda kama inapitisha moto. Baada ya muda vidole vyake vikawa vimebakia na waya rangi ya njano tu baada ya akili yake kutambua kwamba ndio waya wa kuukata ili bomu likome.

Sasa ilikuwa ni kupata ama kukosa.

Kama atakuwa amelikosea bomu litafyatuka na kutekeza wote. Kama atakuwa amefanya mahesabu yake vyema, atakuwa ameokoa watu lukuki waliomo ndani ya jengo hilo.

Alishusha kwanza pumzi ndefu alafu akafunga macho. Kwanguvu zake zote akauvuta na kuukata waya huo wa njano. Bomu likaacha kuhesabu muda. Vitalis akatabasamu kwa kujipogeza. Akaikota bunduki na kumnyooshea Mamba apate kummaliza. Ila kabla uamuazi huo haujapita, akasikia vishindo vya watu vikija.

Wanaume watatu, maafisa wa usalama, walikuwa wanaongozana wakielekea maliwatoni wakiteta. Walipokamata korido ya uchaguzi wa vyoo wakashangaa kumkuta mwanaume, Mamba, amelala chini pembeni yake kukiwa na bomu na bunduki. Walitoa bunduki zao wakapekua pekua wasimuone mtu mwingine yeyote. Walimuweka Mamba chini ya ulinzi wakamtwaa na kumpeleka kituoni.

Kukutwa na ndevu bandia, bomu na bunduki kulimweka Mamba hatiani. Taarifa za habari ziliporushwa kutangaza hatia hiyo, ushahidi wa mlinzi wa soko kuu na mtoto wa marehemu waziri akisaidiana na Sandra ukazidi kukazia kamba kwenye hukumu ya Mamba.

Hakuwa na nafasi yoyote ya kuwa huru tena.



*****



Asubuhi hiyo bahari ilikuwa na mawimbi makubwa yenye hasira yaliyochapa fukwe kwa fujo na kutengeneza sauti ya nguvu. Jua lilikuwa kali pamoja pia na upepo wa bahari.

Ilikuwa ngumu kuamini kama kuna watu ndani ya maji ya bahari yaliyoonekana tu kwa macho kwamba ni marefu na yenye nguvu mpaka pale wanaume wawili: Vitalis na Kaguta, walipotoka kwenye maji hayo baada ya nusu saa wakiwa wamevalia nguo zilizobana miili yao barabara.

Walitembea kwa ukakamavu wakielekea kwenye makazi yao huku wakichonga maneno kuhusu siku ya nanenane. Walipofika ndani walimkuta mtoto tu, Marietta, akiwa amelala, wengine wote walikuwa upande wa pili wa fukwe wakifanya mazoezi mbalimbali ya kutengeneza pumzi na kujenga stamina.

Baada ya lisaa limoja wote walikutana mezani kupata kifungua kinywa, wakawa wanaongea na kupanga yale ya kutendeka ndani ya mkoa wa Dodoma, mkoa utakaoshuhudia sherehe ya nanenane kwa mwaka huo. Tageti yao kubwa ikiwa ni kuwakamata waamerika kusini watatu: Emilio, Cruz na Santanna.

“Tunafahamu fika kutakuwepo na pacha tatu mbili kwenye hiyo shughuli. Tunatakiwa tuwe wepesi zaidi wa kufanya maamuzi kuliko kawaida. Wote hapa tunajua jinsi mapacha walivyo haraka na wenye nguvu. Inahitajika matumizi ya akili zaidi. Hakikisha unatumia vyema sindano zenye dawa kuwafanya wawe dhaifu. Hakikisha pia unakuwa kwenye mawasiliano na wenzako. Na pia hakikisha watu hawa watatu wanakufa kwa gharama yeyote ile.” Vitalis alihutubia akiwatizama wenzake machoni. Wote wakaridhia na kufanya maongezi yawe mafupi zaidi kabla ya kumaliza kula, kupumzika na kisha kwenda kufanyia mazoezi walichopanga siku hiyo ya nanenane wakitumia miti iliyochongwa kama watu.

Zilipopita siku tatu ndipo ikawadia siku ya tukio – siku ya kufa ama kupona – tarehe nane mwezi wa nane. Vitalis akiwa amevalia suti nyeusi isiyo na tai aliongozana na wenzake: Kaguta, Jombi, Sandra, Bakari na Miraji wote wakiwa ndani ya suti nyeusi wakaingia ndani ya uwanja wa sherehe na kuketi juu kabisa.

Bakari alifungua tanakilishi akajaza mtandao. Alipobonyeza vitufe mara tatu akajiona alipo na wenzake kwenye ramani. Akatikisa kichwa na kuweka earphone.

“Tayari, nawaona wote sasa. Embu jaribu na sauti.”

Sandra aligeukia upande wake wa kushoto alafu akaongea maneno kadhaa, yote yakasikika kwa Bakari. Bakari akatikisa kichwa.

“Tayari na sauti pia. Mnaweza mkaenda sasa.”

Baada tu ya hayo maneno wote wakatawanyika wakimuacha Bakari peke yake na tanakilishi yake wakawa wanawasiliana kila mtu akiwa kwenye pande yake.

Baada ya muda mfupi:

“Kuna watu watatu wanaingia ukumbini sasa hivi, nadhani ndio watu tunaowatafuta.”

Sauti ya Vitalis ilifika masikioni mwa Bakari. Punde ikaambatana na picha kwenye tanakilishi.

“Umeziona hizo picha?”

“Ndio.” Bakari alijibu.

“Embu zitizame kama ni wenyewe.”

Bakari alifananisha picha hizo alizotumiwa na zile alizozipakua kwenye mtandao kuhusu kundi la kijambazi, majibu yakaja ni zenyewe baada ya macho kufanyiwa upembuzi.

“Ndio wenyewe.”

“Sawa sawa.”

Vitalis akawasiliana na wenzake kuwataarifu upande ambao mlengwa wao yupo ili wahakikishe hawawapotezi kisha taratibu akawa anatizama saa yake kana kwamba kuna jambo analingoja litokee muda si mrefu.

Uwanja ulikuwa umejaa watu pomoni. Vikundi mbalimbali vya wakulima na washikadau wa kilimo walikuwa tayari wameshajipanga kwa ajili ya maonyesho. Kila kitu kilikuwa kimeshajipanga kwa mujibu ya ratiba, ni waziri tu wa kilimo ndiye alikuwa anangojewa ili tafrija ipate anza.

“Sandra, Miraji, muda umewadia. Fanyeni kazi yenu sasa kabla waziri hajaingia!” Vitalis aliagiza. Baada tu ya hilo agizo mlipuko mkubwa ulitokea upande wa juu kabisa ambapo hamna watu. Watu wakaanza kukimbia huku na huko wakigombania milango ya kutokea nje.

Baada tu ya dakika chache, uwanja wote ulikuwa mweupe kasoro watu wachache mno. Vitalis pamoja na wenzake, pia Emilio, Santanna na Cruz wakiwa pamoja na kundi lao lenye watu kumi na nne – mapacha ndani. Milango yote ya uwanja ikafungwa na Miraji. Alafu sauti ya Bakari ikasema kwenye kipaza:

“Leo ni mwisho wenu, wapendwa.”

Kundi lote linalowalinda waamerika kusini likakusanyika na kuwaweka wakuu wao katikati. Lakini bado hawakujua wala kuona wanaopambana nao. Uwanja mzima walijiona wenyewe tu. Si Vitalis wala wenzake walikuwa wanaonekana wapi walipojificha.

Ni ghafla mlio wa kitu kama kamshale ukavuma. Kutizama, Pacha mmoja alikuwa amedungwa sindano mkono wake wa kuume. Punde tu, pacha huyo akalegea na kudondoka chini kama mzigo.

“Upande ulee!”

Mwanaume mmoja alielekezea kidole chake ilipotokea sindano – upande wa kulia. Wanaume watano wakaanza kukimbilia huko kabla ya sindano nyingine mbili kuruka tokea upande wa kushoto, zikawachoma mapacha wengine wawili na kuwaacha chini wamelegea.

“Upande huu!”

Mwanaume mwingine akaonyeshea kidole chake upande wa kushoto. Ila kabla hawajakimbilia huko, pacha mmoja akawaonyeshea ishara ya kuwakataza kisha akawaelekeza wajigawanye kwa kila upande. Wakafanya hivyo.

Sindano zingine tatu zilirushwa, mapacha waliobakia wakazidaka kwa mikono yao kabla hazijawakuta, wakazivunja na kuzitupilia mbali. Kisha wakakimbia haraka kufuata sehemu ambapo sindano hizo zimetokea. Huko wakakutana na Miraji upande wa kulia na Jombi upande wa kushoto wakiwa wameshikilia pinde zenye sindano.

Kabla mpambano haujajiri, taa zikazima kukawa giza. Zilipowaka zikawaka kwa fujo mno na kuwapiga usoni mapacha hao ambao walishindwa kuhimili – Vinasaba vya wanyama walivyonavyo mwilini haviwezi kustahimili mwanga mkali machoni. Kabla hawajakaa vyema walishashindiliwa sindano kwenye miili yao wakaachwa hoi hawajiwezi kwa lolote kwa chochote. Mapacha wote wakawa historia. Sasa wakabakia binadamu nane wa kawaida ambao hawakuwaumiza kichwa WAGENI kupambana nao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Vitalis alichukua wanaume wawili, vile vile Jombi, Kaguta na Miraji. Waliwasulubu wanaume hao kwa mateke na ngumi takatifu zilizowaacha wakilowea kwenye ulimwengu mchungu wa maumivu huku hakuna yeyote miongoni mwao aliyethubutu kurusha ngumi ama teke lolote lililofanikiwa kumgusa Vitalis au wenzake.

Baada ya hapo hakukuwepo tena na kizingiti kilichosimama mbele ya WAGENI. Hakuna mwanaume yeyote aliyekuwa mbele yao isipokuwa tu wale waliowafuata: Cruz, Santanna na Emilio tena wakiwa wamevaa nyuso za hofu baada ya kuona jinsi watumishi wao walivyosambaratishwa.

“What do you want from us?”





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog