Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

MIFUPA 206 - 5

  





    Simulizi : Mifupa 206

    Sehemu Ya Tano (5)





    “Nashukuru sana” hatimaye nikamwambia huku nikitabasamu kisha nikaitupia

    macho saa yangu ya mkononi. Ilikuwa ikielekea kutimia saa nne asubuhi hali

    iliyonipelekea nishtuke na kujilaumu kwa kulala muda mrefu kiasi kile.

    “Ulikuwa ukiongea na nani kwenye simu?” Iko-Ojo Obaje akaniuliza huku akitoa

    sigara kutoka kwenye pakiti mfukoni na kuibana mdomoni kisha kwa msaada wa

    kiberiti cha gesi kutoka mfukoni mwake akajiwashia na kuanza kuvuta huku mguu

    wake mmoja akiupandisha juu ya mwingine.

    “Mfanyakazi mwenzangu kuna mambo machache ya kiofisi tulikuwa tukiwekana

    sawa” niliongea kwa utulivu huku nikirudi pale kitandani na kujilaza.

    “Huyo mfanyakazi mwenzako anafahamu kuwa wewe upo hapa?” swali la Iko-

    Ojo Obaje likanipelekea nigeuke na kumtazama kwa udadisi hata hivyo sikuona

    tashwishwi yoyote usoni mwake.

    “Hapana” nikamjibu kivivuvivu.

    “Huendi kazini leo?”

    “Nitaenda hata hivyo nimechelewa sana” niliongea huku nikiamka kivivuvivu pale

    kitandani na kuketi tena huku nikimzama Iko-Ojo Obaje na macho yetu yalipokutana

    kila mmoja akaangua tabasamu.

    “Vipi uchovu?” hatimaye nikamuuliza.

    “Umepungua” Iko-Ojo Obaje akaongea huku akiangua kicheko hafifu baada ya

    kuitoa sigara yake mdomoni kisha akaendelea

    “Wewe ni mwanaume uliyenifanya niukumbuke ujana wangu kwa usiku mmoja

    tu” akaongea huku akinikata jicho la mahaba na kutabasamu.

    “Unaonekana mwanamke wa miaka thelathini na kitu lakini kitandani hautofautiani

    na binti wa sekondari” nilichombeza utani na kupelekea wote tuangue kicheko

    mle ndani. Hatimaye nikasimama na kuelekea bafuni kuondoa uchovu. Nilikuwa

    nimekumbuka kazi iliyokuwa ikinikabili mbele yangu hivyo sikutaka kuendelea

    kupoteza muda zaidi mle ndani. Iko-Ojo Obaje akanisindikiza kwa macho yake

    nyuma yangu hadi pale nilipopotelea kwenye kile chumba cha bafu la mle ndani na

    kufunga mlango nyuma yangu.

    Muda mfupi baadaye nilitoka ndani ya kile chumba cha bafu nikiwa mwepesi

    na mbali na uchovu na hapo nikamkuta Iko-Ojo Obaje akiwa tayari amekwisha

    agiza kifungua kinywa chenye taftahi za kila aina. Mle ndani pale kitandani nilikuta

    Iko-Ojo Obaje akiwa ameshazitoa zile nguo kwenye ule mfuko na kuzitandaza

    pale kitandani nami nikajiridhisha kuwa alikuwa amefanya uchaguzi mzuri wenye

    kuzingatia vigezo vyangu. Alikuwa ameninunulia suruali nyeusi ya kadeti,boksa ya

    rangi ya bluu bahari,bukta safi ya rangi nyeupe,singlet nyeupe,fulana moja ya kijivu

    yenye mstari mweusi kifuani na kofia nyeusi ambapo nilipomaliza kuvaa viliubadili

    kabisa muonekano wangu na kunifanya nipendeze na hapo nikageuka kumshukuru

    Iko-Ojo Obaje ambaye alikuwa akinitazama kwa makini pale kwenye kochi alipoketi.

    Nilipomaliza kujiandaa nikasogea kwenye ile meza na kuketi tukipata kifungua kinywa

    kile kwa pamoja. Asubuhi hii mbele yangu nilimuona Iko-Ojo Obaje katika uzuri

    wa hali ya juu. Macho yake yaliponitazama yakapeleka hisia kali za mapenzi moyoni

    mwangu na kunipelekea nijisifu moyoni mwangu kwa kustarehe na mwanamke mzuri

    kama yule. Ingawa nilikuwa sijaamua kabisa kuwekeza kwenye masuala ya mahusiano

    ya mapenzi lakini sasa mbele ya Iko-Ojo Obaje mpango huo taratibu ulikuwa

    umeanza kuumbika kichwani mwangu. Iko-Ojo Obaje alikuwa amefanikiwa kuuteka

    moyo wangu,mwanamke mwenye sifa zote za uzuri ambaye ingenichukuwa miaka

    mingi sana kusahau aliyonifanyia kwenye kitanda cha mle ndani kwa muda wa usiku

    mmoja tu tuliyokuwa pamoja.

    Wakati nikiendelea kupata kile kifungua kinywa nikajikuta nikimtazama Iko-Ojo

    Obaje kwa udadisi mbele yangu. Kwa namna moja au nyingine sikuwa nimemuelewa

    vizuri mwanamke yule kuwa alikuwa ni mtu wa namna gani hasa pale nilipokumbuka

    kiasi kingi cha zile pesa za kigeni,dola za kimarekani kilichokuwa chini ya nguo

    kwenye lile sanduku mle ndani kabatini pamoja na zile kadi nyingi za ATM za benki

    za kimataifa. Kisha nikajikuta nikiikumbuka ile pasi yake ya kusafiria yenye picha yake

    na jina la Chimamanda Okechukwu. Ingawa Iko-Ojo Obaje hakuwa ameniambia

    kiundani zaidi juu ya masuala yake lakini kwa tafsiri ya haraka nilianza kumfananisha

    na mfanyabiashara mkubwa ingawa bado sikuweza kufahamu ni biasha gani ambayo

    angekuwa akiifanya. Labda hakutaka kuniweka wazi jina lake kama walivyo wanawake

    wengi wa zama hata hivyo nikajikuta nikijiuliza ni kwanini alikuwa na kadi nyingi za

    ATM za benki nyingi za kimataifa tena zenye majina tofauti kiasi kile.

    Hatimaye nilimaliza kupata kifungua kinywa kile na kumshukuru Iko-Ojo Obaje

    kwa ukarimu wake kisha nikasimama na kuelekea dirishani ambapo nilisogeza pazia

    pembeni na kutazama mandhari ya chini ya hoteli ile. Nikiwa pale dirishani mawazo

    mengi yakawa yakipita kichwani mwangu nikifikiria juu ya kazi iliyokuwa ikinikabili

    mbele yangu. Sikufahamu kuwa mara baada ya kutoka pale nilipaswa kuelekea wapi

    na kufanya nini hata hivyo niliamini kuwa kuendelea kukaa mle ndani isingekuwa

    suluhisho la kupata majibu ya maswali yangu. Nilihitaji kupiga hatua nyingine zaidi

    katika harakati zangu.

    Wingu zito la mvua lilikuwa limeanza kutanda angani na hivyo kuipelekea miale

    ya jua lile la asubuhi kufifia hali iliyonipelekea nilikumbuka lile koti langu nyuma ya

    mlango wa kile chumba kuwa lingeweza kunisaidia kufanya mizunguko yangu mitaani

    bila kulowana endapo mvua ile ingeanza kunyesha. Hatimaye nikaliacha lile dirisha

    na kufunga pazia kisha nikageuka na kumtazama Iko-Ojo Obaje pale kwenye kochi

    alipoketi.

    “Ni lini umepanga kuondoka hapa Dar es Salaam?” nikamuuliza kwa utulivu huku

    nikimtazama kwa sura ya kirafiki.

    “Viza yangu inaniruhusu kukaa hapa nchini kwa muda wa mwezi mmoja hata

    hivyo kuwenda nikaondoka mapema zaidi kutegemeana na nitakavyoamua” Iko-Ojo

    Obaje akanijibu kwa utulivu baada ya kutoa sigara mdomoni na kuupuliza moshi

    pembeni huku taratibu akiutikisa mguu wake mmoja kwenye lile kochi.

    “Nahitaji kuelekea kazini sasa”nikamwambia Iko-Ojo Obaje huku nikiitazama saa

    yangu ya mkononi kisha nikayapeleka tena macho yangu kumtazama.

    “Usiku wa leo tutaonana?” Iko-Ojo Obaje akaniuliza huku usoni akiumba

    tabasamu hafifu

    “Nipo tayari kuja tena kama utanikaribisha” nikaongea huku nikitabasamu.

    “Nitapenda kukuona tena kama utapata nafasi” jibu la Iko-Ojo Obaje likanipelekea

    niangue kicheko hafifu kwani ni dhahiri kuwa nilikuwa nipo tayari kujifungia mle

    chumbani na mrembo yule hadi pale ambapo angenichoka lakini kizingiti kikubwa

    sasa kilikuwa ni juu ya majukumu yaliyokuwa mbele yangu.

    “Nashukuru sana” hatimaye nikamwambia kisha nikasogea kwenye ule mlango

    na kulichukua lile koti langu na kulivaa halafu nikamuaga Iko-Ojo Obaje na kufungua

    mlango nikitoka nje.

    _____

    NILIKUWA SIJAFIKA MBALI BAADA YA KUSHUKA kwenye teksi eneo

    la posta nikitoka kule Hotel Agent 11 wakati simu yangu ilipoanza kuita mfukoni.

    Haraka nikaingiza mkono mfukoni na kuichukua hata hivyo kabla sijaipokea simu

    ile nikageuka haraka na kuyatembeza macho yangu eneo lile kuzikagua sura za watu.

    Sikuona sura yoyote ya kuitilia mashaka hivyo haraka nikalitazama jina la mpigaji na

    kuiweka simu sikioni kabla ya kubofya kitufe cha kupokelea. Mwasu alikuwa akinipigia

    na tukio lile lilikuwa limenipelekea niingiwe na wasiwasi kwani muda mfupi tu uliyopita

    nilikuwa nimetoka kuongea naye kwa simu. Sauti ya Mwasu ilikawia kunifikia sikioni

    ingawaje nilipotega vizuri sikio langu kusikiliza kwenye ile simu nikagundua kuwa

    Mwasu alikuwa akitembea nusu ya kukimbia huku akihema ovyo.

    “Mwasu kuna nini?”

    “Chaz…”

    “Nakusikia Mwasu zungumza kuna nini?” nikauliza kwa mashaka.

    “Upo wapi?” Mwasu akauliza huku akihema ovyo na kupitia kitetemeshi cha sauti

    yake nikahisi jambo la hatari.

    “Niko maeneo ya posta nje ya jengo la Benjamin William Mkapa Tower. Niambie

    Mwasu kuna nini?”

    “Kuna wanaume watatu wako nyuma yangu wananifuatilia. Chaz tafadhali nahitaji

    msaada wako” Mwasu akaongea kwa hofu.

    “Wanaume watatu?,wameanza kukufuatilia kutoka wapi na wewe upo wapi sasa

    hivi?” nikamuuliza Mwasu kwa udadisi.

    “Walikuja ofisini kukuulizia walipoona haupo wakataka kunikamata nikafanikiwa

    kuwatoroka hata hivyo wamenishtukia na sasa wapo nyuma yangu wananifuata.

    Tafadhali nahitaji msaada wako Chaz hawa watu wanaonekana kuwa si wema”

    Mwasu akaendelea kunitahadharisha huku akitembea kwa kasi.

    “Niambie tafadhali upo wapi?” nikamuuliza Mwasu kwa papara hata hivyo Mwasu

    hakunijibu badala yake nikamsikia akianza kutimua mbio.

    “Mwasu niambie tafadhali upo wapi mbona huongei?” nikamuuliza huku

    nimeshikwa na taharuki. Nikiwa bado nimeishikilia simu yangu sikioni mara sauti ya

    Mwasu ikarudi tena hewani.

    “Nahitani msaada wako wa haraka Chaz hawa watu wanakaribia kunifikia na

    wameshika bastola mikononi mwao” Mwasu akalalamika kwa hofu.

    “Okay!Mwasu niambie mahali ulipo nitafika sasa hivi” nikaongea kwa msisitizo.

    “Nipo kwenye barabara ya mtaa wa Jamhuri nakaribia kwenye mashine za ATM

    za benki ya NMB eneo la posta” Mwasu akaongea kwa msisitizo huku sauti yake

    ikitawaliwa na hofu. Maelezo ya Mwasu yakaipelekea akili yangu kuanza kufanya

    kazi haraka. Kutoka pale nilipokuwa nilitambua kuwa sikuwa mbali sana na sehemu

    alipokuwa Mwasu hivyo bado nilikuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kumuokoa

    kutoka kwa watu wale hatari. Bila kupoteza muda nikaanza kutimua mbio nikishika

    ule uelekeo wa kwenda kukutana na ile barabara ya Jamhuri upande wa kulia.

    “Nakuja Mwasu nipo hapa jengo la Benjamin William Mkapa Tower ondoa shaka

    nafika hapo sasa hivi” nikamtoa hofu Mwasu na kuanza kutimua mbio

    “Fanya haraka Chaz hawa watu ni hatari” Mwasu akasisitiza huku akiendelea

    kutimua mbio

    “Umebeba kitu chochote?” nikamuuliza

    “Nimebeba mkoba wangu na ndani una External hard disc yenye mafaili ya kazi

    zote za ofisini” Mwasu akanitanabaisha.

    “Hakikisha kwa namna yoyote ile hao watu hawafanikiwi kuupata huo mkoba”

    nikamsisitiza Mwasu huku nikitimua mbio kuelekea kule alipokuwa. Baadhi ya

    watu waliopishana na mimi wakati nikitimua mbio kuelekea kule alipokuwa Mwasu

    waligeuka na kunishangaa hata hivyo sikuwatilia maanani badala yake nikaendelea

    kuchanganya miguu nikitimua mbio huku nikitazama huku na kule mbele yangu.

    Nilipofika kwenye ile kona ya kuingia barabara ya mtaa wa Jamhuri nikapunguza

    mwendo na kusita kidogo baada ya kuona kundi kubwa la watu wakitimua mbio

    kutoka kwenye ile barabara. Haraka nikajikuta nikiingiza mkono kwenye koti langu na

    kuikamata vyema bastola yangu hata hivyo nikajikuta nikiachana na mpango ule baada

    ya kuhisi kuwa sikuwa na ushahidi wa kutosha juu ya nini kilichokuwa kikiendelea

    eneo lile. Sikutaka kupoteza muda hivyo bila kusubiri nikaongeza tena mwendo

    nikilipangua lile kundi la watu mbele yangu na wakati nikifanya vile nikasikia baadhi

    ya watu wakisema kule nyuma kulikuwa na majambazi watatu waliokuwa wakitaka

    kuupora mkoba wa dada mmoja wenye pesa.Tathmini yangu ya haraka ikaniambia

    kuwa watu hao hawakuwa majambazi ila wangekuwa ndiyo wale watu waliokuwa

    wakimfukuza Mwasu.

    Mara tu nilipoingia kwenye ila barabara ya mtaa wa Jamhuri nikamuona mwanamke

    mmoja aliyevaa blauzi nyeupe na suruali ya bluu ya jeans akitimua mbio usawa wa

    zile mashine za ATM za benki ya NMB. Alikuwa ni Mwasu nilipomchunguza vizuri

    nikamtambua na mkononi alikuwa amebeba mkoba wake wa ngozi. Mwasu hakuwa

    na viatu vyake virefu vya mikanda miguuni kama nilivyozoea kumuona badala

    yake alikuwa akitimua mbio pekupeku hali iliyowapelekea watu waliokuwa eneo

    lile kumshangaa kwa kitendo kile. Nilipoendelea kuchunguza nyuma yake kiasi cha

    umbali usiopungua hatua thelathini nikawaona wanaume watatu waliovaa suti nadhifu

    nyeusi na miwani nyeusi machoni mwao wakitimua mbio kumfukuza Mwasu huku

    wameshika bastola zao mikononi.

    Kwa mwendo ule wa kasi ya wale watu nilifahamu fika kuwa Mwasu asingefika

    mbali kabla ya wale watu hawajamfikia na kumkamata ingawa nilikuwa na hakika

    kuwa hadi kufikia pale Mwasu alikuwa amejitahidi sana kukimbia katika kuhakikisha

    kuwa wale watu hawamkamati. Sikutaka kusubiri hadi nione wale watu ambavyo

    wangemfikia Mwasu na kumkamata hivyo haraka nikauingiza mkono wangu kwenye

    mfuko wa koti na kuichomoa bastola yangu mafichoni. Muda mfupi uliofuata

    nilikuwa nikikatisha kwenye ile barabara ya Jamhuri na kuelekea ule upande wa pili

    wa ile barabara kumuokoa Mwasu. Hata hivyo sikufanikiwa kwani magari mengi

    yaliyokuwa yakikatisha mbele yangu yakanizuia kama siyo kunichelewesha na wakati

    nikisubiri yale magari yapite mbele yangu ili niweze kuvuka na kwenda upande wa pili

    wa ile barabara jambo moja la kushangaza likatokea.

    Ghafla nikaliona gari moja jeusi aina ya Toyota Noah likichomoza kwa kasi kutokea

    barabara ya Morogoro. Haraka nikafahamu ni maana ya tukio lile hivyo nikapiga

    kelele kumuita Mwasu upande wa pili wa ile barabara. Mwasu akawahi kunisikia na

    kugeuka upande ule kunitazama hata hivyo hakupunguza mwendo kwani wale watu

    walikuwa mbioni kumfikia. Nikiwa nimeanza kuhisi nini ambacho kingefuatia baada

    ya pale sikutaka kuendelea kusubiri yale magari mbele yangu yamalize kupita ndiyo

    nivuke ile barabara. Hivyo nikaongeza kasi na kujitupa kimgongomgongo juu ya

    boneti ya Toyota Cresta iliyokuwa ikikatisha mbele yangu. Dereva wa lile gari kuona vile

    akawahi kushika breki hata hivyo wakati akisimama mimi tayari nilikuwa nimeshatua

    chini upande wa pili wa ile barabara alipokuwa Mwasu na wale watu waliokuwa

    wakimkimbiza. Wale watu ni kama walikuwa hawajaniona au huwenda walikuwa

    wamenipuuza badala yake waliendelea kutimua mbio na bastola zao mikononi huku

    makoti yao ya suti yakipepea kama vishada kumfukuza Mwasu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Mwasu alikuwa ameniona wakati nilipokuwa kwenye jitihada za kuvuka

    ile barabara hivyo nilikuwa na hakika kuwa pia aliamini kuwa wakati ule tayari

    ningekuwa nimeshavuka ile barabara na kuingia ule upande aliokuwa yeye na wale

    watu wanaomfukuza hivyo akageuka nyuma na kunitazama. Macho yetu yalipokutana

    nikaiona hofu iliyotanda usoni mwake hata hivyo Mwasu hakusimama na wakati

    akiifikia ile barabara ya Morogoro ile gari Toyota Noah nyeusi nayo tayari ilikuwa usawa

    wake nikakazana kutimua mbio nikikata upepo kuwakaribia wale watu kwa nyuma.

    Hata hivyo kabla sijawafikia wale watu ghafla nikauona mlango wa ubavuni wa

    ile Toyota Noah nyeusi ukifunguliwa kisha wakashuka watu wawili kwa haraka sana na

    kumkamata Mwasu wakimbeba mzegamzega na kumtupia ndani ya lile gari. Haraka

    nikapaza sauti kumuita Mwasu,Mwasu akageuka kwa taabu kunitazama katika uso wa

    kukata tamaa huku amebebwa juu juu hadi alipotupiwa ndani ya lile gari.

    Matumaini ya kumuokoa yakiwa yamepungua sikutaka kuendelea kusubiri zaidi

    hivyo nikaikamata vyema bastola yangu mkononi. Niliwaona wale watu watatu

    waliokuwa wakimfukuza Mwasu wakizidisha mbio kuukaribia mlango wa ile gari

    Toyota Noah nyeusi na hapo nikajua kuwa wale watu waliokuwa wakimkimbiza

    Mwasu walikuwa shirika moja na watu waliokuwa ndani ya ile gari. Nikiwa naikaribia

    ile gari nikawaona wale watu nao wakiingia kwenye ile Toyota Noah nyeusi. Kuona vile

    nikautupa mkono wangu wa shabaha na kuvuta kilimi cha bastola. Majibu yalikuwa

    ya hakika na yaliyonifurahisha. Risasi zangu mbili nilizozifyatua zikampata vizuri yule

    mtu wa nyuma kabisa kati ya wale watu watatu waliokuwa wakimfukuza Mwasu.

    Risasi moja ikapenya kwenye mfupa wa paja la mguu wake wa kushoto na nyingine

    ikampata begani mwake. Yule mtu akapiga yowe kali la hofu na kupiga mwereka

    wa nguvu akianguka chini huku bastola yake ikimponyoka mkononi. Wale wenzake

    kuona vile wakasita kidogo lakini kitendo cha kugeuka nyuma na kuniona wakawahi

    kujirusha ndani ya ile Toyota Noah nyeusi na hapo ule mlango ukafungwa kwa pupa

    huku ile gari ikiondoka kwa kasi eneo lile.

    Sikukata tamaa nikampita yule mtu niliyemchapa risasi na kuzidi kutimua

    mbio nikilifukuza lile gari kwa nyuma na wakati nikifanya vile nikawa nikiendelea

    kumuita Mwasu kama mwehu. Watu waliokuwa wakifuatilia lile tukio wakasimama

    na kunishangaa hata hivyo sikuwatilia maanani badala yake nikaendelea kutimua

    mbio nikilifukuza lile gari. Lile gari likaendelea na safari kwa mwendo wa kasi na

    lilipomaliza kuuvuka ule mzunguko wa barabara wa Askari Monument nikaona kitu

    fulani kikirushwa kutoka kwenye dirisha moja la upande wa kushoto wa lile gari

    na kuangukia kando ya ile barabara.Mara nikaliona lile gari likipunguza mwendo

    lakini ghafla likaongeza kasi tena pale nilipoanza kulinyooshea bastola. Hata hivyo

    nikaachana na mpango wa kulifyatulia risasi kwani lile gari tayari lilikuwa limeingia

    kwenye eneo la msongamano ingawa dereva wa lile gari alikuwa makini na alipopata

    upenyo mdogo akautumia vizuri kuniacha solemba.

    Muda mfupi uliofuata nikavuka ile barabara nikienda kuokota kile kitu

    kilichotupwa dirishani kutoka katika lile gari nililokuwa nikilifukuza ambalo sasa

    lilikuwa limefanikiwa kunitoroka. Nilipofika lile eneo nikauona ule mkoba wa ngozi

    wa Mwasu na hapo nikapata matumaini kidogo. Haraka nikauokota ule mkoba na

    nilipolitazama lile gari nikaliona kuwa tayari lilikuwa limeshapita eneo la New Afrika

    Hotel na lilipofika mbele likaingia upande wa kushoto kuifuata ile barabara ya Kivukoni

    na baada ya muda mfupi lile gari likawa limepotea kabisa machoni mwangu. Mwasu

    alikuwa ametekwa.

    Niliendelea kusimama lile eneo huku mikono yangu nimejishika kiunoni katika

    hali ya kukata tamaa na mawazo mengi yakipita kichwani mwangu. Watu wakawa

    wakinishanga hata hivyo sikujishughulisha nao. Nilitamani kukodi bodaboda na

    kuanza kulifukuza lile gari hata hivyo wazo hilo nikaliweka kando kwani eneo lile

    halikuwa na huduma ya usafiri wa bodaboda kutokana na sheria za jiji la Dar es

    Salaam kukataza usafiri wa bodaboda maeneo ya mijini katika namna ya kupunguza

    msongamano barabarani. Labda usafiri wa teksi ungeweza kunisaidia lakini nilijua

    kuwa kwa muda ule tayari nilikuwa nimechelewa kwani kutoka pale nilipokuwa

    hadi kwenye eneo la maegesho ya teksi kulikuwa na umbali kiasi kwamba hadi pale

    ambapo ningefanikiwa kupata usafiri lile gari lingekuwa tayari limekwisha fika mbali

    hivyo nikaachana na mpango ule.

    Watu walikuwa wameanza kukusanyika wakinishangaa na kwa kweli sikuipenda

    kabisa hali ile hivyo haraka nikairudisha bastola yangu ndani ya koti na kuanza kurudi

    haraka kule nilipotoka. Nilimkuta yule mtu niliyempiga risasi akiwa bado amelala pale

    chini huku akigugumia kwa maumivu makali ya zile risasi sambamba na damu nyingi

    iliyokuwa ikiendelea kutoka kwenye yale majeraha. Hata hivyo wakati huu yule mtu

    alikuwa amezungukwa na kundi kubwa la mashuhuda ambao mara tu waliponiona

    wakaanza kutawanyika. Sikutaka kupoteza muda eneo lile hivyo nilipomfikia yule

    mtu nikaiokota ile bastola yake kisha nikamnyanyua yule mtu na kumtupia begani

    kwangu halafu nikielekea kwenye maegesho ya teksi yaliyokuwa jirani na eneo lile.

    Muda mfupi uliyofuata mimi na mateka wangu tulikuwa kwenye teksi tukielekea eneo

    la Magomeni sehemu kulipokuwa na hospitali moja ya kichochoroni yenye huduma

    nzuri ambapo niliamini kuwa yule mateka wangu angepatiwa tiba ya kuaminika kabla

    ya mahojiano ya kina kufuatia.



    #254

    CHUMBA KILIKUWA KIKUBWA chenye umbo mraba la kuta safi

    zilizonyooka vizuri. Kulikuwa na mlango mmoja tu wa chuma mkubwa na

    mweusi uliokuwa kwenye kona moja ya kile chumba upande wa kushoto na

    mlango ule ulikuwa umefungwa kikamilifu kwa nje. Ukutani hapakuwa na dirisha

    hata moja na hivyo kupelekea giza zito kutanda mle ndani. Sakafu ya chumba kile

    ilitengenezwa kwa tarazo nadhifu yenye nakshi nzuri za kila namna. Joto la chumba

    lilikuwa kali ingawa hewa ya mle ndani ingeweza kumruhusu binadamu yeyote kuishi.

    Katikati ya chumba kulikuwa na meza ya mbao ndefu na pana kiasi yenye umbo

    mstatili chini ya balbu ya umeme yenye mwanga mkali iliyokuwa imeshikiliwa na waya

    mrefu wa umeme kutoka juu ya dari ya chumba kile. Upande wa pili wa meza ile

    kulikuwa na viti vitatu vya ofisini vyenye foronya laini vyeusi. Upande mwingine wa

    meza ile kulikuwa na kiti kimoja cha chuma chenye mikanda maalum na nikatika kiti

    kile ndipo Mwasu alipokuwa ameketi na zaidi ya pale hapakuwa na mtu mwingine mle

    ndani isipokuwa ukimya wa kutisha.

    Fahamu zilikuwa zimeanza kumrudia Mwasu taratibu huku kumbukumbu sahihi

    zikianza kujitengeneza upya kichwani mwake. Taratibu akayafumbua macho yake kwa

    shida kabla ya kuanza kuyatembeza mle ndani. Hata hivyo ubongo wake ukakawia

    kumletea tafsiri ya haraka juu ya taswira zilizokuwa zikijengeka machoni mwake na

    badala yake akajikuta akipambana na maumivu makali yaliyofufuka upya kutoka

    sehemu ya nyuma ya kichwa chake na kusambaa mwili mzima. Kabla ya kuanza

    kujiuliza pale ni wapi taratibu akajikuta akianza kukumbuka mambo yaliyomtokea

    huko nyuma.

    Akiwa bado ameketi kwenye kile kiti Mwasu akajikuta akiwakumbuka wanaume

    watatu waliovaa suti nyeusi nadhifu wakati walipofika ofisini kwake na kumuulizia

    Chaz Siga huku wakijitia kuwa walikuwa wakihitaji msaada wake wa haraka.

    Akaendelea kukumbuka namna alivyowakaribisha vizuri wanaume wale ofisini kabla

    ya kuanza kuingiwa na mashaka dhidi yao baada ya kumuona mmoja miongoni mwao

    akiwa ameichomeka bastola yake kiunoni kwa hila huku amening’iniza pingu pindi

    alipolisogeza koti la suti yake kwa bahati mbaya wakati alipokuwa akijiandaa kuketi

    katika viti vya wageni vilivyokuwa mle ndani ofisini.

    Mwasu akaendelea kukumbuka namna alivyowahadaa watu wale kuwa ile

    haikuwa ofisi ya Chaz Siga ama mtu waliyekuwa wakihitaji kumuona kauli ambayo

    wale watu hawakuwa tayari kuiamini hata kidogo kiasi cha kutoa vitambulisho

    vyao vinavyowatanabaisha kuwa wao ni wanausalama na kumwonesha huku

    wakimtahadharisha kuwa wangemuweka chini ya ulinzi endapo angekataa kuwapa

    ushirikiano wa kutosha. Mwasu akaendelea kukumbuka namna alivyojitia kukubaliana

    na hoja ya wale watu huku akijidai kuingia kwenye ofisi ya Chaz Siga na kumpigia

    simu Chaz Siga ili kumfahamisha kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wakimsubiri

    pale ofisini. Mwasu akaendelea kukumbuka namna alivyoutumia mlango wa dharura

    uliokuwa kwenye ofisi ya Chaz Siga kuwatoroka wale watu huku wakiwa bado

    wameketi kwenye viti vya wageni vya ile ofisi wakimsubiri.

    Mwasu bado akaendelea kukumbuka namna alivyogeuka nyuma wakati alipokuwa

    akitembea kwenye barabara ya tatu kutoka kule ilipokuwa ile ofisi na kushtukia kuwa

    wale watu aliowatoroka kule ofisini walikuwa nyuma yake hatua chache karibu

    kumfikia hali iliyompelekea aanze kutimua mbio akiwakimbia wale watu kabla ya

    kumpigia simu Chaz Siga na kumfahamisha juu ya tukio lile. Kumbukumbu kamili

    zikiwa mbioni kujengeka kichwani mwake Mwasu akajikuta akikumbuka namna

    alivyoitwa na Chaz Siga katika yale makutano ya barabara ya Jamhuri na barabara ya

    Morogoro muda mfupi kabla hajatekwa na wale watu waliokuwa ndani ya gari nyeusi

    aina ya Toyota Noah iliyokuja na kusimama ghafla kando yake wakati alipokuwa

    akiendelea kutimua mbio kuwakimbia wale watu waliokuwa wakimfukuza nyuma

    yake. Kufikia pale akajikuta akikumbuka namna alivyomuona Chaz Siga akitimua

    mbio kulifukuza lile gari lililotumika kumteka muda mfupi baada ya milio miwili ya

    risasi kusikika nyuma yake kabla ya wale watu wawili miongoni mwa wale watu watatu

    waliokuwa wakimfukuza nao kuingia kwenye lile gari na kisha lile gari kuondoka kwa

    kasi eneo lile.

    Kumbukumbu zile zikapelekea tabasamu jepesi kuanza kuchomoza usoni kwa

    Mwasu pale alipokumbuka namna alivyofanikiwa kuurusha mkoba wake wa ngozi

    kupitia kwenye dirisha moja la lile gari wakati alipogeuka nyuma na kumuona Chaz

    Siga akitimua mbio kulifukuza lile gari nyuma yao. Ni katika ule mkoba wake wa

    ngozi ndiyo kulipokuwa na taarifa zote muhimu za ofisini ikiwemo ile External hard

    disc yenye mafaili chungu mzima ndani yake likiwemo faili la upelelezi wa mkasa wa

    Mifupa 206 ambalo upelelezi wake ulikuwa bado ukiendelea kufanyika pamoja na simu

    yake ya mkononi. Hivyo alikuwa na hakika kuwa hadi kufikia wakati ule wale watekaji

    walikuwa hawajafanikiwa kupata kitu chochote cha maana kutoka kwake na hivyo

    kujikuta akipata faraja.

    Mwasu akaendelea kukumbuka namna alivyopigwa na kitu kizito nyuma ya kichwa

    chake muda mfupi mara baada ya lile gari jeusi Toyota Noah liliyotumika kumteka

    lilipoingia kwenye barabara ya Kivukoni na kuanza kutimua mbio. Kufikia pale

    hakufahamu tena kilichoendelea hali iliyompelekea aamini kuwa alikuwa amepoteza

    fahamu baada ya shambulio lile la nyuma ya kichwa chake.

    Ndani ya chumba kile kikubwa Mwasu akajikuta akiyatembeza macho yake

    taratibu mle ndani huku mawazo mengi yakipita kichwani mwake. Sasa hakuwa na

    shaka yoyote kuwa watekaji wale ndiyo waliokuwa wamemfikisha kwenye chumba

    kile huku akiwa bado amepotewa na fahamu. Alipoanza kujichunguza akagundua

    kuwa mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa kwa mikanda maalum ya kile kiti cha

    chuma alichoketi hata hivyo hali ile haikumshtua kwani alifahamu haraka ni maana

    ya tukio lile.

    Hivyo akaendelea kuyachunguza mandhari yale huku akili yake ikiendelea

    kusumbuka katika kutaka kufahamu pale alikuwa wapi ingawaje hisia zake zilimueleza

    kuwa alikuwa kwenye chumba fulani cha siri katika jengo moja la ghorofa lililoko

    kando kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Giza lililokuwa mle ndani likampelekea ashindwe

    kufahamu muda ule ulikuwa ni saa ngapi na kama mchana au usiku huku akiwaza nini

    ambacho kingefuatia baada ya pale.

    Kelele za ghafla za kufunguliwa kwa mlango wa kile chumba zikayakatisha mawazo

    ya Mwasu na hapo akageuka nyuma na kuutazama ule mlango kama bomu lililokuwa

    limebakisha sekunde chache kabla ya kulipuka. Muda mfupi uliofuata ule mlango

    ukafunguliwa kisha wakaingia wanaume wanne,watatu miongoni mwao wakiwa ni

    wenye umri wa kati ya miaka arobaini na tano hadi hamsini na mbili. Mmoja alikuwa

    kijana wa miaka thelathini na kitu huku wote wakiwa wamevaa suti nyeusi nadhifu

    zilizowakaa vyema katika miili yao mikubwa na mirefu yenye afya.

    Mara tu wale watu walipoingia mle ndani yule kijana akaufunga ule mlango nyuma

    yao wakati wale wanaume wengine watatu walipokuwa wakielekea kwenye vile viti

    vitatu vilivyokuwa upande wa pili wa ile meza katika nyuso zisizokuwa na chembe

    ya mzaha. Walipofika wakavuta vile viti nyuma na kuketi huku yule kijana akienda

    na kusimama kwa nyuma. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata mle ndani huku kila

    mmoja akionekana kumtegea mwenzake kuongea. Mwasu alipoyatembeza macho

    yake kuwatazama wale watu akagundua kuwa wote sura zao zilikuwa ngeni kabisa

    machoni mwake isipokuwa yule kijana aliyesimama mwisho wa ile meza ambaye

    haraka alimkumbuka kuwa alikuwa miongoni mwa wale watu watatu waliofika kule

    ofisini kumuulizia Chaz Siga.

    Mkurugenzi mkuu wa idara ya usalama wa taifa M.D. Kunzugala sasa alikuwa

    ameketi katikati ya kamishina wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini Evans Mchafu

    upande wa kulia na mkuu wa intelijensia ya usalama wa taifa Sulle Kiganja upande wa

    kushoto. Taarifa za kukamatwa kwa Mwasu kama mmoja wa washukiwa waliokuwa

    wakitafutwa kuhusiana na mauaji ya wanausalama wake zilikuwa zimeifikia ofisi yake

    mapema sana na hivyo kurejesha tumaini kubwa la kuendelea kutetea wadhifa wake.

    Na sasa M.D Kunzugala na wanausalama wake waandamizi walikuwa wameingia

    kwenye chumba kile cha siri kufanya mahojiano na Mwasu kufuatia matukio ya mauaji

    ya maafisa usalama yaliyokuwa yakiendelea kutokea jijini Dar es Salaam.

    Ukimya kidogo ulipokuwa mbioni kutawala mle ndani M.D.Kunzugala akageuka

    na kuwatazama wale maafisa usalama wenzake aliyoongozana nao mle ndani kisha

    akakohoa kidogo na kuyapeleka macho yake kwa Mwasu kabla ya kuvunja ukimya.

    “Binti,tunachohitaji sasa kutoka kwako ni ushirikiano wako mzuri katika maswali

    yetu ili kuturahisishia kumpata mhusika wetu tunayemuhitaji na baada ya hapo

    tutakuachia huru ukaendelee na shughuli zako. Lakini vilevile kama utakuwa mkaidi

    bado tunazo njia nyingi za kukulazimisha kuongea ambazo siyo nzuri kwa afya yako

    ingawa hatutakuwa na namna ila kuzitumia pale tutakapohitajika kufanya hivyo”

    M.D. Kunzugala akaweka kituo huku akimtazama Mwasu kwa makini kisha akaingiza

    mkono katika mfuko wa koti lake la suti na kuchukua redio ndogo ya kijasusi yenye

    uwezo wa kurekodi mazungumzo yale ambapo aliiwasha na kisha kuiweka pale juu

    mezani. Kitendo ambacho kiliwapelekea na wale maafisa wengine walioketi kando

    yake kuchukua vitabu vidogo na kalamu kutoka mifukoni mwao na kuviweka juu

    ya ile meza tayari kuandika maelezo yote muhimu ambayo yangefanyika katika

    mahojiano yam le ndani.

    “Jina lako unaitwa nani?” M.D. Kunzugala akavunja tena ukimya.

    “Mwasu”Mwasu akajibu kwa woga huku akitetemeka.

    “Jina lako kamili” mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini Evans

    Mchafu akadakia na kusisitiza .

    “Mwasu Mayanja” Mwasu akaongea huku akiwatazama wale watu kwa mashaka

    “Taja umri wako,kabila na dini” Sulle Kiganja akadakia na Mwasu alipomaliza

    kutaja mahojiano yale yakaendelea.

    “Unaishi wapi hapa Dar es Salaam?” M.D.Kunzugala akauliza.

    “Eneo la Fire” Mwasu akaongea kwa utulivu.

    “Namba ya nyumba unayoishi?” Evans Mchafu akauliza huku akimtazama

    Mwasu kwa makini.

    “Nyumba namba 27” Mwasu akafafanua.

    “Unamfahamu mtu anayeitwa Chaz Siga?” M.D. Kunzugala akauliza huku

    watu wote mle ndani wakimtazama Mwasu kwa uyakinifu. Mwasu akajikuta

    akitaka kushawishika kukataa kuwa alikuwa hafahamu chochote kuhusu Chaz Siga

    lakini alipokumbuka lile onyo alilopewa awali kabla ya kuanza kwa mahojiano yale

    akanyoosha maelezo.

    “Namfahamu”

    “Yeye ni nani kwako?” Sulle Kiganja akadakia.

    “Mwajiri wangu”

    “Umeanza kufanya kazi kwake kwa muda gani?” Evans Mchafu akatumbukiza

    swali.

    “Zaidi ya mwaka mmoja sasa” Mwasu akajibu huku akiyatembeza macho yake

    kuwatazama wale watu

    “Kabla ya hapo ulikuwa ukifanya kazi wapi?” M.D Kunzugala akauliza huku

    wenzake wakiinama na kuandika maelezo yale kwenye vile vitabu vyao katika kila

    hatua muhimu iliyokuwa ikifikiwa katika mahojiano yale.

    “Sikuwa na kazi” Mwasu akafafanua.

    “Kazi gani uliyokuwa ukiifanya katika ofisi ya Chaz Siga?” M.D Kunzugala

    akauliza huku akivigongesha vidole vyake juu ya ile meza.

    “Katibu muhtasi” Mwasu akajibu kwa utulivu na kupelekea kitambo kifupi cha

    ukimya kutokea mle ndani kabla ya Evans Mchafu kuvunja ukimya ule kwa swali.

    “Ofisi yenu inashughulika na nini binti?”

    “Upelelezi binafsi” jibu la Mwasu likawapelekea wale watu mle ndani wageuke na

    kutazamana hata hivyo hakuna aliyemsemesha mwenzake ingawaje kupitia nyuso zao

    kulikuwa na kila hakika kuwa hoja fulani zilikuwa zimeibuliwa vichwani mwao.

    “Ofisi yenu ina leseni inayowaruhusu kufanya hivyo?” M.D Kunzugala akauliza

    “Mimi sifahamu labda mwajiri wangu” Mwasu akajitetea

    “Unatambua kuwa sheria za nchi hii zinamkataza mtu yeyote kuunda jeshi,kikundi

    cha ulinzi au taasisi yoyote ya usalama inayoshabihiana na kazi zinazofanywa na ofisi

    yenu?” Evans Mchafu akatumbukiza hoja.

    “Hapana,sifahamu” Mwasu akajibu kwa woga kabla ya M.D Kunzugala kuendelea.

    “Una hisia zozote juu ya sababu za kwa nini upo hapa?”

    “Hapana” Mwasu akajibu kwa utulivu hata hivyo macho yake yalikataa kudanganya.

    “Mwajiri wako Chaz Siga anahusishwa na mauaji ya watu kadhaa wakiwemo

    wanausalama yanayoendelea kutokea hapa Dar es Salaam. Unafahamu chochote juu

    ya hilo?” Sulle Kiganja akauliza huku akimtazama Mwasu kwa makini.

    “Sifahamu” Mwasu akaitikia.

    “Unaamini kuwa mwajiri wako Chaz Siga anaweza kuhusika na mauaji haya?”

    M.D Kunzugala akauliza kwa utulivu baada ya kuingiza mkono mfukoni na kuchukua

    picha tofauti zilizopigwa kwenye matukio ya vifo vya wanausalama wale na kuzisogeza

    karibu na Mwasu.

    “Siamini”

    “Kwa nini huamini?” Evans Mchafu akauliza.

    “Kwa kipindi chote nilichofanya kazi na Chaz Siga namtambua kama mtu

    mpenda haki utu na wakala mkubwa wa amani hapa nchini kupitia tabia yake. Hivyo

    sioni namna inayoweza kuniridhisha nikubaliane na nyinyi kuwa Chaz Siga ni muuaji

    na ndiye aliyehusika na unyama huu” Mwasu akafafanua kiasi cha kuwapelekea wale

    watu mle ndani watazamane kidogo na kisha kuyapeleka macho yao kwake.

    “Ofisi yenu kwa sasa inahusika na upelelezi wa kesi ya namna gani?” Sulle Kiganja

    akauliza swali lililompelekea kwa mara ya kwanza Mwasu ajikute akibabaika kabla ya

    kudanganya pale alipoanza kuhisi madhara ambayo yangejitokeza baada ya kusema

    ukweli.

    “Upelelezi wa kesi nyingi ambazo siyo rahisi kuzikumbuka zote kwa pamoja”

    Kamishna wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini Evans Mchafu akawa wa kwanza

    kugundua kuwa Mwasu alikuwa akidanganya kabla ya wenzake nao kushtukia hata

    hivyo hakuna aliyetia neno.

    “Taja baadhi ya kesi unazozikumbuka” M.D Kunzugala akatumbukiza hoja huku

    akimkata Mwasu jicho la udadisi. Lilikuwa swali la mtego lililompelekea Mwasu aanze

    kubabaika tena huku akifikiria namna ya kujieleza.

    “Nyingi ni kesi za watu binafsi zinazohusiana na usaliti katika mapenzi” Mwasu

    akadanganya.

    “Na hizo chache zilizosalia?” Evans Mchafu akauliza huku tabasamu la kinafiki

    likichomoza usoni mwake.

    “Zinahusu wizi na ubadhirifu wa fedha katika taasisi binafsi” Mwasu akadanganya

    hata hivyo ni kama aliyejidanganya mwenyewe kwani uongo wake ulikosa ushawishi

    kabisa kwa wale magwiji wa shughuli za kiusalama nchini na kuwafanya waishie

    kutabasamu huku wakifahamu fika kuwa Mwasu alikuwa akikwepa kuzungumza

    ukweli juu ya jambo fulani.

    “Mwajiri wako anaishi wapi?” M.D Kunzugala akauliza.

    “Sijawahi kufika nyumbani kwake kama yeye ambavyo hajawahi kufika kwangu”

    “Hujawahi kumsikia hata siku moja akizungumzia juu ya mahali anapoishi hapa

    jijini Dar es Salaam?” Sulle Kiganja akauliza huku akiacha kuandika na kumtazama

    Mwasu.

    “Hapana” Mwasu akajibu huku akitikisa kichwa kuonesha kukataa hata hivyo wale

    maafisa usalama wakafahamu haraka kuwa Mwasu alikuwa akiwadanganya kwani

    ilikuwa ni vigumu sana kwa ofisi ndogo kama ile halafu wafanyakazi wasifahamiane

    wanapoishi kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja.

    “Kwa nini uliwatoroka watu wangu ofisini kwako wakati walipotaka kuonana na

    mwajiri wako?” Sulle Kiganja akauliza.

    “Nilihisi kuwa hawakuwa watu wema” Mwasu akajitetea na hapo kitambo kifupi

    cha ukimya kikafuatia mle ndani kabla ya M.D Kunzugala kuibua hoja.

    “Wakati watu wetu walipokuwa wakikuchukua kistaarabu kwenye gari

    inasemekana kuwa uliutupa mkoba wako dirishani. Unaweza kutueleza nini maana

    ya kitendo kile?”

    “Ni kama nilivyosema kuwa nilihisi wale watu waliokuja ofisini na hatimaye

    baadaye kuniteka hawakuwa wema ndiyo kisa nikaamua kuurusha nje mkoba wangu

    kwani ndani yake kulikuwa na taarifa muhimu za ofisi na sikujua watu wenu walikuwa

    na nia gani na mimi” Mwasu akajitetea.

    “Mtu uliyemrushia huo mkoba ni nani?” Evans Mchafu akauliza na kumpelekea

    Mwasu ashikwe tena na kigugumizi.

    “Tuambie binti usitupotezee muda wetu” M.D Kunzugala akaongea

    “Mwajiri wangu” Mwasu akaongea kwa woga

    “Chaz Siga?” Sulle Kiganja akauliza kwa shauku

    “Ndiyo”

    “Alijuaje kama wewe ulikuwa pale?”

    “Nilimpigia simu” Mwasu akaongea kwa utulivu na baada kitambo kifupi kingine

    cha ukimya huku wale makachero wakitazamana na kunong’onezana jambo mmoja

    akavunja ukimya.

    “Ofisi yenu ina wafanyakazi wangapi?” M.D Kunzugala akauliza baada ya

    kukumbuka kuwa taarifa za kifo cha mmoja wa maafisa wake wa juu wa usalama

    aitwaye Mbingu Balimenya kilichotokea kule kwenye korido ya jengo moja la ghorofa

    lililoko maeneo posta kilikuwa kimetokana na risasi iliyofyatuliwa na mtu mwingine

    na siyo Chaz Siga.

    “Tupo wafanyakazi wawili tu,mimi na mwajiri wangu Chaz Siga” Mwasu akajibu

    kwa utulivu kitendo kilichompelekea Sulle Kiganja kutumbukiza mkono mfukoni na

    kutoa karatasi ndogo yenye namba za gari alizozipata kutoka kwa vijana wake wa

    kazi,Fulgency Kassy,Pweza na Kombe. Ilikuwa ni namba ya gari la Momba lililokuwa

    likitumika na Koplo Tsega. Sulle Kiganja akaisogeza karatasi ile karibu na Mwasu pale

    mezani kabla ya kumuuliza

    “Unalifahamu gari lenye namba hizi?” Mwasu akainama na kuzitazama zile namba

    za gari kwenye ile karatasi kwa makini kabla ya kutikisa kichwa chake katika namna

    ya kukataa.

    “Sizifahamu”

    “Hujawahi kuliona popote gari lenye namba hizi?” Sulle Kiganja akauliza katika

    namna ya kutaka kupata hakika huku akimtazama Mwasu kwa makini.

    “Hapana” Mwasu akajibu kwa utulivu na hapo Sulle Kiganja akakichukuwa kile

    kikaratasi na kukitia mfukoni huku taratibu akiegemea kiti na kuvigongesha vidole

    vyake juu ya ile meza kama mtu afikiriaye jambo fulani kisha kikafuata kitambo kifupi

    cha ukimya kabla ya M.D Kunzugala kukohoa kidogo na kuvunja tena ukimya.

    “Unadhani ni wapi tunapoweza kumpata mwajiri wako?”

    “Sehemu pekee tunayokutana mimi na yeye ni ofisini zaidi ya pale hakuna sehemu

    nyingine ninayoifahamu” Mwasu akafafanua kisha kitambo kifupi cha ukimya

    kikafuatia tena mle ndani huku wale makachero wakimtazama.

    “Sikiliza binti pengine ukawa hufahamu kuwa sisi ni akina nani na uzito wa suala

    tunalojitahidi kulitatua ili maafa yasiongezeke. Hakuna namna nyingine itakayokuweka

    huru kama hutotupa ushirikiano. Tunaamini kuwa katika mazingira fulani

    tusiyoyafahamu unaweza kutusaidia kumkamata mwajiri wako vinginevyo tunaweza

    kutumia njia zetu nyingine lakini wewe hutokuwa salama na sidhani kama unapenda

    tufike huko” Evans Mchafu akaongea kwa utulivu huku akimtazama Mwasu na

    wakati akifanya vile Sulle Kiganja akawa akiandika maelezo fulani kwenye kile kitabu

    chake kidogo huku akimtazama Mwasu katika uso ulioanza kupoteza uvumilivu.

    “Nitajie namba za simu za mwajiri wako” Sulle Kiganja akauliza kwa makini huku

    akimtazama Mwasu usoni. Lilikuwa swali la kushtukiza lililompelekea Mwasu ababaike

    na kushindwa kujibu haraka. Ukimya kidogo ukapita huku Mwasu akiyatembeza

    macho yake taratibu kuwatazama wale watu mbele yake kama afikiriaye jambo kisha

    akaongea kwa utulivu.

    “Namba za simu ya mwajiri wangu bado sijazishika kichwani” Sulle Kiganja

    kuona vile akashindwa kuvumilia akainuka na kumchapa Mwasu kofi moja la nguvu

    usoni kiasi cha kumpelekea Mwasu apige yowe kali la maumivu huku damu nyepesi

    ikimtoka mdomoni.

    “Chaz Siga mpaka sasa anamshikilia mateka mmoja wa maafisa wangu wa usalama

    baada ya jaribio lake la kumuua kushindikana. Kama hutoshirikiana nasi katika

    kumnasa mwajiri wako basi huyo mateka anayemshikilia huwenda naye akauwawa

    kama ilivyokuwa kwa maafisa usalama wangu wengine na hatuwezi kukubali mtu wetu

    apoteze maisha huku wewe ukiendelea kuishi vizuri katika chumba hiki. Nadhani

    unafahamu ninachokiongea” M.D Kunzugala akafoka huku akimtazama Mwasu kwa

    hasira kisha akasogeza kiti nyuma na kusimama akifuatiwa na wale wenzake kisha

    pasipo kuongea neno wakaanza kuondoka mle ndani wakielekea kwenye ule mlango

    wa kutokea nje ya kile chumba. Yule kijana akawahi kuwafungulia ule mlango na

    walipotoka nje na yeye akafuatia nyuma yao huku ule mlango ukifungwa.

    Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku maswali mengi yakipita kichwani

    kwa Mwasu juu ya mahojiano aliyomaliza kufanyiwa na wale watu waliyotoka mle

    ndani muda mfupi uliopita. Mawazo yake hatimaye yakahamia kwa Chaz Siga na

    kumpelekea kwa mara ya kwanza ajikute akijuta kuwa sehemu ya mkasa huu.

    Muda mfupi mara baada ya wale watu kuondoka akiwa katikati ya mawazo mara

    Mwasu akajikuta akishikwa na wasiwasi baada ya kuusikia ule mlango wa kile chumba

    ukifunguliwa tena na kisha wanaume watatu wengine kuingia mle ndani. Wawili

    walikuwa vijana na mmoja mzee wa makamo. Yule mzee alikuwa amevaa mavazi ya

    kidaktari,koti jeupe, stetheskopu shingoni na miwani yake mikubwa machoni huku

    mkononi akiwa ameshika kisanduku kidogo chenye dhana muhimu za kazi. Wale

    vijana wawili mikononi walikuwa wamevaa glovu nyepesi za mpira huku kila mmoja

    amebeba kiboksi kidogo. Ingawa sura za watu wale hazikuonesha tashwishi yoyote

    lakini Mwasu alipowatazama akajikuta akianza kuwalaani hata kabla hawajamfikia

    huku akianza kuijutia nafsi yake.

    Mlango wa kile chumba ulipofungwa wale watu wakamsogelea Mwasu pale

    kwenye kiti na kumtazama kana kwamba hawakuwahi kumuona kiumbe kama yule

    tangu wazaliwe.

    “Hujambo binti mzuri?” yule daktari mzee akamsogelea Mwasu akimuuliza kwa

    utulivu na kumshika bega huku wale vijana wenye miili mikubwa wakiwa kando yake.

    Hata hivyo Mwasu hakusema neno badala yake akabaki akiwatazama tu.

    “Hatujawahi kumpokea mgeni wa aina yako humu ndani. Kazi yetu ni

    kushughulika na wanaume hasa wale walioshindikana kutupatia taarifa tunazozihitaji.

    Wewe umekuwa changamoto mpya kwetu. Hata hivyo hakuna mtu aliyewahi kuingia

    humu ndani na kutoka na siri yake moyoni kwani tuna hakika na huduma hii. Kwa

    muda wa miaka thelathini na mbili tangu nianze kuifanya hii kazi ni wanaume

    wawili tu waliokufa humu ndani na siri zao moyoni na nikikutazama wewe huelekei

    kuivunja rekodi hiyo. Msichana mrembo kama wewe ingefaa uwe nyumbani kulea

    watoto badala ya kujiingiza kwenye mambo hatari kama haya” yule mzee akaongea

    kwa utulivu huku akitia jitihada za kuvaa glovu mikononi mwake baada ya kuacha

    kumtazama Mwasu na kufungua kile kisanduku chake chekundu chenye vifaa vingi

    visivyoelezeka kikiwemo kibunda cha glovu nyingi za mpira. Yule daktari alipomaliza

    akageuka tena na kumtazama Mwasu.

    “Hiki ni chumba ambacho hakiruhusu sauti ya namna yoyote kupenya na kutoka

    nje hivyo usipoteze muda wako kupiga kelele.

    “Mnataka kunifanya nini?” Mwasu akauliza kwa hofu huku akijitahidi kufurukuta

    kwenye kile kiti bila mafanikio kwani mwili wake ulikuwa umefungwa kwa mikanda.

    “Tunataka utueleze kila kitu unachokifahamu kuhusu huyu mtu anayeitwa Chaz

    Siga ambaye wewe umejinadi kuwa ni mwajiri wako” yule daktari akaongea kwa

    utulivu huku akikisogeza kiboksi kimoja kati ya vile viboksi viwili walivyokujanavyo

    wale vijana.

    “Kitu gani?” Mwasu akauliza huku amejawa hofu hata hivyo hakuna aliyemjibu

    badala yake kijana mmoja aliyekuwa nyuma yake akasogea na kuichana blauzi yake

    kifuani na alipomaliza akafungua na sidiria yake na kuitupa kando kabla ya kuyatazama

    matiti ya Mwasu kwa utulivu kama mtafiti. Yule daktari mzee alipofungua kiboksi

    kimoja akatumbukiza mkono na kuchukuwa kilichokuwa ndani yake. Alipoutoa

    mkono wake ulikuwa umeshika panya buku mkubwa mwenye meno makali

    yaliyojitokeza nje huku akiuchezeshachezesha mkia wake kwa usongo na kupiga

    kelele kali inayoumiza masikio.

    “Mnataka kunifanya nini?” Mwasu akauliza huku akitetemeka kwa hofu.

    “Rafiki yetu John hajakula kwa muda wa siku tatu” yule daktari akaongea huku

    akimuinua juu yule panya na kumgeuzageuza katika namna ya kumchunguza.

    “Naomba mniache nimeshawaambia kila kitu ninachokifahamu?” Mwasu akafoka

    hata hivyo hakuna aliyemsemesha badala yake wale watu kwa pamoja wakaangua

    kicheko cha dhihaka kisha yule daktari mzee akachukua mfuko mweusi wa kitambaa

    kutoka kwa mmoja wa wale vijana na kumtumbukiza yule panya ndani ya ule

    mfuko. Kufumba na kufumbua wale vijana wakauchukua ule mfuko na kumvalisha

    Mwasu hadi sehemu za matiti yake kifuani. Kilichofuata baada ya pale ni yule panya

    buku mwenye njaa kali kuanza kuzitafuna sehemu mbalimbali za mwili wa Mwasu

    yakiwemo matiti yake. Kiwiliwili cha Mwasu kikiwa ndani ya ule mfuko mweusi wa

    nguo wenye panya Mwasu akaanza kupiga mayowe ya hofu iliyotokana na maumivu

    makali ya majeraha ya kutafunwa na yule panya huku akikukurika kwa nguvu zake

    zote pale kwenye kiti. Hata hivyo Mwasu hakufanikiwa kujinasua kutoka katika kadhia

    ile na hapo zoezi lile likaendelea huku yule panya akiendelea kuzitafuna sehemu za

    mwili wake hadi pale yule daktari alipowaambia wale vijana wasitishe na kuuondoa

    ule mfuko wenye panya.

    Ule mfuko ulipoondolewa Mwasu alikuwa akilia kwa maumivu makali yaliyotokana

    na majeraha ya yule panya huku macho yamemtoka na kuwa mekundu kwa hofu

    Yule panya alikuwa amemtafuna na kumtia majeraha kila mahali zikiwemo sehemu

    za matiti yake na kusababisha damu nyingi kumtoka. Mwasu akaendelea kulia huku

    akihema ovyo.

    “Tuambie binti,Chaz Siga ni nani na anapeleleza kitu gani?” yule daktari mzee

    akaongea kwa utulivu huku akichukua sigara moja kutoka katika pakiti yake mfukoni

    alipoiweka mdomoni akajiwashia kwa kiberiti chake cha gesi na kuvuta mapafu

    kadhaa kabla ya kuupuliza moshi pembeni.

    “Nimekwisha waambia kuwa mimi sifahamu chochote zaidi ya hicho nilichowaeleza

    kwenye mahojiano na maafisa wenu” Mwasu akaongea huku akiendelea kulia. Yule

    daktari mzee akamtazama kwa utulivu kabla ya kuvunja ukimya.

    “Sikiliza binti,katika miaka yote niliyofanya hii kazi na kulipwa mshahara mzuri

    wa kumudu kuilea familia yangu vizuri na kusomesha watoto wangu hadi chuo kikuu

    nimekuwa nikichukia sana kitendo cha kuiona roho ya binadamu pale inapouacha

    mwili. Hata hivyo nimejikuta nikifurahi sana pale ninapokutana na mtu mkaidi kama

    wewe”

    “Nimekwisha waeleza kuwa sifahamu chochote” Mwasu akasisitiza huku

    akiendelea kulia hali iliyompelekea yule daktari mzee afungue tena kiboksi kingine

    na kuingiza mkono ndani yake kumchukua panya mwingine mkubwa zaidi ya yule

    wa awali mwenye meno makali zaidi na njaa kali. Yule panya akawa akipiga kelele na

    kuuchezesha chezesha mkia wake huku na kule huku akijipindapinda katika namna

    ya kutafuta nafasi nzuri ya kutaka kutafuna vidole vya yule daktari mzee. Yule daktari

    mzee bila kupoteza muda akamtia yule panya kwenye mfuko mwingine mweusi wa

    nguo na bila kuchelewa ule mfuko akavalishwa tena Mwasu,mara hii akipiga mayowe

    makubwa zaidi ya hofu huku akijitahidi kujinasua kwenye kile kiti bila mafanikio. Hata

    hivyo sauti yake haikwenda popote mle ndani badala yake ikamezwa na sauti nzito

    ya vicheko vya wale wanaume wakati yule panya alipokuwa akianza kuzishambulia

    sehemu mbalimbali za mwili wake.



    KUITAFUTA BENKI YA ZANZIBAR MARINE jijini Dar es Salaam halikuwa

    jambo jepesi hata kidogo kwa kuzingatia kuwa hii ilikuwa ni benki mpya kabisa kuwahi

    kufanya shughuli zake jijini Dar es Salaam. Ni katika benki hii ndipo mtu mwenye jina

    la Aden Mawala aliposemekana kufanya kazi kama meneja wa benki hiyo. Kupitia

    barua yenye ujumbe mfupi ndani ya bahasha ndogo ya kaki ambayo Koplo Tsega

    alikuwa ameiichukua kule nyumbani kwa Balimenya usiku ule baada ya kupambana

    na wale wanausalama wawili na hatimaye kuwaangamiza. Maelekezo ndani ya barua

    ile kutoka kwa mtu mmoja asiyefahamika jina lake yalikuwa yameweka bayana kuwa

    meneja wa benki ya Zanzibar Marine tawi la jijini Dar es Salaam ndugu Aden Mawala

    alikuwa amepewa maelekezo yote muhimu ya kuhakikisha kuwa kiasi fulani cha fedha

    nyingi sana zilizoingizwa kwenye benki yake anazifanyia mgao sahihi kufuatana na

    orodha ya majina yote ya watu waliokuwa wameorodheshwa katika barua ile kutokea

    tarehe fulani. Maelezo yale yaliendelea kuelekeza kuwa watu hao wangefika kwenye

    benki hiyo pamoja na vitambulisho vyao vya kazi huku wakiwa na hundi zao tayari

    kulipwa mgao wao katika fedha hizo. Mtoa taarifa kupitia barua ile ambaye hakutaja

    jina lake aliendelea kusisitiza kuwa shughuli yote ya mgao wa fedha hizo ilipaswa

    kufanywa katika mazingira yenye usiri mkubwa sana ingawa hakueleza kuwa ni lini

    mgao huo ulipaswa kufanyika.

    Kupitia orodha ya majina ya watu waliokuwa katika barua ile Koplo Tsega alikuwa

    ameongeza ziada nyingine katika utafiti wake. Jambo moja muhimu aliloligundua

    ni kuwa majina yote yaliyokuwa katika zile hundi alizozikuta kwenye ile bahasha

    nyumbani kwa Meja Khalid Makame yalikuwa pia kwenye ile barua aliyoikuta

    nyumbani kwa Balimenya isipokuwa majina ya watu wanne tu ambao hakuwafahamu.

    Pili, hundi zile alizozipata nyumbani kwa Meja Khalid Makame zilikuwa ni za benki

    ya Zanzibar Marine. Hivyo kwa namna moja au nyingine ni kuwa meneja wa benki ya

    Zanzibar Marine jijini Dar es Salaam ndugu Aden Mawala alikuwa akifahamu kila kitu

    kilichokuwa kikiendelea akiwemo yule mtu aliyetoa maelekezo yale kwenye ile barua.

    Zanzibar Marine Bank ilikuwa kando ya barabara kuu ya Bagamoyo upande

    wa kulia umbali mfupi baada ya kuyapita makutano ya barabara ya Kawawa na ile

    barabara ya Mwai Kibaki eneo la Morocco kando ya jengo refu la ghorofa la Drive

    Inn Plaza. Baada ya safari ndefu ya kuzunguka katika vitongoji vingi vya jiji la Dar

    es Salaam na ulizauliza ya hapa na pale hatimaye Koplo Tsega akawa ameyafumania

    maficho makini ya benki hii change jijini Dar es Salaam.

    Mchana huu foleni ya magari katika barabara ya Bagamoyo ilikuwa kubwa na yenye

    kukera hivyo Koplo Tsega akaona kuwa lingekuwa ni jambo la usumbufu sana kusubiri

    foleni ile hadi ipungue ili apate nafasi nzuri ya kuchepuka upande wa pili wa barabara

    ilipokuwa ile benki hivyo badala yake akaingia upande wa kushoto na kuegesha gari

    lake kwenye eneo la maegesho ya magari la mgahawa maarufu wa kichina uitwao

    Seafoods kisha akafungua mlango na kushuka akiwa katika mwonekano mpya kabisa

    wa kofia nyeusi ya Sombrero kichwani, miwani nyeusi ya jua machoni, blauzi nyeusi

    ya pullneck aliyoitanguliza ndani ya shati zito la jeans la rangi ya bluu bahari. Chini

    alikuwa amevaa suruali nyepesi ya jeans iliyolichora vyema umbo lake maridhawa la

    kike na buti ngumu za rangi ya udongo aina ya Travolta. Kwa kukwepa aina yoyote ya

    bahati mbaya pale ambapo rabsha zozote zingejitokeza mbele ya safari Koplo Tsega

    alikuwa ameamua kushuka na begi lake la mgongoni jeusi, jembamba na refu lenye

    zana zote muhimu za kazi ikiwemo Sniper Rifle 338 Lapua Magnum, bunduki maalum

    kwa ajili ya kudungulia windo sumbufu la umbali wa masafa marefu.

    Kulikuwa na watu wachache waliokuwa wameketi kwenye sehemu ya nje ya

    mgahawa ule wakijipatia huduma. Wakati Koplo Tsega alipokuwa akishuka kwenye

    gari watu wale waligeuka na kumtazama hata hivyo hakutoa nafasi yoyote ya kugeuka

    kuvutia badala yake akafunga mlango haraka na kuvuka barabara akielekea upande wa

    pili eneo lilipokuwa lile jengo la benki ya Zanzibar Marine huku akikatisha katikati ya

    foleni ndefu ya magari katika barabara ile.

    Akiwa na hakika kuwa hakuna mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia nyuma yake mara

    tu alipomaliza kuvuka barabara ile Koplo Tsega akatembea kandokando ya barabara

    ile akishika uelekeo wa upande wa kulia hadi pale alipokifikia kizuizi cha mbele cha

    kuingia kwenye benki ile kando ya kibanda cha mlinzi kilichokuwa na askari polisi

    wawili ambapo alipita pembeni ya kizuizi kile katika njia ya wazi ya watembea kwa

    miguu iliyopakana na bustani nzuri ya nyasi za kijani kibichi na miti mirefu ya miashoki

    iliyopandwa katika mstari mnyoofu wa kupendeza mbele ya jengo lile la benki.

    Koplo Tsega akaendelea kutembea kwa utulivu akielekea kwenye ile benki huku

    kumbukumbu zake zikimueleza kuwa kabla ya jengo lile kutumika na Zanzibar Marine

    Bank hapo awali lilikuwa likitumika kama makao makuu ya shirika fulani la mtandao

    wa mawasiliano ya simu. Tangu kutokea mauaji ya Sikawa kwenye kile chumba

    namba 18 cha Hotel 92 Dar es Salaam eneo la Ubungo, Koplo Tsega alikuwa ameamua

    kuhamishia makazi yake kwenye chumba kimoja alichokuwa akiishi Sikawa kati ya

    vyumba vingi vya uani vya wapangaji katika nyumba moja iliyokuwa eneo la Mwenge

    mtaa wa Mama Ngoma. Huku akirudi usiku wa manane wakati wapangaji wote

    wakiwa usingizini na kuondoka mapema sana alfajiri kabla ya watu wote hawajaamka

    katika kile chumba kidogo cha kijana wa mjini chenye kitanda kidogo cha futi tano

    kwa sita, kabati dogo la nguo, seti moja ya runinga juu ya meza yenye deki moja ya ya

    dvd, spika dhaifu za muziki wa gheto na ndoo nyingi za maji zilizokuwa kwenye kona

    mojawapo ya chumba kile. Ili kumuenzi Sikawa, Koplo Tsega alikuwa amejiapiza

    kulipa kisasi kwa wote walio husika na kifo chake.

    Nje ya jengo lile la benki ya Zanzibar Marine kwenye eneo la maegesho ya magari

    kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa. Koplo Tsega alipochunguza

    akajikuta akifurahi baada ya kugundua kuwa miongoni mwa magari yaliyokuwa katika

    maegesho yale lilikuwepo gari moja aina ya Landcruiser jeupe lililokuwa limeegeshwa

    katika sehemu maalum ya maegesho yenye utambulisho wa cheo cha meneja wa benki

    ile. Uwepo wa lile gari eneo lile ikawa ni ishara tosha kuwa meneja wa benki ile ndugu

    Aden Mawala alikuwepo ofisini kwake kama kawaida akiendelea na shughuli zake za

    kiofisi kama ilivyo ada. Hata hivyo mandhari ya nje ya ile benki yalitosha kuthibitisha

    kuwa benki ile haikuwa na msongamano mkubwa wa wateja kama zilivyokuwa benki

    nyingine zenye umri mrefu jijini Dar es Salaam.

    Koplo Tsega akaendelea kutembea kwa utulivu akikatisha kuelekea sehemu ya

    mbele ya benki ile yenye baraza pana ya sakafu ya marumaru za kuvutia na juu yake

    imefunikwa na paa zuri na imara ya zege iliyoezekwa kwa vigae na kushikiliwa na

    nguzo mbili upande wa kushoto na kulia. Koplo Tsega alipozifikia ngazi za baraza ile

    akazipanda kwa utulivu kisha baada ya safari ya hatua chache mbele yake akausukuma

    mlango mkubwa wa kioo na kupotelea mle ndani.

    Ndani ya benki ile kulikuwa na watu wachache ambao kwa idadi yao wengi wao

    walikuwa ni wazanzibar kama siyo watu wenye asili ya bara la Asia. Mandhari ya benki

    ile mle ndani yalikuwa tulivu na ya kisomi. Viyoyozi makini vya mle ndani vilikuwa

    vikiendelea kusukuma hewa safi yenye baridi ya wastani. Mara baada ya kuingia mle

    ndani upande wa kushoto kulikuwa na ngazi za kuelekea juu ghorofani kwenye ofisi

    nyingine za idara tofauti za benki ile kama idara ya mikopo, idara za sera, mipango

    na utawala na nyinginezo. Sehemu ya chini katikati ya jengo kulikuwa na nguzo mbili

    kubwa za uviringo zilizoishikilia sehemu ya juu ya jengo lile na sakafu ya mle ndani

    ilifunikwa kwa zulia zuri la rangi ya kijivu.

    Mara baada ya kuingia mle ndani Koplo Tsega akasita kidogo na kusimama

    akijitahidi kuyazoea mandhari ya mle ndani kwa kuyatembeza macho yake taratibu.

    Upande wa kushoto kulikuwa na meza ya ukutani ambayo ilikuwa ikitumiwa na wateja

    wa benki ile kwa ajili ya kuandikia au kujaza taarifa za benki kwenye slips zao. Mara

    baada ya kuipita meza ile kulikuwa na viti vingi katika sehemu maalum ambapo wateja

    wa benki ile wangeketi na kusubiri wakati shida zao zikishughulikiwa na maafisa wa

    benki ile. Baada ya kuipita sehemu ile ya mangojeo mbele kidogo kulikuwa na dawati

    kubwa lenye umbo la nusu mkate mbele ya msichana mrembo wa idara ya huduma

    kwa wateja aliyevaa Hijabu.

    Upande wa kulia mle ndani kulikuwa na vibanda vinne vya tellers wa benki

    vilivyotengenezwa kwa mbao nyepesi ya mahogani sehemu za chini na kuta safi za

    vioo vyenye matundu mbele yake. Ndani ya vile vibanda kulikuwa na wafanyakazi wa

    benki ile waliokuwa wakiendelea kuwahudumia wateja wachache waliokuwa kwenye

    foleni fupi kuelekea vibanda vile.

    Akiwa ameridhishwa na tathmini ya mandhari yale taratibu Koplo Tsega akapiga

    hatua zake kuelekea kwenye lile dawati la huduma kwa wateja ama customer care

    alilokuwa ameketi yule dada mlimbwende aliyekuwa eneo lile akimuelekeza mteja

    mmoja namna ya kujaza taarifa zake kwenye fomu maalum ya benki iliyokuwa juu

    ya lile dawati. Wakati Koplo Tsega akifika sehemu ile yule dada mlimbwende wa

    mapokezi alikuwa tayari amekwisha maliza kumuhudumia yule mteja hivyo haraka

    akageuka na kumtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu la kibiashara.

    “Karibu dada”

    “Ahsante” Koplo Tsega akaitikia kisha kabla ya kusema neno akageuka kidogo

    kuyatembeza macho yake makali yaliyojificha nyuma ya miwani kuchunguza eneo lile

    na alipoona kuwa hali ilikuwa shwari akayarudisha tena macho yake kwa yule dada.

    “Karibu tafadhali naomba nikusaidie dada yangu” yule mlimbwende akasisitiza

    huku akimtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu jepesi. Koplo Tsega

    akasogea vizuri karibu ya lile dawati na kuongea huku usoni akilazimisha tabasamu.

    “Nahitaji kuonana na meneja wa benki”

    “Una shida gani dada yangu labda huwenda nikakusaidia” yule dada akaongea

    kiungwana

    “Nahitaji mishahara yote ya wafanyakazi wa kampuni yetu ipitie kwenye benki

    yenu” Koplo Tsega akaamua kudanganya kwa kutengeneza hoja yenye ushawishi

    mkubwa ambayo kwa namna moja au nyingine aliamini kuwa ilikuwa nje ya uwezo

    wa yule dada wa idara ya huduma kwa wateja.

    “Ofisi ya meneja wa benki ipo mwisho wa hili jengo upande wa kushoto ukifika

    utaona korido. Fuata korido hiyo ukifika mwisho utauona mlango”

    “Ngoja nipige simu ofisini kwake kuuliza kama atakuwa na mgeni yeyote” yule

    dada akaongea kwa utulivu na kabla Koplo Tsega hajatia neno kiwambo cha simu

    ya mezani iliyokuwa juu ya meza fupi kando yake tayari ilikuwa sikioni. Baada ya

    kubonyeza tarakimu kadhaa ile simu ikawa hewani na hapo kukafuatiwa na maongezi

    mafupi baina yake na mtu wa upande wa pili wa ile simu kabla ya yule dada kukata

    simu na kugeuka akimtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu la matumaini.

    “Unaweza kwenda yupo ofisini kwake na hana mgeni yeyote”

    “Nashukuru” Koplo Tsega akatoa shukrani zake huku tabasamu hafifu la

    kutengeza likiumbika usoni mwake

    “Karibu tena” yule dada akaitikia huku akijiandaa kumsikiliza mteja mwingine

    aliyefika eneo lile. Bila kupoteza muda Koplo Tsega akaanza kuzitupa hatua zake

    taratibu akikatisha eneo lile kuelekea mwisho wa lile jengo kama alivyoelekezwa na

    wakati alipokuwa akitembea akagundua macho ya wanaume wote waliokuwa kwenye

    vile vibanda vya tellers wa ile benki yalikuwa yakimtazama kwa uchu kupitia kuta safi

    za vioo zilizowazunguka na hali ile ikampa faraja kidogo huku taratibu akizichezesha

    malighafi muhimu za mwili wake.

    Mara tu alipofika mwisho wa lile jengo upande wa kushoto akaiona korido fupi

    kama alivyoelekezwa hivyo Koplo Tsega akaifuata korido ile. Ilikuwa ni korido fupi

    iliyokuwa ikitazamana na milango mitatu. Mlango mmoja upande wa kushoto,mlango

    mwingine upande wa kulia na mlango wa mwisho ulikuwa mwisho wa ile korido kwa

    mbele. Wakati Koplo Tsega akiendelea kutembea akawa akiyatembeza macho yake

    taratibu kuichunguza ile milango na kupitia vibao vidogo vyeusi vyenye maandishi

    meupe akagundua kuwa mlango wa kwanza upande wa kushoto ulikuwa ni wa ofisi

    ya Line manager wa kitengo cha Import and Export. Mlango uliyofuata upande wa

    kulia ulikuwa ni wa ofisi inayoshughulikia miamala yenye kuhusisha kiasi kikubwa cha

    fedha ama Bulk transaction na ule mlango uliyokuwa mbele mwisho wa ile korido

    ndiyo uliyokuwa wa kuelekea kwenye ofisi ya meneja wa benki ile hali iliyompelekea

    Koplo Tsega ajikute akitabasamu peke yake. Mandhari ya eneo lile yalikuwa tulivu

    mno hata hivyo hali ile haikumaanisha kuwa ndani vyumba vile hapakuwa na shughuli

    za kiofisi zilizokuwa zikiendelea.

    Hatimaye Koplo Tsega akawa ameufikia ule umlango wa kuingia kwenye ile ofisi

    ya meneja wa ile benki. Alipofika pale mlangoni akasimama kidogo akijipa utulivu na

    kujitengeneza vizuri na baada ya kugeuka nyuma na kuhakikisha kuwa hapakuwa na

    mtu yeyote mwingine eneo lile akausogelea mlango wa ile ofisi na kushika kitasa chake

    huku akikisukuma taratibu. Tofauti na matarajio yake mlango ule mzito ukafunguka

    taratibu na hapo Koplo Tsega akaingia mle ndani.

    Kama zilivyokuwa ofisi nyingi za kisasa za zama hizi ofisi ile ilikuwa ya kisasa zaidi.

    Sakafu yake ilifunikwa kwa zulia maridadi la rangi ya kijivu lenye michoro ya maua

    meusi na meupe. Upande wa kushoto kulikuwa na dirisha kubwa lililofunikwa kwa

    pazia jepesi. Kando ya dirisha lile kulikuwa na rafu nne kubwa ya chuma zenye droo

    nyingi zilizosimama wima kama milima meza. Kabla ya kuzifikia rafu zile kulikuwa na

    seti moja ya makochi laini meupe ya sofa yaliyoizunguka meza fupi ya kioo iliyokuwa

    na majarida na vipeperushi vinavyohusiana na huduma zinazotolewa na ile benki.

    Upande wa kulia wa yale makochi kulikuwa na jokofu kubwa la vinywaji baridi

    na kupitia mlango wa kioo wa lile jokofu isingemuwia vigumu mtu yeyote kuona

    kilichokuwa mle ndani. Kiyoyozi makini bado kilikuwa kazini kusambaza hewa safi

    iliyokinzana na hali ya joto kali ya jiji la Dar es Salaam mle ndani.

    Kama zilivyokuwa ofisi nyingi zinazotoa huduma kwa jamii na kuchangia pato la

    taifa,katikati ya ofisi ile ukutani kulikuwa na picha mbili za marais zilizotundikwa. Rais

    wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na rais wa serikali ya mapinduzi ya

    Zanzibar.

    Koplo Tsega akasumbuka kidogo katika kutaka kufahamu ni wapi alipokuwa

    mwenyeji wa ofisi ile mle ndani na hali ile ilitokana na namna ya mpangilio wa ofisi

    ile ulivyokuwa. Baada ya kuufunga ule mlango na kusogea upande wa kulia akizipita

    rafu nyingine mbili ndefu za chuma zilizopakana na rafu nyingine kubwa zenye

    vitabu,mafaili na nyaraka nyingine za ofisi hatimaye Koplo Tsega akamuona meneja

    wa benki ile akiwa ameketi kwenye kiti chake cha utukufu nyuma ya meza kubwa

    ya ofisi yenye kompyuta kubwa ya mezani,tray ndogo yenye ngazi tano kwa ajili ya

    kuwekea nyaraka nyepesi za ofisi,simu ya mezani,mhuri na kidau cha wino pamoja

    na mlima wa mafaili mengi mbele yake. Upande wa kushoto eneo lile kulikuwa na

    meza nyingine ndogo na fupi ya mbao na juu ya meza ile kulikuwa na mashine tatu za

    ofisi printer,scanner na mashine ya kudurufu. Pembeni yake upande wa kulia wa ile

    meza ya ofisi kulikuwa na rafu ndogo ya chuma ambayo isingemlazimu meneja yule

    wa benki kusimama hadi kuifikia. Mbele ya ile meza kulikuwa na kiti kimoja kikubwa

    cha ofisi.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Karibu binti” mzee mfupi mwenye kipara cha afya njema,mnene mwenye kitambi

    cha ukwasi na macho makubwa ya hila yaliyojificha nyuma ya miwani kubwa alikuwa

    amesita kuendelea kufanya alichokuwa akikifanya na kisha kuiegemeza mikono yake

    mezani kabla ya kumkaribisha Koplo Tsega. Uso wake wa duara na ndevu zilizokatiwa

    vizuri kuuzunguka mdomo wake,umri wake usingekuwa zaidi ya miaka hamsini. Uso

    wake ulituama kama maji ya mtungini pasina kuonesha tashwishwi yoyote usoni.

    Koti lake la suti ya kijivu alikuwa amelitundika nyuma kwenye kiti chake cha ofisi

    kinachoweza kuzunguka nyuzi mia tatu sitini na hivyo kuusanifu vizuri mwonekano

    wake mpya wa shati jeusi la mikono mirefu bila tai shingoni hali iliyoupelekea mkufu

    wake mkubwa wa dhahabu uliotia nanga shingoni mwake kuonekana kwa usahihi

    kama mng’aro wa kito cha thamani katikati ya giza.

    “Ahsante” Koplo Tsega akaitikia kwa nidhamu kama iwavyo kwa mtu yeyote

    mgeni aingiapo katika ofisi nyeti za mijini kisha taratibu akapiga hatua zake za woga

    wa kujifanyisha akikaribia kile kiti cha ofisi kilichokuwa kikitazamana na ile meza ya

    ofisini ya yule meneja na alipokaribia akasita kidogo.

    “Karibu uketi binti” yule mzee akaongea kwa mamlaka huku akimtazama Koplo

    Tsega kwa utulivu kabla ya kujiegemeza taratibu kwenye foronya laini ya kiti chake

    cha ofisini.

    “Nashukuru” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu kisha akasogea karibu na kile kiti

    kabla ya kukisogeza nyuma na kuketi. Kibao kidogo chenye utambulisho wa jina na

    cheo cha mhusika wa ofisi ile kikamtanabaisha Koplo Tsega kuwa yule mtu aliyeketi

    mbele yake nyuma ya ile meza ya ofisini ndiye mwenye jina la Aden Mawala,meneja

    wa benki ya Zanzibar Marine jijini Dar es Salaam na hapo akajikuta akimeza funda

    kubwa la mate kuzimeza hisia zake moyoni. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata mle

    ndani huku kila mmoja akiwaza lake kichwani kabla ya yule mzee meneja wa benki

    kuegemeza tena mikono yake mezani na kuvunja ukimya.

    “Nipo tayari kukusikiliza shida yako binti,nimebanwa na kazi na bahati mbaya

    sana leo sina muda wa kutosha”

    “Nahitaji kuonana na ndugu Aden Mawala meneja wa benki hii bila shaka ndiyo

    wewe” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu katika uso wa kazi huku akimtazama yule

    mzee kwa makini.

    “Hujakosea” yule meneja wa benki akaitikia kwa utulivu na Koplo Tsega alipozidi

    kumchunguza moyoni akahitimisha kuwa alikuwa ni mtu mgeni kabisa machoni

    mwake. Yule meneja wa benki kuona vile akapeleka mkono na kuvuta mtoto wa

    meza kabla ya kutoa kabrasha fulani na kuliweka pale mezani.

    “Nimeambiwa kuwa unahitaji mishahara ya wafanyakazi wa kampuni yenu ipitie

    kwenye benki yetu. Unatokea kampuni gani hapa Dar es Salaam?” yule meneja wa

    benki akauliza huku taratibu akianza kupekua karatasi za lile kabrasha aliloliweka

    mezani.

    “T.P.D.F” Koplo Tsega akavunja ukimya.

    “Ndiyo kampuni gani hiyo mbona sijawahi kuisikia tangu nizaliwe” yule meneja

    wa benki akaongea huku akipunguza kasi ya kupekua kurasa za lile kabrasha.

    “Tanzania People Defense Force”

    “Kampuni ya ulinzi?” yule meneja wa benki akauliza huku akiangua kicheko

    hafifu chenye dharau ndani yake.

    “Jeshi la wananchi wa Tanzania” Koplo Tsega akafafanua huku akionesha kuanza

    kuchoshwa na dharau za kisomi. Maelezo ya Koplo Tsega yakampelekea yule meneja

    wa benki asitishe ghafla kile alichokuwa akikifanya na kuyasimamisha macho yake

    akimtazama Koplo Tsega kwa mashaka.

    “Jeshi la wananchi wa Tanzania siyo kampuni nadhani kuna jambo lingine

    lililokuleta humu ndani” yule meneja wa benki akaongea kwa jazba kidogo huku

    akiendelea kumtazama Koplo Tsega kwa udadisi. Pasipo kutia neno Koplo Tsega

    akaingiza mkono mfukoni kuchukua ile bahasha aliyoipata nyumbani kwa Balimenya.

    Kisha akafungua ile bahasha na kutoa ile barua fupi iliyokuwa ndani ya ile bahasha na

    kuitupa pale mezani karibu na yule meneja wa benki. Kuona vile yule meneja wa benki

    akaichukua ile karatasi na kuanza kusoma maelezo yaliyokuwa ndani yake. Koplo

    Tsega akiwa makini kuzitazama nyendo za yule meneja wa benki akashtukia kuwa

    kadiri yule meneja wa benki alivyokuwa akizidi kuyapitia maelezo kwenye ile karatasi

    ndivyo mikono yake ilivyokuwa ikizidi kutetemeka. Mwishowe yule meneja wa ile

    benki akamaliza kuyapitia maelezo kwenye ile karatasi na kuiweka pale juu ya meza

    huku uso wake ukiwa umepoteza utulivu kabisa sambamba na vitone vya jasho jepesi

    vikichomoza kwenye paji la uso wake.

    “Wewe ni nani?” yule meneja wa benki akajikaza na kumuuliza Koplo Tsega kwa

    sauti iliyopwaya.

    “Tiglis Tsega,Koplo na Komandoo wa daraja la kwanza,askari wa jeshi la wananchi

    wa Tanzania” Koplo Tsega akajitambulisha kwa kujigamba huku akimtazama meneja

    wa ile benki kwa udadisi.

    “Nani aliyekupa hii barua?” yule meneja wa benki akauliza kwa hofu

    “Nahitaji ushirikiano wako vinginevyo nisingetumia hila kufika humu ndani”

    Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa benki kwa

    makini. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku yule meneja wa benki akiachama

    mdomo wake kwa mshangao wakati mawazo mengi yakipita kichwani mwake. Sasa

    mshtuko alioupata meneja yule ulikuwa dhahiri usoni mwake huku akionekana kama

    mtu aliyekuwa akifikiria kukurupuka ghafla na kuanza kutimua mbio ingawa mazingira

    yakufanya vile hayakuwepo.

    “Ushirikiano upi unaouhitaji kutoka kwangu?’’ baada ya kubabaika kidogo yule

    meneja wa benki akajikaza na kuongea kwa sauti ya kupwaya.

    “Nafahamu kuwa unatumika na watu wenye mamlaka zaidi juu yako na kutokana

    na mazingira uliyonayo huwezi kukataa.Hata hivyo hiyo haimaanishi kuwa hufahamu

    kinachoendelea na humfahamu kabisa mtu aliyetoa maagizo haya. Niko tayari

    kukulinda wewe na maslahi yako kama utakuwa muwazi na kunipa ushirikiano wa

    kutosha katika kumfichua mtu au watu waliopo nyuma ya mtandao huu mchafu”

    Koplo Tsega akaongea kwa msisitizo huku macho yamemtoka na mishipa ya shingo

    imemtuna hata hivyo kicheko cha mahoka kilichofuata kutoka kwa yule meneja wa

    benki kikampelekea ashikwe na butwaa huku akimtazama yule meneja wa benki kama

    kituko.

    “Binti nadhani umechanganyikiwa bila shaka nani aliyekwambia kuwa mimi

    nahitaji ulinzi kutoka kwako na huo mtandao mchafu unaozungumzia mbona

    sikuelewi?” yule meneja wa benki akaongea kwa dharau huku akiendelea kuangua

    kicheko

    “Kwa hiyo unataka niamini kuwa hilo jina la kwenye hii barua siyo lako na hii siyo

    benki ya Zanzibar Marine?’’Koplo Tsega akauliza kwa jazba huku akimkata jicho la

    hasira yule meneja wa benki.

    “Mimi sikatai kuwa Aden Mawala ni jina langu na hii ni benki ya Zanzibar Marine

    lakini huu siyo ushahidi tosha wa kunifanya nikubaliane na kile unachokiamini binti.

    Jiji hili la Dar es Salaam limejaa matapeli wa kila aina. Mimi ni mtu ninayefahamiana

    na watu wengi kutokana na kazi yangu hivyo mtu yeyote mwenye hila mbaya anaweza

    kulitumia jina langu kujipatia fedha kwa ujanjaujanja” yule meneja wa benki akajitetea.

    “Sikiliza mzee usijaribu kuiondoa hoja yangu ya msingi kwenye mstari. Mimi

    sijafika hapa kufuata pesa na wala sina haja na pesa zako badala yake ninachohitaji

    kufahamu ni kuwa hizi fedha zilizoandikwa kwenye hii barua ambazo hadi wakati huu

    naamini kuwa tayari zimeshaingizwa kwenye benki yako zimetoka kwa nani na ninani

    aliyekupa maagizo haya”

    “Hakuna pesa yoyote ya kiasi hicho iliyoingia kwenye benki yangu na hata kama

    pesa hiyo ingekuwa imeingia taratibu za kibenki haziniruhusu kutoa taarifa za akaunti

    ya mhusika kwa mtu mwingine isipokuwa kwa idhini ya mhusika tu” yule meneja wa

    benki akaweka kituo huku akiunyanyua mkono wake kuitazama saa yake ya mkononi.

    Kuona vile Koplo Tsega akaingiza tena mkono wake mfukoni na kuichukua ile

    bahasha ya kaki aliyoipata kule nyumbani kwa Meja Khalid Makame ambayo ndani

    yake ilikuwa na hundi nyingi zenye majina ya watu tofauti. Alipoitoa ile bahasha

    mfukoni Koplo Tsega akaingiza mkono ndani yake na kuzitoa zile hundi kabla ya

    kuzitupia pale mezani karibu na yule mzee meneja wa benki.

    “Huwenda huo ukawa ni ushahidi tosha kwako kuwa mimi sijachanganyikiwa

    kama unavyodhani na badala yake ninahakika na kile ninachokizungumza.

    Ukichunguza kwa utulivu utagundua kuwa majina ya watu yaliyopo kwenye hundi

    hizo ndiyo yale pia yaliyopo kwenye ile barua niliyokupa awali hivyo sijakosea njia”

    Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akijitahidi kuidhibiti hasira yake kifuani.

    Yule meneja wa benki akainama kwa makini na kuanza kuzichunguza zile hundi pale

    mezani huku akionekana kuingiwa na mshtuko kadiri alivyokuwa akimalizia kupitia

    hundi moja na kuichukua nyingine. Hata hivyo yule meneja wa benki alikuwa mkaidi

    kwani alipomaliza kuzipitia zile hundi akazikusanya kwa pamoja na kuzisogeza karibu

    na Koplo Tsega pale mezani.

    “Hizi ni taarifa nyepesi sana za kufoji binti na huwezi kunifungamanisha nazo

    labda kama unashida nyingine za kibenki mbali na hii nitakusaidia ila kama huna hoja

    za msingi utakuwa muungwana sana ukisimama na kuondoka uniache niendelee

    na kazi zangu” yule meneja wa benki akaongea kwa dharau huku akiunyanyua tena

    mkono wake na kuitazama saa yake mkononi. Koplo Tigls Tsega akazichukua zile

    hundi na kuzirudishia kwenye ile bahasha kabla ya kuitia ile bahasha mfukoni pasipo

    kuonesha tashwishwi yoyote usoni. Hata hivyo Koplo Tsega alikuwa makini kufuatilia

    kwa hila nyendo za meneja yule wa benki hivyo wakati akijitia kuzama katika kuiweka

    ile bahasha ya hundi mfukoni mwake alikuwa amemuona yule meneja wa benki jinsi

    alivyokuwa akiupeleka mkono wake taratibu kuuvuta mtoto mmoja wa ile meza ya

    ofisini.

    Akiwa ameshaanza kuhisi nini maana ya tukio lile Koplo Tigils Tsega hakutaka

    kusubiri hivyo kwa kasi ya ajabu akaisukuma ile meza ya ofisini kwa miguu yake

    kumbana yule meneja wa benki kwenye kiti chake ukutani huku mkono wake mmoja

    ukiwa tayari umezama mafichoni kuikamata vyema bastola yake. Yule meneja wa

    benki alipotaka kufurukuta mahesabu yake yakagonga mwamba kwani mdomo wa

    bastola ya Koplo Tsega ulikuwa tayari ukimtazama usoni. Kisha Koplo Tseakajitetea

    karibu na yule meneja wa benki na kuupenyeza mkono wake katika ule mtoto wa

    meza uliofunguliwa kwa hila na yule meneja wa benki na alipopapasa papasa bastola

    aina ya 22 Caliber Revolver ikaenea vyema kwenye kiganja chake tukio lililompelekea

    yule meneja wa benki ashikwe na kihoro baada ya kuona hila yake imeshtukiwa na

    kugonga mwamba. Koplo Tsega alipoitoa ile bastola akaichomoa magazini yake na

    kuitupa kando kabla ya kugeuka na kumtazama kwa utulivu yule meneja wa benki

    ambaye wakati huu alikuwa amebanwa kwenye kile kiti na ile meza yake ya ofisini

    huku macho yamemtoka kwa hofu.

    “Sura yako inaonekana ni mtu msomi,mkarimu,mtulivu na mzalendo lakini

    matendo yako ni ya kinyama kama walivyo wanamtandao wenzako wengine. Watu

    kama nyinyi hamtakiwi kuundiwa tume ya uchunguzi huku mkiendelea na kazi kama

    ilivyozoeleka badala yake mnastahili kifo cha aibu tena ikiwezekana hadharani ili vizazi

    vijavyo visijifunze chochote kutoka kwenu’’Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku

    akimzunguka yule meneja wa benki pale kwenye kiti.

    “Unajidanganya bure binti hata ukiniua mimi huwezi kufika popote” yule meneja

    wa benki akaongea kwa msisitizo huku akihisi kuzidiwa ujanja.

    “Maelezo yako yanaonesha kuwa mtandao wenu ni mpana sana na una watu

    wengi sana kiasi cha kujipa hakika kuwa hata nikikuua sitofika mbali” Koplo Tsega

    akaongea kwa utulivu

    “Huelewi unachokizungumza’’ yule meneja wa benki akaongea kwa kujiamini

    “Niambie hizi fedha zilizoingia kwenye benki yako zimetoka kwa nani na huo

    mtandao wenu unaongozwa na nani?’’

    “Nimekwisha kwambia kuwa sifahamu chochote kuhusu hizo hundi wala hiyo

    barua uliyokuja nayo. Ndiyo kwanza nimeviona kwako na hakuna kiasi cha pesa kama

    hicho kilichoingizwa kwenye benki yangu” yule meneja wa benki akafoka kwa jazba.

    “Unadhani ninaweza kukuamini kupitia maneno yako?. Huo ni uongo wa

    mwisho usiokuwa na ushawishi niliowahi kuusikia kwa binadamu hapa duniani.

    Nahitaji kuiona Cash flow ya hii benki inayoonesha miamala ya pesa zilizoingizwa

    na kutolewa” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa

    benki kwa makini na alichokiona mbele yake ni mshtuko mkubwa uliojengeka usoni

    kwa yule meneja wa benki.

    “Nimekwisha kwambia kuwa taratibu zangu za kazi haziniruhusu kutoa taarifa

    za namna hiyo kwa mtu asiyehusika” yule meneja wa benki akasisitiza huku akianza

    kutokwa na kijasho chepesi usoni.

    “Nahitaji kuona Cash flow statement ya hii benki ndugu Aden Mawala,usinipotezee

    muda wangu” Koplo Tsega akasisitiza huku taratibu akikata kipande cha waya wa

    simu ya pale mezani,yule meneja wa benki akashindwa kuelewa nini maana ya tukio

    lile.

    “Unataka kunifanya nini?” yule meneja wa benki akauliza kwa hofu baada ya

    kumuona Koplo Tsega akimsogelea pale kwenye kiti na kipande cha waya wa ile simu

    mkononi

    “Cash flow statement…”

    “What…?” yule meneja wa benki kabla hajamaliza kuongea kile kipande cha waya

    tayari kilikuwa shingoni mwake na hapo Koplo Tsega akaanza kukikaza taratibu kwa

    mikono yake. Yule meneja wa benki kuona vile akaanza kufurukuta katika kutaka

    kujinasua huku akitupa mikono na miguu yake huku na kule huku mishipa ya kichwa

    ikimchomoza na ulimi na macho vikimtoka. Jitihada zake za kujinasua hazikufua

    dafu kwani hapakuwa na nafasi ya kuchomeka mikono yake kwenye ule waya

    shingoni na kuuzuia usimkabe. Koplo Tsega akaendelea kuukaza ule waya hadi pale

    alipomuona yule meneja wa benki akianza kuishiwa nguvu ndiyo akalegeza taratibu

    hali iliyompelekea yule meneja wa benki aanze kukohoa ovyo akiurekebisha mfumo

    wa upumuaji wake.

    “Fungua kompyuta yako nahitaji kuona Cash flow statement ya hii benki” Koplo

    Tsega akanong’ona kwa sauti tulivu sikioni mwa yule meneja wa benki.

    “Okay…!” yule meneja wa benki akaitikia kwa shida huku hofu imemshika na

    muda mfupi uliyofuata akaifungua ile kompyuta yake ya ofisini pale mezani huku

    Koplo Tsega akiwa makini nyuma yake. Ile kompyuta ilipofunguka yule meneja wa

    benki huku mikono ikimtetemeka akafungua mafaili kadhaa mle ndani ya kompyuta

    hadi alipolifikia faili lenye rekodi za miamala ya pesa zilizoingia na kutoka kwenye ile

    benki kufikia mwezi ule.

    Kitambo kifupi cha ukimya kikapita mle ndani huku Koplo Tsega akijaribu

    kuichunguza taarifa ile kwa maikini. Aliporidhikanayo akamwambia yule meneja wa

    benki aiprint.Yule meneja wa benki akasita kidogo lakini macho yake yalipokutana

    na macho ya Koplo Tsega hofu ikamuingia tena na hapo akalainika na kufanya vile

    alivyoagizwa. Haraka akaiamuru ile kompyuta kuprint ile taarifa ya benki kwenye

    printer iliyokuwa juu ya meza ndogo kando ya eneo lile.

    Mara baada ya yule meneja wa benki kuprint ile taarifa ya benki Koplo Tsega

    haraka akaichukua na kuanza kuipitia katika namna ya kuichunguza kama angeweza

    kupata taarifa yoyote ya kumsaidia. Kupitia taarifa ile ya benki Koplo Tsega akagundua

    kuwa kulikuwa na miamala mingi iliyofanywa kwenye ile benki kwa kipindi cha miezi

    kadhaa iliyopita na alipozidi kuchunguza akagundua kuwa miamala mingi ilikuwa

    imefanywa na kampuni nyingi zilizokuwa jijini Dar es Salaam ambazo kwa namna

    moja au nyingine hazikupaswa kutiliwa mashaka kutokana na aina ya biashara

    kampuni zile zilizokuwa zikifanya. Kulikuwa pia na miamala mingine iliyofanywa na

    watu binafsi ambayo fedha zao zilikuwa za kawaida kwa vile benki ile ilikuwa imejikita

    kwenye biashara ya uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na uingizaji wa bidhaa ndani nchi.

    Katika kuendelea kuchunguza Koplo Tsega akajikuta akivutiwa na akaunti moja

    ambayo ilikuwa imetumika kufanya muamala wa pesa nyingi sana za kigeni kwa mara

    moja. Akaunti ile ilikuwa na jina moja la Zanzibar Stone City Bazaar. Koplo Tsega

    alipozidi kuchunguza akagundua kuwa kupitia rekodi zilizokuwa kwenye taarifa ile

    ya benki akaunti ile ilikuwa ni mpya kabisa kwani hapakuonekana rekodi nyingine

    zilizoonesha kuwa akaunti ile ilikuwa ikitumika huko siku za nyuma. Lilikuwa ni

    jambo la kustaajabisha lakini vilevile linaloweza kuaminika.

    Koplo Tsega alipozidi kuchunguza mashaka juu ya kile alichokuwa akikihisi

    yakazidi kuongezeka. Muamala wa fedha nyingi uliofanywa kupitia akaunti ile ulikuwa

    umefanyika siku chache baada ya wao kuondolewa kwenye ile tume ya udhibiti na

    upambanaji wa biashara ya dawa za kulevya nchini na hatimaye kuingizwa kwenye

    vikosi vya kijeshi vya kuimarisha amani ya kudumu-MONUSCO nchini jamhuri ya

    kidemokrasia ya nchi ya Kongo. Lakini vile vile jina la akaunti ile lilifanana na jina

    la akaunti iliyokuwa kwenye zile hundi alizozipata kule nyumbani kwa Meja Khalidi

    Makame. Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akajikuta ameganda kama nyamafu

    huku akiendelea kuikodolea macho taarifa ile ya benki kwenye ile karatasi na mkono

    wake mmoja ukiwa umeikamata bastola yake vyema mkononi na kuielekezea kifuani

    kwa yule meneja wa benki ambaye mashaka yalionekana dhahiri usoni mwake.

    “Nahitaji bank statement ya hii akaunti” Koplo Tsega akasogea karibu na

    kumwambia yule meneja wa benki huku akimuelekeza kwa kidole chake kwenye ile

    akaunti ya benki ya Zanzibar Stone City Bazaar. Yule meneja wa benki akaikodolea

    macho ile akaunti kabla ya kusita huku akigeuka na kumtazama Koplo Tsega kwa

    mashaka.

    “Print…” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akifanya ishara ya kichwa

    kumaanisha kile alichokuwa akikisema kisha akaihamisha bastola yake kichwani kwa

    yule meneja wa benki. Yule meneja wa benki kuona vile akainama tena kwenye ile

    kompyuta yake mezani na kuanza kushughulika nayo na baada ya muda mfupi ile

    kompyuta ikaanza kuprint ile Bank statement ya akaunti ya Zanzibar Stone City Bazaar

    ikionyesha kiasi cha pesa,mwaka,mwezi,siku,saa na tarehe ambayo muamala ule wa

    fedha nyingi kwenye ile akaunti ulikuwa umefanyika.

    Jambo moja la kushangaza ni kuwa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ile

    zilionekana kuwa zilikuwa zimetokea kwenye benki mama iliyokuwa kisiwani

    Zanzibar. Koplo Tsega akaendelea kuikodolea macho akaunti ile huku akishindwa

    kuamini kile kilichokuwa kwenye ile karatasi.

    “Kiongozi wa mtandao wenu anaitwa nani?’’ Koplo Tsega akavunja ukimya

    akimuuliza yule meneja wa benki hata hivyo yule meneja wa benki hakuzungumza

    neno badala yake akatikisa kichwa chake kuonesha kuwa alikuwa hafahamu chochote.

    “Kukaa kimya haitakusaidia kitu ndugu Aden Mawala kwani ni vizuri ukawa

    muwazi na kunieleza ni nani anayehusika na ugawaji wa mamilioni ya fedha nyingi

    kiasi hiki huku akisisitiza mambo yenu yafanyike kwa usiri mkubwa’’

    “Nimekwisha kukueleza kuwa mimi sifahamu chochote” yule meneja wa benki

    akasisitiza hata hivyo kabla hajamaliza risasi moja kutoka kwenye bastola ya Koplo

    Tsega yenye kiwambo cha kuzuia sauti ikapenya na kuuvunja mfupa wa paja lake.

    Yule meneja wa benki akapiga yowe kali la maumivu huku akigugumia kwa maumivu

    makali yaliyoambatana na jeraha linalovuja damu.

    “Niambie Aden ni nani anayehusika na fedha hizi?” Koplo Tsega akauliza

    “White…’’

    “White ndiyo nani?” Koplo Tsega akauliza kwa shauku

    “White Sugar…!” yule meneja wa benki akaongea huku akilalama kwa maumivu

    makali ya jeraha la risasi pajani mwake.

    “Niambie,huyo White Sugar ndiyo nani?’’ Koplo Tsega akauliza kwa utulivu.

    “Meneja wa Zanzibar Stone City Bazaar”

    “Anaishi wapi?’’

    “Sifahamu na wala sijawahi kuonana naye” yule meneja wa benki akajitetea lakini

    kitendo cha kumuona Koplo Tsega akiunyoosha mkono na kuelekezea bastola yake

    kwenye paja la mguu wake mwingine akaingiwa na hofu.

    “Duka lake lipo ndani ya Mlimani City Shopping Mall linatazamana na duka

    kubwa la vinyago la African art craft” yule meneja wa benki akafafanua hata hivyo

    mduwao mwingine ukamshika wakati alipouona mdomo wa ile bastola ya Koplo

    Tsega ukielekezewa kwenye kifua chake.

    “Tafadhali usiniue...!”

    “Sikuui Aden nakupumzisha tu!’’ kabla yule meneja wa benki hajaongea neno

    risasi mbili za bastola ya Koplo Tsega zikapenya kifuani mwake na kutengeneza

    matundu makubwa mawili yanayovuja damu kwenye moyo na hapo yule meneja wa

    benki akatikisika kidogo kwenye kile kiti chake cha ofisini kabla ya kutulia huku roho

    yake ikiwa mbali na mwili.

    Koplo Tsega hakutaka kuendelea kupoteza muda hivyo akaingiza mkono

    mfukoni na kuchukua pipi ya kijiti na kuimenya kabla ya kuitia mdomoni. Kisha

    haraka akachukua kilicho chake mle ndani na kuelekea kwenye mlango wa ile

    ofisi. Alipoufungua mlango wa ile ofisi na kutoka nje pale mlangoni akakutana na

    mwanaume mmoja aliyekuwa akielekea kwenye ile ofisi ya meneja wa benki.

    “Subiri kidogo kuna mtu anazungumza na meneja” Koplo Tsega akamwambia

    yule mwanaume wakati akipishananaye kwenye ile korido.

    “Sawa!” yule mwanaume akaitikia huku akigeuza na kurudi kule alipotoka. Muda

    mfupi uliofuata Koplo Tsega alikuwa akikatisha kando ya lile dawati la idara ya

    huduma kwa wateja. Yule dada mlimbwende mfanyakazi wa idara ile alipomuona

    Koplo Tsega akatabasamu na kumuuliza

    “Vipi amekusikiliza haja yako?”

    “Ndiyo nashukuru sana dada kwani amekwisha nielekeza cha kufanya. Nitarudi

    tena mapema sana baada ya kukamilisha taratibu zote” Koplo Tsega akajinadi kwa

    hila huku akijifanya ni mwenye haraka.

    “Karibu tena”

    “Ahsante na kazi njema” Koplo Tsega akashukuru na kuaga huku akielekea

    kwenye mlango mkubwa wa kioo mbele ya lile jengo la benki ya Zanzibar Marine.

    Alipofika akausukuma ule mlango na kutokomea nje huku macho ya yule dada

    mlimbwende wa idara ya huduma kwa mteja yakimsindikiza kwa nyuma.



    SAA TISA ALASIRI KASORO dakika chache Koplo Tsega akaegesha gari

    lake kwenye eneo kubwa la wazi la maegesho ya magari la Mlimani City Shopping

    Mall. Kabla ya kushuka akayatembeza macho yake taratibu kuyachunguza magari

    yaliyokuwa eneo lile kwa utulivu. Mvua ilikuwa imeanza kunyesha hivyo hakumuona

    mtu yeyote eneo lile au kama kungekuwa na watu basi huwenda watu hao wangekuwa

    wamejifungia ndani ya baadhi ya magari yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile.

    Tangu alipotoka kwenye ile benki ya Zanzibar Marine akili yake ilikuwa imejikita

    katika kumtafakari yule mtu aliyekuwa akifahamika kama White Sugar meneja wa

    duka la Zanzibar Stone City Bazaar kama yule meneja wa benki ya Zanzibar Marine

    alivyotanabaisha. Kwa namna moja au nyingine Koplo Tsega aliamini kuwa huyo

    mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la White Sugar ndiye ambaye angekuwa kiungo

    muhiimu sana katika ule mtandao mchafu ulioshiriki kikamilifu katika kusuka

    mpango wa kuwaengua yeye na Sajenti Chacha Marwa kutoka katika tume maalum

    inayoshughulika na udhibiti na upambanaji wa biashara haramu ya dawa za kulevya

    nchini Tanzania.

    Hisia za Koplo Tsega zikamtanabaisha kuwa kumpata White Sugar lingekuwa ni

    jambo muhimu sana katika kuwafahamu watu wote waliohusika na njama chafu dhidi

    yao lakini vilevile kumpata White Sugar kungeweza kutatua maswali mengi yaliyokuwa

    yakiisimanga vibaya nafsi yake. Maswali kama mtandao ule mchafu uliotumika

    kuwahujumu ulikuwa ukimhusisha nani na nani vilevile ulikuwa ukifadhiliwa na nani.

    Meja Khadid Makame,kiongozi wa kijeshi aliyekuwa akiheshimika sana kwa weledi

    wake alikuwa na nafasi gani katika mpango ule mchafu na kama alihongwa fedha

    basi alihongwa na nani na fedha hizo zilikuwa kiasi gani. Kufikia pale Koplo Tsega

    akayahamisha mawazo yake na kuanza kumfikiria yule mwanaume aliyemuokoa

    kutoka mikononi mwa wale wanausalama kule kwenye lile jengo refu la ghorofa

    lililokuwa katikati ya maeneo ya posta jijini Dar es Salaam. Maswali bado yalikuwa

    mengi na majibu yake yalihitaji muda na uchunguzi makini.

    Hatimaye Koplo Tsega akafungua mlango na kushuka kwenye gari kisha akaanza

    kuzitupa hatua zake kwa haraka akielekea kwenye mlango mkubwa wa kuingilia

    kwenye lile duka kubwa la kisasa na la kimataifa-Mlimani city shopping mall. Begi lake

    likiwa mgongoni,kofia ya sombrero kichwani na miwani myeusi machoni taratibu

    Koplo Tsega akawa akiyatembeza macho yake kwa uficho mkubwa na kuwatazama

    watu wote waliokuwa eneo lile. Hakumuona mtu yeyote wa kumtilia mashaka hivyo

    akaendelea kuzitupa hatua zake kwa utulivu kuelekea kwenye lile jengo.

    Kulikuwa na watu wengi ndani ya maduka yale ya kisasa waliokuwa wamefika

    kupata huduma tofauti na baadhi ya watu wale walikuwa wamesimama kwenye korido

    za maduka yale wengine wakinunua bidhaa na wengine wamesimama wakisubiri

    mvua ile iishe ili waondoke baada ya kumaliza kununua mahitaji yao.

    Koplo Tsega alipofika katikati ya korido zile akasimama kwa utulivu akiyachunguza

    mazingira yale. Kulikuwa na korido mbili kubwa na pana,moja upande wa mbele na

    nyingine upande wa kulia. Korido zile zilikuwa zikitazamana na maduka mbalimbali



    baadhi yakiwa ni maduka ya kampuni kubwa na maarufu za jijini Dar es Salaam na

    mengine maduka ya watu binafsi. Maduka yale ya kisasa yalikuwa yamezungukwa

    na kuta kubwa za vioo visafi vinavyomwezesha mtu yeyote kuweza kuona bidhaa

    zilizokuwa ndani ya maduka yale.

    Ile korido ya mbele ilikuwa ikielekea katika Supermarket kubwa ya kisasa iliyokuwa

    na bidhaa nyingi za matumizi ya kawaida ya binadamu yenye wahudumu waliovaa sare

    maalum za kuwatambulisha na vitambulisho vyao vikiwa vimening’inizwa kwa kamba

    maalum shingoni. Ile korido ya upande wa kulia ilikuwa ikitazamana na maduka

    mengi ya bidhaa tofauti zikiwemo ofisi za kampuni za mawasiliano ya mitandao ya

    simu. Koplo Tsega akajikuta akiyakumbuka vyema maelezo ya Aden Mawala yule

    meneja wa benki ya Zanzibar Marine kuwa duka la Zanzibar Stone City Bazaar

    lilikuwa likitazamana na duka la vinyago la Afrikan art craft mle ndani. Hivyo Koplo

    Tsega akashika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata ile korido iliyokuwa ikitazamana

    na maduka mbalimbali.

    Kulikuwa na watu wengi katika korido ile huku kila mmoja akionekana kuzama

    katika hamsini zake. Koplo Tsega wakati akitembea akawa akiyatembeza macho

    yake taratibu kuzichunguza sura za watu aliokuwa akipishana nao kwenye korido ile.

    Hakumuona mtu yeyote wa kumtilia mashaka ingawa baadhi ya watu hawakujizuia

    kumtazama huku dhahiri wakionekana kuvutiwa na mtindo wa uvaaji wake kama siyo

    weusi wake wa asili.

    Ilikuwa ni wakati Koplo Tsega alipokuwa mbioni kufika mwisho wa korido ile

    pale alipoliona duka kubwa la vinyago lenye maandishi makubwa ya African art craft

    upande wa kushoto. Ndani ya duka lile kulikuwa kijana mmoja aliyekuwa akiwaelekeza

    jambo wazungu wawili,mwanamke na mwanaume waliokuwa wakikitazama kinyago

    kimoja kikubwa cha kimakonde cha mti wa mpingo cha mwanamke wa kiafrika

    aliyebeba mtoto wake mgongoni kwa mbeleko. Kinyago kizuri kilichochongwa kwa

    umakini wa hali ya juu.

    Koplo Tsega alipolifikia lile duka la vinyago akasimama mbele yake na

    kuyatembeza macho yake taratibu upande wa kulia. Maelezo ya yule meneja wa

    benki ya Zanzibar Marine yalikuwa sahihi kwani duka la Zanzibar Stone City Bazaar

    lilikuwa likitazamana na duka lile la African art craft kwa upande wa kulia. Kwa dakika

    kadhaa Koplo Tsega akasimama akilitazama duka lile kwa utulivu kama mtu ambaye

    hayaamini vizuri macho yake.

    Duka la Zanzibar Stone City Bazaar lilikuwa ni miongoni mwa maduka

    yaliyokuwa na pilikapilika nyingi za wateja baadhi wakiingia mle ndani na kutazama

    bidhaa zilizokuwa mle ndani huku wengine wakifanya manunuzi ya bidhaa. Lilikuwa

    ni duka kubwa lenye maduka mengi madogo madogo ndani yake ya bidhaa kama

    nguo,simu,vyakula,vyombo vya nyumbani,vifaa vya umeme,vitabu,vifaa vya

    maofisini,viatu,mikoba na vifaa vingine muhimu vya mahitaji ya binadamu. Hata hivyo

    wateja wengi waliokuwa ndani ya maduka yale walikuwa wanawake ambao wengi

    wao walionekana kuvutiwa zaidi na bidhaa kama nguo,viatu,mikoba na vyombo vya

    nyumbani.

    Fikra za mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la White Sugar zikiwa zimeanza

    kujengeka upya kichwani mwake Koplo Tsega akaanza taratibu kuzitupa hatua

    zake akielekea kwenye lile duka la Zanzibar Stone City Bazaar huku akigeuka na

    kuyatembeza macho yake huku na kule katika namna ya kuhakikisha kuwa hakuna

    mtu yeyote aliyekuwa akizifuatilia nyendo zake. Wakati Koplo Tsega akiufikia mlango

    wa duka lile pale mlangoni akapishana na mwanaume mmoja mrefu na mweusi akiwa

    katika mavazi yake ndhifu ya suti ya kijivu ya Marks & Spenser,shati la rangi nyeusi na

    tai ya rangi ya zambarau.

    Mtu yule alikuwa amenyoa upara na macho yake alikuwa ameyafunika kwa miwani

    kubwa nyeusi yenye kumwezesha kuiona dunia pasipo usumbufu wowote. Mkononi

    alikuwa amevaa saa ya gharama sana ya dhahabu aina ya Maurice Lacroix huku akiwa

    amebeba briefcase nyeusi inayotumia mfumo wa codenumber maalum katika kuifungua.

    Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi nadhifu vya ngozi huku marashi yake ya gharama

    yenye harufu nzuri ya tafsiri ya ukwasi yakiongeza ziada nyingine katika utanashati

    wake.

    Akionekana ni mwenye haraka mara tu mtu yule alipopishana na Koplo Tsega pale

    mlangoni akaanza kutembea kwa kuharakisha akishika uelekeo wa upande wa kushoto

    wa ile korido pana mbele ya lile duka huku mara kwa mara akiunyanyua mkono

    na kuitazama ile saa yake ya mkononi kama mtu aliyekuwa nyuma ya muda katika

    tukio fulani. Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akajikuta amesimama pale mlangoni

    na kumtazama yule mtu namna alivyokuwa akitokomea kwenye ile korido kama

    kimbunga kisha akageuka na kuingia mle ndani ya lile duka huku akiyapuuza macho

    ya watu waliokuwa wakimtazama eneo lile kana kwamba alikuwa amebabaishwa na

    kutekwa na muonekano wa yule mwanaume aliyetoka kwenye lile duka.

    Jina la White Sugar likiwa limerudi tena kwenye fikra zake mara tu alipoingia

    ndani ya lile duka Koplo Tsega akajisogeza upande wa kulia sehemu kulipokuwa na

    duka la simu za mkononi za kisasa zilizopangwa ndani ya rafu nzuri ya vioo. Kijana

    mmoja wa kiume aliyekuwa akihusika na biashara ile haraka akasimama kutoka

    kwenye kiti alichoketi nyuma ya ile rafu ya vioo na kusogea karibu na Koplo Tsega

    kama afanyavyo kwa wateja wengine waliokuwa wakiingia mle ndani na kuonekana

    kuvutiwa na bidhaa zake.

    “Mambo vipi dada?’’ yule kijana akamsalimia Koplo Tsega kwa makeke

    “Poa” Koplo Tsega akaitikia huku usoni akiumba tabasamu la kirafiki

    “Karibu sana”

    “Ahsante” Koplo Tsega akaitikia huku akigeuka na kuyatembeza macho yake

    kuzichunguza sura za watu waliokuwa mle ndani kabla ya kuyarudisha tena mbele

    yake na kuanza kuzitazama simu zilizokuwa ndani ya ile rafu ya vioo ingawa dhahiri

    mawazo yake hayakuwa katika zile simu. Yule kijana muuzaji wa lile duka kuona vile

    akasogea karibu akijitahidi kuyapatiliza kwa ukaribu macho ya Koplo Tsega. Koplo

    Tsega alipoyainua macho yake kumtazama yule kijana akavunja ukimya akiuliza swali

    la hila.

    “Hili ndiyo duka la Zanzibar Stone City Bazaar?”

    “Maduka ya humu ndani yote ni ya Zanzibar Stone City Bazaar” yule kijana

    akafafanua huku akishindwa kuelewa hoja muhimu katika swali lile.

    “Ninashida na meneja wa hili duka,unaweza kunisaidia nikaonana naye?’’Koplo

    Tsega akamuuliza yule kijana kwa utulivu huku akimtongoza kwa tabasamu lake

    maridhawa.

    “Shida gani?’’ yule kijana akauliza huku akimtazama Koplo Tsega kwa udadisi

    “Shida binafsi inayohusu biashara” Koplo Tsega akadanganya huku akimtazama

    yule kijana kwa makini.

    “Umepishana naye sasa hivi pale mlangoni wakati ulipokuwa ukiingia humu

    ndani” jibu la yule kijana likapelekea mshtuko mkubwa kwa Koplo Tsega,moyo wake

    ukalipuka kabla ya baridi nyepesi kuanza kusafiri mgongoni mwake huku kijasho

    chembamba kikichomoza taratibu katika sehemu mbalimbali za mwili wake na

    hatimaye utulivu kupotea kabisa moyoni mwake ingawa alijitahidi kuumeza mshtuko

    ule kwa kila hali.

    Kwa sekunde kadhaa akili ya Koplo Tsega ilishindwa kabisa kuamini kuwa yule

    mwanaume aliyepishananaye muda mfupi pale mlangoni wakati akiingia kwenye lile

    duka ndiye angekuwa White Sugar,mtu aliyekuwa akimtafuta. Koplo Tsega akajikuta

    akishawishika kuwa muda uleule atoke kwenye lile duka na kuanza kutimua mbio

    akashika ule uelekeo wa yule mtu kule alikotokomea. Hata hivyo baada ya kufikiri kwa

    kina Koplo Tsega akajikuta akiuweka kando mpango ule pale alipohisi kuwa kwa ule

    muda uliopita yule mtu angeweza kuwa tayari amekwishafika mbali sana na eneo lile

    kwa vile alivyoonekana kuwa na haraka ya kupita kiasi istoshe hakufahamu mtu yule

    alikuwa akielekea wapi.

    “Oh! masikini mimi nimekuwa mzembe kwa kuchelewa” Koplo Tsega akalaani

    kitendo kile huku akishindwa kuamini.

    “Kwani hamfahamiani?” yule kijana akauliza

    “Hatufahamiani ila kuna mtu anayefahamiana naye ndiye aliyenielekeza kwake”

    Koplo Tsega akadanganya wa hila

    “Pole sana basi uache business card yako ili siku atakaporudi nimpe akutafute”

    yule kijana akatoa wazo huku akimtazama Koplo Tsega katika mtazamo wa kimapenzi

    hata hivyo Koplo Tsega akampuuza.

    “Bahati mbaya sana leo nimesahau kutembea na business card yangu. Kwani

    hatorudi tena leo?” Koplo Tsega akamuuliza yule kijana

    “Hapana hatorudi tena na imekuwa ni bahati sana kumuona kirahisi namna

    ile kwani mara nyingi sana huwa yupo safarini nje ya nchi” yule kijana akaendelea

    kutanabaisha na Koplo Tsega alipomtazama akagundua kuwa maelezo yake yalikuwa

    yamekomea pale katika kumfahamu White Sugar na ile ndiyo ilikuwa salama yake.

    “Ameelekea wapi?” Koplo Tsega akauliza kwa utulivu huku akimtazama yule

    kijana kwa makini.

    “Anawahi boti ya kuelekea kisiwani Zanzibar”

    “Kwani anaishi Zanzibar?”

    “Ndiyo maskani yake yalipo’’ yule kijana akafafanua huku akionekana kuwa na

    hakika na maelezo yake na hapo kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku Koplo

    Tsega akizidi kujilaani kwa namna alivyopishana na bahati ile pasipo kujua. Mwishowe

    akavunja ukimya kuuliza

    “Unaweza kunisaidia namba zake za simu?’’

    “Namba zake za simu nilizonazo ukimpigia huwa hapatikani” yule kijana

    akaendelea kufafanua na kupitia maelezo yake Koplo Tsega akatambua kuwa

    asingeweza kupata ziada nyingine kutoka kwake hivyo haraka akaunyanyua mkono

    na kuitazama saa yake ya mkononi na alipomaliza na kuyahamishia macho yake kwa

    yule kijana akaumba tabasamu jepesi lisilo na maana yoyote usoni mwake kabla ya

    kuvunja ukimya

    “Nashukuru sana wacha niende nitakuja siku nyingine”

    “Pole sana dada yangu kama vipi niachie namba yako ya simu ili siku yoyote

    atakaporudi nikufahamishe” yule kijana akasisitiza akijaribu bahati yake na Koplo

    Tsega alipomtazama akayaona macho yake yalivyojawa na uchu wa ngono hali

    iliyompelekea atabasamu kidogo na kuanza kumtajia namba ya simu ya kufikirika

    kichwani isiyopatikana. Yule kijana akawahi kuinakili haraka ile namba kwenye simu

    yake na wakati alipomaliza kubofya tarakimu ya mwisho na kuinua macho yake

    kumtazama Koplo Tsega mbele yake,Koplo Tsega tayari alikuwa amekwisha toka nje

    ya lile duka na kutokomea.





    TAARIFA ZA KUUAWA KWA MENEJA wa benki ya Zanzibar Marine tawi la

    jijini Dar es Salaam lilipo eneo la Morocco zilikuwa zimesambaa haraka kama ubuyu

    na kuvifikia vyombo vya usalama. Ndani ya dakika chache baada ya mwili wa meneja

    wa ile benki kugundulika ofisini kwake taarifa kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa

    benki ile haraka zilikuwa zimekifikia kituo cha polisi cha Oysterbay kilichokuwa na

    dhamana ya kusimamia usalama wa eneo lile. Mkuu wa kituo kile cha polisi alipofika

    eneo la tukio na kutathmini mazingira ya tukio zima akaamua kuomba nguvu ya

    wataalam wa kuchukua vipimo na alama za mwalifu kutoka makao makuu ya jeshi

    la polisi. Taarifa zilipoyafikia makao makuu ya jeshi la polisi juu ya ombi la wataalam

    wake kutokana na unyeti wa tukio lenyewe,taarifa hizo zikawa zimevuja na kuwafikia

    vijana wa Sulle Kiganja waliokuwa wamepandikizwa kila kona katika kuhakikisha

    kuwa mhusika wa mauaji ya wanausalama yaliyokuwa yakiendelea jijini Dar es Salaam

    anakamatwa.

    Hivyo Sulle Kiganja na vijana wake wa kazi wakawa ndiyo watu wa kwanza kufika

    katika eneo la tukio ndani ya ofisi ile ya meneja wa benki ya Zanzibar Marine yale

    mauaji yalipotokea.

    Kamera za usalama za CCTV zilizokuwa zimefungwa katika kila pembe ya lile

    jengo la benki ya Zanzibar Marine ikiwemo kamera iliyokuwa ndani ya ofisi ya meneja

    wa ile benki aliyouwawa zilikuwa zimehifadhi kumbukumbu ya matukio yote muhimu

    ya mtu aliyesemekana kuhusika na kifo cha meneja wa benki ile. Sulle Kiganja na vijana

    wake wa kazi baada ya kumaliza kupitia picha zote zilizonaswa na kamera za usalama

    za jengo lile chini ya mkuu wa idara ya teknolojia ya mawasiliano (IT) akajiridhisha

    na kuhitimisha kuwa muuaji alikuwa ni mwanamke mwenye umri kati ya miaka

    ishirini na sita hadi thelathini ingawa sura yake haikuweza kuonekana vizuri kutokana

    na miwani ya jua aliyoivaa na kofia ya Sombrero aliyojifunika kichwani. Msichana

    mwembamba mwenye umbo kakamavu akiwa amevaa pullneck nyeusi,shati gumu

    la jeans,suruali ya jeans iliyolichora vyema umbo lake,viatu vya rangi ya udongo aina

    ya Travolta miguuni huku akiwa amebeba begi jeusi,jembamba na refu mgongoni

    lisiloeleweka kuwa na kitu gani ndani yake.

    Hata hivyo kulikuwa na mambo mawili matatu yaliyokuwa yamemchagiza Sulle

    Kiganja wakati alipokuwa akizipitia zile picha za matukio ya muuaji zilizonaswa

    na kamera za usalama za ile benki. Kwanza kabla ya kuanza kupitia picha zile za

    matukio moja kwa moja alikuwa ameamini kuwa kwa vyovyote muuaji angekuwa ni

    mwanaume tena kwa hakika angekuwa ni Chaz Siga mwanaume aliyewatoroka siku

    ile chini ya lile jengo la ghorofa lililopo kule maeneo ya posta kwani uchunguzi wa

    awali wa matukio yote ya mauaji yaliyokuwa yakiendelea kufanyika jijini Dar es Salaam

    yalikuwa na viashiria vilivyokuwa vikimhusisha yeye kwa namna moja au nyingine.

    Lakini kitendo cha kuziona picha zile za muuaji zilikuwa ni za msichana kilikuwa

    kimeutibua vibaya ubongo wake na kutengeneza ukinzani mkubwa katika mwenendo

    wa mikakati yake ya kumnasa muuaji.

    Vilvile picha za matukio ya mauaji yale zilizonaswa na kamera za usalama za ile benki

    zilikuwa zimeonesha kuwa kulikuwa na namna ya maongezi ya kawaida yaliyofuatiwa

    na majibishano makali kati ya yule mwanamke aliyeingia ndani ya ile ofisi ya meneja

    wa benki na yule meneja wa ile benki kabla ya mauaji yale kufanyika. Mabishano yale

    kati ya yule muuaji na meneja wa ile benki baadaye yakawa yamepelekea yule dada

    muuaji kutoa karatasi fulani kutoka kwenye bahasha iliyokuwa kwenye mfuko mmoja

    wa suruali yake ya jeans na kuisogeza pale mezani katika namna ya kumtaka yule

    meneja wa benki asome kile kilichokuwa kimeandikwa kwenye karatasi ile. Ingawa

    kamera zilionesha kuwa mara baada ya meneja wa ile benki kumaliza kusoma kile

    kilichokuwa kimeandikwa kwenye karatasi ile alionekana kukataa kukubaliana nacho

    lakini tukio lile lilikuwa limeibua maswali mapya kichwani kwa Sulle Kiganja kuwa

    muuaji hakuwa mwendawazimu kama walivyokuwa wauaji wengine wasio na sababu

    katika kutekeleza unyama wao bali alionekana kuwa na hoja fulani ya kusimamia

    ambayo bila shaka ilikuwa imejificha kwenye karatasi ile.

    Zile picha za matukio bado ziliendelea kuonesha kuwa mara baada ya yule meneja

    wa benki kuonekana kutokukubaliana na kile kilichokuwa kimeandikwa kwenye

    ile karatasi iliyotolewa mfukoni kutoka kwenye bahasha. Yule dada muuaji alikuwa

    ameichukua ile karatasi na kuitia kwenye bahasha kabla ya kuirudisha mfukoni kisha

    kukafutiwa na kitambo kingine cha maongezi ya majibishano makali kabla ya yule

    dada muuaji kutoa tena bahasha nyingine kutoka katika mfuko mwingine wa suruali

    yake ambapo alipoifungua alitoa vipande vya karatasi vinavyolingana na kuvisogeza

    karibu na meneja wa ile benki juu ya ile meza ya ofisini iliyokuwa mle ndani. Kufikia

    pale Sulle Kiganja akawa amemuomba mkuu wa idara ya teknolojia ya mawasiliano

    wa ile benki ambaye ndiye aliyekuwa na dhamana ya kusimamia ufanyaji wa kazi wa

    zile kamera za usalama za ile benki aivute kwa karibu taswira ya vile vipande vya

    karatasi vilivyokuwa vimewekwa pale mezani na yule muuaji na hatimaye kuikuza

    taswira yake. Picha ya karibu iliyoonekana ikathibitisha kuwa vipande vile vya karatasi

    vilivyowekwa pale mezani na yule muuaji zilikuwa ni hundi na hundi zile zilikuwa ni

    za ile benki ya Zanzibar Marine. Sulle Kiganja akazidi kuingiwa na mashaka kuwa

    kulikuwa na jambo la hatari zaidi lililokuwa limefichika hadi kupelekea mauaji ya

    meneja wa ile benki.

    Halafu taratibu Sulle Kiganja alipokuwa akiendelea kuzipitia zile picha hoja

    nyingine zikawa zikiendelea kuibuka kichwani mwake. Kamera ziliendelea kuonesha

    kuwa mara baada ya yule meneja wa ile benki kumaliza kuzipitia zile hundi zilizowekwa

    pale mezani na yule muuaji bado meneja wa ile benki alionekana kukataa kukubaliana

    na hoja ya muuaji kiasi cha kumpelekea yule muuaji kuzichukua zile hundi na

    kuzirudishia kwenye bahasha yake na hatimaye kuzitia mfukoni. Yule muuaji wakati

    akishughulika na kuitia ile bahasha mfukoni kamera zikaendelea kuonesha kuwa yule

    meneja wa benki alikuwa akiupeleka mkono wake taratibu kwa hila kuufungua mtoto

    wa meza yake ya ofisini kabla ya hila yake kushtukiwa na kusukumiwa ile meza ya

    ofisini iliyombana vyema huku akiwa ameketi kwenye kile kiti chake cha ofisini.

    Kitendo cha Sulle Kiganja kumuona muuaji akisimama ghafla na kuichomoa bastola

    yake mafichoni akimwendea yule meneja wa benki pale kwenye kile kiti alipobanwa

    na ile meza ya ofisini kikawa kimempelekea awe makini na kuzidi kusogea karibu

    kulitazama tukio lile. Muuaji alikuwa ameishtukia mapema dhamira ya yule meneja

    wa benki wakati alipokuwa akiuvuta ule mtoto wa meza kwa hila kwani yule muuaji

    alipofika pale kwenye meza na kupenyeza haraka mkono kwenye ile droo na mkono

    ule ulipotoka ulikuwa na bastola ambapo yule muuaji haraka akachomoa magazini ya

    ile bastola aliyoitoa kwenye mtoto wa ile meza na kuitupa mle ndani sakafuni. Tukio

    lile likamaanisha kuwa yule meneja wa benki alikuwa akitaka kuichukua ile bastola kwa

    hila ili aweze kujihami dhidi ya yule muuaji. Hoja nyingine ikaibuka kichwani kwa Sulle

    Kiganja akijiuliza kama meneja wa ile benki alikuwa akimiliki ile bastola kwa kufuata

    misingi ya sheria au lah!.

    Matukio mengine yaliyofuata kupitia zile kamera za usalama za ile benki

    zilimuonesha yule muuaji namna alivyokata waya wa simu ya mezani ya mle ndani

    ofisini kabla ya kuutumia waya ule kumkaba shingoni yule meneja wa benki huku

    akimshinikiza kufanya jambo fulani kwenye ile kompyuta yake ya mezani. Kamera

    bado ziliendelea kuonesha kuwa bado yule meneja wa benki hatimaye aliamua kukubali

    na kutekeleza kile alichoshinikizwa kukifanya kabla ya kuonekana akishughulika

    na kompyuta yake na baadaye kuonekana akiprint taarifa fulani. Kufikia pale Sulle

    Kiganja akamuomba tena yule mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano wa ile benki

    kuvuta karibu ile picha ya ile karatasi iliyotoka kwenye ile printer ya mle ndani na

    kuyakuza maandishi yake. Taswira ile ilipopatikana vizuri afisa mwingine wa ile benki

    aliyekuwa nyuma yao akahitimisha kuwa taarifa ile iliyotolewa na printer ilikuwa ni

    taarifa iliyofahamika kitaalam kama Bank cash flow ya ile benki ya Zanzibar Marine

    na taarifa nyingine iliyofuatia kutolewa na ile printer ilikuwa ni Bank statement na

    taswira yake iliposogezwa karibu jina la Zanzibar Stone City Bazaar likasomeka kwa

    ufasaha kiasi cha kumpelekea Sulle Kiganja kuupindisha mdomo wake kwa dharau.

    Kisha akamgeukia yule afisa wa benki aliyekuwa muda wote amesimama nyuma yao

    akiufuatilia ule mchakato kwa makini ndani ya kile chumba kidogo cha mtaalam wa

    teknolojia ya mawasiliano wa ile benki,kijana mdogo na mtundu wa kompyuta.

    “Cash flow statement na Bank statement zina maana gani kwako?”

    “Cash flow statement ni taarifa ya benki inayoonesha kiasi cha pesa kilichoingia

    na kutoka kwenye benki kwa muda wa mwezi mmoja wakati Bank statement ni ripoti

    inayotolewa na benki katika tarehe maalum kila mwezi ambayo ndani yake huorodhesha

    matukio yote ya kuweka na kutoa pesa kwenye akaunti yaliyofanyika,hundi zilizolipwa

    kama zitakuwepo,riba iliyotozwa na makato ya huduma za benki au faini zilizotozwa

    kwenye akaunti husika” yule afisa wa benki akafafanua kwa ufasaha.

    “Kupitia hiyo Cash flow statement na hiyo Bank statement ambazo meneja wa

    benki yenu alionekana kushinikizwa kuziprint unadhani muuaji alitaka kufahamu

    nini?” Sulle Kiganja akamuuliza tena yule afisa wa benki kwa utulivu huku akiendelea

    kuzitazama zile picha za matukio kwa makini kwenye zile kamera.

    “Sina hakika ingawa nahisi kuwa huwenda alikuwa akitaka kufahamu pesa fulani

    iliyokuwa imeingia kwenye hii benki na kutoka pamoja na jina la mhusika wa akaunti

    iliyotumika kufanya muamala huo” Sulle Kiganja akageuka na kumtazama kwa makini

    yule afisa wa benki kama mtu afikiriaye jambo fulani kisha akawa ni kama aliyeona

    kuwa hapakuwa na swali jingine la ziada la kumuuliza tena yule mtu kwa wakati ule.

    “Okay! nashukuru sana kwa ushirikiano wenu” hatimaye Sulle kiganja

    akawashukuru yule afisa wa benki na yule mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano wa

    ile benki kisha akasogeza kiti nyuma na kusimama.

    “Ningependa kumuona huyo mfanyakazi wenu wa idara ya huduma kwa wateja

    anayesemekana kuwa ndiye aliyemkaribisha huyu mtuhumiwa wa mauaji pamoja

    na huyo mwanaume aliyemuona muuaji wakati alipokuwa akitoka kwenye ofisi ya

    meneja wa benki” Sulle Kiganja akasisitiza akiyakumbuka maelezo ya awali aliyokuwa

    amepewa na yule afisa wa benki wakati alipofika. Kisha akaanza kuondoka taratibu

    kwenye ile ofisi ya idara ya teknolojia na mawasiliano huku akiwa ameongozana na

    vijana wake kuelekea kwenye ile ofisi ya meneja wa ile benki yale mauaji yalipotoke.

    Muda mfupi uliyofuata Sulle Kiganja na vijana wake walikuwa ndani ya ile ofisi ya

    meneja wa benki. Alipofika mle ndani akawakuta vijana wake wakiendelea kuchukua

    vipimo maalum vya kiuchunguzi mle ndani na kutoka katika ule mwili wa yule meneja

    wa benki ukiwa bado haujaondolewa pale kwenye kile kiti chake cha ofisini huku

    kifuani akiwa amelowa damu nyingi iliyokuwa ikiendelea kuvuja taratibu kutoka

    kwenye yale majeraha ya risasi kifuani mwake.

    Dakika chache baada ya Sulle Kiganja kuingia mle ndani ya ile ofisi ya yule meneja

    wa ile benki yule dada mlimbwende mfanyakazi wa ile idara ya huduma kwa mteja

    na yule mwanaume aliyepishana na Koplo Tsega mlangoni wakati ule alipokuwa

    akitoka kwenye ile ofisi ya meneja wa benki nao wakaingia mle ndani. Sulle Kiganja

    alipogeuka na kuwatazama wale watu sura yake ikatengeneza tabasamu jepesi kabla

    ya kuwapa mkono na kusalimiana nao na baada ya pale mahojiano mafupi yakafuatia

    huku akianza na yule dada mlimbwende mfanyakazi wa idara ya huduma kwa wateja

    wa ile benki.

    “Naitwa Sulle Kiganja mimi ni afisa usalama ningependa kusikia maelezo

    machache muhimu kutoka kwako kufuatia hili tukio la mauaji ya meneja wa benki

    yenu wewe ukiwa kama mtu aliyepata nafasi ya kumuona muuaji kwa ukaribu zaidi na

    kuzungumza naye machache” Sulle Kiganja akafafanua.

    “Naitwa Bi.Husna Mansour,afisa wa idara ya huduma kwa wateja wa benki hii”

    yule dada mlimbwende akajitambulisha huku machozi yakimlengalenga.

    “Ulionana na mwanamke aliyeingia humu ndani kabla ya mauaji haya kutokea?”

    Sulle Kiganja akauliza huku akimtazama Bi.Husna Mansour kwa utulivu.

    “Ndiyo”

    “Ilikuwa saa ngapi”

    “Kati ya saa saba na nusu mchana hadi saa nane” Bi.Husna Monsour akaongea

    kwa utulivu huku akijifuta machozi kwa kitambaa chake mkononi.

    “Umewahi kumuona popote hapo kabla?”

    “Hapana” Sulle Kiganja akamtazama Bi.Husna kwa utulivu kabla ya kuendelea.

    “Huyo mwanamke alikwambia shida iliyomleta hapa kukutana na meneja wenu

    wa benki?”

    “Ndiyo”

    “Shida gani?”

    “Aliniambia kuwa alikuwa amefika hapa katika kutaka kujua utaratibu ambao

    ungewezesha mishahara ya wafanyakazi wa kampuni yake iwe inapitia kwenye benki

    yetu”

    “Alikutajia jina la hiyo kampuni au kukuonesha kitambulisho chake?” swali la

    Sulle Kiganja likampelekea Bi.Husna Mansour asite kwani tayari alishagundua kosa

    alilolifanya la kutokuhoji jina la yule dada muuaji kama siyo kuchukua maelezo yake.

    “Hapana” hatimaye akaongea kwa sauti iliyopwaya.

    “Ni kawaida yenu kufanya hivyo?” Sulle Kiganja akauliza tena

    “Hapana nadhani nilifanya makosa kwa vile mtu mwenyewe alionekana kuwa na

    haraka” maelezo ya Bi.Husna Mansour yakapelekea tena kitambo kifupi cha ukimya

    kufuata. Sule Kiganja alipozidi kufikiria akagundua kuwa ile sababu ya kutaka kuonana

    na meneja wa ile benki iliyotolewa na muuaji ilikuwa ni ya uongo wa kutengeneza

    katika namna ya kuhakikisha kuwa muuaji anatimiza lengo lake.

    “Wakati mwingine jitahidi kuwa makini zaidi dada dunia ya sasa imeharibika” Sulle

    Kiganja akasisitiza na kisha kufuatiwa na kitambo kingine cha ukimya huku akifikiria

    jambo fulani.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Rekodi tuliyoipata kupitia kamera zenu inaonesha kuwa muuaji alikaa ofisini kwa

    meneja wa benki yenu kwa muda usiopungua nusu saa. Hili ni jambo la kawaida

    kutokea?”

    “Hakuna muda rasmi wa mteja kuonana na meneja au mtu yeyote wa humu ndani

    kwani hiyo hutegemeana na shida yenyewe na hali itakavyokuwa. Mfano kama meneja

    hana kazi nyingi anaweza kutumia muda mwingi zaidi kuonana na wateja au mtu

    yeyote yule mwingine” Bi.Husna Mansour akafafanua.

    “Ukimuona muuaji unaweza ukamuelezeaje kwa muonekano wake?”

    “Ni dada mrembo,mweusi,mwembamba kiasi na mrefu mwenye umbo zuri la

    kike lakini kakamavu. Sura yake ni nyembamba kiasi ingawa sikuweza kumuona vizuri

    kutokana na kofia aliyoivaa kichwani na miwani myeusi pana ya jua machoni mwake”

    “Wakati alipokuwa akitoka humu ofisini kwa meneja wa benki yenu ulimuona?”

    “Ndiyo”

    “Ukiwa wapi?” Sulle kiganja akauliza kwa makini huku akimtazama Bi.Husna

    Mansour machoni

    “Pale kwenye sehemu yangu ya kazi”

    “Alikuaga?”

    “Nilimuuliza kama alihudumiwa shida yake akaniambia kuwa alishapewa

    utaratibu wa kufanya hivyo angerudi hapa mapema sana baada ya kukamilisha vigezo

    vinavyohitajika”

    Sulle Kiganja akamtazama tena Bi.Husna Mansour kwa utulivu huku akiyatafakari

    maelezo yake kabla ya kuvunja ukimya.

    “Okay! nashukuru sana kwa maelezo yako nadhani sina kingine cha kuuliza

    kwa sasa hata hivyo ningekuomba unipe ushirikiano wa kutosha kama nitakuhitaji

    tena” Sulle Kiganja akamshukuru Bi.Husna Mansour na kumuacha akaendelee na

    majukumu yake kisha akageuka na kumtazama yule mwanaume aliyesimama kando

    yake kabla ya kumuuliza.

    “Unaitwa nani?”

    “Paul Soko” yule mwanaume akajitambulisha huku akionekana kuzama katika

    kuangalia wale makachero wengine walivyokuwa wakichukua vipimo vya kitaalum

    kutoka kwenye ule mwili wa yule meneja wa benki kwenye kiti chake cha ofisini mle

    ndani.

    “Nadhani umeyasikia vizuri maelezo ya yule dada mfanyakazi wa hii benki

    aliyeondoka hapa sasa hivi!”

    “Ndiyo” yule mtu akaitikia huku akitikisa kichwa.

    “Maelezo yake yanaendana na huyo mwanamke uliyepishana naye wakati akitoka

    kwenye hii ofisi ya meneja?” Sulle Kiganja akauliza kwa utulivu huku akimtazama kwa

    makini yule mtu.

    “Yupo sahihi kabisa”

    “Wewe ni mfanyakazi wa hii benki?”

    “Hapana! mimi ni mteja tu na nilikuwa na shida yangu binafsi ya kuonana na

    meneja”

    “Wakati ulipopishana na huyo mwanamke muuaji mlizungumza kitu chochote?”

    “Aliniambia kuwa meneja alikuwa akizungumza na mtu mwingine humu ofisini

    hivyo nisubiri kwanza”

    “Ulifanya hivyo?”

    “Ndiyo,sikuingia badala yake nikaendelea kusubiri pale mlangoni kwa vile namimi

    nilikuwa na haraka” yule mtu akaongea huku akisikitika.

    “Baadaye ikawaje?” Sulle Kiganja akauliza huku akiuvuta mkono wa shati na

    kuitazama saa yake ya mkononi.

    “Niliendelea kusubiri pale mlangoni kwa muda mrefu baadaye nikahisi kukata

    tamaa baada ya kuona kuwa muda ulikuwa ukienda bila huyo mtu anayesemekana

    kuongea na meneja kutoka. Lakini vilevile nilipokumbuka kuwa yule dada aliyeondoka

    hapa alikuwa amenieleza kuwa kabla yangu kulikuwa na mtu mmoja tu aliyenitangulia

    kuingia humu ofisini kwa meneja ambaye ndiye yule dada niliyepishana naye mlangoni

    sikuona sababu ya kuendelea kusubiri zaidi hivyo nikausogelea mlango na kuufungua

    nikiingia humu ndani pasipo kugonga hodi ndiyo nikakuta haya mauaji” yule mtu

    akaweka kituo.

    “Kwa hiyo wewe ndiye mtu wa kwanza humu ndani kuyashuhudia haya mauaji?”

    Sulle Kiganja akamuuliza yule mtu huku akimtazama usoni.

    “Ndiyo na mimi ndiye niliyewajulisha wafanyakazi wa humu ndani juu ya haya

    mauaji”

    “Umewahi kumuona huyo dada kabla ya hapo?”

    “Sura yake ni ngeni kabisa machoni mwangu na sijawahi kumuona” yule mtu

    akaongea huku akitikisa kichwa kuonesha kukataa na hapo Sulle Kiganja akamtazama

    kwa makini kabla ya kumuuliza.

    “Una lolote jingine la ziada la kuniambia juu ya hili tukio la mauaji lililotokea”

    “Hapana”

    “Okay! vizuri na mimi nadhani sina swali jingine la kukuuliza kwa sasa nipe

    namba yako ya simu ili kama nitahitaji maelezo mengine ya ziada kutoka kwako

    uweze kunisaidia” Sulle Kiganja akahitimisha mahojiano huku akitoa kitabu kidogo

    na kalamu kutoka mfukoni na kuanza kuiandika namba ya simu aliyoanza kutajiwa na

    yule mtu na alipomaliza akafunika kile kitabu na kukitia mfukoni.

    “Nashukuru sana kwa ushirikiano wako nadhani unaweza kuondoka na kuendelea

    na shughuli zako” Sulle Kiganja akaongea huku akimpa mkono wa shukurani yule

    mtu.

    “Nashukuru na wewe kazi njema kwako”

    “Na wewe pia”

    Mara baada ya kuagana Sulle Kiganja akaendelea kusimama akimtazama yule

    mtu hadi pale alipofungua mlango wa ile ofisi na kutokomea ndipo akayarudisha

    macho yake mle ndani na kuwatazama vijana wake wa kazi namna walivyokuwa

    wakishughulika na majukumu yao. Wakati Sulle Kiganja akiendelea kuwasimamia

    vijana wake kuchukua taarifa mbalimbali za kiuchunguzi kuhusiana na lile tukio la

    mauaji ya meneja wa ile benki,vijana wake wengine wawili wa kazi Roby na Kaombwe

    wao walikuwa nje ya lile jengo la benki Zanzibar Marine ng’ambo ya barabara

    wakivuna taarifa zote muhimu kuhusiana na mshukiwa wa mauaji yale na waliporudi

    mle ndani walikuwa na jambo la kuzungumza.

    “Mmepata taarifa zozote mpya?” Sulle Kiganja akageuka na kuwauliza vijana wale

    baada ya kuingia mle ndani na kumkaribia pale aliposimama.

    “Mahojiano tuliyofanya na wahudumu wawili wa mgahawa wa Seafoods ng’ambo

    ya barabara yanashabihiana na yule dada tuliyemuona kupitia kamera za usalama za

    hili jengo” Roby akafafanua huku akimtazama Sulle Kiganja kwa utulivu.

    “Wanasema walimuona dada huyo wakati alipokuwa akiegesha gari lake kwenye

    sehemu ya maegesho ya mgahawa ule na kushuka akivuka barabara kuja kwenye hii

    benki na namna ya uvaaji wake ni vilevile kama tulivyoona kwenye kamera za humu

    ndani” Kaombwe akazidi kufafanua vizuri na Sulle Kiganja akawatazama vijana wake

    na kutabasamu.

    “Alikuwa akiendesha gari gani?”

    “Toyota corolla nyeupe yenye mstari wa njano ubavuni na kibandiko cha teksi juu

    yake” Roby akaongea huku akijaribu kukumbuka.

    “Namba za gari?” Sulle Kiganja akauliza. Kaombwe akachukua kitabu kidogo

    kutoka mfukoni mwake na kupekua haraka hadi kurasa fulani na kuweka kituo kisha

    akaanza kuzitaja namba za gari alizoambiwa na mhudumu mmoja wa ule mgahawa

    wa Seafoods ulioko ng’ambo ya barabara nje ya lile jengo la benki. Sulle Kiganja

    aliposogea karibu na kuzitazama zile namba haraka akazigundua kuwa zilifanana na

    zile alizopewa na Fulgency Kassy,Pweza na Kombe ikisemekana kuwa gari lenye

    namba zile ndiyo lililoonekana likitoweka kwa kasi muda mfupi baada ya mauaji ya

    P.J. Toddo kwenye sehemu ya maegesho ya magari ya jengo la Rupture & Capture

    lililokuwa likitazamana na jengo la Vampire Casino siku ile.

    Sulle Kiganja kuona vile haraka akawaita Fulgency Kassy,Pweza na Kombe

    waliokuwa bado wakiendelea na uchunguzi dhidi ya yale mauaji ya meneja wa benki

    mle ndani kisha haraka akawataka waingie mitaani na kuanza kulitafuta lile gari

    lililokuwa likitumiwa na muuaji huku akiwataka waanzie uchunguzi wao Mlimani City

    Shopping Mall kwenye duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar.

    Muda mfupi baada ya Fulgency Kassy,Pweza na Kombe kuondoka eneo lile zoezi

    la kuchukua vipimo vya uchunguzi dhidi ya yale mauaji ya meneja wa benki likawa

    limekamilika. Ule mwili ukaondolewa na kupelekwa hospitali ya taifa ya Muhimbili

    kuhifadhiwa hata hivyo Sulle Kiganja kabla ya kuondoka akautahadharisha ule

    uongozi wa ile benki kutokutoa taarifa zile kwa waandishi wa habari wala mtu yeyotemwingine kwa kigezo kuwa uchunguzi bado ulikuwa ukiendelea.



    AKIWA KWENYE FOLENI YA MAGARI umbali mfupi kabla ya kuyafikia

    makutano ya barabara eneo la Magomeni, Koplo Tsega kupitia vioo vya ubavuni vya

    gari lake akajikuta akishtushwa haraka na gari aina ya Landcruiser jeupe lililokuwa

    likijitahidi kupenya na kuyapita magari yaliyokuwa kwenye foleni ile nyuma yake

    kumkaribia. Aliposogea karibu na kioo cha ubavu wa gari lake na kutazama vizuri

    nyuma yake haraka machale yakamcheza baada ya kuliona gari lile Landcruiser jeupe

    lenye vioo vyeusi tinted namna lilivyokuwa likipenya na kuyapita magari mengine

    kumkaribia. Moyo ukamlipuka kwa hofu,nywele zikamcheza na jacho jembamba

    likaanza kumtoka. Haraka akaingiza gia kisha akaitoa gari yake kwenye mwambata

    wa foleni na kuingia kwa kazi upande wa kushoto kwenye barabara ya watembea kwa

    miguu na kumkosakosa muuza machungwa kabla ya kuligonga toroli lake na kulitupia

    mtaroni huku akiipuuza taharuki ya watu eneo lile.

    Yule dereva wa ile Landcruiser kuona vile naye akaingia upande wa kushoto

    akiifuata ile barabara ya watembea kwa miguu akilifukuza lile gari ya Koplo Tsega.

    Koplo Tsega akaendelea kuendesha gari kwa kasi akiwakwepa watembea kwa

    miguu kwenye barabara ile na haukupita muda mrefu mara mvua ya risasi ikaanza

    kumiminika kutoka kwenye ile Landcruiser. Koplo Tsega akaingiwa na hofu na

    kuanza kuliyumbisha lile gari lake huku na kule akiyakwepa mashambulizi yale.

    Mashambulizi ya risasi kutoka kwenye ile Landcruiser hatimaye yakaanza kuleta

    maafa. Kioo cha nyuma cha lile gari la Koplo Tsega kikachanguka na kusambaratika

    vibaya,taa za nyuma nazo zikapasuka na muda uleule sauti kali ya mpasuko wa

    magurudumu ikasikika. Gurudumu moja la nyuma na jingine la mbele yakapata

    dhoruba na kusababisha lile gari kuanza kuyumba ovyo. Hata hivyo Koplo Tsega

    alijitahidi kuudhibiti usukani wa lile gari kwa jitihada zake zote ingawa lile gari

    Landcruiser nyuma yake halikumpa nafasi ya kujitetea na baada ya muda likawa tayari

    limemfikia na kuanza kumgonga kwa nyuma.

    Wakati ule mtafaruku ukiendelea hatimaye wakajikuta tayari wameyafikia yale

    makutano ya barabara ya eneo la Magomeni. Ghafla Koplo Tsega alipotazama upande

    wa kulia wa ile barabara akaliona lori kubwa la mafuta kwa kasi likitokea maeneo ya

    Kigogo na kukatisha lile eneo la makutano ya barabara kuelekea eneo la Kinondoni.

    Yule dereva wa lile lori hakuonekana kufanya jitihada zozote za kupunguza mwendo

    kwa vile ilikuwa zamu ya foleni ya barabara ile kuruhusiwa. Kuona vile Koplo Tsega

    akakanyaga mafuta na kuongeza mwendo akiwahi kuyavuka makutano yale kabla

    ya lile lori halijamfikia akiifuata barabara ya Morogoro kuelekea Jangwani. Hata

    hivyo mahesabu yake yaligonga mwamba kwani wakati akikaribia kulivuka lile eneo

    la makutano ya barabara lile lori la mafuta tayari lilikuwa limekwishafika katikati ya

    makutano ya zile barabara. Kuona vile Koplo Tsega haraka akakanyaga breki lakini

    kutokana na ule mwendo kasi lile gari likaserereka na kusota huku magurudumu yake

    yakiumana vibaya na lami kulifuata lile tenki la mafuta la lile lori na kusababisha harufu

    kali ya mnuko wa magurudumu yale.

    Hofu ikiwa imeanza kumuingia juu ya kutokea kwa ajali mbaya ya kukatisha

    maisha yake Koplo Tsega haraka akafyatua kabari ya mlango na kujirusha kwa kasi

    akipotelea chini ya uvungu wa lile lori huku macho yake yakiwa makini kuyakwepa

    magurudumu makubwa ya lile lori. Abiria waliokuwa ndani ya daladala maeneo yale

    wakapiga mayowe ya hofu baada ya kuliona tukio lile la kutisha wakati yule dereva wa

    lile gari Landcruiser naye akiminya breki kwa nyuma. Lilikuwa tukio la kushangaza

    sana na kuogopesha.

    Wakati Koplo Tsega akitokezea upande wa pili wa uvungu wa lile lori muda uleule

    sauti kubwa ya mlipuko ikasikika kabla ya moto mkubwa kuzuka eneo lile na moshi

    mkubwa mweusi kutanda angani. Dereva wa lile lori la mafuta alikua amejitahidi

    kulikwepa lile gari la Koplo Tsega kwa kukanyaga breki ya ghafla huku lile gari la

    Koplo Tsega likiwa tayari limeshaingia kwenye uvungu wa lile lori. Tenki la mafuta la

    lile lori lilikuwa limeyumba na kupoteza uelekeo hali iliyopelekea lile lori kupinduka

    yale mafuta kumwagika na hatimaye kulipuka. Watu waliokuwa eneo lile ndani ya

    magari wakashuka na kuanza kutimua mbio kila mtu akishika uelekeo wake huku

    wakipiga mayowe na vilio vya hofu wakiukimbia ule moto.

    Koplo Tsega hakutaka kusubiri huku akiwaza kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi yake

    ya pekee ya kuwatoroka wale watu waliokuwa kwenye lile gari Landcruiser lililokuwa

    nyuma yake. Hivyo haraka akasimama na kuanza kutimua mbio akikatisha katikati ya

    barabara ya mabasi yaendayo mwendo kasi kuelekea posta.

    Fulgency Kassy,Pweza na Kombe baada ya kupata maelezo ya kutosha kutoka

    kwa yule kijana mfanyakazi wa duka la Zanzibar Stone City Bazaar kuwa yule dada

    aliyehusika na mauaji ya meneja wa benki alikuwa amefika pale na kumuulizia meneja

    wa duka lile wakawa wameingiwa na hisia kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa kuwa

    mara baada ya Koplo Tsega kumkosa meneja wa lile duka kwa vyovyote asingejipa

    subira badala yake angefunga safari na kuelekea kisiwani Zanzibar kumfuata yule

    meneja na tukio lile lingemaanisha kifo cha mtu mwingine muhimu katika mtandao

    wao. Hivyo haraka wakaondoa gari kwenye maegesho ya magari ya Mlimani City

    Shopping Mall na kuivuka barabara ya Sam Nujoma wakitokomea vichochoroni.

    Muda mfupi baadaye wakawa wametokezea barabara ya Shekilango ambapo mbele

    yake waliingia upande wa kushoto na kuifuata barabara ya Morogoro wakielekea eneo

    la forodhani bandarini kumuwahi Koplo Tsega kabla hajapanda boti na kuelekea

    kisiwani Zanzibar.

    Koplo Tsega aliendelea kutimua mbio akikatisha katikati ya uwazi uliofanywa

    baina ya barabara ya kwenda na ile ya kurudi katikati ya barabara ya mabasi yaendayo

    mwendo kasi huku watu wakiendelea kumshangaa hata hivyo hakusimama.

    Kumbukumbu ya kifo na mazishi yake katika makaburi ya Mwananyamala jiji Dar

    es Salaam ilikuwa ni historia inayomuwinda ambayo aliapa kuipigania hadi pale

    ambapo ushindi ungepatikana. Hakutaka kamwe Fulgency Kassy,Pweza na Kombe

    wafahamu kuwa bado alikuwa hai na siyo yule waliyemzika kule kwenye makaburi

    ya Mwananyamala kwani endapo wangegundua wangeweza kuzipeleka taarifa zake

    kwenye makao makuu ya jeshi la wananchi na hivyo kujikuta matatani zaidi kwa

    kufanya udanganyifu lakini vilevile kwa kuhusika na vifo vya maafisa kadhaa wa

    usalama ambao alikuwa akiendelea kuwaua jijini Dar es Salaam kama mkakati wake

    wa kulipiza kisasi kwa wale wote waliopanga njama na kuhusika na mpango mchafu

    wa vifo vyao nchini D.R Congo. Fulgency Kassy, Pweza na Kombe hawakuwa

    wamehadaika kirahisi kuwa yule mtu waliyekuwa wakimfukuza alikuwa amekufa

    kwenye lile gari Toyota corolla nyeupe baada ya lile gari kuingia chini ya uvungu wa

    lile lori la mafuta na ajali kubwa kutokea na hivyo kusababisha mlipuko mkubwa wa

    mafuta ya petroli kwenye makutano yale ya barabara zile. Hivyo haraka wakashuka

    kwenye ile Landcruiser nyeupe na bastola zao mikononi wakianza kutimua mbio

    kulizunguka lile lori na kutokea upande wa pili huku wakiamini kuwa yule mwanamke

    waliyekuwa wakimfukuza angeweza kuutumia mwanya ule kuwatoroka.

    Akiwa bado anatimua mbio Koplo Tsega akageuka tena na kutazama nyuma na

    hapo akaliona wingu zito la moshi wa mafuta ya lile lori ukisambaa hewani kwenye

    yale makutano ya zile barabara eneo la Magomeni kabla ya kuwaona wanaume watatu

    waliovaa suti nadhifu nyeusi na bastola zao mikononi wakitimua mbio kumfukuza

    nyuma yake. Hisia zikamueleza kuwa watu wale wangekuwa ni Fulgency Kassy,Pweza

    na Kombe na kwa vile alifahamu kuwa nafasi yeyote ambayo wangeipata wasingeacha

    kuitumia kumshindilia risasi haraka akaamua kuvuka ile barabara na kuhamia upande

    wa kushoto kisha akavizia daladala moja lililokuwa mbioni kumpita akakimbia

    na kudandia mlangoni. Utingo wa daladala lile alitaka kumzuia Koplo Tsega kwa

    vile watu walishaanza kuingiwa na mashaka naye tangu walipomuona madirishani

    akikimbia lakini Koplo Tsega aliwahi kuichomoa bastola yake na kuikamata mkononi

    tukio lililompelekea yule utingowa lile daladala ampishe kwa woga na kumruhusu

    aingie mle ndani.

    Mara tu Koplo Tsega alipoingia mle ndani haraka akawatahadharisha abiria wote

    waliokuwa mle ndani ya lile daladala kuwa wasithubutu kumtaja kuwa alikuwa mle

    ndani huku akitoa vitisho kuwa mtu yeyote ambaye angemtaja angekiona cha mtema

    kuni. Abiria wote ndani ya lile daladala wakawa wamenyamaza kimya na kumtazama

    kwa mashaka kama simba aliyeko usingizini. Koplo Tsega akajichomeka katikati ya

    abiria wengine waliosimama katikati ya daladala lile na kushika bomba la kuning’inizia

    mikono chini ya paa la daladala lile huku akigeuka na kutazama kule nyuma alipotoka

    kupitia kioo cha nyuma cha lile daladala.

    Lile daladala likiwa linaendelea na safari yake taratibu haukupita muda mrefu mara

    Koplo Tsega akawaona Fulgency Kassy,Pweza na Kombe wakikimbia kandokando

    ya ile barabara na bastola zao mikononi huku wakichunguza kwa makini sura za

    watu waliokuwa ndani ya magari yote yaliyokuwa yakiendelea na safari taratibu katika

    barabara ile. Koplo Tsega alipowaona Fulgency Kassy,Pweza na Kombe wakilikaribia

    lile daladala akazidi kujichomeka katikati ya kundi la abiria wale huku akiwatazama

    wale watu kwa makini. Jamaa walikuwa wakihema ovyo na kutokwa na jasho jingi

    huku sura zao zimefura kwa hasira kama mjeruhi wa mbogo.

    Fulgency Kassy,Pweza na Kombe walipolifikia lile daladala alilokuwamo Koplo

    Tsega wakasogea na kuanza kuchungulia dirishani huku lile daladala likiendelea na

    safari yake taratibu kutokana na foleni kubwa iliyokuwa eneo lile. Hata hivyo kwa

    kukosa umakini wakawa hawajamuona Koplo Tsega ndani ya lile daladala hivyo baada

    ya kuchoka kuchungulia madirishani wakaamua kuliacha lile daladala na kukimbia

    mbele zaidi kuyakagua magari mengine. Kuona vile Koplo Tsega akashusha pumzi

    taratibu na kuirudisha bastola yake mafichoni.

    Ile foleni ya magari ilikuwa imeanza kupungua baada ya magari ya barabara

    ile kuruhusiwa kule mbele hivyo lile daladala likawa limeanza kukoleza mwendo

    likimalizia kukatisha eneo lile la jangwani na wakati likiendelea na safari mbele kidogo

    Koplo Tsega akawaona Fulgency Kassy,Pweza na Kombe wakiwa wamesimama kwa

    uchovu,wakihema ovyo huku mikono yao viunoni wakionekana kukata tamaa na

    kuanza kushauriana jambo kabla ya kugeuka na kutazama kule nyuma walipotoka.

    Wakati lile daladala lililokuwa na Koplo Tsega likiwapita Koplo Tsega akageuka na

    kuwatazama kwa makini huku akijitahidi kuimeza hasira yake moyoni hadi lile daladala

    lilipotokomea mbali nao na ile ikawa nafuu kubwa kwa Koplo Tsega.

    Lile daladala kwa kuwa lilikuwa likielekea maeneo ya Kariakoo hivyo lilipofika tu

    maeneo ya Fire Koplo Tsega akasogea mlangoni na kuruka chini akiliacha lile daladala

    likiendelea na safari yake kisha akavuka barabara na kuita bodaboda moja iliyokuwa

    eneo lile. Ile bodaboda ilipokuja Koplo Tsega akapanda na kumtaka dereva wa

    bodaboda ile ampeleke forodhani bandarini kwenye ofisi za boti za kuelekea kisiwani

    Zanzibar.





    SAA KUMI NA MOJA JIONI BOTI aliyoipanda Koplo Tsega ilikuwa ikitoa

    nanga bandari ya Dar es Salaam na kuanza safari ya kuelekea kisiwani Zanzibar baada

    ya kuchelewa kidogo na kuikosa boti iliyotangulia ambayo aliamini kuwa ndani yake

    alikuwepo White Sugar. Mtu aliyekuwa akimtafuta kwa udi na uvumba. Wakati wote

    kabla ya safari kuanza Koplo Tsega alikuwa na wasiwasi mwingi wa kutarajia kuwaona

    Fulgency Kassy,Pweza na Kombe wakifika eneo lile lakini kitendo cha kutowaona

    kikawa kimemtia faraja na kurudisha matumaini makubwa moyoni mwake.

    Jua lilikuwa limeanza kuzama na hivyo ukungu mwepesi wa giza kuanza kutanda

    angani. Koplo Tsega akiwa sehemu ya juu kabisa ya ile boti akaendelea kutazama

    nyuma namna boti ile ilivyokuwa ikikata mawimbi taratibu kuiacha bandari salama

    huku taswira ya majengo mengi marefu ya ghorofa yaliyojazana eneo la posta yakianza

    taratibu kutoweka machoni mwake kadiri boti ile ilivyokuwa ikikata mawimbi na

    kutokomea mbali na eneo lile.

    Wakati Fulgency Kassy,Pweza na Kombe wakifika bandarini Koplo Tsega tayari

    alikuwa yuko mbali na bandari ile kwa muda wa nusu saa huku wasijue la kufanya.





    #321

    NILIMALIZA KUVUTA SIGARA YANGU ya mwisho kisha nikakitupa

    kipisi cha sigara ile kwenye kibakuli kidogo cha majivu ya sigara kilichokuwa

    juu ya stuli ndefu chakavu kando yangu huku nikihisi mapafu yangu kuwaka

    moto. Kwa muda wa masaa machache yaliyopita tayari nilikuwa nimeteketeza pakiti

    mbili za sigara zilizonifanya nianze kujihisi mgonjwa wa maradhi nisiyoyajua huku

    nikiwa nimeketi kwenye kochi moja kuukuu lililokuwa mle ndani wakati mawazo

    mengi yalipokuwa yakipita kichwani mwangu.

    Hiki kilikuwa chumba kidogo kati ya vyumba vingi vya jengo moja la ghorofa

    lililotelekezwa pasipo kumaliziwa baada ya mmiliki wake kujikuta katikati ya mgogoro

    mkubwa na maafisa wa ardhi kwa kujenga eneo lisilostahili kando ya eneo moja

    la ufukwe wa bahari ya Hindi. Jengo hili sasa lilikuwa likitumika kama maskani ya

    watoto machokoraa wa jiji la Dar es Salaam pamoja na vibaka na wakabaji. Nilikuwa

    nimeyagundua maficho haya huko siku za nyuma hivyo nikawa nimeamua kukarabati

    chumba kimoja na kukiwekea ulinzi mkali ambacho ningekitumia kama maficho

    wakati wa harakati zangu au sero ndogo ya kuwasweka washukiwa wangu kabla ya

    kuwatapisha taarifa muhimu ninazozihitaji.

    Baada ya yule mateka wangu niliyempata kutoka katika zile figisufigisu za kutekwa

    kwa Mwasu kule kwenye mnara wa Askari monument eneo la posta nilikuwa

    nimempeleka kwenye hospitali moja ya kichochoroni iliyopo eneo la Magomeni ili

    kupatiwa tiba dhidi ya yale majeraha yake ya risasi kabla ya kumchukua na kumfikisha

    kwenye maficho haya yenye chumba kimoja kidogo kisichopigwa plasta,choo kidogo

    cha ndani na dirisha dogo linalopitisha mwanga hafifu lisilomruhusu mtu kupenya.

    Mle ndani kukiwa na kitanda kidogo cha chuma cha futi sita kwa nne chenye godoro

    la sufi huku kando yake kukiwa na kochi moja kuukuu la sofa,stuli ndefu na kibakuli

    cha majivu juu yake.

    Mara baada ya kutupa kile kipisi cha sigara mkononi mwangu taratibu nikasimama

    kutoka kwenye lile kochi na kuvinyoosha viungo vyangu mwilini kabla ya kupiga

    mwayo hafifu wa uchovu huku nikianza kuzitupa hatua zangu tulivu na kusogea

    kwenye kile kitanda cha mle ndani nilipomlaza yule mateka wangu baada ya kumuona

    akijigeuzageuza pale kitandani kama aliyeshtuka kutoka usingizini. Vile vidonda vyake

    vya majeraha ya risasi begani na pajani vilikuwa vimesafishwa vizuri,zile risasi kwenye

    majeraha zilikuwa zimetolewa na yale majeraha kufungwa vizuri kwa pamba na

    bandeji safi. Sindano mbili za kupunguza maumivu alizodungwa bila shaka zilikuwa

    zimempelekea nafuu ya maumivu mwilini. Nilipotazama kando ya kile kitanda

    kwenye nguzo moja ya chandarua nikagundua kuwa hata ile dripu ndogo ya damu

    niliyomtundikia kwa msaada wa maelekezo ya yule daktari nayo ilikuwa mbioni kuisha

    na hali ile ikanipa matumaini kuwa afya yake ilikuwa mbioni kuimarika.

    Nilipofika pale kando ya kile kitanda nikasimama na kumtazama yule mateka

    wangu kwa makini. Alikuwa amefumbua macho yake na kunitazama kwa utulivu kama

    mtu anayenishangaa halafu akili yake ilipotulia nikamuona ameshikwa na mshtuko

    akajitahidi kunyanyuka pale kitandani hata hivyo hakuwa na nguvu za kufanya vile

    hivyo akarudi tena chini na kukiegemeza kichwa chake kwenye mto mmoja wa pale

    kitandani kwani afya yake bado ilikuwa dhaifu.

    “Unajisikiaje kwa sasa?” nikamuuliza yule mtu na hapo akasimamisha macho yake

    na kunitazama kama ambaye alikuwa akiendelea kukusanya kumbukumbu za kutosha

    kichwani mwake baadaye nikamuona akivunja.

    “Kichwa kinaniuma”

    “Chukua hivi vidonge umeze” nikamwambia yule mtu huku nikiingiza mkono

    mfukoni na kuchukua vidonge vya kutuliza maumivu nilivyopewa na yule daktari

    kule Magomeni kisha nikachukua chupa ndogo moja ya maji kutoka chini ya uvungu

    wa kile kitanda na kumpa. Yule mtu akavichukua vile vidonge na kuvitupia kinywani

    kisha akafungua ile chupa ya maji na kugida mafunda kadhaa kabla ya kuitua ile chupa

    kando yake pale kitandani alipolala ambapo niliichukua na kuiweka chini ya kitanda

    kisha nikasogea na kuketi kitandani karibu yake. Yule mtu akawa ni kama anayejisogeza

    mbali nami pale kitandani hata hivyo niliwahi kumshika miguu na kumzuia.

    “Ondoa shaka sina mpango wa kukudhuru” nikamwambia yule mtu huku

    taratibu nikimshika mkono wakati bado akiendelea kunishangaa kwani ni dhahiri

    hakuwa akifahamu kitu kilichokuwa kimemtokea hadi yeye kuwepo mle ndani katika

    mazingira tofauti kabisa na yale aliyoyazoea.

    “Wewe ni nani?” yule mtu akaniuliza kwa woga.

    “Chaz Siga,mtu mliyekuwa mkimtafuta wewe na wenzako” yule mtu kusikia

    vile akashtuka na kunitazama kwa mshangao sana. Hata hivyo niliupuuza mshtuko

    wake na kumuuliza wakati huo vitu vyake vyote muhimu kama simu,kadi ya benki na

    kitambulisho chake cha kazi kinachomtanabaisha kama afisa usalama kikiwa juu ya

    stuli mle ndani.

    “Unaitwa nani rafiki?”

    “Dan Maro’’ yule mtu akaniambia kwa utulivu baada ya kitambo kifupi cha kusita

    huku akinitazama.

    “CID Dan Maro wa idara ya usalama wa taifa…sivyo?’’ nikamuuliza kwa utulivu

    huku nikimtazama yule mtu. Jambo moja lililonitia matumaini ni kuwa kachero yule

    alikuwa hajanidanganya kwani vitambulisho vyake vyote vilikuwa na lile jina la Dan

    Maro alilojitambulisha nalo kwangu.

    “Unataka nini kwangu?” yule mtu akaniuliza kwa hofu.

    “Labda mimi ndiyo nikuulize swali hilo maana nilisikia kuwa wewe na wenzako

    mlifika kule ofisini kwangu kunitafuta. Sasa huoni kuwa huu ndiyo wasaha mzuri

    wa kuzungumza baada ya kuwa tumeonana?” nikaongea huku nikitabasamu na

    nilipomtazama yule kachero usoni akayakwepesha macho yake na kutazama pembeni

    na hapo nikajua ile hoja yangu ilikuwa imeziteka fikra zake.

    “Wenzako wamempeleka wapi katibu muhtasi wangu?” nikamuuliza pasipo

    mzaha.

    “Mimi nipo humu ndani nitafahamu vipi?”

    “Mbona tukio lenu la utekaji linaonekana kuwa ni jambo mlilokuwa mmelipangilia

    vizuri?”

    “Mimi sikuhusika kwenye utekaji” yule kachero akajitetea huku akitazama pembeni.

    Nikamtazama kwa makini kabla ya kumchapa ngumi mbili za uso zilizomsababishia

    maumivu makali pale kitandani.

    “Nahitaji ushirikiano wako vinginevyo sitokuwa na sababu ya kuendelea

    kukuuguza humu ndani” nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa makini yule

    kachero.

    “Ushirikiano upi ninaoweza kukupa nikiwa humu ndani tena katika hali hii?” yule

    kachero akajitetea huku akiugulia maumivu pale kitandani. Hasira zikiwa zimenishika

    kwa majibu yake yasiyo na tija nikamzaba kibao kimoja cha nguvu.

    “Nahitaji kufahamu ni wapi mlikompeleka katibu muhtasi wangu vinginevyo

    wenzako watakuokota ukiwa maiti” nikamfokea yule mtu kwa hasira huku sura yangu

    ikiwa mbali na mzaha hali iliyompelekea yule kachero aanze kutoa maelezo.

    “Tuna sehemu nyingi za kuwafanyia mahojiano washukiwa wetu na kwa kuwa

    mimi nipo humu ndani siwezi kuwa na hakika ni wapi alipopelekwa katibu muhtasi

    wako” yule kachero akaniambia na nilipomtazama usoni nikagundua hoja yake ilikuwa

    na ushawishi kidogo ingawa sikumwamini.

    “Katibu muhtasi wangu anashukiwa kwa kosa gani?”

    “Tulikuwa tumetumwa kukukamata wewe lakini baada ya kuambiwa na katibu

    muhtasi wako kuwa wewe haupo tukaona tumkamate yeye huku tukiwa na hakika

    kuwa baadaye angetusaidia kukupata wewe”

    “Mlitaka kunikamata kwa sababu gani?” nikamuuliza yule kachero na baada

    ya kitambo kifupi cha ukimya kupita mle ndani huku akionekana kufikiria jambo

    hatimaye akavunja ukimya.

    “Tulipewa amri hiyo na mkuu wetu ya kukukamata”

    “Bado hujajibu swali langu,nimekuuliza mlitaka kunikamata kwa sababu gani?”

    nikamuuliza yule kachero huku nikimtazama usoni.

    “Taarifa kutoka ofisi kuu zinakuelezea wewe kama ndiye mshukiwa namba

    moja wa mauaji ya makachero wa usalama yanayoendelea kufanyika hapa jijini Dar

    es Salaam” maelezo ya yule kachero yakanipelekea kwa sekunde kadhaa nibaki

    nikimkodolea macho huku nikishindwa kuyaelewa vizuri maelezo yake kabla ya

    kuvunja tena ukimya nikimuuliza.

    “Mna ushahidi wowote wa kunitia hatiani kuwa mimi ndiye ninayehusika na hayo

    mauaji ya wanausalama wenu?”

    “Mimi sifahamu” yule kachero akajitetea.

    “Sasa mnawezaje kutaka kunikamata wakati hamna hakika kuwa mimi ndiye

    ninayehusika?”

    “Sisi ni watu wa kutekeleza amri za wakubwa wetu ofini hivyo siyo jukumu letu

    kufahamu sababu ya amri husika inayotolewa”

    “Nani aliyewapa amri ya kunikamata?” hatimaye nikamuuliza yule kachero huku

    nikianza kupata picha kuwa ni kwa namna gani nilikuwa nikisakwa kwa udi na uvumba

    na makachero wale. Kisha wakati nikiendelea kufikiri fikra zangu zikahamia kwa

    yule mrembo aliyeniokoa chini ya lile jengo la ghorofa kule maeneo ya posta siku ile

    dhidi ya wale makachero waliotaka kunikamata. Kwa kuwa mauaji ya makachero hao

    sikuwa nimeyafanya mimi basi niliamini kuwa mshukiwa namba moja wa mauaji hayo

    bila shaka angeweza kuwa ni yule dada ingawa hadi wakati huu sikuweza kufahamu

    ni kwanini mlimbwende yule hatari alikuwa akiendesha kampeni ya kimyakimya ya

    kuwaua makachero wale. Hata hivyo kwa namna moja au nyingine nilikuwa nimeanza

    kuamini kuwa yule dada huwenda angekuwa askari jeshi tena mwenye mafunzo ya

    kijeshi ya hali ya juu ambayo yalikuwa yakimsaidia vyema kutekeleza mipango yake

    bila ya kukamatwa. Kwani vinginevyo kama angekuwa ni mtu wa kawaida mpaka sasa

    tayari angekuwa ameshakamatwa na wanausalama wale na kuswekwa ndani akisubiri

    hukumu ya kifo.

    “Sulle Kiganja” hatimaye yule kachero akatamka kwa kusitasita.

    “Sulle Kiganja ndiyo nani?” nikamuuliza yule kachero huku nikimtazama kwa

    makini.

    “Sulle Kiganja ni mkuu wa intelijensia ya ujasusi ya usalama wa taifa” jibu la yule

    kachero likanipelekea nishtuke kidogo na kumtazama huku kijasho chepesi kikianza

    kunitoka usoni. Sasa nilifahamu kuwa idara ya taifa ya kijasusi ilikuwa na taarifa zangu

    hivyo mpaka kufikia wakati ule niliamini kuwa makachero wa usalama wangekuwa

    tayari wametupa nyavu zao kila kona katika kuhakikisha kuwa wananinasa kabla

    sijafika mbali zaidi katika harakati zangu.

    Nikiwa bado nimeketi kando ya kile kitanda mawazo mengi yakawa yakiendelea

    kupita kichwani mwangu huku nikiwaza namna ya kujiepusha na hatari kubwa

    iliyokuwa mbele yangu pamoja na kumnasua Mwasu kutoka katika mikono ya

    makachero wale hatari. Baada ya kufikiri sana hatimaye nikawa nimepata wazo.Mara

    hii nikayapeleka tena macho yangu pale kitandani kumtazama yule kachero CID Dan

    Maro kabla ya kuvunja ukimya.

    “Nahitaji namba ya simu ya huyo mkuu wako aliyewatuma!”

    “Sulle Kiganja…?”

    “Labda kama kuna mwingine” nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule

    kachero ambaye sasa alikuwa chini ya himaya yangu ndani ya chumba kile cha siri

    chenye dirisha dogo la kupitisha mwanga hafifu. CID Dan Maro akanitazama kwa

    mashaka kama niliyekuwa nikiomba namba ya simu ya mkewe na nilipomuona akizidi

    kusitasita nikamzaba tena makofi mawili ya nguvu yaliyompelekea apige yowe kali la

    maumivu pale kitandani nami nikavunja ukimwa huku nikimtazama.

    ”Mimi siyo muuaji kama mkuu wenu anavyotaka kuwaaminisha. Nimelitumikia

    jeshi la wananchi wa Tanzania kwa muda wa miaka nane kama kamandoo wa daraja la

    kwanza mwenye mbinu zote za kijeshi katika mapambano ya kivita huku nikitekeleza

    vizuri wajibu wangu katika nchi kadhaa barani afrika zenye migogoro ya amani. Lakini

    pamoja na hayo yote siku moja nikajikuta nikipoteza kazi yangu na kutumikia kifungo

    cha jeshi chenye kazi ngumu na mateso makali kwa muda wa miaka minne kwa kosa

    la kutoa ripoti ya siri inayoeleza ni kwa namna gani baadhi ya viongozi wangu wa jeshi

    wanavyonufaika binafsi na migogoro hiyo. Ukweli wangu ukaniponza,nikadhulumiwa

    kazi na mafao yangu lakini nashukuru kuwa hawakuweza kunipokonya maarifa na

    ujuzi kichwani mwangu. Hivyo nikaamua kufungua ofisi inayoshughulika na upelelezi

    wa kujitegemea kama sehemu ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha na sasa sipo

    tayari kuiona idara yenu ya usalama ikinitumbukiza kwenye janga lingine ambalo kwa

    sasa limeanza kuutishia uhai wangu. Ninachohitaji kutoka kwako ni ushirikiano juu ya

    nini kinachoendelea vinginevyo wewe utakuwa ni mtu wa kwanza kufa humu ndani

    kabla ya wengine kufuatia” nikaweka kituo na kukohoa kidogo kisha nikageuka na

    kumtazama yule kachero kwa makini pale kitandani.

    “Nahitaji namba ya simu ya Sulle Kiganja” sauti yangu ilikuwa kavu na yenye

    hakika huku macho yangu yakiwa yameanza kupoteza utulivu. Yule kachero kuona

    vile taratibu akaanza kunitajia ile namba ya simu ya mkuu wa intelijensia ya ujasusi

    ya usalama wa taifa,Sulle Kiganja. Alipomaliza na mimi nikawa nimemaliza kuinakili

    vizuri namba ile ya simu kwenye simu yangu na muda uleule nikaipiga. Kitambo kifupi

    cha ukimya kikafuata kabla ya ile simu kuanza kuita jambo ambalo liliamsha upya hisia

    zangu na kunipa matumaini. Baada ya miito kadhaa hatimaye ile simu ikapokelewa

    upande wa pili na hapo sauti nzito,tulivu na yenye mamlaka ikasikika.

    “Haloo,nani mwenzangu?”

    “Chaz Siga bila shaka wewe ni Sulle Kiganja!” nikauliza kwa utulivu hata hivyo

    sikujibiwa mapema badala yake kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku nikisikia

    kelele hafifu upande wa pili wa ile simu na kutokana na uzoefu wangu nikajua kuwa

    Sulle Kiganja pamoja na watu wake walikuwa katika harakati za kuinasa sauti yangu

    kwenye vifaa vyao maalumu vya kijasusi jambo ambalo halikunipa wasiwasi wowote.

    Baada ya muda mfupi ile sauti ya Sulle Kiganja ikarudi tena hewani huku hisia zangu

    zikinieleza kuwa kando yake kulikuwa na watu wengine tayari kusikiliza maelezo

    yangu.

    “Safi sana Chaz Siga!,nilijua tu kuwa hatimaye utajitokeza mwenyewe na

    kunitafuta. Niambie unazungumza kutoka wapi rafiki yangu?” Sulle Kiganja akaongea

    kwa dhihaka na kuangua kicheko hafifu cha dharau.

    “Mwasu yuko wapi?”

    “Yuko sehemu salama kabisa,ondoa shaka”

    “Nahitaji kuongeanaye sasa hivi”

    “Amelala sehemu tulivu na daktari amesema kuwa hatakiwi kusumbuliwa” Sulle

    Kiganja akaongea kwa kujiamini.

    “Anaumwa nini hadi daktari ampumzishe?” nikauliza kwa hasira baada ya kuhisi

    kuwa Mwasu angekuwa ameteswa sana na kwa muda ule hali yake ilikuwa mbaya

    sana.

    “Uchovu wa kawaida tu” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu huku akiangua

    kicheko cha ushindi.

    “Najua kuwa umemtesa sana Mwasu hata hivyo nakushauri kuwa uachane na

    mpango huo kama bado unapenda kumuona afisa wako CID Dan Maro akiwa

    mzima” maelezo yangu yakapelekea kile kicheko cha Sulle Kiganja kutoweka haraka

    na sauti yake kuingiwa na utulivu.

    “Usijaribu kunitisha Chaz Siga badala yake nakushauri kuwa ujitokeze mwenyewe

    huko ulikojificha vinginevyo watu wangu watakukamata muda siyo mrefu”

    “Sikiliza vizuri na kwa makini Sulle Kiganja,pengine unaongea hivyo kwa sababu

    hujui unazungumza na mtu wa namna gani. Fahamu kuwa sijakupigia simu hii

    kukusalimia kama unavyoendelea kunipotezea muda wangu. Saa mbili usiku wa leo

    nitakupigia simu tena kuzungumza na Mwasu na kama sitoweza kuongeenaye afisa

    wako CID Dan Maro anafahamu vizuri nini nitakachomfanya na tusilaumiane”

    “Okay,okey…nimekuelewa. Sasa na mimi utanihakikishia vipi kuwa afisa wangu

    Dan Maro bado mzima?” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu huku ile hoja yangu

    ikionekana kumuingia vizuri na muda uleule nikageuka na kumchapa Dan Maro kofi

    moja la uso kisha nikamuwekea ile simu sikioni huku bado akilalamika kwa maumivu.

    “Dan…!” Sulle Kiganja nikamsikia akiita upande wa pili wa ile simu.

    “Ndiyo mimi mkuu…!” CID Dan Maro akaongea kwa taabu huku akilalama

    kwa maumivu makali ya kipigo changu hata hivyo niliwahi kuiondoa ile simu sikioni

    mwake na kuiweka sikioni.

    “Afisa wako Dan Maro anaendelea vizuri kama ulivyomsikia,naomba tuwasiliane

    saa mbili usiku bila chenga” nilimwambia Sulle Kiganja na kabla hajatia neno nikawahi

    kukata ile simu kisha nikaizima na kuitia mfukoni.



    #376

    MARA BAADA YA CHAZ SIGA kukata simu, sulle Kiganja akaipiga simu ile

    akirudiarudia mara tatu zaidi bila mafanikio mwishowe akakata tamaa kabisa baada

    ya kuhisi kuwa ile simu ya Chaz Siga ingekuwa imezimwa upande wa pili. Kisha

    taratibu akageuka na kuwatazama maafisa usalama wenzake waliokuwa wakiyafuatilia

    maongezi yale kwa makini wakiwemo Fulgency Kassy,Pweza na Kombe waliokuwa

    wamekuja kumletea ripoti juu ya kutoweka kwa yule dada aliyesemekana kuhusika na

    kifo cha meneja wa benki ya Zanzibar Marine ndugu Aden Mawala.

    “CID Dan Maro bado mzima na lazima tufanye namna ya kumuokoa” Sulle

    Kiganja akavunja ukimya huku akivigongesha vidole vyake mezani katika namna ya

    kufikiri zaidi na hatimaye akayatembeza tena macho yake kuwatazama wale maafisa

    usalama wengine mle ndani.

    “Ningeshauri tusubiri kwanza hadi hiyo saa mbili usiku Chaz Siga atakapokupigia

    simu na kuzungumza na wewe”.Tiblus Lupogo,mwanausalama kutoka kitengo

    maalum cha upelelezi cha ofisi ya mashtaka DPP akatoa ushauri.

    “Tunahitaji vijana wetu wataalam wa masuala ya mawasiliano watakaoweza

    kufuatilia na kujua huyu Chaz Siga alikuwa akizungumza kutoka eneo gani halafu

    baada ya hapo tutaanda mtego mzuri wa kumnasa” afisa usalama na mwanakamati

    ya kudumu ya ulinzi na usalama ya jijini Dar es Salaam,Siraju Chenga akashauri kwa

    utulivu huku ameyatuliza macho yake kufikiria jambo.

    “Mimi siamini kuwa muuaji mkubwa kama huyu Chaz Siga anaweza kukosa

    umakini kiasi cha kufanya mawasiliano yatakayopelekea kukamatwa kwake kirahisi

    namna hiyo. Ngoja tusubiri hadi hiyo saa mbili usiku tukiwa na vijana wetu wa

    mawasiliano na kama wataweza kutambua kuwa simu hii imepigwa kutokea wapi basi

    tutakuwa na nafasi nzuri ya kumnasa” mkuu wa kamati ya dharura ya usalama na itikadi

    za jeshi la wananchi Luteni Kanali Davis Mwamba akafafanua kabla ya wachangiaji

    wengine kuendelea huku kila mmoja akionekana kuridhishwa na mchakato mzima wa

    mikakati ya kumnasa Chaz Siga.

    Kwa kuwa ripoti kutoka kwa Fulgency Kassy,Pweza na Kombe ilikuwa imejaa

    viashiria vyote kuwa yule dada muuaji wa meneja wa benki ya Zanzibar Marine

    alikuwa ameelekea kisiwani Zanzibar hivyo Sulle Kiganja hakuona sababu ya

    kuendelea kupoteza muda badala yake akawataka Fulgency Kassy,Pweza na Kombe

    haraka waondoke usiku ule na kuelekea kisiwani Zanzibar na kuhakikisha yule dada

    anakamatwa kabla hajafika mbali.

    Mara baada ya Fulgency Kassy,Pweza na Kombe kuondoka mle ndani majadiliano

    ya kina yakaendelea zaidi baina ya wale makachero wa usalama katika mkutano ule

    mfupi wa dharura.

    “Uchunguzi nilioufanya kupitia vijana wangu umeanza kunipa uelekeo mzuri

    kuwa huyu Chaz Siga na huyu mwanamke anayesemekana kuhusika na kifo cha

    meneja wa benki ya Zanzibar Marine hawana mahusiano na pengine hawajuani kabisa.

    Lakini vilevile taarifa za uchaguzi kutoka kwa vijana wangu zinaonesha kuwa bastola

    iliyokuwa ikimilikiwa na meneja wa benki ya Zanzibar Marine haikuwa ikimilikiwa

    kihalali na mmiliki wake anaonekana kuwa ni raia wa kisiwani Zanzibar mwenye jina

    la Khalid Makame ingawa uchunguzi wa zaidi bado unaendelea” Sulle Kiganja akatoa

    ufafanuzi wa kina.

    “Mimi nina wazo jipya kidogo” Tiblus Lupogo akavunja tena ukimya na hapo

    wote wakageuka na kumtazama kwa shauku kabla ya kuendelea.

    “Kwa muda mrefu tangu kutokea kwa haya mauaji ya wanausalama wenzetu

    nimekuwa nikifanya uchunguzi na kugundua kuwa wanausalama wote hawa

    waliouwawa walikuwa katika tume ya udhibiti na upambanaji wa biashara haramu

    ya dawa za kulevya iliyoteuliwa na mheshimiwa rais hapa nchini. Sasa hamuoni kuwa

    huwenda hawa wanausalama wenzetu wanaweza kuwa wanauwawa kama sehemu ya

    kuwafumba midomo na kupoteza ushahidi juu ya kile wanachokifahamu kuhusiana

    na uchunguzi unaofanywa na tume yao?” hoja ya Tiblus Lupogo ikaonekana

    kuwaingia vizuri wale wanausalama na hivyo kuibua minong’ono mingi huku kila

    mmoja akizumza kwa mtazamo wake kuhusiana na hoja ile. Hatimaye Siraju Chenga

    akuvunja ukimya.

    “Nadhani hata mimi nimeanza kukubaliana na hoja hii lakini swali ni kwamba

    mnadhani ni nani anayeweza kuwa nyuma ya mpango huu wa kuwafumba midomo

    wanausalama wenzetu?”

    “Anayeweza kufanya hivyo ni dhahiri anapaswa kuwa ni mtu mwenye madaraka

    ya juu zaidi kama siyo wafanyabiashara wenye nguvu kubwa ya pesa” Tiblus Lupogo

    akafafanua.

    “Mimi ningependekeza kuwa mmiliki wa benki ya Zanzibar Marine naye

    achunguzwe” Sulle Kiganja akapendekeza huku akiwatazama wanausalama wenzake

    walioketi kwenye meza ya umbo duara yenye nane vilivyokaliwa na wanausalama wa

    idara tofauti.

    “Hilo nadhani halina mjadala na baada ya hapa nitatoa warrant ya kufanyika kwa

    uchunguzi dhidi ya benki ya Zanzibar Marine” M.D Kunzugala mkurungenzi mkuu

    wa idara ya usalama taifa akatanabaisha. Majadiliano machache yakaendelea kabla

    ya kikao kile cha dharura kufika ukomo na wanausalama wale kuaga na kuondoka

    wakikubaliana kukutana tena.

    Mara baada ya maafisa usalama wale kuondoka mle ofisini wakabaki M.D

    Kunzugala na Sulle Kiganja wakifanya majadiliano mengine ya kina zaidi kabla ya

    kufikia hitimisho huku wakiwa wamekubaliana kuweka mfumo wa siri wa mawasiliano

    kwa maafisa wote wa usalama waliokuwa kwenye kikao kile kama mkakati wa

    upelelezi katika kutaka kufahamu kama kungekuwa na kuvuja kwa taarifa. Hatimaye

    Sulle Kiganja na M.D Kunzugala wakaagana kila mmoja akishika majukumu yake.

    _____

    BOTI ALIYOIPANDA Koplo Tsega ilitia nanga kwenye bandari ya kisiwani

    Zanzibar huku tayari usiku ukiwa umeshaingia. Kama ilivyo miji mingine ya pwani hali

    ya hewa ya Zanzibar ilikuwa imetawaliwa na joto lenye upepo wa wastani. Mwanga

    kutoka kwenye meli kubwa za mizigo za safari za masafa marefu zilizotia nanga katika

    nanga bandarini pale kwa mbali mwanga wa taa kutoka katika majumba ya kale ya

    ghorofa yaliyopakana na ufukwe wa bahari ya Hindi ulipelekea ziada nyingine katika

    kuongeza uzuri wa mandhari ile.

    Safari haikuwa ndefu sana lakini haikuwa imemzuia Koplo Tsega kutongoa walau

    lepe moja la usingizi na sasa alikuwa ameshtuka kutoka usingizini baada ya sauti kali

    ya honi ya meli kusikika wakati boti ile ilipokuwa ikitia nanga bandarini. Koplo Tsega

    haraka akageuka na kuyatembeza macho yake kuwatazama abiria waliokuwa eneo

    lile na kitendo cha kumuona kila mtu akisimama na kuanza kuchukua mzigo wake

    ikawa ni ishara tosha kuwa safari ile ilikuwa imefika tamati. Hivyo haraka na yeye

    akachukua begi lake na kulivaa mgongoni kisha akasimama na kuunga msafara wa

    abiria waliokuwa wameanza kushuka kwenye boti ile huku mawazo juu ya yule mtu

    aliyekuwa akifahamika kama White Sugar yakianza kuumbika tena kichwani mwake.

    Akiwa anaendelea kushuka kwenye ile boti Koplo Tsega akajikuta akiwakumbuka

    Fulgency Kassy,Pweza na Kombe huku hisia za kuwa huwenda wangefanya maamuzi

    ya kuja kisiwani Zanzibar kumtafuta zikitengeneza ushawishi katika mawazo yake.

    Hata hivyo alijipa matumaini kuwa jina la Shamsa Hafidhi alilolitumia kuiabiri boti ile

    lisingekuwa na maana yoyote kwao hivyo akajipa moyo kuwa bado alikuwa salama.

    Mara tu Koplo Tsega alipomaliza kushuka na kutoka kwenye bandari ile ya

    Zanzibar akatembea kwa utulivu kuelekea kwenye maegesho ya teksi yaliyokuwa

    nje kidogo ya eneo lile. Kijana mmoja dereva wa teksi aliyekuwa amejitega kusubiri

    abiria akawa wa kwanza kumuona na kumkaribisha kwenye teksi yake kwa bashasha

    zote. Koplo Tsega akatabasamu kidogo na alipoifikia ile teksi kwenye maegesho yale

    akafungua mlango wa nyuma na kuingia huku akigeuka nyuma na kutazama kama

    kungekuwa na mtu yeyote akimfuatilia. Hakumuona mtu yeyote na hali ile ikampa

    faraja kuwa bado alikuwa salama. Yule dereva wa teksi alipofungua mlango na kuingia

    mle ndani akageuka na kumuuliza Koplo Tsega kwa utulivu.

    “Unaelekea wapi dada?”

    “Nipeleke eneo la Changa,unapajua?” Koplo Tsega akauliza huku kumbukumbu

    ya kisiwa cha Zanzibar ikiwa bado imehifadhika vyema kichwani mwake.

    “Ondoa shaka napafahamu vizuri sana Changa,ndiyo wewe unapoishi?” yule

    dereva akauliza huku akiitoa ile teksi kwenye maegesho yale hata hivyo Koplo Tsega

    hakumjibu badala yake akatumbukiza swali kwenye maongezi yale.

    “Utanitoza pesa kiasi gani?”

    “Utanipa elfu kumi na tano tu dada yangu,bei ya mafuta imeongezeka sana” yule

    dereva wa teksi akajitetea kabla hajaombwa kupunguza hali iliyompelekea Koplo

    Tsega ajikute akitabasamu.

    “Endesha gari” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu na hapo safari ikaanza huku

    ile teksi ikiacha maegesho yale na kushika uelekeo wa upande wa kulia kuifuata

    barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha kandokando ya bahari ile na hapo Koplo Tsega

    akajiegemeza taratibu kwenye siti ya nyuma ya ile teksi.

    Tangu utawala wa kwanza wa Sultan Majid bin Said hadi utawala wa mwisho wa

    Sultan Jamshid bin Abdallah kabla ya kupatikana kwa uhuru wa mtu mweusi kisiwa

    cha Zanzibar kimekuwa ni mji wa kale uliozungukwa na magofu ya zamani mazuri

    yaliyokuwa makazi ya watawala na walowezi kutoka uajemi.

    Muda huu wa usiku kandokando ya barabara ile kuelekea mji wa Stone Town

    wachuuzi wa samaki walikuwa wameweka meza zao na kuendelea kuuza bidhaa

    mbalimbali pamoja na samaki. Wenyeji kwa wageni watalii kutoka mataifa mbalimbali

    duniani walionekana kutembea kwa miguu na kufanya manunuzi katika mtindo wa

    maisha unaowafurahisha. Hoteli mbalimbali za kitalii zilionekana kupandwa katika

    baadhiya maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi na hivyo kuongeza uzuri wa mandhari

    ya usiku ya kisiwa kile.

    Baada ya safari ndefu kidogo hatimaye ile teksi ikaingia barabara ya Mizingani

    iliyokuwa ikipakana na ufukwe wa bahari ya Hindi upande wa kulia. Safari ikaendelea

    huku teksi ile ikilipita eneo la Old Customs House halafu mbele kidogo ikalipita eneo

    la Palace Museum. Hata hivyo kabla ya kulifikia eneo la Forodhani Garden dereva

    wa teksi ile akakunja kona kuingia upande wa kushoto akikatisha katikati ya barabara

    ya mtaa wa Nyumba ya Moto iliyokuwa ikipakana na magofu mengi ya kale. Safari

    ile ikaendelea hadi pale walipoifikia barabara ya Jamatin ambapo yule dereva aliingia

    upande wa kulia akiifuata barabara iliyokuwa ikitokezea kwenye Msikiti wa Jamat

    Khana. Dereva wa ile teksi alipoupita ule msikiti mbele kidogo akaingia upande wa

    kulia akiifuata barabara ya kuelekea Changa.

    “Nishushe hapo mbele ya huo mgahawa wa Café Laaziz” Koplo Tsega

    akamwambia yule dereva wa teksi baada ya kuuona mgahawa ule maarufu ambao

    mbele yake kulikuwa na meza nyingi zilizokuwa na vitafunwa vya kila aina kama

    chapati, vipande vya pweza, vitumbua, kalimati, kachori, kababu, kashata, maandazi,

    tambi, bagia na vingine vingi vyenye majina ya asili.

    Ile teksi iliposimama Koplo Tsega akafungua pochi na kumlipa yule dereva wa teksi

    pesa yake kisha akafyatua kabari ya mlango na kushuka akielekea kwenye ule mgahawa

    huku akifahamu fika kuwa macho ya yule dereva wa teksi yalikuwa yakimsindikiza

    nyuma yake. Akiwa mle ndani yule dereva wa teksi akaendelea kumtazama Koplo

    Tsega kwa utulivu hadi pale alipoingia kwenye ule mgahawa na hapo ndiyo akawasha

    gari na kugeuza akirudi kule kwenye kijiwe chake alipotoka.

    Lengo la Koplo Tsega likiwa ni kuondoa ushahidi juu ya wapi alipokuwa akielekea

    mara tu alipohakikisha kuwa ile teksi iliyombeba ilikuwa imegeuza na kuondoka nje

    ya ule mgahawa haraka na yeye akatoka nje ya ule mgahawa na kukodi bajaji moja kati

    ya bajaji nyingi zilizokuwa eneo lile akimtaka dereva ampeleke eneo la soko la zamani

    la watumwa ama Old Slave Market. Dereva wa bajaji ile kijana machachari akaanza

    safari haraka akiifuata barabara ya Mtaa wa Kajificheni iliyokuwa ikikatisha katikati ya

    makazi ya watu. Baada ya safari ndefu hatimaye dereva yule akakunja kona na kuingia

    upande wa kushoto akiifuata barabara ya New Mkunazini na baada ya kitambo kifupi

    cha safari ile bajaji hatimaye ikasimama eneo la Old Slave Market. Koplo Tsega

    haraka akamlipa yule dereva pesa yake na ile bajaji ilipogeuza na kurudi ilipotoka

    akaanza kutembea kwa miguu akielekea mbele ya ile barabara hadi pale alipoyafikia

    makutano ya barabara ya Benjamin Mkapa na barabara ya Karume. Alipofika pale

    akavuka makutano yale ya barabara na kukodi tena pikipiki ya Vespa akimtaka dereva

    ampeleke mahali lilipokuwa duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar. Dereva wa

    pikipiki ile alikuwa kijana wa mjini aliyeujua vizuri mji na vichochoro vyake hivyo

    haraka akashika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata barabara ya Benjamini Mkapa

    kisha akaipita shule ya Haile Selassie upande wa kulia hadi pale alipoyafikia makutano

    mengine ya barabara ya Benjamini Mkapa,barabara ya Mapinduzi na barabara ya

    Kawawa ambapo aliingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Kawawa.

    Safari ikaendelea huku ile pikipiki ikilipita eneo la The State University of Zanzibar

    kwa upande wa kulia na mbele kidogo akilipita jumba kubwa la Majestic Cinema. Hatua

    chache mara baada ya ile pikipiki kulipita lile jengo la Majestic Cinema yule dereva

    akaingia upande wa kulia eneo la Kibokoni ambapo alipofika mbele akashika uelekeo

    wa barabara ya Sokomuhogo na baada ya safari fupi hatimaye ile pikipiki ikaenda

    kusimama nje ya duka kubwa la kisasa lenye maandishi makubwa yanayosomeka juu

    yake Zanzibar Stone City Bazaar. Kuona vile Koplo Tsega akatabasamu kidogo kisha

    akushuka na kufungua pochi yake akitoa pesa na kumlipa yule dereva wa pikipiki.

    Yule dereva wa pikipiki akaipokea ile pesa na kuitia mfukoni kisha akawasha pikipiki

    yake na kutokomea mitaani.

    Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akasimama ng’ambo ya barabara ile

    akilichunguza kwa makini lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar huku akishangazwa

    sana na uwekezaji mkubwa wa biashara wa namna ile. Hapakuwa na shaka yeyote

    kuwa duka lile lilikuwa ndiyo duka kubwa na la kisasa katika eneo lote la Stone Town.

    Kupitia kuta safi za vioo za duka lile la kisasa bidhaa za kila namna zilionekana ndani

    yake.

    Nje ya jengo lile kwenye eneo la maegesho kulikuwa na magari machache

    yaliyoegeshwa labda kwa vile muda ulikuwa umeanza kuyoyoma kwani maduka

    mengi ya kisiwani Zanzibar yalikuwa tayari yamefungwa. Kadiri Koplo Tsega

    alivyokuwa akilitazama lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar ndivyo taswira ya

    yule mtu aliyekuwa akifahamika kama White Sugar ilivyokuw a ikijengeka upya katika

    fikra zake. Hatimaye akavuka barabara ile kuelekea upande wa pili na kisha kuanza

    kutembea akielekea kwenye mlango mkubwa wa lile duka la Zanzibar Stone City

    Bazaar na muda mfupi baadaye alikuwa mle ndani.

    Kama yalivyokuwa maduka mengi makubwa ya mijini ya kisasa duka la Zanzibar

    Stone City Bazaar halikuwa tofauti sana kwani mle ndani kulikuwa bidhaa za kila

    namna zilizopangwa vizuri katika maeneo tofauti kutegemeana na aina ya bidhaa

    yenyewe. Mle ndani kulikuwa na raia wengi wa kigeni waliofika kufanya manunuzi

    huku wakizunguka korido moja ya bidhaa kwenda nyingine na vitoroli vidogo vya

    kusukuma kwa mikono vyenye magurudumu madogo na vitenga cha kubebea bidhaa

    nyingi kwa pamoja.

    Upande wa kushoto wa lile duka kulikuwa na rafu nzuri za mbao zenye bidhaa

    zilizopangwa katika mtindo unaovutia. Mara baada ya kuingia mle ndani upande wa

    mbele kulikuwa na sehemu zenye mashine za kusoma thamani ya bidhaa kando yake

    wakiwa wameketi wafanyakazi wa duka lile. Upande wa kulia kulikuwa na maduka ya

    simu na vifaa vya umeme.

    Koplo Tsega taratibu akapiga hatua zake hafifu kuelekea kwenye yale maduka

    ya simu na wakati akifanya vile macho ya watu waliokuwa mle ndani yakamtazama

    kwa utulivu huku yakionekana kuvutiwa na namna ya uvaaji wake. Ndani ya duka la

    kwanza la simu aliketi msichana mweupe mlimbwende mwenye asili ya bara la Asia

    aliyevaa Baibui.

    “Habari za kazi?”

    “Salama karibu sana” yule dada akaongea kwa utulivu huku akimtazama

    KoploTiglis Tsega

    “Ahsante” Koplo Tsega akaitikia huku akijitia kutazama simu zilizokuwa

    zimepangwa katika rafu za vioo za lile duka na wakati akifanya vile pia akawa

    akiyachunguza vizuri mandhari ya mle ndani. Kutoka pale kwenye lile duka la simu

    za mkononi upande wa kushoto kulikuwa na ngazi za kuelekea sehemu ya juu ya

    lile jengo kulipokuwa na ofisi za utawala za lile duka. Hivyo kwa namna moja au

    nyingine Koplo Tsega alijikuta akiwaza kuwa White Sugar angeweza kuwa ndani ya

    ofisi mojawapo kati ya zile. Baada ya muda mfupi wateja wengine wakawa wameingia

    mle ndani na kufika pale kwenye duka la simu na hivyo kuongeza idadi ya watu eneo

    lile hali iliyompelekea Koplo Tsega kuweza kufanya uchunguzi wake kwa uhuru zaidi.

    Koplo Tsega akiwa bado anaendelea kununua muda pale kwenye lile duka la simu

    ghafla mlango mmoja kati ya milango mingi ya vyumba vya utawala vilivyokuwa juu

    ya lile jengo ukafunguliwa. Koplo Tsega haraka akageuka na kutazama kule juu. Mara

    baada ya mlango ule kufunguliwa wakatoka wanaume watatu wote wakiwa katika

    mavazi nadhifu ya suti na kuanza kutembea kwa haraka wakazifuata zile ngazi za

    kushukia sehemu ya chini ya lile duka katika korido pana iliyozuiliwa na ukuta mfupi

    wa mabomba ya vyuma.

    Mara moja moyo wa Koplo Tsega ukapoteza utulivu,damu ikamchemka

    mwilini,nywele zikamcheza na jasho jepesi likaanza kumtoka. Miongoni mwa wale

    wanaume watatu mmoja wao alikuwa ni yule aliyefahamika kwa jina la White Sugar

    ambaye Koplo Tsega alikuwa amemkumbuka vizuri kuwa ndiye yule aliyepishananaye

    mlangoni kule kwenye lile duka jingine la Zanzibar Stone City Bazaar lilioko Mlimani

    City Shopping Mall jijini Dar es Salaam. White Sugar alikuwa katika muonekano wake

    uleule wa awali pasipo kubadili mavazi. Upande wake wa kushoto na kulia kulikuwa

    na vijana wawili waliokuwa wakitembeanaye sambamba kama walinzi wake huku

    mmoja akiwa amebeba Briefcase nyeusi ambayo Koplo Tsega aliikumbuka vyema

    kuwa ilikuwa ni ileile aliyomuonanayo White Sugar kule jijini Dar es Salaam.

    Wakati White Sugar akishuka ngazi na wale wapambe wake kuelekea lile eneo

    la chini kwenye lile duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar njiani akapishana na

    wafanyakazi wawili wa lile duka wakiwa katika sare zao za kazi ambapo walimsalimia

    kwa heshima zote huku yeye akiitikia salamu zao kwa kupunga mkono kivivuvivu

    kama mtu asiye na muda. Koplo Tsega akaendelea kumtazama vizuri White Sugar na

    wapambe wake namna alivyokuwa akizishuka ngazi zile kwa madaha kama mfalme

    katika utukufu wake na kupitia mwanga mkali wa taa zilizokuwa ndani ya jengo lile

    Koplo Tsega akajiridhisha vizuri kuwa White Sugar alikuwa mwanaume mweusi sana

    kuwahi kuonekana duniani angawaje afya na rangi yake ya ngozi viliusanifu vizuri

    mwenekano wake wa hali ya ukwasi.

    Mara tu alipomaliza kushuka zile ngazi White Sugar na wapambe wake wakashika

    uelekeo wa upande wa kulia wakiufuata mlango mdogo uliokuwa kwenye kona moja

    ya lile jengo. Wafanyakazi wa lile duka kuona vile wakawa ni kama vile waliotekwa

    umakini huku wakijisogeza karibu na kumsalimia kwa bashasha zote za kirafiki ambapo

    aliwaitikia kwa kuwapungia mkono kivivuvivu kama kawaida yake kisha White Sugar

    akamuita mtu mmoja aliyekuwa eneo lile amevaa suti nyeusi na kumnong’oneza

    jambo. Yule mtu akawa ni kama anayepokea maelekezo fulani yaliyompelekea ageuke

    na kutazama kwenye lile duka la simu jambo ambalo Koplo Tsega hakulielewa maana

    yake.

    White Sugar alipoufikia ule mlango uliokuwa kwenye kona ya lile duka mpambe

    wake mmoja kati ya wale vijana wawili akawahi mbele na kuufungua ule mlango na

    hapo White Sugar akapita kisha wale vijana wapambe wakafuatia nyuma yake kabla

    ya mlango ule kufungwa. Koplo Tsega alipotazama juu ya ule mlango akaona kibao

    cha rangi nyeusi chenye maandishi makubwa meupe yakisomeka EXIT DOOR-For

    Administration use only.

    Kuona vile Koplo Tsega hakutaka kuendelea kusubiri hivyo taratibu akalitoroka

    lile kundi la watu waliokuwa wamesimama nje ya lile duka la simu na kushika uelekeo

    wa upande wa kushoto ulipokuwa mlango wa kutoka nje ya lile duka la Zanzibar Stone

    City Bazaar. Mara tu alipotoka kule nje akaambaa na ukuta akielekea kwenye kona lile

    jengo.Hata hivyo kabla hajafika mara akajikuta akisita na kujibanza baada ya kusikia

    muungurumo wa injini ya gari likiacha maegesho ya magari ya lile jengo. Haukupita

    muda mrefu mara gari kubwa aina ya Ford jeusi likayaacha maegesho yale na kuingia

    kwenye ile barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele ya lile jengo la Zanzibar Stone

    City Bazaar likishika uelekeo wa upande wa kushoto kuifuata barabara ya mtaa wa

    Sokomuhogo eneo la Kibokoni kuelekea kwenye ile kona ya Majestic Cinema.

    Lilikuwa tukio la kushtukiza ambalo Koplo Tsega hakuwa amelitarajia kwani White

    Sugar na wapambe wake walikuwa wakiondoka eneo lile na kuelekea kusikojulikana.

    Kuona vile Koplo Tsega akaiacha ile kona na kuanza kutafuta usafiri wa haraka eneo

    lile hata hivyo hakufanikiwa kwani lile eneo halikuwa na kituo cha usafiri wa namna

    yoyote hivyo akajikuta akianza kutimua mbio kulifukuza lile gari kwa nyuma kama

    mwehu na lile gari likaendelea kutimua mbio likitokomea. Koplo Tsega akaendea

    kukimbia akilifukuza lile gari lakini mwendo wake haukufua dafu kwani baada ya

    muda mfupi tu lile gari likawa limetokomea kabisa mbele yake na hivyo kwa mara

    nyingine White Sugar akawa ameponea kwenye tundu la sindano kitendo ambacho

    Koplo Tsega alikilaani sana.

    Hapakuwa na tumaini jingine la kumfikia White Sugar usiku ule hivyo Koplo

    Tsega akaamua kuchepuka na kuifuata barabara nyingine iliyokuwa upande wa kulia

    wa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa ya kale katika mtaa uliokuwa na

    utulivu na ukimya wa aina yake huku mawazo mengi yakipita kichwani mwake.

    Ile barabara ilikuwa tulivu mno na isiyokuwa na pilika zozote za binadamu

    huku ikiangazwa kwa taa hafifu kutoka katika nguzo za taa zilizokuwa kando yake.

    Wakati Koplo Tsega akiendelea kutembea katika barabara ile akajikuta akiyakumbuka

    matukio yote yaliyojili tangu siku ya kwanza alipoingia jijini Dar es Salaam akitokea

    eneo la Kivu ya kaskazini,jamhuri ya kidemokrasia ya nchi ya Kongo.

    Ilikuwa ni wakati alipokuwa mbioni kufika mwisho wa barabara ile ili aingie

    upande wa kushoto kwenye barabara nyingine pale alipokumbuka kutazama nyuma

    nyake. Kwa kufanya vile mara moja baridi nyepesi ya ghafla ikasambaa mgongoni

    mwake huku moyo wake ukipiga kite kwa nguvu.

    Kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakija kwa haraka nyuma yake kwenye

    barabara ile. Mwanaume mmoja alikuwa akitembea upande wa kushoto na mwingine

    akitembea upande wa kulia na mwendo wao wa haraka ulitia mashaka. Koplo Tsega

    kuona vile akaongeza mwendo huku akiendelea kugeuka nyuma na kuwatazama

    wale watu mara kwa mara huku hofu ikiwa imeanza kumuingia na alipoifikia ile kona

    ya barabara kuingia upande wa kushoto sehemu kulipokuwa na barabara nyingine

    iliyokuwa ikikatisha katikati ya majengo ya kale ya ghorofa makazi ya watu akaanza

    kutimua mbio. Koplo Tsega akaendelea kutimua mbio hadi pale alipofika mwisho wa

    ile barabara ambapo haraka akachepuka upande wa kulia na kwenda kujibanza kwenye

    kona moja ya jumba bovu la kale lililotelekezwa miaka mingi iliyopita ambalo sasa

    lilikuwa halitumiki kama makazi ya binadamu kisha akageuka nyuma na kuchungulia

    kule alipotoka.

    Koplo Tsega akiwa bado amejibanza kwenye ile kona haukupita muda mrefu

    mara akawaona wale wanaume wawili wakichomoza kwenye kona ya ile barabara na

    kuanza kutimua mbio wakija upande ule wa ile barabara kwenye ile kona ya jumba

    bovu alipokuwa bado amejibanza. Koplo Tsega alipowachunguza kwa makini wale

    watu akagundua kuwa walikuwa wameshika bastola mikononi mwao hali iliyopelekea

    hofu ya kukabiliana na hatari ianze kuchipua taratibu moyoni mwake. Wale watu

    wakaendelea kutimua mbio na walipofika pale kwenye ile kona wakapunguza mwendo

    na hatimaye kusimama huku wakishauriana kuwa washike uelekeo upi kwa vile ile

    barabara ilikuwa imegawanyika katika barabara kuu mbili. Barabara moja ikinyoosha

    mbele na nyingine ikiingia upande wa kulia mbele ya lile jumba bovu.

    “Atakuwa ameelekea wapi?” mmoja akasikika akimuuliza mwenzake kwa sauti ya

    chini.

    “Nahisi ni kwenye barabara hii hii kwani kama angekuwa amenyoosha kule mbele

    kwa vyovyote tungekuwa tumemuona tu” mwenzake akasikika akitengeneza hoja

    kisha kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku wale watu wakiwa bado wamesimama

    eneo lile kabla ya kushaurina jambo na kuanza kusogea taratibu kwenye kona ya lile

    jengo bovu la kale. Koplo Tsega kuona vile taratibu akaicha ile kona aliyojibanza na

    kuingia ndani kabisa ya lile jumba bovu huku akienda kujibanza kwenye kona moja

    iliyokuwa na giza zaidi.

    Haukupita muda mrefu mara wale watu nao wakaingia mle ndani ya lile jumba

    bovu huku wakinyata kwa tahadhari na bastola zao mikononi. Walipofika katikati

    ya lile jumba wakashauriana kitu kisha mmoja akaanza kupanda ngazi na kuelekea

    sehemu ya juu ya lile jengo kwa mwendo wa kunyata. Yule mtu mwingine aliyesalia

    pale chini akaanza taratibu kuzunguka kwenye kona za vyumba vya lile jengo

    lisilokuwa na madirisha wala milango. Kuona vile Koplo Tsega akaichomoa bastola

    yake yenye kiwambo maalum cha kuzuia sauti kutoka mafichoni na kuikamata vyema

    mkononi. Yule mtu aliyebaki chini ya lile jengo akavikagua vyumba vyote vya chini

    ya lile jengo na alipoona kuwa hakuna kitu cha maana akarudi mle ndani na kuanza

    kuzikagua kona za eneo lile.

    Koplo Tglis Tsega akiwa bado amajibanza gizani kwenye ile kona akamsubiri yule

    mtu amfikie usawa wake kisha akatupa pigo moja la kareti lililoipokonya mkononi

    bastola ya yule mtu na kuitupa kando. Yule mtu alipotaka kugeuka akajikuta akikabiliana

    na mapigo mengine mawili ya kareti shingoni mwake yaliyolipasua vibaya koo lake

    na kabla hajapiga mayowe ya kuomba msaada Koplo Tsega akawahi kumtundika

    kabari matata shingoni isiyoruhusu hewa kupenya. Yule mtu akafurukuta akitupa

    miguu yake huku na kule na kujitahidi kujinasua lakini ilishindika hivyo mwishowe

    akaishiwa pumzi na kutulia uhai ukiwa mbali na nafsi yake. Kuona vile Koplo Tsega

    akamburuta taratibu yule mtu hadi kwenye chumba kimoja cha lile jengo na kuanza

    kumpekua mifukoni. Hakupata kitu chochote na wakati akimalizia kumpekua mtu

    yule mifukoni mara akamsikia yule mwenzake akishuka zile ngazi za lile jengo bovu

    kuja kule chini hivyo haraka akachepuka na kwenda kujibanza nyuma ya zile ngazi.

    Yule mtu akawa ni kama aliyehisi jambo fulani kwani mara tu alipomaliza kushuka zile

    ngazi akasimama kwa utulivu na kuanza kumuita yule mwenzake kwa sauti ya chini

    “Tino…Tino…!” na yule mtu alipoona kuwa hakuna dalili zozote za kuitikiwa

    akawasha kurunzi yake na kuanza kumulikamulika mle ndani na kwa kufanya vile

    akawa ni kama aliyeziona zile alama za mburuto wa yule mwenzake aliyeuwawa hivyo

    haraka akaikamata vyema bastola yake mkononi na kuanza kuifuatilia ile alama ya

    mburuto kwa tahadhari. Koplo Tsega kuona vile haraka akatoka kwenye yale maficho

    na kumvamia yule mtu kwa nyuma hali iliyowapelekea wote kwa pamoja waanguke

    na kujibwa chini kama mizigo huku bastola zao zikiwaponyoka mikononi. Hata hivyo

    yule mtu aliwahi kusimama haraka na kurusha teke la nyuma lililomtandika vibaya

    Koplo Tsega kifuani na kumtupa tena chini. Pigo jingine la teke lilipomfikia Koplo

    Tsega akawahi kuinama kidogo na hivyo kulipelekea pigo lile likate upepo bila majibu

    kisha akaikita mikono yake chini kwa nyuma akijibetua vizuri na kusimama.

    Kuona vile yule mtu akaruka hewani na kutupa mapigo mawili mengine ya mateke.

    Pigo moja likamzaba Koplo Tsega kichwani na lile pigo la pili Koplo Tsega akawahi

    kulipangua kwa mikono yake miwili kisha akajitupa chini akijiviringisha na kumfuata

    yule mtu kwa kasi ya ajabu na aliponyanyuka akamchapa yule mtu ngumi mbili kavu

    za korodani,mapigo matatu makini ya kareti tumboni na kisha nyumi moja ya nguvu

    ya shingoni iliyompelekea yule mtu apige yowe kali la maumivu huku akipepesuka.

    Kisha Koplo Tsega akajirusha upande wa pili huku akitupa teke la nyuma lililojikita

    vizuri kwenye mgongo wa yule mtu na kumfanya agune kabla ya kuanguka chini. Hata

    hivyo Koplo Tsega akawahi haraka kumrudia yule mtu pale chini kabla hajasimama na

    hapo akaikamata miguu yake na kuanza kumburuta kwa kasi hadi kwenye nguzo moja

    iliyokuwa katikati ya lile jumba bovu ambapo aliigongesha vibaya pacha ya miguu ya

    yule mtu na kumsababishia maumivu makali ya korodani hali iliyompelekea yule mtu

    apige yowe kali la maumivu. Yule mtu alipotaka kufurukuta kajikuta akitazamana na

    mdomo wa bastola ya Koplo Tsega mkononi.

    “Wewe ni nani?”

    “Go to hell…!” yule mtu akajibu kwa jeuri huku akilalama kwa maumivu makali ya

    korodani zake na hapo Koplo Tsega akamshindilia ngumi moja kwenye mwamba wa

    pua yake iliyomsababishia maumivu makali yule mtu.

    “Nakuuliza,wewe ni nani?”

    “Farouk…!” yule mtu akalalama kwa maumivu makali

    “Mnataka nini kwangu?”

    “Tumetumwa tukufuatilie”

    “Nani aliyewatuma?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu huku akishtushwa na

    maelezo yale

    “Bosi wetu…”

    “Bosi wenu nani?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu kwa udadisi na alipomuona

    akisita kunyoosha maelezo akamzaba kofi la uso.

    “White Sugar…” jibu lile likampelekea Koplo Tsega kwa sekunde kadhaa ashikwe

    na mduwao huku akimtazama yule mtu kwa makini. Maelezo ya yule mtu yakawa

    yamempelekea amkumbuke White Sugar wakati alipokuwa akimnong’oneza mtu

    mmoja muda mfupi kabla ya kutoka na wapambe wake kwenye lile duka Zanzibar

    Stone City Bazaar muda mfupi uliopita.

    “White Sugar anaishi wapi hapa Zanzibar?”

    “Sifahamu” yule mtu akajitetea hata hivyo Koplo Tsega hakukubaliananaye

    hivyo akamzaba tena makofi mawili ya nguvu usoni yaliyompelekea yule mtu aanze

    kunyoosha vizuri maelezo yake.

    “Mimi sijawahi kufika nyumbani kwake ila niliwahi kusikia kuwa anaishi eneo

    linaloitwa Bumbwini karibu na Slave Chambers” yule mtu akafafanua na Koplo Tsega

    hakuona sababu ya kuendeleza tena mjadala ule hivyo akaielekeza bastola yake kwa

    yule mtu na kufyatua risasi mbili zilizomlaza yule mtu chali.



    #377

    SAA MBILI KAMILI USIKU ILIPOTIMIA ilinikuta nikiwa mwisho wa korido

    ya ghorofa ya nne ya jengo la Millenium Architectures eneo la Kigamboni jijini Dar es

    Salaam. Kisha nikaichukua simu yangu ya mkononi kutoka mfukoni na bila kupoteza

    muda nikaanza kupekuwa hadi pale nilipoifikia namba ya simu ya mkuu wa idara

    ya intelijensia ya kijasusi ya usalama wa taifa,Sulle Kiganja ambapo haraka nikaipiga

    namba ile na kuiweka simu sikioni.

    Mojawapo ya vitu nilivyokuwa na uaminifu navyo ni katika suala zima la kuzingatia

    muda. Ombi langu likionekana kuzingatiwa vizuri mwito mmoja tu simu yangu

    ikapokelewa upande wa pili na sauti ya mtu aliyepokea simu ile nikaikumbuka haraka

    kuwa ilikuwa ni ya Sulle Kiganja.

    Nikiwa na hakika kuwa mawasiliano ya simu yangu sasa yalikuwa yakichunguzwa

    na sauti yangu kunaswa na vifaa maalum vya kijasusi upande wa pili nikapanga

    kutokupoteza muda katika maongezi na hivyo kukimbilia kwenye hoja yangu ya

    msingi.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Haloo Chaz Siga habari za usiku?”

    “Mpe simu Mwasu nahitaji kuzungumzanaye sasa hivi”

    “Chaz nahitaji kwanza kuonana na wewe,niambie sehemu ulipo nitakuja sasa hivi”

    Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu.

    “Sitaki hadithi nimekwambia mpe simu Mwasu sasa hivi na kama haiwezekani

    nakata na usije kunilaumu” nikasisitiza

    “Unadhani unaweza kuikimbia serikali?” Sulle kiganja akaniuliza kwa dharau.

    “Ndani ya dakika kumi kuanzia sasa maiti ya afisa wako CID Dan Maro utaikuta

    kwenye buti ya gari Mark II pembeni ya njia panda ya Kawe. Usiku mwema…”

    nikaongea kwa hasira na kabla sijakata ile simu nikasikia.

    “Mwasu huyu hapa zungumza naye” kitambo kifupi cha ukimya kikapita baada ya

    sauti ya Sulle Kiganja kutoweka na hapo nikasikia sauti nyepesi ya kike ikiita upande

    wa pili wa simu ile.

    “Chaz…!”

    “Mwasu…!”

    “Bhee…!”

    “Mwasu unaendeleaje?” nikamuuliza Mwasu kwa shauku

    “Naendelea vizuri” Mwasu akanijibu hata hivyo nilipoitathmini vizuri sauti yake

    nikagundua kuwa ilikuwa tulivu kupita kiasi na kile alichokiongea kilipingana kabisa

    na hali yake.

    “Upo wapi Mwasu?”

    “Sipafahamu mahali hapa”

    “Kuna watu wangapi hapo ulipo?” nikamuuliza Mwasu kwa utulivu na baada ya

    kitambo kifupi cha ukimya nikamsikia akinijibu.

    “Tupo watu nane humu ndani”

    “Wamekutesa?”

    “Hapana” Mwasu akaitikia kinyonge hata hivyo niligundua haraka kuwa alikuwa

    akinidanganya kutokana na kushinikizwa kusema vile na watu waliomzunguka.

    “Pole sana Mwasu muda siyo mrefu tutakuwa pamoja”

    “Sitaki kufa Chaz nahitaji msaada wako” Mwasu akaongea kwa huzuni.

    “Ondoa shaka Mwasu muda siyo mrefu watakuachia kwani hauna makosa

    yoyote” nikaongea kwa utulivu nikijitahidi kumtia Mwasu moyo ingawa hadi kufikia

    muda ule sikuona dalili zozote za kuweza kumuokoa kutoka katika mikono ya watu

    wale na kabla Mwasu hajasema neno ile simu ikapokonywa haraka kutoka mikononi

    mwake na hapo sauti ya Sulle Kiganja ikarudi tena hewani.

    “Mwasu anaendelea vizuri kama ulivyomsikia”

    “Hakuna haja ya kunieleza nimekwishazungumza naye tayari” nikawahi

    kumkatisha Sulle Kiganja

    “Afisa wangu Dan Maro anaendeleaje?”

    “Amelala kwa sasa na daktari amesema asisumbuliwe” nikaongea kwa hila

    “Usithubutu kumdhuru vinginevyo urafikiwetu utakwisha” Sulle Kiganja

    akaongea kwa msisitizo

    “Mimi na wewe hatuna urafiki Sulle usijidanganye”

    “Unaweza kusema hivyo Chaz kwa vile unanichukia lakini mimi ni rafiki mwema

    kwako” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu akiununua muda hata hivyo nilikuwa na

    kila hakika kuwa vijana wake walikuwa kazini kuhakikisha wanainasa sauti yangu na

    kuchunguza kuwa nilikuwa eneo gani kwa wakati ule ili waweze kunikamata na hilo

    sikuwa na mashaka nalo kabisa. Nikiwa bado naendelea kufikiria mara sauti ya Sulle

    Kiganja ikarudi tena hewani.

    “Chaz…”

    “Zungumza”

    “Nimeona kuwa sihitaji kuendelea kumshikilia Mwasu hivyo kama utakubaliana

    na mimi tunaweza kubadilishana. Wewe ukamchukua Mwasu wako na mimi

    ukanikabidhi afisa wangu usalama,Dan Maro” nilimsikiliza vizuri Sulle Kiganja na

    kugundua kuwa lile lilikuwa ni wazo la hila lenye lengo la kuandaa mapango mzuri

    wa kunikamata. Hata hivyo niliishilia kutabasamu kwani sikuwa mbumbumbu kama

    vile alivyokuwa akinifikiria huku mpango mpya ukianza kujengeka kichwani mwangu.

    “Lini na wapi?” nikamuuliza

    “Eneo la Mnazi mmoja saa nne kesho asubuhi”

    “Saa sita mchana juu ya alama eneo la makutano ya barabara Uhuru Kariakoo”

    nikaongea kwa hakika

    “Mnazi mmoja ni sehemu nzuri isiyokuwa na msongamano…” Sulle Kiganja

    akatetea hoja yake ya hila

    “Nimesema saa sita mchana eneo la makutano ya barabara Uhuru Kariakoo nje ya

    duka la simu za mkononi la Al-Mustaphar bila hila yoyote” nikasisitiza

    “Okay!,okay!…usijali Chaz hakuna hila yoyote” hatimaye Sulle Kiganja

    akakubaliana na hoja yangu na kabla hajatia neno jingine nikawahi kuikata simu

    yangu na kuizima nikiitia mfukoni. Kisha nikaelekea mwisho wa korido ile na kuanza

    kushuka ngazi na muda mfupi baadaye nilikuwa mbali na jengo lile la ghorofa laMillenium Architectures Dar es Salaam.



    MARA BAADA YA CHAZ SIGA kukata simu Sulle kiganja akajizungusha

    taratibu kwenye kiti chake cha ofisini akibembea kwa utulivu kutoka upande mmoja

    na kwenda upande mwingine huku akiwatazama vijana wake wa kazi kwenye meza

    ile ya ofisini namna walivyokuwa makini kuinasa sauti ya Chaz Siga na kuchunguza

    kuwa muda ule mfupi alipokuwa akizungumza kwenye simu alikuwa eneo gani jijini

    Dar es Salaam.

    “Mmegundua nini?” Sulle Kiganja hatimaye akawauliza wale vijana huku wakiwa

    bado wameziinamia kompyuta zao maalum na vifaa vyao vya kunasa sauti vikiwa

    masikioni.

    “This guy is very clever” mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya ujasusi cha usalama

    wa taifa Micky Sengo akageuka taratibu kwenye kiti chake na kumtazama Sulle Kiganja

    huku akionesha kukata tamaa.

    “Nani?” Sulle Kiganja akauliza kwa shauku kabla ya kuwaamuru vijana wake

    wengine wamchukue Mwasu na kwenda kumfungia kwenye kile chumba mle ndani.

    “Chaz Siga”

    “Kwa vipi?” Sulle Kiganja akauliza.

    “Jana inaonekana alifanya mawasiliano na simu hii akiwa eneo fulani kando

    ya ufukwe wa bahari ya hindi kati ya Osterbay,Msasani au Mbezi beach na sasa

    inaonekana amepiga hii simu akiwa jengo la ghorofa la Millenium Architectures

    eneo la Kigamboni. Inaovyoonekana ni kama ameshtukia kuwa tunaanda mtego wa

    kumnasa hivyo anarukaruka kama ndama kutupotezea timing.

    “Ondoa shaka!,bado kuna njia nyingine ya kumnasa Chaz Siga” Sulle Kiganja

    akaongea kwa kujitapa.

    “Njia ipi?”

    “Kesho saa sita mchana makutano ya barabara ya uhuru kariakoo” maelezo ya

    Sulle Kiganja yakampeleka Micky Sengo amtazame kwa utulivu bila kusema neno

    kisha akawasha sigara na kuitia mdomoni.

    _____

    NIKIWA NDANI YA PANTONI wakati nikivuka bahari kutoka eneo la

    Kigamboni na kuelekea Posta usiku huu nikajikuta nikishawishika kuwasha simu na

    kutazama muda kwa vile saa yangu ya mkononi nilikuwa nimeisahau kule kwenye

    chumba changu cha siri nilipokuwa na mateka wangu kachero CID Dan Maro. Hata

    hivyo nikiwa katika harakati za kutazama muda baada ya ile simu yangu kuwaka mara

    nikaiona namba ya simu ya mzee James Risasi ikianza kuita. Mshtuko ukanipata

    kidogo kwa vile nilikuwa sijatarajia simu yoyote kutoka kwa mzee James Risasi

    hususani muda ule hata hivyo baada ya kuyatembeza macho yangu na kuridhishwa na sura za watu waliokuwa eneo lile na hapo nikaipokea ile simu.



    #379

    “Chaz…” sauti ya mzee James Risasi ikaunguruma upande wa pili.

    “Shikamoo mzee,habari za kazi?”

    “Naomba tuonane saa tatu usiku huu kwenye mgahawa wa Black Coffee eneo la

    Namanga”

    “Kuna shida gani mzee?” nikamuuliza kwa wasiwasi

    “Fanya haraka” mzee James Risasi akamaliza kuongea na kukata simu na kwa

    kweli alikuwa ameniacha njia panda huku nikishindwa kuelewa nini kilichokuwa

    kikiendelea nami nikaizima simu yangu na kuitia mfukoni.

    Muda mfupi baadaye lile Pantoni likatia nanga ukingoni upande wa pili wa Kivuko

    kile huku nikiwa wa kwanza kushuka baada ya kulipangua kundi kubwa la abiria

    waliokuwa wakijitahidi kushuka kwa pupa. Nilipofika nje ya kituo kile cha usafiri wa

    Pantoni kwenye barabara ya Kivukoni nikakodi teksi na kumtaka dereva anipeleke

    eneo la Namanga.

    Yule dereva wa teksi haraka akaingia barabarani akiifuata barabara ya Balack

    Obama Drive kandokando ya ufukwe wa bahari ya Hindi. Muda wa nusu saa baadaye

    teksi niliyoikodi ikasimama nje ya mgahawa wa Black Coffee eneo la Namanga kisha

    nikamlipa dereva pesa yake na ile teksi ilipoondoka nikavuka barabara nikielekea

    ndani ya ule mgahawa na wakati nikifanya vile nikayatembeza macho yangu eneo lile

    na kuiona gari nyeusi Toyota Prado ya mzee James Risasi ikiwa imeegeshwa katika

    maegesho ya magari ya mgahawa ule.

    Black Coffee ulikuwa mgahawa wa kisasa na wenye ubora stahiki. Ndani yake

    kukiwa na meza nzuri za umbo duara zilizozungukwa na viti imara vya mbao za mti wa

    Jakaranda,kuta zake zilipakwa rangi tulivu na safi zinazovutia. Madirisha yake mapana

    ya mbao na vioo yalifunikwa kwa mapazia mepesi marefu yenye rangi rafiki kwa

    macho ya binadamu. Kulikuwa na runinga mbili kubwa zilizofungwa mle ndani,moja

    upande wa kushoto na nyingine upande wa kulia huku harufu nzuri ya vitafunwa

    ikisambaa mle ndani. Wahudumu wake wasichana warembo walikuwa katika sare zao

    safi za kazi na sura za kupendeza. Sehemu ambayo mtu yeyote angeweza kukaa muda

    mrefu zaidi ya malengo aliyojiwekea. Mle ndani kulikuwa na watu wachache baadhi

    yao wakiwa ni wazungu waliokuwa wamezama kwenye kusoma English novels huku

    taratibu wakijipatia kahawa.

    Nilimkuta mzee James Risasi akiwa ameketi kwenye meza moja iliyokuwa kwenye

    kona ya upande wa kulia mle ndani ya mgahawa huku akijipatia kikombe cha kahawa

    chukuchuku bila kitafunwa. Uso wake haukuwa mchangamfu kama nilivyozoea

    kumuona hapo siku za nyuma. Alikuwa amevaa kofia nyeusi ya Pama,koti la suti refu

    jeusi la kijivu lililoishia magotini,shati jeupe na tai nyeusi huku miwani yake kubwa ya

    macho ikiwa imetuama vyema machoni mwake. Nilipofika kwenye ile meza nikavuta

    kiti na kukaa,mhudumu alipokuja nikaagiza kikombe cha maziwa moto.

    “Pole na kazi kijana wangu”

    “Ahsante!,pole na wewe mzee”

    “Nimesaliwa na mwaka mmoja tu wa kustaafu na sasa naona ni mbali sana

    nimechoka na hii kazi” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu huku akivuta funda

    la kahawa na sikutaka kuamini kuwa yale yangekuwa ndiyo maongezi aliyoniitia.

    “Ukistaafu utaelekea wapi?” nikamuuliza baada ya yule mhudumu kuniletea

    kikombe cha maziwa na kuvuta funda moja.

    “Kijijini kwangu Mwisenge,Musoma”

    “Umekuwa mzee sasa,unawajukuu wangapi sasa?”

    “Sina mke,mtoto wala mjukuu,nitajizika mwenyewe na pesa zangu za kiinua

    mgongo” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu na nilipomtazama usoni sikuona

    chembe ya mzaha na jambo lile likanisikitisha sana.

    “Pole sana!”

    “Nimeugua kisukari kwa muda wa miaka mingi sana tangu ujana wangu,kisukari

    sugu kikanipelekea nikose uwezo wa kuzalisha,wanawake wakawa wananikimbia

    baada ya kushindwa kuwatimizia mahitaji yao ya kimwili. Hivyo sikuona sababu ya

    kuoa na suala la watoto na wajukuu kwangu limekuwa ni ndoto ya mchana kweupe”

    mzee James Risasi akaongea kwa utulivu kisha akavuta funda moja la kahawa na

    kunitazama kwa makini kabla ya kuniuliza.

    “Umefikia wapi na kazi yangu?” swali la mzee James Risasi likanipelekea nianze

    kueleza kwa kifupi sana juu ya nilipofikia katika upelelezi wangu huku maeneo

    muhimu nikimuahidi kuwa angekutana nayo kwenye ripoti nzima baada ya kukamilika.

    Nilipomaliza kusimulia mzee James Risasi akavuta tena funda la kahawa na kuvunja

    ukimya.

    “Nataka kufahamu kama Mwasu amekamatwa akiwa na taarifa zozote zinazohusu

    huu mkasa wa Mifupa 206”

    “Ondoa shaka External hard disc yenye mafaili yote ya kiofisi ninayo mimi”

    “Nataka uwe makini kwani sasa hivi unatafutwa kila kona ya jiji la Dar es Salaam

    kwa gharama yeyote ile” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu huku akinitazama

    kwa makini na hapo nikavuta funda moja la maziwa na kuyatuliza vizuri macho yangu

    nikimtazama.

    “Ondoa shaka,hawawezi kunipata mpaka nitakapoikamilisha kazi yangu”

    “Utafanya nini kuhusu Mwasu?” mzee James Risasi akaniuliza kwa udadisi

    “Mpaka sasa bado sijafahamu nini cha kufanya ila kwa kuwa muda upo chochote

    kinaweza kutokea”

    “Taarifa nilizozisikia ofisini zinakutuhumu wewe kama muuaji wa maafisa

    usalama,Guzbert Kojo,Pierre Kwizera,P.J Toddo,Masam na Remmy”

    “Siwafahamu hao watu”

    “Una hakika?” mzee James Risasi akaniuliza akionekana kutaka kupata hakika ya

    jibu langu.

    “Sina sababu ya kuwaua na hadi sasa bado sijawathibitisha kuhusika na kile

    ninachokipeleleza”

    “Unadhani nani atakuwa anahusika na vifo vyao?” mzee James Risasi akaniuliza

    huku akiiondoa miwani yake machoni na kufikicha macho kabla ya kuirudishia.

    “Hiyo ni kazi nyingine yenye malipo yanayojitegemea” nikaongea kwa utulivu na

    kumpelekea mzee James Risasi atabasamu kidogo huku mawazo yangu yakihamia

    kwa yule mwanamke hatari aliyeniokoa mikononi mwa wale wanausalama chini ya lile

    jengo la ghorofa kule Posta. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku kila mmoja

    akionekana kushughulika na kinywaji chake kabla ya kukumbuka jambo na kumuuliza

    mzee James Risasi.

    “Sulle Kiganja anawadhifa gani katika ofisi yenu?”

    “Mkuu wa idara ya intelijensia ya ujasusi ya usalama wa taifa na kabla ya kupewa

    wadhifa huo cheo hicho kilikuwa chini ya Abdulkadir Badru” mzee James Risasi

    akafafanua na hapo nikamtazama kwa makini huku hoja mpya zikichipuka kichwani

    mwangu.

    “Kwanini Abdulkadir Badru aliondolewa kwenye wadhifa wake na kupewa huyo

    Sulle Kiganja?”

    “Baada ya kutokea kwa mauaji ya wanausalama hao unaoshukiwa kuwauwa kamati

    ikamtuhumu Abdulkadir Badru kuwa ni mzembe” mzee James Risasi akafafanua.

    “Sasa hivi Abdulkadir Badru ana wadhifa gani?”

    “Ni afisa usalama wa taifa wa kawaida kabisa asiyekuwa na kazi maalum”

    “Anaisha wapi hapa Dar es Salaam?” nikauliza kwa shauku huku nikimtazama

    mzee James Risasi kwa makini.

    “Block H,jengo la ghorofa la shirika la nyumba la taifa NHC,nyumba namba

    14,mtaa wa Lugalo eneo la Upanga. Abdulkadir Badru ni rafiki yangu wa siku nyingi

    kama una shida naye yoyote kupitia mimi hatoshindwa kukusaidia” jibu la mzee James

    Risasi likanipelekea niupishe utulivu tena kichwani mwangu.

    “Ukitoka hapa unaelekea wapi?” mzee James Risasi akaniuliza kwa utulivu baada

    ya kitambo kifupi cha ukimya.

    “Kanisa la The Last Day Gospel Ministry,nahitaji kuonana na Pastor Romanus

    ana taarifa muhimu juu ya huu upelelezi wa mkasa wa Mifupa 206”

    “Kuwa mwangalifu sana na nyendo zako huku ukitambua kuwa roho yako

    inawindwa”

    “Ondoa shaka”

    Maongezi ya hapa na pale yakafuatia hadi pale tulipoonekana kutosheka na

    vinywaji na hapo tukasogeza viti nyuma na kusimama kisha nikalipia vile vinywaji na

    kuongozana na mzee James Risasi tukielekea nje ya ule mgahawa. Mara tu tulipotoka

    nje ya ule mgahawa tukaagana huku tukikubaliana kuwasiliana tena katika kujulishana

    hali ya mambo itakavyokuwa inaendelea.

    Ilikuw a ni mara tu baada ya kuachana na mzee James Risasi nje ya mgahawa

    ule huku yeye akielekea sehemu alipoegesha gari lake na mimi nikitembea taratibu

    kuelekea kwenye kituo cha teksi kilichokuwa jirani na eneo lile pale nilipoliona gari

    moja aina ya Landcruiser jeupe likichomoza na kuja mbele yangu. Kuliona gari lile

    hisia mbaya zikaniingia akilini na nilipogeuka nyuma kumtazama mzee James Risasi

    nikamuona kuwa alikuwa amebakiwa na hatua chache kulifikia gari lake kwenye

    yale maegesho ya magari. Nilipoyarudisha macho yangu kulitazama lile gari jeupe

    Landcruiser lililokuwa likija mbele yangu likawa tayari limenifikia na hapo nikaona

    kioo kimoja cha dirisha la ubavuni kikishushwa haraka kisha ukachungulia mkono

    wa mtu ulioshika bastola. Sikutaka kusubiri zaidi hivyo nikawahi kujirusha na kujitupa

    mtaroni huku mvua ya risasi ikifuatia nyuma yangu. Hata hivyo mlengaji yule alikuwa

    amechelewa kwani mara tu nilipoingia kwenye ule mtaro wa kando ya ile barabara

    nikaingia chini ya daraja dogo la mfereji ule kujikinga na risasi zile. Ile Landcruiser

    haikusimama badala yake mara tu iliponipita kule mbele nikasikia milio miwili ya risasi

    na kisha nikaisikia injini ya ile gari ikiyoyoma na kutokomea zake.

    Niliendelea kujibanza ndani ya lile daraja dogo kwa dakika kadhaa nikijihakikishia

    usalama wangu kisha nikaichomoa bastola yangu kutoka mafichoni na kutoka sehemu

    ile nikielekea kwenye yale maegesho ya gari la mzee James Risasi. Wakati nikifika eneo

    lile moyo wangu ukaingiwa na baridi ya ghafla kabla ya simanzi kuziteka fikra zangu.

    Nilimkuta mzeeJames Risasi akiwa amelala chini kwenye maegesho yale hatua

    chache kabla ya kulifikia gari lake. Kifuani alikuwa na matundu mawili ya risasi

    yaliyokuwa yakivuja damu nyingi. Alikuwa ametulia kimya huku mdomo na macho

    yake vikiwa wazi kama mtu anayetazama mbingu ingawa nilipomsogelea na kumshika

    shingoni sikuona mjongeo wowote wa damu. Mwili wake ulikuw a ukipoa taratibu

    huku uhai ukiwa mbali na nafsi yake. Mzee James Risasi tayari alikuwa amekata

    roho. Niliendelea kumtazama mzee James Risasi huku machozi yakinilengalenga

    hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya. Nilipogeuka na kuyatembeza macho yangu

    eneo lile nikaona kuwa watu walishaanza kukusanyika hivyo sikutaka kupoteza muda

    badala yake haraka nikampekua mzee James Risasi mifukoni na kuchukua vitu vyote

    alivyokuwanavyo na hatimye kutoweka haraka eneo lile.





    #380

    MAONGEZI YA SIMU KATI YA mzee James Risasi na Chaz Siga yalikuwa

    yamenaswa vizuri na mkuu wa idara ya mawasiliano ya kijasusi ya usalama wa taifa

    Micky Sengo huku akishirikiana na vijana wake wa kazi baada ya namba za simu zote

    za wanausalama kuwa zimeunganishwa katika mfumo wa kitaalam unaomuwezesha

    opareta kuweza kusikia kila kitu pale namba ya simu ya afisa usalama mmoja

    inapopigiwa au kumpigia mtu mwingine.

    Taarifa zile zilipomfikia Sulle Kiganja haraka akawatuma vijana wake kuelekea

    eneo la Namanga sehemu kulipokuwa mgahawa wa Black Coffee huku kwa mara

    ya kwanza akijiridhisha kuwa mwanausalama mwenzao mzee James Risasi ndiye

    aliyekuwa akivujisha nje taarifa za kijasusi za idara ya usalama wa taifa. Lakini bado

    akishindwa kuelewa kuwa mzee James Risasi alikuwa na mahusiano gani na Chaz

    Siga,mtu hatari waliyekuwa wakimsaka kila kona kama shilingi ya mkoloni.

    _____

    MWILI WANGU ULIKUWA MLE NDANI lakini fikra zangu zilikuwa nje

    kabisa ya eneo lile kwenye ulimwengu wa sayari nyingine kabisa ya masafa marefu.

    Kifo cha mzee James Risasi kilikuwa kimenihuzunisha sana na kuacha kovu kubwa

    lisilofutika kamwe moyoni mwangu. Kila nilipotulia na kuupisha utulivu nafsini

    mwangu zile sauti za milio ya risasi zilizohitimisha safari ya uhai wa mzee James Risasi

    hapa duniani zikaendelea kuchukua nafasi kubwa katika mawazo yangu na kunipelekea

    niugue maradhi ya fedheha na unyonge kwenye mtima wangu. Ni dhahiri kuwa wauaji

    wale hawakuwa na sababu za kutosha za kuukatisha uhai wa mzee James Risasi ingawa

    kwa upande mwingine taratibu zake za kazi zingetosha kabisa kumshtaki kwa kitendo

    cha kuvujisha siri za usalama kwa mtu asiyehusika ambaye sikuwa na shaka yoyote

    kuwa mtu huyo ni mimi.

    Nikiwa bado nimezama kwenye fikra zile swali moja likaibuka katikati ya

    fikra zangu kuwa wale wauaji ambao sikuwa na shakanao kuwa walikuwa ni

    wanausalama,waliwezaje kufahamu kuwa mimi na mzee James Risasi tulikuwa

    ndani ya ule mgahawa wa Black Coffee kule Namanga?. Jibu sikulipata hata hivyo

    nilipozidi kufikiri wazo fulani likachipua kichwani mwangu na kunipa faraja kiasi cha

    kushawishika kuuchomoa mche mmoja wa sigara kutoka kwenye pakiti niliyoinunua

    kando ya duka moja lililokuwa karibu na kituo cha teksi kule Namanga na kuibana

    kwenye pembe moja ya mdomo wangu kabla ya kuilipua kwa kiberiti changu cha gesi

    huku taratibu nikijiegemeza kwenye siti moja ya nyuma ya ile teksi.

    Mwanga wa kile kiberiti ukawa umemshtua kidogo yule dereva wa teksi na

    kumpelekea ageuke haraka na kunitazama kupitia kwenye kioo cha mbele cha mle

    ndani kilichokuwa chini ya paa ya ile teksi. Hata hivyo dereva yule akaishilia kunitazama

    pasipo kusema chochote huku akigeuka na kuingiza gia kabla ya kukanyaga mafuta

    katika ile barabara ya Balack Obama Drive iliyokuwa ikikatisha kandokando ya

    ufukwe wa bahari ya Hindi,nikielekea eneo la Posta sehemu lilipokuwa kanisa la The

    Last Days Gospel Ministry. Nilikuwa nimekodi teksi ile muda mfupi baada ya lile

    tukio la kuuwawa kwa mzee James Risasi kule eneo Namanga nje ya mgahawa wa

    Black Coffee.

    Wazo moja lilikuwa limenijia akilini. Miongoni mwa vitu nilivyokuwa nimevipata

    muda ule baada ya kumaliza kuipekua maiti ya mzee James Risasi mifukoni ilikuwa ni

    simu yake ya mkononi,kitambulisho cha kazi,kadi mbli za ATM za benki tofauti na

    bastola moja ndogo iliyojazwa risasi. Hivyo haraka nikaichukua ile simu ya mzee James

    Risasi na kuanza kuichunguza kwa makini. Sikuona chochote hadi pale nilipouondoa

    mfuniko wa betri ya simu ile na kuuchunguza ndani yake.

    Kidude kidogo mfano wa kifungo chembamba sana cheusi. Kinasa sauti

    kinachoweza kusafirisha mawimbi ya sauti kwa umbali wa maelfu ya maili nyingi

    kilikuwa kimepandikizwa kwa hila katika mfuniko wa betri wa simu ile ili kunasa

    maongezi ya namna yoyote ambayo simu ile ingetumika kuyafanya. Sasa nilikuwa na

    hakika kuwa wakati ule mzee James Risasi alipokuwa akinipigia simu nikiwa kwenye

    Pantoni kutokea jengo la ghorofa la Millenium Architectures eneo la Kigamboni

    nilipoenda kuwasiliana na Sulle Kiganja kwa simu kama mkakati wangu wa kumzuia

    kutekeleza mipango yake ya kunikamata kwa urahisi basi maongezi yetu yalikuwa

    yakisikika moja kwa moja na watu wale hatari. Hali iliyowapelekea waweze kufahamu

    kwa urahisi mahali tulipokuwa na hatimaye kutufikia.

    Bila kusita nikawa nimeiwasha ile simu na ilipowaka mara nikaiona ikianza kuita

    na nilipochunguza kwa makini kuwa mpigaji wa simu ile angekuwa nani nikaliona jina

    la Sulle Kiganja. Pasipo kujiuliza nikaipokea ile simu na kuiweka sikioni bila kusema

    neno lolote na kwa kufanya vile nikaisikia sauti ya Sulle Kiganja ikianza kuita upande

    wa pili. Sikuwa na neno lolote la kuzungumza badala yake nikajikuta nikimlaani Sulle

    Kiganja moyoni mwangu kwa kufanya kitendo cha kihuni cha namna ile cha kumpigia

    simu marehemu. Hatimaye nikaikata ile simu na kuizima kisha nikaitia mfukoni.

    Muda mfupi baadaye ile teksi ikasimama barabara ya mtaa wa pili nyuma ya ule

    mtaa wenye lile kanisa la The Last Days Gospel Ministry huku lengo langu likiwa ni

    kuhakikisha hali ya usalama wangu kwanza kabla ya kulifikia kanisa lile. Nikamlipa

    dereva wa ile teksi pesa yake na kushuka. Ile teksi ilipoondoka tu eneo lile nikavuka

    barabara na kuanza kutembea taratibu na kwa tahadhari kuelekea nyuma ya mtaa ule

    huku mkono wangu ukiwa ndani ya mfuko wa koti langu umeikamata bastola tayari

    kwa kumdhibiti mtu yeyote ambaye angejitokeza mbele yangu na kuniwekea kizingiti.

    Sikupata upinzani wa namna yoyote na baada ya safari ndefu kidogo ya miguu

    hatimaye nikapita getini na kuufikia mlango wa mbele wa kanisa la The Last Days

    Gospel Ministry na hatimaye kuusukuma. Mara tu nilipoingia mle ndani nikagundua

    kuwa lile kanisa lilikuwa limemezwa na ukimya wa aina yake. Mapazia meupe marefu

    na mepesi yalikuwa yakipepea taratibu kufuatia upepo mwanana wa usiku uliokuwa

    ukipenya kupitia kwenye madirisha makubwa ya kanisa lile.

    Mle ndani mbele ya kanisa sehemu ya madhabahu kulikuwa na mishumaa

    mikubwa mitatu iliyokuwa juu ya meza moja ndefu yenye umbo mstatili iliyofunikwa

    kwa kitambaa cheupe chenye msalaba mkubwa mwekundu uliyodariziwa kwa ustadi.

    Mishumaa ile ikiteketea taratibu na kuangaza mle ndani. Nikapiga hatua chache

    na kusimama katikati ya kanisa lile huku nikiyatembeza macho yangu mle ndani.

    Sikumuona mtu yeyote na jambo lile likanipa wasiwasi na kujiuliza kama muda ule

    Pastor Romanus angekuwa ndani ya lile kanisa au lah!.

    Hata hivyo sikukata tamaa badala yake nikazidi kujongea taratibu nikielekea

    sehemu ya mbele ya lile kanisa na kwa kufanya vile nikagundua kuwa nyuma ya

    ile meza ya madhabahu mbele ya kanisa lile kulikuwa na mtu aliyeketi kwenye kiti

    huku akiwa katika mavazi ya utukufu kama yale niliyokuwa nimemuona nayo Pastor

    Romanus siku ile nilipofika mle ndani kwa mara ya kwanza japokuwa sikuweza kuiona

    vizuri sura ya mtu yule kwa vile alivyokuwa ameketi kwa utulivu na kuiinamia meza ile

    akionekana kusoma maelezo kwenye kitabu fulani. Hata hivyo kitendo cha yule mtu

    kuinua macho yake na kunitazama haraka na kisha kuendelea kusoma kile kitabu pale

    mezani pasipo kunikaribisha wala kutia neno lolote kikawa kimenishangaza sana huku

    nikijipa moyo kuwa huenda Pastor Romanus alikuwa tayari amenisahau.

    Nilitaka kusogea karibu zaidi ya ile meza ya pale madhabahuni mle ndani kanisani

    ili niweze kumsalimia kwa karibu zaidi yule mtu aliyeketi kwenye kile kiti huku

    nikiamini kuwa angekuwa ndiye Pastor Romanus na hivyo salamu yangu ya karibu

    ingempelekea anitazame vizuri na kunikumbuka. Hata hivyo hilo halikutokea kwani

    wakati nilipokuwa nikikaribia ile meza haraka nikagundua kuwa yule mtu aliyeketi

    kwenye kile kiti nyuma ya meza ile hakuwa mzee kama alivyokuwa Pastor Romanus

    ingawa pia alikuwa amevaa vizuri yale mavazi ya utukufu.

    Kile kitabu alichokuwa akikisoma yule mtu pale mezani nikakitambua haraka

    kuwa ilikuwa ni Biblia ingawa nilipoichunguza kwa makini ile Biblia haraka nikashtuka

    baada ya kuuona mdomo wa bastola ukichungulia chini yake. Yule mtu hakuinua tena

    macho yake kunitazama badala yake akawa amezama katika kusoma maelezo fulani

    yaliyokuwa kwenye kurasa ile.

    Wasiwasi ukiwa tayari umeanza kuniingia haraka nikayapeleka macho yangu na

    kuyatembeza jirani na eneo lile na kwa kufanya vile mara nikaiona michirizi ya damu

    nyingi ya kitu kilichoburutwa na kupelekwa kwenye uchochoro mmoja uliokuwa

    upande wa kushoto wa ile madhabahu. Nywele zikanicheza,moyo wangu ukapiga kite

    kwa nguvu,koo likanikauka ghafla na hapo utulivu ukahama kabisa kichwani mwangu.

    Hatimaye uvumilivu ukanishinda hivyo haraka nikaupeleka mkono wangu mafichoni

    kuichukua bastola. Lakini tayari nilikuwa nimechelewa kwani muda uleule nikasikia

    sauti ya kiume ikinionya nyuma yangu huku mdomo baridi wa bastola ukikitekenya

    kisogo changu.

    “Tupa bastola yako chini Chaz Siga na usithubutu kufanya hila yoyote”

    Kwa kweli nilijihisi kuchanganyikiwa nikataka kugeuka nyuma na kumtazama yule

    mtu kuwa angekuwa nani. Lakini wakati nikiwa katika harakati zile mara nikajikuta

    nikikatizwa na yule mtu aliyekuwa ameketi nyuma ya ile meza pale madhabahuni kwa

    namna alivyoupenyeza mkono wake haraka chini ya ile Biblia na kuichomoa bastola

    yake mafichoni. Kisha akaikamata vyema bastola ile mkononi kabla ya kusimama kwa

    utulivu huku akiielekezea kifuani kwangu.

    Muda uleule wakachomoza watu wengine wawili kutoka kwenye vichochoro

    vilivyokuwa upande wa kulia na kushoto wa lile kanisa pale madhabahuni kutokea

    kwenye vyumba vya maandalizi ya neno huku wakiwa na bastola zao mkononi katika

    mavazi nadhifu ya suti. Nilipogeuka kutazama nyuma yangu nikamuona mwanaume

    mmoja makini aliyeikamata vyema bastola yake mkononi na kuielekeza kwangu na

    nilipotazama kule kwenye mlango wa kanisa nikawaona wanaume wengine wawili

    wakiwa wamesimama mlangoni. Nilijua kuwa nisingeweza kufurukuta tena dhidi

    ya watu wale hatari waliojidhatiti kikamilifu hivyo baridi nyepesi ya hofu ikapenya

    taratibu moyoni mwangu na kunipelekea nijione mzembe kwa kutokuwa makini.

    “Nahitaji kuonana na Pastor Romanus tafadhali!” nikajiongelesha kwa sauti huku

    nikihisi kuchanganyikiwa.

    “Nani aliyekwambia kuwa huu ni muda wa ibada?” yule mtu mbele yangu

    akaniuliza swali la kipuuzi lililowapelekea wale wenzake waangue kicheko cha mahoka

    mle ndani. Sikuwa na namna nyingine ya kufanya hivyo nikaitoa bastola yangu taratibu

    na kuiweka chini sakafuni.

    “Pastor Romanus yuko wapi?” nikauliza huku nikijidai sielewi mada

    “Rafiki yako amekufa” yule mtu mbele yagu akaongea kwa utulivu kisha akasogea

    pale niliposimama na kunichapa ngumi mbili za tumbo zilizonipelekea nihisi kutaka

    kutapika.

    “Mmemuua Pastor Romanus…?” nikauliza kwa hasira huku nikiugulia maumivu

    ya tumbo.

    “Haikuwa kazi rahisi hata hivyo tulilazimika kufanya hivyo” yule mtu akajitapa

    “You bastard you killed God’s servant…?” nikauliza kwa mshangao na hapo nikajikuta

    nikitandikwa ngumi nyingine mbili kavu za mgongoni zilizonipelekea nianze kuhisi

    kichomi.

    “Chaz Siga!...umetusumbua kwa muda mrefu lakini hatimaye tumekutia mikononi.

    Usijaribu kuleta hila za kutoroka kwani bahati huwa haijitokezi mara mbili na mimi

    nitakuwa mtu wa kwanza kukushindilia risasi za kutosha ukafie mbali” yule mtu

    akajitapa huku akinizunguka taratibu na kunitazama kwa dhihaka.

    “Mnashida gani na mimi?” nikawauliza wale watu na nilipowatazama vizuri

    nikajiridhisha kuwa sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu ingawa

    nilifahamu fika kuwa wale wangekuwa makachero waliotumwa na Sulle Kiganja

    kunikamata.

    “Hatuna muda mrefu wa majadiliano na wewe. Tuambie, CID Dan Maro yuko

    wapi?” yule mtu aliyekuwa akinizunguka akaniuliza huku akinipekua mifukoni. Hata

    hivyo hakuambulia kitu chochote kwa vile vitu vyagu nilikuwa nimeviweka mafichoni

    kwenye mfuko wa siri wa lile koti sehemu isiyofikika kirahisi na mtu asiye makini.

    “Kachero wenu CID Dan Maro yupo sehemu salama kabisa ondoeni shaka”

    nikaongea kwa utulivu.

    “Sehemu salama wapi?” yule mtu aliyekuwa akinipekua akaniuliza hata hivyo

    nikalipuuza swali lake na kutumbukiza langu.

    “Kwanini mmemuua Pastor Romanus kama kweli shida yenu hasa ilikuwa ni

    mimi?”

    “Alijitia mkaidi vinginevyo tusingekuwa na bahari naye” yule mtu akanijibu na

    baada ya kukohoa kidogo akaendelea.

    “Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani tumeweza kuigundua sehemu yako hii

    ya tambiko kirahisi namna hii. Jibu ni kuwa kazi ilikuwa rahisi tu kwani mara tu

    ulipofanikiwa kututoroka siku ile kwenye lile eneo la Botanical Garden huku ukipitia

    eneo la chini kwenye mifereji ya maji machafu tulianza kufanya uchunguzi wa kina

    na makini tukiwauliza watu na kuchunguza maeneo tuliyoyashuku. Hatimaye turufu

    yetu ikaangukia hapa na majibu ya kiongozi wako wa kiroho baada ya kumbana vizuri

    akatueleza kuwa ulikuwa hapa. Siri moja tu rafiki yako aliyokufa nayo moyoni ni kuwa

    hakutueleza kuwa ulifika hapa kufanya nini.

    Hatutaki kuamini kabisa kuwa ulifika hapa kwa sababu za kiimani kwa vile

    mikono yako imetapakaa damu za watu wasio na hatia. Hivyo tunaamini kuwa

    kuna sababu nyingine zaidi ya hiyo ambayo hatuna wasiwasi wowote kuwa muda

    utakapofika utazungumza kila kitu. Safari ya kwanza baada ya kutoka hapa tunaelekea

    moja kwa moja sehemu ulipomficha CID Dan Maro na baada ya hapa Sulle Kiganja

    atakuwa anakusubiri kwa hamu sana ofisini kwake” yule mtu aliyeonekana kuwa ndiye

    kiongozi wao akajitapa kwangu na muda uleule akanisogelea mbele na kunivisha pingu

    mikononi na wakati akifanya vile macho yangu yakawa yameweka kituo na kuitazama

    vizuri ile michirizi ya damu iliyoelekea upande wa kushoto kwenye uchochoro hafifu.

    Michirizi ile ya damu ikanifanya nianze kuvuta picha namna risasi za wauaji wale

    zilivyotumika kuukatisha uhai wa Pastor Romanus. Hasira zikanipanda kichwani hata

    hivyo sikuwa na namna ya kufanya badala yake nikameza funda kubwa la mate na

    kupiga moyo konde. Mara tu yule mtu alipomaliza kunifunga ile pingu tukaanza safari

    ya kutoka mle ndani huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.

    Nilifahamu fika kuwa namna yoyote ya kujiokoa kutoka mikononi mwa wale watu

    nilipaswa kuwa makini kwa vile ulinzi niliyokuwa nimewekewa ulikuwa mkubwa tena

    wa watu walionekana kuwa makini na nyendo zangu. Hata hivyo nilifahamu kuwa

    endapo ningekubali kuchukuliwa na wale makachero basi ile ndiyo ingekuwa hatua

    ya kwanza ya kuelekea kwenye kifo cha kinyama chenye mateso makali ya jasho la

    damu kwani ni dhahiri kuwa ukweli wowote ambao ningejitetea nao kuwa mimi siyo

    niliyehusika na mauaji ya makachero wenzao usingenisaidia kitu.

    Sasa nilikuwa nikitembea kwa tahadhari ya hali ya juu katikati ya korido pana

    iliyopakana na mabenchi katikati ya kanisa lile kuelekea nje huku nikiwa chini ya

    ulinzi mkali. Nyuma yangu walikuwa watu watatu,mmoja akiwa ni yule kiongozi

    wao,wawili wakiwa ni wale vijana waliokuwa wamejificha kule kwenye vichochoro

    vya madhabahuni kuelekea kwenye vyumba vya kuandaa neno. Mbele yangu alikuwa

    amenitangulia mtu mmoja tu ambaye ndiye yule aliyekuwa ameielekezea bastola yake

    kisogoni kwangu. Nilipotazama kule mbele kwenye ule mlango wa kanisa nikawaona

    wale wanaume wengine wawili wakinisubiri kwa protokali zote za ulinzi huku mmoja

    akiwa amesimama upande wa kushto wa ule mlango wa kanisa na mwingine akiwa

    amesimama upande wa kulia,wote wakiwa na bastola zao mikononi.

    Tuliendelea kutembea kwa utulivu na tulipofika katikati ya lile kanisa kumbukumbu

    ya lile tukio la kuuwawa kwa mzee James Risasi na taswira ya ile michirizi ya damu

    isiyokuwa na hatia ya Pastor Romanus kule madhabahuni ikavuka kiwango cha

    mwisho cha uvumilivu wangu. Sikuona sababu ya kuendelea kusubiri hivyo kwa

    kasi ya upepo nikasafiri kwa hatua moja zaidi mbele yangu kisha nikatupa teke moja

    makini nikiupiga ule mkono ulioshika bastola wa yule mtu mbele yangu. Ile bastola

    ikamponyoka mkononi na kuruka hewani tukio ambalo lililowashangaza sana wale

    wenzake na kuwapelekea washindwe kufanya maamuzi ya haraka.

    Wale makachero wakiwa bado wanashangaa shangaa nikajitupa hewani kama

    kivuli na kumtandika yule mtu mbele yangu mateke mawili matata ya mgongoni

    yaliyomtupa vibaya kwenye mabenchi yaliyokuwa upande wa kushoto eneo lile.

    Kisha nilipotua chini ile bastola ya yule kachero ikawa imeangukia mikononi mwangu

    huku nikiserereka sakafuni na kupotelea kwenye uvungu wa mabenchi yaliyokuwa

    jirani na eneo lile nyuma yangu nikikoswakoswa na risasi kadhaa za wale makachero.

    Mapigano ndani ya hekalu la Mungu ilikuwa ni zaidi ya laana kwa wanadamu lakini

    kwa kuwa uhai wangu ulikuwa mbioni kununuliwa kwa gharama ya risasi sikuwa na

    namna nyingine ya kujihami.

    Risasi nyingi zikawa zikirindima na kunifuata nyuma yangu kwenye yale mabenchi

    ya kanisa hata hivyo kutokana na giza hafifu la mle ndani wale makachero wakapoteza

    malengo ya shabaha na kuishia kuvunja mbao za mabenchi yale kwa risasi huku

    mimi nikitambaa chini kwa chini. Wale makachero walipoona kuwa nilikuwa mbioni

    kuwatoroka wale wenzao waliokuwa wamesimama kule mlangoni haraka wakawahi

    kuja mle ndani kuongea nguvu. Kachero mmoja akashika uelekeo wa upande wa

    kushoto kwenye uchochoro mdogo uliokuwa kati ya yale mabenchi ya kanisa na ukuta

    huku yule kachero mwingine akianza kaparamia yale mabenchi moja baada ya jingine

    na bastola yake mkononi akitazama chini kunitafuta. Hata hivyo hakufanikiwa kafika

    mbalimbali kwani nilijibanza na kumsubiri hadi pale aliponikaribia kisha nikaikamata

    vyema bastola yangu. Risasi mbili nilizozifyatua moja ikakilenga kiganja cha ule

    mkono wake uliyoshika bastola na kukikata vibaya kidole chake tukio lililopelekea ile

    bastola aliyoishika ianguke chini. Risasi nyingine ikapasua vibaya mifupa ya goti lake

    na hapo akapiga yowe kali na kuanguka chini akiparanganya vibaya na yale mabenchi

    na kulia kama mtoto.

    Nikiwa chini ya yale mabenchi haraka nikayatembeza tena macho yangu na kuiona

    miguu ya yule mwenzie akinikaribia kwa jazba. Tabasamu jepesi likapita usoni mwangu

    na hapo nikajiviringisha vizuri na kuvuta kilimi cha bastola yangu mkononi. Risasi

    moja ikapasua kifundo cha mguu wake na kumpelekea apige yowe kali la maumivu

    na alipotua chini kwenye ile sakafu macho yetu yakakutana na hapo nikamuona yule

    kachero akanisihi sana kwa ishara na kuniomba msamaha kuwa nisiukatishe uhai

    wake na kwa kujenga uaminifu akinitupia ile bastola yake katika namna ya kunionesha

    kuwa alikuwa hataki tena upinzani na mimi. Sikumuacha badala yake nikamlegeza

    kwa risasi mbili za kiuno ambazo zingempelekea atembelee kiti cha walemavu kwa

    sehemu yake ya maisha iliyosalia hapa duniani.

    Muda uleule mvua kubwa ya risasi ikaanza tena kurindima mle ndani ya lile kanisa

    huku risasi zile zikinifuata pale chini ya benchi nilipojibanza. Mbao za mabenchi ya

    eneo lile zikaanza kipukutika ovyo na vibanzi vyake kuniangukia. Zile risasi sasa zikawa

    zikinikosakosa na kunifanya nianze kuhisi hatari ya kifo ikinikaribia. Nilitaka kuanza

    tena hila yangu ya kutambaa chini ya yale mabenchi ili kuikwepa mvua ile ya risasi

    lakini mara moja nafsi yangu ilinionya kuwa mjongeo wowote ambao ningeufanya wa

    kuhama eneo lile ningekuwa nimetoa mwanya mzuri wa shambulio la hakika la risasi

    dhidi yangu na hali ile ingekuwa hatari zaidi. Hivyo nikiwa nimejibanza pale chini ya

    benchi nikaanza kupiga akili nyingine ya haraka ya kujinasua.

    Mle ndani ya kanisa sasa nilikuwa nikishambuliwa na makachero wanne baada ya

    wale wawili kuwa nimefanikiwa kuwapunguza nguvu kama siyo kuwatuliza kabisa.

    Nilipochungulia na kuwatazama wale makachero waliokuwa wakinishambulia

    nikagundua kuwa wawili kati yao walikuwa nyuma yangu wakinishambulia kutoka

    nyuma ya nguzo moja ya kanisa na makachero wengine wawili waliosalia walikuwa

    kwenye korido pana ya katikati ya kanisa.

    Wazo fulani likawa limenijia akilini. Kutoka pale uvunguni mwa lile benchi

    nilikojificha nisingeweza kuwashambulia kwa urahisi wale makachero waliokuwa

    kwenye ile korido ya katikati ya kanisa lakini juu yao kwenye dari ya lile kanisa

    kulikuwa na feni nyingi kubwa za pangaboi zilizotundikwa kupunguza joto la mle

    ndani wakati wa ibada. Hivyo bila kupoteza muda nikaikamata tena vyema bastola

    yangu mkononi na kufanya mashambulizi matatu makini kuelekea kwenye vishikizo

    vya zile feni kwenye dari ya lile kanisa.

    Muda uleule nikaziona feni tatu zikianguka chini kwa kasi ya ajabu usawa wa wale

    makachero wawili pale walipokuwa. Wale makachero kwenye ile korido hawakuwa

    wameelewa vizuri ni maana ya shambulio lile hivyo wakawa wanashangaa shangaa

    na muda uleule feni mbili kati ya zile tatu zikawaangukia vichwani na kuwaangusha

    chini. Ile feni moja iliyosalia ikatua kwenye mabenchi ya jirani na eneo lile na kuanza

    kurukaruka ovyo huku mapangaboi yake yakitishia usalama. Wale makachero

    walioangukiwa na zile feni hawakufurukuta wala kusimama pale chini na hapo nikajua

    kuwa walikuwa kwenye hali mbaya sana huku damu ikiwatoka kwenye majeraha ya

    miili yao yaliyotokana na kukatwa vibaya na mapangaboi ya zile feni.

    Sasa mle ndani kukawa kumesaliwa na makachero wawili tu ambao nao kwa

    wakati ule walikuwa wameacha kufyatua risasi na hivyo kupelekea mle ndani ya kanisa

    kutawaliwa na ukimya wa aina yake. Zile kelele za milio ya risasi zilikuwa zimewashtua

    njiwa waliokuwa wamejenga viota vyao kwenye paa la lile kanisa na sasa njiwa wale

    walikuwa wakipukutisha mbawa zao na kukimbia eneo lile.

    Niliendelea kujibanza chini ya lile benchi huku nikiupima utulivu wa mle ndani na

    nilipoona kuwa hakukuwa na rabsha nyingine taratibu nikaanza kutambaa chini ya yale

    mabenchi kuelekea mbele ya lile kanisa. Baada ya muda mfupi nikawa nimefika kule

    mbele hivyo nikatoka kwenye yale mabenchi na kwenda kujibanza kwenye kona moja

    ya lile kanisa nikisikilizia kama kungekuwa rabsha zozote huku bastola yangu ikiwa

    mkononi. Bado sikusikia kitu chochote ingawa nilikumbuka kuwa yale mashambulizi

    ya risasi yaliyokuwa yakitokea nyuma yangu wakati ule yalikuwa yakitokea kwenye

    nguzo moja kubwa ya kanisa lile ambayo haikuwa mbali sana kutoka pale nilipojibanza.

    Mle ndani ya kanisa hali bado ilikuwa tulivu hivyo nikaanza kunyata taratibu

    nikielekea kwenye ile nguzo kubwa ya kanisa na kwa kufanya vile mara nikamuona

    kachero mmoja akichomoka kutoka kwenye ile nguzo na kuanza kukimbia akielekea

    kule kwenye ule mlango mkubwa wa kanisa huku akigeuka na kuanza kunishambulia

    kwa risasi. Kuona vile haraka nikawahi kujitupa chini na kujikinga mbele ya benchi

    moja lililokuwa jirani na eneo lile na kwa kuwa sikutaka yule mtu anitoroke mle ndani

    hivyo haraka nikajiviringisha sakafuni kuelekea kwenye ile korido ya katikati ya

    ya kanisa

    na nilipofika nikatafuta mhimili mzuri na kufyatua risasi moja kumlenga yule kachero

    aliyekuwa mbioni kuufikia ule mlango wa kanisa ili atoke nje.

    Muda uleule mara nikamsikia yule mtu aliyekuwa akikimbia akipiga yowe kali la

    maumivu huku akisombwa na kutupwa hewani kabla ya kuanguka chini. Ile risasi yangu

    moja ilikuwa imempata kwenye paja la mguu wake wa kushoto. Hata hivyo yule mtu

    alikuwa na roho ngumu kama ya paka kwani haukupita muda mrefu mara nikamuona

    akisimama tena na kuchechemea huku mkono wake wa kushoto ukijitahidi kuusaidia

    kuukokota ule mguu wake wenye jeraha na hivyo kukaza mwendo tena akikimbia kwa

    taabu kuufuata ule mlango wa kanisa ili atoke nje.

    Sikutaka kumpa yule mtu nafasi ya kunitoroka hivyo nikavuta tena kilimi cha

    bastola yangu kuisukuma risasi nyingine. Shabaha yangu makini ikapelekea risasi ile

    nyingine kupenya kwenye paja la mguu wake mwingine wa kulia na hapo nikamsikia

    yule kachero akipiga yowe jingine kali la maumivu kabla ya kutupwa mbele na kuanguka

    chini kwenye ile korido katika mtindo wa kupiga magoti kama mtu anayeungama

    dhambi zake kanisani. Huku akiutazama ule mlango wa kanisa hatua chache mbele

    yake.

    Yule kachero mmoja aliyesalia mle ndani kuona vile akawa ameshikwa na kihoro

    hivyo kufumba na kufumbua akakurupuka kutoka kwenye maficho yake gizani na

    kuanza kuparamia dirisha moja jembamba lililokuwa karibu na ile madhabahu ya

    kanisa na hatimaye kujirusha nje kabla ya kusikia kishindo kikubwa cha mwanguko

    wake chini ya lile dirisha huku risasi zangu mbili zikimkosakosa na kumpunyua begani.

    Muda mfupi uliyofuata mara nikasikia sauti za vishindo vya hatua za yule kachero

    akitimua mbio na kuyoyomea mbali na lile kanisa. Yule kachero akawa amefanikiwa

    kunitoroka.

    Bila kupoteza muda zaidi mle ndani haraka nikatafuta funguo za ile pingu

    niliyofungwa mikononi kutoka katika mfuko wa koti la suti la yule kachero kiongozi

    aliyeangukiwa na feni mojawapo la mle ndani kisha nikajifungua ile pingu na kuitupa

    kando. Muda mfupi uliyofuata nikarudi tena kule madhabahuni na kuanza kuifuatilia

    ile michirizi ya damu iliyokuwa imeelekea kwenye ule uchochoro wa upande wa

    kushoto wa ile madhabahu.

    Nilimkuta Pastor Romanus akiwa amaketi chini kwenye kona moja ya kichochoro

    cha upande wa kushoto wa madhabahu ile huku akiwa katika mavazi yake ya kiraia

    ya shati jeupe,suruali nyeusi ya kitambaa na viatu vya ngozi vya rangi ya udongo

    miguuni. Nilimposogelea na kumshika shingoni sikuona dalili zozote za uhai na mwili

    wake tayari ulikuwa wa baridi roho yake tayari ikiwa imefika kwenye sayari nyingine.

    Nilipozidi kumchunguza vizuri Pastor Romanus nikagundua kuwa tumboni alikuwa

    na majeraha mengi ya risasi yaliyokuwa ukingoni kuvuja damu. Macho yake alikuwa

    ameyafumba ingawa mdomo wake ulikuwa wazi. Mikononi alikuwa ameikumbatia

    Biblia ndogo iliyotapakaa damu. Huzuni ikanishika hata hivyo sikuwa na namna badala

    yake nikainama pale chini na kumfumba vizuri mdomo wake kisha nikaichukua ile

    Biblia ndogo kutoka mikononi mwake huku nikiwa nimekata tamaa kabisa ya kupata

    taarifa zozote za kunisaidia kwenye harakati zangu

    Niliendelea kumtazama mzee yule rafiki yangu mwenye ufahamu wa elimu ya juu

    ya mambo mengi ya ulimwengu huu kisha nikageuka na kuanza kuondoka taratibu

    eneo lile huku mkononi nikiwa nimeichukua ile Biblia yake iliyotapakaa damu.

    Nilipofika katikati ya ile madhabahu ya kanisa sikuona haja tena ya kuondoka

    na ile Biblia kwa kuwa ilikuwa imetapakaa damu nyingi ya Pastor Romanus. Hivyo

    nikaelekea kwenye ile meza ya kanisa yenye mishumaa nikipanga kuitelekeza ile Biblia

    juu yake. Lakini wakati nikiwa katika harakati zile nafsi yangu ikajikuta ikishawishika

    kuifunua ile Biblia na kwa kuwa sikuona sababu yoyote ya kupingana na msukumo ule

    moyoni mwangu nikaamua kusimama na kisha kuifunua ile Biblia. Hatimaye macho

    yangu yakatua juu ya kurasa ya kwanza nyeupe ya kitabu kile iliyoandikwa kwa hati

    inayosomeka vizuri.

    Gabbi Masebo & Milliam Casian

    Wishing you all the best in your wedding day

    Revelation 13;17-18

    Welcome to heaven night club

    Dar es Salaam

    Saturday 6th,July-2005

    Oga & White Sugar

    Nilipozidi kupekuwa kwenye kurasa za ile Biblia katikati nikakuta picha moja ya

    zamani ya wanandoa wakiwa katika mavazi yao ya kupendeza ya harusi na nyuma yao

    walikuwa wamesimama wasimamizi wa ndoa ile mwanamke na mwanaume. Yule

    mwanamke msimamizi wa ile ndoa haraka nilimfahamu kuwa alikuwa ndiye yule

    dada niliyepambana naye ndani ya lile jengo la ghorofa la waabudu shetani lililoko

    maeneo ya Posta Dar es Salaam siku ile akifahamika kwa jina la Oga. Yule mwanaume

    kwenye ile picha sikuwahi kumuona hata siku moja katika harakazi zangu na kutoka

    pale nikiwa nimeanza kupata muunganiko mzuri wa matukio ya nyuma ingawa picha

    bado ilikuwa haijakamilika.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Ingawa nilikuwa siifahamu vizuri Biblia na maandiko yake lakini kwa namna

    moja au nyingine hisia za kuwa Pastor Romanus alikuwa ameniachia ujumbe fulani

    kupitia kitabu kile zikawa zimeanza kujengeka kichwani. Hivyo bila kupoteza muda

    nikaichukua ile Biblia na kuifuta ile damu iliyotapakaa nikitumia kile kitambaa

    kilichokuwa juu ya ile meza ya madhabahu na kuitia mfukoni. Kisha haraka nikaanza

    kuondoka eneo lile nikikatisha katikati ya lile kanisa kuelekea nje huku mawazo mengi

    yakipita kichwani mwangu. Usikuwa bado ulikuwa unamengi ya kuzungumza.





    MWISHO WA MSIMU WA KWANZA

    ENDELEA KUFUATILIA MSIMU WA PILI



    *********MWISHO******

0 comments:

Post a Comment

Blog