Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

NJIA NYEMBAMBA (2) - 5





    Simulizi : Njia Nyembamba (2)

    Sehemu Ya Tano (5)









    "Mkuu, hali si nzuri. Waandamanaji hawa wamekuwa wakimshuku mtu yeyote mgeni ndani ya maeneo yao," alijitetea Rauli.

    "Kwahiyo kama ni hivyo?" Talib aliuliza. "Rauli, ndio maana nikakupa hiyo kazi. Ukae na utazame namna ya kuwapoteza watu hawa.



    Unavyokuja na kuniambia njia yako imefeli, unadhani nina muda wa kusikiliza huo upuuzi wako?"





    Rauli akatikisa kichwa.





    "Ulitaka nini ulichokiainisha kwenye mipango yako nikakunyima?"

    "Hamna, mkuu."

    "Sasa unaniletea porojo gani hapa?"





    Talib akasimama. Alipiga kofi meza akifoka:

    "Toka! Ukirudi hapa pasipo kuniletea cha maana, nitakumaliza mbwa wewe."





    Rauli alisimama, akaenda akitazama chini. Alijihisi vibaya, lakini pia alijihisi amekosewa. Aliminya lips akienenda na kujipaki kwenye gari lake, mercedes benz jeupe toleo la zamani, akatoka ikulu.





    Baadae ilikuja kuripotiwa mwanaume huyu amejiua kwa kujinyonga. Ilikuwa ni punde baada ya kuonana na wenzake na kuwaambia hawezi tena kazi. Hawakumuelewa, labda kwasababu hakusema sana.







    ---







    Waswahili husema mzaa janga hula na wa kwao. Na hakika hawakukosea. Msiba haukosi ndugu.





    Wakati Sierra Leone kukifukuta, Al Saed anafikishiwa habari mbaya kabisa inayomharibia siku. Anahabarishwa watumishi wake wameuawa, ni Rambo pekee ndiye alibaki hai, tena akiwa majeruhi hohehahe.





    Taarifa hizo zilimkuta akiwa anakula chakula cha mchana. Hamu ya kula ilikoma punde akaharakisha hospitali kumuona Rambo apate kumuelezea kilichosibu. Isingelikuwa ni mkuu wa nchi, asingeliruhusiwa kumuona mhanga kwa kuambiwa ampe muda wa mapumziko. Zaidi, uso wake uliwaogopesha wauguzi kwani ulikuwa umefura na kughafirika vya kutosha.





    Hatua zake alizotupa zingekufanya umpishe njia pasipo kuombwa.





    Alijikuta anapigwa ganzi ya mwili alipomuona Rambo akiwa amejilaza kitandani. Alijihisi mwili umepoteza nguvu, magoti yanagongana. Alipata joto la mwili upesi, akaona nguo zinambana. Alitamani hata kuzivua.





    Kwake Rambo kulala kitandani halikuwa jambo dogo hata kidogo, ilikuwa ni ishara ya kushindwa. Ishara ya kuzidiwa. Atafanyaje sasa ilhali wanaume aliowategemea wamalize kazi, wamemalizwa kabla ya kazi?





    Uso wote wa Rambo ulikuwa mwekundu, jicho moja lilivimba rangi ya zambarau. Mkono wake wa kuume ulikuwa umevunjwa. Kichwa kilikuwa kimezungushwa plasta nzito kana kwamba mti umeungwa usianguke. Mguu wa kushoto haukuwepo, wa kulia ukiwa umevunjika.





    Alitia imani. Ungeweza sema amekufa.





    Al Saed alimsogelea karibu zaidi, akashika kitanda. Aliita kwa sauti ya chini, mara tatu, mara Rambo akafungua jicho, lile lililokuwa na afadhali, la kushoto. Nalo lilikuwa limevijilia damu. Hakumudu kuliangaza kwa muda, akalifumba.





    "Mkuu," aliitika kwa shida.

    "Nini kimetokea, Rambo?" Al Saed akauliza. "Nini kimewakumba?"

    "Tuli ... va- miwa, mkuu," alijibu Rambo kwa shida. Alikohoa mara mbili kisha akaendelea: "Tulipang - a vizuri tu ... vizuri ... Tulipo,anza kusha ... mbulia, mabomu mata...tu ya -liru - shwa mbele yetu." Rambo akaweka kituo. Alivuta kwanza hewa, mara kwa mara akiugulia maumivu.

    "Baa ... da ya ha-po, sikumbuki cho-cho-te zaidi ... zaidi ya make - lele ya wenzangu na make... le, le ya risasi. Nasha ... nga .. aa nimefika ... je hapa hai."





    Akaweka kituo kirefu.





    Ilikuwa ni habari ya kuwahiwa kabla hujawahi; pale ujanja wako unapokuwa ujinga mbele ya adui. Kikosi cha wanaume hawa, wakina Rambo, walitanguliwa hatua tatu mbele kimaamuzi. Kila walichokuwa wanafanya kilishatarajiwa tayari, na kikapangiwa namna ya kukikomesha.





    Wakiwa wamepashwa habari na mateka wao, kiongozi wa kamati ya ulinzi na mjumbe wake, walivamia maeneo yale matatu elekezi. Walipovamia eneo moja, hawakukuta kitu, na la pili pia, hivyo basi wakajua la tatu ndilo lenyewe hivyo nguvu zikatiwa hapo.





    Ambacho hawakukijua ni kwamba, maadui zao nao walikuwa wameshalitambua hilo, kwani taarifa za uvamizi wa maeneo mawili ya nyuma walishazipata toka kwa maajenti wao. Hivyo basi, wakajipanga.





    Wakina Rambo walikuta eneo kimya kama vile hamna watu. Walikuja eneoni hapo kwa miguu. Walisogelea jengo hilo kwa kunyatia, na kwa uangalifu.





    Lilikuwa ni jengo la kisasa kubwa la ghorofa, halikuwa limemaliziwa plasta. Kwa nje kulikuwa kuna bustani kubwa likizingira, pamoja na matofali kadhaa.





    Rambo na wenzake wakiwa wanasogea, kuna wanaume wanne waliokuwa wanawatazama, wakiwa wamekaa chumba cha juu. Walipofika eneo la karibu zaidi, wanaume wale wakatazamana, kisha wakapeana ishara. Mmoja akatoa mabomu kwenye kamfuko cheusi kalichokuwepo kando. Akayachomoa pini na kuyarusha kwa mkupuo.





    Yakiwa hewani, wengine wakashikilia bunduki zao tayari kwa mashambulizi.





    Kufumba na kufumbua, mabomu yakatua miguuni mwa wakina Rambo. Hakika wakatoa macho kwa mshangao. Roho zilikuwa mikononi sasa. Walikutana uso kwa uso na kifo.





    "Kimbia!" Mmoja wao alifoka. Kila mtu alijaribu kujiepusha na adha ya kifo kwa kutumia miguuye, ila hawakufika hata hatua mbili, mabomu yakajitusu na kuwarushia mbali.





    Kilichomnusuru Rambo, ni kutulia tuli baada mlipuko huo, alikuwa amepoteza fahamu. Wenzake waliokuwa wanagugumia kwa maumivu, walishushiwa mvua ya risasi, na kisha wahusika wakahepa.





    Ni baada ya masaa matatu, ndipo wakaja waokozi na kubeba miili ya Rambo na wenzake. Walikuwa ni wanajeshi watano waliobebelea silaha. Walipekua nyumba wakapata maganda lukuki ya risasi.





    Walidhani Rambo amekufa pia. Isingekuwa hekima za mfanyakazi wa mochwari, basi alikuwa anatiwa kwenye jokofu kama wenzake waliotiwa humo pasipo kupata huduma yoyote.







    ***







    "Twende basi tukale, mpenzi," Kone alimwambia Fatma aliyekua amejilaza kitandani. Ni majira ya saa mbili usiku sasa na takribani dakika za kutosha.





    Macho ya Fatma yalikuwa mekundu. Alilaza kichwa chake juu ya mkono. Alikuwa amegeuzia uso wake ukutani asimwangalie mumewe. Hakutaka kabisa kuongea na mwanaume huyo tokea aliporudi toka kwa Rose.





    "Mke wangu, utakaa hivyo mpaka lini? Niambie basi kosa langu ni nini."

    "Kone, kama hujui kosa lako, huna haja ya kuomba msamaha," alisema Fatma kwa mara ya kwanza. "We nenda kale, mimi utanikuta hapahapa!"

    "Siwezi nikaenda pasipo wewe. Watoto watajisikiaje?"





    Kimya.





    "Fatma," Kone akaita tena. Aliongea zaidi na zaidi ila Fatma hakusema tena chochote, mwishowe akaamua kwenda kula mwenyewe. Aliwadanganya watoto mama anajisikia vibaya. Watoto walikula wakaenda zao, wakamuacha baba peke yake mezani.

    Baada ya muda mfupi, Kone anajipepesa kutafuta simu mfukoni. Hakupata kitu. Alitazama mezani na maeneo ya karibu, napo hakupata kitu. Moja kwa moja akajua atakuwa ameiacha chumbani.





    Alijinyanyua akaenda chumbani taratibu. Alimkuta mkewe akiwa anatumia simu hiyo, akipekua ujumbe. Aliishia kumtazama akimngojea amalize. Bado macho ya mwanamke huyo yalikuwa mekundu.





    Alimaliza upekuzi, akaiweka simu kando na kugeukia ukutani. Kone hakuichukua simu hiyo, akamtazama mkewe kwa muda wa kama dakika nne pasipo kusema jambo. Alikuwa anatafakari mambo lukuki kichwani.





    Alimgusa mkewe bega, akimuita. Fatma hakuitikia.





    "Samahani, mke wangu. Nimejua kosa langu. Nilipitiwa, hakika nilisahau kabisa. Ila kesho, naapa, nitakupeleka kwenye ile nyumba ukaione."

    "Kesho?" Fatma aliuliza na kisha akaguna. Aligeuza shingo yake akamtazama mumewe. "Unadhani tutakaa hapa mpaka lini? Kila uchwao tuwe tunatoa pesa kulipia nyumba, chakula. Mpaka lini? Uliliona hili halina maana, ukalipuuzia. Umeona ya Guinea na Rose ni ya maana zaidi kuliko familia yako?"





    Fatma aliongea kama chiriku. Kone alikaa kimya kusikiliza. Mwanamke huyo alipochoka, akajilalia zake, akimalizia kwa kusema:

    "Safari njema ya mauaji."





    Kone alishusha pumzi ndefu akiegemeza mgongo wake ukutani. Aliendelea kutafakari mambo kadha wa kadha wakati muda ukisonga. Yalipofika majira ya saa nne, alichukua simu yake akampigia Rose.





    "Vipi tayari?"

    "Ndio, nakungoja wewe."

    "Poa, nakuja."









    *MLENGWA No. 5*



    Kone alinyanyuka akajiandaa, baada ya muda mfupi akawa ameshatoka na kujiweka ndani ya gari lake na kutimka. Alimpitia Rose wakaelekea eneo la tukio wakipewa maelezo vema na Amadu kwa njia ya ujumbe.





    Mlengwa namba tano, ndani ya Sierra Leone. Huyu hakuwa mwingine bali bwana Araphat Saleh; mwanaume aliyewahi kuwa mfanyakazi wa serikali ndani ya ofisi ya jiji la Freetown. Mwanaume huyu amewekwa kwenye orodha kwa kisa cha kuhusika na kikundi cha waandamanaji ambacho kimegeuka kuwa cha waasi.





    Huyu ni kiongozi mkuu wa hiki kikundi. Ndiye yeye anahusika na kuendesha lakini pia kuasisi harakati za hiki kikundi. Yeye ndiye anayeopareti mitandaoni, haswa kwenye kikundi cha whatsapp, akiunga na kuendesha mijadala.





    Jambo ambalo hakulijua ni kwamba, miongoni mwa watu aliowaunga kundini, mmojawapo alikuwa mhusika wa THE GHOST. Ambaye alirekodi na kufuatilia kwa umakini yale yote yaliyokuwa yanatukia. Hakukuwa na siri.





    Kwa mtu huyu, Kone na Rose walikuwa wanatakiwa kumfanyia pekuzi ya baadhi ya taarifa nyeti. Taarifa ambazo hawana ujuzi nazo. Taarifa kubwa ikiwa ni nani anayewafadhili wafanyakazi hawa ambao kiuhalisia wamechoshwa na ukata na hawawezi kumudu kumiliki silaha za moto na mtandao mpana.





    Kone na Rose walifika eneoni, wakazima gari. Walisogelea eneo lao la tukio, nyumba ya Arafat, kwa uangalifu mkubwa kwakuwa tayari walishataarifiwa juu ya hulka ya wananchi kusambaza taarifa waonapo watu wanaowatilia mashaka.





    Nyumba ilikuwa ndogo, vyumba vitatu kama si viwili pamoja na sebule ndogo tu. Kulikuwa kuna mwanga hafifu ndani, kama vile mwanga wa kibatari. Hakukuonyesha kama kuna mtu mazingira hayo.





    Kone alikuwa ameweka bunduki yake ndogo kiunoni, lakini Rose alikuwa ameiweka mkononi tayari kabisa kwa pambano. Walichungulia ndani kupitia dirishani, hakukuwa na mtu. Kulikuwa kuna mwanga tokea kwenye taa ndogo iliyokaa ubavuni mwa meza.





    Walipekua mazingira vema, wakaridhika hamna mtu. Walitazamana kabla hawajaamua kwenda pabu ya karibu wakitumai kumpata huko, na wakimkosa basi waje kumgojea kwenye makazi yake.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Wakiwa wanatoka, wakahisi kuna mtu yuaja. Haraka walijificha kwenye miti wakitupa macho yao kwa umakini. Alikuwa ni Arafat anajirejesha nyumbani, mkono wa kushoto alikuwa amebebelea chupa ya bia, wa kulia akiwa ana simu kubwa aliyokuwa anaitazama.





    Mwanaume huyo hakuwa na hili wala lile. Pengine alikuwa anawaza mambo yake ya kikundi. Mwendo wake ulikuwa wa kistaarabu lakini macho yake yakiwa mekundu kuonyesha alikunywa za kutosha. Na kama haitoshi, akabebelea na ya kumsindikizia njiani.





    Akiwa anatembea, mara anasikia sauti ya majani nyuma yake. Anakurupuka na kuangaza macho nyuma, haoni kitu. Akaendelea na safari yake kama kawaida. Ila punde anasikia tena sauti. Nyuma yake kuna mtu alikatiza ghafla, na mtu huyu alikuwa Rose.





    Arafat alitazama, ila hakuona vema. Macho yake yalitoka kutazama kioo chenye mwanga mkali hivyo akawa anaona maruwekaruwe.





    "Nani?" Aliuliza. Kimya. Alipogeuza macho yake kutazama mbele, uso kwa uso akakutana na mwanga mkali wa kurunzi. Aliona giza. Hakujua cha kufanya. Alijishtukia anazabwa na kuanguka chini kama gogo. Alikuja kufungua macho na kuona vizuri akiwa amefungwa kamba kwenye kiti ndani ya nyumba yake, sebuleni.





    Mbele yake alikuwa amesimama Rose na Kone. Sasa Rose walikuwa wanaonekana vema. Rose alikuwa amevalia gauni refu jeusi la kubana na kuvutika, miguuni viatu vyekundu vya visigino virefu Rose alikuwa ameshika kiuno akiegemea ukuta wakati Kone akiwa amesimama wima, anaperuzi simu ya Arafat ambayo tayari loki yake ilikuwa imetenguliwa na mwenye nayo.





    "Habari Arafat?" Kone alisema kwa utashi. "Tupo hapa kwa muda mchache tu, kutaka machache. Tungeomba utupatie ushirikiano wako."

    "Kamwambieni kiongozi wenu, Talib, hapa ameula wa chuya! Hamtapata kitu!"





    Maneno hayo yalitosha kumghafirisha Kone. Hakuwa na muda wa kupoteza na mtu mmoja ilhali mambo lukuki yanamgoja. Alimtembezea kichapo kizito Arafat mpaka mwanaume huyo akawa nyang'anyang'a kama jojo. Alimvujisha damu uso mzima.





    "Upo tayari kusema? Au niendelee?" Aliuliza Kone. Mikono yake ilikuwa inachuruza damu. Kwa kipigo alichompatia Arafat, mhanga alikuwa hawezi hata kuongea, ilikuwa ajabu kuendelea kumuuliza.





    Mdomo ulikuwa umepoteza meno kadhaa. Lips zilikuwa hazitamaniki. Macho yalizama ndani kwa kuvimba.





    "Kone, tunapoteza tu muda. Twende nimepata wazo," alinong'oneza Rose. Kone alivunja shingo ya Arafat kisha wakautoa mwili huo na kuutupia msituni wakiendeleza safari iliyokomea kama kilomita mbili mbeleni.

    "Kwenye kundi la whatsapp, nimeona kuna admins wawili. Mmoja ni Arafat, na mwingine anaitwa Johnston. Bila shaka kama Arafat hajatupa majibu, huyu aweza kutusaidia," alisema Rose.

    "Sasa huyo Johnston tutampatia wapi?" Akauliza Kone. Macho yake yalikuwa yanatazama mbele aelekeapo.

    "Nimechat naye kwa punde wakati ukiwa unamfanyia intavyuu Arafat, nikapata taarifa za tija. Alidhani anachat na Arafat, hivyo akajieleza yupo wapi kwa sasa."

    "Ni mbali?"

    "Hapana. Bila shaka ni kama baada ya dakika kumi mbeleni."

    "Umejuaje?"

    "Nimetumia GPS kwenye simu ya Arafat."





    Gari lilienda kweli kwa dakika hizo, likasimama na kisha Kone na Rose wakatoka ndani ya gari kufuata nyumba fulani kubwa rangi nyeupe. Nyumba hiyo ilikuwa na uzio mkubwa na mlinzi.





    Ndani ya dakika tatu mlinzi alikuwa tayari yupo chini, ameshauawa, mbwa naye pia na Kone na Rose wakiwa mlangoni wanagonga. Hii ilikuwa kazi murua kabisa ya mwanaume: Kone pasipo makosa. Ujuzi wake uliendesha mikono na miguu akatenda kama anavyopaswa, tena kwa ukimya mkuu.





    "Nani?" Sauti toka kwenye spika ndogo pembeni ya mlango iliuliza.

    "Ni mimi, dear!" Akajibu Rose kwa sauti nyororo. Mara kukawa kimya, punde mlango ukafunguliwa na mwanaume mfupi mwenye asili ya Ulaya. Nywele zake zilikuwa nyeusi ti, na mdomo wake wake ulifunikwa na mustachi wenye afya.





    Kabla hajasema jambo, alikamatwa koo asiweze hata kupiga kelele. Aliingizwa ndani akatupiwa kwenye kochi akinyooshewa bunduki.





    "Johnston!"alibweka Kone. "Tuwie radhi kwa kukuharibia usiku wako, ila unaweza ukaufanya mzuri ama mbaya zaidi."

    "Mnataka nini?" Johnston akauliza.

    "Tunataka taarifa tu, si kingine."

    "Juu ya nini?"

    "Nani anayefadhili kundi la waasi chini ya mwamvuli wa waandamanaji wafanyakazi?"





    Johnston akakunja sura.





    "Sijui mnaongelea nini?"





    Kone akachomoa simu yake na kumuonyeshea Johnston picha ya Arafat aliyekuwa mfu asitamanike sura.





    "Pengine hii inaweza ikafupisha habari," alisema Kone.





    Johnston aliwatazama Kone na Rose kwa macho ya sungura. Ni kana kwamba kuna jambo alikuwa analitatua kichwani. Taratibu aliuzamisha mkono wake kwenye kona ya kochi, ila jicho la Kone halikuwa mbali kutambua hilo.





    "Ukifanya jambo lolote la kijinga, utajutia!" Alitishia Kone. Upesi Johnston akachomoa mkono wake, ulikuwa umebebelea bunduki ndogo nyeusi. Kabla hajafanya lolote, Kone akamuwahi kwa kumfyatulia risasi iliyozama begani na kumliza mwanaume huyo kana kwamba mtoto mchanga achomwaye sindano.





    Rose alikwapua bunduki ya Johnston akaiweka kibindoni.





    Sasa badala ya kujibu maswali, Johnston akawa analia kwa kugugumia maumivu makali begani. Bega lilichuruza damu iliyozidi kumuogofya.





    "Johston, hatuna muda wa kupoteza. Na uhai wako hauna uzito wowote kwetu. Tupe tunachokitaka twende," alisistizia Kone.





    Rose alinyanyua guu lake la kushoto akalituamisha kifuani mwa Johnston, kisigino chake kirefu kiligota shingoni mwa mwanaume huyo. Akakisogeza kidogo akiuliza;

    "Nani anayefadhili kikundi hiki?"





    Macho yake yalitisha. Kwa namna alivyosigima kisigino shingoni, Johnston alishindwa kuongea, Rose alimpa ahueni ndogo avute hewa. Mwanaume akapaliwa kwa kikohozi kirefu. Alipotulia akajibu:

    "Ni Freddy Samuel!"





    Baada ya tu hapo Kone akammaliza mwanaume huyo kwa kumvunja shingo, kisha wakafanya upekuzi wa nyumba nzima. Walikusanya baadhi ya nyaraka wakaenda nazo.





    "Hivi kile alichokisema kinaweza kikawa kweli?" Aliuliza Rose. Walikuwa kwenye gari wakijirudisha kwenye makazi yao.

    "Inaweza ikawa kweli ama uongo," alisema Kone.

    "Ila mimi siamini!" Rose akatia hoja. "Siamini kabisa. Kwa nimjuavyo Freddy, hawezi akafanya haya mambo haya."





    Si bure Rose hakuwa anaamini taarifa ya Johnston, Freddy alikuwa ni miongoni mwa viongozi wazuri waliowahi kutokea ndani ya nchi ya Sierra Leone, na pengine ungeweza haitakuja kutokea kiongozi wa kaliba hiyo.





    Mwanaume huyu mtulivu, aliyeongoza Sierra Leone kwa demokrasia, alipinduliwa na jeshi akiwa nje ya nchi kwa ziara ya umoja wa mataifa. Mmoja wa waasisi wa mapinduzi hayo akiwa ni Assessoko, mwanaume aliyekaimu kiti hicho cha uraisi baadae akilaghai wananchi kuenenda katika nyendo za kidemokrasia.





    Assessoko aliitisha uchaguzi ambao aliuendesha na kuusimamia yeye mwenyewe, akaamua kuwapa upinzani asilimia kumi na tano ya kura wakati yeye akisomba asilimia themanini na tano zilizobakia.





    Katika kipindi chake chote cha uongozi, hakuna aliyejua Freddy Samuel yupo upande gani mwa dunia. Wengine walisema alikuwa nchini Canada pamoja na familia yake akiwa anaishi maisha ya kawaida. Ila jina hili likaanza tena kuvuma masikioni pale mwanaume huyo alipteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa balozi wa amani.





    Sasa akawa anaonekana kwenye vyombo vya habari akisaidia kurejesha amani nchi kadha wa kadha akitumia busara yake kuu iliyoonekana na kuthibitishwa na yale yaliyotukia Sierra Leone, kutolipiza visasi wala kubeba vinyongo na maadui.





    Zaidi ya hapo, hakuna tena mtu aliyesumbuka naye, hakuonekana kama ana madhara, ila leo hii anarudishwa kwa kasi masikioni. Anatajwa na waasi!





    "Pumzika, nitakuja tuyajenge kesho!" Alisema Kone akimshusha Rose kwenye makazi yake.

    "Poa, usiku mwema."





    Kone akatimka mpaka maskani. Alimkuta mkewe akiwa amelala sebuleni akimgojea, alimbeba akaenda kumlaza kitandani kisha akarudi sebuleni kupitia nyaraka alizozipata kwenye nyumba ya Johnston.





    Miongoni mwa nyaraka hizo kulikuwa kuna cheki za benki, risiti kadhaa na vitabu vya mahesabu. Alizipekua nyaraka hizo akiwa ametulia kwa umakini. Alichukua kama dakika kumi na tano, akamaliza.





    Alichokigundua ni kwamba jina la akaunti ya benki iliyokuwa inahusika na mipango yote ya fedha ilikuwa imetunzwa kwa jina la Freddy Samuel. Alishusha pumzi ndefu akakuna kichwa. Aliteka simu yake akamtumia Amadu ujumbe kumjulisha yaliyotokea.





    "Freddy Samuel ahusiki kabisa," ujumbe wa Amadu ulisomeka hivyo.

    "Umejuaje na nyaraka zinaonyesha hivyo?" Amadu aliuliza. Punde ujumbe ukamjibu:

    "Freddy ameshakufa kitambo. Aliuawa na watu wasiojulikana kwa njia ya sumu."









    *MLENGWA NAMBARI MOJA - GUINEA*





    Hatari aliyokuwa amebebelea mikononi na mdomoni mwake ndiyo ilimfanya Sisawo awekwe kwenye orodha. Alitakiwa awe mtu wa kwanza kabisa kuuawa kabla ya mtu mwingine yeyote.





    Kwanini? Kwa jicho la tatu mtu huyu hakuwa mwenyewe, bali alikuwa kikundi. Nyuma yake alikuwa na jeshi tiifu lenye mafunzo. Anaweza akaleta machafuko muda wowote.







    Hivyo basi, kumuangamiza mwanaume huyu, ni kung'oa mbegu hatari ya vita na kupandikiza mazingira mazuri ya amani. Na kuhakikisha hilo linatendeka, Amadu pamoja na Chui wakalivalia njuga.







    Yalikuwa ni majira ya jioni tulivu kabisa, na wateja walikuwa wanaingia ndani ya hoteli ndogo ya kitalii inayovutia machoni kwa mpangilio wake.







    Hoteli hii, milki halali ya Sisawo, ni miongoni mwa hoteli zifanyazo vizuri sana kibiashara ndani ya Guinea. Japokuwa ni ndogo, ilikuwa inapendeza na ni ya gharama mno.







    Majira yakisogea sogea kwenda giza, mara gari mercedes benz nyeusi inaingia ndani ya hoteli hii na kupaki. Ilikaa tuli kwa muda wa kama dakika tano, kisha wakashuka wanaume wawili waliovalia kimaridadi kabisa.







    Walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai rangi ya samawati. Vichwa vyao vilikuwa vimefunikwa na kofia maridhawa zilizoendana na mavazi.







    Wakatazamana kisha wakatikisiana vichwa na kuzama ndani ya hoteli walipokomea mahala mahususi pa mgahawa , sakafu ya chini kabisa.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Walipotua kofia zao na kuziweka mezani, ndipo waonekana kumbe wanaume hawa walikuwa Amadu na Chui. Macho yao yalikuwa tulivu yakiambaa ambaa mazingira.







    Kulikuwa tulivu sana mgahawani. Watu kadhaa wenye heshima na nafasi zao walikuwa wakijipatia chakula cha maana. Hawakuwa wengi sana, ila kutokana na udogo wa eneo pakaonekana kama vile pamejaa.

    Amadu na Chui walikuwa wamekaa kwenye meza ya peke yao, na bado hawakuwa wamehudumiwa.







    "Umemuona?" Akauliza Chui.

    "Hawezi kuwa hapa muda huu," akajibu Amadu bado akiendelea kusachi eneo kwa macho. "Pengine yupo huko juu. Inabidi tuhakikishe hilo."







    Mhudumu akaja: mwanamke mwenye kimo cha wastani aliyevalia nguo ya tamaduni ya kichina yenye vifungo mpaka kooni.







    Alitabasamu akiwatazama watejawe aliowakabidhi orodha ya vyakula na vinywaji.







    "Samahani kwa kukawia, naweza nikawahudumia?"







    Amadu akatabasamu kabla hajajibu:

    "Ndio," na kuongezea: "tungependelea utuletee chakula chako bora kabisa ambacho unachodhani tutakifurahia."







    Mhudumu akatabasamu zaidi, kisha akaondoka kwenda jikoni.







    "Amadu, umejuaje kama tutakipenda chakula chake?" Chui akauliza.

    "Itabidi tuvumilie," Amadu akajibu. "Nia ni kumteka tu, kuna mambo nahitaji kuyafahamu toka kwake."





    Haikupita muda mrefu mhudumu akarejea akiwa amebebelea sinia kubwa mbili za chakula zilizofunikwa vema. Akalitua mezani.

    "Karibuni."





    Chakula kilikuwa ni nyama ya kuku iliyookwa, ndizi za kukaanga na za mchuzi, pamoja pia na tambi zilizokuwa zimechanganywa na mboga za majani.





    Harufu yake ilikuwa maridhawa na ilivutia walaji.





    "Ahsante sana," akasema Amadu akikamata uma na kisu. "Hiki ndicho chakula wakipenda?"

    "Ndio," akajibu mhudumu kwa tabasamu.

    "Nimeshaanza kukipenda kabla hata sijala ... unajua mimi na mwenzangu hapa ni wageni. Na huko tulipotoka, hatujazoea kuona huduma hivi kwa namna ya haraka.





    Bila shaka meneja atakuwepo hapa hapa mgahawani, sio?"





    Mhudumu akatabasamu.





    "Hapana, ni nidhamu tu ya kazi," akajibu na kuongezea: "Meneja yupo huko juu ofisini kwake ametulia tu."





    Amadu akashukuru, mhudumu akaenda zake.





    "Ni muhimu sana kutumia njia ya kuepusha hofu kwa watu kama hawa," akasema Amadu. "Watu hawa tayari wameshafundwa. Pale wanapohisi shaka huwa wanatoa taarifa."





    "Kweli, ulichofanya ni chema. Sasa tumeshajua Sisawo yupo wapi. Kwahiyo tunamfuata?"

    "Tuvute subra kwanza. Hatuna haraka kiasi hiko. Furahia chakula chako, tumelipia."





    Walikula wakiendelea na habari zingine kama kawaida, kama wateja wengine. Wakaagiza na vinywaji vya kusindikizia vilivyozidi kutia hamasa mlo wao.





    Wakiwa wanaendelea kula, mara wanamuona Sisawo akiwa anashuka ngazi. Alikuwa amevalia gauni la kitamaduni rangi ya kaki pamoja na kofia yake kichwani.





    Punde tu alipotokea, wanaume watatu nao wakatokea hatua kama mbili nyuma. Hawa walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai nyekundu.





    Walikuwa ni walinzi wa Sisawo. Macho yao yalikuwa yanazunguka huku na kule wakitembea kwa ukakamavu.





    Sisawo akaonana na msimamizi wa mgahawa, wakateta mambo kadhaa kisha akaenda zake nje akiongozana na walinzi.





    Baada tu ya muda kidogo, Amadu na Chui nao kwa pamoja wakasimama wakiacha sahani zao na mabaki hafifu ya chakula, wakaelekea nje wakitembea kwa mwendo wa wastani usiozaa shaka.





    Walipotoka tu langoni, wakaona gari la Sisawo likiwa linapita getini kuacha hoteli. Haraka wakakimbilia usafiri wao na kujipaki na kuanza kulifuatilia gari hilo.





    Lakini huku hotelini wakaacha shaka!





    Mlinzi wa getini alikuwa mwerevu wa kutosha kuhisi saga lililokuwa linaendelea. Aliwaona Amadu na mwenzake wakikimbilia gari lao pindi walipotazama getini, akili yake ikampigia alarm! Mkuu alikuwa anafuatwa.





    Haraka akanyanyua mkonga wake wa simu na kutoa taarifa:

    "Kuwa makini, kuna gari inawafuatilia."





    Mlinzi huyu ni miongoni mwa wapambanaji wa jeshi la Mandinka. Intelijensia yake ilikuwa juu. Macho na akili yake vilikuwa haraka kwenye kufanya maamuzi. Tena maamuzi sahihi.





    Taarifa yake ilipokelewa na dereva wa Sisawo ambaye naye akaipeleka mara moja kwenda kwenye kikosi kazi cha ulinzi.





    "Kuna nini?" Sisawo akauliza punde simu ilipokatwa.

    "Kuna virusi vinatufuatilia nyuma," akajibu dereva. "Ila usijali mkuu, tushawadhibiti."





    Sisawo akatazama nyuma.





    "Nani anatufuatilia?"





    Walikuwa wameingia kwenye barabara kuu hivyo kidogo ilikuwa ngumu kutambua, magari yalikuwa mengi upande wa kulia, kushoto na nyuma.





    "Ni mercedes benz nyeusi. Haina plate number," dereva akatoa maelezo. Sisawo akapekua mpaka alipolitia machoni gari hilo.

    "Ni mshenzi gani huyu anathubutu kufuata nyayo zangu!" Alisema kwa majivuni akitazama walinzi wake waliokaa kushoto na kulia yake.

    "Hamna wengine zaidi ya wafulani tu!" Akasema mlinzi mmoja. Sisawo akatabasamu.

    "Naona wanakiharakia kifo chao!"





    Akakunja ngumi akisaga meno.





    "Hakikisha mnaua wote! Nyama yao watakula mbwa wangu!"





    Gari likazidi kusogea. Kama dakika kumi na tano mbele yakatokea magari mengine mawili nyuma ya gari la wakina Amadu na Chui.





    Magari haya yalikuwa ni Ford ranger pick up. Rangize nyeusi. Nyuma yalikuwa yamepakia wanaume watatu watatu kila moja. Wanaume hawa walikuwa wamevalia nguo nyeusi tupu, na kofia za soksi vichwani.





    Kwenye sakafu ya gari walikuwa wamelaza bunduki kubwa SMG ambazo huwezi ziona mpaka usogelee gari hizo kwa ukaribu.





    Walisogea zaidi na zaidi, tageti yao ikiwa gari walilopo Amadu na Chui. Lakini kabla hawajakamilisha, Chui anagundua huo mchezo. Akamtaarifu Amadu.





    "Tazama hizo gari mbili, nahisi zinatufuata."





    Macho ya Chui yaliyokuwa yanatazama saiti mira yaliendelea kukodolea hapo kwa umakini. Akaona magari hayo yakijigawa, moja likienda kushoto na lingine kulia.





    Akampasha taarifa hiyo Amadu.





    "Weka silaha yako karibu," Amadu akasema kisha akakanyaga mafuta. Gari likakimbia zaidi. Huku nyuma napo, magari yale mawili yakachochea mwendo.





    "Shikilia vizuri!" Amadu alimwambia Chui. Haraka akaanza kuyakwepa magari mengine kwa mbele akilifuata lile gari lililombebelea Sisawo.





    Sasa ukawa ni mfukuzano wa hatari. Magari yalikimbizwa kama wehu.





    Kwa ustadi wa hali ya juu, Amadu akayakwepa magari mbele yake pasipo kupunguza mwendokasi. Ni punde tu akawa karibu na tageti yake, Sisawo!





    Kufumba na kufumbua wanaume wawili wakachomoza kwenye madirisha ya gari la Sisawo, wakaanza kumiminia risasi kushambulia gari la wakina Amadu. Risasi kama njugu!





    Amadu akajitahidi sana kumudu chombo. Alikipeleka kando na kando kukwepa risasi wakiinamisha vichwa vyao chini. Magari yaliyokuwepo nyuma yao yakatwangwa risasi na mara ajali kubwa ikatokea.





    Magari takribani nane yaligongana na kuharibika vibaya mno. Ajali hii ikabloku njia kwa wafuasi wa Sisawo waliokuwa wamejipaki kwenye Ford Ranger. Hilo likawapa ahueni wakina Amadu.





    "Chui, maliza sasa!" Amadu akapaza sauti. Upesi, Chui akafungua mlango wa gari alafu akachomoza kwa chini akiwa amebebelea bunduki yake ndogo.





    Akafyatua risasi tatu tu kisha akajirudisha ndani na kufunga mlango upesi.





    Bado gari lilikuwa linayumbayumba, lakini risasi za Chui hazikwenda kombo. Zikapasua vichwa vya wanaume wale waliokuwa wanamimina risasi na kuwaacha wafu.





    "Sasa imebaki kazi moja!" Akasema Amadu. Hakukuwa tena na pingamizi mbele yake. Akakanyaga mafuta barabara na kuisogelea kabisa gari la Sisawo.





    Magari yote yalikuwa kwenye mwendokasi mkali mno. Lakini Sisawo bado hakuona kama inatosha.

    "Kimbiza! Kimbiza!" Akasema akimbamiza dereva makofi.





    Moyo wake ulikuwa unaenda mbio akiogopa kifo. Alikuwa anageuza kichwa chake mara kwa mara kutazama wanaomkimbiza. Roho ilikuwa inamuuma kuona anakaribiwa.





    Kufumba na kufumbua, kama miujiza, Amadu analifikia gari la Sisawo. Na pasipo kuchelewesha muda, akalipush kwa nyuma ubavuni mwa gari hilo. Gari likapoteza mwelekeo!





    Liliserereka na kisha likajasimama mbele ya gari la wakina Amadu, likikaa kiubavu. Sisawo akatoa macho kama dafu akistaajabu namna gari la wakina Amadu linavyowajongea kwa kasi.





    Tahamaki, wakasombwa na kupaishwa juu wakibiringita hewani!





    Kwa haraka ya upepo, Amadu akachomoza dirishani mwa gari, akalenga uvungu wa gari la Sisawo lililokuwa hewani. Alipiga risasi tatu akilenga tanki la mafuta.





    Mara punde, gari likalipuka huko juu kwa juu. Amadu akakwepa mabaki yaliyokuwa yanaanguka wakiwa wanaendelea kutimka.





    Misheni ikawa imefanikiwa! Sisawo hakubakia hata jivu, yeye pamoja na dereva wake.





    Amadu aliacha njia kuu akashika njia za kuchepukia ambazo alidumu nazo kwa muda mfupi kabla hawajabadili gari kwa kukwapua lingine.





    Wakaongoza njia mpaka nje kabisa ya jiji walipoachana na gari na kutembea kwa miguu.





    Walitembea kwa ukakamavu wakihakikisha wapo salama na hamna mtu aliyewaona pindi wanatekeleza gari.





    Baada ya mwendo mdogo, wakaona magari mawili yanakuja kwenye uelekeo wao. Basi haraka wakajificha kwenye mojawapo ya chaka. Wakatulia kimya wakitazama kwa umakini.





    Magari hayo yalipita yakitembea taratibu. Yalikuwa ndiyo yale yale, Ford Ranger ya wafuasi wa Sisawo. Wanaume walikuwa wamebebelea bunduki zao mikononi wakitupa macho yao haswa.





    Mara,

    "Wale pale!" Akasema mwanaume mmoja akinyooshea kidole kwenye chaka.







    Hivyo basi hakukuwa tena na muda wa kupoteza, Amadu na Chui wakachoropoka toka chakani na kuanza kukimbia. Nyuma yao risasi zikarushwa kama njugu.







    Magari ya wajumbe wa Sisawo yaligeuza upesi na kuanza kuwakimbiza huku na huko.







    Kuwachanganya maadui, Amadu na Chui wakajigawa, mmoja akaelekea kushoto na mwingine kulia. Walikimbilia kwenye makazi ya watu huko wakijificha.







    Nao wajumbe wa Sisawo waligawa magari yao, kila mmoja likimfuata mwingine.







    Lakini utofauti ulikuwa kwamba, Amadu na Chui walikuwa wanawasiliana wakati watu hawa wa Sisawo wakienda kibubu.







    Walishuka toka kwenye magari yao wakasambaa huko mitaani kuwatafuta walengwa wao. Na hapo ndiyo wakawa wamekosea.







    Palikuwa kimya na giza. Na hata nyumba zilizokuwepo zilikuwa chache mno. Miti ilikuwa mingi pamoja pia na vichaka.







    Wanaume hawa wa Sisawo hawakuwa hata na kurunzi, walitumia macho yao kuangaza. Na kwa upande wa Amadu na Chui pia.







    Lakini Amadu na Chui walikuwa wataalamu wa giza. Muda wao waliokuwa wamejificha na kujifua huko misituni waliutumia pia kuenenda na mazingira ya giza, yasiyo na mwanga.







    Wanajua vema namna ya kukodoa na namna ya kutenda. Huu sasa ukawa muda wao wa kutumia ujuzi huo kumaliza mchezo.







    Mwanaume mmoja mmoja wa Sisawo akadakwa na kumalizwa kwa kunyongwa. Hakuna hata aliyepiga kelele hata zakuomba maji.







    Ndani ya dakika chache tu wakabakia wanaume wawili tu. Wote walikuwa upande wa kumtafuta Amadu.







    Mwanaume mmoja alisogelea kabisa eneo alilokuwa amejificha Amadu ila hakuwa ana hili wala lile.







    Mwanaume huyu alikuwa mrefu na mweusi, ila shati lake la ndani lilikuwa jeupe na ndilo hilo likamweka uchi kwa Amadu kumng'amua upesi.







    Alijikuta anasikia jambo ndani ya kichaka. Basi haraka akamiminia risasi za kutosha hapo akijua anamlenga adui.







    Kumbe Amadu alikuwa nyuma yake, na ndiye alimlaghai mwanaume huyo kwa kurusha kijiwe pembezoni.







    Kufumba na kufumbua, mwanaume huyo alistaajabu kusikia kishindo kizito nyuma yake. Alipogeuka alikula teke kavu lililomvunja taya na kumwagia chini.







    Haraka mwenzake wa pili akatokea. Akamimina risasi kumfuata Amadu.







    Amadu alijimwagia chini upesi akijiviringita na kupotea eneoni. Risasi ziliendelea kumiminika lakini hazikumpata abadani.







    Mwanaume wa Sisawo akiwa anabung'aa na bunduki yake mkononi, anahaha kusaka. Akavutwa mguu na kudondoshwa chini!







    Kabla hajabonyeza triga ya bunduki, akapewa ubapa wa mkono shingoni, akapooza. Mwili ulipigwa shoti ukapoteza nguvu kabisa.







    Ni macho tu ndiyo yalibakia hai wakati viungo vingine vikiwa mfu.







    Amadu akasimama na kumtazama mwanaume huyo akiwa tayari ameshabebelea bunduki yake.







    Punde tu Chui akaungana naye.







    "Salimia huko uendako, waambie tunasafisha jiji!" Amadu alisema kisha bunduki ikakohoa!





    ***

    ***





    *MLENGWA NAMBARI MOJA LIBERIA*





    Siku iliyofuata baada ya mauaji ya Sisawo.





    Baada ya Guinea na Sierra Leone, sasa ilikuwa zamu ya Liberia kutembelewa na THE GHOSTS.







    Ni usiku tena ndani ya jiji la Monrovia. Jiji ambalo halikupumzika toka kwenye mashambulizi ya mfululizo toka kwa kikundi cha AMAA.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Mpaka muda huu, Monrovia ilikuwa imeshuhudia milipuko minne iliyonyofoa roho za watu lukuki.







    Muda wowote sauti za milipuko zingeweza kusikika na isiwe tena kitu cha kushangaza. Ila kwasababu kifo hakizoeleki basi watu wangeangua kilio na kuwalilia ndugu zao.





    Serikali ilikuwa haina msaada tena. Al Saed alishakata tamaa baada ya kufanya kila jambo na kutofanikiwa.







    Alikosa hata msaada toka nje, hakuna taifa lililomshika mkono kwasababu ya kuingia kwake madarakani kinyume na demokrasia.







    Umoja wa mataifa ulikuwa unatoa tu matamko pasipo hatua yoyote kuonekana. Haikujulikana ni watu kiasi gani wakishakufa ndipo watachukua hatua.







    Kuna muda Al Saed alikuwa anajuta kuwa raisi. Hakuwahi kufurahia cheo hiki. Hakujua uchungu wake hapo kabla.







    Alitamani hata angeweza kubadili historia ajirudishe kwenye shughuli yake ya awali, ukulima.







    Alijua sasa ukosoaji ni mwepesi kuliko utendaji. Alipokuwapo nje alipata kukosoa mengi ya serikali na hata kufikia hatua ya kuunda kikundi cha uasi.







    Ila kwa sasa, anatamani kubwaga manyanga. Anaona ikulu chungu. Kila mara tumbo linamvuruga na kichwa kumuuma.







    Alishatayarisha mazingira ya kutorokea endapo mambo yakiwa magumu zaidi. Makazi hayo yalikuwapo huko Paris, Ufaransa.







    Ikiwa sasa ni saa nne usiku, ndani ya chumba kimoja cha hoteli ndogo ipatikanayo mpakani mwa jiji la Monrovia, mikakati ilikuwa inaandaliwa kwa ajili ya kummaliza Mr.X.







    Ndani ya chumba hicho walikuwepo watu wanne: Ulsher, Farah, Mou na Rasta, mwanaume yule aliyekula kiapo cha kuungana na Amadu ndani ya jiji la Freetown.







    Rasta zake zilikuwa fupi sasa. Mwili wake ulikuwa umetengemaa kwa mazoezi zaidi. Alifahamika na wenzake wa THE GHOSTS kwa jina la Ras Killer.







    Jina alilopewa na Farah pindi walipokuwa mazoezini baada ya kutambua na kuheshimu uwezo wa mwanaume huyo kwenye mauaji.







    Watu hawa walikuwa wametandaza ramani mezani, wote wakiwa wanaitazama na kupeana maelekezo.







    Ulsher ndiye aliyekuwa mtengeneza mipango na muelekezaji pia. Kidole chake kiligusa sana ramani akimgawia kila mtu majukumu yake.





    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Kazi haikuwa nyepesi kabisa. Na wao walilitambua hilo ndiyo maana hapa wakatumwa watu wanne.







    Si tu kwamba Mr. X alikuwa na ulinzi mkali, bali pia yeye mwenyewe ni mtu mwenye ujuzi na ufahamu mkubwa kwenye mambo ya ujasusi.







    Anajiweza kimapambano, ni mwepesi na mwenye maamuzi ya tija awapo kwenye uwanja wa vita.







    Sababu hizo ndizo zimemfanya amkoseshe amani bwana Al Saed. Asumbue Liberia nzima kwa mauaji yake. Na azidi kupata wafuasi zaidi waliotokewa kuvutwa na misimamo yake ya kidini.







    Sasa THE GHOSTS walikuwa washatambua wapi makazi yake yalipo. Japokuwa si mtu wa kukaa eneo moja, walijua kwa usiku huo alikuwa analala wapi.







    Zaidi, walijua ameambatana na walinzi wangapi na akiwa amejihifadhi chumba gani.







    Hii ilikuwa kazi nzuri sana ya Farah na Ulsher ambao walifanikiwa kuweka kidaka mawimbi kwenye usafiri apendao kuutumia Mr. X pasipo yeye kujua.







    Kidaka mawimbi hiki kikawasaidia kujua wapi alipo Mr.X na kwa wakati gani.







    Hivyo basi kazi yao sasa ikawa ni kufuatilia tu maeneo hayo elekezi na kuyapembua. Kujua kuna nini kipo karibu na mbali yake.







    Kujua njia ipi ya kuingilia na kutokea. Nyumba ipi wataitumia na ipi wataikimbia.







    Pia kuna idadi ya watu kiasi gani.







    Haya yote yatawafanya watengeneze mipango mathubuti. Ya uhakika na yasiyo na kubahatisha.







    "Kila kitu kipo sawa, si ndio?"akauliza Ulsher. Wote wakaitikia kila kitu kimeeleweka.







    Walikuwa wamevalia nguo za kijani zilizokamata maungo yao. Pamoja pia na kofia kapelo rangi nyeusi.







    Kwa ziada, Ulsher alikuwa amevalia miwani maalum ya kuonea nyakati za usiku.







    Kila mmoja alikuwa na bunduki yake ndogo. Ras Killer na Ulsher wao walikuwa wamevalia pia mabegi madogo meusi mgongoni.







    Wakatoka ndani ya hoteli na kugawanyika ila wote wakielekea upande wa kaskazini. Eneo waliokuwa wanaliendea ilikuwa ni kilomita moja na nusu tu mbeleni.







    Mazingira yalikuwa tulivu sana. Nyumba zilizokuwa zinapatikana maeneo hayo zilikuwa duni tu, chache za kueleweka na kuvutia.







    "Tumefika, mbele kuna wanaume wawili," Ulsher akawataarifu wenzake.







    Ajabu mwanamke huyu alikuwa amevalia khanga akijifunika gubigubi. Alikuwa anachechemea mguu wa kushoto uso wake akiuelekezea chini.







    Kutokana na giza lililokuwepo, na lile begi mgongoni lililofunikwa na khanga, bila shaka ugedhani mwanamke huyo ni bibi mwenye kibiyongo. Ombaomba tu.







    Alijisogeza karibu kabisa na wale wanaume pasipo kuzalisha shaka lolote. Wanaume hao walikuwa wamebebelea bunduki kubwa mikononi.







    Walitazamana kisha mmoja akapaza sauti:

    "We unaenda wapi?"







    Kufumba na kufumbua, Ulsher akanyanyua uso wake na kunyoosha mikono. Yote ilikuwa ina bunduki ndogo. Akafyatua risasi na kuwamaliza wanaume papo hapo!







    Risasi hizo hazikutoa sauti. Zilikuwa zimefungwa viwamba vya kumezea sauti.







    Punde baada ya Ulsher kumaliza hilo zoezi, anawataarifu wenzake:

    "Wawili wameenda: wamebakia nane. Naenda ndani, nahitaji backup."







    Jengo lilikuwa la ghorofa tatu. Mr.X alikuwa amejilaza kwenye sakafu ya juu kabisa. Chumba kilikuwa kimoja tu huko juu, kikubwa na kipana.







    Kwa haraka Ras Killer, Farah na Mou wakajongea mbele ya jengo kuungana na Ulsher. Ulsher akaonyesha ishara ya vidole vinne vikigawanyika kwa mbili.







    Tayari akawa ameeleweka. Farah na Mou walitakiwa wangoje pale mlangoni wakati Ulsher na Ras Killer wakitakiwa kupanda juu mpaka dirishani mwa chumba cha Mr.X.







    Farah na Mou watatakiwa waingie ndani na kushambulia punde tu watakapopewa taarifa na Ulsher, ama wakiona inahitajika kufanya hivyo.







    Mpango wa kwanza wa kumuua Mr. X ulikuwa ni kwa kutumia hewa ya sumu. Ikishindikana basi mpango mbadala itabidi uwekwe kazini.







    Ulsher na Ras Killer wakatoa kamba zenye vishikizi wakazirusha mpaka dirishani mwa chumba. Wakajivuta kwa kamba hizo upesi na kufika dirishani.







    Walipofika walitulia kwanza hapo kabla ya kufanya jambo. Lengo lilikuwa kusikilizia usalama kwanza.







    Chumba kilikuwa giza hivyo ikawa ngumu kujua kama kuna mtu ndani na yupo upande gani. Walinyamaza kusikia kama kuna mihangaiko yoyote.







    Kwa dakika kama tano, kimya.







    Ulsher akaweka kiganja chake kwenye kioo cha dirisha na kukisukumiza. Kilikuwa wazi. Alifungua taratibu sana kauwazi kadogo.







    Akatulia tena.







    Ras Killer akapeleka mkono wake kwenye begi na kutoa bomu la gesi. Akataka kumkabidhi Ulsher.







    Ulsher akatikisa kichwa chake na kumuonyeshea ishara. Muda bado.







    Mwanamke akatazama ndani, akapekua pekua mazingira. Hakuona mtu. Alistaajabu Mr.X angalikuwa upande gani.



    Alimtazama Ras Killer akampa ishara. Hamna mtu.







    Wakiwa hapo bado wanatazamana, mara wakasikia sauti ya kishindo cha mtu. Mara risasi tatu zikapiga dirisha!







    Haraka walitoka upande wa dirisha na kujibanza ukutani. Ulsher akatoa taarifa kwa wakina Farah, muda wa kuzama ndani sasa umewadia.







    Mr. X alikuwa macho. Na alikuwa tayari ameshagundua mchezo. Hivyo hakukuwa na namna nyingine sasa.







    Ilibidi aidha mpango wa kwanza ulazimishwe, au wa pili uingizwe.







    Risasi zilianza kurindima, huko chini Farah na Mou wakipambana na wafuasi wa Mr.X. Milio ilivuma na hata kuwaamsha waliokuwa karibu na maeneo hayo, ila hakuna aliyediriki kusogea.







    Ulsher alimpa ishara Ras Killer. Mwanaume akatupia bomu la gesi ndani ya chumba. Kama haitoshi, Ulsher naye akatupia la kwake humo ndani.







    Wakatoa vinyago vya kuziba hewa wakavivaa.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Punde wakasikia vishindo vya miguu na kisha sauti ya mlango unafunguka. Haraka wakajua Mr. X atakuwa ametoka chumbani. Na ataenda kuongeza nguvu ya mashambulizi dhidi ya Farah na Mou huko chini.







    Hivyo basi wakamalizia kubomoa dirisha Ras Killer akitumia nguvuze zisizo na mithili. Wakazama ndani.







    Kutazama huku na huko, hamna mtu! Chumba kilikuwa cheupe pe, basi haraka Ulsher na Ras wakasonga mbele na huku bunduki zao wamezionyeshea mbele. Huko chini, sauti za milio ya risasi zilikuwa zinarindima kwa fujo!



    Wakafika chini lakini hawakumkuta Mr. X, na Farah na Mou walikuwa wamajeruhiwa kwa risasi. Mou alikuwa amelala chini akiwa anahema kwa tabu, alikuwa ametobolewa kifua kwa ncha ya risasi, Farah yeye alikuwa amedunguliwa bega lake la kushoto lakini nao pia walikuwa wamewamaliza watu kadhaa wakiwa wamelala wafu kando.



    “Mr. X amekimbia!” Alisema Farah akinyooshea kule upande wake wa kushoto. Ulsher akamtaka Ras abaki kuwatazama majeruhi, yeye ataenda kushughulika na Mr. X.



    “Hakikisha unaweka presha za kutosha kwenye majeraha. Fanya pia mpango wa kumuwahisha matibabuni.”



    Ulsher akakimbia upesi kwenda kule alipoelekezwa. Kwa mbali akamwona Mr. X akiwa anayoyoma na basi akamhifadhi asije mtoka mipangoni. Akakimbia kwa kasi mno akijitahi kubana pumzi. Kadiri alivyokuwa anasonga, akawa anamkaribia mlengwa wake.



    Ila hakudumu na hilo, alipokata kona ya pili, ghafla Mr. X akapotea machoni mwake! Hakuonekana wapi alipoelekea. Mtaa ulikuwa kimya na hakukuwa na dalili zozote za mtu kukatiza.



    Ulsher akatazama kila pande, akarusha macho yake dirishani na milangoni mwa nyumba wastani zilizopo kwenye mazingira hayo, ila patupu. Taratibu, akiwa ameshika bunduki yake kwa ustadi, akasonga mbele, macho yake yakiangaza kana kwamba duma mawindoni.



    Mara akasikia kishindo cha mtu nyuma yake, upesi akageuka kuangaza, kurudisha uso wake mbele akakutana na ngumi nzito ya mwanaume ikambwagia chini! Bunduki ikarukia kando asiweze kuinyaka hata kwa kuunyoosha mkono.



    “Habari mrembo?” sauti ya nzito ya kiume ikapaza. Alikuwa ni Mr. X ndani ya kombati nyeusi, kichwa chake kikifunikwa na kofia nzito ya soksi iliyofunika masikio yake. Hakuwa na silaha yoyote pamoja naye.



    “Kwahiyo wewe ndiye wamekutuma uje kunimaliza?” akauliza kwa kabehi. “Watakuwa wamenidharau sana. Sasa wamaenitumia mpambanaji ama mke?” akaangua kicheko kilichoishia kwa kikohozi kikavu. Akamnyanyua Ulsher juu kwa mkono wake wa kuume.



    “Umeingia uwanja mbovu, mwanamama. Muda huu ulitakiwa kuwa chumbani na mumeo si mitaani.”



    Kumaliza kauli yake hiyo, upesi katika kasi ya umeme, Ulsher akadaka mkono wa kuume wa Mr. X kwa kutumia miguu, haraka akitumia uzito wa mwili wake, akambwaga Mr. X kwa njama za judo.



    Dharau hizi!



    Mr. X akanyanyuka kwa kujifyatua. Akakunja sura yake na kumsogelea Ulsher kwa pupa la hasira. Ulsher akajitutumua kurusha mateke na ngumi, ila hakufua dafu, Mr. X alikuwa mkamilifu kumzidi yeye kwenye uwanja wa mapambano, akamsulubu Ulsher kwa ngumi zake nzito na mateke ya kilo nene, Ulsher akawa hoi! Alilala chini akiwa anamimina damu mdomoni huku akihisi maumivu makali.



    “Hakuna wa kunizuia. Sijaona wa kunizuia. Na wewe utakuwa ujumbe mujarabu kwa hao waliokutuma!”



    Mr. X akamkandika Ulsher teke la tumbo, Ulsher akatapika damu akilalama kwa maumivu makali. Akataka kumshindilia teke lingine, Ulsher akawa mwerevu. Haraka akaunyaka mguu huo uliotaka kumwadhibu, alafu akafyatua miguu yake yote miwili kuufagia mguu wa Mr. X, akaudondosha mbuyu chini!



    Asilaze damu akaruka samasoti na kuinyaka bunduki, akamnyooshea Mr. X akimwamuru anyooshe mikono juu.



    “Fuata nitakachokuambia, la sivyo nitatia komo maisha yako!” Ulsher akawaka. Akawasiliana na wenzake na kisha akamtaka Mr. X aweke bayana yale yote atakayomuuliza, akiwa mkaidi atafyatua kitufe cha bunduki akasabahi jehanamu.



    “Nani yupo nyuma ya kikundi chako?!” Ulsher akawaka. Uso wake haukuwa na tone la utani. Mikono yake yote ilikuwa imeshikilia bunduki yake ndogo kwa ukakamavu.

    “Ni Allah!” akajibu Mr. X. “Ni Allah ndiye anafadhili kila kitu. Yeye ambaye tunamwabudu na kumtumikia.”



    Ulsher akapiga risasi mbili za mkupuo pembeni ya Mr. X! Mara mwanaume huyo akaanza kukohoa. Akakohoa mfululizo pasipo kukoma. Akashikilia kifua chake akikohoa mno. Kikohozi chake kilikuwa kikavu kikikwangua kifua. Ulsher akamsogelea akitaka kumjulia hali.



    Kufumba na kufumbua, Mr. X akampoka bunduki na kumtupia maili mbele kwa teke la kusinya! Kisha akaendelea kukohoa, huku akihangaika na kucheka, mkono wake wenye bunduki akimnyooshea Ulsher. Alipokoma kukohoa akafuta mdomo wake kwa mgongo wa kiganja, alafu akamwambia Ulsher huku akihangaika kuhema kwa nguvu.



    “Ok, muda wa kucheza sasa umeshakwisha tutaonana upande wa pili wa dunia!”



    Sauti ya risasi mbili ikavuma tah!-tah! Ulsher akatazama mwili wake akiwa ameachama akikagua ni wapi anavuja damu. Mara akamwona Mr. X akidondoka chini na bunduki yake. Kwa mbali akamwona Ras akiwa amebebelea bunduki, basi akajikuta anatabasamu.



    “Upo sawa?” Ras akauliza akiukagua mwili wa Mr. X.



    “Nipo sawa,” Ulsher akajibu asiamini anachokiongea.



    “Ameshakufa, twende zetu kabla muda haujatutupa mkono.”



    “Vipi Mou, anaendeleaje?”



    “Twende kwanza. Si salama kukaa hapa!”

    Wakaondoka zao wakiwa wameshakamilisha kazi waliyotumwa.





    ***





    Sierra Leone, Freetown. Saa kumi ya jioni.





    “Kila kitu tayari!” alisema mwanaume mmoja aliyevalia kanzu na baghalasia akimwambia Amadu aliyekutana naye mlangoni. Amadu akarudi ndani na kuwashtua wenzake: Chui, Farah, Rasta, Fredy, Thomas na Kone, kwa ishara ya kichwa, wote wakatoka ndani kasoro Ulsher na Rose.



    Wanawake hao walikuwa wamevalia kidesturi ya kiislamu wakihifadhi vichwa na miili yao. Walikuwa ndani ya nyumba duni yenye sebule ndogo ndaniye kulikuwa kuna vitu kadhaa; viti vilivyochoka, meza kuukuu na picha za kale.



    Huko nje watu walikuwa wengi, haswa wanaume, na wengi wao walikuwa wamevalia kanzu haswa nyeupe na za rangi ya kahawia. Watu wao kwa pamoja walijumuika wakashuka chini mpaka makaburini. Wote walikuwa wanaume.



    Dua ikasomwa na mwili ukahifadhiwa kule unapostahili, nyumba ya mwisho ya mwili wa binadamu, kisha watu wakatawanyika wakimuacha mfu yule ardhini peke yake.



    Baada ya nusu saa, THE GHOSTS, wakakutana nje ya makazi waliyofikia. Wakaketi nje wakiwa wamezunguka meza ndogo iliyokuwa imekaliwa na chupa za maji. Wakawa wanateta juu ya mustakabali wao.



    “Mou ametutoka. Mwanajeshi mmoja kaenda chini,” akasema Amadu. “Roho yake haijaenda bure, wala damu yake haijamwagikia mtoni, bali kwenye shamba la haki na uhuru. Hatutaweza kusahau mchango wake kamwe. Tangu mwanzo alikuwa nami, alikuwa nasi. Hakuwahi kuwa na shaka na mipango yetu, wala kusita kuitekeleza, hakika ni pengo kubwa kinywani.





    Na kwa kuenzi yale yote aliyoyafanya, hatuna budi kumaliza alichoshiriki kukianzisha. Kumaliza na kutekeleza yale yote yaliyokuwemo ndani ya makubaliano yetu. Bado tuna watu takribani ishirini wa kuwamaliza. Na ratiba ya kufanya hivyo itatolewa muda si mrefu, ikiambatana pia na watu watakaopewa majukumu hayo.”



    Baada ya maongezi hayo wakakubaliana pia kujipapasa mifuko na kutoa chochote walichonacho kama rambirambi. Lakini pia wakaazimia kujenga nyumba ya kisasa kwa ajili ya familia ya Mou.



    “Tutakutana siku mbili baada ya msiba kukoma,” Amadu akavunja kikao. Lakini kabla hawajatawanyika, wakasikia sauti za wanawake zikipiga yowe! Na mara sauti kali za risasi zikaanza kurururuma kwa fujo!



    “Tumevamiwa!” Kone akatamka kwa uhakika.



    Na kweli walikuwa wamevamiwa! Jeshi la Talib wakiambatana na magari manne na kifaru kimoja walikuwa wameshafika eneoni. Walikuwa wamebebelea bunduki ndefu zenye mijazo ya risasi za kumwaga. Walishajiandaa kwa vita.



    “Hakikisha hakuna anayetoka hai!” sauti ya Talib ikanguruma toka kwenye simu ya redio.



    “Ndio, mkuu!” akaitikia kamanda anayesimamia oparasheni. Alikuwa ameketi kando na dereva wa kifaru. Akabadilisha mawimbi na kuwapa maagizo vibaraka wake.



    “Zunguka eneo lote sasa, hakuna kumruhusu mtu yeyote kutoka, si mwanamke wala mtoto!”



    Magari yakajigawa na kuzunguka eneo lote. Wanajeshi wakashuka na kuamuru watu wote kukusanyika eneo moja wakiwa wamepiga magoti na kunyoosha mikono juu. Hakutakiwa yeyote kuonekana akiwa amesimama ama kutembea, labda kama amechoka pumzi yake!





    ****







    "Vipi? Umewaona?" Akauliza kamanda wa oparesheni.



    "Hapana, mkuu!" Akajibu mwanajeshi aliyetokea ubavu wa kulia wa nyumba akiwa amebebelea bunduki aina ya SMG.

    "Tafuteni! Tafuteni kote!" Kamanda akaamuru. Macho yake yalibeba ujumbe aliokuwa anaumaamisha. Basi watu watano wakajimega upesi na kusambaa kuangazaa, wakazama kwenye nyumba za karibu na wengine wakayatupa macho yao umbali mrefu kama wataona chochote kitu. Lakini mwisho wa siku wakarejea mikono mitupu!





    "Hawa lazima watakuwa wanafahamu!" Akasema Kamanda. Akamnyaka mwanamke mmoja na kumtupia mbele, akiwa amemnyooshea bunduki, akamkaripia:





    "Wenzenu wapo wapi?!"





    Mwanamke yule akiwa analia, akasema hajui. Hata akaapa. Machozi yalikuwa yanamtiririka na uso wake ulikuwa unatia huruma.





    "Sijui! Kweli sijui!"





    Kamanda yule akatishia kumshindilia risasi mwanamke huyo. Akawatazama na wale wananchi wengine akiwatishia wasipo sema basi atammaliza mwanamke yule mbele ya macho yao, lakini hakukuwa na kitu! Watu walikuwa wameinamisha nyuso zao chini kwa hofu. Wengine walikuwa wanamwaga machozi.





    Kamanda akaona zoezi lake halizai matunda, basi akawanyaka na watoto watatu akawaongezea pale mbele, akawalaza chini na kukoki bunduki yake na kisha akapaza sauti kuu akinyooshea mdomo wa bunduki kwenye kichwa cha mtoto mmoja wa kike, kwa makadirio mwenye miaka mitano.





    "Nitafunua ubongo wa mtoto huyu punde itakapofika namba tatu tu!"

    Mtoto huyu asiye na kosa alikuwa anamwaga machozi na makamasi. Hakuwa anajua kinachoendelea hapa lakini macho yake yalimjuza hali ni mbaya na inatisha! Kuona watu wazima wakilia na hata kuhofia, haikuwa kitu cha mazoea. Mkono mpana wa Kamanda ulikuwa umeminya mkono wake mwembamba kwa nguvu!





    Hata wenzake waliokuwa wamesimama kando, wakiwa wameshikiliwa na wanajeshi, nao walikuwa wanalia wakiita wazazi wao wawasaidie dhidi ya kikombe kile. Wakiwa ndani ya nguo zao kuukuu, wakatia huruma ambayo haikufua dafu kwa wanajeshi waliotumwa hapo kutenda kazi.





    "Moja!" Kamanda akahesabu. "Mbili! ... Tat ..."

    "Usimuue tafadhali!" Akasimama mwanaume mmoja mweusi aliyevalia shati la njano. Akaamriwa apige magoti chini upesi!





    "Ni wakina nani mnawataka?" Akaropoka mwanaume huyo. " ... mie nilikutana na watu fulani wakiwa wanakimbilia kusini. Sijui kama ndiyo hao mwawataka! Tunaomba msituue!"





    Kamanda akamuuliza mwanaume huyo juu ya idadi ya watu hao. Baada ya hapo akawaamuru watu wake waelekee huko upesi! Basi magari matatu yaliyopakia wanajeshi , nane kwa idadi, yakaanza safari haraka kwenda kusini.





    Wakatembea kwa umbali wa nusu na robo kilometa kabla hawajamuuliza mkulima mmoja juu ya watuhumiwa wao. Wakapata taarifa kuwa walionekana wakielekea magharibi mwa shamba lake.

    "Watakuwa wanaelekea kuikuta barabara ya lami!" Akasema mwanajeshi mmoja.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Lakini hawataweza kuwasaka watu wao kwa kutumia magari kwani iliwalazimu wazame ndani ya msitu kama walivyofanya watu wanaowasaka. Huenda pia watu hao wakawa wamejificha msituni humo.





    Wakashuka na kuanza kukimbia wakizama ndani ya msitu, wakitumia taarifa za watu waliokuwa wanawauliza njiani. Lakini kadiri walivyokuwa wakizama ndani ya msitu, watu wakawa hawaonekani tena. Sasa wakawa wanafanya kufuatilia alama za viatu, na ishara za kulala kwa majani.





    Baada ya muda mchache wakafika karibia na mtoni.





    "Itabidi tuvuke!" Akasema mmoja.

    "Hapana, ngoja kwanza ..." akatahadharisha mwingine. "Hawa watu hawajavuka mto!"

    "Umejuaje?"

    "Mbona hapa karibia na mto hatujaona tena alama zao za viatu na wakati ndiyo sehemu mbichi?"

    "Vipi kama zitakuwa zimefutwa na maji ya mto?"

    "Tokea kule?" Akanyooshea kidole kwenye kingo ya mbali ya mto.

    "Sasa?"

    "Ni aidha kushoto ama kulia kwetu ndipo wameelekea."





    Mara ghafla, umbali wa kama hatua thelathini kule ng'ambo ya mto, wakaona kitu kikubwa kama gogo kikitumbukia mtoni! Haraka wakanyooshea bunduki zao huko.





    Akili na macho yao yakakazia eneo hilo. Haikupita muda mrefu, kwa mbele kidogo, jiwe kubwa nalo likatumbukia mtoni! Sasa wanajeshi hawa wakawa wamekubaliana kuwa kutakuwa kuna jambo kule.





    Wakiwa kwenye buwazo hilo, kufumba na kumbua, mara wakashangaa wamevamiwa tokea nyuma na watu waliovalia majani.





    Hawakuwa na nafasi yoyote ya kupambana. Bunduki zikaangukia chini!







    ***







    "Mkuu, ni muda sasa umepita, wamekuambia kitu?" Akauliza mwanajeshi mmoja aliyemfuata Kamanda kwenye gari.





    Kamanda akafanya jitihada za mawasiliano na wanaume wake aliowatuma akitumia simu ya redio.

    "Tumekaa kwa muda mrefu sasa na hawa watu wasio na matumizi! Mpo wapi? Mmefanikisha? Ova!"

    "Tumefanikiwa, kamanda. Sasa tunarejea, ova!"





    Sauti ikamjibu na mara mawasiliano yakakatwa. Kamanda akatabasamu.

    "Hatimaye mambo yamekwisha!" Akaangua kicheko kikubwa akionyesha mpaka magego.







    ***







    "Kama ulivyosema, bado wapo ndani ya kijiji."





    "Nilijua hilo, sasa hatuwezi tukaondoka tukawaacha wananchi katika hali ile. Ni lazima tufanye kitu."





    "Yah! Inabidi tukawaokoe, na kuwamaliza wale mbwa waTalib!"





    "Ndio! Lakini inabidi tuwe na mpango, la sivyo tutaharibu kila kitu. Lazima wananchi wawe salama kwenye oparesheni hii!"





    "Ndio! Ni lazima tuhakikishe hilo."







    ***







    Ikapita robo saa.





    Kamanda ndani ya gari alikuwa tayari amesinzia. Mdomo wake alikuwa ameuachama kama shimo la mdako. Ndani ya gari alikuwa mwenyewe wakati wafuasi wake wakiwa wamesimama huko na wananchi wasio na hatia.





    "Piga magoti!" Mwanajeshi alimkaripia bibi mateka aliyekuwa anayumba kwa kuchoka miguu.





    "Tafadhali naomba nilale, miguu inaniuma sana mwanangu," akajitetea bibi yule akitazama kwa sura ya huruma. Macho yake yalikuwa mekundu, akionyesha ni mdhaifu.





    "Hakuna kulala!" Akakaripia mwanajeshi. "Nimesema piga magoti!"

    Bibi akajitahidi kupiga magoti akiwa anahangaika kwa kushindwa kuhimili. Mwanajeshi akakasirika, akapiga hatua zake kubwa kumfuata bibi huyo, lakini kabla hajamfanya kitu, akasikia sauti ikimuamuru:





    "Weka bunduki chini, nyosha mikono juu!"





    Kutazama, akamwona Amadu akiwa amemkaba Kamanda na kumminyia mdomo wa bunduki kichwani.

    "Wote weka silaha chini kabla sijatoboa kichwa cha bosi wenu!" Amadu akanguruma. Wanajeshi wale wakatazamana. Pengine walikuwa wanafikiria kufanya jambo. Lakini mara wenzake na Amadu wakatokea wakiwa wamewazingira na huku wakiwanyooshea bunduki. Basi hapo wakawa hawana namna bali kusalimu amri!





    Wakaweka silaha chini na kunyoosha makwapa.





    THE GHOSTS wakawaruhusu mateka kuondoka. Haraka watu hao wakapotea kana kwamba wanakimbizwa na chatu! THE GHOSTS wakawafunga kamba mateka wao na kuwapaki nyuma ya magari, wakaondoka nao!





    "Pengine mpango wetu wa kummaliza Talib unaweza ukawa mrahisi zaidi ya tulivyowaza," akasema Amadu.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Ni nini alikuwa anawaza? Ni wapi wanaelekea?









    ****



    MWISHO WA MSIMU WA PILI

    ENDELEA KUFUATILIA MSIMU WA TATU



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog