Search This Blog

Friday 18 November 2022

MKONO WA CHUMA - 3

 






Simulizi : Mkono Wa Chuma

Sehemu Ya Tatu (3)





Mishale ya jioni, BQ alikuwa akiingia katika guest nyingine iliyo mtaa wa saba kutoka pale alipokuwa hawali, alionekana amechoka sana, haikujulikana ni kipi kilichomchosha kwa muda huo.



BQ akaenda mapokezi na kuulizia chumba, akaambiwa kipo, akalipia na kisha wakaongozana na yule dada mhudumu mpaka katika kile chumba, BQ akaridhika baada ya kukiangalia kile chumba, kisha akatupa begi lake kitandani,



"mlango huo ni sehemu ya kujisaidia" Muhudumu aliongea huku akiuonesha mlango uliokuwa ndani ya kile chumba,



"sawa" BQ aliongea, na muhudumu akawa anataka kuondoka, ila macho yake yaliona kitu, katika lile begi dogo ambalo BQ alilitupia kitandani, Kuna zip ya mfuko wa nyuma haikufungwa vizuri, bastola ilionekana.

Yule Dada hakutaka kusema kitu, aliondoka kama hajaona kitu, BQ hakugundua kama yule muhudumu kuna kitu kaona.



Yule Dada muhudumu alienda moja kwa moja mpaka sehemu yake, kisha akatoa simu na kuwataharifu polisi juu ya kile alichokiona, akawaelezea polisi namna yule dada alivyo, kwa jinsi maelezo alivyoyatoa yule dada, polisi wakagundua huyo Dada ndio haswa wanayemtafuta.



Wakati hayo yakiendelea, BQ hakuwa na taarifa, alikuwa ndio kwanza ametoka kuoga, kisha akajika mafuta mwilini, akajitupa kitandani na kufungua begi lake, akatoa juisi kubwa na chakula kilichokuwa kimefungwa katika ujazo maalum, kisha akaanza kula bila wasiwasi wowote.



Alipomaliza kula aliingia bafuni na kunawa mikono, kisha akarudi na kutoa lap top yake, ila akasikia Kuna mtu akigonga mlango,



"nani?" BQ aliuliza kwa sauti,



"ni mimi Dada wa mapokezi, nataka nikuletee mashuka masafi" Sauti kutoka nje ilisikika, BQ alitaka kujibu haitaji mashuka kwa sasa, ila akaona acha tu amfungulie.



BQ akasogea mlangoni na kumfungulia, ila cha ajabu alikutana na polisi wakiwa na bunduki, walimvamia na kumpiga kikumbo akaanguka chini, kisha wakamdhibiti barabara. BQ hakuwa na ujanja hakuwa akiamini kile kilichokuwa kinamtokea kwa muda ule.........







"pekua kwenye hiki chumba na kwenye mabegi yake, muangalieni amebeba kithibitisho gani?" Polisi mmoja aliwaambia wenzake ambao kwa haraka sana wakaanza kupekua pekua katika kile chumba, ila hawakukuta kitu mule ndani, ila katika mabegi yale ya BQ, walikuta nguo, karatasi za mikataba, bastola mbili na begi moja lilikuwa na vipande vipande vingi vya chuma,



"hii ni nini?" Askari yule alimuuliza BQ huku akimuonesha lile begi lenye vipande vya chuma,



"sio kitu kibaya" BQ alijibu kwa upole, Ila alishtukia akipigwa kofi kali la shavu,



"ukiulizwa unatakiwa ujibu kulingana na swali, sio unajibu kienyeji kama unamjibu mama yako" Askari aliongea kwa ukali huku akimtazama BQ,



"Kumbe sheria ya nchi yenu inaruhusu kumpiga mtuhumiwa?" BQ aliuliza huku akimtazama yule askari kwa jicho la hasira,



"unajifanya unaijua sheria sana, kila siku unatembea na makaratasi yako ya mkataba ili upewe haki?" Askari aliuliza kwa dharau huku akitabasamu,



"mpelekeni kwenye gari, muda wake wa kuua watu hovyo, umekwisha" Askari aliongea kwa mamlaka kisha wenzake wakatii, wakamtoa BQ huku wakiwa wamemdhibiti haswa, wakampakia katika gari, na safari ya kwenda kituoni ikaanza, walimbeba na yule Dada wa guest kama shahidi wa kutoa maelezo.



********



Sajenti Minja alikuwa nyuma ya meza yake ndogo katika sebule yake, alikuwa akicheza game la mpira katika lap top yake. pembeni yake kulikuwa na sahani iliyoonekana ilikuwa na chakula muda mchache uliopita.



Wakati Sajenti Minja akiendelea kuchezea laptop yake, alihisi simu yake ikiunguruma katika mfuko wa kaptula yake aliyokuwa ameivaa muda huo, akapeleka mkono mfukoni na kuitoa simu yake, na kuangalia jina la mpigaji, alikuta ni mkuu wake,



"naam mkuu" Sajenti Minja aliongea mara baada ya kupokea simu,



"upo wapi Minja?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"nipo nyumbani mkuu" Sajenti Minja alijibu,



"Yule Dada mtuhumiwa amekamatwa jioni hii, polisi wapo eneo la tukio, kama unaweza nenda katika eneo la tukio, unaweza kuambulia chochote" Mkuu wa polisi aliongea,



"sawa mkuu, je ni eneo gani walipomkamatia?" Sajenti Minja aliuliza kisha mkuu wake akamuelekeza eneo ambapo BQ alikamatiwa.



Sajenti Minja akaingia chumbani na kuvaa fulana yake, kisha akatoka kwa mwendo wa haraka mpaka nje na kuingia katika gari yake, akaiondoa gari kwa kasi huku akimshukuru Mungu kwa namna alivyomtendea muujiza wa kumsaidia kupatikana kwa muarifu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya dakika ishirini, gari ya Sajenti Minja ilikuwa ikisimama mbele ya ile guest alipokamatiwa BQ, Sajenti Minja akatelemka na kukuta pako kimya kama hakuna tukio lolote baya lililotokea muda mchache uliopita.

Sajenti Minja akatelemka katika gari na kuingia mpaka katika Ile guest, akamkuta Dada wa mapokezi, Sajenti Minja akamsalimia, kisha akatoa kitambulisho na kumuonesha,



"lakini mimi sio mfanyakazi wa hapa, mimi nimeitwa mara moja kusimamia hapa mara baada ya mfanyakazi wa hapa kuchukuliwa na polisi" Dada aliyekuwepo mapokezi alijibu,,



"Polisi wameondoka na mtuhumiwa muda mrefu?" Sajenti Minja aliuliza,



"mimi sio mkadiriaji mzuri wa muda, ila nadhani wameondoka kama nusu saa iliyopita" Dada alijibu,



"sawa, nashukuru" Sajenti Minja aliongea huku akiondoka eneo lile, alihisi huenda wale polisi walioenda pale ni wa kituo kikuu, sasa na yeye akaamua aelekee huko katika kituo kikuu, na ndipo huko pia ofisi yake ilipo.



**************



Habari za kukamatwa kwa BQ zilimfikia rais, Rais alifurahia hiyo habari, ila kitu ambacho Rais hakuwa anakitaka ni BQ kufikishwa polisi, alihitaji BQ afe kabla hajafika polisi, hakutaka kumshirikisha mkuu wa polisi kuhusu jambo hilo.



Rais alichukua simu yake na kumtafuta yule kijana anayemtumia kwa mambo yake binafsi, simu iliita kwa muda mchache tu, kijana akapokea,



"naam muheshimiwa" Kijana aliongea baada ya kupokea simu,

"nimesikia yule binti amekamatwa?" Rais aliuliza,



"ndio, na hapa nipo kwenye boda boda naifuatilia hiyo gari ya polisi iliyombeba" Kijana alijibu,



"safi, sasa tafuta nafasi na uhakikishe kuwa unafanikisha kummaliza kabla gari haijafika kituoni" Rais alitoa maagizo,



"sawa, ila nahofia hawa polisi, endapo nitaamua kumuua huyu Dada, itabidi na polisi kadhaa nao wafe" Kijana alijibu kwa utulivu,



"hiyo usijali, cha muhimu ni kufanikisha tu kummaliza huyo Dada" Rais aliongea,



"sawa muheshimiwa, hilo nitatekeleza" Kijana aliongea kisha akakata simu.



Umbali uliokuwepo kati ya bodaboda aliyopanda Kijana yule na gari ya polisi, ni kama mita hamsini tu, ila alichokuwa anasubiri yule kijana ni nafasi tu, ila hakuweza kuipata kwa muda huo.



"ebu simamisha, nadhani nimefika" Kijana alimwambia yule dereva bodaboda, kisha dereva bodaboda akasimama, kijana akashuka na kuingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya elfu kumi, kisha akampatia yule dereva, hakusubiri chenji, akaanza kupiga hatua za haraka kwenda mbele huku akimuacha dereva bodaboda akishangaa kuachiwa hela yote, nae dereva bodaboda hakutaka kupoteza muda, akageuza pikipiki na kuondoka huku akiamini yule kijana amesahau chenji.



Yule kijana wa rais, baada ya kukimbia kwa sekunde chache, akatoa kitu kidogo mfukoni, kisha kwa nguvu sana akakirusha kile kitu kuelekea katika gari la polisi, kile kidubwasha kikaenda kunasa kwenye tairi la gari la polisi, kisha yule kijana akasimama na kuiacha ile gari ya polisi iendelee kutembea.



Wakati hayo yanatokea hakuna mtu yoyote aliyeweza kuona hayo matukio, hata polisi waliokuwa mbele na wengine upande wa nyuma kwenye bodi ya gari, ila ni mtu mmoja tu aliyekuwa akiona kila kitu, huyo mtu ni BQ, na aliweza kuona vizuri kwa sababu yeye aliwekwa upande wa mbele katika bodi, na alikuwa akitazama nyuma, na pia mkono wake mmoja wa kushoto ulifungwa pingu iliyoshikana na chuma za kwenye gari.



BQ aliona namna yule mtu alivyorusha kile kitu, hakubahatika kujua ni kitu gani, ila alihisi ni itakuwa ni kitu cha hatari, BQ akataka awaambie wale Askari kuhusu kile kitu, ila akaona atapuuzwa tu, sasa kitu alichokifikiria kwa wakati huo, ni kutaka kuleta vurugu, alijua kabisa hatoweza kuwamudu wake askari kwa sababu yeye kafungwa pingu, ila alichohitaji kufanya ni kuleta fujo tu ili gari lisimame na awaambie kuhusu kile kidubwasha alichokiona kikitupwa.



BQ alichukua mguu wake na kuubana mguu mmoja wa askari, kisha akauvuta na kufanya yule askari aanguke vibaya, wenzake wakataharuki, kwa ufundi mkubwa BQ akampiga askari mwingine teke, nae akaenda chini, tena huyu aliangukia chini ya gari kabisa, wale Askari wengine wakafanikiwa kumdhibiti BQ kwa kumpiga hovyo mwilini huku pia wakimtaka dereva asimamishe gari, dereva akasimamisha gari na kushuka.



Kipindi hicho yule kijana aliyetumwa na Rais alikuwa anafuatilia lile gari akiwa kwa umbali mrefu kidogo, kama mita mia mbili hivi, alivyoona kuna kama vurumai ndani ya gari, alihisi huenda yule mwanamke anafanya mbinu za kujiokoa, akaongeza mbio kidogo, ila akaona askari akianguka kutoka katika gari, hapo ndipo alipoanza kuziamini hisia zake, mara ghafla akaona gari ya polisi ikisimama. Kijana akasimama na kutoa kadude mfano wa remote, na kubonyeza, ukasikika mlipuko mdogo uliofanya lile gari la polisi kurushwa nje ya barabara na kutua ikiwa matairi yapo juu, askari wengine walijeruhiwa na wengine walipoteza yake, watu wachache waliokuwa eneo hilo nyakati hizo za usiku, walitimua mbio kunusuru maisha yao kutokana na ule mlipuko.

BQ hakuna aliyekuwa anajua hali yake, alikuwa yupo chini Ya bodi ya gari na askari kadhaa waliokuwa wamekandamizwa na gari. BQ alikuwa hajakandamizwa ila alikuwa na michubuko kadhaa mwilini, akawa anajaribu kujiondoa chini Ya gari ila pingu aliyofungwa ilikuwa ni kipingamizi kwake, akamvuta askari mmoja na kumpekua mfukoni, akabahatika kukuta ana ufunguo wa pingu, akauchukua na kujifungua kwa kutumia mdomo, kisha akaanza kujivuta kutoka chini ya gari, akajitahidi mpaka akafanikiwa, akavuta na mabegi yake, kisha akasimama na kuyavaa, hakujali watu wachache waliokuwa wakimtazama, kisha akageuka ili aondoke, hapo ndipo alipokutana na yule kijana wa Rais, alikuwa amesimama akimtazama,



"nipo hapa kwa ajili yako" Kijana aliongea kwa sauti kavu, BQ hakuielewa ile kauli,



"umekuja kuniokoa? Asante" BQ alijibu huku akilazimisha tabasamu,



"ndio, nifuate" Kijana alijibu na kuanza kuondoka, BQ bila kufikiria akaanza kumfuata huku akiamini yule mtu huenda ametumwa na kikosi chao kutoka urusi, BQ akaanza kumfuata. Yule mtu alikimbia kwa dakika ishirini huku BQ nae akiwa nyuma yake, waliongozana mpaka walipofika maeneo ya ufukweni mwa bahari,



"RKA" BQ aliita, hilo ni jina la Shirika lao la kijasusi, RKA ikiwa inasimama kama RUSSIA KILLER AGENT.



BQ aliita hivyo ikiwa ni kama alama yao ya kutambuana, ukitaka kumtambua mwenzako, unatakiwa umuite mara tatu, Yaani unapomuita mara mbili hatakiwi kuitika, ila mara ya tatu akiitika tu, ujue ni mwenzako.



"RKA" BQ aliita kwa mara ya pili baada ya kunyamaziwa mara ya kwanza, na hapo pia alikuwa na imani kubwa kabisa huyo ni mwenzake,



"RKA" BQ aliita kwa mara ya tatu huku wakiwa bado wanakimbia, ghafla yule kijana akasimama na kutabasamu, hakuongea kitu, hapo BQ akapata hofu kidogo, kwa maana unapomuita mwenzako "RKA" mara tatu, anatakiwa ajibu "AKR" yaani ile RKA anaigeuza, anaanza kuisoma kutoka mwisho kwenda mwanzo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

BQ akasimama huku hofu ikimtawala,



"wewe ni nani?" BQ aliuliza huku akimtazama yule kijana, kijana akapata kigugumizi kujibu,



"umetumwa kuniokoa?" BQ aliuliza lile swali alilomuuliza mwanzo mara baada ya kuhisi huyu sio mtu wa taasisi yao ya kijasusi,



"hapana, nimetumwa kukuua" Kijana alijibu huku akimsogelea BQ kwa mwendo wa taratibu, BQ akaona hakuna jinsi zaidi ya kujihami, BQ akapiga hatua moja nyuma na kuachia teke kali, yule kijana akainama, akaikusanya miguu ya BQ na kumbeba juu kisha akamtupa BQ chini kwa nguvu,



"unajaribu kupambana au unafanya kweli?" Kijana aliuliza kwa dharau huku akimtazama BQ



BQ akainuka kwa mtindo wa ajabu kabisa, kisha kwa kutumia ule mkono wake mmoja, alishika shati ya yule kijana na kumvutia kwake, kisha akampiga kifuti kikali cha mbavu, cha ajabu BQ akahisi maumivu kwenye goti, ni kama alipiga chuma vile, ila yule kijana alitabasamu, BQ akaanza kurudi nyuma, alishapata uoga wa kupambana na kijana huyo. Kijana alikuwa akitabasamu huku nae akimfuata BQ, BQ alirudi mpaka kwenye ukingo, na chini palikuwa parefu na kulikuwa na bahari, BQ akasimama,



"endelea kurudi" Kijana aliongea huku akiendelea kumsogelea BQ.



BQ akaangalia chini kule baharini, kisha akayavaa vizuri mabegi yake, alishaamua kuruka chini, aliamini yeye ni komando, akijirusha katika maji atatafuta tu njia ya kujiokoa.



Wakati BQ akiwaza hivyo, yule kijana nae akahisi BQ anataka kujitosa majini, kwa kasi ya hatari, kijana alitoa bastola na kumfyatulia BQ, risasi ikampiga BQ kifuani upande wa moyo, BQ akaganda huku akiwa ahamini kinachotokea, yule kijana akafyatua risasi ya pili, hii ilitua moja kwa moja kichwani kwa BQ, BQ akarushwa kutoka juu ya ukingo mpaka chini katika maji, umbali wa mita mia moja na hamsini, kutoka juu mpaka chini,.



Baada ya hapo, yule kijana akakimbilia mpaka ukingoni na kuutazama mwili wa BQ ukiwa unaelea kwa kuingia zaidi ndani ya kina kirefu cha bahari. Kijana nae akataka aruke ili aende baharini, shida yake ilikuwa ni kuipata ile mikataba tu, kwa maana kazi ya kwanza ya kumuua BQ ilikuwa imeshaisha. Kijana akaiweka bastola kiunoni, kisha akarudi nyuma ili ajitupe ndani ya maji,



"wewe muuaji, kwanini umemuua huyo Dada?" sauti toka nyuma ya yule kijana ilisikika, kijana akageuka kwa haraka, akakutana na mdomo wa bastola ukimtazama,



"Sajenti Minja" Kijana aliongea kwa sauti ndogo huku akionesha kukata tamaa..





"lala chini na uweke mikono nyuma" Sajenti Minja aliongea kwa sauti kubwa kidogo kwa maana waliachana umbali wa mita kama sitini hivi.



Yule kijana hakutaka kuyafuatiliza masharti ya Sajenti Minja, ndio kwanza aliichomoa bastola yake,



"kaja kuniaharibia tu utaratibu" Kijana aliongea huku akianza kupiga hatua kumuelekea Sajenti Minja, Sajenti Minja kuona hivyo akaamua kumlenga yule kijana risasi ya mguuni, ila cha ajabu risasi ililenga na kumfanya yule kijana asimame kuungalia mguu wake, kisha akatabasamu, alafu akaanza kwenda mbio kumuelekea Sajenti Minja huku akipiga risasi mfululizo, Sajenti Minja kuona hivyo, akalala chini na kubingirita ardhini, akaenda kukaa nyuma ya mwamba mkubwa huku akiendelea kusikiliza vishindo vya hatua za yule kijana, lakini hakusikia kitu, ukimya tu ulitawala, akasubiri kwa dakika tano nzima, lakini bado ukimya ulitalawa, akaamua achungulie, hakukuta mtu, akatoka kabisa katika ule mwamba huku akiangalia kushoto na kulia, pia hakuona mtu,



"fala huyu, atakuwa amekimbia tu" Sajenti Minja aliongea huku akielekea katika mwamba ule ulio ukingoni ambapo BQ alipigwa risasi, alipofika ukingoni akatupa macho yake baharini, akauona mwili wa BQ ukizidi kuyoyoma kwenye kina kirefu cha maji, Sajenti Minja akaona ni bora azunguke upande wa chini ili aingie mwenyewe ndani ya maji akautoe ule mwili.



Akashuka mpaka upande wa chini na kuingia ndani ya maji, akaanza kuyakata mawimbi, nae alikuwa ni fundi wa kuogelea. Sajenti Minja akazidi kusogea mbele huku akiwa hakati tamaa, alipofika umbali wa mita mia kutoka ulipo mwili wa BQ, alishuhudia kitu cha ajabu, aliona ule mwili ukizungushwa na maji kwa muda wa dakika nzima, kisha ule mwili ukazamishwa pamoja na mabegi yake, Sajenti minja akahisi huenda yule Dada ni mzima, sasa Sajenti Minja akaongeza kasi ya kuogelea, nae alipofika pale pale, akaanza kuzungushwa kwa kasi ya hatari, akaona anaweza kuzamishwa, akajitahidi kushindana na nguvu ya maji, mwisho wake akafanikiwa kujinasua eneo lile na kurudi nyuma,



"hapa itakuwa ni njia ya mto imepita" Sajenti Minja aliongea peke yake huku akipumua haraka haraka, na wakati huo huo alishuhudia begi moja la BQ likiibuka kwa juu, kisha likasukumwa na wimbi na kumsolegea Sajenti Minja, Sajenti Minja akalivuta na kuliweka mgongoni mwake, kisha akawa anasubiri kwa imani kuwa na mwili wa BQ nao utaibuka, alisubiri kwa saa nzima akiwa ndani ya maji, lakini hakuna kilichotokea, akaamua ampigie simu mkuu wake kwa lengo la kuongezewa nguvu zaidi, mkuu wake hakusita, akatuma askari wa doria za baharini.



Baada ya nusu saa wale Askari walikuwa eneo lile huku wakiwa na boti zao.



Sajenti Minja akawaelekeza kwa kuwaonesha eneo alipozamia yule Dada, askari wakamtaka na Sajenti Minja aingie ndani ya boti ili awapeleke eneo husika. Sajenti Minja akaingia, walienda mpaka katika lile eneo,



"hili eneo Kuna mkondo wa mto, ni ngumu boti kuingia hapa" Askari ambaye alikuwa dereva wa boti aliongea,



"nyie humu si ni waogeleaji? Zamieni mjaribu kumtafuta" Sajenti Minja aliongea,



"hapa mkuu ni kuhatarisha maisha tu, kuingia hapa na kutoka salama Haiwezekani, cha muhimu ni kuendelea kufanya doria eneo lote la bahari, huenda mwili wa huyo Dada unaweza kuibuka eneo jingine" Askari mwingine aliongea,



"sawa, nirudisheni nchi kavu, nyie endeleeni na ukaguzi mpaka asubuhi" Sajenti Minja aliongea huku akionekana hajaridhishwa na majibu aliyokuwa akipewa na wale Askari wa doria za baharini.



Ile boti ilimrudisha mpaka ng'ambo Sajenti Minja, kisha akawasisitiza wale Askari wakae mpaka asubuhi wakiutafuta mwili wa yule Dada, baada ya hapo Sajenti Minja akaondoka zake.



*******************



Yule kijana ambaye hutumiwa na Rais, aliondoka huku akiwa na hasira, hasira ya kushindwa kuipata ile mikataba, ambayo inaweza kuingiza hasara katika serikali.



Ingawa BQ alikuwa amekufa, ila bado mikataba iliitajika, kwa maana mikataba uwa inaishi miaka na miaka. Basi yule kijana baada ya kumkimbia Sajenti Minja, hakuondoka eneo lile, alitafuta upande mwingine uliopo mbali kidogo ila ambao unaweza kusimama na kuuona upande wa bahari ambao BQ alikuwa amezamishwa.



Basi yule kijana kwa kusimama eneo lile, aliweza kumshuhudia Sajenti Minja alivyokuwa anaogelea ili amuokoe BQ, pia aliweza kushuhudia lile tukio la BQ kuzamishwa na maji, ila kati ya matukio yote hayo, tukio lililompa furaha ni lile tukio la kuona eneo lile alipozamia BQ, Kuna begi liliibuka, akajua sasa inawezekana kule ndani ya lile begi kunaweza kuwa na mikataba anayoitaka yeye. Sasa wakati yule kijana akitaka kwenda chini kukabiliana na Sajenti Minja ili achukue lile begi, aliweza kuona boti ikija na askari, yule kijana ikambidi asitishe mpango wake, akawa anaangalia namna Sajenti Minja anavyoongea na wale Askari, akaona pia Sajenti Minja na wale Askari walivyoenda eneo lile alipozamia BQ na wao kushindwa kufanya chochote, na mwisho aliweza kumuona Sajenti Minja akiondoka kinyonge huku akiwa na begi lile la BQ. Yule kijana akaanza kumfuata Sajenti Minja, alimfuta mpaka katika lile eneo ambalo yule kijana aliilipua gari ya polisi na kukuta gari ikiwa bado umelala ila majeruhi walikuwa wameshaondolewa eneo la tukio.



Kijana aliweza kumuona Sajenti Minja akiongea na askari kadhaa kwa muda wa nusu saa, kisha akamuona Sajenti Minja akiingia katika gari na kuanza kuondoka, yule kijana akaanza kukimbia taratibu kuifuata gari ya Sajenti Minja, aliendelea kukimbia kwa kuachana kidogo na ile gari, cha ajabu huyu kijana hakuonekana kuchoka ingawa alikuwa anakimbia kwa kasi kulingana na mwendo wa gari.



Alizidi kukimbia na lile gari bila Sajenti Minja kujua kama anafuatiliwa. Baada ya saa zima ndipo Sajenti Minja aliweza kufika anapoishi, alishuka na kufungua geti, kisha akarudi katika gari na kuiingiza gari ndani ya geti, baada ya hapo alitelemka na kwenda kufunga geti, alafu akaelekea katika mlango wa mbele wa sebuleni na kuufungua, kisha akaingia. Alipoingia alienda moja kwa moja katika friji na kutoa maji ya baridi na kuyanywa.



Baada ya hapo akaelekea bafuni na kuvua zile nguo alizokuwa amezivaa, kwa maana zilikuwa zimeloana sana kutokana na kuingia nazo katika bahari kipindi alipotaka kwenda kuuokoa mwili wa BQ. Alipovua nguo aliamua kuoga kabisa.



Baada ya dakika chache, alitoka bafuni na kuelekea chumbani kwake, akavaa kaptula fupi na kurudi sebuleni.



"Yule jamaa aliyempiga risasi yule Dada, alikuwa ni nani? Na alimpiga kwa lengo gani? au huyu Dada ana ugomvi na upande mwingine tofauti na polisi na serikali?" Sajenti Minja alijiuliza maswali mfululizo huku ile taswira ya yule kijana wa rais ikimjia kichwani, kiukwei yeye hakumjua kama yule ni kijana wa rais, hakujua chochote kuhusu yule kijana.



Baada ya muda mrefu wa tafakari, Sajenti Minja akaichukua simu yake iliyokuwa pale mezani, kisha akaitafuta namba ya Tom na kumpigia, simu ikaanza kuita,



"upo wapi dogo?" Sajenti Minja aliuliza baada ya Tom kupokea simu,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"nipo hom, vipi Kaka?" Tom alihoji,



"kuna tukio baya sana limetokea muda mchache uliopita, tunaweza kuonana usiku huu?" Sajenti Minja aliuliza,



"ndio inawezekana, upo wapi kwani?! " Tom aliuliza,



"nipo nyumbani, ila wewe si hupajui? ngoja nije uko" Sajenti Minja aliongea,



"huku usije, we nielekeze tu, nitafika hapo" Tom aliongea,



"kwanini hutaki nije uko?! " Sajenti Minja aliuliza huku akicheka,



"utakuja siku nyingine, wewe nielekeze tu mimi nije uko" Tom alijibu,



"poa basi, we jiandae alafu nipigie simu, nitakuelekeza" Sajenti Minja aliongea,



"Hakuna shida bro" Tom alijibu na kukata simu. Sajenti Minja akainuka na kwenda kuwasha Runinga, aliamua kumsubiri Tom huku akiwa hapo hapo sebuleni.



****************



Wakati Sajenti Minja akiendelea ndani na mambo yake, huku nje yule kijana wa Rais alikuwa anaondoka baada ya kuyajua makazi ya Sajenti Minja. Yule kijana aliondoka kwa mwendo ule ule aliokuja nao, safari yake iliishia nje ya geti la ikulu, akasalimiana na walinzi, kisha akaruhusiwa kuingia, akamkuta Rais akiwa amekaa nje katika bustani,



"mkuu wa polisi amenipigia simu na kuniambia kuwa polisi wake wamejeruhiwa, pia mshtakiwa ametoroshwa" Rais aliongea huku akimtazama yule kijana,



"ndcho nilichofanya" Kijana alijibu,



"umefanikisha kumuua yule binti?" Rais aliuliza,



"ndio, nimemuua" Kijana alijibu huku akijikuna kichwa,



"mwili wake umeuweka wapi? na vipi kuhusu mikataba, umefanikiwa kuipata?" Rais aliendelea kuuliza,



"Yule binti nilimpiga risasi mbili, moja ya kifua upande wa kushoto, na nyingine ya kichwa, akaangukia baharini, sasa wakati nataka kwenda kule alipoangukia ili nikampekue katika mabegi yake, Kuna askari alitokea huku akiwa na silaha, na alinipiga mguuni, inanibidi nikimbie" Kijana alijibu,



"mjinga wewe, kwanini usingemmaliza huyo askari?" Rais aliuliza kwa hasira,



"mheshimiwa, si unajua mimi siwezi kuua mpaka unipe ruhusa?" Kijana aliuliza kwa upole,



"huyo askari ni wapi? nae ni miongoni mwa waliokuwa katika lile gari ulilolilipua?'" Rais aliuliza,



"hapana hakuwepo, ila yule askari mimi namfahamu, ni Sajenti Minja" Kijana alijibu,



"Sajenti Minja??? Ndio nani?!" Rais aliuliza,



"ni askari hodari aliyewahi kupeleleza kesi kadhaa zilizoleta matokeo chanya katika taifa letu" Kijana alijibu,



"kesi kama zipi?" Rais aliuliza,



"ile kesi ya memory card iliyobeba ajenda ya kupindua taifa, na ile kesi ya Tammy Semmy, rais aliyekuachia madaraka" Kijana alijibu kwa utulivu,



"Kwa hiyo huyo Minja ndio amepewa hii kesi tena?'" Rais aliuliza,



"ndio, jukumu la kuifuatilia hii kesi amepewa yeye, ila amekuwa kikwazo kwangu kwa leo, kwa maana nimeshindwa kuipata ile mikataba ingawa yule binti nimemuua" Kijana aliongea,



"kamuue Minja, si ulisema unaua ukiambiwa? Sasa nenda kammalize Minja, maana anaweza kuwa shida hapo mbeleni" Rais aliongea huku akijikuna kipara chake,



"Hakuna shida, hiyo kazi naenda kuifanya sasa hivi mheshimiwa" Kijana alijibu,



"sasa hivi? utampata wapi?!" Rais aliuliza,



"napajua anapokaa" Kijana alijibu,



"sawa kafanye hivyo, alafu kesho endelea kuutafuta ule mwili wa binti" Rais alitoa agizo,



"sawa mheshimiwa" Kijana alijibu,



"unaweza kwenda" Rais aliongea, kisha kijana akasimama na kuondoka.



*********



Sajenti Minja alikuwa bado yupo sebuleni, alikuwa akimsubiri Tom ambaye waliongea nae muda mchache uliopita na akamuelekeza namna ya kufika hapo nyumbani kwa Sajenti Minja.



Baada ya kama dakika tano, Sajenti Minja alisikia mlango wa sebuleni ukigongwa, akainuka huku akijua kuwa Tom amefika, ila alijiuliza mbona amekuja moja kwa moja kugonga mlango wa sebuleni, nani kamfungulia geti?



"au huenda nilisahau kufunga nilipoingiza gari?" Sajenti Minja alijiuliza huku akienda kufungua mlango wa sebuleni, hakuwa na wasiwasi kabisa, kwa maana aliamini nyumbani kwake ni eneo la amani kabisa. Sajenti Minja alipofikia mlango na kutaka kufungua, hata kabla mkono haujagusa kitasa, alishuhudia mlango ukichomoka mzima mzima kwa nguvu na kuja kumpiga, Sajenti akaanguka chini huku mlango ukimlalia kwa juu, akakurupuka huku akijiuliza ni nani aliyeingia kibabe hivyo? Sajenti Minja akainuka na kutupa macho mlangoni, hakukuta mtu, akapigwa na mshangao huku akijiuliza ni nini sasa kimetokea?



"nimetumwa kukuua" Sajenti Minja aliisikia hiyo Sauti ikitoka kwa nyuma yake na kumfanya ageuke kwa kasi, akakutana na mdomo wa bastola ukimuangalia, alipomtupia jicho mtu yule aliyemshikia bastola, akakumbuka, ni yule kijana waliyetoka kurushiana risasi masaa machache yaliyopita. Sajenti Minja akameza mate, ila mdomo ulikuwa umeshakauka muda mrefu tu, kwa hiyo hata hayo mate hayakuwepo mdomoni, na wakati huo yule kijana alikuwa akiikoti bastola yake huku akiwa hana sura ya ubinadamu hata kidogo......



Ila kabla yule kijana hajaruhusu risasi kutoka, Tom aliingia ghafla na yeye akakutana na hilo tukio, akataka kukimbia, yule kijana akarusha risasi iliyopiga chini pembeni kidogo ya mguu wa Tom, Tom akasimama ghafla kisha akadondoka chini kama mzigo, alipoteza fahamu baada ya risasi ile kumkosa, maana alipata mshtuko mkubwa, yeye alihisi imemkosa bahati mbaya, ila mpigaji mwenyewe ndio aliamua kupiga lile eneo makusudi, hakutaka kumpiga Tom.



Sasa Sajenti Minja akatumia mwanya huo kujitetea, akateleza akapita chini Ya meza ambapo kulikuwa na bastola ndogo, kisha akageuka na kumpiga yule kijana risasi nyingi za kifuani, ila alichoshangaa sasa, zile risasi zilikuwa zinatoboa shati tu la yule kijana na kuanguka chini, Sajenti Minja akapata hofu, akainuka na kwenda kujificha nyuma ya friji,



"mtu au robot?" Sajenti Minja alijiuliza huku akipumua haraka haraka, kisha akatoa kichwa ili amchungulie yule mtu, alipotoa tu kichwa, alikutana na risasi nyingi lakini hazikumpata, zote ziliishia katika friji, ila yule jamaa aliendelea kupiga mpaka bastola ikawa inapiga tu kelele ila haotoi risasi, hapo Sajenti Minja akaelewa sasa yule jamaa risasi zimemuishia, akawa anapanga atoke ili akimbie, kwa maana hakutaka tena kupambana na mtu ambaye risasi hazipiti katika mwili wake. Wakati Sajenti Minja akiwaza hayo, yule kijana yeye alikuwa anairudisha ile bastola katika mkanda wake, kisha akaichomoa bastola nyingine inayoitwa BROWNING HI POWER, hii ni bastola iliyotayarishwa na kuanza kutengenezwa na mtu mmoja aitwae John browning mnamo mwaka 1920, ila kabla hajaimaliza kutengeneza hii bastola, alifariki, kwa hiyo matengenezo yalimaliziwa na kampuni ya FN. Hii bastola ilitumika katika vita yote ya pili ya dunia.



sasa tuendelee na mkasa wetu, wakati yule kijana akiichomoa ile bastola, Sajenti Minja akachungulia tena, hapo ndipo alipoweza kumuona yule kijana akiwa anaikagua kama ile bastola ina risasi, Sajenti Minja alipoiona ile bastola, alishtuka, maana analijua balaa la ile bastola, maana risasi zake zilikuwa na uwezo wa kupenya hata katika ukuta mgumu, sembuse hiyo friji aliyojificha nyuma yake?

Sajenti Minja aliinama na kuishika friji kwa chini, aloposimama akainuka na ile friji, yule jamaa akashangaa kwa maana kilikuwa ni kitendo cha haraka sana. Wakati yule kijana akishangaa, alishuhudia ile friji ikirushwa kumuendea, kwa kuwa ilikuwa na kasi, akashindwa kuikwepa, ile friji ikamvaa mwilini na kwenda chini mzima mzima. Sajenti Minja akapata upenyo, akachomoka kwa kasi kuelekea nje na kumuacha yule jamaa akijiinua pale katika sakafu huku ile friji ikiwa pembeni yake. Alijiinua na kusimama, kisha akampita Tom ambaye bado alikuwa amepoteza fahamu, yupo chini.



Yule jamaa akatoka mpaka nje na kupepesa macho kushoto na kulia, kisha akapiga hatua kuelekea nje ya geti, alipotoka tu nje ya geti, alishika ile njia aliyokuja nayo na kuanza kuondoka kwa mwendo wa haraka haraka.



Tom alikuja kupata fahamu baadae sana, alipofungua macho, aliikuta hali ya kutisha pale sebuleni, vitu vilikuwa katika mazingira ya hovyo, alikuta maganda kadhaa ya risasi yakiwa yamezagaa chini. Tom akainuka na kupepesa macho kushoto na kulia, kisha akaona bora aondoke zake, hakutaka kujua hali ya Sajenti Minja, wala hakutaka kujua Sajenti Minja yupo wapi muda huo.



Tom alianza kuondoka kwa mwendo wa kukimbia, ila alipofika getini tu na gari ya polisi nayo ilikuwa inafika hapo nje ya geti,



"huu msala sasa" Tom alijisemea huku akisimama na hasijue atajiteteaje ili polisi wamuelewe.

Polisi wakatelemka kwa kasi, kisha wakamuelekezea mitutu Tom,



"lala chini" Askari mmoja aliongea kwa sauti kubwa, Tom akalala chini huku akijilaumu kwa kuukubali wito wa Sajenti Minja.



"wewe ni nani na unafanya nini kwenye nyumba ya watu?" Askari yule aliuliza huku akiwa anamkanyaga mgongoni Tom,



"muache huyo" Sajenti Minja aliongea huku akitelemka katika gari lile waliotelemka wale Askari wingine, Tom aliisikia sauti ya Sajenti Minja, akapata tumaini, aliona mtu pekee wa kusema ukweli ni Sajenti Minja.



"kwanini tumuache?" Askari mwingine aliuliza,



"wakati tukio linatokea, huyo nae alikuwepo ndani, alikuwa mgeni wangu" Sajenti Minja aliongea huku akimvuta mkono Tom ili ainuke, Tom akainuka huku akimshukuru Mungu kwa namna alivyomtendea wema muda huo.

"vipi, upo salama?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,

"mi mzima" Tom aliongea huku akijifuta vumbi lililomtapakaa baada ya kuangushwa na polisi,

"huyu jamaa aliyenivamia ulimuona wakati akitoka?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,



"bwana we, mimi nimezinduka nimejikuta nipo peke yangu, nimekuta sebule ipo hovyo hovyo, nilichoamua kufanya ni kuondoka mbio tu, ndio kwa bahati mmenikuta hapa mlangoni" Tom aliongea huku akiwatazama Askari wengine ambao nao walikuwa wakisikiliza maelezo yake,



"Mkuu hatujaona kitu chochote cha hatari zaidi ya maganda ya risasi tu, kwa hiyo unaweza kurudi tu ndani kuendelea na shughuli zako" Askari mmoja aliongea huku akitoka ndani kwa Sajenti Minja, na nyuma yake walikuwepo askari wengine watatu walioongozana nae,



"humu sikai tena, hapa nitaingia tu kubadili nguo, alafu nitapahama hapa kwa muda" Sajenti Minja aliongea huku akiingia ndani, na wale polisi walibaki nje wakimsubiri pamoja na Tom.



Sajenti Minja aliingia ndani kwake, akavaa surual na sweta jepesi, kisha akachukua simu zake na kuziweka mfukoni, akachukua pia lile begi la BQ aliloliopoa baharini, kisha akatoka mpaka nje ya nyumba yake na kuwakuta Askari wenzake wakimsubiri.



"sasa mkuu sisi tunaomba tuondoke, nadhani tumeshafanya ukaguzi wa hawali" Askari mmoja alimwambia Sajenti Minja,



"tunaondoka wote, itabidi mnisaidie kutafuta lodge moja tulivu ili nikae kwa muda, kwa maana hapa kwangu sio salama tena" Sajenti Minja aliongea,



"Mkuu si una usafiri wako, kwanini usiutumie huo" Askari aliuliza,

"hapa hakuna kitu ambacho naamini kipo salama, huenda hata yule bwana aliyenivamia ameacha mabomu humu" Sajenti Minja alijibu,



"sawa mkuu, twendeni jamani" Askari mwingine aliongea kisha Askari wakaingia katika gari walilokuja nao,

"Tom, ingia katika gari, bado nina maongezi na wewe" Sajenti Minja alimwambia Tom,



"aah, sawa" Tom alijibu na kwenda kurukia katika bodi ya land cruiser ya polisi, lakini aliteleza na kuanguka chini, polisi wakamcheka,



"mwanaume unatakiwa uwe mkakamavu, sio lazy lazy hivyo" Polisi mmoja alimwambia Tom ambaye alikuwa akiugulia maumivu chini, kisha akasimama kinyonge na kuingia katika gari, gari ikaondoka.



Gari ya polisi ilitembea mpaka nje ya hotel moja kubwa ya ghorofa, ikasimama, na kisha Sajenti Minja akatelemka,



"shuka Tom, tumefika" Sajenti Minja aliongea kisha Tom akashuka katika gari, Sajenti Minja akaagana na wenzake, kisha ile gari ya polisi ikaondoka.



Sajenti Minja alianza kupiga hatua kuelekea katika geti la Ile hotel, Tom alikuwa akimfuata kwa nyuma. Walifika getini na kueleza shida yao, wakaelekezwa sehemu ya mapokezi ilipo, wakanyoosha mpaka mapokezi, wakamkuta dada mmoja nadhifu akiwa amekaa ndani eneo moja zuri lililozungukwa na vioo na kuacha kanafasi kadogo kama dirisha kwa ajili ya kuwasiliana na wateja wanaofika hapo.



Sajenti Minja na Tom wakamsabahi mwanadada yule, nae akaitikia kwa uchangamfu, kwa kweli alijua kuchangamkia wateja,



"nahitaji chumba" Sajenti Minja aliongea mara baada ya salamu,



"chumba au vyumba? maana mpo wawili" Mwanadada aliuliza huku akitabasamu,

"chumba komoja tu, huyu amenisindikiza tu" Sajenti Minja alijibu kwa utulivu,

"sawa kaka, chumba utapata. Je unapenda by ghorofa ya juu, ya kati so chini?" Mwanadada aliuliza,



"chini, juu nitakuwa napata uvivu kupanda" Sajenti Minja alijibu na kumfanya yule mwanadada acheke,



"jina niandike nani?" Mwanadada aliuliza huku akipeleka vidole vyake katika vitufe vya kompyuta yake iliyopo mezani,



"Joel Minja" Sajenti Minja alijibu,



"nipatie na kitambulisho chako" Mwanadada aliongea huku akiandika jina, na wakati huo Sajenti Minja alitoa kitambulisho chake na kuweka katika kidirisha kile, mwanadada akakichukua na kukiangalia kwa muda,



"kumbe ni polisi?, bora uje utusaidie na kulinda" Mwanadada alimtania Sajenti Minja,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"hata usijali, nitakuja kukesha hapa na wewe ili tuimarishe ulinzi" Sajenti Minja nae aliongea kwa utani,



"chukueni funguo hii, lifti ile pale, mkifika ghorofa ya kwanza mtakuta wahudumu wamevaa sare kama nilizovaa mimi, uwape huu ufunguo, watakuongoza mpaka chumba husika" Mwanadada aliongea,



"ok, asante" Sajenti Minja aliongea na kuelekea katika lift huku Tom akiwa nyuma yake. Walifika ghorofa husika na kukuta wahudumu, wakawapa ile funguo, kisha wakaongozwa mpaka katika chumba husika, baada ya hapo muhudumu akaondoka na kuwaacha Tom na Sajenti Minja tu.



"kwa kuwa muda umeenda sana, ngoja nikueleze kitu ambacho niliikutia, na kwa bahati nzuri yule bwana aliyekuja kunivamia umemuona vizuri kabisa, sasa yule bwana usiku huu kabla hajanivamia, nilimkuta kule baharini akimpiga risasi yule dada kichaa anayetuhumiwa kwa mauaji ya vigogo wa serikali" Sajenti Minja aliongea na kumtazama Tom aliyekuwa makini kusikiliza,



"yule dada kichaa amepigwa risasi?" Tom aliuliza kwa mshangao,



"amepigwa bwana, na sidhani kama yupo hai tena, kwa maana alipelekwa na maji mpaka katika kina ambacho kuna muingiliano wa maji ya bahari na mto, ndipo akspotelea hapo. Sasa sijajua huyu jamaa ambaye amekuja kunishambulia, ana uhusiano gani na yule dada, na kwanini amuue, na pia kwanini atake kunidhuru na mimi?" Sajenti Minja aliuliza huku akijua fika kati yao hapo, hakuna mwenye jibu,



"alafu nimekumbuka, yule jamaa ndiye niliyemuona siku ile pale guest, ulipokuja na tukamkuta yule dada wa guest akiwa amekatwa mkono" Tom aliongea,



"kumbe ni huyu? sasa ni nani?" Sajenti Minja aliuliza,



"swali gumu hilo, ila sio mtu mzuri kabisa" Tom aliongea,



"sio mzuri kwangu, kama angekuwa mbaya kwako, angekuua pale kwangu, wewe si ulipoteza fahamu na bado hajakudhuru" Sajenti Minja aliongea,



"kweli, ila huyo jamaa unatakiwa nae umfuatilie kwa ukaribu" Tom aliongea,



"alafu cha kushangaza, yule jamaa huenda sio mtu wa kawaida, maana nimempiga risasi nyingi tu, ila sijakuta hata tone la damu, au unataka kuniambia risasi zote nilimkosa?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,



"sasa mimi nitajuaje kama ulimkosa au ulimpata?" Tom nae aliuliza,



"napata mashaka kuhusu mtu huyu, huenda sio mtu wa kawaida" Sajenti Minja aliongea,



"ndio hivyo, inapaswa umfuatilie kwa ukaribu" Tom alijibu,



"sawa, sasa wewe unaweza kwenda, nilitaka nikupe habari tu za yaliyojili leo uko baharini" Sajenti Minja aliongea,



"alafu hilo begi mbona kama la yule dada kichaa?" Tom aliuliza mara baada ya kuliona begi la BQ,



"ndio unaliona sasa hivi?" Sajenti Minja aliuliza huku akishangaa,



"nimeliona muda tu, nilikuwa natafuta muda sahihi wa kuuliza" Tom alijibu,



"ndio, hili begi ni la yule dada kichaa, liliibuliwa na maji baada ya yule dada kuzama, tena ngoja niangalie kilichopo ndani" Sajenti Minja aliongea huku akilifungua zipu lile begi, akamwaga vitu sakafuni, hakukuta kitu zaidi ya nguo tu.



"Kuna nguo tu" Sajenti Minja aliongea huku akifungua na zipu ndogo ndogo za pembeni, ambazo nazo hazikuwa na kitu.



"haya bwana, acha mimi niondoke, tutawasiliana zaidi" Tom aliongea huku akiinuka kitandani,.



"poa dogo, mimi hata sikutoi" Sajenti Minja aliongea,



"usijali " Tom aliongea huku akitoka nje na kumuacha Sajenti Minja akizirudisha nguo za BQ ndani ya begi.



******************



Ndani ya msitu mmoja wanaonekana watu wawili wenye umri wa makamo, mmoja ni mzungu na mwingine ni mtu mweusi.

Mzungu alikuwa na begi mgongoni na mkononi alikuwa na jembe dogo, wakati mswahili alikuwa na camera aliyeitundika shingoni, na mkononi alikuwa na karatasi kadhaa na katika mfuko wake wa shati alichomeka kalamu.



Walisogea mpaka eneo la mtoni, wakachutama na kuanza kunawa mikono na miguu. Wakiwa bado wanaendelea na zoezi lao hilo, waliweza kuona mabegi mawili yakiongozana ndani ya maji, wakashtuka,



"yatakuwa mabegi ya watalii nini?" Mzungu aliuliza huku akijaribu kuyazuia, lakini yule mswahili hakujibu, aliinua shingo na kutazama kule mabegi yanapotokea, hakuona kitu yalikuwa ni mabegi ya BQ, mara wakaona maji yakija na damu, hapo wakashtuka, maana huo mto una mamba wengi sana, wakatoka pale na kuanza kukimbia kule mabegi yalipotokea, baada ya dakika moja ya kukimbia, waliweza kuona kundi la mamba likishambulia kitu, mamba walikuwa wanagawana tu vipande vya nyama,



"ni mtu yule, atakuwa mtalii ameangukia mtoni" Mzungu aliongea kwa masikitiko wakati mswahili alikuwa bize akichukua picha za lile tukio.....



_____________

Wakati wakiendelea kutazama namna mamba wanavyogawana ridhiki yao, huku yule bwana mwingine akiwa bize na camera yake kuchukua matukio, ghafla aliiondoa camera machoni na kutupa macho pembezoni mwa mto, akapata mshangao,



"Dokta Smith, yule sio mtu kweli?" Yule bwana mswahili alimuuliza yule mzungu huku akionesha kwa kidole upande ule ambapo aliuona mwili wa mtu. Yule mzungu aitwae Dokta Smith, akatupa macho upande ule, akaweza kuuona mwili wa mwanamke ukiwa ufukweni katika mto, Dokta Smith ikabidi asogee mpaka lile eneo, maana sio rahisi kuwe na mtu wa kawaida eneo lile, tena mwanamke kuwepo katikati ya ule msitu wa kutisha.



Dokta Smith alipomsogelea, alimkuta yule binti akiwa amelalia tumbo, pua na mdomo vilikuwa chini, kwa hiyo hakuwa na uwezo wa kupumua, Dokta Smith akamgeuza kwa haraka, akaona ana tundu la risasi kichwani, akashtuka, ila haikumzuia kupeleka mkono wake katika kifua cha binti ili aangalie mapigo ya moyo ya yule dada, hakubahatika kusikia kitu, ikambidi aichane fulana aliyoivaa yule mdada na kumfanya kubaki maziwa yakiwa nje, aligundua kuwa kifuani kwa yule binti Kuna tundu jingine la risasi,



"huyu ni jangili nini amepigwa na Askari wa msituni?" Dokta Smith alijiuliza huku akipapasa tundu la risasi lililopo kifuani kwa yule dada,



"we mzungu unataka kufanya nini hapo? Mbona unampapasa maziwa huyo maiti?" Yule mswahili aliuliza huku akiwa mbali na eneo alilokuwa Dokta Smith,



"sogea ili uone ninachokifanya, huyu dada amepigwa risasi" Dokta Smith aliongea huku akipekeka sikio lake katika kifua cha yule dada, tena upande ambapo moyo unasadikiwa unakaa. Baada ya kupeleka sikio na kulikandamiza kwa nguvu kifuani kwa yule dada, aliweza kusikia mapigo ya moyo ya yule dada yakipiga kwa mbali, Dokta Smith akafungua begi lake na kutoa dawa ya maji na kumnywesha yule binti, kisha akambeba na kumuweka begani,



"beba yale mabegi, yatakuwa ni mabegi yake tu" Dokta Smith alimwambia mwenzake ambaye muda wote alikuwa na camera akichukua kila tukio na kisha alitumia muda mdogo kuandika katika karatasi yake.



"mhmmmm, huyu mzungu nae kwa kujipa majukumu, sasa ameokota mtu anamatundu ya risasi, yeye anabeba tu, hata kama Dokta sio kwa dizaini hii" Mswahili aliongea huku akielekea ule upande ambapo mabegi yalikuwepo, alipoyafikia aliinama na kuyabeba, kisha akafuata ile ile njia aliyoelekea Dokta Smith.



Alitembea kwa mwendo wa dakika kumi mpaka alipofika katika sehemu moja ambapo kulikuwa na uzio wa wavu ulioshikiliwa na vyuma vilivyochimbiwa chini, ule uzio wa wavu ulikuwa umezunguka hema moja kubwa lililokuwa katikati ya uzio ule.



Yule bwana Mswahili alipofika pale alifungua komeo na kisha akaingia ndani ya uzio, alafu akafunga mlango wa uzio kwa kutumia kufuri kabisa, kisha akaelekea katika hema na kumkuta Dokta Smith akiwa amemlaza yule binti ambaye hakuwa na mkono mmoja, na pia Dokta Smith alikuwa akitwanga mizizi ya miti, ambayo ile mizizi ilitoa maji ambayo aliyajaza katika kikombe na kumnywesha yule dada.



"huyo mzima kweli?" Mswahili aliuliza huku akimtupia jicho yule dada ambaye alikuwa hajitambui,



"anapumua kwa mbali, nadhani alizamishwa na maji, maana nilimkamua tumbo na ametapika maji mengi tu, sasa hapa nampa dawa ya kumuongezea nguvu, ili baadae nimuondoe hizo risasi" Dokta Smith aliongea huku akijaribu kumvua suruali yule dada,



"wewe bwana wewe, usimvue" Mswahili aliongea huku akimtazama yule dada kwa uchu,



"mwili wake unahitaji hewa ya kutosha kwa ajili ya kurejesha fahamu yake. Kama hutoweza kuvumilia nenda kakae nje tu" Dokta Smith aliongea huku akiwa ameshaitoa mwilini ile suruali ya dada, kisha akamtoa na nguo ya ndani, na kumuacha hapo, akatoka nje kuendelea na shughuli zake,



"na wewe toka uko ndani, huyo ni nusu mtu nusu mfu, usije ukaendekeza tamaa zako ukamuua bure binti wa watu" Dokta Smith alimwambia yule Mswahili,



"nenda uko, mimi sio mtu wa hivyo" Mswahili aliongea huku akitoka ndani ya hema.



**************



Asubuhi hii ilimkuta Sajenti Minja akiwa njiani akielekea kituo cha polisi, alipanga kuonana na mkuu wake, alitaka kumpa taarifa juu ya upelelezi wake ulipofikia.



Sajenti Minja alifika kituoni na kuelekea moja kwa moja mpaka katika ofisi ya mkuu wa polisi, akagonga mlango na kukaribishwa, akaingia na kutoa heshima kwa ukakamavu,



"kaa" Mkuu wa polisi aliongea kisha Sajenti Minja akakaa katika kiti,



"jana baada ya yule mwanamke mtuhumiwa kukamatwa, nasikia gari ya polisi ilipata ajali na kisha yule mwanamke akatoroka. Je ulifika eneo la tukio?" Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja, Sajenti Minja akakaa kimya kidogo kisha akamuangalia mkuu wa polisi, akakuta yupo bize na makabrasha yake yaliyopo juu ya meza,



"nilifika muda ule ule wakati ajali imetokea, ila nilichogundua ni kuwa ile ajali sio ya bahati mbaya, ni ajali iliyosababishwa na mtu" Sajenti Minja aliongea na kumfanya mkuu wa polisi amtupie jicho,



"kivipi?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"mimi nilifika wakati ajali ikitokea, ila baada ya ajali niliweza kumuona mwanaume mmoja akikimbia na yule dada mtuhumiwa, walikimbia mpaka eneo la ufukweni upande wa juu, mimi nilikuwa nawafuatilia tu. Walipofika pale ufukweni, walisimama na kuanza kuongea, sikuweza kuwasikia kwa kuwa nilikuwa mbali kidogo. Ila ghafla nilishuhudia yule kijana akichomoa bastola na kumuelekezea yule dada mtuhumiwa, nikiwa katika hali ya taharuki, niliweza kumshuhudia yule mwanaume akimpiga risasi ya kifua yule binti, papo hapo tena akampiga risasi ya kichwa, yule binti akaangukia baharini, na mimi nikajitokeza na kumtaka yule kijana ajisalimishe, lakini hakujisalimisha, akaanza kunishambulia, nikajificha nyuma ya mwamba, nilipoona milio ya risasi imepoa, nikachungulia, ila sijakuta mtu, nikatoka mbio mpaka katika eneo alipoangukia yule dada mtuhumiwa, nikamuona akielea ndani zaidi ya maji, ikabidi niingie baharini ili nimuokoe, ila sikufanikiwa, yule dada alizamishwa na maji, baada ya muda liliibuka hili begi tu" Sajenti Minja aliongea huku akilinyanyua lile begi la BQ,



"umelikagua hilo begi?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"Kuna nguo tu, sijabahatika kupata kitu kingine" Sajenti Minja alijibu,



"kwa hiyo huyo dada alikutoroka kwa mbinu hiyo?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"hapana hakunitoroka, ila atakuwa amekufa na amesombwa na maji, ni ngumu sana mtu kupigwa risasi ya kichwa na kupona" Sajenti Minja alijitetea,



"utasemaje amekufa wakati mwili bado haujapatikana? Kupigwa risasi ya kichwa sio sababu ya kufa. Unamfahamu 50 cent yule msanii wa marekani, alishawahi kupigwa risasi tisa, na nyingine zilimpiga kichwani, ila mpaka leo anaishi" Mkuu wa polisi aliongea,



"ni bahati sana kwa mtu kupigwa risasi na kuishi, ila siwezi kukataa husemi wako, kuwa nisiseme amekufa mpaka mwili wake upatikane" Sajenti Minja aliongea,



"sio husemi wangu, hiyo ndiyo kanuni ya kipelelezi" Mkuu wa polisi aliongea,



"sawa mkuu" Sajenti Minja aliongea,



"pia jana nimesikia umevamiwa usiku, na ulirushiana risasi na mtu" Mkuu wa polisi aliongea,



"ni kweli, na aliyenivamia ndio yule yule kijana aliyempiga risasi yule binti mtuhumiwa" Sajenti Minja alijibu na kumfanya mkuu wa polisi avue miwani na kumtazama,



"kwanini alikuvamia, hakukupa sababu?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"hakunipa, nadhani alikuja kuniua tu, hakuja kujadiliana" Sajenti Minja alijibu,



"pia nimesikia ulitumia risasi nyingi sana kupambana na huyo mtu, imekuwaje risasi zote zimemkosa?" Mkuu wa polisi aliendelea kuuliza,



"sio zote zimemkosa, asilimia themanini ya risasi nilizomrushia zilimpiga" Sajenti Minja alijibu na kumfanya mkuu wake ashangae,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"kama umempiga mbona hakupata jeraha na wala hakufa" Mkuu wa polisi aliuliza,



"Yule sio mtu wa kawaida" Sajenti Minja alijibu,



"ni mchawi? kumbuka sisi hatuamini katika hizo imani" Mkuu wa polisi aliuliza huku akiendelea kupekua makabrasha yake,



"sijasema ni mchawi, ila katika risasi zote nilizompiga, hakuna hata moja iliyopenya katika mwili wake" Sajenti Minja aliongea,



"kwa hiyo unataka kusemaje sasa?" Mkuu wa polisi alihoji,



"kwa sasa sina cha kasema, ila nitapofanikiwa kukutana nae tena, nitakuwa nimepata jibu" Sajenti Minja aliongea,



"ila sura ya huyo mwanaume si umeikariri?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"ndio, ingawa sio kwa asilimia mia" Sajenti Minja alijibu,



"ukitoka hapa pitia ofisi namba nane, utakutana na mchoraji, mpe maelezo ili amchore huyo mtu" Mkuu wa polisi aliongea,



"sawa mkuu" Sajenti Minja alijibu,



"vipi kuhusu kifo cha waziri wa katiba na sheria, umefikia wapi?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"na hilo pia nilitaka kulizungumzia, nilichogundua pia, kuwa kifo cha waziri wa katiba na sheria sio kazi ya yule dada mtuhumiwa, itakuwa ni kazi ya yule mwanaume aliyenivamia, kwa kuwa katika mwili wa waziri kulikuwa na matundu ya risasi, tena risasi zenyewe ni kama zile zilizofyatuliwa na yule jamaa aliyenivamia jana" Sajenti Minja aliongea,



"hiyo sio sababu ya kumuondoa huyo mwanamke mtuhumiwa katika katika kifo cha waziri, au labda kama ipo sababu nyungine" Mkuu wa polisi aliongea,



"ni hiyo tu, kwa maana nilifuatilia kuanzia kifo cha mkuu wa wilaya, kifo cha msaidizi wa mkuu wa wilaya, kifo cha mkuu wa mkoa na kifo cha naibu waziri, hakuna hata mmoja aliyepigwa risasi, wote wameuawa eidha kwa kukabwa au kushambuliwa kwa mkono tu" Sajenti Minja aliongea na kumfanya mkuu wake amuangalie huku akionesha hilo neno limemuingia,



"nenda katoe maelezo ya mchoro, kesho mapema ulete huo mchoro" Mkuu polisi aliongea na kumfanya Sajenti Minja ainuke na kutoka nje,



"huyu mzee bwana, mimi naongea yeye anapinga. Ananifundisha kazi??? sasa akaifanye yeye" Sajenti Minja aliongea huku akielekea katika ofisi namba nane, ofisi inayohusiana na mambo ya michoro.



************



Kule msituni, baada ya nusu saa ya kumuacha BQ dawa ifanye kazi mwilini, Dokta Smith alirudi ndani ya hema na kukagua yale matundu ya risasi, kisha akaenda mpaka katika sanduku lake kubwa lililotengenezwa kwa bati, akafungua na kutoa vifaa vipya kabisa via upasuaji, vilikuwa vifaa vya kisasa. Dokta Smith akavaa mipira mkononi, na kuusogelea mwili wa BQ, kisha akapeleka kisu katika kifua upande wa kushoto kabisa, na kupasua kidogo katika eneo ambalo risasi iliingia, kisha akaingiza kifaa kidogo chenye umbo kama la bikali, ila chenyewe hakikuwa na ncha kali.



Baada ya kuingiza kifaa kile, akakivuta juu, kikatoka na risasi, Dokta Smith akaiweka ile risasi katika mfuko mdogo wa nailoni, kisha akamshona BQ katika jeraha.



"umeshaanaza kumtoa risasi kumbe?" Mswahili aliongea huku akiingia ndani,



"ndio, nimeanza na hii ya kifuani kwa kuwa haikuwa eneo baya sana, ingawa ilichimba sana ila ilipita mbali na moyo" Dokta Smith aliongea huku akimalizia kushona jeraha la kifuani kwa BQ,



"sasa hiyo iliyoingia kichwani si ni hatari zaidi?" Mswahili alihoji huku akimtazana BQ ambaye alikuwa amelala bila fahamu,



"hii hatari kweli, ila haijaingia sana, huenda imepasua kidogo fuvu la kichwa, angekuwa mjini angefanyiwa x-ray ili kujua kama imeingia sana" Dokta Smith aliongea,



"sasa si tupeleke tu mjini?! " Mswahili alitoa pendekezo,



"hii risasi kuendelea kukaa kichwani ni hatari zaidi, kwa maana kuna risasi nyingine zina sumu, inavyozidi kukaa mwilini ndivyo inavyozidi kuhatarisha maisha" Dokta Smith aliongea,



"alafu katika mabegi yake hatukukagua" Mswahili aliongea huku akivuta begi moja na kulifungua, akakuta vipande vya vyuma vilivyotengenezwa katika umbo la mkono,



"huo ni mkono wake wa kutumia, si unaona hapa hana mkono mmoja?" Dokta Smith aliongea huku akimpora yule Mswahili ule mkono na kuanza kuuangalia yeye,



"sasa ndio unipore, we mzungu gani una mambo ya kiswahili" Mswahili aliongea kwa jazba huku akilichukua lile begi jingine na kulifungua, akatoa laptop ndogo na kuikagua kwa kuigeuza geuza, kisha akaweka pembeni na kuingiza tena mkono ndani ya begi, akatoa mfuko wa Rambo uliokuwa na karatasi ndani yake, akazitoa zile karatasi,



"hii mikataba" Mswahili aliongea huku akianza kuisoma,



"mikataba inahusu nini?" Dokta Smith aliuliza,



"sasa si ungoje nimalize kuisoma" Mswahili aliongea kisha akaendelea kuisoma, akashtuka baada ya kusoma jina la huyo mwanamke, kisha akasimama na kwenda kumuangalia vizuri,



"vipi?" Dokta Smith aliuliza baada ya kumuona mwenzake akimtazama kwa mashaka binti yule,



"ah hakuna kitu" Mswahili alijibu huku akiendelea kutazama, hata furaha aliyokuwa nayo hapo hawali ilipotea,



"Kuna nini kwani?" Dokta Smith aliuliza huku akiinyakua ile mikataba na kuanza kuisoma yeye, aliisoma kwa muda mchache tu,



"kumbe huyu mwanamke ana utajiri mkubwa? ndio maana umehamaki" Dokta Smith aliongea huku akiendekea kuisoma ile mikataba,



"tatizo sio utajiri, huyo mwanamke namjua vizuri, tena vizuri sana" Mswahili aliongea huku akielekea nje, hakuwa tena na amani kuanzia muda huo.



Dokta Smith akaamua amuache tu, akaona atamuuliza baadae kuwa amemjuaje huyo mwanamke.



Dokta Smith akaendelea na kazi, muda huu alikuwa anamtoa ile risasi ya kwenye kichwa, hii ilimchukua muda wa saa na nusu mpaka alipofanikiwa kumtoa ile risasi, kisha akamfunga bandeji.



Baada ya hapo Dokta Smith aliingia msituni kuendelea kutafuta mizizi na miti kwa ajili ya utafiti anaoufanya wa kutengeneza dawa.



*************



Mswahili tangu asome ile mikataba na kulijua jina la yule dada, alijikuta akiwaza sana, kwani anamfahamu vizuri yule dada, na isitoshe anajua kuwa yule dada alishakufa muda tu kutokana na ajali ya ndege, na mbaya zaidi anamfahamu fika ukatili wa huyo dada.



"huyu sio wa kuishi, ni wa kufa tu" Mswahili aliongea huku akiingia ndani ya hema, akapekua sanduku la Dokta Smith na kuchukua bomba la sindano, kisha akachukua kichupa kidogo cha dawa, kilichoandikwa pembeni "POISON" akaingiza sindano katika kile kichupa na kuivuta ile sumu, kisha akamsogelea BQ aliyekuwa amelala hajitambui, akamchoma ile sindano mkononi katika mshipa, na kuiminya ile dawa, kisha akalitupa lile bomba la sindano na kuirudisha ile sumu katika sanduku la Dokta Smith.



Baada ya hapo Mswahili akachukua camera yake na kuelekea msituni, alishatimiza adhma yake, sasa angalau alipata amani, maana tayari alishaua, aliamini amemuua mtu mbaya kabisa, amemuua kiumbe ambaye hastahili kuishi.

Ni kweli, BQ hakustahili kuishi tena.



Mswahili aliendelea na shughuli zake ndogo ndogo, huku kila muda akijipongeza kwa kutumia muda alioachwa peke yake kwa kumchoma sindano ya sumu yule mwanamke ambaye kwa maelezo yake alionekana anamjua fika yule mwanamke,



"alafu huyu BQ mbona amebadilika sana, au huyu sio yule mwenyewe, kwa maana mwenyewe alishakufa Katika ajali ya ndege" Mswahili alijiuliza mwenyewe bila kupata jibu kamili.



Baada ya saa moja, Dokta Smith alirejea na mizizi yake aliyotoka kuichimba, alipofika alimkuta yule bwana mswahili akiwa nje akikata nyama ya mnyama pori,



"wewe bwege ina maana hujatoka tangu muda ule?" Dokta Smith alimuuliza yule bwana Mswahili ambaye muda huo alikuwa akikinoa kisu kwa kukipitisha katika jiwe gumu la mlimani,



"ningetoka angekupikia mama yako? Mwendawazimu wewe" Mswahili alijibu na kumfanya Dokta Smith atabasamu, walishazoea kuishi katika maisha ya namna hiyo, utani, mizaa na matusi ya hapa na pale bila kuleteana kero.



Wakati Dokta Smith akiingia ndani ya hema, huku huyu Mswahili alikuwa hajiamini kabisa, alijua fika kuwa msala wa kifo cha yule binti ni lazima atapewa yeye,



"shauri yake bwana, hata nikisema nimemuua mimi atanipeleka wapi?" Mswahili aliongea mwenyewe huku akibinua midomo yake.



Wakati Mswahili akiwa katika mawazo hayo, uko ndani Dokta Smith aliingia na kumpima joto la mwili mgonjwa wake, akagundua joto lipo juu kiasi. Dokta Smith akachukua kitambaa na kukiloweka ndani ya sufuria yenye maji, kisha akaanza kumkanda BQ maeneo ya kichwani, alifanya hilo zoezi kwa dakika chache, kisha akaichukua ile mizizi aliyokuja nayo na kuichemsha. Ilipochemka katika kiwango anachotaka yeye, aliipua sufuria, kisha akamimina maji ya ile mizizi katika bakuri, akayapooza yale maji na kumnywesha BQ, kisha akatoka nje na kuungana na jamaa yake Mswahili.



"vipi hali ya mgonjwa?" Mswahili aliuliza,



"kidogo imeimarika, maana hata joto la mwili limeongezeka, tofauti na mwanzo, maana mwanzo alikuwa amepoa kabisa" Dokta Smith alijibu na kumfanya Mswahili ashangae, tena mshangao wa wazi kabisa, kwa maana alijiandaa kupokea habari za kifo, ila sasa anapokea habari tofauti,



"kwanini hafi jamani?" Mswahili aliuliza kwa jazba na kumfanya Dokta Smith amshangae,



"wewe mbona sikuelewi? tangu umezisoma zile katatasi za mikataba ya huyu dada, umeonekana kubadilika sana. Kwanini unamjuaje huyu dada?" Dokta Smith aliuliza huku akimuangalia rafiki yake huyo,



"ujue nini? yule Dada ndio BQ" Mswahili aliongea na kumtupia jicho Dokta Smith ambaye alikuwa bado hajamuelewa mwenzake,



"BQ? BQ ndo nini?" Dokta Smith aliuliza kwa mshangao,



"sio ndio nini, sema ndio nani?" Mswahili alimrekebisha mwenzake kisha akachukua chumvi katika kopo na kuipaka nyama aliyokuwa akiiandaa kwa ajili ya chakula,



"sawa, BQ ndio nani?" Dokta Smith ikabidi aulize kama alivyofundishwa,



"BQ alikuwa ni mlinzi binafsi wa rais aliyeondolewa madarakani, yaani Rais aliyepita kabla ya huyu, na ndio maana kama umesoma vyema ile mikataba, unaona walifanya na mtu aliyeitwa Tammy Semmy, ambaye ndiye huyo Rais aliyepita, ila wakati wakifanya hiyo mikataba, huyo Tammy Semmy alikuwa ni makamo wa Rais" Mswahili aliongea na kumuachia mwenzake nafasi ya kuuliza swali,

"sasa kwa maelezo yako hayo, ubaya wa huyu dada ni upi? maana hapo hawali ulisema huyu mwanamke ni mtu mbaya sana" Dokta Smith aliuliza,



"huyu dada ni elite killer, yaani muuaji wa kulipwa, kabla ya Tammy Semmy kulikuwa na Rais mwingine ambaye aliuawa, na aliyemuua ni huyu dada, ukimuondoa huyo Rais, pia Kuna watu wengi sana aliwaua" Mswahili aliongea na kumfanya Dokta Smith sasa ashtuke,



"kwa hiyo hafai ee?'' Dokta Smith aliuliza kwa hofu,



"hafai kabisa, sio mtu wa kumuachia aendelee kuishi, ndio maana nakushangaa kwa namna unavyoangaika kumtibu" Mswahili aliongea kwa uchungu,



"acha tu tumtibu, huwezi jua, huenda amebadilika au huenda hapendi kuua ila ni katika utafutaji tu wa ridhiki" Dokta Smith aliongea,



"endelea kumtetea, mpaka aje akuue wewe ndio utaona ubaya wake" Mswahili aliongea huku akiwasha moto katika kuni zilizokuwa katikati ya mafiga ya mawe,



"yote kheri, kama ataniua basi ujue ilipangwa iwe hivyo" Dokta Smith aliongea huku akiingia katika hema,



"shauri yako. Ukitoka utoke na wavu wa kuchomea nyama" Mswahili aliongea huku akiweka mafiga vuzuri, na muda huo jua lilikuwa limeshazama, giza ndio lilikuwa linaanza kutawala ndani ya msitu huo wa kutisha.



****************



Wakati hayo yakiwa yanajili, tunamuona yule kijana anayetumiwa na Rais akiwa na gari, alikuwa akielekea ikulu muda huo.



Alikuwa makini na barabara, sterling ya gari aliishikiria kwa nidhamu na mikono yake miwili ambayo ilikuwa ndani ya gloves, na katika kioo cha gari upande alikuwepo, alibandika picha ndogo iliyokuwa ikimuonesha mwanamke mmoja akiwa sura ya furaha akitembea na mtoto mdogo wa kike ambaye nae pia alikuwa na sura ya furaha. Yule kijana akapeleka mkono wa kulia katika ile picha na kuifuta kidogo, kisha akapeleka mkono machoni na kujifuta chozi lililokuwa likitiririka katika jicho lake la mkono wa kulia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Na muda huo gari yake ilikuwa mbele ya geti la ikulu, walinzi wakamfungulia geti, akaipitisha gari na kulipeleka moja kwa moja katika eneo la maegesho, akatelemka na kuelekea moja kwa moja katika ofisi ya Rais,



"vipi mambo?" Rais alimsalimia kijana, na wakati huo Rais alikuwa anajiangalia katika kioo huku akijifuta futa usoni na kitambaa,



"safi mkuu" Kijana alijibu,



"nilisikia umeshindwa kumuua yule askari?" Rais aliuliza,



"sikufanikiwa mkuu, nisamehe sana" Kijana alijibu,



"siku hizi misheni zako zinafeli sana, yule dada ulichukua muda mrefu sana kumkamata na kumuua, ingawa sina uhakika kama amekufa kweli. Huyo Askari wa jana umeshindwa tena kumuua" Rais aliongea huku akiwa hamuangalii yule kijana,



"ni kweli mkuu, ila nadhani ni makosa madogo tu niliyafanya mpaka yule Askari akapata upenyo wa kunitoroka" Kijana aliongea,



"sawa, nina kikao muda huu na wawekezaji, ngoja nikaongee nao, wewe tutaongea baadae" Rais aliongea huku akitengeneza kora ya shati lake la bluu bahari lililokuwa ndani ya koti la suti ya rangi nyeusi.



"sawa mkuu" Kijana alijibu kikakamavu,



"muda huu unaenda wapi?" Rais alimuuliza,



"nataka niingie karakana" Kijana alijibu na kumfanya Rais amuangalie kwa umakini kidogo,



"umepata tatizo?" Rais aliuliza,



"hapana, nataka nikakae tu" kijana alijibu na muda huo mlango wa ofisi ya Rais ulikuwa ukigongwa,



"ingia" Rais aliitikia ile hodi, ataingia binti mmoja mfanyakazi wa mule ikulu,



"Mkuu, muda umefika wa kwenda katika chumba cha mkutano, zimebaki dakika tatu tu" Binti aliongea huku akiwa amesimama kwa heshima mbele ya Rais. Rais akamgeukia kijana wake,



"baadae" Rais aliongea na kutoka nje, kisha yule kijana akafuatia kwa nyuma, ila yeye alitoka moja kwa moja mpaka nje, ataingia ndani ya gari lake, akaliondoa gari.



Alishika barabara mpaka katika nyumba moja kubwa iliyokuwa na uzio mrefu wa ukuta. Gari ilipofika katika geti, geti lilifunguka lenyewe, akaingiza gari kisha geti likajifunga lenyewe. Akatelemka katika gari na kuingia ndani ya nyumba yake, akapitiliza mpaka nyuma ya nyumba ambapo kulikuwa na nyumba nyingine ndogo ndogo. Akaingia ndani ya nyumba hiyo, ambayo ilikuwa na vyuma vingi vipya. Kijana akaenda katika mlango wa chumba kimoja na kuufungua, kisha akaingia. Katika kile chumba kulikuwa na kitanda kidogo cha chuma, na ukutani kulikuwa na kioo.



Kijana akaelekea katika kioo na kujiangalia, kisha akaziondoa gloves zake mikononi, cha ajabu mikono yake ilikuwa ya chuma, kisha akavua shati lake, ajabu nyingine ni kuwa kuanzia chini ya shingo, mwili wake wote ulikuwa chuma, alikuwa kama roboti, kijana akajiangalia kwa muda kisha akasikitika kwa huzuni, akachukua kifaa cha kufungulia nati na kupachika waya wa kile kifaa katika umeme, kisha akakaa chini na kukipeleka kile kifaa katika nati zilizokuwa ubavuni, akaanza kujifungua.



*************



Siku iliyofuata, muda wa saa mbili asubuhi, Sajenti Minja alikuwa hotelin pamoja Tom. Sajenti Minja alimuita Tom hilo eneo kwa lengo moja tu, kuja kuangalia mchoro wa taswira wa mtu anayedaiwa alimvamia Sajenti Minja, pia huyo huyo mtu ndio anadaiwa alimuua BQ.



Tom alikuwa makini akiiangalia ile picha,



"huyu ndiye yeye kabisa, mchoraji ana kipaji kikubwa sana" Tom aliongea huku akiendelea kuuangalia ule mchoro,



"kama na wewe umeridhika na huo mchoro, basi nadhani acha niende kituoni sasa, nikamuoneshe mkuu huu mchoro, maana yeye ndiye aliyetoa maagizo huu mchoro uchorwe jana, kisha leo nimpelekee" Sajenti Minja aliongea,



"basi sawa braza, wewe nenda tu, alafu ukipata muda tuwasiliane" Tom aliongea,



"tuwasiliane?, una habari mpya?! " Sajenti Minja alimuuliza Tom,



"kwani kuwasiliana mimi na wewe ni mpaka niwe na habari mpya bro?" Tom aliuliza huku akitabasamu,



"sawa basi. Hivi si bado hujapata kazi?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,



"bado braza" Tom alijibu,



"sawa basi, tutaongea baadae hilo suala, maana kukaa mjini bila kazi ni mtihani" Sajenti Minja aliongea,



"ila mshahara wangu unaingia, kwa maana kule wilayani nahesabika bado mfanyakazi" Tom aliongea,



"aah, kwa hiyo wewe ni mfanyakazi hewa?" Sajenti Minja aliuliza kwa utani huku akicheka,



"baadae bwana braza, nakuchelewesha tu hapa" Tom aliongea huku akitoka nje, kisha Sajenti Minja nae akatoka na kufunga mlango wa chumba hicho cha hotel. Sajenti Minja akatoka na kuchukua bajaj iliyomfikisha mpaka kituoni, kisha akashuka na kuelekea katika ofisi ya mkuu wake, alipoingia alitoa heshima,



"kaa chini" Mkuu wa polisi alimwambia Sajenti Minja, kisha Sajenti Minja akakaa katika kiti,



"mchoro unao?"Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja,



"ndio mkuu" Sajenti Minja alijibu huku akiutoa ule mchoro kutoka katika bahasha kubwa ya kaki, mkuu wa polisi akaupokea na kuukunjua ule mchoro, akauangalia kwa sekunde tu, akashtuka,



"huyu ndio huyo mtu aliyekushambulia juzi?" Mkuu wa polisi aliuliza kwa mshtuko,



"ndio huyu, pia ndiye aliyemuua yule dada mtuhumiwa wa mauaji" Sajenti Minja alijibu,



"haiwezekani" Mkuu wa polisi aliongea huku akitoa tabasamu la taharuki na kumfanya Sajenti Minja hasielewe ni kitu gani kinaendelea,



"kwanini isiwezekane mkuu?" Sajenti Minja aliuliza kwa mshangao,



"unamjua huyu?" Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja,



"hapana, ni nani kwani?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya mkuu wake ajikune kichwa huku akiwa bado ahamini kitu anachokiona katika ule mchoro, hapo Sajenti Minja akahisi kuchanganyikiwa zaidi baada ya kumuona mkuu wake akiwa hajihamini kabisa, kwa maana tangu ameanza kazi hapo, hiyo ni mara ya kwanza anashuhudia mkuu wa polisi akiwa amekosa amani kabisa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Minja, muda wowote nakuondoa kazini, naona hauna makini tena, huo mchoro sio wa mtu aliye hai, ni mchoro wa marehemu" Mkuu wa polisi aliongea kwa hasira na kuitupa ile picha mezani, Sajenti Minja akatoa macho ya mshangao, alikuwa bado ahamini kile anachokisikia kutoka kwa mkuu wake, ilikuwa ni habari mpya kwake, yaani mtu waliyepambana naye siku mbili nyuma, leo anaambiwa yule mtu ni marehemu, Sajenti Minja hakuamini, na wala hakutaka kuamini, ila ukweli ulikuwa ni ule alioushikiria mkuu wa polisi, kuwa yule mtu alishakufa siku nyingi tu, alikufa miaka mitatu iliyopita......









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog