Simulizi : Oktoba 15 Rais Anaenda Kufa
Sehemu Ya Tano (5)
Walitumia zaidi ya saa moja kujadiliana, walivyofika muafaka waliondoka mahali hapo kila mmoja akaelekea anakokufahamu. Siku iliyofuata tekelezo kuhusu walichojadiliana kikatekelezeka. Aisha, alijirekodi picha ya video kupitia simu akajibu tuhuma zote kisha akatuma mtandaoni. Walivyofikiwa wananchi hawakuacha kuunda makundi kama ilivyo ada kujadili zipi mbichi na mbivu. Makundi yaliyowakutanisha watu wenye itikadi tofauti, kila mmoja akipepea upande wake.
“Huyo hawezi husika, Rais kaamua tu kumchafua,” alisikika mwanaume mmoja aliye katikati ya kundi kubwa la watu waliokuwa wanacheza bao.
“Una uhakika? Ama nawe unaongea sababu itikadi yako ipo tofauti na mheshimiwa Rais?”
“Ninao uhakika. Si mumemsikia mwenyewe alivyoongea?”
“Haa! Kuongea sio kigezo. Ndugu, kabla hujatamka jambo kuchangia huu mjadala, yakupaswa uwe na utambuzi, kuwa sisi sote ni binadamu si malaika. Binadamu hatujakamilika, hivyo kukosea kwetu ni jambo la kawaida.”
“Una maanisha nini?”
“Maana yangu ni kwamba, hata huyo unayomuamini, naye ni binadamu, hajakamilika, yapo anayokosea.”
“Nawe acha siasa zako.”
“Siasa, ndiyo hukawiza maendeleo ya taifa letu.”
“Nani kakuambia? Vitu vingapi vimefanywa na serikali…”
“Acha kufumbwa macho na vitu vichache visivyokugusa. Ama nawe ni mmoja miongoni mwa washabiki wa chama cha wafanyakazi nchini Gundu wanaokesha kufurahia wapinzani walioshika nafasi za kuwatumikia wananchi kuhamia chamani kwao kisha siku za baadaye hurudia uchaguzi utumiao gharama kubwa, na kusahau adha iwakumbayo mara kwa mara ya kupoteza ndugu wengi kwa sababu ya uzembe wa kutokarabati eneo korofi lisababishalo ajali?”
“Huna jipya wewe? Hayo si maamuzi ya mtu?”
“Na vipi kuhusu maamuzi ya serikali kwa wananchi wake? Ama umesahau wiki iliyopita ulipoteza ndugu kwenye kituo chetu cha afya sababu ya ukosefu wa vidonge viwili vya dawa? Ambavyo kiongozi wa serikali ahusikaye na idara ya afya alikataa kuvileta kisa kiongozi wetu wa kundi pinzani alitoa ombi kwa kutanguliza maneno ya kumdhihaki?”
“Aaaah!...usilete mambo yaliyopitwa na wakati hapa.”
Mvutano huo ukajenga matabaka, baina ya wananchi na viongozi pia. Siasa ikaanza gawanya taifa. Kutokana na kila pande kujiona inastahili aminiwa kwa kila jambo lifanyalo. Hakuna walio radhi kujishusha, ama kuonekana wana makosa juu ya mambo mengine watendayo. Viongozi wa kundi tawala walijiona watiifu na wale wa kundi pinzani pia. Tena hawa ndiyo walizidi, kwa kujimilikisha utiifu wa kutotenda chembe ya ovu katika nafasi zao za uongozi. Siasa ikaanza hiaribu Mangaka, miradi mbalimbali ya maendeleo ilizinduliwa kikada. Mpango wa mradi uvumbuliwao na pande pinzani hukutoa nafasi kwa kiongozi wa serikali, waliamini kufanya hivyo kutaipatia sifa serikali badala ya pande hiyo. Na wale wa kundi tawala wavumbuapo mpango wa mradi huruka ruka mithili wametumia jitihada binafsi. Ile kauli ya nimelifanyia nini taifa langu hapa haikuwepo. Iliyotawala ni ile nitapata sifa kiasi gani kwa jamii endapo nikifanya mpango huu. Ama nichangie mradi huu halafu nigeuke upande wa pili nikachukue rasilimali ile.
Itikadi hizo zilijengwa haswa haswa na viongozi wa chini. Na ndiyo daima huchafua hali ya hewa kwa lengo la kujikomba kwa mkuu. Walichanganya wananchi kwa maneno mengi yasiyo na msingi
Haya yote yakamchafua Rais Mlunji. Ndani na nje ya taifa. Japo itikadi yake ya kweli iliyopo moyoni haikubainika kwa wakati huo, sababu hajatuliana kutumikia mamlaka aliyonayo.
“Yanipasa kuachia ngazi,” alijisemeza. Jioni moja alivyoketi Ikulu akiangalia kipindi runingani kiitwacho, tuitafute siasa ya kweli kwa maendeleo ya taifa letu. Wageni waalikwa wakiwa ni Aisha, na Mzee Bandubandu, aliyejivika jina la Mwanaharakati wa mkoloni.
“…ila kabla sijalifanya tukio hilo, lazima nihakikishe wale wote wenye nia ovu nami wanaingia mikononi mwa dola,” aliendelea kujisemeza.
****
Siku za mbeleni, baada ya kuzidi kuandamwa kwa maneno toka kwa vijana wa kundi tawala, marais wastaafu, pamoja na wale vijana wao walijiunga rasmi na kundi pinzani. Aisha, Kanali mstaafu Faidha, Kapteni Maguta na Wambili. Hata mafichoni walikoweka makazi yao muda mwingi walijitoa, wakaanza jionyesha waziwazi sambamba na uonyeshaji wa misimamo yao na mitazamo waliyonayo katika kufikia lengo la kusongesha mbele taifa lao.
“Tumeamua kujiengua kule, baada ya kutupa tuhuma nyingi zisizotuhusu. Kashindwa kujitetea, matokeo yake anatuangushia mpira. Laiti ingelikuwa sisi ndiyo wahusika, hayo mambo si yangelibainika kipindi cha nyuma kabla ya utawala wake?”
“Sahihi. Ila madai yao, wanadai mliwatumia watu kujificha. Mnasemaje kuhusu hilo?”
“Haiwezekani. Huyo mtu tuliyomtumia hajitambui? Kaona mpango mbaya, atakubali vipi? Tena mtu wa Mungu.”
Yalikuwa maongezi baina ya mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga mjini Lidede, alivyowaita wastaafu wa urais kuwahoji juu ya tuhuma walizohusishwa nazo.
Tukio lao, la kuhama kundi likaua sintofahamu kubwa kwa jamii. Werevu wakalichambua kwa namna yao na wale mazuzu pia. Ila wengi walijaa upande wa kufurahia, hasa watu wa kundi pinzani, wakiamini kitendo hicho kitawapa ushindi wa kutwaa nafasi wanayoigombania siku zote. Kutawala nchi. Tena waliwatunuku nafasi kubwakubwa, za kushiriki hadi vikao vya siri vya kundi husika. Ambalo ni Maliga. Pindi wanachama na wengineo wanafurahia kuhamia kwao. Wenyewe walikuwa na mpango mkakati binafsi wenye lengo la kujinufaisha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapa tusha—win, akijifanya kuanzisha upya uchunguzi wake kuhusu ule mradi, tuna watu wengi wataobeba utetezi wetu,” alisema Rais mstaafu, Prof. Kadenge, walivyokutana kwa siri na wenziye usiku wa manane nyumbani kwake.
“Yeah! Maana wanachama wetu hawatokuwa radhi kukubaliana nacho, pia watajaa moyo wa hasira utaosababishwa na hisia za kuona tunaonewa kwa sababu tumehamia upinzani,” mwingine alichangia.
“Huu mpango tumeucheza. Tena vya kutosha, kwani tukishafanikiwa kusimama kwa hili, tunarudi tena kuhitaji kusimama kwa mara nyingine katika mpango wa kumuondoa huyu mtu madarakani, kisha mmoja wetu lazima, arejee madarakani.”
“Hahahaaaaa...” wakacheka.
“Mmmmh! Mpango juu ya mpango.”
“Sahihi! Awamu hii lazima tufanikiwe kwa namna yoyote. Ileile tarehe tuliyofeli mwanzo, itatumika kwa mara nyingine kumuondoa. Madarakani na duniani kwa ujumla.”
****
Rais Mlunji alirejea kwenye nafasi yake, ila si kwa furaha. Kashfa iliyomkumba ilimuumiza sana. Muda mwingi alitekeleza majukumu yake basi tu, nafsi ilikuwa hairidhii hata kidogo. Tamanio lake lilikuwa kuondoka tu madarakani, ili kutoa wasaa mzuri kwa wananchi wamchukue mtu wanayemhitaji awaongoze. Siku za mbeleni akafanya mabadiliko, ya viongozi mbalimbali wa idara za ulinzi na usalama. Safu ya wakuu wa idara hizo alimbakiza Mkuu wa majeshi pekee, wengine wote aliwaondoa. Kitendo hicho kilichangiwa kwa kiasi kikubwa, Mkurugenzi wa usalama wa taifa, Kanali mstaafu Faidha Mwembere, kukimbia idara na kujiunga na upinzani baada ya kuhisi atashtukiwa mienendo yake mibaya aliyoifanya. Sehemu kubwa ya ushauri wake, ikawa kwa mama Tausi, James na Magreth Okuku, ambaye alionana naye Ikulu baada ya kutoka kwenye maadhimisho ya kusherehekea siku ya uhuru wa taifa lao.
Kila jambo lililomtatiza alikutana na hawa kujadiliana ndipo hulitekeleza. Na maamuzi mengine ayachukuayo yasiyosumbua akili yake hupitia kwa hawa pia. Hata Kitendo cha kuridhia kuondoka madarakani aliwashirikisha. Baada ya kuwaeleza kwa kina msukumo wa moyo wake ulivyo, na maono ya wananchi.
“Sisi binadamu, si wakuaminiwa. Tatizo letu huwa ni vigeugeu. Leo tutaongea ama tutafanya hiki, kikienda vibaya huangusha lawama ilhali kulikuwa na maridhiano katika kuchukua hatua za utekelezaji wa hicho kitu,” alisema Rais Mlunji, alivyokutana nao usiku mwingi, uliotanda kiza kizito Ikulu.
“Una maanisha nini mheshimiwa?” aliuliza mama Tausi.
“Yale maamuzi yaliyoandikwa kwenye hotuba, ndiyo maamuzi sahihi kwangu. Ule mpango, bado upo akilini, lazima nijiuzulu. Ili niwaache wananchi huru, kwani likija tokea jambo lingine baya zaidi ya hili lisilotarajiwa, nitageuzwa zaidi ya mkosaji.”
“Ila siku hizi unaanza kukubalika, sasa kwanini unabaki na ung’ang’anizi wa jambo hilohilo?”
“Natakiwa nijifunze kwa wale wanaonichukia. Si hawa wanipendao. Kwani wale ndiyo watanipa dira sahihi ya sehemu ipi niko vibaya.”
“Sawa…tukutakie heri, na kukuhakikishia utekelezaji bora wa kuitafuta amani ya moyo kupitia watangulizi wako.”
“Nawaaminia. Nina hakika hamtoniangusha, na katika hili, najifunza kupitia msukumo uliopo moyoni mwangu.”
Wakati huo, bado James alikuwa anajionyesha onyesha kwa nadra. Lengo, asiwe sehemu ya muendelezo wa matendo washupaliayo wananchi kumchafua Rais Mlunji. Endapo watabainika wakiwa pamoja, watamsema, kuwa analinda wahusika wa uhalifu. Hivyo kuonana kwao, wakawa wanaonana usiku, mchana, hujificha sehemu, akiambatana na Magreth kuratibu mipango ya kumsafisha Rais. Achilia mbali wao. Kikosi kazi nacho, kikapatiwa jukumu la kuhakikisha wanawafuatilia kiundani wale wastaafu na timu yao, sambamba kabisa na kuwachukulia hatua kali za kisheria watapobainika kukosea.
Hatua ya kwanza, ambayo ilikubalika kwa wote, watu hao wafunguliwe mashtaka. Ya uhujumu uchumi na uhaini. Wazo lililofanyiwa kazi siku chache mbeleni. Wakafunguliwa mashtaka katika mahakama ya hakimu mkazi, hasa ile ya uhujumu uchumi, ya uhaini wakafunguliwa katika mahakama ya kijeshi. Lilikuwa tukio la aina yake, lililozua gumzo kubwa mtaani, japo katiba ya taifa lao inaruhusu. Kilichosababisha gumzo hilo ni maneno ya watu wengi wenye itikadi pinzani na serikali. Kwanini wanawachukulia hatua hizo baada ya kujiunga na upinzani.
“Mbona hawakuwashtaki pindi wako kwao?”
“Hiyo ndiyo serikali mjomba. Lengo lao wawadhoofishe, japo haina uhakika kama ule mradi unawahusu ama unahusu hii serikali ya sasa.”
“Hilo nalo neno. Na ikija bainika huu mradi uliwahusu, kundi letu la Maliga litakuwa limejiharibia.”
“Tena sana. Ijapokuwa wengi wetu tumefumbwa macho na u—siasa, kwa kuona kitu chochote afanyiwacho kiongozi wa kundi letu na serikali, hufanywa kwa sababu ya siasa.”
“Wacha tujionee hii ngoma itakuaje.”
Kila mmoja alikuwa na mtazamo wake. Werevu wasiofungamana upande wowote. Nao hawakuwa nyuma kutoa michango kuhusiana na jambo hilo, pamoja na mwenendo mzima wa siasa. Asilimia kubwa, walio wengi waliangukia kwenye hoja moja kuwa siasa ni kichaka cha waovu. Wale wenye misimamo mikali, wakiwa humo, huitwa vigeugeu na waovu, wenye nia ya kuharibu amani ya nchi.
“Ki—uhalisia, tukiangalia, mwanzo wa huu mradi, ni mwaka uliopita. Pindi taifa letu limegubikwa na harakati za kampeni. Pindi, nchi yetu inaongozwa na Prof. Kadenge. Hata watumishi wote walikuwa chini yake. Sasa leo hii, tunavyopakaza hii tuhuma kwa Rais Mlunji, tunakosea. Japo imekuja vuma pindi yuko madarakani. Hivyo hatupaswi kuwakingia watangulizi wake kifua. Tuiachie serikali ifuate sheria zake mwisho tuone matokeo yatakuwaje.”
“Nami nakubaliana na hoja ya mjumbe wa kwanza. Hii kitu ina sintofahamu. Ukihitaji kufahamu hilo, tuangalie mlolongo mzima, toka Rais Mlunji alivyodiriki kuwataja watangulizi wake kuwa ndiyo wahusika wa mradi huu, kwa mwavuli wa Sista Amisa, ambaye aliaga dunia siku chache tu, baada ya Rais Mlunji kutangaza uchunguzi wa kina wa sakata hili. Yule Sista, kuna kitu alikuwanacho kihusianacho na ule mradi, ila hakutaka kuuweka wazi ndiyo maana akadiriki kujiua. Pia, kuthibitisha hawa watangulizi kuna mchezo wameufanya, wakaamua kukimbilia upinzani waufiche mchezo huo. Nasi kwa akili zetu, zisizoruhusu uchanganuzi, tukawaona mashujaa wa kweli, ilhali lengo lao kututumia kama kinga katika kuficha uhalisia wa uovu waliotenda kipindi cha nyuma,” ni maongezi ya wanaharakati fulani, walivyohojiwa na kituo kimoja wapo cha runinga.
Rais Mlunji akaziba masikio, kutosikiliza maneno ya watu. Akajidhatiti kusimamia alichoamua, mambo yakae sawa, pia ajawe na amani, kuuoneshea umma ukweli wa kile walichokuwa wanapigia kelele ni upi. Akakutana na washauri wake wa karibu, wakiongozwa na Magreth Okuku, mtaalamu, mbobezi wa mambo ya ulinzi wa viongozi, akiwa ameitumikia nafasi hiyo tangu taifa lao lipate uhuru. Wakapeana mkazo, kuhakikisha kilichopangwa hakipanguliwi, na kinafanikiwa kwa asilimia zote, pasipo chembe ya upungufu.
“Wakivuka mahakamani, wanatakiwa wale chuma,” alisema Rais Mlunji.
“Usihofu kuhusu hilo. Lazima likamilike.”
Siku husika ya kuanza kusikilizwa mashtaka ilivyowadia, washtakiwa wakapandishwa kizimbani, kuanza kusikiliza shitaka lao la kwanza, la uhujumu uchumi, washtakiwa wakiwa ni Mchungaji Kibunda, Lameck Nchenga na Prof. Kadenge. Huku shitaka la pili liliwaunganisha na kina Aisha, Kalumbwe, Kanali mstaafu Faidha, Kapteni Maguta na Wambili. Watu wenye uhitaji wa kusikiliza hawakuacha kuhudhuria kwa wingi, ila hawakupata nafasi ya kuingia ndani ya ukumbi kutokana na kujazwa mapema na watu waliotangulia, wengi wao wakiwa askari polisi waliovaa kiraia. Lengo kuzuia wananchi wasipate nafasi ya kuingia na kufahamu kiundani kiendeleacho. Hata waandishi wa habari walizuiwa. Na kupewa onyo kali, la kutohitajika kupiga picha ya aina yoyote ama kuandika habari ya aina yoyote mpaka siku ya mwisho. Siku ya hukumu. Na ili waandike habari kuhusu kesi hizo walipaswa kwenda kuomba taarifa maktaba ya mahakama.
Upande wa mashtaka uliongozwa na jopo la mawakili tano, huku upande wa utetezi, ukisimamiwa na mawakili sita. Wote wakiwa wajuvi wa sheria. Mmoja wao, mwanasheria mkuu wa kundi la Maliga. Shitaka lilianza kwa Jaji kusoma maelezo ya kosa wanalotuhumiwa, baada ya hapo wakapatiwa wasaa wa kujieleza kama wanakubaliana na kosa ama lah. Wote wakakana, kisha kufuatia wakati wa mawakili kuingilia kati, kwa kila mmoja kutetea mteja wake. Mahakama ilivyohairishwa, walirejea makwao. Kwani, kuna baadhi ya kinga ziliwalinda wasiingie mahabusu na kufanyiwa vitu vingine vya ovyo watendewavyo watu wengine na jeshi la polisi. Katiba ya taifa lao iliwalinda.
Walivyorejea uraiani, ikawapatia fursa. Za kujipanga na kutimiza matakwa ya mipango waliyojipangia. Wakawa wanakutana kila siku kuratibu hili, kesho lile, mipango mingine wakiwashirikisha viongozi wakuu wa kundi la Maliga, mingine waliijadili peke yao, hasa ile ya kuhitaji kufarakanisha wanachama wa kundi, hadi mmoja wao apate nafasi ya kugombea urais kwa mara nyingine. Katiba ya nchi yao inaruhusu. Rais aliyemaliza muhula wake kugombea kwa mara nyingine, baada ya kumaliza muda wa miaka miwili ya mapumziko.
Mpangilio wa kesi, ukawa kwa wiki mara moja. Nao wakatii mwenendo huo, kwa uhudhuriaji mzuri, na wakati sahihi uliopangwa. Baada ya kusikiliza mashtaka yao katika mahakama ya hakimu mkazi, kwa muda wa wiki mbili, shitaka la uhaini, nalo likaanza sikilizwa. Huku hakukuwa na mawakili, washtakiwa walijitetea wenyewe, upande wa serikali ukiwakilishwa na jeshi la ukombozi. Hakika, lilikuwa balaa, lakini siku za baadaye wakautwaa ukawaida, walivyoanza ita mashahidi wa kuthibitisha tuhuma zao, na wale kuwatetea.
“Mashahidi wakishaanza itwa mahakamani, itakuwa nafasi kwetu ya kutuweka huru,” alisema Prof. Kadenge, walivyokutana kwenye kikao kifupi mara baada ya mahakama kuhairishwa.
“Kivipi?”
“Mashahidi wao hawapaswi kuja mahakamani. Nina maana, wanapaswa kuuwawa.”
“Yeah!...yeah! Umetembea kwenye wazo langu. Huo ndiyo ukombozi wetu.”
“Njia ipi itatumika kukamilisha huo mpango?”
“Mmmmmnh!...kwanza yafaa kuwatambua mashahidi wenyewe ndiyo tupange mbinu sahihi. Ila mimi nina wazo la kumtumia Aisha, kufanya mauaji ya hao watu.”
“Kumtumiaje?”
“Wakiwa wanaume, tuwaanzishie mchezo mchafu wa mapenzi. Aisha ajitongozeshe kwao kisha atekeleze mpango husika. Na endapo kama ni wanawake, basi atumie janjajanja ya mambo ya urembo, ukizingatia watoto wa kike hulainika na hujawa matamanio sana waonapo mwanamke wenzao kapendeza na fasheni ambazo ni adimu.”
“Mpango mzuri. Tusubiri kujionea mashahidi. Nami napendekeza kumtumia huyohuyo.”
Wakakubaliana.
Walivyorejea mahakamani siku nyingine baada ya majadiliano mafupi, upande wa mashtaka ukataja idadi ya mashahidi wanaotaraji kuwasilisha mahakamani, sambamba na majina yao. Ili waweze kuandikiwa samansi za kuwataka wahudhurie mahakamani. Pindi mwendesha mashtaka anataja orodha hiyo, mmoja wao, akawa anaandika majina hadi idadi kamili ilipokamilika, wanaume wakiwa saba na wanawake watatu. Mahakama ikahairishwa.
Walivyorudi nyumbani, wakampanga Aisha. Walimueleza kila kitu, akaridhia kuwatekelezea, sababu wameshirikiana mambo mengi tangiapo. Baada ya hapo wakaanza ingia mtandaoni, kumtafuta mtu mmoja baada ya mwingine. Kitendo kilichowarahisishia, kutokana wengi wao kuwa watumishi wa serikali kipindi cha nyuma wakafukuzwa, wengine bado walikuwa utumishini. Huko walipata data chache, ziwahusuzo. Hasahasa mitandao ya twitter, facebook na instagram. Wakafahamu miji ya makazi yao yalipo, barua pepe zao na namba za simu, ila si kwa wote. Wale wenye namba za simu, walichukua namba zao, wenye barua pepe walichukua pia, na wale wasiokuwanazo Aisha aliwatumia jumbe katika mtandao husika aliojiunga huku akitumia jina bandia. Alijiita Nifaty Makusega.
Mtu wa kwanza kuanza nayo alitambulika kwa jina la Nkumbise. Ambaye ni Mkurugenzi wa mamlaka ya ukusanyaji kodi nchini humo. Aliyetii agizo la kumsamehe Sista Amisa kutolipa kodi ya biashara afanyazo. Huyu, Aisha alichukua namba yake. Usiku akaruka naye hewani, baada ya kujiunga kifurushi cha kutosha ambacho angeweza ongea pasi na hofu ya salio kukata. Alitafuta pozi zuri, sauti akailainisha vyema, kwa mchango wa yai bichi na kulamba asali kiasi kidogo. Akajikohoza kidogo, akiwa anasikilizia simu yake kupokelewa. Iliita kwa sekunde takribani ishirini na mbili, ndipo ikaja pokelewa.
“Mzee, hapa huchomoki,” alijisemeza kimoyomoyo, huku akiusikiliza vyema muungurumo wa sauti ya mtu aliyempigia.
“Hallo!” ilisikika sauti ya upande pili.
“Mheshimiwa, shikamoo,” alisema Aisha, kwa sauti nyororo imtoayo nyoka pangoni.
“Ndiyo. Nani mwenzangu?”
“Mara hii tu, umenisahau?”
“Dah! Sina kumbukumbu kama nakufahamu, maana namba imekuja ngeni kwangu.”
“Mmmh! Sio vizuri hivyo. Naitwa Nifaty, ndugu yake na Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Maliga.”
“Mbona jina ngeni kwangu halafu sikumbuki kama tushawahi onana?”
“Yawezekana umenisahau tu. Naomba kesho tuonane, tujuzane zaidi.”
“Mmmh!...kwa kesho, haitowezekana, labda tufanye siku nyingine.”
“D…! Naomba nipe japo dakika moja tu, halafu hiyo siku nyingine tukutane kwa mambo mengine.”
“Una tatizo gani kwanza ni jambo la kiofisi ama binafsi?”
“Binafsi.”
“Sawa! Tukutane saa nne asubuhi, Matongi hoteli. Si upo Lidede?”
“Ndiyo. Ni mkazi wa Lidede.”
“Basi utafanya nilivyokuambia.”
“Hamna shida. Nashukuru sana.”
“Haya.”
“Usiku mwema.”
“Nawe pia D.”
Naam! Siku iliyofuata, Aisha hakupoteza miadi. Toto lililonona, kwa umbo nene lililokata kwa kutengeneza muonekano uliojaa unofu kukata kiuno kuja chini. Kabarikiwa makalio halisi, ya tingatinga yashtuayo kidume wowote amuonaye, hata wasichana wasiobarikiwa huwa na tamanio la kumuomba awapunguzie japo kidogo nao wapatwe kutazamwa kwa sana. Upande wa juu, ulijijenga vyema pia, kwa skonzi mbili zilizochanua, na kuonesha ukomavu wa kutoguswa guswa sana. Ilivyowadia saa 3:45 asubuhi, tayari alishawasili hoteli aliyoambiwa akatafuta eneo zuri akaketi. Kisha kuanza kutupa jicho huku na kule kumtazamia mwenyeji wake. Mwangalizo huo ulisindikizwa na fundo la kinywaji cha soda aliyogiza dakika chache baadaye punde alivyowasili.
Mnamo saa nne dakika moja, Nkumbise akawasili. Akaongoza kulekule alipoketi Aisha baada ya kutaarifiwa. Alivyomuona tu, akamshangaa, mshangao ulioambatana na swali juu.
“Wewe si Aisha? Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Maliga?”
“Hapana. Naitwa Nifaty, ndugu wa Aisha. Tumezaliwa mapacha.”
“Oooh! Hongereni, mumebahatika kuwa warembo sana,” alisema Nkumbise, pindi akivuta kiti aketi.
“Ahsante.”
Baada ya hapo walisabahiana, kisha Aisha akaanza tupa ndoano yake kwa chombezo, lengo mwanaume huyo aingie ndani ya ngome yake atekeleze alichoagizwa. Kumuondoa duniani. Muda wote akawa anatoa tamko kwa sauti nyororo sana, huku akiacha baadhi ya sehemu zisisimuwazo wazi zishuhudiwe na Nkumbise ajawe uchu. Hasa sehemu ya matiti na mapajani. Kwani alivaa sketi fupi iachayo sehemu kubwa ya mapaja. Kuna muda akawa anatoka toka kwenda maliwatoni kuzuga tu, nia Nkumbise ajionee zigo alilolibeba nyuma.
Maongezi aliyotoa yalisheheni udanganyifu. Akimwambia kuwa ana mzigo wake unatoka nje ya nchi, hivyo anahitaji msaada wa Mkurugenzi kufanikisha, apitishe sehemu yenye vizingiti pasipo usumbufu. Akaenda mbali zaidi, kwa kumhaidi vitu vingine vingi pale atapokubali. Kama vile kushuhudia jinsia yake na kuichezea atakavyo. Pamoja na kiasi kidogo cha pesa kitachomwezesha kusongesha maisha. Nkumbise akawa makini kumsikiliza. Alivyomaliza, aliomba muda wa kutafakari na kumhaidi siku kadhaa mbeleni toka siku hiyo atampatia mrejesho wa ombi lake. Wakaagana.
Kila hatua Aisha akawa anawataarifu wakuu wake, maendeleo aliyoyafikia. Nao kumpatia mchango walionao katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyila kwa ustadi wa hali ya juu.
“Hakikisha, hilo jambo linafanikiwa kabla ya siku ya mahakama. Ina maana haitajiki kabisa kuonekana kufikia siku hiyo,”
“Ondoeni hofu. Hilo lazima lifanikiwe.”
“Okay! Usituangushe.”
Hadi kufikia siku moja nyuma, kabla ya ile inayotakiwa Nkumbise akatoe ushahidi mahakamani, bado hakutoa mrejesho kwa Aisha. Jambo lililomsukuma Aisha kumtafuta kila baada ya dakika chache kuulizia na kuomba miadi ya kuonana. Lakini hakukubaliwa kwa sababu ya kuwa na kazi nyingi za kiofisi, zimkoseshazo muda wa kufanya mambo mengine nje ya kiofisi na ya nyumbani.
“Naomba basi hata kesho asubuhi tuonane. Tuyaweke vizuri.”
“Kesho ndiyo kuzidi, kwani asubuhi na mapema nahitajika ofisini, halafu kwenye mida ya saa tatu tatu hivi ninapaswa nielekee mahakamani nikatoe ushahidi.”
“Fanya, tuonane pindi unaelekea mahakamani. Nitakuwepo Saanne hoteli.”
“Okay! Nitajitahidi kukujuza kama nitafanikiwa. Lakini kwanini tusifanye baada ya kutoka mahakamani?”
“Hapana, asubuhi ndiyo vizuri, Kwani saa tatu nitakuwa na safari kuelekea mkoani.”
“Sawa.”
Mambo yakawa ovyo. Wastaafu walikesha kushinikiza, ikiwezekana Nkumbise atafutwe muda huohuo apigwe shaba, ili asiende kuwaharibia, lakini wengine wakawaomba watulie, kwani walichofikiria kufanya kitawaweka sehemu mbaya itayowasukuma wananchi wawashtumu kwa kitendo hicho. Hivyo wakaombwa wamwachie Aisha, wanachopaswa kuomba mungu, sio kutafuta mbinu nyingine. Aisha naye akawasisitizia, japo hakuisha mashaka kuwa Nkumbise anaweza poronyoka kwenye mtego wake. Siku waliyopaswa kurejea mahakamani kuanza kusikilizwa mashahidi ilivyowadia, roho zilizidi kuwa juujuu, wanaenda umbuliwa. Huku Aisha, akikesha kumsumbua Nkumbise kumtaka afanye jitihada aonane naye kwa kumpigia na kutuma jumbe nyingi zenye mkazo wa kuonyesha yupo katika hali mbaya.
Hadi kufikia muda wa kuanza mahakama, hakukuwa na taarifa yoyote iliyowataarifu kuwa Nkumbise kabadilishwa jina, na upande wa mashtaka nao hawakuwa na taarifa zozote kumhusu. Kila pande wakawa na matamanio na matarajio. Upande mmoja kumuona Nkumbise akiwasili, upande mwingine kusikia Nkumbise hawezi wasili mahakamani baada ya kupatwa na umauti. Mnamo saa 3:30 asubuhi ndipo mahakama ilianza kusikilizwa. Baada ya dakika tano, jaji muongozaji wa kesi hiyo akaomba upande wa mashtaka wawasilishe shahidi wake. Ila cha kushangaza alikuwa bado hajawasili. Alivyopigiwa simu, ilipokelewa na kutoa kauli kuwa anakaribia kuwasili, ikawapa matumaini upande wa mashtaka, na kumuomba mheshimiwa jaji awaongezee muda wa kufanya subira kumsubiri.
Ombi lao lilikubaliwa, lakini hadi kufikia saa 3:50 asubuhi hakuwasili, Alivyopigiwa simu iliishia kuita pasipo kupokelewa. Hali iliyompandisha mheshimiwa jaji hasira, na mawakili wa upande wa utetezi kukazia kwa kumshawishi ahairishe shitaka hilo hadi siku nyingine baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha shahidi wao. Ila mawakili wa upande wa mashtaka hawakukubali, waliendelea kuomba, mpaka ilivyowadia saa 4:01 asubuhi, muda wa mwisho wa ombi alioutoa mheshimiwa jaji, baada ya hapo akatoa maamuzi, ya kughairisha shitaka hilo hadi wiki inayofuata. Maamuzi hayo yakawa furaha kwa wastaafu, kwa kiasi kidogo, wakiamini kuna jambo lililojitokeza. Wakapandwa na shauku ya kutaka kufahamu kwa uharaka nini kimetokea, hivyo punde tu, walivyotoka ukumbini walimpigia simu Aisha kumuuliza. Ila isivyo bahati simu yake haikupatikana. Hata watu wa upande wa mashtaka, kila walivyomtafuta Nkumbise, safari hii simu yake ilikuwa haipatikani. Jambo lililoipa akili kazi ya ziada kuwazua kilichomsibu. Wakajaribu kuwahusisha na watu wengine pia. Hasahasa Rais Mlunji na Magreth Okuku kuomba msaada, ila nao walivyomtafuta majibu hayakutofautiana na yao.
Katikati ya uhangaikaji huo, wakashtushwa na taarifa iliyoibuka ghafla, na kuwashinikiza watu wengi waondoke viwanja vya mahakama wakimbilie nje, umbali wa mita mia moja.
“Kuna nini? Mbona watu wapo wanguwangu sana?” aliuliza Prof. Kadenge, akimuuliza kijana mmoja aliyekuwa anatokea kule walikokuwa wanakimbilia wale watu waliotoka viwanja vya mahakama.
“Kuna mtu kauwawa ndani ya gari.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ikawapa mshtuko. Uliowashinikiza nao waende eneo hilo. Kweli! Walishawishiana, wote wakaridhia, kisha wakapiga hatua kuelekea.
****
Saa 12:10 asubuhi, ndiyo muda ambao Nkumbise aliamka. Akafanya usafi wa mwili, baada ya hapo akapata stafutahi, kisha akafunga safari kuelekea ofisini. Safari hiyo ilianza saa 1:45 asubuhi. Akiwa pekee ndani ya gari. Alivyokaribia kulifikia lango la wigo uliozunguka jengo la ofisi simu yake ilianza ita mfululizo, muito uliomfahamisha anapigiwa. Alivyotupa jicho kwenye skrini, akakutana na jina la Nifaty. Ikabidi apunguze mwendo na kupaki gari pembezoni mwa barabara. Akampigia.
“Ulisema kuwa upo wapi?” aliuliza Nkumbise mara baada ya simu kupokelewa.
“Nipo Saanne hoteli,” alijibu Aisha.
“Okay! Naja sasa hivi,” alisema na kukata simu, kisha akageuza gari kuelekea alikoambiwa.
“…wacha nikaonane naye kwanza huyu ndipo nifanye mambo yangu kwa uhuru,” alijisemeza, huku akizidi kanyaga mafuta.
Hakutumia muda mrefu, akawasili hoteli aliyoelekezwa, akapaki gari eneo la maegesho, na kuongoza mapokezi, ambako alijitambulisha akafuatia kueleza shida ya ujio wake. Wahudumu, wakampigia simu Aisha, kumtaarifu ujio wa ugeni huo, akawapa ruksa ya kumruhusu.
“Unaweza kwenda, chumba namba 801,” alisema mhudumu, aliyekuwa anawasiliana na Aisha mara baada ya kuweka mkonga wa simu ya mezani mahala pake.
“Shukrani,” alisema Nkumbise, na kuanza ondoka kwa kupanda ngazi kuelekea chumba alichoelezwa.
Alivyokifikia, alibisha hodi, iliyopokelewa na Aisha aliyekuwa katika muonekano wa kutamanisha. Alikuwa kavaa taiti ya waziwazi iliyoonyesha sehemu ya mwili, juu kavaa blazia ambayo hata hakuifunga.
“Karibu. Ila samahani kwa muonekano ulionikutanao, najiandaa kwa safari niliyokuambia,” alisema Aisha, akiwa kajibinua, kalio kalielekeza alipoketi Nkumbise, akijipaka losheni mguuni.
“Hamna shida,” alijibu Nkumbise. Domo likiwa limejaa mate, kwa uchu, mwenye jinsia akiwa kavimba na kutaka kuchana suruali aliyoivaa, baada ya kushuhudia sehemu iliyobeba jinsia ya Aisha.
Dakika mbili zilikuwa nyingi. Pasipo hata matarajio, baada ya mizunguko ya kuzuga aliyokesha kuifanya Aisha akizunguka huku na kule mle chumbani na kuivua blazia kwa madai ya kutaka kubadilisha na kuacha wazi sehemu ya matiti, Nkumbise akashindwa kuvumilia, akamvuta na kutua mapajani kwake ambapo mwenye jinsia alishachanua vya kutosha kiasi kwamba hadi misuli ilimuuma. Aisha akajilegeza, akaleta ugumu wa hapa na pale, baadaye akang’ang’ania sehemu ya shingo ya Nkumbise kisha kujizungusha pale mapajani kuongeza msisimko. Punde, wakaanza tomasana, huyu aligusa huku yule kule, mwishowe wakabaki kama walivyozaliwa. Kitendo hicho hakikuchukua muda mrefu, jinsia zikaingiliana. Zilizowabadilisha ulimwengu kwa kuwasafirisha kwenda mbali mpaka wasahau watokako.
Ilivyowadia saa 2:35 asubuhi, tayari Nkumbise alinonoka vya kutosha, hadi akakinai. Baada ya hapo wakaondoka hotelini safari kuelekea mahakamani, Aisha akiwa kaomba lifti amshushe hapo mahakamani aendelee na safari yake. Alivyoulizwa kwanini asipelekwe kwanza anakohitaji kuelekea ambako ni kituo kikuu cha mabasi, alikana kutohitaji. Huku akimzuga kwa kumuonea huruma Nkumbise atachelewa kuwasili mahakamani. Walivyokaribia kufika viwanja vya mahakama, umbali mita mia moja, Aisha akamuomba Nkumbise asimamishe gari kuna kitu fulani anahitaji kufanya. Hakupinga, akaegesha pembeni, kisha akafanya subira, amalize ili waendelee. Subira yake iliambatana na uperuzi wa simu kuangalia taarifa mbalimbali mtandaoni. Zilizomchukulia muda na kumfanya ajiziuke.
Huo ukawa wasaa kwa Aisha. Kwani aliinama akawa anachambua chambua vitu fulani kwenye kibegi chake kidogo. Alikuwa anatafuta pete, iliyorembwa vyema kwa visindano vidogovidogo. Akaivaa, kisha kutumbukiza kidole kwenye kichupa kidogo kilicho na maji nusu yenye rangi nyekundu. Alivyokamilisha, akakitoa, akatupa jicho kwa Nkumbise, akamuona bado akili yake imelala kwenye simu.
“Hii ndiyo nafasi pekee. Haina haja ya kupoteza muda,” alijisemeza. Akiwa anazungusha mikono yake shingoni kwa Nkumbise, ishara ya kumkumbatia. Nkumbise naye, akawa ametulia tu, mwili ukiingiwa msisimko taratibu kwa mapokezi ya kumbatio, lililomghairisha kuchezea simu ili ajionee matokeo vyema.
Aisha naye hakutaka kupoteza. Upotezi utaomfanya ashtukiwe. Haraka sana, akakutanisha viganja vyake, kile kidole alichovaa pete akaking’ang’aniza ngozini, taratibu kabisa, ili mchomo usitoe maumivu makali ya kushtukiwa. Alivyohakikisha kishachoma, kiasi cha kutoa damu na kuingiza yale majimaji, kwenye damu akamwachia.
“Nashukia hapa,” alisema Aisha. Akikusanya vitu vyake.
“Poa, kipenzi changu. Umenifanya niwe mwepesi asubuhi asubuhi,” alisema Nkumbise, pindi akimfungulia Aisha mlango ateremke.
“Okay!” alisema Aisha, akiwa kashateremka.
Nkumbise akapiga jicho la mwisho mwisho kumsaili zaidi alivyonona, kisha akaanza kanyaga mafuta kuendelea na safari. Hata dakika moja haikufikia, akajikuta anaishiwa nguvu ghafla, macho yanajaa ukungu na upoozi wa baadhi ya viungo. Hali iliyomfanya ashike breki kwa nguvu, huku gari ikiwa imepoteza mwelekeo na kwenda kugota kwenye mti wa maembe ulio pembezoni mwa barabara. Tukio lililotoa kishindo kikali kilichowasukuma watu waliosikia kukimbilia eneo hilo kujionea. Baada ya muda mfupi tu, wakajazana watu wengi mno. Wakiwemo askari wa usalama barabarani waliokuja kupima ajali. Wasamaria wema, wakiambatana na hao askari, wakamtoa Nkumbise garini, lakini akiwa amekakamaa, ishara iliyowafahamisha wengi kwa haraka mno.
“Ashafariki…”
“Maskini,…hatunaye tena.”
“Huyu si ndiye mshahidi?”
“Eeh!...ndiyo mwenyewe.”
Walisikika wananchi, huku wakianza ingiwa na simanzi iliyoteka akili. Wastaafu na mawakili wa upande wa serikali, walivyowasili, waliishia kushuhudia pindi mwili unapakizwa ndani ya gari ya askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani. Wakashindwa muona mhusika aliyepatwa na ajali hiyo. Ikabidi wajiunge kwenye makundi ya watu waliokusanyana kusanyana wakiteta jambo. Wastaafu walivyosikia kuwa aliyepatwa na ajali hiyo ni yule wamtakaye, mioyo yao ikachanua tabasamu, lisilopimika. Lilikuwa pomoni, ilhali mawakili wa serikali waliokuwa wanasimimamia hiyo kesi kwa niaba ya jamhuri, walijawa na uchungu, na akili ya haraka ya ufikiriaji. Kwanini kagonga.
Hawakukaa nalo, wakawafahamisha mabosi wao. Wazee wa mipango, wakiongozwa na Magreth Okuku, ambaye alishikia wadhifa huo kwa niaba ya mheshimiwa Rais Mlunji. Alichotaarifiwa, yeye ndiyo hupeleka kwa Rais Mlunji kama kilivyo. Kikifaa kujadiliwa na wawili hukijadili, maamuzi yapatikanayo hufikishwa kwa wote, na chenye kufaa kujadiliwa na wote, hukutana kwa siri usiku sehemu yenye maficho makali hujadiliana. Hivyo hili lilivyofikishwa mikononi mwao, muda huohuo wakaingia kwenye majadiliano mazito, yaliyochukua muda mrefu kufikia tamati. Walifanya majadiliano hayo, kwa njia ya simu. Ambapo mmoja wao, Rais Mlunji, aliwaunga wote kwa pamoja kila mmoja akatoa wazo alilonalo sambamba na hatua stahiki za kunyafa.
Muda wote, wakawa na mioyo iliyojaa tamanio, kujionea mwili wa Nkumbise ulivyo. Hilo halikuwa tabu, wakafanya chaguzi ya haraka, kidedea akapatikana Rais Mlunji aende hospitalini akajionee, ili awafahamishe ukweli. Maana hawakuwa na imani kabisa, kwamba Nkumbise kauwawa kwa ajali ya gari iliyotokea. Mchana wa siku hiyo, Rais Mlunji akaongozana na msafara mdogo hadi hospitali ya taifa, mjini Lidede. Walivyowasili, alionana na mganga mkuu, akamueleza hitajio lake, ambalo halikuwa shida kukubaliwa, baada ya hapo wakaongozana hadi sehemu husika. Monchwari!
Mwili wa Nkumbise ukatolewa, kutoka kwenye jokofu, na kulazwa juu ya kitanda maalamu ambacho alipata nafasi nzuri ya kuusaili.
“Kuna kitu chochote mlichogundua mwilini mwake, ambacho kipo tofauti na chanzo cha ajali aliyoipata?” aliuliza Rais Mlunji, akiwa katupa jicho pima, mwilini mwa Nkumbise, akiusaili kuanzia unyayoni hadi utosini.
“Hapana kiongozi, hamna chochote, chenye kutia shaka. Ni ajali tu ndiyo iliyomuondoa,” alijibu Mganga Mkuu.
“Muna uhakika? Na mumeuchunguza vyema?”
“Tena zaidi ya mara tatu.”
“Naomba mufanye uchunguzi kwa mara nyingine, nina mashaka na kifo chake.”
“Hamna shida kiongozi.”
Mganga Mkuu, akishirikiana na mganga mwenye jukumu la kushughulikia miili chumbani humo, wakaanza mara moja kuwajibika, Rais Mlunji akiwa pembeni anashuhudia. Wakaugeuza huku na kule, lakini hamna walichokibaini chenye shaka, hata Rais Mlunji, akathibitisha hilo na kuwaamuru waurejeshe. Pindi, wanauinua pale kitandani kuuingiza kwenye jokofu, macho ya Rais Mlunji yakatua shingoni kwa Nkumbise, akashuhudia vidoti vitatu vilivyoonekana kuchoma. Akawasitisha.
“Rudisheni huo mwili kitandani. Kuna kitu nimekiona.”
Hawakuwa na budi, wakatii agizo walilopatiwa. Waliurejeshe na kufanya vile walivyoamriwa.
“Angalieni shingoni huko nyuma, kuna alama fulani niliyoiona,” alisema Rais Mlunji, huku akionyesha msisitizo wa kugeuza mwili kwa ishara.
Wale waganga waliugeuza na kutupa macho eneo waliloambiwa. Wakaona, hali iliyowafanya waanze upya vipimo. Vipimo hivyo havikuchukua muda mrefu, robo saa tu, wakafanikiwa kupata majibu, ambayo yalimshangaza kila mmoja alivyoyasikia.
“Kuna sumu iliyoingizwa mwilini mwake, na ndiyo iliyomuondoa,” alisema Mganga Mkuu, pindi akimtaarifu Rais Mlunji. Jibu ambalo lilimduwaza kwa muda, na kumfanya aingie kwenye tafakuri ya kuhitaji kutambua sababu ya kuwekewa sumu ni nini? Na nani katenda kitendo hicho, ijapokuwa hisia za awali zilienda moja kwa moja kwa marais wastaafu.
Kikapita kimya kifupi, kilichobeba ulizo moyoni mwa kila mmoja. Na kukosa jibu sahihi, zaidi ya jibu la hisio. Kikaja katishwa, na Rais Mlunji pindi alivyowaaga na kuondoka. Hakurejea Ikulu, alimwamuru dereva asongeshe msafara nje ya mji wa Lidede, walivyofika umbali fulani, akaamuru kwa mara nyingine msafara usimame. Ulivyosimama, aliteremka, kisha akapiga hatua kadhaa akasimama. Alionekana mwingi wa tafakuri, akitafakari nini afanye, hali iliyowaweka njia panda walinzi wake, na walivyojaribu kuhoji wafahamu shida nini, aliwaomba watulie, wamwachie matatizo yamwandame mwenyewe, wao wasishiriki. Baadaye akamuita mama Tausi, akampatia maelezo fulani, ambayo aliyatekeleza sekunde chache tu alivyohitimishiwa. Ambapo alionekana kuzungumza na mtu kwa njia ya simu kwa muda mfupi kisha akakata. Alivyokata alirejea pale aliposimama Rais Mlunji, akampatia mrejesho uliokubaliwa na utingishaji wa kichwa.
“Twende tukawasubiri,” alisema Rais Mlunji, akianza piga hatua kuondoka eneo hilo akitokomea kichakani akiambatana na mama Tausi, walinzi wengine wakisalia palepale.
Mwendo wa kichakani uliishia kwenye banda moja kuukuu umbali mita mia tatu toka walikoyaacha magari. Kabla hawajaingia walipiga jicho huku na kule, walivyoona mazingira yako tulivu wakazama ndani, punde mama Tausi alivyofungua mlango. Dakika nane baadaye watu wengine wakawasili. Ambao ni James na Magreth. Hawakukawia, walitakiana hali, baada ya hapo waliingia kwenye mazungumzo yaliyomchukua muda Rais Mlunji kutoa mada. Aliwahadithia kuhusu matokeo aliyokutana nayo hospitalini, kisha wakafikia hatua ya majadiliano ambayo kila mmoja alitoa mchango wa wazo alilonalo katika safari ya kufanikisha Rais Mlunji anakuwa msafi kabla hajafikia azma yake ya kujiuzulu. Hatma ya majadiliano yao, ilifikiwa nusu saa baadaye, kisha wakarejea watokako.
Upande wa marais wastaafu, wakiongozwa na Prof. Kadenge, Rais mstaafu awamu ya tano, ambaye ndiye mratibu wa mipango nao walikutana kujadiliana namna ya kuendeleza mipango yao ya kumdhoofisha Rais Mlunji aweze kuachia ngazi ili mmoja wao arejee tena madarakani. Pia walikutana kujadiliana kuhusu Aisha, ambaye walikuwa hawampati hewani kila walivyojaribu kumtafuta. Walihangaika haswa, huku wakijaribu kutembelea baadhi ya maeneo wadhaniayo anaweza kuwepo ila hawakufanikiwa kumkuta. Na walivyojaribu kuulizia watu mbalimbali wanaomfahamu, hawakuwa na mrejesho wenye kuwafurahisha. Wote hawakumuona Aisha. Wala kuwa na dondoo kwamba anaweza kuwepo sehemu fulani.
“Huyu mtu anaweza kuwepo wapi? Asipopatikana nani anaweza kufanya hii kazi?”
“Tunafanyaje kumpata huyu mtu?”
Walikesha kujiuliza maswali mengi, waliyokosa majibu ya papo kwa papo hadi watafakari kwanza. Tena kwa kina ndipo wathubutu kutamka. Hatimaye siku zilikatika, pasipo Aisha kuonekana, wala kupata taarifa zake. Hali iliyowafanya wajawe na moyo wa mashaka, kwamba endapo wakishindwa kuwaondoa mashahidi wa upande wa jamhuri, na wakafanikiwa kufika mahakamani basi mipango yao itafeli na wataumbuka. Akili zao hazikutuliana, kufikiria mbinu za kufanya zenye kuwapatia ushindi, ijapokuwa kuna muda walifikiria kujiondoa duniani kuepuka aibu itayowakumba baadaye wakiumbuka. Hadi ilivyofikia siku nyingine ya kuripoti mahakamani, hawakuwa na habari juu ya Aisha. Na ni siku, ambayo shahidi namba mbili, Afisa uhusiano wa mamlaka ya ukusanyaji kodi Mangaka, Bi. Mwantumu, alipaswa kutoa ushahidi. Muda wa mahakama kuanza ulivyotimu, mheshimiwa jaji aliingia ukumbini, alivyoketi, alivuta faili la shtaka, akasoma maelezo machache kisha akatoa nafasi kwa mawakili waendelee na taratibu za kuwasilisha mashahidi.
Bahati iliyoje, huyu alifanikiwa kuwasili mahakamani. Akapanda kizimbani, akaapishwa, baada ya hapo akaanza toa maelezo anavyofahamu namna marais wastaafu wanavyohusika na mashirika yaliyokuwa yanawaibia wananchi pesa zao. Alivyohitimisha, ukawa wasaa, kwa mawakili wa upande wa utetezi kumuuliza maswali.
“Umesema kwamba ulipokea simu toka kwa Mkurugenzi wako, ambaye sasa ashatangulia mbele za haki, kuwa uweke mahusiano mazuri na Sista Amisa, baada ya kupokea maelezo toka juu, kwanini huyo aliyompatia maelezo Mkurugenzi wako asikupigie wewe moja kwa moja?” aliuliza wakili wa upande wa utetezi. Ajulikanaye Simbili.
“Sijajua. Ila nahisi aliniona ni mdogo ki—wadhfa, ndiyo maana aliwasiliana na Mkurugenzi wangu.”
“Unaamini vipi hayo maagizo ya Mkurugenzi wako yalitolewa ngazi za juu? Je, huhisi kama naye anaweza kuwa mmoja miongoni mwa wabia wa hayo mashirika, hivyo alitumia kauli ya ngazi za juu akufiche uhusika wake?”
“Hapana, hawezi kuwa mshirika. Mshirika ni Sista Amisa, ambaye alikuwa anatumika kuwaficha wahusika halisi. Ambao ni marais wastaafu wa awamu ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano.”
“Kwanini huamini anaweza kuwa mshirika?”
“Hawezi tu.”
“Ndiyo, hawezi. Tupatie ufafanuzi wa kutoweza. Na unaamini vipi, yeye asiwe halafu hawa wateja wangu wawe na uwezo huo?”
Kabla Bi. Mwantumu hajajibu swali hilo, wakili wa serikali akadakia.
“Mheshimiwa jaji, naona wakili wa upande wa utetezi anataka…” naye hakumalizia kutamka kauli yake, akakatishwa na kauli ya mheshimiwa jaji.
“Mwache amalizie.”
Mambo yalikuwa hivyo. Yalikuwa moto, kama wadaivyo vijana wa mjini. Pande zote walikabana kooni kwa hoja, zilizohitaji ufundi wa hali ya juu kuzijibu. Kama ilivyo ada, mahakama ilivyohairishwa, watu walirejea makwao. Wahusika wa pande zote wakiwa tumbo joto, kutofahamu chembe ya mwenendo utakuwaje. Hali iliyowafanya kila siku, wasizohudhuria mahakamani kukutana, kujadiliana nini waendelee kufanya, wajiweke nafasi nzuri zaidi. Marais wastaafu walivyokutana awamu hii, hawakumjadili tena Aisha. Walijadiliana muendelezo wa mbinu walizojipangia na kumtafuta mtu mwingine atayezitekeleza. Awamu hii walimchagua Wambili, pia walibadilisha mbinu, toka ile ya mapenzi na urembo, hadi upigaji wa shaba, huku eneo la tukio wakiliandaa kuwa lango la kuingilia mahakamani. Pasi na sahau, waliongeza mpango mwingine wa kuwaondoa duniani baadhi ya mashahidi wawateteao wao. Ili kuleta ulingani wa kuwaaminisha watu wao hawahusiki na mauaji ya mashahidi wa upande wa jamhuri, pia, kuteka akili za watu vilevile, waonewe huruma kwamba kweli si wahusika ndiyo maana mashahidi wao wanauwawa.
Utekelezaji wa mpango huu mpya ulianza punde, alivyotaarifiwa Wambili, naye akaridhia. Sababu tangiapo huendesha maisha kwa matendo hayo ovuovu. Kumwaga damu ndiyo furaha yake, hivyo alivyotaarifiwa tu, aliruka ruka mithili ya uji jikoni uivapo. Akaandaliwa taratibu zote, akalipwa utangulizi nusu wa gharama wa kile atachofanya. Siku kesi zilivyosikilizwa mahakamani, timizo la mpango huo halikuisha kutekelezwa, Wambili alikuwa anachukua maficho jirani kabisa na viwanja vya mahakama, kwenye hoteli kubwa kubwa ambazo aliweza shuhudia vyema na kwa urahisi mazingira hayo. Zile zilizo katika muundo wa ghorofa.
****
Kikosi kazi ndiyo watu wa kwanza kuzuru kwenye tukio lililompata Nkumbise. Na waliweza shuhudia pindi linatokea, kwani wao walikuwa wanafuatia nyuma yake. Punde walivyofikia, wakagawana, wengine waliteremka garini wakabaki ajalini, waliosalia garini waliunga kumfuata Aisha, ambaye hakuwa na ufahamu kama anafuatiliwa. Gari iliendeshwa kwa kasi sana, walikata kona mbili, walivyoifikia ya tatu, wakamfikia, akiwa anafanya jaribio la kusimamisha bajaji. Kwa ustadi wa mafunzo yao waliteremka chap garini, walivyotua chini, bunduki walizobeba tayari zilishakokiwa na kukitwa vyema kwenye nyama ya bega (nyama ya bure) kama inavyotambulika kitaalamu na wazee wa mashambulizi.
“Mikono juu,” walimuamuru kwa pamoja. Akiwa kanyooshewa mitutu ya bunduki.
Akapatwa na mshtuko wa ghafla, uliomfanya atetemeke kidogo, kisha kuipa akili nguvu ya ufikiriaji. Lakini alikwishachelewa. Kwani askari mmoja wapo aliteremsha bunduki akaivaa mgongoni, baada ya hapo alichomoa pingu akamfunga. Wakambeba mzobe mzobe, kwa mtindo ufahamikao na wengi, tanganyika jeki wakamtupia garini na kuondoka. Watu walivyoanza jazana, kisha askari wa usalama barabarani kufika, wale askari wa kikosi kazi wakaondoka kuwafuata wenzao walipoelekea. Walitaarifiwa kwa njia ya simu.
Makutano yao yalikuwa ndani ya jengo kubwa chakavu. Lililojengwa katikati ya pori, nje ya mji wa Lidede, kama unaelekea jijini Naparavi. Jiji kubwa la kibiashara nchini humo. Jengo hilo lilitawaliwa na michoro ya ajabu ajabu, iliyochorwa kwa mkaa na rangi mbalimbali, michoro iliyochangia kwa kiasi kikubwa jengo kuchafuliwa. Wakakutana humo wakiwa na Aisha. Ambaye alilazwa juu ya machela, kafunikwa uso, mikono na miguu imefungwa pingu.
“Tunampatia adhabu gani?”
“Hatakiwi kuwepo duniani,” alijibu ASP Nendakulola.
“Unamaanisha tumuuwe?”
“Ndiyo. Unashangaa nini? Ama umesahau kiapo chako siku mnahitimu ulitamka utailinda katiba na kumtetea Rais wa jamhuri ya Mangaka?”
“Nakumbuka. Huyu ni kiongozi mkubwa wa upinzani, tukimwondoa, halafu mwili wake ukipatikana, tutaleta vurumai kubwa mtaani.”
“Hey! Umesahau aliyoyafanya kwa mheshimiwa Rais? Ni lazima auwawe.”
“Umepata amri toka kwa mheshimiwa Rais? Ama unajiamulia tu?”
“Hili halina amri toka kwake. Mimi ndiyo naamua, Mkuu wa kikosi hiki,…” alisema ASP Nendakulola na kusita kwa muda, akapatwa na fikra fulani, iliyomuonyesha kasimama mbele ya Rais Mlunji Ikulu akimpatia maelezo. “…natamani hawa watu niwaondoe duniani, taifa letu liwe na amani, ila sijui njia ipi nitumie,” alikumbuka kauli aliyowahi ambiwaga na Rais Mlunji. “Huyu mtu lazima afe. Tena kifo cha kikatili, na mwili wake utazikwa katika makaburi ya mjini Lukwika usiku wa leo,” aliendelea kusema kwa msisitizo.
Ikawabidi wajadiliane, majadiliano yaliyochukua muda mrefu, ya kimyakimya Aisha asisikie, ilhali yale ya awali waliyokuwa wanazozana alishayasikia. Walivyohitimisha, walimsogelea pale kitandani, wakamfungua vitu walivyomfunga funga awe huru. Wakamwacha apumzike kwa muda, huku akiwashuhudia, namna walivyoiva hasira na chuki iliyoonekana kuzalishwa toka moyoni. Hakuwa na budi, muda huo akatumia kuanza kuomba msamaha, akiwa kapiga goti machozi yakimtiririka mithili ya mtoto mdogo. Akawa anamfuata kila mmoja, kwa kutambaa na magoti, ambayo muda mfupi baadaye yalianza kuchubuka kutokana na changalawe zilizosakafiwa chini. Wakati huohuo, alikuwa anajaribu kuwanyemelea, endapo atamuona mmoja wao kasimama kiboya boya amvae na kumpokonya bunduki.
“Tusipoteze muda, tuanze nayo. Mmoja mmoja, fanya ujisikiacho kufanya,” aliamuru ASP Nendakulola. Kauli iliyotoa utii kwa wote.
Wakafanya zamu, mmoja baada ya mwingine, kumfuata Aisha alipo, kisha kufanya anachojisikia. Mwenye kukata kidole, alikata, mwenye kuparua uso kwa wembe, naye alifanya hivyo, hadi pale Aisha alivyotokwa na uhai. Walivyojihakikishia hayuko ulimwenguni, walimfungia kwenye mfuko wa sandarusi kisha wakafunga safari kuelekea kule walikoambizana awali. Mwendo waliotembea nao barabarani haukuwa wa kawaida. Mithili ya maonyesho ya magari yawapo mashindanoni. Mwendo wa gari ulikuwa wa kasi mno, kiasi kwamba mwenye imani ndogo haumudu kuendelea na safari. Mnamo saa tano usiku wakaufikia mji wa Lukwika. Ila waliupita kidogo hadi kwenye pori kubwa litenganishalo kati ya mji huo na ule wa Lumesule kwa upande wa magharibi. Gari wakaenda ificha uchochoroni, kwani ilifikia wakati taa za gari zilizimwa, ili wasiweze bainika na watu wachache ambao kwa muda huo walikuwa na mambo yao.
Walivyofika sehemu waliyokubaliana, waliteremka kwa haraka wakajitwika mwili wa Aisha wakasonga mbele kwa mguu, baadhi yao wakibeba sepetu (chepeo), sururu na jembe, ambazo mara nyingi hutumia gari yao ikumbwapo na tatizo la kukwama. Umbali wa kilomita moja toka eneo walipoliacha gari lao, wakaweka kituo. Wakautua ule mwili, wakaanza kuchimba. Lilikuwa eneo mahususi kabisa kwa maziko, kwani palikuwa na makaburi mengine waliyoweza yatambua kupitia alama za misalaba. Wakafanya chapchap, kwa ushirikiano wa hali ya juu na baada ya saa moja na nusu, walifanikiwa kuchimba shimo refu lililokaribia urefu wa futi tano kwenda chini. Walivyoridhika panastahili, hawakupoteza muda, waliusogeza mwili wakautupia. Pasipo kujali umekaaje, wakaanza ufukia. Hadi panapo majira ya saa saba usiku, walishafanikiwa kumaliza kila kitu, wakaanza safari ya kurejea mjini Lidede.
Wiki moja baadaye, ndipo uvumi wa kutooneka Aisha, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa kundi la Maliga taifa ukaanza sikika. Yote, ilichangiwa na kutohudhuria kwenye vikao vya siri vilivyowakutanisha viongozi wa kundi hilo. Jitihada zao za kumtafuta hazikuzaa matunda, kila walivyojaribu kumpigia simu ama kutembelea alikokuwa anaishi ama nyumbani kwa wazazi wake pia. Mwanzo walianza kwa kificho, ila kadri siku zilivyozidi kwenda mbele wakaamua kuweka mambo hadharani wanachama wengine wafahamu. Kitendo hicho, kikawaibua wananchi upya. Ila si wote, ni wale wenye itikadi pinzani pekee, kuishinikiza serikali, kupitia jeshi la polisi litoe taarifa kuhusu Aisha wapi alipo. Awamu hii kidogo mambo yalikuwa tofauti, haikuwa kama zingine zilizowatoa wananchi barabarani kupambana na vyombo vya dola. Awamu hii walikesha kutoa malalamiko yao kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyopelekea serikali kutowatilia sana maanani, ila wale waliojinasibu kwa kutoa malalamiko yaliyoichafua hawakuwaacha salama. Waliwatafuta kimyakimya, walipofanikiwa kuwapata, baadhi waliangukia jela, wengine kwenye pumziko la milele.
Wakati huo hata ile kazi aliyopewa Wambili ilianza tekelezeka. Wiki hii, akipigwa shaba shahidi wa upande wa mashtaka, wiki inayofuata, anipigwa shaba shahidi wa upande wa utetezi. Tena katika viwanja vya mahakama. Walikuwa wanauwawa pindi washaingia viunga vya mahakama tayari kwa kutoa ushahidi, jambo lililozua taharuki kubwa kwa wananchi. Wale wenye utawalio wa itikadi za kisiasa, wakabaki jibizana kila leo kushutumiana, kwamba kila upande ndiyo hufanya mauaji ya mashahidi wa upande mwingine. Hakika! Huo ulikuwa mchezo, uliowanufaisha kwa kiasi kikubwa marais wastaafu, kuonekana wao watiifu haswa, kama imani inavyotawala siku zote. Mpinzani aguswapo na dola, hicho alichofanyiwa hukimbizwa kwenye siasa moja kwa moja, pasipo hata kulitafutia uchunguzi.
“Wale Wajinga wanaweza toka,” alisema Rais Mlunji, alipokutana na vijana wake wa kazi jioni moja.
“Ila si kwa kote. Wakifanikiwa hii ya kiraia, ipo ile ya kijeshi. Ambayo daima, siku zote haimwachii mtuhumiwa. Mtuhumiwa akipelekwa pale lazima akutwe na tuhuma. Hivyo usife moyo kiongozi wetu,” Magreth Okuku alichangia hoja.
“Unahisi wakiwakataa waendesha mashtaka wote waliochaguliwa itakuaje?”
“Huu si wakati wa kujilaumu kiongozi, ni wakati wa kutenda. Tena matendo yaletayo ushindi. Hamna kitachoharibika. Tuachie kazi sisi watatu, utaona mrejesho wa kile tutachopanga.”
“Muna mpango upi?” aliuliza Rais Mlunji kwa shauku.
“Hupaswi kuambiwa. Subiri matokeo.”
“Haya, natega sikio, na macho nishuhudie.”
“Okay! Sasa tuache tujadiliane.”
Rais Mlunji akaondoka.
Wakasalia watu watatu pekee. James, Magreth na mama Tausi. Rais Mlunji akaenda keti nje ya chumba akisubiri wamalize majadiliano yao waondoke kurejea mjini. Kabla hawajaanza zungumza, Magreth alitoa rununu kwenye pochi yake akabonyeza vitufe kadhaa baada ya hapo akawa kwenye maongezi na mtu wa upande wa pili.
“Tunaanza,” alisema Magreth.
“Hamna shida. Endeleeni na mpango,” ilisikika sauti ya nguvu iliyojaa ngurumo limtishalo mtu yeyote anayewasiliana. Hasa wale waanzao mawasiliano naye. Jenerali Anyilwisye.
Simu ikakatwa.
Baada ya hapo kilifuatia kimya kifupi, kilichochukua takribani sekunde hamsini na tisa, kikakatishwa na Magreth, kwa kujikohoza kidogo kisha akaanzisha maongezi.
“James!”
“Naam!”
“Katika safari yako, ulikutana na neno oktoba 15,...Rais anakwenda kufa,…the bodyguard,…save the VIP & DIE, si ndivyo?”
“Ndiyo, umejuaje hayo?”
“Sisi ni wamoja. Hivyo mengi anayoyafahamu huyu nami nayajua. Nitakupa stori kwa ufupi,…kipindi cha nyuma, enzi za utawala wa Rais wa awamu ya kwanza, Dkt. Chimpele Mwakatubu, sisi, nikiwa na maana na wale wawili waliotangulia mbele za haki, tulikuwa walinzi wa siri wa Rais Mwakatubu. Tukiwa watumishi ndani ya jeshi la ukombozi. Ina maana tulikuwa wanajeshi, na maafisa usalama wa taifa pia. Wenye ubobezi wa hali ya juu. Baadaye tukawa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa idara mbalimbali. Kipindi hicho, wale marais wastaafu wa awamu hizo zingine, walikuwa ndani ya kundi tawala. Wakifanya kazi ya kundi, si serikali. Vilevile walivyo, walikuwa viongozi wa jumuiya fulani iliyopo ndani ya kundi. Sambamba, na marehemu baba yake huyu Rais wetu wa leo. Baba yake alikuwa katibu Mkuu wa kwanza wa kundi tawala. Ambaye itikadi ya uongozi wake, ilikuwa haiendani na wale wastaafu, hivyo wakatokea kumchukia.
“…pindi Rais Mwakatubu anakaribia kuachia madaraka, akatuita kwa siri, akiwemo baba yake Rais wetu, akatuambia, anahitaji amwachie mamlaka Mchungaji Kibunda, pia akaongeza, anatamani, kundi la jumuiya yao, waje kuwa viongozi wakubwa baadaye. Imani iliyokataliwa vikali na wote tuliopo pale. Hatukukubaliana naye, ila Rais Mwakatubu, naye hakuafiki katazo letu la kuwapa mamlaka wale watu. Ambao tuliamini, wamejaa umimi. Akawapa, mwishowe wakapeana. Na ndiyo imani iliyotawaliwa hadi leo, ili uwe Rais wa taifa hili lazima upitie ile jumuiya. Fanya tathmini, utaniamini. Akitoka nje ya ile jumuiya, hawatoisha kumpiga vijembe, ili mradi achukiwe na wananchi. Kwa hiyo hiki kitokeacho kwa Rais Mlunji, ni njama iliyotengenezwa na wao. Ambayo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na baba yake, kutokana na utofauti wa maelewano uliopo baina yao, ambao alikuja uweka bayana siku za baadaye, kwamba anawachukia. Kutokana na umimi wao, wa kujiona wao ndiyo wanastahili ndani ya kundi.
“…hivyo juu ya yote yaliyosababisha haya, Rais Mlunji alilazimika kuundiwa balaa lolote la kumtoa madarakani. Hasa kupitia mzee wake. Ndiyo maana, karibu na Prof. Kadenge kuachia madaraka, baada ya Mlunji kushinda kwenye kura za maoni, walimrejesha baba yake serikalini, ili wapate kianzio kizuri cha kufa naye…”
“Nimekuelewa. Twende kwenye hoja husika.”
“James!...huu ni wakati wa ku—die kama ulivyotaarifiwa kwenye ujumbe uliopatiwa, ili Rais Mlunji aweze kunusurika na hili balaa.”
“Kwanini nife?” James alihamaki.
“Hapana, sio kufa. Die ni D—different, I—image, E—enabling. Unatakiwa uwezeshwe muonekano mwingine tofauti na huo.”
“Upi?”
“Huu uonekanao pichani,” alisema Magreth, huku akimfunulia picha, kumuonyesha maonekano anaopaswa kuonekana.
Viongozi wa kidola walijaa taharuki, walivyofikiwa na taarifa mmoja wa makamanda wa jeshi la ukombozi, aliyekuwa anaongoza kikosi kidogo chenye askari thelathini na mbili (platoon) katika kombania moja wapo ya komandi ya ardhini makao makuu, mwenye cheo cha Luteni, kaacha jeshi, kisha kachukua uamuzi wa kuanzisha kundi la waasi lenye lengo la kuishambulia serikali, hasa Rais Mlunji, kwa madai kanyonya stahiki zake alizopaswa kulipwa. Pia, kuchukua ardhi ya wazazi wake kamkabidhi mwekezaji, wazazi walivyojaribu kupigania haki yao, waliishia kupigwa risasi za kichwa, zilizoondoa uhai wao.
“Siwezi kumsamehe yule mjinga. Lazima akione cha mtema kuni. Ili atambue thamani ya damu amwagayo ya watu wasio na hatia,” alinukuliwa mwanajeshi huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Al maulid Khalfan, alipoojiwa na moja ya kituo cha runinga nchini humo.
“Na vipi kuhusu watu wa kundi pinzani, wakikuhitaji unaweza ungana nao?”
“Wakihitaji msaada wangu nipo radhi kuwapatia. Tena pasipo gharama zozote.”
Mwanajeshi huyo, ambaye alionekana kuwa kijana akakamata mtandaoni. Picha za video zake akijinasibu kwa ubabe zilisambaa vya kutosha, zilizoonyesha akizungumza, nyuma yake kukitawaliwa na maneno lukuki ya furukan, yaliyomfanya ahisiwe moja kwa moja kuwa mtu huyo si mwema kwa taifa. Pindi vyombo vya dola, vinakesha kumjadili namna ya kumkamata, kundi pinzani, likajawa uchu wa kufanya kazi na mtu huyo. Wakatafuta mawasiliano yake, wakawasiliana, na baada ya siku wakaonana. Walivyokutana walijadili mengi, yote yamhusuyo Rais Mlunji na serikali yake kwa ujumla. Miongoni mwa yale waliyoteta, ni hitajio lao la kutaka kumuondoa Rais Mlunji kwa mara ya pili. Walimuomba, waunganishe nguvu, na kumhaidi akifanikiwa kumuondoa duniani, watampatia wadhifa wa ukuu wa majeshi mmoja wao akishajitwalia mamlaka kwa mara nyingine. Al maulid hakupingana nao, alikubaliana, tena kwa urahisi sana pasipo tumia nguvu nyingi.
Watu wa upinzani walivyokuja sikia, kwamba yule mwanajeshi aliyeasi jeshi kaungana na kundi lao walifurahi sana. Wakakesha kumshangilia, na kujiaminisha ndoto waiotayo siku zote ya kuongoza taifa hilo inaenda kutimia. Jambo lingine lililowafanya wamkimbilie kumchukua, lengo awe sehemu ya msaada kuhusu mashtaka ya kijeshi wanayokabiliwa nayo. Ambayo mwenendo wake ulikuwa wa taratibu sana kutokana na watuhumiwa kuwakataa waendesha kesi wote walioteuliwa.
Rais Mlunji alivyofikwa na taarifa hii alizidishiwa mshtuko na ghadhabu moyoni mwake. Kulikoni mambo hayatulii. Likitoka hili, kuna lingine linalochipukia. Hakutuliana, naye akawa anakesha kila sekunde kuwasiliana na mkuu wa majeshi, ikibidi mtu huyo, aliyeibuka ghafla bin vuu auwawe. Sababu ni amri ya Rais, Jenerali Anyilwisye alitii agizo, akaandaa vijana watatu, watokao komandi ya komando akawapatia jukumu la kuhakikisha wanatekeleza agizo la mheshimiwa Rais. Hilo agizo likatekelezwa na idara zingine za ulinzi na usalama pia. Ziliunda vikosi mbalimbali kuhakikisha Al maulid anauwawa. Hakuishia hapo, akawapatia majukumu hadi watu wake wa karibu, wafanye hicho kitu kwa uharaka, baada ya kuona idara za ulinzi zitatumia mlolongo mwingi, ilhali hitajio lake huyo mtu asiwepo duniani.
“Kama hilo jukumu umedondoshea kwetu, waambie vikosi vyote vilivyoundwa kwa minajili ya kupambana naye, wasitishe mipango yao. Tena kwa kutoa tamko lionekanalo wakuu wote wa idara za ulinzi na usalama hawakupendi,”
“Inawezekanaje?”
“Hiyo ndiyo njia pekee, ya kukamilisha utakacho.”
“Mmmmh!...mnaniweka katika wakati mgu…” alisema Rais Mlunji, ila hakumalizia kauli yake, muito wa simu, iliyoonyesha kuna mtu anapiga, halafu jina la Al maulid likijibainisha kuwa ndiye mpigaji kwenye simu ya Magreth likamshtua na kumfanya ajawe hasira iliyomshinikiza awacharukie.
“Ina maana munanisaliti? Jinga kabisa ninyi, siwezi waacha hai,” alisema Rais Mlunji, huku akichomoa bastola na kuwaelekezea, ila ghafla akakumbuka kitu. “Kwanza James yuko wapi?”
“Tulia ufahamishwe,” alijibu Magreth, akipokea ile simu.
“Ndiyo, nakusikia, tupo wote hapa, leta habari.”
“Mpaka sasa nyatio liko vyema. Nishanasa ya muhimu. Bado wana mpango wa kurudia shambulizi, oktoba 15,” ilisikika sauti ya upande wa pili.
“Endelea nao. Mpaka kieleweke.”
“Vipi kuna lingine?”
“Hapana, ni hilohilo, likishafeli ndipo tutakuwa na mpango mwingine. Maana hao kazi yao siku zote kuwadandia wale wenye kujifanya wana uharakati wa kupingana na serikali, ila awamu hii wamepatikana. Acha tuwaonyeshe kazi.”
“Halafu la mwisho, ambalo nililisahau, wanafanya haya yote, nia mmoja wao arejee madarakani. Ambaye ni Prof. Kadenge.”
“Oooh! Habari njema. Endelea kuwa karibu utupatie habari motomoto.”
“Hamna shida.” Alisema yule mtu wa upande wa pili wa simu. Al maulid Khalfan kisha akakata simu.
Kikapita kimya kifupi mle chumbani. Kikafuatia kicheko baadaye, hasahasa Rais Mlunji aliyeonekana kuduwaa. Hii ilikuwa njama juu ya njama, piga nikupige, hadi mshindi apatikane, zilihitajika jitihada za kutosha. Baada ya kikao kile Rais Mlunji alivyorejea Ikulu akatekeleza ombi la Magreth. Lakini alianza kuwaita kwanza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakaeleweshwa ndipo mpango ukatimizwa. Utimizo uliosukwa, kiasi kwamba waliandaliwa askari maalumu, ndani ya idara zote wafanye mgomo, ili wajenge imani kwa wananchi, kwamba ndani ya serikali, wapogo watu waichukiao serikali ila huendelea kubaki humo kutokana na vi—sababu fulani. Watu wenye fikra ndogo, pande zote, wakahusisha tukio hilo katika itikadi za kisiasa. Askari waliogoma waache kazi wajiunge na kundi la Maliga, kukiongozea nguvu kundi hilo
Mwanajeshi aliyefahamika kwa jina la Al maulid Khalfan, alikuwa ni James. Alivishwa sura bandia asitambulike, lengo aingie ngome ya upinzani afahamu mipango waliyonayo. Hilo halikuchukua muda, mapema tu, alinyaka mambo mengi mno yaliyowapa mwanga wapi waanzie. Waliporidhika yanawatosha, waliunda mpango mwingine wa kumuondoa, ili wayafanyie kazi waliyoyapata. Nalo halikuwa na shida sana, kwani walipo wengi, pana mengi. Walikutana, wakajadiliana namna ya kufanya. Majadiliano yaliyochukua zaidi ya saa ishirini na mbili kufikia tamati.
“Hili lazima kikosi kazi kishiriki,” anasema Magreth, akiwaonyesha ramani, jinsi mpango unavyopaswa kutekelezwa ili ulete uhalisia kwa jamii watavyokuja kusikia na kuona.
“Mmh! Kwanini tusifanye kimyakimya?” anauliza mama Tausi.
“Hapana. Inatakiwa iwe wazi. Wananchi waamini, kwamba serikali imehusika moja kwa moja, ili viongozi wa upinzani wasishtuke ulikuwa mpango.”
“Ila uhisi tutakuwa tunampatia mzigo kubwa mheshimiwa? Utaomfanya ashindwe ubeba, maana kwa mtazamo nilionao, nahisi wananchi wataanza mjengea mashaka.”
“Usijali kuhusu hilo. Kikubwa tunachohitaji kujijengea heshima kwa watangulizi wake, na kuwafikisha sehemu sahihi ya kidola. Ambayo itawafanya watangulizi wake, wajutie maamuzi yao ya awali na huu mpango walionao sasa, wa kutaka kurejea madarakani wajisafishe.”
“Okay! Hao kikosi kazi watahusika vipi?”
“Anapaswa aandae kikao. Aidha cha waandishi wa habari, au mkutano mkubwa wa hadhara, ambao atazungumza maneno makali ya kumkashifu mheshimiwa Rais, baada ya hapo, kikosi kazi kitaenda haribu kikao chake kwa kumchukua mzobe mzobe na kuondoka naye.”
“Ni mpango mzuri. Kuteka hisia na akili za wengi, aandae mkutano wa hadhara.”
“Basi iwe hivyo.”
Pindi majadiliano yanafanyika, simu ya James, ilikuwa wazi na kujipiga katika moja ya namba zilizo kwenye orodha ya namba alizopigiwa. Pasipo mwenyewe kufahamu, kutokana na umakini wa kuielekeza akili yake, kwenye kile wanachokijadili. Yule aliyoko upande wa pili, mmiliki wa ile namba iliyojipiga naye akapokea, akaanza ita mfululizo, alipoona hakuna mrejesho wa kujibiwa toka kwa mpigaji, akaingiwa na msukumo uliomshinikiza akate simu. Lakini kabla dole gumba halijafikia kitufe cha kukatia, maongezi aliyosikia kwa uchache yalimshitua, na kumwongezea shauku ya kuendelea kuyasikiliza. Ile nguvu ya kukata, haikuwepo tena, zaidi ya nguvu ya tamanio, kuhitaji simu isikate mapema. Ila haikuwa hivyo, sekunde arobaini na tano tu baadaye, simu ilikata.
Yapo aliyoyaambulia kuyafahamu. Ambayo yalimshangaza, yalimjaza fikirio, zaidi ya mara sitasita kutafakari kama yana ukweli.
“Hapana, sipaswi kuyafumbia macho, niwafikishie viongozi wangu,” alijisemeza, kono lake la kushoto likiwa limeweka tuo shavuni mara baada ya kuweka simu mfukoni… “Ila wataniamije? Wasije niona mchonganishi baadaye, ambaye nufaiko nitalopata baada ya kuwataarifu ni kufukuzwa uanachama. Ningejua ningelirekodi, kidogo ingeliwapa uthibitisho. Lakini,…acha lolote na liwe, lazima niwaambie,” aliendelea kujisemeza. Kijana huyo aliyefahamika kwa jina Ramadhan Kibeloni. Mmoja miongoni mwa vijana wenye ushawishi mkubwa ndani ya kundi la Maliga, kupitia baraza la vijana la kundi hilo.
Baada ya ukinzani wa muda. Wa halmashauri ya kichwa chake, mwishowe aliridhia, kile alichokisia awafikishie viongozi wake. Alianza na Mwenyekiti wa baraza lao, alimpigia simu, akamuomba waonane, ombi lililokubaliwa mapema tu, alivyomjaza shauku ya donge la jambo alilonalo. Alivyohitimisha kwa huyu, alimpigia simu, kiongozi mwingine. Wa kundi, na wengine wabunge. Akafikisha idadi ya watu kumi. Muda waliokubaliana kukutana ulivyowadia, watu wote aliowasiliana nao walitii wito wake. Waliwasili eneo husika, ambalo ni pembezoni kidogo na bustani iliyopo katikati ya mji wa Lidede, itumikayo kupamba shughuli za wengi kwa upigaji wa picha. Katikati ya bustani hiyo, iliyochukua eneo lenye ukubwa wa mita hamsini, urefu kwa mapana, kulikuwa na mkahawa mdogo utoao huduma ya sharubati ya matunda mbalimbali. Nao walienda keti kwenye mkahawa huo. Ijapokuwa kulikuwa na benchi zilizo wazi zilizoko sehemu mbalimbali ya bustani hiyo, iliyopambwa kwa maua ya aina tofauti tofauti, pamoja na michoro iliyobuniwa kwa mawe, inayoashiria asili zipatikanazo nchini Mangaka. Hawakuishia kuketi tu. Walifanya na huduma pia ipatikanayo. Kila mmoja alikuwa na bilauri lililojaa sharubati aipendayo, ambayo Kibeloni, aliahidi kuwalipia, ikiwa kama shukrani la kutii wito wake, sambamba na kukonga koo zao alizohisi kujaa ukavu. Maongezi yakaanza dakika tano baadaye. Kila mmoja alivyopata, zaidi ya bilauri moja la sharubati, Kibeloni, aliyaanzisha, wageni wake wakitega sikio vyema kumsikiliza anenacho. Walivyosikia neno tata kwao hawakuacha kustaajabu. Huku wengine wakijaribu kumsitisha wachangie hoja ama kuuliza swali kutokana na kutoolewa.
“Mwacheni amalizie, mwishoni kila mwenye swali na mchango wowote atatoa,” alisema Kapteni mstaafu, Moomoo Mnukia. Mwenyekiti wa kundi la Maliga, ambaye naye alihudhuria.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kweli! Kibeloni alivyohitimisha, kila mmoja alionekana kuwa na swali. Kiasi kwamba walileta mchanganyiko wa kutaka kuwahi, hali iliyowafanya baadaye waende kwa zamu, kwa uzingatio wa wadhfa. Mtu mwenye wadhfa mkubwa ndiye alitangulia kuuliza. Kama alivyohisi mwanzo. Wengi wao walimuuliza maswali, waliyohitaji jibu la kuwapatia uthibitisho wa kuona kitu. Ambacho kinaonyesha, ama yanasikika maongezi aliyosikia. Kauli ya mdomoni pekee hawakuiyamini. Mpaka wathibitishe, jambo lililopelekea Kibeloni aingiwe na tahayari iliyomtamanisha ajiondoe ndani ya kundi hilo kwa kuhisi hatoaminika tena.
“Ndugu zanguni. Nilichozungumza kina usahihi. Wale marais wastaafu wana njama ya mmoja wao kuja kugombea urais uchaguzi ujao. Nimefahamu hilo kupitia kwa Al maulid Khalfan.”
“Ina maana, unataka kutuambia Al maulid anafahamu pia huu mpango?”
“Inaweza ikawa. Pia nimeingiwa na wasi, kwamba huyu jamaa, alijitoa jeshini, lengo aungane nasi awapeleleze hawa watu,” anasema Kibeloni. Misuli ya shingo ikiwa imekaza kutokana na kutumia nguvu kubwa katika uzungumzaji.
“Hilo nalo neno. Tuwachunguze hawa watu vizuri. Wote kwa ujumla. Kuanzia, Al maulid na wale wastaafu.”
“Sahihi, tena tusikawize. Maana lengo la hawa, kutumia mgongo wetu kujitetea, halafu baadaye wajitwalie mamlaka ya kutawala kundi letu.”
“Mmmmh! Hapa tumeingia mkenge. Kurupuka kurupuka ya kuwapokea watu sababu walikuwa na nguvu kubwa serikalini, inaenda kutuumbua,” anasema Kapteni mstaafu Moomoo Mnukia, huku akifuta kijasho chembamba kilichokuwa kinamtiririka, ijapokuwa eneo hilo, lilitamalaki miti mingi ipepeayo upepo mwanana wakati wote.
Kujihakikishia zaidi, wakampigia James (Al maulid) ila hakupatikana. Jambo lililochangia, wawe na uhakika nusu nusu.
“Huyu ndiye anapaswa kutuaminisha hii kauli. La sivyo, tutakuwa na uchunguzi ambao hatutofahamu kama unatija ama lah!” anakazia Kapteni mstaafu Mnukia pindi wakiondoka.
James alikuja patikana usiku. Kapteni Mnukia alimpigia, akamhoji mambo mbalimbali waliyoteta awali katika kujihakikishia ukweli ni upi. Sababu James, alikuwa na ufundi wa kutosha katika mambo ya usalama, hakumueleza ukweli. Alimwongopea, kwa kumueleza vitu vingine, lengo ndege wasipeperuke kabla hawajitimiza azimio lao. Alimwambia, simu aliwaachia vijana waliokuwa wanajadiliana habari za kiitikadi kwenye shina moja, alilolitembelea kwa ajili ya kupata dondoo za hapa na pale zihusuzo serikali. Walivyohitimisha maongezi, Kapteni Mnukia akawapigia wale wengine, kuwaeleza alichoambiwa na James, ambaye wao walimfahamu kama Al maulid. Ikawafanya wajadiliane simuni, baadaye wakaunda kundi la whatsapp kwa waliokutana mchana pekee wajadiliane waweze kufikia muafaka, sababu wao ndiyo wabebao kundi lao kwa jamii.
“Tunaamuaje katika hili?”
“Kama kanena hivyo, tuendelee na uchunguzi. Tupange muda, kama miezi mitatu, ama miwili matokeo tutayoyapata ndiyo tuyaamulie.”
“Ushauri mzuri. Ni vyema tukaufuata.”
“Sawa.”
Japo aliongopa. Nafsi yake haikutuliana, baada ya kuona kile walichojadiliana kimevuja. Akawataarifu wenziye. Akawahadithia mwanzo mwisho, alivyopigiwa simu alivyoulizwa, hata jumbe za missed call alizopigiwa awali akawa hapatikani. Nao wakaingia kwenye majadiliano, ila mafupi, yaliyotoa matokeo ya kuendelea na mipango waliyopanga mwanzo.
Katika kuelekea safari ya uhakika ya utimizaji, wakawataarifu kikosi kazi, mpango ulivyoratibiwa, wakaridhia kuutekeleza. James naye akatoa ombi kwa uongozi juu ya hitajio la kufanya mkutano wa hadhara, akijinasibu ana mengi aliyoyavumbua toka kwenye kijiwe alichodai alitembelea yafaayo kuwekwa hadharani wananchi wafahamu. Akakubaliwa. Akaandaliwa tangazo, lililorushwa vituo mbalimbali vya runinga, redioni, gazetini na kwenye mitandao ya kijamii. Kila aliyefikiwa na tangazo hili, akajaa mshawasha wa kuhudhuria hata kama yuko mbali kiasi gani na eneo lililoteuliwa mkutano kufanyika. Ukizingatia, ni mara ya kwanza, kwa James (Al maulid) kuonekana hadharani kuongea na wananchi. Wengi walimshuhudia mtandaoni.
Jumamosi, ndiyo siku pendwa iliyopangwa mkutano huo kufanyika. Katika viwanja vya Mwakatubu (Mwakatubu square) vilivyopo mjini Lidede. Wasikilizaji wakaanza kufurika uwanjani kuanzia saa sita mchana. Wengi wakiwa wa hapohapo mjini Lidede na wachache toka miji mingine. Vyombo vya habari, vyenye vibali vya kurusha mubashara mkutano huo viliseti vyombo vyao mapema mno, sambamba na wale ambao walijiandaa kwa ajili ya kurekodi baadaye waanze tuma kwenye mitandao yao.
Mnamo saa nane mchana, mkutano ukaanza. Jukwaa kuu likipambwa na viongozi mbalimbali wa kundi la Maliga, kumsindikiza mwenzao. Hivyo kabla, James ajapanda jukwaa dogo kuhutubia walianza hao wengine, walivyomalizika ndipo akafuatia.
“Katika mkutano wako, usisahau kutamka neno hili, wapinzani huishi kwa kauli. Kauli ambazo wanataka waaminiwe moja kwa moja pasipo kupingwa, hasa zile zihusuzo serikali,” alikumbuka James, aliposimama nyuma ya mimbari, wakati huo akisaili vipaza sauti vilivyojazana, achukue kipi.
Tathmini yake ilivyokamilika, akachukua vipaza viwili. Akaanza tupa neno, pasipo lisahau lile aliloamriwa kulitamka. Kama walivyopanga, maneno aliyoyatamka yalijaa kashfa nyingi, yaliyoshawishi wananchi muda wote wampigie yowe kumshangilia. Hakuna aliyehisi, kuwa huo ni mpango, ulioratibiwa kwa lengo la kuwadhorotesha marais wastaafu japo ungeliitia doa serikali kwa kiasi kikubwa. Hawakujali hilo. Walichozingatia, adui yao awe sehemu mbaya. Dakika kumi baadaye, toka alivyopanda, ving’ora vya nguvu vikaanza sikika. Vilivyowatambulisha watu waliokusanyika mahali hapo kuwa hiyo ni gari ya askari. Hadi ikafikia hatua ya kugeuza macho nyuma yao kuangalia, kulikoni, lakini hawakuambulia kitu, kwa sababu gari haikuwa karibu. Wakarejesha macho jukwaani, kuendelea kumtazama namna James (Al maulid) anavyohutubia, kwa maneno yatoayo cheche.
Mlio ulivyokuja sikika karibu. Ndani ya gari alibaki dereva pekee, huku akizidi kukanyaga mafuta kuelekezea halaiki ilikokusanyika. Jambo lililowashangaza watu wengi, wengine wakijiiandaa kutengeneza njia lipite wasije wakagongwa. Pindi wale walioko nyuma wanahangaika na gari, wale wa mbele wakawa wanashuhudia mengine. Jukwaani palichafuka askari, waliokesha kutembeza kichapo cha rungu mwilini mwa James. Huku wakimbeba juujuu pasipo mpangilio, mithili ya gunia la karanga lisilo na ujazo wa kutosha. Wananchi wakaanza kutawanyika ovyo. Wa mbele, wakajitahidi kukimbilia nyuma, wa nyuma wakajitahidi kukimbilia mbele, wakakutana katikati. Wakatengeneza mgongano mkubwa uliowapatia maumivu mwilini mwao hasahasa waliokutana kwa nguvu.
“Jamani hii nini?” alisikika mama mmoja, aliyekazana kukimbia toka upande wa nyuma kwenda mbele.
“Huoni kuwa pamechafuka? Amani ishatoweka, askari wameingia kati wanapiga watu utazani watoto wadogo,” alijibu, mtu aliyekuwa anatoka mbele kukimbilia nyuma.
Saa zijazo ni uvumi tu, mitandaoni na kwenye vyombo mbalimbali vya habari juu ya kile kilichotokea. Tukio hilo likawapa nafasi wananchi wabwabwaje watakavyo, maneno lukuki yenye machungu kuiendea serikali. Hata Rais Mlunji naye alikuja juu, kuwafokea wasaidizi wake katika hili, ila alitulizwa baadaye, alivyofahamishwa mpango nzima. Al maulid, alivyoadimika, kwa kutooneka sehemu alizopendelea kutembelea, wakaongeza maneno serikali wamemfanyia kitu mbaya, tena lilivyookotwa fuko la sandarusi likiwa na mwili wa mtu aliyeuwawa wakazidi, kupandisha sauti zao, aliyeko kwenye mfuko ndiye Al maulid.
Uzuri, kelele zao zilikuwa za mitandaoni pekee. Ama wakutanapo vijiwe mbalimbali. Wakishayazungumza huishia hapohapo, kisha hupotelea mbali. Ijapokuwa, imani haikuacha kubaki moyoni mwao taratibu, kila tukio baya litokeapo.
“Sasa ndiyo mahususi, weka ile mambo ili tuharibu moja kwa moja,” anasema Magreth. Walipokutana eneo lao la maongezi.
“Hamna shida. Hapa ni mwendo wa kuwachanganya wananchi, ili mambo yaanze kaa mstarini,” mama Tausi akachangia hoja.
“Ni lazima wamkumbuke Rais Mlunji,” James naye akachangia.
Walivyoweka tuo, kuashiria mjadala huo mdogo umehitimishwa, mama Tausi akaivuta kompyuta mpakato iliyo jirani naye, aina ya Huawei mate book X pro akaiwasha, baada ya hapo akawa ulimwengu mwingine wa habari uliomfahamisha yaliyojiri. Baada ya kuperuzi huku na kule, akaingia kwenye moja ya mitandao ya kijamii anayoimiliki. Mtandao wa Instagram, ila alikuwa anatumia jina bandia, na mara nyingi hutuma taarifa za matukio zipendwazo sana na wengi, wale waipendao serikali na wachache wenye itikadi pinzani ambao walivyoona yaongelewayo hutokea. Akaihariri hiyo taarifa. Alivyojihakikishia iko poa, na wenziye walivyothibitisha akatuma mtandaoni.
Dakika tano baadaye, taarifa hiyo ilionwa na wengi. Kiasi kwamba hata watu wamilikio chaneli za youtube walikesha kutengeneza picha za video ihusuyo ujumbe huo kisha kutuma kwenye chaneli zao. Ujumbe huo, uliambatana na sauti. Na ndicho kilichowavuta wengi, waipitie, kwani kila aliyesikia na kusoma hakuacha kumtaarifu mwenziye aingie kwenye mtandao husika alioutumia kusikiliza. Hatimaye ikazua sintofahamu, watu wenye itikadi za upinzani, wakakesha kujitetea, na kuwatetea wahusika waliotajwa kwenye taarifa hiyo, huku wale wa upande tawala, wakikesha kukandamiza taarifa hiyo ni ya kweli.
“Uchaguzi ujao, mmoja miongoni mwa marais wastaafu, waliotimkia Maliga ana lengo la kugombea urais kupitia kundi hilo. Ndiyo maana, wamemwondoa Al maulid kwa kuhofia anaweza kuwapiga bao kwa kujizolea mashabiki tele kutokana na harakati alizozianzisha,” ulisomeka ujumbe huo. Sambamba na sauti iliyotambulisha marais wastaafu wakiteta jambo hilo.
Hiyo habari ikagawanyisha watu. Wenye itikadi pinzani, walilia kusema hiyo ni siasa tu, yenye lengo la kuwachonganisha, itikadi tawala nao wakaendelea na msimamo wao.
“Taifa letu ndipo lilipofikia. Mtu wa upinzani akitenda kosa, halafu likawa rekodedi, aidha kwa sauti au picha ya video, matokeo yapatikanayo, utasikia hivyo vitu ni vya kutengenezwa. Halafu wale waliopo serikalini, sauti au picha za video zao huwa ndizo za kweli.”
“Acha tu. Ila ipo siku ukweli utabainika.”
Marais wastaafu walivyofikiwa na taarifa, walihamaki. Hasira ikawapanda mithili ya mbogo, kiasi kwamba, vifua vyao vilitanuka kutokana na namna walivyofura. Viongozi wakuu wa kundi nao wakawa na mitazamo yao, iliyowahimiza waimarishe uchunguzi kuwachunguza, japo katika majukwaa ya nje walikesha kuteta wanaonewa.
Wastaafu walivyosikia hivyo wakahisi hawajatiliwa shaka. Wakakesha kuendelea na mipango yao. Ambayo baadaye walimshirikisha Kapteni Moomoo Mnukia. Walimueleza kila kitu, wanachohitaji kufanya, hapa walimfungukia juu ya habari ziendeleazo kuenea na kumhaidi donge nono la pesa atapowakubalia. Walitumia njia hiyo baada ya kuhisi walichopanga kinaweza kuleta vurugu kubwa ndani ya kundi.
“Tunaomba, utupatie hiyo ridhaa. Tutakupatia bilioni tatu kama shukrani, pia, tukiingia madarakani, itakuwa njia rahisi ya kundi kuendelea kutawala. Si unaona jinsi tunavyokubalika huko mtaani?” alisema Prof. Kadenge, wakiwa wameketi kwenye moja ya hoteli mjini hapo.
“Siwezi kuwa peke yangu katika hilo. Yafaa kuwashirikisha waasisi wa kundi.”
“Hapana. Wewe ndiyo mwenyekiti. Watu wote wanatupa jicho kwako, ukiridhia tu, hamna atayebisha.”
“Nipeni muda.”
“Hamna shida. Tunaweka utegemezi tu.”
Wakampatia muda, ila walimsisitiza asiwaambie wengine, lengo wasiharibu mambo. Kwani kilichotakiwa kufanywa ni muundo wa amri. Na sio kushirikiana, kuepuka ukinzani wa hoja utaoleta mtafaruku na mpasuko. Muda waliokubaliana ulivyokwisha, wakakutana kwa mara nyingine. Awamu hii hawakuwa na maongezi marefu. Kapt. Mnukia alitoa mrejesho wa kile alichoambiwa. Aliridhia! Hatua iliyowafurahisha mno marais wastaafu. Huku wakijipa imani, kile walichodhamiria kinaenda kufanikiwa. Walisubiri muda tu, apendekezwe mmoja wao, asilimia kubwa akiwa Prof. Kadenge. Kisha atangazwe kwa wanachama.
****
Mwenendo wa kesi mahakama zote ukawa usioridhisha, kwani mashahidi wote waliopaswa kuthibitisha tuhuma zinazowakabili waliteketea mmoja baada ya mwingine, kama mwewe amendeavyo vifaranga. Hali iliyopelekea wawekewe ulinzi, wa askari polisi lakini haukusaidia kwani walizidi kuuwawa, mpaka miongoni mwao wakawa wanakataa kwenda kutoa ushahidi kuhofia ukatishwaji wa maisha yao. Kitendo hicho kikawapa picha, kesi hiyo itakuwa ngumu kukamilika, pia isitoshe, mahakama itachukua muda mrefu kuwatia hatiani. Kiasi kwamba hata muda wa utawala wa Rais Mlunji unaweza malizika kesi bado haijaisha.
“Tunafanyaje hapa? Mambo yanazidi kuwa magumu,” aliuliza Rais Mlunji.
“Nami nashindwa kufahamu. Tuwauwe tu, hamna cha ziada.”
“Lengo si kuwauwa. Nahitaji waahibike kwa wananchi, ili watambue lawama walizokuwa wananipatia sizo.”
“Unahisi hilo litawezekana? Ilhali kila kitu kinakimbiziwa kwenye siasa?”
“Nahitaji sasa liwezekane.”
Kikapita kimya kifupi. Kilichoonyesha kila mmoja akimakinika. James akaja vunja ukimya huo.
“Nimepata wazo,” alisema.
“Lipi tena?” wote waliosalia walimvaa wakamtupia swali hilo. Lililomfanya atulie kwa muda akiwatathmni jinsi walivyojawa na mshawasha wa utambuzi.
“Punguzeni munkari. Cha kufanya ni kitu kimoja tu. Sababu wana nia ya kumuondoa mheshimiwa duniani…” alisema James, ila hakumalizia kauli yake, sauti ya Rais Mlunji, aliyemvaa na moja ya mkono wake mdomoni ilimkatisha.
“Wanataka kuniua?”
“Ndiyo. Huu mpango ulipaswa utokee siku ya kusherehekea taifa letu kupata uhuru, ila sisi tulikukomboa, baada ya kumdungua mtu waliyemwandaa kwa ajili ya mauaji yako.”
“Mungu wangu! Mbona wananiandama hivyo?”
“Wanachohitaji siri yao, ibaki kuwa siri.”
“Hapana! Hapana! Nami sasa yanipasa kuingia uwanjani, nipambane nao ana kwa ana.”
“Si kwa pupa hivyo. Tuachie kazi. Sababu mpango wao bado ni endelevu. Wanahitaji siku nyingine ya kusherehekea taifa letu kupata uhuru mwaka ujao wautekeleze. Ndiyo muda ambao unatakiwa nasi tuoneshe ubabe wetu.”
“Tutawaonesha vipi?”
“Awamu hii, wamedhamiria, wote washike mitutu wakuangamize. Hivyo, tunachopasa kufanya ni kuwadhibiti siku hiyo hiyo ya tukio. Hiyo siku unapaswa uwe na mlinzi mwingine tofauti na mama Tausi, ili aweze kujiunga huku kwetu iwe rahisi kuwadhibiti.”
“Unahisi tutaweza?”
“Yeah! Tena kwa asilimia mia moja.”
Uratibu wa kukamilisha mpango huo ukaanza mapema, punde tu walivyotoka kikaoni. Ambacho askari wa kikosi kazi nao walihudhuria. Wakapangiwa majukumu. Sehemu kubwa ikiwa ni ukaguzi wa makazi waishio hao wastaafu. Kwani waliamini huko makazini mwao kutakuwa na siri kubwa ya kuwasaidia. Hilo halikuwa shida. Waliporejea makwao, jambo la kwanza kila mmoja alifanya utafiti utaomfahamisha mstaafu aliyekabidhiwa mahali gani anaishi. Maana waligawana. Ili siku watayokutana, wakutane kwa lengo la kufanyia kazi matokeo ya utafiti.
Katika kuhakikisha mambo yananyooka, waliyaacha kwa muda makazi yao. Wakawa wanatanga tanga miji husika ambayo waliamini wanapatikana. Ijapokuwa kwa asilimia kubwa, walidumu jijini Naparavi na mjini Lidede. Kilichowarahisishia, kupata mwangaza wa mafanikio, wa kufahamu nyendo zao, ni askari waliokuwa wanawalinda. Kazi yao kubwa ikiwa kuwahabarisha wana kikosi kazi mienendo yote, ukizingatia walikuwa wanaagwa, siku wasizoagwa huulizia kwa watu wengine waliosalia nyumbani. Hasa hasa kwa watoto, wafanyakazi na mama pia wapatapo muda wa kumuona.
Kwa wakati huo, marais wastaafu hawakuwa na ufahamu huo. Kwamba kuendelea kutumia huduma za serikali, hasa za ulinzi zinaenda kuwaangamiza. Waliona poa tu, kama ilivyo kawaida ya watu waishio chini ya jangwa la Sahara, hupenda mteremko. Walijisemeza waache waendelee kuinyonya serikali, huku wakitafuta mbadala wa kunyonya zaidi. Hawakuwa na chembe, kama ipo siku kibao kitageuka. Wao ndiyo watanyonywa badala ya ile sehemu waliyokuwa wanatarajia.
Siku nyingine watokazo nyumbani wakawa wanafuatwa kinyume nyume, wafahamu eneo lipi waendalo. Zoezi lilikuja fanyika miezi minne baadaye tangu mpango ulivyosukwa. Wakafanikiwa kupafahamu. Haikuwa sehemu moja tu, zilikuwa mbili, moja wapo ni katikati ya mapori, nyingine, mjini. Kwenye hoteli tatu kubwa zenye hadhi ya nyota tano zilizozunguka uwanja wa mpira wa miguu, ufahamikao uwanja wa Umoja. Juu ya ufahamu wa maeneo, walienda mbali zaidi, kupata ufahamu mwingine uliowaaminisha kuwa wazee hao wana njama ya kumuondoa Rais Mlunji duniani. Walibaini ufanyaji wa mafunzo ya ulengaji shabaha huko maporini, walifahamu hilo kupitia milio ya risasi. Halafu kule mjini kwenye hoteli walizokuwa wanatembelea, wakabaini, kuwa ndizo hoteli watazotumia kujificha pindi wanafanya shambulizi.
“Kwanini hawa wazee hawataki kukubali? Si waachie haya mambo? Washazeeka halafu wanaendelea kung’ang’ania vitu visivyo.”
“Hiyo ndiyo njia rahisi kwao kujilinda. Wanapaswa kufanya hivyo ili watimize takwa lao, mmoja miongoni mwao kurejea madarakani waendeleze miradi. Kwani wanaamini, kwa yale yote waliyotenda wakikaa kimya watachukuliwa hatua zitazowafedhehesha.”
“Dah! Kazi kwelikweli.”
“Tena sana ila ukweli utabainika hivi punde. Utaowaweka wananchi huru, na si kusukumwa sukumwa kwa mihemko isiyo na msingi.”
Waliteta kikosi kazi, walivyokutana, kufanya tathmini ya hatua waliyofika.
“Kilichosalia, ni kuingia zile sehemu waingiazo. Kule porini lazima tuingie kwenye lile jengo waingialo, halafu hapa mjini zile hoteli. Kwa namna yoyote, tufanikishe hili,” anasema ASP Nendakulola.
“Hamna shida afande. Mpango lazima ukamilike kwa asilimia mia moja. Tumeapa sisi, hivyo lazima tutendee kazi viapo vyetu,” anachangia sajini Zena Chaula.
Kweli! Siku iliyofuata wakagawana majukumu. Mrakibu Msaidizi wa jeshi la polisi Nendakulola, akiambatana na Konstebo Juma Makokola, walijikabidhi kufuatilia jengo la kule porini, huku Sajini Zena na Koplo Malkiadi Makambo, wakajipa kazi ya kufuatilia zile hoteli. Kidogo, ilikuwa kazi ngumu, iliyohatarisha maisha yao moja kwa moja ila walithubutu kujitoa kwa minajili ya kutimiza takwa la mheshimiwa Rais. Hata kama yupo mwenye imani inayokinzana na mwenendo huo. Wale wa porini, walizuru porini mapema sana. Wakiwa na vifaa nyeti vitumikavyo kuvunja milango na sehemu mbalimbali za jengo endapo watashindwa kupata sehemu ya kuwawezesha waingie. Pasi na sahau bunduki za mapigano ya karibu. Wakatafuta eneo zuri wakatega. Kusikilizia waendeleacho kufanya marais wastaafu, walivyowashuhudia washaanza kupiga hatua kuondoka wakajisogeza taratibu kuliendea jengo lilipo. Walilizunguka kwanza. Kabla ya kufanya kitu chochote, waweze kujibainisha ufahamu wa mazingira yatayowawezesha kuingia ndani.
“Tutumie Bleacher tu afande. Ili tusipoteze muda na hizi mbinu zingine ndogo ndogo,” anasema Konstebo Juma.
“Ila si watakuwa hawajafika mbali wanaweza kusikia tukifanyacho.”
“Hapana. Haina haja ya kutanguliza mawazo kama hayo afande. Hapa tunahitaji mawazo ya ushindi pekee.”
“Sawa. Ila hofu haikosekani. Kwani nayo ni sehemu ya ushindi.”
Baada ya majadiliano ya muda mfupi wakaafikiana. Haina haja ya kuendelea kupoteza muda, wafanye kilichowapeleka. Sababu uchumi wa taifa lao ulikuwa unaoendelea, si ulioendelea vifaa walivyokuwa navyo, vilikuwa vya ki—local. Havikuwa vile vya ki—elektroniki. Ambavyo asilimia kubwa utendaji wake uendeshwa na mashine. Wao walikuwa na vifaa, ambavyo utendaji wake, hutegemea nguvu kubwa ya uendeshaji wa binadamu. Walikuwa na bleacher ambazo, hukamatwa huku na huko na watu wawili kutokana na uzito wa kifaa hicho kisha hukiamrisha kubomoa. Daima huitaji nguvu kwa kiasi kikubwa, kwao ikawa rahisi. Kwani, hesabu mara tatu tu, wakafanikiwa kuvunja mlango wakapata mwanya uliowawezesha kuingia. Walipiga hatua za mnyato, kichwani wakiwa wamevaa tochi zilizokesha kutoa nuru iliyowawezesha kuona mule ndani, kwani mlitawaliwa na kiza kikali.
Wakati huo sajini Zena na Koplo Malkiadi walikuwa ndani ya lifti ya moja ya hoteli watembeleazo marais wastaafu. Wakielekea chumba husika walichoelezwa na mhudumu wa hoteli hiyo walivyojitambulisha kinaga ubagha kuwa wana shida na watu hao. Mikononi mwao walikuwa wamekamatia mabegi madogo yaliyoonekana kuwa na vitu vingi kutokana na muonekano wa ujazo uliojinasibu waziwazi. Lifti ilivyofika usawa wa ghorofa husika waliyohitaji ilifunguka. Wakatoka, wakapiga hatua kuelekea maliwatoni ambako walibadili mavazi wakavaa mavazi mengine yaliyowatambulisha kuwa mafundi umeme toka shirika la umeme nchini kwao. Wakiambatanisha na vitambulisho kuwathibitisha wao ni mafundi. Baada ya hapo walipiga hatua hadi chumba husika. Chumba namba 815 ambacho kilikuwa na mlinzi wa pekee tofauti na wale walindao jengo hilo. Walimkuta mlinzi aliyeshiba shiba, kwani kifua kilikuwa kimejaa, dhahiri, kikamtambulisha kuwa ni mtu wa mazoezi. Kimwogopechasho mtu yeyote mwenye roho nyepesi katika anga za kimapigano, achilia mbali rangi ya ngozi yake. Rangi nyeusi, nyeusi hasa, akiwiana na watu wenye asili ya taifa la Kabil.
Muonekano wake, ulikuwa wa kuteteresha. Ila si kwa vichwa vilivyosimama mbele yake. Wao walikuwa wazee wa mazoezi zaidi yake. Japo miili yao iliwatambulisha kuwa dhoofu. Walijitambulisha, kuwa ni maafisa toka shirika la umeme, wapo hapo kwa lengo la kushughulikia hitilafu waliyoarifiwa. Waliongopa. Maelezo yao yakampatia wenge kidogo yule mlinzi. Lililomfanya ajiume ume kwa kushindwa awapatie jibu gani.
“Haruhusiwi kuingia mtu yeyote humo chumbani zaidi yetu,” alikumbuka yule mlinzi. Kauli aliyowahi ambiwaga na marais wastaafu pindi wanampatia tenda ya uangalizi.
Akaduwaa. Huku Koplo Malkiadi akizunguka zunguka kusaili mazingira ya mlangoni yalivyo. Yule mlinzi akiwa bize katumbua macho kumwangalia sajini Zena. Angaza angaza ya Koplo Malkiadi akabaini mwanya mdogo kati ya ulipoishia mlango, na sakafu iliyorembwa kwa malumalu. Akachomoa kitu fulani mfano wa golori ndogo ndogo akatupia kwenye mwanya huo. Hazikupita dakika mbili, wakashuhudia moshi ukitutuma toka ndani uliomshinikiza yule mlinzi alegeze mkazo wake wa kutaka kuwaambia hamna kuingia.
“Tupatie funguo,” alisema sajini Zena, akionekana mwingi wa mambo yamemchanganya hasa moshi ulioendelea kututuma na kutoa harufu ya kuungua kwa kitu.
Kuona hivyo mlinzi hakubisha. Chap, alitoa funguo akawakabidhi. Naye kusogea pembeni kabisa, kama sio kutoka nje kabisa kwa muda fulani akawa anaonekana kuongea na simu. Mule ndani kina sajini Zena wakafanya watakacho. Walikesha kupiga picha baadhi ya vitu walivyokuta. Zikiwemo nyaraka zihusiazo na uratibu wa mpango.
“Haina haja ya kuchukua kitu chochote. Tuviache kama vilivyo. Isipokuwa tuchukue picha ya video na mnato,” wakakumbuka jambo.
Mlinzi kule nje alihaha, tena zaidi ya kuhaha, kwani simu zake alizopiga hazikupokelewa. Baadaye akakata shauri kusubiri wampigie punde wale awapigiao watapofanikiwa kuona missed call zake. Lakini alikata shauri kwa hali ya basi tu, moyo wake hukuridhika, ila angelifanyaje? Hakuwa na namna, aliishia kusikilizia ajionee matokeo yatakuwaje. Dakika saba baadaye akashuhudia kina sajini Zena wakitoka mle chumbani. Nyuso zao zikitawala furaha sababu sehemu ndogo ya mpango wao ushatimia. Walivyomfikia walimuaga, wakamwachia funguo kisha wakapiga hatua kuendelea na safari. Hatua nne toka walivyomuacha, simu yake ikaanza kuita. Akaitoa mfukoni chap, akaangalia jina la mpigaji, alivyombaini aliminya kitufe cha kupokelea kwa haraka akaweka sikioni.
“Mkuu!” aliita.
“Ndiyo, kulikoni?”
“Kuna ajali ya moto ilitokea mkuu chumbani kwenu, wakaja maafisa wa shirika la umeme kushughulikia.”
“Ina maana wameingia ndani?”
“Eeh!...wameingia.”
“Shit! Hiyo hitilafu uongozi wa hoteli wanafahamu? Na vipi kuhusu muito wa alamu kuashiria kuna hatari ilisikika?”
“Dah! Sina hakika kama wanatambua. Maana waliniibukia tu pale chumbani na nilivyoangalia kweli kulikuwa na moshi unaofuka toka ndani. Ila alamu haikulia.”
“Aaakh! Tumechezewa,” alisema. Yule aliyekuwa anawasiliana na mlinzi. Ambaye ni Prof. Kadenge. Kauli iliyowashtua wenziye kwa sababu alitamka kwa nguvu.
Hakuwa na budi, naye akawahadithia wenziye. Wakiwa katikati ya safari kutafuta mjini. Gari ikiendeshwa kwa kasi isiyo ya kawaida wapate kuwahi waweze kufanya mambo mengine. Hata wenziye pia walistaajabu. Hatimaye wakasimamisha gari pembezoni wapate kuteta. Maongezi hayakuwa ya muda mrefu, muda mfupi tu, wakaendelea na safari. Ila hawakufika mbali, mmoja wao akaamuru kwa nguvu gari isimame.
“Kuna nini tena?” watu wote walimtupia swali yule aliyetoa amri hiyo. Rais mstaafu Lameck Nchenga.
“Nimesahau shajara yangu kule porini,” anasema. Akionekana mwenye hamaniko tele.
“Kwa hiyo unashaurije?”
“Sababu tumejipa likizo ya siku tatu ya kufika huko kuanzia leo, ni heri turudi nikaichukue. Si mnajua kuwa ile ndiyo kila kitu kwangu?”
Kikapita kimya kifupi. Kilichochukua takribani sekunde arobaini.
“Haina haja ya kupoteza muda, turudi tu,” anasema Wambili, ambaye ndiye dereva wao. Akakata ukimya huo.
Naam! Ushauri huo ulifikiwa na wote. Gari ikageuzwa safari ya kurejea watokako ikaanza. Mwendo ukiwa zaidi ya ule waliokuwa wanatembea nao mwanzo. Huku wakipepewa na ubaridi kiasi toka kwenye kiyoyozi kilichopo ndani ya gari hiyo. Toyota Land cruiser ZX V8. Iliyo tinted nyeusi iliyowazuia wasionekane japo chembe ya unguo waliovaa.
****
Mrakibu Msaidizi (ASP) Nendakulola na Konstebo Juma walifanikiwa kuingia ndani ya lile jengo. Miale ya mwanga wa tochi walizovaa kichwani zikawapa nuru ya uonaji. Maana mazingira ya ndani yalitawaliwa na kiza kinene ambacho hutoa ugumu wa kuona pasipo kisaidizi. Walizungusha vichwa huku na kule, kwa uchache na uwazi, wakashuhudia mazingira yaliyomo ambayo yaliwatanabaisha kuwa si mema. Na wale watu wana mpango ambao ni mbaya kwa siku za mbeleni. Kama nyapio walilonalo linavyosema. Ndani mlijaa mabango yaliyoshikizwa na vi—miti yakasimamishwa sehemu fulani, umbali mdogo, toka ilipo meza moja iliyojaa maganda ya risasi juu. Mabango hayo yalionyesha picha ya mkaburu al maarufu ma—bull yanavyotambulika na wabobezi wa mashambulizi ya kutumia bunduki.
Hawakutaka kutoka bure, wakapiga picha za mnato pamoja na video baadhi ya vitu ambavyo waliamini vitakuwa sehemu ya ushahidi, kupitia simu na kamera ndogo za kidigitali. Hawakuishia sehemu moja. Walizunguka vyumba vyote vilivyomo. Kisha vile walivyovihisi sehemu ya msaada kwao, walifanya kama sehemu ya kwanza. Katika pita pita wakatumbukia eneo moja lililoegeshwa mazulia kwa juu na kuwekwa kibao kilichoandikwa usipite, lakini wao hawakuona, hivyo walivyoangukia eneo hilo walijikuta wameangukia kwenye chuma kizito kilichotengenezwa kwa umbo la pembe nne, chenye urefu usiozidi mita moja na upana usiozidi mita moja pia. Huku kikiwa na kufuli nyingi zilizofungwa ziashiriazo kuna kitu chini yake.
Wakashawishika. Wajionee kitu kilichopo chini, hivyo mmoja wao alirudi watokako akabeba bleacher akarudi nao pale walipoangukia wakaanza ubomoaji. Sehemu hii kidogo iliwapa shida. Ilikuwa sehemu ngumu, ambayo ugumu wake hautofautiani sana na ule upatikanao kwenye mlango wa strong room benki. Ila hawakukata tamaa. Walijivika ushujaa, kuhakikisha azimio linakuwa timilifu. Awali walifanya kwa ushirikiano. Yaani wote walishika bleacher kisha kubomoa, walipochoka wakafanyiana zamu, mmoja mmoja achokapo mwingine hukamatia gurudumu lisonge mbele. Waliketi eneo hilo zaidi ya dakika kumi na tano, hadi nguvu za mikono zikaruhusu uchovu uliowashinikiza wapumzike kwa muda ndipo waendelee. Walifanya hivyo, kwa kujilaza juu ya lilelile chuma, wakiamini bado halijaanza kuachia ndiyo maana kunakuwa na ugumu katika ubomoaji.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipiga mianguko, huku wakisindikiza na maongezi yahusuyo mbinu wanayopaswa watumie wafanikishe zoezi hilo. Ila maongezi hayo hayakuchukua muda, usingizi ukaanza wanyemelea taratibu mwishowe ukawapitia kabisa pasipo matarajio. Pindi unashikilia akili zao, kwa kuwaficha kiendeleacho, marais wastaafu, wanawasili eneo watumialo kuegesha gari, kisha Rais mstaafu Nchenga akateremka na kupiga hatua kulifuata jengo lilipo. Hatua alizokuwa anapiga ni zile za kukimbia zikichanganyikana na kutembea, picha ya jengo aliendalo alivyoanza liona alipunguza mwendo, akawa anatembea taratibu, hali iliyochangiwa na unyong’onyo pia kutokana na kukimbia. Alivyofika umbali fulani, ambao alishuhudia vyema jengo lilivyo, akashtuka. Mara baada ya kuona mlango uko wazi na hauna mazingira yenye kuridhisha. Akapigwa na butwaa, butwaa lililomkumbusha wenziye. Akatoa simu mfukoni, akampigia mmoja wapo.
“Mambo yameharibika, njooni huku, nahisi kuna mtu ndani, maana mlango umev…” anasema, huku akiwa mwenye mtetemo uliomsababisha ashindwe kuongea vyema.
Yule aliyempigia naye akawafikishia wenziye. Vile alivyoarifiwa, hali iliyowafanya wateremke garini mzobe mzobe na kutoka mbio. Walivyofika, walimkuta Rais mstaafu Nchenga, akaketi mlangoni, akisaili namna ulivyovunjwa. Hakuingia ndani. Aliwasubiri ili wajionee kilichotendeka ndani kwa pamoja. Pale mlangoni walitumia takribani dakika nane, wakijadiliana, yote kutokana na sintofahamu iliyotanda ndani ya mioyo yao. Sintofahamu iliyogubikwa na maswali kemkem wajiulizayo wenyewe, na kushindwa kupatia jibu.
Mshawasha ulivyopanda, wakaingia ndani. Mmoja wao akapiga hatua hadi sehemu ya swichi kuu akawasha umeme na kufanya jengo lote litawaliwe na mwanga uliowawezesha kuona kila sehemu. Wakapiga jicho huku na kule, walipoona hamna kitu chochote, wakahimizana wachukue bunduki ili wafanye uchunguzi wa kina, wa kumtafuta mtu aliyefungua endapo bado yumo ndani, ama kuzungukia maeneo ya karibu yazungukayo jengo hilo. Wakakubaliana, wakaenda hadi kwenye moja ya chumba kilichomo ndani ya jengo hilo, kila mmoja akatoka na bunduki kwa namna walivyopangiana na ufahamu wa matumizi wa mtu husika afahamuvyo kutumia bunduki hiyo.
Hatimaye wakaanza uchunguzi wao. Kwa kuzungukia maeneo yote ya ndani, mwendo ukiwa wa mnyato na wa kimapigano. Kama mwendo watumiao askari wa kikosi cha mapigano ya karibu, CQB (Close Quarter Battle). Mtindo ambao huruhusu askari aketiye nyuma kugeuka kuangalia kundi lao litokako bunduki ikiwa imekitwa vyema kwenye nyama ya bure hakuna kuruhusu ushukaji, lengo, endapo ataonekana adui ashambuliwe kwa wepesi. Pia ni mfumo wa kuweka ulinzi kundi lisishambuliwe na adui atokaye upande wa nyuma. Muda huo wote, hawawi wima, wanapidisha migongo kidogo, pia hubadili badili uelekeo.
Baada ya kuzunguka karibu maeneo yote, eneo la mwisho likawa lile waliloangukia Mrakibu Msaidizi wa jeshi la polisi, Nendakulola na Konstebo Juma. Kama kawaida, walipiga hatua za mnyato na za haraka, mithili ya wabobezi wana timu ya CQB. Ambao mazoezi yao wamechukulia mataifa ya magharibi, hasa Marekani. Pindi walivyokaribia kufika, kishindo cha nguvu kikasikika, sehemu ileile, kishindo kilichowasitisha mwendo, na kufungua usalama wa silaha zao tayari kwa makabiliano na kitu chochote hatarishi watachokutana nacho. wakasita takribani muda wa sekunde kumi na tano, walivyoona kimya, wakaendelea kupiga hatua. Walivyofikia sehemu ya kile chuma, ambacho kilifichwa na unyanyuzi kidogo wa matofali na kuwekwa zulia, walikizunguka. Kwa mtindo wa nilinde nikulinde, ina maana mmoja akitazama mbele, mwingine anatazama nyuma. Huyu akitazama kulia, yule anatazama kushoto.
Hawakukuta kitu chochote, zaidi ya kuona shimo, likaribialo futi kumi na tano kwenda chini, lililofukizwa kiza kinene kilichowashinda wasione ndani. Kile chuma hakikuwepo, wakahisi labda ndicho kilichotoa kishindo baada ya kuangukia ndani, ila wazo hilo lilifutika punde, lilivyokuja lingine juu yake lililowafahamisha sehemu hiyo waliifunga. Ikawabidi wawashe tochi, wajionee kilichomo, walivyomulika huku na kule, katika harakati za kufikia sehemu ndogo ya kona za shimo hilo, lililosakafiwa na malumalu chini na ukutani, wakabaini begi, na viatu, pasi na sahau, walishuhudia mguu ukisogezwa, wakatambua kuna mtu ndani.
“Tunafanyaje?” aliuliza Rais mstaafu Nchenga. Akiwa na muonekano uliogubikwa wasiwasi, kwa sababu washagundulika.
“Tusipoteze muda, tupige mabomu ya machozi na moshi watajileta wenyewe juu,” Wambili alichangia hoja. Kidume aliyetamalaki roho mbaya kuanzia ndani hadi nje.
Wakafanya hivyo.
Kwakuwa kila mmoja alikuwa na mabomu. Yarushwayo kwa mkono, waliyoyahifadhi kwenye vi—peki vidogo walivyovivaa usawa wa tumbo baada ya kuvaa ballistic vest, waliyachomoa wakayakamatia mkononi, bunduki wakizisukumizia mgongoni, ili wafanye zoezi hilo kwa uhuru na uangalifu mambo yasiharibike kwa kuwageukia wenyewe badala ya walengwa. Walivyojihakikishia, kila mmoja ana mabomu mawili mkononi. Bomu la moshi na bomu la machozi lichanganyikalo na moshi kiasi kidogo pasi na sahau mlipuko, mmoja wao akatoa amri nini wafanye.
“Tunaanza na bomu la machozi.”
Amri ilisikika vyema kwa wote. Ukafuatia utekelezaji tu. Ambapo kila mmoja alichomoa fyuzi akashikilia kwa umakini kabisa kwa kulibana vizuri, lisiweze kuachia mwanya wa kuruhusu mlipuko. Walivyotayarika, walisogelea usawa wa mlango wa kuingilia shimoni, wakavitoa mbele kidogo kama kuchungulia, kwamba watakavyotupa, lidondokee ndani moja kwa moja na si kukwama nje, kitendo kitachowaharibia mpango wao. Wakaanza hesabu, ‘…moja!...mbili!...tat…’ hata hawajaimalizia ile tatu, wakashtushwa na sauti ya kitu kilichoonekana kimepita juu ya paa na kutokezea nje toka mule shimoni. Walivyotupa jicho paani, kuangalia ni nini, wakabaini, mbainisho uliohakikishiwa kwa mara nyingine kilivyopita kitu kama hicho sehemu ileile, iliyopita kitu cha mwanzo. Risasi!
Zilifurumushwa nyingi mno, kiasi kwamba zikapoteza nafasi ya utekelezaji wa kile walichopanga kufanya marais wastaafu. Wakabaki na mabomu yao mkononi, huku wakikodoleana macho, yaliyobeba ulizo wafanye nini. Ikawabidi wasogee pembeni kidogo. Wasikilizie kwa muda, wakiamini mpigaji akiishiwa risasi wasogelee kisha wayatupe. Lakini haikuwa hivyo. Risasi ziliendelea kuchakazwa, hali ilivyokuja tulia, hazikupita sekunde sita, zikaendelea kupigwa, hadi wale wastaafu wakachoka na mabomu yao mkononi. Vidole navyo vikaanza achia taratibu, kuiruhusu pini iliyokuwa inazuia bomu lisilipuke, itoe nafasi ya ulipukaji.
Hazikupita dakika mbili. Wote pini zikaachia pasipo matarajio yao, ikawalazimu wayarushe pasipo mpangilio, popote litapodondokea poa tu. Wale wenye nguvu kidogo, waliweza kuyafikisha mbali. Ila ambao hawakuwanazo, yaliishia umbali wa mita tano tu, toka waliposimama, kitendo kilichowafanya waanze kutafutana kwa mbio. Pumziko la mbio zao lilikuwa nje. Walikofikia kuhema, kukohoa na kupikicha macho, kwani sehemu ndogo ya moshi wa bomu uliwapata.
“Ma…okho! Okhoo! Okhoo! Okhoo! Okhoo!...mam…mambo yameharibika,” alisikika Prof. Kadenge. Akiwa anakohoa kohoa na kupiga piga kifua chake.
“Ni wapuuzi sana hawa jamaa. Wanaweza kuwa ni kina nani?”
“Dah! Siwezi wahisi. Wametuharibia vibaya mno. Na endapo tutaachia, tutapoteza malengo yetu yote.”
“Kwa hiyo unashaurije?”
“Tubane sehemu, wakitoka, tuwatambue ni kina nani. Pia tuanze nao muda huo huo. Hakikisho letu, hawa lazima wauwawe.”
“Sahihi! Na hiyo ndiyo njia pekee itayotuwezesha tuendelee na mipango hii. Tukifeli inatulazimu kuandaa mpango mwingine.”
“Haina haja ya kuruhusu kufeli. Ruhusa tunayopaswa ihitaji, ni ruhusa ya ufaulu.”
Walivyoridhia maoni yaliyotolewa kila mmoja akajimwaga upande wake. Kwa kulala kwenye maficho ya nyasi fupi na vishina shina vidogo vidogo vya miti. Wakalala, mlalo wa kifudi fudi, huku wakiinua kichwa kidogo kulitazama jengo.
****
Upande wa sajini Zena na Koplo Malkiadi, mambo yaliwanyookea. Yalienda kama walivyopanga. Walifanikiwa kupata dondoo kemkem, zilizowafahamisha dhamira ya marais wastaafu kuwa ni azimio walilolithubutu kwa namna yoyote. Walifahamu, kwamba wazee hao, wamepanga vyumba kwenye hoteli hizo kwa muda wa mwaka mzima. Siku ya mwisho, ikiwa siku ya kusherehekea taifa hilo kupata uhuru mwaka unaofuata. Pia walifahamu, na kujionea ishara lukuki zilizowatambulisha, zinaenda kutumika kwa lengo la kumshambulia mheshimiwa Rais. Kazi iliyofuata baada ya hapo, ni kupeleka ripoti za uchunguzi wao kwenye kikao cha majumuisho, kitachowapa Magreth, mama Tausi na James uwezekano wa mpango upi wanatakiwa kufanya kusitisha shambulizi. Hivyo wakawa wanawasubiri kina Mrakibu Msaidizi wa jeshi la polisi, Nendakulola wahitimishe, waelekee pamoja sehemu ya majumuisho ambayo walikuwa wanasubiriwa toka waondoke. Kwani James na wenziye hawakuondoa mahali pale tangu walivyotoa hilo jukumu, nia kusiwe na uyumbishaji utaowafanya wapoteze muda pasipo sababu za msingi.
Kule msituni napo, juu ya ASP Nendakulola na mwenziye kushtukiwa, ila kuna dondoo walizinyaka. Wakazinakili kwenye shajara zao walizohifadhi ndani ya peki, zingine walipiga picha kama awali. Mwanga wa balbu zilivyowashwa, uliwashtua, mshtuo uliozalisha mtikisiko kidogo wa kile chuma, ambalo ndilo walilalia. Likaachia kajinafasi kidogo, kwa mshikizo mdogo kwenye kuta za juu ya sakafu, mwishowe ulishindwa kuhimili, ukaachia kwenda chini. ASP Nendakulola na Konstebo Juma wakafuatia nao kutumbukia humo pasipo mpangilio. Hali iliyowapa maumivu baadhi ya sehemu za mwili. Ila hawakuruhusu yawatawale, wangelionekana wazembe, ilhali wao ni wataalamu, maalumu kwa mapambano ya aina hiyo, pia ni wana mazoezi hodari.
Hivyo walijinyoosha. Kwa muda mchache, viungo vilivyotetereka vilivyotengemaa wakajiweka fiti kwa makabiliano. Wakajigawa, mmoja akaendelea na kazi ya uchunguzi, mwingine kukabiliana na watu waliofika, ambao waliwatambua kupitia balbu zilizowashwa, pia miale ya mwanga wa tochi pindi walivyokuwa wanamulika shimoni wakati huo wao wakijaribu kujificha japo hawakufanikiwa.
“Endelea na uchunguzi, hawa niachie nitakabiliana nao,” alisema ASP Nendakulola. Akimwambia Konstebo Juma, pindi akiiweka vyema bunduki yake.
Pindi marais wastaafu wanasogelea shimo, kwa nia ya kurushia yale mabomu, ASP Nendakulola aliwashtukia kupitia vivuli vyao, walivyojaribu kuchungulia. Kuona hivyo hakujadili, akaanzisha mashambulizi, lengo wasisogelee, pia kumpatia mwanya Konstebo Juma wa kufanya uchunguzi kwa makini na uhakika. Alikuja kutuliza mashambulizi, pale aliloulizwa kuhusu jambo fulani, akishajibu huendeleza. Na tulizo la moja kwa moja, lilifikia, marais wastaafu walivyorusha mabomu, moja wapo likadondokea shimoni.
Nao wakatafutana, kama ilivyokuwa kwa marais wastaafu. Kila mmoja alikimbilia kona hii kutafuta unafuu, lakini haikusaidia. Moshi ulikuwa mwingi, uliwaumiza, tena uliwaumiza haswa, ukizingatia hawakuvaa kitu chochote cha kuwakinga, japo walikuwanavyo, walizihifadhi kwenye mapeki. Walikuja kumbuka baadaye sana. Moshi ukiwa umewaathiri vya kutosha. Walifungua mapeki yao wakavaa na kuanza jitihada za kutoka mule shimoni. Utokaji haukuwa mgumu, sababu mlikuwa na ngazi. Wakatumia hizo kutokea. Walivyokaribia sakafu, wakatokeza kichwa kidogo kusoma mazingira, walivyoona yapo sawa, wakatoka mazima.
Hawakuacha kuangaza huku na kule, kusaili mazingira, hali gani imetawala. Ambayo ndiyo itawapa uelekeo wa namna wanayopaswa kutoka ndani ya jengo hilo.
“Washaondoka,” alisema Konstebo Juma, wakizidi kupiga hatua kusonga mbele.
“Wasingeliweza kuendelea kukaa wakati walijilipulia mabomu,” ASP Nendakulola akakazia. Kisha wakafuatia kutoa cheko dogo lililowasukuma kupeana mikono kupongezana, kuwa wameokoka.
Walivyofikia mlango hawakugombaniana, waliachiana zamu kila mmoja apite pasipo usumbufu. Akaanza Konstebo Juma, akafuatia ASP Nendakulola. Walivyoona nuru mawinguni, na walivyopiga jicho huku na kule, wakajihakikishia wamenusurika, dhidi ya wale watu. Ambao moja kwa moja waliwatambua kuwa ni marais wastaafu. Wakajinyoosha, kuweka viungo sawa zaidi, kisha wakatupa jicho mbele kuanza mwendo. Hawakuwa na bahati! Milio ya vitu kugongwa na risasi ikasikika vyema sikioni mwao. Eneo karibu kabisa na pale waliposimama. Ikabidi waingie kwenye purkushani za hapa na pale wajiokoe huku wakijaribu kujibu mashambulizi kuelekea upande wowote waliohisi shambulizi linatokea. Wakawa wanajibu huku wanazama ndani, shida ikawa mlangoni, wakafanya subira ya kutegeana nani aanze kuingia, subira iliochukua sekunde saba na kuwapa marais wastaafu nafasi ya kuzidisha mashambulizi palepale waliposimama. Kitendo kilichoruhusu risasi kadhaa kutua mwilini mwao. Mruko wa damu uliwafahamisha hilo, kuwa kuna risasi zimetua mwilini mwao na ubaridi kiasi, ulioanza chanua maumivu.
Kuona hivyo wakazidisha purkushani, zilizowadondosha palepale mlangoni baadaye wakajivuta kuingia ndani. Ila kabla hawajaingia kabisa, damu iliruka kwa mara nyingine toka maeneo ya begani kwa ASP Nendakulola, iliyomfanya agugumie maumivu na kulala chali palepale. Konstebo Juma ikamlazimu ajikaze, ijapokuwa naye alipatwa na risasi maeneo kadhaa ya maungo ya mwili wake. Hasa mkono wa kuume, juu usawa wa kwapa, pajani, mguu wa kuume na begani, karibu na shingo mkono wa kushoto. Akasimama, akiwa anachechemea akaanza kumvuta kwa tabu sana kutokana na maumivu makali sana yatokanayo na majeraha aliyonayo. Maumivu yalipomzidia alimuacha, naye kujiangusha chini ila kwa kiasi kidogo aliweza kumsaidia, kwani sehemu kubwa ilishaingia ndani, mlangoni ilisalia miguu pekee, hasa usawa wa unyayoni.
Baadaye akajivuta vuta mwenyewe, hadi pale alipojiangusha Konstebo Juma, akajigeuza, wakaanza kujiganga. Kwani walikuwa na visanduku vidogo vya huduma ya kwanza, vilivyo na dhana kadhaa za kuwawezesha kupunguza maumivu na utokaji wa damu, ambao ulitishia kupoteza maisha yao. Zoezi hilo lilichukua muda mfupi tu, walifanya kwa uharaka waweze kujipanga, baada ya kuamini marais wastaafu wanaweza kuwafuata kwa kudhania washawaondoa duniani, ama wako katika hali mbali wasiyojiweza.
“Afande, si tuombe msaada? Maana hii hali tuliyonayo haitoweza kukabiliana vya kutosha na hawa watu. Ukizingatia hawana hata chembe ya jeraha,” alisema Konstebo Juma, aki—malizia kufunga bandeji sehemu ya mwisho ASP Nendakulola kushambuliwa. Usawa wa kifuani, jirani na kwapa la kulia.
“Sahihi, ila kufanya hivyo, ni sawa na kuwaruhusu waandae mpango mwingine, utaotuchukua muda kuufahamu pale wataponusurika.”
“Kwa hiyo tunafanyaje?”
“Acha tupambane. Sisi ni wanaume kamili, wabobezi wa CQB (close quarter battle), SUT (squad unit tactical) hivyo yatupasa kuhakikisha mpango wetu unaenda vile tulivyopanga,” alisema ASP Nendakulola, huku aking’ata meno yaliyosheheni uashirio wa kusikilizia maumivu pindi afungwapo bandeji.
Walivyomaliza, wakajipanga, kuhakikisha wanaondoka eneo hilo na si vinginevyo. Watafanyaje? Mbinu za mafunzo hayo aliyotamka ASP Nendakulola ndiyo yalikuwa mbadala kwao. Mafunzo maalumu, ambayo mara nyingi hutumika katika uokoaji wa mateka kwenye majengo na maeneo mengi tatanishi. Vivyo hivyo kwa mchechemeo, wakakamata vyema bunduki zao, kwa mfumo wa low ready, ambao hutoa nafasi ya maandalizi kwa ajili ya high ready utumikao kwa mashambulizi. Walivyokaribia mlango wakabana ukutani, mmoja wao aliyetangulia, Konstebo Juma, ambaye kidogo alikuwa na nguvu kwa sababu hakupata madhila makubwa toka kwenye yale mashambulizi, alitupa jicho la kujiiba kuchungulia mazingira ya nje yalivyo, kisha akarudisha kumueleza ASP Nendakulola hali aliyojionea.
“Kuko kimya afande.”
“Mmmh!...nahisi hawajatoka,” alisema ASP Nendakulola, sauti ikiwa chini, kama mtu aliyejaa masikitiko.
“Yah! Nilishahisi hilo toka muda, ndiyo maana nikakuambia tuombe msaada kwa wenzetu,” Konstebo Juma akakazia.
“Hapana! Misingi yetu ya kazi inatuambia askari mmoja atokapo mafunzoni, mafunzo ya awali ya jeshi letu, ana jukumu la kukabiliana na raia mia nne, na yule mwenye mafunzo lukuki ya kimapambano, idadi hiyo inaongezeka. Hivyo tuna uwezo wa kukabiliana nao pasipo kujali hali tulizonazo.”
“Sawa. Nipo timamu kwa utekelezaji, afande.”
Wakaafikiana.
Kilichofuata walibadili uelekeo wa kutokea. Badala ya kutumia mlango, waligeuka, na kwenda kutafuta sehemu nyingine itayowawezesha kutoka. Wakatumia takribani dakika mbili kuhitimisha zoezi hilo, wakafanikiwa, kupata sehemu moja iliyojaa ufa nyuma ya jengo. Lilikuwa jengo lililojengwa kwa mawe. Wakaamini, wakifanikiwa kubomoa, watapata sehemu itayowawezesha kuondoka pasipo wasiwasi. Wakatekeleza.
Mmoja wao akafuata bleacher, alivyorudi nalo, ubomoaji usiotumia nguvu ukaanza, nia wasisikie wale wanaowavizia. Walikuwa radhi kutumia muda mrefu, ili—mradi wabaya wao wasisikie. Ikawa hivyo!
****
Sajini Zena, alijumuika na mwenziye, Koplo Malkiadi, chumba cha makutano ya siri yaratibiwayo na Rais Mlunji na watu wake. Pasi na sahau Magreth, mama Tausi na James, wakifanya subira kuwasubiri ASP Nendakulola na Konstebo Juma wafanyie kazi matokeo ya chunguzi zao. Makutano yao yalianza saa 12 jioni, ila huku wakiwa na makubaliano, saa 1:30 usiku, kuhitimisha mjadala, tayari kwa upande wa kina Magreth kuanza kazi. Wakati huohuo pia, Rais Mlunji alikuwa kajifungia ofisini kwake akifanya tathmini ya makala kadhaa aliyoandika siku kadhaa nyuma.
Sekunde zikazidi yoyoma. Pasipo walengwa tarajiwa kuwasili. Hadi panapo saa 1:29:57 usiku hamna dondoo yoyote ya kuwasili kwao. Walivyojaribu kuwatafuta kwa njia ya mawasiliano. Ya simu ya mkononi, au redio za kipolisi kampuni ya Hytera hawakupatikana, jambo lililowapa wasiwasi na kuwaingiza kwenye majadiliano mafupi kipi waamue.
“Kwanini tusitumie hii ripoti ya uchunguzi wetu?” aliuliza sajini Zena.
“Hapana. Ripoti zote muhimu. Ili tukishaanza, tumeanza, hatuhitaji kufanya kazi nusu nusu,” alisema mama Tausi.
“Sasa kama hawatofanikiwa kuja kwa huu muda si tuta…” Koplo Malkiadi alisema, ila hakumalizia. Ikasikika sauti ya kishindo kikubwa nje usawa wa mlango wa kuingilia.
Wakasita kwa muda. Wakanyanyuka, kisha mmoja wao, mama Tausi, akapiga hatua hadi sehemu iliyosikika kishindo hicho. Taratibu, akakamata kitasa akakinyonga, akapata upenyo mdogo uliomwezesha kutupa jicho nje akashuhudia mazingira yalivyo. Alishangaa! Ila mshangao mdogo, ambao hukumchukua muda mwingi. Huku akianza kujawa na tafakuri afanye nini. Aanze kuzungumza na wenziye walio ndani, ama ashughulike na kile alichokiona. Watu! Waliotapakaa damu, mithili walichinjiwa mnyama mwilini mwao. Tafakuri hiyo ilikatikshwa na mkono wa mmoja wa wale watu waliolala mbele yake, ikabidi naye atoe mkono wake aufuate. Kuna kitu alikabidhiwa.
“Waambie tunahitaji msaada,” alisema mmoja wa wale watu. Konstebo Juma.
Chap! Mama Tausi akarejea ndani. Ambako bado wenziye walikuwa na sintofahamu wakiulizana kulikoni? Alivyowafikia alipokelewa na maswali lundo, toka kwa wote. Ambayo alishindwa kuchanganua, aanze lipi kulijibu.
“Ondokeni. Mukawapatie msaada wenzenu,” alisema mama Tausi, kumwambia sajini Zena, huku akionyesha msisitizo wa kile alichozungumza kwa kumpiga begani.
Waambiwa wakanyanyuka, mama Tausi na wenziye wakasalia kupitia ripoti walizokabidhiwa. Ambazo ziliwapa ufahamu wa kutosha, maandalizi yote yaendeleayo kufanywa na marais wastaafu. Kupitia humo walifahamu. Sehemu ipi itatumika zaidi kumshambulia Rais Mlunji, na mtu gani. Taarifa haikumzungumzia mtu mmoja pekee, hata wao, walinzi wa karibu wa Rais Mlunji, ambao kwa namna moja ama nyingine, watahudhuria uwanjani.
Walivyohitimisha kusoma na kupitia picha mbalimbali za zana zitazohusika, walitokwa na mguno, ulioashiria kazi ni nzito, wanapaswa kujipanga haswa kudhibiti tukio hilo lisitokee.
“James! Sisi ni watu wa mlango wa pili. Wewe ndiye mwenye majukumu mazito. Hakikisha, Rais anakuwa salama,” alisema Magreth.
“Naam!...ondoeni hofu. Hakuna atayefanikiwa kumdhuru.”
“Haya, yetu macho na masikio, tutajionea matoke.”
Upande wa pili, sajini Zena na Koplo Malkiadi waliwachukua ASP Nendakulola na Konstebo Juma wakawapeleka zahanati maalumu imilikiwayo na jeshi la polisi kwa ajili ya matibabu. Walivyofikishwa, haraka sana walianza kuhudumiwa na madaktari maalumu waliotaarifiwa pindi wako safari wakienda huko. Madaktari toka hospitali ya taifa. Matibabu yao hayakuwa ya kitoto, yalikuwa matibabu magumu yaliyohitaji uangalizi wa kutosha toka kwa madaktari wanaowahudumia. Kwani pindi, walivyofanikiwa kubomoa, walishtukiwa, na marais wastaafu ambao walishaondoka sehemu walizokuwa wamejificha wakapiga hatua hadi ndani wakajionee kiendeleacho baada ya kuona watarajiwa hawatoki. Kwa muda fulani, hawakuacha kudhania, risasi walizowapiga zimeondoa uhai wao, ama wametoroka. Ila walivyokumbuka kuwa jengo hilo ni la mawe imani ya kutoroka ikaondoka akilini mwao. Ajabu! Walivyoingia. Wakawakuta wanatupa bleacher na mizigo yao mingine waliyokuwa wamebeba mgongoni, peki, wakitupia nje baada ya kufanikiwa kubomoa. Hawakuulizana, kila mmoja aliinua bunduki yake na kupeleka risasi mfululizo. Dhamira yao ilikuwa moja tu, wawaondoe duniani.
“Mabazazi nyie, mnataka kufanya mpango wetu usikamilike,” walisikika marais wastaafu, huku wakipeleka vyema mashambulizi yao.
Miili ya ASP Nendakulola na Konstebo Juma ikaruhusu upokeaji wa risasi. Walichakazwa, walichakazwa haswa, ila hawakukata tamaa, hali hiyohiyo waliyonayo walijikaza na kuruka sehemu ile waliyotoboa wakaangukia upande wa pili. Nje! Kwa sababu hali zao zilikuwa mbaya, hawakuwa na uwezo wa kumudu kuchukua mizigo mizito. Walichambua vitu vya muhimu baada ya hapo kila mmoja alitembea kwa aina ya mtembeo alioumudu na ambao haukuweza kumpatia maumivu makali. Wakajikongoja hadi walivyoifikia barabara, wakapata lifti ya teksi iliyotoka kumpeleka abiria shamba. Dereva wa teksi akawafanyia usamaria wema, kuwapeleka walikohitaji, ambako ni kule eneo la makutano.
Wenzao wakatikisa kichwa kuwahurumia, lakini hawakuwa na namna, zaidi ya kumuomba Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi wapone mapema.
Deal done!
****
OKTOBA 15, 2003.
Kama ilivyo ada. Siku pendwa ya taifa la Mangaka kusherehekea kupata uhuru. Baada ya kufanikiwa kujikomboa na manyanyaso na mateso toka kwa mkoloni. Siku hii husubiriwa kwa hamu kubwa sana na wananchi. Hamu yao hudhiirishwa na namna wajaavyo uwanjani ambao sherehe hufanyika, ama kwa kufuatilia kupitia runinga na redioni. Kikubwa kiwafurahichasho wengi, ni onyesho la paredi, japo, baadhi hufurahishwa na kila kitu kifanywacho ama baadhi. Hotuba ya mgeni rasmi, ikiwa sehemu ya mwisho katika orodha ya vitu vipendwavyo siku hiyo. Ukiorodhesha vitu vichukiwavyo, hushika nafasi ya kwanza.
Siku hii, kwa mwaka huu, ilitengeneza sintofahamu nyingi kwa watu tofauti tofauti. Wapo waliosubiri kuona Rais Mlunji akiaga dunia, wapo waliotawaliwa matarajio ya kumsikia akijiuzulu na wa mwisho, wale waliohitaji kumuona akitamka kuwa hajiuzulu. Naam! Akawa habari ya mjini. Wengi wakakusanyika kwa ajili yake, kuona kile watarajiacho. Sio maonyesho tena, ambayo kila mwaka yafanyikapo mgeni rasmi haonekani na thamani yoyote.
Rais Mlunji alibadili fikra za wengi. Huku wale wenye itikadi za kisiasa, wakiwa roho juu, kuona kilicho fikrani mwao kinatimia. Sababu wengi wao walikuwa na dondoo kuhusu habari za kujiuzulu kwake. Saa rasmi ya kuanza shughuli ilivyowadia, mioyo ya wengi ikapanda mori, kusikia wafikiriacho. Mori hiyo ikazidi kupanda kila sekunde hadi pale aliposimama Rais Mlunji nyuma ya mimbari, tayari kwa kuhutubia, nyuma yake kasimama mlinzi wa kike, mwenye muonekano nadhifu, uliosisimua wengi. PSS ambao nambari tatu, mlinzi mwingine, tofauti na mama Tausi, ambaye alishaanza kuzoeleka na wengi. Mama Tausi yu—wapi?
****
Dhamira ya kutwaa mamlaka ya kuongoza nchi kwa mara nyingine ilizidi kurindima ndani ya mioyo ya marais wastaafu. Amani ya mioyo yao itapatikana, pale tu, mmoja wao atapotwaa kijiti hicho. Baada ya kufanikisha kumshika mwenyekiti wa kundi pinzani, walifuatia kuwashika viongozi wengine, mwishowe nia yao ikawa wazi kwa wanakundi na wananchi wengine. Kimbilio la wananchi wawateteao, vurumai la majibizano yatokeapo hukusu nia hiyo, walikuwa na hoja mbili, ya kwanza; waliamini endapo akirejea madarakani atafahamu alipokesea awali sasa atarekebisha wananchi watakuwa na maendeleo. Ya pili; kubadili mfumo wa kiutendaji. Lakini wote walikuwa nje ya kile kilichopo akilini mwao. Wao walikuwa na mawazo mengine, ya kujisafisha mbele ya umma juu ya tuhuma zote zilizowakabili pindi wako madarakani na baada ya kutoka. Vilevile kuendeleza yale waliyoyaanza. Ambayo Rais Mlunji aliyasitisha. Kupisha uchunguzi, lakini kabla uchunguzi haujaanza akaundiwa zengwe.
Dhana hiyo haikubanduka. Walizidisha mipango tu, hadi siku ya mwisho, siku ya tukio. Taarifa ya tukio hilo kwa upande wa uokoaji ilifahamika kwa wachache tu, nao walifahamu sehemu chache tu ambazo ndizo waliamini wadunguaji wataketi kutekeleza tukio lao. Ila haikuwa hivyo. Walikuwa na mbadala mwingine, tofauti na ule uliofahamika.
****
Magreth Okuku, James na mama Tausi walijigawa katika majengo mbalimbali yaliyotazamana na yale marais wastaafu waliyachagua kufanyia kazi. Pasi na sahau, kikosi kazi, kikiwa na askari wawili pekee, sajini Zena na Koplo Malkiadi nao walichukua maficho sehemu walizopangiwa kuhakikisha lengo linakuwa timilifu, wenzao hali zao bado zilikuwa hazijatengemaa. Muda wote wakawa wanakesha kutazama darubini walizoning’iniza shingoni kuelekea yalipo hayo majengo. Ajabu, kila walivyotupa jicho hamna kitu chochote walichoshuhudia, zaidi ya vyumba kuwa tupu. Hakukuwa na mtu, wala silaha ya aina yoyote.
Wakajikuta wanaingia kwenye mafikirio pasipo kutarajia, wakajadiliana kwa ufupi, walivyomaliza walirudi kutupa jicho kuangalia lakini matokeo hayakuwa tofauti.
“Nini hii?” aliuliza Magreth, swali lililosikika na wote, kupitia visikilizio maalumu walivyopachika sikioni na kuunganishwa na redio zitumiazo mfumo wa mawimbi kwa eneo maalumu kutegemeana na wimbi litakalosetiwa.
“Yawezekana wameghairi,” alichangia sajini Zena. Akipumua kwa shida kutokana na kubana pumzi yake kwa ajili ya kutafuta lengo husika.
“Hapana. Hawawezi kughairi kirahisi hivyo,” James alichangia. Akaendelea… “tupeni macho jukwaani. Jukwaa zote,…”
“Sawa!”
Wakatii oni lake. Kila mmoja akaelekeza darubini jukwaa moja baada ya lingine, ila napo hawakuambulia kitu, jambo lililozidi kuwachanganya. Baadaye wakashauriana kwa mara nyingine. Ushauri uliotoka, watu wa kikosi kazi waelekee ghorofa zote zilizopangwa kutumiwa na marais wastaafu kumshambulia Rais Mlunji wakazikague. Wakatii!
Waliondoka pointi wanguwangu hadi maeneo husika. Wakajitambulisha, kisha kuanza utekelezaji wa kile kilichowapeleka. Matokeo hayakubadilika, yalikuwa vilevile. Walivyorejea pointi zao, wakawataarifu wenzao, walichokutana nacho baada ya hapo yakapita maamuzi.
“Hawa watu wametuzuga, kama wamedhamiria kufanya, basi si mahala hapa. Yawezekana pindi anaondoka uwanjani kurudi Ikulu,” alisema James, wenziye wakiwa tulivu kumsikiliza.
“Sahihi. Tujipange kuulinda msafara wake usidhurike.”
Wakagwaya, mori, ya kusitisha uangalizi ikawatawala. Ambayo waliisikilizia kwa sekunde kadhaa, mwisho wakaifuata. Waliacha! Hatimaye wakakusanya virago vyao kwa ajili ya kwenda kujipanga upya na sehemu nyingine. Ila pindi wanaanza piga hatua tayari kwa kuondoka, yowe la wananchi liliwashtua, na kuwahimiza wakumbuke darubini zao walikoziweka wakatupa jicho jukwaani. Jukwaa la kwanza kulitupia jicho, lilikuwa jukwaa kuu, walivyoangaza, walishuhudia Rais Mlunji kakamatiwa, huku sehemu ndogo ya shati alilovaa ndani, likazuiwa na suti likichafuka. Kuna kitu alirushiwa!
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sambamba na walinzi, wakijitahidi kutaka kumtoa, ila akawa anakataa, kuondolewa baada ya kung’ang’ania kukamata mimbari huku akiendelea kutupa neno.
“Bado wapo,” waliropoka kwa pamoja.
“Tunafanyaje?”
“Lazima tuwapate. La sivyo, watafanikiwa kumuondoa.”
“Hapana. Mheshimiwa hatakiwi auwawe,” Magreth alitilia mkazo. Akaendelea… “tutupe tena majukwaani…”
“Nooo…! Wauwaji wapo jukwaa kuu, tupige jicho hapo,” alisema James.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment