Search This Blog

Friday, 18 November 2022

OKTOBA 15 RAIS ANAENDA KUFA - 4

 






Simulizi : Oktoba 15 Rais Anaenda Kufa
Sehemu Ya Nne (4)




Huo ukawa mwanya kwa wale watu waliosalia ukumbini, kutoka pasipo wasi. Wakishafanikiwa kuwa nje hutumia mbio ili wasibadilikiwe. Ni wachache sana ambao walisalia. Sio ndani ya ukumbi, nje. Wakishangaa pigano lililokuwa linaendelea, huku wakiwa wamesimama umbali wa mita kumi na
tano toka eneo la pambano. Lilichukua dakika nane kumalizika, kwa yule mwanaume mlevi kutiwa nguvuni baada ya kuchangiwa kipigo toka kwa askari wote wa kikosi kazi.

“Kuna kituo cha polisi hapa?” aliuliza ASP Nendakulola, kwa watu waliozunguka wakishangaa pindi wakimpandisha garini yule mwanaume.

“Kipo kijiji cha pili hapo. Kituo kidogo, kituo kikubwa hadi mjini,” walisema wale watu, huku wakitawanyika.



Miongoni mwa walengwa wanaofanikiwa kutoka ndani ya kumbi hiyo ni James. Akiwa kabeba begi dogo mgongoni. Yeye ni mmoja kati ya watu waliotoka mapema kabisa, kabla zoezi la ukaguaji halijaanza. Kwani, alikiona kile kikosi pindi kinaingia. Na kwa sababu kuna anaowafahamu kati yao, akatambua hawajaja kwa amani. Alivyofika nje alitembea kwa uharaka. Muda mwingine alipiga mabio, alipochoka, alitembea. Mbele akaita bodaboda, na kumuamuru ampeleke kituo cha garimoshi. Baada ya kukumbuka kauli fulani aliyoambiwaga na mama Tausi siku chache zilizopita.

“Safari yako iishie kijiji kiitwacho Fidla. Kaa hapo hadi karibu na mida ya mapambazuko, kisha chukua usafiri wa pikipiki ukupeleke kijiji kiitwacho Masyalele. Ukishafika Masyalele, panda treni uelekee mji husika unaotaka kufika. Nina hakika, ukitumia hiyo njia, utakuwa umeepukana na vihunzi vyote vya askari wakeshao barabarani kufanya doria,” alikumbuka James.



Kweli! Ilivyowadia saa 12 asubuhi, tayari alikwishakuwa ndani ya treni. Alifanya sala, kuomba afike salama aendako, kisha akatulia kusubiri muda wa kuanza safari. Ambao ni 12:30 asubuhi.

****



Bodi ya wataalamu wa teknolojia toka ndani ya jeshi la polisi makao makuu, na idara zingine za ulinzi na usalama walikuwa ndani ya chumba maalumu wakiongoza mitambo ya kamera za CCTV zilizotegwa katika barabara za mtaani na zile zielekeazo miji mbalimbali, mikubwa na midogo. Wakiongozwa na Kamishna wa oparesheni na baadhi ya waandamizi wa jeshi la polisi. Muda wote wakikagua matokeo yarekodiwayo na kamera huku wakiteta jambo, ambalo likiridhiwa hutekelezwa na askari wa kikosi kazi.

“Afande,” aliita askari mmoja miongoni mwa wale waongoza kamera.

“Mmh! Niambie ndugu, una jipya?”

“Ndiyo.”

“Lipi hilo?”

“Tunatumia nguvu kubwa kwenye usafiri wa magari, halafu tunashindwa kabisa kuweka nguvu katika vyombo vingine vya usafiri.”

“Unamaanisha nini?”

“Huhisi kuwa mhalifu anaweza tumia hizo njia zingine za usafiri kutoroka? Kama vile, usafiri wa anga, majini na ule wa treni?”

Kimya kilipita. Cha sekunde chache kisha maongezi yakarejea.

“Mmmh!...umewaza kitu chema. Kwa hiyo unashaurije?”

“Tuwekeze nguvu huko pia.”

“Sahihi! Sahihi! Hilo linatekelezwa hivi punde,” alisema Kamishna wa oparesheni, akiwa anapiga hatua kuelekea ilipo simu ya mezani. Alivyoifikia, aliandika namba kadhaa na kufuatia kunyanyua mkonga. Haikuchukua muda mrefu, akawa kwenye maongezi.

“Wape taarifa, makamanda wote wa kamandi zilizopo ndani ya jeshi letu, wawaamuru, makamanda wao wa kamandi za mikoa wafanye doria ya nguvu kumtafuta Sadiki (James),” alisema Kamishna wa oparesheni.

“Sawa afande,” akajibiwa, na mtu wa upande wa pili. Aliyekuwa anawasiliana naye.



Punde amri ikasambaa mikoa yote. Kwa makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa kamandi tajwa. Kamandi ya Anga, kamandi ya majini, kamandi ya reli na ile ya mbwa na farasi. Askari kadhaa wa kamandi husika wakaanza kutekeleza jukumu. Kwa namna walivyojipanga ili watoapo mjeresho kuhusu walivyowajibika wapate cha kuzungumza. Wahusikao na viwanja vya ndege, walikesha kukagua abiria waingiao na watokao kwa umakini, wale wa bandari nao, walikagua haswa meli, boti jahazi na mitumbwi. Vivyo hivyo kwa upande wa kamandi ya reli. Walikagua vilivyo abiria wasafirio na treni.

“Mshakagua abiria wa kituo cha Masyalele?” alisikika Kamanda wa kamandi ya reli, pindi akizungumza na mtu kwa njia ya simu.

“Tuko njiani afande tunaelekea huko, muda mfupi kuanzia sasa, takribani dakika nne tutakuwa tushawalisi,” alijibiwa.

“Basi fanyeni jitihada. Maana zimesalia dakika chache sana treni iondoke.”

“Hamna shida afande, tutaiwahi.”



Kila aliyekamata simu, ndani ya gari ya doria ya askari kamandi ya reli kuangalia muda, ilisomeka 12:27:58, zikisalia dakika mbili treni iyondoke. Dereva akajitahidi kukanyaga mafuta ili wawahi wasitishe safari hadi ukaguzi wa abiria utapokamilika, lakini hawakufanikiwa. Kwani muda ulivyosoma 12:29:59 dereva wa treni akapiga honi ya mwisho kuashiria safari tayari inaanza. Na kuwapa onyo watu wenye kawaida ya kuvuka vuka reli. Pindi honi inapulizwa gari ya doria nayo inawasili. Haraka sana afande aongozaye doria hiyo akateremka na kwenda jengo la utawala kuutaarifu uongozi kama kuna unawezekano wowote wa kuisitishia safari treni kabla mwendo haujachanganya.

“Afande haitowezekana, labda mkaisubirie kituo cha jirani,” alisema kiongozi aliyemkuta chumba cha Meneja wa kituo.

“Tafadhali, nakuomba, hii ni oparesheni ya kitaifa. Hivyo…” alisema afande anayeongoza doria hiyo, ila hakuweza malizia kauli yake. Alikatishwa na Meneja.

“Afande, sijakataa. Hicho nilichokueleza ndiyo utaratibu. Treni ikashaanza safari kamwe kusimama sehemu yoyote mpaka kituoni. Zaidi ya hapo, labda ipatwe na hitilafu.”

“Kwa hiyo utatusaidiaje?”

“Hamna msaada mwingine zaidi ya huo. Pia, nikushauri. Ili mufanye kazi yenu kwa uhuru, ombeni kibali makao makuu ya kupangua ratiba ya usafiri.”

“Ahsante, kwa ushauri, ila umenibania bure. Yamkini mule ndani yupo mhalifu tumtafutaye,” alisema afande aongozaye doria, aliyefahamika kwa jina la Mkaguzi Luambano, wakiwa wamesimama barazani wakishuhudia mabehewa ya treni yanavyomalizikia kuondoka.



Hawakuwa na budi. Walirejea eneo la kazi. Huku wakitoa taarifa juu ya kile walichoshauriwa kwa askari wa vituo vingine pamoja na ngazi za juu. Ushauri ukafanyiwa kazi siku hiyohiyo. Hasa ule wa kuomba kibali cha usitishaji wa safari za treni kwa muda, askari wapate kukagua ndipo taratibu ziendelee. Kamanda wa kamandi ya reli akalipokea hilo na kulifanyia kazi kwa uharaka mno. Akafanya mawasiliano na uongozi wa mamlaka ya usafiri wa reli nchini, akamwelezea hitajio akakubaliwa. Wakapata kibali cha ukaguzi. Muda wa nusu saa, kwa siku inayofuata kitendo kinachopelekea askari walio doria kughairisha kusubiri siku iliyo na kibali maalumu. Ambapo ukaguzi huo utahusisha abiria watarajiao kuanza safari na wale wamaliziao safari.



Hatimaye tangazo rasmi, la dharura likatangazwa kwa abiria na mamlaka ya usafiri vituo vyote, ambavyo treni hupita. Kwa wale abiria waliopaswa ianza safari, hata wale walioko safari muda huo wakiwa na matarajio ya kuhitimisha safari alfajiri ya siku inayofuata. Wakati huo treni aliyopanda James, treni ya shirika la reli nchini Mangaka (Mangaka railway) ilikuwa inakatiza kijiji cha Nahawara kutafuta mji wa mwisho wa safari. Ambao ni Nanderu.



Pindi tangazo linatolewa, na sauti nyororo ya mtoto wa kike kupitia kipaza sauti James alikuwa amelala, hivyo hakuweza sikia kilichozungumzwa. Yote ni kutokana na uchovu uliokithiri kwa kiwango kikubwa mwilini mwake uliochangiwa na safari ya muda mrefu. Takribani saa ishirini na mbili, zikasalia saa mbili ihitimishe safari. Mwisho wa safari ya treni, ndiyo mwisho wa safari ya James. Ambapo yule amfuataye anaishi. Kasanjara Chomeko. Japo hapa napo, alikuwa na kazi ngumu ya kufanya, kama ilivyokuwa atokako. Kwa sababu hamfahamu.



Ilivyowadia saa 12:25 asubuhi, honi ya treni iliyoashiria inawasili stendi ilisikika. Ikiwa mita chache kufika hapo. Watu walio na kawaida ya kuvuka vuka reli, kwa kutumia vyombo mbalimbali vya usafiri na wale watembeao kwa miguu ikawabidi wasitishe kuvuka. Wasubiri iwadie ndipo waendelee na taratibu. Kweli! Dakika tano baadaye iliwasili. Ikapokelewa na lundo la watu wengi walioshindwa kutuliana kwa yowe. Kushangilia upokeaji wageni wanaowasili. Na kufurahia ufanyaji wa biashara, hasa ya usafiri wa bodaboda, bajaji na taksi kutoka hapo kuelekea sehemu watazohitaji wahusika.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Miongoni mwa watu waliokusanyika kwa mapokezi, ni askari. Wale walioandaliwa maalumu kwa ajili ya ukaguzi wa abiria. Wataopata kuteremka, na watarajiao kuianza safari. Ilivyoegeshwa sawa, abiria mmoja mmoja akaanza nyanyuka kwenye siti aliyoketi akijiandaa kuteremka. Hata James wakati huo alishapata kuamka. Akajinyoosha nyoosha kuweka mwili sawa huku akitupa mboni zake nje ya treni kusaili mazingira ya Nanderu yalivyopambika. Alivyoangaza kulia kwake, liliko jengo la utawala wa stendi alipatwa mshituko wa ghafla. Hofu tele ikamvaa iliyomshinikiza atafute mahali pa kujificha kama sio kupata nafasi ya kukimbia kabisa. Japo hakufahamu dhamira ya uwepo wao. Pasipo kutaraji akajikuta anaingia kwenye ukinzani mkubwa wa halmashauri ya kichwa chake kutafuta ufumbuzi achukue hatua gani itayomweka huru.



Alitumia takribani dakika mbili kutafakari. Pasipo kupata maamuzi yamfaayo kuchukua.

“Hawa askari kulikoni?” aliuliza James. Kwa abiria aliyeketi jirani naye.

“Hukusikia tangazo pindi tuko safarini?”

“Aah! Tangazo lipi tena?”

“Kuna ukaguzi wa abiria.”

“Mmmh!...” James alihamaki. Huku akiweka sawa begi dogo la mgongoni alilonalo.



Ikabidi aanze upya kutafakari afanye jambo gani. Kabla hatua hiyo haijakamilika alishtushwa kuona askari wanateremka kwa uharaka pale waliposimama na kuparamia treni kwa fujo wawahi kuingia mabehewani. Kila behewa waliingia askari watatu. Mmoja mlangoni, wawili wakahusika na ukaguzi. Mtu kwa mtu, ukishakaguliwa, unaruhusiwa kuteremka. Wale askari walioingia behewa aliloko James, walifanya zoezi hilo kwa kasi sana. Na kufikia hatua ya umalizo ndani ya muda mfupi.

“Vua kofia na hiyo miwani yako,” alisema askari mmoja walipomfikia James.







James alitii. Akaanza iondoa kofia baadaye akafuatia miwani. Sura iliyoonekana ikawapa mshangao wale askari, na kuwafanya wajadiliane kwa sekunde chache kisha wakamrudia. Kwani kilichowatatanisha ni makovu yaliyojijenga usoni, yaliyochangia kuondoa uhalisia wake kwa namna fulani.

“Tupatie kitambulisho chako.”

“Kimeharibika, kiasi kwamba maandishi na sura yangu havionekani. Hivyo nashindwa kutembea nacho.”

“Utawezaje kutembea pasipo kitambulisho?”

“Kimeharibika afande.”

Baadaye wakarejea kujadiliana kwa mara nyingine.

“Tumwachie aondoke tu, maana hafananii na yule aliyopo pichani,” alisema mmoja wao.

“Hapana. Tusimwachie, kama tuna mashaka tuondoke naye hadi kwa wenzetu nao wakamchunguze vizuri.”

“Sawa. Ila naona kama tunampotezea muda wake tu.”

“Sio sahihi. Tupo kazini, tufanye kwanza kazi, huruma baadaye.”



Walivyohitimisha wakamrudia, wakamuamuru awafuate. Hakupinga. Askari mmoja mbele, James katikati askari wawili nyuma, wakaongozana kuelekea jengo la utawala ambako afande wao aongozaye askari hao alikuwa ameketi. Wakati wote James alikuwa mnyonge. Alikosa namna ya kujitetea kutokana na uwingi wa askari waliopo. Na kuthubutu kupingana nao, kwa kuwakimbia ilikuwa sawa na kujitafutia kifo. Hivyo hakutaka hilo litokee. Ikamlazimu anywee, huku akikesha kufanya sala Mwenyezi Mungu amnusuru.



Pindi anapelekwa wakajenga ulizo moyoni mwa raia na askari wengine waliokuwa wanatoka kwenye mabehewa mengine baada ya kumaliza ukaguzi. Na mshangao mkubwa wa kumtathmini James.

“Kafanya nini tena huyu jamaa?”

“Kaharibu nini tena?”

“Huyu kijana mbona anafanana na yule aliyehusika na mauaji ya dereva teksi Lukwika?”



Walijiuliza raia, maswali waliyokosa jibu rasmi zaidi ya kubashiri. Ila lile la kuhusishwa na mauaji ya dereva teksi, likawavumbua wengi wamwangalie kwa uzuri.

“Eeeh! Ndiyo mwenyewe…”

“Ndiyo yeye. Si unaona mabaka ya kuungua na moto usoni,” walisikika walio wengi. Hasahasa madereva bodaboda, bajaji na teksi.

“Muuaji huyoooo…tuleteeni huku tumwondoe,” waliropoka kwa nguvu. Kauli iliyowashtua watu wengine ambao hawakuwa hata na chembe ya hisia kumuhusu. Ikawabidi nao watumbue macho kumshuhudia kwa uzuri lakini walikwishachelewa, kwani punde sauti hiyo ilivyosikika msafara wao ukaingia ndani ya jengo la utawala.



Moja kwa kwa hadi chumba alichopo afande wao. Mkaguzi Msaidizi wa jeshi la polisi. Mzee akaribiaye umri wa miaka hamsini na nane. Punde wakaingia kwenye majadiliano yaliyoanzishwa na wale askari, yaliyomshinikiza naye kutoa macho pima kumsaili James. Lakini kutokana na tatizo la macho limsumbualo, akashindwa kumng'amua vyema. Maana uwezo wake wa kuona vizuri hadi avae miwani halafu hiyo siku aliisahau.

“Huyu ndiye yule muuaji?” aliuliza, baada ya kumsaili James zaidi ya mara tano kwa kusogeza kichwa chake karibu na uso wa James.

“Nasi tuna mashaka ndiye mwenyewe. Japo kuna utofauti wa sura kidogo. Huyu ana makovu usoni, yule aliyopo pichani hana.”

“Mpigeni picha muwatumie wale wa mawasiliano watupatie uthibitisho kama ndiye mwenyewe ama siyo.

“Sawa afande.”



Hilo likatekelezwa. Kwa wepesi na kutumwa kule wanakohitaji wathibitishiwe. Makao makuu ya jeshi la polisi. Chumba cha mawasiliano na waongozaji kamera za mtaani. Picha ilitumwa na baadhi ya taarifa, wahusika waliopiga picha na jina la sehemu ya tukio. Ujumbe haukuchukua muda mrefu kupokelewa. Ndani mukiwa na mtu mmoja pekee, Kanali mstaafu Faidha Mwembere. Wengine, wahusika wakuu wa kile chumba walikuwa nje wakipata kisabeho. Ambaye alipata kutembelea kujionea kiendeleacho ni nini juu ya jitihada zifanywazo. Sababu alifahamu hatua kadhaa za kiutendaji katika mitambo iliyopo, mlio ulivyosikika aliusikia vyema, na kufahamu mlio huo unamaanisha nini. Akashawishika, kupiga hatua ajionee kihusucho.



Aliisogelea kompyuta husika ambayo ujumbe umeingia, akaanza chezea kwa sekunde chache, kisha akafanikiwa kujionea kilichotumwa. Alivyomaliza, hakufunga aliacha vivyo hivyo wahusika waje kujionea. Na hatimaye kuondoka kwa kasi mule chumbani hadi eneo la maegesho alikopaki gari yake. Akafungua mlango kwa haraka mno, akapanda tayari kuianza safari. Ila kabla hajafanya jambo lolote la kumuondoa alitoa simu yake mfukoni, akabonyeza vitufe kadhaa na kuweka sikioni. Muda mfupi baadaye alisikika akizungumza.

“Wahini Nanderu,”

“Sawa Bosi,” alisikika yule aliyoko upande wa pili.

“Hamtakiwi kufanya uzembe. Fanyeni mlichotumwa.”

“Ondoa shaka kuhusu hilo kiongozi.”

Akakata simu.



Simu aliyopiga ilitua kwa Kalumbwe. Pindi wako doria vijiji mbalimbali wakiutafuta mji wa Nanderu. Walivyopatiwa taarifa hiyo, ikawafanya waongeze kasi na morali, pia kutafuta usafiri utaowawahisha mjini Nanderu. Zoezi hilo lilichukua robo saa. Baada ya hapo wakawa ndani ya basi la abiria. Walisafiri zaidi ya saa kumi kufikia mji husika, wakateremka na kutafuta nyumba ya wageni kwa mapumziko. Wakafanikiwa kupata.



Kazi iliyowapeleka waliianza rasmi siku iliyofuata. Waliomba muongozo kwa Kanali mstaafu Faidha walivyopatiwa wakajua namna ya kujipanga.

“Atasafirishwa mchana wa leo kuletwa makao makuu ya jeshi la polisi na kikosi kazi,” ulisomeka ujumbe waliotumiwa kwenye simu baada ya kuuliza.

****



Muda mrefu sana ulipita. Pasipo kupatiwa mrejesho wa picha na taarifa fupi waliyotuma. Hadi wakaamua kuondoka pale stendi na kwenda kusubiria kituoni. Mchana, majira ya saa saba ndipo walijibiwa. Jibu lililoambatana na ombi la kumsafirisha James mchana wa siku inayofuata. Taarifa ikawafikia kikosi kazi, wakasafiri mpaka mjini Nanderu tayari kwa safari kama walivyoambiwa. Walivyowasili hawakuacha kumchunguza ili nao wawe na dondoo za hapa na pale katika kuelekea kuzipata zile zilizo na uhakika. Wote walivyomuona wakajiridhisha. Pasi na shaka, kwamba huyo ndiye mtafutwa wanaohangaika naye siku zote. Ila hawakuwa na la kumfanya, hata kama kawasumbua kiasi gani. Kwa sababu ya amri waliyopatiwa.



Siku iliyofuata hadi kufikia saa sita mchana, tayari maandalizi ya safari yalishakamilika. Watu wote waliopaswa kuwepo garini, walishapanda. Akasubiriwa dereva afanye mambo yake mara baada ya kumaliza akifanyacho. Alikuwa anaongea na simu. Alivyomaliza alitekenya funguo, gari ikawaka kisha taratibu aliingiza gia safari ikaanza. Waliliacha eneo la kituo, huku gari ikipuliza king’ora muda wote kuomba njia kwa watumia vyombo vya usafiri na wale watembeao kwa miguu. Madereva wenye busara wakafanya hivyo, walipaki gari ama pikipiki pembeni kupisha. Kilomita nne mbele toka kituoni, wakakutana na foleni kubwa iliyowashindwa kupata upenyo wa kupita. Hali iliyowalazimu nao wakae kwenye foleni wasubiri gari zipungue ndipo waendelee. Walivyodiriki kuwauliza watembea kwa miguu watokao foleni ilikoanzia kuja wao walipo, waliambiwa foleni hiyo imesababishwa na ajali ya magari matatu yaliyogongana makutano ya barabara mara baada ya gari moja kushambuliwa na risasi.



Baadaye mmoja wao, akaingiwa na wazo la kwenda kuwasaidia askari wanaoongoza magari yatoke na wale wanaoondoa magari yaliyopata ajali. Wazo lililoridhiwa na wote. Wakateremka. Akasalia dereva na James ndani ya gari, huku akiwa amefungwa pingu mikononi. Umbali lilipo gari yao na eneo lililotokea ajali ni takribani mita mia mbili, wakahimizana watembee kwa haraka wawahi. Wakafanya hivyo. Walivyofika umbali wa mita mia moja na kumi, walishtushwa na sauti ya nguvu iliyotoka nyuma yao.

“Afande!...afande, gari yenu inawaka moto,” ilisikika sauti hiyo. Iliyowalazimu kugeuka nyuma kumuangalia atamkaye na kule walikoiacha gari yao.



Kweli! Walishuhudia gari moja wapo katika zile zilizopo kwenye foleni kufuka moshi. Wakaanza mbio kurudi iliko gari yao. Walivyofika, wakaiamini ile kauli waliyoambiwa. Wakajaribu kuvaa ujasiri kuokoa baadhi ya vitu vya muhimu, na kuuzima moto ulioanzia kwenye tanki la mafuta, lakini hawakufanikiwa, kwani ulianza changanyia kuwaka kwa kasi. Hawakuwa na budi, walisogea pembeni kuangalia namna linavyoteketea huku wakibaki kusikitika na kuwaonea huruma watu waliowaacha ndani, ambao walivyoulizia kwa watu wa kwanza kufika eneo la tukio namna lilivyoanza na wapi wameelekea waliarifiwa kuwa watu hao washaaga dunia baada ya kitu chenye ncha kali kuingia mwilini mwao.

“Wenzenu washafariki, wale pale mnaweza kwenda kuwachunguza,” alisema raia mmoja ambaye alihusika kuwaokoa pindi moto unaanza.



Walienda sehemu waliyoarifiwa na kukuta shuka kubwa jeupe lililolowana damu limefunikwa gubigubi kwa hao watu. Waliuendea upande walioelekezwa vichwa, wakafunua taratibu hadi usawa wa kifua, wakathibitisha walichoelezwa. Mwili wa dereva wao ulionekana kushambuliwa kwa risasi zipitazo tatu kifuani. Ila cha kushangaza mwili wa mtu mwingine, ambaye waliarifiwa, James, haukuonekana. Sehemu aliyolazwa kulikuwa na ubao. Jambo lililowafanya washangaane.

“Huyo mwingine yuko wapi?” waliuliza pamoja.

“Tulimlaza hapo. Ulipokuwa ubao.”

“Inawezekana vipi katoweka? Wakati alipigwa risasi na kafariki?”

“Nasi tunashangaa afande. Yumkini ni mwanga.”

“Hapana! Hapana, hapa kuna namna.”



Dakika chache baadaye taarifa ya tukio ilitapakaa kila kona nchini Mangaka. Wakuu wa vyombo vya dola walifikiwa pindi wako chumba maalumu cha mahojiano wakisubiri msafara unaomsafirisha James. Punde walivyosikia hamu ya kuendelea kuketi ofisini ikatoweka, mshawasha wa kufika eneo la tukio ukatamalaki. Na kuwahimiza watafute namna ya kusafiri muda huohuo. Zilichukua dakika mbili, kufikia tamati kwa jitihada zao, zikiwa na manufaa, baada ya hapo wakaingia ndani ya gari kuelekea sehemu ambayo, Mkuu wa jeshi la ukombozi wa wananchi pekee alilifahamu. Mwendo wa dakika tisa waliwasili mwisho wa safari yao. Katika kambi moja ya kijeshi. Kikosi cha anga, kilichopo pembezoni kidogo na mji.

“Hatuna budi, yatupaswa kufika eneo la tukio muda huu,” alisema Jenerali Anyilwisye. Wakiwa hima kuvuta hatua kuelekea kichakani mlimotawaliwa na miti midogo midogo iliyokauka. Baada ya kukimaliza, walikutana na uwazi uliowawezesha kuona helkopta ya kijeshi imepaki.

“Tutaondoka na hii helkopta kuelekea eneo la tukio,” aliendelea kusema, wakiwa washaifikia.

Haikuchukua muda, walipanda kisha safari ikaanza.



Safari yao iliishia uwanja wa mpira wa miguu wa shule ya msingi Amrimbovu, wakapokelewa na mmoja miongoni mwa viongozi waliopo kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa. Mshauri Mgambo wa mji huo, kisha wakaongozwa hadi eneo la tukio ambako napo waliopekelewa na viongozi wote paswa wa kamati ya ulinzi na usalama. Kile walichoshuhudia hawakuweza amini machoni mwao. Kiliwasikitisha mno, hadi kupelekea maumivu makali yaliyochoma mioyo yao.

“Hakika huyu aliyefanya hivi hapaswi kusamehewa,” alijisemeza kila mmoja kwa namna yake, huku wakiyaangazia mazingira ya tukio yalivyo. Hilo la moto na lile linalohusisha magari yaliyogongana.



Moto na majivu yalivyopoa, waliingia kazini wakuu wenyewe, kufanyia uchunguzi, wakisaidizana na baadhi ya wataalamu wabobezi wa upelelezi ambao washapata kustaafu. Ila hutumiwa katika matukio maalumu kama hilo. Walivyohitimisha uchunguzi wa awali wa gari kuwaka moto walihamia kwenye zile gari zilizoshambuliwa kwa risasi na baadaye kusababisha ajali ya kugongana. Hasahasa walilichunguza kwa makini lile lililoshambuliwa kwa risasi. Walikagua uwiano wa risasi zilizotumika, katika gari ya kikosi kazi na ile iliyochangia kutokea kwa ajali. Zoezi lote hilo, walichukua dakika arobaini na tano kufikia tamati. Na kufikia muafaka kupitia uchunguzi wa mwanzo walioufanya. Wakabaini, ufanano uliopo, wa risasi zilizotumika na ugunduzi wa njama iliyozalisha tukio zima.

“Watu waliohusika na hili tukio, lengo lao mahususi lilikuwa tukio la pili lililotendeka. Walijua, wakishambulia pale makutano ya barabara watatengeneza foleni itayowanasa kirahisi. Na ndicho walichofanya wakafanikiwa,” alisema Jenerali Anyilwisye, walivyokutana viongozi wakuu wa idara za ulinzi na usalama mara baada ya kuhitimisha uchunguzi wao, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya kamanda wa polisi mjini Nanderu.

“Sahihi afande. Tena inajenga wazi kuwa kuna wabaya ambao hawahitaji azma yetu itimie,” alichangia Inspekta wa jeshi la polisi.

“Tufanye uchunguzi wa kina kuhusu hili. Kikosi kazi, kipate mapumziko mafupi, ya siku tatu, baada ya hapo warejee kazini kama kawaida. Awamu hii, watakuwa na kazi mbili, kumtafuta mshambuliaji wa hili tukio la sasa na yule muuaji wa mwanzo.”

“Tunalitekeleza hilo afande,” walisema wale wakuu wengine, huku waki-saluti kwa Jenerali Anyilwisye, kuonyesha utii wao mbele yake sababu alikuwa mkubwa kimamlaka kwao.



Kikosi kazi kilikuwa sehemu ya wahudhuriaji wa kikao hicho kifupi. Majukumu yote waliyokabidhiwa waliyabeba na kuahidi kuyashughulikia ipasavyo japo wameanza pata changamoto ya kufuatiliwa. Wasitimize walichoagizwa.



Pindi wao wanajiwekea upya mikakati ya ushindi itayowawezesha kumweka huru mheshimiwa Rais, Ndg. Mohammed Mlunji aliyoko mafichoni hadi wakati huo, wananchi wanalianzisha upya vurumai baada ya kupenyezewa taarifa kuhusu ahadi waliyopata ahidiwa na vyombo vya ulinzi kuhusu mtu waliyemtuhumu kuwa afisa wa usalama wa taifa kahusika na mauaji ya raia, kwamba atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, matokeo yake wametorokwa. Wao hawakuziamini habari za kutorokwa. Moja kwa moja wakafahamu wamemtorosha makusudi sababu wote ni watu wa idara zinazolandana hivyo lazima wabebane.



Haifahamiki wapi walianzia. Wakajikuta wamejaa barabarani halaiki ya kutosha iliyobeba zana mbalimbali za kimapigano ya jadi sambamba na mabango yaelezeayo hisia zao. Huku wakiimba nyimbo mbalimbali, pasi na sahau kufanya fujo ya kuvamia na kubomoa makazi ya askari waishio uraiani.

Kamata

Pigaaaa

Uonevu

Ku-uaga

Kwa sababu

Mabazazi, hawana huruma

Ukicheka nao, wana-kuvuna.



Walisikika wakiimba. Nyimbo iliyoanzishwa na mmoja wao wengine wakawa wanaitikia. Wakizidi chanja mbuga kuelekea sehemu ambayo hawakuwa na uelekeo nao. Halikuwa tukio la mji mmoja, karibu raia wa miji yote, wale walioguswa na uzembe uliofanywa na idara za ulinzi na usalama kuhusu yule waliyemtaka achukuliwe hatua za kisheria. Habari za kuzidiwa ujanja hawakuzifahamu kabisa, walichojua wao kuwa idara hizo zimedhamiria kumtorosha makusudi.









Miji ikachafuka, kwa moshi na vilio. Vya watu kupigwa, ama mabomu na risasi toka kwa askari wa vikosi vya kutuliza fujo, ambavyo viliingilia kati baadaye. Kuwatawanya waandamanaji wote, ila waandamanaji hawakukubali kirahisi hivyo. Nao walionyesha ubavu walionao, kwa kuhakikisha kilichotawala ndani ya mioyo yao kinatimia.

“Tutoleeni huyo mwendawazimu. Anayesababisha wananchi tuishi kwa tabu,” ilisikika sauti toka kwenye kundi kubwa la kina-baba waliobeba mishale yenye sumu, huku wakiirusha kuielekeza kwa askari waliosimama mbele yao.

“Yaani, wachukue kodi yetu ya kila zao, na kutuondoa ulimwenguni watuondoe? Hapana. Hii kitu hakikubaliki,” mwingine naye alichangia.



Hakika, wananchi walichafukwa. Tena sio kidogo. Kwa kiasi kikubwa, hiyo yote ni kutokana na matendo ya idara hizo kuisapoti serikali hata kama wamekumbwa na matatizo ya aina gani ambayo wana wajibu wa kuyapigania kisheria. Wakifanya, huonekana wamevunja sheria.

“Kwanini huu muandamo wa haya mambo hayaishi?” aliuliza Jenerali Anyilwisye walivyokutana viongozi wakuu wa idara nyeti za ulinzi na usalama.

“Nami nashangaa Afande. Yamkini kuna mtu anayewashawishi hawa wananchi wafanye hivi, wakishawaona wapo kimya kwa muda mrefu. Hasahasa wanasiasa wa upinzani.”

“Haina haja ya kuwatuhumu watu wa upinzani moja kwa moja. Yatupasa nasi wenyewe tujichunguze.”

“Hamna tatizo afande. Ulinenalo, daima hutekelezwa. Tupo tayari kwa tamko lako.”

“Kila mmoja wetu, awajibike ipasavyo katika idara yake. Msivyotekeleza hili, idara zote zitakuwa chini yangu. Ikiwa na maana mtafuata kile nachokiamuru.”

“Tupo timamu afande kwa utekelezaji.”



Sekeseke lilichukua majuma. Huku likitoa matokeo mabaya pande zote. Matokeo yaliyowafanya walaumiane pasipo tambua chanzo kikuu ni nani. Kwani, kila mmoja alimtupia mpira mwenziye. Hadi kuja kutulia, palichukua muda mrefu. Takribani miezi mitatu. Vyombo vya usalama wakitupia lawama wanasiasa wa upinzani kuwa ndiyo chanzo cha yote yaliyojiri, wakisahau, hata wale wanasiasa walioko upande wa utawala wanaweza kuwa visababishi pia.

****



Kalumbwe na Aisha walikuwa ndani ya hoteli kubwa ya kifahari, ifahamikayo BONDENI VIEW, iliyopo katikati ya mji, kilomita chache toka makutano ya barabara kuu. Jengo la hoteli hiyo, lilikuwa ni ghorofa, zipatazo nane, huku likiwa jengo pekee refu kuliko yote mjini Nanderu. Mandhari yake yalisheheni uvutio, kwa yeyote apitaye ama aendaye kupata huduma fulani. Utulivu ulikuwa wa kutosha, uliochangia watu wengi toka miji mbalimbali wafikapo ndani ya mji huo kupitia hapo kupata huduma ya mapumziko kisha kuendelea na ratiba zao. Hakukuwa na pilika pilika zozote ziletazo bughuza watu wapatiwao huduma hutulia sehemu zao hadi wamalize ndipo huonekana wakihangaika huku na kule kuangalia mazingira yalivyopambika. Hata kama mtu kauvaa uenyeji, kutokana na mara kwa mara kupata huduma zake sehemu hiyo, kushangaa hakukukosekana, kwa sababu, kila baada ya siku kadhaa hufanyika marekebisho mbalimbali ya kuongeza ama kuondoa urembo. Hakika, hoteli hiyo ndani ya mji wa Nanderu, ilikuwa sehemu ya kivutio cha utalii.



Hivyo mapema tu, walivyokamilisha taratibu zote hitajika shauku ya kuangalia mazingira yalivyopambika iliwavaa. Walianza na yale ya nje, baadaye wakahamia kila ghorofa na kuhitimisha mwisho kabisa mwa jengo, ambako kulikuwa na banda dogo lililoishia ngazi na ka-uwanja kilichoonekana watu fulani hufanyia mazoezi. Kule juu wakaushuhudia mji wote kwa uzuri. Tena sehemu iliyojibainisha haswa, ni sehemu ya makutano ya barabara.

“Huku kunafaa kwa kazi iliyotuleta,” alisema Aisha. Wakati huo akifanya jaribio la ulengaji wa shabaha kwa kutumia mikono yake.

“…tena kwa mfano kitu chenyewe unachohitaji kukishambulia kipo pale kwenye makutano, unakidungua kwa wepesi kabisa,” aliendelea kunena, Kalumbwe akifanya utafiti wa hapa na pale. Ghafla! Akamvaa Aisha mzobe mzobe kuteremka nayo chini.

“Mbona hivyo kulikoni?” aliuliza Aisha. Akiwa anavutwa kama mbuzi aliyekosa mchungi akamatwapo kala majani ya mahindi mabichi shambani.



Hakujibiwa. Hadi walivyofika chumbani kwao, na kujitupia kitandani wakifuatiwa na mhemo wa nguvu uliosababishwa na uteremkaji wa ngazi. Kwani walikuwa wanateremka kwa kasi.

“Hatupaswi kuzembea, awamu hii, lazima ahangamie,” alisema Kalumbwe, baada ya kupumzika kwa muda mfupi. Takribani sekunde arobaini.

“Umepata mbinu? Maana toka tuje tunashangaa shangaa tu, wala hatufanyi maandalizi yaliyotuleta huku.”

“Maandalizi yashakamilika. Kulekule juu ndipo tutapofanyia tukio.”

“Haya, mimi nasubiri uratibu uliouandaa tu, ili nitekeleze jukumu langu,” alisema Aisha, huku akijibinua binua, kuonesha kitu kimpacho ufahari mbele ya mtoto wa kiume. Makalio!



Walivyomaliza maongezi wakaelekea mapokezi. Wakamuomba muda mhudumu waliyemkuta awaeleze kiundani mazingira waliyojionea, wakakubaliwa. Akaanza waelezea kuanzia ya nje, na sehemu zote ambazo wao walipita.

“Na vipi kuhusiana na uwanja kule juu?”

“Ule ni uwanja wa mazoezi kwa wateja wafikao hapo hotelini.”

“Oooh!...ni mzuri sana. Kwanini pamependekezwa kule juu badala ya huku chini?”

“Vipo viwanja viwili. Yamkini kingine hamjakiona. Upo huku chini na kule juu.”

“Muda wa mazoezi ni upi?”

“Hamna muda maalumu. Muda wowote mtu ajisikiayo kuchangamsha mwili wake ruksa.”

“Ahsante kwa majibu mazuri uliyotupatia. Mna hoteli nzuri sana, hakika hatujuti kufika mahali hapa. Kwani pameweza kutuongezea kitu ndani ya bongo zetu.”

“Nasi tunashukuru pia.”

Wakaagana, kisha Kalumbwe na Aisha wakarejea chumbani kwao.

“Kesho uwanja wa juu ni wa kwetu. Tujitahidi kufanya kila mbinu hilo liwezekane, ili tufanye tukio kwa urahisi,” alisema Kalumbwe.

“Naamini hamna kitachoshindikana,” alichangia Aisha.



Siku iliyofuata, mapema sana. Wakaomba muongozo kwa mkuu wao. Kanali mstaafu Faidha, naye akawapatia utaratibu wa kuhakikisha wanamwondoa yule waliyemdhamiria. James! Lengo asifikishwe mbele ya vyombo vya sheria, mahakamani, kwani ataipatia sifa mbaya idara. Itayowafanya wananchi waamini matendo ovu yaliyotokea kipindi cha nyuma, kama ya kuwakamata wanaharakati, wateteao maslahi ya wananchi, viongozi wa vyama pinzani na raia wa kawaida walio na misimamo mikali wao ndiyo wahusika. Hata kama ni wahusika, ila hawakupaswa wathibitishwe kwa asilimia mia moja. Ilibidi wathibitishwe kwa mashaka. Hivyo kulitekeleza hilo, mhusika wa tukio abainikapo, lazima aondolewe duniani.



Mbali na hilo, shinikizo alilopatiwa Kanali mstaafu Faidha, na watu waonekanao wazito lilichangia. Sio yeye tu, hata watekelezaji, Kalumbwe na Aisha walikuwa sehemu ya shinikizo hilo. Walikuwa kifungoni, kifungo huru, ambacho wakithubutu kutoa neno kuvujisha siri hawawezi eleweka kwa wananchi. Hawatoaminika. Na mara moja maisha yao hai yatakuwa sahaulifu. Kuna mtu alikuwa nyuma yao. Tena sio mtu tu, bali ni watu. Walijipanga kuhakikisha Rais aliyopo madarakani, Ndg. Mohammed Mlunji hafaidi madaraka yake. Ili wao wafanikishe dili zao. Hivyo kwa jitihada kubwa, Aisha akawa sehemu ya wachochezi, wachocheao wananchi kulilia maslahi yao. Ni yeye ndiye aliyewahimiza watu wasiache kuingia barabarani kudai haki yao kupitia akaunti feki mbalimbali za mitandao ya kijamii anayoimiliki. Japo alikuwa sehemu ya wanachama wa upinzani walioshika nafasi za juu, ila uanachama aliokuwa nao ni uanachama wa kupandikizwa, hivyo ili aendelee ku-upalilia watu wa upande walioko wasimshtukie, alilazimika kufanya yote yafanywayo na upinzani yenye kuichafua serikali.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Ilivyowadia mida ya saa tano asubuhi, wakapanda kule juu. Kwa kisingizio cha kwenda kufanya mazoezi. Wakiwa na begi dogo la mgongoni walilohifadhia zana zao za kazi. Silaha, walizozifungua, ili zisibainike. Kitu cha kwanza walivyofika kule juu waliifunga kwa komeo ile sehemu iwezeshayo kutokeza pale juu, pasitokee mtu yeyote wa kwenda zaidi yao. Walivyokamilisha hilo, walitoa vitu vilivyopo begini wakaanza kuvifunga. Zoezi la ufungaji lilikuwa la muda mfupi sana. Dakika moja tu, ikawawezesha kuhitimisha na kupata umbo kamili la kifaa husika. Ambayo ni bunduki, aina ya M4 Carbine iliyotambulishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1993 yenye uwezo wa ulengaji sahihi ndani ya mita mia tano.

“Tupo tayari kuanza,” alisema Kalumbwe, akiwa anatandika kitambaa fulani chenye uzito chini. Sehemu ya kulala, usawa wataokita vyema bunduki yao.



Miongoni mwa vitu vilivyofungwa ni kiwambo. Kifaa pekee kiletacho uzio wa mlio wa risasi kusikika. Ilivyowadia saa 5:55 asubuhi wakafanya jaribio kuhakikisha kama bunduki yao iko imara kwa kazi iliyoko mbele yao. Na halikuwa jaribio ili-mradi, bali ni jaribio litaloleta manufaa katika kufanikisha walichopanga. Wakashambulia moja ya gari pale makutanoni ya barabara. Gari iliyoshambuliwa, ikaenda somba gari zingine zilizopo mbele baada ya kupotezewa uelekeo. Hatimaye ikatokea ajali kubwa, iliyosababisha kufunga barabara moja wapo kwa sababu ya foleni. Na ndiyo barabara ambayo msafara wa kikosi kazi ulikuwa unapita. King’ora kikawatambulisha, kuwa hiyo ndiyo gari waliyokuwa wanaisubiri kwa hamu, kuhakikisha, mmoja wao akavuta darubini aweze kujionea kwa usahihi.

“Ni yenyewe,” alisikika Aisha. Akimwambia Kalumbwe, aliyekuwa anahangaika kulisoma lengo kwa uzuri. Alivyolipatia, hakukawiza, alifanya shambulizi la haraka kisha wakafungua bunduki chap, wakarejea chumbani kwao.



Hakukuwa na haja ya kukaa tena. Walirejesha funguo ya chumba mapokezi wakaondoka zao. Walivyohojiwa ughafla wa safari yao na wahudumu waliokwisha anza nao mazoea, waliwapatia sababu za uongo na kweli.

“Tushafanya yetu,” alisikika Kalumbwe, pindi akiongea na mtu wa upande wa pili. Kwa njia ya simu ya mkononi.

“Mna uhakika mushamaliza kazi?” aliuliza yule wa upande wa pili.

“Sahihi kiongozi, sikilizia matokeo kwenye vyombo vya habari.”

“Kazi nzuri. Yule aliyesalia hatutosumbuka naye.”

“Sahihi,” alisema Kalumbwe na kukata simu.



Dakika kadhaa baadaye wakawa ndani ya gari kuukimbia kabisa mji huo wasibainike. Huku wakiwa na imani, washamuondoa James duniani. Kwa shambulizi walilofanya, lililopelekea kulipua gari zima. Taarifa za tukio wakawa wanasikilizia kwenye mitandao ya kijamii. Namna walivyoleta athari na hatua zilizopangwa kuchukuliwa na vyombo vya dola. Safari yao ikaishia mjini Lukwika. Wakapanga kuketi ndani ya mji huo kusikilizia, kama kuna shughuli nyingine wanayopaswa kufanya iwe rahisi kwao kutekeleza.



Wiki ya mapumziko waliyopatiwa kikosi kazi ilivyomalizika. Ilimalizika kwa tukio. La kuokotwa maganda manne ya risasi juu ya jingo hilo. Habari za tukio hilo liliibuliwa na mmoja wa wateja waliopanda juu kwenda kufanya mazoezi. Tukio likaripotiwa kituo cha polisi, kisha kikafahamishwa kikosi kazi, ambao walizuru eneo la tukio, punde, baada ya kuarifiwa. Wakafanya uchunguzi, uliojaa ubashiri, baadaye wakaenda kutazama kamera waweze kugundua watu wepi walipanda huko juu siku za nyuma. Kwani walishapeleka shaka moja kwa moja, kuwa maganda hayo ya risasi, ndiyo yaliyotumika kwenye shambulizi siku za nyuma.



Taarifa hii iliwafikia Kalumbwe na Aisha kupitia kwa bosi wao. Kanali mstaafu Faidha, kwa njia ya simu. Mara baada ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno, uliosomeka

“Kuna maganda ya risasi yameokotwa juu ya hoteli ya Bondeni View, ninyi ndiyo mlihusika kufanyia hapo tukio?”



Jumbe hiyo ikawafanya wakumbuke jambo, namna walivyofanya tukio na baada ya tukio. Kisha wakamjibu.

“Ndiyo ni sisi.”

“Kwanini mlifanya hivyo? Hamuoni kama mnaenda bainika? Maana hivi ninavyowasiliana nanyi, kikosi kazi kinaenda angalia matukio yaliyorekodiwa na kamera za CCTV waweze watambua watu wa mwisho kupanda kule juu ni nani kabla ya hili tukio la leo.”

“Dah! Mambo yataharibika. Sasa tunafanyaje kukwepa hii?”

“Sidhani kama mtakwepa hapa. Mshaharibu, kujikwamua, labda muondoke nchini.”

“Yeah! Ni jambo jema. Basi tunaomba utufanyie huo mpango, ikibidi, kufikia jioni ya leo, saa kumi na mbili tuwe taifa lingine tofauti na hili tulilozaliwa.”

“Ondoeni sha…” alijibu Kanali mstaafu Faidha, ila hakuweza malizia jumbe yake. Mara baada ya kushtushwa na taarifa ya ujumbe mfupi aliyotumiwa kwenye simu nyingine. Uliosomeka ‘wahusika waliofanya tukio wamebainika,’

Muda huohuo akaacha kuchati na Kalumbwe, akampigia simu yule aliyemtumia ujumbe kwenye simu nyingine.

“Kiongozi, tumekutumia picha ya video whatsapp ya wahusika,” alisikika yule aliyoko upande wa pili, kisha akakata simu.







Hakuchelea, akaingia whatsapp akaipakua video husika, iliyo na urefu wa dakika moja kisha akaanza itazama. Japo picha zilikuwa hazionekani kwa ubora, ila sura za wahusika zilijibainisha. Akazishuhudia picha za watu wawili, wenye jinsia ya kiume na ya kike, walio na muonekano wa mataifa ya nje. Alilitambua hilo kupitia muonekano wao. Akawashuhudia namna walivyopanda, wakiwa na mabegi madogo mgongoni, vilevile walivyoteremka baada ya dakika chache. Sura alizozishuhudia zilikuwa tofauti na zile alizozihisi. Kwamba watakuwa ni Kalumbwe na Aisha, haikuwa hivyo, na alivyoendelea kuichunguza kwa makini, akabaini, utofauti wa tarehe, ile ionekanayo kwenye video na ile iliyofanyika tukio. Kabla hajawahabarisha wenziye, akaanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaficha watu wake, kwani naye angeumbuka endapo wangelionekana. Ila baadaye akahisi yamkini waliomtumia wamekosea, ikabidi awataarifu.

“Tarehe ya hii video ni tofauti na ile iliyotokea tukio,” alisema, pindi akiwasiliana na mtu kwa njia ya simu.

“Unasema kwamba?” aliuliza yule wa upande wa pili.

“Angalieni kwa makini. Tukio lilitokea tarehe 12, hii video ni ya tarehe 11.”

“Eeeh!...eeeh!...sahihi, itakuwa wamekosea kutuma.”

“Jaribu kuulizia imekuaje kuaje halafu utanijuza.”

“Hamna shida afande. Nafuatilia hilo sasa hivi, punde nitavyokamilisha mrejesho kwako,” alisema yule wa upande wa pili, kwa sauti iliyosheheni morali ya kazi, kisha akakata simu.



Dakika saba baadaye simu yake ikaita kwa mara nyingine. Muito uliomwashiria anapigiwa. Alivyoangalia jina la mpigaji, aliliona ni la yule aliyetoka kuwasiliana naye muda chache uliopita. Akapokea.

“Eeh! Afande, nimefuatilia…” alisikika yule mtu wa upande wa pili. Ila kabla hajamalizia kauli yake, alikatishwa na tamko la Kanali mstaafu Faidha.

“Mmmh!...wanasemaje?”

“Hiyo ndiyo picha ya mwisho ya video iliyorekodiwa na kamera za ile hoteli. Ina maana baada ya hapo inapoishia hakuna tukio lolote lililorekodiwa, kwa madai kwamba mitambo iongozayo kamera hizo ilifeli.”

“Ooops!...” alihema Kanali mstaafu Faidha kimya kimya, baada ya hapo akaendelea, “…kwa maana hiyo wale waonekanao kwenye video si wahusika wa tukio?”

“Sahihi afande. Yawezekana wamehusika ama hawajahusika.”

“Kwani maelezo ya wahudumu wanadai lini waliondoka hotelini kwao?”

“Tarehe kumi na moja.”

“Kwa huo mlolongo, wao si wahusika. Tukubali kuwa tumefeli na tujipange kwa mara nyingine.”

“Sawa afande.”



Kanali mstaafu Faidha Mwembere, alikuwa anapokea ripoti hiyo kwa niaba ya wakuu wenziye. Akishataarifiwa, naye huwataarifu, kama watakuwa na cha kujadiliana, watajadiliana maafikiano yakishafikiwa Kanali mstaafu Faidha, hurejesha kwa watendaji. Askari wa chini.



Upande wa pili, James alifanikiwa kuchoropoka. Kwani, zile risasi zilizopigwa, zilimpa mshituko tu, uliomfanya apoteze fahamu. Watu wa msaada walivyokuja wakamhisi moja kwa moja kuwa kashaaga dunia kutokana na mazingira waliyomkutana nayo sambamba na dereva. Ambaye ndiye aliaga dunia baada ya kukutwa na risasi. James alipitiwa na vipande vya vioo tu, vilivyotoboa sehemu ndogo ya mwili wake. Na kumtoa damu kiasi kidogo, vingine viking’ang’ania mwilini. Walivyotolewa garini, wakaenda hifadhiwa eneo fulani, umbali mdogo na gari lilipo, huku mikononi akiwa kafungwa pingu. Iliyowatambulisha wasamaria wema kuwa ni mhalifu, na walivyomchunguza kwa makini, wakambaini ndiye yule anayesakamwa na wananchi kwa kina achukuliwe hatua kali za kisheria baada ya kuhusishwa na mauaji.



Walivyogundua kuwa kashaaga dunia, wala hawakuwa na habari nayo. Wachache waliishia kupiga picha sehemu ya sura yake na kutuma mitandaoni ku—uhabarisha umma yule waliyekuwa wanamlilia siku zote aadhibiwe vikali hayupo tena duniani. Kitendo cha kutuliwa chini na kufunikwa shuka watu wasione one, fahamu ikamrejea. Ila hakuonesha wazi, alisikilizia kwa muda mfupi huku akifunua sehemu ndogo ya shuka iliyomwezesha kuwaangalia watu wafanyacho. Akawaona wengi wako bize kuangalia namna gari inavyoendelea kuteketea kwa moto na jitihada za uokoaji wa zile gari zilizoko karibu na ile iunguayo zisifikiwe na moto huo. Alivyoangaza pembeni yake, akaona ubao fulani ulioenea misumari kadhaa. Akausogeza karibu yake, kisha yeye taratibu akajivuta kwa juu, alivyofanikiwa kuliacha shuka, alipiga hatua taratibu asishtushe watu. Kilichomsaidia, eneo walilohifadhiwa lilikuwa mafichoni kidogo.



Alivyofika umbali fulani, akatoka mbio, mithili ya mwanariadha, ile pingu akiwa ameificha kwa kusundika sehemu ya mikono yake ndani ya shati. Alielekea mafichoni, nje kidogo na mji, vichakani, ili asijenge mshangao na utambuzi wa kufuatwa fuatwa na watu wamuonao. Alivyowasili huko, akawa anatafuta namna ya kuiondoa pingu iliyompa kifungo cha utambulisho wa uhalifu. Kuendelea kuwanayo, ni sawasawa na kujitwalia makaa ya moto mdomoni. Ilimpasa kuiondoa kwa namna yoyote. Pindi akiwa katika harakati za kupambanua mbinu imfaayo, mwishowe alipitiwa na usingizi, uliomchukua muda mrefu kuja kuamka, tena baada ya kushtushwa na mmoja wa watu waliokuwa wanapita kwenda mawindoni. Wao ndiyo wakamsaidia kuiondoa ile pingu. Waliikata kwa kutumia msumeno mdogo watumiao kukatia vyumba vidogo.



Sasa akawa huru. Aliwashukuru kisha akaondoka kuelekea sehemu ambayo hata hakuifahamu baada ya wale wawindaji kuendelea na safari yao. Alikesha kuzunguka huku na kule, pasipo uelekeo maalumu, huku akitafakari namna ya kufanikisha zoezi lililoko mbele yake ukizingatia begi atumialo kuhifadhia nyaraka zake zimuwezeshazo utendaji hakuanazo. Na pasipo hizo hakuna muendelezo wa kufanikisha.

“Inabidi nizipate zana zangu niendelee na kazi,” aliwaza na kukumbuka, mara ya mwisho begi lake dogo alimwachia mmoja wa abiria ambaye aliketi naye jirani. Kisha akakumbuka kauli ambayo aliambiwa na yule abiria.

“Utakuja Mpindimbi klabu kufuata mzigo wako, sitoweza kukusubiri,” alikumbuka. Kauli hiyo alipatiwa na yule aliyemkabidhi begi lake pindi akiongozana na askari kuteremka ndani ya treni.

“Inabidi nifike Mpindimbi klabu,” akawaza.



Jioni, kiza kilivyofukuza mwanga na kuanza kujitwalia nafasi ya kutosha ndipo akaondoka kichakani. Taratibu, kwa mwendo wa kificho wa sura yake isionwe onwe ovyo watu anaopishana nao. Watu wengine ambao aliwahisi hawana ufahamu wowote kumhusu, hasahasa watoto na wazee wakimbiliao kutembea kwa kutumia kisaidizi, hakuacha kuwauliza. Wapi klabu hiyo inakopatikana, alivyopatiwa uelekeo, aliufuata huo, hadi alivyoingia katikati ya mji. Huko nako aliendelea nao, kwa kujificha ficha, mpaka akawasili eneo husika, ambalo ni mahususi kwa mazoezi ya viungo. Akatega sehemu, kusoma mazingira yalivyo. Akaona ingia na toka nyingi za watu wafanyao mazoezi huku akishindwa iona sura ya mtu aliyemkabidhi begi lake. Ila aliendelea kuvumilia. Kwa kuketi sehemu hiyohiyo hadi muda wa kufunga, ndipo akambaini. Akiwa anafunga jengo la klabu hiyo. Chap! Akamkimbilia na kumvaa. Huku akitoa ishara ya kumzuia asiongee neno lolote zaidi ya kutekeleza aambiwacho.

“Nahitaji begi langu.”

“Lipo nyumbani, twende nikakukabidhi.”



James akajifikiria kwa muda, takribani sekunde kumi na tano, alivyopata ufumbuzi wa fikra yake, akakubaliana na takwa la mhusika. Waliongozana hadi nyumbani kwa mtu huyo. Mtaa wa tatu toka pale klabuni. Walivyowasili, hakukuwa na maelezo mengi, James alikabidhiwa begi lake, akathibitisha vifaa vilivyopo ndani kama vipo timilifu, aliporidhia, alimshukuru, akamuaga na hatimaye akaondoka kurudi kichakani. Huko, alitafuta sehemu nzuri ya kulala. Kwani alikubaliana shida zote, ili—mradi apate kuwa salama. Kulivyokucha ndipo akaanza rasmi harakati zake. Kwa kutathmini picha aliyopatiwaga na marehemu Joram Isaac nyumbani kwake. Ile iliyowaonyesha wazee wanne wamesimama mbele ya jengo kubwa lililo na maandishi yaliyosomeka 1950 ukutani. Kwa udadavuzi wa haraka, aliwatambua wazee watatu kati ya wale, mmoja aliyesalia ikawa ngumu kumfahamu japo alifanya kila liwezekanalo amfahamu.

“Yamkini huyu ndiye Kasanjara Chomeko,” aliwaza. Pindi akiirejesha picha begini.



Baada ya hapo alibadili mavazi. Akavaa mavazi makubwa yaliyomzuia sehemu kubwa ya mwili wake usibainike kwa urahisi. Sambamba na kofia kubwa iliyomzuia uso. Alivyojihakikishia, yuko poa, hawezi bainika na mtu hadi achunguzwe kwa undani wa kutolewa mavazi aliyovaa, aliondoka kuelekea mjini. Kazi kubwa ambayo alianza ifanya punde alivyowasili mjini, ni kukesha kushangaa majengo mbalimbali kutafuta lifananalo na lile lililopo pichani.



Asilimia kubwa, majengo karibu yote, yalikuwa na maandishi. Ya mwaka na jina la mhusika wa jengo, lakini lile lililopo pichani halikuwa na jina la mhusika, pia katika yote aliyoyapitia hakubahatika kuona hata jengo moja lililoandikwa mwaka 1950. Muda mwingine akadiriki kuwauliza watu, tena kwa kuwaonyesha ile picha lakini katu hakufanikiwa. Kitendo kilichomfanya ahisi, wenda kakosea mji.

“Dah! Hii kazi inahitaji moyo,” alijisemeza. Akiwa kaketi sehemu atumiayo kustiri mbavu zake. Kwenye jengo moja chakavu, lililoko mbezoni mwa mji, akiperuzi peruzi kitabu.



Baadaye akapatwa na wazo la ghalfa, lililomshinikiza kuachana na kile kitabu alichokuwa anaperuzi, kisha kuchukua kamusi akapekua pekua hadi sehemu aliyoidhamiria. Ukurasa ambao umesheheni michoro mingi na maandishi chini ya mchoro husika. Aliupitia mmoja baada ya mwingine, alivyoufikia ulioonyesha jengo akaweka kituo, akatupa macho chini yake kuitazama maana. Alivyoisoma akainakili sehemu. Akahamia kwenye picha, ile ionyeshayo jengo na watu wanne. Akaigeuza kwa nyuma, akakuta zile namba zilizopo ukutani zikiwa zimejumlishwa, zilisomeka 1+9+5+0=? Akapiga hesabu ya haraka, kupata jumla, nayo akainakili. Baada ya hapo akafanya mjumuisho wa maana kamili. Kati ya jengo na zile namba.



Kamusini, jengo lilimaanisha uwanja, na alivyozijumlisha zile namba akapata jumla ya 15, ambayo maana kamusini ilionyesha mchezo upendwao. Hivyo kumpata mtu aliyemfuata yampasa afike uwanjani, uwanja wa mchezo unaopendwa kwa kina na watu wapatikanao ndani ya mji huo. Ikabidi aanze tafakuri, kwa kutumia masomo waliyopatiwa mafunzoni miaka ya nyuma. Akaorodhesha michezo kadhaa. Akavuta kumbukumbu ya ubashiri pia kumbukizi teule ya mji huo katika ulimwengu wa michezo.

“Mpira wa kikapu!” alijisemeza, baada ya kutumia zaidi ya dakika mbili kutafakari. Na kukumbuka, kuwa mji huo una vilabu vizuri vya mpira wa kikapu.



Siku iliyofuata akaanza tekeleza matokeo ya ubashiri wake. Alihudhuria viwanja mbalimbali vya mpira wa kikapu, vya watoto wadogo na vile viwanja vya wakubwa huku akikesha kutazama sura za wazee kufananisha na ile iliyopo pichani. Halikuwa zoezi la siku moja. Ilimchukua zaidi ya wiki, na kumfanya arejee tena pichani kutathmini kwa uzuri. Hatua kwa hatua, alipofikia mwisho, akagundua uwepo wa alama ya magoli ya mpira wa miguu, moja likiwa mwanzo wa namba, na lingine lilimalizikia mwisho wa namba.

“Mchezo wa mpira wa miguu,” aliropoka. Na kumfanya muda huohuo afungashe virago vyake na kutoka mbio, mithili ya mtu aliyefumaniwa.

“Kesho kuna mechi kali sana, baina ya Wabunifu F.C na Wanasimulizi S. C, mchezo utachezwa uwanja wa mpira wa miguu wa Ninga,” alikumbuka. Kauli aliyotamka kijana mmoja jana, pindi akitazama mazoezi ya mpira wa kikapu yachezwayo na watoto wapatao umri kati ya miaka kumi na mbili hadi kumi na tano. Waliofahamika kwa jina la Wakishua kwa sababu wanatoka familia za ki—tajiri.



Alivyotupa jicho mkono wake wa kushoto, alikovaa saa ndogo nadhifu ya kampuni ya Rado ilisomeka, 14:30, ikiwa na maana ni saa nane mchana. Zikisalia dakika thelathini milango ya uwanja ianze kufunguliwa watu waingie. Akatathminisha muda uliosalia na umbali uliopo, akagundua kuwa akiendelea na mwendo huo hatoweza wahi. Hivyo akazidisha kasi. Ilivyosomeka 14:55, akafanikiwa kulifikia moja ya lango la kuingilia uwanjani. Akalisukumiza taratibu, likaachia nafasi ndogo iliyomwezesha kuingia. Akapiga hatua hadi moja ya jukwaa. Jukwaa kuu litumikalo kuketiwa na viongozi wakuu pawapo na tukio. Akaangaza huku na kule ili aweze kubaini kama kuna uwepo wa mtu yeyote lakini hakubahatika kung’amua maono ya mtu ndani ya uwanja kwa wakati huo. Kutaka kujiridhisha zaidi, akaamua kupanda ngazi kulifuata lile jukwaa kuu. Akapiga hatua, ngazi ya kwanza, ya pili, alivyoifikia ya tatu, akashtushwa na mlio wa risasi, uliotua kwenye kitu kama zigo na kudondoshwa. Ikambidi achukue maficho, kusikilizia kama zitapigwa risasi zingine, alipoona kimya kimetamalaki akatoka mafichoni akakimbilia kule alikosikia anguko la kitu.



Akakuta michirizi ya damu, iliyomtambulisha, kuwa aliyepigwa risasi ni binadamu, na si kitu kingine. Alivyofikia, akathibitisha hilo, tena baada ya kumgeuza, akambaini kuwa ndiye yule aliyopo pichani. Mtu mwenye sura ya kizee, na ilikuwa halali yake kuwa hivyo, kwani ngozi iliruhusu kunyanzi za kutosha kumhusu. Ambazo hutoa utambulisho wa moja kwa moja kwa mtu yeyote umbile lake lipoje.

“The bodyguard…” aliita mzee huyo. Kasanjara Chomeko kwa tabu, kwani roho yake ilikuwa inaenda kutengana na kiwiliwili.



Kabla hajaiitikia, James akaanza patwa na mshangao. Kafahamika vipi? Ila baada ya kutafakari kwa sekunde chache akapatia ufumbuzi tafakuri yake, iliyopatwa hakikishwa mara ya pili alivyoitwa na yule mzee, kuashiria hajakosea atamkacho.

“Oktoba 15, Rais anaenda kufa,…the bodyguard,…sa…” alisema mzee huyo, kauli iliyomtoa James tafakurini na kumfanya asikilize aambiwacho kwa makini. Lakini, punde James anavyoweka mkazo kuuvaa umakini, mzee naye nguvu ya uzungumzaji inakata.



Anahaha huku na kule kupigania uhai wake, ila inashindikana, kwani sekunde chache tu, malaika mtoa roho anafanya kazi yake.

“Hii ni kesi nyingine,” anawaza James. Baada ya kuhisi endapo watu wataanza ingia na kukutwa, atapewa kesi nyingine ya mauaji kama ilivyokuwa mwanzo.



Hatimaye akapiga hatua kuondoka. Maana ndiyo ulikuwa utetezi pekee kwake. Hatua mbili mbele, akakumbana na bahasha iliyomtambulisha kuwa ilikuwa mikononi mwa marehemu ila ilidondokea huko baada ya kitendo cha kupigwa risasi. Akafanya hima kuiokota, kisha akazidi piga hatua kutokomea. Anavyofanikiwa kulifikia lango, malango yakafunguliwa kuruhusu watu waingie.







“Hello!” alisikika mtu mmoja akiita, pindi akiwasiliana na mtu mwingine upande wa pili kwa njia ya simu. Katikati ya kiza kinene kilichotawala moja ya chumba cha jengo la kifahari lililopo jijini Naparavi.

“Ndiyo kiongozi.”

“Mushakamilisha?”

“Kwa usahihi. Hatujathubutu kuingiza dhihaka. Hivi nitetavyo nawe, anatambulika kwa jina lingine.”

“Ni vizuri. Mpango wa kifo chake ulikuwaje? Wa mbali ama karibu?”

“Wa mbali kiongozi,…kama mita mia mbili toka sehemu ambayo alipata kuketi.

“Aaah!...” aligumia yule aliyoko gizani. Kwa sauti iliyomshawishi anayezungumza naye kujawa na shauku ya kufahamu kwanini bosi wake kaonekana kughafirika.

“Bosi kulikoni? Mbona umebadilika ghafla?”

“Huyu alipaswa kuuwawa ana kwa ana, sio njia hiyo mliyotumia. Kwani pindi mnamshambulia hamkuona kabeba kitu chochote?”



Kikapita kimya cha muda mfupi. Kilichosababishwa na ufikiriaji wa yule aliyeulizwa. Karibu sekunde saba, kufikiria namna alivyomuona mzee Kasanjara kabla hajamshambulia kwenye darubini.

“Yeah! Kuna mzigo alibeba. Bahasha,” alikumbuka. Kisha akatoa mrejesho kwa bosi wake.

“Bosi ni sahihi. Alikuwa kabeba bahasha katika moja ya mkono wake.”

“Huo ndiyo mzigo uliokuwa unahitajika kwa udi na uvumba, ili tuendelee kumweka Rais Mlunji matatizoni. Kwani, kitu ambacho kimo ndani ya bahasha, ni karatasi zilizo na hotuba, inayopaswa kusomwa siku ya kusherehekea taifa letu kupata uhuru. Oktoba 15. Hotuba hiyo ikifanikiwa kusomwa, yetu yatakuwa yameisha, ule upendo tuliokuwa tunaupata toka kwa jamii, utageuka na kuwa habari nyingine itayotufanya tuwe wahanga ambao katu, hatutotamani sura zetu zionekane mbele ya mtu yeyote. Tutaaibika, na hata kuuwawa pia. Kwani wananchi watakuwa na chuki zito nasi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Tupe amri bosi, tutatekeleza, ili heshima zenu zisalie zilivyo mbele ya wana—Mangaka.”

“Kuna jambo moja wapo la kufanya kati ya haya mawili. Yote yana ukubwa sawa, sababu yanategemeana. Mosi; kupata karatasi za hotuba zilizomo ndani ya bahasha, pili; Rais lazima auwawe.”

“Ondoa shaka. Hatua moja wapo itakamilika tu.”

Simu ikakatwa.

****



James alifanikiwa kuukimbia mji wa Nanderu. Akafanya safari kuelekea asikokufahamu, kwa kutumia usafiri wa ngalawa. Iliyoongozwa na mzee mmoja afahamikaye kwa jina la Babu wa mjini. Safari ilikuwa ndefu sana. Walitembea zaidi ya saa kumi na nane majini kisha kuwasili mji husika, ambao ni kisiwa. Utambulikao, Mwambani (Kisiwa cha Mwambani). Mji ukaliwao sana na watu wenye mahadhi ya ughaibuni. Waliotapakaa lafudhi ya mataifa ya mashariki ya mbali. Wakichanganyikana na wachache watokao Mangaka, waliovamia mji huo kwa shughuli ya utalii. Ngalawa lilivyotia nanga, akamlipa nahodha nauli, akateremka, kiguu na njia kutafuta uelekeo alioukusudia.



Mwendo ulikuwa wa hadhari, huku akiwatunuku heshima watu anaopishana nao wasimuundie zengwe la kumshangaa, lenye kumketisha kitako waanze kumhoji. Alivyoiacha bandari, akaingia madukani, akanunua mavazi yatumiwayo na wakazi wa mji huo kwa wingi, kisha akaendelea na safari. Mbele, akaingia uchochoroni. Akabadili mavazi, kuvaa yale mapya aliyonunua, alipojiona yupo sawa alirudi barabarani kuendeleza matembezi ambayo hakufahamu mwisho wake ni upi. Baada ya matembezi ya muda mrefu, safari yake ikaishia, kwenye jengo kuukuu lililokosa utofauti na ghofu. Likiwa na mazingira yasiyoeleweka vyema, ila kwa James sehemu hiyo ilikuwa lulu kwake, kwa sababu kaishi maisha ya kutanga tanga muda mrefu. Akasafisha moja ya chumba. Akatafuta maboksi na kufanya kitanda. Kuhusu suala la chakula, alikuwa anapata mlo mmoja tu kwa siku. Mlo wa usiku, ambapo kila siku alihudhuria feri kupata chakula hicho kisha kuendelea na kawaida yake.



Siku za baadaye akaikagua ile bahasha aliyoiokota uwanjani mjini Nanderu. Aliifungua, akakutana na bahasha nyingine iliyofungwa vyema na kupigwa mhuri wa moto uliosomeka Confidential to Mr. President of Mangaka. Kisha akakutana na kikaratasi kidogo chenye ujumbe ulio na maandishi machache yaliyosomeka ‘fikisha sehemu husika, kwani ukombozi wa mheshimiwa wetu upo mikononi mwako.’ Alivyohitimisha, aliigeuza nyuma, akakutana na ujumbe mwingine uliomtatiza kupatia maanisho kihusicho. Uliandikwa Ba+Ba+wasa. Kabla hajaendelea, alinakili ujumbe wa mwisho kupatiwa na Kasanjala kwenye kitabu chake cha kumbukumbu kisha akaendelea. Kutafuta maana ya maneno matatu.



Aliyatekeleza hayo yote akiwa kajipatia likizo ya mwezi mzima, akirudi mzigoni, arudi kwa morali ya hali ya juu yenye kumhakikishia awajibike kwa muda mchache aweze pata mafanikio tele yatayozidi mtangaza. Muda mwingi akawa anashinda kusoma vitabu mbalimbali kumwongezea ujuzi, maarifa, mbinu na mambo mengi kadha wa kadha yenye hitajio la kufikia mafanikio. Muda pangwa, wa mapumziko yake ulivyomalizika. Akasafiri hadi mjini Kisimatuli, kumtafuta mtu aliyesalia katika wale watatu aliotajiwa na mheshimiwa Rais, Ndg. Mohammed Mlunji, Magreth Okuku. Safari ya kutoka kisiwani Mwambani hadi Kisimatuli, ilikuwa safari ya saa arobaini na nane. Ni safari yenye unyong’onyo, kutokana na umbali mrefu wa kusafiri. Lakini James alivumilia, azma yake lazima itimie. Ya kumhakikishia anamsaidia mheshimiwa Rais katika mchezo mchafu alioundiwa. Japo hakufahamu wahusika waliounda mchezo huo, angeliwafahamu ingelimpatia urahisi wa kukabiliana nao.



Alivyowasili Kisimatuli, haikumpa ugumu wa kumtafuta mlengwa. Magreth Okuku. Yale maandishi yaliyoandikwa kwenye kile kikaratasi yalimrahisishia sana kazi. Alivyoweza tambua maana. Kwani alivyounganisha alipata neno lililosomeka Babawasa, akaligeuza. Neno la mwisho kuwa la kwanza, na la kwanza kuwa mwisho, likasomeka sawababa, baadaye akalitenganisha, akapata sawa baba likiwa na maanisho la utii, toka kwa mtoto kwenda kwa mzazi wake. Alivyoenda kamusini, akakutana na maana, lilimaanisha Mjumbe wa mtaa, mtu pekee apatiwaye utii wa kutosha toka kwa wananchi. Hivyo akaanza utafiti, wa kutafuta mtaa upi mjumbe wake ni mwanamke. Utafiti huo alifanya kwa kuwauliza watu mbalimbali, hasa wazee walioelekea kupoteza nguvu za kutembea ama kuona wao wenyewe pasipo kisaidizi.



Halikuwa zoezi jepesi. Lilikuwa ngumu na lilimsumbua vya kutosha, kwani kila aliodiriki kuwauliza hawakuwa na ufahamu juu ya mjumbe awaulizayo. Walivyoomba angalau awaoneshe picha yake ili iwe rahisi kuweza kumtambua alishindwa kuwaonyesha, kwa sababu naye hakuwanayo wala hafahamu huyo mtu anafananaje. Baadaye ikabidi aghairishe, zoezi la kumtafuta Magreth. Akahamia kwenye zoezi la kuifikisha bahasha sehemu husika, kama alivyoambiwa kwenye ule ujumbe. Hivyo ikamlazimu kuelekea jijini Naparavi, ilipo Ikulu, apate ikabidhisha hiyo bahasha kisha aendelee na taratibu zake.



Akasafiri kwa basi toka Kisimatuli, hadi jijini hapo. Jiji pekee maarufu kwa starehe na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kifahari nchini Mangaka. Wakati huo alikuwa hujui liendelealo ndani ya ulimwengu wa matukio nchini na duniani kwa ujumla. Alikuwepo—kuwepo tu, ili mradi aendelee kuishi, sababu ya kuwa na maisha ya mashaka. Kuandamwa na vitu ambavyo hajahusika navyo.

“Hii inabidi ifike Ikulu,” alijisemeza, akiwa anasugua nyayo kutafuta jengo hilo lilipo. Jasho jingi likimtiririka, lililo—lowanisha sehemu kubwa ya shati alilovaa mgongoni.



Hakuwa na taarifa. Kama kuna watu walioandaliwa kwa ajili ya kuitafuta hiyo bahasha. Ambao nao walikesha kuzunguka mazingira ya karibu na Ikulu ili wamuonapo mtu mwenye bahasha waliyoelekezwa waanze nayo shughuli papo hapo. Pasipo hofu ya ulinzi uliopo.

“Ina muhuri mdogo mwekundu usawa wa juu wa kufungulia,” alikumbuka. Kijana mmoja aliyepatiwa kazi hiyo, maelekezo aliyopatiwa na bosi wake pindi wakizungumza kwa njia ya simu. Alivyoomba maelezo ya kutosha kuhusu bashasha ziwekwazo karatasi za hotuba zilivyo.



Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, alilikaribia lango la Ikulu. Mlangoni kukiwa na askari wa kikosi cha kutuliza fujo wakidumisha ulinzi, sambamba na askari wa majeshi mengine waliokuwa wanaranda huku na kule kufanya mawindo ya kumtambua adui. Mwenye nia ovu ya kuvamia jengo hilo takatifu la ki—serikali. Akapiga jicho huku na kule, kuangalia namna walivyojipanga askari hao. Baadaye akaingiwa na ushawishi, amuite mmoja wa askari, waliosimama getini. Akiwa kwenye tafakuri hiyo akashtushwa na kauli iliyotoka nyuma yake, iliyoambatana na kitendo cha kuguswa bega lake na moja ya mkono wa huyo mtu.

“Wewe kijana vipi? Mbona unashangaa shangaa, hufahamu kuwa hili ni eneo hatarishi?” ilisikika sauti hiyo. Sauti ya kike, iliyomshinikiza kugeuka kumwangalia. Akakumbana na sura ya mama Tausi.



Wakashangaana!



Haukuwa mshituko mkubwa, ni mfupi tu, kisha wakavutana pembeni kuteta.

“Kulikoni! Unajileta leta mahali hapa? Hujui kuwa unawindwa vilivyo, unahisi nini kitatokea ukishabainika na kamera zilizotegwa kila kona kama unavyofahamu?”

“Nafahamu yote hayo. Lakini nina ujumbe wa muhimu sana ambao unapaswa kumfikia mheshimiwa Rais.”

“Upi huo?”



James akatoa ile bahasha akamkabidhi. Mama Tausi akaisaili kwa kuigeuza geuza huku na kule kuhakikisha hamna kitu chochote chenye kuwezesha madhara.

“Haya, fanya uondoke,” alisema mama Tausi, huku akitumia kono lake la kushoto kumhimiza James apotee kwa uharaka eneo hilo.



Pindi anafanya kitendo hicho, kijana afanyaye shughuli ya uuzaji magazeti jirani kidogo na jengo hilo, aling’amua ile bahasha, na alama aliyoambiwa. Muhuri. Hivyo moja kwa moja akatambua ndiye yenyewe, ile aliyoelekezwa na bosi wake. Hakukawiza, akainua rununu, akabonyeza vitufe kadhaa kisha akaweka sikioni. Sekunde chache baadaye ikapokelewa na mtu aliyepigiwa upande wa pili. Kisha wakaingia kwenye mazungumzo, yaliyochukua muda mfupi sana.

“Lango kuu, la kuingilia, kuna vilima viwili yupo na ile aalimu,” alisikika yule kijana auzaye magazeti.

“Nimemuona, kaa tayari kwa kazi,” ilisikika sauti ya kike ya mtu wa upande pili, akiwa katika moja ya chumba cha hoteli kubwa, iliyo na ghorofa zaidi ya kumi na nne, akiweka sawa darubini iliyofungwa kwenye bunduki. Aina ya Heckler & Koch MG 4.

“Nipo imara, nakusubiri wewe tu,” alisema kijana muuza magazeti na kukata simu.







Hazikupita dakika mbili, mlio wa risasi ukasikika. Risasi moja iliyopiga katika moja ya nguzo ya chuma iliyo kwenye uzio uzungukao jengo la Ikulu. Na kusababisha ving’ora vilivyoashiria hatari kuanza kulia kwa kasi. Na kushinikiza kusanyiko la askari kwa muda mfupi kuangaza wapi risasi imetokea. Walifanya angaza hiyo wakiwa wamekula maficho kwa kutumia vificho vichache vilivyopo vyenye uwezo wa kuzuia risasi ipigwapo. Wenye Kutumia kamera kuangaza nao walifanya kwa namna yao. Kuangaza mazingira yote jirani yaliyotegwa kamera, lakini katu, hawakufanikiwa kumuona mpigaji. Kwani waliutengeneza umakini huo, kwa kuamini mshambuliaji anaweza shambulia kwa mara nyingine. Ila waliambulia patupu. Mshambuliaji alivyopiga ile risasi akokosa lengo alilolitarajia, hakuona haja ya kuendelea kuwepo. Alifungasha virago chap, baada ya kumaliza kufungua bunduki yake akatokomea kabisa maeneo hayo.



Hiyo yote alifanya kwa mujibu wa sheria iwaongozayo wadunguaji. Kwamba, endapo mdunguaji akipiga risasi ya kwanza akakosa, basi haitajiki kuendelea kuwepo mahali hapo, kama atakaidi, ukaidi wake utakuwa sawa na kujihalalishia ukamatwaji. Kwani, akiendelea kupiga risasi zingine katika usawa huo huo, itamrahisishia mshambuliwa, afahamu upande utokeao mapigo. Na kumpa fursa ya kujipanga.



Risasi ilipigwa kwa lengo la kumshambulia mama Tausi, ili aachie bahasha aliyokamatia kisha yule kijana auzaye magazeti atoke mbio kuipora na kutokomea. Lakini mpango wao hukufanikiwa. Kwani, pindi mdunguaji anaminya trigger tayari kwa kushambulia, wakati huo huo mama Tausi anainamisha mgongo wake kuokota simu yake ndogo iliyomdondoka. Akapishana na risasi kwa namna hiyo. Na alivyopata utambuzi pale chini kuwa kilichopigwa ni risasi, alilala chini ghafla, kisha akafuatia kujiviringisha, alipochoka alitumia mbinu nyingine hadi alivyofanikiwa kuifikia sehemu yenye kizuizi cha kumkinga na risasi.

“Hao wanahitaji hii bahasha,” alijisemeza. Huku akiikagua vyema kwa kuigeuza geuza na kutomasa aweze kufahamu kilichomo ndani ni nini.



Hali ilivyotulizana, watu wote wahusikao na ulinzi wakakutana kujadiliana ubashiri wao juu ya tukio hilo baada ya hapo wakaendelea na kawaida. Huku ikiundwa timu ya kufanya uchunguzi. Wa kutafuta chanzo na lengo la mhusika kufanya hivyo ni nini.

****



Baada ya mvurugano uliobeba dalili za wazi za kuchafua idara ya usalama wa taifa, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Kanali mstaafu Faidha Mwembere, alifanya badiliko la viongozi mbalimbali. Kuanzia waliopo makao makuu, ngazi ya mikoa na wale wa wilaya. Mama Tausi akawa mmoja miongoni mwa waathirika wa badiliko hilo. Alihamishwa, kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, akahamishiwa ofisi ya Rais, kitengo kile kile ambacho alikuwanacho ofisi ya Waziri Mkuu. Ulinzi wa viongozi. Tena akapelekwa moja kwa moja, ndani ya kitengo cha PSS (Presidential secret service) maalum kwa ajili ya ulinzi wa mheshimiwa Rais. Na kushika nafasi ya nambari moja ndani ya kitengo hicho, kwa niaba ya James.



Alifanya badiliko hilo, akiwa na imani, anaenda kutengeneza njia rahisi ya kumuondoa mheshimiwa Rais. Hakufahamu, kama anazidi mwongezea nguvu Rais, Ndg. Mohammed Mlunji itayomfanya adumu na kulindwa dhidi ya mpango huo mchafu. Ambao yeye ni kibaraka tu, wahusika, huucheza wakiwa wameketi tuli majumbani mwao.



Hivyo pindi tukio la shambulizi linatokea Ikulu, mama Tausi alikuwa katika hatua za mwisho za kujiandaa na safari ya kuelekea nchini Msumbiji, kupokea kijiti cha wanaPSS, kwani ile timu iliyoongozana na Rais ilifumuliwa yote na kuingiza watu wapya. Ambao angekuwa nao hadi mwisho wa utawala wake, ama laiti yatafanyika mabadiliko yakawahusu basi wataachia nafasi. Siku mbili baadaye, tangu lilivyotokea tukio la shambulizi, timu mpya ya wanaPSS ikasafiri kuelekea nchini Msumbiji, na iliyopo nchini Msumbiji, ilirejea nchini Mangaka.



Rais Mlunji hakuwa na la kufanya katika badiliko hilo. Zaidi ya kusikilizia matokeo, yatakuwaje siku za baadaye. Watu wa idara za usalama ndiyo walimwongoza. Hakuwa mwongozaji tena, na alilazimika kuwa hivyo ili abaki katika wasaa mzuri kiutawala na maisha yake binafsi pia. Aliwaamini mno, tena kwa asilimia zote, pasi na chembe ya shaka dhidi yao. Kabla hawajaanza rasmi jukumu, walijitambulisha. Kila mmoja nafasi yake imhusuyo baada ya hapo ndipo mtanange ukaanza ramsi. Huku wakizihesabu siku, kuelekea tarehe 15, oktoba, siku pendwa ya kuadhimisha sherehe za taifa la Mangaka kupata uhuru. Sherehe ambazo Rais Mlunji, ndiye mgeni rasmi.

“Dkt. Tausi, maisha yangu yamekuwa ya mashaka,” alisema Rais Mlunji, akiwa ameambatana na mama Tausi wakibarizi kwenye moja ya bustani ipambayo jengo la Ikulu ya Msumbiji.

“Kwanini mheshimiwa? Ondoa hofu. Wapo wananchi wanaokuelewa, si wote hawakupendi.”

“Hapana! Wananchi wa taifa langu, hawana mapendo nami tena. Wamesambaziwa chuki kwa kuaminishwa kitu ambacho hakijafanywa na utawala wangu.”

“Hee! Ina maana unafahamu chanzo cha haya yote?”

“Baadhi, sio yote. Na nahisi, wahusika wa mchezo ni wa…” alisema Rais Mlunji, ila hakumalizia kauli yake. Alikatishwa na chozi lililoanza mdondoka. Baada ya muda kidogo alifuta kisha akaendelea.

“…ona, leo hii namtesa mtoto wa watu. Dkt. Tausi, James anateseka.”

“Ndiyo. Ila ni sehemu ya majukumu yake. Anafanya hayo yote aweze kukuokoa. Uwe na maisha ya raha na amani kama mwanzo.”

“Nahitaji uhuru wangu.”

“Siku si nyingi utaupata.”



Baada ya kufanikisha kukabidhi ujumbe alioamriwa ufikishwe sehemu husika, James alirejea mjini Kisimatuli. Habari za kutokea shambulizi Ikulu alilisoma gazetini, alihuzunika kwa muda, mfupi, kisha akapiga moyo konde kuendelea na mpango uliopo mbele yake. Alivyowasili mjini Kisimatuli, akaanza upya mihangaiko ya kumtafuta Magreth Okuku, mtu pekee aliyesalia ili akamilishe mpango alioagizwa, huku akiwa amekamilisha kwa asilimia tisini na nane. Awamu hii kidogo, ilimpa urahisi. Kwani siku mbili tu, baada ya kuwasili akafahamu mahali anakoishi Magreth. Mtaa wa tatu, nyumba nambari tatu. Aliweza kufahamu kwa wepesi kwa sababu ya shughuli za kampeni za chaguzi ndogo zilizokuwa zinaendelea karibu vijiji themanini na nane ambavyo viongozi wao walijiuzulu, kwa minajili ya kuwaunga mkono wananchi kuwa wanakataa utawala nyonyaji.



Akaweka miadi ya kukutana, kupitia dereva amwendeshaye mama huyo. Miadi ikakamilika siku nne toka ile iliyopangwa. Wakakutana kwa siri katikati ya mtaa mmoja wa pembezoni mwa mji tofauti na ule anaoishi Magreth.

“The Bodyguard,…save the VIP and die,” anasema Magreth, kwa unong’ono, kumnong’oneza James.

“Kwanini nife?”

“Ndiyo njia rahisi ya kusalimika. Pia,…nenda kamwambie mheshimiwa Rais, kuwa asiwaamini wasaidizi wake,” alisema Magreth. Huku akimpiga mpiga James begani kukazia aongeacho.

“Naamini nimeeleweka. Zingatia niliyokuambia. Ila la muhimu zaidi, Rais lazima abaki salama,” aliendelea kuteta. Huku taratibu akipiga hatua kutokomea.



Kama ilivyo ada. Maneno yote aambiwayo na hawa watu huyanakili kwenye kitabu cha kumbukumbu. Hata ya Magreth Okuku naye aliyanakili, na kupata mlolongo mzima. Wa tukio linaloenda kutokea.

“Oktoba 15, Rais anakwenda kufa…the bodyguard, save the VIP and die…” alijisemeza. Baada ya kuyasoma maandishi yote aliyoyanakili kitabuni aliyoambiwa na watu aliohangaika nao muda mrefu kuwatafuta.



Jukumu lililopo mbele yake sasa ni kuhakikisha anamnusuru mheshimiwa Rais kwenye hatari imnyemeleayo. Ya kumuokoa katika mpango wa kifo toka kwa watu wasiojulikana. Alifanya maandalizi, yalivyokamilika alisafiri hadi jijini Naparavi, ambako sherehe ya kusherehekea taifa lao kupata uhuru hufanyikia kila mwaka katika uwanja wa taifa. Jioni ya tarehe 14 oktoba, ndiyo aliwasili jijini humo. Akapokelewa na mtu mzito sana, katika idara ya ulinzi na usalama, Jenerali Anyilwisye. Jenerali alichukua jukumu la kumhifadhi baada ya kutaarifiwa uhalisia wa jambo linaloenda kutendeka na Magreth Okuku, mtu pekee aliyesalimika katika orodha ya watu alioonana na James.

“Nina hakika, utafanikiwa,” alisema Jenerali Anyilwisye, pindi akimkabidhi James bunduki aina ya FN F2000.

“Nakuhakikishia, mambo yatakuwa zaidi ya sawa. Rais wetu atapata heshima yake kama ilivyo mujibu wa sheria.”

“Sina budi kutamka, nakutegemea, japo bado upo kwenye vita kali baina yako na vyombo vya usalama.”

“Lisikusumbue hilo. Ipo siku, ukweli utabainika na mambo yatamalizika.”



Jenerali Anyilwisye alikutana naye kwa siri mno. Huku ni yeye pekee, katika idara yote ya wakuu wa ulinzi na usalama ndiye alikuwa na taarifa naye. Baada ya siku chache za nyuma kupigiwa simu na Magreth akafahamishwa mchezo mzima. Kuanzia mwanzo wa maandamano na yanayojiri kutokea. Pia uhusika wa James katika matukio hayo, na uhusika wa Mkurugenzi wa usalama wa taifa Kanali mstaafu Faidha Mwembere ulivyo. Alivyopandwa na jazba ya kutaka kumtolea maneno machafu Kanali mstaafu Faidha, alitulizwa. Kwa ombi la kuacha mambo yaendelee kama yalivyo, ila ageuke, badala ya kuwa sehemu adui ya James, awe sehemu saidizi ya kukamilisha ngwe iliyobakia.

“Tulia, acha watu waje kuhaibika baadaye,” alisema Magreth. Pindi wakiwasiliana kwa njia ya simu.

“Sawa, hamna shida,” akaridhia.



Usiku wa kuelekea oktoba 15, James hakupata lepe la usingizi. Alikesha kufanya maandalizi. Akayakamilisha usiku wa saa tano. Baada ya hapo akaendelea na mambo mengine yote yenye mchango na kile aendacho kukifanya. Alikuwa kodo—kodo mpaka mapambazuko, ambao ndiyo muda mahususi wa yeye kuingia uwanjani. Alipotayarika alimtaarifu Jenerali Anyilwisye, kisha wakaongozana hadi uwanjani kwa kutumia gari ya mkuu huyo wa majeshi.

“Nimekuja kuhakiki kwa mara ya mwisho, kama ulinzi uko vyema kabla viongozi hawajaanza ingia,” alisema Jenerali Anyilwisye, kuwaambia walinzi walioko getini huku akiwa kashusha sehemu ndogo ya kioo cha gari yake. Kumzuia James asionekane.

“Tupo vyema afande. Hatuwezi kukuangusha,” askari jeshi aliyopo getini alichangia, huku akim—saluti kumuonyesha heshima ya utii.



Walivyohitimisha, Jenerali Anyilwisye aliitekenya gari, ilivyokubali akatia gia kusonga mbele, maana alikuwa anaendesha mwenyewe. Walipofika sehemu moja wapo ya jukwaa akasimamisha. Na kujikuta wanaingia kwenye majadiliano ni upande upi anaopaswa James kuketi.

“Upande upi unaopaswa kukaa?”

Aaah!...mwanzo wa kona nyekundu,” alijibu James, akiwa anapepesa macho huku na kule kuangalia jukwaa la kona nyekundu lilipo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alivyoliona akamuamuru Jenerali Anyilwisye aelekee huko. Naye kufanya hivyo. Alilisogeza gari sehemu husika, na kwa siri kubwa, James akateremka, akaambaa ambaa na ngazi za jukwaa hadi vyumba vya vyoo aambavyo vilikuwa mwanzo wa kona sehemu husika ambayo James alipaswa kuketi. Sababu maandalizi yalishaandaliwa muda mrefu, haikumpatia ugumu, alipanda, moja kwa moja na kutulia kusubiri muda uliopangwa tukio kufanyika. Wakati huo kavishwa kombati za jeshi la ukombozi, naye atambulike kuwa ni mwanajeshi. Ili kusiwe na maulizo na usumbufu kwa watu wengine. Tena kwa uhakika zaidi, wa kumuondolea kadhia, alitengenezewa kitambulisho kilichomwonesha ni mwanajeshi wa namna gani.



Muda ulivyowadia watu walianza ingia. Raia kwa viongozi mbalimbali. James akiwa bado yumo kwenye ki—chumba maalum kilichomwezesha kushuhudia kiendeleacho na sehemu ya mazingira jirani yaliyozunguka uwanja. Hasa majengo makubwa. Mara nyingi akawa anacheza na darubini, kusaili mazingira hayo jirani ambayo aliamini ndiyo yatatumiwa na maadui kutekeleza azimio lao la kumwondoa mheshimiwa Rais duniani.



Hakika! Siku hii uwanja ulifurika watu wengi mno. Haifahamiki, kama walikuja kwa wema au ubaya, jibu lilisubiriwa pindi mheshimiwa Rais atapowasili. Wengi wao wakawa tulivu wameketi kwenye viti, wengine walisimama, hasa hasa waliokosa viti. Mshereheshaji akawa anasindikiza kwa kutambulisha viongozi mbalimbali, na vitu kadha wa kadha vitavyotumbuiza siku hiyo. Watu wa ulinzi wakawa kidete sehemu zao. Wale wa kudhibiti halaiki iliyokusanyika, askari polisi, kikosi cha kutuliza vurugu, MP’s (Military police) na mgambo walikuwa wima muda wote, macho pima, kupepesa huku na kule kuwaangalia watu wafanyao vurugu ama wenye kuleta viashiria vya vurugu.



Askari wengine, walipangwa kwenye majengo yote marefu, yaliyopo jirani na uwanja. Kila jengo lilikuwa na askari wawili wenye bunduki zilizojaa risasi za moto kwenye kisanduku cha kubebea risasi (Magazine) na nyingine ya akiba wakiwa wamehifadhiwa kwenye moja ya mifuko ya kombati zao. Sanjari na watu wa usalama wa taifa ngazi ya mkoa husika na wale wa makao makuu. Dakika ziliyoyoma, huku asilimia kubwa ya viongozi wengi wa kitaifa, walikwishawasili, sanjari na baadhi ya wastaafu wa ngazi hiyo. Mawaziri wakuu, wakuu wa majeshi, wakurugenzi wa usalama wa taifa, na idara zingine nyeti za kiserikali. Isipokuwa wastaafu, nafasi ya urais pekee, awamu zote, kuanzia ya pili hadi ya tano hawakuhudhuria.



Wapo waliojiuliza kulikoni, wengine hawakuona kama walikuwa na haja ya wao kuhudhuria, kila mmoja alikuwa na wazo lake, ila hitimisho lililoondoa sintofahamu hiyo, ilikatishwa na mshereheshaji, ambaye ni mtangazaji wa redio ya taifa.

“Ndg. Wananchi, mabibi na mabwana. Tunataraji kumpokea mgeni rasmi dakika chache zilizosalia kuanzia sasa. Pia tunaomba mtuwie radhi, katika orodha yetu ya wageni waalikwa tulitaraji tuwe na marais wote wastaafu, ila isivyo bahati hawatokuwa pamoja nasi kwenye hafla hii kutokana na sababu mbalimbali,” alisikika mshereheshaji.



Wakati huo msafara wa mheshimiwa Rais, Ndg. Mohammed Mlunji ulikuwa unatoka uwanja wa ndege, punde baada ya kutua na ndege ndogo imilikiwayo na serikali ya taifa la Msumbiji. Walivyotoka uwanja wa ndege, msafara wao uliongoza hadi Ikulu, ambako alisaini kitabu cha mahudhurio kisha kuondoka kwenda uwanjani. Sauti ya ving’ora ikawapa utambulisho watu waliopo uwanjani, kuwa mgeni rasmi anaingia. Na kuwapa nafasi ya kujiandaa kwa mapokezi, punde pikipiki za askari zilivyoanza ingia, wananchi walisimama kuonyesha utii wao kwa mheshimiwa Rais, hadi gari zilivyowasili, kisha ile aliyoko kuanza kuzunguka usawa wa majukwaa waliyoko akiwapungia mkono kuwasabahi bendi za majeshi zikisindikiza mzunguko huo. Huku sura ikitawaliwa na unyonge japo hakuacha kuonyesha cheko kuwaaminisha watu hamna kimsumbuacho moyoni mwake. Mwili tu, ndiyo ulikuwa hapo, akili yake ilikuwa sehemu nyingine. Akiwazua namna aonekanavyo na ataonekana vipi kwa wananchi. Je, atarudi tena mafichoni ama ataendelea kubaki nchini? Ndicho alichokuwa anakifikiria. Mwisho wa tafakuri yake ikaishia pale aliposhtushwa na mtu aliyesimama pembeni yake, Mkuu wa majeshi, Jenerali Anyilwisye kumfahamisha anapaswa kuteremka.

“Tuteremke mkuu,” alisema Jenerali Anyilwisye, pindi Rais Mlunji, akisaili mamia ya watu waliokuja kumsikiliza.

“Yumkini nimeamua kukifuata kifo changu leo hii,” alijisemeza kimoyomoyo, akiwa anateremka kwenye ngazi za gari ya kijeshi iliyowazi, ambayo aliipanda punde alivyofika lango la kuingilia. Aliteremka garini mwake akapanda humo, kama taratibu zinavyohitajika.







Alivyoteremka, akapanda kwenye banda fulani, lililorembwa kwa samani mbalimbali zionyeshazo utaifa. Akapigiwa salamu ya heshima, salamu ya heshima ya Rais, na askari wa majeshi waliosimama uwanjani maalamu kwa onyesho la gwaride. Salamu hiyo iliambatana na uimbaji wa wimbo wa taifa, toka kwa watu wote waliohudhuria wenye ufahamu namna ya kuuwimba. Pasipo kusahau mizinga baridi, ipatayo ishirini na moja ilipigwa na askari jeshi wa jeshi la ukombozi. Zoezi hilo lilivyohitimishwa, alikagua gwaride, baada ya hapo akaenda kuketi jukwaa kuu tayari kwa kuanza hafla hiyo ya kitaifa, ambayo ilikuwa inaonyeshwa mubashara na chaneli mbalimbali za runinga pasi na sahau kutangazwa na vituo vya redio pia.



Ratiba ikaanza fuatwa. Walianza na maonyesho. Onyesho la kwanza likiwa onyesho la gwaride, mengine yakafuatia baadaye. Muda wa maonyesho ulivyomalizika, wakahamia kwenye hotuba. Wakaanza na hotuba za salamu kutoka kwa wageni waalikwa wachache walioorodheshwa ratibani, wakafuatia viongozi kadhaa wa kitaifa. Ambao kwa namna moja ama nyingine wamehusika katika harakati za maandalizi ya sherehe hiyo. Mwisho alimalizia mgeni rasmi. Mheshimiwa Rais, Ndg. Mohammed Mlunji. Aliinuka alipoketi, akapiga hatua hadi nyuma ya mimbari, akisindizwa na wasaidizi wake, waliopo maalumu kwa ajili ya ulinzi. Wa kuhakikisha hadhuriki na kitu chochote.



Kitendo cha kusimama nyuma ya mimbari, pasipo kutaraji, akashuhudia wananchi wakitoa bango walizozisundika ndani ya nguo zao. Walizikunjua, wakazinyoosha juu, kwa kusudi waonyeshe walichoandika. Kweli! Akakishuhudia. Kupitia runinga kubwa iliyofungwa pembeni yake kwa juu ikionyesha sherehe hiyo. Watu waliosimama nyuma ya kamera wakafanya kazi yao vyema, ya kutoruhusu kupitwa na kitu chochote kitokeacho. Wakayakuza maandishi, wakawa na kazi ya kubadilisha tu, lipi walioneshe, maana karibia wananchi wote waliohudhuria walikuwanayo. Ikabidi atulie kwa muda, huku akiyasoma. TUNAAMINI LEO HII UTATUACHIA NCHI YETU…, HATUKUHITAJI. TUMEKUPATIA UTII WA MWISHO KAMA KIONGOZI WETU, ILA HUFAI KUENDELEA KUTUONGOZA. Baadhi ya mabango yalisomeka hivyo. Yakachangia kumdhoofisha, kumpatia hasira na uchungu aliotamani ageuke mnyama akawararue wale wote wamchafuao, ila hakuwa na uwezo huo, zaidi ya kuvumilia. Na kuyapotezea kama hayamhusu japo yalimpatia maumivu.



Akapiga moyo konde, kwa kujikohoza na kupiga fundo la maji yaliyopo kwenye bilauri aliyopelekewa punde baada ya kusimama. Baadaye alivuta bahasha iliyo juu ya mimbari, iliyo na karatasi za hotuba anayopaswa kuhutubia. Akazitoa karatasi zilizopo, akazipanga vizuri, kisha kutathmini maneno ya mwanzo yaliyoandikwa yanahusu nini. Lengo, kama ni maneno mema kwake, ayatumie kuhutubia, na kama sio mema asiyatumie ilhali akili yake haikuwa na ufahamu wa maneno yapi yatafaa kutamkwa yenye uwezo wa kushawishi mamia ya watu waondokane na hisia walizonazo, waingiwe na hisia mpya zitazowasukuma kumfurahia.



Hakika! Aliduwaa. Ila baadaye alishtushwa na kauli iliyotoka nyuma. Kwa msaidizi wake iliyomnong’oneza ‘soma kilichoandikwa humu’ kauli iliyoambatana na makabidhiano ya sirisiri ya karatasi zilizotolewa kwenye begi dogo alilokamatia mama Tausi, ambaye ndiye msaidizi wake nambari moja. Rais Mlunji, wala hakujadili. Alizipokea, akazikagua, alivyoona alama ya mhuri mwekundu kwenye kila karatasi akaingiwa na furaha, iliyomfanya achanue domo lake, na kuonyesha meno yaliyojaa rangi ya shaba kwa mbali. Hakuishia hapo. Alionyesha sura ya tabasamu pia, akahema kidogo na kutoa neno kwa sauti ya chini.

“Ahsante sana James. Siamini kama leo hii naurejea uhuru wangu kwa mara nyingine.”



Akaweka koo vyema, kwa kujikohoza, na kushika shika tai iliyoonekana kumbana, alipojihakikishia yuko sawa akatayarika kuhutubia.



Pindi anajiweka sawa kuhutubia, chumba kimoja wapo cha ghorofa ya saba katika jengo refu lenye ghorofa kumi na tano, lililoko umbali wa mita mia mbili hamsini toka uwanjani inakofanyika sherehe, anaonekana dada mmoja aliyekula maficho kwa kuvaa mavazi mazito na meusi yaliyozuia sehemu kubwa ya mwili wake, akikata kitaalamu kabisa, kwa kutumia chombo maalumu sehemu ndogo ya dirisha la kioo. Alivyomaliza, akaonekana kukita bunduki juu ya meza na kupitisha sehemu ndogo ya mtutu iliyofungwa kiwambo kwenye pango alilotengeneza. Baadaye akaonekana kuongea na simu.

“Ushakamilisha?” aliulizwa na mtu aliyekuwa anaongea naye upande wa pili.

“Ndiyo kiongozi! Nishahitimisha kila kitu,” alijibu msichana huyo, aliyetambulika kwa jina la Lamata Asomaka.

“Okay! Fanya kama tulivyopanga, kwa furaha ya maisha yetu ya sasa na baadaye.”

“Ondoa shaka. Mpango utakuwa kama ulivyopangwa,” akahitimisha kwa kusema hivyo, kisha akakata simu.



Taratibu akaiinamia bunduki. Ilivyokita kwenye nyama ya bega, alitulia na kutupa shabaha kwa kutumia vilengeo vilivyopo. Kidole cha shahada kikiwa juu ya trigger, jicho moja kaliminya aweze ona lengo kwa usahihi kutumia darubini iliyofungwa kwenye bunduki. Baadaye akaanza bana pumzi, alivyozibana kabisa tayari kidole cha shahada kilishafikia trigger na mistari ionyeshayo lengo lipo sahihi kwenye darubini iligota katika paji la uso la Rais Mlunji.

“Kwisha habari yako,” alijisemeza. Akiwa tayari kushambulia.

****



Kipindi cha ukoloni, baada ya harakati za unyonyaji na unyanyasaji kushamiri kwa muda mrefu, iliwapelekea waafrika waanze kuyachoka maisha hayo ambayo hawakuweza kujitetea kwa lolote. Kwani uonevu uliwazidi, ijapokuwa wapo ndani ya taifa lao. Baadaye ikawabidi waunganishe nguvu katika nchi zao waweze kuuondoa utawala huo pasipo kujali itikadi walizonazo, hasa za kidini na kikabila. Walishirikiana pamoja, tena kidete katika kuhakikisha kwa namna yoyote hawakosei kufanikisha walichopanga. Walivyotoka ndani ya nchi kwa wale ambao walifanikiwa mapema kumuondoa mkoloni, walishiriki katika harakati za mataifa mengine, kusaidia nao wajitwalie uhuru.



Zoezi hilo ndani ya Mangaka, liliongozwa na Dkt. Chimpele Mwakatubu. Msomi wa kiwango cha kati, ambaye aliamua kuthubutu kuyaunganisha makabila yote nchini mwao wawe kitu kimoja, na akafanikiwa. Aliliongoza jahazi kwa kusonga naye mbele, hadi alivyofanikiwa kutwaa uhuru, oktoba 22, 1962. Baada ya kujitwalia uhuru, ukafanyika uchaguzi mdogo, uliompa mpini Dkt. Mwakatubu aliongoze taifa hilo mpaka pale watapokuja fanya uchaguzi mkuu. Hata walivyofanya uchaguzi mkuu, aliendelea kuaminiwa, kuliongoza taifa hilo kwa kuchaguliwa dhidi ya wapinzani wake waliojitokeza. Awamu ya utawala wake, aliipatia Mangaka neema kemkem, zilizowafanya wajitegemee kwa kuzalisha bidhaa wao wenyewe na si kutegemea mataifa ya nje. Naam! Alijitwalia baraka na fanaka tele katika nafasi ya uongozi kwa namna alivyokuwa anaongoza vyema taifa, japo kasoro ndogondogo hazikukosekana.



Muhula wake ulivyofikia kikomo, alikabidhi kijiti kwa mtu mwingine, Mch. Anyeli Kibunda. Naye aliingia madarakani baada ya kuwazidi kete wapinzani wake. Wakati huo walikuwa na mfumo wa kundi moja tu la kiitikadi, hivyo uchaguzi ulikuwa unawakutanisha wagombea wa kundini, ashindaye ndiyo huongoza nchi. Hakukuwa na kundi lolote la upinzani, wala mtu mwenye imani ya kwenda tofauti na kundi tawala, japo walikuwepo watu wenye uchu na roho ya madaraka. Akili za watu wengi hazikuwa pevu. Ukizingatia wasomi walikuwa wachache, hivyo waliridhika na mfumo wa serikali iliyopo.



Ilivyowadia awamu ya tatu, ndipo mambo yakabadilika. Nchi ilivyokuwa chini ya Lameck Nchenga. Awamu hii wasomi waliongezeka, na mamia ya wananchi wakaanza pevuka kuhusiana na mambo kadha wa kadha yatendwayo na serikali. Walivyobaini kuna mambo mengi ya ovyo, kundi pinzani zikaundwa, zipatazo mbili, japo si kwa matakwa ya serikali. Serikali hawakufurahia, hicho kitu kuanza, ila ililazimika baada ya shinikizo kubwa la wananchi wachache wenye elimu zao. Chukizo lao wakalionyesha kwa kupandikiza watu wachache wa usalama wa taifa ndani ya kundi hizo wenye lengo la kudukua taarifa zote za siri zipangwazo na upinzani halafu wazipeleke kundi tawala na serikalini. Mambo yakaja haribika zaidi, mara baada ya Rais wa awamu ya kwanza kuaga dunia. Mheshimiwa Rais, Lameck Nchenga akabadili mfumo wa uendeshaji. Akalalia kwenye mfumo wa kibiashara uliowanufaisha watu wa mataifa ya nje badala ya wenyeji. Alizitaifisha rasilimali za serikali, zingine kuzibinafshisha na kujimilikisha viongozi wachache wa serikalini.



Miongoni mwa vijana waliopandikizwa ni Aisha Makusega. Alipatiwa mbinu tele, kuhakikisha anawateka viongozi wakuu wa kundi pinzani na wanachama wa kundi pia. Lengo apatiwe nafasi nyeti ya kiuongozi itayomrahisishia apate watakacho kwa urahisi. Katika kuitafuta nafasi hiyo, Aisha akawa mwanzilishi wa maovu yote yahusuyo serikali. Alikesha kukashfu, miradi na mienendo ya baadhi ya viongozi sambamba na utukanaji wa kuwavua nguo. Hayo aliyafanyia mitandaoni, na kumfanya ajitwalie wafuasi wengi wamwamini. Tabia hiyo aliifanya hadi kwa watendaji wengine wa vyombo vya dola, na hakukuwa na hatua yoyote ya kisheria madhubuti aliyochukuliwa kumwajibisha na kile atendacho. Kwani endapo akikamatwa na kufikishwa mbele ya chombo cha sheria, mahakamani, kesi yake haidumu. Husikilizwa kwa muda mfupi, baada ya hapo hughairishwa, ama ikifika hadi mwisho hukumu itolewayo ni ile impatiayo ushindi.



Kitendo hicho kikawaaminisha wananchi wengi, wamuone ni mpinzani wa kweli na shujaa anayepaswa kutukuzwa ndani ya kundi lao, sababu anaipiga serikali apelekwapo mahakamani. Hakuna mwanachama, aliyekuwa na chembe ya shaka, kwamba Aisha katengenezwa, na hao hao anaowakashfu, wao walimuona ni mwanaharakati aliyechipukia tu, ambaye yupo kwa lengo la kutetea wanyonge. Aisha akauvaa ubingwa, uhodari na ushupavu uliomtengeneza azungumziwe sana na wanachama ama viongozi wakutanapo vikaoni.

“Hii nafasi yamfaa sana yule binti aitwaye Aisha,” alisema mmoja wa viongozi wajuu wa Kamati kuu ya kundi la MALIGA, kundi pinzani nchini Mangaka. Walivyokutana kwa siri moja ya hoteli iliyoko nje kidogo wakijadiliana watu wa kuwapendekeza katika nafasi mbalimbali za uongozi. Kuelekea uchaguzi mkuu ndani ya kundi lao wa viongozi wa kuongoza idara zao.

“Sahihi! Tena kule akishapata hiyo nafasi, nina hakika atawashawishi mamia ya wanachuo wenzake wawe na moyo wa ushupavu,” mwingine naye alichangia. Pindi wakipendekeza mtu anayestahili kuwa mwenyekiti na makamu wa baraza la wanawake Maliga upande wa vyuo vikuu.

“Kwa hiyo tunashauriana vipi?” aliuliza Mwenyekiti wa kamati hiyo. Kapteni. Moomoo Mnukia. Ambaye ndiye Mwenyekiti wa kundi la MALIGA taifa.

“Hamna cha kushauriana zaidi, mawazo yaliyotolewa na hao wajumbe wawili yako sahihi,” walisema wajumbe wote kwa pamoja.



Hilo likapita. Tena wakawashawishi na wajumbe wanaoenda piga kura wamchague Aisha na si mtu mwingine. Kweli! Uchaguzi ulivyowadia, Aisha alishinda kwa asilimia tisini na tisa, dhidi ya mpinzani wake. Ambaye alitoka chuo kingine tofauti na asomacho. Kwani wakati huo alikuwa mwanachuo wa chuo kikuu cha Naparavi, mwanafunzi wa mwaka wa pili akichukua shahada ya sheria. Hatimaye akajitwalia nafasi pendwa ambayo siku zote watawala walimuandalia awe nayo. Nafasi hiyo ilimwezesha kuingia vikao vikuu vya kundi walivyokuwa wanakutana kila baada ya muda fulani kujadiliana mustakabali wa kundi kitaifa, na kupangiana mikakati ya ihusuyo mambo wanayopaswa kuyatendea kundi lao lipate kusonga mbele zaidi.

“Sasa zidisha kasi, ili kila mwanakundi, aamini kuwa ni mpinzani wa kweli,” ilisikika sauti ikimuamuru, akiwa anawasiliana kwa njia ya simu.

“Ondoa shaka kiongozi. Lazima tuende kuua upinzani nchini,” akasema Aisha.





“Nasi tunakuaminia.”

“Ahsante sana.”



Naam! Akazidisha kasi, kila uchao, iliyoendelea kuwapumbaza wanamaliga kwa kuamini wako pamoja naye. Alienda hivyo tawala hadi tawala, ilivyowadia tawala ya tano, akajitwalia nafasi nyingine ya ukuu. Mwenyekiti baraza la wanawake maliga taifa. Nafasi hiyo haikuwa ya kichuo—chuo tena. Bali aliongoza wanawake wote wa kundi la MALIGA nchini. Hapo sasa akawa moto wa kuotea mbali. Kwa kukashfu na kuvumbua madudu mengi yahusuyo serikali. Ambayo ilikuwa chini ya Prof. Dotto Kadenge. Ila kuna kipindi, mambo aliyokuwa anazungumza, alikuwa anapatiwa na viongozi wakuu wa serikali, ayazungumze, ili aonekane mpinzani sahihi mwenye vyanzo vingi vya habari. Ili aaminiwe zaidi na kufuatiliwa kwa kina. Tena alikuwa haishii mitandaoni tu, siku nyingine kwenye mikutano ya hadhara aiandaayo mwenyewe, ama ile ya kualikwa na mashina ya kundi lao.

“Aiseee!...sijawahi ona mwanamke jasiri kama huyu, yaani hana hata chembe ya woga,” alisikika kijana mmoja pindi akiteta na mwenziye mara baada ya kuona taarifa imhusuyo Aisha mtandaoni.

“Huyo ni balaa. Anafaa kuwa kiongozi.”

“Tena haswa. Maana ni mtu anayefahamu mambo mengi sana yahusuyo nchi yetu.”

“Naomba sana aje agombee urais siku moja nimpatie kura yangu.”



Aisha akapata fahamika kila kona ya Mangaka. Kwa udadavuzi wake wa mambo kemkem yenye athari kubwa kwa wanyonge. Jambo lililowavuta wanachama wa kundi tawala wenye imani ndogo na kundi lao, nao waanze kumpenda mwishowe wakadumbukia moja kwa moja upinzani. Juu ya hayo yote, kazi yake hakuisahau. Habari wajadilizo kwenye vikao vya siri hakuacha kupeleka kule alikotumwa, hasa zile mbaya, zenye lengo la kuichafua serikali ama kundi kwa ujumla. Nao wakishafikishiwa, hufanyia kazi haraka sana kisitimie na kwa asilimia kubwa hufanikiwa.

Taarifa zivujapo hawakupeleka shaka kwa Aisha. Hupeleka kwa watu wengine, au huhisi mpango umeharibika kwa sababu ya madhaifu machache ambayo walishindwa kuyadhibiti.

****



Hali ya hewa ilikuwa yenye wingu zito lililotanda kiza, na upepo wastani uliosomba vitu visivyojiweza ardhini. Kama vile nguo zilizoanikwa, mifuko na vingine vingi ambavyo havikuwa katika mpangilio. Wakati huo Rais wa awamu ya tano alikuwa mapumzikoni (likizo) kijijini kwao Nakatete, kupumzika majukumu ya kiutawala kwa muda kulingana na matakwa ya katiba ya nchi isemavyo. Alikuwa kaketi bustanini ipatikanayo nyumbani kwake, pembezoni pakiwa na meza iliyotamalaki magazeti na viji—jarida vichache vihusuvyo uchumi na siasa. Akawa anaperuzi gazeti moja baada ya lingine, amalizapo, huvuta jarida nalo kuanza kulisoma. Upepo ulivyochanganya, akapata shida ya kuyaweka sawa yasipeperuke, lakini hakufanikiwa, kwani katikati ya jitihada zake akapata simu ambayo ilionekana kuwa ya muhimu zaidi kuliko hayo magazeti. Akayaacha yaendelee kupeperuka, akaipokea ile simu kwa uharaka mno.

“Ndiyo mzee wangu,” alisikika mara baada ya kuipokea na kuisogeza sikioni.

“Tushafika,” ilisikika sauti toka upande wa pili. Iliyomshinikiza Rais Prof. Kadenge ageuze shingo kutazama nyuma yake.

“Nimewaona,” akasema na kukata simu.



Akaondoka bustanini, akapiga hatua kuelekea eneo la maegesho, ambako alikutana na wazee watatu, waliotoka safari kumfuata. Walikuwa ni marais wastaafu, awamu ya pili, ya tatu na ya nne. Walisafiri toka jijini Naparavi kumfuata kijijini huko, kufuatia mwaliko wa siri aliowapatia. Kwani hakuna mtu aliyetambua ugeni wao zaidi yake. Hivyo wakaombwa, tukio hilo liwe la siri, lisijulishwe sehemu yoyote. Kuanzia mpiga picha wa Ikulu na wengineo, hawakuruhusiwa. Mtu aliyeleta ukaidi akapiga kwa kujiiba iba, kwa minajili ya kutuma mitandaoni hasa majirani ambao walikuwepo mahali hapo, waliamriwa kuzifuta alipobainika.



Baada ya mambo ya hapa pale, kama vile kusalimia ndugu na kupata chakula kwa wale wageni, wakaelekea banda la maktaba lililojengwa pembeni kidogo na nyumba kubwa wakiongozwa na mwenyeji wao. Rais Prof. Kadenge. Huku walinzi walikizunguka banda hilo kulilinda na kuamriwa wasiingie humo labda itokeapo dharura. Milango na madirisha yote yakafungwa. Kikawashwa kiyoyozi kiwaondolee joto na kuwapa ubaridi kiasi wenye kusindikiza vyema maongezi waliyopaswa zungumzia pasipo mtu mwingine yeyote zaidi yao kusikia.

“Poleni sana na safari, watu tumezaliwa mbali sana na duniani,” alisema Rais, Prof. Kadenge pindi wakipanga viti vyema kisha wakaketi.

“Kawaida, kwani hizi ndizo sehemu ambazo wengi wetu tumezaliwa,” alichangia Rais mstaafu, Lameck Nchenga. Wakafuatia kucheka.

“Okay! Tuachane na hayo. Tuende kwenye mada moja kwa moja iliyonifanya niwahitaji mahali hapa siku ya leo,…” alisema Rais Kadenge na kutulia.

“Sahihi, ili nasi tupate kuwahi kurejea makwetu.”

“…hamna shida, naamini mutawahi.”

“Okay! Endelea kiongozi.”

“Ndugu zanguni, siku kadhaa zilizopita, nilipata kutafakari na kubaini, wastaafu tutakuwa na maisha magumu huko mbeleni. Hasa, pale atapojitokeza mtu wa kuharibu mfumo wa serikali uliopo,…” akatulia, baada ya kukatishwa na Mch. Kibunda.

“Una maanisha nini?”

“…maanisho langu, uchumi utakuwa mgumu kwetu. Kwani vitaundwa vitu vya kutubana na kuondoa asilimia hii ya stahiki itolewayo.”

“Kwa hiyo una nini kiongozi?”

“Mimi sihitaji mupate shida viongozi wangu, ama mwenyewe baada ya kustaafu. Hivyo nahitaji tushirikiane, tuanzishe chombo kitachotufanya tupate pesa ya serikali na kodi ya wananchi kwa urahisi mno. Hata kama watakuja anzisha hayo mambo hapo baadaye.”



Kikatamalaki kimya cha muda mfupi, takribani sekunde kumi, kilichowafanya watazamane kisha wakaanza kujadiliana.

“Ni sahihi, maana sasa hivi dunia inabadilika sana. Toa tu oni lako mkuu, mimi nitakuwa wa kwanza kuliunga mkono,” alisema Lameck Nchenga.

“Yeah! Si jambo baya. Tena hiyo itaturahisishia kupata pesa kirahisi sana,” mwingine naye alitoa wazo lake. Mch. Kibunda.



Baadaye wote waliridhia. Mara walivyoeleweshana nini kifanyike na kwa mtindo upi. Wakafikia maamuzi ya kuanzisha shirika la kibiashara waliloliita WAJUMU ambalo wakalihusisha na mambo ya upokeaji tenda wa shughuli za ujenzi, wa barabara, majengo na nyinginezo, halafu wao ndiyo watafute mkandarasi wa kufanya shughuli hiyo kwa mapatano watayoafikiana. Wakaafikiana mambo yote wanayopaswa kuyatekeleza, likiwemo kujitoa kwenye umiliki na taratibu zote za usajili. Ambazo waka—ahidiana kuzifanyia kazi siku zijazo. Walivyohitimisha majadiliano yao wale wastaafu walirejea makwao jijini Naparavi.



Siku za likizo zilivyomalizika, Rais Prof. Kadenge akarejea kazini kuendelea na majukumu kama ilivyo ada. Wasaa huo akatumia pia, kukamilisha kile walichokubaliana. Akamtafuta mtu wa kumtwika zigo hilo, jambo lililokuwa rahisi kukamilisha, siku mbili tu, alifanikiwa kumpata. Mtawa mmoja, wa kanisa kuu la Roman jijini Naparavi, aitwaye Amisa. Ambaye naye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini humo wanaomiliki makampuni ya kibiashara na shule. Sista Amisa alielezwa kila kitu, kwa usiri wa hali ya juu na kuombwa afanye ridhaa ya kukubaliana ili naye apatiwe wepesi katika biashara zake.

“Tutakupatia asilimia tano ya kila mradi tuuchukuao. Pia nitaweka msamaha wa kodi katika biashara zote unazojihusisha nazo,” alisema Rais, Prof. Kadenge, alivyokutana na Sista Amisa Ikulu.

“Wewe ni kiongozi wangu. Lazima nikubebe kwa lolote utalohitaji kama wengine nao wawezavyo kukubeba katika mambo mengine.”

“Nashukuru sana sista. Utakuwa umenipatia msaada mkubwa ambao katu sitoweza usahau.”

“Nipo tayari kukusaidia kwa lolote utalohitaji kusaidiwa toka kwangu.”



Baaada ya hapo zikafanyika taratibu za usajili. Mpango ambao nao ulichukua muda mfupi kukamilika. Likawa shirika rasmi, iliyotupiwa kila mradi wa ujenzi uliovumbuliwa. Kwani, Rais, Prof. Kadenge alikuwa anakazia kidete kuhakikisha miradi yote inapelekwe kwenye shirika hilo. Tena siku za baadaye likaingia ubia na serikali kuhalalisha. Katika harakati za kuliweka shirika vizuri, siku za mbeleni wakaenda kukopa pesa benki nchini Uingereza katika benki ya RBS (Royal bank of Scotland) yenye makao makuu Edinburgh. Walikopa dola milioni mia mbili za kimarekani (USD 200 million). Wakajifanya kujenga maofisi ya kuzugia na baadhi ya vifaa vya kiofisi, pesa iliyosalia wakatambua kwa kushibisha matumbo yao. Hawakwenda na matakwa ya lengo la mkopo linavyosema.



Kama walivyokubaliana, Sista Amisa, akawa anapata asilimia kadhaa kwa udhamini aliowafanyia wa kuwafichia siri. Huku kwenye miradi yake nako mambo yakawa yanaenda vyema kwa kuingiza faida kubwa kutokana na kutotozwa aina yoyote ya ushuru. Jambo lililomfanya awe tajiri kila uchao uliompeleka kuongoza orodha ya matajiri nchini humo. Tenda zikawa zinamiminika kwao, tena wakawa wanalipwa pesa asilimia zote za gharama ya mradi, deni hubakia kwao kuutekeleza. Walienda hivyo, lakini mbeleni mambo yakabadilika. Tenda walipatiwa za kutosha, tatizo likawa utekelezaji wao. Walianza tabia ya kutotekeleza mradi kwa wakati. Na endapo wakitekeleza, hutekeleza kwa ufinyu, upelekeao mradi watengenezao kutokuwa na ubora stahili. Kiasi kwamba, ukishatumiwa kwa siku chache huaribika.



Wakawa wanapiga pesa kwa namna hiyo. Washtukiwapo, na viongozi wa upinzani na wachache wa serikali wenye misimamo mikali, utetezi wao ulikuwa mmoja tu, kampuni wanayoisimamia imeharibikiwa na baadhi ya vifaa muhimu katika mashine watumiazo, hivyo wanasubiri kifaa kingine toka kiwandani. Ama husubiri mafundi toka nchi husika itokako kampuni. Ambao wako nchi nyingine wakikarabati mashine zingine. Walikuwa na uwongo mwingi, uliowafanya waendelee kuachiwa wajinafasi. Juu ya kasoro hizo zipotezazo mapato ya serikali, bado waliendelea kumiminiwa tenda lukuki. Rais, Prof. Kadenge, alihakikisha hilo hata kama kwa shinikizo.



Miaka minne baadaye, ukiwa ni muhula wa pili wa Rais, Prof. Kadenge, benki ya RBS ikakumbwa na hasara kubwa, iliyochangiwa na poromoko la uchumi wa dunia. Jambo lililowahimiza uongozi wa benki kutafuta wadaiwa wao, warejeshe madeni, kwa wale waliopitiliza siku kwa visingizio mbalimbali. Shirika la Wajumu, ni miongoni mwa wadaiwa, wakapatiwa notisi, iliyowataka kufanya marejesho ndani ya mwezi mmoja kiwango cha pesa walichopaswa kulipwa. Kipindi hicho hali ya uchumi haikuwa imara hata katika shirika hilo pia. Kwani malipo ya tenda wapatiwazo walikesha kuyatumia katika mambo ya starehe na biashara zingine walizozianzisha ambazo hazikusimama vyema. Pesa walizonazo kwa wakati huo, hazikukidhi hata kulipa robo ya deni wanalodaiwa.

“Tunatatua vipi hii mambo?” aliuliza Rais, Prof. Kadenge pindi akiwasiliana na wenziye.

“Kiongozi hilo hatuwezi lizungumzia kwenye simu, yafaa tukutane tujadiliane kwa kina namna gani tunaweza lizuia lisije kutuhaibisha,” lilikuwa jibu pekee alilojibiwa na kila mmoja aliyempigia.

“Basi tufanye jioni ya leo.”

“Hamna shida kiongozi.”





Kweli! Jioni ilivyowadia, wakakutana. Kwa usiri mkubwa kama awali. Wakapanga waliyoyadhamiria, ambayo waliamini yatawawezesha kuwapatia kiasi cha pesa wadaiwacho.

“Biashara ya haraka, itayotuwezesha kuingiza hicho kiasi ni mbili,” alisema Rais Kadenge, baada ya wenziye kuwapatia muda wa kufikiria biashara gani waianzishe wakashindwa zitumia.

“Zipi?”

“Tuchukue tenda ya ukusanyaji wa ushuru. Katika majiji, miji mikubwa na bandarini.”

“Nyingine?”

“Ushuru kwenye kila zao liuzwalo ghalani. Huo uwe kama mfuko maalumu wenye nia ya kumsaidia mkulima, lakini lengo pesa zipatikanazo tuziingize kwenye mambo yetu.”

“Unadhani hilo litawezekana?”

“Yeah! Uwezekano upo. Tena kwa urahisi sana. Kipindi hiki wananchi wamejawa na joto la uchaguzi, hivyo hawatokuwa na hulka ya kufuatilia haya.”

“Okay! Tufanye, halafu tusubiri matokeo.”



Wakakubaliana. Na siku zilizofuata waliratibu mipango yao. Walibadili dhima ya shirika kutoka ile ya awali na kuwa mawakala wa ukusanyaji wa ushuru. Katika sehemu walizozihitaji. Pia waliandika barua, za kugushi, zilizoonekana zimetoka wizara husika, wizara ya kilimo, wizara ya usafirishaji na wizara ya fedha, zilizoidhinisha shirika la Wajumu na chombo kingine walichounda, walichokipatia jina la AAFU TAXATION AUTHORITY kukusanya ushuru na kodi kwa niaba ya serikali. Barua hizo zilionekana kutolewa na makatibu wakuu wa wizara, kwani kulikuwa na saini zao chini ya barua japo hawakuhusika kwa chochote.



Mipango yote ya barua, Aisha ndiye alisimamia. Kuanzia uandikaji na saini zilizopigwa, kisha zikatumwa kwa wakurugenzi wote, wa miji, manispaa na majiji. Sababu ilikuja kama mtindo wa amri, wakurugenzi waliridhia, wakaruhusu mfumo huo kutumika kuanzia siku pangwa iliyoandaliwa tangu barua ziwasilishwe. Wiki moja baadaye.



Mashirika yote yakaingia kazini, kupitia mawakala wa uongo na kweli waliowafoji. Mapato yakusanywayo hupitia kwao ndipo huwafikia walengwa. Kisha wao huchukua asilimia kadhaa inayobaki hupeleka serikalini. Wiki moja tu, ikawawezesha kuwa mabilionea wa kutupwa. Kwani shilingi zilizokuwa zinakatwa kwenye mazao yauzwayo ghalani, yalikuwa hayaendi sehemu yoyote zaidi ya kuongeza akaunti zao. Hayo ndiyo walitumia kulipa deni wanalodaiwa, kiasi kilichosalia hutumia kwenye starehe.



Harakati za uchaguzi, zikafanya mambo hayo yasifahamike. Na pale watokeapo watu kuzungumzia wananchi walikuja juu kwa kuona wanaongopewa ili waondoke kwenye msitari kuhusu mtu waliyodhamiria kumchagua. Uchaguzi uliwafumba sikio. Mengine yatendekayo, wengi wao wakawa hawaamini, ama huona yanaongelewa kwa lengo la kumpoteza mtu fulani asipigiwe kura. Labda kwa wachache washuhudiao ndiyo wataamini pale habari itangazwapo.



Uchaguzi ulivyomalizika kwa mgombea tawala kuchukua nchi. Ndg. Mohammed Mlunji, siku za mbeleni ndipo wananchi wakajionea kile walichokuwa wanaambiwa kwa juujuu wakapuuzia. Wakaanza kesha itupia lawama serikali kwanini imediriki kutenda kitu cha kinyama namna hiyo. Mtaani kukajaa malalamiko yaliyotupwa moja kwa moja kuiendea serikali ya awamu ya sita. Kuwa ndiyo iliyoidhinisha kitendo kidhulumucho jasho la mwananchi.

“Hawa jamaa wanatuonaga hatuna akili wala hatujui matumizi ya pesa zetu,” alisikika baba mmoja aliyetoka kuuza zao la karafuu ghalani.

“Tena sana. Wamediriki kutufanyia unyama ambao huvumiliki,” mwenziye alichangia.

“Sasa hivi hatupaswi kunyamazia, kwani washazoea, kiasi kwamba wanatuona watoto wadogo.”

“Hilo si la kushauri. Watu wamechafukwa huko mitandaoni kuishinikiza serikali irejeshe kiasi chote cha pesa walichochukua tangu walivyoanzisha huu mfumo.

“Hiyo nzuri, awamu hii lazima tuoneshe nasi tuna meno.”



Wananchi walichachamaa, kukataa tozo ya shilingi hamsini kwenye kila kilo moja wauzayo. Sambamba na zuio la kuuza mazao nje ya nchi hata kama soko la ndani linaonekana kutokidhi matakwa ya bei ya mkulima. Aisha akatumia mwanya huo, kuchochea wananchi waendelee kupaza sauti zao kulalamika ikiwezekana waingie barabarani kuonyesha hawakubaliani na kile kiendeleacho.

“Hakikisha wananchi wanaingia barabarani, kumkataa Ndg Mlunji,” alikumbuka Aisha. Jioni moja alivyopatiwa maagizo na marais wastaafu ya kuhakikisha wananchi wanajaa chukizo la kumkataa, baada ya kuhaidiwa donge nono la kwenda kuishi nje ya nchi. Na kumgharamia kitu chochote atachohitaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ngoja nikamilishe huu mpango, nikaishi zangu mbele,” akajisemeza.



Akafanya hivyo. Alikesha kuwachonganisha dhidi ya serikali hadi hitajio lake lilivyokamilika jioni moja iliyowakusanya wananchi miji tofauti tofauti kuandamana huku wakizuru ofisi mbalimbali za serikali kutoa lalamiko la kumkataa Rais Mlunji kwa kutofanya watakacho. Tukio hilo lilijitokeza baada ya Aisha kutuma tamko lililosema, Rais Mlunji hawezi shughulikia tatizo linalowakabili wananchi sababu naye ni mmoja miongoni mwa walaji wa mradi huo.

“Ndugu zanguni wananchi, pasipo kumkataa huyu Rais ni sawasawa na bure. Ataendelea kutunyonya, kwani naye ni mmoja miongoni mwa wanufaika wa huo mradi. Tena sio yeye tu, ni mradi wa familia. Nimewaambatanishia moja ya picha kuonyesha ni mradi wa familia. Picha zingine, na nyaraka za uthibitisho nitawatumia baadaye kuwathibitishia zaidi. Tusimfumbie macho, ni lazima aondoke madarakani,” liliosomeka tamko hilo. Huku kukiwa na picha iliyowaonyesha makatibu wakuu waliopewa kesi ya kuhusika na mradi wakiwa na Rais Mlunji eneo lenye kizakiza.



Baada ya kuona hawasikilizwi na wale watu waliowatembelea kwa lengo la kuwatolea kero zao wafikishe kwa Rais, wakaanza rusha mawe na vitu vingine vingi vilivyoleta uharibifu uliowasukuma watembelewa, ambao walijificha maofisini kuomba msaada polisi. Polisi walivyokuja, hawakuuliza, walifikia kutembeza kichapo kwa yeyote waliyemuona mbele yao. Awe mlemavu, wao walipiga tu kwa lengo la kuwataka watawanyike. Juu ya hivyo wananchi hawakuacha kujitetea, kwa namna wajuavyo kwa wale askari waliozubaa zubaa au kujisahau.



Rais Mlunji ndiye alizuia mwendelezo wa machafuko hayo. Kupitia taarifa ya kurugenzi ya mawasiliano Ikulu. Iliyowaomba wasitishe mapigano aweze kupata muda wa kufuatilia kiundani swala hilo kisha awapatie mrejesho. Taarifa hiyo ilienda sambamba na zuio la kukata kwa ushuru uliokuwa unatozwa kwenye mazao ya mkulima. Walitii. Lakini si kwa muda mrefu. Kwani siku iliyofuata taarifa nyingine ya Aisha mtandaoni ikawaibua na kuwashinikiza kurudisha upya machafuko.

“Tusidanganyike kama watoto wadogo. Huyo hawezi fanya lolote, kwani mwanzilishi wa huu mradi ni baba yake, washirika wengine ni mjomba na shemeji yake. Sasa ataanzaje kuzuia chakula cha wazee wake?” ulisomeka ujumbe aliotuma mtandaoni. Akiambatanisha na picha za barua zile alizotumaga kwa wakurugenzi kipindi cha nyuma.



Pindi taarifa hiyo inatoka, makatibu wakuu, wa zile wizara walikuwa mji mmoja maarufu ufahamikao Namatumbusi, wakisuluhisha wananchi na viongozi wa serikali ya mji kuhusu usafirishaji wa mazao yaliyokamatwa bandarini yakisafirishwa nje ya nchi kwenda kuuza. Usuluhishi huo ulikuwa wa muda mrefu, uliochangiwa na kutofika suluhu kwa pande zote juu ya kila hatua ichukuliwayo. Katikati ya majadiliano, wananchi wachache hasa wenye simu janja wakafikiwa na ile taarifa, iliyowataarifu watu walioko mbele yao ndiyo wamiliki na waanzilishi wa mradi huo.

“Hao wazee wanatuzingua,” alisikika kijana mmoja wao, kwa sauti ya unong’ozi.

“Kwanini?”

“Hao ndiyo wenye huu mradi. Si unaona hizi barua zao walizoidhinisha huu mradi? Hivyo hawawezi ufuta, kwani watashindwa kula,” alisema. Huku akimuonesha mwenziye taarifa aliyoona mtandaoni.



Muda mfupi tu. Wakafanikiwa kuoneshana karibu wananchi wote waliopo. Jambo lililoinua hasira, kwa kuona watu walioko mbele yao hawawezi fanya lolote sababu ndiye wenye mradi. Haifahamiki, ushauri ulipita muda gani kwa wote. Punde wakajikuta wameanzisha vurugu ya kuwapiga wale makatibu na kitu chochote kilichopo mbele yao. Ghafla, eneo lote likachafuka, kwa vurugu kali iliyoumiza miili ya makatibu waliokuwa wanahangaika huku na kule kujitetea.

“Wajinga nyie. Mnahisi siku zote akili zetu ziko vilevile? Yaani mnaanzisha mambo yenu ya ajabu ajabu halafu mnakuja kutuhadaa kwa viji—maneno maneno yenu,” walisikika wananchi kwa sauti ya nguvu.

“Uongozi haupo kwa ajili ya kujihalalishia mambo maovu. Upo kwa ajili ya kuwanufaisha vyema wale uwaongozao.”

“Leo ni lazima tusababishe ondoko la roho zenu, ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wafikiriao uongozi ni halali kwa kujimilikisha rasilimali zote za mwananchi.”



Jitihada zao za kujitetea hazikufanikiwa. Kwani mawe na vingine vilivyorushwa vilitua vyema mwilini, na kuleta majeraha makubwa yaliyoruhusu damu nyingi kutiririka. Si mikono waliyotumia kujikinga na vitu virushwavyo vigote hapo wala magari yaliyokuwa yanasafirisha mzigo kujificha wasionekane, hayakusaidia. Msaada walikuja pata dakika nyingi baadaye. Toka kwa askari wa jeshi la polisi waliowasili punde walivyotaarifiwa na wasamaria wema waliokuwa eneo jirani na lile litokealo vurugu. Kwa kiasi kidogo walisaidiwa, kwa kuwatawanya wale waliokuwa wanafanya fujo pamoja kuchukuliwa na wao kupelekwa hospitalini wakiwa washapoteza fahamu.

****



Hali ilivyoanza chafuka, kwa wananchi kulilia stahiki zao zikatwazo pasipo tambua zinaenda wapi na kwa minajili ipi, wastaafu wa urais. Wakiongozwa na Rais awamu ya tano wakakutana kwa mara nyingine. Kujadili mustakabali wa miradi waliyoianzisha. Makutano yao, yalikuwa ndani ya maktaba ya umma. Itumiwayo sana na viongozi wa kiserikali, taasisi binafsi na wastaafu pia. Walitafuta eneo zuri wakaketi. Walivyojiridhisha hakuna mtu jirani nao. Wakavuta vijarida waonekane wanajisomea ilhali ndiyo wanatumia nafasi hiyo kujadiliana nini wafanye. Lakini sehemu moja wapo kati ya zile zilizowazunguka waliisahau kuikagua na nyuma yake kulikuwa na watu wameketi.

“Tusipokuwa makini tutadhalilika sana.”

“Sahihi! Na endapo tukimuacha huyu jamaa afanye uchunguzi tutabainika.”

“Kwa hiyo tunaamuaje?”

“Hatupaswi kukaa kimya na kujionea afanyacho. Inatulazimu kuondoa uhai wake na hao makatibu wakuu walioonekana ndiyo waanzilishi wa mradi.”

“Yeah! Ni ushauri mzuri. Na ndiyo msaada pekee kwetu utaotufanya tuwe mbali na maovu tutendayo.”

“Sasa ni watu wepi wanaweza tekeleza hili?”

“Wala msihofu. Hawahawa watu wa ulinzi wamlindao, watahusika na mauaji yake.”

“Kwa namna ipi?”

“Tutawashawishi baadhi ya wastaafu wa idara husika, na wengine ni walewale waliopo ajirani.”

“Wacha tukuachie, sisi tusubiri matokeo tu. Maana wewe ndiyo bingwa wa michezo michafu,” walisema wale wastaafu wengine, wakimwambia Rais wa awamu ya tano.

“Ondoeni shaka. Katu wananchi hawatofahamu kuwa sisi ndiyo wahusika wa haya yote.”

Wale walioko upande mwingine ambao hawakuukagua wakawa wanasikia vyema maongezi yao. Tena pasipo pindo la herufi yoyote. Haribio likajitokeza punde simu ya mmoja wao ilivyoita. Na anguko la vitabu vitatu vilivyoacha mwaya uliowabainisha kwa wastaafu.

“Kuna watu wanatusikiliza,” walijikuta wanasema kwa pamoja. Na kutupa jicho kule waliko hao watu, lakini waliambulia kuona migongo ya watu hao wakitokomea.

“Tukiwaacha wanaweza kutuharibia,” walisema, huku wakiinuka na kuwafuatilia walikoelekea.



Wakapiga hatua za kasi ili wawahi kuwatambua lakini haikuwezekana kuwakuta, wakaishia kuwaona kwa mbali wakiwa eneo la maegesho wakiingia garini.

“Ni Guardner’s wastaafu, wale uliowafukuza kipindi cha utawala wako,” walitamka kwa pamoja.

“Kamwe sitowaacha watambe. Lazima niwaondoe duniani, mambo yabaki kama yalivyopangwa,” alisema Rais wa awamu ya tano. Prof. Kadenge.





Kikao chao kikaishia hapo. Wakarejea makwao, wakiwa na lundo tele la fikra kuhusu wale waliosikia maongezi yao. Pamoja na mtu atayeenda kutekeleza mpango wao wa kumuondoa Rais Mlunji. Kwani waliamini, wakifanikiwa, hakutokuwa na mtu yeyote atayeanza wafuatilia fuatilia kuhusu huo mradi. Watakuwa na mikakati pekee ya kuboresha, kusiwe na ono pana la utambuaji kwa wananchi kama wanaibiwa.



Fikirio likahitimishwa, mara baada ya Prof. Kadenge kupendekeza mtu wa kutekeleza maazimio yao. Ambaye ni Mkurugenzi mstaafu wa usalama wa taifa. Kapteni Maguta Mustafa. Wakamwita, wakamhadithia mpango mzima, ila hakuafikiana nao. Wakampatia muda ajifikirie.

“Tunakupa muda, kafikirie, kesho kutwa, tunaomba tuonane utueleze fikirio lako, la sivyo, utajikuta katika orodha ya wahusika wa mradi,” aliambiwa Kapteni Maguta pindi anaagana nao.



Alivyorejea nyumbani, Kapteni Maguta, akalifikiria sana jambo hilo. Kiasi kwamba akili yake haikutulizana, hali iliyomtengenezea fundo la umivu la kichwa. Halmashauri ya kichwa, ilikesha kukinzana, maafikio yapi ayafikie ili nafsi iwe huru na iweze kutakasika. Siku husika, aliyoambiwa akutane nao akaelekea eneo la makutano. Huku bado akiwa na sintofahamu ya maamuzi. Wajihi ulikosa nuru ya uchangamfu ulielezea hali hiyo, lakini akajivika ubandia wasimgundue.

“Tunaamini umejifikiria vya kutosha. Hivyo tupatie mrejesho. Uko tayari kuungana nasi kwenye hii mambo, au hutaki, tukuunganishe kwenye wahusika walioanzisha mradi?” aliuliza Prof. Kadenge. Mratibu wa mipango iwahusuyo marais wastaafu.



Kimya kifupi Kikatamalaki, takribani sekunde thelethini. Kikakatishwa na Rais mstaafu Lameck Nchenga alivyochangia hoja.

“Tunaamini kauli umeielewa. Sasa sijui ni nini kinachokufanya upoteze muda kwa kushindwa kujibu.”

“Nimewaelewa wakuu wangu,…” alisema Kapteni Maguta na kutulia kwa muda, kisha akaendelea “…ila tusigeukane baadaye.”

“Hatuwezi fanya hivyo. Ukikamilisha, tukitakacho. Utaneemeka kama sisi tuneemekavyo. Katu, hatutokutupa.”

“Okay!”



Kazi ikawa mikononi mwa Kapteni Maguta, ya kuhakikisha Rais Mlunji anaondoka duniani. Na wale watu wengine waliosikia maongezi yao. Ambao walikuwa watatu. Joram, Kasanjara na Magreth. Kuanzia siku hiyo akawa anakesha kupanga mbinu atazotumia kuhakikisha kazi aliyopewa inatimia. Kwa sababu umri wake ulishaanza mtupa mkono wa kuweza kufanya kazi mwenyewe, akaruhusu wazo la kupata vijana wataofanya shughuli hiyo kwa niaba yake.

“Lamata na Wambili,” aliropoka. Baada ya kufikiria kwa kina.



Muda huohuo akakivuta kilongalonga chake, ambacho alikiweka umbali mdogo toka alipoketi, akatafuta namba za wahusika aliowatamka, alipofanikiwa kuziona, akaruka nao hewani.

“Hallo!” ilisikika sauti ya upande wa pili.

“Mmmmh!...kuna dili kijana wangu. La mkwanja mnono lilikamilika.”

“Lipi tena kiongozi? Nipe habari mwanao, maana hizo dili zisizo kuwa na uhalali ndicho chakula changu.”

“Tukutane, saa mbili zijazo kuanzia sasa upate kulifahamu.”

“Nitatii huo wito kiongozi.”



Simu ikakatwa.



Baada ya hapo akaunga kwa mtu mwingine. Akawasiliana kwa sekunde chache, kisha akakata simu. Saa walizoahidiana zilivyokamilika, wakakutana. Nje ya mji kidogo, ili maongezi yao yawe ya siri yasinaswe na mtu yeyote, pia wapate uhuru katika uongeaji. Kapteni Maguta akawaeleza uhalisia wa dili husika. Kuanzia mwanzo hadi mwisho, pasipo kuficha kitu chochote ili iwe rahisi katika utambuzi kwa hao ambao aliwahitaji wakafanye.

“Kuhusu hilo usipate tabu. Tupo tayari kufanya. Ili mradi kuwe na chakula kinono tu,” walisema Lamata na Wambili kwa pamoja.

“Chakula kipo. Tena kinono kabisa.”

“Kama ni hivyo, hamna shida.”



Rasmi, kazi ikawa kwa Lamata na Wambili. Vijana waliowahi kuwa usalama wa taifa kipindi cha nyuma, ila wakatoroka, baada ya kuhusishwa na tuhuma ya ujambazi uliofanyika benki ya Maendeleo mjini Lidede. Ambapo pesa kiasi cha shilingi milioni mia tano ziliibiwa. Wakapatiwa picha za wahusika, kisha wakaingia kazini. Walipanga taratibu, waanze vipi na wamalizie vipi, walivyokamilisha utekelezaji ukaanza.

****



Utaratibu wa utekelezaji wa mipango yao walianza na mtu mmoja baada ya mwingine. Walianza na Joram, wakafuatia Kasanjara, ila wa mwisho walishindwa mmalizia. Kwa sababu ya mkanganyiko wa eneo waliloambiwa anapatikana. Walikosa uhakika wa eneo. Lakini hawakutaka kukubali kirahisi kuwa wamemshindwa. Waliomba muongozo kwa Kapteni Maguta nini wafanye, naye akaomba muongozo kwa mabosi wake, alivyoamriwa nini cha kufanya akawapatia mrejesho.

“Hamshieni mpango kwa Rais Mlunji. Huyo hawezi sumbua.”

“Sawa bosi.”



Hilo halikuwa shida. Wakahamishia mipango na nguvu zote kwa Rais Mlunji. Mtu pekee ambaye alipaswa kuuwawa kwa namna yoyote. Kuhakikisha ufanisi wa tukio hilo ili kusiwe na shaka nyingi toka kwa wananchi akashirikishwa Mkurugenzi wa usalama wa taifa aliyopo idarani kwa kipindi hicho, Kanali mstaafu Faidha Mwembere. Naye walimtumia ileile mbinu waliyoitumia kwa Kapteni Maguta. Walimpatia vitisho, kisha wakamhaidi donge nono akamilishapo, akaridhia. Sababu naye hakuwa na uwezo wa kuingia mbele kupeleka shambulizi, aliwatafuta vijana awaaminiao ndani ya idara yao kwa michezo michafu. Akawapata, Aisha na Kalumbwe.



Akawaachia mpango wote. Wafanye wawezavyo katika kuhakikisha hamna kinachoharibika, ikiwa ni sehemu ya kutii takwa la kisheria iongozayo idara yao, na vitisho alivyopatiwa na marais wastaafu, kwamba watamjumuisha kwenye uhusika wa mradi waupigiao wananchi kelele usitishwe. Hivyo, Aisha akawa na majukumu matatu. Ya kutumikia nafasi yake ndani ya kundi pinzani, ambayo alikesha nayo kila kukicha kuwashawishi wananchi wamkatae Rais Mlunji, pili; kumuondoa James duniani na mwisho, kuandaa njia ya mauaji ya Rais Mlunji. Yote akafanikisha. Tena pasipo kutumia nguvu nyingi, akili tu, kwa kiasi kidogo. Akafanikisha mamia ya watu wengi, miji tofauti tofauti kuingia barabarani kushinikiza ondoko la Rais Mlunji kwa sababu hajatekeleza matakwa yao, pia wakaanzisha hoja nyingine ya kutokuwa na imani naye. Hali iliyozua tafrani, baina ya vyombo vya ulinzi na wananchi kupigana vikali kwa kila mmoja kutetea upande wake. Vurugu ilikuwa kali hasa, kwani askari polisi walishindwa ituliza na mwisho wa siku waliifikia Ikulu kuonyesha dhihirisho lao si la kubahatisha.



Chafuko lilivyozidi Rais Mlunji akaachia Ikulu. Kwa kukimbilia nchini Msumbiji, ambako angeishi huko hadi utulivu utapopatikana. Siku hiyo, ikajenga historia mpya katika maisha yake. Kwani achilia mbali, kwa tukio la kukimbia nchi, tukio lingine lilijitokeza pindi yuko safari. Alitumiwa ujumbe mfupi kwenye barua pepe uliosomeka ‘baba yako kashaaga dunia.’ Ambaye ni mmoja miongoni mwa wale makatibu wakuu waliopigwa na wananchi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Hata wale wengine nao walifariki. Na walikuwa sehemu ya familia yake pia.



Aliumia. Umizo alilolionesha kwa huzuni iliyotawala usoni. Akifikiria mlolongo wa tukio ulivyo, na nini anapaswa kufanya ajitetee wananchi wamuamini kwamba si mhusika ili aweze kuifurahia nafasi yake vyema. Fikra zake zilikatishwa na jumbe zingine zilizoingia kwenye barua pepe, zilizotoka kwa wale wazee watatu wakimtaarifu kuna siri wanamhitaji kumwambia ambayo itamweka huru, na taifa litakuwa huru pia. Akawaahidi kutuma mtu wamwambie kwa niaba yake, wakaridhia. Kweli! Walivyowasili nchini Msumbiji, baada ya kuishi kwa siku kadhaa akamtuma mlinzi nambari moja wake akakutane na hao watu.

****



Lamata alikamilisha taratibu zote za mashambulizi ya kumuondoa Rais Mlunji. Taarifa iliyofahamika na watu wawili pekee, kwa upande wa msaada wa Rais Mlunji, James na Magreth Okuku, ambaye naye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa. Wakati huo, James alihangaika huku na kule kuyasaili mazingira jirani ya uwanja kwa kutumia darubini aliyoifunga kwenye bunduki yake. Ila jitihada zake hazikuwa na manufaa ya kumuona mtu mwenye nia ovu zaidi ya askari waliokuwa wanadumisha ulinzi kuhakikisha mheshimiwa Rais hadhuriki. Hakubahatika kumtia Lamata machoni katika duru zake. Kwani alifichwa na vioo vya madirisha, vyenye tinted iliyolandana na rangi ya kiwambo.



Pindi anaendelea na uhangaikaji, Lamata naye akaipa akili utambuzi wa kuruhusu trigger ifanye kazi yake. Kuhalalisha mfumo wa utokaji risasi. Aliongeza nguvu kiasi kidogo katika kidole chake cha shahada kisha akaminya trigger, lakini cha kushangaza risasi haikutoka. Ili—miss fire, ikamshinikiza kuiteremsha kwa haraka, akafungua ajionee tatizo ni nini. Punde tu, alivyoanza kufungua akapata simu, alivyomfahamu mpigaji baada ya kuangalia kwenye skrini, alisita kwa muda kisha akapokea.

“Mbona kimya hadi muda huu?” ilisikika sauti ya upande wa pili.

“Nimepiga lakini risasi haijatoka.”

“Kwa sababu gani?”

“Sijajua tatizo ni nini, nimefungua kuangalia, yamkini baruti ya risasi ama firing pin ina kasoro fulani.”

“Jitahidi, lengo likamilike.”

“Msihofu. Hamna kitachoharibika,” alisema Lamata kisha akakata simu.

Alitumia dakika moja, kufungua na kuifanyia uchunguzi, alipofanikiwa kugundua tatizo akapiga simu kuwataarifu, huku akiifunga taratibu.

“Ni firing pin, imekatika,” alisema.

“Kwa hiyo umefanyaje?”

“Nimejaribu kuiunganisha kiujanja ujanja.”

“Itafanya kazi?”

“Naamini, itafanya kazi. Ila…”

“Fanya uwezavyo, kwa namna yoyote ile, leo iwe mwisho wa siku yake hapa duniani.”

“Sawa.”



Simu ikakatwa.



Pindi anakata simu, anahitimisha na ufungaji pia. Akaiweka mezani na kuanza upya kufanya ulengaji, ila awamu hii, hata kabla hajakamilisha, akasomeka kwenye rada za James, ambaye jicho moja halikubanduka kwenye darubini. Hata kabla kidole chake cha shahada hakijasogea kwenye trigger baada ya kukoki, James alikiwahisha cha kwake, akaminya kidogo mfumo wa utokaji risasi ukakubali kuruhusu mashambulizi.

****



Wakati huo marais wastaafu walikuwa ndani ya hoteli kubwa ya kifahari iliyoko katikati ya mbuga ya wanyama ifahamikayo WATUPOFU, wakiangalia kwa ukaribu kabisa mienendo ya sherehe kupitia runinga. Muda wote mioyo yao ikijaa tamanio na tumaini kuwa Rais Mlunji anaenda kuaga dunia dakika chache zijazo.

“Hauna muda mrefu wa kuendelea kuishi,” walijisemeza.



Cha kushangaza, dakika zilizidi yoyoma pasipo tarajio lao kutokea. Huku Rais Mlunji akizidi tupa neno nyuma ya mimbari aliposimama.

“Ndugu wananchi, baada ya kutoa salamu zangu kwenu Kwa wageni waalikwa, na shukrani za dhati kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetukutanisha hapa, sina budi kuyatoa yangu machache niliyonayo. Yenye lengo la kuwekana sawa, ili tuwe na maisha yaliyojaa heri, amani na kuondoa mifarakano isiyo na msingi. Naamini, tukiyafanyia kazi nitayobahatika kuyatamka, wale wajao, wataoshika mamlaka ya kutawala taifa hili punde nihitimishapo hotuba yangu na kuchukua maamuzi ya kujiuzulu kama mutakavyo, neema tele zitatuandama…



“…ndugu wananchi, maendeleo yanahitaji jitihada. Jitihada zenyewe ni zile zenye hekima, upendo, ubabe na unafiki pia. Ila cha ajabu, leo hii, taifa letu limegubikwa kwa mambo makuu mawili katika kufikia maendeleo tunayoyahitaji. Ambayo ni ubabe na unafiki. Huku unafiki ukiongoza. Unafiki unaongoza kwa pande zote, baina ya viongozi na wananchi pia. Wengi wetu tumeshindwa kuwa wadadisi katika harakati zozote tuzisikiazo, matokeo, huamini moja kwa moja, pasipo tambua kuwa ni jambo lenye manufaa ama sio. Nazungumza haya kwa masikitiko, kutokana, nami ni mmoja miongoni mwa waathirika, ambao nimeshindwa kupewa nafasi ya utetezi, ila hiyo ndiyo aina ya watu tuliopo dunia ya leo. Hatuna muda wa kuamini maneno yatokayo upande unaotuhumiwa. Tumekuwa wepesi wa kukubali upande utanguliao kutamka, pia tumejaa uaminifu, kwa kuangalia namna msukumo wa moyo wetu ulivyo. Kama moyo hauna chembe ya upendo juu yake basi hata kile azungumzacho kamwe hautokipenda. Na endapo, moyo utakuwa na chembe ya upendo kumhusu, aongeacho utakipenda hata kama kina dalili za uongofu ndani.



“…ndugu wananchi, huu ndiyo ukweli, japo utaaminiwa kuwa ni uongo. Ila yote ni kutokana na mitazamo tofauti iliyopo akilini mwetu. Ijapokuwa wengi wetu huukubali mtazamo ulio hasi, nikiwa na maana, daima ukweli ni mchungu, utamkwapo, lazima zifanyike jitihada za kuupindisha. Hasahasa matendo haya, huabudiwa sana na watu waliokithiri imani za kisiasa nafsini mwao. Siasa, ndiyo chanzo cha haya yote yaendeleayo nchini mwetu. Siasa ya kukurupuka, iliyokosa misingi hitajika. Wengi wenye itikadi hizi, hujitanguliza wao mbele, na sio maendeleo, ndiyo maana, hata wakumbwapo na tuhuma halali ya kijinai, hukumbilia huruma za wananchi anaonewa…” alisema Rais Mlunji, kisha akasita kwa sekunde chache, alivyokuta kifungu kidogo chenye maandishi tofauti, yaliyofungwa kwa wino maalumu na kusomeka ‘usiwaamini watu wako wa karibu, wanaenda kukuangamiza.’ Akaisogeza karatasi hiyo pembeni akavuta nyingine, akaendelea…







“…ndugu wananchi, si kila uambiwalo, unapaswa kuliamini. Kwani mengine, huambiwa kwa lengo la kukuhadaa, umuone mwema akuambiaye ilhali nyuma ya kauli zake kabeba njama ya kukudhorotesha. Na watu wafanyao haya daima hufanikiwa, kama hiki mliliacho leo kilivyofanikiwa.



“Ndugu wananchi, juu ya kuwa kimbilio la shibe la viongozi, mumegeuka, kuwa kimbilio la huruma la viongozi waliotawaliwa uasi. Hili limejidhihirisha kupitia kwa watu hawa nitaowataja, wakeshao kila siku kwenu, kuwaeleza maneno yaliyojaa utetezi wa ninyi kudai haki zenu, huku wakificha miradi inyonyayo nguvu zenu. Mosi; wastaafu, nafasi ya ura…” alisema. Lakini kauli yake haikumalizika baada ya kipaza sauti kukata.



Wale marais kusikia hivyo, wakafahamu moja kwa moja wao ndiyo waliokuwa wanatajwa. Wakahamaki, hali iliyowafanya watafute simu zao walikoziacha. Walivyozipata hawakukawiza, waliruka hewani kuwapigia Lamata na Wambili, pasi na sahau Kapteni Maguta, ambaye naye alikuwa anasubiri matokeo ya kifo cha Rais Mlunji. Ili ageuke kuwa mmoja wa mabilionea nchini kupitia donge aliloahidiwa. Pasipo chelea, walianza wapigia simu, ila cha kushangaza hazikupokelewa. Ziliishia kuita mwishowe kukata kabisa. Wakapiga kwa mara nyingine, zaidi ya mara tatu, lakini awamu zote matokeo hayakutofautiana. Jambo lililowapandisha zaidi hasira kwakuwa maficho yao yalikuwa yanafichuliwa.

“Mambo yanaharibika,” alisema Mchungaji Anyeli. Akiranda randa huku na kule chumbani walipo.

“Wamepatwa na nini hawa watu? Au wamegundulika?”

“Au wameamua kutusaliti?”



Walijiuliza, maswali mengi waliyokosa majibu. Huku Rais Mlunji, akiendelea kumwaga ukweli hadharani, uliobadili bongo taratibu na kuwapa wananchi uelewa.



“…ndugu wananchi, sisi viongozi, tumeshindwa kuvidhibiti vile vitu vinne nilivyotamka mwanzo. Matokeo yake, huwa tunavitumia kulingana na watu tulionao kwa wakati huo. Tunaangalia manufaa yapi nipatayo kwa huyo aliyoko mbele yangu. Huwa tunatumia ama kuonyesha hekima; tuwapo na matatizo. Hapa tunatumia ulaghai wa maneno matamu na kukesha kuonyesha nyuso zilizosheheni huzuni ilimradi yule aliyoko mbele aamini, hali niliyonayo si nzuri. Upendo; pia, hii ni silaha, miongoni mwa silaha zenye matunda kwa viongozi. Daima tutafutapo ulaji tunatumia njia hii, sambamba na ile ya hekima kujenga mazingira ya ushindi kwa upande wetu. Kwani tunapokuja, tulio wengi, huja na fikra kichwani mwetu, nikifanikiwa nafasi hii nitakuwa na maisha ya aina fulani. Aina hizi mbili, daima huwa tunatumia tuombapo. Tukishafanikiwa, tunatumia zile zingine. Vilevile, aina hizi hutumia tutakapo kitu tukishakuwa mamlakani…



“…ndugu wananchi, uongozi ni shughuli. Tena shughuli pevu, ambayo inahitaji hizo aina zote nne kuleta matunda kwa jamii. Endapo kimoja kitazidi, hamna manufaa yatayopatikana zaidi ya uonevu wa kundi moja wapo katika jamii. Hili litokealo leo, ni matokeo ya unafiki, uliofanywa na watangulizi wangu. Watangulizi wangu hawakuhitaji mimi niwe Rais wa taifa hili, ndiyo maana leo hii hawapo. Niwape hongera, yao nia imetimia. Kwani walitumia mbinu ya kuingiza familia nzima inihusuyo, ili waweze kuwaaminisha wananchi kwa urahisi kuwa mimi ndiyo mhusika mkuu, huku mkisahau, dondoo za mradi huu zilianza pindi tuko kwenye harakati za uchaguzi…



“…ndugu wananchi, tujenge tabia, ya kupembua habari tusikiazo kwanza ndipo tutolee maamuzi. Ili kuepuka aibu siku za baadaye mambo yaharibikapo. Tuondoe imani, yote yatamkwayo na watu pinzani wa serikali waongea habari za kweli. Wapinzani wengine hutumiwa na watu wa serikalini, kwa lengo la kujilinda wasibainike kuwa wanachuki na kiongozi mwenzao wa serikalini. Hilo limejitokeza nchini, kwa Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Maliga, Bi. Aisha Makusega, kuwa kibara wa watangulizi wangu ili kuhakikisha naondoka madarakani. Kisa, nikiendelea kuwepo nitachunguza undani wa wazee wangu kuhusika kwenye ule mradi. Sijakataa kuondoka, nitaondoka, na leo hii nawahakikishia, kuanzia sekunde hii, mimi, Mohammed Mlunji, naweka historia na kujisikia fahar, kwa kutamka rasmi, najiu…” alisema Rais Mlunji, ila hakukamilisha kauli yake, alikatishwa na kauli iliyotamkwa kwa nguvu toka kwa wananchi.

“Hapana, usijiuzuluu…” walisema wananchi. Kisha kikafuatia kimya kifupi, cha sekunde ishirini na sita baadaye Rais Mlunji akaendelea.



Sherehe ilivyohitimishwa watu walirejea makwao. Na kujenga makundi mengi kujadili kile kilichozungumzwa na Rais Mlunji. Makundi yalijengwa na malumbano ya hoja ya kiimani, baina ya watu wa kundi pinzani na wale wa kundi tawala. Katikati ya mijadala yao, wakafikiwa na taarifa za kifo cha Sista Amisa na Lamata. Taarifa tata kwa namna walivyokuwa wanadadavuliwa matukio yote yalivyotokea. Mmoja walifahamishwa kajinyonga, ambaye ni Sista Amisa, na mwingine, ambaye ni Lamata kapigwa risasi ya kichwa. Taarifa ikaenda mbali zaidi, Sista Amisa, kajinyonga sababu ya tuhuma ambayo ingeenda kumkabili. Awali ya kutolipa kodi (uhujumu uchumi) pili; udhamini alioufanya kuwalinda wastaafu katika mpango nyonyaji wa nguvu kazi za wananchi. Upande wa Lamata, wakawa na dondoo, walizokosa uhakika, kuwa kapigwa risasi kwa sababu alikuwa anataka kumshambulia Rais, wengine nao wakawa na mitazamo tofautitofauti. Hakuna aliyepata taarifa sahihi, mpaka pale jeshi la polisi kupitia kikosi kazi chini ya ASP Nendakulola, kutoa ripoti ya uchunguzi wa awali.



Pindi taarifa hiyo inachukua nafasi kuenea kwa kasi mtaani. Wastaafu, Mchungaji Kibunda, Lameck Nchenga na Prof. Kadenge walishakimbilia kijiji kimoja kilichopo mpakani baina ya taifa hilo na nchi ya Gundu. Hawakuwa pekee, waliambatana na wengine waliokuwa wanawapatia msaada wa kutimiza takwa lao. Ambao ni Aisha, Kalumbwe, Wambili, Kapteni Maguta na Kanali mstaafu Faidha Mwembere.

“Tumechafuka sana, unahisi tutafanya nini kujinusuru na hili?” aliuliza Mchungaji Kibunda.

“Hamna jinsi, tukae chini tupange mbinu ya kujisafisha.”

“Mnahisi kuna uwezekano wa kuwa wasafi katika hili?”

“Upo tena mkubwa sana.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kwa namna ipi?”

“Kwa kutumia siasa. Yeye katumia hoja za kisiasa, basi nasi yafaa kutumia njia hiyohiyo kujinusuru.”

“Jaribu kutudadavulia vizuri.”

“Aisha ndiye anapaswa kutusafisha. Atoke hadharani ajibu hoja alizohutubia Mlunji kuwa hausiki na wala hatuna dili naye. Akishamaliza kwake, ahamie kwetu, atusafishe pia.”

“Kirahisi hivyo? Unahisi wananchi wataelewa?”

“Yeah! Watatuelewa tu. Na kuhamishia mawazo yao yote upande uleule. Kikubwa, ni kuleta ukinzani wa ufikiriaji akilini mwao. Tukifanikiwa kuweka hicho kitu, tutabaki salama.”









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog