Search This Blog

Friday 18 November 2022

FUMBO LA UTAMBUZI - 4

 






Simulizi : Fumbo La Utambuzi

Sehemu Ya Nne (4)





Yule askari alipowafikia nae alitabasamu, alionesha anafahamiana sana na BQ,



"Mbona upo mtaani?, we mtu mzito bwana, muda huu ulitakiwa uwepo kwenye viwanja vya ikulu" Askari aliongea huku akitabasamu na kufanya Tom ahairishe alichotaka kukifanya kwa maana aliamini hata huyo askari ni mwanamtandao ulioamua kuipindua nchi,



"Hata hapa nipo kazini, si unajua mi sielewekagi?" BQ aliongea na kisha wote wakacheka,



"Nimekusimamisha kwa kuwa kuna msafara wa Waziri mkuu unapita sasa hivi, kwa hiyo itabidi uvumilie kidogo" Askari aliongea,



"Sawa, kwa sina haraka" BQ alijibu,



"Poa, acha niendelee na kazi" Askari aliongea kisha akarudi barabarani na kuwasaidia wenzake kusimamisha magari mengine,



"Mbona hutabasamu tena?" BQ alimuuliza Tom huku akitabasamu,



"Kwa hiyo unatakaje sasa?" Tom aliuliza kihasira baada ya mpango wake kutofanikiwa,



"Sitaki kitu" BQ alijibu na kutoa kicheko cha dharau huku akimuangalia Tom.



Baada ya muda msafara wa Waziri mkuu ulipita na magari mengine yakaruhusiwa kupita na BQ akaikamata barabara iliyokuwa inaelekea katika nyumba anayoishi Tom.



Walifika na kuingia ndani, huku Tom akiwa amenuna tu na BQ yeye alikuwa anatabasamu tu kila amuangaliapo Tom, sasa sijui alikuwa anatabasamu kwa namna Tom alivyovimba usoni au alikuwa anafurahi namna Tom alivyonuna.



"Una dawa ya kusafishia vidonda?" BQ alimuuliza Tom,



"Sina" Tom alijibu huku akionekana hataki kuulizwa swali lingine, BQ akatabasamu tena na kutoka zake nje bila kusema kitu na kumuacha Tom akijiangalia kwenye kioo.



Baada ya muda kidogo BQ alirudi huku akiwa na chupa ndogo mbili na pamba katika mkono wake na kufanya Tom ashangae kumuona tena kwa maana alijua huyo Dada ameshaondoka.



"Toa shati nikusafishe vidonda na nikupake dawa" BQ aliongea huku akiwa amesimama anamuangalia Tom,



"Nitaenda mwenyewe hospitali" Tom alijibu kijeuri,



"Acha utoto wewe, mimi kukuhudumia wewe sio kama nakupenda sana au najipendekeza kwako, nafanya hivi kwa kuwa najua shida ya majeraha kama hayo endapo utachelewa kupatiwa Huduma" BQ aliongea huku akiwa hana lile tabasamu lake,



"Kama ungekuwa unajua shida ya majeraha haya, ungenihudumia kule kule kambini kwenu" Tom alijibu,



"Sawa, mimi naenda" BQ aliongea kwa hasira huku akianza kuondoka,



"Kwa hiyo unavyoondoka bila kunitibu unategemea nini?" Tom aliuliza,



"We acha upuuzi, mimi sio mtoto mwenzako" BQ aliongea huku akionesha hafurahishwi na vitendo vya Tom,



"Nitibu bwana" Tom aliongea huku akivua shati na BQ akachukua kichupa kimoja kati ya alivyokuja navyo na kuanza kumuhudumia Tom.



****************



Baada ya BQ kuondoka na Tom, nyumba ilibaki na wanaume tupu, yaani Tammy Semmy, Waziri wa ulinzi, Jimmy na Gabby.



"Mlisema kijana mliyemkuta anaongea na Tom alikuja na gari kama za vigogo wa serikali?" Tammy Semmy aliuliza,



"Ndio, tena inaonesha mmiliki wa hiyo gari ni lazima awe hata Waziri" Jimmy alijibu,



"Mnadai mliifuatilia, je hamkupata namba yake?, yaani namba ya hiyo gari?" Tammy Semmy aliuliza,



"Namba hii hapa, tuliipiga picha" Jimmy aliongea na kuitoa simu yake mfukoni kisha akaanza kuitafuta picha ambayo aliipiga plate namba ya ile gari,



"Mbona unatafuta muda mrefu, au hujapiga?" Gabby alimuuliza mwenzake baada ya kuona ametumia muda mrefu,



"Hii hapa, nimeiona" Jimmy aliongea huku akimpa Tammy Semmy simu,



"Sasa ngoja niwasiliane na mtu wangu, mlinzi wa ikulu ili snipe taharifa juu ya mwenye hilo gari" Tammy Semmy aliongea huku akiitoa simu yake mfukoni,



"Sasa atajuaje taharifa za hilo gari?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Atatumia camera ili kuangalia watu waliotelemka kwenye hiyo gari" Tammy Semmy alijibu kisha akampigia siku huyo mtu na wakaanza kuongea, waliongea kwa dakika tatu na kisha Tammy Semmy akakata simu.



"Ngoja apekue kwenye video za wageni waliofika leo, atanipigia akipata jibu" Tammy Semmy aliongea,



"Hapo atakuwa amerahisishia kazi" Gabby aliongea huku akiwasha sigara na ukimya ukatawala kidogo mpaka simu ya Tammy Semmy ilipoanza kuita tena, mpigaji alikuwa ni yule yule mlinzi wa ikulu, Tammy Semmy akapokea na kuanza kuongea nae, waliongea kwa muda kidogo na mwisho walimaliza maongezi yao.



"Ile gari inasemekana ni ya mkuu wa polisi" Tammy Semmy aliongea huku akishusha pumzi,



"Kwa hiyo yule Jamaa aliyekuwa anaongea na Tom ni polisi?" Gabby aliuliza,



"Inawezekana, kama alikuja na mkuu wa polisi basi na yeye ni polisi" Tammy Semmy alijibu,



"Jamaa anaweza kutusaidia ili tujue wameongea nini?" Gabby alimuuliza Tammy Semmy,



"Sasa hiyo inawezekanaje?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Anaweza kuivuta video kwa karibu na tukajua kwa kutumia midomo yao onavyocheza, au kama vinasa sauti vilikuwa eneo lile pia itakuwa sauti zao zimepatikana" Jimmy alimjibu Waziri wa ulinzi,



"Ebu ngoja niongee nae ili afanye hivyo" Tammy Semmy aliongea kisha akampigia tena simu yule mtu na kumpa maagizo ya kufanya,



"Ngoja aangalie" Tammy Semmy aliongea baada ya kukata simu,



"Mi nadhani huyo polisi aliyekuwa ameongea na Tom ni lazima afe tu, tusimcheleweshe" Gabby aliongea lakini hakujibiwa kutokana na simu ya Tammy Semmy kuanza kuita tena, Tammy Semmy akapokea na kuongea tena kwa muda mchache,



"Anadai ameshindwa kusikia walichoongea, ila inaonekana wameongea kwa muda kidogo" Tammy Semmy aliongea huku akiwaangalia wenzake,



"Ni hatari, hata kama hatujui wameongea nini, ila lazima tumjue mtu huyo ni nani?" Gabby aliongea,



."mwambie akutumie picha ya mtu huyo na aangalie wasifu wake, yaani akutumie kila kitu" Waziri wa ulinzi alimwambia Tammy Semmy.



Tammy Semmy akampigia tena yule mlinzi wa ikulu na kumpa maagizo ya kufanya kisha akakata simu, wakawa wanasubiri majibu.



"Aisee kwanini tusimuue tu huyu dogo ili tuache kuishi kwa presha?" Gabby aliuliza,



"Hata mimi nataka hivyo" Jimmy nae alionekana kumuunga mkono mwenzake, na muda huo simu ya Tammy Semmy ilitoa sauti ya kupokea ujumbe, akaufungua huo ujumbe ambao ulitoka kwa mlinzi wa Ikulu na uliambatanishwa na picha ya Koplo Mbegu, Tammy Semmy akausoma,



"Anaitwa Koplo Said Mbegu, ni askari wa kituo kikuu cha mkoa, ana miaka 27, anaishi Tande, nyumba namba 13" Tammy Semmy alimaliza kuusoma kule ujumbe,



"Koplo? cheo kidogo alafu unataka kupigana na mimi?" Gabby aliongea na kucheka mwenyewe baada ya kukumbuka lile tukio alilofanyiana na Koplo Mbegu mchana,



"Cheo sio muhimu, swali la kujiuliza ni kwamba, Tom aliongea nae nini?" Jimmy aliuliza,



"Si address ya makazi anayoishi mmeshapewa? kamleteni" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Ya nini tuongeze mlundikano wa watu wa kuwafuatilia, kamuueni tu huyu" Tammy Semmy aliongea,



"Hilo ni jambo jema" Gabby aliongea na kunyanyuka na kuikagua bastola yake, akaridhika iko safi,



"Twende zetu" Gabby akamwambia Jimmy na wakaanza kuondoka usiku huo,



"Mimi hamtanikuta, naondoka muda si mrefu" Tammy Semmy aliwaambia,



"Nadhani hata sisi hatutorudi, tutakuja kesho asubuhi" Jimmy alijibu,



"Basi sawa, BQ nae mpaka sasa hivi hajaja, atakuwa ameenda kwake kupumzika" Tammy Semmy aliongea,



"Kesho basi, ngoja tukamalizane na huyo Koplo" Gabby aliongea kisha wakatoka nje na kuchukua gari ambayo waliona itawafaa na kuondoka zao.



Mida ya saa tano usiku walikuwa mitaa ile ile anayoishi Koplo Mbegu, walikuwa wanajaribu kuangalia ni chumba gani anaishi huyu Koplo, ilikuwa ngumu kuulizia kwa kuwa inaonekana muda huo watu wote kwenye hiyo nyumba walikuwa wamelala. Ila walitumia uzoefu na wakagundua chumba anachoishi Koplo Mbegu.



Koplo Mbegu yeye baada ya kutoka viwanja vya ikulu alirudi na kutafuta chakula, akala na akazima taa na muda huo alikuwa anaota tu kutokana na usingizi mzito ulioambatana na mchoko. Usiku huu alikuwa anakoroma tu.



Baada ya wakina Gabby kuridhika na usalama wa sehemu hiyo, Jimmy alishuka huku akiwa amevaa mzula kichwani, bastola kiunoni na kwenda moja kwa moja kwenye mlango mmoja wa ile nyumba, na kufungua taratibu kwa kutumia ufunguo Malaya na kuingia ndani, akamkuta mtu aliyemfuata anakoroma tu kutokana na usingizi. Jimmy wala hakupoteza muda, akatoa bastola na kumfyatulia risasi mbili za kichwa, kisha taratibu akaondoka zake bila mtu yoyote kumshtukia kwa maana hata bastola haikutoa sauti kutokana na kuvikwa kiwambo cha kuzuia sauti.....







Jimmy alitoka taratibu na akafunga mlango kwa nje na akaelekea moja kwa moja kwenye gari lao na kupanda,



"Umefanikisha?" Gabby alimuuliza,



"Tayari, tusepe" Jimmy alijibu na Gabby akawasha gari na wakaanza kuondoka kwa mwendo wa taratibu huku kukiwa hakuna stori kabisa.



"Hivi kwanini mkuu hataki tumuue Tom?" Jimmy alimuuliza mwenzake,



"Mi nadhani ni kutokana na ile flash ya mauaji ambayo na sisi tumeonekana, sasa anahofia tukimuua bila kuipata ile flash mambo yatakuwa sio" Gabby alijibu,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Lakini mtu mwenye ile flash si ni yule mtu wa ajabu? Tom afe tu" Jimmy aliongea,



"Hapa cha muhimu ni kumuua kwanza yule mtu, alafu Tom ndo afuate" Gabby alitoa pendekezo lake,



"Sasa tutawezaje kumuua mtu ambaye hafi?" Jimmy aliuliza,



"Jimmy acha uoga, yule atakufa tu, ngoja nimtaftie namna" Gabby aliongea,



"Mimi naona tumuache tu, kwa maana yeye hana mpango wa kutuua sisi ingawa ana uwezo wa kutuua" Jimmy aliongea,



"Saula la kumuacha halipo, wewe kaa pembeni mi nitakabiliana nae" Gabby aliongea,



"Sawa, je tunaweza kupita bar tupate angalau bia mbili?" Jimmy aliuliza,



"Aisee nimechoka sana, acha niwahi nyumbani" Gabby alijibu,



"Kama ni hivyo basi nipeleke tu na mimi nyumbani, alafu uende kwako" Jimmy aliongea,



"Sawa" Gabby alijibu na kukanyaga mafuta ili mwendo wa gari uongezeke zaidi.



******************



Usiku huu bado BQ aliendelea kumfanyia matibabu Tom, usiku ulikuwa mkubwa ila hilo wala hakujali,



"Una mpenzi au una mtoto?" BQ alimuuliza Tom,



"Sina vyote, vipi kwani?" Tom aliuliza huku akiminya uso kutokana na maumivu anayoyasikia kwa sababu ya kuguswa kwa vidonda vyake,



"Ndio maana hujali, endapo ungekuwa na kimoja wapo au vyote, basi usingekuwa mpumbavu kiasi hiki, kwa maana ungewaweka kwenye hali ngumu" BQ alijibu huku akiendelea kumuweka dawa Tom katika vidonda vyake,



"Ila mimi sijafanya ubaya wowote kule ikulu, nyie mnajihisi tu" Tom aliongea,



"Husichokijua ni kwamba yule polisi uliyekuwa unaongea nae, amekufa muda mchache uliopita" BQ aliongea na kumfanya Tom macho yamtoke kwa mshangao,



"Lakini hajui kitu yule" Tom aliuliza,



"Nani atahamini hilo?" BQ aliuliza,



"Uonevu huo, yule Jamaa hakustahili kifo" Tom aliongea,



" ni kweli hakustahili kifo, wewe ndio ulistahili kifo, ila kwa kutokuwa na akili kichwani mwako ndio unasababisha vifo vya watu wengine" BQ aliongea huku akimaanisha anachokiongea,



"Una maana gani kusema hivyo?" Tom aliuliza,



"Endapo ungetulia tu kwako na kutokwenda maeneo ambayo kuna makutano ya watu mashughuli, na ukaonekana unaongea na mtu, tena kwa kujificha, basi mauti yasingemkuta yule mtu" BQ aliongea,



"Kwa hiyo mnataka niishi peke yangu kama mzimu?" Tom aliuliza,



"Naona hiyo ndiyo njia itakayofanya watu wanaokuzunguka kuwa salama, hakuna njia nyingine" BQ alijibu,



"Basi niachieni tu nisafiri nje ya nchi, hapo nadhani wote tutakuwa huru, mimi na nyinyi" Tom alijibu,



"Ngoja nikaombe nikusafirishe, nikutoe nje ya dunia, hiyo ndiyo itasaidia kuliko kusafiri alafu ubaki ndani ya dunia" BQ aliongea kisha akatabasamu tena,



"Una maana unataka kuniua? si ndio?" Tom aliuliza kwa hamaki,



"Sijui nina maana gani. Mimi naenda, ila kuwa makini na ufanyacho, siku zako za kuishi zitaanza kuhesabika" BQ aliongea huku akimtazama Tom,



"Ebu ngoja nikuulize" Tom aliongea huku akimvuta mkono,



"Sema" BQ aliongea,



"Hivi una mpenzi au una mtoto?" Tom aliuliza,



"Nina mpenzi na nina mtoto" BQ alijibu na kuachia tabasamu laini,



"Kumbe una familia alafu unakuwa katili namna hii?" Tom alimuuliza,



"Mpenzi wangu na mtoto wangu uwa tunashirikiana kufanya ukatili wote ninaoufanya" BQ aliongea huku tabasamu lake likiwa halijamuacha,



"Unashirikiana nao, kwani wapo wapi?" Tom aliuliza kwa mshangao huku akiamini kati ya wale wanaume wakatili, mmoja wapo atakuwa na uhusiano na BQ,



"Mpenzi wangu ni kazi yangu, na mwanangu ni huyu hapa" BQ aliongea huku akiitoa bastola yake na kuibusu, akatoa tabasamu kisha akaondoka zake huku akimuacha Tom akimshangaa tu bila kuongeza neno.



" we mwanamke" Tom aliita lakini alikuwa amechelewa, BQ alikuwa ameshafika mbali.



"Mwanamke mzuri lakini katili, kama tatizo ni pesa si ni bora angetafuta kazi hata za nyumbani kwa mtu?" Tom aliongea huku akitikisa kichwa chake kwa masikitiko.



Kisha akaingia bafuni kunawa, hakutaka kuoga kwa kuhofia kujiumiza vidonda vyake vilivyopakwa dawa, na muda wote alikuwa anamuwaza yule askari waliyekuwa nae mchana, ilimuuma sana kusikia amekufa kwa ajili yake.



********************



Siku mpya ilianza kwa watu Hawa makatili kukutana kwenye kambi yao kwa ajili ya kujulishana mipango mipya, na wote walikuwa wamefika.



"Jimmy na Gabby nipeni taharifa ya mlichofanya jana?" Tammy Semmy aliwauliza huku akiwaangalia,



"Tulifanikisha, tumemuua kwa mafanikio makubwa bila watu wa jirani kutugundua" Jimmy alijibu kwa uchangamfu,



"Safi, sasa kazi iliyopo ni kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama, kuna mtu mmoja itabidi afe" Tammy Semmy aliongea huku akiwaangalia,



"Nadhani ni Waziri mkuu" BQ aliongea huku akimumusa pipi,



"Ndio yeye, kwa maana ameshaanza kampeni za chini za kutaka kuteuliwa kugombea urais kupitia chama chetu, nae sio mtu wa kumbeza, ana watu wengi ndani ya chama" Tammy Semmy aliongea,



"Kwanini tusimteke kwa muda mpaka uchaguzi utakapoisha?" Jimmy aliuliza,



"Kumteka itakuwa hatari kwangu, kwa maana ni mimi na yeye ndio wapinzani ndani ya chama, tutakapomteka ni rahisi watu kujua mimi nahusika na utekaji huo" Tammy Semmy aliongea,



"Kwa hiyo cha muhimu hapa ni kutengenezewa mazingira ya kifo, kifo ambacho hakitatiliwa shaka na mtu kuwa ni cha kupangwa" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Na kazi ya kutengeneza mazingira hayo, nakuachia wewe, maana hata kifo cha rais ni wewe ulipendekeza iwe vile" Tammy Semmy aliongea,



"Au apigwe risasi tu afe, iwe shambulio la kushtukiza?" Jimmy aliuliza,



"Hapana, hiyo kazi ya kupanga ni ya huyu bwana ndevu" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia Waziri wa ulinzi aliyekuwa anatabasamu.



"Kwa hiyo leo kazi ni ile ile ya kupeleleza wabaya tu au tupo huru tukapumzike nyumbani?" Jimmy aliuliza,



"Nendeni mkapumzike, ila dada itabidi twende wote ikulu nikajue nini kitaendelea uko" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia BQ ambaye alikubaliana nae kwa kutingisha kichwa,



"Gabby twende beach mwanangu, leo ni kujiachia" Jimmy aliongea kwa furaha wakati Tammy Semmy na BQ wakiwa wanatoka nje kwa ajili ya safari ya kwenda Ikulu.



"Bakini na mimi tupige story" Waziri wa ulinzi aliwashauri,



"Hapana mkuu, leo nahitaji kuwa na familia yangu, siku kama hizi huja kwa nadra sana" Gabby aliongea huku akichukua funguo ya gari mezani na kuondoka kwa furaha.



******************



Ni kizaa zaa katika mtaa anaoishi Koplo Mbegu, watu waliizunguka nyumba anayoishi Koplo kutokana na tukio la mauaji ya mtu ambaye inasemekana alivamiwa usiku uliopita na kupigwa risasi na watu wasiojulikana.



Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na heka heka, kila mtu alikuwa anataka aende ndani ya chumba kilichotokea hilo tukio kwa ajili ya kuuona mwili wa marehemu, ndani ya chumba hicho juu ya kitanda alikuwepo Koplo Said Mbegu, alikuwa ametulia kitandani huku wanaume wawili wa makamo wakiwa wamesimama pembeni yake, Koplo Mbegu sio kwamba alikuwa maiti, lah ila alikuwa pembeni ya maiti huku akijadiliana na wale watu wa makamo kuhusu tukio hilo la kutisha lililotokea ndani ya nyumba wanayoishi........



"Humu ndani usalama hakuna, inakuaje mtu anaingiliwa na kuuawa bila hata jirani kujua?" Mzee mmoja aliuliza,



"Ni kweli, ila huku uswahilini suala la usalama linakuwa gumu kutokana na kila mmoja kuwa na mambo yake, isitoshe huyu mtu ameuawa usiku wakati kila mtu yupo chumbani kwake, kwa hiyo inakuwa ngumu kujua" Koplo Mbegu aliongea,



"Ina maana hata mlio wa risasi hakuhusikia?" Mzee aliuliza,



"Hakuna aliyesikia, inawezekana wauaji walitumia kiwambo cha kuzuia sauti" Koplo Mbegu alijibu,



"Au alijiua mwenyewe?" Mzee mwingine aliuliza,



"Kama angejiua mwenyewe basi tungekuta silaha ambayo aliitumia kujimaliza" Koplo Mbegu alijibu,



"Sasa kwanini ameuawa?" Mzee aliuliza,



"Hakuna anaejua, huenda ni visasi au madeni" Koplo Mbegu alijibu,



"Au masuala ya wanawake, maana vijana wa siku hizi mnajifanya mashababi sana" Mzee mwingine aliongea na muda huo huo polisi walikuwa wanaingia,



"Aisee poleni, ni muda gani mmegundua hili tukio?" Askari mmoja aliuliza baada ya kuingia,



"Muda si mrefu" Koplo Mbegu alijibu,



"Mlijuaje sasa wakati nasikia mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani?" Askari aliuliza tena,



"Huyu Jamaa uwa anachotaka maji kwa majirani, sasa kuna jirani mmoja alitaka kuchotewa maji asubuhi na akaja kumgongea, lakini aligonga muda mrefu bila majibu ndipo alipoingia wasiwasi" Mzee mmoja alijibu,



"Na mlango mmeuvunja kwa ruhusa ya nano?" Askari aliendelea kuuliza,



"Mimi ni mjumbe wa nyumba kumi, ndiye niliyetoa ruhusa" Mzee mwingine alijibu,



"Sawa, je huyu marehemu ana ndugu?" Askari aliuliza,



"Inawezekana anao, ila sisi hatujawahi kuwaona" Mzee mwingine alijibu,



"Sasa tunaomba tuondoke na huu mwili, nyie endeleeni kusambaza habari ili kama ana ndugu wapatikane, au mtaamua mzike nyie, na mkikosa maamuzi pia mtuambie ili tujue namna ya kuuzika wenyewe" Askari aliongea kisha wakaubeba mwili na kutoka nao nje, wakauweka ndani ya gari lao na wakaondoka eneo hilo.



Mjumbe wa nyumba kumi akatoka nje na kuwatangazia watu kuhusu kutafuta ndugu wa marehemu na akawaambia kuhusu polisi walichokisema ndani na kisha akawataka watu watawanyike kila mtu akafanye shughuli zake, na kama kuna habari yoyote itakuja kuhusu marehemu, watapewa taharifa.



Watu wakatawanyika huku wengi wao wakiwa na majonzi kwa kuwa marehemu alikuwa ni mtu anaefahamika mtaa wote kutokana na shughuli zake za kuwasaidia wakinamama kazi za kuchota maji, kufua na usafi mwingine.



Koplo Mbegu alirudi ndani kwake huku akiwaza hilo tukio lililotokea, ila hakujua kuwa mlengwa wa lile tukio ilitakiwa awe yeye.



Koplo Mbegu alijitupa juu ya kochi na kuanza kukumbuka matukio ya siku iliyopita, ndipo sura ya Tom ikamjia kichwa ni kwake, akaikumbuka na ile habari aliyotaka kupewa na Tom, ila akamlaani Gabby kwa kumtoa Tom nje, yeye alidhani Gabby alikuwa ni afisa usalama tu aliyekuwa anaimalisha ulinzi eneo lile, hakujua kuwa Gabby alikuwa ni mtu ambaye anamfuatilia Tom kwa kila jambo.



"Yule dogo alitaka kuniambia nini?, inaelekea kuna kitu anakijua ila sijajua ni kitu gani?" Koplo Mbegu aliendelea kuwaza,



"Ila aliniambia anafanya kazi radio moja inaitwa TAFU FM, sasa hiyo radio ipo eneo gani? Ngoja niitafute kwenye mtandao" Koplo Mbegu alijiuliza na mwisho aliichukua simu yake na kuanza kuitafuta TAFU FM kwenye mtandao. Alitumia robo saa kupekua na kukipata hicho kituo cha radio, na pia alifanikiwa kujua kinapatikana eneo gani.



"Sina cha kufanya leo, ngoja niende nikamtafute dogo, atakuwa na kitu cha kuniambia" Koplo Mbegu aliongea kisha akasimama na kwenda kutungua shati lake alilokuwa amelitundika ukutani, akavaa na kutoa viatu chini ya uvungu wa kitanda pia akavaa na kutoka zake, safari ya kwenda katika kituo cha radio anachofanyia kazi Tom ilianza.



Alifika eneo la kituo na kuomba aongee na mkurugenzi wa radio, hakupata tabu kumpata, alielekezwa ofisi ya Othman Tafu ilipo na akaenda, alipofika mlangoni alibisha hodi na sauti kutoka ndani ikamruhusu aingie, akaingia na kukaa katika kiti.



"Naitwa Said Mbegu, ni askari kutoka kituo kikuu cha polisi cha mkoa" Koplo Mbegu alijitambulisha baada ya salamu,



"Sawa, nikusaidie nini mkuu?" Othman Tafu aliuliza kwa ustaharabu,



"Nahitaji kumuona kijana wako anaeitwa Tom" Koplo Mbegu aliongea huku akimuangalia Othman Tafu aliyeonesha kushtushwa na huo ujio wa kutaka kuonana na Tom,



"Huyo mtu hayupo hapa" Othman Tafu alijibu,



"Hayupo kivipi? hafanyi kazi hapa au ametoka?" Koplo Mbegu aliuliza,



" huyo mtu alisimamishwa kazi hapa, tena muda mrefu tu na wala hatujui yupo wapi kwa sasa" Othman Tafu alitoa taharifa iliyomshangaza Koplo Mbegu,



"Amesimamishwa kazi? mbona jana alikuwa kwenye viwanja vya ikulu akichukua matukio ya maziko ya Rais?" Koplo Mbegu nae aliuliza swali lililomshangaza Othman Tafu,



"Kwa kweli kuhusu hilo mimi sijui, ila ukweli ni huo niliokuambia hawali" Othman Tafu aliongea,



"Ni sababu ipi ilifanya umsimamishe kazi?" Koplo Mbegu alimuuliza,



"Ni otovu wa nidhamu, alitoka nje ya misingi ya habari na tukatozwa faini na wizara inayoshughulika na habari ikatutaka tumsimamishe kazi" Othman Tafu alijibu,



"Amesimamishwa kwa muda gani?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Kwa muda usiojulikana" Othman Tafu alijibu,



"Unaweza kunipa kijana mmoja anipeleke kwake?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Hakuna anaepajua kwake" Othman Tafu alidanganya,



"Naweza kupata namba zake za simu?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Kwa kweli hakuna mwenye namba yake, maana Mara ya mwisho hata simu hakuwa nayo" Othman Tafu aliendelea kudanganya,



"Sawa, sasa nitaacha namba yangu hapa, akionekana eneo hili mnijulishe" Koplo Mbegu aliongea huku akiandika namba zake kwenye kikaratasi kidogo kilichokuwepo mezani,



"Hakuna shida, kwani amefanyaje?" Othman Tafu aliuliza,



"Kuna mambo muhimu kuhusu usalama wake" Koplo Mbegu alijibu,



"Unaweza kunigusia kidogo?" Othman Tafu aliuliza,



" akionekana unitaharifu, baada ya hapo utajua kila kitu" Koplo Mbegu aliongea huku akiinuka kwenye kiti na kumuacha Othman Tafu akimuangalia,



"asante kwa ushirikiano wako" Koplo Mbegu aliongea kisha akatoka zake ndani ya ofisi ya Othman Tafu na kuelekea nje.



Alipofika barabarani alisimama tu huku akiwa hana pa kwenda, hakutaka kurudi nyumbani kutokana na mkosi walioamka nao asubuhi, mkosi wa kukutwa na msiba wa mtu aliyepakana nae chumba. Maamuzi ya mwisho aliyofikia ni kutafuta sehemu iliyotulia ili apumzishe akili yake, na sehemu aliyoona itamfaa kwa muda huo ni beach peke yake.



Alitafuta usafiri wa kumfikisha beach, alipata bajaj iliyompeleka mpaka maeneo hayo.



Alifika beach na kutafuta sehemu yenye utulivu, eneo ambalo hakukuwa na kelele nyingi, akavua viatu na kukaa chini kwenye mchanga huku akiangalia mawimbi ya maji yanavyotembea.



Alikaa kama saa zima na mwisho aliona ni bora akachukue kinywaji, akanyanyuka taratibu na kuelekea sehemu wanapouza vinywaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Kwa bahati mbaya ambacho hakujua ni kwamba siku hiyo pia Gabby na Jimmy walikuwepo hapo na familia zao.



Koplo Mbegu alikuwa ameshika njia ya kwenda sehemu wanapouza vinywaji huku akiwa bize kubonyeza simu yake ya mkononi na mbele yake alikuwa anakuja Gabby huku akiwa ameshika juisi tatu mikononi, ila uzuri hakuna aliyekuwa amemuona mwenzake. Wakiwa wamekaribiana na wanataka kupishana, waligongana kikumbo na simu ya Koplo Mbegu ikaanguka chini na betri ikatoka, akainama chini ili aikote,



"Aisee samahani sana" Gabby aliongea huku akiwa amesimama anamuangalia na wakati huo Koplo Mbegu alikuwa ameinamisha uso anaokota simu,



"Usijali" Koplo Mbegu alijibu huku akianyanyua uso wake amuangalie Gabby...........





Kabla hajanyanyua sura vizuri, simu ilimponyoka tena na kuanguka chini, akainama na kuanza kuiokota tena,



Pole sana" Gabby aliongea na kuondoka zake kuwahisha juisi na kumuacha Koplo Mbegu akiendelea kuokota vifaa vyake, alipomaliza ndipo alipogeuka nyuma kumuangalia huyo mtu aliyepamiana nae, lakini aliweza kumuona kwa nyuma tu,



"Au kwa kuwa baunsa?" Koplo Mbegu aliongea peke yake baada ya kuuona mgongo mkubwa wa Gabby uliyobeba mabega mazito yaliyoshika mikono miwili yenye misuli mikubwa.



Koplo Mbegu aliiweka vizuri simu yake na kuelekea sehemu ya vinywaji na kuagiza kinywaji anachokitaka, kisha akarudi kukaa katika eneo ambalo alikaa hawali na kufurahia upepo wa bahari.



*************************



Tammy Semmy akiwa na BQ waliingia ikulu na kulakiwa kwa heshima, na baadhi ya ndugu wa rais na vigogo wengine wa serikali ambao bado walikuwa katika eneo hilo la msibani na siku hiyo walitaka kuongea na familia ya rais kuhusu mustakabali wa familia hiyo kuhusu wapi pa kwenda muda huo na mambo mengine kuhusu mafao ya rais.



Tammy Semmy ndiye alikuwa kiongozi wa kikao hicho kutokana na kuaminika na pande zote mbili.



"Shemeji kama unavyojua kuwa kesho ambayo ndiyo mwisho wa Katanga ndio itakuwa mwisho wa wewe kuendelea kuishi hapa, sasa kilichotuleta hapa ni kutaka kujua umejiandaaje na maisha baada ya kutoka hapa?" Tammy Semmy alimuuliza mke wa rais,



"Nitajiandaje tena wakati unajua jambo hili limekuja ghafla tu, kifo hakina maandalizi" Mke wa rais alijibu,



"Swali linamaanisha mtaenda kuishi wapi?, kuna makazi yoyote mliandaa na mme wako?" Tammy Semmy alirekebisha swali lake,



"Mimi nadhani tutarudi kuishi kijijini kwa marehemu mme wangu, kuna nyumba tulijenga kule ambayo tulipanga kwenda kuishi baada ya kumaliza muda wake wa kuwa madarakani" mke wa rais alijibu,



"Sawa, labda kuna msaada wowote mtahitaji kutoka kwetu?" Tammy Semmy aliuliza,



"Msaada nitahohitaji ni mafao ya mme wangu, hilo ndio jambo ambalo naliangalia kwa sasa" Mke wa rais alijibu,



"Hilo ni jambo la lazima ambalo hutakiwi hata kutilia shaka, mafao utawahishiwa haraka iwezekanyo. Jambo lingine utakalohitaji ni lipi?" Tammy Semmy aliuliza,



"Naombeni tu uchunguzi wa kina na apatikane aliyehusika na kifo cha mme wangu, nadhani hilo likifanikiwa basi nitakuwa na amani kidogo" Mke wa rais aliongea kwa huzuni,



"Hilo linafanyiwa kazi na nakuhakikishia kuwa lazima muhusika apatikane" Tammy Semmy aliongea,



"Ni hayo tu, sina jingine" Mke wa rais alimalizia hivyo,



"Sawa shemeji, sasa jiandaeni ili keshokutwa tuwasafirishe ili hii nyumba iwe kwa rais mwingine ambaye atachaguliwa. Cha muhimu ni kupanga mizigo yenu vizuri ili nijue wingi wake na iwe rahisi kuwapatia gari itakayoweza kusafirishia mizigo hiyo" Tammy Semmy aliongea,



"Sawa shemeji, tutafanya hivyo" Mke wa rais alijibu,



"Kuna mtu yoyote ana swali au kitu chochote cha kuongeza?" Tammy Semmy aliuliza huku akiwageukia viongozi wengine wa serikali alioambatana nao,



"Ndio, mimi na wenzangu wachache tumekusanya fungu kidogo hapa, naomba upokee" Waziri mkuu aliongea huku akimpatia kitita cha pesa mke wa rais, hiyo haikuonekana kumfurahisha Tammy Semmy,



"Asante shemeji, mbarikiwe" mke wa rais aliongea huku akipokea zile fedha,



"Hata usijali shemeji, huu ni muda wa sisi kukutazama kwa ukaribu zaidi" Waziri mkuu aliongea,



"Huu utaratibu wa kumchangia pesa shemeji hamkunishirikisha, au ilikuwa ni kwa ajili ya watu maalum?" Tammy Semmy aliuliza huku akitabasamu,



"Inawezekana habari haikukufikia, ila taharifa tuliitoa mapema" Waziri mkuu alijibu,



"Kuna mwingine mwenye chochote cha kuongezea?" Tammy Semmy aliwauliza,



"Hakuna" Mawaziri walijibu kwa pamoja na kufanya Tammy Semmy afunge kikao kile na kisha mawaziri wakatawanyika na kumuacha Tammy Semmy akiwa na mke wa rais,



"Asante sana shemeji, sijui hata nisemeje kwa jinsi unavyoniangakia" Mke wa rais aliongea,



"Ni jukumu langu kufanya hivyo, hata usijali" Tammy Semmy alizungumza huku akinyanyuka na kumpa mkono mke wa rais na kuondoka zake huku mke wa rais akiamini Tammy Semmy ni kama malaika hivi aliyeshushwa kuwafariji, kumbe hakujua kuwa ni shetani, tena shetani hasiyejua lolote kuhusu uwepo wa Mungu, hajui kuwa yule ndio sababu ya ujane wake na huzuni wote aliokuwa nao muda huo.



*************************



BAADA YA MWEZI MMOJA.



Koplo baada ya jitihada zake za kumtafuta Tom mwezi mzima bila mafanikio, huku nae Tom akiwa anaamini Koplo Mbegu ameshakwishakufa, na nchi ikiwa chini ya utawala wa Tammy Semmy ila kwa muda na muda huu kulikuwa na mchakato wa ndani ya chama, mchakato wa kumchagua mtu atayegombea nafasi ya urais wa nchi na upinzani ulikuwa ni watu wawili tu, Tammy Semmy na Waziri mkuu na kwa vyovyote vile atayepita hapo kwenye uchaguzi wa ndani ya chama ni lazima awe rais, kwa maana vyama vingine havikuwa na nguvu kama chama hicho na isitoshe hicho chama chao ndio kiliwaletea Uhuru wa nchi kutoka kwa wakoloni, kwa hiyo wananchi walikiamini sana.



Na kwa wakati uchaguzi ndani ya chama ulipamba moto sana, ilikuwa imebaki wiki moja tu kabla mgombea kupitia chama hicho kuchaguliwa na wanachama wengine.



Tammy Semmy alikuwa na vijana wake ndani ya nyumba yao ya kupangia mipango yao ya kiharifu.



"Kwa hali ilivyo, wewe kupitishwa kugombea itakuwa ndoto, Waziri mkuu ameonekana ana kundi kubwa la watu wanaomkubali" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Hiyo ni kweli mkuu, nafasi yako imekuwa finyu sana kinyume na matarajio yetu" Jimmy alimuunga mkono Waziri wa ulinzi,



"Lakini si tulishakubaliana huyu mtu auawe, na mipango yote nilisema uisuke wewe" Tammy Semmy aliongea huku akimtazama Waziri wa ulinzi,



"Mipango tayari, ila nilikuwa nasubiri tamko kutoka kwako" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Tummalize tu" Tammy Semmy aliongea na kugida glass ya maji,



"Sawa, nipeni siku nne tu" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Nne mbona nyingi hivyo, kesho tu" Tammy Semmy aling'aka,



"Nisikilize mimi, siku nne ndio itakuwa mipango imekamilika" Waziri wa ulinzi aliongea kwa kujiamini,



"Ni aina gani ya kifo ulichomuandalia?" Tammy Semmy aliuliza,



"Hata usiwe na pupa ya kukijua, kesho nitaweka mambo hadharani" Waziri wa ulinzi alijibu na kisha wakaendelea na mipango yao mingine kuhusu mambo yao.



*********************



Usiku mida ya saa nne, Tom alikuwa anajirudisha kwake huku akionekana ni mtu mwenye mawazo sana, mawazo yalipita uwezo wake kiasi kwamba kuna muda Tom alikuwa anaongea peke yake bila kujali watu aliokuwa anaopishana nao. Yeye alijiona yupo sahihi wala hakudhani anaweza kuonekana kichaa mbele yatu.



"Dah yaani nimekuwa mtumwa ndani ya nchi yangu, nimefungwa minyonyoro kiasi kwamba nashindwa kupaza sauti ya kusema ukweli ninaoufahamu, sina pa kukimbilia mnyonge mimi, simuamini mtu tena kwa maana watu waliowekwa kwa ajili ya usalama wa raia wamekuwa sio watu salama kwa raia" Tom aliongea peke yake kisha akasimama baada ya kufika eneo ambalo kuna njia panda, zote zilikuwa zinauwezo wa kumfikisha kwake, ila moja ilikuwa ndefu na nyingine ilikuwa fupi ila ilikuwa inatisha,



"Niogope nini mimi? nimuogope nani mimi wakati nimeshatishiwa na bastola, nimetishiwa na mtu asiyejulikana, mtu asiye na nguo, sasa niogope nini? siogopi kitu, cha muhimu ni kuwahi nyumbani" Tom aliongea peke yake na kisha akaishika ile njia fupi ielekeayo kwake, Tom hakuwa muoga tena na wala hakuwa mtanashati tena kama zamani.



"Kuna watu wamekufa kwa ajili yangu, Mzee bonny alikufa kwa ajili yangu kisa alikubali kunipa siri, siri ambayo inanitesa sasa hivi, kuna askari sijui anaitwa Koplo Mbegu nae aliuawa na wale washenzi kwa sababu walinikuta nimekaa nae, ningejua ningemueleza ukweli yule askari, anaonekana alikuwa ni mtu ambaye anafanya kazi kwa ajili ya Taifa na wala sio kwa ajili ya wapumbavu wachache, ningemwambia, ningemwambia ukweli mapema labda angejua jinsi ya kujilinda na asingedhuliwa na wale washenzi" Tom aliongea peke yake kisha akacheka mwenyewe,



"'Tom, Tom, Tom" Sauti ilimuita, hiyo sauti ya mwanaume iliita kutoka nyuma yake na huyo mtu aliyemuita wala hakuwa nae mbali, walipishana kwa umbali wa hatua kumi tu.



Tom akasimama huku akijiuliza ni nani anaemuita kwenye lile eneo la kutisha? uoga ukaanza kumtawala,



"Tom ni mimi nakuita," Ile sauti iliongea tena, safari iliongea kwa uchangamfu na Tom alisikia vishindo vya huyo mtu vikimsogelea.



Tom akageuza shingo yake taratibu ili amuangalie mtu huyo ni nani, alipogeuza shingo ndipo alipomuona Koplo Mbegu akizidi kumsogelea, tena usoni mwake alikuwa na tabasamu pana, tabasamu lililoonesha furaha yake yeye Koplo Mbegu ya kuonana tena na Tom........







Tom alipogeuka kwanza alimuangalia kwa muda Koplo Mbegu, maana alikuwa anajitahidi kuvuta kumbukumbu ni wapi aliiona hiyo sura,



"Mimi Koplo Mbegu, umenisahau tulikutana kwenye maziko ya rais mwezi uliopita?" Koplo Mbegu aliuliza huku akitabasamu, hapo sasa ndipo Tom akamkumbuka, ghafla Tom akatoka mbio na kufanya Koplo Mbegu ashangae.



Tom aliendelea kukimbia huku akigeuka nyuma kuangalia kama Koplo Mbegu anamfuata, Koplo Mbegu kuona hivyo nae akaamua kumkimbiza Tom, sasa ikawa ni mwendo wa kufukuzana huku Koplo Mbegu asijue ni kwanini Tom anamkimbia?



Tom baada ya kuona Koplo Mbegu anamkimbiza, ikabidi ahache kufuata Barabara na badala yake akaamua aingie katika njia za vichochoroni, kwa uko upande wa vichochoroni kweli alimuweza Koplo Mbegu kwa maana Tom alikuwa ni muenyeji wa mitaa hiyo kwa hiyo vichochoro vyote alivijua.



Koplo Mbegu baada kukunja kona mbili tu za vichochoro hivyo akijikuta hamuoni tena Tom machoni mwake, akajitahidi kuangaza angaza lakini hakufanikiwa kumuona tena,



"Sasa kwanini ananikimbia?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akiendelea kwenda mbele kwa imani ya huenda anaweza kumuona tena lakini imani yake ilimdanganya, ni muda mrefu tu Tom alikuwa ameshatoweka eneo hilo na inawezekana kabisa alikuwa amekwishafika kwake muda huo.



"Huyu dogo ana matatizo gani? au amekuwa kichaa? Kwa maana wakati namfuatilia alikuwa akiongea peke yake" Koplo Mbegu alijisemea mwenyewe na wakati huo aliweza kutokea eneo lililokuwa na watu, eneo lilionekana kuchangamka kidogo nadhani ni kwa sababu ya bar na mabanda ya video yaliyozunguka eneo hilo.



"Dogo hujamuona mtu yoyote akipita anakimbia maeneo haya?" Koplo Mbegu alimuuliza mtoto mmoja aliyekuwa anauza pipi na karanga,



"Sijamuona" Mtoto alijibu huku akiendelea na kazi yake, Koplo Mbegu akauma meno kwa hasira baada ya kumkosa Tom,



"Ningejua hata nisingemuita, ningemwendea moja kwa moja" Koplo Mbegu aliongea huku akiwa amekata tamaa ya kumpata tenaTom usiku huo, akaenda kwenye kijiduka kimoja na kununua maji kisha akayanywa kwa pupa kutokana na mchoko uliotokana na kukimbia sana, kisha akaamua aondoke zake eneo hilo, aliamua kurudi kwake.



__________________________________

JINSI TOM ALIVYOMPATA TOM.

_________________________________



Ngoja nikueleze jinsi Koplo Mbegu alivyompata Tom, Koplo Mbegu siku alivyotoka kwenye kituo cha radio anachofanyia kazi Tom, hakuridhika na majibu ya Othman Tafu, alimuona kabisa kuwa Othman Tafu kuna kitu anaficha kuhusu Tom, kwa hiyo alichofanya Koplo Mbegu ni kurudi pale pale Tafu FM katika siku iliyofuata na kuweza kuongea na Dada mmoja aitwae Juddy ambaye naye alikuwa mfanyakazi wa kituo hicho cha radio, haikuwa rahisi kupata ukweli wa nini Tom alikifanya mpaka kufungiwa, hakuna mfanyakazi aliyejua sababu ya Tom kufungiwa isipokuwa Othman Tafu pekee.



Hilo Koplo Mbegu alilijua kupitia Juddy tena baada ya kumlaghai sana kwa pesa na kumnunulia chakula kila wakutanapo nyakati za mchana maana ndio ulikuwa muda wa Juddy wa kutoka kazini.



Kwa hiyo Juddy hakumwambia Koplo Mbegu sababu ya Tom kufungiwa, kwa maana hata nae hakujua, alichomsaidia ni kumuelekeza mtaa anaokaa Tom ingawa hakumtajia nyumba anayokaa Tom kwa maana hata nae hakupajua.



Kwa hiyo alichokifanya Koplo Mbegu ni kuanza kwenda mtaa ule anaoishi Tom, ilikuwa ngumu kumuona Tom kwa maana alikuwa anashinda ndani tu bila kutoka nje ya geti lao kwa maana kila kitu cha kupika kilikuwa ndani, na kama akihitaji soda au bia alikuwa anamuagiza mtu yoyote anayeenda dukani.



Koplo Mbegu alikuwa anaenda huo mtaa kila siku bila kuchoka kwa maana aliamini ipo siku atamuona, alifululiza wiki nzima bila mafanikio na siku ambayo alimuona ndiyo siku ambayo Koplo Mbegu alipanga iwe ya mwisho kumtafuta Tom.



Siku hiyo Tom alikuwa ametoka mjini kutafuta CD ya kuangalia kwa maana zile zilizopo ndani kwake alikuwa amezichoka, kwa bahati mbaya alizunguka sana kuitafuta CD anayoitaka mpaka usiku ukawa mkubwa, akaamua arudi kwake kwa nia ya kuitafuta tena hiyo CD katika siku inayofuata.



Sasa wakati anarudi, kituo cha daladala aliposhukia ndio kituo cha daladala ambacho Koplo Mbegu alikuwa anangojea daladala ili apande arudi kwake baada ya kumkosa Tom siku hiyo, sasa wakati anasubiri watu watelemke kwenye daladala hiyo ili apande, ndipo alipomuona Tom nae akishuka, akafurahi ila hakutaka kumshtua kwa maana alitaka amfuatilie mpaka ajue anapokaa, Tom alipoanza kuondoka eneo hilo, alimuacha asogee mbele kidogo ili aweze kumfuatilia bila ya yeye Tom kujua.



Walitembea kwa mtindo huo mpaka pale Tom alipofika kwenye njia panda na kusimama, kisha akachagua kuifuata ile njia ambayo ilipita katikati ya makaburi, wakati wakiwa katikati ya makaburi ndipo Koplo Mbegu akaamua amuite Tom kwa maana aliamini kwenye eneo la kutisha kama lile ni bora amuite ili watembee kirafiki kwa kuwa hapo kunatisha, Koplo Mbegu alipomuita Tom aliamini akimjua atamchangamkia kwa maana wameshawahi kuonana, kumbe imani yake haikuwa sahihi, alipomuita Tom alishangaa kumuona Tom akimuangalia kama mtu asiyemjua, na hata Koplo Mbegu alipojitambulisha ndipo aliharibu kabisa, Tom aliamua atoke mbio, ikabidi Koplo Mbegu abaki anamtolea macho tu, mwisho nae akaamua amkimbize bila mafanikio na mwisho ndipo akaamua arudi zake kwake.



*********************



Upande wa Tammy Semmy usiku huu katika kambi yao walibaki wanaume watatu, yaani Jimmy, Gabby na Waziri wa ulinzi wakiwa wanapanga namna ya kutengeneza kifo cha Waziri mkuu,



"Lakini mkuu ulimwambia Tammy Semmy kuwa mipango ya kifo cha huyu bwana tayari umeshaipanga, sasa inakuwaje unasema tuipange muda huu?" Jimmy alimuuliza Waziri wa ulinzi,



"Nilikuwa namtuliza tu, kiukweli sijapanga mpango wowote" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Ebu tuambie basi hata wazo ulilokuwa nalo la namna ulitaka kifo chake kiwe?" Jimmy aliuliza,



"Mimi nilitaka tumkodishe dereva mmoja wa gari, alafu kitakachofanyika ni kuigonga gari ya Waziri mkuu inapokuwa kwenye msafara" Waziri wa ulinzi aliongea na kuwatazama vijana wake,



"Je na asipokufa kwenye hiyo ajali?" Gabby aliuliza,



"Itabidi huyo dereva tutaemkodi tumpe na bastola, ili atakapomgonga ampige na risasi kabisa" Waziri wa ulinzi aliongea na kufanya wenzake wacheke,.



"Huo mpango ni wa kitoto sana mkuu, mipango ya kizamani hiyo" Gabby aliongea,



"Toeni yenu hiyo mipango ya kisasa" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Tufanyeni kitu kimoja, huyo Waziri mkuu tumteke na tumfiche, ili tuangalie wananchi watachachamaa au lah, wakichachamaa tutamuachia baada ya uchaguzi, wakikaa kimya tutamuua" Jimmy aliongea na kuwatizama wenzake,



"Ni mpango mzuri, lakini ningependa niongezee hili, nadhani tuichome nyumba yake moto alafu tumtafute mtu ambaye atakuwa amekufa tumuingize ndani ya ile nyumba ya Waziri, hata tutakapomteka Waziri Mkuu watu hawatajua, watadhani ile maiti tuliyoiweka ndio Waziri mkuu amekufa na itabidi sura ya maiti tutakayoiweka iwe tayari tumeshaiharibu kwa moto" Gabby aliongezea na wenzake wakaonekana kumuunga mkono kwa wazo lake,



"Wazo zuri, je hiyo maiti tutaitoa wapi?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Tom" Gabby alijibu,



"Sasa Tom ni maiti?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Nadhani ni muda wake wa kufa, tena tunatakiwa tumuue ndio tuseme mipango yetu mbele ya Tammy Semmy, vinginevyo Tammy Semmy hatokubali Tom auawe" Jimmy aliongea,



"Na hiyo mipango ya kumuua waziri mkuu ifanyike lini?" Gabby aliuliza,



"Kesho, kesho usiku.



Kwa hiyo Tom mnaenda kumchukua kesho asubuhi?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Leo hii hii usiku, tukimfuata kesho asubuhi itakuwa shazi, kufanya utekaji jua likiwa limechomoza uwa ni ngumu sana" Gabby alijibu,



"Na itakuwa vizuri tukimleta hapa akiwa maiti tayari, maana tunaweza kumleta mzima alafu tukabadili mawazo, maana ana sura ya huruma sana" Jimmy aliongea,



"Hiyo ni kweli kabisa, ila hatutakiwi kumuua kikatili, inabidi afe kifo kilaini sana" Gabby aliongea,.



"Tumuue na (poison powder) unga wa sumu, tuuweke kwenye kitambaa na kumziba nao puani, atakufa haraka na bila maumivu" Jimmy alitoa wazo,



"Limepita hilo, hakuna cha kungoja, twende zetu" Gabby aliongea huku akiinuka kwenye kiti,



"Ninachowapendea ni hicho, uwa hampingani mawazo kabisa, atakachosema mmoja wenu, mwingine anakiunga mkono" Waziri wa ulinzi aliongea huku akicheka wakati vijana wake wakitoka ndani.



*****************



Tom aliingia chumbani kwake huku akihema juu juu baada ya kukimbia sana, mbio alizokuwa anamkimbia Koplo Mbegu. Aliingia na kufikia kitandani huku kila muda akiinuka na kuchungulia dirishani,



"ule ni mzimu wake, yule Jamaa wakina Jimmy si walimuua mwezi uliopita? Alafu amenitokea makaburini unadhani ningefanyaje, ni mbio tu" Tom aliongea huku akiamini alikutana na mzimu wa Koplo Mbegu kwa maana anachojua yeye ni kuwa Koplo Mbegu alishakufa.



Baada ya Tom kupumzika, aliamua kwenda kuoga ili kuondoa jasho lililotokana na kukimbia, alielekea bafuni kuoga, baada ya dakika kadhaa alimaliza kuoga na kurudi chumbani kwake, alipoingia tu ndani kwake, alishangaa mkono wa mtu ukimziba puani na kitambaa cheupe kilichokuwa na unga unga, akajitahidi kufurukuta lakini ilishindikana, Tom akaanza kuona mawenge na mwisho macho yake hayakuona kitu, ni giza tu lilimtawala na hata ubongo wake haukuweza kufanya kazi tena..........



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Aliyekuwa anafanya kitendo hicho alikuwa ni Jimmy, baada ya kuridhika kwa kile alichokuwa akikifanya, alimbeba Tom begani na kutoka nae nje moja kwa moja mpaka kwenye gari yao na kumuingiza katika siti za nyuma.



"Tayari?" Gabby aliuliza,



"Kwisha habari hapa" Jimmy alijibu huku nae akiingia ndani ya gari na kufunga mlango, kisha Gabby akaiondoa gari taratibu bila pupa yoyote safari ya kurudi kambini kwao ikaanza.



"Kesho ndiyo mwisho wa huyo Waziri mkuu, anataka kutuzibia ridhiki zetu" Jimmy aliongea huku akiifungua bia ya kopo iliyokuwa kwenye gari,



"Tusingemuua, ilitakiwa tumteke tu" Gabby aliongea,



"Inabidi tufuate agizo la wakubwa, maana tunaishi kwa ajili yao" Jimmy alijibu,



"Sawa, ila kuna muda inabidi na sisi tufuate hisia zetu bila kuvuruga mipango yao" Gabby alionga huku akiingiza gari ndani ya uzio wa nyumba yao, kisha Jimmy akashuka na kumuweka Tom mabegani na kumuingiza ndani, kisha akaelekea nae mpaka kwenye chumba cha mateso na kumtupa sakafuni, alafu akarejea sebuleni na kumkuta Waziri wa ulinzi na Gabby wakiwa wamekaa,



"Hii kazi inafanyika kesho mchana, Waziri mkuu atakapotoka kwenye kikao cha chama" Gabby aliongea,



"Kwa hiyo basi tumeona suala la kumteketeza kwa kumchoma moto itatuwia vigumu na pia itakuwa na mlolongo mrefu, itabidi tumuue kwa ajali ya kutengeneza" Jimmy aliongea na kumfanya Waziri wa ulinzi atabasamu,



"Ila mimi niliwaambia nyie mkanipinga, sasa mmekubaliana na mimi. Sasa Tom mmeshamuua, mbona amelegea vile?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Hajafa yule, tulimuwekea madawa ya kulevya kidogo tu ili apoteze fahamu, maana tulihisi ingekuwa ngumu kumchukua akiwa na fahamu" Gabby alimjibu Waziri wa ulinzi,



"Basi sawa, mipango itabidi tuipange kesho mapema sana na wote tunatakiwa kuwepo" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Na leo itabidi sisi tulale hapa tukiziangalia kwa umakini ramani za barabara ambayo Waziri mkuu atapita ili iwe rahisi kumtega" Gabby aliongea,



"Ni lazima tujiandae usiku mzima" Jimmy aliongea,



"Ngoja sasa nipike, si kuna nyama kwenye friji?" Gabby alimuuliza Waziri wa ulinzi,.



"Kuna kuku wawili, chukueni mmoja tu" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Miili mikubwa hivi tugombanie kuku mmoja? Gabby pika wote wawili alafu kesho tutawanunulia huyo kuku wao mmoja" Jimmy aliongea huku akicheka,



"Hata tusipowanunulia ni sawa, chakula cha huku ni kwa ajili yetu" Gabby aliongea huku akielekea jikoni.



********************



Koplo Mbegu aliondoka moja kwa moja kutoka ule mtaa anaokaa Tom na kuelekea kwake, njiani bado alikuwa anajiuliza ni kwanini Tom alimkimbia ila hakupata jibu, alianza kuhisi huenda Tom ni kichaa.



Koplo Mbegu kabla hajafika nyumbani kwake, alipitia kwa mama ntilie na kupata chakula cha usiku huku akiwa bado anamuwaza Tom.



Alipomaliza kula alinyoosha moja kwa moja mpaka kwenye mlango wake, alishtuka baada ya kuukuta upo wazi, akapata hofu kwa maana bado alikuwa na kumbukumbu ya mauaji ya mpangaji mwenzie aliyeuawa mwezi uliopita.



Akataka kuita wapangaji wenzake ili wamsaidie kujua ndani kuna nini? ila akapingana na hilo wazo, akaamua achungulie mwenyewe kupitia upenyo mdogo uliopo mlangoni, akamuona Sudy Bakari akiwa amekaa kitandani, Koplo Mbegu akajiuliza amekuja kufanya nini? hakupata jibu, mwisho akaamua aingie ndani,



"Hivi unatumiaga funguo au kitu gani kuingia ndani kwangu?" Koplo Mbegu aliuliza baada ya kuingia ndani, na hakuonekana mwenye kufurahishwa na mlango wake kufunguliwa pasipo ruhusa yake,



"Kitu ambacho hamkijui wanadunia, mimi nimeshakijua zamani sana, na hakuna chochote kitengenezachwo na viumbe nyie alafu kinishinde mie" Sudy Bakari aliongea bila kumtazama Koplo Mbegu,



"Kwanza ni bora umekuja, siku ile msibani nilikuona ukiweka ua kwenye kaburi la Rais, unahusikaje na ule msiba?" Koplo Mbegu alimuuliza huku akivua viatu,



"Nausika na kifo chake" Sudy Bakari alijibu na kufanya Koplo Mbegu amuangalie huku akianza kuamini huyu ndiye muuaji wa Rais,



"Wewe ndiye uliyemuua Rais au unahusikaje?" Koplo Mbegu aliuliza huku akiwa amemkazia macho,



"Kiumbe kiumbe, hicho sicho kilichonileta hapa, hapa nimekuja kwa jambo moja tu" Sudy Bakari alijibu,



"Wewe ni muuaji na unatakiwa kuwa gerezani, alafu unajifanya eti sio mtu wa kawaida" Koplo Mbegu aliongea huku akiwa amemtolea macho,



"Inaelekea hauko tayari kunisikiliza" Sudy Bakari aliongea huku akiinuka,



"Ebu rudi ukae chini nieleze una habari gani?" Koplo Mbegu aliongea huku akimzuia Sudy Bakari,



"Kesho saa nane mchana uje tuonane kwenye Barabara ya Dumizi, eneo la mataa" Sudy Bakari aliongea huku akimsukuma Koplo Mbegu aliyekuwa anamzuia njia,



"Ndio kuna nini hapo?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Nitakukutanisha na muuaji wa Rais" Sudy Bakari aliongea na kutoka ndani,



"Ebu subiri" Koplo Mbegu aliongea huku akinyanyuka, alipotoka nje alikuta mtu hayupo, Sudy Bakari alishapotea kitambo tu.



Koplo Mbegu akarudi ndani huku akijilaumu kumuachia Sudy Bakari aondoke,



"Kesho saa nane mchana, nitaenda ili anioneshe huyo muuaji wa rais, ila mbona ananichanganya, yeye anahusikaje na kifo cha Rais?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akijiweka kwenye Kochi,



"Alafu amesema tukutane barabarani, kwanini asingesema tukutane kwenye hoteli au bar?" Koplo Mbegu alijiuliza bila kupata jibu, ila mwisho aliazimia kuwa bora aende tu akamuone huyo muuaji wa Rais.



********************



SAA 12 ASUBUHI.



Siku mpya ilianza kwa kumkuta Jimmy na Gabby pamoja na Waziri wa ulinzi wakiwa sebuleni huku wakionekana wana furaha, hii ni baada ya kukesha wakipanga njia nzuri ya kumuua Waziri mkuu na wakafanikiwa katika mipango yao, kilichobaki ni utekelezaji tu, watekelezaji ni wawili, Tom ambae atakuwa dereva wa gari litakalogonga gari la Waziri mkuu na BQ ambaye atakaa juu ya jengo refu huku akiwa na bunduki yake kwa ajili ya kumuua waziri mkuu baada ya gari yake kugongwa, na wao yaani Jimmy na Gabby wataenda eneo la tukio kama polisi kwa ajili ya kwenda kumchukua Tom.



Baada ya muda kidogo aliingia BQ huku akiwa na tabasamu pana, akawasalimia wenzake na kukaa kwenye kochi.



"Kamlete Tom ili nae apewe jukumu lake" Waziri wa ulinzi alimwambia Jimmy ambaye alinyanyuka na kwenda kumchukua Tom, akarudi nae huku Tom akiwa na wasiwasi,



"Tom tunakupa kazi ya mwisho, ukiifanikisha hii hatutakusumbua tena, yaani utakuwa huru kufanya mambo yako" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimtazama Tom,



"Kazi gani?" Tom aliuliza huku akionekana amechoka, akaelezwa jukumu lake la kufanya mchana wa leo, ilibidi akubali kwa maana hakuwa na uwezo wa kupinga,



"Kumbuka katika gari utakayopewa uendeshe itakuwa na Bomu, kwa hiyo chochote utakachofanya kinyume na sisi, tutalipua Bomu" Waziri wa ulinzi alimalizia kuongea,



"BQ saa sita unatakiwa uwe umeshaingia eneo lako la shabaha" Gabby aliongea huku akimtazama mwanadada yule aliyekuwa anakula chocolate,



"Usijali baba" BQ aliongea huku akitabasamu,



"Tom baada ya kuligonga gari la Waziri mkuu gari lako linaweza kuzima, chukua kifaa hiki kipo kama bastola, ukibonyeza hapo palipo kama pa kufyatulia risasi basi kioo cha mbele cha gari kitaachia na kudondoka chini, utapata upenyo wa kutokea" Waziri wa ulinzi alimwambia Tom na mjadala ukawa umefungwa, kilichokuwa kinaendelea ni utayarishaji wa vitendea kazi tu.



*******************



_______________________

SAA NANE MCHANA.

_______________________



Koplo Mbegu aliwahi kufika eneo ambalo aliambiwa afike na Sudy Bakari, lakini cha ajabu hakumkuta Sudy Bakari, akaamua asubiri kidogo, wakati akiendelea kusubiri eneo hilo la mataa, aliweza kuona msafara wa kiongozi ukipita eneo lile, ule msafara ulipopita mbele yake aliweza kugundua kuwa ni msafara wa Waziri mkuu.



"Yaani viongozi wana raha kweli, wakiwa wanapita magari yote yanasimama" Koplo Mbegu aliongea mwenyewe wakati msafara ule ukimpita na kuupuuza.



Ule msafara ulipofika eneo la njia panda ambapo kuna mataa, kuna gari iliingia kwa mwendo wa kasi sana na kuigonga gari ya Waziri mkuu upande wa ubavuni kwa mbele, eneo ambalo alikaa Waziri mkuu, kishindo kikubwa kikasikika eneo lile.



Katika lile gari lililogonga gari la Waziri mkuu, dereva alikuwa Tom, baada ya Tom kuigonga gari ile ya Waziri mkuu, aliweza kumuona Waziri mkuu akiangaika huku damu zikiwa zinamvuja kichwani, Tom akakitoa kile kifaa alichopewa mfano wa bastola kwa ajili ya kukifanya kioo cha gari alilokuwepo kuachia, Tom akakibonyeza kile kifaa eneo la kufyatulia, alivyobonyeza tu alishangaa risasi zikitua kwenye kichwa cha Waziri mkuu na kumshuhudia akifa pale pale, akajua tayari BQ amemaliza kazi yake, na kipindi hicho kioo cha gari ya Tom kilikuwa kimeshaachia na Tom alikuwa anaangaika kutoka huku watu wakianza kujaa eneo la tukio.



Koplo Mbegu aliposikia kishindo aligeuka na kushuhudia gari ya Waziri mkuu ikigongwa vibaya sana ubavuni, akawa anajisogeza ili akatoe msaada, ndipo macho yake yakatua kwa dereva wa ile gari iliyoigonga gari ya Waziri mkuu, hakuamini macho yake baada ya kumuona Tom, sasa wakati koplo Mbegu akidhani ni ajali ya bahati mbaya, alimshuhudia Tom akitoa kile kifaa cha kufungulia kioo, kwa jinsi kilivyo basi Koplo Mbegu akaona kama Tom ametoa bastola, na Tom alivyokielekezea kile kifaa kwa mbele ya kioo ambapo ndipo usawa wa Waziri mkuu alipokuwa anaangaika, Koplo Mbegu alishuhudia Waziri akifumuliwa ubongo kwa risasi, hapo sasa ndipo Koplo Mbegu alipoamini kuwa Tom amemfyatulia risasi Waziri Mkuu.



Koplo Mbegu sasa akawa anatoka mbio ili amuwahi Tom asikimbie kwa maana alimuona akiangaika kutoka ndani ya gari....... ..





Watu waliendelea kujaa eneo la tukio na wengi wao walianza kumzonga Tom ili wampige kutokana na uzembe alioufanya na kupelekea ile ajali. Wakati watu wakiwa wanamzonga Tom, kilisikika king'ora cha gari la polisi, baada ya muda gari ilipaki katikati ya lile kundi la watu na wakashuka Gabby na Jimmy,



"Muacheni, sisi ni polisi" Gabby aliongea huku akionesha kitambulisho chake, hiyo ilisaidia kidogo kwa maana watu waliacha kumpiga Tom ila wengine waliendelea.



Gabby na Jimmy walifanikiwa kumuondoa Tom kwenye kikundi cha watu na kumuingiza ndani ya ile gari ya polisi waliyokuja nayo kisha wakaondoka nae kwa mwendo wa kasi.



Koplo Mbegu aliendelea kukimbia kuelekea eneo ambalo magari yale mawili yaliyogongana, ila msongomano wa watu ulimzuia kwa hiyo ikambidi atumie nguvu za ziada za kuwapangua watu mpaka alipofika mbele kabisa, akawa anaangaliana na yale magari mawili yaliyogongana ila Tom hakumkuta,



"Dereva wa hili gari yuko wapi?" Koplo Mbegu aliuliza watu waliokuwepo eneo hilo,



"Ameshachukuliwa na polisi, wameondoka nae na gari lile" Mtu mmoja alijibu huku akilioneshea kidole lile gari walilokuja nalo wakina Gabby, lilionekana likiishia kwa mbali, Koplo Mbegu akaliangalia kwa umakini lakini hili achunguze ni gari la polisi kweli au? lakini hakuweza kupata jibu sahihi juu ya swali lake, akaamua amungalie Waziri mkuu aliyekuwa sio mtu hai tena, tayari alikuwa mfu, Koplo Mbegu akaangalia katika paji la uso la Waziri mkuu na kuona matundu mawili ya risasi, Koplo Mbegu akasikitika na macho akayahamishia kwa dereva wa Waziri mkuu na kumuona alivyokuwa amelala huku damu zikimvuja puani, haikujulikana ni mzima au amekufa?



Wakati Koplo Mbegu akiwa bado anatazama tukio lile, lilifika gari la hospitali na kuuchukua mwili wa Waziri mkuu pamoja na dereva wake na kuondoka nao, watu wakaanza kutawanyika na Koplo Mbegu nae akaanza kuondoka kwenye kundi lile la watu, wakati anaondoka akatupia macho upande wa pili wa Barabara na ndipo alipomuona Sudy Bakari akiwa amesimama huku mikono yake ameiweka mfukoni, kwenye mfuko wa koti lake na pia alikuwa akimuangalia yeye, Koplo Mbegu akaamua amfuate sasa, wakati Koplo Mbegu anamfuata Sudy Bakari, Sudy Bakari alikuwa amesimama tu anamuangalia jinsi Koplo yule anaemfuata.



Katikati yao likapita gari kubwa la mizigo na kuwatenganisha, lile gari lilipomaluza kupita tu, Koplo Mbegu akabaki na mshangao, Sudy Bakari hakuwepo tena ng'ambo ya barabara, sehemu aliposimama kulikuwa patupu, Koplo Mbegu akatoa tusi la nguoni huku akitazama tazama eneo lile bila kumuona mtu yule,



"Ndo nini sasa?" Koplo Mbegu alijiuliza na kuamua kurudi alipotoka huku akiwazia tukio lile la kifo cha Waziri mkuu.



Mwisho aliamua atafute usafiri tu wa kumrudisha kwake, aliziona bodaboda zikiwa mbali kidogo na pale alipo, akaamua azifuate ili apate kuelekea kwake huku mawazo yakiutawala ubongo wake.



Akiwa anarudi alipotoka ndipo alipoona gari la polisi likija na nyuma yake kulikuwa na gari la msalaba mwekundu, magari yote hayo yalikuwa yanakuja eneo la tukio,



"Ndio hatuendelei, yaani gari la wagonjwa linakuja baada ya nusu saa, lile jingine lilokuja ina maana hawajawasiliana mpaka yanakuja magari mawili mawili?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akiangalia eneo lile liliozungukwa na watu,



"Acha nirudi zangu, huu ni msiba mwingine wa taifa" Koplo Mbegu aliongea peke yake huku akianza kupiga hatua za kuondoka kwenye eneo hilo, alitembea mwendo wa dakika chache na kukutana na bodaboda, akaisimamisha na kupanda, safari ya kurudi kwake ikaanza.



Koplo Mbegu alifika kwake na kuingia ndani, akafikia kujitupa kitandani,



"Ndo maana Tom ulinikimbia jana, kumbe wewe ni muarifu, tena muarifu mkubwa tu, Tom nimeshuhudia kwa macho yangu ukimuua Waziri mkuu, huna cha kunificha sasa, ulitaka kuniambia nini siku ile kwenye viwanja vya ikulu? inaelekea unajua kila kitu kuhusu serikali hii, unawajua watu wazuri na watu wabaya ndani ya serikali, Tom muuaji, nakuweka hatiani" Koplo Mbegu aliongea peke yake, alikuwa na hasira nzito sana,



"Sudy Bakari ulisema unataka kunionesha mtu aliyemuua Rais, mbona hukunionesha? mbona uliponiona ulinikimbia? Au Tom ndio muuaji wa Rais? na kama Tom ndiye muuaji wa Rais je nyuma yake yupo nani? anawaua viongozi hawa kwa sababu gani?, Sudy Bakari utakuwa unajua, unajua majibu yote ya maswali yangu, Sudy Bakari na wewe nakuweka hatiani, ni lazima uubebe msalaba huu wa kuhusika na vifo hivi, hata kama auhusiki basi unawajua wahusika, na ndio maana ulionekana siku ile ambapo Rais alikufa, ni lazima uwe muhusika wa hivi vifo, ni lazima ukamatwe ili sheria ifanye kazi yake" Koplo Mbegu aliongea peke yake, alikuwa kama amechanganyakiwa kutokana na tukio aliliona muda mfupi uliopita.



Koplo Mbegu hakuona sababu iliyomfanya aendelee kukaa hapo tena, aliona ni bora akatembee tu mitaani labda inaweza kumsaidia kupunguza mawazo kwa muda huo.



Hakuwa na eneo la kwenda muda huo, isipokuwa ni kwenye mtaa anaoishi Tom, hakudhani kama ataweza kumpata, alichotaka yeye ni kujua tu nyumba anayoishi.



************************



Gabby na Jimmy walipomchukua Tom, walioondoka moja kwa moja mpaka kambini kwao, hakuna mtu aliyeongea kitu kipindi chote wakati gari ikiwa inaenda kambini kwao, walipofika walishuka na kuingia ndani,



"Dogo umefanya kazi nzuri, muda si mrefu utakuwa tajiri, cha muhimu ni kutunza siri tu" Jimmy alimpongeza Tom ambae hakuonekana na furaha muda wote,



"Muache, hayupo sawa" Gabby aliongea na kipindi hicho Waziri wa ulinzi nae alikuwa anaingia ndani, alikuwa anafuraha sana,



"Hapa kazi imeisha, tumemaliza" Waziri wa ulinzi aliongea huku akiwaonesha video aliyoichukua eneo la tukio, cha ajabu sasa kilichomshangaza Tom ni kwenye ile video kuonekana kama ni yeye ndiye aliyempiga risasi Waziri mkuu,



"Mimi sijamuua lakini, hiyo niliyoshika siyo bastola jamani" Tom alilalamika baada ya kuitazama video ile,



"Wewe ndio unajua hivyo, ila mtu asiyejua kitu hawezi kujua kama wewe hujaua, akiiona hii video ni lazima akuhukumu wewe" Waziri wa ulinzi aliongea huku akicheka na kipindi hicho BQ nae alikuwa anaingia,



"Kazi nzuri mwanadada, uwa hukoseagi" Jimmy aliongea huku akigonganisha mikono yake na BQ,



"Nilizaliwa kuua" BQ aliongea na kuachia tabasamu huku akimuangalia Tom,



"Sasa tuna ushahidi wako ukimuua Rais, na pia tuna ushahidi wako ukimuua Waziri mkuu" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuangalia Tom na Kufanya Tom aangalie chini huku machozi yakimtoka, hakuwa na namna ya kupinga kwa kuwa video inaonesha kila kitu ingawa ni kweli yeye hakuua.



"Mkuu ana taharifa hizi za kifo?" BQ aliuliza,



"Hii mipango haijui, habari atazisikia uko uko, huku tutamwambia tu jinsi tulivyopanga shambulio la kushtukiza" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Kila mtu amefanya vyema kwa kile tulichopanga leo, tumeshamsafishia njia mkuu, na kilichobaki ni yeye kutusafishia maisha" Jimmy aliongea huku akiwasha runinga kubwa iliyokuwa ikining'inia ukutani na kukuta habari iliyokuwa ikioneshwa ni juu ya kifo cha Waziri mkuu, chanzo cha habari ilisemekana ni ajali ya gari na dereva aliyesababisha ajali hiyo ilidaiwa amekamatwa, yupo chini ya uangalizi wa polisi.



Wakina Jimmy wakaanza kupongezana kwa maana wapo ndio walijifanya polisi na kuondoka na Tom eneo la tukio.



"Naombeni niondoke" Tom aliongea kwa sauti kavu, sauti iliyobeba hasira,



"BQ mpeleke, muache aende, ameshamaliza kazi yake" Waziri wa ulinzi aliongea na BQ akatii amri, akatoka nje huku akiwa ameambatana na Tom, wakaingia kwenye gari, Tom alikaa siti za nyuma na BQ alikuwa dereva, safari ya kumrudisha Tom ikaanza,



"Umefanya kazi nzuri, nataka nikuombee nafasi Ili uwe miongoni mwetu" BQ alimwambia Tom lakini Tom hakujibu kitu.



BQ akaamua akae kimya kwa maana alijua mtu anapokuwa na hasira uwa yupoje. Gari iliendelea kutembea huku kila mtu ndani ya gari akiwa kimya. Gari ilienda mwendo mrefu kidogo,



"Nishushe hapa hapa" Tom aliongea baada ya kukaribia kufika mtaa wao,



"Natakiwa nikufikishe kwako, ngoja ufike kwako kwanza, hapa utarudi mwenyewe baada ya mimi kukushusha kwako" BQ aliongea,



"Nimesema nishushe" Tom aliongea kwa hasira huku akiwa ametoa macho,



"Ebu nielewe nilichokwambia" BQ aliongea huku macho yakiwa mbele,



"Nimesema nishushe" Tom aliongea huku akimvuta BQ na kufanya gari ianze kuyumba barabarani, ikabidi BQ ampige Tom na kiwiko cha mkono kilichomkuta kwenye shingo, Tom ndipo akamuachia, Tom alipoteza fahamu. BQ aliporudisha macho mbele alishangaa gari ikiwa inaacha njia na ilikuwa inaenda kumgonga mtu aliyekuwa anatembea kando ya barabara, masikini huyo mtu mwenyewe hakuwa na habari kama gari inakuja kwa nyuma kumgonga, BQ akashika breki na ile gari ikaseleleka na kumpiga yule mtu kwa nyuma na kumrusha mbele kidogo, yule mtu akaanguka chini, BQ akashuka kwenye gari na kwenda kumuangalia yule mtu, mtu mwenyewe alikuwa ni Koplo Mbegu, kwa bahati nzuri awa watu hawafahamiani, yaani Koplo Mbegu na BQ.



"Samahani, vipi umeumia?" BQ alimuuliza Koplo Mbegu aliyekuwa anajinyanyua,



"Hapana" Koplo Mbegu alijibu huku akijifuta vumbi,



"Samahani sana kaka yangu, bahati mbaya" BQ aliongea kwa unyenyekevu,



"Hata usijali Dada yangu" Koplo Mbegu aliongea huku akitabasamu,



"unaelekea wapi nikusogeze" BQ alimuuliza Koplo Mbegu kwa maana walikuwa wanaenda uelekeo mmoja,



"Nafika tu hapo mbele, usijali Dada" Koplo Mbegu alijibu huku akimshukuru BQ,



"Twende tu, ukikubali nitakuwa na amani kidogo" BQ alimbembeleza huku akitabasamu,



"Sawa haina shida" Koplo Mbegu alijibu huku akitabasamu na kwenda kwenye mlango wa mbele na kuufungua, Koplo Mbegu akaingia ndani ya gari alilokuwa amepanda Tom........







Koplo Mbegu alikaa kiti cha mbele bila kuangalia nyuma ni nani amekaa, muda wote Tom alikuwa amelala kwenye siti ya nyuma, alikuwa amepoteza fahamu kutokana na kiwiko alichopigwa na BQ katika purukushani yao iliyotaka kusababisha ajali, kwa hiyo muda huo Tom hakuwa na fahamu kabisa, alikuwa amelala kwenye kiti cha nyuma.



Gari ilitembea mwendo wa dakika tano huku ukimya ukiwa umetawala,



"Nishushie hapa Dada, nimefika" Koplo Mbegu aliongea na BQ akapunguza mwendo wa gari na kuisimamisha, kisha Koplo Mbegu akatelemka,



"Kama kama umeumia niambie, usije ukasema hujaumia kumbe una maumivu ya ndani kwa ndani" BQ aliongea huku akitabasamu,



"Hata usijali, au unaweza kunipa namba yako ya simu kama kuna chochote kitanitokea kutokana na hii ajali" Koplo Mbegu aliongea,



"Sina simu, ngoja nikupatie tu pesa" BQ aliongea huku akitoa kibunda cha noti za elfu kumi kumi zilizofungwa na ruber band,



"Hapana usinipe pesa, kama huna simu basi, nadhani sitokuwa nimedhurika" Koplo Mbegu aliongea huku akimzuia BQ,



"Chukua tu" BQ aliongea kwa kusihi,



"Usijali Dada, nashukuru kwa roho yako nzuri" Koplo Mbegu aliongea huku akitabasamu,



"Wewe chukua bwana, acha aibu za kiume" BQ alimbembeleza Koplo Mbegu,



"Haya asante dada, ila hizi umenipa za bure tu, sijaumia kabisa" Koplo Mbegu aliongea huku akizipokea zile fedha,



"Usijali kaka, huwezi jua labda umeumia ila maumivu utayapata kesho" BQ aliongea,



"Mimi mwili wangu naujua, sijaumia kabisa" Koplo Mbegu aliongea huku akifunga mlango wa gari,



"Hiyo nimekupa ya dharula, utaangalia hali yako namna inavyoenda" BQ aliongea kisha akaondoa gari kwa mwendo wa pole pole na kumuacha Koplo Mbegu akitabasamu tu huku akiiangalia ile gari ya kifahari inavyoikanyaga ile barabara ya kimasikini iliyosheheni vumbi.



"Msichana mdogo anamiliki pesa na gari la kifahari, sijui ni mfanyakazi wa wapi huyu?" Koplo Mbegu alijiuliza wakati ile gari ikizidi kupotea machoni pake.



Koplo Mbegu ikaendelea kutembea kwa mwendo wake wa taratibu na nia yake ilikuwa ni kufika eneo lile ambalo alimpoteza Tom machoni siku ile aliyokuwa anamkimbiza.



************************



Tammy Semmy aliingia katika sebule ya kambi yao huku akionekana mwenye furaha sana, aliwakuta vijana wake wakiwa na nyuso zao za kawaida kabisa kama wanavyokuwaga kila siku,



"Leta shampeni kwanza kwa maana furaha niliyonayo sio ya kawaida" Tammy Semmy aliongea huku akicheza mziki laini uliokuwa ukiimbwa kwa lugha ya kigeni,



"Kuna nini mkuu, mbona umefurahi sana?" Jimmy aliuliza,



"Leta shampeni kwanza" Tammy Semmy aliongea kwa kusisitiza huku akiendelea kuselebuka taratibu, na kufanya Jimmy aende katika stoo ya vinywaji na kurudi na shampeni, ambapo Tammy Semmy aliifungua na kuanza kummwagia kila mtu aliyekuwepo pale huku akipiga kelele za furaha,



"Mrembo wenu yupo wapi, mbona simuoni hapa?" Tammy Semmy alimuulizia BQ,



"Ametoka kidogo, mbona leo kama una furaha sana?" Jimmy alimuuliza,



"Si niliwapa kazi mkawa mnajivuta sana, sasa leo imetimizwa kwa uwezo wa Mungu, Waziri mkuu kwisha habari yake, amekufa, ameshakufa tayari kwa ajali ya gari" Tammy Semmy alizungumza kwa furaha na wenzake wakawa wanacheka, akajua na wao wamefurahi kuisikia ile habari,



"Unadhani ajali inaweza kutokea kwenye mataa bila kupangwa? Mzee hiyo mipango ni yetu" Waziri wa ulinzi aliongea na wakaanza kumcheka Tammy Semmy,



"Ina maana mlipanga bila kunishirikisha?" Tammy Semmy aliuliza,



"Hii mipango ilipangwa jana usiku, na ikakamilishwa leo" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Ilikuwaje?" Tammy Semmy akauliza kisha akasimuliwa kila kitu kilivyokuwa na akaoneshwa ile video ya tukio.



"Kwa hiyo Tom ndio alimpiga risasi?" Tammy Semmy aliuliza,



"Tom geresha tu, aliyefanya kazi ya mwisho ni BQ, BQ alikaa juu ya ghorofa moja jirani na pale" Jimmy alijibu na kumfanya Tammy Semmy apige makofi,



"Safi sana, yupo wapi sasa huyu Dada yenu, au hajawaambia alipoelekea?" Tammy Semmy aliuliza



"Amempeleka Tom kwake" Jimmy alijibu,



"Kazi nzuri sana mmeifanya, nashindwa hata cha kuongea, leo nimefurahi sana" Tammy Semmy aliongea huku akielekea kwenye kabati la vyombo na kutoa idadi ya glass kulingana na wao walivyo, kisha akaimimina ile shampeni kwenye kila glass na wakaanza kunywa,



"Sasa hapo tumekusafishia njia, ni wewe tu ushindwe mwenyewe" Waziri wa ulinzi aliongea huku akicheka,



"Mimi ni Rais, mimi tayari ni Rais, kinachofuata ni kuandaa tu baraza la mawaziri ambao nitakuwa nao" Tammy Semmy aliongea kwa furaha,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Mimi nataka niwe Waziri mkuu" Waziri wa ulinzi alijipangia,



"Sasa wewe huwezi kuendelea kuishi na ndevu hivyo, utaishi na mandevu hayo mpaka lini? unatakiwa uende ukabadilishwe sura, kule kule ulipofanyiwa matibabu ya macho baada ya kule mkasa wa memory card" Tammy Semmy alimwambia Waziri wa ulinzi,



"Hiyo haina shida, ila si ni baada ya wewe kukalia kiti cha urais?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Mimi tayari nimeshakuwa rais, itabidi uende haraka iwezekavyo ili ukirudi ukute ndio mchakato wa kutangazwa matokeo ya kura unaanza" Tammy Semmy aliongea kwa kujiamini,



"Kwani kubadilishwa sura uwa inachukua muda gani?" Gabby aliuliza,



"BQ ndio anajua mambo hayo" Tammy Semmy alijibu,



"Na yule Dada yetu anajua kila kitu" Jimmy aliongea huku akicheka,



"Yule nilimchukua kutoka shirika la ujasusi la urusi, na nilimleta ili apambane na Sarah yule mwanadada aliyetusumbua kwenye ishu ya memory card, bahati nzuri yule Dada aliondoka kwa maana alijua kazi imeshaisha" Tammy Semmy aliongea,

.



"Sasa mbona anajua kiswahili vizuri tu?" Jimmy aliuliza kwa mshangao,



."ni mswahili huyu, ila alichukuliwa akiwa mdogo sana na bwana mmoja mmarekani" Tammy Semmy alijibu,



"Sasa kama ni mswahili ilikuwaje akawa anafanya kazi kwenye kitengo nyeti cha nchi isiyo yake?" Gabby aliuliza,



"Hayo maswali mtamuuliza wenyewe, msubirini arudi. Tuendelee kusheherekea tu" Tammy Semmy aliongea huku akizibua kifuniko cha chupa nyingine ya shampeni.



*********************



BQ alimfikisha moja kwa moja Tom nyumbani kwake na wala hakutaka stori zaidi, alimwambia Tom ashuke na wakati huo fahamu zilikuwa zimeshamrudia Tom.



Tom alitelemka na kuingia ndani kwake huku BQ akimuangalia tu, BQ akatabasamu kisha akageuza gari na kuondoka zake.



Tom aliingia ndani kwake na kuitupa mezani ile bahasha ndogo iliyojaa pesa.



"Nimeshakuwa wao sasa, kila baada ya kazi napewa hela, nalipwa kwa kila kazi nayowafanyia, nimekuwa mtumwa, mtumwa ninayelipwa ujira" Tom aliongea na kujitupa kitandani.



"Njaa inauma, naitaji kula" Tom aliwaza huku akivua suruali na kupanda kitandani kisha akachukua shuka akajifunika.



**************



Koplo Mbegu alifanikiwa kufika alipopataka na safari hii aliamua amuulizie Tom kwa vijana wa pale, alifanikiwa kumuulizia na kufanikiwa kupapata anapoishi Tom.



Baada ya kuelekezwa akaamua aende sasa, alidhamiria kumkamata Tom. Wakati anaelekea kwa Tom alipishana na gari analoendesha BQ wakapungiana mikono kisha Koplo Mbegu akaendelea kwenda mpaka alipofika kwenye geti la nyumba analokaa Tom, akamsalimia kijana aliyekuwa amesimama hapo nje ya geti,



"Tom nimemkuta?" Koplo Mbegu alimuuliza yule kijana,



"Yupo, ameingia muda si mrefu" Kijana yule alijibu,



"Chumba chake kipo wapi?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Kile chenye pazia nyeupe" Kijana alimuonesha kwa kidole,



"Nashukuru" Koplo Mbegu aliongea kisha akasukuma geti na kuelekea moja kwa moja mpaka kwenye mlango wa Tom, mlango ulikuwa wazi na hakupanga kugonga hodi, alipanga kuvamia na alijiamini kwa kuwa alikuwa na kitambulisho chake cha polisi na pingu kiunoni....





Koplo Mbegu akasogeza pazia na kuingia ndani taratibu bila fujo yoyote, cha ajabu hakumkuta Tom,



"Ameenda wapi tena? si nimeambiwa yupo ndani?" Koplo Mbegu alijiuliza baada ya kumkosa Tom,



"Au nae yupo kama Sudy Bakari, anaweza kupotea muda wowote?" Koplo Mbegu aliendelea kujiuliza huku akikaa kwenye kochi la sofa lililokuwepo hapo ndani, alidhamiria kumsubiri.



Aliendelea kukaa kwa dakika kumi bila Tom kutokea, akaamua asimame na kuanza kupekua pekua vitu vya Tom kwa dhana ya kupata kitu chochote ambacho kinaweza kuhusiana na vifo vya Waziri mkuu na Rais.



Alipekua kwa muda kidogo lakini hakupata kitu zaidi ya bahasha ndogo kama mbili na zote zilikuwa na pesa, na kilichomshangaza ni aina zile za bahasha ni kama anazopewaga na mkuu wake wa polisi, yaani bahasha zinazowekewa pesa za wafanyakazi wa serikali,.



"Sasa Tom ni mfanyakazi wa serikali au anatumiwa na watu wa serikalini?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akiikagua bahasha moja kati ya zile mbili alizozikuta kwenye chumba cha Tom.



Koplo Mbegu alipomaliza kukagua droo na makaratasi, aliahamia kwenye suruali za Tom sasa, alisachi kila suruali ili aone ni kipi atakipata ila kwa bahati nzuri hakupata chochote zaidi ya pesa chache zilizokuwepo kwenye suruali za Tom, baada ya kuridhika na ukaguzi wake, Koplo Mbegu alirudishia kila kitu kama alivyokikuta na kurudi kukaa kwenye kochi.



Baada ya saa moja la kusubiri bila Tom kurudi, Koplo Mbegu aliamua kutoka nje ya mlango na kuanza kuangaza angaza hapo nje bila mafanikio yoyote ya kuweka kumuona Tom.



Akaamua arudi ndani na kuendelea kusubiri,



"Atakuwa ameenda wapi? ila itakuwa hajaenda mbali kwa maana mlango ameuacha wazi na hela zimekaa hovyo hovyo, atakuwa jirani tu huyu" Koplo Mbegu aliongea huku akikaa kwenye kochi, kisha akachukua magazeti yaliyokuwa chini ya meza ndogo ya kioo na kuanza kuyasoma, hayo magazeti yenyewe yalionekana ni ya muda mrefu kidogo ila wala hakujali hilo.



Saa jingine la pili lilikatika bila Tom kurudi, Koplo Mbegu akaamua atoke sasa, akaenda moja kwa moja mpaka getini ila safari hii yule kijana aliyemkuta hawali hakumkuta tena, inawezekana yule kijana alikuwa amepumzika tu muda ule na safari hii alikuwa ameondoka zake.



Koplo Mbegu akatazama kushoto na kulia hakuona mtu ambaye angemuhitaji muda huo, zaidi aliwaona baadhi ya watu wakiendelea na shughuli zao za kawaida tu.



Sasa Koplo Mbegu akahisi huenda Tom alimuona kipindi anaingia, kwa hiyo Tom ameamua kuondoka.



Alichokifanya Koplo Mbegu ni kuamua kuondoka kwenye nyumba hiyo, aliamua atoke eneo hilo na atafute sehemu iliyokaa vizuri ili akae ila awe anaona mtu yoyote anayeingia na kutoka kwenye nyumba hiyo.



Koplo Mbegu alitembea kwa mwendo wa dakika mbili na kuweza kufika kwenye kijiwe kimoja ambacho kulikuwa na kijana wa makamo akiuza miwa na pipi eneo hilo,



"Dogo nikatie muwa wa mia tano" Koplo Mbegu aliongea huku akikaa kwenye benchi la mbao na macho yake yalikuwa kwenye geti la nyumba ya kina Tom. Kijana muuza miwa akamkatia kipande cha muwa na kumpa, Koplo Mbegu akawa anakila taratibu ili kuvuta muda.



Saa jingine la tatu likakatika Koplo Mbegu akiwa anamuwinda Tom bila mafanikio yoyote, maana alikaa bila kuona mtu yoyote akiingia wala mtu yoyote akitoka ndani ya nyumba ile,



"Dogo unamfahamu Tom?" Koplo Mbegu alimuuliza muuza miwa,



"Tom yupi sasa?, maana kuna Tom wengi" Muuza miwa aliuliza,



"Tom anaekaa nyumba ileee" Koplo Mbegu aliuliza huku akiionyesha kwa kidole nyumba anayoishi Tom,



"Yule mtangazaji, namfahamu vizuri tu, hiki ndio kijiwe chake, sema tu siku hizi amekuwa hadimu sana" Muuza miwa alijibu kichangamfu,



"Leo umefanikiwa kumuona?" Koplo Mbegu alimuuliza,



"Kuna muda aliletwa na gari nyeusi, ila hata hakukaa sana nikaona ametoka" Muuza miwa akajibu,



"Alitoka na hiyo gari?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Alitoka mwenyewe tu, gari iliondoka peke yake" Muuza miwa alijibu,



"Alivyotoka alielekea upande gani?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Alielekea kule, njia hii hajapita" Muuza miwa alijibu,



"Sasa naomba unisaidie kitu, nitakuachia namba yangu ya simu, ukimuona nijulishe" Koplo Mbegu aliongea huku akiandika namba yake ya simu kwenye karatasi,



"Vipi kwani? ndugu yako nini?" Muuza miwa aliuliza,



"Ndio, alafu nimetoka mkoani na nilijua nitamkuta ili nifikie kwake, sina sehemu nyingine ya kufikia" Koplo Mbegu aliongea,



"Aaah, nilijua labda polisi, maana siku hizi Tom kabadilika, ana hela huyo, alafu ana demu mkaliii ndio anamletaga na gari, inasemekana huyo demu ni mtoto wa kigogo, kwa hiyo nikajua wewe ni polisi umetumwa na huyo kigogo umkamate Tom" Muuza miwa aliongea huku akiipokea ile namba ya simu,



"Ndiyo huyo dem amemleta na gari alivyokuja?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Ndiyo huyo huyo anaemletaga kila siku" Muuza miwa alijibu,.



"Huyo mwanamke yupoje?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Kwa hiyo unataka kuniambia humjui?" Muuza miwa alimuuliza,



"Simjui ndio, ningemjua ningekuuliza?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Humjui vipi sasa wakati huyo demu wakati anaondoka na wewe ndio ulikuwa unakuja na niliona mkipungiana mikono" Muuza miwa aliongea na kumfanya Koplo Mbegu ashtuke, maana msichana aliyepishana nae na akiwa anaendesha gari ni BQ, ambaye Koplo Mbegu alipewa lifti kipindi anakuja kwa Tom.



"Yule mdada aliyekuwa anaendesha gari nyeusi ndio mwanamke wa Tom?" Koplo Mbegu aliuliza huku akiwa haamini,



"Ndiyo huyo, unaona anavyoendesha gari Kali? ametokea familia yenye pesa yule" Muuza miwa aliongea huku Koplo Mbegu akiendelea kuwaza,



"Lakini huyo mwanamke hakuja na Tom leo" Koplo Mbegu aliongea maana alikumbuka alipanda gari ya BQ ila hakumuona Tom,



"Yeye ndio amemleta na amemshusha getini, ila Tom anakaaga siti ya nyuma tu, hakaagi mbele kwa sababu hataki watu wajue kama yule ni demu wake" Muuza miwa alijibu na kufanya Koplo Mbegu akumbuke kuwa kweli wakati anaingia ndani ya gari aliona kuna mtu amekaa siti ya nyuma, ila hakutaka kumtilia mkazo sana,



"Dah kumbe alikuwa Tom?" Koplo Mbegu alijikuta anauliza kwa sauti kubwa,



"Ndio, ni Tom" Muuza miwa alijibu bila kujua kuwa Koplo Mbegu aliuliza swali lile bila kutarajia,



"Au basi ngoja nirudi tu nikaendelee kumsubiri kwake, nadhani hatokuwa mbali" Koplo Mbegu aliongea na kuondoka zake, akarudi chumbani kwa Tom, akawasha runinga akawa anaangalia bila ya uoga kama yupo kwaka vile.



******************



Tom baada ya kurudishwa kwake na BQ, alijaribu kulala ila alishindwa kutokana na njaa kumuuma, akaamua aende nje kutafuta chakula, kumbe alipotoka ndipo Koplo Mbegu aliingia.



Sasa Tom alipokuwa anarudi, ndipo alimkuta yule kijana wa getini ambaye aliulizwa na Koplo Mbegu kama Tom yupo. Yule kijana alipomuona Tom alimwambia kuna mgeni wake, Tom alipouliza huyo mgeni yupoje, kwa maelezo ya yule kijana yakaonesha huyo mgeni ni mtu ambaye Tom hamfahamu kabisa, Tom akahisi huenda labda huyo mgeni ni polisi ambao wamemfuatilia kutokana na tukio la ajali aliyoisababisha na kupelekea kifo cha waziri mkuu.



Tom akaamua kuondoka kabisa eneo hilo, akaamua aende kutembea mbali kabisa na hapo ili hata kama huyo mgeni atamsubiri basi atamsubiri mpaka atachoka na mwisho ataondoka.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya masaa matatu Tom aliamua arejee kwake kwa kuamini kuwa mgeni aliyeenda kumuulizia atakuwa ameshaondoka, kitu ambacho hakukijua ni kuwa huyo mgeni mwenyewe ambaye ni Koplo Mbegu alikuwa amekaa sebuleni kwake yeye Tom na anabadilisha tu vituo vya runinga.



Tom akafika mpaka getini na kuona mlango wa chumbani kwake ukiwa umerudishiwa, hapo ndipo akaamini kabisa kuwa ndani hakuna mtu, akawa anaelekea mlangoni kwake bila wasiwasi huku akipiga mluzi.



Koplo Mbegu yeye alikuwa ndani tu na kipindi hiki aliamua kuweka CD kabisa za filamu za nje, akawa anafuatilia kwa makini, alijisahau kabisa kama pale sio kwake.



Wakati Koplo Mbegu akiwa amenogewa na filamu ile anayoiangalia, alishtuka baada ya mlango kufunguliwa.........









Mlango ulivyofunguka, Koplo Mbegu akasubiri kumuona mtu atayeingia, akili zake ziliamini ni Tom ndio anaingia hapo, lakini cha ajabu akaingia yule kijana aliyemkuta hawali pale nje ya geti,



"Bro bado upo?" Kijana alimuuliza Koplo Mbegu,



"Bado nipo dogo, namngoja Tom" Koplo Mbegu alijibu huku macho yake yakiwa katika runinga,



"Nimekuja kufunga mlango, kwa maana huyu mtu inavyoonekana hawezi kurudi muda huu kwa hiyo ni bora nifunge mlango wake, akirudi nitampatia funguo yake" Kijana alimuelewesha Koplo Mbegu,



"Ila mimi si nipo" Koplo Mbegu alimwambia yule kijana huku wakitazamana,



"Tatizo mimi sikujui, kwa hiyo kama kitu chochote kitapotea atanidai mimi kwa kuwa ndiye niliyekuwa getini kipindi anatoka" Kijana alijibu kwa utulivu,



"Kwani wewe unahishi wapi?" Koplo Mbegu alimuuliza yule kijana,



"Chumba hicho kinachofuata" kijana alijibu huku akioneshea kidole mlango unaotazamana na chumba cha Tom,



"Sasa tunafanyaje, maana mimi ni mgeni wa Tom" Koplo Mbegu alijaribu kutumia mbinu ili aendelee kukaa hapo,



"Kwa kukushauri tu, ni bora ukakae pale nje uliponikuta ili umngoje Tom, maana mlango wa kuingilia kwenye hii nyumba upo mmoja tu, kwa hiyo pindi Tom atakapoingia utamuona tu" Kijana aliongea huku akifungua droo ya kitanda na kutoa ufunguo wa kitasa,



"Sawa, kwani ni kawaida yake kuondoka mlango ukiwa hivi na kukaa muda mrefu namna hiyo?" Koplo Mbegu aliuliza huku akivaa shati lake kwa maana alikuwa amelivua,



"Siku hizi imekuwa kawaida, juzi tu alitoka kama hivi, aliporudi akakuta ameibiwa pesa na laptop" Kijana alijibu, ila alitumia uongo ili kumtisha Koplo Mbegu,



"Dah kweli, ebu angalia kama vitu vyote vipo sawa ili nikitoka ubaki na amani" Koplo Mbegu alimwambia yule kijana na kufanya kijana azungushe macho chumba kizima kisha akafungua fungua droo zote za pale chumbani,



"Kupo sawa, unaweza kutoka" Kijana aliongea na Koplo Mbegu akatoka zake nje, Kijana akarudi kwenye drop moja na kuchomoa noti ya elfu kumi na kuitia mfukoni,



"Unawekaje hela kihasara hasara hivi" Kijana aliongea peke yake huku akiurudishia mlango wa Tom, kisha akaenda mpaka getini na kumkuta Koplo Mbegu akiondoka zake taratibu, Kijana akarudi mpaka kwenye mlango wa chumba chake na kuingia,



"Ameshaondoka" Kijana alimwambia Tom,



"Umechungulia mpaka nje ya geti?" Tom alihoji,



"Chungulia dirishani umuone mwenyewe" Kijana alimwambia Tom na Tom akaenda dirishani na kuchungulia, akamuona Koplo Mbegu akizidi kupotea. Tom akatoka kwenye chumba cha huyo kijana na kuingia kwenye chumba chake, kijana akamfuata,



"Nipe changu" Kijana aliongea huku akimtazama Tom, Tom akafungua droo na kuchomoa noti ya elfu kumi akampatia yule kijana,



"Mjini mipango" Kijana aliongea kwa furaha huku akitoka zake nje na kumuacha Tom akijifungia kwa ndani mlango, kisha akazima kila kitu na kubaki na simu yake tu ambayo nayo aliitoa sauti, kisha akajitupa kitandani.



Kumbe wakati Tom aliporudi hakutaka kwenda chumbani kwake moja kwa moja, alianzia chumbani kwa kijana huyo na akamuomba amuangalizie kama bado mgeni yupo katika chumba chake, yaani chumba cha Tom, na wakakubaliana kuwa kama mgeni yupo basi kijana afanye mbinu ili mgeni huyo aondoke na akifanikisha atalipwa elfu kumi.



Ndicho hicho kilichotokea kabla Tom hajaamua kuingia ndani kwake.



**********************



BQ alirejea kambini kwao na kukuta shamrashamra za kupongezana kwa kifo cha Waziri mkuu kilichosababishwa na wao.



BQ alipoingia tu Tammy Semmy alimkumbatia na kummiminia kinywaji kwenye glass na kumpatia, BQ akawa akawa anatabasamu huku akiishangaa ile hali, kwa maana hakutegemea kukuta shangwe ya namna ile,



"Hii part mbona inanitisha, kunani hapa?" BQ aliuliza huku akitabasamu,



"Kazi mliyoifanya ni kubwa imenibidi nifurahi bila kutegemea" Tammy Semmy alijibu huku akiselebuka,



"Mkuu ulitakiwa uandae misosi na vinywaji vya maana, sio kuonja onja kama hivi" BQ alitania huku akitabasamu,



"Hilo nalo neno, hiyo inakuja ila baada ya urais, bado ahadi yangu ya kuwafanyia kitu kikubwa ipo pale pale, mmefanya kazi nzito sana na ni lazima niwalipe kwa kila akili mliyotumia kuniingiza madarakani" Tammy Semmy aliongea na kugida kinywaji,



"Na ni ipi hatma ya Tom baada ya wewe kuuchukua urais?" BQ alihoji,



"Hiyo tutaongea kesho, si unajua si vizuri kutoa maamuzi wakati ukiwa na furaha sana au huzuni" Tammy Semmy alijibu huku akiendelea kucheza,



"Naomba nikae, nyie endeleeni kucheza" BQ aliongea,



"Pumzika tu mama, kazi kubwa umefanya" Tammy Semmy aliongea na BQ akaenda kukaa huku akiwa na tabasamu pana kinywani mwake na kuyafanya meno yake meupe yazidi kupendeza zaidi.



Baada ya dakika kadhaa za mziki kupigwa pale sebuleni, Tammy Semmy aliusimamisha mziki, na kuwataka vijana wake wakae sasa,



"Narudia tena kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya, kesho asubuhi kila mtu nitamuwekea kiasi kidogo cha pesa kwenye account yake ili mkajipongeze na familia zenu" Tammy Semmy aliongea kwa furaha,



"Na mimi nisie na familia?" BQ aliuliza kwa utani,



"Utajua mwenyewe ni kipi ufanye, kamchukue Tom ukatumie nae, maana naona mnapendeza sana mkiwa pamoja" Tammy Semmy alitania na kufanya wenzake wacheke,



"Je vipi kuhusu Tom, hawezi kupata mgawo kidogo kwa kazi alizotusaidia, kwa maana ameshiriki kwa kiasi kikubwa sana kukamilisha hivi vifo?" BQ alihoji,.



"BQ na Tom wako bwana, si nilishakuambia mama kuwa hayo tutayajadili kesho" Tammy Semmy aliongea,



"Anataka na mpenzi wake nae awe tajiri" Jimmy nae alitania na kufanya wacheke,



"Mpenzi wangu ni bunduki Jimmy" BQ aliongea kwa sauti laini huku akicheka,



"Jamani mimi sina jipya hapa, nadhani kesho ndiyo siku ambayo nitatangaza msiba wa waziri mkuu, so muda huu natakiwa niende ikulu nikajue mambo yanavyokwenda. kwa hiyo nyie kuweni huru muda huu, tutakutana kesho kwa ajili ya kupanga mambo mengine" Tammy Semmy aliongea huku akisimama na kisha akaondoka zake, akawaacha vijana wake wakiendelea kupiga story mbili tatu.



********************



KESHO ILIPOFIKA.



Koplo Mbegu hakuridhika kabisa kuondoka kwa Tom bila kumuona, akajiona ni mjinga aliyeshindwa kufanya mambo kiufasaha, kwa hiyo siku ya leo alipanga kwenda kufanya uvamizi mwingine kwa Tom, alidhamiria ni lazima amkamate Tom.



Mishale ya saa sita mchana alikuwa amefika katika kijiwe cha muuza miwa alichokuwa amekaa siku iliyopita.



"Dogo Tom hujamuona akitoka leo?" Koplo Mbegu alimuuliza muuza miwa baada ya kumaliza kusalimiana,



"Leo sijamuona akitoka kwa kweli" Kijana muuza miwa alijibu,



"Jana ulimuona wakati akirudi?" Koplo Mbegu akamtupia swali jingine,



"Kwani wewe hukumuona?" Kijana akamtupia swali Koplo Mbegu,



"Sijamuona mpaka wakati naondoka" Koplo Mbegu alijibu,



"Acha utani bro, au humjui Tom?" Kijana aliuliza huku akimshangaa,



"Namjua, tena vizuri tu. Kwani vipi?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Sasa jana kabla hujaondoka kwa Tom, nilimuona akiingia" Kijana aliongea na kumfanya Koplo Mbegu acheke,



"Acha utani wewe, sasa mbona mimi sijamuona?" Koplo Mbegu akauliza,



"Ndio maana nikakuuliza au humjui Tom?" Kijana akaongea huku akimuangalia Koplo Mbegu,



"Kwa hiyo unataka kusema wakati naondoka jioni ile, Tom alikuwa ameingia ndani?" Koplo Mbegu akauliza huku akiwa bado na mshangao,



"Ndio, tena muda ule ule uliotoka ndio yeye alikuwa ameingia, nikajua mmeshaonana" Kijana alimueleza Koplo Mbegu,



"Sawa, je Tom uwa anatoka saa ngapi nyakati za asubuhi?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Anatoka saa nne au saa tano, ila leo sijamuona akitoka, atakuwa bado yupo ndani" Kijana alijibu,



"Basi acha nikamuone" Koplo Mbegu aliongea huku akiwa anaondoka.



"Inawezekana hata Tom mwenyewe hamjui, atakuwa polisi huyu. Shauri zao bwana" Kijana muuza miwa aliongea na kuchukua kisu chake na kuendelea kukata vipande vya miwa na kuviweka kwenye mifuko laini.



Koplo Mbegu alielekea moja kwa moja mpaka kwenye nyumba anayoishi Tom, akafungua geti na kuingia moja kwa moja mpaka alipoufikia mlango wa Tom, akaukuta umerudishiwa na ndala zikiwa mlangoni, hakuona sababu ya kugonga hodi, akausukuma mlango kwa nguvu na kuingia ndani, alichokutana nacho hata hakuamini macho yake.............







Koplo Mbegu alikuta chumba cheupe kabisa, yaani hakuna kitanda, kochi wala runinga. Yaani kifupi alikuta kapeti peke yake, tena iliachwa kwa kuwa ilikuwa imechoka tu.



Koplo Mbegu akaona kama miujiza au amekosea chumba, akatoka nje na kuangalia vizuri,



"Hataah, ni hapa hapa wala sijakosea" Koplo Mbegu aliongea peke yake na kurudi tena ndani na akakuta hali ile ile kama aliyokutana nayo mwanzo, ikabidi atoke tena nje na kwenda kugonga kwenye chumba kinachoangaliana na chumba cha Tom, akatoka yule kijana wa jana ambaye ndiyo aliyemfukuza chumbani kwa Tom,



"Habari yako bwana" Koplo Mbegu alimsalimia,



"Safi, karibu" Kijana alijibu huku akiwa amesimama mlangoni,



"Huyu bwana imekuaje? mbona nimekuta chumba kitupu?" Koplo Mbegu aliuliza huku akitupia macho kwenye mlango wa Tom,



"Huyu amehama jana usiku" Kijana alijibu,



"Amehamaje sasa ghafla ghafla namna hiyo?" Koplo Mbegu aliuliza huku akionekana amepaniki,



"Hata sisi wenyewe tulishangaa" Kijana alijibu,



"Alisema anahamia wapi?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Hakusema, ila alisema leo anaweza kuja kutuambia alipohamia" Kijana alijibu,



"Dah, huyu fala mjanja sana" Koplo Mbegu aliongea peke yake,



"Kwani hajakwambia anapohamia? wewe si ulisema ni ndugu yako?" Kijana aliuliza huku akimshangaa,



"Kiukweli Tom sio ndugu yangu, ila nikuweke wazi tu, Tom ni muharifu na anatafutwa na polisi" Koplo Mbegu aliongea na kumfanya kijana ashtuke,



"Haiwezekani bwana, Tom ni Muandishi wa habari, huo uharifu ameuanza lini?" Kijana alibisha huku akitabasamu,



"Kijana mimi ni polisi na najua ninachokifanya, nina ushahidi wa kutosha juu ya makosa ya Tom na jana nilikuja kumkamata ila alinipiga chenga na nadhani hicho ndicho kilichomsababisha ahame usiku" Koplo Mbegu aliamua awe muwazi,



"Aisee unanipa habari ngeni sana, hata siamini yaani" Kijana aliongea huku akishangaa,



"Ebu nipe namba ya simu anayoitumia sasa hivi kwa maana zile za zamani hazipatikani" Koplo Mbegu aliongea huku akiitoa siku mfukoni,



"Kiukweli sina namba ya Tom, ila ukiniachia yako itakuwa vizuri zaidi ili akija au nikimuona sehemu nikupe taharifa" kijana aliongea huku akiitoa simu yake mfukoni, Koplo Mbegu akamtajia namba yake na yule kijana akainakiri kwenye simu yake,



"Aisee ningelijua jana jambo hilo mbona ingekuwa rahisi kumkamata, sema jana hukuwa muwazi" Kijana alimwambia Koplo Mbegu,



"Unajua hizi kazi zetu inabidi tuzifanye kiujanja ujanja ili iwe rahisi kumpata mtuhumiwa wa kesi kubwa kama hizi" Koplo Mbegu aliongea,



"Kesi kubwa? kwani amefanyaje?" Kijana aliuliza huku uoga ukimuingia,



"Akipatikana utajua tu alichokifanya, hata nisipokuambia mimi basi vyombo vya habari vitatoa habari zake" Koplo Mbegu alijibu,



"Inaelekea amefanya ishu kubwa sana, nigusie kidogo" Kijana alisihi,



"Nimeshakwambia utajua tu, usiwe na pupa" Koplo Mbegu aliongea huku akianza kuondoka,



"Sawa braza, sasa braza kabla hujaondoka ebu nisaidie buku" Kijana aliongea huku akijikuna kidevu na kufanya Koplo Mbegu atabasamu na kuingiza mkono mfukoni kisha akatoa noti ya shilingi elfu moja na kumpatia,



"Sasa usisahau, ukimuona Tom nipigie" Koplo Mbegu alimaliza na kuondoka zake na kumuacha yule kijana akimtazama tu namna Koplo Mbegu anavyompotea machoni.



"Ndio maana siku hizi ana hela nyingi, kumbe ni jambazi, kweli kuwa uyaone, yaani Tom jambazi?" Kijana aliongea peke yake na kusikitika, kisha akaingia chumbani kwake huku pesa aliyopewa akiwa ameishika mkononi.



Kabla hajakaa hata nusu saa akasikia viatu vya kike vikitembea kwenye korido na kuishia kwenye mlango wa Tom, na kisha akasikia sauti ya mwanamke ikibisha hodi kwenye mlango wa Tom, Kijana akatoka na kusimama mlangoni kwake na kumuangalia huyo mwanamke anayegonga hodi, alikuwa ni BQ,



"Dada huyo mtu hayupo, amehama" Kijana aliongea bila hata salamu na kumfanya BQ amgeukie,



"Amehama? lini?" BQ aliuliza kwa mshangao,



."amehama jana usiku, tena ghafla tu hakuna hata mtu aliyemtaharifu, tulishangaa fuso inapaki nje ya geti na akaanza kutoa vitu vyake" Kijana alimjibu BQ ambaye alionekana kuchanganyikiwa zaidi ya Koplo Mbegu,



"Unapajua alipohamia?" BQ aliuliza,



"Hamna anaepajua" Kijana alijibu,



"Sasa mbona kahama ghafla hivyo, au alitibuana na mwenye nyumba?" BQ aliendelea kuuliza,



"Kwani Tom ni nani yako?" Kijana alimuuliza BQ,



"Ni mpenzi wangu, kwani hunionagi nikija hapa?" BQ alijibu huku akijaribu kumsoma huyo kijana,



"Alikwambia anafanya kazi gani?" Kijana aliuliza,



"Maswali yote hayo ya nini? mimi nimekuuliza hajatibuana na mwenye nyumba?" BQ aliuliza,



"Hayo maswali ninayokuuliza yajibu, maana mwisho ndio kunauwezekano wa kupatikana sababu ya Tom kuondoka hapa ghafla. Haya niambie alikwambia anafanya kazi gani?" Kijana aliuliza,



"Aliniambia ni Muandishi wa habari" BQ alijibu,



"Sasa kwa taharifa yako Tom sio Muandishi wa habari, Tom ni jambazi" Kijana aliongea na kufanya BQ apate mshtuko wa wazi, huku akijiuliza ni kwanini huyo kijana aseme hivyo,



"Mpenzi wangu sio jambazi, wewe nani amekuambia?" BQ aliuliza kwa sauti iliyoambatana na kilio utasema ana uchungu kumbe anaigiza ili kumchimba zaidi yule kijana,



"Wanawake mkishapenda mnakuwa vipofu. Kuna askari alikuja kumtafuta Tom hapa, ilikuwa jana, Tom akamkimbia na jana usiku ndipo Tom alihama baada ya kugundua anatafutwa. Na kwa bahati nzuri huyo askari amekuja na leo ndio amenipa hii taharifa ninayokupa hapa" Kijana aliongea na kufanya moyo wa BQ upasuke zaidi,



"Polisi?, kwa hiyo Tom anatafutwa na polisi?" BQ aliuliza na hili swali lilimtoka moyoni,



"Ndio, tena huyo polisi amesema popote nimuonapo Tom nimpe taharifa" Kijana alimalizia na kutaka kurudi ndani,



"Ngoja basi, huyo polisi amekupa namba yake ya simu?" BQ aliuliza kwa upole huku akiwa ameushika mkono wa yule kijana,



"Sasa nitawasiliana nae vipi kama hajanipa namba ya simu?" Kijana aliuliza,



"Basi nipe hiyo namba ili niwasiliane nae anipe taharifa iliyokamilika" BQ aliongea kwa kusihi,



"Nipe elfu tano nikupe hiyo namba" Kijana aliongea huku akimuangalia BQ,



"Kaka unaniuzia namba ya simu?" BQ alihoji huku akitoa tabasamu la karaha,



"Wewe si una shida nayo, toa pesa nikupe namba" Kijana aliongea huku akifurahi kwa namna anavyomuendesha mtoto huyo wa kike,



"Shika hii hapa" BQ aliongea huku akimpatia elfu kumi yule kijana,



"Unatakiwa uwe na moyo mzuri kama sura yako" Kijana aliongea huku akipokea ile pesa na kisha akampa BQ namba ya Koplo Mbegu.



"Anaitwa nani?" BQ aliuliza huku akitaka aihifadhi ile namba,



"We andika unavyojua wewe, andika hata polisi" Kijana aliongea huku akimuangalia BQ,



"Asante kaka yangu, nakushukuru sana" BQ aliongea huku akianza kuondoka,



"Usijali Dada, siku nyingine uwe unakuja na kwangu, maana Tom ameshaondoka kwa hiyo nipe nichukue nafasi yake" Kijana aliongea kwa utani huku akimuangalia BQ anavyopiga hatua zake za haraka haraka.



BQ alienda mpaka kwenye gari yake na kuingia ndani ya gari na kukaa,



"Huyu kijana anasema Tom ni jambazi na anatangaza hovyo, sasa kama huyo askari akija tena na akamtaka huyu kijana amtaje mtu wa karibu wa Tom si atanitaja mimi? atakuwa amenitafutia matatizo, huyu kijana hatakiwi kuishi, kifo ndio haki yake" BQ aliwaza na kisha akatoa bastola yake aliyoiweka ndani ya gari, akashuka na kurudi ndani, alidhamiria kumuua kijana wa watu, BQ mnyama aliamua kutenda hivyo.



Alienda mpaka kwenye mlango wa yule kijana, alipofika akavuta pumzi ndefu kisha akagonga mlango.......



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Baada ya BQ kugonga mlango, ulifunguliwa na yule kijana na kusimama mlangoni, hakuna aliyemuongelesha mwenzake na badala yake wakawa wanatazamana tu,



"Vipi mbona unagonga hodi alafu unanitazama tu, kuna shida?" Kijana alimuuliza BQ,



"Hapana, nilisahau kukuuliza jina lako" BQ aliuliza huku akitabasamu,



"Yaani ndicho kilichokurudisha hicho?" Kijana aliuliza huku akicheka,



"Kilichonirudisha sicho hicho, ila kwanza ningependa kujua jina lako" BQ aliongea huku tabasamu likifutika usoni mwake,



"Ooooh naitwa Pholly Magai" Kijana alijibu huku akitabasamu,



"Asante, ninaweza kurudi tena baadae" BQ aliongea na kuondoka zake na kumuacha kijana akirudi zake ndani.



BQ aliamua kubadilisha maamuzi yake ili ajaribu kumpata askari anayemtafuta Tom, na aliona njia nzuri ya kumpata huyo askari ni kumtumia huyo kijana kwa maana aliona huyo kijana amejenga uhusiano kidogo na huyo askari.



BQ alipanda gari lake na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu huku akiwaza upuuzi aliofanya Tom, upuuzi wa kukimbia wakati alishamuhakikishia usalama wake dhidi ya kundi hilo la waovu.



"Hapo Tom atakuwa amejitaftia kifo chake mwenyewe, na huyo askari akigundulika ni lazima afe, Hawa ndio kunguni wanaoishi kwa kujificha chini ya godoro na kutoka kipindi watu wakiwa hawana habari nao" BQ aliwaza huku akiingia kwenye Barabara kubwa ya kumfikisha kambini kwao.



Alitembea mwendo wa nusu saa na kufika kambini kwao, alifika huku akiwa na mawazo tele, hata wenzake waliliona hilo kutokana na lile tabasamu lake linaloonekana muda wote, kutokuwepo muda huo, alifika na kwenda moja kwa moja kwenye friji na kuchukua maji ya baridi na kuyagida yote, alipomaliza aliuma meno yake kwa nguvu kutokana na meno yake kushindwa kuhimili lile baridi la maji, baada ya hapo akawasalimu wenzake na kukaa juu ya kochi,



"Vipi mdada, upo sawa kweli?" Jimmy alimuuliza BQ,



"Sipo sawa kwa kweli, kuna shida kubwa imejitokeza" BQ aliongea na kufanya wenzake wapate shahuku ya kutaka kujua ni kipi kilichotokea,



"Nini tena au ndio mabalaa yameanza?" Waziri wa ulinzi aliuliza kwa hofu,



"Tom, Tom amekimbia na pia kuna polisi anamtafuta Tom" BQ alitoa habari ya kutisha,



"Amekimbiaje?" Gabby aliuliza,



"Nyumba anayoishi amehama na haijulikani alipohamia" BQ aliongea,



"Sasa labda alikuwa anamkimbia huyo polisi, na sisi huku tunatakiwa tungoje labda anaweza kuja yeye mwenyewe kutuambia" Jimmy aliongea kwa kujipa matumaini,



"Simu zake hazipatikani na hata kwenye rada zangu nimeshindwa kumpata mtandaoni" BQ aliongea na sauti yake ilikuwa imepoa,



"Inawezekana ni kweli ametukimbia, ila kama angekuwa anataka kutukamatisha si angejisalimisha kwa huyo askari? mimi nadhan hana ubaya na sisi" Jimmy aliendelea kumtetea Tom,



"Hapana, huyo Tom endapo atakamatwa na kubanwa vizuri na askari, ni lazima Tom atatutaja.



Tom inatakiwa apatikane na afe, haina haja ya kuishi na presha hivi, Tom hana umuhimu kwetu kwa muda huu" BQ aliongea kwa hasira,



"Ni bora afe tu" Gabby alipigilia msumari wa mwisho,



"Najua Tammy Semmy atakataa tu tukimshauri Tom auawe" Jimmy aliongea,



"Huyu atafutwe na auawe kimya kimya, Tammy Semmy atapewa taharifa za kifo tu" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Basi hiyo kazi ya kumtafuta ianze leo, nendeni sehemu zote zenye mitandao yetu na waanze kumtafuta kwa kila njia, atapatikana tu na auawe" BQ aliongea na kurudi kwenye friji na kutoa juisi ya box na kurudi nayo kwenye kochi,



"Nini kinafuata muda huu, au tumsubiri Tammy Semmy labda ana mpya?" Jimmy aliuliza,



"Hakuna haja ya kusubiri mtu hapa, nyie wawili mtawanyike na mkasambaze hizo habari ndani ya watu wetu wa usalama wa taifa na ofisi zote zinazotuhusu" BQ aliongea na wenzake hawakuwa na cha kusubiri, wakaondoka kila mtu na gari yake na wakaenda kusambaza huo ujumbe.



"Mimi nitamtafuta mtaani tu, maana sijawahi kufanya kazi usalama wala hakuna taasisi ya ulinzi inayonijua" BQ aliongea na kuigida ile juisi,



"Tom ana balaa sana, haogopi kufa?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Nilishaanza kujenga imani naye, ila kwa tukio hilo ni wazi amenivuruga" BQ aliongea na kujilaza juu ya kochi,



"Ila tujaribu kumpa nafasi nyingine, huenda baadae atakuwa pamoja na sisi" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Hiyo kitu hamna mkuu, mimi nikikutana nae namuua tu" BQ aliongea huku akimaanisha anachokiongea,



"Sawa, basi acha mimi nikajipumzishe kidogo, wewe si bado upo hapo?" Waziri wa ulinzi aliuliza huku akinyanyuka kwenye kochi,



"Mimi sieleweki, muda wowote napotea" BQ alijibu,



"Ukiondoka funga mlango kwa nje" Waziri wa ulinzi aliongea huku akiondoka,



"Sawa" BQ alijibu na Waziri wa ulinzi akaenda zake chumbani kulala na kumuacha BQ akiwa amejilaza juu ya kochi.



********************



Koplo Mbegu alipotoka kwenye nyumba anayoishi Tom hakutaka kuamini kabisa kama ni kweli Tom amehama, alichofanya ni kwenda kwenye kijiwe cha yule kijana muuza miwa na kuangalia watu wanaoingia na kutoka kwenye ile nyumba.



Baada ya muda ndipo alipomuona BQ nae akiingia pale, Koplo akajisogeza na kujipenyeza ndani ya nyumba na akawa anasikia kila neno walilokuwa wanaongea kati ya BQ na yule kijana.



Koplo hakutaka kuwaingilia, wakati BQ anaaga, Koplo Mbegu akaondoka na kurudi kukaa kwenye kijiwe cha miwa na kukaa, ndipo alipomuona BQ akirudi ndani ya gari na baada ya muda tena alimuona BQ akirudi ndani ya nyumba, tena baada ya muda akamuona BQ alirudi tena ndani ya gari na kukaa kwa muda, alionekana amechanganyikiwa kabisa, baadae aliwasha gari na kuondoka. Koplo Mbegu aliyashuhudia hayo yote akiwa kwenye kijiwe cha kijana muuza miwa.



********************



Tom aliamua kuondoka na akachagua kuwa mkimbizi, hakutaka kuwaamini polisi tena na wala hakutaka kuwa chini ya utumwa wa Tammy Semmy, aliamua kuwa kivyake na akili zake.



Vyombo alivyovichukua kwake alivisafirisha moja kwa moja mpaka kwa wazazi wake morogoro na yeye akaamua aendelee kupambana hapa hapa, hakutaka hata kusafiri kwa kuwa aliogopa kuwa Tammy Semmy ana mtandao mkubwa mpaka kwa wafanyakazi wa usafiri wa ndege.



Tom alichoamua ni kuangalia namna ya kufika moja kwa moja kwa mkuu wa idara ya usalama wa Taifa, alitumia njia zote siku hiyo mpaka akafanikiwa kukutanishwa na mkuu wa idara hiyo ya usalama wa Taifa, akaingizwa ofisini,



"Una shida gani kijana?" Mkuu wa usalama aliuliza huku akimuangalia Tom,



"Kwanza kabisa unatakiwa kujua mimi nimejitoa mhanga na sijali lolote kuhusu kufa, kuna habari nyeti ninataka kukwambia kuhusu vifo vya rais na Waziri mkuu" Tom aliongea huku sauti ikiwa kavu kabisa,



"Unaitwa nani kwanza?" Mkuu wa usalama alimuuliza,



.



"Naitwa Thomas Anthony" Tom alijibu,



"Ebu nisubiri kidogo nje ntakuita, inaonekana una jambo muhimu sana" Mkuu wa usalama aliongea na Tom akatoka na kukaa nje ya ofisi, mkuu wa usalama akampigia simu kijana wake mmoja na kuingia ofisini,



"Unamuona huyo kijana aliyekaa hapo, mpelekee supu ya kuku na soda" Mkuu wa usalama alimuagiza yule kijana na kisha akafanya kama alivyotumwa.



Tom akapelekewa supu na soda, akawa anashangaa kwa namna anavyokirimiwa kiasi kile, akaamini huenda ni kutokana na taharifa nyeti aliyoipeleka pale.



Ndani ya ofisi mkuu wa usalama alichukua simu na kumpigia Gabby,



"Tom yupo hapa ofisini kwangu, mfanye haraka mje kumchukua" Mkuu wa usalama aliongea na kukata siku kisha akamuita Tom aingie ndani ya ofisi,



"Haya nieleze kijana, ni kipi unachokijua kuhusu kifo cha rais?" Mkuu wa usalama alimuhoji Tom na Tom akaeleza mwanzo mpaka mwisho,



"Kwa hiyo na wewe ulihusika katika kumuua rais?" Mkuu wa usalama aliuliza,



"Sikuhusika ila nilikuwa nashuhudia chini ya shinikizo la Tammy Semmy na watu wake, ipo video ambayo hilo tukio linaonekana vyema" Tom alijibu,



"Hiyo video anayo nani?" Mkuu wa usalama aliuliza,



"Huyo mtu hata simjui, ni mtu wa ajabu sana, ila hiyo video hata Tammy Semmy aliwahi kuiona na anamtafuta huyo mtu bila mafanikio yoyote" Tom aliongea na wakati huo huo simu ya Mkuu wa idara ya usalama ilikuwa ikiita na akaipokea, akaongea kidogo na kukata simu.



"Ebu ningoje kidogo, kuna watu wameniita nje, usiondoke, nisubiri" Mkuu wa usalama aliongea na kutoka nje, simu akaiacha mezani.



Mkuu wa usalama akatoka mpaka nje kabisa ya jengo la ofisi na kumkuta Gabby akiwa amesimama nje,



"Kumbe ni jengo hili ndipo ofisi yako ilipohamishiwa? mimi nilienda lile jengo nililolizoea" Gabby aliongea,



"Kule nilishahama muda kidogo" Mkuu wa usalama alijibu,



"Nadhani twende ndani nikamchukue huyo mwendawazimu" Gabby aliongea,



"Hii ni hatari Gabby, huyu kijana kama amefikia hatua hii ya kutaka kutafuta sehemu ya kusemea haya mambo, hii kitu inaweza kutusababishia matatizo" Mkuu wa usalama aliongea,



"Ndio maana tunataka tumuue, hilo jambo usimwambie Tammy Semmy, huyu dogo tutamuua kimya kimya" Gabby aliongea huku wakiwa wameukaribia kabisa mlango wa ofisi ya Mkuu wa usalama,



"Ngoja mimi nitangulie kuingia, alafu wewe utafuata baada ya dakika moja" Mkuu wa usalama aliongea huku akifungua mlango wa ofisi yake................





Mkuu wa usalama alipoingia ndani hakumkuta Tom, yeye mwenyewe akashangaa huku asijue kilichotokea. Mkuu wa usalama akafungua mlango na kumwambia Gabby aingie,



"Ameondoka aisee" Mkuu wa usalama aliongea kwa sauti iliyonyong'onyea,



"Ameenda wapi tena? kama ametoka si tungekutana nae njiani?" Gabby aliuliza,



"Ebu wahi getini kabda hajatoka" Mkuu wa usalama alimwambia Gabby na kisha Gabby akatoka nje kwa mwendo wa kasi mpaka getini, lakini hakukuta mtu,



"Nyie hamjamuona kijana mweusi amepita hapa?" Gabby aliwauliza watu wa ulinzi wa getini,



"Anaitwa nani?" Mlinzi mmoja aliuliza huku akifunua daftari wa watu waliongia na kutoka ndani ya jengo hilo,



"Tom, Thomas Anthony" Gabby alijibu na kisha yule mlinzi akatafuta hilo jina na kuliona,



"ndio mtu wa mwisho kutoka hapa, nadhani ameondoka na bodaboda aliisimamishia hapo getini" Mlinzi aliongea baada kuliona jina la Tom,



"Muda mrefu?" Gabby aliuliza,



"Sasa hivi tu hata dakika tano hazijapita" Mlinzi alijibu,



"Kaelekea kushoto au kulia?"Gabby aliulza,



"Kulia" Mlinzi alijibu,



Gabby akaenda kwenye gari alilokuja nalo, akapanda na kuondoka kwa mwendo wa kasi kufuata uelekeo ambao aliambiwa kuwa Tom ameelekea.



Gabby akatoa simu yake na kumtaharifu mkuu wa usalama kuwa anamfuatilia Tom ambaye ametoka nje ya lile jengo muda si mrefu.



Gabby alikuwa anaendesha gari kwa mwendo usiokuwa wa kawaida, alijitahidi kuisogelea kila bodaboda iliyokuwa mbele yake na kuikagua lakini hakufanikiwa kumpata Tom, alijikuta anazunguka zunguka tu mjini bila mafanikio yoyote na mwisho akaamua kugeuza huku akiamini mkuu wa usalama amefanya uzembe kutoka nje na kumuacha Tom ndani akiwa peke yake. Kwa Mara nyingine Gabby alifeli kufanikisha kumpata Tom.



******************



Kipindi chote wakati Tom akijiuliza ni kwanini anafanyiwa ukarimu mkubwa ndani ya ofisi ile kiasi cha kununuliwa supu ya kuku, ndicho kipindi hicho hicho akili yake iliongeza umakini na tahadhari juu ya ukarimu huo.



Na alipoambiwa aingie tena ndani ya ofisi ya mkuu wa usalama, aliingia huku akiwa tofauti kabisa na mwanzo, safari hii alikuwa anajaribu kumsoma Mkuu wa usalama kwa kila anachokiongea huku wasiwasi ukiongezeka zaidi kwa maana kila amuelezeapo mkuu wa usalama juu ya matukio yale ya mauaji, Mkuu wa usalama hakuonekana kutilia sana maanani ila alionekana akifikiria mambo yake.



Na muda ule wakati mkuu wa polisi alikuwa akiongea na simu, Tom alijaribu kuhisi ni nani anayeongea na mkuu wa polisi na huyo mtu kupitia maongezi ya simu alionesha kuwa amepotea ofisi ya mkuu wa usalama, sasa mkuu wa usalama alichokosea ni kuondoka na kuiacha simu mezani.



Mkuu wa usalama alipotoka tu, Tom aliichukua simu ya mkuu wa usalama na kuangalia jina la mpigaji na kukuta limenakiliwa kwa jina la "KIJANA WA TAMMY SEMMY" roho ya Tom ikapata mshtuko, akaamini mkuu wa usalama amemzunguka, akaamini mkuu wa usalama ni mmoja wa watu wabaya wanaoshirikiana na Tammy Semmy.



Tom akatoka haraka ndani ya ofisi ile, na wakati akielekea nje alimuona kwa nje mkuu wa usalama na Gabby wakiongea kwa furaha huku wakicheka na walikuwa wanatembea kuingia ndani ya ofisi zile, Tom ikabidi arudi na kuingia kwenye ofisi nyingine na kujifanya kumuulizia mtu ambaye watu waliopo ndani ya ile ofisi aliyoingia walionekana kutomjua huyo mtu aliyeuliziwa na Tom, akajidai kuelekeza lakini bado watu hao hawakuonekana kumjua.



Tom akatoka nje na akakuta tayari mkuu wa usalama na Gabby wamekwishapita, na yeye hakufanya hajizi, aliondoka kwa mwendo wa haraka mpaka getini na kusaini kitabu cha watu wanaotoka na kuondoka mpaka nje ya geti na kusimamisha bodaboda kisha apanda na kuondoka zake, alipofika mbele kidogo alishuka kwenye bodaboda na kumlipa dereva wa bodaboda na kisha akatafuta bajaji na kupanda, akaenda sehemu ambayo aliichagua kuwa maficho yake kwa muda ambao anatafutwa na polisi na kikosi cha Tammy Semmy.



******************



Gabby alirudi kambini kwao huku akionekana hana furaha kabisa, na pia uso wake ulionesha hasira za wazi kabisa,



"Vipi, mbona hujarudi na Tom?" Jimmy alimuuliza,



"Leo kwa Mara ya kwanza lazy ametuzidi akili" Gabby alijibu huku akivua shati na kufanya kifua chake kipana kama meza ya kioo kionekane vizuri,



"Amewazidi vipi sasa?" BQ aliuliza kwa hasira huku akiamka kwenye kochi kwa maana alikuwa amelala, Gabby akawaeleza kila kitu kilivyokuwa,



"Ni upumbavu, yaani wewe na uzoefu wako wote huo Tom amekuacha kizembe hivyo?" BQ alihoji kwa hasira,



"Usisepe upumbavu sasa, mazingira ambayo nahisi ametumia kutukimbia si nimewaambia?" Gabby aliongea huku akionesha kutofurahishwa na kauli ya BQ,



"Umekuwa mpumbavu sana, lazima nikuambie ukweli" BQ aliendelea kukazania kauli yake,



"Black nitakupiga ujue, naona unazid kuvuka mipaka tu" Gabby aliongea kwa hasira huku akimnyooshea kidole BQ, sasa hapo BQ akatabasamu,



"Siku ukijaribu kunifanyia shambulio lolote ndipo siku utakayojua kifo kiko katika umbile la namna gani" BQ aliongea kwa dharau huku akicheka,



"Analeta dharau huyu, namuheshimu ila aheshimiki" Gabby aliongea huku akisimama na kuanza kupiga hatua kumfuata BQ aliyekuwa amekaa huku akimuangalia Gabby namna anavyomfuata na pia alikuwa akitabasamu,



"Ebu acheni mvurugano, tulieni" Jimmy aliongea huku akimzuia Gabby asimfuate BQ,



"Tukianza kukinzana wenyewe kwa wenyewe hapa hatutafikia malengo" Waziri wa ulinzi aliongea huku Gabby akikaa chini,



"Sikieni, hapa nimeifuatilia ile namba ya huyo polisi anayemtafuta Tom, nimegundua anaitwa Said, Said Mbegu" BQ aliongea na kumtazama Jimmy aliyeonekana kushtuka,



"Kwani yule tuliyemuuaga anaitwa nani?" Jimmy aliuliza,



"Koplo Mbegu, inawezekana wana undugu?" Gabby aliuliza huku akionekana hasira zimemshuka,



"Hawana undugu, ni mtu mmoja kwa maana hata nyumba anayokaa ni ile ile mliyoenda kumuulia" BQ alijibu na kumeza mate,



"Kwa hiyo inawezekana siku ile hakufa?" Jimmy aliuliza,



"Hakuna anaejua, inawezekana ni upumbavu uliotokea leo ndio mlioufanya wakati mnaenda kumuua" BQ alijibu na Gabby akawa anatabasamu tu, hakutaka kuleta usumbufu tena kwa maana alijua BQ ameamka kishari,



"Inabidi afe, ila tufanye uchunguzi wa kutosha kabla hatujamuua" Jimmy alijibu,



"Uchunguzi wa nini? huyo polisi anatakiwa afe, maana inawezekana anatufuatilia hata sisi" BQ aliongea,



"Tena kama inawezekana afe hata leo" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Kwa hiyo twende tukamfanyie uchunguzi muda huu juu ya chumba anachokaa na pia tujue ni yule wa hawali au huyu ni mwingine?" Jimmy aliongea kwa mtindo wa kuuliza,



"Hicho ndicho cha kufanya muda huu" BQ alijibu na kisha Gabby na Jimmy wakatoka na gari mpaka kwenye mtaa anaoishi Koplo Mbegu na kusimamisha gari jirani na nyumba anayoishi Koplo Mbegu na kuanza kufuatilia nyendo za wanaoingia na wanaotoka, kwa bahati nzuri waliweza kumuona Koplo Mbegu na wakajihakikisha huyu ndiye wanaemtafuta, wakajua na chumba anachoishi, wakaamini mwanzoni walikosea chumba kwa hiyo wakajua walimuua mtu mwingine.



Baada ya kujiridhisha na upelelezi wao, Gabby na Jimmy waliondoka zao kwa matumaini ya kurudi usiku kuja kukamilisha kazi yao.



**************†*******



Mishale ya saa tano za usiku, Koplo Mbegu alikuwa anaangalia runinga yake huku akitafakari namna Tom alivyotumia akili kumkimbia.



Baada ya nusu saa aliamua azime runinga ili alale, akazima na taa kwa kutumia bed switch kisha akajifunika shuka na kuanza kuuvuta usingizi.



Kabla hata usingizi haujamchukua, alihisi kuna mtu anafungua mlango wake, akaona akae kimya ili a one huyo mtu atafungua au atashindwa?



Akiwa bado anasubiria tukio hilo, aliona mlango ukifunguliwa na kisha mlango ukafungwa, Koplo Mbegu akawasha taa haraka kwa kutumia swichi ya kitandani na hapo ndipo alipowaona wanaume wawili wenye misuli wakiwa wamesimama huku wakimuangalia, wanaume hao walikuwa ni Gabby na Jimmy na wote walikuwa wakimuangalia Koplo Mbegu.....





Koplo Mbegu alikuwa anashangaa wale watu kwanini wamvamie usiku ule, ila hakupata jibu mpaka alipoiona sura ya Gabby na kumtambua kuwa huyo bwana wameshawahi kukutana kwenye viwanja vya ikulu na walitaka kupigana kisa Tom, sasa Koplo Mbegu akajiuliza tena ule ugomvi wa siku ile ndio umesababisha avamiwe usiku huu?



"Unashangaa nini Said Mbegu?" Jimmy aliuliza huku akitabasamu,



"Nashangaa kwanini mmenivamia?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Unamjua Thomas Anthony?" Jimmy aliuliza,



"Ndio namjua na anatafutwa na polisi" Koplo Mbegu alijibu,



"Kwanini anatafutwa?" Jimmy aliuliza,



"Anahusika na kifo cha Waziri Mkuu" Koplo Mbegu alijibu na kufanya Gabby na Jimmy waangaliane,



"Maswali yanapoteza muda, Kata mti tusepe" Gabby aliongea na Jimmy akachomoa bastola yake na kumuelekezea Koplo Mbegu na kufanya Koplo Mbegu ashangae zaidi,



"Wewe Jamaa si upo usalama wa Taifa, unaniua badala ya kunilinda?" Koplo Mbegu aliuliza huku akimtazama Gabby,



"Ulitakiwa ufe siku nyingi tu, Sema tulivyokuja Mara ya kwanza tulikosea chumba na tukamuua mtu mwingine badala yako" Gabby alijibu na kufanya Koplo Mbegu akumbuke kile kifo cha yule kijana mbeba maji wa chumba cha jirani yake kumbe ndio kilikuwa kifo chake,



"Kwanini mnaniua?" Koplo Mbegu aliuliza,



"Jimmy Fanya mambo, tuokoe muda" Gabby aliongea na Jimmy akawa anajiandaa kumfyatulia risasi Koplo Mbegu ambaye alikuwa kitandani akiangalia namna kifo chake kinavyokuja, ghafla taa za chumbani zikazimika, Jimmy akafyatua risasi kama tatu mfululizo kuelekea sehemu alipokuwa amekaa Koplo Mbegu, kisha taa zikawaka na kukuta matundu ya risasi tu juu ya kitanda na Koplo Mbegu hakuwepo na mlango ulikuwa upo wazi, Gabby akachungulia nje wala hukuona dalili ya kuwepo mtu, wakaangalia chini ya kitanda pia hakuona mtu.



"Tuondoke" Gabby aliongea huku akitangulia nje na Jimmy akafuata, safari yao iliishia ndani gari wakapanda na kuondoka,



"Inawezekana huyu polisi ndo yule mzimu, yaani haiwezekani apotee ghafla namna ile" Jimmy aliongea,



"Hakuna kitu kama hicho, wewe mwenyewe ulileta maswali mengi badala ya kutimiza tendo" Gabby aliongea,



"Ila tutampata tu" Jimmy aliongea,



."tatizo sio kumpata, tatizo ameshatujua wabaya wake na mbaya zaidi anajua sisi ni wafanyakazi wa wapi?" Gabby aliongea,



"Kweli nimefanya uzembe" Jimmy aliongea kwa sauti ndogo,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Sasa tusubiri maneno ya kashfa kutoka kwa BQ" Gabby alijibu,



"Itabidi tuseme hatujamkuta" Jimmy aliongea,



"Mimi sitoongea hata neno, itabidi wewe ndio uongee" Gabby aliongea,



"Sawa, utaniachia mimi" Jimmy alikubali na ukimya ukachukua nafasi yake.



*****************





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog