Simulizi : Fumbo La Utambuzi
Sehemu Ya Tatu (3)
Asubuhi ilimkuta Tom akiwa amelala n
Kwa maana usiku wote hakupata hata lepe la usingizi, akiwa amejikunyata kwenye kona moja ya chumba, mlango ulisukumwa na mwanga ukampiga machoni na alijitahidi kuuzuia ule mwanga kwa kufunika macho yake na viganja vya mikono yake.
"Njoo huku" Jimmy aliongea huku akielekea sebuleni na Tom akamfuata nyuma mpaka sebuleni ambapo Tom alikuta kuna chai mezani.
"Kunywa chai" Jimmy alimwambia Tom lakini Tom hakuwa na hamu hata ya hiyo chai kwa hiyo akabaki anavitazama tu vikombe vilivyopo mezani.
Hakuna aliyemjali kila mtu alikuwa bize na mambo yake, waligutushwa na sauti ya mlango kugongwa,
"Kafungue ila tumia kitambaa ili fingerprints zilizopo hawali zisipotee" Gabby alimwambia Jimmy huku akimtupia kitambaa cheupe, Jimmy akakidaka na kwenda kufungua mlango na Tammy Semmy na BQ wakaingia ndani,
"Vipi mbona mnatumia kitambaa kufungua mlango?" Tammy Semmy aliuliza baada ya kuingia ndani na kisha akasimuliwa yote yaliyotokea usiku uliopita kumuhusu yule mtu wa ajabu aliwatokea na kupotea kimazingara,
"Kwa hiyo sikutaka kuushika huu mlango ili tuangalie kama ni kweli alipitia mlangoni au hakupitia, kwa maana kama alipitia mlangoni alama zake za vidole ndizo zitakuwa za mwisho kuonekana" Jimmy alimaliza kutoa maelezo yake,
"BQ kalete vipimo kule kwenye chumba cha vifaa" Tammy Semmy aliagiza na BQ akaenda kuvifuata,
"Alafu mlisema kuwa huyo mtu baada ya kutokea alisema hiyo video ni yeye ndiye aliirekodi?" Tammy Semmy aliuliza,
"Ndivyo alivyosema" Gabby alijibu,
"Huyu dogo anafahamiana nae?" Tammy Semmy aliuliza huku akimuangalia Tom,
"Aisee huyu dogo nae ametoa hadithi yenye utata kidogo kuhusu huyo mtu" Jimmy aliongea kisha akasimulia yote waliyosimuliwa na Tom.
BQ alirudi na kifaa cha kupimia alama za vidole na akaelekea kwenye kitasa cha mlango kufanya vipimo vyake huku wenzake wakimuangalia.
Baada ya muda alimaliza kufanya vipimo vyake na majibu yalionesha kwenye kitasa kuna alama za vidole vya Jimmy na wote wakabaki wanashangaa,
"Hakuna hata sehemu iliyoharibiwa au kutobolewa akapita?" Tammy Semmy aliuliza huku wasiwasi ukianza kumshika,
"Tumekagua kote, hakuna sehemu ambayo tumekuta kuna tobo" Gabby alijibu,
"Ndani pia mlimtafuta kila sehemu?" Tammy Semmy aliuliza tena,
"Nyumba nzima tumemtafuta" Jimmy alijibu na kumfanya Tammy Semmy ajishike shavu huku akiwaza na kuwazua,
"Basi inawezekana tunapambana na mtu Fundi sana wa kucheza na akili za watu, na huyu ndiye anatakiwa awe adui wetu kwa sasa" Tammy Semmy aliongea kwa sauti ya upole,
"Mzee mimi si mniachie tu, kwa maana mmeshamjua muhusika wa hiyo video" Tom aliongea,
"Wewe bado una umuhimu kwetu, usiwe na shaka kwa maana hatuna nia ya kukuua" Tammy Semmy aliongea huku akiwa hamuangalii Tom,
"Mzee natakiwa nisafiri saa sita mchana wa leo" Tom aliongea kwa kulalamika,.
"Hainihusu. Hey guys natakiwa niende ikulu muda huu nikatangaze kifo cha Rais, nitarudi baadae" Tammy Semmy aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,
"Sawa bosi" Jimmy alijibu na BQ alinyanyuka na kwenda kumfungulia mlango bosi wao, Tom akaona bora atumie mwanya huo kukimbia tu, liwalo na liwe.
Mlango ukiwa wazi na Tammy Semmy akiwa anaelekea mlangoni, Tom aliinuka na kutoka mbio kama swala, alimpiga kikumbo Tammy Semmy na kupita mlangoni mbio, ndani wote wakamahaki wakata kumkimbiza,
"Tulieni" BQ aliongea huku akiitoa kiunoni bastola yake, bastola yenyewe ilikuwa ya ajabu kama toy,
"Angalia pa kumpiga, sitaki afe" Tammy Semmy alimwambia BQ,
"Afe tu, maana anatupa presha zisizo na maana" BQ aliongea na kufyatua risasi iliyoonda moja kwa moja kukita kwenye kisogo cha Tom na Tom akaanguka chini mzima mzima kama gunia la viazi, watu wote ndani wakashika mdomo kwa maana Tom hakutakiwa kufa muda ule.......
Watu wote akiwepo Tammy Semmy walipigwa na butwaa kutokana na kitendo alichokifanya BQ, lakini BQ mwenyewe alikuwa anatabasamu tu huku akiwaangalia wenzake na kufanya wamshangae,
"Huyu hakupaswa kufa lakini" Tammy Semmy aliongea,
"Amekufa kwenye hisia zenu na wala hakufa kihalisia" BQ aliongea huku akielekea sehemu ambapo Tom aliangukia, alipomfikia alimgeuza kisha akatabasamu, akaanza kumburuta kumuingiza ndani huku wenzake wakiendelea kumshangaa.
Alipomuingiza ndani akamgeuza kisha akakichomoa kisindano kidogo kilichokuwa kisogoni mwa Tom na kufanya wenzake wacheke,
"Kumbe ulimpiga sindano ya usingizi? Mimi nilijua umeua" Jimmy aliongea huku akiendelea kucheka,
"Sasa nyie hata hamjashangaa kuwa mbona nilivyompiga risasi hakutoka damu" BQ aliongea huku akitabasamu,
"Hilo mimi nilijiuliza ila silaha uliyotumia ndiyo iliyofanya nijue umeua" Tammy Semmy aliongea,
"Hii inaitwa double barrel pistol, ina matundu mawili, moja ni kwa ajili ya risasi na jingine ni kwa ajili vitu kama hivi, sindano au goroli" BQ alijibu kwa kujiamini,
"Lakini sikumbuki kama kwenye karakana yetu tuna kitu kama hiyo" Tammy Semmy aliongea,
"Hii nilipewa Cuba na mkuu wa majeshi wa uko, ni baada ya kupata alama za juu kwenye ulengaji wa shabaha" BQ aliongea,
"Kwa hiyo dozi uliyompa huyu ni ya muda gani?" Gabby aliuliza huku akimuangalia Tom,
"Baada ya sita atazinduka, ili akute hata muda wa safari yake umeisha" BQ alijibu,
"Sawa basi, ngojeni mimi niwahi nikatangaze hilo tangazo la kifo" Tammy Semmy aliongea huku akiondoka na kuwaacha vijana wake wakiendelea na mipango mingine.
Tammy Semmy alitoka mpaka nje na kupanda gari yake, yeye mwenyewe ndiye alikuwa dereva na hakukuwa na mtu mwingine ndani ya gari. Aliendesha mpaka nyumbani kwake, akaingia na kubadili nguo kisha magari matatu yakiwa yameongozana na pikipiki za polisi yalifika na Tammy Semmy akaenda kuingia kwenye gari mojawapo ambalo katika sehemu ya namba za usajili paliwekwa nembo ya Taifa.
Msafara ule ulioongozwa na ving'ora uliishia ikulu kwenye makao ya Rais, Tammy Semmy alipoingia alielekea moja kwa moja mahali ilipo familia ya Rais na kuwapa pole, kipindi chote hicho Tammy Semmy alionekana ana huzuni sana kiasi kwamba kila muda alikuwa akitoa leso yake nyeupe na kufuta machozi yaliyokuwa yanachomoza kwenye macho yake.
Baada ya kumaliza kutoa pole kwa familia ya marehemu Rais, Tammy Semmy alielekea kwenye ukumbi wa mikutano wa ikulu na kukaa kwenye kiti sehemu ambayo uwa anakaa Rais, kipaza sauti kikawashwa.
Mbele ya meza aliyokuwa Tammy Semmy kwa mbele kuliwekwa video camera na vipaza sauti kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
"Ndugu wananchi, leo ni siku ambayo ni yenye huzuni na masikitiko makubwa kwenye Taifa letu, sipendi kusema haya ila imenibidi niwatangazie kuwa Rais wetu kipenzi hatunae tena duniani, Rais wetu amefariki, tuendelee kufuatilia habari kwa kina kupitia vyombo vya habari ili muweze kujua ni kipi chanzo cha kifo chake.
Kwa dhamana niliyopewa kama kiongozi wa nchi, natangaza kuanzia leo bendera zote zipepee nusu mlingoti kwa muda wa wiki nzima na natoa siku tatu za mapumziko kwa nchi nzima" Tammy Semmy alimaliza kuongea kisha akazima kipaza sauti na kutoa leso yake akaanza kufuta machozi, wasaidizi wake wakaja kumtoa huku wakimliwaza.
Kweli binadamu ni wanafki, yaani Tammy Semmy leo analia kwa ajili ya kifo cha Rais, wakati yeye ndiye aliyefanikisha zoezi la kuuawa kwa Rais kutokana na tamaa zake za kutaka madaraka makubwa ili yawe kinga ya kufanya mambo yake mabaya. BINADAMU SI WEMA.
Tammy Semmy alisogezwa mpaka nje ya ukumbi wa Ikulu na kupelekwa kwenye kochi lililowekwa kwa ajili ya waombolezaji, akachukua daftari la rambirambi na kuweka saini kwa ajili ya rambirambi.
Baada ya muda kidogo alitoka, na muda huo alipigiwa simu, aliipokea na kuongea kwa muda kisha akainuka na kwenda kuiaga familia ya marehemu, akatoka nje na walinzi wake akapanda gari na kuondoka kwa msafara wa ving'ora kama uliomleta hapo hawali.
**********************
Koplo Mbegu alirudi na furaha siku hiyo, furaha ya kumjua muuaji, sasa swali lililokuwa linamuumiza kichwa ni muuaji mwenyewe, mbona hakuwa mtu wa kawaida? ni mtu wa aina gani mwenye muonekano wa ajabu vile? Koplo Mbegu alikuwa akijiuliza huku akiwa amekaa kwenye kochi lake na ule mchoro wa yule mtu ulikuwa mezani mbele ya macho yake.
"Hakunaga mtu wa namna hii katika dunia hii, lakini siwezi kupinga kwa maana walioshuhudia wanasema ndiye huyu waliemuona, mh.....hii kazi imekuwa ngumu sana. Ila hakuna mwenye uhakika wote wanahisi kuwa huenda huyu mtu wa ajabu ndio muuaji lakini hakuna uthibitisho" Koplo Mbegu alikuwa anajiwazia mwenyewe.
Alikuja kugutushwa na mlio wa simu yake aliyokuwa ameitupia kitandani, akanyanyuka na kuangalia jina la mpigaji, alikuwa ni mkuu wake wa kazi, akapokea na wakaongea kidogo, kisha akata simu.
Koplo Mbegu akainuka haraka na kuvaa fulana yake kisha akatoka nje na kuchukua bodaboda iliyompeleka mpaka kwenye baa moja iliyokuwepo mafichoni, akashuka na kumlipa dereva wa bodaboda kisha akaingia ndani ya baa.
Akaenda kwenye kwenye meza moja iliyokuwa imejificha, alimkuta mkuu wake akiwa hapo,
"Mbona baa tena, kwanini sio ofisini?" Koplo Mbegu aliuliza huku akikaa kwenye kiti kilichopo pembeni ya mkuu wake,
"Hii kazi niliyokupa si unajua ni ya siri? Kwa hiyo hata makutano yetu yanayohusu mazungumzo ya hii habari yatakuwa pia ya siri, kwa maana kama nilivyokueleza hawali kuwa hiki kifo ni mipango ya watu na wengi wao wamechomekwa kwenye sekta za usalama kama yetu" Mkuu wa polisi aliongea,
"Sasa kama hiki kifo kimepangwa na watu mnaowajua, kuna umuhimu gani mimi nikafanye upelelezi nje ya taasisi za usalama?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Huwezi kukurupuka tu kwenda uko kupeleleza, watakuwa wamejiandaa kwa kila kitu, kuanzia kujibu na kupotelezea mbali kila mtu ambae ataonekana kuwafuatilia" Mkuu wa polisi alijibu, alionekana ni mwenye uzoefu mwingi katika suala la upelelezi,
"Sasa hata kama nikimaliza upelelezi na ukweli ukapatikana, ni wapi tutaupeleka huo ukweli wakati wako kwenye sekta za usalama ikiwemo mahakama?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Agiza chakula kwanza" Mkuu wa polisi alimwambia Koplo Mbegu baada ya kumuona muhudumu akipita karibu yao, Koplo Mbegu akaagiza chakula anachokihitaji.
"Umefikia wapi katika upelelezi wako?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Ni hatua kiasi nimepiga, nimepata taswira ya muuaji" Koplo Mbegu alijibu,
"Kweli umeamua kupepeleza, yaani haraka namna hiyo na taswira umeipata? Kama unayo hapo ebu nipe niione" Mkuu wa polisi aliongea,
"Nadhani na mkono wa Mungu upo katika kuniongoza kufanikisha kwa jambo hilo" Koplo Mbegu aliongea huku akimkabidhi ile karatasi yenye mchoro,
"Sasa hivi vituko, huyu ni mtu kweli" Mkuu wa polisi aliuliza huku akiushangaa ule mchoro,
"Hicho kiumbe ndicho kilionekana usiku wa tukio" Koplo Mbegu alijibu,
"Nani alikiona na alikiona akiwa kikifanya nini?" Mkuu wa polisi aliuliza na Koplo Mbegu akamsimulia kila kitu mpaka alivyotaka kupigwa na wanakijiji.
"Vizuri sana, ila hukutakiwa kuwaambia wanakijiji wewe ni nani? bado nahisi kuwa hata katika hicho kijiji kuna mtandao wa watu wabaya unachunguza kama mtu yeyote aliona uhalifu wao" Mkuu wa polisi aliongea,
"Ilibidi nitumie njia ile kujiokoa, vinginevyo wasingenielewa" Koplo Mbegu aliongea,
"Hata hivyo hujaharibu sana, sasa unafanyaje ili kukipata hicho kiumbe?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Hatuwezi kuweka picha kwenye vyombo vya habari ili itangazwe?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Hapana, huo ni ujinga kwa maana watagundua kuwa kuna mtu anaifuatilia hii kesi, kwa hiyo itatusababishia matatizo" Mkuu wa polisi alijibu,
"Hatutaandika kuwa huyu mtu ni muuaji, tunaweza kuandika kwa namna nyingine tofauti ila iwe tu ya kutaka apatikane" Koplo Mbegu aliongea,
"Hiyo haiwezekani, wanamtandao wana akili nyingi sana, ni wasomi ambao wamejiandaa kwa kila kitu" Mkuu wa polisi alijibu,
"Mbona kama unawajua?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Hapana siwajui, ila kuna tunaowahisi. Kwa hiyo hatuwezi kumtuhumu mtu kwa hisia tu" Mkuu wa polisi alijibu,
"Kwani haiwezekani kuwahoji kwa siri awa watu?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Jifunze kutumia akili, nikikuhitaji nitakupigia" Mkuu wa polisi aliongea kisha akanyanyuka kwa lengo la kutaka kuondoka, akageuka na kutoa bahasha ndogo ya kaki,
"Kuna pesa kidogo humu za kukusaidia" Mkuu wa polisi aliongea huku akiitupa ile bahasha mezani na kisha akaondoka zake na kumuacha Koplo Mbegu akimuangalia tu.
Koplo Mbegu alipomaliza kula alinyanyuka na kuondoka, alipofika nje ya baa akawa anasubiri bodaboda ya kumrudisha kwake, akiwa anasubiri hapo, simu yake iliita, alipoitazama alikutana na namba mpya, akataka asiipokee ila nafsi ikamshauri aipokee,
"Hallow" Koplo Mbegu aliongea baada ya kupokea,
"Hapo ulipo, geuka nyuma kuna gari nyeusi nipo nyuma ya hiyo gari" Sauti iliongea kutoka upande wa pili wa simu,
"Naongea na nani kwanza?" Koplo Mbegu aliuliza huku akigeuka upande alioambiwa ageukie,
"Acha maswali, njoo hapa mara moja, polisi uwa sio waoga namna hiyo" Sauti ile ilijibu na kisha ikakata simu, Koplo Mbegu akajishauri kwa muda na mwisho akaamua aende tu.
Akaenda mpaka lile eneo, nyuma ya gari, kulikuwa na Giza Nene kidogo, kwa mbele alimkuta mtu akiwa amesimama huku akiwa amempa mgongo, alivaa fulana nyeusi na jeans ya blue na raba,
" simama hapo hapo" Yule mtu aliongea huku akiwa amempa mgongo vile vile,
"Wewe ni nani?" Koplo Mbegu aliuliza huku akiwa amesimama,
"Unataka kunijua?" Yule mtu aliuliza,
"Ndio" Koplo Mbegu alijibu huku akipata wasiwasi,
"Mimi ndio yule kibwengo ulienichora kwenye karatasi yako, nasikia unanitafuta?" Yule mtu aliongea huku akigeuka............
Yule mtu aligeuka na akaanza kucheka, Koplo Mbegu akakasirika baada kuona sura ya yule mtu, alikuwa ni Ghislain.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mambo gani ya kipuuzi hayo? Utani gani huo wa kutiana presha?" Koplo Mbegu aliuliza huku akiwa amekasirika,
"Mwanaume lazima ujiandae kwa kitu chochote kile, ulitakiwa usiteteleke wewe, unakuwa kama mwanamke bwana" Ghislain aliongea huku akicheka,
"Ipo siku utaleta utani sehemu isiyohitaji utani, nakushuti tu" Koplo Mbegu aliongea huku akigeuka na kumfanya Ghislain amfuate huku akicheka,
"Una ishu gani na mkuu wenu wa polisi? maana nilikuona muda mrefu mkiwa kona ya ndani ya baa" Ghislain aliuliza swali lililomshtua kidogo,
"Hakuna kitu, nimekutana nae tu bahati mbaya" Koplo Mbegu alijibu,
"Bahati mbaya wapi wewe, inaelekea kuna kitu mnafanya, kwanini ulimtolea ule mchoro niliokucholea siku ile?" Ghislain aliendelea kuuliza maswali yaliyoonesha kuwa alikuwa akiwafuatilia muda mrefu,
"Bwana acha maswali yako, niache nikapumzike" Koplo Mbegu aliongea kuonesha hataki kuulizwa maswali,
"Shauri yako, kila mficha maradhi ataumbuliwa na kifo" Ghislain aliongea,
"Unamaanisha nini?" Koplo Mbegu aliuliza huku akisimama,
"Kwa utaalam wangu nakuona kabisa kuna kitu kinakusumbua, tena nahisi kuna mtu unamtafuta, itakuwa yule kibwengo niliyekuchorea" Ghislain aliongea na kumfanya Koplo Mbegu haamini kuwa kweli Ghislain ni mpelelezi mwenye uzoefu,
"Mbona kama unanipeleleza na mimi, umetumwa?" Koplo Mbegu aliuliza kwa hasira,
"Mpuuzi wewe nikupeleleze kwa kitu gani ulichofanya? Si bora nipeleleze kifo cha Rais" Ghislain aliongea kwa dharau na kumfanya Koplo Mbegu ashushe pumzi kwa maana alifurahi kujua kuwa Ghislain hajui kama yeye ndio anapeleleza kifo cha Rais,
"Wewe Jamaa yangu una matatizo sana, huishiwi vituko?" Koplo Mbegu aliuliza huku akitabasamu,
"Kuna muda unakhera sana, unajifanyaga msiri kumbe boya tu" Ghislain aliendelea kumponda mwenzake,
"Si yameisha Jamaa yangu? Ebu turudi ndani ya baa nikununulie hata bia mbili" Koplo Mbegu aliongea huku akimshika mkono Ghislain,
"Hayawezi kuisha kirahisi hivi, niambie kuna kesi gani unaifuatilia?" Ghislain aliuliza huku akijiondoa mkononi kwa Koplo Mbegu,
"Twende ndani basi, nitakusimulia, ni kesi moja ya kijinga sana" Koplo Mbegu aliongea huku akimvutia Ghislain ndani. Wakaingia na kutafuta meza moja isiyokuwa na mtu na kukaa kisha Koplo Mbegu akaagiza maji makubwa na Ghislain aliagiza bia tatu, pale alipo alikuwa amelewa ila aliongezea na bia nyingine.
"Utakufa kwa pombe wewe" Koplo Mbegu aliongea huku akicheka,
"Usipoteze mada, niambie ni kesi ipi unafuatilia?" Ghislain aliuliza,
"Ni ya kijinga tu, achana nayo" Koplo Mbegu aliongea ili kumpotezea Ghislain,
"Acha upumbavu, hata kama ya kijinga unapaswa kuniambia" Ghislain aliongea huku akiwa anamaanisha,
"Ni kesi moja nimepewa niifuatilie, eti kuna mzimu unaua watu katika familia, na ndio nikakupa kazi ya kuuchora ule mzimu ukanichorea" Koplo Mbegu alimdanganya mwenzake,
"Sasa si ulitakiwa useme hivyo tangu mapema, umenizungusha we kumbe unaficha ujinga tu" Ghislain aliongea,
"Si ndio maana nilikuwa sitaki kukuambia, kwa maana niliona ni ujinga tu, polisi hatuaminigi imani za Giza" Koplo Mbegu aliongea huku akiamini tayari amempoteza Ghislain,
"Na zile pesa ulizopewa kwenye bahasha ni za nini?" Ghislain aliuliza huku akimimina bia kwenye glass,
"Mkuu amenipa tuu, kuna kazi niliwahi kuifanya kipindi cha nyuma" Koplo Mbegu aliendelea kudanganya,
"Inaelekea hiyo kazi uliyoifanya haikuwa ya halali, kwanini pesa upewe baa wakati kuna ofisi? au haikuwa ya kiofisi?" Ghislain aliuliza,
"Ujue mimi sipendagi kuchimbwa sana, kama hujalidhika na majibu yangu sawa, ila sitaki swali jingine" Koplo Mbegu aliongea huku akijifanya amekasirika, ila kihalisia ni kwamba alihisi Ghislain ametumwa kumchunguza,
"Ngoja ufe miguu juu kama mende, sijui utamlaumu nani? Kwa maana utakuwa umechelewa" Ghislain aliongea kilevi kisha akatema mate chini,
"Unasemaje wewe?" Koplo Mbegu aliuliza kanakwamba hajamsikia vizuri,
"Agiza nyingine ninywe" Ghislain aliongea kama hajasikia swali la mwenzake,
"Bwana mimi naenda, utaagiza mwenyewe, ulizokunywa mwanzo nimeshalipia" Koplo Mbegu aliongea huku akiweka pesa mezani kisha akanyanyuka,
"Sasa hiyo itatosha hata kununua bia tano?" Ghislain aliongea baada ya kuiangalia pesa iliyowekwa mezani,
"Tafuta bwana akulipie hiyo hela ya bia tano" Koplo Mbegu aliongea huku akianza kuondoka,
"Umesemaje?" Ghislain aliuliza huku akimuangalia Koplo Mbegu kwa jicho baya,
"Usiku mwema" Koplo Mbegu aliongea huku akicheka na kuelekea nje, Ghislain akabaki amemtolea jicho la hasira mpaka alipompotea machoni.
**********************
Tammy Semmy ule msafara ulimpeleka nyumbani kwake kisha akawaruhusu waondoke kwa amri ya kwamba atakapowahitaji atawaita, ule msafara ulivyoondoka tu, Tammy Semmy akawasha gari yake na kwenda kwenye nyumba au kambi yake ya waasi.
Alifika na kuwakuta wenzie wakiwa wamekaa, na safari hii waziri wa ulinzi nae alikuwepo,
"Aisee wewe ni bonge la muigizaji" Waziri wa ulinzi alimwambia Tammy Semmy,
"Kwanini?" Tammy Semmy aliuliza huku akishangaa,
"Yaani ulivyokuwa unatangaza tangazo la kifo cha Rais alafu na machozi yalivyokuwa yanakutoka ni kama ulikuwa na huzuni wa kweli vile" Waziri wa ulinzi aliongea na Tammy Semmy akacheka,
"Lazima maigizo yawepo, huwezi kutangaza kifo cha rafiki yako alafu usiweke huzuni, hata wa kinafiki tu" Tammy Semmy aliongea huku akicheka,
"Pia ulipendeza sana kukaa mbele ya bendera ya rais na bendera ya nchi, kweli cheo cha Rais ndio kilikuwa chako, cha umakamo hakikukufaa kabisa" Jimmy aliongea kisha wote wakacheka,
"Mateka wetu anaendeleaje? alishazinduka?" Tammy Semmy aliuliza,
"Bado, ila atazinduka muda sio mrefu" BQ alijibu,
"Vipi ile flash ambayo ilichukua tukio la kifo cha rais na tukionekana katika ile video, unayo?" Waziri wa ulinzi alimuuliza Tammy Semmy,
"Sina, si niliiacha hapa hapa, pale kwenye meza ya TV" Tammy Semmy aliongea,
"Sasa mbona haionekani?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"eti nyie mliokesha humu, flash ipo wapi?" Tammy Semmy aliwauliza Jimmy na Gabby,
"Mara ya mwisho kuiona ilikuwa pale pale uliposema wewe" Jimmy alijibu,
"Mara ya mwisho uliiona muda gani?" Tammy Semmy aliuliza,
"Ilikuwa jana baada ya nyinyi kuondoka" Jimmy alijibu,.
"Sasa mbona haionekani?" Tammy Semmy aliuliza na kukawa kimya, hakuna aliyejibu,
"Yule kijana mateka tumemsachi mpaka tumemvua nguo, hana flash" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Mimi nadhani yule mtu aliyetuvamia jana atakuwa ameichukua" Gabby aliongea,
"Ebu punguzeni uzembe, mjue ni hatari sana kuacha adui awashinde" Tammy Semmy aliongea,
"Tumekuelewa mkubwa, hilo halitokaa lijirudie tena tatizo kama hilo" Jimmy alijibu,
"Vaeni suti sasa twendeni monchwari, natakiwa nikaweke sahihi kuthibitisha kifo cha Rais, nyie mtakuwa kama walinzi wangu, kasoro Waziri wa ulinzi unatakiwa ubaki, wewe bado hautakiwi kujionesha mbele ya watu" Tammy Semmy aliongea kisha vijana wake wakaenda kuvaa vizuri.
Walipomaliza walitoka na kumuacha Waziri wa ulinzi akimlinda Tom.
Tammy Semmy na watu wake walinyoosha moja kwa moja mpaka kwenye hospitali ya Taifa, waliwakuta pamoja na viongozi wengine wa nchi wakiwa nje ya hospitali wakimngoja yeye.
Aliingia na watu wake, ilikuwa ngumu kuwagundua kwa kuwa wengi wa viongozi waliofika hapo hawakuwa wakijua watu wa usalama wa Taifa, kwa hiyo kumuona Tammy Semmy na wale watu waliamini ni miongoni mwa walinzi wa makamo huyo wa Rais.
Tammy Semmy alielekea moja kwa moja monchwari na kutaka kuingia na watu wake,
"Samahani mheshimiwa, unatakiwa uingie wewe na Waziri mkuu tu, wengine watakungoja nje" Mwanajeshi mmoja aliyekuwa mlangoni alimwambia Tammy Semmy,
"Sawa" Tammy Semmy alijibu kisha akaingia ndani ya monchwari akiongozana na Waziri mkuu, ndani walimkuta daktari aliyekuwa akiwasubiri.
"Karibuni waheshimiwa na poleni kwa msiba" Daktari aliongea,
.
"Asante, maiti ya mheshimiwa iko wapi?" Tammy Semmy aliuliza na yule daktari akaenda kwenye jokofu mojawapo na kulivuta, hapo ndipo mwili wa Rais ulionekana huku ukiwa na tobo la risasi katika paji la uso, Tammy akausogelea akawa anauangalia huku akisikitika,
"Usijidai kusikitika, wewe ndio umemuua" Sauti ilisikika nyuma ya Tammy Semmy na kumfanya ageuze shingo nyuma haraka ili kumuona huyo anaeongea.........
Tammy Semmy akageuka nyuma lakini hakumuona mtu mwingine zaidi ya waziri mkuu,
"Umesema?" Tammy Semmy aliuliza huku akimuangalia Waziru Mkuu,
"Hapana sijasema kitu" Waziri mkuu alijibu,
"Dah....basi nna mawazo mengi sana mpaka nashindwa kujielewa" Tammy Semmy aliongea huku akiyarudisha macho yake kwenye mwili wa Rais,
"Unatakiwa uyapunguze mkuu, mwili wako mzuri angalia usiumalize na presha" Waziri Mkuu aliongea huku akitabasamu,
"Mawazo hayaepukiki bwana" Tammy Semmy aliongea na kutupia macho mlangoni ambapo alimkuta mmoja wa walinzi wake akiingia,
"Vipi?" Tammy Semmy alimuuliza,
"Mkuu wa majeshi yupo nje, anasubiri mtoke ili nae apate fursa ya kuuona mwili wa Rais" Mlinzi aliongea,
"Aingie tu, au Waziri unasemaje?" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia Waziri Mkuu,
"Aingie tu" Waziri mkuu alijibu na kisha yule mlinzi akatoka nje ya monchwari.
Baada ya dakika tatu Mkuu wa majeshi aliingia na kutoa heshima kwa wakubwa zake kisha akasogea kusimama karibu na mwili wa Rais ambapo pembeni yake alikuwepo Tammy Semmy,
"Hii no hatari, inaonekana ulinzi umekuwa hafifu sana kwa viongozi wa nchi, na jukumu la ulinzi lenu" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia Mkuu wa Majeshi,
"Hapana, ulinzi upo imara tena sana, ila inasemekana kuwa siku ya tukio, Mheshimiwa Rais hakutaka kutoka na walinzi, in kawaida yake siku kama hiyo kuwapa mapumziko walinzi wake" Mkuu wa Majeshi alijibu kwa heshima,
"Lakini kwa sheria za nchi hairuhusiwi kufanya hivyo, ni lazima hata wangekuwepo watu wa usalama wa Taifa wawe wanamfuatilia kwa nyuma" Tammy Semmy aliongea kwa kulaumu,
"Nadhani imetokea kwa bahati mbaya, kwa maana siyo Mara ya kwanza Mheshimiwa Rais kutoka peke yake, kila wiki uwa ana ratiba za kuwa peke yake" Mkuu wa Majeshi alijibu,
"Msihishi kwa mazoea, inaelekea mtu aliyefanya mauaji haya alishamchunguza kwa muda mrefu sana Rais" Tammy Semmy aliongea,
"Na pia inaelekea huyo mtu ana silaha nzito sana, risasi iliyotolewa kwenye kichwa cha Mheshimiwa Rais ni ya hatari sana" Mkuu wa majeshi aliongea huku kichwa kikiwa chini,
"Ni ya aina ya bunduki?" Waziri Mkuu aliuliza,
"Bunduki ni Riffle, yenye jina la international accuracy, ilitengenezwa mnamo mwaka 1997, INA nguvu sana na ina uzito wa kila sita na nusu (6.5kg), inatumiwa sana na jeshi la uingereza" Mkuu wa majeshi alieleza,
"Na kwa hapa nchini zinapatikana hizo bunduki?" Waziri Mkuu aliuliza,
"Ndio zipo, zinatumiwa zaidi na wadunguaji (sniper) wa jeshi ila wale wa mission maalum zenye ugumu sana" Mkuu wa majeshi alijibu,
"Kwa hiyo unataka kuniambia huu mpango wa kumuua Rais ni wa jeshi?" Tammy Semmy aliuliza huku akimgeukia Mkuu wa majeshi,
"Sijamaanisha hivyo, swali nililolijibu in kuhusu hizi bunduki kuwepo nchini kwetu, ila pia hata waasi wa kongo nao wanatumia hizi bunduki. Pia kama mtakumbuka tulishawahi kukamata bunduki kama hizi katika kambi ya wakimbizi kile kigoma, so inawezekana muuaji alizipata mitaani" Mkuu wa jeshi alitoa maelezo yenye lengo la kujitetea,
"Nafikiri mnatakiwa mchunguze kwa undani zaidi tukio hili" Waziri Mkuu aliongea huku akimtupia jicho Mkuu wa polisi,
"Hilo jambo tayari lipo chini ya usalama wa Taifa, Jeshi liendelee tu na mambo yake ya kuimarisha usalama tu" Tammy Semmy aliongea huku akitoka nje ya monchwari na wanzake wakamfuata,
"Ila ingekuwa bora kama vyombo vyote vya usalama vingetoa mpelelezi mmoja wa kufuatilia hili jambo" Waziri Mkuu aliongea huku akitoka nje kumfuata Tammy Semmy,
"Ebu jaribu kunielewa mheshimiwa, wakati tunakubaliana kuhusu upelelezi wa kesi hii si ulikuwepo? kwanini usingesema matakwa yako katika kipindi kile cha kikao?" Tammy Semmy aliuliza huku akiwa anajitahidi kuzuia hasira zake,
"Kipindi kile nilikuwa na mshtuko wa kifo hiki, kwa hiyo hata akili haikuwa vizuri" Waziri Mkuu alijitetea,
"Nina wasiwasi sana na uwezo wako wa akili, kajiangalie mara mbili na ujitathmini" Tammy Semmy aliongea na kuelekea kwenye gari yake huku akifuatwa na wapambe wake, Jimmy, Gabby na BQ waliokuwa ndani ya suti nyeusi.
"Hata mimi nadhani in vema jambo hili lingesimamiwa na vyombo vyote vya usalama" Mkuu wa majeshi alimuambia Waziri Mkuu baada ya Tammy Semmy kuondoka,
"Huyu mtu in mbishi sana, na hatuna la kufanya kwa maana madaraka yote ya uongozi wa nchi ameyakahimu yeye" Waziri Mkuu aliongea kwa upole,
"Au nitume vijana wangu waendelee na uchunguzi wa chini chini?" Mkuu wa majeshi aliuliza,
"Hapana, kwa kufanya hivyo itakuwa unajitaftia tatizo mbele ya Tammy Semmy, uwa hatakagi kupingwa, cha muhimu tusubiri uchaguzi utamtafuta Rais mwingine wa nchi uishe na apatikane Rais tofauti na yeye Tammy Semmy, hapo ndio utaweka utaratibu wa kuingiza wapelelezi wa idara zote" Waziri Mkuu alimjibu Mkuu wa majeshi,
"We unadhani kuna nguvu yoyote ya kumzuia huyu mtu asiingie madarakani?" Mkuu wa majeshi aliuliza,
"Kwa kweli sidhani kama anazuilika, tutajaribu kuangalia namna" Waziri Mkuu alijibu,
"Mi nadhani hata wewe una nguvu kidogo na isitoshe mna tofauti, yaani hamko sawa kwa maana ya kila mmoja wenu kuwa na wafuasi wake ndani ya chama, no bora ushindane nae kwenye chama ili upate nafasi hiyo wewe" Mkuu wa majeshi alimshahuri Waziri Mkuu,
"Hata mimi nilikuwa na wazo kama hilo, kwa maana kauli aliyoniacha nayo hapa ya kuwa nijitathmini, inanipa mashaka juu ya mustakabali wangu endapo yeye atakuwa Rais, huenda hata uwaziri nisipewe" Waziri Mkuu aliongea huku akiwa na fikra kiasi,
"Nenda kalitathmini hilo, baada ya maziko ya Rais nitakutafuta ili uniambie ulipofikia" Mkuu wa majeshi alimwambia Waziri Mkuu,
"Sawa, haina tatizo ngoja nikafikirie kwa upana na pia nikasikilize washauri wangu" Waziri Mkuu aliongea huku akimpa mkono Mkuu wa Majeshi kisha wakaagana na kila mmoja akaelekea kwenye gari yake, wakaondoka kuelekea njia tofauti.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*******************
Tammy Semmy alipopanda kwenye gari yake alionekana wazi ana hasira,
"Vipi mzee mbona umebadilika ghafla?" Jimmy alimuuliza,
"Waziri Mkuu anajifanya mjuaji sana, eti anashauri vyombo vyote vya usalama vifanyie uchunguzi kifo cha Rais" Tammy Semmy alijibu huku amekunja sura,
"Kama no hivyo sioni sababu ya wewe kukasirika" Jimmy aliongea na kumfanya Tammy Semmy ageuke kumuangalia,
"Huoni sababu?, huoni upelelezi ukifanywa na watu wengi tofauti inaweza kutuletea shida?" Tammy Semmy alihoji kwa hamaki,
"Sijamaanisha hivyo, nilichotaka kuongea ni kuwa lazima umpige chini huyo Waziri, mamlaka yote si yapo chini yako" Jimmy alimjibu Tammy Semmy,
"Bado itakuwa ngumu kumpiga chini, kwa maana nitapewa mamlaka kamili baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais, nikishinda ndio nitachagua baraza langu la mawaziri na watu wengine" Tammy Semmy aliongea,
"Kushinda lazima ushinde. Je Mkuu wa majeshi hana tatizo?" Jimmy aliuliza,
"Yule nimemsoma kwa muda mfupi na nimegundua ni muoga sana, yaani nimemtisha kidogo kuhusu kifo cha rais na amekuwa mpole, yule mitamuacha tu ili baadae nimgeuzie upande wangu" Tammy Semmy aliongea kwa kujiamini,
"Yule mzee no mpole sana, sijui no kwanini alipewa ukuu wa majeshi? Mkuu wa majeshi anatakiwa na sura ngumu na roho ngumu pia" Jimmy aliongea huku akitabasamu,
"Kitu kilichofanywa apewe cheo kile ni elimu yake, uzoefu na utaalamu wake wa kujua vitu vingi vya kijeshi. Kwanza amenitajia jina la bunduki tuliyotumia kumuua Rais na mpaka mwaka ambayo bunduki hiyo imetengenezwa, anasema zinatumika sana na UK army force" Tammy Semmy aliongea kumsifia Mkuu wa majeshi na kipindi hicho gari waliyoipanda ilikuwa inaingia ndani ya ile nyumba ambayo waliitumia kama kambi yao ya kufanyia maovu.
Gari ilipoingia ilipaki na Gabby akafunga Geti. Walipoenda kwenye mlango wa kuingilia walikuta umeegeshwa tu na haujafungwa na funguo, iko kitu sio kawaida kabisa,
"Huyu mwehu atakuwa ametoka nini? Mbona anajiamini sana huyu?" Tammy Semmy aliuliza huku huyo mwehu anayeuliziwa akiwa ni Waziri wa ulinzi,
"Au kalewa?" Gabby aliuliza huku akiusukuma mlango na kuingia ndani ambapo pia hakukuwa na mtu isipokuwa mchirizi wa damu uliotokea upande wa chooni, wote wakashtuka na kila mmoja silaha yake akaiweka mkononi,
"Baki na Mkuu hapa" Jimmy alimwambia BQ kwa sauti ndogo kisha yeye na Gabby wakawa wanafuatilia ule mchirizi wa damu kwa mwendo wa paka bila vishindo kusikika.
Walifuatilia ule mchirizi na kwa mbali kupitia mlango wa bafu ulikuwa umefunguka nusu waliweza kumuona Waziri wa ulinzi akiwa amelala na damu zilikuwa zimemtapakaa mwili mzima.
Wakasogea kwa tahadhari sana huku kila mmoja akiwa amejiandaa kwa tukio lolote, walipokuwa kama bado hatua tano kuufikia ule mlango, mlango ukafungwa kwa ghafla na kwa ndani ikasikika sauti ya komeo ikifungwa.....
" yupo huku" Jimmy aliongea kwa sauti iliyowafikia Tammy Semmy na BQ kule sebuleni na kufanya wajisogeze mpaka walipo Jimmy na Gabby,
"Ni nani?" BQ aliuliza kwa sauti ya chini huku akitayarisha bastola yake,
"Hakuna aliyemuona" Jimmy alijibu,
"Tufanye shambulio la kushtukiza, yaani tusivunje mlango ila tupige risasi tu kuelekea ndani" Gabby alitoa ushauri,
"Hiyo iko poa" Jimmy alimkubalia huku akimuonesha ishara ya dole gumba,
"Ni mimi bwana, msipige risasi" Waziri wa ulinzi aliongea huku akitoka bafuni na pia alikuwa akicheka na kuwafanya wenzake washikwe na bumbuwazi iliyoambatana na hasira,
"Eti huu ni utoto unaofanya ujue?" Tammy Semmy alimuuliza huku akimuangalia kwa hasira,
"Nilitaka kuwapima mmejiandaje kwa tukio kama hili endapo litatokea" Waziri wa ulinzi aliongea huku akicheka,
"Ni upumbavu kufanya jaribio ambalo linaweza kuleta umauti" Tammy Semmy aliongea kwa hasira huku akielekea sebuleni,
"Tom yupo wapi?" BQ alimuuliza Waziri wa ulinzi,
"Yupo torture chamber" Waziri wa ulinzi alijibu huku nae akielekea sebuleni,
"Sema mkuu umetutisha sana, ilikuwa tukufyatulie risasi" jimmy aliongea huku akimuangalia Waziri wa ulinzi,
"Si ndio maana nikawahi kujitokeza, kwa maana nilishasikia mipango yenu" Waziri wa ulinzi aliongea huku nae akitabasamu,
"Na hii damu uliyojipaka ni ya nini?" Jimmy alimuuliza huku akijitupa kwenye kochi pembeni ya Tammy Semmy,
"Sio damu hii, ni maji tu nimeyachanganya na rangi nzito" Waziri wa ulinzi alijibu,
"Ana akili za kitoto sana na ndio maana wale vijana wakina Sajenti Minja walimshinda akili na kumfunga" Tammy Semmy aliongea, alionesha bado ana hasira na waziri wa ulinzi,
"Jamani mnisamehe sikuwa na lengo baya. Nipeni habari ya kilichojili uko"Waziri wa ulinzi aliamua kubadili mada,
"Uko hakuna mpya, mambo yanaenda kama tunavyotaka" Tammy Semmy alijibu,
"Ni habari nzuri, na maziko ya Rais ni lini?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Nafikiri atazikwa kesho, niliwasikia ndugu na familia yake wakizungumza kitu kama hicho, nafikiri habari hizo zitatangazwa baadae" Tammy Semmy alizungumza,
"Basi ni vyema" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Na vipi kuhusu huyo mtu wa ajabu aliowatokea wakina Gabby, wewe hajakutokea?" Tammy Semmy alimuuliza Waziri wa ulinzi,
"Hajanitokea, kwanza mimi siaminigi habari hizo" Waziri wa ulinzi aliongea kwa kujiamini na kufanya Jimmy na Gabby waangaliane kisha wakatabasmu,
"Usiombe akutokee" Jimmy aliongea huku akiendelea kutabasamu,
"Atanifanya nini kwani? mi namtwanga tu risasi mtaikuta maiti yake" Waziri wa ulinzi aliendelea kuongea kwa kujiamini,
"Hivi kwanza ni nini kinafuata ili kuipata ile flash yenye video inayotuonesha sisi tukiwepo kwenye tukio la kumuua rais?" Tammy Semmy aliuliza,
"Hiyo ishu ni ya kusubria kwanza, yaani tungoje tuone kama ataibuka tena huyo mtu, na akiibuka atakuwa na madai gani" Waziri wa ulinzi alijibu Tammy Semmy,
"Je asipoibuka na video ikaanza kusambaa, itakuaje?" Tammy Semmy aliuliza,
" sidhani kama hilo linawezekana, ninachohisi huyu mtu atakuwa ana kitu tu anataka na ndio maana alituletea ile video tuione alafu akaichukua tena, kama angekuwa anataka kuisambaza angeisambaza tu" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Na huyu mtu ni nani?" Tammy Semmy aliuliza,
"Hilo swali halina jibu kwa sasa, tusubiri wakati wake ukifika litajibika" Waziri wa ulinzi aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,
"Kweli, tungoje wakati ndio utazungumza ukweli" Jimmy aliongea huku akiwasha sigara yake yenye rangi kama mbao.
*********************
Koplo Mbegu alichelewa sana kuamka siku hiyo, kilichomuamsha ni simu aliyopigiwa na rafiki yake, siku iliyompa taarifa kuwa awashe runinga kwa maana kifo cha Rais kinatangazwa.
Hakuona jipya la kuangalia ila akaona bora awashe tu, alipowasha aliikuta habari yenyewe inaishia.
Akaamua ashughulikie wazo alilolala nalo usiku uliopita, wazo la kutoa copy za ule mchoro wa ajabu na kuzibandika kila mtaa.
Akajisafisha mwili na kutoka kwake mpaka katika stationary iliyopo jirani na kuwapa maelekezo juu ya ule mchoro na kuambiwa asubiri. Baada ya nusu saa aliletewa copy zipatazo elfu moja na juu ya ule mchoro kulikuwa na maneno yanayosomeka " KIUMBE HIKI NI HATARI, POPOTE MTAPOKIONA MTOE TAARIFA POLISI".
Akazipitia baadhi ya copy, baada ya kujiridhisha alilipia na kuondoka mpaka kwenye vituo vya daladala na kuwapa hiyo kazi makonda wa daladala na kuwalipa 3000.
Alipotoka hapo alienda mpaka nje ya mji kile kulipotokea tukio la mauaji ya rais na alipofika huko alimtafuta yule kijana muongeaji na kumpata,
"Bro tokea siku ile wananchi watake kukupiga sijabahatika kukuona tena mpaka leo" Kijana muongeaji aliongea kwa bashasha kama kawaida yake,
"Mambo mengi ndugu yangu, si unajua kazi zetu hizi?" Koplo Mbegu aliongea,
"Mimi nikajua labda uliingia hofu ukaogopa kurudi tena" Kijana muongeaji aliendelea kuongea,
"Siwezi kuogopa, nitaogopaje majukumu yangu?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Niambie kuna jipya gani lililofanya unitafute?" Kijana mwenye maneno mengi alimuuliza,
"Kuna kazi nataka unisaidie" Koplo Mbegu aliongea huku akimuangalia,
"Kazi gani tena?" Kijana mwenye maneno mengi aliuliza,
"Kazi ndogo tu, nataka unisaidie kuzisambaza hizi picha" Koplo Mbegu aliongea huku akizitoa zile picha kutoka kwenye mfuko wa karatasi,
"Picha gani, au za yule muuaji?" Kijana mwenye maneno mengi aliuliza,
"Ndio huyo huyo" Koplo Mbegu alijibu huku akiwa hamuangalii yule kijana,
"Hii kazi ndogo sana kwangu, naimaliza leo hii" Kijana mwenye maneno mengi aliongea kwa kujidai,
"Itakuwa vizuri sana kama hii kazi itaisha leo, hakikisha zinafika eneo lote na ikiwezekana mpaka maeneo jirani na kijiji hiki" Koplo Mbegu alisisitiza,
"Usijali bro, hii ni kazi ndogo sana" Kijana mwenye maneno mengi aliendelea kumpa moyo Koplo Mbegu,
"Kamata hii itakusaidia" Koplo Mbegu aliongea huku akimpatia yule kijana kiasi cha pesa yenye thamani ya shilingi elfu thelathini,
"Za kwangu zote?" Kijana mwenye maneno mengi aliuliza huku akisita kuzipokea,
"Za kwako ndio, mbona unasita kupokea? au unaziona nyingi sana?" Koplo Mbegu alimuuliza huku akicheka,
"Sio nyingi, ila sijawahi kupewa hela kubwa hivi kwa kazi ndogo kama hii, hizi pesa uwa tunazipata tukianza kuuza mikaa tu, sio bure namna hii" Kijana mwenye maneno mengi aliongea huku akitabasamu,
"Wewe pokea tu, na ukiendelea kunisaidia siku za usoni, utapata nyingine kama hizi" Koplo Mbegu aliongea wakati yule kijana akizipokea zile pesa,
"Nashukuru sana mkuu" Kijana mwenye maneno Mengi aliongea huku akizitia mukoni zile pesa,
"Sasa huu mzigo hakikisha unausambaza wote, sijui utatumia njia gani, ila cha muhimu uusambaze kwa kubandika katika ukuta na kugawa kwa watu mbalimbali" Koplo Mbegu aliongea,
"Usijali bosi wangu, hiyo kazi imeshaisha tayari" kijana mwenye maneno mengi aliongea kisha wakaagana kwa makubaliano ya Koplo Mbegu kurudi tena siku yoyote maeneo ya pale kijijini.
Koplo Mbegu alipotoka pale aliingia kwenye mizunguko yake ya kawaida na pia alijitahidi kuzunguka ndani ya jiji ili kuona kama picha zake zimebandikwa, aliweza kuziona sehemu mbalimbali na akajiridhisha na nafsi yake kuwa kazi kweli imefanyika.
Alipochoka kuzunguka, aliamua kurudi kwake, ila kwanza alipitia kwenye kibanda cha chipsi na kuagiza chakula hicho pendwa kwa vijana, baada ya kuagiza alitengenezewa na kufungiwa kwenye mfuko laini wa nailoni, kisha akamlipa muuzaji na kuanza kuelekea kwake.
Alipofika aliuchomoa ufunguo wa mlango wake kutoka mfukoni na kufungua mlango wake, alipoingia tu alipigwa na mshangao baada ya kumkuta mtu akiwa amekaa kitandani, uso wake aliuelekeza dirishani na mgongo aliuelekezea mlangoni, kwa hiyo Koplo Mbegu alipoingia alimkuta yule mtu amempa mgongo na alikuwa amevaa koti kubwa jeusi lenye kofia yake........
Koplo Mbegu alikuwa bado anamshangaa yule mtu aliyevaa koti kubwa jeusi, suruali ya jinsi ya bluu na buti kubwa kama za wanajeshi na pia nazo zilikuwa nyeusi. Koplo Mbegu akiwa bado ameganda huku akimshangaa yule Jamaa na pia akijiuliza kuwa yule mtu ameingiaje mule, yule mtu wala hakuoneka kushtuka wala kujali ujio wa Koplo Mbegu katika chumba kile.
Sasa koplo Mbegu akawa anajiuliza apige kelele za kuomba msaada wa kukamatwa mwizi au ajaribu kupambana nae mwenyewe? jibu alilolipata ni kupambana nae mwenyewe tu.
"Oya wewe ni nani?" Koplo Mbegu aliuliza kibabe huku akiwa bado amesimama mlangoni,
"Nimeamua kuja mwenyewe baada ya kuona picha zangu kuwa natafutwa na polisi wewe" Yule mtu alijibu huku akiwa bado yupo vile vile yaani kampa mgongo Koplo Mbegu.
Koplo Mbegu baada ya kusikia jibu la yule mtu alijikuta anapata hofu zaidi kwani kwa anavyofahamu yeye kuwa mtu huyo ni wa ajabu wa sura, kingine kilichomfanya aamini kuwa mtu huyu ni wa ajabu ni pale alipomkuta ndani mtu huyu wakati mlango ulikuwa umefungwa.
"Umefuata nini sasa kwangu, si uende polisi?" Koplo Mbegu aliuliza huku sauti yake ikiubeba uoga aliokuwa nao,
"Natafutwa na wewe na sio polisi, acha uoga kiumbe wa kiume" Kiumbe kile kilijibu na kumalizia kwa tabasamu la dharau,
"Ebu nigeukie ili tuzungumze vizuri" Koplo Mbegu aliongea hivyo kwa lengo la kutaka kumuona sura yake huyo mtu, na yule mtu akageuka taratibu kumuangalia Koplo Mbegu...... sasa moyo wa Koplo Mbegu ukaanza kupiga kwa wasiwasi kwa maana aliamini ile sura ya kiumbe cha ajabu ambayo aliiweka kwenye mchoro, sasa anaiona leo kiuhalisia kabisa.
Yule mtu akaendelea kumgeukia mpaka wakawa wanaangaliana uso kwa uso na Koplo Mbegu, Koplo Mbegu akapata mshtuko, maana alikutana na sura tofauti kabisa na ile aliyoisambaza kwenye michoro ya mitaani, sasa Koplo Mbegu akahisi inawezekana huyu mtu sio kile kiumbe anachokitafuta, wazo lake likawa kuwa huyu mtu ni tapeli tu anataka kumuingiza mjini.
"Mimi sio tapeli kama unavyodhani wewe kiumbe, mimi ndimi yule umtafutae" Kiumbe yule aliongea na kumfanya Koplo Mbegu ajiulize yule mtu kajuaje kama yeye amemuhisi tapeli?
"Wewe ni nani sasa? kwa maana mtu ninaemtafuta sio wewe, ni huyu hapa" Koplo Mbegu aliongea huku akimtupia ile karatasi yenye mchoro,
"Huyo mtu aliyepo kwenye mchoro ndiye mimi" Kiumbe yule alijibu bila kuangaika kuichukua ile karatasi aliyotupiwa na Koplo Mbegu,
"Sio wakati wa kupotezeana muda huu, nadhani upo hapa kunivuruga tu, huna cha maana" Koplo Mbegu aliongea kwa hasira baada ya kumuona huyu mto anamzingua tu,
"Sawa, mi naenda ila nisizione tena zile picha mtaani zilizokuwa na sura yangu, ukishindwa kuziondoa wewe, nitaziharibu mimi" Kiumbe yule aliongea huku akisimama, wazo lililomjia Koplo Mbegu muda huo ni kumpiga picha za haraka haraka mtu huyo kupitia simu yake, akaitoa simu yake mfukoni na kuitayarisha kwa ajili ya kupiga picha,
"We ondoka tu, na wala usiendelee kunitolea maneno yako ya kuniamrisha" Koplo Mbegu aliongea huku akisimama na kwenda kufungua mlango ili yule mtu apite.
Yule mtu akasimama na hapo ndipo Koplo Mbegu alipotumia mwanya huo kumpiga picha za haraka nyingi sana, yule mtu alitabasamu kisha akaufuata mlango na kumpita Koplo Mbegu na akatoka nje ya mlango na kusimama. Hapo Koplo Mbegu akawaza kuwa atoe bastola ili amtishie tu ili huyo mtu aondoke machoni mwake,
"Sio kunitisha tu, hata unipige na hiyo bastola yako sitopata tatizo lolote, ewe kiumbe usio na upeo wowote utapata tabu sana kuniona tena" Kiumbe yule aliongea na kumfanya tena Koplo Mbegu awaze kuwa yule mtu amejuaje kama anataka kumtisha kwa bastola,
"Usijisumbue kuwaza najuaje unachowaza, kiumbe mwenye upeo nipo peke yangu katika sayari hii" Kiumbe yule aliongea na kumfanya Koplo Mbegu azidi kumuona huyu mtu ni wa ajabu, kwa maana aliweza kung'amua mawazo ya mtu mwingine.
Wakati Koplo Mbegu akiendelea kumfikiria huyu mtu, kiumbe yule aligeuka na kuondoka zake bila wasiwasi wowote na kumuacha Koplo Mbegu akimtumbulia macho bila kuongea chochote.
Yule kiumbe alipopotea machoni mwake, Koplo Mbegu alirudi zake ndani huku akimfikiria mtu huyu ni mtu wa aina gani? alimfikiria kwa dakika kadhaa kisha akachukua simu yake ili aweze kumuangalia tena kupitia zile picha alimpiga kupitia simu yake ya mkononi, alikutana na kitu cha ajabu, alimuona mtu tu asiye na sura, yaani aliona nguo zimevaliwa na upande wa kichwani aliona ile kofia ya koti ikiwa imevaliwa lakini sehemu ya sura lilionekana giza tu, yaani picha ilionekana kama lilivyo kava la hadithi yetu.
Koplo Mbegu akajihisi kuchanganyikiwa, akaanza kujenga imani kuwa huenda yule Jamaa ndio kiumbe anaemtafuta, kwa jinsi mazingara yale ya kupotea sura ya yule Jamaa kwenye picha yalivyomchanganya alijikuta anacheka peke yake kama mwendawazimu na hata chipsi alizonunua alishindwa kuzila.
**********************
Tammy Semmy bado alikuwa sebuleni na vijana wake wakiongea mawili matatu kuhusu mipango yao.
"Mimi nadhani tumuachie huyu dogo, maana hana jipya na wala sio yeye mwenye ile video mbaya inayotulenga sisi" Tammy Semmy aliwaambia vijana wake,
"Sio mbaya kama ataachiwa, ila kwa sharti la kutotoka nje ya nchi ili iwe rahisi kumfuatilia nyendo zake" BQ alionekana kukubaliana na Tammy Semmy,
"Uzuri wa huyu dogo ni kwamba anatoa ushirikiano wa kutosha, ukimtisha kidogo anasema ukweli wote alionao" Jimmy aliongea kuungana nao wenzake,
"Kama alivyosema BQ hapa, huyu mtu hatakiwi kutoka nje ya nchi kwa maana akiwa nje anaweza kufanya lolote kutuchoma sisi kwa kuwa hatutakuwa na uwezo wa kumkamata kwenye ardhi ya nchi nyingine, anatakiwa abaki hapa" Tammy Semmy aliongea na wenzake wakaitikia kwa kutikisa vichwa vyao,
" kitu kingine ni kuwa anatakiwa ahache kazi ya uandishi wa habari, tumtafutie kazi sehemu itayomuweka bize muda wote ili akose muda wa kujichanganya na watu" Jimmy alitoa ushauri,
"Yeah ni jambo zuri hilo, ngoja tuchukue madaraka rasmi ndio tujue pa kumpachika" Tammy Semmy aliongea kwa sauti tulivu,
"Kwa hiyo nini kinafuata kwa huyo dogo katika muda huu?" Jimmy aliuliza,
"Kamlete huyo dogo, anatakiwa awe huru" Tammy Semmy aliongea na Jimmy akaenda mpaka torture chamber na kumchukua Tom kisha akampeleka sebuleni.
"Cheki alivyo choka, dogo huyu ni lazy sana, hajateswa hata kidogo ila yupo hoi" Gabby aliongea huku akicheka,
"Tom, tunakuachia ila usichoke kutupa ushirikiano pindi tunapokuhitaji" Tammy Semmy alitoa maneno yaliyompa nguvu mpya Tom, kwa maana alishaanza kukata tamaa,
"Dogo haamini yaani, anaona kama mazingaombwe vile" Jimmy aliongea baada ya kumuona Tom akiwa amebung'aa tu,
"Kama ulikuja na kitu chochote sema uletewe" Tammy Semmy alimwambia Tom,
"Kaja kama alivyo" Jimmy alijibu,
"BQ mpeleke huyu" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia yule mwanadada katili,
"Sawa Mkuu" BQ alijibu huku akimuangalia Tom, kisha akanyanyuka na kumfunga Tom kitambaa cheusi machoni na kuanza kumsukuma kuelekea nje,
"Utampatia na hii" Tammy Semmy aliongea huku akimrushia BQ bahasha ndogo ya khaki iliyoonekana ina pesa, BQ akaidaka na kuachia tabasamu laini kisha akaendelea kumuongoza Tom mpaka lilipo gari na kumpakia, kisha akaondoka kwa mwendo wa taratibu.
Gari ilitembea mwendo wa nusu saa na ikasimama, kisha BQ akamtoa Tom kile kitambaa cheusi machoni, na hapo ndipo Tom aliweza kupaona tena kwake, wakatelemka wote na kuingia moja kwa moja kwenye chumba cha Tom ingawa kuna baadhi ya majilani walionekana kumshangaa sana Tom ila wala yeye hakuonekana kujali hilo.
"Kuna mzigo wako hapa" BQ aliongea kwa tabasamu huku akiirusha mezani ile bahasha ya karatasi,
"Kwa hiyo mnateka watu alafu mnawalipa?" Tom aliuliza baada ya muda mrefu wa kukaa kimya,
"Hiyo ni bahati kwako, sisi tukiteka uwa tunaua kabisa" BQ aliongea na kuachia tabasamu na kufanya sura yake ionekane nzuri kama malaika, kumbe ni shetani,
"Mwisho wa haya yote ni nini?" Tom aliuliza kwa hasira,
"Hupaswi kujua ilo, wewe angalia maisha yako tu" BQ alimjibu kisha akapiga hatua kama anataka kuondoka, akasimama na kugeuka nyuma kanakwamba amesahau kitu,
"Nilisahau kukupa ujumbe wako, kuanzia leo unatakiwa uachane kabisa na masuala ya uhandishi wa habari" BQ aliongea kisha akaanza kuondoka,
"Nyie wapuuzi nini? nikiacha hii kazi mtanilisha nyinyi?" Tom aliuliza kwa hasira,
"Mpuuzi baba yako na mama yako, na sitaki utoe neno jingine, cha muhimu fuata maelekezo niliyokupa" BQ aliongea kisha akawa anaelekea mlangoni kwa lengo la kuondoka, ila kabla hajafika mlangoni alishtuka kuona polisi wawili wenye gwanda wakiingia kwa fujo,
"Rudi ndani" Polisi mmoja aliongea kwa mamlaka na kuwafanya Tom na BQ washangae uvamizi huo wa ghafla na hasa mtu aliyekuwa na wasiwasi mkubwa alikuwa ni BQ...
BQ akarudi nyuma kwa tahadhari sana huku akijaribu kuzisoma zile sura za wale polisi,
"Dada kaa chini" Askari mmoja alimwambia BQ na BQ akajiweka kwenye kochi na mkono wake mmoja ulikuwa upo karibu sana sehemu alipohifadhi bastola yake, Tom yeye alishaona ni kitu gani BQ atakifanya kama mambo yanaweza kuharibika muda huo,
"Aisee mbona mmenivamia tu nyumbani kwangu, tunatiana hofu" Tom aliongea kwa sauti ndogo huku akiwaangalia wale askari,
"Kwanza tungependa tukutambue, wewe ndio Thomas Anthony?" Askari alimuuliza Tom,
"Ndio, ni mimi" Tom alijibu huku akihisi kuna kitu kisicho cha kawaida kinaendelea juu yake,
"Sawa kabisa, sisi ni polisi kutoka kituo kidogo cha hapa hapa mtaani, tuliletewa taharifa kuwa siku mbili hizi umepotea na hata simu zako zilikuwa hazipatikani. Hizo ripoti zililetwa kutoka kituo kikuu cha polisi na aliyezipeleka uko ni mtu anayedai ni bosi wako, anaitwa Othman Tafu, kwa hiyo hizo ripoti ilibidi ziletwe hapa kwa kuwa ndio kituo kilichopo karibu na unapoishi, na sisi tulikuwa tunaendelea kukutafuta na tukatoa taharifa kwa majirani zako kuwa ukionekana popote tupigiwe simu, na nashukuru wametii agizo, wametupigia siku muda mchache uliopita na kutujulisha umerudi kwako. Je upo salama?" Askari aliuliza baada ya kutoa maelezo ya kutosha,
"Ndio, nipo salama" Tom alijibu na kumfanya BQ atabasamu kwa maana hakutegemea kama Tom angejibu vile,
"Unaweza kutuambia kipindi hicho chote ulikuwa wapi?" Askari alimuuliza tena Tom,
"Sasa afande hilo ni swali gani, mbona kama mnaniuliza maswali yanayohusu mambo yangu binafsi?" Tom aliuliza huku akijifanya hapendezwi na maswali ya wale polisi,
"Jukumu letu kujua, tunataka tupate majibu ili tuyarudishe kituo kikuu" Askari alijibu kwa ustaharabu,
"Nilikuwa kwa mpenzi wangu, huyu hapa" Tom alijibu huku akimnyooshea kidole BQ,
"Oooh, basi huenda hukuwajulisha wenzako ni wapi ulipo" Askari aliongea,
"Nadhani haikuwa na maana yoyote kuwajulisha, kwanza sio ustaharabu eti kila unapoenda kwa mpenzi wako unatangazia watu" Tom alizidi kutoa majibu yaliyomfanya BQ aendelee kutabasamu,
"Lakini usingezima simu basi, maana ungekuwa hewani haya mambo yasingefika huku kwetu" Askari mwingine aliongea,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sawa wakuu nimewaelewa, nitawasha simu alafu nitamjulisha bosi wangu kuwa nipo salama" Tom aliongea,
"Sawa, sisi acha twende, tunafurahi kukukuta upo salama" Askari aliongea huku akinyanyuka kutoka kwenye kochi,
"Poa, na mie nawashukuru kwa kuwajali raia wenu" Tom aliongea huku akiwapa mkono wale askari,
"Ndio kazi yetu hiyo" Askari walijibu kisha wakaaga na kuondoka zao huku wakimuacha Tom na BQ wakiwa wanawasindikiza kwa macho.
"Una akili sana wewe, maana umeokoa nafsi yako" BQ aliongea huku akitabasamu,
"Nimekuokoa wewe na wala si nafsi yangu" Tom alijibu huku akifuta meza yake ya kioo,
"Umejiokoa wewe, kwa maana chochote kibaya kingetokea basi humu ndani asingebaki mtu" BQ aliongea kwa kujidai,
"Kweli asingebaki mtu, wote tungekuwa polisi" Tom alijibu,
"Sio polisi, wote mngekuwa ahera, ndipo ungeshuhudia unyama wangu vizuri" BQ aliongea huku akitabasamu, uzuri wa huyu dada ni kwamba tabasamu ni kitu ambacho hakimbanduki usoni,
"Hata mimi ungeniua?" Tom alimuuliza,
"We si Mbwa tu, nakuua alafu hakuna atakayenihoji" BQ aliongea huku akiinuka kwenye kochi na kumfanya Tom amuangalie tu,
"Msichana mrembo umejiingiza kwenye unyama, kama tatizo ni pesa si bora ungejiingiza kwenye umama lishe tu" Tom aliongea,
"Tatizo sio pesa, kwa elimu yangu niliyonayo naweza kuajiliwa popote duniani na mshahara nitakaokuwa nalipwa naweza kujenga nyumba za kifahari zaidi ya kumi ndani ya mwaka" BQ alijibu kwa maringo huku akitabasamu,
"Sasa kwanini umeungana na awa wauaji?" Tom alimuuliza,
"Kweli nimeamini wewe ni Muandishi, maswali hayakuishi mdomoni? Ila sio kila swali linajibika kirahisi hata kama swali lenyewe ni rahisi" BQ alijibu kisha akaondoka zake na kumuacha Tom akimuangalia huku akitabasamu peke yake.
**********************
Koplo Mbegu baada ya lile tukio ya picha za yule kiumbe kutoonesha sura, hakuwa na njia nyingine zaidi ya kumtafuta rafiki yake Ghislain ili amsaidie michoro, kwa kuwa sura ya kile kiumbe bado alikuwa nayo kichwani, hakuona sababu ya kuchelewa kumtafuta.
Alichukua simu yake na kumpigia kisha akamuomba aje kwake.
Baada ya saa moja, Ghislain alifika akiwa tayari ameshachangamka kutokana na kupata kinyaji uko atokapo.
"Kweli wewe ni rafiki yangu wa kweli, yaani muda wowote ninaokuhitaji uwa unakuja" Koplo Mbegu aliongea huku akitabasamu,
"Acha habari zako, kwanza leta bia mbili hapa kabla sijajua shida yako" Ghislain aliongea huku akifuta jasho kwa kutumia kitambaa chake cha mkononi,
"Kuna mchoro nataka unisaidie kuchora, baada ya hapo utakunywa bia zaidi ya mbili unazozitaka" Koplo Mbegu aliongea,
"Alafu ule mchoro niliokucholea wa kile kibwengo chako nimeona leo umezagaa kila mahali" Ghislain aliongea,
"Huo mchoro haunihusu, ebu nisaidie kuchora mchoro nilionao kichwani muda huu" Koplo Mbegu aliongea huku akimsogezea vifaa mwenzake,
"Najua katakua kakibwengo kingine unataka nikuchoree" Ghislain aliongea,
"Vifaa hivyo hapo, jiandae nianze kukupa taswira sasa" Koplo Mbegu aliongea huku akijiweka kwenye kochi,
"Anza kumuelezea huyo mtu, mimi nipo tayari" Ghislain aliongea huku akiwa ameshika penseli na kisha Koplo Mbegu akaanza kumuelezea namna kile kiumbe kilivyo na baada ya muda Ghislain alimaliza na kumpatia Koplo Mbegu ule mchoro,
"Swadakta kabisa, huyu mtu ndie ninaemtaka mimi sasa" Koplo Mbegu aliongea huku akifurahi,
"Kafanyaje?" Ghislain alimuuliza,
"Huyu kuna kesi ndogo naishughulikia kuhusu yeye" Koplo Mbegu alimjibu mwenzake,
"Hiyo kesi itakuwa kubwa tu, kama kesi ingekuwa ndogo wala usingeangaika na michoro hiyo" Ghislain aliongea huku akimtazama mwenzake,
"Ushaanza mambo yako, ngoja nikuletee bia kwanza" Koplo Mbegu aliongea huku akielekea kwenye friji na kuchokoa bia tano na kurejea nazo mezani,
"Opener iko wapi, au nifungulie meno?" Ghislain aliuliza huku bia moja ikiwa mkononi, kwa kweli alikuwa na furaha,
"Ngoja wewe, usifungue kwanza" Koplo Mbegu aliongea huku akionekana kutafuta kitu ndani ya kabati lake la nguo, baada ya dakika kadhaa alirudi huku akiwa na begi dogo la mgongoni,
"Hizi utaenda kunywea kwako, mimi nataka kulala muda huu" Koplo Mbegu aliongea huku akizitia ndani ya begi zile bia,
"Wewe mwehu nini? kwa hiyo unaona kazi yako imeisha ndio unanifukuza?" Ghislain aliuliza huku akimshangaa rafiki yake,
"Sio nakufukuza Jamaa yangu, wewe nenda tu mimi nilale, nikisema nikusubiri mpaka umalize bia zote hizi nadhani itakuwa usiku sana" Koplo Mbegu aliongea huku akifunga zipu ya begi,
"Sawa bwana, ila ukiniita tena siwezi kuja" Ghislain aliongea huku akionesha hajapenda kitendo alichofanyiwa na rafiki yake,
"Bwana wewe nenda, chukua na hii ya usumbufu" Koplo Mbegu aliongea huku akimpatia pesa Ghislain,
"Yaani siku hizi una vijisenti ndio maana una kiburi" Ghislain aliongea huku akizipokea zile pesa kisha akalibeba lile begi lenye bia na kuondoka zake.
"Sasa huyu ni nani?, na kwanini awe na mauza uza namna hii?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akiwa ameshika karatasi yenye mchoro wa yule kiumbe.
Hakutaka kujisumbua sana kupoteza muda, aliamua alale tu ili asubuhi ndio aanze kuutafuta uhalisia wa huo mchoro.
Akajitayarisha na kulala zake.
**********
Asubuhi mishale ya saa tatu, Koplo Mbegu alikuwa kwenye bajaji kuelekea kule nje ya mji.
Sema kuna kitu kilikuwa kinamshangaza njiani, kila sehemu ambapo alibandika ile picha yenye mchoro wa ajabu siku iliyopita, picha ilikuwa haionekani ila yalibaki maneno tu, alijiuliza mwisho hakupata jibu sahihi.
Safari yake iliishia katika kile kijiji na kumtafuta yule kijana mwenye maneno mengi na kumpata,
"Bora nimekuona kaka, zile picha zote uliziniachia jana zimefutika" Kijana mwenye maneno mengi aliongea kabla hata hawajasalimiana,
"Zimefutika? zimefutikaje?" Koplo Mbegu aliuliza ingawa alishaona hilo tukio njiani,
"Hakuna hata anayejua, tulishangaa tu picha Hamna ila maandishi yalibakia" Kijana mwenye maneno mengi aliongea,
"Mbona haya mambo yanakuwa ya ajabu hivi?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Ila nilikwambia kuwa hiki kiumbe sio cha kawaida, inawezekana ni jini hilo" Kijana mwenye maneno mengi aliongea,
"Alafu kitu cha kushangaza kuna mtu alinijia nyumbani jana na kudai yeye ndio yule wa kwenye ile picha, ila sura yake ilikuwa ya kawaida na wala sio ya kutisha kama ya kwenye ule mchoro" Koplo Mbegu alimueleza yule kijana,
"Sasa si ungemkamata?" Kijana mwenye maneno mengi aliuliza,
"Ningemkamataje wakati sura yake haikuwa kama ya yule ninaemtaka" Koplo Mbegu aliongea,
"Mtu kama amejileta mwenyewe ulitakiwa umkamate kaka" Kijana mwenye maneno mengi aliongea,
"Ila kweli nilitakiwa nimkamate, ila nitampata tu kwa maana nina picha yake" Koplo Mbegu aliongea,
"Ebu naomba hiyo picha nami nimuone" kijana mwenye maneno mengi aliongea,
"Ikamate vizuri, isichafuke" Koplo Mbegu aliongea wakati akimpatia ile picha na yule kijana akaanza kuitazama,
"Haiwezekani, itakuwa umekosea hii picha" Kijana mwenye maneno mengi aliongea kwa hamaki huku akiwa anaiangalia ile picha,
"Kwani vipi? Mbona umehamaki hivyo, unamjua?" Koplo Mbegu alimuuliza kwa mshangao,
"Ndio namjua" Kijana mwenye maneno mengi alijibu na kumfanya Koplo Mbegu amuangalie vizuri yule kijana na pia alifurahi kwa maana aliona kazi imekuwa rahisi......
Baada ya mlango kufunguka, alitoka Sudy Bakari na kuwapita wakina Jimmy ingawa aliwaona vizuri mikono yao ilivyoshika bastola wala hakuonekana kuwajali,
"We simama hapo" Gabby aliongea kwa sauti ya amri iliyomfanya Sudy Bakari asimame na kugeuka,
"Mnataka nini viumbe?" Sudy Bakari aliuliza huku akiwaangalia,
"Unatakiwa ukae kimya, kuanzia muda huu utafuata kile tunachotaka sisi, vinginevyo tunakufumua ubongo" Gabby aliongea huku akionesha hana mzaha kabisa,
"Sio kila unachoweza kuongea unaweza kukitenda" Sudy Bakari aliongea kisha akageuka na kuanza kuondoka zake,
"We Jamaa ujue hatufanyi utani hapa?" Jimmy aliongea kwa ukali na kufanya Sudy Bakari asimame tena na kugeuka,
"Mnataka nini kutoka kwangu viumbe nyie?" Sudy Bakari aliuliza huku akiwatazama kwa zamu,
"Nyoosha mpaka nje ya geti, tuna mazungumzo tunataka tuzungumze na wewe" Gabby aliongea,
"Hilo halina shida, twendeni" Sudy Bakari aliongea na kuanza kuelekea nje, Gabby na Jimmy pia walikuwa wanamfuata kwa nyuma.
Waliongozana mpaka nje ya geti, walipofika nje ya geti Sudy Bakari alisimama na kuwatazama,
"Mnataka kusema nini?" Sudy Bakari aliwauliza,
"Hatuwezi kuongelea hapa, twende sehemu tukaongelee" Gabby alijibu,
"Twendeni viumbe, mimi sina shida" Sudy Bakari alijibu,
"Ingia ndani ya gari" Jimmy alimwambia huku akiwaza namna wanavyomteka kirahisi mtu huyo bila hata kutumia nguvu kubwa,
"Kuteka sio kitu kigumu, ugumu ni aina ya kiumbe mnachokiteka" Sudy Bakari aliongea wakati akipanda gari na kumfanya Jimmy ashtuke kwa maneno yaliyotolewa na mtu huyu.
"Una maana gani kusema hivyo?" Gabby aliuliza huku akiwasha gari,
"Muulize rafiki yako anaefurahia kuniteka bila kutumia nguvu kubwa" Sudy Bakari alijibu na kumfanya Jimmy aanze kuogopa kwa namna mtu huyo alivyo wa ajabu, yaani ameweza kung'amua ni kitu gani yeye anakiwaza?
"Hakuna anaefikiria kukuteka, na kwanza tukiamua kukuteka hatushindwi" Gabby aliongea huku akiendesha gari, baada ya robo saa walifika na Gabby akaliingiza gari ndani ya uzio wa nyumba yao ya kufanyia maasi.
"Shuka, tumefika" Jimmy aliongea huku akimfungulia mlango, Sudy Bakari akashuka na kuongozana nao mpaka ndani,
"Kaa hapo chini" Gabby aliongea huku akioneshea sehemu ya sakafu,
"Sijawahi kukaa chini, hata kwetu hakuna kiumbe chochote cha kunikalisha chini" Sudy Bakari aliongea huku akikaa kwenye kiti, na kipindi hicho Waziri wa ulinzi nae alijisogeza eneo lile,
"Usilete kiburi ujue, tayari upo kwenye himaya yetu" Gabby aliongea huku akimfuata Sudy Bakari kwa hasira,
"Kiumbe, Inawezekana mawazo yako yako kinyume nyume sana, hauwezi kusema nipo kwenye himaya yenu wakati hamna uwezo wa kunifanya kitu chochote" Sudy Bakari aliongea na kumzidishia hasira Gabby,
"Hivi hunijui vizuri wewe?" Gabby aliongea na kurusha kofi kumuelekea Sudy Bakari, alishtukia tu mkono wake unadakwa hewani,
"Hakuna kiumbe atayeweza kunipiga wala kunidhuru katika jambo la haki" Sudy Bakari aliongea na kumuacha Gabby,
"Nipe bastola yangu" Gabby aliongea huku akimuangalia Jimmy,
"Hatakiwi kufa lakini" Jimmy alimwambia Gabby,
"Viumbe nyie mlinichukua kwa lengo la kuongea au kupigana?" Sudy Bakari aliuliza,
"Hutakiwi kujua" Gabby alijibu kibabe huku akiichukua bastola yake na kuanza kumfuata Sudy Bakari,
"Kama sitakiwi kujua, basi pia sitakiwi kuwa hapa" Sudy Bakari aliongea huku akiinuka na kuanza kuondoka,
"Simama Mbwa wewe" Gabby aliongea kwa hasira huku akiwa na dhamira ya kufyatua risasi endapo Sudy Bakari atakahidi amri, Sudy Bakari akageuka kwa kasi kama mshale na kuipiga ile bastola ikamtoka Gabby mkononi, Gabby akataka kuiwahi ili aiokote, akapigwa kiwiko cha pua na kuanguka, Sudy Bakari akabaki anamuangalia,
"Usifanye chochote, tunafyatua risasi" Waziri wa ulinzi aliongea huku akiwa ameshika bastola sambamba na Jimmy, Sudy Bakari akatabasamu kisha akanyanyua mguu wake na kuikanyaga ile bastola ya Gabby iliyokuwa chini, ikavunjika utasema amekanyaga plastiki, wote wakapigwa na butwaa kuhusu uhalisi wa mtu huyu,
"Viumbe wabishi msio na uoga na matendo ya ajabu ninayofanya, pigeni tu hizo risasi" Sudy Bakari aliongea huku akianza kutoka nje, Waziri wa ulinzi akataka kupiga risasi lakini jimmy akamzuia,
"Muache aondoke" Jimmy aliongea huku akimuangalia Waziri wa ulinzi, Sudy Bakari akatoka na kutokomea zake nje,
"Kwanini umenizuia?" Waziri wa ulinzi aliuliza baada ya Sudy Bakari kupotea machoni mwao,
"Yule sio mtu, yaani Nina uhakika kabisa sio binadamu yule" Jimmy aliongea huku akikaa kwenye kochi,
"Acha upuuzi wewe, uoga wako ndio unafanya uamini kuwa yule sio mtu" Gabby aliongea kwa hasira huku akijinyanyua kutoka chini,
"Si mmeona wenyewe kwa macho yenu namna alivyoikanyaga hiyo bastola na kuitawanya, nani asiyejua kuwa hiyo bastola ni chuma? ni binadamu gani anaweza kuitawanya chuma kwa kukanyaga tu?" Jimmy aliwauliza,
"Mhh...inawezekana kweli lakini, ni ngumu mtu kuitawanya chuma kwa mguu" Waziri wa ulinzi alionekana kukubaliana na Jimmy,
"Mtakuja kujijitea wenyewe kwa Tammy Semmy" Gabby aliongea kwa hasira huku akielekea chumbani kwake na kuwaacha Jimmy na Waziri wa ulinzi wakimuangalia tu.
********************
Tom aliamka mapema na kuamua kufanya usafi chumbani kwa maana ni muda mrefu hajapasafisha, kwa kweli siku hiyo alifanya usafi wa nguvu, alifagia na kudeki, kisha akafuta vumbi ukutani, dirishani na vyombo vyote aliosha, baada ya hapo alianza kufua mashuka na nguo zote chafu, kisha akaoga na kuanza kupitia vijitabu vyake alivyokuwa anaandika habari kuhusu kesi ya memory card, wakati anaipitia ile habari yake, kuna kipengele cha mwisho alikisoma na hapo ndipo alipokumbuka kuwa bado alikuwa hajamaliza kufanya mahojiano na watu wote aliopanga kuwahoji, na mtu muhimu aliyemuona kwa wakati huo ni mke wa marehemu mzee Bonny. Kama unakumbuka kuna hakimu ambaye aliuawa pia alikuwa ni mke wa Mzee Bonny, ila waliachana na mzee Bonny alimuoa mwanamke mwingine, ila Tom alichotaka kwenda kumuhoji mwanamke huyo ni kutaka kumuuliza ni kitu gani anachokijua au anachohisi kilichofanya Mzee Bonny auawe kinyama vile?.
Tom alijitayarisha na kutafuta usafiri uliomfikisha sehemu husika na kwa bahati nzuri alikuwa na kumbukumbu nzuri juu ya nyumba anayoenda.
Alifika katika hiyo nyumba na kumkuta mwanamke ambaye alimtambua ndiye mke wa Mzee Bonny, alimkuta akiwa amekaa kibarazani anasoma magazeti, Tom akamfuata na kumsalimia, kisha akajitambulisha na kumwambia shida yake, yule mama alimuelewa na kwenda ndani kumletea kiti kisha wakakaa,
"Haya niambie mwanangu, ulikuwa unataka kujua nini sasa kuhusu kifo cha Mzee za Bonny?" Mke wa mzee Bonny alimuuliza Tom,
"Nilitaka kujua kuwa kabla ya kifo chake mzee, hajawahi kukuambia kama ana ubaya na mtu?" Tom aliuliza,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapana kwa kweli, Mzee Bonny alikuwa msiri sana na ilikuwa ngumu sana kujua mambo yake" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Na kwanini alijitenga na nyie akaenda kuishi peke yake?" Tom alimtupia swali jingine,
"Kwa kweli sababu haswa siijui, ila kuna maneno ya mafumbo alikuwa anaongea kabla hajahama, ila sijajua mpaka leo alichokuwa anamaanisha" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Maneno gani hayo ya mafumbo ambayo alikuwa akiyaongea?" Tom aliuliza,
"Mara nyingi alikuwa akisema hii nyumba imeingiliwa na virusi, mara aseme kuna shetani kati yetu. Mimi sikuwa namuelewa kwa kweli na hiyo ikasababisha nikwaruzane nae na tukatengana kwa sababu ya hivyo vineno neno" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Kwani hapa mnaishi watu wangapi? labda hivyo virusi alivyokuwa anamzungumzia ni miongoni mwa watu wa hapa" Tom aliuliza,
"Sio kweli, hapa tunaishi watu watano tu nikiwemo mimi, watoto wetu watatu na msichana wa kazi" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Sawa, je unaweza kuniambia ni kwanini mzee Bonny aliachana na mke wake wa kwanza na kuishi na wewe?" Tom alimtupia swali jingine yule mwanamke,
"Yeye mwenyewe alikuwa anadai kule kuna watu walikuwa wanawatisha yeye na mke wake na sababu ya vile vitisho ilikuwa ni kesi ambayo hakuniambia ni kesi gani, na hiyo kesi ilikuwa inaendeshwa na marehemu mke wake" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Na alivyohamia hapa kwako hao watu hawajaja hapa na kuendelea kumpa hivyo vitisho?" Tom aliuliza,
"Hapana kwa kweli, sijawahi kuwaona, labda kama walikuwa wanakuja kwa siri bila ya mimi kuwaona" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Na wewe unafanya kazi wapi?" Tom alimuuliza mke wa mzee Bonny,
"Mimi ni mwalimu tu wa shule ya msingi, leo sijaenda si unajua mtu ukifiwa na mume unapewa muda wa kutosha wa kupumzika?" Mke wa mzee Bonny alijibu kisha akauliza,
"Na watoto wako wapi?" Tom aliendelea kuuliza,
"Watoto wawili wapo mwanza, niliwaacha uko, mmoja yeye anasoma chuo kikuu hapa hapa, muda huu yupo chuo wana mitihani, kwa hiyo hapa nipo na mfanyakazi tu" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Huyo mfanyakazi inaelekea ni wa muda mrefu sana ee?" Tom aliuliza huku akitabasamu,
"Kiasi, maana alikuja kuomba kazi hata kabla mzee Bonny hajahamia hapa, kumbukumbu zangu zinaonesha kuwa baada ya huyu binti kuanza kazi hapa, wiki moja baadae ndio mzee Bonny alihamia hapa" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Sawa mama, nashukuru kwa ushirikiano wako" Tom aliongea huku akikusanya vijidaftari vyake vilivyokuwa mapajani,
"Wewe ni Muandishi wa gazeti gani kwani? maana hukuniambia ulichosema wewe ni mwandishi wa habari tu" Mke wa mzee Bonny aliuliza wakati Tom akinyanyuka,
"Wa radio, inaitwa Tafu FM" Tom alijibu huku akicheka,
"Hata siijui, siku hizi kuna radio nyingi sana" Mke wa mzee Bonny aliongea,
"Samahani mama, unaweza kunisaidia maji ya kunywa?" Tom alimuuliza mke wa mzee Bonny,
"Hata usijali mwanangu, ngoja nimuite Dada wa kazi" Mke wa mzee Bonny aliongea kisha akapaza sauti kumuita huyo dada wa kazi,
"Abee mama" Dada wa kazi aliitika na baada ya muda alikuja na kusimama mbele ya mke wa mzee wa Bonny, Tom hakutaka hata kumuangalia kwa kuwa alikuwa bize na simu yake,
"Kamletee kaka maji" Mke wa mzee Bonny alimuagiza na kisha yule dada akaenda ndani, baada ya dakika moja alirudi na maji yakiwa kwenye glass,
"Haya hapa kaka" Dada wa kazi aliongea na kumfanya Tom aachane na simu, Tom akanyanyua uso wake ili ayapokee maji, hapo ndipo alipotamani kukimbia, maana huyo dada wa kazi hakuwa mwingine, alikuwa ni BQ, tena alikuwa akitabasamu huku akiwa amevaa khanga chakavu na kilemba kikuukuu kilichofubaa.....
Tom alijikuta glass ya maji inamdondoka mkononi na kuanguka chini vipande vipande, Mke wa mzee Bonny akashtuka na kuacha kusoma gazeti,
"Samahani mama" BQ aliongea kwa sauti ya upole na wasiwasi huku akiokota vipande vya glass vilivyosambaratika ardhini,
"Bertha jamani kila ukijaga lazima univunjie vyombo, sasa si utanimalizia vyote, hii itabidi nikukate mshahara wako" Mke wa mzee Bonny aliongea huku akionekana kutofurahishwa na glass kuvunjika,
"Ni mimi mama imeniponyoka bahati mbaya" Tom alijibu huku akitetemeka,
"Aah nilijua labda ni Bertha, maana huyo kuvunja vyombo ni kawaida" Mke wa mzee Bonny aliongea,
"Hata hivyo itabidi niilipe tu hii glass" Tom aliongea huku akiingiza mikono mfukoni,
"Acha tu mwanangu, bahati mbaya" Mke wa mzee Bonny aliongea,
"Nashukuru" Tom alishukuru,.
"Kalete tambala la deki wewe, unazubaa zubaa tu kumuangalia mwanaume" Mke wa mzee Bonny aliongea huku akimuangalia BQ ambayo hapo alikuwa akimuita Bertha. BQ akaelekea kwenda kuchukua tambala la deki na kumuacha Tom akiwa na mawazo na hofu kuhusu mwanamke huyo.
"Mama ulisema kuwa huyu kila akija ndio huvuja vyombo, kwani hakai hapa?" Tom alimuuliza mke wa mzee Bonny,
"Bertha hakai hapa, anakaa kwao ila hata kwao sipajui na wala hajawai kunionesha wazazi wake ingawa aliniambia anao, nimetokea kumuamini tu" Mke wa mzee Bonny alijibu,
"Na kwanini siku nyingine haji?" Tom alimuuliza mke wa mzee Bonny huku akihisi hicho kirusi ambacho mzee Bonny alikuwa akikizungumzia inawezekana ni BQ,
"Uwa anasomea ufundi Cherehani, hata hivyo leo alikuja ghafla tu hata sijamuita, ameniambia ameona hana kazi bora aje kunisaidia kwa kuwa nipo peke yangu" Mke wa mzee Bonny alijibu na wakati huo huo BQ alikuwa anarudi na dekio akaanza kufuta maji,
.sana.
Tom alitembea mpaka kwenye kituo cha daladala na kusimama huku akisubiri usafiri, baada ya dakika mbili mbele yake ilisimama gari nyeusi, ilikuwa land cruiser vx, kioo kikashushwa na aliyekuwepo kwenye gari alikuwa Jimmy na Gabby,
"Ingia twende" Jimmy alimwambia Tom, Tom hakutaka hata kubisha akaingia na kukaa siti ya nyuma pamoja na Jimmy. Gari ilitembea kuelekea katika ile nyumba yao na iliwachukua takribani dakika kumi na tano mpaka kufika, wakatelemka na wote watatu wakaingia ndani, mpaka muda hakuna mtu yoyote aliyekuwa amemuongelesha Tom.
Ndani walimkuta Waziri wa ulinzi na Tammy Semmy wakiwa wamekaa, Tom akawasalimia na kukaa katika kochi,
"Kijana ni habari gani nyingine unayoitafuta wakati unajua kila kitu?" Tammy Semmy alimuuliza Tom,
"Hakuna habari ninayoitafuta" Tom alijibu huku akijifanya kushangaa,
"Kwa mke wa mzee Bonny ulifuata nini sasa?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Aaah kile nilienda kuandika habari nyingine kabisa, wala hazihusiani na nyinyi" Tom alijibu huku akitabasamu na kushtukia anapigwa kofi Kali sana la shingo na Gabby aliyekuwa amesimama nyuma yake,
"Habari ya kifo cha mzee Bonny, si ndio?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Ndio" Tom alijibu huku mkono wake ukiwa umeshika shingoni eneo ambalo alipigwa,
"Shukuru sana Mungu kwa maana BQ alikuwa anakumaliza pale pale na yale maji aliyokuwa amekuletea, tulimzuia tu ndio maana akaangusha glass chini, vinginevyo ungekuwa marehemu wewe" Waziri wa ulinzi aliongea huku akionekana ana hasira,
"Nadhani tunafanya makosa sana kumuacha hai mtu huyu, huyu afe tu" Gabby aliongea na muda huo huo BQ alikuwa anaingia, yaani alikuwa na muonekano tofauti na ule ambao Tom alimkuta nao nyumbani kwa mzee Bonny, BQ alipofika alielekea moja kwa moja sehemu alipokuwa Tom na kumpiga makofi mawili ya haraka haraka,
"Mtu gani wewe umepewa nafasi ya kuishi alafu unataka kujiharibia, Mkuu nipe nafasi nimuue tu kwa maana nimeshaona mwisho huyu mtu anaweza kutusababishia matatizo" BQ aliongea kwa hasira na kwa mara ya kwanza Tom aliweza kumuona BQ mwingine kabisa, sio yule BQ mwenye kutabasamu kila muda,
"Muache kwanza, bado hajajua anachokifanya" Tammy Semmy aliongea,
"Mtu mkubwa kabisa huyu, anafanya mskusudi tu kwa kuwa hatujamkata hata kipande cha ukucha ili ayapate maumivu yetu" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Mpeleke kwake" Tammy Semmy alimwambia BQ, BQ hakupenda hata kuongozana na Tom ila ilibidi atii tu amri ya mkubwa wake,
"Huyu angefungiwa kule torture chamber awe anakula mlo mmoja tu hata mwezi mzima" Jimmy aliongea wakati BQ anamtoa nje Tom.
BQ aliondoka na Tom mpaka nyumbani kwa Tom na kumshusha kisha wakaingia ndani na kukaa kwenye kochi,
"Samahani naomba nikuulize" Tom aliongea baada ya kumuona BQ hana mpango wa kusema chochote na muda wote alionekana ana hasira,
"Unataka kuuliza nini?" BQ aliuliza ila sauti yake ilijitahidi kuficha hasira,
"Unawezaje kujigawa namna hiyo, Mara mfanyakazi wa mzee Bonny Mara uko huku?" Tom aliuliza,
"Bado inaendelea na maswali ya kipumbavu?" BQ aliuliza huku akinyanyuka, alikuwa anataka kuondoka,
"Msichana mzuri ila matendo ya kinyama" Tom aliongea baada ya kumuangalia BQ wakati akiondoka,
"Wewe Mbwa, samahani acha kunifuatilia kabisa, yaani hapo ulipo naweza kukufanya chochote kile" BQ aliongea kwa hasira baada ya kukasirishwa na maneno ya Tom,
"Hutakiwi kusifiwa?" Tom aliuliza lakini hakujibiwa na badala yake BQ aliondoka zake na hapo Tom kweli aliamini siku hiyo BQ alikuwa kwenye hasira kubwa sana, hasira zilizosababishwa na Tom mwenyewe.
"Aende zake uko" Tom aliondoka peke yake baada ya BQ kuondoka zake.
*************
Koplo Mbegu alishachanganywa na matukio yale, alikuwa anaona kama ni masuala ya kishirikina vile,
"Sasa inawezekanaje mtu afe alafu aonekane tena duniani? au msukule?" Koplo Mbegu alijiuliza huku akiwa hana jibu,
"Na kama ndio huyo amemuua rais ni kwa sababu gani au ushirikina?" Koplo Mbegu aliendelea kujiuliza maswali ambayo yeye hakuwa na majibu nayo.
Baada ya kukaa kwa muda huku akiwaza, alipigiwa simu na mkuu wake na kumtaka wakutane sehemu walipokutana mara ya mwisho, Koplo Mbegu akavaa fulana yake na kuelekea mahali alipoitwa na mkuu wake.
Alipofika hata hakupata tabu kujua sehemu alipokuwepo mkuu wake, alijongea na kuvuta kiti kisha akakaa, akamsalimia mkuu wake,
"Niambie ulipofikia" Mkuu wake aliongea huku akimuangalia,
"Hii kesi inanishinda, naona inapoelekea uko siiwezi" Koplo Mbegu aliongea,
"Kwanini ikushinde?" Mkuu wake aliuliza kisha Koplo Mbegu akamueleza kila kitu kilivyokuwa na mkuu wake akabaki na mshangao,
"Sasa fikiria mambo kama hayo unakutana nayo, si mambo ya kichawi kabisa?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Sasa huyo mtu wa ajabu kwanini hujamuuliza anafanya mauji ili iweje?" Mkuu wake aliuliza,
"Ni ngumu kujua kama yeye ndiye anaefanya mauaji na pia jinsi alivyonijia ilikuwa ngumu kumuuliza kwa maana aliingia ndani kimiujiza" Koplo Mbegu alijibu,
"Ni shughuli nzito, sasa wewe usiogope, fuatilia tu kwa maana kama hicho kiumbe kingeamua kukudhuru kingekudhuru tu" Mkuu wake alimwambia,
"Mkuu hii kesi imenishinda" Koplo Mbegu aliongea kwa upole,
"Ninayokupa ni amri sio ombi" Mkuu wake aliongea huku akinyanyuka na kumuacha Koplo Mbegu akimuangalia tu,
"Alafu kesho ndio wanamzika rais, kama utaweza unaweza kuambatana na mimi ili ukafanye uchunguzi ndani ya jumuiko la watu watakaokuwepo kwenye maziko" Mkuu wa polisi aliongea na kuondoka zake huku akimuacha Koplo Mbegu akiuma meno kwa hasira.
"Huu utumwa sasa" Koplo Mbegu aliongea na kuipiga ngumi kwa hasira meza iliyopo mbele yake, kisha akainuka na kutoka nje ya bar na kuanza kutafuta usafiri bila mafanikio, akajaribu kumpigia simu dereva wake anaekodi bajaji yake na yeye pia akawa hapatikani, akaamua akae nje tu ili aombe lifti kwa mtu yoyote mwenye gari.
Akiwa amesimama hana hilo wala lile, bajaji ilikuja na kusimama mbele yake,
"Dah afadhali kwa maana nilishakata tamaa ya kupata usafiri na usiku huu sijui ningefanyaje" Koplo Mbegu aliongea huku akijipakia kwenye bajaji,
"Kituo wapi?" Dereva wa bajaji akamuuliza na Koplo Mbegu akataja sehemu anayokwenda na bajaji ikaanza safari, ilitembea mpaka anapokaa Koplo Mbegu na kusimama pale pale mlangoni kisha Koplo Mbegu akatelemka,
"Unanidai shilingi ngapi?" Koplo Mbegu aliuliza huku akiitoa pochi yake mfukoni,
"Ni msaada tu nimekusaidia" Dereva bajaji aliongea na kumshangaza Koplo Mbegu,
"Msaada vipi? kwani unaniju?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Ndio nakujua" Dereva bajaji alijibu,
"Mbona mimi sikujui" Koplo Mbegu aliuliza huku akiwasha tochi ya simu yake na kummulika usoni dereva wa bajaji, ndipo alipoiona sura yake kidogo akimbie, alikuwa Sudy Bakari na koti lake kubwa jeusi na buti zake za mgambo....
"Nilikuwa nakutafuta sana, ni bora nimekuona" Koplo Mbegu alijikaza na kuongea,
"Ulikuwa unamtafuta nani?" Sudy Bakari aliuliza,
"Wewe " Koplo Mbegu alijibu,
"Unanijua mimi?" Sudy Bakari aliuliza huku akimuangalia machoni Koplo Mbegu, na hapo Koplo Mbegu ndipo alipoyaona vizuri macho ya Sudy Bakari, yalikuwa na mboni ya bluu kama miale ya moto,
"Nakujua, wewe ni Sudy Bakari" Koplo Mbegu aliongea kwa kujiamini,
"kiumbe naomba nikuulize" Sudy Bakari aliongea huku bado akiendelea kumtazama,
"Uliza tu" Koplo Mbegu aliongea,
"Ukimchukua mbuzi ukamvika ngozi ya kondoo, ataendelea kuwa mbuzi au atakuwa kondoo?" Sudy Bakari aliuliza,
"Atakuwa ni mbuzi ila kwenye ngozi ya kondoo" Koplo Mbegu alijibu,
"Safi sana kiumbe, basi mimi sio Sudy Bakari, mimi ni mbuzi kwenye ngozi ya kondoo" Sudy Bakari alijibu kisha akaondoa bajaji na kumuacha Koplo Mbegu akimuangalia tu wakati ile bajaji ikizidi barabarani.
Koplo Mbegu akaingia ndani huku yale maswali yake kuhusu kiumbe hiki yakizidi kuongezeka maradufu,
"Huyu ni dereva bajaji, au jini? mbona macho yake yapo tofauti na binadamu wengine? Na kwanini amekataa yeye sio Sudy Bakari wakati sura na umbo ni la Sudy Bakari? au amevaa mwili wa mtu ila yeye siye Sudy Bakari?" Koplo Mbegu aliendelea kujiuliza,
"Kichwa kinauma bure kwa kuwaza mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wangu" Koplo Mbegu aliongea mwenyewe huku akivua suruali na kubaki na bukta fupi kisha akajitupa kitandani.
*******************
Siku mpya iliwadia, siku ambayo ndiyo yalipangwa yafanyike maziko ya Rais,
"Inabidi tuwahi kufika msibani, maana mimi ni mtu wa karibu sana familia ya marehemu" Tammy Semmy aliwaambia wenzake,
"Kwani ni lazima twende wote?" Jimmy aliuliza,
"Yaani anaetakiwa kubaki hapa ni huyu tu Waziri wa ulinzi" Tammy Semmy alijibu,
"Ni kweli lazima twende wote, si mnaona juzi mlifanikiwa kumuona yule mtu mnaedai ni kiumbe cha ajabu, tukienda wote inakuwa rahisi kufanya upelelezi wetu kwa maana tunajitawanya" BQ aliongea,
"Alafu kitu kingine ni kuhusu Waziri mkuu, nasikia nae anautaka urais, sasa cha muhimu nae auawe" Tammy Semmy aliongea,
"Tusimuue bila kupata uhakika, ni lazima tujiridhishe kwanza alafu ndio tuamue" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Kujiridhisha na nini? yule nilishamuona sio mtu kabisa tokea kipindi kile nipo nae monchwari, naona anajiona ana mamlaka makubwa kuliko mimi" Tammy Semmy aliongea huku akionekana hasira zikianza kumpanda,
"Ila sioni ulazima wa kumuua, ni kumzima tu kisiasa, tunatakiwa kumtaftia kashfa tu" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Alafu na wewe inabidi uende China ili ukafanyiwe madiliko ya sura, nikishachukua nchi natakiwa nikurudishe kwenye wizara yako ya ulinzi" Tammy Semmy alimwambia Waziri wa ulinzi,
"Siutaki uwaziri wa ulinzi, nipe umakamo wa rais au uwaziri mkuu" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Inabidi ushikirie wizara ya ulinzi kwa ajili ya kujua usalama wetu, mshahara wako utakuwa tofauti, utakuwa na pesa nyingi tu" Tammy Semmy alimwambia,
"Sawa, haina tabu" Waziri wa ulinzi alikubali,
"Jimmy na Gabby watakuwa walinzi wako, BQ atakuwa mlinzi wangu" Tammy Semmy aliongea,
"Muda unaenda mkuu, utachelewa msibani" Jimmy aliongea,
"Twendeni" Tammy Semmy aliongea huku akiinuka kwenye kochi na kuanza kutoka nje akifuatwa na wapambe wake. Safari ya kwenda msibani ilikuwa imeiva sasa.
********************
Tom alianza kuamini ana kitu cha ziada na ndio hauawi na wale waarifu, aliamini hivyo baada ya kuona hafanywi kitu chochote na wale watu hata akivunja masharti yao, alianza kuvimba kichwa na kujisahau.
Asubuhi ya leo aliamka huku akiwa hana kitu cha kufanya wala sehemu ya kwenda,
"Hivi kile kiumbe kilichokuwa kinanitokea mbona siku hizi sikioni tena, alafu kiliondoka na nguo zangu" Tom alikuwa anawaza huku akiwa bado yupo kitandani.
Baada ya muda mfupi akaamua Stoke kitandani na kwenda kuoga, alipomaliza aliwasha runinga na kuanza kuangalia, hapo ndipo alipoiona taarifa inayoelezea juu ya ratiba ya maziko ya Rais, na hapo ndipo alipojua kuwa Rais anazikwa hiyo siku, hatia ikaanza kumtafuna, hatia juu ya kifo cha Rais, yeye alijua hakumuua yeye aliwajua wauaji sasa tatizo lilikuwa ni katika kusema ukweli, ni nani ambaye anaweza kumuamini na kumpa ukweli huu? ni nani atakuwa mtu mwema kwa maana awa watu wana mtandao mkubwa sana, unaweza kudhani unaipeleka ripoti sehemu salama kumbe unajipeleka motoni.
"Sasa nitakaa na hii siri mpaka lini? ila nikisema ukweli si wataniua kwa maana nchi ipo chini yao, na nikifa nani atahuzunika na kusema nimekufa kwa kupigania Taifa langu, nani ataumizwa na kifo changu? hakuna zaidi ya wazazi wangu" Tom alikuwa anajiuliza kujijibu mwenyewe.
"Ila ikulu ni lazima wafanyakazi wa pale wawe ni askari watiifu wa serikali, wale ndio wakuwaambia ukweli, ila nitawezaje kuingia kwenye viwanja vya ikulu? sio rahisi hata kidogo mtu kama mimi kuingia kule, sina sifa na hata waandishi wa habari wanaoingia kile ni wale waliochaguliwa tu" Tom aliendelea kuwaza na kuwazua na mwisho aliona bora ajisogeze tu viwanja vya ikulu huku akiwa na kitambulisho chake cha kazi, kwani anaweza kupata bahati ya kuingia.
Akatafuta suti ambayo aliona inamfaa kipindi hicho na kuivaa, akabeba na kitambulisho chake cha kazi na kuondoka zake, safari ya kwenda ikulu ilianza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitafuta bajaji iliyomsogeza mpaka eneo la viwanja vya ikulu ila hakuruhusiwa kuingia, polisi walimzuia nje kwa kuwa hakuwa na sifa za kuingia ndani, na hata alipojitambulisha yeye ni Muandishi wa habari bado alizuiwa kuingia ndani, Tom akakata tamaa na akawa anaondoka zake, alipofika umbali mrefu tu kutoka viwanja vya ikulu, kuna gari la kifahari lilisimama mbele yake,
"Vipi Kijana, umetoka msibani" Mkuu wa polisi alimuuliza huku akiwa ndani ya ile gari,
"Ndio, kwnini umehisi hivyo?" Tom alijibu huku akiwa hajui kuwa yule mtu ni mkuu wa polisi kwa maana alivaa kiraia tu,
"Kwa jinsi ulivyovaa tu. Sasa mbona unaondoka? Au tayari kumejaa na haruhusiwi mtu kuingia, nisije nikaenda alafu nikazuiliwa njiani, kama wanarudisha watu niambie" Mkuu wa polisi aliongea huku akitabasamu,
"Hawarudishi watu, mimi nilitaka kuingia kumbe sisi wengine haturuhusiwi, kuna watu maalum ndio wanaruhusiwa" Tom alijibu huku akitabasamu,
"Kwani wewe unafanya kazi gani na ulitaka kuingia ili iweje?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Mimi ni muandishi wa habari wa radio ndogo ndogo hapa nchini, kwa hiyo nilizuiwa getini kwa sababu vyombo vya habari kama vyetu haviruhusiwi kule" Tom alijibu,
"Unatoka radio gani?" Mkuu wa polisi alimuuliza,
"Tafu, Tafu FM" Tom alijibu,
"Nyie ndio mliuteka mji kwa lile Tangazo lenu lililotaka kueleza muendelezo wa ile habari ya memory card?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Ndio, ni radio yetu ile" Tom alijibu akijiapiza kutosema ukweli endapo ataulizwa ni habari gani waliyotaka kusema kuhusu memory card,
"Una kitambulisho hapo?" Mkuu wa polisi alimuuliza,
"Ninacho, hiki hapa" Tom alijibu haraka na kukitoa na kumuonyesha mkuu wa polisi, Mkuu wa polisi akakipokea na kukiangalia,
"Ingia twende" Mkuu wa polisi alimwambia Tom,
"Unasema?" Tom aliuliza kanakwamba hajasikia alichokisema,
"Ingia twende ukachukue habari" Mkuu wa polisi aliongea na Tom akafungua mlango wa nyuma na kukaa pembeni ya Koplo Mbegu aliyeambatana na mkuu wake.
Gari lile gari la kifahari likaenda mpaka katika geti la ikulu na kuingia bila shida yoyote, lilimpeleka mpaka sehemu ya kushukia mkuu wa polisi,
"Koplo nyie mshukie pale kwenye maegesho ya gari, hapa hamruhusiwi kushuka nyie" Mkuu wa polisi alimwambia Koplo Mbegu wakati anashuka kwenye gari,
"Sawa mkuu" Koplo Mbegu alijibu na gari likaenda mpaka sehemu ya maegesho na koplo Mbegu akashuka, ila alishangaa kumuona Tom akiwa hashuki ila amekaa tu ndani ya gari akimtazama mtu aliyekuwa amesimama eneo hilo la kuegeshea magari, alikuwa ni Gabby na alisimama pale pale kwenye usawa wa mlango ambapo Tom anatakiwa ashukie.
"Dogo telemka basi, au mshamba wa kupanda magari ya kifahari kwa hiyo huwezi kufungua mlango" Koplo Mbegu aliongea huku akimuangalia Tom aliyeonekana ana wasiwasi.
Gabby ambae alikuwa upande wa mlango aliopo Tom, ilibidi ainame kidogo ili amuone huyo mtu ambaye ni mshamba wa kupanda magari ya kifahari.....
Gabby aliangalia lakini hakuweza kuona kitu kutokana na vioo vya giza vilivyokuwepo hapo, na kipindi chote hicho Tom alikuwa anajitahidi kumwambia Koplo Mbegu anyamaze, alikuwa anamwambia kwa ishara ya kidole chake cha shahada kukiweka juu ya midomo yake na kwa bahati nzuri Koplo Mbegu alimuelewa,
"Shuka basi, au wewe unakaa hapa hapa" Koplo Mbegu alimuuliza dereva wake na kumfanya Gabby ahisi kumbe siti ya nyuma hakuna mtu,
"Mimi sitelemki, nangoja hapa hapa" Dereva wa gari la mkuu wa polisi alijibu na kumfanya Gabby aachane na kuwasikiliza, akajiondoa eneo hilo taratibu na kuanza kuzungukia eneo jingine, Gabby yeye alikuwa katika viwanja hivyo na kazi aliyopewa ni kuchunguza kila gari iliyoingia hapo imembeba nani?
"Hivi huyu Jamaa unamjua, maana sura yake sio ngeni?" Koplo Mbegu alimuuliza Dereva wa mkuu wa polisi na alikuwa anamuulizia Gabby,
"Huyu Jamaa yupo usalama wa taifa, sema ni ngumu sana kumjua maana yeye yupo kwenye kitengo cha kuwaangalia vigogo tu" Dereva wa mkuu wa polisi alijibu,
"Inawezekana kabisa, maana sura yake sio ngeni kabisa" Koplo Mbegu aliongea wakati Gabby akipotea katika eneo lile,
"Sasa huyu dogo mbona anamuogopa, au wewe dogo ni muharifu?" Dereva wa mkuu wa polisi aliuliza huku akimgeukia Tom ambaye alikuwa amekaa kwenye siti ya gari,
"Hakuna, mimi sio muharifu" Tom alijitetea huku akijifanya kutabasamu,
"Sasa kwanini unamuogopa huyu Jamaa wa usalama wa taifa?" Koplo Mbegu alimuuliza Tom,
"Huyu ndiye aliyenizuia getini nisiingie, kwa hiyo sikutaka anione kwa maana angenitoa tena nje" Tom alidanganya na wakamuelewa,
"Telemka sasa ukatafute habari, ukisema uendelee kuogopa hapa hutopata habari hata moja" Koplo Mbegu alimwambia Tom ambaye alishuka na kuanza kujitengeneza vizuri nguo zake,
"Hivi wewe Jamaa ni polisi ee?" Tom alimuuliza Koplo Mbegu,
"Maswali gani hayo, au ndio unaanza kutafuta habari hivyo?" Koplo Mbegu aliuliza kwa utani huku akicheka,
"Lazima nijue bwana, ujue ukiwa na marafiki wanaofanya kazi sehemu muhimu kama hizo ni lazima ufurahi" Tom aliongea huku nae akicheka,
"Dah ndugu yangu, kukupa lifti tu tumeshakuwa rafiki zako?" Koplo Mbegu aliuliza na kufanya Dereva wa mkuu wa polisi acheke,
"Naitwa Thomas Anthony" Tom aliongea huku akimpa mkono Koplo Mbegu,
"Sawa, una jina zuri" Koplo Mbegu alijibu huku akiweka mikono yake nyuma ili asipeane mkono na Tom,
"Mikono yangu ni michafu au?" Tom aliuliza baada ya kuhisi ananyanyapaliwa,
"Hakuna umuhimu wowote wa kupeana mikono, kwani bila kunipa mkono hiyo salamu haifiki?" Koplo Mbegu aliuliza,
" sawa, lakini hukuniambia kama wewe ni polisi au sio polisi?" Tom aliuliza ingawa hakujali kuendelea kuonekana mjinga,
"Una maswali mengi sana, na sidhani kama majibu ya maswali yako yana umuhimu wowote kwako?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Kwa muda huu hayawezi kuwa na umuhimu kwako, ila nauhakika endapo utajua umuhimu wangu mimi baada ya kuachana hapa, utapata tabu sana kuonana na mimi tena" Tom aliongea huku akiwa na tabasamu mdomoni ila macho yake yalikimaanisha alichokiongea,
"Sijakudharau dogo, haya niambie umuhimu wako mdogo wangu" Koplo Mbegu aliamua kuwa mpole baada ya kuyasoma macho ya Tom na kugundua kuwa kweli ana kitu,
"Hujanijibu bado, wewe ni polisi?" Tom alirudia swali lake,
"Ndio mimi ni polisi, hujasikia hata mkuu alivyoshuka kwenye gari aliniita koplo?" Koplo Mbegu alimuuliza Tom,
"Wewe upo upande upi, ni walio wema au wale wale?" Tom alitoa swali jingine lililomshangaza Koplo Mbegu,
"Polisi wote ni wema" Koplo Mbegu alijibu huku akimtazama,
"Sio kweli, inaelekea kuna mambo mengi huyajui wewe" Tom aliongea huku akimcheka Koplo Mbegu,
"Mambo gani?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Ngoja kwanza nikatafute habari, kabla hamjaondoka nitakutafuta" Tom aliongea huku akiondoka eneo lile na kwenda kujichanganya kwenye kundi la watu na kumuacha Koplo Mbegu na dereva wa mkuu wa polisi wakimuangalia tu.
"Huyu dogo atakuwa hana akili nzuri" Dereva wa mkuu wa polisi aliongea,
"Inawezekana, ila bado nahitaji kumuamini, macho yake yanaonesha ana kitu kinamchanganya" Koplo Mbegu aliongea huku akiangalia eneo ambalo Tom alipotelea.
"Mi namuona mawenge tu, mjanja mjanja kama tapeli" Dereva wa mkuu wa polisi aliongea,
"Ebu ngoja nikamtafute, atakuwa maeneo yale yale alipoingilia" Koplo Mbegu aliongea huku akielekea kule kule,
"Achana nae bwana, njoo tupige story yule si amesema atakuja?" Dereva wa mkuu wa polisi aliongea huku akihuzunika kwa kitendo cha Koplo Mbegu kutaka kuondoka,
"Nakuja sasa hivi tu" Koplo Mbegu aliongea huku akiwa hana nia ya kurudi.
"Huyu bwege kweli, anadhani nimekuja kuongea huku, watu tunekuja kikazi hapa" Koplo Mbegu aliongea peke yake wakati akiwa amemuacha hatua nyingi yule Dereva wa mkuu wa polisi.
Koplo Mbegu akaanza kuzunguka kila eneo huku akiangaza kule na huku kumtafuta Tom, alizunguka tena tena na wala hakupata bahati ya kumuona Tom, akaenda mpaka maeneo ya vyooni na uko pia hakumuona, akapata wasiwasi,
"Au walinzi wamemuona na kumtoa nje?" Koplo Mbegu aliwaza huku akiwa amesimama peke yake kajitenga na watu wengine, akazungusha shingo yake tena kuangalia kila upande lakini pia hakumuona Tom.
Kwa jinsi Koplo Mbegu alivyokuwa anaangaika, mtu yoyote akimuangalia wala hawezi kupata shida kugundua kuwa mtu yule kuna mtu anamtafuta,
"Wewe mbona hueleweki, we shushushu nini umetumwa kupeleleza?" Gabby aliongea kwa sauti ndogo ila nzito iliyofanya Koplo Mbegu ageuke haraka,
"Kuna mtu namtafuta" Koplo Mbegu alijibu kwa upole,
"Unatakiwa utulie sehemu moja, muda mrefu nakuona unazunguka zunguka tu kila mahali" Gabby aliongea huku akiwa bado amesimama mbele ya Koplo Mbegu,
"Sasa ukiniambia nitulie sehemu moja unakuwa kama unanipangia cha kufanya" Koplo Mbegu aliongea kwa ujeuri,
"Ndio utaratibu wa hapa, unaona kuna mtu mwingine anazunguka zunguka zaidi ya askari?" Gabby aliuliza,
"Sasa unajua mi nani?" Koplo Mbegu alihoji kijeuri,
"Kujua wewe ni nani mimi hainisaidii, unachotakiwa ni kutulia sehemu moja" Gabby aliongea,
"Poa, ila nitatulia nikichoka kumtafuta mtu wangu au nikimpata" Koplo Mbegu aliongea huku akiondoka na kumuacha Gabby akimuangalia tu.
"Jimmy ebu kuwa makini na huyu boya niliyekuwa naongea nae hapa, naona anajiamini sana na ikiwezekana mfuatilie" Gabby aliongea kupitia kifaa kidogo alichokivaa masikioni na waya wake ulifika mpaka mdomoni kwake. Baada ya kumaliza kuongea maneno hayo aliweza kumshuhudia Koplo Mbegu akiendelea kuzunguka tu kama hawali.
Koplo Mbegu alipochoka na kuridhika kuwa kweli ni ngumu kumpata tena Tom, aliamua kurudi kwenye gari walilokuja nalo na kukaa pembeni yake, maana muda huu hata dereva wa lile gari hakumkuta.
Wakati akiwa amekaa alimshuhudia Tom akijongea maeneo yale, Koplo Mbegu akatabasamu kwa kuwa mtu aliyemtafuta muda mrefu mpaka amekata tamaa atimae amekuja tena,
"Nilikuona unazunguka zunguka, ulikuwa unamtafuta nani?" Tom alimuuliza Koplo Mbegu baada ya kumfikia,
"Huyu dereva wa gari, sijui ameelekea wapi?" Koplo Mbegu aliamua kumdanganya,
"Nimemuona kule kati, ila hajaniona" Tom aliongea huku akijitupa chini na kukaa,
"Bora umekuja, ulisema una habari unataka kuniambia, ni habari gani hiyo?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Hakuna kitu, nilikuwa nakuzingua tu" Tom alijibu huku akitabasamu,
"Sasa mambo gani ya kuzinguana, yaani muda wote nakuwaza najua una habari kumbe muongo?" Koplo Mbegu aliongea huku akionekana hajafurahishwa na kauli ya Tom,
"Hivi unajua kuna mtandao mbaya sana serikalini?" Tom aliuliza na kumfanya Koplo Mbegu ashtuke, maana alishawahi kuambiwa hivyo na mkuu wake,
"Mtandao mbaya, upi huo?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Naogopa hata kusema, kwa maana hata nyie polisi miongoni mwenu mpo kwenye huo mtandao" Tom aliongea na kufungua chupa yake ya maji na kunywa,
"Ni miongoni mwetu kumbe, ila sio wote?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Sasa utamjuaje huyu ni polisi mwema na huyu ni polisi mbaya?" Tom aliuliza,
"Ni ngumu kwa kweli, ila cha muhimu niamini" Koplo Mbegu aliongea,
"Una moyo braza?" Tom alimuuliza Koplo Mbegu na kufanya ahisi Tom ana siri nzito,
"Wanadamu wote tuna moyo" Koplo Mbegu alijibu huku akijifanya hajaelewa alichomaanisha Tom,
"Yaani unaweza kujikaza na kuvumilia hiki nitakachokwambia ili ukifanyie kazi?" Tom aliuliza,
"Mimi mwanaume bwana, nitashindwaje sasa kuvumilia?" Koplo Mbegu alijibu,
"Sogea huku sasa ili nikumwambie kila kitu, hii nchi iache tu" Tom aliongea na kujivuta chini ya gari na Koplo Mbegu nae akajisogeza ila yeye alisimama ili asikie Tom anataka kumwambia siri gani?.....
Akili na masikio ya Koplo Mbegu akayaweka sawa kwa ajili ya kusikiliza hiyo habari ya Tom, hakujua habari ambayo angepewa ingehusu kifo cha rais, yeye mawazo yake alijua ataambiwa kuhusu makundi ndani ya serikali, yaani kundi baya na kundi zuri.
"Wewe mpuuzi kumbe upo?" Gabby aliuliza huku akielekea sehemu alipokuwa Tom, na wala hakutaka kusubiri kujibiwa kitu na Tom, alichofanya alienda na kumuinua juu na kuanza kumpeleka nje,
"Muache huyo dogo" Koplo Mbegu aliongea huku akimshika begani Gabby,
"Alafu wewe naona hunijui, muda tu nakuona unavyonipanda kichwani" Gabby aliongea huku akimnyooshea kidole Koplo Mbegu,
"Sasa huyu dogo amekukosea nini? si umuache aendelee na mambo yake" Koplo Mbegu aliongea huku nae hasira zikianza kujijenga kichwani kwake,
"Jiangalie wewe, hujui unabishana na nani _na ndio maana unajifanya kiburi, nitakubadilikia sasa hivi" Gabby aliongea na kumsukuma Koplo Mbegu,
"Wewe ni nani bwana, unalingia kufanya kazi usalama wa taifa?" Koplo Mbegu alihoji huku nae akimsukuma Gabby,
"Ukimchekea Mbwa atakufuata mpaka msikitini" Gabby aliongea na kuachia ngumi kali iliyokuwa inaelekea usawa wa pua ya Koplo Mbegu, Koplo Mbegu akaiona, akanesa kidogo kama nguo iliyopulizwa na upepo, ile ngumi ikamchubua kidogo na ikapita, Koplo Mbegu akawa anajiandaa na yeye kuachia ngumi, akashangaa anadakwa mkono,
"Muwe mnaangalia eneo la kufanya huu ujinga, mnapigania kwenye viwanja vya ikulu?" Dereva wa gari la mkuu wa polisi aliongea huku akiwa bado ameushika mkono wa Koplo Mbegu,
"Si huyu mpuuzi ameanzisha, ungeniacha kidogo nimfundishe kazi" Koplo Mbegu aliongea huku akiachia tabasamu lililobeba hasira juu ya Gabby,
"Sina muda wa kupoteza nguvu zangu kupambana na mende" Gabby aliongea huku akimtoa Tom nje, alitoka nae na kumuingiza kwenye gari kisha wakaondoka nae. Gabby alionekana ana hasira nyingi sana na Tom.
"Jimmy ebu endelea kumfuatilia huyo boya hata akiondoka hapo ondoka nae, maana nilimkuta na Tom ndani ya viwanja hivyo, inawezekana Tom amemwambia kitu" Gabby aliongea kupitia kifaa cha mawasiliano huku akiwa anaendesha gari.
"Mi sijaongea nae kitu chochote" Tom alijibu huku akijua kuwa ni lazima siku hiyo aone cha mtema kuni. Ingawa Tom alijitetea ila wala Gabby hajajisumbua kumjibu, badala yake alitoa sigara yake na kuiwasha kisha akawa anaipuliza kwa fujo kiasi kwamba baada ya sekunde chache moshi ukaenea kwenye gari yote, kwa ushenzi Gabby akafunga vioo vyote na kumfanya Tom aanze kukohoa hovyo. Gabby hakujali hilo alichokuwa anakiangalia ni Barabara tu ili asilete ajali.
Gari ilifika mpaka katika kambi yao na kuiingiza kwa mwendo wa kasi ambao haukuwa na madhara, alipopaki gari alishuka na kumshusha Tom kama anashusha mzigo,
"Sasa mimi nimefanyaje?" Tom aliuliza huku akiwa na sura ya huruma, lakini Gabby hakujali aliendelea tu kumvuta mpaka ndani, alimkuta Waziri wa ulinzi sebuleni ila Gabby hakutaka hata kuongea, alipitiliza mpaka kwenye chumba cha mateso na kumsukuma kwa nguvu Tom akagonga ukutani na kujishika mgongoni kutokana na maumivu aliyoyapata.
Gabby akavua shati na kubaki na vest nyeupe,
"Niambie yule mtu ni nani?" Gabby aliuliza huku akiwa anamaanisha huyo mtu anaemuuliza ni Koplo Mbegu,
"Si ungemuuliza mwenyewe bro, mimi simjui" Tom alijibu kwa unyonge na kushtuka anapigwa kibao kikali cha shavu mpaka akawa akahisi shavu kama linamuwasha vile,
"Niambie umemwambia kitu gani kuhusu sisi?" Gabby aliuliza huku akimuangalia Tom aliyekuwa anajisugua shavu lililopigwa kofi,
"Sijamwambia kitu chochote na wala hajui" Tom alijitete huku akitaka kulia, lakini Gabby hakujali hilo akamuongezea kofi jingine eneo lile lile na kumfanya Tom aangue kilio kama mtoto,
"Niambie kwanza ulifuata nini pale?" Gabby aliuliza bila kujali maumivu anayoyapata mwenzake,
"Nilienda kama Muandishi wa habari" Tom aliongea huku mikono ikiwa mashavuni baada ya kumuona Gabby akitaka kumtandika kofi jingine,
"We si tulikuambia uachane na mambo ya uandishi wako, kumbe hukutii?" Gabby aliuliza kwa hasira mpaka mate yalimtoka,
"Nilitii bro" Tom alijibu kwa huruma,
"Sasa ulifuata nini pale?" Gabby aliuliza na kumtwisha Tom ngumi katika paji lake la uso, Tom akayumba na kuanguka chini huku akiwa amejishika eneo ambalo ngumi ilitua,
"Jibu, ulifuata nini pale?" Gabby alirudia swali lake huku akimuendea Tom pale pale chini,
"Nilienda kuangalia tu namna mambo yanavyoenda kwenye misiba ya wakubwa" Tom alijibu huku akijiandaa kupokea pigo jingine kutoka kwa Gabby,
"Ulipitaje getini wakati watu wanaoruhusiwa kuingia ni watu maalum?" Gabby aliuliza,
"Nilipita tu kawaida, niliamua niwaoneshe kitambulisho cha kazi ndio wakaniachia nipite" Tom alidanganya huku akiwa bado amelala chini,
"Hukomi kudanganya ee?" Gabby aliongea na kuanza kumpiga mateke ya hovyo Tom, alimpiga kila eneo la mwili wake,
"Ukweli ndio huo, niliingia kwa njia ila nilisaidiwa kuingia ndani" Tom aliongea ukweli baada ya kuhisi ataumia zaidi,
"Nani alikusaidia kuingia ndani?" Gabby aliuliza huku akiacha kumpiga Tom,
"Yule Jamaa uliyenikuta nae, ndio walionisaidia walikuwa na gari" Tom alijibu na kumfanya Gabby akumbuke kuwa kipindi wakina Koplo Mbegu wanaingia, aliwaona,
"Mbona sijakuona ukishuka kipindi gari la wale Jamaa likiingia, ulikuwa wapi?" Gabby aliuliza,
"Nilishuka mbona, labda hukuniona tu, ila hata mimi sikukuona, ningekuona ningekufuata tu kwa maana sikwenda kwa ubaya pale" Tom aliongea huku anaugulia maumivu ya kukanyagwa mwili mzima,
"Na wale ni wakina nani?" Gabby alimuuliza huku akimuangalia kwa hasira,
"Siwajui hata wanafanya kazi gani" Tom alijibu,
"Sasa kama huwajui walikupaje lift na kukusaidia kuingia ndani? bado unadanganya?" Gabby aliongea huku akimfuata tena Tom,
"Kweli mi siwajui, niliwaomba tu wanisaidie kuingia ndani nikawaonesha kitambulisho changu ndio wakanisaidia" Tom alijibu huku akijikunyata ukutani,
"Walipofika getini hawakuonesha vitambulisho?" Gabby aliuliza,
"Hawakuonesha, walifunguliwa geti na kupita ndani" Tom alijibu,
"Kaa humu, mpaka niridhike na majibu yako ndio nitakuachia" Gabby aliongea huku akiokota shati lake na kulivaa, kisha akatoka nje ya kile chumba na kumuacha Tom akiwa anamuangalia huku damu zikimtoka katika paji la uso wake.
******************
Jimmy alikuwa bize kumfuatilia Koplo Mbegu muda wote, kwa hiyo katika huo msiba Jimmy alikuwa na kazi zaidi ya mbili.
Muda wa kufanya maziko ya Rais ulifika na walikuwa wanamzikia hapo hapo kwenye viwanja vya ikulu kwa maana sheria iliruhusu hivyo, ila kama familia yake ingetaka asizikwe hapo, pia ingewezekana.
Viongozi mbalimbali wa nchi, akiwemo Tammy Semmy walikuwa wamesimama mbele ya shimo ambayo muda mfupi ujao ndio litakuwa kaburi la Rais, na kipindi hicho wanajeshi waliokuwa na jeneza lililobeba mwili wa Rais walikuwa wamesimama kando ya shimo lile tayari kwa kuushusha chini mwili wa Rais.
Baada ya muda mfupi jeneza lile lilikuwa linashushwa chini taratibu kwa kutumia nyororo zilizofungwa pembezoni mwa jeneza lile, na baada ya shughuli hiyo kukamilika, lile kaburi halikufukiwa na udongo, badala yake liliwekwa mfuniko wa zege kwa juu na shughuli iliyokuwa inafuata hapo ni ya kuweka maua juu ya kaburi lile.
Ilianza familia ya marehemu na baada ya kumaliza, waliokuwa wanafuata ni viongozi wa nchi, Tammy Semmy ndio alikuwa anaelekea kwenda kuweka ua juu ya kaburi.
Kipindi hicho Jimmy na Koplo Mbegu walikaa sehemu tofauti, ila jimmy aliweza kumuona vizuri tu Koplo Mbegu, sasa wakati akiwa anazungusha macho aliweza kumuona kiumbe yule wa ajabu, Sudy Bakari.
Na Koplo Mbegu pia aliweza kumuona Sudy Bakari, kwa hiyo Jimmy na Koplo Mbegu wote macho yao yakaamia kwa Sudy Bakari ambaye alikuwa amesimama na nguo zake anazovaa kila siku na alikuwa tofauti na watu wengine waliokuwa wamesimama hapo kwa maana walikuwa wamevaa suti au nguo za heshima na safi.
Sio Jimmy wala Koplo Mbegu aliyetaka kufanya kitu baada ya kumuona Sudy Bakari, wote walikuwa makini tu kuangalia nyendo zake na yeye muda wote alikuwa amesimama kwa utulivu tu akifuatilia kila hatua.
Sasa uliopofika ule muda ambao Tammy Semmy anatakiwa akaweke ua, Sudy Bakari alichomoka kwa mwendo wa taratibu na kuelekea mahali ambapo Tammy Semmy yupo.
Tammy Semmy yeye hakuwa na habari na ndio kwanza alikaza hatua kuelekea sehemu ya kuweka ua. Jimmy na Koplo Mbegu walikuwa wanashuhudia hilo tukio.
Sudy Bakari alizidi kumsogelea Tammy Semmy na sasa Sudy Bakari alipeleka mkono wake kwenye kiuno upande wa nyuma ndani ya nguo yake, sehemu ambapo watu huweka bastola na huku sura yake ikionesha haina mzaha hata kidogo kwa wakati huo.....
Jimmy akahisi kuna hatari kubwa inataka kutokea kwa mkuu wao Tammy Semmy, Jimmy akachomoka kwa kasi na kuanza kuelekea kumfuata Sudy Bakari aliyekuwa anazidi kumsogelea Tammy Semmy ambae alikuwa ndio anaweka ua juu ya kaburi kisha akainama kutoa heshima na kugeuka ili arudi kusimama sehemu aliposimama hawali, akapishana na Sudy Bakari ambae alikuwa akichomoa ua kutoka kiunoni mwake, na kipindi hicho Jimmy ndio alikuwa anamfikia Sudy Bakari na kumshuhudia akitoa ua na wala sio bastola kama walivyodhani wao, Sudy Bakari akamtupia jicho Jimmy na macho yao yakagongana, Sudy Bakari akatoa tabasamu huku akiweka ua juu ya kaburi na kisha akageuza zake kurudi alipokuwepo, cha ajabu hakukuwa na mtu aliyekuwa akimshangaa kutokana na mavazi yake kuwa tofauti na wengine, wala hakuna mtu aliyeonekana kufuatilia tukio hilo, kifupi ni kwamba watu walikuwa kama hawamuoni Sudy Bakari.
Jimmy akaendelea kumuangalia mpaka kile kiumbe kilipoenda kusimama, na kisha taratibu Jimmy alirudi kusimama eneo alipokuwepo hawali na kumtupia jicho Koplo Mbegu ambaye alimkuta na yeye anamuangalia Sudy Bakari, tena alikuwa anamuangalia kwa umakini wa hali ya juu, Jimmy akahisi huenda Hawa watu wawili wanajuana.
Koplo Mbegu baada ya kumuangalia kwa muda mrefu kiumbe yule, alikata shauri la kumfuata, alimsogelea pole pole mpaka akajikuta yupo nae jirani, ila Koplo Mbegu alikuwa nyuma na Sudy Bakari alikuwa mbele, kwa maana nyingine naweza kusema kuwa Sudy Bakari ilikuwa ngumu kujua au kudhani kuna mtu wa aina fulani nyuma yake,
"Jiangalie, unawindwa" Sudy Bakari aliongea na sauti ilimfikia Koplo Mbegu hakudhani ni yeye anaeongeleshwa, ikabidi Koplo Mbegu aanze kukagua watu waliosimama na Sudy Bakari huku akijiuliza ni nani anaeongea nae kati yao?
"Naongea na wewe, Koplo Mbegu" Sudy Bakari aliongea tena na kumfanya Koplo Mbegu aendelee kushangaa maajabu ya yule bwana,
"Ni nani ananiwinda?" Koplo Mbegu aliongea huku akiwa sambamba na Sudy Bakari,
"Askari gani mpuuzi kama wewe, yaani unawinda bila kujilinda? amini nakwambia kuna mtu yupo anakufuatilia muda mrefu tu" Sudy Bakari aliongea na kumfanya Koplo Mbegu azungushe macho yake kila sehemu na wala hakubahatika kumuona huyo mtu anaemuwinda, Koplo Mbegu akaamua kupuuza kwa maana sio kilichompeleka pale,
"Sasa bwana Sudy Bakari, wewe unahusikaje kwenye msiba kwa maana wanaruhusiwa kuweka maua juu ya kaburi ni wahusika tu" Koplo Mbegu alimuuliza lakini wala hakujibiwa,
"Sudy Bakari si nakuuliza?" Koplo Mbegu aliuliza huku akimuangalia usoni,
"Kiumbe mimi sio Sudy Bakari, nilishakwambia" Sudy Bakari aliongea,
"Lakini hujawahi kuniambia jina lako?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Kiumbe hupaswi kunijua, mimi si wa nasaba ya udongo" Sudy Bakari aliongea na kumfanya Koplo Mbegu ajiulize ni kitu gani amekimaanisha huyu mtu,
"Sawa rafiki, je wewe unahusikaje kwenye huu msiba?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Kiumbe hilo swali jiulize wewe, alafu jibu lake nipe mimi" Sudy Bakari aliongea kisha akaanza kuondoka taratibu kumuacha Koplo Mbegu, lakini Koplo Mbegu hakuonekena kutaka kuachana nae, nae akamfuata.
"Samahani naomba nikuulize swali lingine?" Koplo Mbegu aliuliza huku wakijinasua kutoka kwenye kundi la watu,
"Swali gani hilo?" Sudy Bakari aliuliza,
"Nataka kujua au kuniambia unamjua vipi Sudy Bakari?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Ni marehemu, sina ninachojua kuhusu yeye zaidi ya hilo" Sudy Bakari alijibu,
"Sasa mbona unafanana kila kitu, huna undugu nae?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Kiumbe nilishakujibu, sina unasaba na udongo" Sudy Bakari alijibu na kumfanya Koplo Mbegu asielewe huyu mtu amemaanisha nini?
"Nikisema umemuua utakataa?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Unasema?" Sudy Bakari aliuliza huku akisimama na kumuangalia koplo Mbegu kwa hasira,
"Unahusika na kifo cha Sudy Bakari" Koplo Mbegu aliongea huku akionesha hana uoga wowote,
"Kiumbe umenikosea sana, hupaswi kunihukumu" Sudy Bakari aliongea huku akimkaba Koplo Mbegu na kumnyanyua juu kwa mkono mmoja na kufanya Koplo Mbegu aanze kutapatapa kama kuku aliyeshikwa na kicheche, Sudy Bakari akamtupa chini na kumuacha, Koplo Mbegu akabaki anagalagala huku amejishika koo, baada ya hapo akakurupuka na kukimbilia getini ambapo ndipo Sudy Bakari alipitia. Koplo Mbegu alipita getini kama mwehu na kufika nje, lakini hakubahatika kumuona tena Sudy Bakari,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Huyu mwendawazimu amenikimbia tena" Koplo Mbegu alijilaumu huku akiwa bado amejishika koromeo, kisha akarudi ndani na kwa bahati nzuri hakuna mtu aliyeweza kuliona tukio lake la kupigwa na Sudy Bakari, ila mtu mmoja tu ndiye aliyelishuhudia, ni Jimmy ambae muda wote alipewa kazi ya kumfuatilia Koplo Mbegu.
Jimmy alikuwa makini sana kwa kila hatua inayofanywa na Koplo Mbegu,
"Ina maana yule mtu wa ajabu wanajuana na huyu boya? Ila sasa mbona amempiga?" Ni baadhi ya maswali ambayo Jimmy alikuwa anajiuliza kuhusu watu hawa wawili na kipindi hicho Gabby nae alikuwa anarudi na kumkuta Jimmy akimuangalia Koplo Mbegu ambae alikuwa amekaa mbele ya gari la mkuu wa polisi.
"Vipi umegundua kitu gani kutoka kwake?" Gabby alimuuliza Jimmy,
"Amezidi tu kunivuruga, huyu Jamaa atakuwa anafahamiana na yule mtu wa ajabu, maana walikuwa pamoja" Jimmy alijibu,
"Yule mtu wa ajabu alikuwepo hapa, amefuata nini?" Gabby aliuliza,
"Hata sijajua, ila cha kushangaza na yeye alikuwa ni mmoja kati ya watu walioweka ua kwenye kaburi la Rais" Jimmy alijibu,
"Sasa huyu mtu ni nani? hujajua waliongea nini na yule boya?" Gabby aliuliza,
"Sijajua, ila waliongea vizuri na wakatoka pamoja, ila walipofika pale karibu na geti, yule pale boya alikabwa na yule mtu wa ajabu na sijajua sababu iliyowafanya mpaka yule boya apigwe" Jimmy alimpa maelezo mwenzake,
"Hapa si kila kitu tayari? Mwambie BQ abaki na mkuu hapa, sisi tutatoka na huyu boya, tuifuatilie gari anayoondoka nayo ili tujue mwisho wake" Gabby alimwambia Jimmy,
"Poa" Jimmy alijibu kisha akampa maagizo BQ kupitia kifaa kidogo cha mawasiliano ambavyo walikuwa wanavitumia.
Baada ya nusu saa watu walianza kutawanyika kwenye eneo lile, Jimmy na Gabby walikuwa wametulia tu ndani ya gari lao huku wakisubiri gari ambayo atapanda Koplo Mbegu iondoke ili waifuatilie.
Baada ya muda kidogo waliweza kuiona ile gari ikianza kuondoka na wao wakaanza kuifuata kwa nyuma.
Wakina Koplo Mbegu walifuatwa bila wenyewe kujijua kama wanafuatwa.
Gari ya kina Gabby iliendelea kuwafuata wakina Koplo Mbegu kwa umbali mrefu tu mpaka walipofika kwenye muingiliano wa Barabara nne ndipo waliposimama kutokana na taa za barabarani kuamuru hivyo, wakiwa wamesimamisha gari yao, Jimmy alimuona Sudy Bakari akipita upande wa pili wa Barbara huku mikono ikiwa mfukoni,
"Gabby yule mshkaji yule pale" Jimmy aliongea huku kidole chake kikiwa kimemuelekea Sudy Bakari ambaye hakuwa na habari nao,
"Atakuwa anakaa mitaa hii nini?" Gabby alimuuliza mwenzake,
"Sasa mi nitajuaje?" Jimmy aliuliza huku akimshangaa mwenzake,
"Sasa cha kufanya, piga picha namba ya hiyo gari tunayoifuatilia, alafu tupaki gari yetu pembeni ili tumfuatilie huyu Jamaa, ana umuhimu kuliko huyo boya tunaemfuatilia kwenye gari" Gabby aliongea kisha Jimmy akatoa simu na kuipiga picha plate number ya gari alilokuwepo Koplo Mbegu ambayo ilikuwa mbele ya gari yao.
Taa ziliporuhusu, Gabby alienda kuegesha gari pembezoni mwa Barabara na kuanza kumfuatilia Sudy Bakari aliyekuwa anaelekea kwenye kichochoro, kisha akaingia mitaa ya ndani ndani zaidi na safari yake iliishia kwenye jengo la ghorofa ambalo halikumaliziwa.
Sudy Bakari alipandisha mpaka juu kwa msaada wa ngazi za ghorofa lile, alipofika juu alielekea kwenye chumba kimojawapo cha lile jengo na kuingia ndani, ndani kulikuwa na maboksi tu yametandikwa chini,
"Kumbe ndipo unapoishi hapa?" Gabby aliuliza huku akitabasamu ila Sudy Bakari wala hakuonekana kushtuliwa na huo ujio,
"Viumbe hamridhiki na kila la ajabu ninalolifanya, mmeamua kunifuata sasa" Sudy Bakari aliongea huku akiwa amewapa mgongo,
"Sasa sisi hatutaki mabishano na mbuzi kama wewe, ile flash yenye tukio la mauaji ipo wapi?" Gabby aliuliza,
"Kiumbe aliyeumbiwa udongo uwa anajiamini sana anapodhani ana nguvu" Sudy Bakari aliongea huku akicheka,
"Hatujaja kujadili viumbe hapa, lete flash" Gabby aliongea kwa hasira huku akiichomoa bastola yake,
"Usilete mchezo na kifaa cha moto" Sudy Bakari alimwambia Gabby baada ya kumuona ameitoa bastola,
"Unatupotezea muda, sasa leo nakutwanga risasi ili nione kama wewe sio mtu kweli" Gabby aliongea kwa hasira huku akimaanisha hivyo, maana hata Sudy Bakari alivyomsoma kupitia macho aliweza kuona kuwa Gabby anafyatua risasi muda wowote, Sudy Bakari akapata uoga,
"Usipigeeee" Sudy Bakari alipiga kelele baada ya kuona Gabby amevuta kifyatua risasi, na risasi ikatoka moja kwa moja na kupenya kwenye mdomo wa Sudy Bakari, kisha Sudy Bakari akarushwa na kwenda kujipigiza ukutani, akalala kimya...........
Sudy Bakari alikuwa chini ametulia,
"Umeua na sasa hatujajua hata ile flash ameiweka wapi?" Jimmy aliongea huku akuangalia mwili wa Sudy Bakari aliyekuwa amelala chini,
"Acha afe, kuliko kuendelea kuishi kwa mashaka namna ile" Gabby aliongea huku akiirudisha Bastola sehemu yake,
"Kufa anakufa mwana wa dunia na wala sio mimi" Sudy Bakari aliongea huku akisimama na akionekana anatafuna kitu, na akatema, ilikuwa risasi aliyopigwa, kumbe haikumdhuru ilivyopenya mdomoni na akaitafuna ikasagika kama big G.
Hapo ndipo mshangao ukaongezeka dhidi ya mtu huyo, wakawa kama hawaelewi kilichotokea au naweza kusema kuwa wakawa wanaona mazingaombwe.
"Unashangaa nini? mpige tena" Jimmy alimwambia Gabby na hapo Gabby akaitoa bastola yake ili ampige tena Sudy Bakari, lakini alikuwa amechelewa, hata hakujua kilichotokea maana alijikuta hana bastola mkononi na yeye mwenyewe alikuwa chini huku akijihisi maumivu mkononi na wakati huo Sudy Bakari alikuwa akituwa chini baada ya kumpiga pigo la hatari Gabby, Jimmy akamuwahi Sudy Bakari kabla hajakaa vizuri, Jimmy alimfuata kwa kasi na alipomkaribia aliruka juu kwa lengo la kumpiga teke la kisogoni, hapo ndipo alipoona maajabu mengine, Sudy Bakari akiwa vile vile kampa kidogo, sura iliamia kisogoni, yaani umbo la mbele liliamia nyuma na kisha akaudaka mguu wa Jimmy na kisha akamtupa umbali mrefu kutoka aliposimama yeye.
"Hakuna pigo lolote la mwanadamu litalogusa mwili wa yeye aliye mkuu kwao" Sudy Bakari aliongea huku akimuangalia Jimmy aliyekuwa akigaagaa chini.
Kisha Sudy Bakari akaondoka zake kwa mwendo wa haraka kuzifuata ngazi za kushukia chini na kutokomea zake kusikojulikana.
"Vipi upo sawa?" Gabby alimuuliza Jimmy aliyekuwa bado yupo chini,
"Ndio, ila mguu kama umeshtuka" Jimmy alijibu huku akijaribu kuamka,
"Aisee uchawi anaotumia huyu kiumbe, sio uchawi wa duniani, itakuwa kautoa kuzimu" Gabby aliongea huku akiiokota bastola yake,
"Uchawi?!!!, sio uchawi bwana, nadhani huyu sio binadamu" Jimmy aliongea huku akiunyoosha mguu wake,
"Huyu ni binadamu bwana, acha kuleta habari za kukatishana tamaa, kwa hiyo unataka kusema tunapambana na jini?" Gabby aliuliza,
"Nahisi hivyo" Jimmy alijibu,
"Tuondoke bwana, naona umeanza kuingiwa na uoga" Gabby aliongea huku wakianza kuondoka,
"We fikiria mtu anatafuna risasi kama banzoka, na kingine alichonifanyia wewe hujakiona tu" Jimmy aliongea wakati wakishuka ngazi,
"Yote mazingaombwe yale, anatufanyia viini macho tunaona maajabu tu" Gabby aliongea na kisha ukimya ukatawala wakawa wanaongozana kwenda kwenye eneo ambalo waliegesha gari lao.
*********************
Tammy Semmy na BQ walikuwa wanarudi kambini kwao baada ya kutoka kwenye shughuli ya maziko ya Rais,
"Uliniambia wameelekea wapi wenzio?" Tammy Semmy aliuliza,
"Kuna mtu walimtilia mashaka ndio wanamfuatilia" BQ alijibu huku akiwa makini na Barbara kwa maana yeye ndiye aliyekuwa dereva kwa wakati huo,
"Mashaka juu ya nini?" Tammy Semmy aliuliza,
"Hawajaniambia" BQ alijibu,
"Muda gani waliondoka?" Tammy Semmy aliuliza,
"Muda mfupi kabla hatujatoka sisi" BQ alijibu huku akiingiza gari kwenye uzio wa nyumba yako.
Wakatelemka na kuingia ndani ambapo walimkuta Waziri wa ulinzi akiangalia runinga,
"Gabby leo kavuta bangi?" Waziri wa ulinzi aliuliza baada ya wenzake kukaa,
"Kwanini?" Tammy Semmy aliuliza,
"Kamleta Tom hapa, aisee amempiga sana mtoto wa watu, yupo hoi kule kwenye chumba cha mateso" Waziri wa ulinzi alijibu,
"Eee!!!!! ebu BQ kamlete Tom" Tammy Semmy aliagiza,
"Hakuna ufunguo, Gabby ameondoka nao" Waziri wa ulinzi alijibu huku akisikitika,
"Ni kawaida yake pindi anapokuwa na hasira uwa haitaji mtu aingilie mambo yake" BQ aliongea,
"Sasa hii ya Tom ni kesi yetu sote na wala sio yake" Tammy Semmy aliongea,
"Labda kuna kitu sio cha kawaida amekigundua kwa Tom, na kwanza wamekutana wapi na Tom? au alimfuata nyumbani kwake?"Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Hakuna anayejua, labda walikutana kule kule kwenye viwanja vya Ikulu" Tammy Semmy alijibu,
"Sasa Tom alifuata nini kule?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Wewe ndiye ulitakiwa umuulize Gabby alipokuja na Tom" Tammy Semmy aliongea na kipindi hicho Jimmy na Gabby walikuwa wanaingia huku nyuso zao zikiwa hazina furaha.
"Jamani kwema huko mtokako?" Waziri wa ulinzi aliwauliza,
"Huko hakuna wema, ni balaa tu" Jimmy alijibu,
"Kuna nini kimetokea?" Tammy Semmy aliwauliza na kisha Gabby akawaeleza kila kitu kilivyokuwa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho na mpaka kilichowakuta baada ya hapo.
"Kwa hiyo umempiga Tom baada ya kuhisi anatunguka, si ndio?" Tammy Semmy alimuuliza Gabby,
"Ndio" Gabby alijibu,
"Ebu kamlete" Tammy Semmy aliongea na Gabby akaenda kumchukua.
Baada ya muda alirudi nae huku Tom akiwa ana damu mwili mzima na amevimba kwenye paji la uso.
"Tom unaweza kuniambia ni kitu gani kilikuingiza ndani ya viwanja vya ikulu?" Tammy Semmy alimuuliza,
" nilishamjibu huyu Mbwa" Tom aliongea huku akimuangalia Gabby na hii ilionesha ni jinsi gani alichoka kunyanyasika,
"Mimi Mbwa?" Gabby aliuliza huku akitaka kumpiga,
"Muache, na yule kijana uliyekuwa nae ni nani?" Tammy Semmy aliuliza,
"Kiukweli simjui, alinisaidia tu lifti na sina uhusiano nae mwingine" Tom alijibu,
"Hujamwambia habari yoyote kuhusu sisi?" Tammy Semmy aliuliza,
"Hapana na wala sikuwa na nia ya kumwambia" Tom alijibu,
"Mimi sioni kosa lake, tumuachie tu aende zake" Tammy Semmy aliongea huku akiwageukia wenzake,
"Mkuu huyu tusimuamini sana" Gabby aliongea,
"Tujaribu kumuamini, alafu huyo mtu mnaesema ni kiumbe wa ajabu ndio tusimuamini" BQ aliongea na kisha akatabasamu,
"Mpeleke kwake" Tammy Semmy alimwambia BQ na kisha BQ akainuka na kutangulia nje na Tom akamfuata nyuma huku akiwa na hasira. Wakaingia kwenye gari na muda wote BQ alikuwa anatabasamu tu kila amuangaliapo Tom,
"Tuanzie hospitali au?" BQ aliuliza wakati akiitoa gari ndani
"Nipeleke nyumbani" Tom alijibu kijeuri na BQ akatabasamu na kufungulia radio ya gari huku akiwa makini na barabara,
"Tom utakufa, tatizo lako unaleta dharau unapoona hatukufanyi kitu" BQ aliongea huku macho yakiwa mbele,
"Hakuna binadamu atayeishi milele" Tom alijibu,
"Sawa, kufa wote tutakufa ila aina ya vifo vitakuwa tofauti, basi epuka kufa kifo cha uchungu" BQ aliongea,
'Mungu ndiye anaejua nitakufaje, sio nyie" Tom aliongea kisha akafuta damu iliyokuwa inachuruzika usoni,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sawa, endelea kujikatia tamaa" BQ aliongea na wakati huo mbele yao kulikuwa na askari. Gari yao ilipofika karibu na askari walipo, Gari ilipigwa mkono na ikaamriwa isimame pembeni mwa barabara, Tom akatabasamu na hapo akaweka dhamira ya kupasua jipu mbele ya askari, akadhamiria kusema ukweli endapo askari atakuja kuongea nao dirishani, Tom akatabasamu tena.
"Unacheka nini sasa?" BQ akamuuliza,
"Mwisho, mwisho wa haya mambo" Tom aliongea huku akiendelea kutabasamu ila kauli yake haikueleweka mbele ya BQ, BQ ikabidi nae atabasamu tu huku hajui dhamira ya mwenzie, dhamira ambayo inaweza kuanza kuleta ukakasi katika kambi ya washenzi ...........
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment