IMEANDIKWA NA : ALEX KILEO
*********************************************************************************
Simulizi : Mkono Wa Chuma
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ni nyakati za saa mbili na nusu asubuhi, anaonekana mwanamke mmoja ambaye ukimtazama mara moja tu, hutosita kugundua kuwa mwanamke huyu ni kichaa, chizi, mwendawazimu au ni mtu mwenye matatizo mengi ya akili.
Alikuwa na nywele ndefu zilizokaa kwenye mpangilio mbovu kabisa, yaani zilikuwa shaghalabaghala huku baadhi ya upande wa kichwani kukiwa na uchafu uliokamatana na nywele zake zile ndefu ambazo kila mwanamke alitamani kuwa nazo kutokana na afya na urefu wa nywele ile, zilionekana hazijakuna na mafuta na shampoo kwa kipindi kirefu sana.
Katika uso wa mwanadada huyu, hakukuwa na tatizo, alionekana ana mvuto kidogo ingawa upande mmoja kulikuwa na makovu yalioonekana yameachwa kutokana na vidonda vilivyotokana na moto, makovu yale yalipanda mpaka upande mmoja kichwani na kufanya upande huo mmoja wa juu mbele, nywele kushindwa kuota, kwa hiyo alitumia mbinu za kuzilaza baadhi ya nywele zake upande ule wenye kovu na kufunika kwa kiasi kikubwa lile kovu lake la kichwani.
Endapo hutojali na kuamua kutumia muda wako mrefu kumuangalia huyo dada, utagundua kuwa huyo ni dada hata ngozi ya mwili wake ni nzuri, tena zile ngozi zilizozoea mafuta ya bei ghali ila alijitahidi kuificha ile ngozi na kuonekana kama mtu aliyetoka kufukuliwa kwenye shimo la mkaa.
Na kitu kingine ni kuwa huyu mwanamke hakuwa na mkono, mkono mmoja wa kulia ulikuwa umekatika, umekatikia juu ya kiwiko na kufanya kuwa na kipande cha mkono, ule mkono mwingine wa kushoto ulikuwa hauna kasoro na alikuwa ameshika mfuko wa nylon wenye rangi ya ubuluu, mifuko ile yenye mchoro wa muigizaji maarufu wa kimarekani mwenye hasili ya uitaliano na umarekani ajulikanaye kama Silvester Stallone, almaarufu kama RAMBO. Mifuko hiyo huku uswahilini tunaiita mifuko ya Rambo.
Dada yule alitembea mwendo wa polepole na gauni lake fupi la kulalia lilioishia juu ya magoti na lilikuwa na rangi halisi ya maziwa, ila kutokana na kufubaa, lilibadilika rangi na kuwa na rangi kama tatu mchanganyiko ambazo ni ugoro, weusi na maziwa.
Dada yule hakuonekana kujali namna watu wanavyomkwepa na wanavyomuangalia, aliendelea kutembea na mkono wake mmoja uliokuwa na mfuko wa Rambo ambao ndani yake kulikuwa na karatasi zisizojulikana.
Safari ya dada huyu iliishia kwenye ofisi kubwa ya serikali, ofisi ya mkuu wa wilaya. Dada akapita getini
"wewe unaenda wapi?" Mgambo aliyekuwa getini alimuuliza huku akimfuata kwa lengo la kumtoa nje, aliamini huyu mwanamke ni kichaa,
"leo si ni jumatatu? Mheshimiwa si kila jumatatu anasikiliza malalamiko ya wananchi wa eneo lake?" Dada yule aliuliza kwa sauti ya upole huku akimuangalia yule Mgambo,
"ndio, na wewe una malalamiko?" Mgambo aliuliza huku akiwa anaona kama anaongea na mwendawazimu,
"ndio, nahitaji kuonana nae"" Dada aliendelea kuongea kwa utulivu na kumfanya yule mgambo atoe cheko la dhihaka na kufanya mapengo yake yaonekane vyema,
"ebu nieleze hayo matatizo yako, nitayashughulikia" Mgambo aliongea na kumfanya yule dada atabasamu, meno yake meupe yakaonekana,
"anatakiwa ayasikie mkuu wa wilaya na wala sio mlinzi wa getini" Dada aliongea na kupiga hatua akielekea ndani, ila yule Mgambo alihisi amedharauliwa sana kwa ile kauli, kauli kutoka kwa mwendawazimu, Mgambo akakimbia na kusimama mbele ya yule mwanamke,
"hujaruhusiwa kuingia ndani, humu wanaingia watu wenye akili timamu tu" Mgambo aliongea kwa jazba,
"kwa hiyo mimi sina akili timamu? mimi na wewe nani chizi?" Dada aliongea huku akimuangalia Mgambo kwa dharau, Mgambo akaamua atumie nguvu sasa, akaanza kumsukuma yule mwanamke, mwanamke alitaka kujaribu kushindana ila alishindwa kwa kuwa hakuwa na nguvu na pia alikuwa akitumia mkono mmoja ingali mwenzie alitumia mikono miwili.
Katika kusukumana, yule dada akaangusha mfuko wake wa Rambo chini na yeye pia akaanguka chini. Alipofika chini alimkata jicho la hasira yule Mgambo ambaye bado pia nae alionekana pia ana hasira na yule mwanamke.
Yule mwanamke akainuka kwa hasira sasa ili kukabiliana na huyo Mgambo,
"kuna nini hapa?" Sauti ya ukali ilisikika ikiuliza na kumfanya yule mgambo ahache kukabiliana na yule mwanamke,
"si huyu mwendawazimu analazimisha kuingia ndani akaonane na mkuu wa wilaya" Mgambo alijibu huku akihema haraka haraka,
"eti ni kweli?" Kijana aliyejibiwa na Mgambo aliuliza huku akimuangalia yule mwanamke,
"sijalazimisha, ila kama utaratibu unavyokuwaga siku kama ya leo ni rasmi mkuu wa wilaya aliitenga kwa ajili ya kuongea na sisi wananchi wake, ndio nimekuja nashangaa napita getini huyu mlinzi ananizuia" Yule mwanamke alijibu kwa utulivu huku akimuangalia yule kijana aliyevaa mavazi nadhifu,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"yaani una maongezi na mkuu wa wilaya, si ndio?" Kijana aliuliza huku akiwa bado anamshangaa yule mwanamke ambaye alionekana ni mwehu ila aliongea vuzuri tu,
"ndio, nina malalamiko kidogo" Dada alijibu,
"ingia hapo, utakuta kuna foleni watu wamekaa kwenye benchi nao wanahitaji kuonana na mheshimiwa kama wewe unavyohitaji, kwa hiyo ukifika Kaa kwenye benchi subiri zamu yako" Kijana aliongea na kisha yule mwanamke akainama na kuokota mfuko wake wa Rambo, kisha akaelekea kwenye mlango alioelekezwa,
"ila mheshimiwa huoni umemruhusu mwendawazimu akaonane na mkuu wa wilaya?" Mgambo aliuliza,
"huwezi jua, huenda kuna malalamiko ya maana anayo, pia yule ni mwanadamu, ana haki ya kusikilizwa" Kijana aliongea kisha nae akaelekea pale pale alipoingia yule mwanamke, ila alimkuta yule dada amesimama kwenye mstari ila mbali kidogo na wa mbele yake.
"sogea karibu na mwenzako, mnatakiwa kuwa karibu karibu" Kijana alimwambia yule dada,
"kuna watu watatu waliokuwepo mbele yangu ila wametoka na wamekaa pembeni" Dada aliongea huku akitabasamu na kumfanya yule kijana ageuze shingo na kuwaona wanawake watatu wakiwa wamekaa pembeni,
"usijali, sogea mbele umsogelee wa mbele yako" Kijana aliongea huku akiwa amemshika bega yule dada. Yule dada akasogea mbele, cha ajabu mtu wa mbele yake nae akachomoka na kwenda kukaa pembeni,
"ndivyo wote wamefanya hivi, nadhani ni kutokana na muonekano wangu" Dada aliongea, hakutaka kuliacha tabasamu lake limtoke mdomoni,
"usijali, sogea tena mbele" Kijana aliongea,
"hapana, endapo nitamsogelea kila mtu atatoka kwenye mstari, nitakuwa nimeharibu utaratibu, ni bora mimi nikae pembeni na wao warudi mstarini, nitamkariri mtu wa mbele yangu" Dada aliongea huku akitoka kwenye mstari na kumfanya yule kijana aondoke na kuingia kwenye ofisi moja, kisha akatoka na kiti cha plastic,
"njoo ukae hapa" Kijana aliongea na kisha yule dada akaelekea kilipo kiti na kukalia, cha ajabu baada ya yeye kutoka tu kwenye foleni, baadhi ya watu waliotoka kwenye mstari kwa sababu yake, walirudi kwenye foleni na kukaimu nafasi zao, dada yule baada ya kugundua hilo, aliachia tabasamu hafifu huku akiwaangalia.
Baada ya nusu saa, zamu ya yule dada ilifika, akainuka taratibu na kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye mlango mweupe uliokuwa na maandishi yaliyoandikwa (DC) na kubandikwa juu ya mlango. Aliendelea kupiga hatua huku nyuma kuna baadhi ya watu walikuwa wakimsema chini chini.
Alipoufikia mlango alisukuma na kuingia, ndani akakuta watu wawili, Mwanaume mmoja ambaye ndiye alimtambua kama mkuu wilaya ambaye alikuwa amekaa kwenye kiti nyuma ya meza kubwa ya kifahari na pia huyo mkuu wa wilaya alikuwa nae alikuwa amemtolea macho huyo dada mwenye muonekano kama kichaa.
Pembeni ya mkuu wa wilaya alikuwa amekaa msichana ambaye alikuwa ameshika kalamu na daktari ndogo, alikuwa anaandika maelezo ya kila mtu aliyekuwa anaingia hapo ndani, pia huyo msichana alikuwa amemtolea macho huyo dada aliyeingia hapo.
Dada mwenye muonekano kama kichaa akaachia tabasamu ili awatoe wasiwasi, ila watu hao wala hawakucheka, walikuwa wamemkodolea macho tu,
"nani amekuruhusu kuingia?" Msichana alimuuliza yule dada,
"Japan!!!!!!! kwani kuingia humu kuna utaratibu gani zaidi ya kupanga foleni nje?" Dada alijibu huku akishangaa,
"toka nje" Msichana aliongea huku akimuangalia yule dada mwenye muonekano wa kichaa,
"sasa mbona unanifukuza hata kabla sijamueleza mheshimiwa shida yangu?" Dada aliuliza huku akitabasamu na muda huo mkuu wa wilaya alisimama na kutoa noti ya elfu kumi na kumpatia yule dada kichaa,
"chukua hii, itakusaidia" Mkuu wa wilaya aliongea huku akimpatia pesa yule dada kichaa,
"siko hapa kwa ajili ya kuomba pesa, nina shida tofauti kabisa" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"una shida gani wewe, kama hutaki hela toka bwana" Msichana aliongea huku akiinuka ili amtoe nje yule dada,
"muache, Ebu niambie una shida gani?" Mkuu wa wilaya alimuuliza yule dada na kufanya yule dada auweke mfuko wake juu ya meza na kutaka kuufungua kwa kutumia ule mkono wake mmoja,
"hapana, usitoe karatasi, wewe sema tu nitakusikia" Mkuu wa wilaya aliongea na kufanya dada kichaa asitishe zoezi lake,
"nina mikataba hapa, ila imekiukwa na watu niliowekeana nao" Dada kichaa aliongea huku akiwa amesimama, maana hakukaribishwa hata kiti,
"mikataba hiyo inahusu nini?" Mkuu wa wilaya aliuliza,
"ni kuhusu majengo mawili ya mjini, yaani jengo la wizara ya fedha lile la ghorofa kumi na mbili, na jengo la jirani lile la benki kuu" Dada kichaa aliongea huku akimuangalia mkuu wa wilaya,
"yamefanyaje hayo majengo?" Mkuu wa wilaya aliuliza,
"kulingana na mikataba, yale majengo ni mali yangu" Dada kichaa aliongea na kufanya mkuu wa wilaya na yule msichana anayemsaidia wakatazamana na kucheka chini chini, sasa waliamini kabisa huyo dada ni kichaa kabisa,
"hiyo mikataba ulifanya na nani?" Mkuu wa wilaya aliuliza huku akitabasamu,
"rais aliyepita, Tammy Semmy, nilifanya naye hiyo mikataba kipindi akiwa makamo wa rais" Dada kichaa aliongea na kufanya mkuu wa wilaya acheke tena, tena safari hii alicheka wazi wazi kabisa bila kujificha,
"sasa hapo umejidhihirisha ukichaa wako, yaani wewe ulivyo hivyo ni rais yupi anaweza kukaa na wewe, achana na suala la kusainishana mikataba, yaani kukaa tu na wewe haiwezekani" Mkuu wa wilaya aliongea huku akiinuka kwenye kiti,
"lakini mheshimiwa nina hii hapa kwenye mfuko" Dada kichaa aliongea huku akiuonesha mfuko wake,
"yaani yaani mikataba mikubwa ya kumiliki majengo makubwa unaiweka kwenye rambo?" Msichana msaidizi wa mkuu wa wilaya aliongea na kucheka kwa dharau na kipindi hicho mkuu wa wilaya alikuwa akifungua mlango,
"nani amemruhusu huyu mwendawazimu aingie humu ofisini kwangu?" Mkuu wa wilaya aliongea kwa sauti kubwa huku akiwa amesimama mlangoni na kufanya watu wote wamuangalie,
"mimi hapa mheshimiwa" Kijana aliyempokea yule dada kichaa kwa ukarimu alijibu,
"njoo umtoe humu, sio kila mtu anayefika hapa basi anastahili kuongea na mimi" Mkuu wa wilaya aliongea kwa ukali,
"Ila ungenisililiza kwanza" Dada kichaa aliongea huku akiwa amesimama pembeni ya mkuu wa wilaya,
"toka nje, siwezi kusikiliza zaidi ya ulichonieleza, namaanisha siwezi kusikiliza upumbavu tena" Mkuu wa wilaya aliongea kwa ukali na kumshika yule dada na kumsukumia nje, akadondoka chini yeye na mfuko na wake, kisha akaokota mfuko wake na kusimama, akamgeukia mkuu wa wilaya na kutaka kuongea kitu, ila akasita kisha akitabasamu, alafu akageuka na kuanza kuondoka huku watu wakimuangalia,
"huyu hakutakiwa kuruhusiwa kufika hapa, hastahili kuingia ofisini kwangu, huyu hastahili kuwa hapa labda mirembe" Mkuu wa wilaya aliendelea kubwata huku yule dada akiendelea kupiga hatua, hakuonekana kujali maneno ya mkuu wa wilaya ila aliyasikiliza.
Yule dada alitembea mpaka alipofika usawa wa yule Kijana aliyemkarimu mwanzo, Dada akasimama ila hakutaka kumtazama yule Kijana usoni, ila dada alitabasamu huku akiamini fika yule Kijana anamtazama,
"sikustahili kuwa hapa, nilistahili kuwa mirembe, ila nadhani kesho asubuhi kila mtu atakutwa anapostahili" Dada kichaa aliongea kisha akaanza kuondoka na kumuacha yule Kijana akiyashangaa yale maneno ya yule dada kichaa huku hasijue maana yake.
Baada ya yule dada kuondoka kila mtu eneo lile alicheka huku kila mmoja akiongea neno lake, isipokuwa yule Kijana tu, alikuwa bado anahisi kabisa yule dada kichaa hakutendewa haki.
*****************************
Siku iliyofuata, mishale ya saa moja asubuhi, yule kijana mkarimu alikuwa amevaa kitanashati, alikuwa akiwahi kazini, ila alishangaa kuona kundi kubwa la watu likikimbia kuelekea ilipo shule ya msingi, akapuuza, alihisi ni mwizi tu anakimbizwa.
Akaendelea kusogea mbele kwa hatua za haraka haraka, akapishana na kundi jingine la watu wakielekea upande ule ule, tena safari hii hakutaka kupuuza,
"kuna nini uko?" Kijana alimuuliza Msichana mmoja aliyekuwa nae anakimbilia uko,
"kuna mtu amekufa, amepigiliwa misumari juu ya mti" Msichana alijibu huku akikimbia.
Kijana akaona ni bora na yeye akashuhudie, haikuwa tukio lililozoeleka eneo hilo, hilo lilikuwa tukio jipya kabisa.
Kijana akaanza kupiga hatua kuelekea eneo la shule, alipofika aliweza kuona kundi la watu likiwa limeuzunguka mti, Kijana akaanza kupangua watu na mwisho anajikuta yupo mbele ya mti, juu ya mti kuna mwili wa mwanaume ukiwa umetundikwa, yaani mikono yake imegongelewa na misumari kwenye shina la mti na mwili wake ulikuwa ukining'inia, na mwili haukuwa na nguo, ulikuwa mwili wa mwanaume.
Yule kijana akauangalia ila hakumgundua yule maiti, kijana kwenye kutupa macho kuwaangalia baadhi ya watu waliopo pale, aliweza kumuona yule dada kichaa nae akiwa miongoni mwa mashuhuda wa tukio lile, hakutaka kumfuatilia sana.
"mshusheni sasa, mnangoja nini?" Ilikuwa sauti ya polisi mmoja akiwaambia wananchi.
Vijana kadhaa wakatoka na kwenda kutafuta ngazi, baada ya muda wakarudi, wakapanda na kuutelemsha ule mwili, sasa hapo ndipo watu walishtuka, ulikuwa ni mwili wa Mkuu wa wilaya, kundi zima likakazima kwa mshtuko, mpaka polisi wenyewe wakashikwa na mshangao.
Yule kijana ndio akachanganyikiwa zaidi, maana ndio boss wake,
"kuna karatasi kwenye pua" Kijana aliongea baada ya kuona kuna kikaratasi kidogo kilichojitikeza kwenye pua ya mkuu wa wilaya, watu wote wakaiangalia pua ya mkuu wa wilaya, kweli kulikuwa na karatasi. Polisi mmoja akaichomoa ile karatasi na kuisoma kimya kimya,
"kuna ujumbe gani?" Polisi mwingine akauliza,
"imeandikwa "kesho kila mtu atakuwa anapostahili" Polisi yule aliusoma ule ujumbe na kumfanya yule kijana afikirie Yale maneno amewahi kuyasikia wapi? akumbuka kuwa yale maneno yaliongewa siku iliyopita na yule dada kichaa, yule kijana akamtupia jicho yule dada kichaa na akakuta pia yule dada anamtizama, yule dada akatabasamu.
Yule kijana akamsogelea polisi na kuongea nae,
"yule dada nahisi anajua kitu kuhusu hili tukio" Kijana aliongea huku akiwa ameinamisha kichwa chini ili dada kichaa hasijue kinachoendelea,
"Dada yupi?" Polisi aliuliza,
"humuoni huyo dada kichaa mbele yetu?" Kijana aliuliza huku akiinua kichwa, cha ajabu hakumuona tena yule dada kichaa, kijana akashangaa, akapanda juu ya ngazi iliyotumiwa kuutungua mwili wa mkuu wa wilaya.
Kijana akapanda na kuanza kuzungusha macho kuona kama ataweza kufanikiwa kumuona yule dada, ila hakumuona, yaani alipotea ghafla tu.
Kijana akashuka na kutaka kutoka katikati ya lile kundi ili akamtafute yule dada,
"wewe utakuwa mshukiwa wa kwanza wa hili tukio, kuna unakijua wewe" Polisi aliongea na kumshika mkono yule kijana na kwenda kumuingiza kwenye gari huku yule kijana akilalamika bila polisi yoyote kujali malalamiko yake.......
Polisi waliuchukua mwili wa mkuu wa wilaya na kuuingiza ndani ya gari, kisha wakaondoka huku wakiwa pamoja na yule kijana mkarimu.
Mwili wa mkuu wa wilaya wakauacha hospital kisha gari la polisi likaelekea moja kwa moja kituoni. Walipofika walitelemka na kisha yule kijana akapelekwa moja kwa moja katika ofisi ya Mkuu wa kituo,
"Huyu kijana inaelekea kuna kitu anakijua kuhusu kifo cha mkuu wa wilaya" Polisi aliongea huku akiwa amesimama kikakamavu mbele ya Mkuu wa kituo,
"kifo cha mkuu wa wilaya?" Mkuu wa kituo aliuliza kwa mshangao,
"Ndio, ule mwili tulioenda kuuchukua katika eneo la shule, ni mwili wa mkuu wa wilaya hii" Polisi alijibu kikakamavu na kumfanya mkuu wa kituo hazidi kutahamaki,
"Na huyu kijana ni nani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"Hata mimi simjui, ila kuna ujumbe ulikutwa kwenye mwili wa marehemu, huyu kijana akadai anajua aliyeandika hayo maneno" Polisi aliongea huku akimpatia mkuu wa kituo kile kikaratasi, mkuu wa kituo akayasoma yale maneno kwa sekunde kadhaa,
"eti kijana unajua nini kuhusu hiki kifo?" Mkuu wa kituo alimuuliza yule kijana mkarimu,
"kusema kweli kuhusu kifo cha mkuu wa wilaya mimi sijui chochote, ninachojua ni kuhusu hayo maneno yaliyoandikwa kwenye hicho kikaratasi" Kijana mkarimu aliongea kwa utulivu,
"haya maneno yana nini?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hayo maneno kuna kichaa mmoja aliyaongea siku iliyopita, tena aliyaongea muda mfupi baada ya kutoka katika ofisi ya Mkuu wa wilaya, tena inaelekea hakupendezwa namna mkuu wa wilaya alivyokuwa anamfukuza ofisini kwake" Kijana mkarimu alijibu,
"kichaa?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"ndio" Kijana mkarimu alijibu,
"huyo kichaa alifuata nini kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"sijui kwa kweli" Kijana mkarimu alijibu,
"tungeweza kupata kilichoongelewa ndani ya ofisi ingekuwa nafuu kwako, sasa hatujui ni kipi walichoongea" Mkuu wa kituo aliongea huku akivua miwani yake,
"kuna dada mmoja huenda akawa anajua kilichoongelewa baina ya Mkuu wa wilaya na huyo kichaa" Kijana mkarimu aliongea,
"huyo dada ni nani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"Ni msaidizi wa mkuu wa wilaya, uwa anamsaidia kuandika mahojiano anayofanya mkuu wa wilaya na wananchi wake" Kijana mkarimu alijibu,
"unapafahamu anapokaa huyo dada?" Mkuu wa kituo aliuliza,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ndio" Kijana mkarimu alijibu kisha akamuelekeza mkuu wa kituo kwa kumtajia mtaa na namba ya nyumba na jina la mtu anayehitajika.
Mkuu wa kituo akawaita askari wawili na kuwaagiza waende wakamuangalie yule Msichana na wakimkuta wamlete kituoni muda huo, Askari wakatoka mpaka nje, wakaingia kwenye gari ndogo yenye namba za usajili binafsi, kisha wakaondoka kuelekea uko kwa huyo dada.
Walipofika waliweza kumuona huyo dada akiwa amejitanda kanga, alikuwa anataka kuingia ndani ya gari lake. Polisi wakashuka na kumfuata, wakawasalimia,
"Unahitajika polisi" Polisi mmoja alimwambia,
"kuna nini?" Dada aliuliza huku akishangaa, macho yake yalikuwa mekundu kutokana na kulia muda mrefu,
"kuhusu kifo cha mkuu wa wilaya" Polisi alijibu kifupi,
"sasa mimi nahusikaje?" Dada aliuliza,
"hauhusiki, ila Unahitajika, utaenda kuhojiwa alafu utaachiwa" Polisi aliongea na kisha yule dada akakubali kuongozana nao, wakaingia nae ndani ya gari na kuondoka.
Walifika mpaka kituoni na kuingia moja kwa moja kwa mkuu wa kituo, wakamkuta mkuu wa kituo akiwa bado yupo na yule kijana mkarimu, yule dada akashangaa kumkuta mfanyakazi mwenzie ndani,
"Kaa hapo binti" Mkuu wa kituo aliongea huku akimuonesha kiti yule dada na wale polisi waliomleta walikuwa bado wamesimama.
Yule dada akakaa kwenye kiti,
"Ni kweli jana wakati mpo ofisini kuna dada mmoja kichaa aliingia?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"ndio" Msichana alijibu,
"alikuwa anataka nini?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"alikuwa anadai ameingia mkataba na Rais aliyetoka madarakani, na mkataba wenyewe ni ule wa yale majengo makubwa mawili mapya ya serikali" Msichana alijibu huku hajui kwanini anahojiwa maswali hayo,
"hakuna jingine?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hakuna, kwa maana baada ya kuongea maneno hayo tu, mheshimiwa alimfukuza" Msichana alijibu,
"hayo maneno yaliyokutwa kwenye hiyo karatasi yaliongelewa wapi?" Mkuu wa kituo aliuliza huku akimtazama yule kijana mkarimu,
"wakati anaondoka alipofika jirani na mimi" Kijana mkarimu alijibu,
"mnafahamu anapopatikana huyo kichaa?" Mkuu wa kituo aliuliza, lakini yule kijana mkarimu na yule Msichana wakajibu kwa kutikisa kichwa kuashiria hawajui,
"lakini sura yake mnaweza kuitambua?" Mkuu wa kituo aliuliza swali jingine,
"Mimi naijua sura yake, hata pale kwenye tukio alikuwepo" Kijana mkarimu alijibu,
"kama alikuwepo kwanini hukuwapa taharifa polisi?" Mkuu wa kituo alihoji,
"niliwaambia, ila yule kichaa alitoweka ghafla eneo lile" Kijana mkarimu alijibu,
"Basi naomba hili jambo msimwambie mtu, kufanya hivyo itakuwa inatusaidia kufanya uchunguzi wetu kimya kimya bila mtu yoyote wa kujua kama tunafanya upelelezi, sawa?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"sawa" walijibu kwa pamoja,
"Na popote mtapomuona huyo kichaa mnitaharifu, nitawapa namba zangu" Mkuu wa kituo aliongea,
"Sawa mkuu" Kijana mkarimu alijibu,
"mnaweza mkaondoka sasa" Mkuu wa kituo aliongea huku akiwapa karatasi ndogo aliyoandika namba yake ya simu.
Yule Msichana na yule kijana mkarimu wakatoka mpaka nje ya kituo,
"hivi ni kweli inawezekana ni yule kichaa amefanya haya mauaji?" Msichana aliuliza,
"atakuwa ni yeye tu, maana yale maneno aliongea mwenyewe kabisa" Kijana mkarimu alijibu huku akimtazama yule Msichana ambaye alikuwa akisikitika,
"Basi acha mi nirudi nyumbani nikachukue gari ili nielekee msibani" Msichana aliongea,
"Sawa, hata mi naelekea msibani, tutawasiliana basi" Kijana mkarimu aliongea kisha wakaachana huku yule Msichana akisimamisha bajaj na kuondoka na pia yule kijana mkarimu akishika njia yake na kuondoka taratibu huku sura ya yule dada kichaa ikiwa inamrejea kila dakika katika kichwa chake.
********×***
Madaktari waliufanyia uchunguzi mwili wa mkuu wa wilaya, na majibu waliwakabidhi polisi.
Askari baada ya kuisoma ile taharifa ya uchunguzi, waligundua kuwa kuna alama za mikono zimeonekana kwenye shingo ya Mkuu wa wilaya, yaani kulikuwa na uwezekano kuwa alikabwa kabla hajauawa.
Ikabidi polisi wawaite tena yule Msichana na yule kijana mkarimu ili wawe wa watu wa hawali kabisa kuangaliwa alama za mikono yao.
Kijana na yule Msichana walifika polisi, kisha wakachuliwa mpaka hospitali na kuangaliwa alama za mikononi, baada ya vipimo zile alama za mikono yao zikalinganishwa na alama zile zilizotokea kwenye shingo ya Mkuu wa wilaya, kwa kweli alama hazilufanana kabisa,
"sasa tuendelee kumtafuta huyo kichaa, huenda akawa ndio jibu la hili swali letu" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa" Kijana mkarimu alijibu,
"mnaweza kuondoka, ila mnaweza kuhitajika tena muda wowote" Mkuu wa kituo aliongea na kisha yule kijana mkarimu na Msichana wakaondoka huku yule Msichana akionekana kutopenda namna wanavyosumbuliwa na polisi.
Msichana alienda mpaka kwenye gari yake na kuingia, akaondoa gari kwa kasi kuwahi msibani, ila alipofika maeneo ya sokoni aliamua ashuke ili anunue mahitaji kidogo ya nyumbani, akatelemka kwenye gari na kuingia sokoni.
Baada ya muda alirudi kwenye gari huku akiwa na mifuko mikubwa miwili mkononi, akafungua mlango wa nyuma na kuiweka, kisha akaingia mbele, ila alipotupa macho siti ya pili aliona kuna mtu, alipomuangalia usoni alikuwa ni yule dada kichaa, alikuwa akitabasamu na kumfanya yule dada ashtuke, huku akiwaza yule kichaa ameingiaje wakati mlango alifunga?
"usiogope, za tangu jana?" Dada kichaa aliuliza,
"safi" Msichana alijibu huku akiwa na uoga moyoni,
"najua umetoka polisi muda huu, je polisi wamefikia wapi katika uchunguzi wa kifo cha boss wako?" Dada kichaa aliuliza huku akitabasamu,
"hamna, mimi sijui kitu" Msichana alijibu huku akitetemeka na kumfanya yule dada kichaa atabasamu,
"jana si ulikuwa na ujasili wa kunifukuza ofisini, vipi leo umekuwa muoga namna hiyo?" Dada kichaa aliuliza, lakini yule Msichana hakujibu kitu,
"nilikuja kukuonya tu, popote unionapo mimi usiwape taharifa polisi, kufanya hivyo ni kuhidhinisha kifo chako" Dada kichaa aliongea kisha akatelemka chini na kuanza kupiga hatua na kuondoka kwa mwendo wa taratibu.
Yule dada kichaa alipofika mbali kidogo, yule Msichana akatoa simu na kuwataharifu polisi kuhusu kumuona yule dada kichaa, alafu yeye hakuondoa gari, alibaki pale pale alikuwa akimuangalia yule dada kichaa akiuvunja mhogo aliopewa na muuzaji wa sokoni.
Baada ya dakika tano gari ya polisi iliingia kwa kasi eneo lile la polisi kisha askari wapatao saba wakaruka chini kabla gari halijasimama vizuri.
Wale Askari walivyoshuka na yule Msichana akatelemka kwenye gari yake na watu wote sokoni waliacha kazi zao na kutazama wale polisi wamekuja kufanya nini.
"Yupo wapi?" Askari aliuliza huku akimtazama yule Msichana aliyepiga simu,
"yule pale" Msichana alijibu huku akimuoneshea kidole yule dada kichaa ambaye muda huo alikuwa amekaa chini ya mti huku akiutafuna mhogo wake, na kipindi yule kijana mkarimu nae alikuwa anafika eneo lile baada ya kupigiwa na yule Msichana.
Polisi wakasogea mpaka alipo yule dada kichaa na kumshika, wakamnyanyua kwa nguvu, dada kichaa akaanza kuleta vurugu, hataki kushikwa na polisi,
"mnanipeleka wapi?" Dada kichaa aliongea huku akiendelea kuleta vurugu,
"muacheni, muacheni kwanza" Kijana mkarimu aliongea na kufanya polisi wamtazame,
"Wewe unaongea kama nani?" Polisi mmoja aliuliza kwa hasira, ila dada kichaa aliwachomoka polisi na kwenda kumshika yule kijana mkarimu,
"wanataka kwenda kunibaka, nisaidie" Dada kichaa aliongea huku akiwa amemshika kijana mkarimu kwa mkono mmoja kwa maana alikuwa na mkono huo huo mmoja,
"Ni watu wema tu, wanataka wakupeleke polisi wakakuhoji kuhusu tukio la kifo cha mkuu wa wilaya, baada ya hapo watakuachia" Kijana mkarimu aliongea,
"tunaenda wote, na wewe?" Dada kichaa alimuuliza,
"Ndio, na mimi naenda" Kijana mkarimu alijibu,
"haya twende" Dada kichaa aliongea, kisha yule kijana akaanza kuelekea kwenye gari ya polisi huku akiwa amemshika mkono yule dada kichaa,
"popote unionapo usiwape taharifa polisi, kufanya hivyo ni kuhidhinisha kifo chako" Dada kichaa aliongea kwa sauti ndogo ila ilisikika vizuri tu masikioni mwa yule kijana,
"usiwe na shida" Kijana mkarimu alijibu huku akitabasamu ingawa hiyo kauli ilimtisha,
"sijakuambia wewe, nilimuonya yule Msichana" Dada kichaa aliongea huku akimtazama yule Msichana ambaye alikuwa akimsaidia mkuu wa wilaya na kipindi hicho yule Msichana alikuwa akiingia kwenye gari yake.
Kijana mkarimu aliyapuuza tu maneno ya dada kichaa, aliamini huenda akienda polisi hawezi kutoka leo wala kesho,
"usiwe na imani hiyo, nakuhakikishia tu leo hii naachiwa" Dada kichaa aliongea na kumfanya yule kijana ashtuke, maana akishangaa yule dada kichaa kujua kitu anachokiwaza, ila kijana hakuuonesha mshtuko wake, badala yake alitabasamu na kipindi hicho gari la polisi lilikuwa likitoka eneo lile la sokoni huku watu wasijue kinachoendelea baina ya polisi na Dada huyo ambaye ni kichaa........
Gari ya polisi ilienda mpaka kituoni na kisha ikasimama, kisha polisi wakatelemka na Dada kichaa akashuka, polisi hawakutaka kumshika, walimuacha huru tu.
Polisi wawili wakatangulia mbele na kisha katikati waliokuwepo dada kichaa na kijana mkarimu na nyuma walikuwa polisi watano.
Ule msafara uliishia katika ofisi ya Mkuu wa kituo,
"mtuhumiwa huyu hapa" Polisi mmoja aliongea kwa ukakamavu mbele ya Mkuu wake na kumfanya mkubwa wake na kumtazama yule dada kichaa kwa muda,
"sawa, nyie askari nendeni nje, tacheni na hawa watu, yule Msichana mwingine aliyetoa taarifa yupo wapi?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"anakuja" Kijana mkarimu alijibu na kipindi hicho yule Msichana alikuwa akiingia katika ofisi hiyo na wale Askari wengine wakatoka nje,
"Kaa hapo" Mkuu wa kituo alimwambia dada kichaa huku akimuonesha kiti, yule dada kichaa akakaa,
"Naomba hayo maji, nina kiu" Dada kichaa aliongea huku akiiangalia chupa kubwa iliyokuwa mezani, mkuu wa kituo akampatia ile chupa,
"Dada mwenyewe ndo huyu?" Mkuu wa kituo aliuliza huku akiwatupia jicho yule Msichana na yule kijana mkarimu,
"ndiye huyu huyu" Msichana alijibu kwa sauti kubwa na kumfanya yule dada kichaa amgeukie kisha akatabasamu,
"Binti unamjua mkuu wa wilaya?" Mkuu wa kituo aliuliza huku akimtazama yule dada kichaa,
"namjua, si yule aliyekutwa amekufa asubuhi ya leo?" Dada kichaa aliongea kisha akaendelea kupasua muhogo wake kwa kuupiga juu ya meza ya Mkuu wa kituo,
"kabla ya tukio la leo umeshawahi kumuona tena?" Mkuu wa kituo alihoji,
"Ndio, jana nilienda ofisini kwake, nilikuwa na malalamiko" Dada kichaa aliongea,
"malalamiko juu ya nini?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"siweii kuyaeleza hapa, kwa maana sio sehemu husika, au huyo dada anaweza kueleza kwa maana na yeye alikuwepo" Dada kichaa aliongea,
"sawa, tuachane na hayo, je nitakosea kama nitakuhusisha na kifo cha mkuu wa wilaya?" Mkuu wa kituo alimuuliza,
"Mimi? Au naonekana kama muuaji?" Dada kichaa aliongea na kutabasamu,
"Twende hospitali tukaangalie alama za mikono yako" Mkuu wa kituo aliongea huku akimtazama yule dada kichaa,
"sio mikono, sema mkono kwa maana ninao huu huu mmoja" Dada kichaa alimrekebisha mkuu wa kituo,
"sawa, tunaweza kwenda" Mkuu wa kituo aliongea huku akisimama na kufanya watu wote wasimame, kisha wakatoka mpaka nje.
Wakaingia kwenye gari huku na askari wengine wakiongezeka. Wakaelekea mpaka hospitali na moja kwa moja wakaongea na Daktari.
Daktari akaingia kwenye chumba cha vipimo huku akiongozana na Dada kichaa na Mkuu wa kituo.
Walipofika ndani wakaanza kumpima alama za mikononi yule dada kichaa. Zoezi halikuchukua muda mrefu.
"sasa hapa tumemaliza, baada ya nusu saa nitakuwa na majibu ya vipimo" Daktari alimwambia mkuu wa kituo huku wakitoka nje,
"sawa, tutarudi baada ya muda huo" Mkuu wa kituo aliongea,
"Kwa hiyo sisi tuondoke?" Msichana aliuliza huku akimuangalia mkuu wa kituo,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nyie mnaweza kuondoka, ila huyu mrembo namrudisha kituoni" Mkuu wa kituo aliongea huku akimshika bega yule dada kichaa,
"sawa" Kijana mkarimu alijibu kisha polisi wakaanza kuondoka na yule dada kichaa, yule dada kichaa alipofika karibu na kijana mkarimu na yule Msichana, alisimama na kutabasamu, kisha akamuangalie yule Msichana,
"Wewe ndo umesababisha mimi kusumbuliwa hivi na kushindwa kufanya mambo yangu mtaani" Dada kichaa aliongea kwa sauti ambayo polisi hawakuisikia,.
"Kwani tatizo nini? usiniletee ukichaa wako hapa" Msichana alijibu kwa jeuri tena kwa sauti kubwa,
"Tatizo nini?, tatizo polisi" Dada kichaa alijibu huku akiondoka na kuelekea kwenye gari la polisi, kisha akapanda gari na kuondoka pamoja na askari,
"sidhani kama huyu dada ni kichaa kweli" Kijana mkarimu aliongea huku akimtazama yule Msichana,
"atajijua mwenyewe, kama ni kichaa au sio kichaa" Msichana alijibu kwa jazba huku akijifuta uso na kitambaa,
"haya bwana, unaelekea wapi muda huu?" Kijana mkarimu alimuuliza yule Msichana,
"narudi msibani" Msichana alijibu,
"nipe lifti, na mimi naelekea huko huko" Kijana mkarimu aliongea,
"Twende" Msichana aliongea kisha wakaingia kwenye gari na kuondoka.
*****************
Mkuu wa kituo na Dada kichaa walienda moja kwa moja mpaka kituoni,
"tumuweke lock up?" Askari mmoja alimuuliza mkuu wa kituo,
"Jamani nina njaa, niachieni nikatafute chakula mtaani" Dada kichaa aliongea kwa upole,
"unaenda kununua chakula wapi?" Mkuu wa kituo alimuuliza huku akimtazama,
"naenda Kuomba tu mtaani" Dada kichaa aliongea,
"Ebu kamchukulie chipsi" Mkuu wa kituo aliongea na kumpa pesa askari aliyekuwa hapo,
"Asante sana baba, kufanya hivyo utakuwa umenisaidia sana" Dada kichaa aliongea,
"Twende ofisini kwangu" Mkuu wa kituo aliongea huku akielekea ndani na kisha yule dada kichaa akamfuata kwa nyuma mpaka ofisini, kisha akakaa kwenye kiti,
"nyumbani wapi?" Mkuu wa kituo alimuuliza,
"Mimi sina kwetu, naishi mtaani tu" Dada kichaa alijibu huku akitabasamu,
"umezaliwa mtaani?" Mkuu wa kituo aliuliza tena,
"urusi" Dada kichaa aliongea na kumfanya mkuu wa kituo aanze kuona huyu mtu sio mzima kweli,
"Kwa mkuu wa wilaya ulienda kwa mazungumzo gani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"nilishakwambia yule Msichana ndio umuulize, mimi siweii kukujibu" Dada kichaa aliongea na kipindi hicho askari aliyeagizwa chakula alikuwa anaingia na mfuko laini ukiwa mkononi, kisha akampatia yule dada kichaa.
"nisaidie kujibu, alafu nitakupatia pesa leo" Mkuu wa kituo alimshawishi yule dada kichaa,
"pesa?? we unadhani una pesa nyingi kuliko mimi?" Dada kichaa aliuliza na kutabasamu na kumfanya mkuu wa kituo nae atabasamu, alishaamini kabisa kuwa yule binti ni kichaa,
"pesa zako Zipo wapi?" Mkuu wa kituo aliuliza kwa utani na kufanya yule dada kichaa haache kula na kumtazama kwa dakika mpaka mkuu wa kituo akapata hofu,
"sio vyema kuniongelesha wakati ninakula, naweza kupaliwa na chakula" Dada kichaa aliongea na kisha akaendelea kula huku mkuu wa polisi akitabasamu.
Baada ya saa moja, mkuu wa kituo akaondoka na yule binti kichaa na polisi wawili, walikuwa wanarudi hospitali kuchukuwa majibu ya vipimo vya alama za mikono ya dada kichaa.
Walifika hospitali moja kwa moja, kisha Mkuu wa kituo akaingia ofisini kwa Daktari na kumuacha yule dada kichaa akiwa na wale Askari wawili nje.
Baada ya nusu saa mkuu wa kituo alitoka huku akiwa na bahasa ya kaki mkononi,
"muachieni aondoke" Mkuu wa Polisi aliwaambia wale Askari ambao walitii, wakamuachia yule dada kichaa, akatabasamu,
"Naomba nauli, kwa maana mmenitoa mbali sana" Dada kichaa aliongea kwa upole kisha Mkuu wa kituo akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu mbili, akampatia,
"Asante" Dada alipokea na kuanza kuondoka kwa mwendo wake wa taratibu huku wale Askari wengine wakitazamana mpaka alipopotea machoni kwa.
"vipimo vinasemaje mkuu?" Askari mmoja aliuliza,
"alama za mkono wake hazifanani na zile zilizokuwa kwenye mwili wa mkuu wa wilaya" Mkuu wa kituo alijibu huku nae akiondoka na kufanya wale Askari wamfuate kwa nyuma.
***********
Uko msibani kulikuwa na kikao kidogo cha wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa wilaya, waliamua wakae kikao ili wao kama wao wachange rambirambi kwa ujumla wao na kukabidhi kwa familia ya marehemu, na wakakubaliana kuwa pesa zote za mchango zitashikwa na yule Msichana, na mpaka kesho asubuhi kila mtu awe amekabidhi pesa yake kwa yule Msichana.
Kikao kikafungwa namna hiyo, kila mtu alionekana kukubaliana na hayo maamuzi.
************
Siku mpya ilikucha, jua likachomoza tena na kuangazia dunia mwanga wa asili.
Kwenye barabara alionekana yule kijana mkarimu akielekea msibani, ilikuwa yapata saa tatu na robo asubuhi.
Alipofika msibani alikuta wenzie waliokuwa wote kwenye kikao siku iliyopita wakiwa wamekaa pamoja, akawafuata na kuwasalimia,
"muda wa kuwasilisha rambirambi kwa wahusika wa msiba ni saa tatu na nusu, ila mpaka muda huu Zawadi hajafika". Mmoja kati ya wenzake aliongea kwa hasira kidogo. Zawadi ni jina la yule Msichana ambaye alikuwa akimsaidia mkuu wa wilaya.
"mmejaribu kumpigia simu?" Kijana mkarimu aliuliza,
"tumempigia zaidi ya mara kumi, lakini hapokei" Mwenzake alijibu na kufanya kijana mkarimu achukue simu yake mfukoni na kuanza kupiga namba ya Zawadi, simu iliita bila kupokelewa, akajaribu tena na tena ila hali ikawa ile ile, kijana mkarimu akapata hofu,
"sio kawaida yake kutopokea simu, Ebu twendeni nyumbani kwake" Kijana mkarimu aliongea na kisha wote wakaelekea kwenye gari ya mwenzao mmoja na wakaingia, safari ya kuelekea nyumbani kwa Zawadi ikaanza.
Iliwachukua dakika kumi na tano kufika kwenye nyumba anayoishi Zawadi, kilichowashangaza ni kukuta kundi kubwa la watu wakiwa wameizunguka nyumba ya Zawadi, na nje kulikuwa na gari la polisi,
"kuna nini hapa?" Mmoja kati yao aliuliza,
"Ebu twendeni ndani tukaangalie" Mwingine alijibu kisha vijana wale wakatelemka na kujipenyeza kwenye kundi la watu mpaka wakafanikiwa kufika sebuleni kwa zawadi, walichokiona ndicho kiliwatisha, ulikuwa mwili wa mwanamke ukiwa hauna nguo hata moja, ulikuwa umepigiliwa misumali ukutani na kufanya uning'inie.
Vijana wale hawakupata shida kuutambua kuwa ule mwili ni wa Zawadi, ulitisha kwa kweli, yaani mikono yake ilitandazwa na kugongelewa misumali ukutani na kisha miguu ikawekwa sehemu moja na kupigiliwa misumali, ilikuwa ni kama picha ya mtu ametundikwa msalabani.
Meno yake aliyauma kwa uchungu na hiyo ilionesha kuwa kabla ya kufa alipata maumivu makali sana.
Na pembeni yake kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa damu, hayakusomeka vizuri kutokana na hati mbaya iliyotumiwa na muandishi.
"aliyeweza kuyaelewa hayo maneno atusomee hapo" Askari mmoja aliongea na kufanya vijana wale watupie macho kwa pamoja yale maandishi, walitupia macho kwa dakika mbili nzima huku kila mmoja akijaribu kusoma bila mafanikio,
"Tatizo ni polisi" Kijana mmoja alisoma kwa tabu sana na wengine wakaona ni kweli pameandikwa hivyo,
"dah, ameua tena!!!!!" Kijana mkarimu aliongea kwa mshangao na kufanya wenzake pamoja na maaskari wamtupie jicho lenye viulizo.......
"nani?" mwenzake aliuliza huku akimtazama,
"Ni dada mmoja hivi kichaa" Kijana mkarimu alijibu na kufanya wenzake washangae,
"kwanini aue sasa?" Askari mmoja aliuliza huku akimtazama yule kijana mkarimu,
"Mimi sijui" Kijana mkarimu alijibu,
"Wewe itabidi tuondoke wote, kuna kitu unajua" Askari aliongea huku akimfunga pingu yule kijana,
"mimi sijui kitu jamani" Kijana mkarimu aliongea lakini askari hakujali maneno yake, aliondoka nae na kumuingiza ndani ya gari kisha akaondoka nae.
Huku waliobaki ndani kila mmoja alikuwa akiwaza ni kitu gani kinachoendelea,
"Jamani Ebu twendeni polisi ili tujue kinachoendelea" Kijana mmoja aliongea huku akiwatazama wenzake,
"twendeni" Kijana mwingine aliongea na kisha wote wakatoka nje na kuingia kwenye gari waliyokuja nayo, wakaondoka kwa lengo la kwenda kufuatilia mustakali wa mwenzao aliyechukuliwa na polisi muda mfupi uliopita.
********************
Katika lile kundi la watu ambao walijaa nje ya nyumba ya Msichana aliyeuawa, alikuwepo pia yule dada kichaa, baada ya kuona mambo yanavyoenda na pia alishuhudia pia yule kijana mkarimu akiondoka na polisi.
Dada kichaa akajichomoa katikati ya watu na kisha akaanza kupiga hatua ndogo ndogo za kuondoka eneo lile.
Dada yule kichaa aliendelea kutembea kwa mwendo wa taratibu mpaka kwenye jengo moja ambalo kulikuwa na maduka, akaelekea kwenye mlango mmoja ambao ulikuwa umechorwa nembo moja ya chama cha siasa na pia juu ya mlango huo kulikuwa na bendera ya chama husika. Akaingia na kumkuta mzee mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha plastic nyuma ya meza kubwa ya mbao, mzee alikuwa bize anaweka betri kwenye radio yake, betri zilikuwa kuukuu zilizopondwa pondwa.
Mzee alimuona huyo Dada kichaa ila hakuonekana kumjali sana,
"shikamoo babu" Dada kichaa alimsalimia yule Mzee,
"marahaba, naona umerudi tena" Mzee aliongea huku akiendelea na shughuli yake,
"ndio, nimerudi kwa sababu sijafanikisha tatizo langu" Dada kichaa alijibu,
"kwanini? Mbona nilikuelekeza vizuri tu" Mzee aliuliza,
"mkuu wa wilaya amekufa, sasa huwezi kunisaidia wewe?" Dada kichaa aliuliza,
"kama nilivyokueleza ulivyokuja mwanzo, mimi ni mwenyekiti wa mtaa tu, sina nguvu ya kusikiliza shauri lako, ndio maana nikakwambia uende kwa mkuu wa wilaya" Mzee alizungumza kwa upole,
"mkuu wa wilaya amekufa sasa, na nikisema nisubiri mpaka achaguliwe mwingine nitakuwa napoteza muda, nina haraka sana" Dada kichaa aliongea,
"kama una haraka basi unaweza kwenda kwa mkuu wa mkoa, alafu yeye anaweza kukusaidia au akakuonesha mahali ambapo utasaidiwa" Mzee aliongea huku akimbinya mende mdogo aliyetoka kwenye radio yake,
"sawa, nashukuru kwa maelezo yako" Dada kichaa aliongea,
"haya mama, ukikwama tena urudi unione" Mzee aliongea huku akitabasamu,
"sawa babu, umeshakunywa chai?" Dada kichaa aliuliza,
"bado mama" Mzee alijibu kisha Dada kichaa akaingiza mkono ndani ya sidiria na kutoa noti mpya mpya zilizonyooka,
"hii utakunywa chai, na hii utanunua betri za radio yako" Dada kichaa aliongea huku akiweka noti mbili juu ya meza,
"alafu mkono wako mmoja ambao haupo, ulikatwa au ulizaliwa hivyo?" Mzee aliuliza huku akichukua zile hela juu ya meza,
"mamba, mkono uliliwa na mamba baada ya mimi kuangukia mtoni" Dada kichaa alijibu,
"pole sana" Mzee aliongea kwa huruma,
"asante, sasa mimi acha niondoke nikashughulikie suala langu" Dada kichaa aliongea huku akigeuka,
"sawa mama, mafanikio mema" Mzee aliongea na kisha yule Dada kichaa akaanza kuondoka kwa mwendo wake wa taratibu na kupotelea mtaani.
Huku mzee alibaki huku akitabasamu mara baada ya kuziokota zile noti mbili zilizoachwa juu ya meza na yule dada.
**********
Ndani ya selo ya polisi, watu mbalimbali, kila mmoja ana kesi yake iliyopelekea yeye kuwepo Ndani ya chumba hicho kisichofaa.
Jirani ya mlango wa chumba hicho alikuwepo kijana mkarimu ambaye ilikuwa ni saa la pili tangu aingizwe kwenye chumba hicho. Alionekana akiwa na mawazo mengi, kilichokuwa kinamtatiza sio yeye kuwepo ndani ya chumba hicho, kitu kilichokuwa kinamuumiza kichwa ni swali moja tu, kwanini yule Dada kichaa anaua watu hovyo?
Kijana mkarimu akiwa amekaa chini pembeni ya mlango, alishuhudia mlango ukifunguliwa, kisha akaingia askari mmoja, akapepesa macho kwa sekunde kadhaa,
"we mheshimiwa, nifuate" Askari aliongea huku akimuoneshea kidole kijana mkarimu.
Kijana mkarimu akainuka kwa haraka na kumfuata yule askari, safari yao iliishia kwenye ofisi ya mkuu wa kituo, wakaingia ndani kisha yule askari akatoka nje,
"kaa hapo" Mkuu wa kituo aliongea bila kumuangalia usoni, kijana akakaa kwenye kiti huku akionekana hana wasiwasi,
"unajua nini kuhusu tukio la kifo cha mfanyakazi mwenzio?" Mkuu wa kituo aliuliza huku akimtazama,
"sijui kitu" Kijana mkarimu alijibu,
"unaitwa nani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"Thomas Anthony" Kijana mkarimu alijibu,
"sasa bwana Tom, umesema hujui kitu chochote kuhusu kifo cha mfanyakazi mwenzio, ila askari waliokukamata wanadai unamjua muuaji, ni kweli?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"maelezo yangu ni yale yale kama ya hawali kwenye kifo cha Mkuu wa wilaya, kuwa yale maneno yaliyokutwa kwenye ukuta wa nyumba ya mfanyakazi mwenzangu, ni maneno aliyoongea jana yule Dada kichaa" Tom alijibu,
"ujue mwili wa mfanyakazi mwenzio tumeukuta na alama za vidole shingoni kama alama zile alizokutwa nazo Mkuu wa wilaya, tena zinafanana, kwa kuwa alama zako tunazo na za Dada kichaa zipo, tumezijaribu kufananisha na hazionekani kufanana, sasa kwanini tuendelee kumng'ang'ania Dada kichaa wakati alama hazifanani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"bado mimi naimani kuwa anahusika na hivi vifo au anamjua muhusika, au anajua sababu ya vifo hivi" Tom alijibu,
"kwa hiyo wewe kama raia mwema, unatushauri nini sisi polisi?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"sioni haja ya nyie kumkamata huyu mtu, mimi naona ni bora mumfuatilie kimya kimya bila yeye kujua, tena mumfuatilie kwa siku nyingi ili mjue ni kipi anakifamya katika mji huu" Tom aliongea na kumfanya Mkuu wa kituo afikirie kwa Muda kidogo, kisha akachukua simu yake na kupiga, kisha akakata, baada ya Muda wakaingia askari watatu,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"jana nadhani tulikuwa wote wakati tukifuatilia vipimo vya vidole vya yule Dada kichaa, kwa hiyo sasa ingieni mtaaani na mumtafute yule Dada kichaa, mkimuona msimkamate, fuatilieni nyendo zake" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa mkuu" Askari walijibu kwa pamoja,
"msitumie gari yenye namba za polisi, tumieni gari ya kawaida tu, alafu mkimuona mnitaharifu" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa" Askari walijibu,
"mchukueni huyu mumrudishe selo" Mkuu wa kituo aliongea na kumfanya Tom ashangae,
"si niruhusu nifuatane nao?" Tom aliuliza,
"rudi ndani, hiyo kazi itafanywa na polisi" Mkuu wa kituo aliongea,
"sasa nitakaa ndani mpaka lini?" Tom aliuliza,
"usijali, utaachiwa tu" Mkuu wa kituo aliongea wakati askari mmoja akimuinua Tom aliyekuwa amekaa.
************
Askari waliingia mtaani na kuanza kumtafuta kimya kimya Dada kichaa, hawakupata kazi sana, walielekea eneo la sokoni walipomkuta siku iliyopita na kuegesha gari yao, ilichukua saa moja tu ndipo walipomuona yule Dada kichaa akikatiza eneo Hilo, wakaanza kumfuatilia, wakachukua simu na kumtaharifu Mkuu wa kituo.
Askari wakiwa ndani ya gari waliendelea kumfuatilia yule Dada kichaa, wakamshuhudia akiingia kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa. Polisi wakatoa simu na kumjulisha mkuu wao.
Mkuu wa kituo akaamrisha Tom apelekwe eneo hilo ili aonane na huyo Dada kichaa na waone kama anaweza kuongea nae kitu chochote kuhusu tukio la yule msichana kufa.
Dada kichaa alitembea mpaka eneo la mapokezi na kuomba kuonana na mkuu wa mkoa, ilikuwa ngumu kukubaliwa kutokana na muonekano wake, ila bahati nzuri wakati Dada kichaa akiendelea kuomba, mkuu wa mkoa nae alikuwa akitoka,
"afadhali mkuu umetoka, huyu Dada anataka kuonana na wewe" Binti wa mapokezi aliongea na kumfanya mkuu wa mkoa asimame,
"una shida gani?" Mkuu wa mkoa aliuliza huku akimtazama Dada kichaa,
"ni vyema tungeongelea ofisini, hapa sio sehemu nzuri ya kuongea shida yangu" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"sema tu ni shida gani, maana natakiwa nikale muda huu" Mkuu wa mkoa aliongea,
"sawa basi, kwa kuwa nina shida acha tu niongee, Kuna mikataba hii naomba unisaidie kupata haki yangu" Dada kichaa aliongea huku akijitahidi kutoa karatasi moja iliyokuwepo kwenye mfuko wa Rambo na kumpa mkuu wa mkoa, mkuu wa mkoa akasoma kwa muda kisha akamtazama usoni,
"sasa mbona hii mikataba haifanani na wewe? na kipindi hicho unafanya mikataba na Tammy Semmy wewe ulikuwa na wadhifa gani?" Mkuu wa mkoa aliuliza,
"nilikuwa mlinzi binafsi wa Tammy Semmy" Dada kichaa alijibu,
"basi ni hivi, Tammy Semmy alikuwa ni muuaji, na watu wake wote wa karibu walifungwa na wengine walikufa, sasa mimi nakushauri bora uachane na hayo madai" Mkuu wa mkoa aliongea,
"kwa hiyo niiache haki yangu ipotee?" Dada kichaa aliuliza,
"kwanza kwa namna unavyoonekana, hakuna mtu wa kuweza kukubali kukusikiliza, na ukiendelea kufuatilia hili jambo, utaishia pabaya" Mkuu wa mkoa aliongea,
"pabaya? Haki yangu inipelekee pabaya? Itakuwa hujui nini maana ya neno haki na ndio maana unasema hivyo" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"haya ondoka eneo hili haraka kabla sijabadilika, nenda kwa wanaojua haki" Mkuu wa mkoa aliongea kwa hasira huku akiitupa chini karatasi aliyopewa na yule Dada kichaa, Dada kichaa akatabasamu na kuiokota,
"mimi nadhani watu kama nyinyi hamkustahili kupewa madaraka, kwa sababu hamsikilizi shida za watu" Dada kichaa aliongea huku akiirudisha karatasi yake kwenye mfuko wa Rambo,
"walinzi mpo wapi? Njooni mumtoe chizi huyu" Mkuu wa mkoa aliongea kwa sauti kubwa huku akiangaza angaza kuangalia walinzi,
"hata chizi anastahili haki" Dada kichaa aliongea na kuanza kuondoka taratibu kuelekea nje, alipofika mlangoni alikutana na yule kijana mkarimu akiingia, wote wakasimama, wakatazamana kwa muda huku Tom akionekana anataka kuuliza swali ila anashindwa, anapata uoga,
"kama unaenda kuonana na mkuu wa mkoa, mkumbushe kuwa hata chizi ana haki" Dada kichaa aliongea na kutabasamu, kisha akaondoka na kumuacha Tom akishangaa tu bila kuongea kitu.
Tom akaomba kurudishwa ofisini kwa mkuu wa kituo, askari aliyemleta akafanya ambavyo Tom alitaka.
Walipofika kituoni, Tom akaelekea moja kwa moja kwa mkuu wa polisi,
"nasikia umeshindwa kuongea nae" Mkuu wa kituo aliuliza,
"kweli, ila Kuna neno ameongea, nahisi mkuu wa mkoa yupo hatarini" Tom aliongea kwa wasiwasi,
"neno gani?" Mkuu wa kituo akauliza,
"aliniambia nimkumbushe mkuu wa mkoa kuwa, hata chizi ana haki" Tom aliongea,
"sasa Hilo neno ndio linakutia hofu, mbona halina shida?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"tatizo lipo, haya maneno ya mwisho ambayo ananiambiaga mimi, ndio uwa yanakutwa katika maiti ya watu walioongea maneno hayo, mimi nadhani mkuu wa mkoa anatakiwa alindwe leo" Tom aliongea,
"kweli, ila sasa njia nzuri ya kumlinda ni kutompa taharifa wala nyumbani kwake kusijazwe polisi" Mkuu wa kituo aliongea,
"camera zinatakiwa ziwekwe kila eneo la nje" Tom aliongea.
*******
Mishale ya saa mbili usiku mkuu wa polisi, Tom na Askari wengine, walikuwa wapo kwenye ofisi ya mkuu wa kituo wakitazama runinga ambayo iliunganishwa moja kwa moja na camera iliyofungwa ndani ya eneo la ndani la nyumba ya mkuu wa mkoa, na pia kulikuwa na polisi wengi tu walikuwa wamemwagwa maeneo ya jirani na nyumba ya mkuu wa mkoa.
Mkuu wa kituo na wenzake waliendelea kuangalia tu huku masaa yakikatika bila kuona kitu.
Masaa yakazidi kuyoyoma tu, usiku mzima ukapita, na hatimaye saa mbili asubuhi iliwakuta wakiwa bado wanatazama runinga yao ambayo haikuonesha mtu wala kiumbe chochote kikiingia kwenye nyumba ya mkuu wa mkoa.
"Tom umefanya tumekesha bure" Mkuu wa kituo aliongea huku akisimama,
"nisameheni sana, ila mjakesha bure, si mlikuwa mnaimarisha ulinzi?" Tom aliongea kwa sauti ndogo, na wakati huo huo simu ya mkuu wa kituo iliita, akapokea, aliongea kidogo tu na kukata simu, sura yake ilibadilika kabisa,
"vipi mkuu?" Askari mmoja aliuliza,
"Mkuu wa mkoa ameuawa nyumbani kwake" Mkuu wa kituo aliongea na kufanya watu wote hapo washangae huku wakiendelea kutazama runinga yao ambayo bado haikuonesha mtu wala kitu chochote kinachoingia wala kutoka katika nyumba ya mkuu wa mkoa, yaani hakuna walichoona zaidi ya mazingira tu ya nyumba ya mkuu wa mkoa.......
Watu wote waliokuwa katika ofisi Ile ya mkuu wa kituo walipigwa na butwaa, hakuna aliyeamini kauli Ile ya mkuu wa kituo wakati wote walikesha pale wakitazama Ile camera iliyofungwa kwa mkuu wa mkoa na ikaunganishwa moja kwa moja kwa mkuu wa kituo,
"aliyekupigia simu anamjua mkuu wa mkoa au anaongea tu bila kujua kitu? Au ndio muuaji tunayemtafuta anajaribu kukuchezea akili?" Askari alimuuliza mkuu wake maswali mfululizo na kumfanya mkuu wake amtupie jicho kali,
"aliyenipigia hii simu ni polisi ninayemuamini kuliko nyie wote hapa" Mkuu wa kituo alijibu huku akionekana kutopendezwa na maswali ya askari wake,
"basi twendeni kwa mkuu wa mkoa ili tukajionee wenyewe, ila kama kweli ameuawa itakuwa ni tukio la ajabu sana kwangu, yaani huyo muuaji atakuwa sio mtu wa kawaida, apite katika camera na tushindwe kumuona?" Tom aliuliza huku akitoa mguno wa mshangao,
"wote twendeni ili tukaone hayo maajabu" Mkuu wa kituo aliongea huku akiinuka katika kiti, na Askari wengine pamoja na Tom wakainuka na kumfuata mkuu wa kituo ambaye aliingia katika gari ya polisi na kisha wale Askari wengine nao wakaingia, Tom pia akaingia, kisha Ile gari ya polisi ikaondoka.
Gari ya polisi ilishika njia inayoelekea kwa mkuu wa mkoa, njia nzima hakuna aliyekuwa akiongea kitu, sio mkuu wa kituo, sio Askari wake, na wala sio Tom aliyediriki kunyanyua mdomo wake, wote walikuwa kimya na kila mmoja akiwaza jambo lake.
Ndani ya dakika tano tu, gari ya polisi ilikuwa inasimama mbele ya geti la nyumba ya mkuu wa mkoa, akatelemka mkuu wa kituo na vijana wake, moja kwa moja wakapitiliza sebuleni katika nyumba ya mkuu wa mkoa. Hapo sebuleni waliweza kuwakuta Askari kadhaa wakiwa pembeni ya mwili wa mkuu wa mkoa uliokuwa umelazwa sakafuni, huku mikono yake ikiwa imetandazwa kama mtu aliyelala msalabani, na katika viganja vya mikono ya mwili wa mkuu wa mkoa, vilikuwa vimepigiliwa misumari mikubwa iliyozama ardhini, na tumbo la mwili wa mkuu wa mkoa lilikuwa limepasuliwa na karibia viungo vyote vinavyopatikana ndani katika mwili wa binadamu, vilikuwa vimewekwa Juu ya meza. Tom alikuwa amejishika mdomo na kiganja, alikuwa akijizuia kutapika kutokana na vitu alivyoviona, wakati Tom akiwa katika Hali hiyo, kwa upande wa mkuu wa kituo na Askari wengine wao walikuwa makini kuutazama mwili ule wa mkuu wa mkoa.
"familia ya marehemu ipo wapi?" Mkuu wa kituo alimuuliza Askari waliyemkuta pale,
"wamepelekwa hospital, kwa maana wote walikuwa wamepoteza fahamu" Askari alimjibu mkuu wake,
"wapo wangapi?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"mke wake, watoto wawili na binti mmoja, nadhani ni msichana wa kazi" Askari alijibu,
"shabaaash, sijasema utaje wasifu wao, nimeuliza wapo wangapi?" Mkuu wa kituo aliuliza kwa hasira huku akimtazama yule askari,
"wapo wanne mkuu" Askari alijibu,
"wamepelekwa hospital gani?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hospital ya wilaya" Askari alijibu,
"sawa, twendeni" Mkuu wa kituo aliongea huku akiondoka na kumfanya Tom na wale Askari aliokuja nao wote waondoke.
Walitoka pale sebuleni na kutembea kuelekea nje, ila mkuu wa kituo akasimama ghafla na kutazama Juu katika ukuta,
"Ile camera tuliyoiunganisha na runinga ya ofisini si tuliificha kwa pale?" Mkuu wa kituo aliuliza huku akiwa bado anaangalia pale Juu ya ukuta,
"ndio mkuu" Askari mmoja alijibu kikakamavu,
"ebu panda na uangalie kama ipo sawa" Mkuu wa kituo alimpa amri, kisha yule Askari akarukia Juu ya ukuta na kuitazama Ile camera kwa muda, akagundua kitu, akatabasamu be kufanya wenzake wamtumbulie macho,
"nini wewe unacheka cheka kama binti?" Mkuu wa kituo alihoji,
'"camera haipo sawa mkuu" Askari alijibu,
"ina nini?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"njoo uone" Askari alimwambia mkuu wake,
"ebu tafuteni ngazi" Mkuu wa kituo aliongea na kufanya Askari waanze kuzunguka katika ile nyumba wakitafuta ngazi, baada ya muda waliipata, wakaiweka ukutani usawa wa Ile camera, mkuu wa kituo akapanda Ile ngazi mpaka juu, akafanikiwa kuiona camera, akapigwa na butwaa, maana katika ile camera kwa mbele ilizibwa na kikaratasi kidogo cheupe, mkuu wa kituo akakibandua kile kikaratasi na kukigeuza, akagundua kuwa kile kikaratasi ni picha, ni to ndogo ambayo ilikuwa ikionesha mazingira ya nyumba ya mkuu wa mkoa, mkuu wa kituo akatikisa kichwa kwa masikitiko,
"genius killer, inawezekana tumemtega nguruwe kwa mtego wa panya" Mkuu wa kituo aliongea kwa sauti ndogo,
"kweli mkuu, huyu muuaji ana uwezo mkubwa sana" Askari aliyekuwa juu na mkuu wa kituo alionekana kumuunga mkono mkuu wake.
Mkuu wa kituo akatelemka kutoka juu, hakuongea kitu chochote, akaelekea moja kwa moja katika gari waliyokuja nayo,
"twende hospital ya wilaya" Mkuu wa kituo aliongea na kisha dereva akawasha gari na kushika barabara inayoelekea uko hospital.
"kwenye camera kulikuwa na nini?" Tom alimuuliza mkuu wa kituo,
"ilibandikwa picha mbele ya camera, kwa hiyo usiku kucha tumekesha tukiangalia picha tu" Mkuu wa kituo alijibu katika sauti ya kuchoka,
"ila hujawauliza Askari walikuwa wanaimarisha ulinzi katika nyumba ya mkuu wa mkoa, hujawauliza kama hawajaona chochote usiku" Tom aliongea,
"hiyo ni kesi yao, lazima waandike maelezo na wanikabidhi kuhusu hili tukio" Mkuu wa kituo aliongea,
"huenda walizidiwa akili" Tom aliongea,
"sio huenda walizidiwa, ila ni ukweli tumezidiwa akili" Mkuu wa kituo aliongea wakati gari ikiegeshwa katika eneo la wazi la hospital ya wilaya.
Mkuu wa kituo pamoja na Askari wake wakatelemka na kuingia moja kwa moja mpaka ndani ya hospitali, kwa bahati nzuri walikutana na Dokta mkuu wa hiyo hospital, huyo Dokta anafahamiana na mkuu wa kituo, wakasalimiana kwa uchangamfu,
"kilichonileta hapa ni kujua hali ya mke wa mkuu wa mkoa" Mkuu wa kituo aliongea,
"yupo vizuri sasa hivi, hata fahamu zimemrejea" Dokta mkuu aliongea na kumfanya mkuu wa kituo ashukuru Mungu,
"mmegundua ni kipi kilichosababisha wapoteze fahamu?" Mkuu wa kituo alimuuliza Dokta,
"kwa uchunguzi wa hawali, tulichogundua ni kuwa walivuta hewa ambayo inafanya ubongo uwe mzito na ushindwe kufanya kazi vizuri, hali hiyo hupelekea kupoteza fahamu kwa muda, ila haina mengine kwa baadae, hukaa mwilini muda mchache tu, baada ya mtu akishapata fahamu, basi ujue na yenyewe ndio imeisha mwilini" Dokta alimuelezea mkuu wa kituo,
"sawa sawa, je watoto nao wamepata fahamu?" Mkuu wa kituo alihoji,
"ndio, nao wameshazinduka, ila bado hatujawakutanisha na mama yao" Dokta aliongea,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"je, mmemwambia mke wa mheshimiwa kuwa mheshimiwa amekufa?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hapana, kutokana na mazingira ya kifo chake, nadhani kutoa taarifa za kifo chake, sio kazi yetu" Dokta alijibu huku akitabasamu,
"sawa, tupeleke katika wodi aliyolazwa mke wa mheshimiwa" Mkuu wa kituo aliongea na kisha Dokta akaongoza njia kuwapeleka katika wodi aliyolazwa mke wa mkuu wa mkoa, walipofika wote waliingia pamoja na Tom na kumkuta mke wa mkuu wa mkoa akiwa amekaa kitandani huku akilia, wakamsalimia,
"mama, nieleze kidogo tu, ni nini kilitokea jana usiku?!" Mkuu wa kituo aliuliza,
"wanangu wapo wapi?" Mke wa mkuu wa mkoa aliuliza huku akifuta machozi,
"wapo wote, ni channel wazima wa afya" Dokta alijibu huku akilazimisha tabasamu,
"mume wangu yupo wapi?" Mke wa mkuu wa mkoa aliendelea kuuliza, ila hilo swali lilikuwa gumu kidogo kwa Dokta, ukimya ukatawala, hiyo hali ikamfanya mke wa mkuu wa mkoa aanze kulia,
"yupo, ila amelazwa, hali yake bado haijaimalika vyema" Mkuu wa kituo alijibu na kumfanya mke wa mkuu wa mkoa ashushe presha kidogo,
"lakini ana fahamu?" mke wa mkuu wa mkoa aliuliza,
"yupo sawa tu, alitaka kuja kukuona, ila madaktari wakamtaka apumzike kidogo" Askari aliyekuwa nyuma ya mkuu wa kituo alijibu,
"mama samahani, unaweza kutueleza ni kitu gani kilitokea usiku uliopita?" Mkuu wa kituo aliuliza kwa upole,
"ndio nakumbuka, ila kidogo sana" Mke wa mkuu wa mkoa alijibu na kumfanya mkuu wa kituo asimame vizuri,
"tueleze hicho unachokikumbuka" Mkuu wa kituo aliongea,
"ni ilikuwa usiku, sikujua ni wa saa ngapi, ila nilishtuka usingizini na kumuona mtu akiwa amesimama upande watu wa miguu kitandani, kisha akamuamuru mme wangu asimame na amfuate, mimi nikamuuliza mume wangu huyo mtu ni nani? ikaonekana hata yeye hamjui, nikaanza kupiga kelele, akatoa kitu kama kopo la body spray na kunipulizia puani, nguvu zikaniishia na kupoteza fahamu, sijajua kilichoendelea tena" Mke wa mkuu wa mkoa alieleza,
"huyo mtu uliyemuona alikuwa ni mwanamke au mwanaume?" Tom aliuliza na kumfanya mkuu wa kituo amtupie jicho kali,
"nadhani ni mwanamke, kwa maana alivaa suruali iliyomshika mwili vizuri vizuri na kufanya umbo lake lionekane vyema, lilikuwa ni umbo la kike, sijamuona vizuri kwa sababu ya taa ya chumbani, chumbani uwa tunaweka taa ya rangi yenye mwanga hafifu" Mke wa mkuu wa mkoa alijibu,
"alikuwa na mkono mmoja au yote?" Tom alikurupuka na kuuliza tena,
"asante mama, sisi tunaenda ila tukiwa na swali jingine, hatutasita kukufuata" Mkuu wa kituo aliongea, hakutaka swali la Tom lijibiwe. Mkuu wa kituo alitoka nje huku Askari wengine pamoja na Tom wakimfuata, wakaingia katika gari na kuondoka.
"sasa mbona mkuu hukutaka yule mama ajibu swali langu?" Tom alimuuliza mkuu wa kituo,
"wewe pale uliuliza kama nani? wewe sio polisi wala huna uzoefu wowote wa kufuatilia kesi, alafu unauliza maswali ya kijinga" Mkuu wa kituo aliuliza kwa hasira, hapo Tom akanywea, ni kweli yeye hakustahili kuuliza, ila maswali yale yale ya Tom yalimpa mwanga mkuu wa kituo, alipata mwanga baada ya mke wa mkuu wa mkoa kujibu kuwa mtu aliyewavamia usiku ni mwanamke.
"na nyie wengine, mtafuteni yule dada kichaa na mumpeleke selo" Mkuu wa kituo aliongea,
"umeanza kuamini maneno yangu? yule Dada kichaa ndio mtuhumiwa" Tom aliongea,
"simamisha gari" Mkuu wa kituo alimuamrisha dereva, dereva akatii, gari ikasimama,
"Tom shuka, nitakutafuta nikikuhitaji" Mkuu wa kituo aliongea kwa hasira, kisha Tom akashuka.
Kiukweli mkuu wa kituo hakupenda kwa namna Tom ansvyotaka kuwafundisha kazi.
Tom alivyoshuka alitabasamu huku akiliangalia gari ya polisi ikiondoka, aliona amewaweza.
Mkuu wa kituo baada ya kurudishwa ofisini kwake, vijana wake waliingia mtaani kumtafuta yule Dada kichaa, kwa bahati nzuri walimpata, kwa maana walijua anapopatikana. Walivyomkamata moja kwa moja wakampeleka selo, ingawa haikuwa kazi rahisi, ila walifanikisha.
*********
_________________
BAADA YA WIKI.
_________________
ikiwa tayari mkuu wa mkoa akiwa amezikwa siku kadhaa nyuma, siku huyo mkuu wa kituo aliwatuma polisi kumuita mke wa mkuu wa mkoa.
Baada ya nusu saa, polisi walirudi wakiwa na mke wa mkuu wa mkoa. Mke wa mkuu wa mkoa alipofika alisalimiana na mkuu wa kituo, kisha akakaa katika kiti,
"nimeitikia wito" Mke wa mkuu wa mkoa aliongea mara baada ya kukaa,
"Kuna mwanamke tumemkamata, tunahisi anaweza kuwa muhusika wa hili tukio la kifo cha mkuu wa mkoa" Mkuu wa kituo aliongea na kumfanya yule mama mke wa mkuu wa mkoa ashtuke kidogo,
"aisee, nitashukuru sana kama mtakuwa mmepiga hatua kubwa sana" Mke wa mkuu wa mkoa aliongea huku akijifuta machozi kwa kukumbushwa kifo cha mme wake,
"basi ngoja tumlete huyo mwanamke ili uweze kumuona, alafu utaangalia kama anaendana na yule uliyemuona" Mkuu wa kituo aliongea na kuwaamuru vijana wake wamlete yule dada kichaa, wale Askari wakatoka kwenda kumchukua yule Dada kichaa.
Baada ya dakika tano, mlango wa ofisi wa mkuu wa kituo ulifunguliwa, wakaingia Askari wakiwa wameongozana na yule Dada kichaa, Mkuu wa kituo akamuamuru yule Dada kichaa asimame mbele ya mke wa mkuu wa mkoa, Dada kichaa akasimama,
"mama, huyu ndiye dada tunayemtuhumu kamuua mme wako, ebu muangalie kama anafanana na yule uliyemuona ule usiku" Mkuu wa kituo alimwambia mke wa mkuu wa mkoa, kisha yule mama akageuka na kumtupia jicho kwa dakika nzima, ghafla akshtuka baada ya kumuangalia vizuri, Kuna kitu aligundua.....
Kisha mke wa mkuu wa mkoa akamgeukia mkuu wa kituo,
"huyu Dada ni mzima?" Mke wa mkuu wa mkoa aliuliza,
"hapana, nadhani ana matatizo ya akili" Mkuu wa kituo alijibu,
"kwa hiyo nyie mkaona mtu wa namna hii ni wa kumuhusisha na mauaji, hii sio sawa, huu ni udhalilishaji mkubwa" Mke wa mkuu wa mkoa aliongea kwa masikitiko,
"hapo mama unaingilia kazi za kipolisi, sisi uwa tunamchunguza mtu yoyote bila kuangalia ana tofauti ipi?" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa, endeleeni na uchunguzi wenu" Mke wa mkuu wa mkoa aliongea na kutoka zake nje,
"muachieni huyo dada aondoke" Mkuu wa kituo alimwambia vijana wake na kumuachia yule Dada kichaa aondoke zake, akaondoka huku akitabasamu.
Dada kichaa alitembea mpaka chini ya jengo na kumpita mke wa mkuu wa mkoa, kisha ghafla yule Dada kichaa akasimama na kumgeukia mke wa mkuu wa mkoa,
"samahani mama, ni wapi ilipo wizara ya katiba na sheria?" Dada kichaa aliuliza, ila yule mama alimuangalia tu huku akipata kigugumizi kumjibu,
"nisaidie tafadhali" Dada kichaa aliongea kwa upole,
"zipo mbali na hapa, sidhani kama utaweza kufika" Mke wa mkuu wa mkoa alijibu,
"nitafika tu kwa maana nina shida na hapo itakuwa ni sehemu muhimu kwangu" Dada kichaa aliongea kisha mke wa mkuu wa mkoa alimuelekeza,
"nashukuru mama, Mungu akubariki" Dada kichaa aliongea na kugeuka, kisha akaanza kuondoka taratibu huku mke wa mkuu wa mkoa akimuangalia.
****************
Mkuu wa kituo alibaki ndani ya ofisi peke yake, alikuwa na mawazo mengi sana, kilichokuwa kikimuumiza kichwa ni vifo vya viongozi wa mkoa.
Akachukua laptop yake na kuangalia video waliyorekodi usiku kupitia camera waliyoitega kwenye nyumba ya mkuu wa mkoa. Aliiangalia kwa muda mrefu tu huku akitafakari ni muda gani picha iliwekwa mbele ya camera.
Mkuu wa kituo akachukua simu na kupiga, aliwapigia Askari wa ubaoni (kaunta), na aliwaagiza wamlete Tom, kisha mkuu wa kituo akakata simu.
Baada ya dakika Tatu mlango wa ofisi ulifunguliwa na Tom akaingia huku nyuma kukiwa na Askari,
"ebu toka nje, niache na huyu" Mkuu wa kituo alimwambia yule Askari aliyemleta Tom, kisha yule Askari atatoka nje na kuwaacha watu wawili tu ofisini,
"pale kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kazi yako ilikuwa ni ipi haswa?" Mkuu wa kituo alimuuliza Tom,
"kazi yangu ilikuwa ni kusikiliza matatizo ya wananchi kipindi mkuu wa wilaya anapokuwa hayupo, na kama yupo kazi yangu ilikuwa ni kuakikisha watu wote wanapata nafasi ya kuweza kueleza matatizo yao kwa mkuu, mimi nilikuwa nasimamia foleni" Tom alijibu,
"na elimu yako ni ya ngazi ipi?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"nimesoma na kuhitimu chuo cha Mtakatifu Augustino, tawi la mwanza, na nimesomea mambo ya habari" Tom alijibu,
"sasa kama umesomea mambo ya habari, imekuaje unafanya kazi tofauti na ulichosemea?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"huku nililetwa tu na viongozi wa serikali, nililetwa baada ya kufanikisha kutoa siri za hayati Tammy Semmy, rais aliyeuawa wakati akikimbia nchi" Tom alijibu na kumfanya mkuu wa kituo ashtuke,
'"Wewe ni usalama wa taifa?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hapana, mimi ni muandishi wa habari" Tom alitoa jibu lakini mkuu wa kituo hakutaka kuliamini, tayari akili yake ilishamwambia kuwa Tom ni usalama wa Taifa,
"basi mimi nakuachia huru, ila ninachokuomba ni uondoke ndani ya wilaya hii" Mkuu wa kituo aliongea kwa utulivu,
"sasa mkuu nitaondokaje wakati wilaya hii ni kituo changu cha kazi?" Tom aliuliza,
"fanya mpango uhame, kwa maana wewe kuwa hapa, utaendelea kuhesabika kama mtuhumiwa wa haya matukio ya mauaji" Mkuu wa kituo aliongea,
"lakini mtuhumiwa si anatakiwa awe yule Dada kichaa?" Tom aliuliza,
"kwa ushahidi upi?" Mkuu wa kituo alihoji.
"sasa na mimi natuhumiwa kwa ushahidi upi?" Tom Aliuliza,.
"ushahidi unaoweza kukuweka hatiani ni wewe kutuambia ujumbe ambao tumeukuta kwenye nyumba ya mkuu wa mkoa" Mkuu wa kituo aliongea,
"lakini siku Ile mkuu wa mkoa anauawa si tulikesha wote hapa?" Tom aliuliza,
"kukesha wote sio tatizo, ila tatizo ni wewe kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na muuaji, alafu unamsingizia yule Dada mwendawazimu" Mkuu wa kituo aliongea,
"mna uhakika gani kama yule ni mwendawazimu? mmeshawahi kumpima akili?" Tom aliuliza,
"tumpime vipi wakati muonekano wake tayari umeshasadifu akili zake" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa, kama mtu anapimwa kwa muonekano tu" Tom aliongea huku akitabasamu,
"haya sasa unaweza kuondoka, ninakupa wiki moja ya kuwa ndani ya wilaya hii" Mkuu wa kituo aliongea,
"yule Dada kichaa mara ya mwisho kumuona ni lini?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"ametoka hapa muda si mrefu" Mkuu wa kituo aliongea,
"naomba unipe nafasi ili nimfuatilie" Tom aliongea,
"nafasi gani unayoitaka? unataka kuwa polisi?" Mkuu wa kituo aliuliza,
"hapana, nadhani kwa kazi yangu ya uandishi wa habari niliyoisomea, naweza kudadisi mambo vizuri tu, kwa hiyo basi nipe nafasi ili nimfuatilie yule Dada kichaa kwa ukaribu zaidi" Tom aliongea,
"hiyo kazi siwezi kukupa, ila unaweza kufanya kama msamalia mwema tu" Mkuu wa kituo aliongea,
"sawa, naomba niondoke" Tom aliongea huku akisimama,
"ruksa, nenda tu" Mkuu wa kituo aliongea huku akiitoa miwani yake na kuipachika machoni,
Tom akageuka na kuanza kuondoka,
"kumbuka kuwa una wiki moja tu ya kukaa hapa wilayani, zaidi ya hapo nitatuma Askari wakukamate" Mkuu wa kituo aliongea na kumfanya Tom asimame kwa muda, kisha akatoka zake nje.
Tom alivyotoka tu nje ya jengo la polisi, alisimama kwa muda huku akifikiria, baada ya dakika mbili akaanza kupiga hatua za haraka kuelekea kwake.
Ilimchukua dakika ishirini mpaka kufika kwake, akasalimiana na wapangaji wenzake ambao walimpa pole kwa matatizo yaliyomkuta, kisha akaingia chumbani kwake, akaelekea bafuni na kujisafisha mwili, kisha akarudi na kujitupa kitandani.
Akawa anawaza aanzie wapi ili kuupata ukweli juu ya matukio ya mauaji ambaye yeye aliamini kwa asilimia Mia kuwa muhusika wa mauaji yale ni yule Dada kichaa.
Tom akainuka na kuvaa nguo, kisha akachukua begi dogo na kuweka nguo kadhaa. Alipanga ahame kwake kwa muda, na muda huo alikuwa akijiandaa kwenda kwa rafiki yake wa kike anayeishi mkoa huu huu ila wilaya nyingine.
Tom alitoka mpaka kwenye kituo cha basi ndogo ndogo zinazofanya safari za wilaya hadi wilaya, alipofika akaingia kwenye gari moja ambayo halikuwa na abiria wengi, akaenda kukaa siti ya mwisho kabisa upande wa dirishani, akawa anachezea simu yake.
Hazikupita hata dakika tano, akatupa macho dirishani na kumuona yule Dada kichaa, ila safari hii hakuwa na zile nguo zake chafu, alivaa suruali nyeusi iliyomkaa vizuri na pia katika bega lile la mkono mzima alitundika mkoba wake mweusi, Tom akakaza macho zaii kwa maana hakutaka kuamini kwa haraka,
"ndio yeye" Tom aliongea na nafsi yake huku akiendelea kumtazama yule Dada kichaa. Akamshuhudia yule Dada kichaa akiingia katika lile lile gari, Tom akapata uoga, alihisi yule Dada anamfuatilia, Wakati yule Dada akiingia kwenye gari, Tom akainamisha kichwa na kujifanya akichezea simu yake, na muda huo abiria walikuwa wameongezeka ndani ya gari.
Dada yule akakaa siti za mbele karibu na mlango, kisha akatoa kitambaa na kujifuta jasho, harufu ya manukato aliyojipaka yalienea gari yote, kisha akatoa simu janja yake na kuanza kuchezea, ilikuwa simu ya bei ghali sana, Tom bado alikuwa akishangaa huku akiwa bado ahamini,
"nilimwambia yule mkuu wa kituo, huyu demu sio chizi, hawa wanakuwaga usalama wa taifa, au waalifu wa kimataifa" Tom aliendelea kusema ndani ya nafsi yake huku akimtazama yule Dada ambaye alikuwa bize na simu yake.
Na wakati huo gari ilikuwa imeshajaa na dereva alikuwa akiiondoa hapo kituoni. Njia yote Tom hakuwa na amani kabisa, muda mwingi macho yake aliyaweka katika siti aliyokalia yule Dada kichaa, alikuwa makini kwa kila anachokifanya.
Kituo ambacho Tom alitakiwa kushuka kilikuwa ndio kinafuata, ila hakutaka kabisa kushuka kwa kuwa hakutaka yule Dada kichaa ajue. konda akauliza kama kuna mtu wa kushuka kituo kinachokuja, ila watu hawakujibu, konda akauliza tena kwa sauti kubwa zaidi, yule Dada kichaa akasema anashukia hapo.
"huyu ananifuatilia mimi nini?" Tom alijiuliza baada ya kugundua yule Dada kichaa anashukia kituo anachotakiwa kushukia yeye Tom.
Gari ikasimama kituoni na kisha yule Dada kichaa akatelemka, Tom akawa anajishauri ashuke au akashukie kituo kinachofuata? Wakati akijishauri, gari ilianza kuondoka,
"we konda bado nashuka" Tom aliongea kwa sauti huku akisimama na kufanya abiria wengine wamshangae kwa maana gari iliposimama hakushuka,
"braza ulikuwa umesinzia au mgeni wa jiji?" Konda aliuliza huku akigonga bodi ya gari na kufanya gari isimame pembezoni mwa barabara. Tom akashuka na kutupa macho kwenye kituo aliposhukia yule Dada kichaa, akaweza kumuona akiingia mtaani, nae akaanza kumfuatilia kwa mbali.
Kilichomshangaza na kumuogopesha Tom ni namna yule Dada alipokuwa anaelekea, ni kule kule ambapo Tom alikuwa anatakiwa aende.
Yule Dada kichaa aliendelea kusonga tu huku Tom nae akiendelea kumfuata tu, ila kwa mbali Tom alimuona rafiki yake wa kike, ambaye ni mpenzi wake, akiwa nae anakuja upande ambao Tom yupo, Tom akahisi huenda rafiki yake huyo alikuwa akienda kumpokea kwa maana alimpa taarifa juu ya ujio wake, ila pasipo kutegemea, alimshuhudia rafiki yake yule wa kike akisimama na yule Dada kichaa, kisha wakawa wanaongea, na mwisho rafiki wa kike wa Tom aligeuza na kushika njia ya kurudi alipotoka, huku wakiwa wameongozana na yule Dada kichaa, hapo ndipo Tom alichoka zaidi....
Tom alisimama kwa muda huku akijiuliza maswali mengi, mpenzi wake anashirikiana na yule Dada kichaa au kuna nini kinaendelea?
Tom aliendelea kusimama huku akitafakari, na wazo la mwisho aliloliona linafaa ni kurudi alipotoka, hakuwa na imani na mpenzi wake tena. Tom akageuza na kuanza kurudi kwenye kituo cha basi, ila hata kabla hajapiga hatua tano, alisikia sauti kutoka nyuma ikimuita, wala hajaumiza kichwa kuijua sauti hiyo ni ya nani? Ilikuwa ni sauti ya mpenzi wake, Tom akasimama na kugeuka,
"vipi mbona unaelekea uko wakati nyumbani ni huku?" Mpenzi wake Tom aliuliza huku akishangaa,
"nilikuwa narudi kule juu kuchukua vocha" Tom aliongea huku akitabasamu,
"jamani!!!! Mbona hata pale jirani na kwangu kuna maduka tu" Mpenzi wake Tom aliuliza kwa kudeka,
"OK, basi turudi. Kwema lakini?" Tom aliuliza huku akigeuza njia,
"kwema, nilichelewa kuja kukupokea kwa maana nilikutana na Dada mmoja alikuwa akiulizia nyumba ya kulala wageni mtaa huu, ikabidi nikamuoneshe" Mpenzi wa Tom aliongea huku akichukua begi kutoka kwenye mikono ya Tom.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"huku kuna guest kumbe? umempeleka guest gani sasa?" Tom aliuliza huku lengo lake likiwa ni kupafahamu alipofikia yule Dada kichaa,
"we twende tu nitakuonesha, kwa maana tunapita hapo hapo, ndio njia ya kuelekea kwangu" Mpenzi wake Tom alijibu,
"tunapita hapo hapo??? Kwani hakuna njia nyingine?" Tom aliuliza kwa mshangao kwa maana hakutaka kupita ile njia kwa kuhofia kuwa akipita ile njia, huenda yule Dada kichaa anaweza kumuona,
"hee!!! Mwenzangu mbona hivyo!? Kwani hii njia ina nini mpaka uhamaki hivyo? Au una mwanamke mwingine huku?" Mpenzi wa Tom aliuliza kwa hasira huku chembe za wivu zikiuteka moyo wake,
"sijamaanisha hivyo, ujue nimechoka sana, sasa nilitaka kujua kama kuna njia rahisi zaidi ya hiyo ili niwahi kufika nikapumzike" Tom alijitetea kwa njia hiyo ili kumpoza mpenzi wake huyo,
"twende, njia ni hii hii moja, usijifanye hujui mazingira ya huku" Mpenzi wake Tom aliongea huku akiwa ametangulia mbele.
"sawa twende, mimi sitii neno tena" Tom aliongea huku akimfuata kwa nyuma,
Ukimya ukawazingira, njia nzima hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Walitembea katika hali hiyo mpaka walipofika kwenye usawa wa duka moja dogo, mpenzi wake Tom akasimama,
"duka Hilo hapo, si ulikuwa unataka vocha?" Mpenzi wake Tom aliongea huku akimtazama Tom,
"twende bwana, nitarudi baadae kununua, nimechoka sana" Tom aliongea huku akimpita mpenzi wake, hakutaka kusimama,
"khaaa, yaani wewe mwanaume kigeugeu, nilikukuta unarudi barabarani kutafuta vocha, nikakuzuia, sasa tumefika dukani hutaki tena vocha!!" Mpenzi wake Tom aliongea huku akitikisa kichwa,
"na wewe ukishaanzaga kuongea uwa humalizi, nambie umeniandalia chakula gani?" Tom alijaribu kubadili maongezi,
"Wewe twende tu, utachokikuta ndicho utachokula" Mpenzi wake alijibu huku akiwa anasonga mbele,
"alafu, mbona hukunionesha Ile guest uliyosema ipo njia hii?" Tom aliuliza,
"ile pale mbele, Ile yenye rangi ya zambarau" Mpenzi wake alijibu huku akionesha kwa kidole,
"aaha, kuna wateja kweli huku? Maana huku ni uswahilini sana" Tom aliongea,
"wapo wateja wengi tu, wazinifu wenzako ndio wanapapenda huku" Mpenzi wake alijibu,
"basi yaishe, naona hauko sawa" Tom aliamua kutotaka kuuliza maswali kutokana na majibu aliyokuwa akipewa,
"na bora yaishe, maana maswali yako ya kijingajinga, sijui utakuwa lini wewe Thomas?" Mpenzi wake aliongea kwa hasira huku akimtazama Tom aliyekuwa akitabasamu tu.
Ukimya ulitawala mpaka walipofika kwenye chumba ambacho anakaa mpenzi wake, wakaingia na Tom akafikia kitandani na kujilaza,
"nisaidie kuvua viatu basi" Tom aliongea huku akiwa anamuangalia mpenzi wake,
"lazy, yaani hubadiliki tu, kuanzia tabia mpaka matendo" Mpenzi wake aliongea kwa kulalamika,
"basi kama hutaki kunivua viatu, nibandikie maji ya kuoga" Tom aliongea huku akianza kuvua viatu,
"isiwe shida, nabandika tu, jiko lenyewe la gesi, yaani ni chap na kwa haraka" Mpenzi wake aliongea na kuingia jikoni, kisha akachukua sufuria na kuinjika kwenye mtungi wa gesi, kisha akaweka maji ya kutosha.
Muda wote Tom alikuwa akitabasamu tu, alipenda sana namna mpenzi wake anavyoongea, na ndio maana alipenda kumchokoza kila muda ili mradi amsikie tu akiongea.
*********
Ndani ya nyumba ya wageni, Dada kichaa alipoingia tu, kitu cha kwanza alienda mariwatoni, akajiswafi mwili, kisha akarudi na kujifunga shuka. Akakaa kitandani na kuchukua mkoba wake, kisha akatoa laptop ndogo sana, akaiwasha na kupachika moderm pembeni, akaanza kubofya na kisha akapata kitu anachokitaka, ilikuwa ni ramani ya wizara ya katiba na sheria, kisha akasoma pia baadhi ya vipengele kwenye sheria za kimataifa, baada ya hapo akachomoa moderm na kuzima laptop.
Akainuka kwenye kitanda na kutoa kaptula kwenye pochi na kuvaa, akaenda mpaka sehemu ya mapokezi,
"samahani Dada, hapa chakula kinapatikana wapi?" Dada kichaa alimuuliza Dada wa mapokezi,
"chakula gani unachohitaji?" Dada wa mapokezi aliuliza,
"nadhani chipsi inatosha" Dada kichaa alijibu,
"nipe hela, nitamuagiza mtu aniletee, alafu nitakuletea ndani" Dada wa mapokezi aliongea,
"sawa, nitashukuru" Dada kichaa alijibu na kutoa pesa kisha akampatia yule Dada wa mapokezi.
Baada ya hapo, Dada kichaa akarudi ndani kwake na kukaa kitandani, akawa anaandaa mipango yake ya siku inayofuata.
**********
Siku iliyofuata, asubuhi ya saa moja, Dada kichaa alitoka kwenye Ile nyumba ya wageni huku akiwa amevaa baibui yake nyeusi na hijabu pia, na begani alitundika pochi yake.
Alitoka kwa mwendo wa kawaida mpaka kwenye kituo cha daladala na kuingia kwenye daladala moja.
Daladala haikukaa sana kituoni, ikaondoka. Daladala ilivipita vituo viwili, kituo cha Tatu yule Dada akatelemka na kushika njia iliyokuwa inaelekea kwenye jengo refu la ghorofa tano lilikuwa na maandishi makubwa yalioandikwa kwa uzuri kabisa "WIZARA YA SHERIA NA KATIBA".
Dada kichaa akapiga hatua kadhaa mpaka kwenye mlango wa lile jengo na kuingia mpaka eneo la mapokezi na kumkuta mwanaume mmoja aliyekuwa amekaa.
"habari kaka, samahani unaweza kunielekeza ilipo ofisi ya waziri?" Dada kichaa aliuliza,
"ulikuwa na mihadi nae?" Kijana aliuliza,
"hapana, ila nina shida muhimu sana, naomba unisaidie tu" Dada kichaa aliongea kwa upole,
"hapo sina msaada, ungekuwa na mihadi nae ningekusaidia, ila huna mihadi nae, cha kukusaidia ni kukupa barua pepe ya hapa, alafu urudi nyumbani ukaandike maombi ya kuonana na mheshimiwa, alafu kama utakubaliwa, utapangiwa siku ya kuja tena hapa" Kijana aliongea huku akimtazama yule Dada kichaa,
"kaka nisaidie kwa maana nimetoka mbali sana, alafu sina pesa ya kukaa muda mrefu mjini, naomba unisaidie tu ndugu yangu" Dada kichaa aliongea kwa kulalamika,
"Dada nielewe, hii ofisi ina utaratibu wake, fuata maelezo niliyokupa" Kijana aliongea, ila safari hii aliongea kwa hasira baada ya kuona yule Mwanamke anamsumbua,
"kaka hunionei huruma hata ulemavu nilionao?" Dada kichaa aliuliza huku akiutazama mkono wake uliokatika,
"Dada naomba ukae pembeni, kuna watu wengine wanataka kusikilizwa pia" Kaka yule aliongea baada ya kuona watu kadhaa wakiwa wamepanga foleni nyuma ya yule Dada.
Dada kichaa akageuka nyuma na kuona watu kadhaa wakiwa nyuma yake, akasogea pembeni na kuwaacha wasikilizwe, waliposikilizwa wote, Dada kichaa akarudi tena pale kwenye sehemu ya mapokezi,
"kaka hivi nyumbani huna mama? Mbona hunijali mimi mwanamke kama alivyo mama yako?" Dada kichaa aliuliza kwa upole,
"Dada acha usumbufu, kwanza waziri hayupo, yupo ziarani mkoani" Kaka yule alijibu kwa ukali,
"yupo tu, sema unanijibu hivyo kwa kuwa unaona nakusumbua, unataka tu niondoke" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"Ni kweli hayupo, yupo mkoani kwa ziara" Dada mwingine aliyekuwepo mapokezi alimsaidia kuongea yule kaka,
"basi mimi nitasubiri hapa mpaka muda wa kufunga ofisi utapofika" Dada kichaa aliongea na kwenda kukaa kwenye makochi yaliyokuwepo eneo hilo.
Alikaa hapo kwa muda wa nusu saa, kabla yule kijana wa mapokezi hajapokea simu na kuanza kuongea huku akimtazama yule Dada, maongezi hayakuwa marefu sana, kisha yule kijana akakata simu na kumtupia jicho yule Dada,
"nenda ghorofa ya Tatu, ofisi namba 31" Kijana wa mapokezi alimwambia yule Dada kichaa, yule Dada akainuka taratibu na kuelekea kwenye ngazi.
"nani amemuita juu?" Dada aliyepo mapokezi alimuuliza yule kijana,
"naibu waziri, alikuwa anatuona kupitia camera jinsi tunavyobishana nae hapa, amenitaka nimruhusu akaonane nae" Kijana wa mapokezi alijibu.
Dada kichaa alipanda mpaka ghorofa husika, akaelekea kwenye mlango namba 31, ulikuwa na maandishi yaliyosomeka "NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA" , Dada kichaa akatabasamu na kugonga hodi, akaruhusiwa kuingia, alipofungua mlango macho yake yakagongana na mwanamke aliyekuwa amekaa kwenye kiti na mbele yake juu ya meza kulikuwa na kibao kinachomtambulisha kuwa huyo ndiye naibu waziri, hakuwa mtu mzima, ila alikuwa ni mama wa miaka 35-40.
"karibu" Naibu waziri aliongea huku akimuonesha kiti cha kukalia yule Dada kichaa,
"asante" Dada kichaa aliongea na kukaa,
"muda mrefu nimekuona ukiwa mapokezi, una shida gani?" Naibu waziri aliuliza,
"nina shida ya kisheria, nahitaji msaada wenu nyinyi kama serikali" Dada kichaa aliongea na kumtazama naibu waziri,
"shida ipi sasa, ongea maneno yote, usiongee nusunusu" Naibu waziri aliongea huku akiendelea kuandika makaratasi yake yaliyokuwa mezani,
"nina mikataba yangu hapa, ambayo ina makubaliano tuliyofanya na makamo wa rais, ila sasa serikali imenigeuka, haitaki kufuata mkataba unachotaka" Dada kichaa aliongea na kuweka mfuko wake mezani, kipindi hicho naibu waziri alishtuka, akaacha kuandika na kumtupia macho yule Mwanamke,
"ebu nione hiyo mikataba" Naibu waziri aliongea huku akimtazama yule Dada kichaa, Dada kichaa akatoa Ile mikataba kutoka kwenye mfuko na kumpatia naibu waziri, naibu waziri akavaa miwani na kuanza kusoma zile karatasi, alisoma kwa muda kidogo, kisha akamtupia jicho yule Dada,
"sasa mbona ukisema ufuate sheria, wewe ndiye utaingia kwenye matatizo, kwa maana mtu uliyefanya nae mkataba tayari alishakufa na pia alikuwa akitakiwa akamatwe kutokana na mauaji ya rais wa kipindi kile" Naibu waziri aliongea,
"hicho sicho kilichonileta hapa, nadhani umesoma mikataba vizuri, hiyo ndio iliyonileta hapa" Dada kichaa aliongea na kutabasamu,
"sawa ondoka, siwezi kukusaidia" Naibu waziri aliongea kwa hasira,
"kwa hiyo unataka kuniambia kuwa rais amekuweka eneo ambalo hustahili? Kwa maana unashindwaje kunisaidia wakati hayo masuala yanahusu wizara yako?" Dada kichaa aliuliza,
"Binti toka nje, ulikuja kuomba msaada na wala sio kunifundisha kazi" Naibu waziri aliongea kwa jazba,
"sasa nakuomba kitu kimoja, andika barua inayoonesha umekubaliana na hii mikataba na pia utie sahihi chini ya barua" Dada kichaa aliongea na kumtazama naibu waziri,
"hivi una kichaa wewe? Ngoja nikuitie security" Naibu waziri aliongea na kupiga simu kuwaita walinzi wa jengo lile, kisha akashusha simu chini, Dada kichaa alikuwa akimuangalia tu huku akitabasamu,
"kabla security hawajafika, roho yako itakuwa imeshafika mbele ya haki'" Dada kichaa aliongea na kucheka, naibu waziri wala hakushtuka, alijua yule Dada hawezi kuwa na silaha kwa maana mpaka ufike ndani ya jengo lile, ujue umekaguliwa ipaswavyo, na kweli alikuwa sahihi, ila kitu ambacho hakukijua ni kuwa yule Dada kila kitu kwake ni silaha.
Wakati naibu waziri akiwa anamtazama yule Dada, alimuona akivuta karatasi moja kutoka mezani na kuishika, pasipo kutegemea, Dada kichaa aliirusha Ile karatasi kwa ufundi na ikachana kidogo koromeo la naibu waziri, naibu waziri akainuka kwa mshtuko na kujishika shingo, alihisi damu zikimvuja, akaanza kupiga kelele za kuomba msaada, Dada kichaa akainuka kwa kasi akiwa na kalamu mkononi, akapiga hatua za haraka za kwenda mlangoni, alipofika mlangoni akageuka kwa kasi na kuirusha Ile kalamu kumuelekea naibu waziri, Ile kalamu ikapenya moja kwa moja kwenye shingo ya naibu waziri, sauti ikakata, damu ikawa inaruka kama kuku aliyechinjwa, kisha Naibu Waziri akapiga magoti na kuanguka kifudifudi, ulikuwa mwisho wa uhai wa naibu waziri, kisha yule Dada kichaa akachovya damu na kidole na kuandika sakafuni, "KAMA HUJUI KAZI YAKO, HAMNA HAJA YA KUENDELEA KUWEPO HAPA" , kisha akainuka, akachukua karatasi zake za mikataba na kuziweka kwenye pochi, akaanza kupiga hatua kuelekea nje, ila hata kabla hajaufikia mlango, mlango ulifunguliwa kwa fujo na kundi la Askari likaingia, wote walikuwa na silaha mkononi. Askari walipoingia tu, wakatupia macho kwenye mwili wa naibu waziri, kisha wote wakamuangalia yule Dada kichaa,
"ametaka mwenyewe" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu na pia mkono wake aliunyoosha juu, ishara ya kujisalimisha....
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"mfunge pingu" Askari mmoja aliyekuwa na cheo alimuamrisha mwenzake,
"wee, asithubutu mtu kunisogelea, msidhani nilivyoinua mkono juu kujisalimisha basi ndio mnifunge pingu" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"ebu mkamateni bwana, anatupotezea tu Muda hapa" Askari aliongea kwa hasira.
*************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment