Search This Blog

Thursday 29 December 2022

C.O.D.EX 4 (A MISSING SOLDIER) - 5

 

  Simulizi : C.o.d.ex 4 (A Missing Soldier)

Sehemu Ya Tano (5)



“Naona sasa mmeunganika na kuwa kitu kimoja.” Aliongea Jenero huku akitoka nyuma ya jeshi aliloliita, na kusogea hadi mbele, akawa anaonekana vema. “Kuna C.O.D.EX na Roboti.” Akaongeza huku anawaonyeshea kidole Idris na Merice pamoja na The Lens. “Ninao pia, C.O.D.EX na Maroboti wangu hawa.” Muda huohuo, wale C.O.D.EX wanamichezo, wakajitokeza mbele na kuungana na Jenero huku wale aliowaita maroboti, nao wakianza kujitengeneza.


“Hao sio maroboti, ni Transformers.” The Lens alitoa sauti kurekebisha kauli ya Jenero baada ya watu wake kujibadilisha na kuwa maroboti makubwa, sawa na The Lens.


“Hapana. Transformers, wanatoka kwenye magari, ndege, helikopta, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri. Ila hawa wangu, wanatoka kwenye nyama ya binadamu. Na wewe wako huyo…” Akamuangalia The Lens. “Huyo ni Iron Man.” Akamalizia kauli yake na kuanza kucheka. Alimfananisha The Lens na yule bwana wa kwenye filamu ya Iron Man.


“Hapana. Naitwa The Lens.” The Lens akabadilika na kuwa kioo, kisha mwanga mkali wa jua ukamtoka na kuurusha mbele ya wale wanajeshi wachezaji. Mlipuko mkubwa ukajitokeza huku wachezaji wale wakirushwa kushoto na kulia, pembeni na katikati kwa sababu ya mlipuko na wakati huohuo, wale maroboti wa Jenero, walimkinga Jenero ili asidhulike na mlipuko ule.


The Lens alichomoka ghafla na kufika hadi eneo ambapo F.O.F wanne walikuwa wamemkinga Jenero, na kisha kwa nguvu nyingi alizonazo, alitoa muale mwingine wa jua na kuwapiga wale maroboti, nao wakatupwa mbalimbali kama walivyotupwa wale wachezaji wa C.O.D.EX. Jenero akajikuta yupo wazi na uso wake unatazamana na The Last ambaye alishuka toka ndani ya The Lens.


“Umekosea njia Mzee. Na utajuta kwa nini umepita hii njia.” The Last alimwambia Jenero kwa sauti kavu na kumpiga ngumi nzito ya tumbo. Mzee yule alishika tumbo lake huku kainama na kumpa nafasi The Last ya kumfunua kwa kumpiga kwa goti lake sehemu ya kidevu. Damu zikamruka Jenero na wakati huo, maroboti yake yalinyanyuka na kutengeneza silaha mikononi mwao tayari kwa kumvamia The Last.




Katika hali ambayo hamna aliyeitegemea, Idris alitokeza akiwa angani huku kanyanyua mokono wenye panga kali sana, na kisha akashuka nalo kwenye mikono ya wale maroboti kila mmoja kwa wakati wake. Silaha ambazo waliziandaa kumvamia The Last, zikawadondoka chini huku miili yao ikijirudi na kuwa binadamu wa kawaida.


Idris alianza kuwatembezea kipigo huku Merice naye akijiunga na kusababisha wale mabwana waliyoletwa na Jenero kujutia kuonekana eneo lile ambalo lilikuwa ni weka mbali na watu wazima na pia watoto.


Dakika tano pekee, zilitosha kuwanyong’onyeza wale mabwana na walikuwa hoi huku hawatamani hata kunyanyuka na kupambana. Idris na Merice waliwafunga wale mabwana kwa kamba za chuma ambazo zilijitengeneza mikononi mwao na kisha wakamtazama The Last alipofikia.


“Nakuuliza tena, Uzo yupo wapi?”Swali lilikwenda kwa Jenero ambaye alikuwa kachakaa kwa kipigo kikali toka kwa The Last. Vyeo vilivyokuwa vimetapakaa mwilini mwake, havikufua dafu mbele ya kijana mweusi aliyekuwa kifua wazi na fulana yake akiwa kajifunga kwenye kidonda


“Mzee, hapa utajisumbua tu. Utanipiga na kuniua, lakini hatutoi siri yoyote ile, ndivyo wanajeshi tulivyo.” Jenero aliongea huku kachanua tabasamu baya kuwahi kuonekana kwenye maisha haya. Tabasamu lilichanganyika na damu toka mdomoni na puani.


“Mimi siyo mzee.” The Last akampa kofi zito lililomfanya Jenero ateme damu nyingine. “Usinizeeshe.” Akampa onyo. Jenero akatema mate pembeni na kisha akamtazama The Last ambaye hakuwa na utani katika mambo yake.


“Uzo ndiye mrithi wa hii teknolojia mpya ya F.O.F, yaani Future Of Forever.” Akaongea kwa umakini na kuwaonyeshea vidole wale wanajeshi waliyopokea kipondo toka kwa Idris na Merice. “Hao hamuwezi kuwasimamisha hata mje na jeshi zima la China, Japan, Malyasia na wote mnaojijua.” Maneno hayo yalikwenda sambamba na tabasamu lake baya ambalo hamna mtu ambaye alitaka kuendelea kulitazama. “Labda kidole cha MUNGU pekee.” Akamaliza Jenero.


“Sasa mbona ni wale pale hawana hali tena ya kupambana.” The Last alimuuliza kwa kejeli.


“Hapana. Siyo hawana hali ya kupambana. Hawataki kuleta madhara kwa wengine ambao hawana kosa wala tatizo nao. Lengo lao kubwa ni wewe.” Akaongea Jenero.


“Basi nitaanza kukumaliza wewe, kisha nitawafuata wao na kuwafutilia mbali.” The Last aliongea na kisha akanyoosha mkono wake na mkono wa The Lens ulikuja na kuingia mahali pake na kutoa chupa ambayo ilikuwa mfano wa sindano kubwa sana. Bila kusita alikamata kichwa cha Jenero na kukiangalizisha juu tayari kwa kuingiza sindano ile ya chupa kwenye shingo ya Jenero. “Salamu zao kuzimu.” Aliongea The Last lakini kabla sindano ile haijaingia shingoni, alijikuta akirushwa vibaya sana na mpira ambao ulimpiga tumboni na kisha kulipukia hapo.


Maradona, Mwanajeshi mcheza mpira alikuwa kapiga mpira wake na kumtupia mbali The Last . Idris na Merice walimkimbilia The Last na kumnyanyua na wakati huo, jeshi la wachezaji nalo lilimnyanyua Jenero na kumtoa kabisa eneo lile.


Idris, Merice na The Last wakasimama na kuwatazama wale wanamichezo ambao kwa pamoja nao walikuwa wamepanga mstari na kuwatazama pia wabaya wao.

Katika hali ya taharuki, vyuma vilisikika vinakatika nyuma ya mstari walioupanga Idris na wenzake. Walipotazama, walishuhudia wale wanajeshi wa F.O.F wakianza kuwa wakubwa na kusababisha zile kamba za chuma kukatika bila kupenda.


Walipomaliza kujibadilisha na kuwa maroboti, waliruka angani na kisha kwenda kutua nyuma ya jeshi la wana michezo.


“Naona jeshi lao limeongezeka.” Idris aliongea huku katabasamu kana kwamba kulikuwa hamna tatizo.


“Hawana shida hawa.” Man’Sai, The Last, aliongea na kubonyeza vitufe vya kwenye saa yake. The Lens, yule roboti alianza kujipangua na kujitokeza maroboti wengine wawili wenye maumbo sawa lakini walizidiwa ukubwa na wale F.O.F


“Hata bila The Lens, hawa tunawamaliza bila shida.” Merice aliongea kwa kujiamini na wakati huo, Mcheza Rugby alianza kuuzungusha mpira wake tayari kwa uvamizi.


“Katika maisha yangu, nimeishi Tanzania na Marekani. Lakini Tanzania, ni nchi ambayo inawatu wenye ukarimu na upendo kuliko Marekani ambapo ubaguzi pamoja na kujiona, kumetawala kupita maelezo.” Idris aliongea maneno yake huku macho yake yakiwa makini kuwatazama wapinzani wake ambao walikuwa wanajiandaa kwa uvamizi. “Nakuomba Man’Sai, kama sitafanikiwa kutoka hapa, fikisha salamu zangu za upendo kwa Watanzania wote hasa Limasi na mwanangu atakayemzaa.” The Last alimtazama Idris na kujikuta akiingiwa na furaha kwa maneno yale kuhusu nchi yake.

“Hamna atakayepotea leo hii, labda mimi nisiwepo.” The Last alimjibu Idris na hakutaka maongezi zaidi kuhusu upendo wa nchi yake. Akarudi kwenye vita. “Mimi wangu hao maroboti. Nyie malizaneni na hao wajinga wengine.” The Last aliongea na kubofya saa yake kama kawaida. Mwili wa The Lens ukaanza kujiunga tena na kisha kumpa nafasi kijana yule wa Kitanzania kuingia ndani yake tayari kwa kuundesha.


Mcheza Rugby ambaye alikuwa kachochea mpira wake, alirusha mpira wake kwa nguvu zake zote kuwaelekea wapinzani wake na mpira ulipofikia umbali fulani, Idris alitoa mkono mrefu ulioukamata mpira ule pale ulipo na kisha kuuminya na kuupasua vibaya. Mlipuko mkubwa ukachukua nafasi yake huku moto ukitanda angani. Mpira ambao ulikuwa bomu, ulileta tatizo pale katikati ya jeshi la Uzo na jeshi la Dokta Ice na The Last.


Moshi ulipotulia, Wachezaji walikutana uso kwa uso na Merice na Idris ambao walifika pale walipo bila taarifa wala hodi.


“Sisi ndiyo C.O.D.EX bora kuundwa kwenye maabara yenu. Na tunawadhihirishia hilo sasa hivi.” Idris aliongea na kisha alimpiga ngumi nzito ya kidevu mcheza Rugby. Akapaa juu na akiwa hukohuko juu, mkono wa Idris ambao ulikuwa na asili ya chuma, ukarefuka tena na kumuongezea konde lingine la nguvu.


Wakati huohuo, Merice alikuwa anapambana na Mwanadada mcheza Tenis ambaye alikuwa anajaribu kupangua mapanga ya Merice kwa kutumia fimbo yake ya kuchezea Tenis. Akiwa anahaha kupangua mikato kadhaa ya panga la Merice, Merice alipotea ghafla na kutokea nyuma yake kumpiga kareti ya uti wa mgongo. Mcheza tenis mambo yakamuwia ugumu hasa kwa sababu pigo lile lilinyamazisha viungo vyake vyote kucheza. Akapiga goti moja na kutumia fimbo yake kusimama. Akawa anaonekana kama mwanariadha ambaye anataka kuanza mbio. Uso uliangalia chini na wakati huo Merice alitokeza pembeni yake na panga ambalo alitaka kulishusha shingoni kwake lakini kabla hajafanya hivyo, alihisi kuna kitu kinakuja nyuma yake. Akanyoosha mkono wake na kitu hicho ambacho kililenga kichwani kwake, akakidaka kwa ustadi na kukiangalia.


Kilikuwa ni kichuma kilichokuwa kama kifuniko cha kikopo cha mafuta. Na wakati anakitazama, Mwanamichezo mwenye viatu vya matairi akiwa anatereza huku kakamata fimbo ambayo alitumia kukipiga kile kichuma, alikuwa anakuja kwa kasi na Merice ambaye alikuwa katika ubora ambao hakuwahi kuwa nao, alikirusha kichuma kile kwa mchezaji yule, nacho kikaingia kwenye koo lake na kumfanya yule mwanajeshi adondoke na kutereza hadi pale aliposimama Merice.


Mwanadada Merice akainama na kuchukua ile fimbo ya mterezaji ambaye alikuwa kakamata koo lake huku macho kayakodoa kama aliyekabwa kwa kiazi kitamu.


“Hii ndio silaha yako?” Merice akauliza huku anaitazama ile fimbo huku na huko na wakati Idris na The Last walikuwa wanaendeleza ubabe mbele ya wale wanajeshi wengine. “Na hii ndio sehemu ya kulipua eeh.” Merice akaongea tena baada ya kuona kitufe fulani kwenye ile fimbo. Mterezaji alikuwa anashindwa hata kujibu mapigo.

Merice akabofya kile kitufe, chuma kidogo kilichokuwa shingoni kwa mchezaji yule kikajitokeza visu vingi na kuanza kuzunguka kwenye koo la mchezaji yule huku kinajikita zaidi ndani. Mchezaji alikuwa anatapatapa na mwisho wake alitulia tuli mbele ya macho ya mwanamichezo mwenzake wa Tennis. “Zamu yako.” Merice aliongea na kunyanyua tena mkono wake wenye panga lakini kabla hajaushusha, Mcheza Tenis alipiga yowe kubwa ambapo lilimfanya abadilike na kuwa mweupe sana. Mwili wake ulizungukwa na mwanga fulani kama upepo. Alikuwa kajichochea nguvu zake ambazo akiziunga na wenzake, anakuwa bomu baya sana la nyuklia. Ndilo ambalo lililipuka kule kwenye barafu na kusababisha maporomoko makubwa.


Hata wale wengine waliposhuhudia mmoja wa wanajeshi mwenzao ameaga dunia kwa kujiua kwa silaha yake mwenyewe, nao walijikuta wakipandisha hasira na kujitengezea nguvu zao binafsi ambazo sasa ziliweza kuwasaidia kupambana na Merice pamoja na Idris.


Kwa upande wa The Lens, alikuwa anatoa kipigo kwa wale F.O.F zamu kwa zamu. Aliweza kujitawanya mbele yao. Yaani alijitengeza miili miwili ambayo iliweza kuumiliki mchezo vema sana. F.O.F walikuwa vizuri kuzuia mapigo ya The Lens lakini hawakuwa vema kushambulia. Hali hiyo ilimzuia The Lens kuwamaliza mapema wale mabwana na wakati huo, nguvu zake zilikuwa zinakwisha.


The Lens alipoona anazidi kuishiwa nguvu, aliruka angani na kujichochea nguvu zake zote, na kisha alitua katikati ya wale maroboti na wakatio huohuo, The Last alijitupa pembeni kabisa akiuacha mwili wa The Lens ukijibamiza chini na kulipuka palepale na kuwakatakata na kuwabomoa kabisa F.O.F na wakati huo zile athali za mlipuko ule, zikiwarusha Idris, Merice na wale wengine pembeni kabisa. The Last akalala chini na mlipuko ule kupita mbali naye.


Kimya kikatanda. Ni sauti za moto ndizo zilisikika eneo lile pamoja na moshi mkubwa. Hali ilipotulia, eneo ambapo The Lens alitua palikuwa na shimo kubwa jeusi na pembeni kulikuwa na vipande vyake pamoja na vya wale F.O.F. Wanajeshi wa Uzo pamoja Idris na Merice, waliathiliwa sana na miale ya The Lens, hivyo walikuwa wanajizoa zoa kwa shida toka pale chini waliporushwa. Nguvu zao hazikuwepo kwa muda ule. Walitakiwa kupata muda mdogo wa kuzirudisha.


The Last alinyanyuka kwa shida na huku anapepesuka, akaanza kwenda pale Idris alipokuwepo na Merice ambaye alikuwa bado hajainuka vema kama mwenzake Idris ambaye tayari nguvu kiasi zilianza kumrudia.




The Lens alipoona anazidi kuishiwa nguvu, aliruka angani na kujichochea nguvu zake zote, na kisha alitua katikati ya wale maroboti na wakatio huohuo, The Last alijitupa pembeni kabisa akiuacha mwili wa The Lens ukijibamiza chini na kulipuka palepale na kuwakatakata na kuwabomoa kabisa F.O.F na wakati huo zile athali za mlipuko ule, zikiwarusha Idris, Merice na wale wengine pembeni kabisa. The Last akalala chini na mlipuko ule kupita mbali naye.


Kimya kikatanda. Ni sauti za moto ndizo zilisikika eneo lile pamoja na moshi mkubwa. Hali ilipotulia, eneo ambapo The Lens alitua palikuwa na shimo kubwa jeusi na pembeni kulikuwa na vipande vyake pamoja na vya wale F.O.F. Wanajeshi wa Uzo pamoja Idris na Merice, waliathiliwa sana na miale ya The Lens, hivyo walikuwa wanajizoa zoa kwa shida toka pale chini waliporushwa. Nguvu zao hazikuwepo kwa muda ule. Walitakiwa kupata muda mdogo wa kuzirudisha.


The Last alinyanyuka kwa shida na huku anapepesuka, akaanza kwenda pale Idris alipokuwepo na Merice ambaye alikuwa bado hajainuka vema kama mwenzake Idris ambaye tayari nguvu kiasi zilianza kumrudia.


ENJOY


“Idris,” The Last akaita huku anaenda pale alipokuwa anajikusanya Idris. “Upo vipi mzee.” Akamuuliza huku anafuta moshi ambao ulikuwa umemtinga machoni mwake.


“Nitakuwa sawa, Man’Sai. Ila Merice naona bado hajawa sawa. Hajazoea kabisa nguvu ambazo anazo sasa hivi. Hivyo kuna muda zinamzidi na kumuathili kwa asilimia kubwa sana.” Akajibu Idris huku anajaribu kumrudisha Merice katika hali yake na wakati huo, The Last naye alikuwa amekaribia kufika eneo lile.


Wakiwa wamekaribiana wote watatu, ndipo walianza kusikia ardhi waliyokuwepo ikianza kutikisika kama vile tetemeko la ardhi. Hali ilizidi kuwa tete eneo lile na walipotazama, waliweza kushuhudia miili ya wachezaji wale ikiwa inatetemeka kwa nguvu nyingi sana na mioto mikali ikiwa inaonekana ikiwatoka wale wachezaji ambao miili yao ilikuwa inajiingiza nguvu tena kwa ajili ya kufanya jambo la hatari zaidi.


“Hapafai hapa Idris.” The Last aliongea baada ya kuona hali ile ikizidi kuwa mbaya zaidi. “Nadhani wanajiunga ili kujitoa sadaka.” Akaweka bayana hali ambayo alikuwa anaifikiria.


“Ndiyo hivyo Man’Sai. Na hatutofika mbali, tayari watakuwa wamejitoa sadaka na kutumaliza na sisi pia.” Idris akamjibu The Last huku akijaribu kujikakamua kumnyanyua Merice ambaye bado hakuwa katika hali yake.


“Hawa wameundwa kishenzi sana. Wanaweza kuwa hata nyuklia na kuangamiza dunia nzima.” The Last aliongea huku akisubiri litakalotukia.


“Uzuri kuna mavazi yao ambayo huvalishwa na kupachimwa vifaa vingine ambavyo wakijilipua, basi huwa hatari karibu eneo kubwa la nchi. Naona hapo walishtukizwa tu, hawajavaa hayo mavazi ila bado sisi tupo hatarini.” Akaelezea Idris.


“Sasa wewe, si waweza kupotea na kuonekana? Kwa nini usipotee na kisha tukajikuta tupo Miami au Texas?” The Last alimuuliza Idris.


“Uwezo wangu kupotea na kutokea, ni kwenye eneo lisilozidi mita mia mbili. Tofauti na hapo, siwezi kufika mbali.” Akajibu Idris na wakati huo, wanajeshi wachezaji walikwishajiunga na kuanza kuzunguka angani huku miili yao ikizidi kung’aa kama mwanga wa jua.


“Nadhani mwisho wetu umewadia kutokana na maelezo yako.” The Last akaongea.


“Siwezi nikazuia nguvu zao kwa pamoja Man’Sai. Nikifanya hivyo, nitajiumiza zaidi na watakula nguvu zangu zote na kuzidisha hatari nyingine kwa taifa.” Idris akaongea kwa masikitiko. “Bora waniue nikiwa hapa kuliko kwenda kuwazuia na kuninyonya nguvu zangu.” Akaongeza.


“Siyo kosa lako Id. Umefanya kilicho bora.” The Last akamwambia huku akimgonga gonga begani.

Wakiwa pale chini, waliangaliana wote kwa pamoja na wakati huo, mlio mkubwa ulisikika. Ni miili ya wale wachezaji ililipuka na moto mkubwa ukaanza kushuka ardhini kutokea juu.


“Tunakufa bila kumaliza kazi.” Idris alinong’ona.


“Wapo watakayoimaliza Brother. Wapo kila mah…” Hakumaliza sentensi yake.

****

BAADA YA MIEZI MIWILI

Den Haag – Uholanzi


Kesi kubwa ilikuwa inanguruma kwenye Mahakama Kuu Ya Makosa Ya Jinai. Limasi akiwa na wenzake, waliweza kukubaliwa kufungua kesi hiyo huko Afrika Kusini na kwa bahati nzuri, kesi hiyo ilikuwa na vithibitisho vyote vinavyoweza kuishitaki nchi, pamoja na wahusika wa kuunda kemikali hatari za C.O.D.EX.


Uzo akiwa mtuhumiwa nambari moja, aliweza kukamatwa na kuwekwa kizuizini ndani ya muda wote wa kesi na wakati huo, Idris, Merice na The Last, wakiwa hawajulikani walipo tangu mlipuko wa wanajeshi wachezaji ulipochukua nafasi yake miezi miwili iliyopita.


Kila kesi ile ilipokuwa inasikilizwa, haikupata muafaka wa mwisho kwa sababu ya ushahidi mwingine kuwa nyeti sana kiasi kwamba ililazimu, mahakama ikae peke yake ili iweze kuupitia ushahidi mmoja baada ya mwingine na pia kuepuka macho ya vyombo vya habari ambavyo vingeonyesha na kutoa taarifa za kila kitu kuhusu kesi ile ambayo ilizidi kuvuta vichwa vingi hapa duniani.


“Si kama mlivyodhania. Hii kesi kidogo imekuwa ngumu na inavushwa vushwa kila mara. Lakini tuwape muda wakuu hawa wafanye kazi.” Aliongea mwanasheria mkuu aliyechaguliwa na Limasi kusimamia kesi ile.


“Hamna shida. Tumeelewa na tupo hapa kupambana hadi ipatikane.” Alijibu Limasi kwa niaba ya wenzake wengine.

Mimba ya Limasi ilikwishaonekana. Ilikuwa na miezi mitano, hivyo kumfanya Limasi aonekane ni mwanamke mpambanaji hasa kwa sababu ya hali yake pamoja na maswahibu yanayomkumba.


“Cha msingi, ni kuwa wavumilivu.” Bwana Desh De Reek, mwanasheria na mmiliki wa kampuni kubwa ya Kisheria nchini Afrika Kusini, aliwaambia wakina Limasi. Nao wakakubaliana wakiwa ndani ya mahakama wakisubiri hatma mpya ya kesi yao.


Baada ya dakika zipatazo thelathini, kundi la mahakimu lilirudi tena kortini na kumrudisha pia Uzo kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayomkabili.


“Tumepitia tena ushahidi wenu. Na unaonekana bado mgumu sana kufanyiwa ufumbuzi ndani ya siku hizi.” Aliongea hakimu mkuu aliyepewa mamlaka ya kusimamia kesi ile. “Tumetuma nakala za ushahidi wenu kwa mtaalamu wetu ili aweze kuthibitisha kama video na karatasi zenu, ni kweli ziliandikwa na Dokta Ice. Hivyo, wiki ijayo, tutakuwa hapa tena kwa ajili ya kuendelea kusikiliza hii kesi.” Akameza mate kidogo na kuangalia nyuso za wanasheria waliokuwa wanaisimamia ile kesi. “Baraza la mahakama, linaahirisha kesi hii, mpaka baada ya siku saba.” Akagonga nyundo kwenye kigongeo maalumu kilichopo kwenye meza yake mle mahakamani. Kesi ikawa imeahirishwa huku Limasi na kundi lake wakiwa katika hamaniko kubwa.


Baada ya kesi kuahirishwa, iliwapasa wapange kurudi kwenye makazi yao, lakini kabla hawajakwenda kwenye gari lao, Limasi aliomba faragha ya dakika kadhaa ili aende uwani kujisaidia.


Akiwa uwani, alitokea mwanadada mmoja ambaye alikuwa kavalia suruali nyeusi iliyombana na kung’aa sana. Suruali ilikuwa imetengezwa kwa matirio ya mpira. Na juu alivalia fulana fupi iliyoacha kitovu chake nje, huku pia akimalizia kwa koti jeusi la leiza.


“Limasi.” Akamuita mwanadada yule kwenye mlango wa choo alichoingia. Limasi akiwa hajui ni nani aliyemuita. Akaitika kwa woga. “Tunakupenda sana mdogo wetu. Lakini unapotaka kuingia, ni kubaya sana. Tunakuomba ulee mimba yako badala ya kupambana na watu usiyowajua.” Mwanadada yule alimpa taarifa Limasi na kisha akapenyeza mkono wake juu ya mlango, na kumtupia Limasi kikaratasi kilichokunjwa kwa mtindo wa sigara. “Elewa kilichomo humo.” Mwanadada akaondoka ndani ya vyoo vya wanawake akimuacha Limasi akivaa nguo zake haraka na kukifungua kile kikaratasi.


“SIKU NNE PEKEE ZA KUONDOKA UHOLANZI. UKIKAA, UTAUMIA NA KUUMIZA WATU WAKO. ONDOKA HARAKA.” Kipande cha karatasi kiliandikwa hivyo na kumfanya Limasi apagawe na kuhisi tumbo baya la kuhara likimkamata. Akajikuta mwenye uhitaji wa kuendelea kujisaidia.

****

“Unasemaje Lim?” Buja Bujiku, Mnaijeria ambaye alikuwa bega kwa bega na Limasi kwenye kesi yake, alimuuliza kwa hamaki Limasi ambapo tayari wote walikuwa wamerudi kwenye makazi yao.


“Nasema hivi. Hii kesi tuachane nayo. Wote tutaangamia.” Limasi alirudia kauli yake aliyoitoa na kumsababisha Buju kumuuliza tena.


“Yaani kwa sababu ya huu upumbavu?” Buju alimuuliza Limasi na kukiokota kikaratasi alichopewa Limasi chooni na kukinyanyua. “Haiwezekani Lim. Hapo utakuwa unatuonea tu.” Akaongeza Buju.


“Lakini hii ni kwa ajili ya usalama wetu na tunaowapenda.” Limasi akaongea kwa sauti ya kubembeleza.


“Kwa hiyo tunajipenda sisi tu. Hao wengine tunaowatetea hawastahili upendo wetu?” Chameli. Mwanadada wa Kihindi, alimuuliza Limasi ambaye alikaa kimya bila kuweka neno.


“Lim. Hii si kwa ajili yako mama yetu, ni kwa ajili yetu wote. Hatuwezi kumuacha ng’ombe ambaye tayari tumekwishamchuna ngozi na kumchoma na tayari amewiva. Kazi imebaki kumla tu! Leo unatuambia tumuache ni haramu.” Buju aliongea kwa huzuni huku anakaa kwenye sofa moja na Limasi.


“Jamani, nimewaita mimi ili tushughulikie hii kesi…” Hakumaliza sentensi yake, akakatishwa.


“Na tuache tushughulikie na tuimalize.” Faruq ndiye alimkatiza kauli yake na kumfanya Limasi abaki bila usemi. “Tunajua umempoteza Idris. Lakini huko alipo, atakuwa na furaha kama akiona kesi hii utashinda. Lim, muda ndio huu, usiogope hivyo vitisho.” Akaongeza Faruq, kijana wa Kioman. Limasi akawa kimya akiwa hajui aongee nini ili wale wenzake wamuelewe. Kimya kikatawala.


“Sikilizeni vijana.” Desh De Reek, mwanasheria mkuu, alikata ukimya. “Hamna ambaye anamjua aliyemtumia huu ujumbe Limasi. Lakini watu ambao tunapambana nao, si rahisi kutuacha sisi salama. Niamini mimi nachowaambieni.” Desh akaendelea. “Usione kesi inaenda enda hivi kama gari bovu lisilokuwa na dereva, ni hatari hata kwa mahakimu. Kila kukicha wanabadilisha mahakimu. Mara tunapeleka kwa wataalam. Ina maana hao wataalamu hawapo kwenye baraza lao?” Akaacha swali hewani na hakutaka mtu ajibu. “ Wapo hatarini. Hii kazi mliyoingia, inapaswa kujitoa kila kitu. Tutawapoteza wengi hapa. Na tutapotea wengi vilevile. Huu ujumbe si wa kupuuzia. Sasa tukubaliane, tunaacha au tunaendelea?” Akauliza Desh.


“Mimi nitaendelea.” Akaanza Buju kujibu na wengine wakafuata kuwa wataendelea na kisha Desh akamaliza kuwa atakuwa nao.


“Nadhani mmesoma kwa makini kesi hiyo. Ni wangapi walipotea walipotaka kuifumua. Sasa kazi ni kwetu. Roho zetu zipo toharani japokuwa tu wazima.” Desh alimaliza na kutoka ndani ya chumba kile.

****

Siku ya nne ilipowadia, Chameli mwanadada wa Kihindi akiwa anakimbia barabarani kama kunyoosha viungo vyake asubuhi ile, alishitukia ghafla gari dogo jeusi likisimama mbele yake, na kioo kimoja kufunguka. Mkono ukajitokeza kwenye kioo hicho ukiwa umekamata bastola. Risasi moja ikachomoka kwenye bastola na kutua kwenye paji la uso la Chameli. Mwanadada akadondoka na kupoteza uhai hapohapo huku kipande cha karatasi kilichonyongwa kama sigara, kikitupwa kwenye mwili wake na gari lililohusika kwenye tukio, likiondoka kwa kasi.


Hamna aliyeelewa kilichotokea ndani ya dakika zisizozidi mbili. Ni gari lilisimama, na kisha mkono ukachomoza ukiwa na bastola. Risasi ikafyatuliwa, na mkono huohuo, ukarusha kikaratasi kilichoandikwa, ”TUNAANZA KUTIMIZA AHADI ZETU.” Kisha gari hilo kutokomea. Hayo ndio maelezo yaliyotolewa kituo cha polisi na baadhi ya mashuhuda wa tukio lile.




“Kuna vitisho vyovyote ambavyo mlivipokea kabla ya tukio hili?” Bwana mmoja aliyepewa jukumu la kufuatilia kesi ile, alimuuliza Buju ambaye aliingiia chumba kilichotengwa kwa ajili mahojiano kwenye kituo cha polisi, na kuanza kuhojiwa maswali kadhaa na mpelelezi wa kesi ile.


“Ndio. Kuna karatasi alipewa mwenzetu ambaye ndiye aliyeifukua kesi tunayohangaika nayo kwa sasa.” Akajibiwa mpelelezi.


“Karatasi hiyo ilisemaje?” Akaulizwa tena Buju.


“Iliandikwa kama onyo, kuwa ni siku nne Limasi anatakiwa kuondoka. Asipoondoka, ataumia yeye na sisi.” Akajibu.


“Na leo ni siku ya ngapi toka mpokee karatasi hiyo?” Akaulizwa tena.


“Ni siku kama ya nne hivi.” Akajibu tena baada ya kufikiria kwa muda kidogo.


“Kwa nini hamkuja kutoa taarifa kituo cha polisi?” Akaulizwa tena na Buju hakuwa na jibu la kutoa kwa swali hilo. “Mnaona matokeo yake sasa?” Akaulizwa kwa kulaumiwa Buju. “Mmempoteza rafiki yenu kwa sababu ya ujinga wenu.”


“Kwani Insipekta, hata kama tungekuja kutoa taarifa, tungezuia kifo chake? Mbona unakuwa kama unatulaumu tu hapa.” Buju alikuja juu baada ya kuona mpelelezi wa kesi ile akiongea shutuma juu yake na wenzake.


“Sikulaumu wala kuwalaumu. Ila mngefanya la maana kama mngeondoka hii nchi. Vinginevyo, mtapotea wote tena mmoja baada ya mwigine.” Alijulikana kama Insipekta Pox Maxmilian, yeye alipenda kujiita Insipekta Pox Max. Alikuwa ni mtaalamu wa kufuatlia kesi nyingi za mauaji na kufanikisha kuzitatua mapema iwezekanavyo.


Kwa habari za chinichini, Insipekta Pox Max, aliikuwa anashiirikiana na mitandao mikubwa ya mauaji. Hivyo mauaji kama ya Chameli yakitokea, basi huwafuata wakubwa wa makundi ya mauaji na kuwauliza kama wanafahamu waliyofanya tukio hilo na anapopata majibu, huwashughulikia haraka wauaji lakini baada ya kuomba kibali cha mabosi wa wauaji hao.


“Kwa hiyo unaona haki ilitendeka kwa hawa wanaotengeneza hizi kemikali za mauaji?” Akauliza Buju.


“Hapana. Hawajatenda haki kabisa. Lakini hiyo kesi tayari iliyawafukia wengi sana. Yawezekana ikakufukia hata wewe. Sasa kwa nini usitii amri yao na wewe kurudi kwenu Naijeria kwenda kubangua dengu?” Pox akamkejeli Buju.


“Ni kheri nife wakati napigana kuliko kufa kama muoga, au niliyeshindwa. Nitapigana na hii kesi hadi pumzi ya mwisho ya uhai wangu.” Akajibiwa Pox.


“Ohooo.” Pox akaongea huku ametabasamu na kuanza kumpigia makofi ya pongezi Buju. “Bravo sana, Bravo.” Alimpa hongera.


“Haijalishi hayo makofi yako ni kweli au kejeli, ila nitapigana kufa na kupona.” Buju naye hakuwa nyuma kuonyesha ujasiri wake kwenye kila tendo toka kwa Pox.


“Vema. Tutaona mwisho wake.” Akajibu Insipekta Pox Max na kwenda kwenye kioo cheusi na kutoa ishara fulani. Mlango wa chumba kile ukafunguliwa na Buju akaruhusiwa kutoka mle huku njiani akipishana na Faruq ambaye naye aliingia kwenye chumba kile alichotoka mwenzake.


Faruq aliingia ndani ya chumba kile na kumkuta Pox akiwa kasimama kwenye kona fulani ndani ya chumba kile. Akamtazama vema kijana yule na kuanza kumuuliza maswali yaleyale ambayo aliulizwa Buju. Na majibu yalikuwa yaleyale. Vitisho vilikuwa vilevile lakini hamna ambaye alitaka kuendelea kusikiliza ushauri wa Pox.


“Unajua kuwa haya maongezi ni ya mimi na wewe tu. Hamna ambaye anayasikia, awe huyo nje ya kioo hichi cheusi au yeyote yule. Sasa kwa nini usisikilize ninalokwambia tu! Ili uondokane na kifo.”


“Nitakusikiliza vema kama ukiwaambia Wamarekani waache ubabe wa kijinga dhidi ya nchi za Kiislam pamoja na nchi za Ujamaa.” Akajibu Faruq. Kijana toka Oman.


“Ahaa! Umeshaanza kuleta na mambo ya siasa.” Akaongea Pox.


“Siyo siasa, huo ndio ukweli.” Faruq alijibishana kwa muda mrefu na Pox na baadaye aliachiwa kama ilivyokuwa kwa Buju.


“Naona hamna ambaye yupo tayari kuiachia hii kesi na naona hamna ambaye anataka kusikiliza ushauri wangu. Lakini wauaji hawa ambao wametumwa, hawana utani hata kidogo. Na ni watu hatari duniani, ni hatari hata kwa taifa letu.” Aliongea na mkuu wa kituo cha polisi, Insipekta Pox Max.


“Kama hawataki, basi kuna njia moja tu.” Akaongea Mkuu wa Polisi.


“Njia ipi?” Akauliza Pox.


“Kuwalinda.” Akajibu kwa utulivu Mkuu wa Polisi na kumshangaza Pox.


“Mkuu, hawa watu ni hatari balaa. Si wa kawaida. Hawatumii silaha kama zetu na wala risasi zetu haziingii kwao. Ni hatari hawa. Wameundwa kutosikia maumivu. Unadhani tutasalimika kwenye huo ulinzi?” Pox alikuja juu.


“Nimekwishakwambia, walinde kwa lolote lile. Hawa ndio wanaweza kuwasimamisha hao wauaji wasiweze kuundwa tena. Fanya, ufanyalo, bora ufe wewe, lakini hawa wawe wazima.” Akajibiwa na mkuu wa polisi wa Uholanzi.


“Lakini mkuu, japo upo sahihi, lakini hii ni kazi ngumu kwangu.” Pox alionyesha wasiwasi wake pia.


“Unahitaji nini toka kwetu?” Akaulizwa.


“Silaha za kweli. Zenye mchanganyiko wa kemikali. Kama zile ambazo tulizikamata uwanja ndege miezi miwili iliyopita. Ni zile pekee zinazoweza kuwasimamisha wauaji hawa.” Akajibu Pox.


“Limepita hilo Insipekta. Hakikisha hamna kifo tena hapa.” Akahakikishiwa kuwa anaweza kupatiwa silaha ambazo anazihitaji.

Baada ya hapo, akapewa mikakati kabambe ya kuwalinda wanasheria wale waliyobaki. Na mikakati hiyo, ilienda sambamba na yeye kuwa anawafuatilia kimya kimya bila wao kujua.

****

Baada ya kuitwa kituo cha polisi na kuhojiwa kuhusu mauaji yaliyofanyika asubuhi ile, kundi zima la wanasheria likiwa linaongozwa na Limasi, wakaruhusiwa kurudi nyumbani kwao tayari kwa kujiandaa na kuzika maiti ya Chameli ambapo wazazi wake walikwishapata taarifa na kuzisambaza kwa watu wengine wa karibu. Na utaratibu wa kumzika Chameli, ulikuwa ni kumchoma moto, na kisha majivu yake kusafirishwa hadi India kwa ajili ya kuzikwa kwa kumwagiwa baharini.


Wakiwa wenye huzuni, wanasheria wale walitoka kwenye kituo cha polisi abacho kilikuwa kikubwa sana na chenye uzio mpana wa kuweka magari. Magari mawili yaliyokuwa yamewabeba wale wanasheria, yalikuwa yamewekwa mbali kiasi na kituo cha polisi. Hivyo baada ya kutoka ndani ya kituo kile, wakiwa kwa ukaribu kabisa na mmiliki wa kampuni ya Uanasheria ya Afrika Kusini, walianza kufuata magari yao tayari kwa kurudi walipoweka makazi yao ya muda.


Wakiwa kama hatua ishirini kabla ya kuyafikia magari yao, walisikia sauti kali ikimuita Limasi. Wote kwa pamoja waligeuka na kumtazama aliyekuwa anamuita Limasi. Walimuona Insipekta Pox Max akija mbio huku anapunga mkono wake.


“Mbwa huyo sitaki hata kumuona. Anashirikiana na wauaji.” Theresa Tyrese, mwanadada wa Kiingereza na mwenye mahusiano ya kimapenzi na Buju Bujiku, aliongea kwa kisirani na kuanza kwenda kwenye gari ambalo lilikuwa na asili ya Noah. Gari lenye uwezo wa kubeba abiria wapatao nane.


“Noo.” Sauti kali ikasikika toka kwa Pox lakini hamna aliyeelewa anachomaanisha.

Buju alimtazama Theresa ambaye alikuwa amebakiza hatua chache sana za kulifikia gari analotakiwa kulipanda, ndipo alielewa maana ya Pox kuwasimamisha.


“Theresaaaa.” Buju alipaza sauti yake kumuita Theresa na mwanadada yule aligeuka na kumtazama Buju ambaye alikuwa kasimama bila kujielewa anataka kufanya nini kwa wakati ule.

Theresa akauliza kwa ishara ya mikono, huku midomo yake akionekana akiuliza “Kuna nini?” Na ndipo hapo jibu lilipatikana kwa mlipuko mkubwa kutokea eneo lile. Mlipuko ambao uliliinua gari ambalo wanasheria wale walitaka kulipanda na baadaye gari lile kutua chini na kuzidi kulipuka kuanzia injini yake hadi tanki la mafuta na wakati huo, mlipuko ule ukisababisha kupasua vioo vya magari ya pale na upepo wake kuwatupa vibaya sana wakina Limasi ambao walikuwa mbali kidogo na gari lile.


Mlipuko ulipotulia, Buju alisimama haraka na kukimbilia eneo ambalo Theresa alirushwa na kuathiriwa vibaya na ule mlipuko wa bomu lililotegwa kwenye gari lao.


“T.” Buju alimuita Theresa kwa kifupi huku kampakata kwenye mapaja yake. Damu zilikuwa zinamtoka usoni pamoja na sehemu kubwa ya mwili wake. Theresa alipotaka kuongea, damu zilikuwa zikimtoka mdomoni na kushindwa kabisa kusikika anachoongea. “Usiongee T, usiongee chochote mpenzi. Utapona mpenzi wangu.” Aliongea kwa uchungu Buju Bujiku.


“Don’t Stop… Don’t Stop.” Alijikakamua Theresa akimuhasa Buju kuwa asisimame kwa kile alichokianza.


“I will never stop my love.” Buju naye akamuahidi mpenzi wake kuwa hawezi kusimama. “Ila naomba utulie. Nyamaza ili usipoteze nguvu nyingi kwenye kuongea.” Buju aliongea lakini wakati huo, Theresa alikuwa anamuachia taratibu na kisha akamuachia kabisa na macho yake yakabaki yamefumbuka na damu zikiendelea kutoka sehemu kubwa ya mwili wake. “T.” Buju alimuita Theresa lakini hakuona muitikio wowote. Akamuita tena safari hii kwa kumtikisa, lakini hamna jibu lolote alilopewa na mwanadada yule.

“Theresaa.” Aliliita jina la mpenzi wake kwa nguvu huku anaangalia angani. Buju alilia kwa uchungu baada ya kugundua mpenzi wake hakuwa naye tena duniani.


Limasi na wenzake walikuwa wamemzunguka na wao kwa pamoja walianza kudondosha machozi ya uchungu baada ya kugundua kuwa hawakuwa naye tena rafiki yao kipenzi.


“T. Nitataniana na nani tena mpenzi wangu. Nitampa nani tena siri zangu. T, kwa nini umeniacha mimi T? T amka. Amka mke wangu tukajenge familia tuliyoipanga baada ya kesi hii. Amka T. Nakupenda T, tafadhali usiniache T.” Buju alizidi kuwafanya na watu wengine wazidi kulia kwa maneno yake ya uchungu ambayo alikuwa anayotoa.


Pox alikuwa amefika pale na kuanza kuangalia huku na huko kuona kama kutakuwa na kitu chochote cha hatari au labda kuwaona wahusika. Lakini hakuweza kupata chochote hadi baada ya dakika mbili mbele alipoona gari dogo jeusi likitoka sehemu ya kuegeshea magari na alipolitazama vizuri, aliweza kumuona bwana mmoja ndani ya gari lile akiwa upande wa abiria, na bwana yule akamuonyesha alama ya bastola kama anayemfyatulia. Kisha kwa mwendo wa kasi, gari lile likatoka eneo lile na kumuacha Pox akiliangalia kwa macho ya gadhabu.


“Heeey.” Pox akaongea kwa sauti ya juu kidogo baada ya kuona wale Wanasheria hawana la kufikiria zaidi ya kulia. “Hapa si salama kwenu, muda wowote yanalipuka mengine.” Ikabidi awatishe ili waweze kumfuata yeye a wakati huo, ving’ora vya magari ya zima moto na huduma ya kwanza, vilisikika kwa mbali vikija eneo lile.


Wote wakasogea alipokuwa Pox na kumsikiliza huku Buju akimtazama Theresa ambaye alikuwa si mali tena ya dunia, bali sehemu nyingine ambayo binadamu wengi tunaamini ndipo makao mapya.





“Kuna mambo mnatakiwa kuwa makini sana kabla hamjaamua kuyafanya.” Akaanza kuongea Pox baada ya wale Wanasheria kumsogelea na wakati huo, mwili wa Theresa ulikuwa unachukuliwa picha kwa ajili ya upelelezi pamoja na eneo zima la tukio.


“Unataka tuwe makini na tuiache hii kesi?” Buju alimuuliza kwa utulivu huku macho yake yakiwa mekundu.


“Nisikilize kijana. Tena naomba tega sikio lako kwa maki…” Kabla hajaendelea, tayari Buju alimdaka kauli yake na kuongea anayoyawaza kichwani mwake.


“Acha upumbavu mbwa wewe. Angali hii ni nini..” Akamuonyesha mikono yake ambaye ilikuwa imetapakaa damu. “Damu ya mwili wa mwanamke ambaye nilimpenda, na kumthamini na kumuona kama mwanamke ambaye atakuja kunitoa kwenye huu upweke. Sababu ya hawa wajinga, leo hii kapotea, halafu unataka sisi tusimame na kutazama huu ujinga wao. Wangapi wamekufa na wanazidi kupotea kwa ajili ya hawa wajinga? Halafu unatueleza tuwe makini, how? Kivipi yaani tunaweza kutulia?” Aliongea kwa uchungu Buju.


“Umemaliza?” Pox alimuuliza badala ya kujibu zile shutuma. “Nadhani umemaliza, zamu yangu kuongea sasa, naomba ukae kimya.” Pox hakutaka tena kumsikiliza Buju kwa maneno yake. “Wakati mpo hapa, watu ambao nahisi ni wauaji, wamepita na gari ileile ambayo imetolewa taarifa ndiyo iliyoonekana kwenye tukio la mauaji ya yule binti wa Kihindi. Na kulikuwa na mtu ambaye alininyooshea alama ya bastola kwa kutumia vidole vyake.” Akaeleza kwa kifupi Pox lakini kabla hajaendelea, mwanadada Brighita alidakia na kumuuliza.


“Alikunyooshea hiyo alama, wewe kama nani kwenye hii kesi?” Akauliza Brighita.


“Baada ya kuongea na mkuu wa polisi wa eneo hili, nimepewa mamlaka ya kuwalinda ninyi nyote na kuhakikisha kuwa hamna anayepoteza uhai.” Akajibu Pox.


“Tayari T kapoteza uhai. Kwa hiyo kibarua chako kimekwisha.” Akajibu Buju na kuwataka wenzake waondoke pale.


“Unadhani walipanga afe tu huyu mwanamke?” Pox akawauliza wale Wanasheria ambao tayari walikwishaanza kuondoka wakiwa na hasira ndani ya mioyo yao. Pox aliuliza kwa sauti na kuufanya umati wa watu wamtazame yeye. Na waandishi wa habari baadhi walivutiwa na tukio lile, hivyo kamera pamoja na vipaza sauti vikawaelekea watu wale.

“Walipanga mfe wote. Wote nyie mngekuwa ni majivu leo hii,” Aliongea Pox huku anawafuata wale wanasheria na vipaza sauti vikiwa vinamfuata kwa makini lakini alivisukumia pembeni. “Walikuwa wanawasubiri ninyi nyote mpande ndani ya kigari chenu kisha wabonyeze rimoti yao na nyie kupotea hapa duniani. Nimewaita na kuwasimamisha kwa sababu nilikuwa na hisia hizo. Lakini huyu mwenzenu sababu ya chuki zake, akaniona kama mpumbavu. Angalia kilichomtokea.” Wanasheria wakakaa kimya na maneno yake yakawaingia.

“Sina haja ya kuwalinda nyie hata kidogo. Ila ni jukumu la mkubwa wangu ndilo limetoka. Na sina jinsi bali kulibeba kwa sababu ndicho kiapo nilichokiapa mbele ya mkuu wa nchi hii kuwa nitailinda amani ya nchi pamoja na watu waliomo ndani yake. Lakini kwa hili, najua ni mzigo mkubwa nimebebeshwa.” Safari hii Pox alisogea mbele yao na kuendelea kutiririka.

“Unadhani sina watoto na familia? Unadhani hawa watu watawaacha salama? Mnajua ni wauaji gani hawa ambao mnacheza nao? Ni haohao wenye kemikali mwilini. Huwezi kuwaua kirahisi. Lakini nimebeba msalaba wa kuwalinda nyie na familia yangu. Nyie mnaweza? Au mnadhani nacheza hapa?” Akabwata kwa hasira.


“Unataka tufanyaje Insipekta?” Limasi akamuuliza kwa upole.


“Mtafanya ninachowaambia, vinginevyo, wote mtapotea kabla ya kesi yenu hamjaimaliza.” Akawajibu.


“Kwa hiyo unaturuhusu tuendelee na hii kesi?” Buju akauliza.


“Ndivyo mkuu wangu kaniagiza. Ni lazima muimalize hii kesi salama na mrudi makwenu salama. Nadhani dunia itakuwa salama pia.” Pox akawajibu na wote wakatazamana bila kuamini kama wamepewa kibali cha kuendelea na ile kesi.


“Kama ni hivyo, tunaweza kukusikiliza na si kutuambia tuwe makini. Tupo tayari kufa kwa sababu wenzetu tayari wamekwishapotea.” Buju aliongea lakini bado moyoni mwake alikuwa hamuamini kabisa Pox. Mwanasheria wao mkuu, yeye hakuwa na hamu tena ya kukaa eneo lile. Kila kitu alichokuwa anakiona, kwake kilikuwa kama filamu fulani ya kusisimua.


“Buju. Yapasa tumuamini huyu kwa sasa. Hamna jinsi.” Limasi aliongea kwa sauti ya unyonge huku anamtazama Buju. Brighita pamoja na Faruq nao wakamtazama Buju ambaye hakuwa na moyo rahisi kukubali.


“Mtajua wenyewe. Mimi nitakuwa na nyinyi hadi mwisho, lakini siyo huyo. Na sitaki aniamrishe.” Buju akaweka bayana yaliyokuwa moyoni mwake.


Wakati hayo yanaendelea, waandishi wa habari walikuwa wanarekodi kila kitu na mambo yale yalikuwa yanarushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari hasa runingani.


“Naona Max kaamua kuingilia hii kesi.” Bwana mmoja akiwa katika ofisi yake na mabwana wengine wawili, alizima runinga iliyopo humo na kuwageukia wenzake akiyatoa maneno hayo.


“Watu wawili walitosha sana kuwamaliza hawa mbwa. Ila kwa uwepo wa huyu mbwa mwingine, yatupasa kuwaongeza wengine wanne.” Bwana aliyekuwa kavalia suti ya rangi ya udongo, na pembeni ya kiti chake alikuwa kaegesha fimbo ya silva na kishikio chake kikiwa cha nyoka, alitoa wazo huku kakunja miguu yake kwa mtindo wa nne.


“Unadhani kuna haja ya kuongeza wanajeshi wetu kwenye hii kesi?” Akauliza mwenzake ambaye yeye alikuwa kavaa suti ya damu ya mzee, na mdomoni kwake hakuacha kutema moshi kutokana na sigara kubwa aliyokuwa anaivuta.


“Unajua yule ndiye alikamata silaha zile za kemikali. Na kingine ni mtu wa karibu sana na wauaji wengine. Si ajabu akaongeza timu yake ya ulinzi. Na kibaya zaidi, kumbuka yule ni mtu ambaye hata Interpol na mashirika mengine ya kipelelezi duniani, yanahitaji sana huduma yake. Hiyo ni kutokana na ubora wake kazini.” Akajibu mwenye suti ya rangi ya udongo.


“Kwa nini tusichukue moyo wake kwanza?” Akauliza mwenye suti ya rangi ya damu ya mzee.


“Ukitaka na wewe uchukuliwe mioyo yako yote uliyonayo, basi jaribu kuchukua moyo wake.” Akajibiwa.


“Mbona ni kama muoga sana wewe Ortis?” Akauliza kwa sauti kali kidogo.


“Simuogopi. Ila hii vita na huyu mtu, tusijaribu kushirikisha familia zetu. Nadhani wajua sheria zetu. Ukitaka kushirikisha familia, basi jiandae kupoteza familia yako pia.” Ortis ambaye ndiye mwenye suti ya kijivu, alijibu mapigo akitaka kuweka mbali vita ile na familia zao au mioyo yao kwa sababu ndivyo vitu wanavyovipenda.


“Nashauri, tuivurumishe familia yake.” Akamaliza bwana mwenye suti ya rangi ya damu ya mzee.


“Nashauri tuongeze wanajeshi wengine.” Ortis Morgan, Mmarekani aliyekuwa anamiliki maabara nyingi sana Australia, na ambaye alikuwa mnunuzi mkubwa wa kemikali za C.O.D.EX aliweka bayana wazo lake mbele ya Burden Hussein ambaye yeye alikuwa mnunuzi mkubwa wa wanajeshi wa C.O.D.EX katika nchi za Kiislamu pamoja na kiongozi wao ambaye yeye alikuwa kimya akiwasikiliza.


“Bwana Burden. Kama wataka kuingiza na familia, basi kubali kuwa sisi hatutohusika na hiyo kesi. Yaani familia zetu tunaomba zikae mbali kabisa na uhusike wewe peke yako.” Alianza kuongea kiongozi wao ambaye alijulikana kama Microchip Degteck na ndiye mtu wa karibu ambaye alikuwa anawasiliana na Uzo na yeye ndiye alikuwa msambazaji wa bidhaa za C.O.D.EX maeneo mengine duniani.


“Kwa nini sasa Micro?” Akauliza kwa hamaki Bwana Burden.


“Kwa sababu umetaka hiyo njia.” Akajibiwa. “Lakini kwa wazo la Ortis, basi tulitazame na liwe la kwanza kufanyiwa kazi kabla ya lako.” Akaongeza Microchip.


“Sawa kabisa.” Ortis alikubaliana na wazo hilo kisha akanyanyuka na kuanza kutoka ndani ya ofisi ile. Tayari kikao kilikwisha.

****

Kutokana na matukio ya mauaji yaliyotokea siku kadhaa zilizopita, siku ya kesi ya Uzo pamoja na uongozi mzima uliyoshiriki kuunda wanajeshi wa C.O.D.EX , mahakama kuu ilijaa kuliko siku zote za nyuma. Vyombo vya habari vikubwa duniani, vilijumuika eneo la mahakama kwa ajili ya kuifatilia kesi ile.


Hakimu mkuu wa kesi ile akiongozana na jopo la mahakimu wengine, waliingia kwenye ukumbi wa mahakama kuu na mahakama yote kwa ujumla ilisimama kuwakaribisha watu hao. Baada ya hakimu kukaa, wahudhuriaji nao walikaa na kisha hakimu mkuu alifungua kesi ile rasmi kwa kumuita Uzo apande kizimbani kwa ajili ya kujibu mashtaka binafsi ya kuua familia ya Idris pamoja na kuhusika kwa ukaribu sana kuunda wanajeshi wa C.O.D.EX ambao walikuwa wanaundwa kinyume na matarajio. Yaani wanajeshi wale, walitokana na wafu ambao wengine, waliuawa kwa makusudi ili wapate wanajeshi bora.


“Uzo Buzzin. Upo tayari kujibu mashitaka yanayokukabili?” Hakimu alimuuliza Uzo baada ya kupanda kizimbani na Uzo akatabasamu bila kujibu neno.

Wanasheria walioandaliwa, walienda kumuuliza maswali Uzo baada ya kula kiapo kuwa atasema ukweli na hamna atakaloficha. Kesi ikaanza kuunguruma.


Masaa mawili yalifika na kesi ile iliendelea kuunguruma huku kila upande ukivutia kwake. Pesa, utajiri na vitisho, ndivyo vilikuwa muamuzi mkuu wa kesi ile. Haki ilikuwa ndogo sana na kesi ilionekana kuwaelemea wakina Limasi ambao sasa walikuwa wanatokwa na jasho la kuogopa kushindwa.


“Tutarudi baada ya nusu saa. Tuchukue mapumziko.” Hakimu mkuu aliongea na kusimama huku wengine wakisubiri atoke kabisa na wao ndio watoke.


Baada ya hakimu mkuu na jopo lake kutoka, na watu wengine walitoka huku Limasi na kundi lake wakiwa wa mwisho kutoka ndani ya mahakama ile.

Wakiwa wanashuka kwenye ngazi za mahakama waliweza kuongea hili na lile bila kuangalia wanapoelekea. Lakini mbele yao kulikuwa na bwana mmoja mwenye asili ya Kihindi, alikuwa anawafuata kwa kasi huku mikono yake kaitumbukiza ndani ya koti.


Ni Pox ambaye hakuonekana alipotekea, aliweza kujitupa mbele ya yule bwana na kumkata ngwara nzito, na wakati anatua chini, akamsindikiza kwa teke zito la tumbo yule bwana. Macho ya Wanasheria na watu waliokuwepo pale, yakashindwa kuelewa kinachoendelea lakini waliweza kumuona yule bwana aliyeadhibiwa na Pox akikimbia toka pale alipokuwa kadondokea na kurudi alipotoka. Pox akaenda hadi yule bwana alipodondokea, akaokota simu aliyoidondosha na kuwaonyesha wakina Limasi.


“Siyo simu hii.” Akaifungua kwa nyuma na kuwaonyesha kilichopo. “Angefika tu hapo mlipo, angelifyatua bomu hili na kuwaua nyie wote.” Akawalezea lile bomu ambalo ilisemekana kuwa haliwezi kutoka ndani ya mita kumi. Ni lazima mhusika asogee karibu na mtu anayetaka kulipuka naye, ndipo bomu hilo litafanya kazi vema.


Wakati wanaendelea kushangaa, mara damu zilimrukia Limasi. Na kabla hajajua la kufanya, aliweza kumuona Brighita akidondoka huku pembeni ya kichwa chake kukiwa na shimo la risasi.


“Sniper.” Akabwata Pox akimaanisha risasi ile imepigwa na mdunguaji. “Wote laleni chini.” Hamna ambaye hakutii, hata Pox mwenyewe alilala lakini macho yake yakawa yanaangaza huku na huko kwenye maghorofa yaliopo maeneo yale.


Wakati anaendelea kuangaza, gari moja aina ya VX 8, lilisimama na kisha watu wawili wenye vinyago wakashuka na kuanza kutupa mabomu ya moshi na kusababisha eneo lile kujaa na moshi pekee.



Lilikuwa ni tukio la kushtukiza na la haraka sana. Hata waandishi wa habari hawakuweza kugundua ni nini kilichotokea ndani ya muda ule. Brighita, alikuwa hana uhai tena, Limasi, Faruq, Buju, na mwanasheria wao mkuu, Bwana Reek, nao walipotea ghafla baada ya moshi ule kutulia. Kila mmoja alikuwa katika taharuki ambayo hamna wa kumpa majibu ya haraka.


Ndani ya gari ambalo liliwachukua vijana wale, kulikuwa kuna utulivu mkubwa sana. Wanasheria wote walikuwa wametulia wakiwatazama wale mabwana waliowateka kwa uoga mkubwa. Bado walikuwa wamevaa vinyago vyao usoni na waliendelea kuvaa huku gari ambalo liliwekwa vioo vya ‘tinted’ likizidi kukata mitaa kwa kasi kubwa.


Ndani ya dakika kumi, gari lile lilifika eneo moja na wale mabwana wenye vinyago pamoja na dereva wao, walishuka na kisha kuwaamuru wakina Limasi pia washuke. Vijana wale walishuka huku wakiwa bado na uoga mkubwa.


“Embu vueni hayo madudu yenu, mnaogopwa.” Dereva wa gari lile aliwaamuru na wale watu walivua vile vinyago na kujionyesha sura zao.


“Agent Zero?” Limasi aliuliza kwa hamaki huku akianza kupambwa kwa tabasamu mwanana usoni kwake. Akachomoka pale alipo na kwenda kumkumbatia Agent Zero. “Merice. Kumbe upo dada yangu.” Akamtazama mwanadada Merice ambaye naye alichonga tabasamu lake.


“Nipo dada yangu.” Merice akajibu na wakati huo, wale wanasheria wengine walikumbwa na ahueni baada ya kuona Limasi kawatambua wale mabwana.


“Na wewe naye? Ni nani?” Akauliza Limasi. “Au ndio Idris kwa muonekano mwingine?” Akaendelea kuuliza lakini aliambulia tabasamu pekee kutoka kwa yule bwana ambaye alikuwa dereva wa lile gari lililowabeba.


“Hapana Limasi. Naitwa Agent Unknown, au The Last au Man….” Hakumaliza kauli yake ya kujitambulisha, Limasi, Agent Zero na Merice, wakamalizia kumtambulisha. “Sai…” Wote kwa pamoja walijikuta wakicheka baada ya kumaliza utambulisho huo.


“Yaonekana mimi ndio najulikana sana kuliko yeyote hapa.” Akaongea The Last huku katabasamu.


“Una majina mengi sana Bro. Yaani kama sijui linini.” Akaongea Agent Zero na kuzidi kuleta amani toka eneo lile ambapo kulikuwa ni ndani ya valanda kubwa mfano wa ghala, lakini mbele yake kulikuwa na ngazi ambazo ukizipanda, utakutana ofisi kadhaa.


“Unadhani mimi napenda haya majina dogo? Ni nchi yenu ndio inanipa haya majina. Na mimi nayakubali tu. Sasa nitafanyaje?” Akajibu The Last.


“Aaah! Nchi yetu au yetu wote. Na mfano nikikuuliza The Last ulipewa kipindi gani na kwa nini, utajibu vipi?” Akauliza Zero.


“Ishi! Sasa hilo nalo ni swali?” The Last akashangaa. “Nani asiyejua shughuli niliyoifanya kule Korea kwenye yale majina yaliyokuwa kwenye ukurasa wa hamsini na sita? Dunia nzima ilishituka na dunia nzima ilinipigia magoti na kuniabudu. Hapo ndipo jina la The Last lilitokea. Walishindwa kuniita jina la kuabudiwa kama MUNGU na nilikataa wasifanye hivyo. Waliniita mimi ndio alpha na omega, sijui na madudu gani mengine.” The Last aliongea. Na hadithi yake ilikuwa inawavuta wote wanaomsikiliza.

“Ila baadaye, ndipo Rais aliponiita na nikakukuta wewe umeanza kuiva.” Akamuangalia Agent Zero. “Na hapo nilipendekeza kwenye hizi misheni za ndani ya nchi, uwe unatumwa wewe na ukishindwa, ndipo mimi niitwe. Yaani niwe wa mwisho. Hapo ndipo Rais akaniita The Last. Nikaona linafaa sana kwangu kuliko kujiita majina ya kujibatiza U-MUNGU. Kwanza ni dhambi kubwa sana. Mimi sistahili kuitwa hata Malaika.” The Last aliongea na wote wakatabasamu kusikia historia ya jina lake.


“Na hili Agent Unknown.” Akauliza Limasi.


“Hilo hata dogo huyo anajua kwa nini naitwa Unknown.” Man’Sai akajibu huku anamtazama Agent Zero na kuchanua tabasamu. “Ila kwa kifupi, kwenye shirika letu, tunapewa majina ya kipelelezi. Zero ni namba ya kwanza kabisa. Na mle kazini kuna hadi Agent Sixty. Na anamajukumu yake ambayo hamna mwingine anayeweza. Sasa huyu alipopata jina la Zero, wakaona atakuwa kama juu yangu. Ikabidi waniite Unknown badala ya namba. Yaani mimi ni namba isiyojulikana. Dogo alinuna sana siku hiyo. Hahahaaa.” Man’Sai alihadithia na kucheka sana.


“Bro unazingua sasa. Ujue tutazichapa hapa hapa. Mimi sioni unachonitisha ujue.” Zero aliongea huku ni wazi tayari alionekana kukasirika.


“Dogo utakula nazi za kumwaga. Ohoo! Sema kwa sasa, tuangalie hili la mbele. Sisi tutamalizana tu!” Unknown ambaye naye alionekana mwenye kutaka kupandwa na hasira, alitumia busara zake huku wengine wakiwa kimya wakitazama zile tambo.


“Na Id yupo wapi?” Akauliza Limasi baada ya utani wa hapa na pale kuchukua nafasi kwa muda mrefu.


“Na tulipata taarifa mlikufa kwenye ule mlipuko wa nyuklia pale New York, vipi tena?” Buju ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu, aliwauliza.


“Twendeni hivi.” Masai aliwaambia huku akiwaonyesha kule kwenye ofisi zao. “Siku ile ilikuwa kweli tupoteze uhai, lakini tunamshukuru kijana wetu huyu.” Alimuoneshea kidole Zero na wakati huo wakiwa wanazidi kuzielekea zile ngazi. Akaanza kusimulia kilichotokea siku ile.


ILIVYOKUWA.


“Siyo kosa lako Id. Umefanya kilicho bora.” The Last akamwambia huku akimgonga gonga begani.

Wakiwa pale chini, waliangaliana wote kwa pamoja na wakati huo, mlio mkubwa ulisikika. Ni miili ya wale wachezaji ililipuka na moto mkubwa ukaanza kushuka ardhini kutokea juu.


“Tunakufa bila kumaliza kazi.” Idris alinong’ona.


“Wapo watakayoimaliza Brother. Wapo kila mah…” Hakumaliza sentensi yake The Last, mara masikioni mwake zilisikika sauti za nzi wengi sana. “Pumbavu Zero.” Akatukana baada ya kugundua ni Agent Zero ndiye anayetumia kitambulisho hicho kuja eneo fulani.

Na hapohapo, walifunikwa na vyuma na wakiwa ndani ya vyuma hivyo, taa zikawaka na kwa pamoja waliweza kumuona Agent Zero akiwa nao kakaa mkao kama anakula ubwabwa.


“Vipi wazee. Mnaonekana mlikwishakata tamaa kabisa ya kuishi. Hata wewe roboti.” Akaongea Zero na wakati huo ukasikika mtikisiko mkubwa zaidi na hata mle ndani pakaongezeka joto. Zero akabonyeza saa yake, na hali ya ubaridi ikaingia kwenye vile vyuma.


“Sasa mbona umechelewa kuja?” Akauliza The Last huku akikaa sawa ndani ya vyuma vile ambavyo vilijenga nyumba kubwa unayoweza kujitanua utakavyo.


“Huu ulikuwa siyo ugomvi wangu kaka. Kwa hiyo nilikaa pembeni nikiwatizama mnavyopambana. Ila nilipoona mmeamua kukubali kushindwa, ndipo nikaja kuwasaidia.” Akajibu Zero. “Au nimefanya kosa?” Akawauliza.


“Hamna Soldier. Umefanya vema sana.” Akajibu Idris.


“Ahsante Kaka.” Akashukuru Zero na kumuangalia Unknown ambaye naye alimtazama tu.


“Ila umechelewa.” Akajibu Unknown. Merice alikuwa bado hayupo sawa kifikra.


“Tutakesha hapa. Ngoja niyaache hayo.” Zero aliongea na kubonyeza tena saa yake. “Tunaondoka hapa.” Akatoa taarifa na hali ya nyumba ile ya chuma, ilionekana wazi inanyanyuka. Na baada ya kunyanyuka, Zero akabofya tena saa yake, vile vyuma vikapotea na wote wakawa wanaona hadi nje lakini bado wapo angani. Ni kama walikuwa ndani ya kioo. Hapo waliona jinsi Jiji la New York lilivyoweza kuathiliwa na ule mlipuko wa wale wachezaji.


“Hatari sana hawa watu.” Aliongea The Last na nyumba yao ikazidi kuondoka eneo lile.

****

“Ndivyo tulivyopona wenzenu.” The Last aliongea wakati huo walikuwa wamefika kwenye mlango mmoja na kuufungua.


“Idris.” Limasi alipiga ukelele na kwenda kumrukia Idris ambaye alimdaka na kisha wakakutanisha midomo yao na kubadilishana hisia fulani ambazo ni ngumu kuzielezea.


“Pole sana mama yangu. Naona jinsi unavyohangaika. Lakini sasa, hutoweza kuhangaika. Tumenunua mchezo wote.” Idris aliongea huku bado kambeba mkewe, ambaye badala ya kujibu, alilala kabisa kwenye bega la Idris.


“Mama Kijacho tutachelewa kesi.” Buju ilibidi awatoe wale wapenzi kwenye hisia zao za hatari.


“Kesi hiyo, nadhani leo ndio mwisho. Na inavyoonekana, yule hakimu, wamemuingizia madudu yao.” Aliongea The Last.


“Madudu gani?” Mwanasheria mkuu, Reek, aliuliza kwa hamaki.


“Wale mahakimu, huwa hawakubali rushwa kirahisi na ni mahakimu wanaoaminiwa na dunia nzima. Lakini kuna kemikali fulani wananusishwa bila wao kujua. Hizo kemikali ni kama uchawi, utafanya kile ambacho wanataka wao. Ama la! Basi alitekwa bila yeye kujijua. Yaani kuna njia za kutekwa. Unaweza ukawa umelala ndani, wakakupulizia madawa, na kisha wakakupandikiza madudu yao mwilini. Mara nyingi huwa madudu ya Kisayansi. Yanaungwa kwenye kompyuta, na kisha wanakuendesha watakavyo.” Akajibu The Last.


“Kwa hiyo itakuwaje?” Akauliza mwanasheria.


“Tuachieni sisi. Nyie nendeni mkamalize kesi.” Akajibu The Last. “Na yule Pox, muamini tu. Hana shida. Ni mtu mzuri lakini bado muoga.” Akaongeza na Buju alionekana kushusha pumzi.


“Tuaomba turudi sasa. Maana walitupa nusu saa. Na hadi sasa, zimebaki dakika kumi tu.” Faruq aliongea.


“Tutawalinda. Hamna tena damu kumwagika. Labda yao.” Idris aliongea na wote wakikumbwa na ahueni na hari mpya.


“Zero. Fanya yako basi.” Unknown aliongea na Zero akabetua midomo yake na kubofya saa yake. Vyuma vingi vyenye sauti ya nzi, vilitokea na kutengeza nyumba ileile ambayo iliwaokoa kwenye mlipuko wa wale wachezaji. Wanasheria wakapanda. Na Zero akabonyeza tena saa yake, vyuma vikawa vioo. Wakaagwa na vioo vile vikapotea ghafla eneo lile.

****

Limasi pamoja na wenzake, walijikuta waesimama nje ya mahakama waliyokuwepo na geti la mahakama ile lilikuwa wazi huku watu wengi wakizidi kurudi ndani yake.


“Twendeni.” Mwanasheria mkuu aliongea na wote wakaanza kwenda ndani ya mahakama ile kwa kujiamini kuliko hapo mwanzo. Pox aliwaona kwa mbali na kujikuta akiwakimbilia na kuanza kuwauliza maswali kadhaa lakini hakupata jibu wala kusikia sauti za wale vijana waliyokuwa wamedhamiria kumaliza kesi waliyoianza.


Wakaingia ndani ya mahakama na watu walishangaa kwa sababu zilibaki dakika tatu pekee ili kesi ile kuisha. Kama wasingeonekana, basi ushindi wa kesi angepewa Uzo. Lakini wanasheria walioshitaki, waliingia ndani ya mahakama na watu wote walitabasamu kuwaona tena. Kesi ikaanza kuunguruma na safari hii, vijana waliyoongozwa na Limasi, waliweza kufanya kazi kubwa kuuliza upande wa mahakama pamoja na watuhumiwa.


Ilikuwa ni mshike mshike hasa pale video zile za mauaji zilipoombwa ziwekwe hadharani ili kila mmoja azione na waseme kama kweli kulikuwa kuna kitu walichokidanganya. Video zile zikawekwa na watu waliokuwepo, waliweza kuona kila kitu na walishangaa kwa nini hakimu alikuwa mgumu kuukubali ule ushahidi. Kesi iliendelea kwa masaa matatu zaidi. Hali ilikuwa ngumu kwa Uzo na wenzake.


“Namaliza kesi hii, kwa kumuachia huru Uzo…” Sauti ya hakimu ilisikika na miguno ndani ya mahakama ilisikika kwa uamuzi ule ambao uliamuriwa na baraza lote la mahakama. Na hata baada ya minong’ono, hakimu alisisitiza kumuachia huru Uzo na nyundo yake ikatua mezani kuonyesha kesi imeisha.




Uzo akawatazama wale wanasheria waliyomshitaki yeye pamoja na serikali yake kwa kosa la kuunda wanajeshi wa C.O.D.EX. Wakati anawatazama, askari wa mahakamani walikuwa wanamfungua pingu na yeye taratibu akachanua tabasamu hasa pale alipoona uso wa Limasi ukimuangalia kwa macho ya chuki.


Akatoka kizimbani huku anasugua mikono yako sehemu ambazo pingu zilipita. Akasogea hadi vilipokuwepo viti walivyokalia wakina Limasi na kuwatazama.


“Hatujawahi kushindwa. Huwa hatushindwi. Subirini zamu yenu.” Maneno yalimtoka Uzo na kuanza kuondoka ndani ya mahakama ile akifuatiwa na watu karibuni saba waliokuwa wanamtetea pamoja na wengine walioshitakiwa naye.


“Anadhani ameshinda. Subiri aone.” Akanong’ona kwa kisirani Limasi. Kisha baada ya hapo, wakakusanya vitu vyao walivyokuja navyo na wao wakutoka nje ya mahakama na hapo wakakutana na jopo kubwa la waandishi wa habari likimuhoji Uzo.


“Unadhani haki imetendeka kwa ulichokifanya?” Akauliza mwandishi wa habari mmoja wa kiume ambaye alimuelekezea kipaza sauti mdomoni.


“Haki?... Haki?...” Akauliza mara kadhaa na waandishi wa habari wote walikuwa wanasubiri ajibu swali hilo. “Haki haipo kila mahali. Kwangu, kwako na hata kwa hao walinionishitaki. Haki ipo sehemu moja tu.” Akaongea Uzo.


“Ipo wapi?” Akauliza yule mwandishi wa habari.


“Ipo kwenye kifo. Hio ndiyo haki pekee ambayo kila mwanadamu aliahidiwa kuwa atakutana nayo. Tofauti na hapo, hamna haki nyingine.” Akajibu Uzo.


“Kifo.” Akaongea hilo neno yule mwandishi wa habari. “Sawa mkuu.” Akamaliza swali lake na akaanza kuwapangua watu waliopo pale tayari kwa kuondoka na wakati huo, macho ya Limasi na wenzake, yalimuelekea Uzo hasa kwa maneno machafu aliyokuwa anayotoa dhidi yao.


“Tuondokeni hapa. Mnajua kuwa hatujamuaga wala kumuona Brighita tangu auawe?” Akasema Buju na wengine wakaona hilo jambo ndilo la busara kuliko kuendelea kumsikiliza Uzo.


Wakati wanashuka ngazi, wakiwa tayari wamewapa mgongo waandishi wa habari pamoja na Uzo, mara walisikia kelele kubwa toka kwa wale waandishi wa habari. Waligeuka na hapo walimuona Uzo akiwa anagalagala na kubingirita kwenye ngazi. Yaani alikuwa anazishuka ngazi nyingi za mahakama huku anagalagala na kulikamata koo lake. Alifika hadi kwenye miguu ya wanasheria wale na kuacha kubiringita ila alikuwa kakamata koo lake na damu zilimtoka machoni na puani na alionekana wazi pumzi zilikuwa hazimtoshi.


“Haki ya kweli ni moja tu!” Aliongea Buju.


“Kifo.” Limasi naye alimalizia kauli ambayo ni yeye Uzo ndiye aliitoa kwenye mahojiano ya yule mwandishi aliyeondoka baada ya kumaliza swali lake.

Na hata baada ya kuitikia kauli hiyo aliyoianzisha Buju, Limasi na wenzake hawakuwa na msaada kwa Uzo bali kuondoka na kumuacha Uzo akiwa kabadilika macho na kuwa meusi kama mkaa.


Gari moja la kitajiri, lenye muonekano kama hiace, lilifika haraka eneo lile na watu wawili wenye suti nyeusi, walifika haraka na kumnyayua Uzo kutoka pale alipokuwa ametulia na kumuingiza kwenye gari.


“Tumemchukua Jenero. Ila hali yake si nzuri kabisa.” Mmoja wa wale mabwana waliomchukua Uzo, aliongea kwenye simu wakati gari hilo likianza kuondoka mahali pale. Upande wa pili ukamjibu na yeye akaitikia sawa na kukata simu.


“Jenero kasema anamtaka akiwa hai. Hivyo kasema apigwe sindano ya T-Plus.” Akaongea yule bwana alichoambiwa na mkuu wake wa kazi na bwana mmoja bila kuchelewa, alifungua mkoba wa huduma ya kwanza na kuchomoa dawa pamoja na sindano.

T-Plus ni dawa ya sindano ambayo inaweza kumrudishia mtu mapigo ya moyo na msukumo wa damu kwa siku tatu mfululizo. Na baada ya hapo, mgonjwa anaweza kufa kama atakosa tiba ya kilichotaka kumuua. Sindano hiyo, huchomwa mara moja mwilini.

Uzo alikuwa anapokea sindano hiyo na wakati huo, gari alilowekwa, lilikuwa linakata mitaa kwa kasi ya kushangaza wananchi. Uzo akadungwa sindano ya T-Plus na mara macho yake yakaanza kuwa masafi na baadaye alipumua pumzi ndefu.


“Pumbavu sana.” Uzo aliongea kwa shida huku akijaribu kuinuka lakini alirudishwa chini ili aendelee kupumzika.


“Nini kilitokea Mkuu.” Akaulizwa Uzo na mmoja wa wale waliokuwa wamembeba.


“Kuna mwandishi mmoja nadhani alikuja na sumu. Aliponiuliza vimaswali kadhaa, akaondoka. Nadhani huyo ndio sababu.” Akajibu Uzo.

Pox Maxmilian alipewa jukumu la kumuua Uzo atakapotoka mahakamani. Alivaa sura nyingine katika uso wake na kisha kuchukua kipaza sauti na kukipaza sumu ambayo inaweza kumdhuru mtu kama ikifika sentimita moja ya pua yake. Pox alijitahidi kusogeza kipaza sauti chake karibu na pua ya Uzo na alifanikiwa kwa asilimia kubwa. Ndipo baada ya hapo, akaondoka haraka eneo lile akijua kuwa, naye kaivuta sumu ile sababu alikuwa anamuuliza maswali Uzo kwa kutumia kipaza sauti hicho hicho.

Baada ya kuondoka, alielekea kwenye gari lake na kutoa sindano ambayo ilikuwa ni dawa pekee ya kuondoa sumu ile iwezayo kuuchukua uhai wa binadamu kwa dakika tatu pekee. Na ndicho kilimkuta Uzo.

“Pumbavu yule mbwa. Labda nisipone.” Alizidi kutukana Uzo huku akijaribu kujizoa zoa tayari kwa kuinuka.


Lakini kabla hajaamka vema, gari lao lilisimama ghafla na dereva akabaki anatizama kile ambacho anakiona mbele yake.


“Nini tena?” Akauliza mwenzake ambaye alikuwa sehemu ya nyuma.


“C.O.D.EX” Akajibu dereva kile abacho anakiona mbele yake. Alikuwa Idris pamoja na Merice wakiwa wamevalia nguo za jeshi la Marekani na mikono yao wakiifunga kwa nyuma.

Wote waliokuwa kwenye gari wakainuka na kutazama kile ambacho wameambiwa kipo mbele yao. Na wao wakashuhudia ile mizimu waliyodhani ilishakuwa majivu. Uzo naye kwa kujikakamua, aliweza kuinuka na kutazama kile ambacho wenzake wanakitazama.


“Hamna kama Dokta Ice.” Aliongea maneno hayo ya kumsifu Dokta Ice na hapo Idris alitoa mikono yake nyuma na kurusha vichuma vilivyokuwa kwa mfano wa vifuniko vidogo vya kopo la mafuta. Vikaenda kunata kwenye gari lile na baada ya hapo, Merice alichomoa rimoti iliyoundwa kwa mfano wa peni ya kubonyeza. Naye bila hiyana, akaibonyeza na mlipuko mkubwa ukasikika eneo lile. Gari liliruka juu na kutua chini na kuendelea kuungua hadi lilipochoka kuungua.


Waokoaji mbalimbali walikuja kutaka kusaidia lakini moto ambao ulikuwa unawaka kwenye gari lile, hamna ambaye aliweza kuusimamisha hadi pale kikosi maalumu cha kuzima moto kilipokuja na kuanza kazi ya kuokoa maiti zilizokuwepo ndani ya gari lile.

****

“Pumbavu hawa. Wamemuua Uzo.” Alibwata kwenye simu Bwana Microchip Digtec, ambaye ndiye wakala mkuu wa kununua dhana za C.O.D.EX na kuzisambaza nchi nyingine. “Tunafanyaje sasa Jenero?” Aliuliza tena kwenye simu akiwa ofisini kwake. “Sawa. Nafanya hivyo mkuu.” Akajibu haraka na kukata simu.


“Boss, kuna mgeni wako hapa nje.” Mwadada mwenye rangi nyeusi lakini anaasili ya watu wa Asia hasa Korea, China na Japan, aliingia ndani na kumpa taarifa tajiri wake aliyekuwa kawehuka baada ya kugundua kuwa Uzo na wanajeshi waliotumwa kumchukua, wamepoteza uhai baada ya gari lao kulipuliwa.


“Mwambie sipokei wageni kwa sasa.” Akajibu kwa hasira.


“Tayari nimeingia mkuu wangu.” Pox Max alikuwa ameingia ndani ya ofisi ya Microchip na kumtaka yule mwanadada aondoke mle ndani. Na baada ya kuondoka, akafunga mlango vema na kwenda hadi kilipokuwa kiti cha wageni, akakaa hapo. “Nadhani unanijua na wajua nimefuata nini.” Akaongea Pox.


“Ulichokifuata, hapa hakipo.” Akajibu kwa kiburi Microchip Digteck.


“Ohoo! Hiyo nzuri, lakini na wenzangu hapa wanaweza kunisaidia ujibu.” Pox alipoongea hayo, Idris pamoja na Merice waliingia mle ndani kama mizimu kwani walionekana wapo ndani bila milango wala madirisha kufunguliwa.


“C.O.D.EX Soldiers.” Akaongea Microchip.


“Hapana. Dokta Ice Soldiers.” Merice akamjibu Digteck na kupotea tena kisha akatokea nyuma yake anamkanda mabega. Microchip aliishiwa nguvu na kuanza kutetemeka kama mgonjwa wa tetenasi.


“Wangapi wanashiriki kuwaua wale wanasheria?” Akauliza Pox huku kakunja mguu wake kwa kuuweka juu ya paja lingine.


“Sifahamu hilo Pox.” Akajibu kwa mtetemo na hapohapo Merice akayabonyeza mabega yake kwa nguvu na kumfanya Microchip apige ukelele wa nguvu. Na hata kabla kelele hizo hazijaenda mbali, Idris alitoa upepo kwenye mkono wake na sauti ya Microchip ikazama humo.


“Huwezi fanya lolote ndugu yangu. Jamaa uliyekuwa unacheza na mke wake, anaweza kuzuia sauti yako isifike popote. Ni bora kuongea tu kuliko kuanza kukupiga sindano za kukufanya uongee.” Pox aliongea na wakati huo Idris alitoa sindano na dawa na kuanza kuinyonya dawa iliyopo humo kwa manjonjo. Kisha kabonyeza dawa ile iliyojaa ndani ya sindano na kuirusha kwa juu kidogo.


“Inaitwa ‘More Damage’, ni sindano inayoweza kuuubongonyoa ubongo wako na kuwa vipande vipande na kisha kuufanya useme chochote tutakachokuuliza. Sindano hii ilitengenezwa Ujerumani katika vita vikuu vya pili vya dunia ili kuwafanya mateka wao waseme lolote watakaloulizwa. Na sasa, ipo mikononi mwetu.” Pox aliongea na Idris alianza kwenda pale alipokuwa kawekwa Microchip.


“Mipango imesukwa na Ortis Morgan na Burden Hussein. Hawa ndio tulipanga nao kuwaua hao wanasheria na tuliagizwa na Jenero.” Akajibu Microchip kwa haraka. “Naomba myanusuru maisha yangu.” Akaendelea.


“Sawa. Tutaanusuru maisha yako. Kama ulivyoyanusuru ya wale wanasheria.” Pox alijibu na kumpa ishara Merice ambaye mkono wake ulibadilika ghafla na kuwa kisu kikali, kisha kuichana vibaya shingo ya Microchip.


Baada ya tukio hilo, Merice na Idris walipotea ghafla na kumuacha Pox akitoka ofisini peke yake ambapo pale mapokezi alikutana na yule sekretali wa Microchip.


“Dada unakazi nyingine a kufanya tofauti na hiyo hapo?”Pox akamuuliza yule Sekretali.


“Tofauti na hapa, sina kwingine.” Akajibiwa Pox Maxmilian.


“”Kwa lolote, nitafute kwa namba hizi.” Akamuwekea kadi ya biashara mezani kwake ambapo kadi hiyo ilionesha mawasiliano ya Pox na anapofanya kazi pamoja na anapopatikana. “Unaweza kuwa sekretali wangu baada ya hapa kufungwa.” Akamwambia yule dada aliyeonekana hana ajualo kwa kilichotokea. “Boss wako tayari ni marehemu.” Pox akamaliza na kumuacha yule mwanadada akiwa katika taharuki.


Usiku uleule ambao mchana wake, Digteck alikutwa amekufa kwenye ofisi yake, ndio ulikuwa usiku mwingine wa maruweruwe kwa mtu aliyeitwa Ortis Morgan.

Akiwa katika hotel moja ya nyota tano katika Jiji la Amsterdam, aliweza kunywa na kula kila alichoona kinafaa kuliwa huku walinzi kadhaa wakionekana wakiangalia huku na huko kama kuboresha hali ya usalama.




Baada ya furaha ya hapa na pale, ndipo aliamua kwenda kujipumzisha mwili wake huku walinzi wake wakimfuata kwa nyuma. Ndani ya lift waliokuwa wameipanda kuelekea ghorofa ya juu, walikuwepo wao pekee na ghafla lift ile ilisimama na walinzi wote wakaweka mikono yao kwenye kiuno tayari kwa kuchomoa bastola lakini lift ile ikarudi katika hali yake lakini ikaanza kuelekea juu kwa kasi ya ajabu na kukataa kabisa kutulia japo walinzi walihangaika kubonyeza vitufe vya kuisimamisha. Lift ilienda kusimama kwenye ghorofa ya thelathini lakini bado haikufunguka milango.


“Show time.” Pox aliongea kwenye chumba cha kuendeshea mitambo kwa kompyuta na kisha akabonyeza ‘enter’ kwenye kiparaza cha kompyuta mojawapo, na lift aliyokuwepo Ortis ikaanza kushuka chini kwa kasi na baadae kugonga chini vibaya sana. Mshindo mkubwa ukasikika na lift ile ilikuwa imejibonyeza vibaya na hata wahusika waliokuwa ndani yake, walikuwa wote ni maiti.


Na wakati hayo yanaendelea, upande mwingine wa nchi ya Uholanzi, bwana Hussein Burden, alikuwa kawekwa katikati na Merice pamoja na Idris.


“Watu uliowatuma wawaue wale wanasheria, wanapatikana wapi?” Akauliza Merice kwa hasira.


“Mnadhani mnaweza kuwamaliza F.O.F?” Burden aliuliza kwa umakini mkubwa.


“Ohoo.. Kwa hiyo ni wanajeshi wa Jenero.” Idris aliingilia maongezi na kutabasamu.


“Hata kama wangekuwa wa nani, lakini hao hamuwawezi, bora muanze maisha yenu tu.” Burden akazidisha utamu wa maongezi.


“Sawa. Kwa kheri Burden” Merice hakusubiri majibu ya kwa heri yake, akamnyonga Burden akiwa katika chumba chake cha kufanyia sala.


“F. O. F” Idris akaongea kifupi cha maneno aliyoyasikia kwa Burden na ara kadhaa toka kwa Jenero. Na akakumbuka wale wanajeshi maroboti waliojiunga kule makao makuu ya C.O.D.EX.


“Future Of Forever.” Merice akatamka kirefu cha maneno aliyotaja Idris kwa kifupi.


“Hatari nyingine inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.” Idris akaweka bayana wasiwasi wake.


“Tunatakiwa kusimamisha huu mpango Id.” Merice alitoa ushauri.


“Kivipi sasa. Hayo mbona sisi hayatuhusu?” Idris akamtazama Merice.


“Ni nchi yetu hii Idris. Tunatakiwa kuikomboa katika majanga haya.”


“Mimi kwetu Tanzania. Huku nyie wazungu hata siwaelewi.” Merice akasikitika kidogo kwa maneno hayo.


“Idris,” Akamuita yule mwanajeshi kwa upole. “Yawezekana ni kwenu huko. Lakini vipi wakasambaza teknolojia hiyo hadi huko? Au ni vipi wakamchukua na mtoto wako naye akawa F.O.F?” Merice akaongea kwa upole wa kike na maneno hayo yakamuingia Idris. “Tuwatafute hawa na tuwaangamize. The Last, Zero na Pox, nina imani watatusaidia japo kidogo tu.”


“Upo sahihi Merice. Tuwasiliane na hawa mabwana ili tuone kama wataweza. Najua Man’Sai hawezi kukataa maana anapambana na wabaya wa teknolojia wao. Ila Zero na Pox, watatusaidia kufika tu huko. Vitakavyobakia, ni sisi na hao F.O.F” Idris akamaliza na maongezi mengine yakaendelea huku wakiwa tayari wamekwishatoka kule walipofanya mauaji.

*****


Mauaji mbalimbali yaliendelea kufanyika kwa wote ambao walihusika na kutengeneza wanajeshi wa C.O.D.EX . Na baada ya mwezi mzima nchi ya Marekani ilikuwa bado haijamjua ni nani aliyehusika na mauaji hayo. Mtu pekee ambaye alishindikana kuuawa, alikuwa ni Jenero ambaye anamamlaka ya kuunda wanajeshi wapya wa F.O.F.


Idris akiwa katika fukwe za Cabana huko Brazil, alikuwa anamuangalia kwa mbali Limasi katika fukwe hizo akiwa anafuraha tele moyoni mwake na tumbo lake lilikuwa tayari limekuwa kubwa zaidi. Idris akamfuata Limasi pale alipo na kukaa pembeni yake na kumshika kiuno.


“Lim.” Akamuita Limasi ambaye alikuwa kakaa chni ya mwamvuli wa ufukweni huku kavaa mawani myeusi ya jua.


“Yes Honey.” Akaitika kwa mahaba.




“Baada ya kujifungua, fungua ile kesi tena. Nadhani tutashinda safari hii. Uongozi wote mbovu tayari tumekwishauondoa.” Idris akamueleza mpenzi wake dhamira yake.


“Ahsante sana mume wangu.” Limasi aliongea kwa furaha na kumkumbatia Idris.


“Nilifanya kosa sana kukukataza usiifungue tena. Na nikaona ni kiasi gani uliumia, ila leo, nakupa ruhusa ya kuifungua tena.” Idris akaongeza na Limasi akazidi kumkumbatia.


“Hukufanya kosa. Nilielewa kuwa unatakiwa kwanza kusafisha njia ya sisi kushinda kesi ile. Na nashukuru kwa hilo Baba Nanii.” Limasi akaongea na utani ukaanza hapohapo ukisindikizwa na mabusu motomoto.

Wakati wapo katika hali hiyo, masikioni mwao walisikia sauti za nzi wengi sana na wote kwa pamoja walishituka na kubwata kwa kulitaja jina la Agent Zero. Walipotazama mbele yao, walimuona Agent Zero na The Last ambaye alivalia fulana iliyokatwa mikono bila mpangilio maalum.


“Mlidhani mmejificha?” Akauliza Agent Zero. Na The Last akabaki anacheka baada ya swali lile.


“Mnataka nini wazee?” Akauliza Idris huku akimruhusu Limasi aondoke eneo lile na mwanadada yule aliondoka huku akiwapungia mkono Watanzania wenzake na tabasamu mwanana likimchanua.


“Nasikia ulimpiga huyu dogo nusu ya kumuua. Na mimi siku ile ukataka kunifanya vilevile ukiwa na mkeo Merice.” Akaongea The Last.


“Ndio maana yake. Wote mlipokea kichapo nyie.’ Akajibu Idris huku katabasamu.


“Sasa ni zamu yetu kukupa kichapo.” The Last akaongea huku ananyoosha mikono yake.

Na mara Idris akapotea pale alipo na kutokeza nyuma ya Agent Zero na kutaka kumpiga ngumi kali ya kisogoni lakini mara nguo za Zero zikageuka na kuwa vyuma vingi vilivyomdaka Idris na kumvaa kama nguo. Hapo nao wakapata nafasi na kuanza kumtwanga Idris ambaye kwa hasira, aliwaka moto na kuyayusha vile vyuma lakini bado aliendelea kurushiwa vyuma vingine na kuendelea kupigwa na vijana wa Kitanzania.


“Omba msamaha dogo.” Akaongea The Last huku anampiga ngumi za shavu na wakati huo Limasi alikuwa amekwishafika kwenye nyumba ambayo walipangisha na kutulia huko akijua wazi kuwa watu wale walikuwa wanamaongezi yao hivyo hakupaswa sana kuyashuhudia.


“Najua nyie mkikamataga, hamuachii. Mkimbana tu mtu, atajuta.” Leo mmeshinda kwangu, ila bado hamjaishinda hii vita.” Idris aliongea huku anatazama nyuma ya wakina The Last, nao wakageuka nyuma na kukutana na uso wa Merice.


“Mmetukumbuka eeh?” Merice akaongea na kisha kupotea ghafla. Alipotokeza, alikuwa mbele ya The Last, akamfyatua kwa konde zito lililompaisha hewani lakini wakati yupo hewani, The Last alichomoa kamba fulani mikononi mwake na kwenda kukaba shingo ya Merice na kamba ile kila Merice alipotaka kutoroka, ilizidi kumkaba. Mwanadada akatulia.


“Tumewaletea teknolojia mpya. Tulikuwa tunaijaribu, na kweli inafanya kazi.” The Last aliongea huku katabasamu na kuwaachia wakina Idris. Wote kwa pamoja wakakutana na kucheka sana.


“Zamu ya Jenero.” Wote wakaongea na kuweka mikono yao pamoja kuonyesha muunganiko wa kwenda kumuhangamiza Jenero ambaye yeye alisimamia jeshi jipya la F.O.F.


“Ila mnajua alipo au mmeongea tu kuwa ni zamu yake?” Akauliza Merice.


“Nyie si mmesema mnajua alipo.” Akaongea kwa mshangao Zero.


“Ndio tunajua na Pox kathibitisha hilo. Lakini kuna taarifa mbaya kuhusu eneo analopatikana.” Akaongea Merice.


“Taarifa ipi sasa.” The Last akadakia.


“Yupo Cuba.” The Last na Zero wakawa wa kwanza kupokea kauli hiyo kwa mshangao na masikitiko.


“Sasa Cuba wamepokeaje hawa wajinga?” Akauliza The Last.


“Ni ubabe tu umetumika hapo. Hamna ambalo naweza sema halijatumia ubabe.” Maneno hayo yakapoteza hali za The Last na Zero na kujikuta wanakaa kwenye ule mwamvuli aliyokuwa kakaa Limasi.


“Mimi nikienda kuwaomba wale wenzangu wanisaidie The Lens kwenda naye Cuba, sidhani kama wataniruhusu hata kama nitawapa sababu zenye mashiko.” The Last akaweka bayana hali ambayo atakutana nayo kwenye shirika lake la kipelelezi ambalo analitumikia. “Cuba na China ni marafiki sana. Hawawezi kuniruhusu.” Akaendelea The Last.


“Ila na wewe kwa nini uliamua kwenda kufanya kazi China?” Akauliza Merice kwa utani ndani yake.


“Ni shirika letu la Tanzania ndilo lilinitaka nikafanye nao huko. Hivyo kule mimi nasaidia nchi yangu kupitia shirika la siri la kipelelezi la China. Na wanatusaidia sana tu. Na huwa hawanikatazi nikitaka kwenda kuisaidia nchi yangu.” Akajibu na wote kwa pamoja wakatulia wakifikiria utatuzi.


“Ila nadhani kuna njia nyingine.” Idris akaanzisha tena maongezi na wote wakakaa kitako kumsikiliza. “Mnaweza kutusaidia sisi kuingia ndani tu. Kisha nyie mkarudi makwenu. Ama la! Tunaweza kumuhangamiza Jenero akija Marekani.” Akaweka mezani wazo lake.


“Kumuhangamiza Jenero wala si njia ya kuwasimamisha F.O.F. Ila hiyo ya kuwasindikiza, nadhani ni bora zaidi. Ila kwa maelezo ya wanaowajua hao F.O.F sidhani kama peke yenu mtaweza.” Zero aliongea na wote wakatulia wakitafakari kwa muda.


“Mimi nadhani tusindikizeni Cuba. Tupeni na vifaa vyenu. Kazi yenu itakwisha nje. Msiingie ndani maana huko tunaweza kulipua, na nyie kama mtaonekana, basi kesi itawarudia na mtaingiza matatizoni nchi zenu na Cuba. Bora twende wenyewe.” Idris akamaliza maneno hayo na The Last pamoja na Zero, hawakuwa na jinsi.

****

CUBA SAA 3:30 USIKU


Katika pori moja kubwa Idris na Merice wanatua kwa parachuti kimyakimya, na kuanza kulikusanya parachuti hilo na kulificha kwenye vichaka vilivyopo maeneo hayo. Wawili wale wakiwa wamevalia sare za jeshi zenye mabaka meusi na kijani, waliangaza huku na huko na kisha kubonyeza saa zao.


“Tayari tupo eneo la tukio.” Idris aliongea na sauti ikamjibu kuwa imemsikia vema. Baada ya sauti hiyo, Idris na Merice wakaanza kukimbilia lilipokuwepo jengo kubwa sana lenye ulinzi mkali wa senyenge zenye umeme pamoja na taa kali zilizokuwa zinawaka usiku kucha.


Wakati hayo yanajiri kwa Idris na Merice, upande mwingine, The Last na Zero wakiwa kwenye mavazi yao ya jeshi na usoni wamejipaka rangi nyeusi, walikuwa juu ya miti huku wamekamata bunduki za ndefu kwa ajili ya udunguaji. Walikuwa wameachana kwa umbali wa mita mia mbili kila mmoja na wote bunduki zao zilieelekea kwenye jumba lile ambalo Merice na Idris wanakimbilia.


“Kuna walinzi nane chini ya jengo. Hao wanatembea tu chini.” The Last alitoa taarifa ambayo iliwafikia washirika wake wote.


“Juu wapo kumi. Ghorofa la kwanza wapo wanne na la pili wapo wanne. Kwenye vile vibanda vya taa, viwili, wapo wawili.” Agent Zero akatoa taarifa huku anaendelea kuchungulia kwenye lens ya bunduki yake.


“Chukua wa juu, mimi nitachukua wa chini.” The Last akaongea na wote wakakubaliana. Merice na Idris wakafika kwenye tuta moja kubwa ambalo lipo mita chache kabla ya kuufikia uzio wa jengo walilopanga kwenda. Wajibanza kwenye tuta hilo wakisubiri The Last na Zero wasafishe njia.


Baada ya dakika moja, walinzi waliochukua jukumu la ulinzi eneo lile, walikuwa wanapokea risasi za kichwa ambazo zilitoka bila mlio wowote. Na kila zilipotua vichwani mwao, vichwa vyao vilipasuka kimyakimya.


“Papo safi sasa.” Alitoa taarifa The Last na Idris pamoja na Merice wakaanza kukimbilia zilipo senyenge za jengo lile na walipofika, wakabandika vitu fulani ambavyo vilifanya senyenge ile itokwe na umeme. Idris pamoja na Merice wakakata haraka nyavu na kisha wakaingia ndani kwa umakini mkubwa na kushuhudia miili kadhaa ikiwa imelala bila vichwa.


Walifika chini ya ghorofa na kutazama juu. Kisha wakabonyeza saa zao na kuelekeza mikono hiyo yenye saa juu. Kamba moja ndefu ilichomoka toka kwenye saa zao na kwenda kunasa kwenye ghoofa ya pili na kisha ikaanza kuwavuta toka chini hadi huko juu.


“Zero wewe ni noma.” Idris alimfia Agent Zero kwa ile teknolojia ya saa yenye kamba. Zero akacheka kwa tambo.

Walipofika ghorofa ya pili, waliingia kwenye uzio wake na kutizama ndani ambapo waliweza kushuhudia mitambo mingi ambayo ilikuwa inatengeneza wanajeshi kwa haraka kupita malelezo. Ndani ya dakika moja, wanajeshi watano walitolewa ndani ya mitambo wakiwa katika hali ya utayari wa mapambano. Idris na Merice wakawa wanatizama hali ile wasiamini kama wapo dunia hii au nyingine.


Wanajeshi walitapakaa kila mahali na walikuwa hawana idadi halisi. Vyumba vilipewa majina na wanajeshi waliingia humo na kupuliziwa dawa ambayo iliwafanya walale. Vilikuwa ni vyumba vya mfano wa kioo au kama lift jinsi vilivyokaa. Vilitaakaa jengo zima. Idris akashusha pumzi asijue afanyaje.


JE NINI KITATOKEA HAPO?

WATAPONA WATU HAWA?

AU WATALIPUA HILO ENEO.

MIMI NA WEWE HATUJUI.

TUKUTANE TENA SIKU ZINGINE ILI TUJUE HUU MSALA ULIISHAJE.

KAZI BADO INAANDALIWA. ITAKUJA IKIWA TAYARI.


MWISHO WA C.O.D.EX 4.


0 comments:

Post a Comment

Blog