Search This Blog

Thursday 29 December 2022

ZAWADI YA USHINDI - 3

 

 Simulizi : Zawadi Ya Ushindi

Sehemu Ya Tatu (3)







lisimtawale. Hofu. Naam, hakuipenda hofu. Kwa ujumla, aliichukia akijua kuwa kuna ujirani mkubwa kati ya hofu na mauti. Hata hivyo, uwezo kamili wa kuishinda ulikuwa ukimtokea kwa vipindi tu. Si sasa ambapo giza lilimfunika na dunia kutulia kama inayoomboleza kifo chake. Si sasa ambapo alikuwa na bunduki mkononi hajui adui yu wapi na iwapo angeweza kweli kumjua adui huyo kabla hajafa yeye. Si sasa wakati ambapo bila shaka jamaa zake huko nyumbani walikuwa wakilia na pengine hata kuomboleza juu yake.


Ni hofu hiyo ambayo ilimrejesha katika yale maswali ambayo siku hizi yalitawala akili yake na kumfanya awe nayo akilini kama wimbo usio na msaidizi, wimbo wa bubu na kiziwi. Kwamba ni kweli kuwa sasa yuko mstari wa mbele! Mbele ya nchi na taifa zima! Mbele ya wazalendo wote, tayari kuua, tayari kufa kwa ajili yao! Ni kweli au ndoto! Kama ni kweli kujinadi nafsi yake kiasi hiki ametumia busara kweli? Swali ambalo alikuwa akijitahidi kulifuta akilini kwa kujihisi mwenye hatia kwa mawazo hayo duni, pamoja na kujikumbusha ujana wake, afya yake na wajibu wake kwa taifa.


Lakini, kadhalika, hayo pia yalikuwa yakimzulia swali jingine. Wajibu ni nini? Hilo lilifuatiwa na lingine. Yeye ni nani na wajibu wake ni upi? Taifa litamlipa nini kwa kumwaga damu yake? Na kwa nini iwe yeye? Kuna maelfu mangapi ya vijana ambao walikuwa wakizurura mitaani?








Labda amekuwa mjinga kuamua kufanya hivyo? La, alijikanusha hima. Ni kufuru kubwa kuwaza hivyo. Yeye ni shujaa, shujaa miongoni mwa mashujaa. Nchi inamtegemea na kuwategemea wote wenye ari kama yake.


Lakini ni kweli yeye ni shujaa? Ushujaa ni nini? Na nini tuzo ya shujaa iwapo atakufa na kuoza kama mzoga? Manufaa yake ni nini? Maswali hayo yaliendelea kuzuka akilini mwake na kuota mizizi. Yalianza tangu usiku ule ambao alijikuta akiparamia lori na kuanza safari ya kuja hapa alipo.


Ulikuwa usiku wenye giza zito kuliko hili la leo, giza la kutisha, giza ambalo lingeweza kuwa ahera iwapo nuru ya taa za umeme katika kambi yao zisingekuwepo na kuunajisi unene wake.


Gari lilikuwa limesimama barabarani likiwasubiri. Wakawa wakiliendea mmoja baada ya mwingine kila mmoja akiwa kamili kwa hali na mali na bunduki zikiwa mikononi, mafurushi makubwa yenye mavazi na mahitaji mengine migongoni. Kadhalika, mioyoni walikuwa wameivaa ile hali ya kusikia furaha na utukufu, hali ambayo humpata yeyote anayefahamu kuwa uhai wake ni tegemeo pekee la wengine.



Hata hivyo, pengine hii haikuwa sare katika mioyo yao wote, Sikamona akiwa mfano. Yeye japo alifurahi na kujisifu kimoyomoyo lakini bado hofu haikukoma kupenya katika ari hiyo na hivyo kumfanya awe na mashakamashaka. Wakati wakihutubiwa ile hotuba ya mwisho ambayo








ilikuwa ndefu yenye maneno mengi ndani ya neno moja tu, “Tunawategemeeni” yeye alijisikia kama anayesomewa sala ya mwisho kaburini. Wakati akipanda lori hili alijiona kama anayeingia katika jeneza. Gari lilipoanza kuondoka na kujitoma gizani alihisi kaanza ile safari ya mwisho, safari ya kuzimu. Alitulia akitetemeka kindanindani, macho kayakaza kutazama mandhari ya nchi yake, kwa mara ya mwisho.


Alikuwa akiilinganisha hali hii na ile aliyowahi kuiona miaka michache iliyopita, pindi alipofiwa na mdogo wake. Wakati huo alikuwa bado mtoto, alipendana sana na nduguye huyo, kwa jina Marubu. Kisha, usiku mmoja aliamshwa usingizini kwa ndoto mbili mbaya zinazotisha. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umelala juu ya mgongo wa Marubu hali wa kulia kaufanya mto. Kitisho cha jinamizi hilo kilimfanya atetemeke na kutweta. Hivyo, akaanza kumwamsha Marubu kwa kumsuka polepole. Marubu hakuamka. Alimsukasuka kwa muda mrefu bila mafanikio. Akashangaa. Mwisho alimsukuma kwa hasira. Marubu aliviringika kama gogo na kuanguka uvunguni. Lakini bado hakuamka. Hali hiyo ilimjaza Sikamona hofu mpya. Akafanya haraka kuwaamsha wazazi wake ambao baada ya kumtazama mara moja waliangua kilio, kilio ambacho kilithibitisha kuwa Marubu asingeamka tena. Siku ya pili walimshonea sanda na kumlaza katika jeneza. Kisha, wakamchimbia kaburi na kumzika. Sikamona alilia sana akitegemea machozi yamrudishe ndugu yake. Lakini haikutokea.








Akaendelea kulia ingawa si kwa machozi bali majonzi na maombolezo, kilio ambacho kilifufuka kuwa machozi kila alipokumbuka na kuhisi akiona jeneza la Marubu likididimizwa kaburini.


Ndio hali ambayo Sikamona aliihisi wakati alipokuwa anapanda na kuelekea vitani, hali ya kujihisi kamkumbatia Marubu na kushonewa pamoja katika sanda, kupakiwa katika jeneza na hatimaye kuelekezwa kaburini. Na ni hali hiyo ambayo ilimjaza hofu, hofu ya kutisha na kutatanisha, hofu ambayo ilimlazimisha kujiuliza maswali ambayo aliamini ni ya kike kwa wakati kama huo.


Alijisikia kupiga uyowe wa hofu, aruke toka katika jeneza hilo na kujitoma porini, amwepuke Marubu na wafu wengine. Lakini hakufanya hivyo. Hakufanya asilani. Polepole kelele, shangwe na vigelegele toka kwa wenzake viliurejesha moyo na roho yake katika ukumbi wa furaha na utukufu. Akajikuta mshirika katika vigelegele na nyimbo za kuukashifu uvamizi na hekima za mvamizi. Akaupenda sana ule wimbo uliomfafanua Amini kama “mroho” askari zake “Malaya”



“Vijana twendeni. Wote twendeni. Tukamtoe nchini mroho wa madaraka.


Tumtoe, tumtoe mroho mwenye njaa ya ukubwa. Tukawatoe nchini Malaya wa Amini.


Tukawatoe, tukawatoe, Malaya, makahaba wa Amini.”








Huo pamoja na nyingine kadha wa kadha zilimfanya abadilike kabisa moyoni na kumaliza safari hali akijiona kama aendaye harusini badala ya vitani.


Ari hiyo iligeuka hasira mara tu alipowasili Kagera na kuushuhudia unyama wa Amini na askari wake katika nchi yao. Alilakiwa na magofu ambayo juzi tu zilikuwa nyumba bora za thamani. Sasa zilikuwa zimechomwa na kubomolewa kwa vifaru, kung’olewa milango na madirisha pamoja na kila chenye thamani.


Si hayo tu, mashamba ya mibuni, migomba na miwa yalikuwa yamechomwa moto pamoja na kuvurugwa hata yakawa kama uwanja ambao ulitumiwa kucheza ngoma ya kikatili. Hayo yalikuwa pamoja na kuharibiwa viwanda, hospitali, shule, barabara na kila kitu ambacho askari hao walifahamu kuwa kina manufaa ama kilimgharimu mwanadamu muda na fedha kukitengeneza. Ukatili ulioje huu? Hasara iliyoje? Alijiuliza huku akitikisa kichwa kwa uchungu.


Eneo hili walilokuwa wamefikia ni lile la Kyaka, ambalo lilikuwa limetekwa na majeshi ya Idd Amini. Kikosi cha Sikamona kilikuwa kimefika kuungana na vikosi vilivyotangulia. Kwa bahati mbaya au nzuri walikuta kazi ya kuyaondoa majeshi hayo ya Amini imekwishatekelezwa. Walichoambulia ni harufu ya vita na mabaki yake. Hata hivyo, walitegemea mashambulizi wakati wowote, na hivyo, walilazimika kuwa makini wakati wote.








Jioni moja Sikamona alitoka kwenda kutembeatembea katika mashamba haya ambayo yaliharibiwa na ukatili wa hao wakatili. Alijipenyeza katika vichaka na migomba iliyosalia. Kisha, macho yake yalivutwa na kitu fulani ambacho aliona kimelala katika kimoja cha vichaka vilivyonusurika. Alikisogelea na kutazama kwa makini. Kelele za hofu au uchungu zingeweza kumtoka. Hakujua kwa nini alifanikiwa kujizuia asifanye hivyo. Badala yake alijikuta akisaga meno na kufunga ngumi kwa nguvu. Alikuwa akiushuhudia unyama wa Amini na askari wake kwa macho yake mwenyewe, unyama wao kwa viumbe wa Mungu. Zile sifa zote ambazo alizisikia kwa maneno sasa alizisadiki baada ya kuona hiki alichokuwa akikiona, maiti ya mwanamke! Ilikuwa imelazwa chali juu ya nyasi. Ukatili si tu kule kumwua, bali njia ambazo zilitumika. Yaonekana alikuwa hakufa kwa silaha ya aina yoyote. Alikufa kwa vidole. Macho yake yote mawili yalikuwa yameng’olewa, ulimi umevutwa nje, sehemu za siri zimetatuliwa na vidole vya mikono na miguu kuvunjwa. Kando yake kitoto kichanga kilikuwa kimelala, maiti vilevile. Hiki ilionyesha kilifariki kwa njaa na kilio kwa kumpoteza mama ghafla.


Sikamona alizitazama maiti hizo kwa muda mrefu. Hasira zikampanda na kisasi kukamilika katika nafsi yake. Haistahimiliki… haivumiliki. Alifoka kimoyomoyo. Ni hapo ambapo alijikuta akijilisha kiapo upya, kiapo cha rohoni kabisa, kwamba asingesita kujitolea kikamilifu kumwadhibu huyu ambaye anafanya vitendo vya








aina hii.


Aliporejea hakujua kuwa alikuwa ametokwa na machozi hadi alipofika mbele ya Mdoe ambaye alikuwa akimsubiri mbele ya handaki lake. “Una nini?” Mdoe alimwuliza kwa mshangao.


“Ninalia!” sikamona pia alishangaa. Kisha, “Ah! Nadhani ni upepo tu.” Alimdanganya.


“Upepo! Tangu lini?” Hakumjibu.



ILIENDELEA kutulia katika handaki lake akifanya kila juhudi kuushinda usingizi ambao sasa ulimnyemelea. Angewezaje kualala wakati walikwishaambiwa kuwa


adui hawako mbali na walitarajiwa kupita eneo hilo? Giza ambalo lilikwishaimiliki nchi nzima lilimnyima uwezo wa kuona chochote, hali ambayo ilimfanya aone kama vivuli vinavyotembea na hivyo kurejewa na hofu mara kwa mara. Hakuchoka kupambana na hofu hiyo.


Ukimya ambao ulikuwa umetanda ulinajisiwa na sauti ya bundi ambayo ilianza kulia ghafla. Sikamona alimsikiliza bundi huyo kwa muda, kisha akatabasamu. Alikumbuka ile imani ya kabila lake, kwamba bundi ni ndege wa wachawi na aliapo uwa anabashiri maafa, imani ambayo ilidumu katika nafsi yake hadi mwalimu wake alipoipotosha kwa kuwaambia kwama bundi








ni ndege kama wengine na kwamba imani hiyo ni ya kale isiyotofautiana na zile mila za mtoto kutokula mayai ama mama mjamzito kuambiwa akila samaki asiye na magamba angezaa zeruzeru. Labda ni kweli kuwa imani hiyo ilikuwa duni iliyoachwa nyuma na wakati. Lakini mbona bundi huyu analia hapa, saa hizi, ambazo maafa yako usoni na mashaka yakimchungulia? Mara ngapi mila za kale zimetokea kuwa tunu njema kwa maisha ya kileo? Alinong’ona kimoyomoyo.


Hakuyamaliza mawazo yake. Ile ishara waliyokuwa wakiisubiri ilisikika ghafla. Ikamfanya aduwae kwa muda huku miguu ikilegea na mwili mzima kumtetemeka. Kisha, alizikusanya nguvu zake. Akafanya hima kuiandaa bunduki yake, huku mgongoni akijifunga furushi lake la vifaa.


Walitulia kwa muda ambao sikamona aliuona mrefu kupindukia. Muda ambao ulimrejesha katika hofu. Mikono yake ilitoa jasho huku mwili ukimtetemeka. Alijisikia kwenda haja lakini hakuthubutu. Wala hakujua kama haja hiyo ingemtoka. “…. Tulieni… sikilizeni muone vijana wetu watafanya nini…” yalimrudia maneno ya Mwalimu. Yakamfanya ajisikie aibu na hatia kwa hofu yake, kisha “…Utarudi salama…. Utanikuta… Nikukabidhi zawadi ya Ushindi…” hayo yaliambatana na hali ya kuhisi akiuona uso wa Rusia ukimtazama na kushuhudia alivyokuwa akitweta hovyo. Aibu ikamzidi. Yeye ni kijana. Ujana wake unategemewa sana dakika hii kwa manufaa ya nchi nzima. Vipi aanze hofu na kukata



tamaa! La, asingeruhusu uzembe kama huo. Akajikaza kiume na kuahidi na kujikumbusha tena, kwamba ilimlazimu awe imara.


Wakati huo mapambano yalikaribia. Walisubiri kwa dakika kama kumi tu, mara wakawaona maadui waliokuwa wakiwajia kwa kundi kubwa kama la ngombe waendao malishoni. Akainua bunduki yake na kuielekeza katika kundi hilo tayari kuifyatua. Lakini alijisahihisha upesi alipokumbuka kuwa alikuwa hajapewa amri ya kufanya hivyo. Akajilazimisha kutulia. Macho yake kayakaza kuwatazama adui ambao walizidi kuwakaribia.


Kamanda ana nini? Amepatwa na jambo gani hata aache adui kutufikia bila ya kufanya lolote? Sikamona alijiuliza kwa hofu na mshangao.


Halafu, ishara ikatolewa. Ikafuatiwa na ngurumo ya mlio wa bunduki na mlindimo wa risasi ambazo zilimiminwa katika genge la maadui. Maadui hao, ambao bila shaka hawakujua kuwa mbele yao kuna mtego, waliduwaa kwa muda kwa ajili ya mshindo wa wingi wa risasi ambazo zilimiminika toka kila upande. Kisha, kama walivyo askari wote waliofundishwa walijitupa ardhini ghafla na kuanza kupigana. Si mapigano ya kuteka nchi tena, bali kujaribu kuziokoa roho zao.


Ni hapo ilipofuata mvua ya ajabu, mvua ambayo ilikuwa na ngurumo za kutisha, pamoja na vilio vya watu waliokuwa wakihanguka huku na huko.


Haikuchukua muda mrefu kama alivyotegemea








Sikamona. Baada ya dakika kadhaa hali ilirudi kama kawaida. Zile kelele, mingurumo na vilio vilipoa ghafla na nafasi yake kumezwa na ukimya wa hali ya juu. Kama wengine wote, macho ya Sikamona yalitulia juu ya mizoga iliyotapakaa huku na huko pamoja na miili ambayo ilikuwa ikitapatapa kwa maumivu na kukata roho. Miili ya adui.


“Hee, kilikuwa kipigo chema au sio?” Mtu mmoja alitamka. “Kipigo halali yake: chastahili kupewa jina. Kipigo cha kumtoa nyoka pangoni au sio?”


Si kwamba hakumjibu tu, hali kadhalika hakumtazama. Hivyo, hakujua ni nani ambaye alimsemesha. Mawazo yake yalikuwa yamepaa na kutua katika dunia nyingine, dunia yenye huruma na uchungu. Hali hiyo ilimtokea baada ya kuutazama kitambo mwili wa adui mmoja na kushuhudia mateso aliyoyapata. Si hayo tu, alikuwa pia amesikia hata sauti yake ikikoroma na kudai “I am dying for nothing.”


Pengine ni kweli alikuwa akifa bila sababu. Sikamona alijiuliza akitembea polepole toka nje ya umati huo wa mzoga. Bila ya sababu! Kwa vipi? Alilazimishwa kuja vitani? Mtu anawezaje kulazimishwa kufanya jambo kubwa kama hilo?


Hakuwahi kupata muda wa kulijibu swali lake. Kelele za ghafla zilisikika. Alipogeuka aliiona maiti moja ikiinuka na kukurupuka mbio. Hakuwa peke yake, askari mwingine alikuwa akimkimbila. Walikuwa wakimjia. Akaharakisha kuielekeza bunduki yake kifuani mwa adui huyo huku








akifoka, “Simama.” Kabla hajafoka tena mkimbizi huyo alijikwaa na kuanguka chini. Askari aliyekuwa akimkimbilia alimfikia na kumchoma sime mgongoni.


“La, la, acha!” Sikamona alifoka huku akimkimbilia. Alimvuta askari mwenzake mgongoni na kufoka tena. Mwache…”


Askari huyo akainua uso kutazama. Ikamshangaza kukuta si mwingine zaidi ya Mdoe ambaye alimtazama kwa muda. Kisha, kama aliyetishwa na kitu fulani katika macho yake, akafanya haraka kuichomoa sime yake toka katika mwili wa adui huyo na kuondoka zake.


Sikamona akainama kumtazama mateka huyo. Alikuwa ametapakaa damu mwili mzima. Damu ya mtu ilikuwa ikimwagika hadharani. Kwa nini? Alijiuliza. Yeye hakujua kwa nini anakufa? Aliendelea kujiuliza. Hakujua ajipe jibu lipi, hakujua awaze nini. Akayaepuka macho ya mtu huyo na kujivuta tena nje ya uwanja huku askari wenzake wakisogea na kumthibiti adui ambaye aliendelea kutapatapa kama anayekata roho.




NDIO nilizaliwa katika nyumba masikini. Labda tuseme ilikuwa na umasikini zaidi ya masikini wengi waliotapakaa huko na huko katika kata yetu, umasikini unaotisha. Ndio, kwani si kwamba ulinifanya nitembee matako wazi tu, bali pia uliniwezesha kuona viraka vilivyoshonana nyuma ya suruali ya baba, wala si kwamba ulitufanya tuishi kwa dhiki tu bali pamoja na kutulazimisha kumfungia baba chooni kila wakusanya kodi walipokuwa wakipita kijijini petu. Ni mengi mno ambayo yalitupata. Mengi kupindukia. Yanatosha kabisa kumfanya mtu aamini kuwa dunia, kama si jehanamu, ni gereza. Sijui kwa nini hali hiyo ilituzidi mno sisi kuliko jirani zetu. Labda ilikuwa kwa ajili ya malazi ya mama mara kwa mara. Ama ilitokana na mapenzi ya baba kwa pombe. Sijui! Kitu nijuacho ni kimoja, kwamba pamoja na umasikini wote huo nilikuwa


na furaha.”








Kiasi Sikamona alimwogopa Mdoe. Akamtazama usoni na kushangaa macho yake yalivyokuwa yakichezacheza na kutoa nuru kali iliyodhihirisha uchungu na simanzi.


“Naam, furaha tosha kabisa. Sikuwa na wasiwasi wowote wa maisha. Sikuuchukia umasikini wala sikupata maumivu yake. Niliyazoea yote. Pengine hali hiyo ilitokana na kule kuwa mmoja miongoni mwa wengi wenye hali kama yetu. Si kuna mtu aliyewahi kusema, kifo cha wengi harusi?” basi mimi pia nilikuwa harusini, katikati ya kundi linalosheherekea, nikicheza ngoma waliyokuwa wakiicheza na kuimba nyimbo walizokuwa wakiziimba, zaidi ya yote hayo nilikuwa na mpenzi.”


Sasa alikuwa kama anayeota na kuzungumza katika ndoto yake hiyo aliposema, “Msichana mzuri mwenye heshima na adabu. Umbo lake lilikuwa na kila ambacho mwanamume anakihitaji. Mwenendo wake ulikamilisha yote ambayo ndoa inayataka. Alikuwa kama nuru gizani, maji jangwani, shibe njaani na faraja matangani. Si kwangu tu, bali kwa kila aliyemwona. Kila mpita njia aliyetazamana naye hakukosa kutazamana naye tena usingizini. Na kila aliyemgusa hakukosa kujikuta akimkumbatia katika ndoto zake. Naam, alikuwa ua la roho, ua lililochanua. Lakini alikuwa wangu. Wangu peke yangu.” Akameza mate kulainisha koo kabla hajaendelea.


“Mapenzi yalianza kama ndoto, ni kweli kuwa alikuwa jirani yangu. Ni kweli pia kuwa alikuwa na hali kama yangu, mtoto wa masikini kama baba yangu.




na hali kama yangu, mtoto wa masikini kama baba yangu. Lakini si hiyo sababu ya mapenzi yetu. Ni kitu baki kabisa. Kitu ambacho mpaka leo kinanifanya nishindwe kukifafanua. Ninachojua ni kwamba kitu hicho kilinyang’anya starehe ilipokaa bila ya kumwona, kikanifanya mgonjwa niliposhinda pasi ya kuisikia sauti yake. Nilipojikakamua na kumweleza habari hiyo ikanishangaza aliponifahamisha naye alikuwa na shida kama zangu. Halafu nikaelewa. Yalikuwa mapenzi. Tukawa tukiandamana naye huku na huko. Sikuyaonea aibu matako yangu ambayo yalikuwa wazi kama ambavyo yeye pia hakujali kuvaa gauni lililotatuka kifuani mbele yangu. Mavazi pekee ambayo yangefaa kuitwa mavazi, zilikuwa sare zetu za shule. Tulipofikia umri wa kutosha, matiti yakiwa kamili kifuani mwake, wima kama yanayodhihaki, nilimtajia ndoa. Akanicheka na kunishauri nisubiri tumalize shule.”


“Wakati huo uhuru ulikuwa mikononi mwa mtu mweupe. Ingawa nilikuwa mdogo, lakini nilihisi kasoro katika uhuru huo. Hayo yalinijia baada ya kumsikia baba akifoka kila baada ya kulewa. ‘Tumejidanganya… Tumejidanganya… Uhuru nini kama kodi iko palepale? Uhuru nini kama umasikini uko palepale?’ Ndio nilihisi kasoro kwani nilikuwa nimeshuhudia watu walivyoshambulia kwa nguvu usiku huo wa uhuru. Nikadhani kitakachofuata si kidogo. Lakini sikukiona. Hata hivyo, niliamini umasikini wa baba ulisababishwa na pombe. Hivyo, nikaiepuka na kuapa kwamba








nisingeinywa kamwe. Mara nikaanza kutaabika mawazoni ningepata wapi mahari ambayo ingeniwezesha kumwoa Maida, mpenzi wangu. Huo ukawa mwanzo wa kupotelewa na furaha yangu. Hata hivyo, nilijifariji kila nilipokadiria uzito wa penzi kati yetu. Lazima angekuwa radhi tutoroke tukaishi kokote ambako hakuna ndugu yake wa kudai mahari wala yangu wa kunilaumu. Nikawa nikisubiri kwa kiu kubwa siku ambayo ingenitukia kuwa naye kitanda kimoja nikimkumbatia na kumbusu mwili mzima.”


“Sio kwamba nilikuwa sijamkumbatia. Nilimkumbatia sana, huku nikimshika na kumgusa nipendavyo, nikifarijika na kuburudika nilivyoweza. Lakini ilikuwa ndotoni tu. Njaa yangu ilikuwa lini ndoto hizo kuondokea kuwa kweli.


Sikamona alimwona Mdoe alivyoyaepuka macho yake na kutazama ardhini aliposema, “Haikutokea. Haikutokea ndugu yangu. Maida kwangu alikuwa kama ndoto tu. Ndio, ndoto nzuri na ya kupendeza. Lakini ndoto. Hayo niliyagundua baada ya kumaliza shule. Nilimkumbusha mara kwa mara juu ya ndoa lakini alicheka tu na kuniambia “Tusubiri.” Nikasubiri hadi siku ile ambayo nilikuta… kwao kuna sherehe kubwa. Vipi? Nikauliza.


“Kuna harusi.”


“Ya nani?” Niliuliza kwa wasiwasi. “Maida.”


“Ameolewa!”








“Ndio. Anaolewa na mwalimu wake anaye…”


Sikuweza kumsikiliza zaidi. Sikuwa na hali. Nilijikuta nikipata maradhi ya ghafla. Nikaanguka kwa kizunguzungu. Simjui msamaria ambaye alinizoa na kunipeleka nyumbani juu ya kitanda changu cha kamba ambacho hakikuwa na shuka ya pili. Nijiue? Au nimwue Maida pamoja na mume wake! Nilijiuliza niliporudiwa na fahamu. Kisha, nilipokea barua yake. Ilikuwa na machache yayoeleweka. ‘…kama kweli ulinipenda Mdoe, hutanilaumu kwa uamuzi wangu. Nilijua usingepata mahari. Kadhalika, maisha yetu yangekuwa mabaya mno. Umasikini ungepotosha starehe katika ndoa yetu…’ Ni hapo nilipogundua tusi la masikini. Nikagundua unyonge wa masikini. Hapendezi, hapendeki… ni hapo furaha yangu ilipoingia dosari.”



“Kabla sijafahamu kama ningemchukulia Maida hatua ipi, kikatokea kifo cha mama yangu. Kikadhulumu nusu ya furaha na matumaini niliyobakia nayo. Halafu baba akafa. Alikuwa kiungo cha mwisho kati yangu na furaha, matumaini na hamu ya maisha. Nikajikuta nimetua katika dunia ya dhiki, kebehi na misukosuko. Dunia ambayo si kwamba ilininyima chakula na mavazi tu, bali pamoja na kunifanya niwe kichekesho hata kwa mafukara wenzangu. Unyonge ulionijia nusura ungenitia wazimu.”


“Siku moja nilipokuwa nikipitapita katika mitaa ya vichochoroni, nilipita mbele ya kilabu cha pombe. Nikachungulia ndani. Nilimwona








kijana mmoja mwenya hali kama yangu” shati lililotatuka mgongoni, viatu vya magurudumu na suruali yenye viraka visivyokadirika. Alikuwa amelewa barabara na sasa hana habari ingine zaidi ya kucheza na kucheka kwa furaha.”


“Alinivutia kijana huyo. Si kwa ajili ya mchezo wake wala ulevi wake. Ilikuwa kwa ajili ya furaha aliyokuwa nayo. Nimekwishakuambia kuwa niliishiwa na matumaini yote ya maisha mema? Lakini nilichohitaji ni furaha. Nilijua kuhuzunika kwangu kusingenipa mahitaji yangu. Nilihitaji kufurahi ili niendapo kaburini nife mwenye furaha. Furaha ilikuwemo katika ulevi, ulevi ambao uletwa na pombe. Pombe… pombe… pombe… nikajifunza kuinywa pombe. kila senti yangu ambayo niliipata kwa kibarua kigumu ama kuiokota kwa kudra za Mwenyezi Mungu niliitupia katika mkoba wa muuza pombe. Nikawa mlevi mashuhuri mwenye kila sifa ya unywaji pombe, mapenzi kwa kazi hiyo na zaidi ya yote mwenye furaha. Niliyafurahia maisha. Na nikasahau kabisa kudhani kuwa ulevi wa baba ndio uliokuwa kisa cha umasikini wetu. Badala yake niligundua kuwa alijua alichokuwa akikifanya. Ni pombe ambayo ilimsahaulisha uchungu wa kukosa shamba, majonzi ya kutokuwa na kazi na msiba wa kuniona mimi nikifuata mkondo wake. Pombe tu, hakuna zaidi.”


Nzi ambaye alikuwa akimtambaa usoni alimrukia mdomoni. Akamtema na kumponda kwa dole gumba. Sikamona alitamani kucheka.








Lakini kicheko kikagoma kumtoka.


“Hata hivyo, bwana sidhani kama kweli naweza kuiita hali hiyo kuwa ni furaha, kwani furaha ilinitokea kwa muda mfupi tu, muda ule ambao pombe ilikuwa ikielea kichwani mwangu na kunifanya niwe kama ninayeelea katika bahari iliyochafuka. Nyakati ambazo sikupata nilijikuta nikijuta kama kawaida. Nilijuta kuzaliwa, nikajuta kuishi. Nikaanza kumtafuta rafiki mwingine, rafiki ambaye angenitoa katika hili gereza ambalo ni baadhi tu wanaoliita dunia, kifo. Naam, ilikuwa ndio dawa pekee.”


Alisita tena. Safari hii ilikuwa kwa ajili ya kusikiliza nje. Alidhani amesikia sauti ikiita.


“Kifo hakikuja upesi. Na sikuwa shujaa wa kujiua kwa urahisi. Hata hivyo, badala ya kifo ilifuata faraja mpya. Tumaini pekee la mtu kama mimi, Azimio la Arusha.” Alisita na kumtazama Sikamona usoni. “Naam, lilitangazwa. Likatoa sheria mpya na zenye manufaa kwetu ambao tulikuwa na shida na kwa kila mmoja ambaye aliwahurumia watu wote wenye dhiki. Nilifafanua makosa ya uhuru wetu, kwamba ulikuwa kilemba cha ukoka. Uhuru si kubadili rangi ya bendera, bali kubadili mfumo wa maisha, yaani kumfanya kila mwananchi ajisikie huru, si kwa maneno bali kwa vitendo. Huru katika siasa. Huru katika uchumi. Huru katika utamaduni. Likakomesha misingi yote ya baadhi ya watu kukalia uchumi hali wengine wakitaabika. Likafutilia mbali umilikaji wa ardhi, kugawa kazi kwa mjuano na



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog