Search This Blog

Thursday, 29 December 2022

ZAWADI YA USHINDI - 5

 

 Simulizi : Zawadi Ya Ushindi

Sehemu Ya Tano (5)





imekwisha ila tu kulikuwa na mabaki ambayo yalikuwa yamehama miji na kujificha misituni. Hawa walijipenyeza mijini mara kwa mara na kufanya uhuni ambao hawakuona aibu kuuita, “Kuikomboa Nchi Kutoka Tanzania.” Tatizo hili halikumtia wasiwasi Sikamona. Lilikuwa jambo la kutegemea. Kila vita uwa na mabaki ya aina hii, yakitumia nafasi hii kujineemesha na kujitajirisha huku wakisema hili na lile. Hivyo, Sikamona alifahamu dhahiri kuwa hii haikuwa sababu ya kumnyima furaha.


Lakini hakuwa na furaha.


Hakuwa na furaha kama ile ambayo ingemstahili kuwa nayo baada ya ushindi mkubwa kama huu. Kwa nini? Alijiuliza. Ushindi si jambo dogo. Hasa ushindi dhidi ya kiumbe kama Idd Amini, kiumbe mwenye sifa za unyama, dunia nzima, kiumbe ambaye ulimwengu mzima umeona na kushuhudia alivyoitaabisha Uganda na kuwababaisha majirani. Nchi ngapi zilitumia serikali ya Tanzania salamu za pongezi, zikionyesha furaha yao kwa kuanguka kwa fashisti huyo? Haiyumkini ushindi huu uliifuraisha dunia kwani ulihitajika na dunia nzima.


Hata hivyo bado hakujiskia furaha.


Kwa nini? Ama hali hii ilitokana na kule kupona kwa Idd Amini? Alikuwa ametoroka na kuanza maisha ya udobi katika nchi mojawapo ya Kiarabu. Hakuna mtu yeyote aliyependa kuliona jambo hilo likitokea. Lakini alipona, baada ya kuyapotosha matumaini ya watu na kuwafanya








Waganda wote kutapatapa wakielekea huko na huko, akiwachezesha kama wanawe.


Kwa nini dunia inakua hivi? Mtu mmoja, binadamu wa kawaida kama watu wengine, vipi apate uhuru na nguvu ya kuifanya nchi nzima apendavyo? Vipi ajaliwe uwezo wa kuyatawala maisha ya watu, kunyayasa starehe zao na kukomesha haja zao za maendeleo? Vipi abahatike kupata amri juu ya kuishi na kufa? Uwezo wa kila mwananchi na mamlaka katika kila jambo atendalo?


Baada ya kuchekelea vifo na maisha ya watu wenye dhiki, sasa mtu huyohuyo, yuko salama salimini. Hana shaka lolote, hofu ya mlo wa kesho wala dhiki ya mavazi. Waliokufa wengine, wanaotahabika wengine…


Labda kweli askari ni mbwa…


Kwa vipi? Askari ni kama watu wengine, mwananchi kama alivyo kila mwananchi. Kama kijana basi yu kijana wa taifa, mtoto wa mkulima na mfanyakazi. Kama taifa linaathiriwa na ujinga, umasikini na maradhi basi athari hizo humkumba askari kama zimkumbazo kila mwananchi. Hayo Sikamona aliyafahamu kitambo, kitambo sana, kabla ya Amini kuivamia nchi. Na ni hilo ambalo lilimfanya aingie jeshini. Hakuwa mwanajeshi. Lakini alifahamu fika maslahi yake yalimtaka kuyalinda, kama mwananchi, kama mmoja miongoni mwa wote ambao wanayategemea maslahi yao.








Na askari wa Amini je?


Hapo alijisahihisha mara moja. Alikuwa amekosea. Tafsiri aliyoitoa ilikuwa tafsiri ya askari wa Tanzania. JW “Jeshi la Wananchi” tafsiri halisi kwa maneno na vitendo. Hayo aliyathibitisha kwa macho yake mwenyewe baada ya kushuhudia Waganda wanavyowalaki kwa nyimbo na maua.


Ndiyo, tafsiri hiyo haikuwahusu askari wa Amini kamwe. Idd Amini alikuwa nduli. Alikuwa na kiu kubwa ya kunyayasa na kutesa. Uwezo wa kutimiza kiu yake hiyo hakuwa nao. Alihitaji msaada. Ndipo alipogeuza jeshi la nchi kuwa watumwa wake baada ya kuua waliopinga ujeuri huo na kuajiri aliodhani wangefaa katika kutimiza kiu yake. Aliliamrisha jeshi kuwa sugu katika kuwakandamiza raia, kukomesha nia zao za kujiinua pamoja na kuwasumbua jirani. Kama mbwa wa tajiri, akawashibisha askari hawa kwa vinono zaidi ya chakula cha watu. Akawahonga si malipo tu, bali pamoja na maneno ya uongo hata wakaishiwa aibu na kuwa kama malaya wasio na aibu wala hofu mbele ya wazazi wao. Wakafanya yote ambayo bwana wao aliwaamuru kutenda. Hata wakaritoroka jeshi lake hilo na kwenda kuishi ugenini. Waliosalia miongoni mwao ndio wale waliojiunga na jeshi la ukombozi.


Wala si jeshi tu ambao Amini aliwageuza malaya wake. Viongozi wake wote aliwalazimisha kuifumbia macho haki na halali, wakawa viziwi wasisikie malalamiko na vilio. Hivyo, mkulima akaendelea kuwa mtumwa katika nchi yake



mwenyewe, akivuna mavuno mengi na kuambulia faida duni, akifanya kazi ngumu na kulazimika kuona jasho lao likiwastarehesha “wateule” wachache. Kadhalika, mfanyakazi akawa punda asiyejua kuchoka wala kuhitaji malipo halali. Alikesha viwandani na kushinda juani akizalisha faida kubwa ambayo ilimnenepesha Amini, kuimarisha jeshi lake na kustarehesha mabwana zake ndani na nje ya nchi. Hayo pamoja na kule kuiweka Uganda nzima katika jehanamu isiyopungua vilio na maombolezo ndio kisa cha vita. Ndio kisa kilichoifanya Tanzania isisite kuwaunga mkono waganda. Ndio kisa cha adhabu aliyoipata Amini adhabu ya kipigo ambacho kamwe kisingemtoka katika fikra na ndoto zake, kipigo ambacho kimeihakikishia dunia kwamba Waganda walikuwa tayari kununua upya uhuru wao hata kwa bei ya damu. Na kwamba Tanzania ilidhamiria kuleta mapinduzi ya kweli nchini na barani Afrika kwa gharama yoyote, gharama zote, jasho, damu, maisha…


Mdoe!


Umbo na sura yake vilimrudia Sikamona akilini tena. Siku zote kila alipowaza juu ya vita na ukombozi, sura ya Mdoe haikukosa kumjia akilini. Alimwona katika kila hali, mara akiwacheka maadui baada ya kuwazuia kuingia kambini, mara akifoka aliposema “…anastahili kipigo,” na pengine ilimjia ile sauti yake ya mwisho aliponong’ona “…Umekuwa mwisho wa kiume…” hayo yalimfanya Sikamona ajikute akizidi








kumheshimu siku baada ya siku na kuuthamini mchango wake katika kuilinda nchi na kuitetea haki ya Waganda, mchango usiosahaulika, mchango wa maisha, mchango wa uhai kwa hiari!


Nani mwingine anayestahili kuitwa shujaa zaidi ya mtu kama huyu? Mtu ambaye amekuwa tayari kuyapoteza maisha yake kwa ajili ya watu! Kwa ajili ya maslahi, mahitaji na matumaini yao? Mtu aliyezaliwa katika ukoo masikini, akaathiriwa na umasikini na siasa potofu; kisha akaona nuru ikitokea, tumaini la mnyonge, akaitumaini nuru hii na kuanza kuonja matunda yake; kisha giza likatishia kuizima, akaiacha nuru na matumaini na kulipinga giza hata likakubali kuwa limepingwa. Kwa bei ya maisha yake ameinunua nuru upya. Si kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya watu wengine, kwa faida ya maisha yao ya baadaye. Kama si ushujaa ni nini basi?”


Kuna watu wengi ambao majina yao yanaishia miongoni mwa watu, kwa ajili ya kujitoa kulisaidia taifa. Akina Lumumba wa Zaire, Nguabi wa Kongo, Mkwawa wa Tanzania, Mao wa China, Lenini wa Urusi n.k. wengi mno. Wote hao majina yao yanaishi kwani matendo yao yalikuwa nuru iliyokusudia kuleta ufanisi palipodorora, faraja penye dhiki na shibe penye njaa. Orodha ya majina yao imo katika fikara za dunia. Jina la Mdoe lilikwishaingia katika kurasa hizo, Sikamona alijikumbusha.


Damu ni nzito kuliko maji. Thamani ya damu ni kubwa, kubwa machoni pa mwanadamu








na Mungu. Haikadiriki. Hakuna aijuaye bei yake. Kama kuichezea damu hiyo, kuchezea maisha, kama alivyofanya Idd Amini ni dhambi isiyosameheka si wazi kuitetea damu na maisha ya utukufu usiosahaulika? Tanzania ni nchi masikini. Pamoja na umasikini wake imejijengea misingi ya siasa ambayo kila mwananchi ataufurahia uananchi wake. Azimio la Arusha ni njia inayomwelekeza huko Mtanzania.


Ingawa bado tumo njiani, lakini mafanikio ambayo yamekwishafikiwa si haba. Yamewafanya si waanze kuyafurahia matunda na uhuru wao tu, bali pamoja na kuwahurumia jirani ambao wanataabishwa zaidi ya wakimbizi katika nchi zao wenyewe.


Hatimaye, wakawahurumia na kuliafiki ombi lao. Baadhi ikawalazimu kufa, akina Mdoe na wenzake. Huu si upendo usio na kifani? Kuacha maisha yenye matumaini! Kuacha uhai! Kwa ajili ya jirani ili kukomesha mkondo wa damu isiyo na hatia uliokuwa umechimbwa na Amini.


Wameukausha! Wameukomesha! Kwa damu yao! Damu isiyo na hatia!


Kama kupanda mbegu ya haki na upendo katika bahari iliyojaa uonevu, chuki na kukata tamaa!

















NAAM. Damu ya Mdoe na wote waliolala katika ardhi ya Uganda haikuwa imepotea bure. Ilikuwa mbegu. Hayo Sikamona aliyafahamu. Lakini bado hakujisikia furaha kama alivyodhani ingemstahili. Kwa nini? Hakulijua jibu. Pengine furaha hiyo ingekamilika hapo ambapo mbegu hiyo waliyopanda itakapotoa matunda, hapo ambapo matunda hayo yatakapoonekana kwa kila mtu na kuwashibisha wananchi labda! Kwani bei ya damu haikadiriki, wala hakuna aijuaye thamani


yake, isipokuwa hapo tu ambapo itachanua.


Akaendelea kuuegemea mti, akiitazama nyumba ya mkimbizi Amini tena na tena. “Baada ya siku itakuwa gofu,” alijiambia akitabasamu kimoyomoyo. Mchana ukatoweka na usiku ukaingia. Akainuka na kujivuta kambini kwao ambako alipata chakula cha usiku. Usiku wa leo








ulikuwa usiku wake wa zamu. Akajivuta hadi mahali pa zamu ambapo alijificha na kutulia akitazama huko na huko.


Kwa Sikamona ulikuwa usiku mrefu, tena wenye kiza kinene zaidi ya kawaida. Hivyo, ilimlazimu kuangalia kwa makini ili aweze kutimiza wajibu uliomleta hapa. Si kutazama tu. Ilikuwa pamoja na kushindana na usingizi ambao uliyatongoza macho yake mara kwa mara. Mawazo yake yakamwacha Amini na ukimbizi wake na kurudi nyumbani, Tanzania. Akawafikiria wazazi wake, akajiuliza watafurahi kiasi gani pindi wamwonapo akirejea salama. Mzima sana, isipokuwa kovu dogo la ile risasi iliyomjeruhi paja! Lakini hiyo ilimfurahisha, kwani kuwepo katika paja lake ni kumbukumbu ambayo kamwe isingefutika, kama shahada ya ushujaa wake.


Halafu akamkumbuka Rusia. Furaha iliyoje pindi watakapoonana tena? Watakumbatiana, watacheka, watashangilia! Atapokelewa kwa lile tabasamu lake makini linalofariji na kuburudisha. Zaidi ya yote atapewa zawadi yake ‘ya ushindi.’ Zawadi… ni zawadi ipi ambayo Rusia alikusudia kumpa? Alijiuliza tena swali hilo. Angepewa kitu gani? Hakuwa na jibu. Badala yake alijisikia ile hamu ya kurejea nyumbani ikimkumba kwa nguvu zaidi. Alitamani aondoke dakika hiyohiyo, apae na kuruka hadi nyumbani. Ndiyo, akatue hadi katika kifua cha Rusia. Lakini akaishia kuhuzunika kwa jinsi jambo hili lilivyokuwa mbali na uwezo wake. Angeruka hapo tu atakapoamriwa kufanya hivyo,




siku chache zijazo. Hata hivyo, asingeruka kwa mbawa zake, ingekuwa safari ndefu ya gari.


Aligutuka ghafla. Alihisi ameona kitu kikitambaa katikati ya giza. Akayakaza macho yake kwa makini. La, hakuona chochote. Haiyumkini? Alikuwa amewaza tu. Akaendelea kuwaza hili na lile, akifika huku na kule na kuonana na kila anayemtaka, kimawazo. Kisha alihisi kuona kitu tena. Akayalazimisha macho yake kushindana na giza kulivuka. Naam, hakukosea. Kivuli cha mtu kilionekana kikipenya katikati ya giza hilo, polepole kama wingu. Alikuwa akitoka katika makambi yao! Sikamona alishuku mara moja kuwa huyu hakuwa rafiki wala askari mwenzao. Rafiki asingewatembelea katika muda kama huu na askari mwenzao asingewatembelea kwa mwendo huu bila yeye mlinzi kuwa na taarifa. Akainua bunduki yake na kumlenga huku akipanua mdomo na kutaka kusema “Simama” lakini aliiteremsha bunduki hiyo mara moja baada ya kupata wazo jingine.


‘Bila shaka huyu ni adui,’ Aliwaza. Kama ni hivyo alikuwa ameingilia katika kambi zao kwa upelelezi, ikiwa na maana kuwa alikuwa amegundua yote aliyohitaji kuyagundua na alikuwa akielekea kuwasilisha kwa wakubwa wake. Hivyo, kumwua kusingemaliza ukorofi wao. Haja ilikuwa kung’oa mzizi wa fitina kumaliza vitisho kabisa ili Waganda wapate uhuru wao na kuijenga upya nchi yao. Hivyo, badala ya kumwua alimwacha ili awe daraja ambalo lingemwezesha kuyafikia








maficho yao. Ni wazo hilo ambalo lilimfanya aache kumpiga risasi na badala yake ayaache maficho yake na kuanza kumnyatia kwa adhari na ungalifu kama paka anayemnyemelea panya. Sikamona alifahamu fika kuwa alikuwa akivunja amri zote za jeshi, kuchukua uamuzi huo bila ruhusa. Lakini hakuona kama kulikuwepo na wasaa wa kungoja ruksa.


Waliandamana kwa muda mrefu. Wakauacha mji na kuanza kufuata kichochoro kilichowaelekeza msituni. Hapo Sikamona aligutuka. Aingie porini? Vipi kama angepotea ama kujikuta akitokeza katika umati wa watu? Ni lipi ambalo angefanya kuyaokoa maisha yake? Akaanza kuulaumu uamuzi wake. Labda ingembidi kumwarifu mkuu wa Kombania ili wawafuate pamoja! Lakini huo muda angeupata wapi? Akasita, akiwa hajaamua kama ilimlazimu kuendelea au la.


“Tulieni…. Sikilizeni muone vijana wetu watafanya nini…” maneno ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Nyerere, yalimjia akilini. Ni nani kijana zaidi yake? Ni kipi wananchi watakachokisikia zaidi ya kitendo kama hiki?”


“…Umekuwa mwisho mzuri… Mwisho wa kiume… Mwisho unaomstahili mwanaume…” si maneno tu aliyohisi kuyasikia bali pamoja na umbo zima la Mdoe likitamka kwa majivuno na faraja.


“…Utarudi salama… Ndipo nitakapokukabidhi zawadi ya ushindi…” kadhalika hakuyasikia maneno ya Rusia tu, bali ilikuwa pamoja na




kuhisi uso wake mchangamfu ukimtazama kwa tabasamu. Hayo, kama hirizi ya usalama wake ama taji la ushujaa wake, yakamfanya aanze kumfuata adui huyo kwa moyo wenye ari na matumaini.


Hakukubali kumpoteza. Wala hakuwa tayari adui huyo afahamu kuwa anafuatwa. Alimnyemelea, akajitahidi kadiri ya uwezo wake kuepuka kukanyaga vijiti, visiki na kutumbukia katika korongo. Akaushukuru ujuzi na mazoea yake ya kutembea porini. Zaidi ya yote alilishukuru giza. Zamani alipokuwa mdogo alilichukia na kuliogopa, sasa alilitegemea na kuliona rafiki mkuwa.


Baada ya mwendo wa kutosha waliwasili katika kambi yao. Ingawa giza halikumruhusu kuona lakini kadri alivyozoea, hakushindwa kugundua vibanda vyao vilivyojengwa huku na huko. Kisha, aliweza kuona vichwa vya watu waliokuwa wamesimama hatua kadhaa mbele yake. Walikuwa wakizungumza kwa kunong’ona, asingeweza kusogea tena pasi ya kuonekana. Hivyo, alijifutika katika kichaka huku akimtazama kiongozi wao ambaye aliingia katika kundi hilo. Alihisi wakimlaki kwa shangwe. Akawasikia wakinong’onezana maneno kadhaa. Alihuzunika kwa kule kuwa mbali kiasi cha kutoweza kusikia walichokuwa wakizungumza. Kitu kimoja alikuwa na hakika nacho, kwamba maongezi yao yote yalikusudia kuwaangamiza wao. Laiti angeisikia mipango yao! Akasaga meno kwa uchungu.








Halafu alifahamu kinachotokea. Hujuma hiyo ilikuwa ikipangwa kufanyika muda huohuo! Aliyagundua hayo baada ya kuona vikosi vikitayarishwa na kupangwa tayari. Asingeruhusu hilo litokee, kuacha kikosi chao, ama kijiji chao, kivamiwe ghafla. Ni hilo alilofuata kulikomesha. Hivyo, bila ya kufikiri kwa mara ya pili aliinua bunduki yake na kupiga risasi juu kwa namna ya kuwatahadharisha askari wenzake waliobaki kambini. Mlipuko wa bunduki yake uliwafanya adui wote waduwae na kubaki kimya kwa muda. Lakini mlipuko huohuo uliyafichua maficho yake. Hivyo, wakati adui hao wameduwaa yeye aliinuka na kuanza kukimbia. Hakupiga hatua tatu kabla ya adui mmoja hajafahamu kilichokuwa kikitokea na kuanza kumfuata mbio. Alikuwa adui mwenye mbio nyingi, labda kwa ajili ya kuwa mwenyeji katika msitu huo, kila hatua yake moja alizidi kumkaribia Sikamona. Ndipo Sikamona alipoona kukimbia kusingemfikisha popote. Akasimama na kumgeukia. Adui alipomkaribia , alimpiga risasi na kuanza kukimbia. Lakini sasa alikuwa akifuatwa na kundi zima. Alijua asingefika mbali. Hivyo, aligeuka kuwakabili, hakuwa na muda wa kulala chini. Hakuwa na nafasi ya kufanya hivyo. Wima, kama kisiki, akaiwasha bunduki yake na kuwamiminia adui risasi bila hata ya kulenga shabaha. Wengi walianguka na kufa, wengi wakageuka na kukimbia, lakini ni wengi pia ambao walizidi kumjia kwa uchu kama kundi la mbwa mwitu lililomfumania mwanakondoo. Hatimaye, risasi zikamwishia. Alifahamu








kukimbia kusingemsaidia. Hivyo, alijitosa katika genge la maadui na kuanza kuwapiga kwa sime. Haikumchukua muda kabla hajajikuta angani akipigwa kwa kitako cha bunduki hii na kudakwa kwa singe ile.


Maumivu aliyoyasikia hayakuwa na kifani. Hata hivyo, aliyasikia kwa muda mfupi tu kwani dakika chache baadaye, badala ya kuelekea hewani, alijisikia akididimia polepole katika shimo refu lenye kiza kinene.












alipozinduka alijikuta kalala juu ya kitanda katika chumba chenye harufu tofauti na ile aliyoizoea, harufu ya mchanganyiko wa madawa. Uso wake


mzima ulikuwa umefunikwa na bandeji nzito ambazo zilimzingira hadi mikononi na kifuani. Alipojaribu kujigeuza alalie ubavu alipambana na maumivu makali, maumivu ambayo yalimfanya akikumbuke kile kipigo alichokipata toka kwa adui. “Niko wapi?” aliuliza.


“Kampala. Hospitali,” sauti ilimjibu.


Alipogeuka kuangalia macho yake yaligongana na yale ya Brigedia wake, Chunga. Akagutuka kidogo kwani hakutegemea. Akajaribu kuinua mkono ampigie saluti lakini hakufanikiwa.


“Usisumbuke Sikamona,” Brigedia alimjibu akitabasamu. “Unahitaji kupumzika kwa muda,”








akasita. Kisha, alianza tena, “Umekuwa hapa hospitali bila fahamu kwa siku tatu. Kwa kweli, tulianza kukata tamaa. Sasa hatuna shaka kuwa utapona.” Akasita tena. Kisha akaendelea, “Kitendo chako kamwe hakitasahaulika. Licha ya kuokoa maisha yetu ilituwezesha kuwaangamiza adui ambao walikuwa wakitusumbua sana. Hata hivyo, bado hatujafahamu uliwezaje kufahamu kambi ziliko na kwa nini ulianza kupambana nao peke yako.”


Sikamona angependa kueleza yote, tangu alivyomwona adui, alivyomfuata na hata alipofyatua bunduki ya kuwataadharisha. Hata hivyo, kwa ajili ya maumivu makali aliishia kuongea machache tu. Brigedia alisikiliza kila kitu kwa furaha, huku kasahau tabasamu usoni kwake. Baada ya kusikia yote alitikisa kichwa na kusema. “Ushujaa wako hautasahauliwa. Laiti kila kijana wa kitanzania angekuwa na roho yenye uamuzi na nia kama yako! Nasikitika tulichelewa kidogo kufika hapo ambapo ulikuwa umewadhibiti adui. Hata hivyo, tulifanikiwa kuwateka wote wale ambao walikuwa wamekuzingira na kukukanyagakanyaga kama vifaru wenye vichaa. Nadhani watajuta milele kwa ujinga wao wa kusahau yote waliyostahili kuyakumbuka na badala yake kukuvamia wewe.


Sikamona hakuyasikia yote. Uchungu mkali ulimrudia tena. Vitu kama nyundo vilimpiga kichwani. Ghafla akajiona akididimia tena katika lile shimo refu lenye kiza cha kutisha.








***


Sasa alikuwa hajambo kiasi. Aliweza kukiacha kitanda chake na kujikongoja hatua chache nje ya jengo la hospitali. Aliweza hata kula mwenyewe, ingawa alipata matatizo katika kulenga mdomoni na kutafuna. Alidhani hayo yalisababishwa na plasta zilizomzingira usoni, hivyo yangetoweka mara tu zitakapoondolewa.


Askari wengi walimjia kumpa pole na hongera, wengi sana, wadogo kwa wakubwa, rafiki kwa watu baki. Wote walikifurahia kitendo chake na kumwomba awasimulie tena na tena alivyofaulu peke yake kuwakabili maadui wengi kiasi kile. Lakini Sikamona hakuwa tayari kufanya hivyo. Asingekubali kurejea tena katika ndoto hiyo ya kutisha. Badala yake alikuwa akijiuliza vipi alinusurika katika mapambano chungu nzima, makali mno na kuja kuhatarika katika pambano dogo la mwisho kama hili. Miongoni mwa mapambano hayo ambayo kamwe yasingetoweka katika fikra za Amini na vikaragosi wake ni pamoja na kile kipigo cha Kagera. “Kumtoa Nyoka Nyumbani,” kile cha Lukaya “Asiye Sikia la Mkuu,” kile cha Entebbe “Joka Limekamatwa Kiwiliwili” na kile cha Kampala “Kupondaponda Kichwa cha Joka” yote hayo alishiriki kikamilifu na kuokoka isipokuwa hili. Hata hivyo, huku pia si kupona? Alijikumbusha. Kwani kupona ni nini? Haja si kuweka jina katika historia? Yeye ameongeza uzito wa jina lake katika kurasa za historia!


***








Halafu akawa amepona. Bandeji zikaondolewa na akaruhusiwa kuondoka. Akajisikia furaha kuvaa tena magwanda yake badala ya kanzu za hospitali. Akainua mkono wake ili auguse uso wake ambao alikuwa hajaugusa kwa muda mrefu. Alichokigusa kilimtisha. Alihisi kushika kitu zaidi ya uso wake, kitu baki kabisa, kitu kikavu na kinachokwangua kama kisiki. Ni kitu gani? Akagutuka. Hofu ilimshauri kutoka nje upesi. Huko pia alikutana na mwujiza. Watu wote aliofahamiana nao si walimtazama kwa hofu na mshangao tu, bali pamoja na dalili zote za kutomjua. Akaduwaa kwa muda, kisha alirejea ndani upesiupesi. “Kioo” alifoka akiangaza huku na huko. Ndipo alipokumbuka kioo kilichokuwa bafuni. Hima, akaelekea huko. Alipofika akasimama mbele ya kioo kujitazama. Mbele yake alimwona mwanajeshi mwingine kasimama akimtazama. Kilichomshangaza ni uso wa mtu huyo. Hakujua kama ulistahili kuitwa uso au vipi. Ulikuwa kama kinyago ambacho kilichongwa kwa makosa, kinyago chenye kovu zito na jeusi nusu ya uso mzima, jicho moja, hali la pili limetoweka na nafasi yake kuchukuliwa na kovu hilo, pua lilipondwa na nusu iliyosalia kuinamia upande, mdomo wa juu ukiwa umeng’oka, hali wa chini umerudishiwa kwa kushonwa na shavu ambalo lilisinyaa na kukauka kabisa. Kwa mshangao, Sikamona aliinua mkono kukuna kichwa. Akashangaa zaidi alipoona mtu huyo akifanya vivyohivyo. Kisha akaelewa. Alikuwa akijitazama mwenyewe katika kioo. Mtu wa kutisha alikuwa








yeye!


Ndipo alipoangua kicheko na kuondoka.


Alipofika kambini kwake, Gulu, alilakiwa na nyuso zilezile za mshangao. Hakujali. Alicheka na kuingia hemani ambamo alipata silaha na kutoka tena haraka. Aliifuata njia ileile ambayo alimnyemelea yule adui. Akafuata uchochoro uleule. Hatimaye, akawasili katika msitu wenyewe. Aliufahamu kwa kuona miti ilivyoumia kwa ukali wa risasi. Ni hapo ambapo aliupoteza uso wake. Ni hapo pia ambapo alikusudia kuupoteza uhai wake. Vinginevyo angewezaje kuishi katika hali hii? Angewezaje kustahimili mishangao ya watu? Angewezaje kutazamana na watu waliomjua? Ndugu zake, rafiki na zaidi ya wote Rusia! Mpenzi wake.


Alifahamu fika kuwa amekwishampoteza. Huu si uso ambao ulimfanya Rusia ampende. Hivyo, ni uso ambao utamfanya amdharau. Akajaribu kujikumbusha sura yake ilivyokuwa. Hakuweza kuikumbuka. Ilikuwa imekwishamtoka hata akilini. Alichofahamu peke yake ni kwamba alikuwa na sura nzuri, sura inayowavutia wasichana na kuwababaisha akina mama, sura ambayo ilimfanya Rusia ampende tangu walipoonana kwa mara ya kwnanza. Mara ngapi aliwaona wasichana wakimtazama kwa tamaa? Mara ngapi aliwafumania akina mama wakiteta kuwa ana sura nzuri? Ni yupi tena atakayemtazama kwa namna hiyo? Nani atakayewaza kuwa alikuwa na sura nzuri? Amepoteza kila kitu. Ameupoteza








uzuri, ameupoteza ujana na amempoteza mpenzi.


Jioni ile ambayo kamwe uwa haimtoki akilini ikamrudia tena mawazoni.


Alikuwa amejilaza juu ya kitanda chake akisikiliza redio. Kisha, ikamjia ile hamu yake ya sikuzote, hamu ya kumwona Rusia. Alikurupuka toka kitandani hapo na kumfuata nyumbani. Kwa bahati walikutana njiani. Rusia alikuwa akimjia, pengine kwa kiu ya kumwona vilevile. Wakarudi hali wameshikana mikono, maongezi na tabasamu za Rusia ziliifanya safari yao kuwa fupi zaidi. Walipofika ndani Rusia alijitupa kitandani kujipumzisha. Sikamona akamfuata na kujilaza pembeni yake. Kama kawaida tabasamu la Rusia lilimlaki. “Joto,” Sikamona alinong’ona akivua nguo zake. “Vipi ukilivua hilo gauni Rusia?” Rusia akatii. Ngozi yake laini, nyeusi ilimeremeta kwa namna ambayo iliufanya moyo wa Sikamona upoteze baadhi ya mapigo. Uso wake vilevile, ukisaidiwa na tabasamu laini, ulimfanya aonekane si malaika mzuri tu, bali pia ua zuri lililochanua ambalo linaalika nyuki na vipepeo. Yeye alijisikia kama nyuki anayealikwa. Subira ikamtoka. Akajikuta akimsogelea Rusia na kumkumbatia. Joto la mwili na ngozi laini, matiti yake mororo kifuani na tabasamu lake vilimfanya Sikamona ajihisi mwili wake ukitaka kutoka nje ya ngozi yake. Akapiga hatua ya pili. “La, la, la, Sika, tafadhali…” Rusia alisema bila kumsukuma. Sauti yake haikuwa na hasira, lakini tabasamu lilikuwa limeuacha uso wake.








“Tafadhali Rusia,”


“Hapana. Sio leo, Sika.”


“Kwa nini?” sauti yake ilikuwa na uchungu. Rusia alimtumbulia macho yaliyojaa aibu. Kisha akamwuliza kwa sauti ndogo, “Hujui mwenzio bado bikra?” maelezo ambayo yalimfanya Sikamona si azidi kumpenda tu, bali pamoja na kumheshimu kuliko wasichana wote aliowafahamu. Akaairisha chochote alichokusudia kukifanya. Ndipo tabasamu la Rusia liliporejea. Likamfariji. Wakatulia hali wamekumbatiana, wakiisubiri siku halali kwao wote.”


Kumbe haikutokea siku hiyo. Mapenzi yao yalikuwa yamefikia ukingoni. Ilikuwa kama ndoto, ndoto nzuri ya kupendeza, lakini ndoto ambayo ingeendelea kuwa ndoto. Siku hiyo ingesalia kama kumbukumbu tu katika maisha yake, kumbukumbu katika roho yake. Kumbukumbu ambayo itaandamana naye kaburini na kuishi naye huko kuzimu.


Akairekebisha bunduki yake na kuilekeza kichwani kwake. Akajiandaa kuifyatua. “Kwa heri dunia, kwa heri Rusia…”


“Sikamona.”


Sauti hiyo, kali yenye amri, ilimfanya asite kuifyatua bunduki yake na kugeuka. Alikutana na uso wa Brigedia Chungu pamoja na askari watatu nyuma yake.


“Usifanye hivyo Sikamona” Brigedia alisema



walipomfikia. “Sisi tumekuchukulia kama shujaa wetu. Lakini unataka kuuharibu ushujaa wako kwa kujiua. Kujiua ni kitendo cha uoga. Ni tabia ya kukata tamaa. Wewe umekwishaudhihirisha ushujaa wako. Umewashinda maadui zako. Vipi uipoteze heshima yako, kijana? Usiliharibu bure jina lako, bwana mdogo. Huna sababu ya kufanya hivyo. Tafadhali turudi kambini.”


Sikamona akageuka na kuwafuata.


Hakuna sababu ya kujiua? Pengine sura hii ni shahada ya kazi aliyoifanya? Rusia amemkosa, amempoteza. Hayo hakuwa na shaka nayo. Ambacho hakupenda ni kuyaona machozi yake. Asingekuwa tayari kushuhudia maombolezo ya kifo cha mapenzi yao. Hivyo, akaamua kumkwepa maisha yake yote.













HATIMAYE, ule wakati ambao aliuogopa na kuuhofia kuliko nyakati zote ukawa umewadia ,wakati wakukutana macho kwa macho na Rusia akiwa


katika hali hii, wakati ambao hakutaka utokee.


Lakini kumbe hofu yake ilikuwa ya bure. Haikutokea kama alivyotegemea. Rusia si kwamba asingemkubali tu, bali alikuwa amemdharau kiasi cha kumcheka hadharani. Hayo yaliuzidisha msiba wake rohoni na moyoni. Yako wapi machozi ambayo alitarajia kuyaona katika uso wake? Iko wapi huzuni ambayo alidhani ingemkumba? Alikuwa amekosea. Alikosea kila aliloliwaza. Uchungu wa kujua hilo ndio uliomfanya aanguke na kuzirai. Aliporudiwa na fahamu alishangaa kumwona Rusia bado kasimama palepale akimtazama.


“Rusia… kweli Rusia unanicheka?” alifoka kwa








sauti kubwa. “Si kitu. si kosa langu wala lako. Nakuomba jambo moja la mwisho, ondoka mbele yangu na hakikisha hatuonani tena maishani. Nenda.”


Maneno ya Sikamona yakazidi kumshangaza Rusia. Amekuwaje? Akajiuliza. Sikuzote, tangu Sikamona alipoondoka amekuwa akiisubiri dakika hii kwa njaa kubwa, dakika ya kukutana naye tena. Aligundua hilo mara tu baada ya kuondoka kwake. Wala haikuwa hilo peke yake, bali pamoja na kufahamu kikamilifu kuwa asingeona faraja yoyote katika maisha, pasi ya kuwa na Sikamona.


Zamani, kabla hajakutana naye aliishi katika dunia yake peke yake, dunia isiyo na haja ya mpenzi wala mapenzi. Katika dunia hiyo vijana kadha wa kadha wenye kila hali, wakitumia kila aina ya lugha, walimjia na kumtaka mapenzi. Hakukubali. Hakukubali, si kwa kuwa hakutaka tu, bali kwa sababu hakuona hata hicho walichokitaka ni kipi. Maneno yao ya kubembeleza yalipozidi ndivyo alivyozidi kuwachukia. Vitendo vyao vya kumwonyesha mapenzi, yeye vilimfanya awakinai na kuwaona kama wendawazimu.


Lakini alipotokea Sikamona yote hayo yalitoweka katika fikra zake. Huyu hakumtongoza wala kumwonyesha chochote, lakini umbo lake, alipojitokeza mbele yake kwa mara ya kwanza, liliuondoa moyo wake pale ulipokuwa na kuuweka panapostahili, mahali penye njaa na kiu. Si kiu ya maji wala njaa ya chakula. Wala haikuwa njaa ya kupendwa ama kiu ya mapenzi la, ilikuwa kiu ya








kuwa na Sikamona daima, kiu ya kuisikia sauti yake mara kwa mara na njaa ya kuuona uso wake tena na tena. Kiu na njaa hiyo vilikuwa vikitoweka kila walipokutana, akajisikia furaha na faraja kubwa ambayo si kwamba vilimfanya ayapende maisha tu, bali pamoja na kuiona thamani yake.


Hivyo, kipindi hiki ambacho Sikamona alikuwa vitani, Rusia alikuwa taabani akimfikiria. Mara kwa mara alikuwa akizinduka usingizini huku akitetemeka kwa hofu iliyotokana na ndoto mbaya ambazo zilimtisha juu ya maisha ya Sikamona. Hofu yake kubwa ilikuwa pale alipokumbuka kuwa alikuwa ameshiriki kwa njia moja au nyingine kumshawishi Sikamona kwenda huko. Ni hapo alipoapa kuwa kama Sikamona asingerudi, basi angemsubiri hadi ahera ambako wangetimiza ahadi yao.


Wakati mwingine alipata ndoto za kuvutia. Alijiona akiwa na Sikamona katika bustani nzuri zenye maua ya kupendeza, wakiwa wameketi na kukumbatiana. Lakini alipoamka na kujikuta kakumbatia mto badala yake, hofu ilikuwa ikimrudia na machozi kumtoka.


Leo hii, alipopata habari kuwa mashujaa wanarudi, alikuwa wa kwanza kuwahi katika ukumbi ule, muda wote akiangaza macho huku na huku kumtafuta Sikamona. Vipi basi baada ya kumpata akiwa salama, awe na vituko visivyoeleweka? Alijiuliza kwa uchungu na mshangao.


Kwa mshangao huo alimtumbulia macho








Sikamona, macho ambayo yalimshinda nguvu Sikamona, hata akajikuta ametulia akiyatazama, kinyume cha matakwa yake. Kila kitu kilikuwa wazi katika macho hayo, jambo ambalo lilimfanya Sikamona ajikute amemwangukia Rusia kifuani na kumkumbatia kwa mara nyingine, huku kilio cha kwikwi kikimtoka taratibu.


“Mpenzi,” Rusia alikuwa akinong’ona kwa sauti dhaifu. “Nilikuahidi zawadi… Zawadi ya ushindi… ipokee zawadi yako, tafadhali. Nipokee. Tangu leo, mie wako… ukitaka nimeze, ukitaka nitafune…”


Sikamona hakuyaamini masikio yake. Ni kweli kuwa alimwamini rusia na kuliamini kila neno lake. Lakini hakuamini kama bado kulikuwa na uwezekano huo. Kwa nini ampe taabu, aibu ya maisha, msichana huyo mpole? Kwa nini aendelee kuwa kichekesho mitaani na simulizi ofisini maisha yake yote?


“Haiwezekani Rusia,” aliropoka. “Yaliyopita yamepita. Ilikuwa ndoto nzuri… tuendelee kuiacha iwe ndoto. Tusiiharibu…” alimaliza akijikwanyua na kuanza kuondoka tena.


“Sika… tafadhali…” Rusia alisema akizidi kumshikilia mkono. “Sika… sika… mbona sikuelewi?”



TAMATI



0 comments:

Post a Comment

Blog