Search This Blog

Thursday 29 December 2022

MALAIKA WA SHETANI - 1

  Simulizi : Malaika Wa Shetani

Sehemu Ya Kwanza (1)


Simulizi : MALAIKA WA SHETANI

Mwandishi : BEN R. MTOBWA

Imeletwa kwenu na: BURE SERIES


Sehemu ya 1


LANGO uligongwa tena. Safari hii mgongaji aligonga kwa nguvu zaidi. Kwa mbali, sauti yake ilisikika ikinong’ona, ikiwa na kila dalili ya hofu na wasiwasi, ikisema, “Tafadhali


nifungulie… dakika moja tu ya muda wako…”


Joram aligeuka kumtazama Nuru ambaye alikuwa chali, juu ya kitanda, vazi jepesi la kulalia likiwa pazia pekee lililouweka sirini mwili wake laini; unaolazimisha kutazamwa tena na tena. Hata hivyo, halikuwa pazia maridadi kiasi hicho. Wepesi na ulaini wa vazi hilo haukuwa kipingamizi cha haja dhidi ya macho ya Joram ambayo yaliweza kuona waziwazi hazina ya uzuri usiochuja, iliyokuwemo katika umbo hilo; hazina ambayo Joram alikuwa akijifariji kwa kuitazama na kuipapasa; vidole vyake vikistarehe; roho ikiburudika na nafsi yake kuridhika; muda mfupi tu kabla ya yeyote aliyekuwa hapo mlangoni akibisha hajafika.


Macho ya Nuru, ambayo yalikuwa yameanza kulainika kwa mguso wa vidole vya Joram Kiango, vilivyohitimu kugusa, yalirudiwa na uhai yalipoona maswali katika macho ya Joram. Kama aliyejua Joram anauliza nini alitamka kwa upole, “Mfungulie.”


“Anaweza kuwa nani? Na anataka nini saa hizi?”


“Majibu yenye uhakika utayapata hapo baada ya kumfungulia mlango.”


Joram alisita tena, hakuweza kufikiria nani anaweza kufanya






ziara chumbani kwake usiku huo, saa sita kasorobo! Zaidi hakuhitaji kabisa kupata mgeni yeyote muda huo alikuwa akijiandaa kwa mara nyingine kufanya ile ziara ya kila siku katika bustani isiyokinaisha iliyofichwa katika umbo la Nuru, safari ambayo kamwe haimchoshi na bado kila anaposafiri inakuwa kana kwamba ni mpya zaidi. Kama jana alisafiri kwa kila kitu kama ndege, leo itakua kana kwamba yuko katika jahazi linalosukwasukwa kwa mawimbi mazito, ambayo badala ya kutisha na kuogofya yanafariji na kusisimua. Na kesho ataivinjari bustani hiyo huku akielekea angani. Kesho kutwa…


Hapana. Si hilo lililomfanya asite kufungua mlango. Hasa ni hisia. Zilikwishamfanya aamini kuwa mgeni huyo hakuleta habari njema. Si kwamba Joram alikuwa mwoga wa habari mbaya, bali alikuwa ameamua kujitenga kwa muda na dunia aliyoizoea, dunia ya Joram Kiango.


Utashangaa kuwa chumba hiki walichokuwemo kilikuwa kidogo chenye kitanda kimoja kikiwa hoteli ya daraja la nne, au mwisho, katika kimojawapo cha vijimitaa kisicho na jina, katika vitongoji vya Tandale; kijihoteli ambacho Joram hata hakujishughulisha kufahamu jina lake ambalo lilimtoka mara baada ya kupatiwa ufunguo!


Joram, ambaye maisha yake yote ni katika miji mikuu na mahoteli ya daraja la kwanza! Joram ambaye sura yake ni maarufu katika magazeti na televisheni zote duniani, akiwa na uzito wa aina yake katika masikio ya karibu kila mtu. Naam, Joram yuleyule ambaye sasa yuko katika chumba hiki chenye kuta zilizochakazwa kwa utandu wa buibui, chumba ambacho kingeweza kutoa harufu ya kutatanisha, endapo mafuta yenye harufu nzuri ya Nuru yasingeibabaisha harufu hiyo!



Hata hivyo, hilo halikuwafanya waepuke ukatili wa kunguni na mbu jeuri, wasiosikia dawa, waliokuwa tele katika vyumba vyote vya hoteli hii. Zaidi ya wadudu hao, panya wenye ukubwa wa paka mdogo waliwadhihaki sana kwa kuwatazama kwa macho ya kebehi na kisha kuwarukia kitandani walipoona Joram na Nuru hawajishughulishi nao.


Joram na Nuru walizistahimili kwa sababu moja tu, ya kuepuka kupigiwa hodi kama hizi, ambazo zingeleta mgeni wasiyemhitaji. Hapa alikuwa mafichoni. Na amekuwa katika maficho hayo leo wiki ya pili na siku mbili, tatu, wakati huohuo






wakibadili majina haya na yale na kuvaa sura mbalimbali za bandia ili wasifahamike; tabia au mwenendo ambao waliuanza tangu waliporejea kishujaa toka huko Afrika Kusini ambako walifanya yale yaliyofanyika, yale ambayo hayatasahaulika.


Kwa kweli, stahili yao haikuwa kuwa katika chumba hiki, wakati kama huu. Haki yao ilikuwa wawe katika chumba chenye hadhi, miongoni mwa watu wenye hadhi. Ni hilo ambalo Taifa lilihitaji kuwatendea tangu ilipodhihirika kuwa ni wao walioachia lile pigo takatifu ambalo watawala dhalimu wa Afrika Kusini kamwe wasingelitoa mwilini, pigo ambalo baada ya kuandikwa sana magazetini, kutajwa katika redio na televisheni, bado waandishi mbalimbali wamejitokeza kuiweka kumbukumbu hiyo katika vitabu. Hapa nchini mwandishi mmoja hakubaki nyuma, tendo hilo la kishujaa amelitungia kitabu alichokiita Tutarudi na Roho Zetu? Ushujaa huo wa Joram Kiango na yule msichana wa aina yake, Nuru, ulimfanya Rais aamuru Joram atafutwe ili apewe tuzo ya Kitaifa na kutangazwa hadharani kuwa shujaa wa taifa na afrika. Ni kutopenda sifa za aina hiyo kulikowafanya waamue kujificha huku ili wasubiri roho za binadamu ambazo ni nyepesi kusahau mema na mashuhuri kuhifadhi mabaya zitakaposahau mchango wao, ndipo wangejitokeza na kurudia mzunguko wao wa maisha.


Jambo la kushangaza ni kwamba safari hii binadamu hakuelekea kusahau. Uchunguzi wao uliwathibitishia kuwa upelelezi ulikuwa ukiendelea kufanyika nyumba hadi nyumba, kichochoro kwa kichochoro, kuwatafuta chini ya uongozi wa Inspekta Kombora.


Ndipo wakaendelea na ukimbizi huu.


Na sasa mtu anabisha hodi, mtu ambaye kwa vyovyote si mtumishi wa hoteli hiyo. Aliendelea kugonga.


“Mfungulie,” Nuru alisema tena akiinuka na kujitupia mavazi zaidi mwilini mwake.


Joram alivuta taulo akalifunga kiunoni mwake. Kisha, akauendea mlango na kuufungua. Mtu aliyekuwa hapo mlangoni hakuwa na afya nzuri. Joram hakuona kwa nini aligonga mlango wake badala ya mlango wa daktari yeyote aliyekuwa karibu. Hali yake ilimfanya amkaribishe kwa ustaarabu kuliko alivyotegemea. Akamwongoza na kumketisha juu ya kiti hiki kikuu kuu ambacho zamani kingeweza kuitwa kochi. Sura yake ilikuwa ngeni machoni






mwa Joram. Alipoanza kusema, sauti yake ilikuwa ngeni vilevile masikoni mwa Joram na Nuru, ambaye sasa alikuwa ameketi kitandani; akimtazama kwa mshangao. Kwa kila hali mgeni huyo alionekana kuwa mtu aliyetoka nje ya nchi, jambo ambalo liliwafanya wamsikilize kwa makini zaidi. Alikuwa hasikiki vizuri.




“Jikaze kidogo… haya… unasemaje?”


Joram alimnong’oneza akiwa amemshika begani. “Joram… Kiango wewe?” aliuliza kwa udhaifu. “Ndiye. Unasemaje?”


“Nak… nakufa…” alilalamika.


Ndiyo. Kifo hakikuwa mbali sana na roho yake. Hilo Joram hakuwa na haja ya kuambiwa. Lakini bado hakuona kama hilo lingeweza kumtoa mtu huyo kokote huko alikotoka na kuja kumwambia hivyo mtu ambaye hakuwa na undugu, wala urafiki naye. Hivyo, aliendelea kumshawishi aseme kilichomleta.


“Nimetafuta s… sana wewe. Nak… nakufa… la, la,la… sifi kabla ya kutimiza… kazi… kazi niliyotumwa na… Rais wetu,” aliendela kutokwa na maneno kwa taabu.


“Rais!” Joram aliuliza. “Rais gani?”


“Ra… Ra… Rais wa Pololo… ame… nini… nituma. Nikuite… yuko hata… hatarini…”


Uwezo wa kuzungumza ulionekana kumtoka harakaharaka. Mara akaegamia kiti alichokikalia na kuanza kutapatapa huku akibubujikwa na maneno ambayo hayakuleta maana yoyote katika masikio ya Joram na Nuru. Mara alitulia kimya, macho yenye hofu yakiwa yamemtoka pima, pindi roho ikimkimbia. Dakika iliyofuata alitulia kimya kabisa, katika hali ya utulivu mkubwa; kama ambaye anasubiri tuzo baada ya kuifanya kazi aliyotumwa.


Joram na Nuru walitazamana kwa mshangao. Kwa muda hakuna aliyejua la kusema. Kisha, Joram alitabasamu na kusema polepole, “Nadhani sasa nimekuwa mtu maarufu duniani. Kama mtu anaweza kusafiri toka umbali wa kilometa nyingi kuja kufia katika mikono yangu! Mama yangu ana haki ya kujipongeza kupata mtoto wa aina yangu.”


“Joram!” Nuru alimkatiza. “Hili sio jambo la kufanyia mzaha. Lazima tujue la kufanya. Sasa hivi tuna mzigo mzito mikononi mwetu. Mzoga wa tembo ni mwepesi kuliko maiti ya mtu. Na tuko nayo chumbani. Kumbuka tumepanga kwa majina ya






bandia. Hilo peke yake linatosha kututia hatiani. Lazima tuamue la kufanya haraka.”


Joram alitabasamu tena. Safari hii tabasamu lake lilikuwa halisi, likiufurahia ushujaa wa msichana huyu. Msichana wa kawaida sasa hivi angekuwa akitetemeka, machozi yakimtoka. Mwingine angekuwa amezimia au kutapika kwa hofu ya maiti. Huyu alikuwa imara, kama alivyo. Baada ya tabasamu hilo Joram alimrudia marehemu na kumtazama kwa makini zaidi.


Mwili wa marehemu ulionyesha kuwa hakuwa mtu aliyejua sana amani. Alikuwa mkakamavu, mwenye makovu hapa na pale. Hata hivyo, makovu hayo hayakuwa kisa cha kifo chake cha ghafla. Joram aliendela kumkagua. Katika mfuko wake mmoja alipata hati yake ya usafiri. Mfuko wake mwingine ulikuwa na ramani pamoja na pesa chache ambazo jicho la mtu aliyehishiwa lingeziona nyingi sana. Ni katika mfuko wa siri sana, uliofichika mapajani, ambapo Joram alipata bastola ndogo.



Baada ya kuhakikisha kuwa hakuacha kitu chochote katika mwili wa marehemu, alimfunika kwa shuka moja ya chumba hicho. Kisha, alirejea kitandani ambako alianza kuvichunguza vitu vya marehemu kwa dhamira ya kupata chochote ambacho kingeweza kumsaidia katika mkasa huu wa kutatanisha.


Hati yake ya usafiri ilimwonyesha kama mwandishi wa habari, jina lake likiwa wazi kwa herufi kubwakubwa, Patauli Kongomanga. Umri wake ulikuwa miaka arobaini na mbili. Hati hiyo ilikuwa na mihuri ya nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya ambako aliwahi kutembelea. Alikuwa mtu wa safari mara kwa mara. Ni macho yake katika picha hiyo ambayo yalimwonyesha Joram kile alichohitaji kukiona, kuwa kama alikuwa mwandishi wa habari, hakuwa mwandishi wa kawaida. Hiyo ilikuwa kazi yake ya ziada tu. Kazi yake hasa ingekuwa mbali sana na uandishi na karibu zaidi na ukachero. Hilo lilikuwa wazi katika macho ya mtu huyo pichani. Joram asingeshindwa kuyafahamu macho ya watu hao, hasa yanapomtazama mpiga picha. Huwa yana aina yake ya utazamaji ambayo makachero wengi hushindwa kuificha.


Pesa alizokuwa nazo zilikuwa za nchi mbalimbali pamoja na Tanzania. Upande mmoja wa noti zao, ulikuwa na picha ya Rais wao, ikiwa sura ya mtu aliyeshiba, macho ya mtu mwenye njaa. Upande wa pili ulikuwa na picha ya vitu mbalimbali kama mazao






mashuhuri, wanyama maarufu; na kadhalika.


Joram alimtazama kwa makini Rais huyo, mtu ambaye inasemekana anamwita! Anamwita kweli? Na anamwitia nini? Na kwanini mtu aliyetumwa kumwita akate roho kabla hajaukamilisha ujumbe wake? Kitu gani hasa kilimwua?


Jibu lisingeweza kuwa karibu kiasi hicho. Alijua kwa vyovyote alikuwa ametumbukia pasi ya hiari katika shimo lenye kiza kinene ambacho kilimhitaji yeye kama Joram Kiango kulivinjari na kupata jibu.


“Utafanya nini?” Nuru, ambaye alikuwa akimtazama kwa utulivu muda wote huo, aliuliza.


“Naona kama sina la kufanya zaidi ya kumtii marehemu.


Naitwa na Rais wa Pololo.” “Utakwenda?”


“Vipi nisiende? Nawaheshimu sana maraisi wetu, hasa wale waliopigania uhuru. Unajua wamebaki wachache sana.”


“Utakwenda!” Nuru aliuliza kwa mshangao. “Una hakika gani kuwa unaitwa? Yawezekana huyo alisema hayo kwa kutapatapa tu pindi roho ikimkimbia. Na kama sivyo, huoni kuwa yaweza kuwa safari ya hatari sana? Kama mjumbe aliyetumwa tu kukuita ameweza kupoteza maisha kabla hata hajaufikisha ujumbe wake kikamilifu, wewe unayeitwa utakuwa katika hali gani?”


Joram alitabasamu kidogo. Akaushika mkono wa Nuru na kuutomasatomasa taratibu. Kisha, akasema, “Tangu lini umeanza kujenga tabia ya uoga? Usinidanganye, unapenda sana kwenda huko vilevile. Huwezi kujua. Pengine naitwa nikawe Waziri Mkuu au Mkuu wa Majeshi. Yawezekana tukapokelewa kwa shangwe na kupewa heshima ya hali ya juu na huduma zote za kifalme. Siwezi kuichezea bahati kama hiyo. Binadamu uishi mara moja tu.”


Nuru alijua wazi kuwa Joram alikuwa hasemi kweli. Katika yote aliyoyategema kwenye ziara kama hiyo heshima ya kifalme haikuwemo kabisa akilini mwake. Akamtazama kwa macho yaliyomfaya amsikie wazi kama anayesema, “Wacha mzaha.”



Hilo lilimfanya Joram acheke tena na tena na kusema polepole, “Hata kama kuna hatari, naamini hatari hizo si mbaya kama kuadhibiwa na kunguni kusimangwa na mende, kuchezewa na panya huku ukiumwa na mbu wasio na huruma. Unajua,



Waafrika wengi hadi leo bado tunakufa kwa malaria zaidi ya risasi? Tutaendela kujificha hadi lini tukisubiri kifo cha malaria. Tutakwenda zetu safari hii fupi. Tutakaporudi wanaotutafuta watakuwa wamekwishachoka kama si kutusahau kabisa.”


Aligeuka kuyatazama maiti ambayo bado yalikuwa yamelala juu ya kiti kwa utulivu, yakiwa hayana dalili zozote za kufahamu uzito wa mkasa yaliouweka mikononi mwa wenyeji wake. Kisha, Joram alimgeukia Nuru na kumwuliza kwa sauti nyembamba, “Unafahamu nini juu ya nchi ya Pololo?”

KAMA nchi zote nyingine nyingi za Kiafrika, Pololo imetengwa na dunia ya nje kwa milima mirefu, mito mikubwa na misitu ya kutisha kiasi cha kuifanya isionekane vizuri wakati kamera za wataalamu wa ramani zilipoanza kazi. Ni hilo ambalo lilisababisha nchi isijulikane kwa kila mtu. Isipokuwa watu wachache wenye macho ya udadisi na mioyo ya utafiti. Vinginevyo ingeweza kuwa nchi ya kufikirika tu kama kufikirika au kusadikika zilizofikirika na kusadikika katika kichwa cha


hayati Shaabani Robert.


Misitu hiyo iliyoizunguka nchi hii ilikuwa ifadhi nzuri ya wanyama pori wakali kwa wapole, wanaotisha kwa wanaovutia; wenye thamani kwa wasio na thamani, kiasi cha kuifanya nchi kuwa kipenzi cha wapenzi wa maliasili toka duniani kote. Milima pia ilikuwa na utajiri. Licha ya mtu kutoka atokako na kusafiri hadi huku kwa nia ya kuiona tu milima hiyo, bado katika ardhi ya miamba yake muumba aliifanya kuwa ifadhi malizawa ya madini mbalimbali ya thamani kama dhahabu, shaba na almasi, madini ambayo yaliipatia nchi chochote cha kuridhisha. Wala si hayo tu. Mito na maziwa yalikuwa na samaki wanono na ardhi ilijaa rutuba iliyoafikiana na karibu kila zao lililopandwa.


Zaidi ya rasilimali hizo asilia bado nchi ilikuwa na watu wengi, wenye vipaji mbalimbali ambavyo vilitumiwa kulinufaisha taifa. Kama ilivyo kwa kila serikali, serikali hii pia ilikuwa vitani usiku






na mchana ikipambana na wavivu, wazembe na wazururaji kwa kuhakikisha wanatumia muda wao kwa manufaa yao na taifa lao.



Lakini kama nchi nyingine zote duniani nchi hii pia ilikuwa na tatizo la binadamu kutothamini kazi yake. Mafundi wengi walikwishapoteza moyo wa kuuheshimu ufundi wao, jambo ambalo lilichangia katika uzalishaji wa bidhaa duni. Wasanii hawakuiona haja ya kuuthibitisha usanii wao; matokeo yake yakiwa kutokidhi kiu ya halaiki. Hivyo, kama kote kwingineko kasoro zilikuwa tele katika kila kitu; nyimbo hazikuwa maridadi kama za kale, michoro haikupendeza kama awali; waandishi hawakuandika kwa roho moja kama ilivyotakiwa; wahunzi hawakukamilisha kila walichotengeneza; wachezaji hawakuitia akilini michezo, n.k. Wakati ulikuwa umeondoka na tabia ya mtu kuiheshimu kazi yake.


Watu wa aina hiyo walikuwa tele katika kila wizara na kila idara. Idara ya uhamiaji ikiwa na sehemu yake, jambo ambalo lilichangia kufanikisha hila za Joram Kiango na mpenzi wake, Nuru, hata wakaingia nchini humo kwa majina ya bandia na mizigo yao yenye vitu hatari bila kushukiwa na mtu yeyote.


Walitua kwa ndege ambayo ilitua katika uwanja huu ambao Joram hakuona kama kweli ulistahili kuitwa “Wa Kimataifa.” Wakiwa hawajui kama walikuwa wageni wanaohitajika katika nchi hiyo waliamua kuingia kwa siri wakitumia hati zao bandia. Afisa wa Uhamiaji aliyekagua hati hizo hakushuku chochote kuhusu picha ya wazee wawili waliokuwa katika hati hizo na hawa wawili ambao walisimama mbele yake wakimtazama.


“Mmekuja kwa…” aliuliza.


“Hamtaki wageni baba?” Joram alimwuliza.


Afisa huyo alitabasamu kabla hajajibu, “Tunawapenda sana


wageni, mzee. Kuuliza ni moja ya kazi zetu. Si kwa nia mbaya.” “Hapana shaka, baba. Tumekuja kutembea,” Joram alimjibu. “Kutalii” Nuru alimsahihisha kwa sauti ya kizee. “Safari kama


hii inaitwa utalii kwa sababu hatuna shida maalum.”


Afisa huyo alicheka akigonga muhuri juu ya hati zao. “Mtafikia


hoteli ipi?” aliuliza huku akisogeza fomu mbele yao.


“Inaitwa nini hoteli kubwa kuliko zote katika mji huu?” lilikuwa swali ambalo lilikusudiwa kuwa jibu la Joram. “Umri huu sio wa kufikia hoteli ndogondogo.”






“Fikieni Golden View,” aliwashauri. “Lakini ni ghali sana.” “Tunataka ghali… andika hiyo,” Nuru alimjibu.


Mambo hayakutofautiana na hayo pindi mizigo yao ikikaguliwa. Si macho wala mikono ya mkaguzi huyo iliyoweza kuifikia mifuko ya siri ambayo ilihifadhi silaha za kujihami ambazo Joram hakupenda kutengana nazo.


Muda mfupi baadaye walikuwa katika kimojawapo kati ya vyumba mia nne vya hoteli hiyo. Walipobaki peke yao walitazamana, wakatabasamu. Kilichowachekesha ni jinsi walivyojiona kama watu wengine badala ya wao wenyewe kwa jinsi walivyojibadili ki mavazi na kuvaa vitu mbalimbali vya bandia kiasi cha kuonekana kama wazee wenye umri unaozidi miaka sitini.


Kilikuwa chumba cha hali tofauti kabisa na kile walichokiacha nchini Tanzania. Hiki kilikuwa Self contained, kikiwa na vitanda viwili vyenye hadhi, simu, kochi kubwa la sofa na kila hitaji ambalo mtu mwenye pesa angehitaji. Hali ya hewa pia licha ya kupozwa na kiyoyozi ilikuwa tulivu kutokana na upeo mpana uliokuwa wazi mbele ya hoteli hiyo, ukitoa nafasi kwa bustani kubwa yenye maua ainaaina ambayo ilienea hadi pwani ya ziwa Bululu.



Rangi mbalimblai za maua hayo, pamoja na mng’aro wa maji; hasa nyakati za asubuhi na jioni, ndizo zilizoifanya hoteli hiyo iafikiane na jina lake.


Walifuatana bafuni ambako walioga na kuusheherekea ujana wao. Kisha, waliurejea uzee wao kwa mavazi na hila mbalimbali. Ndipo Joram alipopiga simu kwa wahudumu kuomba chakula na vinywaji. Vilipoletwa walikula na kunywa kwa utulivu.


Ni wakati huo wa kunywa Joram alipokiruhusu kichwa chake kuuvinjari upya mkasa uliokuwa mbele yao, ambao uliwafanya wafike katika nchi hii bila mategemeo.


Kutembelewa na mgeni, aseme kuwa Rais anakuita, kisha akate roho papo hapo ni jambo ambalo lisingekosa kumvutia mtu yeyote, hasa Joram Kiango aliyechoshwa na kuwa mkimbizi katika nchi yake. Kadhalika, kilichomfanya aamue kuifunga safari hii haraka ni baada ya kuchunguza kifo cha mtu huyu aliyejiita Patauli Kongomanga.


Kwa Joram haikuwa kazi kubwa kufanya uchunguzi huo. Alichofanya ni kuichukua mizigo yao na kuhamia hoteli nyingine katika wilaya hiyo ya Kinondoni, alfajiri hiyohiyo. Kisha, aliinua






simu na kuipigia polisi akiiarifu kuwa katika hoteli fulani, chumba fulani kuna mtu ambaye anaonekana kama roho yake imemkimbia.” Baada ya hapo hakuwa na kazi nyingine zaidi ya kushuhudia wenye hoteli hiyo wanavyoadhiriwa na vijana wa Jeshi la Polisi kwa maswali kemkem ili waeleze chochote walichokijua juu ya marehemu. Wakiwa hawana wanalolijua hawakuwa na kipingamizi chochote ambacho kingeweza kuwaepusha wasihifadhiwe ndani kuisaidia polisi pindi uchunguzi unaendelea. Joram akayahamisha macho na masikio yake toka huko na kuyaelekeza Muhimbili ambako marehemu alikuwa akifanyiwa uchunguzi. Hakuchelewa kupata fununu zenye uhakika kuwa marehemu alikufa kwa aina fulani ya sumu ambayo inaweza kukaa katika mwili wa binadamu kwa siku tatu hadi nne kabla ya kutimiza wajibu wake.


Ni hilo lililomvutia zaidi Joram. Vipi mtu atumwe kwake akiwa na sumu mwilini? Sumu hiyo aliinywa mwenyewe au kunyweshwa bila ya yeye binafsi kuwa na habari? Na kwa nini? Yawezekana kuwa ilikusudiwa kuwa mara baada ya kuitamka siri hiyo asiishi muda mrefu? Yawezekana kabisa, kwani haikuwa kazi ndogo kumpata Joram Kiango kwa jinsi alivyokuwa amejificha. Siri gani hiyo ambayo ni nzito kiasi hicho?


Maswali yalikuwa tele na ziada. Jibu hakuwa nalo hata moja, jambo ambalo lilimfanya aamue kuingia katika nchi hii kama ilivyo; kwa siri sana kwani hakujua kama alikuwa mgeni anayehitajika au la.


Naam. Tayari amefika. Iliyobaki ilikuwa kumwona Rais ili aone kama kweli aliitwa. Lakini kabla ya kumwona Rais Joram aliamua kufanya uchunguzi mdogo juu ya marehemu na wenyeji wake.



Akiwa katika hali ya uzee bandia hakujisikia uchangamfu wowote kuweza kufanya kazi nzito kama hizo katika nchi ngeni kama hiyo. Hivyo, alichofanya ni kwenda katika maduka ya vitabu na maktaba ambako alijipatia vitabu mbalimbali ambavyo vilihusu nchi hii, wananchi wake na hasa Raisi wao. Kwa bahati, zaidi ya vitabu vitano vilikuwa vinavyomhusu Rais binafsi, kimoja kikiwa kimeandikwa na Rais mwenyewe. Siku tatu zikafuata Joram alikuwa mzee hasa, mvivu wa kutembea hovyo; na badala yake alipenda kutulia chumbani mwake akijisomea kwa makini. Pale ambapo alihitaji mawaidha ya mtu hai zaidi ya mahubiri






ya mwandishi alijadiliana na Nuru ambaye daima alikuwa na majibu yaliyomsaidia Joram kwa njia moja au nyingine.


Siku tatu baadaye Joram alijiona ameelimika tosha, juu ya nchi hii. Alikuwa tayari kuanza upelelezi wake.


Wafanyakazi wa hoteli walisikitika walipoagwa na wazee hawa wawili, wenye tabia nzuri, sura nzuri na wasio na mikono ya birika kama watu wengi wenye umri huu. “Mnarudi nyumbani?” wafanyakazi wa hoteli waliwauliza.


“Hapana tunaendelea na safari za hapa na pale. Tuna miezi mitatu kutembelea nchi zetu za Kiafrika. Ulaya kumetuchosha,” yalikuwa majibu ambayo baadhi ya wafanyakazi waliyapata.


Wafanyakazi wakasaidia kuitoa mizigo yao hadi nje ya hoteli ambapo walikodi gari lililowaelekeza uwanja wa ndege. Lakini hawakufikia huko. Dereva wa gari hilo hakuona haja ya kudadisi chochote alipoelekezwa kuwapeleka mahala pengine badala ya uwanja wa ndege. Nauli ya mara mbili ya kawaida iliumeza moyo wake wa udadisi.


Saa kadhaa baadaye wafanyakazi wa Golden View walipokea wageni watano. Miongoni mwao walikuwemo vijana wawili, bibi na bwana, ambao jicho la kawaida lisingewapita bila ya kutulizwa juu yao. Walihitaji chumba. Wakakipata. Walipofika kwenye mlango wa chumba hicho hawakustahimili tabasamu lililowajia ghafla. Kilikuwa chumba chao kilekile walichokiacha muda mfupi uliopita. Chumbani waliangua kicheko ambacho pia kilisheherekea kurudi kwao katika dunia ya ujana. Safari hii walihitaji hila ndogo sana kuwafanya wasijulikane kama Joram na Nuru. Joram alikuwa haachani na miwani pamoja na vijidevu vichache ambavyo vilimchafulia sura. Nuru alibadili rangi ya nywele na ngozi. Wakiwa mbali kiasi hiki hawakuona vipi wangeweza kushukiwa kama Joram na Nuru, hasa kwa hati zao nyingine bandia ambazo walizipata katika ule mzunguko wa hapa na pale uliowafikisha hadi Afrika Kusini.


“Sasa naweza kuanza upelelezi wangu kivitendo badala ya kinadharia,” Joram alimweleza Nuru. “Nataka kumfahamu vizuri zaidi rafiki yetu marehemu Kongomanga kabla ya kumkabili Rais.”




***


Haikuwa kazi kubwa kwa mtu kama Joram kupata mwanya






ambao ulimwezesha kuanzisha uchunguzi dhidi ya hayati Kongomanga. Wakati huo habari zake zilikuwa zikiandikwa sana magazetini, japo kwa ufupi.


‘Mwandishi wa habari ambaye amefariki kimiujiza nchini Tanzania. Yalisema. Maiti yake yaliokotwa katika vichaka vya pwani ya Bahari ya Hindi.’


Gazeti moja lilitia chumvi. ‘Kisa cha kifo chake hakijafahamika. Walikubaliana. Uchunguzi bado unaendelea.’


Siku mbili tatu baadaye ilifahamika kuwa alifariki kwa sumu. Hapo tena zikaanza kupikwa habari za kuchekesha katika magazeti yote. Mara ‘Alipewa sumu na wanawake ambao walikuwa wakimgombea.’ Mara ‘Aliamua kujiua, baada ya kugundulika kuwa alikuwa na virusi vya UKIMWI.’ Mara ‘Aliuawa kwa hila baada ya kugundua mambo fulanifulani ambayo serikali ya Tanzania haikutaka yatolewe hadharani,’ na kadhalika. Kwa siku mbili maongezi ya kifo hicho yalitawala mitaani, jambo ambalo lilimpa Joram mwanya wa kupenyeza maswali yake juu ya marehemu.


Na siku ambayo maiti yalirejeshwa nyumbani Joram alikuwa miongoni mwa watu walompokea marehemu. Macho yake hayakufanya kazi ya kulitazmaa jeneza. Alikuwa akitafuta macho ambayo yangeweza kueleza chochote cha ziada. Hakufanikiwa sana. Watu wote walikuwa wakimtazama kama mtu wa kawaida tu. Hata hivyo, jicho la Joram lilimwona kwa mbali mtu ambaye alionekana kama mwenye mengi zaidi ya watu wengine. Katika pilikapilika zilizofuata mtu huyo alijikuta yuko bega kwa bega na Joram.


“Amekufa akiwa kijana sana.” “Kabisa. Kufa kabla hajaoa!”


“Alikuwa mwandishi maarufu sana nchini.”


“Ndiyo… Lakini umaarufu wake mimi ulinitatiza… mandishi yake hayaonekani mazuri kuliko ya wengine… Ajabu ni jinsi alivyokuwa akipata safari za nchi mbalimbali mara kwa mara…”


“Kana kwamba alikuwa na kazi nyingine ya ziada.”


“Kama hivyo…” kisha ghafla mtu huyo aligutuka. Kwa mara ya kwanza akageuka kumtazama Joram. Hofu ilikuwa wazi katika macho yake hasa baada ya kugundua kuwa alikuwa akizungumza na mtu asiyemfahamu, “Wewe nani?” aliuliza.


Joram akamfariji kwa tabasamu lililodhamiriwa kurejesha






uhusiano. “Naitwa Brown Paul ni…”


Mwenyeji wake hakumsikiliza. Alifanya haraka kujipenyeza katika makundi ya watu na kutokomea, Joram akatabasamu tena, safari hii likiwa tabasamu la uchungu. Mtu wa kwanza aliyeonekana mwepesi wa kuufumbua mdomo wake alimtoroka kabala hajaropoka chochote cha haja, jambo ambalo lilimwashiria ugumu wa kazi iliyokuwa mbele yake. Upelelezi katika nchi ya kigeni ni sawa na kutembea katika pango kubwa lenye kiza totoro.


Naam, hayo Joram aliafikiana nayo kikamilifu baada ya siku mbili za kuhangaika pasi ya kugundua chochote cha haja kuhusu marehemu. Aliyoyafahamu ni yale yale ya kawaida: alikuwa hajaoa, hakuwa na rafiki wa kike maalum; alikuwa na safari nyingi kiasi cha kuwa mgeni katika nchi yake mwenyewe; awapo mjini alipendelea kula hoteli hii na kunywa baa ile; elimu yake ilikuwa ya shahada ya kwanza ya Chuo Kikuu ambayo aliipata humohumo nchini; na mengi ya kawaida. Jorm alihitaji yale ya zaidi ya kawaida. Hakuyapata. Na hakuthubutu kusisitiza maswali ambayo wasikilizaji wake wangemtilia mashaka. Hivyo, akaamua kuukomesha upelelezi wake.


“Sasa unafanya nini?” Nuru alimwuliza.


“Sina haja ya kuupoteza zaidi muda wangu.” Lilikuwa jibu la Joram. “Nimeitwa na Rais wa nchi hii. Nadhani ataniamabia yote ambayo nahitaji kuyafahamu. Kwanza, nastahili lawama. Mtu aliyekuwa akifa aliniomba nimwone Rais ambaye yuko hatarini. Lakini hadi leo sijafanya hivyo. Aibu iliyoje!”




***


Kama ilivyo kwa marais wengi wa nchi za Kiafrika ambao waliongoza mapambano ya kupigania uhuru hadi ulipopatikana, Abdul Shangwe alikuwa Rais ambaye jina lake lilikuwa zito sana masikioni mwa watu. Aliimbwa katika tungo na mashairi anuwai, akipambwa kwa sifa zote njema na kuombewa kila la heri, hali ambayo ilimfanya kila mtu ajikute akimpenda, hata mwananchi wa kawaida, akiamini kuwa alikuwa na kiasi fulani cha uungu katika utu na fikra zake. Vinginevyo, angewezaje kuwatetemesha Wazungu ambao waliwachapa viboko baba zetu mbele yetu? Angewezaje kuwafukuza watu hawa walioapa kwa damu kuwa wasingeondoka katika nchi hii? Watu ambao licha ya viapo vya






maneno walikuwa na silaha zote na jeshi lililohitimu kila aina ya ukatili? Lakini yeye aliwatoa kwa maneno tu. Kwa siasa. Walitoka huku wakicheka. Kila palipokuwa na mtu Mweupe pawekwa mtu Mweusi. Ndiyo; walilalamika kichinichini lakini mbele yake walimsifia na kumtakia heri. Na bado hadi leo wanaipa nchi yake mikopo na misaada kila anapohitaji. Binadamu gani wa kawaida anayeweza kufanya hayo?


Sifa hizo ziliambatana na simulizi ambazo hazikuweza kuthibitishwa, ambazo hazikuwa na idadi juu ya mambo mbalimbali yaliyokuwa yakitendeka enzi za madai ya uhuru, kwamba kuna wakati mkoloni alimkamata Shangwe na kumfungia katika chumba chenye baridi kali kwa dhamira ya kumwangamiza. Siku ya tatu walikuta tayari amekufa na kukaukiana. Kwa furaha wakoloni hao walimshonea katika gunia na kumpeleka ziwani ambako walimtumbukiza majini. Kisha, walirejea mjini wakiwa na haraka ya kuvifikia vyombo vya habari ili watangaze kuwa Shangwe ametoroka. Lakini walipofika mjini walishangazwa kukuta mkutano mkubwa sana ukiwa umekusanyika katika uwanja wa shule moja ya sekondari. Wananchi walikuwa wakimshangilia kiongozi wao ambaye alikuwa akihutubia kwa nguvu kuwataka wasiogope chochote bali waendelee kushikamana hadi watakapojipatia uhuru wao. Wazungu hao waliokuwa wametokea ziwani kumtupa Shangwe hawakuweza kuyaamini macho yao kwani mhutubu hakuwa mwingine zaidi ya Shangwe, na akiwa na afya njema kabisa.


Katika tukio jingine inasemekana Shangwe alikuwa katika moja ya safari zake za ng’ambo katika harakati za kudai uhuru. Wenyeji wake ambao walimchukia na kumwogopa walimwandalia chumba ambacho kiliandaliwa maalumu kwa ajili ya kumwangamiza. Chini ya chumba hicho kulikuwa na shimo kubwa, chini ya kitanda. Huko shimoni iliwekwa mikuki na mishale ambayo ingechomwa na kumwua. Lakini Shangwe alilala juu ya kitanda hicho bila ya wasiwasi. Kulipokucha alianza harakati zake za hapa na pale akimwona huyu na yule kupigania uhuru. Adui zake walishangaa. Mmojawao alipokikaribia kitanda hicho ili aone kilichotokea alitumbukia shimoni na kupoteza maisha yake.


Hadithi hizo ni pamoja na nyingine nyingi za kutegwa mabomu ambayo hayakulipuka, kupigwa risasi ambazo hazikuingia;


kupewa sumu ambazo hazikumdhuru na kadhalika. Zilienea sana mitaani, mababu wakisimulia wajukuu zao, wengi wao wakidai kuwa hayo waliyaona kwa macho yao wenyewe. Ni hadithi ambazo zilithibitisha umashuhuri wake miongoni mwa wananchi. Wengi waliamini bila yeye nchi isingekuwa kama ilivyo. Wako ambao walikuwa na hakika kuwa yeye alikuwa mteule wa Mungu kwa ajili ya nchi ya Pololo.


Yote hayo Joram aliyasikiliza sana lakini hakuyasikia. Hakuwa mgeni wa nchi mbalimbali za Kiafrika. Alijua viongozi wengi wa Kiafrika wanavyopenda sifa na utukufu zaidi ya pesa na uhai. Hivyo, ambayo aliyasikiliza na kuyasikia ni yale ambayo alikuwa anayasoma katika vitabu mbalimbali vya historia, yale ambayo yamemchora Shangwe kama Shangwe binadamu.


Historia yake ilianza miaka sitini na minane iliyopita, alipozaliwa akiwa mtoto pekee katika familia yenye baba mmoja na mama wanne. Baba yake alikuwa askari aliyestaafu baada ya vita vikuu vya kwanza. Alikuwa akikaribia kufa bila mtoto hadi mkewe wa kwanza alipofanya hayo maajabu ambayo yalisimuliwa kijijini hapo kwa siku nyingi, kujifungua mtoto mzuri wa kiume wakati hata umri wake ulianza kumsuta. Baba mtu akamfanya mtoto huyu kama nusu Mungu. Akataka ampe kila kitu. Lakini mtoto hakutaka chochote zaidi ya elimu. Mara akawa ameyamaliza madarasa yote yaliyokuwa katika nchi hiyo. Mara ikaletwa barua, anaitwa kwenda ng’ambo kuongeza elimu. Mara elimu imemtosha sasa anataka uhuru, kumfukuza Mzungu toka katika kiti cha enzi. Wazazi wake hawakuweza kumwelewa. Iliwashangaza zaidi kuona watu wote nchini wako nyuma ya hako katoto kao, wakikasikiliza kwa makini na kukashangilia kwa nguvu. Na kisha, kama ndoto, siku moja, baada ya makelele ya miaka mingi; bendera ya mtu Mweupe ikashuka na mtu Mweusi ikapanda. Baba mtu hakuweza kuyaamini macho yake hadi siku ile ambayo alifuatwa na gari lisilo na namba, lililopambwa kwa bendera; likamchukua yeye na mkewe hadi Ikulu ambako walipigiwa saluti njia nzima hadi walipoingia katika chumba ambacho walimkuta mtoto wao kakalia kiti kilichoonekana chenye hadhi kuliko viti vyote nchini. Walimkumbatia na kuangau kilio kwa sauti kubwa.


Mtu anaweza kusema kuwa Abdul Shangwe alikuwa mtu aliyeumbwa ili aongoze. Uongozi ulikuwa katika damu na mishipa






yake. Uongozi ulikuwa katika vitendo na maneno yake. Ni hayo yaliyomwezesha kuwa Rais wa nchi, mwenyekiti wa chama pekee kinachotawala; Amiri Jeshi na mkuu wa vyuo vikuu vyote; pamoja na vyeo vingine tele ambavyo havikuyafikia masikio ya wananchi wa kawaida. Watu wote wa chini yake walikaa na kumsikiliza, wakitimiza wajibu wao bila shaka wala minong’ono. Kama kuna manung’uniko hayo pia hayakuyafikia masikio ya kawaida.


Machoni mwa wananchi wote, na hasa katika vyombo vya habari, Shangwe alikuwa na angeendelea kuwa mtukufu, mtakatifu, mwanamapinduzi shujaa, mwenye roho ya chuma na akili za ajabu. Mtu yeyote ambaye angethubutu kutamka chochote kisicho cha kawaida dhidi yake alionekana kama punguani au mchafu anayekusudia kuleta fujo.




***


Joram alikuwa ana yote akilini mwake alipoifanya ziara hii nyumbani kwa Rais. Akiwa kafuatana na Nuru, siku zote tatu ambazo alikwenda Ikulu kuomba kuonana na Rais kwa madai kuwa wao ni wageni toka Tanzania ambao walikuwa na hamu sana ya kumwona Rais Shangwe baada ya kuzisikia sifa zake kwa muda mrefu, uongo wake ulizaaa matunda wiki nzima baadaye. Na hata hivyo, hayo yalitokea baada ya kujaza fomu nyingi zinazotatanisha na kujibu maswali yanayokera. Zaidi ya hayo, badala ya kuonana naye Ikulu walijikuta wakipakiwa katika gari ambalo liliwaleta nyumbani kwake. Waliwavuka walinzi wote baada ya maelezo mafupi yaliyotolewa na askari wawili waliowaleta. Wakaongozwa ndani.


Ilikuwa nyumba kubwa kama yalivyo majumba ya marais wengine. Na ilikuwa imezungukwa na bahari ya bustani nzuri, yenye matunda na maua ainaaina. Ndani ilikuwa msitu wa vyumba mbalimbali ambavyo vilihitaji mwenyeji sana kuweza kuvuka hadi chumba cha maongezi. Ni huko walikomkuta Rais, kasimama mlangoni akiwasubiri.


Ni jambo la ajabu jinsi ambavyo picha huyalaghai macho. Picha, gazetini na katika televisheni yaweza kukufanya mtu umwone tofauti kabisa na alivyo. Ndivyo Joram na Nuru walivyomwona Shangwe. Katika picha hizo alionekana mtu ambaye daima yuko kikazi, macho yake maangavu yakitisha na






kulazimisha. Hivyo, kiasi walitegemea kukutana na mtu ambaye daima yuko kazini na ambaye angewafanya wamwogope na kumwona kama baba yao. Lakini ilitokea kinyume chake kabisa. Shangwe alitokea kuwa mtu mpole na mcheshi. Aliwapokea kwa mikono, akiwakumbatia na kuwaita ‘Marafiki wapenzi,’ lakini akilini Joram alijiona kama mjukuu wake badala ya rafiki.


Huku akiwa amewashika mikono, kila mmoja upande wake, aliwaongoza hadi katika chumba cha maongezi. Huko aliwaelekeza kukalia makochi ambayo yaliwalaki kwa ulaini. Kisha, yeye pia akaketi katika kochi lililowaelekea. Askari waliokuwa bado wamesimama mlangoni walipoona Rais katulia waligeuka na kuondoka taratibu.


“Ndiyo vijana,” Shangwe alikuwa akiongea. “Ni jambo la kupendeza sana kusikia mtu akitoka mbali kama nyinyi mlivyofanya kwa nia ya kuniona tu. Inafanya nidhani kuwa nafanya mema, yanayoifaa nchi na watu wangu. Poleni sana kwa usumbufu mliopatiwa na vijana wangu kabla ya kuruhusiwa kuniona,” alisema kwa upole.




Kila neno lilisindikizwa na tabasamu. Kiingereza chake kilikuwa chepesi, kinyume na viongozi wengine waliosoma zamani ambao hupenda kutumia maneno magumu na kuiga sauti ya Mzungu fulani kwa dhamira ya kumfanya mtu anayezungumza naye ajione kuwa hakusoma vizuri.


“Lakini ebu niambieni kweli,” aliendelea kuzungumza. “Ni kweli kabisa kuwa mmetoka kwenu kwa ajili ya kuniona mimi tu, au ni pamoja na safari zenu za ujana?”


Joram alikohoa kidogo kuitengeneza sauti yake kabla hajajibu. “Nia pekee ya safari yetu ni kukuona wewe,” hatimaye alisema.


“Kwa ajili ya sifa zangu? Nimefanya lipi la haja ambalo linaweza kulinganishwa na mengi ya ajabu yaliyofanywa na Rais wenu wa kwanza, Julius K. Nyerere?”


Kuwa mwanasiasa na hasa Rais wa nchi ni kuwa mwigizaji. Mwanasiasa mzuri daima ni mwigizaji mzuri. Atajitia ukali mahala pasipo na ukali, kadhalika, atajitia upole mahala panapohitajika ukali; mradi dhamira yake ifanikiwe. Ni hilo ambalo huwafanya marais wote ulimwenguni kuweza kusimama mbele ya halaiki kubwa ya watu na kulaani kwa ukali kitu ambacho rohoni wanakiamini. Na siku chache baadaye wanaweza kukitetea kitu hichohicho, katika halaiki hiyohiyo; na bado wakaungwa mkono.






Naam, uigizaji umo katika damu za marais wote ulimwenguni, Shangwe akiwa na sehemu yake. Hayo Joram aliyasikia kwa namna ya hisia katika sauti yake. Aliona kama aliyekuwa akichezewa kwa maneno yasiyo na msingi, wakati Shangwe akiwa na hakika kamili ya msafara wake. Hivyo, aliamua kuukatiza mchezo huo kwa kumwambia taratibu, “Mtukufu Rais. Kwanza sina budi kukutaka radhi kwa uongo mwingi ambao nimekuwa nikiutumia tangu nilivyoingia nchini mwako hadi nilipofika mbele yako. Kwanza kabisa, ningependa kukuomba uyasahau majina yetu yote tuliyotaja na kujaza katika hati mbalimbali. Kwa jina halisi mimi ni Joram Kiango na mwenzangu hapa ni Nuru.”


Kama alivyotegemea Joram hakuuona mshangao wowote katika macho ya Rais. Badala yake aliona tabasamu jembamba likijitokeza na kupotelea katika kona moja ya mdomo wake mpana. Baada ya tabasamu hilo Shangwe alijibu kwa kusema, “Kumbe sina budi kuwapongeza vijana wangu kwa uchunguzi wao. Hawakuamini kabisa kuwa nia yenu ilikuwa ya kuniona na kunipongeza. Hamkuelekea kuwa kama watu ambao wanaweza kuupoteza muda wao kwa ajili ya kumwona Rais wa nchi yoyote ile. Hivyo, wakati wakiwazungusha kwa fomu hii na ile wao walikuwa wakiwachunguza kwa makini. Waligundua ninyi ni nani. Ambacho hawakuweza kugundua ni dhamira ya safari yenu. Hamkuonekana kama watu wenye dhamira mbaya. Hivyo, waliamua kuwaruhusu mnione ili mnieleze kisa hasa cha safari yenu,’ alibadili kiasi sauti yake, kuifanya ya kikazi zaidi aliposema, “kwa hiyo nadhani huna haja ya kuniomba radhi kwa hila zako. Dunia nzima inakufahamu kwa hila hizo. Unaonaje basi ukiyafupisha maongezi yetu na kunieleza haja hasa ya kutaka kwako kuniona?”


Hilo kiasi lilimshangaza Joram. Alimgeukia Nuru kumtazama usoni, alimwona yeye pia katulia, mshangao ukiwa wazi katika macho yake. Akaurejesha uso wake kumtazama Rais na kuruhusu tabasamu dogo kabla hajasema, “Nadhani umeona nilivyoshangaa mtukufu Rais. Nilidhani mara tu baada ya kulitaja jina langu ni wewe ambaye ungeweza kuniambia kitu kilichonileta hapa.”


Shangwe alionyesha kutokwa na macho ya mshangazo zaidi yao. “Sijakuelewa kijana. Nadhani enzi ya kuzungumza kwa mafumbo ilipita zamani. Enzi tuliyonayo sasa haitupi muda wa






kutosha kucheza na maneno. Tuna mengi ya kufanya kuliko babu zetu. Ebu zungumza kifupi basi.”


Ilikuwa dhahiri kuwa ustahimilivu ulianza kutoweka katika sauti ya Rais. Hata macho yake yalionyesha kwamba akilini mwake alikuwa ameishiwa na hamu ya kikao hicho na kuanza kufikiria mengine. ‘Na hii pia ni sehemu ya maigizo?’ Joram alijiuliza. Kwa sauti alisema, “Samahani mzee. Labda nimtaje hayati Patauli Kongomanga. Unafahamu nini juu yake?”


“Patauli… Patauli… Patauli yupi?”


“Yule mwandishi wa habari ambaye maiti yake imeokotwa huko Tanzania.” Ni Nuru aliyeongeza.


“Alaa! Yule!” Rais alifikiri kwa muda kabla ya kuuliza,


“Anahusika nini katika maongezi haya?”


Joram pia alianza kuchukizwa na mchezo huu. “Nilifanya uchunguzi mzee. Uchunguzi wangu ulinithibitishia kuwa hakuwa mwandishi wa habari tu. Alikuwa mtu wako. Mmoja kati ya watu wako wachache ambao mara nyingi wamekuwa wakipokea majukumu yao toka kwako binafsi,” alisema huku kamkazia macho Rais.


Rais alitabasamu kidogo kisha akasema polepole, “Naanza kukupenda pamoja na kukuchukia Joram. Kukupenda kwa jinsi kichwa chako kinavyofanya kazi haraka na kukuchukia kwa jinsi ulivyo na uwezo wa kufichua siri zote za nchi yangu. Umeingia nchini kwa hila na kwa hila hizohizo umeiba siri ambazo vijana wangu wengi hawajui,” alisita kwa muda. Kisha, akaongeza, “Haya tuseme alikuwa kijana wangu. Hilo linahusiana vipi na maongezi. Yetu?”


“Kama unakubali kuwa ni kijana wako nadhani utanifanyia hisani ya kukubali kuwa ulimtuma kwangu,” Joram alieleza.


“Kumtuma kwako! Sijakuelewa.”


Joram alimtazama kwa makini kuona kama kweli Rais alikuwa hamwelewi. Macho yake yalikuwa yaleyale yaliyosomeka kwa urahisi. Alimtazama tena Nuru, kisha akaanza kumweleza kwa tuo tangu alivyotembelewa na marehemu usiku ule, marehemu alivyokata roho kabla hajafaulu kueleza kwa ukamilifu kisa au mkasa uliomleta. “Uchunguzi aliofanyiwa marehemu ulionyesha kuwa aliuawa kwa sumu kali ambayo inaweza kukaa mwilini kwa siku hata saa kadhaa kabla ya kudhuru moyo wa mtu aliyeila,” Joram aliongeza. “Ni kifo hicho kilichonitia ari ya kuja






hadi hapa. Nilidhani kuwa ni kweli kulikuwa na tishio kubwa katika maisha au serikali yako. Na kwamba kifo chake zilikuwa juhudi za wapinzani ambao hawakutaka aufikishe ujumbe huo kwangu.”




Sasa alitulia akimtazama na kumsikiliza Rais. Alipokuwa akieleza alishuhudia jinsi mshangao ulivyokuwa ukitoweka polepole toka katika uso wake na nafasi yake kumezwa na kitu kama hofu. Kitu hicho kilidumu katika uso huo kwa nusu dakika tu, dakika iliyofuata nafasi yake ilichukuliwa na tabasamu baridi, ambalo liliendelea kutulia usoni hapo kwa muda mrefu baada ya Joram kumaliza maongezi kana kwamba lilikuwa limesahauliwa hapo; mwenyewe akiwa maili nyingi nje ya chumba hicho. Mara tabasamu hilo liligeuka kicheko, ambacho kilifuatwa na sauti ileile, yenye utulivu na uhakika.


“Sidhani kama ni kweli.” “Kweli?” Joram aliuliza.


“Kwamba naweza kuwa mashakani kiasi hicho. Sijafanya dhambi yoyote katika utawala wangu kiasi cha mtu kumwaga damu kwa ajili yangu. Katiba iko wazi kabisa, kama nina makosa au nakiuka utaratibu mwananchi yeyote anaweza kusema, vikao vikakaa na kuniondoa madarakani wakati wowote.”


Vikao ambavyo kama mwenyekiti wake sio wewe basi ni mtu wako. Kwa nini mmeondokea kuamini kuwa kila mtu ni kiziwi na kipofu? Joram alisema kimoyomoyo. Kwa sauti alisema, “Usitazame upande mmoja mzee. Kuna maadui wa nje vilevile, ambao hawaipendi serikali wala maendeleo yako. Hao wanaweza kufanya lolote vilevile.”


“Pengine,” alinong’ona. “Lakini kwa nini?” kisha aliyarudisha macho yake toka angani na kuwatazama Joram na Nuru kwa makini. Akasema, “Lakini sioni inawezekana vipi.”


“Unachohitaji kunieleza ni kuwa hukumtuma hayati Patauli kuja kwangu?” Joram aliuliza.


“Nitakuwa na muda gani wa kuchezea kiasi hicho, kijana? Nimtume mtu wangu kwako akuite, ufike hapa mie nikatae?” alimjibu kwa swali jingine.


Jibu hilo lilimfanya Joram amshike Nuru mkono na kuinuka taratibu huku akisema, “Kwa hali hiyo sina budi kukuomba radhi kwa kuupoteza bure muda wako. Pengine ni ndoto iliyonitokea, na kama si ndoto basi yaliyosemwa na marehemu






ni yale ambayo husemwa na mwanadamu anapotapatapa kwa hofu ya kifo kinapomsubiri mbele yake. Tungeomba uturuhusu tuondoke.”


Rais alikuwa ameinuka kitambo na kuwashika mikono akiwaongoza mlangoni huku akisema, “Hamna haja ya kuondoka harakaharaka. Ninyi bado ni wageni wangu wapenzi. Tutakaa tena siku moja kabla hamjaondoka tulijadili suala hili kwa urefu zaidi. Leo nina wageni ambao wananihitaji zaidi.”


‘Kama hapa pia anaigiza,’ Joram alikuwa akiwaza kwa hasira ingawa tabasamu lilikuwa usoni mwake, ‘basi ni mwigizaji mzuri.’


KITU fulani kilimkereketa Joram rohoni. Kitu hicho hakuweza kukifafanua kwa maneno japo Nuru alijitahidi vilivyo kuzungumza naye ili aseme kinachomsumbua. Angewezaje kueleza akaeleweka kwamba kitu mfano wa hasira za hisia za aibu, uchungu wa kujifikiria juha au mambo kama hayo ndiyo yaliyokuwa yakimsumbua? Kwamba alikuwa hajielewi, hamwelewi hayati Patauli wala kumwelewa Rais Shangwe na mkasa mzima uliokuwa mbele yake? Alijiona kama aliyeko katika safari ndefu, mara afike katika kituo asichofahamu na


kuambiwa, “Haya shuka, umefika uendako.”


Vinginevyo imekuaje Rais akatae katakata kuwa hakumtuma marehemu nchini Tanzania kumtaka msaada? Ilikuwaje basi marehemu huyo akafanikiwa kugundua huko alikojificha? Zaidi ilikuwaje apoteze maisha yake katika hali kama ile? Nani hasa angehitaji roho ya Patauli kwa kiu kubwa kiasi hicho na kwa nini asitumie njia za mkato hata akamruhusu kumfikia yeye wakati punje ndogo tu ya risasi ingetosha kabisa kumfanya marehemu kuwa marehemu mapema zaidi?


Kwa kila hali, Joram aliona kuwa bado alikuwa hewani akielea juu bila ya kuufikia msingi wa mambo. Ni hicho kilichomsumbua sana akili yake, kujiona yuko angani, akielea kama kishada. Angeweza kufanya chini juu kupeleleza kisa na kiini cha mambo haya, walao kwa ajili ya kuitoaa roho yake katika bwawa hilo






la mashaka. Lakini isingekuwa rahisi kiasi hicho. Akiwa mgeni katika nchi hii, Rais ambaye alitegemea kuwa angemsaidia kwa chochote hicho alichomwitia keshakanusha na kuhusika kwake, yeye Joram angefanya nini? Angeanzia wapi katika upelelezi wake? Na kama kweli lipo jambo la haja katika madai ya hayati Patauli, basi ambacho upelelezi wake ungempatia katika mkasa huu ni hakika ya kujipatia shahada ya risasi kichwani mapema zaidi.


Hayo yalikuwa yakipita katika kichwa cha Joram pindi wakiwa wamekaa chumbani mwao, katika hoteli yao, saa tatu baada ya kurejeshwa toka nyumbani kwa Rais. Njia nzima Joram hakuonyesha hamu ya maongezi kwa askari aliyevaa kiraia, ambaye aliwaendesha hadi hotelini. Joram aliyaepuka maswali yake kwa kumpa majibu ya mkatomkato. Alipoona askari kanzu huyo hatosheki Joram alianzisha maswali yenye dhamira ya kuisifu nchi, siasa na Rais wao, kwa maneno mengi; jambo ambalo lilimkinaisha askari huyo mara moja hata akakoma kuendelea na maongezi. Walipowasili hotelini walifuatana katika chumba cha vinywaji ambapo waliagiza soda na kuanza kunywa kwa utulivu.



“Unamfikiriaje?”


“Nani?”


“Rais.”


Joram akatabasamu kidogo kabla hajaongeza, “Sikia Nuru, Rais wa Kiafrika sio mtu wa kujadiliwa na mtu kama mimi na wewe mahala kama hapa. Tunaweza kesho tukajikuta mahabusu, badala ya hotelini, kujibu maswali yasiyoeleweka.”


Nuru naye alicheka. “Usinidanganye Joram,” alisema baada ya kicheko hicho kizuri. “Najua unahitaji muda wa kufikiri. Ameivuruga akili yako. Ulichotegemea sicho ulichokikuta. Akasita tena. Alipomwona Joram yuko kimya akaongeza, “Hata mimi sina budi kusema kuwa amenishangaza. Tulivyopokelewa nyumbani kwake badala ya Ikulu nilidhani ameamua kutusimulia hicho alichotuitia. Sasa utafanyeje, Joram?”


Kama alitegemea jibu, basi alikosea sana. Badala yake Joram alimshika mkono na kumwongoza kwenye lifti ambayo iliwapandisha hadi ghorofani kilikokuwa chumba chao. Chumbani aliendelea kuyakoroga maswali yote ya Nuru juu ya Rais huyo. Ulipofika wakati wa mlo walikuwa wa kwanza kufikia






chumba cha maakuli. Walikula huku wakitazama televisheni ambayo ilikuwa ikionyesha kikundi cha utamaduni kilichokuwa kikiwatumbuiza wageni fulani uwanja wa ndege. Wageni hao walipopita baada ya kuwatazama wachezaji kidogo, kikundi hicho kilisahauliwa na umuhimu kuhamishiwa kwa wageni. Historia zao za nchi zao zilisimuliwa, zikafuatiwa na majibu yao kwa waandishi wa habari. Joram aliyatazama yote hayo ilihali hayaoni. Mara baada ya mlo na bia mbilimbili za kuteremshia aliushika tena mkono wa Nuru na kumwongoza chumbani, ambako sasa alitulia kama awali; akiendelea kutafakari.


Kwa muda aliusahau mkasa huo na kujifikiria mwenyewe. Alikosa nini kwa Mungu hata apewe moyo huu wa kufuatilia mambo yasiyomuhusu ambayo mara zote uifanya roho yake iponee chupuchupu? Kitu gani kilichomwambukiza ugonjwa huu hatari? Tamaa ya kufichua kila siri, kiu ya kumfichua kila mwenye hatia, njaa ya kumpokonya silaha kila mwenye nia mbaya unapochanganyika na uroho wa kushuhudia mibabe iliyokubuhu ikilia hadharani; kama si ugonjwa ni nini?


Joram hakuweza kukumbuka ni lini na nani alimwambukiza maradhi hayo. Yako magonjwa mengine ambayo mwanaume huzaliwa nayo. Pengine Joram ni mmoja wao.


Baba na mama yake wasingesahau jinsi mtoto wao huyu pekee alivyokuwa machachari tangu alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Akiwa mtoto aliyepatikana baada ya miaka saba ya kutafutwa kwa namna zote, madaktari na wahenga walishirikishwa, alipopatikana alikuwa kama mboni ya jicho kwa baba na yai la dhahabu kwa mama. Kila mmoja alipenda kumlea kutwa. Lakini iliwashangaza kuona kwamba mtoto huyu hakupenda kabisa kubebwa. Kila aliposhikwa mikononi alisumbua kwa kurusha viteke na vigumi hata akarejeshwa kitandani ambako alitulia.




Hayo yalifuatwa na jinsi alivyoanza kutambaa, kusimama na hatimaye kutembea akiwa katika vikundi vya watoto wakubwa zaidi akishiriki katika michezo na maongezi. Alikuwa hodari katika kila kitu, jambo ambalo lilimfanya apendwe na watu mbalimbali, shuleni na mitaani. Katika vikundi hivyo mara nyingi alionekana kama kiongozi na msemaji mkuu. Hata katika timu zao za mpira, mchezo ambao hakuumudu kama mingine, bado alichaguliwa kuwa kiongozi.


Huyo ndiye Joram Kiango utotoni, utoto ambao aliupitisha






katika mitaa ya California nchini Marekani ambako baba yake alikuwa akifanya kazi kwa Mzungu mmoja aliyeondoka naye hapa nchini kukimbia ‘adha ya uhuru’ mara tu ulipopatikana. Shule zilimpa Joram elimu nzuri. Alijipatia shahada ya M.A katika historia, fasihi na siasa. Mara akaliacha somo hilo na kuanza kusomea Sayansi. Kabla ya kuhitimu aliamua kuacha masomo na kutulia nyumbani, muda wake mwingi akiutumia katika mazoezi ya kareti, ngumi na sarakasi. Haya pia aliyaacha na kukaa bure.


Hakuwa mzigo kwa wazazi wake. Kwa kweli walipenda sana mtoto wao akae nao muda wote, hasa baada ya daktari kuwahakikishia kuwa Joram alikuwa yai pekee lenye uhai katika tumbo la mama yake. Hata hivyo, iliwashangaza kuona kuwa pamoja na mtoto wao kuwa mtu mwenye hekima na uwezo wa hali ya juu katika mambo mbalimbali, bado alikuwa kama mtu ambaye hakujua alihitaji nini katika maisha yake. Hata kati ya wasichana wengi ambao alikuwa akiwaleta nyumbani hakuonyesha dalili ya kumpenda yeyote. Aidha, kila aliyediriki kuzidisha dalili za mapenzi Joram alimwepuka mara moja. Hilo lilimtia hofu mama yake. Hakuona kama Joram angekuwa mtu wa kuoa na kutulia kama watu wengine. Asingependa kufa kabla ya kumwona mjukuu. Zaidi angependa Joram achukue jukumu ambalo yeye alishindwa kulitekeleza, aijaze nyumba kwa watoto.


Hakubahatika kuishi hadi hilo litokee.


Siku moja Joram alikwenda disko ambako alichelewa hadi saa nane za usiku. Aliporudi nyumbani alishangaa kukuta taa zinawaka, wazazi wake wakiwa nje wakimsubiri. Baba yake alikuwa akivuja damu puani na mdomoni.


“Kuna nini?” aliwauliza. “Tumeibiwa,” walimweleza.


Majambazi manne yenye silaha yaliivamia nyumba yao na kumpiga baba yake, kisha yakamlazimisha kutoa pesa zote alizokuwa nazo humo ndani. Yalipozipata yalichukua pia televisheni na kinyago chao kikubwa, kinyango ambacho kilimshangaza kila mtu mjini hapo kwani kilikuwa mwanzo wa uchongaji wa vinyago dhania vya mashetani. Mmakonde huyo alikuwa amechonga binadamu mwenye vichwa sita, akiwa ameinama kulipapasa tumbo lake. Hiyo ilikuwa amali yao pekee ambayo iliwapa sifa katika mtaa huo kiasi cha kuwafanya






wajivunie nchi yao, kila walipoulizwa msanii gani aliyeweza kuchonga kitu kama hicho na alitumia vifaa gani.


Joram aliyasikiliza maelezo ya wazazi wake kwa makini. Aliwauliza maswali mawili, matatu kwa nia ya kuelewa dalili za watu hao. Wazazi wake hawakuwa na maelezo marefu. Lakini huo haukuwa mwisho wa maswali ya Joram. Alipeleleza kwa urefu katika majumba ya sanaa, kuulizia kama kuna watu waliokuwa wakiuza aina fulani ya kinyago. Majibu yalimjia toka New York, kwa simu kuwa kinyago alichohitaji kililetwa hapo na wauzaji ambao hawana ujuzi na vinyago wala sanaa kwa ujumla. Alipaa hadi mjini hapo. Aliporudi alikuwa na anuani kamili ya watu aliowahitaji. Usiku wa siku iliyofuata aliwatembelea ghafla. Aliwakuta wawili kati yao. Walipomwona, kijana mdogo kiumri, akiwa mikono mitupu walimcheka na kumdhihaki. Lakini walishangaa kuona akidiriki kuwarushia makonde yaliyokuwa mazito kuliko umri wake. Walishangaaa zaidi kuona akikwepa kila konde walilomrushia. Muda mfupi baadaye, walijikuta hoi, hawajitambui. Hivyo, hawakua na upinzani Joram alipowaburura hadi nyumbani kwao, wakiwa wamekibeba kinyago hicho. Nyumbani aliwalazimisha kuwapigia magoti na kuwalamba miguu wazazi wake. Baada ya hapo aliwafukuza.


Kuwafukuza badala ya kuwapeleka polisi, kama wazazi wake walivyomshauri, lilikuwa kosa ambalo Joram atalijutia hadi siku ya kwenda kaburini; kwani usiku wa siku ya pili yake nyumba yao ilitembelewa na majambazi hayo. Safari hii hayakuja kwa mzaha. Yaliifunga milango yote kwa nje na kuimwagia petrol nyumba nzima, kisha yakailipua moto. Ulikuwa moto mkali ambao uliwachukua zima moto saa kadhaa kuuzima. Hata hivyo, hawakufaulu kuyaokoa maisha ya baba na mama Joram Kiango. Walikutwa wamefia bafuni baada ya juhudi zao za kuzima moto kwa maji ya bomba kutozaa matunda.



Joram hakuyaamini macho yake alipofika nyumbani toka kokote alikokuwa na kukuta maiti mbili zilizoungua zikibebwa na polisi kupelekwa katika gari la wagonjwa lililokuwa nje. Wala hakuelewa chochote pindi majirani walipoanza kumpa pole na kumkaribisha nyumbani kwao. Kwake ilikuwa kama moja ya zile ndoto mbaya ambazo humtukia mtu kushuhudia jambo la kusikitisha. Hivyo, alijitoa katika mikono yenye huruma ya majirani hao na kuendelea kuitazama ‘picha’ hiyo ya kutatanisha.






Tahamaki fahamu zake zilioana na hali halisi. Akaanza kulewa. Ikampambazukia kuwa miili iliyokuwa ikipakiwa katika gari hilo ilikuwa ya wazazi wake.


Bado hakujisikia chochote. Damu yake ilikuwa imetulia, fahamu zikiwa kimya. Chochote alichotegemea kuwa humwingia au kumtoka mtu ambaye amewahi kushuhudia kifo cha aina hiyo kwa wazazi wake yeye hakukihisi. Ubaridi ambao amesoma vitabuni kuwa humwingia mtu hadi rohoni yeye hakuusikia. Machozi ambayo ameyaona mara nyingi katika macho ya watu yeye hayakumtoka. Alikuwa kimya kama alivyokuwa. Angeweza kucheka, angeweza kulia, lakini hakufanya lolote zaidi ya kutulia kimya, akitazama.


Ukimya na utulivu wake uliwashangaza majirani na kuwatisha polisi ambao walikuwa wakisubiri kuzungumza naye. Jirani walizoea mtu anayeomboleza, si huyu asiyeeleweka. Askari wangependa kumtupia maswali mtu anayebabaika, si aliyetulia kama huyu. Hata hivyo, askari mmoja alimshika mkono na kumwongoza mtaa wa pili ambako kulikuwa na baa. “Listen, you need a drink,” alimwambia akimwagizia pombe kali. Joram aliipokea na kuinywa taratibu. Kisha, askari alianza kumwuliza maswali ambayo yalikuwa yakimtatiza muda wote huo. “Unaweza kukisia nani aliyetenda kitendo cha kinyama kama hiki?” Aliuliza kwa upole. Joram hakumjibu. “Au hujawa tayari kuzungumzia suala hili… unajua, tungependa kuwakamata mapema.” Aliongeza. Joram hakumjibu. Badala yake aliaga kwamba anakwenda kujisaidia.


Askari huyo alisubiri hapo kwa dakika ishirini. Hakuamini. Wasiwasi ulipomzidi alimfuata Joram maliwatoni. Hakumkuta. Wanywaji aliowauliza kama wamemwona hawakuwa na la kumjibu. Alihangaika huko na huko bila mafanikio. Ikamlazimu kurudi kituoni kutoa taarifa.


Alfajiri hiyohiyo maiti mbili ziliokotwa nyuma ya nyumba moja ambayo iliungua moto. Marehemu waliuawa kwa mikono baada ya kupigwa na kuvunjwavunjwa viungo. Mwuaji hakuonekana. Lakini uchunguzi ulionyesha kuwa marehemu walikuwa miongoni mwa magaidi manne yaliyokuwa yakiisumbua sana wilaya hiyo kwa wizi na mauaji. Mara mbili tatu yaliwekwa ndani kwa makosa madogomadogo. Ushahidi mzuri wa kuyaweka kizimbani au kitanzini ulikuwa haujakamilika. Hivyo, kufa kwa



wawili kati yao haikuwa habari mbaya sana kwa polisi japo wangependa zaidi kumfahamu mtu aliyewasaidia kazi hiyo.


Mtu wa tatu katika kikundi hicho aliokotwa siku chache baadaye, akiwa maiti; katika kitongoji fulani. Yeye pia aliuawa kwa mikono ingawa alikuwa na majeraha mengi mwilini. Polisi waliwaagiza wafungwa kumzika, kisha walianzisha upelelezi mkali kumtafuta mtu aliyehusika na mauaji hayo. Haikuchukua muda kugundua kuwa mwuaji alikuwa Joram Kiango ambaye alikuwa akilipiza kisasi dhidi yao kwa madai kuwa ni wao waliwateketeza wazazi wake kwa moto. Msako mkali ukaanzishwa dhidi ya Joram. Vyombo vya habari vikapewa jina na picha na kumtangaza kama mtu hatari.


Polisi hawakuwa na haja ya kujisumbua kumtafuta. Siku chache alionekana katika kituo cha treni akiwa na mateka wake ambaye alifungwa kamba. Wote walikuwa mahututi. Joram alikuwa taabani kwa majeraha mengi ya visu na risasi, ambayo yalianza kuvunda kwa kutopatiwa matibabu halisi. Mateka wake pia alikuwa hoi kwa kipigo ambacho alikipata tangu walipoanza mapambano. Walivutana hadi katika kituo cha polisi ambapo Joram alimwamuru mateka wake kujieleza kwa mara nyingine jinsi walivyoshoriki kuwaangamiza wazazi wake. Mbele ya polisi jambazi hilo lilijaribu tena kukataa, jambo ambalo liliamsha hasira za Joram. Pamoja na udhaifu wake, aliwashangaza polisi alipopaa angani na kutua katika uso wa jambazi hilo kwa kichwa, kitendo ambacho kiliufumua uso huo na kuchafua sakafu kwa damu. Walimkamata Joram na kumpeleka hospitali chini ya ulinzi wa polisi.


Joram alitibiwa hapo kwa wiki nzima. Japo alijisikia nafuu, lakini aliendelea kujifanya mahututi akisubiri siku na wasaa aliouhitaji. Hatimaye, uliwadia. Mchana askari wa zamu alikuwa mmoja tu. Daktari aliingia katika chumba chake na kuyachunguza majeraha yake. Kisha, akamshauri Joram kwenda katika chumba cha X-ray kuzipima tena mbavu ambazo alidai kuwa zinamwuma sana ingawa picha hazikuonyesha madhara yoyote. Ni chumbani humo ambamo Joram aliamua kuchukua uhuru wake. Alimshangaza daktari kwa kumtia mweleka ambao ulifuatiwa na kufungwa kamba zilizotokana na shuka ya kijitanda cha chumba hicho. Kabla hajaamua la kufanya alisokomezwa tambara mdomoni kwa namna ambayo





ilimfanya asiweze kupiga kelele. Kisha, alivuliwa nguzo zake, ambazo Joram alizivaa harakaharaka huku akitamka kitu kama ‘samahani.’ Mara akatoka kuelekea nje.


Safari yake iliishia benki ambako alichukua akiba yake yote. Toka hapo alikwenda uwanja wa ndege ambako alikata tiketi ya New York. Alijificha kwa muda katika mji huo akisubiri vyombo vya habari vichoshwe na suala lake ambalo lilipambwa mambo mengi ya uongo. Idd Amini alipojiita Mungu, Mugabe alimng’oa Ian Smith na kuiita nchi Zimbabwe na mambo mengine. Habari hizo zilimeza nafasi ya jina la Joram katika magazeti ya Marekani. Akasahauliwa. Ni hapo aliponunua hati ya usafiri ya bandia na kupanda ndege ambayo ilimchukua hadi Afrika, Dar es Salaam; Tanzania.


Jiji la Dar es Salaam halina hiana. Pamoja na ukweli kwamba Joram alikuwa mgeni sana nchini hapa, isipokuwa kwa safari chache alizokuja alipokuwa likizo; bado lilimlaki kama Mtanzania mwingine yeyote. Alieleweka alipoomba kufungua ofisi ya upelelezi binafsi, ingawa haikueleweka kama taifa au yeye angepata faida kutokana na kazi hiyo. Ikiwa kazi ngeni hapa nchini haikumchukua muda kupata kibali cha ofisi na kile cha kumiliki bastola kwa ajili ya kujilinda.


Wateja wakaanza kumjia. Wengi wakiwa na matatizo madogomadogo ambayo aliyatatua mara moja. Yale ambayo hayatatuliki aliyatupa kapuni. Kuna waliotaka msaada wa ushahidi wa vitendo vibaya katika ndoa, kuna wale ambao walidhulumiana; wengine ni wale ambao walipotelewa na mali au amali zao; n.k. yote hayo Joram aliyafanya shingo upande kwa ajili ya kujipatia kitu cha kutia tumboni. Zaidi, alihitaji mikasa mizito ambayo inatisha na kutatanisha.


Ni hilo lililomfanya ajitume kwa hiari katika mkasa wowote uliotokea. Na ni katika moja ya mikasa hiyo alipokutana na Neema ambaye aliondokea kuwa mwenzi wake wa kudumu hadi kifo kilipowatenganisha, mkasa ambao uliyafikia masikio ya waandishi wa habari na kupambwa sana na gazeti la Kiongozi ni ule wa mauaji ya Ngarenaro, Arusha, ambao waliuita Lazima Ufe… Baada ya huo ndipo macho na masikio ya watu wengi yalielekezwa kwake, jambo ambalo lilifanya mikasa na maafa yaanze kumwandama kila anapopita.


Kwa ajili ya njaa, kijana mmoja anayejifanya mwandishi




aliibuka na tabia ya kuandika kila mkasa uliomkumba. Matokeo ya kazi hiyo ni msululu wa vitabu kama Dimbwi la Damu; Najisikia Kuua Tena; Mikononi mwa Nunda; Salamu Toka Kuzimu na Tutarudi na Roho Zetu, Mikataba ya Kishetani na vingine vingi. Jambo ambalo lilimzidishia umaarufu ndani na nje ya nchi na kumfanya ajikute katika nchi hii ya Pololo ambayo hakutegemea kuitembelea katika maisha yake.




***


Naam, huyo ndiye Joram Kiango, Joram ambaye sasa, kwa mara ya kwanza maishani mwake, alijikuta akiilaani kazi yake na kuilaumu bahati yake. Mungu alimpa au kumnyima nini mpaka akapenda kuhangaika vichochoroni na makuburini akipeleleza mambo ya watu wengine badala ya kutulia katika ofisi moja yenye kiyoyozi nyuma ya meza kubwa yenye fomica na kufanya shughuli zake kwa utulivu? Afrika imeipa nini roho yake wakati nchini mwake hakuwahi kupewa walao ujumbe wa nyumba kumi?


Alitulia kwa muda akiitazama dari. Hapana. Alikuwa haioni. Alikuwa mbali zaidi, nje kabisa ya chumba hicho; akiyatazama mengi ambayo yamepata kumtukia, mengi ya kutisha na kutatanisha. Yote yaliifanya roho yake iponee chupuchupu. Lakini hakuna kilichomfurahisha zaidi ya kuwa mshindi kati ya yote hayo. Na ni hilo ambalo lilimsumbua, kuona pamoja na ushindi wake wa kila mara, leo hii ameondokea kuonekana mtu wa kwanza kwa ujuha; utoke kwenu, ulipe nauli, hadi nchi ya watu, mbele ya Rais wa watu na kudai madai yasiyoeleweka wala kuelekeza kama si ujuha ni nini? Ujuha huu umemwanza lini? Na utaendelea hadi lini?


“Utafanya nini Joram?” Sauti ilimzindua.


Joram akageuka kumtazama. Nuru alikuwa amelala kando yake. Mikono yake ilikuwa imekizunguka kiuno cha Joram, uso wake ukimtazama. Joram alikuwa amemsahau. Wakati wote ambao alikuwa nje ya chumba hiki kimawazo, alikuwa amesahau kabisa kuwa alikuwa mikononi mwa msichana mzuri, pengine kuliko wote duniani katika karne hiyo, kwani imedaiwa mara nyingi kuwa Nuru alikuwa mmoja kati ya wale wanawake ambao huja duniani kwa makosa, wakiwa wamekusudiwa kuwa



malaika, kosa ambalo Mungu hulifanya mara moja tu katika kila miaka mia moja.


Nuru, akiwa anaufahamu uzuri wake na jinsi uzuri huo unavyowasumbua wanaume wengine wote, awali Nuru alishangazwa kuona kuwa hauna madhara yoyote katika akili za Joram Kiango. Mwanzoni, hilo lilimwudhi sana. Kisha, alilisamehe. Ilikuwa baada ya kujiuliza kuwa pengine Joram pia sio binadamu wa kawaida. Kama ni kweli, wanavyotania waandishi wa habari kuwa yeye alikusudiwa kuwa malaika basi pengine Joram pia alitayarishwa kuwa malaika wa kiume.


Kwa kweli, huo ulikuwa mzaha tu uliokuwa ukipita katika kichwa chake katika vipindi kadhaa ambavyo kichwa hakikuwa na kazi nyingine muhimu, kama wakati huo alipokuwa ametulia na kujaribu kumtoa Joram katika dimbwi la mawazo lililokuwa limemmeza gubigubi. Alipomwona kazama kabisa, utulivu usio wa kawaida ukiwa umemkumba, macho yake yakiwa wazi kama maiti, ndipo Nuru akaamua kutulia, ili asivuruge mkondo wa mawazo yake, hadi alipomwona Joram akirudi chumbani humo toka kokote alikokuwa. “Utafanya nini?” alilirejea tena swali lake. Joram aligeuka kumtazama. Akatabasamu. Tabasamu hili lisingeweza kumlaghai Nuru. Lilikuwa tabasamu la uchungu lililobeba hasira na maumivu makubwa. Badala ya kutoa jibu Joram alitoa ulimi na kuusogeza kinywani mwa Nuru ambaye aliukwepa kwa kumsukuma pembeni akisema, “Usijisumbue.


Hujisikii kustarehe. Akili yako yote imevurugika kwa kukosa kazi ya kufanya kama ulivyotegemea.”


Tabasamu la Joram liligeuka kuwa halisi, kama alivyotaka Nuru. “Nadhani hujanielewa mpenzi,” alimwambia.


“Kinachonisumbua siyo kazi ya kufanya. Tanzania ina misitu mingi ambayo inahitaji jasho langu kugeuzwa mashamba. Kama shida yangu ingekuwa kazi, ningerudi kufanya hivyo mara moja. Kinachonisumbua ni marehemu ambaye alitutafuta usiku na mchana, na hatimaye kufia mikononi mwetu, baada ya kufikisha ujumbe ambao niliondokea kuuamini. Unadhani alikufa akifanya mzaha? Kuna mzaha wa aina ile? Mtu ufanye utani hata dakika ya mwisho wa maisha yako?”


“Sasa utafanya nini? Rais ame…”


“Hilo ndilo tatizo langu,” Joram alimkatiza. “Nitafanya nini?


Nifanye nini?”





ILIKUWA usiku usio na furaha kwa Joram na Nuru. Walilala ndiyo, wakiruhusu miili yao kustareheshana kama kawaida, mikono ikijifariji kwa kugusa hapa na


pale; miguu ikiburudika kwa mguso huo. Hata hivyo, faraja hiyo haikufikia kiwango cha kuzifuta chembechembe zisizoelezeka ambazo zilienea katika fikra za Joram. Akijua hayo Nuru alifanya kila alilolifanya kwa dhamira ya kumsahaulisha msiba wake walau kwa muda. Alipoona havitimizi wajibu alijaribu kutumia maneno, kwa sauti yake laini, iliyopenya katika kiza kilichotanda chumbani humo baada ya kuzimwa taa zote, Nuru alimwambia. “Mpenzi nadhani hakuna asiyejua kama wewe ni shujaa.”


“Wanakosea wanaonifikiria hivyo,” lilikuwa jibu la Joram kwa


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog