Simulizi : Bomu
Sehemu Ya Kwanza (1)
MEANDIKWA NA : HALFANI SUDY
********************************************************************************
Simulizi : Bomu
Sehemu Ya Kwanza (1)
DANIEL Mwaseba aliamka ghafla kutoka katika usingizi aliodumu nao kwa saa zisizozidi tatu. Alifumbua macho kwa haraka huku sura yake ikionesha kukereka na kitu kilichomuamsha katikati ya usingizi. Macho yake yote mawili yakiwa wazi huku yakionesha kuwa bado yalihitaji kufumbwa, ili mmiliki wa macho hayo alale. Ndipo simu ya Daniel iliita tena. Hapo ndipo alipogundua kitu kilichomfanya aamke ghafla usiku wa manane, kumbe ilikuwa ni simu yake ya mkononi kuita ule usiku wa manane.
Daniel alinyoosha mkono wake wa kushoto hadi chini ya mto, mahali alipokuwa ameihifadhi simu yake. Aliichukua simu yake na kuipeleka katika paji lake la uso ili kuangalia, ni nani alikuwa mpigaji. Wakati huo bado simu ilikuwa inaendelea kuita. Huku mkono wake wa kushoto ukitetemeshwa kila simu ilipokuwa inatoa mlio.
"Namba ngeni, ni nani huyu anayenipigia simu muda huu?" Daniel alisema kwa sauti ndogo huku akiwa makini kuiangalia ile simu.
Wakati anaipokea simu macho yake yalitua ukutani ambapo kulikuwa na saa kubwa ya mshale ikining'inia katika chumba cha hoteli. Saa ya ukutani ilikuwa inaonesha kuwa yalikuwa majira ya saa tisa na dakika kumi na tatu usiku.
"Hallo" Daniel alisema kivivu simuni.
"Bila shaka naongea na Daniel?" Sauti kavu ya kiume iliuliza simuni. Daniel alihisi kuifahamu ile sauti.
"Ndio, ni Daniel" Daniel alijibu.
"Kuna tatizo kidogo limetokea kwa hawa wageni wenzio uliokuja nao....." Ile sauti ilisema, lakini Daniel hakuiruhusu imalize ilichokuwa inasema.
"Kuna matatizo gani?" Sauti ya Daniel sasa iliingiwa na fadhaha. Aliuliza kwa pupa huku akiinuka kutoka kitandani.
"Hawapo katika vyumba vyao..." Ile sauti ilisema huku ikiambatana na uwoga.
"Wakina Dr Luis hawapo katika vyumba vyao? Haiwezekanii.." Daniel alisema huku akiwa amesimama wima katikati ya chumba cha hoteli. Shuka alilokuwa amejifunika lilikuwa limeanguka chini. Lakini hakujari. Alichokuwa anataka kwenda kukifanya kilikuwa ni bora kwa sasa kuliko lile shuka la hoteli.
Harakaharaka alivua lile pajama la rangi ya bluu alilokuwa amelalia. Alichukua tshirt yake nyeusi juu ya kabati na kuivaa, maandishi mbele ya ile tshirt yalikuwa meupe huku yakisomeka 'Force'. Chini alivaa suruali ya bluu ya 'jeans'. Aliifunga vyema kwa mkanda wake mweusi. Chini alivaa raba nyeusi huku pembeni zikipitiwa na maneno ya rangi nyeupe nayo yakisomeka 'Force'. Alitumia chini ya dakika moja kuvaa vitu vyote hivyo.
Mkuumkuu Daniel alitoka ndani ya chumba cha ile hoteli. Alisimama katikati ya mlango wa kutokea chumbani. Pande zote mbili za kiuno chake akiwa amechomeka bastola nyeusi. Alikuwa tayari kwa kazi. Kazi ya kwenda kumsaka Dr Luis na mkewe waliopotea ndani ya hoteli ya Dos Santos...
***
Daniel Mwaseba, alikuwa ni mfanyakazi katika idara ya usalama wa Taifa. Idara hii ilikuwa inasimamiwa moja kwa moja na ofisi ya rais. Jukumu kuu la idara hii lilikuwa ni kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya maadui wote, wa ndani na wa nje, kwa wakati wote.
Asubuhi ya jana, Daniel Mwaseba aliitwa ofisini kwa bosi wake. Baada ya kuitikia wito alipewa jukumu la kwenda kumpokea mgeni majira ya usiku katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere. Mtu aliyepaswa kumpokea alitambulishwa kwa jina la Dr Luis Hamerton, mzee wa kizungu mwenye umri wa miaka themanini na moja, raia wa Marekani.
"Yakupasa kwenda uwanja wa ndege saa nne usiku. Kwa maana tumewasiliana na wenzetu wa Marekani kwamba ndege aliyopanda Dr Luis itatua katika ardhi ya Tanzania saa tano na dakika kumi usiku" Mkurugenzi wa usalama wa Taifa alimpa maagizo Daniel hiyo asubuhi.
"Sawa, nimekuelewa Chifu..nitafika muda huo pale uwanja wa ndege" Daniel alikubali kwa utii.
"Ukishampokea utampeleka hoteli yoyote ambayo itakuwa bora kwa huduma na salama kwake. Daniel, hakikisha Dr Luis haimkaribii hatari yoyote ile akiwa hapa nchini. Keshokutwa asubuhi inabidi umpeleke ikulu ili akaonane na Mheshimiwa rais ataporejea kutoka Nigeria. Kumbuka, Dr Luis ni mtu muhimu sana kwetu na kwa Marekani pia, hivyo hakikisha anakuwa salama salmini akiwa hapa nchini. Dr Luis hapaswi kupatwa na baya lolote lile. Na hii ndio maana nimekuchagua wewe Daniel ukampokee Dr Luis. Ninakuamini sana Daniel na ninaamini utaifanya kazi hii ndogo kwa ufanisi mkubwa" Mkurugenzi wa usalama wa Taifa alisisitiza.
"Nimekuelewa Chifu..na ninakuahidi mgeni wetu hatopatwa na baya lolote lile" Daniel aliahidi mbele ya bosi wake.
Waliagana.
Saa nne kamili usiku Daniel alikuwa katika viunga vya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, alisubiri hadi ndege iliyombeba Dr Luis ilipofika.
Kumbe Dr Luis alikuja na mkewe. Hilo kidogo lilitia shaka katika moyo wa Daniel. Maagizo aliyopewa na Chifu ni kuwa Dr Luis atawasili peke yake, leo hii alikuwa na mwanamke wa kichina pembeni yake. Mwanamke aliyemtambulisha Daniel kuwa ni mkewe.
Je huyu mwanamke ni mke Dr Luis kweli? Dr Luis amepoteaje hotelini? Je Daniel atafanikiwa kumpata?
Daniel aliwapokea Dr Luis na mkewe katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere. Aliwaingiza katika gari yake. Ndani ya gari ilikuwa kimya. Hakuna aliyeongea neno lolote lile ndani ya gari wakiwa njiani. Ilikuwa kimya cha kaburi, na moja kwa moja aliwapeleka katika hoteli ya Dos Santos iliyopo maeneo ya Kijitonyama.
Walipofika mapokezi walikutana na kijana mmoja mtanashati. Aliwakaribisha vizuri.
"Tunahitaji chumba kimoja cha kulala" Daniel ndiye alisema pale mapokezi.
"Sawa, chumba mmepata. Na karibuni sana katika hoteli ya Dos Santos" Yule kaka wa mapokezi alisema kwa sauti kavu huku akisogeza vizuri kitabu cha wageni pale mezani.
"Sijui niandike nani?" Yule kijana alisema huku akimwangalia usoni Daniel Mwaseba.
"Mgeni wangu anaitwa John Voosx" Daniel alidanganya jina. Yule kijana aliandika bila wasiwasi wowote.
Baada ya kuandika mambo yote yaliyohitajika katika kile kitabu cha wageni, na kulipa, yule kijana wa mapokezi aliwasindikiza hadi chumbani.
Walifika hadi nje ya mlango. Yule kijana alitoa funguo moja na kufungua ule mlango.
"Karibuni sana hoteli Dos Santos..karibuni sana, hiki ni chumba namba sabini na nane" Yule kijana alisema.
"Ahsante sana. Nimefurahishwa sana na huduma zenu hapa, sijui unaitwa nani kaka?" Daniel aliuliza.
"Ni jukumu letu kaka kutoa huduma bora kwa wateja wetu. Ninaitwa Kelvin Mbinu. Ila wengi hapa wamezoea kuniita Kevi" Yule kijana alisema.
"Nami nitakuita Kevi.." Daniel alisema huku akitabasamu.
"Karibuni tena" Kelvin alisema huku akiwaonesha kwa mkono ndani baada ya kufungua mlango wa kile chumba.
Daniel naye aliwakaribisha ndani ya chumba wageni wake kwa lugha ya kiingereza. Chumbani, waliongea kwa muda wa dakika sita pekee. Huku wakipeana miadi ya kuonana kesho yake asubuhi, kabla Dr Luis hajaonana na mheshiwa rais kesho kutwa.
"Nina wasiwasi sana na usalama wa Dr Luis. Sipaswi kwenda nyumbani kwa Leo, yanipasa na mimi nipange chumba ndani ya hoteli hiihii ili niwe karibu na Dr Luis. Ingawa Chifu hajanambia Dr Luis ni nani hasa, na kwanini kaja nchini lakini bila shaka ni mtu muhimu sana" Daniel Mwaseba alikuwa anawaza wakati akielekea upande wa mapokezi alipokuwa Kelvin.
"Samahani Kevi, naomba nami unipe chumba hapa" Daniel alisema alipofika mapokezi.
"Vyumba vipo kaka" Kelvin alisema huku akivuta kitabu chenye orodha ya wageni.
Daniel naye aliandikishwa kwenye daftari la wateja wa hoteli ya Dos Santos bila kusahau namba ya simu. Daniel akapewa chumba namba tisini na tatu. Hakikuwa mbali sana na chumba walichopewa wakina Dr Luis. Usiku huohuo Daniel alienda katika mgahawa wa hoteli ile na kupata chakula cha usiku. Hadi Daniel anaingia kulala ilikuwa ni saa sita na dakika kumi na tatu usiku.
Daniel alilala kwa muda wa saa tatu tu ndipo simu yake iliita. Baada ya kuipokea ndipo anapewa taarifa za kushangaza kwamba Dr Luis na mkewe wamepotea ndani ya hoteli ya Dos Santos.
Wamepoteaje sasa?
***
Daniel alikuwa anakimbia katika shuruba ndefu ya hoteli ya Dos Santos akielekea upande kulipokuwa chumba namba sabini na nane. Chumba ambacho walikuwa wamepatiwa wakina Dr Luis na mkewe ambao nao walipotelea humo.
Maneno ya aliyopewa na Chifu asubuhi yalikuwa yanarejea kichwani mwa Daniel Mwaseba.
"Ukishampokea utampeleka hoteli yoyote ambayo itakuwa bora kwa huduma na salama kwake. Daniel, hakikisha Dr Luis haimkaribii hatari yoyote ile akiwa hapa nchini. Keshokutwa asubuhi inabidi umpeleke ikulu ili akaonane na Mheshimiwa rais ataporejea kutoka Nigeria. Kumbuka, Dr Luis ni mtu muhimu sana kwetu na kwa Marekani pia, hivyo hakikisha anakuwa salama salmini akiwa hapa nchini. Dr Luis hapaswi kupatwa na baya lolote lile. Na hii ndio maana nimekuchagua wewe Daniel ukampokee Dr Luis. Ninakuamini sana Daniel na ninaamini utaifanya kazi hii ndogo kwa ufanisi mkubwa"
Na sasa hiyo hatari ndio ilikuwa inamkaribia kwa kasi sana Dr Luis.
Sekunde kumi na nane tu zilimfikisha Daniel mbele ya kile chumba. Nje ya chumba kulikuwa na watu saba. Daniel alimtambua mmoja tu kati ya watu wale saba.
Alikuwa Kelvin Mbinu..
"Vipi Kevi? Kimetokea nini?" Daniel aliuliza kwa pupa huku akimfata Kelvin.
"Kuna mambo ya ajabu sana yametokea katika hoteli yetu" Kelvin alisema kwa sauti iliyosawajika.
"Mambo gani hayo Kevi?" Daniel aliuliza huku hofu dhahiri ikitamalaki usoni mwake.
"Kama nilivyokwambia katika simu, wageni wako wametoweka katika mazingira ya kutatanisha sana hapa hotelini" Kelvin alisema.
"Hebu nieleze Kevi, wametowekaji?" Daniel aliuliza.
"Nilikuwa naangalia kamera ya CCTV majira ya saa nane na dakika tano usiku. Huwa ni kawaida yangu kuangalia mazingira ya nje na ndani ya hoteli. Nilianza kuangalia maz..." Wakati Kelvin akielezea ndipo alipokatishwa kwa ukali na Daniel Mwaseba.
"Kijana upo chini ya ulinzi, naona tunaleteana mas'hara hapa" Daniel alisema kwa jazba huku mdomo wa bastola yake ukimtazama Kelvin.
"Vipi tena kaka, si umeomba nikuelezee nini kilitokea? Sasa mbona wanionesha mimi bastola" Kelvin aliuliza kwa sauti kavu huku uwoga ukiwa mbali sana na yeye.
"Naitwa Daniel Mwaseba. Kama ni mara yako ya kwanza kulisikia jina hili basi jua tu Daniel sio mtu wa kufanyiwa mas'hara na mambo ya kijinga. Najua unapoteza muda hapa kwa maelezo yako yasiyo na maana. Sijajua malengo yako, lakini ninakuahidi nitayajua tu" Daniel alisema kwa hasira.
Kelvin alibaki kimya. Huku akiwaangalia wale watu sita kwa zamu.
Kwa kasi Daniel aliingia katika chumba namba sabini na nane akiwaacha wakina Kelvin pale nje. Hakukuwa na mtu ndani ya chumba namba sabini na nane. Alizungusha macho yake mle chumbani kuyaangalia mazingira ya kile chumba. Sekunde hizo chache aligundua kwamba mabegi ya kina Dr Luis hayakuwemo mle chumbani. Alipiga hatua kuelekea bafuni, huku bastola yake ikiwa imetangulia mbele. Nako hakukuwa na mtu.
"Nipeleke kwenye kamera za CCTV, nikaangalie nini kilitokea.. " Daniel alisema kwa amri.
Kelvin aliongoza njia bila kutia neno. Waliifata ile shuruba ndefu ya hoteli ya Dos Santos hadi chumba cha pili kutoka mwisho mkono wa kulia. Juu ya mlango mweusi kulikuwa kumeandikwa 'Control room'. Walipofika Kelvin Mbinu aligonga mlango. Baada ya kama sekunde tano mlango ulifunguliwa.
"Devi nimekuja na mwenyeji wa yule mzungu" Kelvin alisema kwa dharau.
Macho ya Daniel Mwaseba moja kwa moja yalitua mle chumbani. Kwa haraka haraka aliona video tatu, zote zikionesha maeneo mbalimbali ya hoteli ya Dos Santos.
"Nahitaji kuona picha zilizonaswa wakati Dr Luis anatoweka" Daniel alisema.
"Unahitajika kuwa na kibali cha meneja ili tuweze kukuonesha picha za CCTV" Devi alisema kwa dharau.
"Hivi mnajua mnaongea na nani ninyi?" Daniel alighadhibika.
"Huo ndio utaratibu kaka. Sina haja ya kujua wewe ni nani? Siwezi kukuonesha chochote katika CCTV mpaka uje na kibali kutoka kwa meneja" Devi alishikilia msimamo wake.
"Huyo meneja yupo wapi kwa sasa?" Daniel aliuliza.
"Meneja amesafiri leo asubuhi, ameelea Misri" Safari hii Kelvin nd'o alijibu.
Daniel aliwaangalia kwa tuo wale vijana wawili. Alikuwa anajitahidi kudhibiti hasira zake ambazo alikuwa anashindwa kuzihimili.
"Hawanijui hawa, ngoja niwafunze adabu" Daniel aliwaza.
Daniel aliruka hatua ndefu kumwelekea Devi. Goti lake la kulia lilitua katika kende za Devi. Devi alitoa yowe la uchungu huku akirushwa juu na kujibamiza ukutani.
Kwa kasi, Kelvin nae alikuwa anamsogelea Daniel, alikutana nayo...Daniel aliruka teke la kuzungusha na kumkumba Kelvin upande wa kulia wa uso wakw. Nguvu ya teke lile lilimporomoshea Kelvin katika video moja iliyokuwepo mle ndani. Daniel alisimama wima katika kile chumba huku akiwaangalia kwa zamu wale vijana wawili.
Ni Kelvin tena ndiye aliyenyanyuka kwa kusuasua na kumwelekea Daniel. Safari hii akiwa na bastola mkononi.
"Simama hivyohivyo Daniel, la sivyo nakupasua kichwa chako!!" Kelvin alimtahadharisha Daniel.
Daniel alikuwa anapiga mahesabu yake vizuri ili aweze kumpora Kelvin ile bastola nyeusi.
Lakini alichelewaa...
Hawa kina kelvin ni kina nani hasa? Je Dr Luis na mkewe wapo wapi?
RIWAYA; BOMU
MWANDISHI; HALFANI SUDY
Sehemu ya Nne
Wale watu sita waliowaacha kule mlangoni, katika chumba namba sabini na nane alichopewa Dr Luis waliingia mle ndani. Wote wakiwa na bastola mikononi.
"Daniel huu ndio mwisho wako" Jamaa mmoja, aliyekuwa mrefu na mweusi kuliko wote kati ya wale sita alisema.
Daniel aliwaangalia kwa zamu wale watu. Alikuwa haelewi kabisa ni kitu gani kinatokea. Na wale watu ni kina nani? Na wamejuaje ujio wake katika hoteli ya Dos Santos? Lilikuwa fumbo tata ambalo Daniel Mwaseba hakuweza kulifumbua hata kidogo.
"Nyoosha mikono yako juu!!" Yule jamaa mrefu na mweusi alimuamuru Daniel Mwaseba.
Daniel alinyoosha mikono yake yote miwili juu. Huku akiruhusu bastola zake zote mbili kuonekana kiunoni.
"Dingo mchomoe hizo bastola.." Yule jamaa mrefu mweusi alisema huku akimwangalia kijana mmoja mfupi kuliko wale wote.
Dingo alimsogelea kwa tahadhari Daniel huku akimtazama usoni. Alijua kuwa Daniel sio mtu wa kumwingia kwa pupa. Ilihitajika tahadhari ili kuwa karibu yake. Dingo alifanikiwa kuchomoa bastola mbili kutoka kiunoni mwa Daniel Mwaseba. Kisha akampekua mifukoni kama kuna lolote la hatari. Katika mifuko ya mbele ya Daniel Mwaseba hakukuwa na kitu. Lakini alipomsachi katika mfuko wa nyuma, aliikuta 'wallet'. Dingo akaichukua na kuiweka ile 'wallet' katika mfuko wake.
"Dingo muongoze kutoka nje ya hoteli. Nakuonya Daniel, ukifanya ujanja wowote ule nakuapia kwa Shetani nakupeleka kuzimu kwa mkono wangu mwenyewe!!" Yule jamaa mrefu mweusi alisema huku akiipitisha bastola yake katikati ya shingo.
Dingo alizificha katika koti lake kubwa jeusi bastola mbili alizozichomoa kiunoni mwa Daniel. Sasa alikuwa sambamba na Daniel mwenyewe walitangulia mbele, wakati Kelvin, David na wale watu wengine wakifata nyuma. Wote walikuwa wameficha bastola zao sehemu wanaozijua wao.
Daniel alitembea bado mikono yake ikiwa juu. Alitembea kwa mwendo wa taratibu huku akiwapigia mahesabu wale jamaa.
"Shusha mikono yako chini. Sitaki watu wajue kama tumekuteka" Yule jamaa mrefu mweusi alisema.
Daniel alishusha mikono yake chini. Kwa siri kubwa aliuingiza mkono wake wa kulia mfukoni. Kwa chini kabisa ya mfuko ambapo Dingo hakufika wakati anampekua aligusa kitu kigumu, chenye umbo kama kifungo cha shati. Alianza kukibonyaza huku akipiga hatua za taratibu kuelekea yalipokuwa mapokezi ya hoteli ya Dos Santos.
Baada ya kama sekunde kumi za kubonyeza kile kifungo kule mfukoni, Daniel alitabasamu.
Alikuwa amefanikiwa...
"Nimeingia tena kwenye dirt game" Alisema kwa sauti ndogo. "Hii ndio michezo michafu niipendayo. Sasa ninaenda kujua hawa watu ni kina nani? Na wana lengo gani mpaka wakaamua kumteka Dr Luis?" Daniel aliwaza wakati wakipita pale mapokezi ili kutoka nje ya hoteli ya Dos Santos.
Alitabasamu tena...
***
HANNAN HALFANI alikuwa ni msichana mdogo aliyeajiriwa katika ofisi ya usalama wa Taifa. Alikuwa na wiki tatu tu tangu atoke nchini Cuba katika mafunzo ya juu ya kijasusi. Alifuzu vyema, na moja kwa moja alijiunga na idara ya usalama wa taifa Tanzania. Na alivyotua tu nchini alipata bahati ya kuwa ofisi moja na mpelelezi Daniel Mwaseba.
Muda huu wa saa kumi na dakika saba usiku Hannan alikuwa amelala nyumbani kwake Sinza Kijiweni. Akiwa amelala fofofo ndipo simu yake ikatoa mlio wa ajabu. Hannan alikurupuka usingizini, hakuifata simu yake, moja kwa moja alivaa nguo za kazi na kuchukua zana kadhaa za kazi. Alitoka nje na simu yake mkononi. Akaingia katika gari lake dogo jeusi aina ya Spacio. Akachukua simu yake na kuiunganisha na waya mdogo. Mbele ya 'dashboard' ya gari kikiwa na ramani ya jiji la Dar es salaam. Huku kialama chekundu kikiwa kinatembea.
"Huyu ni Daniel Mwaseba.." Hannan alisema kwa sauti ndogo huku akikiangalia kile kialama chekundu kikichojongea.
Akawasha gari na kuanza kuifata ile alama nyekundu. Ambayo ramani ndani ya gari la Hannan ilionesha kuwa kipo katika mataa ya Sayansi, Kijitonyama.
Naye aliongeza moto gari lake kuelekea huko.
Kutoka Sinza Kijiweni alipokuwa anakaa hadi katika taa za Sayansi hakukuwa mbali sana. Na kwa vile usiku hakukuwa na foleni, kubwa, ukichanganya na mwendo wa kasi akioendesha basi palizidi kuwa pafupi.
Ndani ya dakika kumi alikuwa anaiona gari ambayo alihisi ndio ilikuwa imempakia Daniel Mwaseba mbele yake.
Ndani ya gari Daniel Mwaseba alikuwa amewekwa katika kiti cha kati cha gari aina ya Noah nyeusi. Alikuwa amefungwa kitambaa cheusi usoni kisichomuwezesha kumuonesha wapi wale watu walikuwa wanaelekea. Mikono yake yote ilikuwa imefungwa kwa kamba ngumu kwa nyuma, na miguu pia ilifungwa kwa kamba imara. Daniel alikuwa hawezi kufurukuta. Bila kuwahi kukibonyeza kile kifungo mfukoni basi pengine alikuwa amekwisha.
Ndani ya gari ilikuwa kimya. Hakuna aliyekuwa anaongea. Kijana mmoja mweupe kuliko wote alikuwa anaongoza usukani, huku wale majamaa wengine wote walikuwa wanamlinda Daniel Mwaseba. Wote walikuwa wanajua kwamba Daniel Mwaseba alikuwa sawa na Bomu!! Muda wowote ule lingeweza kuwalipukia.
Gari waliomo kina Kelvin ilikuwa maeneo ya Kinondoni, usawa wa chuo kikuu huria. Haikuwa inaenda kwa kasi sana ili kutowatia shaka watu watakaoliona gari hilo likipita barabarani. Ulikuwa ni mwendo wa kawaida, mwendo wa kumpeleka Daniel Mwaseba kusulubiwa.
Hakuna aliyekuwa anajua kwamba nyuma ya magari mawili kulikuwa na Hannan Halfani, mwanamke aliyekuwa na lengo moja tu, kufatilia ni wapi alipokuwa anapelekwa mpelelezi Daniel Mwaseba ili amwokoe.
Dakika ishirini baadae msafara ulifika maeneo ya Mbagala. Walisimama kama dakika mbili pale Mbagala rangi tatu. Hakushuka mtu ndani ya gari. Hannan yeye alisimamisha gari yake usawa uliopo ukumbi wa Dar Live, huku akiruhusu macho yake kutopotewa na watu wale ambao aliamini kwamba walikuwa na nia ovu dhidi ya Daniel Mwaseba.
Baada ya dakika hizo mbili gari iliyombeba Daniel Mwaseba ilianza safari tena.
"Mambo yapo safi. Hakuna kidudumtu chochote kinachotufatilia" Yule dereva mweupe aliongea huku akitabasamu.
"Sawa Brian, lakini usiache kuangalia mara kwa mara. Kama kuna gari au pikipiki yoyote unaitilia shaka, twambie tucheze nayo" Yule jamaa mrefu mweusi ambaye alionekana kuwa ndiye kiongozi wa wale majamaa alisema.
"Najua jukumu langu" Brian alisema kwa kifupi.
Safari ya wakina Kelvin ilifika katika mji wa Mkuranga. Mkuranga ni mji mdogo uliokuwepo mkoa wa Pwani. Iliwachukua dakika arobaini na tatu wakina Kelvin kufika katika mji huo.
Katika nyumba moja iliyokuwepo eneo la peke yake maeneo ya Mkuranga shamba ndipo gari aina ya Noah lililompakia Daniel Mwaseba lilikuwa limepaki. Daniel alikuwa ameshushwa katika gari hilo na kusukwasukwa na wale jamaa, kisha kutupwa katika chumba kimoja kidogo pembezoni ya nyumba hiyo.
Kwasasa, Daniel Mwaseba alikuwa amekaa katika kona moja ya chumba hiko huku bado akiwa amefungwa kwa kamba ngumu mikono na miguu. Huku kitambaa cheusi kikiweka kambi ya kudumu katika uso wake.
Watu waliofanikisha kumleta Daniel katika chumba hiko walikuwa ndani wakijipongeza kwa kufanikisha kazi hii ambayo walihisi itakuwa ngumu sana kwao. Kumbe haikuwa hivyo, kazi ya kumteka Dr Luis na kumweka mikononi mwao Daniel Mwaseba ilitokea kuwa rahisi sana kuliko kawaida.
"Hongereni sana Kelvin na David. Mmetusaidia sana leo katika kufanikisha kazi hii. Yule mzungu hakupaswa kabisa kukutana na Mheshimiwa rais Mgaya. Dr Luis angekutana tu na rais basi ungekuwa ndio mwisho wa Roho. Roho amefurahi sana kusikia kuwa tumefanikiwa kumteka Dr Luis. Dr Luis alikuwa ni bomu baya sana kwetu, lakini kwa sasa tumefanikiwa kulitegua bomu hilo bila ya kuleta madhara yoyote yale" Yule kiongozi wao mrefu mweusi alisema wakiwa wamekaa katika ukumbi wa mikutano wa nyumba hiyo.
"Nasi tumefurahi sana kwa kuweza kufanikisha kazi hii. Maana haikuwa kazi ndogo sana, baada ya kusikia kwamba ni Daniel ndiye atakayekuja nae Dr Luis hotelini, mimi na David tuliingiwa na uwoga sana. Najua hakuna asiyejua uwezo wa Daniel Mwaseba katika mambo haya, lakini kwa kushirikiana na yule mwanamke Cynthia tulifanikisha hili jambo kwa urahisi sana" Kelvin alisema kwa kirefu.
"Ni kweli, sote tunaujua uwezo wa Daniel, na ndiomaana tukamwandaa Cynthia kutoka China kuja kufanikisha jambo hili.
Sasa tulisema tutawapa milioni arobaini kwa kazi hii, wewe na Devi. Kwa maana kila mmoja apate milioni ishirini" Yule kiongozi alisema huku akiwaangalia kwa zamu wakina Kelvin.
Kelvin na David waliitikia kwa kichwa kwa pamoja huku sura zao zikionesha tabasamu.
"Mtazikuta hizo hela katika akaunti ya kila mmoja wenu. Ila kuweni makini sana, maana mnaweza kuanza kuchunguzwa na polisi kuhusu kupotea kwa Dr Luis katika hoteli ya Dos Santos. Kuweni makini sana na majibu yenu. Na hakikisheni ham'watii shaka yoyote ile jeshi la Polisi" Yule kiongozi mrefu mweusi alisema.
"Msiwe na shaka kabisa na sisi. Tutafumba midomo yetu. Hatutosema lolote lile kuhusu kilichotokea usiku wa leo pale hotelini" Kelvin alisema, kisha wakaagana na wale watu sita. Walitoka nje katika uwa mpana wa nyumba ile. Lakini hawakuwahi kufika hata getini. Migongo yao ilikuwa haitamaniki. Walikuwa wamechakazwa na risasi zisizo na idadi. Hiyo ilikuwa ni kazi ya Carlos, kiongozi wa wale jamaa sita.
"Hakuna pesa ya bure namna hii...Nisalimieni kuzimu!!! Naitwa Carlos!!" Yule jamaa mrefu mweusi alisema kwa kebehi huku bastola yake ndogo ikifuka moto.
Mlio wa risasi kutoka katika bastola ya Carlos ulisikiwa vizuri sana na masikio ya Daniel Mwaseba kule kibandani, akahisi kwamba Hannan amefika kwa lengo la kuja kumuokoa. Akajua kazi imeanza, naye akaanza kutafuta namna ya kufungua zile kamba, ili atoke nje kusaidiana na Hannan.
Kule nje pia, mlio ule wa risasi kutoka katika bastola ya Carlos ulisikiwa vizuri sana na masikio mawili ya Hannan Halfani. Yeye moyo ulimpiga vibaya sana. Akijuta kwanini alichelewa kuingia mle ndani kumuokoa Daniel. Aliamini kwamba risasi zile alizozisikia zilikuwa zimeingia katika mwili wa Daniel Mwaseba.
Kumbe haikuwa hivyo.
Hannan alifanya himahima kwenda kuvamia ile nyumba.
"Kama wamemuua Daniel, nao hawastahili kuishi hata dakika moja katika sayari hii. Lazima nao wauawe!" Hannan alikuwa anaapa kimoyomoyo wakati akiisogelea ile nyumba ya wale jamaa.
Daniel anawaza kujiokoa huko ndani, wakati huohuo Hannan akija wakawaka kumuokoa Daniel...Je nini kitatokea huko ndani? Tuwe wote katika sehemu ijayo.
Ndani ya kibanda alichofungwa Daniel kulikuwa na giza totoro, ingawa jua la asubuhi lilikuwa limeanza kuchomoza huku nje.
Lakini kwa bahati mbaya, katika chumba alichofungiwa Daniel kama mateka hakukuwa na madirisha hivyo mwanga wa jua haukuruhusiwa kuingia mle ndani hata chembe.
Ndani ya chumba, kulikuwa na kiti kidogo cha mbao kilichokuwa katikati ya chumba. Ukiondoka hiko kiti kikuukuu hakukuwa na kitu kingine chochote kile.
Daniel alikuwa amesweka pembeni kabisa ya kile chumba. Bado alikuwa na kitambaa cheusi usoni, kisichoruhusu aone chochote kile mle ndani. Giza la kitambaa alichofungwa ukijumlisha na giza lilikuwemo mle ndani ya chumba, utaelewa ukubwa wa giza alilokuwa anatazama nalo Daniel. Ukiondoa giza bado alikuwa amefungwa kamba kwa nyuma katika mikono yake yote miwili, na miguuni pia alikuwa amefungwa kamba ngumu na imara.
Tangu wanatoka katika hoteli ya Dos Santos, ambapo Dr Luis ndipo alipopotelea ndani yake kama alivyodai Kelvin, pia katika hoteli hiyo ndipo mahali Daniel Mwaseba alikuwa ametekwa.
Sio kwamba Daniel alikuwa hawezi kuwatoka wale majamaa kulekule hotelini ama ndani ya gari. Daniel alikuwa anaweza sana, tena alikuwa ana uwezo zaidi ya huo. Ila hakufanya kitu. Alijiambia awe na subira..kwa maana Wahenga waliwahi kusema siku zote subira yavuta heri.
Nia yake ilikuwa kuona wale watu watampeleka wapi. Alikuwa anajua lazima wale majamaa watampeleka katika chimbo lao ambapo alikuwa anaamini Dr Luis pia atakuwa huko.
Hivyo, alichofanya ni kukigusa kifaa chake kilichopo mfukoni ili kumwamsha Hannan ambaye alikuwa anajua nini cha kufanya pindi tu ataposikia mlio huo. Na kweli, Hannan aliweza kufatilia mahali alipokuwa anapelekwa. Hii ilikuwa na maana kama kutakuwa na lolote la kumsaidia basi amsaidie.
Mle ndani ya chumba, Daniel aliipitisha mikono yake juu ya kichwa ili mikono yake iliyofungwa kamba iwe kwa mbele. Lilikuwa ni zoezi gumu pengine lingefanywa na mimi au wewe. Lakini, sio kwa Daniel Mwaseba. Mpelelezi namba moja nchini Tanzania. Kijana anayeaminika zaidi katika idara ya usalama wa Taifa. Hilo kwa Daniel lilikuwa ni miongoni mwa mazoezi rahisi sana aliyowahi kuyafanya katika harakati zake za kipelelezi.
Mikono ya Daniel ilipofika mbele aliipeleka mdomoni na kufungua fundo lililofungwa. Mikono ya Daniel Mwaseba kwa kutumia meno. Ndani ya dakika tatu mikono ya Daniel ilikuwa huru sasa. Na hivyo kazi ya kufungua zile kamba za miguuni kuwa kama kumsukuma mlevi.
Ndani ya dakika mbili, Daniel alikuwa kasimama wima katikati ya kile chumba. Alikuwa hana kamba katika mikono yake wala miguu. Na kile kitambaa cheusi kilichokuwa usoni kilikuwa sakafuni.
Daniel alivua shati alilokuwa amevaa na kuangalia kwenye kola. Alitumia sekunde kama kumi hivi kulifumua. Akatoa kitu kidogo cha chuma.
Ilikuwa funguo malaya...
Aliishika mkononi ile funguo baada ya kuvaa tena lile fulana.
"I am coming Kelvin..." Daniel alisema kwa sauti ndogo huku akifungua mlango kwa ile funguo aliyoishika. Mlango ukafunguka, akauvuta ule mlango kidogo na kuanza kuchungulia kwa nje.
Ndipo alipoona...
Mbele ya macho yake alikuwa anazitizama maiti za wakina Kelvin na David zikiwa zimelala katika dimbwi la damu!!!
Afanaleeek...
"Nani kawauwa hawa vijana? Ni Hannan au?" Daniel alijiuliza mwenyewe, hakukuwa na wa kumjibu.
Daniel alirudi tena ndani ya kile chumba alichofungiwa. Alifunga tena ule mlango kwa kutumia ule funguo wake malaya. Akasimama karibu na mlango kusikilizia.
Sekunde tisa tu tangu alipoingia ndani mlango ulikuwa unafunguliwa na mtu kutoka nje.
Ndipo alipoingia Ndimbo wa Ndimbo..
Mwanaume anayejulikana kwa jina la Ndimbo wa Ndimbo, ndiye aliyekuwa kiongozi wa ulinzi katika nyumba hii ambayo Daniel alikuwa ameletwa. Na nd'o yeye ndiye aliyejipa jukumu la kwenda kumuhoji Daniel Mwaseba katika chumba cha mateso.
Hakujua kwamba Daniel Mwaseba hakuwa sawa na yule waliyemleta muda uliopita. Kwa sasa, alikuwa huru kufanya kitu chochote kile atakacho. Alikuwa huru kwa maana sahihi ya neno huru. Huru miguuni kwa maana hakuwa kamba miguuni. Huru mikononi kwa maana pia hakuwa na kamba mikononi. Kile kitambaa cha kukera, kitambaa kilichomletea giza walichombandika usoni nacho kilikuwa kimelala sakafuni.
Ndimbo wa Ndimbo, ambaye kwa makadirio ya umri alikuwa kama na miaka arobaini mbili, aliufungua ule mlango akitanguliwa na bastola yake mbele. Pamoja kwamba alijua Daniel alikuwa amefungwa kamba lakini aliweka tahadhari mbele. Mlango nao haukuwa na hiyana, ulifunguka baada ya kusukumwa na mdomo wa bastola...
Alipoona kuna harufu ya amani, Ndimbo wa Ndimbo aliutosa mguu wake wa kulia kuvuka katika kizingiti cha mlango, kisha ukafatiwa na mguu wake wa kushoto huku macho yake mekundu na ya kutisha yakiangalia pale mahala walipomtupia Daniel.
Daniel Mwaseba hakuwepo!!
Mshangao dhahiri ulitamalaki katika macho yake mekundu. Kwa jinsi walivyomfunga Daniel alikuwa na uhakika Daniel asingeweza kujisogeza hata nukta moja kutoka pale chini. Cha kushangaza sasa, Daniel hakuwepo pale mahali.
Hakuwepo...
Sekunde hiyohiyo likapita jambo la kushangaza zaidi katika kichwa chake. Kile kitambaa cheusi walichomfunga Daniel usoni kilikuwa kimelala pale sakafuni.
Daniel hakuruhusu mshangao mwengine kwenda kwa Ndimbo wa Ndimbo...
Alijisogeza taratibu kutoka nyuma ya mlango akitanguliwa na teke la mguu wa kulia lililoukwapua ule mkono wa Ndimbo alioshikilia bastola. Lilikuwa ni shambulio la kustukiza kwa Ndimbo wa Ndimbo lilikompeleka sakafuni bila kupenda, huku bastola yake ikiruka juuu na kutua konani kabisa ya kile chumba.
Harakaharaka Daniel Mwaseba aliufunga ule mlango kwa funguo yake..
Sasa mle ndani giza lilirejea kama awali, huku wanaume wawili wakiwemo ndani yake. Walikuwa wanatazamana gizani mithili ya midume ya nyani.
Ilikuwa jasho na damu!!
Daniel alimfata Ndimbo wa Ndimbo kulekule upande aliokuwa, wakati huo Ndimbo akifanya jitihada za kunyanyuka pale chini.
Kwa kasi na nguvu, Daniel alirusha tena teke kwa mguu wake wa kushoto. Ndimbo aliliona lile teke. Alilikwepa kwa ufundi mkubwa na kumfanya Daniel akose 'balance'. Alipepesuka kidogo kuelekea kulia, na ndipo Ndimbo wa Ndimbo alipopata nafasi ya kushambulia..
Alirusha ngumi ya nguvu iliyotua chini kidogo ya tumbo la Daniel. Daniel aligugumia kwa maumivu huku akitoa sauti kidogo. Ndimbo akaona ile ndio nafasi pekee ya kuitumia. Alirusha ngumi nyingine kwa mkono wake wa kushoto, Daniel aliiona. Aliinama chini kidogo, ile ngumi ikapita sentimita chache sana kutoka katika kichwa chake.
"Nakuua!!" Ndimbo wa Ndimbo aliipata sauti yake kutoka huko ilipokuwa.
Daniel hakumjibu kwa maneno. Alimjibu kwa vitendo. Hii ilikuwa ni maneno dhidi ya vitendo. Kwa mguu wake wa kulia aliruka hewani na kudanda katika ukuta ambapo alipata nguvu ya kurusha teke la kwa mguu wake wa kushoto. Teke lilienda moja kwa moja usoni kwa Ndimbo na kupangusa pua ya Ndimbo. Ndimbo alianza kuchuruzika damu kutoka katika pua yake.
Daniel hakumpa nafasi, kwa kasi alizunguka nyuma yake na kumkaba kabali. Kabali iliingia bara'bara katika shingo ya Ndimbo wa Ndimbo. Kila alipokuwa anataka kuitoa ndio Daniel alikuwa anapata nafasi ya kumkaba zaidi.
Baada ya kama dakika mbili ya ile kabali, Ndimbo wa Ndimbo aliishiwa nguvu kabisa.
Alizimia.
Harakaharaka Daniel alichukua zile kamba alizofungwa yeye na kumfunga yule jamaa. Sasa Ndimbo wa Ndimbo alikuwa mateka wa Daniel Mwaseba.
Baada ya kama dakika saba Ndimbo wa Ndimbo alifungua macho yake. Alijikuta mbele ya Daniel Mwaseba, tena akiwa amefungwa kamba.
"Sasa utanieleza kila kitu kibaraka wewe" Daniel alisema huku akimwangalia Ndimbo wa Ndimbo.
Ndimbo wa Ndimbo alibaki amekodoa macho tu akiwa haamini ni kitu gani kimetokea?
"Mmetumwa na nani kumteka Dr Luis?" Daniel Mwaseba aliuliza huku akimwangalia kwa ghadhabu yule jamaa.
"Fala wewe usidhani mimi ni mateka wako na nitakueleza kila kitu. Ingawa umenifunga kamba hapa ila jua bado upo katika himaya ya Roho.." Ndimbo wa Ndimbo alijibu kwa majigambo.
Sitaki ngonjera zako hapa.." Daniel alisema huku akimtandika kibao katika shavu lake la kushoto.
"Nakuuliza kwa mara nyingine, nani kawatuma kumteka Dr Luis?" Daniel aliuliza.
Ndimbo wa Ndimbo alikaaa kimya.
"Nakuuliza kwa mara ya mwisho, na kawatuma mumteke Dr Luis?" Daniel aliuliza.
Bado yule jamaa alikaa kimya.
"Hanijui huyu.." Daniel alisema kwa sauti ndogo ambayo ilisikiwa vyema na Ndimbo wa Ndimbo.
Kwa kasi, bila kutarajia alinyoosha mkono wake wa kulia kuelekea katikati ya mapaja ya yule jamaa. Alikipata alichokuwa anakitaka.. Alizinasa korodani za Ndimbo wa Ndimbo. Zilijaa vizuri mkononi katika mkono wake imara. Akaanza kuzibinya taratibu.
Kila sekunde zilivyosogea mbele Daniel alizidi kuzibinya.
Ndimbo wa Ndimbo alianza kutaharuki, akataka kulia kwa nguvu, Daniel akamziba mdomo kwa mkono wake wa kushoto, huku mkono wa kulia akiendelea kumbinya kwa nguvu zile korodoni.
"D..ani..ell" Ndimbo wa Ndimbo aliita.
Daniel alikuwa kama hamsikii. Sasa alizinasa gorori zilizomo ndani ya korodani. Akazibinya kwa nguvu.
"Na..s..emaa.." Ndimbo wa Ndimbo alisema kwa shida.
"Haya niambie..nani aliyewatuma kumteka Dr Luis?" Daniel aliuliza huku akilegeza mkono wake uliokuwa umezibana korodani za Ndimbo wa Ndimbo hapo awali.
Je Ndimbo wa Ndimbo atasema nini? Tuwe wote katika sehemu ijayo. Inaitwa Bomu. Unapomaliza kuisoma like na kutoa maoni yako. Usipite kimyakimya.
"Dan..iel, sisi tumetu..mwa na kiu...mbe kinachoi..twa Roho" Ndimbo wa Ndimbo alijibu kwa sauti ya kukatakata.
"Roho? Ndio nani huyo kiumbe anayeitwa Roho?" Daniel aliuliza.
"Hakuna aliyewahi kumuona kwa macho yake huyo Roho. Katika kundi letu sidhani kama kuna anayeisikia hata sauti yake" Ndimbo wa Ndimbo alifikiria kidogo kisha akasema "Labda Dingo".
"Dingo ndio nani?" Daniel aliuliza tena.
"Dingo ndio kiongozi wa 24 Mission" Ndimbo wa Ndimbo alisema.
"24 Mission?"
"Ndio. Hiki kikundi chetu kinaitwa hivyo"
"Kazi yenu kuu hasa ni nini?"
"Huwa tunafanya kazi za kihalifu, kama kuvamia benki, vituo vya mafuta au maduka makubwa. Huwa tunapewa kazi na Dingo ambaye yeye huagizwa na Roho" Ndimbo wa Ndimbo alisema. Daniel aliyaangalia macho mekundu ya yule mzee yalionesha kwamba alikuwa anasema kweli.
"Ok niambie ilikuwaje kuwaje hadi mkajua kwamba mimi na Dr Luis tutafikia hoteli ya Dos Santos?" Daniel aliuliza huku macho yake yakimwangalia Ndimbo wa Ndimbo usoni.
"Hii mission pia ilitolewa na Roho mwenyewe kwa kupitia Dingo. Kwa kutumia pesa Dingo aliwashawishi wahudumu wote wa hoteli hapa jijini kutoa taarifa pindi tu yule mzungu atapowasili katika hoteli anayofanyia kazi, na alisambaza picha yake pia kwa kila mhudumu.." Ndimbo wa Ndimbo alisema.
"Unavyohisi wewe kwanini Roho aliwaagiza mumteke yule mzungu?" Daniel aliuliza tena.
"Kwa kweli mimi sifahamu kitu chochote kile kuhusu yule mzungu. Hata hivyo huwa tukipewa maagizo hatuulizi sababu. Kazi yetu kuu kutekeleza maagizo. Dingo pekee nadhani anaweza kujua sababu ya mission hii.." Ndimbo wa Ndimbo alisema.
"Huyo Dingo yupo hapa?" Daniel aliuliza.
"Ndio, Dingo yupo huko ndani na wenzangu. Na bila shaka watakuwa wananitafuta sasahivi" Ndimbo wa Ndimbo alisema.
"Kwani hukuwaambia kama unakuja huku?"
"Niliwaambia. Lakini wataona nimechelewa sana kurudi"
Daniel alifikiria. Akauona ukweli katika maneno ya yule jamaa.
"Kwasasa mmempeleka wapi yule mzungu?" Daniel lilimtoka swali.
"Yule mzungu alichukuliwa kwa gari jana usiku na mwanamke mmoja..."
"Mwanamke?" Daniel aliuliza kwa wahka mkubwa.
"Ndio, ni mwanamke ingawa mimi simfahamu. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumuona. Maagizo kutoka kwa Dingo yalikuwa ni kumteka yule mzungu na kumkabidhi kwa huyo mwanamke" Ndimbo wa Ndimbo alisema.
"Huyo mwanamke aliwachukua pamoja na mkewe?" Daniel aliuliza huku damu ikimchemka.
"Hapana. Yule mwanamke hakumchukua..." Ghafla aliacha kuongea, alikatishwa na makelele ya kugongwa na mlango wa chumba cha mateso kwa nje.
"Ngo ngo ngooo!!" Mlango uligongwa kwa nguvu huku jamaa kule nje akijaribu kuzungusha kitasa.
"We Ndimbo wa Ndimbo upo wapiii.." Jamaa aliamua kuita kabisa.
"Ukijifanya kuleta ujanja wowote nakupeleka kuzimu" Daniel alionya huku mdomo wa bastola ukiwa usoni mwa yule jamaa.
Baada ya kama dakika tano za kugongwa kwa fujo ule mlango, baadae kukatulia.
Daniel akitanguliwa na bastola aliyompora Ndimbo wa Ndimbo alisogea kule mlangoni. Kwa kutumia ule funguo bandia aliufungua ule mlango taratibu. Alichungulia kidogo.
Aliyoyashuhudia huko nje...
Kule nje Hannan alikuwa bado anatafuta namna ya kuingia katika nyumba ile iliyokuwa na ukuta mrefu. Ambapo ndani yake Daniel Mwaseba alikuwa amefungwa.
Baadae aliipata..
Nyuma ya ile nyumba iliyozungukwa na ukuta mrefu kulikuwa na mti aina ya mwarobaini. Mti ambao Hannan aliiona fursa ya kuweza kumuingiza mle ndani. Kwa umakini mkubwa sana aliupanda mti ule. Bastola yake ilikuwa imara katika mkono wake wa kulia wakati akipanda. Alikuwa tayari kuidungua hatari yoyote ile kabla haijamletea hatari.
Sekunde sabini na tatu tu zilimfikisha Hannan kileleni mwa ule mti. Alijivuta kidogo na kuugusa ukuta wa ile kwa kutumia mguu wa kulia, kisha akapeleka na mguu wa kushoto.
Sasa alikuwa amekaa juu ya ukuta akiwa katika harakati za kushuka chini. Ili kuingia ndani ya ile nyumba, kwenda kumuokoa Daniel Mwaseba..
Hakuwahi kuruka...
Katika bega lake la kulia ziliruka damu kwa nguvu!!! Hannan alishindwa kuhimili maumivu yaliyokuja baada ya damu zile kuruka. Alidondoka mzimamzima akiambatana na yowe la maumivu kuelekea ndani ya ile nyumba.
Alikuwa amepigwa risasi!!!
Kule chini akiwa katika maumivu ya hali ya juu alijaribu kujiviringisha ili kuwaepuka watu wale waliogeuka kuwa wabaya kwake. Lakini hakuweza, pale chini zilivurumishwa risasi kama mvua. Na risasi tano ziliingia moja kwa moja katika sehemu mbalimbali za mwili wa Hannan. Ilikuwa hali ya hatari sana kwa Hannan Halfani!!!
***
Wakati Hannan anashambuliwa na risasi zisizoeleweka zilikuwa zinatokea wapi, ndio wakati huohuo ambao Daniel Mwaseba alikuwa anatoka katika kile chumba cha mateso. Alishuhudia vumbi lilivyokuwa linatimka karibu na ukuta. Hakujua ni nani anashambuliwa pale ukutani lakini alifanya kitu.
Daniel alilenga shabaha kuelekea upande ilipokuwa zinatoka zile risasi. Risasi yake moja tu ilitosha kukomesha mmimino ule wa risasi. Daniel akiwa mwishoni kabisa mwa ukuta wa chumba cha mateso alipiga shabaha kali sana. Alimdungua mtu ambaye aliyekuwa anapeleka dhahama kwa Hannan.
Aliambaaambaa na ule ukuta akielekea mahali ambapo risasi za yule jamaa zilikuwa zinaelekea.
Akiwa katikati ya ule ukuta na chumba cha mateso naye alianza kushambuliwa. Harakaharaka alilala chini huku akijiviringisha chini bila mwelekeo maalum. Alifanikiwa, alipoteza shabaha ya mpigaji.
Daniel alijiviringisha ardhini, akawa amelala chali, akiwa amelala chali aliikutanisha mikono yake yote miwili na kuikamata imara bastola yake, alifinya jicho moja na kuitomasa triga kwa nguvu. Kitu kilikubali...
Risasi ilitoka kwenye bastola ya Daniel na kwenda kuzama katika uso wa mshambuliaji aliyekuwa pembeni kabisa ya ile nyumba.
Ilikuwa shabaha kali sana ambayo Daniel Mwaseba aliipiga akiwa katika mazingira magumu kabisa.
Daniel alijiandaa kusimama ili kuelekea kule ukutani, kumwangalia yule aliyekuwa anashambulia.
Hakuwahi kufika..
Ulisikika mlio wa ajabu angani. Harakaharaka Daniel alilala tena chini kusikilizia. Mara ule mlio ulizidi kuongezeka.
Daniel akagundua kwamba ulikuwa ni mlio wa helkopta!!
Ilichukua sekunde tisa tu tangu alipogundua kuwa ilikuwa helkopta..jamaa waliachia Bomu zito kuelekea katika ile nyumba!!
Mara moto mkubwa ulizunguka!!
Nyumba ya wale jamaa ilianza kuteketea kwa moto.
E bwana wee!!
Wakati Daniel anaenda kumuokoa Hannan, nyumba ya wale jamaa inateketezwa kwa moto. Je Daniel atafanya nini? Simulizi ya Bomu sasa nd'o inaanza. Tuwe wote katika sehemu ijayo
Moshi wa bomu ulikuwa mkubwa sana ndani ya ile nyumba. Huku moto uliotokana na lile Bomu ukiendekea kuteketeza vibaya sana ile nyumba.
Daniel Mwaseba alipata nguvu za ajabu sana. Akiwa katikati ya moshi mzito alielekea kule ukutani. Alipambana moshini kwa shida sana lakini alifika alipotaka kufika...
Alifika mahali alipokuwa yule mtu.
Aliinama chini ili kumtazama yule mtu, alimtambua.
"Hannaan" Daniel aliita huku akimpapasa kwa fadhaha yule mwanamke.
Huku, moto uliendelea kuteketeza ile nyumba, huku moshi nao ukiendelea kusambaa hewani.
Daniel Mwaseba alijaribu kumbeba yule mwanamke wakiwa katikati ya moshi. Lengo ni kumuepusha na like dhahama, lakini hakuweza. Hakuweza katu.
Baada kama ya sekunde tatu moshini, ndipo alipogundua kwamba hakuwa na nguvu hata za kuuinua unyoya wa kuku, sembuse nguvu za kumuinua Hannan.
Mwanamke mwenye kilo sitini na tano.
Thubutu!!!
na hakuthubutu katu.
"Ha..nn..an.." Daniel alijaribu kuita tena, sasa ndio aligundua hata sauti yake mwenyewe ilikuwa inamsaliti. Sio tu aliishiwa nguvu. Daniel Mwaseba aliishiwa hadi sauti. Sauti ya Daniel ilikuwa inakatakata, huku sauti nyingine ikipotelea moshini.
Alimwangalia Hannan aliyekuwa yupo hoi pale chini. Hajui Aa wala Bee. Hana lolote alitambualo litokealo hapa duniani.
Alipozidi kumwangalia, ndipo alipoona..
Majimaji mazito yenye rangi nyekundu yalikuwa yametapakaa katika bega la Hannan.
"Damu!!" Daniel alisema kimoyomoyo.
Daniel aliingalia ile nyumba iliyokuwa inamalizikia kuteketea.
Akamwangalia tena Hannan.
"Tumekwisha" Alisema tena kimoyomoyo.
Mara, alianza kuona maluweluwe. Alijihisi kila sekunde zikivyoyoyoma ndio jinsi nguvu zake zikivyopungua kwa kasi sana...
Sasa hata nguvu ya kufungua macho yake mwenyewe ilimpotea, usiseme ile nguvu ya kusimama mbele ya Hannan. Ghafla, Daniel Mwaseba alidondoka chini, pembeni kidogo ulipokuwa mwili wa Hannan.
Sasa Daniel alikuwa hana ujanja. Mabaharia walikuwa wamechomoa betri, na kwa bahati mbaya Daniel Mwaseba na Hannan Halfan walikuwa wanaenda kuteketea na moto ule mbaya, moto uliosababishwa na Bomu.
Daniel hakukata tamaa. Alijitahidi kunyoosha mkono wake kwa shida sana. Akamgusa tena Hannan. Akapapasa katika mfuko wa Hannan.
Aligusa kitu kigumu.
"Simu" Daniel aliwaza kimatumaini.
Daniel akajitahidi kuingiza mkono mfukoni na kuitoa simu ya mkononi ya Hannan. Alijilazimisha kufungua macho katikati ya moshi mwingi. Lilifunguka jicho moja tu, jicho la upande wa kushoto. Alilitumia jicho hilohilo kuiangalia ile simu ya mkononi ya Hannan. Akaanza kubonyezabonyeza ile simu. Kwa shida sana, lakini aliweza kuiandika.
Namba ya Chifu.
ITAENDELEA
Simulizi : Bomu
Sehemu Ya Pili (2)
Alipiga ile simu na kuiweka sikioni. Akaanza kuita wakati lile jicho la kushoto nalo lilipoamua kufunga kwa hasira.
Kwa bahati nzuri sana simu ilipokelewa upande wa pili.
"Tu..na..kufa...aa" Hilo ndilo neno pekee alilojaaliwa kulitamka huku sauti yake ikikatakata.
Dakika hiyohiyo alihisi maumivu makali ya mvuke wa moto. Huku ile hewa iliyojaa moshi ikiwasulubu vilivyo. Walikuwa katika hali ngumu sana.
"Tunakufa kweli kwa moto!!" Daniel aliwaza kimoyomoyo. Hakuona namna inayoweza kuwafanya watoke hai ndani ya moto ule mzito.
Baada ya kama dakika nne, Daniel Mwaseba hakuelewa chochote kinachoendelea hapa duniani.
Alitekwa na moshi ule mzito...
ZILIKUWA zimepita siku mbili tangu kutokea ile ajari mbaya ya moto huko Mkuranga. Ajari ambayo ilikuwa imeacha maswali mengi sana, lakini haikuleta jibu hata moja.
Watu pekee ambao walikuwa wanatarajiwa kutoa majibu, walikuwa wamelala hoi katika vyumba vya hospitali ya taifa ya Muhimbili, ghorofa ya nane, katika wodi namba arobaini na nne katika jengo la Mwaisela.
Daniel Mwaseba na Hannan Halfani walikuwa katika wodi iliyokuwa na vitanda viwili pekee. Kitanda cha kushoto alikuwa amelazwa Daniel Mwaseba wakati upande wa kulia alikuwa amelazwa Hannan.
Wote wawili walikuwa hoi vitandani ndani ya saa ishirini na tangu wapelekwe Muhimbili. Kwa mujibu wa Dr Yusha, Daniel na Hannan walikuwa wameathiriwa kwa ndani na moshi waliovuta. Huku Hannan akipata madhara makubwa zaidi baada ya kukutwa na risasi sita ndani ya mwili wake.
Upasuaji wa kuondoa risasi katika mwili wa Hannan ulikuwa umefanikiwa kwa asilimia kubwa ndani ya saa arobaini na nane. Na sasa madaktari na manesi wa hospitali ya taifa ya Muhimbili walikuwa wamepambana sana kupunguza athari za moshi ambazo walikuwa nazo wote wawili.
Kwasasa, Daniel Mwaseba alikuwa ameamka kama dakika tano zilizopita. Tangu alivyoamka kutoka huko alipokuwa alikuwa anasema neno moja tu, tena kwa sauti ndogo sana.
"Tunakufa, tunakufa, tunakufa"
Pembeni ya kitandani cha Daniel Mwaseba kulikuwa na watu watatu, wakioenda sambamba na kila mrindimo wa pumzi za Daniel Mwaseba. Walikuwa wakipumua nae, huku kila mmoja akiomba dua ya aina yake ili Mwenyezi Mungu amponeshe salama Daniel.
Kulikuwa na mkuu wa majeshi ya Tanzania, Jenerali Bruno Ngoma. Pembeni yake, alikuwepo mkuu wa jeshi la Polisi la Tanzania, IGP John Rondo sambamba mkurugenzi wa idara ya usalama wa Taifa, ambaye alizoeleka kuitwa kwa jina la Chifu.
Wote walikuwa na sura zilizoonesha kuwa na matumaini baada ya kumuona Daniel Mwaseba akifumbua macho yake. Na walifarijika zaidi baada ya kumsikia akiongea.
"Pole sana Daniel.." Chifu alisema kwa sauti ndogo.
Daniel aligeuza shingo yake upande wa kushoto ambapo walikuwa wamekaa wale viongozi. Akatikisa kichwa chake juu, kisha akarudisha chini. Aliitikia ile pole kwa kichwa.
"Daniel.." IGP Rondo aliita.
Daniel aligeuza tena shingo yake ule upande wa kushoto.
"Pole sana kwa maswahibu yaliyoyokukuta Daniel" IGP John Rondo alisema.
Daniel aliitikia tena kwa kutikisa kichwa kama awali.
"Pole sana afande" Jenerali Ngoma naye aliitupia pole yake kabla Daniel Mwaseba hajageuza tena shingo yake.
"Ahsante sana afande" Kwa mara ya kwanza tangu apatwe na matatizo Daniel Mwaseba alijibu kwa mdomo.
"Daniel, wote unaotuona hapa tulikuwa na shauku sana ya kusikia sauti yako. Siku zote mbili ambazo ulikuwa haujitambui zimekuwa ngumu sana kwetu. Sio sisi tu hata kwa mheshimiwa rais. Hakuna anayeelewa kitu gani kilitokea pindi tu ulipotoka kumpokea Dr Luis uwanja wa ndege zaidi yako na Hannan, ambaye naye yupo hoi kitandani.. Tunaomba tusikie kutoka kwako ili tujue wapi pa kuanzia ili tumuokoe Dr Luis" Chifu alisema kwa kirefu.
"Chifu, nilitekeleza maagizo yako kama ulivyonambia" Daniel aliongea kwa sauti ndogo. "Nilienda kumpokea Dr Luis na mkewe katika uwanja wa ndege wa Julius nyerere majira ya ...."
"Ulienda kumpokea Dr Luis na mkewe?" Chifu aliuliza kwa wahka mkubwa.
"Ndio Chifu, Dr Luis alishuka na mwanamke wa kichina aliyesema kuwa ni mkewe" Daniel alisema sauti yake ikiwa chini mno.
"Dr Luis hajawahi kuoa tangu azaliwe.." IGP John Rondo alisema.
"Dr Luis hajawahi kuoa?" Daniel alishangaa. "Nakumbuka kabisa alinitambulisha kwa mdomo wake mwenyewe kule uwanja wa ndege kuwa yule mwanamke ni mkewe kabisa" Alisema.
"Ni hivyo Daniel, Dr Luis hajawahi kuoa hata kwa bahati mbaya. Lazima kutakuwa na kitu kilichojificha juu ya huyo mwanamke aliyekuja nae na kudai ni mkewe. Jukumu letu ni kukijua hicho kitu kilichojificha" IGP John Rondo alisema.
"Haya mambo yanashangaza sana kwakweli. Haya endelea kutusimulia Daniel ni kitu gani kilitokea baada ya kumpokea Dr Luis na huyo mwanamke aliyekutambulisha kama mkewe" Chifu alisema.
"Nilifanya kama ulivyoniagiza Chifu. Nilimpokea Dr Luis kule uwanja wa ndege na kwenda naye Kijitonyama katika hoteli ya Dos Santos. Baada ya kufikiria kidogo niliona si sahihi kumuacha Dr Luis alale peke yake pale hotelini, na mimi nililala palepale hotelini kwa ajili ya kumlinda Dr Luis.
Lakini cha kushangaza ilipofika saa tisa usiku nilipigiwa simu na mfanyakazi wa hoteli ile akiniambia kuwa Dr Luis amepotea. Nilianza harakati za kumtafuta, na katika harakati za kumtafuta nilijikuta nimetekwa na kupelekwa huko Mkuranga. Nikiwa njiani kama mateka, nilimtaarifu Hannan kwa ishara zetu kuwa nilikuwa katika hali ya hatari, naye alinifuata kwa gari.
Waliponifikisha huko Mkuranga, nilifungiwa kwenye kichumba kidogo. Kabla ya kujiokoa baada ya kusikia milio ya risasi nje. Nilivyotoka tu nilimuona mtu pembeni kabisa ukutani akigalagala. Wakati nikielekea kumuokoa ndipo ilipotokea helkopta yenye rangi ya jeshi na kuilipua ile nyumba..."
"Unasema helkopta yenye rangi za jeshi ndio iliyolipua ile nyumba?" Jenerali Ngoma alishangaa.
"Ndio Mkuu. Kwa macho yangu mawili niliishuhudia helkopta yenye mabaka ya jeshi ikiachia Bomu zito na kuiangamiza ile nyumba!" Daniel alisema.
"Bila shaka wakitaka kuficha kitu ndio maana waliiripua hiyo nyumba" Chifu alisema kwa sauti ndogo.
"Bila shaka. Hawa watu wana siri kubwa sana ambayo waliamua kutumia njia hiyo kuificha. Swali la msingi ni hawa watu ni kina nani? Na kwanini wamemteka Dr Luis?" IGP John Rondo aliuliza.
"Majibu ya maswali hayo uliyoyauliza sisi ndio wenye dhima ya kuyatafuta. Mheshimiwa rais ameacha kazi hii mikononi mwetu. Hivyo tujadiliane hapa ili kujua tunaanzia wapi kumpata Dr Luis? Pia lazima tujue kutekwa kwa Dr Luis kina nani wanahusika?. Tukiunganisha vyombo vyetu vya ulinzi bila shaka tutajua wahusika wa jambo hili" Chifu alisema.
"Umesema kweli Chifu. Hapa tupo viongozi wakuu wa ulinzi wa nchi hii. Lazima tufanye kitu kuhakikisha Dr Luis anapatikana. Mimi ushauri wangu tutoe mtu mmoja kila mmoja wetu katika sekta yake ili kuhakikisha suala hili linafika mwisho" Jenerali Ngoma alisema.
"Huo ni ushauri mzuri, nakubaliana nao" IGP John Rondo alisema.
"Nami pia naafiki" Chifu nae alisema.
"Kwakuwa hili ni jambo la haraka. Na lazima tulifanye kwa haraka kabla hawajamdhuru Dr Luis, pia hawajaleta madhara mengine, tuchague hapahapa watu ambao watachunguza jambo hili" Jenerali Ngoma alisema.
"Sawa, mimi katika jeshi la Polisi nitamtoa kijana wangu mahiri sana, anaitwa Adrian Kaanan" IGP John alisema.
"Mimi katika jeshi la Wananchi wa Tanzania nitamtoa kijana wangu David John. Ni mahiri sana katika uwanja wa vita, lakini kwasasa aliniambia ana hamu sana kujaribu uwezo wake mtaani. Na ishu hii kwakuwa inahusisha ndege ya jeshi basi itamfaa sana" Jenerali Ngoma alisema.
Kisha wote macho yao yakamwangalia Chifu.
"Mimi ninamteua Daniel Mwaseba.."
"Khaaaa!" Jenerali Ngoma na IGP John Rondo walishangaa kwa pamoja.
"Ndio, namwamini Daniel Mwaseba. Ni yeye ndiye aliyelianzisha jambo hili, na kwa kushirikiana na hao mliowachagua bila shaka wataenda kulimaliza" Chifu alisema kwa uhakika.
"Daniel si anaumwa? Unamaanisha tumsubiri Daniel mpaka apone ndipo tuanze operesheni hii? Mheshimiwa rais amesema tufanya haraka kumsaka Dr Luis" IGP John alisema.
"Ninaweza. Nilipata madhara kidogo ya moto kohoni. Lakini ninaweza kuifanya kazi hii kwa umakini mkubwa sana. Nitakuwemo katika kikosi hiko" Daniel alisema.
"Kwakuwa mwenyewe amekubali sawa, tutamuuanganisha na wakina Adrian ili waanze uchunguzi wao" IGP John Rondo alisema.
Baada ya maongezi hayo, IGP John alimpigia simu Adrian Kaanan huku Jenerali Ngoma akimpigia simu David John. Nusu saa tu zilitosha kuwafikisha askari hao katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
"Karibuni sana wakina Adrian. Kuna kazi ya haraka imetokea hapa nchini. Sisi kama viongozi wenu tumewachagua nyinyi katika kuchunguza jambo hili. Kiongozi wenu katika operesheni hii atakuwa Daniel Mwaseba. Najua nyote mnamfahamu Daniel Mwaseba. Ni yeye ndiye atakayewaambia operesheni hii inahusu nini, na ndiye atakayewapa majukumu yenu katika uchunguzi" Jenerali Ngoma alisema.
Adrian Kaanan na David John waliitikia kwa kichwa.
"Jukumu letu kama viongozi wenu limeisha. Sasa kazi hii ipo mikononi mwenu vijana. Daniel, kama mkuu wa kikosi hiki utaripoti moja kwa moja kwa Chifu. Naye atatuarifu sisi. Una ruhusa ya kuongeza mtu au watu katika kazi yako, awe mtu kutoka idara ya usalama wa taifa, jeshi la polisi au jeshi la wananchi la Tanzania. Mna ruhusa ya kutumia chombo chochote kile cha serikali, ili kukamilisha lengo kuu" IGP John alisema.
Baada ya maongezi yaliyodumu kama dakika kumi, viongozi wakaondoka pale hospitali, wakiwaacha wale vijana watatu.
Daniel, aliwaeleza wakina Adrian kila kitu jinsi Dr Luis alivyopotea. Wote walielewa nini wanatakiwa kufanya.
"Kikosi chetu tutakiita kikosi B. Kwa maana kikosi Bomu. Lengo kuu kama nilivyowaambia ni kumsaka Dr Luis popote pale alipo. Na kujua ni kina nani wapo nyuma juu ya utekaji huu. Naamini ninyi wote ni mahiri katika kazi hizi, sasa hii kazi lazima tuoneshe umahiri zaidi.
Tuna siku tatu tu tumepewa za kuhakikisha tunampata Dr Luis, tumeelewana?" Daniel aliuliza.
"Tumeelewana" Waliitikia.
"Na..omb..a mnijum..uish.e katika kik..osi B" Kwa sauti ya kukatakata Hannan alisema.
"Hannan, relax my dear. Ngoja upone kwanza. Hii kazi tunayoenda kuifanya ni ngumu sana, huwezi kuifanya ukiwa katika hali hiyo" Daniel alisema huku akimwangalia Hannan aliyelala kitandani.
"Da..ni.el Nita..ifanya kazi hii..nihesabu ...na mi..mi" Hannan alisema akigugumia.
"Utaifanye kazi hii ukiwa katika hali hiyo? Subiri kwanza upone Hannan" Daniel alisisisitiza.
"K..abla si..jaingia k..atika kaz..i hii nilis..omea IT, nahitaji ko..mpyuta yan..gu tu ni..kiwa hapa kitan..dani, amini ni..tawasaidia..." Hannan alishindwa kuongea.
"Ok tutafanya hivyo. Nitakuletea kompyuta yako hapa. Tuone tutaimalizaje hii kazi" Daniel alikubali.
Saa moja baada ya kikosi cha B1, chini ya kiongozi wake Daniel Mwaseba kupewa kazi ya kuchunguza mahali alipo Dr Luis. Katika nyumba moja kubwa iliyopo huko Kigamboni kulikuwa na kikao cha siri.
Kilikuwa ni kikao cha watu watatu.
"Nashukuru sana tumefanikisha zoezi la kumteka Dr Luis, huyu mzee ni muhimu sana katika hii mpango wetu wa kutengeneza kirusi cha DH+. Kwa kutumia kirusi hicho na jinsi tulivyoipanga mipango yetu lazima tutamfanya Dr Luis akubaliane na matakwa yetu" Mzee mmoja mnene mweusi alisema mle ndani.
"Ni kweli mzee Msangi. Ni suala la kushukuru sana baada ya kufanikiwa kumpata Dr Luis. Na pia tulifanya maamuzi ya busara sana kumteka yule Daniel, na kumripua kwa Bomu kule Mkuranga. Tuna hakika Daniel kingekuwa kikwazo kikubwa sana katika mpango wetu. Lakini kwasasa tumefanikiwa kuondoa hiko kikwazo. Sasa mpango uliobaki ni mmoja tu, kwenda kumfungua Dr Luis atwambie nini lilikuwa lengo la rais kumleta hapa nchini. Pia ni lazima tumpe mpango wetu wa kutengeneza kirusi DH+" Kijana mwengine wa makamo alisema.
"Upo sahihi Lameck. Tufanye hiyo mipango yetu mapema na kwa haraka kabla hawa washenzi hawajajua nini lengo letu" Mzee Msangi alisema.
"Kwani Dr Luis yupo sehemu gani?" Kijana mwengine aliuliza.
"Kwani hujui Luca. Yupo sehemu salama ndani ya nyumba hiihii. Hii nyumba imejengwa maalum kwa kazi kama hizi. Chini kabisa ya nyumba hii kuna chumba cha siri ambacho ndimo Dr Luis amewekwa. Atahojiwa hukohuko. Baada ya kutwambia lengo la rais kumleta hapa nchini. Tutampa Dr Luis mpango wetu wa kutengeneza kirusi DH+" Mzee Msangi alisema.
"Tutaenda na Carlos kumuhoji Dr Luis?" Lameck aliuliza.
"Kwani hujui Lameck. Watu wa kule Mkuranga wote waliuwawa kwa shambulio la Bomu. Roho alipata wasiwasi baada ya kusikia Daniel alikuwa katika harakati za kutoroka mle ndani. Alitoa maamuzi magumu ya kuilipua ile nyumba na wote waliomo ndani. Kina Carlos, Dingo na wote waliuwawa mle ndani, akiwemo Daniel Mwaseba" Mzee Msangi alisema.
"E bwana wee!! Sasa nani ataenda kumfungua Dr Luis huko chini. Carlos ndiye tuliyekuwa tunamtegemea katika kazi ya kuwafanya watu waseme hata yale wasiyoulizwa. Sasa nani ataifanya kazi hiyo kwa Dr Luis?" Luca aliuliza.
"Tuna Imma Ogbo. Imma Ogbo amekuja leo kutoka nchini Nigeria kwa kazi hiyo" Mzee Msangi alisema.
"OK, twendeni na huyo Imma Ogbo kwa Dr Luis tukamfungue" Lameck alisema.
"Hapana, sisi hatutaenda huko chini. Tutashuhudia kila kitu kutokea hapa. Chumba cha mateso kimeunganishwa na kamera ambazo tutashuhudia kila kitu Imma Ogbo atakachofanya" Mzee Msangi alisema.
Watu wote wakatulia.
Mzee Msangi aliwasha runinga kubwa iliyopo ukutani. Akabonyazabonyaza rimoti kisha picha ilionekana katika ile runinga iliyapachikwa ukutani.
Chumba cha siri kilikuwa kinaonekana.
Mzee mmoja aliyechoka wa kizungu alionekana katika kile chumba. Alikuwa amekaa katika kiti akiwa na mawazo mengi.
"Yule ndio Dr Luis" Mzee Msangi alisema.
"Anaonekana ana mawazo mengi" Lameck alisema.
"Tulifanya makusudi kumwacha kwa muda ili aingiwe na wasiwasi. Sasa ni muda muafaka wa Imma Ogbo kwenda kumfungua kila kitu, na kumpa kazi yetu." Mzee Msangi alisema.
Akachukua simu yake na kuibonyaza. Akaitafuta namba ya Imma.
Akapiga.
"Imma, unaweza kwenda sasa kumuhoji Dr Luis. Hakikisha anasema kila kitu. Unaruhusiwa kumtesa uwezavyo, lakini hakikisha hafi. Tunamuhitaji sana Dr Luis katika mambo yetu" Mzee Msangi alisema.
"Usiwe na hofu mzee. Atasema tu huyu mzungu" Imma Ogbo akasema kwa kifupi.
"Nakuamini Imma Ogbo"
"Sijawahi kukosea katika kazi hizi" Imma Ogbo alisema kwa kujiamini.
Mzee Msangi akakata simu.
Kupitia ile runinga ya ukutani ya mzee Msangi walimwona Imma Ogbo akiingia katika kile chumba cha mateso.
Imma alikuwa amezaa suruali ya jeans nyeusi, huku juu akiwa amevaa fulana nyeusi iliyokuwa imembana vyema. Aliingia katika kile chumba bila wasiwasi wowote ule. Alipoingia mle ndani moja kwa moja alimsogelea Dr Luis aliyekuwa amekaa katika kile kiti.
"Ninaitwa Imma Ogbo. Nipo hapa kwa kazi mbili tu ambazo bila shaka ninategemea utanipa ushirikiano" Imma alisema.
Dr Luis aliinua sura yake kivivu na kumwangalia yule kijana.
"Kwanini mmenileta hapa?" Dr Luis aliongea kwa kiswahili.
"Hapa kuna mgawanyo wa majukumu. Mimi kama Imma Ogbo jukumu langu ni kuuliza maswali, na wewe kama Dr Luis jukumu lako ni kujibu tu. Ukifanya vingine utafahamu upande wangu wa pili wa shilingi" Imma alisema kwa utulivu.
Dr Luis alikaa kimya huku akimwangalia yule kijana aliyejitambulisha kwa jina la Imma Ogbo.
"Tunajua umekuja hapa jijini baada ya kupewa mwaliko na rais Mgaya. Swali ni mwaliko huo ulihusu nini?" Imma Ogbo aliuliza.
Dr Luis alikaa kimya.
"Nimekuja hapa kama rafiki. Ninaomba tuhojiane kirafiki bila ya kupeana mateso na kumwaga damu!!" Imma Ogbo alipiga mkwara.
"Kwani mnataka nini ninyi watu? Kama mnataka hela niambieni. Nitawapa kiasi chochote kile cha pesa mnirejeshee uhuru wangu..." Dr Luis alisema kwa kulalama.
Imma Ogbo hakuuliza tena swali. Alienda konani kabisa ya kile chumba ambako kulikuwa na kabati dogo, alilifungua kabati na kutoa kisu, na chupa ndogo nyeupe iliyokuwa na majimaji meupe ndani yake. Bila kufunga lile kabati alimsogelea tena Dr Luis.
"Nadhani hujaelewa nimemaanisha nini niliposema hapa kuna mgawanyo wa majukumu. Ngoja nikuoneshe sasa" Imma Ogbo alisema huku akishika mkono wa Dr Luis.
"Nakukata kidole!! Na natavimaliza vidole vyako vyote endapo utaenda kinyume na ninachokueleza" Imma Ogbo alisema akiwa kaushika mkono wa Dr Luis.
Nimekuelewa. Nimekuelewa. Nitafanya kama ulivyonielekeza" Dr Luis alisema huku akitetemeka. Aliiona sura ya Imma Ogbo haikuwa na utani hata chembe.
"Nashukuru sana kwa kuwa muelewa Dr Luis. Hapa uko peke yako. Na ukweli wako pekee ndio utakaokutoa salama mikononi mwa nyumba hii" Imma alisema huku akimwangalia Dr Luis. Dr Luis hakutia neno, alikuwa anamwangalia tu yule mwanaume.
"Eeh nambie, nini lengo la Mheshimiwa rais kukuleta hapa nchini?" Imma Ogbo aliuliza tena.
"Kwa kweli mimi sijui lengo la rais kuniita hapa. Nililetewa ujumbe tu kuwa ninahitajika Tanzania kwa kazi maalum. Sijawahi kukutana na rais maana ameenda nchini Nigeria hivyo sijui ni kazi gani maalum aliyoniita" Dr Luis alijibu.
"Huo ujumbe kwamba unaitwa na rais kwa kazi maalum ulitoka kwa nani? Na wewe ulikufikia kwa njia gani?" Imma Ogbo aliuliza tena.
"Mtu aliyeniletea ujumbe alijitambulisha kwa jina la Irene Dembwe. Na alinitumia ujumbe kwa njia ya email" Dr Luis alisema.
"Unamfaham huyo Irene Dembwe?"
"Hapana simfaham. Nilitegemea ni yeye ndiye atakayekuja kunipokea uwanja wa ndege. Lakini hakuja yeye. Kwahiyo hadi sasa simfahamu huyo Irene Dembwe ni nani?" Dr Luis alisema.
"Kwa hisia zako tu, unahisi ni kitu gani alichokuitia rais hapa nchini?" iImma aliuliza.
"Kwakweli mimi sijui. Pengine ningekutana naye ndipo ningejua rais alikuwa anaiitia nini?"
"Hii ni mara yako ya kwanza kuja Tanzania?"
"Hapana, nimekuja mara nyingi tu Tanzania. Lakini nilikuwa nakuja mwenyewe kwa ajili ya kufanya utalii. Hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania kwa kuitwa na rais"
"Sawa Dr Luis. Nimeyasikia naongezi yako. Nina imani haujanidanganya hata kidogo. Ninaenda kuchunguza juu ya haya uliyonambia. Ukiwa umenidanganya tu jua maisha yako yatakuwa matatani" Imma Ogbo alisema..
Dr Luis alikaa kimya.
Imma Ogbo alitoka katika kile chumba alichofungiwa Dr Luis.
***
Daniel Mwaseba, David na Adrian Kaanan walikuwa wamekaa sebuleni katika nyumba ya siri iliyokuwa inamilikiwa na idara ya usalama wa Taifa. Walikuwa wanapanga mipango yao jinsi ya kuifikikisha mwisho kazi waliyopewa.
Daniel alikuwa tayari amepelekea kompyuta yake Hannan kule wodini.
Sasa wote watatu walikuwa tayari kuchunguza mahali alipopelekwa Dr Luis.
"Adrian na David bila shaka tumeona nguvu ya watu tunaoenda kupambana nao. Utumiaji wa helkopta kule Mkuranga na kuachia Bomu katika kupoteza ushahidi inaonesha kwamba hawa sio watu wa mchezo. Hapa, yatupasa kutumia umahiri wetu ili kuhakikisha tunampata Dr Luis. Tena tunampata akiwa hai" Daniel Mwaseba alisema.
"Ni kweli Daniel. Yatupasa kutumia umahiri wetu katika fani hii ya upelelezi, pia umakini mkubwa sana unahitajika. Hatujui nani yupo nyuma ya utekaji wa Dr Luis. Hivyo yatupasa tuwe makini sana" David alisema, huku Adrian akitingisha kichwa kukubaliana nae.
"Mpo sawa ndugu zangu. Kazi yetu inaeleweka, sasa la msingi ni kujua tunaanza wapi katika kuchunguza jambo hili. Muda tuliopewa ni mdogo sana, hivyo lazima tufanye nambo kwa uharaka mkubwa sana" Adrian alisema. Wote wakamwangalia Daniel.
"Siku aliyetekwa Dr Luis nilipigiwa simu na mfanyakazi wa hoteli ya Dos Santos anayeitwa Kelvin. Baadae nikaja kugundua kwamba Kelvin anashirikiana na wale watekaji. Sasa mimi naona tuanze na huyu Kelvin. Tuisake namba ya Kelvin. Kisha tutamwambia Hannah aichunguze namba hiyo tuone alikuwa anawasiliana na nani mara kwa mara kabla ya tukio lile.
Pia lazima tujue Kelvin alikuwa anaishi wapi? Kama tukikuta hakuna mtu wa kumtilia shaka katika mawasiliano ya simu yake tutawauliza majirani ni nani akiyeenda kumtembelea mara kwa mara. Tutaanzia hapo uchunguzi wetu" Daniel alisema.
Adrian na David walitikisa vichwa kuonesha kuwa wamekubaliana na mpango wa Daniel.
"Sasa tunaipataje namba ya kelivin?" David aliuliza.
"Ni jambo dogo sana hilo. Nina namba ya meneja wa hoteli ya Dos Santos katika kitabu changu ninachohifadhi namba zangu muhimu za simu. Ngoja nikachukue tumpigie ili atupatie namba ya Kelvin" Daniel alisema.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment