Simulizi : Top Secret: Nyaraka Namba 12333 Kutoka Whitehouse
Sehemu Ya Nne (4)
Pia waingereza hawakupenda mfumo huu mpya wa bunge la Majlis kwani kulianza kuliizwa maswali kuhusu mikataba ya uchimbaji mafuta nchini humo.
Waingereza wakaingiza maafisa wao wa ujasusi na wakaanza npango wa kushawishi na kuwahonga wabunge wa Bunge la Majlis wamuondoe madarakani Waziri Mkuu aliye chaguliwa na Shah na kumuingiza madarakani mwanasiasa machacjari aliyeitwa Reza Khan.
Mpango huu ulifanikiwa na mwaka 1925 Waziri Mkuu wa kwanza wa Iran akaondolewa madarakani na kuingizwa madarakani waziri Mkuu mpya Reza Khan.
Kitendo hiki pia kilimchukiza Ahmad Shah Qajar na kukaanza kutokea sintogahamu ya chini kwa chini kati yake na serikali ya Uingereza.
Wanasema ukidharau mwiba mguu huota tende, na Waingereza hawakutaka madhara yatokee waanze kujilaumu baadae hivyo wakaanzisha mpango wa kumuondoa Shah katika kiti cha Ufalme.
Wakamtumia Waziri Mkuu mpya waliyemuingiza Bw. Reza Khan kulishawishi Binge la Majlis kumpigia kura ya kumuondoa kwenye kiti cha ufalme Ahmad Shah Qajar.
Mpango huu ukafanikiwa na Ahmad akaondokeqa kwenye Ufalme na Waziri Mkuu mpya Bw. Reza Khan akajivika yeye cheo hicho na kuwa Reza Khan Shah Pahlavi.
Huu ndio ukawa mwisho wa koo ya Qajar (Qajar Dynasty) kukalia kiti cha kifalme cha Shah na mwanzo wa koo ya Pahlavi (Pahlavi Dynasty) kukalia kiti hicho cha Shah.
Mwanzoni mwa utawala wake Reza Khan Shah Pahlavi akipendwa sana na wananchi kwani kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza alifanya Nazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii.
Lakini kadiri siku zilivyo songa Shah Pahlavi alibadilika na kuwa zaidi ya mfalme, alianza kuwa na chembe chembe za udikteta.
Hakuwa mtu mwenye kusikiliza maoni ya Bunge lake la Majlis na aliukandamiza upande wa Upinzani kwa mabavu makubwa. Watu wote ambao walipingana nao walitiwa gerezani na wengine kuuwawa.
Katika miaka ya kati kati vugu vugu la upinzani lilikuwa limepamba moto na hoja kubwa ilikuwa ni kuishinikiza serikali ijiondoe kwenye mikataba kandamizi ya uchimbaji mafuta kati yake na serikali ya Uingereza.
Moja ya vinara wa vugu vugu hili alikuwa ni kijana aliyeitwa Mohammad Mosaddegh.
Kijana huyu alijitengenezea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kuliteyea taifa la Iran.
Shah Pahlavi aliona tishio la kijana huyu Mosaddegh na mwaka 1940 akamtupa gerezani.
Mwaka 1941 Reza Khan Shah Pahlavi akarothiwa kiti cha Ufalme na mtoto wake wa kiume kijana wa miaka 22 aliyeitwa Mohammad Reza Khan.
Baada ya kuchukua madaraka Mohammad Reza Shah Pahlavi pia kama watoto wengine wengi wanaorithi Ufalme hakuwa na kiongozi imara kama baba yake Reza Khan. Lakini Uingereza walimpenda kwakuwa alikuwa kibaraka wao aliyefanya kila kitu walichohitaji.
Baada ya upande wa upinzani kugundua udhaifu wa Shah mpya, wakarudisha tena vugu vugu lao.
Kwanza kabisa wakaanza kumshinikiza Shah mpya awaachilie wafungwa wa kisiasa waliofungwa na baba yake.
Mohammad Shah Pahlavi kutokana na uchanga wake wa kiuongozi akafanya 'kosa' kubwa la kuwaachia wafungwa wa kisiasa akiwepo Mohammad Mosaddegh.
Mara tu baada ya Mosaddegh kuachiliwa gerezani akaanzisha tena vugu vugu la kudai visima vya mafuta viwe chini ya Iran peke yake pasipo umiliki wa pamoja na serikali ya Uingereza.
Ili kufanikisha lengo hili, Mohammad Mossadegh aliviunganisha vyama vyote vya upinzani na kuunda 'Ukawa' yao iliyoitwa National Front.
Hoja yao kuu ikiwa ni kurudisha visima vya mafuta kwa taifa la Iran kutoka kwa wanyojani.
Mtaani kulikuwa na kikundi kilichojiita Fadaiyan e-Islam ambacho kiliongozwa Ayatollah Kashani (huyu ndiye mlezi wa kiroho wa Ayatollah Khomeini aliyekuja kuwa kiongozi Mkuu wa kiroho wa Iran (Iran Supreme Leader)).
Kikundi hiki kilimuunga mkono Mosaddegh wakimuona ni mzalendo.
Wakaenda mbali zaidi na kufanya shambulizi lililomuua Waziri Mkuu wa kipindi hicho aliyeitwa Haj Ali Razmara.
Hii ikapelekea kuitishwa upya kwa uchaguzi mkuu mwaka 1951. Mosaddegh na 'Ukawa' yake ya National Fron wakashiriki na kupata ushindi wa kishindo kwa kuingiza wabunge wengi kwenye Bunge la Majlis.
Baadae Bunge likapiga kura kumchagua Mohammad Mosaddegh.
Hii inaitwa, "usiyempenda kaja".
Mohammad Mosaddegg mpinzani anayechukiwa zaidi na Shah wa Iran na mwanasiasa mwenye Sera zinazopingwa vikali na Uingereza sasa ndio Waziri Mkuu wa Iran.
Haikumchukua mda mrefu baada ya kuapishwa akaanza 'kuwasomesha namba'.
Kwanza akaanza na Shah. Akapeleka Bungeni hoja kwamba Shah apunguziwe madaraka kwani hakuna maana katika nchi ya kidemokrasia kuwe na "mfalme mwenye mamlaka". Hoja yake aliwaeleza kwamba anataka Shah abakie lakini cheo chake kiwe ni alama tu (Ceremonial) lakini asiwe na mamlaka ya kuamuru uendeshaji wa serikali.
Mwenyewe Mosaddegh katika waraka aliouwalisha bungeni alitumia sentesi tamu zaidi, "Shah anatakiwa kutawala, lakini sio kuwa na malaka" ("reign, but not rule")
Bunge likakubaliana na hoja hiyo. Mohammad Shah Pahlavi akaondolewa madaraka yote ya kiserikali, akabakishwa kama Picha ya kikaragosi, mtawala asiye na mamlaka. Mamlaka yote ya kiserikali yakaamishiwa kwa Waziri Mkuu.
Baada ya kumsomesha namba Shah kwa uzuri kabisa akawageukia wazungu wa Uingereza. Tena akataka kuwasomesha namba kwa staha na ustaarabu kabisa.
Akawapa 'ofa' kuwa hataki kuwanyang'anya visima bali anawaomba waboreshe mikataba.
Kwanza kabisa akataka mgawanyo wa fedha usiwe kwenye "faida" pekee bali mgawanyo uhusu mapato yote. Pia akawaambia si sahihi wao wenye mafuta wapewe asilimia kiduchu (16%) hivyo akapendekeza iwe 50%.
Waingereza wakakataa kataka kata.
Mosaddegh hakuangaika nao, wanasema "ukisusa wenzio twala".
Akapeleka muswada bungeni wa kutaifisha visima vyote vya mafuta nchini Iran.
Waingereza wakashikwa na bumbuwazi, bumbuwazi likageuka kihoro, kihoro kikazaa chuki na vichwani mwao likatawala wazo moja tu. Mohammad Mosaddegh lazima ang'oke madarakani.
Lakini huyu alikuwa ni "heavyweight" tofauti na viongozi wengine wa Iran waliofanikiwa kuwang'oa.
Nchi nzima nzima mpaka ngamia walimuunga mkono Mosaddegh. Hata wakundi ambayo ilikuwa ni ngumu kwao kuunga mkono wanasiasa kwa mfano kikundi cha msimamo mkali cha Fadaiyan e-Islam na kiongozi wao Ayatollah walimuunga mkono Mosaddegh.
Mosaddegh alionekana ni shujaa wa Taifa. Mosaddegh alionekana ni "Musa" mwenye maono wa kuipeleka Iran kwenye "maziwa na asali".
Uingereza wakang'amua mapema 'ligi' hii hawaiwezi.. Hili ni zigo ambalo hakuna 'mnyamwezi' wao wowote mwenye uwezo wa kuliinua, au kama ni fupa bado hajazaliwa fisi uingere,a mwenye uwezo wa kuliuma.
Ni hapa wakaona umuhimu wa kuwageukia na kuomba msaada kwa 'kaka zao' na maswahiba wao U.S.A. wazee wa "fitna za daraja la kwanza".
Walichowaahidi ni kuendelea kuwaunga mkono kwenye vita vya Korea. Pia wakawaonyesha data za 'reserve' za mafuta chini ya bahari ya Iran na wakawaahidi kuyaruhusu makampuni ya kimarekani kwenda kumiliki baadhi ya visima vipya vya mafuta.
Ndio hii inatupeleka kwenye kikao cha tarehe 13 march 1953 ndani ya Oval Office, whitehouse. Kikaoni kati Rais Eisenhower, waziri wa mambo ya nje John Dulles na Mkurugenzi wa CIA Allan Dulles.
Ambapo Rais akatoa agizo CIA kuandaa mpango kabambe wa kumuondoa madarakani Mohammad Mosaddegh.
Na CIA kupitia Idara yake maalumu ya SAD ikaja na mpango mwanana kabisa…
TPAJAX PROJECT (OPERATION AJAX).
Ili kutekeleza agizo la Rais Eisenhower kuhakikisha serikali ya Iran inayoongozwa na Waziri Mkuu Mohammad Mosadegh inaondoka madarakani, CIA kupitia idara yake ya SAD (Special Activities Division) wakaja na mango kabambe waliouita TPAJAX PROJECT (au kwa jina linvine Operation Ajax).
Katika kipindi hiki kitengo maalumu cha SAD kilikuwa kinasimamiwa na Kermit Roosevelt Jr. (Mjukuu wa Rais wa zamani wa Marekani Theodore Roosevelt).
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment