Search This Blog

Thursday 29 December 2022

BOMU - 2

   

Simulizi : Bomu 

Sehemu Ya Pili (2)



Daniel alienda katika chumba kimoja kilichokuwa mle ndani. Akarudi na kitabu kidogo mkononi.




"Hii hapa namba ya meneja wa hoteli ya Dos Santos" Akasema.




David aliichukua kile kijitabu kidogo mikononi mwa Daniel. Akaziandika zile namba katika simu yake na kupiga. Kisha akampa simu Daniel.




"Hallo bosi Fadhili" Daniel akasema.




"Hallo, habari yako?" Meneja Fadhili alijibu.




"Unaongea na Daniel Mwaseba" Meneja Fadhili alisema.




Meneja Fadhili alihema kidogo baada ya Daniel kujitambulisha kisha akasema.




"Aaah Daniel, nambie"




"Nina shida moja ndogo" Daniel akavuta pumzi. "Nahitaji namba ya mfanyakazi wako Kelvin"




"Kelvin?" Mbona aliuwawa katika mripuko wa bomu huko Mkuranga.




"Nafaham, ila naiihitaji namba yake"




" Ook nakutumia"




Ilichukua kama dakika tano. Meneja Fadhili alimtumia namba Daniel. Naye moja kwa moja aliituma kwa Hannan ili aichunguze watu waliowasiliana na namba ile.




Majibu yaliyotoka kwa Hannan, yalimwacha kila mtu mdomo wazi.








Hannan alimpigia Daniel simu dakika kumi baadae, ili kumpa majibu ya kazi aliyopewa ya kuichunguza namba ya Kelvin aliyekuwa mfanyakazi wa hotel ya Dos Santos.




"Naomba niongee na Daniel, David" Hannan alisema alipopiga simu ya David.




"Hannan huyu hewani anataka kuongea na wewe" David alisema huku akimkabidhi simu Daniel.




"Eeh nambie Hannan, umepata nini katika simu ya Kelvin?" Daniel aliuliza.




"Daniel, hii namba inaonesha imetumika mfululizo kwa miaka mitatu sasa. Na mtumiaji kwa mujibu wa usajili wake ni huyo Kelvin, lakini cha kushangaza hakuna kumbukumbu yoyote ile katika hii namba" Hannan alisema.




"Unasemaje Hannan?"




"Nd'o hivyo Daniel, nimejaribu kuichunguza hii namba, hakuna kumbukumbu yoyote ile. Hakuna kumbukumbu za watu waliompigia, waliopiga wala meseji. Lakini namba inaonesha kwamba ilikuwa inatumika ndani ya miaka mitatu mfululizo" Hannan alirudia tena.




"Wametuwahi hawa mbwa" Daniel alisema kwa sauti ndogo.




"Yani hawa watu wanafanya mambo yao kwa umakini sana. Wamefuta kumbukumbu zote za hii namba" Hannan alisema.




"Wamejaribu lakini bado hawataweza. Lazima tutawagundua tu hawa watu ni kina nani? Na wana nia gani na Taifa hili?" Daniel alisema.




"Nakuombea sana Daniel muwatie mikononi watu hawa. Nina hasira nao sana kwa jinsi walivyotumbukiza risasi katika mwili wangu. Yani natamani ningekuwa mzima ili niungane na nyinyi ili kuwakamata hawa mafedhuli" Hannan alisema kwa hasira.




"Pole sana Hannan. Msaada wako ni mkubwa sana. Hesabu tu nawewe upo ndani ya kazi hii. Jina lako litaandikwa kwa wino wa dhahabu siku tutakayoifanikisha kazi hii. Na kuliacha salama taifa letu. Lakini vipi unaendeleaje kwa sasa Hannan?"




"Operesheni za kuondoa risasi imekwenda vizuri sana. Kwa sasa ninauguza vidonda tu. Nitakuwa sawa sio muda na bila shaka nitaungana na nyinyi katika kikosi B1" Hannan alisema kwa hisia.




"Kila sekunde ninakuombea Hannan. Bila shaka utakuwa sawa mdogo wangu. Tumekumiss sana kazini" Daniel alisema.




Waliongea kidogo na Hannan, kisha waliagana simuni.




Daniel aliwasimulia wakina Adrian taarifa alizopewa na Hannan. Wote walishangaa sana. Sasa mpango ukabaki mmoja tu, wa kwenda nyumbani kwa Kelvin.




***




Imma Ogbo aliwasiliana na kina mzee Msangi juu ya aliyoyapata kutoka kwa Dr Luis. Bila kujua kwamba walisikia na kuona kila kitu. Aliwaambia pia jioni ndio ataenda rasmi kumueleza mpango wa kutengeza kirusi cha DH+.




"Hawa watu wamejuaje kama nilitakiwa kufika siku ile. Mara zote ninapofika Dar es salaam ujio wangu huwa wa siri sana. Ni rais pekee ndiye anayejua kuwa ninakuja. Safari hii nilishangaa sana baada ya rais kuniambia nitapokelewa na mtu mwengine badala ya Irene Dembwe kama ilivyo kawaida yetu. Bila shaka hapo ndipo siri juu ya ujio wangu ilipoanza kupotea. Najua rais Mgaya atachanganyikiwa sana akisikia nimetekwa. Atafanya juu chini kunitafuta, nipatikane ili siri yake isije ikavuja. Hawa watu walioniteka wamehisi nini kitu kinachonifanya nije Tanzania mwanzo na mwisho wa mwezi? Ila hawawezi kujua. Nilitazama sura ya yule mtu aliyekuja kunihoji inaonesha hajui chochote. Pengine kuna mambo yao mengine kabisa yaliyofanya waniteke. Niliahidi nitatunza siri ya rais Mgaya siku zote za maisha yangu. Na itakuwa hivyo. Sitoisema kwa mtu yoyote yule.




Hawa jamaa wanaonekana makatili sana, niliona macho ya yule jamaa yalivyobadilika alivyotaka kunikata kidole. Lakini niseme tu, sitasema kitu chochote kile juu ya siri ya rais Mgaya" Dr Luis alikuwa anawaza.




Kipindi Dr Luis anawaza juu ya kuificha siri ya rais, Daniel Mwaseba, Adrian Kaanan na David John walikuwa wanaelekea nyumbani kwa Kelvin.




Ilikuwa mitaa ya Mikocheni jijini Dar es salaam. Katika nyumba moja yenye geti kubwa jeusi iliyokaribu na hospitali ya Kairuki. Walipewa hadi namba ya nyumba na meneja wa hoteli ya Dos Santos baada ya Daniel kumpigia tena.




Wakiwa njiani walikutana na foleni kubwa sana. Foleni haikuwa ya kawaida. Wakiwa katikati ya foleni ndipo walipoanza kusikia tetesi kwamba mbele kuna nyumba inaungua moto. Wote waliingiwa na uwoga kusikia taarifa hiyo. Kwakuwa mahali walipokuwepo hapakuwa mbali sana na mahali walipoelekezwa kuwa anaishi Kelvin.




Adrian Kaanan alishuka kwenye gari na kuelekea upande ilipokuwa nyumba ya Kelvin.




Alipokaribia, alipigwa na butwaa!!!. Nyumba ya Kelvin ndio iliyokuwa inawaka moto!




Watu wengi walijaa eneo lile wakishuhudia ile nyumba kubwa ikiteketea. Adrian Kaanan aliiweka mikono yake yote miwili mdomoni. Macho yamemtoka pima.




Akiwa haamini. Haamini hata kidogo...




"Wameichoma moto nyumba ya Kelvin. Bila shaka kuna kitu wamekificha tena hapa. Walifuta mawasiliano ya Kelvin wakificha kitu na sasa wameichoma nyumba yake katika mwendelezo wao wa kuficha vitu vyao. Lakini hawa watu waliomteka Dr Luis ni kina nani hasa? Na wana lengo gani?" Adrian Kaanan aliwaza.




Hakukaa tena eneo lile. Maana hakukuwa ni kitu chochote kile ambacho kingemsaidia katika uchunguzi wake. Alirejea kule alipowaacha wakina Daniel.




"Tuambie, umefanikiwa kufika?" Davis aliuliza Adrian alipowasili tu.




"Nimekuta nyumba ya Kelvin inaungua moto!!" Adrian alisema kwa sauti ya kuchoka.




"Ni meneja Fadhili wa Dos Santos" Daniel aliropoka. "Bila shaka ndiye anayevujisha siri zetu. Mpigie Hannan aifatilie simu ya meneja tujue yupo wake. Tumfuate sasahivi. Huu ni mwisho wake wa kutuchezea michezo ya kijinga" Daniel Mwaseba alisema kwa hasira.




Je nini kitatokea? Ni meneja fadhili ndiye anayewauza au kuna msaliti mwingine? . Tuwe wote sehemu ijayo




David aliitoa simu yake mfukoni na kumpigia Hannan.




"Inaita simu.." David alisema wakati akimpatia simu Daniel.




"Hallo Daniel ?" Hannan alisema simuni pindi tu alipopokea simu ya David.




"Hannan unaendeleaje?" Daniel aliuliza.




"Naendelea vizuri kwasada. Alikuja daktari kuniona dakika chache zilizopita. Kaniambia afya yangu inaimarika kwa kasi sana." Hannan alijibu.




"Safi sana. Nakuombea sana kwa Mungu upone Hannan. Ni mimi ndiye nilikuingiza katika hayo matatizo. Na ninakuahidi nitawatia mikononi watu wote waliokufanyia kitendo hiko cha kikatili" Daniel alisema.




"Sawa Hannan. Ingawa usisikitike sana. Nilikuwa katika majukumu yangu niliyoapa. Hii ni ajari kazini.




"Ni kweli, ingawa ahadi yangu kwa hawa washenzi ipo palepale. Lazima wajutie kwa hiki walichokufanyia" Daniel alisema. Kisha akaendelea "Sasa Hannan tuna kazi ya kufanya nataka utusaidie.."




"Ninakusikiliza Daniel. Nipo kwa ajili yenu"




"Nataka uichunguze namba ya meneja wa Dos Santos. Kuna mambo yanatia shaka kidogo juu yake" Daniel alisema.




"Ninarudia tena nipo kwa ajili hiyo kazi. Pamoja na kutaka sana hao wahalifu wakamatwe pia nina kisasi binafsi juu yao kwa hiki walichonifanyia. Nitumie hiyo namba sasahivi"




"Ninakutumia" Daniel akasema.




Simu ikakatwa.




Sekunde hiyohiyo, Daniel alimtumia namba ya meneja Fadhili, Hannan.


Baada ya kama dakika kumi Hannan alipiga simu.




"Hallo Daniel? Nimefanikiwa kuichunguza namba ya meneja Fadhili" Hannan alisema baada ya Daniel kupokea simu.




"Eeh yupo eneo gani kwa sasa?" Daniel aliuliza.




"Kwa mujibu wa simu yake Meneja Fadhili yupo eneo la Sinza Kijiweni, yupo katika nyumba inayotazamana na hoteli ya Deluxe. Nimejaribu kudukua taarifa katika mtandao wa hoteli ya Dos Santis, nimegundua mahali hapo ndipo anapoishi meneja wao" Hannan alisema.




"Nashukuru sana Hannan, kazi nzuri sana. Tupo njiani tukielekea Sinza Kijiweni. Tutawasiliana kadri ya tutakavyokaribia eneo hilo" Daniel alisema na kukata simu.




"Twendeni Sinza Kijiweni sasahivi. Lazima tumuwahi meneja Fadhili. David chepuka pembeni ya barabara tuwahi haraka sana" Daniel alisema.




David alilitoa gari katikati ya foleni na kuanza kupita pembeni ya barabara. Hawakutembea hata dakika tano wakasimamishwa na askari wa usalama barabarani. Kabla yule askari hajasema kitu David alionesha kitambulisho chake.




"Tupo kazini afande" Akasema.




Askari hakuwa na neno. Mkukumkuku wakina Daniel walielekea Sinza Kijiweni.




Wakati wakiwa maeneo ya Sayansi simu ya David iliita tena.




"Hannan anapiga" David alisema huku akimkabidhi simu Daniel Mwaseba.




"Target yetu inasogea" Hannan alisema pindi tu simu ilipopokelewa.




"Inaelekea wapi?" Daniel aliuliza.




"Kwa sasa ipo stendi ya Sinza Kijiweni, inaelekea barabara ya Shekilango" Hannan alisema.




"Sawa Hannan. Sisi tupo Sayansi hapa. Endelea kumfuatilia.." Daniel alisema.




"Jitahidini mumuwahi Daniel" Hannan alisema.




Simu ikakatwa.




David aliongeza kasi ya gari. Pale Sayansi alikata kushoto akipita barabara ya mchepuko iliyokuwa inapita nyuma ya chuo cha Ustawi wa Jamii. Njia hiyo iliwafikisha hadi katika baa ya Hongera, ambapo walikata kushoto tena kuishika njia inayoelekea Shekilango. Mwendo ambao gari lilikuwa linaendeshwa haukuwa wa kawaida. Walikuwa wanamuwahi meneja Fadhili ambaye walihisi kuna kitu anahusiana nacho na hii misheni yao.




Walipofika maeneo ya Sinza Mapambano simu ya David iliita. Kwakuwa simu alikuwa nayo Daniel akaipokea.




"Daniel kuna jambo la kushangaza kidogo limetokea sasahivi" Hannan alisema kwa wahka mkubwa.




"Jambo gani hilo Hannan?" Daniel aliuliza.




"Niliifatilia target yetu hadi usawa wa hoteli ya Rombo. Cha kushangaza target yetu imepotelea hapohapo. Siioni kabisa simu ya meneja Fadhili katika laptop yangu" Hannan alisema.




"Ni kitu gani unahisi kimetokea Hannan?" Daniel aliuliza.




"Meneja Fadhili amezima simu. Bila shaka amegundua kama anafatiliwa" Hannan alisema.




"Kwanini unahisi hivyo?" Daniel aliuliza.




"Nilianza kupatwa na wasiwasi kutokea alipotoka kule nyumbani kwake Sinza Kijiweni. Target yetu ilikuwa inaenda kwa kasi sana. Bila shaka alikuwa anakimbiza gari. Hivyo nilihisi anawakimbia ninyi. Lakini kupotea ghafla simu ya meneja Fadhili katika laptop yangu imeniaminisha hisia zangu. Meneja Fadhili hajazima simu yake kwa bahati mbaya. Imepangwa." Hannan alisema.




"Amejuaje sasa kama tunamfatilia?" Daniel aliuliza.




"Hiyo hata mimi sijajua bado. Lakini hisia zangu zinaniambia hivyo. Meneja Fadhili amegundua kama anafatiliwa" Hannan alisema.




"Hannan ngoja kwanza. Naona kuna wingu la moshi mbele. Bila shaka kuna nyumba inaungua moto" Daniel alisema harakaharaka na kukata simu.




"Ni nini ile?" Daniel aliuliza huku akionesha kwa kidole mbele. Kipindi hiko gari lilikuwa linapita pembeni ya barabara maana foleni ilikuwa imeanza tena.




"Sijui kuna nini? Kuna moshi mzito mbele umeanza sekunde chache baada ya wewe kuanza kuongea na Hannan" Adrian alisema.




Gari ikatembea kidogo ikasimama kabisa. Foleni ilikuwa imeshamiri. Hakukuwa na namna tena ya kusogea mbele.




"David baki hapa na gari. Mimi na Adrian tutakodi pikipiki kwenda kuona kitu gani kimetokea?" Daniel alisema.




"Sawa Daniel"




Daniel na Adrian walishuka katika ile gari. Na kukodi pikipiki mbili ziwafikishe maeneo ya hoteli ya Rombo. Ambapo walihisi moshi ule wanaouona ndipo ulipoanzia.




Dakika tano tu kwa kutumia pikipiki ziliwafikisha mahali ambapo ilikuwa ndipo chanzo cha ule moto. Walichokutana nacho, wote walipigwa na butwaa...








Walikutana na mabaki machache ya moto. Huku mashuhuda wakisema kwamba mabaki yale lilikuwa ni gari ambalo liliwaka moto ghafla. Hawakuwa na haja ya kuuliza. Hisia zao tu ziliwaambia kuwa lile lilikuwa ni gari la meneja Fadhili. Ndio, gari la meneja Fadhili lilikuwa limeteketea kwa moto.




"Kwa mara nyingine tena wametuwahi hawa watu. Hadi sasa sijaelewa ni kwa namna gani wanazipata taarifa zetu. Pale walipogundua kuhusu Kelvin kufuta mawasiliano yake katika simu na pia kuamua kuchoma nyumba yake moto nilihisi kwamba meneja Fadhili anahusika katika kuvujisha siri zetu. Maana ni yeye ndiye tukiyewasiliana kuhusu Kelvin. Lakini sasa meneja fadhili mwenyewe nae ameuwawa kwa bo..." Daniel alipotaka kusema neno Bomu akasita. "Aaaaah nimegundua kitu Adrian..." Daniel alisema.




"Umegundua kitu gani Daniel?" Adrian aliuliza.




"Matukio haya matatu yote yamehusisha kitu cha mripuko. Ambacho katika hisia zangu kinaniambia kuwa ni mabomu. Kule Mkuranga nilishuhudia kwa macho yangu helkopta ikiachia bomu na kuiteketeza ile nyumba tuliyofungiwa. Leo sijaishuhudia nyumba ya Kelvin ikivyoteketea. Ni wewe ndiye uliyeenda. Lakini nahisi nyumba ya Kelvin nayo itakuwa imeripuliwa kwa bomu. Na sasa hili gari la meneja Fadhili. Hili gari limeripul..." Daniel hakumaliza alichotaka kusema. Alimsukuma kwa nguvu Adrian kwa mikono miwili!!.




Adrian aliyumba vibaya na kudondoka chini akifuatiwa na Daniel juu yake!


Sekunde ileile risasi moja ilipita na kuchimba chini, palikuwa ni mahali ambapo kilikuwa kimesimama kifua cha Adrian sekunde moja iliyopita!




E bwana wee!!.




"Mdunguaji" Daniel alimnong'oneza Adrian wakiwa wamelaliana pale chini. Adrian hakulipata neno. Alikuwa haamini kama amenusurika kifo kwa namna ile.




"Mdunguaji yupo juu kule katika hoteli ya Rombo" Daniel alisema tena. Sasa alikuwa na bastola yake mkononi.




Sekunde hii Adrian naye aliupata ufahamu wake. Naye alichomoa bastola yake kiunoni, tayari kwenda kumsaka Mdunguaji ghorofa ya juu katika hoteli ya Rombo.




Mkuumkuu, Daniel Mwaseba na Adrian Kaanan walielekea ilipo hoteli ya Rombo. Huku wakiwaacha watu waliokuwa wakishuhudia ile ajari ya kuungua kwa moto wakiwa hawaelewi ni kitu gani kimetokea. Kilikuwa ni kitendo kilichodumu si zaidi ya dakika moja.




Kule juu ya ghorofa ya hoteli ya Rombo, The sniper alikuwa katika mtatiziko wa nafsi. Alikuwa haamini kilichotokea. Hii, ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika maisha yake kukosa shabaha kwa mtu aliyepanga kumdungua. Hakuelewa kwa namna gani wale jamaa waligundua kuwa wanataka kudunguliwa. Na kusukumana namna ile.




The sniper, kwa macho yake mawili, alishuhudia wale jamaa wakisukumana kiajabu na kulaliana vumbini. Huku wakimkosesha shabaha yake matata aliyoilenga kikamilifu.




Harakaharaka, alibadili mwonekano wake.




Dakika moja baadae hakuwa The sniper tena. Alikuwa katika vazi la baibui, huku bunduki yake ya gharama akiitelekeza katika ndoo ya taka kulekule ghorofani. Alijua hawezi kutoka salama ndani ya Rombo hoteli akiwa na silaha.




The sniper alianza kushuka mkuumkuu. Alipokaribia katika ghorofa ya pili alipunguza mwendo. Alipishana na kina Daniel wakiokimbia kwa kasi wakielekea juu katika korido ya ghorofa ya pili. Daniel alibahatika kuusikia uturi wa mwanamke waliyepishana nae akiwa mbiombio. Na huyo ndiye Daniel Mwaseba. Milango yake ya fahamu inafanya kazi kikamilifu wakati wote.




Hakuna aliyehisi kuwa yule mwanamke ndiye waliyekuwa wanamkimbilia kule juu. Haikuwaingia akilini mdunguaji afike pale kwa sekunde zile chache.




Hawakujua. Hawakujua.




Yule hakuwa mwanamke, alikuwa ni The Sniper, Mdunguaji hatari sana!!




Mbio za kina Daniel Mwaseba ziliwafikisha juu kabisa ya hoteli ya Rombo. Baada ya dakika tano za kutafutatafuta, walichobahatika kukutana nacho ni bunduki iliyotelekezwa katika ndoo ya taka. Kwa kutumia kitambaa Daniel aliishika ile bunduki. Kitu kimoja tu kilipita katika pua yake.




Harufu ya uturi..




Ndio, harufu ya uturi waliyopishana nao kutoka kwa mwanamke aliyevaa baibui katika ghorofa la pili, ndio harufu ileile ya uturi aliyosikia katika ile bunduki ya Mdunguaji.




"Tumepishana na Mdunguaji.." Daniel alisema kwa sauti ndogo.




"Tumepishana nae wapi? Wakati hii hoteli haina lift. Na ina njia moja tu. Pia wakati tunakuja huku juu tumepishana na mtu mmoja tu, tena mwanamke kule ghorofa la pili, ambaye kwa vyovyote vile hawezi kuwa ametokea huku. Hakuna mwanadamu mwenye kasi hiyo, ya kutoka huku hadi kufika ghorofa ya pili kwa muda mfupi vile" Adrian alisema.




"Yule mwanamke mwenye buibui ndiye Mdunguaji..." Daniel alisema.




"Kivipi Daniel? Mbona sikuelewi..."




"Nusa hii bunduki yake" Daniel alisema.




Adrian aliinusa ile bunduki. Alistuka sana.




"Namjua mdunguaji..." Adrian alisema.




"Unasemaje Adrian? Unamjua mdunguaji?" Daniel aliuliza kwa wahka mkubwa.




Ghafla, simu yake iliita.




"Namba ngeni..." Adrian alisema huku akiipokea.




"Haloo naweza kuongea na Daniel?" Sauti ya kike ilisema simuni harakaharaka.




"Simu yako..." Adrian akisema huku akimpa simu Daniel.




"Daniel, kuna jambo la kushangaza limetokea.." Mwanamke alisema simuni. Sauti ambayo Daniel alipoisikia tu aliitambua.




Ilikuwa sauti ya Hannan Halfani.




"Jambo gani Hannan?" Daniel aliuliza.




"Nimeipata katika mtandao simu ya meneja Fadhili" Hannan alisema.




"Hannan unasemaje simu ya meneja umeipata? Wapi Hannan?" Daniel aliuliza akiwa haamini.




"Simu ya meneja Fadhili imewashwa maeneo ya Tegeta mwisho. Nyumba namba kumi na saba. Imewashwa ndani ya dakika mbili halafu ikazimwa" Hannan alisema.




"Inawezekana vipi hiyo Hannan? Meneja Fadhili na gari yake wameteketea kwa moto hapa Sinza Legal. Na wakati tukiwa eneo la tukio nasi tukashambuliwa. Hapa tulipo tunamsaka mtu aliyetushambulia" Daniel alisema.




"Inawezekana walimtoa Meneja Fadhili kabla, kisha wakachoma gari moto kupoteza ushahidi. Nendeni Tegeta haraka nakwambia meneja Fadhili yupo huko.." Hannan alisema kwa msisitizo.




"Tupo njiani Hannan" Daniel alisema.




"Do did" Hannan alisema na kukata simu.




Do did lilikuwa ni fumbo lao la siri kati ya Daniel na Hannan. Ni wao tu wawili ndio waliokuwa wanaelewana hapa Duniani baada ya kusema Do did.




Baada ya kuambiwa 'Do did'. Daniel alipatwa na hasira za ajabu sana. Ghafla!! Alimwangalia Adrian kwa jicho la hasira. Adrian hakuelewa ni kitu gani kimetokea.




"Vipi Daniel. Mbona umebadilika ghafla baada tu ya kutoka kuongea na Hannan? Mmeongea nini?" Adrian aliuliza kwa sauti ya hofu.




"Tuna..zun..guka..na.." Daniel alisema kwa sauti ya kukwaruza. Macho yake yakiwa mekundu hayajawahi kutokea hapa duniani.




"Wamenichokoza hawa mabwege. Wamechezea sharubu za simba. Hawanijui. Hawanijui. Hawanijui hata kidogo.. Nitawafanya kitu kibaya sana nakwambia hawa watu. Hawatanisahau. Hawatanisahau kamwe. Vizazi vyao vyote hawatamsahau mtu mwenye jina la Daniel Mwaseba. Maana watasimulia vizazi na vizazi. Nitawaonesha mimi ni nani? Nitawakomesha.." Daniel alisema kwa hasira.




"Mbona sikuelewi Daniel? Ni kitu gani kimetokea kwani? Hannan amekwambia nini?" Adrian aliuliza.




Daniel hakujibu kitu. Badala yake alibonyazabonyaza ile simu ya Adrian, kisha akaiweka sikioni.




Simu ilianza kuita.




Daniel Mwaseba alikuwa anampigia Martin Hisia.








Wakati simu yake inaita, Martin Hisia alikuwa Mlimani city. Alikuwa anasukuma kitorori kilichojaa bidhaa mbalimbali za nyumbani katika duka la Discount centre.




Pembeni yake kulikuwa na msichana mzuri. Mwenyewe, alizoea kumuita Malaika. Msichana huyo mrembo jina lake halisi alikuwa anaitwa Felisia Nyenyembe.




"Simu yako inaita.." Felisia alisema kumwambia Martin.




"Nimeisikia. Ila nikiwa na Malaika wangu sipendi kupokea simu. Nikiwa na wewe napenda niutenge muda wangu kwa ajili yako tu. Sipendi kuchanganya na mambo mengine" Martin alisema bila kujihangaisha kuitoa simu yake mfukoni.




Simu iliita, hadi ikakata.




Baada ya sekunde moja tu, simu yake iliita tena.



ITAENDELEA


     


Simulizi : Bomu 


Sehemu Ya Tatu (3)




"Pokea simu mpenzi wangu. Inawezekana ni simu muhimu" Felisia alisema kwa kubembeleza.




"Hiki sio kimeo kweli.." Martin aliwaza wakati akiitoa simu yake mfukoni.




"Hallo" Martin alisema huku akiomba atakayoisikia isiwe sauti ya kike.




Dua yake ilikubaliwa.




"Daniel, Daniel Mwaseba hapa naongea" Ilikuwa sauti ya kiume.




"Ahhaaa nambie Comrade. Mbona umetumia namba mpya?" Martin alisema.




"Martin nitakueleza kuhusu kutumia simu ngeni. Lakini kwasasa kuna jambo la muhimu sana limenifanya nikupigie" Daniel alisema.




"Jambo gani hilo Daniel?" Martin aliuliza kwa hofu.




"Mama mgonjwa sana Martin. Inabidi twende kijijini Somanga haraka iwezekanavyo" Daniel alisema.




"Mama anaumwa? Upo wapi kwasasa Daniel?" Martin aliuliza.




"Kwasasa nipo Sinza Legal. Ila niambie wewe upo wapi nikufuate" Daniel alisema.




"Nipo Mlimani city hapa" Martin alisema.




"Ndani ya dakika kumi nitakuwa hapo" Daniel alisema na simu ikakatwa.




"Malaika, kanipigia simu kaka Daniel. Amenipa taarifa kwamba mama mgonjwa sana huko kijijini Somanga, inabidi tukamwone" Martin alisema akimpigapiga begani Felisia.




"Tutaenda wote baby, nami nataka nikamwone mama" Felisia alisema.




"Nitaenda nawe siku nyingine Malaika. Hiyo itakuwa safari maalum kwa ajiri yako" Martin alisema.




"Sawa mpenzi wangu" Felisia alikubali kwa shingo upande.




"Ndio maana nakupenda sana Malaika wangu. Tangu nikutane na wewe maisha yangu yamekuwa tofauti sana" Martin alisema. Felisia alicheka kwa aibu.




"Sasa mpenzi, wewe nenda nyumbani na hivi vitu. Mimi nitaenda na kaka Daniel kijijini Somanga leo. Nitakufahamisha hali ya mama nikifika" Martin alisema.




"Sawa mpenzi wangu. Nitakumiss sana" Felisia alisema akilengwalengwa na machozi.




"Nitakumiss pia Malaika wangu" Martin alisema huku akimkumbatia Felisia.




Walipoacha kukumbatiana na kupigana mabusu ya kutosha. Felisia alishika usukani wa kukisukuma kitorori kuelekea nje ya jengo la Mlimani city.




Alipofika katika mlango wa kutokea. Alisogea pembeni. Akatoa simu yake na kuibonyazabonyaza.


Akaiweka sikioni.




"Ulikuwa sahihi Imma Ogbo" Akasema simuni.




"Vipi, mtego wetu wa miezi kadhaa umenasa?" Imma Ogbo aliuliza.




"Hakika, we ni kichwa. Uliyapanga haya mambo ukiwa jijini Lagos nchini Nigeria. Na sasa yanaenda kutokea kama ulivyoyatarajia hapa jijini Dar es salaam nchini Tanzania. Daniel kampigia Martin sasa hivi. Wameongea kwa mafumbo kuwa mama yao mgonjwa hivyo wanataka kumwona. Mwenyewe alidhani ananificha, kwasababu hajui mimi ni nani? Nilielewa kila kitu" Felisia alisema kwa majigambo.




"Mpango wao upoje sasa?" Imma Ogbo aliuliza.




"Wamekubaliana Daniel aje hapa Mlimani city. Mipango yao itaanzia hapa" Felisia alisema.




"Wasitoke salama hapo!!" Imma Ogbo alisema.




"Imma sio tufanye ule mpango wetu wa awali?" Felisia aliuliza.




"Ule mpango ulikuwa mzuri. Na tulitega kila kitu katika nyumba yetu kule Tegeta. Wauaji wapo tayari wakisubiri ujio wa Daniel. Lakini nahisi kama Daniel hajatilia maanani sana" Imma Ogbo alisema.




"Au amefahamu kama mmemteka yule msichana wake kule hospitali?" Felisia aliuliza.




"Hawezi kujua. Tulimpigia Daniel na kumwelekeza aje Tegeta nyumba namba kumi na sita kwa kutumia yule msichana tuliyemteka. Na kila kitu kilienda sawa. Sisi tulitegemea Daniel atakuwa njiani kuelekea Tegeta. Lakini badala yake yeye amempigia simu Martin.." Imma Ogbo alisema.




"Imma, huoni pengine anataka kwenda na Martin huko Tegeta?" Felisia aliuliza.




"Aaah inawezekana Felisia. Umewaza jambo la maana sana. Natuma watu hapo kwa ajili ya kuwafatilia wakina Daniel. Kama uekekeo wao hautakuwa wa Tegeta, itabidi tuwalipue tu kwa Bomu" Felisia alisema.




"Nimekuelewa Imma" Felisia alisema na kukata simu.




Daniel Mwaseba, Adrian Kaanan na David walikuwa njiani wanaelekea Mlimani city.


Kule Sinza Legal kulikuwa shwari sasa. Jeshi la zimamoto wakishirikiana na jeshi la polisi walikuwa wamefanikiwa kuondoa mabaki ya gari la meneja Fadhili lililoteketa kwa moto. Na shughuli katika njia ya Shekilango ziliendelea kama kawaida.




Baada ya Daniel kuongea na Martin Hisia, kidogo hasira zake za ajabu zilikuwa zimepungua. Alihisi ameutua mzigo mzito kwakuwa alijua Martin Hisia kwa kushirikiana na wao wataumaliza mchezo. Lakini, kila dakika, hisia kwamba kuna msaliti miongoni mwao zilikuwa zinautekenya ubongo wake.




Swali gumu lilikuwa, je msaliti kati yao ni nani?.




"Adrian, naomba unisamehe kwa yaliyotokea muda mfupi uliopita. Nilipatwa na hisia za ajabu sana ambazo nilishindwa kuzimiliki" Daniel alisema wakati wakiwa ndani ya gari.




"Wewe ni kaka yangu Daniel. Mwalimu wangu katika uga huu, hauna haja ya kuniomba msamaha.." Adrian alisema.




"Kuomba msamaha hakuangalii cheo, wala umri. Unapohisi umekosea ni huna budi kuomba msamaha" Daniel alisema.




"Basi nimekusamehe Daniel" Adrian alikubali, wakati David akiwa haelewi watu wale wamekoseana nini?.




"Adrian, ulisema unamfahamu mdunguaji?" Daniel aliuliza ghafla.




"Nahisi hivyo Daniel" Adrian alisema.




"Mdunguaji ni nani?" Daniel aliuliza.




"Wakati tupo katika mafunzo ya kijasusi kule Cuba, kuna mwanafunzi mwenzetu mmoja ambaye habari zake hazijulikani hadi sasa. Hayupo katika jeshi lolote lile duniani. Hata ukisachi katika mtandao ni ngumu kuzipata habari zake. Mwanafunzi huyo alikuwa anapenda kutumia uturi unaonukia harufu uliyoninusisha katika bunduki ile. Uturi kutoka Uturuki.." Adrian alisema kwa kirefu.




"Anaitwa nani huyo Mdunguaji?" daniel aliuliza kwa shauku.




"Alikuwa anaitwa Mark. Mwenyewe alikuwa anapenda kujiita The Sniper. Mark alikuwa namba moja katika mafunzo ya udunguaji kule Cuba. Hakuna mtu akiyemkaribia hata robo katika kulenga shabaha.." Adrian alisema.




"Inawezekana Mark akawa ndiye aliyetushambulia pale. Na ndomana alianza kukulenga wewe ambaye anakufahamu" Daniel alisema.




"Ni kweli Daniel. Hivi ulijuaje kama kanilenga yule jamaa?" Ilikuwa zamu ya Adrian sasa kuuliza.




"Mdunguaji alifanya kosa, kosa le.." Daniel hakumalizia kuongea. Adrian aliropoka.




"Tunafatiliwa Daniel.." Adrian alisema huku akiangalia nyuma. Yeye alikuwa amekaa katika siti za nyuma.




Kipindi hiko walikuwa kataka foleni ya mataa ya Ubungo.




Ghafla! David aliyekuwa dereva akatoa bastola yake kiunoni na kumuelekezea Daniel ambaye alikuwa pembeni yake.




"Tulia hivyohivyo! Ukijitikisa tu naipeleka roho yako kuzimu!" David alionya kwa nguvu.




Ilizuka patashika katikati ya foleni pale Ubungo.




Je nini kitatokea? Ina maana David ni msaliti? Kivipi yaani? Tukutane kesho hapahapa.










"Unataka kufanya nini David?" Daniel aliuliza swali huku akitabasamu.




"Fuata maelekezo yangu Daniel!! Mimi sitanii nitakupasua kweli na risasi!!" David alionya.




"Tatizo nini David?" Adrian naye aliuliza kule nyuma.




"Nawe tulia! Usijione upo salama, angalia nyuma yako huko!" David alisema kwa hasira.




Adrian aligeuka nyuma. Ile sehemu ya ndani wanapowekea mizigo. Pua yake iligusana na mdomo mweusi wa bastola.




"Tumetekwa" Adrian alisema akiwa amekata tamaa.




"David, wamekulipa shilingi ngapi hawa watu kiasi ukaamua kuisaliti nchi yako namna hii?" Daniel aliuliza huku tabasamu lake likiwa vilevile.




"Adrian! Ruka katika usukani hapa. Utafuata maelekezo yangu. We Daniel ruka nyuma kule. Ukakutane na muhuni.." David alisema kwa amri.




Daniel Mwaseba na Adrian Kaanan walifanya kama walivyoagizwa.




"Adrian tunaenda Tegeta. Ukileta ujanja wowote ule sitaki kurudia tena kukwambia nitakufanya nini!" David alionya tena.




"Sifiki Tegeta mimi" Daniel alimjibu kimoyomoyo.




+(vipande vyote 36 vinapatikana kwa Tshs 1000 tu, lipa kwenda Halopesa namba 0621249611 kisha nitext whatsapp au njoo inbox hapahapa Fb nikutumie kama huna whatsapp)+




Songa Nayo....




Taa ziliruhusu. Gari la kina Daniel ambalo kwasasa lilikuwa linaendeshwa na Adrian lilikata kulia likiifuta barabara ya Sam Nujoma.


Ndani ya gari kulikuwa na utulivu mkubwa. Kila mmoja akiwaza lake moyoni.




Walipita Mlimani city, Daniel alichungulia kwa nje dirishani lakini hakumuona Martin Hisia.




"Tutaonana soon brother" Daniel alisema kwa sauti ndogo.




Gari lilishika kasi. Adrian alikuwa analiendesha bila wasiwasi wowote ule. Hakutishwa na mdomo wa bastola uliokuwa unamgusagusa shingoni. Zilikuwa ni kazi zao kugusana na bastola.




Walifika Mwenge, gari lilikata kushoto kuelekea Tegeta. Adrian na Daniel mara kwa mara walikuwa wanaangaliana kwa kutumia kioo cha kati. Walikuwa wanawasiliana kwa alama zao.


Na walielewana.




Gari liliendelea kusonga mbele.


Kuelekea Tegeta.




Adrian pia aliangalia nyuma yao kwa kutumia vioo vya pembeni. Lile gari aliloliona tangu wakiwa kule Ubungo ambalo alihisi kuwa linawafatilia bado lilikuwa nyuma yao.




"Hawa watu ni kina nani? Kwanini wamemteka Dr Luis? Siamini, na David naye ni miongoni mwao? Kajuana nao lini hawa watu wakati muda mwingi alikuwa msituni? Nina maswali mengi sana ambayo yanipasa niyapate majibu. Na nitayapata kutoka kwa David mwenyewe" Daniel aliwaza.




Daniel alikiangalia tena kioo cha kati, na Adrian naye alikiangalia.


Waliangaliana.


Macho yao yaliongea tena.


Walielewana.




Safari iliendelea huku ukimya wa kifo ukiwa umetawala ndani ya gari . Mateka walikuwa kimya, watekaji nao walikuwa kimya.




"Hannan alinipa taarifa kwamba simu ya meneja Fadhili ilionekana imewashwa na kisha kuzimwa Tegeta. Niliamini taarifa ile, na nilitaka kwenda kweli Tegeta. Lakini mwishoni kabisa aliniambia 'Do did'. Najua aliyekuwa nao huko hawakumuekewa. Hilo neno tunalitumia mimi na yeye tu endapo mmoja wetu atakapokamatwa na kulazimishwa kumleta mwenzie mtegoni. 'Do did' leo imetusaidia.


Ila hawa jamaa wana roho mbaya. Unamtoaje mgonjwa katika hali hospitali na kumteka. Lakini lazima watalipa kwa haya mambo wayafanyayo" Daniel aliwaza.




Akanyanyua tena sura yake katika kioo cha kati. Adrian naye alifanya vivo hivo. Akamkonyeza kwa jicho lake la kushoto.




"Its the time" Daniel alisema kwa sauti ndogo aliyoisikia mwenyewe.




Sekunde hiyohiyo, Adrian aliliyumbisha gari kwa nguvu na kwenda kulikwaruza gari la pembeni. Gari lao liliyumba vibaya huku likielekea kugongana uso kwa uso na roli, likilotokea Tegeta. Adrian alikata kona kwa haraka na ustadi mkubwa na kurudi upande wake. Walihitaji mstuko mdogo tu kutoka kwa wale watu.


Na waliupata.


Daniel Mwaseba alikuwa ameshafanya kitu....




Wakati yule jamaa aliyumbishwa na ule myumbo wa kwanza wa gari, Daniel aliitumia nafasi ile kupiga kwa nguvu kiganja cha yule jamaa, na bastola ilidondoka chini. Jamaa alitoa yowe dogo la hofu lisilo na mwendelezo, kwani alikutana na mkono wa kiume wa Daniel ulioizungusha shingo yangu kwa nguvu kuelekea kushoto. Ulisikika mlio kama kijiti kikavu kimevunja. Jamaa alienda katika sayari nyingine palepale. Wakati gari lilkikaa sawa barabarani, Daniel Mwaseba alikuwa ameimaliza kazi.




David alikuwa anatetemeka huku akiwa bado kamuelekea bastola yake Adrian. Hakuna aliyemsemesha.




"Hawa wajinga wanaotufuata watatutambua leo!!" Daniel alisema kwa jazba.




Adrian alifanya alitulia katika usukani. Safari ya kuelekea Tegeta iliendelea..




David akiwa vilevile, na mtetemo wake wa haja huku bastola yake ikiwa imeelekezwa kichwani kwa Adrian Kaanan.




***




Imma Ogbo aliingia katika chumba ambacho alikuwa amewekwa Dr Luis. Safari hii ndio alipanga kwenda kumwambia Dr Luis lengo lao kuu la kumteka. Alimkuta Dr Luis amekaa katika kiti akiwa mwingi wa mawazo.




"Tumekutana tena rafiki yangu.." Imma Ogbo alisema huku akitabasamu.




Dr Luis alimwangalia tu.




"Dr Luis, ni wewe pekee ndiye unayeweza kupigania maisha yako. Huko nje hakuna harakati zozote za kukutafuta. Rafiki yako mheshimiwa rais hana habari na wewe. Hapa ni wewe na wewe tu ndio wenye nafasi ya kujiokoa" Imma Ogbo alisema.




"Kwani mnataka nini kwangu ninyi watu? Kama mnataka kiasi chochote cha pesa mimi nitawapa. Naomba niachieni nirudi kwetu. Mmeniteka bila sababu, maswali yenu yote nimeyajibu sasa mnataka nini tena kutoka kwangu?" Dr Luis alisema.




"Sikiliza Dr Luis. Huu si wakati wa kulalamika. Hapa si mahali sahihi pa kulalamika. Hakuna atakayekuonea huruma kwa malalamiko yako. Sikiliza tutachokwambia, nawe utekekeze. Huo ndio usalama wako"




Dr Luis alibaki kimya.




"Tunataka ututengenezee kirusi cha DH+...." Imma Ogbo alisema kwa sauti ndogo.




"Unasemaje!!!?" Mshangao mkubwa ulionekana katika macho ya Dr Luis.




Hakuamini maneno yale kutoka kwa yule mtu. Kabla ya dakika hii aliamini ni yeye pekee ndiye anayejua kuhusu kirusi cha siri cha DH+ hapa duniani.




Kumbe katu haikuwa hivyo.




Moyoni akahisi, hata siri yake na rais Mgaya sasa itakuwa hadharani kwa hawa watu.




Hili lilikuwa ni Bomu kwake!!!




Je nini kitatokea? Mmeelewa kwanini Hannan alimwambia Daniel Mwaseba DO DID? Tukutane hapahapa kesho. Cha muhimu ni wewe kulike na kushea kwa wingi kwenye magroup ili tusonge mbele.




"Sijaelewa unazungumzia nini kijana?" Dr Luis alisema hofu dhahiri ikiwa katika sauti yake.




"Nimesema nataka ututengenezee kirusi cha DH+" Imma Ogbo alirudia tena.




"Unafaham nini kuhusu kirusi cha DH+?" Dr Luis aliuliza huku akiwa katika hali ya wasiwasi.




"Hapa kuna mgawanyo wa kazi. Wewe hauna jukumu la kuuliza maswali. Jukumu lako ni moja tu, kutekeleza kila nikwambiacho" Imma Ogbo alisema.




"Hawa watu wamejuaje kuhusu kirusi cha DH+. Dh+ ni kirusi kibaya sana. Endapo nikitengeneza kirusi cha DH+ na kuwakabidhi watu hawa ambao sijui wanataka kukifanyia nini itakuwa ni hatari sana. Katu siwezi kuwatengenezea kirusi cha DH+. Najua madhara yake ambayo hadi sasa yanamtesa Mheshimiwa rais" Dr Luis akawaza.




"Dr Luis umenielewa nikichokwambia?" Imma Ogbo aliuliza.




Dr Luis alikaa kimya.




"Dr Luis, napenda tuumalize mjadala huu kistaarabu. Sitaki tuumizane ili utekeleze nikwambiacho. Utatutengenezea kirusi cha DH+?" Imma Ogbo aliuliza.




Dr Luis alikaa kimya.




"Hii ni mara ya mwisho kukwambia kistaarabu. Naona unataka kuujua upande wangu wa pili. Mimi ni tafsiri sahihi ya neno ukatiri!!"




"Nitawatengenezea kirusi cha DH+, lakini kwa masharti mawili" Dr Luis alisema kwa uwoga.




"Haujaja kutupa masharti hapa!!" Imma Ogbo alifoka.




"Basi kama hutaki nikupe masharti, niseme tu sitowatengenezea hiko kirusi. Nifanyeni mnavyoweza" Dr Luis alisema.




"Narudia kwa mara ya mwisho Dr Luis, sitaki nitumie nguvu ili kutekeleza hiki nikwambiacho!" Imma Ogbo alisema.




Dr Luis alikaa kimya.




"Bila hayo masharti yako, upo tayari ututengenezee kirusi cha DH+?" Imma Ogbo aliuliza.




"Siwezi kuwatengenezea" Dr Luis alijibu kwa ufupi. Huku macho yake yalimaanisha alichokuwa amekisema.




Mara, simu ya Imma Ogbo iliita. Alikuwa ni mzee Msangi.




"Eeeh nambie mzee..bado naendelea na mahojiano.." Imma Ogbo alisema simuni.




"Tumesikiliza majadiliano yako na Dr Luis. Naomba mpe nafasi akwambie hayo masharti" Mzee Msangi alisema.




"Ni nje ya utaratibu mzee. Hatuwezi kupewa masharti na mtu tuliyemteka" Imma Ogbo alisema.




"Mimi ni bosi wako hapa. Naomba fanya nilichokuagiza!" Mzee Msangi alifoka.




"Siwezi kufanya maagizo yako. Hujanileta wewe hapa! Mimi napewa oda na aliyenileta tu, ambaye ni..."




"Come on Imma Ogbo. Toka humo ndani!!" Mzee Msangi alifoka.




"Mzee unajua unachokifanya. Kwanza umekosea kufatilia majadiliano haya. Ndio maana kamera zote za huku zimezimwa. Bila shaka umeweka kamera zako za siri. Hilo ni kosa. Haya ni majadiliano ya siri. Kwahiyo ulikuwa unanichunguza? Umeniuzi sana. Na sasa unataka kuingilia kazi isiyokuhusu. Jua haya si majukumu yako. Na sipo tayari kuteleza usemayo" Imma Ogbo alisema.




Kwa hasira Mzee Msangi alikata simu.




"Twendeni huko shimoni!" Mzee Msangi aliwaambia wenzake. Kila mmoja akatoa bastola yake.




"Imma Ogbo hastahili kuifanya kazi hii" Mzee msangi alisema wakiwa katika korido kuelekea katika chumba cha mateso kilichokuwa chini kabisa ya jengo hilo.




Dakika saba ziliwafikisha shimoni. Cha kushangaza waliukuta mlango wazi. Na tangu kimejengwa chumba hiko hakikuwahi kuwa wazi. Kwa umakini mkubwa wakina mzee Msangi waliingia mle ndani.




Walikutana na jambo la kushangaza sana..




Hakuwepo Imma Ogbo wala Dr Luis...




Harakaharaka Dr Luis alitoa simu yake na kumpigia mkuu wa ulinzi wa lile jengo.




"Simon, kuna watu wawili wametoroka humu ndani. Hakikisha hatoki mtu ndani ya jengo hili. Fikisha taarifa kwa watu wako wote!" Mzee Msangi alifoka.




"Sawa mkuu" Simon alijibu.




Dakika hiyohiyo msako wa kuwasaka Imma Ogbo na Dr Luis ulianza mle ndani ya nyumba.




"Huyu kijana hajui kwa namna gani amefanya jambo la hatari sana. Hajui Dr Luis ni mtu wa muhimu kwetu kwa kiasi gani? Atajutia kwa hiki alichokifanya" Mzee Msangi aliwaza.




Mara simu yake iliita. Alikuwa Simon.




"Vipi Simon mmewapata?" Mzee Msangi aliuliza.




"Hatujafanikiwa mzee. Lakini nyuma ya nyumba tumekuta walinzi wetu watatu wameuwawa. Bila shaka hawa watu wameruka ukuta kwa nyuma. Msako inabidi utoke ndani ya jengo" Simon alisema.




"Umeruhusuje hilo Simon?" Mzee Msangi aliuliza.




"Jamaa walikata mawasiliano. Hata kamera zetu hazikuweza kuwanasa wakati wanatoroka. Wakati mafundi wakijaribu kurudisha nawasiliano yetu, kumbe hao watu ndio walikuwa wanatoroka" Simon alisema.




"Daah tumefanya kosa kubwa sana. Tutamwambia nini Roho?" Mzee Msangi aliwaza.




"Nitakuelekeza cha kufanya Simon. Ngoja nifikirie kidogo" Mzee Msangi alisema.




Ilipokatika simu ya Simon, mzee Msangi akapiga simu kwa Mark the Sniper.




"Vipi mzee, sisi bado tunaliwinda windo lendo" Mark alisema simuni.




"Mark kuna tatizo huku" Mzee Msangi alisema sauti yake ikiwa na uwoga.




"Tatizo gani tena mzee?" Mark aliuliza.




"Imma Ogbo ametoroka na Dr Luis!!"




"Unasemaje mzee?"




"Imma Ogbo ametoroka na Dr Luis" Mzee Msangi alirudia kusema.




"Kwanini Imma amefikia hatua hiyo?"




"Kulitokea kutoelewana na kutoelewana kidogo kati yangu na Imma. Na yeye nd'o akachukua hatua ya kumtorosha Dr Luis" Mzee Msangi alisema.




"Hilo limewezekana vipi? Katika nyumba yenye kamera za ulinzi na walinzi kama hiyo?"




"Imma Ogbo ameweza, ameua walinzi wetu watatu, huku akiacha ameuharibu kabisa mfumo wetu wa ulinzi" Mzee Msangi alisema.




"Hiyo ni mbaya sana kwetu. Si unajua Roho anarudi leo usiku. Na kesho asubuhi inabidi akutane na Dr Luis kwa mahojiano. Tutamweleza nini sasa na tulishamueleza kuwa yupo mikononi mwetu?"




"Yaani hata sielewi. Hapa nimechanyikiwa. Naomba rudini hapa tuone tunafanya nini? Lakini, lazima tumsake Imma Ogbo, apatikane kabla hakujakuchwa. Hii ni kwa kulinda kazi yetu" Mzee Msangi alisema.




"Sasa kuhusu hawa majamaa. Si unajua Ninja na yule mwanajeshi wamewateka wakina Daniel. Hapa tunaelekea Tegeta kwenda kuwamaliza hawa jamaa" Mark alisema.




"Haina shida. Ninja atamaliza kila kitu. Ninyi rudini kwanza huku ili tulimalize hili. Kisha tutamalizana na hao majamaa, kwakuwa wapo mikononi mwetu hakitoharibika kitu"




"Sawa mzee"


Mark The Sniper alisema. Alimwamuru dereva wao ageuze gari na kuelekea Kigamboni.




Mambo yalikuwa yameharibika. Na mharibuji alikuwa ni Imma Ogbo.




***********************




"Jamaa wanageuza gari.." Adrian alisema baada ya kuangalia katika vioo vya pembeni.




"Wamestukia nini kama tumemuua mwenzao?" Daniel aliuliza.




"Sidhani kama wamestukia. Sasa yatupasa na sisi tugeuze tuwafatilie wanaenda wapi??" Adrian alisema.




"Jamani, watoto wanguu.." David alisema kwa kulalama.




Daniel na Adrian walimwangalia tu yule mwanajeshi msaliti. Hakuna aliyesema kitu. Huku hasira dhahiri zikionekana usoni mwao.




Adrian akageuza gari na kuanza kuwafatilia wale majamaa. Sasa mchezo ukageuka. Sasa wafatiliaji wakageuka kuwa wafatiliwaji...




"Bila shaka wanatupeleka alipo Dr Luis" Daniel akawaza.








Martin Hisia bado alikuwa Mlimani city akimsubiri Daniel Mwaseba kama simu ilivyomwagiza.




Baada ya kusubiri zaidi ya nusu saa hisia zake zilimwambia kwamba kuna tatizo. Daniel Mwaseba alikuwa mtu wa kutimiza ahadi, sasa kwanini hadi muda huo alikuwa hajafika?




Felisia Nyenyembe, mpenzi wake alikuwa amekaa katika kona moja akimwangalia Martin Hisia. Alikuwa anasubiri watu ambao wametumwa na Imma Ogbo ili waje waumalize mchezo. Sehemu alipojibanza alikuwa anamwangalia kwa chati Martin huku akihakikisha hafanyi kosa lolote lile. Alikuwa anamjua Martin katika medani hizi.




"Siku Martin akigundua kwamba mimi nimewekwa kwa ajili ya kumchunguza sijui itakuaje?. Martin anaonekana kuniamini sana kwakuwa hajui mimi ni nani? Ila sijui kama nifanyacho ni sahihi? Martin ananipenda sana. Upendo wa Martin kwangu sio wa kawaida. Je ni sahihi kumfanyia ninachotaka kumfanyia Martin. Namuuza Martin..." Felisia aliacha kuwaza. Simu yake ilikuwa inaita.




"Hallo Imma?" Felisia alisema.




"Felisia bado upo Mlimani city?" Imma Ogbo aliuliza.




"Ndio, na jamaa bado anamsubiri Daniel Mwaseba hapa Mlimani city. Nashangaa kwanini amechukua muda mrefu sana kufika hapa" Felisia alisema.




"Mambo yamebadilika Felisia. Hapa nilipo tushavurugana na majamaa" Imma Ogbo alisema.




"Umevurugana na majamaa gani?" Felisia aliuliza.




"Nimevurugana na wakina mzee Msangi. Nimechoka na tabia zao za kufatilia kazi ambazo sio zao" Imma Ogbo alisema.




"Bado sijakuelewa Imma"




"Haya sio mambo ya kuongea simuni. Maana mambo yamebadilika. Nimekuwa adui kwao sasa. Nataka kuungana na wewe ili tuwashinde. Naomba uwe upande wangu" Imma alisema.




"Wewe unanijua Imma kuliko mtu yeyote yule. Sijawahi kuwa na jibu la hapana kwako. Ni wewe ndio ulioniingiza katika misheni hii tangu ukiwa Nigeria. Naanzaje kusema hapana kwako Imma" Felisia alisema.




"Nakuamini sana Felisia. Sasa mimi nipo Vikindu huku, unapajua?"




"Hapana, sipafaham"




"Chukua taksi yoyote hapo Mlimani, mwambie akulete Vikindu. Atakuleta" Imma alisema.




"Sawa Imma. Ninafanya hivyo sasahivi. Vipi kuhusu huyu Martin Hisia?" Felisia aliuliza.




"Achana nae. We njoo Vikindu. Tutapanga mipango yetu kuanzia hapa. Tunaelekea kuwa mabilionea soon" Imma Ogbo alisema.




"Nipo njiani brother" Felisia alisema.




Simu ikakatwa.




"Imma Ogbo amevurugana nini na hawa jamaa zake. Ni yeye ndiye aliyenitambulisha kwa hawa jamaa na nikawa pamoja katika misheni hii ya kumteka Dr Luis. Sasa limetokea tatizo gani tena. Ngoja niende huko Vikindu nikajue" Felisia akawaza.




Felisia alienda mahali wanakopaki teksi. Aliongea na dereva mmoja, wakakubaliana bei. Felisia alikaa siti za nyuma za gari, gari likawashwa.




Safari ya kuelekea Vikindu ikaanza.




Ndani ya gari mawazo yote yalikuwa juu ya misheni hii ambayo kwa sasa imebadilika. Pia alikuwa anawaza Imma Ogbo ataenda kumueleza kitu gani?.




***




Gari ya kina Adrian ilikuwa nyuma ikilifatilia gari la wale majamaa. Ndani ya gari ilikuwa kimya kabla Daniel Mwaseba kumuuliza swali David.




"David, hebu nambie kitu gani kimetokea hadi ukaamua kutusaliti na kuwa upande wa hawa jamaa?"




David akiwa bado amemuelekezea bastola Adrian alisema..




"Daniel, mimi sielewi walijuaje kuhusu mimi?" David alisema kwa majonzi.




"Walijuaje kuhusu nini?" Daniel aliuliza.




"Sikuwa na nia ya kuwasaliti ndugu zangu. Najua jukumu zito lililopo mbele yetu. Na tumiaminiwa sisi katika taifa lenye zaidi ya watu milioni hamsini. Lakini, mambo hayo yalianza ghafla tu nusu saa baada ya kupigiwa simu na mkuu wa majeshi na kupewa kazi hii" David alisema.




"Mbona unafichaficha David?. Kuwa muwazi ili tujue tunakusaidiaje. Kikanuni, si unayajua malipo ya msaliti katika misheni kama hizi? Ni kifo!


Tena kifo cha kuumiza. Huwa hatuhoji wasaliti kama nifanyavyo. Nimekupa nafasi hii adimu sana, naomba itumie. Na ni mara yangu ya kwanza katika maisha yangu kumuhoji msaliti" Daniel alisema.




"Daniel, jamaa wameiteka familia yangu..."




"Wameiteka familia yako? Lini? Mbona hukutuambia David?" Adrian akiwa katika usukani alidakia.




"Waliiteka familia yangu nusu saa tu baada ya kupewa kazi hii. Mke wangu, Hellen na watoto wangu mapacha, Candy na Cindy wapo mikononi mwa hawa jamaa. Walitumia kuiweka mateka familia yangu ili kunishinikiza niwaambie kuhusu mipango yetu" David alisema.




"Inamaana ni wewe ndiye ukiyewaambia mambo yetu?" Daniel aliuliza akishangaa.




"Samahanini sana brothers. Nimefanya kosa kubwa sana. Hapa nafsi inanisuta. Ila jamaa walinishika pabaya sana. Familia yangu ni kila kitu kwangu. Nimeshinda vikwazo vingi vigumu katika medani huko msituni, lakini kikwazo hiki nilishindwa kabisa" David alisema.




"Lakini kwanini usituambie kabla David ili tuone namna ya kuiokoa familia yako?" Daniel aliuliza.




"Walinionya nisithubutu kuwaambia lolote. Huku wakinipa kazi ya kuwaeleza direction yetu. Na hilo ndio kosa kubwa sana nililolifanya" David alisema.




"Mimi ninakusamehe David. Hii ni misheni yako ya kwanza mjini, ulizoea misheni za msituni. Na hili ni kosa lako la kwanza pia. Lakini bado nina maswali kwako"




David alitingisha kichwa kukubali.




"Ulikuwa unawasiliana vipi na hao watu?" Daniel aliuliza.




"Kuna mtu mmoja alikuwa ananipigia simu, na wakati mwengine tukiwasiliana kwa meseji" David alisema.




"Na ni wewe ndiye uliyewaambia kuhusu Hannan?"




"Ni mimi" David alisema kwa majonzi.




"Ulikosea sana David. Ona umemweka Hannan katika hatari kubwa sana. Anaweza kuuwawa muda wowote ule" Daniel alisema.




"Naamini atakuwa salama. Walimchukua Hannan kama chambo kukusaka wewe. Ninaapa nitaungana nanyi, tumsake Hannan mpaka tumpate. Na ninaomba sana nanyi mnisaidie kuiokoa familia yangu.." David alisema.




"Nakuahidi nitakusaidia. Na tutawapa mke na watoto wako. Wewe unahisi ni nani aliyewaambia hao watu uhusika wako nusu saa tu baada ya kuchaguliwa?" Daniel aliuliza.




"Mimi sifahamu. Lakini kuna watu sita ninawahisi, kati ya hao kuna mmoja au zaidi wanahusika" David alisema.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog