Simulizi : Malaika Wa Shetani
Sehemu Ya Pili (2)
sauti nzito yenye dalili ya uchovu.
“Hivyo, inanishangaza kuona ukivunjika moyo kwa tatizo dogo kama hili. Unautia dosari ushujaa wako.”
Joram alikohoa kidogo kabla ya kumjibu. “Yaleyale ya waoga wanaodai, ‘Asiyekubali kushindwa si mshindani.’ Sikiliza Nuru…” Lolote alilokusudia kulisema lilikatizwa na mlio wa simu iliyokuwa kando yao. Simu hiyo iliwashangaza kidogo kwa sababu nyingi. Wakiwa wageni ambao hawakujulikana kabisa katika nchi hiyo, hawakuwahi kupigiwa simu na mtu yeyote, toka nje. Wala wafanyakazi wa hoteli hiyo hawakuwahi kuitumia kwa jinsi walivyokuwa wageni wasio na madai mengi. Zaidi ya
yote hayo saa hizi ilikuwa yapata saa saba za usiku? Maswali hayo ndiyo yaliyomfanya Joram aidake mara moja na kuitika.
“Samahani bwana,” sauti toka upande wa pili iliitika. “Tafadhali unaombwa kufika mapokezi kuna mgeni wako ambaye anakusubiri.”
‘Mgeni wa saa hizi! Anatoka wapi? Anataka nini?’ Joram alitamani kumuuliza hivyo operata huyo. Lakini alihairisha maswali hayo kwa kumjibu kuwa angefika mara moja. Akawasha taa na kujitupia mavazi ambayo yalikuwa karibu.
“Vipi?” Nuru alimtupia.
“Kuna mgeni hapo nje. Naenda mara moja.”
Nuru hakuelekea kulifurahia wazo hilo. “Kwa nini humkaribishi hapa ndani?” alimwuliza. “Nahisi wito huo hauna wema.”
“Nadhani hatukufuata mema huku, Nuru. Tungeyataka mema tungeendelea kuishi Dar es Salaam katika mahoteli ya Embassy na Kilimanjaro,” alimjibu huku akimaliza kuvaa na kuanza kutoka.
“Nisubiri basi,” Nuru aliita akikurupuka toka kitandani. “Usijisumbue. Nitarudi mara moja.”
Pengine Nuru hakumsikia, kwani Joram alisema huku akiufunga mlango nyuma yake.
Aliiendea lifti na kuisubiri. Ilipofika aliingia ndani ambamo alimkuta abiria mmoja tu, ambaye alikuwa amelewa. Alimsumbua Joram kwa harufu ya pombe kali ambayo ilijaa chumba hicho kila alipopumua. Joram alipofika chini alikwenda moja kwa moja katika chumba cha mapokezi.
Alikuwemo mgeni mmoja tu. Alikuwa ameketi juu ya kochi, sigara mdomoni; kitabu wazi mkononi. Uso wake ulimezwa na ndevu nyingi zilizoyafunika
masikio. Alivaa mavazi ya kawaida kuliko ilivyo kwa watu wengi wa umri wake katika nchi hiyo; shati jeusi, ambalo halikuchomekewa na suruali ya kijivu. Joram alimkisia kama mtu mwenye umri wa kati ya miaka sitini na sabini. Macho yake yalikuwa yamezama katika kitabu cha riwaya ya kiingereza, Fear to Live alichokuwa akikisoma. Hisia zilimwambia Joram kuwa huyo ndiye mgeni wake. Hivyo, alimsogelea na kuketi naye.
“Natumaini hujambo,” alimsalimu.
Mgeni huyo aliinua uso mara moja na kumtazama Joram. Kisha, alikikunja kitabu chake na kumsogelea Joram zaidi.
“Joram Kiango?” aliuliza bila ya kuzijibu salamu za mwenyeji wake. Sauti yake haikuwa ngeni masikioni mwa Joram. Alijaribu kujiuliza aliisikia wapi. Hata hivyo, mgeni wake hakumpa nafasi ya kuendelea kufikiria. Alikuwa amenaza maelezo kwa sauti ndogo ambayo ni dhahiri ilikusudiwa kuishia katika masikio ya Joram peke yake.
“Nina ujumbe wa siri sana,” alieleza. “Rais ameomba radhi kwa jinsi alivyopuuza habari ulizomletea jana. Baada ya kufikiria kwa makini ameona kuwa yawezekana kweli marehemu alikuwa na habari muhimu ya siri ambayo alikusudia kukuletea. Hivyo, anakuomba uendelee na upelelezi wako kwa siri sana kuchunguza jambo lolote ambalo lilikusudiwa kutendwa dhidi ya taifa. Ameahidi kukupa msaada wowote ambao utahitaji pamoja na ulinzi kwa maisha yako kwa lolote litakalotishia usalama wako.”
Joram alikuwa akimsikiliza kwa makini. Sasa sauti hiyo haikumtatanisha tena. Alijua anaongea na nani. Aliupenda sana mchezo wa aina hiyo. Kwa kuufanya mchezo uendelee alisema, “Nadhani ningependa kumsikia Rais mwenyewe akinipa maagizo hayo badala ya mtu mwingine. Kama sikosei, iwapo kuna lolote linalotisha katika mashaka haya basi litakuwa suala linalotishia maisha ya Rais zaidi ya mtu yeyote mwingine.”
“Ukinisikiliza mimi umemsikiliza Rais,” alijibu. “Wewe ni nani kwake?”
“Msiri wake mkuu.”
Joram alitabasamu kidogo. “Nadhani umri wako ni mkubwa sana, kuwa nje ya nyumba yako usiku kama huu na katika baridi kali kama hii. Ungeniita tu, mzee…”
“Usijali,” alijibiwa baada ya kumjibu Joram kwa tabasamu lake lililochanua na kutoweka mara moja. “Usijali,” aliongeza. “Wazee vilevile tunapenda kujikumbusha matembezi ya usiku yanavyoburudisha. Zaidi suala hili ni la siri sana. Rais asingeweza kumwamini mtu mwingine zaidi yangu.”
Wakatazamana na kucheka tena katika hali ya kuelewana. “Unaelekea kijana mwepesi sana wa kuona,” aliongeza.
“Natumaini hutasahauu kuwa nimekutembelea usiku huu na kukupa ujumbe mzito kama huu. Nadhani inafaa tuagane. Utapokea mahitaji yako yote kesho mchana. Usisite kuomba msaada mwingine wowote ule.”
Waliinuka pamoja na kupena mikono.
“Itakuwa siri,” Joram alimwambia. “Nani atakayeniamini katika dunia hii nikijitia kutamba kuwa niliwahi kutembelewa na Rais katika hoteli yangu?”
Rais yupi?” mgeni huyo aliuliza akiondoka.
Mara moja akamwona yule mlevi waliyeshuka naye katika lifti akichomoza toka katika kimoja kati ya vyumba vya hoteli hiyo na kumfuata mgeni huyo kwa mwendo ambao ulitangaza yeye ni nani katika duia hii. Hata chembe moja ya ulevi haikuwemo tena mwilini mwake. Koti lake lilituna kidogo mgongoni kuonyesha kuwa alikuwa kamili. ‘Kidogo nishangae,’ aliwaza kimoyomoyo. ‘Nilidhani hatimaye nimekutana na mmoja wao anayejiamini. Hawajiamini walo kwa dakika moja.’ Taratibu aligeuka kuiendea lifti.
Alishangaa kumkuta Nuru nje ya lifti hiyo. Hakushangaa alipoulizwa kwa sauti ndogo, “Ni nani yule mzee aliyekutembelea saa hizi? Na alitaka nini?”
“Kwa nini hukulala hata ujisumbue kunifuata kwa siri?
Ulidhani naitwa na mwanamke? Ulitaka kunifumania?”
“Acha mzaha, Joram,” Nuru alisisitiza. “Ulitegemea kuwa ningestarehe juu ya kitanda wakati wewe umeitwa usiku wa manane na mtu mwenye madevu ya kutisha kama yule?” alipoona hajibiwi aliongeza, “Ni nani lakini yule Joram?” Lifti ikafika. Wakaingia.
“Mbona hunijibu Joram?”
“Kukujibu nini?” aliuliza akipapasa mfuko na kutoa sigara. “Yule mzee. Ni nani na alitaka nini?”
Joram alikuwa akishughulikia sigara yake. Alivuta mara moja, ikazima. Akaiwasha tena. Lifti ikawafikisha. Wakashuka na kufuatana chumbani kwao.
“Ni nani? Au hutaki kunijibu?” lilikuwa swali la kwanza mara walipoingia chumbani kwao.
“Kwani hukumwona?” Joram aliuliza. “Nimemwona, sikumtambua.” “Alikuwa Rais.”
“Rais yupi?” “Abdul Shangwe.”
Nuru alitabasamu kwa hasira. “Naona hutaki kuniambia
ukweli, Joram. Tumeanza lini kufichana mambo?”
“Tangu ulipoanza kutoniamini.” Alipoona Nuru hajamwelewa, aliongeza, “Kwa nini huamini kuwa Rais wa nchi hii ametutembelea? Nuru ninayemjua mimi hawezi kudanganywa na madevu yale ya bandia na mavazi ya kubabaisha aliyoyavaa.”
***
Moyo wa Joram ulijaa furaha alipoingia katika baa ya tatu kati ya nne ambazo aliambiwa kuwa hayati Patauli Kongomanga alizipendelea, baa iliyojulikana kwa jina la Glamour Site ikiwa moja kati ya zile maarufu sana katika mji huu wa nchi ya Pololo, Baubu.
Katika baa zilizotangulia Joram alidokezwa na mtu mmoja kuwa alipata kumwona marehemu akifuatana na msichana mmoja aliyefanya kazi hapo Glamour Site katika hali ya mtu na mpezi wake. Hayo aliyapata baada ya maswali mengi, uongo mwingi na ahadi zisizo na idadi kwa wafanyakazi mbalimbali; hasa wa kike, katika baa mbalimbali. Haikuwa kazi ngumu kwa mtu kama Joram kupata mwanya wa kumfikisha hapo. Jina la marehemu Kongamanga likiwa bado moto masikioni mwa watu, hasa kwa waandishi wa habari; ilimchukua dakika chache tu kupenya toka baa hadi baa hata kufikia hii ambayo aliamini ingekuwa kichochoro ambacho ama kingemwongoza katika barabara kuu au msitu mkuu wa chochote alichokuwa anakitafuta.
Alianza upelelezi rasmi baada ya ile ziara ya Rais usiku wa manane. Kutembelewa na Rais wa nchi! Usiku kama ule! Katika hali kama ile kulimzidishia ile njaa aliyokuwa nayo rohoni, kutaka kujua ni kitu gani kinapikika sirini, katika nchi; kiasi cha kuyapoteza maisha ya kijana asiye na hatia kama Kongomanga. Na nani mpishi wa chungu hicho.
Nuru aliondokea kuwa tatizo dogo lililojitokeza mwanzoni mwa uchunguzi wake. Hakuafiki kuachwa nyuma. Joram akijua kuwa suala hilo kama lilikuwa lianze katika mabaa; basi ingekuwa toka katika midomo ya wanawake, ambao wasingejisikia kumkaribisha endapo angekuwa akifuatana na msichana, kisha mzuri kama Nuru. Alijaribu kumshawishi Nuru kubaki nyuma, haikusaidia. Siku ya kwanza ilibidi wafuatane. Matokeo yake Nuru mwenyewe aliyaona. Siku ya pili alikubali kubaki hotelini kwa masharti ya kufahamishwa ratiba nzima ya mienendo ya
Joram. Ni siku hiyo ambayo Joram alifaulu kuzungumza kwa mapana na watu mbalimbali, akianzia mbali na kuishia katika maongezi ya marehemu Kongamanga.
Hata hivyo, baada ya maongezi yake, alimwona Nuru akiingia na kuketi meza ya mbali sana. Joram alijaribu kumsalimu kwa macho lakini Nuru akajifanya hamwoni wala hamsikii. Badala yake aliyaona macho yake yakimtia moyo kwa tabasamu la kumvutia mzee mmoja ambaye tangu alipoingia hakuchoka kumtazama, kinywa wazi; ulimi nje; kila dalili ya tamaa ikiwa wazi katika macho yake. Baada ya muda mzee huyo alihamia katika meza ya Nuru na kuanza kumwaga vinywaji na maongezi kama aliyepagawa. Joram alihisi wivu kiasi. Lakini mara moja alijicheka kwa wazo la kuwa na wasiwasi na ‘zee’ kama lile. Akaendelea na shughuli zake. Akayapata anayoyataka. Alipotosheka aliaga na kutoka nje ambako aliita teksi. Wakati akifungua mlango na kuingia aliisikia sauti ya kike ikimsemesha. “Samahani,” ilisema kwa upole. “Kama unaelekea Golden View Hotel naomba lifti.”
Joram alimtazama kidogo kisha akatabasamu kabla ya kuuliza, “Na yule bwana wako?”
“Achana naye.”
Wakainggia na kuondoka. Hawakuzungumza chochote hadi chumbani kwao ambako Joram alimgeukia tena Nuru na kumwuliza, “Umeanza lini dada yangu, tabia ya kujiuza kwa wanaume katika mabaa?
Ilikuwa sauti yenye mzaha, Nuru alijibu kimzahamzaha. “Unadhani nitakuruhusu ukaukwae Ukimwi kwa wanawake
wa baa?”
“Utafanyaje kunizuia?”
“Nikiona maongezi yanakuwa si ya kawaida nitaanzisha fujo na kukupora wewe na huyo hawara yako.”
Wakacheka na kujitupa kitandani.
***
Naam, hayo yalikuwa ya jana. Leo Joram yuko katika baa yenye matumaini makubwa. Alikuwa tayari kununua habari kwa bei yoyote ile, hata kwa kutazamana na Ukimwi ana kwa ana. Asingekubali Nuru alete wivu au mzaha ambao ungevuruga uchunguzi wake. Hivyo, alifanya hima kuvaa lile tabasamu lake ambalo huwaloga wanawake, tabasamu ambalo mara
nyingine humletea matatizo bila ya kutegemea kwa kutafsiriwa vibaya na wanawake ambao hakuwakusudia. Leo alilielekeza kwa kila mwanamke. Macho yake yakiwa kazini kutafuta uso wa mwanamke aliyekuwa akimhitaji. Isingekuwa kazi ngumu kumfahamu mwanamke ambaye amepoteza mpenzi siku mbili, tatu, zilizopita.
Tabasamu lilifanya maajabu. Haukupita muda, mara akawa nyota katika baa hiyo, macho ya kila mwanamke yakimwelekea; kila mhudumu akitaka kumhudumia. “Samahani, nimekwishahudumiwa,” alieleza kwa mara ya tatu.
Kinywaji chake kilipoletwa alikunywa kwa utulivu, akiendelea kutupa jicho lake huku na kule. Haukupita muda alipouona uso aliouhitaji, uso wenye furaha ya bandia na tabasamu lililokusudiwa kufunika msiba ulokuwa moyoni. Ulikuwa uso wa msichana mzuri wa sura, mwenye umbo dogo lililokatika kike kiunoni na kujaza tosha nyuma, nywele zake ndefu zilizosukwa kileo zikiwa zimeuzunguka uso wake mzuri na kuufanya kama kisiwa cha kupendeza katikati ya bahari nyeusi. Msichana huyu, aliyekuwa katika mavazi yake ya kikazi; alikuwa akipita hapa na pale katika meza za wanywaji.
Joram alimkonyeza. Akajifanya haoni. Akamkonyeza tena. Bado alijifanya haoni. Joram akaamua kumwacha kwa muda. Akaichoma na kuishughulikia sigara yake. Alipoinua uso, msichana huyo alikuwa kasimama mbele yake akiuliza kwa upole, “Naweza kukusaidia?”
“Eh! Ndiyo. Bia mbili, moja kwa ajili yako.”
Msichana huyo alimtazama Joram kama anayetafuta kitu katika macho yake. Kama ambaye alikipata au hakukipata alinong’ona, “Ahsante, lakini bado niko kazini. Kama unanitaka kwa maongezi zaidi naweza kumwomba ruhusa msimamizi wetu. Ghorofa ya pili toka hii kuna vyumba vya mapumziko. Nenda kapate chumba, kisha nipigie simu, naitwa Betty.”
Baada ya nusu saa nitakupigia simu,” Joram alijibu.
Alikunywa bia yake taratibu. Alipomaliza alimtupia Betty jicho la kumuaga, kisha akainuka kuelekea mlangoni. Ndio kwanza akamwona Nuru aliyekuwa ameketi katika meza ya tatu tu nyuma yake, pamoja na wanaume wengine wanne. Nuru alikuwa amevaa katika hali ambayo isingekuwa rahisi mtu yeyote aliyemwona jana kumfahamu. Alikuwa katika suruali ya degrizi,
fulana nyeusi na nywele za bandia. Matiti yake yalisimama wima kama yanayowaringia wanawake wote katika baa hiyo na kumdhihaki kila mwanaume. Sura yake nzuri, yenye macho maangavu ilikuwa kama bahari tulivu ambayo iliwatia wivu wanawake wazuri wa kuvutia wanaume machachari. Kwa muda, Joram alijikuta amesahau kwamba huyo alikuwa Nuru wake, akimsubiri; na badala yake moyo wa tamaa na wivu ukamshika. Akajikuta akitamani kumwendea na kumtoa katika kundi hilo la wanaume wenye kiu kubwa kumgusa. Lakini alipomtazama Nuru na kutoiona dalili yoyote ya kutofahamiana na mwanaume yeyote kati yao akakumbuka kuwa yuko kazini. Akatabasamu kimoyomoyo na kuendelea na safari yake.
Alijipatia chumba kidogo ambacho kiti pekee chumbani humo kilikuwa kitanda. Kando ya kitanda kulikuwa na kijimeza ambacho Joram hakuona kama kilikuwa na kazi nyingine zaidi ya kuwekea nguo. Hewa chumbani humo ilikuwa nzito kiasi kwamba Joram aliifikiria kama hewa iliyojaa dhambi. Kadhalika, kulikuwa na harufu kali ya ukahaba. Ilimchukua dakika mbili tatu kabla ya kuubatilisha uamuzi wake wa kumwalika Betty chumbani humo.
Betty aliingia kikazi. Alikuwa katika mavazi tofauti na yale ya kazi. Hili lilikuwa vazi jepesi, fupi ambalo Joram hakujua aliite gauni au sketi. Liliruhusu mwili wake wa ndani, ngozi inayomeremeta kwa rangi yake ya kunde, na mapaja laini, mekundu, yawe kama siri isiyohitaji kuwa siri katika mavazi hayo. Sura yake nzuri ilizidi kuwa nzuri kwa tabasamu lililochanua ghafla usoni mwake. “Bwana wangu mzuri… una bahati wewe?... utafurahi…” Betty alisema huku akijifungua fundo moja nyuma ya mgongo wake ambalo lilifanya gauni hilo lifumke na kuwa kipande kimoja cha kitambaa kilichoteleza toka mwilini mwake na kumwacha kama alivyozaliwa. “Siku ya leo… hutaisahau…” alisema akimsogelea Joram.
Naam, ilikuwa sura ambayo ilitosha kabisa kuufariji ubongo uliochoka kwa kusoma aina mbalimbali za vitabu, uso ambao ulibebwa na umbo ambalo ni burudani kamili kwa fikra za mtu ambaye muda mwingi wa maisha yake aliutumia kuandika burudani za watu wengine, mtu kama hayati Patauli Kongomanga. Hayo yalipita katika kichwa cha Joram pindi akiendelea kujiuliza ama hisia zake zilikuwa kweli kuwa huyo ndiye
aliyekuwa hawara au mpenzi wa Patauli. Kadri anavyowafahamu waandishi walivyo watu wanaoishi katika ndoto za ajabuajabu, na wanaopenda kufanya maisha halisi kuwa ndoto na dunia sehemu tu ya ndoto hiyo; aliamini kuwa hata mapenzi kwao ni ndoto ya mahaba, ndoto isiyo na upande wa pili ambao ni dhiki na maudhi. Nani ambaye angefaa kuikamilisha ndoto hiyo zaidi ya mwanamke, mzuri aliyehitimu katika kila fani ya kumstarehesha mwanaume? Mwanamke ambaye kula yake inategemea jitihada na mafanikio yake kitandani. Na ni yupi mwanamke huyo katika baa hiyo zaidi ya Betty?
Betty ambaye sasa alikuwa kajilaza chali kitandani, macho kayalegeza huku kwa sauti ndogo ya huba akinong’ona, “Njoo… Nadhani naweza kukuamini… Malipo baadaye…”
Ilikuwa picha ya aina yake, picha inayotisha na kupendeza kwa wakati mmoja, picha inayoshawishi na kuvutia, moja kati ya zile picha ambazo hufanya akili ya mwanaume ihamie kisogoni na kujikuta ikifuata matakwa ya mchezaji katika jukwaa, badala ya akili yake timamu. Hata hivyo, haikuwa picha mpya kiasi hicho kwa Joram Kiango. Alichofanya ni kuendelea kusimama katikati ya chumba hicho, akiimalizia sigara yake. Kisha, kwa sauti tulivu alisema, “Vipi Betty… sikujua kama nawe hu shemeji kula.”
“Kwani vipi jamani?” Betty aliuliza kwa mshangao kidogo. “Mimi ni shemejio,” alieleza. “Nilichohitaji ni kuzungumza
nawe tu.”
“Kuzungumza!” Betty alifoka kike. “Kuzungumza! Wakati wenyewe wanasubiri nusu ya chochote utakacholipa! Wewe vipi kaka! Unajua niliondokea kukuheshimu sana?” akasita kidogo. Kisha, “Kwanza yamekuaje hayo ya shemeji! Kwa nani?”
“Hayati Patauli… alikuwa rafiki yangu mpenzi…”
Betty alimkatiza kwa ukali kidogo, “Mwongo! Nipishe niende zangu. Kumbe nawe u mmoja wao! Hamchoki kunifuatafuata? Nipishe…”
Kiasi Joram alishangaa kidogo. Hakutegemea kama ingekuwa rahisi kiasi hicho. Alichotegemea hasa ungekuwa ubishi mwingi na Betty kujifanya hamfahamu kabisa marehemu. Baada ya ubishi huo angeambulia kununua ukweli au uongo ambao angeuchambua na kuungaunga hata apate uchochoro aliokuwa akiuhitaji. Hata hivyo, hiyo pamoja na urahisi huo, hisia fulani zilimfanya Joram ahisi kuwa ukali katika sauti ya Betty ulikuwa
wa bandia na hata maneno hayo aliyatamka kama aliyeyakariri kwanza. Hivyo, alimtazama kwa makini pindi akijifunga vazi lake taratibu na, hatimaye, kuanza kutoka.
“Usiwe na haraka kiasi hicho bi Betty,” Joram alimshika mkono. Akamwambia taratibu, “Nimekuita tuzungumze tu juu ya marehemu, mpenzi wako. Nipo tayari kuilipia kila dakika ambayo nitakupotezea. Au hujui kuwa alikupenda sana?”
Betty alimbetulia macho na kumtazama Joram kwa makini zaidi, “Alinipenda ndiyo… mie pia nilimpenda… lakini wewe ni nani? Watu wengi sana wamekuwa wakinifuatafuata kwa maswali ambayo hata sielewi yanaelekea wapi. Hata nahofia maisha yangu sasa. Sijui wanataka kuniua kama walivyomwua yeye…”
Ilikuwa nafasi ambayo Joram asingeipoteza. “Unadhani ni kweli walimwua?”
“Bila shaka,” Betty alifoka. Kisha, dalili za hofu ziliurudia uso na sauti yake alipouliza tena, “Wewe ni nani? Sijisikii vizuri kuzungumza na mtu nisiyemfahamu.”
Hisia ziliendela kumfanya Joram ajione kama anayechezewa akili zaidi ya anavyomchezea yeye. Bado Betty alikuwa kama anayeigiza mchezo ambao alikwishaufanyia mazoezi kwa muda mrefu. Hilo lilimfanya Joram aamue kujitokeza toka kichakani na kuingia hadharani. “Sikia Betty. Mimi ni mgeni katika nchi hii. Nimetoka nchi ya mbali sana kukufuata wewe ili unieleze chochote unachojua juu ya maisha na kifo cha mpenzi wako, Patauli. Unaonaje ukiketi chini na kunieleza kwa tuo?”
Betty alitabasamu kidogo kabla ya kumjibu, “Sura yako inanifanya nijisikie kukuamini ingawa roho hainiruhusu. Nadhani hujui, tangu alipofariki nimekuwa nikifuatwa na watu mbalimbali na kuulizwa maswali tofautitofauti. Wote huanza kwa kunitaka mapenzi na tunapofikia chumbani huishia kunitupia maswali mazitomazito. Wote hujifanya rafiki wa hayati Patauli. Wengine wamediriki hata kunitisha kwa sababu nisiyoielewa. Hata nimekuwa simjui nani rafiki nani adui yake.” Akasita na kumtazama Joram kwa wizi. “Kwa hiyo, kaka, nashindwa kujua nikuweke katika kundi lipi.”
‘Mwanzo mzuri!’ Joram aliwaza. “Huitaji kuniweka katika kundi lolote. Kama nilivyokwambia mimi ni mgeni tu nchini, ambaye niliondokea kuvutiwa na mtindo wake wa uandishi. Kifo
chake cha ghafla, nchini mwetu, kilinifanya niwe na shahuku
kubwa ya kuelewa kilivyotukia.” “Umetokea Tanzania?” “Hujakosea.”
“Unaitwa Joram Kiango?”
“Hauko mbali sana na ukweli.” Kisha Joram aliliweka usoni tabasamu lake ambalo anaamini ni moja kati ya silaha zake kali kwa wapenzi na maadui. “Ndiyo. Wananiita Joram Kiango. Bila shaka marehemu alikuwa akinitaja sana katika maongezi yake.”
“Hapana, alikutaja katika ndoto,” Betty alimfahamisha. “Sijakuelewa… ndoto vipi?” Joram aliuliza.
“Aliwahi kukutaja usingizini,” Betty alifafanua. “Wakati ule ambapo alikuwa mtu aliyebadilika sana na kuwa mkimya, msiri, mwenye wasiwasi sana. Katika usingizi wake wa mchana aliwahi kuweweseka akitamka mambo mengi. Mojawapo lilikuwa jina lako.”
“Alisemaje?”
“Sikumbuki vizuri. Lakini ilikuwa kitu kama… nitakwenda Tanzania… Joram kiango anafaa…” mambo kama hayo. Sikuelewa maana yake hadi baada ya kusikia kuwa amefia Tanzania.”
Joram alimtazama kwa makini zaidi. Maongezi hayo yalimvutia kuliko alivyotegemea. Alijihisi kama anayekunywa chai iliyozidi sukari. “Mambo gani mengine aliwahi kuongea ndotoni Betty?”
“Mengi tu,” Betty alieleza, “Alikuwa kama anayeropoka tu, kama ambaye alianza kuharibikiwa na akili. Siku hiyohiyo alisema vitu kama … Waziri Mkuu…. Kumwaga damu… kwa ajili ya mapenzi… hapana… nani ataamini… Joram’ “Maneno kama hayo kisha ghalfa Betty aliinuka na kumtazama Joram kwa hofu. “Nafanya nini?” aliuliza. “Haya ninayoyazungumza kwako sijapata kumwambia mtu yeyote. Nadhani ni haya yaliyomwua. Tafadhali usiniulize zaidi.”
“Sikiliza Betty,” Joram alimwambia. “Bado nahitaji sana kuzungumza nawe. Nadhani utanisaidia sana.”
“Basi sio hapa,” lilikuwa jibu la Betty. “Waonaje nitakapomaliza kazi tukilala wote tuzungumze kwa urefu. Nina chumba changu ambacho hakina bugudha wala kupigiwa hodi.”
“Leo si rahisi, Betty. Labda tukutane kesho wakati huko kazini, tupange kwa ukamilifu na kuzungumza kwa marefu na
mapana.”
“Vizuri… saa ngapi? Unajua sisi tunaoishi kwa kuuza miili yetu hatuna muda wa kutosha? Lazima uwe na ahadi za kiungwana. Ukichelewa hunikuti, ukiwahi hunipati. Saa ngapi?”
***
Saa nne ya asubuhi hiyo ilimkuta Joram akiwa mtaa wa pili toka hotelini hapo. Alisimamisha teksi ya kwanza ambayo ilisimama na kumchukua. Akampa dereva jina la mtaa na namba ya nyumba aliyohitaji. “Mapalala, jengo la Edward namba 104. Fanya mwendo wa kiume rubani,” alimweleza.
Haikuwa kazi kubwa kwa Joram kumtoroka Nuru. Alimwacha kitandani, akaingia bafuni ambako alioga na kupiga simu kwa wahudumu akiomba chai iletwe chumbani humo. Kisha, alifanya kama aliyekumbuka kitu, akainuka na kutoka. Akawa ameondoka. Nyendo za mchana zikiwa nje ya kawaida yao tangu walipofika katika mji huo Nuru hakuwa na sababu yoyote ya kushuku kuwa anaachwa.
Uamuzi wa kumtoroka Nuru ulimjia usiku wa jana baada ya kumaliza maongezi yake na Betty kwa ahadi ya kukutana mchana huo na kurudi ambako alimkuta Nuru katika kundi la wanaume walewale. Wakiwa wamelewa kiasi, kila mmoja alianza kuonyesha dalili ya kumtaka Nuru kwa heri au shari, hali ambayo ilimfanya Nuru ainuke na kutoka zake nje. Joram alimfuata huko na kumshika mkono huku akimwambia, “Leo mwisho kujiuza kwa bei rahisi kiasi hicho.”
Nuru alimgeukia na kumwambia kwa mzaha, “Nimekubali baada ya kushuhudia ukiukataa mwili mzuri wa msichana mzuri kama yule. Nimeanza kukuamini Joram…”
Ndiyo kwanza Joram akafahamu kuwa Nuru alimnyemelea na kumchungulia. Pamoja na kwamba Nuru hakuwa na nia mbaya, bado Joram alifahamu madhara mengi ambayo yangeweza kusababishwa na mzaha au mapenzi katika kazi kwa visingizio vya “Usalama wako.” Ndipo akaamua kumtoroka Nuru katika kila safari ambayo ingekuwa na umuhimu katika upelelezi wake, alikuwa na hakika kuwa angejifunza mengi ambayo yangemsaidia kujua kitu gani anatafuta.
Gari lilimteremsha robo saa kabla ya muda alioahidiana na
Betty. Hakuwa tayari kufuata matakwa ya Betty ya kufika kwa
muda uliopangwa kama angekwenda msikitini au kanisani, kwani moja kati ya mambo ambayo anayathamini katika maisha ya mpelelezi ni tabia ya kutomwamini mtu yeyote na kumshuku kila mtu, hata marehemu. Kupanga muda ni kati ya makosa makubwa. Unaweza kuwa unashirikishwa kupanga muda wa kifo chako. Hivyo, ni vizuri kukifumania kifo kikijiandaa kukuchukua au kukichelewesha kidogo. Ubovu wa gari na uzembe wa dereva kwa kutojua vyema ramani ya mji huo ndio uliomfanya aipoteze robo saa nyingine.
Kilikuwa kitongoji ambacho kilikuwa na haki ya kumshukuru Meya wa Jiji hilo kwa kukikumbukakumbuka. Mitaro ilikuwa safi, barabara ya kuridhisha na taa za barabarani zilienea kila upande. Nyumba nyingi katika mtaa huo zilikuwa za kuridhisha. Hata wakazi wake walikuwa na dalili nyingi za “Hatujambo” kuliko vingine vya mji huo ambavyo Joram aliwahi kuvitembelea. Watu hao, wake kwa waume, walipita katika shughuli zao, bila kumtupia jicho la pili Joram ambaye tayari alikuwa akipiga hodi mlango wa nyumba aliyoihitaji.
Ilikuwa nyumba kubwa, yenye zaidi ya vyumba ishirini. Mlango ulifunguliwa na msichana ambaye kitabia alikuwa ndugu yake Betty. Lakini baada ya Joram kumtaja msichana huyo alilimeza tabasamu ambalo alikuwa amekwishaliumba usoni mwake. Kwa sauti ya kebehi alilalamika, “Kila mtu anamtaka Betty… mgejua alivyo malaya wala msingejisumbua. Mwanamke gani ambaye halali bila ya wanaume kumi kumshughulikia?” baada ya maneno hayo alirudi chumbani kwake na kufunga mlango wake kwa nguvu.
Kabla Joram hajajua afanye nini mlango mwingine ulifunguka. Uso mwingine wenye dalili za mapigo ya Betty ukachungulia. “Ni wewe unayemtaka sio?” aliuliza bila ya kusalimu. “Sijawahi kukuona hapa. Utawezana naye? Sasa hivi ameingia ndani na mwanaume. Kama utasubiri zamu yako njoo chumbani. Huwezi nenda zako… haturuhusu watu kukaa ukumbini. Mtatufukuzia baraka.”
Ilimlazimu Joram kutabasamu. Alishindwa kufahamu ni mtu gani au shirika lipi hili lililojenga nyumba kama hii na kuwapangisha watu ambao kitabia walifanana kama pacha. Badala ya kujibu alifuata mlango ambao wote walikuwa wakielekeza macho yao na kugonga. Hakuitikiwa. Akagonga
tena. Bado hakuitikiwa. Alipoitazama saa yake ilikuwa dakika tano kabla ya muda ambao waliahidiana na Betty. Akaujaribu. Mlango ukafunguka taratibu na kumruhusu kuingia chumbani, chumba ambacho pia kilitumika kama ukumbi wa maakuli na maongezi.
Picha kubwa, iliyoegemezwa ukutani ikiwa katika fremu ya kioo, ilimhakikishia Joram kuwa hakupotea. Katika picha hiyo Betty alikuwa kavaa sidiria na chupi peke yake, akiwa kakalia mwamba wa jiwe kando ya mto mkubwa. Kwa mbali, wavuvi wawili wakiwa ndani ya mtumbwi wao, walionekana wamesimama wakimwangalia. Ikiwa picha ya miaka miwili au mitatu iliyopita, akiwa hana madoido mengi ya kuongeza uzuri mwilini mwake, Joram aliona jinsi Betty alivyowahi kuwa msichana mzuri. Kama madoido yalikuwa yamemuongezea kitu mwilini, basi nyongeza hiyo haikuwa chochote zaidi ya kuutia dosari uzuri wake.
Macho ya Joram yalipoikinai picha hiyo yalitambaa chumbani kote, yakapima hiki na kile. Ziara ya macho hayo ilipokoma, ilimfanya Joram kubakiwa na hakika kuwa Betty hakuwa akifanya biashara ya kujiuza kwa shida, labda alikuwa na silika ya kupenda wanaume. Kitanda chake kiligharimu pesa za kutosha kuwekea msingi wa nyumba, redio yake ilimeza mishahara ishirini ya kima cha chini, makochi yangetosha kabisa kumfanya awe na pikipiki na zulia lingemwezesha kumiliki gari dogo. Juu ya kijimeza cha kando kulikuwa na simu, kando yake kabati ambalo lilikuwa limefunikwa na vitabu anuwai. Kwa mbali, Joram aliweza kuyaona majina ya waandishi kama James Hadley Chase; Harold Robbin; Mario Puzo na wengine.
Vitabu vyote humo vilikuwa katika hali ya vuruguvurugu ambayo ilimfanya Joram ahisi kwamba Betty alichelewa kuamka na hivyo, hakuwa mbali. Akajituliza juu ya kochi kumsubiri. Subira yake ilipungua baada ya kuteketeza sigara mbili bila ya kumwona mwenyeji wake. Akainuka na kuanza kuchungulia huko na huko. Jikoni hakukuwa na mtu. Akagonga mlango wa bafuni. Haukuitikiwa. Akasita kabla ya kuufungua na kuchungulia. Macho yake yalivutwa moja kwa moja na beseni la kuogea.
Kama angekuwa mtoto mdogo angecheka kwa kumwona mtu akioga katika maji ya rangi, maji mekundu. Lakini utu uzima wake ulimfanya agutuke kidogo na kisha kulisogelea sinia hilo.
Yeyote yule aliyeifanya kazi hiyo alikuwa hodari sana wa kazi yake. Betty alikuwa na jeraha moja tu, dogo sana, katika ubavu wake wa kushoto. Kitu chochote kilichoingia katika jeraha hilo kiliufikia moyo na, hivyo, kufanya damu itoke nyingi kuliko ilivyohitajika. Ustaarabu mwingine wa mwuaji huyo ni jinsi alivyomlaza marehemu katika sinia lake kwa uhakika hata tone moja la damu lisidondokee sakafuni.
Kiasi, Joram alisikia kichefuchefu. Haikuwa picha ambayo aliitarajia hata kidogo. Akamtazama marehemu kwa muda, kisha akarudi sebleni ambako aliduwaa akijiuliza kwa nini Betty ameuawa. Ni kweli kuwa maongezi yake ya jana usiku na ahadi yao ya kuonana leo ndiyo kisa cha mauaji hayo? Betty alikuwa na lipi la haja? Na ni nani huyo ambaye alikuwa akizichunguza nyendo zake kiasi hicho hata kumwua mtu pekee ambaye alielekea kuwa nyota pekee katika anga hii yenye kiza cha kutisha?
Hasira zikachemka katika ubongo wa Joram. Kwa hasira hizo akatabasamu. Sasa asingelala usingizi hadi amegundua jambo gani linatukia katika nchi hii. Mara akainuka na kuanza kupekuapekua katika makabati na masanduku ya Betty. Alikuwa na hakika kuwa mwuaji asingeacha kuharibu kitu ambacho kingemsaidia katika upelelezi wake. Hata hivyo, aliendelea kutafuta, ingawa hakujua anatafuta nini. Aliangalia hiki akaacha, akasoma kile na kuacha akashika hiki. Mara simu ikalia na kumkatiza. Aliitazama kwa mashaka kidogo, moyo ukimshauri aache kuipokea. Moyo mwingine ulimshawishi kupokea. Pengine ingemsaidia kuisikia sauti ya binadamu yeyote ambaye alihitaji kuzungumza na Betty.
Akainua mkono wa simu na kuitikia akiitaja namba iliyoandikwa kwenye simu hiyo.
“Nani mwenzangu?” sauti iliuliza. “Wewe unamtaka nani?”
Kimya kifupi kilifuata. Kisha, sauti hiyo ilizungumza tena. “Wewe ni Joram Kiango?”
“Kama ndiye?”
“Sikiliza…” sauti hiyo ilinguruma. “Unasikia, Joram? Unajua unachokitafuta? Unatafuta kifo chako.”
Baada ya maneno hayo simu ilikatwa. Joram akatua yake na kutabasamu kidogo. Hili lilikuwa tabasamu la furaha. Ilikuwa
hatua moja mbele, hatua ya ushindi. Kama aliyepiga simu hiyo alikusudia kumtisha, basi alikosea sana. Alichofanya ilikuwa kumtia ari na matumaini zaidi. Adui anapoanza kukutisha ameanza kukuogopa.
Akarudia upelelezi wake. Hakupata chochote cha haja. Wakati akikaribia kukata tamaa, karatasi moja ilidondoka toka chini ya matandiko aliyokuwa akiyafunua. Alipoigeuza alishangaa kukuta ni picha. Ilikuwa ni picha yake ya siku mbili tatu zilizopita. Hilo lilimshangaza. Vipi Betty ambaye wamefahamiana jana tu awe na picha yake? Na vipi aifiche kiasi hicho? Zaidi alipigwa lini picha hii bila ya yeye mwenyewe kujifahamu?
WAZIRI Mkuu… kumwaga damu… kwa ajili ya mapenzi… Hayo yalikuwa maneno pekee ya haja kati ya yote ambayo hayati Betty aliyatamka. Kama angekuwa hai
hadi sasa, au endapo kifo chake kingekuwa cha kawaida maneno hayo pia yangeweza kuwa ya kawaida au uzushi tu. Lakini sasa amekufa. Hapana, ameuawa! Yawezekana kuwa maneno hayo au mengine ambayo angeweza kutoa yakawa ndiyo kisa cha kifo chake? Haiwezekani kuwa amechinjwa na mwuaji wa kawaida kwa sababu zake binafsi? Wangapi ambao wameua hata wana wao bila ya sababu? Lakini, kuna ile simu… na ile picha…
Hayo yalielea katika kichwa cha Joram wakati akirudi nyumbani baada ya kuiacha nyumba hiyo ya maafa kwa siri. Aliamua kutembea kwa miguu ili apate wasaa wa kuyatafakari hayo yaliyokuwa yakitendeka. Jitihada zake zote za kuwaza na kuwazua zilizidi kumdidimiza katika shimo lenye kiza kizito lisilo na nuru wala mwanga wa kutokea.
Kwanza, mtu atoke mbali aje kufia mikononi mwako, akuambie kuwa unaitwa na Rais! Rais akatae, kisha akuombe uendelea na upelelezi. Mtu wa kwanza mwenye uwezekano wa kukupa habari auawe dakika chache kabla hujamfikia. Kisha, ije simu, ikikutishia ili uache uchunguzi wako. Katika upekuzi wako uikute picha yako ikiwa imefichwa humo ndani. Hujui ilifika vipi.
Kitu pekee ambacho kilimtia Joram moyo katika suala zima ni simu hiyo. Ilimdhihirishia kuwa sio bure, liko jambo. Na asingestarehe hadi angelifahamu. Kwamba maisha yake yangekuwa hatarini, hatari zilikuwa ladha na burudani zake pekee. Zaidi, usalama wake ulikuwa katika kugundua ukweli wa jambo hilo kuliko kuukimbia kwani, kwa namna moja au nyingine, aliwishajiingiza katika mkasa huo. Mtu yeyote angefanya mauaji hayo kumchinja kama alivyomfanyia Betty, hawezi, wala kumpa sumu kama Patauli sio rahisi, lakini asingesita kumzawadia risasi ya kichwa wakati wowote atakapoona hana budi. Zaidi, kifo cha Betty yeye, akiwa mtu wa mwisho kuonekana akiingia kwake, kabla maiti yake haijagunduliwa, kwa tabia ya polisi angekuwa mtu wa kwanza kushtakiwa. Na asingekuwa na lolote la kujitetea, wala muda wa kukaa mahabusu kwa miaka kusubiri polisi hao wavivu wampate mwuaji wa kweli au Rais akutetee. Kwa kila hali alilazimika kuanza msako kwa nguvu zaidi. Dawa ya moto ni moto.
‘Waziri Mkuu… kumwaga damu….’ Aliyakumbuka tena maneno ya Betty. Bado hakuona kama yalikuwa na kichwa au miguu. Wala hakujua kama ‘Waziri Mkuu’ lilikuwa jina la mtu, jina la kikundi cha majambazi au cheo cha mkuu wa kikundi cha majambazi. Pengine Betty angeweza kumsaidia kupata walao fununu, lakini amekufa! Joram alifahamu Waziri Mkuu mmoja tu katika nchi hii. Mtu wa pili kwa madaraka serikalini, mtu mkubwa sana. Ni yeye anayeweza kuwa tishio kwa Rais na taifa lake? Ni yeye ambaye anaweza kuwa nyuma ya mauaji haya ya kinyama? Anachotaka ni kipi? Ukuu wa nchi?
Yalikuwa maswali yaleyale ambayo yalimfanya apige hatua moja mbele moja nyuma, maswali ya kupoteza muda. Mtu ambaye angemsaidia alikwisha kufa. Iliyobaki ni yeye mwenyewe kupambana. Njia ilikuwa moja tu, kumwona Waziri Mkuu. Lakini mtu huenda vipi kwa mtu mkubwa kama huyo na kumshutumu kwa mauaji? Na kama kweli ni mwuaji kiasi hicho si atakuwa anajipeleka mwenyewe katika domo la simba lililo wazi, likimsubiri?
Hapana… lazima aende. Walao kumwona tu.
Alipofika hotelini alimkuta Nuru ameamka kitambo na sasa ameketi kitandani kwa namna ya mtu mwenye wasiwasi na maswali mengi kichwani. Joram alimwendea na kumbusu
shavuni. Nuru hakuonekana kulipokea busu hilo. Busu la pili vilevile halikuzaa matunda yoyote. Joram akacheka na kumwachia. Akaamia kwenye kochi ambako aliketi na kuiwasha sigara yake.
“Huna haja ya kununa. Mke mwenzio amekwishakufa.” “Nani?”
“Betty… Yule msichana wa jana.”
Macho ya mshangao yakamtoa Nuuru. “Amekufa! Amekufaje?” Joram akamweleza kila kitu, pia akampa ile picha aliyoikuta humo ndani. Kwa sauti iliyojaa masikitiko Nuru alinong’ona, “Alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kukusaidia, kama kweli angekusaidia. Kinachonishangaza ni hii picha yako. Aliipataje?
Na kwanini awe ameificha? Kama alikupenda si angeiweka
hadharani tu?”
“Yote hayo tutayajua hii karibuni,” lilikuwa jibu pekee la Joram.
***
Waziri Mkuu, Shubiri Makinda alikuwa mtu mwenye historia ndefu kama ilivyo historia ya nchi hiyo ya Pololo, kama si zaidi. Jina lake lilijitokeza katika kila orodha yenye majina mashuhuri ambayo yalihusika kwa njia moja au nyingine, tangu zilipoanza ndoto za uhuru; ndoto zilipotukia kuwa kweli na hadi sasa ambapo serikali huru ilikuwa ikijitawala. Mara nyingi jina hilo lilifuata nyuma ya lile la Shangwe, ingawa mara nyingine lilihama na kushuka chini ya orodha. Kwa sasa lilikuwa la pili kutoka juu.
Hayo Joram aliyaona tena baada ya kuanza utafiti wake juu ya nchi na siasa ya nchi hii, hasa akiitafuta nafasi halisi ya Waziri huyo. Haikuwa kazi kubwa kujipatia vitabu vingi ambavyo vimeyaelekeza yote hayo kwa mapana na marefu. Hata hivyo, kama alivyotegemea humu, yote yalikuwa mema yaliyompamba Shubiri Makinda kama mtu mtukufu na mtakatifu sana, ambaye hakuwa mbali sana na malaika. Siku zote alikuwa shujaa, mwenye hekima za ajabu, mpenzi wa nchi na wananchi, mwaminifu kwa Rais, asiye na tamaa wala ndoto za kibinafsi na kadhalika. Kalamu za waandishi wote, walao kwa kukosea, hazikumchora kama binadamu wa kawaida ambaye anaweza kupotoka wala kuropoka.
Kitu pekee kilichomsisimua Joram katika maandishi hayo
duni ni pale aliposoma kuwa Shubiri na Rais Shangwe walikuwa marafiki tangu wakiwa shule ya msingi, kwamba tangu hapo walikuwa pamoja katika kila darasa na kila chuo hadi walipokwenda ng’ambo ambako walirudi na ndoto za uhuru.
‘Yawezekana kuwa madaraka aliyonayo shubiri yanatokana na urafiki wa Rais Shangwe kutokana na tabia ya viongozi wengi wa Afrika kupeana vyeo kama zawadi? Joram alijiuliza wakati akiendelea na uchunguzi wae.
Baada ya kupitia vitabu vyote vilivyoelezea historia ya maisha yake alianza kusoma vile ambavyo viliandikwa na Shubiri mwenyewe. Alikuwa ameandia kitabu kimoja tu kwa lugha ya kiingereza: This way Men. Vingine vyote vilikuwa ni mkusanyiko wa hotuba zake mbalimbali. Katika maandishi hayo Joram aliipata picha ya Shubiri kama mtu mwenye ndoto zote za kujenga nchi ya Ujamaa ingawa mara nyingi aliepuka kutaja Ujamaa huo kwa jina. Zaidi, alionyesha kama mtu ambaye alikuwa akiwalilia watu na taifa zima liongeze juhudi na moyo katika kuinua uchumi, elimu ushirikiano na kujitegemea kikamilifu. Ilikuwa dhahiri kuwa hakuridhika na mafanikio ya nchi yake katika kila fani, akiamini kuwa wangeweza kufanya vizuri zaidi. Katika maandishi hayo Joram hakuona kile ambacho alizoea kukiona katika vitabu na maandishi ya viongozi wengi wengine, tabia ya kuwatupia lawama mfanyakazi na mkulima, kama kwamba wangefanya hivi ingekuwa hivi… na kadhalika. Shubiri alielekea kama mtu aliyesimama njia panda akiangalia kila upande, jambo ambalo lilimfanya Joram ajikute akisahau kuwa anamchunguza Shubiri kama adui na badala yake akaanza kumpenda, mapenzi ambayo yalitoweka mara moja alipopata jalada lenye picha mbalimbali za Waziri Mkuu huyo toka katika ofisi moja ya chama.
Picha zote zilimwonyesha Shubiri kama mtu mkatili asiye na muda walao kumwonyesha meno mpiga picha ili wasomaji wa magazeti waone kuwa anacheka. Karibu picha zote alikuwa mkimya, mtulivu, aonekanaye kama aliyenuna. Kwa nadra sana, kama picha mbili tatu, Joram aliona dalili za tabasamu katika uso wake. Hata hivyo, tabasamu hilo lilikuwa kitu kingine kilichoyavuta macho ya Joram. Lilikuwa tabasamu lililoficha au kufichua kitu kama msiba au maombolezo katika fikra au moyo wake. ‘mtu mwenye jina kubwa na maisha mazuri, mtu anayepokelewa kwa hadhi ya kifalme popote duniani; mtu wa
pili kwa ukubwa, katika nchi nzima yenye mamilioni ya watu, vipi awe na msiba rohoni mwake? Mungu ampe nini zaidi?’ Joram alijiuliza.
Aliendelea kuzichunguza picha za Shubiri. Pamoja na kutokuwa na furaha, Joram aliridhishwa na sura yake yenye paji pana la uso, ndevu fupi zilizokizunguka kidevu kinene kilichojaa na kukizingira kinywa ambacho kilionekana kuafikiana na pua yake ndogo nyembamba. Umbo lake refu nene lenye dalili zote za ukakamavu lilikubaliana na suti zake nyeusi ambazo alipendelea kuvaa, suti ambazo zingependeza zaidi kama kando yake kungekuwa na aina fulani ya mavazi ambayo… kama…
Mara Joram akakumbuka kitu kipya. Wako waliosema kuwa nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa huwa yuko mwanamke. Katika watu waliofanikiwa Shubiri yu miongoni mwao. Kati ya maandishi yote aliyosoma hakukumbuka kuona kitu chochote juu ya ndoa au talaka ya Shubiri. Wala katika picha zote hakupata kuona maelezo yoyote ya mtu na mkewe. Vipi? Shubiri hajaoa? Kisa na mkasa?
‘Waziri Mkuu… kumwaga damu…. Kwa ajili ya mapenzi….’ Maneno ambayo hayati Betty alidai kuyapata toka katika ndoto za mpenzi wake, Patauli Kongomanga, yalimrudia akilini. Mapenzi! Mapenzi yapi? Kitu mapenzi hakikuwemo kabisa katika historia yote ya Shubiri, iliyoandikwa.
Lakini kuna historia ambayo haikuandikwa. Kila binadamu ana mambo yake ambayo angependa kufa kuliko kuyaona yakiandikwa na kusomwa hadharani. Bila shaka
Shubiri, kama binadamu, anayo yake. Ni hayo ambayo Joram aliyahitaji. Si haya ambayo yamechujwa na kutiwa chumvi na sukari ili yapendeze machoni na masikioni mwa dunia.
Joram aliyahitaji hayo mengine. Mara akaona anapoteza bure muda wake kushinda katika maktaba hiyo kwa saa nyingi siku nenda rudi akisoma kile ambacho ameandaliwa, kama kipofu anayepewa fimbo na kuongozwa njia. Akayabwaga majitabu hayo na kutoka zake nje.
***
Uzee ni maktaba isiyo kifani. Kuna wale wazee ambao historia imewasahau au kuwatupa kando wakati ikiendelea na mkondo wake, wazee ambao utake usitake ni kama punje moja ya
mchele uliomo katika gunia; kulifanya liitwe gunia la mchele. Kwa njia moja au nyingine wameshiriki na kuwa sehemu ya historia wakitazama inavyopita taratibu mbele yao, ikibadili sura na kuneemeka au kumeguka hapa na pale. Japo historia imewasahau wazee hao, lakini wao hawakuisahau. I hai katika fikra na mioyo yao.
Mmoja kati ya wazee hao alikuwa Pondamali Kalulu. Huyu alijaa habari nyingi za kale. Na alizikumbuka kwa uhakika kama kanda ya video ambayo ikishanasa imenasa. Na hakuna alichopenda zaidi ya kusimulia historia hiyo, kutwa kucha. Pengine ni hilo ambalo lilimfanya ajione sehemu ya historia hiyo. Joram alimfikia mzee huyo baada ya kuongea na watu mbalimbali ambao hawakumsaidia sana zaidi ya kulitaja jina la mzee huyo mara kwa mara. Ndipo akafanya safari hii fupi ya kuuacha mji na kuja huku kitongojini ambako alielekezwa nyumbani kwa mzee huyu. “Naandika kitabu cha historia, kitabu hasa. Unajua hivi vyote vilivyoandikwa havina historia kamili? Nataka kitabu ambacho kimeandikwa kwa msaada wa mtu anayeijua historia. Nimeambiwa wewe unaifahamu, Mzee
Pondamali, utanisaidia?”
Ni hayo tu ambayo yalimfanya babu huyo ajikongoje kuwapeleka Joram na Nuru hadi chini ya mti uliokuwa na kivuli kikubwa, mbele ya nyumba yake, ambapo kulikuwa na viti maalumu vya wacheza bao. Walipokwishaketi alitabasamu akiruhusu meno yake manane tu yaliyosalia mdomoni yaonekane. “Kitabu sio, bwana mdogo? Usiwe na shaka kitabu chako kitakuwa na uhakika. Kitanunuliwa kama peremende. Utakuwa tajiri sana. Lakini mimi sitaki pesa. Nimebakiwa na siku chache za kuishi. Huko niendako pesa hazihitajiki,” aliwatupia tena kicheko kingine wageni wake kabla ya kuuliza, “Unataka kuandika juu ya nini?”
Badala ya kufurahi Joram alisikitika kidogo alipomwona mzee huyo alivyokuwa na hamu ya kuzungumza naye. Hakujua kama maongezi yake yangeweza kumpotezea maisha. Tangu juzi Betty alipouwa kikatili kwaajili ya kuzungumza naye Joram alikwishajenga tabia ya hofu sana kwa maisha ya watu. Hakupenda awe kisa cha mauti ya watu wasio na hatia. Kwa bahati mbaya, hakuwa na njia nyingine ya kuwasaida watu bila ya kuzungumza na watu. Hata hivyo, sasa alikuwa akizungumza
na watu ambao alizungumza nao hadharani bila dalili yoyote iwezayo kumwonyesha mtu anayemchunguza kuwa anapeleleza. Wengine alizungumza nao kwa siri sana. Mfano ni huyu mzee. Akiwa na hakika kuwa kuna watu wanaomchunguza kwa makini, wakiwa na silaha mfukoni, waliondoka na Nuru hotelini kwa mwendo wa mtu na mpenzi wake wanaopunga upepo. Huko mbele walipanda basi na kuteremka mahali ambapo walipenya katika uchochoro hadi mtaa wa pili ambako walipanda basi jingine. Hadi kufika hapo walikuwa wamebadili mabasi mara nne.
Kitu kingine ambacho kilimfanya aongeze uangalifu ni tangazo la mkuu wa polisi baada ya maiti ya Betty kupatikana. Mkuu huyo alitokea katika televisheni akisema kuwa mwuaji angepatikana baada ya muda mfupi kwani watu wengi walimwona akiingia chumbani humo na kwamba wasingesita kumtambua mara watakapomwona tena. Aliongeza kuwa wasanii wa polisi walikuwa wakikamilisha michoro inayoonyesha sura za watu mbalimbali ili mashahidi hao waeleze alivyofanana, picha ambayo ingetolewa gazetini. Lakini saa chache baadaye mkuu huyo wa polisi alibadili kauli na kusema kuwa inaaminika muuaji wa mama huyo ni mwendawazimu mmoja ambaye alikamatwa na jisu lenye damu mtaa wa jirani akikusudia kumwua mtu mwingine. Ni hilo lililomshitua Joram. Alijua kuwa mabadiliko hayo yalifanywa kwa ajili yake na mtu mkubwa serikalini. Rais, au mtu wake wa pili kwa ajili ya kumlinda yeye. Lilimsumbua kwa kuona kuna mtu au watu wanaoangalia kila mwenendo na kitendo chake, jambo ambalo si la kupendeza hata chembe katika shughuli kama hizi. Yeye alikuwa mtu wa kujilinda si kulindwa, na hasa kulindwa na mtu ambaye humfahamu; mtu usiyejua ana nguvu kiasi gani na iwapo ni adui au rafiki.
Hali hiyo ilimfanya atembee kwa adhari kama chui aliyejeruhiwa. Watu wa kawaida, wenye macho ya kawaida walimwona kama kijana mwingine wa kawaida ambaye yumo katika matembezi ya kawaida. Aidha, walimwona Nuru kama msichana mzuri mwenye starehe zote akilini na rohoni, fikra zake pekee zikiwa anasa na mahaba. Hawakujua kama wawili hawa walitembea huku miili yao imebeba silaha hatari ambazo zingetosha kuteketeza kikosi cha jeshi ambalo halikufundishwa vizuri. Bastola, silaha ya kawaida, zilikuwa mgongoni mwa Joram
na katika mapaja ya Nuru. Bomu la machozi, hewa ya sumu, vinasa sauti, kamera ndogo za kijasusi pamoja na vikorokoro vingine vilikuwa katika hifadhi nzuri miilini mwao.
Hata hivyo, kitu fulani kilimnong’oneza Joram kuwa iwapo kweli hukumu ya kifo ilikuwa imetolewa dhidi yake, yeyote yule anayeitoa hukumu hiyo alikuwa hakupanga tarehe maalumu ya kifo hicho. Vinginevyo, muuaji asingeshindwa kutumia fursa nyingi zilizojitokeza. Wala isingekuepo haja ya kumwua Betty na kumwacha yeye hai na badala yake kujisumbua kumtisha kwa maneno badala ya risasi. Japo isingekuwa rahisi kumwua Joram kama adui huyo alivyofikiria, lakini bado Joram aliamua kuzidisha uangalifu kwa makini zaidi. Daima macho yake yalikuwa wazi, masikio yakiwa makini na mwili mzima timamu kwa lolote.
“Kitabu chako, bwana mdogo,” Mzee Kalulu alikuwa akiendelea baada ya kujiwashia sigara yake yenye harufu kali. “Kitanunuliwa utashangaa.” Alijiweka vizuri juu ya kiti chake na kuruhusu mapengo yake yaonekane tena kwa tabasamu lake ambalo huko nyuma liliwatesa sana wasichana. “Unajua kuwa nafahamu mambo mengi ambayo hata wazee zaidi yangu hawayafahamu?”
“Kwa mfano,” aliendelea. “Hawa vijana wanaoongoza nchi, kama Rais na baraza lake la mawaziri. Hawa mimi nawafahamu nje ndani. Nazifahamu hata siri zao ambazo kama wangejua kuwa nazifahamu wangeninyonga. Ni siri ambazo wangependa kuzifuta kabisa katika maisha yao.” Alicheka ghafla kabla ya kuuliza, “Unajua kuwa wanachangia mwanamke?”
Mzee hakuhitaji jambo lolote zaidi ya swali hilo kumfanya Joram na Nuru wawe wasikivu zaidi ya walivyowahi kumsikiliza mwalimu yeyote duniani. Hata hivyo, wakiwa watu wanaoifahamu kazi yao vizuri hawakuonyesha dalili yoyote ya kuvutiwa sana na habari au ubaya huo zaidi ya kawaida. “Mwanamke?” Joram aliuliza baada ya kumtazama Nuru na mzee huyo kwa tabasamu. Nani na nani wanaochangia mwanamke?”
“Rais na Waziri Mkuu wake.” “Mwanamke yupi? Hawara…”
“Mke! Mke wao,” Mzee Kalulu alimkatiza Nuru. “Ni hadithi ndefu sana, tamu sana, ya siri sana na ilitokea zamani sana. Wao wanafikiri hakuna mtu anayeifahamu, lakini sisi wazee
ambao tunaona kila kitu tuliona na tunaendelea kuona…” “Wakati huo nilikuwa kijana bado. Wao walikuwa watoto.
Niliwafahamu kwa kuwa mwalimu wao wakiwa darasa la kwanza hadi la nne alikuwa rafiki yangu mpenzi. Alikuwa mwalimu wa ajabu kwa jinsi alivyoipenda kazi yake na wanafunzi wake. Kila nilipotoka zangu nyumbani kwa bwana Pony, aliyekuwa mkuu wa wilaya, mimi nikiwa mtumishi wake nilimkuta Puta, huyo mwalimu rafiki yangu akiwa nyumbani kunisubiri. Tulifuatana kilabuni ambako tulikunywa na kuongea. Wakati huo ukiwa na shilingi mbili utakunywa bia na kuku mzima wa kuchoma, tulijisikia kama tunaoishi peponi. Kila mtu kijijini hapo alituheshimu. Yeye kama mwalimu na mimi mtumishi wa bwana mkubwa. Hivyo, mara nyingi tulilewa kwa kutumia wadhifa badala ya pesa.” Hilo lilimfanya mzee Kalulu atokwe na tabasamu jingine.
“Mwenzangu alikuwa hana maongezi zaidi ya kusimulia mambo ya wanafunzi wake. Huyu hivi, huyu vile, michezo yao, utukutu wao, akili yao darasani na mengineyo. Siku moja alinieleza juu ya wanafunzi wawili ambao anasema siku waliyoanza shule tu, walipigana hata kutoana ngeu, lakini baada ya ugomvi huo sasa ilikuwa imepita miaka miwili wakiwa marafiki, chanda na pete…”
“Watoto hao walikuwa hawaachani popote waendapo. Huyu akitumwa huyu, huyu anatoroka hadi amfuate mwingine. Wala hawanyimani kitu, cha huyu ni cha huyu. Na kwamba kitu kikubwa kilichomfanya mwalimu huyo kuwatia maanani ni akili zao. Walikuwa wakiongoza darasani katika kila mtihani. Huyu akiwa wa kwanza huyu atakuwa wa pili. Wala alama zao hazikutofautiana sana, jambo ambalo lilifanya walimu kushuku kuwa walikuwa wakionyeshana. Lakini baada ya uchunguzi mkubwa ilidhihirika kuwa kila mtu alikuwa na akili zake ingawa wakati fulani walisaidiana.”
“Urafiki wao uliendelea hadi walipomaliza shule ya msingi na kuchaguliwa kwenda sekondari. Huko pia walikuwa katika bweni moja. Huko pia akili zao zilichemka na kuongoza si darasani tu bali katika maongezi ya kawaida na mijadala ya hadhara pia. Walipowekwa katika upande mmoja wa kongamano upande wa pili hawakufua dafu. Na walipokwenda pande mbalimbali ulikuwa ubishi mzito ambao haukuelekea kupata mshindi.
Kadhalika, walikuwa mstari wa mbele katika michezo yote, pamoja na gwaride. Uhodari wao haukuchelewa kuwapitia uongozi mwaka wa pili tu wa maisha yao hapo sekondari, mmoja wao akiwa kiranja mkuu.”
“Nilishangazwa na jinsi mwalimu huyo alivyokuwa akipata habari zao za huko sekondari, iliyokuwa maili kumi na tano toka hapo kijijini kwetu. Lakini yeye aliniambia kuwa kila jumapili watoto hao walimtembelea nyumbani kwake na kumsimulia maendeleo yao. ‘Wangefaa kuwa pacha,’ alikuwa akinisumbua mara kwa mara. Nilipolewa nilimwambia awafanye kuwa pacha badala ya kunipigia kelele.” Alitabasamu akimtazama Joram na Nuru kwa shahuku.
“Ikaja siku ambayo rafiki yangu alikuja na habari mpya zaidi. ‘Wanataka kuoa’ alinieleza. “Nani?” nilimwuliza. ‘Wale watoto,’ alinieleza. ‘Wamepata wachumba kijiji cha Pongwe, si unakikumbuka? Harusi yao itakuwa ya ajabu kama walivyo watoto wa ajabu.’ “Kwa nini?” Alinieleza kwamba wamepata wasichana wazuri sana ambao ni pacha, kwamba watoto hao wamefanana sana ambapo huwezi kuwatofautisha. Wasichana hao wamewapenda sana wanafunzi hao na walikuwa tayari kufunga nao ndoa mara tu wamalizapo shule. Ilisemekana kuwa harusi zao zingefanyika pamoja, siku moja.
“Siku chache baadaye mwenzangu alikuwa na habari nyingine ya kusisimua. ‘Wamekwenda Ulaya kuongeza masomo! Aliniambia kwa furaha kana kwamba ni watoto wake. Sikuwa na haja ya kumwuliza ni akina nani hao. Picha zilitokea siku chache baadaye katika magazeti, wakiwemo miongoni mwa watoto wanane waliokuwa wakienda zao kuongeza masomo nje ya nchi. Wakati huo kwenda Ulaya ilikuwa sawa na kwenda peponi, wajukuu zangu mnaweza kufahamu majina hayo yalivyoongeza uzito!”
Mzee alitulia kwa muda akishughulikia sigara yake. Ghafla, aliwakazia macho Joram na Nuru. Kisha akaangua kicheko kabla ya kuongeza kwa sauti ya majivuno, “Halafu na mie nilipata habari ya kumsimulia rafiki yangu huyo.” Alisita tena. “Ilikuwa baada ya miaka minne tu tangu walipoondoka nchini. Nilimkuta bwana
D.C wakifoka kwa ukali huku majina ya wale watoto wawili. Abdul Shangwe na Shubiri Makinda, yakitajwatajwa. Baada ya kuwasikiliza kwa makini nilielewa kilichowafanya wazungu hao
kuwa na wasiwasi. Kweli, walikuwa watoto wa ajabu. Siku hiyo niliona kama saa haziendi ili nirudi nyumbani kumshangaza rafiki yangu kwa habari hiyo mpya. Saa zilienda taratibu zaidi ya kinyonga. Zilipotimu niliendesha baiskeli kama kichaa hadi nyumbani. Nilimkuta rafiki yangu ndiyo kwanza anafika. “Watoto wako wanataka uhuru,” nilimwambia. Nikamweleza kwa tuo kwamba wamerudi nchini na kuanzisha chama cha kudai uhuru; na jinsi chama hicho kilivyokuwa kinaungwa mkono na watu wengi.
“Ilinishangaza kuona rafiki yangu Puta hakushangazwa sana na habari hiyo. Alichofanya ni kucheka kidogo na baadaye kuniuliza ‘Sikukuambia kuwa ni watoto wa ajabu? Uongozi wao pia utakuwa wa ajabu. Shubiri atakuwa Rais wa aina yake,’ alinieleza.”
Habari hiyo zilifuatwa na pilikapilika za vita vya uhuru. Maneno yakiwa silaha, vijana hao walishangaza ulimwengu kwa jinsi walivyoshinda uongo, hila na vipingamizi vyote vya mkoloni. Waliandamwa pia na vitisho vya kuwekwa gerezani na kutishiwa kufa. Hawakukata tamaa. Mmoja alipowekwa gerezani wa pili alisimama hadharani kulaani unyama huo hata mwenzake akaachiwa. Na alipotoka neno la kwanza lililomtoka mdomoni lilikuwa ‘Uhuru.’ Taratibu, wakati wenye roho nyepesi wakianza kukata tama, dalili za uhuru zilianza kujitokeza.
‘Atakuwa Rais wa ajabu!’ mwenzangu aliendelea kunong’ona. ‘Unajua pamoja na shughuli zake nyingi kila anapopata fursa anakuja kunisalimu?’ aliuliza. Hilo kwa kweli sikulitegemea. Wakiwa watu wenye shughuli nyingi, wasiolala usiku na mchana, huku wakiwindwa na serikali ya mkoloni sikuona vipi wangeweza kupata wasaa wa kumtembelea mzee huyo ambaye licha ya kwamba hana lolote la kuwaambia bado waliachana naye miaka mingi ya utoto wao. “Wanakuja?” nilimwuliza. ‘Anakuja, Shubiri anakuja. Hata usiku wa manane anakuja. Na kila akija ananiletea zawadi, walao ndogo. Juzi kaniletea tochi. Unajua hajabadilika kabisa yule mtoto? Tabia yake bado ileile. Mkimya na msikilizaji kuliko alivyo msemaji. Kila akija nategemea awe na la kuniambia, lakini naishia mimi kumsimulia yeye. Na sijui namsimulia nini. Naona kama anafurahia kuisikia sauti yangu tu.’
“Na siku chache mwenzangu alinitembelea katika hali ya
huzuni na msiba mkubwa. ‘Tuna msiba,’ aliniambia, ‘Tumefiwa na mke wetu,’ “Mke yupi?” nilimwuliza. Alinieleza kuwa mmoja kati ya wale pacha wazuri, wachumba wa Shangwe na Shubiri alikuwa amefariki kwa ajali ya kutumbukia mtoni na kuliwa na mamba. “Ni mchumba wa nani aliyepotea?” nilimwuliza. ‘Hilo ndilo tatizo’ alinijibu kwa huzuni kubwa. ‘Wasichana wale wanavyofanana, hakuna anayefahamu nani alikuwa mchumba wa nani zaidi ya msichana mwenyewe. Nina mashaka hata wazazi wao watapata matatizo hayo. Hofu yangu ni kwamba vijana hawa wanaweza kukosana kwa suala hili. Mwanamke ni ibilisi bwana.’ Nilijaribu kumweleza kuwa vijana hao wana akili nyingi na timamu, kamwe wasingeweza kuharibu kazi na hadhi yao kwa jambo dogo kama hilo, lakini mwenzangu hakuelekea kuniamini sana. ‘Pengine uniambie kuwa kwa jinsi wanavyopendana wote wataamua kumwacha msichana huyo,’ alieleza.
“Miezi kadhaa ilipita. Ikafika siku ambayo harusi ya kufana ilifanyika jijini. Abdul Shangwe alimwoa Tunu Mtoro, rafikiye Shubiri akiwa mshenga. Ilikuwa sherehe kubwa ambayo ilikumbukwa na watu kwa muda mrefu.
“Siku chache baada ya harusi hiyo bendera ya mtu mweupe ilishuka na Mtu Mweusi kuchukua nafasi. Wazungu, machozi yakiwatoka, waliporomoshwa toka madarakani. Kiti cha Gavana kilikaliwa na Shangwe, mtu wa pili akiwa Shubiri. Waliitangaza katiba yao mpya, ambayo ilikuwa nuru kwa Mtu Mweusi. Matunda yake ndiyo tunayaona na kuyala sasa…”
Mzee aliposita ili kuwasha sigara nyingine Joram alipata fursa ya kupenyeza swali. “Mzee, yu wapi huyo rafiki yako mwalimu? Siku hizi hakutembelei?” Joram aliuliza.
“Uzee, baba, uzee umemzidi nguvu. Huu mwaka wa nane sasa sijamtia machoni. Lakini hajafa. Kama angekufa ningepata habari mara moja. Yuko hai katika kijumba chake cha mbavu za mbwa kijiji cha Polo ambacho toka hapa ni mwendo mfupi tu.”
Kisha mzee huyo alishituka kidogo baada ya kulitazama jua ambalo lilikuwa likielekea kuaga. “Mungu wangu,” alifoka. “Saa zimekwisha na wala hatujaanza. Anza kuuliza maswali yako. Unataka kuandika kitabu cha nini vile?”
***
Jua lilikuwa likifikia kiota chake cha magharibi wakati Joram
na Nuru walipomwacha mzee huyo kwa ahadi ya kurudi kesho kuanza kuandika kitabu chao. Nuru ya kawaida ilikuwa tayari imemezwa na ile nzito ya dhahabu ambayo pia ilikuwa ikitoweka taratibu na kiza kuchukua utawala. Joram alilifurahia sana giza hilo. Alikuwa ameushika mkono wa Nuru akimwongoza kama mwenyeji, toka kichochoro hadi kichochoro hata walipofika kituo cha basi. Joram hakupenda kubahatisha. Hivyo, ingawa alikuwa na hakika kuwa hakuweza kuonekana na mtu yeyote wa hatari pindi wakimwendea Mzee Kalulu bado walitumia hila nzito za kujihadhari kwa kubadili magari na kujipitisha huku na huko. Walipoingia jijini walichagua baa nzuri ambayo waliamua kuitumia kwa kupozana koo kwa kutumia bia mbilimbili, ambazo ziliwapa hamu ya chakula; kilichohitaji kuteremshwa kwa bia nyingine.
Ilikuwa yapata saa nne na robo za usiku walipoifikia hoteli yao. Walipofika mapokezi na kumsalimu msichana aliyekuwa zamu aliwapa ufunguo na ujumbe mfupi ambao uliandikwa juu ya kipande cha karatasi ukisema: Mara ufikapo tafadhali nipigie. Joram hakuitaji kuuliza ni nani aliyeleta ujumbe huo bila jina.
Alikuwa na namba moja tu ya simu. Na asingeweza kutumia simu ya ndani. Hivyo, alimtaka Nuru radhi na kurudi nje ambako alifuata kibanda cha simu. Akazungusha namba hizo moja baada ya nyingine.
Sauti ya mtu aliyeipokea haikuwa ngeni masikioni mwake, “Ulikuwa wapi” iliuliza. “Nimejaribu kukupigia mara tatu bila mafanikio.”
“Nilitoka kidogo.” “Kwenda wapi?”
Hilo lilimshangza na kumkera Joram. “Ni lazima ujue kila ninalofanya na popote niendapo?”
“Ndiyo… hapana… lakini unajua hujanipa taarifa yoyote ya maendeleo yako tangu umeanza kazi? Wakati huohuo Napata taarifa za kutatanisha juu yako. Juzi tu ilikuwa uchukuliwe hati kwa kuua mtu. Mimi sikuamini. Nadhani mambo yanatisha kuliko nilivyofikiria awali. Hivyo, nahitaji kupata taarifa yako mara kwa mara. Sawa?”
Joram hakufahamu kwa nini sauti au amri hii ilimchukiza kiasi hicho. Hakuwa mtu wa kuchukizwa kwa vijambo vidogovidogo kama hivyo. Wala hakuwa mtu wa kufundishwa la
kufanya na mtu yeyote duniani. “Sikia mzee,” alijibu. “Nadhani ulipoamua kunipa kazi hii ulikuwa tayari umearifiwa tabia yangu ya utendaji kazi. Sina tabia ya maneno ila vitendo. Vinginevyo, siwezi kusema lolote.”
Joram akasikia pumzi ikishushwa upande wa pili. Ilifuatwa na kicheko kidogo. “Nadhani nazidi kukuelewa, bwana mdogo. Mimi pia sina muda wa kupoteza. Wasiwasi wangu mkubwa ni juu ya maisha yako. Hawa ni viumbe hatari sana. Siwezi kujisamehe iwapo lolote litakutokea kwa uzembe wangu. Hivyo, napenda sana kuhakikisha nyendo zako hazikupeleki hatarini.”
“Usijali mzee, najua kujiangalia. Mie sio mtoto mdogo.” “Nakutakia kila la kheri.”
Simu ikafa masikioni mwa Joram. Akaitua na kurudi hotelini. Nuru alikuwa tayari ametangulia chumbani. Joram akasubiri lift na kumfuata. Alipowasili chumbani hakumwona Nuru kitandani kama alivyotegemea. Bila shaka alikuwa bafuni. Akaamua kumfuata huko, rohoni akifanya sherehe kidogo kwa matumaini ya kumkuta Nuru kama alivyozaliwa; ili naye avue na kuoga naye, jambo ambalo walikuwa hawajalifanya kwa muda mrefu. Nuru katika ngozi ya Nuru, na ulaini wa mwili huo, vingekuwa burudani tosha ambayo ingeikamilisha siku hiyo na kumfanya asahau uchafu wa siku nzima.
Alikwenda bafuni. Na alimkuta Nuru kama alivyotaka, lakini uso wake ulikuwa na kitu ambacho hakukitegemea. “Vipi?” aliuliza akimfuata pale aliposimama akichungulia ndani ya karo. Joram aliyafuata macho ya Nuru. Mara akakiona kilichomfanya uso wake uwe ulivyokuwa. Kilikuwa kipande cha karatasi, kilicholazwa ndani ya karo kikiwa na maneno yaliyoandikwa kwa wino mzito mwekundu: ‘Joram unatafuta kifo chako.’
Joram alifungua bomba la karo hilo kufanya maji yaloweshe karatasi hiyo. Ilipolainika aliichana vipandevipande na kisha kumgeukia Nuru. “Ni hilo tu lililokufanya upoteze uzuri wa sura yako na kuwa mnyonge kiasi hicho? Alimuuliza kwa mahaba.
“Kwako wewe na hili pia ni mzaha?”
“Sio mzaha. Ni dalili ya uoga. Huoni kama wananiogopa hata wanaanza kunitumia vitisho vya kitoto?”
“Joram!” Nuru alifoka akijitoa katika mikono yake alipojaribu kumkumbatia “Usifanye utani Joram. Kama wameweza kuingia hadi huku na kuacha maandishi kama hayo wangeweza pia
kutega bomu ambalo lingetufanya sasa hivi kuwa marehemu.” “Ndiyo,” Joram alimjibu akitabasmau “Ni hapo ninapowaona
waoga. Kwa nini wasitege bomu badala ya kuleta vitisho vya maneno? Pamoja na kumwuliza Nuru swali hilo lilikuwa likimkereketa. Kwa nini watege maneno badala ya bomu?
CONGO ukiuzidisha kwa uongo matokeo yake ni wazimu. Uongo huohuo ukiujumlisha na uongo mwingine matokeo yake ni kitu kilekile cha kutatanisha. Nao ukweli ukiujumlisha na uongo bado jibu utakalopata ni mkorongonyo
wa mambo yasiyo na kichwa wala miguu.
Lakini ukiufanya ukweli uutoe uongo utabakiwa na kitu fulani kinachoeleweka. Ukweli ukiujumlisha na ukweli, utoe uongo, umbeya, unafiki, hila, hisia na mengineyo jibu utakalopata linaeleweka na kukubalika. Daima ndilo linalohitajika.
Hayo yalikuwa yakielea katika ubongo wa Joram Kiango jioni hii, akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu. Nuru, alikuwa ubavuni mwake katika kiti cha nyuma ya gari hili walilolikodi.
Hakuona kama ilikuwepo njia nyingine ya kuikamilisha kazi iliyokuwa mikononi mwake bila ya kumwona, kumsikia na kumsikiliza Waziri Mkuu huyo. Kila alichopata kilimfanya azidi kumshuku. Kumsikia tu ndiko ambako kungemfanya ama athibitishe au ayapuuze mawazo yaliyoanza kujengeka kichwani mwake. Ndiyo, Waziri huyo kama binadamu wengine, hasa akiwa kama anavyofikiriwa, asingekosa kuwa na sehemu yake ya uongo pamoja na ile ya ukweli. Baada ya kuipata akiba nyingine ya uongo kama hiyo na ukweli ndipo Joram angekalia meza na kuanza tena mahesabu ya ukweli toa uongo, zidisha
na hisia gawanya kwa hakika na kadhalika. Alikuwa na hakika kabisa kuwa baada ya kazi hiyo kama asingeiona siri iliyofichika basi angeiona njia ambayo ingemwongoza kuifikia.
Safari hii ya kumwendea Waziri Mkuu kiasi ilikuwa kama ya uvamzi. Aliamua kuifanya bila taarifa kwa hofu ya kumfanya ajiandae na kumpokea kiungwana. Joram alipenda kuwapata wasailiwa wake kabla hawajajiandaa. Alichofanya ilikuwa kumnong’oneza Nuru taratibu, “Leo tunamtembelea Shubiri Makinda.”
“Saa ngapi?” “Sasa hivi.”
Dakika mbili baadaye wakawa ndani ya teksi hii ambayo iliendeshwa kwa mwendo wa kistaarabu. Dereva wake, kama walivyo madereva wengi wa teksi, alikuwa mtu mwenye hamu sana ya maongezi, aliongea juu ya kila lililomjia kichwani. Siasa, uchumi, utamaduni, mapenzi, ujambazi na hata yale ambayo hayakumuhusu. Joram na Nuru hawakumtia moyo sana, kwa jinsi ambavyo hawakujiingiza katika maongezi hayo kikamilifu kama alivyotaka. Walichofanya ilikuwa kutia kicheko au neno moja moja ili aendelee. Kimawazo walikuwa mbali sana.
Joram alikuwa akifikiri vipi atakavyomkabili waziri mkuu huyo na kumfanya aseme chochote, licha ya uongo. Si rahisi kumwendea Waziri Mkuu, ambaye fununu zinaonyesha kuwa kwa sababu moja au zaidi anakusudia kumwangamiza Rais wake. Umfikie mbele na kumwuliza maswali ya kijinga. Hiyo isingetofautiana sana na kutia kichwa katika domo la mamba mwenye njaa. Madamu haikuwepo njia nyingine, kazi ya Joram ilikuwa kumfanya azungumze. Hilo ndilo lililomfanya asifanye usiri wowote katika msafara huo kama roho nyingine ilivyomtuma. Alikuwa na uhakika kuwa kuingia kwa Shubiri ingekuwa rahisi kama kwenda kanisani, lakini kutoka… hilo ni jingine lililomsumbua, kubuni mbinu au hila ambayo ingewawezesha kutoka na kuifikia hoteli yake huku wakiwa na roho zao kifuani? Mwilini hakuwa na silaha zozote za haja isipikuwa ile bastola ndogo ambayo maficho yake yasingeweza kufikiwa na wakaguzi wa kawaida. Hiyo tu, silaha nyingine zisingewezekana. Huwezi kwenda kwa Waziri Mkuu na bastola katika mfuko wa koti na ukatarajia kurudi utokako.
Gari liliendelea kutafuna lami, likiiacha mitaa na miji na
kuanza kuvinusa vitongoji vya Borongo, eneo ambalo hukaliwa na wazito wengi. Dereva aliendelea kuzungumza, sasa alikuwa akisimulia jinsi alivyofanya alipomchukua mwanamke mmoja ambaye ana wazimu wa kupenda, “kama alivyodai yeye…” kama huna moyo utaanguka naye nakwambia. Mapaja kayaachia, macho kayalegeza huku mkono wake ukikukuna polepole. Ukimtazama akukonyeza…”
Joram aliinua uso kumtazama alipoikatiza ghafla hadithi yake. Mara alikiona kilichomfanya asite. Hatua chache mbele yake, gari aina ya Dutsan lilikuwa likiwajia kasi kwa mwendo mkali likiwa upande wao kabisa. Lilikuwa tukio la ghafla mno. Haikuwepo nafasi walao ya kufikiria. Alichokifanya Joram ni kufungua mlango ghafla na kumshika Nuru kiunoni huku akiruka nje ya gari. Dakika hiyohiyo mlio wa kutisha ulisikika wakati magari hayo yalipogongana uso kwa uso. Joram aliviringika toka alipofikia na kisha kuinuka ghafla. Aliyatupa macho kwa Nuru na kumwona kama aliyezirahi. Alipoyainua macho kutazama magari yaliyogongana aliambulia kumwona dereva wa gari lililowagonga akiviringika toka alipoanguka na kusaidiwa na dereva mwingine ambaye alisimamisha gari lake ghafla katika eneo hilo kulipanda gari hilo la aina ya Landrover, kabla Joram hajafahamu kinachotendeka aliiona landrover hiyo ambayo ilisimama kwenye gia ikiondoka kwa mwendo wa mshale. Hakujishughulisha kusoma namba ya gari hilo. Akageuka kumtazama Nuru tena. Alimwona akijipindapinda kwa juhudi za kuinuka. Akamwendea na kumsaidia kusimama. Nuru aliinuka kwa shida na kuchechemea hatua mbili tatu kabla hajarudi tena sakafuni.
“Pumzika kidogo,” Joram alimwambia akimtua chini na kutazama kilichokuwa kikimsumbua. Hakuona damu wala dalili yoyote. Pengine ilikuwa hofu tu. Akamwacha hapo na kumwendea dereva wa gari lao. Alikuwa hatazamiki.
Kichwa chake kilikuwa kimekatwa vipande vitatu. Sehemu iliyobaki shingoni ilikuwa ya pua na kinywa ambacho kilikuwa wazi kama kinachocheka kipumbavu na kutema mate ya damu. Kifua chake pia kilikuwa kimefumuliwa na usukani ambao ulivunjika na sehemu yake kupotelea mwilini mwake. Sehemu ambapo palistahili kuwa miguu sasa palijaa damu na mchanganyiko wa kitu kama nyama na mifupa iliyosagwa.
Ilikuwa picha nyingine ya kusikitisha sana. Ilimfanya Joram asikie kichefuchefu. Akafumba macho yake na kugeuka nyuma. Alipomfikia Nuru aliinama na kuutazama mguu wake. Akaona sehemu za magoti zikianza kuvimba.
***
Simu iliita tena. Safari hii iliita kwa muda mrefu, ikatulia kwa dakika mbili na kuanza tena. Joram aliendelea kuipuuza. Aliitazma kwa jicho lililoikinai huku akijaribu kuyalazimisha masikio yake kutosumbuliwa na mlio huo mkali. Iliendelea kuita kinyume cha matarijio yake kuwa mpigaji angechoka. Akainuka na kuiendea, akainua mkono wa simu na kuutia mezani. Kisha, alikirudia kitanda chake na kujilaza tena chali.
Kitanda cha pili kililaliwa na Nuru. Vidonge vya usingizi alivyopewa vilikuwa vikitimiza wajibu kwani kwa muda mrefu sasa alikuwa ametulia kimya katika hali ya utulivu bila ya kujitupa huko na huko kama alivyofanya kabla ya kumeza dawa hizo, kutokana na maumivu makali ya mguu ambao ulikuwa umeteguka gotini.
Hayo yalikuwa matokeo ya ile ajali ya gari nyumba mbili tatu toka nyumbani kwa Waziri Mkuu, ajali ambayo mtu mwenye macho asingeweza kuiita ajali.
Hivyo, ilimshangaza Joram alipoona wananchi wengi wakilijia eneo hilo na kulizunguka huku wakitazama kwa macho ya huzuni. Ilimshangaza zaidi polisi wa usalama barabarani walipojitokeza na kuanza kupimapima wakati hata haikuwepo haja. Macho yangetosha kueleza kuwa ilikuwa ajali ya kukusudia. Ajali iliyopangwa. Gari la wagonjwa lilipofika na kumchukua marehemu pamoja na Nuru kwenda hospitalini Joram aliomba kuandamana naye.
“Hapana. Wewe unatakiwa kituo cha polisi,” “Kuna nini?”
“Ushahidi wako unahitajika.” “Nitakuja baadaye.” “Tunakuhitaji sasa hivi.”
Joram aliafiki kwenda nao polisi. Huko aliruhusu kuulizwa maswali yote ya kijinga na aliwapa majibu ya kipumbavu kama walivyotaka. Rohoni alijua fika wangemtafuta dereva wa landrover iliyosababisha ajali hadi kufa na wasingempata. Licha ya namba kuwa za bandia yawezekana pia gari hilo lilikuwa
limeibiwa mahala au kununuliwa maalum kwa shughuli kama hizo. Askari hao walipotosheka na maswali yao na kuchukua jina na anwani yake ya bandia, aliondoka kumfuata Nuru hospitali. Akamkuta tayari amepimwa kwa x-ray na kuonekana ameteguka, ndipo waliondoka kurudi hotelini baada ya matibabu mafupi na kuchukua dawa za kuchua.
“Siku mbili tu kitandani, utakuwa umepona.” Alimweleza Nuru wakati akimsaidia kuvua na kujilaza.
“Siku mbili niwe nimelala tu?” Nuru alilalamika. “Hakuna njia nyingine.”
Na mara tu usingizi ulipomchukua ndipo simu ilipoanza kumsumbua, simu ambayo Joram hakuipenda kuijibu kwani hakuwa na jibu. Alijua ingetoka kwa watu wawili tu, Rais angependa kumwona au yule mtu mwingine ambaye angependa kumtisha. Wote hakuwa tayari kuwajibu. Hakuwa na lolote la kumwambia Rais na asingeweza kumwambia kuwa “Nimeshindwa” hasa baada ya damu nyingi kumwagika kwa ajili yake. Lazima damu hii ilipizwe. Bei ya damu ni damu. Yeyote aliyesababisha kumwagika kwa damu hiyo Joram alimhitaji kwa udi na uvumba kama asingejisamehe kumwacha mtu huyo aendelee kusheherekea hewa safi ya dunia baada ya kumwaga damu nyingi zisizo na hatia.
“… Unakitafuta kifo chako.” Maneno ya mbaya wake yalikuwa wazi masikioni mwake yakikusudiwa kumtisha. Awali yalimchekesha, akijua kuwa ni moja kati ya sura nyingi za woga. Sasa yakimjia akilini, wakati Nuru akiwa chali kitandani, uso wake ukionyesha wazi maumivu yaliyokuwa yakimsumbua japo yumo usingizini ambayo yalimfanya Joram kuhisi kitu fulani kikiibuka tumboni mwake na kujikita moyoni, kitu kichungu, chenye maumivu yasiyoelezeka, kitu ambacho huwezi kukipambanua baina ya hofu na hasira wala asingeweza kukipambanua kwani hakumbuki lini aliwahi kuonja hasira ya hofu na kuijua. Tangu utoto wake hofu kwake ulikuwa msamiati usio na hisia zozote katika nafsi yake.
Ndiyo kifo alikifahamu sana na ni moja kati ya vitu ambavyo hakupenda vimtokee katika umri huu aliokuwa nao. Hakukipenda hasa kwa kutojua kipi humtokea binadamu baada ya roho yake kutengana na moyo. Lakini kuna tofauti kati ya kifo na kifo. Kifo chake yeye binafsi ni jambo ambalo lingemshitua
lakini lisingemtisha. Ni jambo ambalo kila binadamu timamu hana budi kulitarajia kwani hujafa hujazaliwa. Hata hivyo, kifo cha mtu mwingine, asiye na hatia, kwa ajili ya shahuku yake ya kutaka kujua mambo yasiyomhusu ni jambo lililomtesa sana Joram. Kwanza, yule mwandishi wa habari Patauli, kIsha yule msichana, Betty, na leo hii yule kijana mchangamfu, dereva wa teksi. Hayo yalimsumbua sana Joram. Watu wangapi watapoteza maisha yao kabla hajaupata ukweli? Na angeendelea kuketi kizeezee hadi lini akiwatazama watu wanavyouawa kinyama kwa ajili yake? Lini angejibu shambulio?
Akayahamisha macho yake toka kokote yalikokuwa na kuyasafirisha hadi kitanda cha pili, aliuona uso wa Nuru ulivyokuwa, bado dalili zote za maumivu zilikuwa wazi machoni mwake japo alilala kwa utulivu. Akamtazama kwa makini zaidi, utulivu wake ukamtia uchungu mkali moyoni mara alipowaza kile ambacho hakupenda kukiwaza, msichana huyu hivi sasa angekuwa maiti?
Kisha, likamjia wazo jingine zito kuliko la awali. Pengine yule mwuaji hakupenda kuwamaliza? Pengine alichokusudia ni kuwajeruhi tu na kuwatisha kwa kifo cha dereva! Vinginevyo, kwa nini asitumie njia nyingine kuwamaliza wakitapatapa sakafuni baada ya kunusurika?
Maswali hayo yalimwongezea Joram hasira. Aliona dhahiri kuwa adui alikuwa akimchezea kama mtoto mdogo na kumdhihaki kwa vifo vya watu wengine wasio na hatia hali kifo chake kikiendelea kuhairishwa. Ni nani na anachotaka ni nini mtu kama huyu! Na vipi ameondokea kujiamini kiasi hicho? Joram alijiuliza. Au amejiimarisha sana hata anamwona Joram kama chui jike aliyefungwa kamba shingoni, tayari kusulubiwa wakati wowote? Bila shaka machachari yake yote ya kupeleleza kwao yalikuwa mzaha usio na maana yoyote.
Hasira ina nafasi ndogo sana katika kichwa cha Joram. Hutokea kwa nadra sana. Hasira zikimteka akili na kumfanya achukue uamuzi wa pupa. Leo zilimshika. Yeye ni Joram Kiango. Na angeendelea kuwa Joram Kiango kama asingekubali kuwa chui jike au kondoo wa mtu yeyote anayeishi na kamba shingoni. Aliitazama saa yake na kuyasubiri mapambazuko kwa shahuku kubwa. Kesho angekwenda tena kumwona huyo anayejiita Waziri Mkuu. Angemfata ofisini na hakuna mtu
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment