Search This Blog

Thursday, 29 December 2022

MTAMBO WA MAUTI - 3

   

Simulizi : Mtambo Wa Mauti

Sehemu Ya Tatu (3)







alikuwa hasemi ukweli. “Meja,” akaita kwa sauti yenye hasira kidogo. “Unajua kuwa unajiweka mahala pabaya? Unafahamu hilo?”


Beka naye alianza kuchoshwa na vitisho hivyo, akamwambia, “Inspekta, na wewe unajua kuwa toka umeniita hapa na kuanza kunisaili kama mhalifu hujaniambia kosa langu?”


“Hujui kosa lako?” Kambambaya alishangaa. “Hujui kama umekiuka kiapo chako cha kutotoa nje siri za jeshi? Huoni kama huo ni uhaini? Hujui kama kumsaidia mhalifu ni uhalifu? Alihoji, kwa mbali akitwetwa.


“Sijatoa siri yoyote Inspekta,” Meja Mfumue alisisitiza. “Na kuwasiliana na Joram Kiango ninayemfahamu mimi sidhani kama ni uhaini wa aina yoyote. Hakuna asiyejua mchango na harakati zake zilivyoinusuru nchi hii na Afrika nzima mara kwa mara. Kama ni mhalifu basi leo ndio nafahamu, toka kwako.”


Kambambaya hakuutegemea ujasiri huo toka kwa Meja Beka Mfumue. Kwa ujumla, alitumia njia ya vitisho kwa matarajo ya kupata chochote ambacho kingemsaidia kumpata Joram Kiango. Alikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa kumpata Joram ilikuwa sawa na kuupata ufunguo ambao ungemfungulia mlango wa siri ya mikasa na maafa haya makubwa ambayo yanazidi kutokea.


Awali, ilianza kama mauaji ya kawaida, ambayo kwa kila hali inafanya Joram Kiango awe mtuhumiwa wa kwanza. Katika kumtafuta Joram Kiango yakaibuka mauaji makubwa zaidi; polisi wanne, daktari mmoja Manzese. Mgonjwa wa bandia aliyesababisha yote hayo si mwingine zaidi ya Joram Kiango.


Kana kwamba hayo hayatoshi, alfajiri hiyohiyo iliambatana na habari za kutisha zaidi. Tukio la mapambano makali ya silaha na mlipuko wa bomu la mkono katika hoteli ya New Africa, lililopelekea vifo vya watu watatu, watumishi wawili wa hoteli na mtu mmoja anayedaiwa kujibamiza mwenyewe kwenye gari kubwa kwa kila hali lilikuwa chachu nyingine ya kumpata upesi zaidi Joram Kiango.


Tukio hilo lilimfikia kwa taarifa ya maandishi. Ilikuwa baada


ya kutoka hospitali ya Muhimbili, ambako alishuhudia maajabu





ya kutoweka kwa mwili wa marehemu ambaye anaelekea kuwa chanzo cha zahama hii alikuta jalada likimsubiri juu ya meza yake. Lilikuwa bado halijakamilika. Hivyo, lilieleza kwa ufupi tu, kama taarifa, juu ya yaliyotokea hotelini hapo, kwamba alfajiri hiyo. Mzee mmoja mchovumchovu alitokea mapokezi na kutaka chumba. Wakiwa na hakika kuwa hangekuwa na uwezo wa kulipia bei ya vyumba vyao walimwambia kuwa kuna vyumba. Kwa mshangao mzee huyo alitoa pesa na kukabidhiwa chumba chake, kwamba muda mfupi baada ya makabidhiano alitokea mgeni mwingine, mwanamke, ambaye alitaka kumwona mzee huyo. Walizungumza kidogo kwenye simu kabla mama huyo hajapanda lifti kumfuata mzee huyo ghorofani.


Mtoa habari huyo, ambaye ni mmoja wa wapokeaji wageni aliyekuwa zamu, anasema toka hapo hakumbuki kilichondelea kwani ulifuatia mlipuko mkubwa wa bomu ambao ulimfanya yeye na kila kitu ukumbini hapo wapae angani na baadaye kutua chini wakiwa nyang’anyang’a, yeye akiwa amevunjika miguu yote miwili na kuungua sehemu kubwa ya kichwa na kisogo. Alitoa taarifa hiyo akiwa Muhimbili, kitengo cha MOI, ambako anapatiwa matibabu.


Jambo lililofanya Kambambaya ahisi kuwa mzee yule, pale New Africa hakuwa mwingine zaidi ya Joram na taarifa alizoziandikisha:


Jina: Kondo Mtokambali! Kabila: Mtanzania!


Anakotoka: Dar es Salaam. Anakokwenda: Dar es Salaam


Majibu hayo na uwiano wa muda toka lile tukio la Manzese hadi lile la katikati ya mji, pamoja na mlolongo wa matukio, yaliyofuata ndivyo vilivyomfanya Kambambaya asiwe na chembe yoyote ya mashaka kuwa Joram Kiango yumo katikati ya dimba hilo.


Hivyo, wafumbuzi wa mafumbo walimthibitishia kuwa ile simu ya maandishi ilitoka kwa Joram Kiango pamoja na kumpatia jina la mmoja wa maafisa wa polisi, ambaye alipelekewa ujumbe ule, Kambambaya hakuona kama ilimpasa kuvuta subira. Alimtaka Joram Kiango. Na alimtaka






haraka sana, kabla ya maafa zaidi kutokea. Ndipo akataka aitiwe Meja Beka Mfumue na kumketisha mbele yake huku akimsukumia vitisho kwa matarijio ya kupata ukweli mara moja.


Hivyo, Mfumue alipobadilika na kuipoteza ile hali ya ushirikiano aliyoionyesha mwanzo wa mahojiano hayo, Kambambaya alianza kuuona ugumu wa kazi iliyokuwa mbele yake. Ni kweli kuwa katika hatua hii alikuwa hana namna ya kumtuhumu Meja Mfumue kwa lolote. Kwa mujibu wa Katiba ya Jhamuri ya Muungano wa Tanzania Meja Mfumue, kama mtu huru, ana haki na uhuru wa kukutana na mtu yeyote huru, kuzungumza naye na kushirikiana naye, mradi hawavunji sheria. Joram bado alikuwa mtu huru. Tuhuma juu yake, pamoja na yote yanayoendelea kutokea, bado zilikuwa ni hisia tu, hadi pale itakapothibitika vinginevyo.


“Sikiliza Meja,” Kambambaya alitamka ghafla, akimkazia Mfumue macho. “Kwa sasa unaweza kusema chochote unachojisikia kusema. Lakini unafahamu vizuri sana kuwa kuna mambo ya kutisha ambayo yametokea katika saa ishirini na nne zilizopita, mauaji ya watu wasio na hatia, milipuko ya mabomu; na mengineyo. Nadhani unafahamu pia, kwa njia moja au nyingine, kuwa Joram Kiango anahusika au kuhusishwa na hali hii. Hivyo, lazima apatikane, haraka iwezekanavyo. Wewe kama afisa wa jeshi, kama mtu uliyekula kiapo cha kuilinda na kuitetea nchi hii, una wajibu wa kusaidia kufanikisha jitihada hizi. Uongo?”


“Kweli, mzee.”


“Na utatusaidia haraka zaidi kwa kutuwezesha kumpata, au walao kuwasiliana na Joram Kiango. Uongo?”


“Kweli.”


“Kwa hiyo,” Kambambaya aliongeza. “Kama kweli hujaujibu ujumbe wake wa maandishi nenda kaujibu. Mpe maelekezo ya kukutana naye mahala. Utajua namna ya kumweleza. Lakini hakikisha unaniarifu, mimi binafsi, maendeleo ya jitihada hizo. Kuanzia leo, mimi na wewe tutakutana kila siku jioni, ili unipe taarifa za jukumu hilo. Sawa?”


Halikuwa ombi. Ilikuwa amri. Mfumue hakuwa na kauli zaidi ya “Sawa, Inspekta.”






Ulikuwa mtego mwingine kwa Meja Beka. Kitu ambacho hakujua, kitu ambacho wengi hawajui, ni kwamba ziko njia nyingi za kunasa ujumbe wa maandishi toka simu yoyote ya mkononi kwenda nyingine. Moja wapo ya njia hizo ni kile ambacho watu wengi hawajui, kuwa ujumbe unapotumwa toka simu fulani hubakia ndani ya simu hiyo hata kama umeufuta. Zamani kidogo ujumbe huo ulikuwa unakaa katika kadi. Siku hizi, baada ya maendeleo zaidi katika teknolojia, ujumbe huo hukaa katika hifadhi ya kumbukumbu. Simu za kisasa zaidi huweza kuhifadhi maelfu ya ujumbe wa maandishi. Hivyo, mtu akiinasa simu yako anaweza kusoma simu zako mbalimbali za maandishi bila mwenyewe kujua.


Lakini kuna njia nyingine, ya uhakika zaidi. Unapotuma ujumbe wa maandishi, ujumbe huo hupitia katika kituo chako cha mawasiliano, hapa nyumbani vituo maarufu vikiwa ama Vodacom, Airtel, Zantel au Tigo. Hawa, pamoja na kuupeleka ujumbe wako kama ulivyoagiza, nakala ya ujumbe huo hubakia katika hifadhi yao kwa muda mrefu. Kumbukumbu ya simu iliyopigwa huweza kuhifadhiwa kwa kati ya miezi sita hadi miaka mitano kabla ya kuteketezwa. Hivyo, mtu yeyote mwenye nyenzo na utaalamu angeweza kuchimba katika msitu huo wa ‘meseji’ na kupata kile anachokitafuta.


Kambambaya alilijua hilo. Na tayari watu walikuwa kazini kuchimba chochote ambacho kilikuwa kimepita baina ya simu ya Joram Kiango na Meja Beka, au mtu mwingine yeyote, katika siku hizo mbili tatu.


Hivyo, kama Meja Beka alidhani angemlaghai Kambambaya, Kambambaya aliamini kuwa angekuwa akijidanganya mwenyewe.




***


Toka bustani ya Mnazi Mmoja Joram aliifuata Barabara ya Lumumba na baadaye kuingia ya Uhuru, akielekea Kariakoo. Alihitaji nafasi ya kutulia ili awaze na kuwazua hadi atakapokifikia kiini cha fumbo au kitendawili hiki, utulivu ambao, kwa hali ilivyokuwa aliamini kuwa hakuna mahala pengine ambapo angeupata zaidi ya katikati ya msongamano wa watu. Utulivu wa aina yoyote mwingine, kama ule






alioutafuta wodini Manzese na hoteli ya New Africa tayari ulikuwa umepelekea kutokea kwa maafa makubwa. Mitaa ya Kariakoo, hasa ile ya Msimbazi na Kongo, kwa vyovyote vile, ilikuwa sehemu muhafaka kwa sasa. Pamoja na maafa yote hayo bado Joram hakuamini kuwa yeyote huyo anayemfuatilia angeweza kuuteketeza mtaa mzima uliofurika watu kwa ajili ya roho moja, Joram Kiango.


Akiwa katika mavazi yaliyomfanya afanane sana na mamia ya vijana wa mitaa hiyo, kofia pana ikiwa imefunika uso wake, Joram alitembea mtaa huu hadi ule bila wasiwasi wowote. Alikuwa mmojawao, mmoja wa Wamachinga, mmoja wa wabangaizaji wa jiji la Dar es Salaam ambao kwao vumbi, jasho na msongamano ni sehemu tu ya maisha yao katika jitihada za kutafuta riziki ya siku hiyo.


Lakini kama mtu angebahatika kuingia katika kichwa chake angeshuhudia jinsi ubongo wake ulivyokuwa kazini, ukiwaza kwa nguvu zake zote, wazo kubwa zaidi likiwa ni kujaribu kutafuta kiini cha maficho yake yote kugundulika mara moja kana kwamba alikuwa akijianika hadharani huku akipiga mbiu kumwashiria adui yake wapi aliko.


Ndiyo, alibaini madhara ya simu na kuitupilia mbali. Hata hivyo, bado aliamini kuwa haraka iliyotumika kumfikia kule Manzese haikotokana na matumizi ya taaluma hiyo dhidi ya simu za mkononi. Kwa vyovyote, ingechukua muda, ikiwa pamoja na kulikagua eneo la mraba lisilopungua ekari tano kabla ya kubaini mahala alipo. Hali kadhalika, taaluma hiyo ilifanikiwa pale tu mwenye simu hiyo anapoitumia. Joram hakuwa amepiga wala kupigiwa simu pale New Africa. Waliwezaje kufika haraka kiasi kile?


Huku akitembea aliendelea kujikagua kuona kama alikuwa na chombo chochote kingine kinachoweza kutumiwa kusafirisha mawasiliano. Aliitoa kalamu yake na kuitazama. Ilikuwa aina ya packer, ya kawaida kabisa, tena iliyonunuliwa toka kwa mmachinga. Aliitazama saa yake, Omax, ambayo amekuwa nayo miaka sita sasa. Hajawahi kumwazima mtu, wala haijawahi kwenda kwa fundi ambako ingewekewa kwa siri vyombo vya mawasiliano.


Ni wakati akiitazama saa yake hiyo, alipoiona ile pete




kubwa ya Mona Lisa, ikiwa imetulia katika kidole chake. Joram alikumbuka vizuri kilichopelekea pete hiyo iwe hapo kidoleni pake.


“Unaogopa!” “Naogopa nini?” “Mchumba wako.”


“… Mchumba! Mchumba gani? Mie bado niko single. Sina mume wala mchumba.”


“Umeanza kuwa mwongo… pete hiyo hapo inakusuta. Kama sio ya uchumba ni ya ndoa…”


Maongezi baina yake na Mona Lisa, yakiwa mzaha tu, lakini uliopelekea Mona Lisa kuivua na kumwachia Joram Kiango pete hiyo.


Ingawa maongezi hayo yalifanyika siku mbili tatu tu zilizopita, Joram aliyahisi kama yaliyofanyika miaka nenda rudi, kwa jinsi matukio mengi na ya kutatanisha yalivyolifuatia tukio hilo. Joram aliitazama kwa makini zaidi pete hiyo, pete ya Mona Lisa; msichana aliyemfia mikononi mwake huku yeye akiwa usingizini kama mzoga, msichana ambaye mauti yake yamejaa utata mkubwa. Alikufa… yeye mwenyewe aliushuhudia mwili wake pale kitandani… mara mwili huo unadaiwa kutoweka toka katika chumba cha maiti… mara sauti ya Mona Lisa huyohuyo ikimfikia Joram na kumtaka wakutane… sauti ambayo mara zote ilifuatiwa na umwagaji mkubwa wa damu, bila shaka za watu wasio na hatia.


Joram alichunguza kwa makini zaidi pete hiyo. Aliyaamuru macho yake kupuuza mng’aro wa madini yaliyotumika kuitengeneza, badala yake akayakaza kutazama ndani kabisa ya ua hilo lililokuwa likimeremeta. Akahisi kuona kitu cha ziada, kitu kidogo sana, kilichokaa katikati ya ua hilo, ambacho kilikuwa hakimeremeti pamoja na pete nzima. Joram alishuku jambo. Akaipeleka pete hiyo sikioni na kusikiliza kwa makini. Kama alivyohisi, kwa mbali sana alisikia mlio wa tik-tak-tik- tak toka katika pete hiyo.


Joram akatabasamu. Hakuwa na shaka tena kuwa amebaini kisa cha kufanya maficho yake yawe yakibainika ghafla kila mara. Chombo hicho kidogo, kilichofichwa ndani ya pete hiyo, bila shaka kilikuwa aina fulani ya mtambo wenye nguvu






za kieletroniki, ambazo zilimwezesha mtu fulani, mahala fulani, kujua pete hiyo ilipo na, hivyo, kuweza kumpata kila alipojichimbia.


Hata hivyo, kwa Joram Kiango ugunduzi huo bado haukuwa ufumbuzi. Kwa ujumla alihisi kama ulikuwa nyongeza tu ya utata mzima. Hakuwa na shaka kuwa pete hiyo ilibeba chochote cha mawasiliano, kilichokuwa kikiyafichua maficho yake. Lakini kilichomtatiza ni jinsi alivyopata pete hiyo. Kwa kila hali, Mona Lisa alikuwa amempa kimapenzi tu, bila ajenda yoyote ya siri. Na hakuitoa mahala pengine zaidi ya kidoleni, alipokuwa ameivaa. Wala hakuifanyia utaalamu wowote kabla ya kumkabidhi. Kama hivyo ndivyo, Joram aliwaza, ni wazi kuwa Mona Lisa mwenyewe alikuwa akiitumia bila kufahamu matumizi yake. Kwa maneno mengine, ni kwamba mtu ambaye amekuwa akimfuatilia yeye, bila shaka amekuwa akimfuatilia Mona Lisa pia. Na kama huo pia ndio ukweli ni wazi kuwa mtu huyo ama ndiye aliyemuua ama anahusika sana na kifo chake, aliwaza.


Mawazo hayo yaliibua maswali mengi zaidi, ni nani huyu mtu? Alitaka nini kwa Mona Lisa? Mswada wa “Ubongo wa Mwalimu Nyerere?” na kama ni ule kwa nini alimuua Mona Lisa badala ya kuuchukua tu na kuondoka? Na kwa nini alimwacha yeye akiwa hai badala ya kumuua pamoja na Mona Lisa? Hlafu, kama aliamua kumwachia kwa nini sasa anamwinda huko na huko? Na huyu msichana anayejiita Mona Lisa, mwenye sauti kama ya Mona Lisa, ambaye amekuwa akizuka kama kizuka kila anapojificha, ni nani na anahusika vipi na yote hayo?


Msitu wa maswali ulikuwa mpana sana. Joram alihisi kuwa angeweza kutembea kwa miaka katika msitu huo na asipate jibu, kama angeendelea kuwa mtu wa kuwindwa badala ya kuwa mwindaji, mtu wa kutafutwa badala ya kutafuta. Akafanya uamuzi. Toka dakika hiyo atakuwa mwinda badala ya mwindwaji.


Akaiinua pete ya Mona Lisa na kuibusu. Pete, aliinong’oneza, ni wewe utakayenipeleka mbele ya adui kama ulivyomwezesha adui kufika mbele yangu. Utake usitake.


Baada ya sala hiyo aliirejesha kidoleni huku akiendelea






kupigana vikumbo na wapita njia wenzake waliofurika mitaani.




***


Kwa Papaa Mulumba mchana wa siku hiyo ulijaa maajabu ambayo hakupata kuyaona tena maishani mwake. Kwanza kabisa, alikuwa mkavu kabisa mfukoni. Alifika kazini hapo kibahatibahati baada ya kutumia utoto wa mjini uliomlainisha kondakta wa daladala apokee shilingi mia mbili tu, badala ya mia nne ambayo ni nauli halali. Kutwa nzima hiyo alijaribu kuchora kila aina ya mchoro ili apate walao elfu moja ya kianzio bila mafanikio. Ghafla sasa hivi alikuwa na shilingi elfu hamsini zilizomjia “hivihivi tu,’ bila jasho.


Si hilo tu. Kazi yake ngumu pia ilikuwa imechukuliwa na mtu, yeye akiwa na uhuru wa kwenda zake, ama kuitumia fedha yake ya bure ama nyumbani kwake hadi kesho. Mgeni huyo wa ajabu aliyeinunua kazi yake kwa elfu hamsini tayari alikuwa amevaa viatu vyake vya mpira, joho lake refu la plastiki na kofia yake ya kapero na sasa yuko kazini akisafisha vyoo na masinki kwa utaratibu wa kawaida kabisa. Mtu yeyote ambaye angeingia maliwatoni humo, kama asingemsemesha angetoka huku akiwa na hakika kuwa mtumishi huyo hakuwa mwingine zaidi ya Papaa Mulumba.


Papaa Mulumba ni mtoto wa mjini. Ingawa alitoka kwao Mahenge miaka tisa tu iliyopita, mara baada ya kumaliza shule ya msingi, tayari mitaa ya Ilala, Magomeni na Kinondoni ilimpokea na kumkubali kama mmoja wa vijana wa mjini. Kila alipopata pesa zake alizipanga katika mafungu muhimu matatu; kuvaa, kula na kunywa.


Alikuwa hodari wa kuchagua mashati na suruali za mitumba kwa makini kiasi kwamba kila alipozivaa, alionekana kuvaa nguo mpya za kutoka ughaibuni. Unywaji wake pia aliufanya kwa uangalifu. Kwake ilikuwa mwiko kunywa katika baa za vichochoroni. Alipendelea baa kubwakubwa, zenye majina, huku akijichanganya na watu wakubwawakubwa, wenye pesa na vyeo; jambo lililompatia marafiki wa maana. Mmoja wa marafiki hao ndiye aliyempatia kazi Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.


Papaa Mulumba wala halikuwa jina lake halisi. Alizaliwa






na kubatizwa kwa jina la Paskali, baba yake akiitwa mzee Kirumba. Vaa yake ya kufungia suruali tumboni, mwili uking’ara kwa pafyumu na vipodozi, huku akiwa hakosekani katika kumbi za muziki bandia za Maquis inapotumbuiza, ni miongoni mwa sababu zilizofanya jina la Paskali life na ‘Papaa’ kuzaliwa.


Sababu nyingine iliyompa jina hilo ni lugha. Kuupenda kwake u-Kongo kulimfanya abadili lafudhi ya Kiswahili chake kiasi kwamba watu wengi wasiomfahamu walimfikiria kuwa ni Mkongo, tena mwanamuziki. Lafudhi hiyo iliambatana na ‘lugha’ yake katika kuwatoa rafiki zake ‘kitu kidogo’ kila anapojikuta hana pesa mfukoni, jambo lililolifanya jina la Papaa lishamiri zaidi.


Papaa alikuwa mtumishi wa Mamlaka ya Viwanda vya Ndege. Aliajiriwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Mwenyewe alipenda sana kuutambulisha kwa Kiingereza, “Niko Dar International Airport,” akiamini kuwa kuutaja kwa Kiswahili kuliupunguzia hadhi na, hivyo kumpunguzia yeye mwenyewe hadhi. Kila alipohojiwa yuko idara gani hapo uwanjani alijibu harakaharaka “Huduma ya Jamii,” akikwepa kuitaja kazi yake halisi ya utunzaji wa vyoo, kazi ambayo alikuwa ameipokea shingo upande, baada ya elimu yake kuonekana kuwa isingempatia nafasi nyingine. Lakini baadaye alikuja baini kuwa haikuwa kazi mbaya kama ilivyofikiriwa. Kwanza, sare zake za kazi, ikiwa pamoja na joho refu, kofia ya kapero na glovu zilifanya hata mtu anayemfahamu kwa karibu anapomkuta kazini ashindwe kumtambua. Pia, kazi hiyo ilikuwa na pesa kuliko alivyotegemea. Watu wengi wenye magendo yao, hasa dawa za kulevya, walikuja chooni kuficha bidhaa zao. Kila mara walimwachia ‘kitu kidogo’ kama bakshishi. Baadhi alidiriki kuwatolea au kuwaingizia bidhaa zao hizo na, hivyo, kumwachia ‘kitu’ ambacho hakikuwa ‘kidogo’ hali iliyomwezesha kumudu vikao vya high table na rafiki zake baadaye.


Jana tu aliondoka kazini hapo na elfu ishirini. Alitegemea angetumia elfu tano tu, lakini walipokwenda Diamond Jubilee ambako Kanda Bongo Man alikuwa akitumbuiza na bia mbili tatu baadaye ndipo akajikuta akiamka na mia mbili mfukoni.






Hivyo, ujio wa huyu ‘brother’ wa kutaka aachiwe kazi hiyo ngumu, kutwa nzima ya leo, na shilingi elfu hamsini juu, ilikuwa kama nyota ya jaha.


“Natumaini huna ajenda ya siri, ambayo itaniharibia kazi,” Papaa alionya.


Kicheko. “Sina ajenda yoyote. Kuna kitabu naandika. Sehemu mojawapo ya kitabu hicho inamhusu mtu aliyekuwa akifanya kazi kama hii. Hivyo, ili nitoe picha halisi ya kazi yenyewe lazima nifanye angalao kidogo, badala ya kuandika hisia tu. Ukitaka unaweza kukaa hapo kuniangalia. Ingawa mimi nakushauri uende zako popote unapotaka.”


“Nitatoka kidogo. Nitakuwa nikirudi kukutazama kila baada ya muda fulani. Saa za kazi zikiisha nitakuja kuchukua vifaa vyangu na kuvifungia.”


“Bila wasiwasi,” mgeni huyo wa ajabu alijibu.


Mgeni ambaye hakuwa mwingine zaidi ya Joram Kiango. Ndani ya mavazi ya kazi ya Papaa, Joram Kiango alikuwa amejikamilisha. Pamoja na silaha na vifaa alivyonunua pia alikuwa ameipitia kamera ndogo ya video wakati akija Uwanja wa Ndege. Alikuwa akimsubiri Papaa aondoke ili ategeshe vifaa hivyo, pamoja na kuiweka ile pete mahala muafaka. Alikuwa na hakika kuwa usingepita muda mrefu kabla ya ugeni mwingine, mzito zaidi, kuingia katika eneo hilo.


Alikuwa tayari, akisubiri.



W 7 X


AKATI mikono ya Joram ikiwa shughulini kusafisha vyoo vya pale uwanjani, mikono ya Inspekta Haroub Kambambaya nayo ilikuwa kazini ikichambua mamia


ya taarifa ambazo ziliendelea kumiminika mezani pake, taarifa ambazo ziliambatana na namba za simu zilizowahi kupigwa kwenye simu ya Joram Kiango; nakala za simu za maandishi; majina ya baadhi ya watu wenye simu hizo; na kadhalika. Kambambaya aliichambua kila taarifa kwa makini kabisa, akitafuta neno lolote au jina lolote lile ambalo lingefanikisha kupata ama fununu ya kila kinachoendelea, ama kauli ambayo ingemwezesha kubaini alipo Joram.


Haikuwa kazi rahisi. Joram hakuwa mtumiaji mzuri wa simu. Na hizo chache alizowahi kupiga hazikuwa na lolote lile ambalo ambalo lingefanikisha kupata ama fununu ya kila kinachoendelea, ama kauli ambayo ingemwezesha kubaini alipo Joram.


“Atapiga tu. Naamini hataitumia tena simu yake wala simu yoyote ya mkononi. Lakini endeleni kufuatilia simu zote za watu aliopata kuwasiliana nao. Simu ya Meja Mfumue itazamwe kwa makini zaidi. Naamini atahitaji kuwasiliana naye kwa namna moja au nyingine,” Kambambaya aliwaagiza wasaidizi wake.


Wasaidizi wake walishangazwa sana na mabadiliko ya






ghafla katika wajihi wa bosi wao. Katika muda wa saa arobaini tu zilizopita mzee alikuwa amekonda, uso umesinyaa na mvi kuongezeka kichwani mwake maradufu. Alionekana kama mtu ambaye kipindi hicho hakupata kula wala kulala vizuri. Kwa ujumla, alionekana kama mtu aliyeko katika mateso makubwa, kimwili na kiakili, kiasi cha kulisahau tumbo lake na kuipuuza afya yake.


Haikuwa uongo. Ubongo wa Kambambaya ulikuwa katika changamoto nzito kuliko zote zilizowahi kumkuta kazini. Vifo vya watu, askari kwa raia wasio na hatia vilimchanganya sana. Matarajio ya maafa mengine, wakati wowote, mahala popote, huku wanausalama wakiwa hawana uwezo wa kuyathibiti, yalimchanganya zaidi, nusura kumtia kichaa.


Kutoweka kwa Joram Kiango, kutoweka kwa mwili wa msichana anayeshukiwa kuwa aliuawa na Joram toka chumba cha maiti, mlolongo wa mauaji ambayo, kwa namna zote, yanahusiana na matukio haya yaliendelea kuwa kiini cha akili yake kuhangaika kupita kiasi.


Idara yake na jeshi zima la polisi walikwishafanya kila ambacho walistahili kukifanya, kwa nia ya kuimaliza kadhia hii mapema; bila mafanikio. Kila polisi alipewa picha ya Joram Kiango na kuamriwa kutoa taarifa mara atakapoonekana. Zaidi ya watu mia tayari walinaswa kwa kufananishwa naye. Vituo vyote vya mabasi, viwanja vyote vya ndege, stesheni za treni na, hasa, vichochoro vya miguu vinavyotoka nje ya Dar es Salaam viliwekewa ulinzi mkali kwa dhamira hiyo. Bado si Joram wala mtu yeyote anayeelekea kuhusika na maafa haya aliyekamatwa.


Hali kadhalika, maiti aliyetoweka Muhimbili naye alitafutwa kwa namna zote bila mafanikio. Vibali vyote vya mazishi vilipigwa marufuku kwa muda, kila mwili unaosafirishwa ukikaguliwa na kupekuliwa kwa makini kabla ya kuruhusiwa kuondoka. Ule mwili mzuri, wa aliyekuwa Mona Lisa, haukupatikana. Ilikuwa kama ametoweka kama zile hadithi za Alfu Lela u Lela.


Pengine nuru pekee ambayo Kambambaya alianza kuiona katika mkasa huu ni ile ya kufahamika kwa jina la marehemu huyo aliyetoweka. Moja ya taarifa za karibuni ilikuwa ile






ya kuitambua picha ya marehemu Mona Lisa kama mmoja wa wapangaji wao ambaye alikuwa hajaonekana hotelini hapo kwa siku mbili bila taarifa yoyote. Vitabu vya wageni vilimtambulisha kama mkazi wa Arusha aliyetokea Zanzibar na kuja Dar es Salaam ambapo tayari alikaa kwa wiki moja. Nafasi ya kabila ilimtaja kama Mmanyema.


Siku zote, mwanausalama anapopata jina huwa ni hatua moja mbele. Lakini haikuwa hivyo katika hili. Hali hiyo ilitokana na pale picha hiyohiyo ilipopelekwa kwa yule mtumishi wa hoteli ya New Africa aliyelazwa MOI alipomtambua kama mgeni aliyefika hotelini hapo alfajiri na kuomba kuonana na mgeni mwingine aliyejiandikisha kama Kondo Mtokambali, mgeni ambaye mara tu alipoanza kukiendea chumba cha Mtokambali mlipuko mkubwa wa bomu ulitokea ukifuatiwa na yale mauaji ya kutisha.


Madai hayo yaliongeza utata katika fikra za Kambambaya na wapelelezi wenzake. Haikumyukinika mtu aliyeuawa, tena kwa risasi, maiti yake ikapotea kimiujiza toka chumba cha maiti, adaiwe kuwa alionekana alfajiri akidai kuonana na mtu anayetuhumiwa kwa mauaji yake. Kambambaya aliamua kumchukulia majeruhi yule wa New Africa kama mtu ambaye ama kwa ajili ya hofu ama kutokana na akili yake kuathiriwa na mlipuko wa bomu, hakuwa na hakika na madai yake.


Uchunguzi mkali uliofanyika katika chumba cha marehemu pia haukumsaidia sana. Zaidi ya nguo zake chache, vitabu vya riwaya na vipodozi hakikupatikana kitu chochote ambacho kingewezesha kufahamika haraka kwa habari za marehemu huyo.


Hivyo, wakati polisi wa Arusha wakipewa jukumu la kutafuta habari za marehemu mwenye jina hilo, Kambambaya aliendelea kuyatia matumaini yake yote katika haja ya kupatikana kwa Joram Kiango, haraka iwezekananvyo. Aliamini kuwa hiyo ingekuwa njia ya mkato zaidi ya kufikia ufumbuzi wa kadhia hii.




***


Mageuzi ya uchumi, kwa lugha nyingine mfumo wa ubepari, ambao ulipokelewa na kuhalalishwa nchini Tanzania kwa jina




la kutatanisha, utandawazi, yaliambatana na kuchangamka vilivyo kwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Idadi ya ndege za kuingia na kuondoka, iliongezeka kila siku, jambo ambalo lilipelekea kuwapo kwa pilikapilika nyingi za watu, magari na mizigo uwanjani hapo. Hazikupita dakika mbili bila ya ama gari lingine kufika, ama kuondoka; likiwa na abiria. Aidha, kama ilivyokuwa katika vyumba vya kusubiria safari, eneo la nje pia lilikuwa na watu wengi, baadhi yao wakisindikiza, baadhi wakiwapokea wageni wao, baadhi wakiendesha biashara zao mbalimbali.


Ni katika hali hiyo teksi moja ilipomshusha abiria mmoja mkimya, aliyekuwa na kijimfuko kidogo tu mkononi. Abiria huyo alilikodi gari hilo toka mtaa wa Uhuru, Kariakoo. Kwa kiasi fulani, alionekana abiria wa ajabuajabu kwa dereva wa teksi iliyomleta. Alikuwa mkimya sana, kinyume kabisa na abiria wengi wa jijini Dar es Salaam. Mara baada ya kutamka maneno “Airport… mwendo wa haraka, tafadhali.” Hakutia neno jingine. Jitihada za dereva huyo kumshirikisha maongezi hazikuzaa matunda.


Dereva wa teksi hiyo aliamua kumchukulia abiria wake kuwa ni wa ajabu tangu pale abiria huyo alipolifuata gari lake na kuomba kupelekwa Uwanja wa Ndege. Alikuwa ameshuka toka katika teksi nyingine yenye namba za Ilala, jambo ambalo lilimfanya dereva huyo ahisi kuwa ama ni mkorofi katika malipo au hajui anakokwenda. Hivyo, hakuwa na hakika ya malipo yake alimtajia bei ya juu zaidi. Abiria huyo alikubali kwa kichwa huku akifungua pochi yake na kutoa pochi nyingine ndogo iliyokuwa ndani yake, akaifungua hiyo pia na kutoa pesa alizomlipa dereva.


Jambo jingine lililomshangaza dereva huyu kwa abiria wake ni mavazi. Pamoja na abiria huyo kufunika sehemu kubwa ya sura yake kwa miwani mipana ya jua, huku nusu ya kichwa chake ikiwa imemezwa na kofia pana ya jua vilevile, bado dereva alipata hisia kuwa mavazi hayo yalimficha kiumbe mmoja mzuri sana. Kilichomshangaza ni pale alipogundua kuwa kiumbe huyo alikuwa amevaa suruali ya jeans ambayo ilionyesha kuchakaa kidogo na jaketi lililofanana na suruali hiyo, ambalo nalo lilikuwa na dalili ya ama kuchafuka au






kutumiwa kwa muda mrefu zaidi.


“Unasafiri au unatarajia mgeni?” dereva alijaribu tena


maongezi. “Mgeni.”


“Anatokea wapi?” Kimya.


“Wewe mwenyewe unaishi hapa jijini au nje?” Kimya.


Dereva akaamua kuufyata mkia hadi alipowasili uwanjani na kumfungulia mlango. Alishuka taratibu, akauendea ukuta wenye ratiba za safari na kuusoma kwa dakika mbili tatu. Baadaye, alichanganyika na watu wengine ambao ama walikuwa wakisubiri wageni ama wakisubiri safari.




***


Joram Kiango alimwona mgeni huyo kitambo. Alimwona pale alipoketi na wageni wengine, akiwa na gazeti la Daily News mkononi. Ni gazeti hilo ambalo lilimsaidia Joram Kiango kumshuku haraka. Alikuwa halisomi kwa makini, kwa ujumla, alikuwa alisomi kabisa bali alilitumia kama ngao ya kuuficha uso wake, wakati macho yake yakitazama huku na huko kwa makini sana.


Kabla ya kulinunua gazeti hilo mwanamama huyo alikwenda maliwatoni mara mbili na kutoka akiwa na dalili za mshangao mkubwa machoni mwake. Msala aliouingia mara zote hizo ni ule ambao Joram aliutumia kuificha ile pete, nyuma ya sinki la maji. Mgeni wake alikwenda moja kwa moja na alikaa huko kwa dakika mbili nzima. Kisha alitoka na kutazama huku na huko kwa takribani dakika tano nzima kabla hajakwenda tena. Alipotoka ndipo aliponunua gazeti na kuketi kwa utulivu, lakini macho yake yakiwa kazini.


Joram hakuwa na shaka kuwa huyu alikuwa ndiye mgeni wake. Ingawa alikuwa hajapata wasaa wa kumkaribia, lakini umbile lake na mwendo wake vilitosha kumfanya apoteze mpangilio mzima wa ratiba yake ya awali. Hii ilitokana na ukweli kuwa umbile lile na mwendo ule haukuwa wa binadamu mwingine yeyote yule zaidi ya Mona Lisa! Mona Lisa ambaye ni marehemu! Mona Lisa ambaye pamoja na kuwa marehemu amekuwa akimfuatafuata kila anakokwenda!


Joram angeweza kumwendea msichana huyo, palepale alipokuwa, na kumuuliza yakoje mambo haya. Angeweza kumlazimisha ili aupate ukweli wa kitendawili hiki kinachomsumbua. Hata hivyo, alisita kufanya hivyo mara moja kwa sababu nyingi; kubwa ikiwa kwamba sehemu hiyo haikuwa mwafaka kwa majadiliano mazito kama hayo.


Pia, haukuwa wakati mwafaka kwani Mona Lisa hakuwa mgeni pekee wa kutatanisha uwanjani hapo. Muda mfupi kabla Mona Lisa hajafika macho mazoefu ya Joram yaliwaona wageni wengine wa kutiliwa mashaka. Walikuwa wanaume wawili. Waliketi mahala wakinywa soda na kusoma magazeti. Walikuwa kazini, macho yao yakikitazama kila kitu na kila mtu kwa makini. Mara kwa mara mikono yao iliingizwa katika mifuko yao ya koti, ambayo kwa uzoefu wa Joram Kiango, ilihifadhi silaha.


Joram aliwatazama watu hawa kwa muda mrefu. Aliwashuku zaidi pale mwanamke huyo mwenye umbile la Mona Lisa alipofika, ambapo mmoja wao alitoa simu yake ya mkononi na kuzungumza kwa muda mfupi. Baada ya hapo wote walionekana makini zaidi.


Si hao tu. Polisi na wanausalama uwanjani hapo walikuwa wengi kuliko kawaida. Joram angeweza kumnusa polisi yeyote hata akiwa mita mia moja toka alipo, awe na magwada asiwe nayo. Kwa hesabu za harakaharaka Joram aliona kama idadi ya askari wasio na magwanda, wanaopita huko na huko wakiwa maradufu. Wote walionekana kama waliokuwa na majukumu yasiyo ya kawaida, majukumu ya ziada, ambayo yalifanya wasiwe na ile hali ya utulivu na kujiamini kama ilivyo kawaida yao.


Subira Joram, Subira! Ni subira pekee itakayokuwezesha


kufikia mradi wako, Joram alijinong’oneza kimoyomoyo.


Aliitazama saa yake. Ilikuwa inakaribia saa moja na robo za usiku, robo saa zaidi ya muda ambao Papaa Mulumba aliahidi kuja kukusanya vifaa vyake, jambo ambalo lilimtia hofu Joram Kiango, kuwa ujio wake huo ungeweza kutibua mpangilio aliokuwa nao na, hivyo, kutibua mwelekeo wa mambo. Kwa bahati, Papaa alichelewa.






Joram akaendelea kusubiri, mikono yake ikiendelea kusugua vyoo na sakafu za choo baada ya choo, macho yake yakiendelea kufuatilia kila tukio katika maeneo yote yaliyofikiwa na upeo wa macho hayo. Na kila alipopata mwanya aliitumia mikono yake ndani ya mavazi yake kuhakikisha kuwa silaha na vifaa vyake vyote viko salama na angeweza kuvifikia muda wowote wakati utakapojiri.


Mambo yalitokea ghafla na haraka kuliko Joram alivyotegemea. Alikuwa ameinama kuokota kishungi cha sigara iliyotupwa na msafiri mmoja aliyeonekana mlevi. Wakati akiinuka alimwona mmoja wa wale wanaume wawili akimlenga bastola yule mwanamama mwenye sura na umbile la Mona Lisa. Kulikuwa na sekunde chache tu kati ya uhai na kifo cha mwanamama huyo, ambaye alikuwa amegeuka upande mwingine. Joram hakufikiria mara mbili. Aliichomoa bastola yake na kumlenga mtu huyo kwenye bega la mkono wake wa kulia. Akavuta kifyatulia.


Mlipuko wa bastola hiyo, kilio cha ghafla cha mtu aliyejeruhiwa na kuanguka kwa bastola aliyokuwa ameishikilia mkononi, vilizua purukushani ya ghafla chumbani humo. Umati wa watu ulilipuka na kuanza kukimbia huku na huko, wengi wakiwa hawajui kitu gani kimetokea.


Mtu wa pili alipoona mwenzake kaanguka, damu nyingi zikimvuja toka begani naye aliitoa bastola yake na kumlenga mwanamama yule. Alikuwa amechelewa. Risasi mbili zilimwingia mwilini, moja ikiwa imetoka katika bastola ya Joram, ya pili ikiwa imetoka katika bastola ya mwanamama huyo na ilimwingia barabara kifuani. Alikata roho hata kabla hajaifikia sakafu ambayo aliiangukia kifudifudi.


Matuko hayo ambayo yalitokea ndani ya sekunde ishirini tu yalizidi kuwasha moto wa hofu na purukushani uwanjani hapo. Wako walioendelea kukimbia huko na huko, wako waliojilaza chini ya viti na wako pia walioduwaa wima wakiwa hawajui lipi la kufanya.


Ni wanausalama waliokuwa katika eneo hilo ambao walimtia hofu Joram. Wote walichupa chini na kuzielekeza bunduki zao kwa mwanamama huyo huku mmoja wao akitoa amri ya kumtaka adondoshe silaha yake chini. Mmoja kati






ya wanausalama hao alikuwa amemwona Joram na kumpiga risasi bila ya kulenga vizuri. Risasi hiyo ilimchubua paja la mguu wake wa kushoto. Risasi ya pili Joram aliikwepa kwa kujirusha chini na kujikinga kwa pipa la taka. Wakati huohuo mkono wake ulikuwa ukiishughulikia ile chupa yake yenye moshi wa pilipili aliyoinunua duka la silaha. Aliifungua na kuirusha katikati ya chumba hicho. Ilipotua ilipasuka kwa mlio mkubwa wa kitu kama bomu, lililofuatiwa na ukungu mkubwa wa moshi unaowasha kupita kiasi. Kila mtu alifumba macho yake akilia kwa maumivu makali.


Kila mtu, isipokuwa Joram Kiango ambaye, alikuwa amejiandaa. Yeye aliutumia mwanya huo kuchupa hadi alipokuwa yule mwanamama na kumshika mkono huku akimwelekeza mlangoni. “Twe’nzetu,” alimhimiza. “Joram Kiango?” mwanamama huyo aliuliza.


“Ndiye, twende!” Joram alimwamuru akimvuta kutoka nje. Akiwa ameshikwa kwa mkono wenye nguvu kama koleo, akiwa haoni, huku machozi yakimtoka kwa maumivu ya macho, mwanamama huyo alikubali kuongozwa kikondoo


toka ndani ya chumba hicho.


Hakuna asiyejua hofu ya bomu. Toka ugaidi ulipopamba moto duniani, toka Marekani na ubabe wake uliposhindwa kufanya lolote wakati yale majengo yake marefu zaidi kati ya machache ya aina hiyo duniani yakilipuliwa kwa ndege za abiria zilizogeuzwa mabomu; toka nchi ya Irak ilipogeuka uwanja wa majaribio ya kila aina ya bomu; hofu ya bomu iliingia katika moyo wa kila binadamu anayeishi katika karne hii.


Kwa Watanzia hofu ya mabomu iliongezeka maradufu Agosti 7, mwaka 1998, pale wakazi wa Dar es Salaam waliposhuhudia bomu moja tu likiulipua Ubalozi wa Marekani pale Oysterbay, Barabara ya Bagamoyo, bomu ambalo lililipuka sambamba na lile la Nairobi, ambalo nalo liliulipua Ubalozi wa Marekani nchini humo na kuteketeza mamia ya watu wasio na hatia, hofu ambayo ilizidishwa nguvu na vyombo vya habari, vikiongezwa nguvu na vile vya Marekani yenyewe, ili iweze kuhalalisha malengo yake ya kisiasa na kiuchumi duniani.


Ni hofu hii ambayo ilimkumba kila mtu aliyekuwa uwanjani



hapo jioni hii. Joram na mateka wake walipotoka nje ya jengo walikuta hali iliyokuwa nje haikuwa tofauti na ya ndani. Watu walikuwa wakilia ovyo, kila mmoja akikimbilia huku na kule bila mpangilio; wote wakiamini kuwa wakati wowote uwanja huo ungelipuka kwa bomu kubwa zaidi.


Hali hiyo ilikuwa mwafaka kabisa kwa Joram Kiango, ambaye alimvuta mwanamama huyo hadi katika eneo la kuegesha magari. Madereva wengi walikuwa wameyasahau magari yao na kukimbia bila hata kufunga milango. Dereva mmoja yeye hata ufunguo wa kuwashia gari aliuacha ukining’inia sehemu yake. Joram alimsukumiza mateka wake katika gari hilo, kisha akaingia upande wa dereva na kuliwasha moto kuelekea mjini.


Gari hili lilikuwa aina ya Mark II Grand. Mwendo wake ulikuwa wa uhakika na petrol ilikuwa nusu tenki. Ingeweza kumfikisha Joram na abiria wake popote alipotaka. Hivyo, aliliendesha kwa mwendo wa kasi, akipita gari baada ya gari, huku akiangalia kwa makini kwenye kioo cha ndani kama hafuatwi. Nyuma yake barabara ilionekana nyeupe. Ukiacha magari mengi ya kupishana nayo Joram hakuona gari lolote nyuma yake, ambalo lingeweza kumtia mashaka.


Pamoja na kutazama magari, Joram Kiango alikuwa makini vilevile kumtazama abiria wake. Toka alipomwona akichupa angani na kutua sakafuni bila kishindo chochote kama paka shume kuufuatia ule mlipuko wa bastola, na alivyomwona akiitoa bastola yake kwa wepesi wa ajabu na kummiminia risasi yule mtu aliyetaka kumwua pale uwanjani, Joram alijua huyu si mwanamke wa kawaida. Macho yake hayakuonyesha dalili yoyote ya hofu wala mshituko hata pale mlipuko wa lile bomu la bandia ulipotokea. Ni pale tu chumba kilipojaa moshi wenye pilipili ndipo, kama watu wengine, alishindwa kujizuia na kupata upofu wa muda, huku machozi yakimtiririka, machozi ambayo yalianza kunyauka, lakini mwenyewe akaendelea kuyafumba macho yake na kutulia pale kwenye kiti katika hali ya ukimya na upole; tofauti kabisa na yule chui jike aliyecharuka dakika mbili tatu zilizopita pale uwanjani, chui ambaye hadi sasa aliishikilia bastola yake, japo kwa kuificha katika mfuko wake wa mkononi. Joram hakuwa na






shaka kuwa wakati wowote mwanamama huyo angeweza kucharuka tena na kuanzisha purukushani. Wakati wowote angeweza kuua, na safari hii marehemu mtarajiwa asingekuwa mwingine zaidi ya Joram Kiango, wazo ambalo lilimfanya aongeze umakini wa kumchunguza.


Kitu kimoja kilimsumbua Joram katika sura na umbile lake. Toka alipoanza kumchunguza pale uwanjani mpaka sasa akiwa naye ubavu kwa ubavu, mwanamama huyu hakuwa mwingine zaidi ya Mona Lisa. Urefu wake wa kadiri, umbile lililokatika kati kike kabisa, ngozi laini ya maji kunde; Mona Lisa mtupu! Lakini kile alichokiona pale uwanjani, alivyomwona anavyocharuka kama kifaru aliyejeruhiwa mara alipohisi kutishiwa uhai wake, alivyolenga shabaha na kumuua yule mtu kwa wepesi na utulivu wa ajabu, Joram aliapa kimoyomoyo; Hapana huyu si Mona Lisa. Kwanza Mona Lisa alikuwa amekufa pale kitandani, mbele ya macho yake. Kisha, Mona Lisa yule hakuwa mtu wa kuweza kumuua hata mende huku akiwa ametulia kama tembo aliyekanyaga sisimizi.


Mwanamke huyu ni nani? Ni swali ambalo alikusudia mwanamke mwenyewe alijibu mara wakati utakapojiri, ampe jibu hilo na pengine majibu ya mlolongo mzima wa kitendawili hicho. Alikuwa na kila hakika kuwa mwanamke huyo alikuwa ama kufuli ama funguo wa mengi yaliyofichika katika kadhia hii. Ni hilo lililomshawishi akubali kuhatarisha maisha yake kwa kumteka nyara, na kumwingiza katika gari hili, ili aweze kupata mahala ambapo angehakikisha anapata majibu yote, kwa bei yoyote.


Walipofika katika makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela taa za barabarani ziliwazuia. Ilibidi wasubiri. Ni mwanga toka gari la nyuma yao uliomfanya Joram ashituke kwa jinsi alivyolowa damu. Lile jereha la risasi, ambalo awali aliliona dogo, lilikuwa linavuja damu nyingi kiasi cha kumfanya ajikute amekalia kiti kilichojaa damu, huku yale mavazi ya Papaa Mulumba ambayo alikuwa hajayavua yalowe chapachapa.


Hilo lilimsumbua Joram kiasi. Hakuona kama alikuwa na


nafasi ya kutosha ya kujisafisha. Kadhalika, gari alilokuwa






akiliendesha lilikuwa la kupora. Alitarajia kulibadili mara baada ya kuingia mjini, hatua ambayo pia ililenga kumpoteza mtu yeyote ambaye anaweza kuwa anawafuata au trafiki ambao punde watapewa taarifa ya wizi wa gari na namba zake. Akiwa ametota kwa damu, akiwa na abiria asiyetabirika wala kuaminika, hata kwa sekunde; Joram hakuona kama ulikuwepo uwezekano wa kushuka ndani ya gari hilo na kukodi jingine. Akaamua kuendelea nalo.


Kitu kingine ambacho kilimsumbua Joram ni utulivu wa mwanamama huyo. Alivyotulia pale juu ya kiti, macho kayafumba kana kwamba yuko usingizini, kana kwamba ni mwanamke wa kawaida anayesafiri na mumewe; ni jambo lililomtisha Joram. Liliashiria ukongwe na uzoefu wake. Kwa jinsi alivyoifahamu ile sumu ya pilipili, baada ya dakika tano huwa imekatika machoni, kwa mwanamke ngangari kama huyu, dakika mbili au tatu zilimtosha awe amefumbua macho na kuanza kutazama uwezekano wa kuendelea na ratiba yake.


Kwa Joram utulivu wake uliashiria jambo moja tu, uzoefu, hakuna jambo jingine. Joram aliamini kuwa ndani ya ukimya na utulivu huo mwanamama huyo alikuwa kazini akiandaa mikakati mipya, mikakati ambayo kwa vyovyote haikumkusudia tena lolote.


Joram hakuona kama alikuwa na la kufanya katika hatua hiyo. Akaendelea kusubiri. Subira yavuta heri! Alijikumbusha. Taa ziliporuhusu aliliondoa gari kwa kuiacha Barabara ya Nyerere na kuifuata ile ya Mandela. Ilimchukua hadi inapokutana na ile ya Morogoro. Taa zilikuwa zikiwaka kijani. Hivyo, alivuka na kuifuata ile ya Chuo Kikuu, Mlimani. Aliifuata hadi mwenge, ambako aliicha na kuingia ile ya Ali


Hassan Mwinyi.


Alijua anakoelekea.




***


Ndiyo, purukushani za pale Uwanja wa Ndege zilimshitua takribani kila mtu. Mameneja waliziacha ofisi zao na kukimbilia vyooni, maafisa wa kawaida wakikurupuka kukimbilia huku na kule huku watu wengine, abiria kwa






wasio abiria, wakihaha ovyoovyo. Mamia waliumia vibaya kwa kugongana au kuanguka. Watu watatu walipoteza maisha kwa kukanyagwakanyagwa na watoto kadhaa walipotezana na wazazi wao.


Hata hivyo, hali hii ilimsisimua sana mtu mmoja. Huyu alifuatilia kila tukio na kila kitendo kwa makini, tabasamu jembamba likiwa limechanua usoni mwake. Mtu huyu alikuwa na majina mengi. Zamani kidogo aliwahi kumtania mmoja wa waajiri wake aliyekuwa amemtumia zaidi ya mara mbili kwa kumwambia, “Utapendelea kuniita nani?” pale mwajiri huyo alipomuuliza ana majina mangapi baada ya kumtajia majina mapya kila walipoonana.


Safari hii bwana huyu alijiita Othman Mchopanga, jina ambalo lilikuwa kwenye kitambulisho chake bandia kinachomtabulisha kama mkurugenzi wa fedha katika kampuni moja inayojihusisha na uagizaji wa vipuri vya magari na mitambo mbalimbali.


Mchopanga alifika uwanjani hapo muda mfupi kabla ya kuanza kwa purukushani. Alisimama nje ya uwanja, sigara mdomoni, mikono mfukoni, macho yake yakiwa kazini yakimtazama kila mtu anayeingia na anayetoka. Alimwona yule mwanamke aliyeshuka harakaharaka kwenye gari na kuingia ndani ya chumba cha kusubiria.


Pia, aliwaona wale watu wawili waliokuwa wakimfuatilia mama huyo, sura zao zikionyesha wazi kuwa walihitaji roho yake. Aidha, alimwona pia yule mtunzaji wa vyoo na kubaini mara moja kuwa hakuwa mfagizi wa kawaida.


Baada ya kumtazama sana Mchopanga alibaini kuwa mfagizi huyo alikuwa nani, jambo lililofanya tabasamu lake lizidi kuchanua.


Lakini kitu kilichomvutia zaidi ni yule msichana mwenye miwani na kofia pana ya jua. Alimjua fika msichana yule. Alimjua toka sauti, ukucha hadi unywele wake wa mwisho. Alikuwa amemfuatilia kwa wiki nzima, usiku na mchana, kabla hajapewa ile amri ya mwisho, ya kumuua. Na alimuua kwa mkono wake mwenyewe, pale kitandani na kumwacha bwana wake akikoroma kama nguruwe lililochoka, kazi ambayo aliifanikisha kwa urahisi baada ya kupenyeza mvuke






wa dawa za kulevya chumbani humo na, hivyo, kuwafanya walale fofofo, nusu maiti, kwa muda mrefu.


Mchopanga hakuwa mtu wa kuua wanawake. Wala hakuwa mtu wa kuua binadamu waliolala usingizi. Kwa kawaida, alipenda kumuua mtu huku marehemu mtarajiwa akikiona kifo kinavyomchukua. Alipenda kuyaona macho ya anayeuliwa yakitoka pima; kumtazama muuaji wake pindi risasi inapopenya kifua na kuuchoma moyo.


Hivyo, ingawa kazi ya kumuua mwanamke yule, ilikuwa nyepesi kuliko kazi zote alizowahi kufanya, ikiwa na malipo murua kuliko yote aliyowahi kupokea, bado aliona nzito sana; si kwa ajili ya kumuua mwanamke tu, tena akiwa usingizini. La hasha! Ugumu wake ulitokana na mwanamke anayeuawa. Alikuwa msichana mzuri, mzuri, mzuri. Mchopanga hakupata kukutana na mwanamke aliyekamilika kama huyu, sura ya kusisimua, umbile la kupendeza na mwendo wa kuvutia. Zile siku saba za kumfuatilia, kwake ilikuwa adhabu kubwa. Alitamani kuzungumza naye, aisikie sauti yake. Kusikia tu! Alitamani agusane naye ili aionje ladha ya ngozi yake. Kuionja tu! Uwezo alikuwa nao. Moja ya kumi ya pesa alizolipwa kwa kazi ndogo ya kumwondoa duniani zingetosha kumfanya msichana huyo apate wazimu.


Hata hivyo, Mchopanga alijitahidi kumshinda nguvu shetani wake. Maadili ya kazi yake hayakumruhusu kufanya mzaha wa aina yoyote. Vilevile, hakuona kama mwajiri wake alikuwa mtu wa kuvumilia upuuzi wa aina yoyote. Lakini, kubwa zaidi ni msichana mwenyewe. Muda wote wa kumfuatilia alimwona kama mtu asiye wa kawaida. Wakati wote alikuwa makini, macho yake yakiwa na kila dalili ya hadhari kama anayejua kuwa anafuatiliwa, hali iliyomfanya ajione kama kitendo chake cha kumfuatilia kilikuwa sawa na kucheza na chui jike aliyejeruhiwa. Hakujua kwa nini alilipata wazo hilo. Badala yake aliendelea kumfuatilia na kutoa taarifa ya nyendo zake zote kwa mwajiri wake hadi pale alipopewa amri ya kumuua usiku ule.


Amri hiyo aliitekeleza kikamilifu, lakini, saa ishirini na nne baadaye akaarifiwa kuwa alikosea na kumuua mtu asiyehusika. Na kwamba mtu aliyemwacha hai, pale kitandani,





alikuwa Joram Kiango, mtu ambaye alitakiwa kufa mara elfu moja na zaidi badala ya yule msichana.


Taarifa hiyo ilimchanganya Othman kuliko jambo lolote jingine. Katika maisha yake ya ajira hakuwahi kukosea wala kuua kwa bahati mbaya. Alikuwa makini na alilifuatilia windo lake kwa makini kabla ya kuitekeleza kazi yake. Alikuwa na hakika asilimia mia moja kuwa aliyemuua ndiye aliyekusudiwa, uhakika ambao ulianza kuingia mashaka pale alipomwona mtu yuleyule, akiwa katika mwendo na tabia ileile, japo katika mavazi tofauti pale uwanjani. Mashaka yake yaliongezeka zaidi pale alipomwona mwanamama huyo, akibadilika ghafla na kuwa kama paka shume aliyetishiwa maisha yake. Othman Mchopanga alimhusudu alipomwona akichupa angani na kutua chini kwa utulivu kama unyoya. Alimhusudu zaidi kwa wepesi wake na shabaha sahihi wakati alipoitoa bastola yake huku angali angani na kumuua mmoja wa maadui zake bila kuonyesha jitihada yoyote katika kulenga shabaha.


Othman Mchopanga alisisimkwa na damu zaidi alipomwona yule mfagizi akipata uhai ghafla na kuyaweka mambo chini ya himaya yake. Alimwona alivyo mwepesi wa mwili na akili. Aliona vidole vyake vilivyokuwa ‘sharp’ katika kuchezea bastola na hila aliyoitumia katika kulilipua lile bomu lisilo na madhara, lililokusudiwa kuongeza mparanganyiko wa mambo uwanjani hapo ili apate mwanya wa kutoroka. Alimwona alivyomnyakua yule msichana kama kuku na kinda lake na kumwongoza nje. Alimwona pia alivyopokonya gari na kulitia moto. Hata alifanikiwa kunukuu namba ya gari lile. Othman Mchopanga hakuhitaji ushahidi zaidi ya kuhakikishiwa kuwa mtu huyo hakuwa mwingine zaidi ya Joram Kiango.


Awali, jukumu lililomleta Mchopanga uwanjani hapa lilikuwa dogo tu, kuhakikisha yule msichana ameuawa na kisha awaue wale wauaji wake ili kufuta uwezekano wowote wa kuvuja kwa kiini cha mauaji hayo. Na kama wauaji hao wangeshindwa tena kumuua msichana yule mdogo yeye aliagizwa kutekeleza mara moja.


Angeweza kuitekeleza kazi hiyo kwa urahisi kabisa. Ule moshi wa pilipili uliowapa watu upofu wa muda yeye haukumfikia. Hali kadhalika, milipuko ya lile bomu la kuparanganyisha






watu yeye haikufanikiwa kumtisha kwani alikwishaizoea. Hata hivyo, alisita kufanya hivyo kwa sababu mbili za msingi. Moja, ni mabadiliko ya mambo yaliyotokea. Kuwepo kwa Joram Kiango katika eneo hilo la kujiingiza kwake kikamilifu katikati ya dimba la mambo hayo kulimfanya asite kufyatua bastola yake ambayo ilikuwa imemlenga vizuri sana kisogoni, wakati akimvuta yule msichana kuelekea kwenye gari.


Lakini sababu nyingine, ambayo Othman Mchopanga aliiona ya msingi zaidi ilitokana na malipo. Fedha alizolipwa, japo zilikuwa nyingi, bado hazikumhusisha Joram Kiango. Uzito wa jina lake na ukali wa kiu ya damu yake kwa mwajiri wake vilifanya aamini kuwa pato lake lingepanda maradufu kama angezungumza kabla sio baada ya kuitekeleza kazi hiyo. Hivyo, wakati Joram Kiango na msichana wake wakiondoka uwanjani hapo yeye pia aliliendea gari lake, aina ya pajero, na kulitia moto. Aliwafuata kwa mwendo wa wastani akiruhusu magari matatu au manne kuwatenganisha. Wakati huohuo simu yake ya mkononi ilikuwa hai ikitoa taarifa ya mwenendo


wa mambo uwanjani hapo.


“Joram tena!” Sauti upande wa pili ilifoka. “Na bado hukumwua!”


“Ningeweza kumwua. Hata sasa bado naweza kumwua vizuri tu, yeye na yule msichana wake anayeonekana anataka kufa mara mbili. Lakini unajua hatujazungumza mzee?”


“Kuzungumza nini tena?” “Dau.”


“Dau?”


“La kichwa cha Joram Kiango.”


“Akh! Hilo tu! Ungemuua, halafu tukazungumza.”


“Unajua huwa sifanyi kazi kwa mkopo mzee? Joram anaweza kufa wakati wowote, usiku huuhuu. Lakini si kabla ya kupokea dau langu.”


Sauti upande wa pili ilionyesha hasira kidogo iliposema, “Huu ni usiku sana. Kesho saa mbili utalipata dau lako. Lakini Joram na huyo malaya wake lazima wafe usiku wa leo. Jua likichomoza kesho, wangali hai, kazi itakuwa imekushinda.”


Mchopanga aliitafakari kauli hiyo kwa muda. Aliujua ugumu wa kumwachia Joram Kiango usiku huo ili apate malipo yake


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog