Search This Blog

Thursday, 29 December 2022

MPANGO WA NJE NI PIGO BUTU LA KIFO - 4

   

Simulizi : Mpango Wa Nje   Ni Pigo Butu La Kifo

Sehemu Ya Nne (4)





Dokta Omary hakuridhika na alichokitoa kifuani mwake laiti angalikuwa na mke ni wazi angalimtapikia siri zote akabaki uchi ila hakuwa na mke Daktari huyu wala Papi. Waliishi wabweni hawa mabwana. Usiku wa siku hiyo chungu kama Mualovera, Dokta Omary Maboli siki alichukua kitabu chake kidogo akachota namba za simu kutoka kwenye kitabu hicho ambacho kilikuwa na namba tatu tu akataka kupiga mahali hata hivyo akapuuzia wazo lake, akafikiri kwa muda mtu atakaye kumpigia alikuwa yu mahala gani kwa majira hayo, akapata kujua kuwa kijana huyo alikuwa zamu ya usiku hospitalini basi akakata shauri na kuamua kuipiga namba hiyo.




"Dokta, Gabriel?" Aliita Dokta Omary baada ya simu ya ofisi ya upande wa pili kupokelewa.




"Naam, baba?" Dokta Gabriel Nyagile kijana ambaye alikuwa akimheshimu sana Dokta huyo kwa ukubwa kiumri na ukongwe kazini.




"Kama sitakuwepo leo au kesho waambie wamtafute Musa!" Akakomea hapo. Ilikuwa ni kauli tata iliyomuacha Dokta Gabrie Nyagile kijana mdogo katika utata uleule. Akauliza kuhusiana na mtu huyo aitwaye Musa hata hivyo hakukuwa na maelezo mengine ya kuridhisha zaidi ya kusema kuwa wapo kwenye vitisho vikubwa. Hakujua yeye na nani? Hili nalo likamchanganya Dokta Gabriel. Akabaki akining'inia asijue aende wapi.




"Tazama usalama wako!" Akamuongezea utata mwingine kisha akaifisha ile simu na kuitua mezani. Mkono ukimtetemeka akakirudisha kile kitabu kidogo cha kumbukumbu akakiweka kwenye kichanja cha meza akasubiri ujio wa watu hao watishi kama upo au ni vitisho tu pekee hakutaka kufanya chochote kwa jeuri.




Kwa upande wa Dokta Lumoso Papi Mmbai mambo yalikuwa ni tofauti na yalivyokuwa upande wa pili. Yeye hakumpa taarifa mtu yeyote juu ya kitisho alichopokea, alichokifanya yeye ni kujificha kwenye maabara yake ya nyumbani akaanza kuandika ripoti ambayo ilikuwa ndefu sana, hii aliandika kutokana na maelezo aliyopewa, kichwa cha ripoti ile ilikuwa kuhusiana na uchunguzi ambao hata hakuufanya kisha akaandika neno U.N.G.A.M.O kwa hati hafifu ya mkono chini kabisa kwenye kona ya karatasi, ilihitaji utulivu wa akili kuweza kuigundua hati hiyo kwa namna ilivyoandikwa kwa kificho. Kuna baadhi zilichapwa na hizo zilikuwa ni kutoka kwenye hifadhi ya chunguzi zake baada ya hapo akaambatanisha na ile ripoti ambayo ilihatiwa kwa mkono chini ya karatazi ya kuchapwa akaandika neno "Musa" ambalo aliliwekea funga na fungua semi akiwa na maana kuwa lilikuwa ni jina tata.




Kuna baadhi zilichapwa na hizo zilikuwa ni kutoka kwenye hifadhi ya chunguzi zake baada ya hapo akaambatanisha na ile ripoti ambayo ilihatiwa kwa mkono chini ya karatazi ya kuchapwa akaandika neno "Musa" ambalo aliliwekea funga na fungua semi akiwa na maana kuwa lilikuwa ni jina tata.




"Ushahidi wa watakaotutafuta kama tutatekwa ama kuuawa!" Akajisemea kisha akaitazama radio kaseti ya kizamani ambayo ilikuwa ikimrekodi kwa kila alichokuwa akikifanya akasikiliza akaona inafaa sana akaweka tena rekodi na kuunganisha na waya mwembamba sana wa rangi nyeusi ambao aliupenyeza sehemu ambazo katu zisingeweza kuonekana kwa urahisi huu ulikwenda hadi chini ya rafu ya vitabu. Akasema.




"Chini ya rafu ya vitabu!" Kisha akaiweka radio ile kwenye sehemu ambazo aliamini jicho la mtu yeyote lisingeweza kuiona labda awe makini na mpelelezi wa hali ya juu sana. Alipohakikisha kuwa kila kitu amekifanya sawia, akatulia pale mezani na kuendelea na tafiti zake za utambuzi wa dawa kupitia mimea na mchangacho wa baadhi ya kemikali. Ilipotimu saa sita kasoro dakika tano usiku, Dokta Lumoso Papi Mmbai alisikia kishindo mlangoni baada ya mlango kufunguliwa. Kishindo hiki kikamjulisha kuwa ni watu waliyomuahidi kuja. Walipofika walimuuliza maswali kadhaa akiwa hapo kwenye chumba cha uchunguzi naye akajibu vile atakavyo na kuwauliza maswali akiwa na maana maalumu baada hapo walimvuta hadi sebuleni kisha kumuuliza kama amefanya uchunguzi ambao alipewa maagizo yake.




"Uchunguzi upi?" Akawauliza.




"Hukuandaa ripoti yoyote?" Wakauliza tena. Walikuwa ni vijana wawili weusi waliyovaa mavazi meusi pia huku yule mweupe akiwa haonekani.




"Inayohusiana na nini?" Akawauliza tena pia, hakuwajua kwani aliyekuja mchana alikuwa ni mzungu na hawa walikuwa ni watu weusi, ni lazima ahoji kile alichohojiwa. Mara kishindo kingine cha kufunguliwa kwa mlango kikasikika. Akaingia Tally yule mrusi.




"Tayari mwenzake yuko garini ameshalala." Akasema kisha akamkwida na kumburuza hadi kule chumbani ambako kulikuwa na tafiti akimuhoji swali hili na lile na Dokta Lumoso akijibu vile atakavyo na kuwahoji atakavyo akijua kuwa ile radio ilikuwa ikirekodi hivyo kwake ni ushahidi utakao bakia.




"....nyinyi ni akina nani na kwangu mnataka nini....?"


".....wewe ukifikiria unadhani sisi tumekuja kufanya nini kwako....? Unadhani tumekuja kwa ajili ya kupata matibabu labda au kuja kupima magonjwa mbalimbali kama gono, kaswende, pangusa, ukoma au kifua kikuu....? Au unafikiri nini zaidi Dokta....?


Hayo ndiyo yalikuwa maswali ya kimajibizano baina ya Dokta Lumoso na watu hao na mwisho ikawa ni.




".....Musa anakuhitaji kwa udi na uvumba na ndiye aliyetutuma tukupeleke kwake.....hakuna cha kutupotezea muda. Mchome sindano ya usingizi tuondoke naye." Amri ilitolewa. Ndipo dokta Lumoso alipopiga kelele za maumivu kisha wakamtitika baada ya kulegea na kumtoa nje huku wakiufunga ule mlango kwa nje wakiwa na uhakika hakuna alama yao waliyoiacha.




__________




Dokta Lumoso Papi Mmbai alifumbua macho na kujikuta akiwa kwenye chumba safi kilicho na kitanda safi pia. Akajitazama alivyo, akatazama mahali alipo ni kama alikuwa hajui nini kimeweza kumkuta, hali halisi ya hapo alipo ilikuwa tofauti sana na iliyomtisha. Chumba japo kilikuwa kikubwa chenye kila kitu kifaacho kwa mwanadamu anayeishi kutokana na hali yake ya hewa aliyohisi hata hivyo hakikuwa kile alichokizoea. Alipotazama vizuri akagundua kuwa chumba hicho kilikuwa kikubwa na chenye giza ambalo halikuweza kumuonesha yaliyo mengi kwa usahihi. Upande wa mbele magharibi mwa chumba kile kulikuwa na kitanda kingine na juu yake kulikuwa na mtu ambaye alilifahamu hilo mara baada ya mtu huyo kupiga chafya kali.




"Nani huyu....? Kwani hapa niko wapi....?" Akajiuliza angalau aone namna ubongo wake unavyofanya kazi. Jibu hakulipata la yule ni nani ila hili la yuko wapi? Likajenga mlolongo wa kumbukumbu dhidi ya waliokuwa wakimpa vitisho hadi kufikia hapo.




Tumetekwa! Akawaza mara baada ya kumbukizi ile kumpa majibu ya kuwa huwenda yuko sambamba na Dokta mwenzake, Dokta Omary Maboli Siki. Walikuwa hapo kila mmoja akiifungua tafukuri kichwani mwake kwa namna ya pekee, mlango ukafunguliwa taratibu kisha mwanga mkali kuwaka mara baada ya mtu aliyeingia humo kuiwasha taa iliyofanikiwa kulitorosha giza lililokuwa limekimeza chumba hicho.




"Mmeamka? Karibuni sana Sami Ado wataalamu natumai mtayapenda mazingira haya mapya hata hivyo ni mazingira mazuri yasiyo na vurugu. Mtakuwa mkifanya kazi kwa malipo na mtaishi kwa amani kubwa ila tu hamtakuwa huru kutokana na unyeti wa jambo hili namna lilivyofanyika. Pumzikeni na ifikapo saa tano asubuhi mtapata kifungua kinywa kizito kishapo mtajua kilichowaleta hapa." Aliongea kijana yule ambaye Dokta Lumoso Mmbai alikuwa akimfahamu kwa jina la Tally. Baada ya kuongea hayo akawaacha na kutoka. Akapita kwenye Kori moja ndefu ambayo ilikuja kumfikisha kwenye subule ile wapendayo kukutania.




"Wameamka tayari." Aliongea Tally. Malfrey akamtazama na kusema.




"Nadhani wapelekewe tu kifungua kinywa muda huu, sasa ni saa nne hivyo ni vema ikawa haraka kwani hali ya Maleley ni mbaya sana kwa sasa hivyo vipimo vinahitajika kwa haraka ili tiba ianze. Hilo lilikuwa ni agizo na si ombi. Tally Man akatoka hapo na kupeleka taarifa mahali husika. Kifungua kinywa kilipokuwa kikiandaliwa, akaenda kuwapa taarifa wageni wale kuwa wanaweza kujisafisha vinywa vyao kwani kila kitu kilikuwa humo kwani hicho ndicho kingekuwa chumba chao.




Hakuna aliyemsikiliza.


Wakaletewa kifungua kinywa wakalazimishwa kula kwa vitisho na kuambiwa kama hawaitaki amani wataishi kwa mateso makali wakiambiwa kuwa ole wao Maleley afe kwa uzembe wao. Hii ikamfanya Dokta Lumoso afikirie sana akaona hakuna namna kwani walipo ni ugenini na njia waliyotumia kufikishwa hapo haikuwa ya kutambulika.




"Inabidi tuishi kwa matakwa yao." Akaongea Dokta Lumoso. Dokta Omary akamtazama mwenzake kisha akasema.




"Ndugu yangu, sikusomea hii taaluma nije kuwa mtumwa bali nimesoma kwa shida ili nilisaidie taifa langu. Nitakubali kufanya kazi hii kwa sharti moja pekee, mtu wao akipata afueni tunarudi nyumbani." Dokta Lumoso akafikiri kwa mapana akaona namna mwenzake alivyo akijidanganya. Upo utaratibu wa kufanya kazi hata nje ya nchi kwa kufuata misingi ambayo itakuruhusu kufanya kazi kisha baada ya kazi kwisha urejee kazini kwako. Hii haikufuata taratibu na haijulikani huyo mgonjwa anasumbuliwa na nini. Mwenzake alikuwa akijidanganya.




"Sawa tuombe Mungu japo sidhani maana ujio wetu hapa si wa kiungwana kabisa." Akasema Dokta Lumoso akiwa anakula taratibu. Walipomaliza kula walipumzika kidogo na kuchukuliwa hadi kwenye chumba maalumu ambacho kilitengenezwa kama wodi. Kulikuwa na kitanda kimoja tu cha kulazia mgonjwa ambacho kilikuwa kimezungushiwa msutu na msutu ule ulipofunuliwa juu ya kitanda hicho wakamuona bwana mmoja wa kizungu ambaye alikuwa amekonda sana kiasi cha mbavu na mitulinga kuanza kuonekana. Sura ilikuwa imenyauka kama Karara lililopigwa na jua, macho yaliingia ndani na kubakiwa na mashimo makubwa huku vifupa vya taya na juu kidogo ya mashavu vikionekana waziwazi. Alitisha kumtazama. Walimuwekea utaratibu wa kujisaidi kutokana na hali yake ilivyotete. Hakuwa na fahamu kwa wakati huo.


"Anamuda gani tangu kuwa kitandani?" Akauliza Dokta Lumoso Papi Mmbai. Alikubaliana na hali halisi kwani akilini mwake kulikuwa na kauli isemayo 'Nanga kwa amari yafuata mkumbo'. Mwenye nguvu anazo ambaye huna jiteteme uikinge roho.




"Miaka nane sasa kichwa kiuchagoni hanyanyuki, uzima wake ni mtikisiko wa ukakamavu umjiapo," akajibu Malfrey ambaye naye alikuwa yu adema maana nguvu zilipungua kwa kukosa amani juu ya afya ya pachaye. Labda ndio ile imani kuwa pacha hushirikiana kwa kila kitu hadi maradhi.




"Mlishajua anasumbuliwa na nini?" Alihoji Dokta Omary Maboli.




"Hakutaka atibiwe na tabibu yeyote yule kutoka nje alikuwa akiwasubiri ninnyi maana hili ni anguko la maudhi lililomuangukia. Hakuna zaidi mtakachotakiwa kujua zaidi ya kumtibia baada ya kujua mgonjwa ni nini anachosumbuliwa nacho, kinyume na hapo ni siri na hampaswi kujua kwanini hakutibiwa nje au kwanini hakutafutwa tabibu wa nje." Alijibu kwa jeuri Malfrey. Akaongezea.




"....Vipimo vifanyike sasa ili nijue ndugu yangu anasumbuliwa na nini na nini itakuwa tiba yake." Alipomaliza kusema hayo wataalamu hao wakaingizwa kwenye chumba kingine ambacho kilikuwa ni maabara kubwa iliyokamilika kwa kila kitu. Watu hao walijipanga vya kutosha hadi hali hii ikaanza kumtisha Omary Maboli kwani kama watu hao walikuwa na uwezo wa kununua hadi mashine za mionzi vifaa vingine vya gharama kubwa kwa ajili ya matibabu yao binafsi na kuweka ndani huwenda maisha yao yakaishia hapo kama madaktari watakaokuwa chini ya mapacha hao. Moyoni alipinga kabisa na kujihakikishia kuwa lazima aondoke baada ya mtu huyo kutengemaa na kama mwenzake atabaki ni yeye na si yeye. Walivaa mavazi ya kazi na kuchukua vifaa vya kazi kwa ajili ya kuchukua vipimo. Walifanya kazi hiyo kwa muda mrefu sana na mwisho wakaamua kupata uchunguzi kamili kwa kuamua kumpima mgonjwa kwa kutumia mashine maalumu ambao huonesha taarifa zote kwenye mwili wa mwanadamu. Waliingia maabara na kutulia kwa takribani masaa kumi na nane.










Walivaa mavazi ya kazi na kuchukua vifaa vya kazi kwa ajili ya kuchukua vipimo. Walifanya kazi hiyo kwa muda mrefu sana na mwisho wakaamua kupata uchunguzi kamili kwa kuamua kumpima mgonjwa kwa kutumia mashine maalumu ambao huonesha taarifa zote kwenye mwili wa mwanadamu. Waliingia maabara na kutulia kwa takribani masaa kumi na nane. Waliweka kando kula na miili yao ikaingia kazini huku akili zao zikiwa macho wakati wote.




"Aisee!" Akahamaki Dokta Lumoso Papi Mmbai.




"Kuna chochote umegundua?" Akauliza Dokta Omary Maboli akilitoa jicho lake kwenye Hadubini akiwa anawavuta baadhi ya bakteria aliyowatoa kwenye vipimo kuwapatia utambuzi wa maumbo na majina yao.




"Ana Saratani ya Ubongo!" Aliongea Dokta Lumoso Papi Mmbai akijiweka kwenye kiti sasa baada ya kusimama kwa kitambo kidogo.




"Kunauvimbe ubongoni?" Akauliza Zaidi Dokta Omary akijisogeza kwenye mtambo ambao ulileta majibu hayo, akiwa hajajibiwa aliona, akakubaliana na matokeo hayo.




"Yaa, anauvimbe mkubwa kiasi ndani uliogemea fuvu sehmu ya ubongo wa kati," akasema huku akirudi kitini kwake.




"Achana na vyote tuandae ripoti tukitoka hapa ni kula na kupumzika ndipo tuwape matokeo ya vipimo vyetu." Alitoa wazo Dokta Lumoso, wazo hilo likakubalika na wakaanza kazi hiyo ya kuandaa ripoti ya uchunguzi iliyoshiba, wakaipeleka kwenye ofisi nyingine hapo ndani ikachapwa na kukusanywa pamoja. Wakapumzika hadi kulipokucha. Walichoka sana hata hivyo ilikuwa ni lazima wawaambie kile kilichokuwepo maana hakukuwa na namna nyingine. Walipata staftahi asubuhi hiyo kisha wakakutana kwenye chumba cha maongezi kwa ajili ya kuwasomea ripoti hiyo ya kitabibu. Dokta Omary Maboli alimuachia kazi hiyo mwenzake kutokana na yeye kuwa bingwa wa maradhi husika.




"Nini kinamsumbua ndugu yangu Daktari?" Akauliza Malfrey akiwa ametoa macho akisikiliza pembeni yake akiwapo Tally Man.




"Ndugu yako alikuwa akitumia dawa za kulevya au?" Akauliza Dokta Lumoso Mmbai.




"Ni muda mrefu tulikuwa tukitumia wote mimi nikaacha ila mwenzangu akawa bado anatumia na aghalabu huwa namuona akitumia Buruma."




"Huwenda hiyo Buruma ndiyo anayoitumia kuvutia. Nduguyo ana Saratani ya Ubongo," akasema Dokta Lumoso huku akichomoa sigara moja kutoka kwenye pakiti na kuiwasha kwa kiberiti cha gesi akapuliza moshi kwenye pembe ya mdomo. Aliuona mshtuko mkubwa uliyomkumba bwana huyo hata hivyo hakujisumbua kujiingiza kwenye huzuni aliyonayo huyo bwana, alifanya kazi yake kama Daktari. Aliifunua karatisi moja ya juu na kuchungulia ndani kisha akamtazama bwana huyo aliyetayari kusikiliza akaifunika na kusema.




"Hii ndiyo ripoti nzima ya uchunguzi wetu na namna ya ugonjwa huu ulivyo na unavyotibiwa." Akaweka tuo na kuifunua tena akavuta sigara yake na kusoma kilichomo.




"....kama mjuavyo kuwa Ubongo ni moja wapo ya kiungo muhimu katika mwili na ni kitovu cha mtandao wa mishipa ya kusafirisha damu mwilini. Ubongo na Uti wa mgongo vinaweza kuwa na uvimbe wa Saratani ingawa ni nadra sana, ugonjwa huu ni hatari sana ikiwa hautatibiwa mapema." Akamtazama vizuri Malfrey kabla ya kuendelea.




"....kisababishacho Saratani ya Ubongo hakijulikani hata hivyo kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha ugonjwa huu na ni kama yafuatayo; unaweza kuwa na saratani kwenye sehemu nyingine ya mwili na ukiwa na Saratani katika sehemu nyingine za mwili huweza kusambaa hadi kwenye ubongo. Pia kufanya kazi katika kampuni za kusafisha mafuta, kutumia dawa za kulevya kwa kunusa muda mrefu, kampuni za kutengeneza bidhaa za mipira au hata kampuni za kutengeneza madawa kwa muda mrefu vinaweza kukusababishia Saratani ya Ubongo." Hapa Dokta Lumoso Papi Mmbai akatulia.na kuivuta sigara yake taratibu.




"Ndugu yangu hakuwahi kufanya kazi kwenye kampuni hizo sasa hii inakujaje Dokta?" Akauliza Malfrey akiwa katika utulivu wa hofu.




"Kama umemsikiliza Daktari vizuri mwanzoni alisema kuwa ugonjwa huu visababishi vyake huwa havijulikani, hivi vinavyoorodheshwa hapa ni moja ya sehemu tu ambazo ni visabishi vinavyotambulika." Alijibu Dokta Omary Maboli. Malfrey akatulia na Dokta Lumoso akaendelea.




"Dalili ya ugonjwa huu wa Saratani ya Ubongo huwa haitabiriki. Uvimbe unaweza kujitokeza katika sehemu yoyote ya ubongo na kwa hali hiyo hivyo ni lazima dalili zitofautiane. Mathalani uvimbe ukitokea sehemu ya mbele (frontal). Mgonjwa huweza kuhisi hali hizi zifuatazo; anaweza kuumwa na kichwa, anaweza kupata ulegevu wa mwili, kufa ganzi sehemu moja ya mwili, kupatwa na mabadiliko ya haraka mwilini kama hisia, moyo au hata mabadiliko ya tabia, pia mgonjwa anaweza kuchanganyikiwa na akili. Uvimbe ukitokea sehemu sawia (parietal). Pia mtu anaweza kuumwa na kichwa, kushikwa na kifafa, mwili kufa ganzi, mgonjwa anaweza kupata shida anapoandika hati, kupata shida anapojaribu kusonga au kujongea kwa namna fulani, pia mgonjwa anaweza kushindwa kufanya hesabu hata rahisi tu. Vilevile akipatwa na uvimbe sehemu ya nyuma (occipital). Hapa pia mgonjwa anaweza kuumwa na kichwa, kushindwa kuona vizuri, kuona maluweluwe, mazingara, mazingaombwe yaani hali ya kujitisha mwenyewe. Hapa mgonjwa anaweza hata kupayuka kwa kupiga mayowe kwa kitu ambacho hakionekani kwa watu wengine ila yeye anakiona, pia hapa mgonjwa huweza kushikwa na kifafa. Hata hivyo uvimbe unaweza kutokea ghafula na kwa muda mfupi (temporal). Yaani si ule ambao huanza taratatibu. Aina hii ya uvimbe pia humfanya mgonjwa kuumwa na kichwa, kushikwa na kifafa vilevile, kushindwa kufuata maagizo ya pamoja yaani yeye hufuata kile anachohisi kinafaa kwa wakati huo na si makubaliano ya pamoja, mpingifu, pia anaweza kushindwa kupambana na mwangaza." Akaweka tena tuo akaitazama sigara yake iliyokuwa ikiteketea kwenye pacha ya vidole vyake akaikung'uta jivu kwenye kikombe kigumu cha udongo cha majivu akaivuta kwa utulivu mkubwa na kuuvuta moshi ndani kabla ya kuutoa kwa mkupuo kinywani na kwenye tundu zake za pua. Akamtazama Malfrey aliyekuwa akimtazama yeye kwa kila kitengo alichokuwa akikifanya kama Paka aliyeona Samaki anayechuruzika mchuzi ulioungwa kwa nazi kwenye mikono ya Daktari huyo asiye na papara katika kueleza.




"Dokta.....!" Akaita Malfrey kwa lengo la kuuliza hata hivyo Dokta Lumoso Mmbai akamuwahi.




"Lakini vilevile mtu anaweza kupata uvimbe kwenye mtandao wa mishipa, muhanga akipatwa na uvimbe kwenye mtandao wa mishipa huweza kumfanya ashindwe kusimama wima, kutapika na kubadilika ghafula kwa hisia." Akanyamaza na kumtazama huku akiivuta sigara yake kwa pozi kubwa akimtaka aulize sasa alichotaka kuuliza.




"Sasa Dokta imaana ndugu yangu ndiyo basi tena, hawezi kupona ndugu yangu au hata kuudhibiti huu ugonjwa usiendelee angalau asimame basi!" Alichachawa Malfrey, sura yake ikiwa nyekundu kwa hofu ya kumkosa nduguye. Dokta Lumoso Mmbai alimtazama kwa masikitiko kama sifa ya mwanadamu mwenye upendo na ujalifu kwa wanadamu wenzake kisha akaipachika sigara kwenye kingo za midomo yake na kuivuta.




"Hapana Malfrey, ugonjwa huu unao namna ya kudhibitika, kuna uwezekano wa kuudhibiti na nduguyo akatengemaa, Mungu anaweza kusaidi kwenye hili." Akatulia kidogo na kusema.




"....kwa kawaida Saratani inaweza kutibiwa kwa kufanya upasuaji, tibakemo, matibabu kwa njia ya Eksirei, matibabu ya tibamaradhi, matibabu ya monokloni ya kingamwili au njia nyingine. Uchaguzi wa upasuaji hutegemea mahali uvimbe ulipo na daraja lake na hatua ya ugonjwa huo pamoja na hali ya jumla ya mgonjwa (hali ya utendaji). Idadi kadhaa ya matibabu ya Saratani ya Ubongo ya majaribio hayajatengenezwa kikamilifu; hii inamaana gani? Hii inamaana ya kuwa mgonjwa mwenye Saratani ya Ubongo ana asilimia chache sana za kupona kiukamilifu. Mgonjwa anaweza kupunguziwa makali ya ugonjwa lakini uvimbe huo huweza kutunga sehemu nyingine au pale pale ulipoondolewa na kusababisha mgonjwa wa namna hii kufanyiwa upasuaji mara kwa mara ili tu kumfanya aendelee kuishi lakini pia kuzuia ugonjwa usisambae sehemu nyingine za ubongo na kuleta ugumu wa matibabu yake zaidi." Akavuta pumzi kidogo na kuendelea.




"....kuondolewa kikamilifu kwa saratani bila kuharibu sehemu nyingine za mwili ndilo lengo la matibabu. Pamoja na njia nyingine za kutibu ugonjwa huu hata hivyo wakati mwingine jambo hili linaweza kutimizwa kwa upasuaji hata hivyo iwe ni kabla ya Saratani hii haijavamia tishu zilizo karibu au kuenea kwenye maeneo ya mbali kupitia uenezi mdogo sana kiasi kwamba hauwezi kuonekana kwa macho aghalabu huzuia ufaafu wake. Ufaafu wa tibakemo aghalabu huzuiwa na kiwango cha kusumisha kwenye tishu zingine katika mwili na hata mnururisho unaweza kuharibu tishu kawaida. Kuhusiana na mgonjwa wako Malfrey, ni hatari sana kutumia tiba nyingine. Hatari hii inaweza kusababisha maafa makubwa na nduguyo kuingia kwenye kupooza kabisa maana unaweza.....unaweza kujikuta umegusa tishu nyingine au kuhamisha vimelea vya ugonjwa huu mahali pengine ikawa ni kuzalisha kazi mpya badala ya kumaliza kazi. Uvimbe wa mgonjwa wako upo ndani na umeegemea fuvu la kichwa la kati, kuwepo kwa uvimbe hapa ndiyo maana mgonjwa wako akawa na dalili ambazo nilikuorodheshea hapo juu na kadiri uvimbe huu unavyokuwa ndivyo huzidi kuleta mgandamizo mkubwa kwenye ubongo kiasi kwamba mgonjwa wako angefikia hatua ya kuwehuka au kupoteza kabisa nguvu ya kufanya maamuzi ya kawaida au hata kupoteza maisha. Kama uvimbe ungekuwa umetokea sehemu nyingine ya mwili lingekuwa ni jambo linalowezekana kutimia kwa haraka na hata kwa njia nyingine za kimatibabu lakini uvimbe huu uko sehemu ya kati tena ya ndani kabisa ya Ubongo, ni hatari sana kufanya hivyo na hakuna njia nyinge zaidi ya upasuaji." Akahitimisha Dokta Lumoso Papi Mmbai na kuisogeza ripoti ile pembeni akaimalizia kuivuta sigara yake kwa pafu kubwa kisha akaitupia kwenye kikombe cha majivu.








Kama uvimbe ungekuwa umetokea sehemu nyingine ya mwili lingekuwa ni jambo linalowezekana kutimia kwa haraka na hata kwa njia nyingine za kimatibabu lakini uvimbe huu uko sehemu ya kati tena ya ndani kabisa ya Ubongo, ni hatari sana kufanya hivyo na hakuna njia nyinge zaidi ya upasuaji." Akahitimisha Dokta Lumoso Papi Mmbai na kuisogeza ripoti ile pembeni akaimalizia kuivuta sigara yake kwa pafu kubwa kisha akaitupia kwenye kikombe cha majivu.




"Inamaana Dokta upo uwezekano wa ndugu yangu kusimama?"




"Ndiyo, hata hivyo si kama awali japo anaweza kuendelea na taratibu zake"




"Nitafarijika sana Daktari na utakuwa umefanya jambo la maana kuliko yote uliyowahi kuyafanya kwenye maisha yako" alisema Malfrey. Dokta Lumoso akamtazama bwana huyo akamuona jinsi anavyouendeleza ubaguzi wake na ushetani wa kutokumjua Mungu kupitia maneno yake, yaani yeye hakuna jambo lenye umuhimu alilowahi kulifanya kwenye maisha yake na hilo la kufanikisha kumtibia nduguye ni la kwanza.




Upuuzi.




Hata hivyo Dokta Lumoso hakuwa na namna wakaahidi kuwa ifikapo saa sita mchana Maleley angeingizwa kwenye chumba cha upasuaji. Wakaondoka hapo na kuelekea mahala pengine ambapo huko walitulia kwa muda mrefu huku wakipitia vitu mbalimbali ambavyo vingeweza kuwaongezea umakini wawapo ndani ya chumba cha upasuaji. Waliweka akili sawa na muda ulipofika waliagiza mgonjwa huyo aingizwe chumba cha upasuaji.




"Malfrey, cha msingi ni kumuomba Mungu, hakuna kazi ngumu kama kufanya upasuaji. Kibinadamu huwa hatuombi kazi yetu ifeli japo tunafanya kazi ambayo tunaamini ina majibu ya aina mbili kufeli na kufanikiwa. Kufanikiwa hakuna shaka sababu unaweza kufanikiwa kikamilifu au unaweza kufanikiwa kwa uchache na ikawa rahisi kurekebisha. Huku kwenye kufeli ndiko kwenye shida maana unaweza kufeli kidogo tu hii ukarekebisha na kufauli hata hivyo unaweza kufeli vibaya sana na ukaambulia kifo. Mungu awe mbele ya kazi yetu na Mungu atuongoze katika kile tunachokwenda kukifanya. Sisi tumemtanguliza Mungu mbele basi hata wewe huna budi kumtanguliza Mungu mbele ili maombi yetu yatakapokutana yawe na nguvu ya uhitaji wa msaada mbele zake." Alifanya maombi Dokta Lumoso Papi Mmbai na kumwambia Malfrey. Malfrey akaweka dharau pembeni hata mbele za Mungu na kuitikia kwa moyo wa uhitaji.


Amen.




_________




Dokta Lumoso awapo kwenye kazi ya kuokoa maisha ya mtu huwa na huruma sana hapa huweka chuki pembeni na kuvaa sura ya kazi. Hakuwa na haja ya kuwaza kurudi nyumbani wakati kulikuwa na mtu alikuwa akiihitaji taaluma yake ili Mungu azidi kumfanya aweze kumhuisha tena kiakili na kimwili. Waliingia kwenye chumba hicho wakiongezewa muuguzi mmoja kwa ajili ya kutoa msaada huu na ule. Wakavaa mavazi husika ya chumba hicho kisha wakaingia kazini. Haikuwa kazi nyepesi, ilimaliza masaa nane hadi kwisha kwa upasuaji huo. Walimrudisha tena wodini kwa ajili ya kuendelea na huduma nyingine huku akisubiriwa arejewe na fahamu.




Majuma mawili yalitosha kumuamsha Maleley kitandani akawa anaweza kutembea na kufanya kazi nyingine. Akili yake ilikuwa sawa na alichoamka nacho ni kuhakikisha anasimama tena na kuwaondoa wale wote waliokuwa kauzibe kwenye mapambano yake. Alipanga timu yake iliyokuwa ikiongozwa na Tally man shughuli ya mauaji ikaanza tena ilianza kwa kasi mno huku Maleley akiwa mstari wa mbele kama siyeye mwenye afya mgogoro inayohitaji mapumziko makubwa. Wiki moja baadaye katikati ya mauaji yasiyoeleweka, waziri wa nishati na madini alikoswa kuuawa kwa kuchomewa nyumba yake akiwa akiwa safarini huku wachomaji wakidhani alikuwa ndani, pamoja na kwamba yeye alipona ila familia yake iliteketea yote kwani ndiyo pekee iliyokuwa imesalia ndani huku waziri wa afya aliyeshirikiana na waziri wa nishati na madini akipigwa risasi akiwa ziarani jijini Haika, huyu hawakutaka wakosee tena. Jambo hili lilikuwa kama kumsukuma mlevi tu. Hofu ikaibuka upya baada ya kutulia, viongozi waliyoponea chupuchupu wakajificha. Malfrey akakasitika kwani kwenye orodha yake ya kuua alibakiwa na Jaji wa mahakama kuu Kiago Mathias, mwendesha mashitaka Masuka Mvungi, mkuu wa kituo kikuu cha Muavengero Mansuli Bingwa na Maviza kavishe pamoja na waziri wa nishati na madini aliyepita kwenye tundu la sindano hapo awali ambao walikuwa sumbufu kwenye mipango yake kwa namna tofauti tofauti.




"Kazi iliyobakia ni ndogo sana kwani sasa hivi hakuna wa kunizuia kwenye njia yangu. Nitauwa kila niliyemuwekea 'X' na nitaua kweli." Alipiga kelele Maleley akiwa amesimama kwa kutegemea fimbo maalumu ya kutembelea kwa kuwa mwili wake haukuwa na nguvu. Akiwa hapo na watu wake wa karibu, Dokta Lumoso Papi Mmbai na Dokta Omary Maboli Siki waliingia kwenye chumba hicho alichokuwa akibwata bwana huyo mwenye chuki na viongozi wa taifa hilo utadhani kaonewa. Maboli akasimama mbele ya mabwana hao akiwa mkavu wa sura utani kauweka pembeni na kudai kuwa sasa kazi iliyowaleta hapa nchini imekwisha hivyo anahitaji kurudi nyumbani. Hii ilikuwa ni kauli iliyosababisha mapigo ya moyo ya Maleley Kobra kuharibu upigaji wake kwani wale aliwaona ni kama Miungu inayomfanya aishi japo aliwanyima uhuru wa kutembea na akiwafungia ndani ya himaya hiyo tu wakitoka ni kwenye bustani kuota jua na kurudi ndani, wakitaka kumkimbia na kumuacha katika hali tete inayohitaji huduma yao kila wakati. Hali hii kwa Dokta Maboli ilikuwa ni kama roho ndani ya moto wa Jehanamu. Kumuomba malaika mtoa roho akupe muda wa nyongeza na ilhali siku zako za kuishi hapa duniani zimekwisha. Alikuwa akijipalia makaa ya moto pasipokujua Daktari huyo.




"Unasemaje wewe nyani mweusi?" Akauliza kwa hamaki mzungu huyo mwenye dharau ya kurithi kutoka kwa mizimu ya babu zake iliyofia huko nchini Uingereza.




"Nahitaji kurudi nyumbani kazi yetu imekwisha." Akajibu kwa kiburi pia Dokta Omary.




"Hivi mnajua kuwa hata ndugu yangu ni mgonjwa na anahitaji huduma yenu, hivi mnajua....hamjui...? Labda hamjui....! Hamuwezi kwenda mahali sema tu kama unahitaji kufa wewe.!" Alifoka Malfrey.




"Ni sawa tu kama mtaniuwa lakini mimi siwezi kuishi kwenye mazingira haya kama Mbwa wa kufugwa, mimi ni Mbwa koko nimezoea kuzurura niacheni niende bwana?" Akafoka Dokta Maboli hadi Dokta Lumoso akamshika mabega na kumsihi atulie kwani hapo walipo hawana sauti. Dokta Maboli alimjia juu hata mwenzake na kumwambia kama yeye ameridhika kuishi hapo na aishi tu ila yeye anataka kuondoka. Dokta Lumoso alitaka kumwambia kuwa watanzania hawezi kukubali kupotea kwao hivyo wawe wapole kwani kuna alama ameiacha nyuma ambayo itawafikisha wapelelezi wao hapo hata hivyo aliona kama angeweza kupasua jibu na alishachelewa tayari. Kwa hali ile ikabidi kuwa mpole. Maleley alimuona Dokta Lumoso ni kama malaika mpole. Akasimama wima akiiweka sawa ile fimbo yake.




"Lumoso, wewe ndiye ninayekutegemea kwa kuwa hata ugonjwa wangu unakuhitaji wewe, sijawahi kupandwa utosini na kuku wa kinyavu mimi," alipokwisha kusema hivyo akarusha ile fimbo ambayo ilimpiga Dokta Omary Maboli Siki kichwani. Dokta Omary akapiga kelele sana kwa maumivu makali huku ile fimbo yenye chuma chini ikampasua utosini na kufanya damu zianze kumtoka kwa fujo kisha Maleley akamsogelea Dokta huyo na akamtandika ngumi nzito ambayo ilitua usoni kwa Dokta Omary ambayo ilimpeleka chini hata hivyo yeye mwenyewe ilimpeleka chini kutokana na kukosa muhimili kutoka mwilini mwake.




"Mvueni nguo na mumfunge kama ndafu nimle!" Alitoa amri Maleley kwa watu wake. Shughuli ya kumvua nguo ikafanyika akafungwa kidhalili sana Dokta Omary Maboli Siki. Kisha bwana huyo akamtazama na kusema.




"Sitakufukuza wala kukuwa. Nitakufanya mke wangu pale niwapo na kiu ya ngono, sitafikiria tena kusafiri kwenda mbali maana wewe upo, aaaah! Kweli Mungu hamtupi mja wake, nilikuwa nawaza kuwa nitamalizia wapi haja zangu za kibinadamu kama mwanaume rijali. Leo naonesha mfano kuwa utanifaa. Akameza kidonge cha kumsimumua mishipa ya mwili na kuipa uhai wa kuzidi zakari yake, na baada ya dakika tatu kupita Maleley akavua nguo zake za chini na kubakiwa mtupu kisha bila aibu wala huruma na hofu ya Mungu akachukua jukumu baya kabisa na linalomchukiza Mungu la kumuingilia Dokta Omary Maboli Siki kinyume.




Alimlawiti.


Dokta aliyekuwa akipigania haki ya kuwa huru, Dokta aliyejitoa kumsaidia mpuuzi huyo hadi anapona akiamini baada ya pale angerudi nyumbani Aaghr! Dokta Maboli Siki aliingiliwa kinguvu na kwa maumivu makali huku akikosa msaada hata wa kujitetea kwani mikono na miguu ilifungwa huku akifungwa madhubuti asiweze hata kutetereka. Alilia kwa uchungu sana, alilia mno kilio cha ndani kabisa ya moyo wake. Hakuwahi kufanyiwa ujinga huo leo anafanyiwa mbele ya kadamnasi haa! Iliuma sana. Bwana huyo na kile kidonge alichomeza alichukua muda kumaliza na hata alipomaliza bado walimuacha hapo wakaondoka. Dokta Lumoso hakulala siku hiyo, alilia usiku kucha kwani hakuwahi kudhani kama kwenye dunia hii kuna watu wamevishwa ngozi tu lakini roho zao ni sawa na vitukuu wa shetani.




Dokta Omary Maboli alikuja kufunguliwa siku ya pili akiwa hoi anayenuka kinyesi chake mwenyewe. Ilikuwa ni fadhaa kubwa, alijihisi haya kubwa sana hata kuwatazama wanaume wenzake machoni. Alishindwa kumtazama Dokta Lumoso usoni kwa aibu, akafikiri namna taarifa zake zitakapoingia nchini kwake ya kuwa kalawitiwa. Akaifikiria nchi ile jinsi ambavyo jambo hili ni la ajabu sana na litawashangaza wengi huku akikosa mahali pa kuuweka uso wake kama akirudi nyumbani. Chozi lilimdondoka kwa uchungu zaidi. Akaenda mbali zaidi katika kuwaza, akaisikia ile sauti ya mtu yule aliyemfanyia ukatili ilivyokuwa ikiunguruma mgongoni kwake kwa kufurahishwa na ukatili aliokuwa akimfanyia, mbaya zaidi akakumbuka kuwa mtu yule aliahidi kumfanya mkewe pale ahisipo hamu ya kufanya ngono.




Na nani sasa....? Swali likajitenga jibu alikuwa nalo kuwa hakuna mwingine ispokuwa yeye. Aaaaghr....! Aliumia Dokta Omary akaapa moyoni kuwa hana muda mrefu atakufa. Akawa wa kulia kila wakati hata akashindwa kumtazama mwenzake usoni mara zote muda wote akaishi akitazama chini mithili Kondoo.




Alipatwa na haya, haya isiyofichika.




USODOMA NA GOMOLA UPO NA UNAENDELEA KUWEPO.










Na nani sasa....? Swali likajitenga jibu alikuwa nalo kuwa hakuna mwingine ispokuwa yeye. Aaaaghr....! Aliumia Dokta Omary akaapa moyoni kuwa hana muda mrefu atakufa. Akawa wa kulia kila wakati hata akashindwa kumtazama mwenzake usoni mara zote muda wote akaishi akitazama chini mithili Kondoo.




Alipatwa na haya, haya isiyofichika.




"Sina muda mrefu nitakufa!" Omary Maboli alisema kwa sauti mbele ya Dokta Papi Mmbai huku bado akiendelea kutazama chini. Hakusema Kitu Dokta Mmbai, hakuwa na neno zuri la kumwambia mwenzake ambalo labda lingekuwa faraja kwake, kimya kirefu kikapita kati yao Lumoso na Maboli hata hivyo Dokta Lumoso akaona atakaa kimya hadi muda gani.




"Huu wote ni mpango wa nje Maboli tutarudi nyumbani na yatakwisha," akajaribu bahati yake Lumoso akimaanisha kuwa zile ndizo zilikuwa taratibu za watu weupe na hilo jambo halikuwa geni kwao kwani huko kwenye mataifa yao wenyewe wanaoana waume kwa waume. Akaahidi kuificha siri ile akamwambia yeye hajaona kitu chochote alichofanyiwa apige moyo konde lakini Maboli akakazia hapohapo kuwa hana muda mrefu atakufa. Dokta Lumoso Papi Mmbai akabaki na kauli hii asiyoijua ilibeba maana gani kwenye maisha ya mtu huyo. Chakula kwake hakikupita, hakula kabisa na hakukitaka chakula, alikuwa wa kulia kujiliza kila wakati.




Usiku ulipoingia kimya kilichukuwa nafasi hakuna aliyekuwa akitikisika kila mmoja aliamini mwenzake amepitiwa na usingizi, ilipotimu saa nane za usiku, Omary Maboli Siki akajinyanyua kutokea kitandani taa ilikuwa ikiwaka kwani hakuna aliyepata wazo la kuizima walipolala, akamtazama mwenzake na kumuona alivyotulia pale kitandani, akajisogeza kwa utaratibu hadi kilipo kitanda cha Lumoso. Lumoso alikuwa amefumba macho na kujifanya yu katika usingizi mzito kumbe alighilibu muda wote alikuwa macho na kilichomfanya kuwa macho hasa ni ile kauli ya mwenzake ya kuwa hana muda mrefu atakufa. Alimuona Omary Maboli Siki akijitoa mule chumbani bilashaka ni baada ya kujiridhisha kuwa yeye amepitiwa na usingizi. Alitoka pale akaufungua mlango na vyote hivyo alivifanya kwamwendo wa minyato sana. Hili lilimtisha sana Dokta Lumoso hakulifumbia macho hata kidogo akaonelea ni vema kama atajua ni nini mwenzake anataka kufanya akaamua kumfuatilia kwa nyuma taratibu huku akiwa makini sana. Alimfuta akamuona akiingia kwenye maabara, akazidi kushikwa na tahamaki akajituliza mahali ambapo anaona kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani. Dokta Omary Maboli Siki alikuwa akishika kemikali hii na ile, ile na hii. Akazidi kutulia ili ashuhudie kile kilichokuwa kikifanyika. Lo! Akagundua kuwa mwenzake alikuwa akitengeneza msombo. Aliogopo sana kuona kitu cha namna hiyo akajiuliza ni nini ambacho Dokta Omary anataka kufanya? Hakuwa na jibu la haraka ila utulivu. Akaendelea kutulia hadi pale alipomuona anaunyonya ule msombo kwenye bomba la sindano kisha kutoka mule maabara. Akakimbia Dokta Lumoso ili kutafuta kona nyingine ya kujificha, akamuona akielekea kwenye chumba ambacho alikuwa akikitumia Maleley Kobra.




"Mungu wangu! Omary anataka kuuwa?" Akahamaki. Ni mara baada ya kumshuhudia akipotelea ndani kabisa mwa chumba cha Maleley Kobra kwani mlango ule haukuwa umefungwa. Dokta Lumoso akazidi kusogea taratibu akachungulia akamuona Dokta Omary Maboli akiwa amesimama pembeni ya kitanda cha Maleley akilia kwa kwikwi ya chini kudhihirisha hasira zake na uchungu mwingi aliyonao dhidi ya mwanaume huyo. Aoliogopa sana Dokta Lumoso maana alijua fika nini kitakwenda kutokea baada ya mwenzake kuua. Kitu cha ajabu akakiona, alimshuhudia Dokta Omary akivua nguo zake zote na kubakiwa mtupu kabisa kisha akaushika mkono wa Maleley Kobra na kuidunga sindano kidogo hakuwa na wasiwasi kwani alikuwa akiyafahamu maisha ya Maleley Kobra kuwa alikuwa akiishi kwa kutumia dawa za kumuongezea usingizi hivyo hapo aliizamisha ile sindano taratibu baada ya kuidunga kwenye ngozi ya mkono wa bwana huyo, akamwaga msombo ule hadi nusu ya bomba kisha akachomoa na kusimama pembeni ya mtu yule ambaye alimuona jinsi atakavyokufa usingizini punde. Alisimama kwa dakika mbili ndipo akaliweka lile bomba la sindano pembeni kisha akamvua nguo Maleley Kobra muda huo wakati hayo yakiwa yanaendelea, Dokta Lumoso Papi Mmbai alijikuta akipata msukumo mkubwa wa kuvamia mule chumbani na kuichukua ile sindano na kutok nayo ili ndugu yake asiwahi kujiia. Akawaza namna itakavyokuwa pindi mwili wa Maleley ukikutwa umekufa tena kwa sumu, ni adhabu gani angepata Omary endapo akigundulika kuwa yeye ndiye msababishi wa jambo lile. Akaumia kuona hakuna namna ambayo angeweza kumuokoa na kifo kile kwani hata hivyo alishachelewa sana kufanya maamuzi kwani Dokta Omary Siki alishamaliza kumvua nguo Maleley Kobra na alipomaliza kumvua nguo zote hadi kufanana naye. Akajipandisha kitandani na kumpa mgongo mtu yule aliyemnasibisha na firauni, sura zao zikiwa zimeelekea sehemu moja ni kama mke na mume walalavyo kitandani. Akalikamata bomba la sindano barabara mkononi mwake akajichoma kwa nguvu kwenye bega lake la kushoto na kujisukumia msombo ule akalichomoa lile bomba na kulitupa pembeni, muda mfupi baadae akaanza kutetemeka kidogo na kutulia akiwa hana uhai. Dokta Lumoso aliumia vibaya sana hakuwa na namna ya kufanya kwa mtu yule ambaye kwa kitendo cha aibu alichofanyiwa tena mbele ya wanaume wenzake akaamua kujiuwa na kuuwa hii ilikuwa na maana kuwa alikuwa radhi kupoteza maisha pamoja na mtu yule aliyemfanyia kitendo cha kidhalili na kikatili.




Wakafa wote kweli.


Dokta Lumoso Papi Mmbai alielekea chumbani kwake akakitazama chumba kilivyokuwa kikubwa na jinsi jazanda la Dokta mwenzake litakavyokuwa likimzengea na kumletea shida usingizini ama hata mawazoni. Alikitazama kitanda cha mwenzake huku akiwa na imani kuwa mtu huyo asingeweza kulala tena mahala pale labda nafsi yake irudi pasi na mwili.




Siku iliyofuata Dokta Lumoso alishtuliwa na ukunga wa Tally Man sambamba na wafanyakazi wengine wakinadi kuwa Malfrey alidondoka na kupoteza fahamu baada ya kumkuta nduguye akiwa mfu. Kifo kile kilikuwa kichungu sana kwa Malfrey hata hivyo akashindwa kutoa hukumu aliporejewa na fahamu zake kidogo kutokana na namna alivyoshuhudia picha ilivyo. Bomba la sindano lilichukuliwa kutoka chini ya kitanda ilipojikatishia uhai miili ile na kuchunguzwa ili ijulikane ni nini kilisabisha kifo kile. Dokta Lumoso akasema kuwa ule ulikuwa ni mchanganyiko hatari sana wa kemikali ambazo kwa kuchanganya kwake ziliunda sumu hatari yenye kuuwa kwa sekunde sita hadi nane. Taarifa hii ikadhoifisha maisha ya Malfrey hata hivyo iliyarekebisha maisha ya mtu huyo kwa namna moja ama nyingine kwa kuweza kutoa japo uchache wa thamani kwa mtu huyo aliyekuwa akimuhudumia. Hali yake ilikuwa tia maji tia maji. Ndoto za Dokta Lumoso za kurudi nyumbani siku moja zikafifia na kupotea kabisa. Kwani yeye ndiye aliyetakiwa kusimamia hali ya kiafya ya Malfrey baada ya kuangushwa na ugonjwa usieleweka sababu wala dalili lakini alikuwa akiumwa kweli kiasi kwamba kuna wakati unaweza kuhisi kuwa mtu huyo angemfuata ndugu yake na kuna wakati alikuwa mzima kabisa na kumsahau kama ni mgonjwa mwenye kuhitaji msaada. Mtu pekee aliyekuwa akitoa msaada mkubwa hakuwa mwengine zaidi ya Dokta Lumoso Papi Mmbai. Alipewa akitakacho japo alinyimwa uhuru wa kutoka nje ya himaya hiyo. Dokta Lumoso hakuisha kufanya maombi kwani alibeba imani kuwa kwa usalama wa taifa lake aliamini ipo siku angekuja kuokolewa na kuishi maisha ya furaha kama ya awali na kuondokana na maisha ya upweke, maisha ya kuishi kwa ndoto zisizokwisha za kumuota mwenzake kila siku huku na yeye akiona huwenda kile kilichompata mwenzake pengine kingejirudia kwake. Akaona namna atakavyo kufa kwa presha.




Kuhemewa na mwanaume mwenzio...! Ebo!




Miaka ilizidi kukatika na ukafikia ule wasaa wa Malfrey kuamua kurudisha kesi yake upya. Bwana huyo akapanga mipango ya kuihuisha kesi ya kampuni yao upya ili kuitafuta haki yao hata hivyo hakufanikiwa aligonga mwamba kila alipojaribu alikutana na kigingi kizito kilichomrudisha nyuma, alijiona ni mkosaji. Hakuona kama anafaida tena ya kuishi kama angeshindwa kupambana akatepeta, nguvu akakosa akarudi Sami Ado kutokea muavengero akiwa hoi kiakili na kimwili. Aliposhuka kutokea kwenye Chopa yake akadondoka na kupoteza fahamu. Hali ikawa mbaya kwake akafanyiwa vipimo naye akagundulika anauvimbe mdogo ambao uko mbali sana kwenye ubongo wa mbele (frontal). Akafanyiwa matibabu kwa haraka sana ila siku aliyokuja kutoka nje akawa ndani ya machela. Na hakuamka tena huku akisemekana kuwa upande wa chini kuanzia kiunoni alipooza.




__________




"Huu ni muda wa kuzifunga kurasa na hakutakuwa na matatizo wala hofu kwa upande wetu tena kila kitu kinarudi kwenye upande wao. Hakuna kulia tena Malfrey kwani sababu ya kulia haipo. Watapambana na Mpango wa nje sisi watengenezaji tukiwa watazamaji tu." Aliongea kwa kujiamini sana Mr. Polgeo baada ya Malfre Kobra kueleza namna nduguye alivyohangaika kufanya kila kitu kwa ajili ya kuhakikisha anarejesha mali zake hata hivyo akafa kama Mbu kwenye Neti kwa sababu ya tamaa za ki-ngono. Mr. Polgeo akanyanyuka na kumsogelea Malfrey pale kwenye machela, akamtazama kwa muda kisha akasema.




"Waliyosalia watakufa na wasiyohusika watawauwa wenyewe kama Rais wa nchi hii akiwa na utaahira wa ubongo au akiwa kiziwi wa kuona ama kipofu wa kusikia."




"Ninayo matumaini sasa tena hili lianze sasa na lisikawie Mr. Polgeo. Himaya ya Musa inakusubiri huko Sami Ado nenda ukaishi kwa amani huku tukifanya yetu kwa kasi ya kimondo." Aliongea Malfrey akiupokea mkono wa Mr. Polgeo. Mr. Polgeo alitoka akifuatana na familia yake huku nyuma Malfrey alibakia na watu wake akatoa maagizo kwa Amsuni Bhehe ya kukutana na Black Scorpion ili wajue ni hatua gani wamefikia na kama itahitaji msaada kwake haraka sana taarifa hizo zifike. Akaondoka kwa kukokotwa hadi alipofika nje ambako Chopa yake ilikuwa ikimsubiri akaondoka na kuelekea Sami Ado ambako ndiko kulikokuwa na makazi yake. Japo waliishi kwenye jiji moja na Mr. Polgeo hata hivyo walifanya makutano yao Muavengero na si Sami Ado kwani jumba hili la Muavengero ndilo jumba waliloteuwa kwa makutano na si vinginevyo japo nalo pia lilikuwa na kila kitu kwa ajili ya afya yake isiyotabirika kama chumba kidogo cha maabara na kadhalika hata hivyo waliamua kupafanya ni kwa makazi ya muda mfupi na makutano. Hawakutaka kuyahusisha makazi yao na kazi hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kuu




___________




NILIJITANDA KHANGA NA VITENGE MITHILI YA MWANAMKE WA PWANI, nilikuwa nimevaa kipwani pwani zaidi japo sikuwa nimejidabagiza mapambo yenye kuleta walakini machoni mwa watu niliingia kama mtu niliye na ukaribu na familia ya wafiwa. Nilijiweka mbelembele ili niweze kuona yote yenye kuendelea. Usiku huu ulipoa sana eneo hili la msiba na anga kwa majira hayo ilikuwa ng'avu isiyo na dalili ya mvua hii ikaleta utulivu kwa walalao matanga msibani. Shughuli za kawaida zilikuwa zikiendelea ambazo zilikuwa ni za hapa na pale, wakina mama waliyokuwa jikoni walikuwa, wakina mama wakandao maandazi walikanda, wale wachomao maandazi walichoma na wanaume waliyokuwa wakibadilishana mawazo na wengine wakielezea namna marehemu alivyo na vinginevyo, ilikuwa hivyo alimradi muda ulikuwa ukienda namna hiyo.




"Mazishi yatakuwa ni kesho sivyo?" Aliuliza dada mmoja aliyekuwa amekaa pembeni yangu.




"Ndiyo, wanazika kesho mapema tu nilimsikia mzee mmoja akisema kuwa hawataki ndugu yao akae sana kwenye barafu," dada mwengine alijibu.










Shughuli za kawaida zilikuwa zikiendelea ambazo zilikuwa ni za hapa na pale, wakina mama waliyokuwa jikoni walikuwa, wakina mama wakandao maandazi walikanda, wale wachomao maandazi walichoma na wanaume waliyokuwa wakibadilishana mawazo na wengine wakielezea namna marehemu alivyo na vinginevyo, ilikuwa hivyo alimradi muda ulikuwa ukienda namna hiyo.




"Mazishi yatakuwa ni kesho sivyo?" Aliuliza dada mmoja aliyekuwa amekaa pembeni yangu.




"Ndiyo, wanazika kesho mapema tu nilimsikia mzee mmoja akisema kuwa hawataki ndugu yao akae sana kwenye barafu," dada mwengine alijibu. Nilikuwa kimya nikiwa msikilizaji hata hivyo kwa wakati huo nilikuwa makini na mtazamo wangu kwa mama mfiwa. Sikutaka jicho langu limpoteze hata kidogo alikuwa katikati ya wanawake waliyojaribu kumliwaza kwa kumpigisha soga hizi na zile.




"Masikini baba wa watu hakuwa mtu mwenye uhasama na mtu hawa majambazi si watu kabisa." Mwengine akaongezea kabisa akiamini kitendo kile cha mauaji kilichomkuta Masuka Mvungi kilisababishwa na majambazi yaliyotaka kumpora.




Majambazi...? Kuna jambazi anaweza kuharibu risasi zake mahali ambapo si pa kumuingizia kitu...? Nilijiuliza hata hivyo ndiyo walivyoamini inabidi kuacha ili angalau watu wapeane faraja. Wakati tukiwa hapo kuna mwanamke mmoja aliingia hapo na kumuulizia Binti Mbaruku. Alikuwa ni msichana mdogo mwenye umbo jembamba na sura aliyoifunika kwa kuitanda na Khanga nikatazama saa yangu, nikagumia ndani kwa ndani. Muda ulikuwa ukiyoyoma sana.




"Nani ananiita Saumu?" Aliuliza Binti Mbaruku sura yake ikiwa na tashwishi.




"Ni mzee mmoja bila shaka kuna jambo anataka kukuuliza."




"Yukoje?" Akauliza dada yake na binti Mbaruku hakutaka mdogo wake aingie katika usumbufu tena. Alishachoshwa na njoo nenda, nenda njoo zilizokuwa zikimkuta mdogo wake. Nikamtazama yule dada. Sikuwa nimekurupuka kusema kuwa ni dada yake. Nilimjua kwa kufanana kwao na kwa namna walivyokuwa wakiitana, uchunguzi wangu ulishiba kwani nilifika muda mrefu hapo msibani.




"Amevaa kofia ya pama, ana koti kubwa jeusi na mkongojo mkononi mwake, haoneshi kama ni mtu mwenye kuleta shaka ni mzee aliyekuja kulala matanga maana amebeba na shuka mkononi na bilashaka anakufahamu." Akajibu yule dada.




"Usiku huu jamani hajui kama mimi ni mfiwa na nahitaji utulivu, haya ngoja nikamsikilize," akanyanyuka na kutoka taratibu akiangaliwa na watu vile anavyotembea kwa kujisukuma. Alikuwa amechoka ila basi tu afanyeje sasa.




Jicho langu lilikuwa likitazama zaidi ya mtazamo wa kawaida, akili yangu nayo ilikuwa ikijiuliza kuhusiana na mtu ambaye alikuwa akimuita mama mjane usiku huo.




Saa nne sasa yenye kukimbilia saa tano...? Niliwaza.


Nikajinyanyua taratibu kisha nikatoka nikiongozana na yule dada aliyekuja kuleta wito ule.




"Umesema aliyemuita dada ni mtu wa namna gani?" Nilimuuliza dada yule huku nikijinasibisha na undugu wa mama mfiwa, nilijua hawezi kunijua kwani hata sura yangu hakuwa akiijua.




"Ni mzee tu asiyejiweza." Alinijibu kwa mkato huku akichukua uelekeo mwingine. Hakujua kwa nini namuuliza na pengine hakutaka kuijua maana yangu. Sikujali sana nikaangaza macho yangu baada ya kuwa mwenyewe. Nilitazama kila mahali nikaona watu wakiwa wamekaa vikundi vikundi huku wengine wakiwa wameshajifunika shuka gubigubi katika namna ya kuupitisha usiku. Niliangusha macho chini baada ya kuhisi jambo lisilo la kawaida ni machale yalinicheza maana hii hali haikuwa ya kawaida. Nikapita pembeni mwa maua na kutokea kwenye kona moja iliyokuwa ikielekea nyuma ya ile nyumba. Kulikuwa kimya.




"Mbona gizani babu?" Nilisikia sauti ikisema upande huo wa huko nyuma, nilipoisikiliza katika utulivu wangu kichwani kwa kuirejesha rejesha, nikaing'amua. Ilikuwa ni ya Binti Mbaruku. Nikasita, sikusogea wala sikutazama waliko. Nikaendelea kuwepo hapo kwa sekunde za kuhesabika kisha nikageuza shingo yangu taratibu kuwatazama waliko, nikawaona wakienda nyuma ya banda la uwani. Nikachepuka kwenye watu wachache waliyokuwa wamjilaza karibu na moto katika namna ya kupambana na baridi ya usiku huku soga zikiwa zinaendelea.




"Wapi tena huku bibie?" Akauliza mtu mmoja nilipokuwa namalizia kuwapita. Sikumjibu kwa kuwa nilikuwa mbali nao tayari, nilipita upande wa pili wa lile banda la uwani na kwenda kujibaniza kwenye kona ya banda lile rangi ya nguo nilizovaa kwa muda ule wa usiku zililisharabu giza na nilivaa hivyo kwa kukusudia kabisa.




"Pole sana mama kwanza kwa kupatwa na msiba mzito sana," hapo sasa niliweza kuwasikia vizuri, sauti ya kiume ilianza, nikashtuka. Haikuwa sauti ya mzee kama yule msichana mleta taarifa alivyosema, ilikuwa ni sauti ya wastani yaani umri wa katikati ya uzee na ujana.




"Asante kwani wewe ni nani na mbona huku kote?" Akauliza Binti Mbaruku. Huyo niliijua sauti yake.




"Utulivu, napenda sana sehemu tulivu kwani ni sehemu nzuri zenye kukupa amani.....vipi kuhusu usumbufu wa watu wanaopeleleza kesi ya mauaji ya mumeo, hawakusumbui maana wapelelezi bwana, kwenye sakata kama hili huwa ni wasumbufu sana?"




"Wapo na walinisumbua sana leo?"




"Kweli?....nilijua, lazima wakusumbue. Vipi unauhakika wa kufikia mafanikio ya kuwapata waliyohusika na mauaji ya mumeo?" Akazidi kuuliza yuke mtu. Kimya kikachukua nafasi, nikaendelea kujipa utulivu mkubwa huku nikiwa msikilizaji inaonekana yule dada alikuwa kwenye mafikirio labda kutokana na kuchelewa kujibu hata hivyo hakuchelewa sana.




"Wewe ni nani?" Nilimsikia akiuliza Binti Mbaruku. Yule mtu akatulia kisha nikamuona akitazama huku na huko. Nilikuwa tayari nimewakaribia hivyo niliwaona jinsi walivyokuwa wamesimama na wao wakiwa hawanioni. Baada ya kuangalia sana kwa mtindo ule akasema.




"Unajua kama umefanikiwa kuziona sura za watu waliyotenda mauaji ya ndugu yako hii inaweza kuwa ni rahisi sana kuwasaidia wanausalama katika kupeleleza kwao. Hiki ndicho nilitaka kujua, kwani ulifanikiwa kuona hata sura ya muuaji mmoja?" Jibu la huyu mtu lilinichanganya kwani jinsi alivyojibu si kama alivyoulizwa. Alitakiwa kujibu na si kuuliza swali kama alivyofanya.




"Hapana, sijafanikiwa....sijathubutu hata kutaka kuwajua walikuwa wanatumia silaha za moto unadhani ningeweza kuwa na ujasiri huo wa kutaka kuwajua?" Nilimsikia akijibu Binti Mbaruku akijibu. Hapa nikamuona yule mtu akijipapasa kwenye koti lake hiki kilikuwa ni kitisho. Huyu mtu hakuwa mwema hadi hapa nilimtilia shaka. Nilichepuka na kunyata kisha nikaibuka nyuma yake nikimuwekea kasiba ya Colt Officer's ACP nyuma ya kichwa chake.




"Tulia hivyo hivyo na uniambie wewe ni nani na kwanini unafanya mahojiano gizani namna hii?" Nilimwambia hapa nikamuona akishika kitu kutokea kiunoni, nilimpiga na liwato kichwani akatokwa na mguno wa maumivu.




"Mikono juu, ukileta kujua unajua nini kitakutokea," nilimwambia huku nikimtaka utulivu mama mjane kwani sasa yuko kwenye mikono salama.




"Nini jamani...? Kwani kuna baya gani nimefa....!" Hakumalizia alichotaka kusema kwani nilikuwa tayari nimeshaichomoa bastola yake kiunoni na kumuongeza na pigo jingine la liwato.




"Hata kama ukiamua kumuua huyu dada huwezi kupata chochote kwani ushahidi wote uko mikononi mwetu." Nilimwambia. Alishtuka waziwazi na kutaka kugeuka hata hivyo nilimgutusha na sauti ya kuitoa usalama bunduki yangu akatulia. Nikampiga mtama mmoja matata sana akadondoka chini hata hivyo alijigeuza kwa kasi na kusimama. Binti Mbaruku kuona hivyo akakimbia kabisa hilo eneo. Alinifuata kwa mapigo mchanganyiko huku akininyima nafasi ya kuyachomoa mapigo yangu. Giza lilikuwa likimsaidia kwa kiasi kikubwa sana. Nilikuwa nikimtafutia mwanya na sikuupata. Aliniletea ngumi moja safi ambayo nilifanikiwa kuipisha kisha hapo hapo nikampelekea ya kwangu ambayo ilimpata mdomoni. Nikamtandika na ngumi nyingine mbili za kifua na kumsukumia mbali na guu langu la kuume. Akapepesuka hata hivyo hakugusa chini. Nilidhamiria kumjua ni nani hivyo nilimfuata kwa kasi ya kimondo na kumpelekea mapigo mengi ambayo yalimshinda kukinga. Akadondoka chini.




"Wewe ni nani?" Nilimuuliza hata hivyo hakusumbuka kunijibu. Alisimama taratibu nami nikamuwahi kwa kumtandika teke la shavuni akarudi chini kwa manung'uniko madogo.




"Utakufa ukiwa mkaidi?" Nilimwambia. Huyu jamaa alikuwa makini na mjanja sana kwani alikuwa akijifanya kugaagaa hapo chini nikamsogelea kwa lengo la kumuuliza vizuri, akageuka na kunichota mtama ambao ulinitupa chini akanyanyuka na kutimua mbio huku akiwa anachechemea nikamrukia nikalikamata koti lake akalivua na kuniachi. Hapa nikamuona vizuri alikuwa ni yule jamaa niliyepambana naye usiku ule uliyopita nyumbani kwa Jaji Kiago Mathias. Nikalitupa lile koti chini na kumfukuza. Nilimkimbiza kwa kasi kubwa naye hakuwa mdogo kwenye mbio. Nilienda naye akipita mitaa hii na ile tukaja kutokea kwenye barabara iliyokuwa ikitokea mjini kati, akaivuka nami nikavuka, nilikuwa nikimkaribia kwa hatua chache sana. Sikujua dhamira yake ilikuwa nini na sikutaka kutumia bastola kumuadhibu. Nilimuona akiambaa na ukuta wa uzio wa nyumba fulani hivi, sikumuacha. Punde alidandia ukuta na kudondokea ndani nami nikafanya hivyo. Yule jamaa akaongeza kasi na kuparamia gari moja iliyokuwa imeegeshwa mule ndani kisha akadandia ukuta kwa upande mwingine na kuchumpia nje.






Nilimuona akiambaa na ukuta wa uzio wa nyumba fulani hivi, sikumuacha. Punde alidandia ukuta na kudondokea ndani nami nikafanya hivyo. Yule jamaa akaongeza kasi na kuparamia gari moja iliyokuwa imeegeshwa mule ndani kisha akadandia ukuta kwa upande mwingine na kuchumpia nje. Sikulaza damu. Sasa nikaona ananipotezea muda, nikachomoa bastola yangu na kumuelekezea nilikuwa na lengo la kumfyatulia risasi na kumvunja miguu ili niweze kumuhoji vizuri. Nilichelewa, gari kubwa la mizigo lilipita kati yetu na kutuziba. Nilitukana tusi zito sana, hadi lilipopita yule jamaa akatoweka kwenye macho yangu. Nikatazama huku na huko ili kujua nilipo, sikujua. Niliifutika bastola yangu kiunoni na kurudi kwa kuchepuka njia hii na ile nikiwa kwenye mwendo wa haraka sana nilielekea maskani kwangu na kwenda moja kwa moja chumbani ambako niliiwasha Tarakilishi yangu nikaelekea upande wa barua pepe nikachapa ujumbe fulani na kuutuma. Jibu halikuchelewa. Nikatabasamu baada ya kujua Amiri alikuwa macho kwa majira hayo. Nikaichukua tarakilishi yangu na kuelekea nayo chini ya lile jengo ambako moja kwa moja nilifika kwenye mashine moja na kuitumbukiza ile picha kisha ikai-skani na kuiingiza kwenye tarakilishi yangu moja kwa moja nikaambatanisha na ujumbe ambao ulimtaka Amiri aitumbukize picha ile kwenye mtandao na afanye tafutishi zake kama picha ile ingeweza kumletea picha na maelezo ya utambuzi ya mtu huyo kwa uhalisia. Nilisubiri kwa muda kidogo huku nikiwa na mawazo mengi kuhusiana na yule mtu ambaye ni mara ya pili nilikuwa nikimkosa.




Nikiwa naendelea kusubiri, nikakumbuka kuwa nilimpokonya bastola yake. Nikaitoa niliko kuwa nimeihifadhi na kuiweka mezani niliichunguza nikagundua ilikuwa ni bastola aina ya Belleste Molina iliyotengenezwa huko Argentina. Nikairudisha mezani na kuyaruhusu mawazo yajiendeshe yenyewe kichwani mwangu. Nilikuwa na mambo mengi sana ya kufikiri na kuyafanyia kazi. Hii kazi nilianza kuiona ugumu wake kwani hadi wakati huo nawaza sikuwa nimegundua chochote walau.




Nilisikia sauti ya ujumbe ukiingia kwenye tarakilishi yangu, nikaufungua nikaanza kuusoma baada ya kuingia upande wa barua pepe, ujumbe huu ulijaa maelezo mengi sana ambayo yalikuwa yakiihusu ile picha sambamba na ambato la picha halisi ambayo Amiri alidai kuwa ilimsumbua sana kuipatia majibu. Mwisho akatanabaisha utambuzi wake kwa picha ile. Aliitwa Welason Mpopoki alizaliwa nchini Ungamo na ni mwenyeji wa jiji la Muavengero, anaishi mtaa wa Kwetu kambi mita mia moja na hamsini kutokea soko kuu mjini nyumba namba 18. Nilitabasamu huku nikiurudia kuusoma huu ujumbe hakika ulikuwa ukinipeleka kwenye lengo langu husika. Ni usiku huu. Niliwaza. Muda ulikuwa umekwenda sana maana sasa ilikuwa ikikimbilia saa saba za usiku. Ni lazima niende ili kesho niangalie mambo mengine ya msingi. Niliwaza zaidi kisha nikanyanyuka na kwenda kufungua Friji ambapo nilikuta maziwa yakiwa mengi tu kwenye chupa. Hivi ni miongoni mwa vitu ambavyo nilitegemea kuvikuta vyote hivi AKM aliniandalia. Niliyatoa na kuelekea jikoni nikayachemsha maziwa hayo kwa kutumia jiko la umeme kisha nikachukua vipande vitatu vya mkate na kuvipaka Siagi ya karanga nikaanza kuziba nafasi zenye mapengo ya njaa tumboni. Nilikunywa maji mengi sana baada ya kutulia kwa dakika tano nilipomaliza kula ndipo nilitoka nje ambako niliikuta gari yangu ikiwa imetulizana. Niliingia ndani yake na kuliungurumisha kisha nikatoka nikichukua uelekeo wa mjini. Kulikuwa kumepoa sana usiku huu japo baadhi ya sehemu bado zilikuwa na watu waliyokuwa wakipitapita huku wengine wakiwa bado wanaendeleza biashara. Nilitafuta kituo cha kujazia mafuta ili nilijaze gari langu maana nilijua nitokako ila sikujua niendako.




"Weka ya shilingi elfu ishirini." Nilimwambia kijana aliyekuwa akitoa huduma. Nikamuona akibofya namba na kuniwekea mafuta hayo alipomaliza nililipa kiasi cha pesa cha huduma husika nikaondoka.




____________




Niliwaza mengi kwa wakati huo, akili yangu ilidhamiria kuumaliza usiku huu kwa mafanikio mazuri huku ukiwa ni mwanzo mzuri kwangu. Niliapa kuhakikisha namjua huyu mtu anayesemekana ndiye hasa aliyeonekana akifanya mauaji ya Masuka Mvungi. Nilipofikiri kuhusu Masuka Mvungi, ghafula nikamkumbuka mkewe binti Mbaruku. Moyo ukaniuma, nilimhurumia mwanamke yule kwa namna anavyopitia wakati mgumu kutokana na adha ya kifo cha mumewe namna kilivyo mtafutano mkubwa. Niliwaza kumfuta baada ya mazishi hapo kesho kisha nimshauri akimbie mbali na mji huo ili aweze kukaa mbali na wauaji wanaoiwinda roho yake. Nilipojiaminisha kuwa huo ungekuwa ushauri mzuri kwangu kwenda kwake niliachana na wazo hilo na kuirudisha akili yangu barabarani. Hata hivyo ilikuwa siyo rahisi kwani nilijiuliza sababu hasa ya kuwindwa kwake. Sikuipata kwa haraka hadi nilipoipa akili yangu utulivu ndipo nilipogundua kuwa ni kutokana na kusema kuwa aliwahi kuiona sura ya muuaji kiasi hadi picha ya muuaji huyo ikapatikana kupitia maelezo yake.




Muuaji anashirikiana na mtu niliyemkosa muda mfupi uliopita. Niliwaza kisha nikajiona mshindi ninayeukaribia ushindi.




Nilikuwa nimeshaingia ndani ya mtaa wa Kwetu kambi. Niliendesha taratibu huku nikisoma namba za kwenye nyumba. Hapa nilikuwa siko mbali sana na nyumba husika maana nilikuwa kwenye nyumba moja ya kisasa ambayo langoni ilikuwa na namba 11. Nilibakiza nyumba saba za upande niliyopo ili kuifikia nyumba namba 18. Nikaangaza macho yangu nje kisha nikaegesha gari baada ya kuona mahali sahihi pa kuegesha gari yangu. Hapa nilikuwa na uhakika kuwa ningeweza kwenda na kurudi nikaikuta ikiwa bado iko kwenye usalama. Nilipiga hatua za haraka ili kuendana na wakati, nilibadili mavazi, sikuwa nimejitanda kama nilivyotoka msibani hapa nilivaa suruali ya jeans ya kuvutika (mnyonyo). Chini nilivaa kiatu cheusi cha ngozi na chepeo ya wazi. Nilizihesabia vema hizo nyumba huku nikizirusha hatua zangu kwa utulivu mkubwa hadi nilipokuwa nikitazamana na nyumba niliyoikusudia. Ilikuwa ni nyumba ya kawaida ambayo ujenzi wake ulikula chumvi nyingi. Ilikuwa na baraza fupi iliyojengewa hadi usawa wa kiuno cha mtu yeyeote mwenye urefu sawa nami, taa zilikuwa zikiendelea kuangaza eneo hilo. Sikuwa na papara ya kutaka kulikaribia hilo eneo, nilitulia kwanza nikiyasoma mazingira. Naam, nilijiridhisha vema kuwa eneo hilo ndilo lenyewe japo lilikuwa si tulivu kwa kuwa nyuma ya nyumba hiyo namba 18 upande wa mashariki kulikuwa na duka kubwa la vyakula na Grosari. Vijana wakicheza pool table na kunywa pombe hata hivyo eneo hili halikuwa na njia ya kukatiza watu hovyo hivyo sikuwa na shaka ya kushtukiwa uwepo wangu hapo. Niligeuka huku na huko nikiwa kwenye nguo nyeusi nikiwa nimejibana kwenye uzio wa nyumba ya jirani na nyumba namba 18, hakukuwa na kiumbe aliyekuwa akinifuatilia. Nikapapasa kiunoni nikakiona chuma kikiwa kimetulia, safari hii sikuwa nimebeba Colt Officer's ACP, hii sikupenda sana kuitumia na sina sababu za msingi za kwanini sikupenda kuitumia. Nilikuwa na chombo makini nikipendacho, Caracal Pisto. Hii ndiyo hasa niliipenda, ukinikosa na hii basi unaweza kunikuta na Baretta 8000 au Brawning Buck Mark. Bastola pekee zinazonifurahisha niwapo nazo kazini. Niliingia kwenye mlango wa ile baraza na kuukuta mlango wa mbele, nikatulia huku nikiyapa masikio yangu usikivu mkubwa, nikachungulia kwenye tundu la funguo baada ya kuusukuma mlango na kugundua kuwa ulikuwa umefungwa. Ndani kulikuwa kukiwaka yaa na hakukuwa kumechomekwa ufunguo kwa ndani. Ilikuwa afadhali kwangu. Nikatumbuliza ufunguo wangu wa kazi taratibu kisha nikatulia kabla ya kuanza kuuzunguusha, kimya changu kilikuwa na maana kubwa sana kwani kilikuwa kikiyapa masikio kazi ya kusikiliza kinachoendelea ndani mule. Muziki laini ukapenya masikioni mwangu, ulikuwa ni muziki mtamu sana wenye kulazimisha usingizi au kuamsha hisia wakati ukiwa unafanya ngono maana haukuwa kero kwenye masikio.




Ndani kuna mtu. Niliwaza.


Ni baada ya kusikia muziki kwani ni mara chache sana mtu kuacha muziki ndani halafu yeye awe hayupo. Niliuzungusha ufunguo wangu mara mbili kitasa kikaachia. Nikauchomoa na kuurudisha mfukoni kisha nikazungusha mkono wa kitasa taratibu hadi pale nilipo hakikisha kuwa naweza kuusukuma bila kelele. Nikausukuma ukakubali kusukumika, niliusukuma hadi nilipoweza kupata upenyo wa kuchungulia ndani. Hakukuwa na mtu sebuleni zaidi ya sofa pekee. Nikajiingiza kisha nikaurudisha mlango nyuma yangu. Kulikwa na seti ya sofa, meza ya kioo ambayo juu yake kulikuwa na chupa mbili za bia moja ikiwa imekwisha na ya pili ikiwa imesalia kidogo. Niliona simu ndogo pembeni ya bilauri nilipoichunguza nikagundua kuwa ilikuwa imezimwa, sikuiwasha niliiacha kama ilivyo. Nikazidi kushangaa. Sofa moja linalobeba watu wawili halikuwa katika hali nzuri, lilikuwa limechanguliwa huku vimito vidogo vikiwa wanguwangu kimoja chini.




Mh! Nikaguna.


Nilijua humu ndani hakukuwa salama, ni lazima kutakuwa na mwanamke akishughulikiwa. Niliwaza. Sikuchunguza tena pale sebuleni bali nilitazama korido ndogo iliyokuwa ikielekea kwenye vyumba vingine. Nikaifuata, ilikuwa nyembamba. Nilikipita chumba cha kwanza kilichokuwa kimefungwa, sikujisumbua kukifungua. Mbele kidogo kutoka kwenye mlango wa chumba kilichofungwa kulikuwa na chumba kilichokuwa wazi huku sauti ya muziki ikiwa inasikika vizuri.




Kweli kuna mwanamke. Nilijihakikishia kwani baada ya kusikia mguno mmoja wa kimahaba kisha miguno mingine ya mahaba kuendelea kusikika, nilikumbwa na manukatoa yaliyochanganyikana na jasho la watu wawili, ilihitaji moyo kiasi maana ilichefua. Nikasogea na kuchungulia. Lahaula! Nilimuona kijana akiwa amenipa mgongo huku kiuno chake nikikifananisha na mjongeo wa Kiwavi jeshi kwa jinsi alivyokuwa akijisukuma mbele na kujirudisha nyuma. Mwanamke alikuwa akipiga kelele mchanganyiko kuashiria kuwa dunia aliyopelekwa hakuwa amewahi kwenda hapo kabla. Zilikuwa ni kelele za raha. Taa yenye mwanga hafifu wa rangi ya kibuluu ilikuwa ikiongeza chachu ya ngono ile ambayo sikuwa na uhakika nayo kama ilifuata misingi ya kidini au ni kama hizi tufanyazo vijana wengi huku tukijiona tuko kwenye usahihi na hatuwazi tena kuoa wala kuolewa. Sikuwa na papara niliendelea kusubiri kwani niliamini hawako mbali kumaliza maana jasho lilikuwa likiwakatika haswa kama wako kwenye mashindano ya mbio ndefu. Punde nilimsikia kijana akipiga kelele zile ambazo ni wanaume wachache ndiyo wanaweza kuzihimili hasa wakaribiapo kufika mshindo au wafikapo mshindo kabisa, nikajua hapo tayari. Nikazama chumbani mule kwa fujo.


Aisee!


Yule kijana alikuwa wa ajabu sana na mwepesi kwani alijitoa mwilini mwa yule msichana baada ya kuhisi kavamiwa akataka kujirusha kuliko na mto mmoja mkubwa sehemu ya uchago wa kitanda hicho nikamuwahi maana nilijua anachokimbilia. Nilimshika mguu na kumvuta nyuma akaserereka na shuka.




"Kwanini umenileta huku kama unajua kuna malaya wako mwengine?" Alibwata yule mwanamke huku akiwa kasimama ukutani uchi wa mnyama kama sanamu la kukifu huku akijitahidi kuyakaza macho yake yaliyolegea kwa kuzidiwa na utamu wa mahaba aliopewa na kijana huyo.




"Malaya ni wewe uliyekuwa ukiongea lugha usiyoijua hapa au mimi...? Mpuuzi wewe!" Nilimjibu yule msichana huku nikimtandika ngumi yule kijana pale kitandani akagumia kwa maumivu ya ngumi ya tumbo akabingilia na shuka akasimama huku akilivilingita shuka lile kiunoni katika nmna ya kuuzuia utupu wake.








"Malaya ni wewe uliyekuwa ukiongea lugha usiyoijua hapa au mimi...? Mpuuzi wewe!" Nilimjibu yule msichana huku nikimtandika ngumi yule kijana pale kitandani akagumia kwa maumivu ya ngumi ya tumbo akabingilia na shuka akasimama huku akilivilingita shuka lile kiunoni katika nmna ya kuuzuia utupu wake.




"Wewe ni nani unayejaribu kuharibu starehe za watu?" Akaniuliza yule kijana ambaye hadi hapo nilikubali kuwa alikuwa ni Welason kwa kufananisha sura yake na ya picha huku nikimuona akijaribu kunikathmini kama ni kilo ya mchele au uzito wa pamba, hakung'amua.




"Nimekuja kwako kijogoo Welason Mpopoki." Nilimjibu nikamuona akishutuka hata hivyo haukuwa mshtuko mkubwa. Akautupia mbali mshtuko ule ili nisimshtukie.




"Unanidai?" Akaniuliza.




"Ndiyo," nikamjibu huku nikiwatazama wote wawili kwa namna ya kupendeza.




"Unanidai nini malaya wewe? Mbona sikumbuki kama niliwahi kukuona kwenye maisha yangu?" Alisema akihamaki.




"Nakudai roho ya Masuka Mvungi, risasi zako mbili zilimaliza uhai wake," nilimwambia nikimtazama kwa udadisi. Akainama kidogo chini kama afikiriaye kisha akanitazama usoni kama chatu mwenye shibe.




"Wewe ni nani?" Akatoa swali jepesi.




"Green bird,"




"Kutokea wapi mbona kama unajichanganya?" Akaniuliza. Sikumjibu kwanza nilimtazama jinsi alivyokuwa akitweta baada ya kutoka kifuani punde na kukutana na jambo asilolielewa kisha nikamtazama na yule mwanamke ambaye aliupindisha mdomo kama wa Kwembe.




"Kwanini mnaua kiholela kama vile mlitumwa na muumbaji jambo hilo?" Nilimuuliza nikilipuuza swali lake.




"Hata wewe naona umekifuata kifo chako mpuuzi wewe," alisema kisha akanifuata kwa hatua mbili akarusha ngumi nne za chapuchapu nikafanikiwa kuzitoka mbili huku mbili nikizipotezea maboya kwa kuzipangua, yule mwanamke akahamaki kwa kukiachia wazi kinywa chake baada ya ufundi niyouonesha kisha nikamuona akitaka kutoka. Nilimtandika kofi la uso na kumwambia akae chini akajibweteka chini akibweka Mbweha kwenye ardhi yenye ukame huku akiyatanua mapaja yake kama anayemsubiri ngariba. Nilikuwa makini na Welason kwani baada ya kumsulubu malaya wake alikuja mbogo. Nilijitahidi kwa kadiri yangu ili kumkabili hata hivyo ngumi mbili za mwisho zikanipata na kunitoa kwenye mchezo. Niliyumba kama mlevi kwa ngumi zile nzito za kifua, akaja kwa kasi kuu hapa sikumpa nafasi ya kujiona ni bora kuliko mimi, nilimpisha juu akapiga hewa, nikacheka na tumbo lake changa akaachama kinywa chake, ngumi ya mwisho nikaikita kwenye taya nikamrusha nyuma akajaa kitandani. Akajishika kidevu huku akilia kwa maumivu makali. Akasimama pale kitandani na kunirukia kama mwanasarakasi nikampisha akatua chini mithili ya nyani akajibinua na kunikabili hata hivyo akanikuta niko makini zaidi ngumi moja matata ikamsukuma nyuma baada ya kutua kwenye paji lake la uso nikamsikia akimuita mama, nikacheka kumoyo. Hakukubali akanivamia na kunisumia nyuma nikaparamia kabati la nguo kwa nyuma na kuvunja kioo akanishindilia ngumi za tumbo tatu zikanipeleka chini akaninyanyua na kunipigiza kwenye kioo kingine nacho kikavunjika huku kikinichana kwenye shavu la kushoto nikamtukania mama yake huyo huyo aliyemuita, maumivu makali yakanitambaa mwilini. Hakuacha lile zoezi, sasa akataka kunipigiza kichwa changu kwenye mbao ngumu za kabati lile. Nikampapasa kwenye mabega akavimbisha nyama za mabega na kwa vile alikuwa kifua wazi mikono yangu ikateleza. Nikakumbuka kitu kimoja ambacho sikukawia kukifanya, nilijikunja na kumpiga kigoti cha kwenye korodani kabla haja nipigiza kwenye mbao akaniachia huku akilia kwa maumivu mimi nikiyumbayumba kwa kukosa muhimili. Akakaa kitandani akiwa analalama nikaona nikimuacha ataiwahi ile bastola ambayo nilikuwa na uhakika ilikuwa chini ya mto, nikajirusha kama kondoo kwenye radi nikamchapa kichwa cha tumboni akalia tena huku akilala chali kitandani na kujaribu kunyoosha mkono wake kuikaribia silaha yake, nikaurukia ule mkono na kuurudisha nyuma akapata nafasi ya kunigeuza chini yeye akawa juu. Akaanza kunishindilia ngumi za kila mahali lakini nijilitahidi kuzizuia huku nikimuwekea pingamizi la kuipata ile silaha. Nikajikunja na kumsukumia nyuma na maguu yangu akajipigiza kichwa chake kwenye ukuta akadondoka chini. Yule mwanamke kuona vile akatoka mbio kutaka kukimbia ili kuuwahi mlango, akanikuta tayari nimeishika ile bastola ambayo Welason alikuwa akiihitaji nilichomoa magazini na kumrushia miguuni yule mwanamke ambayo ilimbabatiza na kumpigisha mweleka akadondoka vibaya akiita mama. Nikaichomoa bastola yangu toka mafichoni na kumnyooshea Welason.




"Ni nani anayewatuma ninyi kufanya mauaji?" Nilimuuliza huku nikikaa kitandani nikijaribu kuifuta damu iloyokuwa ikichuruzika shavuni.




"Haita kusaidia mwanamke wewe mpuuzi kwa kuwa hutafika popote." Alijibu akiwa anatweta vibaya mno.




"Wewe fala nini...yaani bado unajitia kiburi na kuamini sitafika nipatakapo...? Wewe utakufa papa hapa, nitafika niendako kama nilivyofika kukupokonya roho yako." Nilimwambia kwa kiburi.




"Kumbe nia yako ni kuniuwa sasa mbona unakawia? Niuwe sasa hivi kabla hujakufa wewe," aliongea kwa kiburi Welason.




"Siwezi kukuuwa kama hujaniambia chochote," nikamwambia. Akacheka cheko kubwa sana hata hivyo hakufika mwisho wa cheko lake, nilimpiga teke zito kwa kiatu changu kigumu mdomoni, mdomo ukalegea huku akiyapokea meno yake matatu kiganjani toka kinywani mwake.




"Unadhani nimekuja kukupongeza hapa kwa uhodari wako wa kufanya ngono? Nipo kwa ajili ya kazi mjinga wewe, sema?" Nilifoka baada ya kujua analeta utani.




"Sijui chochote kuhusu unachotaka niseme maana hukuniambia unachotafuta." Akajibu. Nikamuinamia nikamwambia.



ITAENDELEA


Simulizi : Mpango Wa Nje - Ni Pigo Butu La Kifo 


Sehemu Ya Tano (5)




"Nataka kumjua mshirika wako na anayewatuma ninyi?"




"Simjui ha....aaaghr!" Nilimtandika ngumi ya mwamba wa pua baada ya kuendeleza kiburi chake akabweka kama Mbwa aliyepigwa na jiwe kwa kushtukiza.




"Bhehe.....anaitwa Amsuni Bhehe, ana anakaa mjini," aliongea kwa hamaniko baada ya kuhisi huwenda akafa akizidi kukaidi.




"Mjini tu...? Huoni kama mjini ni sehemu kubwa sana na miji iko sehemu nyingi? Unalenga nini hasa?" Nilimuuliza zaidi huku nikiweka utulivu.




"Kanisa kubwa la Anglikana upande wa magharibi jengo la shirika la nyumba la taifa ghorofa ya pili tafuta mlango wenye herufi 'C'..." Akanieleza kwa ufasaha.




Wakati nikiwa namtazama na huku nikiipandisha risasi kwenye chemba tayari kumchapa nayo, nikasikia sauti ya mlango kufunguliwa taratibu sana.




Upepo....? Nikajiuliza hata hivyo nikajipuuza pia, hakuna upepo wa hivyo eneo hili ambao ungeweza kusukuma mlango, nikatulia tena nikausikia ukilia tena.




Mtu! Nikajionya.


Nikaminya kilimi cha bastola yangu yenye kiwambo cha kuzuia sauti, risasi ikalichapa paji la uso la Welason Mpopoki, ubongo ukamwagika sambamba na damu risasi nyingine ikamdhibiti yule mwanamke asipige kelele na kumgutusha mtu ajaye. Sikuwa na lengo la kumuua ila kwa kuulinda usalama wangu sikuwa na namna nyingine. Nilipowamaliza nikasogea pale kizingitini ambako yule mwanamke alikuwa amelala.




Kama siyo kuhisi mtu ajaye, nisingekuuwa.


Nikamwambia kisha nikachungulia kwenye korido kuelekea sebuleni. Nikasikia mlio wa simu wa kuashiria ujumbe mfupi wa maneo umeingia simuni. Akili yangu ikanikumbusha kuwa ni ile simu pale mezani imewashwa.




Ni nani huyo...? Nikawaza kichwani mwangu hata hivyo sikuwa na jibu zuri nikarudi chumbani mule na kufanya upekuzi wa haraka hakuna nilichopata zaidi ya noti sita za shilingi elfu kumi, nikazitupia mulemule nilipozikuta kisha nikalielekea dirisha nikalisogeza pazia pembeni. Kulikuwa na nondo. Nikajua kutoka hapa itakuwa ngumu na mtu aliyeingia atanikuta, sikumjua ni nani hivyo ni lazima nitafute namna ya kuondoka. Nikaufuata mlango na kuufunga kwa ndani madhubuti kabisa kisha nikachungulia kila mahali mule ndani na kuona chuma kimoja kirefu mithili ya bomba nikalivuta kutokea uvunguni na kuchomeka pale kwenye nafasi ya nondo moja na nyingine nikatumia nguvu kusukuma chini hadi nondo zile zilipopinda. Nikapata nafasi ya kupenya. Nikahakikisha kuwa kila kitu kiko sawa kwangu na sikuacha alama yoyote, nikakamata dirishani kwa juu na kujivuta nikatoka pale dirishani kisha kutokea upande wa pili wa dirisha lile. Nililirudisha lile pazia na kupotelea gizani.




TWENDE KAZI SASA.








Nikapata nafasi ya kupenya. Nikahakikisha kuwa kila kitu kiko sawa kwangu na sikuacha alama yoyote, nikakamata dirishani kwa juu na kujivuta nikatoka pale dirishani kisha kutokea upande wa pili wa dirisha lile. Nililirudisha lile pazia na kupotelea gizani. Nilikuja kutokea kwenye gari langu nikachunguza kama kuna mtu yoyote mwenye kuwepo eneo lile sikumuona, nikaingia garini. Wakati nikiwa navua glovu zangu, mbele mita kama hamsini hivi nikaona pikipiki kubwa ikiwa imeegeshwa chini ya mti wenye mwanga hafifu wa taa uliokuwa ukimulika kutoke nyumba ya jirani na mti huo.




Haikuwepo hapo awali. Niliwaza.


Nilikuwa na uhakika kabisa kuwa wakati nafika hapo lile pikipiki halikuwapo pale.




Huwenda ni wenzake wamekuja. Nikajiliwaza hata hivyo sikutaka kupoteza muda, niliwasha gari yangu Peugeot 404 nikaiondoa hapo bila kuwasha taa hadi nilipofika mbali kabisa na eneo hilo. Nilipokuwa barabarani nilitazama saa yangu, ilikuwa tayari ni saa tisa usiku. Nilichoka.




___________




Huu msiba ulikuwa na mauzauza kwa upande wa Binti Mbaruku, kitendo cha kushuhudia mapigano baina ya mtu asiyemjua na mtu asiyemjua, ilikuwa ni hatari kubwa sana kwa upande wake akahisi huwenda hata yeye roho yake inawindwa na wauaji wa mumewe. Aliweza kuwatofautisha watu wale kwa jinsia zao tu. Mmoja alikuwa ni mwanaume umri wa kati aliyekuja kwake kwa kujifanya mzee na mwingine akiwa ni msichana. Kwanini walipambana? Huyu mwanaume hakuwa mwema kwake na huyu mwanamke alitokea kama malaika mwokovu wa maisha yake. Hili hakutaka lipite yaani macheo yafike akiwa nalo rohoni, ni dhambi. Akaitafuta namba ya simu ambayo aliachiwa na mtu aliyejitambulisha kwake kama Raurent Mbuva akiwa ni Inspekta wa polisi kituo cha kati ambaye ndiye aliyekwenda naye kuchora picha ya muuji mchana. Alimpigia simu hiyo mara baada ya vurumai lile kwenda mbali kabisa na nyumba yake akiwa na lengo la kumueleza yote yaliyojiri. Hakusema kitu baada ya hapo hata aliporudi ndani japo sura yake ilijaa tashwishi kubwa. Onyo alilopewa na Frank Matiale Bambi ambaye yeye alimfahamu kama Raurent Mbuva, kuwa asiseme chocho atakachokishuhudia kwa watu bali ampe taarifa yeye kupitia namba alizomuachia, alilizingatia vema sana. Hivyo wakati mwanadada makini Catherine akiwa anamtimua gizani yule mtu asiyemjua, huku nyuma onyo lake lilipuuzwa na Bint Mbaruku na alikuwa akitoa taarifa kwengine. Binti Mbaruku aliona bora kumuamini Raulent Mbuva kuliko binti asiyemjua.




Simu ilimgutusha Frank Matiale akiwa ndani ya nyumba moja tulivu akiwa anayasoma maelekezo aliyoyapata kutoka kwa wataalamu wa utambuzi wa kitafutishi kuhusiana na ile picha ya mchoro. Maelezo hayo yalikuwa yamempa uelekeo mzuri na ulioshiba kuhusiana na mtu aliyekuwa akimtaka. Alimfahamu mtu huyo pichani kwa jina la Welason, aliyeishi katika mtaa wa Kwetu kambi nyumba namba 18. Simu ile ikamfanya kuacha kila kitu alichokuwa akikifanya na kuipokea.




"Ni mimi Bint Mbaruku kaka wewe si ndiye askari uliyenipa kadi kazi Raurent Mbuva...?" Sauti isiyokuwa na utulivu ilizungumza simuni.




"Ndiyo, ni mimi dada vipi kuna shida?" Aliuliza Frank akiwa makini zaidi ya hata alivyoipokea.




"Shida kubwa. Njoo nyumbani mara moja na haraka kaka askari!" Iliongea tena sauti hiyo kwa mtindo ule ule usio na utulivu.




"Ok, nakuja." Alijibu Frank kisha akatoka ndani mule akiwa ameweka vitu vyake vizuri alichokumbuka kubeba ni ile picha tu akaifutika mfukoni akaliendea pikipiki lake akiwa ameufunga mlango wa nyumba hiyo madhubuti. Nusu saa mbele akawa amefika kwenye nyumba yenye msiba akaegesha pikipiki mbali na pale palipo na watu. Muda huu watu wengi walikuwa wamelala tayari. Simu yake ikaita akatazama aliyempigia, akaona ni namba ile ile akapokea.




"Bado hujafika kaka askari? Siwezi kulala usingizi umenipaa." Iliongea sauti hiyo simuni.




"Nimefika tayari uko wapi?" Alijibu Frank Matiale Bambi.




"Nikukute nyuma ya jengo la uwani." Sauti simuni ikatoa maelekezo, Frank akaelekea huko na kutulia. Muda huohuo Binti Mbaruku akafika akiwa matumatu macho juu hofu kwa mtima wake.




"Walipigana hapahapa mama yangu!" Akaongea kwa mpayuko Binti Mbaruku.




"Subiri kwanza dada, huyo mtu yukoje kwani?"




"Mwanamke au mwanaume?" Akauliza swali ambalo hata hivyo hakusubiri jibu akawahi kujibu mwenyewe ajuavyo.




"Mwanaume haeleweki, sijui mfupi, kikongwe, anatembea na mkongojo, mnene vile...? lakini alivaa pama jeusi na koti nakumbuka." Hata wewe ingekubidi ushangae maelezo haya, yalikuwa hayaja nyooka ati!




"Unahisi kwanini huyo mwanamke alitokea na kumvamia huyo mwanaume wakapigana? Kuna maswali yoyoye alikuwa akikuuliza kwani?" Akauliza Frank Bambi.




"Ndiyo, alikuwa akitaka kujua kama nilimuona kweli muuaji!" Akashtuka Frank.




Anataka kumjua muuaji...? Au anataka kujua kama huyu mjane aanamjua muuaji? Akawaza.




Kwanini sasa? Akawaza tena. Huwenda kuna jasusi ndani ya hii Operesheni Safisha. Akawaza tena. Ni nani....?




"Kama asingelikuwa huyo mwanamke....aaa! Ningelikuwa mfu tayari maana hakuonesha kama alikuwa mwema kwangu." Sauti ya Bini Mbaruku ikamtoa mawazoni Frank. Frank akatulia na kufikiria kwa muda. Kuna kitu alikuwa akijishauri nacho ni kumjua kwanza muuaji kisha kupitia huyo anaweza akawa amesaidia hili tata. Huyu mwanamke aliyetoa msaada kwa huyu mjane angemjua siku yoyote ile.


"Kuwa makini usitoke ndani hata kwa wito, mwenye shida na wewe atakufuata, sawa?.....nitakuja kesho kwenye mazishi, tutazungumza au kama nisipofika basi huna budi kufanya haya; lazima kesho uondoke ukishamaliza kuzika ama kabla ya mazishi. Nenda unapoona kwako kuna unafuu na amani ya maisha yako, huyu muuaji atarudi tena kwani ninahakika kabisa ndiye aliyesababisha kifo cha mumeo na kama ndiye anajua kuwa ulimuona wakati anafanya mauaji hivyo anataka kukuziba mdomo ili asikamatwe mapema. Nenda mbali binti Mbaruku, nenda tu." Akamaliza Frank kisha akaondoka na kurudi kwenye pikipiki lake akimuacha Binti Mbaruku akiyatafakari yale maneno na ndani yake akaona ukweli hivyo akaonekea usiku huo huo aliweke wazi jambo lile akaelekea ndani. Frank alitazama muda ilikuwa ni saa nane kasoro usiku. Akawasha pikipiki na kuelekea mahali ambako ile picha ya mtu anayedhaniwa kuwa ni muuaji yupo.




__________




Maelekezo aliyoyapata kutoka kwa wataalamu wa tafutishi, yalimsaidia kufika maeneo husika akatafuta maegesho mazuri ya pikipiki yake ili isiweze kuonekana, akaona mti mmoja uliokuwa umeweka giza la wastani chini yake akasogea hapo na kuiegesha. Akiwa bado juu ya pikipiki akiangaza macho yake huku na huko, aliweza kuona gari ikiwa imeegeshwa mita kama hamsini kutokea mahali alipo. Akalijengea hofu lile gari, akateremka kutokea kwenye pikipiki na kulifuata lile gari kwa umakini mkubwa sana hakutaka kujihakikishia usalama kirahisi namna ile. Alipofika lilipo gari lile hakuona kiumbe yoyote ndani yake wala nje, ilikuwa yenyewe.




Nimwenye hii nyumba labda? Akajinyuka swali mawazoni hata hivyo akaliacha na kulimeza jibu lake. Akazidi kulichunguza akagundua kuwa ilikuwa ni Peugeot 404. Gari makini sana ya kizamani. Alipojihakikishia usalama wake ndipo akarudi kwenye ile nyumba, alipofika akausogelea mlango na kunyonga kitasa kujihakikishia kama ulifungwa ama la. Hakuwa na imani kama kwa majira yale mtu ndani yake angekuwa macho kodo bado. Alikuwa na uhakika muhusika ni lazima awe yuko kwenye ndoto ya mwisho kabda ya kuamshwa na adhana ya kwanza kutokea kwenye msikiti wowote wa jirani na hapo. Alipokinyonga kitasa na kuusukuma mlango, ajabu! Malango ulisukumika bila pingamizi.


Akaogopa.


Haraka sana akaitazama bastola yake mafichoni kama ipo. Ilikuwepo hivyo hakuwa na shaka tena. Akausukuma mlango na kupiga hatua moja ndani huku akiwa ameamua kuishikilia bastola yake kabisa mkononi. Wakati anafungua mlango, sauti ya mlango ile ndiyo iliyomgutusha Catherine ndani mule akajiweka sawa. Wakati anaurudisha mlango ule, hapo Catherine ndipo alipokubaliana na usikivu wake kuwa huyo alikuwa ni mtu.




Frank Matiale Bambi alifika mezani moja kwa moja baada ya kufanya upekuzi wa macho kwa umakini na utulivu mkubwa, hakuona kitu chenye kumpa hofu zaidi kilichomvuta ilikuwa ni simu iliyoko mezani. Akaichukua na kuiwasha baada ya kugundua imezimwa alijitahidi kuuzuia mlio wa simu hiyo wakati wa kuiwasha hata hivyo punde tu ilipowaka ikaingia ujumbe wa maneno ambao ulileta sauti iliyopelekea kumtahadharisha Catherine mule chumbani. Alishtuka kidogo Frank baada ya mlio ule wa ujumbe mfupi wa maneno kusikika, halafu akastaajabu kuona simu iko hapo sebuleni ikiwa imezimwa huku chupa mbili za bia zikiwa zinamshangaa ingali moja imetumika. Kulikuwa na mtu kama hakulala basi kuna jambo yu afanya, alijiaminisha hivyo.








Alishtuka kidogo Frank baada ya mlio ule wa ujumbe mfupi wa maneno kusikika, halafu akastaajabu kuona simu iko hapo sebuleni ikiwa imezimwa huku chupa mbili za bia zikiwa zinamshangaa ingali moja imetumika. Kulikuwa na mtu kama hakulala basi kuna jambo yu afanya, alijiaminisha hivyo. Ila baada ya ule ujumbe kuingia kwa sauti kuna kitu kama kikohozi cha mbuzi kilisikika. Kwa uwelewa wake wa kijasusi akajua fika hiyo ni bastola, bastola iliyotenda kazi huku ikiwa imevishwa kiwambo cha kuzuia sauti. Hapa akaitumbukiza simu mfukoni na kuikamata silaha yake madhubuti akajiweka tayari kuvamia chumbani mara, mlio mwengine kama ule akajua ohooo...! Kuna viumbe watu walikuwa wakifyekwa roho zao huko chumbani.




Na nani....? Swali hili lilikuwa ni gumu kujibika maana hakujua. Alichojua ni sababu ya mlango kuwa wazi pekee. Hiyo ndiyo sababu, mvamizi muuaji hakuthubutu kuufunga mlango baada ya kuufungua. Akapiga hatua na kujaa kwenye ile korido kasiba ya bastola ikiwa tayari kufanya lolote litakalojiri. Hapa Catherine alikuwa tayari ameshairudisha sura yake ndani baada ya kuchungulia na kuikuta korido itupu. Wakati Frank akiwa anazidi kusonga mbele zaidi kuukaribia mlango, akasikia kishindo cha kufungwa kwa mlango wa chumbani mule kisha kufungwa kwa ndani kabisa, purukushani za mtu anayehangaika zikaanza kusikika mara kimya kikuu kikachukua nafasi baada ya sekunde thelathini kumalizika.




"Fungua mlango kabla sijachukua hatua mbaya kwako." Aliongea Frank kwa sauti hata hivyo kimya bado kilishika hatamu vivo hivyo. Akasubiri kwa dakika nzima akitega sikio mlangoni.


Bado kimya.


Akakata shauri na kuamua kupiga risasi moja sehemu ambayo alijihakikishia kuwa hapo ndipo komeo la ndani liliposhikilia mlango. Mlango ukacheka na kulia kwa maumivu ya kuchangulia komeo lake ukapenuka penuu!


Lo! Chumba kilijaa miili miwili iliyopokonywa roho huku yote ikiwa mitupu bila nguo.




Nani kachukua roho zenu...? Akaiuliza ile miili iliyolala pale chini kidhalili.


Maajabu! Maiti nayo yaulizwa...?




"Nani kafanya haya?" Akabadili swali lenye maana ileile ila awamu hii alijiuliza mwenyewe japo swali hili nalo lilikuwa ni la kipuuzi pia maana jibu lisingepatikana kwa wakati ama kabisa kwani alijua fika anachojiuliza jibu lake ni kwa aliyeuwa na kumkimbia waliyouawa na kulala hovyo humo ndani wangali hawana nguo. Frank Matiale akabaki kukishangaa kile chumba kwa namna ya kudadisi. Kweli kilikuwa kitupu hakuna kingine zaidi ya vilivyomo kawaida na vigeni vikiwa ni miili afu chini sakafuni. Akavaa glovu na kuigeuza geuza hadi alipoziona nyuso zao. Nyuso zilijaa haya ya umauti maana roho zao zilitoka baada ya kutoka kuivunja amri ya sita ya Mungu. Miili ilibaki na soni kwa kuachwa na roho ikiwa bila nguo tena ikinuka janaba la ngono zembe.


Makubwa!


Midomo yao ilikuwa wazi kwa kuona au kushuhudia namna ya muuaji alivyokosa utani katika kutenda alichokitaka.




Ametenda kweli na alichokitenda ni kile ambacho nilidhamiria kukitenda mimi kwa huyu jamaa ambaye picha yake ninayo. Hakika ni yeye! Akawaza Frank Matiale Bambi akiwa amesimama katikati ya chumba akistaajabu ya firauni angali Musa hayupo.




Ni nani lakini ambaye anafanya kile nilichotaka kukifanya mimi..? Akawaza zaidi bila majibu. Hakuwa na sababu ya kuendelea kuwepo hapo kwani kazi aliyotaka kuifanya imekamilishwa na mtu asiyemjua ni nani na kwanini anaua anaotaka kuwaua. Akaitoa simu ile mfukoni na kuusoma ule ujumbe. 'Ni kesho saa kumi kamili alasiri nyumbani kwa Abdallah Juma Kimbo. Hakikisheni mnamaliza mapema isiwe kama awali.' Ujumbe ulikoma.




Munguuu! Akashtuka Frank Bambi.


Abdallah Juma Kimbo alikuwa ni waziri wa Nishati na Madini kwenye awamu iliyopita ya uongozi, alishawahi kukoswa kuuawa kopindi hicho cha nyuma huku akiipoteza familia yake.




Sasa anakufa na yeye? Akawaza


Frank akiwa anaitazama ile simu kwa macho ya shauku ya kutaka kujua kama kweli anakufa ama la!




Simu haisemi wala haimtazami.


Akatoka wanguwangu ikiwa ni saa kumi za usiku adhana ya kwanza ikiwa imeadhiniwa muda mfupi tu nyuma. Akaifuata pikipiki yake na kuondoka.




__________




Alishtuka kutokea usingizini ikiwa ni saa nne na upuuzi wa dakika na sekunde kama tatu kwenda nne na zaidi. Aliamka kivivu sana akiwa hakumbuki kama alilala kwa maamuzi au alilala akiwa hajui kama analala. Muda ulikwenda akakiri mara baada ya yeye mwenyewe kutazama saa. Akajinyanyua toka kitandani na kujinyoosha viungo ambavyo vilikubali mnyoosho huo mara baada ya kupiga kelele kama kuna vijiti mathalani vya kuti kavu vilikuwa vikivunjwa. Akafanya mazoezi mepesi na kuelekea maliwatoni, alipotoka huko angalau sura ikaanza kutabasamu. Alikuwa akilisikia tumbo linavyounguruma kwa njaa, akajiuliza muda ambao alikula siku iliyopita akakumbuka ni saa nne usiku alikula msosi wa maana kabla ya kusoma maelezo ya hayati Welason mtu pekee aliyekuwa akihitaji kumfuatlia. Frank akajua ni ila ya tumbo lake maana alikuwa na uhakika kuwa taksiri huunda ghiliba yenye kukupa msukumo hasi wende chanya kwa kukuhakiki hukutenda. Akautupa msonyo kwenye meza ya chumbani hapo ukachutama na kulishangaa tumbo lililopuuzwa.




Kwanini ahisi njaa wakati alikula? Mjadala huu ukaundika upya mara baada ya minyoo ya njaa kuchachamaa tumboni. Akapata kufikiri sana ndipo akagundua kuwa ni mbiombio za usiku kucha ndizo zilizopelekea kumuacha na njaa asubuhi hiyo. Akajikalisha kitandani na kujenga fikira nzito ambayo ilikuja kumpa majibu yaliyomfanya ajinyanyue haraka hapo kitandani na kukimbilia kabatini na kubadili nguo zake. Alikumbuka ujumbe wa kwenye simu kuwa ni saa kumi nyumbani kwa Abdallah Juma Kimbo. Huu ulikuwa ni ujumbe na hakutakiwa kuupuzia. Akabadili haraka akavaa suruali nyeusi kiatu safi kisha akaifutika bastola yake mahala pa siri kama ada keshapo akatoka nje ya hiyo nyumba yake ya siri na kulifuata pikipiki maegeshoni. Hii ilikuwa ni safari ya kwa mkuu wake wa kazi kwenda kumpa hizi taarifa.




____________




Kiti kilimshangaa sana Amsuni Bhehe tena kilimshangaa mno maana haikuwa ada yake kwa kukisulubu namna hiyo. Alikuwa akikizungusha kiti hicho kwenye chumba chake cha mipango kama bembea kwa watoto. Kite cha maudhi kilikuwa kikipishana kwa umbali wa sekunde za kuhesabika. Anajua nini kitakwenda kumtokea kwa hili lililokwenda kutukia ghafula namna hiyo.




"Kwanini sasa?" Akapiga kelele kama mwendawazimu mwanzwa nao. Akatoa macho kwa kulazimisha ilhali aliona mwanga sawia. Hakuona anacho kitazama, akabaki anashangaa kisicho shangaza, akacheka cheko kubwa la kujiliwaza ilhali hakuna cha kuchekesha mwisho akaangua kilio ndani ya kicheko.


Kipo kilichomliza hakika.




"Welason Mpopoki ameuawa ndani ya nyumba yake akiwa na malaya....wameuwawa!!!" Akapata mchecheto wa hofu akiwa anajisemea mwenyewe hapo ndani. Kifo cha Welason kilikuwa kama mwiba wenye kuumiza katikati ya kitufe kinachosababisha mapigo ya moyo kupiga. Akauona moyo wake ukisimama kwa lazima kisha kumnyima pumzi kwa muda na kuendelea tena kupiga.


Haa!


Aliogopa matusi, dharau, kejeli na lawama za kijinga kwa bosi wake.




Kazi gani hii likitokea dosari kidogo tu hofu mtindo mmoja utumbo mkubwa unacheza hadi kinyesi laini kinajitengeneza na kunya sinyi ni mtikisiko tu wa tumbo kwa miungurumo ya mashaka mithili ya mvumo wa radi. Akawaza.


Mara simu ikaita akaiogopa kama vile si yake akaitazama kiooni kama vile anayepiga ni jini mauti litazamikalo kwa picha.


Ebo!


Alikuwa ni mliwaza wake binti mdogo anayempa penzi matata hadi anasahau kama kuna dunia yenye lawama, dhambi isababishayo mauti na upumbavu. Akajichekesha kama mjinga. Akajicheka mwenyewe kwa kutokuwa na msimamo na ukatili wa maamuzi ya kuamua chochote cha kujibu kwani si maji yakishamwagika hayazoleki. Akaipokea simu ile baada ya kulisawazisha koo lake ili kupata sauti tamu yenye kumlegeza mtoto ahisi yu pamoja naye.




"Nimekusubiri sana lakini hutokei sijui utakuja saa ngapi?" Sauti muruwa ikamuuliza, akajiona yu mtu mbele ya watu akajiweka sawa kujibu jibu ambalo lingempa mtoto wa kike faraja ya moyo. Ghafula, Toop! Toop! Toop! Simu ilikuwa ikiingia wakati akiwa anaongea na mtoto mzuri wa kike, habibi wake. Akaitoa haraka sikioni kama inayomuunguza. Akatazama kiooni.




"Haa!" Akamaka kama anayepiga ni malaika mtoa roho ambaye alimuahidi kifo cha mama yake mzazi. Mfu anayeishi alikuwa akipiga simu. Ule ujasiri wa kuwa anao uwezo wa kupokea na kuzungumza chochote kwa kuwa kilichotokea kimetokea, ukayeyuka kama unga wa ubuyu kwenye ulimi wa binti mjamzito aliyedabukwa na mate. Amsuni Bhehe akajitoa ufahamu na kulisoma jina la mtu anayepiga simuni 'Malfrey Kobra'. Jina lilisome simuni. Akajikuta anakata simu iliyopigwa na kuiacha hewani ile aliyokuwa akiongea nayo hapo awali.




TUTASONGA.












Ule ujasiri wa kuwa anao uwezo wa kupokea na kuzungumza chochote kwa kuwa kilichotokea kimetokea, ukayeyuka kama unga wa ubuyu kwenye ulimi wa binti mjamzito aliyedabukwa na mate. Amsuni Bhehe akajitoa ufahamu na kulisoma jina la mtu anayepiga simuni 'Malfrey Kobra'. Jina lilisome simuni. Akajikuta anakata simu iliyopigwa na kuiacha hewani ile aliyokuwa akiongea nayo hapo awali.




"Mbona huongei baby jamani leo nina hamu sana na wew....!"




"Booo! Bado ni wewe kwani!" Akachachawa masikini ya Mungu. Hakuwa akijua nini kilikuwa kikimtokea, ile sauti za mahaba zilipotea ghafula kwa mpenzi wake, kifo cha Welason kimetokea ghafula sana na kimetokea wakati kazi muhimu ilitakiwa ifanyike, kazi ya kummaliza awliyewahi kuwa waziri wa nishati na madini, lazima achanganyikiwe mtu mzima. Akaitazama simu ile kwa macho ya huruma hata hivyo hakukuwa na namna yenye kubadilisha alichokiona kimetokea. Akaitupa simu mezani na kujilaza kitini akiuma midomo yake ya chini. Simu ikaita tena kwa fujo, Amsuni Bhehe akakereka zaidi akainyakuwa na kuropoka.


"Nitakupigia mpenzi niko na kazi mkononi.....!"


"Amsuni, Amsuni.....ni ujinga gani unaongea wewe mpuuzi!" Akastaajabu Amsuni. Kumbe aliyepiga safari hii hakuwa mpenziwe bali mkuu wake katika majukumu aliyojitwisha kichwani. Akalegea, ile sauti simuni ikaendelea.


"....hivi wewe ni mtu wa aina gani unayejali mapenzi yanayokuvuna pesa kila siku huku chanzo cha pesa hiyo unayohonga kwa wasiokupa faida bali hasara unakiacha kinateketea?"




"Na..na, ha..hahap.....!"




"Acha ujinga nyani wa msitu wa Kakamega wewe. Welason ameuawa sijui unajua?....hivi unajua kweli kama Welason ameuawa usiku wa kuamkia leo? Kazi yangu itafanikiwa vipi ya kumuondoa duniani waziri yule mpuuzi aliyesababisha kufungwa kwa kampuni yangu mama....? Yule mpuuzi aliyetoroka kifo hapo awali?" Alizidi kutoa shutuma kali sana Malfrey Kobra akikataa kumpa nafasi ya kuongea bwana Bhehe.




"Najua mkuu ila imekuwa ghafula sana kiasi kwamba nashindwa kuelewa namana ya kufanya!" Akajitetea Amsuni Bhehe.




"Jengo la mazungumzo leo kabla ya saa sita." Alitoa amri Malfrey Kobra kisha akakata simu. Amsuni Bhehe akapumua kwa nguvu sana akiwa haamini kama yameweza kuisha kiaina ile yale maongezi. Kuitwa Nyani wa msitu wa Kakamega na kadhalika wala hakujali alichoangalia ni namna ambavyo ya kwake yanakwenda.




Sitafanya ujinga tena. Akawaza huku akinyanyuka kwa lengo kujiandaa.




___________




Saa 14:15 adhuhuri. Malfrey Kobra akiwa na msaidizi wake walikuwa wakiingizana ndani ya jumba kubwa la makutano huko Muavengero wakiwa hai hai. Waliingia mahali ambapo hukutania wakawakuta Amsuni Bhehe na kijana wake Abdi Hussein wakiwa wametulia kimya kama wajane. Malfrey akawatazama kisha akatulia kimya kama si yeye, dakika moja mbele kijana mwingine akaingia, huyu alikuwa ni Black Scorpion.




"Tally Man nadhani kikosi kimekamilika sivyo?" Akauliza bwana mkubwa.




"Ndiyo, bosi." Akajibu Tallya Man. Kimya kikachukua muda kwa sekunde nane nzima ndipo bwana huyo akasema.




"Hii ni hatari kubwa sana, kila mmoja anaijua hii hatari iliyopo japo wapo wapuuzi miongoni mwetu wanajua halafu wanafanya ujinga. Nchi hii imevamiwa na watu hatari japo sijajua watu hao wanatokea ndani ama wamechangamana na watu kutoka nje....kama mimi najua haya kwa uchache nani mwengine anajua....? Amsuni Bhehe unajua chochote?" Alifoka Malfrey, alifoka vibaya sana kwani hakuna kitu asichokipenda kwenye maisha yake kama kazi yake iingiliwe. Kufa kwa mmoja wa vijana wake wa kazi ni wazi kuwa sasa kazi ilikuwa inaanza rasmi.




"Ninachokijua mimi mkuu ni kifo cha Welason Mpopoki na sina hakika kama aliyehusika na kifo hicho ni mwanausalama wa kawaida au ni jasusi." Akajibu Amsuni.




"Kwanini hujui, kwanini.....!" Hakumalizia.




"Bosi!" Aliita Black Scorpion na ndiye aliyeikata kauli ya bosi huyo. Malfrey akageuza shingo kwa kumtazama mtu huyo.




"Ndani ya nchi hii wapo wapelelezi hata hivyo pia kuna jasusi ameingia nchini." Akashtuka Malfrey baada ya kusikia kuna jasusi ameingia nchini kwanini jasusi aingie nchini na ni jasusi kutokea taifa gani? Maswali kama hayo yalikuwa yakiushambuli ubongo wake. Black Scorpion akaendelea.




".....hisia zangu zinaniambia hivyo kwani huwa najua nyendo zote za ufanyaji kazi wa wapelelezi wa nchi hii ila ndani ya ufanyaji kazi huu wa kushtukiza lipo jambo jipya ndani yake sasa hii ni hatari sana. Ufanyaji huu wa kushtukiza au kung'ang'ania jambo hufanywa na wapelelezi wa Tanzania mkuu, sasa nina mashaka sana na hilo huwenda ndani ya nchi hii tunae jasusi wa kike....kwanini nasema jasusi wa kike....?" Akauliza na kuweka tuo kwanza akatazama kila pande kama anayetaka kujua idadi ya watu waliyomo mule ndani. Akaendelea.




".....nimekutana na kiumbe anayejua kushambulia, mwepesi, mbishi na mwenye malengo mabaya ya kuuwa kwa adui. Kiumbe huyo ni kiumbe mwanamke na upiganaji wake naulinganisha na wa jasusi hatari sana wa kike anayetokea Tanzania ambaye anafahamika kwa jina la Catherine....!"




"Unamjua?" Akauliza Malfrey Kobra.




"Ndiyo, ila sijawahi kukutana naye ana kwa ana...!"




"Sasa unamjua vipi?" Akauliza tena huku watu wengine wakiwa makini kumsikiliza.




"Sijaanza leo kazi hii ya upelelezi na tangu niwapo kazini nchini Tanzania nilikuwa najitahidi sana kuhakikisha nawajua wapepelezi wengi hatari wa nchi nifanyayo kazi. Namfahamu Roi kwa sura kabisa hata hivyo namfahamu binti anayekwenda kwa jina hilo nililokutajia awali, huyu namfahamu kwa utendaji wake wa kazi, ni mpole awapo kazini na upole wake umebeba hatari kubwa ya ufanyaji maamuzi ya kweli sijui labda kwa kuwa ni mwanamke maana tunaamini mwanamke ni hatari zaidi katika kushambulia na kufanya maamuzi hii iko kihistoria. Huyu binti niliwahi tu kuiona sura yake pichani na kuzisikia sifa zake kwa uchache kama nilioueleza." Akaweka tuo tena na kuzungusha macho yake. Alikuwa kwenye mavazi yake ya kujificha kama ilivyo ada yake.




"Huyu mwanamke nimekutana naye mara mbili kwenye harakati zangu na nimepambana naye hata hivyo sikufanikiwa kumzidi ujanja na hakufanikiwa kunizidi ujanja pia.....!"




"Unataka kuniambia nguvu zenu zinalingana?" Akauliza kwa hamaki Malfrey.




"Hapana, silingani naye nguvu hata kidogo, ni dhaifu mno binti huyo na nimejihakikishia kupitia mapambano yangu naye, nilichokigundua ni kwamba alitaka kulazimisha kunifahamu, nilipogundua hilo nikawa makini zaidi hii ndiyo pekee iliyopelekea mimi naye tushindwane. Mkuu kumbuka ni mapema mno mimi kugundulika ukizingatia mimi bado ni mfanyakazi nikiwa kama usalama wa taifa nchini Tanzania, sikutaka anifahamu mapema namna hii."




"Namtaka huyo jasusi wa kike haraka iwezekanavyo je, mnaweza kuniambia namna ambavyo nitamtia mikononi? Huyo anaweza akawa kikwazo kizito sana kwenye mpango wetu halafu ni vema kama mngejua yuko hapa nchini kwa minajili ipi." Aliongea Malfrey.




"Kama yuko hapa nchini basi ujue yupo kwa ajili ya kuwatafuta madaktari waliyopotea nchini Tanzania." Akasema Black Scorpion, Malfrey akashtuka, hili lilikuwa jipya kwake, madaktari waliyopotea nchini Tanzania. Akajua kweli nchi hiyo ni ving'ang'anizi. Miaka zaidi ya ishirini pengine iliyopita? Akashangaa.




"Mbona walikuwa kimya miaka yote hiyo na hawakuwahi kupiga hatua kubwa namna hii?" Akauliza Malfrey akiwa ameanza kujua ugumu unakujaje.




"Awamu zilizopita zilikuwa pozo sana, hii ni awamu ya tano, awamu hii haijawahi kufikiria kurudi nyuma hata kidogo mkuu na ni awamu ambayo kiongozi wake hutoa amri yenye kuhitaji matekelezo na si maneno matupu. Rais wa nchi hiyo amesema ni lazima wataalamu wake wapatikane hai ama wafu kinyume na hapo hategemei." Akasema Black Scorpion.




"Nataka sasa....nataka mniambie nampataje huyo malaya wa kike nije kuzaa naye mtoto wa ugonjwani, namtaka na mnipe mbinu papa hapa nitakayoikubali ndipo niwape ruhusa ya kwenda kuniletea, sitajali hata akiwa maiti ni sawa tu ila sura yake niione nijihakikishie. Huyo Rais wenu ni juha....juha tena juha bwege mtozeni, anawataka wataalamu wake?" Akacheka cheko kubwa sana kisha akatulia baada ya pumzi kukata kisha akasema tena.








"Nataka sasa....nataka mniambie nampataje huyo malaya wa kike nije kuzaa naye mtoto wa ugonjwani, namtaka na mnipe mbinu papa hapa nitakayoikubali ndipo niwape ruhusa ya kwenda kuniletea, sitajali hata akiwa maiti ni sawa tu ila sura yake niione nijihakikishie. Huyo Rais wenu ni juha....juha tena juha bwege mtozeni, anawataka wataalamu wake?" Akacheka cheko kubwa sana kisha akatulia baada ya pumzi kukata kisha akasema tena.




"Hajui....hajui kama mmoja amekufa kifo cha kunitia uchungu, hajui kuwa huyu aliyebakia ndiye maisha yangu na akiondoka huyu sina uhai. Sitaki huyu aondoke kwa kuwa sitaki kutibiwa nje ya nchi hadi kisasi changu cha kurudisha mali zangu zilizopotea kitimie.....Mzuieniiii! Nasema mzuieni huyo malaya na mnileteeeee.....! Nipeni mbinu basi nipeni mbinu Amsuni!!" Aliongea kwa kufoka akizidhihirisha hasira zake na mwishoni Malfrey Kobra alimuita Amsuni kwa sauti ya mkoromo wa hasira. Amsuni akamtazama kama nani sijui.




"Wewe ni mtu hatari sana ila bado hujaonionesha chochote, kuanzia sasa nataka ukunjue kucha zako ili wajue kuwa sina mpuuzi kwenye kazi yangu. Nataka kabla Mr. Polgeo hajauingiza mpango wake wa nje hapa nchini, huyu malaya wa kike awe ndani ya vitengele vya mikono yangu. Tukimuacha huyu lazima atataka kumjua Musa na akimjua Musa maana yake mimi na ninyi yaani sisi sote tumekufa. Hawezi kumjua Musa bila kupitia sisi lazima atumalize sisi ndipo amfikie Musa." Akasema kwa marefu Malfrey. Kimya kikuu cha kufikiria mpango utakuwaje ili mkuu huyo aukubali kilishika hatamu hapo ndani. Kimya hicho kiliweka himayani mwake dakika tatu nzima kila mmoja kwa dakika hizo zilizopotea alikuwa akimtazama mwenzake kama ndiye mwema ama mwenye kujua zaidi.




"Amsuni!" Aliita Black Scorpion akiwa ndiye pekee aliyefanikiwa kuutia ukimya ule kibindoni mwake.




"Naam!" Amsuni Bhehe akaitika. Black Scorpion akavuta pumzi za kutosha kisha akauliza.




"Taarifa ya kumpa Welason kuhusu kumuondoa waziri wa nishati na madini ilitoka kwako muda gani?"




"Ilikuwa ni saa saba na nusu usiku hata hivyo simu ilikuwa haina uhai bilashaka maana ujumbe wa kuonesha kuwa simu hiyo iliwashwa ni saa nane na dakika arobaini na mbili ndiyo majibu ya kuwa ujumbe wangu umefika kwa Welason ulirudi kwangu." Alijibu Amsuni hapa Malfrey na Tally Man walimtazama Black Scorpion kwa jicho la tatu. Huyu mtu hakuwa mdogo kifikra hili hawakuwa wameling'amua.




"Ujumbe huo haukusomwa na Welason Mpopoki." Akasema Black Scorpion.




"Kwanini?" Akauliza kwa hamaki Amsuni. Black Scorpion akatulia kabla ya kuamua kujibu.




"Ujumbe uliutuma saa saba na nusu. Muda huo Welason alikuwa amezima simu alivyo mpuuzi na kujikita kwenye starehe ya ngono na malaya aliyemnunua na kumuingiza ndani kwake. Najiamini kusema simu ilikuwa imezimwa kwa kuchelewa kwa majibu kwenye simu yako. Hii starehe ya ngono ndiyo iliyomfanya hata akiwa anavamiwa asijue chochote akauawa na malaya wake. Ujumbe huu ulikuja kurudi kwako saa nane na dakika arobaini na mbili, muda huo muuaji wa Welason Mpopoki alikuwa tayari ameshajichukulia jukumu la malaika mtoa uhai na kuamua kuiwasha simu, ujumbe wako umenaswa na adui tumtakaye sisi hapo mtakuwa mmenielewa vizuri?" Akauliza baada ya kuwapa maelezo hayo.




"Hili sikuwa nimeliwaza nadhani ugonjwa huu unazidi kuniathiri zaidi ubongo wangu hadi kuwa mzito kuchanganua ila najivunia kuwa na mtu au watu makini kama ninyi. Nini mpango wako sasa hapo Black Scorpion?" Akauliza mwishoni Malfrey Kobra mara baada ya kukubaliana na maelezo ya mtu huyo.




"Mtego." Akasema, wakajiweka vizuri kusikiliza mbinu za mtego huo, Black Scorpion akaendelea.




".....lazima huyu muuaji wa Welason Mpopoki na adui yetu kwa ujumla ategwe. Anategwa vipi.....? Mtego huu utatokana na ujumbe ulioutuma Amsuni kwa Welason. Yeye ataamini moja kwa moja leo waziri wa nishati na madini kuwa anauawa. Hivyo basi sisi tunatakiwa kuwa hapa na tuwe macho kwelikweli. Muda huo wa kuwa macho ni muda wa ufanyaji kazi pia. Lazima waziri wa nishati na madini Abdallah Juma Kimbo afe hata hivyo muuaji wa Welason naye afe. Ni ndege wawili kwa jiwe moja." Akahitimisha. Malfrey Kobra akacheka cheko kubwa sana, alicheka kuliko uwezo wa binadamu kucheka kwa siku. Papo hapo Tally Man alimpa mkono wa hongera Black Scorpion kwa kujua namna ya kufanya kazi kwa akili nyingi.




"Kazi hii ni yako Amsuni Bhehe na ni lazima kwa nusu saa hii uwe umeandaa vijana wa kutosha, narudia tena wa kutosha hata hivyo kuwe na Chopa ambayo itahakikisha huyu mwendawazimu hapotei kwenye macho yetu kipumbavu." Akatoa agizo Malfrey Kobra.




"Hapo kwenye hao vijana hakikisha anapatikana mdunguaji mwenye shabaha kali hata akiwa amefumba macho yake yote mawili. Nasema hivyo kwa maana kubwa, nyumba ya Abdallah Juma inatazamana na ghorofa moja ndefu na kwa kuwa nyumba yake ina uzio mfupi, nadhani itatusaidia sana sisi kufanya mauaji ya watu hawa wawili kwa wakati mmoja. Ni rahisi sana kutekeleza mauaji kwani nyumba ya huyu muheshimiwa imejengwa kwa vioo kwa asilimia kubwa sana. Mdunguaji atakaa kwenye chumba kimoja cha ghorofa ya kati ambacho kitakuwa kikiangaliana na nyumba ya muheshimiwa huyu kwa kiasi kikubwa. Tutakuwa na mawasiliano na mawasiliano hayo ni kwa watu wachache ambao watatumika kama viungo muhimu kwenye kazi hii." Akaongea kwa marefu Black Scorpion.




"Mdunguaji nitakuwa mimi mwenyewe na nitakuwa nikiwasiliana na wewe utakapokuwa ndani vivo hivyo nitakuwa nikiwasiliana na vijana nitakao wapanga kikazi ili kuhakisha hakuna njia atakayoitumia kutorokea." Akamaliza Amsuni Bhehe kuongea. Wakafurahi kwa mpango huo. Mipango na maandalizi yakapangwa kikamilifu huku muda ukisubiriwa.




_____________




"MABULE UNAJUA MUDA UNAKWENDA LAKINI SEMBUYAGI HAJAREJEA BADO, NAJUA WEWE UKO KARIBU NAYE SANA AMEKWAMBIA MAHALI ALIKOKWENDA?" Aliuliza Marietha alipokuwa akiingia ndani akitokea nje ambako alikuwa amekaa akiyatazama mandhari ya eneo walilopangiwa kuwepo kwa kazi yao nzima. Mabule alimtazama binti huyo kisha akasema kuwa aliagwa na mtu huyo kuwa anakwenda mjini kuna mambo anayafuatilia.




"Alisema ni mambo gani anayoyafuatilia au hakukuambia?" Akauliza tena Marietha.




"Ni jambo lililopo ndani ya kazi yetu."




Kwanini hakutaka tuongozane?" Mabule akafikiria kwa muda kabla ya kujibu hilo swali aliloulizwa.




"Sijui sababu ya kutokuongozana hata hivyo hakuwa ameiwekea mkazo safari hiyo pia aliahidi asingechelewa kurudi si unajua tangu tutoke kwa mkuu kumueleza tulipofikia na mkuu akakalipia sana kwa kuwa watu wanakufa hovyo bila mpangilio na hatujafanikiwa kumkamata au kumkaribia muuaji hata mmoja. Kumbuka pia tulipotoka kwenye nyumba ya marehemu Masuka Mvungi na kumuhoji mke wa marehemu. Hii imemfanya Sembuyagi kuwa kimya muda wote asiseme chochote na leo akaamua kutoka mwenyewe huku akisema anataka kuona kitu huwenda akapata mwanzo mzuri. Tumekuwa watu wa namna gani sisi Marietha, tusianze kulaumiana wenyewe kwanza tujiulize kwanini hatufanikiwi? Kwanini kila mahali tunakuwa wa kukomea njiani...hatukumaliza mahojiano na binti Mbaruku, badala ya kumuhoji hadi mwisho ili tupate njia tukashauriana tumuache hadi siku inayofuata matokeo yake siku iliyofuata ikasemekana hata mumewe hakumzika amekimbia na kwenda kujificha pasipojulikana. Haya, ila tutafika tu na itajulikana." Akazungumza Marietha akiwa haelewi mwenendo wa kazi yao ya upelelezi ilikuwa inakwenda kwa namna gani.


"Sijawahi kuwa mpelelezi wa hivi Mabule." Akasema Marietha huku akikaa kitini na kumtazama Mabule usoni ambapo alikutana na mshangao wa kuuliza akaendelea.


"......Sembuyagi kuna kitu anakijua na bado anatufanya sisi ni watoto wadogo. Kuteuliwa yeye kuwa kiongozi isiwe sababu ya kutuona hatujui kitu Mabule. Tuna wiki ya tatu sasa na hatujafanya kitu cha maana cha kuonekana au wewe una hatua yoyote uliyopiga? Tumekuwa tukiyafuata maamuzi yake, hakuna kikao cha pamoja ambacho sisi na yeye tulikaa na kupanga chochote kuhusiana na kazi hii au anadhani uzito wa kazi hii umemuelemea yeye tu kama kiongozi?"




"Unamaanisha nini kwenye lawama zako Marietha?" Akauliza Mabule huku akimtazama binti huyo usoni. Binti ambaye alikuwa mrembo kwelikweli.


"Sembuyagi anaifanya hii kazi mwenyewe kwanini na wakati sisi ni wamoja, huoni kama anajipalia makaa ya moto au unataka sisi tuwe na kazi ya kumuokoa atakapo patwa na matatizo ambayo hatutayajua chanzo chake?"




"Unavyoonekana humuamini Kiongozi Marietha?" Akasema Mabule akiwa anamtazama binti huyo kwa umakini zaidi.




"Sina maana hiyo Mabule."




"Ila?"




"Ni muda mrefu sana hadi sasa tangu alipoondoka, ameondoka hapa saa sita kamili na sasa ni saa nane na dakika zake. Sembuyagi yuko kwenye matatizo Mabule si kawaida hii." Akaonesha wasiwasi wake Marietha akiwa anamaanisha zaidi huku akiendelea kumtazama Mabule usoni vilevile akilipuuza swali la shutuma la Mabule. Mabule akatabasamu kwa kejeli kisha akasema.






"Ni muda mrefu sana hadi sasa tangu alipoondoka, ameondoka hapa saa sita kamili na sasa ni saa nane na dakika zake. Sembuyagi yuko kwenye matatizo Mabule si kawaida hii." Akaonesha wasiwasi wake Marietha akiwa anamaanisha zaidi huku akiendelea kumtazama Mabule usoni vilevile akilipuuza swali la shutuma la Mabule. Mabule akatabasamu kwa kejeli kisha akasema.


"Si yule....yule hawezi kuingia matatizoni kirahisi ni makini sana labda kama unajingine akilini mwako.....ngoja, ngoja tusubirie kwa muda wa masaa mawili tuone, ikifika saa kumi hajatokea lazima tumfuatilie haraka sana." Akasema Mabule. Marietha akanyanyuka kwa hasira na kutoka pale sebuleni. Akawaza mengi kichwani mwake, kuna jambo lilikuwa likimsumbua kichwa chake na bado hakuwa amekipangilia vizuri. Huu ulikuwa ni mchanganyano mkubwa sana. Akazimeza hasira zake na kutulia asubirie hiyo saa kumi aone. Hakutaka waingie matatizoni mapema ikiwa hata hawajafanikisha chochote.




__________




Frank Matiale Bambi alikuwa barabarani akiwa juu ya pikipi lake akiwa anatokea mahali aishipo baada ya safari ya kutoka kwa mkuu wake wa kazi kukamilika na kuanza kuifuata njia iliyokuwa ikimpeleka nyumbani kwa waziri wa nishati na madini muheshimiwa Abdallah Juma Kimbo. Alipotazama muda kwenye saa yake ilikuwa ni saa tisa kamili. Akaongeza mwendo na kuhakikisha anawahi mapema kabla ya muda husika. Alifika katika eneo ambalo nyumba ya muheshimiwa huyo ipo. Alikuwa tayari ameitafutia mahali pa kuegesha pikipiki yake hivyo hapo alipo alikuwa akizirusha hatua zake taratibu na kuingia ndani ya jengo moja lililopo mashariki mwa nyumba ya muheshimiwa waziri. Nyumba aliyoingia Frank ilikuwa ya ghorofa mbili, hii aliona itamfaa kwa kuwa nyumba ya waziri ilikuwa ni ya chini na uzio wake ukiwa mfupi kiasi. Akapanda hadi juu na kujibana kwenye madishi ya ving'amuzi mbalimbali yaliyokuwa yamefungwa juu ya jengo lile. Akiwa hapo juu alikuwa na uwezo wa kuona chochote kile kilichokuwa kikitokea popote kwani jengo lile lilikuwa katika njia zote zilizokuwa zikitoka na kuingia kwenye nyumba ya muheshimiwa huyo. Kwa mbali akiwa pale aliona gari iliyokuwa ikija eneo ambalo yeye yupo hata hivyo gari hiyo ilisimama umbali fulani kwenye duka moja la vipodozi kisha kwa muda mfupi uliopotea, akateremka binti mrefu kiasi mwenye urembo uliojificha kwenye kofia pana ya urembo akiwa amevaa suruali ya jeans ya rangi nyeusi ya kuvutika na kiatu nyeusi cha ngozi chenye soli ngumu. Mkononi alivaa saa ndogo yenye mikanda ya chuma ya rangi ya dhahabu. Frank alizidi kumfuatilia yule binti na alikuwa ameanza kuzitupa hatua zake za haraka kuikabili nyumba ya waziri Abdallah Juma Kimbo huku akiwa makini kwa kutazama kila mahali. Gari ile ilimfikirisha sana Frank, ni kama kuna mahali aliiona na si siku nyingi sana. Ni usiku wa siku hiyo tu ndiyo alipata kuiona. Huwenda gari zilikuwa zikifanana sawa; ila kwanini binti huyo aielekee nyumba ya muheshimiwa huyo. Frank alikuwa akiwaza huku akimuona binti yule akiukaribia ukuta mdogo wa nyumba ya muheshimiwa kisha akauparamia ukuta na kuingia ndani ya uzio. Haraka sana Frank akamtilia mashaka huyu binti baada ya namna alivyomuona akiuruka ule ukuta na namna alivyokumbuka kifo cha Welason. Akajipa uhakika kuwa lile gari peugeot 404 ndilo alilokutana nalo usiku na huyo binti atakuwa ndiye muuaji wa Welason kwani hata alivyotoka ndani ya nyumba ya Welason, ile gari ilikuwa imekwishaondoka. Akakumbuka na zile purukushani za mule ndani ya nyumba ya Welason akaziunganisha. Sasa alikuwa na muuaji kamili mbele ya macho yake, akafungua begi lake alilokuwa amelibeba mgongoni akatoa vilivyomo. Akavifunga kwa haraka ya kijeshi kisha akabandua na kifuniko kigumu kilichokuwa kimefunika lenzi ya kuonea mbali ya bunduki hiyo ya kudungulia ambayo ilikuwa imekamilika na aliilaza vema kwenye visimamio vyake, akaiweka sawa mashine yake ile ambayo ilikuwa ni H.S Precision Pro Series. 338 Lapua magnum iliyobuniwa huko U.S.A mwaka 2000. Akajilaza vizuri pale chini ya madishi ya ving'amuzi mbalimbali akihakikisha hawezi kuonekana kirahisi na kiumbe cha aina yoyote. Akaweka jicho lake nyuma ya Darubini ya mashine ile hatari. Akachungulia na kumuona mlinzi wa jengo lile akiwa amekamata mtutu wa bunduki yake iliyokuwa ikining'inia begani akiwa anazunguka hapa na pale. Pia akamuona yule binti akiwa anamnyatia yule mlinzi hata hivyo hakuwa kwenye wazo la kutaka kumuua. Akashangaa Frank kuona kuwa huwenda binti hakuwa pale kwa lengo la kuuwa. Waziri alikuwemo ndani mwake bado kwani Frank alikuwa anaushahidi juu ya hilo baada ya kumfuatilia muheshimiwa huyo mara tu alipokuwa na taarifa dhidi ya kutaka kuuawa kwake. Hata hapo aliweza kumuona akiwa anzunguuka ndani ya nyumba yake akiwa anashika hiki na kile kabla ya kupotelea chumbani muda huo. Alimuweka kwenye kumi na nane zake huyo binti akiwa na lengo la kumchapa risasi ambayo alikuwa na hakika isingemuua bali ingemdhoofisha na kumuweka chini. Akiwa anazidi kumtafutia nafasi, akasikia sauti ya Chopa ikiwa inakaribia eneo hilo akasita. Yule binti akapata mwanya wa kuzama kabla hiyo Chopa haijafika usawa huo kwani hakujua inalengo gani na pia hakudhani kama inahusiana na kazi yake.


Hakusumbuka nayo.




Baada ya kufanikiwa kumpita vema mlizi yule ambaye macho yake yalikuwa yakiitafuta Chopa hiyo ilipo akiwa bado nje ya ule uzio, akaambaa na ukuta kimya kimya kuelekea kwenye mpango. Frank aliporudisha macho kwenye lenzi yake akakuta mahali alipokuwa yule binti hayupo hii ni baada ya kutoka kuitazama Chopa ile ambayo ilitua nyuma ya lile jengo refu lililoko upande wa kuli wa mkono wake. Akarekebisha lenzi yake ili iwe na nguvu ya kuona hadi ndani kupitia vile vioo vya madirisha akamuona yule binti akiwa anatafuta mahali pa kujificha, akamuona akisogeza sofa kando na kujibana mahali. Frank akasita kumshuti kwani Chopa sasa ilifika mahala ambapo alikuwa na uhakika kama angetingishika waliyoko chopani wangemuona kwani kuna baadhi ya watu hakuwa akiwaelewa kabisa eneo hilo ila hakujua wapo hapo kwa minajili ipi na hakujua kama wanashirikiana na huyo binti ama lah!. Akavuta subira huku akiitazama Chopa ile kwa kuichunguza huku kwa wakati huo huo akimfuatilia yule binti asiyemjua. Ilikuwa ni Chopa inayomilikiwa na mtu binafsi.




Kwanini imezunguka na kusimama kwenye uwanja mdogo nyuma ya jengo hilo refuna. Akawaza.


Wakati Frank anaiona ile Chopa ikiwa inazunguka hatimaye kutua, hakuwa akijua kama Amsuni Bhehe alikuwa ameshaweka makazi kwenye jengo la ghorofa alilokuwa amelipa ubavu ambalo nyuma yake ndiko iliko hiyo Chopa na alikuwa kwenye ghorofa ya katikati kama ya tatu hivi kwenye dirisha la chumba kimoja ambacho kilikuwa kikitazamana na jengo la waziri Abdallah Juma.




"Kumepoa sana eneo hili huwenda hakuna mtu kabisa ambaye amefika je, bado tunasubiri maana nilimuona muheshimiwa akiingia chumbani kwake na amejituliza humo, kwa hii mashine yangu siwezi tena kumuona." Kwa upande ule wa lile jengo refu la ghorofa Amsuni Bhehe aliongea kupitia kisafirisha sauti ambacho alikivaa kwenye kola ya suti yake nyeusi akiwa amechutama nyuma ya lenzi ya FR F1 Refle zao la mwaka 1966 huko nchini Ufaransa.




"Tazama kama kuna mdudu eneo hilo maana nataka kuingia ili kuing'oa roho ya huyo waziri pia hakikisha vijana wanakuwa tayari kwa lolote maana adui yetu ni hatari kama nilivyowapa mshabaha wake." Sauti kutoka kwa Black Scorpion ilirudi kwa Amsuni. Amsuni akamagaza huku na huko kupitia lenzi ya bunduki yake ya kudungulia asione kitu.




"Kuko sawa, hakuna mtu zaidi ya yule mlizi pekee." Alisema Amsuni Bhehe. Mara chini ya lile jengo refu ambalo ndanimwe alikuwamo Amsuni, kuna gari ilipiga bteki na garini humo akateremka Black Scorpion akiwa kwenye mavazi ya kujificha kama ambavyo huwa anavaa muda wote akapiga hatua za haraka haraka hadi kwenye ule uzio wa ile nyumba ya muheshimiwa. Akatazama mahali mlinzi alipo. Muda wote huu Frank alikuwa akimfuatilia huyu mtu wa ajabu ambaye alikuwa amevaa kiajabu ajabu. Akachekecha kichwa chake hasa ubongoni akajua hapo si salama na mtu huyo si mwema pengine kuliko yule binti. Akamuona yule mtu akiruka uzio na kwa kasi ya ajabu akichomoa kisu na kumrushia yule mlinzi ambacho kilimpata kooni. Mlizi yule akalishika koo lake huku akishuka chini kama anayetaka kukima goti chini alipofika mwisho wa kuchutama akapinduka na kunyoosha miguu. Frank alikuwa na nafasi ya kumuua huyu mtu hata hivyo hakufanya kama alivyowaza kwanza alitazama chini ili kujionea mtu huyo alitokea wapi. Akazunguusha lenzi yake kila mahali kulizunguka lile jengo refu. Lo! Kulikuwa na watu wasiyoeleweka wakiwa wamevaa mavazi tofautitofauti huku wakiwa wanazunguka chini ya jengo lile refu la ghorofa la ubavuni mwake, pia kulikuwapo na gari tatu zenye vioo vya giza huku zenyewe zikiwa nyeusi.




"Mpango wa kumuuwa waziri huu!" Akajisemea moyoni. Akarudisha lenzi kwa yule mtu aliyekuwa anaingia ndani,




"Shiit! Nimechelewa." Akang'aka Frank kisha akarekebisha tena lenzi yake. Sasa akawa na watu wawili wa kuwatazama. Yule msichana ambaye alijibana kwenye upenyo wa sofa na sofa sambamba na huyu mtu aliyevaa mavazi ya kujificha kama Spider Man. Yule mtu akamuona akitazama huku na huko kisha kuifuata korido iliyokuwa ikielekea mahali vyumba vilipo.




"Korido hiyo hiyo mbele utakunja kona huko ndiko alikoelekea muheshimiwa baada ya hapo sitakuona tena." Akasema Amsuni akiwa makini na lenzi ya bunduki yake palepale juu dirishani. Hapo hapo akamuona mtu akisimama nyuma ya Black Scorpion kwenye nafasi ya sofa na sofa, alikuwa mwanamke mwenye kofia kubwa la urembo kichwani mwake akiwa na bastola mkononi.




"Shiit! Alituwahi mjinga, yupo ndani muuaji wa kike nyuma yako na anasilaha mkononi kunja kona haraka wacha nimsubiri akipiga hatua nimmalize." Akasema Amsuni kisha akabadili maongezi baada ya kurekebisha kisafirisha sauti chake.




"Kaeni 'stand by' yupo ndani muuaji na hakikisheni hatoki."




"Tumekupata mkuu!" Alijibu kiongozi wa watu wa chini ambaye alikuwa akiongoza kikosi cha wapambanaji wa ana kwa ana na silaha pia, kilichochaguliwa naye. Akaweka umakini mbele.




Frank alikuwa njia panda asijue ampige nani kati ya wale wawili mule ndani. Sasa alimuona yule mtu aliyevaa kiajabu ajabu akiwa anapotea kwenye kona ambayo yeye hakuweza kumona tena kama ilivyo kwa Amsuni. Yule binti akapiga hatua moja mbele kama atakaye kukimbia hata hivyo alisita baada ya ishara ya mtu yule ambaye alivaa kiajabu ajabu kuonekana dhahiri kuwa alikuwa akitumia kisafirisha sauti kilichobanwa kitaalamu kwenye vazi lake. Ile hali ikamshtua yule binti na kuhisi hatari kubwa ilikuwa ikienda kumkali na kwa uzoefu wake alijua kuwa lipo jambo na linaweza kuyagharimu maisha yake. Yule binti alitazama kushotoni kwake kisha akarudi nyuma na kujibana palepale kwenye sofa. Risasi kutoka kwa Amsuni ikapasua kioo na kumkosa.




"Mjinga wewe aaghr!" Alibwata Amsuni baada ya kupoteza risasi yake baada ya kumkosa hakukaa. Na ile risasi ilipopasua kioo Frank alikuwa kama kachachawa sasa alijikuta kuwa na lengo la kumsaidia yule binti kwani aliona jinsi alivyo kwenye hatari kuliko alivyofikiria. Akatazama mahali risasi iliyomkosa yule binti ilipotoka huku akiwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa aliyefanya vile alikuwa ni mdunguaji. Hapakuwa na mtu licha ya kuona uwazi kwenye dirisha moja hii ikimaanisha kuwa mdunguaji alikuwa hapo. Akakasirika kwa kupiga ngumi chini, wajinga walikuwa wajuzi kuliko.










KUMBUKA INAPATIKANA BADO KWA SH. 3000 NO. ZA MALIPO HIZO HAPO JUU.




Akatazama mahali risasi iliyomkosa yule binti ilipotoka huku akiwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa aliyefanya vile alikuwa ni mdunguaji. Hapakuwa na mtu licha ya kuona uwazi kwenye dirisha moja hii ikimaanisha kuwa mdunguaji alikuwa hapo. Akakasirika kwa kupiga ngumi chini, wajinga walikuwa wajuzi kuliko.




Yule mtu aliyevaa kiajabu alizama hadi chumbani alipofika alimkuta muheshimiwa akitokea maliwatoni. Akasikia sauti ikimwambia masikioni kuwa;


"Mpuuzi nimemkosa na bado yumo ndani kajificha kuwa makini." Aliposikia hivyo hakuwa na mjadala na muheshimiwa waziri alichokifanya ni kummiminia risasi na kutoka mule chumbani sasa akiweka umakini maana alijua mbele yake yupo adui hatari zaidi.




____________




"Hatuwezi kuzidi kusubiri Mabule muda unakwenda na hatujui mwenzetu yuko wapi twende sasa!" Aliongea Marietha huku akiwa anatoka nje na kuparamia pikipiki.




"Nakubaliana na wewe sasa huwenda Sembuyagi akawa matatozoni, twende mjini." Alijibu Mabule huku akirukia juu ya pikipiki ambalo lilikuwa limekwisha kuondolewa na mtoto huyo wa kike aliyecharukwa. Waliendesha kwa kasi sana hadi walipofika katikati ya mji.




"Tutajua alipo kweli?" Akauliza Mabule akiwa nyuma.




"Lazima tuju.....!" Akataka kuongea Marietha hata hivyo alishindwa kumalizia mara baada ya Mabule kumkatisha.


"Tazama hizo gari nyeusi hatuna budi kuzifuatilia maana zimetoka kwa kasi hapo maegeshoni na kuna yule jamaa aliyeondoka na pikipiki hapa kuna hatari Marietha tunafanyaje?" Aliuliza Mabule akiwa amechanganyikiwa.




"Subiri tuegeshe pikipiki kwenye kingo za hili jengo refu." Akajibu Marietha kisha akapiga breki na kusimama ghafula. Wakashuka kutoka juu ya pikipiki na kutaka kuanza kukimbia kwa miguu kuona nini kilichokuwa kikiyakimbiza hayo magari. Punde walipamiana na mtu aliyekuwa akitokea upande wa nyuma wa lile jengo refu akiwa anaambaa chini ya jengo lile akiwa amechanganyikiwa na hofu kuu ikiwa juu yake.




"Samahani, msikae hapa....hapa ni hatari hamuoni?" Akasema yule mtu aliyekuwa anaitokea huko nyuma ya jengo kwa kukimbia.




"Sembuyagi nini?" Aliuliza Marietha akiwa amechanganyikiwa baada ya kumuona mtu huyo vizuri usoni.




"Ah...ah....ah! Ni, ni nyinyi, ooh! Afaghali mmefika hapa maana itasaidi." Akasema kisha akatulia kidogo sembuyagi kujipa utulivu. Akaendelea.


".....muuaji yule wa kike aliyekuwa akifanya mauaji hapa mjini ameonekana leo na huwenda amefanya mauaji ya muheshimiwa waziri msataafu aliyekuwa waziri wa nishati na madini. Hatuna muda wa kupoteza ni lazima muuaji huyo tumkamate sisi ili tujue ni kwani anaua? Haraka nifuateni kwa kuwa najua uelekeo aliochukua." Alipiga kelele Sembuyagi Mpauko. Hii hali ikamchanga sana Marietha, kusema kuwa kulikuwa na muuaji wa kike hii huwenda ikawa sawa ila namna muonekano wa Sembuyagi ulivyo na jinsi alivyokuwa akijikanyaga baada ya kuwaona hapo. Hili lilikuwa ni tukio jipya kuliona kwa mtu huyo. Akakata shauri na kuona ngoja azidi kuwa mvumilivu huwenda wakafanikiwa kufikia lengo. Wakaanza kukimbiza wakiwa wanamfuata Sembuyagi nyuma huku ile kauli ya muuaji wa kike ikijirudia kichwani mwake asijue Sembuyagi amemjulia wapi huyo muuaji wa kike.




___________




Kichwani nilikuwa na maelezo ya yule mjinga niliyemuua usiku uliopita. Maelezo yake hayakuwa ya kupuuza hata kidogo na lengo langu kubwa lilikuwa ni kumpata mtu aliyekuwa akiitwa Amsuni Bhehe. Maelezo ya marehemu Welason Mpopoki yalinifanya kwa wakati huu niwe mjini na nilikuwa katikati ya mji nikianza kulitafuta kanisa la Anglikana ambapo niliambiwa kuwa mtu nimtakaye ndipo alipokuwa akiishi. Wakati nikiwa nakunja kona moja huku nikiwa nawaza hili na lile, niliona pikipiki kubwa ikiwa imenipita kwa kasi kubwa sana. Nilishangaa kwenye kona kama hii na huku njia yenyewe ikiwa imejaa waenda kwa miguu iweje mtu awe kwenye mwendo mkali hivi. Nikawa niko nyuma ya pikipiki hilo sasa baada ya kupunguza mwendo baada ya kunipita, nikaliona kwa ukaribu zaidi hilo pikipiki. Lilikuwa ni pikipiki kubwa na pikipiki hili ni mara kadhaa sasa naliona. Nikavuta kumbukumbu zangu huku nikionesha ishara kuwa nataka kuingia upande wa kulia baada ya mtu mwenye pikipiki lile ninalolifahamu akielekea huko. Nilikuwa nimeacha uelekeo wa kwa Amsuni sasa nilikuwa nikilifuata hili pikipiki ambalo nililijengea mashaka makubwa sana. Mbele yangu kulikuwa na duka kubwa la vipodozi na hapa ndipo mtu aliyekuwa akiendesha hilo pikipiki aliposimama na kuliegesha pikipiki lake. Akavua kofia ya ulinzi kichwani kisha akaelekea kwenye jengo moja la ghorofa mbili. Akaingia ndani. Nikiwa ndani ya gari yangu Peugeot 404 niliweza kuuona mwendo wa mtu huyo. Naam, alikuwa ni yule kijana ambaye nilimfahamu kama mpelelezi ambaye nilimgundua zaidi baada ya kuchunguza kifo cha Masuka Mvungi japo ni mara kama mbili hivi niliwahi kumuona na sehemu ya kwanza kabisa kumuona ni kule kwenye soko kuu wakati tukio la kuuawa Mansuli Bingwa likiwa limetokea.




Hapa palikuwa na shida. Niliwaza.


Nikiwa hapo garini bado huku nikimfikiria Amsuni Bhehe mtu aliyetajwa na marehemu Welason, akili yangu ikaniasa niachane na huyo kijana na niendelee na kazi yangu ambayo hitimisho lake ni kuwapata madaktari waliotekwa nchini Tanzania na kusemekana wameletwa kwenye nchi hii. Akili yangu hiyo hiyo ikaniomba samahani kwa kunitaka utulivu huku ikinipiga kofi na kunikumbusha kuwa yule kijana niliyemfahamu kama mpelelezi alikuwa amebeba begi jembamba na refu mfano wa mwanamuzi aliyebeba gitaa mgongoni. Hapa nikakurupusha pumzi zangu na kuzitoa kwa nguvu puani huku nikijisukuma mbele na kuyapeleka macho yangu juu ya lile jengo la ghorofa mbili ambalo aliingia huyo kijana.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog