Simulizi : Kiguu Na Njia
Sehemu Ya Pili (2)
SURA YA SITA
Kwa treni hadi Tabora
Ben R. Mtobwa
afari ya Mwanza hadi Tabora ilikuwa ya kusisimua sana. Ilikuwa safari yangu ya kwanza maishani kusafiri bila kutumia nguvu za miguu
au mikono yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono au miguu yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono yangu kupiga makasia hadi tulipowasili majuzi. Safari hii kazi yangu ilikuwa kukaa kitako, kando ya dirisha, huku macho yangu yakifaidi kilometa zote 453 za safari kwa kuburudishwa na mazingira aina aina.
Tulisafiri kwa aina mpya ya usafiri iliyotambulishwa nchini na utawala wa Mjerumani, gari moshi. Ujenzi wa reli, vyuma imara ambavyo vilitumiwa na gari moshi hiyo kuteleza juu yake, ambao ulianza huko Darisalama mwaka 1912 uliweza kufika Mwanza 1923, ikiwa moja ya matawi ya reli hiyo lililoanzia Tabora. Reli hiyo, maarufu kama reli ya kati inayokata nchi toka mashariki hadi magharibi na toka kaskazini hadi kusini inakadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 2600. Ni moja kati ya kumbukumbu za utawala wa mjerumani, ambazo kamwe hazitafutika katika historia ya nchi hii.
Reli hii ni kiungo pekee muhimu kinachoiunganisha nchi toka bahari ya hindi kwa upande mmoja hadi ziwa
la Tanganyika kwa upande wa pili, jambo linaloifanya iwe tegemeo kubwa kwa usafirishaji wa watu na mizigo si kwa nchi yetu pekee bali pamoja na zile za Burundi, Kongo na Rwanda pia.
Licha ya sababu hizo za kiuchumi reli ilikuwa pia mshirika mkubwa katika masuala ya kiutamaduni na kijamiii nchini. Kwanza iliwezesha makabila yapatayo mia na ishirini ya Tanganyika kufahamiana kwa urahisi. Mzaramo wa pwani angeweza kukutana na Mmanyema wa Kigoma, au Mchaga wa Kilimanjaro kufahamiana na Mfipa wa Mpanda kwa urahisi zaidi ya siku zile za akina Livingstone kutumia miaka maporini toka pwani ya Bahari ya Hindi hadi pwani ya ziwa Tanganyika.
Na hilo halikuwa kwa makabila ya ndani tu. Ujenzi wa reli hiyo ulimfanya mkoloni wa Kijerumani alete vibarua wengi wa kazi hiyo toka nchini India. Hawa ni chanzo cha msamiatai wa ‘kuli’ neno lililozaliwa kutokana na lile la kiingereza ‘Coolie’ wakatii huo likitumiwa kama kashfa kwa vibarua wasio na ujuzi wowote. ‘Kuli’ haikutofautiana sana na ‘manamba’ wa hapa nyumbani ambao walikamwatwa kwa visingizio mbalimbali kubwa ikiwa kushindwa kulipa kodi ya kichwa, na kupelekwa kufanya kazi za mikono katika mashamba ya mkonge kaskazini magharibi mwa nchi yetu.
‘Kuli’ wengi walitoka India, ama walinogewa, ama hawakuwa na uwezo wa kurudi kwao, ama yote mawili, wakaishia kuwa wakazi wa hapa. Leo hii jamii mpya ya akina Gulamali, Manji, Adamjee; na kadhalika inapatikana sehemu yoyote ya Tanganyika; hasa vijijini.
Jing – janga – jing – jang – jing - jang garimoshi lilihangaika kuvuta mabehewa sita wa abiria na manne ya mizigo yaliyofanya tuwe kama joka refu linaloteleza kwa kujikongoja.
Injini ya garimoshi hilo, ambayo sikuhitaji kuambiwa kuwa ilikuwa ikitumia kuni kutengenezea mvuke wa kuiendesha ilikuwa ikitoa moshi mwingi na mzito sana. Moshi ambao ulilala juu ya treni kama wingu jeusi lisilopendeza machoni. Nadhani hiyo ni sababu pekee iliyowafanya waswahili waamue kuita usafiri huo wa ‘garimoshi.’
Nikiwa nimeketi raha mustarehe dirishani pangu nililitazama kwa masikitiko ziwa nililolipenda la Nyanza likitokomea machoni mwangu taratibu. Ziwa hilo lilinilea, lilinihifadhi na kunifadhili kwa muda wa kutosha. Ndilo lililonifundisha kuogelea na kutafuta pesa. Ziwa lililonitoa Kagera na kunifikisha Mwanza. Hilo ndilo ziwa ambalo leo naliacha bila kuwa na uhakika wa kuliona tena. “Nitarudi!” nilinong’ona taratibu.
“Nini?” jirani yangu, mzee wa makamo ambaye tulichangia kiti, alinihoji akidhani nazungumza naye.
Sikumjibu.
Tukapinda na kupenya katikati ya majabali marefu mfano wa milima. Tuliacha jabali moja baada ya jingine, mbuyu mmoja baada ya mwingine huku tukivuka vijito na mito ya hapa na pale.
Mara tukazama katika mapori na misitu mikubwa, kwa mbali tukawaona wanyama mbalimbali kama ngedere waliokuwa wakirukaruka kwenye miti au mbuzimawe ambao walirandaranda juu ya majabali ya hapa na pale. Katika eneo moja lenye mabwawa tuliwaona ndege aina ya flamingo wenye miguu mirefu na midomo myekundu wakiwinda samaki au wadudu ndani ya maji hayo. Ndege wengine, aina mbalimbali pia walikuwa wakiruka huku na huko kama wanaotushangaa au kutushangilia hadi tulipotokomea.
“Mantare!” Yule jirani yangu aliropoka.
Ikawa zamu yangu kumshangaa, “Nini?” nilimuuliza.
“Tumefika stesheni ya Mantare,” alifafanua.
Kweli. Nililiona garimoshi likipunguza mwendo na hatimaye kusimama kando ya nyumba mbalimbali ambazo zilionekana kuwa za wafanyakazi wa reli hiyo.
Palikuwa na purukushani fulani, watu wakipanda wengine wakishuka. Miongoni mwa watu hao walikuwepo pia wafanyabiashara wenye bidhaa mbalimbali kama vyakula, mapambo na mifugo. Walionunua walinunua, wasionunua tulijifanya hatuoni.
Tulisimama hapo kwa dakika kumi tu. Mara garimoshi hilo lilianza tena safari yake kwa mwendo wake wenye maringo, taratibu kama halitaki na baada ya kuchochea huku likikohoa kwa uzito wa mabehewa.
“Kwimba!” mzee aliropoka tena. Nilikuwa nimeanza kusinzia. Nikafunga macho na kuona tukiingia katika stesheni nyingine. Nikatoa kichwa dirishani na kuwatazama wanaoshuka na kupanda.
Tukaondoka.
Jirani yangu huyo alikuwa amejipa kibarua. Kila tulipokaribiakituofulani nilimsikiaakitamkakwanguvu,“Malya,” kisha “Seke.” Sikufumbua macho yangu hadi pale aliponitikisa kwa nguvu huku akiniambia, “Amka tumefika Shinyanga!” nilifumbua macho. Jina la Shinyanga lilikuwa na uzito wake katika kumbukumbu zangu. Hata hivyo, nilimwambia taratibu “Siendi Shinyanga. Nakwenda zangu Tabora.”
“Tabora! Kuna nini Tabora?”
Sikumwelewa, “Kuna nini Tabora?” nikamjibu kwa swali jingine. “Kwani Shinyanga kuna nini?”
Kumbe mzee alikuwa na hamu ya maongezi. Alianza kwa kutabasamu. Baadaye aliporomosha sifa za Shinyanga. Kuna kila kitu ambacho binadamu anahitaji. Ardhi bora yenye rutuba tele. Misitu imejaa wanyama kila aina. Ng’ombe wa hapa wamenenepa na wanatoa maziwa mengi kuliko popote pale. Hata Wazungu wengi siku hizi wanatembelea milima yetu mara kwa mara. Kuna fununu kuwa huko ardhini kuna mali nyingi ambazo huko kwao ni utajiri mkubwa.”
Nilitabasamu lakini sikumjibu. Sikuwa na jibu la haraka.
“Enhe na Tabora?” alihoji. “Tabora nini?” nilimuuliza. “Kuna nini Tabora?”
Niliamua kumnyamazisha kwa kumpa kile ambacho nilikipata vitabuni, ambacho nina hakika kuwa alikuwa hakijui. “Tukianza na reli hii tunayoitumia sasa. Roho yake iko Tabora.”
“Kwa vipi?” alihoji akicheka.
“Tabora ni kituo pekee muhimu sana. Pale Tabora ndipo ambapo reli hii inajigawa, moja ikienda Kigoma, ambako inafika hadi ziwa Tanganyika linalotuunganisha na nchi za Kongo, Burundi na Zambia. Pia, kuna reli inayokwenda hadi Mpanda, kusini mwa nchi yetu.”
Wakati akitafakari hilo nilimpa la pili. “Unaijua eropleni?” nilimuuliza.
“Ndege Ulaya!” alisema akicheka. “Sio naijua, nimeipanda mara nyingi.”
“Kutoka wapi kwenda wapi?” nilimuuliza kwa mshangao. “Burma,” alinijibu. “Kwenye vita kuu ya kwanza nilikuwa mmoja wa wapiganaji tuliorushwa kwa ndege kwenda kusaidia
wenzetu waliozingirwa na maadui,” alisita kidogo kabla ya kuniuliza, “Ndege ina uhusiano gani na Tabora?”
“Tarehe 22 Julai mwaka 1920 ndege ya kwanza kutua nchini Tanganyika ilitua katika uwanja wa ndege Tabora. Ndege hiyo ndogo ya Mwingereza iliruka toka Nairobi Kenya hadi hapa na kuweka historia ya pekee kwa nchi ya Tabora.
Mzee alicheka. “Hilo tu?” aliniuliza.
“Yako mengi, “ nilimjibu. “Yule kiboko wa Waarabu, Mtemi Milambo, aliishi katika ngome yake Iselemagazi iliyokuwa Tabora. Yule Mwingereza Davidi Livingstone aliyekataa kurudishwa kwao na akafia Zambia alipata kuishi Tabora kwa muda, kabla hajahamisha makazi yake Ujiji, Kigoma. Tabora ulikuwa mmoja kati ya miji michache nchini iliyokuwa na watu wengi, toka miaka ya 1700, mji mdogo huo?”
Mzee aliyatafakari maneno yangu. “kichwa chako kinafanya kazi vizuri sana, mjukuu wangu. Naweza kutabiri unakwenda Tabora kufanya nini.”
“Naenda kufanya nini?” nilimjaribu. “Kusoma,” alinijibu. “Kweli au uongo?” “Kweli tupu.”
Mzee akacheka kabla hajaongeza, “Naweza hata kukuambia jina la shule unayokwenda.”
“Shule gani?”
“Unakwenda Tabora School. Shule ya misheni inayopokea watoto wa machifu. Kweli au uongo?”
“Ni kweli,” nilimjibu kwa mashangao. “Umejuaje mzee?” “Uzee dawa. Uzee ni kuona mengi ni kuona mbali. Jinsi ulivyovaa, jinsi ulivyotulia, jinsi unavyoongea, ni wazi kuwa wewe ni mtoto wa Chifu. Na nina imani kuwa utafika mbali
katika safari yako ya maisha.”
Nilitamani kucheka, nilitamani kulia. Sikujua nifanye lipi katika hayo. Kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu nikamkumbuka babu yangu, mzee Kionambali.
Mtoto wa Chifu!
* * *
Tulifika Tabora siku mbili baadaye.
Stesheni ya Tabora ni sehemu moja yenye kila aina ya pilikapilika. Ilikuwa na watu wengi wenye purukushani hii na ile, huyu akihangaika kupanda behewa, huyu akishuka, yule akibadili behewa kuhamia lile, huyu akipiga kelele kuuza asali na bidhaa nyingine na kadhalika na kadhalika. Lakini purukushani kubwa zaidi ilikuwa ya magarimoshi yenyewe. Vichwa vilikuwa vingi mno, vikienda hapa au pale, kuhamia reli hii au ile huku vikicheua moshi na honi za mara kwa mara, hali iliyofanya pawe mahala ambapo mtu asingependa kukaa kwa muda mrefu.
Nilishuka, nikachukua mzigo wangu na kutoka nje ya stesheni. Huko nje kitu cha kwanza kilichovuta macho yangu ni wingi wa maembe. Barabara nzima toka stesheni hadi mjini zilizingirwa na miembe mikubwa, kila upande kwa namna iliyofanya iwe na kivuli murua cha kusisimua. Nilipiga hatua moja kwenda nyingine kuifuata barabara hiyo ya aina yake. Kila hatua ilinifanya nione kuwa wingi huo wa miembe haukuwa wa kando ya barabara pekee. Mapori yote ya mji yalitawaliwa na miembe mingi, mikuwa, ambayo baadhi ilikuwa na maembe yaliyoiva, ambayo yalionyesha kuwa watoto wa mji huo walishachoka kuyala.
Mji wa Tabora ulikuwa mdogomdogo, wenye nyumba za kawaida, ambazo hazikutofautiana sana na zile za Mwanza. Tofauti pekee kubwa niliyoiona ni mavazi na lafudhi. Kimavazi
nilishangaa kuona watu wengi wakiwa wamevaa mavazi yenye asili ya Kiarabu, kanzu nyeupe na kiko mdomoni kwa wanaume na baibui jeusi lililofunika moja ya kumi ya mwili isipokuwa sehemu ndogo ya uso kwa wanawake. Katika mazungumzo yao nilibaini pia kuwa lafudhi ya wengi wao ilikuwa ya Pwani zaidi. Japo walizungumza kwa namna iliyofanya nihisi ama wanaibembeleza lugha ama inateleza kwenye ndimi zao.
‘Karibu Tabora mwanangu!’ nilijikaribisha.
Nikauliza njia ya kwenda shule ya Tabora School. Nikaelekezwa. Nikaifuata njia hiyo taratibu, mzigo mkononi, mluzi mdomoni, ndoto za mafanikio zikiwa tele moyoni.
Nilipokelewa na mlinzi nje ya geti la kuingilia shuleni. Nikajitambulisha kwake. Alinifungulia geti na kunielekeza iliko ofisi ya mkuu wa shule. Nilikwenda kwa mwendo wa kujiamini, huku nikiwa tayari nimetoa barua yangu ya utambulisho toka kwa ‘baba yangu,’
Chifu Masanja mwana Kasanga. Wanafunzi wenzangu tayari walikuwa madarasani. Niliweza kuwasikia baadhi ya walimu wakifoka kwa sauti kubwa katika jitihada za kujaribu kuingiza kitu fulani katika vichwa vigumu vya wanafunzi.
Karani wa mkuu wa shule alinipokea, akaipokea barua yangu na kuiingiza chumbani kwa bosi wake. Muda mfupi baadaye niliitwa katika ofisi hiyo.
Mkuu wa shule alikuwa Mzungu. Mtu mnene miraba minne, ambaye angefaa zaidi kuwa mwalimu wa ngumi badala ya taaluma. Nilimkuta kasimama nyuma ya meza yake, barua yangu ikiwa mkononi mwake. Alinikazia macho makali kwa dakika moja au mbili kabla hajatamka neno moja tu “Keti.” Nikaketi kwenye kimoja wapo cha viti viwili vilivyomuelekea mwalimu mkuu, miguu yangu ikianza kupoteza nguvu, mikono
ikianza kutetemeka kwa sababu ambayo sikuifahamu. “Barua yako hii?” alinihoji baadaye.
“Ndiyo.” “Umeipata wapi?”
“Kwa nini? Nimepewa na Chifu… baba… nikuletee.” “Chifu nani?”
“Masanja mwana Kasanga.”
Mkuu huyo wa shule alinitazama kabla hajaongeza swali jingine, “Unaitwa nani?”
Nusura nitaje jina langu halisi. “Cheyo,” nikatamka.
Nilimwona mkuu wa shule akizidi kushangaa. Mara akawa kama kakumbuka jambo. Akatoka na kumnong’oneza jambo karani wake. Kisha akarudi na kuketi. Muda mfupi baadaye mlango uligongwa, mwanafunzi mmoja akaingia na kuelekezwa kuketi kiti cha pili kilichokuwa wazi.
Mkuu wa shule akimkazia macho kama alivyofanya kwangu kabla ya kumuuliza, “Ulisema wewe ni nani, unatoka wapi na baba yako ni nani?”
“Naitwa Cheyo. Kwetu Mwanza. Mimi ni mtoto wa Chifu Masanja mwana Kasanga.”
Miguu yangu iliishiwa nguvu. Nilitamani ardhi ipasuke, inimeze yaishe. Ardhi haikufanya hivyo. Nikahisi nimeanza kutetemeka mwili mzima, jasho jembaba likinitoka.
Mkuu wa shule alikuwa akinitazama kwa makini. “Nani anasema uongo, nani anasema ukweli kati
yenu?” aliniuliza. “Juzi tu,” aliongeza. “Alikuja huyu kijana, akatuambia kwamba anaitwa Cheyo na ni mtoto wa chifu Masanja. Kwa maelezo yake baba yake hataki aje shule, anataka akae nyumbani kusubiri kurithi Uchifu wake atakapokufa. Kwamba amekuja hapa shuleni kwa kutoroka baada ya
jitihada za kumsihi baba yake kumruhusu kushindikana. Na kwa jina na nafasi yake ilikuwa wazi bado tumempokea na kumruhusu kuendelea na masomo. Leo umekuja wewe. Unadai wewe ni Cheyo mtoto wa Chifu Masanja na una barua yake ya kuomba upokelewe hapa. Nataka kujua nani mkweli nani mwongo kati yenu,” aliniuliza akitutazama kwa zamu. Cheyo naye alishangaa. Akageuka kunitazama. Nilijitahidi kuinua uso wangu nimtazame pia, ilikuwa kazi ngumu kuliko zote nilizopata kufanya. Hicho kidogo nilichobahatika kuona katika uso wake kilionyesha wazi kuwa si kwamba hatufahamiani tu, bali pia tulikuwa hatufanani kwa namna yoyote ile. Pale ambapo mimi nilikuwa mng’avu yeye alikuwa mweusi tii, pale nilipokuwa mrefu yeye alikuwa mfupi na mwenye kiribatumbo. “Mnafahamina?” mkuu wa shule aliuliza baada ya
kutupa dakika za kutumbuliana macho.
Wote tulitikisa vichwa kukataa.
Mkuu wa shule akacheka, “Iweje watoto wa mtu mmoja, tena waotumia jina moja wawe hawafahamiani?”
Hatukumjibu.
Haikumchukua mkuu wa shule muda mrefu kubaini ukweli wa mambo hayo. Kutokana na udadisi wa Chifu Masanja juu ya kumpeleka mwanae shule, bila shaka kwa muda mrefu sasa, ndipo akabuni hila ya kuteua mtu mwingine ili aache kusumbuliwa, jambo ambalo limetibuka baada ya mwanawe kutoroka nyumbani na kuja shuleni bila ridhaa wala khiari yake.
Mkuu huyo alinikazia macho kama anayesubiri uthibitisho wa kile kinachopita katika fikra zake bila kutamka. Nilitamani asome jibu la ‘ndiyo’ katika nafsi yangu ili yaishe, niondokane na aibu hiyo. Nadhani alisoma hilo katika macho
yangu, kwani nilimsikia akisema taratibu, “Sipendi kuchezewa. Sipendi kudanganywa. Natoa dakika kumi tu, yule ambaye anafahamu kati yenu kuwa si mtoto halali wa Chifu masanja aondoke mbele yangu na ndani ya eneo la shule yangu. Vinginevyo, nitamchukulia hatua kali za kisheria.”
Sikungojea dakika hizo kumi. Moja tu ilinitosha. Niliinuka, nikachukua begi langu na kutoka taratibu. Nyuma yangu nilisikia kicheko, kicheko ambacho kiliashiria mwisho wa ndoto yangu ya kupata elimu zaidi ya ile ndogo niliyokuwa nayo.
* * *
Niliduwaa kwa muda nje ya eneo la shule. Nilihisi akili yangu ikiwa imedumaa kiasi kwa kuwa mvivu wa kufikiri, hali ambayo ilitokana na uchovu wa ubongo wangu kwa ajili ya tukio hilo zito. Nikatafuta kivuli na kukaa.
Kelele za wanafunzi ambao walikuwa wakitoka, ndizo zilizonizindua hapo chini ya mwembe nilipoketi. Nikainuka nikachukua begi langu na kuitumia miguu yangu kuniondoa hapo. Sikujua naelekea wapi. Lakini sikushangaa pale miguu yangu iliponifikisha stesheni ya treni, mbele ya dirisha la mkata tiketi.
“Nipe tiketi,” nilimwamuru. “Ngapi?”
“Moja.”
“Ya kwenda wapi?”
Niende wapi? Nilijiuliza. Sikuhitaji kujiuliza sana, “Tiketi yoyote ile. Kigoma, Dar es Salaam au Mpanda,” nilimjibu.
Mkata tiketi huyo alinitazama kwa macho ya mshangao wa muda, akinichungulia toka katika kijidirisha chake.
“Unaumwa?” baadaye alinihoji.
Sikutarajia swali hilo, “Kuumwa! Kuumwa nini?” “Chochote kile. Kama akili hivi?”
Ikawa zamu yangu kumshangaa, “Kwa nini uniambie hivyo?” nikafoka.
“Mtu yeyote asiyejua anakokwenda ama ni mngonjwa wa akili, ama ameiba anataka kukimbia. Wewe uko katika kundi gani katika hilo?”
Lilikuwa swali la kifedhuli kuliko yote. Lakini nadhani alikuwa akinitendea haki. Mwenyewe pia nilianza kujishuku. Ninakwenda wapi? Ninakimbia nini? Nimechanganyikiwa kwa kupoteza nafasi yangu nyingine ya kupata elimu? Lakini mara ngapi nimesikia kuwa kukosa elimu ya darasa siyo mwisho wa elimu duniani? Wangapi duniani wamefanya maajabu na kuingia katika vitabu vya kihistoria kwa kiwango cha elimu kama yangu au ndogo zaidi.
Wazo hilo lilinifanya niangue kicheko. Nilicheka kwa muda wa dakika mbili nzima mpaka nikapaliwa. Nikaanza kukohoa.
Kicheko changu kilifanya mkata tiketi huyo aamini hisia zake, kuwa naumwa. Na siumwi kitu kingine zaidi ya akili. Nilimwona akichukua simu na kuzungusha namba kadhaa. Alizungumza kwa sauti ya kunong’ona huku akiwa amenikazia macho ya tahadhari. Baada ya hapo alifunga dirisha lake.
Huku nikicheka niliinua begi langu na kuanza kuondoka eneo hilo. Lakini sikuweza kupiga zaidi ya hatua kumi kabla sijajikuta nikivamiwa na watu wawili waliovaa sare za polisi, shati na kaptula za kaki, kofia zilizovaliwa upande, soksi na viatu vyeusi. Mkononi kila mmoja alikuwa na rungu.
“Polisi! Tulia kama unanywolewa!” mmoja aliniamuru.
Nikiwa nimeshikwa na mkanda wa suruali kwa nyuma, hali iliyofanya nining’inie juu juu na kutembelea ncha za vidole vyangu sikuwa na nguvu zozote za kujitetea. Niliburuzwa hadi katika chumba chao kidogo ambako nilisukumwa na kufungiwa kwa nje bila kuulizwa swali lolote.
“Nimefanya nini jamani?” niliwapigia kelele. Hakuna aliyenijibu.
SURA YA SABA
Lyampa Mfipa
ilipohoojiwa na polisi kwa dakika kumi tu kabla hawajathibitisha kuwa nilikuwa na akili zangu timamu. Lakini ilikuwa baada ya kufungiwa
chumbani humo kwa siku nzima.
Alikuja mmoja kati ya wale walionikamata, akiwa amefuatana na mtu mwingine mfupi, mnene, ambaye alinukia dawa za hospitali. Sikuhitaji kuambiwa kuwa mtu huyo alikuwa daktari, pengine wa maradhi ya akili, toka hospitali ya Kitete. Walipoingia ndani yule daktari aliketi mbele yangu na kunikazia macho. Mie pia nikamkazia macho. Hata hivyo, nusu dakika baadaye niliyakwepa macho yake kwa kuinamisha uso wangu.
Akiwa bado amenikazia macho daktari yule alitabasamu, mimi sikutabasamu. Aliangua kicheko. Mimi sikufanya hivyo. Kisha alitikisa kichwa chake kwa kujiyumbisha huku na kule kama aliyekusudia nifuate mfano wake. Sikufanya hivyo. Nikamwona kama mtu aliyepatwa na mshangao.
“jina lako?”
Nikamjibu kwa kutaja lile nililopewa na chifu Masanja, “Cheyo.”
“Kabila lako?”
“Msukuma. Ingawa sikijui vizuri.” “Kwa nini?”
“Nilizaliwa na kukulia Buha. Nafahamu Kiha kuliko kisukuma.”
“Mwakeye!” Akanijibu.
“Saa hizi sio mwakeye, ni mwidiwe,” nikamsahihisha.
Akatabasamu. Nadhani akiba yake ya Kiha ilikuwa inaishia pale, kwani alirudi kwenye Kiswahili. “Enhe, una tatizo gani?” alihoji.
“Nadhani hawa walionifungia hapa ndio wenye matatizo. Wamenikamata bila sababu na kunifungia humu bila maelezo,” nilisema kwa sauti yenye hasira.
Daktari huyo alinitazama kwa makini, toka kichwani hadi miguuni. Mavazi yangu yalikuwa safi, viatu vyangu viking’ara kwa kiwi. Hata mwili wangu pia ulikuwa safi, ukimeremeta kwa afya na mafuta niliyopaka kabla ya kwenda mbele ya mkuu wa shule ile iliyonikataa. Begi langu pia lilikuwa safi, jipya, lililofura mali ambazo mgonjwa wa akili hawezi kuwa nazo. Daktari huyo aliacha kunitazama mie akawa akimtazama yule askari. Nilihisi kuwa alikuwa katika wakati mgumu wa kuamua nani mgonjwa wa akili kati yangu na hao walionikamata. “Wamekuhangaisha bure,” alisema baadaye. “Ilikuwa tukukamate, upelekwe Dodoma kwenye hospitali ya wenye maradhi ya akili. Unaonekana huna tatizo loolote.”
Askari huyo hakuweza kunitazama usoni kwa aibu.
Mara niliporuhusiwa, nilichukua begi langu na kurudi katika dirisha lilelile la mkata tiketi. Nilimkuta karani yuleyule bado akiwa kazini. “Nataka tiketi,” nilimwamuru.
Aliponitazama alishtuka kama aliyeguswa na waya wa umeme. “Ya kwenda wapi?” alinihoji kwa sauti ambayo
haikuwa imara kama awali.
“Popote,” nilimjibu kama awali.
Alitazama huko na huko kama anayetaka kuomba msaada. Kisha akasema, “Leo kuna treni mbili. Moja inakwenda Kigoma, itapita usiku. Nyingine inakwenda Mpanda, itaondoka hapa baada ya nusu saa.”
Nipe ya Mpanda.” Nilisema bila ya kufikiri sana.
“Shilingi tano, njia moja.”
“Nipe,” nilimjibu nikimlipa. Nikapokea tiketi na chenji zangu na kuzitia mfukoni. Nikaenda mgahawa mmoja uliokuwa karibu ambapo nilinunua wali kwa maharage, nikayashushia kwa chai ya rangi. King’ora cha abiria wa treni ya Mpanda kilipolia nilikuwa mmoja wa abiria wa kwanza kuiparamia.
* * *
Sikuhitaji kufikiri sana kabla ya kukata tiketi hiyo kwa sababu nyingi. Kwanza, nilikuwa na hisia kuwa Tabora haukuwa mji wangu wa bahati. Kuumbuliwa na mkuu wa shule kwa kiwango kile kulinitia doa na dosari kubwa iliyofanya nijisikie aibu isiyo na kifani. Mimi sio yatima. Nina baba na mama. Nina babu mwerevu kuliko mamia ya mababu ninaowajua. Kiu ya elimu haikuwa sababu nzuri ya kunifanya nikubali wazo la kipuuzi la kufanywa mtoto wa kambo wa Chifu Masanja.
Ni wazo hilo lililofanya nitupilie mbali wazo la kurejea Usukumani. Ningemwambia nini Chifu?
‘Nimebainika. Mtoto wako halisi yuko shuleni, kwa hiyo nitafutie hifadhi mpya!’ Aibu iliyoje. Ningemwambia nini mkewe na watumishi wa himaya yake ambao bila shaka wengi waliijua kinachoendelea?
Ndipo nilipowaza juu ya kurudi nyumbani. Nipande garimoshi hadi Kigoma, huko nitafute njia ya kufika Kasulu. Huenda tayari kulikuwa na malori ambayo yalibeba watu na mizigo kama sehemu nyingine za nchi.
Hata hivyo, hilo pia sikulitekeleza kwa sababu tele. Moja ilikuwa aibu. Mwanamume akitoka ametoka. Akirudi ana kitu cha kuonyesha kijijini. Ama vyeti vya kuhitimu masomo yako ama fedha au mtaji au kujenga nyumba bora zaidi. Mimi ningerudi na aibu tupu. Sikuwa tayari kufanya hivyo.
Sababu nyingine iliyonizuia kwenda nyumbani ni babu yangu. Ni kweli alinipenda sana na angefurahi sana kuniona. Lakini sikupenda kujitokeza mbele yake kichwa kitupu, mikono mitupu. Alitegemea nirudi na elimu. Alitegemea nirudi na mali. Kamwe asingefurahi kuona nikirudi mnyonge, kama kinda la ndege, linalotegemea mama akutafutie, akutafunie, umeze.
Lakini kuna sababu nyingine, kubwa zaidi, iliyonifanya nisijisikie kumtazama babu machoni. Hirizi yake. Hirizi hiyo ya familia, ambayo kwa mujibu wa maelekezo yake ilivaliwa na babu yake, baba yake na kisha yeye mwenyewe. Hirizi ambayo ilimpeleka Ughaibuni na kumrejeshha salama. Naam, hirizi ambayo aliivua na kunivisha mimi, badala ya baba, ili nipate kile ambacho aliamini kingeinua ukoo na familia yetu.
Hirizi ambayo niliipoteza kwa uzembe!
Haikuwa kweli kuwa chanzo cha migogoro yangu hii mipya, ikiwa pamoja na kukataliwa nafasi ya kusoma, kwa namna moja au nyingine ilihusiana na kupotea kwa hirizi ile? Mara kwa mara niliwaza.
* * *
Gari moshi liendalo mpanda hulazimika kueleka magharibi kwa kilometa kadhaa kabla ya kuchepuka kuelekea kusini. Kwangu mimi ilikuwa sawa na kuelekea nyumbani, Kigoma. Tuliiacha stesheni ya Tabora, tukatafuna reli hadi Usoke. Toka hapo tuliingia Urambo. Tuliacha Urambo na kufika Kaliua ambako tulianza safari ya kusini.
Kama ilivyokuwa safari ya kutoka Mwanza safari hii pia ilikuwa sawa na kusafiri katikati ya bustani ya Eden. Kila upande tulizungukwa na ama misitu minene iliyoashiria kila aina ya hazina, ama mapori ya kutisha yaliyoonya juu ya wingi wa mbolea katika ardhi yake.
Mara kwa mara tulipishana na wanyama ainaaina waliokuwa kando wakitushangaa, pamoja na ndege ainaaina walioruka hapa na pale juu ya miti, wakifaidi asali ya maua na wadudu wadogowadogo. Baadhi ya maeneo kulikuwa na mabwawa makubwa yaliyoshawishi kilimo cha mpunga au mito ambayo ilinikumbusha samaki wa ziwa Nyanza.
Toka Kaliua tuliingia Mfulu, baadaye Ugalla na hatimaye tukawasili Mpanda. Huo ulikuwa mwisho wa reli hii, lakini haikuwa mwisho wa safari yangu.
Pamoja na shahuku yangu kubwa ya kuondoka Tabora, ndoto yangu ya kuja Mpanda ilikuwa na malengo yake. Zilikuwepo fununu za hapa na pale kuwa maeneo mbalimbali ya huku yalikuwa dhahabu. Uchimbaji wa dhahabu hiyo sikuona kama kwa namna yoyote ile ungenishinda. Kuchimba udongo hadi ufikie mchanga maalumu kuchekecha mchanga huo hadi uone chembechembe za dhabahu na kuiokoteza, vipi kungenishinda?
Hilo lilikuwa wazo la kwanza. Wazo la pili, ambalo nilikuwa na hakika nalo zaidi ni uvuvi. Toka Mpanda hadi
Ikola au Kerema ambayo ni miji ya kandokando mwa ziwa Tanganyika haikuwa safari ndefu. Ningeweza kufika huko hata kwa miguu. Nilipanga, kama kazi ya kuchimba dhahabu ingeshindikana ningeelekea huko na kujiunga na uvuvi. Ndiyo, nasikia ziwa Tanganyika lina kina kirefu kuliko maziwa yote duniani. Kama kuna ukweli kwa hilo bila shaka samaki wake pia ni wengi zaidi na watamu zaidi. Ningekuwa mmoja kati ya walaji wake. Wala nisingeishia kula tu; samaki hao wangenipatia fedha za mtaji ili nirudipo kwetu nirudi kishujaa. Hivyo ndiyo ilikuwa ndoto yangu. Kwa bahati, nzuri au mbaya, haikwenda kama nilivyotarajia. Hali hiyo ilitokana na kukutana kwangu ana kwa ana na mtu ambaye sikutarajia kamwe kumwona tena katika maisha yangu, mtu ambaye sikupata hata kulifahamu jina lake. Alikuwa mmoja kati ya wale Wamanyema wawili waliofuatana na Mwarabu katika safari yetu ya miguu toka Buha hadi kwa Wahaya, miaka zaidi
ya mitano iliyopita.
Ni yeye aliyeniona kwanza, “We mtoto wewe! Kama nakufahamu vile?”
Nikageuka kumtazama. Mara moja nilimkumbuka, “Mmanyema! Unafanya nini huku?” niliuliza kwa mshangao.
“Wewe je? Umefikaje huku?” Sikujua nimweleze nini. “Babu yako hajambo?”
Sikuwa na jibu. Nikainamisha uso kwa aibu.
Nadhani Mmanyema alisoma kitu fulani katika uso wangu, kwani alinitazama kwa muda kabla hajanikaribisha chai kwa mihogo ambayo alikuwa akiila. Nikapokea kikombe cha chai ya maziwa na kipande cha muhogo. Njaa iliyoanza kuninyemelea ikakimbia mara moja.
Wakati tukinywa chai hiyo yapata saa kumi na moja za alfajiri. Gari moshi lilikuwa limechelewa sana njiani kutokana na mafuriko katika maeneo mbalimbali. Ilibidi gari hilo liendeshwe taratibu sana. Tulikuwa tumeketi nje ya stesheni, kwenye benchi la chuma ambalo bila shaka lilijengwa kwa ajili ya wasafiri.
Nilishangaa pale Mmanyema aliponiambia kuwa tulisafiri katika behewa moja toka Tabora hadi hapo. Kuwa aliniona lakini hakuwa na hakika na macho yake hadi aliposikia sauti yangu na kuniona nikimkumbuka.
Alikuwa mzungumzaji sana mzee huyu. Alinieleza jinsi alivyoacha kazi ya kumtumikia yule Mwarabu baada ya kufilisika. “Yaelekea Mwarabu yule hakuwa na ujuzi wowote zaidi ya biashara ya watumwa. Kila alichojaribu kushika kiliteleza. Hata mishahara yetu alishindwa kulipa. Tukaachana naye na kuanza shughuli zetu binafsi,” Alinieleza kwamba yeye sasa alikuwa akifanya biashara ya kununua dagaa toka kwa wavuvi wadogowadogo wa kandokando ya ziwa Tanganyika na kuwauza kwa walanguzi wakubwa ambao waliwapeleka Tabora, Dodoma na Dar es Salaam kwa matumizi ya binadamu na mifugo. Kwamba sasa hivi alikuwa na mtaji wa kutosha ambao utamwezesha kupeleka mwenyewe dagaa hao hadi Dar es Salaam ili apate faida kubwa zaidi. “Toka huku nitanunua nyavu na vifaa vingine vya uvuvi na kuwauzia watu Kigoma na Kongo. Nikijaliwa miaka miwili baadaye nitakuwa mmoja wa matajiri wakubwa wa nchi hii,” alisema kwa kujipamba.
“Sasa unakwenda wapi? Mbona huku hakuna dagaa?” nilimuuliza.
“Nakwenda Sumbawanga.” “Kufanya nini?”
Alinitazama na kucheka kidogo kabla hajasema, “Unaonekana wewe ni mtoto mdogo sana kuliko umbile lako. Hujui watu huenda Sumbawanga kufanya nini?”
Mie: Sijui
Yeye: Pole sana. Kwa hiyo, hata maana ya jina Sumba
- Wanga hujui?
Mie : Sijui
Alitikisa kichwa kwa namna ya kunisikitikia. Kisha alisema, “Sumba-Wanga maana yake ‘Tupa Uchawi.’ Kwa maana ya kuwa mji huo ni wa watu wazito, watu waliokomaa. Hivyo, ukiingia huko na vijiuchawiuchawi vyako utaumbuka. Ni huko ambako watu wazima huenda kugangwa, ili wasichezewechezewe ovyo kishirikina. Huwezi kufanya biashara kama hujafundwa ukafundika.”
Ilikuwa habari mpya kwangu. Niliipokea kwa mshangao na kutoamini. “Lakini Biblia inasema…” nilijaribu kumwambia. “Achana na Biblia. Mimi ni Mwislam. Tunatumia Msahafu wa Mwenyzi Mungu. Ulioshushwa toka peponi kwa
mkono wa mtume Mohamed S.A.W.”
“Lakini hata Uislam unakataza ushirikina.”
“Kujikinga sio ushirikina. Hayo ni mambo ya wakoloni tu, walipoamua kututawala miili na mioyo yetu. Walitarajia kuwa mila na tamaduni zetu kupotea huku wao wakihifadhi za kwao. Kila binadamu ana nyota na anahitaji kuisafisha mara kwa mara. Kila binadamu ana wahenga ambao anahitaji kuwaenzi kwa sadaka na tambiko. Asiyefanya hivyo kamwe hawezi kufanikiwa.”
Lilikuwa somo jipya kwangu, somo ambalo sikuwa na ujuzi nalo. Nikaamua kunyamaza. Mmanyema alichukulia ukimya wangu kama dalili ya kumwelewa.
“Haya na wewe nieleze ukweli wa kile kilichokufanya ufike huku. Kama nakumbuka vizuri babu yako alikupeleka Uhayani ukasome. Nadhani ulipata shule kwani nilipoonana naye mwaka mmoja baadaye alinidokeza kuwa ulishaingia shuleni,” alisema.
Nusura niruke kwa shauku, “Ulionana na babu?” “Ndiyo!”
“Wapi?”
“Nyumbani kwenu. Kasulu. Tulilala pale siku mbili na alituchinjia beberu mkubwa sana. Babu yako ni mkarimu sana.”
Bila kutegemea nilijikuta nikitokwa na machozi. Babu yuko hai! Babu alirudi salama! Sikupata kupokea habari njema kama hiyo kwa miaka nenda rudi.
Sikuiona haja yoyote ya kumficha chochote Mmanyema huyu. Nilimwona kama baba yangu. Kama malaika, kwa kuweza kunipa walao fununu tu ya habari za nyumbani. Nikamweleza kila kilichonisibu, toka mwanzo wa mikasa yangu hadi nilipofikia.
Alinisikiliza kwa makini sana, mara kwa mara akitikisa kichwa kwa masikitiko. Mwisho wa maelezo yangu alinishika mkono na kuninong’oneza, “Pole sana mtani. Usijali. Hujafika mwisho wa safari yako kimaisha. Nitakusaidia.”
Nilimwamini. Sikujua kwa nini nilimwamini haraka kiasi hicho.
* * *
Safari ya Ikola au Karema ilikufa. Ndoto ya kuchimba dhahabu nayo ilikufa. Safari ya Sumbawanga ikazaliwa.
Tulikaa kwa siku mbili kabla ya kupata gari lililotufikisha
Sitalike. Hapo tulipumzika tena kwa siku tatu tukifaidi kula nyama pori ambazo zilikuwa tele toka katika mbuga za Katavi. Tukaondoka hadi Kisi, Chala, Nkundi na hatimaye Sumbawanga.
Wakati huo sumbawanga kilikuwa kimji kidogo tu, chenye wakazi wachache lakini kikiwa na mambo makubwa. Mandhari ya mji, ambayo yalipambwa na mlima Malonje wenye urefu wa mita 2418 toka usawa wa bahari, mito na misitu tele yalifanya nitamani kuishi hapo kwa muda mrefu zaidi.
Lakini Mmanyema ambaye baadaye alinitajia jina lake kuwa ni Baraka Khalfan alikuwa na ratiba tofauti na yangu. Alikuwa na majina ya vijiji mbalimbali na waganga mbalimbali ambao alipanga kuwaona. “Huku ni Ufipa, mdogo wangu. Lyampa Iya Mfipa, umepata kulisikia?”
Sikupata.
“Lyampa Iya Mfipa kwa tafsiri ya kawaida ni mlima mdogo tu, ambao unatambaa hadi kando ya ziwa Tanganyika na kupita chini hadi Kongo, katika eneo la Moba, nchi ya Watabwa. Lakini kwa wajuzi wa mambo Lyampa Iya Mfipa linabeba uzito wa pekee. Ni jiwe la tambiko ambalo ukikaangwa juu yake hakuna mtu yeyote atakayekuchoma. Na hayo hafanyiki mjini, isipokuwa vijijini kwa wazee, waliofundwa na babu zao,” alinieleza.
“Watu wengi wenye nafasi zao wamepitia huku. Watu toka sehemu mbalimbali za dunia huja huku kufanyiwa mambo. Watabwa wa Kongo nao huja huku, ingawa ni kweli pia kuwa wazee wa huku katika kuimarisha uwezo wao huvuka ziwa kwenda Kongo,” aliongeza.
Hivyo, zilianza safari za hapa na pale. Mara Chapota, mara Kasanga, mara Wampembe na kwingineko. Safari hizo
zilitufikisha Pwani ya ziwa Tanganyika na kuniwezesha kuona milima ya Kongo mbele yetu na ile ya Zambia kushoto kwetu. Ziwa hilo lilinikumbusha hamu ya kurudi nyumbani, kwani kwa kuambaa nalo tu, nikielekea kulia ningeweza kufika Kigoma. Kwa bahati mbaya, sikuwa tayari kwa safari hiyo.
Mmanyema alikuwa na pilikapilika nyingi. Mara kwa mara aliniacha peke yangu na kwenda hapa na pale na aliporudi alikuwa kachanjwa chale ama za kwenye paji la uso ama katika viwiko vya mikono na miguu. Wakati mwingine alinituma kumtafutia vifaa mbalimbali kama mayai viza, mizoga ya paka au njiwa weusi.
Siku moja aliondoka alfajiri na hakurudi. Nililala peke yangu katika chumba tulichofikia cha mwenyeji wetu mmoja. Kwa kuwa nilikuwa peke yangu nililala mapema sana, mara baada ya chakula cha usiku. Nilipofumbua macho tena ilikuwa alfajiri. Baridi kali iliyotokana na upepo ziwani nadhani ndiyo iliyoniamsha. Nilipotazama huko na huko sikuweza kuyaamini macho yangu. Nililala ndani, juu ya kitanda, lakini niliamka nikiwa nje, tena juu ya mbuyu mkubwa ulikuwa mbele ya nyumba hiyo. Isitoshe nilikuwa mtupu, bila nguo yoyote mwilini! Nilishuka harakaharaka na kuingia ndani. Nguzo zangu zilikuwa zimetupwa ovyoovyo chumbani humo. Nikaziokota na kuvaa harakaharaka. Ni wakati nikivaa nilipobaini kuwa nilikuwa nimechanjwa chale mbili katika paji langu la uso na
kupakwa vitu vyeusi kama masizi ya mkaa.
Nilikosa raha. Niliduwaa katikati ya chumba hicho huku nikitetemeka kwa hasira.
Mara mlango uligongwa na kufunguka kabla sijaitikia. Mwenyeji wetu, mzee Imilio Kahigi aliingia ndani. Alikuwa akicheka huku anatikisa kichwa. “Mtoto, mbona unasafiri
ukiwa mwepesi hivyo?” aliniuliza.
Sikumwelewa, hivyo sikumjibu.
“Uko mtupu mno. Mwepesi kupita kiasi. Kwani hukuaga kwenu?” aliuliza tena.
“Niliaga!” nilimjibu.
Alicheka kabla ya kusema, “Hukuaga. Na kama uliaga wazazi wako ni watoto vilevile. Jana watoto wenzako wameamua kukupima baada ya kuona huelewekiheleweki. Wakakuta ni mwepesi mno. Ndiyo maana wakakuacha pale juu ya mti baada ya kukuchezea usiku kucha.”
Sikujua mzee huyo alitarajia jibu gani kwangu. Hivyo, niliendelea kukaa kimya wima, nikiwa nimemkodolea macho.
“Utafanyaje?” aliniuliza ghafla.
Nilijua nitakachofanya. “Nitaondoka, leo hii hii,” nilimjibu.
Alicheka tena kabla hajasema, “Unadhani utafika
unakokwenda?”
“Nitafika. Kwa nini?”
“Wenzako wamekutia alama. Popote utakapokwenda wajuzi wa mambo watakubaini mara moja na kukugombea kama mpira wa kona, maana una alama, alama ya shari.”
Nilizidi kuduwaa. Nadhani hata mdomo wangu niliusahau ukiwa wazi wakati nikiwa nimemtumbulia macho. “Huyu Mmanyema unamfahamu kwa kiwango gani?”
Aliniuliza ghafla.
“Simfahamu vizuri. Tulikutana naye safarini miaka mingi iliyopita. Tumekutana naye tena majuzi na kufuatana naye. Basi.”
Mzee Kahigi alitikisa kichwa kwa namna ya kunihurumia sana. Kisha aliongeza swali jingine, “Alikuambia anatafuta
nini huku?”
“Waganga.” “Wa?”
“Kujiganga. Anataka kinga.”
Mzee akacheka tena. “Humjui vizuri,” alisema. “Humjui hata kidogo. Huyu bwana anatafuta kizimba, dawa ya mali. Ametakiwa kutoa kichwa cha mtu. Alitakiwa atoe mtoto wake wa kwanza, ageuzwe ndondocha, awekwe chini ya maji kumswagia dagaa. Hana mtoto wake wa kuzaa. Anachofanya sasa ni kukutoa wewe. Utageuzwa akili, utawekwa chini ya maji maisha yako yote, hadi kifo cha kweli kitakapokutokea.”
Sikuyaamini masikio yangu. “Mmanyema!”
“Naam!”
“Mimi!”
“Naam… tena mipango yake inakwenda vizuri sana. Kesho au keshokutwa utakufa, tutakuzika. Lakini wajuzi wa mambo tutaona tunavyozika mgomba huku wewe ukiongozwa kikondoo kupelekwa ziwani.”
Baada ya taarifa yake hiyo ‘njema’ alinikazia macho kabla hajaniuliza tena, “Utafanya nini?”
Bado sikujua alitaka nimjibu nini, “Nitaondoka,” nilimjibu.
“Nimekwishakwambia umetiwa alama. Hutafika mbali.” “Nitaondoka nikafie mbali. Siyo hapa.”
Baada ya kuwaza sana alisema, “Nitakusadia. Utaondoka hapa salama ufike salama kokote uendako. Siwezi kukubali mtu wa kuja afanye ushenzi katika milki yangu. Kaa kama kawaida, kula kama kawaida, usiku ufunge vitu vyako vyote tayari kwa safari.”
Sikujua ilinipasa kumshukuru au la. Kwa ujumla, sikujua kama nilipaswa kumwamini au kutomwamini. Nilichojua ni kwamba maisha yangu yalikuwa katika mashaka makubwa. Unapopigania roho yako, bila kumjua nani adui nani rafiki, sio suala la mzaha.
Nilifanya kama nilivyoelekezwa. Sikumwambia mtu yeyote juu ya masaibu yaliyonipata usiku huo. Nilioga, nilikula na baadaye kutembeatembea kijijni hapo kana kwamba hakuna lolote la ajabu lililonipata.
Mmanyema alirudi mida ya saa nne hivi. Alionekana mtu mwenye furaha na matumaini makubwa. Huku akitabasamu alinivuta chemba na kuninong’oneza, “Mdogo wangu mambo yamekwisha. Kama nilivyokuambia baada ya miaka miwili tutakuwa watu katika watu. Pesa halitakuwa tatizo tena. Wewe, kwa kuwa umesoma kuliko mimi utakuwa mhasibu. Utatunza hesabu ya fedha na mali zetu zote.” Aliongeza kwa kunidokeza kuwa jioni hiyo angesafiri tena. Atakaporudi tutakuwa tayari kurudi Kigoma.
“Unakwenda wapi safari hii?” Nilimuuliza.
“Nakwenda Kipili hadi Mtakuja. Nitajitahidi kurudi keshokutwa. Nikirudi tu yamekwisha,” alinijibu. Kisha alinitazama usoni na kuniuliza “Hapo umefanya nini?”
“Nilijikuna,” nikamjibu.
Nilihisi hakuniamini. Alizikagua chale zile kwa muda mrefu kidogo.
“Sidhani,” alisema. “Nikirudi tutaangalia suala lako vilevile. Isije kuwa washenzi wanakuchezea, maana umekaa mweupemweupe kama kinda la ndege.”
Nilitamani sana kumwamini. Sikubahatika kuipata fursa hiyo.
Mara tu alipoondoka nilifunga vifaa vyangu katika begi langu. Baada ya mlo wa usiku nilijilaza mapema nikisubiri usingizi unichukue ili kesho ifike nione mzee Kahigi atanisaida vipi ili niweze kuondoka nchi hiyo ya Wafipa salama.
Sikujua usingizi ulitokea wapi. Nilihisi ghafla kama naota, mlango ukifunguka na mzee Imilio Kahigi akiingia chumbani humo. Alikuwa mtupu, isipokuwa kwa kipande kidogo cha kaniki alichofunga mbele ya kiuno chake. “Inuka,” aliniamuru. Niliinuka. “Chukua begi lako unifuate,” nilifanya kila alichoniamuru na kumfuata hadi nje ya nyumba.
Hapo kulikuwa na ungo mkubwa wenye vikorokoro mbalimbali ambavyo sikuweza kuvifahamu. “Ingia ukae hapo,” aliniamuru tena. Nikamtii.
Mara alianza kuimba kwa lugha ya Kifipa, maneno ambayo sikuweza kuyaelewa. Akaninyunyizia kitu fulani chenye harufu mbaya kwa usinga wake huku akiendelea kuimba. Ghafla nikaona ungo ukianza kupaa. Ulipaa, ukapaa, ukapaa hadi mawinguni. Naota? Nilijiuliza. Kama ilikuwa ndoto, basi ilikuwa ndoto ya aina yake ambayo ningependa nirudie kuiota mara kwa mara.
SEHEMU YA NANE
Kwa Hadi Mbeya
ilizinduka toka usingizini. Nadhani kilichonizindua ni baridi kali iliyoambatana na upepo wa kipupwe ambao ulinipiga mwili na
kunifanya nijikute nikitetemeka, meno yangu yakigongana. Nilikuwa katika kituo cha mabasi, peke yangu. Jogoo waliokuwa wakiwika huko na huko waliniashiria kuwa ilikuwa alfajiri.
“Niko wapi?” nilijiluliza nikiinuka na kutazama huko na huko. Begi langu lilikuwa miguuni mwangu, kama nilivyolifunga jana. Kwa mbali nilianza kuona mtu mmojammoja wakipita hapa na pale, baadhi yao wakija kituoni kuwahi usafiri. Baadhi ya magari yalianza kuwashwa.
Niliinama na kuliinua begi langu, ambalo nililiinua kwa taabu sana. Vidole vyangu vilikuwa vimekufa ganzi. Hata pale nilipojaribu kutembea miguu yangu ilikuwa kama haipo kwa ajili ya baridi hiyo kali. Nikajikongoja hadi nilipomfikia taniboi mmoja ambaye alikuwa akimimina maji katika injini ya gari lake, tayari kwa safari.
“Samahani, hapa ni wapi?” Nilimuuliza.
“Huwa tunasalimiana kwanza,” alisema akinitazama kwa mshangao.
Sikumjibu. Si kwa ajili ya ujeuri bali kwa kuwa sikujua
alitaka salamu za aina na lugha gani, kwani lafudhi yake ilikuwa tofauti kabisa na ile ya watu wa Sumbawanga. Alipoona kimya aliniuliza kwa mshangao, “Kwani wewe umetoka wapi hata uulize hapa ni wapi?”
“Nimetokea Sumbawanga.” “Umekuja na gari gani?”
Sikuwa na jibu, jambo ambalo lilimshangaza zaidi. “Ulilewa?”
“Hapana.”
“Ulikuwa unaumwa?” “Hapana.”
“Sasa umewezaje kutoka Sumbawanga hadi hapa Mbeya bila kujua unapokwenda?”
Sikuendelea kumsikiliza. Mbeya! Niliwaza kwa mshangao. Niliyakumbuka maongezi yangu na Mzee Imilio Kahigi na ahadi yake ya kunisaidia. Nikakumbuka tukio la usiku, aliponijia katika mavazi ya ajabuajabu na kuniamuru kuketi katika ungo, nikiwa nimepakata begi langu. Nilikumbuka kwa mbali nyimbo zake alizoimba akichezesha usinga wake hata nikaanza kupaa! Mbeya! Nimekuja Mbeya kwa ungo! Sikuamini.
Lakini sikuwa na sababu ya kutoamini. Baridi kali ambayo ilianza kunila mifupa ilikuwa ushahidi tosha kuwa niko katika eneo jingine, lililo juu zaidi ya usawa wa bahari zaidi ya Sumbawanga. Hata mavazi ya watu wengi waliokuwa wakiongezeka mitaani yaliashiria hali ya hewa nyingine kabisa. Makoti au majaketi makubwa, kofia au vitambaa kichwani na viatu vizito miguuni. Majina mengi yaliyokuwa yakitajwatajwa pia yalikuwa mapya masikioni mwangu; Mwakipesile, Mwangonda, Mwamasika, Mwanjelwa na kadhalika.
Nilipapasa mifuko yangu. Pesa nilizopewa na Chifu Masanja bado zilikuwemo. Nikajikongoja hadi nilipopata mgahawa mdogo na kujinunulia chai ya moto sana. Nilikunywa vikombe viwili chapchap na cha tatu taratibu kabla ya kubaini kuwa chai hiyo ilinichubua midomo na ulimi kwa kiwango kikubwa sana.
Toka hotelini hapo nilitafuta nyumba ya wageni ya bei nafuu ambamo nilionyeshwa mapipa ya maji ya moto na kuchota ndoo moja niliyoitumia kuoga. Baada ya hapo nilipanda kitandani na kujilaza, nikiwa nimejifunika mablanketi mazito mawili. Usingizi mzito ulinichukua na kwa muda ukawa umenisahaulisha masaibu yote yaliyonitukia katika muda mfupi wa maisha yangu. Hata hivyo ulikuwa usingizi wa mang’amung’amu kwani niliandamwa na ndoto za kutisha, mara nikiwa juu ya mbuyu, mara nikipaa angani, mara nikiwa nimezingirwa na wachawi wanaopanga kunila nyama na kadhalika.
Nililala mchana kutwa na usiku kucha. Nilipoamka kesho yake jambo la kwanza nililofanya ilikuwa kwenda madukani ambako nilinunua mavazi yanayoendana na hali ya hewa ya Mbeya; koti, sweta zito, kofia na soksi nzito.
Katika pitapita yangu mjini hapo niliingia duka la vitabu ambamo nilinunua ramani ya mji na vitongoji vya Mbeya. Nikaketi mahala na kuisoma. Jambo la kwanza lililovuta macho yangu ni urefu wa safari ambayo nilisafiri kwa miujiza toka Sumbawanga hadi Mbeya. Kama ningelazimika kusafiri kwa gari ningetumia zaidi ya siku mbili njiani kwa kupita katika miji na vijiji mbalimbali kama Mpui, Ndalambo, Tunduma, Ihanda, Iwanda na hatimaye Mbalizi.
Jambo jingine lililovuta macho yangu ni kubaini kuwa
mkoa wa Mbeya ulikuwa mpakani mwa Tanganyika na Zambia kwa upande mmoja, nchi ya Malawi kwa upande wa pili. Mji mkubwa zaidi wa mpakani kwa upande wa Zambia ukiwa Tunduma na kwa upande wa Malawi mji mkubwa zaidi ukiwa Kyela na Itundi. Mbeya ilikuwa na sifa nyingine. Ilibahatika kuwa na ziwa kama yale ya Nyanza na Tanganyika, ingawa kwa asilimia ndogo. Bahati hiyo iliwezesha si kuvua samaki tu, bali pamoja na kuwawezesha kuwa na bandari, Itungi, ambayo ilihudumia miji ya Karonga kwa upande wa Zambia na mikao kama Iringa kupitia wilaya ya Ludewa.
Ramani hiyo ilinionyesha kuwa Mbeya haukuwa mji mdogo kama ulivyokuwa ukionekana. Ulikuwa na mengi ya kusisimua kiutamaduni, kiuchumi na kimazingira. Pamoja na ukweli kuwa kabila lililojulikana zaidi la mkoa huo lilikuwa la Wanyakyusa bado kuna makabila mengine tele kama Wandali, Wasafa na Wasangu ambao ni wenyeji asilia. Aidha, kuwepo kwa mkoa huo mpakani kulichangia kufanya uhamiaji wa kutokea nchi za Malawi na Zambia kuwa sehemu ya wakazi.
Sikuhitaji ramani hiyo kusoma ukweli kuwa wakazi wengi walikuwa wakulima. Mazao kama mahindi, mpunga, migomba, viazi na mimea mengine ilikubaliana sana na ardhi na hali hewa ya huko, jambo lililofanya katika pitapita zangu nipishane na wakulima waliobeba mazao ama kwenye baiskeli ama katika mikokoteni wakielekea sokoni.
Lakini Mbeya ilikuwa na kitu kingine cha ziada. Dahabu. Purukushani za kutafuta dhahabu, kwa mujibu wa maelezo toka kwa baadhi ya watu niliobahatika kuzungumza nao, zilianza tangu mwaka 1905 kufuatia fununu za kuwepo kwa madini hayo. Hata hivyo, miaka kumi na mitano baadaye ndipo ilipodhihirika rasmi kuwepo kwa madini hayo katika
mji wa Chunya. Hali hiyo iliyopelekea mji huo mdogo upanuke ghafla na kupokea watu wa aina mbalimbali, wa makabila na mataifa mbalimbali, kila mmoja akijaribu kuutumia mwujiza wa dhahabu kujipatia chochote. Walikuwemo wachimbaji, madalali, wanunuzi, wauzaji wa vifaa vya uchimbaji na vyakula na wengineo.
“Nafikiria kwenda huko kesho,” nilimwambia mmoja kati ya watu niliobahatika kuzungumza nao juu ya suala hilo. Alikuwa mtu wa makamo, ambaye muda mwingi nilimwona kakaa mbele ya hoteli niliyofikia. Sikupata kujua kazi yake ilikuwa ipi.
Mtu huyo alinitazama kwa mshangao, “Nani, wewe?” aliniuliza.
“Ndiyo,” nilimjibu. “Unakwenda kufanya nini?” “Kuchimba.”
Akacheka na kunitazama kwa dharau ya dhahiri. “Inahitaji mtu kichaa sana kwenda kuchimba madini,” alisema.
Ikawa zamu yangu kumshangaa. “Kwa vipi?” nilihoji. “Kwanza hutarudi salama. Na ukirudi utakuwa masikini
kuliko hapo ulipo.” Alinionya.
Sikumwelewa. “Mbona kuna watu huko na wanachimba?”
“Mdogo wangu, hao walioko huko huwa hawarudi. Kazi ile ni kama laana hivi. Unaweza kuchimba maisha yako yote bila kupata chochote cha maana. Unaweza kubahatika kupata mali ya maelfu lakini siku mbili tatu ukawa huna hata shilingi moja. Fedha za madini ni kama za mashetani. Hupotea kimiujiza kama zinavyopatikana.”
“Na hawa wanaotajirika?” nilihoji.
“Hao sio wachimbaji. Ni wanunuzi au wamiliki wa maeneo utakayochimbia. Wachimbaji wa kawaida wako huko, wanazeekea huko na kufa huko!” alisisitiza.
Laiti angejua taarifa yake ilinikata maini. Toka nilipofika mjini hapo kimiujiza nilikwishafanya uamuzi. Uamuzi wangu ulikuwa kwenda Chunya, kujiunga na wachimbaji madini ili nikibahatika nirudi kwetu sina elimu lakini nina mali. Taarifa za kwenda kuzeekea huko na kufia huko ziliniacha hoi, taabani. Mshauri wangu aliweza kusoma msuguano wa mawazo yangu, nilidhani, kana kwamba anapigilia msumari wa mwisho kichwani mwangu, aliongeza, “Kama umetoka kwenu kwa nia ya kwenda machimboni isahau kabisa ndoto hiyo. Utakufa siku si zako. Utaugua kifua kikuu kwa vumbi la machimboni, utazikwa hai kwa kubomokewa na kuta za shimo, utauawa na wachimbaji wenzako ukibahatika kupata mali nyingi. Kuna
hatari elfu moja na moja.”
Ushauri wake wa bure ulianza kunichosha. “Kuna kazi gani duniani ambayo haina hatari kwa namna moja au nyingine?”
“Nyingi tu,” alijibu harakaharaka. “Kama?”
“Udaktari kwa mfano,” alijibu harakaharaka.
Nikacheka. “Daktari lazima asome kwa miaka nenda rudi. Huwezi kuamua tu kwamba unataka kuwa Daktari.”
“Tunazungumzia kazi, sio kisomo.”
Nikabaini kuwa nazungumza na mtu mweye asili ya ubishi. Nikaamua kumuuliza yeye binafsi anafanya kazi gani.
“Wengine kazi zetu huwa hazitajwi hovyo.” Alisema.
Nikaanza kuamini hisia zangu kuwa hana kazi. Hiyo
ilikuwa siku yangu ya tatu toka nilipofika Mbeya na kila
siku namwona ameketi anazungumza na watu mbalimbali. Nikaamua kupuuza hata mawaidha yake juu ya hatari za uchimbaji madini. Watu hujiunga na jeshi, wakijua fika kuwa kazi yao ni kwenda vitani ambako kifo ni jambo la kutarajiwa. Watu hujifunza urubani, wakiwa wanajua vizuri sana kwamba ndege ikidondoka kupona ni nadra sana.
Nadhani sihitaji ushauri wako zaidi, nilitamani kuwambia hivyo. Hata hivyo, sikuthubutu. Nilimwona kama mtu ambaye asingekuwa mwepesi wa kusahau na kwa kila hali sikuhitaji maadui bila sababu za msingi.
* * *
Nilikaa Mbeya kwa wiki nzima zaidi. Bado nilikuwa na hamu kubwa ya kwenda Kiwira kujaribu bahati yangu machimboni. Tatizo lilikuwa usafiri. Hakukuwa na magari ya abiria ya mara kwa mara isipokuwa yale ya kuvizia tu. Na hayo ilikuwa lazima kuwe na mtu atakayekudokeza gari fulani, linakwenda siku fulani. Sikuwa nimebahatika kumpata mtu wa aina hiyo.
Hivyo, niliutumia muda wangu mwingi kutembea huku na huko katika mji na vitongoji vya Mbeya. Nilifurahia sana vijilima vingi vilivyotapakaa huku na huko na kufanya safari zangu ziwe za kupanda na kushuka toka kitongoji hadi kitongoji. Salamu za Kinyakyusa ‘Ugonile,’ ziliniandama kila nilipokwenda. Nami sikujivunga, nilijibu kwa kujiamini, ‘Ndaga,’ ingawa ilipofuata midahalo mirefu ya kilugha niliufyata ulimi wangu na hivyo kufanya nijulikane kuwa mimi ni ‘Wakuja.’
Kama fedha zingeniruhusu ningeweza kusafiri hadi
maeneo mbalimbali maarufu kama Tukuyu, Mbarali, Ileje,
Kyela na Rungwe ambako nilisikia kuna mlima mrefu kwa mita 2961 juu ya usawa wa bahari.
Mto Kiwira pia ni kitu kingine kilichonivutia sana huko Mbeya. Ukiwa unapokea maji yake toka vijito vya Matogola, Sinini, Kipoke, Kilosi na Mulagala mto huo ulisafiri hadi Ziwa Nyanza ambamo ulimwaga maji yake siku hadi siku. Kama ilivyo kawaida ya bahari na maziwa, kamwe ziwa Nyasa halikupata kushiba wala kutapika kwa wingi wa maji hayo. Pengine ni kweli kuwa hiyo ndiyo kanuni ya maisha? Samaki mkubwa hummeza mdogo!
Ziwa hilo la Nyasa halikuwa pekee kwa Mbeya. Walibahatika kurithi sehemu nyingine ya ziwa jingine ambalo lilijikita katikati ya Mbeya na Rukwa. Hilo ni ziwa Rukwa. Wakati Rukwa walilifaidi kwa sehemu kubwa ya kusini, Mbeya walilitumia kikamilifu upande wa Kaskazini. Wakazi wa miji kama Manda na Ngomba walilitumia kwa masuala mbalimbali, ikiwa pamoja na uvuvi wa samaki.
Kitu kingine kilichonisumbua hapo Mbeya ni lile shamba la aina yake la maua na miti asilia. Shamba au pori hilo lililoko Kitulo lilikuwa kama moja ya mashamba ya wafalme wa kale, hata kabla ya kalenda ya sasa kuanza, jambo lililofanya liwe hazina ya pekee duniani. Kwa kweli shamba hilo lilinifanya nimkumbuke babu yangu. Alivyokuwa mpenzi wa miti na mitishamba kama angebahatika kufika shambani humo angekuwa mtu wa kushinda maporini akinukuu na kukariri hiki na kile.
Mfuko wangu ulianza kukaa vibaya. Akiba yangu ya pesa nilizopewa na Chifu ilianza kuyoyoma, hali iliyofanya nianze kufikiria umuhimu wa kupata ajira mapema zaidi. Nikiwa kijana, mwenye nguvu na afya tele sikuwa na wasiwasi kwa kazi yoyote ambayo ingenitokea mbele yangu. Hivyo, alipotokea
mzee Ayubu Mwalongo na kuniuliza kama ningependa kuwa mmoja wa wafanyakazi wake wa lori la abiria na mizigo kama kondakta sikusita kukubali.
Nilikutana na mzee huyo kwa namna ya ajabu kidogo. Kwa mara ya kwanza tulikuwa hotelini. Nilikuwa nikinywa uji wa ulezi. Nilipata hisia kuwa kuna mtu ananitazama sana. Nikainua uso na kukutana na mzee mmoja mwembamba na mfupi sana. Kwa kweli, ni mvi na ndevu zake ndizo zilizonifanya nijue kuwa ni mzee. Vinginevyo umbo lake lilikuwa la mtoto mdogo. Hata mavazi yake nadhani alitoa vipimo vya mtoto. Tulipokutanisha macho alinitazama kwa muda kama mtu aliyepata kuniona mahala lakini hakumbuki ni wapi. Mimi binafsi, nikiwa na hakika kuwa sijapata kumwona mahala popote nilimpuuza na kuendelea kuufaidi uji wangu.
Kesho yake, nikipitapita zangu katika kituo cha magari kwa matarajio ya kusikia taarifa za gari liendalo Kiwira nilimwona tena. Na alikuwa akinitazama kwa jicho lilelile la aina fulani. Wakati nikiamua kuondoka alinifuata. “Samahani kijana,” aliniambia aliponifikia. “Hivi tulionana wapi?”
“Nina hakika hatujapata kuonana. Mimi ni mgeni huku
na nimefika majuzi tu,” nilimweleza.
Hakuoneka kuamini, “Unaitwa Nani?” aliuliza tena. “Kwa nini unahitaji jina langu?”
“Bado ninahisi nilipata kukuona mahala,” alijibu na kuongeza. “Ulipata kuishi Iringa?”
“Mimi! Hapana.” “Tanga?”
“Hapana.” “Morogoro?” “Hapana.”
Akazidi kushangaa, “Unaitwa nani?” aliuliza tena.
“Jina la nini?” nami nikahoji.
“Siulizi kwa nia mbaya. Ninapata hisia kuwa nakufahamu. Kama sikufahamu wewe nitakuwa namfahamu baba yako. Kwani unakotoka hasa ni wapi?”
“Kigoma,” nilimjibu.
Akaonekana kuchanganyikiwa zaidi. Nadhani hakupata
kufika huko.
“Unafanya kazi gani?”
“Sina kazi. Natafuta kazi.” Nikamwona akitafakari kabla ya kuuliza, “Unajua kusoma na kuandika?”
“Mie! Vizuri sana.” “Unajua mahesabu?”
“Najua. Kwa kiwango cha kutosha tu,” Nilimjibu
Ndipo aliponieleza kuwa yeye ni mfanyabiashara wa magari. Kwa jina alijitambulisha kuwa anaitwa Ayubu Mwalongo.
Alikuwa nayo magari manne ya mizigo yanayokwenda huku na huko. Moja likiwa jipya ambalo halijaanza safari. “Tayari nimepata dereva. Bado nilikuwa na shida ya kondakta. Kama wewe umesoma na unataka kazi umepata. Unasemaje?”
Nikatae? Tuliafikiana na kupangiana mshahara na
majukumu. Nilitakiwa kuripoti kazini kesho yake.
Mtu mmoja aliniona wakati nikizungumza na yule mzee pale stendi. Mara tu tulipoachana aliniita kwa jina. Sikujua alijuaje jina langu. Ni yule aliyejitokeza kuwa mshauri wangu wa masuala ya madini wa pale nyumba ya wageni niliyofikia.
“Unamfahamu yule mzee uliyekuwa unazungumza naye?” alinihoji.
“Nani? Mzee Ayubu? Namfahamu.” “Unamfahamu vizuri?”
“Kwa nini? Nimemfahamu leo tu. Najua ni
mfanyabiashara mkubwa wa magari na anayo mengi. Kesho naanza kazi katika moja ya magari yake,” nilimwambia.
“Nini?” alishtuka. “Unaanza lini?” “Kesho”
“Kwenye magari…!”
“Yake,” nilimjibu. “Kwani kuna tatizo gani?”
Alinitazama huku akitikisa kichwa kwa namna ya kunihurumia. Mdogo wangu hujipendi. Naona mji umeingia kwa pupa. Acha tabia ya papara. Kaa na watu uliza, kabla hujakurupuka. Oh! Shauri yako!”
Hasira zikanipanda. “Kwani lini nilipata kukuteua wewe kuwa mshauri wangu? Shika hamsini zako, acha nishike zangu. Nitakapohitaji ushauri labda nitakuomba, siyo leo.” Nilisema nikiondoka zangu na kumwacha akiwa kanikodolea macho.
Kwa namna fulani nilihisi kuwa nimefanya makosa. Pengine isingenigharimu chochote kumsikiliza mshauri huyo wa bure, kumsikia tu, sio kumsikiliza, kwani nilikwishamchukulia kama mtu mwenye muda mwingi wa kuzungumza na tabia ya kujifanya anajua kuwa ningeishia kuwa kama yeye, kuketi toka asubuhi hadi adhuhuri akizungumza kwa hofu ya kufanya hili na lile.
Vilevile, sikutaka mtu yeyote anishawishi kuacha fursa ya kazi hiyo ya kusafiri. Tangu nilipoanza safari toka Buha hadi Uhayani na kisha Usukumani hadi Ufipa na sasa huku kwa Wanyakyusa nilijikuta nimeanza kupatwa na maradhi ya kupenda safari. Nilifurahia sana kuona sura mpya za nchi za watu, mazingira mapya na tamaduni mpya. Sikutaka mtu yeyote anishawishi vinginevyo kwa hilo.
9SURA YA 9
Nchi Ya Mkwawa, Ya Wajerumani.
ati ya wageni walioingia katika nchi yeti kwa mikiki, jeuri na ukatili mkubwa ni pamoja na Wajerumani. Baada ya kusikia sifa za uzuri
na utajiri wa Tanganyika, toka kwa Waarabu na Wareno ambao walifika kwanza katika pwani ya nchi yetu wajerumani walishikwa na tamaa isiyo kifani.
Tamaa hiyo ilichochewa zaidi na bwana mmoja aliyeitwa John Rebman tarehe 11, mwezi wa tisa mwaka 1848 alipoondokewa kuwa mtu mweupe wa kwanza kuutia machoni mlima mrefu kuliko yote afrika, Kilimanjaro. Mlima huu, huko Kaskazini mwa nchi yetu, unakwenda angani kwa mita zipatazo 5895, ukiwa umepambwa kwa theluji nyingi inayong’ara kwa kumeremata kwa namna ya kufanya uwe kama shada la ufalme wa Afrika na dunia pia. Hali nzuri ya hewa iliyootesha vizuri aina mbalimbali za mimea na utulivu wa wakazi wake vilimtia Rebman wazimu. Aliporudi kwao nchi yake ikapata wazimu, wazimu wa mapenzi kwa Tanganyika.
Hivyo, mwaka 1884, Novemba 23, Mjerumani aliposimika bendera yake kule Bagamoyo na mwaka mmoja baadaye, February 27 kujitangaza wamiliki wa Tanganyika haikuwa muujiza kwa mtu yeyote. Uvamizi huo wa Wajerumani
kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kwa ajili ya hila zilizofanywa na mtu wao mmoja, aliyeitwa Karl Peters, ambaye alipita huko na huko akiwaingiza Machifu na watu wengine katika mikataba ya ujanja ujanja kuhalalisha utawala wao. Kwa upande mwingine, vitisho vilivyoambatana na mauaji, kwa kutumia silaha zao ambazo zilikuwa bora zaidi ya zetu kulifanikiwa azma yao ya kuimeza nchi yetu.
Mnamo mwaka 1991, Mjerumani mmoja, kwa jina Julius Von Sodden aliteuliwa kuwa gavana wa kwanza wa Ujerumani kwa Tanganyika. Ni yeye aliyeamua kuhamisha makao makuu ya serikali yao toka Bagamoyo hadi Dar es Salaam.
Kam Sodden na magava wenzake waliomfuatia, akina Von Echele, Von Wissman, Von Libert na wenzao wengine; Von Gotzen, Von Rechenberg na yule wa mwisho Von Schnee walidhani kuwa walikuwa wameipita Tanganyika kwa urahisi kiasi kile basi walikuwa wamejidanganya.
Huko Tabora aliibuka shujaa mmoja, Isike Mkasiwa, ambaye alipigana nao kwa muda mrefu hadi Januari 9, 1893 alipozidiwa na kuamua kujiua badala ya kuchukuliwa mateka. Huyo hakuwa mhanga pekee. Huko Kilimanjaro mnamo
Machi 2, 1900 Machifu tisa wa koo mbalimbali za makabila ya huko walinyongwa hadharani kufuatia upinzani wao mkali dhidi ya Wajerumani. Miongoni mwa Machifu mashuhuri kati ya walionyongwa alikuwemo Mollelia wa Kibosho, Ngalami pamoja na Meli wa Moshi. Madai ya watawala wa Kijerumani ni kuwa walikuwa wakichochea upinzani dhidi ya utawala wao.
Haikuwasaidia, kwani ndio kwanza Watanganyika walizidisha mapambano. Vita ya majimaji vilienea sehemu mbalimbali za kusini ikiwa pamoja na Songea, Mtawara, Lindi na kwingineko. Majimajii walishambulia misheni ya
Mikukuyumbu Nachingwea, wakateka makao ya Wajerumani ya Liwale, misheni ya Masasi na kuteketeza ile ya Nyangao, Lindi. Hali hiyo ilipelekea Septemba 1, 1905 Wajerumani waombe msaada zaidi wa kijeshi toka kwao, ambao uliwezesha kurejesha utawala wao.
Uamuzi waliouchukua baada ya kuona hata baada ya kumteka Kinjekitile Ngware mganga aliyekuwa akiwapa kinga wapiganaji ili wasidhurike na risasi za Mjerumani na kumnyonga hadharani katika kijiji cha Muhoro, Rufiji bado mapambano yalizidi kuwa makali.
Chifu mwingine, akitokea Iringa, kwa jina Singoyangili Mkwawa hatasahulika kwa kupambana na Wajerumani kwa nguvu zake zote. Chifu huyu alitokea katika kabila la Wahehe, makazi yake yakiwa kijijini Kalenga, aliwachachafya Wajerumani kwa kiwango ambacho hawatakaa wasahau.
Mara kadhaa majeshi ya Mkwawa yaliwateketeza Wajerumani na kuvunjilia mbali ngome zao. Hali hiyo iliwasababishia Wajerumani waamue kujenga ngome imara ambayo ilikuja kuwa chanzo cha mji na baadaye mkoa wa iringa. Mji huo ulijengwa karibu na ngome ya Mkwawa ya Kalenga. Ndiyo, Mkwawa pia alishindwa na kuamua kujinyonga badala ya kukamatwa akiwa hai, lakini mji wa Iringa ukawa kielelezo tosha cha nguvu na misimamo thabiti wa babu zetu dhidi ya utawala wa kigeni.
Niliyafikiria yote hayo nikiwa ndani ya gari karibuni kuingia katika mji huo wa kihistoria. Ilikuwa safari yangu ya kwanza kama kondakta. Nilikuwa na muda mwingi wa kufikiri na kutafakari yale ambayo nilibahatika kuyasoma shuleni na katika vitabu mbalimbali vilivyopata kunipitia mbele yangu. Mambo hayo yalikuja kama ndoto kutokana na macho yangu
yaliyokuwa yakitazama nje ya gari muda mwingi zaidi.
Tulisafiri kwa zaidi ya siku tatu, toka Mbeya hadi kuufikia mji wa Iringa. Tulishusha hapa na kupakia pale, mara abiria ama mizigo, mara mizigo na abiria. Mara kadhaa tulilala porini kwa ubovu wa magari, mara nyingine ilikuwa kusubiri mzigo ya michele au matunda yaliyokuwa yakivunwa.
Kinyume na nilivyoahidiwa kuwa ningetumia gari jipya, gari hili lilikuwa chakavu lililochakaa sana. Kama lingekuwa binadamu lingeweza kusema hivyo na kuacha lipumzike kwa amani, lakini kwa kuwa halikuwa na uwezo huo liliacha liburuzwe kama ng’ombe mzee huku mlio wake ukionyesha kuteseka sana kwa mashine yake hata kwa mtu asiye na ujuzi wa ufundi wa magari. Lilikuwa lori, aina ya Bedford. Kila baada ya kilomita kumi tulilazimika kusimama na kujaza maji katika rejeta ambayo ilikuwa ikiyakausha kwa kasi ya pekee.
Alichoniambia tajiri yangu juu ya kutumia gari hilo badala ya lile jipya nililoahidiwa sikupata kukielewa vizuri. Alitumia maneno kama ‘Ngoja uzowee’ au ‘Vibali vimechelewa.’ Kauli ambazo sikuona kama alitaka nizielewe vizuri. Kwa kuwa wahanga wanasema ‘mchagua jembe si mkulima,’ nikapokea jukumu hilo bila maswali zaidi.
Lakini dereva wangu alinishangaa zaidi pale nilipomuuliza juu ya gari hilo. Alionekana kuwa mtu mwema, mchangamfu na mkimya. Nilimkadiria kuwa alinizidi umri kwa zaidi ya mara mbili. Kwa jina alijitambulisha kuwa ni Kalinga. “Gari jipya?” alinihoji akicheka sana. “Alikuambia analo
jipya? Basi litakuwa hili,” aliongeza.
“Kwa vipi? Kwani hana gari jipya?” nilihoji.
“Huu kwangu mie ni mwaka wa tatu toka niandikishwe kazi kwake. Na nilijiunga kwa hadithi hiyohiyo ya gari jipya.
Sikupata kuliona hata kwa macho.”
Nilipatwa na mshangao wa mwaka. “Kwanini basi anasema uongo?” nilimuuliza.
“Hata mimi najiuliza hilo mara kwa mara,” Kalinga alinijibu. “Mtu mzima kwa nini useme uongo? Unajua madereva wawili kabla yangu na makondakta watatu wameshaacha kazi kwa jili ya ahadi hizo za gari jipya?”
Ghafla nikajiwa na wazo. “Kwa hiyo mimi nimeingia
baada ya kondakta wa mwisho kuacha kazi?” nilihoji. “Kawambwa! Yeye hakuacha,” alisema.
“Ila?” “Alikufa.”
“Alikufaje? Ajali?” nilizidi kudadisi.
“Wala haikuwa ajali. Kifo chake kina utata mwingi. Nadhani tuachane na maongezi hayo. Hayakufai kwa sasa,” alishauri.
Nikamuuliza Kalinga juu ya magari mengine saba aliyonayo tajiri yetu. Hilo lilimfanya aangue kicheko.
“Mbona unacheka. Hana?”
Kalinga alikohoa kwa namna ya mtu aliyepaliwa kabla ya kusema taratibu, “Anayo.”
Nilimwona kama mtu aliyeacha neno alilotaka kulisema. “Anayo, lakini?” nilimshurutisha.
“Lakini ni mabovu kuliko hili. Yote yako katika magereji mbalimbali, taabani hata mafundi wameyakatia tamaa. Wanamwambia akayavute, mwenyewe anasema yatatoka yakitembea.”
Ilibidi nami niangue kicheko. Kilikuwa kicheko cha uchungu. Sikujua kama nilikuwa nikijicheka mie au kumcheka mwajiri wangu mpya, tajiri wa magari mabovu. Kwa namna
fulani nilihisi fahari. Niliona kama mimi na dereva Kalinga ndio tuliokuwa matajiri wenye ufunguo pekee za kumkwamua tajiri yetu ili anunue gari jipya na kufufua yale mengine yaliyoozea kwa mafundi. Fikra hizo zilinifanya nitupile mbali wazo ambalo lilianza kunijia la kuacha kazi hiyo mara moja na kutafuta nyingine.
Nikakumbuka yule mshauri wangu wa masuala ya madini na kubaini kuwa kweli alikuwa na jambo la kunishauri juu ya tajiri yangu, mzee Ayubu Mwalongo. Kwa mara ya kwanza nilijilaumu kwa kutomsikiliza.
* * *
Hali ya hewa ikiwa, kwa kiasi fulani, kama ile ya Mbeya, mji ukiwa juu ya vilima kwa takribani mita 1550 juu ya usawa wa bahari nilijikuta nikiridhika sana na maisha yangu ya hapa na pale katika mji, vitongoji na vijiji vya Iringa.
Tulikuwa watu wa safari kila siku. Tulikwenda Mafinga, ambako baridi ilizidi ile ya mjini kwa kiwango kikubwa. Tulikwenda Kilolo ambako niliweza kuupanda mlima Luhembelo na kuvutiwa na wanyama wa ainaaina katika pori moja lililoitwa Udzungwa. Wanyama ambao walikuwa tele kama wale tuliowaona pia kule Ruaha. Tulifika Makete, tulifika Njombe, tulifika pia Ludewa.
Kila nilipopata wasaa nilitembelea kijiji cha Kalenga ili kuona kumbukumbu za yule mzee shujaa, Mkwawa na ngome yake. Kaburi lake lilikuwa pale, nasikia alizikwa bila kichwa, kwani Wajerumani walikipokonya na kukipeleka kwao ili kuchunguza uwezo wa ajabu wa mtu huyu aliyewatoa jasho vigogo waliokaribia kuitawala dunia.
Nilipata pia kutembelea kijiji cha kumbukumbu cha
Isimila. Niliweza kuona michoro na vifaa vilivyochongwa kutokana na mawe ambavyo ni sehemu ya uthibitisho kuwa mtu wa kale, zaidi ya miaka 70,000 aliishi Tanganyika. uthibitisho huo umefanywa na wataalamu mbalimbali waliobobea katika taaluma za macho ya kale.
Uzoefu wangu mkoani humo ulinifanya nibaini kuwa hata jina la Iringa lilitokana na udhaifu wa matamshi ya wageni hao kwa lugha ya Kihehe, kwamba wenyewe walikuwa wakiuhita mji huo Lilinga, kwa maana ya ng ngome.
Biashara yetu ilikuwa ikienda vizuri, kama kila mmoja wetu alivyotegemea. Kwanza gari lilipunguza tabia ya kuharibikaharibika mara kwa mara. Jambo lililomfanya dereva Kalinga ambaye pia ni fundi anichekelee na kunisifu kuwa nina ‘nyota’ ya biashara, “Sio siri, gari hili lilianza kushindikana. Mimi mwenyewe nilishaamua kuifanya safari hii iwe ya mwisho,” alinitobolea siri yake.
Aliyefurahi zaidi , alikuwa tajiri yetu mzee Ayubu. Kila tuliporejea Mbeya tulikuwa na fedha nyingi za kumpa na taarifa chache tu za kuharibika kwa gari lake. Kwa mara ya kwanza nilimwona akitabasamu. Miezi miwili mitatu baadaye nilipomtazama nilihisi amenenepa na kurefuka kidogo.
Kwa bahati mbaya, mafanikio hayo yalianza kuambatana na ajali za mara kwa mara. Ajali hizo zilikuwa ngumu kuelezeka. Ya kwanza, ilitokea katika maeneo ya Ruaha. Nilikuwa nimeshuka nje ya gari nikimsaidia abiria mmoja mwenye mguu moja kushuka. Mara alipofika chini mbele yetu, lilisimama gari dogo, aina ya Landrover, lililokuwa na Wazungu wawili. Waliniita. Nikawaendea. Mara tu nilipowakaribia gunia la mahindi lililokuwa juu ya gari liliporomoka kwa kasi na kutua palepale nilipokuwa. Kasi ya gunia hilo lilimwangusha yule
abiria na kumfanya ateguke mguu wa pili. Ilibidi tumrudishe kwenye gari na kumpeleka hospitali moja ndogo huko Iringa.
Ajali ya pili ilikuwa mbaya zaidi! Ilikuwa katika milima ya Kitonga. Gari letu kongwe lilipanda kwa taabu sana milima hiyo kiasi kwamba abiria wengi walishuka na kutembea taratibu, wakiwa wamelitangulia gari. Tulibakiwa kwenye gari mimi na dereva pekee. Mara gari ikaanza kurudi nyuma kwa kasi. Kwa kila hali lilielekea kuporomokea katika yale mashimo makubwa ambayo hufanya abira wengine wafumbe macho kila wanapofika hapo, kwa uoga. “Ruka nje!” dereva aliniamuru.
“Na wewe?” nilimuuliza. “Ruka.” Alifoka
Nikafungua mlango na kuchupa nje. Dakika hiyohiyo gari liliangukia upande nilioshukia na kunikosa kwa nusu nchi tu! Mimi pamoja na abiria wangu ambao walikuwa wakishuhudia purukushani hiyo tulilikimbilia gari kumwahi dereva. Tulimkuta akifungua mlango na kutoka nje akiwa safi bila hata vumbi kana kwamba alijilaza tu. Kila mtu alishangazwa na ajali hiyo.
Lakini ajali ya tatu ilishangaza zaidi. Ilitokea miezi miwili baada ya ile ya mwisho. Tena ilitokea katika kituo cha kazi, Mbeya. Tulikuwa tukilikagua gari kwa makini kabla ya kuanza safari yetu nyingine ndefu ya mijini na mashambani.
Baada ya dereva kuwasha gari na kubaini kasoro fulani katika mlio wake, alikagua maji, oili, mafuta ya breki na kila kilichohitajika. Kila kitu kilikuwa safi. Alipoiwasha bado ilitoa mlio usioeleweka. Akaniamuru niingie chini ya gari kuangalia kama kulikuwa na nati au sukurubu yoyote iliyolegea. Nilikuwa tayari nimevaa vizuri, shati jeupe, suruali nyeusi na tai shingoni. Nilijitazama, kisha nikakutazama huko chini
nilikotakiwa kuingia. Kulijaa vumbi na topetope la manyunyu ya ukungu wa baridi.
“Hakufai,” nilimwambia dereva.
Aliponitazama aliridhia kuwa sikustahili kuingia huko. Akaniamuru kuingia ndani ya gari, niwashe na kupiga resi wakati yeye akikagua huko chini. Haikuwa kazi kubwa kwangu kufanya hayo. Katika safari zetu nyingi nilikwishajua kuendesha gari vizuri, ingawa uzoefu mdogo ulifanya niwe na wasiwasi kidogo.
“Washa!” dereva aliita toka chini. “Kanyaga resi!”
“Kanyaga breki!”
Ni wakati nikikanyaga breki hiyo lilipotokea jambo ambalo hakuna aliyeweza kuelewa. Nilisikia mlio wa ‘ka ka ka ka’ kana kwamba kuna kitu kinachokatika. Haikuwa uwongo kwani mara hiyohiyo niliona nyufa zikitokea kwenye bodi ya gari na baadaye sehemu iliyobeba injini ikaanza kudidimia.
“Kalinga! Toka haraka!” Nilipiga kelele nikifungua mlango na kuruka nje.
“Kanyaga bre….” Ilikuwa kauli yake ya mwisho kabla injini haijadondoka chini na kumpondaponda vibaya sana. Majirani walijitokeza na kumsaidia kumtoa chini ya injini hiyo ambayo ilikuwa bado ikinguruma. Alikuwa akipumua, lakini hakuwa mtu wa kuishi. Uso mzima ulikuwa umepondeka, kichwa na kiwiliwili vikiwa kama vimeachana.
Sikupata kuona kitu cha kutisha kama kile maishani mwangu. Nilitetemeka mwili mzima huku machozi yakinitoka. Nilitetemeka zaidi pale nilipokumbuka kuwa mimi ndiye niliyetakiwa kuwa chini ya gari lile. Kwa maneno mengine, mimi ndiye ambaye ningekuwa taabani, nusu maiti. Nilishukuru
pale nilipohisi mtu mmoja akinishika mkono na kuniongoza taratibu hadi katika chumba changu cha nyumba ya wageni na kuniketisha kitandani.
“Pumzika. Ikiwezekana lala. Usitoke kwenda kula nje hadi masuala yote ya kumshughulikia marehemu yatakapokwisha,” alisema.
“Ame… amekufa!” niliropoka. “Kwa vyovyote vile.”
Nikainua macho kumtazama mfadhili wangu huyu. Hakuwa mwingine zaidi ya yule mshauri wangu wa masuala ya madini, ambaye mara ya mwisho nilipuuza kumsikiliza. Alikuwa akinitazama kwa huzuni, lakini nilihisi macho yake yalikuwa yakinicheka na kunidhihaki kama yanayosema, “Si unaona? Nilikuambia nini!”
Kwa sauti alinieleza kile ambacho alidai alitaka kunieleza toka awali, lakini, ‘nikampuuza!’kuhusu sifa mbaya za mzee Ayubu, “Ni mtu hatari sana. Ni mshirikina kupita kiasi. Marehemu Kalinga ni mtu wa tano aliyepoteza maisha katika mazingira ya ajabuajabu katika ajali.”
“Kwa vipi?” nilimuuliza. “Inakuwaje mambo hayo?” “Ushirikina.”
“Ushirikina?”
Akaamua kunifafanulia. “Inaaminika mzee Ayubu alipata utajiri wake kwa njia ya ushirikina. Kabla hajawa na kitu alifiwa na mkewe katika mazingira ya kutatanisha. Mara akaibuka na kununua magari kwa mpigo. Kipindi fulani alionekana kulegalega kiuchumi mtoto wake mkubwa naye akafa kiajabuajabu. Akaibuka tena na kuongeza magari. Lakini kwa kuwa mali ya haramu haidumu magari yake nayo yaliandamwa na mkasa huu na ule. Mara yapate ajali, mara yaharibike. Mawili yalipata kuibuka bila sababu yoyote.”
Nilimsikiliza kwa mshangao. Nikayakumbuka yaliyonikuta mimi mwenyewe kule Sumbawanga ya Mmanyema kudaiwa kutaka kunigeuza ndondocha.
“Hivi ni kweli mambo haya yapo?” nilimuuliza.
Swali hilo ambalo lilimfanya anitazame kama mdudu kwa dharau. “Unauliza ni kweli? Huna hakika! Hujui kuwa ni wewe uliyekusudiwa? Kalinga amekufa kwa bahati mbaya tu. Wewe ndiye hasa uliyehitajika!” alisisitiza.
“Mimi! Kwa nini mimi?”
“Kwani hukumbuki mara ngapi umenusurika?” alinijibu kwa swali jingine. “Ni wewe uliyekuwa chaguo lake. Damu za wengine wote waliokutangulia hazijafaa. Wewe toka alipokutia machoni alishajua u chaguo lake,” alinijibu.
“Alijuaje kuwa damu yangu itamfaa?” nilisisitiza. Aliendelea na mtindo wake wa kunijibu swali kwa swali,
“Kwani hujui?” alinihoji. “Unataka kusema kuwa hujui kuwa una alama?”
“Alama! Alama gani?” Nilihoji kwa mshangao uliochanganyika na hofu.
Akaangua kicheko. baadaye alisema taratibu., “Usijifanye mtoto kuliko ulivyo. Una alama ya shari. Iko wazi usoni mwako kwa kila mjuzi wa mambo atakayekutazama usoni mara moja. Hapo ulipo una elimu ya kutosha lakini haikusaidii! Una nyota lakini haing’ari! Wewe si mtu wa kuhangaika kama unavyohangaika. Unahitaji kusafishwa, kufutiwa alama hiyo. Vinginevyo, maisha yako yataendelea kuwa kama ya mbwa koko asiye na mwenyewe.”
Niliyatafari maneno na hoja zake. Chembechembe za ukweli zilikuwa nyingi kuliko uongo. Kwa mara ya kwanza nilijikuta nikipatwa na hofu kubwa juu ya maisha yangu, hofu ya kufa Kama mbwa koko kama alivyonieleza. Leo niko
hapa kesho niko pale! Kila ninachoshika hakishikiki! Nadhani machozi yalinilengalenga au kunitoka bila taarifa, kwani nilihisi mkono wa jamaa yangu huyo ukiwa begani kwa namna ya kunifariji; kitendo ambacho kilifuatiwa na sauti yake yenye huruma aliponiambia, “Usijali mdogo wangu, nitakusaidia.”
“Utanisaidiaje?” nilinong’ona.
“Nitakupeleka mahala, utasafishwa vizuri. Baada ya
hapo utaona milango yote uliyofungiwa ikifunguka.”
Bado nilikuwa na wasiwasi. “Utanipeleka wapi?” Nilimuuliza.
“Kilwa.”
“Kilwa?”
“Naam. Kuna wajuzi wa mambo haya na gharama zake ni nafuu. Utaoshwa utasafishwa na kukaangwa upya. Hakuna atakayekugusa.”
* * *
Mipango ya safari ya Kilwa ilianza mara baada ya mazishi ya dereva Kalinga. Yalikuwa mazishi yaliyoudhuriwa na takribani kila mkazi wa Mbeya, waliomfahamu na wasiomfahamu. Wakati wote wa msiba hadi matanga lilisemwa hili na lile kufuatia muujiza ule wa kifo chake. Jina la mzee Ayubu lilikuwa mdomoni mwa kila mtu. Wako waliomwita ‘mchawi’ wengine walimwita ‘mshirikina.’ Lakini walikuwepo wengine waliokuwa wakimtetea kwa madai kuwa anarogwa na watu wenye kijicho kwa mali na jitihada zake. Mradi kila mmoja alikuwa na lake la kusema.
Mzee Ayubu mwenyewe alikuwa mtu wa kuhurumiwa sana. Katika kipindi chote hicho cha msiba alikuwa mkimya muda wote akiwa kajiinamia. Haikuwa rahisi kujua iwapo minong’ono na macho ya kusengenya ya waombolezaji wengine
ilihusiana na ukimya wake au la.
Nilimhurumia zaidi pale nilipomwita chemba na kumuarifu kuwa kazi kwake basi. Alishtuka kama aliyeguswa na waya wa umeme. Nilihisi machozi yakimlengalenga pale aliposema, “Unajua ni wewe ninayekutegemea? Nakuhitaji sasa zaidi ya wakati mwingine wowote ule. Kuondoka kwako itakuwa sawa na kuondoka kwa roho yangu.”
Nilitamani kumsikiliza. Nilitamani kufutilia mbali uamuzi wangu na kurudi kazini kwa kumhurumia. Lakini nilijihurumia pia, zaidi ya nilivyomhurumia yeye. Nikapiga moyo konde na kuung’ang’ania msimamo wangu. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kunilipa madai yangu kisha tukaagana bila kuangaliana machoni.
Mfadhili au mshauri wangu mpya, ambaye sasa nilimfahamu kwa jina kuwa aliitwa Bushiri Mtanashati, alinipongeza kwa uamuzi wangu wa kiume. “Ni muhimu sana kwa mtoto wa kiume kujua na kusema ‘ndiyo’ au ‘hapana’. Ukishindwa hilo utaishia kuwa hamnazo.”
Akili yangu ilikwisha hama kabisa toka Mbeya sasa ilikuwa Kilwa. Nilikuwa nikitafakari kile ninachofahamu juu ya mji huo ambao una historia kubwa kote duniani.
Kufika kwangu Kilwa kungefanya nifike Pwani na kuiona bahari kwa mara yangu ya kwanza, bahari maarufu ya Hindi ambayo jiografia inaonyesha kuwa ndiyo inayolinganisha bara letu la Afrika na lile la Asia. Bahari hiyo naambiwa ina maji mengi lakini hayanyweki kwani yana chumvi tofauti kabisa na maji ya maziwa yetu kama Nyanza na Tanganyika ambayo yanafaa kila aina ya matumizi.
Kihistoria Kilwa ni miongoni mwa miji michache katika Pwani ya Bahari ya Hindi ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya watu walioishi pamoja. Hali hiyo ilisababisha uwe mji wa
kwanza kibiashara katika nchi yetu. Historia hiyo ilijengeka zaidi April 15, 1497 pale inapodaiwa kuwa mtu mweupe wa kwanza alipokanyaga ardhi ya Tanganyika, kupitia Kilwa katika jitihada zao za kutafuta biashara. Juni 2, mwaka uliofuata Mreno aliyeitwa Vasco da Gama, akiongoza kundi kubwa la watu walifika Pwani ya Tanganyika. Tamaa na uroho wa da Gama vinaaminika kuwa chanzo cha ukoloni wao nchini. Hivyo ilipofika mwezi wa Julai, tarehe 16, mwaka 1500 wakazi wa Kilwa walikuta bendera ya utawala wa Kireno ikipepea juu ya vichwa vyao. Miaka miwili baadaye wakazi hao wa Kilwa waliamriwa kuanza kulipa kodi ya kichwa kwa serikali ya Ureno na hivyo kuufanya mji huo kuwa koloni la kwanza la wageni katika Tanganyika.
Utawala wa Wareno haukuja kwa urahisi kiasi hicho. Baada ya da Gama lilifuata kundi la pili, lililoongozwa na Pedro Cabral, kamanda katika jeshi la wanamaji. Waliuvamia mji kwa mizinga, kusambaratisha wakazi na wengi kuuawa kabla ya kufanikiwa azma yao. Baada ya hapo walimwekea gavana wao wa kwanza, Antonio Fernandes kama mtawala wa kwanza wa Wareno nchini Tanganyika.
Miaka iliyofuata Kilwa iliondokea kuwa lango kuu la biashara. Biashara iliposhamiri sana hapa miaka ya 1901 hadi 1914, ingawa ilipigwa marufuku tangu 1873, ilikuwa ile ya utumwa. Lakini pia biashara za meno ya tembo, dhahabu, vipusa na simbi zilifanyika kwa kasi mjini hapo zikivuta wafanyabiashara toka nchi mbalimbali za dunia kama China, Uarabuni na India.
Mzunguko huo wa biashara pia uliwezesha mazao mbalimbali kama mahindi, viazi na korosho. Aidha, matunda kama vile mapera na mapeasi na mananasi ni sehemu ya ujio
huo wa Wareno waliopo nchini. Pamoja na vyakula athari za Mreno katika utamaduni wa Tanganyika hazitaweza kufutika. Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili maneno kama gereza, meza, leso, karata, mvinyo na mbolea yana athari kubwa ya lugha ya Kireno.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zangu maeneo mengi ya Kilwa ni vivutio vikubwa kwa macho ya mwanadamu. Kwa wapenzi wa mazingira kitu cha kwanza kitakachonasa macho yake ni ile delta kubwa ya mto Rufiji. Delta hii ya aina yake inapambwa zaidi na miti aina ya mikoko iliyoizunguka miti, miti ambayo huota majini na hivyo mashina yake yenye mizizi kuwa maficho na mazalio ya samaki aina mbalimbali hasa kamba.
Kwa mwanahistoria delta hii ni hadithi ya pekee. Ni humo ambamo nguvu za Mjerumani katika Tanganyika zilipata pigo lake la kwanza pale manowari yake ya kivita, Konigsberg ilipopatwa na mkasa wa kuharibika na hivyo kuruhusu kipigo ambacho hawatakisahau. Magofu ya Kilwa Kivinje, Kilwa Visiwani, visiwa vya songo mnara, Songalungu, Sanje na Kati na Sanje ya Majoma, mapango ya Chetasui, Mkondaji, Mbaga
, Kiinja na Maloho, Jiwe la Mzungu, Kilola Mbani ni miongoni mwa maeneo ambayo mwanahistoria angesisismkwa sana kuyaona kwa macho yake.
Na mwana utamaduni naye atavutiwa na ule mchanganyiko wa tamaduni za makabila mbalimbali ya eneo hilo kama Wamatumbi na Wangino na ule wa Waarabu na kuzaa kitu ambacho baadhi ya watu hupenda kukiita ‘waswahili’. Makabila hayo makuu pamoja na na yale ya Wasongo, Wambana, Wambamula, Wamasoko na Washirazi ni sehemu ya utamaduni wa Kilwa. Wengine ni Wamachinga,
Wamakonde, Wayao, Wamera na wengineo. Wengi kati yao wamerithi dini na mila za kiarabu kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, ndani kabisa ya mioyo yao wengi wao bado ni watu walewale, wenye imani na tamaduni zilezile za asili yao.
Kwa mfano, wakati kwa Waarabu watu wa Kilwa wamerithi utamaduni ule ambao hufanya mtoto wa baba mkubwa na wa baba mdogo waweze kuoana bila pingamizi lolote, bado taratibu zao za jadi katika masuala kama jando na unyago ni za asili zaidi. Mtoto wa kiume hupelekwa itani, yaani jandoni afikapo umri wa kati ya miaka kumi na kumi na nne. Baada ya hapo hupelekwa utagoni, ambako hukaa muda mrefu wakifundwa mila, tamaduni na wajibu wao kwa jamii. Hatua ambayo inapokamilika hufuatwa na sherehe maalumu yenye chakula maalum ngando ambacho huandaliwa kwa majani ya mti maalumu, mfulu, ambao umefanana sana na vidole vya ndege wanayemwita kituku, kwetu akiwa ni njiwa.
Masuala hayo ya jando huenda sambamba na yale ya unyago kwa wasichana. Hata hivyo unyago hauna mambo mengi sana. Siku ya kwanza binti ambaye amefikia hadhi ya mwali hukamwatwa na kufungiwa ndani akiitwa ‘kukujike.’ Siku ya pili hutapishwa kwa dawa maalumu, chini ya uongozi wa kungwi mkuu. Siku ya tatu hurudishwa nyumbani kwao ambako huogeshwa, kupakwa mafuta na kuvishwa kanga mpya. Toka hapo yuko huru kwa mchumba yeyote anayestahili kumposa.
Hiyo ndiyo Kilwa, Kilwa ambayo niliifahamu vilivyo kinadharia, baada ya kusoma na kusikiliza simulizi za watu mbalimbali juu ya mji huo wa kihistoria, mji ambao siku mbili tatu zijazo ningeutembelea na kujionea kwa macho yangu mwenyewe siri ya umaarufu huo. Siri hiyo ingesaidia
kuniondolea ‘alama’ katika uso wangu.
Maandalizi ya safari yalikuwa yakiendelea vizuri. Rafiki na mshauri wangu mpya, Bushiri Mtanashati, alikuwa mtu wa kushughulika kinyume kabisa na siku za awali ambazo nilimwona akiwa amekaa bure muda mwingi. Alienda huko na huko kufanya utafiti wa njia bora zaidi, gari lipo na lini linaondoka. Mara mbili alichukua pesa kwangu kwa maelezo yaleyale ya ‘Maandalizi ya safari.’
Nilikuwa na pesa za kutosha na nilitaka ‘alama’ iondolewe haraka katika paji langu la uso. Hivyo, sikuwa mtu wa kusita kila nilipotakiwa kutoa. Lakini pale alipokuja kwa mara ya tatu, akiwa amelewa, na kuniomba nimpe pesa zaidi nilianza kumtilia mashaka. “Leo unataka za nini?” nilimuuliza.
“Maandalizi.” “Yapi?”
“Kwani hujui?” aliuliza kwa sauti yenye hasira kidogo “Hii ni safari ndefu. Safari ngumu lakini muhimu sana kwako. Kivuli cha kifo kinakufuata popote uendapo. Usipokiondoa huna uhai, pesa unazotafuta hutazifaidi.”
Sikupenda kubishana naye. Nikampa, shingo upande. Siku hiyo sikumwona tena hadi kesho yake akiwa mchovu sana, bila shaka kwa ulevi. “Safari imewiva. Kesho mchana tunaondoka. Usiwe na wasiwasi mdogo wangu,” aliniambia akijilaza juu ya kitanda changu na kupitiwa na usingizi.
Wasiwasi nilikuwa nao. Bushiri alinitia wasiwasi. Tabia yake, maneno yake na sasa vitendo vyake vilianza kunipa picha tofauti kabisa na ile ya awali, kabla hajautia mkono wake katika mfuko wangu. Alikuwa ameshinda amekaa, ghafla amekuwa hapatikani. Alikuwa halewi, mara amekuwa mlevi! Nilimtazama wakati kalala chali, akikoroma kama nguruwe
aliyejeruhiwa. Karatasi mbili tatu katika mfuko wake wa shati zilikuwa zikichungulia nje. Nikashawishika kuzichomoa ili kujua kama zilikuwa tiketi au la. Haikuwa tiketi. Moja ya karatasi hizo kilikuwa kipande cha kodi ya kichwa cha miaka miwili iliyopita. Ni jina kwenye cheti hicho ambalo liliniacha hoi zaidi. Abdallah Jongo! Mkazi wa Kisarawe! Sio Shubiri Mtanashati tena! Wala hatoki tena Newala ambako alisema ni jirani sana na Kilwa!
Nikakumbuka alivyonieleza kwa taabu sana jina na historia yake fupi baada ya kumsaili mara wa mara.
Mimi: Unajua hujapata kunitajia jina lako? Yeye: Hivi sijakutajia? Naitwa … Bushili.
Mimi: Bushili au Bushiri? Yeye: Bushiri
Mimi: Kabila lako? Yeye: M-makonde
Yeye: Mmakonde wa wapi? Wa Msumbiji?
Yeye: (Akicheka) Hapana. Wa Tanganyika hapahapa. Ingawa nina wajomba wengi huko Nampula, Msumbiji. Mimi natoka Newala. Ndiyo maana Kilwa naijua vizuri sana.
Mie: Mimi nilidhani wewe Mnyakyusa, Mbungu au Muandali wa hapahapa Mbeya.
Yeye: (Akacheka tena) Hapana. Wengi wanafikiri hivyo. Wengine wananiita Mmalila, wengine Msangu, wengine Mbungu. Sijui kwa nini. Mimi Mmakonde bwana.
Mie: Mbona huna ndonya? Wamakonde wengi wana
ndonya.
Yeye: Nilinusurika. Sikukulia kule sana. Hata kilugha naongea kwa taabu sana.
Maongezi hayo sasa niliyatilia mashaka kutokana na
kulibaini jina lake jingine kwenye cheti hicho. Karatasi ya pili ilikuwa bili ya vinywaji ambavyo ama alikunywa ama anadaiwa. Senti hamsini! Fedha ambazo zilitosha kununua shati jipya, suruali mpya na viatu! Nikaweka nadhiri kutompa hata senti yangu moja bila uthibitisho wa kile ninachokwenda kufanya.
Safari ya kesho, ambayo tayari niliitilia mashaka, ilipatwa na pigo jingine. Tajiri yangu wa zamani, mzee Ayubu alikufa ghafla. Maiti yake ilikutwa ikining’inia kwenye kamba, juu ya mwembe uliokuwa nyuma ya nyumba yake. Alikuwa amejinyonga. Nilisikitika sana na kujikuta nikilia kama mmoja wa jamaa zake wa karibu.
Mara baada ya mazishi jambo jingine, kubwa zaidi, lilitokea na kubadilisha kabisa ramani ya safari yangu iliyokuwa kichwani.
SURA YA KUMI
Tanga, kama Manamba
osa langu, ambalo nililifanya bila kukusudia ni kujisahau. Kwa maneno mengine, ni kuyafumbia macho mabadiliko ya umri na maumbile yangu
kwa muda mrefu. Ni kosa hilo lililoniletea matatizo ya kisheria, dhidi ya serikali ya Mwingereza na mfalme wao George.
Nilikuwa nimebadilika. Nilirefuka kiasi cha watu wengi wanaoitwa warefu kulazimika kunyanyua nyuso zao ili kunitazama usoni. Sikupata kuwa mnene, lakini mwili wangu ulijaza vizuri na kunipa ukakamavu na kila dalili ya afya njema. Nadhani sura yangu ilivutia, kwani nilipata hisia kuwa wasichana wengi walipenda sana kuzungumza na mie, wakati mwingine bila sababu za msingi. Na pale nilipowakazia macho wengi wao waliinama kwa aibu kuyakwepa macho yangu.
Rafiki zangu huko mtaani nao walinishangaza. Walianza kunipisha kila nilipotokea, huku ‘shikamoo,’ zikiwatoka baadhi yao. Heshima hizi zilinifanya nisite kuzipokea kwa ukunjufu huku nikijawa na mshangao ulioambatana na maswali tele. Yakoje mambo haya? Au mavazi mazuri ninayovaa na usafi wa mwili wangu vinachangia kunipa heshima?
Lakini ni jana tu nilipoweza kupata majibu ya fumbo hilo. Nilikuwa nimetoka kuoga, tayari nimepaka mafuta na sasa
najikagua kwenye kioo chenye ukubwa wa kiganja changu. Niliridhishwa na nywele zangu nyeusi, zilizosheviwa vizuri. Nilivutiwa na sura yangu ang’avu, yenye pua lililochongoka kiasi cha baadhi ya watu kunifananisha na Watutsi. Mara macho yangu yakavutwa na kitu kigeni katika uso wangu huo. Kwenye kidevu changu, chini ya mdomo, palikuwa na vijinywele vitatu ambavyo havikupaswa kuwa pale. Nilidhani ni nywele zilizokatika toka kichwani wakati nachana, lakini pale nilipovikung’uta kwa kidole na kuona haviondoki ndipo nilibaini kinachotokea. Ndevu! Nimeanza kuota ndevu! Hatua ambayo ilikuwa na tasfri moja tu; Nimekua!
Sina budi kukiri hapa kuwa kubaini hilo kulinishtua sana. Sikuona kuwa ilikuwa habari njema kwangu kuingia katika safari ya utu uzima bila kutarajia. Sikuwa nimejiandaa, si kielimu si kiuchumi. Bado nilikuwa na ndoto za kurudi shule na kujipatia elimu ili niweze kupata ajira yenye hadhi na wajibu mkubwa zaidi, ambao kwa kawaida huambatana na malipo makubwa zaidi. Kwa kuona dalili za kuzeeka zikianza, nilianza kupata mashaka iwapo nitakaa niyafikie matumaini hayo.
Mawazo hayo yalitembea kichwani mwangu jana tu, leo nilipata majibu. Tulikuwa nje ya hoteli yangu, tukibishana na Bushiri Mtanashati, au Abdallah Jongo, juu ya kumpa fedha zingine za kile alichokiita ‘kukamilisha’ mikakati ya safari. Nilimkatalia katakata na kumwambia wazi kuwa hata safari yenyewe naifikiria kwa mara ya pili.
Alinitazama kwa macho yake makali, yaliyowekwa katika hali ya kunitisha na kunihurumia pamoja. Kisha, kwa sauti ya upendo aliniambia, “Mdogo wangu naona hujipendi. Hizo fedha zitakusaidia nini kama kila uendako unafuatwa na
kivuli cha mauti? Angalia, utakufa siku si zako.”
Mie pia uvumilivu ulianza kunishinda. “Hivi wewe ni nani hasa hata uwe na kauli juu ya kifo au uhai wangu?” Nilimuuliza. “Wewe ni nani?” niliongeza, “Mungu au Shetani?”
Kauli yangu ilimshangaza kuliko kitu kingine chochote kile. Macho yake yalibadilika na kuwa makali kama simba aliyeona kila dalili ya windo lake kupokonywa. Alifungua mdomo wake kutaka kutamka jambo. Lolote alilotaka kusema lilitoweka pale tulipowaona tarishi watatu wa bomani, walipotujia na kusimama kwa namna ya kutuzingira.
“Toeni vipande vyenu,” tarishi mmoja kati yao aliamuru baada ya kutuuliza majina yetu.
Nilimwona Bushiri Mtanashati akitetemeka. “Vipande gani?” aliuliza.
“Vipande vya kodi,” alifafanua.
“Kodi?” niliropoka. “Ilikuwa mara yangu ya kwanza maishani kuulizwa kodi. Ni hapo nilipobaini kuwa utoto ulikwishanitoka na nimeingia ukubwani. “Lakini mimi sijaanza kulipa kodi,” nilijitetea.
“Kwa nini?” Yule msemaji wao alihoji.
“Mimi bado. Umri haujafika. Isitoshe mimi ni
mwanafunzi.”
Askari huyo na wenzake waliangua kicheko. “Umri bado!” mmoja wao alisema.
“Mwanafunzi!” mwingine alitamka “Mwanafunzi!” aliongeza yule msemaji wa kwanza. “Tunakuona mwaka mzima hapa unafanya kazi mbalimbali, leo umekuwa mwanafunzi! Pita huku!” Nilielekezwa upande ambao kulikuwa na watu wengine kadhaa, bila shaka mateka kama mimi.
Nikaenda na kujiunga nao.
“Na wewe?” walimgeukia Bushiri Mtanashati.
Huku akitetemeka alijishikashika mifukoni na kuchomoa pochi yake ambayo ilikuwa na vyeti na nyaraka zake kadhaa. Alitoa mojawapo kwa wasiwasi na kuitazama. Akataka kuirejesha mfukoni. Tarishi mmoja akawa mwepesi wa mkono. Aliipokonya pochi hiyo na kutoa nyaraka hizo ambazo alizisoma taratibu na kisha kumtazama Bushiri kwa mshangao.
“Inaonekana umelipa kodi mara ya mwisho miaka miwili iliyopita,” alimhoji.
Bushiri alikubali kwa kichwa.
“Halafu,” tarishi huo aliongeza akiwa kamkazia macho, “Umesema jina lako ni nani vile?”
Bushiri alibadilika. Niliona akitokwa na jasho huku miguu yake ghafla ikionyesha kukosa nguvu za kukibeba kiwiliwili chake. Alifunua mdomo kutaka kutamka neno ambalo halikutamkika au kusikika.
Tarishi alimkazia macho. “Hujui jina lako?” alimuuliza
tena.
Tarishi wengine walivutiwa na mjadala huo. Wakakiomba
kitambulisho hicho na kukitazama kwa zamu. Kila mmoja alitikisa kichwa huku akimtazama Bushiri.
“Za mwizi arobaini,” mmoja wao alisema. “Arobaini za leo zimetimia. Unajiita Bushiri Mtanashati wakati jina lako ni Abdallah Jongo! Jongo tunayemfahamu sisi, ambaye anatafutwa kwa miaka miwili sasa ni mhalifu aliyemwibia mwajiri wake fedha nyingi kule Pangani. Kumbe muda wote umejificha hapa? Twende,” walisema wakimkamata na kumtia pingu.
“Naomba nizungumze faragha na mdogo wangu,” Bushiri au Abdallah alisihi akinitazama mimi.
“Nani mdogo wako? Huyu?” Waliuliza.
“Mimi siyo mdogo wako” niling’aka mara moja. “Nimemfahamu hapahapa, tena kwa jina la Bushiri Mtanashati. Hatuna uhusiano wowote wa damu wala kabila.”
“Mtanashati sio?” Tarishi mmoja alisema akicheka. “Basi atafanya utanashati wake akiwa jela. Wewe suala lako ni dogo. Tutakupeleka bomani ukalipie kodi ya faini. Kama huna utapelekwa manamba, Tanga, ukajifunze kutafuta fedha kwa kukata mkonge.”
***
Safari ya Kilwa ilikufa. Safari ya Tanga ikazaliwa. Nilikuwa katika kundi la watu wasiopungua arobaini, wenye umri tofauti, waliokuwa wakiisubiri safari hiyo. Nadhani mimi nilikuwa mdogo kuliko wote kiumri. Lakini kwa ajili ya umbile langu niliweza kujumuika katika kundi hilo bila ya yeyote kunishuku.
Sikuwa na sababu kubwa ya kuwemo katika kundi hilo. Nilikuwa na fedha ambazo zingetosha kulipia kodi na bado nikabakiwa na akiba. Aidha, barua ile ya Chifu Masanja na madaftari yangu toka shule yangu ya awali Uhayani, ambayo niliyatunza kama roho yangu, vingetosha kumwonyesha mkubwa wa hapo bomani na angeniachia mara moja. Lakini sikufanya hivyo. Sikuona haja yoyote ya kubakia kusini, ambako sikuwa na kazi wala mipango yoyote inayoendelea kiuchumi au kielimu. Hivyo, sikuona ubaya wowote kusafiri bure, ukihudumiwa chakula na matibabu, hadi katika nchi mpya maishani mwako. Si kuna mhenga mmoja aliyepata kusema kuwa bahati ya mwanaume iko kichwani, miguuni na mikononi mwake? Huwezi jua, pengine huko ambako miguu yangu inanielekeza ndiko iliko bahati yangu.
Hilo ni moja. La pili lililofanya nipokee masaibu hayo ni umbali wa huku nyumbani. Lakini habari za watu wengi wa kutoka kwetu waliokwenda huko kwa njia na mazingira kama haya zilikuwa nyingi. Wengi wao wakiwa wamelowea hukohuko na kufanya makazi ya kudumu. Hivyo, uhakika wa habari na hata uwezekano wa kusafiri toka huko hadi nyumbani ulikuwa mkubwa sana.
Ni kwa mtazamo huo ndipo niliufyata ulimi wangu nisiweze kujitetea na baadaye kukusanya vitu vyangu vyote ambavyo ningesafiri navyo kuelekea Mashariki ya Tanganyika.
Tulisubiri safari kwa takribani wiki nzima, tukiwa tumefungiwa katika ukumbi mmojawapo wa Bomani. Mtu mmoja ambaye sikupata kumfahamu alikuwa ameingiza nakala mbili tatu za magazeti ya Ngurumo na Mamboleo ambayo hayakuwa na msomaji zaidi yangu. Gazeti jingine la lugha ya kiingereza, Tanganyika Standard, ambalo lilikuwa limeanza mwaka 1930 niliweza kupata nakala yake ya miezi kadhaa iliyopita. Ingawa nililisoma kwa taabu kidogo kutokana na kiwango changu cha lugha ya Kiingereza bado nililielewa na kunivutia kwa habari zake.
Bila mwenyewe kuwa na habari, tabia hiyo ya kujisomea kwangu ilivuta macho ya mateka wenzangu pamoja na watekaji wenyewe. Afisa mmoja Mzungu alipotembelea makazi yetu kukagua afya zetu aliponikuta nimejiinamia nikisoma Tanganyika Standard alishangaa sana. Alishangaa zaidi pale aliponihoji maswali mawili matatu kwa Kiingereza na nikamjibu vizuri. Akaniuliza kwa nini niko pale. Nilipomjibu kuwa ni tatizo la kodi alitikisa kichwa kwa masikitiko na kuondoka zake. Baada ya tukio hilo nilianza kupewa jukumu la ukarani kwa kuratibu mambo mbalimbali ya manamba wenzangu,
kuwaelekeza wagonjwa matumizi ya dawa walizopewa na wakati mwingine ukalimani kwa wageni ambao hawakufahamu kiswahili.
Sikubahatika kumwona tena bwana Bushiri Mtanashati au Abdallah Jongo. Tangu pale alipotiwa pingu na kuburuzwa huku akinitupia jicho la ‘kwa heri’ lililoonyesha chuki na hasira dhidi yangu kwa kile alichokichukulia kama kumsaliti, alitupwa gerezani kusubiri safari ya pwani kujibu tuhuma dhidi yake. Kwa jumla, nilishukuru kutengana naye, kwani nilihisi kuwa angenielekeza shingoni badala ya kileleni. Ndiyo, alinishauri mengi juu ya masibu katika maisha. Lakini gharama ya ushauri wake ilikuwa kubwa kuliko mahitaji halisi. Kwa vyovyote vile, kama ningeendelea naye ningejikuta katika lindi kubwa la umasikini pengine na madeni pia badala ya faraja aliyoniahidi. Kubainishwa kwake mapema kuwa ni mtu wa aina gani kuliniokoa na mengi.
Safari ilianza alfajiri ya siku ya nane toka tulipokamwatwa. Tulisafirishwa kwa lori kuukuu, ambalo mlio wake ulinikumbusha lori la hayati Ayubu ambalo nililitumikia kama kondakta kwa muda mrefu. Sasa tulikuwa zaidi ya watu tisini baada ya wengine kuletwa siku mbili kabla ya safari. Tulijazwa nyuma ya lori hilo, watu na mizigo yetu na kung’ang’ania kuta za bodi ili kujiepusha na kuanguka kwa kuyumba kwa gari kulikosababishwa na ubovu wa barabra. Ilikuwa safari yangu nyingine ngumu, ndefu na ya kukatisha tamaa. Lakini Mungu si Athumani, siku ya nne tangu tulipoanza safari tulifika Muheza ambako tulishushwa ili kusubiri kugawanywa katika mashamba ya mkonge.
* * *
Umepata kulisikia kabila la Wandorobo? Hawa kwa kiasi fulani ni watu wa porini. Wanapenda kuvaa kiutamaduni, pande la ngozi ya nyama (Lusira) au kaniki, ikiwa imefunikwa sehemu tu ya mwili wake. Nywele zao huwa ndefu na hupendelea kuzivuta kwa nyuma. Kwa wanaume mara zote utamwona akiwa ameshika upinde, podo la mishale ubavuni na kishoka, ambacho wenyewe hukiita ‘kitodyo’ mkononi.
Kwa kawaida Wandorobo ni watu wa kuhamahama, mara msitu huu mara ule. Chakula chao kikuu ni nyama za porini, mizizi na asali. Aidha, ni wa matunda ya porini yatokanayo na mimea kama ngabaito na olugumu. Wakati wa mvua Wandorobo hujisitiri kwa kujenga mabanda ya ngozi za wanyama, mfano wa mahema.
Watu hawa ni mashujaa wa aina yake. Si waoga, hivyo hawapendi au kujali sana umoja. Mtu na mkewe wanaweza kukaa porini kwa miaka bila hofu wala kuhitaji msaada wa watu wengine. Inaaminika pia kuwa wana uwezo mkubwa wa kutumia miti shamba kuyatawala mazingira yao kiasi cha wanyama wakubwa kama simba, chui na majoka kuwakimbia.
Kuna hadithi nyingi za miujiza ya watu hawa. Moja ni ile inayosimulia juu ya wawindaji saba walioingia katika msitu mmoja mkubwa kwa matarajio ya kupata wanyama. Si kwamba hawakufanikiwa tu, bali pia walipotea mchana kutwa wasiweze kujua njia ya kurudi kwao. Ulipofika usiku, wakiwa wamekata tamaa waliona mbuyu mkubwa wenye pango kwenye shina, ambalo lingetosha kuifadhi watu kumi na wa tano au zaidi. Wawindanji hao waliingia katika pango hilo kwa matarajio ya kupitisha usiku. Ikatokea kuwa pango hilo lilikuwa makazi ya joka kubwa aina ya chatu. Lilirejea na kuingia pangoni humo. Wawindaji wale, kwa hofu kubwa walitimka mbio kila mmoja akikimbilia anakokujua, kuokoa roho yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment