Simulizi : Mtambo Wa Mauti
Sehemu Ya Tano (5)
“Tutawahi,” Joram alisema akiendelea kuyakodolea macho maajabu aliyokuwa akiyaona katika kompyuta hiyo.
“Tano!”
Joram alichukua diski mpya na kuanza kunakili yale aliyokuwa akiyaangalia.
“Nne!” “Tutawahi?” “Bila shaka.”
“Tatu!”
“Mbili!”
“Una hakika Joram?” “Bila shaka yoyote.”
Alikuwa tayari amemaliza kunakili. Aliificha diski moja chini, katika kipoza hewa, huku jicho lake likiitazama screen, la pili likiwaangalia polisi ambao sasa walikuwa wakishughulika na mlango wa mbele wa nyumba yake. Joram aliupeleka mkono wake katika tufe moja chini ya kompyuta hiyo. “Sasa ni wakati wangu wa kuwapa polisi zawadi yangu ya kusisimua,” alisema huku akibonyeza kitufe hicho.
Mara tu sauti ya Kambambaya ilipotamka “Moja!” kitu ambacho hakikutarajiwa kilifuatia. Milipuko mikubwa ya mabomu iliibuka ghafla toka sehemu mbalimbali za nyumba hiyo. Polisi waliokuwa tayari wameingia katika eneo la nyumba hiyo, wale waliokuwa nje, pamoja na watu wote walitimka kuziokoa roho zao, Inspekta Kambambaya akiwa mmoja wao. ‘Mona Lisa’ aliduwaa, hasa alipomwona Joram Kiango
akiangua kicheko.
“Ni mabomu yasiyo na madhara yoyote, niliyoyabuni kwa ajili ya mazingira ya aina hii,” alisema huku akimvuta msichana huyo mkono na kumwambia. “Ni wakati wetu wa kuondoka katika nyumba hii.”
Akiwa tayari amezima jenereta lake, watu wakikimbia huku na huko mitaani, Joram, kwa kutumia vijia vyake vya siri, alimwongoza Margareth kupenya taratibu hadi nje ya nyumba; nje ya ua na nje ya eneo hilo.
***
Ilimchukua Inspekta Kambambaya dakika moja baadaye kuelewa kuwa mabomu hayo yalikuwa ya bandia. Ilimchukua dakika moja nyingine kuwakusanya vijana wake wote. Mmoja alichoropoka toka huku, mmoja toka kule; wote wakiwa wamechakaa kwa uchafu baada ya kujirusha hapa na pale, katika maeneo ambayo walidhani yangepunguza madhara ya mabomu hayo.
Kambambaya mwenyewe, mara mlio wa kwanza wa bomu uliposikika alichupa chini na kutambaa hadi nyuma ya mbuyu
uliokuwa kando. Bastola yake ikiwa tayari mkononi, macho yake yakiwa wazi, aliyatumbua kuangalia kitu ambacho kingefuatia; mlipuko mkubwa wa moto, wingu zito la moshi na kuporomoka kwa majengo. Haikuwa hivyo. Ndipo alipoelewa kilichotokea.
“Tumechezewa akili. Hizi ni mbinu za Joram Kiango. Ama anajaribu kutoroka ama tayari ametoroka. Tawanyikeni mara moja kuziba kila njia na kila uchochoro unaotoka nje ya eneo hili. Wale mliokuwa na jukumu la kuingia ndani fanyeni hivyo mara moja. Kumbukeni, namtaka akiwa hai,” aliamuru.
Hata kabla maelekezo yake hayajatulia vizuri katika vichwa vyao jambo la ajabu zaidi lilitokea. Anga ambalo lilikuwa kimya na tulivu, ghafla lilipata uhai. Ndege mbili za kivita ziliibuka ghafla na kulizunguka eneo hilo mara mbili kabla ya kuachia miale ya moto ambayo iliilenga nyumba ya Joram Kiango.
Kambambaya hakupata kuona kitu cha aina hii katika uhalisia wake. Dakika iliyopita mbele yake kulikuwa na nyumba, ambayo alikuwa akiwaelekeza vijana wake waivamie. Dakika iliyofuata hakukuwa na nyumba. Mabomu ya mfululizo yameiteketeza kabisa na kuacha kifusi cha majivu na moto kidogo hapa na pale; Ndege zilizofanya kazi hiyo tayari zikitokomea kuelekea zilikotokea.
Nini hiki! Kambambaya alijiuliza akiwa ameduwaa. Kwa mara ya kwanza katika uhai wake, hakujua la kufanya wala kusema.
Angeweza kuapa kwa kichwa chake kuwa aliiona nembo ya Jeshi la Ulinzi la Tanzania chini ya moja ya ndege zilizofanya shambulio hilo. Ingawa hakuwa mtaalamu sana wa masuala ya anga, lakini alikuwa na hakika kuwa ndege alizoziona kama hazikuwa F-7 au F-6 basi zilikuwa F-5 MiG 17UTI zilizonunuliwa toka China, mtengenezaji wa awali akiwa Mrusi.
Nini hiki! Alijiuliza tena.
W 10 X
SIKU huo haukuwa wa kawaida jijini Dar es Salaam na Tanzania nzima. Taarifa za nyumba kuteketezwa kwa mabomu, tena yaliyofyatuliwa na ndege za Jeshi
la Wananchi wa Tanzania zilimwacha kila mtu taabani kwa namna yake.
Wako raia ambao hawakujua kilichotokea,wale ambao waliona tu miale mikali ya moto ikifuatiwa na kishindo kikubwa na kisha, kimya cha kutisha. Wako majirani na wakazi wengine wa eneo la Bunju waliziona ndege hizo zikiibuka na kuelea ghafla angani, kabla hazijalipua mabomu ambayo yaliliteketeza jumba zima na eneo la mraba lisilopungua ekari moja; na kulifanya ligeuke jivu. Hawa walipatwa na kiwewe. Waliokuwa mitaani walikimbia huku na huko, waliokuwa majumbani walikusanya watoto na vitu vyao tayari kukimbilia wasikokujua; wakiamini kuwa vita vimeanza; Dar es Salaam imevamiwa. Wachache miongoni mwa hawa, waliokuwa jasiri zaidi, walipata muda wa kuzikumbuka simu zao na kupiga huku na huko, jambo lililosaidia sana kusambaza hofu na mashaka katika jiji zima na nchi nzima.
Mitandao ya simu ilijikuta ghafla ikiwa na kazi nzito nusura ishindwe. Huyu alitaka kuongea na yule, yule alitaka kumwarifu huyu; na kadhalika.
Viongoz wa ngazi za juu ndio waliokuwa taabani zaidi. Simu
za mawaziri, wakuu wa vikosi vya usalama na vya ulinzi, watu wa Usalama wa Taifa na wengineo hazikupumua hata kwa sekunde moja.
Na kwenye orodha hiyo Kambambaya alishika namba ya juu. Wakati simu yake ya ofisini ikiita mfululizo bila kupumua, simu ya mkononi nayo kila alipoikata baada ya kuzungumza na mtu mmoja ilinguruma tena. Kilele cha simu hizo kilifikia pale Rais wa Jhamhuri mwenyewe alipompigia tena kutaka ufafanuzi.
“Nadhani operesheni hiyo ulikuwa ukiiongoza mwenyewe, Inspekta,” Rais alisema kwa utulivu, lakini taharuki ikiwa wazi ndani yake.
“Ni kweli, mzee.”
“Na pia naambiwa hadi sasa uko katika eneo la tukio.” “Kweli kabisa.”
“Niambie,” sauti hiyo iliongeza. “Kitu gani hasa kimetokea? Hapana, usinieleze kuwa nyumba hiyo imelipuliwa na ndege za kijeshi. Wala usinieleze kuwa ndege hizo ni za JWTZ. Hayo nimekuwa nikielezwa na kila ninayezungumza naye. Ninachotaka kuelewa ni kitu kimoja tu; nani aliyetoa amri ya kurusha ndege hizo na kulipua nyumba ya raia wangu mwema. Hilo tu.”
Kambambaya alikuwa na jibu rahisi sana. Neno moja tu; Sijui. Lilikuwa jibu lake pekee, jibu ambalo yeye pia amekuwa akilipata toka kwa kila aliyempigia simu kumuuliza swali lilelile ambalo Rais ameliuliza. Ilikuwa kama muujiza! Kila mtu alidai kuwa hajui! Mkuu wa Majeshi hajui! Mkuu wa Kikosi hajui! Kumbe hata Amiri Jeshi Mkuu pia hajui!
“Unasikia, Inspekta?” sasa Rais alikuwa akifoka. “Ndiyo, Chifu.”
“Nasubiri jibu lako.” “Kwa kweli. Mzee, si…”
“Sikiliza Inspekta,” Rais alimkatiza. “Inaelekea nchi imetushinda kuendesha. Acha kila unachokifanya tangu sasa. Badala yake wewe na wakubwa wenzako wote nawataka hapa Ikulu saa moja kuanzia sasa. Tumeelewana?”
“Ndiyo, Chifu.”
Mara tu baada ya Rais kukata simu, iliita tena.
“Nani mwenzangu?”
“Mimi ni mwandishi wa habari. Naitwa…”
Kambambaya alikata simu na kuizima kabisa. Ilikuwa rahisi kwake mara mia moja kumkabili Rais aliyekasirika kuliko mwandishi yeyote wa habari kwa wakati huo.
***
“Ni yeye!” “Una hakika?”
“Bila shaka yoyote. Namfahamu vilivyo. Amemshika kila mtu na ana uwezo wa kumnunua mtu yeyote kwa bei yoyote,” Margareth alifafanua huku ameushikilia mkono wa Joram Kiango, ambaye alikuwa bado ameduwaa; bado hajui kama alipaswa kuyaamini macho yake kwa kile anachokiona au la. Alikuwa ameshuhudia ndege mbili za kivita zikiibuka ghafla toka upande wa magharibi ya Dar es Salaam na kuelea juu ya nyumba yake. Kwa macho yake mwenyewe alishuhudia nyumba yake ikiteketezwa kwa mabomu na kufutika kabisa juu ya ardhi, kitendo ambacho awali kilimfanya aduwae; kisha akurupuke na kuanza kukimbia kuiendea nyumba hiyo. Kama Margareth asingemzindua kwa kumshika mkono, pengine bomu la mwisho lingemkuta akiwa amesimama katikati ya
magofu ya iliyokuwa nyumba yake.
Kichwani Joram alijaribu kufanya tathmini ya harakaharaka ya hasara aliyoipata. Hakuona kama inathaminika. Tatizo halikuwa jengo au gharama yake, la hasha! Kilichomtesa akilini hasa ni maabara yake ambayo ilisheheni vifaa vyake mbalimbali vilivyomsaidia katika kazi zake. Pamoja na maabara, maktaba yake iliyosheheni kumbukumbu na nyaraka mbalimbali pia ni kitu kingine kilichoiumiza sana roho yake. Ingemchukua maisha yake yote yaliyobakia kujenga upya maktaba kama ile. “Kwa hiyo, sio kwamba tunashughulika na mtu hatari tu,
bali mtu ambaye pia ni kichaa,’ Joram alisema. “Kichaa! Tena asiyestahili kuendelea kuishi.” “Nani aliyekuambia kuwa kesho ataliona jua?”
Joram alikitupia jicho la mwisho kifusi cha iliyokuwa nyumba yake. Kisha, akageuka na kumwambia Margareth, “Twen’zetu,” huku akimvuta mkono. Alimwongoza katika vijia
vya uchochoroni vilivyowawezesha kufika Boko na, hatimaye,
Tegeta Kibaoni; bila matatizo yoyote.
Hapo Kibaoni, homa ya hofu ikiwa bado imetanda huku na huko, Joram haikumchukua muda kupora gari ambalo lilikwishasahauliwa kituoni. Milango ilikuwa imeachwa wazi, ufunguo wa kuwashia ukining’inia katika tundu lake. Hivyo, mara baada ya Margareth kuingia Joram aliliwasha kwa utulivu na kuliondoa taratibu, kama lake.
“Atatusamehe!” Joram alinong’ona. Tuko katika majukumu ya kitaifa!”
“Ya kimataifa!” Margareth alimkumbusha.
“Naam, ya kimataifa!” Joram alirudia. Kisha, alimgeukia msichana huyo na kumwambia taratibu, “Tuna wasaa mfupi wa amani. Baadaye tutakuwa katika kazi ngumu. Huwezi kujua. Wote yunaweza kupoteza maisha, au mmoja wetu. Unaonaje tukiutumia wasaa huu ili unifafanulie kwa mapana zaidi yote yale ambayo siyafahamu baina yako na hayati Mona Lisa na kisha juu ya uhusiano wako na huyu mnyama tunayemtaka?”
“Lipi zaidi unalohitaji kujua Joram?” Magreth alisema akitabasamu. “Unataka kujua ilikuwaje nikampiku Mona Lisa uliyemjua na kumpenda kabla yangu? Hilo si tayari tumelizungumza? Si nimekuambia kuwa mimi na yeye tulikuwa damu moja na roho moja? Kila alichokipenda mie pia nilikipenda. Kwa bahati tulilelewa katika mazingira tofauti. Kwake yeye kusema uongo, ilikuwa dhambi kubwa, kufanya mapenzi kabla ya ndoa ilikuwa ni laana isiyostahimilika. Hivyo ule mchezo wangu wa kuichukua nafasi yake hadi juu ya kitanda chako ilikuwa moja ya mizaha mingi niliyokuwa nikimfanyia ndugu yangu bila yeye kujua. Nilijua kamwe asingekuridhisha kimwili na nilivyokujua wewe si mtu wa kuoa.”
Margareth alibadilika kidogo, tabasamu likiuacha uso wake pale alipoongeza, “Kwa bahati mbaya sana, nilijikuta nimekupenda. Sijui ni baada ya kubaini kuwa wewe ndiye yule Joram Kiango ambaye nimekuwa nikisoma sifa zake au la. Nilijikuta nimekupenda vibaya sana. Hata kwa mara ya kwanza nilianza kumwonea wivu dada yangu. Mungu
atanisamehe.” Baada ya maneno hayo alimwangukia Joram kifuani na kumkumbatia huku akimnong’oneza kwa sauti ndogo, “Sina bahati… Sikuwahi kuwa na bahati maishani mwangu. Naamini Mona Lisa atanisamehe… Amekuwa akinisamehe maisha yake yote… Wewe utanisamehe, Joram?”
Alisema huku machozi yakimlengalenga na kuteleza juu ya mashavu yake laini.
Kama sauti yake, sura yake pia ilikuwa imebadilika. Katika macho au hisia za Joram Kiango aliyekuwa akiyasema hayo hakuwa yule Mona Lisa machachari, Mona Lisa katili mwenye bastola kibindoni, Tayari kuua… Tayari kufa… Huyu alikuwa Mona Lisa wake! Mona Lisa halisi; mpole, mtaratibu na mwenye haiba.
Masikioni, Joram alisikia maneno mengine kabisa. Aliisikia sauti ya Mona Lisa pale alipopata kumwambia, Hujui Joram. Hujui, huelewi. Na huwezi kuelewa… Sijui kitu gani kinanitokea. Lakini naamini nimekuweka katika hatari kubwa…
Pamoja na hisia zote alizokwishajenga juu ya pacha hewa, Mona Lisa na Margareth, pamoja na kuziamini hisia hizo, bado Joram alijikuta akihitaji kuisikia sauti ya Margareth mwenyewe ikimtengulia kitendawili hicho. Hivyo, alisimamisha gari kando ya barabara na kumwambia, “Ndiyo, tunahitaji kuzungumza.”
Margareth aligeuka kumtazama usoni. Sekunde kadhaa zilipita bado kamtumbulia Joram macho. Kisha, taratibu, machozi yalikoma kumtoka na tabasamu jipya kuanza kuchanua usoni mwake. Halikuwa tabasamu lile ambalo Joram alilishuhudia muda mfupi katika uso huo. Hili lilikuwa tabasamu jembamba, lisilopendeza hata kidogo, tabasamu ambalo lilifuatiwa na swali, “Bado tu unataka kunifahamu kwa mapana zaidi? Sijawahi kumsimulia mtu yeyote duniani ukweli kuhusu maisha yangu. Mona Lisa, ndugu na rafiki yangu pekee amekufa bila hata kujua kama ana ndugu. Kwa kuwa leo unaweza ukawa usiku wangu wa mwisho duniani nitakusimulia. Lakini lazima nikuonye mapema. Jiandae kusikia moja ya hadithi chafu, za kutisha na kusikitisha. Baada ya kuutua mzigo huu nitakuwa tayari kumfuata dada yangu, ili kama tutaonana tena huko aliko niweze kumtaka
radhi.”
Joram alikuwa akisubiri.
“Hujali kusikiliza hadithi mbaya Joram?” Margareth alimuuliza. “Usije ukajilaumu baadaye.”
***
“Ilinichukua miaka kumi na sita ya umri wangu kujua kuwa mimi ni Mtanzania, mimi ni pacha na kuwa ndugu yangu alikuwa hai, hapahapa Tanzania,” Margareth alieleza.
“Awali ya hapo nililelewa kwa uongo na kuamini kila nilichoambiwa. Walinifanya niamini kuwa mimi ni yatima niliyetelekezwa na mama yangu mzazi hospitalini, mara tu baada ya kujifungua, kwamba, mama baada ya kitendo kile cha kunitelekeza katika hospitali moja Entebe, alipotelea katika madanguro ya wanawake Malaya mjini Kampala. Msamaria mmoja aliyekuwa safarini kuelekea Nairobi aliniokota na kunipeleka Nairobi ambako alinikabidhi katika himaya ya watunzaji wa watoto yatima. Huko ndiko nilikopata mfadhili mwingine, tajiri, aliyenichukua na kunipeleka katika shule mbalimbali za kimataifa. Mfadhili huyo baadaye alichukua nafasi ya baba na mama yangu na kuhalalisha jambo hilo kwa mujibu wa sheria za Kenya.”
Margareth aligeuka na kutazama nje ya gari kwa muda. Kisha, alimgeukia tena Joram na kuendelea, “Robo tatu ya hadithi hiyo ni uongo, Joram, uongo mtupu. Mimi sikuwahi kuwa yatima wala sikupata kutekelezwa na mama. Mama yetu alitupenda sana na alitulea vizuri sana hadi walipomwua kikatili, wakayatupa maiti yake katika ziwa Victoria na kututenganisha, mimi na mdogo wangu.
Kwa mujibu wa maelezo yake mama yake, msichana ambaye alikuwa akijiandaa kufanya mtihani wake wa kidato cha nne, alipewa mimba na padre wa kanisa moja mjini Bukoba. Alimwendea padre huyo kwa ajili ya kuungama lakini padre akamshawishi kufanya naye mapenzi, jambo lililopelekea apoteze bikra yake na kupata ujauzito. Kutokana na hofu ya kupoteza upadri na hata kufungwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania padre huyo alimsihi sana msichana huyo kutomtaja. Badala yake alimtoroshea mjini Mwanza
ambako alimficha katika moja ya hoteli za kitalii na kuanza kumhudumia mahitaji yake yote huku akimshawishi kuitoa mimba hiyo, “Jambo ambalo mama alikataa katakata.”
“Vishawishi vilipoanza kukoma na vitisho kuchukua nafasi yake mama aliamua kuondoka hotelini hapo, akaenda kujificha Igoma alikokuwa akiishi shangazi yake mmoja. Shangazi huyo alimlea vizuri na kuhakikisha anajifungua salama, mapacha wa kike, mimi nikiwa mmoja wao. Tulipofikia umri wa miezi miwili shangazi alitusafirisha kurudi nyumbani ambako wazazi wa mama walitupokea kwa furaha zote hata wakaandaa sherehe kubwa iliyoambatana na vinywaji anuwai.”
“Sherehe hiyo ilikuwa mwanzo wa balaa. Ingawa mama alikuwa hajapata kumtaja mtu aliyehusika na ujauzito wake, lakini minong’ono iliyokuwa ikitembea ilisafiri huku na huko hata kumfikia padre huyo, kuwa anahusika. Alipatwa na hofu kubwa hata akaanza upya kubuni mikakati ya kusafisha jina lake.”
“Ikaja siku moja,” Margareth aliongeza. “Mama na watoto wake walitoweka. Tulitafutwa huku na huko bila mafanikio. Wiki moja baadaye mama aliokotwa akielea juu ya Ziwa Victoria, sehemu kubwa ya mwili wake ikiwa imeliwa na samaki. Miili ya watoto haikuonekana. Watu wakachukulia kuwa tayari tuliliwa na sangara. Upelelezi wa ndugu za mama na vyombo vya dola haukufanikisha kumtia yeyote hatiani. Hadithi ikawa imeshia hapo.”
Lakini kwa upande wa watoto huo haukuwa mwisho bali mwanzo wa sura ya pili ya maisha yao. “Yaelekea mtu au watu waliopewa jukumu la kutuangamiza alituonea huruma. Badala ya kutuua pamoja na mama alitutorosha hadi Mwanza. Huko, kweli alitukabidhi katika kituo kinachojihusisha na watoto yatima KULEANA. Nao wakiwa hawana ujuzi wa kushughulika na watoto wenye umri kama wetu, walitupeleka hospitali ya Bugando ambako tuliishia katika mikono ya akina mama huruma wa Kanisa la Katoliki. Tukajiunga na jamii mpya, jamii inayochipukia, ya watoto yatima. Muda waliojiwekea wa kusubiri watu waliopotelewa na watoto wao wajitokeze na kututambua ulipopita tuliorodheshwa rasmi na kuanza kutafutiwa wafadhili.”
“Miezi sita baadaye, mimi nilipata mtu ambaye alikuwa tayari kunilea. Nadhani, kwa lugha sahihi, nilinunuliwa kwani nilikuja kubaini baadaye kuwa kwa kutumia mawakala, au kwa majina tofauti mfadhili wangu alichukua zaidi ya watoto mia moja, katika nchi na miji tofauti duniani na kuwapeleka huku na kule kulingana na mahitaji ya mtoto. Tuliokuwa wachanga tulipatiwa vituo vya kulelea watoto ambavyo ama alivipata vizuri ama alivimiliki.”
“Mfadhili huyu hakuwa na tatizo la fedha. Tuliishi vizuri sana, wenye akili tukitafutiwa shule na vyuo vya maana popote duniani.”
“Mfadhili huyu alikuwa msiri sana. Si kwamba alihakikisha kuwa sisi tulio katika himaya yake hatujuani peke yake, bali sisi wenyewe hatukumjua. Mimi binafsi nilikujamwona kwa macho nikiwa na miaka kumi, darasa la tano. Alikuja shuleni kwetu usiku. Nikaitwa na kutambulishwa kwake kama baba yangu. Wakati huo sikuweza kumwona vizuri, lakini nilihisi kuwa ama alikuwa mtu mweupe sana ama chotara. Alizungumza nami kwa kiingereza kizuri, akiniomba radhi kwa kutoonana naye mara kwa mara. Akaniambia kuwa mama alifariki wakati wa uzazi wangu lakini yeye amenilea na atanilea vizuri kwa kadri ya uwezo wake. Kuwa itakuwa vigumu kuonana naye mara kwa mara lakini popote alipo atanikumbuka. Akanitaka nikazane na masomo yangu kwa kuwa amenitegemea sana katika urithi wa shughuli zake.”
“Nilirudi bwenini nikiwa nimejawa na furaha kubwa kwa kubaini kuwa kumbe sikuwa yatima wala mtoto wa mtaani. Nilikuwa na baba! Baba mwenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na mapenzi mazito kwangu! Furaha hiyo ilinifanya niongeze juhudi katika masomo na majukumu yangu yote hata nikaondokea kuwa mwanafunzi bora karibu katika kila somo.” Margareth alionekana kuwaza kwa muda kabla hajaendelea, “Mabadiliko yangu ya kitabia yalikwenda sambamba na yale ya kimaumbile ya kitoto yakitoweka na taratibu niliibukia kuwa msichana mzuri ambaye kila mtu, hata wasichana wenzagu, walinimezea mate. Nilimaliza elimu ya sekondari kwa taabu kutokana na vishawishi vya walimu na wanafunzi wenzangu. Nilisoma Chuo Kikuu kwa shida kwa ajili ya usumbufu wa
wanafunzi na hata maprofesa wangu. Nikajifunza kushindana na vishawishi hivyo hata nikawa sugu, asiyebabaishwa na lolote.”
“Katika miaka yote hiyo ya sekondari na chuo sikumwona baba, zaidi ya kupokea simu zake na zawadi za mara kwa mara. Nilipojaribu kuwasiliana naye nilikosa mafanikio kutokana na simu zangu kupokelewa na makarani wake ambao walikuwa na kila aina ya majibu; mara, “Yuko mkutanoni,” mara, “Amesafiri,” mara, “Acha namba atakupigia,” nakadhalika.
“Furaha niliyokuwa nayo juu yake ikaanza kufifia.”
Walikutana tena na baba yake wakati Margareth akisheherekea shahada yake ya pili huko Montreal, Canada. Mzee alitokea ghafla chuoni na kumtafuta. Margareth alipofika mbele yake alionekana kutahayari waziwazi kwa uzuri wa sura na umbile lake.
“Mpenzi… mpenzi wangu…” alitamka akimbusu na kisha kumkumbatia. “Nakwambia mimi na wewe tutafanya makubwa duniani.”
Alimhamisha Margareth toka chuoni hapo usiku huohuo na kumpeleka katika mojawapo ya mahoteli makubwa. Alimchukulia chumba bora zaidi hotelini humo na kumkabidhi kadi ya benki yenye maelfu ya dola.
“Toka hapo hakuniacha tena. Kila jioni alifuatana nami sehemu mbalimbali za starehe na kuninunulia mvinyo huku yeye akinywa wiski. Kauli yake kubwa ilikuwa moja tu siku zote, “… mimi na wewe tutafanya mambo makubwa …” kila nilipopata wasaa na kumdodosa juu ya mama yangu alikwepa kuzungumza lolote kwa kisingizio cha ‘Usinikumbushe, iko siku tutazungumza.’
Margareth alisita kwa muda mrefu tena kabla hajayafumba macho yake na kisha kunong’ona kama anayezungumza peke yake, “Halafu ukaja ule usiku ambao alinibaka.” Alinyamaza kwa muda kama anayesikiliza kwa mara nyingine maumivu ya usiku huo.
Joram alitulia, akisubiri pasi ya kumhimiza.
“Usiku ambao kamwe sitausahau,” Magreth aliendelea, “Tulikuwa Florida, Marekani. Kutwa hiyo nzima alionekana mtu mwenye furaha tele. Hakukubali nimwache walao kwa
dakika chache. Muda mwingi aliutumia kwa kunywa wiski zake, mara chachechache akiinuka kwenda kupiga simu. Mimi pia alinishawishi kunywa kitu chenye nguvu zaidi ya ule mvinyo niliouzowea. Nilikataa, nikiendelea na kinywaji changu cha kawaida. Nadhani alitumia mwanya fulani kuniwekea dawa za kulevya kwani baada ya muda fulani nilijiona taabani, macho mazito mwili ukiwa umelegea. Nikahisi kumwona akinibeba hadi chumbani kwake ambako alinivua nguo na kunifanyia kile ambacho sikuwahi kufanya maishani.”
“Kesho yake, fahamu ziliponirudia kikamilifu alikuwa bado amenikumbatia kitandani! Mshituko nilioupata haukuwa na kifani. Baba yangu mzazi! Niliwaza kwa uchungu huku nikiangua kilio. Lakini yeye alinibembeleza na kuamua kunitobolea ukweli.”
“Mimi si baba yako Margareth. Wala sina undugu wowote wa damu nawe. Mimi ni mfadhili wako tu, aliyeondokea kukupenda na ambaye siku moja atakuwa mfalme wa dunia hii, wewe ukiwa malkia,” alisema akizidi kunipapasa hapa na pale.”
“Nilitetetemeka, nilichanganyikiwa, nikatamani ardhi ipasuke; inimeze. Nikajikaza na kujaribu kuuficha mshangao wangu ili nimwelewe vizuri zaidi mtu huyo ambaye miaka yote niliamini kuwa ni baba yangu mzazi. Kila alivyojieleza, kila alivyozidi kufafanua harakati zake, ndivyo nilivyozidi kuamini kuwa kichwa chake kilikuwa na aina fulani ya mushkeli. Alijawa na ndoto za ajabu, ndoto za alinacha. Na kila ndoto zake hatima yake ilikuwa ni kuitawala dunia, kuwa mfalme wa dunia.”
“Sikumwelewa. Wala sikuona iwapo ingetokea siku nikamwelewa. Nikaanza kubuni mbinu za kutoroka. Kwa bahati mbaya, sikumjua kwa karibu mtu yeyote zaidi yake, wala sikuwa na ndugu yeyote duniani. Hivyo, nikaamua kujifanya kama niliyeziafiki ndoto zake na kuamua kuishi naye milele.”
“Tuliishi pamoja kwa miezi sita. Hatukuishi muda wote huo kwa mfululizo, la hasha! Alikuwa mtu wa hapa na pale, mtu wa kutoweka ghafla kwa wiki na hata miezi na kurejea ghafla wakati na saa yoyote. Kwa bahati, katika kipindi
hicho nilibahatika kufahamu kuwa asili yangu ni Tanzania, si Uganda wala Kenya kama nilivyoelezwa awali. Toka hapa niliongeza jitihada kubwa za upelelezi hata nikayabaini yote yaliyonihusu, baba aliyenisusa, mama aliyeuawa na pacha mwenzangu ambaye tulitenganishwa toka tungali wachanga. Nikaongeza juhudi. Niliwasiliana na vituo vyote vya kulelea watoto yatima Afrika Mashariki, ofisi zote za Ustawi wa Jamii, shule na vyuo mbalimbali. Juhudi zangu zililipa takribani mwaka mmoja baadaye, nilipoletewa picha ya msichana aliyesimama katika mojawapo ya mitaa ya Dar es Salaam, ambaye ningeweza kuapa kuwa alikuwa mimi. Tulifanana reale kwa ya pili. Nilitetemeka mwili mzima huku nikiangua kilio, hasa baada ya kupewa historia ya msichana huyo kuwa aliitwa Mona Lisa; alilelewa na Wamisionari wa dhehebu la Katoliki, akaelimishwa katika vyuo vyao na baadaye kwenda nchini Uingereza ambako alipata shahada yake ya pili majuzi tu. Kwamba, alikuwa amesomea fani ya uandishi wa habari za kubuni na mengine mengi.”
Joram alihisi akianza kupata mwanga zaidi. Alimkumbuka Mona Lisa na mswada wake wa ‘Ubongo wa Mwalimu Nyerere.’ Alikumbuka msichana huyu alivyomjia na kumtaka ushauri. Akaukumbuka ule mswada mzuri, ambao ungeweza kuwa kitabu cha kusisimua sana kama kile kifo cha kusikitisha kisingemkuta, tena juu ya kitanda chake. Hasira zikampanda na kumfanya amkazie Margareth macho makali yaliyojaa maswali.
Maswali ambayo Margareth aliendela kuyatolea ufafanuzi katika simulizi yake.
“Kiumbe huyu ambaye alianza kama baba kisha akawa mume na baadaye kuondokea kuwa adui yangu mkubwa, siku zote alikuwa na ndoto juu ya nchi hii ya Tanzania. Kila mara aliita, ‘Nchi yangu.’ Wakati mwingine alizungumza hata akiwa usingizini, akiitaja Tanzania. Siku moja alinivuta faragha na kuniambia, “Unafahamu kuwa tutaitawala dunia kutokea Tanzania?” bado sikuweza kumwelewa. Wakati huo tulikuwa tukifanya ziara nyingi za siri humu nchini na kufungua miradi mingi chini ya mwamvuli wa uwekezaji.”
“Wakati hayo yanatokea tayari nilikwishapewa mafunzo
makubwa ya ujasusi, upelelezi na matumizi ya silaha anuwai. Nilipelekwa Israel, Lebanon, Marekani na Pakistan ambako nilikutanishwa na Osama bin Laden ambaye alinipenda ghafla na kujaribu kunirubuni. Nikamwacha, lakini si kabla ya kuchota mengi toka kwake kitaaluma.”
“Taaluma hiyo iliniwezesha kujua na kutumia vitendea kazi vya aina mbalimbali, kimojawapo ikiwa ile pete ya mawasiliano ambayo nilifanya hila hata marehemu akaipokea na kukubali kuivaa akiamini kuwa ni zawadi toka kwa mtu mwingine kabisa, pete ambayo, nikiwa umbali usiozidi kilomita moja niliweza kusikiliza maongezi yake yote bila ya yeye kujua. Kadhalika, iliniwezesha kujua mahala alipo muda wote.”
Margareth alisita tena, kama anayesikiliza maumivu ya hadithi yake mwenyewe. “Lazima nikiri kuwa niliishi kwa taabu sana katika kipindi hicho, Joram,” aliendelea. “Fikiria, ndugu yako wa damu, hujapata kuzungumza naye kwa miaka, toka mlipokuwa mkigombea titi la mama, halafu unamwona, unamsikiliza. Lakini huwezi kujitokeza na kujitambulisha kwake.”
“Kwa nini hukujitokeza?” Joram aliuliza.
Margareth alimtazama Joram kwa mshangao, akamwambia taratibu, “Wewe si mtu wa kuuliza swali kama hilo Joram.”
Ni kweli, Joram aliwaza. Kujitambulisha kwa Mona Lisa lilikuwa ni jambo ambalo Magreth asingeweza kulifanya kwa sababu nyingi sana. Kwanza, alikuwa akiishi katika dunia ile ambayo Wamarekani huiita ‘Underground World’ dunia ya kujificha mchana na kutembea usiku. Kama angejitokeza ingekuwa sawa na Osama bin Laden kuitangazia dunia amejichimbia wapi. Kwa upande mwingine, Joram alifahamu kuwa Margareth alisita kufanya hivyo kwa kuchelea kuhatarisha maisha ya ndugu yake huyo wa pekee duniani. Mwajiri au mfadhili wake alikuwa mtu hatari ambaye asingesita kumuua msichana huyo asiye na hatia kwa ajili ya kulinda maslahi yake. Angemuua kwa kukusudia, si kwa bahati mbaya kama alivyofanya. Lakini, vilevile maisha yao tayari yalikuwa na tofauti kubwa sana. Wakati Mona alikuwa kama malaika, Magreth alijiona kama shetani asiye na lolote la kuzungumza naye.
“Mshenzi yule,” Margareth aliendelea. “Alikuwa ananiamini sana. Lakini pamoja na hayo alikuwa akinificha baadhi ya mikakati yake nyeti. Ni majuzi tu, akiwa amejawa na furaha, aliponiita na kuniambia, ‘Tayari. Hakuna tena kitakachotuzuia kuitawala dunia. Tutaanza na Tanzania. Baada ya muda mfupi tutaichukua Afrika na muda si mrefu dunia nzima itakuwa chini ya himaya yetu.’ Sikumwelewa. Ni kweli kuwa alikuwa na hela, tena nyingi sana na zilizochimbiwa sehemu mbalimbali duniani. Ni kweli pia kuwa alikuwa na mtandano mkubwa; viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijeshi, wasomi na watu wa kada nyinginezo wakipokea maelekezo toka kwake. Sikuwa na shaka kuwa angeweza kuandaa na hata kuangusha utawala wa nchi yoyote duniani, hasa zile nchi dhaifu kiuchumi. Lakini kuitawala dunia…”
“Alibaini kuwa nilikuwa sijamwelewa. Ndipo aliponifungulia kompyuta yake na kunionyesha hicho nilichokionyesha, ambacho alikitaja kama silaha yake pekee ya kuitawala dunia, silaha ya maangamizi ya kutisha ambayo mimi niliichukulia kama mtambo wa mauti. Niliogopa, nikatetemeka sana na kumwambia waziwazi kuwa siafikiani naye. Kwa hulka yake nilijua kuwa kauli yangu ilikuwa hukumu ya kifo changu mwenyewe, lakini sikujali. Kifo changu kilikuwa kheri mara elfu moja kuliko kuiacha dunia nzima iteketezwe kwa ajili ya ndoto za mwendawazimu mmoja.”
Ndipo nikaelewa kwa nini alifanya kila njia kuhakikisha naajiriwa katika Jeshi la Polisi la Tanzania na baada ya kuhakikisha kupitia kwangu amepata kile alichotaka akanitoa kwa kubuni ule mpango wa ajali ambao ulisababisha kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.
“Nikiwa ndani ya polisi ndipo nilipoanzisha ule utani wa kujiita ‘Mona Lisa’ kama njia pekee ya kuwa karibu na ndugu yangu, jina ambalo kwa ajili ya maumbile yangu lilikubalika mara moja na kudumu hadi kilipotokea ‘kifo changu’.
Baada ya kusita kwa muda, Margareth akaendelea, “Nililazimika kutumia busara juu ya mkakati wake wa kishetani. Nilijitia kumsikiliza wakati akijitahidi kunishawishi na kunipamba kwa joho la ‘Umalkia wa Dunia.’ Usiku huohuo nilinakili toka katika kompyuta yake mpango wake
huo na kutoroka. Ndipo ulipoanza ule mchezo wa paka na panya. Alifungulia majeshi yake yote na kuniwinda kwa udi na uvumba. Pale kitandani kwako, pamoja na mzaha wangu wa kawaida kwa hayati ndugu yangu niliitumia fursa ile kwa masuala mawili. Moja ilikuwa kujificha. Lakini pili, nilikuwa nikitafuta nafasi nzuri zaidi ya kukufahamu na kuona kama ungeweza kukidhibiti kichaa changu. Lazima nikiri kuwa sikujua kama alikuwa na mtandao mpana kiasi kile nchini. Nadhani ni kwa ajili ya kufanana kwangu na Mona Lisa ndiyo sababu walinifikia haraka kiasi kile na kuishia kumuua yeye badala yangu.”
Margareth alisita tena, machozi yakianza tena kumtoka. Alitetemeka mwili mzima, jasho jembamba likimtoka. Kwa mara nyingine tena, alimwangukia Joram kifuani na kunong’ona, “Samahani sana. Mimi ni mwanamke mbaya sana, muuaji na katili mkubwa. Mona Lisa hakustahili kuwa ndugu yangu. Nadhani hata wewe sistahili kukukumbatia, Joram. Lakini bado nitaua! Kwa mara ya mwisho! Baada ya hapo nitakuwa radhi kufa!”
W 11 X
WAKATI watu mbalimbali wakitaabika usiku huo, mtu mmoja alikuwa akichekelea. Kwa jina aliitwa Christopher Marlone, ingawa kwa sasa hakujulikana kwa jina hilo.
Marlone alikuwa na kila sababu ya kuchekelea. Aliamini kabisa kuwa usiku huu ulikuwa mwisho wa ndoto yake kuitawala dunia na mwanzo wa ndoto hiyo kutimia. Kesho ingekuwa siku nyingine kabisa katika historia ya maisha yake, historia ya Tanzania na historia ya dunia. Kesho atakuwa Ikulu, akitoa maagizo ambayo nchi nzima itayatekeleza. Mwaka kesho Afrika nzima ingemtii na muda mfupi baadaye dunia nzima ingetekeleza matakwa yake. Zimebakia saa tu! Aliwaza.
Safari ya kuifikia tamati ya ndoto yake haikuwa fupi. Kwa ujumla, ilikuwa ndefu, ngumu na iliyohitaji uvumilivu mkubwa. Tangu pale mikakati yake ilipoharibika kwa bahati mbaya, mwaka 1995, kufuatia ajali mbaya ya gari jijini London, Uingereza na kumfanya King Halfan ambaye angekuwa mtu wake pale Ikulu achoropoke toka mikononi mwake. Marlone, hakuipoteza ndoto yake. Badala yake ndio kwanza aliivalia njuga na kuzama katika mbinu na mikakati mbalimbali ya kujiandaa kuichukua nchi yake na baadaye dunia nzima.
Matarajio yake hayo yalipata nguvu zaidi pale mmoja wa ‘watoto’ wake, ambaye alimfadhili katika masomo ya sayansi
alipoibuka na ugunduzi wa kuumba upya na kisha kuviumbua virusi vya UKIMWI. Kwa kutumia maabara ya siri aliyomjengea msichana huyu yatima, ambaye wazazi wake wote walipoteza maisha kutokana na tatizo hilo, alifanikiwa kuumba kirusi ambacho kilifanya kazi ya kuteketeza chembechembe nyeupe katika damu kwa kasi ya kutisha, chembechembe ambazo pia alikuwa na uwezo wa kuziteketeza kwa kasi ileile kwa kuziagiza vinginevyo.
Msichana yule, ambaye alikuwa amefanya kazi katika maabarambalimbalizinazojihusishanavirusinakuwashangaza mabingwa wa taaluma hiyo duniani, aliufanya ugunduzi huo kwa nia njema kabisa. Alitarajia ufumbuzi wake uwe mwisho wa zahama ya UKIMWI ambayo inatishia kuiangamiza dunia. Lakini mfadhili au ‘baba’ yake alikuwa na mawazo tofauti, “Usimwambie mtu yeyote juu ya hili. Tutaitumia hii kuitawala dunia. Wewe na mimi. Wewe utakuwa malkia, mimi nikiwa mfalme!” alisema.
Msichana hakuelewa. Lakini alipomwagiwa fedha nyingi na vifaa mbalimbali vya uzalishaji wa virusi hivyo viliponunuliwa, huku maabara kubwa zikijengwa kwa siri katika nchi mbalimbali za dunia na mitandao ya kuzisafirisha na kuzisambaza kuundwa ndipo alipoelewa. Ndio kwanza akaelewa kuwa mfadhili wake huyo alikuwa mwendawazimu. Alijaribu kuiharibu fomula yake lakini akawa tayari amechelewa. Marlone alikuwa tayari ameinakili na kumfundisha mmoja wa wasaidizi wake mwenye ‘kifua’ zaidi ya msichana huyo.
Jaribio la awali kwa binadamu dhidi ya virusi hivyo lilikuwa lile la kupenyeza nyama zilizosagwa katika tafrija ya harusi moja kubwa jijini Dar es Salaam. Kila aliyekula nyama hiyo alipoteza maisha katika saa ishirini na nne zilizofuata. Jambo ambalo lilimsisimua sana Marlone na kumthibitishia kuwa alikuwa amepata silaha pekee aliyohitaji.
Majaribio ya virusi hivyo yalipoanza kufanyika kwa watu wasio na hatia, na kufanya madaktari bingwa duniani washindwe kuamini kile wanachokiona binti wa watu alifanya kitu pekee alichokuwa na uwezo nacho. Alijiua kwa kutumia virusi alivyovibuni mwenyewe.
Marlone hakujali. Aliendelea na maandalizi yake ya
kuidhoofisha na kisha kuitawala dunia.
Fedha haikuwa tatizo. Biashara zake halali kwa haramu pamoja na hujuma mbalimbali alizopata kufanya maishani mwake zilikuwa zimemwingizia mamilioni kwa mamilioni, ambayo aliyachimbia katika benki mbalimbali katika nchi mbalimbali duniani.
Hapa nchini, sura yake ya hadharani ilimchora kama mwekezaji mashuhuri anayejihusisha na uchimbaji wa madini, uingizaji na usafirishaji wa mafuta, umiliki wa viwanda vya chakula; na kadhalika. Kwa majina ya bandia alimiliki benki, kampuni ya bima na maduka kadhaa ya kubadili fedha. Kwa siri sana, alikuwa msafirishaji mkubwa wa dawa za kulevya mara nyingi akitumia ndege zake binafsi ambazo ziliandikishwa kwa majina bandia vilevile.
Katika daftari lake la siri la mishahara, Marlone alikuwa na orodha ndefu sana ya waheshimiwa sana katika kila pembe ya dunia. Wako marais ambao bila msaada wake ama kiuchumi ama kijeshi wasingeweza kuiona Ikulu. Wako majemedari, madaktari, wahandisi, wanasiasa na wengineo ambao waliishi kwa fadhila zake. Wengi kati ya hawa ama hawakumfahamu kabisa au walimfahamu kijuujuu katika sura na jina alilotaka yeye, kulingana na mazingira.
Wakati akikamilisha mtandao wake wa kusambaza virusi hivyo duniani, kupitia katika maji na chakula, ndipo lilipozuka tatizo la yule msichana wake kujiua, kwa maana ya kupingana na harakati zake, tatizo ambalo halikumsumbua sana kwani tayari alikuwa amelipatia ufumbuzi kitambo kirefu. Na baada ya hilo likafuata lile la Margareth…
Kwake Margareth alikuwa zaidi ya kila mtu. Alimtegemea kwa kila hali, kuliko yeye mwenyewe alivyofahamu. Uzuri wake usio wa kawaida ulikuwa chombo kilichomsaidia sana kunasa marafiki au maadui zake. Ujasiri wake katika matumizi ya mwili wake, akili zake na silaha yoyote anayoitia mkononi, ulikuwa msaada usio kifani kwake. Hata ile hatua ya kumwingiza katika jeshi la polisi la Tanzania, na baadaye kumtoa kwa kisingizio kuwa alikufa katika ajali ya gari, ilikuwa moja ya harakati zake za kuujenga vizuri zaidi mtandao wake katika jeshi hilo.
Hivyo, Margareth naye alipooneka kupingana na mkakati wake na baadaye kutoweka na siri zake lilikuwa pigo kubwa kwake, pigo ambalo hakulitegemea kamwe. Hata ile kauli yake ya kuamuru Margareth auawe aliitoa shingo upande, kinyume kabisa na tabia yake ya kuhukumu mtu kifo kwa urahisi kama anayeamrisha kuku achinjwe.
Akiwa anafahamu fika Margareth alivyofundwa akafundika katika taaluma ya ujasusi, Marlone alisita kuutumia mtandao wake wa kawaida katika kazi hiyo. Badala yake akamkodi mtu wa nje ambaye mara nyingi alitumiwa kwa mauaji. Ikamshangaza kuona muda mfupi baadaye mtu huyo akidaiwa kuikamilisha kazi aliyopewa. Hakuamini ingawa alikubali kummalizia malipo yake.
Hivyo, hakushangaa zilipoibuka taarifa za Margareth, aliyetarajiwa kuwa marehemu, kuonekana tena mitaani katika hali ya kuchanganyikiwa. Marlone alipoletewa picha ya marehemu alishangaa kuona kuwa ilikuwa ya Margareth yuleyule aliyemjua, jambo ambalo lilichanganya sana akili yake. Ndipo akachukua uamuzi wa kufanya lile jambo la hatari, kuuiba mwili wa marehemu toka jengo la maiti la Muhimbili na kuupeleka katika misitu ya Pugu ambako alikwenda kuukagua, kazi ambayo ilikamilika kwa kuhakikisha yule mlevi, Super D, anauawa kwanza na maiti yake kuchukua nafasi ya marehemu.
Marehemu alikuwa Margareth! Marlone hakuyaamini macho yake. Ni pale tu, kupitia mtandao wake aliouamini, alipofahamishwa juu ya ‘Margareth’ mwingine aliyeishi hoteli ya New Africa kwa siku kadhaa ndipo alipobaini kuwa walikuwa pacha. Ilimwuma kuona kuwa aliishi gizani kwa muda mrefu bila kujua kuwa Margareth alikuwa na ndugu, mzuri kama yeye, aliyekuwa akiitwa Mona Lisa.
Aliamuru mwili wa marehemu uzikwe humo msituni na
kaburi lake kufichwa vilivyo.
Mkasa huo wa kifo kisichokusudiwa ungeweza kabisa kuvuruga mikakati yake ambayo hadi hapo ilikuwa ikienda kwa mujibu wa mpangilio. Hivyo, alitoa amri nyingine, ya kuhakikisha Margareth anauawa haraka, mahala popote na wakati wowote, amri ambayo aliitoa kwa watu kadhaa bila
wao kufahamiana, miongoni mwao wakiwemo wale waliokuwa na jukumu la kufuta ushahidi kwa kumuua muuji kabla hajafungua mdomo wake.
Kitu kingine kilichomsisimua Marlone ni taarifa kuwa mtu aliyeachwa hai pale kitandani, baada ya aliyedhaniwa kuwa Margareth kuuawa, alikuwa Joram Kiango! Kiango, kijana hatari na machachari, ambaye amekuwa akivuruga harakati nyingi za hujuma hapa nchini na nje ya nchi, Joram ambaye alisababisha makaburu wa Afrika Kusini wabadili siasa zao na kumruhusu Nelson Mandela, mtu mweusi, aichukue nchi, baada ya harakati zao kubwa kutibuliwa, Joram mwenye roho ya paka! Joram anayeweza kuponyoka hata katika mikono ya nunda au kuchoropoka katika dimbwi la damu! La, hakuwa mtu wa kuishi. Amri ya kifo cha Margareth iliambatana na ile ya kumuua pia Joram Kiango mahala popote na wakati wowote.
Haikuwa kazi rahisi. Joram Kiango alitoweka, Margareth Johnson aligeuka mbogo. Badala ya kuuawa ni yeye aliyeua, sirini na hadharani. Hali iliyopelekea Marlone aanze kuingiwa na hofu. Hakuna uwezekano wowote wa kuendelea na program yake huku Margareth akipumua, Joram akimvizia.
Faraja na matumaini vilimrejea alipoarifiwa juu ya Joram Kiango na Margareth Johnson kuonekana wakipanda gari moja na kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kwa gari moja na baadaye kuripotiwa kuingia katika vyumba vyake, huko Bunju. Taarifa za polisi wa kiraia na wenye sare kuizingira nyumba hiyo pia zilimfikia. Mmoja wao, akiwa mtu wake, alimletea taarifa zote, hatua kwa hatua.
Haikuwepo namna yoyote ya Marlone kuipoteza nafasi hii adimu, Marlone aliamua. Akatoa amri ya kwanza kwa mtu wake mzito katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nyumba ya Joram Kiango ilipuliwe, Joram, Margareth na kila kilichomo ndani ya nyumba hiyo kiteketezwe kabisa, amri ambayo ilitekelezwa mara moja.
Margareth alikuwa marehemu! Joram Kiango amekuwa historia! Hakuna tena ambacho kingesimama kati yake na azma yake ya muda mrefu.
Ni hayo ambayo yalimfanya achekelee, tabasamu likichanua
mara kwa mara katika uso wake. Sasa alikuwa na muda mfupi tu wa kusubiri kabla hajatoa amri nyingine. Baada ya hapo atatoa amri zote akiwa ndani ya Ikulu ya Dar es Salaam, akiwa juu ya kiti cha enzi.
Mara kwa mara Marlone aliitazama saa yake. Aliiona kama inayochelewa. Alikuwa akiwasubiri wajumbe wa kikao cha Ikulu watimie, Rais achukue nafasi ili aitoe amri yake hiyo, ya mwisho akiwa uraiani.
“Bado watatu Chifu,” aliendelea kupokea taarifa katika simu yake.
“Bado wawili.”
Na baadaye kidogo, “Bado mmoja!” Kisha, “Sasa anasubiriwa Rais tu!”
Marlone lishusha pumzi kwa nguvu. Akaitazama tena saa yake. “Dakika kumi tu baadaye,” alinong’ona akilazimisha tabasamu ambalo aliliona likianza kutoka kwa shida kuliko awali.
“Rais anaingia, Chifu!”
***
Kilikuwa kimoja kati ya vile vikao adimu sana, kikao cha watu wazito ambao dhamana ya uhai na usalama wa Taifa uko mikononi mwao. Alikuwapo mkuu wa Majeshi ya Ulinzi; alikuwapo Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Taifa; alikuwapo Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mawaziri wa Baraza zima walialikwa pia.
Ukiwa mkutano wa dharura ulioitishwa ghafla kufuatia tukio la dharura, kila mmoja kati yao alikurupuka na kuja kikaoni. Wako waliotokea kwenye hafla mbalimbali, ambao suti na tai zao zilikuwa bado zinaning’inia katika shingo zao. Wako waliotokea kitandani, ambao walijitupia vazi lolote lililokuwa karibu. Wako ambao walitokea kazini, ambao hawakupata hata muda wa kubadili sare zao zilizolowa jasho na kuchakaa kwa vumbi. Miongoni mwao alikuwamo Inpsekta Haroub Kambambaya.
Si kwamba yeye alichakaa mwili na mavazi tu, bali pia alikuwa amechakaa kwa uchovu, njaa na ukosefu wa usingizi. Alikuwa hajapata mapumziko wala fursa ya kutia
chochote mdomoni kwa takribani saa ishirini na nne sasa. Akiwa Bunju, macho yake yakishuhudia nyumba ya raia na chochote kilichomo kikiteketezwa mbele yake, wito wa kuja Ikulu aliutelekeza bila kupitia nyumbani wala ofisini. Alikuwa mmoja kati ya waliotangulia kuingia ukumbini hapo na kusubiri kimya juu ya kiti chake. Akiwa mmoja kati ya viongozi wakuu wa operesheni ile, kila mmoja alijaribu kumdodosa juu ya tukio hilo, “Ni kweli haya tunayosikia? Ilikuwaje?”
“Hicho ulichosikia kizidishe mara nne ndipo utaupata ukweli wa tukio zima,” Kambambaya limjibu mmoja wao, akimwonyesha dalili kuwa hataki mazungumzo zaidi.
Minong’ono ilizimika ghafla mlango wa Ofisi ya Rais
ulipofunguka naye kuingia taratibu.
Rais hakuwa mrefu sana. Kwa ujumla, alikuwa mtu mfupi, mnene, mwenye afya. Tumbo lake lililobeba kilo zisizopungua mia na kumi lilimfanya kila mtu ainue kichwa chake na kukaa kwa nidhamu kabla ya kusimama.
“Kaeni,” alisema baada ya yeye mweyewe kuketi.
Alionekana mchovu, aliyekosa mapumziko kwa muda mrefu. Kichwa chake pia kilionekana dhahiri kuwa kilikuwa msitu mkubwa wa mawazo. Utategemea nini zaidi kwa Rais anayeongoza moja ya nchi zinazoitwa masikini zaidi duniani ingawa ardhi yake inafoka kwa madini, bahari, mito na maziwa yake yanafurika kwa samaki na misitu yake imejaa utajiri wa wanyama na maliasili nyinginezo? Utategemea nini kwa Rais anayeongoza nchi kubwa ambayo zaidi ya asilimia tisini ya watu wake pato lao ni chini ya dola moja kwa siku, zaidi ya asilimia tisini ya vijana wake hawapati elimu ya sekondari na zaidi ya asilimia hizo tisini hawana ajira? Utategemea nini kwa Rais ambaye wakati nchi nyingine zinatenga fedha za kupeleka wataalamu wake kufanya utafiti katika sayari nyingine, yeye anawatuma mawaziri wake kwa wanaoitwa wafadhili kuomba fedha za kufanikisha kujenga madarasa na kununua vitabu kwa ajili ya elimu ya msingi? Utategemea nini kwa Rais ambaye maradhi madogomadogo kama kipindupindu na malaria bado yanaua maelfu ya watu wake kila mwaka huku yale makubwa kama, UKIMWI na Kifua Kikuu yakiwateketeza vijana kwa watu wazima, huku dawa na lishe vikiwa bidhaa
adimu? Naam, Rais alikuwa na kila sababu ya kuonekana ameelemewa.
Pamoja na yote haya sasa limekuja na hili. “Samahani kwa wito wangu wa ghalfa,” alisema baada ya kutulia juu ya kiti chake cha enzi. “Nimewaiteni hapa kwa ajili ya suala moja tu, ambalo nadhani karibu nyote mnalifahamu, ingawa kwa minong’ono. Ndege zetu za kivita, toka katika kituo kimojawapo cha Kijeshi, zimepaa angani na kuja Dar es Salaam kufanya shambulio la aibu katika nyumba ya raia mmoja na kuiteketeza kabisa. Inaaminika kuwa yeye na kila kilichokuwamo katika nyumba hiyo vimeteketea. Kilichofanya niwaiteni hapa ni kujua nani aliyetoa amri ya kurusha ndege hizo. Taarifa ninazopata zinatatanisha. Kila mmoja anasema hajui, ingawa watu wa rada na marubani waliozirusha wanasema walipokea amri halali na kupatiwa ramani ya eneo la tukio kwa taratibu zote.” Rais alisita kwa muda kabla hajaendelea, “Kati yetu hapa, kuna mtu anayefahamu vizuri zaidi tukio hili. Namtaka ajitokeze na aeleze kwa kina kilichotokea.”
Ukumbi mzima ulimezwa na ukimya mzito. Kila mmoja alijiinamia huku akimtazama mwenziwe kwa wiziwizi. Ni Rais peke yake aliyewakazia macho, akimtazama kila mmoja kwa zamu.
“Sikilizeni,” Rais alisema baada ya dakika nzima ya ukimya. Labda sijaeleweka. Sijasema kuwa kilichotokea ni kitu cha ajabu sana duniani. Yanatokea mara nyingi, amri kutolewa kwa bahati mbaya na ikaleta maafa makubwa. Tatizo hapa ni kuelewa tu, amri hiyo ilianzia kwa nani hadi kuwafikia watekelezaji. Wao wanaijua sauti ya mtu aliyetoa amri, ambaye yuko hapahapa. Mwenyewe ama haijui sauti yake ama anaikana. Tungeomba awe mwungwana, ajitokeze na kutupa ufafanuzi wa kilichopelekea atoe amri nzito kama ile.”
Kimya kingine kikaumeza tena ukumbi mzima. Hakuna aliyejitokeza.
Uso wa Rais ulianza kuondokana na ile hali ya diplomasia iliyokuwepo kwa muda mrefu. Alianza kukasirika. “Sasa nitafanya jambo moja,” aliwaambia. “Nitawapeni dakika tano za kujadiliana. Baada ya hapo natarajia kupata jibu. Vinginevyo….” Aliiachia sentesi hiyo hewani na kuinuka.
Akarejea katika ofisi yake.
Mmoja kati ya waalikwa hao alikuwa akitetemeka. Japo chumba kilikuwa na ubaridi tosha toka katika kiyoyozi yeye mikono yake ililoa kwa jasho jembamba. Aliificha mikono hiyo katika mifuko ya koti lake huku mara kwa mara akifuta paji lake la uso kwa leso.
Muda mfupi uliopita bwana huyu alikuwa akichekea tumboni. Alijua fika kuwa kikao hiki kilikuwa cha mwisho kwake kama mwalikwa au msikilizaji. Vikao ambavyo vingefuata yeye ndiye angealika huku akiwa mbele yao, nyuma ya meza ile pana, juu ya kiti cha enzi! Kwa bahati mbaya, wote waliokuwamo chumbani humo hawatakuwepo kumshuhudia akiendesha vikao hivyo. Hawatakuwa hai. Aibu iliyoje! Angependa wawepo, wawe mashahidi. Kwa bahati mbaya hilo lisingewezekana. Mara tu atakapokiacha chumba hiki mwisho wao utakuwa umewadia.
Lakini jasho lilizidi kumtoka. Aidha, alihisi akitetemeka waziwazi. Alihisi pia kuwa kila mtu alikuwa akimtazama. Akainuka na kuelekea maliwatoni. Miguu yake ilikuwa haina nguvu na iligongana magotini. Akajikongoja hadi huko, ambako alijifungia msalani na kutoa simu yake ya mkononi. Kwa mikono inayotetemeka alibonyeza namba kadhaa harakaharaka. Simu haikumjibu.
Hakukuwa na mtandao!
Alijaribu mara kadhaa kabla hajayaona maandishi katika uso wa simu hiyo yakisema waziwazi kwa lugha ya Kiingereza ‘No service.’ Hakuyaamini macho yake. Sasa aliloa jasho mwili mzima huku akitetemeka waziwazi. Alijikongoja akijaribu kutoka nje ya jengo hilo na kuliendea gari lake, lakini vijana wawili wa usalama walimzuia.
“Samahani mzee, tumeagizwa kutomruhusu mtu yeyote kutoka kabla ya Rais kufunga kikao hiki,” mmojawao alimwambia.
“Lakini… lakini… sijisikii vizuri. Na… Nadhani nina homa,” alijaribu kuwaambia.
“Pole sana,” alijibiwa. “Itabidi uhudumiwe na daktari wa Ikulu.”
Mtu huyo aliitazama saa yake. “Haiwezekani!” alifoka.
“Lazima nitoke mara moja!”
“Pole sana. Lakini haiwezekani!”
***
Akiwa Dar es Salaam, akiwa kama mwekezaji. Christopher Marlone alipenda kuishi katika nyumba yake ya ghorofa mbili iliyojengwa katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo la Kunduchi. Alijitahidi sana kuifanya iwe nyumba ya kawaida, kama zilivyo za majirani zake wengine, ikiwa na ulinzi wa kawaida wa akina Knight Support, Simba Security, Goha Security; na wengineo. Yeye alitumia walinzi wa Simba. Aidha, geti lake liliunganishwa na waya wa umeme ambao uliashiria hatari mara ulipoguswa na mtu au kitu ambacho hakikukusudiwa.
Joram Kiango na Margareth waliifikia nyumba hiyo kupitia upande wa nyuma. Waliambaa katika msitu wa maua uliofunika ukuta wa nyumba hiyo hadi walipoufikia upenyo wa siri ambao zaidi ya Marlone ni Margareth peke yake aliyeufahamu. Walipoufikia mlango Joram alitoa vifaa vyake na kushughulikia kitasa harakaharaka. Dakika tatu baadaye tayari walikuwa wameingia ndani bila ya walinzi wa kampuni ya Simba, waliokuwa wakilizunguka jengo kila baada ya dakika kumi, kuwaona.
Akiwa mwenyeji tosha katika jumba hilo Margareth alimwongoza Joram kupita toka uchochoro huu hadi ule, chumba hiki hadi kile hadi walipofika mbele ya mlango wa chumba ambacho alikielezea kuwa maktaba ya Marlone.
“Atakuwa humu,” alimwambia Joram. “Muda wake mwingi huutumia katika chumba hiki.”
Huku bastola mbili zikiwa zimemtangulia, Joram aliupiga teke mlango huo na kuingia nao ndani. Aliviringika mara mbili kabla ya kusimama, bastola zake zote zikiwa zimemlenga Christopher Marlone ambaye aliduwaa, wima, nyuma ya meza yake kubwa.
“Nani… umeingiaje humu ndani?” aliuliza kwa sauti iliyojaa mshangao.
“Naitwa Joram Kiango. Na niliyefuatana naye ni msichana unayemfahamu vizuri zaidi yangu. Anaitwa Margareth
Johnson,” Joram alimjibu kwa kebehi.
Wakati huo Margareth alikuwa akiingia chumbani humo taratibu, hatua baada ya hatua. Yeye pia alitanguliwa na bastola kubwa iliyoshikwa barabara katika mkono wake wa kuume.
Marlone alitokwa na macho ya mshangao. “Wewe!” alifoka, “Uko hai!” hakuyaamini kabisa macho yake.
Toka alipopokea taarifa ya nyumba ya Joram kuteketezwa kabisa, huku yeye na Margareth wakiwa wamejichimbia humo, polisi wakiwa wametanda kila kona ya nyumba hiyo, aliamini kuwa wamekufa na hakuwa tena na jambo lolote la kuhofia. Ni imani hiyo iliyofanya asione haja ya kuchukua hadhari zaidi, wala kujishughulisha kuitazama screen ya kompyuta yake ndogo ambayo ilikuwa ikimwonyesha mazingira yote ya nyumba hiyo. Ndiyo, imani hiyo pamoja na taharuki aliyokuwa nayo juu ya tukio zito ambalo alilitarajia kujiri muda wowote kuanzia wakati huo viliimeza kabisa akili yake.
Badala yake muda wote macho na masikio yake vilikuwa kwenye simu yake maalumu akisubiri iite, imthibitishie kuwa kila mjumbe alikuwa ameketi kwenye kiti chake katika kikao cha Ikulu, ili baada ya uhakika huo atoe amri yake kuu, amri ya mwisho akiwa uraiani.
Ilimshangaza Marlone kuona simu aliyotarajia ikichelewa kuingia. Si hilo tu, hakupata kupokea simu yoyote katika muda wote wa kusubiri, jambo ambalo awali lilimfariji lakini baadaye likaanza kumshangaza.
Simu aliyoitarajia ingetokea kwa mtu wake ambaye muda huu alikuwa katika kikao cha Ikulu. Kwa kiasi fulani, Marlone alikuwa akimhurumia rafiki yake huyo kwa kumtumia kama alivyomtumia. Ndiyo, alikuwa amemtajirisha sana na kumsaidia kuuficha utajiri wake katika mabenki ya nje ya nchi. Lakini hakuwa na namna ya kumwacha hai. Ulikuwa ulaghai mtupu alipomfanya aamini kuwa baada ya tukio angempa yeye Ikulu ya Tanzania na kiti hicho cha enzi, ulaghai ambao ulimsaidia sana kufanikisha mtandao wake katika vyombo vya dola, mipango ambayo kwa mara ya kwanza alianza kuyatilia mashaka mafanikio yake kufuatia ujio wa Joram na Margareth, ambaye taratibu vilevile, hatua baada ya
hatua, alitembea hadi mbele ya Marlone na kumjibu taratibu, “Unataka kujua kama niko hai? Nitazame vizuri usiogope.”
Marlone alijaribu kutabasamu. Tabasamu likakataa. “Usiogope… Nitazame,” Margareth alimwamuru tena. “Si ulitegemea kuwa nimekufa? Ulipanga kuniua mara ngapi mshenzi wewe?” alihoji.
Macho ya Margareth yalikuwa yakimtazama Marlone kwa makini sana alitazama kila hatua ya mwenendo wa mwili wake. Margareth alijua chini ya meza hiyo, hatua mbili tu toka aliposimama Marlone, kulikuwa na kitufe ambacho kama angekibonyeza kwa mguu wake kila kilichokuwa mbele yake kingechakaa kwa risasi.
Joram pia alikuwa amedokezwa juu ya hilo. Hivyo, yeye pia alikuwa makini, kukichunguza kila kitendo cha Marlone. Alimsogelea na kumwambia, “Mbona humjibu huyu msichana? Ulitegemea kumwua mara ngapi?”
Hakujibu.
“Christopher Marlone,” Joram aliita tena. “Kichaa mwenye ndoto za kishetani za kuiangamiza nchi hii na dunia nzima kwa kuubadili uvumbuzi wa kisayansi uliofanywa kwa nia njema kuwa maangamizi makubwa ya maisha ya binadamu. Christopher Marlone, kwa jina la Jhamuri ya Muungano wa Tanzania nakuamuru uinue mikono yako juu na utoke nyuma ya meza hiyo.”
Marlone alimkodolea Joram macho.
“Nitahesabu mara tatu,” Joram alionya. “Baada ya hapo kichwa chako kitakuwa halali yangu.”
Marlone aliendelea kusimama. “Moja!”
Kimya. “Mbili!”
“Ta…” Marlone alifanya kama alivyotegemewa. Alichupa kukiendea kitufe chake cha kufyatulia silaha za siri. Kwa bahati mbaya, hakujua kuwa si Joram wala Margareth aliyekuwa na muda wa kuendelea kuvistahimili vitendo vyake. Akiwa hukohuko angani tayari sura na kifua chake vilichakaa na kufumuka kwa zaidi ya risasi kumi za Daringer .41, Semi- Automatic na .38 Colt Special, zilimnyeshea mithili ya mvua.
Alianguka chali na kutapatapa kwa sekunde chake, kisha akakata roho.
Joram na Margareth waliuinamia mzoga wa aliyekuwa Christopher Marlone kana kwamba walitaka kuhakikisha kuwa amekufa. Kichwa chake kilikuwa kimefumka, ubongo uliochanganyika na damu ukimwagika juu ya sakafu kama uji wa moto. Hali kadhalika, kifua chake kilikuwa kimekatika kabisa, mbavu na sehemu kubwa ya moyo wake vikiwa vimetoka nje.
Hakuna binadamu aliyeumbwa na Mungu ambaye angeweza kuwa hai katika hali hiyo.
“Ulistahili kufa zamani sana, Marlone.” Joram alimwambia maiti.
“Kwa ujumla, ulistahili kufa kifo kama hiki mara tatu au zaidi,” Margareth naye alimwambia. Kisha alimtazama Joram na kumwambia taratibu, “Mpenzi nadhani sasa naweza kuungana na ndugu yangu huko aliko, ingawa nadhani yeye atakwenda peponi, mimi motoni.”
Hata kabla Joram Kiango hajajua lipi Margareth alikusudia kufanya alimwona akiielekeza bastola yake katika kifua chake na kuvuta kiwambo cha kufyatulia.
“Margareth!” Joram aliita akichupa kumwendea.
Alikuwa amechelewa sana. Risasi mbili zilikwishapenya katika moyo wake na kuufumua kabisa. Alianguka juu ya sakafu na kugugumia kwa maumivu. Baadaye alitulia na kumtazama Joram ambaye alikuwa bado kapigwa na butwaa. “Samahani Joram. Nilikupenda na bado nitaendela kukupenda… lakini sitahili kuishi… nimefanya madhambi
mengi sana na makubwa sana…”
Uso wake ulibadilika taratibu. Maumivu yakaonekana kuuacha na tabasamu kuchukua nafasi yake, tabasamu jepesi, tabasamu murua ambalo machoni mwa Joram halikuwa tena tabasamu la Margareth; isipokuwa lile alilolizoewa na kulipenda sana.
Tabasamu la Mona Lisa!
HITIMISHO
ASUBUHI hiyo iliondokea kuwa ya kawaida kama zilivyowahi asubuhi nyingine zote. Wanafunzi walidamka na kuwahi mashuleni kama ilivyo ada, watu wazima walikimbilia makazini, wafanyabiashara waliendelea na pilikapilika zao. Waliobakia majumbani nao waliendelea na yao. Ile hofu iliyowakumba usiku, ilitokana na uvumi wa ama Tanzania kuvamiwa, ama shambulio la ugaidi ilitoweka usiku huohuo baada ya Rais kulihutubia taifa kupitia vituo vya televisheni na redio.
Hotuba ya Rais ilichukua dakika tano tu, ikiwa na ajenda mbili muhimu. Kwanza, Rais aliwatoa hofu wananchi kwa ‘Uvumi usio na msingi’ wa Tanzania kuvamiwa ama na magaidi ama na nchi jirani. “Nchi yetu ni imara, haina wasiwasi wowote. Jeshi letu ni imara na halijapatwa kubabaishwa na wala halitababaishwa na mtu wala Taifa lolote. Fanyeni shughuli zenu kwa utulivu pasi na kubabaishwa na uvumi wowote.”
Akizungumza kwa kujiamini, sauti yake ikiwa imara, uso wake ukiwa hauna dalili yoyote ya kuficha kitu, wananchi walimwamini Rais mara moja na kupuuza kila walichosikia.
Ajenda ya pili katika hotuba ya Rais ilikuwa ya kutisha. Kwa ujumla iliwashitua na kuwashangaza wengi. “Taifa limepata msiba. Kiongozi wenu, Mpenzi wenu, ambaye amelitumikia Taifa hili kwa mapenzi makubwa kwa uaminifu na mapenzi makubwa kwa zaidi ya miaka kumi na mitano, katika nyadhifa mbalimbali amefariki dunia.
“Kifo chake kimetokea ghafla usiku huu kutokana na ugonjwa wa moyo wakati akiwa Ikulu, katika shughuli za Kitaifa, akiendelea kuitumikia nchi yake.”
“Atazikwa kwa heshima zote za Kitaifa. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
Watu walimwona marehemu muda mfupi uliopita, akiwa hai, mchangamfu na mwenye afya tele hawakuamini masikio yao. “Binadamu hatuna thamani, tunatembea na kifo,” mtu mmoja alinong’ona mtaani.
“Kweli kabisa,” aliungwa mkono.
***
Kesho yake vyombo vya habari vilipamwa na habari na picha za mheshimiwa huyo. Televisheni, redio na magazeti yote yalikuwa na taarifa za kifo chake ‘cha kishujaa’ na historia ya maisha yake.
Habari za nyumba iliyoteketezwa kwa madege ya Kijeshi kule Bunju hazikupata nafasi. Habari za kifo cha tajiri, mwekezaji maarufu, Christopher Marlone, zilidokezwa kidogo tu katika gazeti moja, tena katika ukurasa wa tatu, chini ya kichwa kidogo cha habari ‘Tajiri auawa na majambazi.’ Kwamba tajiri huyo alipambana kiume na majambazi hayo na akafanikiwa kuliua moja la kike; lakini jambazi la pili limefanikiwa kutoroka na fedha nyingi.
Mmoja kati ya watu wachache waliofanikiwa kuisoma habari hiyo ni Joram Kiango. Alilitupa gazeti hilo mezani huku tabasamu la uchungu likichanua usoni pake, tabasamu ambalo alilifukuza kwa kumeza fundo la kahawa chungu iliyokuwa mbele yake.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment