Search This Blog

Thursday 29 December 2022

MTAMBO WA MAUTI - 1

  

Simulizi : Mtambo Wa Mauti

Sehemu Ya Kwanza (1)


Simulizi : MTAMBO WA MAUTI

Mwandishi : BEN R. MTOBWA

Imeletwa kwenu na: BURE SERIES


Sehemu ya 1



W 1 X


HILI lilianza kama tamthiliya, tena tamthiliya yenyewe nyepesi tu, ya mapenzi. Kama waigizaji katika tamthiliya hiyo, si Joram Kiango kwa upande mmoja;


wala msichana huyu, kwa upande wa pili, alipata angalau kuhisi tu kuwa mwanzo wa tamthiliya hiyo ulikuwa sawa na kuanza kwa mkasa mzito kama mkondo wa mto unaopita katika majanga ya nchi yenye kila aina ya ukatili na unyama usiomithilika.


Dar es Salaam ikiwa imefurika wasichana warembo kupindukia, wengi wao wakiwa wameuongeza urembo wao wa asili maradufu kwa vipodozi lukuki vilivyofurika madukani, msichana huyu, machoni mwa Joram alikuwa wa kawaida kabisa. Hata hivyo, baada ya kumtazama kwa makini zaidi alibaini kuwa alikuwa na ziada moja juu ya urembo wake. Si ile ngozi yake ya maji ya kunde, la hasha. Ilikuwa ngozi ya kawaida ingawa weusi wake uliifanya imeremete na kushawishi kuigusa. Si lile tabasamu lake la mara kwa mara. Hilo pia ni jambo la kawaida katika nyuso za wasichana wa kileo na lingeweza kununuliwa kwa fedha tu iwapo mwenyewe angejali kujiunga na chuo kimojawapo cha usanii na kuhitimu. Hali kadhalika, ziada hii haikutokana na macho yake maangavu, pua yake iliyochongoka; wala meno yake meupe yaliyojipanga kikamilifu kinywani mwake kama mistari miwili ya punje za






mahindi kwenye kibunzi.


Alikuwa na ziada!


Lakini ziada hii ilikuwa ipi? Joram alijiuliza akimtazama kwa hila mrembo huyo aliyeketi kando. Macho yao yakagongana. Yale ya msichana yalihimili kwa sekunde moja dhidi ya yale ya Joram, sekunde ya pili yakawa yameangukia chini huku lile tabasamu lake likigeuka kuwa katika sura nyingine. Ni hapo Joram alipobaini ile ziada iliyomvuta katika sura na umbile la msichana huyu.


Haya!


Alikuwa msichana mwenye haya! Mmoja kati ya wasichana wachache kabisa duniani waliobakia na haya. Wengi wao, toka walipoanza kuvaa suruali kama wanaume, huku wakienda kazini na kurudi jioni kama wanaume, kile kirusi kinachoitwa ‘haya’ kilitoroka zama za kale katika maumbile yao na, hivyo, kuwaacha wakavu kama wanaume.


Akiwa amevutwa na hilo, kwa mara ya kwanza Joram Kiango alijikuta akimtilia maanani na kuamua kumsikiliza, badala ya kuishia kumsikia tu.


“Umesema unaitwa nani vile bibie?” alimuuliza. “Mona.”


“Mona?” “Mona Lisa.”


Joram alipata kuziona mara nyingi nakala za ule mchoro maarufu duniani wa Mona Lisa. Aidha, aliwahi kuiona nakala halisi ya mchoro huo katika jumba moja la kumbukumbu za Sanaa nchini Ufaransa. Mchoro huo ulichorwa na msanii maarufu aliyeishi mwaka 1452 hadi 1519 huko Italia, Leonardo da Vinci, akimwigiza mrembo huyo Mona, aliyezaliwa kati ya mwaka 1503 na 1506; mchoro ambao mtu mmoja, Vincenzo Peruggia aliwahi kuuiba toka katika jumba hilo na kuuficha kwa kuamini kuwa ulikuwa umeibiwa na Napoleon wakati wa vita vilivyoifanya Ufaransa iitawale Italia kwa muda mrefu. Lakini mchoro huo ukakamatwa na kurejeshwa tena Ufaransa mwaka 1913, baada ya kibaka huyo kujaribu kuuza.



Aliyempatia msichana huyo jina hilo hakubahatisha. Isipokuwa kwa tofauti ya rangi, Mona huyo akiwa maji ya kunde, yule wa historia akiwa mweupe, vinginevyo walikuwa






mtu na dada yake. “Jina lako halisi hilo!” alimuuliza kwa mshangao.


“Nadhani,” alijibu kwa sauti yake ileile, laini inayobembeleza, sauti iliyofuatiwa na tabasamu lilelile la pekee; Tabasamu la Mona Lisa.


“Unadhani? Huna hakika? Kwa nini?”


“Nadhani! Kwa kuwa toka nimepata akili nimejikuta naitwa Mona Lisa. Hata cheti changu cha kuzaliwa kimeandikwa hivyo.


Joram alimtazama kwa makini zaidi. Mara akaanza kubaini mengine katika umbile la msichana huyu ambayo pia yalikuwa ya ziada. Kwa mfano, alibaini kuwa nywele zake fupi zilikuwa asilia, hazikupata kuwekewa aina yoyote ya dawa ili kuzipa mvuto uliokuwa nazo. Hali kadhalika, ngozi yake pia haikupata kuathiriwa na yale madawa ya kileo, yanayowababaisha wasichana wengi kwa faraja ya muda mfupi na athari za maisha. Huyu alikuwa kama alivyozaliwa. Sifa zake hizo zikiwa zimepambwa kwa mavazi yenye heshima, sketi ndefu iliyovuka magoti na blauzi nyepesi iliyokifanya kifua chake kitoe picha ya uhai wa matiti yake.


“Utanisaidia?” msichana huyo alimzindua Joram baada ya kumwona kamtumbulia macho, kimya, kama anayetafakari jambo ambalo binti huyo hakulielewa.


“Hivi ulisema unachohitaji kwangu ni nini vile?” Joram alimwuliza.


Msichana akaangua kicheko. “Acha mzaha, Joram. Unajua, kukupata leo peke yake ni bahati ya pekee? Nimekutafuta wiki mbili katika mahoteli yote na baa zote za jiji hili. Leo imetokea kama ndoto!”


Hilo lilikuwa jingine ambalo Joram aliishangaa akili yake kwa kutolitafakari mapema. Msichana huyu amewezaje kumpata katika hoteli hii ambayo si kila mtu anafahamu kuwa hupenda kuitumia?


‘Comfort Hotel’ moja kati ya hoteli mpya zinazojengwa kwa fujo katika ufuko wa bahari ya Hindi, ilimvuta Joram Kiango kwa upya wake. Toka alipoamua kukaa kimya, baada ya kutoridhika na tamati ya mambo katika mkasa ulioandikiwa kitabu na kuitwa Nyuma ya Mapazia Joram alijikuta hana






raha. Ndiyo, King Halfan alifanikiwa kuponyoka toka katika mikono ya yule muuaji hatari, Marlone, na kufanikisha taarifa za mauaji ya kutisha yaliyoandaliwa kufanyika kwenye ule mdahalo wa kihistoria wa kumtafuta Rais anayefaa zaidi kuiongoza Tanzania; bado mwisho ule haukumridhisha kabisa Joram. Kutoweka kwa Marlone kabla ya yeye kumtia risasi ya kichwa kulimsononesha sana na ukimya wake hadi sasa ulimkosesha kabisa usingizi.


Wapambe wake jijini London walikuwa wamedokeza juu ya ‘ajali ya kamera’ katika uwanja wa Heathrow, ajali ambayo baadaye hisia zilielekeza kuwa iliandaliwa itokee katika hoteli ya Kilimanjaro, kwenye mdahalo. Lakini Mungu akaingilia kati na kuiepusha. Hata hivyo, mshenzi aliyeyaandaa mauaji hayo alitoweka kama tone la maji baharini, pasi ya kuacha alama yoyote ya kuwepo kwake. Kwa Joram Kiango hilo lilikuwa sawa na bomu lililo hai, ambalo wakati wowote lingeweza kulipuka na kusababisha maafa ya kutisha.




Kutokana na hisia kuwa kwa namna moja au nyingine alikuwa ameshindwa kutimiza wajibu wake, ndipo Joram alipoamua kuingia gizani kwa kujiepusha na vikao vyake vya kawaida, ikiwa pamoja na kumwepuka msaidizi wake mkuu, Nuru, na badala yake kuamua kujichimbia hapa na pale; mara kwa mara katika hoteli hii, ambayo kama wapo watu waliomfahamu kwa jina lake halisi ni wachache sana.


“Utanisaidia?” Mona Lisa alimzindua tena Joram.


Joram akamtazama kisha akamuuliza, “Hebu niambie Mona, umejuaje kama napatikana hapa?”


“Ni hadithi ndefu. La msingi ni wewe uelewe tu kuwa nimekuja hapa Dar toka Arusha kwa ajili yako. Na kwamba nimekutafuta kwa wiki mbili kamili kabla ya bahati kunitokea leo.” Mona alisita na kumtazama Joram. “Tafadhali niambie kama utanisaidia,” akasema kwa msisitizo.


Joram alimtazama. Macho yake yakagongana tena na yale laini, yanayobembeleza, ya Mona Lisa, macho ambayo si kwamba yanabembeleza tu, bali pia yanashawishi na kushurutisha.


“Tutaangalia uwezekano,” alimjibu.


Mona akatoa tabasamu la shukrani. “Lini? Leo?”






“Hata sasa hivi. Kuna ubaya gani?” lilikuwa jibu la Joram. “Hapana. Labda jioni, nina disketi tu. Hatuna kompyuta. Lakini hoteli niliyofikia ina chumba cha kompyuta za kukodi.


Naweza kwenda kuiprint na kuja nayo jioni. Utakuwepo?”


Ndio kwanza Joram akakumbuka msichana huyo alihitaji msaada gani toka kwake. Alikuwa ameandika riwaya ya upelelezi. Tayari ilipitiwa na wahariri kadhaa ambao walimhakikishia kuwa ilikuwa riwaya nzuri sana. Hata hivyo, alisita kuipeleka kwa wachapishaji hadi hapo itakapopitiwa na mpelelezi mashuhuri, kama Joram Kiango, ambaye ana uwezo wa kudodosa kasoro zinazoweza kukifanya kisifikie kiwango kinachohitajika.


“Lakini mimi sio mwandishi wala mhariri. Bado sioni naweza kukusaidia kwa namna gani,” Joram alionya.


“Sihitaji msaada wa ajabu, Joram. Ukikitazama tu utaona kama kinafaa au la. Kama hakifai…”


“Sitasita kukueleza,” Joram alimalizia.


“Usisite, tafadhali. Naomba uniruhusu nikaprint ili niulete jioni,” Mona aliomba huku akiinuka.


“Kuna ubaya gani?” Joram alimjibu na kuongeza, “Nitatoka na kurudi hapa saa moja na robo usiku. Saa tatu kamili nina mihadi mahala. Nadhani muda wa saa moja unatosha kuutazama mswada wako na kutoa maoni yangu ambayo naamini hayatakusaidia sana.”


“Mie naamini yatanisaidia sana,” Mona Lisa alisema hali akiinuka na kuondoka.




***


Ndiyo, kwa kila hali alikuwa msichana wa kawaida. Macho yake yenye haya yasingekuwa na uwezo wa kuficha chochote ambacho angependa kuficha bila ya Joram Kiango kumshuku. Hata hivyo, hilo halikuondoa ule ‘u-Joram Kiango’ katika fikra za Joram Kiango. Si wahenga walisema kuwa tabia haina dawa? Ni tabia hiyo, au ‘u-Joram Kiango’ huo uliomfanya Joram kupitia katika kioo cha moja ya madirisha ya hoteli hiyo amchunguze msichana huyo toka alipotoka hotelini, alivyotembea kwa mwendo wake wa kusisimua, hadi alipoifikia teksi iliyomleta hotelini hapo. Mara tu gari hilo



lilipoondoka Joram naye alitoka nje ya hoteli na kuliendea gari lake la kukodi, akaliwasha na kulielekeza mjini, akilifuata gari la Mona Lisa.


Aliiacha njia ya kutokea hotelini na kuingia barabara ya Bagamoyo. Gari moja, Toyota Hilux lililokuwa likiendeshwa kasi bila sababu za msingi lilimpita kwa kasi na kumtenganisha na lile la Mona Lisa jambo hilo lilimfurahisha Joram. Hakutaka Mona amwone au kuhisi kuwa anafuatwa au kuchungwa.


Waliiacha tegeta, wakaingia Kunduchi, Mbezi na, hatimaye Tangi Bovu. Hadi wanaingia Mwenge tayari yalikuwepo magari matano baina yake na lile la Mona Lisa. Mawili kati ya hayo yakiwa daladala, moja likiwa gari la abiria na mawili yaliyosalia magari madogo.


Umbali huo baina yake na gari la Mona haukumsumbua hata kidogo. Alikwishazisoma namba za gari hilo. Hali kadhalika, aliweza kuona vizuri hatua zote ambazo dereva wa gari hilo alikuwa akichukua, kama kusimamia, kulipita gari lingine au kupinda kona kabla ya dereva huyo kufanya hivyo. Pengine kilichokuwa kikimsumbua Joram Kiango wakati huo ni hatua yake hii ya kumfuatilia msichana mpole kama huyo. Mona Lisa hakuonekana kuwa na madhara ya aina yoyote. Zaidi, alikuwa ameahidi kurejea hotelini hapo jioni hiyohiyo akiwa na mswada wa riwaya yake ya upelelezi aliyoiandika. Ya nini kumfuatilia hadi huku? Joram alijiuliza. Kisha, alijicheka kimoyomoyo alipokumbuka usemi wa mwanamke wa kiingereza; Never marry a Cop. Usilogwe kuolewa na polisi kwani akikosa mtu wa kumshuku kwa


uharifu ataanza kukushuku hata wewe mwenyewe.


Wakati huo walikuwa wakimalizia barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Gari ya Mona Lisa lilipoonyesha ishara ya kuingia kushoto kuifuata barabara ya Maktaba. Joram naye alihamia kushoto na kuifuata barabara hiyo. Waliifuata moja kwa moja kuelekea baharini. Gari ya Mona Lisa ilipoonyesha ishara ya kuingia hoteli ya New Afrika Joram, ambaye alikuwa magari manne nyuma, alipinda kushoto kuifuata barabara ya Samora hadi mbele ya ukumbi wa MAELEZO ambapo alisimama na kupaki.


Kabla hajashuka alifunua kiti cha abiria na kutoa miwani






yake mieusi, kofia pana ya Cowboy na ndevu zake za bandia ambazo alizivaa mara moja huku akizidi kujishangaa kwa hatua zote. Alijipapasa katika sehemu yake ya siri ambapo huficha bastola yake, na baadaye kuanza safari yake fupi ya mguu kuiendea hoteli ya New Africa.


Mbele ya lango kuu la hoteli, Joram alimpita Mona Lisa amabaye alikuwa akibishana jambo na dereva wake. Baadaye alimsikia akimwambia ‘nisubiri’, na kuingia ndani. Kama ambavyo Joram alitegemea, msichana huyo hakuonyesha dalili yoyote ya kumjua. Badala yake alimpita baada ya kumtupia ‘shikamoo’ ambayo Joram aliitikia kwa kutikisa kichwa. Alitembea mwendo wa haraka hadi kaunta ambako aliomba kadi ya kufunguliwa mlango wa chumba chake na kisha kuiendea lifti.


Hotelini humo Joram alielekea ukumbi wa baa. Aliagiza toti mbili za John Walker ambazo alizinywa kavukavu kwa mikupuo mitatu na kuisindikiza kwa sigara moja ambayo aliivuta nusu, akaizima na kuisindika katika kasha la taka.


Huku akiwa na hakika kuwa hakuna mtu yeyote anayemtazama zaidi ya mtazamo wa kawaida, alitoka katika ukumbi huo na kuiendea lifti. Ilikuwa chini kama inayomsubiri. Aliingia na kubonyeza tufe la ghorofa ya tano. Aliutumia upweke katika lifti hiyo kubandua ndevu zake za bandia na kuvua miwani yake mieusi na kufutika vitu hivyo katika moja ya mifuko yake ya koti. Aliyesimama hapo mbele ya chumba namba 512, alikuwa Joram Kiango yuleyule ambaye Mona Lisa alimwacha kule Comfort Hotel dakika arobaini zilizopita. Mkono wake wa kulia ulikuwa ukigonga mlango taratibu hadi ulipofunguka na uso mzuri wa msichana huyo kuchungulia.




***


“Joram!” Mona Lisa alitamka kwa mshangao. “Siamini macho yangu!”


“Shauri yako. Ni macho yako mwenyewe. Ukiyaamini sawa, usipoyaamini sawa,” Joram alimtania akitabasamu. “Nakaribishwa nyumba hii au sitakiwi?”


“Lakini si nimekuacha ufukweni muda mfupi uliopita?” Mona Lisa alizidi kusaili.






“Si tulikuwa wote?” Joram alimhoji. “Mimi nilikuja kwa gari.”


“Mimi nimekuja kwa helkopta,” Joram alizidi kumtania. “Nakaribishwa humu ndani?”


Mona Lisa alimpisha kuingia. “Karibu sana. Keti tafadhali,” alimhimiza. Hata hivyo bado ilikuwa dhahiri kuwa ujio huo wa Joram ulikuwa umemshangaza sana. “Sikujua kuwa siku hizi Dar mnazo helkopta za kukodi,” alichokoza mara baada ya Joram kuketi kwenye kochi.


“Zipo ingawa hazionekani kwa macho ya kawaida,” Joram aliongeza mzaha. “Bibi yangu alinifundisha namna ya kuruka kwa ungo.” Alipoona msichana huyo akizidi kuduwaa Joram aliamua kumtoa wasiwasi kwa kumweleza, “Usijali mpenzi. Mimi ni mtu wa utani kila wakati. Unajua sikuwahi kupata mapenzi ya bibi wala babu? Unajua sina binamu? Hivyo, napenda kulazimisha utani kwa kila mtu. Kwa kweli, nimekuja hapa kwa gari kama wewe. Kilichonileta hapa ni hiki!” alitia mkono wake katika mfuko wa koti na kuutoa ukiwa umeshikilia pochi. “Uliisahau pochi yako. Nikaona nikodi gari kukufuata kwa kuhofia kuwa ungepata shida ya kumlipa dereva wako na mahitaji mengine. Ndipo nikakodi gari kukufuata. Kwa bahati mbaya dereva wangu aliendesha gari kwa mwendo wa kinyonga. Wakati nafika hapa niliambulia kukuona ukiingia katika lifti. Nikauliza namba ya chumba chako mapokezi na kukufuata.


Mona Lisa alipokea pochi hiyo kwa furaha. “Loo, masikini!


Pole sana. Kumbe niliisahau kwako!”


Laiti angejua Joram alikuwa ameisogeza ili apate chochote ambacho angehitaji kupata juu ya msichana huyo! Kwa bahati mbaya hakuambulia chochote zaidi ya kukuta noti za elfu kumi kumi zisizopungua ishirini. Hakukuta kielelezo wala kitambulisho chochote, jambo lililopelekea kujiri kwa safari yake hadi chumbani humu.



“Karibu sana… Jisikie nyumbani,” Mona alimkaribisha tena Joram Kiango, “Sijui nikupe kinywaji gani? Aliuliza.


Joram alichagua John Walker, kavu. Mona alimsogezea chupa nzima na glasi na kuviweka juu ya kijimeza cha kioo kilichokuwa mbele ya kochi alilolikalia Joram. “Tafadhali,






jihudumie. Natoka mara moja kumtoa dereva wangu. Nadhani kwa sasa atakuwa na wasiwasi kuwa nimemwingiza mjini,” alisema akiichukua pochi yake na kuelekea mlangoni.


“Take your time… Mie niko nyumbani hapa,” Joram alisema akijiweka katika mkao wa kunywa. Aliifungua chupa hiyo iliyojaa pomoni na kumimina nusu glasi ambayo aliitia mdomoni. Mara tu Mona alipotoka nje ya chumba hicho na kufunga mlango nyuma yake, macho ya Joram yaliingia kazini. Alichunguza uvunguni, nyuma ya kabati, paa na kila uchochoro wa chumba hicho. Alitupa macho paani na sakafuni.


Macho hayo yenye uzoefu hayakumfanya ashuku chochote. Kwa kila hali kilionekana chumba cha kawaida, chenye kila hadhi ya chumba cha hoteli ya kisasa. Mlango wa maliwatoni uliokuwa wazi nusu ulimwonyesha marumaru ya kung’ara iliyofunika sakafu na ukuta mzima, huku masinki ya choo, ya kunawia na kuogea, yaking’ara kwa usafi. Kitanda futi sita kwa sita kilifunikwa vizuri kwa shuka nzito ya mauamaua. Kando ya kitanda hicho ilikuwepo televisheni ndogo, friji na shefu ya vitabu. Juu ya kitanda kulikuwa na mashine ya hewa ambayo iliendelea kusambaza hewa safi chumbani humo. Meza ya pili chumbani humo ilibeba kompyuta, printer na begi la nguo.


Kwa kila hali, kilikuwa chumba cha kawaida, kama ambavyo msichana aliyekikodi alivyokuwa wa kawaida. Tulia Joram! Akili yake ilimwambia. Si kila wakati ni wakati wa hatari. Sio kweli kuwa kila chui huvaa ngozi ya kondoo! Mona Lisa ni msichana wa kawaida kabisa. Anahitaji ushauri tu katika riwaya yake ya upelelezi.


Hata hivyo, zile hisia za u-Joram Kiango ziliendelea kumpigia kengele za kuwa makini na msichana huyu; yote yang’aayo si dhahabu, nafsi yake nyingine ilimnong’oneza.


“Mbona hunywi?” Mona ambaye aliingia chumbani humo kimyakimya alimzindua Joram.


Joram alitabasamu, “Kinywaji cha upweke kamwe hakipandi, mpenzi. Ungekuwa chumbani humu, macho hayo mazuri yakiendelea kuniloga, chupa hili lingekuwa limekauka kitambo,” alisema kwa utani.


Kauli hiyo ilimfanya Mona Lisa aangue kicheko. “Kweli






hukupata mapenzi ya bibi,” baadaye alisema. Akaketi na kujimiminia toti mbili za pombe hiyo kali na nusu glasi ya soda ya maji. “Unalazimisha utani hata pale ambapo haupo! Nina nini mie hata kuwepo kwangu kukufanye unywe mzinga mzima kama huo!”


“Hujui una nini!” Joram alimjibu, kauli ambayo ilimfanya Mona Lisa azidi kucheka huku haya zake zikianza kumrudia. Shingo yake ndefu aliilaza upande kidogo, macho yake kiasi yakilainika huku vidole vikiitua glasi ya kinywaji chake na kuanza kutekenyana.




Ilikuwa picha ya kusisimua, picha ya kuvutia, picha ambayo, kwa muda ilifanya fikra za Joram zichukue likizo na nafasi yake kuchukuliwa na hisia za ajabu, hisia za kimaumbile zilizomfanya Joram Kiango awaze; faraja iliyoje kumkumbatia msichana huyo akiwa kama alivyozaliwa! Fahari iliyoje kukumbatiwa na mikono hiyo laini! Hadhi iliyoje kumbusu mrembo kama huyu!


Mara Joram akainuka.


Mona Lisa akazinduka, “Vipi, mbona umeinuka?” alimuuliza kwa mshangao.


“Nadhani ni wakati muafaka wa kuondoka.”


“Kwa nini? Nilidhani kwa kuwa huko hapa ningefungua kompyuta na kuchapa sura mbili tatu za kitabu changu ili uziangalie,” Mona aliongeza.


“Hata mimi ningependa iwe hivyo,” Joram alimjibu. “Kwa bahati mbaya haiwezekani.”


“Kwa nini?”


“Unamfahamu mtu anayeitwa Mike Tyson?”


“Kama ni yule bondia, Mmarekani mweusi, nadhani namfahamu.” Mona Lisa alimjibu, kiasi akionyesha mshangao.


“Unafahamu kuwa aliwahi kufungwa?”


“Nafahamu. Alibaka,” Mona alijibu kwa haya kidogo.


“Nani anafahamu kuwa alibaka?” Joram alihoji. “Kinachofahamika ni kuwa alimkaribisha msichana mrembo chumbani kwake hadi kesho yake. Siku mbili baadaye msichana huyo alidai kuwa amebakwa. Tyson akaenda jela.”


Mona Lisa alimkazia Joram macho. Kiasi fulani hasira na mshangao vilijitokeza katika macho hayo, ingawa sauti yake






ilikuwa ileile ya upole, “Sijakuelewa, Joram. Una maana kuwa mimi pia naweza kukugeuka kuwa ume… umenibaka!”


Joram akatabasamu kumtoa wasiwasi. “Ninachojaribu kusema hapa,” alimwambia. “Ni kile ambacho watu wengi hapa nchini hawajakitia akilini. Kuwa bunge letu limeshapitisha sharia kama ileile iliyomfanya mbabe Mike Tyson asote gerezani kwa muda mrefu. Mimi ni mtu mwenye maadui wengi katika nchi hii. Na nimejikaribisha mwenyewe chumbani humu. Chochote kinaweza kutokea.


Joram alipomwona Mona Lisa bado kaduwaa, aliongeza harakaharaka, “Isitoshe, nina miadi na msichana mrembo sana jioni hii hotelini kwangu.”


“Msichana gani tena huyo?” Mona Lisa aliuliza. “Anaitwa Mona Lisa. Kwani hutakuja?”


Mona Lisa aliangua kicheko. Bila kutegemea alijikuta akimkumbatia Joram, ambaye, yeye pia bila hiari yake, alijikuta akimbusu.


Mona aliupokea ulimi wa Joram. “Ni-ta-ku-ja!” alinong’ona kwa taabu.


W 2 X


BONGO WA MWALIMU NYERERE! Joram alisoma kwa sauti maneno hayo na kuachia tabasamu jepesi. Aliinua uso wake kumtazama Mona Lisa ambaye aliketi kimya,


upande wa pili wa kijimeza kilichowatenganisha, macho yake yakimtazama Joram kwa shauku.


“Hili ndio jina la kitabu chako?” Joram alimuuliza.


“Ndiyo. Jina la awali… kama kitafaa na kama kitapata mchapishaji, nadhani kwa kawaida atakuwa na uhuru wa kuchagua jina litakalofaha zaidi,” Mona alieleza.


Joram akatabasamu tena kabla ya kuongeza, “Sijasema kuwa halifai. Naliona kama jina kali na zito sana kwa riwaya ya kwanza kwa mwandishi. Lakini… ni riwaya yenyewe itakayoafikiana au kutofautiana na jina…” akawasha sigara nyingine. Kabla ya kuivuta alimeza fundo moja la wiski yake, ambayo kama kawaida aliinywa kavukavu. Kisha, akameza fundo la moshi na kuuhifadhi katika mapafu yake kwa muda wa robo dakika hivi kabla ya kuupeperusha angani, taratibu, huku macho yake yakiwa tayari yamezama na kupotelea katika msitu wa maandishi yaliyolala juu ya mapaja yake.


Ni usiku. Usiku wa manane. Isipokuwa kwa milio ya magari, mingurumo ya ndege angani na mashine ya kurekebisha hewa, jiji la London lilikuwa kimya, kama lililokufa. Kama taa za barabarani zisingekuwa ziking’ara kama ilivyo kawaida,






tungeweza kusema kuwa mji huu maarufu duniani ulikuwa kuzimu.


Kama ilivyo tabia ya maumbile, utulivu huu uliwahusu hawa, uliwasahau wale. Katika jengo moja kongwe jijini humo, lililohifadhi hospitali maarufu ya St. Thomas, watu mbalimbali walikuwa wakitaabika. Wako waliokuwa wakitaabika kwa mateso ya maradhi, wako pia waliokuwa wakitaabika kwa kuhangaikia wagonjwa wao. Madaktari, manesi na wataalamu mbalimbali wa uhai wa binadamu pia walikuwa katika hekaheka kubwa.


Wengi kati ya hawa, hali haikuwaruhusu kujua kama huo ulikuwa usiku wa manane au mchana.


Miongoni mwao alikuwamo mgonjwa mmoja mashuhuri, Julius Nyerere. Alikuwa amelala kwa utulivu baada ya kuteseka sana. Saratani ya damu, iliyomvamia ghafla, ilikuwa imemtesa sana toka kijijini kwake Butiama, jijini Dar es Salaam hadi hapa Uingereza. Maradhi haya yalikataa kuitii kila aina ya dawa yaliyopatiwa. Yalikataa kuwaheshimu madaktari bingwa waliokesha usiku na mchana kumsaidia. Yalikataa kusikia maombi na kilio cha maelfu ya Watanzania waliomtakia kila la heri. Yalikataa katakata, angalao kuitii mizimu ya Wazanaki, ambayo Mwalimu hakuwahi kuipuuza.


Na sasa Mwalimu alilala kwa utulivu katika chumba cha wagonjwa mahututi, mabingwa wa maradhi hayo duniani wakiendelea kukuna vichwa vyao na kupekua tena na tena kamusi ya misahafu ya taaluma zao…


Joram aliinua uso na kumtazama Mona Lisa usoni. Msichana huyo, ambaye alikuwa akimtazama Joram kwa makini pindi akiyasoma maandishi yake aliyakwepa macho ya Joram Kingo kwa aibu. Badala yake alichukua glasi ya mvinyo aliokuwa akinywa na kumeza mafunda mawili matatu.


“Umeandika wewe, riwaya hii?” Joram aliuliza taratibu. “Ndiyo… kwani inafaa?” aliuliza kwa sauti ya juu kidogo.



Joram akacheka. “Huko hatujafika,” alimjibu. “Niambie jambo moja! Ulikuwa London wakati wa maradhi ya Mwalimu Nyerere?”


“Ndiyo na hapana,” lilikuwa jibu la Mona Lisa. “Una maana gani?”






“Maana yangu ni kuwa, kweli nimewahi kufika London. Na nilifika huko wakati wa maradhi ya Mwalimu Nyerere. Lakini pia sio kweli kwa maana unayofikiria wewe. Sikufika St. Thomas wakati Mwalimu akiwa amelazwa pale. Sikuhusika kwa namna yoyote na matibabu yake. Nilichoandika hapo ni utunzi tu wa kawaida kabisa, kwa lengo la kumuenzi kisanii.” Joram alimeza funda jingine la wiski. Akawasha sigara nyingine. Kisha, akazama tena katika mswada huo ambao


haikuwa siri tena kuwa ulianza kumvutia;


… Wakati Mwalimu akipambana kiume na maumivu hayo, pale nje, katika chumba cha mapumziko, kundi jingine dogo lilikuwa likipambana na mengi. Kundi hili lilijumuisha wapenzi na waumini wa Mwalimu.


Alikuwapo Mama Maria, siku ya tatu leo hajapata usingizi. Moyo wake uligubikwa na huzuni huku macho yake yakishindwa kuhimili machozi ambayo yalimtoka mara kwa mara. Kando ya Mama Maria binti yake… alitulia kimya, macho kayafumba akihesabu rozari. Ingawa sauti ilikuwa haitoki bado midomo yake iliashiria kuwa alikuwa katika sala ndefu, sala iliyoanzia Butiama, akaendela nayo hadi Dar es Salaam; akaruka nayo Bahari ya Atlantic na sasa anaendelea nayo katikati ya jiji la London.


Pembeni, ya kochi, alikuwepo Makongoro Nyerere na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru. Walikuwa wakinong’ona kwa sauti ndogo; Makongoro, kiko akiwa amekisahau, Mzee Kingunge makeke yakiwa yamemtoka.


Hawa, pamoja na baadhi ya Watanzania waishio London, walijumuika katika mkesha huo, macho yao yakiwa yameelekezwa mlangoni, kumsubiri daktari kwa shahuku kubwa.


“Weitaa!” Joram aliita bila kuinua uso wake toka kwenye maandishi hayo. Kinywaji chake kilikuwa kimekwisha. Alimwelekeza mhudumu huyo kumletea kinywaji kingine kwa mkono, bila kutoa sauti.


Macho yake yalihama kutoka kwenye mswada huo pale tu alipoyainua kumtazama Mona Lisa, ambaye alitabasamu pia kwa aibu. Akayarejesha kwenye maandishi na kuendelea.


Nusu kilomita tu toka hospitalini hapo, katika moja wapo






ya hoteli za Sheraton zilizotapakaa jijini humo, kundi jingine dogo lilijifungia katika chumba mahususi likijadili hatima ya Mwalimu. Hili lilikuwa kundi la wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali. Mmoja wao alikuwa mtu mfupi, mnene mwenye kipara kilichong’ara kana kwamba hakuwahi kuota nywele toka utotoni. Kati ya kundi hili la watu wanne kati yao hakuna aliyemfahamu kwa jina. Walichofahamu ni kuwa alikuwa ameingia jijini humo usiku huohuo kwa ndege ya jeshi la anga la Marekani. Alijitambulisha kwa jina mola la Ignatius, ambalo lina asili ya Kigiriki kwa maana ya kitu kama moto au joto. Lakini kila mmoja alijua kuwa lilikuwa jina la bandia. Alijitambulisha pia kuwa alikuwa na ujumbe mahususi toka serikali ya Marekani, ingawa kila mmoja alihisi kuwa alikuwa mjumbe wa CIA.



Mwingine katika kundi hilo alikuwa daktari bingwa wa upasuaji wa vichwa na ubongo, Dkt. Brown Abraham. Katika dunia ya wanataaluma mabingwa wa upasuaji hakuna ambaye hakupata kumfahamu, sifa ambayo iliongezeka maradufu pale alipofanikiwa kuhamisha ubongo wa binadamu na kuupandikiza katika kichwa cha kondoo na ule wa kondoo akauweka kwa binadamu. Viumbe hao waliishi kwa saa ishirini na nne kabla ya kufa. Hata hivyo, inaaminika kuwa waliuawa na wanataaluma wenzao ili kuepusha kasheshe ambayo ingeweza kutokea. Dkt. Abraham mwenyewe aliadhibiwa kwa kupokonywa leseni yake kwa kipindi chote cha uhai wake. Hata hivyo, hatua hiyo haikufanya wanataaluma waliomheshimu wasite kumtumia kwa siri kila walipokwama…


Kinywaji cha Joram kikafika. Akainua glasi na kumeza funda la pili. Akawasha sigara nyingine na kupeperusha moshi angani. Akageuka kumtazama Mona Lisa. Macho yao hayakugongana. Mona Lisa alikuwa amegeuka kumtazama mlevi mmoja ambaye alikuwa ameiacha meza yake na kusimama katikati ya uwanja akicheza mayenu kwa nguvu kuliko muziki wenyewe ulivyoashiria.


Mona Lisa alicheka. Joram akatabasamu.


Akarejea kwenye riwaya yake.


…Mwingine chumbani humo, ambaye hasa alichukua






nafasi ya uenyeji alijitambulisha kama mtumishi wa ubalozi wa Marekani nchini humo, ingawa wajihi wake ulimweka miongoni mwa wale maafisa wa ubalozi wenye nyadhifa za ziada. Kwa mfano, ni yeye aliyetuma tiketi ya ndege na fedha zilizomwezesha Dkt. Abraham kuwa hapa leo toka Afrika Kusini alikokwenda kwa mapumziko. Ni yeye pia aliyekodi chumba hiki na kufanikisha kikao hiki. Yeye, kwa mujibu wa kadi yake, alitajwa kama Thomas MacBain, mwambata wa utamaduni.


Mtu wa nne na wa mwisho katika hafla hii alitajwa kama Dkt. Fabian Winston, bingwa katika matibabu ya kansa ya damu katika hospitali ya St. Thomas jijini humo.


“Ninachotaka kufahamu kabla ya yote,” Ignatius alikuwa akisema. “Ni iwapo, kwa utaalamu wako Dkt. Winston, ipo nafasi yoyote ya Julius Nyerere kupona.”


“Kwa hatua aliyofikia, nafasi hiyo ni finyu sana,” Dkt.


Winston alieleza.


“Na katika hali kama hiyo Dkt. Abraham,” Ignatius aliendelea. “Ubongo wake bado uko katika kiwango chake kwa asilimia mia moja?”


Dkt. Winston alikuwa na tabia ya kukohoa na kisha kukuna kichwa kabla hajaingia katika uchambuzi wa kitaalamu. Alifanya hivyo. “Hakuna binadamu ambaye ubongo wake uko asilimia mia moja, Bw. Ignatius, awe mzima awe mgonjwa. Isipokuwa, katika hatua hii, ninachoweza kusema ni kuwa hakuna namna yoyote ambayo inaweza kufanya virusi vya kansa ya damu vishambulie ubongo wake. Taarifa ya kitaalamu aliyoileta Dkt. Winston hapa inaonyesha kuwa ubongo wake haujaathiriwa.


Ignatius alishusha pumzi ya faraja. “Kwa hiyo,” baadaye alisema. “Tunaweza kuendelea na mpango wetu bila wasiwasi wowote.”


“Unajua, hujatuambia hadi sasa ni mpango gani ulionao ambao umetukutanisha hapa ghafla, katika mazingira ya usiri kama haya,” Dkt. Abraham alisema.


“Tunauhitaji ubongo wake kabla hajafa.”


“Ubongo wa Julius Nyerere!” Dkt. Abraham na wengine wote chumbani humo walitokwa na macho ya mshangao.


“Siamini masikio yangu!” Dkt. Winston alisema. “Nadhani



hujui hospitali ile inavyolindwa! Si hayo tu, muda wote amezungukwa na madaktari bingwa toka pembe zote za dunia. Hapa tunavyoongea wako wenzangu wamekizingira kitanda chake wakimhudumia.”


“Tunataka ubongo wake… kwa bei yoyote ile,” Ignatius alisisitiza, akamgeukia Dkt.Abraham, “Kazi hiyo inawezekana?” “Bila hofu ya ulinzi mkali uliopo, bila vipingamizi vya daktari wenzangu, manesi na jamaa zake wanaokesha pale usiku na mchana, mimi nahitaji dakika ishirini tu kuhamisha ubongo


wake na kuweka…”


Ignatius alimkatiza, “Achana na hofu ya ulinzi uliopo. Sahau madaktari waliomzunguka. Hayo mwachieni McBain. Anajua la kufanya. Kwa hili hakuna hata kujadili bajeti.


Amepewa uwezo wa kutumia kiasi chochote cha fedha zinazohitajika. Amepewa amri ya kutumia silaha yoyote atakayoona inafaa. Ikibidi hospitali nzima ipitiwe na usingizi wa pono kwa hizo dakika unazohitaji kukamilisha kazi yako. Akilazimika kuua kwa hili ruksa.”


Dkt. Abraham alitokwa tena na macho ya mshangao. “Kwa nini mnauhitaji kiasi hicho ubongo wa binadamu wa kawaida?” Ignatius alitikisa kichwa kwa masikitiko na kusema, “Mie pia natimiza amri niliyopewa. Lakini kwa machache ninayoyajua juu ya Julius Nyerere hakuwa binadamu wa kawaida. Fikiria, Mwafrika gani wa kawaida aliyeweza kuiyumbisha CIA, BOSS, MOUSAD na wengineo kwa miaka nenda rudi hadi anaachia madaraka kwa hiari yake? Waulize akina Nkurumah, akina Lumumba, akina Mondlane na wengineo. Waulize kipi


kiliwakuta.”


Haya, fikiria Mwafrika gani ameweza kufanya kile ambacho marais watano wa Marekani walishindwa kufanya. Aliweza kumng’oa Idd Amin na kuweka utawala aliotaka nchini Uganda. Sisi Marekani tulishindwa kufanya hivyo Vietnam, Kambodia, Iran na hata Congo.


Fikiria alivyoiyumbisha IMF na Benki ya Dunia hata zikashindwa kutekeleza sera zao katika nchi mbalimbali za Kusini mwa dunia kwa wakati muafaka hadi alipoachia madaraka.


Fikiria alivyoweza kuitawala Tanzania, nchi masikini yenye






makabila zaidi ya mia na ishirini na dini mbalimbali kuwa kitu kimoja na kupata hadhi kubwa duniani. La… hakuwa mtu wa kawaida. Na tunauhitaji ubongo wake katika maabara zetu, kwa bei yoyote.


“Mpaka hapa riwaya yako inaonyesha matumaini makubwa,” Joram alimwambia Mona Lisa, akiitua mezani na kuanza kushughulikia sigara nyingine. “Ina mvuto na msisimko wa kutosha ingawa sifahamu dhamira yako kuu. Lakini lazima nikuonye mapema, mimi si mtaalamu wa lugha wala uhakiki. Hivyo, sitakusaidia sana kwa vitu kama tamathali za semi mfano: takriri, tashbiha, tafsida na kadhalika. Hata hivyo, kwangu mimi imefika mahala ambapo natakiwa nianze kuisoma kwa makini zaidi ili niwe katika nafasi ya kujaribu kutoa ushauri wangu mdogo.”


“Naamini hautakuwa mdogo kama unavyofikiria wewe. Kuna mengi humo ndani ambayo ama hayaaminiki ama hayawezekaniki,ambayo naamini kwa uzoefu wako hutasita kunidokeza ili ama niyarekebishe kama yanarekebishika, au nikitupilie mbali kama hayarekebishiki,” Mona alimwambia kwa sauti yake yenye haya.



Joram alimzawadia tabasamu, bila shaka la kumtia moyo. “Sidhani kama suala la kukitupa litakuwepo,” alimwambia. “Kama kingekuwa kitabu cha kutupwa nisingesoma zaidi ya kurasa mbili. Ningekinai zamani na kukurudishia…”


Mhudumu alitokea na kumwongezea Joram kinywaji. Mona Lisa alikataa kwa maelezo kuwa mvinyo aliokunywa ulikuwa unatosha.


“Nadhani nirudi mjini,” alimwambia Joram taratibu. “Mara hii?” Joram aliuliza. “Una haraka gani, wewe


msichana? Unajua nimeanza kukuzoea. Halafu, unajua kuwa hatujafahamiana hata kidogo? Nilidhani tutakaa, tuongee, tule chakula cha usiku pamoja na ikiwezekana tuingie muziki.”


Mona aliachia moja ya zile tabasamu zake za kusisimua, tabasamu ambalo lilimfanya Joram aanze kujutia mzaha wake. “Nashukuru sana kwa ofa yako. Ni vile tu sikujiandaa, ningechangamkia. Nitakupitia kesho kutwa nione umefikia wapi kwenye riwaya yangu.”


“Kesho kutwa! Kwa nini isiwe kesho!” Joram alisema






akiinuka. Akauchukua mkono wa Mona Lisa na kuufinya kidogo, kabla hajaubusu. Kisha, aliutua taratibu huku akisema, “Kumbe! Haya nimeelewa.”


“Nini?” Mona Lisa aliuliza kwa mshangao.


“Nimeelewa kwa nini umekataa ofa yangu ya kuingia muziki.”


“Umeelewa nini?” “Unaogopa!” “Naogopa nini?” “Mchumba wako.”


Mona Lisa akaangua kicheko. “Mchumba! Mchumba gani?


Mie bado niko single. Sina mume wala mchumba,” alisema. “Umeanza kuwa mwongo,” Joram alimwambia. “Pete hiyo


hapo inakusuta. Kama si ya uchumba ni ya ndoa.”


Mona alicheka tena. “Watu wengi wanasema hivyo,” baadaye alisema. “Kila mtu anadhani hii ni pete ya uchumba. Hii naivaa kama mapambo tu, jamani,” alisema akiishikashika.


Joram alionyesha kutomwamini.


“Kama huamini,” Mona alisema akiivua. “Nitakuachia uivae hadi kesho kutwa nitakapokuja.”


Joram aliipokea na kuitazama. Ilikuwa pete kubwa, iliyotengenezwa kwa mchanganyiko wa madini ya Tanzanite na ruby. Kwa ndani ilikuwa na kito kinachong’ara, ambacho Joram hakuweza kujua mara moja kama ilikuwa almasi au kioo.


“Hii ni pete ya thamni kubwa,” Joram alisema baada ya kuitazama. “Unaiacha kwa roho nyeupe?”


“Bila wasiwasi.”


“Mchumba wako utamwambiaje?”


“Si nimeshakwambia sina mchumba?”


“Uliipata wapi basi pete ya bei mbaya kama hii?”


“Ni hadithi ndefu. Tuiache hadi kesho kutwa nitakapo kuja.”


Huku akimshika mkono, Joram alimwuliza, “Bado umeng’ang’ania kesho kutwa. Mimi nakuhitaji hapa kesho.”


“Kesho! Ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Kurasa mia mbili na arobaini utakuwa umezimaliza kesho!”


Joram alicheka. “Bila shaka,” alisema. “Nina tabia ya






kuamka saa kumi za alfajiri na kufanya mazoezi hadi saa kumi na mbili. Toka hapo kazi yangu huwa ni kusoma magazeti yote yaliyochapishwa nchini siku hiyo. Kama naweza kusoma magazeti ishirini na tatu, yenye zaidi ya kurasa kumi na sita kila moja,nitashindwa kusoma na kuimaliza riwaya tamu kama hii kabla ya saa nne asubuhi?”



Mona Lisa alimtazama kwa mshangao. Hakuelekea kuamini. Hata hivyo, alisema, “Nitajitahidi kuja kesho jioni basi, kama nitapata wasaa.”


“Nitakuwa juu ya kiti hikihiki nikikusubiri,” Joram alimwambia.


Mona akaendea mojawapo ya magari ya kukodi yaliyokuwa nje ya hoteli na kutokomea.


Mara tu Mona Lisa alipotoweka machoni mwake hisia za upweke zikamjia Joram Kiango. Alihisi hali ambayo hakupata kuhisi huko mbeleni, hali ya kitu kama unyonge au kupungukiwa kitu fulani.


“Nimeanza kuwa mzee, nini?” alijiuliza akiichezea pete aliyoachiwa. Jana alimtazama Mona Lisa kwa namna iliyofanya ajiwe na hisia za mapenzi na kujenga matumani ya mahaba mazito toka kwake, hisia zilizomfanya hata afikie hatua ya kumkumbatia na kumbusu, lile busu moja tu, busu la kwanza, ambalo lilimloga zaidi.


Leo alijitahidi vilivyo kuziweka nyuma ya kisogo chake hisia zile ingawa hakufanikiwa sana. Huyu ni msichana mdogo tu, Joram. Alijinong’oneza mara kwa mara. Ndiyo, ni mzuri… na mwili wake unafariji… lakini bado ni mdogo tu, tena anahitaji msaada wako. Uko wapi ule ushujaa wako?... Uko wapi ule msimamo wako usiotetereka? Ni hayo ambayo muda wote yalikuwa yakipiga kengele katika kichwa chake hadi pale Mona Lisa alipoinuka na kuaga. Vipi sasa ajisikie kama anavyojisikia? Vipi afikie hatua ya kukubali kubaki na pete yake?


Nadhani ni kweli… Uzee unaninyemelea, alinong’ona tena, akiagiza kinywaji kingine.


“Leta chupa nzima… Huchoki kuleta hivi vitoti? Alimwamuru mhudumu.






***


“Mpenzi nimerudi,” sauti ilimzindua Joram Kiango. Ilikuwa ile sauti tamu, ambayo muda mfupi uliopita ilikuwa ikimfariji. Joram aliinua uso wake kumtazama Mona Lisa. Kama muda mfupi uliopita alikuwa mzuri sasa alikuwa malaika. Alikuwa amejipulizia pafyumu nyepesi iliyofanya hewa iliyomzunguka ijae hisia za mahaba. Kama awali uso wake uling’ara, sasa ulimeremeta kwa aina ya poda au mafuta aliyoyatumia. Nywele zake, ambazo awali zilifungwa kichwani sasa ziliachiwa na kujimwaga hadi mabegani mwake na, hivyo, kufanya suala la kujua kama msichana huyu ni Mbantu, Mhindi au Muajemi liwe tatizo. Kilichohitimisha u-malaika wake katika ujio wake huu lilikuwa vazi lake. Alivalia vazi la usiku, nguo laini,


iliyofichua vilivyo ubora wa umbile lake.


Joram alihamisha macho yake toka juu ya umbo hilo la kuvutia na kuitazama saa yake, tano na dakika arobaini. Saa tatu zilikuwa zimepita toka Mona Lisa alipoondoka hapo kwa ahadi ya kurudi kesho. Dakika ishirini zilibakia kabla ya kuingia siku mpya ya Jumamosi. Na zilisalia saa kumi na mbili kabla ya kufikia miadi yao. Kulikoni?


Mona Lisa alikuwa kama anayeyasoma mawazo ya Joram. “Naona hujaridhika na ujio wangu,” alisema. “Samahani sana kama nitakuwa nimekuudhi. Hisia za upweke zilinibana


nikashindwa kuvumilia. Naweza kuondoka kama…” “Hapana, hapana,” Joram alisema akiinuka kumkaribisha.




“Ujio wako umenifurahisha sana . Ni vile tu sikukutegemea hadi kesho. Keti, tafadhali… jisikie uko nyumbani,” alisema akimshika kiuno na kumkumbatia. Akambusu, busu ambalo lilijibiwa kwa mbwembwe zote.


“Utakunywa nini?”


“Kama hutojali nitapenda kuonja hicho ulichokunywa wewe. Ni John Walker, sio?”


“Ndiyo.”


Joram aliagiza glasi ya pili. Tayari alikuwa amemaliza chupa nzima ya wiski hiyo, jambo ambalo aliamini kuwa lilitokana na hisia za upweke toka pale Mona Lisa alipoondoka. Hivyo, kichwa chake alikiona chepesi huku macho yake yakiwa mazito kiasi. Lakini hilo halikumfanya ashindwe kuiona tabia ya kinyonga






katika msichana huyu. Ama nusu glasi aliyokunywa ilikuwa imemaliza haya zote, ama alikuwa akinywa toka alipoondoka hapa.


Alikuwa hazungumzi sana. Lakini alichekelea kila kauli ya Joram huku akitia neno hapa na pale, jambo ambalo lilimfanya Joram acheke. Aidha, aliongea kwa maneno na vitendo. Mara kwa mara mikono yake iliruka na kutua hapa na pale katika mwili wa Joram. Mara achezee vidole vyake. Mara mkono utue na kutulia juu ya paja lake.


Ukiwa usiku mwingi, upepo mwanana wenye marashi ya karafuu ukiwapepea toka visiwani. Kama binadamu, kama mwanamume rijali Joram hakuwa na uwezo wa kustahimili hali ile. Bila kutegemea alijikuta yeye pia akiingia katika mchezo wa mikono. Alimshika hapa na pale. Mona alionekana kuridhia. Taratibu walianza kubusiana.


Mara Mona aliinuka na kumshika Joram mkono. “Twende zetu,” alimwambia.


“Wapi?”


“Kwani huna chumba?”


Ilimshangaza Joram kuona kuwa pamoja na mwili wake kusisimkwa na matarajio, roho yake ilikuwa nzito. Hisia fulani, ambazo hakuweza kuzifafanua ziliashiria shari badala ya heri. Hivyo, wakati akiongozwa kupelekwa chumbani kwake, alihisi kama mwanakondoo anayepelekwa madhabauni kutolewa kafara, badala ya kijana mzuri, aliyefuatana na msichana mzuri, anayetarajia kuufurahia ujana wake.


‘Umeanza kuwa mzee, Joram…’ kitu ulani kilianza tena kumnong’oneza, kauli ambayo ilimezwa pale kitanda kipana kilipowapokea na kuwakumbatia.




***


Muda mfupi baadaye. “Joram!”


“Na…am!”


“Unajua unachokifanya?” “Si…jui.”


“Ni kweli hujui… Hujui kuwa unabaka! Na unambaka afisa


wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi,” sauti ya Mona ilisema,






ikisindikizwa na kicheko.


“Sikujua,” Joram alijibu. “Nilidhani mimi pia nimebakwa.” Kicheko.


“Ni wazi kuwa hujaipitia sharia ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”


“Siijui.”


“Miaka ishirini na nane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haikutoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”


Kicheko.


“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”


“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”


Kicheko. Usingizi uliwachukua huku wakiwa wamekumbatiana, wakiwa bado wanacheka.


W 3 X


I kitu kama unyevunyevu uliomgusa ghafla ubavuni, ambacho kilimfanya Joram Kiango aamke toka katika usingizi wa pono, uliokuwa umemchukua. Akiwa bado ameyafumba macho yake aliuondoa mkono wake toka kifuani mwa msichana aliyelala kando yake na kuutuma kuupeleleza unyevunyevu huo. Vidole vyake viligusa kitu kama maji mazito mithili ya uji uliopoa. Kitu gani hiki? Alijiuliza akiutoa mkono


wake huko ulikokuwa na kuuleta puani ili kuunusa.


Ilikuwa harufu ngeni, lakini aliyoifahamu vilivyo. Harufu ya damu! Mara moja akayalazimisha macho yake, ambayo aliyaona mazito kuliko kawaida yake, kufunguka.


Damu! Mkono wake ulikuwa umejaa damu!


Hakuamini. Akakiinua kichwa chake kizito kumtazama msichana aliyelala kando yake. Alikuwa amelala kwa utulivu kupita kiasi. Uso wake ulikuwa na tabasamu lililofanya kama kusahauliwa pale. Kifuani alikuwa na tundu kubwa lililokuwa likiendelea kuvuja damu ambayo ilianza kuganda, damu nzito ambayo ndiyo iliyokuwa imetambaa hadi kuutembelea ubavu wa Joram.


Hii ni ndoto, au… Joram alijiuliza akiinuka harakaharaka. Kwa dakika moja au mbili aliduwaa wima, katikati ya chumba hicho, akimtazama kiumbe aliyepoa pale kitandani. Kiumbe ambaye muda mfupi uliopita alikuwa hai, hai kuliko uhai






wenyewe, wakacheka na kucheza pamoja hadi usingizi ulipowatenganisha, kiumbe ambaye sasa alikuwa marehemu. Katika kipindi hicho kifupi cha kuduwaa mbele ya maiti, mambo elfu na moja yalipita katika kichwa cha Joram Kiango. Yalimjia mfululizo, bila mpangilio, kiasi cha kufanya ashindwe kujua aanzie wapi aishie wapi katika kuutafakari mkasa huo mzito uliomsibu. Kwanza, alishangazwa na uzito wa ubongo wake katika kufikiri. Aliiona akili yake kama iliyoduwaa, kinyume cha kawaida yake anapokuwa katika masaibu hayo. Pia, aliduwazwa na udhaifu wa mwili wake. Hata macho yake alihisi kuwa anafanya kuyalazimisha kuwa wazi. Vinginevyo, alijisikiakama mtu aliyekuwa tayari kuendelea kupiga usingizi wake, hadi wakati muafaka, atakapoamka na kisha kuanza


kujiuliza nini kinachotokea.


Changamka Joram! Uko hatarini! Hatari yenyewe kubwa kuliko unavyofikiria! Amka! Chemsha ubongo wako! Sauti fulani, toka nyuma ya kisogo chake ilimhimiza.


Joram aliitii. Dakika iliyopita alikuwa ameduwaa, ubongo ukiwa umeduwaa. Dakika iliyofuata akili yake ilikuwa makini. Alianza kwa kujikumbusha kuwa kwanza alihitaji kutuliza akili yake. Katika hali hiyo ya utulivu aliitazama saa yake. Ilimwambia kuwa ilikuwa alfajiri, saa 11:45. Hata alipotupa macho nje aliona miale ya mwanga wa jua ikianza kuashiria mapambazuko.


Baada ya hapo Joram aliutupia macho tena mwili wa marehemu. Hakuhitaji daktari kuthibitisha kuwa alikata roho kitambo. Hali kadhalika, hata kipofu angejua kuwa kifo chake kilitokana na tundu la risasi iliyopenya kifuani mwake na kusababisha damu nyingi imwagike toka mwilini mwake.



Nani aliyemuua? Kwa nini amemuua? Aliwezaje kuingia chumbani humu na kufanikiwa kumuua msichana huyu asiye na hatia bila yeye kujua? Na ilikuwaje yeye Joram, mwenye maadui lukuki akaachwa hai? Hayo ni miongoni mwa mamia ya maswali yaliyokisumbua kichwa cha Joram Kiango. Hata hivyo, hakuona kama ulikuwa wakati muafaka kujaribu kutafuta majibu. Kitu fulani kilikuwa kikimnong’oneza kuwa yeyote aliyefanya mauaji hayo ya kinyama alikusudia yeye aonekane kuwa ndiye muuaji, jambo ambalo lingemfanya






achukue miaka, huku akiwa mahabusu, kuihakikishia dunia vinginevyo.


Joram hakuwa na wasaa huo, wasaa wa kukaa gerezani huku mtu fulani anayeitwa wakili akiipigania roho yake. Alikuwa mtu wa kujipigania, mtu wa kisasi kwa yeyote aliyekatisha maisha ya Mona Lisa, msichana mwenye umbo la malaika.


Harakaharaka, Joram alianza kukusanya vifaa vyake muhimu. Aliliendea begi lake. Lilikuwa wazi. Na, kama alivyotegemea, bastola iliyotumika kumuulia Mona Lisa ilikuwa humo. Ilikuwa bastola kubwa, maalumu kwa majeshi ya polisi na usalama; K.45 Joram akaifungua. Ilikuwa na risasi tano. Moja tu ilikuwa imetumika. Bila shaka ni ile iliyomuua Mona. Joram aliitia mfukoni mwake na kuifungua mifuko ya siri ya begi lake hilo.


Ilikuwa mitupu!


Silaha zake zote zilikuwa zimechukuliwa!


Akauacha mfuko huo na kuiendea meza ndogo ya chumbani humo. Macho yake yalikwenda moja kwa moja pale alipouweka mswada wa marehemu; UBONGO WA MWALIMU NYERERE.


Nao ulikuwa umetoweka!


Katika mtoto wa meza Joram aliipata simu yake ndogo ya mkononi. Akaichukua na kuitia katika mfuko wa suruali yake nyepesi ambayo aliivaa. Pia akavaa shati jeusi, viatu na kofia yake ya kawaida. Alifikiria kufuta alama za vidole vyake katika mwili wa marehemu na kila kitu chumbani humo. Wazo ambalo alilipuuza mara moja kwa kuzingatia kuwa uongozi wa hoteli ulikuwa na kumbukumbu zake zote, aidha wateja wote wa hoteli hiyo walimwona pindi akiburudika na msichana huyo ambaye sasa ni marehemu. Isitoshe, jaribio la kufuta alama hizo ni dalili ya kwanza kabisa ya mauaji ya kukusudia kwa mpelelezi mzoefu.


Mlango wa chumba ulikuwa wazi. Joram hakuutumia. Alimtupia marehemu jicho la mwisho. Huyo, akapenya dirishani kudondokea nje.


Dakika tano baadaye alikwishaliacha eneo la hoteli na kuingia katika mitaa iliyomwelekeza mjini.






***


Katika uhai wake wote wa kimatibabu Daktari Omari Shaka, hakupata kupokea mgonjwa wa aina hii, mgonjwa ambaye alijileta mwenyewe hospitali, huku akigugumia kwa maumivu, lakini akakatalia vipimo na dawa zote isipokuwa ‘kitanda’ na ‘vidonge vya usingizi tu.’ Mgonjwa huyohuyo alionekana mchovu kiafya na kiuchumi, bila kudaiwa, alitoa shilingi 50,000 kama malipo ya awali ya gharama za matibabu yake.



Daktari alichukulia siku hiyo kama siku mpya, ambayo ilianza na maajabu.


Ilikuwa ndio kwanza anaingia kazini, kushika zamu ya daktari mwenzake ambaye alimaliza saa kumi na mbili asubuhi. Ikiwa hospitali yao binafsi, mpya, iliyojengwa katika eneo la watu wenye kipato cha chini, siku zote kwao wagonjwa waliendelea kuwa bidhaa adimu. Si kwa kuwa magonjwa yalikuwa yamepungua, la; isipokuwa gharama za matibabu ndizo zilizokuwa zikiwakimbiza. Wengi waliugulia majumbani na kupoteza maisha. Wengi walikimbilia kwa waganga wa jadi ambao waliwapokonya hadi senti za mwisho bila uhakika wa tiba. Wengi, kati ya wachache waliokuja hospitalini hapo, waliondoka na madeni makubwa na, hivyo, kutorejea tena.


Hivyo, anapokuja ‘mgonjwa’ mwenye shilingi elfu hamsini mkononi, na madai ya kuujua vizuri ugonjwa wake, kwamba anachohitaji ni kitanda cha mapumziko na vidonge vya usingizi, baada ya hapo ndipo atakubali vipimo, nani amkatalie?


Alilitupa chini gazeti alilokuwa akilisoma na kuvuta jalada jipya ambalo aliliandika tarehe na kisha kumgeukia mgonjwa wake.


“Jina lako?”


“Sharif Mkono wa Birika.” “Umri?”


“Miaka sitini na tano.” “Unakoishi?” “Kinondoni B”


“Mjumbe…” na kadhalika na kadhalika.


“Una hakika kuwa usingependa kupimwa walao presha?


Unajua tuna taratibu zetu…”






“Daktari vipimo vyote utachukua. Lakini baada ya mapumziko yasiyopungua masaa ishirini na nne. Najifahamu, Daktari. Niwahishie kitanda, tafadhali.”


Alipatiwa kitanda katika chumba pekee maalumu hospitalini hapo. Kilikuwa chumba chenye vitanda vitatu, yeye akiwa mgonjwa pekee, jambo ambalo lilimfurahisha sana. Baadaye nesi alipomletea vidonge viwili vya piritons, alivipokea na kusingizia kuvimeza. Alikunywa maji matupu, akamrejeshea nesi glasi na kisha kujifunika gubigubi. Muda mfupi baadaye alisikika akikoroma kwa mbali.


Joram alikuwa amejisingizia ugonjwa ili apate nafasi ya kujificha, akiwa ametulia, ili aweze kupata fursa ya kufikiri na kutafakari kwa kina kitu gani kinamtokea, nini kinachofuata na achukue hatua zipi kukabiliana na hali hiyo.


Kutoweka lilikuwa jambo la awali na muhimu sana. Alijua kwa vyovyote usingepita muda kabla ya mauaji hayo kuarifiwa polisi na yeye angekuwa mtuhumiwa wa kwanza. Kwa tabia ya polisi wa Tanzania, na pengine kote duniania, alijua ambacho wangefanya ni kumkamata kwanza na kuanza upelelezi baadaye. Akiwa na pingu mkononi, nyuma ya nondo kubwa, Joram alijua kuwa huo ungekuwa mwisho wa ndoto yake ya kukielewa kiini cha mkasa huo na mwisho wa dhamira yake ya kumwadhibu yeyote ambaye amemuua msichana mpole kama yule, mzuri kama yule, malaika asiye na hatia yoyote.


Uamuzi wa kujificha hapa kwa muda aliuchukua mara alipotoka pale hotelini. Alijua fika kuwa pindi taarifa za mauaji zitakapowasilishwa kwenye vyombo husika, na yeye kutajwa kama mtuhumiwa, msako kabambe dhidi yake ungetangazwa. Nchi jirani na zote zilizo katika mkataba wa INTERPOL pia zingeusishwa. Hoteli na majumba yote ya wageni yangepekuliwa, madanguro na magenge yote yangekaguliwa. Hata magari mabovu na magofu yote jijini yangechunguzwa. Joram alikuwa na hakika kuwa mahala pa mwisho ambapo polisi wangepafikiria kumtafuta, ni hapo, wodini.


Kichwani mwake hakuona kama ni jambo jema sana kujisingizia ugonjwa, akichelea kuwa unaweza kumchukiza Mungu ukajikuta umekuwa mgonjwa kwelikweli.


Aliwahi kusoma mahala fulani, juu ya mtu mmoja kule



Harare, wakati ule wa shida kubwa ya mafuta kufuatia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi ile, kwamba walisubiri mgao wa mafuta tangu saa mbili usiku na kuja kuyapata saa tisa alfajiri. Magari pekee yaliyotiliwa maanani yakiwa yale yaliyobeba wagonjwa au maiti. Hivyo jamaa fulani walilazimika kununua jeneza na sanda, mmoja wao akijilaza katika jeneza hilo na kuvishwa sanda. Wakapatiwa mafuta na kuondoka zao. Lakini walipofika mbele ya safari na kusimamisha gari ili wamtoe mwenzao walimkuta tayari amekufa kikweli kweli. Msiba wa kusingizia ukaanza upya.


“Yasije yakanitokea hayo…” Joram aliwaza huku akicheka kimoyomoyo ndani ya shuka zake za hospitali alimojifunika.


Akaituma akili yake kuanza kufikiri kwa makini zaidi. Jambo la awali ambalo hakuona kuwa lilihitaji kumpotezea muda ni vipi muuaji alivyoweza kuingia chumbani mule na kumuua Mona Lisa kwa risasi, yeye akiwa kwenye usingizi wa pono. Bila shaka muuaji huyo aliwapulizia dawa ya usingizi na, hivyo, kuingia chumbani humo na kufanya mauaji yake kwa kutumia bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti bila yeye kuwa na habari.


Alihisi dawa hizo hadi sasa bado ziliufanya ubongo wake ushindwe kufanya kazi yake kwa kiwango chake halisi.


Hata hivyo, akiwa kitandani hapo, taratibu aliona kama utandu katika ubongo wake ukianza kudondoka na mambo kadhaa aliyokuwa akiyaona katika hali ya ukungu yakianza kutoweka na kuonekana katika hali yenye uhalisia zaidi.


Kilichozindua akili yake ni pale alipokumbuka kumwona Daktari Omari, wakati akimwandikia cheti, aliandika kitu kama jumatatu, tarehe 25 Septemba! Hata gazeti lililolala pale mezani pake lilikuwa la Jumatatu.


Jumatatu! Joram alishangaa. Alikumbuka vizuri sana, kwamba alikutana na Mona Lisa siku ya Jumamosi na aliingia naye chumbani mle usiku mwingi wa Jumamosi ileile. Ilikuwaje aamke, akiwa amemkumbatia Mona Lisa yuleyule, au maiti yake, siku ya Jumatatu? Inawezekana kuwa walilala chumbani mule kwa takribani saa ishirini na nne? Inawezekana!


Joram aliituma akili yake kufikiri. Alizirudisha fikra zake






kama mkanda wa picha toka pale Mona aliporejea ghafla na kumwambia “Mpenzi nimerudi…” kinyume cha rai yake ya awali kurudi kesho yake. Aliufikiria uchangamfu wake uliomfanya ajikute yuko naye chumbani. Aliufikiria utundu wake kitandani uliopelekea ajione kuwa yuko peponi anayeburudishwa na malaika halisi. Akaifikiria ile kauli yake ya mwisho, kabla usingizi haujampitia.



Muda mfupi baadaye.


“Ni kweli hujui… Hujui kama unabaka. Na unambaka afisa


wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi…” Kicheko.


“Sikujua… nilidhani mimi pia nimebakwa.” Kicheko.


“Ni wazi kuwa hujaipitia vizuri sheria ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”


“Sijui.”


“Miaka ishirini na minane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haitoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”


Kicheko.


“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”


“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”


Kicheko. Usingizi…


Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyomjia Joram hayo yalikuwa maongezi yake ya mwisho na Mona Lisa kabla hajaamka na kujikuta akiwa amekumbatia maiti yake, tundu kubwa la risasi kifuani pake likiendelea kuvuja damu.


Huo ulikuwa usiku wa Jumamosi au alfajiri ya Jumapili. Kilichomshangaza ni hii hadithi mpya ya kuwa leo ni Jumatatu. Ukweli ni upi, Jumapili au Jumatatu?


Joram hakuona kama alikuwa na haja ya kuupoteza muda wake kufikiria kama leo ilikuwa Jumapili au Jumatatu. Kama daktari ameandika tarehe ya Jumatatu na kama hata gazeti lilikuwa la Jumatatu, kwa vyovyote siku ya leo ni Jumatatu. Alichohitaji kufanya ilikuwa ni kukusanya akili yake ili imwambie kitu gani kilimtokea hata akalala kwa saa ishirini na nne bila kujua kinachoendelea.


Ilikuwaje? Alijiuliza.






Taratibu, ule utandu uliokuwa ukiudumaza ubongo wake ukaanza kumtoka na picha mpya kuingia akilini. Ilikuwa kama mkanda wa video ambao unarudishwa nyuma na kuchezeshwa upya.


Sasa alikumbuka vizuri kabisa kuwa mara baada ya Mona kumwambia, “Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…” na usingizi kuwachukua, Mona Lisa alitoweka.


Joram alibaini kutoweka huko pale alipoamka na kushituka mida fulani baina ya saa tatu au nne na kujikuta peke yake. Ubavuni mwake, pale alipolala Mona Lisa, sasa palikuwa na mto ambao yeye, Joram, aliukumbatia. Hakujali, akijua kuwa msichana huyo alikuwa ameondoka kimyakimya kwa kuchelea kumsumbua. Akaurudia usingizi wake ambao aliuchapa hadi saa saba za mchana huo. Baada ya kuoga, kunywa supu na chupa mbili za club soda alirejea chumbani kwake ambako alijilaza chali na kuendelea na mswada wa Mona, UBONGO WA MWALIMU NYERERE.


Ilikuwa riwaya tamu. Ilimvutia na kumsisimua kiasi kwamba alijikuta amezama moja kwa moja katika msitu huo wa maneno yaliyopangiliwa kisanii. Ilimwia vigumu zaidi kuamini kuwa mbunifu mwenyewe alikuwa msichana mpole na mrembo kama yule. Ufundi wa matumizi ya lugha, hila katika mpangilio wa matukio na zaidi ya yote uhalisia wa matukio ya mambo katika hadithi hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram amezwe moja kwa moja, bila kujua kuwa muda umekwenda, hadi aliposikia mlango wake ukigongwa.



Kabla ya kuinuka kuufungua aliitazama saa yake ya mkononi. Tatu kasoro! Hakuamini. Alipoufungua mlango umbile zuri la Mona Lisa lilikuwa limesimama pale, tabasamu lenye hayahaya na kutojiamini likiwa limechanua usoni pake. “Darling! Karibu sana,” Joram alisema akimshika mkono na kumvuta ndani ambako alimkaribisha tena kwa busu jingine. Kiasi fulani Mona Lisa alionyesha kushangazwa na mapokezi hayo. Alimtazama Joram kwa muda, kisha akayakwepa macho yake na kujiinamia. Joram pia alishangazwa na hali hiyo. Muda mfupi tu uliopita ulikuwa mchangamfu kuliko mie, mara hii umebadilika tena! Achana na tabia hizo za kinyonga!






Alitamani kumweleza. Lakini hakufanya hivyo. Badala yake alimwambia taratibu, “Chumba hiki chako, chagua kukaa ama kitandani, ama kwenye kochi.”


Mona aliliendea kochi na kuketi.


“Kitabu chako kimenishika kwelikweli,” Joram alimwambia. “Sikujua kama muda umeisha kiasi hiki. Nikuagizie chakula na kinywaji gani?”


Mona alitabasamu, “Kizuri?” “Kitu gani?”


“Kitabu. Ni kizuri kweli?”


Joram akatabasamu. “Kizuri kama alivyo mtu aliyekiandika. Kikitoka utapata washabiki kila pembe ya dunia. Utakula nini?”


“Unaamini kitakubaliwa?” Mona alihoji tena kwa shahuku. “Ni mchapishaji kipofu wa taaluma peke yake anayeweza kukataa kitabu kama hiki. Ingawa kuna mambo mawili matatu atakayoyatoa na kuyaongeza. Hata hivyo, sijafika mwisho,”


Joram akasita, “Hujaniambia utakula nini na utakunywa nini.”


Ilikuwa dhahiri kuwa akili za Mona hazikuwa kwenye chakula wala kinywaji, bali kwenye maandishi yake, hali ambayo ilimshangaza Joram. Jana hakukitaja kabisa kitabu hicho, leo hataki kusikia jambo lolote zaidi ya kitabu.


Kinyonga!


“Siwezi kukaa hapa na msichana mrembo kama wewe, bila kumkirimu walao maji ya uhai. Nawapigia jikoni watuletee kuku mzima, chupa mbili za wiski na tonic. Sawa?”


Joram alisubiri jibu la Mona Lisa.


“Samahani sijisikii kula wala kunywa chochote.” “Kwa nini? Za jana bado zipo kichwani?”


“Jana!” ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Jana nimekunywa wapi! Sijawahi kunywa pombe toka nizaliwe.”


Joram hakuyaamini masikio yake.


“Wacha mzaha Mona,” akamwambia akicheka. “Jana umerudi hapa ukanipa company ya nguvu, ukanywa kiasi cha kunifariji hapo kitandani hadi ulipotoweka bila kuniaga!”


Kilichofuata baada ya hapo Joram hakukitegemea. Joram alimwona Mona Lisa akisimama na kumtumbulia macho






ya mshangao, akiwa ameusahau mdomo wake wazi, huku akitetemeka mwili mzima. Taratibu mshangao ulianza kutoweka katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na hasira, hasira za mwanamke, hasira ambazo Joram, pamoja na ujabali wake wote hakupata kuziona kwa mwanamke yeyote yule. Lakini hali hiyo pia ilitoweka taratibu katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama msiba au maombolezo, jambo lililofuatiwa na kilio cha kwikwi, kwa sauti ndogo, huku machozi mengi yakimtoka.




Kwa Joram Kiango ile picha ya kusisimua ilikuwa imerudi, picha ya msichana mpole, mrembo, mwenye maumivu fulani rohoni mwake, picha ya malaika anayeteseka! Ambayo mwanaume yeyote asingeivumilia. Hivyo, bila ya kujipa wasaa wa kutafakari zaidi alimwendea na kumkumbatia. Akamvuta taratibu hadi kitandani ambako alimketisha na baadaye kumlaza huku akiwa amemkumbatia, mkono wake wa pili ukijipa kazi ya kumfuta machozi.


Mona alinyamaza kidogo na kumuuliza Joram kwa sauti ya mnong’ono, “Unaniambia kweli, Joram?”


“Kwamba?”


“Kwamba jana nimerudi hapa na kuwa nawe hadi asubuhi ya leo?”


“Kwa nini nikudanganye?” Joram alimjibu kwa swali vilevile. “Kwani kulikoni, Mona, mbona sikuelewi!”


Mona akaanza kulia tena. Baadaye alinong’ona tena kama anayezungumza peke yake. “Hata wewe! Hata Joram Kiango! Nifanye nini jamani?”


“Kuna nini?” Joram alihoji tena. “Kuna jambo gani la muujiza wewe kurudi hapa na kuwa nami?”


“Hujui Joram, hujui; huelewi. Na uwezi kuelewa,” Mona alisema na kuongeza, “Hujui kuwa tayari nimeyaweka maisha yako hatarini. Sijui kitu gani kinachonitokea. Lakini naamini nimekuweka katika hatari kubwa sana katika maisha yako.”


“Hatari gani?” “Ya kifo.”


Joram akaangua kicheko. “Yaani kufurahi na wewe usiku mmoja kwangu ni hukumu ya kifo! Acha mzaha Mona. Mie sio mshirikina kiasi hicho!”






“Joram, hufahamu,” Mona aliongeza. “Kwanza, hukulala na mimi. Halafu, suala la ushirikina halipo.”


Joram akacheka tena. Akasema, “Kwa hiyo tuachane na ushirikina. Twende kwenye elimu ya akhera. Ni kwamba nimelala na jini linalotumia sura yako, jini ambalo baadaye litaniua, sio? Usinichekeshe Mona”


“Huwezi kuelewa,” Mona alinong’ona tena. Ingawa sasa kile kilio cha kwikwi kilikoma, machozi yaliendelea kutiririka juu ya mashavu yake laini, Joram akiendelea na kazi ya kuyafuta na kumfariji.


Kuna ugonjwa fulani. Ugonjwa adimu, ambao ni madaktari wachache hadi sasa wanaoufahamu. Ni aina fulani ya matatizo ya akili ambapo mhusika hujikuta amesahau yeye ni nani na kujihisi kama mtu mwingine kabisa mwenye jina na tabia tofauti. Akiwa katika hali hiyo anaweza kufanya chochote, hata kuua bila kujua analolifanya.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog