Simulizi : Mtambo Wa Mauti
Sehemu Ya Nne (4)
kwanza, halafu aanze kumtafuta baadaye. Ingekuwa sawa na kurudia kosa. Yule msichana vilevile, roho yake ilitakiwa kwa udi na uvumba. Mamilioni ya fedha yalikuwa tayari yametapanywa kwa watu mbalimbali kwa dhamira hiyo bila mafanikio. Kumpoteza ingekuwa kosa jingine.
“Haya, nimekubali,” alisema baadaye. “Umekubali?”
“Kuwaua usiku huu, kesho nione pesa zangu zikiwa tayari katika akaunti yangu. Kama utashindwa kufanya hivyo, elewa kuwa kichwa chako kitakuwa asusa yangu kesho hiyohiyo.”
Mchopanga alisikia kitu kama kicheko cha kebehi toka upande wa pili, kicheko kilichofuatiwa na neno “Vizuri,” na kIsha, “Bila wasiwasi wowote.”
Maneno hayo yalimfariji. Akautia mkono wake mfukoni na kuipapasa bastola yake Smith & Wesson 459, iliyokuwa imejaa risasi. Mfuko wa pili ulikuwa na visu viwili vya aina mbalimbali; kamba ya nailoni maalumu kwa kunyongea, kijaluba chenye unga wa cocaine na vikorokoro vingine. Chini ya kiti cha gari hilo alihifadhi bunduki kubwa, AK-47, lensi yake na kasha la risasi. Pembeni ya bunduki hiyo palikuwa na nyundo, lundo la funguo bandia na chupa mbalimbali za ainaaina za sumu.
Niko barabarani, Othmani aliwaza, akilifuata gari la Joram kwa makini zaidi.
Gari lao lilipovuka kuifuata barabara ya Mwenge, yeye alipinda kuifuata ya Chuo Kikuu cha Mlimani. Alijua angewakuta wapi.
Kwa ujumla alijua wanakoelekea.
W 8 X
LE wimbo uliozoeleka, wa “Hali ngumu ya uchumi,’ ambao uliimbwa zaidi na viongozi wa serikali na chama tawala kuanzia miaka ya themanini uliambatana na vikolombwezo lukuki. Miongoni mwa vikolombwezo hivyo ni kutoweka kwa uhuru wa kujitawala kichumi na badala yake kina IMF na Benki ya Dunia kushika hatamu. Na walizishika kwelikweli. Walimimina amri baada ya amri, zote zikielekeza serikali kujitoa katika huduma nyingi za jamii. Elimu, ambayo awali ilitolewa bure, ikawa ya kulipia, na hivyo, kufanya watu wengi washindwe kuimudu, huduma za afya kadhalika zikawa hazishikiki, mashirika ya UMMA yakauawa moja baada ya jingine huku maelfu ya waliokuwa watumishi wake wakitupwa nje ya soko la ajira. Kitu kinachoitwa ruzuku toka serikalini
kikafanywa nuksi.
Viongozi wengi, wakitembelea magari ya gharama kubwa na kuishi katika majumba ya fahari, walipokea kwa furaha kila amri toka juu. Walifumbia macho ukweli kuwa huko zinakotoka amri si wakulima tu bali hata ng’ombe wao walikuwa wakilipwa ruzuku. Aidha, waliziba masikio ukweli kuwa kila raia asiye na kazi, tangu mtoto mchanga, alikuwa akilipwa posho hadi anapopata ajira, na kwamba mwananchi kupata ajira lilikuwa jukumu la serikali pia, si raia pekee.
Hivyo, katika hali hiyo hakuna aliyeona kama ni jambo la
ajabu pale wizara inayohusika na masuala ya ardhi, kama wizara nyinginezo, ilipojisahau kwa miaka kadhaa na kulifanya suala la mipango miji kama mojawapo ya anasa. Upimaji wa maeneo mapya ulisimama, uendelezaji wa miundombinu ukasahauliwa. Wakubwa walikuwa ‘busy’ kugombea ubunge, wakubwa kidogo wakihangaikia semina na warsha mbalimbali huku wale wenzangu na mie wakiikimbiza shilingi, ambayo ilionekana kama imeota matairi.
Lakini maisha yalikuwa yakiendelea. Watu waliendelea kufa, watu waliendelea kuzaliwa. Jiji la Dar es Salaam lilizidi kuwa dogo, hivyo likaendelea kupanuka. Wajanja wachache waliwasukuma wenyeji toka katika maeneo yao asilia ya Kigamboni, Tabata, Tegeta, Bunju na kwingineko na kujenga mahekalu yao. Wenzangu na mie walivamia vichochoro, mifereji ya maji machafu na mabonde yote yaliyolizunguka jiji la Dar es Salaam na kuweka vibanda vyao. Mradi wawe karibu na Dar es Salaam. Karibu na neema.
Ni katika hali hiyo, pale Bunju, eneo moja la ekari tano lilipopata mwenyewe. Likalimwa, likapandwa miti na matunda na kuzungushiwa seng’enge. Katikati ya shamba hilo jengo dogo, la ghorofa mbili, likaibuka. Hakuna aliyelishangaa wala kulitilia maanani kwani majengo hayo yalikuwa yakiibuka kama uyoga kila upande wa jiji bila mpangilio.
Hali kadhalika, hakuna aliyeshangaa jengo lilipokamilika na mzee mmoja wa Kimamkonde alipokabidhiwa kulilinda, mwezi, miezi, mwaka na, hatimaye, miaka bila ya wenyewe kuhamia. Hilo pia halikuwa la ajabu kwani majengo ya aina hiyo yalikuwa mengi katika miji mipya ya kandokando ya jiji la Dar es Salaam. Baadhi ya majengo ya aina hiyo yaliwahi kukaa zaidi ya miaka kumi kwani mwenye nyumba alikuwa nazo nyingine pengine tatu au nne, watoto na wajukuu zake wakiishi Ulaya au Marekani huku ndugu wengine wakiwa wamesahauliwa vijijini.
Lakini jengo hili lilikuwa na muujiza mmoja. Mlinzi wa Kimakonde hakupata kumfahamu mwajiri wake kwa sura wala jina. Si kwamba hakuwahi kumwona au kutajiwa jina lake, la hasha. Alimwona zaidi ya mara tatu. Lakini kila alipomwona mwajiri huyu alikuwa na sura au umbile tofauti.
Hata mavazi yake pia hayakumsaidia sana. Kila safari alikuja na vazi tofauti na awali; mara joho la ki-Naijeria, mara suti ya Kiingereza, mara jeans za wachunga ng’ombe wa Texas; na kadhalika.
Mara zote hizo alitajiwa jina. Lakini lilikuwa gumu, la lugha iliyofanana sana na Kihabeshi au Kifaransa. Mmakonde hakulishika na asingeweza kulishika. Laiti angejua kuwa hakukusudiwa kulishika..
Kazi yake haikuwa ngumu, kutunza mazingira ya nyumba kwa kufyeka majani yanapozidi, kumwagilia maua na kutunza nyumba. Mshahara ulikuwa mnono. Wakati walinzi wengine waliambulia shilingi 15,000 kila mwezi, yeye alipokea 50,000 huku akiletewa chakula kingi ambacho kilimshinda.
Mzee wa Kimakonde alinenepa, akanawiri. Mashavu yake yaliyoanza kuingia ndani kwa lishe duni na upungufu wa meno mdomoni yalianza kujaa tena, sura yake ikirudia ujana. Tahamaki miaka yake sitini na minane ya umri ilishuka na kuwa arobaini na minane machoni mwa watu wengine, hali iliyomwezesha ajikute akiishi na msichana wa Kidigo, mwenye umri wa miaka ishirini, kama mama watoto wake.
Mafanikio na uhuru huo wa muda mrefu ulimfanya aanze kujisahau kuwa yeye ni mlinzi tu wa nyumba hiyo, badala yake akajiona kama mwenye nyumba. Hata aliwaambia hivyo rafiki zake wasiomjua vizuri, kwamba mwanawe anayeishi Japan ndiye aliyemjengea nyumba hiyo. Alianza hata kuota ndoto zinazoashiria mawazo hayo. Ndoto ambazo zilimwonyesha kuwa siku za karibuni mwanawe huyo angemletea gari la kutembelea na kumfungulia mradi wa bwawa la kuogelea.
Njozi zake hizo za usiku na mchana zilikoma ghafla, usiku wa saa tatu kasoro, pale kengele za geti zilipolia. Alipokwenda kufungua mwajiri wake aliingia na gari taratibu katika banda la kuhifadhia magari. Alikuwa katika mavazi ya ajabu zaidi machoni mwa Mmakonde. Na alifuatana na mwanamke! Mwanamke mzuri! Lakini kilichomvutia zaidi Mmakonde si mwanamke bali kile alichokiona katika mavazi ya tajiri wake wakati akishuka toka ndani ya gari.
Damu!
Nguo zake zilikuwa zimeloa damu!
Mmakonde huyo alipata mshituko mkubwa zaidi pale alipomwona tajiri wake akimvuta mgeni wake huyo ambaye alifungwa pingu za mikononi. Yeye pia alikuwa na michubuko usoni na mikononi.
“Funguo, tafadhali,” aliomba huku akijaribu kumtoa wasiwasi mlinzi huyo kwa kumzawadia tabasamu jepesi.
“Funguo zipi?”
“Za geti. Sitaki mtu yeyote aingie wala kutoka humu ndani leo. Sawa?”
“Sawa… bo… bosi,” alijibu akitoa funguo hizo na kumkabidhi.
***
Kama ilivyo katika mambo yake mengine, Joram Kiango aliijenga nyumba hii kwa siri kubwa. Akiwa amejenga katika shamba alilonunua kwa mzee wa Kizaramo aliyeamua kurudi Bagamoyo, Joram hakuhitaji kutumia jina lake halisi. Na hata maombi yake ya hatimiliki ya eneo hilo pale Wizara ya Ardhi yalikuwa katika moja ya majina yake ya akiba. Mafundi aliowatumia aliwatoa nje ya nchi na hakuonana nao mara kwa mara isipokuwa tu pale ilipobidi. Wao pia walimjua kwa majina tofauti na walikuwa wakibadilishwa kila hatua, kiasi kwamba hakukuwa na fundi yeyote mwenye ramani halisi ya jengo hilo.
Kazi nyingine, nyeti zaidi, Joram Kiango alizifanya kwa mkono wake mwenyewe, usiku na mchana, akitumia vitendea kazi ambavyo ama alinunua ama alikodisha kwa hila vilevile. Alifunga umeme kwa njia na namna zake, aliunganisha maji na mashine za kupozea hewa kwa mitindo yake na kuweka milango na madirisha kwa namna ya kukidhi mahitaji yake. Alikuwa na vyumba vya siri na milango ya siri ambayo mtu yeyote asingebaini bila matakwa yake.
Ilipokamilika ilikuwa nyumba ya pekee, ingawa wapita njia waliichukulia kama mojawapo ya nyumba za kawaida. Kumwajiri mzee yule wa Kimakonde ili ailinde, badala ya kuitumia moja ya kampuni lukuki za ulinzi zilizopo jijini, kwa Joram ilikuwa sehemu ya kuendeleza usiri wa jengo lake hilo. Mzee hakuwa mdadisi, wala hakuwa makini. Mara nyingi
sana Joram amekuja nyumbani hapo na kufanya shughuli zake huku mzee akiwa hana habari. Mara mbili aliwahi kulala usiku mzima na kuondoka zake alfajiri huku mlinzi wake akikoroma.
Hivyo, kadhia hili zito, ambalo liliambatana na vifo na maafa ya kila dakika, lilimfanya Joram Kiango alazimike kuja hapa. Hakuona wapi pengine panafaa kumweka kitako msichana huyo wa ajabu anayejiita Mona Lisa na aliyefanana naye reale kwa ya pili, msichana ambaye hashikiki, hatabiriki.
Haikuwa kazi rahisi kumfikisha hapo. Mara mbili walinusurika kifo kufuatia vurumai ambayo aliianzisha ghafla mara walipokaribia Barabara ya Bagamoyo. kwa bahati, joram alikuwa tayari. Ule utulivu na ukimya wa muda mrefu aliokuwa nao toka Uwanja wa Ndege haukumpumbaza Joram. Alikuwa makini, jicho lake la wizi likiwa halijamwacha hata kwa dakika moja. Hivyo, pale Joram alipomwona akifumbua macho kwa hila na kisha kuyafumba, huku mkono wake mmoja ukipelekwa taratibu katika mfuko wake wenye bastola, Joram alimsubiri. Mara tu alipoipata bastola hiyo Joram alimpokonya, kitendo ambacho kilifuatiwa na pigo kali la kareti toka kwa msichana huyo. Pigo hilo lilimpata Joram Kiango barabara shingoni, likalifanya gari liyumbe, nusura kupinduka. Kwa bahati, Joram aliwahi kulizima gari huku akizuia pigo la pili na kuachia lake lililompata shingoni na kumlegeza msichana huyo. Joram aliitumia fursa hiyo kumkamata na kumtia pingu za mikono. Alishangaa kuona Mona Lisa huyo akiruhusu kufungwa pingu kwa utulivu kabisa, kinyume na matarajio yake.
“Uko tayari kuzungumza?” Joram alimhoji msichana huyo.
Hakujibu. Badala yake alifumba macho yake na kukilaza kichwa chake kwenye kiti.
Jaribio la pili alilifanya wakati gari likikaribia kuvuka daraja linaloitenga Tegeta na Bunju. Kwa kuitumia mikono yake yenye pingu, aliuvamia usukani na kuupinda akilielekeza gari kutumbukia mtoni. Joram alitumia nguvu za ziada kulirejesha barabarani. Lakini haikuwa kabla ya gari hilo kugonga ukuta wa daraja na kubonyea vibaya upande wa kushoto. Kwa bahati, magari yalikuwa yamepungua sana njiani. Vinginevyo,
hadithi ingekuwa nyingine.
‘Mona Lisa’ alitulia tena. Hakufanya vurugu ya aina yoyote tangu gari lilipoondoka eneo hilo, likaiacha Barabara ya Bagamoyo na kufuata njia ndogo iliyowafikisha yalipo makazi ya Joram Kiango. Wala hakuwa mbishi wakati geti lilipofunguliwa naye kuongozwa hadi ndani ya jumba.
“Tunahitaji kuzungumza,” Joram alimwambia mara walipofika ndani. “Bila shaka mazungumzo yetu hayatakuwa mafupi. Hivyo,” aliongeza, “Nadhani unahitaji kuoga. Umechakaa sana.” Alimwelekeza kwenye kimojawapo cha vyumba vya wageni na kumfungulia akimwambia, “Humo kuna bafu, sabuni na dawa za meno. Nadhani utapata hata nguo za kubadili. Tumia muda wako, usiku bado mbichi huu.” Joram alitoa funguo za pingu na kumfungua mikono.
“Usijisumbue kufikiria kutoroka,” alimwambia. “Ni rahisi sana kuingia katika nyumba hii, sio kutoka,” alisema akivuta mlango wa chumba na kuufunga kwa rimoti.
Yeye pia alihitaji kuoga. Alikuwa mchovu na mwenye njaa. Hali kadhalika, hakuwa amechafuka tu, bali kuchakaa. Mchanganyiko wa damu, jasho na vumbi mwilini mwake ulimfanya ajisikie kunuka. Alitamani sana aingie katika beseni lake la kuogea, ajilaze katika maji ya baridi na kukaa humo kwa saa moja au zaidi.
Lakini hakuwa na muda huo. Alikuwa na mengi ya kufanya. Awali ya yote, alihitaji kukaa mbele ya kompyuta yake. Alihitaji majibu ya maswali aliyoyasambaza kwa rafiki zake kupitia mtandao wa E-mail. Hivyo, alikiendea chumba chake cha kujisomea na kuiwasha kompyuta yake ndogo, lap top aina ya Mackintosh toka katika kiwanda cha yule kijana tajiri kuliko watu wote duniani, Bill Gate. Pia, akafungua mtandao wake wa huduma ya bure, hotmail, na kuita moja ya anuani zake zenye majina bandia.
Alikuwa hata hajatulia vizuri wakati mlio wa risasi za SMG
uliposikika ghafla toka mbele ya geti lake.
***
Othman Mchopanga alikuwa amemfuata Joram Kiango hadi nyumbani kwake kwa urahisi kuliko alivyotegemea. Kuna
wakati aliwatangulia na kuruhusu magari kadhaa kati yao, mara moja walimpita kasi na kuendelea na safari yao. Kwa mbali alizishuhudia zile purukushani za yule msichana na Joram Kiango pale darajani. Angeweza kuwaua kwa urahisi sana na kulilipua gari lao kwa tenki la gari lao lakini alisita kufanya hivyo. Alitaka kazi yake iwe nzuri, ya kujivunia, si kubahatisha.
Faida moja ya kuishi katika dunia ya kile marafiki zake wanachokiita ‘dunia ya mafichoni’ ni kujua mambo mengi ya watu wengine hali yako hayajulikani, mfano mzuri ukiwa safari hii ya kumfuatilia Joram Kiango. Hakuwa na papara ya kufanya lolote kwa kuwa alijua wanaelekea wapi. Alipata fununu muda mrefu kuwa jengo lile lilikuwa la Joram Kiango. Hakupata kufikiria kuwa fununu hizo zingekuwa na manufaa yoyote kwake hadi leo, wakati akiwafuata kwa kazi moja tu.
Wakati huohuo alikuwa na hakika kabisa kuwa hakuna mtu yeyote aliyejua kuwa mbili kati ya zile boti ziendazo kasi kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni zake. Hali kadhalika, kama wapo waliofahamu ni wachache sana, kuwa hoteli nne za kitalii jijini Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar ni zake. Walichofahamu majirani zake kule Makongo Juu ni kuwa yeye alikuwa mfanyabiashara wa jumla wa vipodozi toka Dubai na Falme za Kiarabu. Aidha, walimtambua kama mtu mpole, mkarimu na muumini mzuri wa dini ambaye alikosa sala kwa nadra sana.
Mtu ambaye hakumtambua zaidi ya watu wote ni mkewe. Binti Kalenga, mtoto wa Kifipa aliyezaliwa na kukulia Dar es Salaam aliolewa angali kinda, mara baada ya kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari. Baba yake, mzee Kalenga, akiwa amezibwa macho kwa kitita cha fedha za kishika uchumba, mama yake akiwa amelogwa kwa zawadi za mavazi na hereni za dhahabu kutoka Dubai, binti yao angepata lipi la kusema? Yeye pia, mara baada ya kuingia katika ‘hekalu’ la mume wake na kukabidhiwa umalkia wa kila kitu katika nyumba hiyo moyo wake haukuwa na nafasi ya kumchunguza mume wake. Na pale alipopewa usimamizi kamili wa bidhaa zote toka nje, huku mara mojamoja wakisafiri pamoja kwenda nje, alijikuta akiondokea si kumwamini tu bali kumwabudu
mume wake. Hakuhoji chochote pale mume alipotoweka ghafla kwa siku na hata wiki kadhaa na kurejea akiwa na hadithi za ‘safari ya ghafla.’ Hakushangaa pindi mumewe anapoondoka mikono mitupu na kurejea na fuko lililofurika noti.
Ni siku moja tu ambapo alipata kumshuku mumewe. Alikuwa amempigia simu kuwa angesafiri ghafla kwenda Nairobi. Lakini usiku wa manane alirejea akiwa na jeraha baya la risasi katika ubavu wake wa kushoto. Hadithi yake ilikuwa fupi tu, “Nimevamiwa na majambazi.” Lakini binti Kalenga alipomshauri atoe taarifa polisi alikataa katakata kwa kisingizio kuwa hakuwa na muda wa ‘kuwasaidia polisi.’ Hata alipomshauri kwenda hospitali vilevile aligoma kwa maelezo kuwa angelazimika kupata fomu za PF3 ambazo zingewafanya polisi wamlazimishe ‘kuwasaidia.’
Mkewe alilazimika kuchukua nafasi ya udaktari na unesi. Kwa maelekezo ya mumewe, alimtibu jeraha hilo usiku na mchana kwa wiki mbili bila kumhusisha wala kumweleza mtu yeyote juu ya ‘ugonjwa’ wa mumewe. Jeraha lilipopona mumewe alimpa zawadi ya kutembelea Ufaransa na Ubelgiji, akiwa na ruhusa ya kunua chochote ambacho angekitamani. Aliishia kununua magauni sita ya mmeremeto, kwani kila alichohitaji alikuwa nacho.
Maisha yalikuwa matamu kama ndoto ya kuvutia si kwa Binti Kalenga tu, bali pamoja na Othman mwenyewe. Hakukoma kushangaa kwa jinsi hali yake ya uchumi ilivyokuwa ikipanda kwa kasi siku baada ya siku toka baada ya ile ‘kazi’ yake ya kwanza, kazi ambayo ilisambaza sifa zake na kumpa hadhi kubwa katika dunia yao ya giza.
Ilikuwa ndio kwanza anarejea nchini toka katika gereza moja nchini Pakistan, ambako alifungwa maisha kwa kukamatwa na dawa za kulevya alizobeba kwa matarajio ya kulipwa chochote iwapo angefanikiwa kufika nazo jijjini Dar es Salaam. Kwa bahati, alitumikia kifungo hicho miaka miwili tu na kufanikiwa kutoroka wakati ulipozuka mgomo gerezani humo, uliofuatiwa na mapambano makali baina ya polisi na wafungwa. Alikuwa miongoni mwa wafungwa wanane waliobahatika kutoroka. Akapata hati za bandia na kuvuka mipaka ya nchi hadi nchi hadi alipofika Dar es Salaam. Akiwa
amejifunza mengi gerezani humo, akiwa ametaabika sana kwa njaa na karaha nyinginezo wakati wa ukimbizi wake, Mchopanga aliapa kuwa asingekubali tena kurudi katika umasikini.
Hasira zake dhidi ya umasikini zilianzia kwa mtu aliyemtuma kuchukua mzigo ule Pakistan na kisha kumtelekeza mara alipokamatwa. Alikuwa mtu mzito kisiasa na kibiashara. Alikataa katakata kumfidia Mchopanga kwa masaibu yaliyompata kwa maelezo kuwa uzembe wake ulimsababishia hasara kubwa. Kwa ujumla, alimfukuza kama mbwa na kumpiga marufuku kukanyaga nyumbani kwake. Hata pale Mchopanga alipomtishia kuwa angelipa kisasi tajiri huyo alicheka na kumpuuza.
Lakini wiki moja baadaye alipookotwa chini ya uvungu wa kitanda chake, kichwa chake kikiwa kimetenganishwa na kiwiliwili chake kwa kisu, huku sefu lake la fedha lilikutwa tupu; ndipo sifa za Mchopanga ziliposambaa kama upepo. Haukupita mwezi kabla hajaombwa kumtoa roho polisi mmoja aliyelishikilia jalada la kesi ambayo ingewaumbua wakubwa fulani. Huyu kifo kilimkuta wakati akila chakula cha usiku na familia yake. Mtutu wenye bastola iliyowekwa kiwambo cha kuzuia sauti ulimchungulia dirishani na kumfumua moyo. Wakati familia hiyo ikitokwa na mshangao na kupiga mayowe. Mchopanga tayari alikuwa mtaa wa pili wa eneo hilo.
Matukio hayo yalifanya atumiwe na watu mbalimbali, wanasiasa wenye visasi na wenzao, wafanyabiashara waliodhulumiana, washitakiwa waliokusudia kufutilia mbali ushahidi; na kadhalika. Na kati ya waliomtumia, kila ambaye alijaribu kukiuka makubaliano roho yake ilikuwa halali yake. Wakati wote huo, machoni mwa jamii isiyojua chochote kinachoendelea nyuma ya mapazia, Othman Mchopanga aliendelea kuwa mfanyabiashara halali, aliyelipa kodi zote na kustahi heshima zote. Tabasamu zake za mara kwa mara, uchangamfu wake kwa kila mtu na misaada kwa wahitaji mbalimbali hakukumpa mtu yeyote fursa ya kufikiria tu
kuwa angeweza kuwa mtu wa aina yake.
Hivyo, ilipokuja kazi mpya, ya kuua kasichana tu, tena kakiwa kamelala kitandani, kwa mamilioni ya fedha; aliona
kama aliyekaribishwa katika mchezo wa kitoto. Hakukutana na tajiri wake huyo ana kwa ana. Lakini mjumbe wake alipokuja na kila kitu alichokihitaji; picha ya marehemu mtarajiwa, ratiba ya mwenendo wake, namba ya chumba atakacholala na, zaidi ya yote, fuko la mamilioni ya malipo yake, aliitekeleza kama mchezo vilevile, ingawa alikuwa amemfuatilia wiki nzima kwa taabu sana.
Hivyo, kuambiwa kuwa alikosea na kupewa mtu mpya ambaye yeye alikuwa na hakika kuwa ndiye yuleyule ambaye alimuua tokea majuzi; pamoja na mtu anayeitwa Joram Kiango kuongezwa kwenye orodha hiyo, ndipo Mchopanga alipojikuta akianza kuvutiwa na ‘mchezo’ huo.
Hivyo, aliruhusu dakika ishirini zipite kabla hajaanza kunyata kuuendea upande wa pili wa uwanja wa jengo hilo, ambako alitegemea kukata seng’enge ili apenye ndani. Giza likiwa limetanda huku na huko, nyumba za jirani zikiwa ekari moja au zaidi pembeni, huku kichaka cha miti na nyasi kikiwa kimeshamiri upande huo; Othman Mchopanga hakuwa na shaka yoyote ya kuvurugikiwa na ratiba yake hiyo.
Mshangao wa kwanza aliupata pale alipoifikia sehemu nzuri na kugusa seng’enge ili aanze kuzikata. Alijikuta akitupwa angani na kisha kuanguka chini kama gunia. Umeme! Aliwaza. Nyaya zilikuwa zimetegeshwa umeme. Alijikusanya, akajifuta vumbi na kisha kutoa vifaa vyake ili aone kama alikuwa na kitu chochote ambacho kingemwezesha kukata nyaya hizo bila kugusa umeme.
Ni wakati akifanya hivyo alipopatwa na mshangao wa pili. Alijikuta akimulikwa ghafla na kurunzi yenye mwanga mkali, mwanga ambao ulifuatiwa na sauti kali iliyotokea ghafla kichakani humo ikisema; Polisi! Weka mikono yako juu!”
Hakuyaamini masikio yake. Polisi! Wametokea wapi na wanafanya nini hapo?
Weka mikono yako juu! Amri ya pili! Aliamrishwa tena. Mchopanga hakuwa mtu wa kutii amri, hasa za polisi.
Badala ya kuweka mikono yake juu aliipeleka mfukoni mwake na kutoa bastola. Pamoja na ukweli kuwa alikuwa kipofu kwa nuru kali iliyokuwa ikimmulika machoni, pamoja na kuwa hakupata muda wa kulenga; lakini bado aliachia
risasi mbili za harakaharaka kufuata kurunzi hiyo. Alisikia kilio cha mtu, kikifuatiwa na kurunzi kudondoka. Ni hayo tu aliyoweza kuyaona kwani sekunde hiyohiyo alinyeshewa na mvua kubwa zaidi ya risasi ishirini ambazo zilimfanya akate roho hata kabla hajaanguka.
***
Utajisikia vipi pale utakapojikuta ukipigiwa simu na Rais wa Jhamuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama? Zaidi utajisikia vipi wakati Rais akikumiminia maswali mazito, tena ya harakaharaka, ambayo wewe huna majibu yake.
Hayo ndiyo yaliyomkuta Inspekta Haroub Kambambaya jioni hiyo. Alikuwa bado kaduwaa ofisini mwake, juu ya kiti chake, mikono yake yote miwili ikiwa inakilea kichwa chake ambacho alikiona kizito zaidi kufuatia taarifa mpya toka Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Vifo vya watu watano, wawili kwa risasi, watatu kwa kukanyagana, huku wengine kwa makumi wakikimbizwa mahospitalini, taabani kwa kukanyagwa ama kujipigiza kwenye kuta na ajali za magari, vilimfanya achanganyikiwe.
Kilichomchanganya zaidi Kambambaya ni taarifa ya kuonekana uwanjani hapo kwa yule mwanamke wa miujiza, ambaye kila anapotokea maisha ya watu wengi huteketea, mwanamke ambaye kama kawaida yake alitoweka tena wakati watu wengi, wakiwemo wanausalama, wakiuguza maumivu makali ya ile sumu ya macho.
Uamuzi wa Kambambaya kuweka ulinzi mkali katika vyanzo vyote vya kutokea jijini Dar es Salaam ulitokana na matarajio ya kumpata Joram Kiango, ambaye aliamini angekuwa ufunguo wa kadhia hii ya kutatanisha. Badala yake aliyetokea tena ni yule mwanamke, ambaye ameondokea kuwa kama mjumbe wa kifo.
Kutoweka kwa maiti yake pale Muhimbili na kudaiwa kwake kuwa anazuka hapa na pale, kuzuka kunakoambatana na vifo hakukumwingia akilini Kambambaya. Kama angekuwa anaamini miujiza na ushirikina angeweza kuapa kuwa mwanamke huyu ni mzimu wa yule aliyetoweka chumba cha
maiti kule Muhimbili. Kambambaya hakuwa na imani hiyo. Hivyo, akajikuta akiishia kukilea kichwa chake, kilichojaa maswali mengi majibu sifuri.
Na wakati akiendelea kuwaza na kuwazua ndipo ikaingia kengele ya simu yake maalumu, ambayo haikuorodheshwa mahala popote. Alipoipokea, sauti nzito ambayo daima haina mzaha, ilinguruma kutaka aeleze kinachoendelea. “Nchi imekumbwa na hofu kubwa. Vifo na maafa kila dakika. Unadhani ni kitu gani kinachotokea?” Ile sauti iliuliza.
Kambambaya alikuwa hana jibu sahihi. Aliropoka hili na lile ambalo bila shaka Rais alilipuuza na badala yake akaongeza swali jingine, “Kitu gani ambacho mnafanya, ambacho mnadhani kitakomesha maafa haya mara moja?”
“Tunafanya kila tunaloweza mzee,” Kambambaya alijikongoja. “Tunachukua kila hadhari. Nadhani tutafanikiwa tu.
“Nasikia mnamtafuta Joram Kiango. Mmeshampata?” “Bado mzee, lakini…”
“Lakini!” Rais alikatiza tena. “Siku zote niliamini Joram Kiango ni kijana wetu. Na amefanya mengi ambayo yameliletea taifa letu sifa na hadhi kubwa duniani. Leo yakoje tena mambo hayo?”
“Ndiyo maana tunamtafuta mzee. Ili atusaidie. Tunaamini tukimpata tutapata mwanga mapema zaidi,” Kambambaya alijitetea.
“Ningependa hali hii isiendelee tena katika saa ishirini na nne zijazo,” Rais alisema. “Nadhani umenielewa, Inspekta.”
“Ndiyo, mzee.”
Simu ikakatwa upande wa pili.
Kambambaya aliona simu kama imezidisha tani elfu moja zaidi juu ya kiroba kizito kilichomwelemea kichwani.
Hivyo, ilikuwa kama faraja kubwa kwake nusu saa baadaye alipopokea taarifa ya Joram Kiango kuonekana akiingia katika nyumba moja huko Bunju, huku akimburuza mwanamke mmoja.
“Nakuja,” alitamka mara moja, akiinuka na kuuendea mlango, aliikumbuka bastola yake iliyokuwa katika kijaluba cha meza. Akaikagua na kuona kuwa ilijaa risasi. Akaitia
mfukoni na kulikimbilia gari lake.
“Bunju! Kwa mwendo wa kupaa,” alimwamuru dereva wake ambaye alikwishalitia gari moto.
Kuwa mkubwa wa Idara kuna raha na karaha zake. Karaha ni pale mambo yanapokwenda mrama kama sasa, lawama zote hutupwa juu ya mabega yako. Lakini ziko nyakati za neema, nyakati ambazo utafurahia madaraka yako si kwa ajili ya mshahara mnono, nyumba nzuri na marupurupu mengine peke yake. Zaidi ni kwa kuwa katika nafasi ya kujua na kuhifadhi mambo mengi kuliko wasaidizi wako, kujua mkubwa yupi ana siri ipi, yupi anaumwa na anaumwa ugonjwa upi, yupi anaiba na fedha zake amezificha wapi, yupi amemkabidhi yupi kulinda miradi yake haramu; na kadhalika.
Kuzijua siri nyingi za Joram Kiango kwa Kambambaya ilikuwa miongoni mwa neema hizo za ukubwa. Hakuna msaidizi wake hata mmoja aliyejua kuwa amejenga. Hata pale alipowaagiza askari wanne kuilinda nyumba hiyo, usiku na mchana, hakuwaambia ni nyumba ya nani. Hivyo alipopata simu ikimwarifu juu ya Joram Kiango kuonekana huko Bunju akiingia kwenye ‘nyumba moja’, alifurahi kuona moja ya mitego yake ikifyatuka.
Dereva wa Kambambaya alikuwa ‘kichaa’ barabarani. Alikwishapewa amri ya ‘mwendo’ wa ‘kupaa,’ alipaa kikwelikweli. Alitafuna lami, akiyapita magari upande huu na ule kana kwamba yuko katika mashindano. Alivuka Lugalo, akitafuna Mbezi Beach na kuimeza Tegeta katika muda wa dakika nane tu. Lami inayovutia toka Tegeta hadi Bunju ililifanya gari liteleze kwa dakika nne tu hadi walipoufikia uchochoro unaoelekea kwenye nyumba waliyohitaji.
Kwa maelezo ya Kambambaya waliliacha gari mita kadhaa nje ya eneo la nyumba hiyo na kutembea kwa miguu. Milio ya risasi iliwafikia wakiwa mita tano tu toka kwenye eneo la tukio. Huku akiitoa bastola yake mfukoni, Kambambaya alikimbia kuliendea eneo hilo.
Alikuwa tayari amechelewa. Askari wake watatu, silaha zao mkononi waliduwaa wakiitazama miili ya watu wawili waliolala chini wakiwa maiti. Maiti mmoja alikuwa msaidizi wake, afande Chaku Chikaya. Maiti wa pili alikuwa raia.
Kambambaya aliyatazama harakaharaka na kushusha pumzi alipoona kuwa marehemu hakuwa Joram Kiango.
“Kitu gani kimetokea?” aliuliza.
Askari mmoja alieleza jinsi walivyomwona marehemu huyo akifanya jitihada za kujipenyeza ndani. Na kwamba alipopewa amri ya kusimama ili ajitambulishe alitoa bastola yake na kumuua mwenzao aliyekuwa akimmulika kwa kurunzi, kitendo ambacho kilifanya walazimike kummiminia risasi ili kuokoa maisha yao.
Kambambaya aliamuru gari la wagonjwa liitwe mara moja na kuwachukua marehemu. Aliamuru pia mpigapicha apige picha za yule raia kwa makini zaidi pamoja na kuchukua alama za vidole vyake ili uchunguzi kamili juu yake uweze kufanyika.
“Natumaini Joram Kiango bado yumo ndani.” “Yumo afande.”
“Na mateka wake.” “Bila shaka.”
“Mnadhani kuna watu wengine zaidi yao ndani ya nyumba hii?”
“Ndiyo, afande. Yumo mlinzi wake, mzee mmoja mlevimlevi na mkewe.”
Kambambaya alifikiri kwa muda kabla ya kutoa amri nyingine, “Tuko wangapi hapa? Sita.” Aliuliza na kujijibu. Halafu akatoa amri, “Nataka kila pembe ya ua huu iwe na mtu mmoja. Kila mmoja awe makini kuhakikisha hatoroki. Mimi na askari wawili tuliobaki tutaingia kupitia geti la mbele. Sawa?”
“Sawa, afande.”
“Sawa. Sasa kuna kitu kimoja. Bado tunamtaka sana Joram Kiango, akiwa hai. Zaidi, tumechoshwa na vifo vya hapa na pale. Hivyo, kila mmoja wenu awe makini katika kutumia silaha. Zitumike pale tu inapobidi, si vinginevyo.”
Askari waliitikia kukubali. Kisha kila mmoja akachukua sehemu yake. Kambambaya aliuendea mlango wa geti la mbele kwa nia ya kuusukuma.
“Mzee, ametegesha umeme” mmoja wa askari aliokuwa nao alimwonya.
“Ametegesha umeme!” Kambambaya alirudia maneno hayo kwa mshangao. “Sidhani kama itamsaidia sana.”
Alirudi kwenye gari lake na kumwamuru dereva wake ampe kipaza sauti. Alipopewa alirudi getini na kukielekeza ndani ya nyumba hiyo. “Joram Kiango,” alinguruma. “Tunajua uko ndani. Tunajua unao watu wengine watatu. Wote inueni mikono yenu juu na mtoke mara moja. Hii ni amri halali ya jeshi la polisi.”
Kambambaya alisubiri dakika moja kisha aliirudia tena amri hiyo kwa sauti kubwa kuliko awali.
“… amri ya pili,” alimaliza.
Baada ya kusubiri dakika moja nyingine alirudia ujumbe uleule kwa mara ya tatu na kumalizia akisema “… amri ya tatu na ya mwisho.”
Bado hakujibiwa. Hivyo, akaongeza “Sasa tutatumia nguvu, kwa mujibu wa sheria halali za nchi.”
Kwa kutumia redio yake ya mkononi Kambambaya aliagiza askari ishirini zaidi waletwe eneo hilo. Aidha, aliagiza eneo hilo likatwe umeme mara moja ili waweze kukata nyaya hizo kwa urahisi.
W 9 X
MBIU ya Inspekta Kambambaya ilimfikia Joram Kiango vizuri kabisa chumbani humo. Mbiu hiyo ilifuatia mlio wa risasi toka nyuma ya jengo lake. Hata hivyo, hii ikiwa nyumba yake, aliyoijenga kwa mkono wake, Joram alijikuta akimhurumia Inspekta huyo. ‘Atasubiri sana.’ Aliwaza. Macho yake yalikuwa bado yamezama kwenye tovuti ya hotmail vidole vyake vikigonga hapa na pale kwenye bodi ya maandishi.
Angeweza kushangazwa na wepesi wa polisi hao kufika nyumbani kwake hapo dakika chache tu baada ya kufika kwake. Angeweza kushangaa zaidi kwa kuzingatia kile alichoamini kwamba polisi walikuwa wakimfikia haraka kwa kufuatilia nyendo za mwanamama huyu anayejiita Mona Lisa, ambaye yeye binafsi alifanikiwa kuyabaini maficho yake yote kwa kuongozwa na ile pete aliyokuwa akiivaa, pete ambayo aliitelekeza katika choo kimojawapo cha Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Msichana huyo sasa akiwa mateka wake, naye akiwa na kila hakika kuwa hakufuatwa na mtu yeyote, achilia mbali polisi, toka uwanjani hadi hapa, angeweza kushangazwa na wepesi huo wa polisi.
Hali kadhalika, Joram angeweza kushangazwa au kujiuliza risasi zilizotembezwa huko nje zilikuwa baina ya nani na nani. Kwa bahati mbaya, Joram hakuwa na muda huo kwa sasa. Kitu alichokuwa akikisoma katika kompyuta hiyo
kilimshangaza na kumvutia zaidi. Ulikuwa ujumbe mfupi, toka kwa mmoja wa rafiki zake aliowasambazia ili wampe kile walichokifahamu juu ya mtu anayeitwa Mona Lisa, nchini Tanzania na duniani.
Wengi walikuwa hawajamjibu lolote. Wawili watatu walimkumbusha juu ya yule Mona Lisa aliyepata umaarufu duniani baada ya kuchorwa kule Italia takribani miaka mia sita iliyopita. Lakini kati yao mmoja ndiye aliyemsisimua zaidi.
Mona Lisa: Jina la utani alilopewa toka utotoni Jina halisi: Margareth Johnson
Kuzaliwa: Agosti 28,1958
Kufa: Agosti 28, 2000 Sababu ya kifo: Ajali ya gari.
Kazi yake: alikuwa askari, Jeshi la Polisi Kituo: Moshi mjini, Kituo cha kati.
“Joram Kiango…” sauti ya Inspekta ilinguruma tena na kumfikia Joram. “Tunajua uko ndani… inueni mikono yenu juu na mtoke mara moja… Amri ya tatu.”
Joram alipuuza. Alifungua maandishi juu na kufungua kiambatanisho kilichotumwa na taarifa hiyo. Kilikuwa na picha mbili. Moja ilikuwa picha ya mazishi, polisi wakitoa heshima zao za mwisho kwenye jeneza lenye maandishi; SJN MARGARETH JOHNSON. Picha ya pili ilikuwa ya ‘merehemu,’ enzi za uhai wake. Alikuwa amesimama, katika mavazi yake ya kijeshi, huku akitabasamu.
“… Amri ya nne na ya mwisho… sasa tutatumia nguvu…” Kambambaya alikuwa akiendelea kufoka katika kipaza sauti.
Joram hakumsikia. Au hasa hakumsikiliza. Alikuwa amekodoa macho kuitazama picha hiyo.
Haikuwa ya mtu mwingine zaidi ya Mona Lisa.
Mara ikamjia kumbukumbu ya usiku ule wa chanzo cha balaa. Yale maneno ya Mona Lisa yakamrudia akilini aliposema, “Ni kweli hujui… Hujui kama unabaka. Na unambaka afisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi…”
Mona Lisa ambaye ni mateka wake katika chumba kimojawapo katika nyumba hiyohiyo! Mona Lisa ambaye majuzi tu alikufa hali wamekumbatiana pale hotelini! Mona Lisa ambaye maiti yake yalitoweka toka chumba cha maiti
Muhimbili! Mona Lisa ambaye amekuwa akimtokea tena na tena, huku kutokea kwake kukiambatana na maafa makubwa! Mona Lisa…
Chochote ambacho Joram alijaribu kukiwaza kilitoweka pale umeme ulipokatika ghafla na kiza totoro kukimeza chumba hicho na jengo zima.
***
Inspekta Kambambaya hakuyaamini macho yake pale umeme uliokatizwa katika eneo lote hilo ulipowaka ghafla katika jengo zima la Joram Kiango. Ilichukua dakika moja tu kiza kutanda katika nyumba hiyo, dakika ya pili nuru ya uhakika, kama ileile ya awali, ilitamalaki.
Laiti angejua kuwa kitendo cha kukatika kwa umeme unaomilikiwa na Tanesco katika jengo la Joram ni kufyatua mtambo mwingine wa umeme, uliounganishwa kwenye envetor ambayo ilipokea umeme utokanao na mwanga wa jua, kupitia katika betri kubwa ya gari na kusambazwa katika njia zote za umeme kama kawaida, kamwe asingejisumbua kuamuru katizo la umeme.
Kambambaya aliduwaa kwa dakika moja mbili, akitafakari afanye lipi jingine. Alikuwa na taarifa ya kuunganishwa kwa umeme kwenye nyaya zilizoizunguka nyumba hiyo. Na alikuwa na hakika kuwa isingewachukua vijana wake dakika kumi kutumia vifaa vyao kukata nyaya hizo na kuingia ndani. Lakini hakujisikia kufanya hivyo. Hakuona kama ingekuwa hekima kuwapeleka vijana wake, ‘mchana kweupe,’ mbele ya mtu kama Joram Kiango na hasa akiwa pamoja na mwanamke yule ambaye amekuwa kama anayefuatana na kifo popote alipo.
Wakati akiwaza hayo mara alisikia sauti ya kike ikiangua kilio toka ndani ya nyumba hiyo, sauti ambayo ilifuatiwa na kishindo kwa kupigwa mlango mara kwa mara.
“Nifungulieni nitoke… sitaki kufia humu,” mwanamke huyo
alisikika akisema katikati ya kilio chake.
***
Aliyekuwa akilia ni yule msichana wa Kidigo, Natasha, mke
wa mzee wa Kimakonde.
Hofu ilianza kumwingia msichana huyo toka pale alipoona mumewe akifungua mlango na kuwaruhusu yule mwanamume na mwanamke wake kuingia huku wakivutana. Watu hao walimtia hofu, mwanamume akiwa kaloa damu, bastola mkononi, huku akimkokota mwanamke yule mzuri, ambaye pia alichakaa. Huku akitetemeka, Natasha aliwachungulia hadi walipoingia kwenye vyumba vyake.
Mume wake alimwongezea hofu pale yeye pia alipoonyesha kila dalili ya kuduwaa, akiwa hana uhakika kama huyu ndiye mwajiri wake au la, na kama ndiye kwa nini awe na damu, bastola mkononi, huku akimburuza mtu muda huo.
Hofu yao iliongezeka maradufu pale risasi zilipoanza kurindima huko nje, risasi ambazo muda mfupi baadaye zilifuatiwa na tangazo la polisi likiwataka kutoka nje.
Natasha alikurupuka kukimbilia nje. Kwa mikono yake inayotetemeka alijaribu kufungua mlango huo ili atoke. Hakufanikiwa. Ilimchukua muda kubaini kuwa kitasa cha kawaida cha mlango huo hakikuwa kimefungwa, bali kitasa kingine, ambacho kilifunguliwa kwa nguvu za electroniki ndicho kilichochukua nafasi.
Halafu, umeme ukakatika.
Halafu, ukarudi tena ghafla.
Ndipo alipoangua kilio akiamini kuwa maisha yake yamefika ukingoni. Akaulaumu umasikini wa wazazi wake uliomfanya ashindwe kuendelea na shule na, hivyo, kuja mjini kwa matarajio ya kupata kazi, kazi ambayo iliishia kuwa ya kuuza pombe za kienyeji katika vilabu. Akailaani ‘bahati’ yake iliyofanya jioni ile, baada ya kununuliwa kuku na viazi, akubali kuondoka na mzee huyu mwenye umri zaidi ya baba yake mzazi. Akaishutumu zaidi tamaa yake pale alipoletwa katika jumba hili na kukuta lilivyojaa tele vitu vya anasa na vyakula ainaaina, jambo lililopelekea ajikute akisahau kurejea katika geto lake kule Mabwepande na kujikuta mke katika jengo hili, ambalo sasa lilielekea kuwa kaburi lake.
Kichwani mwake alikuwa na hadithi tele za watu wasio na hatia waliokufa mikononi mwa polisi. Moja ya hadithi hizo ikiwa ya shoga yake ambaye walipata kuishi nyumba moja,
akatoweka, hadi siku tatu baadaye picha yake ilipotolewa katika vyombo vya habari kama mmoja wa majambazi sugu yaliyouawa katika mapambano na polisi.
Hayo ndiyo yaliyofanya azidiwe na hofu. Alipomtazama ‘mume’ wake alimwona yeye pia haelewi la kufanya. Hivyo, akaendelea kulia huku akiupiga mlango kwa nguvu zake zote.
***
‘Mona Lisa’ katika chumba kingine, pia alikuwa akiutazama mlango katika hali ya kukata tama. Kama angekuwa na machozi katika macho yake angeweza kuangua kilio cha kwikwi. Kwa bahati mbaya, hakuwa nayo. Yalikauka kitambo kutokana na purukushani ngumu na dhoruba tele katika maisha yake.
Kama binadamu wengine, hakuumbwa kwa chuma wala mfupa. Alitumia damu mwilini na ubongo kichwani mwake. Kama binadamu wengine, mwili wake ulijua kuchoka na ubongo wake ulihitaji mapumziko.
Kwa takribani siku tatu sasa si mwili wala akili yake iliyopata fursa ya mapumziko hayo. Muda wote alikuwa mashakani, akikimbiza mtu huku yeye pia akikimbizwa, akijua kuwa anamkimbiza mtu hatari; akijua vilevile kuwa anakimbizwa na watu hatari. Kila dakika ilimkuta macho kimwili na kiakili, kuisaka roho ya mtu huku akiilinda roho yake mwenyewe.
Aliitaka roho ya Joram Kiango. Aliitaka kwa bei yoyote ile. Na angeweza kumuua kitambo kirefu. Safari yao toka Uwanja wa Ndege hadi hapa ilikuwa fursa nzuri sana kwake kuitimiza azma yake. Hata hivyo, jambo moja tu lilimfanya ashindwe kufanya hivyo; mashaka. Alitaka uhakika, kupitia katika sauti na macho ya Joram Kiango mwenyewe kama kweli ndiye aliyemuua au la. Toka alipopata taarifa kuwa nani aliyemuua, haikumwingia akilini kuwa angeweza kuwa Joram.
Joram, ambaye waliburudika naye usiku kucha! Joram, ambaye alikuwa mwanamume wake wa kwanza kumtia kichaa cha mapenzi hata kwa mara ya kwanza vilevile akafikiria kuolewa! Joram, aliyekuwa mcheshi na mchangamfu sirini na hadharani! Joram, ambaye nuru katika macho yake ilikuwa ikimshawishi kutapika uwozo wote uliofurika katika moyo wake
na kumlazimisha kumfuata popote ambapo angemwelekeza!
Haikumwingia akilini.
Na ni mashaka hayo yaliyomfanya Joram Kiango awe hai hadi sasa.
Ama hilo, ama uchovu wa mwili na akili, ama yote kwa pamoja, kwani alipokabidhiwa chumba na kuliona beseni la maji likimeremeta kwa usafi juu ya marumaru iliyofurika kila pembe ya ukuta na sakafu, chumba cha pili kitanda kipana kikimwalika kwa shuka safi zilizotandikwa vizuri; zile tani elfu moja na moja za uchovu alizoziacha kando zikamrejea. Kuoga alitamani, kulala alitamani. Zaidi ya yote njaa, ambayo kwa muda wote huo hakupata kuisikia, ilianza kumkereketa.
Ni wakati akiwa bado ameduwaa katikati ya chumba hicho, hajui aanze lipi, aishie lipi, aliposikia mlio wa risasi toka nje.
Mara hii! Aliwaza akiuendea mlango na kubaini kuwa ulikuwa umefungwa. Alijaribu moja ya funguo zake bandia. Hakufanikiwa. Akakumbuka kumwona Joram Kiango akitia mfukoni mwake rimoti ndogo mara baada ya kumfungulia. Hakujisumbua kupigana na mlango huo kama yule msichana wa Kidigo. Badala yake aliyatuma macho yake huku na huko kuangalia uwezekano wa kuweza kutoroka chumbani humo. Hakuiona namna zaidi ya kupitia mlangoni. Dirisha lilikuwa na nondo na vioo. Na hata bila hivyo kupitia dirishani kichwa chake kingekuwa halali ya risasi za hao wanaosubiri nje.
Onyo la kwanza lilitolewa wakati bado ametulia mbele ya
mlango huo akifikiri kwa nguvu zake zote.
“Joram Kiango… Tunajua uko ndani…” maneno ya Kambambaya yalimfikia vizuri chumbani humo. Joram Kiango! Sio Mona Lisa! Alijiuliza, hali iliyopelekea aamini kuwa polisi pia bado walikuwa gizani. Kwa kila hali aliamini kuwa si polisi tu, bali umati mzima ambao ulikuwa ukiiwinda roho yake kwa udi na uvumba ungenufaika mara elfu moja na moja kwa kumpata yeye badala ya Joram Kiango.
Halafu, umeme ukakatika.
Ghafla, ukawaka tena.
Hakuwa mwoga wa kifo, hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa kifo ni ada ya kila binadamu. Lakini hakuwa tayari kufa kabla ya kupata majibu ya mashaka yake. Hakuwa tayari kabla ya
kutekeleza jukumu lake la pili, ambalo lilihusiana na kutimiza wajibu wake kwa taifa lake, dunia yake na muumba wake.
Ni baada ya hapo tu ndipo angekuwa radhi kuwaachia roho yake. Si kabla!
***
“Hujaoga tu?” Joram alimuuliza ‘Mona Lisa’ mara tu alipofungua mlango na kumkuta kasimama katikati ya chumba, bastola mkononi.
Yeye binafsi alikuwa ametumia dakika tatu kuoga, kufunga jeraha lake kwa plastiki na kubadili nguo, hali iliyomfanya awe tofauti kabisa na Joram Yule aliyeingia muda mfupi uliopita akinuka kwa mchanganyiko wa jasho, damu na uchafu. Usoni alionekana mtulivu, asiye na wasiwasi wowote kwa bastola iliyokuwa ikimtazama kifuani wala polisi walioizingira nyumba yake.
“Sidhani kama nahitaji kuoga. Polisi watakapoingia hapa watayakuta maiti yangu. Lakini itakuwa baada ya kukuua wewe,” msichana huyo alivuta pumzi kwa nguvu na kurekebisha kifyatulio bastola. “Kitu kimoja tu kitakachonichelewesha kufyatua bastola hii ni utata unaojitokeza. Nieleze, kwa nini uliamua kuniua?”
Kwa mshangao wa msichana huyo Joram Kiango aliangua kicheko. Akautia mkono wake mfukoni na kutoa pakiti ya sigara ambayo aliiwasha kwa mikono iliyotulia kabisa. Akaitia mdomoni. Kwa sauti yenye utulivu vilevile akauliza taratibu, “Margareth Johnson, utakufa mara ngapi? Hata yesu wa Nazareth alikufa mara moja, akafufuka. Hajawahi kufa tena na wala hatarajiwi kufa tena.”
Msichana huyo alitokwa na macho ya mshangao. “Wapi ulikolipata jina langu?”
Joram akacheka tena, “Sio jina lako tu,” akamwambia. “Najua mengi kuliko unavyofikiria wewe. Naijua hata tarehe ya kifo chako cha kwanza. Si ulikufa katika ajali ya gari, barabara ya Moshi/Arusha, mwezi Agosti tarehe ishirini na nane mwaka elfu mbili?”
Joram alimwona msichana huyo akiduwaa. “Labda nikukumbushe zaidi. Ajali hiyo ilitokea eneo la Boma Ng’ombe,
barabara ya Arusha/Moshi, usiku wa manane. Katika gari ulikuwepo wewe na dereva wako. Miili yenu wote iliteketea vibaya kwa moto uliofuatia ajali hiyo. Hakuna aliyefanikiwa kuwatambua. Hivyo, mlizikwa katika kaburi la pamoja kwa maelekezo ya mwajiri wenu, Jeshi la Polisi. Sivyo?”
“Naanza kukukubali kuwa wewe ni mpelelezi hodari. Nimeishi maisha yangu yote kwa hila, nikimlaghai kila mtu. Sikutegemea kama fumbo la maisha yangu lingeweza kufumbuliwa. Hata hivyo, unachofahamu ni kidogo sana katika maisha yangu.” Ilikuwa sauti ya msichana huyo. Alivuta pumzi kwa nguvu kidogo kabla hajaongeza, “Hata hivyo, bado hujaniambia kwa nini uliniua?”
“Kukuua!” Ilikuwa zamu ya Joram Kiango kushangaa. “Bado unasisitiza kuwa nilikuua. Sikiliza mpenzi. Kama unataka tuzungumze kama watoto wa shule ya msingi ni juu yako. Lakini aliyekufa ni Mona Lisa mwingine, pacha mwenzio. Wewe, ukitokea unakokujua mwenyewe uliingilia kati penzi letu. Ulitumia hila kunilaghai hata nikahadaika na kudhani kuwa niko na Mona Lisa kitandani. Kwa nini ulifanya vile?”
Kwa kiasi fulani, Joram alikuwa akiongea kwa uhakika. Lakini, kwa namna nyingine, alikuwa akitafuta kitu katika macho ya msichana huyu ili kupata uthibitisho wa hisia zake, hisia zilizomjia toka alipopata taarifa ya mtu aliyeitwa kwa jina la utani Mona Lisa, ambaye jina lake halisi ni Margareth, aliyekufa kitambo kwa kilichoelezwa kuwa ni ajali ya gari, alipolinganisha vitendo vyake na ujasiri wake, aliamini kuwa kitendawili cha kufa na kufufuka kwa ‘Mona Lisa’ kilikuwa kimefikia tamati. Mona Lisa aliyekufa pale kitandani alikuwa Mona Lisa halisi. Mona Lisa mpole, mtaratibu, mwenye haya! Mona Lisa ambaye aliondokea kumpenda, ingawa hakupata kumgusa! Huyu alikuwa Mona Lisa mwingine. Mona Lisa asiye na tone la haya wala chembe ya woga katika moyo wake. Mona Lisa ambaye si kwamba anacheza na mauti peke yake, bali anaonyesha kufurahishwa na mchezo huo. Naam, Mona Lisa wa bandia.
Chochote ambacho Joram alitegemea kukiona katika macho ya msichana huyo kilimezwa na tabasamu jembamba lisilopendeza hata kidogo, tabasamu ambalo lilibeba hasira,
chuki na kisasi.
“Labda huelewi Joram,” alitamka baadaye. “Nadhani huelewi,” alirudia. “Kumwua Mona Lisa ni kuniua mimi. Yeye ni sehemu yangu, sehemu ya mwili wangu; sehemu ya uhai wangu. Tuliishi pamoja miezi tisa tumboni. Tukachangia na kugombea titi la mama kwa miezi miwili kabla mama yetu hajapokonywa roho yake na kutuacha yatima. Tukatenganishwa kama mifugo na kupokonywa fursa yoyote ya kuonana, achilia mbali kujuana. Na fursa hiyo ilipotokea tayari ameuawa…”
Kwa mara ya kwanza Joram aliyaona machozi yakilengalenga na hatimaye kuteleza toka katika macho hayo mazuri, machozi ya mwanamke mwenye huzuni. Machoni mwa Joram Kiango hakuwa tena yule ‘Mona Lisa’ mwenye kisasi, ‘Mona Lisa’ aliyekuwa tayari kwa lolote; Tayari kufa… Tayari kuua… Badala yake, aliyesimama pale alikuwa Mona Lisa yuleyule aliyemfahamu, Mona Lisa aliyempenda. Mona Lisa mpole, mtaratibu, mwenye haya!
Bila yeyote kati yao kujua wanachokifanya, walijikuta wamekumbatiana, kichwa cha ‘Mona Lisa’ kikiwa kimelala kifuani mwa Joram Kiango, mikono yake ikiwa imemkumbatia kiuno. Naye Joram alijikuta kamkumbatia, huku mkono wake ukimfuta machozi.
“Nisamehe Joram Kiango,” msichana huyo alinong’ona. “Nisamehe kwa yote,” aliongeza. “Kwa kukurubuni hata ukaamini kuwa umelala na dada yangu. Nisamehe pia kwa kukufikiria kuwa ulimwua au kuhusika kumwua Mona Lisa. Kitu fulani kimekuwa kikininong’oneza vinginevyo. Sasa nimepata uhakika. Nadhani namfahamu aliyemuua Mona. Nakuhakikishia kuwa leo hii atamfuata Mona Lisa kwa mkono wangu huu,” alisema akijikwanyua toka katika fungate la Joram.
“Mie pia sitalala usingizi hadi nifumue kichwa cha yeyote aliyemwua msichana yule. Unadhani ni nani hasa?” Joram alisema na kuuliza.
“Ni haditi ndefu kidogo. Kumbuka polisi wanatusubiri hapo nje. Unadhani wataturuhusu tukaifanye kazi hiyo?”
Joram akacheka kabla hajasema, “Watasubiri sana. Hii ni
nyumba yangu.”
“Una hakika?” Margareth aliuliza. “Unajua siwahofii sana polisi? Zaidi yao kuna watu wenye kiu kali zaidi ya damu yangu. Wanaisubiri kwa hamu kama tai anayenyemelea kifaranga. Na kinachowasumbua ni hiki,” alitoa kitu kidogo mfano wa kalamu na kumkabidhi Joram Kiango, “Hiyo ni diski. Kama una kompyuta na kama una hakika kuwa tunaweza kupata walao dakika tano tu ifungue uone kile ambacho kinafanya waitafute roho yangu.”
“Tuna muda wa kutosha,” Joram alimhakikishia. “Polisi wanaweza kusubiri hapo nje hadi mwisho wa dunia. Nimekuambia hii ni nyumba yangu. Na nimeijenga kwa mikono yangu.”
***
Kabla ya kurejea kwenye chumba chake cha kompyuta Joram alifanya mambo mawili. Kwanza aliitumia rimoti yake kufungua mlango kwa muda. Kisha, alimwendea mlinzi wake na mke wake na kuwaambia kwa sauti ya upole, “Poleni sana, msiwe na hofu. Hakuna lolote litakalokupateni. Tokeni taratibu, mkiwa mmeiweka mikono yenu juu. Polisi watawasumbua kidogo kwa maswali ya kipuuzi. Wanaweza hata kukutisheni, lakini baadaye watawaachieni huru. Mambo yakipoa rudini hapa na mtaendelea kuishi kama kawaida.
Akiwa ametiwa moyo kwa utulivu aliouona katika macho na sauti ya Joram Kiango mzee huyo alitii. Akamwongoza mkewe kutoka nje.
Natasha, mtoto wa Kidigo hakuitegemea fursa hiyo ya kutoka katika nyumba hiyo akiwa hai. Akakumbuka alivyopata kuwaona katika mkanda wa video, wateka nyara walioiteka ndege ya abiria walivyojitoa huku wakipepea vitambaa vyeupe juu ya vichwa vyao. Polisi waliwapokea na kuwapokonya silaha kabla ya kuwafunga pingu. Ni hivyo, alivyofanya yeye pia. Alichopoa toka mwilini mwake moja ya kanga zake na kuanza kuipunga huku na huko, huku kwa sauti akipiga kelele, “Msituue, tunakuja…”
Kwa bahati mbaya, kanga yake haikuwa nyeupe. Ilikuwa na rangi mbalimbali, maandishi yake makubwa, La uvundo
halina ubani yakionekana waziwazi. Lakini polisi waliwaelewa. Mara tu geti lilipofunguka na kuruhusu watu hao wawili, geti lilijifunga tena. Polisi wawili waliolidaka pindi likifunguka ili waingie ndani walirushwa kwa mkondo wa umeme na
kuanguka huko na kule.
“Msifanye pupa!” Inspekta Kambambaya alionya. “Maadam yumo ndani sisi tuko nje, tutampata tu,” alisema akimaanisha Joram Kiango.
Kama alivyotabiri Joram Kiango, mzee wa Kimakonde na mkewe wa Kidigo walitiwa pingu na kupakiwa ndani ya gari la polisi. Kabla hawajapelekwa kituoni Kambambaya aliwahoji maswali ya harakaharaka; watu wangapi wako ndani? Wana silaha au hawana? Wanatumia nini kufunga na kufungua milango? Wanafanya nini? Na mengineyo.
Mengi kati ya majibu aliyoyapata aliyategemea; wamo watu wawili tu! Ndiyo, wana silaha! Wana rimoti ya kufunga na kufungulia milango. Hapana, haijulikani wanachokifanya kwani mwanamume amejifungia chumba chake cha kujisomea, mwanamke amefungiwa chumba cha pili!
Wanafanya nini! Kambambaya alijiuliza. Wanapanga kufanya nini! Ni swali lililomtatiza zaidi. Hakuona kama Joram Kiango alikuwa mtu wa kukubali kujiweka katika mazingira ya aina hiyo, yasiyo na tofauti yoyote na mtu ambaye ni mfungwa, kwa kujichimbia ndani, huku polisi wakiwa wameizingira nyumba nzima.
Askari wengine kumi, wenye magwanda kwa wasio nayo, gari la wagonjwa, na ya kuzimia moto na daktari, kama alivyokuwa ameagiza Kambambaya tayari waliwasili katika eneo hilo wakisubiri amri yake. Kwa upande mwingine vijana wake, wakitumia vifaa maalumu vya kujikinga na umeme walikuwa tayari wamekamilisha kukata sehemu kubwa ya nyaya zilizoizunguka nyumba hiyo wakisubiri amri ya kuingia.
Amri ambayo aliamua kuitekeleza baada ya kutoa wito mwingine kwa kutumia kipaza sauti.
“Joram Kiango hili ni onyo la mwisho kabisa. “Tunakupa dakika mbili tu uwe umetoka ukiwa umeiweka mikono yako juu. Nitahesabu mara kumi. Baada ya hapo utajilaumu mwenyewe,” alisita kidogo kabla ya kuanza kuhesabu, “Kumi!”
Baadaye kidogo alinguruma tena, “Tisa!”
Huku akiwaelekeza askari wanne, waliofuzu katika sanaa ya mapambano ya mikono kujipenyeza ndani, Kambambaya aliendelea kuhesabu, “Nane!”
*** “Saba!”
Joram alimsikia vizuri sana. Lakini alikuwa amezama tena katika kompyuta. Kitu alichokuwa akitazama katika uso wa kompyuta hiyo kilimfanya ashindwe kuyaamini macho yake.
“Una hakika hii siyo moja ya filamu za vitisho, iliyobuniwa ili kusisimua watu?” alimuuliza Margareth ambaye alikuwa amesimama nyuma yake, akiwa pia kainamia kompyuta.
“Roho yangu inatafutwa kwa udi na uvumba kwa ajili ya hicho unachoita mchezo wa kusisimua. Watu wote waliopoteza maisha na wanaoendelea kupoteza ni kwa ajili ya hicho unachoita mchezo wa kuigiza. Mona Lisa, sehemu ya mwili na roho yangu, ameuawa kwa ajili ya huo mchezo wa kuigiza…”
“Sita!”
Joram aliitazama saa yake. Kisha alikumbuka kuitazama screen nyingine iliyokuwa pembeni mwa kompyuta hiyo. Kama alivyotegemea, aliwaona askari wakipenya katika tundu walilotoboa na kujipenyeza ndani. Walikuwa wakitembea kwa kunyata, hatua baada ya hatua, mitutu ya bunduki zao ikiwa imewatangulia.
Margareth alikuwa amewaona pia. “Tutawahi kutoka?” alimuuliza Joram. “Nisingependa kufa kabla ya kuhakikisha nimekifumua kichwa cha mwendawazimu aliyebuni kitu hicho. Awali ilikuwa kwa ajili ya dada yangu pekee. Sasa ni pamoja na kupigania dunia.”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment