Search This Blog

Thursday, 29 December 2022

BOMU - 4

   

Simulizi : Bomu 

Sehemu Ya Nne (4)





Adrian Kaanan akishirikiana na Martin Hisia pia walifanya kazi kubwa katika misheni ya kumsaka mwanamke muuaji mwenye kasi na shabaha ya ajabu. Kwa majina aliitwa Red Butterfly. Kutokana na kufanikisha misheni kadhaa hakuna mwenye kuhoji juu ya uwezo wa askari huyu kijana. Ambaye watu wengi wakimtazamia kuwa mrithi wa Daniel Mwaseba.




Sasa, alikuwa mbele ya nyumba ya kulala wageni ya Platnumz akiwa na bastola nyeusi katika mkono wake wa kuume. Dhamira yake kuu ilikuwa ni kummaliza kwa mkono wake mtoto wa kinigeria, wa kuitwa Imma Ogbo.




Pembeni ya nyumba hiyo alikuwepo David. Mwanajeshi imara ambaye ameshinda vita kadhaa huko msituni.




David alikuwa ni mtu katili na asiyekuwa na msamaha kwa wavunja amani. Alifanya kazi kadhaa chini ya mwamvuli wa umoja wa Afrika huko katika misitu ya Kongo na kuhakikisha waasi hawafurukuti. Kabla ya kwenda Sudan kwa mwamvuli wa umoja wa mataifa kwenda kupambana na kikundi cha kigaidi cha Al shabab. Mote alifanya kazi yake kwa usahihi na kutunukiwa tuzo mbalimbali. David hakuwa na mashara na wavunja amani. Lakini leo, David alikuwa katika misheni yake ya kwanza mjini. Misheni ambayo alianza kwa kufanya kosa, na sasa alikuwa anataka kusahihisha kosa.




Ataweza?




Sasa, alikuwa na bunduki aina ya SMG mkononi mwake. Kichwani alikuwa na wazo moja tu, la kuua tu...akiamini kwamba watu wanaowawinda hapo ndio wameiteka familia.




Misheni hii ya hatari ilikuwa inaongozwa na mpelelezi namba moja nchini Tanzania, kwa majina Daniel Mwaseba. Ndiye ambaye alikuwa anawaongoza wenzake kwa kupitia vile vifaa vyeusi walivyoweka masikioni mwao.




"Taratibu na kwa umakini mkubwa tusonge mbele. Kuweni makini kuhakikisha hawatutoroki hawa jamaa. Ama zao, ama zetu..." Daniel alisema kwa sauti ambayo ilisikiwa na kila mmoja.




"Tumekupata, tumekupata" David na Adrian waliitikia kwa pamoja.




Kule mbele Adrian aliingia ndani kwa kupitia mlango wa mbele. Alikutana na ukumbi mkubwa wa vinywaji uliokuwa unatazamana na mapokezi ya nyumba hiyo ya kulala wageni. Alipoingia tu, watu wote waliokuwa wanapata vinywaji mbalimbali huku wakiangalia mpira walimwangalia yeye. Nyuso za uwoga zikiwatamalaki.




Adrian hakujali.




Bastola yake bado ilikuwa mbele huku macho yake yakifanya kazi isivyo kawaida.




Kwa harakaharaka aliwaangalia wale watu waliokuwa wanakunywa vinywaji mle ndani. Walikuwa watu kama kumi na tano. Lakini hakumwona Imma Ogbo, hakumwona Dr Luis.




Moja kwa moja alielekea mapokezi. Ambapo kulikuwa na dada mmoja akihangaika kupanga vinywaji katika friji. Yule dada alipogeuka nyuma, alikutana na macho ya Adrian. Mtetemo ulionekana kwa yule mwanamke.




Kutazamana na mdomo wa bastola si kazi ndogo!




"Samahani kwa kuingia namna hii. Maneno mengi tutaongea baadae, kwasasa nielekeze chumba alichopanga Imma Ogbo" Adrian alisema.




Yule mhudumu alikaa kimya. Macho yake yakionesha kuwa hakumwelewa hata kidogo.




"We msichana sina siku nzima hapa!" Adrian aling'aka.




"Sijakuelewa kaka yangu..huyo Imma nani sijui mi simfaham. Na hatuna mteja mwenye jina hilo hapa" Yule mhudumu aliipata sauti yake.




Adrian akajipekua katika mfuko wa nyuma wa suruali yake. Akatoa picha na kumrushia yule msichana. Huku akisindikizwa na maneno...




"Namtaka huyo!!"




Yule mwanamke aliidaka ile picha na kuiangalia. Mstuko dhahiri ulionekana katika macho yake. Alikuwa anatazamana na mtu anayemjua.




"Yu..po ch..umba cha Li..on" Mtetemo dhahiri uliambatana na sauti yake.




"Nipeleke" Adrian alisema.




Yule mhudumu alitoka mle kaunta. Na kuongozana na Adrian kuelekea katika chumba cha Lion, kwenda kuwakamata wakina Imma Ogbo.




Upande wa Daniel Mwaseba alikuwa amekaribia kuingia nyumba ya kulala wageni ya Platnumz kwa kupitia mlango wa nyuma. Alikuwa na maelezo yote kuhusu chumba walipo wakina Dr Luis na Imma Ogbo. Kwa kupitia vile vifaa walivyoweka masikioni, wakati Adrian akimuhoji yule Mhudumu.




Chumba cha Lion...




Daniel aliingia ndani, akiongozwa na bastola yake ambayo ilikuwa tayari kwa lolote. Alipita uwani ambapo kulikuwa kumepandwa migomba kadhaa. Alitembea kidogo na kuingia sehemu ambapo kulikuwa na vyumba vya uwani vya 'guest' hiyo.




Akaanza kuhesabu vyumba..




Hali ilikuwa tulivu. Hakukuwa na pilikapilika katika vyumba hivyo vya uwani.




"Tiger" Alisoma moyoni.




"Elephant" Akasoma chumba kingine.




"Rabbit" Akasoma tena mlango mwingine.




"Rhino.." Akasoma tena.




Akapiga jicho mlango wa tano. Hapo ndipo alipokiona..




"LION!!" Alisoma kwa nguvu moyoni huku damu yake ikisisimka.




"Humu ndimo walimo wakina Imma Ogbo" Daniel alisema kimoyomoyo huku akiusogelea ule mlango. Mlango uliokolezwa kwa wino mwekundu. Maandishi yakisomeka..




LION.






Daniel akagonga mlango wa chumba cha Lion kwa kutumia mdomo wa bastola.




Ngo ngo ngo..




Mlango ulikuwa kimya. Kimya cha kaburi.




Akagonga tena.




Ngo ngo ngo..




Ikawa kimya tena kama awali. Hakuna aliyejibu.




Kwa mbali, akasikia sauti za miguu kutoka mlango alioingilia. Akajua pale si mahali salama. Alipiga hatua tano kubwa kukimbilia ule upande lilipo bafu. Akabana katika kona moja. Macho yake yote mawili yakiwa katika mlango wa chumba cha Lion..


Je ni nani alikuwa anakuja?




Zile kelele za miguu alizozisikia zikaishia katika chumba cha Lion. Kutoka pale alipokuwa Daniel aliwaona vizuri watu wale wawili.




Alikuwa Adrian Kaanan na yule dada Mhudumu.




Daniel alimwona Adrian akigonga ule mlango kama alivyokuwa anagonga yeye. Sasa mlango ule uligongwa kwa mara ya tatu na watu wawili tofauti.




Daniel na Adrian..




Adrian akagonga tena. Huku hofu dhahiri ikionekana katika sura ya yule mhudumu kila mlango ulipokuwa unagongwa. Bila shaka alikuwa anahisi kwamba walikuwa wanaibishia hodi hatari.




Adrian akashika kitasa cha mlango. Akakizungusha. Kikazunguka taratibu. Na mlango ukaanza kufunguka.




Adrian alikuwa anausukuma taratibu mlango kwa mkono wa kushoto. Huku mkono wa kulia ukiwa umeshikilia bastola iliyoondolewa usalama. Tayari kufanya shambulio!!




Tayari kwa kumfyatua Imma Ogbo!




Kwa mwendo wa taratibu akajitosa mle chumbani. Huku akimwacha yule mhudumu kwa nyuma. Ngoja sasa tumtambue jina lake, alikuwa anaitwa Merina.




Adrian alikutana na chumba kisichokuwa na mpangilio. Godoro lilokuwa chini huku kabati kubwa likiwa limeegeshwa upande. Chandarua kilikuwa kimekatwa. Runinga ikionesha picha bila sauti.




Macho ya kipelelezi ya Adrian yalitazama kila mahali mle ndani. Kwasasa wala hakukuwa na mtu, lakini kwa mazingira waliyoyakuta ilionesha kwamba kulikuwa na watu, tena wamefanya vurugu ya kutosha.




Alitumia dakika tano kupekuapekua mle ndani. Hakuna chochote cha maana alichokipata.




"Nipo chumba cha Lion. Chumba kimevurugwa hasa. Hakuna mtu yeyote humu ndani" Adrian alisema kupitia kile kifaa cha mawasiliano.




"Nipo karibu na hiko chumba. Nakuja" Daniel alijibu.




"Mimi nipo pembeni hapa. Sehemu ambapo kuna jiko la hii guest. Nimeona michirizi ya damu. Nimejaribu kuichunguza, sio damu ya mnyama ni damu ya binadamu. Tena ya moto!" David alisema.




"Angalia mwelekeo wa hiyo damu. Inaweza kuwa damu ya adui" Daniel alisema.




"Nafanya hivyo Daniel" David alijibu.




Wakati huo Daniel alikuwa anarudi kuelekea chumba cha Lion. Huku akiwa makini kama awali.




Alifika.




Aliusukuma mlango na kuingia ndani, Merina akiwa nyuma yao. Naye aliushuhudia mvurugano akiousema Adrian. Chumba kilikuwa kimevurugwa haswa!!




"Nini hiki?" Merina alishangaa.




Hakuna aliyejibu.




Daniel kwa kutumia macho yake ya kipelelezi alianza kukichunguza kile chumba. Naye hakugundua kitu chochote kipya. Macho yake yalitembea mlemle yalipotembea macho ya Adrian.




"Tunyanyue godoro" Daniel alishauri.




Kwa kushirikiana na Adrian walilinyanyua lile godoro na kuliweka mahala pake.




Hapo ndipo walipoona kitu cha kushangaza..




Pale mahali lilipokuwa godoro walikutana na damu!




Kengele za hatari zikagonga kichwani mwao. Na maelezo ya David yaliwarejea vichwani mwao.




"Mimi nipo pembeni hapa. Sehemu ambapo kuna jiko la hii guest. Nimeona michirizi ya damu. Nimejaribu kuichunguza, sio damu ya mnyama ni damu ya binadamu. Tena ya moto!" Hayo yalikuwa maneno ya David.




"Damu!! Ina maana kuna mtu amejeruhiwa humu?" Adrian aliuliza.




"Bila shaka. Hii ni damu ya mwanadamu..kuna mtu alijeruhiwa humu ndani kabla hawa watu hawajatoroka" Daniel alisema.




"Tumechelewaa" Adrian alisema akiwa amekata tamaa.




"Usikate tamaa Adrian. Amini tunaenda kuwakamata hawa watu. Tupo karibu nao sana hivi sasa kuliko wakati wowote tangu sakata hili lianze" Daniel alisema.




Adrian alishusha pumzi kwa nguvu.




Mara sauti ilisikika katika vile vifaa vya masikioni. Ilikuwa ni sauti ya David.




"Hii michirizi ya damu imeenda hadi huku nyuma kabisa ya hii guest, porini huku. Hapa nimeikuta damu nyingi zaidi, inaonesha walipumzika hapa" David alisema.




"Baada ya hapo inaonesha hiyo michirizi ya damu ilielekea wapi?" Adrian aliuliza.




"Imekomea hapahapa. Hii michirizi haiendi sehemu yoyote tena.." David alisema.




"Tusubiri. Tunakuja hapohapo" Daniel alisema.




"Merina, hapa mlipangisha watu hatari sana. Kuweni makini sana msiruhusu guest yenu kuwa kichaka cha wahalifu" Adrian alisema.




Merina aliitikia kwa kichwa. Huku akijitahidi kuzuia machozi yakiyoanza kujenga ujirani na macho yake.




"Adrian twenzetu mahali alipo David. Tukiwa watatu bila shaka tutagundua kitu hapo.." Daniel alisema.




"Na Merina hakikisha hamumpangishi mtu chumba hiki. Pengine tutarudi tena na kukihitaji kukitumia kikiwa hivihivi. Pia usiwaambie chochote wahudumu wenzako wala wale wateja, fanya kama hakijatokea kitu. Lakini kama watakuja tena hao watu, piga mara moja namba hii" Daniel alisema huku akimpa business kadi Merina. Wakati akimpa akamtekenya kidogo katikati ya mkono. Merina alistuka kidogo na kumlegezea jicho Daniel. Daniel akalifinya jicho lake la upande wa kulia pia. Merina akalainika..




"Tutawasiliana" Daniel alimtoa katika mawazo Merina kwa kauli hiyo.




Kisha wakaondoka.




Je kina Daniel wataenda kukutana na nani huko? Je michirizi ya damu ni ya nani? Vipi tena Daniel na Merina, umewaelewa?






Daniel Mwaseba na Adrian Kaanan Kaanan kwa tahadhari kubwa sana walielekea kule nyuma ya ile nyumba ya kulala wageni ya Platnumz.




Daniel alikuwa mbele, Adrian akifuatia nyuma. Bastola mikononi mwao. Macho yakizunguka kila upande kwa umakini na kasi. Yakiitafuta hatari!. Yakimsaka adui!.




Kule porini alipokuwa David bado alikuwa anaangaza huku na kule. Lakini hakuambua lolote, michirizi ya damu ilikuwa imeishia palepale, na kutengeneza kidimbwi kidogo cha damu.




"Nini kilitokea hapa?. Mbona hii michirizi ya damu hakuna inapoelekea. Kwanini michirizi hii iishe ghafla. Au walipofika hapa waligundua kwamba hii michirizi ya damu itakuwa tatizo kwao?. Na kuamua kuidhibiti?" David alikuwa anajiuliza mwenyewe, lakini hakuwa na jibu hata moja.




Alikata shauri kuwasubiri kina Daniel Mwaseba watafute majibu kwa pamoja.




***




Martin Hisia, mwanaume mwenye Hisia zake nd'o alikuwa anaingia Vikindu. Kichwani mwake alikuwa anawaza kitu kimoja tu, kuhakikisha mpenzi wake, Felisia, anakuwa salama.




Leo hii aliamini usahihi wa hisia zake tangu siku ya kwanza aliyokutana ba Felisia. Alikumbuka kila kitu kilivyotokea siku ile katika klabu ya Bilcanas. Lakini kwa sasa hakujari hayo. Alikuwa anataka kitu kimoja tu, kuhakikisha Felisia anakuwa salama. Alitambua sana matokeo ya kitendo cha hatari alichokifanya Felisia. Huku akijua kwamba adhabu yake ni moja tu endapo atastukiwa.


Kifo!!




Na yeye hakutaka hata kidogo Felisia afe kwa namna yoyote ile.




Felisia Nyenyembe. Mwanamke waliyekutana kama bahati tu katika klabu ya usiku ya Bilcanas...




Siku hiyo Martin alikuwa ametoka kukamilisha misheni moja ya hatari sana. Misheni ambayo iliisha kwa mafanikio makubwa sana kwake, na kuhakikisha bilioni sita zilizoibwa kutoka katika benki ya wakulima zinarudi salama katika benki hiyo. Huku watu wote waliohusika na wizi katika benki hiyo wakitiwa katika mikono ya dola.




Siku hiyo jioni ndipo alipoenda katika klabu ya muziki ya Bilcanas kujipongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya.




Baada ya kunywa sana pombe, ndipo alipoamua kuingia sehemu ya kuchezea naye aoneshe ujuzi wake katika fani hiyo. Wimbo uliokuwa unapigwa ni 'Fool again' wa kundi la muziki la West life.




Martin aliucheza haswa wimbo huo, akichagizwa na pombe zilizokuwa zimejaa pomoni kichwani mwake.




"Tunaweza cheza pamoja?" Sauti ya kike nyembamba ilipenya katika masikio yake. Martin alimwangalia mmiliki wa sauti hiyo aliyekuwa mbele yake.




Blauzi nyeupe yenye kung'aa, suruali ya jeans fupi iliyombana vyema na viatu vya mchuchumio kwa chini vilikuwa ni vitu alivyovitazama kwa haraka.




"Huyu ni mtoto haswa" Alijisemea kimoyomoyo.




Martin hakuwa na nguvu za kukataa ombi la binti huyo, ingawa hisia zake zilimwambia kwamba hakuwa mtu mzuri.




Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Martin Hisia alipingana na Hisia zake. Hisia zilizoanza tangu akiwa mtoto mdogo na kuaminiwa na kila mtu.




Ilikuwa Martin alikuwa akihisi kitu basi lazima kitatokea. Na hili lilimfanya jina la babaye mzazi liondoke na kuitwa Martin Hisia.




"Usijari dada. Twaweza cheza, tena hadi majogoo ukitakaa" Martin alisema kwa sauti ya kilevi.




Na DJ alibadili wimbo. Sasa ulikuwa unaimbwa wimbo wa 'My love' toka katika kundi hilohilo la West life.




DJ kama alijua kuweka wimbo huo. Maana penzi jipya ndio lilikuwa linazaliwa mjini. Hadi wimbo laini wa 'My love' ulipoisha Martin alikuwa ameshadadisi kila kitu. Sasa alikuwa analijua jina la yule binti, mahali anapoishi na kazi anayoifanya hapa mjini. Yote hayo waliulizana wakati wimbo wa 'My love' ukikita katika spika za klabu ya Bilcanas.




Martin alihisi lakini hakutilia maanan. Pombe, ukichanganya na hisia kali za mapenzi basi zilimfanya aendelee kuzidharau hisia zake. Hakujua kwamba yule alikuwa ni wakala wa Imma Ogbo aliyetumwa kwake kwa kazi maalum.




Tangu siku hiyo Felisia akawa mpenzi wa Martin Hisia, huku akipeleka taarifa mbalimbali za Martin kwa Imma Ogbo.




Katika moyo wa Martin Hisia alitokea kumpenda sana Felisia. Felisia alikuwa mwanamke aliyekamilika haswa. Wa kupendwa na kila mtu. Hata wewe...




Ukiacha weupe wake wa asili sio wa kuchanganya na carotone na maji ya diana, sura nzuri na shepu ya kufa mtu, Felisia alikuwa na ya zaidi. Alikuwa mpishi mzuri sana jikoni. Alikuwa anajua kupika kila aina ya chakula na kuwa kitamu sana. Pia Felisia alikuwa malaya sana kitandani. Alikuwa anaweza kufanya mitindo ya kila aina ya mapenzi tena kwa umahiri wa ajabu sana. Huku akilia kwa milio ya kushangaza. Hili la kitandani lilimmaliza sana Martin. Akawa hana uthubutu wa kumuacha hata kidogo ingawa alikuwa anamtilia shaka mara kadhaa kwa matendo yake.




Siku moja, usiku wa manane wakiwa wamelala kitandani simu ya Felisia iliita. Felisia aliamka na kumwangalia Martin kama amelala. Martin alijifanya ametopea usingizini.


Kumbe haikuwa hivyo..


Martin alikuwa anasikia kila kitu!




Felisia alinyanyuka pale kitandani taratibu. Kuhakikisha hamuamshi Martin, alielekea bafuni na simu yake mkononi. Martin naye aliamka kitandani na kumfuata kwa nyuma Felisia hukohuko bafuni.




Kule bafuni Felisia alipiga simu yake kwa Imma Ogbo. Akawa anaongea kwa sauti ndogo sana. Martin alijaribu sana kusikiliza akiwa nje ya mlango wa bafu, lakini aliambulia maneno mawili tu.




Misheni na Daniel Mwaseba..




Felisia alikata simu, na kuelekea chumbani. Alimkuta Martin akiwa amelala vilevile. Akaamini kwamba maongezi yake na Imma Ogbo hayajasikiwa na kiumbe chochote kile hapa duniani.




Kumbe haikuwa hivyo.




Martin kichwa kilimuuma kwa mawazo, huku akiwa anatamani amfahamu huyo aliyekuwa anaongea na Felisia usiku wa manane. Hisia za wivu zilimtawala zaidi ya hisia za kipelelezi. Maneno mawili aliyoyasikia kwenye simu yalikuwa ya muhimu sana kwake kuyafanyia kazi, lakini alipotezea. Mapenzi yalikuwa yamemlevya. Akadharau kazi.




Asuhuhi kulikucha. Kabla hawajatoka kitandani wakafanya mapenzi ya asubuhi. Wenyewe walikuwa wanaita 'morning glory'.




Kwa utundu alioufanya Felisia asubuhi hii, yalimsahaulisha kila kitu Martin Hisia.


Kila siku mwanamke huyu alikuwa mpya kitandani, alikuwa anakatika kiajabu huku akitoa kilio mithili ya ndege chiriku.




Alivyotoka hapo alimpikia chai yenye viungo mbalimbali na chapati zilizokaangwa kikike. Huku pembeni kukiwa na supu ya kuku iliyopikwa ikapikika. Hapo alikuwa tayari katoka kuogeshwa kwa maji ya moto na kusuguliwa kila sehemu ya mwili wake.




Unafikiri hata alikumbuka simu ya jana usiku?




Alichokumbuka ni kumweka kifaa kidogo maalum mithili ya punje ya mchele, katikati ya nywele za Felisia zilizosukwa kwa mtindo wa yebo fasta, kifaa hiko kikimwezesha Martin kujua uelekeo wa Felisia..




Yote hayo ulikuwa ni wivu tu..




***




Imma Ogbo na Dr Louis walikuwa katika nyumba ya balozi wa Nigeria hapa nchini. Walitoka kule Vikindu kwa mtindo wa ajabu wakisaidiwa na balozi Agdir na kusalimika kutiwa mkononi na wakina Daniel Mwaseba.




Felisia yeye, alikuwa katika stoo ndogo iliyopo ndani ya nyumba hiyo, akiwa uchi wa mnyama huku akiwa amefungwa kamba ngumu mikononi na miguuni.




Mwili mzima ukiwa umevimba huku akiwa anabubujikwa na damu sehemu kadhaa. Jicho lake moja lilikiwa likiwa limetolewa na kubaki shimo baya na la kutisha! huku mkono wake wake wa kulia akiwa hana kidole cha mwisho. Kilikuwa kimekatwa!


Hiyo ilikuwa kazi ya Imma Ogbo katika kumfanya Felisia aseme alikuwa anampigia nani simu kule chooni.




Lakini pamoja na mateso yote hayo bado Felisia alikuwa mgumu kufunguka, huku akidai alienda bafuni kujisaidia sio kupiga simu. Utetezi huo haukuingia hata kidogo katika kichwa cha Imma Ogbo na kumuahidi atarejea tena!


Na hapo ndipo atasema hata asivyoulizwa.




Je nini kitatokea?








Stoo yote aliyokuwepo Felisia ilikuwa imetapakaa damu, na nyingine ikianza kuganda sakafuni.




Maumivu aliyokuwa anayasikia Felisia sehemu mbalimbali katika mwili wake hayakuwa na mfanowe. Alikuwa anasikia maumivu kuanzia utosini hadi nyayoni. Imma Ogbo alimfanyia unyama wa hali ya juu!!




Kama Felisia alikuwa anadhani aliwahi kukutana na mtu katili hapa duniani, basi hiyo itakuwa labda kabla ya kukutana na Imma Ogbo!




Imma Ogbo alikuwa katili na nusu!




Imma Ogbo, mwanaume wa Kinaijeria ambaye aliamini kuwa ni rafiki wa kweli kwake lakini kwasasa haikuwa hivyo. Alikuwa ni adui namba moja kwake.




Na aliapa kumuua kwa mkono wake endapo akipata tu nafasi hiyo!!




Felisia, hakujua kwamba Imma Ogbo hakuwa na urafiki hata kidogo na yeye, alikuwa ni rafiki maslahi. Alikuwa anakuwa rafiki anapokuhitaji, adui asipokuhitaji.




Muda huu, Imma Ogbo, Dr Louis na balozi Agdir walikuwa katika ofisi ndogo ndani ya nyumba hiyo. Walikuwa wanapanga mipango yao kwa umakini mkubwa na kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.




Kuhakikisha kina Imma Ogbo wanatoka Tanzania salama..




"Balozi Agdir tunashukuru sana kwa kuweza kututoa kule porini na kutufikisha hapa. Yaani tulilikuwa tumekwama kabisa. Na tungechelewa kidogo tu tulikuwa tunatiwa mkononi na wale jamaa. Yaani yule malaya ni mshenzi sana. Nilimstukia kwamba alienda kuongea na watu wake kule bafini. Halafu kumuuliza ananiletea ujuaji. Nilikuwa sina namna zaidi ya kumkata kidole!




Lakini bado alijifanya mtukutu...




Akaleta ujanja mpya tulipotoka kule chumbani. Ujanja wa kuchuruzisha damu yake kila tulipokuwa tunapita ili iwe rahisi kwa hao watu wake kutufatilia!




Na hapo ndipo nilipoamua kumtoboa jicho!!" Imma Ogbo alisema kwa hasira.




"Achana na habari za yule malaya. Zawadi uliyompa ya kumtoboa jicho na kumkata kidole nd'o zawadi aliyokuwa anastahili. Na sasa hakuna kingine anachostahili zaidi ya kifo! Hiyo ndio zawadi kuu ya msaliti!" Dr Louis alisema kwa nguvu.




"Imma Ogbo, hamna haja ya kunishukuru mimi hata kidogo. Ni kitu kidogo sana nimekifanya katika kuwaokoa ukilinganisha na mliyoyafanya nyinyi kwa Nigeria. Nyinyi mmefanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha mnayalinda maslahi ya nchi yenu. Niwaambie tu nami nilijisikia fahari sana kupokea simu ya rais Abayo ikinitaka kuhakikisha nawatoa kule porini, na kuwasaidia kuhakikisha mnatoka salama hapa Tanzania" Balozi Agdir alisema.




Kikapita kimya kifupi kabla ya Imma Ogbo hajaongea tena.




"Tuyaache hayo. Tu'focus ya mbele, maana kwa sasa mpango wa kuulipua ubalozi wa Uganda bila shaka umefeli. Nimewasiliana na Mark na kunambia mpango huo tayari umeshamfikia Rais. Bila shaka kupitia kwa huyu mwanamke. Sasa sijui tutatumia njia gani tena ya kutuwezesha kutoka nje ya Tanzania?"




"Ni swali zuri sana. Kwanza ule mpango wa kulipua ubalozi wa Uganda ulikuwa mzuri sana. Lakini kwasasa si mpango tena, mpango umeingia kidudu mtu, lazima tutafute njia nyingine ya kutufikisha Nigeria. Na njia hiyo lazima iwe ya haraka sana" Dr Louis alisema.




"Msiwe na shaka, nitaongea na rais Abayo tuone atatupa mbinu gani kututoa nje ya nchi? Yule ni rais hawezi kukosa namna ya kututoa hapa nchini" Balozi Agdir alisema.




Daniel Mwaseba, Adrian Kaanan, David na Martin Hisia, ambaye aliwasiliana na kina Daniel na kuelekezwa eneo walipo walikuwa wamesimama pale kulipokuwa na kidimbwi cha damu.




Walijaribu kuchanganya akili zao lakini hawakugundua pale kilitokea nini? Ukweli ulibaki uleule, Michirizi ya damu iliishia palepale walipomkuta David na hakukuwa na dalili yoyote ya kuonesha wakina Imma Ogbo walikuwa wamenda wapi?




Walijaribu kutafuta nyayo za miguu, lakini uwepo wa nyasi nyingi eneo hilo zilikwamisha kabisa zoezi hilo. Wakina Daniel wakabaki tena katika sifuri. Wakiwa hawana lolote la kufanya..




Walikuwa wametorokwa kiajabu!!


ITAENDELEA




Simulizi : Bomu 


Sehemu Ya Tano (5)






"Sasa tunafanyaje hapa? Jamaa wameyeyuka hapa kwa mtindo usioeleweka. Si mashariki, si magharibi, si kusini na kaskazini pote hakuna dalili za kuonesha kwamba hawa jamaa walielekea? Sijui walipaa hapa? Tunafanyaje kuhakikisha tunawapata?" Adrian aliwauliza wenzie.




"Hawa jamaa ni wajanja sana. Sijui wametumia mbinu gani kutoroka. Lakini niwaambie tu kwa sasa tupo karibu yao kuliko wakati wowote ule. Na tutawakamata tu hawana ujanja!" David alisema kwa hasira. Zilikuwa ni mchanganyiko wa hasira za kutekwa familia yake.




"Martin Hisia. sijui una mawazo gani mwenzetu? Sisi wote watatu hapa tupo watupu, lakini angalau tumepunguza tishio la kulipuliwa kwa ubalozi wa Uganda baada ya kumtaarifu IGP John Rondo, bila shaka vyombo vyetu vya ulinzi vitahakikisha hilo halitokei. Lakini swali ni tunafanyaje kuwakamata hawa wahalifu wenye nia ovu na nchi yetu?" Daniel aliuliza.




"Felisia, Felisia.." Martin alisema. Na hili ni neno pekee ambalo alilokuwa analitamka tangu afike eneo hilo.


Kuambiwa hali ilivyokuwa kabla ya ujio wake, na kuona damu ambazo kwake yeye aliamini ni za Felisia zilimnyong'onyesha sana. Macho yake yalikuwa mekundu huku yakitoka machozi kila dakika. Midomo ilimtetemeka sambamba na mikono.




Safari hii, alikuwa amepigwa penyewe!




Daniel akaona hakuna msaada kwa kumtegemea Martin Hisia. Hakukuwa na nafasi ya kuzitumia hisia zake. Sasa, Martin alikuwa anaelekea kuwehuka, kupotea kwa Felisia kulimuumiza isivyo kawaida.




"Hapa lazima turudi maskani kwetu tukajipange upya. Ila kiukweli hadi sasa tumepiga hatua kubwa sana. Tumejua ushiriki wa Rais Abayo katika sakata hili. Pia tumejua kwamba Dr Louis anaushirikiano wa karibu na Imma Ogbo. Hii ni hatua kubwa sana ambayo tumepiga kwa leo" Daniel alisema.




Wote walikubali kwa kutikisa kichwa, kasoro Martin Hisia.




"Lakini Daniel, kwanini tusiombe nafasi ya kwenda kuonana na Mheshimiwa Rais Mgaya? Tumueleze mheshimiwa rais juu ya uhusika wa rais Abayo katika upoteaje wa Dr Louis?" Adrian aliuliza akiwa anamwangalia Daniel usoni.




Wakati wakina Imma Ogbo wakipanga kumueleza Rais Abayo awasaidie kutoka nchini, Adrian anatoa wazo nao wamwambie rais Mgaya juu ya uhusika wa rais Abayo katika sakata hili. Je nini kitatokea? Tuwe wote katika sehemu ijayo.










"Adrian umeongea jambo zuri sana. Sijui muda wote huu hatujawaza hivyo. Hili sulala lilipofikia lazima tumfahamishe mheshimiwa rais. Uhusika wa rais Abayo katika suala hili ni jambo zito sana!. Lazima rais ajue nani adui wake mkuu kwasasa.




Lakini tatizo Ikulu si mahali unapoweza kuingia kiurahisi. Lazima uwe na jambo muhimu na zito, pia uwe na mtu anayeweza kufanikisha ukaingie ndani ya jumba hilo tukufu. Ngoja niwasiliane na Chifu ili atutafutie namna ya kuonana na Mheshimiwa rais. Tukimueleza kuwa tuna jambo zito la kumwambia rais juu ya kutekwa nyara kwa Dr Louis lazima tutaipata hiyo nafasi. Bila shaka yeye atatupa namna sahihi ya kulimaliza hili suala" Daniel alisadiki maneno ya Adrian.




Suala la michirizi ya damu liliishia pale. Kilibaki ni kitendawili juu mahali walipoelekea wakina Imma Ogbo. Wote wanne walitoka eneo lile na kuelekea mahali ambapo walikuwa wamepaki gari yao. Wakajitosa ndani ya gari na kurudi katika maskani yao.




Nyumbani kwa Daniel Mwaseba.




"Kipindi hiki ambacho tunasubiri kukubaliwa ombi letu la kuonana na Mheshimiwa rais mnaonaje tukaenda kuwasaka watu wetu waliotekwa?" Adrian aliuliza.




"Umeongea jambo zuri sana Adrian. Unajua mwanzoni tulikuwa tumeweka nguvu kubwa sana ya kumsaka Dr Louis. Lengo ni kumkomboa kabla hajapatwa na madhara makubwa zaidi. Lakini kwakuwa tumegundua Dr Louis yupo na watu wake, itakuwa vizuri tukaitumia nafasi hii kuwasaka watu wetu, Hannan na familia ya David" Daniel aliunga mkono hoja.




"Tutaanzia wapi sasa kuwasaka? Maana hadi sasa sidhani kama tumepata sehemu sahihi pa kuanzia msako wetu.." David aliuliza, huku akionekana kabisa furaha ilikuwa imechanua usoni kwake.




"David, tunapo pa kuanzia msako wetu!" Daniel alisema kwa uhakiks huku akichukua simu ya Adrian.




Moja kwa moja akampigia mshkaji wake, Mwanasheria mlevi..




"Hallo Mwanasheria mlevi?" Daniel alisema pindi tu simu yake ilipopokelewa upande wa pili.




"Eeh nambie Daniel Mwaseba. Nimeona kimya sana, vipi mlifanikiwa kuwapata wale majamaa?" Mwanasheria alisema.




Daniel alivuta pumzi kidogo.




"Hatujafanikiwa kuwapata Mwanasheria, ingawa tupo katika mwelekeo mzuri sana. Unajua mambo yale tuliyoyagundua baada ya kutumiwa ujumbe na Felisia ni mazito sana. Tumeona kwa uzito wake kuna umuhimu wa kumshirikisha Rais" Daniel alisema.




"Sidhani kama ni sahihi kumweleza Mheshimiwa rais kwasasa. Unajua yale ni mamho mazito sana. Yanahusisha nchi nyingine. Kwanini msimalizie uchunguzi wenu hadi mwisho na kisha mumueleze rais mkiwa ushahidi uliokamilika?" Mwanasheria mlevi alipinga wazo la Daniel.




"Umesema vyema Mwanasheria, lakini tumewaza sana na wenzangu hapa. Tumeona umuhimu wa kumueleza Mgeshimiwa rais sasa kabla maji hayajakorogeka. Hatujui rais ana mpango gani na nchi ya Nigeria, lazima tuhakikishe anasimamisha uhusiano wake na nchi hiyo". Daniel alisema.




"Sawa Daniel. Ni kutofautiana tu maoni na mawazo, lakini kama mnahisi hiyo ni njia sahihi, basi tupo pamoja. Mimi nitawaunga mkono kwa kadri ya uwezo wangu"




"Upo sahihi Mwanasheria, wote tunajenga nyumba moja, na sisi ni watoto wa mama mmoja. Mama Tanzania.




Vipi, bado upo ofisini?" Daniel aliuliza.




"Ndio bado nipo ofisini. Mambo yamekuwa mengi sana hapa ofisini. Vipi ulikuwa unataka nije nini, nami nivae jezi tuingie wote uwanjani?" Mwanashetia aliuliza kimas'hara.




"Hapana kijana, kuna kitu kidogo nilikuwa ninataka unisaidie" Daniel alisema.




"Nitakusaidie kitu chochote kile, kama kipo ndani ya uwezo wangu basi hesabu kitu hiko kmekwisha!" Mwanasheria alisema kwa uhakika.




"Ninakuamini jamaa yangu. basi nipe dakika moja ninakutumia ujumbe mfupi" Daniel alisema.




Simu ikakatwa.




Daniel aliangalia ile namba ya simu aliyoitumia Hannan kupiga na kisha kumwambia akiwa Rombo hoteli. Aliandika pembeni katika karatasi ndogo, akaandika pamoja na muda simu hiyo ilipopigwa.


Akaandika katika simu yake, kisha akamtumia meseji Mwanasheria mlevi.




Alivyohakikisha ujumbe umefika kwa Mwanasheria mlevi. Akasindikiza na meseji ya pili iliyokuwa inasomeka.




"Nipe location yake"




Zilipita kama dakika mbili, majibu yalirudi kutoka kwa Mwanasheria mlevi. Ilikuwa ni meseji yenye eneo na namba ya nyumba aliyokuwepo Hannan.




"Tunaelekea Tegeta sasahivi" Daniel alisema kwa sauti iliyosikiwa na wote.




***




Taa mbalimbali zilikuwa zinawaka ndani ya Ikulu ya Tanzania, iliyopo maeneo ya Posta, jijini Dar es salaam. Walinzi maalum wa rais, wenye silaha za kisasa walikuwa wanazunguka eneo hilo kuhakikisha usalama unaendelea kudumishwa ndani ya jengo.




Nje nako kulikuwa kumejaa walinzi lukuki wenye bunduki. Wakihakikisha kila kitu kinakaa mahali pake.




Katika chumba cha faragha cha Mheshimiwa rais, kulikuwa na watu wawili. Walinzi na wahudumu walitolewa nje, wakiwaacha watu wawili tu ndani ya chumba hiko.




Kilikuwa ni chumba kidogo chenye kila kitu ndani yake. Samani za ghali na za kisasa, friji ndogo pembeni iliyojaa matunda na kila aina ya sharubati, kompyuta ya bei, kutoka kampuni ya Apple mezani, air condition ikiyotoa hewa mujarab ukutani huku kabati dogo lililojaa mafaili mbalimbali likiwa pembeni konani mwa chumba hiko. Kilikuwa chumba kidogo lakini kilichopangiliwa vizuri sana. Chumba hiko kizuri kwasasa, sofa zake ghali na za kisasa zilikaliwa zimekaliwa na watu wawili tu..




Mheshimiwa Rais Mgaya na Mohammed Msangi.




"Safari hii mzee Msangi umeniangusha sana. Sikutegemea suala la kumpata Dr Louis litakuwa gumu na kuchukua muda mrefu namna hii?" Rais Mgaya alisema baada ya kusafisha koo lake kwa sharubati ya embe.




" Niombe tena msamaha kwa hilo Mheshimiwa Rais. Hili suala limekuwa tata na gumu. Yaani sijui hata nisemeje. Kama nilivyokwambia awali, Tulifanikiwa kumtia mikononi mwetu Dr Louis lakini yule kijana uliyetuletea kutoka kwa rais Abayo ndiye aliyeharibu kila kitu, alimteka Dr Louis na hadi sasa hatujui wapi amempeleka. Lakini sisi bado hatujakata tamaa, tunaendelea kumsaka Dr Louis hadi apatikane" Mzee Msangi alisema.




"Kusema kweli nimesikitishwa sana na kitendo alichokifanya huyo kijana. Nimemweleza Rais Abayo juu ya kitendo alichokifanya kijana wake. Naye amesikitishwa sana, na amesema atatusaidia kwa namna yoyote ile kuhakikisha tunampata Dr Louis pamoja na huyo kijana" Rais Mgaya alisema.




"Kwakuwa umemwambia rais Abayo haina shida, lakini nikuhakikishie tu sisi wenyewe tumejipanga vizuri, na nakuahidi tutampata Dr Louis" Mzee Msangi alisema kwa uhakika.




"Nakuamini sana Mzee Msangi. Ila kuchelewa kwenu kumpata Dr Louis ndo kunanipa mashaka. Sikudhami kama suala hili litachukua muda mrefu namna hii. Nimewaagiza wakuu wa usalama wafunge mipaka yote ya nchi kuhakikisha mnawakamata watu hao lakini bado majibu na yaleyale, bado bado!!.." Rais Mgaya alisema huku akigonga meza.




"Mheshimiwa rais usiwe na shaka. Hii ni ahadi yangu ya mwisho kwako. Nakuahidi nakuletea Dr Louis hapa" Mzee Msangi akameza mate. Kisha akauliza.




"Kwani kuna kitu gani cha siri kati yenu kinachokufanya umsake sana Dr Louis? Mimi ni mshirika wako na sidhani kama kutakuwa na ubaya wowote nikifahamu. Pengine itachochea msako wake" Mzee Msangi aliuliza swali.




Rais Mgaya alikaa kimya. Alimwangalia Mzee Msangi huku uso wake ukionesha hajapendezwa na swali hilo.




"Bila shaka kuna siri kubwa sana kati ya rais na Dr Louis. Na siri hiyo nikiijua kwangu itakuwa ni hela. Lazima nimsake Dr Louis kwa nguvu kubwa sana ili niitie mikononi mwangu siri hiyo! Siri ya kutengeneza mabilioni!" Dr Louis alijisemea kifuani.




"Mzee Msangi, sidhani kama sasahivi ni wakati sahihi wa kukwambia kwanini ninamsaka sana Dr Louis. Ipo siku nitakwambia sababu, na siku hiyo ni utakayoniletea Dr Louis mbele yangu" Rais Mgaya alisema.




Rais Mgaya na mzee Msangi waliongea kama muda wa robo saa, kisha wakaagana.




Mzee Msangi alipotoka tu nje, alimpigia simu Antony Kyando..




Je kuna siri gani kati ya Rais na Dr Louis?






Wakina Daniel Mwaseba walikuwa wameshawasili Tegeta, au ili tupajue zaidi palikuwa panaitwa Tegeta Nyuki. Gari yao moja kwa moja ilipaki katika nyumba ambayo walielekezwa na Mwanasheria mlevi.




Kwa kutumia miguu, kutoka katika kiduka kidogo, mahali walipopaki gari yao, walifika katika nyumba aliyokuwemo Hannan Halfan. Walitumia dakika tatu kuichunguza nyumba hiyo. Kisha walijipanga vizuri kuvamia, nyumba ambayo walikuwa wameshaichunguza na kuona maeneo yote dhaifu ya kuwawezesha kuwaingiza ndani.




Walinzi wawili wenye silaha za moto walikuwa karibu na geti. Mmoja alikuwa amesimama karibu kabisa na geti huku mwengine alikuwa katiks kibanda kidogo kilichokuwa pembeni ya geti.




Mlinzi wa tatu alikuwa katika mlango wa kuingilia ndani wa nyumba hiyo. Alikuwa anaranda pale mlangoni, huku akiikumbatia bunduki yake.




Mlinzi wa nne alikuwa nyuma ya nyumba hiyo. Naye pia alikuwa na short gun machine mkononi.




Lakini walinzi hao wanne wenye silaha, hawakuwaogopesha hata kidogo wakina Daniel Mwaseba. Ingawa hawakujua ndani ya nyumba hiyo kuna walinzi wangapi.




Hofu ilikuwa maili nyingi sana katika mioyo yao..




Daniel Mwaseba na David walielekea m mbele ya geti la nyumba hiyo. Mahali ambapo waligundua kuwa kulikuwa na walinzi wawili.




Adrian Kaanan alizunguka nyuma ya nyumba hiyo, lengo ni kuhakikisha anaenda kumsambaratisha yule mlinzi mwenye short gun machine mkononi.




Wakati Martin Hisia alibaki ndani ya gari. Kuhakikisha eneo lote la nje linakuwa salama- salmin.




Kutokea upande wa mbele, Daniel Mwaseba aligonga geti kwa kutumia mkono wa kushoto.




Yule mlinzi aliyekuwa karibu na geti, alifungua mlango mdogo wa geti na kutoa kichwa chake kwa nje kumsikiliza mbisha hodi. Huku akiisahau bunduki yake ndani ya geti.




Mwenyewe alikuwa anajiamini, akiamini hakuna kitu kibaya kitakachotokea, lakini nikwambie tu nd'o lilikuwa kosa kubwa sana kuwahi kufanywa katika maisha yake.




Daniel alikuwa tayari amejipanga kwa kitendo hiko. Na pengine zaidi ya kitendo hiko...




Kwa kasi, aliikandamiza ile sura kwa kitambaa cheupe chenye unga mweupe alichokishika mkononi huku akimvutia kwa nje. Mlinzi aliburuzwa bila kupenda.




Yule mlinzi mwengine aliyekuwa katika kibanda karibu kabisa na geti akapatwa na shaka na mwenzake.




Alimshuhudia jinsi alivyoka nje katika namna ya ajabu!


Naye akiwa na silaha yake mkononi alielekea ule upande wa geti.




Wakati huohuo, Adrian Kaanan alikuwa amefanikiwa kwa siri kukwea ukuta mrefu wa ile nyumba na kujitosa ndani ya ile nyumba bila kutoa sauti yoyote ile.




Mlinzi aliyekuwa upande ule alikuwa ameugekia ukuta, akiupisha upepo huku akijarubu kuiwasha sigara yake.




Kwa mwendo wa kunyata, wa taratibu sana. Huku akihakikisha nyayo zake hazitoi ukelele wowote ule, Adrian Kaanan alikuwa anamsogelea yule mlinzi. Alipomkaribia kwa mita chache sana, mlinzi alihisi kitu. Aligeuka kwa kasi na bunduki yake mkononi.




Tayari kwa kumpasua mtu!




Lakini kwa bahati mbaya sana kwake, alikuwa amechelewa. Kisu kikali kilikita upande wake wa kushoto na kumdondosha chini akiisahau bunduki yake kwa muda. Mlinzi alitaka kutoa ukelele wa maumivu, lakini haukotoka.




Utatoka vipi?




Wakati Adrian alikuwa amemuwahi kwa kasi na kuubana kwa nguvu mdomo wa mlinzi kwa mkono wake wa kushoto.




Sauti ya mlinzi ilirudi tumboni kwake mwenyewe...




Kule kwa mbele, David alikumbana katikati ya mlango mdogo wa geti na yule mlinzi mwengine, kipindi ambacho Daniel akimsweka kichochoroni yule mlinzi mwengine aliyemvutisha unga uliomlalisha bila kupenda.




Teke la nguvu na kasi la David liliikwapua bunduki ya yule mlinzi na kuirudisha kule ndani ya geti. Mlinzi alijaribu kujitetea kwa mikono yake lakini ilikuwa ni kazi bure kwa David Ngocho.




Jamaa alikuwa ni mwamba msituni!




Kwanza alimvuta kwa nje kumtoa machoni kwa yule mlinzi aliyekuwa anarandaranda kule mlangoni kwa mbali.




Mpambano ulianza.




David alipangua kwa ustadi mkubwa sana kila pigo la yule mlinzi, aliyekuwa anarusha ngumi na mateke kwa pupa. Na yeye akipiga sehemu muhimu tu kila alipopata nafasi.




Walidumu katika mapigano ndani ya dakika mbili tu kabla ya yule mlinzi kulazwa chini. Damu zikimvuja puani na masikioni.




Alikuwa amekata moto!




Daniel Mwaseba aliungana na David na kujitosa ndani. Walikuwa wanaenda kwa umakini huku wakijificha katika maua mengi yaliyopandwa mle ndani. Hatimaye walifika. Walikuta Adrian ameshazunguka kwa mbele na kumpa pumziko la kudumu yule mlinzi aliyekuwa katika mlango wa mbele.


Sasa walikuwa wamevimaliza vikwazo vyote vya nje. Wakaingia ndani.




Walianza kukagua nyumba yote, huku wakitembea kwa umakini na silaha zao mikononi.




Hakukuwa na mlinzi yoyote yule mle ndani..Katika chumba cha mwisho kabisa upande wa kulia ndipo walipomkuta Hannan baada ya kuvunja mlango. Hannan alikuwa salama kabisa.




Lakini familia ya David haikuwemo mle ndani.




Walimchukua na kuondoka naye.




Hannan anaokolewa na kina Daniel, lakini familia ya David hawajaikuta, je itakuwa ipo wapi




Dakika ishirini na tano baadaye ndipo Anna, mfanyakazi wa nyumba aliyosekwa Hannan alirudi katika makazi yao. Alikuwa amebeba kapu kubwa la rangi ya kahawia mkononi, kapu lenye vitu mbalimbali. Alikuwa ametoka sokoni..




Alipigwa na bumbuwazi tangu akiwa mbali, mita kadhaa kutoka katoka getini, alienda na bumbuwazi lake hadi alipowasili.




Kuona geti la nyumba yao kuwa wazi haikuwa kawaida hata kidogo. Ile, ilikuwa ni nyumba maalum kwa kazi maalum. Umaalum huo haukuruhusu lile geti jeusi liwe wazi zaidi ya dakika tano.




Aliongeza kasi ya kutembea kuelekea getini, alipofika ndio alishuhudia unyama uliotendeka ndani ya nyumba yao.




Hakusubiri hata dakika moja. Ampigia simu Mzee Msangi kumtaarifu kilichotokea.




Wakati huo mzee Msangi alikuwa sebuleni kwa Antony Kyando, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani hapa nchini, chama cha Tanzania People Party.




"Mambo bado magumu sana Mheshimiwa Mwenyekiti. Hadi sasa hatujafanikiwa kumpata Dr Luis atueleze hiyo siri tuisakayo. Ni Dr Luis pekee ndiye anayeweza kutuambia madhara ya kirusi DH+ baada ya kufanikisha kumpaka rais. Nilifanya jukumu la kumpaka, lakini sielewi kinatokea nini baada ya kumpaka kirusi cha DH+. Na hayo matokeo ndio siri tuitatayo." Mzee Msangi alisema.




"Lakini mzee Msangi, mwanzoni si ulisema mmefanikiwa kumpata Dr Louis na kumficha kitalu B huko Kigamboni? Sasa nini kilitokea huko? Au mlifanya kazi ya rais Mgaya badala ya kufanya kazi yangu?" Mwenyekiti Antony aliuliza huku akimwangalia mzee Msangi.




"Kama nilivyokwambia Mwenyekiti. Ni kweli tulimpata Dr Luis katika hoteli ya Dos Santos, lakini kwa bahati mbaya kuna mwenzetu mmoja alitusaliti kule kitalu B na kutoroka naye. Na nikwambie tu, hadi hivi sasa tupo katika harakati za kumtafuta huyo mwenzetu" Mzee Msangi alijitetea.




"Je, mlivyomkamata ulimdokeza kuhusu kututengeneza hiko kirusi cha DH+?" Antony aliuliza kwa shauku kubwa.




"Kazi ya kumhoji alipewa jasusu mmoja kutoka Nigeria, anaitwa Imma Ogbo. Ni miongoni mwa vijana aliopewa rais Mgaya kutoka kwa rais Abayo. Nilimdokeza Imma Ogbo amuulize Dr Luis kuhusu kirusi cha DH+. Unajua rais Mgaya hakutaka hata kidogo Dr Luis ahojiwe. Agizo lake lilikuwa ni kumteka na kumsubiri yeye arejee kutoka Nigetia. Hivyo ni mimi ndiye niliyefanya Dr Luis ahojiwe, na lengo lilikuwa tujue ana siri gani ya rais Mgaya? Pia tujue kuhusu kirusi DH+. Lakini sasa kabla hatujambana zaidi juu ya hiko kirusi, na kumwomba atutengenezee ndio akatoroshwa na Imma Ogbo baada ya kupishana kauli na mimi.." Mzee Msangi alisema.




Maneno hayo yalipenya katika masiko mawili ya Mwenyekiti Antony Kyando. Mwenyekiti alikaa kimya akitafakari. Huku akichambua kila neno la Mzee Msangi.




"Mwenyekiti, lakini kuna kitu kimoja kinaniumiza sana kichwa" Mzee Msangi alisema wakati Antony Kyando akiwa katika tafakuri.




"Kitu gani hiko?" Mzee Msangi aliuliza harakaharaka. Hakuwa na haja ya kuzama katika tafakuri wakati kulikuwa kuna cha kuuliza.




"Mimi, najua wewe sababu ya kumsaka Dr Luis kwa udi na ubani. Lengo ni kwaajili akutengenezee kirusi cha DH+. Lakini unadhani ni nini sababu ya Rais Mgaya kumsaka Dr Luis namna hii?" Mzee Msangi aliuliza swali ambalo alikuwa na jibu lake.




"Mzee Msangi, wewe ndiye mtu wa karibu sana na Mheshimiwa rais, nadhani mimi nd'o ningekuwa katika nafasi nzuri ya kuuliza hilo swali. Wakati wewe ndiye ungekuwa unajibu" Antony alikwepa kujibu.




"Nimeuliza hivyo kwasababu leo hii, nimejaribu sana kumdadisi Rais Mgaya, lakini hakuwa tayari hata kidogo kunambia siri hiyo" Mzee Msangi alisema.




"Basi hata mimi sifahamu..ninachojua mimi chanzo cha siri hii, ni matokeo ya kirusi cha DH+ uliyompaka akiwa amelala.." Antony alisema.




"Lakini Mwenyekiti, huoni fursa ya kutengeneza pesa nyingi sana kupitia hiyo sababu ya rais kumsaka Dr Luis? Ukimsikiliza kwa umakini mheshimiwa rais anavyoongea inaonesha kuwa kuna siri nzito sana kati yake na Dr Luis. Na siri hiyo tukiigundua inaweza ikawa dili la kupata pesa nyingi sana. Kwanini tusikazanie kuijua siri ya Mheshimiwa rais Mgaya kwake mwenyewe kuliko kupitia kwa Dr Luis ambaye imekuwa ni kitendawili kumkamata?" Mzee Msangi alisema.




Mwenyekiti Antony alikaa kimya. Akitafakari kwa umakini maneno ya mzee msangi.




"Umewaza sana Mzee Msangi. Na niseme tu umewaza kitu kikubwa sana Leo. Umeiona fursa adhimu sana. Lakini pamoja na kuijua hiyo siri ambayo wewe umeigeuza kuwa pesa, mimi ninakitaka kirusi chenyewe, nahitaji DH+ kiwe mikononi mwangu.." Antony alisema kwa hamasa.




"We cha nini kirusi DH+?" Mzee Msangi aliuliza.




Mwenyekiti Antony alikaa kimya. Aliinama chini akifikiri. Huku akicheza vidole vyake vya mkono wa kushoto.




Hakuhangaika hata kidogo kujibu swali la mzee Msangi.




Na hapo ndipo simu ya mzee Msangi iliita.




Simu ilikuwa inatoka kwa mfanyakazi wake, Anna.




***




Wakina Daniel Mwaseba walifika salama salmin wakiwa na Hannan nyumbani kwake Mikocheni.




Hapo ndipo walipopachagua pawe sehemu sahihi ya kupanga mikakati yao.


Ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa, yenye kila kitu ndaniye.




Walikuwa wamekaa sebuleni. Kama kawaida wakipanga mipango yao. Huku wakimsubiri daktari kwa ajiri ya kuja kuiangalia afya ya Hannan. Ingawa kwa macho ya kawaida alionekana yupo fit.




"Tumefanikiwa kumwokoa Hannan. Zoezi limekuwa rahisi sana. Tumerudi wote salama, tena tukiwa na Hannan. Ni suala la kumshukuru Mungu sana.




Nini kifuatacho sasa?




Sasa ni zamu ya kwenda kuikoa familia ya David popote pale ilipo. Kwa damu au kwa jasho, lazima familia ya David tukaikoe, ili tumrejeshee furaha mwenzetu" Adrian alisema.




"Ni kweli Adrian. Hiyo ni kazi yetu ya pili baada ya kumwokoa Hannan.




Katika kazi hii tuna pa kuanzia pia. David alikuwa anatumiwa meseji na mtekaji wa familia yake. Tunaweza kum'track huyo mtu akiyetuma hizo meseji kwa David. Tukimjua tutajua nini cha kufanya.


David, hebu nipe namba ambazo akiyotumia huyo mtu kukupa maagizo yake" Daniel alisema.




Harakaharaka, David alipekua katika simu yake, na kumpa Daniel simu yake, ikionesha meseji mojawapo ya huyo mtu.




"Safi sana. Hii namba itatusaidia sana kuelekea mahali tunapopataka. Kama mnakumbuka Mwanasheria mlevi alisema namba hii imesajiliwa kwa majina ya Elia Kilasi. Sasa ni lazima tupige hatua nyingine mbele. Tumfamu vizuri huyo Elia Kilasi ni nani haswa?" Daniel alisema.




"Na uzuri leo hapa sebuleni tunaye Hannan. Kwa kiasi kikubwa sana atatusaidia kufumbua fumbo hili tata.




Fumbo la Elia Kilasi!!" Adrian alisema.




Watu wote pale sebuleni wakamwangalia Hannan. Ambaye alikuwa amekaa sofa la mwisho kabisa karibu na runinga. Alikuwa ndani ya suruali ya jeans iliyombana vyema, huku juu akivaa T-shirt ya bluu iliyoandikwa maandishi meusi katikati, neno likisomeka (FORCE).




"Laptop yangu waliichukua wale jamaa. Daniel kama una kompyuta ya ziada humu ndani nipe nianze kazi" Hannan alisema kwa kujiamini sana.




Daniel alitoka pale sebuleni na kwenda chumbani kwake. Alirudi kama baada ya dakika tatu, alikuwa amebeba tarakilishi nyeusi. Kwa nyuma ilisomeka Toshiba. Akamkabidhi Hannan.




sekunde ileile, Hannan aliiwasha ile tarakilishi. Akachomeka 'modem' iliyokuwa juu ya meza pale.




Ndani ya dakika thelathini na tano alizitumia kuingiza programs mbalimbali anazozijua yeye.




Kisha akaiomba ile namba ya Elia Kilasi.




Ukumbi mzima ulikuwa kimya, unamwangalia yeye. Kwa muda huu yeye ndiye alikuwa tumaini lao. Tumaini jipya. Tumaini la pekee.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog