Simulizi : Hekaheka Msituni
Sehemu Ya Kwanza (1)
IMEANDIKWA NA : KALMAS KONZO
********************************************************************************
Simulizi : Hekaheka Msituni
Sehemu Ya Kwanza (1)
Bantu Military Movemnt (BMM) killikuwa ni kikundi cha waasi ambacho kilikuwa kikiendesha harakati zake kusini mwa nchi ya Bantu. Kikundi hiki kilikuwa kina nguvu sana na kadri siku zilivyokuwa zikizidi kusonga mbele ndivyo ambavyo kilikuwa kikizidi kujiimarisha. Kikundi hiki kilikuwa kimeiimarisha kwa jeshi kubwa pamoja na silaha nyingi na za kisasa. Kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele kikundi hiki kilizidi kuwa tishio kwa serikali ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ikiongozwa na Rais Ditrick Mazimba.
Kwa upande wake mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba alikuwa ni Rais kipenzi cha wengi. Wannanchi wengi wa Bantu walimpenda sana Rais huyu kwani alikuwa ni Rais ambaye alikuwa akiwajali sana. Alikuwa ni Rais ambaye alikuwa anajali utu na kutambua thamani ya binadamu. Alikuwa ni Rais ambaye alikuwa akiwajali wananchi wake na kuwasaidia kwa kadri ya uwezo wake na wa serikali yake.
Hata wananchi wenyewe waliwashangaa wale wanajeshi ambao walikuwa wakiendesha harakati za mapinduzi. Waliwaona kama walikuwa ni wendawazimu. Na kwa mtazamo dhahiri ni kweli wanajeshi wale hawakuwa na sababu nyingine ya uasi wao kwa serikali zaidi ya uroho wa madaraka. Ilikuwa ni uendawazimu kuendesha harakati za uasi kwa serikali sikivu na yenye kuwajali wananchi wake kama serikali ya Bantu.
Hata Umoja wa Mataifa ulikuwa ukilipigia kelele suala la waasi wale kila uchao. Umoja wa Mataifa ulikuwa ukiwarai waasi wale kuweka silaha zao chini na kukaa meza moja ya mazungumzo ya amani na serikali ya Bantu ili waweze kueleza shida yao hasa ilikuwa ni nini?
Wanajeshi wale hawakutaka kusikiliza rai za Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zilikuwa zikijihusisha na haki za binadamu duniani. Wenyewe waliendelea kudai tu kwamba Rais Ditrick Mazimba pamoja na serikali yake hawakustahili kuwepo madarakani.
Harakati hizi za uasi zilikuwa zikiendeshwa na Kanali Edson Makoko mwanajeshi muasi kutoka katika Jeshi la Wananchi wa Bantu. Mwanajeshi huyu alikuwa ameacha jeshi na kuingia msituni ambako aliwakusanya wanajeshi kadhaa ambao walimuunga mkono na kuanzisha kikundi cha uasi. Walitafuta silaha na kuzidi kujiimarisha.
Katika kujijengea uwezo kiuchumi kikundi hiki kilianza kufanya shughuli za ujambazi ambapo kilivamia na kupora mali na pesa kutoka kwa watu makampuni na taasisi mbalimbali. Hii ilikifanya kikundi hiki kizidi kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi.
Baadaye wanajeshi hawa walianza kuwateka watoto na vijana na kuanza kuwafunza matumizi ya silaha na baaddaye kuwaweka katika jeshi. Kikundi hiki sasa kilianza kuwa tishio kwa nchi zilizopakana na Bantu pamoja na Afrika nzima kwa ujumla.
Harakati hizi za uasi zilianza miaka saba iliyopita ambapo palikuwa na uchaguzi mkuu nchini Bantu. Uchaguzi huu ulikuwa ni wa Rais, wabunge pamoja na madiwani. Ulikuwa ni uchaguzi ambao ulikuwa na changamoto nyingi sana. Na huu ndiyo ulikuwa uchaguzi ambao ulimwingiza madarakani mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba katika kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi.
Uchaguzi ule ulikuwa na mchuano mkali sana kati ya mahasimu wawili wakubwa wa kisiasa nchini Bantu. Mahasimu hawa walikuwa ni mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini Bantu kwa kipindi kile bwana Shukuru Kizibo.
Wanasiasa hawa walichuana vikali sana kila mmoja akimwaga sera zake ambazo aliamini kwamba zitawavutia wananchi wa Bantu kumpa kura. Kila mmoja alijiona ni bora kuliko mwenzake.
Katika uchaguzi ule bwana Shukuru Kizibo alijipa asilimia kubwa sana ya ushindi kwa sababu yeye alikuwa akitokea katika chama kikuu cha upinzani nchini Bantu.
Chama hiki kilikuwa na nguvu sana na kilionyesha kuwa na wafuasi wengi sana. Wafuasi wa chama hiki walikuwa ni wafuasi ambao walikuwa na ashki kubwa sana ya kuchukua madaraka ya uongozi wa serikali ya Bantu.
Uchaguzi ule uliendeshwa kwa vurugu nyingi sana. Wananchi hawakutulia hata kidogo kwani kila mmoja kwa upande wa chama chake alijihesabu kwamba ni mshindi wa uchaguzi ule.
Uchaguzi ulifanyika kwa muda wa siku moja na baada ya hapo uhesabuji wa kura ulianza. Katika kipindi chote cha kuhesabu kura, wananchi walikuwa wakifanya vurugu nyingi sana. Wafuasi wa chama pinzani walikuwa wakitaka muda wote wawe jirani na vyumba ambamo shughuli ya kuhesabu kura ilikuwa ikiendelea.
Dhumuni lao kubwa hasa lilikuwa ni kuzilinda kura zisiibiwe. Walitamani hata kulala hapohapo. Jambo hili liliwafanya waingie mgogoro na vyombo vya usalama ambavyo vilikuwa vijiraibu kuwatawanya. Baada ya siku tano za kuhesabu kura, hatimaye majibu yaliwekwa hadharani hasa kwa kura ya urais kwani majibu ya ubunge na udiwani yalikuwa yametoka mapema. Mheshimiwa Ditrick aliibuka kidedea kwa uchaguzi ule na kutangazwa kuwa mshindi.
Jambo hili lilimkasirisha sana bwana Shukuru Kizibo pamoja na wafuasi wa chama chake ambao walianzisha vurugu kubwa sana. Vurugu zile ilikuwa kubwa sana ambapo wafuasi wa chama kile pinzani walikuwa wakipambana na vyombo vya usalama vya nchini Bantu.
Katika ghasia zile watu takribani elfu moja na mia moja waliuawa. Bwana Shukuru Kizibo alijikuta akishikiliwa na polisi na baada ya vuguvugu la uchaguzi kwisha na Rais mpya kutangazwa, alipelekwa mahakamani. Alionekana na hatia na mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka kumi na tano gerezani. Hukumu hiyo iliwahusu wafuasi wa bwana Shukuru Kizibo ambao walimsaidia katika kufanya vurugu zile.
Lakini baada ya mwaka mmoja wa kutumikia adhabu ile, mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba alitoa msamaha kwa bwana Shukuru Kizibo na wafuasi wake. Hii yote ilikuwa ni katika kutafuta amani na utulivu wa kisiasa nchini Bantu.
Kwa upeo wake uliojaa busara mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba alidhani kwamba kwa kufanya vile atakuwa ameutatua mgogoro wa kisiasa ambao ulikuwa ukifukuta nchini Bantu baina ya chama tawala na chama kikuu cha upinzani. Yaani ilikuwa ni afadhali ambapo bwana Shukuru Kizibo alikuwa akishikiliwa gerezani.
Kumpa msamaha mfanyabiashara na mwanasiasa huyu lilikuwa ni kosa kubwa sana ambalo mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba alikuwa amelifanya. Kosa hili lilimgharimu sana na muda wote huwa anajilaumu kwa kuchukua maamuzi yale ambayo yapo kwa mujibu wa katiba ya nchi ya Bantu.
Bwana Shukuru Kizibo aliporudi uraiani tu alianza kufanya vuguvugu la uasi wa chini kwa chini. Lengo lake kubwa lilikuwa ni hapo baadaye kuja kufanya mapinduzi makubwa sana ambayo yataistaajabisha dunia.
Bwana Shukuru Kizibo alikuwa ameyadhamiria hasa mapinduzi haya. Hakuwa na huruma hata kidogo kwa raia wenzake wa Bantu juu ya madhara ambayo yatatokea katika utekelezaji wa mapinduzi hayo. Kwa sasa alikuwa amechafukwa kabisa. Moyo wake kwa sasa haukuwa tofauti na moyo wa mnyama mkali na katili wa mwituni.
*******
Bwana Shukuru Kizibo alikuwa ameyadhamiria hasa mapinduzi haya. Hakuwa na huruma hata kidogo kwa raia wenzake wa Bantu juu ya madhara ambayo yatatokea katika utekelezaji wa mapinduzi hayo. Kwa sasa alikuwa amechafukwa kabisa. Moyo wake kwa sasa haukuwa tofauti na moyo wa mnyama mkali na katili wa mwituni.
SASA ENDELEA
Kwanza kabisa bwana Shukuru Kizibo alianza kwa kuumiza kichwa ni namna gani atapata jeshi ambalo litamuunga mkono katika mapinduzi yake aliyoyakusudia. Aliwaza sana lakini mwishoni alikuja kujipa moyo kwamba katika dunia hii kila kitu kinawezekana. Aliamini kwamba kwa kutumia pesa ambayo alikuwa nayo, basi angeweza kuunda jeshi imara ambalo litaweza kupambana na serikali kwa mafanikio makubwa.
Jambo la kwanza ambalo alipanga kuanza nalo katika kuutekeleza mchakato ule lilikuwa ni kumpata mwanajeshi mmoja ambaye ndiye angekuwa inchaji katika kuelekea kuliunda jeshi ambalo alikuwa akilitaka.
Mwanajeshi huyu ambaye alimhitaji kuwa inchaji alitaka awe ni mwanajeshi wa ngazi ya juu jeshini ambaye amehudumu jeshini kwa muda mrefu hivyo anafahamu mbinu mbalimbali za kijeshi.
*******
Kanali Edson Makoko alikuwa ni mwanajeshi mtumishi katika Jeshi la wananchi wa Bantu. Alikuwa ni mkuu wa kambi ya jeshi ijulikanayo kama KJ 05. Kanali Edson Makoko alikuwa amelitumikia jeshi kwa muda mrefu sana. Alikuwa ni mwanajeshi ambaye alikuwa ana sifa kubwa sana katika Jeshi la wananchi wa Bantu. Alikuwa ni mwanajeshi makini kabisa ambaye hakuwa akipenda utani pindi linapokuja suala la kazi.
Sambamba na hilo pia Kanali Edson Makoko alikuwa ni mwanajeshi mwenye sifa ya ukatili kupita kiasi. Yeyote ambaye alikuwa amekosea na kuingia katika anga zake, basi hakika alipata tabu sana.
Sifa hizi na zingine kedekede ndizo ambazo zilimfanya apande vyeo harakaharaka. Na sasa alikuwa ni mkuu wa kambi KJ 05 kambi ambayo ilikuwa ni muhimu sana kwa jeshi la wananchi. Kambi hii ilikuwa inatunza silaha mbalimbali za jeshi na pia ilikuwa na gereza la kijeshi ambapo wafungwa wa kijeshi walikuwa wakifungwa humo.
Kanali Edson Makoko alikuwa na kasoro moja tu katika maisha yake. Kanali Edson Makoko alikuwa ni mtu ambaye alikuwa na tamaa sana. Hakuwa ni mtu wa kutosheka kwa chochote alichonacho au akifanyacho.
Tabia hii ilimfanya awe ni mtu wa matumizi makubwa sana kuliko kipato ambacho alikuwa akikipata. Hii ilimfanya muda mwingi asiwe imara kiuchumi.
Kanali Edson Makoko alianza kufikiria namna mbadala ya kuweza kuongeza kipato tofauti kabisa na mshahara ambao alikuwa akipokea. Aliamini kwamba kwa kufanya hivyo basi maisha yake yangeliweza kumnyookea.
Na ni katika wakati huu ndipo ambapo alizipata habari za siri za mfanyabiashara maarufu nchini Bantu bwana Shukuru Kizibo za kutaka kufanya mapinduzi kwa serikali. Kanali Edson Makoko aliona kwamba hii ilikuwa ni fursa pekee kwake ambapo angeweza kutengeneza pesa nyingi sana ambazo angezitumia vyovyote apendavyo mpaka anaingia kaburini. Hii ilikuwa ni kwa kushirikiana na bwana Shukuru Kizibo kaika kuyatekeleza mapinduzi yale.
*******
Bwana Shukuru Kizibo alikuwa ametulia ndani ya baa ijulikanayo kama Oceania Bar. Chupa moja ya pombe kali aina ya Silicov inayotengenezwa nchini Urusi ilikuwa tuou. Hii ilimaanisha kwamba bwana Shukuru Kizibo alikuwa amekwishaimaliza pombe ile. Chupa ya pili kwa sasa nayo ilikuwa imekatwa robo.
Bwana Shukuru Kizibo alikuwa ni fundi mkubwa sana katika kukata masanga. Alikuwa na uwezo wa kunywa pombe nyingi sana pasi kulewa chakari. Kichwa chake kilikuwa ni kizuri sana. Hata watu wake wa karibu walimshangaa sana.
Pia pombe ni kitu ambacho bwana Shukuru Kizibo alikuwa akikipenda sana katika maisha yake. Bwana Shukuru Kizibo anapokuwa na mawazo mengi sana kichwani mwake, basi hupenda kujituliza kwa kuzitandika chupa nyingi za pombe kali.
Na kama ambavyo nilikudokeza hapo awali ni kwamba bwana Shukuru Kizibo kwa sasa alikuwa na mawazo mengi sana muda wote. Mawazo yake yalikuwa ni katika kuelekea kuliunda jeshi lake ambalo litashiriki katika mapinduzi ya serikali ya Bantu.
Akiwa katika burudani yake ile ya pombe, ghafla mhudum mmoja wa baa ile ambaye alikuwa ni mlimbwende hasa alikuja katika meza ya bwana Shukuru Kizibo. Mkononi alikuwa ameshikilia gazeti. Mlimbwende yule aliliweka gazeti lile mbele ya bwana Shukuru Kizibo. Pasi kusema chochote mlimbwende yule aligeuka na kuanza kutembea kuelekea kule ambako alikuwa ametoka.
Bwana Shukuru Kizibo alibaki ameduwaa kwani hakuelewa ni nini ambacho kilikuwa kikiendelea. Hakuelewa ni kwa nini mlimbwende yule alikuwa ametenda kitendp kile. Kwa kweli hakuelewa maana yake.
Baadaye aliamua kulichukua gazeti lile ili aweze kupitisha macho yake ndani. Akiwa katika kulifunufunua, ghafla kipande cha karatasi kilidondoka kutoka kurasa za katikati za gazeti lile.
“NAOMBA KUKUTANA NAWE HAPA NJE KATIKA GARI LAKO. NI MUHIMU SANA HASA KWA MIPANGO YAKO!” huu ulikuwa ni ujumbe ambao ulikuwa umeandikwa juu ya karatasi ile.
Macho ya bwana Shukuru Kizibo yalibaki yakiwa yameduwa juu ya maandishi ambayo yalikuwa yameandikwa katika karatasi. Pia kichwa chake kilikuwa kikiwaka moto kujaribu kuutafakari na kuuelewa ujumbe ule ambao ulikuwa umeandikwa katika karatasi ile.
Baadaye bwana Shukuru Kizibo alikiinua kichwa chake na kujaribu kumtazama mrembo yule ambaye alimletea gazeti lile ambalo lilikuwa na kipande kile cha karatasi chenye ujumbe lakini hakuweza kumwona. Alijaribu kuangazaangaza macho yake katika ukumbi wa baa ile huenda macho yake yangeweza kumwona mtu ambaye alikuwa ndiye mhusika na ujumbe ule, lakini aliambulia patupu.
Hapo awali alitaka kuupuuza ujumbe ule lakini upande wa pili wa akili yake ulimkataza kufanya vile. Upande ule wa akili yake ulimsisitiza kuitikia wito kwani hakufahamu umuhimu wa wito ule.
Bwana Shukuru Kizibo aliinyanyua chupa ile ya pombe kali na kupiga mafunda mawili ya mfululizo. Baada ya hapo alisimama na kuanza kutembea. Alipopiga hatua ya pili bwana Shukuru Kizibo alitaka kupiga mweleka ambapo alijishikilia katika kiti ambacho kilikuwa pembeni yake. Alitulia kidogo na kuuweka mwili wake sawa. Baada ya hapo alianza kutembea kuelekea nje ya baa ile kuitikia wito ule.
Dakika tatu zilitosha kumfikisha mpaka mahali ambapo alikuwa ameliegesha gari lake. Aliangaza macho yake kama angeweza kumwona mtu ambaye alikuwa akimhitaji lakini hakufanikiwa. Baadaye aliamua kuingia ndani ya gari ili aweze kumsubiri mtu huyo akiwa ndani ya gari.
Aliuingiza ufunguo wa gari katika tundu la mlango na kasha aliuzungusha. Baada ya hapo alikikamata kitasa na kukinyanyua. Mlango ulisalimu amri na kufunguka.
********
Aliuingiza ufunguo wa gari katika tundu la mlango na kasha aliuzungusha. Baada ya hapo alikikamata kitasa na kukinyanyua. Mlango ulisalimu amri na kufunguka.
SASA ENDELEA
Bwana Shukuru Kizibo alipigwa na butwaa mara baada ya macho yake kumwona mtu mmoja akiwa amekaa pembeni ya siti ya dereva.
“Wewe ni nani na umeingiaje humu ndani wakati mlango wa gari nilikuwa nimeufunga?” bwana Shukuru Kizibo aliporomosha maswali mawili mfululizo huku akimtazama mtu yule ndani ya gari lake.
“Acha maswali ya kitoto. Ingia ndani ya gari acha kupoteza muda. Hilo ni jambo dogo sana” Kanali Edson Makoko aliongea. Bwana Shukuru Kizibo hakujibu kitu. Alichofanya mi kuingia ndani ya gari kama vile ambavyo aliamriwa.
“Habari yako bwana Shukuru?” Kanali Edson Makoko alimsabahi bwana Shukuru Kizibo.
“Salama tu. Wewe ni nani na umefuata nini hapa?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.
“Usijali bwana Shukuru. Nitajitambulisha na utanifahamu kwa kina” Luteni Edson Makoko alijibu.
“Kwanza kabisa naitwa Kanali Edson Makoko mwanajeshi wa Jeshi la wananchi wa Bantu. Mimi ni mkuu wa kambi ya jeshi ya KJ 05” Kanali Edson Makoko alianza kujitambulisha.
Ghafla mwili wa bwana Shukuru Kizibo ulishikwa na ganzi. Pombe aliyokunywa yote ilimtoka na macho aliyatumbua mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango. Utambulisho ule ulimshtua sana.
Hakufahamu ni nini ambacho kilikuwa kinaendelea. Alihisi huenda harakati zake za mapinduzi zitakuwa zimevuja na sasa wanajeshi walikuwa wamekuja kumsomba na kumpeleka kizuini. Alichoka sana. Ubongo uligoma kufanya kazi kwa muda.
“Ok, wahitaji nini kutoka kwangu bwana Makoko?” bwana Shukuru Kizibo alijitutumua na kuuliza swali.
“Kuwa mpole bwana Shukuru Kizibo. Hautakiwi kuwa na jazba kama ambavyo ninakuona ulivyo. Mimi nimekuja hapa kwa kheri kabisa na wala si kwa shari. Hivyo kuwa huru kabisa bwana Shukuru Kizibo!” Kanali Edson Makoko aliongea akimtoa wasiwasi bwana Shukuru Kizibo.
“Nimekuwa nikikufuatilia kwa muda mrefu sasa harakati zako kisiasa. Hakika wewe ni mtu wa pekee sana ambaye unastahili kupongezwa na kuungwa mkono!” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Ahsante sana!” bwana Shukuru Kizibo alijibu.
“Sasa mimi nipo hapa kwa ajili ya kukuunga mkono. Nahitaji kukuunga mkono kwa huo mpango ambao unao. Mpango wako unahitaji watu kama sisi” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Mpango gani? Mbona sikuelewi” bwana Shukuru Kizibo alijibu huku akihisi kwamba Kanali Edson Makoko alikuwa akimtega.
“Usijifanye huelewi bwana Shukuru Kizibo. Nadhani nilikwishakwambia hapo awali kwamba hupaswi kuwa na woga kwani mimi nimekuja hapa kwa kheri na si kwa shari. Hebu tuache utoto na tuongee mambo ya maana” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Sasa nitaamini vipi kama haupo hapa kwa ajili ya kunikaanga?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.
“Wewe ulikuwa una shida ya kupata wanajeshi kwa ajili ya kuunda jeshi. Sasa ni kwa nini unashindwa kuniamini kama mimi nipo tayari kwa ajili ya kukuunga mkono?” Kanali Edson Makoko aliuliza.
“Jambo linalonitia hofu ni kwamba, wewe ni mtumishi wa jeshi. Sasa utawezaje kushiriana name pasi kuleta matatizo jeshini?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.
“Hilo ni jambo dogo sana bwana Shukuru Kizibo. Mimi niko tayari kuacha jeshi kwa ajili ya kuuratibu na kuutekeleza mpango huu. Mpango huu ni muhimu sana kwangu kuliko huduma yangu jeshini. Mimi mwenyewe nilikuwa na ndoto za kuufanya mpango huu kwa muda mrefu sasa lakini sikuwa nimepata mtu wa kuweza kushirikiana naye. Nadhani kwa sasa Mungu amejibu maombi yangu na amekuleta wewe kwangu. Usiwe na shaka bwana Shukuru Kizibo” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Unajua wanipa mtihani mzito sana. Lakini ngoja nikuamini. Nadhani mimi pamoja nawe kwa ushirika wetu tutaweza kulifanisha jambo hili kwa mafanikio makubwa sana. Jambo la muhimu ni kuaminiana. Jambo hili ni jambo ambalo lina matunda makubwa sana hapo mbeleni. Ni jambo ambalo litayabadilisha kabisa maisha yetu na tutaishi kama wafalme mpaka tunaingia kaburini” bwana Shukuru Kizibo aliongea.
“Kuhusu uaminifu kwangu ondoa shaka. Nadhani mimi ni mtu sahihi ambaye ulipaswa kunishirikisha mpango huu kwani sote tuna mawazo yanayooana. Wewe hesabu mafanikio tu bwana Shukuru Kizibo” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Sasa tunaanzia wapi mchakato huu huu maana ni kwa muda mrefu nimekuwa ninashindwa namna ya kuanza?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.
“Hili ni jambo dogo sana. Kwanza kabisa tunatakiwa kuunda jeshi. Mchakato huu utatuhitaji kuwa na bajeti ya kutosha kwani tutahitajika kuwa na silaha za kutosha pamoja na chakula cha kutosha pia” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Kuhusu bejeti, hilo lisikupe hofu hata kidogo. Nimejipanga vilivyo katika kuhakikisha mchakato huu unafanikiwa. Hivyo masuala yanayohusu ffedha wala yasikuumize kichwa. Itakuwa ni utekelezaji tu” bwana Shukuru Kizibo aliongea.
“Safi sana. Hizo ni habari nzuri. Basi kama hali iko hivyo basi mchakato huu utafanikiwa mapema sana. Kama nilivyosema hatua ya kwanza itakuwa ni kulikusanya jeshi. Katika jeshi letu kutakuwa na watu mchanganyiko. Kutakuwa na wanajeshi wenye taaluma ya jeshi na pia kutakuwa na watu wa kawaida ambao ni vijana na watoto”
“Tutahitajika kuweka kambi kubwa mahali Fulani msituni ambapo tutakuwa tumepachagua. Tutaendesha mafunzo ya kijeshi kwa watoto hao pamoja na vijana. Niamini, jeshi letu litakuwa ni jeshi lenye nguvu sana!” Kanali Edson Makoko aliongea maneno ambayo yalimfurahisha sana bwana Shukuru Kizibo.
“Umebnifurahisha sana bwana Makoko. Maneno yako yananifanya nizidi kukuamini na pia kuamini kwamba kuna mafanikio makubwa sana mbele yetu. Hakika leo nimempata mtu sahihi kabisa katika mipango yangu” bwana Shukuru Kizibo aliongea.
“Usijali bwana Shukuru. Kila kitu kitakwenda kama ambavyo kimepangwa” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Sasa katika wiki hili nitafanya mchakato wa kuacha kazi. Kuacha kazi kwangu hakutakuwa katika mfumo wa kawaida. Kutakuwa ni kwa kutoweka tu kazini. Naamini jeshi litanisaka lakini halitanipata. Na pia ndani ya wiki hili litafanya ziara ya kuangalia ni mahali gani katika nchi hii ambapo patatufaa kuweka kambi ya jeshi letu” Kanali Edson Makoko aliongea.
“Basi sawa. Nadhani tutawasiliana kwa kila hatua” bwana Shukuru Kizibo aliongea.
*******
ITAENDELEA
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment