Search This Blog

Thursday, 29 December 2022

MALAIKA WA SHETANI - 3

  

  Simulizi : Malaika Wa Shetani

Sehemu Ya Tatu (3)


ambaye angemzuia.


Kulipokucha alikuwa mtu wa kwanza kuamka. Kama kawaida yake, alifanya mazoezi ya viungo kwa saa moja, mwili ukiwa umetoka jasho alielekea bafuni ambako alijimwagia maji na kisha kuoga vizuri. Aliporudi chumbani alimkuta Nuru kaamka akijaribu kusimama. “Usifanye hivyo,” Joram alimwonya. “Jipumzishe kitandani tu.”


“Huna budi...”


Haikuwepo haja ya kubishana. Nuru alipojaribu kupiga hatua ya pili tu toka kitandani hapo maumivu makali yalimrudia mguuni. Akaukunja uso wake kwa uchungu na kukirejea kitanda. Macho yake yalitazama mguu wake kwa hasira. “Kitandani siku tatu! Kama maiti,” alinong’ona. Joram alimwendea na kumbusu shavuni. Kisha, alimwacha na kurudi mezani ambako alichukua kitabu cha simu na kuanza kukipekua. Baada ya muda alionekana kuipata namba aliyohitaji. Akainakiri katika daftari lake. Kisha akapiga simu kuagiza chai iletwe chumbani kwao. Chai ilipoletwa alisogeza meza ndogo mbele ya Nuru na kumshawishi kula. Nuru, ambaye alikuwa hajaoga ilibidi apate msaada wa Joram hadi bafuni ambako alijimwagia maji kisha akajikongoja peke yake kurudi chumbani. Alimkuta Joram kaiacha meza ya chakula yuko kwenye simu. Alikuwa akiomba gari la kukodi.


“Unataka kwenda wapi?” Nuru Aliuliza. “Kumwona Waziri Mkuu.”


“Joram!” Nuru alifoka kwa hofu na mshangao. “Bado una hamu ya kumwona. Jana tu tungekuwa maiti kwa ajili ya kutaka kuwona. Nadhani tutafute njia nyingine.”


“Hatuna njia nyingine zaidi ya kumwona. Leo nitamwona. Nitamfuata ofisini ghafla na kutumia mbinu ambayo itaniwezesha kumwona bila kipingamizi chochote,” Joram alimhakikishia.


Alipomwona Nuru akikusudia kuendelea na ubishi alimwacha na kuliendea kabati la nguo. Akatoa suti yake aliyoipenda zaidi. Akachagua viatu maridadi na kuvaa. Akalifungua kasha lake la silaha. Akaitazama bastola yake kubwa 45 kwa tamaa lakini hakuthubutu kuichukua badala yake alirudi kitandani na kupenyeza mkono wake chini ya mto. Ulipotoka ulikuwa umeshikilia ile bastola yake ndogo yenye ukubwa wa kalamu. Akaihifadhi mwilini mwake. Pale ambapo mkono wa binadamu






wa kawaida usingeweza kufika kwa urahisi. Kisha, akachukua ile kalamu yake ambayo haikuwa kalamu ya kawaida bali silaha kali ambayo ingeweza kuua mtu wakati wowote endapo angepata mwanya wa kubonyeza mahala fulani na kuachia hewa ya sumu iliyokuwa imeifadhiwa humo ndani kumfikia binadamu huyo. Aliiweka kalamu hiyo mfukoni. Baada ya kujikamilisha aligeuka kumuaga Nuru. “Nusu saa tu, mpenzi. Baada ya hapo nitarudi hapa mara moja.”


Uso wa Nuru ulikuwa na dalili zote za mashaka. “Joram, nadhani usifanye safari hiyo.”


“Kwa nini?”


“Sijisikii vizuri… naogopa.”


Joram akaangua kicheko. “Huna haja ya kuogopa chochote. Hakuna mtu atakayethubutu kuingia hapa mchana. Na akitokea nadhani hutomruhusu kutoka na roho yake. Bastola yako iko mahala pake. Na sina mashaka kuwa una uwezo wa kuitumia zaidi ya wanawake wote ninaowafahamu. Licha ya bastola kuna bomu la machozi, kuna king’ora cha kumtia hofu, kuna nuru ya kumlewesha, kuna…”


“Hujanielewa Joram,” Nuru alimkatiza. “Siyahofii maisha yangu kwa kubaki peke yangu. Nakuhofia wewe… Huko uendako… Nadhani usingeifanya safari hii. Imekuwa ya ghafla mno. Hukuiandaa.”


“Hiyo hasa ndiyo dhamira yangu.” Joram alimjibu akicheka. “Kumwendea bila ya kujiandaa. Niende kama raia yeyote wa kawaida ambaye atatoka ofisini bila ya kumwona Waziri huyo? Kujiandaa nusura kutupotezee maisha jana. Yawezekana tunapojiandaa wenzetu nao wanajiandaa…” alisita kidogo kumtazama Nuru. “Usijali Nuru, muda mfupi baadaye tutakuwa pamoja.


“Joram!”


Joram alimwendea na kumbusu, kisha alitoka nje taratibu. “Joram!”


Hakugeuka kumsikiliza.


Gari lilikuwa likimsubiri nje ya hoteli. Dereva alikuwa mzee mkimya ambaye alikuwa na macho yenye asili kama anayeuonea wivu ujana wa Joram Kiango. Joram alimsalimia na kumpa anuani ya ofisi aliyohitaji. Dereva akalitia moto gari lake. Mara tu gari lilipopamba moto naye alibadilika na kuanza kutokwa






na maongezi kama aliyetiwa funguo. Alizungumza lolote lililomjia akilini akitumia lugha zote za mitaani. Joram alitabasamu na kuendelea kumsikiliza ilhali hamsikii.


Nje ya jengo hilo Joram alimlipa dereva na kuiendea ofisi ya mapokezi. Walikuwa askari ambao maswali yalijaa midomoni mwao kama kanda iliyorekodiwa miaka nenda rudi iliyopita, maswali ya aina ileile, wakitegemea majibu yaleyale. Hivyo, hawakujua wanachokifanya walipojikuta wakijaa hofu ambayo zilimruhusu Joram kuwaendea maofisa wa usalama ambao wangemsikiliza zaidi yao. Askari mmoja alijitokeza kumwongoza katika ofisi yao, walipita hapa na pale na hatimaye, kupanda lifti hadi ghorofa ya nane ambako walifika tena mapokezi. Askari huyo alimwacha Joram hapo.


Maswali mengine yakafuata. Uongo mwengine ukafuata. Hatimaye, fomu nyingine zikajazwa. Zikapelekwa katika nyumba mbalimbali kuchunguzwa. Ziliporejea Joram aliruhusiwa kuendelea na msafara wake. Akajitokeza mtu mwingine kumwongoza. Walipanda tena lifti kushuka chini. Ghorofa ya nne waliteremka. Joram akaelekezwa katika chumba fulani ambacho hakikua na anwani yoyote mlangoni. Aliingia katika chumba hicho kwa mashaka kidogo. Ramani ya ofisi hiyo aliyokuwa nayo kichwani, katu haikuwa na chumba cha aina hiyo, chumba kidogo chenye meza moja tu kubwa iliyozungukwa na viti sita ambavyo havikukaliwa na mtu yeyote. Hewa katika chumba hicho ilikuwa nzito, licha ya mashine ya hewa kufanya kazi kama kawaida. Joram alipiga hatua ya pili kuingia. Ghafla hisia za hatari zikamjia. Akageukua taratibu kumtazama mwenyeji wake. Aliambulia kuona tabasamu la kifedhuli likichanua usoni mwake huku mkono wake ukitoka mfukoni, ukiwa umeshikilia bastola kubwa. Joram alifanya haraka kuupeleka mkono wake kunako silaha yake. Hakuwa mwepesi kiasi hicho kwani mkono huo haukuruhusiwa kutoka kwa jinsi mwenyeji wake alivyoudaka ghafla huku akiisogeza


bastola kifuani mwa Joram.


“Keti,” aliamuru kwa sauti ya utulivu.


Joram hakuwa na la kufanya zaidi ya kumtii. Alikalia kimoja kati ya viti vilivyokuwepo. Akilini alikuwa akijilaani kwa kuruhusu uzembe mkubwa kiasi hicho. “Vipi?” alijitia kuliza. “Sikutegemea mapokezi kama haya katika ofisi kubwa kama hii.






Kama unataka pesa sina chochote.”


Badala ya jibu mwenyeji wake aliangua kicheko ambacho kilikatizwa ghafla pindi mkono wa mtu huyo ulipoinuliwa tena na kubonyeza dude fulani lililokuwa kando ya mlango. Kabla Joram hajajua lipi la kufanya aliambulia kuona chumba kikimezwa na kiza ghafla. Alijitupa kuelekea mlangoni. Haikusaidia. Alikuta tayari mlango umefungwa kwa nje, sauti ya kicheko cha mwenyeji ikipotelea upande wa pili.


‘Nimefanya nini?’ Joram alijiuliza kwa hasira. Upuuzi gani kuacha ajiingize katika mtego ulio wazi kiasi hiki! Uzembe na upofu umemuanza lini? Mikono yake ilitambaa huko na huko ikipapasa hapa na pale. Alipata swichi nyingi ambazo alijaribu kuziwasha. Swichi ya kwanza alipobonyeza tu alihisi chumba kikianza kujawa na joto kali. Akaizima mara moja na kuwasha nyingine; iliyosababisha ubaridi mkali sana. Akaizima na kuendelea kupapasa. Akagusa nyingine. Aliiwasha kwa mashakamashaka. Kiasi hii aliiona imemsaidia. Ilitoa nuru nzito ya bluu ambayo ilimwezesha kuona ingawa kwa tabu kidogo. Akauchunguza mlango. Haikuwepo haja yoyote ya kujaribu kupambana nao. Ulikuwa mlango imara, maalumu kwa shughuli hizo. Akauacha na kurudi mezani. Alijaribu kuvuta droo, lakini zote zilikuwa zimefungwa. Juu ya meza hakukuwa na chochote cha haja; zaidi ya vifaa vya ofisi vya kawaida. Akaiacha meza hiyo na kurudi mlangoni. Alishangaa kuona miguu yake ikiwa mizito mno. Kila hatua aliipiga kwa tabu sana mithili ya mgonjwa wa miaka mingi anayejaribu kukiacha kitanda chake. Sasa hata macho yake aliyaona mazito, yakitokwa na uwezo wa kuona. Tahamaki chumba kilianza kuzunguka machoni mwake.


“Shit,” Joram alifoka kwa hasira akijaribu kujitahidi aufikie mlango. Alikuwa na hakika kuwa hali hiyo ni matokeo ya aina fulani ya sumu ya kulevya au kupumbaza ambayo alikuwa ameichokonoa mwenyewe baada ya kuwasha ile swichi yenye mwanga hafifu. Hivyo, alichohitaji ilikuwa kuifikia swichi hiyo na kuizima. Haikuwa kazi rahisi. Sasa alijiona taabani, kila hatua ikizidi kuwa ngumu kana kwamba mgonjwa huyo anajaribu kuupanda mlima Kilimanjaro. Kizunguzungu kilimzidi. Nayo macho yalikuwa hayataki tena kukaa wazi.


Hatua moja zaidi… Jitahidi tena….






Inua mkono…


Haikusaidia. Miguu ilipoteza uwezo wa kukichukua kiwiliwili chake. Macho yakaishiwa nguvu za kuona. Taratibu alijikuta… akiangukia zulia na kulikumbatia, akili yake ikizama katika usingizi mzito mtamu usio na kifani.




***


Zilimrudia taratibu kama zilivyomtoka. Zilianza fahamu, ambazo zilimfanya ajikumbuke. Zikafuatwa na mwili wake kuupata tena uwezo wake. Aligeuka kutazama huko na huko. Hakushangaa kujikuta katika chumba kingine, bila shaka katika jengo jingine, nje ya mji. Hayo Joram aliyahisi baada ya kusikia utulivu, kinyume cha mjini. Sauti pekee iliyomfikia ilikuwa ya gari moja ambalo lilisikika likipita kwa mbali. Joram alikitazama kwa makini chumba hicho. Kilijengwa kwa kuta nzito za mawe na dari ambalo bila shaka hewa chumbani ilikuwa nzito ingawa mapangaboi ya feni yalikuwa yakifanya kazi.


Chumba kilikuwa na mlango mmoja tu ambao Joram alishangaa kuuona ukiwa wazi. Kisha akageuka kujitazama. Hakufungwa miguu wala mikono. Akainuka mara moja na kugeuka nyuma. Haikuwepo dalili yoyote kuwa analindwa. Akapiga hatua mbili tatu za haraka kuuendea mlango. Mbele ya mlango alisita kidogo. Yawezekana kuwa alikuwa huru kiasi hiki? Alijiuliza. Akaamua kuthubutu. Taratibu akaushika mlango na kuufungua. Ukiwa mlango mzito wa chuma, ulifunguka taratibu. Joram akachungulia nje. Macho yake yakakutana na yale ya pande la mtu ambalo lilikuwa limeketi juu ya kiti nje ya chumba hicho, likivuta sigara kwa utulivu kama linalomsubiri!



Lilikuwa pande la mtu hasa. Uso wake, ulifunikwa na ndevu nyingi ambazo zilishuka hadi juu ya kifua chake kipana, ambacho hakikuhifadhika vizuri katika shati lake. Lilikuwa na midomo mipana ambayo ilidhihirisha unyama na ukatili. Mikono yake ambayo ilifunikwa na nywele nyeusi ilikuwa kitu kingine cha kuogofya zaidi. Ilitosha kabisa kuwa nyenzo ambayo ingepoteza maisha ya binadamu kwa kulikaba koo kwa dakika moja tu. Kitu cha kuogofya zaidi katika mtu huyo yalikuwa macho yake. Licha ya kwamba yalitisha sana bado hayakuonekana kama macho ya kawaida. Yalikuwa makavu, baridi, kana kwamba si macho ya binadamu hai bali ambaye ndio kwanza anatoka kaburini katika






nchi ya wafu, macho ya mauti.


Joram alijua kuwa maisha yake yalikuwa mashakani iwapo uhai wake ulikuwa mikononi mwa kiumbe huyu. Kupambana naye isingetofautiana na kuinadi roho yake kwa bei rahisi. Hivyo, hakuiona njia nyingine zaidi ya kujaribu kujenga urafiki na dude hilo, ingawa hakuona vipi lingehitaji urafiki.


“Kaka, samahani,” Joram alisalimu akijaribu kuunda


tabasamu usoni mwake. “Hivi nimefikaje chumbani humu?”


Kitu mfano wa tabasamu kilipenya katika uso huo. Tabasamu kiasi liliufanya uso wake ufanane na uso wa binadamu. Lakini lilidumu usoni hapo kwa sekunde mbili tu, mara likatoweka na kumezwa na ukatili uleule. “Umeamka sio?” sauti yake ilishangaza. Ilikuwa kinyume kabisa na sura yake. Ilikuwa ndogo kama ya msichana.


“Nenda zako,” aliongeza.


Hilo Joram hakulitarajia. Akajifanya hakusikia. Badala yake


akalirudia tena swali lake, “Nimefikaje hapa?”


“Nasema toka, nenda zako,” msichana katika jitu hilo alinong’ona tena.


Kwenda ilibidi Joram ampitie mtu huyo. Macho yake yalionyesha wazi kuwa kuambiwa aondoke ilikuwa dhihaka tu. Jitu lilikuwa likimsubiri kwa shahuku kubwa. Hata hivyo, alijaribu kumpita ili aondoke zake baada ya kuona kuwa jitu hilo halikuwa na dalili yoyote ya kuelekea kuzungumza zaidi. Alipiga hatua moja, ya pili na ya tatu kwa hadhari, ingawa hakuonyesha dalili yoyote. Hatimaye, alimfikia na kumpita kwa hatua moja. Ni hapo kilipofuata kile ambacho alikihofia. Lilikuwa pigo ambalo Joram alilitegemea na alilisubiri ili alikinge au kulikwepa. Lakini hakutegemea kuwa lingekuwa kali na kwamba lingepigwa kwa wepesi kiasi hiki. Alitahamaki teke likimwingia barabara ubavuni na kumfanya apepesuke na kutua sakafuni. Akaviringika na kuinuka hima huku akizipanga, tabasamu la hasira likichanua usoni mwake.


Kitu kingine mfano wa tabasamu kilijitokeza katika uso wa jitu hili, pengine kwa furaha kuona Joram akiwa tayari kupambana. “Unaitwa Joram, sio?” lilikebehi. “Hodari kwa kila kitu. Nilikuwa na hamu kubwa ya kupambana na wewe ana kwa ana. Umetusumbua kwa muda mrefu sana. Kwa nini unakuwa husikii unapoonywa?”






“Kuonywa! Kwa jambo lipi?” Joram alijaribu kuuliza. “Kwa nini unataka kumwona Waziri Mkuu?”


“Kuna ubaya gani ku…”


Joram alikatizwa na pigo jingine kali. Aliliona pigo hilo likija, lakini bado hakuweza kuliepuka. Lilimtia mweleka mwingine na kuinuka harakaharaka, akichupa angani na kuachia teke kali lililokilenga kifua cha jitu hilo. Pigo hilo ambalo jitu hilo halikulitegemea, bado halikumfikia. Alilikwepa kwa wepesi wa ajabu na kujibu kwa teke lake ambalo lilimnasa Joram tumboni. Yalifuata mapamabano makali. Joram alijikakamua na kuutumia ujuzi wake wote wa kareti na judo, akibadili mtindo kwa mtindo. Alipiga kwa nguvu na wepesi kuliko alivyowahi kupigana. Lakini ni vipigo vichache sana ambavyo viliufikia mwili wa jitu hilo. Wakati huohuo Joram alipokea vibao vingi vilivyomlegeza, hata akaanza kutweta huku jasho likimtoka ovyo. Aliongeza jitihada, akipigana kwa nia moja. Bado juhudi zake hazikuzaa matunda. Ilikuwa dhahiri kuwa asingekufua dafu kwa adui yake huyu ambaye alionekana kuufurahia sana mchezo huu, macho yake yakionyesha hamu ya kitu kimoja tu; kuua. Joram alishangaa kwa nini jitu hilo lilikuwa halijafanya hivyo. Pamoja na kumchelewesha sana Joram katika mapambano haya, ilikuwa dhahiri kuwa alikuwa akichelewesha mapambano


hayo makusudi ili auone ujuzi na juhudi za Joram.


Naam, ulifika wakati ambapo jitu hilo lilionekana kukinaishwa na mchezo huo. Likaachia pigo moja ambalo lilimwingia Joram barabara na kumfanya apepesuke na kuanza kuanguka. Lakini jitu hilo halikumruhusu kuifikia ardhi. Lilimrudisha kwa pigo jingine kali zaidi. Ndipo ikafuata mvua ya vipigo, mapigo makali ya harakaharaka; kila pigo likiwa limekusudiwa liingie wapi. Mapigo hayo yalimlegeza kabisa Joram hata akawa hawezi kujitetea wala kukinga. Bado hakuruhusiwa kuanguka, badala yake alisogezwa ukutani ambako aliegemezwa na kuendelea kuadhibiwa.


Maumivu hayakuwa na kifani. Yalimfanya Joram aishiwe hata nguvu za kulalamika na kubaki kimya, kinywa wazi; macho yakiwa yamemtoka pima katika kusubiri vipigo vingine. Mara mbili tatu alielekea kuzirai, lakini fahamu zilikuwa zikimrudia tena; zikifuatwa na maumivu makali. Joram, alitamani afe, ayaepuke mateso hayo. Wala hakufahamu vipi roho yake






iliendelea kuwa sugu kiasi hicho.


Mvua ya mawe iliendelea kumnyeshea. Hatimaye, Joram alielewa kilichokuwa kikimtokea. Adui yake alikuwa hapigi kwa nia ya kuua bali kumchezea tu, na alikuwa akiufurahia sana mchezo wake. Hata upigaji wake ulikuwa wa aina yake. Alijua apige wapi. Na alijua kiwango cha maumivu ambayo Joram aliyapata. Alikuwa akimchezea kwa mapigo hayo, akimlegeza na kumtesa. Joram alipoonyesha dalili za kuzidiwa kupita kiasi lile jitu lililegeza mapigo yake hadi akili zilipomrudia sawasawa, ndipo lilipoanza tena kupiga. Kama mwanamke hodari wa kufanya mapenzi ambaye humchukua mwanaume kimahaba hadi anapokuwa tayari kufika kilele, na kumfanya ahairishe kilele hicho na kuanza upya mara kadhaa hadi wakati unaoruhusiwa kumaliza unakuwa mwisho mtamu ambao huacha kumbukumbu toka fikra za mwanaume huyo. Ndivyo lilivyokuwa jitu hilo. Tofauti ni kwamba yeye alikuwa akiwakilisha burudani hiyo kwa maumivu badala ya starehe. Kipigo kilimlewesha Joram hata akaanza kuyazoea maumivu kiasi cha kutamani kuendelea kupigwa. Hata alipoacha kupigwa alikuwa akitamani kulalamika, amwambie mpigaji huyo aendelee, kama mwanaume anayemwabia yule mwanamke hodari wa mapenzi aendelee.


‘Binadamu gani wa kawaida anayeweza kuwa hodari wa kupigana kwa mapenzi na ukatili kama huyo?’ Joram alijiuliza katikati ya maumivu hayo. ‘Nani? Nani? Ah!’ mara akakumbuka. Ninja! Aliwahi kusoma mahala fulani ninja walivyo wataalamu wa kupigana, upiganaji ulio na utaalamu mkongwe, zaidi, unaojumuisha judo na kareti. Ninjutsu, utaalamu ambao unadaiwa chimbuko lake ni baina ya China na Japan, kwamba pamoja na mazoezi magumu, hila nyingi, mbinu mbalimbali bado unajumuisha uchawi na mazingaombwe pia. Naam, hiyo ndiyo sababu pekee ambayo ilimfanya ashindwe kupambana na mtu huyo kwa kila hali.


‘Ninja katika nchi ya Kiafrika!’ Joram alijiuliza kwa mshangao. ‘anafanya nini…’ na kwa… Mvua ya maumivu iliyokuwa ikiendelea kumnyeshea ilimfanya ashindwe kufikiri vizuri. ‘Oh! Akh! Shida yote hii kwa nini?’ alijiuliza. ‘Akh!’


Kwa nini adhabu kubwa kiasi hiki! Kosa lake ni lipi hasa. Kutaka kumwona Waziri Mkuu! Vipi kumwona Waziri Mkuu iwe kama kuthubutu kumwona Mungu au Shetani? Akh! Oh!



NURU alikua amechoka kuitazama saa yake. Masikio yake pia yalichoshwa na subira ya kutegemea simu ile na kumletea ujumbe wowote. Tayari usiku ulikua


umeingia, zaidi ya saa kumi zimepita, Joram, ambaye aliahidi kukaa saa moja, hajatokea! Wala hajaleta ujumbe wowote! Hofu na wasiwasi ambao ulimnasa tangu Joram alipompa kisogo tu, asubuhi, ulikua ukimzidi kila ilipoongezeka dakika moja zaidi pasi ya kutokea kwake.


Na sasa ni usiku!


Hisia zilimwambia kwamba liko jambo. Vinginevyo Joram si mtu wa kuvunja miadi na kumwacha akae roho juu kiasi hicho. ‘lakini ni kitu gani hasa kilichomtokea?’ alijiuliza kwa mashaka, ‘kifo?’ wazo hilo lilimfanya atetemeke ndani ya mwili wake. Nuru hakuwa kipofu, alikua akiona wazi kabisa kuwa shughuli za Joram zilimfanya awe akitembea na kifo chake mkononi kwani alikuwa na maadui wengi kuliko marafiki; wote wakiwa na hatari kuliko hatari yenyewe. Na kati yao wote, adui wa safari hii aliwatangulia kwa madhara. Kwanza, walikuwa hawamfahamu; kisha haikuwa siri kuwa adui huyo alikuwa akiwadhihaki kama mvuvi anayemchezea samaki ambaye tayari amenasa kwenye ndoana yake. Vifo! Ajali! Vifo! Yote hayo machoni mwa Nuru yalikuwa katika jumla ya dhihaka na mateso kabla ya ile adhabu yenyewe,






adhabu ambayo isingekuwa nyingine isipokuwa kifo.


Ndiyo Nuru alimwamini sana Joram. Alimwamini. Alimtegemea, alimheshimu, alimtukuza na zaidi alimpenda kwa ajili ya hekima, ujasiri na vilevile umbile lake. Nuru hakuona kama yuko kijana mwingine wa kiafrika, anayeipenda Afrika na kuthamini utu na haki ambaye angeweza kumzidi Joram. Ni hayo ambayo yalimfanya aitupe kazi yake, aisahau elimu yake, awaasi wazazi wake na hata kutojali uzuri wake ambao wengi wanadai kuwa si wa kawaida ili awe pamoja na kijana huyu ambaye roho yake ameifanya sadaka na mwili wake kafara kwa ajili ya bara la Afrika. Nuru alisherehekea kila dakika ya kuwa naye. Na asingejali kufa naye, huku amemkumbatia. Nuru alimwamini sana. Hofu ya kifo ilikuwa mbali sana na roho yake kila alipokuwa naye. Hata hivyo pamoja na imani yake kwake, safari hii aliona wazi kuwa Joram alikuwa akitapatapa, haoni aendako wala atokako, jambo ambalo lingefanya kifo chake kisiwe tatizo sasa.


Bila hiari aliitupia saa yake jicho jingine. Saa tatu!


Sasa alihisi akitetemeka mwili mzima. Alikisogeza kando chakula alicholetewa na watumishi ili ale. Alijikongoja kuinuka. Mguu uliendelea kumsumbua. Akaamua kuyapuuza maumivu hayo na kwenda hadi bafuni. Ikamshangaza kuona anaanza kurudiwa na uwezo wake. Baada ya shughuli zake za bafuni alirudi chumbani na kuketi kitini akifikiri la kufanya. La kufanya hakuliona. Alikuwa amewaza mengi na kuyawazua yote. Ilimjia kwenda polisi. Hilo alilifukuzia mbali mara moja. Licha ya kwamba Joram asingefurahi kusikia hivyo bado Nuru anaufahamu udhaifu wa kabila la watu hao wanaojiita polisi. Wangeanza uchunguzi baada ya maiti ya Joram kuokotwa barabarani na wasingegundua chochote hadi kiama.


Kumfuata ofisini au nyumbani kwa Waziri Mkuu huyo bado isingekuwa hekima. Kwanza, hajui Joram alitumia hila na njia gani kuingia huko. Zaidi, ingekuwa sawa na kujipeleka mwenyewe kaburini. Asingefurahi adui wajifariji kwa kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Subira. Hilo ndilo wazo pekee ambalo aliliona la busara. Subira, hadi kwa wakati unaofaa. Saa kumi tu baadaye. Wakati huo mguu wake utakuwa umepona.


Lakini kusubiri ilikuwa kazi nzito zaidi ya neno lenyewe.






Kusubiri ukiwa chali kitandani ilihali hujui yaliyompata mwenzi na mpenzi wako! Wala hujui lipi linakusubiri! Haikuwa rahisi. Nuru alijikuta hatulii. Alitembeatembea, mara bafuni, mara dirishani; kusikiliza. Na alipotulia kidogo ni wakati alipokuwa akiirudia bastola yake na kuipapasapapasa. Mikono yake haikuchoka pia kuzishika silaha nyingine ili kuhakikisha kuwa ziko timamu kwa matumizi ya dharura.


Saa sita!


Nuru alishangaa. Akaruka toka kitandani na kukimbilia dirishani, bastola mkononi. Hakuona chochote. Akaiendea simu na kuinua mkono wa kusikiliza. Kisha, akakumbuka kuwa hakuwa na mahala popote pa kupiga. Akatulia na kurudi kitandani. Mara akagundua jambo ambalo hakulitegemea. Alikuwa akitembea kwa ukamilifu. Maumivu aliyokuwa akiyasikia yalikuwa ya mbali sana, yasingeweza kumfanya ashindwe kufanya kazi kesho. Akafurahi na kurudi kitandani ambako alijinyoosha, akiisubiri kesho kwa hamu kubwa.


Saa nane! Saa tisa!


Nuru aliduwaa. Kisha, akajisahihisha. Saa tisa! Maana yake bado saa tatu tu kupambazuke, aanze kazi. Hofu ya nini! Akainuka kwenda mlangoni kuhakikisha kuwa ameufunga. Kisha, akavua nguo zake na kujilaza kitandani, mkono wake wa kuume ukiwa umeikumbatia bastola yake. Akazima taa na kujilazimisha kufumba macho.


Hakumbuki kama alipitiwa na usingizi ama la. Alihisi kama anayeona mtu anaingia chumbani humo taratibu. Akafumbua macho na kutazama huku na huko. Hakuona chochote. ‘Upuuzi,’ alinong’ona akiyafumba tena macho yake na kujaribu kuubembeleza usingzi. Mara tu alipotulia hisia zilimrudia tena, kwamba kuna mtu aliyeingia chumbani humo. Alijilazimisha kuzipuuza hisia hizo, lakini hazikuelekea kumtoka. Aliendelea kuhisi kama kuna mtu aliyeingia, anamcheka. Akayafumbua macho yake taratibu na kuitazama nuru nyembamba iliyokuwa ikiingia toka dirishani ambayo haikumwezesha kuona vizuri. Lakini chumba kilikuwa kitupu. Alipotaka kuyafumba tena macho yake alihisi kama aliyeona kitu katika pembe moja ya chumba. Akayakaza macho yake kutazama. Naam, kulikuwa na kitu, kilisimama kimya kama kivuli mfano wa mtu. Kilikuwa






kikitingishika, kikimjia kimya bila kishindo kama mzimu. Nuru akaupeleka mkono wake kuwasha taa ilihali mkono wa pili ukiinuka kulenga bastola. Ndipo lilipotokea jambo la ajabu. Kivuli hicho kilipata uhai ghafla, kikajitupa kitandani na kuunasa mkono wa Nuru ambao ulikuwa na bastola; mkono wa pili ukimziba mdomo ili asiweze kupiga kelele.


Alikuwa binadamu mwenye nguvu za ajabu. Juhudi zote za Nuru kupiga kelele hapa na pale kwa nguvu zake zote zilikuwa kazi bure. Ilikuwa kama anayeupiga mwili wa chuma. Jitu hilo halikuonyesha dalili yoyote ya maumivu. Kinyume chake liliendelea kumnyonga Nuru mkono hadi lilipompokonya bastola na kuitupa kando. Kisha, likaanza kumfunga kamba.


Nuru alipambana kufa na kupona. Alitumia viungo vyake vyote, akirusha mikono na mateke. Alitafuta mwanya azipige sehemu za siri za jitu hilo kwa goti, hakufaulu. Kila pigo lake ambalo lingeweza kuleta madhara lilikingwa kwa uhodari. Nuru akashangaa. Binadamu gani huyo asiyepigwa akapigika? Akajiviringisha shingo kumtazama usoni. Macho yake yalipambana na uso wa kutisha kuliko uso mwingine wowote aliopata kuuona, uso ambao haukutofautiana naye. Yalikuwa macho yake kabisa, macho ya mauti. Yalimtazama Nuru kwa uadui kama yasiyo na uhai wala chembe yoyote ya kuthamini uhai wa mtu mwingine.


Hofu ikamshika Nuru.


“Unataka nini?” alijaribu kufoka. Sauti haikutoka.


Akaacha kupambana na kujilegeza ili kulibabaisha jitu hilo lijisahau, ili aweze kunyoosha mkono wake ufikie chini ya mto lilipokuwa lile bomu lake. Lakini jitu hilo halikuelekea kufanya makosa. Lilimfunga Nuru barabara mikono kwa miguu. Kisha, likaanza kumkunjia katika shuka nyeusi aliyoivuta toka katika kitanda cha pili.


Kidogo hilo lilimfariji Nuru. Pamoja na ukatili wake, pamoja na kutofanya makosa katika mapambano, bado kiumbe huyo ni kiumbe dume. Nuru alijua silaha ambayo inawafaa viumbe hawa. Na alikuwa nayo, silaha ambayo wahenga na wanasayansi wote kamwe wasingeipatia dawa. Ni silaha hiyo ambayo aliitegemea zaidi. Angeitumia. Mwanaume ni mwanaume tu. Huyu asingekuwa tofauti.


Hivyo, hakuwa na hofu sana aliponyanyuliwa na kutupwa




beganikwaurahisikamaunyoya,walajituhilolilipoanzakutembea bila kishindo kama kivuli hadi mlangoni ambako liliuchomoa ufunguo wake malaya lililoutumia kuingia, na kuuweka mfukoni. Likaurudisha mlango nyuma yake na kuiendea lifti. Huko chini lilitumia hila ileile kufungua milango hadi nje ya hoteli. Nje ya hoteli kulikuwa na walinzi wawili waliokuwa wanazungumza mbele ya ofisi yao. Nguo nyeusi lililozivaa jitu hilo, na mwendo wake wa utulivu kama mzimu vilimwezesha kupitia hatua chache nyuma yao, kandokando ya ukuta hadi nyuma ya hoteli ambako kulikuwa na gari likiwasubiri. Nuru alitupwa ndani kwa kupitia mlango wa nyuma. Jitu hilo likaingia mlango wa mbele na kulitia gari moto.


‘Ni mwanaume… atafanya makosa…’ Nuru alijifariji.


***


Kama Joram angewahi dakika tano tu angeliona gari lililomchukua Nuru likiondoka. Mwendo wake wa udhaifu na mzunguko wa safari aliyoifanya ni mambo ambayo yalimchelewesha.


Kiasi alijiona kama aliyeko ndotoni au hadithini kuwa hai na huru wakati huo. Kama si ndoto wala mwujiza basi ilikuwa dalili nyingine ya wazi kuwa maadui walimdharau sana hata hawakuiona haja ya kummaliza. Vinginevyo, asingeliacha jengo hilo isipokuwa kwa msaada wa jeneza. Kipigo alichopata toka kwa lile jitu ni kitu ambacho kamwe kisingemtoka akilini katika uhai wake. Roho yake isingeweza kustahimili dakika tatu zaidi ya adhabu ile. Adui yake, kama mpishi hodari ambaye alikuwa akipima chumvi na sukari kwa uhakika, aliacha ghafla kumpiga. Joram aliporomoka na kuanguka sakafuni. Fahamu zikamtoka. Zilipomrudia alijiona yuko palepale alipoangukia, peke yake na maumivu yake. Alitulia kwa muda akisikiliza. Haikumjia sauti yoyote. Taratibu, alijikongoja kuinuka. Akapiga hatua mbili tatu. Kisha, akatulia kusikiliza tena. Bado hakuisikia dalili yoyote ya kiumbe mwingine hai katika jengo hilo. Alikuwa peke yake. Huru! Hakuamini. Akaanza tena kujikongoja kidhaifu hadi alipoufikia mlango wa chumba hicho, akaufungua na kutoka nje taratibu. Alitokea katika chumba kingine ambacho kilikuwa kama ukumbi uliozungukwa na vyumba vingi. Kila mlango ulikuwa na amaelezo yake. Joram aliyasoma maandishi hayo harakaharaka.






Maabara… mkemia mkuu…. Quality Control…


Akajikokota hadi mbele ya mlango wa maabara. Mlango ulikuwa umefungwa. Alipojipapasa mfukoni mshangao wa pili ulimkumba. Funguo zake malaya zilikuwa salama kama ilivyokuwa bastola yake, kalamu yake, ambayo ni tochi na silaha; bomu lake dogo la machozi na vikorokoro vingine. Mshangao wake ulipomtoka nafasi yake ilichukuliwa na hasira. Vipi watu hao wamemdharau kiasi hicho hata wasijisumbue na chochote alichonacho mfukoni! Hasira hizo zikamfanya atabasamu, kiu kubwa ikizidi kuchemka rohoni mwake, kiu ya kuendelea kupambana na watu hao wanaojiamini. Hakuna ambacho Joram anapenda zaidi ya adui wa aina hiyo.


Mawazo hayo yaliupa mwili wake nguvu mpya ambazo hakujua zilikotoka. Akajikuta akitembea kwa uhakika zaidi katika jengo hilo toka chumba hadi chumba, funguo zake zikitimiza wajibu; bastola ikiwa imemtangulia. Baada ya kuingia vyumba vya kutosha alijua hakuna anachotafuta hapo zaidi ya kupoteza muda. Jengo hilo halikuwa na chochote cha haja kwake. Wala halikuwa kambi ya maadui kama alivyofikiria awali. Bali lilikuwa jengo la watu wenye shughuli zao nyingine kabisa, utafiti wa dawa za kienyeji, ingawa maandishi mbalimbali aliyoyasoma katika mafaili yalionyesha kuwa ofisi hiyo ilikuwa imefungwa na wafanyakazi wote kwenda likizo isiyo na malipo baada ya wafadhili wa serikali kushindwa kuihudumia. Bila shaka, maadui hao walilitumia jengo hilo kwa vipindi fulani wanapokuwa na shughuli zao. Hivyo, Joram akatafuta njia ambayo ilimtoa nje ya jumba hilo.


Mbele ya jengo kulikuwa na kichaka kikubwa cha miti, majani na maua mbalimbali; baadhi yakiwa aina ya mitishamba inayotumiwa katika utafiti. Katikati ya kichaka au msitu huo palikuwa na barabara nyembamba yenye kiza inayoelekea barabara kuu. Joram alijishauri sana kabla ya kuamua kuitumia. Ilikuwa nzuri sana, yenye uhakika wa kumfikisha mtu kuzimu haraka kuliko inavyoweza kumfikisha barabarani, hasa kwa jinsi ilivyokuwa na kiza cha kutisha. Adui yake angeweza kuwa popote, na kumwangamiza kwa silaha yoyote. Hakuna pigo baya kama lile ambalo linakupiga bila kutegemea wala kujua litatokea upande upi. Na ni mchezo ambao dude kama lile linalotumia mbinu za kininja linaupenda kuliko michezo mingine, kuua






huku anayeuawa hajui anapigwa na nani.


Hata hivyo, Joram aliamua kuifuata njia hiyo. Alijua kabisa kuwa hiyo haikuwa siku yake ya kufa. Vinginenvyo, angekwishayapoteza maisha yake muda mrefu uliopita.


Kabla ya kuondoka aliyatazama vizuri mazingira ya jengo hilo. Ramani ya nje na ndani ikijichora akilini mwake kikamilifu. Kitu fulani kilimwambia kuwa angerudi tena katika jengo hilo. Hakuwa mtu wa kuchukua kipigo kama kile alichokipokea na kisha akastarehe hotelini. Angekuwa mtu wa aina hiyo asingekuwa Joram Bin Kiango.


Alipiga hatua mbili kuingia kichakani, akasimama kusikiliza. Hakusikia chochote. Halafu akajitazama. Mavazi yake, suti nyeusi aliyoivaa ilimfanya awe sehemu ya kiza hicho. Kitu pekee kilichomtia dosari ni shati jeupe alilolivaa chini ya koti. Akaamua kulifunika vyema kwa koti lake. Kisha, akaanza safari yake kwa utulivu na adhari. Hata alipoifikia barabara tayari alikuwa amepata wazo. Asingekwenda hotelini moja kwa moja. Angemtembelea tena Waziri Mkuu.


Joram alijua fika kwamba kipigo alichokipata hakikukusudia kumwua. Adui alitaka kumtia hofu moyoni mwake ili akome kuendelea na upelelezi wake. Kwa bahati mbaya, hawakujua moyo wa Joram ulivyo. Badala ya kuogopa ndio kwanza walimzidishia ari. Sasa hivi, wakiwa na hakika kuwa yuko mahututi akijuta na kuomboleza ilikuwa nafasi yake nzuri ya kumtembelea Waziri Mkuu.


Barabarani alikaa muda mrefu bila kuona teksi. Saa yake ilikuwa imevunjika kioo katika mapambano, hakuweza kuiamini kama ilikuwa sahihi ilipoonyesha saa saba za usiku. Magari kadhaa ya binafsi yalipita bila kumtupia jicho japo alijaribu kupepea. Teksi mbili tatu pia zilimpita, ingawa moja haikuwa na abiria. Joram akaamua kujivuta taratibu kwa miguu akielekea mjini. Baada ya mwendo wa dakika kumi alifika mahala ambapo aliona gari limesimamishwa kando ya barabara, mlango wa dereva ukiwa wazi. Hatua kadhaa kando ya gari hilo, chini ya mti, Joram aliwaona kwa shida vijana wawili ambao walikumbatiana wima wakifanya wanachokijua. Walikuwa wanaume watupu. Lakini kutokana na mkao hali ilikuwa wazi kuwa mmoja alijifanya mwanaume zaidi ya mwingine, akijaribu kuchukua nafasi ya mwanamke. Hayo Joram aliyathibitisha baada ya kusikia busu






zito likifuatiwa na sauti ya kiume inayojaribu kulia kwa namna ya mahaba.


“Wapumbavu kama hawa wanastahili kurudi makwao kwa miguu,” Joram alisema akiingia katika gari hilo na kufunga mlango taratibu. Kama alivyotegemea swichi ilikuwa imeachwa katika tundu lake. Akaitekenya na kuondoka kwa kasi. Hakujisumbua kuwasikiliza majuha wawili ambao walipiga kelele nyuma yake huku wakimkimbilia. Likiwa gari aina ya Peugeot 505 mpya nalo lilimchukua kwa mwendo aliouhitaji. Dakika kumi baadaye alikuwa mjini. Huko alichukua ramani nyingine ambayo ilimwongoza hadi kwa Waziri Mkuu.


Kama alivyotegemea, walinzi wawili walikuwa wakisinzia katika kibanda cha usalama mbele ya geti la kuingilia katika nyumba hiyo. Lakini waliamka na kuzishika bunduki zao vyema mara tu Joram alipokanyaga breki mbele yao. Waliinuka na kuzielekeza bunduki zao kifuani mwake mara walipomwona akitoka na kuwafuata kwa mwendo wenye uhakika.


“Nani?”


Joram alizidi kuwafuata. “Simama hapohap ulipo.” Alicheka na kuzidi kuwaendea.


“Amri ya mwisho, simama,” askari huyo alifoka akirudi nyuma.


Joram akacheka na kuwatoa wasiwasi. Akasimama na kuwauliza kwa upole, “Vipi? Mapokezi haya hapa hata kwangu?”


“U nani wewe?”


“Tafadhali msijifanye hamnifahamu.”


Askari walishangaa. Yawezekana kuwa wanamsumbua mtu mkubwa sana katika idara ya usalama! Walijiuliza wakiangaliana. “Tunaomba kitambulisho tafadhali,” mwingine aliropoka.


Hiyo ilikuwa nafasi ambayo Joram alikuwa akiisubiri. Alitia mkono mfukoni na kuutoa ukiwa umeshikilia bunda la makaratasi. Aliyachambuachambua taratibu. Akatoa pochi nene ambayo aliifunua na kuchambua kitambulisho chake kimojawapo, ambacho kilikuwa na maelezo mengi yaliyoandikwa kwa herufi ndogondogo sana, makusudi kwa ajili ya kumsumbua msomaji. Akamkabidhi askari aliyekuwa karibu. Askari wa pili alisimama kando akisubiri.


Joram aliutia tena mkono wake mfukoni na kuipata moja kati






ya sigara zake maalumu. Akaitoa na kuiwasha. Aliitia mdomoni na kuvuta moshi, lakini alikuwa mwangalifu sana kuhakikisha haumezi. Alichofanya ni kuupuliza kwa hila usoni mwa askari hao, wakati huohuo akiwa ameziba pumzi. Askari hao wakiwa hawana habari kama wanavuta hewa yenye sumu kali ya kulevya, waliendelea kukikagua kitambulisho cha Joram kwa makini.


“Hiki kina uhusiano gani na Waziri Mkuu?” aliuliza baada ya


kuhangaika na herufi hizo.


Maelezo ya Joram yalikuwa mengi. Ilikuwa hila nyingine ya kuipa muda wa dawa yake ifanye kazi katika miili yao. Wakati huo alikwisha itoa sigara mdomoni mwake na kuacha moshi uendelee kuwaendea askari usoni. Aliyaona macho yao yalivyokuwa yakibadilika harakaharaka kuwa katika hali ya usingizi. Akaendelea kuwasimulia uongo mwingi juu ya udugu wake na Shubiri.


Dakika iliyofuata binadamu hao walikuwa nusu wafu. Walianguka mmoja baada ya mwingine, kila mmoja akianguka taratibu miguuni mwa Joram ambaye alifanya hima kuwabeba hadi katika kibanda chao, akiwafunga kamba mgongo kwa mgongo na kisha kuondoka haraka kuelekea ndani.


Haikuwa kazi ngumu kuingia katika jumba hilo, wala haikuchukua muda kufika chumba ambacho alikihitaji. Ramani ya jengo hilo ilikuwa wazi katika ubongo wake kihisia kama anavyozifahamu nyumba za wakubwa. Mbele ya mlango huo alisita kwa muda kusikiliza. Hakusikia chochote, kinyume na baadhi ya vyumba ambamo alisikia watu wakikoroma au kupumua kwa namna ya usingizi. Hivyo ilimshangaza chumba hiki kuwa kama kilivyokuwa, kimya kiasi hicho. Pengine mzee alikuwa macho akifanya shughuli zake? Alijiuliza. Akainama na kuchungulia katika tundu la ufunguo. Zaidi ya ukimya chumba kilimezwa na kiza kizito. Taratibu, kwa hadhari Joram alizitumia funguo zake malaya kuujaribu mlango. Ni ufunguo wa tatu ambao ulifaulu kufungua. Kabla ya kuingia alisikilza tena. Ukimya ukazidi kumwalika. Kimya kama ukimya wenyewe, aliingia chumbani humo. Alipofika katikati ya chumba aliitumia tochi yake kutazama huko na huko.


Nuru hafifu toka katika tochi hiyo yenye muundo na ukubwa wa


kalamu ilimwezesha kuona wazi kuwa chumba kilikuwa kitupu.






Kitanda hakikuwa na dalili yoyote ya kulaliwa. Makochi yalikuwa yametandikwa kwa utaratibu wa kawaida. Kwa uangalifu na hadhari ileile, Joram akafanya ziara bafuni na chooni. Akafunua hata kabati la nguo lililochimbiwa ukutani, hakuona mtu. ‘Yuko wapi Waziri Mkuu?’ alijiuliza kwa mshangao. Haja yake ilikuwa kumwona ana kwa kwa ana, amsikie na kumsaili.


Joram aliitumia nafasi hiyo ya upweke kupekuapekua, ingawa hakufahamu alihitaji nini hasa. Upekuzi wake haukumpatia chochote cha haja zaidi ya vitabu mbalimbali, hotuba zinazoandaliwa; na maandishi mbalimbali. Yote hayakumsaidia. Hata hivyo, wakati akitoka mguu wake, uligusa karatasi moja ambayo ilidondoka toka katika vitabu hivyo. Akainama na kuiokota. Ilikuwa karatasi ya kawaida ambayo mwandishi aliitumia bila kujua, pengine wakati akiwa na mawazo mengi kwani ilichorwa ovyoovyo na kisha chini ya michoro hiyo yalikuwepo maandishi.


…aondoke madarakani! Ni msaliti na mhaini!


Chini ya maneno hayo kulikuwa na alama ya kuuliza ambayo ilichorwa kwa wino mzito zaidi.


Joram aliyasoma tena maandishi hayo. Bado hakuyaelewa kikamilifu. Akaisokomeza karatasi hiyo mfukoni mwake na kuanza kutoka tena, uangalifu ukiwa umemtawala.


Alipofika kibanda cha askari aliingia na kuwatazama. Mmoja wao alikuwa ameanza kuamka. Joram akamsogelea na kumgusa koo kwa kisu ambacho alikichomoa katika vazi la askari huyohuyo. “Sikia,” alimnong’oneza. “Nitakuchinja usiponiambia aliko Waziri Mkuu.”


“Siwezi kusema… siwezi kumsaliti… ukitaka nichinje,” lilikuwa jibu la askari huyo kwa sauti ya kugugumia.


Joram alimchana kidogo kwa kisu shingoni. Ikamlazimu Joram kucheka kimoyomoyo kwa jinsi askari huyo alivyoshituka na kutoa macho. Alikuwa mwanaume mwingine mwenye moyo wa kike, mwoga kuliko kunguru.


“Nakuchinja.”


“Usinichinje,” alibembeleza. “Sijaona. Wala… yalaa… ngoja niseme.”


Hakuhitaji ushawishi zaidi. Alieleza yote aliyoyafahamu, yote ambayo aliapa kuwa asingeeleza, kwamba huo ulikuwa mwezi




wa pili Waziri Mkuu hakiwa halali katika nyumba hiyo, alikuja mchana na kufanya shughuli zake hadi usiku ambapo alitoweka ghafla.


“Analala wapi?”


“Sijui… hakuna anayejua.” MaelezoyakeyalimchanganyaJoramzaidiyayalivyomnufaisha.


Ndipo aliporudi hotelini kwa mwendo wa uchovu na maumivu makali kuliko alivyotegemea. Na ndipo alipofika hotelini na kukuta Nuru akiwa ametoweka. Kichwani mwake mlikuwa na maswali mengi, ‘Kwa nini Waziri Mkuu aihame nyumba yake? Na analala wapi?’ maswali ambayo yalitoweka mara baada ya kuona kuwa Nuru pia alikuwa ametoweka.









ITANDA kilimlaki Joram kwa namna ya mapenzi ambayo huko mbeleni hakupata kuyaonja. Mara tu ubavu wake ulipoligusa godoro hilo laini, huku akiwa na mavazi yake yote; pamoja na viatu; alijikuta akimezwa na lindi zito la usingizi.


Ukweli kwamba Nuru alikuwa mashakani, mikononi mwa watu au mijitu yenye kiu ya damu kama nunda; na ambayo starehe yao kubwa ilikuwa kuua; ukweli kwamba kichwa chake kilikuwa na maswali mengi yaliyohitaji kujibiwa haraka ili kulifumbua fumbo hili ambalo lilimtia Rais wa nchi nzima hatarini; bado haukumpokonya usingizi. Yote yangeweza kusubiri. Usalama wa Nuru haukumtia hofu kuuawa. Alikuwa na hakika kuwa kama yeye ameruhusiwa kuwa hai hadi sasa Nuru pia anasamehewa kwa muda. Kwa sasa hakuna alichokihitaji zaidi ya mapumziko ili aipate tena afya yake ya mwili na akili kwa kiwango chake halisi kumwezesha kumwokoa Nuru na uhuru wa nchi hii. Usingizi ukiwa dawa pekee ya mapumziko, ndipo akalala.


Na alilala…


Usingizi mzito, ambao haukuwa na ndoto zozote, isipokuwa ile aliyoifikiria kama ndoto ambayo ilimfanya adhani kuwa kila mara alikuwa akisikia kengele ya simu. Alipofumbua macho hakuweza kuona chochote kwa jinsi chumba kilivyojaa giza. ‘Vipi?’ Alijiuliza alipowasha taa na kuitazama saa ya ukutani. Alikuwa na hakika kuwa alilala jana, mnamo saa kumi na moja






za alfajiri. Vipi tena saa mbili za usiku? Yawezekana kuwa alilala zaidi ya saa kumi na tano?


Akajizoakitandanihukuakipepesuka.Ndiokwanzaakagundua amedhoofika kiasi gani kwa uchovu, maumivu na pengine njaa ya muda mrefu. Alikuwa mtu mgonjwa. Akakitazama tena kitanda kwa tamaa, na kilimwalika. Hata hivyo, aliishinda hamu hiyo ya kulala tena kwa kujilazimisha kuyavua mavazi yake na kisha kupepesukia bafuni. Maji ya baridi kali, ambayo aliacha yauchezee mwili wake kwa muda wa kutosha, yalimrudishia nusu ya afya yake.


Nusu ya pili ya uhai ilimrudia baada ya kufanya zoezi lake la viungo kwa robo saa.


Sasa alikuwa Joram Kiango tena. Sura yake ilichangamka kama kawaida, ikivutia katika suti yake ya kijivu ambayo aliivaa. Sasa aliiendea simu ili aombe room service wamletee chochote ambacho kingeweza kuila njaa yake. Mara tu alipoifikia simu hiyo ilipata uhai na kuangua kilio. Joram alipuuza. Iliponyamaza aliizungusha namba za huduma hiyo na kuagiza viazi kwa kuku mzima, pamoja na vinywaji mbalimbali.


Mhudumu alileta chakula hicho cha ziada. Matunda ya aina mbalimbali yaliimeza sahani moja pana iliyowekwa kando ya chakula juu ya kimeza kilicholetwa kwa kusukumwa. Pembeni zaidi kulikuwa na kijibahasha ambacho juu kiliandikwa jina lake bandia alilokuwa akilitumia hapo hotelini. Kadhalika, kulikuwa na ujumbe ambao uliandikwa katika karatasi za hapo hotelini.


“Hivi nimepewa hapo mapokezi, mzee,” mfanyakazi huyo alieleza. “Wanasema hawakuweza kuziwakilisha jana kwa kuwa hawakuwa na uhakika kama upo au la, baada ya simu zote kutopokelewa.”


“Vizuri sana,” Joram alimjibu. “Ziache, nitasoma baadaye.”


Mtumishi huyo alipoondoka Joram aliyasogeza kando maandishi hayo. Akijua kuwa asingetegemea habari yoyote njema katika nchi hiyo, hakupenda aipoteze hamu yake ya kula. Hivyo, akakaa mkao wa kula na kuanza kushughulika. Dakika kumi baadaye tayari alikuwa amevichakaza viazi, kumteketeza kuku na kunyanyasa matunda. Akakisindikiza chakula hicho kwa kinywaji. Baada ya hapo ndipo alipozichukua barua hizo na kuanza kuzisoma.


Ujumbe ulikuwa mfupi tu, “Mara tu ufikapo nipigie. Namba






ni ileile.” Joram alijua kuwa unatoka kwa Rais. Hakuwa na la kumwambia, hivyo akaamua kutompigia. Barua ya pili, kifurushi ambacho kililetwa hapo kwa express ya posta kilimchukua muda kufungua kwa jinsi kilivyofungwa kwa gundi lenye uhakika. Ndani mlikuwa na kidole cha mtu. Damu iliyoganda juu ya kidole hicho haikumfanya Joram ashindwe kuona kuwa kilikuwa kidole cha mwanamke.


‘Kidole cha Nuru?’ alijiuliza kwa wasiwasi.


Jibu lilikuwa katika kijikasha hichohicho, katika kijikaratasi ambacho kililetwa hapo kwa express ya posta kilimchukua muda kusoma kwa jinsi mwandiko wake ulivyokuwa mbaya.


… Ni msichana mzuri sana. Hatapendeza iwapo atapoteza vidole vyote. Hivyo, hili liwe onyo la mwisho. Kila siku ambayo utaendelea kuishi katika nchi hii tutamkata kidole kimoja. Na ni msichana ambaye hana hiana. Kabla ya kumkata kidole tunafurahi naye. Kazi anaijua…


Moyo wa Joram ulidunda kwa hasira. Akayasaga meno yake. Hakutegemea kama wangeweza kuwa katili kiasi hicho, hasa kwa mtu asiye na hatia kama Nuru. Asingewaruhusu kumkata kidole kingine. Na kwa kidole hicho walichomkata, kamwe asingejisamehe kwa uzembe huo alioufanya. Wala asingewasamehe washenzi hao.


“Watajuta kuzaliwa,” alinong’ona akiinuka kuanza kuutoka.


Baada ya kupiga hatua mbili kuelekea mlangoni alisita na kujiuliza anakokwenda. Akajikumbusha kuwa alihitaji kuwa na akili zake zote. Kumkata kwao Nuru kidole kimoja kulidhamiriwa kumtisha na kumkoroga akili. Ili alipize kisasi hicho alihitaji kuwa timamu kimwili na kiakili, si kufanya pupa wala papara.


Wazo hilo likamfanya akirudie tena kiti chake na kuketi chini. Kisha, alikichukua tena kidole hicho na kukitazama kwa makini zaidi. Akakirejesha katika kasha hilo na kukificha mahala ambapo watumishi wa hoteli wasingeweza kukiona. Kisha, akainuka na kuanza kutoka, tabasamu likiwa wazi usoni mwake.




***


Kijiji cha Polo kilikuwa pacha kwa vijiji vingi vya nchi masikini duniani. Barabara ya kukifikia isingestahili kuitwa barabara tena kwa jinsi ilivyomezwa na makorongo pamoja na mapori. Na hapo kijijini dalili pekee ya uhai ulikuwa moshi uliokuwa ukitoka






katika vibanda mbalimbali ambavyo wenyewe waliviita nyumba. Vinginevyo, kwa mtu aliyetoka katika mji mkuu, maili chache tu kutoka hapo; alijiona kama anayetoka peponi na kuingia kuzimu; badala ya dunia halisi. Dunia ya wakulima. Uti wa mgongo wa taifa kiuchumi! Giza zito, milio ya bundi na vyura na ukimya wa kutisha ni baadhi tu ya mengi yasiyopendeza yaliyokuwepo.


Ikiwa yakaribia saa nne za usiku, wakati ambapo pirikapirika za starehe zilikuwa zikiendelea mjini hapa, karibu kila mtu tayari alikuwa amejifungia ndani ya nyumba yake; ama anayeiogopa dunia yake, kana kwamba wanauogopa uhai wa usiku kuusubiri mchana ambao daima ulileta nuru ambayo ni neema na matumaini yao pekee, ahadi ya Mungu. Si zile za binadamu ambazo hazikuelekea kutimia. Yako wapi mabomba waliyoahidiwa hata kabla ya uhuru? Uko wapi umeme? I wapi mikopo ya kujenga nyumba bora? Zawadi au ahadi pekee iliyotimizwa ni shule. Lakini hii elimu haitumiwi ili wawaibe vijana wao wenye nguvu na afya toka hapo kijijini na kwenda kuwatumia mijini?


Hayo yalikuwa mawazo ya baadhi ya wanakijiji. Yalikuwa pia mawazo ya Joram Kiango wakati alipokifikisha kijiji hicho na kujikuta kamezwa na kiza hicho cha kutisha.


Sasa alikuwa amefika katikati ya kijiji. Alilizima gari lake na kufikiri namna ya kuanza kuuliza. Aliihitaji nyumba ya mzee Puta.


“Mwalimu Puta?” mtu mmoja ambaye alikuwa anapita hapo kwa bahati alilijibu swali la Joram. “Mbona umefika,” alisema akimwelekeza kwa kidole.


Ilikuwa moja kati ya zile nyumba zinazoitwa “bora” katika nchi kama hizi, nyumba pekee kijijini hapo ambayo ilijengwa kwa saruji na kuezekwa bati, kuta zake zikiwa zinavutia kwa rangi nzuri. Kwa mujibu wa maelezo ya mtu huyo aliyemwelekeza Joram, nyumba hiyo ilijengwa na Waziri Mkuu baada ya kibanda chake kuanza kuutishia uhai mfupi wa mzee huyo. Akiwa mzee mjane, asiye na mtoto, msaada huo kwake ulikuwa kama kapewa uhai mpya.


Kama nyumba nyinginezo, nyumba hii pia ilikuwa kimya, giza likiwa limetawala, wakati Joram alipoifikia na kuugonga mlango. Alipogonga kwa mara ya pili aliisikia sauti dhaifu ikiitikia toka ndani, “Nani?”






“Mgeni” alijibu.


“Mgeni! Unatoka wapi?” “Nifungulie tafadhali.”


Zilipita dakika zaidi ya tano kabla ya taa kuwashwa humo ndani na, hatimaye, mlango kufunguka taratibu.


Puta, umri ulikuwa unamshinda nguvu. Mwalimu huyu ambaye alikuwa mtu mrefu, mwenye mwili mkubwa, sasa alikuwa kama mzigo wa mifupa mitupu ambayo iliunganishwa pamoja na ngozi ambayo pia ilichoka kupindukia. Sauti na uhai kuwa katika umbo hilo dhaifu ilikuwa kama mwujiza. Hayo Joram aliyaona pindi akilitazama umbo la mzee huyo katika vazi lake la usiku; kaptula iliyokunjamana na fulana nyepesi. Alisimama huku akitetemeka, katikati ya mlango kama anayemnyima Joram ruhusa ya kuingia. Badala yake aliuliza tena, “Wewe nani?”


“Mgeni mzee… labda ungenikaribisha ndani ili tuzungumze.


Nimetoka mbali sana…”


“Una shida gani?” Joram alikatizwa. “Ni usiku sana. Siwapendi wageni wa saa hizi. Hawaleti jema lolote.” Sauti yake ilikuwa ikitetemeka kama mwili wake.


“Siwezi kuzungumza hapa nje. Labda niseme tu kwamba ningependa kuzungumza nawe juu ya rafiki yako mpenzi, Waziri Mkuu bwana Shubiri,” Joram alieleza.


Mzee alifanya kama kushituka kiasi, kisha alimkazia macho makali kwa muda. Baada ya muda ambao Joram aliuona mrefu, mzee alisimama kando ya mlango na kutamka neno moja tu, “Ingia.”


Ndani vilevile kulikuwa hakujambo. Taa ya chemli iliyokuwa imewekwa mezani ilimwezesha Joram kuchagua akalie kochi lipi kati ya seti moja unusu iliyokuwemo ukumbini. Aliketi juu ya lile ambalo liliekea mlangoni.


Mzee Puta alimfuata na kusimama mbele yake. “Ulitaka kusema nini juu ya waziri mkuu?’


“Si ungekaa ili tufahamiane vizuri, mwalimu?” Joram alieleza akiachia tabasamu lake bandia kwa nia ya kumtoa wasiwasi mzee. Lakini mzee huyo hakuwa rahisi kiasi hicho. Bado sauti yake ilikuwa na kila dalili ya uadui na kutomwamini Joram.


“Kama ungependa kufahamiana,” alisema. “Ungekuja mchana, si kuvizia saa hizi. Tafadhali, sema unachomtakia Shubiri.”



“Namtafuta,” Joram alieleza. “Nahitaji kumwona. Unaweza kunisaidia, mwalimu?”


Mwalimu wa kale alimezwa na kimya kingine. Kisha, akaiendea meza na kuvuta fungameza. Joram alimtegemea kuutoa mkono wake ukiwa na sigara. Lakini kilichotoka humo haikuwa sigara isipokuwa bastola aina ya revolver. Na ilikuwa ikimwelekea Joram kifuani. “Sasa utasema ukweli. Vinginevyo, utatoka huku ukiwa maiti. Sema upesi, wewe ni nani na nani amekutuma?” mzee huyo alinguruma kwa mnong’ono.


Kwanza Joram aliduwaa kwani hilo hakulitegemea. Kisha, akatamani kucheka kwa jinsi alivyomwona mzee huyo akitetemeka mwili mzima kwa kule kuishika tu bastola. Angeweza kuipokonya kwa urahisi wakati wowote bila ya mzee huyo kuwahi walao kuifyatua. Hata hivyo, hakuthubutu kucheka kwa kuchelea kutia mafuta katika mkaa wa moto. Hakupenda kubahatisha, bastola ifyatuke bure na mlio wake kumdhuru mzee wa watu.


Pengine mzee huyo anapenda kuongea na watu katika hali hii, akajikumbusha alivyokuwa akiongea na wanafunzi wake hali fimbo mbili zikimlinda juu ya meza. Hivyo, Joram akaamua kujitia aliyeshtushwa sana na tukio hilo, “Vipi kwani, mzee?”


“Sema wewe nani?’


Joram hakuona ubaya wowote kujieleza. “Naitwa Joram… toka nchi ya Tanzania. Niko hapa kwa ombi la serikali hii kujaribu kupata kiini cha maafa yanayotishia usalama wa nchi hii. Bwana shubiri anahitajika sana…


“Kwa nini unamtafuta usiku?” mzee alikatiza.


Joram alikuwa na jibu tayari. “Namtafuta usiku na mchana.


Nimejar…”


Mzee alimkatisha tena. “Kwa nini kila mtu anamtafuta? Kwa nini mnamwinda kama simba mwenye kichaa wakati yeye ni mtu mkubwa mwenye hadhi na heshima? Inakuwaje hamumfuhati ofisini kwake mchana, wala anapokuwa mikutanoni hadharani bali mnasubiri giza liingie? Hamna shukrani wala fadhila nyie. Mnadhani bila yeye hii ingekuwa nchi? Bila hekima na mapenzi yake kwenu mgekua watu nyie? Mzee akasita kidogo akitweta kwa hasira, jasho jembamba likimtoka usoni. “Naye upole umemzidi,” aliongeza. “Nilimwambia kitambo aiondoe roho hiyo na kuwa mwanaume, hasikii. Sasa anachezewa kama ngedere;






hata na vijitu kama wewe! Nitakuua.”

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog