Search This Blog

Thursday 29 December 2022

MALAIKA WA SHETANI - 4

  

  Simulizi : Malaika Wa Shetani

Sehemu Ya Nne (4)



“Sikia mzee,” Joram alijaribu kusema kwa utulivu kama awali. Lakini mzee alimkatiza kwa ukelele mkali wa hasira uliofuatiwa na machozi mengi. Kwa sauti kali alinguruma, “Nitakuua… naua


mtu…”


“Subiri kidogo mzee, anaweza kufa baadaye. Mimi pia nahitaji kumwona.” Ilisema sauti mpya, yenye uhakika ikitokea katika kimojawapo cha vyumba hivyo. Msemaji alikuwa akiwajia.


Joram na mzee Puta waligeuka kumtazama.


Joram hakuhitaji kuambiwa kuwa alikuwa ana kwa ana na mtu ambaye alihitaji sana kumwona. Hakuoana kabisa na picha zake nyingi katika vitabu na magazeti.


“Ndugu Shubiri,” alisalimu.


“Naama. Hujambo Joram Kiango? Nilikuwa na kiu kubwa ya kuonana nawe,” akamgeukia Puta na kumwambia, “Samahani, mwalimu. Huyu ni Joram Kiango. Anayeweza kufa baadaye…”




***


Hakuna kitu kinachotisha kama kilio cha mzee. Ama kwa kuwa hakupata kumsikia mzee wa umri kama huu akilia kwa sauti ama kwa kuwa hakutegemea mtu ambaye alijitia ushujaa kiasi hicho kulia. Masikioni mwa Joram ulikuwa muziki wa kutisha sana, kama unaoimbwa na mzuka.


Kwa muda alimtazama mzee alivyolia huku akilalamika kwa sauti ambayo iligugumia hata analosema lisisikike. Kisha, ghafla, kama alivyoanza; mzee alinyamaza; mwili wake ukakoma kutetemeka. Akaitazama bastola yake, kisha akamtazama Shubiri.


“Na huyu unamsamehe, mwanangu?” alinong’ona kwa udhaifu. Hakusubiri jibu. “Unamsamehe!” vipi mtoto wewe unakuwa na moyo wa barafu kiasi hicho? Watakuchezea hadi lini? Na wana haki gani ya kukuchezea kiasi hiki?” mzee alisita kidogo. Alipoanza tena kuzungumza sauti yake ilikuwa ya mnong’ono zaidi, kana kwamba aliwasahau Joram na Shubiri na sasa anazungumza peke yake. “Aibu iliyoje. Kila mtu anajua nchi hii ni yako. Kila mtu anakuhitaji. Wala hakuna asiyefahamu kuwa bila wewe nchi hii isingekuwa hapa ilipo. Na hii ndiyo fadhila ya wema wako, kuishi mithili ya popo, huku ukiwindwa kama mhalifu. Nchi hii ni yako mwanangu. Yako… yako… yako,”






alifoka ghafla.


Kisha, alianza tena kulia. Akaitazama tena bastola. Mara akajitupa chini na kuondoka zake kurudi chumbani, huku akipepesuka kwa jinsi macho yake yalivyojaa machozi.


Walipobaki peke yao ndipo Joram alipomkumbuka Waziri Mkuu na kumtazama. Aliona kuwa yeye pia alikuwa ameduwazwa na machozi ya mzee ingawa tabasamu dogo lilienea usoni mwake na kuwa kama lililosahauliwa hapo.


‘Tabasamu katika uso wa Shubiri!’ Joram alishangaa, kitu ambacho hakupata kukiona kamwe katika picha zote zinazotokea magazetini! Vipi wapiga piche wote wasilione tabasamu hili?


“Keti.”


Sauti yake ikamzindua Joram. Akaketi kumwelekea mkuu huyo ambaye tayari alikuwa ameketi, akiipapasa mifuko yake kutafuta sigara. Joram aliwahi kwa kutoa paketi yake na kumchagulia sigara moja. Waziri aliipokea na kuivuta bila ya wasiwasi. Hilo pia lilizidi kutia nyongeza katika mshangao wa Joram Kiango.


Mtu aliyekuwa mbele yake hakuonekana tishio kama alivyostahili kuwa. Hasa alikuwa kama rafiki wa kawaida tu, si Waziri Mkuu wa nchi. Na hasa si yule Shubiri ambaye kila kidole kilikuwa kikimwelekea kutokana na maafa yaliyokuwa yakiikabili nchi, mtu ambaye vifo vingi vilitokea kwa ajili yake, mtu ambaye kumwona tu kumetia roho yake na ya mpenzi wake Nuru katika mashaka makubwa.


Nuru… mara Joram akamkumbuka hasira kali iliumeza moyo wake. Akamkazia Waziri huyo macho yaliyojaa maswali mengi hata asijue aanze na swali lipi na kumaliza na lipi. Ni waziri huyo aliyemrahisishia jukumu hilo kwa swali lake lililoulizwa kwa sauti ya kawaida kabisa. “Bwana Joram Kiango sio? Yule mpelelezi mashuhuri kutoka Tanzania. Ndiye au siye?”


“Nadhani ndiye,” Joram alimjibu.


“Ninayo furaha kubwa kukuona ana kwa ana. Sifa zako ni nyingi sana kijana. Kama waandishi wa habari hawatii chumvi, basi wewe u mtu mwenye roho ya paka.” Akasita kidogo. “Nilikutegemea kuwa jitu la kutisha sana,” aliongeza. “Si mtu wa kawaida, kama ulivyo. Kitu gani kilichokutoa kwenu na hata kuja hangaika katika nchi kama hii?” Aliuliza.


Joram hakujibu mara moja. Sauti ya Shubiri ilikuwa






ikimshangaza. Alikuwa akizungumza bila wasiwasi wowote, wala dalili ya uadui. ‘Mwigizaji mwingine?’ alijiuliza. Hata hivyo Joram alijisikia salama sana kuzungumza naye kuliko alivyopata kujisikia kwa mtu yeyote. Hasira zikazidi kumpanda. Ndivyo walivyo waovu. Huwezi kuwafikiria. Akaamua kutouzunguka mbuyu. Badala yake alieleza kama ilivyokuwa, macho yake yakifanya kazi ya kuuchunguza uso wa Shubiri ili kuona alizipokea vipi habari hizo.


“Niko hapa kwa ombi la serikali yako…” alieleza. Akaendelea kueleza tangu alivyotembelewa na hayati Kongomanga, hayati huyo alivyopoteza maisha yake baada ya kuufikisha tu ujumbe huo; msichana Betty alivyopoteza maisha yake mara tu baada ya kueleza yale aliyoeleza na jinsi maisha yake na Nuru yalivyokuwa mashakani kwa ajili tu ya kujaribu kumwona yeye.


Ilikuwa hadithi ndefu, kisha kama tamu vile masikioni mwa Shubiri aliyekuwa akisikiliza huku tabasamu lake likizidi kuchanua usoni mwake tabasamu ambalo lilipotea na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama mshangao au kutoamini kila Joram alipoeleza juu ya vifo na maafa. Hali hiyo ilibadilika na kuwa kicheko Joram alipogusia suala la mapenzi na kudai kuwa yanaweza kuwa moja ya sababu zinazomfanya yeye Shubiri ashukiwe kuwa kiini cha mauaji hayo.


“Kama mapenzi ama tamaa ya cheo tu hilo si shauri langu. Hata hivyo, kinachonishangaza ni jinsi ulivyo tayari kumwaga damu isiyo na hatia kwa ajili ya kukidhi haja zako, ni dhambi isiyosameheka.”


Maelezo hayo ya Joram yalikikatiza kicheko cha Shubiri. Badala ya kumjibu, aliuliza, “Umesema umekwishamwona Rais?”


“Ndiyo.”


“Naye pia alishangaa?” “Nadhani.”


Baada ya kimya kifupi aliuliza tena, “Na unaonaje? Ni wewe tu uliyekuwa ukinitafuta au kuna watu wengine?”


“Sijui kama wapo.”


“Swali la mwisho tafadhali,” Shubiri alieleza. “Unafikiri vipi. Watu waliokuwa wakikushambulia kila ulipojaribu kuniona nia yao ilikuwa kuua kabisa au kukunyima fursa ya kuniona tu?”


“Nadhani hawakutaka nikuone,” Joram alimjibu. “Wewe






ulitaka?” akaunganisha swali lake. “Nilikuwa na hamu kubwa ya kukuona.”


“Kitu gani kimekufanya hata uihame nyumba yako na


kujificha humu?


“Huwezi kuelewa,” lilikuwa jibu la Shubiri. Kisha, alimezwa na mawazo mengi. Mara akautia mkono wake katika mfuko wa shati na kuutoa ukiwa na karatasi mbili za hundi. Moja aliirejesha mfukoni, ya pili aliiweka mezani na kuandika juu yake. Kisha, alimsogelea Joram na kumpa hundi hiyo.


Joram aliipokea na kuisoma. Iliandikwa jina lake. Paundi za kiingereza elfu kumi. “Za nini?” aliuliza.


“Usumbufu,” Shubiri alimweleza. “Ningekushauri kesho uondoke na ndege ya kwanza kwenda zako kwenu,” aliongeza, “Kucheza na mauti ni jambo jema. Ya Kaisari mwachie Kaisari.” Joram aliitazama tena hundi hiyo. ‘Hakuna pesa zinazonuka,’


aliwaza akiitikia mfukoni.


“Sina budi kukushukuru. Hata hivyo, naomba niulize swali la mwisho kabla sijaondoka.


“Uliza.”


Chochote ambacho kilikusudiwa kuulizwa na Joram hakikuwahi kuulizwa. Mshindo wa kuanguka kitu toka chumbani kwa mzee Puta uliwashitua wote. Wakatazamana. Kisha, Waziri aliinuka na kuelekea chumbani huku, akifuatwa na Joram. Walimkuta mzee akiwa ameanguka chini toka kitandani. Joram aliinama kumgusa kifuani. Uhai ulikuwa umemwacha kitambo. Akamtazama Shubiri kwa macho ambayo hayakuhitaji maelezo zaidi.


“Am… kufa,” Shubiri alitahayari. Machozi yakaanza kumtoka?... sasa nenda zako tafadhali. Nikikuona tena… nitakuua.”


Ilikuwa sauti iliyobeba msiba, huzuni na hasira zake zote. Ilimsikitisha Joram zaidi ya ilivyomtisha. Bila kuaga, taratibu aliinuka na kutoka.




ARI lake la kuiba lingeweza kumpeleka popote. Usiku kwake ulikuwa bado mchanga sana na alikuwa na mengi ya kufanya. Sasa angependa kufanya safari ya kumtafuta Nuru na kumtoa katika mikono ya binadamu hao wenye kiu kali ya damu. Lakini alisita kulifanya. Hakuwa na shaka zaidi mateso na majeraha ya hapa na pale Nuru yuko hai na salama. Vinginevyo angekwishapokea furushi la kichwa chake badala ya kidole. Zaidi ya hayo, Joram alikuwa na hakika kuwa maadamu majambazi hayo yalikuwa na Nuru katika himaya yao, yalikuwa na hakika kuwa Joram asingethubutu kwenda kinyume cha maagizo yao. Hivyo, alijiona kuwa alikuwa katika nafasi nzuri ya kwenda atokako na kufanya atakalo katika upelelezi wake. Lakini angekwenda wapi zaidi? Alijiuliza kwa masikitiko. Kama kumwona kwake Waziri kulimwongezea chochote katika uchunguzi wake, basi nyongeza hiyo haikuwa zaidi ya kitu kama kumimina sukari katika bakuli la mboga kwani alichanganyikiwa zaidi. Kwanza, alimwona kwa urahisi zaidi ya alivyotegemea; jambo ambalo, licha ya kushangaza lilimchukiza. Alitegemea kumwona kwa taabu, kama anayeonana na kifo; huku risasi zikimkosakosa. Si kwa ajili ya Waziri Mkuu huyu ambako kulifanya msichana wa watu Betty, auawe kinyama? Si kumwona Waziri huyuhuyu ambako kumeyahatarisha maisha ya dereva asiye hatia. Si






kwa ajili yake huyuhuyu ambako sasa hivi kunamfanya Nuru awe mikononi mwa mauti, tayari kufa wakati wowote? Sio Waziri huyu?...siye?


Na kama ndiye basi imekuwa rahisi kumwona! vipi kuonana naye imekuwa kama kumwona mtu yeyote wa kawaida, si mtu ambaye mauaji ya kutisha yanatokea kwa ajili yake? Na vipi maongezi yake yamekuwa ya kawaida kiasi hicho, sauti yake ikiwa haina dalili yoyote ya hofu wala hatia kwa yote aliyosimuliwa? Zaidi, vipi Waziri huyo aonyeshe kushangaa kwa maelezo ya Joram. Au ni mwigizaji mwingine mzuri?


Kisha, Joram alikumbuka kitu kingine alichokipata katika macho na sauti ya Shubiri. Naam, kulikuwa na kitu zaidi ya mshangao, kitu kama huruma. Shubiri alikuwa kama anayemhurumia Joram zaidi ya anavyojihurumia mwenyewe. Kwa nini? Au angesema mengi iwapo kisingetokea kile kifo cha uzee cha mwalimu Puta?


Maswali yaliongezeka kila dakika, majibu yakiwa ndoto iliyokuwa mbali mno na kichwa chake. Kitu pekee alichokuwa na jibu lake ni kwamba mkasa huo ulimvutia katika kiza kizito zaidi, kinachotisha na kutatanisha.


Laiti ingekuwa hadithi tu, au ndoto, aamke kesho na kujikuta yuko Tanzania, katika chumba chake kilekile chenye kunguni na mbu. Lakini haikuwa ndoto. Alikuwa macho na akishuhudia au kujihusisha na vifo vya kikatili. Watu walikuwa wakiteketea. Nchi ilikuwa mashakani. Nuru alikuwa mikononi mwa mauti. Kisa na mkasa?


Wakati msongamano huo wa mawazo ukikisumbua kichwa chake, Joram alikuwa amekiacha kijiji kitambo na kuingia mjini. Tena, tamaa ilimshika ikimshawishi ageuze gari na kuelekea huko ambako aliamini angeweza kumkuta Nuru, amtoe mikononi mwa wauaji hao kwa gharama yoyote. Lakini roho nyingine ilimshikashika ikimtaka aiharishe safari hiyo na kusubiri wakati unaostahili. Hivyo, akalielekeza gari hotelini kwake. Akaliacha mtaa wa pili na kwenda hotelini kwa miguu.


Mapokezi alipewa karatasi yenye maagizo yaleyale; piga namba ileile mara ufikapo pamoja na kifurushi kingine kidogo. Ndani ya lifti alifungua kifurushi hicho. Mlikuwa na kidole kingine. Hakujishughulisha kukitazama kwa makini. Badala yake aliingia nacho hadi chumbani mwake ambamo alikitupia






mezani na kuwasha taa. Alipoyatupa macho yake kitandani hakuweza kuamini.


Juu ya kitanda hicho alilala mwanamke. Shuka laini alizojifunika hazikufaulu kufanya siri kuwa mwanamke huyo alikuwa kama alivyozaliwa. Mwili wake ulipendeza na kuvutia sana katika shuka hizo.


Hakuwa Nuru. Hilo Joram alikuwa na hakika nalo. Mwanamke huyu ni nani basi na aliingiaje katika chumba hiki ambacho kilikuwa kimefungwa? Na hasa anataka nini? Joram alimtazama kwa muda. Akasogea na kujiketisha juu ya kitanda taratibu. Kwa utulivu huohuo aliivuta shuka toka usoni mwa mgeni huyo na kumtazama. Alikuwa mwanamke wa makamo. Lakini uzuri ulikuwa wazi katika sura hiyo japo macho yalifumbwa. Nywele ndefu laini, nyusi nyingi nyeusi, pua pana iliyonyooka na kinywa kidogo cha kuvutia vilikuwa dalili tosha ya uzuri wa umbile la mwanamke huyo aliyelala kwa utulivu kama yuko kwake.


Joram alikuwa na hakika kuwa mtu huyo yuko macho. Alikuwa na hakika pia kuwa kuna jambo zaidi ya jambo ambalo lilimleta. Hakuonekana kuwa na haraka. Hivyo, Joram aliamua kumpa muda wote anaoutaka kwa kutomwamsha. Badala yake aliinuka taratibu kukiendea kitanda cha pili ili alale.


“Usinikimbie Joram,” sauti ya kike ikanong’ona ghafla.


Joram akageuka kumtazama.


Msemaji alikuwa akitabasamu alipoongeza, “Au naonekana mzee sana kwako?”




***


“Naonekana mzee?” aliuliza tena. Sasa alikuwa amekiacha kitanda chake na kusimama kama alivyozaliwa, akiyaruhusu macho ya Joram kutalii juu ya umbo lake. Alikuwa katika kila hali ya kujiamini, kwamba Joram asingekosa kuridhika na anachokiona. Na alikuwa na kila haki ya kujiamini kwani umri ulikuwa haujadokoa chochote cha haja katika umbo lake. Zaidi ya idadi ya miaka, bado alikuwa msichana. Matiti yake mekundu, laini yanayomeremeta yalikita kifuani kama yanayoshindana na wakati. Kiuno chake chembamba kilichokatika kama kinavyostahili kilikuwa daraja zuri lililounga umbo hilo na mapaja laini ambayo yalimeremeta kwa wekundu. Uzuri huo ulikamilishwa na sura nzuri ya kupendeza, yenye macho ya






kuvutia na kinywa cha kusisimua, kinywa kilichobeba tabasamu ambalo lilipendeza zadi kwa jinsi lilivyokuwa mchanganyiko wa haya, kushawishi na kubembeleza pamoja. Hata sauti yake sasa ilikuwa yenye haiba aliponong’ona, “Kama nimekuudhi…”


Joram hakuyasikia yote. Rohoni alikuwa akitaabika kwa kutiana mieleka na shetani wake ambaye alimtaka ainue mkono na kuugusa mwili huo ambao ulikuwa umejitunuku kwake. Alimtazama mama huyo kwa makini zaidi kwa nia ya kumtia aibu avae, aondoke zake. Lakini haikuwa hivyo. Kinyume chake, Joram alijikuta akizidiwa na tamaa kiasi cha kujikuta akijihurumia zaidi ya alivyokuwa akimhurumia mwanamama huyo. Kisha, Joram alikumbuka jambo. Alikumbuka kuwa alipata kumwona huko mbeleni mama huyo mzuri. Wapi vile? Wapi?


Asingeweza kukumbuka kikamilifu. Akili yake ilikuwa haifanyi kazi kikamilifu. Baadhi ya shurubu zilikuwa zikichezacheza huku nyingine zikikaza kuliko inavyostahili. Hata hakuiamini sauti yake alipouliza, “Kama nimepata kukuona mahala!”


Tabasamu la mama huyo lilipata nguvu zaidi. “Ndiyo,” alijibu akizidi kumsogelea Joram na kuketi kando yake. “Lakini, ya nini?” Aliuliza akiuchukua mkono wa Joram na kuanza kuchezea vidole. “Tuna usiku mrefu sana mbele yetu,” aliongeza taratibu. “Hadi kesho tutakuwa tumefahamiana vya kutosha.” Alikuwa havichezei tena ila kunyonya vidole vya Joram. “Uwe mwanangu mzuri,” sauti yake iliendelea kunong’ona kama kinanda.


Na sasa alikuwa amelishika titi lake na kumnyonyesha Joram. Lilikuwa zito, lililojaa, lenye uhai na joto, titi zuri, la mwanamke mzuri. Joram ni mwanaume shujaa. Lakini ni mwanaume kwanza, shujaa baadaye. Alikuwa na kila chembe ya udhaifu wa kiume. Yawezekana hali hiyo ilisababishwa na kutokuwepo mpenzi wake Nuru? Kwani muda si mrefu alijikuta akishuhudia mavazi yake yakitolewa moja baada ya jingine… alitaabika mikono hiyo laini ilipoanza kuteleza juu ya mwili wake katika kila kichochoro ambacho kilihifadhi faraja iliyoburudisha mwili na kuifariji roho… aliteseka zaidi mikono hiyo ilipoacha kazi hiyo na kinywa kuichukua, kililamba hapa, kunyonya pale na kuonja huku. Kisha…


“Wewe… wewe nani?...” Joram aliuliza kidhaifu. “Baadaye…”






“…Ndiyo… Baadaye.” alijibu akiushuhudia mkono wake mmoja, bila hiari yake, ukiuacha mwili wake na kusafiri hadi katika mwili wa mwanamke huyo, ukitomasa hapa na kupapasa pale. Mkono wa pili ulimtoroka na kusaidia kazi hiyo. Ni hapo lilipotokea jambo ambalo Joram hakulitegemea. Mwanamke huyo aliacha ghafla kufanya alichokuwa akifanya mwilini mwake na kutulia mara tu mguso wa Joram ulipomkolea. Kisha, ghafla mwili huo uliokuwa mtulivu ulianza kutetemeka kwa nguvu, huku akiangua kilio chembamba kwa sauti laini, machozi mengi yakimmiminika.


Kwanza, Joram hakuelewa. Alisita chochote alichokuwa akiutendea mwili wa mwanamke huyo na kumkazia macho ya mshangao. ‘Anakufa?’ alijiuliza. Kisha alielewa. Pamoja na orodha yake ndefu ya wanawake mbalimbali, wenye tabia mbalimbali kitandani huyu alikuwa mwanamke wake wa kwanza ambaye mahaba yangeweza kumwua. Alikuwa na njaa au kiu kubwa ya mahaba, kama mtu ambaye ameokotwa katikati ya jangwa baada ya siku nyingi ya ukosefu wa maji na chakula. Hayo Joram aliyafahamu baada ya kuisikia sauti yake dhaifu ikinong’ona, “Endelea…” mara alipoduwaa.


Aliendelea. Na ilikuwa safari ya kihistoria. Paa lingeweza kufunuka kwa kelele. Kitanda kingeweza kugeuka bahari kwa machozi… lakini aliendelea. Ni baada ya muda mrefu sana, ndipo waliachana lakini bado walikuwa wamekumbatiana.


Joram aliuiba mkono wake mmoja na kuutumia kuvuta kijimeza chenye sigara zake. Akauiba mkono wa pili na kujiwashia sigara moja. Alivuta huku akifikiri. Fikara zake zilikuwa nyingi, za kutatanisha na zilimhusu mwanamke huyo aliyelala ubavuni mwake. Hakuhitaji tena kumwuliza kuwa ni nani. Saa chache walizosumbuana kitandani zilifanya agundue kuwa huyo ni mke wa Abdul Shangwe, Rais wa nchi. Kitandani na mke wa Rais wa nchi! Hilo lilimtisha Joram, lakini halikumsumbua sana. Alijua kuwa mwanamke huyo alikuwa na yake, angeyajua kitambo si kirefu. Ambalo lilimsumbua Joram ni jinsi mwanamke huyo, pindi wakifanya mapenzi alivyosahau kuwa yuko na Joram Kiango, badala yake bila ya kujifahamu alilia “…Shubiri ….Shubiri…” sauti hii haikuwa ya hila. Ilitamkwa kimapenzi kabisa, toka katikati ya fungate la moyo wa mwanamke anayempenda. Ni hilo lililomtatanisha Joram. Alikuwa na kila hakika kuwa Shubiri






anayetajwa si mwingine zaidi ya Shubiri Makinda, Waziri Mkuu. Kwamba kuna mapenzi mazito kiasi hiki, baina ya mwanamke huyu na Shubiri, hilo Joram hakulitegemea. Pamoja na upelelezi wake mgumu, pamoja na vifo vya watu wengi, pamoja na marehemu mmoja kufa baada tu ya kutoa siri ya mapenzi haya bado Joram alikuwa na mashakamashaka juu ya ukweli wa suala hilo, mashaka ambayo yalianza kukamilika usiku huu baada ya kuonana na Shubiri ana kwa ana na kumwona alivyoyapuuza maswali yake yote. Ni hapo Joram alipoanza kushuku kuwa kuna jambo jingine zaidi ya mapenzi na tamaa ya vyeo katika mkasa huu. Lakini sasa mashaka hayo yalielekea kusambaratika tena na kumwacha palepale alipokuwa, katika lindi la bahari ya kutatanisha, yenye kiza na mashaka kwani mapenzi yalikuwa wazi katika macho na sauti ya mwanamke huyu. Mapenzi halisi. Au anaigiza? Aweza kuwa mwigizaji mzuri kiasi hicho? Naye Joram amekuwa kipofu na kiziwi kiasi gani hata ashindwe kuona nuru ya mapenzi halisi katika macho na tetemo la huba katika sauti ya mwanamke huyu? La. Lazima liko


jambo zaidi ya jambo.


Akanyoosha mkono na kupapasa titi lililoshiba, ambalo lilikuwa wazi likimtazama kama linalomdhihaki. Mtoto wa kike aliamka. Akafumbua macho na kuachia miayo mirefu. Kisha, alimtazama Joram. Tabasamu likaumeza ghafla moyo wake, tabasamu refu, pana, ambalo lilisema yote ambayo mwili wake ulipenda kusema. Yote, ingawa yalijumuishwa katika neno moja tu “Ahsante.” Naam, kuridhika kulikuwa wazi katika macho yake, kutosheka kukiwa dhahiri katika sauti yake alipoongeza kwa mnong’ono, “Sikujua, kumbe nimekuwa nikiusumbua bure mwili wangu katika kitanda cha mwanaume ambaye hajui thamani ya mwili wa mwanamke. Nusu ya maisha yangu imepotea bure kabisa. Damu ya ujana wangu imekauka bila thamani. Kama ningejua!”


Joram alimtazama. Macho yake maangavu, japo hayakudhihirisha hasira wala furaha, yalimfanya mama huyu akose raha na kunong’ona kitu kama “Samahani” ingawa Joram hakumsikia vizuri.


“Ulifikiri unafanya nini kujipenyeza chumbani humu kwa siri na kunisubiri uchi kitandani?” aliuliza. Mwanamke huyo alipochelewa kujibu Joram aliongeza, “Na unadhani ni heshima






kwa mke wa Rais wa nchi kubwa kama hii kujiuza kwa bei rahisi kiasi hicho?” mama huyo alipofunua mdomo wake kujibu Joram alimkatiza tena. “Usijisumbue kunidanganya. Naifahamu tabia ya wanawake wa aina yako. Umalaya na uongo ni mchezo wenu wa kawaida.”


Haja yake ilikuwa kumtia hasira na aibu. Kumpokonya ushujaa ambao alikuwa nao kwani Joram alikuwa na kila hakika kuwa tamaa ya mwili lisingekuwa jambo pekee lililomleta chumbani humo. Alikuwa mjumbe. Mjumbe wa nani? Ni hilo alilotaka kulifahamu. Ni hilo lililomfanya amruhusu mwanamke huyo kumchezea kimwili, ili apate siri. Hawakusema kuwa kitanda hakina siri?


“Nadhani huna haki ya kuniita malaya mapema kiasi hicho,” mwanamke alisema. “Kuwa mke wa Rais hakunifanyi kuwa mwanamke, mwenye kila udhaifu wa kike.” Alisita kwa muda. Halafu akaendelea, “Ningeomba uelewe kuwa niko hapa kwa ajili ya kuiokoa roho yako. Sikuwa na njia nyingine zaidi ya kujifanya mwanamke malaya na kumhonga mhudumu mmoja ili aniruhusu kukusubiri chumbani humu.”


“Mume wako…”


“Hana habari. Yuko nje ya nchi. Hukusoma gazeti la jana? Ameenda Ethiopia kuudhuria mkutano wa viongozi wa nchi huru. Nadhani atarudi leo.”


“Walinzi wako…”


“Kwao, sasa hivi niko nyumbani, chumbani kwangu; nikimsubiri mume wangu. Hakuna anayejua kuwa nilitumia mlango wa siri hadi nje ambako nilikodi gari iliyonileta hapa.”


“Na ni kipi kilichokuleta?” “Kuyaokoa maisha yako…” “Ongea kwa tuo, tafadhali.”


Mwanamke alimtazama Joram kwa utulivu. Kisha akatabasamu. “Kijana mzuri,” alisema. “Kwanza umejuaje kuwa mimi ni mke wa Rais?” aliuliza.


“Kwa jinsi unavyotapatapa kitandani kama samaki anayekaangwa hai,” Joram aliamua kumtusi tena. “Hakuna ambaye angeshindwa kufahamu.”


Kwa mshangao wake Joram hilo pia halikumkera mwanamke huyo. Ndio kwanza alicheka na na kusema, “Hujui. Usiku wa leo umekuwa wa aina yake katika maisha yangu. Sikutegemea…”



“Nielewe kuwa ulikuja kufaidi, au kuyaokoa maisha yangu?” “Kuyaokoa.”


“Kwa vipi?”


Ndipo ilipokuja ile hadithi ndefu, ya kale, ambayo Joram aliisubiri kwa hamu. Mwanamke alieleza taratibu bila haraka, tangu alipozaliwa akiwa pacha, yeye na ndugu yake Lulu; yeye akiitwa Tunu… “Tulipendana kama tulivyofanana. Tulikuwa radhi kuichangia punje ya mhindi kuliko kumwacha mmoja ale, mwingine akose.”


“Watu walisema kuwa tulikuwa wasichana wazuri. Walitutazama kwa tamaa na mshangao, jambo ambalo lilitufanya tuwe na kiburi sana, tukimringia kila mwanaume aliyemtaka yeyote kati yetu. Tuliringa sana, na tungeendelea kuringa kama asingetokea Abdul na Shubiri. Vijana hao, wazuri wa sura na tabia; wakiwa wanapendana kama tulivyopendana siye; tulijikuta tumefanya nao urafiki; urafiki uliozaa uchumba. Kama ndugu yangu Lulu asingekufa, tungefunga ndoa siku moja, saa moja…” “Kitu gani kilichosababisha kifo cha Lulu?” Joram alitaka


kujua.


“Mapenzi.” “Mapenzi?”


Tunu alisita kujibu na kumkazia macho Joram. “Unaweza kutunza siri?” aliuliza. “Jibu la swali lako ni siri ambayo nimeishi nayo miaka nenda rudi. Sijapata kumwambia mtu yeyote. Kila mtu anaamini kuwa alikufa kwa ajili ya kuchukuliwa na mto. Ni mimi tu ninayefahamu kuwa haikuwa ajali. Alijiua. Maiti yake ilitafunwa siku nyingi bila kuonekana. Ikaaminika kuwa ameliwa na mamba au viboko waliokuwa chini ya mto huo.”


Sauti yake ilimshangaza Joram. Kama kweli walipendana kiasi hicho vipi anazungumza kujiua kama anayesema “Kulala” I wapi dalili yoyote ya majonzi inavyowastahili wapendanao? Kwa sauti aliuliza, “Alijiua… kwa ajili ya mapenzi! Nifafanulie tafadhali.”


“Nisirinyinginenzitoambayonakuibia,”alieleza.“Nimekwambia kuwa tulimpenda Abdul na Shubiri? Sio kweli sana. Ukweli ni kwamba tulimpenda mmoja wao. Wote tulimpenda sana Shubiri. Lakini ilikuwa siri yetu. Tuliificha vilivyo. Tusingeweza kuwavunja mioyo kwani wao walikuwa zaidi ya chanda na pete. Hivyo, tukalazimika kuendelea kukubali uamuzi wao wa kutugawa kama mifugo Shubiri akiwa amenichagua mimi na






Abdul akimtaka ndugu yangu Lulu.


“Nadhani waliyapenda majina yetu tu kwani, kama nilivyosema awali, kwa sura tulikuwa sarafu kwa ya pili. Hivyo, tulikuwa tukiwachezea tulivyopenda. Leo mie nilijifanya Lulu, Lulu akawa Tunu, tukaandamana nao na kufanya yote waliyotaka kufanya. Hawakuiona tofauti yoyote, hata kitandani. Tungeweza kuendelea na mchezo wetu huo milele kama kisingetokea kipingamizi cha ndoa. Ingetulazimu kutengana. Tunu angelazimika kuwa Tunu na Lulu, Lulu. Ni hapo ulipozuka msiba wa mapenzi. Nani akawe Tunu wa Shubiri? Wote tulimpenda. Tukaamua kumkataa Abdul na kuolewa uke wenza kwa Shubiri lakini tulipomwambia hilo kwa siri, alitucheka na kutuomba tuache upuuzi. Tarehe ya harusi ilipokaribia ndipo Lulu alipoamua kujiua.”


Alisita kidogo, Joram alipokosa swali aliongeza, “Mimi nikiwa mchumba halisi wa Shubiri nilijikuta nikiwa na furaha kwa kifo cha ndugu yangu. Hata hivyo, furaha hiyo iliyeyuka nilipotakiwa na wazazi wangu kuolewa na Abdul badala ya Shubiri. Kisa? Atakuwa Rais wa nchi. Nilipomtaka Shubiri ushauri nilikuta nae kapambazika kama wazazi wangu “Siwezi kumyang’anya Rais mke,” alisema. Nilipomweleza kuwa mimi ni Tunu si Lulu hakunisikia. Baada ya kulia sana ndipo nilipoyaona machozi katika macho yake. Nikajua kuwa alinipenda sana. Ati ni hilo tu lililonifanya nikubali kuolewa na Abdul baada ya Shubiri kunisihi sana. Hata hivyo, ingawa miaka nenda rudi imepita, lakini bado nampenda Shubiri zaidi. Naye ananipenda. Iko siku haki itatawala ki-mapenzi baina yake na miye. Abdul amenikinaisha kabisa. Laiti angeupasua moyo wangu na kuuona ukweli huo, angeninyonga au kujinyonga mwenyewe.”


Alikuwa akisema kweli tupu. Hilo Joram hakuwa na shaka nalo. Mwanamke huyu asingekuwa hodari wa kutunga hadithi na bado awe fundi wa kuigiza kwa kiwango hicho. “Kwa nini humpendi Abdul? Ana kosa lipi?” alimwuliza.


“Ni mzembe sana kitandani. Anavyosifiwa hovyo na watu na kupendwa amefikia hatua ya kujipenda sana. Hata mwili wa mwanamke ukiwa uchi kando yake haupendi kama anavyojipenda. Inachukiza zaidi anapotaraji kusifiwa hata kwa uzembe huo, kisha asifiwe na mkewe.”


Joram alimwelewa. Baada ya kumtazama, tena kwa makini zaidi, aliuliza swali jingine, “Nadhani hukuja hapa kuniibia siri






hizo. Ulitaka kunionya. Sio?”


“Nimekuja kukuomba urudi kwenu. Maisha yako yapo hatarini sana, panda ndege ya kwanza leo hiihii.


Joram akacheka. “Usijisumbue kunitisha kwa maneno. Kwa taarifa yako nimekwishatishiwa kwa silaha na damu. Sitishiki kwa urahisi.”


“Sikusudii kukutisha. Nimekuja kukuomba.”


Joram akacheka tena, kicheko kingine cha kebehi. “Na unaweza kuniambia mapenzi yako kwangu yalianza lini, hata uhatarishe ndoa na hadhi yako kwa ajili ya kunionya?” alisukuma swali jingine. Alipoona Tunu akibabaika kulijibu aliongeza, “Pengine hilo si swali la maana kwa sasa. La muhimu, ambalo lingenifanya niamue kuondoka hapa ni iwapo utaniambia ukweli, ni nani aliyekutuma kwangu?”


“Nadhani, kulingana na sifa nilizozisikia juu yako umekwishamfahamu.”


“Sijamfahamu.”


“Ni mpenzi wa moyo wangu. Kila mtu anampenda kama ninavyompenda miye. Siku mbili tatu zijazo atachukua uongozi wa nchi hii. Siku chache baadaye tutakuwa mume na mke…”


Alikuwa akiongea kama anayeota, kana kwamba anaiomba miungu hilo litokee, si kama mtu anayewakilisha ujumbe muhimu ambao ametumwa kuuwakilisha. “Ni yeye aliyekutuma kuufikisha ujumbe huo kwangu?” Joram alimwuliza.


“Ndiyo,” alijibiwa. “Usiwe na shaka. Nenda zako uwanja wa ndege na utamkuta mkeo akikusubiri.”


“Ni yeye aliyekuambia hilo pia?” Tunu alikubali kwa kichwa.


Jibu lake lilimshangaza Joram. “Amekuambia lini maneno hayo?”


“Jana.”


“Saa ngapi?” “Usiku wa jana.”


Joram hakuhitaji kuongeza swali jingine ili kuthibitisha kuwa mwanamke huyo sasa alikuwa akisema uongo. Alikuwa na hakika kuwa Shubiri asingekuwa mwepesi kiasi hicho, katika usiku mmoja aonane na mke wa Rais wake kwa siri; usiku huohuo asafiri hadi kijijini ambako alijificha kwa sababu isiyoeleweka. Kilichomshangaza Joram ni kwa nini mwanamke






huyo alikuwa akimdanganya ilihali muda mfupi uliopita alikuwa akisema ukweli mtupu.


Huku akitabasamu Joram alisema, “Mama, hivi nimewahi kukuambia kuwa u-mwaname mzuri sana kwa sura?”


Pamoja na kushangazwa kwa badiliko hilo la ghafla, la mkondo wa maswali ya Joram, bado alionyesha kuburudishwa sana na maelezo hayo. Kama mwanamke yeyote mwingine yeye pia alipenda sana kusifiwa uzuri.


“U-malaya mzuri sana, wa sura na umbile,” Joram aliendela. “Hata hivyo, sina budi kukuambia kuwa roho yako ni mbaya kuliko shetani.” Akasita na kuacha tusi hilo lizame katika akili ya Tunu. “Ndiyo, shetani ni afadhali kuliko wewe…”


“Tafadhali,” Tunu alibadilika. “Sidhani kama una haki wala hadhi ya kunitukana kiasi hicho. Kujitupa kitandani mwako kusikufanye usahau kuwa mimi ni mke wa mkuu wa nchi hii. Tamko langu moja linatosha kukutupa gerezani kwa maisha yako yote yaliyosalia.”


“Linatosha pia kunitupa kaburini kama ulivyokusudia.” Tunu alionekana kama ambaye hakumwelewa Joram. “Wengi umekwishawapeleka kuzimu kabla ya wakati wao.


Mimi umeamua kunichelesha kidogo na kujisingizia mapenzi. Kama inavyomstahili kabisa shetani mzuri wa kike.”


“Sikuelewi…”


“Huwezi kuelewa.” Sasa alikuwa kama anafoka. “Utanielewa vipi wakati kuua mtu asiye na hatia kwako ni mchezo mdogo tu? Utaelewa vipi wakati kumtesa mwanamke mwenzio ni jambo dogo sana kwako?”


“Bado sijakuelewa.”


“Huwezi kuelewa,” Joram alisema tena akiinuka na kuiendea meza. Alimrudia Tunu huku akiwa ameshikilia lile kasha aliloletewa. Akalifungua na kutoa kidole, ambacho sasa kilianza kuelekea kuvunda. Akakisogeza mbele ya macho ya Tunu na kumwonyesha huku akisema, “Labda utafurahi zaidi kukiona hiki?”


“Nini hicho?” “Kidole.”


“Cha?” “Binadamu.”



Tunu alionekana kubadilika. Kitu kama kichefuchefu


kilionyesha dalili katika uso wake kiasi cha kumfanya ashindwe kutamka lolote ingawa alimtazama Joram kwa macho yenye maswali elfu moja.


“Ni kidole cha mpenzi wangu,” Joram alimpa moja ya majibu ya maswali hayo ambayo hayakutamkwa. “Hana hatia. Mmemteka nyara na kumtesa kiasi hiki bila kosa lolote, nia yenu ikiwa kunitisha niondoke nchini. Kwa taarifa yako, ukitaka kamwambie pia aliyekutuma, kwamba siondoki katika nchi hii bila kulipwa vidole vya mpenzi wangu na damu za watu wengi wasio na hatia. Ningependa pia mjue kuwa bei ya damu ni damu na deni la damu hulipwa kwa damu.”


Ilikuwa dhahiri kwa Joram Kiango kuwa Tunu hakuelewa chochote ambacho alieleza. Macho yake yalionyesha mshangao na kushitushwa sana na maelezo hayo lakini hakuna alichokielewa. Akaomba aelezwe kitu kizima, kwa tuo. Ndipo Joram akamsimulia, tangu alivyoitwa toka Tanzania; mjumbe huyo alivyoyapoteza maisha yake; Betty alivyochinjwa kama kuku; dereva teksi alivyouawa na wao kuponea chupuchupu; mateso aliyoyapata; mwalimu Puta alivyofariki kwa hasira na akamaliza kwa kumkumbusha juu ya vidole vya Nuru ambavyo vilikatwa bila huruma. “Nadhani umeelewa kwa nini unastahili kuitwa mwovu kuliko shetani. Kuwa kwako katika njama chafu kama hizi kunakufanya uwe mwanamke wa mwisho kwa roho nzuri ambaye anaishi duniani. Kwa kweli, nilistahili kukuua, mara tu nilipokutia machoni,” Joram alimaliza.


Macho yalimtoka pima Tunu. Alionekana kama ambaye hakushangazwa tu bali kutishwa sana na hadithi hiyo, kana kwamba hakuitegemea wala kuamini. Mara chozi lilimtoka na kuteleza juu ya shavu lake. Likafuatiwa na la pili. Joram aliamua kuitumia nafasi hiyo. “Kuyafanya maisha ya binadamu kama mifugo ni dhambi sana. Mtu yeyote ambaye anayafanya, pamoja na kujificha kwake katika fumbo lisiloelezeka, bado nitamtia mikononi na kuhakikisha anayalipia madhambi yake yote hapahapa duniani. Wewe uko katikati ya mgogoro huu, mpenzi u-kama ufunguo ambao unaweza kurahisisha kazi yangu. Unaonaje kama utaniambia kinachotokea?”


Tunu alijaribu kutabasamu, tabasamu ambalo lilimgomea na kufanya sura yake iwe katikati ya kicheko na kilio. Alijaribu kusema, neno likakataa kutamkika. Akausogeza mkono wake






na kuvuta saa yake ya dhahabu ambayo ilikuwa juu ya kijimeza. Alitahayari kuona kuwa ilikuwa yakaribia saa kumi na mbili za asubuhi. Mara moja akaamka na kuanza kuvaa nguo zake, suruali ya degrizi na tisheti nyepesi ya kijani ambayo iliyafanya matiti yake yasimame na kuvutia sana. Alizishughulikia nywele zake harakaharaka; kisha, akavaa miwani yake myeusi na kukifunika kichwa chake kwa kofia kubwa ya jua. Akasimama mbele ya kioo kujitazama. Aliyekuwa akionekana katika kioo hicho hakuwa mwingine wa mjini ambaye vijana wangemwita changudoa. Hakuna mtu ambaye angediriki kumshuku. Alimgeukia Joram na kumnongoneza kwa sauti ambayo ilimtoka kwa dhiki “Bado nakushauri urudi kwenu.”


“Siwezi…”


Tunu alisita na kufikiri kwa makini. Kisha, aliitazama tena saa yake. “Mungu wangu, muda umekwenda,” aliropoka. Akamgeukia Joram na kusema, “Unajua kuwa unacheza na kifo?”


“Siogopi kufa!”


“Ningependa kukusaidia,” aliendelea. “Ni hadithi ndefu sana. Muda haunitoshi. Unaweza kufika mtaa wa Lolongo, nyumba namba arobaini leo saa nne? Nitakuibia siri ambazo zitaitingisha nchi hii.”


Joram alikubali.


“Na iwapo utabadili mawazo na kwenda zako kwenu bado nitashukuru sana,” aliongeza. “Kwani kila dakika unayoishi katika nchi hii inakusogeza karibu zaidi na mauti yako.”


“Nitafika…” Joram alisisitiza. “Saa nne sio?”


***


Kwa Joram kiango, kuisubiri saa nne haikuwa kazi ndogo. Zaidi ya saa tano zilihitaji kuuawa kabla ya kuifikia saa nne. Saa tano ukiwa chali juu ya kitanda, katika nchi hiyo ambayo ilinuka maafa, ilikuwa sawa na kukisubiri kifo miaka mitano juu ya kitanda hichohicho.


Hata hivyo, hakuwa na jingine la kufanya. Kufunga virago vyake kwenda uwanja wa ndege kama alivyoshauriwa, ingekuwa aibu ambayo hakuwa tayari kuifanya. Angekuwa radhi kufa na kuzikwa ugenini zaidi ya kukimbia baada ya kufanywa juha kiasi hicho kwa sababu ambayo hakuifahamu, hasa baada ya maisha






ya watu wengi kuteketea kwa ajili yake. Na hasa kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuishinda kiu yake kubwa ya kulifumbua fumbo hili la kutatanisha.


Kwamba Nuru alikuwa huru, akimsubiri uwanja wa ndege hilo lilimsisimua Joram lakini halikumvutia. Pamoja na ukweli kwamba alifurahi Nuru kuwa hai, bado asingeruhusu kuwa chambo ambacho kingemshawishi kuondoka katika nchi hiyo kabla hajalipwa maovu yote aliyotendewa. Nuru si mgeni Tanzania. Acha atangulie. Watakutana baadaye, kama si Dar es salaam hata mbele ya milango ya kuingilia ahera.


Saa moja kasoro Joram alikiacha kitanda na kuingia bafuni. Toka huko alivaa na kwenda chumba cha maakul ambako alijiamsha kwa staftahi kamili, kisha akapitia magazeti mawili ya kila siku. Habari zilizoongoza gazeti hilo zilikuwa suala ambalo lilimfanya Joram alivamie gazeti hilo mara moja na kurudi nalo chumbani ambako aliketi na kulisoma kwa makini.


WAZIRI MKUU KUJIUZULU?


…Katika barua hiyo ambayo ndugu Shubiri amemwandikia Rais amedai kuwa hana sababu maalumu ya kujiuzulu kwake isipokuwa kujipumzisha tu. Akiwa mtu ambaye ni mmoja kati ya nguzo za nchi hii, aliyepigania uhuru tangu utoto wake na ambaye alifikiriwa kuongoza iwapo Rais atapumzika, uamuzi wake wa ghafla umemshangaza kila mtu. Gazeti hili limewasiliana na mawaziri wengi na kuwataka mawaidha yao. Kila mmoja ameonyesha kushangazwa na uamuzi huo. Rais alipohojiwa hakuwa na la kusema isipokuwa kwamba ameshangazwa na uamuzi huo na kuongeza kuwa leo saa nne za mchana kamati kuu ya nchi itakutana katika ukumbi wa Makao Makuu kulijadili suala hilo…


Joram aliisoma tena habari hiyo. Hakuelewa. Ulikuwa mwanzo au mwisho wa mchezo huu wa kutatanisha? Alijiuliza. Hakupata muda wa kujijibu. Mlango wake ulikuwa ukigongwa kwa nguvu. Kabla hajaitikia ulifunguka.


Waliingia askari wawili wenye vyeo vya Captain, bastola zao zikining’inia viunoni. Walimkagua kwa macho na kisha mmojawao, ambaye Joram aliona kuwa alifanana sana na samaki, alimwuliza kwa ukali, “Wewe ni Joram Kiango?”


“Kama ndiye?”


“Tumeamriwa kukuondoa nchini mara moja. Na ni kwa



usalama wako.”


“Nilidhani hiyo ni kazi ya askari wa uhamiaji,” alisema, “Zaidi, sijui kosa langu.”


Yule aliyefanana na askari alimjibu kwa ukali zaidi. “Hakuna muda wa kuyajibu maswali yako. Inuka uondoke.”


“Siruhusiwi kufunga vitu vyangu?”


“Huruhusiwi kugusa chochote,” aliyejibu ni yule aliyefanana na binadamu.


Joram aliwatazama kwa hasira, ingawa alikuwa akitabasamu. “Nadhani walao mnaweza kuniambia ni amri ya nani inayonitoa kinyama namna hii?” alisema akipima uwezekano wa kuwashughulikia. Isingekuwa kazi kubwa sana, lakini hakuwa tayari kuifanya chumbani humo. Alihitaji sana saa nne, na alitaka imkute akiwa hai na huru.


“Ukiuliza swali moja zaidi utatoka chumbani humu juu ya machela kama si jeneza,” aliyefanana na samaki alisema bila mzaha.


Joram alijisikia kucheka alipomtazama tena, hasa alivyonuna wakati alikuwa na kila hakika kuwa kiumbe huyo aliyekosewa kimaumbile hakuijua hata sababu moja inayofanya aamrishwe ghafla kiasi hicho. Badala ya kucheka akajisikia kumhurumia. Pengine akili yake ilifanana na ya samaki.







NENDA zako.” “Wapi?”


“Kokote. Uko huru.” Alipomwona kimya aliongeza, “Na ukichelewa hapa nitakutafuna hai kwa ajili ya mbwa wangu.”


Nuru hakuyaamini masikio yake. Alimtazama tena msemaji huyo, lile pande la mtu lenye macho ambayo yalibeba kila dalili ya ukatili na sauti yenye dalili zote za mwuaji, jitu ambalo liliutumia muda wake mwingi kumtesa, kumsimanga na kumdhihaki huku likichekelea. Naam, jitu ambalo si roho tu bali umbile lake li mbali sana na binadamu wa kawaida na karibu zaidi na shetani. Na ni jitu hilohilo ambalo sasa lilisimama kando ya mlango likiwa limeuacha wazi kumwamuru kwenda zake.


Kana kwamba lilisoma kutoamini katika macho ya Nuru jitu hilo lilicheka kicheko kinachoweza kumliza mtoto. Kisha, likasema, “Huamini tu? Nakwambia uko huru. Mpenzi wako anakusubiri Uwanja wa Ndege mrudi kwenu. Huamini?”


Kuamini! Hilo halikuwa tatizo la Nuru. Asingeshindwa kumwamini kiumbe huyo ambaye ulimi wake haujui neno lolote la mzaha. Kuamini halikuwa tatizo. Tatizo la Nuru lilikuwa hasira zake dhidi ya jitu hilo. Hakutegemea kama baada ya aibu na mateso yote yale, ilimstahili kuondoka kimyakimya na kwa amani kiasi hicho. Katika kipindi chote hicho, alikuwa akiomba kufia katika michezo ile ya hatari badala ya kutoka hai. Uhai






pia alikuwa akiuomba kwa nia moja tu; ya kulipiza kisasi. Vinginevyo, asingestahimili yote yale!...


Mbwa!


Walipomchukua toka hotelini, akiwa nusu mzoga, walimleta katika jumba hili kubwa lililofichika, na kumbwaga juu ya meza. Fahamu zilipomrudia alishangaa kujikuta katika hali kama hiyo, bila kamba wala ulinzi wowote wa haja. Mlinzi pekee aliyekuwa mlangoni ni jibwa kubwa jeusi ambalo lilikuwa likimtazama, domo wazi, udenda ukilitoka. Nuru alijitazama na kujinyoosha kuupima mwili wake. Akajiona mzima wa afya. Akajaribu kuinuka.


Ni hapo jibwa hilo lilipotoa mlio mdogo wa onyo. Nuru alimgeukia mbwa na kuupima uwezo wake ki-ulinzi. Alikuwa na dalili zote za mbwa aliyehitimu mafunzo yake.


Kareti ni moja kati ya michezo mingi ya Nuru na Joram wanapokuwa na wasaa. Wamejizoeza pia kucheza na mbwa. Nuru asingeshindwa kucheza na jibwa hili, japo lilitisha kiasi hicho. Hata hivyo, alijua kuwa lisingekufa kabla ya walao kubweka mara moja, jambo ambalo lingeweza kumfanya adui yake atokee ghafla. Hivyo, Nuru alisita na kusikiliza kwa makini. Zaidi ya kupumua kwa mbwa huyo hakusikia chochote. Ilipomdhihirikia kuwa jumba zima waliokuwemo ni yeye na mbwa aliamua kuuchukua uhuru wake.


Huku akiwa amemkazia macho mbwa aliinuka taratibu na kuketi juu ya meza hiyo. Mbwa alitoa onyo jingine kwa kukoroma taratibu. Nuru akachukua pande la ubao lililokuwa kando ya meza hiyo na kuinuka. Kisha, alilirusha bao hilo kumwelekea mbwa huku naye akiruka kumfuata. Matumaini yake yalikuwa kwamba mbwa angelidaka bao hilo kwa meno hili naye atumie fursa hiyo kumkaba koo. Hilo halikutokea. Mbwa alilikwepa bao hilo na kumdaka Nuru kwa kucha zake. Huku akikoroma kwa sauti nzito ya kutisha badala ya kumwuma Nuru, alianza kuyapambua mavazi yake kwa meno na kucha. Nuru alijaribu kujitetea kwa kumpiga mbwa huyo hapa na pale, lakini mbwa alikuwa mwepesi kuliko Nuru. Alikwepa kila pigo la Nuru na kuruka huku, kila alipotua alikuwa na kipande cha nguo yake.


Hilo Nuru hakulitegemea. Wala hakuwa amejifunza kupambana na mbwa anayeshambulia mavazi yake badala ya yeye mwenyewe. Alijitahidi kwa nguvu zake zote kupiga, akirusha






mateke, ngumi na hata vichwa, lakini bado hakufaulu kumpata mbwa huyo. Badala yake, dakika chache baadaye alijikuta kasimama kimya, uchi kama alivyozaliwa, mbele ya mbwa huyo ambaye sasa aliketi, akimtazama, domo wazi, kwa namna ya tabasamu.


Kama angekuwa mliaji, kama walivyo wanawake wengine, Nuru angeweza kulia; tena kwa sauti. Lakini kulia, machozi yamtoke, ni jambo ambalo lilimtokea kwa nadra sana. Hivyo, aliendelea kusimama palepale, akitweta kwa hasira; macho yake yakimtazama mbwa huyo kwa uadui mkubwa. Mbwa pia aliendelea kumtazama, lakini kwa namna tofauti. Sasa udenda ulikuwa ukimtoka mwingi zaidi, macho yakiwa yanalegea. ‘Anamtamani?’ Nuru alijiuliza kwa hofu na mshangao. ‘Mbwa anamtamani?’ Hilo ni jingine ambalo hakulitegemea. Kwa hasira zilizochanganyika na aibu, aligeuka na kuirudia meza ambako aliketi na kujaribu kujificha, kama alivyofanya mama yetu Hawa, baada ya kulila lile tunda ambalo lilituletea balaa.


Mbwa alimfuata Nuru kwa macho, tamaa sasa ikiwa wazi katika macho hayo. Hata sauti ndogo, ya mlio wa kitu kama maumivu au kubembeleza ilisikika ikimtoka mbwa huyo. Nuru alitamani tena apige kelele, lakini bado sauti haikuweza kumtoka. Akatamani afumbe macho. Lakini hakuthubutu. Asingeweza kumwamini mbwa huyo. Kwa mara ya kwanza maishani mwake akailaani bahati yake na kumlaumu mama yake aliyemleta duniani. Akailaani pia siku ambayo alimtia Joram machoni kwa mara ya kwanza. Balaa lilioje! Kwa nini akanyimwa moyo wa kike, wa kutulia nyumbani azae na kulea? Mbwa!


“Usiogope. Akela ni mbwa aliyeendelea sana,” sauti ilisema ghafla toka chumbani humo. Nuru alipogeuka macho yake yalikutana na yale yenye kebehi ya lile jitu baya kama mbwa wake. Lilikuwa limeingia chumbani humo kimyakimya, kama kivuli na kushuhudia kila kilichokuwa kikitokea. “Usimwogope kabisa mbwa huyu. Si mgeni kwa mabibi wa kibinadamu,” aliongeza.


Nuru hakupata kumwona binadamu mwingine mwenye sura mbaya kama hii, sura ambayo ilitisha, hasa kwa madevu yake yaliyofunika hata kifua na macho yake. Zaidi kilichomtisha ni hayo macho. Licha ya kwamba hayakuwa macho ya binadamu halisi, bado hayakuwa na dalili yoyote ya mwanaume mwenye






uwezo wa kutamani. Kwake Nuru, pamoja na uzuri wake, pamoja na kuwa kama alivyokuwa, alionekana kama maiti au kipande cha mti kilichotupwa. Ni hapo matumaini ya Nuru yalipozidi kudidimia. Alitaraji kuyaokoa maisha yake kwa silaha ya mwisho, silaha pekee ya mwanamke. Amlaghai mapenzi na, hatimaye, kupata fursa ya kutoroka au kuliangamiza, fursa ambayo sasa ilikuwa ndoto ya mchana, kwani pamoja na kuupenda uhai wake bado Nuru asingekubali binadamu duni kama huyo amguse; mtu ambaye machoni mwa Nuru angeweza kuwa ametoka moja kwa moja kaburini.


Jitu hilo lilikuwa likiendelea kucheka huku likizidi kumsogelea Nuru. “U mwanamke mzuri,” lilisema kwa sauti yake mbaya. “Mbwa wangu atafurahi sana kama nitamruhusu kujipatia chakula bora kama hiki.”


Mbwa! Nuru alitamani ardhi ipasuke, immeze.


Jitu hilo lilipomfikia liliuinua mkono wake na kuligusa titi la Nuru. Nuru alijaribu kuusukuma mkono huo. Ilikuwa sawa na kusukuma kipande cha chuma chenye kilo mia. Mkono huo uliliacha titi hilo na kuhamia la pili. Ghafla, ukaliacha titi hilo na kumshika penyewe. Nuru aliachia kibao kikali ambacho kilidakwa kama mchezo. Mkono ukaendelea kumchezea, huku jitu lenyewe likiwa halionyeshi dalili yoyote. Lingeweza kuwa linachezea kipande cha ubao!


Kisha, ghafla kama lilivyoanza lilimwacha Nuru na kusogea kando. Likatulia na kumtazama, huku likichekelea. Ni hapo lilipotokea jambo jingine ambalo Nuru hakulitegemea. Mwili wake ulianza kuwasha. Kila ambapo kono hilo lilipagusa paliwasha sana, kwa namna ya kuvutia. Kwanza, Nuru alijaribu kustahimili. Akashindwa. Akaanza kujikuna. Vidole vyake vilaini vikishuka toka kifuani hadi katikati ya miguu. Alijikuna huku akitetemeka na kulialia bila kujali tena aibu wala macho ya shetani huyo na mbwa wake.


Kila Nuru alivyotahabika na kujigeuzageuza kama anayehitaji mwanaume kwa nguvu zake zote, ndivyo jitu hilo lilivyozidi kuchekelea kwa furaha. Mara likakurupuka na kutoka chumbani humo. Liliporudi lilikuwa na kamera ya picha za video. Liliwasha na kumlenga Nuru. Nuru, hasira zilizidi kumpanda. Hata hivyo, hakuwa na hali. Alizidi kutaabika, machozi yakimtoka. Alivitumia vidole vyake kwa juhudi, havikumsaidia sana. Sasa hangeweza






hata kuliruhusu jitu hilo. Alilitazama kwa namna ya kuliambia hivyo, lakini halikuelekea. Starehe ya kumshuhudia Nuru akijinyonganyonga kama samaki anayekaangwa hai ilisisimua zaidi.


Ni mbwa peke yake ambaye alikuwa akitaabika pamoja na Nuru. Ulimi ulikuwa karibu udondoke, macho nusura yamtoke kwa tamaa. Alikuwa akimsogelea Nuru hatua moja baada ya moja. Sasa alikuwa amemfikia na kuanza kulialia kama mbwa kwa mbwa. Nuru alitamani alie kwa nguvu, paa lipasuke; apae na kutoweka. Aliomba tena ardhi ifunguke, immeze na kumfunika. Yote hayakutokea… badala yake sasa mbwa alikuwa akimlamba miguu! Ulimi wake ulikuwa ukipanda taratibu! Nuru alitamani ampige. Uwezo wa kufanya hivyo hakuwa nao. Jambo la kushangaza zaidi lilikuwa likimtokea. Alihisi ulimi huo ukifariji na kusaidia kumkuna. Alihisi akitamani kumkumbatia, lakini hakuthubutu.


Mbwa!


Alihisi akili zake zikipaa. Bila ya kujua atendalo alitokwa na teke kali lenye nguvu zake zote nyuma yake, teke ambalo lilimmaliza yeye mwenyewe na kumfanya apoteze fahamu.




***


Haya, sasa yuko hai. Na analoambiwa ni kwenda zake kwa amani kana kwamba hakuna lolote lililotokea. Kuondoka baada ya yote yale, hakuona kama ingewezekana. Ama aondoke chumbani humo akiwa maiti, ama aache maiti. Vinginevyo angewezaje kuyakabili macho ya Joram Kiango na walimwengu wengine? Hata hivyo, Nuru alijua wazi kuwa kuonyesha hasira zake kusingemsaidia. Hivyo, alichofanya ni kuuliza tena, kwa unyonge, “Kweli niko huru?”


“Nenda,” jitu lilinguruma likiufungua mlango. “Nje kuna gari ambalo litakupeleka Uwanja wa Ndege.” Lilimtazama tena Nuru na kuongeza, “Na ujihesabu mwanamke mwenye bahati kubwa duniani. Si kila mtu anayeingia humu hutoka hai.”


Hai! Baada ya unyama kama ule! Heri angekufa. Nuru aliwaza.


Akasema kwa sauti, “Sijui kama nikushukuru au la?”


Aliyatazama mavazi aliyokuwa amevaa. Sketi nzuri ya kijivu na kijikoti chake. Nuru alikuwa hakumbuki muda gani ulikuwa umepita tangu alipoanza kutendewa unyama hadi






sasa. Hakukumbuka chochote. Akatoka na kufuata mlango kwa mlango hadi nje ya jumba hilo.


Gari lililokuwa likimsubiri ilikuwa teksi aina ya Datsun. Dereva alikuwa kijana mfupi, mnene, ambaye alikuwa ameulalia usukani akisoma gazeti. Alikuwa mgonjwa wa wanawake. Mara tu alipomtia Nuru machoni hamu ya gazeti ilikwisha. Alifungua mlango wa pili na kumkaribisha ndani, huku akiruhusu meno yake yote kuonekana kwa tabasamu. “Sikujua kama abiria wangu angekuwa malaika,” alisema baada ya kuwasha gari.


“Mimi siyo malaika,” Nuru alimjibu, kichwani akianza kubuni mbinu za kisasi.


“Basi umefanana nao sana.” “Ulipata kuwaona?”


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog