Simulizi : Zawadi Ya Ushindi
Sehemu Ya Kwanza (1)
Simulizi : ZAWADI YA USHINDI
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
Sehemu ya 1
SHANGWE na vigelegele ambavyo viliutoka umati huu mkubwa vilipaa hewani na kujaza anga lote. Sauti za kila aina zilitamkwa kwa kila rangi kiasi
kwamba zilitoa kelele, si kelele za shangwe tena bali mngurumo ambao uliitetemesha ardhi. Naam, ilikuwa siku ya furaha, siku ambayo haitasahaulika, siku ambayo wazee waliusahau uzee wao na kujitoma uwanjani kifua mbele, wakikoroma mikoromo ambayo ilizaa ngurumo ya furaha, siku ambayo vijana waliikumbuka afya yao na kuihadharisha uwanjani kwa kurukaruka huku na huko huku, midomo yao ikiimba nyimbo za ushindi, siku ambayo hata watoto waliukana utoto wao na kujikuta katikati ya wazazi wao wakipiga vigelegele na kucheka.
Naam, siku ya siku! Nani ambaye asingefurahi leo? Siku ambayo mashujaa walikuwa wakirejea
toka katika ile safari yao ndefu ya kumwangamiza nduli, fashisti, dikteta Iddi Amini ambaye alikuwa ameivamia nchi na kuyahatarisha maisha ya mamia ya wananchi wasio na hatia.
Ngoma ziliendela kupigwa ingawa mlio wake ulitawaliwa na vifijo na vigelegele hata visisikike kabisa. Wachezaji waliendelea kucheza na kuimba ingawa macho ya wachezaji yalikuwa juu, kila mmoja akiwatazama wanajeshi ambao walikuwa wakiteremka toka katika magari yao yaliyokuwa yakiendelea kuwasili. Wanajeshi hao walipowasili walijiunga na wenzao katika magoma na vigelegele.
Kila mara mtu mmoja au wawili walionekana wakiiacha ngoma ghafla na kumkimbilia mwanajeshi ambaye ndio kwanza anateremka toka garini. Walimkumbatia na kuviringishana kwa furaha huku machozi ya faraja yakiwaponyoka na kuteleza mashavuni. Pengine alitokea mzee akajikongoja kumkimbilia mtu, alipomfikia alisita ghafla moyoni akinong’ona “siye.”
Hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu, lakini hatimaye ngoma zikatelekezwa na nyimbo kusahauliwa, kila mmoja akawa ama kamkumbatia huyu au kaduwaa akimtazama yule.
Waliolia kwa furaha walilia, waliocheka kwa faraja, walicheka. Baadhi walitulia wakitetemeka kwa hofu, mioyo yao ikiwa na imani yenye shaka: Atafika kweli? Atarudi salama? Mungu atajua…
***
Huyu aliteremka polepole, mzigo wake ukining’inia mgongoni. Kama wengine wote alikuwa amevaa mavazi rasmi ya kijeshi, mavazi ambayo yalimfanya aonekane si kama kichaka kinachotisha tu bali kadhalika kama chui anayeranda baada ya kuliangamiza windo lake. Alikuwa akitabasamu. Au tuseme alifahamu mwenyewe kuwa anatabasamu kwani haikuwa rahisi kwa mtu baki kufahamu. Hakuwa mgeni katika mji huu wa Dodoma. Ingawa si mzaliwa wa hapa lakini miaka minne aliyoishi hapa kama haikufaulu kumweka katika orodha ya wenyeji basi ilimfuta katika ile ya wageni. Hivyo, hakuwa na shaka ya kupokewa na watu aliowafahamu. Akatazama huko na huko kwa shahuku. Naam, haukupita muda kabla hajamwona mtu anayemfahamu. Mzee philipo Matayo, mfanyakazi mwenzake, alikuwa akimjia. Akajiandaa kumpokea kwa kuongeza ukubwa wa lile tabasamu lake huku akipanua mikono amkumbatie. Lakini ah! Mzee alimpita bila dalili yoyote ya kumfahamu. Alijaribu kumwita lakini sauti haikufua dafu miongoni mwa kelele nyingi zilizokuwepo. Pengine hakumwona! Aliwaza.
Sasa alitokea Luoga, jirani yake, kijana, ambaye kila jioni walizoea kuketi mbele ya nyumba yake wakicheza karata au kuzungumza tu. Huyu alikuwa akimjia huku kamkazia macho. Hakua na shaka kuwa anamwona. Walipokutana Luoga aligutuka kidogo alipoona akikumbatiwa. Akaduwaa katika hali ya mshangao kwa kukumbatiwa na mtu ambaye hakumfahamu
hata kidogo.
“Samahani, nadhani sijawahi kukuona,” alitamka baada ya kujikwanyua toka katika mikono hiyo yenye nguvu.
“Hunifahamu?” mwenzake alihoji kwa mshangao. “Hukumbuki? Humkumbuki mwenzio sikamona?”
Luoga hakuyaamini masikio yake. “Umesema nani? Sika! Ndio wewe sika!” alifoka badala ya kuuliza. Akamkazia macho kwa mara nyingine. Macho yake yalilakiwa na yote yale ambayo kwanza yalimtisha na kumshangaza. Sasa yalimuhuzunisha na kumsikitisha. Kwa muda akajisahau akiwa kamkodolea macho kama anayedhani yanamdanganya na kuota ndoto za mchana.
“Ah!” ikamtoka baada ya kimya hicho kirefu. “Mungu ni mkuu!” Kisha, kama anayetoroka kitisho ama anayeepukwa kutokwa na machozi hadharani aligeuka na kuondoka taratibu huku kajiinamia.
Kitendo cha Luoga kilitonesha au kukumbusha jeraha ambalo Sikamona alikuwa ameanza kulisahau. Hapana, si kulisahau bali kujaribu kufanya hivyo. Jeraha ambalo limekaa katikati ya roho na kuuvisha moyo wake msiba usiovulika wala kufarijika, msiba wa kupotelewa na kilicho chako na kuvisha usicho kitamani, kisichotamanika.
Yale mawazo ambayo yalikuwa yamemjia awali,
mawazo ambayo angeweza kuyatekeleza kama si askari mwenzake kumuwahi muda mfupi kabla ya kuyakamilisha ya kujiua, yakamrudia tena. Naam, ajiue. Angewezaje kuwakabili ndugu zake akiwa katika hali hii? Zaidi ya ndugu zake, Rusia! Angejitokeza mbele yake? Hapana asingekubali kushawishika tena. Lazima atekeleze. Lazima ajiue. Lazima… akafoka kimoyomoyo huku akianza kuondoka kasi.
Alipenya kati ya umati huu mkubwa bila ya kujali chochote. Hakushughulika kujitambulisha kwa waliomjua kadha wa kadha ambao aliwaona. Hakujali alipomwona mtu au watu ambao aliwaona. Hakujali alipomwona mtu au watu ambao waliduwaa wakimtazama kwa mshangao. Wala hakutahabika kuwatazama wale ambao walikumbatiana na jamaa zao wakisheherekea kuonana tena. Alikuwa na yake. Alifanya haraka kwenda asikokujua, akafanya kile ambacho alikijua fika kuwa kingemtenga na macho ya walimwengu milele, na hivyo kumnyima hiyo fursa ya kuchekwa na kusikitishwa kwa wakati mmoja.
Sasa alikuwa mbali kabisa na umati. Akasita kwa muda akijiuliza aende upande upi ambako angepata faragha tosha ya kulikamilisha lengo lake. Wapi? Makore? Tambuka reli? Chamwino? Hapana. Vichochoro vya One Way vinatosha. Silaha? Akafurahi alipokumbuka kuwa bado alikuwa na silaha zake zote. Akaondoka na kuanza kuelekea One Way huku ameridhika kabisa.
“Sika.”
Akagutuka kisha akajisahihisha mara moja. Si yeye anayeitwa. Nani awezaye kumfahamu katika hali yake hii mpya aliyonayo? Hakudhani. Akaendelea na safari yake akiwa katika mwendo wake uleule.
“Sika.”
Ilikuwa sauti ya kike. Yaekelea mwitaji alikuwa akimkimbilia. Hata hivyo, hakujishughulisha kugeuka.
“Sika!”
Sasa hakuwa na shaka kuwa ni yeye anayeitwa, kwani mwitaji alikuwa amemfikia na kumshika mkono. Ndipo alipogeuka na kumtazama.
“Rusia.” Akafoka kwa mshangao, bila ya kufahamu anachokifanya. Kiumbe wa mwisho kati ya wote ambao angependa kuonana nao akiwa katika hali hii! Kiumbe ambaye alikuwa hasa ndio kiini cha safari hii ili ajitenge nae milele! Kiumbe ambaye kabla hajaondoka kuelekea huko vitani alimnong’oneza “Utarudi salama… Utanikuta salama ili nikukabidhi zawadi yako…. Ya ushindi…” Kiumbe ambaye… kiumbe…
Hakujua awaze nini. Badala yake alijikuta ameusahau msiba wake na kubaki kimya akimtazama Rusia ambaye pia alisita akitweta kwa mbio alizopiga kumfuata. Uso wake maji ya kunde uliokuwa umezingirwa na nywele nyingi ulimfanya aonekane kama malkia machoni mwa
Sikamona.
“Sika, kwa nini ulikuwa ukinitoroka? Hujui kama siku zote hizi sikuwa na kheri wala afya kwa ajili yako? Sika…” akasita na kumwangukia kifuani. Sikamona akampokea na kumkumbatia kwa nguvu.
Kimya kilichofuata kilikuwa cha faraja. Yote yalikuwa yamesahaulika. Rusia alikuwa amefarijika kwa kumtia Sika wake mikononi baada ya miezi kadhaa ya hofu na mashaka ya kutomuona tena. Sikamona alikuwa ameusahau msiba wake na badala yake kujikuta, kama zamani, yumo katika kifua cha mchumba wake mpenzi. Wakajisahau kama alivyoyasahau macho ya wapita njia.
Kisha, Sikamona akajikumbuka. Akaikumbuka sura yake mpya. Akawaza harakaharaka na kuona kuwa mapenzi yake na Rusia sasa ni ndoto tu, ndoto ambayo kamwe isingetukia kuwa kweli. Ni hapo ambapo alimsukuma Rusia kando polepole na kuanza kuondoka zake.
“Sika! Kwa nini unanifanya hivi? Ni kosa lipi nililokukosea?” Rusia alihoji kwa uchungu ambao ulichanganyika na mshangao.
“Hapana, Rusia. Yaliyopita yamepita. Mapenzi yetu yalikuwa ndoto tu. Ndoto ambayo aslani haiwezi kuwa kweli. Sasa yamekwisha. Sikufahi…” alifoka kwa juhudi ambayo hakujua ilipotoka.
“Yaani… sijakuelewa Sika!” alimjibu kwa sauti yenye majonzi. “Labda huamini kuwa sikuwa na
furaha hata siku moja tangu ulipoondoka hadi leo baada ya kukusubiri kwa hamu kubwa huku nikisononeka mchana na usiku kucha nikilia kama mtoto mdogo. Una nini Sika, jamani?”
Sauti yake ilikuwa na huzuni. Ikamtia Sikamona huruma. Akamgeukia tena Rusia na kumwambia polepole, “Nadhani hujaniona vizuri mpenzi, ebu nitazame.”
Rusia akageuka kumtazama.
Ndio kwanza akashuhudia uharibifu uliokuwa umetendekea katika sura ya Sikamona. Kitu ambacho alikuwa akikitazama hakikustahili kuitwa uso wa binadamu bali kinyago cha Mmakonde ambaye ama hakuwa hodari wa kazi yake au alikusudia kuwashangaza watu. Pua lilikuwa limebomoka na kulalia upande, mdomo mmoja ulikuwa umekatika na kushonwashonwa na wa pili uliambatanishwa kwa shida sana na mashavu yake, jambo ambalo lilimfanya daima mate yawe yakitiririka hadi juu ya kovu hilo jeusi. Jicho moja halikuwepo. Nafasi yake ilimezwa na kovu zito, jeusi, ambalo lilionekana kama lililonona sana.
Hayo yalikuwa machache kati ya mengi ya kutisha na kusikitisha yaliyokuwamo katika uso huo. Kwa muda yalimfanya Rusia aduwae akimtazama Sikamona. Kisha ghafla akaangua kicheko.
UCHEKWA! Kisha na mtu kama Rusia! Ni jambo ambalo kamwe halikuigusa akili ya Sikamona.
Kwa kweli, tangu siku ile ambayo alitahamaki na kujikuta kavaa sura hii mpya alifahamu wazi kuwa amekwishakuwa kichekesho miongoni mwa watu. Hata hivyo, kicheko hicho alifahamu kuwa kingekuwa cha kusikitisha. Kila ambaye angemcheka kicheko chake kingekuwa cha uchungu. Wala asingemlaumu yeyote ambaye angemcheka kwani hata mwenyewe alijicheka kwa uchungu siku ile ambayo alijitazama katika kioo kwa mara ya kwanza.
Lakini kilikuwa kicheko cha uchungu. Na kila amchekaye alicheka kwa uchungu. Si kama kicheko na hili tabasamu la Rusia, tabasamu ambalo halina hata chembe ya huzuni kwa kipigo ambacho kimeutokea uso wake. Kwa kweli,
kadiri alivyoyafahamu mapenzi yake, alitegemea kumwona akilia kwa nguvu na aliamini kuwa kilio hicho kingekuwa sherehe ya mwisho kwa mapenzi yao, kwani baada ya kulia angemwepuka daima na kumkwepa kila wakutanapo. Na iwapo ingemtokea kumfumania mahala lazima Rusia angetoa visingizio kadhaa vya kumtoroka, kumbe sababu si nyingine zaidi ya kumwogopa, kumdharau na kutomwamini tena. Sika kwa kuifahamu fika sura yake ilivyo sasa alikuwa ameamua kitambo kuwa asingemlaumu Rusia kwa uamuzi huo.
Ni hayo ambayo yalimshawishi kujiua. Hakutaka kuyaona machozi ya Rusia yakimiminika hadharani kwa ajili yake. Wala hakuwa tayari kushuhudia mwisho wa mapenzi yao ukitokea katika hali kama hiyo. Wala usingekuwa mwisho wa mapenzi yao tu, bali pamoja na ule mwisho wa kumpata mpenzi mwingine yeyote duniani.
Kumbe alikosea. Alikosea kwa yote aliyofikiri. Badala ya mwisho wenye majonzi ambao aliutegemea, umetokea kuwa mwisho wa vicheko na tabasamu, vicheko vya dharau na tabasamu la kashfa. Tabasamu ambalo licha ya kudhihirisha kuwa sura yake haifai kabisa ni ushahidi tosha kuwa asingependeka milele. Kama Rusia kiumbe ambaye alidhani wanapendana, anamcheka watafanyaje wale wasiomjua? Wale ambao hawakuwahi kuitamani sura yake ilipokuwa timilifu? Mawazo hayo yalimwongezea mori wa kujiua upesi ajifiche, asipambane tena na nyuso
zenye huruma, unafiki na tabasamu zenye uchungu. Hakuwa tayari kuendelea kuishi. “Lazima afe… lazima…” alinong’ona kwa uchungu huku akianza kuondoka. Lakini baada ya kupiga hatua mbili tatu kizunguzungu kilimshika, akapepesuka na kuanguka chini. Alijikongoja kuinuka lakini akaanguka tena. Rusia alimuwahi na kumshika mkono, kumwongoza katika kivuli cha mti. Lakini Sikamona hakuhisi mikono hiyo. Wala fikara zake hazikupokea sauti wala ujumbe ambao Rusia alijaribu kumwambia. Badala yake hisia hizo zilikuwa zimehama ghafla na kusafiri maili nyingi nyuma ya wakati zikimfanya aone upya yote ambayo yalikuwa yamemsibu, yote yale ambayo yalimfanya aambulie kuvaa sura kama hii na kuishia kuchekwa na mtu wa mwisho katika wote aliowategemea kumcheka.
SIKU hiyo alikuwa ameamka mkakamavu mno. Alihisi afya na kujisikia uchangamfu mwili mzima. Alijisikia akicheka kimoyomoyo. Furaha iliyoje kuwa hai hali
ujana u kamili katika roho na nafsi yako? Aliwaza akichupa toka kitandania na kuvaa mavazi yake harakaharaka. Kisha, alikumbuka kuwa ilimpasa aoge. Kwani jana yake hakuwa amefanya hivyo kwa ajili ya uhaba wa maji. Akavua nguo zake na kujifunga taulo kiunoni. Akavuta ndala toka uvunguni na kuzipachika miguuni. Huyoo, akaelekea bafuni. Huko alikutana na mengine. Maji yalikuwa yamekatika tena. “Haya ndio matatizo ya mkoa huu.” Aliteta moyoni akirejea chumbani ambako alivaa tena nguo zake. Akasugua meno na uso kwa maji ya chupa kisha akaondoka zake kuelekea kazini.
Vinginenvyo, ilikuwa asubuhi njema vilevile,
asubuhi ambayo iliendana vilivyo na hali yake, asubuhi yenye hali ya hewa nyepesi, yenye ule ubaridi unaofariji na kuburudisha.
Kwa mwendo wake wa hatua ndefu aliuacha mtaa wake wa Iringa na kujikuta katikati ya mji wa Dodoma, mji ambao unakusudiwa baadaye uwe Makao Makuu ya Chama na Serikali. Tahamaki akajikuta tayari amewasili kazini kwake CDA, alipita mlangoni na kuiendea ofisi yake huku akipiga mluzi, akiimba wimbo wa mwanamuziki mmoja maarufu duniani.
“Makini kabisa,” alizijibu salamu za wafanyakazi wenzake.
“Vipi! Mbona unaoneka mchangamfu sana leo?” mmoja wao alimtania. “Au ndio umepiga maji alfajiri?”
Alimjibu huku akicheka “Tangu lini nikanywa pombe? Ni kawaida yangu kufurahi na kwa nini ninune? Nna wasiwasi gani mie? Niko huru, katika nchi huru.”
“Wacha, bwana. Mbona jana tu hukutaka kuzungumza na mtu?” Mfanyakazi huyo aliendelea kutania. “Kama hukulewa basi umeshinda bahati nasibu, zawadi ya kwanza.”
Wakacheka kwa nguvu Kisha wakazama kazini.
Saa za kazi zilipokatika Sikamona hakupoteza muda wake. Alifanya haraka kurejea nyumbani kwa mwendo uleule alioujia. Jua lilikuwa kali
na joto jingi, siku zote joto hili lilimuudhi na kumfanya achukie kuishi hapa.
Asingesahau wakati alipotoka kwao Iringa na kuhamia hapa. Siku ile ya kwanza tu alilakiwa na joto kali ajabu. Alipokimbilia bafuni ili aoge alikuta bomba kavu likikoroma kana kwamba linamdhihaki. Usumbufu huo alidhani ungemtia kichaa. Lakini haikutokea kuwa hivyo. Badala yake alijikuta akizoea na kujifunza ustahimilivu.
Lakini leo joto hilo hakuliona hata chembe. Kwani hali ilikuwa ya kawaida, hali ambayo haikuwa na maudhi wala ukatili wowote. Amani, furaha, afya na starehe iliyojaa katika moyo wake ilikuwa vimelimeza kabisa tishio lolote la joto na vumbi ambalo lilikuwa likipeperuka huku na huko.
Kisha, aliishuku furaha yake. Ni kweli kisa cha furaha yote hii ni ujana, uhai na afya peke yake? Haiwezekani. Alijikanusha. Angekuwa mnafiki mkubwa kudai hivyo kwani alifahamu fika asili hasa ya furaha hii ilikuwa ile shahuku ya mkutano wake na Rusia jioni ya leo, mkutano ambao waliuandaa jana ukiwa na ajenda moja tu, kupanga lini wafunge ndoa.
Ni hilo ambalo lilizaa furaha rohoni mwake na kufichua afya katika ganzi yake kwani hilo ndilo lililokuwa njaa yake ya kila siku, njaa isiyoshibika kila usiku hakupata usingizi unaomstahili kwa ajili ya kutokuwa na Rusia. Na mchana aliona hauna amani kwake bila ya Rusia kuwa mbele yake. Sasa maadamu siku ya njaa hiyo kudidimia
milele ilikuwa imewadia angekosaje kusahau joto na kudharau jua? Angeshindwaje kuikumbuka afya yake na kuuona ujana wake?
Jioni baada ya kula na kuyaoga yale maji aliyokuwa ameyaifadhi kwa ajili ya dharura alijikuta mitaani. Mguu na njia akielekea Makole kumchukua Rusia. Alijilazimisha kadiri ya uwezo wake kupunguza mwendo ingawa hakufaulu. Mara kwa mara alijifumania kakaza mwendo kupita kiasi hali saa ikimwambia muda walioahidiana ulikuwa mbali.
Njiani alikuta vikundivikundi vya watu wakizungumza kwa sauti ambazo hazikuwa za kawaida. Akahisi lipo jambo lililotokea. Lakini hakuwa na muda wa kujiingiza katika magenge na kuanza maongezi. Aliendelea na safari yake, hatua moja baada ya nyingine.
Mbele yake kulikuwa na watoto wawili. Walikuwa wakienda huku wakizungumza jambo ambalo ingawa hakulielewa, lakini alilisikia kikamilifu.
“Wacha bwana!”
“Kweli kabisa. Atapigwa hadi aone haya.” “Unamtania Idd Amini! Afrika nzima hamna
shujaa kama yeye.”
“Nakwambia atapigwa!” ilikuwa sauti isiyo na shaka. “Ngoja uone. Jeshi letu rafiki yangu ni la pekee. Hivi hujasikia ile methali ‘Debe tupu alihachi kuvuma?’ Ana bahati mbaya sana Amini.
“Siamini.”
“Utaamini tu.”
Sikamona aliwapita na kwenda zake. Maongezi ya Idd Amini yalikuwa yamemchosha siku nyingi, Kwa kadiri alivyofahamu Amini alitawala maongezi si hapa tu bali duniani kote. Vyombo vya habari daima havikukosa cha kuandika juu yake.
Alipoitazama tena saa yake ilimshauri kuongeza mwendo. Akafanya hivyo. Haukupita muda mrefu kabla ya kuwasili mbele ya nyumba yao Rusia. Ule ushujaa aliokuwa nao moyoni ukaanza kudididimia. Siku zote hali hii ilimtokea kila alipokabiliwa na jukumu la kugonga mlango wa nyumba hii, mlango wa akina Rusia. Ukweni, aliwaza akicheka kimoyomoyo. Hata hivyo, baada ya dakika mbili za kujishauri, jitihada zilishinda hofu yake. Akagonga. Bahati ilikuwa upande wake. Aliyefungua mlango hakuwa mwingine zaidi ya Rusia.
Alihisi uso wa Rusia hauna ile hali ambayo huwa nayo siku zote.
Kwa nini? Akajiuliza.
Alikaribishwa ndani ambako aliongozwa hadi chumbani kwa mchumba wake.
“habari za hapa?” alihoji baada ya kuketi kitandani.
“Kidogo nzuri.”
Sauti ya Rusia kadhalika ilikuwa na upungufu fulani katika masikio yake
“Una hakika ni nzuri?” Alihoji tena ili kufukuza ukimya ambao ulianza kutanda.
“Bila shaka, wewe waonaje kwani?” Rusia aliuliza akijiketisha kando yake. Sauti yake ilibishana na maneno yale.
“Sioni kama una hali ya kawaida.” Kimya kikawateka tena.
Ni katika kimya hiki sikamona alipoigundua ile siri ambayo siku zote alikuwa akijuliza juu ya mafanikio, siri ya mapenzi yake kwa Rusia, yaani sababu hasa iliyomfaya ampende na kuamua awe mwandani wake milele. Hakupata kuifahamu hadi leo baada ya kumwona Rusia akiwa amenuna kinyume cha kawaida yake.
Kumbe hakuna kilichomvutia zaidi ya ule uchangamfu na tabasamu zake ambazo hazikukoma kububujika kila wakutanapo, kila siku, isipokuwa leo.
Sio kweli kudai kuwa Rusia hakuwa mzuri. Alikuwa mzuri. Mzuri zaidi ya wazuri wengi. Alijaliwa uso mpana ambao ulibeba pua nyofu, mashavu wastani yaliyonona, macho maangavu yanayocheka daima. Umbo lake kadhalika halikuitupa sura. Lilikuwa lile lenye urefu wa kadri na unene wa kadri kama unavyomtshili kabisa mwanamke. Mavazi yake hali kadhalika, yalikuwa kiungo ambacho kilitumika kukamilisha ubora wake. Hakuvaa kiuni wala hakutegemea kuvaa nguo fupi na kujipamba kwa bidhaa zitokazo kiwandani ili kuongeza uzuri.
Siku moja aliwahi kumwambia Sikamona juu ya hilo, “Tabia hiyo ni moja ya utekaji nyara, unamlazimisha mtu akuhusudu bila ihari. Haikuwa uongo, nguo zake zilikuwa za heshima, nywele zake asilia, ngozi yake ya kuzaliwa lakini alimvutia kuliko wengi ambao walitumia maelfu ya pesa kujitengeneza. Machoni mwa Sikamona alivutia kuliko wote.
Hata hivyo, si hayo tu yaliyomfanya Sikamona ajikute hana heri bila kumwona kwani mwenye sura na tabia nyofu kama hiyo hakuwa peke yake. Walikuwa wengi. Wengi tosha. Sikamona aliwastahi wote na kuwahusudu lakini hakuwapenda wala kuwaza chochote juu yao zaidi ya ile hadhi ya kawaida isipokuwa Rusia.
Mapenzi yao na hatimaye, uchumba ni vitu ambavyo vilitokea kama muujiza
***
Ilikuwa asubuhi moja yenye kila hali ambayo Sikamnoa haipendi. Mawingu yalikuwa yametanda angani bila dalili yoyote nyingine ya mvua kunyesha. Mingurumo hafifu ilisikika mara Kusini mara Kaskazini na kuzidi kuchafua mandhari. Sikamona alikuwa njiani kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa shughuli za kikazi. Alipoingia ofisi aliyoihitaji alipokelewa na karani ambaye alimlaki kwa namna ambayo hakuwahi kulakiwa huko nyuma. Ukarimu, heshima na zaidi ya ya yote tabasamu laini vilichangia katika kumkaribisha. Ni tabasamu ambalo lilimkoga
Sikamona vilivyo. Lilkuwa tabasamu ambalo lilimfanya ajisikie mwenyeji ghafla kiasi cha kujiona kama yuko nyumbani kwake.
“Naitwa Sikamona.” Alijitambulisa pasi ya kutegemea.
“Ndio. Ndio. Nami jina langu Rusia. Rusia Rashidi.”
Kwa muda Sikamona akajisahau na kujikuta ameketi akimwuliza Rusia habari ambazo hazikuhusiana kabisa na shughuli za kikazi zilizomleta. Baada ya muda alihoji lile swali ambalo lilimtatiza tangu alipokaribishwa “Hivi uliwahi kuniona huko mbeleni?”
“Hapana, kwa nini?”
“Kwa jinsi ulivyonikaribisha. Nilidhani wanifahamu.”
Tabasamu la Rusia likageuka kicheko.
“Hata mimi nilidhani wewe wanifahamu. Niliona uso wako una dalili zote za kujuana.”
Wakacheka
Kisha Sikamona akaongeza harakaharaka, “Najua tulikowahi kuonana
“Wapi?” “Ndotoni.” Wakacheka tena
Yalifuata maongezi marefu, wakiongea hili na lile hadi mgeni, ambaye alikuwa akizungumza
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment