Search This Blog

Thursday 29 December 2022

BOMU - 3

   

Simulizi : Bomu 

Sehemu Ya Tatu (3)




"Ni watu gani hao?" Adrian alirukia.




"Ni mkuu wa majeshi, mkuu wa Polisi, Chifu, wewe, Daniel ama Hannan. Watu hao sababu ndio pekee walijua kuchaguliwa kwangu katika misheni hii. Nahisi aliyepanga mpango wa kuiteka familia yangu yupo kati ya watu hao sita" David alisema kwa uhakika.




Daniel na Adrian walitazamana kupitia kioo cha kati. Kipindi hiko walikuwa wanapita juu ya daraja la Kigamboni wakiifatilia ile gari.




"David umeongea jambo zito sana. Lakini tutalifanyia kazi tujue ni nani yupo nyuma ya hawa watu." Daniel alisema.




"Hiyo namba ukiyowasiliana nayo iko wapi?" Adrian aliuliza.




"Hii hapa" David alisema huku akiitoa simu yake mfukoni.




"Ninamuhitaji sana Hannan kipindi hiki. Ni yeye ndiye angeichunguza hii namba ya nani? Tumpoteza Hannan, lakini hii kazi lazima iendelee. Ngoja nimpigie Mwanasheria mlevi, najua kwasasa yupo katika kitengo cha mawasiliano pale usalama wa Taifa. Ni yeye ndiye atakayetupa majibu wa ukweli juu ya namba hii" Daniel aliwaza.




"Naomba simu yako nimpigie mtu" Daniel alisema.




"Usiitumie simu yangu Daniel, wameitrack. Watasikia kila kitu" David alisema.




"Nipe simu yako Adrian tumpigie Mwanasheria mlevi..." Daniel alisema.




Je nini kitatokea? Msaliti mwingine ni nani eti? Tuwe wote katika sehemu ijayo.




Ukimaliza kusoma like na comment. Wewe unayesoma bila kutoa maoni unafanya simulizi hii ichelewe.






Songelael Ntenga P.A.K Mwanasheria mlevi alikuwa amekaa makao makuu ya usalama wa Taifa. Alikuwa amekaa ofisini, mbele yake kukiwa na meza kubwa yenye mafaili mbalimbali, yakiyopepewa na upepo wa feni.




"Sijazoea kabisa hizi kazi za kukaa ofisini. Mi furaha yangu ni kuwa katika hekaheka mtaani na kuwasaka wahalifu. Lakini kwasasa Chifu amenipa heshima kubwa sana ya kuwa mkuu wa kitengo cha mawasiliano hapa makao makuu. Lakini, roho yangu haijakongeka hata kidogo. Nimemiss sana mikimiki ya mitaani, na kufumbua mafumbo magumu yanayoumiza kichwa. Naupenda sana upelelezi..Hakuna ka.." Mwanasheria mlevi akakatishwa katika mawazo yake. Simu yake ya mkononi iliyokuwa juu ya faili moja, ilikuwa inaita.




"Nani huyu anayenipigia simu? Namba hii wanaojua ni watu wachache sana, lakini sio namba ngeni?" Mwanasheria mlevi alijiuliza.




Akaipokea.




"Daniel Mwaseba hapa naongea" Sauti ilisema simuni.




"Daniel, kulikoni? Mbona umenipigia kwa namba ngeni?" Mwanasheria mlevi aliuliza.




"Tutaongea kwa kirefu baadae Mwanasheria. Lakini kwa sasa kuna kazi moja naomba uisaidie" Daniel aliongea harakaharaka.




"Kazi gani hiyo Daniel?" Mwanasheria aliuliza.




"Najua kwasasa upo katika kitengo cha mawasiliano hapo makao makuu. Sasa kuna namba moja ya simu nataka uichunguze. Nataka unambie namba hiyo inamilikiwa na nani? Na watu gani inayowasiliana nao mara kwa mara?" Daniel alisema.




"Nitumie hiyo namba Daniel. Hesabu hilo limekwisha. Nitakupa majibu soon. Eeh nambie kingine unachohitaji kutoka kwangu?" Mwansheria aliuliza.




"Kwasasa nahitaji hilo tu la namba. Ni muhimu sana, nikitaka kitu kingine nitawasiliana na wewe" Daniel alisema.




"Halafu unadrive Daniel? Unaenda kwa kimada nini?" Mwanasheria mlevi alibadili namba.




"Hapana, ila nipo kwenye gari. Kuna wachawi ninawafukuzia hapa"




Mwanasheria mlevi akapiga ngumi ya nguvu katika meza.




"Nimemiss sana maisha hayo!" Akasema kwa hisia.




Daniel Mwaseba alikuwa ameshakata simu.




Muda huohuo, Mwanasheria mlevi akatoka mle ofisini. Akaenda kwenye chumba cha pili ambapo kulikuwa na kompyuta mbili katika meza tofauti. Akaenda kukaa katika kiti, mbele ya kompyuta mojawapo. Sekunde hiyohiyo, mlio wa meseji ulisikika katika simu yake. Ilikuwa ni namba ya simu aliyotumiwa na Daniel Mwaseba. Akaingiza ile namba katika kompyuta ambayo ilikuwa na program ya kutambua namba za watu.




Majibu aliyokutana nayo huko...yalimwacha mdomo wazi....




***




Viongozi mbalimbali walikuwa wamejaa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Ilikuwa ni siku maalum ambayo rais Mgaya alikuwa amemaliza ziara ya wiki moja nchini Nigeria, hivyo anarejea nyumbani. Ziara ya wiki moja nchini Nigeria iliisha kwa mafanikio makubwa sana, baada ya rais Mgaya na rais Abayo wa Nigeria kusaini mikataba mikubwa mbalimbali ya ushirikiano, lakini mkataba mkuwa ulikuwa ni ushirikiano katika suala la mafuta.




Itifaki ilizingatiwa katika uwanja wa ndege. Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kama mkuu wa mkoa mwenyeji alikuwa amesimama na viongozi mbalimbali. Makamu wa rais, waziri mkuu, spika wa bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na jaji mkuu walikuwa wakipiga makofi wakati rais Mgaya akishuka ndani ya ndege ya shirika la ndege la Tanzania.




Vikundi mbalimbali vya ngoma vilikuwa vinaburudisha pale uwanjani. Huku wanasarakasi nao wakibiringita ardhini kuonesha umahiri wao.




Rais Mgaya, aliyekuwa amevaa suti nzuri ya kijivu. Alikuwa anashuka katika ngazi ndefu za ndege akifuatiwa na walinzi wake kwa nyuma. Alionekana ni mtu mwenye furaha machoni kwa kumwangalia, hakuna aliyekuwa anajua lililokuwa linapita kichwani mwake. Alikuwa hana furaha hata chembe.




Pale uwanja wa ndege ilifanyika hafla fupi ya pongezi. Viongozi mbalimbali walihutubia, na mwishoni kabisa hotuba ikimaliziwa na mheshimiwa rais Mgaya.




Baada ya hotuba hiyo, msafara ulianza kuelekea ikulu. Ndani ya gari rais Mgaya alitulia kimya. Alionekana ndani ya gari kimwili, lakini mawazo yake yalikuwa yanawaza kitu kimoja tu, Dr Luis.




"Mzee Msangi ameniangusha sana katika kazi hii. Nimemtumia katika kazi zangu za siri nyingi na ngumu sana. Lakini nashangaa ameshindwa kufanya kazi hii ndogo sana. Kazi ilikuwa ni kumteka Dr Luis na kumuua!!.


Zoezi la kwanza lilifanikiwa kwa ufanisi mkubwa sana, sasa iweje washindwe kumuua mtu aliyekuwa mikononi mwao?.


Ni kosa kubwa sana amefanya, haitakiwi hata kidogo Dr Luis awe hai. Siku akifumbua mdomo wake na kusema siri zangu. Basi ndoto ya kugombea awamu ya pili ya urais itakuwa imefutika. Na hilo sitaki litokee kwa namna yoyote ile. Nitatumia nguvu zangu zote kama rais kuhakikisha Dr Luis anakufa!




Nilitegemea kupokea simu ya mzee Msangi kuwa zoezi limekamilika, eti ananambia Dr Luis ametoroshwa na Imma Ogbo.




Who is Immanuel Ogbo. Ni rais Abayo wa Nigeria ndiye aliyenitambulisha kwa mtu anayeitwa Imma Ogbo. Nikifika Ikulu nitampia simu nimweleze kitendo alichokifanya mtu wake. Hakutumwa kuja kufanya kazi ya kuteka watu hapa..." Rais Mgaya alikatishwa mawazo yake na simu.




Alikuwa ni mkuu wa Polisi IGP John Rondo.




"Shikamoo mheshimiwa rais" IGP Rondo aliamkia.




"Marhaba IGP, vipi mnaendeleaje na kazi ya kumtafuta Dr Luis?" Rais Mgaya aliuliza.




"Na hilo ndilo lililonifanya nikupigie mheshimiwa rais. Nimeongea na Daniel Mwaseba sasahivi. Anasema zoezi linaenda kufika mwisho. Hivi sasa wanaenda mahali alipofichwa Dr Luis huko Kigamboni. Hivyo Dr Luis atakuwa mikononi mwetu sio muda mrefu kutokea sasa" IGP Rondo alisema.




"Kazi nzuri sana IGP wangu. Mimi nipo njiani naelekea ikulu. Nitakupigia nitakapofika ikulu" Rais Mgaya alisema na kukata simu.


Alikuwa ameyakatisha maongezi harakaharaka kwa makusudi.




Kisha akampigia simu mzee Msangi....








Mzee Msangi alikuwa amechanganyikiwa sana, sigara aliyokuwa anaivuta ilikuwa ni sigara ya kumi na tatu tangu Imma Ogbo amtoroshe Dr Luis kitalu B. Alikuwa anazunguka meza ya ofisi yake huku akiteketeza sigara isivyo kawaida. Kichwa chake kilikuwa na mambo mengi sana, lakini jambo kuu ilikuwa ni kutoroshwa kwa Dr Luis na Imma Ogbo.




Wakati akiwa katika mzunguko wake mwengine wa meza, mara simu yake iliita. Aliitoa simu yake mfukoni na kuiangalia. Alikuwa rais Mgaya..


Akaipokea.




"Hallo Mheshimiwa rais" Alisema simuni.




"Mzee Msangi mnafanya kitu gani? Mbona umekuwa mpuuzi kiasi hiki safari hii?" Rais Mgaya alisema kwa hasira.




"Kuna nini mheshimiwa rais? Msako wa Dr Luis unaendelea vizuri. Namsubiri Mark hapa tukaanze msako. Tutatampata tu hakuna tatizo. Au kuna tatizo gani tena?" Mzee Msangi aliuliza.




"Mzee Msangi mnafanyaje kazi ninyi? Kikosi cha B1 kimegundua mahali alipofichwa Dr Luis, na sasa kipo njiani wanakuja Kitalu B!" Rais Mgaya alisema.




"Wamepagundua Kitalu B? Kivipi? Hii ni nyumba ya siri na tunafanya mambo yetu kwa siri sana, ni ngumu sana kupagundua hapa jinsi palivyo. Sasa Bi wamepangunduaje?" Mzee Msangi aliuliza.




"Huu sio muda wa kuulizana maswali. Huu ni muda wa utekelezaji. Lipua kwa Bomu hiyo nyumba haraka sana!!. Nanyi mhamie kitalu C haraka iwezekenavyo. Mtafanya kazi hii kutokea kitalu C" Rais Mgaya alisema.




"Sawa mheshimiwa nimekuelewa" Mzee Msangi alisema.


Simu ikakatwa.




Msafara wa Mark the sniper ulikuwa unakaribia katika makazi yao, kitalu B kama walipozoea kupaita. Mara walianza kuona moshi mkali ukiwa juu ya anga.




"Motooo!!" Mark aliropoka.




"Kitalu B kinaungua" Mwenzie aliyekuwa pembeni alisema.




"Afanalek!!, nani kachoma moto kitalu B?" Mark aliuliza swali ambalo hakukuwa mwenye majibu.




"Tusiende pale, ni hatari!" Jamaa aliyekaa siti ya pembeni mwa dereva alisema.




"Lazima twende Elia ! Pale tuliacha wenzetu wapo katika hali gani?" Mark alisema.




"Ni hatari Mark.." Yule jamaa aliyekuwa pembeni alikatishwa na simu ya Mark. Mzee Msangi alikuwa anapiga.




"Mark tukutane kitalu C sasahivi" Mzee Msangi alisema harakaharaka na kukata simu.




"Amenipigia mzee Msangi" Mark aliwaambia wenzake.




"Kasemaje?" Wote waliuliza kwa pamoja.




"Twende kitalu C sasahivi" Mark alisema.




"Huu moto ni wa kupangwa. Its our bomb!" Elia alisema.




"Elia, unataka kuniambia kuna watu waligundua makazi yetu?" Mark aliuliza.




"Itakuwa hivyo. Mzee Msangi hawezi kuruhusu kitalu B kiteketezwe kwa Bomu. Ni nyumba ya gharama sana ile. Kuna vitu vingi sana vya thamani" Elia alisema.




"Inawezekana wamekusudia kuteketeza kitalu B. Twendeni kitalu C kama tulivyoagizwa" Mark alisema huku akigeuza gari kwa kasi. Kwakuwa waligeuza gari ghafla wakina Daniel hawakujipanga kwa hilo. Wao hawakuweza kukata kona. Walipishana na gari la wakina Daniel.




Kwakuwa Mark alishusha kioo kidogo, Adrian alimwona Mark.


Alipigwa na mshangao. Lakini Mark hakumwona Adrian kutoka na giza la kioo.




"Mark!!" Adrian aling'aka




"Vipi unamjua yule dereva?" Daniel aliuliza.




"Nilijua tu siku hii itafika, huyu ndiye aliyejifanya mwanamke aliyevaa baibui kule Rombo hoteli. Ndiye mwenye ile harufu ya uturi uliounusa katika bunduki ya mdunguaji kule juu ya ghorofa katika hoteli ya Rombo. Ndio, ulikuwa ni Uturi wa Mark" Adrian alisema.




"Ndio maana ulisema unamjua Mdunguaji tulivyokuwa kule juu katika hoteli ya Rombo? Who is the Mark?" Daniel aliuliza.




"Mark the sniper. Alikuwa mwenzetu lakini katika mafunzo huko Cuba, lakini alihasi pindi tu tulipomaliza mafunzo. Hakujulikana alienda wapi?




Baadae ikatoka taarifa kwamba Mark amefariki kwa ajiri ya gari huko nchini Nigeria. Lakini mimi haikuniingia akilini hata kidogo. Sikuamini katu. Nilihisi ni ajari ya kutengeneza.




Ulipita mwezi tu tangu taarifa ya kufariki kwa Mark ndipo rais wa nchi ya Sokonja aliuwawa kwa risasi. Kwa jinsi alivyodunguliwa niliamini hisia zangu. Ulikuwa aina ya udunguaji wa Mark the sniper. Nchi ya Sokonja walimtafuta mtu aliyemuua rais wao bila mafanikio..." Adrian alisema wakati akigeuza gari kulifata tena gari la kina Mark. Hakukata kona ghafla ili kuwapoteza maboya wakina Mark.




Gari lilivyokaa sawa Adrian aliendelea kuongea "Miezi miwili baadae rais wa Konjana naye alidunguliwa kwa risasi. Alidunguliwa kwa namna ileile aliyodunguliwa rais wa Sokonja. Si unajua rais wa Sokonja na Konjani walikuwa maadui kutokana na mzozo wao wa mipaka.


Dunia mzima hawakujua nani mdunguaji wa marais hao? Ingawa wengi waliamini nchi ya Sokonja walilipiza kisasi kutokana na kuuwawa kwa rais wao.




Umoja wa Afrika ukatuma wapelelezi wao kuchunguza undani wa vifo hivyo. Baada ya kutokea mzozo mkubwa kila nchi ikikataa wapepelezi wa mwenzake kuimgia nchini mwao.




Mimi, niliteuliwa kuungana na wapelelezi wanne. Mmoja alikuwa anatoka nchini Nigeria, mwengine nchini Zambia, kuna wa Misri na Afrika ya kusini. Lengo ni kufanya uchunguzi wa siri juu ya vifo hivyo. Tilisafiri hadi nchi ya Sokonja nikiwa na wenzangu, kisha tukaenda Konjani. Majibu tuliyoyapata kwamba ile ilikuwa kazi ya Mark.




Kamera za uwanja wa ndege wa nchi zote hizo zilinasa sura ya Mark akiwasili wiki moja kabla ya hayo matukio kutokea. Mark alitumia pasi zenye majina tofauti kuingia katika nchi hizo mbili. Tulipeleka taarifa yetu katika baraza la usalama la umoja wa Afrika. Lakini hakuna aliyetuamini, wote walitudharau na kuamini Mark alikuwa amekufa katika ajari ya gari huko Nigeria!


Nilirudi nchini baada ya kazi hiyo iliyoisha kwa kudharauriwa, lakini moyoni mwangu niliamini Mark the sniper yu hai. Na ndiye aliyewauwa hao marais...Ingawa sikujua kiini cha kuwauwa marais wale" Adrian alisema.




"Daah huyu mtu inaonesha ni hatari sana.." David alisema.




"Mark sio tu ni mtu hatari sana. Mark ni zaidi ya hilo neno hatari linavyomaanisha. Nakumbuka tukiwa mafunzoni hakuwahi kukosa kulenga shabaha. Alikuwa ni namba moja katika udunguaji. Wapo waliokuwa wanaamini Mark alikuwa anatumia uchawi ndio maana alikuwa Mdunguaji mzuri. Waliamini uturi wa Mark ni uchawi aliyopewa na mganga huko Nigeria ambao unamsaidia katika ulengaji wa shabaha. Maana Mark hawezi kufanya udunguaji bila kujipaka uturi. Na inasemekana kwamba Mark hawezi kabisa kulenga shabaha ikiwa hajapaka uturi. Ingawa hilo halijathibitishwa" Adrian alisema.




"Daah Adrian hizo habari mpya kabisa. Sijawahi kusikia mtu wa aina hii tangu niingie katika taaluma hii. Sasa Mark yupo Tanzania, ni nini hasa kitakuwa kimemleta hapa nchini?" Daniel aliuliza.




"Hakuna anayejua ni nini kilichomleta hapa nchini zaidi ya Mark mwenyewe. Lazima tumpate Mark atujibu nini kimemleta hapa? Na pia atuambia kwanini aliwauwa marais wa Sonjani na Sokonja? Na alikuwa wapi baada tu ya kumaliza mafunzo kule Cuba?" Adrian alisema.




"Atatujibu tu soon" Daniel alisema.




Kipindi hiko walikuwa katika chuo cha uhasibu. Gari la kina Mark lilikuwa limekata kushoto, likielekea upande wa Mbagala. Gari la sita nyuma lilikuwa ni gari la kina Daniel Mwaseba.




Hapo ndipo kikatokea kitu cha kushangaza sana....








Walipokuwa hatua chache usawa wa chuo cha Uhasibu, simu ya Adrian iliita. Adrian akaitoa mfukoni simu yake, huku mokono mwengine ukibaki kaushikia usukani. Simu ambayo iliwafumbua baadadhi ya vitu wakina Daniel Mwaseba.




"Mwanasheria mlevi anapiga" Adrian alisema huku akimpa simu Daniel.


ITAENDELEA


   


Simulizi : Bomu 


Sehemu Ya Nne (4)






Daniel akaipokea simu kutoka kwa Adrian , kisha akaipokea.




"Daniel" Sauti ya Mwanasheria mlevi ilisikika simuni.




"Nambie Mwanasheria?" Daniel alisema.




"Hii namba uliyonipa niichunguze umeitoa wapi?" Mwanasheria mlevi aliuliza.




"Kuna kimeo tunakifatilia. Sasa katika harakati za uchunguzi tukakutana na hiyo namba" Daniel alisema.




"Kaka hii namba ya ajabu sana. Sidhani kama kuna mtu angeweza kugundua mawasiliano ya namba hii zaidi ya sisi, usalama wa taifa. Namba imefichwa katika code ngumu sana. Ni namba ya mtandao wa simu wa Telecom lakini mawasiliano yake hayapo katika database za Telecom " Mwanasheria mlevi alisema.




"Daah mambo ya kushangaza sana. Lakini umefanikiwa?" Daniel aliuliza kwa wahka mkubwa.




"Swali gani hilo Daniel? Sasa kwani imewahi kushindikana kitu kwangu. Program waliyoitumia ni ya kitoto sana ukilinganisha na programs zetu. Mwanaume nimegundua kila kitu" Mwanasheria mlevi alisema kwa majigambo.




"Eeh nambie hiyo namba inamilikiwa na nani?" Daniel aliuliza kwa shauku.




"Namba imesajiliwa kwa jina la Elia Kilasi" Mwanasheria mlevi alisema.




"Elia Kilasi?" Daniel alirudia jina huku akiwatazama kwa zamu Adrian na David, wote walikataa kwa kichwa kuwa hawamfahamu mtu mwenye jina hilo.




"Elia Kilasi, Tutamtafuta mtu mwenye jina hilo. Eeh hiyo namba inawasiliana zaidi na namba gani?" Daniel aliuliza.




"Hapo ndipo penye utata mkubwa sana Daniel" Mwanasheria mlevi alisema.




"Utata gani?"




"Hii namba imewasiliana na namba tano tu tangu isajiliwe" Mwanasheria mlevi alisema.




"Ni namba zipi hizo?" Daniel aliuliza.




"Namba nne zipo katika uficho. Inahitajika program ya juu zaidi ili kuzigundua. Nimezituma namba hizo kwa rafiki yangu, yupo katika kitengo cha ujasusi cha CIA Marekani. Muda mfupi ujao tutakuwa na majibu ya namba hizo nne ni za kina nani?. Lakini namba moja ambayo nimeigundua ni ya Mohammed Msangi" Mwanasheria mlevi alisema.




"Mohammed Msangi!!" Daniel aling'aka kwa nguvu.




"Ndiyo, Mohammed Msangi. Aliyekuwa mkuu wa usalama wa Taifa" Mwanasheria mlevi alisema.




"Nimestushwa sana na kitu ulichokigundua mwanasheria mlevi. Mzee Msangi ni mmoja wa viongozi makini sana kuwahi kutokea katika idara ya usalama wa taifa. Alistaafu bila makandokando yoyote yale. Na hiyo ilimfanya awe rafiki sana na rais aliyepita na hata huyu wa sasa. Namba yake kukutwa katika orodha ya Elia Kilasi ambaye ndiye alikuwa anampa amri David ni jambo la kushangaza sana" Daniel alisema.




"Hivi unajua hujanambia unachunguza nini Daniel? Na huyo David ni nani?" Mwanasheria mlevi aliuliza.




"Haya mambo si ya kuongea kwenye simu. Yatupasa tukutane ana kwa ana. Nahitaji pia mchango wako katika uchunguzi wangu, pia naihitaji sana idara yako katika kazi hii ambayo wewe ni mkuu" Daniel alisema.




"Nihesabu nipo ndani ya misheni yako. Dakika yoyote ukinihitaji au kutaka msaada wangu wowote nipo tayari.."




"Nitakucheck Mwanasheria, simu yangu inaita" Daniel alisema.




Mwanasheria mlevi alikata simu, Daniel akapokea simu iliyokuwa inapigwa. Alikuwa ni Martin Hisia.




"Daniel mbona umeniweka tu hapa Mlimani city?" Martin aliuliza pindi tu simu yake ilipopokelewa.




"Mambo mengi Martin. Kuna jamaa walituteka wakati nakuja kwako. Nilipofanikiwa kuwatoka ikatokea dharura ya haraka, nikasahau kabisa kuhusu miadi yetu" Daniel alisema.




"Pole sana Daniel"




"Ndio kazi zetu. Kutekwa ni njia ya kuwafahamu wahalifu. Mara nyingi ukitekwa wanakupeleka katika makazi yao, hivyo ukifanikiwa kutoka unakuwa umepiga hatua kubwa sana" Daniel alisema.




"Ni kweli Daniel. Upo wapi kwasasa ?" Martin aliuliza.




"Nipo mitaa ya Aziz Ally kwa sasa, kuna kimeo nakifukuzia hapa" Daniel alisema.




"Nipo njiani nakuja pande hizo. Siwezi kukaa tu hapa wakati mwenzangu upo kazini" Martin alisema.




"Njoo haina shida. Tutawasiliana maana mwelekeo wangu ni uelekeo wa hawa jamaa" Daniel alisema.




"Sawa Daniel" Martin aliitikia.




Dakika hiyohiyo Martin Hisia alikodi teksi na kuelekea uelekeo wa Mbagala, kuwafuata wakina Daniel Mwaseba.




***




Imma Ogbo alikuwa katika nyumba ya kulala wageni huko pembeni kidogo ya kijiji cha Vikindu. Alikuwa amekaa huku akimwangalia Dr Luis aliyekuwa amelala kitandani. Haikuwa rahisi kutoka na Dr Luis Kigamboni hadi Vikindu. Imma ilimpasa atumie mbinu za kijasusi hasa, hadi ikafikia hatua ya kumtoa fahamu Dr Luis ili ijulikane kwamba alikuwa anampeleka mgonjwa hospitalini.




Baada ya vikwazo vingi njiani ndipo alipofanikiwa kufika katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz. Nyumba ya kulala wageni iliyopo nje kidogo ya kijiji cha Vikindu.




Utulivu wa nyumba hiyo ya kulala wageni, na umbali wake kutoka kijiji cha Vikindu ndicho kilichomfanya Imma Ogbo aamini kwamba pale palikuwa ni sehemu sahihi.




"Nimefanikisha hii misheni kwa awamu ya kwanza. Awamu ya kumtorosha Dr Luis mikononi mwa wale jamaa. Sasa yanipasa kwenda awamu ya pili na ngumu zaidi. Kumtoa Dr Luis Tanzania!!


Lazima niwasiliane na rais Abayo tuone jinsi ya kumsafirisha Dr Luis hadi Nigeria. Najua itakuwa kazi ngumu sana, lakini kwa msaada wa rais Abayo lazima tumpeleke huyu mtu nchini Nigeria. Hatuwezi kuruhusu Dr Luis akauwawa hivihivi, ametusaidia sana katika misheni ngumu na za siri katika nchi mbalimbali Duniani.." Wakati Imma Ogbo anawaza simu yake ikaita.




Alikuwa Felisia.




"Umefika wapi Felisia?" Imma Ogbo aliuliza alipopokea simu.




"Nipo Mwandege hapa" Felisia alisema baada ya kumuuliza dereva teksi.




"Mwambie akushushe hapohapo" Imma alisema.




"Sawa Imma" Felisia alisema




Baada ya Felisia kumlipa yule dereva teksi, alishuka. Akiiruhusu ile teksi irejee ilipotoka. Baada ya kama dakika tano Imma Ogbo alipiga simu.




"Felisia, tafuta dereva teksi hapo mwambie akupeleke Kongowe" Imma Ogbo alisema. "Wakati ukienda Kongowe kuwa makini, hakikisha hakuna mtu yeyote anayekufatilia"




"Usiwaze Imma" Felisia alisema na kukata simu.




Felisia alifanya kama alivyoambiwa. Alikodi teksi hadi Kongowe. Alipofika Kongowe alimpigia tena simu Imma. Imma akamwambia akodi bodaboda amreheshe Mwandege tena, kisha ashuke, apande daladala hadi Vikindu. Wakati huo Imma Ogbo alitoka katika ile nyumba ya kulala wageni, alikuwa Vikindu stendi kwenye duka kubwa la dawa. Alikuwa anaangalia usalama wa pale stendi. Aliridhishwa nao. Felisia alipowasili pale stendi, alimpokea na kuelekea mahali ilipo nyumba ya kulala wageni ya Platnumz.


Bado walimkuta Dr Luis amelala kitandani, hajarejewa na fahamu.




"Imma umenizungusha sana. Kumbe mahali penyewe ni hapa" Felisia alisema.




"Ilikuwa ni lazima nifanye vile, kama itatokea mtu wa kufuata nyayo zako iwe ngumu kukufikia" Imma Ogbo alisema.




"Upo sahihi Imma. Eeh nambie kilitokea nini kule kitalu B hadi ikafikia hatua ya kutoelewana na kina Mzee Msangi na kumtorosha Dr Luis?" Felisia aliuliza.




"Felisia wewe ni rafiki yangu wa siku nyingi sana. Tumefanya misheni nyingi sana na wewe na kufanikiwa kwa kiwango cha juu. Sitaki kukudanganya chochote kwa kuwa ninakuhitaji sana katika misheni hii" Imma Ogbo alisema wakati Felisia alikuwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa.




"Felisia, mimi nimetumwa na rais Abayo kwenye misheni hii"




"Umetumwa na rais Abayo?" Felisia alishangaa.




"Ndio, nimetumwa na rais Abayo kuja kumtoa mikononi mwa wale jamaa Dr Luis na kumrejesha nchini Nigeria" Imma alisema.




"Rais Abayo anamtaka wa nini Dr Luis?" Felisia aliuliza.




"Kuna vitu vingi bado haujavifahamu kuhusu Dr Luis. Kwanza inatakiwa ujue Dr Luis ni Jasusi mkubwa sana wa Nigeria!!!" Imma alisema.




"Unajua sikuelewi Imma. Hebu niweke wazi nikuelewe. Hapa unanichanganya tu"




"Kama nilivyokwambia Felisia. Dr Luis ni jasusi wa Nigeria. Alikuja hapa nchini kwa kazi maalum. Dr Luis amefanya kazi kubwa sana na kufanikiwa, hata mikataba waliosaini juzi kati ya rais Abayo na rais Mgaya ni kazi ya Dr Luis. Ndani ya mikataba ile kuna siri kubwa sana ambayo wananchi hawajui. Rais Mgaya hajasaini mikataba ile kwa kupenda, kuna shinikizo nyuma yake, na shinikizo hilo limeletwa na huyu kiumbe aliyepoteza fahamu hapa" Imma alisema.




"Imma umenieleza mambo makubwa sana, ingawa hujataka kunifafanulia. Nilikuwa sijui kitu kuhusu Dr Luis, wala kuijua kwa undani misheni hii. Lakini kwanini umenieleza mimi yote hayo?" Felisia aliuliza.




"Kwa sababu nataka unisaidie"




"Nikusaidie nini Imma?"




"Kama ujuavyo, kuna ulinzi mkali sana katika viwanja vyote vya ndege na mipakani. Lakini mimi ninataka kumtorosha Dr Luis na kumrejesha nyumbani. Najua kwasasa itakuwa ngumu sana kwakuwa Dr Luis anasakwa usiku na mchana. Lakini yanipasa kumtoa Dr Luis hapa nchini kwa namna yoyote ile. Na katika kazi hiyo ngumu nimekuteua wewe Felisia unisaidie kumtoa Dr Luis hapa nchini kwenu. Nikuahidi tu kazi hiyo ina malipo makubwa sana. Tukifanikisha kazi hii unaenda kuwa bilionea Felisia. Na pengine kuwa mwanamke wa kwanza tajiri hapa nchini kwenu" Imma alisema.




"Imma wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu sana. Tumefanya misheni nyingi za kifo na wewe. Katika kazi hii unayonipa huna haja ya kunitangazia pesa. Ninakuahidi ushirikiano na kuhakikisha Dr Luis anarejea Nigeria salama. Lakini naomba nijue baadhi ya vitu kama hautojari" Felisia alisema.




"Uliza chochote kile, kama kipo ndani ya uwezo wangu nitakujibu"




"Kwanza nataka kumjua zaidi Dr Luis. Na kama hautajari nambie nini hasa kilimleta hapa nchini ambacho kwa sasa kinasabanisha atake kuuwawa?. Na ni nani hasa ambaye yupo nyuma ya mipango ya kuuwawa kwa Dr Luis?"




Imma Ogbo aliinamisha kichwa chini "Felisia kauliza maswali magumu sana. Namwamini sana Felisia lakini sipo tayari kumueleza juu ya hayo aliyouliza. Hizo ni siri ya nchi yetu, kumueleza Felisia ni jambo la hatari sana. Ni sawa na kumvua nguo rais Abayo.."




"Imma Ogbo" Felisia aliita wakati Imma Ogbo akiwa katikati ya mawazo.




Je nini kitatokea? Tuwe wote katika sehemu ijayo.






"Nikuombe kitu kimoja Felisia" Imma Ogbo alisema.




"Nakusikiliza Imma" Felisia alisema huku akimwangalia Imma kwa chati.




"Naomba nisikujibu maswali yako kwasasa. Naomba hayo maelezo niliyokupa yatoshe. Lakini nikuahidi tu siku ambayo mpango wa kumtoa Dr Luis hapa Tanzania utafanikiwa ndio siku ambayo nitakueleza kila kitu" Imma Ogbo alisema.




Falisia aliinama chini, kisha akasema kwa unyonge


" Sawa".




"Najua Felisia hajaridhika na majibu yangu. Lakini sipaswi kumwambia kila kitu Felisia. Katika hizi kazi usimwamini mtu kwa asilimia mia moja. Muda wowote anaweza kukugeuka. Ingawa sina mashaka hata kidogo na Felisia. Nimemfahamu kitambo sana. Hawezi kuwa double agent lakini pia sipaswi kufunguka kila kitu kwake" Imma Ogbo aliwaza.




"Sasa Imma umepangaje ili kuhakikisha Dr Luis anatoka nje ya mipaka ya Tanzania?" Felisia aliuliza.




"Kama nilivyosema awali. Kwa kutumia njia ya ndege za abiria ama kumtorosha kupitia mipaka itakuwa ni kazi ngumu sana. Kuna kitu nimewaza. Ila ninahitaji sana ushirikiano wako ili kuweza kukifanikisha" Imma alisema.




"Kitu gani hiko ulichowaza?" Felisia aliuliza.




"Nataka kupoteza tension ya vyombo vya ulinzi. Unajua kwasasa vyombo vya ulinzi vyote vimejiandaa katika msako wa Dr Luis. Sasa mimi ninataka niwabadilishe uwelekeo wao" Imma alisema.




Felisia alibaki kimya, akisikiliza.




"Nataka tufanye tukio ambalo litabadilisha uelekeo wa vyombo vyote vya usalama hapa Tanzania" Imma Ogbo alisema.




"Unataka tufanye tukio gani Imma?"




"Nataka tuulipue ubalozi wa Uganda hapa Tanzania!!" Imma alisema.




"Imma Ogbo!!" Felisia aliita kwa sauti.




"Felisia, hiyo ndiyo njia pekee itakayotuwezesha kumtoa Dr Luis nje ya nchi. Tukiulipua ubalozi wa Uganda hapa nchini, macho na masikio ya nchi yataelekea katika tukio hilo, na kusahau kuhusu habari za Dr Luis. Hapo ndipo tutakapopata nafasi ya kwenda Nigeria" Imma Ogbo alisema.




"Inawezakana kuna ukweli katika maneno yako. Lakini sio rahisi kama usemavyo. Hilo ni jambo kubwa na la hatari sana. Na ni jambo ambalo linaweza kuleta mtafaruku mkubwa kati ya Uganda na Tanzania, na jumuia ya Afrika Mashariki kwa ujumla" Felisia alisema.




"Come on Felisia. Lengo letu kuu ni kuhakikisha Dr Luis anatoka hapa Tanzania kwa namna yoyote ile. Mambo ya mtafaruku sijui hatari ni out of our business" Imma Ogbo alisema.




"Imma, huo sio mpango wa kufanywa na watu wawili. Unajua jinsi balozi zinavyolindwa, suala kwenda kulipua ubalozi si la kitoto" Felisia alisema.




"Hatupo wawili. Tupo watu watatu mahiri sana. Sisi ni jeshi. Sisi sio tu tunaweza kuulipua ubalozi wa Uganda, tunauwezo wa kulipua hata dunia mzima tukitaka. Mimi, wewe na Mark the sniper tunaweza kufanya chochote kile. Suala ni kukubaliana tu na kuanza mpango wetu. Hiyo ndio njia pekee ya kumtoa Dr Luis Tanzania" Imma Ogbo alisema.




"Ina maana na Mark yupo upande wetu?" Felisia alishangaa.




"Mimi na Mark tupo katika misheni moja. Wote tumeletwa na rais Abayo kwa lengo la kumsaidia Dr Luis, na kuhakikisha anarudi salama Nigeria" Imma Ogbo alisema.




Felisia aliinama chini kufikiri " Ni kweli Imma Ogbo ni rafiki yangu sana. Tumesaisaidiana katika misheni mbalimbali kama ndugu. Lakini hii misheni ya sasa ni ngumu sana kwangu. Kuungana na Imma katika misheni hii ni kuisaliti nchi yangu na kuiunga mkono nchi ya Nigeria. Hii ni misheni yangu ya kwanza ngumu kuamua..."




"Felisia" Imma Ogbo aliita na kumtoa Felisia mawazoni.




Felisia alinyanyua kichwa chake. Alikutana na Dr Luis akiwa kafumbua macho.




"Dr Luis ameamka!!" Felisia alishangaa.




"Nilimnusisha dawa ambayo ilimtoa duniani kwa saa mbili" Imma Ogbo alisema.




Dr Luis alipiga chafya mara tatu mfululizo.




Na akarejea tena duniani.




***




Hannan Halfani bado alikuwa ametekwa katika nyumba moja huko Tegeta. Watekaji walijitahidi kumtibu Hannan ili atengemae. Waliamini kwamba Hannan ni silaha ambayo wanaweza kuitumia hapo baadae.




Hannan mwenyewe afya yake ilikuwa nzuri kidogo ingawa alijifanya bado anaumwa ili asiwape nafasi wale watekaji kufanya walichotaka kufanya. Kila sekunde alikuwa anawafikiria wakina Daniel na misheni yao. Alijilaumu kwa kukamatwa kijinga kule hospitali.




"Wameniteka kama kuku hawa wajinga. Hii ni kwasababu sipo sawa kiafya. Waache waniweke hapa ipo siku watajuta kwa kitendo chao cha kukaa na nyoka nyumba moja. Nitawashangaza. Nashukuru wananihudumia vizuri, na hii inanifanya nizidi kuwa imara kila sekunde. Lakini hawa watu ni kina nani? Ingekuwa ni majambazi wasingeniweka hapa na kunihudumia vizuri namna hii. Jinsi walivyoniteka kule hospitali inaonesha ni watu wenye mafunzo maalum. Kwakuwa afya yangu inaanza kuwa imara lazima nianze kuwapeleleza kuanzia usiku wa leo" Hannan alikuwa anawaza akiwa katika chumba chake. Mara mlango ulifunguliwa. Aliingia msichana ambaye alikuwa anamuhudumia tangu aingizwe katika ile nyumba.


Yule msichana alienda hadi mezani na kuanza kutoa vyombo vya chakula ambavyo alishavitumia.




"Uliniambia unaitwa nani vile?" Hannan aliuliza.




Yule msichana aliacha kutoa vyombo na kumwangalia Hannan.




"Naitwa Anna"




"Anna. Samahani ninaomba unisaidie kitu" Hannan alisema.




"Nikusaidie nini dada?"




"Kwani hapa ni wapi Anna?" Hannan aliuliza.




"Hapa ni Tegeta" Anna alijibu wakati huku akianza tena kukusanya vyombo.




"Mdogo wangu naomba unisaidie simu. Mama yangu mgonjwa sana, nataka nimjulie hali" Hannan alitupa karata yake.




"Dada ombi lako haliwezi kufanikiwa. Mtu yoyote anayeingizwa katika chumba hiki hatakiwi kuwa na mawasiliano yoyote yale na nje" Anna alisema.




"Kwani ninyi ni kina nani?" Hannan aliuliza.




"Hannan , nimeshangaa sana wewe kuletwa hapa. Wewe ni msichana mdogo sana, na unaonekana ni innocent. Na hii ndo sababu iliyonifanya nifungue mdomo wangu kuzungumza na wewe. Hii nyumba wanaletwa magaidi na watu walioshindikana, na wakiingia tu humu ndani watafunguka kila kitu. Sasa wewe sijui umefanya jambo gani la kuhatarisha usalama wa nchi hadi ukaletwa hapa" Anna alisema.




"Kwani ninyi ni askari?" Hannan aliuliza.




"Sisi ni zaidi ya askari. Akija Ayoub Ndondo atakueleza kila kitu kuhusu sisi. Na nikushauri tu usilete ujuaji mbele ya Ayoub Ndondo, atakuchakaza!!. ayoub hana huruma. Mjibu kila atakachokuuliza, tena umwambie ukweli mtupu!" Anna alisema.




Hannan alimwangalia Anna kisha akasema " Kwahiyo huwezi kunisaidia nilichokuomba? Unachoweza wewe ni kunitisha tu!" Hannan alisema.




"Msubiri Ayoub Ndondo!!" Anna alisema kwa mkato na kutoka nje na vyombo vya chakula.




Imma Ogbo anapanga kuulipua ubalozi wa Uganda, je watafanikiwa? Wakati Hannan anaambiwa akisubiri kiumbe kinachoitwa Ayoub Ndondo, je ni nani huyo Ayoub? Endelea kuisoma Bomu upate majibu.










Gari ya kina Daniel Mwaseba ilikuwa Mbagala Zakheim. Bado ilikuwa ikiifuata gari ya kina Mark the Sniper ambayo ilikuwa Mbagala Rangi Tatu. Simu ya Adrian iliita.




"IGP John Rondo anapiga" Adrian alisema huku akiipokea simu.




"Adrian mbona kimya sana. Hujanambia misheni yenu ya huko Kigamboni iliendaje? Na kwasasa mpo wapi?" IGP John Rondo aliuliza.




"Mkuu samahani sana sikukwambia juu ya ile misheni yetu. Ile misheni hatukufanikiwa mkuu. Tulikuta nyumba ambayo tuliamini Dr Luis alikuwepo imelipuliwa na Bomu mita chache kabla hatujaifikia!" Adrian alisema.




"Nimeipata hiyo taarifa ya mlipuko wa bomu huko Kigamboni. Na vijana wetu wapo huko wakifanya uchunguzi. Kumbe hiyo nyumba iliyolipuliwa na bomu ndiyo mliyokuwa mkienda ninyi?" IGP John Rondo aliuliza.




"Ndio mkuu. Ingawa hatukufanikiwa kufika pale lakini tunaamini Dr Luis alikuwa pale muda mchache kabla hilo bomu halijalipuliwa" Adrian alisema.




"Basi inawezekana walifahamu kama mnaenda pale?" IGP John Rondo alisema hisia zake.




"Aaah umeongea kitu ambacho mimi na wenzangu tulikuwa hatujawaza bado. Inawezekana mkuu walifaham kama tunaenda kuvamia pale nao wakaamua kuilipua ile nyumba" Adrian alisema. Daniel naye alimgeukia Adrian.




"Ni nani mwengine mlimjulisha kuwa mnaenda kuivamia hiyo nyumba ukiacha mimi?" IGP John Rondo aliuliza.




"Zaidi ya wewe, hakuna mwengine tuliyemjulisha" Adrian alijibu.




Ukapita ukimya kidogo. Kabla ya IGP Rondo hajaongea tena.




"Hapo kuna kitu hakipo sawa Adrian. Haiwezekani nyumba aliyokuwepo Dr Luis ilipuliwe muda mchache wakati mkienda kuichunguza. Huoni kwamba inawezekana kuna mtu aliwapa taarifa hao watu ndio wakaamua kuilipua?"




"Mwanzoni hatufikiria hivyo. Lakini sasa nauona ukweli katika maneno yako. Tutafanya uchunguzi pia juu ya hisia zako mkuu" Adrian alisema.




"Unaweza ukamuhisi mtu yoyote kuhusika katika kuvujisha siri?" IGP John Rondo aliuliza.




"Kwasasa hapana, hakuna tunayemuhisi, maana nd'o kwanza umetufumbua macho. Lakini naomba tupe muda. Tutamfahamu tu huyo Nyang'au. Je wewe kuna mtu yeyote yule uliyemwambia baada ya kukuambia juu ya operesheni tuliyokuwa tunataka tuifanye?"




IGP John alifikiri kidogo, kisha akasema " Hapana sikumwambia mtu"




"Basi sawa mkuu. Tutakujulisha baada ya kuwapata hawa watu tunaowafatilia kwenye gari" Adrian alisema.




Na simu ikakatwa.




IGP John Rondo akiwa kituo kikuu cha Polisi, simu yake ilipokata tu, hakukaa hata dakika nne. Simu yake ilipata uhai tena.Ilikuwa ni simu kutoka kwa mheshimiwa rais Mgaya.




"Habari za sahivi IGP?" Rais Mgaya alisalimu.




"Nzuri mheshimiwa rais. Sijui zako?"




"Huku Magogoni ni salama kabisa. IGP vipi watu wako walifanikiwa kuwapata wale watekaji?" Rais Mgaya aliuliza.




"Mheshimiwa rais hawakufanikiwa. Kulitokea tatizo kidogo"




"Tatizo gani hilo?"




"Nyumba waliyohisi kwamba Dr Luis alikuwemo ililipuliwa kwa bomu dakika chache kabla hawajawasiri!"




Kilipita kimya kidogo.




"IGP John, hiyo ni habari mbaya sana. Matukio ya milipuko ya mabomu yameshamiri sana hapa jijini. Hii sio Tanzania tuliyoizoea. Umefika muda wa kujipima sasa kama unastahili kukalia kiti hiko" Rais Mgaya alisema kwa sauti ya mamlaka.




"Mheshimiwa rais usiwe na shaka na mimi. Tunaenda kuwakamata hawa watu muda mfupi ujao. Kikosi changu kwa sasa kinawafukuzia kwa siri watu hao ambao bila shaka wanahusika na utekaji wa Dr Luis. Nitakupa majibu baada ya muda mfupi mafanikio yao" IGP John alisema.




"Ok sawa. Nasubiri matokeo ya ufatiliaji wao" Rais Mgaya alisema na kukata simu.




Rais Mgaya alipokata simu hiyo, simu yake ilipata uhai tena. Rais Mgaya alikuwa anampigia simu mzee Msangi.




"Mzee Msangi mambo gani mnafanya? Kwanini mmekosa umakini kiasi hiki?" Rais Mgaya alisema kwa hasira.




"Kuna nini mheshimiwa rais?" Mzee Msangi naye alirusha swali.




"Gari yenu moja inafatiliwa sasahivi na kikosi cha B1. Bila shaka ni ile inayokwenda kitaluni. Na unajua kwamba kitalu C ndipo mahali tulipohamishia makazi yetu kwa sasa" Rais Mgaya alisema.




"Inafatiliwa? Ngoja niwasiliane na kina Mark wajitoe mbele ya macho ya hao jamaa" Mzee Msangi alisema harakaharaka.




Na rais alikata simu.




Dakika ileile Mzee Msangi aliwapigia simu wakina Mark Sniper na kuwaeleza kwamba walikuwa wanafatiliwa.




***




Katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz huko Vikindu, Imma Ogbo, Felisia Nyenyembe na Dr Luis walikuwa na kikao kizito. Bado walikuwa wanapanga juu ya mpango wao wa siri wa kuulipua ubalozi wa Uganda nchini Tanzania ili kuharibu 'tension' ya polisi juu msako wao wa kumtafuta Dr Luis.




"Sasa nimeongea na rais Abayo. Ameubariki mpango wetu wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Amesema hiyo ndiyo njia pekee rahisi inayoweza kumtoa Dr Luis nje ya nchi hii. Rais amesema tuulipue ubalozi wa Uganda haraka iwezekenavyo" Imma Ogbo alisema.




"Safi sana. Nafurahi sana kusikia kwamba rais kaubariki mpango huu. Hii imeonesha kiasi gani ananijari. Ila unajua huu ni mpango mgumu sana. Kuulipua ubalozi wa nchi nyingine si jambo la kitoto hata kidogo. Pamoja na ugumu wake lakini inabidi ufanywe kwa siri sana. Maana siri ikifichuka kama ni sisi ndio tuliolipua ubalozi huo kwa maagizo ya rais Abayo inaweza kuleta ugomvi ama vita hata nchi kwa nchi. Sijui tumejipanga vipi ili kuhakikisha siri hii inabaki kuwa siri milele na milele?." Dr Luis aliuliza.




"Kuhusu ugumu wa mpango huu msamiati huo ondoa Dr Luis. Rais Abayo ameahidi kuwaleta majasusi watano kutoka taasisi yetu ya ujasusi nchini Nigeria. Majasusi hao watatusaidia kutekekeza mpango huu. Maana nilimgusia rais Abayo juu ya kumuhitaji Mark the Sniper katika mpango huu wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Alichosema rais ni kwamba tumwache Mark akae upande uleule ili aweze kuchota siri zao na mipango yao, na hivyo badala yake kaahidi kuleta majasusi hao watano kesho asubuhi.




Kuhusu suala la siri hilo usiwe na shaka nalo hata kidogo. Mpango huu utakuwa siri hadi kiama. Naamini si sisi wala hao majasusi hakuna atakayeweza kuutoa nje mpango huu" Imma Ogbo alisema kwa kirefu.




"Ni lini sasa tunaenda kuulipua ubalozi wa Uganda?" Felisia aliuliza.




"Hao majasusi watano wataingia kesho saa mbili asubuhi pale uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere. Na kesho hiyohiyo usiku tunaenda kutekeleza shambulio letu, na usiku huohuo wakati Polisi wakihahaha kusaka wahusika wa shambulio hilo sisi tutaanza safari ya kutoroka hapa nchini" Imma Ogbo alisema.




"Tunaondoka kwa njia ipi sasa?" Dr Luis aliuliza.




"Rais Abayo amesema hao majasusi watakuja na ndege binafsi. Ambayo ndiyo tutakayoitumia kuondoka nayo" Imma Ogbo alisema.




"Good plan mtu mbaya Imma Ogbo. Hakika safari hii tutawaacha midomo wazi wapelelezi wa nchi hii wanaojiweka matawi ya juu katika mambo ya kipelelezi" Dr Luis alisema kwa furaha.




"Kwa hakika watajuta!" Felisia alisema kwa nguvu huku akimalizia kutuma ujumbe wake kwa mtu fulani kwa siri.




Kati yao, hakuna aliyejua kwamba alikuwa anawarekodi kwa siri...




Je mpango wa kulipua balozi ya Uganda utakamilika? Vipi kuhusu msako wakina Daniel na Mark the Sniper? Na je Felisia anatuma ujumbe kwa nani?










Wakati huohuo teksi iliyompakia Martin Hisia ilikuwa maeneo ya Buguruni. Pamoja na dereva teksi kujaribu kukimbiza kwa kasi kila apatapo nafasi, lakini foleni ya haja ilizizima mbio zake mara kwa mara.




Pindi walipokuwa katika foleni hapo Buguruni ndipo simu ya Martin Hisia ilipoingia meseji. Martin aliitoa simu yake mfukoni ili kuiangalia hiyo meseji. Ulikuwa ni ujumbe uliongia kwa njia ya mtandao wa Whatsapp. Martin alifungua whatsapp yake. Akaona ni ujumbe uliongia kutoka kwa mpenzi wake, Felisia. Lakini uliingia kwa mtindo wa 'voice note'. Martin alitoa 'earphone' kutoka katika mfuko wake mwengine wa suruali. Akazichomeka katika simu yake.




Akaanza kusikiliza.




Wakati huohuo kule katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz. Felisia aliomba kwenda kujisaidia chooni nakutoka mle chumbani ambapo walikuwepo wakina Imma Ogbo. Alinyanyuka bila kuomba ruhusa. Alitoka nje ya mlango wa chumba walichofikia. Akakata kushoto akiifuata korido ndefu ambapo ndipo kulikuwa na choo. Mara kwa mara alikuwa anageuka nyuma ili kuona kama kuna hatari yoyote ile ilikuwa inamfuata. Hakuiona hatari, wala harufu ya hatari. Aliingia moja kwa moja bafuni. Akafungulia bomba la maji, akiruhusu maji kutoa sauti wakati yakiingia katika ndoo ya chuma. Sekunde ileile alitoa simu yake mfukoni na kumpigia Martin Hisia. Alisikiliza kidogo, kwa bahati mbaya alikuta simu ya Martin Hisia ilikuwa inatumika. Martin Hisia alikuwa anaongea na simu nyingine.




Hofu dhahiri ilishamiri katika moyo wa Felisia. Aliujua uhatari uliopo kwa kitendo alichokuwa anakifanya. Alifahamu vizuri sana adhabu atakayopewa na Imma Ogbo pindi atakapogundua kwamba alikuwa anamsaliti. Lakini hakuwa na namna, kuungana na Imma Ogbo safari hii ilikuwa ni kuisaliti nchi yake Tanzania. Na yeye hakuwa tayari kwa hilo.




Akiwa anatetemeka kwa woga Felisia alipiga tena simu ya Martin Hisia. Lakini bado majibu yalikuwa yaleyale. Simu aliyokuwa anaipigia ilikuwa inatumika.




Hii ilimpa mawazo mengi sana Felisia. Maana hakujua kwamba Martin aliusikiliza ujumbe wake aliomtumia ama lah. Alitamani Martin apokee simu yake hata sekunde moja na kumjulisha kwamba aliusoma ujumbe wake.


Angejisikia amani..




Alipiga tena simu kwa mara ya tatu.




"Come on Martin pokea simu" Felisia alisema kwa sauti ndogo. Lakini majibu ya simu yalikuwa yaleyale, bado ilikuwa inatumika.




"Hapa sina jinsi. Yanipasa nitoke tu nje. Maana jamaa wasije wakanitilia shaka kwakuwa nimechelewa sana kutoka chooni" Felisia aliwaza. Akafunga lile bomba la maji na kuelekea mlangoni. Alipofika mlangoni na kufungua tu ule mlango, alikutana na jambo la kushtusha sana!!




Felisia alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola nyeusi iliyoshikwa imara na mkono wa nguvu wa Immanuel Igbo!!




Kimbembe....




Wakati Felisia akitazamana na mdomo wa bastola, mpenzi wake, Martin Hisia alikuwa anaongea kwenye simu na Daniel Mwaseba. Alikuwa ameshamtumia ule ujumbe uliotoka kwa Felisia. Na Daniel aliituma ule ujjumbe pamoja na namba ya Felisia kwa Mwanasheria mlevi. Ndipo walipoweza kufanikiwa kupafahamu mahali alipo mtumaji wa ujumbe ule. Sasa safari yao ilibadilika, kwa kasi walikuwa wanaelekea Vikindu mahali ambapo waligundua kwamba ndipo alipokuwa Dr Luis.




"Kazi imekuwa rahisi sana. Sikutegemea kwamba tutampata Dr Luis kirahisi namna hii" Adrian alisema.




"Adrian, usiseme kazi ni rahisi. Hatujui Dr Luis yupo katika mazingira gani? Na hatujui tunaenda kupambana na watu wa aina gani? Hapa lazima tujipange kamili ili kuhakikisha tunampata Dr Luis" David alisema.




"Lakini jamani kuna mambo ya kushangaza kidogo juu ya hizi sauti alizotutumia Martin Hisia. Inaonesha kwamba Dr Luis hajatekwa, yupo na watu anaowafahamu kabisa huku naye akishiriki katika mpango wao wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Hii ipo vipi?" Daniel aliuliza.




"Hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali hilo kichwani mwangu. Lakini hatuna haja ya kuumiza kichwa. Dakika chache zijazo Tunaenda kukutana na hawa watu, na tutajua tu mbivu na mbichi" Adrian alisema.




"Hili swala limekuwa kubwa sana. Uhusika wa rais Abayo katika sakata hili ndo limezidi kulifanya kuwa kubwa. Lakini niahidi tu tutazifukia hila zote za watu hawa na kuziweka hadharani. Tutampata Dr Luis na kumfikisha kwa mheshimiwa rais, na lazima tuziseme hila zake. Pia lazima tuhakikishe ubalozi wa Uganda haulipuliwi abadaan, sambamba na kuwatia mikononi hao majasusi watano wanaokuja kutoka nchini Nigeria.




Pamoja na hayo lazima tuhakikishe tunamkomboa Hannan na familia ya David. Hizo ndio kazi zetu kuu, na nina hakika tutazikamilisha" Daniel alisema kipindi hiko gari yao ilikuwa Kongowe.




Walikuwa wameshapoteana na gari ya kina Mark ambao nao walihisi wanawakimbia wakina Daniel. Kumbe haikuwa hivyo, wakina Daniel walikuwa wamepata misheni ndani ya misheni.




Kwa mwendo wa gari la kina Daniel, Dakika saba tu ziliwafikisha Madafu kutokea Kongowe. Walipofika Madafu walimpigia simu Mwanasheria mlevi ili awape mwelekeo sahihi waliopo wakina Dr Luis.




"Mwanasheria, tupe mwelekeo, tupo Madafu hapa" Daniel alisema.




"Sasa Daniel ninavyoona hapa katika mtandao, hapo Madafu upande wenu wa kulia kuna kituo cha mafuta. Mita chache kutoka kituo cha mafuta upande huohuo wa kulia kuna nyumba ya kulala wageni. Hapo ndipo hiyo simu ilituma ile meseji" Mwanasheria alisema.




"Sawa Mwanasheria nd'o tupo katika kituo cha mafuta hapa, tunaelekea hilo eneo. Vipi hiyo namba iliwasiliana tena na mtu mwengine?" Daniel aliuliza.




"Hapana Daniel. Nimekuwa nikiichunguza namba hii muda wote. Ilijaribu kuwasiliana na namba moja ambayo nayo ilikuwa inaongea wakati akiipigia. Nilijaribu kuichunguza namba hiyo ikiyopigiwa nikagundua imesajiliwa kwa jina la Martin Hisia. Nikachunguza tena huyo Martin Hisia alikuwa anaongea na nani kwa muda huo? Nikagundua anawasiliana na simu iliyosajiliwa kwa majina ya Adrian Kaanan, hivyo nikagundua alikuwa anawasiliana nanyi" Mwanasheria mlevi alisema.




"Pengine huyo mtu alikuwa anataka kumpa taarifa nyingine Martin" Daniel alisema.




"Inawezekana. Maana alijaribu kupiga simu zaidi ya mara mbili"




"Sawa Mwanasheria. Sisi tunaingia kazini. Nitakupigia baada ya kutoka hapa. Tuna kazi kubwa sana kesho asubuhi kama ulivyosikia katika hizo records. Nitakuhitaji ili kuikamilisha hiyo kazi" Daniel alisema.




"Nipo tayari saa yoyote, sehemu yoyote. Mimi ni Mwanasheria..."




"Mwanasheria mlevi" Daniel alimalizia.




Na simu ikakatwa.




Daniel alimwangalia Adrian, kisha akamwangalia David.




"Wanaume, sasa tunaenda kuvamia hii nyumba ya kulala wageni ambayo tuna uhakika yupo mtu anayeitwa Imma Ogbo. Pengine hamumjui vizuri Imma Ogbo. Mimi nimemjua Imma Ogbo kupitia Mwanasheria pindi nilipomtumia zile record alizoturushia Martin Hisia. Katika record zile kuna sauti tatu, ya Dr Luis, mwanamke ambaye ndiye amevujisha siri hii na mwengine ni sauti ya Imma Ogbo. Sisi shabaha yetu ni Dr Luis, lakini tujue kwamba Dr Luis yupo sambamba na kiumbe hatari kinachoitwa Imma Ogbo.




Imma Ogbo ni nani?




Imma Ogbo ni jasusi namba mbili kutoka nchini Nigeria. Licha ya ujasusi Imma ni mlinzi namba mbili wa rais wa Nigeria, rais Abayo. Kupambana na jasusi namba mbili wa nchi kama Nigeria, nchi yenye maelfu ya majasusi na yeye kupewa namba mbili si jambo la kitoto. Kwa Afrika Imma Ogbo anashika namba sita. Mmeona uhatari wa huyu jamaa? Lazima tuwe makini sana ndugu zangu. Ukimwona Imma Ogbo cha kwanza mpige risasi ya kichwa kisha ndo umuhoji!! Nataka leo ndio uwe mwisho wa hila za hawa manyang'au!!!." Daniel alisema huku akiwaangalia wenzie kwa zamu.




Wote waliitikia. Sura zao zikionesha walikuwa na hamu kubwa ya kuingia katika mapambano haya magumu na ya hatari.




"Haya sasa...Twendeni tukaivamie hiyo nyumba ya kulala wageni. Iwe iweje..lazima tuhakikishe tunawatia mkononi Dr Luis na Imma Ogbo!!" Daniel alisema.




Wote watatu, walishuka kwenye gari, wakiwa tayaritayari, na kwa kutumia miguu yao walielekea katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz kuwatia mbaroni watu ambao waliwapachika jina la Manyang'au...










Daniel Mwaseba alipita upande wa nyuma kuelekea nyumba hiyo ya kulala wageni. Alikuwa ana bastola mbili kiunoni mwake zikizosubiri kutumika. Upande wa kulia na upande wa kushoto.




Bastola ya tatu ilikuwa katika mkono wa kulia ikiwa tayari imeondolewa usalama.




Tayari kuilipua hatari yoyote.




Mgongoni kwake, kulikuwa na begi dogo jeusi lenye zana kadhaa za kazi. Begi ambalo lilikuwa halikosekani mgongoni mwake akiwa katika misheni.




Daniel alikuwa ananyatia kimyakimya na kwa umakini mkubwa huku akijificha mara kwa mara katika mashina ya miti miarobaini iliyopandwa bila mpangilio maalum. Au pengine ilijiotea yenyewe.




Masikioni mwake, kulikuwa na kifaa kidogo cheusi. Hiki kilikuwa ni kifaa cha mawasiliano ambacho kilimwezesha kuwasiliana na wenzake. Sekunde na dakika yoyote.




Upande wa mbele wa nyumba ile ya kulala wageni alikuwepo Adrian Kaanan. Askari polisi imara ambaye alionesha umahiri mkubwa katika misheni mbalimbali.




Misheni yake ya kwanza aliifanyia huko maeneo ya Mkuranga. Misheni ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa sana na kufumbua fumbo gumu, misheni hiyo ilipachikwa jina la Briefcase.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog