Simulizi : Kiguu Na Njia
Sehemu Ya Tatu (3)
Kumbe muda wote ule alikuwepo Mndorobo mmoja aliyekuwa akiwatazama. Mndorobo huyo aliwaita na kuwataka watulie. Kisha akaenda kwenye pango lile la mbuyu na kutamka maneno kadhaa. Mara kwa mshangao wa wawindaji wale joka lile lilitoka taratibu na kutokomea porini. Mdorobo akawataka wawindaji kurejea pangoni na kulala bila wasiwasi wowote. Walilala na kesho uake wakafanikiwa kupata njia ya kurudi kwao.
Pengine jina hili la Wandorobo lilitokana na tabia yao katika ulaji wa uwindaji. Ni hodari sana kwa kutumia mishale. Mshale mmoja wa Mdorobo huua wanyama wawili kwa mpigo si jambo la ajabu. Mara nyingi, wanapowinda uwalenga zaidi wanyama wanaonyonyesha. Mara wanapomwona mnyama wa aina hiyo humpiga mshale na anapoanguka hukimbilia na kunyonya maziwa yake na damu yake kama mdudu aitwaye Ndorobo anavyonyonya damu ya binadamu na mifugo. Huanza kwa kunyonya maziwa. Akitosheka hutafuta mshipa unaotoa damu na kuinyonya hadi ashibe. Baada ya hapo ndipo huchukua kibuyu chake wanachokiita ululu na kukijaza kwenye ziwa. Baadaye Mdorobo hurudi nyumbani ambako humchukua mkewe na wanawe na kurudi kwenye windo lao ambalo hulichuna na kulila wakitunza ngozi, mafuta na mifupa kwa matumizi ya baadaye.
Watu hawa, ambao kwa viwango vya dunia ya sasa ni masikini sana, kwani hawana tabia ya kuweka akiba ya chakula wala mifugo, hawajengi wala kulima, hawatilii maanani suala la elimu wala kujishughulisha na masuala ya serikali kwa namna yoyote, wanaaminika kuwa ndiyo wakazi wa asili wa Tanga. Tabia yao ya kuhamahama pia inawafanya wapatikane katika maeneo ya Arusha na Manyara na Singida.
Simulizi za kale zinaonyesha kuwa makabila maarufu ya sasa mkoani Tanga, maarufu kama Waseuta lilipata msaada mkubwa toka kwa Wandorobo hata wakawashinda Wareno na kuweza kuanzisha himaya yao. Simulizi hizo zinaanza kwa mfalme mkuu Seuta. Waseuta walianza ugomvi na Wareno kule Vumba, wakakimbilia Sonjo na Nguu. Baadhi walitimka hadi Kondoa Irangi.
Seuta anaelezewa kutawala Waseuta ambao ni mjumuiko wa makabila ya Wazigua Wanguu, Wabondei, Wakilindi wa Waluvu. Katika makabila hayo awali, lilikuwa moja kabla ya kutawanyika, kila ukoo ukishika njia yake, na kuibuka katika mazingira na lafudhi tofauti, ingawa wote wanalichukulia jina la Seuta, mfalme wao kuwa ni mzimu wao unaowaepusha na balaa na kuwafanikishia masuala yao pale wanapomtambikia.
Seuta alianza kutawala akiwa na miaka kumi na miwili tu. Alizaliwa eneo liitwalo Nguu (Kilindi) baba yake akiitwa Kuba Kaluli. kwa msaada mkubwa wa mishale aliyopewa na Wandorobo, Seuta aliweza kuwateketeza Wareno waliokuwa wakiwaandama. Mbinu nyingine ilikuwa ile ya kuwaachia Wareno vijiji, huku wakiwa tayari wemeteketeza au kuharibu mahitaji yote muhimu kama chakula na maji jambo lililowaacha hoi Wareno. Na wakati wakihangaika ndipo mishale ya Waseuta iliwanyeshea kama mvua na kufanya bunduki zao zishindwe kutimiza malengo yao. Wachache walionusurika walirejea Pwani, ambako huko nako balaa lilikuwa likiwasubiri. Waarabu toka Oman waliwashambulia na kuwafanya waikimbie kabisa Pwani ya Afrika Mashariki.
Hao ndio Waseuta na hiyo ndiyo Tanga. Mkoa mwingine uliobahatika kuwa katika Pwani ya Bahari ya Hindi, kwenye wilaya za Handeni, Lushoto, Korogwe, Muheza, Kilindi na
Tanga yenyewe. Nje ya makabila ya Waseuta makabila mengine ni pamoja na Wadigo, Wasegeju na Wadaiso.
Lakini hadithi ya Tanga katika vita na mapambano hiishii hapo. Mjerumani na mikiki yake alipoingia Tanganyika ghafla aliipenda Tanga. Mwaka 1889 akaiteua kama ngome yake ya vita. Pendekezo lililorasimishwa miaka miwili baadaye. Tanga ilionja kali ya vita kuu novemba 4, 1914 pale mapambano makali yalipoibuka. Mwingereza ambaye alitokea Kenya alitandikwa.
Majeshi yake yaliyokuwa na wapiganaji wapatao 8,000 ambao hawakuwa na ujuzi wa kutosha yalisambaratishwa na kukimbilia maporini, ambako huko nako walishambuliwa na kundi kubwa la nyuki hata vita hivyo vikaitwa ‘vita vya nyuki.’ Lakini ilipofika julai 7 mwaka huohuo, baada ya kujizatiti Mjerumani alizidiwa hata kamanda wa Wajerumani, Von Lettow – Vorbeck, akiwa na bendera nyeupe akamfuata jemedari wa Waingereza, Arthur Aitken na kumwangukia.
Jambo hilo liliokoa maisha ya majeshi yake na likampa hadhi kubwa nchini Ujerumani.
Naam, hiyo ndiyo Tanga. Tanga niliyoifahamu kupitia vitabuni na simulizi za wazee walioshiriki vita hiyo kwa hali na mali. Tanga ambayo sasa nilikuwa sehemu ya wakazi wake, nikiishi Pangani, kilometa zipatazo arobaini na tano toka mji mkuu.
Niliandikishwa kazi katika shamba la Mgiriki mmoja, bwana Nicodemus, ambalo halikuwa mbali sana toka mji mdogo wa Tongwe ambao ulibahatika kuwa kando ya barabara inayotokea Mzundu, inavuka mto Pangani na kwenda hadi Majongo na hatimaye Tanga mjini. Tongwe ilikuwa na bahati nyingine kubwa. Reli. Ni ile inayotoke Pwani na kuelekea
Tanga, kabla ya kuchepuka pale Korogwe ambako inaenda hadi Kilimanjaro na Arusha.
Kazi ya kilimo cha mkonge sio mchezo. Inahitaji ujuzi na maarifa kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Wageni ambao hawakuwa na ujuzi wa kutosha katika wiki mbili zao kwanza walitaabika sana na baadhi kuugua kwa kuchomwa na ncha ya katani au kudondokewa na maji yake ambayo yanawasha sana. Hali ambayo pia ilichangia kuwanyima mapato.
Mimi, kama kawaida yangu, nilijihisi mwenye bahati. Nadhani tajiri huyo alidokezwa jambo juu yangu, kwani mara tulipoanza kugawiwa majukumu mimi nilifanywa mnyapala na karani wa shamba moja wapo. Jukumu langu lilikuwa pamoja na kutoa ripoti ya kiwango cha kazi ya kila kibarua, kusimamia utendaji wao na kumwandalia tajiri taarifa za malipo ya kila wiki. Haikuwa kazi rahisi kama mtu mwingine anavyoweza kufikiri. Kukimbia hapa na pale, kugombana na huyu au yule, huku muda wote tajiri akiwa nyuma yako akifoka na hata kutukana pasipo sababu za msingi ni miongoni mwa mambo yaliyofanya niichukie tangu siku ya kwanza ya ajira.
Nikaanza kupanga namna ya kutoroka.
Hata hivyo, azma yangu haikutimia hadi mwaka mmoja na nusu baadaye. Kipindi ambacho kilinipa uenyeji wa kutosha wa mkoa huo. Kwa mfano, ni huko Pangani ambako kuliniwezesha kutimiza ile ndoto yangu ya kuona Bahari ya Hindi kwa mara ya kwanza maishani mwangu, ndoto ambayo awali nilitarajia kuitimiza katika ile safari yangu ambayo haikuwa ya kwena Kilwa.
Niliona kile nilichokuwa nikisikia toka utotoni juu ya tabia ya bahari kupwa asubuhi na kurejea jioni. Kwa macho yangu nilijionea eneo la bahari likiwa kavu kana kwamba
halikupata kuwa na maji lakini jioni bahari ikarejea na kulifanya sehemu ya bahari. Majahazi ya wavuzi na wasafiri wakitembea juu yake kama kawaida.
Nilijionea, kuwafahamu na kuwaonja samaki wa maji chumvi; pweza, samaki mtamu mwenye miguu lukuki na kichwa ambacho mgeni wa Pwani huwezi kufahamu ni kipi. Samaki wengine walionitoa macho kwa mshangao nilipodokezwa kuwa waliliwa pia ni kasa ambaye alifanana na kobe na nguva anayefanana umbo na binadamu, hasa mwenye jinsia ya kike, kwa umbile lake. Sikupata kumtia machoni samaki huyo wa ajabu. Lakini picha nilizopata kuona na simulizi za watu zilifanya niamini kuwa nguva ana maziwa kama mwanamke. Wale vibua, kolekole, changu, kamba, ngisi na hata kaa niliwaona na kuwala kama kawaida.
Jambo jingine ambalo lilinivutia macho Pangani ni minazi. Hapana, sio mnazi kwa maana ya urefu wa mti wake, La hasha! Walionishangaza ni wakwezi wa mnazi. Mimi nilizaliwa na kukulia porini. Kupanda miti na hata kuruka toka tawi hili au lile lilikuwa jambo la kawaida kwangu. Lakini wakwezi wa minazi ya Pangani, mti mrefu takribani futi 30 au zaidi, ukiwa hauna tawi lolote la kushikilia, kulifanya niwatazame kwa mshangao mkubwa wakwezi hao waliofuata nazi na madafu au kugema mnazi huko angani. Kila nilipomwona mtu akikwea mnazi sikuchoka kumtazama kwa hofu hadi nilipomwona akishuka akiwa salama.
Sitaisahau Pangani wa sababu nyingi. Kubwa ni kunipa fursa ya kumwona kwa macho yangu mwenyewe yule mshairi gwiji, aliyekuwa akiwanyanyasa wakoloni kwa mafumbo yake mazito katika beti za tungo zake. Mtu huyu alitamba sana katika magazeti mbalimbali kama Ngurumo, Kiongozi na Lipuli. Kwa jina aliitwa Shaaban Robert.
Mtu huyu alinisisimua kwa mengi, kubwa likiwa hekima zake ambazo zilichongwa na kufichwa vilivyo katika lugha ya kiswahili, aya baada ya aya, tenzi baada ya tenzi huku zikimsuta mkoloni na kumshawishi Mtanganyika kujiandaa kuichukua nchi yake. Isingekuwa kwa utaalamu huo wa kucheza na lugha Shaaban Robert asingeweza kuajiriwa na serikali hiyohiyo aliyokuwa akiipiga vita kama karani wa Forodha katika kituo cha Pangani kwa miaka kumi na minane kabla ya kuhamishiwa Tanga mjini.
Msisimko wangu kwake, hasa ulitokana na kubaini kuwa elimu yake ilikuwa ya muda mfupi tu darasani, nikiwa nimemzidi kwa miaka miwili, lakini upeo wake wa kufikiri, kuchambua mambo na kuitumia vilivyo lugha ya Kiswahili upeo na uwezo wake uliwazidi kwa mbali watu wengi wenye shahada. Kwa mujibu wa maandishi yake mwenyewe, Shaaban alisoma katika shule ya msingi ya Msimbazi iliyoko Dar es salaam kati ya mwaka 1922 hadi 1926.
Titi la mama ni tamu Japo liwe la Mbwa,
Ni moja kati ya beti za mashairi yake ambayo kamwe hazijapata kunitoka akilini.
Jambo jingine lililonisisimua katika uhai wangu wa Pangani na Tanga kwa ujumla ni kule kujikuta katika mazingira tofauti kabisa na yale ya kwetu na sehemu nyingi nilizozipitia. Mazingira ya Kiswahili kile nilichokuwa nikisoma na kusikia, kwamba Waarabu walifika miaka nenda rudi katika Pwani ya mwambao mzima wa Afrika Mashariki, sasa nilikiona kwa macho yangu. Wanawake wengi walijificha nyuso zao kuonekana. Wanaume wengi walivaa kanzu na vilemba au baragashia. Idadi kubwa ya wakazi walikuwa Waislam huku tamaduni na hata lafudhi zao zikiwa za Kiarabu
zaidi. Watoto walipenda madrasa wakiwa bado wadogo na wengi wao waliondokea kuwa hodari wa Koran kuliko hata Waarabu wenyewe. Familia nyingi, isipokuwa kwa ajili ya rangi, wangeweza kabisa kuwa sehemu ya wakazi wa Oman, Baghdad au Cairo.
Moja kati ya familia hizo ni ile ya Sheikh Msa. Yeye na wanawe hawakupata kukosa sala hata moja. Kila mmoja, hadi yule mjukuu wa miaka kumi na tatu, tayari alikuwa na ‘sijida’ katika paji lake la uso inayoonyesha jitihada za uadilifu wake katika kumcha Mungu.
Ilitokea bahati nikafahamiana na mzee huyu. Alikuja kazini kwangu akiwa na barua ya Kiingereza ambayo alitaka nimsomee. Barua hiyo iliondokea kuwa fomu iliyotakiwa kuijaza ili kupata uthibitisho wa ushiriki katika vita vikuu vya kwanza. Ni katika kumjazia niliposhangaa alipodai kuwa asili yake ni Kigoma.
“Kigoma! Kigoma ipi?” Nilimuuliza
“Kwani kuna Kigoma ngapi, Sheikh?” alinijibu kwa swali vilevie. “Kigoma ni moja tu ya Wamanyema na Waha.”
“Wewe ni Mmanyema?” Nikahoji tena.
“Hapana, Muha, ingawa huku tunaruhusiwa kuitwa Wamanyema…”
Nikazidi kuvutiwa naye, “Muha wa wapi?”
“Kasulu, baba alipotea maeneo ya Nyamasovu, akalowea huku.” Ikawa zamu yake kushangaa. “Siye tunafahamu unatokea Mbeya! Kumbe ‘mwanangu’ allah akbar!”
“Ni hadithi ndefu,” nikamjibu “Nyumbani hasa ni Buha. Kwenda Mbeya na kufika hadi huku ni katika jitihada za kutafuta maisha.”
“Allah akbar” alisema tena akiwa amenikodolea macho ya mshangao.
Tulizungumza sana na mzee huyo maongezi ambayo yalikolea pale nilipomtajia jina la babu yangu na akajikuta amemkumbuka mara moja.
“Wewe ni mjukuu wa Kionambali? Oh ni mwanangu kabisa!” alimaka. Akanieleza alivyokutana na babu katika vita kuu ya kwanza, walipochukuliwa kama wapagazi, wakaishia kupewa bunduki. “Babu yako alikuwa mkorofi sana. Hakupata kumfyatulia adui bunduki hata mara moja. Wajerumani wakamfanya mpishi. Huko nako alikuwa na vituko vyake vingi tu. Halafu akatoweka. Nadhani Wajerumani walimwua. Walikuwa katili sana.”
Nilihisi machozi yakinilengalenga kwa simulizi hiyo ambayo babu hakupata kunisimulia hata mara moja. Mzee alishangaa zaidi pale nilipomwabia kuwa yuko hai, alirejea Buha zamani sana.
“Sishangai. Ni mtu wa miujiza sana babu yako.
Hatabiriki!”
Nikawa nimepata ndugu, udugu ambao ulipelekea mzee huyu anitazame kwa jicho tofauti na lile la kawaida, kabla hajasema taratibu, “Mwanangu una nini? Kwa kila hali hustahili kuwa hapa ukifanya kazi hizi za kitumwa. Umesoma una busara, na una afya tele. Kuna kitu kimepungua au kuzidi katika nafsi yako. Ni hicho kinachofanya uwe mtu wa kutangatanga. Ama nyota yako imefifia. Inahitaji kusafishwa.”
Ben R. Mtobwa
SURA YA KUMI NA MOJA
jahazi hadi
wa mara ya kwanza niliitumia bahari kusafiri. Kwa ushauri wa mzee wangu na mshauri wangu mpya kwa masuala yanayohusu maisha, Sheikh
Msa, haikuwepo haja ya kutumia barabara ambayo gharama yake ilikuwa kubwa zaidi na magari yalipatikana kwa shida sana. Bahari ya Hindi ilitosha.
Safari yangu ilikuwa ya kwenda Bagamoyo, dhamira ya safari ikiwa ileile iliyotaka kunipeleka Kilwa, kusafisha nyota yangu kwa kuondoa ‘wingu’ la mkosi ambalo lilifunika bahati yangu, safari ambayo ilitokana na maelekezo ya mzee Msa, baada ya maongezi marefu baina yetu toka siku ile alipoishuku nyota yangu kuwa na kasoro.
Sikuwa na sababu yoyote ya kutomwamini mzee huyu. Akiwa mtu mwenye heshima zake, mtu anayejiweza kiuchumi kwa kumiliki mashamba na vyombo vya uvuvi, huku watoto wake wanne wakishindana kumletea mahitaji mbalimbali; asingekuwa na sababu yoyote ya kunihujumu kama alivyokusudia yule Bushiri Mtanashati, hapana. Nilimsimulia mkasa mzima wa safari yangu, toka zilipoibuka fununu za kunitoa kafara kwa ajili ya mvua hadi safari yangu ya nchi ya
Wahaya kutafuta elimu na hata kupotea kwa hirizi niliyopewa na babu.
“Unaona? Unaona? Nilijua zamani una jambo mwanangu. Sasa lazima usafishwe, uoshwe. Hirizi yako lazima irudi,” kauli ambayo ndio hasa iliyozaa safari hii ya Bagamoyo. Naikumbuka vizuri tarehe ya kuanza kwa safari yangu.
Ilikuwa tarehe 7 Januari, 1938. Sikuwa na namna ya kuisahau kwani ni siku hiyo serikali ya Mwingereza, kwa kauli ya gavana wake nchini, wakati huo bwana H.A Mac Michael, alipoitazama rasmi eneo la Pangani kuwa wilaya kamili.
Safari ilianza alfajiri, mara baada ya pepo za kusi toka kaskazini kuanza kuvuma. Tulisafiri kwa jahazi litumialo matanga yaliyopokea upepo vizuri sana na kwa ujuzi wa naodha wetu aliyekuwa akitoa maelekezo kwa mahabaharia wake haikuchukua muda kabla ya jahazi letu kushika kasi likifuata mwambao wa bahari kuekelekea kusini. Tulipepepa hadi Mwera, tukaacha na kuingia Mkwaja, tukaipita hadi Saadani kabla ya kutia nanga Bagamoyo mjini saa kumi na moja za jioni.
Pamoja na uzoefu wangu wa mambo ya majini sina budi kukiri hapa kuwa nilifika Bagamoyo nikiwa taabani. Upepo wa kusi ambao tulianza nao safari ulikuwa ukibadilikabadilika mara kwa mara. Ziko sehemu ambazo tulipambana nao, ukituelekeza takribani hukohuko tunakotoka, lakini kwa uhodari wa naodha chombo hakikupata kwenda mrama. Ziwa Nyanza lina mawimbi. Lakini mawimbi yale na haya niliyopambana nayo baharini ni vitu viwili tofauti kabisa. Kama wimbi la ziwani ni kubwa kama nyumba la bahari liliweza kuwa kubwa kama mlima. Chombo chetu kilipaa na kushuka juu ya mawimbi hayo kama unyoya, huku naodha wa baharia
wetu wakifanya hili na lile kuhakikisha usalama.
Harufu ya maji chumvi nayo ilikuwa kero nyingine. Ilikuwa harufu aina fulani, kavu, ambayo ilishawishi kutapika. Hata hivyo, sikuthubutu kukubali kushawishika. Hakuna aibu katika safari za majini kama kutapika. Wazee wengi husema kuwa hayo ni maradhi ya wanawake.
Jahazi hilo lilikuwa na abiria wawili tu, mimi na Ramadhani, mtoto wa nne wa mzee Msa, ambaye aliteuliwa kunisindikiza. Awali, ilikuwa Msa mwenyewe anilete Bagamoyo, lakini siku mbili kabla, alibanwa na mshipa wa ngiri, uliofanya ashindwe hata kutoka kitandani kuniaga. Hivyo, Ramadhani ambaye tulikaribiana kwa umri akabebeshwa jukumu hilo la kuniongoza. Na alianza kwa kunifikisha salama mikononi mwa mjomba wao aliyekuwa akiishi hapohapo Bagamoyo. Tulikaribishwa vizuri, tukapewa chakula na malazi hata kabla ya kueleza kiini cha safari yetu.
Kesho yake Ramadhani alinitambulisha kwa mjomba wake huyo kama ‘ndugu yetu’ ambaye mola kamleta mikononi mwetu ili kumnusuru na pepo mbaya aliyemkumba.’ Akaeleza kwa ufasaha kila alichoelekezwa na mzee Msa kukieleza.
“Hilo mbona tatizo dogo tu.” Mwenyeji wetu, ambaye baadaye nilibaini kuwa ni Imam wa msikiti mashuhuri wa hapo Bagamoyo, alisema. Kwa jina aliitwa Al Haji Suleiman. Sikupata kuuliza kama Al Haji ni jina lake au wadhifa ambao muislam hupata baada ya kutimiza nguzo mojawapo muhimu ya dini ya kwenda Hijja.
“Tatizo ni dogo sana,” aliongeza. “Kesho pia pumzikeni. Kesho kutwa nitawapeleka Mlingotini, kwa Sheikh Mahmoud. Atamsafisha mara moja na kama kuna mkono wa mtu, mtu huyu ana bahati mbaya sana.”
Nilikuwa nimechukua likizo ya wiki mbili kazini kwangu. Hali ya mfuko wangu kifedha pia haikuwa mbaya. Hivyo, mapumziko hayo ya siku moja kabla ya kukutana na ‘mtaalam’ wa kusafisha nyota niliamua kuyatumia kwa kuvinjari vilivyo Bagamoyo.
“Unafahamu kuwa pamoja na mambo mengine kufika hapa Bagamoyo peke yake ilikuwa ni moja ya ndoto zangu kubwa maishani?” nilimwambia Ramadhani.
“Kwa nini ?” alihoji.
“Huu ni mji wa kihistoria,” nilimwambia. “Wataalamu wa historia na mambo ya kale wanaamini mji huu ni wa kale kuliko yote Afrika Mashariki. Wanaamini ulikuwepo kabla ya kalenda tunayoitumia sasa, yaani kabla ya Issa bin Mariam hajazaliwa kule Nazareth. Huoni kama ni bahari ya pekee kuwa katika mji huu leo na kujionea kwa macho yako kile ambacho umekuwa ukisimuliwa na kujisome?”
Ramadhani alikuwa na tabia moja ambayo sikuipata kuipenda. Tabia ya kuiminya midomo yake kila unapomwambia jambo ambalo anahitaji kulitafakari. Tabia hiyo huchukua nafasi yake ya kutabasamu, kucheka na kununa. Ndivyo alivyofanya nilipomweleza jambo hilo. Sikujua kama anatabasamu au amenipuuza. Nilisubiri kwa dakika nzima kabla ya kuipata kauli yake. Hivyo, nikaamua kumwambia, “Kama wewe hupendi kutembea nitakwenda peke yangu.”
Aliiminya tena midomo yake kabla hajasema, “Uwe mwangalifu sana.”
“Kwa nini? Nitapotea?” nikamuuliza.
“Si afadhali upotee!” alisema. “Hii ni Bagamoyo ndugu yangu. Jina halisi la hapa ni ‘Bwaga moyo’ maana ukifika hapa sahau kwenu, sahau yote unayojivunia. Hapa ni mwanzo na
mwisho wa maarifa.
Sikumwelewa. “Kwa hiyo,” nikamuuliza.
“Kwa hiyo, maana yake ni kwamba uwe makini sana na nyendo zako. Usione paka ukampiga jiwe. Utashangaa anageuka binadamu na kukuliza, ‘wanipigia nini? Nikikupiga miye utaamka weye?’
Nikaangua kicheko.
“Usicheke,” Ramadhani alinionya. “Sikutanii. Haya ni mambo ya kawaida hapa. Vilevile usithubutu kutamani mwanamke. Ukimtamani mke wa mtu utarudi kwenu umeota busha la tende. Na ukikutana na msichana mzuri ukamtaka, utashangaa atakavyokuchangamkia hata kukushawishi ufike nae kwao. Huko utakuta nyumba nzuri, vijakazi tele na utalazwa kwenye kitanda murua kinachonukia manukato. Lakini utakapomka kesho utajikuta umelala makaburini, peke yako.”
Hadithi zake zilinivunja nguvu. Hazikuwa hadithi mpya. Lakini zinakuwa na uzito wa pekee pale zinapozungumzwa ukiwa juu ya ardhi ya Bagamoyo, mzungumzaji mwenyewe akiwa mtu anayekuongoza kwenda kwa mnganga. Kwa kweli, zilipunguza sana ari yangu ya kuvinjari mji wa Bagamoyo.
Nadhani Ramadhani aliyasoma mawazo yangu. Nilimwona akiuvuta tena mdomo wake. Nikahisi kuona dalili za kicheko au tabasamu katika macho hayo, dalili ambazo zilifuatiwa na kauli yake aliyoitoa kwa sauti ndogo “Usiogope. Nenda katembee. Mimi najisikia uchovu bado. Natamani kulala usingizi mchana.”
Wafanyabiashara wa Kihindi na Waarabu ni sehemu moja ya kihistoria ya Bagamoyo. Wajerumani na Wamisionari wa dini ya kikristo ni sehemu ya pili ya mji huu wa kale wa Bagamoyo. Historia ilianza rasmi kunukuu kuwepo kwa mji huu toka karne ya kumi na tatu, wakazi wake wengi wakiwa wavuvi na wakulima. Mnamo karne ya kumi na nane familia kadhaa za kiislam, za ukoo wa mtu aliyejulikana kama Shamvi la Magimba aliyeishi Oman zilihamia Bagamoyo na kuifanya makazi yao. Wakaanza pia kuwatoza wenyeji kodi. Wakati huohuo biashara za chumvi, shanga na nguo zikishamiri. Biashara ambazo zilifuatiwa na ile ya watumwa wa pembe na za ndovu toka sehemu za ndani ya nchi kama Morogoro, Kigoma na hata Kongo. Wakati biashara ya utumwa ilipigwa marufuku rasmi mwaka 1873, mjini Bagamoyo biashara ilishamiri hadi mwishoni mwa karne ya kumi na tisa.
Hayo niliyafahamu kinadharia.
Sasa nilikuwa nikiyaona kwa macho yangu mwenyewe. Nilianza kwa kwenda kaskazini mwa mji huo ambako kulikuwa na eneo la Wamisionari wa kikatoliki. Lilikuwa eneo kubwa lenye majengo kadhaa likiwemo kanisa, shule, karakana za ufundi na miradi ya kilimo. Kwa mujibu wa kumbukumbu zangu misheni hii ilianzishwa mwaka 1868 kwa waislam kutoa ardhi hiyo kwa wakristo. Jambo hilo linaelekezwa kuwa lilizusha upinzani mkubwa toka kwa wenyeji, Wazaramo, ambao hawakuridhika wageni kugawa ardhi kwa wageni wengine ili waanzishe dini ngeni ambayo ilipingana na maadili yao.
Nilitembea nje ya majengo hayo, nikichungulia hapa na pale na kuvutiwa na kila nilichokisoma. Wafanyakazi wa misheni walikuwa katika pilikapilika zao, wanafunzi
wakiwa madarasani. Kwa mbali, nilimwona padri mmoja akitembea taratibu, rozali mkononi. Mara nikayakumbuka maisha niliyoyaacha katika misheni kama hiyo kule Kagera. Nikaikumbuka nafasi ya elimu niliyoipoteza. Kisha nilikumbuka hirizi yangu, hirizi ambayo niliamini kupotea kwake ndio chanzo cha mikosi na mikasa iliyoniandama. Nilihisi machozi yakinilengalenga. Nikageuka na kurudi nyumbani taratibu.
“Mbona mapema?” Ramadhani aliniuliza. “Hamu yako ya kuiona Bagamoyo imeisha mara hii?”
Badala ya kumjibu niliiminya midomo yangu kama ilivyokuwa kawaida yake. Nadhani alinielewa, kwani kwa mara ya kwanza nilimwona akiangua kicheko. Mie pia nikaangua kicheko. Tulicheka pamoja kwa dakika moja au zaidi bila sababu za msingi. Mimi nikimcheka yeye na yeye akinicheka mimi; tukio dogo, ambalo lilinifanya nijisikie karibu zaidi na ndugu yangu huyu. Nadhani naye alijisikia hivyo kwani toka hapo alikuwa rafiki zaidi kuliko ule udugu wetu wa awali.
Kesho yake Alhaji Suleiman alituamsha alfajiri, ili tujiandae kwa safari ya Mlingotini. Tulioga, tukapata kifungua kinywa na kisha kuanza safari hiyo ya miguu tukielekea kusini mwa mji. Nusu saa baadaye tulikuwa mbele ya nyumba ya Sheikh Mahmoud. Tulikaribishwa vizuri sana na mkewe na kukaribishwa kahawa kwa kashata na tende, ambazo nilizifurahia sana. Lakini pale mwenyeji wetu alipomweleza mama huyo haja yetu ya kumwona mzee, nilijiona nilivyokuwa mtu mwenye bahati mbaya.
“Hayupo,” “Kaenda wapi?”
“Kasafiri. Tena kaondoka alfajiri ya leo tu. Wamekuja
watu toka Darisalama kumchukua, akawasidie. Kama
mngejua, jana kashinda hapa hana kazi yoyote.”
Wote watatu tulitazamana kwa zamu. Kisha mwenyeji wetu akamgeukia mama Mahmoud na kumuuliza, “Atarudi lini?”
“Hakusema. Lakini huwa hakai nje muda mrefu. Anaweza kurudi kesho au kesho kutwa. Ningeshauri mje tena kesho au kesho kutwa, huenda akawepo.”
Tulishukuru tukaaga na kuondoka.
Mimi sikurejea nyumbani mara moja. Niliwataka udhuru wenyeji wangu kuwa ningependa kuendelea kuvinjari maeneo ya kihistoria ya Bagamoyo. Jiografia yangu ilionyesha kuwa toka hapo Mlingotini haikuwa umbali mrefu kuyafikia magofu ya Kaole, mji ule wa kale ambao kitendawili chake bado hakijateguliwa hadi leo.
Waliniruhusu. Wakashika hamsini zao nami nikashika hamsini zangu.
Nilipenya katika vichaka hadi kuyafikia magofu ya mji huo. Ilibidi kukaza macho ili kuweza kuona mabaki ya majengo ambayo yalionekana kama misikiti na majumba ya watu. Baadhi ya majengo hayo tayari yalifunikwa na ardhi na mimea kuota juu yake. Lakini kuta kubwa za mawe, milango yenye nakshi ya aina yake na sakafu imara zilitoa kila dalili ya maendeleo au ustaarabu wa watu walioishi mji huo. Kitu kingine kilichovuta macho yangu ni wingi wa makaburi yaliyojengwa kando ya majengo hayo. Ilionyesha kuwa wakazi hao ama hawakupenda kuwazika wafu wao mbali, ama mji huo ulikuwa maalum kwa ajili ya mazishi.
Mji wa Kaole machoni mwa wataalamu ni kama kitendawili kwa sababu kadhaa. Kwanza, kwa kila hali unaonyesha kuwa ulikuwa mji mkubwa uliokaliwa na watu
wengi. Lakini hadi sasa hakuna mtaalamu yeyote ambaye alipata kubaini bila mashaka nini kiliutokea mji huo na wakazi wake walikwenda wapi. Baadhi ya wataalamu hupata hisia kuwa huenda yalitokea maradhi mabaya ambayo yaliwateketeza wenyeji wote. Hisia hizo hupingwa mara moja kutokana na utafiti ambao haujapata kuonyesha mafuvu au mifupa ya watu iliyozagaa kuthibitisha tukio la aina hiyo.
Baadhi ya watafiti katika mji huo waliwahi kuchimbua sarafu iliyopata kutumika katika karne ya kumi na mbili. Sarafu ya Kilwa inaaminika kuwa ni moja ya zile za Sultan Ali Hassan ambaye alitawala Kilwa katika kipindi hicho. Uthibitisho mwingine unaoashiria kuwa Kaole na Kilwa ziliwasiliana kibiashara miaka hiyo.
Nilitembea katika magofu hayo moja baada ya jingine. Viumbe pekee hai niliowaona wakiwa ndege, mijusi na digidigi wawili niliowakurupusha. Nilipojiridhisha kuwa nimetimiza wajibu wangu kutembelea eneo hilo nilirejea nyumbani.
Kesho yake Alhaji Suleiman alikuwa na wageni. Alituruhusu mimi na Ramadhani kwenda peke yetu kwa Sheikh Mahmoud. Tuliarifiwa kuwa hajarudi.
“Jaribuni tena kesho,” mkewe alituelekeza.
Asubuhi hiyo mimi niliendelea na safari zangu. Nilitembelea lile jengo maarufu ambalo awali lilikuwa soko kuu la watumwa, binadamu wakipigwa mnada kama mifugo, jengo imara lenye kuta pana zilizopanda juu ambazo pia ziliweza kuhimili silaha hafifu za enzi hizo.
Wajerumani walipoitawala Tanganyika waliitumia ngome hii kama makao yao makuu ya jeshi. Hata hivyo, mwaka wa kwanza tu wa vita vikuu vya kwanza wajerumani walisalimu amri na kuikimbia Bagamoyo pale majeshi ya
Uingereza walipowamiminia mabomu toka katika mizinga yao ya melini.
Nilishuhudia kwa macho yangu makovu ya mabomu hayo na kushika kwa mkono wangu, mmoja wa mizinga ya Mjerumani iliyotekwa. Nikafurahi sana kwa fursa hiyo.
Kesho yake tuliamkia tena kwa Sheikh Mahmoud. “Hajarudi. Hatujui kapatwa na nini maana si kawaida
yake,” mkewe alisema sura yake ikiwa na dalili za wasiwasi na mashaka.
Niliendelea kuivinjari Bagamoyo. Kwa ushauri wa mmoja wa vijana mjini hapo nilitembea hadi eneo la Mbegani ambako nilishangazwa na wingi wa wanyama mbalimbali wa porini, wengi wao wakitembea hadi Pwani ya bahari kama mifugo. Walikuwa twiga, swala, korongo na pundamilia. Ndege wa aina mbalimbali pia waliipamba burudani hiyo ya aina yake kiasi cha kufanya nijione kama natazama picha ya sinema badala ya hali halisi.
Toka hapo nilitembea hadi mdomo ambao mto Ruvu uliingiza maji yake katika bahari, upande wa pili mji wa Bagamoyo. Hapo pia kuna burudani yake, kuona maji ya mto yanavyoshindana na yale ya bahari na bahari ikasalimu amri. Yakiwa maji yanayopita maeneo mbalimbali, maji haya yalibeba aina mbalimbali za taka ikiwa pamoja na udongo ambao ulifanya rangi ya maji eneo hilo hadi baharini ibadilike.
Nilirudi nyumbani nikiwa taabani kwa uchovu. Kesho yake nilichoka zaidi pale tulipokwenda tena kwa Sheikh Mahmoud na kukuta pana msiba, akina mama wakilia ndani, watani wakipita na kusema hili na lile bila kujali huzuni ya wafiwa.
“Kuna nini?” mmoja wetu aliuliza.
“Mzee Mahmoud amefariki.” “Lini?”
“Hatujapata uhakika. Kafia Darisalama. Maiti imeletwa
leo alfajiri.”
Nilipigwa na butwaa. Nguvu zikaniisha. Nikamkodolea macho Ramadhani ambaye pia alionekana kuduwaa, hajui lipi ni lipi.
Baadaye tulipata nusu ya ukweli toka kwa mtani wao mmoja Mluguru ambaye aliinuka na kuangua kicheko kabla hajasema, “Yako wapi? Siku zote nilimwambia akawa mbishi. Alijitia yeye bingwa wa kutoa majini na roho za watu. Mbona hili limemshinda? Achezee majini ya Kizaramo siyo ya Kimanyema. Amekwenda Darisalama, amelitania jini limemshikisha adabu. Yako wapi?”
Nilishtushwa sana na uzito wa maneno ya mtani huyo, ukizingatia kuwa hata maiti alikuwa yungali ndani. Ndugu wa marehemu walikasirika lakini hawakuwa na la kufanya. Hali ambayo ilifanya mtani huyo aongeze vijembe.
“Mnajua alitoa roho ngapi mzee wenu huyu? Mnajua kila roho inamngojea huko aendako na kijinga cha moto mkononi? Toka leo yeye ni mtu wa kuungua tu, usiku na mchana,” aliongeza huku akionyesha jinsi marehemu atakavyokuwa akirukaruka kwa maumivu ya moto.
Haikuwa rahisi kujizuia. Hata baadhi ya wafiwa
walicheka.
Mazishi yalifanyika mchana huohuo. Alhaji Suleiman aliendesha ibada ya mazishi msikitini na baadaye kwenye mazishi. Alisoma dua kadhaa hadi marehemu alipolazwa katika mwanandani. Tukatawanyika. Wana ndugu na majirani wakienda kulala matanga. Siye wengine tukirudi majumbani.
Mimi binafsi niliduwaa. Kitu fulani kilinifanya nishuku kuwa kifo hiki ni katika jumla ya mateso na mikasa dhidi yangu. Vinginevyo, kwa nini afe ghafla? Kwa nini afe hata kabla sijamtia machoni na kusikia ambacho angeongea juu ya masaibu yangu? Kitu gani hasa kinanitokea?
Mawazo hayo yalinitinga kiasi kwamba alinisemesha mara mbili bila ya kumsikia. Aliporudi kwa mara ya tatu nilisikia sauti yake bila ya kumwelewa. Nikamtaka radhi.
“Naona uko mbali sana,” alisema. “Nilikuwa nikikwambia kuwa wajuzi wa masuala yale wako wengi. Usivunjike moyo kwa kifo cha Sheikh Mahmoud. Kesho tu Alhaji atatupatia mtaalamu mwingine.”
Sikujua kama bado nilikuwa na hamu ya wataalamu zaidi, baada ya kifo cha kutatanisha cha mtalaamu huyu.
12
Ben R. Mtobwa
SURA YA KUMI NA
‘Mgeni’ Siku
K
esho yake ilikuwa Jumapili. Niliamka alfajiri, kabla ya mtu yeyote mwingine katika nyumba ya Alhaji Suleiman. Nikachukua ndoo ya maji
toka kwenye pipa la maji ya akiba na kuibeba hadi maliwatoni ambako nilioga. Nikarudi ndani na kuvaa nguo zangu safi, nikachana nywele zangu, kisha huyoo; nikaondoka zangu.
Kwa kweli, sikuwa na pa kwenda. Haja yangu ilikuwa kupata nafasi ya upweke ili niweze kuifikiria hatma yangu kwa kina. Upekee huo niliupata ufukweni, nilipoketi juu ya gogo la mnazi ulioanguka nikiitazama bahari. Macho yangu yaliweza kuiona mitumbwi ya wavuvi wawili watatu waliokuwa baharini wakitafuta riziki zao. Niliweza pia kuviona visiwa vya Zanzibar na Unguja, ambavyo kutoka hapa Bagamoyo ni mwendo wa kilomita thelathini tu kuvifikia.
Nikapata wazo. Kwa nini nisiachane na imani za kishirikina za kuwekwa alama au nyota kuchafuka na kuijaribu bahati yangu katika biashara? Kipindi nilichokaa hapo Bagamoyo nilikwishasikia na kujionea mwenyewe biashara mbalimbali zilizokuwa zikiendelea baina ya mji huo na visiwa vile. Biashara kubwa iliyonivutia ni ile ya chumvi.
Uzalishaji wa chumvi, toka katika mabwawa mengi
yaliyochimbwa kandokando mwa bahari nje kidogo ya mji wa Bagamoyo ilikuwa imeshamiri sana na iliuzwa maeneo mbalimbali ya pwani na bara. Niliichukulia kama biashara isiyo na madhara sana kwani kila mtu anahitaji chumvi katika chakula chake na ni bidhaa ambayo haiharibiki haraka kama nyanya au samaki. Kwa kuwa bado nilikuwa na akiba yangu ya fedha nilishawishika kumshauri kiongozi wangu wa msafara, Ramadhan, tuifanye kazi hiyo kwa muda kabla ya kurejea Pangani.
Wazo hilo lilinipa uhai mpya. Nikajiona nimechangamka. Nikainuka na kuanza kurandaranda juu ya mchanga wa bahari, ambao maji yake yalikuwa hayajarudi.
Mara nikasikia kengele ya kanisa ikilia kwa mbali. Ikanizindua. Nikakumbuka kuwa nilikuwa sijahudhuria ibada kwa muda mrefu sana, toka lilipotokea lile tukio la hirizi na kukimbia kwangu. Kuna ubaya gani nikienda kanisani? Nilijiuliza. Sikuhitaji jibu. Niligeuka na kuanza kutembea, kuelekea kwenye kanisa ambalo linadaiwa kuwa la kwanza Afrika Mashariki. Nilikuwa miongoni mwa waumini wa kwanza waliofika kujumuika na wenzao katika kumcha bwana.
Kana kwamba padri alijua kuwa katika waumini wake alikuwemo mmoja ambaye yuko njia panda kati ya imani ya bwana na ushirikina, mahubiri yake yalielekea katika kulaani vitendo hivyo na kumtegemea Yesu. “Alizaliwa kama mmoja wetu, akasulubiwa, akafa na siku ya tatu akafufuka. Damu yake ilitusafisha na laana ya asili. Tumefunguliwa minyororo yote ya dhambi. Jina lake ni dawa na jibu pekee la kila tatizo letu.” Padri alisema. Kuna wakati nilihisi kama alikuwa amenikazia macho mimi, kana kwamba anaisoma roho yangu kupitia katika macho yangu.
Mwisho wa ibada nilifikiria kumfuata padri ili niungame, lakini nikasita. Nitaungama kwa lipi? ‘Baba nimetenda dhambi! Nilipoteza hirizi ya babu! Nikamsukuma padri na kukimbia! Sasa naona mambo yangu yanakwenda mrama. Baba nisamehe!’ niliwaza. Atanielewa kweli? Niliwaza nikicheka mwenyewe kimoyomoyo.
Baada ya kutoka katika eneo la kanisa niliona bado ni mapema kurejea nyumbani. Nikaamua kurudi ufukweni na kuvinjari taratibu kuelekea kusini. Nilipita nikiitupia macho mikoko iliyonawiri katika maeneo mbalimbali ya mwambao huo wa bahari. Bila kutegemea nilijikuta nimefika tena Kaole. Nikachepuka na kuingia katika eneo lenye magofu yale ya kale, nikichungulia hapa na kupapasa pale kana kwamba nilitarajia kitendawili cha mji huo kiteguke, nijue ni watu gani hasa walioishi hapo, walianza kuishi lini na masaibu gani yaliwakuta.
Mawazo yangu yalisitishwa na mlio wa kitu kama chuma kilichogongana toka upande wa pili wa jengo la msikiti niliokuwa nikiukagua. Nilishtuka sana, nywele za utosini zikanisimama. Nikatulia na kusikiliza kwa makini. Zaidi ya nyimbo za ndege wa angani na milio ya wadudu wasiofahamika, palikuwa na ukimya mkubwa. Nadhani masikio yangu yamenidanganya; Niliwaza nikianza tena kutalii. Mlio ule ukasikika tena. Safari hii ukifuatiwa na sauti ya mtu aliyekohoa. Huku nikiwa na hofu, nilinyata kuelekea upande ule. Nikawaona. Watu wawili, mwanamume na mwanamke, walikuwa wameinamia gari wakihangaika kulitengeneza. Nadhani, kwa maelezo ya mwanamume, mwanamke aliingia ndani na kuwasha. Mlio uliosikika ulionyesha kuwa gari hilo lisingewaka kamwe. Mafuta yalikuwa hayaingii kwenye kabreta. Nikawasogelea.
Waliponiona wao pia walishituka kama mimi. Lakini baada ya kuniona kuwa ni mtu wa kawaida, sio mmoja wa mizimu ya watu wa kale, walichangamka na kunisalimu kwa Kiswahili chao cha mashaka. Niliwaitikia, baadaye nikawauliza kwa Kiingereza changu ambacho nadhani kwao kilikuwa cha mashaka pia, “Kuna tatizo gani?”
Walichangamka zaidi kuona naongea lugha yao. Mwanamume akaeleza. Gari lilikuwa linawaka, halipandi mafuta. Na joto lilikuwa likipanda kwa kasi kiasi kwamba gari isingeweza kutembea kwa dakika kumi kabla ya kuishiwa maji. “Unamjua fundi?” waliuliza.
Sikuwa mgeni wa magari mabovu. Uzoefu wangu wa lile gari la mzee Ayubu Kilole kule Mbeya na malori ya shambani mwa bwana Nicodemus Pangani vilinifanya nijue wapi pa kuanzia kabla ya kumhitaji fundi. Nikawaomba nichungule kidogo. Wakanipisha. Nikafunua tenki la maji. Yalikuwa yamekauka. Nikafunua gudulia la maji yatokayo kwenye injini. Lilikuwa limejaa pomoni. Nikayachukua na kuyamimina kwenye lile tenki la kupozea injini. Kisha nikakagua na kugundua mpira mmoja wa kupitisha hewa ambao ulikuwa umechomoka. Nikaurudishia. Nikaingia ndani ya gari na kuliwasha. Likawaka. Nikaiendesha kidogo kabla ya kusimama na kuwakabidhi ufunguo wao.
Hawakuamini. Walinikodolea macho ya mshangao huku mwanamke akitangulia, “Wewe ni nani?” aliuliza. Kisha akajitambulisha haraka. “Sisi ni mume na mke. Mimi naitwa Mary Leakey. Mume wangu ni Dkt. Louis Leakey. Tunatoka Uingereza. Lakini muda wetu mwingi tunautumia kufanya utafiti wa mambo ya kale. Hapa tunatafuta chochote ambacho tunaweza kupata juu ya masuala hayo.”
“Kwa kweli tunajihusisha na mambo ya kale zaidi ya haya,” mume wake aliingilia kati. “Tunatafuta ushahidi juu ya binadamu, kwamba aliishi Afrika Mashariki miaka milioni nyingi iliyopita. Hapa tumekuja kama kupitia tu. Tunafanya shughuli zetu zaidi huko Kondoa Irangi katika Bonde la Ufa.” Mumewe aliongeza.
“Wewe ni nani?” mkewe alirudia swali.
Walikuwa wakiongea Kiingereza kwa haraka sana. Lafudhi yao ikiteleza kiasi kwamba niliwaelewa kwa taabu. Nikajitahidi kuwajibu kwa Kiingereza changu cha kujikongoja. Nikawatajia jina langu na kazi yangu ya ukarani katika mashamba ya mkonge.
Mke alimtazama mume kama anayesubiri atamke neno fulani. Mume alimwelewa. Akanigeukia na kuniuliza, “Kwa nini usifanye kazi na sisi? Mikono yako ina miujiza kwenye mashine za gari. Bila shaka unajua kuendesha pia. Na unazungumza Kiingereza kwa ufasaha. Utatusaidia katika ukalimani pia.”
Mke akaongeza, “Hatuna pesa nyingi. Tunaishi kwa michango ya watu wengine pamoja na kujitolea. Lakini tuna hakika utakachokipata kitakuwa bora kuliko hicho unacholipwa huko kwa Wagiriki.”
Huku nikitabasamu, niliwashukuru kwa kunifikiria. Hata hivyo, niliwaambia, “Nimeamua kujaribu bahati yangu katika biashara.”
“Biashara gani?” Mmoja wao aliniuliza. “Ya chumvi” nilimjibu.
“Ina faida kweli?” mwingine aliuliza. “Nadhani. Watu wengi wanaifanya…”
“Hakuna kosa kubwa katika biashara kama kudhani,” Leakey mwanamume alinikatiza. “Biashara ni mahesabu.
Fanya hesabu zako kwa makini, toa gharama zote, jumuisha muda wako na uione faida kabla hujatumia fedha zako. Kinyume na hivyo ni hatari sana,” aliongeza.
Mkewe akadakia, “Nadhani unahitaji kulifikiria pendekezo hili. Tuko hapa siku mbili zaidi. Tutakuonyesha mahala tulipofikia. Kama utabadili mawazo tutakupokea kwa furaha.”
Tulirejea wote mjini. Kwa namna niliyoichukulia kama majaribio zaidi, akina Leakey walinitaka niendeshe mimi. “Lakini sina leseni,” nilijitetea, utetezi ambao hawakuafikiana nao. Nikawafikisha nyumbani kwa afisa mmoja wa Kiingereza, ambaye alitajwa kuwa mtaalamu wa masuala ya samaki wa baharini na uvuvi, nikawaacha. Nikatembea taratibu hadi kwa wenyeji wangu.
* * *
Kuna ule wimbo au shairi maarufu kwa wakazi wa Pwani, ambalo lilipendwa sana hapo Bagamoyo. Kama nakumbuka vizuri beti za shairi hilo zinasema;
Mgeni siku ya kwanza, mgeni siku ya pili,
mpe mchele la panza, Mpe maziwa na samaki,
Mtilie kifuuni, mali ikizidia,
Mkaribishe mgeni. mzidishie mgeni.
Mgeni siku ya tatu, Mgeni siku ye nne,
Nyumbani hamna kitu, mpe jembe akalime
Mna vibaba vitatu akirudi muagane
pika ule na mgeni. ende zake mgeni!
Mgeni siku ya tano, Mgeni siku ya sita, Mwembamba kma sindano mkila mnajificha, Nyumbani haiishi mnong’oni muingie vipembeni, atetwa yeye mgeni. afichwa yeye mgeni.
Mgeni siku ya saba Mgeni siku ya nane
si mgeni; ana baa! Njoo ndani tuagane!
Hata moto mapaani akitoka nje;
Atia yeye mgeni ! kwa heri, nenda mgeni.
Mgeni siku ya kenda, Mgeni siku ya kumi,
Enenda bwana, enenda! Kwa mateke na magumi,
Usirudi nyuma, hapana afukuzwaye,
Usirudi mgeni! Afukuzwa yeye mgeni.
Nilipata hisia kuwa wenyeji wangu, nyumbani kwa Alhaji Suleiman walikuwa wakiniimbia wimbo au shairi hilo nyuma ya kisogo. Hisia hizo ziliniingia akilini kuanzia Jumapili ya jana tu, mara baada ya kurudi toka kanisani na matembezini ambako nilikutana na akina Leakey.
Nilirejea nyumbani hapo kama saa tisa hivi. Ramadhani hakuwepo, Sheikh alikuwa chini ya mwarobaini, kando ya nyumba yake akisoma msahafu. Akina mama na watoto walikuwa katika pilikapilika zao kama kawaida. Hakuna mtu yeyote aliyeonekana kunichangamkia kama awali. Zaidi, hakuna yeyote aliyezungumza chochote juu ya chakula. Mie njaa ilikuwa ikiniuma, chango likinguruma tumboni kudai chochote. Nikatupa jicho la upelelezi jikoni. Jiko nalo lilikuwa limenuna. Halina dalili ya moto wala moshi. Nikadhani pengine nyumbani hapo hamkuwa na chakula siku hiyo. Hivyo, nikatoka
taratibu hadi sokoni ambako nilinunua changu wakubwa wanne, kilo kumi za mchele, nyanya, vitunguu na mchicha. Nikajitwisha mfuko wangu na kuupeleka nyumbani, ambako niliutua jikoni bila kupokelewa na mtu yeyote. Nikatoka tena na kutembeatembea ili nikirudi chakula kiwe tayari.
Nilirejea mida ya saa kumi na mbili. Jiko lilikuwa bado limenuna.
Nikalala na njaa yangu. Ramadhani alichelewa sana kurudi, akakuta tayari nimelala. Kesho yake nilipoamka kwenda maliwatoni nilishangaa kuwaona wale samaki wazuri niliowanunua wakiwa wametupwa katika pipa la taka. Sikuelewa. Mtoto mmoja wa kike wa Alhaji alikuwa akifagia uwanja. Nikamsogelea na kumuuliza kisa cha samaki wale kutupwa.
“Mama alisema walishachina, wasingefaa kuliwa.”
Sikuamini maneno yake. Ndiyo, mimi ni mzaliwa wa bara lakini si mshamba wa samaki wala mgeni wa mambo ya pwani. Maisha yangu katika ziwa Nyanza na katika Bahari ya Hindi pale Pangani yalikwishanitoa kabisa katika ugeni wa mambo hayo. Sikuwa mtu wa kununua samaki aliyeharibika. “Mbona hamkuniambia niwarudishe?” nilimhoji mtoto
huyo.
“Sijui mwenyewe mama,” alinijibu.
Ni hapo wimbo ule wa watu wa Mafia uliponirudia
akilini.
‘Mgeni siku ya kwanza…’ nikaingia maliwatoni. Nilipotoka nilimwamsha Ramadhani na kumuuliza kulikoni. “Ukarimu wa wenyeji wetu umetoweka ghafla. Hata chakula nilichonunua kimetupwa. Waswahili mnamsemo kuwa ‘Akufukuzwaye hakuambii toka,’ nisingependa kuamini hivy
lakini kuna kila dalili, kulikoni?”
Ramadhani alisita kwa muda, kisha akanitaka nimsubiri naye aoge ili twende tukazungumze faragha. Tulikwenda hadi kwenye kijimgahawa ambako kwa njaa niliyokuwa nayo nilikunywa vikombe vitatu vya chai na chapati sita. Ramadhan alikunywa kikombe kimoja kwa chapati mbili.
“Ni kosa lako mwenyewe.” Baadaye alisema. “Kosa langu! Kosa gani?”
“Kwa nini ulikwenda kule?” “Kwenda wapi?
“Kanisani.”
Nikashangaa. “Kwani kuna ubaya gani kwenda kanisani?” Nikamuuliza. Ramadhan aliiminya midomo yake kama ilivyo kawaida yake kabla hajatoa hotuba yake fupi, “Kwako wewe hakuna ubaya wowote. Lakini si kwa Alhaji Suleiman. Yeye dini haiko rohoni mwake pekee. Iko akilini na katika damu yake. Ukizingatia kuwa ameutumia muda wake mwingi kukutafutia maalim ambaye anagekusaidia, akijua fika kuwa wewe mwislam safi, taarifa za kuonekana kwako kanisani zilimsononesha sana. Kwa bahati mbaya hata mimi sikujua hilo. Nafikiri hata baba hakujua wala kupata kufikiria kuwa wewe si mwislam!”
Nikazidi kushangaa. Kwa nini mtu amezwe na dini kiasi hicho? Sisi wote ni viumbe wa Mungu. Suala la imani ni la mtu binafsi. Wengi wetu tumerithi dini toka kwa wazazi wetu ambao nao walirithi kwa wazazi wao. Suala la kuwa dini fulani ndiyo hasa inayokubalika na Mwenyezi Mungu ni midahalo ileile ambayo haijapata na haitokaa ipate ufumbuzi. Nilitamani kumwambia hayo Ramadhan, lakini nilisita. Yasingenisaidia mimi wala kumsaidia yeye kwa lolote lile.
“Kwa hiyo, sina budi kuondoka,” nilimwambia. Alitafakari kidogo kabla ya kuuliza, “Lini?”
“Leo.” Nilimjibu. “Haifai kuishi chini ya paa la mtu ambaye unamkera na kumkinaisha.”
“Leo hakuna jahazi la kurudi Pangani. Kesho lipo,” alinidokeza.
Nilimshangaza pale nilipomwambia kuwa sina mpango wa kurudi Pangani haraka. Nikamweleza nia yangu ya kumshirikisha katika biashara ya chumvi kati ya Bagamoyo na Zanzibar. “Tutapata hela za kutosha. Tutarudi pangani tukiwa matajiri.”
Ramadhan aliyatafari maneno yangu kwa makini. Nilihisi akishawishika. Lakini kitu fulani kilimfanya asite. Nilishuku kuwa kitu hicho kilitokana na mkasa wa dini ambao uliibuka kati yetu na kujenga ukimya ambao haukuwepo. Baada ya ukimya mrefu aliniambia kuwa lazima arudi Pangani, asingefanya shughuli yoyote bila idhini ya baba yake.
Kwa hiyo inabidi tuagane,” nilisema nikitia mkono wangu mfukoni na kutoa fedha ambazo nilizichambua na kumkabidhi sehemu ya fedha hizo.
“Za nini?” Aliuliza kabla hajazipokea. “Zitakulinda njiani. Lolote laweza kutokea.”
Akazipokea. Macho yake yalionyesha masikitiko makubwa. Mie pi nilinyong’onyea kumpoteza ndugu na rafiki ambaye nilikuwa na ndoto za kufanya naye mambo mengi.
Tuliporejea kwa Alhaji tulikuta tayari ametoka. Nikamshukuru mkewe na wanawe na kuwataka radhi kwa lolote nililowakosea. Niliwaona wakiyakwepa macho yangu. Nikaingia ndani na kuchukua kilicho changu, kisha huyoo, nikatokomea katika mji wa Bagamoyo. Sikutaka kuisubiri siku
ya kumi kama yule mgeni wa kale. Ya tatu tu ilitosha.
Wakati nikitafuta nyumba ya wageni nilifikiri harakaharaka. Wazo la biashara ya chumvi lilianza kunitoka. Niliona wazi kuwa nisingeweza kuifanya peke yangu; kubeba, kupakia na kupakua magunia ya chumvi nzito. Pia, sikuwa na mwenyeji ambaye kwake pangekuwa kituo changu cha biashara. Chumvi si biashara ya kuweka katika vyumba vidogo vya wageni. Hivyo, nikafikia uamuzi wa kuacha. Wazo la kurudi Pangani kuendelea na kazi ya unyampala katika mashamba ya mlonge niliachana nalo. Licha ya mshahara duni kazi yenyewe haikuwa ya kimaendeleo. Sikuwa na jipya la kujifunza wala matarajio yoyote kukua kitaaluma. Ni hapo nilipowakumbuka wale Wazungu na kuamua kuipokea kazi yao ya ajabuajabu.
Jioni hiyo niliwafuta na kuwaarifu juu ya uamuzi wangu. Walifurahi sana.
* * *
Tulianza safari kesho yake. Haikuwa safari ya Kondoa moja kwa moja. Leakey aliamua tupite Dar es Salaam ambako alitaka gari lipate matengenezo makubwa. Pia alikuwa na nyaraka fulani ambazo alihitaji kuziwasilisha.
Safari ya Dar es Salaam ilinisisimua sana. Nilikuwa nimesikia mengi juu ya mji huo. Mji mkuu wa nchi ambao ulikuwa na bandari maarufu katika mwambao huu wa bahari. Chimbachimba zangu katika vitabu vya historia zinaniambia kuwa Dar es Salaam ni mji wa kale pia ingawa ni sawa na Kilwa au Bagamoyo. Kwamba, mji huo asili yake ni kijiji kidogo cha wavuvi kilichoitwa Mzizima, ambacho haikujulikana kilianza vipi au lini. Kumbukumbu za maandishi juu ya Dar
es Salaam zinaanzia mwaka wa 1865 pale Sultan Sayyid Majid wa Zanzibar alipoitembelea Mzizima. Alivutiwa sana na shughuli za uvuzi na biashara zilizokuwa zikifanyika hapo kwa amani na utulivu. Akaamua kuhamishia himaya yake hapo na kupaita Bandur ul Salam. Jina hilo lilibadilika taratibu na kuwa Dar es Salaam kwa maana ileile ya bandari salama.
Kama ilivyokuwa kawaida ya Waarabu wengi enzi hizo, Sultan aliifanya Dar es Salaam kituo kikubwa cha kupokelea biashara haramu ya watumwa, mizigo na pembe za ndovu. Bidhaa hiyo zilisafirishwa hadi Zanzibar na baadaye nchi za mbali. Sultan huyo alifariki mwaka 1870.
Mrithi wake alikuwa na mapenzi na Bagamoyo zaidi ya Zanzibar. Mashua nyingi za biashara zikahamishiwa huko. Umaarufu wa Dar es Salaam ulipungua zaidi baada ya mwaka 1873 pale jitihada zilizosimamiwa na Waingereza za kuteketeza biashara ya utumwa zilipozaa matunda. Lakini uhai huu ulirejea tena 1887 pale Wajerumani walipoipokonya Tanganyika na kuanzisha ujenzi wa bandari ya Dar es Salaam kwa kasi. Na mwaka 1912 pale ujenzi wa reli ya kati ulipoanza kwa kishindo Dar es Salaam ilizidi kushamiri. Dar es Salaam ilitamalaki zaidi baada ya vita kuu ya pili, pale Mwingereza alipomshinda Mjerumani na kuifanya Dar es Salaam makao makuu ya serikali yake.
Safari ya Dar es Salaam, toka Bagamoyo ni fupi sana. Ni umbali wa kilometa zipatazo sabini na tano hivi kwa ajili ya uduni wa barabara, ikiwa na mashimo mengi, sehemu nyingine mchanga na hata makorongo ilituchukua masaa manne kuwasili katika mji huu. Tulipita vijiji mbalimbali vyenye watu na nyumba chache; Kaega, Bunju, kunduchi na vinginevyo. Njiani mito ya msimu kama Mpiji, Tegeta na
Kunduchi ambayo yote, nyakati za masika huendeleza tabia ya asili kumimina maji yake yote, hadi tone la mwisho, katika bahari, ambayo kamwe haitosheki.
Leakey na mkewe ni watu ambao hawakujua kitu kinachoitwa uchovu. Mara baada ya kufika kwa mwenyeji wao, kula na kuoga waliamua kuingia mjini kuendelea na shughuli zao. Mie waliniruhusu kupumzika. Lakini mie pia sikuwa mtu wa kupumzika. Nilifuatana nao. Leakey aliendesha gari kwa uangalifu zaidi, kwani tofauti na Bagamoyo hapa hazikupita dakika tano kabla ya kupishana na gari jingine. Kwa maelekezo ya mwenyeji wake alilipeleka gari lake Kariakoo, kwa fundi wa Kigoa, ambaye aliaminika zaidi.
Kariakoo, enzi hizo ikiwa kama kijiji ndani ya mji, ilikuwa na sifa zote za mji. Eneo maarufu zaidi lilitemwa kando kidogo ya soko kuu zamani pakiitwa ‘pombe shop’ ambapo mamia ya watu walijumuika kila jioni kunywa pombe ya mnazi, kahawa kucheza bao na pilikapilika nyingine tele. Bendi mbalimbali za muziki pia zilitumbuiza siku za sikukuu na mwisho wa wiki.
Eneo jingine lililotamba likiwa lile la kilabu cha wazee walioshiriki vita kuu. Jengo lao likiwa kandoni mwa barabara iendayo Morogoro, likiwa na ukubwa wa ukumbi wa muziki, eneo la kuuzia ‘mnazi’ na vinywaji vingine lilikuwa fahari kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam. Hadithi za matukio ya vita zikisimuliwa, waliopotea vitani wakikutana na kubadilishana mikasa, waliopoteza maisha walikumbukwa, umaarufu wa eneo hilo ulikuwa mkubwa.
Fundi huyo na wasaidizi wake walilivamia gari kama nzige. Huyu alishika spana hii na kufungua pale, huyu alifunua kile, huyu alilala chini ya gari dakika kumi baadaye injini nzima ilikuwa imefumuliwa. Fundi mkuu alikagua
kifaa baada ya kifaa na kutuagiza kurudi baadaye ili awe ameandaa orodha ya vifaa vitakavyohitajika kununuliwa na vipi vitafanyiwa matengenezo. Nilitumia fursa hiyo kuagana na akina Leakey kwa maelezo ya kukutana nao hapo kwa fundi baadaye.
“Angalia usipotee. Hapa siyo Bagamoyo.” mkewe alitania.
Nikacheka kabla ya kumjibu, “Kama kupotea ningepotea zamani. Nimekuwa mtu wa kiguu na njia toka utotoni.”
Mara tu walipoondoka niliuliza lilipo soko la Kariakoo. “Shuka hapa, mtaa ule ingia kushoto, utaliona,” mmoja kati ya mafundi wasaidizi wa Goa alinielekeza. Nikayafuata maelekezo yake.
Soko lilikuwa pale, likinisubiri. Pilikapilika tele za biashara za nafaka, dagaa, samaki, nazi, matunda na kila unachoweza kufikiria zilikuwa zikiendelea kama kawaida. Kwa mara nyingine nikawa shahidi wa historia ya yote niliyopata kusikia juu ya soko hili.
Toka hapo niliomba kuelekezwa iliko shule ya Msimbazi. Haikuwa mbali kutoka hapo. Nilienda na kujionea mwenyewe majengo ambayo yalimhifadhi Shaaban Robert kwa miaka minne na kumpa ule ujasiri wa aina yake. Yalikuwa pale. Na wanafunzi wengine walikuwa pale, pia waliandaliwa au kujiandaa kuyakabili maisha yao ya baadaye.
Kelele za wanafunzi waliokuwa nje ya madarasa, usafi wa sare zao na utulivu wa wale waliokuwa madarasani, vitabu vilifanya, kwa mara nyingine tena niyakumbuke maisha ya shule na kuyatamani. Nikayakumbuka hata madaftari niliyoyaacha Pangani, ambayo sikupata kutengana nayo kwa miaka nenda rudi iliyopita. Ndoto za kurudi shuleni zikanirudia
huku nikijinong’oneza. Umeshakuwa mtu mzima Mtukwao. Huoni ‘shikamoo’ zinavyokuandama?
Haikua uongo. Kama ilivyokuwa Pangani, Bagamoyo na sasa Dar es Salaam nilipokea heshima. Nami nikajifunza kuitoa kwa kila aliyeonekana kunizidi umri. Kwa wale ambao hirimu yetu ilionekana moja tulipeana ‘Assalaumaleikum’ au ‘Saballakheri’ kabla ya maongezi zaidi. Tabia hiyo nilijifunza hasa kule Pangani baada ya tukio moja lililonitia aibu. Kuna jambo nilitaka kuuliza; ama njia ama kumuulizia mtu. Mzee mmoja mwenye upara na ndevu nyingi nyeupe aliketi juu ya kiti mbele ya nyumba yake. Nilimsogelea na kumuuliza hicho nilichotaka kumuuliza. Alinikodolea macho kama mtu ambaye hanisikii. Nilirudia swali langu mara tatu bila mafanikio. Nikamwacha na kwenda nyumba ya jirani. Baada ya kuwauliza hicho nilichotaka kuuliza niliwahoji iwapo yule jirani ni bubu.
“Hapana kwa nini?” Walihoji kwa mshangao. “Maana namsemesha hajibu,” niliwaeleza.
Wakacheka, kisha mmoja wao akaniuliza kama nilimwamkia kabla mzee Yule.
“Hapana.” Nilikiri.
“Unaona?” Alisema akicheka. “Mzee yule kama hujamwamkia hata umwulize mara ngapi hakujibu.”
Niliporejea gereji akina Leakey walikuwa hawajafika. Niliketi na mafundi ambao tayari walimaliza kazi yao wakimsubiri. Walikuwa katika ubishi, juu ya mechi ya mpira ambayo ingechezwa mwishoni mwa wiki ijayo. Ilielekea kuwa kati ya mafundi hao walikuwemo washabiki wa klabu moja waliyoitaja kama Yanga na ya pili waliyoiita Sunderland. Yanga ilitajwa kama timu kongwe zaidi ya Sunderland. Sikuwa mjuzi wa masuala ya mpira wa miguu, hivyo sikufatilia sana mdahalo huo.
Akina Leakey waliporudi walionyeshwa vifaa vilivyohitaji kununuliwa. Wakatoa pesa, tukaondoka kwa ahadi ya kulichukua gari hilo kesho yake jioni. Hali hiyo iliyonipa nafasi nyingine nzuri ya kuendelea kuivinjari Dar es Salaam ya enzi hizo. Niliwaomba akina Leakey na wakaniruhusu kulala mjini, katika nyumba ndogo ya maeneo hayohayo ya Kariakoo, badala ya kufuatana nao Oysterbay.
Jioni hiyohiyo nilianza kufaidi Pwani ya Dar es Salaam. Nilikuwa nikipita katika moja ya mitaa ya kitongoji hicho. Macho yangu yakavutwa na kundi kubwa la watu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto ambao walikuwa wakitembea huku wakicheza na kuimba. Mchezo wao ulikuwa wa kusisimua sana. Wakiongozwa na mdundo wa ngoma, ambazo wapigaji wawili walizipiga kifundi wachezaji walikuwa wakichezesha viungo vyao, miguu ikipiga hapa na pale huku wakirusha viuno ambavyo vilifungiwa kanga iliyokunjwa. Nyimbo zao pia zilikuwa za kusisimua, sehemu mchanganyiko wa beti za ngonjera, mashairi na sehemu zilizojaa mafumbo na ucheshi. Wimbo mmoja ulisema;
Nimeinama, nimeinuka, Nimeokota kidude.
Wachezaji walicheza huku wakionyesha ishara za kuinama na kuinuka. Kila ngoma ilipokolea msafara ulisimama kwa dakika mbili tatu na kuwaburudisha watazamaji kabla ya kuendelea tena. Hali iliyopelekea watu wengi zaidi kutoka majumbani mwao, kuja kushangilia, huku wengi wao wakijiunga na msafara huo wa kushiriki katika kucheza na safari ambayo ni wachache waliojua ambako ingeishia.
“Mdundiko huo kijana,” mzee mmoja aliniambia. Yeye alikuwa hatazami ngoma. Alikuwa akinitazama mimi, bila
shaka akiwa amevutwa na mshangao aliouona katika macho yangu. “Mdundiko mwanangu,” aliongeza. “Ngoja ya Kizaramo, ingawa Wandengereko, Wakware na makabila yote ya Pwani yanaicheza.”
“Inaashiria nini?” nilimuuliza.
“Mambo mengi. Inawezekana mwali anatolewa nje mahala fulani au msichana anachezwa unyago,” aliongeza.
“Mbona kila mtu anacheza?”
Alicheka, “Mdundiko haina uchoyo. Ni ngoma pekee duniani ambayo haina mwenyewe. Kila mtu ana uhuru wa kuiburudisha roho yake kwa kujimwaga uwanjani na kuonyesha uwezo wake. Ngoma hiyo inaweza kwenda hadi Ilala na hata Temeke bado ikawa na umati mkubwa hivyohivyo. Ikiisha utasikia taarifa za watoto na hata watu wazima kupotea, kwani wengi huifuata bila kuangalia wanakotoka au wanakokwenda,” aliongeza.
Wakati huo ngoma ilikwishatuacha na kuendelea na hamsini zao. Nami nikashika hamsini zangu kwa kuendelea kukata mitaa. Nilitembea taratibu na kuiacha Kariakoo, kwa kuifuata barabara ya Morogoro hadi nilipofika bandarini.
Bandari ya Dar es Salaam kweli ni ‘Bandari Salama.’ Jiografia yake inathibitisha hivyo. Bahari kuu ikiwa nje ya bahari hiyo, upo mdomo wa bahari ambao unawezesha meli kuingia na kutoka bandarini humo kama mtu anavyoingia ndani ya nyumba yake baada ya misukosuko mingi ya baharini kama dhoruba za upepo mkali pengine pamoja na viumbe kama papa ambao hawawezi kuvumilia maisha katika eneo finyu kama hilo.
Nilitembea kuifata pwani hiyo hadi mbele ya mdomo wa bahari hiyo, ambayo ulitenganisha mji na sehemu
niliyodokezwa kuwa inaitwa Kigamboni kwa eneo la takriban meta mia mbili. Eneo ambalo lilikaliwa na wavuvi wengi. Nikiwa nimesimama hapo, nilipoambiwa kuwa panaitwa Magogoni, niliweza kuona mitumbwi ya wavuvi ama ikijishughulisha na uvuvi au kuvusha watu toka upande mmoja hadi mwingine.
Niliamua kupoza kiu yangu kwa kunywa maji ya dafu baada ya kumwona muuzaji akipita karibu yangu na tenga la madafu juu ya baiskeli yake.
“Unataka gumu au laini?” Aliniuliza. “Kwani kuna tofauti gani?”
“Gumu ni lenye nyama na maji matamu zaidi. Laini halina nyama, maji yake kidogo yana chumvi.”
Niliomba laini. Nikanywa maji na kufaidi ujiuji wake badala ya gumu ambalo nyama zake mara nyingine hufanana na nazi.
Wakati nikirejea, juu kidogo ya Pwani hiyo ya Magogoni nilionyeshwa jengo ambalo nilidokezwa kuwa ni makazi na ofisi ya Gavana. Sikuweza kuvumilia, nikachungulia. Macho yangu yalivutwa na bustani kubwa ya miti mbalimbali iliyooteshwa, mingi ikiwa ya asili. Niliweza kuiona miti kadhaa, ambayo babu alipata kunitajia majina yake wakati tukisafiri kwa miguu miaka ile iliyopita.
Kitu kingine kilichonivutia katika Ikulu hiyo ni ndege. Ilionekana kama shamba la wanyama kutokana na ndege aina mbalimbali waliokuwa wakiruka, kuimba na kucheza toka mti huu hadi ule, tawi hili hadi lile. Ndege walionivutia zaidi ni tausi. Walikuwa wengi, waliimba na kutembea kwa maringo kana kwamba wao ndio walikuwa wafalme na malkia wa bustani hiyo. Tausi mmoja, mwenye mkia mrefu na rangi ya kuvutia, alinizawadia kwa kunifunulia mkia wake na kuufanya
ugeuke kuwa mfano wa ……. mzuri wenye mchanganyiko wa rangi ya dhababu, almasi na lulu.
Ningeendelea kuduwaa hapo kama askari mmoja asingetokea na kunifukuza. Nikaondoka na kuifuata barabara inayotokea hapo Ikulu, ambayo nayo ni burudani tosha kwa miti asilia tele, iliyooteshwa kila upande na kuipa barabara kivuli na hewa murua tofauti kabisa na maeneo mengine ya mjini ambayo hayakutofautiana sana na jangwa.
Sikuwa na haraka. Nilitembea taratibu nikitazama hapa na pale. Nilipita katika bustani ya Mnazi mmoja, yenye maua na miti ya vivuli. Nikaiacha na kufika maeneo ambayo hayakuwa na watu hadi nilipofikia hoteli yangu. Ilikaribia saa mbili za usiku.
Wakati tayari nimeoga na kupiga mswaki nikijiandaa kulala mtaa wa pili zilisikika kelele za muziki. Sikuwa mpenzi sana wa muziki. Lakini ile midundo na tungo zao mara nyingi zilinisisimua. Hivyo, sikuhitaji kuambiwa kuwa muziki huo ulikuwa wa mwanamuziki mahiri, Hamisi Machapti aliyekuwa akiongoza Dar es Salaam jazz, bendi kongwe iliyozaliwa mwaka 1933.
Nilimsikiliza kwa muda kabla ya usingizi kunichukua.
Kiguu n1a Njia
3
SURA YA KUMI TATU?
Ya Kingalu wa Morogoro?
“Petro!”
Nilishtuka kidogo lakini sikugeuka. Nani
ananifahamu mimi katika mji huu wa Dar es
Salaam? Zaidi, nani ananifahamu kwa jina hilo la Petro ambalo sina tabia ya kulitumia mara kwa mara? Nikaendelea na hatua zangu, moja baada ya nyingine; nikiwafuata kina Leakey ambao walikuwa wamesimama nje ya gari lao, tayari kwa safari yetu ndefu.
“Petro!” Sasa mwitaji alikuwa nyuma yangu. Pumzi yake, wakati akiniita, ikikifikia kichogo changu. Nikahisi mkono wake ukinigusa bega. Kwa sauti ya kujiamini zaidi nilimsikia akisema, “Wewe ni Petro Kionambali. Sidhani kama nitakuwa nimekosea.”
Nikageuka kumtazama. Aliyesimama pale alikuwa mtu ambaye kamwe nisingeweza kumsahau, mtu ambaye alisababisha safari yangu ya kielimu ivunjike mwanzo tu wa safari. Mtu huyo ndiye chanzo cha mikasa na masaibu yote yanayonipata. Nikamkodolea macho ya mshangao.
“Usiniambie kuwa hunikumbuki?” alisema akitabasamu. “Wewe si yule Petro wa hirizi”
“Ndiye” nikamjibu “Na wewe nakukumbuka vizuri sana.
Unaitwa Byabato. Tulikuwa wote kule Kagera.”
“Naam halafu ukapoteza hirizi yako,” akakumbushia. “Naam, na wewe ukaiokota.”
“Kabisa. Nikaipeleka kwa faza Backhove akaamua kuichoma moto hadharani…”
“Mie nikaikwapua na kukimbia nayo.”
Tulipofika hapo Byabato akaangua kicheko kisha akasema huku akiendelea kucheka, “Ikakuponyoka tena. Nikaiokota tena. Nikamrudishia faza. Akiwa amekasirika sana faza aliichukua na kuitumbukiza ndani ya moto kwa mkono wake mwenyewe.”
Taarifa yake ya mwisho ilikuwa habari mpya kwangu. Kumbe hirizi yangu ilipatikana na ikatiwa moto? Nikamtazama kwa macho yenye maswali mengi ambayo aliyasoma na kuyajibu baadhi.
“Hirizi haikuungua,” alisema. “Haikuungua? Ilikuwaje?” “Ilikataa kuungua!”
“Ilikataa kuungua! Kwa vipi?” nilizidi kushangaa. “Ilikataa tu. Ilikuwa hirizi ya ajabu sana na imeacha
historia kubwa. Kila ilipotupwa katika moto ilidunda na kuchupa kama chura hadi nje ya moto huo. Tukio hilo lilirudiwa zaidi ya mara tano, lakini hirizi haikukubali kuungua. Kila mtu alishangaa. Padri akaamua ikatupwe ziwani, mbali kabisa ya nchi kavu. Nadhani walifanya hivyo, ingawa baadhi ya wanafunzi wanadai padri aliihifadhi ili ipelekwe kwao ikafanyiwe uchunguzi wa kina.
Hirizi yangu ilikuwa na maajabu hayo! Niliwaza kwa mshangao. Nikamkazia macho Byabato kuona kama alikuwa akisema ukweli au uongo. Siku zote shuleni pale alijulikana
kama mwanafunzi mzushi, mchangamshi na mwongo lakini kwa hili alionekana kuwa alikuwa akisema ukweli.
Nikamtazama kwa makini. Zaidi ya kuwa mnene zaidi na mweusi zaidi hakuwa amebadilika sana. Alikuwa amevaa nguo za kuvutia. Viatu vyeusi, suruali nyeusi na shati jeupe ambalo liling’ara zaidi kutokana na tai nyekundu iliyokuwa ikining’inia shingoni mwake. Sauti yake pia ilikuwa ya kujiamini zaidi.
Yeye pia alikuwa akinitazama kwa makini. Alivutiwa na suruali yangu ya kijivu, shati la buluu na jaketi la kahawia nililovaa. Miguuni nilikuwa na viatu vya bei ya kuridhisha. Nilimwona akiwa na dalili zote za kuridhishwa na hali yangu ya kiuchumi.
“Haya, ulipata wapi?” alihoji ghafla.
“Nini?”
“Hirizi ile. Unajua haikuwa hirizi ya kawaida uliipataje
ile?”
“Achana na mambo yale.” Nilimwambia. “Yamepitwa na
wakati.”
Akacheka kabla hajaongeza swali jingine. “Halafu kwa nini ulikimbia?”
“Ilikuwa utoto tu.” Nilijibu na mimi na kumtupia swali harakaharaka. “Na wewe kwa nini ulipoiokota uliipeleka kwa padri badala ya kunirudishia mwenyewe?”
“Ilikuwa ni utoto vilevile.”
Jibu lake lilinifariji kiasi. Nikamchukulia kuwa amekuwa kiakili na kitabia hivyo, nikataka kujua mengi zaidi juu yake. Nikamuuliza anafanya nini hapo Dar es salaam.
“Naishi huku. Huu mwaka wa tatu sasa. Niko shule ya Minaki. Naendelea na kidato cha tano.” Alisema kwa sauti ya
majivuno kidogo. “Na wewe?”
Nilifikri kidogo kabla ya kumpa hadithi yenye uongo kidogo iliyochanganyika na ukweli mwingi. “Mie nilipowaachia ile shule yenu nilienda Uganda. Kule nilimaliza kidato cha nne na sasa nipo mwaka wa pili wa Chuo Cha Makerere. Nipo hapa na maprofesa wangu. Wale pale wananisubiri. Tuko katika utafiti wa mambo ya kale. Hivi unanvyoniona tumetokea Bagamoyo kwenye magofu ya Kaole na tunaelekea bonde la ufa kwa ajili ya utafiti wa mtu wa kale.”
Kama kuna mtu aliyepigwa na butwaa siku hiyo hakuwa mwingine zaidi ya Byabato. Alipogeuka na kuwaona wazungu wale wakiwa wamesimama nje ya gari lao katika hali ya kunisubiri pengine pamoja na ubora wa mavazi yangu aliamini mara moja. “Unajua tulidhani umeliwa na fisi kule porini ulipokimbilia?” Baada ya muda alisema.
“Fisi au mamba wa ziwa Nyasa?” Nilihoji nikicheka. “Hapana. Niko hai. Tuko pamoja katika kuitafuta elimu ili tuweze kuitumia vyema kuitumikia nchi yetu mara mkoloni atakapoondoka.” Nilisema kwa kujiamini huku nikimtaka radhi ili niwawahi ‘Maprofesa’ wangu.
Nilimwacha kasimama palepale. Macho kayakodoa kwenye gari hadi ilipowashwa na kuondoka kwa mwendo wa kasi.
* * *?
Gari lilikuwa limepona. Mlio wa mashine ulidhihirisha hivyo, ukiulinganisha na ule wa awali, kabla ya matengezezo ambao haukutofautiana na ule wa ng’ombe mgonjwa anayevutwa kupelekwa malishoni kwa nguvu. Tuliteleza tukaiacha Kariakoo, Ubungo na hatimaye kibaha. Toka
hapo tulifika Chalinze ambako tulisimama kidogo, akina Leakey wakibisha iwapo tuelekee kaskazini kwa kuifuata njia inayoelekea kaskazini ambayo ingetupeleka hadi Kilimanjaro na Arusha kabla ya kwenda Kondoa Irangi au ile ya moja kwa moja ambayo ingetufikisha Morogoro, Dodoma na hatimaye Kondoa. Waliafikiana tuifuate ya Morogoro.
Ilikuwa safari yangu nyingine ya kuvutia. Mazingira yaliyoizunguka barabara yalikuwa na rasilimali tele za kusisimua. Uwanda mpana wa mto Ruvu. Ambao ulitosha kuwa malisho murua ya ng’ombe ulikuwa pale, umetulia tuli kama bustani ya aina yake, iliyokuwa ikisubiri kutumiwa. Bustani ambayo kwa wakati huo ndege kama yangeyange na korongo walikuwa tele mbele ya macho yetu wakiifaidi.
MilimayaUluguru,ambayoilitulakiilikuwaimeusimamia mji kama inayoulinda, ilikuwa burudani nyingine ya kuvutia. Ukiwa unameremeta kwa rangi ya kijani, iliyotokana na msitu mkubwa uliouzingira, mlima huo uliashiria kila dalili ya kuwa chanzo cha mvua kubwa, mbolea na utajiri wa kila aina ya mti, wanyama, ndege na wadudu waliojihifadhi humo. Nilikumbuka kusoma mahala fulani kuwa msitu huo, ambao unaangukia upande wa pili wa mji, unakisiwa kuwepo kwa zaidi ya miaka milioni ishirini na tano. Waluguru wengi hadi leo wanadaiwa kuendesha matambiko yao kimila ndani ya msitu huo.
Licha ya msitu, Morogoro ilijaliwa mito na mabwawa mengi kama mto Wami, bwawa la Mindu, Kidatu na Kihansi ambayo si kwamba huwapatia wavuvi mahitaji yao tu, bali pia pamoja na nguvu za umeme ambazo sehemu kubwa ya nchi inazitegemea.
Mama Leakey hakuweza kujizuia. Mara kwa mara alishuka kwenye gari na kupiga picha za maeneo na matukio
mbalimbali, huku uso wake ukiwa na furaha tele.
Tulisimama kidogo hapo Morogoro ili tupate mlo wa mchana. Tulisimama mbele ya hoteli moja ndogo, katika eneo la Kinole. Kwa mshangao wetu tulikuta hoteli hiyo imefurika, kitu kama sherehe za kikabila zikiendelea.
“Kuna nini hapa?” Leakey aliuliza.
“Nipe dakika tano nitakuwa na jibu,” niliwaambia wakiketi katika viti ambavyo meza yake ilikuwa tupu.
Mimi nilijichomeka katika kundi la watu waliokuwa wakiimba na kushangilia jambo. Katikati ya umati huo, waliketi watu watatu, mmoja kati yao ambaye alionekana kijana zaidi alionekana kama mgeni rasmi wa shughuli hizo.
“Kuna nini?” nilimuuliza jirani yangu mmoja ambaye alikuwa akichekelea kila tukio kwa macho, meno na hata mikono yake.
Mtu huyo alinitazama kwa macho ya mshangao uliochanganyika na dharau kiasi kabla hajaniuliza kwa sauti ya juu kuliko nilivyotegemea, “Hujui kuna nini hapa leo?”
“Sijui,” nikakiri.
“Una maana kuwa hata yule aliyeketi pale humjui?” aliniuliza akielekeza mkono wake kwa yule kijana.
“Simjui.” Nikakiri tena.
Alinitazama kwa namna ya kunisikitikia. Kisha akaamua kunielimisha, “Yule pale ni Kingalu.”
“Kingalu ndiye nani?”
Alinisikitikia zaidi, “Kingalu rafiki yangu, huko kwenu ni Chifu au Mtemi. Sisi Waluguru tumewaita Kingalu. Huyu hapa ni Kingalu mwana wa wa Banzi mpya. Amerithi wadhifa huo majuzi tu. Alipoamua kutembelea hoteli hii ambayo ni ya mwanafamilia, watu waliosikia habari, wameamua kuja
kumwona, kumpa heshima yake na kupokea baraka zake.” Maongezi yaliyofuata baada ya hapo yalikuwa matamu
zaidi.
Nilisimuliwa historia ya kabila la Waluguru. Kwamba
baadhi ya watu wanaamini kuwa Mluguru alitokea kusini, katika mipaka ya Msumbiji na Ruvuma na kupita Mahenge, Kilosa hadi Kasanga na hatimaye Morogoro mjini ambako Kingalu Mkuu aliweka makao yake rasmi.
Kingalu Banzi, aliyekuwa akishangiliwa hotelini hapo, niliarifiwa, alikuwa mmoja kati ya akina Kingalu Banzi wengi ambao walipata kushika wadhifa huo kabla ya kuurithisha kwa wengine. Ikiwa na maana kuwa jina hilo ndio hasa la ukoo na kila mrithi aliwajibika kulitumia. Akiwa Chifu Mkuu, Kingalu alikuwa na machifu wengine wengi wa koo mbalimbali kama akina Chifu au Chifu Kingo. Wote walifanya kazi zao za kusimamia masuala ya koo, kuamua kesi, kusimamia matambiko na mara nyingine kutoa baadhi ya dawa za asili zenye miiko maalum.
Machifu hawa, kama Kingalu, hawafanyi kila kitu peke yao. Ama hukasimu madaraka kwa watu wengine, ama huwatumia wasaidizi wao maalumu, wanaoitwa ‘Wandewa’ kwa tafsiri ya Kiswahili ‘Waheshimiwa’ ambao kwa sasa tunaweza kuwalinganisha na baraza la mawaziri au madiwani.
Kwa mujibu wa mwalimu wangu huyo wa masuala ya Waluguru, Mluguru ni mali ya mama zaidi ya alivyo baba. Kwamba chanzo cha utamaduni huo kinaendana na historia ya kale ya kabila zima la Waluguru. “Kama nilivyosema tunaaminika tulitokea kusini. Mababu wanatuambia kuwa ujio wetu ulitokana na ugomvi wa ndugu wawili katika familia. Waligombana sana hadi mmoja wao akaamua kuondoka hapo
na kwenda eneo la mbali kuanzisha makazi yake mapya. Hakupenda kuondoka peke yake. Alimchukua dada yake na kuondoka naye. Kumbe dada yake huyo alikuwa mjamzito. Haikujulikana ujauzito huo ulikuwa ni wa nani, jambo lililopelekea mtoto huyo awe mali ya mama. Na kwakuwa mtoto huyo aliyezaliwa ndiye aliyekuja kuwa chanzo cha ukoo na hatimaye kabila la Waluguru utamaduni wa kuwaenzi wajomba zaidi umeendelea kushamiri.”
Mwenyeji wangu huyo, ambaye sasa tuliketi kwenye viti, mimi nikila wali na kuku wa kienyeji, yeye akinywa bia niliyomnunulia, aliendelea kujibu hata maswali yale ambayo sikupata kumwuliza, bila hiyana.
“Unajua sababu ya majina ya akina Mkude na akina Mbena kuwa mengi kwa Waluguru?” aliniuliza na kujibu mwenyewe. “Ni majina ya ukoo. Mimi hapa naitwa Mbena. Ukoo wa mama yangu ni Mwenda. Hivyo, nikipata mtoto wa kike ataitwa jina la ukoo Mwenda. Japo kama baba naweza kumpa jina jingine lakini jina litakalotambuliwa na ukoo mzima ni lile la Mwenda. Mwenda akizaa mtoto wa kiume atamwita Mkude. Majina hayo vilevile yana maana nyingi. Kwa mfano jina la Banzi lina maana ya kibanzi cha kuni. Jakka lina maana ya kibanzi kilekile cha kuni lakini kinachowaka. Chinga ni kibanzi kikubwa zaidi. Bonzo ni kibanzi kikubwa zaidi ya vyote.”
Nilipomaliza chakula changu nilikishushia kwa chupa ya fanta baridi, kisha nikamshukuru kwa ukarimu wake na kujiunga na akina Leakey ambao nao walikuwa tayari. Tukaendelea na safari yetu. Njiani nilisimulia kila nilichoweza kukielewa juu ya Chifu au Kingalu na kabila lake.
Niliongeza kile nilichojua juu ya Morogoro na vitongoji vyake. Niliwatajia makabila ya Wapogoro, Wakaguru na
Wasagara kuwa ni baadhi ya makabila ya eneo hilo.
Shughuli za kiuchumi? Nje ya uvuvi niliwaambia kuwa wakazi wengi zaidi ni wakulima. Mazao kama nyanya, uwele, mpunga, cocoa, simsim na muhogo na baadhi ya kilimo cha Morogoro. Niliwakumbusha pia kilimo cha miwa na katani ambacho kilishamiri sana katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo uliojaliwa rutuba na mvua kwa takriban mwaka mzima.
“Kwa mfano, upande wa pili wa mlima wa Uluguru ni pori na msitu mkubwa uliojaa wanyama aina aina. Msitu huo umeambaa hadi kuungana na mto Rufiji ambao nao ni habari nyingine kubwa.” Nilimweleza kwa kujigamba.
Nilitamani kuwaeleza pia kuwa miujiza ya Mlima Kolelo, ulioko kusini mwa mji wa Morogoro katika eneo liitwalo Mvuha. Simulizi za mababu toka enzi zao hadi sasa zimejaa hadithi za vituko vya kusisimua toka ndani ya mapango ya mlima huo.
Ukiwa mlima mwingine ulio katika himaya ya Waluguru, Kolelo unatumiwa na wazee kwa tambiko na tiba kwa matatizo mbalimbali. Kwa mfano, Uluguru inapokumbwa na ukame wa muda mrefu wazee huenda mlimani, wakatoa kafara na kuomba mvua, hazipiti siku mbili kabla ya mvua kubwa kunyesha na kurutubisha ardhi. Kwa upande mwingine wanandoa wanapojikuta wameishi muda mrefu bila kupata ujauzito. Hata hivyo, watoto wa aina hiyo wanakuwa na miujiza yao; akikosa usimpige wala kumkaripia kwa hasira nyingi, atakufa ghafla. Aidha, mtoto huyo akiugua usimpe dawa za hospitali wala mitishamba unayoifahamu wewe. Mpeleke mlima Kolelo atambikiwe, kesho anakuwa mzima kana kwamba hakupata kuugua.
“Mna bahati kubwa sana Watanganyika.” Mama Leakey alisema.
“Kwa nini?” Nilimuuliza.
Nchi yetu kubwa sana na ina kila kitu. Wengine wana nchi kubwa, lakini sehemu kubwa ni jangwa ambalo si mnyama wala binadamu anayeweza kuishi. Wengine eneo kubwa la nchi zao ni milima isiyopitika au iliyofunikwa na barafu kiasi cha kutishia uhai wa viumbe hai wa huko. Nyie sivyo. Ardhi yenu imejaa rutuba. Ndani ya ardhi kuna kila dalili za madini. Mmezungukwa na mito, maziwa na bahari, jambo ambalo linafanya kamwe msiijue shida ya maji wakati huohuo mkila samaki wa kila aina. Maana mapori na misitu iliyofurika wanyama na ndege wa kila aina. Hali ya hewa hapa kwenu ni nzuri kabisa kwa maeneo tofauti. Mungu awape ni zaidi?” aliuliza.
“Atupe uhuru,” nilimjibu. “Uhuru wa …”
Kutumia rasilimali zetu, nguvu na akili zetu kwa faida yetu. Kwa sasa hatuna uhuru huo. Mwarabu alikuja akatuvuruga kwa biashara zake za utumwa. Mreno na udikteta wake akafuatia. akati tunajipanga kupambana naye akingia Mjerumani na sera zake za kikatili. Ndiyo, alifanya mengi ya maendeleo kama kusomesha watu wapatao laki moja katika shule zake na kutujengea reli. Lakini hakupata kutushirikisha kikamilifu katika mipango ile. Aliwafanya babu zetu vijakazi na watwana, jambo ambalo lilipunguza ufanisi. Na ilipokuja vita kuu babu zetu walilazimishwa kushiriki bila hata kujua wanapigania nini. Wakafa, wakaparanganyika, uchumi wa nchi ukadidimia. Kisha akaja Mwingereza. Naye alikuwa na yake, kwa faida yake. Hadi leo hatujapewa nafasi ya kujipanga na utamaduni na uwezo wa kutumia rasimali zetu kwa faida yetu,” nilimjibu.
Ilikuwa moja ya hotuba zangu ndefu nilizopata kuzitoa. Nadhani ilikuwa hotuba ya maana kwani nilimwona Mary akinitazama kwa namna ya kuniunga mkono. Kupitia kwenye kioo cha dereva nilimwona pia mume wake, Leakey, ambaye alikuwa akiendesha gari, akitikisa kichwa huku tabasamu dogo likiwa limechanua usoni mwake.
“Uhuru una matatizo yake,” Mary alinichokoza tena. “Bila shaka. Lakini hilo tutahangaika nalo baada ya
kupata uhuru, sio kabila.”
Leakey hakuweza kujizuia. Aligeuka na kunitazama usoni kwa muda kana kwamba ndiyo kwanza ananiona maishani hivyo angependa kunifahamu zaidi. Kama angekuwa mtumishi wa serikali nilikuwa na hakika kuwa msimamo huo ungefanywa nitupwe jela kwa miaka kadhaa na viboko tele kwa tuhuma za uchochezi. Kwa bahati akina Leakey hawakuwa wa aina hiyo. Walikuwa na yao.
Wala mimi sikuwa mwanasiasa. Nilikuwa na uchungu tu wa kuiona nchi yangu ikiwa chini ya wageni, tena ambao hawakuujua wala kuuthamini utu na utamaduni wetu. Walijipa amri ya maisha yetu na kujichukulia madaraka juu ya uchumi wetu. Watu ambao kwao, kwa mujibu wa vitabu na habari za redio na magazeti walijitawala wenyewe huku wakichota rasilimali zetu na kuzipeleka kwao kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wao.
Msimamo wangu huo ulikuwa ukichochewa na sauti za watu, akina Nkurumah kule Ghana na Wamarekani weusi ambao walianza kupiga kelele wakitaka watu weupe waondoe kwato zao Afrika.
SURA YA KUMI NA NNE?
Na ‘Idodomya’ Yao
G
ari lilitafuna ardhi kwa kasi ya wastani. Dakawa, Magole, Gairo. Tukaingia katika ardhi ya Dodoma eneo la Kongwa.
Sura ya Dodoma kwa ile ya Morogoro ilitofautiana kama samaki na panya. Tulipokelewa na dalili nyingi za jangwa, isipokuwa kwa mti mmojammoja aina ya ‘mikungu’ ambayo iliota hapa na pale, tofauti kabisa na ile ya Morogoro iliyokuwa na misitu mikubwa na mapori yaliyoashiria neema. Milima ya hapa Dodoma pia ni jambo jingine la kuchekesha. Mingi ilikuwa midogo midogo, iliyoumbwa kwa mawe au majabali ambayo hayakuwa na mpangilio maalum.
Ukame au umbile hili la nusu jangwa limemwezesha mpita njia kuona mbali sana ya eneo alilopo. Hivyo, tuliweza kuona nyumba mbalimbali za Wagogo zikiwa zimejengwa hapa na pale. Majengo yao ni hadithi nyingine ya kusisimua. Wakati makabila mengi hujenga nyumba za kuta za udongo na paa la majani, au kuta na paa za majani matupu Wagogo zao zilikandikwa na udongo juu na chini, paa zao zikiwa za tambarare kama sakafu. Nyumba hizi fupifupi kiasi cha kumlazimisha mtumiaji kuinama anapoingia au kutoka na kuketi au kulala muda wote anapokuwa ndani. Ujenzi huo
ulishawishiwa na uhaba wa miti na nyasi katika eneo lao, pamoja na vipindi virefu vya ukame na mvua ndogo ambayo isingekuwa na madhara makubwa kwa majengo yao.
Katika maeneo mbalimbali tuliyopita, hasa eneo la Masalato, lililo karibu zaidi ya mji wa Dodoma tulikutana na mashamba kadhaa ya zabibu, wakulima waliendelea na shughuli zao.
Nilibaini baadaye kuwa Dodoma ni nchi pekee duniani ambayo zabibu hulimwa kwa misimu miwili ndani ya mwaka mmoja bila kuhusisha kilimo cha umwagiliaji. Kwa eneo ambalo mvua zake ni rasharasha na msimu wa ukame ni wa muda mrefu, toka Aprili mwanzoni hadi Disemba mwishoni, uzalishaji huo wa zabibu niliuchukulia kama moja kati ya ile miujiza midogomidogo ya dunia.
Tulitafuna kilometa zote 486 za safari toka Dar es Salaam na kuingia Dodoma. Tukatafuta mahali pa kulala, kwani akina Leakey walionyesha dalili ya uchovu. Tulipata hoteli ndogo lakini safi kuliko tulivyotegemea. Ukiwa mji mdogo sana enzi hizo, Dodoma ilikuwa haina pilikapilika nyingi licha ya ukweli kuwa ramani ya barabara ilionyesha kuwa Dodoma kilikuwa kituo muhimu cha safari toka nchi ya Misri hadi Afrika Kusini bado uchangamfu wake haukufika ule wa Dar es Salaam wala miji mingine niliyopata kuitembelea.
Akina Leakey walioga, wakala wakanywa mvinyo kidogo, kisha wakaingia chumbani kwao kulala. Mimi sikufanya hivyo. Niliamua kuitumia nuru ndogo ya jua ambalo lilikuwa likielekea kuzama magharibi mwa nchi na kuvinjari kidogo katika mitaa ya mji huo. Nilipenda sana kusikia lafudhi za makabila. Hapa niliwasikia Wagogo na Wakaguru wakizungumza. Ingawa sikuelewa wanazungumza nini bado
nilifurahi pale nilipozilinganisha lafudhi hizo na zile za makabila mengine niliyopata kukutana nayo. Lugha za baadhi ya makabila zilifanana sana hata nikaweza kuokota maneno mawili matatu na kuyatafsiri kwa Kiswahili.
Kiza kilipoanza kuingia nilirejea hotelini na kuketi na baadhi ya wageni wenzagu ambao walijipumzisha nje ya jengo hilo.
Mabadiliko ya hali ya hewa yalinishangaza. Lile joto la mchana lilitoweka ghafla na hali ya ubaridi ulioambatana na upepo wa kipupwe ikachukua nafasi. Nilijikuta nikitetemeka kidogo.
“Mbukwenyi!” alinisalimu mtu mmoja. Sikuwa mgeni sana wa salamu hizo za Kigogo.
“Mbukwa,” nikamjibu huku nikigeuka kumtazama.
Alikuwa mzee mmoja. Aliketi pia nje ya hoteli hiyo akinywa chai. Alikuwa ameona ninavyohangaika kwa baridi, “Hujapata kufika Dodoma?” aliuliza.
Nikamwambia kuwa hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza.
“Pole sana,” alisema. “Hali ya hewa ya Dodoma inadanganya sana. Mchana joto usiku baridi. Ukijidanganya kwa joto la mchana uje hapa bila koti wala blanketi utaadhirika na kuathiri afya yako.”
Lafudhi na umbile la mzee huyu ni mambo ambayo hayakuhitaji kuambiwa kuwa yeye ni mwenyeji wa hapohapo Dodoma. Pamoja na kuvaa nguo za kileo, koti, tai, na suruali nzuri bado alikuwa na alama mashuhuri, ambayo huonekana mara nyingi katikati ya nyuso za Wagogo walio wengi.
Wenyewe wanaiita ‘nindi.’ Katika enzi za kale jamii ya Wagogo waliitumia na kuamini kuwa ilikuwa kinga na tiba ya
tatizo la maradhi ya macho, tatizo ambalo ama kwa ajili ya pepo nyingi za kipupwe, ama uhaba wa maji, ama yote mawili, lilishamiri sana katika eneo hilo.
Niliingia ndani nikavaa sweta juu shati langu kisha nikatoka na kuketi tena na mzee yule. Nadhani sura yangu imekaa katika hali ya kupenda kusikiliza zaidi ya kuzungumza. Kwani hata kabla sijakaa vizuri mzee huyu alianza kuzungumza. Mazungumzo hayo kwangu yalikuwa somo la kusisimua.
“Unajua kwa nini hapa panaitwa Dodoma?” alianza kwa kuniuliza.
“Sijui.”
Akacheka kabla hajaendelea, “Kwa kweli, hata kuitwa hivyo nimekosa tu. Wageni, hasa Wazungu wanaposhindwa kutamka jina fulani huishia kulitamka kivyao na kuliandika hivyohivyo. Hapo jina hasa ni ‘Idododmya.’
Haikuwa habari jema kwangu.
“Unajua jina hilo lilitokeaje?” aliuliza tena. “Sijui.”
Akacheka tena, “Zamani sana.” Akaeleza, “Enzi za mababu wa mababu zetu, palikuwepo na bwawa kubwa ambalo wakati wa mvua lilitoa maji mengi kiasi cha kuitwa mto. Bwawa hilo lilikuwa kando ya mti mkubwa wa mkikuyu, hali iliyosababisha bwawa hilo liitwe mto Mkikuyu. Enzi hizo wanyamwa walikuwa wengi na walitembea ovyo. Tembo, mmoja ambaye bila shaka alikuwa na kiu, alitembea hadi katika bwawa hilo kwa nia ya kukata kiu yake. Mara akaanza kudidimia. Tembo alihangaika sana kutoka kujiokoa lakini wapi. Watu wengi walikuja na kushuhudia tukio hilo. Walimwona tembo akizidi kudidimia hadi akatoweka machoni mwao. Kwa enzi hizo, ambazo matukio kama hayo yalikuwa machache hiyo
ilikuwa habari kubwa, ikaenea na kubadili kabisa jina la eneo na kuwa ‘Idodomya’ au Dodoma kama mnavyoita leo.”
Haikuwa hadithi jema masikioni mwangu. Hata hivyo, nilimzawadia kwa kujifanya nimeshangaa sana. Hali iliyompendeza na kufanya aanze simulizi nyingine juu ya Dodoma mara moja. “Ulipata kusikia chochote juu ya mtu aliyeitwa Mburumatare au Stanley?”
“Naam, nimemsoma katika vitabu vya kihistoria,” nilimjibu. “Naam, ameandikwa sana na aliandika sana vitabu vinavyohusu safari yake. Moja ya safari hizo ilimfikisha hapa Dodoma. Ni yeye aliyekuwa mgeni wa kwanza kuliweka jina la Dodoma katika maandishi.” Alitulia midogo, akameza mate. “Huo ulikuwa mwaka 1874” aliendelea kueleza. “Aliporejea tena mwaka 1886 Stanley aliliangalia eneo la Wagogo kwa tamaa. Hakuweza kujizuia, akaandika, “Nilikaa pale kwa miezi sita. Nilikuwa na hakika Ugogo ingeweza kufanywa ya kupendeza na tulivu, kuwa mahala pa rehema kwa wakazi wake na wagine. Hakuna nchi katika Afrika iliyonipendeza sana kuliko hii.”
“Mgeni mwingine mashuhuri,” mzee huyo aliendelea. “Jenerali Cameron alipata kupumzika Dodoma mnamo 1873 katika safari yake ya miguu katika bara la Afrika alisema ‘katka majira ya mvua mambo yote ni tofauti, nchi yote ni kijani, yenye uhai. Mapande makubwa makubwa ya ardhi yamefunikwa na mtama, maboga na tumbaku…”
Hali hiyo ya mabadiliko makubwa ya kimaumbile mwaka baada ya mwaka, raha na karaha zikipokezana, ilikuwa na athari zake kwa wagogo. Koo nyingi zilitawanyika na kuhamahama kutafuta ardhi yenye rutuba na malisho ya mifugo yao, hali iliyosababisha pasiwepo na utawala wowote
mkubwa, wa kudumu ambao ulijumuisha kabila zima.
Lakini jiografia ya Ugogo ilikuwa hazina tosha. Ikiwa katikati ya nchi, kwenye njia kuu iliyotokea pwani hadi ziwa Tanganyika, watu na biashara zote toka pande zote zilipitia hapo. Baadhi ya misafara iliyosheheni bidhaa za chumvi, meno ya tembo, nguo, silaha za watumwa ilisimama hapa kwa siku kadhaa wakijipanga kabla ya ngwe ya pili ya safari.
Pamoja na kutokuwa na himaya yenye nguvu Wagogo hawakukubali ardhi yao itumiwe bure. Watemi mbalimbali waliwatoza wageni hao ushuru mdogomdogo ambao Stanley aliulalamikia sana na kuuita ‘kero’ na kuongeza “Utaweza kufikiria kama ilikuwepo shule mahala fulani nchini Ugogo ya kuwafunza ujanja mdogomdogo na ubaya wa machifu ambao ni mabingwa wa kazi hii.”
Lakini msafiri mwenzake, Cameron alitofautiana naye. Alisema kama ungekuwepo utaratibu maalum malipo hayo yangekuwa ya halali kabisa kwani kama Wagogo wasingelikuwa wanaishi katika eneo hilo, wakilima na kufuga, pamoja na kutunza vyanzo vya maji eneo hilo lisingepitika kamwe.
Lakini unyama uliofanywa na Mjerumani mmoja, Carl Peters, dhidi ya msimamo huo wa Wagogo kamwe hautafutika katika kurasa za historia ya unyama wa baadhi ya watu weupe dhidi ya wageni. Mtu huyu, ambaye aliacha nyayo za damu kila alikopita, toka nchi ya Wamasai, alifika Ugogo mnamo 1890. Alifika katika kijiji cha Mtemi mmoja aliyeitwa Makenge. Alipiga kambi yake bila ridhaa. Alipotakiwa kutoa ushuru alikataa na kutema cheche za vitisho vingi. Baada ya ugomvi wa maneno alifika mjumbe wa Mtemi aliyemwambia, “Sultani anataka amani nawe. Atakupa ushuru wa pembe za ndovu na ng’ombe dume.” Kwa maneno yake mwenyewe Carl Peters
anaandika hayo na jibu alilotoa akisema, “Sultani atapata amani. Itakuwa ni amani ya milele. Nitawaonyesha Wagogo, Wajerumani ni watu wa aina gani.”
Ndipo, kwa maelezo yake mwenyewe alipoanza kutekeleza mpango wa kuteketeza na kuiteka sehemu hiyo, “Nilisonga mbele dhidi ya kijiji cha mwanzo. Wagogo walijaribu kujilinda, lakini baada ya wengi wao kupigwa risasi walitimka ovyo kupitia lango la kusini. Kijiji kikawa mikononi mwetu.”
“Teka nyara kijijini humo, choma nyumba zote, vunjavunja kila kitu ambacho hakikuweza kuungua… walijitahidi kukimbiza mifugo yao lakini tuliweza kupora ng’ombe mia mbili au tatu, huku tukiwapiga wale waliokimbia. Bunduki yangu ilikuwa ya moto sana kutokana na kupiga risasi kila mara hata ikawa shida kuishika.”
“Asubuhi yake zilipokelewa ripoti za kuuawa zaidi ya watu hamsini. Makenge akaomba tena amani. Peters alijibu, “Mwambie kuwa sitaki amani naye. Wagogo ni waongo, lazima waangamizwe kabisa duniani. Lakini ikiwa Sultani atataka kuwa mtumwa wa Wajerumani hapo tena yeye na watu wake wataweza kuishi.” Baada ya maneno hayo aliomba na kupewa ushuru wa ng’ombe dume, kondoo, mbuzi, maziwa na asali. Kisha akaahidi kuwapelekea bendera ya Ujerumani.
Unyama huo wa Peters ulifanyika pia Mpwapwa na sehemu nyingine ambako Chifu mmoja aliyeitwa ‘Muniama,’ Chifu wa Kigogo wa Kogollo, aliwaua wapagazi wake wawili. Peters alihakikisha anamuua yeye na watu wake na kuteka silaha zake ikiwemo bunduki aina ya mauser.
Lakini utawala wa Wajerumani Dodoma ulikuwa na sura tofauti. Wakati wa ujenzi wa reli, june 2, 1910 ilipotolewa amri ya kuchukua eno fulani la ardhi kwa ajili ya kupisha
majengo ya serikali watu mbalimbali waliokuwa na majengo na mashamba katika eneo husika walilipwa fidia. Miongoni mwao ni bwana Ndogwe aliyelipwa fidia ya rupia 27. Bwana mwingine aliyeitwa masala alipokea rupia 15. Kweche na Kihale kila mmoja alilipwa rupia kumi.
“Wajerumani pia walianza mchakato wa kuhamisha makao makuu ya Tanganyika hapa Dodoma tangu wakati ule,” alieleza mzee huyo kwa sauti ya majigambo.
Aliutaja mwaka 1921 kuwa ulikuwa na mengi yaliyofanyika kwa ajili ya azma hiyo ambayo haikupata kuwa baada ya himaya ya Mjerumani kutimuliwa nchini.
Kwangu, maelezo hayo lilikuwa somo kubwa la kisheria. Somo ambalo si rahisi kulipata toka katika kumbukumbu za mtu mmoja. Hivyo, nilimtazama mzee huyo na kumuuliza, “Wewe ni mwalimu?”
Alicheka kabla hajasema, “Hapana. Mengine nimeyaona kwa macho yangu, mengine nimesimuliwa na baba na babu yangu. Yaliyobakia nayasoma katika vitabu. Nakuhakikishia mwanangu ipo siku na haiko mbali sana utukufu wa Idodomya utakumbukwa na mji utakuwa na kustawi kuliko unavyoona leo.
*?
*?
*
Umbali wa safari toka Dodoma hadi Kondoa
haukutofautiana sana na ule wa Dar es Salaam hadi Morogoro. Hata hivyo, ilikuwa safari ndefu na ngumu zaidi. Barabara haikuaminika sana, katika sehemu nyingi ilitulazimu kupita kwa uangalifu mkubwa kutokana na makorongo yaliyotafuna nusu ya barabara na madaraja mabovu ya hapa na pale.
Toka Dodoma kuja Kondoa ilitulazimu kupita kwa uangalifu mkubwa kutokana na makorongo yaliyotafuna nusu ya barabara na madaraja mabovu ya hapa na pale.
Toka Dodoma hadi Kondoa ilitulazimu kubadili mwelekeo. Badala ya kuelekea Magharibi kama tulivyofanya toka Dar es Salaam sasa tulielekea Kaskazini. Tulipita vijiji mbalimbali ambavyo sikuweza kushika majina yake yote isipokuwa Melamela, Babaiyo Nafakwa. Hapo tukavuka Mto Mbu na kuingia kwa Mtoro, eneo lenye maajabu yake.
Kwa Mtoro lilikuwa eneo kame zaidi. Ardhi yake ilitawaliwa na mchanga mwingi. Ungeweza kumwona mtu aliye umbali wa kilometa hadi tatu bila kuhitaji darubini wala jitihada za ziada. Kwa mtazamo wa harakaharaka ungeweza kudhani kuwa eneo hilo lisingeweza kuwa na watu. Lakini watu walikuwepo. Nyumba moja mbili, aina ya tembe, zilionekana hapa na pale, wenyeji wake wakionekana kwa nadra sana. Na kila aliyetokea alionekana nusu mtupu kwa mavazi duni waliyovaa. Aidha, karibu kila mmoja alionekana kupauka kwa vumbi na jua kali. Hilo halikupata kunishangaza sana. Kwani sikuwa nimepata kuona dalili ya maji ya kisima wala bwawa katika umbali mrefu wa safari yetu. Hata kile kilichoitwa mto mara nyingi yalielekea kuwa makorongo tu, ambayo hupata maji kwa vipindi vifupi vya mvua kabla hayajakauka tena.
“Wanaishije watu upande huu wa dunia?” alihoji Mary Leakey akitazama huku na huko.
“Wanayo namna yao ya kuishi,” mumewe alijibu. Jibu ambalo lilithibitika pale tulipofika mahala na kukuta watu wawili wakichimba katika mkondo wa mto mmoja uliokauka
ili kupata maji kwa matumizi yao na mifugo yao “Unaona?” Leakey alimwonyesha mkewe.
Tulisimamisha gari, nikashuka ili kuwauliza jambo. Ni hapo nilipokutana na mwujiza wangu wa kwanza katika eneo hilo. Watu hao, wakiwa weupe zaidi ya weupe wa kawaida kwa Mwafrika walisimama na kunitazama kwa mshangao. Kila dalili ikionyesha kuwa hawakuelewa lugha yangu.
“Nawasalimu, hamjambo?” Nilirudia tena. Nilipoona bado hawanielewi nilirudia salamu hizo kwa lugha ya Kigogo ‘mbukwenyi’ niliwaona wakitabasamu, dalili ya kuelewa. Kazi ilikuwa pale mmoja wao aliponijibu. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuisikia lugha kama ile. Kwanza nilihisi kuwa anaondoa kitu mdomoni mwake kwa ulimi pale alipobandika ulimi wake kwenye fizi na kutoa sauti mnato.
Aliporudia tena, na baadaye kupokewa na mwenzake kwa namna ileile ndipo nikabaini kuwa wanajaribu kuniambia kitu kwa lugha yao, ambayo nadhani haiyandikiki kwa herufi hizi za kizungu tunazotumia.
Wasandawe! Nikakumbuka. Kwa kiasi fulani nililinganisha lugha yao hiyo na ile ya Wamang’ati au Wandorobo ambao si Wabantu. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kugeuka na kurejea kwenye gari, tukaendelea na safari.
Dalili za neema katika ardhi hiyo zilianza kujitokeza pale tulipofika mji wa Kondoa. Ulikuwa mji mdogo lakini watu wengi na pilikapilika nyingi kuliko nilivyotegemea. Kulikuwa na nyumba ya wageni, maduka mawili ya Waarabu na kituo kidogo cha afya. Hii ilikuwa nchi ya Warangi, ambao ni Wabantu zaidi. Aidha, wengi wao walizungumza Kiswahili
kwa ufasaha, lafudhi ya Kiarabu ikiwa imetamalaki katika matamshi yao. Dini ya Kiislam pia ilijikita zaidi, kwani hata kabla hatujatulia tulilakiwa na sauti ya ‘wahadhini’ ambao walikuwa wakiwakumbusha waumini kwenda msikitini kwa sala ya jioni.
Tulipata nyumba tukapumzika. Kesho yake pia tuliamua kupumzika. Leakey aliandaa ratiba ya pilikapilika zake za safari, mimi nilivinjari katika mitaa na vitongoji vya Kondoa. Fursa ambayo iliniwezesha kuona na kujua mengi juu ya mji huo. Kwa mfano niliweza kubaini kuwa kihistoria haukuwa mji mdogo kama unavyofikiriwa. Ulikuwa na sehemu yake, kubwa tu katika kurasa za kihistoria ya vita kuu zilizohusisha Tanganyika.
Kondoa ni mji mdogo lakini una mengi ya kusisimua. Kinyume na Dodoma, Kondoa ilikuwa na sehemu yake katika historia ya vita kuu. Pale wakazi wa eneo hilo walionja makali ya vita hivyo kuliko wale wa Dodoma, jambo lililofanya Wajerumani waiweke Kondoa katika hifadhi ya kumbukumbu zao za matukio muhimu ya vita ile.
Kiutamaduni Kondoa pia ina nafasi ya pekee. Wakati wakazi wa Dodoma wakisubiri maji kwa msimu Kondoa wao mizimu ya babu zao iliwazawadia maji ya kudumu yanayotoka hadi hivi leo.
Ntomoko ni jina la mlima wenye chemchem ya maji safi yanayotoka kwenye jiwe kubwa lililoko kwenye mlima huo. Mlima huo ni mkali na uhitaji ushujaa mkubwa kuupanda. Kuna maelezo kuwa jina hilo la Ntomoko, kama ilivyo ‘Idyodoma’ lilitokana na mapigano kati ya Warangi na Wamasai. Kwamba
Wamasai walikuwa wakivizia mara kwa mara na kuwaibia Warangi ng’ombe. Hali hiyo iliwachosha Warangi ambao waliishi juu zaidi ya kilima hicho. Hivyo siku moja walizingira kilima chote na kuanza kuwashambulia Wamasai kwa mikuki na mishale. Wamasai wakawa wakikimbia kwa kujirusha katika kichaka kilichokuwa na miti mingi bila kujua kuwa pale kulikuwa na chemchem. Kila aliyejirusha hapo alididimia na kufa. Warangi walipoona hali hiyo ndipo wakaliita eneo hilo ‘Ntomoko’ kwa maana ya mahala ambapo watu hutokomea.
Baadaye Wamasai walilifanya eneo hilo mahala pa tambiko kwa kuwakumbuka wahanga waliotokomea katika eneo hilo. Inadaiwa kuwa tambiko hilo liliambatana na kumpeleka ng’ombe aliye hai na kumfungia. Wanaporudi baadaye hukuta ng’ombe huyo kachinjwa na kuchunwa. Nusu ya nyama hiyo waliila nusu wakiiacha hapo kwa ajili ya mizimu.
Awali, kabla ya kuhusishwa na teknolojia ya kisasa katika chanzo hicho cha maji zilikuwepo taarifa nyingi za miujiza. Ilielezwa kuwa mtu aliyekwenda hapo ghafla bila kuhusisha wazee wafanye tambiko alijikuta akipakwa kinyesi cha binadamu bila kujua nani kampaka. Usiku zilisikika sauti za ngoma na watu wakicheza lakini hawakuonekana. Wakati mwingine unapokaribia maji, maji hayo yalibadilika rangi ghafla na kuwa kama maziwa au yaliyojaa tope. Mara nyingi saa za usiku wakazi walidai kuona mlima ukiwaka taa. Hali iliyopelekea wazee wa Kirangi kufanya tambiko hapo kwa kupeleka kondoo mweusi kila mwaka ili maji yasikauke.
Kiongozi mmoja wa serikali aliamua kwenda Haubi,
kilipo chanzo cha maji. Alipoona maji hayo yanavyotoka kwa wingi alitamka kuwa anadhani kama ungechimbwa mfereji mkubwa maji hayo yangeweza kuhudumia watu katika maeneo mengi zaidi ya Kondoa. Kwamba mara baada ya kauli yake hiyo maji yalibadilika ghafla na kuwa machafu. Wazee wakashauri kufanya tambiko. Baada ya tambiko maji yakarejea hali yake ya kawaida, ikiwa ishara kuwa mizimu iliafiki wazo lake. Miaka kadhaa baadaye mradi mkubwa wa kuchimba mfereji wa kufikisha maji hayo katika vijiji vipatavyo kumi na vinane vya Irangi nchini. Baadhi ya vijiji hivyo ni Busi, Mairinya, Kirere cha Ng’ombe, Goima, Chandama na vinginevyo. Watu wapatao 30,000 wakinufaika na huduma hiyo.
Siku mbili baadaye Leakey aliniarifu kuwa alikuwa tayari kwa kile alichonilezea kama ‘maandalizi’ ya kazi yake. Maandalizi yalikuwa magumu kuliko hata kazi yenyewe. Kwa msaada wa mzee mmoja wa Kirangi, Msii, ambaye alipewa ajira ya muda tulikuwa watu wa kusafiri katika maeneo mbalimbali ya Kondoa, safari nyingi zikihusisha kutembea kwa miguu katika mapori, majangwa, milima na mabonde ambayo Leakey aliyapendekeza kutokana na ramani yake. Mara kwa mara tulishinda porini, mara kadhaa tukilala huko huko ili tuweze kuamka alfajiri na kuendelea na kazi. Haukupita muda mrefu kabla mzee Msii hajatutoroka na kutoweka bila hata ya kuchukua ujira wake.
Safari hizo zilitufikisha Serya, Mondo, Goima, Sombwa, Mnenya na baadaye Kolo ambako kwa mara ya kwanza niliona Leakey akitoa tabasamu lake la kwanza. Ilikuwa baada ya kugundua mapango na majabali kadhaa yaliyokuwa na michoro
ya ajabuajabu. Michoro ambayo baada ya kuichunguza sana Leakey na mkewe waliniambia kuwa ilichorwa na watu wa kale.
“Leo ni siku ya kihistoria. Nina hakika makazi ya kale zaidi ya watu wa kale. Michoro hii inaweza kuwa na umri wa miaka isiyopungua elfu thelathini hadi leo,” alisema kwa furaha akiyumba huku na kule kama mtu aliyegundua machimbo ya dhahabu.
Mingi kati ya michoro hiyo ilikuwa ya wanyama hasa swala na nyati. Mingine ilikuwa ya watu waliokuwa katika mawindo, silaha zao mishale au mawe ikiwa mkononi tayari kuua mnyama. Vifaa walivyotumia kuchora ndivyo vilivyoniacha zaidi ya michoro yenyewe. Ilikuwa aina fulani ya rangi ambayo iliweza kuingia kwenye jiwe na kudumu kwa miaka mingi ikistahimili jua, mvua na misukosuko mingine tele ya kimaumbile.
Tulikaa katika eneo hilo kwa wiki mbili. Mary akiitumia kamera yake kupiga picha kila mchoro na kila kifaa walichokishuku kuwa ni cha kale. Tulifanya pia, kazi ya kuchimba hapa, kufukua pale. Kazi hiyo iliwezesha kukusanya vifaa vingi kama silaha, mawe ya kusagia, mabaki ya mifupa ya wanyama walioelekea kuuawa na binadamu na vitu vingine tele. Dalili ambazo zilizidi kuthibitisha hisia za Leakey na mkewe kuwa mtu wa kale zaidi ya duniani aliishi hapo au maeneo hayo.
Hisia ambazo zilithibitishwa na wenyeji pale alfajiri moja tuliposhangaa kuwaona wazee watatu, mmoja wa kike waliovaa kimila wakija katika eneo hilo na kuendea moja ya
jabali yenye michoro na kuanza tambiko la kimila. Waliimba na kucheza kabla ya kumwaga mchele na vyakula vingine kama zawadi kwa wahenga.
Baadaye tulibaini kuwa eneo hilo hutumiwa na wenyeji tangu enzi za mababu zao kwa ajili ya matambiko ya kuita mvua au kujiepusha na maafa mbalimbali kama mlipuko wa maradhi au vita. Kwamba ilikuwa nadra sana matambiko katika eneo hilo kutojibiwa kwa neema.
Eneo hilo lililojaa miamba, ardhi yake ikiwa nusu jangwa kama ilivyokuwa sehemu kubwa ya ardhi ya Dodoma iliashiria kuwepo kwa ardhi nzuri, yenye miti, majani na wanyama tele miaka mingi iliyopita.
“Mtu wa kale aliishi hapa,” Leakey alisisitiza akitazama huko na huko. “Naweza kusema kuwa aliishi hapa miaka milioni mbili iliyopita. Naamini uchunguzi wa kimaabara kwa baadhi ya vifaa hivi tulivyopata utathibitisha hivyo,” aliongeza.?
Nilimtazama kwa kumpongeza. Pia, nilijipongeza kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya uvumbuzi huo.
SURA YA KU5MI TANO?
S
Bonde Ufa na Morani?
ikumbuki niliishi na akina Leakey kwa muda gani. Hazikuwa siku wala miezi. Wala haukuwa mwaka. Niliishi nao kwa miaka, tukihangaika
pamoja katika mapori, miamba, mito, milima na mabonde mbalimbali ya Bonde la Ufa.
Tulichimba hapa, tulifukua pale, tuliokota hiki, tulitupa kile ilimradi mtu asiyejua tunachokifanya angeweza kutufananisha na genge la wendawazimu.
Haikuwa kazi nyepesi. Ilihitaji vifaa na watu wa kutosha. Mara kwa mara tulilazimika kutoa ajira za muda kwa watu ambao walitusaidia kwa shughuli hizo ngumu. Hali kadhalika, hatukuwa na kituo kimoja. Tulipiga kambi katika miji na vijiji mbalimbali vya Babati, Mbulu, Manyara na kwingineko. Kupokea na kusikiliza kwa makini simulizi za wazee na hata hadithi za mapokeo ilikuwa sehemu ya kazi yetu kwa ajili ya utafiti tuliokuwa tukiufanya.
Eneo la kazi nalo lilikuwa pana sana. Bonde la Ufa ni uwanja mrefu sana. Unakadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 6,000 ukiwa umeambaa toka nchi ya Syria, Lebanon, Jordan, Israel, Kenya, Tanganyika hadi Msumbiji. Mto Jordan ambao hupeleka maji yake katika bahari mfu na Galilaya, milima ya
Virunga na Luenzori, maziwa kama Tanganyika, Nyanza na Magadi au Nakuru ya Kenya ni sehemu ya Bonde la Ufa. Baadhi ya milima kama Kilimanjaro, mlima Kenya na mengineyo inaaminika kuwa ilikuwa ikipata milipuko ya Volkano miaka ya nyuma. Mlima Oi Doinyo Lengai hadi sasa hupatwa na mlipuko huo wa volkano.
Katika Bonde hilo la Ufa ndimo lilimo eneo la Olduvai Gorge, wenyeji wakiliita ‘Oldupai.’ Likiwa katika uwanja wa Serengeti, ambao pia una wanyama wengi kuliko mahali popote pale duniani, lilikuwa na mito, milima na maziwa madogo kwa makubwa. Moja ya maziwa hayo likiwa Olduvai. Maumbile ya eneo yalionyesha dalili za kuwepo kwa jambo kubwa kama tetemeko kubwa la ardhi na jambo jingine kubwa zaidi ambalo lilitikisa dunia na kufanya ididimie katika Bonde hilo la Ufa huku maeneo mengine yakiwa yameathirika zaidi. Bonde la Olduvai. Pia liko katika maeneo hayo.
Zipo hisia kitaalamu kuwa eneo ilo lilikaliwa na watu, takribani miaka milioni mbili iliyopita. Dalili nyingi zilithibitisha hivyo. Ni humo ambalo Leakey aliendesha utafiti wake kwa muda mrefu na kuchimbua vitu mbalimbali ambavyo vilizidi kuashiria hilo.
Jitihada hizo zilizaa matunda siku ile alipogundua fuvu la kichwa cha mtu wa kale. Fuvu ambalo lilipopimwa kwa njia za kisasa zaidi lilibainika kuwa lilikuwa la mtu wa kale zaidi duniani. Kwa maneno mengine, mtu wa kale zaidi duniani aliaminika kuishi katika maeneo ya Tanganyika. Ugunduzi huo ulimpa Leakey sifa kubwa miongoni mwa wataalamu wa masuala ya mambo ya kale. Hali hiyo ilimsababisha awe mtu wa safari nyingi sana, katika nchi mbalimbali za dunia. Aliudhuria warsha na semina nyingi hapa na pale,
alikaribishwa katika vyuo vikuu mbalimbali kutoa miadhara, alitembelea majumba ya kumbukumbu za mambo ya kale huku na kule na kuendesha mikutano mingi ya kuchangia fedha ili zimwezeshe kuendelea na utafiti wake mrefu na mgumu.
Safari hizo zilinifanya niwe mtu wake wa karibu zaidi Tanganyika, mara kwa mara nibakie kuwa kiongozi na msimamizi wa shughuli zake. Nilikuwa na uwezo wa kuajiri na kufukuza. Nilihifadhi nyaraka na kumbukumbu za utafiti. Kwa kweli sikuwa tena mtu mdogo kama yule kondakta wa gari bovu kule Mbeya au Mnyampala wa mashamba ya katani kule Pangani.
Posho au mshahara wangu haukuwa mbaya, aidha matumizi hayakuwa mengi. Muda mwingi uliishia maporini ambako sikuhitaji kutumia fedha zozote. Hali iliniwezesha kufungua akaunti benki na kujiwekea akiba kidogo kidogo. Hiyo ni faida nyingine niliyoipata katika ajira yangu kwa akina Leakey.
Lakini faida kubwa ilikuwa elimu. Sikubahatika kupata elimu ya darasani. Ndoto ya kurudi shule zilikwishayoyoma tangu niliposahau madaftari yangu kule Pangani na kwenda Bagamoyo, baadaye Dar es Salaam hadi huku. Nilitafuta elimu vitabuni. Leakey na mkewe walikuwa watu wa vitabu. Walisoma kila kitu; toka historia, sayansi, jiografia hadi riwaya. Walisoma vitabu vya dini, majarida na makabrasha ya kila aina. Walipobaini kuwa mimi pia nilikuwa ‘mgonjwa’ wa vitabu waliniruhusu kusoma kitabu chochote nilichokitamani. Ingawa sikuwa na kiongozi wa kunielekeza kile ninachokisoma bado nilijifunza mengi na kupata ufahamu wa kutosha.
Lugha ya kiingereza ni jambo jingine ambalo nilinufaika nalo kwa kuwa nao. Mara kwa mara, walizungumza nami
kwa lugha yao, hali iliyopelekea niondoe hali ya kutojiamini na kuwajibu bila kujali kama nakosea au la, kama ambavyo wao pia waliongea Kiswahili bila kujali kama wanapatia au la. Taratibu nikajikuta naimudu vizuri lugha yao. Hata pale nilipokutana na watu wengine, wawe wageni wasiojua kabisa Kiswahili, au wasomi wa vyuo mbalimbali, niliweza kuzungumza nao kwa ufasaha hata wakashindwa kuamini kuwa elimu yangu haikuvuka daraja la kati.
Habari ulikuwa ugonjwa wangu mwingine. Pamoja na ukweli kuwa muda mwingi niliutumia maporini, ambako redio nyingi hazikuweza kusikika na ilikuwa ndoto kuona magazeti, bado kila niliporejea mijini niliyafuta hata yale ya mwezi mmoja uliopita. Nilisoma habari, makala, matangazo, hadithi na mashairi. Gazeti jipya la Mwangaza lililoanzishwa Mei 10, 1951 na lile la kwetu la tangu 1943 likihaririwa na Chifu Thomas Mareale II (OBE) ni miongoni mwa magazeti ya Kiswahili ambayo pamoja na upatikanaji wake wa nadra bado yalininufaisha sana kuelewa mtazamo wa mtu mweusi katika nchi yake.
Habari ya Pangani kufanywa wilaya (Janua 7, 1938), samaki wa aina ya sangara kupandikizwa katika ziwa Nyanza, ambalo sasa liliitwa Victoria (1950), Laurian Rugambwa kuteuliwa kuwa askofu wa kwanza Mwafrika nchini Tanganyika (Desemba 13, 1951), kuanzishwa kwa Chama cha TAA kikidai haki za watu weusi (1949). Amri ya serikali kuitangaza rasmi Serengeti kuwa hifadhi ya taifa (April 20, 1948 na kadhalika).?
Vyombo hivyo vya habari viliniwezesha pia kufahamu kuwa sensa ya mwaka 1948 ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na idadi ya watu 7,744,600 kati yao 183,860 au
asilimia 2.4 pekee wakiishi mijini. Idaidi ambayo miaka tisa baadaye (1957) ilibadilika na kuwa watu 9,087,6000 nchi nzima, 364,070 au asilimia 4.0 wakiishi mijini.
* * *?
Alfajiri moja nilipata mtihani wangu wa kwanza wa kiutamaduni nikiwa kama mkuu wa kambi ya Leakey. Tulikuwa tumepiga kambi katika maeneo ambayo hayakuwa mbali sana na ziwa Manyara. Akina Leakey walikuwa nje ya nchi kwa miezi kadhaa. Usiku huo mzima ngoma za Wamasai ambazo wenyeji zaidi yangu walizitambua kama ‘Omorata’ ambayo huchezwa majira ya tohara, miezi hiyo ya julai zilitumbuizwa. Niliamshwa toka usingizini kwa kelele za mtu aliyekuwa akilia nje ya hema langu kwa sauti huku akiita kwa nguvu, “Nisaidie. Baba nisaidie…” nilipotoka nilikuta msichana mdogomdogo akiwa hapo nje, kapiga magoti, akilia na kutetemeka kwa hofu. Alikuwa msichana wa Kimasai. Alipambwa kwa shanga kwenye kichwa chake chenye nywele fupi, shanga nyingine tele shingoni, masikioni, mikononi na miguuni. Alivaa vazi la buluu, lililomfunika hadi miguuni. Hakuwa na viatu. Nadhani msichana huyu alitegemea zaidi kumwona mtu mweupe akitoka humo ndani badala ya mweusi kama mimi, kwani niliona dalii za kukata tamaa katika macho yake. Hata hivyo aliendelea kupiga magoti huku akisema “Nisaidie baba…?
naomba unisaidie.”
“Kuna nini?” niliuliza.
“Na… niko naogopa…” alisema kwa Kiswahili chake cha?
shida.
“Unaogopa nini?”
“Naogopa. Naogopa sana. Kufa …”
“Kufa!”
“Ndiyo… kufa. Ndito mmoja kafa jana. Damu… damu nyingi. Naogopa,” aliendelea kusema huku mara kwa mara akigeuka nyuma alikotokea kwa dalili za hofu.
Ndipo nikaelewa. Msichana huyu alikuwa akikimbia tohara, jambo ambalo wasichana wote wa Kimasai, kabla ya kuolewa, hutakiwa kufanyiwa. Kwa maana hiyo msichana huyu alikuwa Ndito. Alikuwa hajafikia hadhi ya kuitwa kokoo. Yeyoo au Shangiki ambazo ni hadhi maalumu za wanawake wa kimasai waliopitia hatua mbalimbali za kimila na kimaisha.
“Wewe unatoka wapi?” nilimuuliza.
“Enkang,” alinijibu, akiwa na maana ya boma lao. Mimi nilitaka kujua kama anatokea Kenya au
Tanganyika. Nikamuulia hivyo. “Hapana.”
“Hapana? Hutoki Kenya?” “Ndiyo.”
“Kwa hiyo wewe n Mtanganyika?” “Hapana.”
Nikashangaa. “Kwa hiyo wewe ni raia wa nchi gani?” “Siye ni Wamasai,” alinijibu.
Ilinibidi nicheke kidogo. Alinikumbusha tabia ya Wamasai ya kujiona kuwa wao ni raia wa nchi hizo mbili. Tabia hiyo ilijengeka katika fikra zao kutokana na kukulia katika utamaduni wa kuahama hama wakifuata malisho ya mifugo yao bila kujali kama wameruka mpaka au la.
“Nisaidie… wanakuja…” alisema akiinuka na kukimbia ndani ya hema langu. Nilipotanabahi, nilikuta hema zima limezingirwa na vijana wa Kimasai wapatao ishirini, wakiwa na ngao zao mikononi, mkuki mkono wa pili. Walikuwa tayari
kwa lolote. Tayari kwa vita, tayari kwa mauaji.
“Iko naficha yeye wapi?” mmoja wao aliniuliza. Nikamtazama. Alikuwa ‘Layoni’. Mwenyewe akiwa bado hajatahiriwa, hajaua simba wala kuoa lakini hawaogopi isipokuwa wakati wao bado.
Walikiri kuwa nikweli msichana mmoja alifariki usiku huo katika kufanyiwa tohara. Lakini walilielezea tukio hilo kuwa la bahati mbaya tu, ambalo hutokea kwa nadra sana. Wakasisitiza msichana huyo kufanyiwa tohara ili aweze kuwa mtu mzima, abebe majukumu ya kifamilia.
“Ataolewaje bila emorata? Atapataje watoto na familia? Ndito lazima apitie mila zote alizopitia mama na bibi yake,” mmoja wao alisisitiza.
“Lakini huyo hataki,” nilijaribu kutetea.
“Siyo suala la kutaka au kutokutaka. Ni suala la ukoo. Akikataa atatengwa na jamii nzima. Atafukuzwa kila anakokwenda. Hataolewa milele. Huoni kama hilo pigo kubwa kwake kuliko kifo?” alinihoji kijana huyo wa Kimasai.
Kama wenzake alivaa nguo nyekundu. Nywele zake ndefu zilizosukwa vizuri kurudi nyuma zilipambwa kwa rangi au udongo mwekundu. Mikononi na miguuni alivaa bangili za shanga ambazo zilifanya kila hatua aliyopiga wakati tukizungumza itoe mlio ambao nadhani huchangia kumchanganya hata simba kwa wale waliopata kupambana nao.
Wamasai ni watu wanaothamini utamaduni wao kwa kiwango kilekile wanachotamani ng’ombe wao. Ujenzi wa maboma yao, ambayo nilipata kuyatembelea mara kwa mara unathibitisha hilo. Vijiji vinavyoitwa ‘Enkang’ hujengwa kwa mduara, ng’ombe wao wakilala katikati ya duara hilo ili
kuwaepusha na wanyama wakali pamoja na wezi wa mifugo. Vijiji huwa havidumu sana kwani mara malisho ya mifugo yao yanapoonyesha dalili za kupungua, au kifo kinapotokea katika eneo hilo huondoka mara moja na kuhamia sehemu nyingine. Maamuzi mengi ya Wamasai hufanywa na ‘Laibon,’ ambaye ni kiongozi na pia kuhani wao kwa mungu wao, wanayemwita ‘Enkai’. Kutoboa masikio pili aweze kuvaa bangili, kung’oa watoto meno ya mbele ili aweze kulishwa uji wakati akiumwa na kuhakikisha mtoto wa kiume anapotahiriwa hapigi kelele za kuogopa maumivu ni baadhi ya mila za Kimasai ambazo zimedumu miaka nenda rudi. Lugha yao ‘maa’ pia wanaithamini sana kiasi kwamba kuwa hawafanyi jitihada za?
haja za kujua lugha za watu wengine.
Tofauti na makabila mengi nchini, kazi za ujenzi wa nyumba zao hufanywa zaidi na wanawake wakati wanaume wakijihusisha na ulinzi wa makazi na mifugo.
Kwa Wamasai tohara ni tukio la aina yake. Ndilo ambalo humtoa msichana au mvulana katika hadhi moja kwenda ya pili. Hivyo, tukio hilo huambatana na mbwembwe nyingi, zikiwemo ngoma maalumu ambazo huchezwa miezi ya Julai na kufuatiwa na tukio lenyewe ambalo hufanyika alfajiri, kabla jua halijachomoza. Tukio hufanyiwa karibu na zizi, moto mkubwa huwashwa na ng’ombe mmoja kuchomwa mkuki shingoni. Damu ya ng’ombe huyo hukingwa na kuhifadhiwa katika kibuyu maalumu kiitwacho ‘Eng’oti’. Damu hiyo huchanganywa na maziwa na watahiriwa wote kunyweshwa kabla ya tohara.
Kilimo ni moja ya mambo ambayo hayawavutii sana Wamasai. Chakula chao kikuu ni nyama ama kupika ama ya kuchoma. Nyama za kupika zina maadili yake. Huchanganywa
na dawa mbalimbali. Kwa mfano dawa ya ‘Okiritaraswa’ humfanya mtu awe na hasira sana. Dawa nyingine ni ‘Orumukatani’ ambayo nayo hupikwa na humpa mtumiaji nguvu. Mara nyingi watumiaji wa dawa hizi ni wale walio tayari kwenda vitani au kupambana na simba. Dawa ya tatu, ‘Orokirotiti’ humfanya mtumiaji kuwa na hamu ya kula pamoja na kuwa mchangamfu. Nyingine ni dawa za kuondoa mafuta mwilini, kujikinga na maumivu ya misuli na kujenga mwili.
Hawa ndio Wamasai. Watu wanaojipenda na kujithamini. Watu wanaoupenda na kuuthamini utamaduni wao kiasi kwamba ujio wa wageni mbalimbali nchini, toka makabila yaliyoingia toka kila upande wa nchi, Waarabu waliotoka mbali na ujanja wao, Wazungu na hila zao na wengine hawakupata kuwatikisa Wamasai na imani zao. Watu wa aina hiyo ambao walikuwa tayari kwa lolote, ikiwa pamoja na kutoa uhai wao, ili kulinda hadhi yao, mimi ni nani hata nibadili imani yao katika muda wa saa moja? Niliwaza nikiingia ndani ya hema kwa dhamira ya kumtoa dada yao.
Nilimkuta akibubujikwa na machozi huku akitetemkea mwili mzima. “Tafadhali, usiwaruhusu wanichukue. Naogopa… Nitakufa!” alinisihi akipiga magoti miguuni mwangu.
Nilipatwa na huruma. Nikahisi machozi yakinilengalenga hasa pale nilipomtazama usoni na kuona alivyonitumbulia macho ya huzuni kama mfamaji aliyekata tamaa, anayetegemea msaada wangu pekee.
Huko nje Morani walisikiliza wakianza kupiga kelele. Nadhani walihisi kuwepo kwa jambo linaloendelea humo ndani. Mara wakaanza kuimba nyimbo zao zinazoashiria vita huku wakirukaruka kulizingira hema langu. Ghafla mmoja mmoja akaingia ndani ya hema, mkuki wake ukiwa umetangulia.
Mwingine akafuatia, sime mkononi. Walimwendea ndito moja kwa moja na kuanza kumvuta nje. Msichana akazidi kulia akinitazama kwa macho yake yaliyoloa machozi.
Sikufikria mara mbili. Nilichupa na kuichukua bunduki
ya Dakta Leakey na kuilekeza kwao huku nikifoka, “Mwacheni!”?
Hawakuamini macho yao. Walinitazama kwa mshangao na hasira kali.
“Tokeni!” Nilifoka tena.
Yule mwenye sime alipandwa na hasira. Akamwachia msichana na kunifuata huku akichomoa sime yake. Lakini mwenzake alimshika na kumnong’oneza jambo.
Nadhani alikuwa hajasahau maafa ya risasi kwa miili yao. Pengine alikumbuka tukio la kinyama la mamia ya watu wao waliouawa na Stanley walipopambana naye kwa mikuki na sime zao. Mwezie alimsikiliza. Kama kondoo, waligeuka na kutoka nje ambako waliwashawishi wenzao kuondoka. Lakini haikuwa kabla ya kunitupia jicho kali, la kisasi, ambalo hadi leo sijapata kulisahau katika njozi zangu za usiku na mchana. Mara walipoondoka, nilimrudia msichana yule na kumtaka yeye pia aondoke. “Nenda zako, wakirudi hapa?
hawatafikiria mara mbili,” nilimhimiza.
Aliinuka, akanitupia jicho la shukrani kisha kwa sauti ndogo alisema, “Umesaidia mimi sana. Ahsante Laibon.”
Laibon! Heshima aliyonipa haikuwa ya kawaida. Nilimtazama akigeuka na kuondoka taratibu. Nje ya hema alitazama huko na huko kabla ya kuondoka akielekea upande wa pili wa walikoelekea wabaya wake.
Wasaidizi wangu walinifuata baadaye, mmoja akinipongeza wa pili yule anayejua Kimasai akinipa pole.
“Pole ya nini?” Nilimwuliza.
“Hujui? Unadhani Mmasai ni mtu wa kuvumilia kitendo ulichokifanya? Kwao umedhalilisha kabila zima. Lazima watataka kulipa kisasi. Kama si leo kesho, kama si kesho keshokutwa au hata mwakani,” alinifafanulia.
Kwa kuamini kuwa Wamasai wasingependa kucheza na risasi, hasa baada ya kuona bunduki mikononi mwangu, niliipuuza hofu yake. “Enzi zile zimepita ndugu yangu. Sasa wanajua bunduki, wanajua utawala wa sheria,” nilimweleza.
Hakuonekana kuafikiana na fikra zangu, ingawa hakutia neno jingine. Niliamini hivyo jioni hiyo aliponitaka ruhusa ya kwenda nyumbani kwake kuitazama familia yake. Hakukuwa na kazi nyingi. Hivyo nilimruhusu. Msaidizi wa pili alitoweka bila kuaga. Bila shaka kwa hofu ileile.
Usiku huo nilijikuta peke yangu katika kambi, katikati
ya uwanda mpana wenye jangwa na majani hafifu.
Sina budi kukiri kuwa kwa kiasi fulani nilishikwa na hofu. Nilikusanya magogo na kuwasha moto nje ye hema langu kwa dhamira ya kutishia wanyama wakali waliozowea kutembelea makambi yetu hasa nyakati za usiku. Ulipofika wakati wa kulala niliweka bunduki yangu kando ya kitanda na kujilaza chali na huku nikijiambia kuwa nisingeruhusu usingizi unichukue.
Usingizi ulinichukua. Tena ule wa pono.
Nadhani nililala kwa masaa manne au matano kabla ya kuzinduka ghafla kwa hisia ambazo sikufahamu zilitokana na nini. Nilihisi kuwepo kwa mtu au kitu cha ziada hemani humo. Nikafumba macho na kutazama kwa makini huku mkono wangu ukiwa tayari kuichukua bunduki yangu.
Je nini kilifuata?
Huyo mtu ni nani?
ITAENDELEA
Usingizi ulinichukua. Tena ule wa pono.
Nadhani nililala kwa masaa manne au matano kabla ya kuzinduka ghafla kwa hisia ambazo sikufahamu zilitokana na nini. Nilihisi kuwepo kwa mtu au kitu cha ziada hemani humo. Nikafumba macho na kutazama kwa makini huku mkono wangu ukiwa tayari kuichukua bunduki yangu.
Kweli kulikuwa na kitu. Hapana, mtu! Kwa nuru ndogo iliyotokana na moto uliokuwa ukiendelea kuwaka pale nje,
niliweza kuona kiwiliwili cha binadamu kikipenya kimyakimya, kama mzimu, kunifuata kitandani. Niliinuka mara moja na kusimama huku nikianza kuinua bunduki yangu
“Shhhh! Hapana kelele,” ilinong’ona sauti ya mtu huyo. Ilikuwa sauti ya kike! Sauti ya yule msichana aliyetoka hemani humu asubuhi hii.
“Kuna ni…” Nilijaribu kumuuliza. Lakini kwa mara nyingine alinizuia kuzungumza, safari hii kwa kuniziba mdomo kwa kiganja chake cha mkono wenye baridi.. Kitendo kilichofuatiwa na sauti yake ya mnong’ono vilevile ikisema, “Haraka… Ondoka. Wanakuja kukuua.”
“Nani?” Nilinong’ona kama yeye.
“Morani. Wanakuja…” Hata kabla hajamaliza kunifafanulia. Nilisikia hatua za watu wanaotembea kulifuata hema. Nilipochungulia nje, niliona viwiliwili vya miili ya watu wapatao ishirini, silaha mkononi, wakitembea kulifata hema langu.
“Kimbia!” Alisema akinisukuma kutoka nje. “Wewe?”
“Acha mimi… nitakufa… peke yangu. Wewe hapana.” alinong’ona.
Sikuafikiana naye. Nilimshika na kumvuta mkono kutoka naye nje, huku tukiwa tumeinama. Nje ya hema tulinyata taratibu kuelekea upande wa pili, kulikokuwa na vichaka na miti miwili mitatu.
Hata kabla hatujafikia vificho hivyo, Morani walikwishafika kwenye hema na kulizingira. Walipita huko na huko wakikagua hema baada ya hema. Walipobaini kuwa mahema yote hayakuwa na watu, waliutumia moto niliouwasha mwenyewe kuteketeza mahema yote. Walifanya
hivyo huku wakiimba nyimbo za kivita au za ushindi, wengine wakirukaruka juu kama waliopagawa.
Bila ya msichana yule kunishikilia, ningeweza kurudi waliko ili kupambana nao. Moto, ambao niliushuhudia ukiteketeza mahema hayo, kwangu ulikuwa pia ukiteketeza ndoto na matumaini yangu ya maisha.
Achilia mbali vitabu na nyaraka zangu binafsi, nyaraka zote za Dakta Leakey na mkewe, baadhi ya vifaa vyake katika shughuli zake za utafiti na kumbukumbu mbalimbali za muhimu zilizotafunwa na moto huo. Kama mchezo wa kuigiza. Ilikuwa dhahiri kuwa nisingeweza kuwa naye, kwani nisingeweza kumweleza chochote ambacho angekielewa.
Nadhani nilitokwa na machozi kama mtoto. Nadhani miguu yangu iliishiwa nguvu, kwani nilijikuta nimeketi chini huku mikono ya msichana huyo mdogo ikiwa imenikumbatia kwa namna ya kunifariji. Yeye pia alikuwa akilia. Bila shaka akijiona chanzo cha mkasa huu mzito katika maisha yangu.
Nilimtazama, mara nikajikuta nikimuonea huruma badala ya kujionea huruma mimi mwenyewe. Nilimwona katika nuru tofauti. Si kama msichana aliyekimbia tohara bali shetani au malaika aliyetumwa kuvuruga maisha na matarajio yangu kama ilivyokuwa ada katika maisha yangu. Nikainuka na kisha kumwinua.
Aliinuka kwa taabu. “Twende!” Nilimwambia.
“Wapi?” Alinong’ona kwa sauti yenye kwikwi .
Wapi! Nilijiuliza vilevile. Ndio kwanza ikanipambazukia kuwa toka muda huo sikuwa na mahala pa kwenda. Nilikuwa nimerudi nilipoanzia; Mtu wa kutangatanga kama ndege asiye na makao maalum.
Niende wapi? Nilijiuliza tena. Ningeweza kwenda polisi kutoa taarifa ili Morani wale watafutwe na kuadhibiwa, lakini hilo lisingesaidia. Ni vigumu sana kuwapata Morani katika uwanda huo mpana. Kesho wanaweza kutorokea Arusha, kesho kutwa wakawa Kenya. Zaidi ya hayo sikuona vipi adhabu hiyo ingeweza kunisaidia. Kamwe isingerudisha chochote kati ya yote yaliyoteketea.
Nilimvuta taratibu kuelekea nje ya eneo hilo. Tulitembea taratibu, tukikurupusha wanyama hapa na pale hadi tulipofikia mti mmoja mkubwa. Msichana yule alininong’oneza jambo akielekeza kidole chake kwenye mti ule. “Unasemaje?” Nilimhoji.
“Jana nashinda juu ya mti ule. Nalala juu yake hadi nasikia ngoma ya vita. Nakuja ita wewe,” alisema
Nilimwelewa, nikawa nimepata jibu la swali lililokuwa likinisumbua, la kutaka kufahamu alijuaje kuwa ndugu zake walikusudia kunidhuru. Ukiwa juu ya mti huo mkubwa, unaweza kuona hadi mbali. Na ukiwa msikivu, unayezifahamu mila zako, hutashindwa kujua ngoma inayopigwa kwa mbali inaashiria nini.
Alinishauri tulale juu ya mti ule.
Nikaafiki.
Tulipata tawi kubwa, lililofanya tuketi bila hofu kubwa ya kuanguka. Kwa ajili ya baridi kali, usiku huo, pengine na hofu ya uzito wa matukio, binti huyo aliniegemea kifuani, usingizi ukamchukua. Joto lake na uwepo wake ulinifariji. Lakini sikuweza kupata usingizi. Jogoo wa kwanza alipoanza kuwika, nilimuamsha taratibu. Aliamka kiasi akishikwa na aibu kwa jinsi alivyonikumbatia. Mimi sikuwa huko. Akili zangu zilikuwa mbali maili nyingi nje ya eneo hilo.
“Nadhani nianze safari ya kuondoka.” Nilimwambia.
“Wewe nakwenda wapi?” aliniuliza akifikicha macho
yake kutoa usingizi.
“Sijui ninakokwenda lakini sihitaji kukaa hapa.
Nitakwenda popote.”
Alinitazama kwa makini kabla hajatamka taratibu, “Nakwenda na wewe.”
“Unakwedna na mimi! Wapi?”
“Sijui. Popote nakwenda wewe mimi nakwenda,” alisema.
“Mimi sijui nakwenda wapi.” Nilimwambia.
“Hata mimi yenyewe sijui. Nabaki hapa itaniua. Wewe nasaidia mimi. Hapana acha iniue.”
Niliishiwa nguvu. Nikaduwaa
Jogoo wa pili walianza kuwika. Sikutaka alfajiri inikute hapo. Nikashuka kwenye mti na kuanza safari. Msichana wa Kimasai alishuka na kunifuata.
?
16
Ben R. Mtobwa
SURA YA KUMI SITA?
Na Wangu Hadi
K
una fasihi simulizi nyingi nchini ambazo zamani nilidhani zilikusudiwa kumsisimua msikilizaji wake peke yake. Nyingi kati ya hizo ziliwalenga
watoto. Baadhi zilikuwa hadithi za kusisimua au kutisha sana kiasi cha kuwatoa machozi wasikilizaji wake, wengine zikiwakosesha usingizi.
Moja ya hadithi hizi ni zile za kubeba ‘mzigo’ ambao mhusika alishindwa kuutua kwa urahisi, kwa mfano, kuna ile inayosimulia kijana ambaye alikuwa akitembea porini peke yake. Kwamba alifika mahala penye mto ambao alitakiwa kuuvuka. Kando ya mto huo alikuta msichana mdogo, mzuri sana aliyetaka kuvuka vilevile lakini alikuwa akiogopa mkondo mkali wa mto huo. Hivyo alipomwona kijana huyo msichana aliangua kilio akimsihi amsaidie kuvuka. Kwa huruma zake, kijana alikubali. Akambeba binti huyo mgongoni na kuogelea naye hadi upande wa pili ambako alijaribu kumtua. Lakini msichana huyo alikataa. Alipotanabahi kijana huyo alibaini kuwa alibeba kikongwe ambacho kilimng’ang’ania mgongoni usiku na mchana hadi mvulana akakosa nguvu.
Nyingine inayofanana na hiyo, ni ile ya mvulana mwingine aliyekuwa akivuka mto vilevile. Yeye alielezewa
kukuta kikongwe kikilia kando ya mto huo kikiomba msaada wa kuvushwa. Kilikuwa kibibi kichafu kinachonuka na kutoa tongotongo na kamasi muda wote. Mhusika alikihurumia. Akakitia mgongoni na kukivusha. Kinyume na mhusika wa kwanza, huyu mara tu alipokitua, alibaini kuwa kikongwe kile kilikuwa msichana mrembo sana, mwenye uwezo wa kimalaika. Walipendana, wakaoana. Maisha ya mvulana huyo yakiwa yamebadilika toka kwenye ufukara na kuwa tajiri na mtu maarufu sana nchini kwao.
Awali sikupata kufikiria uzito wa falsafa iliyokuwemo katika simulizi hizo. Sasa nikiwa na matukio yale, nilizichukulia kwa uzito unaostahili. Tatizo ni kutokujua nilikuwa katika nafasi ipi kati ya wahusika wale wawili.
Hayo yalipita akilini mwangu baada ya kumtazama kwa mara nyingine yuleyule msichana wa Kimasai aliyeniganda kama kupe. Jitihada zangu zote za kumwacha ashike hamsini zake nami nishike zangu hazikupata kuzaa matunda. Nilijaribu kumtelekeza hapa na pale lakini machozi yalimtoka na macho yake yenye huruma aliyonikazia yalinipokonya ujasiri. Hali iliyopelekea nijikute nikipanda naye lori la kwanza lililopita barabarani alfajiri hiyo
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment