Simulizi : Urithi Wenye Umauti
Sehemu Ya Tano (5)
Sofia hakuwa na uwezo wa kufurukuta hata kiduchu, maana nilikuwa nimemfunga sawa sawa.Mitiririko ya jasho ikawa ikimtoka mwilini baada ya kuiona ile bastola niliyokuwa nimekamata mkononi.Mawazo mengi yalikuwa yakinipitia kichwani ya jinsi na ambavyo ningewapa adhabu wale watu wawili.Nikiwa katikati ya mawazo Yale,mlango ukagongwa na mtu kutoka nje pia akijaribu kuusukuma ndani ila akashindwa maana ulikuwa umekomelewa."Said harakisha tunahitajika na bosi!"Yule mtu wa nje alipaza sauti kumwambia mwenzake tuliyempata kwenye penzi zito na mpenzi wangu Sofia.Kimya kikafuata ila kwa kifupi kabla ya yule mtu kuongea tena.
"Muda umekwenda Said,mbona hutoki au yule hawara amekutendea nini?"Yule mtu akasema.Niliusogea mlango kisha nikazungusha kitasa polepole,ukafunguka.Mwanamume mwenye urefu wa makamo akajitoma ndani muda huo nikiwa nimejibanza kando ya mlango.Alipofika ndani akamaka baada ya kumwona mwenzake amefungwa na Sofia.Nikauona mkono wake wa kulia ukifikia kiunoni nami sikuwa zumbukuku,nikang'amua njama ile mapema.Njama ya kuchomoa bastola."Usidhubutu!"Nikatoa amri kali iliyomshtua na kulazimika kugeuka,akawa akiangaliana na domo la bastola.Mshangao uliompata haukuwa wa kikawaida ila akawa akijikaza asiuonyeshe kwa vitendo."Iweke bastola chini pole pole la sivyo ninaufumua ubongo wako!"Nikamwamrisha kwa ukali.Lisilo budi hubidi,aliiweka bastola chini Kisha nikamwamuru asonge nyuma hatua nne,nami nikaitwaa ile bastola na kuiondoa usalama.Nikamnyoshea ile niliyokuwa nayo awali na kuvuta triga ikatoa mlio wa vyuma viwili vikigongana-kiashiria kuwa sikuwa nimebakiza risasi yoyote.
Yule mtu kweli akaudhika,akiniangalia kwa macho yenye ghadhabu huku akijaribu kusaili jinsi angejiondoa mtegoni.Niliisundika bastola yangu kiunoni kisha nikaichukua ile ya yule mtu na nikampiga risasi moja mkononi.Sauti mbovu ya mfyatuko kutokana na kukosa kuwa na kiwambo cha kuzuia sauti ikasikika.Nikamwongezea nyingine iliyokifumua kichwa chake vibaya.Ubongo ukamwagika na kujipaka ukutani.Hali ya taharuki ikazuka mle ndani.Abdi akausogea mlango na kuchungulia Kisha akaniita kwa sauti."Roy,king'ora cha polisi!!".Nilimtazama Said kisha nikaamua kutomwacha bure.Nilimpiga risasi mbili kifuani,nikarukia mlango ila nikateleza na nilipokuwa niking'ang'ana kusimama,kidole changu kikavuta 'triger' risasi ikamcharaza Sofia begani upande wa kulia.Yowe Kali likamtoka.
Niliungana naye Abdi tukatoka mle ndani na kuwafuata wale wanafunzi waliokuwa wikiparamiana ovyo ovyo.Waliokuwa nusu uchi hawakujali soni ila muda huo ulikuwa wa kuokoa maisha.Tulipishana na polisi wa kitengo cha ugaidi wakiingia kwa namna ya kupendeza.Nilikuwa nimeificha bastola niliyomnyang'anya yule mshirika wa Said kiunoni.Tulitokeza nje na kufululiza mpaka kwenye gari letu,tukajiweka vitini,Abdi akaiwasha nasi tukatokomea.Njiani tukapishana na magari aina ya lori,nne za wanajeshi wakielekea chuoni Romi.Tulifika jijini Sogomo kwake Abdi ikiwa imewadia saa nne usiku.Tuliingia ndani na kuoga Kisha Abdi akaanza kupika.Mimi nikaisogelea runinga ndogo mle ndani na kuiwasha.Nilitazama kwa muda kisha habari zikaanza kutangazwa.Butwaa iliyo
nipata baada ya kuiona tukio ambalo tulilifanya chuoni Romi haikuwa ya kumithilika."Natumai u mzima mpenzi mtazamaji.Moja kwa moja tunaanza habari za leo rasmi ya mwanzo ikiwa tukio lililotokea chuoni Romi,moja ya chuo ambacho kinaaminika na kukubalika kama sio kuheshimika katika ukanda huu wa Afrika mashariki.Hii leo kumetokea tukio la kigaidi ambalo limetekelezwa na vijana wawili barobaro mmoja akijulikana kwa jina moja la Roy.Tukio hili lilitokea mida ya saa nane mchana wakati wanafunzi wengi walikuwa wamekwenda katika masomo ya mchana.Licha ya hayo kulikuweko na miili miwili ya wanaume kati ya miaka ishirini hadi thelathini.Hata hivyo msichana mmoja pia alipatikana akiwa na risasi moja begani muda huo akiwa amezirai.Mkuu wa idara ya usalama,Jenerali Yusuf Yudy amesema tukio hili linachunguzwa kwa undani."Mtangazaji akamaliza."Roy mambo yanakuwa magumu."Abdi akaniambia."Nikidhani yanibidi mimi mwenyewe nijitwike haya.Pole kwa kukuingiza katika hatari hii Abdi."Nikamweleza."Hamna shida Roy,usiwe na wasiwasi,mimi na wewe ni kama ndugu sasa.Mbona nikuachie msiba huu peke yako?"Abdi akaniambia.Kweli maneno yake yaliniliwaza kwa asilimia kubwa.Kwisha maliza shughuli za upishi,tulijiandaa na kujibwaga kitandani.
Tukiwa tumelala,mara Abdi akanigusa begani akiomba tusemezane kabla ya kulala."Vipi Abdi?"Nikamwuliza."Roy,nimetafakari kuhusu hali iliyoko kwa Sasa.Kweli si hali nzuri ukijumlisha na hatari inayotukabili siku baada ya siku.Huwezi jua haya yote yatakwisha lini na vipi.Kulingana nami,naona Ni vyema ikiwa nasi tusake silaha za moto"Abdi alisema.Ukimya ukashika hatamu,takribani dakika tano kabla yangu kumjibu."Ni wazo zuri Abdi ila kuna ugumu fulani"."Ugumu upi?"Akauliza."Tutapata wapi zana hizi za moto?Pili,hatutakuwa tumewavuta karibu wanausalama na wanaintelijensia wa nchi hii?"."Hakuna ugumu wa yote hayo.Nina rafiki yangu humu mjini ambaye anakodi silaha halali ila si halali kwa asilimia fulani.Pia kuhusu kuziweka usiwe na wasiwasi.Tutatoboa sakafu ya chumba hiki kisha tunaunda kikabati cha saruji.Humo ndimo tutaziweka"Abdi akaelezea.Nikawa nimependezwa na mawazo yake.Tulijadili hili na lile muda mfupi tu,kisha tukalala.
Alfajiri,tukaamka kujiandaa kuanza siku yetu.Nilipika chai tukanywa na silesi za mkate kisha Abdi akaanza kunipa maelezo ya jinsi na ambavyo tungempata yule rafiki yake,muuza silaha."Ila pesa ndiyo tatizo Roy.Mimi nimeishiwa kabisa,nimebakiza tu hela ya chakula"Abdi akasema."Usijali,ninazo za kutosha"nikamwahidi.
'Jerusalem',ndilo jina lililokuwa limeandikwa mlangoni.Jumba lenyewe halikuwa limekamilika kujengwa.Vyumba kadhaa vilikuwa bado na vumbi na kokoto sakafuni.Mwenyeji wetu,kijana wa umri wa makamo ila aliyejengeka kimwili,alikuwa akitupitiliza hapa na pale mpaka ramani ya mle ndani ikanipotea akilini.Muda mchache,tukatokelezea kwenye chumba kilichokuwa kimepambwa kwelikweli.Kochi za mbonyeo,za kuvutia zilikuwa zimezunguka mle ndani.Tuliketi kisha Abdi akaanzisha mazungumzo moja kwa moja."Ni siku nyingi sana Yolanda tangu tuwe pamoja"Abdi akamsemesha yule kijana aliyemwita Yolanda."Kweli sahibu wangu,ila si tumekutana leo?"Yolanda akasema huku akitabasamu.Mazungumzo machache ya kirafiki yakachukua hatamu baada ya utambuzi kisha Abdi akamsimulia Yolanda masahibu yetu.Alimwelezea yote kuhusu kuuawa kwa wazazi wangu mpaka na matukio yaliyofuata baadaye."Pole sana Roy,kweli yote ambayo umeyapitia ni Rabuka tu ayajua"Yolanda alinipa pole huku akinipapasa mgongoni.
Machozi yakawa yakinitiririka huku rundo fulani la uchungu likinipanda kooni.Abdi na Yolanda wakawa wakinituliza.Yolanda akasogea kwenye friji na kuchukua soda tatu aina ya Fanta,akavifungua na kutukaribisha."Hebu tuwe na kinywaji kabla ya kuendelea maana hali iliyopo si ya kupendeza na salama kwa rafiki Roy Sikazwe."Yolanda akasema.Kadri muda ulivyokuwa ukisonga ndivyo hasira ikaanza kunitoka,nikarudi katika hali ya kawaida."Sasa vipi kuhusu mihela ndugu zangu?"Yolanda akatuuliza."Hamna shida Bratha maana tumekuja tayari tayari"Abdi akamwambia."Ok,tuingie ghalani"Yolanda akasema.Nikasimama tayari kwenda kuzikagua zile silaha ila Yolanda akacheka pamoja na Abdi."Tulia Roy,twaenda sote tena kwa njia ya ajabu"Abdi akasema.Kwisha sema hivyo,nikamwona Yolanda akibonyeza kitufe fulani chini ya meza kikatoa mlio hafifu kama lile la mtu anapolikanyaga tawi lililokauka.Polepole sakafu ikawa inazama,kisha tukapokelewa na giza totoro ambalo halikudumu sana.
Tukatua kwenye chumba fulani ardhini lenye upana mkubwa.Kilichonishangaza zaidi ni kuwa vile vyumba vyote vilikuwa na muundo sawa,pia samani ikiwa na mkao ulioshabihiana na mwingine.Sehemu kulikokuwa na friji kule juu ndiko kulikokuwa na friji huku chini.Lile sakafu ambalo lilituleta mle ndani likajirudisha kule juu baada yetu kuliondokea.Yolanda alisogea kochi moja refu Kisha akainama na kubonyeza kitufe fulani,nacho kikatoa sauti mfanano na ule wa kwanza.Kochi lile likajivuta nyuma na kuuwacha uwazi mkubwa tu kiasi ulioweza kuturuhusu kutumbukia ndani.Muda huo wote,hamna aliyemsemesha mwenzake.Tukafika ndani ya chumba chenye ukubwa kama wa ule wa juu.Tofauti ikiwa tu kuwa chumba tulichofikia kilikuwa kimejazwa silaha aina ainati ukutani.Kulikuwa na bunduki za walenga shabaha,zile ambazo niliweza kuziona kwenye runinga tu,nazo zikiwa mle ndani.Upande mmoja kulikuwa na bastola fupifupi,nami nikavutiwa na moja iliyolandana kimuundo na ile niliyokuwa nimewapokonya wale watu kwetu nyumbani."Chukua glovu hizi ndipo mzikague silaha hizi"Yolanda akatuambia huku akitukabithi glavu nne.Nilianza kuangalia moja kwa moja kila silaha iliyokuwa imenivutia."Ukuta ule unasilaha ndogo ndogo Kama vile visu vya kininja,sindano za kupuliza zenye sumu hivyo mjichunge navyo.Pia kuna grenedi za kurushwa na za kutega ardhini.Navyo msisahau mkachomoa pini ya usalama kwani zitalipuka."Yolanda alieleza akituonyesha ukuta wa nyuma kabisa.
Baada ya ukaguzi wa hapa na pale,tukaanza kukusanya silaha moja moja mezani.Tukachukua bastola sita za aina tofauti,magazine mia moja zilizojaa risasi,bunduki nne za kijeshi,vilipuzi aina ya grenedi za kutupa na kutega na zile silaha ndogo zenye sumu.Kwisha maliza kuchagua,tukaanza kuvipaki kwenye begi tulilokuja nalo.Baadaye safari ya kurudi kule juu ikaanza.Tulipofika kwenye chumba cha kwanza,tukaketi tena kochini kujadiliana."Pesa zangu nitapata vipi?"Yolanda akatuuliza."Nakutumia hivi sasa kwenye simu yako"Nikamwambia."Sawa ila sifikiri ni njia nzuri maana hivi sasa wewe watafutwa na wale watu wasiojulikana.Ningeomba ile kadi yako ya mawasiliano niifutie mtandao wa 'tracking'"Yolanda akasema.Nikampatia ile kadi,naye akaipachika kando ya tarakilishi iliyokuwa kando yake,kisha akabonyeza vitufe kadha wa kadha na kuitoa ile kadi."Sasa nimeiwekea usalama na kuitolea ile ya awali.Upo huru kuitumia sasa."Yolanda alisema.Akanipa ile kadi,nikaipachika kwenye simu yake Abdi na kufanya malipo ya silaha zile.Nilibaki na kiwango kikubwa cha pesa kwenye akaunti yangu ya benki ya rununu.Tulimuaga Yolanda kisha tukaondoka huku akitusindikiza."Nawatakia kila la heri ila msisite kunijulisha iwapo mwahitaji msaada wowote"akatuambia."Ndio Bratha.Tukishindwa Lazima tukujulishe maana licha yetu kuwa wawili,bado methali isemayo;kidole kimoja hakimwui chawa,inakubalika"Abdi akamwambia Yolanda.
Tulirudi kwake Abdi ikiwa imetimu saa nne usiku maana tulichukua muda mrefu kwake Yolanda,karibia siku nzima.Saa saba usiku ikatupata mezani,kwa harakati za kupanga namna ya kuanza vita vile."Ni vizuri tukianza uchunguzi nyumbani kwenu"Abdi akasema."Mmmh,vyema sana ila tutapita vipi mpaka ndani maana wale watu ninao uhakika watakuwa wameniwekea mtego"nikamweleza Abdi."Ndio maana tulitafuta silaha.Licha ya hayo,operesheni yote itafanywa usiku tukianza kesho.Kando na hayo,tutatumia majina bandia,wewe nitakuita Ahmed Musa nami utaniita Janito Kimbili"."Kwa nini tuitane majina bandia?"Nikamwuliza."Ili kuepuka uwezekano wetu kujulikana"Abdi alisema."Nimekumbuka kitu Abdi linaloniletea wasiwasi"."Lipi hilo?"."Iwapo Sofia atahojiwa na polisi na kunitaja itakuwaje?"
MWISHO WA SEASON 1
ENDELEA KUFUATILIA SEASON 2