Search This Blog

Saturday 5 November 2022

MIKONONI MWA NUNDA - 2

 








Simulizi : Mikononi Mwa Nunda

Sehemu Ya Pili (2)





Gari likaelekezwa Upanga. Akaisaka nyumba ya Ukeke hadi alipoipata. Lakini aligundua kuwa ameupoteza bure muda wake baada ya kukaribishwa na mke wa marehemu kwa vilio na machozi mara tu alipolitaja jina la marehemu. Yote mengine aliyouliza yalijibiwa kwa machozi yaliyomtoka mama huyo kama chemchemi ya maji. Machozi yake yaliwafanya wanawe nao kuangua kilio. Hivyo, alichofaidi Joram ni kuitumia nafasi hiyo kuitazamatazama nyumba, vifaa vya ndani na mapambo mengine.



Kadhalika, alimtazama mama huyo ambaye alikwisha kuwa mjane, na wanawe waliofanywa yatima. Hapo huzuni ikamwingia, huzuni ambayo iligeuka kuwa hasira, hasira ambazo kama kawaida yake zilibadilika na kuwa kiu ya kumnasa upesi zaidi mwuaji huyo.



Alijitahidi kuwafariji kidogo. Waliponyamaza aliwaaga kwa ahadi ya kuwatembelea siku nyingine. Akaianza safari ya kurudi ofisini. Hata hivyo alipofika nusu ya safari aliahirisha wazo la kwenda huko, badala yake aliamua kurudi zake nyumbani. Hakuiona sababu ya kwenda ofisini kwake zilisalia dakika chache tu kuwadia saa zake za kufunga. Mahala fulani alikiona kibanda cha simu.



Akasimamisha gari na kumpigia Neema simu akimjulisha kuwa asingefika tena ofisini. Baada ya hapo aligundua kuwa njaa ilikuwa ikimwuma. Akajitoma katika moja wa migahawa ambamo alijipatia maakuli. Kisha alirejea Ilala, nyumbani kwake. Jioni sana alilitia gari moto hadi Buguruni ambako alipenya uchochoro huu na ule akiitafuta West Bar. Alipoipata aliingia ndani na kujiketisha kiti cha mbali. Akajiwashia sigara na kutulia, akiwatazama wahudumu na wahudumiwa.



Sura na mazingira ya Bar hiyo hayakumvutia. Aliiona kama nafasi ambayo ingeweza kutumiwa na watu wengi ambao wanaiogopa sheria na polisi. Hayo yalimjia akilini kutokana na sauti za wanywaji waliokuwemo. Baadhi yao walikuwa wakipiga kelele bila kujali. Baadhi walikuwa wakicheza hovyo, nyuma au mbele ya meza; bila ya kufuata utaratibu wowote. Wengine waliacha viti na kukalia meza.



Mmoja kati ya wahudumu alimwona Joram alivyotulia peke yake, akamwendea. Alikuwa mwanamke mwenye umri baina ya kijana na mzee. “Nikusaidie nini kaka?” alimwuliza Joram.



“Bia moja tu,” Joram alimjibu. Kisha akajisahihisha, “Hapana, lete mbili. Uje ukae hapa tunywe na kuangalia yatakayofuata.”



“Vizuri.” Alisema akitabasamu.



Chupa zao zilipofika Joram alianza upelelezi wake mara moja. “Napenda kukuuliza, tafadhali. Ulikuepo usiku ule lilipokuja gari la marehemu. Ukeke? Ulimwona?



Tabasamu lililokuwepo katika macho ya mwanamke huyo likadidimia ghafla. Nafasi yake ikatawaliwa na kitu kama hasira,

“Na wewe u mmojawao? Mbona huonekani kama mmoja wao?



“Wao! Akina nani?”



“Askari,” alijibiwa. “Wanatusumbua sana siku hizi. Kuja kwa lile gari hapa; kama ni kweli lilikuja, imekua kama tumemwua sisi. Mnadhani tulimwua?”



Joram akaruhusu moja ya vicheko laini kuupenya uso wake alipomjibu mwanamke huyo, “Usiniogope. Mimi si askari wala polisi. Ni raia tu mwenye nia ya kufahamu kama yanayosemwa ni kweli au uongo.”



“Alaa! Basi huna haja ya kujisumbua kwa kifo cha mlevi kama yule, anaweza kuwa alifika hapa au hakufika. Hatujui. Si kazi yetu kujua nani kafika nani hakufika. Anaweza kuwa alipitia baa nyingine nne au zaidi kabla hajakutana na hayo majambazi yaliyomwua. Hatujui. Hivyo, sioni kama iko haja ya kuendelea kutuhangaisha bure.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Wakati mama huyo akizungumza hayo, macho ya Joram yalivutwa na msichana mrembo ambaye alijitokeza nyuma ya kaunta. Ilikuwa sura nzuri yenye dalili zote za ujana. Kuweko kwake miongoni mwa wanawake wengine huko nyuma ya kaunta kuliwafanya hao wenzake waonekane kama vichaka vilivyoota kulizunguka ua zuri.



Akajikuta akitamani binti huyo amtazame ili amkonyeze. Kwa bahati mbaya, hilo halikutokea. “Kwanini auharibu uzuri wake katika mabaa? Joram aliwaza.



Ghafla, alijikuta hana hamu ya kuendelea kumsikiliza mwanamke huyu mzee aliyekaa kando yake. Akamgeukia na kumweleza polepole, “Ahsante kwa maelezo yako sasa unaweza kwenda zako.”



Mama huyo alimtazama Joram kwa mshangao. Joram hakuujali mshangao wake. Kinyume chake aliiacha chupa yake iliyojaa nusu na kuhamia kaunta ambako aliparamia stuli ndefu na kuketi.



Macho yake yalikuwa yakimtazama mtu mmoja tu, Yule binti ‘dogodogo’ na mzuri. Lakini binti huyo alikuwa hamtazami wala kutazama upande wake. Alikuwa akishughulika kuwahudumia wateja wengine kwa kuwapa pombe na maongezi matamumatamu. Hata hivyo, Joram aliridhika kwa nafasi hiyo aliyoipata, nafasi ya kuketi akimtazama binti mzuri, ambaye hajui kuwa anatazamwa, nafasi ambayo ilimwezesha kutazama yote aliyoyahitaji katika uso huo.



Yote aliyoyaona yalimvutia. Yote yalikuwa mema. Hata hivyo, Joram alihisi upungufu wa jambo moja katika sura ya msichana huyo. Jambo moja tu, tabasamu, kamwe hakuona likijitokeza kuwafariji wateja. Kama ni dosari basi ilikuwa hiyo tu katika sura ya binti huyo.



SURA YA TATU



Jiji la Dar es Salaam si dogo. Ni kubwa tosha. Na lina wingi wa watu, watu mbalimbali. Kadhalika, kila mmoja akiwa na shughuli mbali na mwingine. Wakati wengine wakilima, wengine huvua, wakati wengine wakinadi wenginne hufua, na kadhalika.



Hivyo, usiku ule ambao Joram Kiango aliketi katika moja ya baa za Buguruni akimtazama yule msichana mzuri, mtu mwingine alikuwa kajifungia katika chumba chake cha kuchorea; akikamilisha picha yake mpya. Huyu alikuwa Silivano Rashidi, mchoraji ambaye sifa zake zilikwishatapakaa Afrika Mashariki nzima na kupenya hadi ughaibuni. Picha zake zilikuwa nzuri za kuvutia. Kila mtu alitaka awe na moja ya picha hizo katika nyumba yake, lakini si kila mtu aliyeweza kuzinunua kwa ajili ya ukubwa wa bei zake. Hivyo, wateja wake wengi walikuwa matajiri na watalii ambao walikuwa tayari kutoa pesa zozote.



Pamoja na umaarufu wake ni watu wachache sana waliomjua Silivano kwa sura. Hata baadhi ya watu walioishi Buguruni, jirani zake, hawakumfahamu kwa sura zaidi ya kusoma habari zake magazetini. Na waliomwona wakielekea kushindwa kuamini kama kweli huyu ndiye Silivano aliyeweza kuchora picha ainaaina.



Walimwona kama mfupi mno, mkimya mno na asiyejua kitu. Baadhiwalidiriki kumwambia hivyo. Yeye aliwajibu kwa tabasamu akisema, “Ubora wa mtu umo kichwani tu.”



Hata hivyo, waliendelea kushangaa wakidai kwenye miti hakuna wajenzi, kwani ingawa Silivano alikuwa tajiri lakini hakujua namna ya kuutumia utajiri wake



Haikuwa uongo. Hata mara moja Silivano hakuingia baa yeyote kuinywa fedha yake. Anapoulizwa hudai ulevi ungempunguzia muda wa kuchora na kumvurugia kipaji. Sinema alikwenda kwa taabu. Mara nyingi ilikuwa baada ya kubembelezwa au kulazimishwa na mke wake. Alikuwa amejenga nyumba kubwa kwa ajili ya usalama wa afya yake na wanawe. Gari alilinunua kwa kuwa alihitaji kurahisisha safari zake. Kama hizo ni starehe basi zilikuwa starehe zake pekee. Vinginevyo, hakukubali kuupoteza muda wake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Chumba chake cha kusomea kilikuwa na dirisha lililotazama barabarani. Mara nyingi, wakati akiyapanga mawazo yake kabla ya kuanza kucheza na rangi, huacha macho yake yatazame nje ya dirisha hilo yakiwaona wapitanjia hali mawazoni hawaoni. Kisha huinama na kuanza kazi.



Usiku wa leo alichora hali dirisha li wazi kwa haja ya kuburudika kwa upepo asilia wenye baridi badala ya ule wa feni. Mara akaona kipande cha karatasi kikipeperuka na kuangukia kwenye meza yake. Karatasi hiyo ilikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa wino mwekundu. Maandishi ya aina yoyote humvutia Silivano, kama apendavyo kuyaandika. Haya ambayo aliamini kuwa yamepeperushwa toka nje hadi mezani kwake, yalimvutia zaidi. Akayatwaa na kuyasoma. Hakuyaamini macho yake. Akayasoma tena kwa makini.



Ndugu Silivano Rashidi,

Waraka huu kwako sio ombi bali ni amri. Kesho saa sita usiku tupa shilingi laki moja nje ya chumba chako. Mtu ataziokota. Usipofanya hivyo ama ukijidanganya kuiarifu polisi, kesho hiyohiyo utakuwa marehemu. Wakumbuke marehemu Ukeke na Matoke.

Sina mchezo wala huruma. Wala sifanyi makosa nikikusudia kuua.

Ndimi,

NUNDA MLA WATU.



Silivano alipomaliza kuisoma barua hiyo kwa mara ya tatu alijikuta akitetemeka mikono ikiwa imeloa jasho. Yote aliyoyaandaa ili kuyachora, yalitoweka ghafla, nafasi yake ikiwa imemezwa na kitu kingine, hofu ya kufa. Kwa mikono inayotetemeka, akalifunga dirisha lake na kukifuata kitanda ambacho alikesha juu yake.



Kwake fedha haikuwa na thamani zaidi ya maisha, uhai, ili achore, ili asifike. Kifo kingekuwa mwisho wa kusifika kwake. Hivyo, kulipopambazuka alioga, akasahau kufungua kinywa na kuwa mtu wa kwanza kufika benki. Ilipofunguliwa alitwaa fedha aliyoamriwa na kuhifadhi nyumbani kwake. Saa ilipowadia alifanya kama alivyoelekezwa.

Alipoamka kesho yake na kukuta fedha haipo, ndipo alipostarehe.

***

Barua kama hiyo ziliendelea kuwafikia watu kadha wa kadha wenye ukwasi. Kila aliyeipata alitetemeka kama aliyesalimiwa na mauti. Kila mmoja wao alitii kama kifo na kutekeleza yote aliyoamriwa kufanya. Hofu ya kifo ilikuwa na nguvu zaidi ya tamaa ya fedha. Naam, ilikuwa hivyo kwa kila mtu; Tendwa Mkoroma.



Yeye barua hiyo aliiokota chini ya meza alipokuwa akinywa pombe katika moja ya baa za Magomeni. Alidhani ni noti iliyodondoka toka katika mfuko wa mmoja wa wanywaji wenzake. Alipoitazama akashangaa kuona kuwa ni barua yake, ikimdai fedha! Akaisoma tena kwa makini zaidi. Kisha aliielewa. Akacheka. “Awe Nunda mla watu ama Nunda mla nchi, hata senti moja toka katika milki yangu hataipata,” alisema kwa nguvu alipokuwa akiinuka, kuelekea polisi.



Kuidharau kauli ya NUNDA MLA WATU alikokufanya Tendwa ni jambo ambalo lisingeweza kumshangaza mtu yeyote aliyemfahamu. Alijulikana kote Magomeni, si kwa ajili ya utajiri wake mkubwa tu bali hasa kwa ajili ya ubahili aliokuwanao, ubahili wa ajabu. Wanawe walikuwa wakivaa matambara ambayo ni yeye tu aliyeyaita nguo. Mke alikuwa na hali kama hiyo, nyumba ilikuwa gofu lisilo na dalili ya utajiri na ilisemekana kuwa hata chakula hakikuwa na tofauti na kile cha fukara asiye na senti. Hilo pia lingeweza kudhihirika kwa jinsi yeye na wanawe walivyokuwa wembamba mithili ya wagonjwa waliotoka hospitali.



Chanzo cha utajiri wake ambao ulimpatia magari manane ya abiria, baa mbili na vilabu vinne, hoteli tatu na mashamba makubwa ni siri ambayo hakuna aijuaye. Wengine walidai kuwa alifanikiwa kuchuma kwa ajili ya kujinyima. Wengine walidai kuwa alifanya magendo na ujambazi, pamoja na hadithi chungu mbovu ambazo hazikuweza kuthibitishwa.



Hadithi iliyovuma sana, ikasimuliwa na kila mtu ni ile inayodai kuwa alisafiri toka kwao Kilimanjaro, akiwa fukara zaidi ya ombaomba, akaenda hadi vijiji vya Mwanza ambako yuko mzee mkongwe sana mwenye njia ambazo humwezesha mtu shujaa kujipatia utajiri wa haraharaka.



Ilielezwa kwamba Tendwa alipomfikia babu huyo na kumweleza haja yake mzee alimwambia ajiandae kufunga safari ndefu ya milimani. Tendwa hakupinga, kesho yake saa sita za usiku, baada ya kuelekezwa njia na kuonywa kuwa asiogope wala kurudi nyuma, akakubali. Safari ilimchukua hadi chini ya mlima uliokuwa na pango lenye giza kuliko usiku wenyewe.



Aliingia katika pango hilo na kuendelea na safari yake ikiwa kupapasapapasa kuta. Kila alivyopapasa aligusa wadudu kama nge na nyoka ambao walikoroma kwa ukali. Hakuogopa wala hakukata tamaa. Badala yake akaendelea na safari hiyo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Tahamaki akasikia sauti za watu wasioonekana, wakinong’ona na kumfokea kwa kila neno la kutisha. Alipatwa na hofu na kutetemeka lakini hakurudi. Hatimaye, akawasili sehemu ambayo ilikuwa na nuru hafifu. Hapo aliona vitu vya kutisha zaidi. Maiti, nyingi zikiwa hazina macho, meno ama zilizokatwa kichwa. Zote alihisi zikimnong’oneza maneno ya masimango kwa lugha ya kutisha.



Hakutishika. Akazipita hadi mbele ambako alihisi ni mwisho wa pango. Alisimama hapo kwa muda hadi macho yake yalipolizoea giza. Ndipo alipoliona joka kubwa kupindukia lililokuwa likimtazama, domo wazi tayari kumgonga. Mbele ya domo hilo yalikuwepo maiti ya mtu, mwanamke; yakivuja damu. Kizee kilimwambia kuwa chochote ambacho angekiona mdomoni mwa joka hilo akitwae, ndio utajiri wenyewe.



Hivyo, kwa mikono inayotetemeka akayavamia maiti haya na kuanza kurudi alikotoka. Kwa mshangao wake joka halikumfuata wala maiti hayakuwa mazito. Kila alivyozidi kwenda ndivyo yalivyozidi kuwa myepesi. Alipofika nje ya pango alijikuta hana maiti tena ila kifurushi kidogo ambacho kilikuwa na vipande vingi vya almasi. Akamwendea yule kizee ambaye alimweleza kuwa huo ndio utajiri wenyewe.



Hayo na mengine mengi Tendwa aliyasikia na kutabasamu tu. Kamwe hakujishughulisha kuyaafiki wala kuyakanusha.



“Tazameni hii. Oneni kisa cha vifo vya watu wote wanaoangamia siku hizi. Kumbe ni hii…” Tendwa alisema alipofika polisi na kuitupa ile karatasi mezani.



Polisi aliyeipokea aliitazama kwa mshangao. Kisha alimtazama Tendwa na kumwuliza, “Umeipata wapi barua hii?”



“Nimetupiwa chini ya meza…” ikafuata habari kamili. Jinsi alivyoipata, wapi, lini na kadhalika.



“Niwie radhi kidogo, mzee,” askari huyo alisema, akiondoka na kumezwa katika jumba hilo kubwa. Alirejea hima na kumtaka Tendwa amfuate ndani.



Walifuatana hadi mbele ya Inspekta Kombora ambaye alimkaribisha Tendwa kiti na kumruhusu yule askari kuondoka.

“Ulichofanya ni jambo la kijasiri,” Kombora alimweleza baada ya kujuliana hali. “Jambo ambalo litayaokoa maisha ya watu wengi wasio na hatia pamoja na kutuwezesha kumkamata mwuaji au wauaji hawa mapema zaidi. Kwa kweli, bila wewe tungepata shida kumkamata. Si rahisi kuwagundua wauaji bila ya kufahamu chanzo cha mauaji yao. Sasa tumefahamu, ni fedha. Haikosi wamekwishawatisha watu wengi na kuvuna wasichokipanda.”



Akasita na kumkazia macho Tendwa ambaye alitulia juu ya kiti chake, mikono ikichezea kasha la jivu la sigara lililokuwa mezani hapo.



“Bado tutauhitaji zaidi msaada wako ndugu Tendwa,” Kombora alimwambia. “Sijui ni watu wangapi waliokuona ukija hapa?”



“Sidhani. Sijamweleza mtu jambo hili.”



“Vizuri. Tutafanya hivi. Pesa wanazozitaka ndizo zitakazowanasa. Tutakupa pesa hizo. Ziweke mahala walipokuamuru. Tutamnasa yeyote atakayekuja kuzichukua. Hata kama atanusurika kwa njia hiyo bado atakuwa mikononi mwetu kwani noti zote zitakuwa zimenakiliwa namba. Itakua rahisi sana. Rahisi kuliko nilivyotegemea.” Kombora alimaliza akitabasamu.



“Ningependa sana kusaidia,” Tendwa alijibu. “Lakini hofu yangu ni kuhatarisha maisha yangu. Kumbuka walivyouawa kikatili akina Ukeke na Matoke. Nisingependa kufa sasa hivi.”



Kombora akacheka, “Usiwe na hofu. Tunayathamini sana maisha yako. Mpaka sasa tunavyozungumza nimekwishatuma makachero ambao wanainyatianyatia nyumba yako kuhakikisha usalama wako na familia yako. Usiku, wakati ukipeleka fedha hizo, makachero wengi watakuwepo tayari kwa lolote, tayari kumwua adui yako kabla dhara lolote halijatokea. Usihofu, ndugu Tendwa. Kila kitu kimepangwa kwa uangalifu, kama inavyostahili.”





Wakakubaliana, Tendwa akapewa furushi la noti, kama alivyoamriwa. Akaenda nazo hadi nyumbani ambako alilihifadhi akisubiri saa aliyopangiwa.

Saa sita za usiku aliinuka na kuichukua fedha hiyo. Akatoka nje na kuufuata mti alioelekezwa. Akaiweka. Kesho yake, alfajiri alichungulia dirishani na kuona mfuko wa fedha ukiwa palepale. Hatimaye, alimpigia simu Inspekta Kombora ambaye alimweleza kuwa mpango umeharibika.

Kachero mmoja alipewa amri ya kuzitwaa na kuzirejesha kituo cha polisi.

***

Konko wa Mankonko aliipata barua yake kwa njia ya ajabu kidogo. Aliikuta katika moja ya mifuko yake ya shati. Hakujua iliingiaje humo. Alipoisoma akakuta ni amri;

…mwue Tendwa Mkoroma kabla ya kesho kutwa. Usipofaulu utakufa badala yake. Sina mzaha wala hili si ombi ni amri.

Ni mimi,

NUNDA MLA WATU.

Kupewa amri ni jambo ambalo liliongoza orodha ya mambo yote ambayo Mankonko hakuyapenda. Kamwe hakuwa tayari kupokea amri yoyote toka kwa mtu yeyote. Ni kuichukia amri ambako kulimfanya ashindwe angalao kuhitimu darasa la kwanza. Kuchukia amri ndiko kulikomfanya ashindwe kufanya kazi ya kuajiriwa ambayo alitafutiwa na wazazi wake. Kwa kutopenda amri akajikuta anavunja sheria na kujikuta gerezani mara kwa mara. Huko alikuwa akifanya kila awezalo hadi akatoroka. Hali hiyo ilimfanya atukie kuwa gaidi wa kutisha ambaye alitetemesha jiji zima la Dar es Salaam, gaidi aliyefanya ujambazi wake peke yake, kuua ukiwa mchezo aliouona wa kawaida kama yote mingine. Majuzi tu picha yake ilitolewa gazetini akisakwa kwa kosa la kumuua polisi. Hivyo, alikuwa akiishi kwa mbinu hii na ile, akibadili majina na tabia kama kinyonga abadilivyo rangi ya ngozi yake.

Kumwua Tendwa ni jukumu ambalo lisingemchukua dakika tano. Alikuwa hodari wa kutumia bastola kwa umbali wowote unaoruhusu. Na shabaha yake haikuwa na mashaka. Lakini alijikuta akilikataa jukumu hilo kwa hasira mara tu alipoona neno “amri” katika waraka huo.

Ingawa alikuwa amesoma magazetini sifa na ukatili wa mwuaji huyo asiyejulikana, lakini kamwe hakujisikia kutii amri yake. Kama watu wengine, yeye pia alikuwa akijiuliza ni nani huyu mwuaji katili? Alikuwa hata hafahamu kisa cha mauaji yake wala jina la mwuaji huyo hadi jana aliposoma gazeti na kugundua kuwa alijiita NUNDA na haja yake ikiwa fedha.

“Pamoja na ununda wake mimi hanibabaishi,” Makonko alinong’ona akikiacha chumba chake kilichojificha katika vichochoro vya Buguruni na kufuata kimoja cha vibanda hasara vya karibu ambapo aliizima hasira yake kwa bia. Alipolewa barabara aliirejea kambi yake ambako alijitupa kitandani na kuruhusu usingizi mnono kumchukua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kesho yake aliifuata ratiba yake ya kawaida, kunywa, kulewa na kulala.

Siku ya tatu alianza kuwa mwangalifu zaidi. Hakuruhusu ulevi kumtawala. Na aliporejea chumbani kwake hakuuacha usingizi ummiliki. Badala yake alitandika kitanda chake vizuri akatwaa moja ya mablanketi yake na kulikunja vizuri, mfano wa mtu, juu ya kitanda hicho. Mwenyewe akavuta stuli na kutulia juu yake, katika moja ya kona ya chumba chake. Bastola yake ikiwa mkononi, macho kayakaza mlangoni, alikesha akiisubiri habari yoyote ambayo ingetokea.

Hakuna kilichotokea. Hadi kulipokucha bado alikuwa hajaona wala kusikia chochote kilichoashiria hatari.

Hakukata tamaa. Kesho yake aliurejea utaratibu uleule. Usingizi haukumsumbua kama usiku uliotangulia kwa jinsi alivyoupunguza mchana.

Usiku wa manane alihisi kusikia kitu alichokihitaji, vishindo hafifu na mchakacho kwenye mlango wake. Akaishika bastola yake vizuri zaidi na kuendelea kusubiri. Kikafuata kimya kirefu. Baada ya kimya hicho zilisikika tena hatua za mtu, zikifuatwa na minong’ono hafifu. Kisha chakarachakara za funguo zikasikika. Ghafla, kama ndoto mlango ukafunguka polepole na kuruhusu viwiliwili vya watu walioshikilia bastola kuingia. Wakaufunga mlango polepole nyuma yao.

Blanketi alilolikunja Makonko halikutofautiana na kiwiliwili cha mtu aliyekuwa katikati ya usingizi mnono. Watu hao wenye silaha walitazamana na kutabasamu kidogo kwa kudhani kuwa wamelifumania windo lao katika hali nzuri.

“Hakuna haja ya kuharibu risasi,” alinong’ona mmojawao. “Tumwue kwa kisu. N’nacho kifaacho. Hiki hapa.” Akakichomoa na kumwonyesha mwenzi wake. Nuru hafifu ya mwezi iliyopenya kupitia dirishani ilifanya kisu hicho kimeremete.

“Bila shaka,” mwenzake alijibu. “Mlio wa bastola utawaamsha majirani kiasi cha kutufanya tuanze kukimbia bure. Tukimchinja tutatoka hapa kwa usalama kama watokao dansini. Tena tufanye hima.”

“Haya”

Mwenye kisu alikisogelea kitanda na kujiandaa kukichovya katika kifua cha windo lake. Alikatizwa kwa sauti nzito iliyonong’ona kwa ukali ikisema, “Angusheni silaha zenu chini, wote.”

Walipogeuka walishangaa kumwona Makonko akiinuka toka juu ya stuli aliyokuwa kaikalia kwa namna ya starehe na kuwajia polepole, bastola imemtangulia.

“Silaha zenu chini,” alifoka kwa sauti ileile, ndogo na kali. Wakamtii hima na kuiweka mikono yao juu huku wakitetemeka.

Makonko aliwafahamu sana vijana hawa. Walikuwa majambazi wadogowadogo toka katika kikundi cha White Satans ambacho kiliongozwa na mzee mmoja aliyekuwa jela. Angeweza kuwaua bila matatizo yoyote mapema zaidi. Hakufanya hivyo kwaajili ya mshangao wake wa kujua kuwa Matamba, kiongozi wa kikundi hicho ndiye aliyekuwa akijiita NUNDA na kuua ovyoovyo. Hakutegemea kama kikundi hicho kingefikia hatua kama hiyo. Na bado hakukuwa na hakika. Hiyo ilikuwa sababu pekee iliyomfanya aahirishe adhabu ya kifo, ili ahakikishe.

“Sogeeni hapa.”

Wakamtii na kumkaribia.

“Nani ajiitaye Nunda kati yenu?” alihoji.

Hakuna aliyemjibu.

“Nani?” alifoka.

Wakatikisa vichwa vyao kukana.

“Au ni yule Matamba anayejihita hivyo?”

Bado wakakana.

“Sijakueleweni. Manataka kuniambia nini? Kwamba hamumjui NUNDA? Nani basi aliyekupeni jukumu la kuniua?”

“Kwakweli hatumfahamu NUNDA. Jukumu la kukuua ni amri tuliyopewa na mkubwa wetu akidai kuwa ameamriwa na NUNDA kufanya hivyo. Eti asipotii atakufa badala yako,” mmoja wa mateka hao alijitahidi kueleza huku akitetemeka.

“Mna hakika kuwa Matamba sio NUNDA?” Makonko aliendelea kuuliza.

“Hakika tunayo kwani mzee mwenyewe anamwogopa sana NUNDA.”

“Yaani mlikubali kuua, kuniua, hali hamumjui NUNDA?”

“Ndio. Ilikuwa hofu tu. Kama alivyosema bosi.”

“Mna bahati mbaya sana. Ningeweza kuwasamehe, kwakuwa sina kisasi nanyi. Lakini sitafanya hivyo, haijanitukia hata mara moja kumwacha hai mtu yeyote aliyekusudia kunitoa roho. Vilevile ninyi ni wapumbavu na waoga ambao hamfai kuishi. Mnawezaje kuitii amri ya mtu msiyemfahamu kwakuwa tu anajiita NUNDA MLA WATU? Sitakuhurumieni kwa sababu hizo. Fumbeni macho…”

Badala ya kufumba wote waliyatoa kwa hofu na kuanza kutetemeka. “Tafadhali…li, …tu…tu” walijaribu kusema lakini sauti zao zikamezwa na milipuko ya bastola ambayo ililipuka na kualika kama umeme kuvuruga utulivu wa usiku.

Wakati mshindo huo ukipoa ulimkuta Makonko akiwa mbali mitaani, akienda zake; mikononi akiwa na rasilimali zake zote muhimu.

Alikuwa akiumaliza mtaa wake, aingie mtaa wa pili alipogeuka nyuma baada ya kusikia akiitwa. Alilazimika kuirudisha mafichoni bastola yake ambayo alianza kuitayarisha, alipoona akifuatwa na mwanamke. La, msichana. Alikuwa mdogomdogo, mwenye sura nzuri ingawa ilifunikwa na kitu kama huzuni au msiba. Kilichomvutia Makonko si usichana wake tu bali kanga moja tu ambayo aliivaa binti huyo kiasi cha kulifanya umbo lake la ndani kuonekana kama lilivyo; lililojaa na kubonyea panapostahili kwa namna iwezavyo kumletea njaa ya mapenzi mwanaume yeyote. Makonko, akiwa mmoja wao, alijikuta kasahau kuwa ilimpasa kutoweka eneo hilo haraka. Badala yake alisogelea na kuuliza polepole, “Unasemaje shangazi?”



“Samahani kaka,” binti huyo alimjibu hali kamkazia macho. “Nauomba msaada wako. Unisaidie nifike nyumbani tu, tafadhali. Naogopa kuvamiwa na wahuni.”



“Kwani wewe ni nani sista? Na unatoka wapi na kwenda wapi saa hizi?



“Ya Mungu, mengi kaka yangu. Yaliyonikuta hayasemeki.” Sauti yake ilikuwa na huzuni kama uso wake. “Mambo yenu nyie wanaume ya hatari sana. Kanifuata mwenyewe nyumbani, kanibembeleza kwa fedha na hongo hadi nikakubali kwenda naye kwake. Kumbe ana mke. Sijui alikuwa kamficha wapi mke wake. Mara nikaona mke wake akitokea uvunguni. Wakaanza kunipiga. Nimeponea chupuchupu baada ya kukimbia. Tazama nilivyo. “Sina hata nguo, masikini.”



Makonko, ambaye huruma iko mbali na roho yake, alihisi kitu fulani rohoni. “Unaishi wapi? Nitakupeleka.”



“Ahsante sana kaka. Sijui nikushukuru vipi.”



“Usijali. Unaishi wapi?”



“Twende tu. Nitakuonyesha.”







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog