Search This Blog

Saturday 24 December 2022

OPERATION ENTEBBE - 4

  http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/operation-entebbe.html

Simulizi : Operation Entebbe

Sehemu Ya Nne (4)



Baraza la mawaziri la Israel likamuomba Amin aongee na watekaji wakubali kusogeza siku mbele ili kuipa serikali ya Israel muda wakutosha kushughulikia lojistiki na kushawishi Ujerumani na Ufaransa ili waweze kutimiza sharti la kuachiwa kwa wafungwa wa kipalestina 53 wanaotuhumiwa kwa ugaidi.


Rais Idd Amin baada ya kushawishiwa sana akakubali ombi hili na akaieleza serikali ya Israel kwamba ni siku tatu tu pekee zinaongezwa, yaani ikimaanisha kwamba siku zitaongezwa mpaka tarehe 4 July, saa 8 mchana. Serikali ya Israel ikakubliana na hili.


Mchana wa siku hiyo, serikali ilitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari wakilaani vitendo vya kigaidi na hususani matukio ya utekeji wa raia wasio na hatia, na pia ikaendelea kusisitiza kuhusu sera yake ya kutojadili na magaidi. Lakini taarifa hii ikamalizia kwa kueleza kuwa kwa kujali zaidi uhai wa zaidi ya raia 200 ambao bado wanashikiliwa na magaidi hayo, na kujali maumivu ambayo familia zao na taifa zima linapitia, wamekubali kutimiza sharti la magaidi hao la kuwalipa fedha za kimarekani dola milioni tano pamoja na kuachiwa kwa wafungwa wa kipalestina 53 wenye tuhuma za ugaidi.


Ilikuwa ni moja ya matukio machache ambayo yaliishangaza dunia kwa Israel kukubali kushindwa hadharani. Kwa upande wa maadui wa Israel hii ilikuwa ni sherehe kubwa kwao. Na kwa upande wa Isarel na maswahiba zake hii iikuwa ni maombolezo makubwa.

Amin na wenzake kule Uganda walikuwa wanasherehekea baada ya taarifa hii kutolewa kwa vyombo vya habari. Walihsi kabisa harufu ya ushindi inanukia kwenye pua zao.


Kitu ambacho walikuwa hawafahamu ilikuwa ni kwamba, Israel walikuwa wanawafanyia ‘mchezo’ wa kisaikolojia ili Amin, jeshi lake na watekaji wajiamini kwa kuona kuwa ushindi umeegemea upande wao na hatimaye wajisahau kutokana na kujiamini huku.


NYUMA YA PAZIA


Huko Tel aviv, makamanda wa IDF na maafisa wa Mossad walikuwa wamekusanyika katika conference room ya mako makuu ya wizara ya ulinzi kuweka mkakati wa oparesheni ya uokozi (rescue mission) wa mateka wanaoshikiliwa katika uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda.

Kati ya watu muhimu ambao walikuwepo kwenye kikao hiki alikuwa ni Waziri Mkuu Rabin na Ehud Barak ambaye kipindi hicho alikuwa kamanda wa ngazi za juu kwenye jeshi anayeongoza kitengo cha Intelijensia ya jeshi (Military Intelligence).


Moja kati ya vitu muhimu ambavyo viliwasaidia ilikuwa ni taarifa ya intelijensia iliyoletwa na Mossad kwamba uwanja wa ndege wa Entebbe ulijengwa na kampuni ya Kiisrael inayoitwa Solel Boneh.


Kwahiyo muwakilishi kutoka katika kampuni hii ya ujenzi naye akaitwa kikaoni kwa ajili ya kuwasilisha michoro kuhusu jengo lote na uwanja wa ndege wa Entebbe ulivyo.

Lakini pia wakati huo huo kulikuwa na maafisa wa Mossad ambao walikuwa ufaransa kuwahoji wale mateka ambao walikuwa wameachiwa awali. Mtu muhimu zaidi ambaye alitoa taarifa nzuri kwa Mossad alikuwa ni yule afisa wa jeshi niliyemuelezea awali kwamba alikuwa na uraia wan chi mbili (Israel na Ufaransa) na siku hii alikuwa ametumia passport ya nchi ya ufaransa hivyo watekaji walimuachia pamoja na wenzake wa kundi la kwanza lile la watu 48.


Bwana huyu alitoa taarifa muhimu zaidi kuhusu kilichokuwa kinaendelea katika uwanja wa ndege wa Entebbe, kwa kuwa yeye tofauti na wenzake kutokana na uzoefu wake wa jeshi alikuwa aliweza kuwaeleza Mossad kuhusu ni salaha za namna gani watekaji walikuwa nazo, kulikuwa na ndege za aina gani za kijeshi pale uwanjani (Idd Amin aliamuru Air Force ya Uganda kulinda uwanja huo masaa 24), pia aliweza kuwaeleza kuhusu ‘rotation’ ya ulinzi ya jeshi la Uganda pamoja na taarifa nyingine muhimu ambazo abiria wengine wasingeweza kuzitilia maanani au kkuzieleza kwa ufasaha.


Baada ya kupata intelijensia ya kutosha, mkakati wa awali ambao ulipendekezwa na jeshi ulikuwa ni kutumia ndege ya kijeshi na kisha kudondosha makomando kwenye ziwa Viktoria na kutoka hapo watatumia boti za mpira kuvuka mpaka nchi kavu na hatimaye kuelekea uwanja wa ndege ambao haukuwa mbali sana na ziwa Viktoria.


Mkakati huu ulikuwa ni mzuri lakini ulihairishwa baada ya kupewa taarifa kuwa ziwa Viktoria lilikuwa na mamba wengi na ingeweza kuhatarisha uhai wa hawa makomando kabla hata ya kufika kwenye uwanja wa ndege. Kwahiyo ilikuwa dhahiri kwamba mkakati wowote ambao utawekwa ni lazima uwe wa kuvamia kutokea nchi kavu na ikiwezekana kutoka nchi jirani.


Changamoto kubwa zaidi ilikuwa ni usafiri. Yaani kwamba oparesheni hii ilikuwa si tu kwamba makomando wanaotumwa kutekeleza wanaenda kupambana na magaidi wanne tu walioteka ndege, bali ilikuwa ni kana kwamba wanaenda kupambana na jeshi zima la Uganda. Kwa hiyo kikosi cha makomando ambacho kitatumwa kwenda huko lazima kiwe na watu wengi wa kutosha na pia lazima wachukue silaha nzito za kutosha. Ili kufaniskisha safari yenye makomando wengi hivi na vifaa vizito ilikuwa ni lazima kutumia ndege kubwa za kijeshi zenye uwezo mkubwa pia na hakukuwa na chaguo zuri zaid ya kutumia ndege za kijeshi za LOCKHEED C-130 HERCULES. Sasa changamoto ilikuwa inakuja kwamba huwezi kurusha dege kubwa kama hii kwenda na kurudi kutoka Israel mpaka Uganda bila kujaza mafuta tena japo mara moja.


Katika kipindi hiki bado Israel walikuwa hawajawa na uwezo wa kufanya ‘Aerial Refuel’, yaani ndege kujazwa mafuta kwa kutumia ndege nyingine ikiwa angani. Lakini pia ilikuwa ni lazima madege hayo yakikaribia Uganda yaruke chini chini ili kukwepa kudunguliwa na kuikwepa rada ya kijeshi. Kwa hiyo ilikuwa ni lazima kupata nchi ndani ya afrika Mashariki ambao watakubali madege hayo ya kijeshi ya Israel kutua kwenye uwanja wake wa ndege na kujaza mafuta lakini pia kujiandaa na kuanzisha operation kutokea hapo na pia anga lao kutumika kuanzisha shambulizi la kijeshi kuelekea Uganda.





Sasa japokuwa nchi zote za Afrika Mashariki zilikuwa hazikubaliana na kitendo cha Rais wa Uganda kushirikiana na watekaji, lakini hakukuwa na hata nchi moja ambayo ilikuwa iko tayari kuingia kwenye mzozo na Idd Amin kwa kuruhusu viwanja vya vya ndege kutumika na ndege za jeshi la Israel au wanajeshi kujiandaa kuvamia Entebbe au pia kuruhusu anga lao kutumia na jeshi la Israel.


Ndipo hapa ambapo kwa haraka sana siku hiyo hiyo Waziri Mkuu Rabin akamtuma Ehud Barak na maafisa wachache wa Mossad kwenda Kenya kushawishi serikali ya Mzee Jomo Kenyatta iruhusu ndege za jeshi la Isarel kutumia kiwanja chao cha ndege. Ehud barak na wenzake hawakwenda tu moja kwa moja kwa Mzee Kenyatta, bali kwanza walienda kwa Waziri wa kilimo wa kipindi hicho Bw. Bruce McKenzie ambaye huyu aliwahi kuwa afisa wa Idara ya ujasusi ya Uingereza, MI6 na pia alikuwa swahiba mkubwa wa Ehud Barak.


ehud-barak-jpg.524098

Ehud Barak enzi za utumishi jeshini


Kwa hiyo Israel ikamtumia Bruce McKenzie kumshawishi Mzee Jomo Kenyatta kuruhusu anga la Kenya na viwanjavya ndege kutumiwa na makomando wa Israel na ndege zao.

Ehud Barak na maafisa wa Mossad hawakuishia hapa tu, bali pia walifanya vikao vya siri na wafanyabiashara wakubwa nchini Kenya wenye asili ya Israel na wale ambao walikuwa na ‘marafiki’ wa Israel kuwaomba watumie ushawishi wao wa kisiasa na kiuchumi wasaidie kumshawishi Kenyatta kukubali ombi la seriakli ya Israael viwanja vyao kutumika na ndege za kijeshi za Israel na makondo wake.

Baada ya mashinikizo haya kutoka kila upande, Mzee Kenyatta hakuwa na chaguo linguine zaidi ya kukubali ombi lao.


Bwana huyu McKenzie pia alikuwa na ndege yakebinafsi, na Ehud Barak akaona fursa. Walitumia ndege hii ya kiraia kuruka mpaka Uganda mijini Entebbe na kukatiza juu ya anga la uwanja wa ndege wa Entebbe na walipokuwa wanapita juu ya anga la uwanja wa ndege, Ehud Barak akatumia fursa hii kupiga picha kila eneo la uwanja. Kwa kuwa hii ilikuwa ni ndege ya kiraia, jeshi la Uganda hawakushughulika nayo.

Picha hizi zilizopigwa na Ehud Barak zilikuja kuwa na umuhimumkubwa katika maandalizi ya mwisho ya oparesheni ya makomando wa Isarel Kuvamia uwanja huu.


Mpaka kufikia hapa maandalizi yote muhimu yalikuwa yamekamilika.


WAKATI HUO HUO


Upande wa watekaji kule Uganda walikuwa wanasubria mifwedha yao dola milioni 5 za kimarekani.

Rais Idd Amin naye baada ya kufikia makubaliano na Israel kuwa masharti ya fedha na wafungwa wa kipalestina kuachiwa tarehe 4 July, naye ‘akarelax’ na akaona huo ndio muda wa kutekeleza majukumu Mengine akisubiria tarehe 4 July ifike.


Katika kipindi hiki Idd amin ndiye alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa kuzingatia utaratibu wa uenyekiti kuzunguka kwa kila nchi kwa mwaka mmoja mmoja na wiki hii alikuwa anatakiwa kwenye kikao cha Umoja wa Afrika kilichokuwa kinafanyika Mauritius. Kwa hiyo Amin akafunga safari kuelekea Mauritius kwenda kukabidhi kijiti cha Uenyekiti.


Ehud Barak aliposikia taarifa hii, kwa kutumia akili yake kubwa ya kuzaliwa aliyojaliwa na uzoefu wake wa ujasusi, aliona fursa adhimu kabisa hapa. Akawasiliana na walioko kikaoni huko Tel Aviv na kuwaeleza taarifa ambazo awali wote hawakuielewa.


Ehud Barak: “Idd Amin akiwa ndani ya Uganda huwa anatumia Mercedes Limousine katika msafara wake”


Waziri Mkuu Rabin: “Ok! Limefanyaje?’


Ehud Barak: “Nataka mtafute gari kama hiyo… Mercedes Limousine”


Waziri Mkuu Rabin: “la kazi gani?”


Ehud Barak: “siku ambayo kikosi cha makomando wakipanda kwenye ndege kutoka huko Israel kwenda Uganda, gari hilo nataka pia lipakiwe ndani ya ndge!”


Kwa dakika kadhaa wote ambao walikuwa wanamsikiliza pale kikaoni kupitia simu hakuna ambaye alielewa nini hasa Ehud Barak alikuwa anapendekeza.


Yalikuwa yamebaki masaa machache tu ambapo, weledi, ushujaa na uzalendo uliotukuka ulikuwa unaedna kudhihirika.


imeandikwa na THE BOLD kutoka jamiiforum

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog