Simulizi : Operation Gothic Serpent
Sehemu Ya Pili (2)
Kwa mfano, kikundi kingine cha waasi wa SNM walijiamulia kutangaza moja ya eneo la nchi ya Somalia kama nchi huru na kuibatiza jina jipya la Somaliland na kiongozi wao Abdirahman Ahmed Ali Tuur kuwa Rais wa nchi hiyo mpya. Mgogoro huu bado ungalipo mpaka leo hii wananchi wa eneo hilo wakitaka kutambulika eneo lao kama nchi huru.
Hata kikundi cha USC chenyewe nacho kiligawanyika baada ya makamanda wake wakuu Farah Aidid na Ali Mahdi Mohamed kutofautiana wakigombea madaraka na utawala wa mji wa Mogadishu.
Wapiganaji wa USC waliokuwa wanamuunga mkono Aidid na upande mwingine ambao walikuwa wanamuunga mkono Mahdi walianza kupigana wenyewe kwa wenyewe kugombea kutawala mji mkuu wa mogadishu.
Baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali, mwaka 1992 ilibidi Aidid na Mahdi wakubaliane kuugawanya mji wa Mogadishu katika pande mbili… kusinu na kaskazini. Ukawekwa mpaka katikati ambao hakuna upande ulikuwa unaruhusiwa kuvuka.
Nchi ya Somalia ilikuwa imefikia kuwa kiroja cha namna hiyo. Ikiwa imegawanyika vipande vipande. Kila ukoo ukitawala eneo fulani. Kwa maneno mengine nchi haikuwa na serikali wala jeshi la pamoja bali kila ukoo ulkkuwa na lwake.
Ndipo hapa ambapo mwaka 1992 Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa walipitisha resolution namba 733 kuunda UNOSOM I (United Nations Operation in Somali I) kwa lengo la kusaidia kupeleka misaada ya kiutu nchini Somalia.
Mwezi desemba tarehe 3 mwaka huo 1992 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walipitisha resolution nyingine namba 794 kuunda kikosi maalumu cha UNITAF (United Task Force) kwa ajili ya kulinda watoa huduma za kiutu na kulinda amani nchini Somalia.
Mwezi January mwaka 1993 vikosi hivi vya umoja wa mataifa kwa ajili ya kazi hii maalumu. Hakuna ambaye alikuwa na hofu au shaka juu ya utekelezaji wa oparesheni hii. Ilikuwa inategemewa kwenda sawia na murua kabisa na amani kurejea nchini Somalia.
Jambo moja la msingi ambalo hawakuliangalia au hawakuling'amua mwanzoni ni kwamba… hakuna weledi au ushujaa unaotosha kupambana na wananchi wenye hasira au imani. Na kama waswahili wasemavyo, "usiingile ugovi wa ndugu… wakipatana watakurarua wewe". Ndicho kinachofanana kabisa na aambacho kilikuwa kinaelekea kutokea nchini Somalia.
Ni kweli nchi ilikuwa imemegeka vipande vipande… na vita vilipiganwa hovyo baina ya ukoo na ukoo kugombea utawala wa maeneo. Lakini kitendo cha Umoja wa Mataifa kuingiza majeshi nchinu Somalia ilikuwa ni kana kwamba kuwapa koo hizo adui mmoja wa wote kupigana nae.
Lilikuwa ni suala la muda tu kabla ya vikosi vya Umoja wa Mataifa vikiongozwa na Marekani kugundua kosa kubwa ambalo walikuwa wamelifanya. Kosa ambalo lilikuja kupelekea kufanyika kwa moja oparesheni ya za kijeshi hatari zaidi kwenye historia… Operation Gothic Serpent. Operation ambayo imeacha vidonda kwa pande zote mbili… Marekani na Somalia. Na kuchangia Somalia kutotengamaa mpaka leo hii.
Tuwe pamoja kuichambua mpaka mwisho.
OPERATION GOTHIC SERPENT: NGUVU YA ITIKADI, IMANI NA USHUJAA ULIOTUKUKA
SEHEMU YA PILI
Somalia ilikuwa imegawanyika. Kulikuwa na vikundi vinne vyenye nguvu ambavyo vyote vilikuwa vinapambana kutaka kuongoza nchi. Kukikuwa na Somali Salvation Demecratic Front (SSDF), kulikuwa na Somali Patriotic Movement (SPM), Somali Democratic Movement (SDM) na Somali United Somali Congress ambayo ilikuwa imegawanyika pande mbili, upande unaomuunga mkono Ali Mahdi Muhammad na upande unaomuunga mkono Mohamed Farrah Aidid.
Vikundi vyote hivi vilikuwa vinapambana kutaka kuunda serikali na kutambulika kama ndio uongozi rasmi wa nchi ya Somalia.
Mapigano haya yaliibomoa nchi sana na kuifanya sekta ya kilimo nchini Somalia kuporomoka kabisa na hatimaye kupelekea uwepo wa njaa kali kwenye nchi.
Jamii ya kimataifa ilianza kufanya kampeni na mikakati ya kuingiza misaada ya kiutu nchini Somalia hasa hasa chakula. Lakini misafara hii ya misaada hasa ya chakula ilikuwa inatekwa na shehena kuchukiliwa na wapiganaji wa vikundi hivi ambao walikiwa wanaenda kubadilishana chakula hicho na silaha kwenye nchi za jirani. Ilifikia kipindi ambacho 80% ya vyakula vyote vya msaada vinavyoingizwa Somalia vilikuwa vinaporwa na wapiganaji wenye silaha.
Hii ilifanya tatizo la njaa nchini Somalia kuwa la ukubwa wa kutisha. Inakisiwa kwamba kwenye mwaka 1991 mpaka 1992 pekee jumla ya watu 300,000 walikufa njaa huku wengine milioni moja na nusu wakibaki kwenye hali mbaya ya uhitaji wa chakula.
Hii ndio ilikuwa sababu kuu ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kutuma vikosi vya kijeshi vya UNITAF (United Task Force) kwa ajili ya ulinzi wa misafara ya vyakula vya misaada, maghala na kuratibu shughuli nzima ya usambazaji wa vyakula hivyo nchi nzima.
Katika sehemu iliyopita nilieleza kwamba katibu mkuu wa umoja wa Mataifa wa kipindi hicho Bw. Boutros Boutros-Ghali alitoa mapendekezo kwa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kwamba UNITAF ipandishwe daraja na kuwa UNISOM (United Nations Operation in Somali) chini ya resolution namba 794 ili kuruhusu vikosi hivyo viratibu pia urejeshaji wa amani nchini Somalia na kupatikana kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Kwa hiyo mwanzoni mwa mwaka 1993 kama ambavyo nilieleza vikosi vya Umoja wa Mataifa viliwasili nchini Somalia vikiongozwa na Marekani.
Walipowasili mara moja tu kazi ilianza. Kwa mfano kwenye wiki mbili tu mwanzo baada ya kuwasili Vikosi vya Marines viliweza kuuweka kwenye himaya yao zaidi ya robo ya mji wa Mogadishu pamoja na Bandari, na kiwanja cha ndege.
Vikosi vingine viliweza kuifungua tena njia ya Mogadishu kwenda Baidoa na Kismayo.
Kwa haraka sana vikosi vya Umoja wa Mataifa taratibu walianza kudhihirisha uwezo wao wa kuituliza tena nchi ya Somalia na kudhibiti vikundi vya wapiganaji.
Ndipo hapa ambapo mwezi March mwaka huo 1993 ilibidi kuitishwa Kongamano kubwa la Kitaifa ambalo likifanyika Adis Ababa nchini Ethiopia na kukutanisha vikundi vyote vya wapiganaji vya nchini Somalia kwa lengo la kufanya usuluhishi na kuunda serikali ya pamoja.
Jumla ya vikundi kumi na tatu vilihudhuria. Masharti yakawekwa na hatimaye March 15 makubaliano ya pamoja yakafikiwa na wote kukubaliana kuunda serikali ya pamoja ya umoja wa kitaifa.
Lakini wakati michakato hiyo ikiendelea kwa kasi kuharakisha serikali hiyo ya kitaifa kuundwa, ilipofika mwezi May Mohammed Farrah Aidid alianza kuonyesha nyendo za kuashiria kwamba ana dhamira ya kuvunja makubaliano ya mwezi March ambayo kikundi chake kilihudhuria kwenye kongamano na yeye mwenyewe kutia saini makubaliano.
Aidid alianza kurusha matangazo kupitia Radio Mogadishu ambayo yalikuwa yanalenga kueneza propaganda na kuchochea wananchi kupinga uwepo wa vikosi vya UN nchini mwao.
Makamanda wakuu wa UNOSOM wakiongozwa na Luteni Jenerali Çevik Bir walitoa karipio kali kumtaka Aidid aache mara moja uenezaji wa propaganda hiyo kwa wananchi kupitia matangazo ya redio. Hofu yao ilikuwa ni kwamba sumu inaweza kuwaingia wananchi wa Somalia na hatimaye kuwageuzi kibao wanajeshi wa UN ndani ya Somalia.
Aidid hakuelegeza msimamo, aliendelea kurusha matangazo.
Safari hii kamanda Bir alitoa amri kwamba Radio Mogadishu ifungwe. Lakini Aidid aliweka msimamo kwamba redio hiyo itaendelea kuwepo na kurusha matangazo na kamwe haitofungwa.
Ubaya ni kwamba, katika makao makuu ya UNOSOM kulikuwa na wafanyakazi wa kiraia, raia wa Somalia. Mwanzoni U.N hawakulijua hili lakini kumbe Aidid alikuwa amepandikiza watu wake ambao walikuwa wanafanyakazi kama waajiriwa wengine hapo makao makuu. Kwa hiyo taarifa nyingi na mipango mingi ya UNOSOM Aidid alikuwa anaijua hata kabka haijaanza kutekelezwa.
Baada amari ya kufungwa kwa kituo cha redio cha Radio Mogadishu kupuuzwa, kuna taarifa zilimfikia kamanda wa UNOSOM Luteni Jenerali Çevik Bir kwamba pia kwenye majengo ya redio hiyo kuna vyumba vinatumiwa na Aidid kuhifadhi kiwango kikubwa sana cha silaha.
Jenerali Bir aliamua kutuma kikosi cha wanajeshi kutoka Pakistan ambao walikuwa sehemu ya UNOSOM kwenda kufanya ukaguzi kwenye kituo hicho cha redio ili kujua kama intelijensia waliyoipata ilikuwa ni sahihi na ina ukweli wowote. Kama kweli silaha zilikuwepo kwenye majengo ya kituo hicho cha redio basi hii ilikiwa ni sababu nzuri kwao kuitumia kukifunga kituo hicho cha redio kwa lazima.
Kikosi cha wanajeshi wa Pakistan ambao walikuwa ni waliwasili kwenye majengo ya kituo cha Radio Mogadishu. Hii ilikiwa ni siku ya June 5 mwaka 1993 majira ya asubuhi kama saa nne hivi.
Taarifa hii ya wanajeshi wa UNOSOM kuwasili kwenye majengo ya Radio Mogadishu zilimfikia Aidid. Lakini hazikumfikia kwa usahihi. Watu wake walimpasha habari Aidid kwamba kikosi hicho cha wanajeshi kimeenda pale Radio Mogadishu kukifungia kituo hicho wakati uhalisia ni kwamba wanajeshi wale walifika pale kukagua uwezekano wa uwepo wa silaha kama amabavyo walikuwa wamepata taarifa za intelijensia.
Aidid akaamuru wapiganaje wake wafanye shambulio la kushtukiza kwa wanajeshi wale wa UNOSOM walioko kwenye majengo ya Radio Mogadishu.
Shambulio hili la wapiganaji wa Mohammed Farrah Aidid lilisababisha vifo vya wanajeshi 24 wa pakistan huku wengine 57 wakijeruhiwa vibaya na pia mwanajeshi mwingine mmoja wa nchi ya Italia naye kujeruhiwa vibaya na wanajeshi wengine watatu wa Marekani.
Hili lilikuwa ni pigo kubwa ambalo liliushitua ulimwengu. Aidid alikuwa amevuka mpaka safari hii. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa vikundi hivi vya wapiganaji wa Kisomali kushambulia moja kwa moja wanajeshi wa U.N na kuwaua. Ulimwengu mzima ulikuja juu kwa hasira.
Kesho yake, tarehe 6 June 1993 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walipitisha resolution namba 837 wakitaka kukamatwa na kushtakiwa kwa Mohammed Farrah Aidid kwa kosa la kupanga na kutekeleza shambulio dhidi ya walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Mara moja kampeni za kijeshi zikaanza kumsaka Aidid ndani ya jiji la Mogadishu. Mikakati hii ilianza siku ya June 12, 1993 na zilifanywa oparesheni mfulululizo kwa siku nne mpaka tarehe 16 June lakini waliambulia patupu. Aidid aliwa hajulikani alipo.
Siku ya June 17, Admiral Jonathan Howe alitangaza zawadi ya dola 25,000 za Kimarekani kwa mtu atakayesaidia kutoa taarifa itakayopelekea kupatukana kwa Mohammed Farrah Aidid.
Lakini hii nayo haikufua dafu… Aidid hakupatikana.
Mohammed Farrah Aidid
Siku ya tarehe 19 June 1993 wakiwa kwenye harakati hizi za kumsaka Aidid, vikosi vya jeshi la Marekani sehemu ya UNOSOM walifanya kosa kubwa sana ambalo naamini mpaka leo hii linajutiwa na Wamarekani. Kosa ambalo liliamsha hasira za Wasomali. Kosa ambalo lilipelekea kuanzishwa kwa Opaleration Gothic Serpent. Oparesheni iliyosababisha kumwagika damu nyingi ambayo haikuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa nyuma.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment