Search This Blog

Saturday, 24 December 2022

OPERATION GOTHIC SERPENT - 5

   http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/operation-gothic-serpent.html

Simulizi :  Operation Gothic Serpent

Sehemu Ya Tano (5)


Chopa ya Super 64 ambayo ilikuwa imeenda kusaidia makomando waliokuwemo kwenye Super 61 nayo ilikuwa imeshambuliwa kwa bomu la RPG.


Kile kitendo cha Super 64 kujipigiza chini katika uelekeo sahihi (matairi chini) ndicho ambacho kilisaidia kuwafanya wote kuwa hai baada ya chopa kujipigiza chini ardhini. Japo kuwa walikuwa hai lakini walikuwa wamejuruhiwa vibaya sana.

Rubani Mike Durant alikuwa amevunjika mbavu kadhaa huku nyama ya paja la kulia ikiwa imechanika. Kabisa.Rubani wake msaidizi, Ray Frank naye alikuwa na majeraha kama yake. Wenzao wawili ambao walikuwa kwenye siti za nyuma walikuwa na hali mbaya zaidi kushinda wao kutokana na siti za nyuma kuundwa tofauti na siti za marubani.




Zilipita karibia dakika kumi wote wakiwa hawana ufahamu… Durant hatimaye alipopata ufahamu na kuamka na kuanza kuwaza sawaswa alishuhudia namna ambavyo wenzao walioko kwenye siti za nyuma walikuwa wametapakaa damu na wakiwa kwenye hali mbaya japo walikuwa hai, msaidizi wake Ray Frank alikuwa amejikongoja na kujivuta mpaka nje ya chopa akiwa ametapaa damu lakini akiwa amekaa kwenye mkao wa kuwa tayari kumfyatulia risasi adui yeyote Yule ambaye angethubutu kusogelea eneo hilo.


Taarifa tayari ilikuwa imetumwa kwamba Super 64 nayo imedunguliwa na imedondoka… ubaya ni kwamba nguvu kubwa na akili yote ilikuwa imeelekezwa kufanya uokozi kwenye chopa ya kwanza ambayo ilikuwa imedondoka, yaani Super 61. Kwa hiyo ingechukua muda mrefu kiasi mpaka wenzao kujipanga upya ili kufika hapa ambapo chopa hii nayo imedondoka.


Lakini kwa upande wa wasomali hii ilikuwa ni kama sherehe kwao. Walijua fika kwamba kitendo cha chopa mbili kudondoka lazima ingewabidi makomando wa marekani kujigawanya mara mbili ili kuweza kutoa msaada kwa sehemu zote mbili na hii maana yake ufanisi wao makomando wa Marekani usingekuwa mkubwa sana nah ii ilikuwa ni faida kwao.


Vijana wa kisomali walio na silaha za moto, wenye mapanga, majembe, mundu, akina mama na mpaka watoto, kama vile tai wakisikia harufu ya mzoga mahala… walimiminika kwa makundi ya mamia ya watu wakikimbia kuelekea Super 64 ilikodondoka. Hii ilikuwa ni siku ya sherehe na siku ya msiba… siku ya kupimana misuli kati ya imani na itikadi dhidi ya misuli ya weledi na ushajaa.


Itaendelea…


Habibu B. Anga ‘The Bold”

To Infinity and Beyond



FINALE



Kwa muda wa siku kumi na moja Mohammed Farrah Aidid aliendelea kumshikilia rubani wa Super 64 Michael durant. Kwa siku zote hizi Farrah Aidid alikuwa akitoa matakwa yake juu ya vitu ambavyo alikuwa anataka vifanyike ili amuachie Michael Durant. Na sharti lake kuu alikuwa anataka vikosi vya UNOSOM wakiongozwa na Marekani kuondoka Somalia.

Lakini pia Adid alisambaza video za propaganda zikimuonyesha Michael Durant akiongea kupinga uwepo wa Wanajeshi wanzake wa Marekani juu ya uwepo wao ndani ya Somalia. Ni dhahiri kabisa kwamba Michael Durant alikuwa analazimishwa kusema kile ambacho alikuwa anakiongea.


Mpaka leo hii kuna utata mkubwa ya ni namna gani hasa Marekani waliweza kumshawishi Aidid kumuachia Michael Durant.

Ziko ripoti ambazo zinaeleza kwamba Marekani walilipa kiasi cha dola Milioni 10 ili kuachiwa kwa Michael Durant na mjadala juu ya malipo haya unazua nadharia juu ya kushamiri kwa uharamia katika pwani ya bahari ya hindi na hasa hasa kwenye pembe ya Afrika (tukipata nafasi tutajadili zaidi suala hili).


Mohammed Farrah Aidid alimuachia Michael Durant kwa shirika la misaada la msalaba mwekundu baada ya siku kumi na moja za kumshikilia. Baada ya Michael Durant kupatikana tu haraka alichukuliwa na jeshi na kusafirishwa kwenda nchini Ujerumani kwenye kituo cha tiba za kijeshi cha Landstuhl Regional Medical Center ambako alikaa kwa wiki kadhaa akitibiwa na kufanyiwa upasuaji kurekebisha paja na sehemu ya uti wa mgongo ambazo alivunjika kwenye ajali ya chopa ya Super 64.


Nilieleza kwamba miili ya wanajeshi wa Marekani ambao ilikuwa imechukuliwa kutoka kwenye chopa zilizodondoka, yaani Super 61 na Super 64 ilichukuliwa na wananchi na kuburuzwa barabarani na kudhalilishwa mno.

Wiki moja baadae jeshi la Marekani waliwabana viongozi wa koo za kisomali wakitaka miili ya wanajeshi wao irejeshwe. Ulikuwa ni mzozo mkubwa kweli kweli mpaka kufikia hatua ya Marekani kutishia kuingiza majeshi zaidi nchini Somalia ndipo ambapo viongozi wa koo za kisomali wakafanya juhudi za kusaka miili hiyo mpaka kupatikana na yote kurejeshwa kwa jeshi la Marekani. Miili ilikuwa katika hali mbaya kabisa na mengine ikiwa haina vichwa.


Mapigano haya ambayo nimeyaeleza kwenye makala hii ambayo kwenye vitabu vya historia yameandikwa kama "Vita ya Mogadishu" ni moja ya vipigo vya aibu kabisa na maumivu makali ambayo jeshi la Marekani limewahi kupata.

Kutokana na maumivu haya ba aibu hii, waziri wa ulinzi wa Marekani wa kipindi hicho Les Aspin alilazimika kujiuzuru na kuchukua lawama zote kutokana na kufeli kwa aibu kwa opareshenu hiyo. Moja ya masuala ambayo Waziri Aspen analaumiwa sana ni kitendo cha kukataa kuidhinisha kutumika kwa vifaru na magari ya silaha nzito na katika mapigano hayo.



Siku ya octoba 6 1993, Rais Bill Clinton aliitisha kikao kikao cha tathimini katika Ikulu ya Marekani ambapo kupitia kikao hicho alimuagiza Mwenyekiti wa kamati ya Majemedari (Chairman of the Joint Chiefs of Staff) Jemedari David E. Jeremiah kuagiza vikosi vya jeshi la Marekani vilivyopo nchini Somalia kujiondoa katika mapambano yoyote yale dhidi ya wapiganaji wa Aidid isipokuwa tu kama ni kwa ajili ya kujilinda.


Kuanzia Tarehe 31 March 1993 majeshi ya Marekani yalianza kuondoka nchini Somalia. Vikosi kadhaa vya Marines vilibakia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba raia wa kawaida wa Marekani walioko ndani ya Somalia wanaondoka wakiwa salama.


Kujitoa huku kwa Marekani kulileta mpasuko mkubwa katika diplomasia za kimataifa kutokana na mataifa mengi kutounga mkono kujitoa kwao ghafla hivyo. Tukumbuke kwamba vikosi vya Marekani vilikuwa ni sehemu ya vikosi vya umoja wa mataifa vya UNOSOM kwa ajili ya kusaidia usambazaji wa misaada ya kiutu nchini humo.

Nchi ya Somalia ilikuwa bado haijatulia, mapigano ya kikabila yalikuwa yameshika kasi na Aidid alikuwa amejilimbikizia madaraka makubwa sana. Kwa hiyo kujitoa kwa Marekani katika misheni hiyo bila kukamilika kwake ulikuwa ni usaliti mkubwa kwa jumuiya ya kimataifa.

Lakini vyombo vya habari vya Marekani vilikuwa vimeikalia kooni serikali ya Rais Bill Clinton. Picha za maiti za wanajeshi wa Marekani zikiburuzwa na kupigwa mawe kwenye mitaa ya Mogadishu zilionyeshwa kwenye televisheni. Wananchi walijawa na hasira. Na katika Bunge, wawakilishi wa chama cha Republicans walishupaa kweli kweli kwamba wanataka jeshi lao liondolewe nchini Somalia, hawawezi kuvumilia kuona jeshi likidhalilika namna hiyo. Hii ndio ilikuwa presha iliyomfanya rais Bill Clinton kuagiza vikosi vya Marekani virudi nyumbani.



Jinamizi hili la kudhalilika nchini Somalia ndilo ambalo Marekani walitumia kujitetea kwa kushindwa kwao kuingilia kuzuia mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.



Vita ya Mogadishu na Operation Gothic Serpent kwa ujumla inabakia kama moja ya misheni za machungu zaidi kuwahi kushuhudiwa na jeshi la Marekani. Ubaya zaidi kuna masuala mengi sana ambayo yalipata mwanya masuala mengine makubwa nyuma ya pazia. Kama amabavyo nimesema kwamba tukipata wasaa unaofaa tutajadili namna ambavyo uharamia katika pembe ya Afrika ulipata mwanya wa kushamiri baada ya kipindi hiki.


Lakini suala lingine ambalo kwa kipindi kile halikutiliwa maanani sana ni Osama Bin Laden. Kwa kipindi kile Marekani walikuwa wanajua juu ya uwepo wa Al-qaida na Osama Bin Laden lakini hakikuwa kitu ambacho wanakitilia maanani sana kwa kuwa hawakuwahi kutekeleza misheni yoyote kubwa ya kuigharimu nchi ya Marekani. Jambo ambalo hawakulifahamu kipindi kile ni kwamba, nyuma ya pazia ya umahiri wa wapiganaji wa Mohammed Farrah Aidid alikuwa ni Osama Bin Laden.

Kama umesoma kwa makini makala yangu ya "Behind The Curtain" utakumbuka kwamba katika kipindi hiki ndipo ambapo Osama Bin Laden alikuwa amejificha ndani ya nchi ya Somalia. Ni vijana wa Osama Bin Laden wakiongozwa na Mohamed Atef ambao walihusika kuwapa mafunzo mapiganaji wa Mohammed Farrah Aidid. Katika kitabu changu ambacho kitatoka siku si nyingi, nimejadili pia namna ambavyo kuna kijana wa Kitanzania kutoka Zanzibar ambaye alikuja kuigharimu sana nchi yetu na ulimwengu (tuhifadhi jina kwa sasa (sio Mohammed Ghailani)) alivyosafiri mpaka Somalia kwa mualiko wa Mohammed Atef kwa niaba ya Osama Bin Laden na kupata mafunzo pamoja na vijana wa Mohammed Farrah Aidid.


Lakini pia ni Al-Qaida ambao waliwezesha kudungua chopa zile mbili za Black Hawk na kuwatia wazimu Wamarekani.


Masuala haya (Al-Qaida kumsaidia Aidid) yalithibitishwa pia na Osama Bin Laden mwenyewe alipofanya mahojiano na John Miller wa kituo cha habari cha ABC cha nchini Marekani mwaka 1998 katika eneo lisilojulikana. Katika mahojiano yale ukimsikiliza Osama namna ambavyo anawakashifu wanajeshi wa Marekani kama 'cowards', unawez kuelewa ni kwa namna gani kukimbia kwa vikosi vya Marekani nchini Somalia kulitumiwa na watu kama Osama kipropaganda kuwatia moyo vijana wake wasiogope jeshi la Marekani.


Kuna mengi ya kujifunza kijeshi, kiitikadi na hata kiimani na pengine kuchochea ushujaa kutoka kwenye kisa hiki cha Vita ya Mogadishu na Operation Gothic Serpent. Licha ya vikosi vya Marekani kuwa na silaha za kisasa zaidi na weledi zaidi wa kijeshi, lakini vijana wenye mori ya itikadi na imani wakiwa na mapanga na mundu tu mikononi waliweza kuwatoa jasho na mpaka kusalimu amri. Ni mara chache sana katika maisha ambapo tunapata kukumbushwa na kushuhudia kwa macho yetu namna nguvu hii ya itikadi na imani lakini pia hatupaswi kubeza ushujaa uliotukuka ulioonyeshwa na makomando wa Marekani.



MWISHO



Makala mpya inakuja wiki hii…


Ramadhan Kareem


0 comments:

Post a Comment

Blog