Simulizi : Cosa Nostra
Sehemu Ya Kwanza (1)
COSA NOSTRA: SEHEMU YA I
Kwa miaka mingi sasa kumekuwepo na hadithi nyingi sana kuhusu Kundi maarufu la uhalifu la Mafia.
Hadithi hizi zimewafanya wengi kutamani kufahamu umahiri, mbinu na usiri unaotawala katika ulimwengu wa kundi hili maarufu la uhalifu la Mafia au 'Cosa Nostra' kama wenyewe wanavyojiita.
Tofauti na watu wengi wanavyodhani kuwa Mafia ni kikundi Fulani cha uhalifu, hii sio sahihi.
Mafia sio 'kikundi' cha uhalifu bali ni mkusanyiko wa vikundi vingi vya uhalifu vinavyo julikana kiitaliano kama "cosca". Vikundi ambavyo kiuhalisia ni koo (familia) kila kimoja kinakuwa na eneo lake la kufanyia shughuli zake ambalo wenyewe wanaliita "Borgata".
Vikundi hivi vyote kwa pamoja vinakuwa chini ya Mwamvuli mmoja ambao wenyewe wanauita "Cosa Nostra" kwa kiitaliano ambayo inamaanisha "Kitu Chetu" (Our thing).
Neno lenyewe Mafia lina maana ya "Ujasiri na Uzuri" (boldness, bravado).
KUANZISHWA KWA MAFIA.
Kwa karne nyingi katika jimbo la Sicily nchini Italia, kiasi kikubwa cha ardhi kilimilikiwa na watu wachache ambao walikuwa ni wakulima wakubwa.
Mwaka 1860 Sicily ikatengwa kutoka Italia na kuwa jimbo linalojitegemea.
Hii ikapelekea mamlaka za jimbo la Sicily kuchukua kutoka wakulima wote wenye ardhi kubwa na kuigawa kwa wananchi.
Lakini mamlaka za mji wa Sicily ikaamuru kuwa kila mwananchi ambaye atapewa ardhi atatakiwa kulipa "kipande" kidogo kwa mmliki wa ardhi ambaye ardhi yake ilichukuliwa na serikali na kugaiwa kwake. Kipande hiki kilitakiwa kulipwa kila mwaka kutoka kwa mkulima mdogo kwenda kwa mkulima mkubwa aliyepokonywa ardhi na serikali.
Hatua hii ilikuwa na faida pamoja na changamoto. Faida yake ilikuwa ni kwamba wakulima wengi sasa walikuwa na ardhi ya kulima.
Lakini hasara yake ilikuwa ni kwamba ilianza kupandikiza hisia kwa wananchi kuwa wakulima wakubwa wanawanyonya na kuwaonea.
Wakulima wengi wakaanza kukaidi agizo la kuwalipa kipande cha kila mwaka wakulima wakubwa na baadhi yao wakaanza kuvamia makazi ya wakulima wakubwa na kuiba.
Katika kipindi hiki jimbo la Sicily lilikuwa na changamoyo kubwa ya kutokuwa na Polisi wa kutosha.
Jimbo zima lilikuwa na askari 350 pekee.
Hii ilifanya kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu kuwa ngumu na hii ikasababisha uhalifu kuongezeka kila siku.
Ndipo hapa wakajitokeza wahalifu ambao walijiunga katika vikundi na kutoa huduma ya kuwalinda kwa malipo ya fedha matajiri na kufuatilia madeni yao kwa wakulima wadogo.
Vikundi hivi viliundwa na wahalifu wenye weledi ambao wao walitoa huduma kwa matajiri kuwatafuta watu waliwaio waibia mali zao na hata wale ambao hawataki kulipa vipande kwa ajili ya ardhi waliyopewa.
Kutokana na ufanisi wa vikundi hivi, mamlaka za kisheria pia zikaanza kuvutiwa na huduma zao.
Kama nilivyosema awali kuwa katika kipindi hiki mji wa Sicily ulikuwa na upungufu mkubwa wa polisi. Lakini si hivyo yu bali pia ufanisi wa vikundi hivi ulikuwa ni mkubwa kuliko polisi kutokana na uwezo wao wa kuwakamata wahalifu au kurejesha vitu vilivyoibiwa.
Baada ya vikundi hivo kuanza kutengeneza faida kubwa, baada ya kugunduliwa kwa malighafi ya Sulphur katika mji wa Sicily, wahalifu wakubwa wakaanza kutengeneza vikundi ndani ya faimilia/koo zao.
Hii ilikuwa ni miaka ya 1900.
Kugunduliwa kwa malighafi ya Sulphur katika jimbo la Sicily kulimaanisha kuwa vipato vya watu viliongezeka kutokana na shughuli za uchimbajo malighafi hii, hii ilimaanisha kuwa pia uhitaji wa kujilinda na kulinda mali uliongezeka pia. Hii maana yake kuwa huduma za ulinzi wa Mali na mtu zinazotolewa na familia hizi za kihalifu uhitaji wake ukaongezeka maradufu.
Baada ya shughuli za familia hizi za kihalifu kuongezeka maradufu, ukaonekana umuhimu wa kufanya kikao cha pamoja ili familia hizo zote zikubaliane namna ya utendaji kazi wake na maeneo ya utendaji kazi ili kuepusha kujikuta wanaingia kwenye malumbano au vita ya kugombea maeneo ya kufanyia shughuli.
Ni katika kikao ambapo wakakubaliana kuweka mfumo wa ufanyaji kazi unaofanana kwa familia zote, na wakaweka Sheria ambazo wenyewe waliziita "umirta".
Sheria hizi zilihusu usiri (kutunza siri za shughuli zao), kujitenga/kutoshirikiana na polisi, alama (signal) za siri za kutambuana na kujitenga na jamii ya kawaida (kutochangamana).
Ni katika kikao hiki ambapo viongozi wa kila familia wakaanza kuitwa "Don" (Sir). Na ni katika kikao hiki ambapo umoja wao huu wa familia zao ukaanza kuitwa "Mafiosi" (Mafia) wenyewe wakiwa na maana ya "Men of honour" (Watu wa Heshima).
Baada ya kutengeneza mtandao huu, na kugawana maeneo ya kufanyia kazi ndani ya jimbo la Sicily, ndipo hapa ambapo shughuli za Mafia zikaanza kubadilika kutoka katika kuzuia uhalifu na badala yao wao wenyewe wakageuka wahalifu, tena wahalifu wa daraja la kwanza.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment