Simulizi : Cosa Nostra
Sehemu Ya Tano (5)
Don Riina alienda mbali zaidi mpaka kufikia hatua ya kupanga mauaji ya mabosi wa familia zilizokuwa zimekataa kujiunga na umoja wa Carleonesi.
Hapa ndipo vita kuu ya pili ilipoanzia.
Wanachama wa familia nyingine nao wakaanzisha oparesheni za kulipa kisasi kwa kuuwa wanachama wa familia zilizojiunga katika umoja wa Carleonesi.
Lakini Don Riina alikuwa na mbinu adhimu za kihalifu. Alichokifanya ilikuwa ni kuwahonga baadhi ya wanachama wa familia pinzani ili kuwaua wenzao wanaoendeleza vita dhidi ya umoja wa Carleonesi.
Hadi kufikia mwaka 1978, Don Riina alifanikiwa kuiweka kiganjani Tume ya Mafia kwa kuingiza mabosi wa familia za umoja wa Carleonesi pekee na yeye mwenyewe akijipa cheo cha uongozi wa Tume ya Mafia.
Ndipo hapa alipopachikwa jina la "Boss of Bosses".
Baada ya mafanikio haya Don Riina akavimba kichwa zaidi.
Don Riina akaanzisha vita na waandishi wa habari walioiandika Mafia vibaya, akaanzisha vita na mauaji ya Polisi ambao waliendesha oparesheni zilizokuwa kinyume na mafia.
Don Riina akaenda mbali zaidi akaaendesha utekaji na mauaji ya viongozi wa serikali ambao walikuwa wanaipinga Mafia.
Mauaji haya yalikuwa ni mengi katika miaka ya 1980 kiasi kwamba ikaamsha hasira za wananchi.
Kwa miaka yote wananchi walikuwa wamejiweka kando (neutral) katika ugomvi wa serikali na Mafia.
Lakini kutokana na mauaji yaliyokuwa yanaendelea ikawafanya wananchi waanze kuipinga Mafia wazi wazi na kuanzisha harakati za kuishinikiza serikali kuitokomeza Mafia nchini Italia.
Mwaka 1988 serikali ikaanzisha rasmi oparesheni ya kuwasaka mabosi wa familia za Mafia.
Mwaka 1993 wakafanikiwa kumkamata Don Riina na kumtupa gerezanj.
Kitendo hiki kilikuwa kama kimewawehusha wanachama wa Mafia kwani wakaanza kutekeleza matukio ya kigaidi kitu ambacho hakikuwahi kushudiwa kikifanywa na Mafia hapo kabla.
Wanachama wa mafia wakaanzisha matukio ya kulipua majengo ya serikali, vituo vya mabasi, mahoteli na sehemu za utalii. Lengo lao kubwa lilikuwa ni kuishinikiza serikali kumuachia Don Riina.
Serikali ikasimama imara na kukataa kata kata kumuachia Don Riina.
Ndipo hapo ilipobidi Don Leoluca Bagarella arithishwe uongozi mwaka huo 1993.
Lakini Don Bagarella akafanya makosa ya kuendeleza staili ile ile ya uongozi ya Don Riina. Kuiandama serikali, waandishi wa habari na kuuwa wanachama wa familia nyingine ambazo hazipo kwenye umoja wa Carlonesi.
Hii ikisababisha Don Bagarella kutodumu sana kwenye uongozi kwani miaka miwili baadae yaani 1995 alikamatwa na serikali ya Italia na kutupwa gerezani.
Hii ikatoa fursa kwa uongozi mpya kushika hatamu, ambapo Don Bernardo Provenzano akachukua madaraka ya uongozi wa familia za Mafia.
Mara baada ya Don Provenzano kuchukua madaraka akajiapiza kuirudisha Mafia katika misingi yake ya weledi, ufanisi na kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe (Loyalty).
KUREJEA TENA KWA MAFIA KATIKA "UTUKUFU" WAKE.
Don Provenzeno kwanza kabisa akapiga marufuku kwa wanachama wa Mafia kufanya mauaji ya viongozi wa serikali, waandishi wa habari na polisi.
Pia akapiga marufuku wanachama wa Mafia kuuwa mashahadi wa kesi za serikali dhidi ya Mafia na kama mbadala alianzisha utaratibu wa kuwahonga mashahidi na kuwatorosha wakaanze maisha sehemu nyingine.
Pia akamaliza kwa kusuluhisha vita zote za kifamilia katika mtandao wa Mafia na kuwasisitiza wao wote wako kwenye timu moja, kwamba ni wote ni ndugu chini ya mtandao wa Mafia.
Baada ya miaka kadhaa Mafia ikatulia na kurudi katika weledi na ufanisi wake.
Kuna tuhuma ambazo hazijathibitishwa zinazoeleza kwamba Don Provenzena aliwasiliana na Bw. Silvio Berlasconi ambaye alikuwa katika harakati za kuanzisha chama chake cha Ferzo Italia ili aweze kugombea Uwaziri Mkuu wa Italia.
Inasemekana kwamba Don Provenzeni alimpa ofa Berlasconi kuwa watamsaidia ashinde katika jimbo la Sicily na maeneo mengine ya nchi ambayo wanaushawishi.
Ombi lao kwao ni kwamba akiingia madarakani alegeze sheria zinazopinga Mtandao wa Mafia (anti-Mafia law) hasa hasa kipengele maarufu kinachojulikana kama "article 41-bis".
Shutuma hizi zimepingwa vikali na Silvio Berlosconi mwenyewe na chama chake lakini baadae Berlosconi alishinda uwaziri Mkuu akipita kwa kishindo katika jimbo la Sicily.
Pia mwaka 2002 kifungu cha sheria cha "article 41-bis" kiliacha kutumiaka, kitendo ambacho kilizua maswali mengi.
Don Provenzeno hakuishia hapo tu kudhihirisha kuwa japokuwa watangulizi wake walipenda utengano yeye anapendelea zaidi ushirikiano.
Ndipo hapa ambapo aliwasiliana na nguli wa mihadarati kutoka Mexico Bw. Joaquin Guzman au maarufu kama "El Chapo" na wakaanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya mtandao wa Mafia na genge la Sinaloa Cartel linalomilikiwa na El Chapo.
Pia Don alianzisha utaratibu maalumu wa kuwafanya wahalifu wa Mafia wawe wa kipekee.
Utaratibu huu aliuita "Pax Mafiosa" (Mafia Quietness (ukimya wa Mafia)).
Chini ya utaratibu huu aliamuru kwanza wanachama wote wa Mafia kuacha kujigamba na kujitanabaisha katika jamii. Aliamuru wanachama wa Mafia kuishi kama mashushushu bila watu kuwafahamu na shughuli zao ziendeshwe kimya kimya na kwa usiri mkubwa.
Chini ya Don Provenzena Mafia ikarudi katika "ubora" wake.
Ingawa Don Provenzena alikamatwa na kutupwa gerezani mwaka 2006, lakini bado alama yake ya kiuongozi (legacy) inaendelea kuiongoza Mafia mpaka leo hii chini ya Don Messina Denaro ambaye ndiye kiongozi wa sasa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment