Search This Blog

Tuesday, 20 December 2022

D.B. COOPER TUKIO HALISI LA KUSISIMUA LILILOGEUKA HADITHI YA 'ALFU LELA ULELA' - 1

 


http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/db-cooper-tukio-halisi-la-kusisimua_10.html

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi :  D.b. Cooper Tukio Halisi La Kusisimua  Lililogeuka Hadithi Ya 'alfu Lela Ulela'

Sehemu Ya Kwanza (1)



KIDOKEZO MUHIMU..


Kwa wale wapenzi wa tamthilia ya Prison Break watakuwa wanakumbuka katika msimu wa kwanza wa tamthilia kipindi muhusika mkuu wa tamthilia Michael Scofield akijaribu kuwashawishi wafungwa kadhaa aliowachagua wamuunge mkono kwenye mpango wake kabambe wa kutoroka kutoka katika gereza la Fox River, kulikuwa na mzee wa makamo aliyeitwa Charles Westmoreland ambaye alimpa changamoto kubwa kukubalia kujiunga na mpango huu.


Watu ambao Micheal aliwachagua kila mmoja alimteua kwa sababu maalumu kutokana na umuhimu fulani alionao ambao utahitajika katika kufanikisha tukio la kutoroka. Mfano alimchagua cell mate wake Fernando Sucre ili aje kuwasaidia katika mpango wa kuingia nchi ya Mexico kiurahisi baada ya kutoroka, alimchagua John Abruzzi ili aje kusaidia kupata usafiri wa ndege watokomee pindi tu wakitoroka Fox River, na wengineo wote waliojumuishwa kwenye mpango huo walikuwa na umuhimu maalum.


Kujumuishwa kwa Charles Westmoreland kwenye mpango huo ni kutokana na Michael kung'amua mapema kwamba watahitaji fedha za kujikimu mara tu wakifanikiwa kutoroka na hatimaye kuingia nchini Mexico.


Swali je, fedha wanapata wapi? Ndipo hapo anapoingia Charles Westmoreland, ambaye licha ya kutumia jina hili la Charles Westmoreland, Michael Scofield aliamini kuwa huyu mzee ni D.B Cooper jambazi aliyefanikiwa kuiteka ndege na serikali kukubali kulipa dola milioni moja ili aiachie, jambazi ambaye mpaka mda huo alikuwa bado anatafutwa na FBI, jambazi pekee aliyefanikiwa kuweka historia katika nchi ya marekani kufanya tukio la utekaji ndege kwa mafanikio na kesi kushindwa kuwa kuwa solved na FBI kwa miaka 45! Licha ya Charles Westmoreland kukataa katakata kuwa yeye siye D.B Cooper lakini Michael aliamini yeye ndiye na fedha alizofanikiwa kulipwa na serikali bado hajazitumia ziko mahali fulani amezificha..


Baada ya majaribio kadhaa ya kumshawishi kushindikana, mwishoni kabisa Charles anakubali kuungana katika mpango wa kutoroka baada ya kugundua kuwa hatopewa fursa ya kumuona binti yake aliyekuwa anaumwa na ana karibia kufa, na kuthibitisha hilo anamuonyesha Michael noti ya fedha ya marekani yenye serial number D 1192589 ambayo ni moja ya noti katika fedha alizolipwa na serikali ili aweze kuiachia ndege aliyoiteka na baadae kabisa anakiri kwa Michael kuwa hakulipwa dola milioni moja kama inavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari bali alilipwa dola milioni tano.


Katika msimu wa pili wa tamthilia sehemu kubwa inahusu jinsi wafungwa waliofanikiwa kutoroka (Michael, Burrows, T-bag, Sucre e.t.c) wanavyofanya juhudi ili wazipate November Charles Westmoreland (D.B Cooper) katika eneo la Utah.!


TUKIO LA KWELI KATIKA MAISHA HALISI.


Siku ya November 24 mwaka 1971, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji wa Portland jamaa aliyevaa suti nyeusi na koti refu jeusi kwa juu akiwa amebeba brief case nyeusi alifika katika counter ya kampuni ya ndege ya Northwest Orient Airlines na akatoa fedha cash dola 20 kununua tiketi ya ndege Flight 305 kwenda mjini Seattle, ambayo kwa kawaida ni safari inayochukua dakika 30. Jamaa huyu alijitambulisha kama 'Dan Cooper'.


Baada ya kuingia kwenye ndege akakaa kwenye siti namba 18C, baadae akakaa siti namba 18E na baadae 15D.


Ilipofika mida ya saa nane na dakika hamsini mchana ndege ikaruka na baada ya ndege kuruka Mr. Cooper akawasha sigara na akaagiza soda!


Siti ambayo alikaa Cooper ilikuwa siti ya nyuma kabisa na alikaa karibu kabisa na siti ya muhudumu wa ndege wa kike aliyeitwa Florence Schaffner.

Baada ya dakika chache Cooper alitoa kikaratasi mfukoni kilichochapwa kwa unadhifu na maandishi yakiwa yameandikwa kwa herufi kubwa na kisha akampatia Bi. Schaffner kikaratasi hicho.


Baada ya Bi. Schaffner kupokea kikaratasi, kutokana na mazoea akajua ni kawaida tu abiria alikuwa ametokea kumtamani na hivyo amempa namba ya simu, kwa hiyo Bi. Schaffner hakukisoma kikaratasi bali alikiweka moja kwa moja kwenye mkoba. Mara baada ya kukiweka kikaratasi kwenye mkoba, Cooper akainama kidogo na kumnong'oneza Bi. Schaffner na kumwambia "Miss you would better take a look at that note. I have a bomb" (Bibie ni vyema ungekisoma hicho kikaratasi. Nina bomu).


Baada ya kumueleza hivyo kimya kimya akamuamuru muhudumu huyo akae karibu nae na kuanza kumpa maagizo. Lakini kabla ya hapo yule mhudumu akataka ampe uhakika kama kweli ana bomu. Cooper akachukua briefcase yake na kuifungua kidogo tu ili muhudumu aangalie na alipoangalia ndani ya briefcase akaona cylinders nane, nne zikiwa chini na nne zikiwa juu zikiwa zimeunganishwa kwa nyaya nyekundu ambazo nazo zinaenda kuunganika kwenye battery yenye rangi nyekundu pia ikiyopo pembezoni mwa briefcase. Baada ya kuchungulia muhudumu akaamini kweli Cooper alikuwa na Bomu.


Cooper akampa maagizo muhudumu akaongee na marubani kwa kupitia intercom kuwa wawasiliane na uwanja wa ndege wa Seattle na wawaeleze juu ya ndege kutekwa na mtu mwenye bomu na yuko tayari kulipua ndege hiyo na abiria wote 36 na watumishi wa ndege 6 waliopo umo ndani.. (Ndege ilikuwa haijajaa yote, ilijaa kama theluthi moja tu (1/3)).


Ili asilipue ndege hiyo Cooper alihitaji apewe 'Fedha halali za kimarekani' dola 200,000 (msemo huu 'fedha halali za kimarekani' utakuja kuleta maana sana huko mbele kwenye upelelzi wa FBI). Pia aliamuru apewe parashuti nne na ndege itakapofika uwanja wa ndege wa Seattle kuwe na gari ya kujaza mafuta inasubiri ili ijaze ndege mafuta na kumpeleka sehemu atayoitaka.


Muhudumu Bi. Schaffner akawasiliana na mapilot na kuwahakikishia kuwa ni kweli jamaa ana bomu na akawapa orodha ya vitu alivyokuwa anavitaka.


Baada ya kupewa orodha ya demands za Bwana Cooper, marubani wakawasiliana na uwanja wa ndege wa Seattle na watu wa uwanja wa ndege wakawasiliana na vyombo vya ulinzi na baada ya mtiririko wa mawasiliano kati ya uwanja wa ndege, wamiliki wa ndege na vyombo vya ulinzi kufanyika wakakubaliana kuwa ili kuepusha hasara ya kibiashara na kupoteza maisha ya watu 42 ni vyema wakampatia mtekaji anavyovitaka lakini vyombo vya ulinzi vitaangalia kama kutapatikana fursa yoyote waweze kumkata au kumdungua mtekaji huyo.


Hivyo basi wahudumu wote waliopo kwenye ndege waliamuliwa wampe ushiriakiano Cooper ili kuepusha hatari yoyote na pia wamueleze kuwa awape mda kidogo ili kukamilisha kupata vitu alivyokuwa anavihitaji.


Baada ya jibu hilo kurudishwa juu kwenye ndege na marubani kuwasiliana na muhudumu Schaffner kupitia intercom, muhudumu alirudi kwenye siti aliyokaa Cooper na alikuta sasa amevaa miwani meusi ya jua na yuko amerelax kabisa bila presha wala wasiwasi wowote! Akampatia jibu walilopewa kutoka chini kwenye uwanja wa ndege.


Baada ya kupewa jibu hilo Cooper akaitikia kwa kichwa kisha akawasha sigara nyingine na kuagiza Soda nyingine na maji ya kunywa, na kwa mshangao akalipia na chenji iliyorudi akampa 'tip' muhudumu Schaffner.


Muda wote huu abiria wengine walikuwa hawajui kinachoendelea ndani ya ndege na ili kuepusha wasije wakapata wasiwasi kutokana na kuchelewa kutua wakatangaziwa kuwa kulikuwa na tatizo la kiufundi hivyo itawalazimu wachelewe kutua mpaka tatizo litakapo shughulikiwa.



    0 comments:

    Post a Comment

    Blog