IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Dili La Dola Bilioni Nne
Sehemu Ya Kwanza (1)
Wasichana zaidi ya kumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walinyamaza ghafla huku macho yao yakimwangalia kijana mmoja ambaye alikuwa akipita mbele yao.
Mwendo wake ulikuwa wa taratibu sana, alitembea kwa kujiamini mno, alijua kwamba alikuwa mzuri wa sura, wanawake wengi walimbabaikia huku akizungumziwa sana midomoni mwao na ndiyo maana hata alipokuwa akitembea mbele ya wasichana, mwendo wake ulikuwa ni wa kunyata sana kana kwamba alikuwa akimsubiri mtu aliyekuwa nyuma yake.
Wote waliokuwa wakimwangalia walivutiwa naye, kulikuwa na wasichana ambao walitamani hata kumsimama kijana huyo na kuzungumza naye tu ili kesho waanze kuzusha kwamba walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi pamoja naye lakini hilo halikuwezekana kabisa.
Kila mmoja alitulia na kumwangalia kwa makini kabisa, alikuwa kijana mwenye sura nzuri ambaye kila msichana chuoni hapo aliyemwangalia alitamani sana siku moja awe naye kimapenzi na kuwa mume wake wa ndoa. Kijana huyo aliitwa Richard Mawelle.
Richard alikuwa tofauti na vijana wengine, muda mwingi alikuwa kimya, hakuwa mzungumzaji hata kidogo, hakupenda mazoea na wasichana na ndiyo maana muda alipenda kujitenga huku kama ilikuwa ikitokea kuzungumza na watu wengine, basi alikuwa akiwafuata marafiki zake wawili, Robinson na Robert.
Wasichana walimbabaikia, mara kwa mara kulikuwa na ugomvi wa wasichana kwa wasichana, wengi walikuwa wakigombana kwa ajili yake, si kwamba walizungumza naye bali kujitamba mbele ya mashoga zao ndiyo hali iliyokuwa ikileta ugomvi katika chuo hicho.
Kulikuwa na makundi ya wasichana waliokuwa wakichukiana kisa Richard, kulikuwa na watu ambao kila walipoonana ilikuwa ni kugombana kisa kijana huyo ambaye wala hakuwa na taarifa na msichana yeyote yule.
Kutokupenda kwake wanawake kukamfanya watu kuanza kumfuatilia, walihisi kwamba kulikuwa na siri kubwa na nzito nyuma yake, ilikuwa ni vigumu kwa mvulana yeyote kutotaka kuwa kwenye mahusiano na msichana yeyote yule, hasa wasichana wengi warembo ambao walikuwa wakipatikana chuoni hapo.
Kwenye ufuatiliaji wao, hawakugundua kitu chochote kile, alikuwa mzima wa afya, hakuwa na urafiki na wanaume wengi, hao wawili, Robinson na Robert ndiyo walikuwa kila kitu kwake, alibadilishana nao mawazo na hata kujadili mambo mengi ambayo walitakiwa kufanya mara baada ya kumaliza chuo.
Kila siku Richard alikuwa mtu wa kupokea maboksi ya zawadi kutoka kwa wasichana mbalimbali, chuoni hapo ilikuwa ni kama ushindani, kila mmoja alitaka kumuonyeshea kijana huyo kwamba alikuwa akimpenda na alitakiwa kuuchukua moyo wake na kumfanyia lolote lile alilotaka.
“Richard...kwa nini unanifanyia hivi?” aliuliza msichana mmoja aliyeitwa Jesca ambaye alisimama mbele ya Richard.
Siku hiyo ilionekana kuwa kama muujiza, kijana huyo hakuwa akitoa nafasi ya kusimama na msichana yeyote yule, kwa Jesca ilikuwa ni bahati kubwa kwa kuwa alimkuta akifikiria mambo mengine kabisa, alimfuata kwa kushtukiza.
“Unasemaje?” aliuliza Richard huku akionekana kushtuliwa kutoka kwenye lindi la mawazo.
Msichana huyo akarudia maneno yake kwa mara nyingine huku Richard akimwangalia. Alitamani kumfukuza, hapo alipokuwa alikuwa akiwasubiria marafiki zake, Robinson na Robert ambao walipanga kuonana mahali hapo kwa ajili ya kuzungumza kitu cha muhimu sana.
Alisita kumfukuza kwa sababu kila mtu aliyekuwa canteen alikuwa akimwangalia yeye na msichana huyo ambaye aligoma kabisa kuondoka, alichokuwa akitaka ni kujua ukweli kama Richard alikuwa akimpenda au la.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alichokifanya ni kusimama, akamshika mkono na kuanza kuondoka naye. Kila mmoja alishangaa, uondokaji wake haukuwa wa kawaida hata kidogo, ni kama kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Waliokuwa wakitaka kuona mwisho wa mchezo ni kitu gani kingeendelea wakaanza kufuatilia kimyakimya, wale ambao hawakuwa mule canteen ambao walimuona Richard na msichana huyo wakiwa wameshikana mikono walipigwa na butwaa kwani kwa mwaka wa pili mfululizo walijaribu kuzungumza na Ricard lakini ilishindikana kabisa.
Siku hiyo ilikuwa ni kama kituko fulani hivi, safari yao hiyo iliishia katika bweni la wavulana ambapo moja kwa moja wakaelekea katika chumba alichokuwa akilala na kumuweka kitandani.
Jesca hakujua sababu ya kupelekwa mahali pale, alibaki akimshangaa Richard, alihisi kama kijana huyo alitaka kuzungumza naye lakini kwa jinsi alivyoonekana, hakuwa sawa kabisa.
“Jesca! Nisikilize kwa makini,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo usoni.
“Sawa. Nakusikiliza baba,” alisema msichana huyo kwa adabu zote.
Richard alitaka kuzungumza kitu lakini akashindwa, alichokifanya ni kuchukua begi lake na kulifungua, humo akatoa kadi nyingi, maua, saa mpya, cheni na vitu vingine vingi ambavyo alitumiwa kama zawadi na wasichana mbalimbali chuoni hapo.
“Hebu niambie! Kati ya hawa wote na wewe nimkubali nani?” aliuliza Richard huku akimwangalia msichana huyo ambaye hakuwa akishangaa vitu vile kwani kwa jinsi Richard alivyokuwa mzuri wa sura, alistahili kuvipokea kutoka kwa wasichana hao.
“Richard....” aliita Jesca.
“Hebu nijibu kwanza! Nimkubali nani? Nyie mnanichanganya sana. Unajua mimi siangalia wanawake, mimi naangalia pesa, kichwa changu kinafikiria mambo mengi kuhusu pesa. Jesca, sina muda na wanawake,” alisema Richard huku akionekana kuwa na hasira mno.
Jesca alibaki kimya, alimwangalia Richard, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, mishipa ilivyomtoka ilionekana kabisa kwamba hakuwa na masihara hata kidogo, kile alichokuwa akimwambia ndicho ambacho alikimaanisha kutoka moyoni mwake.
Baada ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, Jesca akaanza kutabasamu, alijua dhahiri kwamba Richard alikasirika, hakutaka kumuona akiendelea kwenye hali hiyo na ndiyo maana akaamua kulitumia tabasamu lake kama silaha ya kumaliza hasira za Richard.
“Unacheka?” aliuliza Richard.
“Hapana! Natabasamu. Naomba nipige picha na wewe, nakuomba!” alisema Jesca huku akitoa simu yake aina ya iPhone X.
“Jesca....”
“Nakuomba,” alisema Jesca na kujivuta mbele ya Richard na kujipiga picha moja iitwayo ‘selfie’ kisha kuondoka mahali hapo.
Moyo wa Jesca ukauma mno, hakuamini kile alichokuwa ameambiwa. Alijiona kuwa msichana mrembo mno, alifuatiliwa na wanaume wengi lakini wote hao hawakuwa na nafasi kwake, mwanaume ambaye alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati alikuwa huyo Richard ambaye aliamua kumkataa na kumwambia kwamba hakufikiria mapenzi, moyo wake ulifikiria zaidi pesa.
Alitembea kwa kujiachia, kila mtu ambaye alimuona alipoingia ndani na Richard aliamini kwamba walimalizana vizuri na inawezekana kabisa msichana huyo alikubaliwa kwani hata tabasamu lililokuwa likionekana usoni mwake lilikuwa la matumaini tele.
Jesca aliamua kulitumia tabasamu lake kama kuficha kile kilichokuwa kimetokea ndani. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, alilia kwa ndani lakini machoni mwake alionyesha kuwa na furaha kupita kawaida.
Alitembea mpaka kwenye bweni lao, akaingia mpaka chumbani na kulala kitandani kwake, hapo ndipo alipoanza kulia kwa uchungu mkubwa moyoni mwake.
Kwa miaka ishirini na mbili aliyokuwanayo alijiapiza kwamba ilikuwa ni lazima aendelee kuishi bikira mpaka siku ambayo angeolewa ili iwe zawadi kwa mume wake lakini kitu cha ajabu kabisa baada ya kuanza chuo na kumuona Richard, akaamua kuachana na ahadi yake kwa mume wake mtarajia hivyo kutaka bikira hiyo itolewe na kijana huyo.
“Richard! Kwa nini umenifanyia hivi?” aliuliza Jesca huku akiendelea kulia kama mtoto mdogo.
Wakati yeye akilia na kuomboleza, upande wa pili maisha ya Richard yalikuwa kama kawaida, alizoea kuyaona machozi ya wanawake, wale wachache ambao walibahatika kuzungumza naye wengi waliyatumia ili kumlaghai lakini msimamo wake ulikuwa uleule kwamba hakutaka kuwa na uhusiano na msichana yeyote yule mpaka pale ambapo angekuwa na pesa nyingi.
Kupendwa na wanawake haikuwa chuoni tu bali hata nyumbani kwao, Magomeni Mapipa Richard alikuwa gumzo, kila msichana aliyekuwa akimuona alimpenda, alivutiwa naye na kutamani kuwa naye lakini hali ilikuwa vilevile.
Wake za watu walikuwa kwenye wakati mgumu, hawakuweza kujizuia, waliwaambia wanawake wengine jinsi walivyokuwa wakimpenda kijana huyo ambaye hakuonekana kuwa na habari na msichana yeyote yule.
Ndoa nyingi zilitingishika, waume zao walikasirika lakini hawakuwa na la kufanya kwa kuwa walijua ukweli juu ya kijana huyo kwamba hakuwa mtu wa wanawake, aliishi maisha yake ya peke yake huku kila siku akiwaambia watu kwamba pamoja na umasikini aliokuwa nao na familia yake lakini kuna siku moja angekuja kuwa na pesa nyingi.
“Ipo siku. Iqram, ipo siku mshikaji wangu,” alisema Richard mara kwa mara alipokuwa akikutana na rafiki yake, Iqram Maduro.
“Itakuwaje?”
“Nitakuwa bilionea mkubwa sana!”
“Kama ni hivyo, nitafurahi, ila kwa nini usianze kuwa na mademu wa kishua? Angalia unavyofagiliwa, kwa nini usimchukue hata Amanda. Demu ana pesa, atakutoa,” alisema Iqram.
“Hujui kichwa changu kinafikiria nini. Iqram, sifikirii laki, milioni wala bilioni. Kichwa changu kinafikiria trilioni,” alisema Richard.
“Trilioni?” aliuliza Iqram kwa mshtuko.
“Ndiyo! Nisikilize! Kuna siku nitazipata hizi pesa. Nakuambia ukweli, kuna siku nitazipata, nitakuchukua na kukupeleka Paris kwenye mnara wa Eiffel na nitakwambia Iqram I made it,” alisema Richard huku akionekana kuwa na imani kubwa ndani yake.
“Utafanikiwaje?”
“Hahah! Nimezungukwa na vichwa viwili hatari sana, yaani vichwa hatari mno, utaona,” alisema Richard huku akimwangalia Iqram.
“Basi wote tuseme Insh allah!” alisema Iqram huku akitabasamu.
“Aisha, umeona picha nilizokutag jana?” aliuliza msichana mmoja kwenye simu.
“Hapana!”
“Hujaingia Facebook?”
“Mh! Nilijaribu kuingia lakini password yangu ilikuwa ikikataa, sijui kulikuwa na tatizo gani manake hata simu yangu kama siielewielewi hivi, ngoja niingie tena. Wewe umeingia leo?” aliuliza msichana huyo, Aisha.
“Hapana! Ngoja niingie,” alisema na kukata simu.
Watu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikuwa bize na kompyuta na simu zao, kilichokuwa kikiendelea kilimshangaza kila mmoja. Hakukuwa na aliyeamini kama akaunti zao za mitandao ya kijamii hazikuwa zikifanya kazi kwa wakati huo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hawakujua tatizo, kila mmoja chuoni hapo ambaye alijaribu kuzifungua, hakukuwa na mtu aliyeweza kuona kitu chochote kile.
Simu na kompyuta zao zilionekana kama kuvamiwa na virusi kwa kuwa kila walipokuwa wakijaribu kufungua kulikuwa na neno lililosomeka Robit ambalo kwa jinsi lilivyokuwa likisomeka ilionyesha kabisa lilikuwa virusi ambavyo vilitengenezwa na mtu ambaye alihakikisha kinaingia kwenye simu na kompyuta ya mtu yeyote ambaye angeiunganisha na huduma yoyote ya internet katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Maprofesa hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani kazi ilianzia kwa mitandao ya kijamii na baadaye kuhamia katika tovuti ya chuo hicho, kila password iliyokuwa ikiingizwa, haikuwa ikikubali hata kidogo.
Hilo likawafanya kuwapigia simu mafundi wa kitengo cha IT ambao walifika chuoni hapo na kuanza kulifanyia kazi. Walihangaika, waliingia na kuona kulikuwa na tatizo gani.
Kama ambavyo iligundulika mwanzo kwamba kulikuwa na virusi vilivyojiita Robit ndivyo walivyokutana navyo. Mara ya kwanza haikuonekana kuwa tatizo kwani walikuwa na anti-virus wakali hivyo kuanza kuwatumia.
Hakukuwa na kitu kilichowezekana, walijaribu kufanya hivyo mara kadhaa lakini hawakufanikiwa. Ndani ya chumba walichokuwa wamekaa, vipara vyao vilikuwa vikitoka jasho, hawakuamini kama kulikuwa na virusi hatari ambavyo vilivuruga mawasiliano kama hivyo ya Robit ambavyo hawakujua vilitengenezwa na mtu gani.
Kazi hazikufanyika chuoni, materials yote ya chuo ambayo yaliwekwa katika tovuti ya chuo hicho yalifichwa, vyeti, fomu za kujiunga na chuo hicho na vitu vingine vyote vilifichwa kitu kilichoonyesha kwamba walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanatatua tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
Kwa siku tatu mfululio hakukuwa na kitu chochote. Waliposhindwa kabisa wakaamua kuwasiliana na wakuu wengine wa vyuo ambao hao waliwasiliana na viongozi wa serikali akiwemo rais ambaye yeye akawapeleka vijana wa IT ambao walikuwa hatari, walioilinda mafaili ya ikulu na kwenda kufanya kazi hiyo.
Kwa macho ilionekana kuwa nyepesi mno lakini baada ya kuanza kuifanyia kazi, ilionekana kuwa kazi kubwa na ngumu kupita kawaida.
Wataalamu hao kutoka serikali nao wakaona joto la jiwe, walifika chuoni hapo kwa mbwembwe kubwa na kujiona lakini baada ya kushindwa kazi hiyo wakawa wadogo kama pritoni.
“Vipi?” aliuliza Profesa Mjuni.
“Kazi ngumu!”
“Ngumu? Ngumu kivipi?”
Walijaribu kumwambia ugumu ulipokuwa, kwa siku zote hizo walikuwa chuoni hapo wakiifanya kazi hiyo lakini hawakufanikiwa hata kidogo.
Hilo likawaonyeshea kwamba walitakiwa kutafutwa wataalamu wa IT bora kuliko wao hivyo serikali kuamua kuwapigia Waafrika Kusini ambao waliahidi kufika Tanzania haraka iwezekanavyo.
Wakati wakiwasubiri watu hao, mambo yalikuwa magumu chuoni hapo, bila internet hakukuwa na kitu cha maana kilichokuwa kikiendelea. Tatizo kubwa lilikuwa ni huduma ya internet iliyokuwa mahali hapo ambayo hiyo ilitumiwa kitaalamu na kuingiza virusi kwenye simu na kompyuta ambazo zilikuwa zikitumia huduma hiyo chuoni hapo.
Huduma zote zilizokuwa zikipatikana katika Jengo UDBS, CoET, Utawala na sehemu nyingine chuoni hapo kote hakukuwa na huduma ya internet kwa mitandao ya kijamii wala tovuti ya chuo.
“Yaani huyu mtu aliyefanya hivi ametumia akili kubwa,” alisema jamaa mmoja ambaye naye kidogo alikuwa na ufahamu kuhusu mambo ya teknolojia.
“Ipi?”
“Yaani kama umewahi kuiunganisha simu au kompyuta yako na huduma yoyote ya internet hapa chuoni, virusi wameingia kwenye kifaa chako hivyo huwezi kuingia tovuti ya chuo, Facebook, WhatsApp wala Instagram,” alisema jamaa huyo.
“Ila kama hujaunganisha baada ya kuvamiwa?”
“Hapo poa, mimi si unaona natumia bando la huduma ya simu, nipo poa tu,” alisema kijana huyo.
Waandishi wa habari hawakuwa nyuma, kama kawaida yao wakaanza kuizungumzia hali iliyokuwa ikiendelea chuoni hapo kwamba kulikuwa na tatizo kubwa ambalo liliwafanya wanafunzi kutokusoma tena kwa kuwa hakukuwa na huduma ya internet.
Hawakuishia hapo tu bali waliendelea kutoa taarifa kwamba hakukuwa na mategemeo ya wanafunzi wapya kujisajili kwa sababu fomu zote ambazo zilitakiwa kufunguliwa katika tovuti ya chuo, tovuti yenyewe haikuwa ikifanya kazi, yaani virusi ambavyo vilitumwa viliharibu kila kitu.
Baada ya siku mbili wataalamu kutoka nchini Afrika Kusini wakafika Tanzania na moja kwa moja kupelekwa katika chuo hicho na kuanza kufanya kazi.
Kama walivyokuwa wale wa kutoka serikalini, hata nao walianza kupuuzia lakini baadaye wakagundua kwamba walikuwa wakipambana na virusi hatari sana ambavyo kama wasingekuwa na uzoefu wa ziada basi wasingeweza kufanikiwa.
Wakaweka umakini wao wote mahali hapo lakini bado hawakuweza kufanikiwa. Ilikuwa ni moja ya kazi ngumu sana ambayo waliwahi kukutana nayo katika maisha yao.
Tovuti ile haikufunguka na kurudi katika hali ya kawaida, kila kitu ambacho walikifanya kuhakikisha kwamba wanafanikiwa walishindwa kabisa kufanikiwa.
“Siku ya tatu leo, vipi jamani?” aliuliza profesa.
“Hali bado tete! Ila tutafanikiwa.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa.”
Wakati wataalamu hao wakiendelea kuhangaika na kompyuta zao, kijana Robinson Frank alikuwa nyumbani kwao, Mwananyamala A alipokuwa akiishi huku akiwa na kompyuta yake iliyochoka mapajani mwake.
Huyo ndiye alikuwa chanzo cha kila kitu. Japokuwa alitoka kwenye familia ya kimasikini lakini alikuwa na akili mno, katika maisha yake alifanya mambo mengi ambayo yalidhihirisha kwamba alikuwa na akili ya ziada ambayo watu wengine hawakuwa nayo kabisa.
Alipenda kompyuta tangu alipokuwa mdogo, alipambana kwa kudunduliza pesa na hatimaye akafanikiwa kununua kompyuta yake hiyo ambayo alidumu nayo kwa miaka mitano na ilikuwa imechoka kupita kawaida.
Hiyo ndiyo aliyoitumia kufanyia utundu wake. Alipenda sana IT, alijifunza mambo mengi kwenye mitandao na vitabu mbalimbali, ndoto yake ilikuwa ni kuwa mmoja wa watu hatari sana katika teknolojia na ndiyo maana alijifunza kwa nguvu kubwa huku akiamini kwamba kuna siku angekuja kufanikiwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa na pesa nyingi kupitia teknolojia.
Wakati akiwa amejifunza mambo mengi mno ndipo akaamua kutengeneza virusi vyake na kisha kuingiza kwenye database za chuoni kwake na nyingine akaingiza katika system ambayo watu waliamini kwamba duniani hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kuingiza virusi humo na kuvipitisha kupitia mfumo wa internet.
Yeye alifanya na kufanikiwa, akavipa virusi hivyo kwa jina la Robit, yaani Rob ya kuiba lakini pia alipenda zaidi jina hilo kwa sababu nalo lilionyesha mwanzo wa jina lake.
Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake, alitamani kuona virusi wale wakisumbua, maprofesa wasipate usingizi ili kuona kama alifanikiwa kuwa mkali ama la.
Alipoona kwa siku tatu mfululizo maprofesa walikuwa wamehangaika huku na kule ndipo akawaambia marafiki zake wawili, Richard na Robert kuhusu mchezo aliokuwa ameufanya, wao wenyewe walishangaa.
“Acha masihara, yaani wewe ndiye unawasumbua watu hivi?’ aliuliza Richard huku akionekana kutokuamini.
“Yeah! Nataka wasumbuke tu! Nyie akaunti zenu vipi, zimezingua niwarekebishie?” aliuliza Robert.
“Sina simu ya android, kwanza mimi na mitandao wapi na wapi? Kompyuta yenyewe sina,” alisema Richard huku akionekana kuwa na huzuni moyoni mwake.
“Na wewe Robert au kama kawaida unatumia Nokia ya Tochi?”
“Mulemule mzee baba! Internet mpaka nikadowee kwa washikaji,” alisema Robert huku akitabasamu kana kwamba hali ile ilimfurahisha kumbe ukweli ni kwamba ilimuumiza mno ndani ya moyo wake.
Wote hao walikuwa masikini, hawakuwa wakijiweza. Walisoma kwa moyo mmoja na kufanikiwa kufaulu kwa alama za juu kabisa. Walikutana hapo chuoni na kuanza kusoma pamoja na kuwa marafiki wakubwa kiasi kwamba watu wengine walishangaa kwani hao wote majina yao yalikuwa yakianza na herufi R ambayo iliwafanya wengi kuona ndiyo maana waliendana na kuwa marafiki wakubwa.
“Ila nina wazo moja kubwa la kutengeneza pesa, mpo tayari?” aliuliza Robert huku akiwaangalia wenzake, yeye muda wote kichwa chake kilifikiria pesa na biashara tu.
“Tuambie mfanyabiashara wetu.”
“Kuna wazo la kipuuzi limenijia kichwani, mnaonaje mkija nyumbani na tukazungumza kuhusu hili?” aliuliza.
“Nyumbani kwenu?”
“Ndiyo!”
“Kule Manzese Kwa Mfuga Mbwa?”
“Hukohuko!”
“Sawa. Kwangu hakuna tatizo, ila ni la pesa kiasi gani?” aliuliza Robinson.
“Kama dola bilioni tatu hivi, ila kama mtataka tumshirikishe na mwingine, basi dola bilioni nne,” alijibu.
“Hold up! Hivi unajua unaposema dola bilioni tatu unazungumzia kiasi gani mzee baba?” aliuliza Richard.
“Zaidi ya shilingi trilioni sita!”
“So unataka sisi tufanye biashara ya kuingiza kiasi hiki cha pesa?”
“Tena inawezekana! Ila kama tutaelewana, cha kwanza tufanyeni mchakato wa kuonana na kuyajenga, tukikubaliana, mpaka mwaka keshokutwa tutakuwa tumefika robo ya kiasi hicho,” alisema Robert.
“Mh!” aliguna Robinson.
“Niamini!” alisema Robert huku akitoa tabasamu pana. Japokuwa hakuwa na pesa lakini alikiona kichwa chake kikiwa na utajiri mkubwa.
Miongoni mwa wanafunzi waliokuwa na akili ya kufanya biashara katika Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam alikuwa mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Robert Temba. Alikuwa mcheshi mno, kila wakati mazungumzo yake yalikuwa ni biashara tu.
Muda mwingi alipokuwa darasani, akizungumza na wenzake na hata kufanya mambo mengine huku kichwa chake kikifikiria ni kwa namna gani angeweza kufanya biashara na kuingiza pesa.
Katika mwaka ambao aliingia shuleni hapo, aligundua vitu vingi havikuwa vikifanyika na alitakiwa kuhakikisha mambo hayo yanafanyika haraka iwezekanavyo.
Hakukuwa na huduma ya kupatikana kwa vocha, ili wanafunzi waweze kununua vocha ilikuwa ni lazima kununua nje ya chuo, hakukuwa na sehemu za kuuza magazeti na hata vyakula ambavyo vilikuwa vikiuzwa mahali hapo vilikuwa ni bei kubwa.
Hilo likamfanya kufikiria sana na ndipo akaamua kuwaweka vijana wake ambao walikuwa na kazi ya kuuza vocha ndani ya chuo hicho, aliwaombea ruhusa maalumu kutoka kwenye uongozi, kila kitu alichokuwa akikifanya, kilimuingizia pesa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuishia hapo, akaomba ruhusa pia ya kupika chipsi humo kwa kuwa vyakula vya aina moja aliamini vingemchosha kila mtu, alipewa ruhusa hiyo na hivyo kuendelea kuingiza pesa.
Alijua biashara, kichwa chake kilikuwa kipana kufikiria ni kwa namna gani angeweza kuingiza pesa nyingi zaidi. Katika maisha yake chuoni hapo ndipo akafanikiwa kukutana na marafiki wawili, Richard na Robinson na hivyo kuwa karibu kupita kawaida.
Yeye ndiye ambaye alimshauri Robinson kuwa na mchezo wa kutengeneza virusi halafu pia watengeneze anti virusi, yote hiyo ni kwa sababu kila mtu ambaye kompyuta yake ingekuwa na virusi basi anunue anti virus kutoka kwake.
Hakuishia hapo, kwa kutumia internet ya chuo alikuwa akipakua muvi nyingi na kuwauzia wanafunzi chuoni hapo. Ilikuwa biashara kubwa kwa sababu asilimia tisini ya wanafunzi hawakuwa wakiweza kupakua muvi kutoka kwenye tovuti mbalimbali.
Japokuwa watatu hao walikuwa masikini lakini kidogo yeye alikuwa nafuu, aliingiza kiasi cha pesa ingawa si kikubwa sana lakini hichohicho ndicho ambacho kilikuwa kikimuwezesha kuendelea na maisha yake.
Baada ya siku kadhaa ndipo akapata wazo jingine la kutengeneza pesa, hazikuwa pesa ndogo kama za chuo, alikuwa na mpango wa kutengeneza pesa nyingi zaidi ya trilioni.
Wazo hilo hakutaka kubaki nalo kichwani, aliamua kuwashirikisha marafiki zake, wakakutana sehemu na kuanza kuongea. Wote walimwamini, alikuwa mtu hatari, hakuwahi kufeli kwenye mipango yake, alikuwa mtu makini sana hasa kwenye mambo yote yaliyokuwa yakihusu pesa.
Richard na Robinson walipoitwa na Robert na kuambiwa kwamba kulikuwa na ishu ya biashara fulani nao wakaungana naye, wakakubaliana na kuamini kwamba hicho ambacho angekwenda kuwashirikisha kilikuwa kitu kizuri na inawezekaa kabisa wangetengeneza pesa.
“Robert! Hebu hold up! Hivi unazijua dola bilioni tatu wewe?” aliuliza Richard, bado hakuamini kama mwanaume huyo alikuwa akikizungumzia kiasi hicho cha pesa.
“Nazijua!”
“Tuambie mpango upo vipi!”
“Mpango ni mkubwa sana! Tutakuwa tunadili na watu na kompyuta zao, simu, hasa kwa wale mastaa wakubwa duniani, katika hili tutakuwa tunasaidiana, kwanza tutaanzia nchini Tanzania halafu tunahamia duniani kote ikiwepo nchini Marekani,” alisema Robert.
“Bado hujafafanua!”
“Ishu ni kwamba tunaanza kutengeneza pesa kwa kuchukua picha zao za utupu na kutaka kuzivujisha!” alisema Robert, wawili hao wakaangaliana, kile alichokiongea kilionekana kuwa upuuzi mkubwa.
“Robert! Yaani picha?”
“Ndiyo! Ni biashara nzuri sana, tutafanya biashara kubwa sana, hasa tukimtumia huyu Richard,” alisema Robert.
“Mmh! Mnitumie mimi tena?”
“Ndiyo! Richard, niamini! Kupitia hili jambo tunakwenda kutengeneza pesa nyingi sana, unabisha?” alisema Robert na kuuliza.
“Nabisha! Bado haijaniingia akilini!”
“Kwa sababu wewe si mfnyabiashara! Hebu niambie demu mwenye pesa hapa chuo tumjaribu!” alisema Roert.
“Kwa hapa! Labda Natasha, yule video vixen!”
“Ooh! Yule demu wa wasanii?”
“Yaap!”
“Okay! Ngoja tuanze na huyu, ili kukuonyeshea kwamba huu mzigo utatiki, tutahitaji shilingi milioni tatu kutoka kwake,” alisema Robert.
“Robert! Unajua mimi sijakuelewa kabisa.”
Ni kweli, kwa kile alichokuwa akizungumza kwa mtu kama yeye ambaye alikuwa akifikiria biashara ilikuwa ni vigumu sana kugundua, aliongea katika lugha ngumu mno ambayo kwa mtu ambaye hakuwa akifanya biashara ilikuwa ni vigumu mno kugundua kitu hicho. Alibaki akitabasamu, kichwa chake kilikuwa na mambo mengi, moyo wake ulikuwa na furaha kwa sababu aliamini kwamba baada ya kufanya mambo yote hayo basi angefanikiwa kuingiza kiasi kikubwa cha pesa.
“Richard! Mademu wanasema wewe ni mzuri sana, si ndiyo?” aliuliza.
“Yeah! Kwa hiyo?”
“Fanya juu chini umchukue Natasha na uwe naye kimapenzi!”
“Halafu!”
“Siku moja mkiwa chumbani, mpige picha za uchi, tena kwa kutumia simu yake,” alisema.
“Kisiri?”
“Hapana! Muombe, akuruhusu kwa ridhaa yake,” alisema Robert.
“Mh! Hiyo ndiyo biashara yenyewe?”
“Yeah! This is how we are going to make money! Guys, this is the deal,” (Yeah! Hivi ndivyo tutakavyotengeneza pesa. Washikaji hili ndilo dili lenyewe) alisema Robert.
“Oops! Halafu!”
“Tutahitaji tupate barua pepe yake na neno la siri ya akaunti yake ya iCloud ambayo anaitumia kwenye iPhone yake,” alisema Robert.
“Halafu?”
“Hiyo tutampa Robinson ambaye ataidukua na kuingia kwenye mafaili yake na kuiba hizo picha,” alisema.
“Halafu?”
“Richard acha utoto! Hizo picha si ndiyo tutamtisha kama tunataka kuzivujisha, hapo tutamwambia atupe pesa, vinginevyo Tanzania nzima itamuona akiwa uchi,” alisema Robert.
“Wazo zuri sana! Wewe mtu hapo umepigilia msumali wa mwisho,” alisema Robinson.
“Kwa hiyo tuanzie wapi?” aliuliza Richard.
“Tuanze na wewe kwenda kumtafuta msichana huyu, hakikisha anakuwa mpenzi wako, tukifanikiwa kwake, tutahamia kwa viongozi mbalimbali Tanzania, yaani pesa itapatikana tu,” alisema Robert.
Mpango haukuwa hapo tu, aliwaambia kwamba ili kuendelea kufanya mambo mengi ilikuwa ni lazima wahakikishe wanahamia katika nchi za nje, walijua kabisa kwamba wangekutana na kesi nyingi na nzito kwani biashara hiyo ingebadilika na kuanza kudili na watu waliokuwa na nguvu duniani, hivyo ilikuwa ni lazima wajipange hata watakapokabiliana na kesi, iwe rahisi kushinda.
“Hapo tutafanyaje na hizo kesi? Tutafungwa na kuacha mabilioni yetu benki,” aliuliza Robinson.
“Kazi rahisi sana! Nashauri kitu kimoja!”
“Kipi?”
“Tumtafuteni kijana mmoja anayesomea sheria, tuzungumze naye na tumwambie kwamba sisi tutamsomesha mpaka nje ya nchi kwa pesa zetu ila lengo litakuwa moja, akiwa mwanasheria mkubwa, mwenye umaarufu duniani ndiyo tutamtumia kutusimamia kesi zetu,” alisema Robert.
“Mh! Sasa sisi hizo pesa za kumsomesha mpaka nje ya nchi tutazipata wapi?” aliuliza Richard.
“Rich! Hukumbuki kama hapo tutakuwa tunapata pesa kwa kutaka kusambaza picha za watu, pesa hizo ndizo zitakazomsomesha! Hahaha,” alisema Robert na kuanza kucheka.
“Hapo nimekuelewa sasa! Na mfano tukishindwa?”
“Hiyo si tatizo! Tutazungumza na Pamela atuazime pesa halafu tukipiga hizi dola bilioni nne, tutamlipa,” alisema Robert.
“Dola bilioni nne tena na si tatu?”
“Ndiyo! Yaani hiyo bilioni moja tumeiongeza kwa kumlipa huyu mwanasheria lakini pia kumlipa pesa huyu Pamela! Yaani hizo dola bilioni tatu ziwe zetu, hiyo moja tuwagawie wagawane, halafu hapo tutakuwa mabilionea wakubwa,” alifafanua Robert.
“Duuh! Wewe jamaa hatari sana, mahesabu yako si ya nchi hii,” alisema Robinson, kila alipomwangalia Robert, hakummaliza, mtu huyo alionekana kuwa na akili ya kipekee.
Huo ndiyo ulikuwa mpango wao, walitakiwa kuukamilisha haraka iwezekanavyo. Wote hawakuwa na pesa za kutosha lakini waliamini kwamba hapa duniani kulikuwa na pesa nyingi mno.
Mpango huo ulitakiwa kufanyika haraka sana lakini kabla ya yote walitaka kuona kama ungefanikiwa na ndiyo maana walitakiwa kujaribu kwa msichana mrembo, aliyeringa mno chuoni hapo, aliyekuwa akionekana kwenye video za wasanii wengi, Natasha.
Jukumu la kumfuata msichana huyo lilikuwa la Richard, yeye alikuwa na sura nzuri hivyo alitakiwa kufanya kila liwezekanalo anaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo kisha kuchukua barua pepe aliyokuwa akiitumia katika akaunti ya iCloud.
Hilo kwake halikuwa tatizo, akakubaliana nao na hivyo kuanza kuitafuta namba ya msichana huyo kwa udi na uvumba. Kuipata haikuwa kazi kubwa kwani kwa jinsi alivyokuwa maarufu chuoni hapo, ilikuwa rahisi kabisa kuipata na hivyo Richard kukabidhiwa.
“Fanya mambo! Namba hiyo, jifanye umekolea sana kwake, akikubali, hakikisha unampiga picha za uchi, sawa?” aliuliza Robert.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa. Hizo milioni tatu ngoja tuanze nayo,” alisema Richard na hivyo kuondoka, kazi iliyokuwa imebaki ni yeye kufanya kile alichoambiwa akifanye.
“Mungu tuongoze tushinde haya mapesa,” alisema Richard katika kipindi alichokuwa kwenye daladala akielekea nyumbani tayari kwa kuanza kazi hiyo.
Natasha alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili aliyekuwa akisomea uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa msichana mrembo aliyekuwa na umbo la kuvutia ambaye kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia alitamani kuwa naye kitandani.
Umbo lake lilijitengeneza vilivyo, hakuwa na kitambi, kwenye kitovu chake aliweka kipini kilichotoboa upande huu mpaka upande mwingine. Mwendo wake ulikuwa wa mapozi huku kichwani mwake akiwa amenyoa mtindo wa kisasa kabisa.
Mavazi yake yalikuwa ni yale yaliyokuwa na mitego mikubwa, alijua kwamba alikuwa na mwili wa kuvutia, mweupe hivyo alipendelea sana kuvalia sketi fupi ambazo ziliyaacha mapaja yake wazi kwa kiasi kikubwa.
Wanaume hawakuacha kuulizia namba ya simu, si wanafunzi wa chuo hicho tu bali hata wale waliokuwa nje, waendesha bodaboda, daladala na watu wengine walitamani sana siku moja wawe na msichana huyo aliyejua kuwaringia wanaume.
Wakati siku zikiendelea kwenda mbele huku akiwa gumzo kutokana na urembo wake, wasanii wakasikia kuhusu msichana huyo hivyo kumtafuta kwa lengo la kulala naye.
Walijua alikuwa mgumu lakini kwa kuwa walikuwa wasanii, wenye silaha za kumpata msichana yeyote yule, wakafanya mawasiliano naye na kumwambia kwamba walitamani sana awe video vixen kwenye video zao.
Kukubali kwa Natasha ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuvuliwa sketi yake na wanamuziki hivyo kuanza kugawa penzi huku akipewa nafasi kubwa ya kuonekana kitu kilichozidi kumfanya kuwa staa zaidi na zaidi.
Ni ndani ya mwaka mmoja tu, alionekana kwenye video zaidi ya kumi huku kila msanii, maprodyusa na wengine wengi wakiwa wamelala naye, kwa pesa au hata kwa kumwambia kwamba kama asingetoa penzi basi vipande vyake vyote kwenye video vingekatwa.
Aliogopa na hivyo kwa hiari yake kupanda kitandani, akafungua zipu ya sketi zake na wanaume kulala naye. Alijua kuutumia mwili wake, alijua jinsi ya kumchanganya mwanaume awapo kitandani.
Alicheza michezo yote ya hatari kiasi kwamba kila aliyepata nafasi ya kulala naye msichana huyo alibaki kwenye kichwa chake kwamba aliwahi kulala na msichana aliyekuwa akijua kufanya uchafu wote kitandani.
Wanaume ambao hawakuwa na pesa waliumia, walisikia tetesi kwamba msichana huyo alipenda sana kutoa penzi kwa watu wenye pesa na wale maarufu, wao, hawakuwa na kitu hivyo kuendelea kula kwa macho kwa kumtamani kwenye televisheni na kuwa wapenzi watazamaji tu.
Kwenye akaunti zake za Instagram na Facebook alipata wafuasi wengi, alijua kuwadatisha, picha alizokuwa akiziweka humo ndizo zilizowafanya mapedeshee wamtafute na kutangaza dau.
Maisha yaliendelea mpaka siku ambayo alitangaza kwamba naye angeanza kuimba, alitengeneza pesa nyingi kwenye kuzipendezesha video za watu wengine sasa aliona ni nafasi yake naye kujifanya muimbaji kwa kuamini kwamba kwa ule uzuri aliokuwanao kusingekuwa na mwanaume yeyote ambaye angeacha kuangalia video yake, yaani hata kama angeimba utumbo bado watu wangependa kuangalia video hiyo kwa jinsi tu alivyokuwa akijiachia.
Kimasihara sana akaanza kutengeneza pesa, alijiwekea himaya yake, dau lake la kulala na wanaume kwa siri likaongezeka na wale ambao walipata nafasi hata ya kukiona kifua chake walikuwa ni wale waliokuwa na pesa nyingi, wanaume wanaohinga kuanzia milioni mbili kwenda juu.
Muziki ukamtoa, hakuwa akijulikana nje ya Afrika Mashariki lakini alianza kupata mafanikio makubwa. Kila siku alipokuwa chumbani kwake, alivua nguo zote na kusimama mbele ya kioo kisha kujiangalia.
Mwili huo ndiyo uliompa pesa, ndiyo uliomfanya kuwa maarufu na ndiyo ambao uliwafanya wanaume kugombana kwa kuwa kila mmoja alitamani sana kulala naye kitanda kimoja.
Mwaka wa pili wa chuo ulipoingia, alipata marafiki wengi, alipendwa na wengi lakini hakutaka tena kutoa penzi kwa mwanaume yeyote chuoni hapo, alikuwa mgumu, hakutaka kuona akivua nguo zake kwa mwanaume ambaye hakuwa na pesa alizokuwa akizitaka.
Baada ya siku kadhaa ndipo akasikia kuhusu Richard, aliambiwa kwamba alikuwa mmoja wa wanaume waliokuwa na sura nzuri, hakuwahi kumuona, alitamani kukutana naye kwani tangu alipofika chuoni hapo hakuwahi kusikia sifa za mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa huyo aliyemsikia.
“Kwani yupo vipi?” aliuliza Natasha huku akimwangalia rafiki yake Angelina.
“Nani?”
“Huyo Richard!”
“Rich Rich? Weee! Mzuri huyo!” alisema Angelina kwa staili ambayo alimaanisha kabisa na alitamani kuona rafiki yake huyo akiuona uzuri wa Richard kupitia macho yake.
“Mh!”
“Yaani wewe acha, ukimuona nadhani utajuta kwa nini ulitolewa usichana wako na mwanaume mwingine,” alisema Angelina maneno yaliyomfanya Natasha kuwa na hamu ya kumuona Richard kwani tayari kichwa chake kilimtengeneza Richard wake, mzuri aliyekuwa na mvuto kupita kawaida.
Wakati yeye akijitahidi kumtafuta mwanaume huyo, naye Richard alikuwa bize kumsaka Natasha, alitamani sana kuonana naye, amwambie jinsi alivyokuwa akimpenda lakini cha ajabu, walikuwa wakipishana sana.
“Rich! Umemuona Natasha?” aliuliza Robinson, alikuwa amempigia simu kuuliza kama tayari alifanikiwa.
“Hapana!”
“Njoo huku canteen namba tano, yupo,” alisema Robinson.
Haraka sana Richard akatoka bwenini na kuelekea huko, alionekana kuwa na haraka sana na kila mtu aliyekuwa akimwangalia alimshangaa. Wasichana walijaribu kumuita na kumsalimia lakini hakujali, alikuwa bize kwenda kumuona msichana huyo ambaye alimuona kama mara mbili tu na kumpotezea.
Hapo canteen watu walikuwa wakipiga stori, wasichana walikuwa wakila lakini kuingia kwake tu, wasichana wote wakabaki kimya na kumwangalia, wale waliokuwa kwenye viti vilivyokuwa na nafasi wakaanza kusogea pembeni ili kumpa nafasi mwanaume huyo aende kukaa naye lakini Richard alisimama na kuanza kuangalia huku na kule.
“Natasha! Richard huyo hapo,” alisema Angelina kwa sauti ndogo huku akiwa na msichana huyo wakila.
Macho ya Natasha yakagongana na macho ya Richard, kwanza wakaganda kwa sekunde kadhaa wakiangaliana tu kiasi kwamba kila mmoja aliyekuwa mahali hapo aliona kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Richard akapiga hatua na kumfuata Natasha pale alipokuwa na kukaa mbele yake. Msichana huyo alimwangalia Richard, zile sifa alizokuwa amepewa na rafiki yake aliziona kuwa ndogo sana kwani kwa jinsi Richard alivyokuwa na sura nzuri, hakika alikuwa mwanaume wa aina yake.
“Mambo!” alisalimia Richard kwa sauti ya kujiamini.
“Poa! Karibu,” aliitikia Angelina huku Natasha akiwa kimya tu akimwangalia pembeni kwani alihisi kuchanganyikiwa na uzuri aliokuwanao.
Richard alikuwa kimya, macho yake hakutaka kuyatoa kutoka usoni mwa Natasha, hakumpenda kabisa lakini kwa sababu kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ilikuwa ni lazima ajifanye anampenda.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walikaa na kuanza kuzungumza. Wasichana waliokuwa wakimuona Natasha akizungumza na Richard, walikasirika, mwanaume kama huyo hakutakiwa kuwa na msichana kama Natasha ambaye kila mmoja aliyajua maisha yake, kuonekana vile ilikuwa ni sawa na kwenda kujiua.
“Umebadilika sana, si kama mwaka jana ulivyokuwa,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo.
“Mh! Kwani wewe ni wa mwaka wa ngapi hapa?”
“Wa kwanza!”
“Umejuaje kama nimebadilika na wakati hukuwepo mwaka jana?” aliuliza Natasha.
“Nilikuwa nakuja kumuona bro. Siku moja akaniambia nije kumuona msichana mrembo kuliko wote chuoni hapa, akanionyeshea wewe,” alisema Richard huku akiachia tabasamu pana lililommaliza Natasha kabisa.
“Jomoniiiiiiiiii!”
“Kweli! U mzuri mno, ni kama ndoto kuja kuzungumza na wewe. Una nafasi baadaye nikuone?” aliuliza Richard.
“Muda gani?”
“Hata usiku!”
“Nitakuwa kwenye shoo!”
“Basi nitakusindikiza, ila kama shemeji hatokuwepo!” alisema.
“Shemeji? Shemeji gani?”
“Kwani upo singo?”
“Ndiyo!”
“Inawezekanaje mwanamke mzuri kama wewe kuwa singo! Au hatujiamini hata kuja kuomba namba ya simu?” aliuliza Richard huku akiendelea kutabasamu.
“Sijajua! Ila wakati mwingine ni maamuzi tu,” alisema Natasha.
“Mmh! Aya bwana!”
Walizungumza mambo mengi huku kila mmoja akionekana kumtamani mwenzake, muda wote huo Angelina alikuwa pembeni, siku hiyo alitaka kumfaidi sana Richard kwa sababu kila siku alikuwa akimuona kwa mbali, siku hiyo alitamani sana kumuona akiwa karibu yake na ndiyo maana alibaki mahali hapo akimsikiliza na kumwangalia mwanaume huyo japokuwa alionyeshewa na Natasha dalili zote za kuondoka hapo ila hakutoka.
Baada ya dakika kadhaa wakabadilishana namba za simu na Richard kuondoka huku mooyoni akiwa na furaha tele kwamba kazi aliyokuwa amepewa ilionekana kukamilika muda wowote ule.
Wakati akiondoka, wasichana wale wawili walikuwa wakimwangalia huku wote wakitabasamu, ilikuwa ni kama ndoto kuzungumza na mwanaume mzuri aliyekuwa akisifika chuoni hapo.
“Umemuonaje sasa?” aliuliza Angelina huku akimwangalia Natasha.
“We acha! Nilikuwa natetemeka mno, yaani nilipagawa,” alisema Natasha!
“Kwa hiyo?”
“Mmh! Sijui nifanyeje! Ila amechukua namba yangu, nadhani atanitafuta!”
“Akutafute! Wee! Sijui, huyu mwanaume anavyoshobokewa na mademu, akutafute wewe Natasha, sidhani! Akichelewa kukupigia, mpigie yeye!” alisema Angelina.
“Namba yake?”
“Hilo si tatizo, ninayo! Nitakupa ila akipokea tu, sema Natasha hapa bila hivyo atakukatia,” alisema.
“Kwa nini?”
“Haongeagi na mademu! Mimi alishanikatia kama mara sita hivi,” alisema Angelina na wote kuanza kucheka.
“Mh! Basi nitamtafuta hata leo!” alisema Natasha, nao wakasimama na kuondoka mahali hapo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment