Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

DILI LA DOLA BILIONI NNE - 2

 






Simulizi : Dili La Dola Bilioni Nne

Sehemu Ya Pili (2)









Moyo wa Natasha ulikuwa na presha kubwa, kile alichokutana nacho siku hiyo kilimshtua mno. Kukutana na Richard na kuzungumza naye kulimfanya kuamini kwamba alikutana na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kuliko wote katika dunia hii.

Alipokuwa kwenye gari lake akirudi nyumbani, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mwanaume huyo tu, kwake alionekana kuwa mtu wa tofauti, mwenye muonekano wa kitofauti kuliko wanaume wote ambao aliwahi kuwa nao.

Alibahatika kutembea na wanaume wenye maumbo mazuri, muonekano mzuri na wa kuvutia lakini hao wote kwa Richard walifunikwa kwa kitu kimoja tu, sura nzuri aliyokuwanayo.

Walibadilishana namba za simu na Richard, kama alivyoambiwa na Angelina kwamba kama angelaza damu basi mwanaume huyo asingempigia hivyo aliona alikuwa na kila sababu ya yeye kuwa wa kwanza kumpigia na kuzungumza naye.

Alichukua nusu saa njiani ndipo akafika Sinza E alipokuwa amepanga. Akateremka na kuelekea ndani. Kichwa chake kilivurugwa, hakutaka kuwafikiria mabwana zake wengine, mtu pekee aliyekuwa akimfikiria ni Richard tu.

Ilipofika majira ya saa moja usiku simu yake ikaanza kuita, ilikuwa ikitoka kwa bwana wake, Waziri Abdallah Sungura ambaye aligombana naye baada ya kugundua kwamba mwanaume huyo alikuwa na mchepuko mwingine baada yake.

Hakumpenda Sungura, alitembea naye kwa sababu alikuwa waziri, alifanya hivyo kwa kuwa tu alikuwa na pesa nyingi. Uhusiano wao wa kimapenzi ulikuwa ni siri kubwa, hakukuwa mtu aliyekuwa akijua kama wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, walikuwa wakifanya kila kitu kwa siri kubwa.

Hayo ndiyo aliyokuwa akiyapenda Natasha, alitamani sana siri hiyo iendelee kwa sababu mbali na Sungura pia alikuwa akitoka kimapenzi na mawaziri wengine wawili ambao nao hawakuwa wakijuana na kila mmoja alijua kwamba yupo peke yake.

Aliingiza pesa, alihongwa kwa sababu hata kitandani alikuwa moto wa kuotea mbali, alicheza michezo yote ya hatari kiasi kwamba wanaume hao walichanganyikiwa na kumuhonga pesa nyingi zaidi.

Natasha hakuipokea simu hiyo kwanza, alibaki akiiangalia kwa sekunde kadhaa, alikuwa akijiuliza kama lilikuwa jambo sahihi kuipokea ama la. Baada ya sekunde kadhaa, akaamua kuichukua na kuipeleka sikioni.

“Unasemaje?” aliuliza huku akijifanya kukasirka.

“Mpenzi naomba unisamehe, ni kweli nimekukosea, nakiri lakini naomba unisamehe nipo chini ya miguu yako,” alisikika Sungura kwenye simu.

Japokuwa alikuwa mwanaume wa mikwara mingi, watu walimuogopa, viongozi na wafanyabiashara wengine walimuona kama Mungu lakini mwanaume huyohuyo kwa Natasha alikuwa mdogo kama pritoni, kila alipoambiwa fanya hivi, pasipo kuuliza swali lolote lile alikuwa akilifanya bila tatizo lolote lile.

Natasha alijua kama anapendwa na mwanaume huyo hivyo hakutaka kabisa kuona akijilegeza, akitawaliwa na mwanaume huyo na kumfanya alivyotaka. Yeye ndiye aliyependwa hivyo alikuwa na kila sababu ya kumfanya mwanaume huyo amnyenyekee kuliko hata mke wake.

“Naomba unitafute kesho!” alisema.

“Ila mpenzi....”

“Umenielewaaa?”

“Laki...”aliuliza Sungura lakini hata kabla hajamalizia swali lake, simu ikakatwa na haikupokelewa hata alipopiga zaidi ya mara sita.

Natasha hakutaka kuwafikiria wanaume wengine, kwake, mtu ambaye alikuwa kwenye mipango yake alikuwa Richard tu ambaye alimwambia ampigie lakini hakuwa na uhakika kama mwanaume huyo angefanya hivyo ama la.

Ilipofika saa mbili usiku huku akiona kimya kabisa, akachukua simu yake na kuanza kumpigia mwanaume huyo. Simu iliita kwa sekunde kadhaa tu, Richard akapokea na kuanza kuzungumza naye.

Kitendo cha kusikia sauti ikiita ‘haloo’ moyo wake ukapiga paaa...alishtuka, kwake, sauti hiyo ilionekana kuwa na msisimko wa ajabu masikioni mwake kiasi kwamba alihisi kama ngoma za masikio yake zikisikiliza aina fulani nzuri ya muziki.

“Rich..unaendeleaje mpenzi?” aliuliza, japokuwa hilo neno la mpenzi alilitaja pasipo kutarajia lakini hakuwa na uwezo wa kulibadilisha.

“Poa tu sijui wewe mtoto mzuri,” alisema.

“Nipo poa. Utakuja?”

“Wapi?”

“Kwenye shoo yangu!”

“Mh! Itakuwa usiku sana, sijui kama nitaweza!”

“Naomba ujitahidi, hata ukitaka nikupitie, nitafanya hivyo,” alisema.

Richard hakukubaliana naye, alikataa na kumwambia kwamba isingewezekana kwenda klabu kwa ajili ya kuangalia shoo yake. Huo ndiyo ulikuwa mpango ambao ulipangwa na alitakiwa kuufuata.

Hakuwa mtaalamu wa wanawake, hakujua walihitaji nini na walichukia nini. Maujanja yote alipewa na Robinson ambaye mbali na utaalamu wake wa IT lakini alikuwa mzee wa totozi.

Alijua njia nyingi za kuwavua nguo za ndani watoto wa kike, alijua jinsi ya kuwaghai, kuzungumza nayo na hata kumfanya kile alichotaka kumfanyia.

Wanawake wengi walikuwa wagumu kuvua nguo kwa siku ya kwanza baada ya kuonana na mwanaume lakini kwa Robinson alikuwa masta, alijua jinsi ya kuzungumza nao kwa lugha nyepesi na kuwaambia jinsi alivyokuwa akiwapenda, kuwajali na alikuwa tayari hata kuwatukana marafiki zake, ndugu zake kitandani lakini si kuona akimkosa mwanamke.

Yeye ndiye aliyemwambia Richard kwamba msichana anapotokea kumpenda hakutakiwa kumuonyesha kwa asilimia zote, alitakiwa kuleta mapozi, nataka sitaki na hakutakiwa kufanya kila kitu ambacho msichana huyo alihitaji akifanye kwa sababu angeonekana kuwa mtu dhaifu sana.

Alimwambia kuhusu Natasha, alimuonya kwamba hakutakiwa kwenda kwenye shoo aliyomwambia aende kwani hiyo ingemuonyeshea thamani na kuonekana kama hana haja na msichana huyo na ndiyo maana Richard alikataa japokuwa alilazimishwa sana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Basi nikitoka kwenye shoo nitapitia kwako,” alisema Natasha.

“Haina shida. Karibu,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.

Kwa Natasha ilikuwa ni kama mateso, mtu aliyelazimisha penzi lakini upande wa pili Richard alikuwa akifurahia tu, pembeni yake alikuwa na washikaji zake, aliwaambia kuhusu msichana huyo, jinsi alivyokuwa akizungumza naye.

“Huyu mtoto unamla,” alisema Robinson.

“Kwani suala lilikuwa ni kumla ama kumpiga picha?” aliuliza Richard.

“Picha kwanza! Kwani hutaki kumla?”

“Hapana! Siwezi!”

“Daah!” alisema Robinson huku akishusha pumzi ndefu.

Walikuwa wakitembea kwenye mipango yao, alichokisema Robinson ni kwamba Richard alitakiwa kujifanya anaumwa hili msichana huyo atakapofika nyumbani kwao basi asifanye naye mapenzi.

Hilo likakubalika na hatimaye kufanya hivyo. Majira ya saa tisa alasiri msichana huyo alipopita kwa akina Richard, akamkuta mwanaume huyo akiwa nje akimsubiri huku akionekana kutokuwa sawa kabisa.

Natasha akashtuka, kuumwa kwa Richard kulimfanya naye kuhisi kaugonjwa fulani hivi, akamsogelea na kuanza kumuuliza, alichomwambia ni kwamba alitapika na alisikia tumbo linauma sana.

Akamshauri kwenda hospitali lakini akakataa na hivyo kwenda chumbani kulala. Natasha hakumsumbua japokuwa walilala pamoja, alijua kwamba mwanaume huyo alikuwa mgonjwa kumbe ukweli ni kwamba hakutaka kufanya naye mapenzi.

Siku ziliendelea kukatika, kitu alichokuwa akikitumia Richard ni kumuonyeshea msichana huyo kwamba alikuwa akimpenda lakini ukweli wa mambo ni kwamba moyo wake haukuwa kwake kabisa.

Marafiki zake waliendelea kupanga mipango, kwa kuwa walijiamini sana kwa kile walichokuwa wakienda kukifanya na kuamini kwamba walikuwa wakienda kuwa matajiri wakaamua kumuita mwanaume mmoja aliyekuwa akisomea sheria, mwanaume huyu aliitwa Vonso almeida.

Huyo ndiye ambaye walitakiwa kufanya naye mipango, wamsomeshe kwa lengo la kuja kuwasaidia huko baadaye. Mwanaume huyo akakutana nao na kuanza kuzungumza.

Walimwambia wazi kwamba walitaka kumsomesha kwa kipindi chote cha maisha yake, walitaka kuhangaikia ada na vitu vingine mpaka wahakikishe anapata masta yake na kuendelea na kazi zake.

“Lengo?” aliuliza Vonso huku akiwaangalia, kile alichoambiwa hakikuaminika kabisa, aliona kama walikuwa wakiigiza.

“Upate masta na uwe mtaalamu wa sheria ili baadaye uje kutusaidia,” alisema Robert.

“Niwasaidie? Kwenye nini?”

“Kesi zetu!”

“Yaani mnataka kufanya makosa?”

“Vonso, tumekuita ili tuzungumze na wewe, tukubaliane, tutimize ndoto yako ya kusoma mpaka nchini Marekani, sasa maswali yanapokuwa mengi, hatuelewi kabisa, au unataka tumtafute mtu mwingine?” aliuliza Robinson huku akionekana kukasirika, katika vitu ambavyo hakuvipenda kabisa basi ni kupotezewa muda.

“Subirini kwanza! Sasa si ninauliza nisije kuingia choo cha kike!”

“Sawa. Sasa sikia, huu ni mkatabata, kausome, ukikubaliana nao, saini na tuanze kufanya kazi,” alisema Robinson na kumpa karatasi halafu kuondoka mahali hapo.

Vonso aliwashangaa, kwake mambo hayo yalionekana kama vituko fulani, ilikuwaje watu wamfuate, wamwambie kwamba walitaka kumsomesha, kumlipia kila kitu kwa ahadi za kumtimiza ndoto zake na kumpa mkataba?

Akaondoka na kwenda bwenini, akaanza kuusoma mkataba huo kila kipengele. Vilikuwa vipengele vilivyompendelea yeye, alivisoma vyote na mwisho kabisa akaambiwa kwamba angelipwa dola milioni mia tano.

“Haiwezekani! Inawezekana vipi hii?” alijiuliza pasipo kupata majibu.

Hata kama asingekuwa na akili ilikuwa ni lazima kusaini mkataba huo, akafanya hivyo harakaharaka na kesho yake kuwafuata vijana hao na kuwapa, wakabaki na orijino na yeye kumpa kopi.

“Hii ni siri yako, nadhani umeona hicho kipengele pia, ukisema kwa yeyote, mkataba unaishia hapo,” alisema Robert.

“Sawa. Haina shida. Siri milele!”

Wakati hayo yakiendelea huku upande wa pili Natasha alikuwa moto, alichanganyikiwa mno. Kila siku alimsumbua Richard kwamba alitamani sana kukaa naye na kuzungumza.

Hilo halikuwa tatizo, walikuwa wakikaa, wanabadilishana mate lakini hawakufanya mapenzi. Natasha hakuelewa sababu, alijua tu kwamba mwanaume huyo alikuwa akimuogopa kwa sababu alikuwa msanii hivyo kumwambia wakapime Ukimwi ili asiogope lakini msimamo wa Richard ulikuwa vilevile.

“Richard! Mwili huu ni kwa ajili yako, yaani simpi yeyote yule, sasa kwa nini hutaki?’ aliuliza Natasha.

“Kwa sababu sipo kwenye hali nzuri, mawazo mengi,” alijibu.

“Mawazo kuhusu nini?”

“Sina pesa!”

“Nakutumia milioni moja baadaye. Richard mpenzi ninahitaji kukuona ukiwa na furaha mpenzi,” alisema Natasha, hakutaka kusema tu, ilikuwa ni lazima kufanya matendo kumuonyeshea mpenzi wake huyo kwamba alikuwa akimpenda sana.

Kuhusu kumtumia pesa hazikuwa stori bali alifanya kweli na kumpa mwanaume huyo kiasi hicho cha pesa ambacho alikichukua na kuanza kugawana na wenzake kisha kuendelea kujibebisha kwa msichana huyo.

Alihitaji kumteka, alichokifanya ni kwenda mjini ambapo huko akanunua maua, nguo za ndani za kike, akazifunga sehemu nzuri na kumpelekea msichana huyo.

Natasha alipofungua boksi na kukutana na zawadi hizo akachanganyikiwa, zilimpagawisha. Kwenye maisha yake alipewa zawadi nyingi na mabwana zake, magari lakini hizo alizokuwa amezipata kutoka kwa mwanaume huyo zilimchanganya kupita kawaida.

“Bebi nashukuru! Ila naomba tufanye kitu kimoja,” alisema Natasha huku akimwangalia Richard.

“Kitu gani?”

“Nataka nikakutambulishe kwa mashoga zangu!”

“Mh!”

“Unaogopa?”

“Hapana! Haina shida.”

Natasha aliamini kwamba alikuwa na mwanaume mzuri kuliko wote katika dunia hii, hakutaka kuona akiwa kwenye uhusuano naye tu huku marafiki zake wakiwa hawamfahamu, alitaka kuwatambia, kuwaonyeshea kwamba alikuwa na bwana mzuri kuliko yeyote yule.

Siku ambayo alipanga kuondoka na Richard kwenda kumtambulisha kwa marafiki zake alijiandaa mno, alipendeza kupita kawaida kiasi kwamba ule uzuri aliokuwanao uliongezeka maradufu.

Wakaondoka na baada ya dakika kadhaa wakafika katika Hoteli ya Serena ambapo hapo akakutana na marafiki zake na kuanza kumtambulisha kwa Richard.

Alijisikia raha moyoni mwake, marafiki zake walishangaa, nao hawakuamini kama duniani kungekuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Richard.

Walimwangalia, mioyo yao wenyewe ikatokea kumpenda, walikaa na kupiga naye picha mahali hapo ili nao pia waende kuwatambia mashoga zao kwamba walikutana na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri sana.

Kwa kifupi Richard aliwachanganya mabinti hao, hapo walipokaa, kila alipokuwa akizungumza wote walibaki kimya na kumkodolea macho.

Miongoni mwa marafiki waliokuwa mahali hapo, msichana ambaye alimpenda kwa moyo wa dhati alikuwa Judith. Huyu alikuwa amsichana aliyeishi maisha ya kitajiri, alilelewa kama yai na wazazi wake waliokuwa wakiishi Masaki, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kupendwa sana, kuonyeshwa mapenzi ya kila aina na kutakiwa kutulia ndani lakini Judith hakuelewa hata kidogo ndiyo kwanza alikuwa mtu wa kutoka mitoko ya usiku, kwenda klabu na marafiki zake na kufanya mambo mengi tu.

Siku hiyo alipomuona Richard yeye mwenyewe alimpenda, alimjua rafiki yake huyo, alipenda kuwa na wanaume wengi, kila alipomwangalia Richard aliona kabisa mwanaume huyo alikuwa akienda kufa au kuumizwa vibaya huku mbeleni hivyo alihitaji kumuokoa, kumtoa katika mikono ya Natasha na kuwa naye yeye mwenyewe.

“Haiwezekani malaya kama Natasha awe na Richard...yaani haiwezekani, kama tutagombana, nipo tayari lakini si kuona akiwa na huyu mwanaume. Mimi mwenyewe nina moyo wa nyama, wenye kupenda kama watu wengine,” alijisemea Judith huku akionekana kupenda kweli kiasi kwamba hata macho yake aliyokuwa akiyatumia kumwangalia mwanaume huyo yalielezea kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.





Kitu alichokihitaji Natasha kilikuwa ni kufanya mapenzi na Richard tu, alimpenda, kuwa mpenzi wake pasipo kufanya mapenzi ilikuwa sawa na bure. Alipambana, alimwambia kila aina ya maneno matamu lakini Richard hakuwa radhi, kila siku kazi yake ilikuwa ni kumwambia kwamba alimpenda na alitamani sana kulala naye lakini alikataa kwa kumpa visingizo ambavyo kwake havikuwa na mashiko hata kidogo.

Siku ziliendelea kukatika, Natasha alikuwa msiri, hakuacha kuwapiga pesa mawaziri, alilala nao kwa siri kubwa huku akipewa kila kitu alichokuwa akikihitaji. Kwao, alifanya mapenzi kwa nguvu kubwa, alijua kucheza na mwanaume lakini alihisi kabisa kwamba moyo wake ulihama kabisa.

Hakuwa na wasiwasi na Richard, alimjua mwanaume huyo, hakuwa mtu wa kushika simu yake kabisa, hata alipokuwa akimuacha nayo, alipokuwa akirudi hakukuwa na kitu chochote kilichotokea, hakujua kama mwanaume huyo alikuwa na mahesabu yake makubwa.

Upande mwingine wa rafiki yake Natasha, Judith alikuwa akihangaika, hakukuwa na kitu alichokitamani muda huo kama namba ya simu ya Richard. Alitokea kumpenda mwanaume huyo, asingeweza kuvumilia kumuona rafiki yake akiwa na mwanaume mzuri kiasi hicho hivyo alitaka kufanya mapinduzi makubwa.

Akaanza kuitafuta namba ya Richard, kuchukua simu ya rafiki yake Natasha ilikuwa vigumu mno, rafiki yake huyo aliwajua, walikuwa na tabia ya kuchukuliana mabwana hivyo kitu pekee alichokuwa akiamini kuwa anaweza kuzungukwa kilikuwa ni huyo Richard.

Alimshtukia Judith, kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimwangalia Richard aliamini kabisa alimpenda, alihitaji kuwa naye hivyo kazi kubwa aliyokuwanayo ilikuwa ni kuilinda simu yake kwamba kama angezubaa angechukua simu na kuiiba namba hiyo.

Judith alihangaika lakini hakufanikiwa, alichoamua ni kuanza kumtafuta mwanaume huyo chuoni. Hakuwa msomi mahali hapo, alimfahamu Natasha kama rafiki yake ambaye alikutana naye katika mishemishe zake za kusaka mabwana katika klabu ya Next Door jijini Dar.

Walizoeana na kuanza kutembeleana huku naye akifanya kazi ya Video Vixen na alionekana kwenye video za wasanii mbalimbali. Alipofika chuoni humo akaanza kumtafuta Richard, hakutaka kuulizia kwani aliamini kabisa ni lazima rafiki yake angepata taarifa kwamba alifika mahali hapo na kumuulizia mwanaume huyo.

Kuonekana kwa Richard haikuwa kazi ndogo, alisumbuka zaidi ya saa moja lakini ilishindikana kabisa kumuona hivyo kuamua kuulizia tu. Jibu alilopewa ni kwamba kijana huyo alikuwa uwanjani, hakutaka kusubiri, katika vitu ambavyo alitamani sana kilikuwa ni kuonana na mwanaume huyo ili amwambie ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

Akaondoka na kwenda huko, alipofika, akamuona akiwa pembeni kabisa na marafiki zake wawili, Robinson na Robert, kwa mwendo wa kujiamini akaanza kuwafuata.

Alipowafikia, macho ya Robinson yalipotua kwa msichana huyo tu, moyo wake ukapiga paaa. Alipenda mademu mno, kwake, hata kama kwenye mademu mia moja ungemwambia achukue mademu tisini na tisa bado angekutumia meseji za lawama kwamba kwa nini hukumruhusu ammalizie na yule mmoja.

“Habari zenu,” alisalimia Judith huku akiwaangalia, uso wake ukawa na tabasamu pana.

“Poa tu mrembo, umependeza kama Priyanka Chopra,” alisema Robinson huku akimvua Judith nguo kwenye mawazo yake na kumuweka kitandani na kuanza kufanya mambo.

“Ahsante. Samahani Richard, unanikumbuka?” aliuliza Judith huku akimwangalia mwanaume huyo aliyekuwa akimuumiza moyoni mwake, Richard akaanza kumwangalia vizuri.

“Sura si ngeni,” alijibu Richard, alimkumbuka sana msichana huyo lakini hakutaka kumwambia.

“Naweza kuzungumza na wewe kidogo?”

“Haina shida. Unataka kunipa hela?”

“Hahaha! Hapana! Ila napo ukihitaji si tatizo,” alisema msichana huyo.

Wakaelekea pembeni, walizungumza kidogo tu. Muda wote Judith alikuwa akimwangalia mwanaume huyo kwa uso wenye bashasha kubwa, alitamani sana kumwambia lengo lake la kwenda hapo lakini alihofu moyoni mwake na kuona kama asingeweza kukubaliwa na mwanaume huyo.

“Unazunguka sana Judith! Unahitaji nini?” aliuliza Richard.

“Naomba namba yako!”

“Ya simu ama?”

“Ndiyo!” alijibu.

“Si tatizo!”

Richard akampa msichana huyo namba ya simu na kuondoka zake. Mpaka kufikia hapo akahisi kabisa alishinda vita hivyo. Alipofika nyumbani kwake, akachukua daftari lake na kuiandika na kwa pembeni pia kwani alihisi kama simu ile ingepoteza namba hiyo.

Kazi ikabaki kwake, akawa anampigia simu Richard na kuanza kuzungumza naye, alijishtukia, hakutaka kumwambia kama alimpenda, alihitaji kumzoea na kuzungumza mambo mengine lakini mwisho wa siku kitu alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni kimoja tu.

Wakati hayo yakiendelea, tayari Natasha akaambiwa kwamba msichana huyo alionekana hapo chuoni akizungumza na Richard, alikasirika, hakuamini kama Judith angediriki kwenda chuo kwa siri kubwa na kuonana na Richard.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alikuwa rafiki yake mkubwa, alimwamini sana, kwa kile alichokifanya kwake ilionekana kama dharau. Akampigia simu na kuomba kuonana naye, walipoonana tu, wakaanza kutukanana kama wanawake wa uswahilini.

Kutukanana kwao kukawakusanya watu, picha zikapigwa na kutupwa kwenye mitandao ya kijamii. Ugomvi huo haukuisha, ulihamia mpaka kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kutupiana vijembe, walitoleana siri za ndani lakini Judith hakuwa radhi kusema kwamba Natasha alikuwa chakula cha mawaziri nchini Tanzania, aliogopa kwani alihisi kama angetafutwa.

Natasha alilia sana, moyo wake ulikuwa na majonzi kupita kawaida, alijiona kama kumkosa Richard kwa sababu Judith aliingilia na alikuwa mzuri zaidi yake. Hakutaka kuona akimkosa Richard, akampigia simu na kuomba kuonana naye.

“Ili?” aliuliza Richard.

Swali hilo likaufanya moyo wa Natasha kupiga paa. Hakuamini kama angeulizwa swali hilo, ilimaanisha kwamba Judith alimwambia mambo mengi mwanaume huyo kiasi kwamba hakutaka kuonana naye.

Natasha akaanza kujishtukia, akaanza kuomba msamaha hata kama hakujua kama aliwahi kumfanyia kosa lolote lile. Aliomba kuonana na Richard na mwisho wa siku mwanaume huyo kukubaliana naye.

“Ila usijaribu kujitetea, sawa?” aliuliza Richard maneno yaliyomfanya msichana huyo kushtuka.

“Sawa.”

“Basi nakuja kwako!” alisema Richard.

Mpango wote huo ulisukwa na mtaalamu Robinson. Aliuona ugomvi wa wasichana hao kwenye mitandao ya kijamii, haraka sana akampigia simu Richard na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Alimueleza kwa kina kwamba huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa kupata kile walichokuwa wakihitaji kwa nguvu zote. Richard hakuelewa ni kwa jinsi gani wangepata lakini Robinson alimwambia kuwa ajifanye kama mtu aliyeambiwa mambo mengi kuhusu msichana huyo lakini mwisho wa siku achukue simu yake na kuomba kutolewa namba za siri, aingie kwenye ile barua pepe ya iCloud na kuchukua neno la siri.

Ndani ya dakika kumi, wawili hao wakaonana nyumbani kwa msichana huyo kwa lengo la kuzungumza. Richard alijifanya kuwa na hasira mno, kila alipomwangalia Natasha alionyesha ni kwa jinsi gani moyo wake ulijaza mambo mengi, ulikuwa na hasira kutokana na yale aliyokuwa ameambiwa.

Natasha alitetemeka kwa hofu, siku hiyo alikuwa tayari kufanya lolote lile lakini si kumkosa mwanaume huyo. Wakaingia chumbani na kukaa kitandani.

Kabla ya yote Natasha akaanza kuomba msamaha, alimwambia Richard jinsi alivyokuwa akimpenda, alivyofanya mambo yake mengi kwa siri, kwa hayo yote alihitaji msamaha wake kwani moyo wake uliamini kuwa Judith alimwambia kila kitu.

“Natasha! Unaniona mimi mtoto sana,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo.

“Naomba unisamehe!”

“Nilikataa kufanya mapenzi na wewe kwa sababu nilikuwa nakuchunguza, ni kazi kubwa sana kwa msichana kuniona nikiwa mtupu, nilikuwa nakuchunguza tu na niliyoambiwa, yanatisha,” alisema Richard huku akionekana kuwa siriazi mno kiasi kwamba Natasha akawa anaogopa.

“Naomba unisamehe.”

“Hebu simu yako!” alisema Richard, moyo wa Natasha ukapiga paa! Hakukuwa na kitu alichoogopa kumpa mwanaume huyo kama simu yake.

“Simu yangu!”

“Natasha, nipe simu yako,” alisema Richard kwa hasira na sauti ya juu, huku akitetemeka, akampa simu yake mwanaume huyo na kuanza kuifungua.

“Nipe namba ya siri!”

“0088.”

Richard akaingiza na kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda kwenye upande wa picha. Huko ndipo alipokutana na majanga, aliambiwa na marafiki zake kwamba ampige picha za uchi msichana huyo lakini kwa zile picha ambazo aliziona humo zilitosha kabisa kutumiwa kwenye lile dili lao walilokuwa wamepanga.

Richard aliyahamisha macho yake na kumwangalia msichana huyo, alikuwa akitetemeka, kwa jinsi alivyoonekana tu aliogopa, alitamani asimwambie kile ambacho alikutana nacho kwenye simu ile.

“Kuna mengi sana unanificha Natasha, kwa nini?” aliuliza Richard huku akimwangalia msichana huyo.

“Naomba unisamehe! Naomba unisamehe mpenzi,” alisema Natasha huku akipiga magoti na kumuomba msamaha.

“Nipe password yako ya iCloid, nahisi kuna uchafu mwingi sana huko,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo.

“Bebi! Hakuna vitu vingine.”

“Naomba password yako ya iCloud,” alisema Richard, alijifanya kukasirika mno.

“NatashaX0X0,” alijibu.

Haraka sana Richard akafungua kwenye akaunti hiyo ambayo tayari iliandikwa natasha89@icloud.com, akaingiza namba hiyo ya siri na kuangalia kila kitu kilichokuwa humo zikiwepo picha nyingine ambazo zilifichwa sana.

Yote hayo alikuwa akiyaangalia alibaki akitabasamu, alifurahia mno, akamrudishia simu hiyo Natasha na kuanza kuzungumza naye kwa amani kabisa.

“Natasha! Kwa nini umeamua kufanya hivyo?” aliuliza Richard.

“Naomba unisamehe mpenzi!”

“Siyo tatizo! Ila kwa nini? Yaani mawaziri wote hawa umefanya nao mapenzi? Wameuona utupu wako? Why?” aliuliza Richard.

Natasha hakujibu chochote kile, alikuwa akilia, aliumia moyoni mwake, alijuta kupiga picha hizo, alitegemea kwamba zingekuwa siri, mpenzi wake huyo asizione lakini mwisho wa siku, akaziona na kumuuliza maswali mengi kuhusu picha hizo.

“Halafu unataka kufanya mapenzi na mimi! Unataka kuniua?” aliuliza Richard.

“Hapana mpenzi!”

“Basi sawa. Sharti ni moja, ukitaka kufanya mapenzi na mimi, ni lazima tukapime, upo tayari?” aliuliza Richard.

“Nipo tayari!”

Richard hakutaka kubaki mahali hapo, alimwambia Natasha kwamba siku inayofuata angemfuata na kwenda kupima afya zao na baada ya hapo wangekuwa huru kufanya mapenzi. Natasha akafurahi kidogo, yale maumivu yaliyokuwa moyoni mwake yakapungua.

Richard alipofika kwenye kituo cha bajaji, akaingia na kuondoka. Akamtumia Robinson akaunti ile na namba za siri ambapo moja kwa moja mwanaume huyo akaingia kwenye simu ya Natasha pasipo msichana huyo kugundua lolote lile.

“Bingo!” alisema Robinson huku akionekana kuwa na furaha, akaanza kuzipakua picha hizo mfululizo.





Robinson alizipakua picha zile harakaharaka, macho yake yalishangaa, hakuamini kile alichokiona. Msichana mrembo kama Natasha kulala na mawaziri wakubwa kwake lilikuwa jambo la ajabu mno.

Yeye na mawaziri ambao alipiga nao picha chumbani walikuwa watupu, aliziangalia picha hizo huku mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu, japokuwa walikuwa na mpango wa kuchukua pesa kutoka kwa Natasha lakini akaona kabisa kwamba kulikuwa na kila sababu ya kuchukua pesa kutoka kwa mawaziri hao pia.

Baada ya kumaliza na kuzihifadhi kwenye kompyuta yake akawapigia simu wenzake na kuhitaji kuonana nao, hilo halikuwa tatizo, ni ndani ya dakika ishirini wote walikuwa chumbani kwake na kuanza kuzungumza.

Kitu cha kwanza kabisa walitakiwa kuwa na namba ya simu ya siri ambayo ndiyo wangeitumia kuwasiliana na watu hao. Hilo halikuwa tatizo, walijipanga na hata namba ya namna hiyo walikuwanazo tatu ambazo waliamini kwamba kusingekuwa na mtu ambaye angewajua kwa kuwa hata vitambulisho ambavyo walijisajilia havikuwa vyao.

“Tufanyeni na Natasha, baada ya hapo, tutahamia kwa hawa mawaziri, wapo wawili,” alisema Robinson na kuwaonyeshea wenzake picha hizo.

“Sawa. Naona ni jambo zuri! Huyu Natasha tumuombe milioni tatu halafu hawa mawaziri milioni thelathini! Tupo sawa hapo?” aliuliza Richard.

“Nadhani si tatizo,” alisema Robert.

Mipango yao ilitakiwa kufanyika haraka sana, hawakuwa na muda wa kupoteza, ili kupata pesa za haraka ilikuwa ni lazima wahakikishe wanapata kile walichokitaka kwa haraka mno.

Japokuwa Robinson alitamani sana kupiga simu siku hiyo, wenzake wakakataa na kumwambia asubiri baada ya siku mbili kwa sababu kama angepiga siku hiyo basi kulikuwa na uwezekano wa msichana huyo kumgundua Richard kwamba ndiye mtu aliyekuwa amesababisha hayo.

Hilo halikuwa tatizo, wakasubiri huku Richard akimzingua Natasha kwamba alikuwa akiumwa hivyo asingeweza kufanya naye mapenzi.

Natasha aliumia mno, hakukuwa na kitu alichohitaji kwa nguvu kubwa kama kulala kitanda kimoja na Richard, alilalamika sana, alimwambia jinsi alivyokuwa akiteseka lakini kijana huyo alimwambia kwamba anaumwa.

Siku ya kumpigia simu ilipofika, Robinson akamwambia Richard ajifanye anaumwa kiasi cha kwenda kulazwa hospitalini. Hilo halikuwa tatizo, Richard akajifanya anaumwa na hivyo kwenda hospitalini na kuhitaji mapumziko.

Akawekwa humo na kulala kwa siku nzima huku akiwasiliana na Natasha kwamba aliumwa na hakuweza hata kula chakula kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia mwilini mwake.

Natasha alipoambiwa hivyo, moyo wake ulimuuma, hakutarajia kuona mtu aliyekuwa akimpenda akiumwa mpaka kufikia hatua ya kulazwa. Nyumbani hakukukalika tena, haraka sana akaondoka na kuelekea hospitalini.

Huko akawakuta vijana wote watatu, walikuwa kwenye sura za huzuni mno, Richard alikuwa kitandani huku akionekana kuwa mpole kupita kawaida. Kwa jinsi alivyoonekana kitandani pale ilikuwa ni rahisi kugundua kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa mgonjwa.

Alijipa kazi ya kuzungumza, aliongea kwa sauti ya chini na kumwambia Natasha kwamba alikuwa akiumwa mno. Msichana huyo aliumia kupita kawaida na kila alipomwangalia Richard alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.

“Utapona bebi! Utapona mpenzi wangu,” alisema Natasha huku akimwangalia Richard aliyekuwa hoi.

Walizungumza kwa muda na muda wa kuona wagonjwa ulipokwisha, wakaondoka. Ndani ya gari alionekana kuwa na mawazo tele, bado moyo wake ulikuwa na huzuni tele, alimfikiria Richard, alikuwa mwanaume mzuri, aliyekuwa akihangaika naye kufanya mapenzi lakini alikataa kwa kumpa visingizo vingi.

Alipofika nyumbani kwake, akaelekea chumbani, baada ya kuvua nguo tu simu yake ikaanza kuita, akaichukua na kuangalia namba, ilikuwa ngeni, hakutaka kuipuuzia kwani alihisi kwamba inawezekana alikuwa mtu fulani aliyekuwa akihitaji kufanya biashara ya muziki pamoja naye.

“Halo!” aliita.

“Halo! Natasha?” Aliuliza mwanaume huyo, alikuwa Robinson.

“Ndiyo! Nazungumza na nani?” aliuliza msichana huyo.

“Hutakiwi kunijua, ila nataka nikwambie kitu kimoja tu, nina picha zako za utupu, ninahitaji milioni tatu,” alisema Robinson maneno yaliyomfanya Natasha kushtuka lakini baada ya sekunde chache, akaanza kucheka.

“Unasemaje?”

“Ninahitaji milioni tatu, vinginevyo nitazivujisha,” alisikika Robinson.

Kwanza Natasha akaanza kucheka, alishangaa, hakuamini kama kulikuwa na mtu aliyekuwa na picha zake za utupu, alipuuzia na kucheka sana kiasi kwamba mpaka Robinson akakata simu kwa hasira.

Alizungumza simpo sana na ndiyo maana hata Natasha hakushtuka. Akaiweka simu yake pembeni na kuendelea na mambo yake. Baada ya muda, akasikia simu ikitoa mlio wa kuashiria kwamba kulikuwa na meseji imeingia, haraka sana akaifungua na kuanza kuisoma.

“Unajifanya una dharau sana! Njoo WhatsApp! Kuna picha zako na kesho naziweka mitandaoni,” ulisema ujumbe huo.

Natasha alitaka kupuuzia lakini kwa sababu mwanaume huyo alimwambia aende WhatsApp, akafanya hivyo na kuufungua mtandao huo.

Alikutana na picha hizo hazikuwa zikionekana vizuri hivyo akaanza kuzipakua. Zilipokuja kuonekana vizuri machoni mwake, moyo wake ukapiga paaaa.

Zilikuwa ni picha zile zile zilizokuwa kwenye simu yake, alipiga na mawaziri wakiwa kitandani tena utupu kabisa. Akahisi moyo wake ukitetemeka na kijasho chembamba kikianza kumtoka.

Hakuelewa ni kwa namna gani picha zile zilifika kwa mtu huyo, hakuwa amemuonyeshea mtu zaidi ya mawaziri hao, alishangaa mno.

Mwili ulimtetemeka, akajikuta akiwa mpole na haraka sana kumpigia simu mwanaume huyo kwa ajili ya kuzungumza naye.

Simu ikaanza kuita, iliita na kuita lakini haikupokelewa. Kawa na presha kubwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya ili kuzuia picha hizo kutokutolewa kwenye mitandao kama alivyoambiwa.

Simu haikupokelewa, alipiga zaidi ya mara kumi na nne lakini kote huko aliambulia patupu kitu kilichomfanya kutuma meseji huku akiomba sana picha hizo zisiwekwe kwenye mitandao kwa kuwa zilikuwa ni za hatari sana ambazo mawaziri wale wangehisi kwamba yeye ndiye aliziweka kwa lengo la kujitafutia kiki.

Alituma meseji nzito lakini haikujibiwa kabisa, na ndiyo kwanza simu ikazimwa. Natasha alikuwa na presha kubwa, mawazo yake hayakuwa kwa Richard, yalihama haraka sana na kufikiria hatari ambayo ingekuwa mbele yake mara baada ya picha hizo kuonekana.

“Mungu naomba unisaidie,” alisema Natasha huku akiendelea kumpigia simu Robinson lakini haikupokelewa.

Hakujua afanye nini, alibaki akiogopa mno, muda ulizidi kwenda mbele na ilipofika majira ya saa mbili usiku, akapiga tena simu ile ikapokelewa na sauti ya Robinson kusikika.

“Halo! Kaka naomba tuongee,” alisema Natasha huku akiomba sana kwani alijua kabisa kwamba kama asingefanya hivyo basi kitu ambacho kingetokea mbele ya safari kingekuwa kikubwa ambacho kingemfanya kujuta sababu ya kutokumuomba mwanaume huyo.

“Wewe ni jeuri sana! Sasa nataka kukuonyeshea mimi ni nani,” alisema Robinson.

“Naomba unisamehe kaka yangu! Naomba unisamehe!” alisema Natasha.

“Nikusamehe? Yaani wewe uliyenijibu kwa nyodo nikusamehe! Haiwezekani,” alisema Robinson na kukata simu.

Huo wote ulikuwa ni mchezo alioamua kumchezea msichana huyo, alitamani sana kumuona akiwa na presha kubwa ili wafanikiwe kile walichokuwa wakihitaji kutoka kwake.

Natasha akajua kabisa kwamba mwanaume huyo alikuwa siriazi na kama asingefanya jambo lolote lile au kumpa kile alichokuwa akihitaji basi ingekuwa balaa.

Wakati mwingine alitamani kuwaambia wale mawaziri ili awasaidie lakini hakuona kama hilo lingewezekana, kama picha hizo zilizokuwa kwenye simu yake zilionekana, basi ilikuwa ni lazima apambane yeye kama yeye lakini si kuwashirikisha watu hao.

“Naomba tuonane, naomba tuonane,” alituma ujumbe mfupi wa maneno, baada ya dakika chache, akapigiwa na kuanza kuzungumza na Robinson.

Mwanaume huyo alisistiza kwamba ni lazima picha zile alizokuwa amezipata azichukue na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii ili kila Mtanzania aone uchafu ambao alikuwa akifanya na mawaziri hao.

Natasha alilia sana, aliomba mno na mwisho wa siku Robinson kujifanya kukubaliana naye kishingo upande kwamba ataacha kuziposti kwenye mitandao kwa kuwa zile milioni tatu alizohitaji kutoka kwake zingelipwa.

“Nitakulipaje?” aliuliza.

“Unazo hapo? Una saa moja tu za kunilipa,” alisema Robinson.

“Nitakulipaje?”

“Unapajua Magomeni Usalama?”

“Ndiyo!”

“Nenda hapo, utakuta pipa la takataka, weka pesa hizo kwenye bahasha na uziweke humo. Una saa moja kumbuka,” alisema Robinson.

“Sawa! Nakwenda sasa hivi, naomba picha hizo usizisambaze pleaseeee!”

“Hilo wala usijali! Wahi Magomeni, kwenye saa moja zimebaki dakika hamsini na tano,” alisema Robinson na kukata simu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Natasha alikuwa akitetemeka, kiasi cha pesa alichokuwa ameambiwa atoe kilikuwa kikubwa lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima afanye hivyo kwa kuwa kama picha zile zingevuja basi ingekuwa balaa kwake.

Haraka sana akaondoka nyumbani kwake na kuelekea katika ATM ya Benki ya Mzalendo iliyokuwa Sinza Kijiweni ambayo ilikuwa na uwezo wa kutoa hata kiasi cha shilingi milioni tatu. Alipofika huko, akasimama kwenye foleni huku muda wote macho yake yakiwa kwenye saa yake ya mkononi.

Ilipofika zamu yake, akaingia na kutoa kiasi hicho cha pesa na kuondoka nacho kuelekea Magomeni huku akinunua bahasha na kukiweka humo. Aliendesha gari kwa kasi kama mtu aliyekuwa ameliiba sehemu.

Hakuchukua muda mrefu, akafika Magomeni ambapo moja kwa moja akateremka alipoelekezwa na kulifuata pipa la uchafu na kuitumbukiza bahasha ile na kuondoka zake huku akionekana kutokujiamini.

“Received...” (umepokelewa) alitumiwa meseji.

Robinson aliyekuwa pembeni ya kituo cha usalama huku akiwa na kofia yake akasimama na kulifuata pipa lile, alipolifikia, akaingiza mkono kwa ndani na kuchukua kiasi hicho cha pesa na kuondoka zake kwa kupanda bodaboda.

Akakutana na wenzake, kitu cha kwanza wakapongezana sana kwamba hatimaye lile dili walilokuwa wamepanga lilianza kufanya kazi hivyo walichotakiwa ni kuwasiliana na wale mawaziri wawili na kuwaambia kuhusu picha zao walizokuwanazo.

“Kwa staili hii, dola bilioni nne zitapatikana kwa haraka sana!” alisema Richard.

Wakagawana pesa hizo. Kila mmoja alikuwa na furaha, wakanunua simu za smartphone na laptop mpya kila mmoja kwa ajili ya kufanyia kazi zao kwani kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yakija huko mbele.

Wakati wakiendelea na maisha kama kawaida, Robinson akawapa wazo kwamba ilikuwa ni lazima kufuatilia vyuo vya nchini Marekani ambavyo vilifundisha sheria kwa lengo la kumpeleka Vonso aende kusoma huko.

Haraka sana wakaingia na kuanza kuangalia vyuo kumi bora. Kwenye vyuo hivyo wakakubaliana kumpeleka katika Chuo cha Kikuu cha Florida State kilichokuwa Tallahassee hukohuko Florida nchini Marekani.

Baada ya kuchagua chuo hicho wakawasiliana na Vonso na kumwambia kilichoendelea kwamba walitaka kumpeleka katika chuo hicho kwa ajili ya kusoma ambapo baadaye walijua kabisa kwamba wangefanikiwa kumtumia katika kutatua kesi zao kwa kiwango kikubwa.

Vonso aliwaangalia, kila alilokuwa akiambiwa hakuamini, alijua kama utani lakini kila alipokuwa akiwaangalia watu hao walionekana kumaanisha kwa kile walichokuwa wakikizungumza.

Kutuma maombi halikuwa tatizo, akaangalia ada yao, ilikuwa ni milioni arobaini kwa mwaka. Kilikuwa kiasi kikubwa mno lakini walimwambia kwamba wangekitoa na yeye kwenda kusoma huko Marekani kitu ambacho hakuwahi kukifikiria hata mara moja.

“Haya yote mnafanya kwa ajili yangu?” aliuliza Vonso.

“Ndiyo! Tunataka ututetee kwenye kesi zetu, zitakuwa nyingi mno, utatakiwa kuwa mtaalamu mwanzo mwisho,” alisema Robert huku akimwangalia kijana huyo.

“Sawa. Haina shida!”

***

Kanisa zima lilisimama huku likishangilia kwa furaha baada ya kutangazwa kwa tangazo maalumu kwamba Nehemiah Matimya alikuwa akijiandaa kwenda kusomea uchungaji katika Chuo Kikuu kilichokuwa Dodoma.

Mchungaji wa kanisa hilo alisimama huku akiwaangalia watu kwa tabasamu pana, kila mmoja alishangazwa kwa kilichokuwa kikiendelea, hawakuamini kama Nehemiah aliamua kwa moyo mmoja kwenda kusomea uchungaji kutokana na cheo kikubwa alichokuwanacho serikalini.

Alikuwa Waziri wa Madini nchini Tanzania, aliheshimika mno, kwake, alikuwa na uwezo wa kupata kiasi kikubwa cha pesa na kufanya alichokuwa akitaka lakini kwa moyo wake mmoja aliamua kupanga safari ya kwenda kusomea Biblia na mwisho wa siku kumtumikia Mungu katika maisha yake yote.

Aliitwa na mchungaji na kusimama mbele ya kanisa. Moyo wake ulijisikia amani na furaha kubwa, watu walimpigia makofi kwa shangwe kubwa kiasi kwamba akahisi kama alikuwa akiishi katika mlango wa wa kuingia Mbinguni.

Baada ya kuzungumziwa sana na mchungaji, naye akaanza kuwaambia watu kuhusu maono ambayo alifunguliwa na Mungu kwamba alitakiwa kuachana na mambo yote hayo na hatimaye kwenda kumtumikia Mungu.

Aliamua kwa moyo mmoja kuelekea huko kusoma, alikuwa na uwezo wa kusimamia jimbo lake na majukumu ya nchi lakini kipindi hichohicho awe akisomea uchungaji katika chuo hicho.

Pale mbele ya kanisa akaanza kuzungumzia mambo mengi kuhusu kumtumikia Mungu, jinsi alivyokuwa mtu mwema, mtakatifu ambaye kila siku alikuwa akimuabudu Mungu huku akiyaona matendo yake makuu katika maisha yake.

“Mungu ni wa ajabu sana,” alisema huku akiliangalia kanisa, akaendelea:

“Nimekuwa nikimtumikia Mungu katika maisha yangu yote, amenitendea mambo makubwa na ndiyo maana nimeamua kwenda kumtumikia,” alisema Nehemiah huku akiliangalia kanisa.

Aliendelea kuzungumza mambo mengi na baada ya hapo, akarudi kwenye kiti na ibada kuendelea. Muda ulizidi kwenda, baada ya kumalizika tu huku akianza kusalimiana na watu wengine, simu yake ikaanza kuita, kuangalia, namba ilikuwa ngeni, akaomba radhi kwa watu aliokuwa akizungumza nao na kuipokea.

“Halo! Waziri a.k.a mzee wa mademu mambo vipi?” alisalimia mwanaume aliyekuwa upande wa pili, Nehemiah akashtuka.

“Umeniitaje?”

“Ingia WhatsApp kwanza! Utakachokikuta wasiliana nami, una saa tano za kufanya ninachokitaka,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.

Nehemiah hakutaka kusumbuka, alichohisi ni kwamba mtu huyo alikuwa mmoja wa matapeli, hakutaka kwenda WhatsApp kuangalia kuna nini zaidi ya kuendelea na mambo yake.

Alizungumza na watu wengi, walimsifia kwa uamuzi sahihi aliokuwa ameufanya na baada ya dakika kadhaa akaichukua familia yake na kuondoka kuelekea nyumbani.

Alipofika huko, akaendelea na majukumu yake kama mzazi, wakati hayo yakiendelea ndipo akakumbuka kuhusu ile simu aliyokuwa amepigiwa akiwa kanisa. Alipewa saa tato na hapo zilibaki saa mbili tu, haraka sana akaingia WhatsApp kuona kulikuwa na nini.

Alipoingia humo, akakuta ametumiwa picha mbili, akazipakua na kuziangalia. Moyo wake ukapiga paaa! Hakuamini alichokuwa akikiona, kulikuwa na picha yake na Natasha wakiwa kitandani uchi wa mnyama na nyingine wakiwa wanapapasana.

Alishtuka, kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Mtu wa kwanza kabisa ambaye alimfikiria kwenye kichwa chake alikuwa Natasha, huo ulikuwa mtihani mzito ambao hakuutegemea kuupata hasa katika kipindi kama hicho.

Alibaki akitetemeka, aliogopa, alijijua jinsi alivyokuwa, siku hiyo alitoka kanisani, alisimama mbele ya kanisa na kusema kwamba aliamua kumtumikia Mungu na siku hiyohiyo akatumiwa picha hizo.

Aliogopa, alihisi kabisa kwamba mtu huyo alitaka kwenda kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii. Kama angefanya hivyo lingekuwa jambo baya sana katika maisha yake, alitakiwa kupambana kuhakikisha picha hizo hazitolewi kwenda sehemu yoyote ile.

“Huyu atakuwa Natasha,” alisema huku akionekana kuwa na hasira.

Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akamuaga mkewe kwamba alipigiwa simu ya kazi hivyo kuondoka. Ilikuwa ni haraka mno, alipofika sehemu nzuri akampigia simu Natasha na kuanza kuzungumza naye.

Kwanza alimlaumu kwa alilolifanya, hakutakiwa kuzisambaza picha zile kwa watu kwani wakati wanapiga walikubaliana kwamba ziwe picha zao wawili, asizione mtu yeyote yule, walikubaliana.

“Sikumpa mtu picha hizo,” alisema Natasha.

“Sasa amezipataje?”

“Hata mimi sijui! Mimi mwenyewe nimetumiwa, yaani nimechanganyikiwa,” alisema Natasha, hakuishia kumwambia hivyo tu bali akascreenshot mawasiliano yake na Robinson na kumtumia.

Waziri huyo alibaki akitetemeka, hakujua mwanaume huyo alihitaji nini, kama zile picha zingevujishwa basi lingekuwa jambo baya sana katika maisha yake. Kanisa lake lingemuona mnafiki, Tanzania ingemuona kuwa waziri wa hovyo kuliko wote waliowahi kupita katika nchi hiyo.

Haraka sana akawasiliana na Robinson na kumuomba mno asizisambaze picha zile kwani angempa kitu chochote ambacho alikihitaji kutoka kwake.

“Hahaha! Hapana! Pesa ninazozihitaji huwezi kunilipa, ni lazima nizisambaze WhatsApp,” alisikika Robinson, alianza kumpiga mkwara ili aonekane kwamba hakuwa mtu wa kupenda pesa, alichokuwa akikihitaji ni kuzisambaza tu.

“Nakuomba! Nakuomba! Nipo chini ya miguu yako!”

“Hahaha! Hivi unahisi mimi naweza kununuliwa kirahis hivyo? Hakuna chini ya jua,” alisema Robinson.

Kiasi walichokuwa wakikihitaji kilikuwa ni milioni thelathini lakini baada ya kugundua kwamba cchuo kile alichotakiwa kwenda kusoma Vonso ada yake ilikuwa ni milioni arobaini waliona ni lazima wafanye jambo ili pesa zote hizo zitolewa kwa mtu mmoja.

Lengo la kujifanya kutokuhitaji pesa lilikuwa ni kumfanya mwanaume huyo aongeze dau yeye mwenyewe vinginevyo angezisambaza picha hizo. Kwa kuwa Nehemiah alikuwa akiogopa, akamwambia kwamba angemtumia milioni hamsini ili picha hizo zisisambazwe.

“Milioni hamsini?” aliuliza Robinson kwa dharau.

“Naomba unisaidie! Nionee huruma, najua kwamba nilifanya uchafu, naomba unionee huruma,” alisema Nehemiah, alikuwa ndani ya gari lake alilolipaki sehemu, kwa jinsi alivyokuwa akongea mpaka machozi yalikuwa yakimtoka.

“Haiwezekani!”

“Naomba unisaidie mimi kama baba yako, nisaidie mimi kama ndugu yako,” alisema Nehemiah.

Japokuwa Robinson alijifanya kukataa sana lakini mwisho wa siku akakubaliana naye na hivyo kumwambia amtumie milioni hamsini haraka sana vinginevyo ngezisambaza picha hizo haraka sana.

Kiasi alichokuwanacho kilikuwa ni milioni kumi tu, benki hazikuwa zimefunguliwa siku ya Jumapili, akawapigia marafiki zake ambao walimsaidia pesa hizo kwa ahadi ya kuzilipa siku inayofuata na hivyo kuwasiliana na Robinson.

“Ninazo hapa!”

“Unapajua Tandale?”

“Ndiyo! Huwa ninapita bosi!”

“Kuna sehemu inaitwa Mbuyuni, nenda hapo, utamkuta fundi viatu, ukifika mgawie hizo pesa. Yaani ukichelewa hata dakika ishirini tu, picha zako zitasambzwa dunia nzima, nitawatumia na Global Publishers wazitoe gazetini,” alisema Robinson.

“Nitafanya hivyo, naomba usizsambaze,” alisema Nehemiah.

Wakati wakizungumza, tayari upande wa pili Robert alijipanga na kuelekea Tandale, huko akatafuta meza ndogo, akanunua viatu, alipofika huko akavipanga na kuchukua kiwi na blashi na kujifanya kama alifungua fundi viatu mahali hapo.

Wakazi wa eneo hilo walibaki wakimshangaa, mwanaume huyo aliwashangaza, alikuwa kijana msafi sana, alivalia vizuri na alichomekea, kufungua kwake ufundi wa viatu ulimshangaza kila mtu kwani ilikuwa ni ghafla sana.

Baada ya saa moja, gari la kifahari likasimama barabarani, mwanaume mmoja aliyevalia kofia akateremka na kumfuata Robert, alipomfikia, akampa ile bahasha, akarudi garini na kuondoka zake.

Robert alipoona ameondoka, naye akasimama, akaacha kila kitu mahali hapo na kutokomea huku akiwaacha watu waliokuwa hapo wakijiuliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea? Kila walipojiuliza, wakakosa jibu, waziri Nehemiah alipigwa milioni hamsini kirahisi sana ili picha zake alizokuwa utupu chumba na msanii Natasha zisivujishwe kama alivyoambiwa.





Upinzani wa vyama vya siasa nchini Tanzania ulikuwa ukitikiza, kila kona wanasiasa ilikuwa ni kupeana madongo kwenye majukwaa kwamba mtu fulani alifanya hivi na vile hivyo hakutakiwa kabisa kuongoza jimbo fulani.

Hali ilikuwa mbaya kwa wanasiasa, skendo zilikuwa zikichukuliwa kutoka sehemu za siri na kupelekwa sehemu nyingine kabisa, watu wengi walipata aibu, kipindi hicho kilikuwa ni cha hatari ambacho wagombea wengi walitakiwa kuwa makini na maisha yao.

Watu waliokuwa na siri za viongozi fulani walikuwa wakipigiwa simu na kupewa pesa, muda huo haukuwa wa kuchafuana, kila mmoja alitakiwa kupambana na hali yake.

Katika kipindi hicho ambacho uchaguzi mkuu nchini Tanzania ulitakiwa kufanywa ndicho kilikuwa kipindi ambacho watu wengi walikuwa wakiuawa. Wale waliobeba siri kubwa za viongozi walitekwa na kupelekwa kusipojulikana na baada ya siku kadhaa maiti zao zilikutwa kwenye viroba ufukweni.

Hali ilikuwa ni mbaya, kila mmoja aliogopa, wale waliokuwa na siri kubwa za viongozi wengi walijificha, hawakutaka kugundulika na hata wale waliokuwa na siri kubwa zaidi waliamua kuwauzia wanasiasa kwa makubaliano ya kutokutajwa sehemu yoyote ile.

Wakati huo Waziri Wa Fedha, Peter Kisiju alikuwa jimboni kwake Kinondoni akiendelea na kampeni kama kawaida yake. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, alijua jinsi alivyokuwa akikubalika, kila kona alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha mwaka huo anaondoka na kura nyingi na kuwashinda wapinzani wake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wakati akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Biafra Kinondoni ndipo akapigiwa simu na mwanaume mmoja na kuanza kuzungumza naye. Alikuwa Robinson, alimpigia simu na kumwambia kwamba alikuwa na picha zake za utupu ambazo alipiga akiwa na msichana aliyekuwa na jina kubwa kipindi hicho, Natasha.

Kwanza akacheka sana, alijua dhahiri kwamba huo ulikuwa ni uongo, hakutaka kuzungumza kitu chochote zaidi ya kmwambia kwamba angempigia baada ya mkutano ili waongee vizuri.

Muda wa kusimama ulipofika, akaanza kuhutubia huku akiwaomba watu kura zao. Alisimama imara, hakuwa mwanaume wa kuteteleka, alikuwa na roho mbaya iliyomfanya afanye mauaji mengi kwa watu waliokuwa wakisimama mbele mbele ya kumuwekea zengwe.

“Eti kuna kijitu kinajitokeza porini na kusema kwamba kana picha zangu cha utupu, hivi hizi adobe photoshop ndizo zinawafanya watu kuedit na kutuwekea vipicha vya utupu ili kutuchafua, sasa tunasema hivi, tumewashtukia. Hebu tuseme wote TUMEWASHTUKIAAAA...” alisema na uwanja mzima kulipuka.

“Tumewashtukiaaaa...” walisema.

Huyo ndiye mwanaume aliyekuwa na jina kubwa, kila alipopita watu walimuheshimu na kumshangilia, alipigiwa makofi kila kona kwa kuonekana kuwa mtu mahiri ambaye alipambana kuhakikisha anakuwa hapo alipofika.

Baada ya dakika kadhaa akamaliza na kuelekea kwenye kiti na kukaa. Moyo wake haukuwa na hofu kabisa, hakukumbuka kama aliwahi kupiga picha za utupu na msichana yeyote yule, aliijichukulia kuwa mwanaume msafi ambaye hakutaka kuona mambo ya kijinga mbele yake.

Baada ya saa moja akaanza kurudi nyumbani kwake. Ndani ya gari akapigiwa simu na Robinson na kuambiwa vilevile kuhusu picha zake, muda huo kijana huyo akaamua kumtumia kabisa.

Kisiju akaifungua picha hiyo na kuanza kuiangalia. Aliikumbuka mno, yeye mwenyewe alishangaa ni kwa namna gani mtu huyo alikuwa na picha hiyo kwani alikumbuka kabisa kwamba aliipiga kwa siri yeye na Natasha na haikuwa hiyo tu bali kulikuwa na picha zingine tatu.

Haraka sana akampigia simu Natasha na kuanza kuzungumza naye. Alimuuliza kuhusu picha hizo, msichana huyo akashtuka, hakuamini kama mtu huyo aliituumia nafasi hiyo kumuonyeshea picha hizo waziri kwa lengo la kuchukua pesa kutoka kwake.

“Hapana! Sikumpa picha...bebi nina wakati mgumu sana,” alisema Natasha huku akilia.

“Wakati gani? Kuna jambo gani limetokea, hebu niambie,” alisema Kisiju.

Natasha hakuwa na la kufanya zaidi ya kumwambia kuhusu simu yake. Alimdanganya kwamba iliibwa na mtu mmoja chuoni alipokuwa akisoma na mtu huyo alilijua neno lake la siri na ndipo alipoziona picha zile na kuanza kumsumbua.

“Alizijuaje? Hivi iPhone unafananisha na visimu vya android?” aliuliza Kisiju, alizijua sana simu hivyo akagundua kabisa kwamba Natasha alikuwa akimdanganya.

“Kweli bebi! Kuna mtu ameiba simu yangu, alinipigia na kuchukua pesa kutoka kwangu. Mpenzi niamini, nimechanganyikiwa,” alisema Natasha na kuanza kulia.

Kisiju alikasirika, akakata simu akiwa na hasira nzito na kutulia chumbani kwake. Alipanga mipango mingi, suala la picha hizo hakutaka kabisa kuona likimuumiza kichwa chake. Wakati akiwa amekaa hapo, akapigiwa simu na Robinson na kuanza kuzungumza naye.

“Nikusaidie nini?” aliuliza.

“Nina picha zako!”

“Kwa hiyo?”

“Ninahitaji milioni hamsini, vinginevyo kesho utazikuta kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Robinson.

“Mbona unachelewa sana kuzitoa? Ziweke sasa hivi basi mpumbavu wewe,” alisema Kisiju na kukata simu.

Upande wa pili Robinson alishtuka, hakuamini kama kulikuwa na mwanaume aliyekuwa mbishi kama Kisiju, aliwaambia wenzake kilichotokea kwamba mwanaume huyo aliruhusu picha zake ziwekwe kwenye mitandao hata kama alikuwa utupu kabisa kitandani lakini si kutoa pesa.

Richard na Robert walishangaa, walimuuliza mara mbilimbili Robinson lakini majibu yake yalikuwa yaleyale kwamba mwanaume huyo aliruhusu hilo litokee tena aliongea kwa kujiamini na kumwamwambia awahi kufanya hivyo.

“Jamani! Kuna hela hapa tena ama tunapoteza muda?” aliuliza Robinson huku akiwaangalia wenzake.

“Hapana hakuna hela!” alijibu Richard.

“Hapana! Pesa ipo, unajua ipo vipi?” alisema Robert na kuuliza swali.

“Kivipi?”

“Subiri!”

Alichokifanya ni kuwapigia simu marafiki zake na kuwaomba namba ya mwenyekiti wa chama cha upinzani ili awasiliane naye kuhusu picha zile alizokuwanazo.

Kuzipata namba za mwanaume huyo halikuwa tatizo, akapewa na hivyo kuwasiliana naye na kumwambia kwamba alikuwa na habari njema ambayo ingewashtua watu wote ambao wangekwenda kuisikia na kuona.

“Habari gani?” aliuliza mwenyekiti aliyeitwa kwa jina la Maliki.

“Kwanza mnalitaka jimbo la Kinondoni?” aliuliza.

“Ndiyo! Kuna nini lakini?”

“Basi mmeshalichukua!”

“Kwa nini?”

“Nina picha za utupu za huyu Kisiju akiwa kitandani na demu flani staa,” alisema Robert.

“Unasemaje?”

“Habari ndiyo hiyo ngoja niseti mitambo nikutumie, waambie na wenzako, nakutumia,” alisema Robert na kukata simu.

Hiyo ndiyo ilikuwa njia ya mwisho kabisa ambayo waliamini kwamba ni lazima mwanaume huyo achanganyikiwe baada ya kuona kwamba suala la picha zake lilifika mpaka kwa chama cha upinzani. Robert alimwambia kwamba awaambie wenzake kwa lengo la mmojawapo kutoa siri na kuzungumza na mwanaume huyo.

Hilo likafanyika, Maliki akawaita watu wake na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea kwamba alipigiwa simu na kijana mmoja na kumwambia kuhusu picha hizo. Hilo lilikuwa jambo kubwa ambalo lilionyesha kabisa kwamba walikuwa wakienda kushinda vita hivyo.

Kama ambavyo Robert na wenzake walivyohisi ndivyo ilivyotokea, ni ndani ya nusu saa tu tayari Kisiju alikuwa na taarifa kuhusu picha zake. Kwanza akashtuka, hakuamini kama kweli mwanaume huyo angewasiliana na upinzani na kuwaambia kuhusu picha hizo.

Kama kweli picha zingekabidhiwa kwa Maliki ilikuwa ni lazima kuzitoa, chama chake kingesemaje? Hata ile nguvu ya kusema kwamba zimeeditiwa isingekuwa na nguvu kwa kuwa zilifika mikononi mwa mtu aliyekuwa akijulikana na kuaminika sana nchini Tanzania.

Akawaita wenzake na kuzungumza nao, alihitaji ushauri ni kitu gani alitakiwa kufanya kwani vinginevyo picha hizo zilikuwa zikienda kuvuja na kulikuwa na uwezekano mkubwa wanachama wakashinikiza atolewe kwenye kinyang’anyoro hicho.

“Kwa hiyo tufanyeje?” aliuliza Kisiju.

“Tumuue mtoa taarifa,” alisema mwanaume mmoja.

Huo ndiyo uamuzi uliokubaliwa, ilikuwa ni lazima wamuue Robinson kwa sababu alikuwa na picha za utupu alizokuwa amepiga na mwanamuziki Natasha.

Haraka sana akampigia simu Robinson na kuanza kuzungumza naye, kwanza kitu cha kwanza kilikuwa ni kumuomba sana asifanye kile alichomwambia kwani vinginevyo alikuwa akienda kudhalilika kwa kuzitoa picha hizo.

“Naomba unisamehe kwa kukukaripia, nipo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa,” alisema Kisiju huku akijifanya kuwa na hofu kumbe hakuwa na lolote lile.

“Umejifanya mbishi sana, sasa utatoa milioni sitini!” alisema Robinson.

“Nipo tayari! Naomba msitoe picha zangu, nawaombeni sana, nifichieni hii aibu,” alisema mwanaume huyo.

Aliomba sana na ndipo Robinson akakubaliana naye na kumwambia baada ya dakika kadhaa angemwambia ni wapi alitakiwa kuzipeleka pesa hizo, ampe na kufanya mambo yake.

“Vipi?” aliuliza mwenzake.

“Kila kitu tayari! Sasa cha kufanya, popote atakaposema picha zipelekwe, vijana wanatakiwa kuwepo, baada ya kuchukua pesa hizo, achukuliwe na kutekwa haraka sana. Sawa?” aliuliza Kisiju.

“Sawa.”

Baada ya nusu saa Robinson akapiga simu na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia kwamba maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam pembeni ya kituo cha Mafuta cha TSN kulikuwa na pipa la takataka, hapo ndipo alipotakiwa kwenda na kuzitumbukiza pesa hizo kisha aondoke haraka sana.

Hilo halikuwa tatizo, simu ilipokatwa, akawaambia vijana wake waondoke na kuelekea huko, walipofika, wakajifanya kuwa bize na mambo yao huku wakiliangalia pipa dogo mfano wa ndoo kubwa ambalo lilikuwa limewekwa tayari eneo moja mahali hapo kama mita nne kutoka kwenye mtaro.

Baada ya dakika kadhaa mwanaume mmoja akatokea akiwa na mfuko mkubwa na kwenda kuuweka kwenye pipa lile kisha kuondoka. Vijana wale waliokuwa pembeni wakajiandaa, mtu yeyote yule ambaye angekwenda mahali pale ilikuwa ni lazima achukuliwe, atekwe na kupelekwa sehemu ya siri.

Wakati hayo yote yakiendelea, Robinson alikuwa njiani akielekea kule eneo la tukio, alipofika Mwenge, akateremka na kwenda karibu na mahali pale na kuanza kuangalia huku wanaume wale wakiwa pembeni wakifuatilia kila kitu, walitaka kumuona huyo mtu ili wakamteke, hata walipomuona Robinson, hawakugundua kama ni yeye, walitaka kuona mpaka atakapokwenda katika pipa lile na kuchukua pesa hizo ndipo wafanye yao.





Vijana watatu waliokuwa na akili walikuwa wakijadili ni kwa jinsi gani walitakiwa kupata kiasi cha milioni sitini kutoka kwa Waziri Kisiju ambaye alisema kwamba alikuwa tayari kutoa kiasi hicho cha pesa ili picha zake zisisambazwe kwenye mitandao ya kijamii.

Alikubaliana nao hivyo kutaka kujua ni mahali gani makabidhiano hayo yalitakiwa kufanyika. Kabla ya kujibu, kwanza Robinson akakata simu na kumwambia kwamba wangewasiliana.

Ilikuwa ni lazima watafute sehemu ambayo ingekuwa salama kwao kufanya makabidhiano hayo. Walizungumza kwa dakika tano tu, walichogundua ni kwamba inawezekana kabisa waziri huyo alikuwa na mpango wake wa siri aliotaka kuufanya kwao, ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanamuepuka na kupata pesa hizo kilaini.

Wakati wakifikiria ni kwa namna gani wangeweza kuchukua pesa hizo kutoka kwake ndipo Richard aliwaambia kwamba pembeni ya sheli ya TSN iliyokuwa Mwenge kulikuwa na sehemu iliyokuwa na mtaro, huo mtaro ulipita karibu na shimo kufulani ambalo kwa juu lilifunikwa kwa chuma ambapo kwa ndani yake kulikuwa na maji machafu.

“Jamani! Kuna sehemu nimeipata,” alisema Richard huku akiwaangalia wenzake ambao walibaki wakimsikiliza.

Aliwaambia kuhusu sehemu hiyo, aliwaelezea kwamba kama kweli walitaka kwenda kuchukua pesa kutoka kwa mwanaume huyo basi wamwambie kwamba alitakiwa kwenda kuziweka pesa katika mfuniko wa shimo hilo ambalo kwa chini kulikuwa na mfereji wa kupitisha maji machafu.

“Halafu!”

“Robert! Ila si unajua mahali shimo hilo lilipo? Pembeni kidogo mwa barabara,” alisema Richard.

“Nadhani nitapafahamu nikipaona, kwa hiyo baada ya hapo?”

“Tunatakiwa kupata pipa dogo mfano wa debe au mfano wa ndoo kubwa ambapo kwa chini tutalitoboa usawa wa lile tundu la shimo, chini ya hilo pipa tutapatoa kote na kuweka makaratasi kama takataka,” alisema Richard.

Mpango wake ulikuwa mkubwa sana, kwa sababu yeye ndiye alikuwa mratibu wa mambo hayo, akawaambia wenzake kwamba alitakiwa kuondoka mahali hapo na kwenda huko.

Haraka sana akaondoka akiwa na begi la nguo mbayambaya, breki ya kwanza ilikuwa ni kwenda kununua hilo pipa dogo, akalipeleka kwa mkataji na kulikata kwa chini na hivyo kuwa wazi pande zote mbili, yaani chini na juu.

Alipomaliza, akaondoka na kuelekea Mwenge. Alipofika njiani, akaingia kwenye choo cha kulipia, kwa kuwa alikuwa na nguo zake mbayambaya, akazitoa na kuzivaa kisha kutoka.

Alitakiwa kuwa makini, mchezo ambao walikuwa wakienda kuucheza ulikuwa hatari lakini ungewafanya kupata mamilioni ya pesa na kuondoka nazo.

Hakuchukua muda mrefu akafika Mwenge, kwa jinsi alivyokuwa akionekana, alivyo mchafu ilikuwa ni rahisi kusema alikuwa muokota chupa za maji, alikuwa na gunia lake chafu na alikwenda moja kwa moja na pipa lake dogo kama ndoo kubwa na kwenda kwenye lile shimo kwa barabarani.

“Kwanza niutoe huu mfuniko,” alijisemea na kuanza kuuvuta.

Ilikuwa barabarani, watu walikuwa wakimwangalia lakini hakuonekana kujali, kwa chini kulikuwa na maji machafu ambayo yalikuwa yakiendelea kupita, hakujali, aliuvuta mfuniko mpaka ulipotoka, akalichukua pipa lile na kuliweka pale kisha kuchukua makaratasi mengi kuyatumbukiza ndani ya pipa hilo kwa lengo la kuziba tundu lile kwa chini na pia ionekane kama kulikuwa na takataka zilizowekwa.

Baada ya kumaliza akachukua simu yake na kumpigia Robinson na kumwambia awaambie watu hao waonane mahali hapo na kwenda kuziweka pesa hizo kwenye pipa hilo.

Alipomaliza kuongea huku akiwa na mfuniko wa chuma wa lile shimo, akaondoka na kwenda mtaroni upande wa pili wa barabara, akaingia, kulikuwa na maji machafu lakini hakutaka kujali, watu waliomuona, wengine wakahisi kama alikuwa kichaa kutokana na uchafu mwingi aliokuwanao.

Ubishoo aliuweka pembeni, akaingia mtaroni, akatambaatambaa mpaka usawa wa lile shimo, akaingia huko. Kulikuwa na maji machafu, yalimmwagikia lakini hakutaka kujali, alizidi kwenda mbele zaidi ndani kwa ndani, umbali kama wa mita kumi ndipo akafika usawa wa lile pipa kwa chini, akaangalia kwa juu, akayaona yale makaratasi na kutulia hukohuko chini akisubiri huo mzigo wa pesa uletwe, auchukue na kuondoka nao.

Alisubiri kwa dakika kama arobaini na tano, ulikuwa muda mchache lakini harufu mbaya ya mule, panya kulimfanya kuona kama alikaa kwa saa ishirini na nne, dakika hizo zilipotimia tu, akasikia kitu kikiangushwa ndani ya pipa hilo. Haraka sana akachukua simu yake na kumpigia Robinson.

“Vipi?” aliuliza.

“Mzigo umewekwa,” alisema.

Kwa taratibu mno akaipitisha mikono yake, akaanza kuyatoa makaratasi hayo kwa kuyavuta kwa chini, yakatoka mpaka alipoufikia mfuko uliokuwa na pesa na kuuvuta kwa chini, akauweka ndani ya bei lake na kuanza kuondoka kwa kutambaa kwa kushika huku na kule kuelekea kwenye ule mtaro.

Hakutumia dakika nyingi, akafika kwenye mtaro huo ambapo akaendelea mbele mpaka kama mita kumi na tano, akasimama na kuanza kuondoka zake huku watu wakimuona kama mtu fulani aliyekuwa akiokota makopo au kichaa fulani pasipo kujua kwamba begi alilokuwa amelibeba lilikuwa na milioni sitini.

Akamwambia Robinson kwamba alichukua mzigo huo, vijana hao wakachukuana na kuondoka, walipopanda daladala akampigia simu Waziri Kisiju kwa lengo la kuongea naye.

“Mbona kimya, nakusubiri sana hapa uje kuchukua huo mzigo,” alisema Waziri Kisiju kana kwamba alikuwa eneo la tukio.

“Mzigo nishachukua. Nashukuru sana! Tutaonana miaka mingine,” alisema Robinson huku akicheka, akakata simu.

Waziri Kisiju aliposikia hivyo, hakuamini, haraka sana akawasiliana na vijana wake waliokuwa huko na kuanza kuwaambia kile alichoambiwa. Hawakuamini, walimwambia kwamba walikuwa hapo muda wote na hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikwenda kuchukua zile pesa zilizokuwa kwenye lile pipa.

“Mnasema hakuna mtu aliyekwenda?” aliuliza Kisiju.

“Ndiyo bosi! Hakuna!”

“Hilo pipa mnaliona?”

“Ndiyo! Tunaliangalia na tupo nalo makini sana!” alijibu kijana wa upande wa pili.

“Na hakuna aliyekwenda kuchukua hizo pesa?”

“Hakuna bosi!”

“Mbona kijana ameniambia tayari amechukua? Hebu kaangalieni kama zipo,” alisema.

Vijana hao walikuwa na uhakika kwamba hakukuwa na mtu aliyekwenda kwenye lile pipa na kuchukua pesa hizo, walipolifikia na kuangalia, walichokiona hawakuamini macho yao.

Chini waliona shimoni huku maji machafu yakipita, hakukuwa na pesa hata kidogo. Kwa hasira huku wakionekana kuchanganyikiwa wakaliondoa lile pipa, sehemu hiyo ilitakiwa kuwa na mfuniko wa chuma, haukuwepo na tayari watu walifanya yao kwa kuchukua pesa hizo na kuondoka nazo.

Wakalifuatilia hilo shimo ambalo kwa ndani kulikuwa na mfereji wa maji machafu, ulikwenda mpaka kwenye mtaro wa pembezoni mwa barabara ambapo walipofika hapo, wakayaona yale makaratasi yaliyokuwa mule kama uchafu yakiwa hapo.

“Tumepigwa!” alisema mwanaume mmoja.

Wakampigia simu bosi wao, Kisiju na kumwambia kwamba mwanaume huyo alizichukua pesa hizo kwenye mazingira ambayo ni vigumu kuamini kama yangefanyika nchini Tanzania.

Kisiju hakuamini, alichoambiwa kilionekana kama mchezo wa maigizo, milioni sitini zilikuwa nyingi mno, alikuwa na uhakika kwamba mtu huyo asingezipata, hivyo akaenda yeye mwenyewe kwenda kuhakikisha.

Alichoambiwa ndicho alichokutana nacho, mwanaume ambaye alimpigia simu lijipanga mno, alijua kucheza mchezo hatari ambao ulikuwa mgumu kwa mtu yeyote yule kugundua kama ungechezwa.

“Ameondoka na mamilioni yangu, ameondokaje na pesa zangu?” aliuliza huku machozi yakianza kumlenga, kila alipokuwa akiuangalia ule mtaro wa maji machafu, alishindwa kuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angepenya moja kwa moja mpaka kwenye shimo lile lililokuwa upande wa pili ambapo mfereji wake ulipita katikati ya barabara kwa chini.

Wakati yeye akiendelea kulalamika, Robinson na wenzake wakakutana na kuanza kupongezana. Kiasi cha shilingi milioni sitini kilikuwa kikubwa mno, walipanga kugawana milioni ishirini kila mmoja lakini wakakumbuka kwamba kulikuwa n Vonso ambaye alitakiwa kwenda Marekani kusoma.

Wasingeweza kuchukua pesa zao japokuwa walikubaliana hilo. Taama ya pesa ikawaingia, wakaona pesa tamu hivyo walichokubaliana ni kwenda mahali kukopa kiasi cha shilingi milioni mia moja kuahidi kurudisha baada ya miaka mitano.

“Mh! Benki zitaweza kutukopesha kweli?” aliuliza Richard, kiasi hicho kilikuwa kikubwa mno.

“Nadhani! Tufungueni biashara, halafu twende tukakope,” alisema Robert.

“Hapana! Hapo tutakuwa tunajichelewesha, kwa nini tusizungumze na Upendo?” aliuliza Robinson.

“Upendo yupi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Upendo Massawe, yule demu anaweza kutusaidia, tumuiteni tuzungumze naye,” alisema Robinson.

Upendo Massawe alikuwa binti wa mfanyabiashara mkubwa Massawe aliyekuwa na biashara nyingi Afrika. Baba yake alifanikiwa mno, alikuwa na pesa nyingi huku akitajwa kuwa bilionea wa kwanza nchini Tanzania.

Upendo aliishi maisha aliyotaka, alifanya alichokitaka na kwenda popote pale alipojisikia kwenda. Hakuwa mtu wa starehe, alikuwa msichana wa kushinda sana chuoni na jioni kurudi nyumbani.

Alimiliki gari aina ya Aston Martin, lilikuwa na gharama zaidi ya milioni mia sita lakini cha kushangaza hakutaka kabisa kulitumia gari hilo, kila alipokuwa akienda chuo alichukua gari yake ya kawaida aina ya Vitz na kuelekea huko.

Watu walichukia, wengine walitamani sana wawe na utajiri wa baba yake lakini msichana huyo hakuwa na habari. Akaunti yake ilikuwa na pesa nyingi, zaidi ya bilioni moja lakini maisha yake yalikuwa ya kawaida mno.

Mbali na utajiri aliokuwa nao, biashara alizokuwa akizisimamia za baba yake sifa nyingine aliyokuwanayo Upendo ulikuwa ni ubaya wa sura.

Upendo alikuwa mbaya, tena mbaya hasa. Wanaume hawakutaka hata kumwangalia mara mbili, hakuvutia, mbali na ubaya huo wa sura yake lakini hakuwa na umbo zuri, alikuwa mnene ambaye kwa kumwangalia ilikuwa ni vigumu kujua kiuno kilikuwa wapi.

Alikuwa tipwatipwa na hata jinsi alivyokuwa akitembea ilikuwa ni rahisi kujua kwamba muda wowote ule angepiga mwereka.

Katika maisha yake yote mpaka kipindi hicho Upendo alikuwa msichana bikira, hakuwahi kuguswa na mwanaume yeyote yule kwa sababu hao wanaume wenyewe hawakutaka kuwa na msichana kama yeye.

Hilo lilimpa wakati mgumu mno. Alikuwa na pesa ila bila kuwa na mwanaume likaonekana kuwa tatizo kwake. Akajitahidi kuwatongoza wanaume mbalimbali lakini kitu cha ajabu kabisa hakukuwa na aliyetaka kuwa naye hata kidogo, ndiyo alikuwa na pesa lakini kuwa na mwanamke kama Upendo ilikuwa ni aibu mno.

Alikuwa akilia tu chumbani kwake, alipenda wanaume wengi lakini hakuwa na uwezo wa kuwapata na hakujua angetumia njia gani kuwanasa kwani hata zile pesa alizokuwanazo hazikuonekana kumsaidia hata kidogo.

Huyo ndiye ambaye Robinson alimkumbuka, alijua kwamba alikuwa na pesa hivyo ilikuwa ni lazima amfuate na kumuomba msaada. Hakuwa na namba yake, ila kuipata haikuwa tatizo, akaomba kwa wanafunzi wenzake, alipopewa tu, akaanza kumpigia.

“Halo!” aliita.

“Halo! Naongea na nani baby?” aliuliza msichana huyo, alikuwa na hamu ya kuwa na mpenzi na ndiyo maana kila aliyempigia simu na kugundua alikuwa mwanaume, alimuita bebi kuona kama angebahatika kuwa naye.

“Unaongea na Robinson. Naweza kukuona hapa Utawala?”

“Hakuna tatizo beby! Nipe dakika kadhaa!” alisema Upendo na kukata simu.

Ni ndani ya dakika tano tu msichana huyo akawa mahali hapo. Alikutana na wanaume watatu ambao walimchangamkia sana, aliwaangalia huku moyo wake ukijisikia amani kabisa, uliburudika kuliko siku zote.

Kila aliyekuwa akipita aliwashangaa watu hao, kwa nini walimuita Upendo na kutaka kuongea naye na wakati alikuwa mbaya namna ile. Wao hawakutaka kujali, walichohitaji kilikuwa ni pesa, hivyo wakamvuta pembeni, wakakaa sehemu na kuanza kuzungumza naye.

Kwanza walimwambia mambo mengi, mipango yao ya kufungua biashara na kuwa mabilionea wakubwa. Upendo alifurahi kwani hakukuwa na kitu alichokuwa akikipenda kama kufanya biashara. Aliwaangalia, akatoa tabasamu.

“Tunahitaji msaada wako Upendo!” alisema Robinson.

“Upi?”

“Tunahitaji utukopeshe milioni mia moja, halafu tutakurudishia ndani ya miaka mitano, tunakuahidi na hata kuandikishana tuandikishane,” alisema Robinson huku akimwangalia msichana huyo.

“Mna uhakika mtanirudishia?”

“Ndiyo! Tutakurudishia!”

“Mna uhakika?”

“Ndiyo!”

“Basi pesa si tatizo na hata kuandikishana si tatizo pia, kama kweli mtanirudishia, nitawakopeni ila kwa sharti moja dogo,” alisema Upendo huku akiwaangalia, tabasamu halikuisha usoni mwake.

“Lipi?”

“Ndani ya hiyo miaka mitano, nataka mniruhusu niwe na uhusiano wa kimapenzi na huyu Richard!” alisema Upendo, kila mtu akashtuka ila mshtuko wa Richard ulikuwa mkubwa zaidi.

“Unasemaje?” aliuliza Richard.

“Niwe na uhusiano wa kimapenzi na wewe kwa miaka mitano, tuonyesheane mapenzi ya dhati, mapenzi ya njiwa, kama mpo tayari kwa hilo, nawaandikia cheki ndani ya nusu saa,” alisema Upendo huku akiwaangalia.

“Ooppss...” Richard akashusha pumzi ndefu, hakuamini kile alichokisikia, yaani kijana yeye, mwenye sura nzuri atembee na Upendo? Wawe wapenzi, kila mtu ajue, hivi wangemuonaje? Kwake lilionekana kuwa suala gumu sana.

“Hilo halina tatizo,” alisema Robinson huku akimwangalia Upendo.

“Unasemaje wewe?” aliuliza Richard huku akionekana kupaniki, jicho alilomkata Robinson halikuwa la nchi hii.



Kwa Richard ulikuwa mtihani mgumu mno, hakuamini kusikia kauli kama ile kutoka kwa msichana aliyekuwa na sura mbaya kama Upendo akilazimisha kuwa naye kimapenzi.

Kwake lilikuwa suala gumu mno, hakuwa tayari kuwa na msichana huyo kwa kuwa hakumpenda, hakuwa mzuri wa sura na kitu ambacho kilimpa mawazo mengi ni kwa namna ambavyo watu wangegundua kama alikuwa akitoka na msichana huyo.

Alipendwa na mademu wakali, ambao walilala usiku na mchana huku wakimfikiria, alitongozwa na warembo mno na alijua kabisa kwamba angekuwa kwenye mapenzi na msichana huyo basi ingekuwa lazima kila mtu ajue kile kilichokuwa kikiendelea.

“Upendo! Kwani hakuna sharti jingine zaidi ya kuwa mpenzi wangu?” aliuliza Richard huku akimwangalia msichana huyo.

“Nilikuwa najiuliza swali linalofanana na lako, hivi hakuna mtu mwingine wa kumkopa pesa zaidi yangu?” naye Upendo aliuliza.

“Richard! Mbona ishu nyepesi sana hiyo! Kwanza mtoto wa kishua, utakula raha, yaani wewe tu! Halafu Upendo, hivi lile gari lako la Aston Martin si lipo?” alisema Robinson na kujifanya kumuuliza.

“Lipo!”

“Sasa je! Huo ndiyo muda wako kuendesha gari zuri! Piga mtoto huyu tupate hela tufanye biashara,” alisema Robinson huku akimwangalia Richard.

Ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa Richard lakini hakuwa na jinsi kwa sababu tu msichana huyo ndiye alikuwa mtu pekee ambaye angewasaidia. Akakubaliana nao na hatimaye uhusiano ukaanza siku hiyohiyo.

Kwa Upendo ilionekana kuwa furaha kubwa, alikuwa pembeni ya Richard huku akionekana kuwa na furaha kubwa. Alimuhitaji mwanaume huyo, kwake, kila wakati alikuwa akitamani kuwaaminisha watu kwamba alikuwa mrembo na ndiyo maana alimchagua mwanaume aliyekuwa akitetemekewa na wanawake wengi chuoni hapo.

Watu waliomuona Upendo na Richard hawakuamini macho yao, ilionekana kama kituko fulani kilichojaa mshangao mkubwa. Hawakuamini kama yule mwanaume mzuri wa sura, aliyetetemekewa na kila mtu leo hii alikuwa na mtu kama Upendo.

Ubaya wa Upendo ndiyo uliowafanya wanaume wengi kumkimbia japokuwa alikuwa na pesa, hakukuwa na mtu aliyejua kilichokuwa kikiendelea, kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea msichana huyo alikilipia kwa kuwakopesha kiasi kikubwa cha pesa.

Baada ya siku moja, Upendo akawakopesha vijana hao pesa walizokuwa wakizihitaji na hivyo kumuita Vonso na kuanza kuzungumza naye. Walimwambia kwamba muda ulifika, alitakiwa kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani kwa ajili ya kusoma.

Barua ya kuomba nafasi iliandikwa, ilijibiwa na ni yeye tu ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa. Baada ya kuongea na vijana hao, wakakubaliana na hatimaye akaanza safari ya kuelekea nchini Marekani kuanza masomo katika Chuo Kikuu cha Florida State kilichokuwa huko Tallahassee hukohuko Florida.

Kwenye kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa kama ndoto, hakuamini kama vijana hao watatu, waliokuwa na umri kama wake ndiyo ambao walimsafirisha na kuelekea nchini humo.

Huko nchini Tanzania, vijana hao hawakutaka kuendelea kubaki chuoni, ilikuwa ni lazima waondoke na kwenda kutafuta maisha, hawakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kuendelea na shule na wakati kulikuwa na michongo mingi ya kupiga pesa sehemu nyingine.

Walichokifanya ni kukutana na kupanga mikakati, wakakubaliana kuondoka kuelekea nchini Kenya, ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo wapate pesa mpaka kufikia kiasi cha dola bilioni nne kama walivyokuwa wamepanga.

“Ila kwanza tuanzisheni akaunti yetu ambapo humo tutaweka milioni hamsini na kuendelea na ishu zetu,” alishauri Richard.

“Hakuna shida.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hilo ndilo walilolifanya, wakafungua akaunti na hatimaye kukiweka kiasi cha pesa walichotaka kikae humo na hivyo Robinson na Robert kuondoka kuelekea nchini Kenya huku wakimuacha Richard aendelee kula bata na mpenzi wake mpya.

Hawakutaka kufikia Nairobi, ili waanze kupata mambo mengi, kufanya mambo yao kwa uhuru ilikuwa ni lazima waelekee Mombasa kwanza. Wakaenda huko na kuanza kujipanga ni kitu gani walitakiwa kufanya.

***





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog