Search This Blog

Saturday 5 November 2022

DILI LA DOLA BILIONI NNE - 5

 





    Simulizi : Dili La Dola Bilioni Nne

    Sehemu Ya Tano (5)







    Robinson, Richard na Robert walikuwa nchini Marekani katika hoteli ya King Lear wakiendelea na mambo yao kama kawaida. Siku hiyo walitakiwa kupanga mipango yao, kikubwa zaidi kulikuwa na kitu ambacho walitakiwa kufanya, kitu ambacho waliamini kwamba kama wangefanikiwa basi wangefanikiwa kuwa na pesa nyingi zaidi.

    Ilikuwa ni lazima wasafiri kutoka hapo Marekani na kuelekea Mexico kuonana na mwanaume aliyejulikana kwa jina la Kamacho. Walijua kwamba ni vigumu kupatikana kwa mwanaume huyo ila ilikuwa ni lazima wahakikishe wanakwenda na kuonana naye.

    Hawakutakiwa kwenda wote watatu, kwa sababu kulikuwa na mambo mengi ya kufanya, huko akatumwa Richard, yeye ndiye ambaye alitakiwa kwenda Mexico na kuhakikisha mwanaume huyo anapatikana haraka iwezekanavyo.

    Huku nyuma Robinson na Robert walitakiwa kubaki, wao ndiyo wangekuwa wanampa maelekezo juu ya kitu gani alitakiwa kufanya. Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu hapo New York mpaka Texas hakukuwa mbali sana, wakaanza kufanya harakati za kupata kibali cha kuingia nchini humo.

    Walikuwa na pesa, hakukuwa na tatizo lolote lile, Richard akafanikiwa kupata kibali cha kwenda Mexico na hivyo siku hiyohiyo kupanda ndege na kuelekea jijini Texas. Walipanga mipango yao, hawakutaka atumie ndege, walihitaji atumie gari kwa sababu huko mpakani ambapo ndipo alipotakiwa kupita kulikuwa na michezo mingi ya uingizaji wa madawa ya kulevya iliyokuwa ikichezwa.

    Safari hiyo kutoka hapo Texas mjini mpaka El Paso, mpaka wa Mexico na Marekani alitumia saa kadhaa akafika huko ambapo kulikuwa na bango kubwa lililoandikwa ‘Welcome Mexico’ ambalo lilisomeka vizuri kabisa.

    Kulikuwa na msururu mrefu wa magari, kila mtu mahali hapo alionekana kuwa bize mno, hakukuwa na mtu aliyekuwa na mpango na mwenzake, kila mmoja alifuatilia kile kilichomfanya kuwa mahali hapo.

    Zamu yake ya kuangaliwa hati ya kusafiria, ikaangalia, ilipoonekana kufaa, ikapigwa mhuri na kuingia nchini Mexico. Hakujua ni kwa namna gani angeweza kumpata huyo Kamacho, alisoma kwenye mitandao kwamba alikuwa mtu katili ambaye hakuwa na huruma hata kidogo.

    Kwake, hakuogopa kwa kuwa alikuwa na kitu ambacho aliamini kabisa mwanaume huyo angemuhitaji kuliko mtu yeyote yule.

    Akaondoka mpakani na kuelekea katika hoteli ya El Pablo iliyokuwa umbali wa kilometa sita kutoka El Paso, alipofika huko akachukua chumba na kutulia chumbani.

    Aliwasiliana na wenzake, aliwaambia tayari alifika na alichokihitaji kilikuwa ni kuonana na mwanaume huyo ili ampe taarifa kwamba alikuwa na mpango kabambe wa kumtoa ndugu yake, Hernandez katika gereza kubwa nchini Marekani, kama kweli alihitaji msaada wake, basi alitakiwa kumsikiliza.

    “Nitampataje?” alijiuliza.

    Aliwasiliana na wenzake na kuwaambia ugumu ulivyo, walijua ni kwa jinsi gani wangesumbuka sana kuonana na mwanaume huyo lakini kwa sababu alikuwa muuzaji wa madawa mkubwa, waliamini alikuwa na watu wengi waliokuwa wakimpelekea taarifa, hasa huko mpakani.

    Alichokifanya ni kusubiri, kulala na asubuhi ilipofika tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumfuata dada wa mapokezi na kuanza kuzungumza naye.

    Siku iliyopita mtu aliyekuwa hapo alikuwa mwanaume, huyu wa sasa hivi, msichana mrembo ndiyo kwanza alikuwa amemuona, macho yake yalivyotua kwa Richard akashtuka mno.

    Ni kweli aliwaona wanaume weusi wengi, wenye sura nzuri lakini huyu aliyekuja leo alionekana kuwa tofauti mno, alipendeza, alikuwa na sura nzuri kiasi kwamba hata yeye mwenyewe alihisi kabisa hakukuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama huyo.

    “Hi!” alimsalimia, msichana huyo alimkodelea macho, hata salamu ile hakuisikia.

    “Haloooooo....” aliita huku akimchezea mkono wake mbele ya macho yake, msichana huyo akashtuka.

    “Oh! Welcome...” (Oh! Karibu..) alisema msichana huyo huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

    Alishindwa kuvumilia, tabasamu lake lilikuwa usoni mwake, alitokea kumpenda mwanaume huyo kwa kuwa alikuwa mzuri wa sura. Alitamani amwambie kitu chochote kile kizuri ili akae naye kwa muda mrefu na kuzungumza.

    “I need your help,” (nahitaji msaada wako) alisema Richard huku naye uso wake akiuwekea tabasamu pana lililomchanga kabisa msichana huyo.

    “No problem! What can I help you?” (hakuna tatizo! Nikusaidie nini?) aliuliza msichana huyo.

    Richard alianza kuzungumza naye, alimwambia kwamba alifika nchini Mexico kwa lengo la kuonana na mwanaume aliyeitwa kwa jina la Kamacho.

    Hakujua alipokuwa akiishi ila alitamani sana kuonana naye kuliko mtu yeyote yule. Msichana huyo aliposikia hivyo, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, kwake haikumuingia akilini kwa mwanaume mzuri kama alivyokuwa Richard kumuulizia Kamacho, mwanaume aliyekuwa na roho mbaya mno.

    “Kamacho?” aliuliza huku akimwangalia.

    “Ndiyo! Ninahitaji kuonana naye,” alisema Richard.

    Msichana huyo alichomwambia ni kwamba hajawahi kumuona hata siku moja. Ni kweli alimsikia sehemu mbalimbali akitafutwa au hata kuwatuma watu wake kufanya utekaji na mauaji lakini hakuwahi kumuona hata siku moja zaidi ya kwenye magazeti tu ambayo yalikuwa yakimzungumzia yeye.

    “Hujawahu kumuona hata kidogo?”

    “Kweli! Na simjui kabisa,” alisema msichana huyo.

    Richard hakutaka kuzungumza zaidi, akatoka na kuelekea matembezini, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakujua namna ya kumpata Kamacho kwani ingekuwa ni rahisi kuambiwa mahali alipokuwa akipatikana na kwenda yeye mwenyewe.

    Alizunguka huko kwa saa zima kwa kuhisi kwamba inawezekana angeweza kuonana na mtu yeyote ambaye angeweza hata kumwambia kuhusu mwanaume huyo lakini hilo halikuwezekana.

    Baada ya kutembeatembea kwa saa mbili akaamua kurudi hotelini na kuingia chumbani. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwasiliana na wenzake na kuwaambia kuhusu ugumu wa kile alichokuwa amekutana nacho.

    “Kwa hiyo hujampata kabisa?” aliuliza Robinson.

    “Ndiyo! Nimejitahidi mno kuulizia,” alisema Richard.

    Alichokisema Robert ni kwamba Richard alitakiwa kuhakikisha anafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anampata mwanaume huyo na njia pekee ya kumpata ilikuwa ni kumuulizia kila mtu kuhusu mwanaume huyo.

    Ulikuwa ni mtihani mkubwa lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kama alivyoambiwa hivyo kuondoka na kwenda chini kulipokuwa na mgahawa.

    Alipofika huko, akaanza kuwauliza wahudumu kuhusu Kamacho. Kila mtu alibaki akishangaa, haikuwa kawaida kwa mtu kumuulizia mwanaume huyo kama ambavyo yeye alimuulizia.

    Kila mmoja alimuuliza maswali juu ya sababu iliyomfanya kutaka kuonana na mwanaume huyo lakini hakutaka kuwaambia ukweli, msimamo wake ulikuwa uleule kwamba alihitaji kuonana na mwanaume huyo tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakusaidiwa kwa lolote lile, akaondoka na kurudi chumbani. Bado alikuwa na shaka kubwa kuhusu kumpata Kamacho, hakujua ni kitu gani kingetokea huko mbele kwani hakuweza kumpata na mbaya zaidi kila mtu aliyemuuliza kuhusu mwanaume huyo alibaki akimshangaa tu.

    Siku ziliendelea kukatika, siku ya pili, na ya tatu ikaingia lakini hakuwa amefanikiwa kwa lolote lile. Siku hiyo alilala chumbani kwake, alisikia mlango unagongwa, haraka sana akaiangalia saa yake, ilikuwa ni saa tano usiku.

    Hakujua ni nani alikuwa akipiga hodi, akausogelea mlango, kabla ya kuufungua, akachungulia kwenye kitundu kidogo cha mlango, hakuona mtu lakini bado alisikia mlango ukigongwa kumaanisha mgongaji alikuwa pembeni, alijificha, hakutaka kuonekana na mtu huyo.

    “Who is it?” (nani?) aliuliza huku akiwa ndani.

    “Linda!”

    “Who the hell is Linda?” (Linda ndiye nani?) aliuliza.

    Msichana huyo akamwambia kwamba alikuwa mhudumu, kulikuwa na jambo alihitaji kuzungumza naye. Alichanganyikiwa, hakujua kulikuwa na jambo lipi msichana huyo alihitaji kuzungumza naye.

    Akamuuliza, akamjibu kuhusu mwanaume aliyekuwa akimtafuta, Kamacho, alipata taarifa kwamba alikuwa sehemu fulani, hivyo alihitaji kumwambia.

    “Mh!” aliguna.

    Kwa sababu alikuwa na hamu na Kamacho, akaufungua mlango kwa lengo la kumsikiliza huyo Linda. Mlango ulipofunguka, wanaume watatu waliokuwa wamejificha kwa pembeni ambao walikuwa na bastola mikononi huku miili yao ikiwa imechorwa tatuu, wakaingia ndani, wakamsukuma na kumlaza kitandani.

    “Ukipiga kelele tu, ubongo utasambaa kitandani,” alisema mwanaume mmoja kwa sauti iliyokuwa nzito.

    Hata kabla hajajibu kitu, hapohapo akapigwa na kitu kizito, akaanza kuona giza, ni ndani ya sekunde kadhaa tu, akapoteza fahamu.

    Richard alikuja kupata fahamu baada ya saa mbili, akayafumbua macho yake, akajikuta akiwa ndani ya chumba kimoja kilichokuwa na mwanga hafifu, alikalishwa kwenye kiti huku akiwa amefungwa kamba miguu na mikono.

    Hakujua ni kwa namna gani alikuwa ndani ya chumba hicho, akaanza kuangalia huku na kule kwa macho yake yaliyokosa nguvu. Akajitahidi kuyafumbua na kuangalia huku na kule, akaanza kukukuruka ili ajitoe kwenye kamba zile lakini alishindwa.

    “Halooooo!” aliita kwa sauti ili kuona kama kungekuwa na mtu yeyote yule ambaye angefika mahali hapo.

    Aliendelea kupiga kelele kwa dakika kadhaa, mara mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia huku akiwa amevalia pensi na shati lililofunguliwa vifungo vyote.

    Alimwangalia Richard pale alipokuwa, hakuzungumza kitu ila kwa jinsi alivyomwangalia, macho yake tu yalitosha kumwambia kwamba hakutaka kusikia akipiga kelele tena.

    Richard akaogopa, hakujua alikuwa mahali gani na watu waliomteka walikuwa akina nani. Alitulia kwa nusu saa, mlango ukafunguliwa tena na wanaume sita kuingia huku mmoja akiwa amevalia kofia ya Marlboro na suti nyeupe.

    Watu wengine wakasimama nyumba kabisa na mwanaume aliyevalia suti akamsogelea pale alipokuwa kwa lengo la kuongea naye. Richard hakujua mwanaume huyo alikuwa nani, aliogopa, hakuona kama kungekuwa na dalili za kutoka ndani ya chumba kile akiwa mzima kabisa.

    “Wewe ni nani?” aliuliza mwanaume huyo.

    “Richard!”

    “Umetoka wapi?” aliuliza mwanaume huyo.

    “Nimetoka Afrika,” alijibu.

    Mwanaume huyo akacheka sana, alichokifikiria ni kwamba alidanganywa. Akawaambia vijana wake wamchukue Richard na kutoka naye.

    Wakafanya hivyo na kumpeleka kwenye chumba kingine kilichokuwa na mashine kubwa huku pembeni kukiwa na watu wengine wakiwa wamefungwa kamba.

    Mashine moja ikawashwa, mwanaume mmoja miongoni mwa wale waliokuwa wamefungwa kamba akachukuliwa, akaanza kupiga kelele za kuomba msamaha lakini jamaa mwenye suti hakutaka kujali kabisa.

    Akachukuliwa na kuingizwa kwenye mashine ile ambapo ikaanza kumvuta na kumsagasaga huku nyama yake ikienda kuangukia sehemu nyingine iliyokuwa na ndoo.

    Richard akaogopa mno, aliona kabisa kwamba huyo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Jamaa yule mwenye suti akamsogelea na kumuuliza tena alitoka wapi kwani halikuwa jambo jepesi mtu kutoka barani Afrika na kumuulizia Kamacho.

    “Yule aliyetumbukizwa, alitapeli madawa ya kulevya yenye thamani ya dola milioni mbili. Alitukimbia lakini tukamakamata, hiyo ndiyo adhabu yake. Huwa hatuoni shida kuua, kwanza ndiyo tunasikia burudani kabisa mioyoni mwetu. Una nafasi ya mwisho, umetoka wapi?” alisema mwanaume huyo na kumuuliza.

    “Nimetoka Afrika! Naomba unielewe, huo ndiyo ukweli wangu, nimetoka Afrika,” alijibu Richard huku akitetemeka.

    “Nuno! Mtumbukizeni kwenye mashine,” alisema jamaa huyo, hapohapo Richard akabebwa mzimamzima na kuanza kupelekwa kwenye mashine ile kama ilivyokuwa kwa mwanaume yule mwingine.





    Wakati vijana wa Kamacho wakiwa wamemshika Richard kwa lengo la kumtumbukiza kwenye ile mashine ili asagwe ndipo akaanza kulitaja jina la Hernandez, aliwaambia alikuwa hapo kwa ajili ya mwanaume huyo aliyekuwa amekamatwa na kufungwa gerezani nchini Marekani.

    “Nimekuja kuzungumza nawe kuhusu Hernandez,” alisema Richard kwa sauti, kila mtu aliposikia hivyo, akashangaa, si wao tu bali hata Kamacho naye alishtuka hivyo kuwaambia vijana wake wamuachie ili amsikie vizuri alichokuwa akikijua kuhusu Hernandez.

    Wakamchukua na kumpeleka kwenye chumba kingine ambapo huko kulikuwa na meza na kumwambia akae kwenye kiti kwa ajili ya kuzungumza. Hakumfahamu mwanaume huyo lakini kwa jinsi alivyomtaja ndugu yake, akahisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.

    Kwanza akapewa maji na kuanza kunywa, baada ya dakika kadhaa, Kamacho akatoka katika chumba kimoja na kuingia mule na kuanza kumuuliza maswali kuhusu ndugu yake huyo na sababu iliyomfanya mpaka kumtaja.

    “Umemjuaje ndugu yangu?” aliuliza Kamacho.

    “Nilimfuatilia kwenye mitandao pamoja na wenzangu,” alijibu Richard.

    “Kwa sababu gani?”

    “Tunataka kumtoa gerezani,” alisema Richard huku akimwangalia Kamacho.

    Mwanaume huyo aliposikia hivyo, akaangaliana na wenzake, kwake, kile alichoambiwa kilikuwa ni kitu kigumu sana kufanyika. Aliwahi kuwatumia polisi wa nchini Marekani kwa kuwapa kiasi kikubwa cha pesa lakini hawakufanikiwa kumtoa mtu huyo gerezani.

    Hilo lilimpa mawazo mengi, kitendo cha Richard kumwambia kwamba alikuwa na mpango huo, moyo wake ukaridhika na kuanza kuhisi kuwa kijana huyo angefanikisha mpango huo, alichotakiwa ni kumwamini tu.

    “Ndugu yakoana thamani gani?” aliuliza Richard, sasa akaanza kujiamini kwani Kamacho pamoja na ubabe wake, akawa mdogo tu.

    “Unamaanisha nini?”

    “Utatoa kiasi gani kwa ajili ya kumleta mpaka mikononi mwako!” alisema Richard.

    “Dola milioni moja!”

    “Unahisi inatosha hiyo?”

    “Wewe unataka kiasi gani?”

    “Kumbuka tupo watatu, itakuwa jambo zuri sana kama tutapata dola milioni sita ili tukuletee mpaka mlangoni,” alisema Richard.

    Kamacho akanyamaza, kiasi alichoambiwa atoe kilikuwa kikubwa mno, hakuwahi kufikiria hata siku moja angatoa kiasi kikubwa namna hiyo tena ndani ya muda mfupi tu.

    Lakini mbali na kufikiria kiasi hicho cha pesa akaanza kuufikiria ukaribu wake na Hernandez, alimpenda mno, kwake, huyo alikuwa karibu naye, ni zaidi ya upendo, yaani ni zaidi ya kitu chochote kile.

    Walizungumza lakini Richard hakutaka kushusha bei, alimwambia ugumu wa kazi hiyo, kama kweli alijitahidi kumtoa mwanaume huyo gerezani na kushindwa, ilimaanisha kazi hiyo ilikuwa ngumu mno.

    Hakuwa na jinsi, alikubaliana naye na hivyo kumsindikiza Richard mpaka mpakani El Paso na kuahidi kumtumia siku inayofuata ili kazi ibaki kwake na hao wenzake.

    Huku nyuma Kamacho hakutaka kumwambia kitu chochote kile, aliambiwa kwamba hakutakiwa kuamini habari yoyote ile ambayo ingeonekana mbele yake kwa sababu dili walilokuwa wakienda kulifanya ili ndugu yake atolewe gerezani lilikuwa kubwa mno, hivyo hakutakiwa kuwa na hofu hata kidogo.

    Richard akaondoka mpaka jijini Texas ambapo hapo akapanda ndege na kuelekea jijini New York kuonana na wenzake. Aliwaambia kila kitu kilichotokea kwamba Kamacho alikubaliana naye na alikuwa tayari kutoa kiasi hicho cha pesa kwa ajili yao.

    “Safi sana! Hebu tufanyeni kazi ya kiume sasa,” alisema Robinson, akayapeleka macho yake kwa Robert ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kutumia kichwa chake kuuelezea mpango jinsi ulivyotakiwa kufanywa.

    “Kitu cha kwanza ni lazima tumtafute daktari ambaye anafanya kazi ndani ya gereza hilo. Huyo tutaongea naye kirafiki kwamba aende katika gereza hilo kwa lengo la kumchoma sindano Hernandez, hiyo sindano itakuwa na kazi moja, kuyasimamisha mapigo yake ya moyo kwa muda wa saa sabini na mbili,” alisema Robert na kuendelea:

    “Daktari akimpima, atasema kwamba mwanaume huyo amekufa, hivyo atatakiwa kwenda kuzikwa kwenye makaburi yaliyopo nje ya gereza hilo,” alisema.

    “Kwa hiyo atazikwa?”

    “Hapana! Hawezi kuzikwa kwa sababu tutakwenda na maiti yetu hapo ambayo ndiyo tutaizika,” alisema Robert.

    “Tutaizika? Kivipi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Taarifa zitatolewa kwamba Hernandez amekufa, daktari atakwenda kumpima na kugundulika kwamba amekufa kwa sababu mapigo yake ya moyo yamesimama, kumbuka kwamba huyu daktari ni wetu, yaani yeye atacheza dili kuhakikisha mchezo unachezwa vizuri kabisa.

    “Sasa ikishaonekana Hernandez amekufa, watapigiwa simu watu wa kitengo cha kuzika, bado sijawajua, ila tutatafuta namba zao, wewe utazidukua, simu ikipigwa kwao kwa lengo la kwenda huko kuzika, simu itakuja kwetu, kwa hiyo sisi ndiyo tutakwenda na mwili wetu ndani ya gari,” alisema Robert, wenzake walikuwa kimya tu wakisikiliza mipango yake.

    “Halafu?”

    “Kwenye kuzika tutauzika mwili mwingine, halafu mwili wa Hernandez tutauingiza ndani ya gari na kuondoka zetu,” alisema Robert.

    “Bado kutakuwa na tatizo hapo! Najua tutakapokuwa tunazika, polisi wa magereza watakuwa wanatuangalia, sasa tutabadilishaje mwili? Halafu kwani ni lazima twende na mwili? Hatuwezi kuzika mdoli?”

    “Ni kazi nyepesi sana. Huyo daktari tutampa baruti, tutamwambia ampe kijana mmoja na kumdanganya kwamba ni mabomu ambayo yatafanya ukuta ubomoke na kutoroka. Hapo ni lazima atuhusishe sisi, yaani amwambie kwamba kuna watu watakuja kumzika Hernandez, kwa sababu polisi watakuwa bize kutuangalia sisi, basi wao watumie nafasi hiyohiyo kupiga baruti hizo, ukuta ubomoke na watoroke, sasa wakati baruti hizo zitalia kwa sauti kubwa, hawa polisi waliokuwa huku kwetu hawatoweza kubaki, ni lazima watakimbilia gerezani, hiyo itakuwa nafasi yetu ya kumtoa Hernandez na kuuweka huo mdoli kaburini kisha kuondoka,” alisema Robert.

    “Mimi ndiyo maana napenda kufanya kazi na Wachaga,” alisema Richard na kuanza kucheka.

    Mipango ilipangwa, ilikuwa kabambe lakini suala moja tu ndiyo lilikuwa gumu ambalo Richard hakuwa amelifafanua, nalo lilikuwa ni kuhusu huyo daktari, kama wangempa pesa, alitakiwa kupewa kiasi gani ili afanye kazi hiyo.

    “Na daktari tutamlipa kiasi gani?” aliuliza Robinson.

    “Dola 0.00,” alijibu Robert.

    “Unanichanganya kidogo!”

    “Namaanisha hatolipwa!”

    “Kwa nini?”

    “Guys! Hivi mnajua kwa nini nilisema Vonso aende akasome katika Chuo Kikuu cha Tallahassee hukohuko Florida?” aliuliza.

    “Hapana! Ndiyo utuambie”

    “Basi hii ndiyo sababu! Hiki kitu nilikipanga kabla, nilijua tu kuna siku tutakuja kuchukua pesa nyingi kizembe kabisa,” alisema.

    “Kivipi?” aliuliza Richard, Robert akabaki akitabasamu tu.

    ***

    Maisha yalikuwa yakiendelea vizuri kabisa chuoni. Vonso alikuwa mwanaume mkimya ambaye alipenda sana kujifunza mambo mbalimbali. Alihitaji kuwa mkali kwenye sheria kwa sababu alijua kulikuwa na watu waliolipia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili yake.

    Hakutaka kuwaangusha, alipambana usiku na mchana, alijisomea vitabu vingi, alipitia kesi nyingi za zamani, jinsi watu walivyokuwa wakitumia vifungu mbalimbali katika kushinda kesi zao.

    Ilikuwa ni lazima ajue mambo mengi kuhusu sheria, alihitaji kuwa mtu muhimu katika dunia hii. Hapo chuo, kutokana na kujifunza mambo mengi na kuwa mkali, wanafunzi wengi wakaanza kumzoea na kuhitaji kujifunza mengi kupitia mtu huyo.

    Miongoni mwa watu ambao walikuwa wakipenda sana kupiga naye stori alikuwa msichana Vivian James, msichana mrembo ambaye baba yake alikuwa daktari mkubwa katika Hospitali ya St. Joseph iliyokuwa Florida hapohapo nchini Marekani.

    Alikuwa msichana mrembo mno, alipenda pombe, alipenda starehe, kwenye kila sherehe ambayo iliandaliwa chuoni hapo, hakukosa, alitamani kwenda kwenye kila sherehe kiasi kwamba wenzake walimzoea na hata siku alipokosa, walikuwa wakiulizana kama alikuwa akiumwa ama la.

    Vivian hakuwa na leseni ya udereva, alipokonywa baada ya kukamatwa mara kadhaa akiwa anaendesha gari huku amelewa. Hilo kwake halikuwa tatizo, alichohitaji ni kwenda kwenye kila sherehe kwa sababu tu alipenda kufanya hivyo.

    Wanaume nao hawakuwa nyuma, kupitia ulevi wake, walipambana mpaka kulionja penzi lake. Kwake, hilo halikuwa tatizo, hakuwa msichana mgumu, kila mwanaume aliyekuja na mipango yake, alifanikiwa kumchukua na kumfanya chochote kile.

    Baada ya kukaa kwa miezi kadhaa, huku akipewa taarifa na vijana watatu waliokuwa wakimlipia ada kwamba walikuwa nchini Marekani, akaambiwa aandae sherehe ya kuzaliwa kwake ambayo ingekwenda kufanyika mwezi huo na wao wangesimamia kila kitu.

    Hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa watu hao walimwambia wangelipia kila kitu, wakakubaliana naye na hivyo kuwaambia marafiki zake kuhusu sherehe hiyo.

    Kwa Vivian, aliposikia, alichanganyikiwa, kwake, sherehe ilikuwa kila kitu hivyo akaanza kujipanga na marafiki zake na hatimaye kusubiri siku ya sherehe hiyo kufanyika.

    Siku zilikwenda kama kawaida na baada ya siku kadhaa, hatimaye siku husika ikafika na hivyo watu kujiandaa usiku kwenda huko kusherehekea na Vonso katika siku yake ya kuzaliwa.

    Sherehe ilifanyikia katika nyumba moja kubwa ya kukodi iliyokuwa ufukweni, watu walicheza na kufurahi pamoja. Waliokuwa wanywaji, walikunywa sana, waliokuwa wakitaka kufanya mapenzi, hakukuwa na mtu aliyezuiliwa.

    Vivian alikuwa amekaa na marafiki zake, walikuwa wakipiga stori kwa sauti kubwa kwani walikuwa wamelewa mno kwani hata sauti zao tu zilionyesha ni kwa jinsi gani pombe ziliwaingia vichwani mwao.

    Baada ya dakika kadhaa, akafika mwanaume mmoja pale walipokuwa, alikuwa Richard. Alipowafikia, akaanza kuwaangalia kwa macho ya kuvutia huku mkononi akiwa na chupa ya Heinekenn ambayo ndani yake kulikuwa na vidonge vya usingizi.

    “Hey girls! You look stunning...” Hey warembo! Mmependeza) aliwaangalia na kuwasifia.

    Wasichana hao wakaangalia na kuanza kucheka, kwa kuwa walilewa, hakuona kama kungekuwa na ugumu wowote ule. Richard akakaa kabisa karibu na Vivian na kumwangalia.

    “I just need your company miss,” (nahitaji kampani yako mrembo) alisema Richard.

    “Me?” (mimi?)

    “Yaap! I was looking for you,” (ndio! Nilikuwa nakutafuta?)

    “Why? Do we know each other?” (kwa nini? Tunafahamiana?) aliuliza Vivian kwa sauti ya kilevi.

    Richard hakutaka kuzungumza kitu, alichokifanya ni kuchukua glasi iliyokuwa chini na kumuwekea ile pombe aliyokuwa akinywa na kumtaka kunywa.

    Hilo halikuwa tatizo, Vivian akaichukua na kuanza kunywa, si yeye tu bali hata wenzake nao wakaanza kunywa mfululizo pasipo kugundua kama pombe ile iliwekewa madawa ya usingizi.

    Ni ndani ya dakika tano tu, wote wakapitiwa na usingizi, alichokifanya Richard ni kumuinua na kuanza kuondoka naye kwenye gari. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu yoyote ile, walijua ni mtu ambaye alilewa hivyo alikuwa akipelekwa kwenye gari.

    “Oya washikaji! Mtu wenu huyu hapa,” alisema Richard huku akimuingiza Vivian ndani ya gari hilo.

    “Safi sana!” alisema Robinson, akawasha gari na kuondoka mahali hapo kwa mwendo wa kawaida tu.



    Vivian alikuja kurudiwa na fahamu akiwa ndani ya chumba kidogo kilichokuwa na mwanaga hafifu. Alishangaa, hakujua ni kwa namna gani alifika ndani ya chumba kile. Alikalishwa kwenye kiti na mikono yake ikiwa imefungwa kwenye kiti kile.

    Alijaribu kujitoa lakini alishindwa, hakuishia hapo tu bali akajaribu hata kuitoa miguu yake, akashtuka kuona nayo ikiwa imefungwa kama ilivyokuwa mikono ile. Aliumia, alijaribu kufikiria ni kwa jinsi gani alifika mahali pale.

    Alikumbuka mara ya mwisho alikuwa kwenye sherehe ya mmoja wa wanachuo wenzake, Vonso, huko alikula na kunywa na mwisho wa siku hakukumbuka kilichokuwa kimeendelea baada ya hapo.

    Akaanza kuita kuomba msaada, alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa na hofu tele, alihisi kabisa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake, asingeweza kutoka, asingeweza kuwasiliana na mtu yeyote pale na mwisho wa siku angekufa ndani ya chumba hicho kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.

    Wakati akipiga kelele, mara mlango wa chumba kile ukafunguliwa na Robinson kuingia, hakumfahamu mtu huyo kwani hata uso wake ulifichwa na nguo iliyotengenezwa kwa staili ya kininja. Akaanza kumuomba msamaha japokuwa alikuwa na uhakika hakuwa amefanya kosa lolote lile.

    Robinson alimwangalia, msichana huyo ndiye ambaye angewafanya wapate pesa nyingi, kwa kumtumia huyo ndiye ambaye wangewafanya kuendelea kutafuta dola bilioni nne. Vivian alipoona Robinson hamsaidii kwa lolote lile zaidi ya kusimama na kumwangalia tu, akaanza kupiga kelele za kuomba msaada kitu kilichomfanya Robinson kuchukua gundi ya plastiki na kumfumba mdomo.

    Baada ya sekunde chache mlango ukafunguliwa na Richard kuingia, kama alivyokuwa Robinson naye alivalia kininja, alibaki akimwangalia msichana yule, alikuwa dili kubwa mno ambapo baada ya kuzungumza na baba yake basi wangejua ni kitu gani kilitakiwa kufanywa.

    Walizungumza kwa dakika moja na kutoka ndani ya chumba kile huku wakiwa na simu ya Vivian, huko walipokwenda, wakachukua namba ya mzee James na kumpigia kwa lengo la kumpa taarifa kwamba binti yao alikuwa kwao, walimtaka kufanya jambo moja tu, vinginevyo basi wangemuua kama walivyowaua watu wengine.

    Kwa jinsi mzee huyo alivyosikika kwenye simu, alionekana kuogopa, alijawa na hofu na mpaka simu inakatwa walijua dhahiri kwamba angefanya kile walichotaka akifanye.

    “Ila si wanaweza kudukua simu yake na kujua alipo?” aliuliza Richard na Robinson kuanza kucheka.

    “Yaani waidukue simu ambayo ipo mikononi mwangu! Basi nitakuwa nimeshuka kiwango kwa kiwango kikubwa sana,” alisema Robinson huku akicheka, kwa kile alichoambiwa, kilimfanya kutoa tabasamu pana.

    ***

    Dokta James alichanganyikiwa, kilichotokea kilimtisha mno, aliogopa, alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha ya binti yake. Hakumuona binti yake usiku uliopita, alimpa ruhusa ya kwenda kwenye sherehe ya rafiki yake lakini mpaka asubuhi ya siku hiyo hakuwa amerudi nyumbani.

    Alimpigia simu lakini haikupokelewa na baada ya dakika kadhaa haikuwa ikipatikana kabisa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea huko, alichanganyikiwa, mke wake hakuwa na amani hata kidogo, alikuwa mtu wa kulia tu, moyo wake ulimwambia kwamba kulikuwa na jambo baya lililokuwa limetokea hivyo walitakiwa kuhakikisha wanawasiliana na polisi ili kuanza kufuatilia kila kitu.

    Hawakutaka kuchelewa, simu ikapigwa mpaka katika kituo cha polisi ambapo wakafika hapo na kuanza kuzungumza nao. Waliwaambia kila kitu, ni kwamba binti yao aliaga usiku uliopita lakini kitu cha ajabu kabisa mpaka muda huo hakuwa amerudi nyumbani.

    Polisi walichukua maelezo yao, wakachukua namba ya simu na kuanza kumtafuta. Kwa sababu waliambiwa na wazazi hao kuhusu uwezekano wa kutekwa, wakawasiliana na maofisa wa FBI (Federal Bureau of Investigation) na kuwaambia kila kitu, yaani kwa sababu wao ndiyo walikuwa na uwezo zaidi yao wa kuwatafuta watu waliotekwa, wakaamua kuwaachia hao.

    Maofisa wa FBI wakawasiliana na wazazi wa Vivian na kuanza kuongea nao, walihitaji kupata maelezo kidogo kuhusu binti huyo, kama ilivyotokea ndivyo walivyowaambia hivyo watu hao kuanza kazi ya kumtafuta msichana huyo.

    Kitu cha kwanza kabisa ambacho walikuwa na uhakika ni kuipata simu yake. Walijua ni lazima huko alipokuwa alikuwa na simu hivyo lingekuwa jambo zuri kama wangeidukua na kujua kila kitu. Wakafanya hivyo, kitu kilichowashangaza ni kwamba simu ilionekana lakini cha ajabu haikujulikana mahali ilipokuwa.

    Hilo likawashtua kidogo, wakahisi kulikuwa na jibu, wakaendelea kuitafuta, ilishindikana kabisa kitu kilichowafanya kuhisi kuwa msichana huyo alitekwa na mtu ambaye alikuwa na utalaamu mkubwa wa kucheza na network.

    Maofisa wa FBI hawakutaka kukata tamaa, walihitaji kufuatilia kamera, michoro yao na kila kitu lakini bado hawakupata kitu. Hawakuishia hapo, kitu ambacho walikuwa na uhakika ungekuwa mwanzo mzuri ni kuzungumza na marafiki zake ambao walikuwa katika sherehe hiyo.

    Wakawasiliana nao na kuonana, wakawauliza maswali mengi kuhusu usiku huo ambao Vivian alitekwa na watu wasiojulikana.

    “Alikuwa amelewa sana, yeye na watu wengine, alikuwa na kijana mmoja hivi, akamchukua na kumpeleka ndani ya gari,” alisema msichana mmoja.

    “Ilikuwa ni majira ya saa ngapi?”

    “Ni kama saa nane usiku hivi!”

    “Aina ya hiyo gari?”

    “BMW nyekundu,” alisema.

    “Ulibahatika hata kuona namba?”

    “Hapana! Niliona ubavu ubavu tu,” alijibu.

    “Na ndani ya hilo gari kulikuwa na watu wengine?”

    “Nahisi hilo kwani mlango ulipofunguliwa, nilimuona kama mtu mwingine hivi, ila sikumfahamu hata kidogo,” alijibu.

    “Na huyo mtu aliyemchukua alikuwa Mzungu ama mweusi?”

    “Mweusi!”

    “Tunashukuru!”

    Hivyo ndivyo vitu ambavyo walihitaji kusikia kutoka kwa watu hao, waliwahoji wote mpaka Vonso ambaye ndiye aliyekuwa amewaalika watu hao, kwenye mahojiano hayo aliwaambia kwamba hakufahamu kitu chochote kile.

    Ni kweli hakufahamu, mpango uliokuwa umefanyika ulimficha, walimuandalia sherehe pasipo kujua kama watu hao walikuwa na mpango wao kwenye hilo.

    Maofisa wakaendelea na kazi yao, waliamini kwa kile walichokuwa wamekipata kingewasaidia lakini mpaka siku tatu baadaye hawakuwa wamefanikiwa kumpata msichana huyo kitu kilichowafanya kuhisi walikuwa wakipambana na watu waliokuwa hatari sana.

    “Mambo yamekuwa magumu sana, taa za barabarani zinaonyesha matukio, ila ikifika majira ya saa 8:23 usiku, kamera zinaonekana kuzima na baada ya dakika kadhaa kuwaka. Nadhani hawa watu waliofanya huu mchezo ni hatari sana kwenye mambo ya teknolojia na hata kuzidukua kamera za barabarani,” alisema ofisa mmoja ambaye alilifuatilia jambo hilo kwa siku tatu mfululizo lakini hakuwa na majibu juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

    ***

    Dokta James na mkewe walikuwa kwenye majonzi makubwa, hawakuwa na raha, muda wote walihisi kabisa binti yao alikuwa ameuawa mahali fulani na mwili wake kufukiwa sehemu.

    Walikata tamaa, walimuomba Mungu kwamba kama binti yao huyo hajauawa basi Mungu amlinde mpaka siku ambayo wangemtia mikononi mwao. Waliwategemea maofisa wa FBI na polisi kwamba wangefanikiwa kumpata binti huyo lakini kitu cha kushangaza mpaka siku tatu zinakatika hakukuwa na mategemeo yoyote yale.

    Baada ya kutimia siku ya nne, mzee James akapokea simu kutoka kwa namba ambayo haikuonekana kwenye kioo cha simu yake, mtu aliyepiga alimwambia kwamba kulikuwa na mazungumzo walitakiwa kuongea ambayo kama yangekwenda vizuri basi angempata binti yake akiwa salama kabisa.

    “Nataka kwanza nisikie sauti yake,” alisema mzee James, hilo halikuwa tatizo, Vivian akapewa simu na kuisikia sauti yake akilia huku akiomba msaada.

    “Nadhani umeridhika,” alisema Robinson.

    “Niambie unataka nini!”

    “Tunataka kitu chepesi sana ambacho utaweza kutupatia haraka sana,” alisema Robinson.

    “Kitu gani?”

    “Tunataka ukamtoe Hernandez gerezani,” alisema Robinson.

    Mzee James alishtuka, hakujua mwanaume huyo alimaanisha nini, hakuhusika na gereza, hakukuwa na jambo lolote lile kuhusu yeye na mfungwa huyo. Alijua alifungwa katika gereza lililokuwa na ulinzi mzito, isingekuwa kazi nyepesi kumtoa lakini watu hao walimwambia kwamba ingewezekana kama tu wangeshirikiana.

    “Hivi unalijua lile gereza lilivyokuwa na ulinzi mkubwa?” aliuliza mzee James.

    “Najua sana! Lakini huwezi kuamini, mbali na ulinzi huo lakini bado unaweza kumtoa mtu huyo gerezani,” alisema Robinson.

    Kwa kuliangalia lilikuwa jambo gumu sana kwake lakini Robinson aliendelea kumsisitiza kwamba lingekuwa jambo jepesi mno.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Robert akapewa simu na kuanza kuzungumza na mzee huyo, alimwambia mpango wao, kitu cha kwanza alitakiwa kutafuta dawa zilizokuwa na nguvu ya kusimamisha mapigo ya moyo kwa saa sabini na mbili lakini pia walitakiwa kuwa na baruti ambazo angepewa kijana mmoja huko gerezani, jinsi ya kuonana na kijana huyo ni yule ambaye angekuja ofisini mwake kutibiwa na kumpa hizo baruti na kiasi cha dola elfu moja na kumwambia aende akazipige ndani ya gereza hilo majira ya saa kumi jioni, muda ambao vijana hao watatu watakuwa nje na daktari huyo kwa lengo la kumzika Hernandez.

    Aliambiwa kila kitu na mwisho kabisa akaambiwa kwamba kama mpango huo usingekamilika basi ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha ya binti yake.

    Maneno hayo yalimshtua na kumfanya kuhisi kwamba alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha mpango huo unafanyika. Baada ya kumalizia kila kitu, akaambiwa aende katika park ya Santana iliyokuwa hapohapo New York ambapo huko angekutana na baruti, kiasi cha pesa na hivyo kutakiwa kuanza kazi hiyo siku inayofuatia.

    “Haina shida.”

    Hiyo ndiyo kazi aliyopewa, kwa jinsi maelekezo juu ya kile alichotakiwa kufanya alivyopewa aligundua kabisa kwamba watu hao hawakuwa na masihara hata kidogo, walikuwa ni watu wenye akili kubwa ambao walikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile.

    Kwa kile alichoambiwa, hakuwahi kufikiria hata kidogo kama kuna mtu angemwambia hivyo, mbinu hizo zilikuwa kubwa, za kisasa ambazo zilimpa uhakika kwamba kusingekuwa na mtu yeyote yule ambaye angegundua kama mtu huyo alitoroshwa.

    “Nitafanya hivyo! Nitapambana kwa ajili ya mtoto wangu,” alijisemea mzee huyo huku akiwa na uhakika wa kufanikiwa kwa kile alichoambiwa.





    Ulikuwa ni mpango uliosukwa na kusukika, mzee James hakutakiwa kuhofia jambo lolote lile kwa sababu watu waliokuwa wamemteka binti yake walionekana kuwa hatari kupita kawaida. Alichukua kila kitu alichowekewa kwenye park ile na kurudi nyumbani.

    Hakutaka kumwambia mke wake, alijua jinsi mioyo ya wanawake ilivyokuwa dhaifu katika kutunza siri, hakutaka kuwa muwazi kwa jambo lolote lile na ndiyo maana aliamua kunyamaza kabisa. Polisi waliendelea kufuatilia kila kitu, hakutaka kuwaambia kitu chochote kile.

    Hofu yake ilikuwa ni kwa binti yake tu, alijua dhahiri kwamba mtu aliyemteka binti yake alikuwa akimfuatilia kwa kila hatua hivyo kama angethubutu kuwaambia polisi kwa kitu chochote kile basi angejua na hivyo kumuua kabisa.

    Hakutaka kuona hilo likitokea na ndiyo maana alikuwa tayari kwa jambo lolote lile. Siku hiyohiyo akachukua dawa iliyokuwa ikitumika kusimamisha mapigo ya moyo ya binadamu, alitakiwa kuitumia dawa hiyo kwa kwenda kuyasimamisha mapigo ya moyo ya Hernandez kama alivyoambiwa.

    Dawa hiyo iliitwa Phormephysoliyn ambayo haikuwa ikipatikana kwa urahisi, iliuzwa kwa madaktari wakubwa au wale ambao walisomea mambo ya kitabibu. Alipoichukua, siku iliyofuata akachukua vitu vyote na kuondoka zake kuelekea gerezani kuendelea na kazi yake.

    Mtu wa kwanza kabisa aliyetakiwa kumpata alikuwa ni kijana ambaye alikuwa na tamaa ya vitu vidogo, ambaye alikuwa radhi kufanya jambo lolote lile lakini pia awe mtu aliyekuwa na kiu ya kutaka kuondoka hapo gerezani.

    Hilo halikuwa tatizo, akamtafuta mwanaume aliyeitwa Cassian ambaye alifungwa maisha na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia kwamba alikuwa na baruti ambazo endapo angezilipua kwenye ukuta wa gereza basi ungeweza kuvunjika na yeye kutoroka zake.

    Cassian alivyoambiwa hivyo alishangaa, hakuamini kile alichoambiwa, ilikuwaje dakktari huyo amwambie maneno hayo? Alikuwa na mpango gani kwani hakikuwa kitu chepesi hata kidogo. Alipoonekana kusitasita, akamwambia amtafute mtu mwingine kwa kuwa yeye hakutaka.

    “Unasitasita sana. Ngoja nitafute mtu mwingine,” alisema mzee James.

    “Hapana! SI kwamba nakataa! Ni kwamba una uhakika?”

    “Asilimia mia moja. Umekwishawahi kusikia stori kuhusu The Joker?” aliuliza.

    “Yule jamaa aliyetoroka gerezani?”

    “Unahisi yule alitumia kitu gani?”

    “Mmh! Basi na mimi nataka!” alisema.

    “Ila kumbuka iwe siri.”

    “Sawa.”

    “NA hii inatakiwa kufanyika kesho majira ya saa sita kamili mchana. Chukua hii saa, saa sita kamili, lipua, muda huo askari wanakuwa bize sana na mambo yao!” alisema.

    “Sawa. Haina shida!”

    Alimwambia kwa maneno matamu mno na mwisho kabisa akampa pesa kwa kumwambia kwamba ni lazima atunze siri kwani endapo polisi wangegundua basi kungekuwa na tatizo kwake. Hilo likakubaliwa na hatimaye kijana huyo kuondoka huku akimtuma kwenda kumuita Hernandez kwa kuwa kulikuwa na dawa alitakiwa kumpa.

    Mpango ulionekana kwenda kama alivyotaka, alitulia ofisini kwake na baada ya dakika kadhaa Hernandez kufika mahali hapo. Alichoka, kwa kumwangalia tu ilitosha kuonekana mtu huyo hakutaka kuendelea kuishi gerezani, alimwangalia daktari, alimuita kwa lengo la kuzungumza naye, hakuwa anaumwa, hakuwa na dozi sasa mwanaume huyo alihitaji nini kutoka kwake?

    Alikaa na kuzungumza naye, alianzia mbali kabisa na baada ya maongezi ya dakika tatu nzima ndipo akamwambia kuhusu mpango wake wa kumtia gerezani na kumrudisha kwa kaka yake. Hernandez akashindwa kuvumilia, hapohapo akaanza kucheka kwani kile alichoambiwa kwake kilionekana kuwa kituko mno.

    “What did you say?” (umesemaje?) aliuliza Hernandez huku akionekana kuwa na tabasamu pana.

    “I want to take you out of here?” (nataka nikutoe hapa) alijibu mzee James.

    “Hahaha! How? I’ve spent almost five years, my brother tried, he failed, how can you take me out of this shit?” (Hahaha! Kivipi? Nimekaa karibu miaka mitano, ndugu yangu alijaribu, akashindwa, utaweza vipi kunitoa mahali hapa?) aliuliza Hernandez huku akiendelea kucheka.

    “I got company, a intelligence man I’ve never seen,” (nina mtu, mwenye akili sipata kuona) alimjibu.

    Hernandez bado aliendelea kushangaa, kwake haikuingia akilini kabisa, akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Kabla ya kukubali alitakiwa kufikiria sana kuhusu jambo hilo, hakutakiwa kukurupuka tu.

    Alijua dhahiri kwamba alikuwa na kesi kubwa mno, kitendo cha kukubali harakaharaka kilimaanisha angeyaweka maisha yake kwenye wakati mgumu. Kichwa chake kiliwafikiria CIA, aliamini maofisa hao wa kijasusi waliweka mpango mzito kuhakikisha anatolewa gerezani ili wamuue kwa urahisi.

    Alimwambia mzee James kwamba hakuwa tayari. Mzee huyo alishtuka, hakuamini kile alichoambiwa. Kitendo cha Hernandez kukataa kilimaanisha kwamba basi binti yake angeweza kuuawa kule aliposhikiliwa, alichokifanya ni kuanza kuomba.

    Alimuomba mno, Hernandez alishangaa, hakujua ni kwa sababu gani mwanaume huyo alimuomba kumtoa gerezani. Hilo likazidi kumpa hofu na kuwa na uhakika kwamba inawezekana kabisa kulikuwa na jambo kubwa la kumpoteza ambalo lilikuwa limepangwa kikamilifu. Mzee huyo alimuomba mpaka kuanza kulia.

    “I can’t do that shit,” (siwezi kufanya hivyo) alisema na kuinuka.

    “Please! They will kill my daughter, help me,” (tafadhali! Watamuua binti yangu, nisaidie) alisema mzee huyo huku akilia.

    “Who?” (akina nani?) aliuliza.

    Hernandez alikuwa ndani ya mpango huo hivyo ilikuwa ni lazima amwambie ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea. Hakutaka kumficha, alimwambia kuhusu kutekwa kwa binti yake na watu ambao alikuwa na uhakika walitumwa na ndugu yake kumtorosha hapo gerezani.

    Hernandez alimsikiliza kwa makini, kwa jinsi alivyokuwa akiongea mpaka kulia, aliamini kabisa kwamba kile alichokisema kilikuwa kweli kabisa. Akakubaliana naye na hivyo kuchomwa sindano ambayo ingeanza kufanya kazi baada ya saa nne, mapigo yake ya moyo yangesimama kwa saa sabini na mbili.

    Baada ya kumaliza kila kitu, akatoka na kuelekea katika chumba chake. Mzee huyo alibaki akiwa na mawazo tele, kile alichoambiwa afanye, alikifanya na kilichobaki kilikuwa ni umaliziaji wa kazi hiyo. Aliendelea na kazi yake na aliporudi nyumbani akapigiwa simu na Robinson na kumwambia kilichotokea.

    “Basi sawa! Sisi tutafika saa 05:50,” alisema Robinson.

    Kazi ya mwanaume huyo ilikuwa ni kuangalia namba za watu wa kuzika ambao walikuwa wakitumiwa na gereza hilo. Hakukuwa na kazi yoyote ile kuipata, kila kitu kiliwekwa kwenye mtandao hivyo kuichukua namba hiyo na kuahidi siku inayofuata ilikuwa ni lazima kuidukua.

    Hilo ndilo lililofanyika, siku iliyofuata, asubuhi na mapema tu akaidukua na kuanza kuisubiria simu kutoka katika gereza hilo. Wakati hayo yakiendelea, upande wa pili tayari mzee James alienda gerezani kuendelea na mambo yake, siku hiyo ndiyo ilikuwa ni ya kufanya kazi, ilikuwa ni lazima ifanyike kwa asilimia mia mia.

    Asubuhi hiyohiyo akapewa taarifa kwamba usiku uliopita, mfungwa mmoja, Hernandez alisemekana kufariki gerezani, kwanza akajifanya kushtuka kwa kutokuamini kile alichoambiwa. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kutaka kuuona mwili huo, aliambiwa usiku uliopita ulipelekwa humo, haukutakiwa kupelekwa mochwari mpaka pale ambapo vipimo vingefanyika kuthibitisha kama kweli alikufa.

    Akachukua vipimo vyake na kuanza kumpima mbele ya mkuu wa gereza, mapigo ya moyo hayakuwa yakifanya kazi, kila kitu katika mwili wake kilisimama, ili kumuhakikishia mkuu wa gereza, naye akampa kifaa cha kusikilizia mapigo ya moyo, haukuwa ukidunda, ulisimama kumaanisha kwamba tayari mwanaume huyo alifariki dunia.

    Gerezani hapo ilikuwa ni balaa, fujo za kila aina, watu walihisi kwamba mkuu wa gereza aliamua kumuua mwanaume huyo kwa kuwa aliamini siku yoyote ile kaka yake angeweza kumtoa gerezani. Waandishi wa habari wakapigiwa simu na kuambiwa kilichotokea, haraka sana wakafika hapo na kuchukua picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea na kutolewa kwani wakati mazishi yanafanyika, haikuwa ruhusa kubaki mahali hapo, hivyo wakaondoka.

    Upande mwingine, Kamacho aliiona taarifa ya kifo cha ndugu yake kwenye televisheni, kwanza hakuamini, alishangaa, alipanga na Richard kwamba atamtoa ndugu yake gerezani, sasa iweje siku mbili baadaye itoke taarifa kwamba ndugu yake huyo alifariki dunia? Hilo lilimchanganya, wakati akifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya, simu yake ikaanza kuita, haraka sana akaipokea.

    “Unaongea na Richard!”

    “Niambie! Kwa nini umemuua ndugu yangu?” aliuliza Kamacho huku akionekana kuwa na hasira tele.

    “Huo ndiyo mpango wenyewe.”

    “Mpango wa kumuua?”

    “Hapana! Hajafa.”

    “Ila taarifa zinasema amekufa, na daktari amethibitihsa!”

    “Sawa. Kubaliana na mimi. Cha msingi familia itoe tamko la kulitaka gereza limzike ndugu yako hukohuko!” alisema Richard.

    “Yaani sijaelewa.”

    “Kamacho! Ni kweli unamtaka ndugu yako au humtaki?” aliuliza Richard kwa sauti ya ukali kidogo.

    “Ninamtaka!”

    “Basi toa tamko hilo haraka sana! Ukitoa tamko, kesho tunakuletea ndugu yako,” alisema Richard na kukata simu.

    Kamacho alichanganyikiwa lakini hakuwa na jinsi, aliambiwa kitu cha kufanya, hakujua ni ujanja gani alitumia jamaa huyo lakini kwa sababu alitamani kumuona ndugu yake, hakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana naye.

    Haraka sana akawapigia simu ndugu zake na kuwaambia kuhusu kutoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari. Kwanza walishangaa, hawakuamini kile alichokisema Kamacho, ilikuwaje Hernandez azikwe huko gerezani na wakati alikuwa ndugu yao?

    Walibisha lakini kwa kuwa Kamacho ndiye alikuwa sauti ya mwisho, akawaambia na hivyo tamko kutolewa mbele ya waandishi wa habari na kutangazwa kwenye televisheni hivyo uongozi wa gereza hilo ukawapigia simu watu wa kuzika kwa lengo la kufika mahali hapo na kuuchukua mwili huo kuuzika kwenye makaburi ya gereza.

    Kwa kuwa Richard aliidukua simu hiyo, ilipopigwa, moja kwa moja ikaenda mpaka kwake na kuanza kuzungumza nao. Aliambiwa kwamba kulikuwa na maiti nyingine hivyo walitakiwa kwenda kuizika. Haraka sana akawaambia washikaji zake, wakachukua nguo ambao zilitengenezwa tayari na kuondoka mahali hapo kuelekea gerezani huko huku wakiwa na vifaa vyote vya kuchimba kaburi.

    Walipofika, wakaonyesha vitambulisho vyao na kuingia huko, kwanza wakaenda kusaini na kutoka kwenda kusubiri nje ya gereza huku kukiwa na askari kila kona wakiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani na hata nje ya gereza.

    Hapo, wakatoa jeneza, ndani hakukuwa na kitu, wakaliweka tayari kwa nje na hivyo kusubiri mwili wa Hernandez utolewe huku Robinson na wenzake wakianza kuchimba kaburi. Walifanya haraka haraka na ilipofika majira ya saa 05:50 walimaliza hivyo kusubiri mwili wa Hernandez.

    Ilipofika majira ya saa 05:58 mwili ukatolewa, haraka sana wakauchukua na kujifanya kuuandaa kuuweka kwenye jeneza. Saa ilipogonga 06:00, sauti kubwa kama ya mlipuko ikasikika gerezani. Kila askari aliyekuwa nje, juu ya ukuta akaanza kukimbilia ndani.

    Walikumbuka vilivyo kwamba hiyo ilikuwa ni njia mojawapo ya wafungwa kutoroka gerezani na ndiyo ambayo walikuwa wakiifanya kwenye kila gereza nchini Marekani. Hawakutaka kuona mfungwa yeyote akitoroka na ndiyo maana walikuwa radhi kufanya jambo lolote lile, waache kazi yoyote lakini si kuona mfungwa akitoroka gerezani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wa ukutani, waliondoka, wa hapo nje na sehemu nyingine wote waliingia ndani na kubaki Robinson na wenzake. Walichokifanya ni kumtoa Hernandez, wakamuingiza kwenye boneti la gari na kuliingiza jeneza lile kaburini na kulifukia harakahara na walipomaliza, wakaenda gerezani kuripoti kwa mkuu wa gereza.

    Walipoingia, macho yao yalikuwa kwa wafungwa waliotolewa na kuwekwa chini, askari walikuwa na bunduki, waliwaambia wasifanye kitu chochote kile cha hatari. Maaskari wengine walikuwa ndani ili kuona ni kitu gani kilikuwa kimetokea.

    Kwa jinsi hali ilivyokuwa humo, ilitisha, kila mtu aliogopa, mkuu wa gereza alikuwa akiweweseka, kitendo cha mfungwa yeyote yule kutoroka kwake ingekuwa skendo kubwa mno ambayo ingeharibu faili lake kwa maisha yake yote.

    Askari walikuwa wakihaha, hata wao akina Robinson walipotaka kuongea na mkuu wa gereza walishindwa kwa kuwa alichanganyikiwa na alitembea huku na kule kuhakikisha usalama unaendelea kuwepo.

    Akawaambia waende akaunti kuchukua malipo yao na kuondoka haraka sana mahali hapo kwani hali ilichafuka. Hawakutaka kuchelewa, wakaondoka mahali hapo na kuelekea akaunti ambapo huko wakapewa pesa yao na kuondoka huku Hernandez akiwa kwenye boneti la gari lao.

    “Hureeeeee......” alisema Robert kwa sauti huku akishusha pumzi ndefu.

    “Siamini kama tumefanikiwa. Kwenye kazi zote, hii ilikuwa ya hatari sanaaaa....” alisema Robinson huku akikenua, mikono yake ilikuwa kwenye usukani na alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kawaida tu, alipoishika barabara ya lami, akaongeza mwendo na kuondoka mahali hapo lengo likiwa ni kufika Texas ambapo huko wangempigia simu Kamacho na kumwambia aende kumchukua mtu wake, na upande wa pili walimtumia meseji mzee James na kumuelekeza mahali binti yake alipokuwa, amfuate na kumchukua.





    Kazi ilifanyika kikamilifu, Hernandez alichukuliwa na kutolewa gerezani, hakukuwa na mtu aliyejua lolote lile, wale askari wa gerezani waliendelea kuwazuia wafungwa pasipo kugundua kulikuwa na mtu muhimu sana alichukuliwa kutoka hapo gerezani.

    Kila mmoja alijua kwamba hernandez alikufa na kuzikwa katika makaburi yaliyokuwa ndani ya eneo la gereza hilo, hakukuwa na yeyote aliyejua kama mwanaume huyo alichukuliwa na vijana wale watatu ambao walijifanya kutoka katika kampuni iliyokuwa ikihusika na uzikaji wa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini Marekani.

    Safari ilikuwa ikiendelea, walipofika jijini Texas wakawasiliana na Kamacho na kumwambia kuhusu kile kilichotokea, walikuwa na ndugu yake mikononi mwao, walihitaji awamalizie kiasi kilichobaki ili waweze kumruhusu kumchukua mtu huyo.

    Kamacho hakutaka kukubaliana nao, kwake, hilo lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo, kwa gereza kama lile alilofungwa ndugu yake, kwa jinsi lilivyokuwa na ulinzi mkubwa, jinsi alivyopambana kumtoa gerezani na kushindwa, kwake ilikuwa ni vigumu kukubaliana nao kwamba walifanikiwa kumtoa mtu huyo humo.

    Hawakutaka kupoteza muda kuongea naye sana, walichokifanya ni kumpiga picha na kumtumia. Kamacho alipoziona picha hizo, hakuamini, alitamani kushangilia lakini hakutaka kufanya hivyo mpaka pale ambapo angekuwa na uhakika kwamba kweli mtu yule aliyekuwa akimuona alikuwa hernandez.

    Aliwaambia kwamba alitaka kumuona ndugu yake huyo, lilikuwa jambo gumu kumruhusu mpak pale ambapo angewatumia kiasi hicho cha pesa kwani kwenye mambo makubwa na ya kibiashara kama hayo, hawakutakiwa kumuamini mtu yeyote yule.

    Kwa Kamacho, japokuwa alikuwa mtu katili, lakini kwa jinsi watu wale aliozungumza nao walionekana kujiamini na bila kuwa na hofu yoyote ile, akawaambia ni lazima waondoke na kwenda Mexico, wakutane huko na kuzungumza vizuri huku wakiwa na huyo Hernandez.

    Ugumu ulikuwa ni mpakani El Paso. Hawakujua kama wangevuka salama lakini kwa sababu walizungumza naye na kuwaambia kwamba kusingekuwa na tatizo, wakakubali na kuanza kuondoka kuelekea huko.

    Walipofika njiani, yaani sehemu ambayo ilikuwa na janga kubwa, wakakutana na gari moja la kifahari, Audi nyeusi ambapo wakasimamishwa, wanaume wawili wakateremka huku wakiwa na bastola, kwa kuwaangalia isingekuwa tatizo kugundua kama walikuwa Wamexico, waliwasimamisha kwa kuwa walitumwa na Kamacho kuhusu mtu waliyekuwa wamembeba.

    “Hatuwezi kuwaruhusu muondoke naye bila sisi,” alisema Robinson huku akiwaangalia.

    “Kwa nini?”

    “Kwa sababu tunahitaji kuonana naye, lakini bado hajatumalizia pesa yetu,” alijibu Robinson.

    Japokuwa kwa kila mtu waliyekuwa wakimfuata na kugundua kama walitumwa na Kamacho alionekana kuogopa lakini kwa watu hao hali ilikuwa ni tofauti kabisa, hakukuwa na yeyote aliyekuwa na hofu, walijiamini kana kwamba nao walikuwa wakimiliki watu waliokuwa na bunduki na mabomu.

    Hapohapo simu ikapigwa mpaka kwa Kamacho, wakazungumza naye na kumpa Robinso kuongea naye. Yeye alimwambia kwamba walifurahi kufanya naye kazi na ndiyo maana waliifanya kazi hiyo hata kabla ya kupewa pesa zote kama malipo, hivyo hakutakiwa kuwa na hofu nao hata kidogo.

    “Sawa. Hao watawalete huku. Msijali kuhusu mpakani, kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Kamacho.

    Kama alivyowaambia ndivyo ilivyotokea, hapo mpakani, El Paso hakukuwa na tatizo lolote lile, walivuka na kuingia nchini Mexico.

    Gari liliendelea kwenda mpaka katikati ya Jiji la New Mexico ambapo hapo likaingia ndani ya jumba moja kubwa na la kifahari ambapo huko wakakutana na Kamacho aliyewapokea huku akionekana kuwa na furaha tele.

    Kitu cha kwanza kabisa alihitaji kumuona kaka yake, hilo halikuwa tatizo, mlango ukafunguliwa na Hernandez kutolewa.

    Alipomuona, akamsogelea, hakuwa ameamka, bado alilala kutokana na dawa ile kuendelea kuwepo mwilini mwake. Akaagiza achukuliwe na kupelekwa ndani ambapo huko akalazwa kwenye kitanda na kurudi sebuleni kuongea na vijana hao.

    “Mliweza vipi kumtoa gerezani?” lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa Kamacho, hakuwa akiamini kile kilichotokea, kama vijana wake walifanya kila liwezekanalo, alitumia pesa lakini bado akashindwa, alijiuliza mno kuhusu vijana hao, walitumia njia gani mpaka kumuondoa Herandez kule gerezani?

    Hawakuwa radhi kumwambia, walichokijibu ni kwamba kulikuwa na mipango ambayo waliifanya na mwisho wa siku kufanikiwa. Kwa jinsi walivyoongea, kwao, kwa kile walichokifanya kilionekana kuwa kitu cha kawaida mno ambacho wangekifanya kwa mtu yeyote yule.

    Kamacho alichanganyikiwa, akagundua kwamba watu hao walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kitu chochote kile, hivyo kama lingekuwa jambo zuri basi awape kazi nyingine ya kufanya ambayo ingekuwa na malipo makubwa zaidi.

    “Kazi gani?” aliuliza Robinson.

    “Ni ya hatari sana, ila ina malipo makubwa,” alisema Kamacho huku akiwaangalia wote.

    “Itatuingizia kiasi gani cha pesa?”

    “Dola milioni hamsini kila mmoja,” alijibu huku akiwaangalia.

    Robinson, Robert na Richard wakaangaliana, kwao lilionekana kuwa jambo la ajabu sana kwa mtu kama huyo kuwapa kiasi kikubwa kama hicho. Kwa maana hiyo, kwa kazi hiyo ambayo hawakuijua ingekuwa ni ipi wangelipwa sawa na kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mia moja kwa kila mmoja kwa pesa za Kitanzania.

    Zilikuwa pesa nyingi sana ambazo hawakuzitarajia lakini pia hazikuwa pesa ambazo walitaka kuingiza, walichokiitaji kilikuwa ni dola bilioni nne ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni nane za Kitanzania ili kila mmoja achukue shilingi trilioni moja.

    “Kazi gani?” aliuliza Robinson ambaye alikuwa muongeaji mzuri.

    “Kuna watu watatu ninawahitaji mikononi mwangu,” alisema huku akiwaangalia.

    “Watu gani?”

    “Ni mabilionea wakubwa sana. Ni kwamba tulikuwa tukifanya biashara kwa kushirikiana kwa kipindi kirefu sana lakini baada ya kuona ninatafutwa na Marekani, wakaamua kunizika na kuchukua kiasi changu cha pesa, dola bilioni tano, wakanidhulumu, waliona kabisa siwezi kuwapata kwa kuwa siwezi kutoka ndani ya Mexico, nilikasirika sana, ninachohitaji ni kuwaona watu hao mbele yangu, niwaue kwa mkono wangu,” alisema Kamacho huku akiwaangalia vijana hao ambao muda wote vichwa vyao vilifikiria pesa tu.

    “Sawa. Ila ulitapeliwa kiasi cha dola bilioni tano, si ndiyo?” aliuliza Robert.

    “Ndiyo!”

    “Kwa maana hiyo baada ya kuwapata, bila shaka utawaambia wakurudishie kiasi hicho cha pesa, si ndiyo?” aliuliza Robert.

    “Ndiyo!”

    “Sasa kama wakikurudishia dola bilioni tano, utatupa dola milioni mia moja na hamsini, yaani sisi tukuingizie dola bilioni tano halafu wewe utuingizie dola milioni mia moja na hamsini, huu ni utani Kamacho,” alisema Robert.

    “Naomba mnisaidie!”

    “Hilo si tatizo. Hiyo ni kazi ngumu sana, hatuwezi kukuingizia kiasi hicho na sisi kutulipa kiasi kidogo cha pesa,” alisema Robert.

    Alichokisema kilikuwa kweli kabisa, kazi ambayo walitakiwa kuianza ilikuwa kubwa mno, ni ya hatari ambayo ingeweza hata kuwafanya kukamatwa, hivyo kama ilikuwa ni ya hatari sana ilikuwa ni lazima walipwe pesa nyingi pia.

    Mzee Kamacho aliwabembeleza na mwisho wa siku wakakubaliana naye kufanya kazi hiyo kwa kuingiza kiasi cha dola bilioni moja kwenye akaunti yao ambacho kilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni mbili.

    Hilo likawafurahisha, wakainuka na kumpa mkono wa pongezi Kamacho na kumwambia kwamba kazi ile ingefanywa katika utaalamu mkubwa, walitoka barani Afrika na kwenda Marekani mpaka hapo Mexico kwa kuwa walikua na uhitaji wa kutafuta pesa, na kama hizo zilikuwa mbele yao basi waliona ni jambo jema kama wangeziingiza kwenye akaunti zao haraka sana.

    Kilichofanyika, zile pesa ambazo walikuwa wakimdai, akawaingizia kwenye akaunti yao na hivyo kuanza kazi ya kuwaambia ni kitu gani kilitakiwa kufanya.

    Kulikuwa na mabilionea watatu, mmoja aliitwa Ryan Godlove, huyu alikuwa akiishi nchini Australia. Alikuwa na hoteli nyingi na za kifahari, alikuwa na hisa kubwa katika Shirika la Ndege la Orange Airline lakini pia alikuwa akimiliki ardhi ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa.

    Utajiri wake ulikuwa mkubwa, alikuwa ni mwanaume mwenye pesa ambaye kwenye akaunti yake alikuwa na utajiri wa dola bilioni kumi na sita, alikuwa bilionea namba moja nchini Australia.

    Ukiachana na huyo kulikuwa na mwingine aliyeitwa Scott Anderson, huyu alikuwa bilionea mkubwa nchini Ukraine. Alikuwa akimiliki hoteli nyingi, majengo makubwa na alikuwa na hisa nyingi katika makampuni mengi nchini humo.

    Pamoja na kuwa na utajiri huo lakini alishirikiana na Kamacho katika biashara haramu na hakukuwa na yeyote ambaye alilifahamu hilo na utajiri wake kwenye akaunti yake ilikuwa ni dola bilioni kumi na tatu.

    Ukiachana na huyo, wa mwisho alikuwa Hussein Abdoulaziz. Huyu alikuwa Mwarabu aliyekuwa akiishi Dubai. Alikuwa mmoja wa watu wenye pesa ndefu ambao walikuwa msaada mkubwa kwa nchi hiyo. Alipenda kula bata, alikuwa amewekeza katika biashara nyingi na kwenye akaunti yake alikuwa na kiasi cha dola bilioni ishirini na mbili, alikuwa ni tajiri namba sita hapo Dubai, na pesa yake ilikuwa ikiingia kupitia biashara ya mafuta aliyokuwa akiyachukua kutoka hapo Dubai na huko Kuwait.

    Hao ndiyo watu ambao Kamacho alitaka kuwaona mbele ya macho yake. Hakujua alikuwa na ulinzi kiasi gani, alichokuwa akihitaji ni kuona watu hao wakiwa mbele yao. Alikuwa na hamu nao kwa sababu waliuumiza moyo wake na aliamini kabisa kwamba watu hao walikuwa na uwezo mkubwa wa kumfanya kupata alichokuwa akikitaka.

    “Sawa. Dili la dola bilioni moja lipo sawa?” aliuliza Robinson.

    “Hakuna tatizo! Ila nitawapata?”

    “Hilo ondoa shaka. Tutaifanya kazi hiyo kama CIA. Tutafanikiwa ila utatakiwa kutupa dola milioni tano kama pesa ya kutumia katika mishemishe zetu!” alisema Robert.

    “Na hizo zitakuwa ndani ya hiyo dola bilioni moja?”

    “Hapana! Hiyo ni nje kabisa. Hatuna pesa kabisa, kwa hiyo tupe hiyo tuanze nayo!” aliingilia Richard.

    “Basi sawa. Nitawapa pesa hiyo. Naomba sana kazi ifanyike!”

    “Hakuna tatizo!”

    Baada ya kukubaliana hawakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana wakaondoka kuelekea hotelini na siku mbili mbele ambapo Hernandez alirudiwa na fahamu, wakaondoka kurudi Marekani huku wakimwambia Kamacho kwamba ile kazi ambayo aliitaka ifanyike, ingefanyika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutaka kufuatilia kuhusu hao matajiri, walikuwa wakiishi maisha gani? Biashara zipi walikuwa nazo na ni kwa namna gani wangeweza kuwapata? Hiyo yote ilikuwa ni ya kufuatilia.

    ***

    Robinson, Richard na Robert walikutana ndani ya chumba cha hoteli na kuanza kuzungumza kile kilichokuwa kikiendelea. Kulikuwa na pesa nyingi zilizokuwa mbele yao ambapo walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanazipata.

    Kiasi cha dola bilioni moja ambazo kilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa pesa za Kitanzania kilikuwa kiasi kikubwa kupita maelezo, kama wangefanikiwa kupata kiasi hicho ha pesa kilimaanisha kwamba wasingekuwa na shida yoyote ile maisha yao yote na hata kama wangetumia kwa fujo bado pesa hizo zingekuwa nyingi sana mpaka kuzimaliza.

    Katika kikao chao hicho wakaanza kukumbushana kuhusu maisha yao ya nyuma, jinsi walivyokuwa wamepigika lakini ghafla tu wakaanza kufanikiwa kwa kufanya mambo ya kijanja na hatimaye kuwa matajiri wakubwa wanaochipukia. Kwao ilikuwa kama ndoto, kila kitu kilichokuwa kimetokea nchini Tanzania, Kenya na mpaka hapo Marekani bado walihisi kama walikuwa wakipita katika maisha fulani hivi ya maigizo na baadaye kuambiwa picha limeishia hapo.

    Pesa waliyotangaziwa na Kamacho ilikuwa nyingi sana, pesa hiyo ingetoka yote baada ya kukamilisha kazi hiyo, ilikuwa ni lazima waifanye hata kama ilikuwa ngumu kiasi gani. Walijipanga, ilikuwa ni lazima kupambana kwa asilimia mia moja na kufanikisha suala hilo zima.

    Kabla ya kufanya kitu chochote kile ilikuwa ni lazima kuangalia mafaili ya watu hao, wajue walikuwa wakiishi maisha gani huko, familia zao na mambo mengine. Mtu wa kwanza kabisa ambaye walihitaji kumfanyia kazi alikuwa bilionea Ryan Godlove.

    Wakaanza kumwangalia mwanaume huyo. Walisoma sifa zake nyingi lakini lililowatisha ni kuwa mwanaume huyo alisomea masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard hapohapo Marekani kabla ya kuamua kuondoka kurudi nyumbani kwao huko Australia.

    Alikulia maisha ya kitajiri, mwanzo walifikiri kwamba alikuwa na akili sana mpaka kusoma katika chuo hicho kumbe haikuwa hivyo, ni kwa sababu baba yake alikuwa na pesa hivyo aliamua kumsomesha katika chuo hicho.

    Kipindi hicho alikuwa na miaka arobaini na moja, alikuwa akiishi na familia yake jijini Melbourne hapohapo Australia huku akiendelea kufanya biashara zake kama kawaida. Kila mtu nchini humo alikuwa akimuheshimu, alimsikiliza na alikuwa huru kufanya kitu chochote kile kwa ajili ya watu wengine.

    Hakuwa mtu wa starehe, alikuwa mtu wa kushinda nyumbani kwake na ofisini tu, alipenda kufanya kazi kuliko kitu chochote kile katika maisha yake. Kwa jinsi walivyosoma faili lake waligundua ilikuwa ni vigumu sana kumpata mwanaume huyo kwa sababu hakuwa mtu wa klabu au sehemu nyingine yoyote ile, kazi yake kubwa ilikuwa ni kukaa nyumbani na familia yake huku muda mwingine ofisini kwake.

    “Hii kazi naiona kama ngumu hivi,” alisema Richard huku akiwaangalia wenzake.

    “Na ndiyo maana ina pesa nyingi sana. Lakini wakati mwingine hatutakiwi kuiona kazi ngumu mpaka tuondoke na kwenda sehemu ya tukio. Hebu tuondokeni kwanza, tukifika huko ndiyo tutajua kama kazi ni ngumu ama si ngumu,” alisema Robinson.

    Hilo ndilo walilotakiwa kulifanya, hakukuwa na sababu ya kupoteza muda nchini Marekani, haraka sana wakaomba viza katika ubalozi wa Australia na walipopata tu wakaondoka nchini humo kuelekea huko.

    Ndani ya Ndege ya Shirika la Alliance Airlines kila mmoja alikuwa na mawazo yake, hakukuwa na mtu aliyeuona urahisi wa kazi hiyo, kila mmoja aliona kabisa mbele yao kulikuwa na ugumu mno hivyo walitakiwa kupambana mpaka kuhakikisha wanampata mwanaume huyo na wenzake na kuchukua pesa walizokuwa wameahidiwa.

    Ndege ilichukua saa kumi na mbili ikaanza kutua katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Melbourne ambapo wakateremka na kwenda nje ambapo wakaingia ndani ya gari la wateja waliokuwa wakifikia katika Hoteli ya nyota tano ya Bayview Eden iliyokuwa pembeni kidogo mwa jiji hilo.

    Walipofika, wakachukua vyumba vitatu ambavyo waliweka oda na kabla ya kulala ilikuwa ni lazima kukutana na kuzungumza kile kilichokuwa kikiendelea. Mipango ilitakiwa kusukwa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufahamu mahali mzee huyo alipokuwa akiishi, baada ya kujua huko ndipo wangeanza kufikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapo, wakajifanya kama wageni waliofika kwa lengo la utalii, siku iliyofuatwa wakaanza kutembezwa sehemu mbalimbali huku wakijifanya kupiga picha kila kitu kilichoonekana kuwa kigeni. Walizungumza na watu wengi, waliwaambia kwamba wao walikuwa Wamarekani ambao walifika hapo kwa lengo la kuitazama Australia kwani hawakuwahi kufika.

    Kuamini kama hawakuwa Wamarekani weusi ilikuwa vigumu mno kwani kwa jinsi walivyokuwa wakiongea kwa slang, ilikuwa ni lazima kuamini kila kitu walichokuwa wakikizungumza.

    Kutokana na ucheshi wao mkubwa wakapata marafiki wengi ambao waliwatembeza sehemu mbalimbali lakini lengo lao kubwa lilikuwa ni kutaka kujua mahali alipokuwa akiishi Godlove.

    Siku hiyo hawakutaka kuwa na presha yoyote ile, ilikuwa ni lazima kujifanya wageni wakubwa na siku zinazofuata ndiyo ambazo wangetumia kuuliza mambo mengi kuhusu mwanaume huyo.

    Hapo Melbourne mtu ambaye walimpata kwa ajili ya kuwatembea huku na kule alikuwa kijana mdogo wa makamo yao aliyeitwa Pegg Ball. Kijana huyo ndiye alichukua jukumu la kuzunguka naye huku wakimwambia kwamba wangemlipa kiasi cha dola elfu mbili kila siku huku kula na vitu vingine vikiwa ni juu yao.

    Ilikuwa pesa nyingi kwake ambayo ingemfanya kuwafanyia kitu chochote kile ambacho watu hao wangekihitaji. Walihitaji kumzoea kwa siku kadhaa, kama mbili hivi ndipo wakaanza kumuuliza kuhusu bilionea Godlove.

    “Ryan Godlove! Kuna watu wana pesa bwana!” alisema Ball huku akiwaangalia.

    “Huwa anaishi wapi?”

    “Mh! Anaishi wapi?”

    “Seacombe Grove upo katika mji mdogo wa Brighton,” alijibu Ball.

    “Mtaa huo upo vipi?”

    “Ni wa kitajiri sana! Sisi walalahoi huwa haturuhusiwi kufika huko,” alijibu.

    “Kwa nini?”

    “Utaanzaje kufika huko? Umesahau kitu gani? Kuna ulinzi wa kila aina! Mnamuulizia sana, kuna lolote mnahitaji?” aliuliza Ball huku akiwaangalia.

    “Yeah! Tunahitaji kufungua kampuni ya utalii! Sasa tunahitaji kukutana naye,” alijibu Richard.

    “Sasa si muwasiliane naye?”

    “Sasa tutawasiliana naye vipi?”

    “Kwani hamna namba yake?”

    “Hatuna. Wewe unayo?”

    “Hapana!”

    “Hata sehemu ambayo tunaweza kuipata?”

    “Hapana! Sijui sehemu yoyote ile,” alijibu Ball kikawaida pasipo kugundua watu hao walikuwa na mpango gani kwa huyo bilionea.

    Ball hakuonekana kuwa na msaada wowote ule zaidi ya kuwatisha kwamba mtaa aliokuwa akiishi Godlove haukuwa ukiingilika na watu wengine kwa sababu kulikuwa na ulinzi mkubwa mno.

    Hawakutaka kukata tamaa, walifika nchini Australia kwa ajili ya mwanaume huyo na ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha wanampata na kuondoka naye kwenda kumficha sehemu fulani.

    Waliendelea kukaa nchini humo kwa siku kadhaa huku kila siku wakawa wanaonana na kuzungumza kama namna mojawapo ya kuona kama kulikuwa na njia nyingine ambayo waliipata kuitumia kumuingiza mwanaume huyo katika mikono yake.

    Baada ya kukaa kwa wiki moja huku Kamacho akiwapigia simu na kuwauliza walipofikia ndipo wakapata wazo la kwenda ofisini kwake. Hawakupajua lakini waliamini kama wangemuuliza Ball angewaambia mahali alipokuwa akifanyia kazi.

    Haraka sana wakamuuliza, alichowajibu ni kuwa hakufahamu ofisi yake ilipokuwa ila angeweza kuuliza na kuwaambia, hivyo walitakiwa kusubiri kwa siku moja mpaka atakapokutana na marafiki zake.

    “Hivi nyie huyu Ball mnamuonaje? Mimi naona kama anatuzingua. Manake kila kitu hafahamu, sasa wa kazi gani?” aliuliza Robert huku akionekana kuwa na hasira.

    “Kama vipi tumteme!”

    “Hapana! Tumeanza naye mbali, amesema kwamba atawauliza marafiki zake, tumpeni muda, tutajua tu,” alisema Robinson.

    Hilo ndilo walilolifanya, kwa sababu kijana huyo alihitaji muda, akapewa na siku iliyofuata akawapa majibu kwamba mwanaume huyo alikuwa akifanya kazi katika jengo kubwa la Richmond lililokuwa na ghorofa ishirini na nne na ofisi yake ilikuwa ni kuanzia ghorofa ya kumi na nane kwenda juu.

    Kulikuwa na wafanyakazi wengi humo na kampuni hiyo ilikuwa ikijihusisha na mambo ya majengo. Wakapanga na hivyo kumtuma Richard kuelekea huko. Alitakiwa kujua kila kitu kilichokuwa kikiendelea, ofisi ilikuwaje na kulikuwa na ulinzi gani mpaka kumuona bosi huyo, yaani kwa kifupi alitakiwa kujua kila kitu.

    Siku iliyofuata asubuhi na mapema Richard akaondoka kuelekea huko. Hakuchukua muda mrefu akafika na kuhitaji kuonana na meneja wa ofisi hiyo ambapo akasaini na kupewa kitambulisho maalumu na kuanza kupandisha juu kwa kutumia lifti.

    Kwa jinsi alivyovaa, alipendeza, alivalia na miwani iliyomfanya kupendeza kupita kawaida na kwa jinsi alivyokuwa na sura nzuri, kila msichana aliyekuwa akimuona, alichanganyikiwa, alipendeza na wengi walitaka japo kuisikia sauti yake.

    Hakuzungumza na mtu yeyote mpaka alipofika katika ghorofa husika, akateremka na kwenda sehemu ambapo akapewa kitambulisho kingine na kuruhusiwa kuingia ndani. Kila alipopita, kulikuwa na kamera, alikuwa makini, aliziangalia huku akiwaza ni kwa namna gani wangefanikiwa kuingia humo na kuondoka na mtu huyo.

    “Ninahitaji kuonana na meneja wa ofisi hii,” alisema Richard sehemu ya mapokezi.

    “Una miadi naye?”

    “Hapana!”

    “Huwezi kuonana naye!”

    “Kabisa?”

    “Kabisa!”

    “Hata mkurugenzi?” aliuliza.

    Wasichana waliokuwa hapo mapokezi waliangaliana, wakaanza kutoa tabasamu. Hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angefika mahali hapo na kumuulizia mkurugenzi. Kumuona Godlove lilikuwa jambo gumu sana, si kwa watu wengine, hata kwao pia, kama wafanyakazi hawakuwa na uwezo wa kuusogelea mlango wa ofisi yake na kuzungumza naye.

    Godlove alikuwa mtu wa kazi nyingi, hakuwa na muda wa kuzungumza na watu humo, alipenda kukaa peke yake akifanya mambo yake kivyakevyake na taarifa zote kuhusu ofisi alikuwa akipelekewa na meneja wake, ilikuwaje Richard afike mahali hapo na kutaka kuonana na mkurugenzi wao.

    “Mbona mnanicheka?” aliuliza Richard huku akitabasamu.

    “Hatukucheki! Bali tumeshangaa!”

    “Mmeshangaa nini?”

    “Kumuulizia mkurugenzi. Hivi unamjua Godlove kweli?” aliuliza msichana mmoja.

    “Na ndiyo maana nilihitaji kuzungumza naye.”

    “Samahani! Huwezi kumuona.”

    “Hata nyumbani kwake?”

    “Yaani huko ndiyo kabisaaaa.”

    “Kwa hiyo huwa haonekani?”

    “Inawezekana!” alijibu msichana mmoja.

    ***

    Richard hakuzungumza kitu, alibaki akiwaangalia wasichana wale, walimjibu kwa nyodo kiasi kwamba mpaka akasikia hasira moyoni mwake. Hakutaka kuona akiendelea kudharauliwa vile, alichowaambia ni kwamba alihitaji kuondoka na angerudi siku nyingine.

    Wakati akiondoka, wasichana wale walibaki wakimwangalia. Walishangaa, mtu ambaye alisimama mbele yao sekunde chache zilizopita alikuwa mzuri wa sura na waliamua kumzingua makusudi ili waweze kupata kile walichokuwa wakikihitaji.

    Haraka sana msichana mmoja akasimama na kumuagiza mlinzi aliyekuwa humo amsimamishe na kumwambia arudi. Mlinzi huyo alifanya kama alivyoambiwa, huku akiendelea kuwa humo ofisini, akasimamishwa na kuambiwa kwamba alikuwa akihitajika, hivyo akarudi.

    Kwa muonekano ambao walionekana wasichana hao kipindi hicho hakuwa na maswali mengi kwamba ni kitu gani walikuwa wakihitaji, macho yao yalionyesha kila kitu, akatoa tabasamu kidogo kitu kilichowachanganya wasichana hao.

    “Umekasirika?” aliuliza msichana mmoja, swali la kipumbavu kabisa kwa Richard, akakosa jibu, akabaki akiwaangalia kwa zamu tu.

    “Tulikuwa tunataka kuuona msimamo wako. Naitwa Rose,” alisema msichana mmoja huku akimpa mkono.

    Richard akashusha pumzi ndefu, hakuamini alichokuwa akikiona mahali hapo, wasichana haohao walimjibu kidharau huku wakimwambia lingekuwa jambo gumu kuonana na Godlove lakini mwisho wa siku akashangaa kuona akiitwa na kuulizwa swali hilo.

    “Jamani naomba tusamehe. Mimi naitwa Gwen,” alisema msichana mwingine, naye akampa mkono.

    Kwa kuwa lengo lake halikuwa limefanikiwa ndani ya ofisi hiyo, Richard akatoa tabasamu pana na kuanza kuzungumza naye. Kitu walichokihitaji ni kwamba walitaka kula naye chakula cha mchana katika mgahawa wa ofisi hiyo na huko wangeongea mengi kuhusu Godlove lakini pia wangemsaidia kuonana naye.

    “Ila mliniambia kwamba haiwezekani!” alisema Richard.

    “Tulisema, ila nahisi inaweza kuwezekana,” alisema Rose.

    Yeye ndiye alikuwa na shida ya kuonana na Godlove hivyo hakuwa na jinsi, alihitaji kuwasikiliza wasichana hao kujua ni kitu gani walikuwa wakihitaji. Alibaki humo huku akizungumza nao mambo mengi, walifahamiana kwa mengi lakini kwenye yote ambayo aliyazungumza, hakutaka kuwaambia ukweli alikuwa nani hasa na alitoka wapi.

    Ilipofika majira ya saa sita mchana, wakatoka na kwenda mgahawani. Kila mtu alikuwa akimwangalia Richard, alikuwa mwanaume mzuri, mpole ambaye hata kutembea kwake ilikuwa ni rahisi kugundua kama alikuwa mtu aliyejiheshimu.

    Wakaelekea mpaka kwenye mgahawa huo na kuanza kula chakula. Muda wote Richard alionekana kuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria huyo Godlove, japokuwa kimwili alikuwa mahali hapo lakini mawazo yake yalikuwa sehemu nyingine kabisa.

    Walizungumza mambo mengi, wasichana wale walijisikia raha kuzungumza naye. Uzuri wake wa sura uliwafanya mpaka wengine kuja pale na kuwasalimia, walichokihitaji ni kumsikia Richard akiongea, sauti yake ilifananaje? Alikuwaje kwa karibu?

    “Unamfahamu Godlove?” aliuliza Gwen.

    “Kwa kumuona kwenye picha, ila si uso kwa uso,” alijibu Richard.

    “Kwa hiyo ulikuwa unakuja kumuona mtu ambaye hukuwahi kumuona ana kwa ana?”

    “Ndiyo! Kuna biashara ningependa kufanya naye, hivyo nilihitaji ushauri wake kidogo!”

    “Biasharara gani?”

    “Kuchuna watu ngozi!” alijibu Richard huku akitabasamu, tabasamu lililowafanya wasichana wote hao kuanza kucheka kwani walijua alidanganya na hakutaka kuwaambia ukweli.

    Hawakujua jinsi ya kumsaidia, na hawakuwa na uwezo huo ila ilikuwa ni lazima waonyeshe kwamba wangemsaidia ili wamtie katika mikono yao. Walichomwambia ni kuwaachia namba ya simu, wao wangezungumza na Godlove na kupanga siku ya kuonana kwani walimwaminisha kwamba kwao asingeweza kupindua hata kidogo.

    Richard hakuwa na jinsi, akafanya hivyo, akawapa namba yake na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulikuwa na uhakika kama angefanikiwa na hata alipofika kwa wenzake aliwaambia kazi ilikamilika na ni kitu kidogo tu ndicho kilikuwa kimebaki.

    “Kwa hiyo wamesema watakupigia simu?” aliuliza Robinson.

    “Ndiyo! Watanipigia!”

    “Una uhakika?”

    “Kabisa! Hawawezi kunidanganya. Hivi unaweza kweli kumdanganya handsome kama mimi?” aliuliza Richard huku akiwaangalia wenzake.

    Hawakumjibu swali lake, walibaki wakiangaliana tu na kuendelea na mambo yao. Wakati hayo yote yakitokea huku akiendelea kusubiri simu kutoka kwa Rose na Gwen ndipo akaanza kuyafikiria maisha yake.

    Suala la Upendo lilimuumiza kichwa chake, bado alimfikiria msichana huyo mno, alimwambia kwamba alikuwa na mimba yake, alichokikumbuka ni kwamba siku zote amekuwa mtu wa kutumia kinga na hakukumbuka kama kuna siku aliwahi kufanya bila kinga.

    Aliambiwa kwamba siku ile ambayo mpia ulipasuka ndipo mimba hiyo ilipoingia, hakukubaliana na hilo kwa sababu siku hiyo aliikumbuka vilivyo. Alihisi kabisa kulikuwa na jambo nyuma ya pazia, moyo wake ulimwambia asubiri mpaka pale ambapo mtoto angezaliwa ili aone kama kweli alikuwa wake ama la.

    “Nitapima DNA,” alisema Richard.

    Hilo ndilo lilimjia kichwani mwake lakini bado alikuwa na mambo mengine mengi ambayo yalimsumbua. Hofu aliyokuwanayo kuhusu ujauzito huo ilikuwa kubwa kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe akabaki akishangaa.

    Alichokifanya ni kuwashirikisha wenzake, ilikuwa ni lazima wajue kile kilichokuwa kichwani mwake, aombe msaada ili kujua ni kitu gani wangemshauri katika suala hilo.

    “Hofu yako nini?” aliuliza Robert.

    “Hiyo mimba jinsi ilivyoingia!”

    “Sasa wewe unaogopa nini?”

    “Yaani nina hofu kubwa sana. Mimi sijawahi ndani, sasa hiyo mimba imeingiaje mazee?’ aliuliza Richard.

    Marafiki zake hao wakaangaliana na kuanza kucheka. Walijua ni kwa jinsi gani aliumia, waliujua ukweli kwamba Richard hakumpenda Upendo hata kidogo, alifanya mambo yote yale kwa sababu tu kulikuwa na sababu ya hayo yote.

    Richard alikuwa siriazi kuwaambia wenzake kuhusu mambo yake yaliyokuwa yakimsumbua lakini wenzake ndiyo kwanza walikuwa wakicheka na kumwambia kwamba mimba ni yake na alitakiwa kumlea mtoto, asikimbie majukumu hata kidogo.

    “Mtoto wako huyo, litakuwa bonge la handsome?”

    “Naomba tusikilizane! Tuacheni utani, naomba mnisaidie, tufanye nini katika hili!” alisema Richard huku akionekana kukasirika.

    “Hakuna cha kushauriana. Tusubiri mtoto azaliwe kwanza!”

    “Nyie hamuoni kama nitakuwa nimeuziwa mbuzi kwenye gunia?”

    “Kwamba ulipiga lakini mtoto siyo wako au kuna jamaa mwingine alimfuata Upendo na kupiga kisha akapata mimba? Richard! Come down. Hivi kuna jamaa gani hapa anaweza kutembea na Upendo zaidi yako?” aliuliza Robert huku akimwangalia Richard ambaye alionekana kuwa na hasira zaidi.

    Richard hakuzungumza kitu, akaachana na suala hilo akaendelea na mambo yake kama kawaida. Siku iliyofuata akapokea simu kutoka kwa namba ngeni, alipoichukua na kuipokea, akagundua kwamba ilitoka kwa Rose hivyo akaanza kuzungumza naye.

    Msichana huyo alimwambia kuhusu kuonana naye, alikuwa na mengi ya kumwambia hivyo ilikuwa ni lazima kukaa sehemu na kuzungumza naye kwa kirefu kuhusu huyo Godlove aliyekuwa akihitaji kuonana naye.

    Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akawaambia wenzake kwamba mambo yalitiki na hivyo alitakiwa kuondoka kwenda kuonana na msichana huyo mahali na kuzungumza kile alichokuwa akihitaji.

    Akaondoka na kwenda kwenye mgawa wa Marrybrown uliokuwa hapohapo Melbourne. Waliponana, wakatafuta kiti na kutulia, wakaanza kuzungumza, kitu alichotaka Rose kumwambia Richard ni kuhusu moyo wake, jinsi alivyompenda mwanaume huyo lakini kichwa cha Richard muda huo kilikuwa kikifikiria kuhusu Godlove, mwanaume ambaye aliamini kwamba kama angebahatika kuonana naye, basi kila kitu kingekwenda kama kilivyotakiwa.

    ***

    Upendo alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Richard, hakujua ni kitu gani ambacho kingetokea kama siku moja mwanaume huyo angekuja kugundua kile kilichotokea.

    Hakutaka kuona hilo likitokea, alichokifanya kilikuwa siri kubwa na ndiyo maana hata wahusika ambao alishirikiana nao walikuwa ni Wazungu, watu waliosafiri kutoka mbali kabisa na kwenda kuifanya kazi hiyo.

    Hakuwa na amani, moyo wake ulikuwa na mawazo tele, alichokifanya alijua kabisa hakikuwa sawa lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kitokee kile kilichotokea kwa sababu tu mwanaume huyo hakuwahi kukubali kufanya naye mapenzi bila kutumia kinga.

    Aliendelea kwenda hospitalini, alihitaji kujua kuhusu afya yake, aliwasiliana na baba yake na kumwambia ukweli kuhusu mimba hiyo, mzee wake alifurahi sana, aliwapigia simu marafiki zake na kuwaambia kwamba hatimaye binti yake alipata mimba.

    Mzee mwenyewe alijua jinsi binti yake alivyokuwa mbaya, hakuwahi kuhisi kama kungetokea mwanaume yeyote ambaye angemfuata na kumwambia nakupenda, hivyo hakuwa na uhakika kama kuna siku Upendo angekuja kufanya mapenzi na mwanaume, mtu huyo ambaye angejitolea kufanya naye basi alikuwa na moyo wa kishujaa sana.

    Alimuuliza mara mbili mbili kama kile alichokizungumza kilikuwa kweli ama la, alimhakikishia kwamba ni kweli alikuwa mjauzito, akaona hiyo haitoshi, akamuonyeshea mpaka vipimo alivyokwenda kupima hospitalini, aone jinsi majibu yalivyokuwa.

    Mzee Massawe alichanganyikiwa mno kiasi cha kuanza kulengwa na machozi machoni mwake. Hakutegemea kupata majibu hayo kwamba binti yake alipata mimba, hakutaka kujua ni mwanaume gani alimpa hiyo mimba, yeye alichokifurahia ni kile kilichokuwa tumboni mwa Upendo tu.

    Hakutaka kuwasiliana tena na Richard, alijua kabisa mwanaume huyo hakuwa akimpenda, alifahamu kabisa kama alikuwa na ugumu wa kuikubali mimba hiyo, alimwaha aendelee na maisha yake lakini alichokuwa akikiangalia ni kwa jinsi gani mtoto wake huyo angeishi baada ya kuzaliwa.

    Wiki ya pili baada ya Richard kuondoka na wenzake kuelekea nchini Marekani ndipo akapokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakumfahamu. Simu ile ilitoka kwa namba ambayo ilipigwa kutoka nchini Tanzania na mtu aliyekuwa akisikika alikuwa ni mwanamke ambaye alikuwa na kitu cha kumwambia.

    “Kitu gani?” aliuliza Upendo huku akionekana kuwa na wasiwasi kwani kwa jinsi alivyokuwa akiongea, ilionyesha kulikuwa na jambo kubwa mno lililokuwa likiendelea.

    “Nasikia una mimba ya Richard!” alisema msichana huyo. Alishtuka, suala la yeye kuwa na mimba alilifanya siri, hakutaka mtu mwingine yeyote afahamu zaidi yake na Richard tu, akahisi kwamba mwanaume huyo ndiye aliyekuwa amemwambia mtu aliyekuwa akiongea naye.

    “Haikuhusu dada!” alisema.

    “Najua! Ila ni afadhali hata ungeipata kwa kupitia ile kitu, yaani yenyewe. Kumbe mimba yenyewe ni ya kutengeneza! Yaani mwanamke mtu mzima unafanya Surrogation. Na Richard hajui, ila ni lazima nitamwambia,” alisikika mwanamke huyo kutoka kwenye simu.

    Moyo wa Upendo ukapiga paaa! Hakuamini alichokuwa amekisikia kutoka kwa msichana huyo. Hakuwa na la kusema, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kile alichokisikia kilikuwa kama ndoto.

    “Unasemaje?” aliuliza kwa hofu lakini hapohapo simu ikakatwa.

    Akasimama pale kwenye kitanda na kuanza kuzunguka huku akiita lakini hakukuwa na majibu yoyote yale kwenye simu. Hilo lilimchanganya mno, kile alichokifanya kilikuwa ni siri kubwa, ni yeye na Manka tu ndiyo waliokuwa wakijua kuhusu mimba ile.

    Mwili wake ulikuwa ukitetemeka mno, alitamani kumfahamu mtu huyo, ampe pesa ili asiweze kutoa siri hiyo. Alijua kungekuwa na tatizo kubwa endapo angethubutu kuufumbua mdomo wake na kumwambia Richard kwamba ile mimba aliyokuwanayo ilikuwa ni ya kutengeneza, aliiona kabisa aibu kubwa ikija mbele yake.

    “Haiwezekani!” alijisema Upendo, hakutulia hapo chumbani, alikuwa akihangaika, na kilichomchanganya zaidi ni kwamba kila alijaribu kumpigia simu mwanamke huyo, hakupatikana.

    Upendo alizidi kuchanganyikiwa, siri ambayo aliamini ingedumu milele katika maisha yake kumbe upande wa pili kulikuwa na mtu ambaye alifahamu kila kitu, hiyo ilimuuma sana na muda mwingine alihisi kabisa kungetokea tatizo fulani kama tu asingemnyamazisha mtu huyo kuufumba mdomo wake.

    Hakuwa na raha tena, muda wote alikuwa na mawazo tele, alihitaji mimba ya Richard, aliipata lakini hakuwa na amani hata kidogo. Moyo wake ulimuuma, alitamani kuonana na mwanamke huyo na kumuomba sana, asimwambie Richard kwani endapo angejifanya mjanja basi kusingekuwa na siri tena.

    Alichokipanga ni kumtafuta mtu huyo, ilikuwa ni lazima afanye hivyo kwani hakutaka kuona akipata aibu kubwa. Alikuwa na pesa, aliamini katika jambo lolote lile, kama angetumia pesa basi lisingekuwa tatizo lolote lile, kusingekuwa na kitu chochote ambacho kingeharibika.

    Alikuwa na mawazo, hakumwambia mtu yeyote yule, aliendelea kuwa hivyohivyo na hata wazazi wake walipomuuliza juu ya kile kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kuwaambia lolote lile zaidi ya kujifanya hakukuwa na kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea.

    Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, ya pili ikaingia, siku ya tatu akapigiwa simu na namba ileile na kuanza kuzungumza naye. Kitu cha kwanza, Upendo akaanza kumuomba sana asimwambie Richard kwani alijua endapo angefanya hivyo mwanaume huyo angeweza kumfunga.

    “Hakuna shida. Utatakiwa kuulipia mdomo wangu usitoe siri,” alisema mwanamke huyo kwenye simu.

    “Niambie kiasi chochote kile,” alisema Upendo.

    “Ninahitaji bilioni moja kuunyamazisha mdomo wangu,” alisema msichana huyo.

    Upendo akashtuka, hakuamini kama mtu huyo angehitaji kiasi kikubwa cha pesa namna hiyo, alichohisi ni kwamba angehitaji milioni kumi ama ishirini.

    Alibaki akitetemeka, akaishiwa pozi la kuongea, simu ilikuwa sikioni mwake lakini alikuwa kimya kabisa.

    “Kwa heri,” alisema mwanamke huyo baada ya kuona ukimya umekuwa mkubwa.

    “No! Naomba usikate simu!” alisema Upendo.

    “Sasa mbona huongei?”

    “Umeniambia kiasi kikubwa sana. Bilioni moja?”

    “Kwa hiyo hiyo unaiona nyingi sana? Hivi hujui kesi ikifika mahakamani Richard anaweza kuhitaji kiasi gani? Hujui waandishi wa habari wakiiandika habari yako utapata aibu kiasi gani? Jamii itakuonaje? Upendo! Baba yako ana pesa sana, fanya unitumie hiyo pesa, vinginevyo, nitamwambia Richard akirudi kutoka alipokwenda,” alisema mwanamke huyo.

    “Naomba unisaidie mwanamke mwenzako!”

    “Niambie kitu kimoja! Utatoa pesa hiyo au hautotoa?” aliuliza msichana aliyesikika kwenye simu, alionekana kuchoshwa na vilio vya Upendo, alihitaji kusikia jibu moja tu.

    “Naomba unionee huruma!”

    “Hilo si jibu ninalolitaka. Niambie! Utatoa au hutotoa?” aliuliza tena.

    Upendo hakujua ni kwa namna gani angelijibu swali hilo, jibu lake lilikuwa jepesi mno, yaani ni ‘ndiyo’ au ‘hapana’ lakini hakuwa radhi kutoa jibu lolote lile.

    Aliendelea kuomba sana lakini mwanamke huyo hakumuelewa hata kidogo. Alisisitiza kwamba ni lazima amwambie Richard kilichofanyika kama tu hakutaka kutoa kiasi cha pesa alichokuwa amekitaka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Upendo akafikiria biashara zake, akamfikiria baba yake na mwisho wa siku akamwambia mwanamke huyo kwamba alikuwa tayari kutoa kiasi hicho cha pesa, ila alihitaji kupewa mwezi mmoja mpaka kukamilisha mpango huo.

    “Sawa. Haina shida. Leo ni tarehe kumi, inamaana mpaka tarehe kumi ijayo nataka pesa iwekwe kwenye akaunti hii, 01J2030341600,” alisema mwanamke huyo.

    “Sawa.”

    Simu ikakatwa.



    MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog